Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sophia Mattayo Simba (4 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu ili na mimi niweze kutoa yangu machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na utukufu kwa kuniwezesha kuwa mmoja wenu katika Bunge hili. Aidha, nawapongeza Wabunge wenzangu ambao wamefanikiwa kuingia katika Bunge hili. Nakupongeza wewe kwa nafasi hiyo, nampongeza pia Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wenzio, nawatakia kila la kheri katika kazi hiyo na najua mnaimudu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi sikupata nafasi ya kuzungumza wakati wa kuzungumzia hotuba ya Mheshimiwa Rais, naomba kidogo nichukue nafasi hii na mimi kumpongeza Mheshimwia Rais, kwanza kwa ushindi mnono alioupata lakini pia kwa hotuba nzuri sana aliyoitoa ambayo imegusa nyoyo zetu sisi na wananchi karibu wote. Kwa kweli Mheshimiwa Rais ameonyesha uwezo mkubwa na ameonyesha ukweli wake. Kwenye kampeni alikuwa akisema nipeni nifanye kazi, msema kweli mpenzi wa Mungu na kweli tunamuona anatenda yale ambayo alisema angefanya. (Makofi)
Mheshimwia Mwenyekiti, kabla sijaingia kwenye Mpango, napenda nimfahamishe kijana wangu ambaye alizungumza hapo awali, nadhani ni Mbunge wa Liwale, ni kijana madogo kwa hiyo anahitaji kusaidiwa. Amenigusa alivyoanza kuzungumzia Mtwara Corridor, misamiati, kaulimbiu zinazotolewa, Mheshimiwa Rais Mkapa amekuja na Mtwara Corridor ipo wapi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekuja na maisha bora yapo wapi. Mheshimiwa Mbunge pengine kwa ajili ya umri wako, leo unaizungumzia Mtwara Corridor! Sasa hivi wenyewe wa Mtwara wanasema Mtwara kuchele. (Makofi)
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mtwara Corridor isingewezekana bila ya kuwa na miundombinu na moja ni barabara. Wakati Mheshimiwa Mkapa akizungumzia Mtwara Corridor hata barabara ilikuwa hakuna, daraja lile la Mkapa lilikuwa halipo na limepewa jina sahihi kabisa, limejengwa katika ku-facilitate Mtwara Corridor. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa ukienda Mtwara siku nyingine unaweza ukalala mwezi mzima daraja la Mkapa hujafika kule. Leo Mheshimiwa Mbunge najua kwa umri wako pengine wakati ule hujawahi hata kusafiri, lakini mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kazi nzuri imefanywa na Mtwara Corridor, ule mradi wote wa gesi umeanzia huko kwa Mkapa. Maendeleo ni mchakato, maendeleo hayaji siku moja. Mchakato ule ndiyo sasa unaonekana kule Mtwara, viwanda vinajengwa na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, inauma sana ukimsikia mtu anasema maisha bora kwa Mtanzania ilikuwa inapitapita tu, kweli tulikuwa hivi, hata Bunge halikuwa kubwa kama hili. Sekondari za Kata mara hii mmezisahau, vituo vya afya, zahanati kila kona, nchi hii imefunguliwa kwa kuwa na mtandao wa barabara, kama siyo maisha bora kwa kila mwananchi ni nini hiyo? Isitoshe angalieni UDOM hiyo ni kazi ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wake university ngapi zimeongezeka hapa nchini? Ndiko tunakoenda kuchukua maisha bora kwa kila Mtanzania ndugu zangu. Pamoja na simu zilizokuwa mifukoni kwa kila mwananchi yale yote ni matokeo mazuri ya maisha bora kwa kila Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye vipaumbele. Kwanza nampongeza sana Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri aliyoifanya na wameweka vipaumbele vizuri. Nataka nimkumbushe kwamba Mheshimiwa Rais alipokuwa akisoma hotuba yake alisema tutakamilisha miradi ya mwanzo na kuanzisha mipya. Hivyo basi, ni bora tukakumbuka miradi mikubwa ambayo ilikuwepo kabla ya Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni suala zito sana duniani, huko tunakokwenda ukiangalia mabadiliko ya tabianchi, wataalam wanasema vita ya tatu itatokea kutokana na kugombea maji.
Kwa hiyo, miradi mikubwa ya maji ambayo napenda kuikumbusha, napenda wakumbuke kwamba zaidi ya miaka kumi iliyopita kuna mradi mkubwa wa maji wa Kipera, tuliambiwa kule Kibada kuna bahari ya maji kule chini, mradi ule upo wapi? Tunakazania Mradi wa Mto Ruvu lakini kuna bwawa la Kidunda silioni! Bwawa la Kidunda ni lazima lijengwe, vinginevyo tunaachia maji yanaenda baharini, bahari haina shida ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mikubwa ya Ziwa Viktoria kupeleka maji Lamadi, Magu na Tabora. Hebu tuhakikishe miradi hii ya maji na mengine inakamilika. Maji ni suala linalomhusu mwanamke na watoto, mwanamke anaamka asubuhi sana kutafuta maji, watoto wengine hawaendi shule ili waende kutafuta maji. Kwa hiyo, sisi wanawake linatugusa sana suala hili la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni la elimu. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuja na utaratibu wa elimu bure. Ndugu zangu kama nilivyosema maendeleo ni mchakato, elimu bure tulianza kwanza kujenga shule nyingi sasa wengi wataweza kusoma kwa elimu bure. Tatizo langu tunahitaji kuwa na elimu bora (quality education). Hiyo quality education isianzie sekondari tunahitaji elimu ya awali iweze kujenga msingi bora kwa watoto waweze kujiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi ilivyo sasa hivi mtu anamaliza university hajiamini, lakini ameanza toka kule kwenye msingi kujifunza kwa uoga. Kwa hiyo, naomba sana kwenye elimu tuwasaidie walimu kwa kuwaendeleza zaidi, tupate walimu bora ili watoto waweze kupata elimu bora zaidi na hasa elimu ya awali. Mimi naamini sana akitoka na elimu nzuri kwenye elimu ya awali hawatapata tabu huko watakapokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mchana huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kuwa mmojawapo wa kuchangia bajeti hii ya mwanzo kabisa, bajeti ambayo inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 mpaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyofanya kazi nzuri katika kutekeleza hii Ilani, lakini katika kutekeleza yale aliyosema mabadiliko ya kweli. Ni kweli, Mheshimiwa Rais tunaona katika bajeti hii ni vipi mabadiliko ya kweli yanaweza yakapatikana. Hongera sana Mheshimiwa wetu, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uendelee kuwa na nguvu ya kutusimamia na hivyo kuleta maisha bora kwa Watanzania wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nachukua nafasi hii pia, kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri waliyoifanya. Pia nakupongeza wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa jinsi unavyoendesha Bunge lako kwa busara, kwa umakini na kwa jinsi unavyohakikisha unaleta nidhamu ndani ya Bunge hili, ukitumia weledi wako mkubwa wa kutafsiri Kanuni za Bunge tulizojiwekea wenyewe. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla bajeti ni nzuri, lakini inahitaji sana Watanzania tubadilike, tunahitaji discipline ya hali ya juu katika ukusanyaji na katika utumiaji wa fedha hizo. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge, tupo pamoja na Rais wetu, tunakubalina naye kwamba tutabana matumizi kama tulivyoanza na pia tutahakikisha huko Majimboni kwetu kila mtu anafanya kazi. Kabla sijaendelea naomba niunge mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwapongeze sana Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa kazi nzuri waliyofanya. Nawapongeza sana wadau wangu akinamama nadhani wanne au watano, wamefanya kazi kwa umahiri mkubwa sana. Pia nawapongeza na akinababa ambao walikuwanao, lakini walionesha umahiri wao kwa vile wamesheheni weledi katika taaluma zao na wanazielewa vizuri, kwa hiyo, nawapongeza sana. Kwangu mimi nikiwa Mwenyekiti wao, I am proud of them, wamefanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kazi hiyo, moja ambalo limenifanya niwapongeze ni pale walipogundua lile tatizo kubwa ambalo wameliona na wamepeleka mapendekezo, ingawa sijui kama yamechukuliwa katika ukurasa wa 11. Moja ya pendekezo lao ni lile walilosema, ziongezwe shilingi bilioni 30 kwenye bajeti ili kumaliza zile Zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo zahanati ambazo wananchi wamejitolea kujenga. Nilipokuwa nikitembea mikoani wakati wa kampeni kilio kikubwa walichonacho akinamama, walikuwa wanasema, unaona boma lile, ndiyo Zahanati yetu, haijakwisha. Hivyo basi, kama hatukuwasaidia hawa katika hizi zahanati, kwanza tunawavunja moyo wa kujitolea, lakini kubwa zaidi akinamama wanaendelea kufa kutokana na kukosa huduma za afya. Baya zaidi, vipo pia Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa vizuri, lakini havina vyumba vya upasuaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbona saa inaenda upesi! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini fedha hizi zingesaidia sana katika kutengeneza hizo theater ili tupunguze vifo vya akinamama. Pia, waliozungumzia kuongeza tozo ile ya senti 50 kuwa sh. 100/= kwa ajili ya Mfuko wa Maji. Nawaunga mkono mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wenyewe siyo rafiki, lakini napenda niwapongeze sana kwa jinsi walivyotenga pesa ya kutosha kwenye miradi ya maji. Nashukuru sana kama pia wangetenga pesa ya kutosha kwenye miradi ya mazingira. Kazi yote tunayoifanya kwenye maji haitakuwa na maana kama mazingira yetu yanaendelea kama yalivyo. Tunahitaji kuwe na Mfuko wa Mazingira uweze kupanda miti mingi sana. Kwa hiyo, hilo naomba liishie hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia Mheshimiwa Waziri afafanue, kuna uwoga ndani ya jamii kuhusu huu ushuru wa simu pamoja na benki; hizi ada. Wananchi na sisi wenyewe tuna wasiwasi; mzigo usije ukarudi kwa wananchi. Hali siyo nzuri. Wananchi hawana hali nzuri ya kifedha, pesa imepotea; sasa tusiwaongezee tena matatizo katika masuala ya simu. Hata mkisema watakaolipa ni wale wenye Makampuni ya Simu, lakini mwisho wa siku hawa ni wafanyabiashara, watatafuta ujanja zitarudi kwetu tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu shilingi milioni 50. Mimi na wenzangu ambao wako humu tulikuwemo katika kutengeneza ile Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Nataka nitanabahishe, tuelewe. Tuliposema vijiji 50 tulikuwa na maana ya Vijiji, Mitaa na Shehia. Kwa hiyo, kwa sababu kila mtu anazungumzia vijiji, wale kule mitaani wanaweza kudhania hawamo. Wamo! Hata hivyo, nawapongeza sana kwa utaratibu mliouchukua wa kufanya kwanza pilot project ya mikoa 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi shilingi milioni 50 tulisema zitakuwa revolving fund katika kile kijiji, hazitoki. Kwa hiyo, leo wanapata hawa, kesho wale, ni za kijiji, hazi-revolve kutoka nje. Kwa hiyo, hilo likumbukwe, nia yetu ilikuwa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gratuity kwa Waheshimiwa Wabunge kutozwa kodi siyo sahihi. Zile sababu zilizosababisha kusamehewa, bado zipo mpaka leo. Warudi kwenye makabrasha yao wasome, zile sababu zimekwisha? Ahsante.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Naanza kabisa kwa kumpongeza Mwanasheria Mkuu pamoja na Wizara ambazo zimehusika kutengeneza marekebisho mengi ya sheria. Nakiri kwamba marekebisho ya safari hii yaliyokuja mengi ni mazuri na yanaenda kurahisisha kazi hasa ile ya usajili wa Makandarasi na nyinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kushukuru sana Serikali kwa kuleta sheria na kuweka adhabu ya ukeketaji. Siku zote ukeketaji ilikuwa kesi zake zikienda Mahakamani inachukuliwa kuwa amemjeruhi, basi, lakini sasa imepata kifungu chake na adhabu yake. Tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo limenifurahisha sana ni kuongeza kiwango katika usimamizi wa mirathi, kwamba Mahakama zetu za Wilaya ziweze kushughulikia hizi kesi ambazo zamani ilikuwa ni shilingi milioni 10 na sasa shilingi milioni 100. Nashukuru, kwani akina mama wengi walikuwa wakisumbuliwa kwa kusubiri kesi ziende kwenye Mahakama za juu zaidi. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama, kwanza napenda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba, mtoto ni yule aliye chini ya miaka 18, ndiyo Sheria ambayo tumeitunga mwaka 2009 tukasema yeyote aliye chini ya miaka hiyo 18 ni mtoto. Napongeza sana Wizara ya Elimu kwa kuliona hili la watoto kupata mimba. Nadhani litaenda kufanya kazi nzuri na kwamba ni kweli adhabu watakayopewa inaweza ikasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatoa adhabu kwa wale ambao watawapa mimba watoto wa shule wa sekondari na msingi; mbona tunawasahau wale watoto ambao hawakupata nafasi ya kwenda sekondari? Hawakupata nafasi ya kwenda shule? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imekuja na utaratibu wa shule bure, lakini tulipo hapa sasa kuna wengi ambao hawakupata fursa hiyo. Shule bure inaanza mwaka huu, lakini huko nyuma tunao wengi sana ambao hiyo fursa hawakuipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana sana na Kamati, kwanza naipongeze sana Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na naungana nao sana, kwani wamezungumzia kuhusu hili; vipi wale watoto wengine? Tusiwe na double standards! Hawa ni watoto! Mtoto hata kama hayuko shule bado huyu ni mtoto. Kwa hiyo, naomba sana kwa sasa nadhani yaweza isiwezekane, lakini tulifikirie. Nchi yetu imesaini mikataba mbalimbali ya Kimataifa na ndiyo iliyotusababisha mpaka tukatunga Sheria ya Mtoto na tukasema, aliye chini ya miaka 18 ni mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, niulize, kwa nini mtu atake kumuoa mtoto? Kwa wale akinababa; nimesikia maneno hapa! Kuna mwingi anakwambia, huyu mtoto amefika miaka 14 ameshabalehe, hana la kufanya nyumbani, nimfanyeje? Ni mwanao, mtunze mpaka afike miaka 18. Ubaya uko wapi? Si mtoto wako! Umemtunza miaka 14, bado miaka minne afike 18 ndiyo umuoe! Kwa hiyo, hizo excuse za watoto wadogo kuolewa siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, adhabu. Huko nyuma kidogo kama mwaka 2007 na 2008 tuliweka adhabu, tukaomba na utafiti ukafanywa kuhusu huyo aliyepewa mimba kwamba naye inakuwaje? Kwa nini asirudi shule kama wazazi wake wanakubali kulea mtoto? Naomba Wizara ya Elimu ilitizame hilo. Kuna wengine pale wangeweza kuwa Maprofesa kabisa, lakini wamekatishwa masomo! Tuwape hiyo opportunity waweze kuendelea na masomo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina lingine ambalo linanitia wasiwasi. Ni vyema kutoa adhabu kali, lakini huko nyuma tumetoa adhabu kali, matokeo yake watu wamekuwa wakificha ushahidi. Kwenye Sheria ya SOSPA, Makosa ya Kujamiiana, kesi nyingi zinakosa ushahidi. Mtu anaona afadhali akahonge shilingi milioni 10 ili yule mtuhumiwa asiende akafungwa kifungo cha maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa tunamfunga huyu aliyempa mimba miaka 30, mimi nasema afungwe, lakini wasiwasi wangu ile miaka 30 huyu mtoto atalelewa na nani akishazaliwa? Tunam-deny huyu mtoto hata kupata mapenzi ya baba. Kwa hiyo, afungwe pengine miaka mitano akitoka mtoto ana miaka mitano anaendelea kumlea. Tunamfunga huyu miaka 30, akitoka mtoto ana ndevu wala hamjui yule baba. Huyu mama tumempa mzigo wa kulea huyu mtoto kwa miaka yote 30! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili nalo tulifikirie, tunapoweka adhabu kali. Na mkumbuke adhabu kali hii tuliyoiweka kwenye makosa ya kujamiiana, makosa hayo yameendelea kuzidi! Tunachotakiwa ni sisi jamii kubadilisha mitazamo yetu. Elimu zaidi, lakini tunaweza tukawajaza watu huko, tukawa na watoto ambao hawana baba wanatembea barabarani. Kwa hiyo, yule ambaye amempa mimba, nashauri sana tupunguze apate miaka mitano na faini ili mtoto yule aweze kulelewa badala ya kumwacha alelewe na mama na anakosa mapenzi ya baba yake. Ikumbukwe hata kama amepewa mimba tu, yule mtoto bado atamtafuta baba yake siku moja, hata miaka 30, lakini yule baba hajamlea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa ule Muswada mwingine ambao sikuupata na ninampongeza kwa kuleta Mahakama ya Mafisadi. Aliisema kwa sauti kubwa na leo tunaipitisha kwa nguvu zetu zote. Nampa hongera sana. Pia nampa hongera Waziri wetu wa Sheria, Mwalimu wangu amefanya kazi nzuri, upesi upesi ameileta na tunakubaliana nao kwamba tunahitaji sheria hiyo haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie suala lililopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kuwapongeza sana Wizara hii ya Ardhi; Waziri na Naibu wake, tumewaona wanavyohangaikia migogoro ya ardhi na leo wamekuja na sheria ambayo itawasaidia zaidi katika kupunguza migogoro hii ya ardhi. Kabla sijaendelea, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Rais wetu mpenzi kwa jinsi alivyoshughulikia tatizo la pale Dar es Salaam kwenye quarter za Magomeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pale ameonesha ubinadamu wake na utu wake, kwa kweli lile tatizo lilikuwa kubwa, lakini wananchi tunamwambia hongera sana na aendelee hivyo. Ameonesha jinsi anavyowajali watu wa pale Magomeni, karibu nusu ya wale ni civil servants wa siku nyingi sana ndiyo wako pale. Kwa hiyo, kama wenzao waliuziwa nyumba, kwa nini wao wasipewe wakae pale miaka mitano? Nashukuru sana kwa hatua ambayo imefikia. Namshukuru Mheshimiwa Waziri ambaye amelifikisha mpaka limefika kwa Mheshimiwa Rais; sisi Wabunge wa Dar es Salaam tumekuwa tukipata taabu sana kwa malalamiko yao. Pia namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu asogee kidogo afike Ilala pale quarter tumalize lile tatizo ili mambo mazuri yaonekane pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye sheria hii. Sheria hii imekuja wakati muafaka; pamoja na kwamba imechelewa, lakini ni sheria ambayo nadhani itatusaidia sana. Inakwenda kupunguza migogoro ya ardhi na kubwa zaidi ninaloliomba Mheshimiwa Waziri, elimu ifike kwa wananchi, hawajui haki zao. Wananchi wengi wamepoteza haki kutokana na kutokujua, inakuja Manispaa, anakuja Mthamini wa Manispaa, anathamini, analipa anavyotaka au halipi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kule Dar es Salaam ile Avic City, wananchi wamedhulumiwa vibaya sana pale, kama kungekuwa na kitu kama hiki. Kungekuwa na sheria kama hii, nadhani wengi wamekufa pale wameondolewa, tunaona kuna Avic City lakini wenyewe waliokuwepo pale sasa ni maskini kabisa. Haya mambo kwa Dar es Salaam yamekuwa makubwa kwa sababu kumejitokeza Wathamini wengi sana ambao wanaenda wanachukua ardhi analipwa mtu shilingi milioni moja yeye anakwenda kutengeneza shilingi milioni 100 bila hata huruma. Kwa hiyo, nadhani wananchi wakijua kuna sheria hii, kabla hawajauza watakuwa wanathaminisha ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pia itatusaidia hasa kutakapokuwa na uthamini ambao uko registered, vizuri kabisa, wakati tukitaka kutoa collateral kutafuta mikopo mbalimbali, wakati mwingine thamani inathaminishwa inakuwa ndogo kumbe ni kubwa. Kwa hiyo, kwa sababu sasa itatengenezwa na wenyewe kabisa, nadhani itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limekuwa likiwakuta hawa Wathamani, anaweza akaenda akathamini jengo la mtu, siku benki inataka kwenda kuchukua mkopo wake, wanauza nyumba ya mtu kwa thamani ya chini sana. Nyumba ambayo imejengwa kwa pesa nyingi lakini kwa sababu benki inataka pesa zake, hawajali yule Mthamini anaithaminisha kwa pesa kidogo, matokeo yake wewe mwenye nyumba hupati kitu chochote. Nadhani hapa tumepata mwarobaini sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wakati tunajaribu kugawana mali tukiachana, matrimonial assets, hivyo hivyo akina baba walikuwa na mchezo anakwenda anaongea na Wathamini wanathamini nyumba kwa pesa ndogo, mashamba kwa pesa ndogo; kwa hiyo, akina mama walikuwa wanaonewa pale. Kwa hiyo, akina mama nadhani tulielewe hili sisi kama Wabunge wanawake tukawaelimishe akina mama wasikubali vitu hivi vithaminiwe na Wathamini vishoka. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nimekipenda ni kwamba hii ardhi ikishathaminiwa baada ya miezi sita inaanza ku-attract riba na miezi sita mingine ina-attract riba zaidi tena, lakini baada ya miezi 24 (miaka miwili), basi uthamini ule umekwisha na inarudi kwako. Nimeona hilo ni jambo zuri na litaifanya Serikali au yule ambaye anatakiwa awalipe alipe haraka tofauti na ilivyokuwa Kipawa. Kipawa watu wamekaa miaka 28 hawafanyi jambo lolote. Waliokuwa na hoteli wengine walishazivunja baadaye hakuna kulipwa fidia, wamekaa muda mrefu sana mpaka wamekuja kulipwa, wengine wameshakufa. Kwa hiyo, nadhani kwa hali ilivyo kutakuwa na speed ya kulipa. Wengine kama kule Kigamboni pia wamepata hasara sana kwa sababu ya kusubiri subiri mambo kama haya ingawa sasa hivi naona mambo yanakuwa mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sheria hii mnazungumzia kutoa notice pia, ni jambo zuri kwa sababu wale ambao nyumba zao kulikuwa na miradi inapita, zile alama, zile “X” nyeusi, “X” nyekundu, kijani, zilikuwa zinawapa hofu sana wananchi. Naamini kwamba sasa zile “X” zitaenda baada ya maelewano; baada ya kuzungumza, wananchi waelewe, wakubaliane, baadaye ndiyo hizo “X” ziwe pale tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza na ninaomba tu kwa hapa tulipofikia, sheria mbalimbali ziwe harmonized. Maana yake huko kwenye Local Government wana sheria zao, kila mahali wametengeneza sheria zao ili hii sheria iweze kutumika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.