Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sophia Mattayo Simba (3 total)

MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ni chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi mijini kwa kuangalia wananchi wakijenga maeneo ambayo hayaruhusiwi na wanajenga majengo makubwa, mazuri na matokeo yake Serikali inashindwa kulipa fidia kutokana na gharama kubwa. Je, Serikali itaweka utaratibu gani wa kuwapa nguvu maafisa mbalimbali wa chini
wakiwemo Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa kuhakikisha maeneo haya hayavamiwi? (Makofi)
(b) Kwa kuwa wananchi walioamishwa Kipawa kupelekwa Kinyamwezi baadhi yao mpaka leo hawajalipwa fidia. Je, Serikali inasema nini kwa sababu imewaletea wale wananchi umaskini, inabidi wauze vile viwanja na kwa hiyo umaskini unaendelea. Naomba anihakikishie, hawa ambao wako Kinywamwezi siku nyingi, wamepelekwa hawana la kufanya, hawana pesa ya kujengea watalipwa lini sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza amezungumzia habari ya kupewa nguvu wananchi ili kuweza kuzuia pasiwepo na ujenzi holela kwa sababu watu wanajenga majengo katika maeneo yasiyoruhusiwa na baadaye wanabomolewa. Naomba niseme tu kwamba, nadhani ilikuwa ni Aprili kama sikukosei ambapo Wizara ilichukua hatua mahsusi ya kushirikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika maeneo mbalimbali kwa kuwapatia ramani na tulianzia kwenye Mkoa wa Dar es Salaam. Lengo la Wizara kutoa ramani hizi kwa viongozi wa maeneo hayo ni kutaka pia kuwafanya wao wawe na wajibu wa kuweza kulinda maeneo yao. Kwanza watambue eneo lao na matumizi ya ardhi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni wazi wakishaona ile ramani na kwa sababu walielezewa pia, kwa sababu kumpa ramani peke yake bila kufungua akili na mawazo yake na akajua maana ya michoro ile inakuwa ni kazi bure lakini walielezwa wapi pana maeneo ya wazi, wapi panastahili kujengwa nini na wapi hapastahili kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo la Serikali kutaka kuwapa nguvu kwanza ni kuwapa yale mamlaka yao kamili kuweza kuwa sehemu ya ulinzi wa maeneo yao kuepuka ujenzi holela ambapo wakati mwingine watu wanabomolewa kwa kujenga maeneo yasiyoruhusiwa, maeneo ambayo yanahitaji pengine kuwa na jengo fupi mtu anajenga jengo refu lakini hayo yote tumewawezesha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Kamati zao waweze kuyatambua. Napenda kusema kwamba tunatakiwa kuendelea kutoa ramani hizo kwa Wenyeviti ili kero ya Dar es Salaam isije ikaenda na maeneo mengine ili tuanze kudhibiti kabla haijafika ingawa kuna maeneno mengine pia yana tatizo hilo hilo.
Kipawa na Kinyamwezi ni lini watalipwa stahiki zao waache kusumbuliwa ili waweze kujenga nyumba zao? Nimesema kabisa kwamba, sheria iliyotumika kipindi kile cha kuwalipa ilikuwa inazungumzia suala zima la Land Acquisition Act ya mwaka 1967.
Mheshimiwa Naibu Spika, ile sheria ilikuwa inataka tu mtu alipwe kwa maendelezo yaliyopo na anapewa kiwanja ili aweze kwenda kujenga tena katika maeneo mengine. Kusema kwamba Serikali pengine itawawezesha ili waweze kujenga, hilo halitawezekana kwa sababu sheria haitaki ifanyike hivyo. Sheria ikishakupa thamani ya maendelezo yako, ikakupa na kiwanja, sasa ni jukumu la wewe kufanya hivyo. Uzuri ni kwamba thamani inayotolewa ni ile iliyoko katika soko. Kwa hiyo, tuna uhakika kwamba pengine inaweza ikamwezesha mwananchi kurudia katika hali yake.
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi alivyojibu kwa umakini sana na hususani pale alipozungumzia kwamba walimu wanapata mafunzo zaidi, refresher course ambazo kwa kweli wengi wanazihitaji. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali je, haioni kwamba kuanza kutumia kiingereza kama lugha ya kufundishia kuanzia masomo ya sekondari inasababisha kuleta ugumu sana kwa wanafunzi na matokeo yake wanakuwa wanakariri hasa katika masomo ya sayansi na teknolojia, kitu ambacho kinapelekea wasifanye vizuri sana katika masomo hayo wakati wa mitihani yao, na wale ambao wapo kwenye shule za private wanafanya vizuri zaidi? Sisemi shule zote, lakini hii ni sababu mojawapo ya shule za sekondari za private kufanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu wa kipekee kabisa kuhakikisha kiingereza kinatiliwa mkazo kwa sababu kwenye soko la ajira mara nyingi unaona inatokea kwamba interview zinafanywa kwa kiingereza. Hata mashirika mengine ya umma wakienda vijana interview unawauliza mmefanyiwaje anasema ni kwa kiingereza. Isitoshe sisi tunawakaribisha wawekezaji lakini wale wawekezaji wanahitaji wale ambao wana lugha ya pili ambayo ni kiingereza ili ku-communicate. Je, Serikali haioni kwamba tunapoteza ajira nyingi kutokana na ukosefu wa kujiamini wa kuongea lugha ya kiingereza na matokeo yake uakuta hata kwenye EPZ wako Wakenya, Waganda na Wazimbabwe wameajiriwa na mashirika haya ya uwekezaji. Naomba anijibu hilo tunafanya nini, ajira zinapotea. Ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda ifahamike lugha ya kiswahili ni lugha ambayo ni lugha ya taifa, na ni lugha ambayo inafahamika na wananchi wengi toka wakiwa wadogo. Mwanafunzi anapofundishwa lugha ambayo ameiozoea na amezaliwa nayo ni rahisi zaidi kupokea mitaala anayowekewa kuliko pale ambapo unamfundishia lugha mpya kabisa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo tunasema kwamba, sisi kwa kuzingatia kwamba kiswahili ndiyo lugha yetu ya msingi tunasema kwamba mtoto aanze kufundishwa kwa lugha hiyo, lakini mara anapofika darasa la tatu dozi ya kiingereza inaanza kuongezeka kama nilivyosema mpaka kufikia vyuo vikuu. Kwa siku za nyuma kulikuwa na upungufu zaidi kwa sababu unakuta kwamba walimu walikuwa wanaweza kufundisha somo la Kiingereza hata kama alikuwa hana ufaulu wa kutosha. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile unakuta mwalimu mmoja alikuwa anafundisha masomo mengi. Kadiri tunavyoenda na kuimarisha sifa za walimu na kuongeza idadi ya walimu kutakuwa na specialization kiasi kwamba sasa mwalimu atakuwa anafundisha somo husika na somo alilofaulu na hivyo kiingereza kitazidi kuimarika. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa suala la kukosa ajira nipende tu kusema ukweli kwamba kiingereza kimekuwa kikiendelea kuzingatiwa; na niseme tu kwamba kwetu Watanzania yawezekana pengine unyanyapaaji wetu nao unachangia katika kuwafanya watoto waogope somo la kiingereza; na kila wakati kutokujiamini na kutokuzungumza kiingereza kwa hofu kwamba nitaambiwa sijui kiingereza. Mimi nasema kwamba kiingereza ni lugha sawa na lugha nyingine, mtu zungumza bila uoga sawa na ambavyo wengine wanaweza kujaribu kuzungumza kiswahili bila uoga na watu tunaelewana. Mheshimiwa Mwenyekiti, serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuboresha somo la kiingereza katika shule na kuongeza mijadala katika shule au midahalo, lakini vilevile kupata hata wataalam mbalimbali wanaopenda kuja kujitolea katika nchi yetu kutoka nchi mbalimbali. Kwa hiyo, niwaombe wote tushikamane kuona kwamba lugha hii ya pili ambayo itatusaidia zaidi katika masuala ya mawasiliano hasa ya kibiashara ili nayo iweze kupata nguvu sawa na ambavyo tunasisitiza katika lugha yetu nzuri lugha ya kiswahili, lugha ambayo ni ya upendo na upole. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali kadhalika tunasema kwamba bado lazima tuongeze jitihada hata katika lugha za alama kwa sababu huyu mwanafunzi si kiingereza peke yake, ni pamoja na lugha ya alama…
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, na ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini kidogo yananitatanisha.
Mheshimiwa Spika, anazungumzia ujenzi wa magereza 11 katika kipindi cha miaka 20. Speed hii si nzuri, na pia hayo magereza pamoja na kwamba amesema hayajamalizika lakini wanayatumia, nadhani hapo pana hitilafu kubwa.
Ningependa niulize katika hayo magereza yanayojengwa ni lini anafikiri wanaweza wakaboresha ile mahabusu ya watoto iliyopo Upanga Dar es Salaam; ni mahabusu ya miaka mingi na ni ndogo na haifanani kuwa mahabusu ya watoto? Na sidhani kama zipo mahabusu nyingi kama hizo, Waziri wa Ardhi ana viwanja vingi Dar es Salaam ni vyema akaihamisha pale, ni lini watafikiria kuiondoa ile mahabusu pale?
Mheshimiwa Spika, la pili, kumejitokeza msongamano mkubwa sana kwenye mahabusu na magereza, hasa mahabusu pale wanapokamata watu wengi kwa wakati mmoja. Ningependa kujua hivi kule polisi au magereza wana utaratibu gani wanapokamata watu wengi kwa pamoja, wa kuweza kupunguza wengine kwenda maeneo mengine kwasababu pale ndipo kuna gross breach ya human rights, watu wanapumuliana, wale watuhumiwa wanashindwa hata kukaa na wanalala wakiwa wamesimama.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua kuna utaratibu gani kupunguza hilo tatizo kwa sababu ni la muda tu wanakamatwa kwa muda? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kasi ya kuongeza idadi ya magereza ama kuboresha magereza yaliyopo, naomba tu nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inajitahidi sana kuhakikisha kwamba magereza yetu yanaendelea kuongezeka ukubwa kwa kupanua na kujenga mabweni mapya. Na mfano mzuri wa hilo ni bajeti ya mwaka huu ambayo tumeipitisha hivi karibuni; ambapo tumetenga takribani shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kazi hiyo ambayo itahusisha ukarabati mabweni karibu 15 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo hayo ni kama vile Nzega, Babati, Ushora, Tarime na kadhalika. Lakini pia itahusisha kukamilisha kwa mabweni kama saba ambayo yameshaanza kujengwa ambayo yapo maeneo mbalimbali, likiwemo hilo la Chato, Mpwapwa, Biharamulo, Mkuza, Urambo na kadhalika; pamoja na kuimalisha maeneo ya huduma katika magereza yetu ambapo itahusisha ujenzi wa jiko katika Gereza la Segerea pamoja na mazingira mengine ya magereza yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi hiyo inafanyika hatua kwa hatua kadri hali ya uchumi utakavyoruhusu na tutaendelea kufanya hivyo katika bajeti ya kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na lile Gereza la Watoto la Upanga ambalo Mheshimiwa Sophia Simba ameliulizia; ni kwamba kimsingi lile lipo chini ya Wizara ya Afya kwenye Idara ya Ustawi wa Jamii. Kwa hiyo, sisi tunachokifanya ni kwamba hatuna magereza ya watoto ukiachia Gereza la Vijana la Wami ambalo lipo Morogoro; linalochukua vijana wa miaka 16 mpaka 21, kimsingi watoto wanopatikana kwenye hatia katika magereza hupelekwa katika Idara ya Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kuhudumiwa kama watoto na si wafungwa. Kwa hiyo, kimsingi jibu la swali lake lilikuwa hivyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusu kupunguza msongamano magerezani. Kuna njia mbalimbali zimefanyika, ukiachia hizi ambazo tumezungumza za kuona jinsi gani tunapanua mabweni na kujenga magereza mapya pia kuna hatua mbalimbali ambazo zimesaidia kufanikisha kupungua kwa idadi ya wafungwa kutoka 38,000 mpaka sasa hivi takribani 34,000 tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingia madarakani.
Mheshimiwa Spika, hali hiyo ilitokana na hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha kwamba tunatumia njia za parole, huduma za jamii, probation na njia nyingine ili kuona sasa wafungwa ambao wana kesi ndogo ndogo ama wana hatia ndogo za miaka michache kukaa magerezani basi watumie vifungo vya nje badala ya kurundikana magerezani na kusababisha msongamano usio ulazima. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, niseme kwanza nimefurahi kukuona hapo.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa majibu mazuri. Ni kweli kwamba mahabusu za watoto ziko chini ya wizara yangu, lakini nataka kumthibitishia mama Sophia Simba kwamba katika mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha kwanza makazi ya wazee lakini pia tutaboresha hizo nyumba za kuwarekebisha tabia watoto. Tunajaribu ku-avoid neno mahabusu kwa sababu tunataka kuwarekebisha tabia, ndilo neno ambalo tunapenda kulitumia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mama yangu Sophia hatukuwa na mpango wa kulihamisha lakini sasa kabla hatujaboresha naomba nichukue hoja yako tuone kama je, tuboreshe au tulihamishe tulipeleke sehemu nyingine. Nakushukuru sana. (Makofi)