Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Silafu Jumbe Maufi (4 total)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI kuhusu swali langu, nina swali la nyongeza.
Pamoja na jitihada na changamoto walizonazo na kuhakikisha kwamba masomo haya yanapatikana katika maeneo yetu ya Rukwa na hasa katika Mikoa yetu ya pembezoni. Kwa kuwa tumechelewa kupata elimu hii na speed ambayo wanakwenda nayo naona kana kwamba haitaweza kuleta mafanikio mazuri kwa mikoa yetu ya pembezoni. Swali langu dogo napenda kuuliza kwa niaba ya Mkoa wa Rukwa, ni lini sasa Wilaya ya Nkasi na Wilaya ya Kalambo masomo hayo yatafikishwa kwani Makao Makuu ya Wilaya hizi umeme umekwishafika?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukiri kwamba suala la kompyuta sasa hivi na elimu ya TEHAMA ni jambo la msingi sana kama tunataka twende katika maendeleo ya kasi. Tumejielekeza sasa hivi, kama jibu langu la msingi lilivyosema kwamba, tutatumia kila liwezekanalo kuhakikisha tunawezesha vijana katika shule hizi kupata elimu hii ya kompyuta.
Suala la Nkasi na Kalambo ni kweli, katika maeneo mbalimbali ambayo tunataka tuyape nguvu hasa ukiangalia mkoa huu una changamoto kubwa sana, jambo hili hata Mheshimiwa Keissy na Mbunge wa Viti Maalum huwa eanalizungumzia sana, siyo hilo tu na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nieleze wazi katika michakato ambayo tutaifanya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sababu Mkoa wa Rukwa ni Mkoa wenye changamoto kubwa sana, tunaita mikoa ya pembeni, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo katika program zetu Wilaya hizi tuwape kipaumbele, kwa sababu maeneo mengine ya mijini kama vile Dar es Salaam, Arusha na Mikoa mingine ni rahisi zaidi vijana ku-access mambo ya kompyuta kuliko mikoa ya pembezoni. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa na hasa katika Wilaya ya Nkasi na Wilaya ya Kalambo.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya kitaalam ambayo kwa namna moja au nyingine akina mama zangu wa Mkoa wa Rukwa na hususan wa Bonde la Tanganyika, bado hawajatendewa haki. Tunasema ya kwamba tunazuia magonjwa na vifo vya wamama na watoto, katika maeneo haya hatutakuwa tumezuia vifo vya akina mama na watoto, bali tutaendeleza vifo hivyo.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Waziri anahusika vilevile na suala zima la mawasiliano, afahamu ya kwamba kata ya Kara haina mawasiliano ya barabara na wala haina mawasiliano ya simu. Huu utaalam wa TARURA watakuwa wamewapa umuhimu upi wa kuweza kuyafanyia kazi katika hizi barabara zetu za Ziwa Tanganyika na vilevile zinazoelekea kwenye barabaa za Ziwa Rukwa ziko katika hali hiyo hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kupata majibu yaliyokuwa sahihi hasa kuhusu akina mama zangu wa Bonde la Tanganyika na Bonde la Rukwa, wanasaidiwa vipi juu ya hizi barabara na hao ndugu wa TARURA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi kwa namna anavyoshirikiana na Wabunge wenzake katika kufuatilia masuala mbalimbali ya maendeleo ya watu wa Mkoa wa Rukwa na vilevile Mkoa wa Katavi. Sina uhakika kwa nini wanashirikiana wakati ni watu wa mikoa miwili tofauti, lakini nadhani ni kwa sababu maeneo yao yanafanana. Mara nyingi barabara anazoziongelea nyingine zinaunganisha mikoa yote hii miwili, kwa mfano, barabara zinazoenda kwenye Ziwa Rukwa zinapita katika mikoa hii yote miwili.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie, kama ambavyo tumeweka katika bajeti, barabara hizo tutazishughulikia kwa kadiri bajeti ilivyopangwa. Kwa mfano, barabara inayounganisha mikoa hiyo miwili, lakini vilevile na Mkoa wa Songwe anafahamu kwamba tumeanza kujenga daraja linalounganisha mikoa hiyo na tukishamaliza kujenga daraja, tutaanza sasa kuiangalia barabara yenyewe.
Mheshimiwa Spika, kubwa nimhakikishie kwamba Serikali inafahamu sana na wala haina nia hiyo anayoiongelea. Barabara hizo zitashughulikiwa na TARURA kwa kiwango na kwa kasi ile ile ambavyo angetegemea kwa kuzipandisha hadhi. Kwa sababu TARURA na TANROADS kwa sasa wana hadhi sawa na uwezo sawa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata kwenye upande wa rasilimali fedha nako huko tunakuangalia, ili kuhakikisha taasisi hizo mbili zinatekeleza ahadi zetu na ahadi za viongozi katika maeneo hayo ambayo yameulizwa kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru hayo majibu niliyopewa na Mheshimiwa Waziri, lakini niliuliza swali kwamba kufufuliwa Kambi ya JKT, sikuuliza swali la kwamba mabadiliko ya matumizi ya Kambi ya JKT, la hasha. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa tunajua wazi kwamba kujiunga kwa vijana wetu kwenye JKT ndiko ambako kuna chachu ya kuwawezesha wao kujiunga na Polisi, kujiunga na JWTZ na kadhalika. Sasa je, ni sababu zipi zilizopelekea kutoka JKT na kuwa Kikosi cha Jeshi na kusababisha Mkoa wetu wa Rukwa kukosa Kambi ya Jeshi?
Swali la pili, je, vijana wetu ambao wanauhitaji wa kujiunga na JKT wa Mkoa wa Rukwa kutokana na wingi wao wa kila mwaka kuongezeka ndani ya jamii, je, hawa vijana watanufaika vipi na vikosi hivyo ambavyo vimebadilishwa makambi yao kuwa ni vikosi vya Jeshi au watajengewa Kambi ya Jeshi upande gani? Naomba uniambie katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge kwa kuguswa kwake na vijana hasa hasa wa Mkoa wa Rukwa na hoja yake ya kutaka vijana wapate fursa hiyo, lakini nimhakikishie tu ninapojibu maswali yake yote mawili kwa pamoja ni kwamba Kambi la Jeshi kubwa hasa linaloangaliwa ni suala la kibajeti.
Natambua katika nchi nzima vijana wengi hata maeneo ambako kuna Kambi wengi sana wanajitokeza kuomba nafasi hizo, unaweza ukakuta Wilaya ambako wamejitokeza vijana kama 500, idadi inayotakiwa kupatikana labda ni 50 mpaka 60 kwa maana hiyo sisi kama Serikali tunapokea tu hoja ya Mbunge na uhitaji mkubwa huo wa kuona vijana wanataka kujitolea kwenda kujenga Taifa ili tuliangalie kwenye upande wa bajeti kwasababu kwenye upande wa makambi hilo ni jambo rahisi tu ambalo wanaweza wakakaa tu katika Kambi yoyote ile na mafunzo haya yakaendelea kama ambavyo inafanyika katika mikoa mingine.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu suala hili, bahati nzuri mwenyewe anayezungumza ni ametoka Mkoa wa Rukwa, kwa hiyo, barabara hii anaifahamu vilivyo. Akina mama wengi na watoto wanapata shida kwenye barabara hii wanapokuja kupata huduma ya afya Namanyere.
Napenda kuiuliza Serikali, je, ina mpango gani kwa hivi sasa kwa sababu tupo katika kipindi cha bajeti kuweza kutenga fedha za kutosha kuikamilisha hii barabara badala ya kuendelea kutengeneza maeneo korofi kila mwaka hadi mwaka na kuonekana kana kwamba ni mradi wa Serikali? (Makofi)
Swali la pili, ninapenda kuiomba Serikali ijaribu kuona hizi barabara zetu za Bonde la Lake Tanganyika na Bonde la Lake Rukwa, barabara hizi ni tata, zinahitaji matengenezo yaliyokamili kama vile Kitonga na inavyoelekea kutumika katika kipindi chote cha mwaka mzima.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba barabara hii ina changamoto kubwa maana kuna maeneo ambayo kuna milima mikubwa sana na azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wa Ninde wanapata barabara inayoweza kupitika kwa vipindi vyote.
Mheshimiwa Spika, kabla ya hapo ilikuwa hakuna barabara kabisa na ndiyo maana Serikali kwa kulitambua hilo ikaanza kutenga kiasi cha shilingi milioni 350 na maeneo yaliyokuwa korofi zaidi ilikuwa ni maeneo ya madaraja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ilimradi madaraja yameshajengwa ambayo ndiyo yalikuwa ni changamoto kubwa sana, nia na azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yaliyobaki yataweza kutengenezwa kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
Katika swali lake la pili, ameongelea Ukanda wa Ziwa Rukwa. Sifa ya Ukanda wa Ziwa Rukwa na hii barabara aliyoitaja ya kwenda Ninde hazina tofauti sana na Mbunge, Mheshimiwa Malocha amekuwa akiipigia kelele sana na kwa mara ya kwanza Serikali imesikia kilio chake na barabara hii inaweza kuimarishwa ili iweze kupitika katika kipindi chote.