Contributions by Hon. Stella Ikupa Alex (36 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie Kanuni ya 60(11), kwa idhini yako naomba nizungumze nikiwa nimekaa.
NAIBU SPIKA: Endelea Mheshimiwa.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha mahali nilipofika, kwa kupitia watumishi wake mbalimbali ambao wamekuwa wakiniombea mchana na usiku.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda niwashukuru sana wazazi wangu Alex na Anitha Mwabusega kwa jinsi ambavyo walinilea kwa mapenzi makubwa na hata kunifikisha mahali nimefika leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitakuwa ni mpungufu wa fadhila nisipowashukuru mama zangu UWT, Mkoa wa Dar es Salaam, ambao wameniwezesha kufika mahali nimefika leo pamoja na mama zangu UWT taifa. Mungu awabariki sana. (Makofi)
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa hotuba yake nzuri ambayo aliitoa katika Bunge hili Tukufu tarehe 20 Novemba, 2015. Hotuba hii
ilijitosheleza kila eneo kwa maana iligusa maeneo yote ya Mtanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumpongeza maana hotuba yake imeanza kutekelezeka haraka sana. Tumeona matunda mengi ambayo yametokana na hotuba hii, tumeona jinsi ambavyo matumizi ya siyo lazima yamepunguzwa, tumeona jinsi ambavyo mapato yameongezeka lakini pia tumeona jinsi ambavyo majipu yameendelea kutumbuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo imeweka uwakilishaji kwa kundi la watu wenye ulemavu. Uwakilishaji ni wa jinsi gani? Ni ule uwakilishaji wa kutupatia nafasi kubwa za ngazi ya juu ikiwemo Unaibu Waziri pamoja na Unaibu Katibu Mkuu. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaongea mengi, naomba nijikite kwenye ukurasa wa 9 ambapo Mheshimiwa Rais aliongelea makundi maalumu kwa kusema kwamba haki za makundi maalumu zimekuwa zikikiukwa, walemavu, wazee, wanawake na watoto na kadhalika.
Nitajikita kuchangia kwa upande wa watu wenye ulemavu pamoja na wazee.
Mheshimiwa Naibu Spika, kweli kumekuwa na ukiukwaji wa haki za watu wenye ulemavu ikiwemo haki ya kuishi. Tumeshuhudia jinsi ambavyo wenzetu wenye ulemavu wa nguzo wamekuwa wakitendewa vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kukatwa viungo vyao na
kuuwawa. Ni juzi tu hapa mwezi Disemba kuna mama mmoja kutoka Tanga alikatwa kidole, ni mtu mwenye u-albinism. Kwa kweli ni vitendo ambavyo havistahili na ni vitendo ambavyo kiukweli vinatakiwa kupigiwa kelele sana. Pia Watanzania ambao muda huu wanatutazama
wavikemee kwa hali na nguvu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho kimekuwa kikikiukwa kwa upande wa kundi hili ni haki ya ajira. Kuna sheria kabisa ambayo inawataka waajiri wawe na asilimia tatu ya wafanyakazi wao ambao ni watu wenye ulemavu lakini sheria hii imekuwa haitekelezeki.
Niombe Serikali Tukufu ya Chama cha Mapinduzi ifuatilie utekelezaji wa sheria hii kwa kufuatilia kila mwajiri na kuhakikisha wana asilimia hii ambayo imewekwa katika sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo halitekelezeki ni haki ya habari. Kwa upande wa wenzetu ambao ni viziwi wanahitaji kupata habari. Kwa mfano tu wa haraka haraka na mfano halisi hata sisi Wabunge wakati tunaendesha kampeni zetu, ni nani ambaye katika kampeni zake alikuwa akizunguka na mkalimani wa lugha ya alama, hayupo! Mtu huyu unategemea akupigie kura, atapigaje kura na wakati hajajua kitu ambacho umekiongelea katika sera zako? Kwa hiyo, hili pia ni jambo la kuangalia sana. Pia ni endelee kuiomba Serikali
ya Chama changu cha Mapinduzi kutoa agizo kwa wamiliki wa vyombo vya habari ikiwemo television waajiri haraka sana wakalimani wa lugha za alama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho pia napenda kukiongelea ni haki ya elimu kwa watu wenye ulemavu. Tunashukuru kwamba tuna shule chache lakini hazitoshelezi kwa sababu si wazazi wote ambao wanauelewa wa kuwapeleka watoto katika shule hizi. Kwa hiyo, mimi
niombe Serikali zilezile shule za kawaida iziboreshe kwa kuweka mazingira ambayo yataweza kufikika ama yatakuwa ni rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niongelee suala la uandaaji wa shughuli za Kitaifa. Katika uandaaji wa shughuli za Kitaifa pia umekuwa hauzingatii mahitaji maalumu. Naomba nitolee mfano mmoja ambao mimi mwenyewe niliguswa. Samahani, ilikuwa ni kipindi kile cha
msiba wa Mheshimiwa Celina Kombani, tulipofika mahali pale hakukuwa na mkalimani wa lugha za alama, ufinyu wa nafasi lakini ule mwili uliwekwa juu inakubidi upande kitu ambacho mimi niliogopa naweza nikasukumwa kidogo nikaanguka wakati nilihitaji kwenda kumuaga yule Mheshimiwa. Kwa hiyo, naomba panapokuwa pana uandaaji wa shughuli za Kitaifa hivi vitu vizingatiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda niongelee haki za wazee. Tumeona wazee wetu ambao wamestaafu miaka ya nyuma wamekuwa wakilipwa pensheni ndogo sana. Kwa hiyo, niioombe Serikali iangalie ni jinsi gani ambavyo inaweza ikawapandishia pensheni wastaafu
hawa ili waweze kufaidi matunda yao ya utumishi wao katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja, ahsante sana.
(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ulinzi, rehema na fadhila zake kwangu pamoja na familia yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda niitumie nafasi hii kumpa pole sana Mheshimiwa Naibu Waziri Engineer Stella Manyanya kwa kuondokewa na mama yake mpendwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba niitumie tena fursa hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo imetekeleza kwa haraka sana ahadi yake ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Kama tunavyofahamu kwamba, hata mbuyu ulianza kama mchicha, pamoja na changamoto zilizopo lakini Serikali yetu inastahili kupewa pongezi kwa jinsi ambavyo imefanya na kwa jinsi ambavyo inaendelea kutatua changamoto ambazo zimejitokeza ikiwemo changamoto ya madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee tatizo la ufaulu wa msomo ya sayansi, biology pamoja na mathematics. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake ameliongelea hili, lakini naomba niongelee kwa msisitizo. Kweli kumekuwa kuna tatizo kubwa la ufaulu wa masomo haya kwa watoto wetu, tatizo ambalo linasababishwa na Walimu lakini pia ukosefu wa maabara pamoja na vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa upande wa Walimu, iangalie watu ambao wanakwenda kuchukua course ya Ualimu, wawe ni wale watu ambao wamefaulu sana katika haya masomo yaani chemistry, biology na physics. Inakuwa inatia simanzi sana kuona kwamba Mwalimu ambaye labda yeye alipata „D‟ lakini ndiyo huyo anayekwenda kusoma Ualimu wa physics au Ualimu wa chemistry. Kwa hiyo, naishauri sana Serikali iliangalie hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee suala zima la ukosefu wa maabara pamoja na vifaa katika hizi maabara. Inatia simanzi sana kuona kwamba vyumba vipo, lakini vifaa vya maabara hakuna tatizo ambalo linapelekea wanafunzi kufundishwa theory, lakini baadaye inabidi aende akafanye practically, vifaa hamna vya kumwezesha mwanafunzi huyu kufanya hizi practical, mwisho wa siku anaingia kwenye chumba cha mtihani anakutana na swali hata ambalo ni rahisi la titration anashindwa kufanya, anakutana na kifaa kama test tube, anashindwa kugundua kama hiki kifaa kinaitwa test tube.
Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iliangalie hili, iangalie uwezekano mkubwa wa kuweka vifaa kwenye hizi maabara zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niongelee suala zima la changamoto ya elimu kwa wanafunzi ama watoto wenye ulemavu. Changamoto ziko nyingi sana, lakini naomba niongelee changamoto chache kwa sababu ya muda. Kuna changamoto kubwa ya Walimu kwa watoto hawa wenye ulemavu. Changamoto hii ni ya muda mrefu na ni changamoto kubwa. Niiombe sana Serikali kwa habari ya Walimu wa kundi hili maalum, wawachukue wale Walimu ambao wana uweledi wa kuwafundisha watoto hawa ndiyo ambao wakachukue course hii ya kufundisha watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niiombe Serikali itoe motisha kwa sababu kiukweli kufundisha makundi maalum ni kazi. Kwa hiyo, itoe motisha kwa maana ya pakages za mishahara ziwe kubwa tofauti na Walimu wa wanaofundisha watoto wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee suala zima la changamoto ya miundombinu kwa watoto wenye ulemavu ama wanafunzi wenye ulemavu. Changamoto hii ni kubwa kuanzia primary school mpaka vyuoni. Naomba nitolee mfano mdogo wa Chuo Kikuu cha UDOM, hiki chuo ni kipya, kimejengwa miaka ya hivi karibuni, lakini cha kushangaza miundombinu yake si rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie suala zima la kuboresha miundombinu kwa wanafunzi ama watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna changamoto ya uhaba wa shule za haya makundi maalum. Shule ni chache sana ukilinganisha na uhitaji. Kwa mfano, unaweza ukakuta labda shule inapatikana Dar es Salaam, lakini mtoto yuko Mtwara, ama yuko Mwanza ama yuko mahali ambako panakuwa hapana shule, inakuwa ni ngumu sana kwa sababu tuelewe kwamba wazazi wengi wenye watoto hawa wana kipato cha chini. Kwa hiyo, inakuwa ni ngumu mzazi huyu kumleta mtoto wake shule halafu aje amfuate, ukizingatia kwamba pia kulikuwa kuna ile pesa ambayo inatolewa kwa ajili ya kumwezesha mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu kuweza kumpeleka mtoto wake shuleni, hizi pesa siku hizi hazitolewi tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe sana Serikali izirudishe hizi pesa, iwapatie wazazi wenye watoto wenye ulemavu pamoja na walezi ili waweze kusafiri kuwapeleka watoto hawa kwenye maeneo ambayo yana shule maalum. Pia niiombe Serikali kuboresha sana hizi shule ambazo zipo kwenye maeneo, kwamba watakapoziboresha hizi shule katika maeneo husika, itaondoa huu usumbufu wa wazazi kusafiria huduma hii ya shule kwenda mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala zima la changamoto ya vifaa saidizi kwa watoto wenye ulemavu. Unaweza ukakuta kwamba mtoto ana uwezo wa kwenda shule, wa kusoma lakini sasa changamoto yake aidha ni wheel chair au ni brail au ni vifaa vingine vinavyofanana na hivyo. Changamoto hii ni kubwa sana na inawafanya watoto wengi washindwe kwenda shule kwa sababu ya ukosefu wa hivi vifaa saidizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara ya Elimu, ishirikiane na TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu kuwabaini watoto ambao kweli wana uhitaji wa hivi vifaa saidizi na waweze kupatiwa hivi vifaa tofauti na sasa hivi, vifaa hivi vinaweza vikawa vinatolewa lakini haviwafikii wale walengwa, kwa maana kwamba utakuta mtu yule aliyenacho ndiye anaongezewa, kwamba mtu ambaye ana uwezo wa kupata hiki kifaa ndiye huyo ambaye anapewa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili la utambuzi linawezekana kabisa kwa sababu mimi mwenyewe binafsi nimeshawahi kufanya hilo zoezi. Ni juzi tu hapa nilimtumia Mwenyekiti wangu wa Serikali za Mitaa, nikamwambia kwamba naomba nifahamu idadi ya walemavu waliopo kwenye mtaa huu pamoja na changamoto zao na ilikuwa ni within a week yule Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa alinipatia orodha ya hawa watu wenye ulemavu pamoja na changamoto zao. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Elimu ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Bunge, Sera, Ajira na Walemavu pamoja na TAMISEMI kuwabaini watoto hawa na kuweza kuwapatia hii huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niongelee suala la hivi Vyuo vya VETA. Kumekuwa kuna ongezeko kubwa la ombaomba wenye ulemavu pamoja na tegemezi. Niiombe sana Serikali, ili kupunguza hili wimbi la ombaomba wenye ulemavu, iwasaidie kwa kuwawezesha kusoma katika hivi vyuo vya VETA ikiwezekana iwe ni bure kabisa ili waweze kupata ujuzi wa kuweza kumudu maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee na niiombe Serikali kwa habari ya suala zima la lugha ya alama. Kumekuwa kuna changamoto kubwa ambayo tumekuwa tukiiongea kila siku, uhitaji wa Wakalimani wa lugha za alama, lakini nashauri kwamba lugha hii ya alama ifundishwe kama somo mashuleni, kwa maana kwamba mtoto huyu ambaye anasoma sasa hivi darasa la kwanza, anafika form six, ndiye mtoto ambaye tunamtegemea kwamba aje kuwa Daktari amuhudumie mtu ambaye ni kiziwi, aje kuwa ni Polisi, aje kuwa ni Nesi ambaye atamzalisha mtu ambaye ni kiziwi. Pia itasaidia hata kwenye jumuiya zetu kwamba unakutana na mtu ambaye ni kiziwi, lakini kwa sababu ulishasoma hii lugha ya alama inakuwa ni rahisi ku-communicate naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niongelee suala zima la Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu ambao ulianzishwa kwa Sheria namba 9 ya mwaka 2010. Mfuko huu upo lakini umekuwa hautengewi fedha wala haupatiwi fedha. Niiombe Serikali sana kwamba sasa umefika wakati Mfuko huu utengewe na kupatiwa pesa, pesa hizi zitasaidia kwa habari ya mahitaji ya watoto wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuongelea msongamano wa watoto kule Buhangija. Kule kumekuwa kuna msongamano mkubwa wa hawa watoto, naishauri Serikali kwamba ifanye kuwatawanya kwa yale maeneo ambayo yako safe ambapo kwa mfano, kama Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro ni mikoa ambayo iko safe ambayo haijaripotiwa na haya matukio ya mauaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kila mmoja wetu aliyeko mahali hapa. Pia nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati zote waliowasilisha taarifa zao leo na kipekee kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Naendelea kumpongeza kwa sababu ya haya mengi ambayo anaendelea kuyafanya katika nchi yetu ambayo yanatupelekea kuwa Tanzania ya kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika maoni ya Kamati ya Masuala ya UKIMWI maeneo mengi imeshauriwa kwamba kama Serikali tuweze kujitegemea kwenye masuala ya UKIMWI. Kwa hiki anachokifanya Mheshimiwa Rais anatupeleka kwenye Tanzania ambayo baadaye tutaweza kuwa ni watu wa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichangie katika eneo la mashirikiano kati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika eneo la mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Niseme tu kwamba ushauri wote ambao umetolewa na Kamati hii ya Masuala ya UKIMWI umepokelewa, lakini naomba nitoe ufafanuzi kidogo. Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kuna mashirikiano mazuri kabisa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mapambano ya dawa za kulevya kwa njia gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upande wa Zanzibar tuna Tume, lakini upande huu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano tuna Mamlaka. Kwa hiyo hii Mamlaka inashirikiana vizuri kabisa na Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Zanzibar, kuna vikao mbalimbali ambavyo vimekuwa vikifanyika vya Baraza la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Tume imekuwa ikishiriki kikamilifu kabisa. Hata hivyo, pia kumekuwa na jumbe mbalimbali ambazo zinatoka Tanzania kwenda Kimataifa katika eneo hili la madawa ya kulevya. Tume pia imekuwa ikishirikishwa vizuri kabisa.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza sasa hivi, Tume ya Zanzibar ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, iko katika mchakato wa kufanya mabadiliko na kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Sambasamba na hilo, Tume pia iko katika mchakato na harakati za mwisho kabisa za kufanya marekebisho ya Sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya ili sasa ile Sheria ya upande wa Zanzibar iweze kufanana na Sheria ya upande wa Tanzania Bara. Ni kwa nini tunafanya hivyo, kwa sababu ilionekana kwamba kuna gape kidogo kati ya upande wa Tanzania Bara na upande wa Tanzania Zanzibar. Kwa hiyo marekebisho hayo yakishafanyika ina maana kwamba sasa udhibiti wa dawa za kulevya utaenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Spika, vile vile kulikuwa na hoja ya kwamba hatuna Sera ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Ni kweli sera hii haipo, lakini, Tume iko katika hatua za mwisho kabisa za kuandaa huu mchakato wa Sera ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya. Katika hili pia kwa sababu Serikali yetu, Serikali ambayo inapenda ujumuishi, iliandaa utaratibu mzuri kabisa wa kukusanya maoni na walijiwekea kwamba watakusanya maoni kutoka kwa Wadau wapatao 120, lakini pia kutoka kwenye Kanda zetu zote tano. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza tayari tumekwishakusanya maoni kutoka kwenye kanda nne bado kanda moja. Tukishakamilisha kanda zote tano, watakaa chini na ku-compile maoni haya na hatimaye utaratibu wa kupatikana kwa sera utaendelea(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie katika eneo la kukinzana kwa Sera Mipango na Sheria mbalimbali za UKIMWI, lakini pia kuna mapendekezo ya Kamati ambayo yametolewa kwamba Sheria ifanyiwe mapitio. Niseme kwamba ushauri huu mzuri kabisa umepokelewa, lakini sambamba na hilo, naomba nitoe ufafanuzi kidogo, Serikali kupitia Wizara husika, Wizara ya Afya tayari imekwishaandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria Na. 28 ya mwaka 2008. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mapendekezo haya ya mabadiliko ya Sheria, kuna baadhi ya vifungu ambavyo vitafanyiwa marekebisho. Vifungu hivi ni kifungu cha 13, 15, pamoja na 27. Katika kifungu cha 13 kinaongelea upimaji wa VVU, katika vituo ambavyo vimethibitishwa. Katika mapendekezo ya Sheria yanasema kwamba sasa hivi upimaji wa VVU uwe ni kwa hiyari lakini mtu aruhusiwe kujipima mwenyewe mahali popote alipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili tunaamini kwamba tutapata matokeo mazuri ya ile 90 ya kwanza, kwa sababu inaonekana kwamba katika ile 90 ya kwanza tupo nyuma kidogo tofauti na ile 90 ya pili, ambayo tumefikia asilimia 91 na ile 90 ya tatu ambayo tumefikia asilimia 87.
Mheshimiwa Spika, sambasamba na hilo, pia kuna mapendekezo kwenye umri wa kuweza kupima virusi vya UKIMWI kwa hiari bila ridhaa ya mzazi. Katika sheria yetu, kifungu cha 15(2) kilikuwa kinalazimisha mtu anayepima UKIMWI awe ni yule mtu ambaye anakuwa na umri wa miaka 18 na kuendelea ambapo hapo sasa anakuwa anapima mwenyewe kwa hiari yake bila ridhaa ya mzazi lakini chini ya hapo mtu alikuwa haruhusiwi kupima mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi sheria inapendekeza kwamba umri wa mtu kupima kwa hiari bila ridhaa ya mzazi/ mlezi uwe ni miaka 15. Tumesikia Waheshimiwa Wabunge wengi wameliongelea hilo na Serikali yenu sikivu imelisikia na muda siyo mrefu mapendekezo haya yataletwa mbele ya Bunge lako Tukufu ili Waheshimiwa Wabunge waweze kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna kifungu kingine ambacho pia kinatarajiwa kufanyiwa marekebisho, kifungu cha 27 ambacho kinaelezea adhabu ya kosa la mtu ambaye anatangaza tiba ya UKIMWI kinyume cha sheria. Mwanzoni adhabu ilikuwa ni shilingi milioni moja ama kifungo cha miezi sita lakini sasa hivi inapendekezwa kwamba adhabu iwe shilingi milioni milioni tano au kifungo cha miaka mitatu.
Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na suala la mahusiano kati ya shughuli za kiuchumi na ongezeko la maambukizi ya UKIMWI sanasana kwenye maeneo yale ambayo yanakuwa na msongamano mkubwa ama sehemu za miradi mbalimbali kama barabara, migodini na sehemu nyingine. Pamoja na elimu ambayo inatolewa, Serikali pia imeenda mbali zaidi kwa kutoa dawa kinga kwenye maeneo haya ili kuhakikisha makundi haya yanaendelea kuwa salama. Dawa kinga hii ni Pre-exposure Prophylaxis ambayo inasaidia kwa makundi haya ili yasiweze kuambukizwa na magonjwa ya VVU.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada hizo tumefika mbali kwa sababu tulianza kutoa dawa hizi mwezi Machi, 2018 kwa pilot ya mikoa tisa. Machi 2018 mpaka Septemba, tulikuwa tumeshafikia mikoa tisa lakini malengo yetu ilikuwa ni kufikia watu wapatao 16,000 na ndani ya mikoa tisa tulikuwa tumeshafikia watu 9,000. Kuanzia Oktoba tuliongeza mikoa mingine 12 na kufanya jumla ya mikoa kuwa 21. Tunategemea kabisa tutavuka lengo kwa sababu katika mikoa tisa tulikuwa tumefikia watu 9,000 lakini katika mikoa hii mingine iliyoongezeka tunategemea kwamba tutaenda kuvuka lengo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna suala la Mfuko wa UKIMWI wa Taifa ambao huu unatupelekea kuondokana na ile dhana ya kutegemea wafadhili. Mfuko huu unafanya vizuri sana ambapo mwaka 2017 tuliweza kununua dawa za Septrin zenye gharama ya shilingi milioni 660. Pia kwa mwaka huu umeidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 455 ambayo inaenda kununua hizi dawa za Septrin. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda na mimi naomba niunge mkono hoja za Kamati zote hizi tatu ambazo zimewasilisha taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha tena siku ya leo kuwa mbele ya Bunge lako Tukufu ikiwa ni mwaka 2018 nilipochangia bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitumie nafasi hii kuendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miongozo na maelekezo ambayo ameendelea kunipatia katika nafasi hii ambayo ninahudumia kama Naibu Waziri ambaye nashughulikia masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miongozo ambayo imeniwezesha na imeendelea kuwezesha kundi hili la watu wenye ulemavu mahitaji yao kuweza kutekeleza vizuri. Pia naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, dada yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jenista ni mama, ni mlezi. Kwa kweli ninakushukuru sana Mheshimiwa Jenista kwa upendo wako, lakini pia kwa miongozo na maelekezo ambayo umeendelea kunipatia. Kwa kweli nashindwa nitumie lugha gani rahisi kuweza kumwelezea Mheshimiwa Jenista. Amekuwa ni rafiki wa karibu, amekuwa ni dada na mama, yaani amevaa nafasi zote kwa nafasi hii ninayoitumikia katika Ofisi hii ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Angellah Kairuki dada yangu, kwa muda mfupi ambao nimekuwa naye katika Ofisi ya Waziri Mkuu ameendelea kunielekeza na kunipatia maelekezo ambayo yanaendelea kunisaidia katika utendaji wangu. Pia naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu Mheshimiwa Antony Peter Mavunde kwa ushirikiano ambao ameendelea kunipatia. Ni ushirikiano mkubwa, sisi ni marafiki. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Antony Mavunde kwa ajinsi ambavyo ameendelea kunipatia ushirikiano mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Makatibu Wakuu wote watatu kwa majina yenu, kwa sababu ya muda naomba nisiyataje kwa jinsi ambavyo mmendelea kunifanya niweze kutekeleza majukumu yangu katika Ofisi hii ya Waziri Mkuu. Vile vile nawashukuru Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwemo watumishi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu. Naomba niseme kwamba nawashukuru sana kwa jinsi ambavyo mnaniwezesha kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja kwa sababu ya muda, naomba niende kwenye ufafanuzi wa hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na Kamati yetu ya kudumu ya masuala ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja kwamba Serikali iweze kuimarisha kitengo kinachohudumia masuala ya watu Wenye Ulemavu. Ushauri huu wa Kamati ni ushauri mzuri na ndani ya Serikali tayari tumeshaanza kuona ni jinsi gani tunaweza tukaongeza watumishi katika kitengo kinachohudumia na kuratibu masuala ya watu wenye ulemavu. Kuongezeka kwa watumishi hawa kutawezesha usimamizi na uratibu kuweza kufanyika kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika mwaka huu wa fedha kifungu cha Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kimeweza kuanzishwa ambacho ni Kifungu Na. 2034 na kupitia kifungu hiki, pia tunaona masuala mengi ya watu wenye ulemavu yataweza kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kuendelea kuimarisha Kitengo hiki cha Watu Wenye Ulemavu, Serikali tunaona kwamba iko haja ya kuwajengea uwezo watumishi wa kitengo hiki kwa sababu masuala ya watu wenye ulemavu yako mengi, lakini pia yanaibuka kila kukicha. Kwa hiyo, uko umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi hawa na tumekuwa pia tukifanya hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna suala la Baraza la Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu. Baraza hili, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba litatangazwa hivi karibuni, muda siyo mrefu. Litakapokuwa limetangazwa baraza hili, basi tunaamini kwamba litatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria inavyoitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya Mfuko wa Taifa kwa Watu Wenye Ulemavu. Sheria yetu inatuongoza kwamba tunatakiwa kuwa na Mfuko huu wa Taifa kwa Watu Wenye Ulemavu. Maandalizi ya Mwongozo yanaendelea kukamilika na tayari kwa mwaka wa fedha ujao 2019/2020 tumetenga fedha zipatazo shilingi milioni 103 ambazo ni mbegu kwa mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nitoe rai kwa wadau mbalimbali kuweza kuchangia mfuko huu kwa sababu una matumizi mengi kwa kundi hili la watu wenye ulemavu. Ruzuku za Vyama vya Watu Wenye Ulemavu zinategemea mfuko huu na pia elimu na mafunzo vinategemea mfuko huu. Pia, tafiti mbalimbali ambazo zinahusiana na masuala ya watu wenye ulemavu yanategemea mfuko huu. Pia kuna masuala ya Utengemano kwa Watu Wenye Ulemavu yanategemea mfuko huu. Kwa hiyo, ni rai yangu kwamba Serikali tumeshaanza kwa kutenga hiyo fedha, basi na wadau mbalimbali waendelee kujitokeza kuchagia mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja ya kwamba, Serikali ihakikishe kwamba inatatua migogoro mbalimbali ambayo inajitokeza kwenye Vyama vya Watu Wenye Ulemavu. Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Kiraia lakini pia kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu. Ni kweli kuna migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mara kadhaa imeweza kuwaita wahusika wa vyama hivi na kuweza kutatua migogoro ambayo imekuwa ikiendelea. Sambamba na hilo, tumekuwa tukihakikisha kwamba chaguzi zinakuwa zinafanyika na mikutano inakuwa inafanyika kwa mujibu wa katiba na sheria ambavyo inataka ifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu sasa hivi kinaendelea kushughulikia kuhakikisha kwamba Mkutano Mkuu unaitishwa na Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Viungo Tanzania (CHAWATA) na kuweza kufanya mkutano ambao imekuwa ni changamoto kubwa kwa chama hiki kwa muda mrefu. Kwa hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu inalishughulikia hili kwa kushirikiana na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo Tanzania kuona kwamba, mkutano unaitishwa na hatimaye uchaguzi ule unaweza kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya miundombinu ambayo inakuwa ni rafiki kwa watu wenye ulemavu. Serikali ihakikishe kwamba miundombinu inakuwa ni rafiki kwa watu wenye ulemavu. Serikali yetu inazo sheria ambazo zinaelekeza kabisa kwamba, miundombinu inatakiwa iweje ili iweze kuwa jumuishi kwa watu wote. Niendelee kutoa rai kwa mamlaka ambazo zinahusika na upitishaji wa michoro mbalimbali katika miji yetu, kuhakikisha kwamba inazingatia hii sheria, kwamba isipitishe michoro ambayo inakuwa haijaonesha ni jinsi gani miundombinu itakuwa ni rafiki kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Serikali imeendelea kutoa elimu kwa mamlaka mbalimbali lakini pia hata kwa jamii zetu kuelekeza kwamba ni jinsi gani basi miundombinu inafaa kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu. Waheshimiwa Wabunge, hata nyumba ambazo tunakuwa tunajenga tuweze kuona kwamba ni jinsi gani zinakuwa ni rafiki kwa makundi yote. Mimi huwa nakuwaga na msemo kwamba; sipendi sana kusema kuwa kila mtu ni mlemavu mtarajiwa, lakini napenda kusema kila mtu ni mzee mtarajiwa. Kwani hata uzee hatuutaki, si kila mtu anapenda awe mzee, kwa hiyo kama unapenda kuwa mzee, kuna miundombinu ambayo itafika mahali haitakufaa utakapokuwa mzee. Kwa hiyo suala la miundombinu ni suala ambalo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kwamba, miundombinu inakuwa ni rafiki kwa makundi yote. (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya kwamba, Serikali iwasaidie watu wenye ulemavu wanapokuwa wanapatikanika ama wanapokuwa na kesi zao. Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba, haki za watu wenye ulemavu zinafuatwa kwa kutumia Ofisi zetu za Ustawi wa Jamii, lakini pia niendelee kutoa rai kwa asasi mbalimbali ambazo zinashughulika na masuala mbalimbali ya kisheria, kuona kwamba ziweze kuzingatia masuala mbalimbali yanayohusiana na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wanasheria ambao wamekuwa wakijitolea katika eneo hili pia, niendelee kuwapongeza na kuwashukuru na wamekuwa wakijitangaza kwamba wanaweza wakasaidi kundi hili la watu wenye ulemavu wanapokuwa wanapatikanika na kesi. Pia sisi kama Serikali tumekuwa tukifanya hivyo mara kadhaa hata mimi mwenyewe nimeweza kuwaunganisha watu wenye ulemavu na Wizara ya Katiba na Sheria na wamekuwa wakisaidika. Kwa hiyo, ushauri huu mzuri tumeupokea na tutaendelea kuutekeleza kama ambavyo inatakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kusimamia na kudhibiti ile asilimia mbili ambayo inatolewa na halmashauri. Niseme kwamba, Serikali tumepokea ushauri huu mzuri, lakini pia tumeanza kuandaa kanuni kwa kushirikiana na Ofisi ya Mheshimiwa Rais, TAMISEMI kuandaa mwongozo na kanuni ambazo zitawezesha utolewaji na usimamizi wa hii asilimia mbili ambayo inatolewa na halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ama ushauri ambao ulitolewa kwamba Serikali ihakikishe inashughulikia ama kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinahusiana na watu wenye ulemavu, kwa maana ya kwamba kuweka uratibu mzuri kwa masuala ya watu wenye ulemavu. Serikali imeendelea kufanya hivyo na kwa kuliona hilo tumeweza kuanzisha madawati katika Wizara zetu zote, pamoja na taasisi, madawati ambayo yanashughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia tumeweza kufanya warsha mbalimbali kwa sababu tunatambua kwamba, ajira imekuwa ni changamoto kubwa kwa watu wenye ulemavu. Tumeweza kuandaa warsha mbalimbali ambazo Serikali kwa kushirikiana na CCBRT, tulifanya warsha ambayo iliwahusisha waajiri na kupitia hapo tukawaomba waajiri kwamba waweze kuendelea kuwaajiri watu wenye ulemavu. Kupitia warsha ile, kuna waajiri ambao pale pale waliweza kujitolea kwamba, wataajiri watu wenye ulemavu kadhaa, pale kadhaa, pale kadhaa.
Kwa hiyo, ilikuwa ni warsha nzuri ambayo iliendelea kuwa na mafanikio. Niendelee kutoa rai kwa waajiri wote kuendelea kutenga nafasi katika ofisi zao kwa ajili ya kuajiri watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi ambayo yamefanywa na Serikali, lakini naona tayari nimeshagongewa kengele ya kwanza, pia sambamba na hilo tumeweza kufanya semina kwa wajasiriamali wenye ulemavu na hii ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaonesha fursa ambazo zinapatikana ndani ya Serikali yetu sikivu ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Rais wetu, ambaye amejipambanua kwa vitendo kuendelea kulijali na kulipenda kundi hili la watu wenye ulemavu. Semina hii pia ilikuwa na mafanikio makubwa kwa sababu wajasiriamali wale wenye ulemavu waliweza kufahamu fursa mbalimbali ambazo wanaweza wakazitumia ndani ya Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye masuala yanayohusiana na UKIMWI, kulikuwa kuna hoja ya Kamati ambayo iliweza kusema kwamba, Serikali iweze kukamilisha mwongozo wa namna ya kamati zile ambazo zilikuwa zinatumika na masuala ya UKIMWI, basi ziweze kushughulikia masuala ya dawa za kulevya. Serikali yetu imepokea ushauri huo na tayari Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekwishakasimu mamlaka ama shughuli za kupambana na dawa za kulevya kwa hizi Kamati za UKIMWI kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kulikuwa kuna hoja ya kwamba, Serikali iweze kuona umuhimu wa kutenga fedha zake za ndani za maendeleo angalau asilimia 75, kwa ajili ya masuala ya UKIMWI kutekeleza hizi afua za UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ushauri huu mzuri pia umepokelewa na tayari Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na UKIMWI imeandaa mkakati wa jinsi gani itaweza kukusanya fedha na pia umeweza kuonesha ama kuainisha vyanzo vya mapato vya ukusanyaji wa fedha hizo. Tunaamini kwamba kupitia mkakati huu, tutaweza kuondokana na utegemezi wa kutegemea ufadhili kutoka nje na hasa tukizingatia kwamba, Mheshimiwa Rais wetu ni Rais ambaye anapenda sisi kama Taifa tuweze kujitegemea kwa mapato ama kwa fedha zetu ambazo tunazipata ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya Kamati kwamba Serikali iweze kuanzisha chanzo maalum ama mahususi ambacho kitawezesha kutunisha fedha ya Mfuko wa UKIMWI. Hii walipendekeza kwamba, iwe ni tozo labda kutoka kwenye maji na vitu kama hivyo. Ushauri huu pia ni mzuri sana na utawezesha kiukweli kwamba tutaweza kuendelea kujitegemea. Serikali imepokea ushauri huu na inaendelea kuufanyia kazi kuona ni jinsi gani tunaweza tukaanzisha tozo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja ya kwamba Serikali iweze kubuni uwekezaji katika kutekeleza afua za UKIMWI kwa kushirikiana na sekta binafsi. Hoja hii pia ni nzuri na imepokelewa, lakini pia niweze kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI tayari ipo katika hatua za mwisho za kuajiri mtaalam ambaye atasaidia katika upatikanaji ama ni jinsi gani sasa fedha zipatikane. Sambamba na jukumu hilo, atafanya na jukumu hili la kuhakikisha kwamba basi, hizi sekta binafsi zinaweza kushirikishwa na hatimaye kuweza kufikia lengo ambalo limetarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya kwamba Serikali kwa ku… (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kusema haya, nami naomba niunge mkono hoja ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. STELLA A. IKUPA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa fursa ya kuweza kuchangia jioni hii ya leo. Awali ya yote ninaomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa jinsi ambavyo ameendelea kutulinda mpaka tumefikia Mkutano huu wa Kumi na Tano na hatimaye Kikao cha 51 cha Bunge letu. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu, wengi walitamani kufika, lakini hawajaweza kwa hiyo, tunaposimama ni lazima tumshukuru Mungu kwa sababu, ni neema tu wala siyo kama tunastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba kuunga mkono hoja ambazo ziko hapa mbele yetu, lakini pia, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri kwa jinsi ambavyo wanasimamia Wizara zao na kwa jinsi ambavyo wanamshauri vizuri Mheshimiwa Rais wetu. Pia natumia fursa hii, kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Rais shupavu, ni Rais mahiri, ni Rais ambaye ana ubunifu ambao kwa kweli, ukikaa ukiutafakari, mpaka unashangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubunifu huu na umahiri wa Mheshimiwa Rais wetu ndiyo ambao umesababisha uchumi wetu kuwa imara mpaka hivi tunavyozungumza. Dunia imetikiswa sana, lakini pamoja na kutikiswa kwa dunia uchumi wetu umeendelea kuwa imara. Kwa hiyo, ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kuendelea kumshukuru na kuendelea kumuombea kwamba, Mwenyezi Mungu aendelee kumpa maarifa na ubunifu wa kuendelea kuliongoza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, uchumi wetu uko imara, lakini Serikali inapaswa iendelee kuchukua tahadhari dhidi ya vitu ambavyo vinaweza vikasababisha uchumi wetu kushuka, miongoni mwa vitu hivyo ni mabadiliko ya tabianchi. Tunaona jinsi ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kutikisa dunia kwa hiyo, iko haja ya Serikali kuweka mikakati ya kuona ni namna gani inakabiliana na mabadliko haya, ili yasiweze kuathiri uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Serikali iweze kuona ni kwa jinsi gani inapunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje na badala yake kutoa kipaumbele kwa bidhaa ama mazao ambayo tunazalisha sisi wenyewe likiwemo zao la ngano. Yako mambo mengi, lakini kwa sababu ya muda, ninaomba niyataje hayo kwa uchache. Kwa hiyo Serikali iendelee kuangalia mambo ambayo wanashuku kwamba, yanaweza yakasabaisha uchumi wetu ukashuka, ili uchumi wetu uendelee kuwa imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninaomba kuongelea suala la misamaha ya kodi. Kuna malengo ambayo yamewekwa kwamba, misamaha ya kodi isivuke asilimia moja ya Pato la Taifa, lakini mpaka hivi tunavyozungumza misamaha hii imekwishavuka, iko asilimia 1.3. Sasa, kwa staili hii ama kwa jinsi hii, iko haja ya Serikali kuweza kuipitia upya misamaha ambayo ilitolewa kuona kama ina tija kwa Taifa letu au kama inaendana na wakati tulionao hivyo, iweze kuipitia na kuona kwamba, ni kwa jinsi gani inaiondoa na kuweka ile misamaha ambayo itakuwa na tija kwa Taifa na itaendana na wakati tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba kuongelea suala la kulinda viwanda vyetu. Ninaishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa imara katika kulinda viwanda vyetu, hasa tukiangalia hata kwenye hizi taarifa ambazo tuko nazo. Imeonesha wazi kwamba, inaenda kufanyia mabadiliko Sheria ya Kudhibiti Uingizwaji wa Bidhaa Kutoka Nje, Sura Na. 276 na kuanzisha Tozo ya Maendeleo ya Viwanda (Industrial Development Levy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la kupongezwa sana, lakini pia, Waswahili wanasema; “ukibebwa bebeka.” Viwanda vyetu vya ndani iko haja ya kuona ni kwa jinsi gani bidhaa ambazo inazitengeneza zinakuwa shindani. Kwa maana ya kwamba, ziweze kuwa shindani ndani ya Taifa letu, lakini pia, na nje ya Taifa letu.
Mheshimiwa mwenyekiti, naomba kutolea mfano mdogo wa kiwanda cha vitenge. Kiwanda hiki kinatengeneza vitenge ambavyo vinauzwa kwa bei ndogo, lakini pamoja na hilo, wanawake wa Kitanzania na Watanzania kwa nini wanashawishika kununua vitenge vya shilingi 30,000, vitenge vya shilingi 100,000, mpaka shilingi 300,000? Ni kwa sababu ya ubora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninasema ukibebwa bebeka. Viwanda vyetu vione ni kwa jinsi gani bidhaa ambazo vinazitengeneza zinakuwa shindani. Pale ambapo bidhaa zinakuwa shindani ama zinakuwa na ubora unaotakiwa ni faida ya Watanzania. Kwa mfano, unakuta kwamba, labda kiwanda kama kilianzishwa Pwani, kutokana na ubora wa bidhaa zake, kiwanda hiki kinaanza kujitanua, kinaanza kuwa na branches. Kupitia zile branches ama matawi unakuta kwamba, ajira zinaendelea kuongezeka kwa vijana wetu na hivyo pato letu pia linaendelea kuongezeka. Kwa hiyo, mimi nadhani, iko haja ya Serikali kuona viwanda ni watoto wetu na kuendelea kuvifuatilia. Kadiri ambavyo tunafuatilia tunatengeneza uchumi wetu, lakini pia, tunaongeza Pato la Taifa na tunatengeneza ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba kuongelea suala zima la kuongeza wigo wa makusanyo. Ninaipongeza sana Serikali wigo wa makusanyo haya kadiri ambavyo miezi inaongezeka na miaka inaongezeka tunaona kwamba, yanaongezeka, lakini bado hatujafikia, yaani vile vyanzo vya mapato tulivyonavyo bado hatujavikusanya ipasavyo. Kama tungekuwa tumekusanya ipasavyo, yamkini tungepunguza hii kuumiza kichwa kwamba, tunapata wapi hiki? Tunapata wapi hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naiomba Serikali iweze kuona ni jinsi gani inarasimisha sekta isiyo rasmi. Pia iweze kuona ni kwa jinsi gani mifumo tuliyonayo na taasisi zote zinajiunga na hii mifumo, lakini pia mifumo hii iweze kusomana kwa sababu, ipo lakini haisomani, hivyo inasababisha kuvuja kwa mapato yetu, ninaomba sana Serikali iweze kuliona hili. Mifumo yetu isomane na taasisi zote ziunganishwe kwenye hii mifumo, ili tuweze kupata mapato ambayo yanastahili ama tuweze kukusanya kulingana na vyanzo tulivyonavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo Serikali inaweza ikalifanya, limekwishazungumzwa, lakini na mimi naomba kuwekea mkazo. Kwa jinsi ambavyo tunazunguka kwenye nchi za wenzetu ni jambo ambalo linawezekana, kutumia kadi kwenye malipo yetu, linawezekana kabisa. Tuliweza Kwenda nchi jirani tu hapa, tunashukuru Bunge, kama kamati tulienda pale, tuliona ni kwa jinsi gani ambavyo makusanyo yanakusanywa kupitia kadi ama kupitia, tunaita electronic payment. Sasa kwa nchi yetu tunaona kabisa kwamba, tukiwa kama Watanzania yamkini tunaweza tukaona kwamba, ni jambo gumu, lakini hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kiasi kilekile ambacho ungetoa fedha taslimu, ndiyo hichohicho unakilipia kupitia kadi yako kwa hiyo, ni kitu ambacho kinawezekana kabisa. Naiomba Serikali iweze kuona ni kwa jinsi gani tunaelekea huko kwa sababu mbuyu nao ulianza kama mchicha, tusisubiri mpaka hiki na kile, lakini tunaweza tukaanza taratibu. Kwa mfano tunaweza tukaweka amount kwamba, labda kiwango kinachozidi kiasi fulani kilipiwe kwa kadi, ama kiwango kinachopungua kiasi fulani ndiyo kilipwe kwa fedha taslimu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, unaweza ukahitimisha. Muda wako umeisha.
MHE. STELLA A. IKUPA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ninaomba kuhitimisha kwa kusema kwamba, wakati sasa tunasubiri kuelekea huko kwenye huu ushauri ambao nimeutoa kuna zile namba ambazo zimetolewa, ambazo zipo, zile za TRA ambazo zinakuwa zinatumika labda kama kuna shida unaweza ukaripoti. Naomba namba hizi ziingizwe kwenye mifumo, kama kwenye meseji labda kwamba, tuwe tunatumiwa mara kwa mara. Kwa sababu, unakuta mtu unakumbana na tatizo kwamba, haujapewa risiti, unadai risiti, huna mahali pa kuripoti na hujui unaripoti kwa namna gani. Kwa hiyo, mimi naomba hii namba iwe inazunguka kwenye messages zetu za kila siku, ili kila mwananchi aweze kufahamu kwamba, nisipopewa risiti, naripoti wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naishukuru Serikali kwa hatua kali ambazo inazichukua za kuweza kukabiliana na mauaji ya watu wenye ualbino ambayo yametokea hapa nchini. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, ninaomba tena nitumie Kanuni Na. 60 (11) nichangie nikiwa nimekaa.
NAIBU SPIKA: Tafadhali endelea,
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, moja kwa moja nitaenda kwenye pongezi, napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa utendaji wake mahiri, chini ya Rais wetu mpendwa John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yaliyofanyika ni mengi siwezi kueleza moja moja, pia ninapenda nimshukuru Rais wetu kwa kusikia kilio cha watu wenye ulemavu kwa kutuhamishia Ofisi ya Waziri Mkuu, kilikuwa ni kilio chetu cha muda mrefu, tunashukuru kwamba alisikia ombi letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijikite moja kwa moja kwenye masuala ya watu wenye ulemavu kwa sababu mengi yemeongelewa mambo ya maji watu wanaongelea, barabara, umeme na kadhalika.
Moja kwa moja ninaomba niongelee suala la elimu kwa watu wenye ulemavu. Katika sehemu hii ya elimu ninaiomba Serikali iangalie ni kwa jinsi gani ambavyo inaweza ikawasaidia watu wenye ulemavu hasa katika suala zima la kuongeza shule ambazo ni maalum na ambazo watu wenye ulemavu wanaweza wakapata elimu pasipo kipingamizi chochote. Ukiangalia suala zima la kusema kwamba majengo yaongezwe inaweza ikawa ni ngumu, lakini naiomba Serikali iboreshe majengo yaliyopo kwa upande wa miundombinu pamoja na walimu ili watu wenye ulemavu waweze kupata elimu pasipo vikwazo vyovyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninaomba nizungumzie suala la mikopo kwa watu wenye ulemavu vyuoni. Mimi pendekeza kwa Serikali kwamba kusiwe kuna vipingamizi kwa mtu mwenye ulemavu kupata mkopo ambaye tayari amechaguliwa na chuo fulani kujiunga hapo. Ninaomba sana Serikali iliangalie hili suala la mikopo ili kusiwe kunakuwa kuna vikwazo kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaomba niongelee suala la ajira. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 18 ameongelea suala la ajira lakini ametoa takwimu za vijana. Katika sehemu hii haioneshi kwamba Serikali inatekeleza vipi ile Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 kwa upande wa ajira kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali iangalie ni kwa jinsi gani ambavyo Sheria hii ya mwaka 2010 inatekelezwa hasa katika suala zima la ile asilimia tatu kwamba kila mwajiri awe na asilimia tatu ya watu wenye ulemavu katika wafanyakazi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaomba niongelee suala la mauaji kwa wenzetu wenye ulemavu wa ngozi. Suala hili kwanza napenda niishukuru Serikali na kuipongeza kwa jinsi ambavyo mauaji haya yamepungua kwa kiasi kikubwa, lakini bado kuna taarifa ambazo zinaendele kuripotiwa za kupotea kimya kimya kwa hawa wenzetu wenye ulemavu wa ngozi. Ninaiomba Serikali pamoja na ulinzi ambao inatupatia, pia ijikite katika suala nzima la elimu kwa jamii yetu. Pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge katika Majimbo yao wanapopata fursa ya kukaa na wapiga kura wao watoe elimu hii kwa jamii kuhusiana na suala zima la mauaji kwa watu wenye albinism.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongelee suala la kodi kwenye mishahara ya waajiriwa ambao wana ulemavu. Tumeona kwamba mishahara ya waajiriwa wenye ulemavu imekuwa ikikatwa kodi ninaiomba Serikali iondoe suala zima la kodi kwenye mishahara ya watu wenye ulemavu. Kama tunavyofahamu kwamba ulemavu ni kikwazo, sasa unapokata tena ile kodi ina maana kwamba unampunguzia huyu mtu uwezo wa hata kumwezesha kumpa posho mtu ambaye ni msaidizi wake. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iondoe kodi kabisa kwenye mishahara ya waajiriwa ambao ni walemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la vyombo vya usafiri ambavyo vinaagizwa na watu wenye ulemavu. Kumekuwa kuna sheria kwamba ili mlemavu asamehewe kodi ya chombo alichokiagiza ni mpaka kile chombo kiwe kina vifaa maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Binafsi ni mlemavu, lakini mimi huwa naweza kuendesha gari yoyote ambayo ni automatic, kwa hiyo, ninaomba sheria hii irekebishwe mradi tu kwamba mtu aliyeagiza kile chombo ni mlemavu basi ile kodi asamehewe siyo mpaka kile chombo kiwe na vifaa maalum kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la malipo ya road license kwa vyombo vya watu wenye ulemavu. Naomba Serikali itusamehe kodi hii ya barabara katika vyombo ambavyo tunavitumia sisi watu wenye ulemavu, kwa sababu hili suala lipo ndani ya uwezo wa Serikali ninaamini kabisa kwamba inaweza ikaondolewa na vyombo hivi tukawa hatulipi hii road license badala yake tukawa tunalipa tu insurance.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu. Mfuko huu ninajua kwamba upo na ulishaanzishwa, ninaiomba Serikali kama vile ambavyo imekuwa ikitenga pesa kwa ajili ya barabara, pesa kwa ajili ya umeme, pia Serikali itutengee fungu maalumu kwenye huu mfuko ili huu mfuko uweze kutusaidia sisi watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala zima la Halmashauri na Manispaa hasa kwa wale watu wenye ulemavu ambao hawana kipato chao kujitosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa wafanye utambuzi wa watu wenye ulemavu ambao hawajiwezi na baada ya kufanya utambuzi huu waweze kuwapatia zile shughuli ambazo zinapatikana kwenye Halmashauri zao ikiwemo shughuli mbalimbali kama kuzoa takataka, vyoo vya city, hili limefanyika katika Halmashauri ya Ilala kuna choo kimoja ambacho walitengewa watu wenye ulemavu, kwa hiyo hawa watu wenye ulemavu ambao walikuwa wanaomba barabarani, walikuwa wanapita pale kila asubuhi mtu anachukua shilingi 1,000 kwa sababu kile choo kilikuwa kina uwezo wa kupata shilingi 250,000 kwa siku, hivyo ilipunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la ombaomba wenye ulemavu katika eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri kuna ile asilimia ambayo inawataja wanawake na vijana tu, nilikuwa ninaomba asilimia hii iweze pia kuwataja na watu wenye ulemavu ili weweze kunufaika isiwe general, iwataje na wao kama vile ambavyo inataja vijana na wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya ninaunga mkono bajeti hii ambayo ipo mbele yetu, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na timu ya wataalam wa Wizara kwa hotuba nzuri yenye kuonyesha nuru ya Tanzania ijayo ya viwanda kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 inavyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie katika suala zima la viwanda hasa upande wa ajira kwa watu wenye ulemavu. Ninamuomba Waziri mwenye dhamana aliangalie suala zima la ajira kwa watu wenye ulemavu katika viwanda ikiwa ni utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninaongelea viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Kuna kazi nyingi ambazo zitaweza kufanywa na watu wenye ulemavu hasa za kiufundi na zisizo za kiufundi. Hii itasaidia kupunguza ama kuondoa wimbi la ombaomba ama tegemezi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba pia Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kati ya viwanda vitakavyoanzishwa, kiwepo kiwanda ama viwanda vitakavyokuwa vinatengeneza vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia vifaa hivi saidizi vipatikane kwa gharama nafuu lakini pia ita-create ajira kwa watu wenye ulemavu kwani wengi wao wana utalaamu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali yangu sikivu ya CCM izingatie maombi ama ushauri niliotoa hapo juu. Vifaa saidizi vinauzwa kwa bei kubwa sana ikilinganishwa na uwezo halisi wa watu wenye ulemavu.
Pia ninapenda niongelee suala zima la viwanda na upatikanaji wa umeme ama stability ya umeme nchini. Kama tunavyofahamu viwanda vingi karibu asilimia zote mia vinategemea uwepo wa umeme sana.
Nimuombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya viwanda na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati, washirikiane katika utendaji wao ili suala zima la umeme liweze toa mwelekeo wa uwepo na ustawi wa viwanda nchini kama Ilani ya chama changu cha CCM inavyosema. Ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha atoe ufafanuzi wa mambo niliyozungumzia hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja naomba nianze na pongezi kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa kuendesha zoezi zima la uchangiaji wa damu. Katika ukurasa wa 57 wa kitabu cha hotuba ya Waziri imeonesha ni kwa jinsi gani Tanzania inahitaji damu salama kwa ajili ya wanawake wanaojifungua, lakini siyo tu wanawake wanaojifungua, pia na watu wote wanaokuwa na uhitaji wa damu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya hii Wizara, Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara kwa hotuba nzuri ambayo wameiandaa na kuiwasilisha hapa, lakini pia kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la bajeti la Wizara hii. Kutokana na maelezo ya hotuba hii inaonesha kwamba, mpaka kufikia Machi mwaka huu ni asilimia 31 ambayo tayari Wizara hii ilikuwa imeshapelekewa. Pia kwa upande wa mishahara, inaonesha kwamba ni 4.1 billion ambayo ilikuwa imeshapelekwa kufikia mwezi Machi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja atoe ufafanuzi kwamba hii mishahara kama imetolewa asilimia ndogo hivi, amesema kwamba ni asilimia 37, hawa wafanyakazi ni kwamba wanakopwa ama hawapo labda walipunguzwa ama labda bajeti ya fungu la mishahara lilikuwa kubwa ukilinganisha na wafanyakazi waliopo? Kwa hiyo, naomba ufafanuzi katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala la huduma ya saratani. Naipongeza Wizara kwa mipango yake mizuri kwa mwaka ujao wa fedha. Naomba niishauri Serikali kwamba huduma hii ni muhimu sana, lakini katika hii hotuba tunaona kwamba, kipaumbele kimepewa kwa Hospitali moja ya Ocean Road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhalisia wa nchi yetu ya Tanzania ni kwamba, watu wengi ambao wanatoka pembezoni, hawana uwezo. Kwa hiyo, utakuta mtu anafariki kwa kukosa tu ile nauli ya kumtoa huko mahali alipo na kumpeleka Dar es Salaam kupata hii huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapokuwa mgonjwa anahitaji mtu wa kumsaidia, kwa hiyo, hapo inabidi mtu atafute nauli yake yeye mwenyewe mgonjwa na nauli ya mtu ya kwenda kumsaidia kule Dar es Salaam anapokwenda kupatiwa huduma hii. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwamba hii huduma iboreshwe katika maeneo yote ya Tanzania ili watu wasiwe wanakufa kwa kukosa hata nauli ya kuwafikisha hospitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niishukuru Serikali kwa ajili ya lotion kwa ajili ya watu wenye albinism. Huduma hii inapatikana KCMC. Naiomba Serikali ifanye mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa lotion hizi kwa sababu imekuwa ikipatikana kikanda. Kuna baadhi ya maeneo lotion hizi hazifiki. Serikali ishirikiane na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba huduma hii inapatikana all over the country. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia huduma ya Mifuko ya Bima ya Afya. Sijui nitumie lugha gani rahisi, lakini niseme tu kwamba, Mifuko hii inabagua baadhi ya huduma, yaani baadhi ya gharama. Utakuta mtu ndiyo ameshamwona Daktari vizuri, anapokwenda kuchukua dawa, anaambiwa kwamba hii dawa haigharamiwi na Mfuko huu; ama kuna hili suala zima la vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu. Mifuko hii haigharamii vifaa saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi nikailaumu mifuko hii, nadhani ni zile sera na sheria ambazo zipo. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie ni jinsi gani ya kubadilisha hizi sera na sheria ambazo zinatekelezwa na Mifuko hii ambayo inasababisha baadhi ya huduma kushindwa kutolewa na Mifuko hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee suala zima la wazee. Kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, imeongelea huduma bure kwa wazee. Tunaishukuru Serikali kwa huu mpango na huduma hii ambayo inaendelea, lakini naiomba Serikali iboreshe sana huduma hii, kwa sababu kuna kilio kikubwa cha wazee kwamba wanapofika pale hospitali, kuna baadhi ya huduma ambazo ni nyingi ikiwemo dawa, baadhi ya vipimo kwamba havipatikani kwa sababu tu kwamba, huduma ile inakuwa haipatikani mahali pale. Kwa hiyo, naiomba Serikali iboreshe na iangalie kwa jicho la pekee huduma bure kwa wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, naomba niongelee suala zima la ukatili wa kijinsia. Katika ukurasa wa 89 wa hii hotuba inaelezea takwimu zilizopo, kwa kweli zinasikitisha. Naomba nitumie Bunge lako Tukufu kulaani vitendo vya ukatili kwa watoto pamoja na wanawake. Matukio ni mengi ambayo yameendelea kuripotiwa ya watoto kubakwa, kulawitiwa, lakini pia vipigo ambavyo vinawasababishia watoto hawa na wanawake ulemavu wa maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema namalizia, lakini bado points mbili. Pia naomba Serikali iangalie suala zima la Bima ya Afya kwa watu wenye ulemavu. Kuna msemaji ambaye ametoka kuongea hapa, alikuwa ameshanifilisi lakini naomba nami nitilie mkazo. Kundi hili kiukweli linahitaji Bima ya Afya. Ukiangalia ni kwamba hata mlo wa siku moja inakuwa ni tatizo. Kwa sababu katika kitabu hiki inaonesha kwamba Serikali itahamasisha watu wenye uwezo wa kuchangia Mifuko hii waweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia mtu mwenye ulemavu, anakuwa hana uwezo hata kupata mlo mmoja kwa siku. Kwa hiyo, naiomba Serikali huduma hii ipatikane bure kwa kundi hili la watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa na kuaminiwa na wananchi wa Tanzania kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Nampongeza pia Mheshimiwa Rais kwa kuunda Baraza la Mawaziri lenye ueledi wa hali ya juu wakiwemo Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kuishauri Serikali kupitia Wizara hii likiwemo suala zima la mabalozi wa utalii. Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa kuwa na vivutio vya aina mbalimbali na vingi. Naishauri Serikali iwahimize Mabalozi wetu walio kwenye nchi mbalimbali watangaze utalii na vivutio vyetu ili nchi yetu ipate watalii wengi, iwe ni miongoni mwa kazi na wajibu wa Balozi kutangaza vivutio na utalii wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee ama nishauri kuhusu ulinzi wa Watanzania wanaoishi ughaibuni. Serikali ichukue hatua za makusudi kuhakikisha wananchi ama Watanzania hawa wanaoishi ughaibuni maisha yao yanakuwa salama kwa maana ya uhai. Matukio mengi ya kikatili yameendelea kuripotiwa wanayofanyiwa Watanzania hawa ikiwemo mauaji na vitendo vya udhalilishaji. Serikali ijitahidi kupunguza ama kuondoa kabisa kupitia Balozi zetu vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa Watanzania hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri mwenye dhamana amezungumzia ukarabati wa majengo ya Balozi zetu. Nami naomba nitumie fursa hii kuishauri ama kuomba Serikali ihakikishe inaipatia Wizara hii fedha ya ukarabati wa majengo ya Balozi zetu kama ilivyoombwa na kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018.
Awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ulinzi na mambo mengi ambayo anatujali sisi Waheshimiwa hapa ndani, na hasa mpaka tukafika kipindi hiki kuweza kuchangia mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda niipongeze sana Serikali kwa sababu mimi ni Mbunge ambaye nipo katika kundi la vijana, katika mpango huu Serikali imeonesha ni jinsi gani ambavyo vijana wanaweza wakapunguziwa ugumu ama ukali wa maisha. Ukiangalia katika ukurasa wa 55 limeongelewa suala zima la ajira pamoja na mambo ya biashara, lakini pia yameongelewa na mambo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu mimi ni mlemavu ninaomba niongelee masuala ambayo yanahusiana na watu wenye ulemavu katika mpango huu. Mpango huu ni mzuri na jukumu letu sisi Wabunge ni kuangalia ni mambo gani ambayo yanakosekana ili tuweze kuyaboresha ama tuweze kuyaongezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu mtu mwenye ulemavu ninamuona sehemu moja katika ukurasa wa 55, naomba ni nukuu, kuna hiki kipengele kimeandikwa kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu. Kifungu (d) kinasema kwamba; “Kutenga maeneo maalum ya biashara ili kuwezesha vijana na wenye ulemavu kujiajiri.” Ni hapa tu ambapo ninamwona mtu mwenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishauri ama niiombe serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwamba masuala ya ulemavu ni mtambuka, kwa hiyo ninapendekeza yafuatayo, nitaenda page wise nikianzia na huu ukurasa wa 55 hapa ambapo inaelezea kwamba; “kuendelea kutekeleza programu ya kukuza ajira kwa vijana.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba isomeke kwamba; kuendelea kutekeleza programu ya kukuza ajira kwa vijana na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna suala la kuimarisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana. Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 inaelezea jinsi ya kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu. Mfuko huu ulianzishwa kisheria. Ukiangalia katika hii sheria kifungu namba 57 (1) kinaelezea unazishwaji wake na kifungu kidogo cha (2) kinaelezea vyanzo vya mapato. Katika hivi vyanzo vya mapato fedha inayoidhinishwa na bunge hili ni fedha ambayo ni mojawapo ya chanzo kikubwa cha mapato, kwa hiyo mimi niiombe Serikali kuutengea mfuko huu fedha
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha tatu kinaelezea kazi za mfuko huu. Mfuko huu unakazi nyingi, na iwapo Serikali itautengea fedha kama ambavyo imefanya kwa Mfuko wa Vijana, mfuko huu utasaidia mambo mengi sana ya watu wenye ulemavu zikiwemo tafiti mbalimbali, mambo ya elimu lakini pia uwezeshwaji wa vyama vya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa hivi ni zaidi ya miaka mitatu ama miaka minne hivi vyama vya walemavu havipatiwi hata ruzuku, hivyo uwepo wa mfuko huu utasaidia mambo mengi sana kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakimbia kwaajili ya muda ninaomba niende ukurasa wa 56, niongelee suala la kilimo. Hapa naomba ninukuu, inasema; “kuongeza ushirika wa vijana katika kilimo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba iseme kwamba; kuongeza ushiriki wa vijana na watu wenyeulemavu katika kilimo. Kwa nini ninasema hivi? Ninasema hivi kwa sababu katika maeneo mengi ambayo nimefanya ziara ama nimetembelea watu wenye ulemavu nikakuta ni wakulima, wanalima, kwa hiyo ni vizuri wakajumuishwa katika hili kundi. Watu wenye ulemavu wanalima si kwa kutumia matrekta, wanalima kwa nguvu zao. utakuta ni mtu mwenye ulemavu amekaa chini kabisa lakini analima pale pale chini alipo kaa, mimi nimeshuhudia kwa macho yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo niombe watu wenye ulemavu wajumuishwe katika hiki kipengele ili waweze kupewa elimu ya kilimo pamoja na biashara ili kuweza kuwaondolea ugumu wa maisha, lakini pia kuendelea kupunguza wimbi la omba omba la wenye ulemavu na tegemezi Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niongelee suala la afya. Kwenye suala zima la afya mtu mwenye ulemavu pia anaingia…
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la afya pia ni muhimu sana kwa hili kundi la watu wenye ulemavu kwa sababu hata wakati naendelea na hizi ziara zangu afya ni moja ya vitu ambavyo watu wenye ulemavu waliviongelea na waliiomba sana Serikali iwasaidie kwenye suala la afya. Na pia niliulizwa maswali mengi ikiwemo bima ya afya, kuna watu wenye ulemavu ambao hawajiwezi kabisa.
Kwa hiyo, niiombe Serikali katika mpango huu iingize ama itenge fungu maalumu ambalo litawawezesha watu wenye ulemavu kupatiwa bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niunge mkono hoja, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuleta mapendekezo ya Mpango na Mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi kwa ufupi naomba nijazie vitu vichache ama niungane na wachangiaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu. Mfuko huu ni halali maana uliundwa kisheria ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwemo suala la elimu na kadhalika. Naiomba Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 mfuko huu utengenezwe na kupelekewa fedha za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ruzuku za vyama vyenye watu wenye ulemavu, naomba vyama hivi vipewe ama vipelekewe ruzuku kama ilivyokuwa zamani ama miaka ya nyuma. Vyama vya watu wenye ulemavu vinashindwa kujiendesha na vingine vinaelekea kufa kabisa maana vimekosa fedha za kuviendesha. Naomba sana Serikali yangu ya CCM iliangalie tena na tena suala la ruzuku na Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kifungu maalum kupitia Bunge, Sera, Ajira, Kazi na Walemavu; naiomba Serikali iweke kifungu maalum na kifungu hicho kipewe fedha kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya watu wenye ulemavu. Watu wenye ulemavu wana mahitaji mengi ikiwemo mafuta maalum kwa watu wenye ualbino, baiskeli za miguu mitatu au miwili, fimbo nyeupe, vifaa vya kuongeza usikivu (hearing aids) na kadhalika. Uwepo wa kifungu hicho chenye fedha, utasaidia mahitaji tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, matengenezo ama ukarabati wa shule maalum, vitengo na shule zote za awali, msingi, sekondari na vyuo ili zifae kwa watoto ama wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa vya kufundishia na kufundishiwa (teaching and learning aids), kuna uhaba mkubwa wa vifaa hivi kwa wanafunzi wenye ulemavu. Naiomba Serikali itoe kipaumbee kwa upatikanaji wa vifaa hivi ili WWU (Watu Wenye Ulemavu) waweze kupata elimu ambayo ndiyo mkombozi wa maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkalimani wa lugha ni chakula kwa mlemavu; kiziwi, hivyo naiomba Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 itengwe bajeti na waajiriwe wakalimani hawa (kwenye Televisheni ya Taifa, Hospitali za Serikali, Viwanja vya Ndege, Vituo vya Polisi na kadhalika); kwa vyombo binafsi kama televisheni, hospitali na kadhalika. Serikali itoe tamko la kuviamuru vyombo hivi viajiri wakalimani hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika nchi nzima na ambayo tayari imekwisha kufanyika. Mawaziri hawa ni mahiri, wasikivu na wachapakazi sana. Hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mengi yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na Wizara hii, naomba nishauri yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyombo vya Usafiri kwa Watu Wenye Ulemavu (Mabasi). Ipo haja kwa Serikali kuliangalia hili kwa kuwaagiza wamiliki wa Public Transport kuhakikisha vyombo vyao vinazingatia mahitaji maalum. Hili litawezekana endapo kutakuwa na Sheria ya kuwabana wamiliki hawa wakati wa usajili; kuwa chombo hakitasajiliwa kwa huduma za kijamii kama kitakuwa hakijakidhi vigezo ama kama kitakuwa hakina miundombinu ya kuwezesha mtu mwenye ulemavu hasa wa viungo kupanda pasipo shida yoyote ama pasipo kubebwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndege. Kwa ndege ndogo (kati ya abiria 5 – 25) zinazofanya safari zake ndani ya nchi yetu miundombinu yake si rafiki kwa watu wenye ulemavu kwani upana wa ngazi zake ni mdogo sana na hakuna Ambulift. Ushauri wangu ni; Unguja wana ngazi pana (Uwanja wa Unguja) ngazi hii ni ya mbao, inatumika pale inapotokea mtu hawezi kupanda kwa kutumia ngazi za ndege husika (yaani zile ndege ndogo hasa coastal na kadhalika)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu kumpakia kwenye ndege si sahihi kabisa, hivyo naomba sana Serikali yangu sikivu ihakikishe uwepo wa Ambulift na hizi ngazi za mbao kwenye viwanja vya ndege kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa Ambulift, lift na hizi ngazi za mbao kwa ndege ndogo zitasaidia wagonjwa, wazee na watu wenye ulemavu kutobebwa wakati wa kupanda ndege kitu ambacho ni hatari kwa anayebebwa na anayebeba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, awali ya yote niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya maana Wizara hii ina mambo mengi mno.
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee wakalimani wa lugha ya alama kwa viziwi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri aseme kitu kuhusiana na hili maana Watanzania hawa wako njia panda na hawaelewi kinachondelea. Namwomba sana Mheshimiwa aseme kitu Watanzania viziwi wapone maana wako gizani, wanakosa habari nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee katazo la uchambuzi wa magazeti kwenye redio na televisheni. Nampongeza Waziri kwa katazo hili naelewa kuwa ameangalia maslahi ya wafanyabiashara ila amepitiwa kuangalia makundi mengine hasa wasioona wote Tanzania. Ikumbukwe kuwa uwezo wa kuchapisha nukta nundu kwenye magazeti haupo na ni gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ushauri; kuliko kuendelea kuwaweka gizani Watanzania hawa wasioona kwa kukataza uchambuzi wa magazeti. Naomba Serikali ije na njia ya jinsi gani Watanzania hawa watapata hizi habari ndipo hili katazo liendelee.
Mheshimiwa Spika, vazi la Taifa; mchakato ulishaanza umefikia wapi? Naomba ufafanuzi wa hoja hizi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu ya muda nitaenda haraka haraka. Nikiwa kama kijana, napenda na mimi niweze kuongelea kwa uchache kuhusiana na dawa za kulevya kwa sababu ni janga ambalo linaharibu ama linapoteza nguvu kazi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niiombe sana Serikali kuitengea hii Tume ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya fedha za kutosha na kuipelekea ili iweze kufanya kazi yake vizuri kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee suala la ulinzi kwenye mipaka yetu kwa sababu tunaona kwenye airport nyingi imeshadhibitiwa lakini bado kwenye mipaka yetu ulinzi hauko vizuri. Kwa hiyo, niiombe Serikali iimarishe ulinzi kwenye mipaka ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa vya kitaalamu ambavyo vitaweza ku-detect dawa hizi za kulevya kwa wale wanaopita kwenye hii mipaka yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niongelee suala la elimu hasa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kwanza kabisa, napenda niishukuru Serikali kwa kuweka ulemevu kama ni kigezo kimojawapo cha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Naomba nitoe mapendekezo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa watu wenye ulemavu kwa kuwa idadi ya watu wenye ulemavu ambao wanapata fursa ya kufika chuoni ni ndogo sana, hivyo niombe kabisa Serikali isitoe kama mikopo kwa watu wenye ulemavu bali itolewe kama ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kwa habari ya elimu ya kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha sita. Watu wenye ulemavu ambao wanapata fursa ya kwenda shule ni wachache sana na ipo ndani ya uwezo wa Serikali kuwapa elimu bure watoto wenye ulemavu kuanzia darasa la kwanza ama kindergarten mpaka kidato cha sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niende ukurasa wa 45 wa Taarifa ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Ukurasa huu unaongelea mkakati wa kuongeza walimu. Naomba ninukuu; “Kamati imebaini kuwa, kuna upungufu wa walimu hususani wa masomo ya sayansi na hisabati, hali ambayo imekuwa ikiathiri kiwango cha elimu nchini. Kutokana na hali hiyo, Kamati inaazimia Wizara iandae mkakati maalum wa kuendeleza walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ili kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa wataalamu hao katika masomo hayo.”
Mheshimiwa Mwenyikiti, mimi napendekeza kwamba kifungu hiki kisomeke kwamba; “Kamati imebaini kuwa kuna upungufu wa walimu hususani wa masomo ya sayansi, hisabati na elimu maalum hali ambayo imekuwa ikiathiri kiwango cha elimu nchini. Kutokana na hali hiyo, Kamati inaazimia Wizara iandae mkakati maalum wa kuendeleza walimu wa masomo ya sayansi, hisabati na elimu maalum ili kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa wataalamu hao katika masomo hayo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa haraka haraka, naiomba Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ijitahidi kutembelea shule…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Ikupa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi anavyoisimamia Wizara hii na uchapakazi wake akitumia uzoefu na umahiri mkubwa alionao. Naomba nimpongeze Naibu wake na watendaji wa Wizara hii kwa jinsi wanavyotekeleza majukumu yao.
Kipekee kabisa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano mkubwa alionipa kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja ambao uliniwezesha kutekeleza vema majukumu yangu katika eneo langu la uwakilishi (kundi la watu wenye ulemavu). Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali dogo kuhusu kifuta machozi kwa waathirika wa katazo la usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi, kitatolewa lini? Na je, kitatolewa kwa uhalisia wa gharama walizotumia waathirika hawa? Naomba ufafanuzi wa kina kwa jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wameendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia Wizara hii, hakika naiunga mkono Tanzania mpya ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri mwenye dhamana na kwa weledi mkubwa, juhudi na jinsi anavyojituma kupitia Wizara hii, hakika ni Waziri mchapakazi. Pia niipongeze sana timu ya Wizara kwa jinsi ya utendaji wao na kuwapatia Watanzania tumaini la viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha General Tyre, naomba ufafanuzi wa kina wa kiwanda cha General Tyre kwani maelezo yanayotolewa ama maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa ndani ya Bunge hili na maelezo ya hotuba ya leo yanakinzana. Maelezo kuhusu Kiwanda cha General Tyre kwenye Hotuba za bajeti kwa miaka 2015/2016 na 2016/2017 ni tofauti (kila mwaka yanaletwa maelezo mengine mapya. Naomba ufafanuzi wa kina, maelezo gani ni sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa mtoa hoja anifafanulie wakati anahitimisha hoja yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nipende kumshukuru sana Mungu kwa ajili ya kila mmoja wetu aliyeko hapa ndani kwa sababu ni wengi walitamani kuwepo hapa siku ya leo lakini wameshindwa, si kwamba sisi ni wema sana ila ni kwa
rehema tu za Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie fursa hii kutoa pole nyingi sana kwako Mheshimiwa Naibu Spika, Spika wa Bunge lakini pia kwa Wabunge wote kwa kuondokewa na mpendwa wetu, Mheshimiwa Dkt. Elly Macha. Kundi la watu wenye ulemavu tumepoteza, Tanzania na duniani kote, kwa sababu ikumbukwe mwaka jana Mheshimiwa Dkt. Elly Macha alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Wasioona Duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo aliyoyafanya katika kipindi hiki cha mwaka mmoja ni mengi na yanafahamika.
Mheshimiwa Jenista Mhagama pongezi nyingi, Mheshimiwa Dkt. Possi tulikuwa naye na hata sasa hivi ametuachia alama kwamba hata kwenye upitishaji wa sheria mbalimbali watu wenye ulemavu wanaonekana; kwenye uundwaji wa bodi tunaona watu wenye ulemavu tunaonekana, kwa hiyo Mheshimiwa Dkt. Possi ameacha alama. Nimpongeze Mheshimiwa Mavunde, amekuwa pamoja na sisi kipindi hiki
ambacho Mheshimiwa Dkt. Possi ameondoka, amekuwa ni msikivu sana. Kwa hiyo naomba niwapongeze sana kwa utendaji wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda niishukuru sana Serikali kwa kupatia mwarobaini tatizo la vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kilikuwa ni kilio cha watu wenye ulemavu ama watoto wenye ulemavu lakini Serikali imetoa mwarobaini wake kwa kutatua tatizo hili la vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa asilimia kubwa. Lakini pia katika bajeti ya mwaka huu yapo mambo mengi ambayo yameongezeka ambayo kwa bajeti ya mwaka jana hayakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kuna suala zima, ukisoma kwenye randama ndipo unaona hivi vitu. Wakati napitia randama ndipo nilipoona; kuna suala zima la ununuzi wa madawa, mambo ya ununuzi wa kuni kwa habari ya vyuo vya watu wenye ulemavu, lakini pia bajeti ya chakula imeongezeka kutoka milioni 38 ya mwaka wa fedha huu tunaoumaliza na kufikia milioni 126 kwa mwaka huu wa fedha ambao ndio tunapitisha sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda niipongeze sana Serikali kwa kuwakumbusha tena wakuu wa mikoa kwa habari ya uundwaji wa kamati za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kijiji mpaka mkoa. Kwa nini nasema kuwakumbusha tena; Serikali ilishatoa agizo, nakumbuka
ilikuwa Januari mwaka huu wakati likijibiwa swali langu la nyongeza, Serikali iliagiza kwamba hizi kamati ziundwe. Sasa ushauri wangu katika hili kuwakumbusha tu haitoshi ama kwa sababu agizo tayari lilishatolewa kikubwa ambacho ningeomba ni kwamba ingetolewa time frame, kwamba hizi kamati ziwe zimekwishaundwa ifikapo lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua naomba nitoe mfano mdogo, watu wawili wanaweza wakaja kwangu, mmoja akaniambia Ikupa unatakiwa ufanye kazi hii, akaondoka. Mwingine akaniambia Ikupa ifikapo kesho saa tano asubuhi uwe umekwisha kufanya hii kazi. Kwa vyovyote vile mimi nitafanya haraka sana kwa huyu aliyeniambia kesho ifikapo saa tano asubuhi hii kazi iwe imekwishakamilika. Kwa hiyo, niiombe Serikali itoe time frame kwa habari ya huu uundwaji wa hizi kamati ili pia hawa wakuu wa mikoa waweze kujipanga kwa habari ya bajeti na waweze kutoa kipaumbele kwa habari ya uundwaji wa hizi kamati. Muda hautoshi sana kuelezea manufaa ya hizi kamati lakini nafahamu kwamba Waheshimiwa Wabunge mnafahamu na Serikali inafahamu umuhimu wa kamati hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niipongeze Serikali kwa kuvikumbusha vyombo vya habari kuhusu kutumia lugha ya alama ama kuajiri wakalimani wa lugha ya alama. Nasema kuwakumbusha kwa sababu mwaka jana ilishatolewa time frame na Waziri mwenye dhamana kwamba ifikapo Machi mwaka huu, 2017, hivi vyombo vya habari viwe tayari vinatumia lugha ya alama ama vimeajiri wakalimani wa lugha ya alama lakini sasa kinachotakiwa ni ufuatiliaji, kwamba ni chombo gani ambacho kinatumia lugha ya alama na ni chombo gani ambacho hakitumii na ni kwa sababu zipi. Kwa hiyo naishauri Serikali, kikubwa sasa hivi si kuvikumbusha tena bali ni kuvifuatilia kwamba ni vipi vinatumia na vipi havitumii kwasababu zipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee idara ya watu wenye ulemavu. Wakati napitia kwenye randama idara hii haina kifungu na idara hii ina umuhimu mkubwa sana. Tukiongelea vyuo vya watu wenye ulemavu ambavyo sasa hivi ni vyuo vipatavyo vitano vimekwishafungwa na ni vyuo viwili tu ambavyo vinafanya kazi na vyenyewe kwa kusuasua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara hii ina umuhimu sana, itahudumia vyuo vya watu wenye ulemavu, itahudumia hizi sherehe za Kitaifa za watu wenye ulemavu lakini pia itahudumia mafunzo kwa ajili ya watu wenye ulemavu, jambo ambalo sasa kwa kuinyima idara hii kifungu ama kutokuitengea fedha ina maana inakwamisha ufanisi wa haya mambo ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naendelea kupitia randama inaonekana kwamba hii idara inahudumiwa kwenye hifadhi za jamii; sasa kwenye hifadhi za jamii sio mambo yote ambayo yamekuwa accommodated, mengi yameachwa kwa sababu bajeti ya pale naona pia sio kubwa
sana. Kwa hiyo niiombe sana Serikali idara hii ni muhimu, ipatiwe kifungu na itengewe fedha ili iweze kufanya kazi yake ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee Baraza la Ushauri la watu wenye ulemavu. Baraza hili ni muhimu, kama ambavyo niliuliza swali mwezi Januari na nikajibiwa kwamba litatengewa fedha. Fedha iliyotengwa ni kidogo, ni kiasi cha Shilingi milioni 4.3 tu ndiyo ambayo imetengwa kwenye hili baraza. Fedha hii haitoshi kwa sababu shughuli za baraza ni kubwa, kwa kikao kimoja inaweza ikatumika shilingi milioni nne mpaka milioni tano, kwa sababu lina wajumbe wapatao 20. Sasa kwa kuitengea shilingi milioni 4.3 hii fedha ni ndogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwenye hili eneo la baraza fedha iongezeke angalau ifike hata Shilingi milioni 20, katika Shilingi milioni 20 vikao vinavyofanyika ni vinne. Kwa hiyo, kama vinafanyika vikao vinne ina maana hapo tunakuwa na wastani wa angalau Shilingi milioni tano kwa kila kikao, Shilingi milioni 4.3 ni ndogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ikumbukwe kwamba vyanzo vya fedha vya hili baraza mojawapo ni fedha ambazo zinaidhinishwa katika Bunge hili Tukufu na hiki ndicho chanzo pekee cha uhakika vyanzo vingine ni vya wafadhili; wafadhili si chanzo cha uhakika. Nitoe mfano mdogo, mtoto anakuwa na uhakika wa chakula anachopika mama yake nyumbani kwake na si chakula cha kutegemea kwa jirani. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali itoe hizi fedha, iongezee hili baraza fedha angalau ifike hata Shilingi milioni 20 ili tuwe na uhakika kwamba hili baraza litafanya kazi kama ambavyo niliahidiwa Januari wakati swali langu linajibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu. Mfuko huu ni muhimu na hata wakati nachangia mpango mwezi Januari niliongea, kwamba once huu Mfuko utakapopatiwa fedha mambo mengi ya watu wenye ulemavu yatakuwa solved tofauti na
sasa hivi. Unajua tunachoongelea sasa hivi ni kwa sababu hakuna fedha, ni kwa sababu bajeti inayotengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu inakuwa ni ndogo sana ndiyo maana mambo mengi yanakwama.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, naomba niunge mkono hoja iliyopo Mezani na naomba kuwasilisha.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. IKUPA S. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia machache katika Wizara hizi mbili. Awali ya yote, naomba niiungane na wenzangu ambao wametangulia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa yale makubwa ambayo ameendelea kuyafanya. Pia tumeona mambo mengi yamefanyika ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja. Kwa kweli napenda nimpongeze sana. Kwa ajili ya muda sitaweza kuyataja, lakini naomba tu pongezi zangu zimfikie mahali popote alipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Simbachawene na Mheshimiwa Waziri Angella Kairuki kwa hizi taarifa zao. Nimezipitia kwa ufupi na uchache, mengi yamefanyika, pongezi zangu ziwafikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja naomba niongelee ile asilimia kumi ya vijana na wanawake. Naishukuru sana Serikali kwa kutenga hii asilimia kumi kwa ajili ya wanawake na vijana katika Halmashauri, lakini nina ushauri kidogo kuhusiana hii asilimia kumi na pia nimekuwa nikiongea mara kwa mara, naomba niweke msisitizo tena juu ya hii asilimia kumi. Naiomba Serikali na pia Wabunge wenzangu tuungane katika hili, kwamba hii asilimia kumi igawanywe, angalau basi hata asilimia mbili au hata kama ni asilimia moja iwe ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Kuna siku niliuliza swali, nikaambiwa kwamba hii asilimia kumi unaposema kwamba wanawake na vijana, inaaccommodate na watu wenye ulemavu, lakini kiuhalisia watu wenye ulemavu huwa hawapewi kipaumbele katika
hii asilimia kumi. Ni malalamiko ambayo tumekutana nayo hata katika ziara mbalimbali; ukifuatia kwamba je, hii asilimia kumi mnanufanika nayo vipi? Wanasema hapana, tunapofika pale tunaambiwa kwamba ni kwa ajili ya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba kuna watu wenye ulemavu ambao siyo wanawake na wala siyo vijana; nafiki hapo naeleweka. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iliangalie hili; hii asilimia 10 igawanywe either iwe asilimia mbili kwa walemavu, halafu asilimia nne ibaki kwa
wanawake na asilimia nne ibaki kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee takwimu za watu wenye ulemavu. Kiukweli Tanzania hatuna takwimu halisi. Yaani tunasemea tu kwamba kwa sababu ndivyo ambavyo inajulikana kwamba katika population duniani asilimia kumi inakuwa ni ya watu wenye ulemavu kwa
kila nchi, lakini tunatakiwa kuwa tupate uhalisia wa takwimu halisi za watu wenye ulemavu ili tuweze kupanga bajeti accordingly; kwa sababu sasa hivi tunabaki tu kama tuna hisia hisia, kwa hiyo hata ile bajeti yenyewe ambayo inatakiwa kwa ajili ya mambo fulani kwa ajili ya watu wenye ulemavu, inakuwa ni ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kufanyaje? Kupata takwimu yake, ni rahisi na ambayo inakuwa haina gharama ya aina yoyote. Kwa kuwatumia hao Wenyeviti wa Serikali za Mitaa; nirudie tena kusema kwamba mimi mwenyewe binafsi nimeshawahi kufanya hivyo, yaani ile
kuona kwamba hili jambo linawezekana? Nilimtumia Mwenyekiti wangu wa Serikali ya Mtaa nikamwambia naomba nifahamu, huu mtaa wako una watu wenye ulemavu wangapi? Ilikuwa ndani ya muda mfupi, yule Mwenyekiti akawasiliana na viongozi wake kwa maana ya Mabalozi, kila Balozi akaja na takwimu kwamba mimi katika nyumba zangu nina watu wenye ulemavu kadhaa. Kwa hiyo, mwisho wa siku yule Mwenyekiti akawa na takwimu sahihi kwamba watu wenye ulemavu nilionao kwenye Mtaa wangu ni watu kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku sasa hao Wenyeviti wanaweza wakawa wanakusanya zile takwimu wanapeleka kwa Wakuu wa Wilaya; Wakuu wa Wilaya wanazipandisha mpaka kwenye mikoa, hatimaye tunapata takwimu ya nchi nzima, kwamba watu wenye ulemavu wako wangapi, ambayo haitaigharimu Serikali gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee suala zima la miundombinu kwenye shule zetu kwa maana kwamba shule za msingi mpaka shule za sekondari. Hapa naongea kwa sababu tunaongelea suala zima la inclusive education, tukiongela suala la inclusive education miundombinu bado siyo rafiki.
Kwa hiyo, naendelea kuiomba Serikali iendelee kuboresha hii miundombinu. Hapa naomba niipongeze sana Serikali kwa sababu kuna baadhi ya maeneo nimetembelea kwenye hizi shule za msingi na kuna fedha zimepelekwa kwa ajili ya kurekebisha ile miundombinu. Sasa kupelekea tu ile fedha, haitoshi; nafikiri wakati zile fedha zinapelekwa, pia liwe linatolewa agizo kwamba hii miundombinu inakarabatiwa. Pia mnapokuwa mnafanya ukarabati, mzingatie mahitaji ya watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika kila shule itakuwa ni vizuri sana kukiwa kuna choo ambacho kinaweza kumsaidia mtoto mwenye ulemavu kujisaidia kwa urahisi. Kwa sababu wakati nafanya hizi ziara, nilijaribu pia kuangalia miundombinu ya vyoo. Miundombinu ya vyoo siyo mizuri
kabisa ukiangalia kuna ulemavu mwingine mtu anakuwa anatambaa chini, sasa ukimchanganya, kwamba aende kwenye vyoo vya public na watoto wenzake, inakuwa ni shida sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie hilo pia kwamba hata kama ule ukarabati wa jumla utakuwa labda unachukua gharama kubwa, lakini pia suala la choo lingeanza, ingekuwa nzuri zaidi kwamba angalau kila shule ipate choo ambacho kitamsaidia mtoto mwenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, naomba niongelee suala la TASAF. Naipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo imefanya. Kweli katikati wakati niko kwenye ziara zangu, watu wenye ulemavu walizungumzia sana suala la TASAF kwamba wao wamekuwa wakiachwa na badala yake wanakuwa wakiwekwa watu ambao wana uwezo wao kabisa. Kwa hiyo, naipongeza Serikali, lakini pia naomba katika zile qualifications za kuingizwa kwenye huu mfumo wa TASAF, pia suala la ulemavu liangaliwe kwa maana kwamba ule ulemavu ambao mtu anakuwa hajiwezi kabisa, anakuwa ni maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mmoja amekuwa akinisumbua sana hata sasa hivi, anasema kwamba yeye hana uwezo; nikajaribu kumwambia kwamba hebu basi awasiliane hata na Mwenyekiti Serikali za Mitaa, anaweza akamsaidia kwamba aanzie wapi au jinsi gani anaweza akaorodheshwa kwenye huu mpango; anasema hapana, hawa watu wanapeana, unakuta sisi ambao tunakuwa tuna shida, tunaachwa, wanapeana watu ambao hawana shida. Kwa hiyo, pia naomba Serikali iliangalie sana hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi, naomba kuunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kwa yote yaliyotekelezwa ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja kupitia Wizara hii. Pili niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa utendaji wenu mahiri na jinsi mnavyojituma kulitumikia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee Mental Health Act 2008 sheria namba 28. Sheria hii ipo toka mwaka 2008 lakini mpaka leo ni miaka tisa kanuni hazijatungwa ama kuandaliwa. Kutokuwepo kwa kanuni kumesababisha sheria hii kutoanza kutumika na hivyo kupelekea wagonjwa wa akili na walemavu wa akili kukosa haki zao za msingi. Naomba kufahamu, ni lini kanuni hizi zitaandaliwa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana? Pia kuna upungufu wa madakatari (kuna madaktari 15 tu nchi nzima).
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee msamaha wa matibabu kwa wenye ulemavu. Wakati linajibiwa swali langu Bungeni, Serikali ilikiri kutokuwa na utaratibu wa kuwabaini watu wenye ulemavu wenye vipato duni hivyo kupelekea Watanzania kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali ikubali kuwaingiza watu wenye ulemavu ambao wana vipato duni kwenye huu msamaha wa matibabu. Kwanza iwabaini kwa kuwapatia vitambulisho ili wanapofika hospitali pasiwe na usumbufu kwao. Nafahamu kuna mpango wa Serikali wa kuwapatia Watanzania wote bima ya afya. Naipongeza Serikali kwa mpango huu. Mpango huu ni long term, hivyo ninaiomba Serikali wakati tunasubiri ione ni jinsi gani itawaangalia watu wenye ulemavu kwa masuala mazima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee watoto wenye vichwa vikubwa. Kadi Toto Afya haiwakubali watoto wenye vichwa vikubwa, wanaambiwa wao ni wagonjwa, kadi hii kwa nini inawabagua watoto hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee upungufu wa dawa za walemavu wa akili. Ninaiomba Serikali iongeze bajeti ama itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa za akili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watu wenye ualbino, limekuwa ni ombi la muda mrefu kuwa sunscreen lotion zinunuliwe ama ziagizwe na Serikali kama dawa zingine zinavyoagizwa ama kununuliwa. Ninaiomba Serikali yangu sikivu ilizingatie ombi kwani mafuta haya ni muhimu na ni kama chakula kwa wenzetu wenye ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna uhitaji mkubwa wa vifaa vya ku-detect kansa kwa hatua za awali (Kliogan).Vifaa hivi vitakuwa msaada mkubwa si tu kwa watu wenye ualbino bali kwa Watanzania wote maana kansa imekuwa tishio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa zoezi la ugawaji wa vifaa mbalimbali kwenye hospitali zetu vikiwemo vitanda. Katika vitanda hivi, je Serikali ilizingatia ombi letu la vitanda vya kujifungulia wanawake wenye ulemavu? Kama haikuzingatia kwa kweli wanawake wenye ulemavu tuna uhitaji mkubwa wa vitanda hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye hospitali zetu kuna uhitaji mkubwa wa wakalimali wa lugha ya alama kwa wagonjwa ambao ni viziwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kodi kwenye taulo za kike (pads), ninaiomba Serikali iondoe kodi kwenye taulo hizi kutokana na umuhimu wake na kulinganisha na vipato vya wanawake wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ninaomba ufafanuzi wa hoja zangu wakati mtoa hoja anamalizia.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wenye dhamana ya Fedha na Mipango kwa kazi kubwa wanayoifanya ili kuhakikisha Ilani ya CCM 2015/2020 inatekelezeka. Baada ya pongezi hizi, nina maombi yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uangalie uwezekano wa kuutengea na kuuwekea fedha Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu kama ambavyo Mfuko wa Vijana unatengewa. Mheshimiwa Waziri, Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu (WWU) ni muhimu sana ukatengewa fedha, hii itasaidia sana ustawi wa WWU na hasa ikizingatiwa kuwa wana mahitaji mengi ikiwemo hitaji la mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, fedha iongezwe kwenye Kasma 280400 Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu ambapo mwaka 2017/2018 Kasma hii ilitengewa shilingi 600,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Idara ya Watu Wenye Ulemavu haina sub vote, hivyo ninaomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hili maana mchakato ulishaanza.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
AIBU WAZIRI, OFISI YA WZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kwa ajili ya muda naomba niende haraka haraka nikiwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote mbili za Sheria Ndogo pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee kidogo kuhusiana na hoja ya Kamati ya kutokuwa na mafungu ya moja kwa moja kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kibajeti kwa ajili ya maendeleo ya vijana pamoja na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ikumbukwe kwamba masuala ya watu wenye ulemavu pamoja na vijana ni mtambuka, kwa maana kwamba yapo ambayo yanayoshughulikiwa moja kwa moja na Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini pia yapo yanashughulikiwa na Ofisi ya Mheshimiwa Rais, TAMISEMI, na pia Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Ofisi ya Waziri Mkuu sasa hivi inaendelea na zoezi la kukamilisha uundwaji wa Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu. Mfuko huu utasaidia sana watu wenye ulemavu kwa kuwa mambo mengi ambayo yanahusu watu wenye ulemavu yatakuwa solved, ikiwa ikiwa ni pamoja na tafiti za watu wenye ulemavu, pia mambo ya elimu pamoja na mafunzo kwa watu wenye ulemavu, mambo pia ya ruzuku za vyama vya watu wenye ulemavu na mambo mengine ambayo yanahusu mambo ya ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuna Idara ya Maendeleo ya Vijana, idara hii ina mfuko wa vijana na mfuko huu unasaidia sana kwa habari ya mikopo ya vijana ambao wanafanya biashara mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema vijana ni pamoja na kundi la watu wenye ulemavu, kwa hiyo hii hoja ni ya msingi na kwa ufupi wake nimeitolea ufafanuzi kwa jinsi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haraka haraka tena kulikuwa na hoja kwamba Serikali itenge fedha kwa ajili ya Baraza la Ushauri la Watu Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Baraza la Ushauri la Watu Wenye Ulemavu na hivyo limeendelea kufanya vikao vyake vya kuishauri Serikali kama ambavyo Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu inavyoelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kulikuwa kuna masuala ya utengwaji wa bajeti ya watu wenye ulemavu pamoja na vijana. Kama ambavyo nimeeleza hapa mwanzoni ni kwamba Serikali imeendelea kutenga fedha ingawa….(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii adimu. Nami moja kwa moja niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wameyashughulikia masuala haya ya watu wenye ulemavu kupitia Wizara hii ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako pamoja na Mheshimiwa Stella Manyanya wamekuwa ni mama zetu kwa maana kwamba wamekuwa ni wasikivu sana. Muda wote ambapo tumekuwa tukiwahitaji kwa ajili ya masuala ya watu wenye ulemavu wamekuwa wakipatikana kirahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa ni mpungufu wa fadhila nisipoishukuru Serikari kwa jinsi ambavyo imetoa kipaumbele cha elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu. Kwa sababu ya muda nitataja baadhi ya maeneo na si kwa umuhimu basi hakuna mengine. Kuna ukurasa wa 22 aya ya 45; ukurasa wa 23 aya ya 46, lakini kuna ukurasa wa 26 aya ya 53, hiyo nitaomba niisome kwa sababu ni kitu kigeni kidogo. Inasema:-
“Imeandaa Kiongozi cha Mwalimu wa Masomo ya Sayansi kwa wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu. Uwepo wa kiongozi hiki utasaidia wanafunzi wasioona wa sekondari kwa mara ya kwanza kuwezeshwa kusoma masomo ya sayansi”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni habari njema sana kwa watu wenye ulemavu. Pia shukrani zangu zinaendelea ukurasa 29 aya ya 55 mpaka (56) na ukurasa wa 30 aya ya 57 mpaka 59.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niipongeze sana Serikali, wakati Mheshimiwa Waziri akisoma hotuba yake siku ya Jumamosi alikiri kwamba kuna changamoto ya miundombinu na vifaa saidizi. Niiombe tu Serikali tunaongelea mambo ya elimu jumuishi lakini haiwezi kuwa kama miundombinu haitaboreshwa. Kwa hiyo, niiombe Serikali iiendelee kutoa kipaumbele kwa habari ya uboreshaji wa miundombinu ili elimu jumuishi iweze kuwezekana katika Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hili niombe Serikali kwamba katika vyuo vyetu vya ualimu, kwa sababu sasa hivi kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa elimu maalum, kwa hiyo katika vyuo vyote vya ualimu nchini elimu hii ifundishwe. Kwa hiyo, Mwalimu anapotoka chuoni anakuwa ana ufahamu ama uelewa wa elimu maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapoongelea elimu jumuishi ni pamoja na Walimu, tusipokuwa na Walimu wa kutosha ambao wanafahamu elimu maalum hili halitawezekana. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweke mkazo ama iweke msisitizo kwamba katika vyuo vyote vya ualimu elimu maalum ifundishwe ili mwalimu anapotoka pale anapokwenda shule yoyote ana uwezo wa kumfundisha mwanafunzi mwenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee Walimu wenye ulemavu. Inawezekana Serikali ikawa haina takwimu sahihi za Walimu wenye ulemavu lakini Walimu hao wapo. Kwa hiyo, niiombe Serikali iwe na takwimu sahihi za Walimu wenye ulemavu ili waweze kujua changamoto na mahitaji walionayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pPamoja na ugawaji wa hivi vifaa ambavyo vimegawiwa lakini Walimu hawa wasipoangaliwa itakuwa pia ni kazi bure. Kwa maana kwamba Serikali ikiwa na takwimu sahihi za hawa Walimu wenye ulemavu itawawezesha ili waweze kuwa na sifa, maarifa na weledi kama Walimu wengine. Walimu hao wanahitaji pia kujengewa uwezo kwa njia ya mafunzo. Kwa hiyo, niiombe Serikali pia itoe kipaumbele sana kwa ajili ya mafunzo ya hawa Walimu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee tena kwa mara nyingine kwa sababu nimeshawahi kuongea kwenye Bunge lako Tukufu, kwamba Serikali ione sasa umuhimu wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu ya Tanzania. Kwa nini nasema hivyo? Kila siku hapa tunalalamika kuhusu wakalimani wa lugha ya alama lakini kama hii lugha ya alama itafundishwa kwenye elimu yetu kuanzia darasa la kwanza mpaka form four, huyu mtu tunamuandaa kuwa Mwalimu, Mbunge, Daktari, Polisi, kiongozi wa madhehebu ya dini, kwa hiyo ataweza kuwasiliana na mtu ambaye ni kiziwi kwa urahisi. Kwa hiyo, niombe sana Serikali yangu sikivu ilione hili na kwa hapo baadaye tutengeneze kizazi ambacho kitakuwa kinaweza kuwasiliana na viziwi kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee pia takwimu za watahiniwa wenye ulemavu kuanzia darasa la saba, form four mpaka cha kidato cha sita. Kwa nini nasema hivi? Mheshimiwa Profesa Ndalichako atakuwa ni shahidi hapa katikati nilimsumbua sana kwa habari ya uhamisho wa mwanafunzi ambaye alikuwa na ulemavu. Hizi takwimu za watahiniwa zitasaidia wakati wa selection. Unapomalizika mtihani wa darasa la saba Serikali ikafahamu kwamba tuna wanafunzi wenye ulemavu wa aina hii kwa hiyo watawapangia shule kutokana na aina ya ulemavu walionayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kuwa na takwimu sahihi za watahiniwa wenye ulemavu, hii itasaidia kwa habari ya selection. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Profesa Ndalichako kwamba ule uhamisho ulifanikiwa na mtoto anaendelea na masomo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niishukuru Serikali sana kwa sababu mimi ni mwakilishi wa watu wenye ulemavu kuhusiana na wale watoto mapacha walioungana kule Iringa, Consolata na Maria ambao kiukweli Serikali imesimamia elimu yao na watoto wanakiri kwamba hakukuwa na shida kwao kwa sababu hata wakiwa pale shuleni wakati wa kidato cha sita walijengewa kajumba ambako kalikuwa ni maalumu kwa ajili yao peke yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili niongeze, ulemavu wa jinsi hii, Mheshimiwa Profesa Ndalichako yule mtoto ambaye nilimwomba uhamisho kwa ajili yake, amepangiwa shule ya Jangwani, lakini bado kuna changamoto kwa sababu ulemavu wake unahitaji usaidizi, yaani anahitaji mtu wa kumsaidia hawezi kushika kijiko kula mwenyewe. Kwa hiyo, niiombe Serikali ione jinsi gani ya kuandaa wasaidizi kwenye hizi shule kwamba anakuwepo matroni maalum kwa ajili ya watoto wa jinsi hii. Matroni atamuogesha, atamsaidia kwenda chooni lakini pia atamsaidia hata chakula na kumfulia nguo. Kwa hiyo, niombe Serikali pia hili iliangalie kwa jicho la tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na si kwa umuhimu naomba niongelee Bodi ya Mikopo. Nimekuwa nikiomba na imekuwa ni kilio changu cha muda mrefu kwamba wanafunzi ama watoto ambao wanafanikiwa kufika kidato cha tano na sita mpaka kufika chuoni ni wachache sana. Kwa hiyo, hii elimu bure inayotolewa naomba Serikali itolewe bure kwa watu wenye ulemavu yaani mtoto mwenye ulemavu kama atafanikiwa kuingia kidato cha tano na mpaka kufika chuo, asomeshwe bure na Serikali kwa sababu wako wachache. Kwa hiyo, hata gharama ni ndogo haitakuwa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ya kwangu kwa leo ni hayo, naomba kuwasilisha. Naunga mkono hoja ya Wizara hii. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE.STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Naomba niendelee kumshukuru Mungu kwa ajili ya muda huu, lakini pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais akisaidiwa na Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo anaendelea kuitekeleza Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi. Pia naomba niendelee kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri wake na timu nzima ya Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja naomba niongelee huduma kwa wastaafu. Napenda niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo imeboresha mfumo wa malipo ya pensheni kwa wastaafu wetu, lakini pia naungana na maoni ya Kamati kuhusiana na wastaafu ukurasa wa 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili nina ushauri ufuatao:-
Serikali ni kweli imeongeza kima cha chini kwa pensheni kwa wastaafu wetu na kufikia laki moja. Kima hiki cha chini ukiangalia na uhalisia wa maisha ya sasa hivi ni kidogo sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali ama naishauri Serikali kima hiki kiendane na uhalisia wa maisha. Pia Serikali iangalie kwamba mtu anapokuwa mzee na gharama zinaongezeka. Ndiyo katika umri huu ama muda huu ambapo mtu anakuwa na magonjwa anahitaji kujitibia lakini pia anakuwa anahitaji ale hata lishe bora tofauti na mtu wa kawaida unaweza tu ukala ugali na maharage siku imepita lakini kwa Mzee anahitaji kula vizuri na anahitaji huduma za matibabu. Naomba Serikali iliangalie hili iendee kuboresha pensheni kwa hawa wastaafu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee pia msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wenye ulemavu. Ikumbukwe kwamba watu hawa walio wengi ama walio wachache pia wameamua kujitoa kwenye eneo la utegemezi na kuona kwamba wajishughulishe na biashara, aidha, wameona kwamba wasiwe ombaomba. Kwa hiyo naiomba sana Serikali iondoe kodi kwenye biashara za watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala la zima la kodi kwa vyombo vya moto vinavyotumiwa na watu wenye ulemavu yakiwemo magari ama kama ni bajaji. Katika eneo hili naishukuru Serikali kwamba inatoa exemption kwa vyombo vile ambavyo vimefungwa vifaa maalum vinavyoonesha kwamba chombo hiki kinatumika na mtu mwenye ulemavu, ikumbukwe kwamba kuna mtu mwenye ulemavu mwingine ambaye anaendeshwa ama anasaidiwa kwa mfano ukichukulia mtu ambaye haoni, kwa vyovyote vile lazima ataendeshwa na mtu anayeona, sasa ukimfungia kifaa maalum, halafu atakitumiaje hii inakuwa haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie tu kwamba kama kifaa hiki kinatumika na mtu mwenye ulemavu isiangalie kwamba lazima hiki chombo kiwe kimefungwa kile kifaa maalum kwa mtu mwenye ulemavu. Kwa mfano, mimi naendesha gari mwenyewe lakini gari yangu haina vile vifaa maalum ambavyo vinatumika na watu wenye ulemavu, kwa hiyo sasa nisinyimwe exemption kwa sababu tu ile gari haijafungwa vile vifaa maalum, naomba sana Serikali iondoe kodi kwenye hivi vyombo vinavyotumika na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la road licence hata mwaka jana wakati nachangia bajeti hii niliongelea hilo pia. Serikali itoe msamaha wa road licence kwa watu wenye ulemavu. Kwa nini nasema hivyo kwa mfano mtu kama mimi natumia gari ambalo kwangu siyo luxury ni hitaji la lazima. Kwa hiyo Serikali inaponitoza kodi ya road licence kwenye gari yangu ina maana kwamba inalipisha ile miguu. Gari pale inasimama badala ya miguu ya mtu mwenye ulemavu ama inasimama badala ya hata macho kwa mtu mwenye ulemavu. Kwa hiyo, road licence iondolewe kwenye magari ama vyombo vinavyotumika na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na si kwa umuhimu natoa rai kwa Watanzania wenzangu, kumuunga mkono Rais wetu katika juhudi za ulipaji wa kodi kwa kudai na kutoa risiti pale ambapo mauzo na manunuzi yanapofanyika. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu bado kuna wimbi kubwa la udanganyifu kwenye suala zima la kodi. Unaenda dukani ama kwenye kituo cha mafuta unadai risiti, mtu anakwambia mashine ni mbovu, ukipita tena siku nyingine anakwambia mashine ni mbovu. Hawa wafanyabiashara hizi mashine za EFD wanazo ila wanatumia hii ya kusema kwamba mashine ni mbovu kama ni njia ya ukwepaji wa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie hili, kuna wafanyabiashara wanakwepa ulipaji wa kodi kwa kudanganya kwamba mashine ni mbovu. Niwaombe sana Watanzania tuwe na uzalendo katika ulipaji wa kodi. Mambo mengi leo tunaona kwamba hayaendi kwa
sababu makusanyo yanakuwa si mazuri na ni madogo kwa sababu sisi wenyewe hatuwajibiki katika suala zima ya ulipaji wa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. STELLA A. IKUPA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana pamoja na Naibu wake kwa kuchapa kazi na jinsi wanavyojitoa kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa salama (ulinzi wa nguvu kazi ya Taifa letu). Pili, niwapongeze watendaji wote wa Wizara hii wanaowasaidia Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi; utambuzi wa watu wenye ulemavu wenye vipato duni ili waweze kupatiwa vitambulisho kwa ajili ya matibabu tofauti na ilivyo sasa ambapo mtu mwenye ulemavu mpaka apatiwe barua ya utambulisho. Madhara ya barua ya utambulisho ni pale mtu mwenye ulemavu anapougua ghafla usiku ama akapatwa na ugonjwa akiwa nje ya eneo linalomtambua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kuwa Wizara iliangalie hili na ikiwezekana zoezi hili liende sambamba na zoezi linaloendelea sasa la kuwapatia vitambulisho wazee.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema jambo tajwa hapo juu, naunga mkono hoja hii ya hotuba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote niseme nitajikita zaidi upande wa UKIMWI na niseme kwamba UKIMWI bado upo kwa hiyo, ni jukumu la kila mtu binafsi kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI kwa kubadili tabia, lakini pia kuendelea kujilinda na zile njia nyingine ambazo zinasababisha maambukizi ya UKIMWI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja za Kamati, Kamati imeshauri kwamba hii sera ya Taifa ya udhibiti wa maambukizi ya UKIMWI imepitwa na wakati. Niseme kwamba mchakato wa mapitio ya sera hii ulianza kufanyika toka mwaka 2010. Baada ya mapitio haya, iligundulika kwamba kuna upungufu na upungufu huu uliwasilishwa kwenye Secretariat Cabinet ambapo katika ile Secretariat Cabinet ilishauri kwamba ufanyike uthamini mpya wa utekelezaji wa sera hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi kinachofanyika ni kwamba TACAIDS wanaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuona kwamba sasa lile agizo ambalo lilitolewa la upitiaji upya wa hii sera unafanyika. Kwa kipindi hiki cha mpito, Serikali imeendelea kutekeleza vile vipengele ama ule upungufu ambao ulionekana katika mapitio ya hii sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee suala la ushauri ambao umetolewa na Kamati kwa habari ya vile vyanzo vya Mfuko wa udhamini wa Mfuko wa UKIMWI. Kamati imependekeza kwamba kama ilivyo kwenye Road Fund, basi huu Mfuko kuwe kuna tozo ambayo itakuwa inasaidia kutunisha huu mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepokea ushauri huo na tayari utekelezaji umeshaanza kufanyika na naamini kwamba mapendekezo yatakapoletwa kwenye Bunge lako Tukufu basi Waheshimiwa Wabunge wataunga mkono utekelezaji wa hayo mapendekezo ambayo yatakuwa yameletwa kwa habari ya zile tozo ambazo zitakuwa zimependekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali pia imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha udhibiti wa masuala ya UKIMWI. Fedha hizi mpaka kufika mwaka jana Desemba, 2017, kiasi cha shilingi bilioni 1.3 zilikuwa zimekwishatolewa kwa ajili ya kuhakikisha masuala ya UKIMWI yanaenda vizuri. Fedha hizi zimekuwa zikitolewa kupitia Wizara ya Afya ambapo mwaka jana ilitolewa milioni 660 ambayo ilitumika kununulia dawa za septrine kwa ajili ya waathirika wa UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la data za maambukizi katika nchi yetu ya Tanzania imekuwa ni changamoto. Kuna Mbunge ambaye alichangia mchana akasema kwamba hizi data ni za miaka mingi. Niseme kwamba hizi data sio za miaka kumi iliyopita kama ambavyo Mbunge amesema, hizi data ni za mwaka jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani mwaka jana tarehe 1 Desemba hizi ndio data ambazo zilitolewa na hiyo ni sambamba na hoja ya Mheshimiwa Mjumbe wa Kamati, Mheshimiwa Masoud kwamba Dodoma sio kweli kama ambavyo iko. Hizi ni data ambazo zimetolewa mwaka jana tu Desemba na Dodoma ina maambukizi ya 5.0, sasa hizo za kwako sijui ni za lini lakini kutokana na hizi data za mwaka jana Dodoma inaonesha kwamba kiasi cha maambukizi ni 5.0.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Mjumbe alichangia kuhusiana na Njombe kwamba Njombe wanaonewa, hizi ni data halisi na Njombe inasemekana kwamba maambukizi ni kiasi cha asilimia 11.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote natoa pongezi nyingi kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mengi ambayo yametekelezwa katika kipindi hiki kifupi cha uongozi wake akisaidiwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Naibu Mawaziri wake wawili pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi wanavyojitoa kuhakikisha sekta inafanya vizuri na kuleta tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mapendekezo/maombi yafuatayo sambamba na mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vingi kama siyo vyote vya usafiri (public transport) havina miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu hali inayopelekea wengi wao kushindwa kusafiri toka sehemu moja mpaka nyingine au kutumia gharama kubwa kwa kutumia usafiri wa kikundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri/mapendekezo/ maombi kwa changamoto hii, kuwe na ukaguzi wa miudnombinu itayowezesha mtu mwenye ulemavu kupanda pasipo shida yoyote ama kuwe na ukaguzi maalum wakati wa uagizaji wa vyombo hivi nchini/miundombinu (uwepo wa miundombinu hii) iwe ni kigezo kimojawapo cha mtu anayetaka kufanya biashara ya usafirishaji kukidhi kabla ya kupewa leseni ya usafirishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii pia ipo kwenye usafiri wa treni zinazosafirisha abiria ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Watu wenye ulemavu wanashindwa kutumia usafiri huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba zinaweza kutengenezwa ngazi ambazo zitasaidia watu wenye ulemavu kuitumia anapohitaji kupanda. Vilevile nashauri kuwe na msisitizo wa sheria kwenye majengo mapya pamoja na miundombinu ya barabara mpya zinapojengwa vikidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, zinapotokea fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika Wizara hii, ni ombi langu kwamba kundi hili lifikiriwe. Fursa hizo ni pamoja na ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba upatikanaji wa habari na mawasiliano uwe rafiki kwa watu wenye ulemavu hasa wasioona na viziwi kwa kuzingatia matumizi ya lugha ya alama na maandishi ya nukta nundu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote, napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipatia kibali cha kuweza tena kuzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu na ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia hoja ya bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ambavyo imewasilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye ndiye Waziri wangu na dada yangu mpendwa kwa miongozo ambayo wameendelea kunipatia ambayo inaniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya kila siku nikiwa kama Naibu Waziri ninayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba pia nimshukuru sana Mheshimiwa Antony Peter Mavunde, Naibu Waziri mwenzangu. Kiukweli ushirikiano anaonipatia unaniwezesha kutekeleza majukumu yangu kila iitwapo leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia hotuba hii na sana sana nitajikita katika kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge lakini ufafanuzi mwingine utatolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu pamoja na Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu. Uanzishwaji wa mfuko huu ni hitaji la kisheria, Sheria Na.9 ya mwaka 2010 inaeleza wazi kwamba ni lazima kuwe na Mfuko ambao unashughulikia maendeleo ya watu wenye ulemavu. Mfuko huu una faida nyingi ikiwa ni pamoja na kusaidia kufanya tafiti za watu wenye ulemavu, lakini pia elimu ya watu wenye ulemavu pamoja na mafunzo yaani vocational training kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya fedha vya Mfuko huu ni pamoja na fedha ambayo inatengwa na Bunge lako Tukufu, lakini pia fedha ambayo inatokana na wadau mbalimbali. Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwaka huu wa fedha tayari imekwishatenga fedha ambazo zitasaidia sana katika uanzishwaji wa huu Mfuko.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara taratibu zitakapokamilika za kuanzishwa kwa huu Mfuko utazinduliwa rasmi. Nitoe rai kwa wadau mbalimbali wa masuala ya watu wenye ulemavu kwamba Mfuko huu utakapokamilika kuanzishwa basi wajitokeze kuuchangia kwa sababu chanzo kimojawapo cha fedha za huu Mfuko ni wadau mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ilijitokeza pia hoja kwamba tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda basi Serikali ihakikishe inajali kundi la watu wenye ulemavu kuona kwamba wanapatiwa ajira. Pia hili ni takwa la kisheria. Sheria Na.9 ya mwaka 2010 kifungu cha 31 kinaeleza wazi kwamba waajiri wanatakiwa kuajiri watu wenye ulemavu yaani mwajiri ambaye anakuwa na waajiriwa kuanzia 20 na kuendelea basi ahakikishe kwamba asilimia tatu inakuwa ni watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu kama Serikali imepokea ushauri huu na itaendelea kusimamia sheria hii kuona kwamba waajiri wanaajiri watu wenye ulemavu kwenye viwanda vyao ili na wao waweze kufaidi keki yetu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nitoe rai sana kwa waanzishaji wa viwanda kwamba wazingatie miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Tunaposema miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu hatumaanishi tu kwamba zile ramp maana yake tukisema miundombinu watu wanafikiria kwamba inakuwa tu ni ramp. Unapokuwa umeanzisha kiwanda chako na uka-install zile mashine zako kwa jinsi ambavyo mtu mwenye ulemavu hawezi kuzitumia tayari umeshamwekea kikwazo. Kwa hiyo, niombe sana waanzishaji wa hivi viwanda wazingatie miundombinu ambayo itakuwa ni rafiki ili watu wenye ulemavu waweze kuajiriwa katika viwanda vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ambavyo tumesikia kwenye hotuba yake imeanzisha kanzidata ambayo itakuwa inajumuisha wale wahitimu wote wenye ulemavu ambao wamehitimu kutoka kwenye vyuo mbalimbali. Kanzidata hii itasaidia sana kuweka mfumo rahisi kwa watu wenye ulemavu kuweza kuajiriwa na kupata ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaendesha Programu ya Kukuza na Kurasimisha Ujuzi na katika programu hii na watu wenye ulemavu pia ni miongoni mwa watu ambao ni wanufaika na wataendelea kunufaika. Kupitia programu hii watu wenye ulemavu wataweza kukuziwa ujuzi wao na kurasimishiwa ujuzi ambao utawawezesha kujiajiri na kuajiriwa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja ya uboreshaji wa vyuo vya watu wenye ulemavu. Hivi vyuo ni vile vyuo ambavyo vinatoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu, Serikali imeendelea kuviboresha vyuo hivi. Kama tunavyofahamu kwamba vyuo vilikuwa vingi na kama vinne hivi bado havifanyi kazi, lakini Serikali imejikita kuhakikisha kwamba Chuo cha Yombo na Singida kinapewa miundombinu ambayo inakuwa ni rafiki kwa kukarabatiwa kupitia Serikali yenyewe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukarabati unaendelea kufanyika lakini pia Serikali inahakikisha kwamba vyuo hivi vinakuwa na vifaa ambavyo vinatakiwa, vifaa saidizi, vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili sasa iwe rahisi kwa watu wenye ulemavu kuweza kupata mafunzo stahiki sambamba na mahitaji yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee hoja ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge ya upungufu wa Walimu, walezi, wapishi pamoja na walinzi kwenye shule zetu za watoto wenye ulemavu. Nikiri wazi kama Serikali kwamba ni kweli tatizo hili lipo ama upungufu huu upo. Hata hivyo, Serikali yetu sikivu tayari Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Mheshimiwa Rais – TAMISEMI ilishafanya kikao Januari, 2018 ambapo tulijadili changamoto nyingi ambazo zinawakabili watu wenye ulemavu ikiwemo changamoto hii ambayo imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba changamoto hii imechukuliwa na inafanyiwa kazi na Serikali yetu sikivu. Kutokana na ukubwa wa tatizo si kama hili tatizo litakuwa solved kwa muda mfupi, lakini Serikali yetu tayari imeshaanza kulifanyia kazi kuona kwamba hawa walimu, wapishi pamoja na walezi na walinzi basi wanaweza kupatikana katika haya maeneo ambayo yameainishwa kwa maana ya shule za watoto wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia kuna hoja kwamba Serikali sasa ilete sheria kwa sababu matamko yamekuwa ni mengi kwa ile asilimia 10. Niseme kwamba ushauri huu Serikali imeupokea na itaufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja kwamba vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu viendelee kutolewa maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya vijijini kwa sababu maeneo ya vijijini yameonesha kwamba yana uhitaji mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Serikali yetu sikivu imelichukua hili na itaendelea kusambaza vifaa hivi kama ambavyo tumeona katika shule mbalimbali ikiwemo shule za vijijini vifaa hivi vimeendelea kusambazwa kwa wanafunzi. Pia nafasi inapopatikana tumeona kwamba vifaa hivi vimekuwa vikitolewa hata kwa watu wenye ulemavu ambao pia siyo wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia pendekezo kwamba VETA itoe kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya kupata zile stadi za mafunzo. Niseme kwamba kama Serikali tumelichukua pendekezo hili na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na hoja kwamba kuna idadi kubwa ya watu wenye ulemavu ambao wanakaa vijijini, hivyo Serikali iangalie jinsi gani ya kuwawezesha kwa kuwatengea fedha. Hilo kama Serikali pia tumelichukua kama ushauri na tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kwa hoja ambazo nilikuwa nazo nimeweza kuzikamilisha na niseme kwamba naunga mkono hoja iliyopo mbele yetu ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ambavyo imewasilishwa. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. IKUPA S. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kwa miongozo yake ambayo imepelekea nchi yetu kuendelea kuwa na amani na utulivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Masauni kwa kazi kubwa wanazozifanya na jinsi wanavyojitoa kwa ajili ya Taifa letu. Baada ya pongezi hizo nina maombi au ushauri ufuatao kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; zoezi la ukamataji mtu mwenye ulemavu unapotenda kosa sambamba na uwekwaji ndani (mahabusu). Mikataba ya Kimataifa tuliyosaini kama nchi sambamba na sheria na sera ya watu wenye ulemavu inataka kuwe na utofauti wa ukamataji wa nguvu inayotumika kati ya mtu mwenye ulemavu na asiye na ulemavu. Pia mtu mwenye ulemavu awekwe kwenye mahabusu au magereza inayoendana na ulemavu wake, miundombinu iwe rafiki kwa watu wenye ulemavu, mahabusu na magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; vibali vya mikutano ya hadhara vizingatie kundi la watu wenye ulemavu. Utolewaji wa vibali vya mikutano ya hadhara uzingatie uwepo wa ama matumizi ya lugha ya alama. Mwombaji kibali aoneshe kama kunakuwa na mkalimali ama wakalimali kwenye mkutano wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na utaratibu pia wa kutenga maeneo maalum ambayo yatatumika ama yatakaliwa na watu wenye ulemavu kwenye mikutano hii, hii itawafanya watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu kwenye mikutano hii tofauti na ilivyo sasa ambapo ushiriki wao ni mdogo kwa kuhofia usalama wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; vitambulisho vya Taifa viwe na kipengele kinachoonesha ama kumtambua mtu mwenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kabla sijaendelea naomba niunge mkono hoja hii iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa upendeleo mkubwa alionipatia na kuweza kuingia tena ndani ya Bunge hili ambalo mimi ni mara yangu ya pili, Bunge la Kumi na Mbili. Pia naomba nitumie nafasi hii kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi kwa kuweza kutenga nafasi maalum kwa kundi la watu wenye ulemavu, nafasi ambazo zilikiwezesha chama kunichagua mimi kuwa Mbunge wa Bunge hili la Kumi na Mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana akinamama wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa jinsi ambavyo wameendelea kuniamini, pia akina mama wa UWT, Baraza Kuu ambao wameniwezesha tena kuingia ndani ya Bunge hili niweze kuwakilisha wanawake, watu wenye ulemavu pamoja na Watanzania wote kwa ujumla. Ahsanteni sana akinamama, nawaahidi ya kwamba sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nitumie nafasi hii kuishukuru sana familia yangu, lakini pia watumishi wa Mungu ambao wamekuwa wakiniombea mchana na usiku, maombi ambayo yameniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo kila iitwapo leo. Naomba niendelee kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli, jembe letu, tingatinga kwa ushindi mkubwa ambao ameupata katika uchaguzi uliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kuwaza kwa sauti, hivi Watanzania tungekuwa ni watu wa aina gani na kwa kweli niseme hata shetani angeweza akatushangaa kumnyima kura Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa hospitali hizi alizotujengea, lakini kwa umeme huu aliotuletea, barabara na pia kwa jinsi ambavyo alihakikisha kwamba kizazi chetu kinasimama imara kwa kukomesha dawa za kulevya. Kwa jinsi ambavyo ameweza kusimamia vitendo vya rushwa na kutokomeza kabisa rushwa ndani ya Taifa letu. Hakika shetani angeweza kutushangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya, lakini katika hotuba zake, nimesoma hotuba yake vizuri, nimeirudia tena hotuba yake ya mwaka 2015 na ya 2020. Hotuba hizi zimejieleza vizuri na zinaonesha kabisa ni kwa jinsi gani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amedhamiria kulitoa Taifa letu kutoka sehemu moja na kulipeleka sehemu nyingine lakini pia ameweza kuonesha kwa vitendo katika awamu yake ya miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana tukiwa kama Watanzania, lakini pia kwa kundi la watu wenye ulemavu hatuna budi kuendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jinsi ambavyo ameendelea kuyasimamia masuala ya watu wenye ulemavu na kuhakikisha kwamba kundi la watu wenye ulemavu na lenyewe linapata heshima katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri mambo mawili kwa upande wa kundi la watu wenye ulemavu na hasa kwenye eneo la matibabu. Wakati wa kampeni niliweza kutafuta kura pia kwenye kundi la watu wenye ulemavu na changamoto mojawapo ambayo waliiongelea ilikuwa ni changamoto ya matobabu ambapo hapo kabla kulikuwa na utaratibu ambao ulikuwa unatumika, utaratibu wa utambulisho. Yaani mtu mwenye ulemavu anapoumwa yule ambaye hana uwezo, basi anaenda kwa mtendaji wa Kijiji ama Mwenyekiti wa Kijiji na hatimaye anaweza kutibiwa. Waliweza kuniambia kwamba utaratibu huu sasa hivi hauko vizuri sana, kwa hiyo suala la matibabu kwao inakuwa ni changamoto. Niiombe Serikali sana iweze kuuhuisha utaratibu huu wakati tunasubiri sasa ule mfumo wa Bima ya Afya kwa watu wote ili sasa kundi hili la watu wenye ulemavu liweze kunufaika na utaratibu wa matibabu kwa wale ambao hawana uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nitumie nafasi hii kuweza kuishauri Serikali na kuiomba na kuungana na Wabunge wenzangu waliotangulia kwenye eneo la TARURA.
Tumeona kwamba mabadiliko ya tabianchi yameendelea kutuathiri sana na hivyo mvua za mara kwa mara zimekuwa zikiathiri miundombinu yetu. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kuipa nguvu kubwa TARURA ili sasa hii miundombinu yetu iweze kuwa vizuri wakati wote. Mara nyingi tunapokuwa tunawasiliana na TARURA kama Wabunge wanalalamikia changamoto ya bajeti, kwa hiyo niiombe sana Serikali iweze kuliangalia hili na kulipa kipaumbele ili sasa miundombinu yetu iweze kuwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuendelee kumwombea Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili aendelee kuliongoza Taifa letu na Mwenyezi Mungu aendelee kumpa hekima na maarifa ya kuliongoza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi awali ya yote ninaomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ulinzi wake katika kipindi chote cha miaka ambayo nimekuwa ndani ya Bunge lako tukufu toka 2015.
Mheshimiwa Spika, lakini pia nitumie kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kumsaidia kwenye eneo hili la watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo Serikali yake imeweza kumdhamini mtu mwenye ulemavu na kuhakikisha kwamba mambo mbalimbali ya watu wenye ulemavu yanashughulikiwa na hatimaye ustawi wa mtu mwenye ulemavu kuweza kuonekana iliwa ni pamoja na kumjumuisha kwenye maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Rais hatuna kitu cha kukulipa sisi kama watu wenye ulemavu zaidi ya kuendelea kukuombea afya njema lakini pia ulinzi, pia baada ya hapa maisha ya hapa dunia ninaamini kuna maisha mengine basi usima wa milele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu ninakushukuru sana kwa miongozo ambayo umeendelea kunipatia na hatimaye nimeweza kutekeleza majukumu yangu vizuri na kuendelea kukusaidia kwenye eneo hili la watu wenye ulemavu, Mheshimiwa Waziri Mkuu ninakushukuru sana nimeweza kufurahia vizuri maisha ndani ya ofisi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Jenista dada yangu kwa jinsi ambavyo ameendelea kuniongoza kwa jinsi ambavyo ameendelea kunielekeza sita koma kumshukuru kwa kweli amekuwa ni dada yangu mzuri sana na kuniongoza katika utendaji wangu wa kazi Mheshimiwa Jenista nakushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia sambamba na hilo nikushukuru Mheshimiwa Angella Kairuki, dada yangu kwa jinsi ambavyo umeendelea kuniongoza na kunipa maelekezo mbalimbali niweze kukushukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu Mheshimiwa Antony Peter Mavunde kwa ushirikiano mkubwa ambao umenipatia katika kutekeleza majikumu yangu ndani ya ofisi ya Waziri mkuu nikushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika wewe mwenyewe pamoja na Naibu Spika kwa jinsi ambavyo mmeweza kuliongoza Bunge letu, pia kwa jinsi ambavyo umeyashughulia masuala ya watu wenye ulemavu tunaona umehakikisha kwamba maeneo mbalimbali ndani ya viwanja hivi vya bunge yanakuwa ni rafiki kwa watu wenye ulemavu ninakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana makatibu wakuu ndani ya ofisi ya Waziri Mkuu, makatibu wakuu wako watatu, kipekee kabisa nikushukuru Adrew Masawe umenipatia sana ushirikiano mkubwa sana katika kutekeleza majukumu yangu. Ninaomba nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi za kuweza kutenga nafasi mbili za watu wenye ulemavu ambazo zimeniwezesha kuingia mimi na Mheshimiwa Amina Mollel pacha wangu Mbunge machachari hakika amekuwa akifuatilia vizuri utekelezwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru wakinamama UWT Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia UWT ngazi ya mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na visiwani. Ninaenda haraka haraka kwa sababu ya muda naomba nijikite sasa kwenye hoja zilizotolewa na waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ambayo inaitaka Serikali kuweza kuimarisha kitengo cha watu wenye Ulemavu pia Baraza la Ushauri kwa watu wenye ulemavu, kushughulikia migogoro ya vyama vya watu wenye ulemavu. Serikali ya Awamu ya Tano tunaposema kwamba imetekeleza imetekeleza masuala ya watu wenye ulemavu imetekeleza kweli kweli na inaendelea kuyatekelez kwa kishindo.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la kitengo cha watu wenye ulemavu tumeendelea kuhakikisha kwamba fedha zinatengwa rasilimali fedha zinatengwa kwa ajili ya kitengo hiki kupitia kifungu cha 2034, lakini pia tumeendelea kukipatia vitendea kazi vya kisasa kitengo hiki. Sambamba na hilo tumeongeza watumishi katika kitengo hiki ikiwa ni pamoja na kuteuwa kaimu mkurugenzi wa kitengo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa baraza Serikali imeweza kulizindua Baraza la Ushauri kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa lilikuwa limemaza muda wake. Mheshimiwa Rais aliteua Mwenyekiti na hatimaye Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aliweza kuteua wajumbe wa baraza hili na baraza hili liliweza kuzinduliwa mwezi Juni, 2019 na linaendelea kutelekeza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na pia tumeendelea kulitengea fedha.
Mheshimiwa Spika, pia kwa upande wa migogoro ya watu wenye ulemavu tumeendelea kuvifuatilia vyama hivi na kuvishauri kuhakikisha kwamba vinatekeleza katiba ambazo vimeweza kujiwekea vyenyewe. Katika hilo katika eneo la kutatua migogoro basi mfano mmoja wapo mzuri ni Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA) ambacho kilikuwa kimeshindwa kufanya uchaguzi kwa takribani miaka kumi. Serikali iliweza kuingilia kati na kufuatilia mgogoro huu pia tulienda mbali zaidi kwa kuwapatia rasilimali fedha na hatimaye uchaguzi wao uliweza kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja pia ya kwamba Serikali iweze kutekeleza Mkataba wa Marakesh. Ikumbukwe kwamba 2019 Septemba, 11 Bunge lako liliweza kuridhia Mkataba huu wa Marakesh na hatimaye kusainiwa na Mheshimiwa Rais. Baada ya hapo ulipelekwa nchini Geniva ambapo kwenye Shirika la Hati miliki (World Intellectual Property Organization) ambako sasa umepelekwa kwa ajili ya uhakiki na hatimaye uweze kutelezwa kama ambavyo inatakiwa.
Mheshimiwa Spika, tunaposema kwamba Serikali yetu imetekeleza mambo mengi imetekeleza kweli kweli. Pamoja na hilo Serikali imeweza kuvifufua vyuo vitatu vya ufundi kwa watu wenye ulemavu. Vyuo hivi kimoja kipo Mkoani Tabora ambacho Ruwanzari, lakini pia Mkoani Tanga (Masiwani) na Mirongo Mkoani Mwanza na kupelekea kwamba idadi ya vyuo hivi kuwa vyuo vitano na pale mwanzoni vilikuwa viwili.
Mheshimiwa Spika, hili lilikuwa ni tamanio kubwa la watu wenye ulemavu kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinafunguliwa na vinasaidia watu wenye ulemavu ambao wanashindwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Serikali imeweza kukamilisha uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa kwa watu wenye ulemavu kwa kuufungulia akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania. Sambamba na hilo Serikali imeweza kupendekeza Mfuko huu uweze kutengewa shilingi milioni mia mbili.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya machache ninaomba nitumie Bunge lako Tukufu hili kuwatakia Waheshimiwa Wabunge wote kila la kheri na upendeleo wa Mwenyezi Mungu na kibali kiendelee kuwa pamoja na sisi ili tuweze kurejea katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante nawasilisha na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya uzima na uhai ambao anaendelea kunipatia kila siku.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumtakia heri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mpendwa wetu mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, niendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu siha njema, hekima na maarifa ya kuendelea kuliongoza Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Serikali kwenye maeneo mengi, kwenye eneo la watu wenye ulemavu kwa yale ambayo yamekwisha kufanyika na yale ambayo yanaendelea kufayika. Kwanza, naomba nianze na eneo la kamati za watu wenye ulemavu. Serikali imekimbizana na kuhakikisha kwamba kamati za watu wenye ulemavu zinaundwa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu lakini bado kuna maeneo ambayo kamati hizi hazijaundwa. Niishauri Serikali ihakikishe kwamba zoezi hili la uundwaji wa kamati za watu wenye ulemavu linakamilika nchi nzima. Pia kwa yale maeneo ambayo tayari kamati hizi zimekwisha kuundwa basi Serikali iziwezeshe ili ziweze kufanya kazi kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kamati hizi ni muhimu sana. Mambo mengi ambayo yanaendelea huko chini ambayo hayagunduliki kwenye eneo la watu wenye ulemavu yatakuwa solved kama hizi kamati zitaanza kufanya kazi kama ambavyo zilikuwa zimetarajiwa na sheria. Kwa hiyo, Serikali kupitia TAMISEMI iweze kuliona hili na kutenga fedha ili kamati hizi ziweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Serikali na kuishukuru sana na watu wenye ulemavu wamenituma niliseme hilo kwa kuweza kusikia kilio chao na hatimaye kuweza kufanya marekebisho ya kanuni za mikopo ya halmashauri zetu. Takumbukwa kwamba katika Bunge la Kumi na Moja, Waheshimiwa Wabunge pia waliweza kuishauri sana Serikali kwamba ione namna ya kufanya marekebisho ili basi mtu mwenye ulemavu mmoja mmoja aweze kupata mkopo. Suala hili Serikali yetu sikivu imekwisha kulifanyia kazi. Kuna swali ambalo nilileta lakini sasa sioni hata umuhimu tena wa swali hili kuweza kujibiwa ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali kwamba iendelee kuzihimiza halmashauri zetu kutenga fedha lakini pia kununua mafuta ya watu wenye ualbino na hatimaye kuyasambaza kama ambavyo maelekezo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara. Zipo halmashauri ambazo zinatenga fedha lakini kutenga tu haitoshi. Mtu anaishia kutenga, ukifuatilia kweli fedha imetengwa, lakini mwisho wa siku fedha zile hazikuwahi kufanya kazi ambayo ilikusudiwa. Pia kuna maeneo mengine unakuta mafuta yananunuliwa lakini hayawafikii walengwa. Kwa hiyo, niombe Serikali iweke mkazo mkubwa kwenye eneo hili la mafuta kwa watu wenye ualbino.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisema na naomba nirudie tena; vifaa hivi visaidizi kwa sisi watu wenye ulemavu ni kama chakula. Kama vile ambavyo binadamu wa kawaida anahitaji kula, vivyo hivyo mtu mwenye ulemavu hivi vifaa kwake inakuwa ni kama chakula ambacho akikikosa kwa kweli inakuwa inamhatarishia maisha yake. Nimeshuhudia mimi mwenyewe kwa macho yangu kwa sababu nimekuwa kwenye eneo hili kwa muda mrefu; watu wenye ualbino wanateseka na kansa za ngozi. Hata kama itatokea mtu ukaona picha yenyewe kwa kweli sijui unaweza ukafanyaje lakini ni muhimu sana haya mafuta yakawafikia wenzetu.
Mheshimiwa Spika, pia elimu kubwa iendelee kutolewa kwa watu wenye ualbino ili iwasaidie na/ama iwawezeshe ni jinsi gani pia wanaweza wakajikinga na hizi kansa za ngozi. Kwa sababu unakuta mtu mwingine mafuta amepaka ndiyo lakini nguo aliyoivaa inamhatarishia maisha kwa sababu anakuwa anajiachilia kwenye mionzi ya jua.
Mheshimiwa Spika, naomba niiombe Serikali kwenye eneo la ajira na hasa TAMISEMI, zile ajira zikiwa zinatangazwa basi itolewe angalau hata idadi fulani maalum kwa watu wenye ulemavu. Kwa mfano, sasa hivi kuna ajira 6,000, hata zikatengwa nafasi 300 ama 200 kwamba hizi ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kama hawatapatikana basi zitaendelea kuchukuliwa na watu wengine.
Mheshimiwa Spika, kwa harakaharaka naomba nizungumzie suala la miundombinu kwenye shule zetu na hasa vyoo. Vyoo vimekuwa ni tatizo kubwa sana, watoto wenye ulemavu wanapata shida, kwa hiyo, Serikali iendelee kuweka nguvu kubwa na kutenga fedha kuhakikisha kwamba angalau basi katika kila shule kunakuwa na tundu moja ambalo litamuwezesha mwanafunzi mwenye ulemavu kuweza kulitumia.
Mheshimiwa Spika, pongezi zangu zienda kwa Serikali, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika aya ya 73, 74 mpaka 75 imeonesha ufaulu wa watoto wenye ulemavu. Pia kuna ongezeko la uandikishwaji na fedha ambazo zimeweza kununua vifaa visaidizi ambazo ni takribani shilingi bilioni tatu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa jinsi anavyonilinda, anavyonitetea na anavyonipigania katika majukumu yangu ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jinsi anavyoendelea kumpa hekima, busara na maarifa ya kuliongoza Taifa letu. Nina hakika tunaona ni kwa jinsi gani anavyoendelea kuupiga mwingi kwenye maeneo mbalimbali, yaani kwenye sekta mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo imeendelea kuyapa kipaumbele masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu. Tukianzia kwenye Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ilieleza mambo mengi kwenye eneo la watu wenye ulemavu; na pia kwenye Hotuba hii ya TAMISEMI, imeeleza mambo mengi ambayo yanatarajiwa kufanyika na yale ambayo yameshafanyika.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa kwenye maeneo ya shule zetu, ni uzio. Shule nyingi zilikuwa hazina uzio ambapo sasa ilikuwa inasababisha kuhatarisha maisha ya watoto mbalimbali na hasa ikizingatiwa kwamba, watoto wengi kwenye maeneo hayo unakuta ni walemavu wa akili, pia kuna watoto wenye ualbino, kwa hiyo, ilikuwa ni changamoto kubwa. Naipongeza sana Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba changamoto hii inaenda kutoweka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, naipongeza na kuishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga mabweni kwenye shule za watoto wenye ulemavu. Kwenye maeneo mengi watoto wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya umbali, lakini sasa uwepo wa mabweni haya utawezesha watoto wengi wenye ulemavu kuweza kusoma na hatimaye kuwa na uhakika wa masomo yao kwa kadiri ambavyo wanaendelea. Kwa kweli sisi kama watu wenye ulemavu Tanzania, tunaishukuru sana Serikali na tunaendelea kuiombea mipango hii iweze kutekelezeka kwa wakati kama ambavyo imepangwa.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba hii pia limeongelewa suala zima la utambuzi wa watu wenye ulemavu. Pale ambapo suala hili la kuwatambua watu wenye ulemavu limefanyika imekuwa ni vizuri kwa sababu, wanapotambuliwa inakuwa pia ni rahisi kufahamu na mahitaji yake. Hotuba imeeleza wazi kwamba, wamewatambua na hatimaye wameweza kuwapatia mahitaji mbalimbali miongoni mwa wale waliotambuliwa. Hivyo pia, nikiwa kama mwakilishi wao, ninawashukuru sana na kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, limeendelea zoezi la uandikishwaji watoto kwa maana ya kuanzia elimu ya awali, msingi na kuendelea; na tunaona kabisa kwamba idadi ya uandikishwaji inaongezeka. Ilikuwa ni kilio cha muda mrefu na changamoto kubwa kwamba, watoto wengi wenye ulemavu walikuwa hawaendi shule, lakini kwa trend hii inayoendelea, tunaona kabisa kwamba kundi hili la watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma na hatimaye na wao wanaenda kupata elimu kama watoto wengine. Ninaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi, yako mambo mengi ambayo yamefanyika kwa mujibu wa hotuba hii, na kwa kadiri ya ambavyo tunayaona sisi watu wenye ulemavu. Kipekee kabisa nilete salamu nyingi za watu wenye ulemavu kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Tunamshukuru Rais wetu kwa sababu aliweza kutualika Ikulu ya Chamwino, tukakaa naye, tukazungumza naye, tukawasilisha changamoto zetu mbalimbali ambazo kwa kweli, Mheshimiwa Rais changamoto zile, nyingi zimeshaanza kufanyiwa kazi na nyingine zimeshapata suluhisho na nyingine ziko katika hatua ya utekelezaji. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo kuna baadhi ya changamoto ambazo ninaomba niziwasilishe mbele ya Serikali. Changamoto ya kwanza ni utolewaji wa mafuta ya watu wenye ualbino kwenye Halmashauri zetu. Hii imekuwa ni changamoto ya muda mrefu; miongozo ipo, kanuni zinaongea wazi, lakini suala hili halitekelezeki kwenye Halmashauri zetu. Nimekuwa nikipokea simu mbalimbali kutoka kwa watu wenye ulemavu wakilalamikia suala hili kwamba, Halmashauri hazitoi mafuta haya.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisema kwamba mahitaji ya watu wenye ulemavu ni kama chakula. Vile ambavyo binadamu mwingine anahitaji kula, hivyo, mahitaji haya ni ya muhimu sana kwa kundi hili la watu wenye ulemavu. Naiomba Serikali, suala hili liweze kutekelezeka kwa maana ya kwamba, Halmashauri ziweze kutenga, kununua na kusambaza mafuta haya kwa watu wenye ualbino. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbali na hilo, namwomba Waziri anapokuja kuhitimisha, basi aweze kulielezea suala hili kwa kina, ni kwa nini halitekelezeki? Pia, niseme wazi kwamba, maelezo ya Mheshimiwa Waziri yasiponitosheleza, nitashika shilingi yake na nitaondoka na huo mshahara wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile ieleweke wazi kwamba familia nyingi ama watu wenye ulemavu walio wengi wanaishi kwenye kipato cha chini sana kiasi cha kushindwa kumudu matibabu yao. Naishauri na kuiomba Serikali iweze kufanya zoezi ambalo lilifanyika kwa wazee, kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wale ambao hawana uwezo wa kupata matibabu ili basi, vitambulisho vile viwawezeshe kutibiwa kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, suala hili ni muhimu sana kwa sababu, wengi wanapata changamoto kubwa. Sasa unakuta mtu anakupigia simu, Mbunge nisaidie matitabu; na idadi ilivyo kubwa unajikuta unashindwa kusaidia kwa ukamilifu wake kwa wale ambao wana uhitaji. Hivyo, naiomba Serikali iweze kuwatambua watu wote ambao wanashindwa kumudu matibabu kama ilivyofanya kwa wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kabisa, kwa sababu muda umekuwa siyo rafiki, niwahamasishe watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuweza kuhesabiwa, lakini pia elimu hii kwa wale viongozi wa watu wenye ulemavu waweze kuitoa kwa wenzao. Kwa maana kuhesabiwa ni muhimu, yamkini mambo mengi hayatekelezeki kwa sababu Serikali haina idadi yetu kamili. Hivyo, niwaombe sana watu wenye ulemavu wajitokeze kuhesabiwa; na pia watu ambao wanaishi na watu wenye ulemavu wasiwafiche kuhesabiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. STELLA A. IKUPA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake shupavu na mahiri unaopolekea maslahi ya watumishi wa umma kuboreshwa na kuongezeka kwa ajira kwenye kada mbalimbali ambazo zilikuwa na uhaba mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wa Wizara hii kwa jinsi wanavyomsadia Mheshimiwa Rais kutimiza ndoto zake kwa wananchi na ahadi zilizo ndani ya Ilani ya CCM kupitia mipango mbalimbali inayoandaliwa na Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali katika ajira zinazotolewa walau iwe inatengwa hata asilimia kati ya 10 mpaka 12 kutegemea na idadi ya ajira zilizotangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii ya kuniwezesha na mimi kutoa mchango mdogo katika Wizara hii ya Afya. Kabla sijaendelea ninaomba niunge mkono hoja iliyopo mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameweza kumpongeza kwa kuongeza mishahara ya Watumishi wa Umma jambo ambalo linaenda kupelekea ongezeko la mzunguko wa fedha ndani ya nchi yetu. Pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaendelea kuipa kipaumbele sekta hii ya afya na hasa kibajeti. Tunaona bajeti ya afya jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri amei-present imekuwa na mambo mengi ambayo yanatoa tumaini la sekta hii kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimwia Waziri Ummy Mwalimu Dada yangu kwa jinsi ambavyo anaendelea kuchapa kazi yeye pamoja na timu yake ya Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 mwezi wa Nne mwaka huu niliweza kuuliza swali lakini pia Januari mwaka huu niliweza kuuliza swali nikitaka kufahamu mpango wa Serikali ni jinsi imejipanga kuona kwamba inaandaa vyumba maalum vya kujifungulia wanawake wenye ulemavu. Ninaishukuru Serikali kwa jibu ambalo lilitolewa lakini mpango ambao ulitolewa ni mpango wa muda mrefu kutokana na umuhimu na unyeti wa jambo hili niiombe Serikali iliangalie jambo hili kwa jicho la tatu, kwa kuja na mpango wa muda mfupi ambao utawezesha upatikanaji wa vyumba hivi vya kujifungulia wanawake wenye ulemavu kwa haraka, tofauti na ambavyo sasa kwenye jibu lile ilisema kwamba wameandaa ramani ambazo zimeandaliwa sasa hivi kwa maana ya vituo vya afya ama hospitali ambazo zitajengwa basi zitazingatia jambo hili, ninaiomba sana Serikali iliangalie jambo hili kwa jicho la tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT Ndugu Brenda Msangi jambo hili aliposikia tu nilipouliza kazi swali yeye alilifanyia kazi kwa haraka sana na hivyo pale CCBRT sasa hivi wanawake wenye ulemavu wanajifungua vizuri na wanafurahia kuleta viumbe duniani kama wanawake wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nichangie kwenye eneo la wagonjwa wa akili lakini mimi nipo tofauti kidogo na wachangiaji ambao wamepita. Kwa kadri ambavyo nilikutana na kundi hili ambalo pia ni kundi ambalo ninaliwakilisha, waliweza kuzungumzia changamoto ya upatikanaji wa dawa za wagonjwa wa akili. Dawa hizi kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wake lakini hata zinapopatikana zinapatikana kwa gharama kubwa, hivyo niiombe sana Serikali iweze kuangalia kwamba dawa hizi ziweze kupatikana kwa gharama nafuu lakini pia ziweze kupatikana kwa wingi kwa kadri ambavyo wamekuwa wakizihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo la mwisho ambalo ninaomba nilichangie ni kuhusiana na upatikanaji wa matitabu kwa watu wenye ulemavu. Hata mwaka jana kwenye bajeti niliweza kuchangia lakini pia Mheshimiwa Waziri alipokuwa anawasilisha bajeti yake mwaka jana aliweza kuongelea mpango mzuri ambao umeandaliwa kwa wazee na mimi nikatumia nafasi hiyohiyo kwamba Serikali sasa inaonaje kwenye ule mpango mzuri wa wazee, alisema zimeandaliwa t-shirt wazee kwanza, nikasema kwa nini Serikali sasa isiongeze neno ikawa kwamba wazee na watu wenye ulemavu kwanza ili kuweza kuleta huduma hii ya matibabu kiurahisi kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina ufahamu mpango mzuri ambao unaandaliwa na Serikali, Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanakuwa na Bima za Afya hili ninalitambua lakini kwakuwa bado tupo kwenye mchakato katika kipindi hiki cha mpito basi Serikali iweze kuona utaratibu mzuri wa kundi hili kuweza kupatiwa matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii ya kuchangia jioni hii ya leo. Awali ya yote naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima na uhai kwangu binafsi, pia na Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani ukiwemo pia na wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa leo utajikita zaidi kwenye kuishukuru Serikali na kuipongeza kwa mambo makubwa ambayo imeyafanya kwa kundi la watu wenye ulemavu, nikiwa kama Mbunge wa kundi hili. Naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo imeendelea kuleta mageuzi kwenye elimu ya kundi hili la watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi ya kuishukuru Serikali, lakini kwa masilahi ya muda, nimekuwa nayo machache hapa ambayo kwa kweli yamekuwa ni mageuzi makubwa sana kwa kundi hili la watu wenye ulemavu. Naishukuru Serikali kwa kuanzisha shule za nyumbani. Kwa nini naishukuru Serikali kwa ajili ya jambo hili?
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa sababu watoto wengi wenye ulemavu uliozidi walikuwa wanashindwa kupata haki yao ya elimu kwa kushindwa kwenda shuleni. Kwa hiyo, uwepo wa miongozo ya shule za nyumbani unawawezesha watoto hawa kuweza kupata haki yao ya elimu. Walimu wanawafuata nyumbani wanawafundisha na hatimaye wanatungiwa mtihani, wanafanya kama watoto wengine. Haya ni mageuzi makubwa sana kwa Elimu ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naomba niishukuru Serikali kwa kuwa imeendelea kutenga fedha za kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, lakini pia kununua vifaa visaidizi kwa kundi hili la wanafunzi wenye ulemavu. Hii ni hatua kubwa sana. Kama tunavyofahamu na kama ambavyo nimekuwa nikisema mara nyingi, kwamba suala la vifaa visaidizi kwa kundi la watu wenye ulemavu ni kama chakula, yaani mtu hasemi kwamba alikula jana leo asile. Vifaa hivi ni muhimu sana, kwa sababu anapokuwa nacho leo, kesho kinaharibika, kinahitajika kingine. Kwa hiyo, ni kama chakula kwa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu. Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutenga fedha na kununua vifaa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naomba niishukuru sana Serikali kwa kuendelea kufanya upimaji wa usikivu kwa kundi la wanafunzi viziwi; na baada ya kufanya upimaji huu, Serikali pia imekuwa ikitoa vifaa vya kuwasaidia kwenye eneo hili la usikivu (hearing aids). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu wenzetu viziwi, yaani huwezi tu kununua kifaa ukampatia. Sasa hatua hii ambayo imechukuliwa na Serikali ya kuwapima kwanza na kuona ni kwa jinsi gani wameathirika na kuwapatia hivi vifaa ni hatua kubwa sana. Kwa hiyo, naishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa hatua hii kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naishukuru Serikali kwa kuongeza vyuo vya kudahili walimu wa elimu maalum. Kama tunavyofahamu, kumekuwa kuna upungufu wa walimu wa elimu maalum, hivyo Serikali imeongeza Chuo cha Kabanga na Chuo cha Mpwapwa ili viweze kuongeza udahili wa walimu hawa. Kwa hiyo, hii ninaamini kwamba inaenda kupunguza hii changamoto ya kuwa na upungufu wa walimu wa elimu maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee tena kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwa imekuwa ikifanya mafunzo kwa walimu wa elimu maalum lakini pia na walezi wa mabweni. Kama tunavyofahamu kwamba walimu wa elimu maalum wapo wachache, kwa hiyo, kwa kadiri ambavyo wanaendelea kupewa mafunzo ya mara kwa mara, pia na hawa walezi wa mabweni wanavyoendelea kupewa mafunzo ya mara kwa mara inawaweka kwenye nafasi nzuri ya kuliangalia kundi hili na kuwasaidia ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kushukuru na kupongeza ni kuomba tena. Yapo mambo kadhaa ambayo nimekuwa nikiishauri na kuiomba Serikali kwa kundi hili la watu wenye ulemavu na ninaomba niyakumbushe tena siku ya leo. Pamoja na kwamba Serikali imeweka huu mkakati mzuri wa kuongeza chuo cha Kabanga na Mpwapwa ili kuweza kudahili walimu wa elimu maalum, ushauri wangu ambao nimekuwa nikiutoa kwa Serikali ni kwamba, ni kwa nini Serikali isione umuhimu wa kwamba hii elimu maalum iwe ni lazima kwa kila mwalimu anayesomea ualimu?
Mheshimiwa Spika, kwa nini? Ni kwa sababu kila mwalimu akifahamu elimu maalum, mtoto huyu mwenye ulemavu anaweza akasoma kwenye eneo lake, tofauti na ilivyo sasa hivi ambapo mtoto mwenye ulemavu ambaye anahitaji mwalimu ambaye amesoma elimu maalum inamlazimu mpaka aende kwenye shule jumuishi, ama inamlazimu mpaka aende kwenye zile shule zetu maalum. Hii inaleta changamoto kwa sababu kuna maeneo ambayo shule ipo karibu, lakini hakuna walimu ambao wanafahamu elimu maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuwafanya walimu wote kujifunza elimu maalum, itasaidia kila mtoto asome kwenye mazingira aliyopo badala ya kumpeleka kwenye elimu jumuishi. Unakuta kwenye ile elimu jumuishi hakuna bweni na hakuna miundombinu ya kumwezesha kufanya vizuri kwenye masomo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ikiliona hili, kila mwalimu akajua A, B, C akajifunza elimu maalum na elimu hiyo ikawa ni kitu cha lazima, basi tutaondoa kwanza hata hii changamoto ya ukosefu wa walimu wa elimu maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wakati Bunge lililopita zilitangazwa nafasi za walimu wa elimu maalum, zilikuwa nafasi kama 400 kama sijasahau ama kama ninakumbuka vizuri, lakini walimu hawa walikosekana, wakapatikana walimu 200 tu. Kwa hiyo, sio walimu wengi wanasoma hii elimu maalum. Naomba sana Serikali iweze kuliona hilo na kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika ushauri wangu mwingine, nilikuwa naiomba Serikali, pamoja na kwamba Serikali sasa hivi inakalimani vitabu vya masomo kwa lugha ya alama, lakini pia iweze kuona ni kwa jinsi gani kila mwanafunzi anajifunza. Yaani hii lugha ya alama iwe ni somo la lazima kwa kila mwanafunzi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumechelewa, lakini tutatengeneza kizazi kijacho ambacho kitakuwa kina uwezo wa kuwasiliana na wenzetu viziwi. Hapa hatutakuwa tena na changamoto ya wakalimani, hatutakuwa tena na changamoto ya walimu. Kwa hiyo, Serikali iweze kuona ni kwa jinsi gani hii lugha ya alama ikawa ni somo la lazima kwa kila mwanafunzi ili tutengeneze kizazi kijacho ambacho kitaweza kuwasiliana na wenzetu viziwi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Serikali kwa kutenga fedha na kununua vifaa visaidizi kwa kundi hili la watu wenye ulemavu. Naiomba Serikali, mwitikio wa wazazi na jamii yetu kwa ujumla kwa habari ya elimu kwa watu wenye ulemavu sasa hivi umekuwa ni mkubwa sana. Hivyo vifaa hivi vinakuwa havitoshi. Naiomba Serikali iongeze bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivi visaidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nilikuwa naomba niishauri Serikali kwenye eneo la uanzishaji wa chombo maalum cha kuratibu na kusimamia elimu jumuishi nchini. Sasa hivi hakuna chombo hiki, lakini kwa nchi nyingine, naomba nisizitaje, kuna nchi ambazo tayari zimeshaanzisha hivi vyombo na vinafanya vizuri. Hii elimu jumuishi inaratibiwa vizuri na inasimamiwa vizuri, uwepo wa chombo hiki utasaidia sana kuhakikisha kwamba hii elimu jumuishi inaratibiwa vizuri na inatekelezwa vizuri kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia hii nafasi. Awali ya yote naomba niunge mkono hoja hii ambayo iko mbele yetu na moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada kuunga mkono hoja hii na kama ambavyo hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu imeelezea, hiki kilikuwa ni kilio cha wafanyakazi kwa muda mrefu sana kama ambavyo imeelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida zake kwenye hotuba imeelezwa pia kwamba ni kwa nini sasa hii mifuko inaunganishwa ama kwa nini wafanyakazi walikuwa wakililia kwamba mifuko hii iunganishwe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ilitokana na kwamba kulikuwa kuna utofauti mkubwa wa mafao kati ya mfuko mmoja na mwingine, lakini pia gharama za uendeshaji wa hii mifuko na mengine mengi ambayo yameongelewa kwenye hii hotuba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitafafanua kwa ufupi tu fao la kifo. Fao hili ni fao ambalo linatolewa pale ambapo mtumishi bado anakuwa yuko kwenye utumishi na bahati mbaya akafariki. Fao hili limewekwa siyo kama tunataka watu wafe kabla ya umri, lakini kwa hali ilivyo ni lazima liwepo kwa sababu ni hali ambayo imekuwa ikijitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili fao ni zuri kwa maana ya kwamba kwa jinsi ambavyo limewekwa, yaani wanufaikaji pale ambapo huyu mtumishi anapofariki akiwa kwenye utumishi. Ukiangalia kwenye hii sheria inafafanua kabisa na inaonesha kwamba ni akina nani ambao wanakuwa ni wanufaika pale ambapo mtumishi anafariki akiwa bado kwenye utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kuna watoto, lakini pia kuna mjane, kwa maana ya mgane ama mjane; pia kwa upande wa watoto wanaendelea kuhudumiwa mpaka pale wanapofikisha umri wa miaka 21. Pia watoto hawa ama mtoto anaweza akaendelea kuhudumiwa endapo atakuwa na ulemavu wa aina yoyote. Kwa hiyo, huyu ataendelea kuhudumiwa kwa muda wake wote, yaani kwa maisha yake yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili fao ni zuri kwa maana kwamba linanufaisha wale ambao wanakuwa wamebaki ama ambao walikuwa ni wategemezi wa Marehemu. Siyo hilo tu, kama Marehemu alikuwa hana mke wala watoto wanaomtegemea, lakini ana wazazi, hili fao pia linakuwa lina umuhimu kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, muunge mkono hoja hii iliyoko mbele yetu ili iweze kupitishwa kwa maslahi mapana ya Watanzania wote na kwa maslahi mapana ya nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba niendelee kuunga mkono hoja hii.