Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Stella Ikupa Alex (13 total)

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Singida wamejikita katika shughuli za ujasiriamali ili kuondokana na umaskini, lakini wanakosa mbinu za kitaalam za kuwawezesha kupiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia kazi wanazofanya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mbinu endelevu, zana za kisasa pamoja na mitaji ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwapatia vijana wa Singida mbinu endelevu na zana za kisasa pamoja na mitaji ya kufanyia kazi kwa ufanisi, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujasiriamali. Hadi kufikia mwezi Oktoba jumla ya vijana 11,340 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi wa fani mbalimbali na wengine wanaendelea na mafunzo ya kujenga ujuzi kutoka katika mikoayote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano dhahiri wa mafunzo ya kukuza ujuzi ni pamoja na utumiaji wa teknolojia ya kitalu nyumba (green house) ili kuwawezesha vijana wetu kufanya kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza tija ya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa mikoa yote kushiriki katika program hii, mikoa ilielekezwa kutenga eneo la kujenga green house ya kufundishia; kutenga maeneo ya kilimo kwa vijana pamoja na kuweka miundombinu muhimu na upatikanaji wa maji; kuandaa vijana wenye nia ya kujifunza kilimo kwa kutumia teknolojia ya green house.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote Wizara yangu imeendelea kusimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana wote wa Tanzania.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Watanzania wenye ulemavu wanakabiliwa na kero mbalimbali za kimaisha ikiwemo ukosefu wa ajira kama ilivyo kwa Watanzania wengine, aidha, zipo changamoto za jumla kama vile kijana mwenye ulemavu wa ngozi asiye na ajira ana changamoto ya mahitaji ya kujikimu na pia ana changamoto za kipekee za mahitaji ya kiafya na kiusalama.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu umuhimu wa kuwatazama vijana wenye ulemavu mbalimbali kwa namna ya pekee na kama zipo sera na mikakati ya kiujumla kwa vijana wote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua vijana wenye ulemavu kuwa ni kundi mojawapo miongoni mwa Watanzania wenye ulemavu nchini ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma maendeleo yao. Mojawapo ya changamoto hizo ni ukosefu wa ajira, huduma za afya, uwezo mdogo wa kuyamudu mahitaji ya kujikimu, umaskini na changamoto ya kiusalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la watu wenye ulemavu wakiwemo vijana wenye ulemavu, Serikali iliunda Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ambalo kazi yake kubwa ni kutoa ushauri kwa Serikali na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya watu wenye ulemavu juu ya namna bora ya kushughulikia changamoto zao, kuzijumuisha zile za kundi la vijana wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kuunda Kamati za Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya Mkoa, Halmashauri ya Wilaya, Kata na Mtaa/Kijiji. Kazi kubwa ya Kamati hizi ni kuhakikisha kuwa masuala ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa katika mipango yote ili kuondoa kero mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu elimu, ajira, afya na mikopo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nichukue pia fursa hii kuwakumbusha na kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia ipasavyo utekelezaji wa suala hili ambalo liko kisheria na pia ikizingatiwa kuwa maagizo kadhaa yamekwishatolewa kwa maneno na kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha vyuo vya mafunzo ya ufundi vya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kuajiriwa na kijiajiri na kupata ujuzi mbadala wa kumudu maisha yao.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Tanzania ina idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Je, Serikali inajua idadi kamili ya watu wenye ulemavu na aina ya ulemavu waliokuwa nao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2012 inaeleza kuwa, ulemavu ni hali inayotokana na dosari ya kimwili au ya kiakili ambayo inampunguzia mtu uwezo na fursa sawa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii. Upungufu huo unaweza kuchochewa na mazingira na mtazamo wa jamii kuhusu ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina mbalimbali za ulemavu ambao umegawanyika katika makundi yafuatayo:-
Ulemavu wa viungo, wasioona, viziwi, wasioona, ulemavu wa akili, wenye ualbino, ulemavu wa vichwa vikubwa na mgongo wazi, ulemavu wa matatizo ya afya ya akili, yaani walioupata ukubwani bada ya kuugua kwa muda mrefu pamoja na ulemavu wa ngozi yaani walioathirika na mabaka mabaka ya ngozi mwilini. Sababu za kiujumla ni pamoja na ukosefu wa chakula bora au lishe duni, magonjwa kama malaria, uti wa mgono na surua, ajali mbalimbali, urithi na hali ya mama yaani umri na hali ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maelezo hayo, naomba kujibu sasa swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na wingi huo wa aina za ulemavu, Sense ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imejumuisha vipengele mahususi kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusu watu wenye ulemavu hivyo Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani watu 44,928,923 ambao sasa kwa hapo mgawanyo wake uko kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye ualbino ni 16,477,000 ambayo ni sawa na asilimia 0.04, wasiiona ni 848,530 sawa na asilimia 1.19, ulemavu wa uziwi ni 425,322 sawa na asilimia 0.97, viungo ni 525,019 sawa na asilimia 1.9, ulemavu wa kumbukumbu ni 401,931 ambayo ni sawa na asilimia 0.9, ulemavu wa kushindwa kujihudumia ni 324,725 sawa na asilimia 0.74, na ulemavu mwingine yaani kwa ujumla wake ni 99,798 ambao ni sawa na asilimia 0.23.
MHE. CATHERINE N. RUGE aliuliza:-
Upatikanaji wa vifaa vya walemavu ni mdogo sana lakini gharama zake ni kubwa sana hali inayofanywa walemavu kushindwa kumudu, kwa mfano mguu bandia mmoja unauzwa shilingi milioni mbili.
Je, ni lini Serikali itatoa agizo la kufutwa kodi za vifaa hivyo kama ilivyo katika nchi nyingine na kwa kuzingatia kauli mbiu ya Serikali ya kumkomboa mnyonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa watu wenye ulemavu ni kundi kubwa miongoni mwa Watanzania ambalo linakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kujimudu vikiwemo miguu bandia ambayo huuzwa kwa gharama kubwa kiasi cha kuwafanya Watanzania wenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kuwepo kwa vifaa hivyo vya kujimudu kwa watu wenye ulemavu, Serikali ilitunga Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 inayotoa tamko juu ya upatikanaji wa nyenzo mbalimbali za kujimudu kwa watu wenye ulemavu ili kuwarahisishia utendaji wao wa kazi na katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo pamoja na kuwarahishia mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo bado kumekuwepo na changamoto ya upatikaji wa vifaa hivyo kwa bei kubwa ambayo inakuwa vigumu kwa wananchi wengi kuweza kumudu na pia vifaa hivyo kuagizwa nchi za nje kwa kuwa hapa nchini vinapatikana vichache. Hivyo, Serikali kwa kutambua changamoto hiyo na kwa lengo la kumkomboa mnyonge, ilifuta kodi kwa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kama alivyoeleza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mbunge) kupitia hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2017.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Utekaji nyara na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) vilikithiri kwenye miaka ya 2000 hali iliyopelekea Serikali kuanzisha kambi maalum kwa ajili ya usalama wao.
(a) Je, Serikali imeanzisha kambi ngapi mpaka sasa na ni katika Mikoa na Wilaya zipi?
(b) Je, ni watu wangapi wenye ulemavu wa ngozi wanaoishi katika makambi hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b)kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kambi iliyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi hadi sasa, isipokuwa kuna shule katika baadhi ya Mikoa kama vile Shule ya Buhangija iliyoko Mkoani Shinyanga ambayo imepokea watoto wenye ulemavu wa ngozi kwa kuletwa na wazazi, viongozi wa vijiji, Maofisa Ustawi wa Jamii na Polisi. Hii yote ni katika kunusuru uhai wao, kwani Sera ya Taifa ya watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 inakataza watu kuishi kwenye Kambi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la (b) jibu ni kwamba idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi waishio kwenye Shule ya Buhangija ni 309 ambapo wanaume ni 152 na wanawake ni 157.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Mfuko wa Watu wenye Ulemavu ulianzishwa kwa Sheria Na.9 ya mwaka 2010 na lengo la mfuko huo ni kusaidia Baraza la Watu Wenye Ulemavu kufanya kazi zake kwa ufanisi, kuendesha tafiti mbalimbali na kubaini changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu. Hata hivyo mfuko huo haukutengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2016/2017.
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mfuko huo ili uweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Watu wenye Ulemavu umeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza matakwa ya sheria hii, Serikali ilizindua rasmi Baraza la Ushauri la Taifa kwa Watu wenye Ulemavu mnamo Novemba, 2014 ambalo limejumuisha Wizara zinazohusika na masuala ya watu wenye ulemavu, Vyama vya Watu wenye Ulemavu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Chama cha Wafanyakazi. Aidha, kupitia Serikali ya Awamu ya Tano Baraza limeanza Rasmi kazi na Serikali imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa vikao ambavyo kwa mujibu wa sheria vinafanyika vinne kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa kuwa na Baraza la Taifa la Ushauri kwa Watu wenye Ulemavu umeshakamilika, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2018/2019 imetenga fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) ina mikakati mbalimbali ya kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI (VVU).

Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha inafanikiwa na Kampeni ya Mpango wa asilimia 90, 90, 90 hasa ukizingatia jiji la Dodoma UKIMWI umeongezeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Hassan Mbunge wa Mtambile kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maafikiano ya malengo ya Tisini Tatu yaliyopitishwa na wadau wa Kanda zote za UNAIDS, Serikali ya Tanzania ilianza kuyatekeleza kwa kufanya yafuatayo ili kuhakikisha tunafikia malengo ya 90, 90, 90:-

(i) Kuanzia mwenzi Oktoba, 2016 ilitoa Waraka nchi nzima wa kuridhia utekelezaji wa Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kupima VVU na kutibu bila ya kuzingatia kiwango cha kinga mwilini (CD4);



(ii) Imeweka utaatibu wa kuhakikisha watu wote wanaogundulika kuwa na VVU wanaanzishwa dawa za kufubaza VVU (ARV) mara moja;

(iii) Kuandaa kampeni mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU ili kujua hali zao na hasa mkazo mkubwa umeelekezwa kwa Wanaume ambao utafiti umeonyesha kuwa hawajitokezi sana kupima na kujua hali zao;

(iv) Kufanya mapitio ya Mkakati wa kudhibiti UKIMWI wa Mkoa wa Dodoma (2017) ili kuhuisha mahitaji ya afua za UKIMWI baada ya Serikali kuhamia Dodoma na kuongezeka kwa wawekezaji katika Jiji la Dodoma;

(v) Kurekebisha Mwongozo wa huduma za VVU na UKIMWI wa mwaka 2014 kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa ili kuboresha mikakati ya kuwapatia huduma za UKIMWI, ikiwemo upimaji wa VVU; na

(vi) Kuanza mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI (Kuazuia na Kudhibiti) Sura ya 431 ili kushusha umri wa watoto kuruhusiwa kupima VVU kutoka miaka 18 hadi 15 na kuanzisha utaratibu wa wananchi kuruhusiwa kujipima wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wananchi wote kuendelea kupima afya zao ili watambue hali zao na kuchukua hatua stahiki.
MHE. MAULID S. MTULIA aliuliza:-

Walemavu wana mahitaji maalum ukilinganisha na watu wasiokuwa na Ulemavu na idadi ya walemavu imekua ikiongezeka siku hadi siku kutokana na ajali za barabarani hasa zitokanazo na usafiri wa bodaboda:-

(a) Je, Serikali inaweza kutoa orodha ya idadi ya watu wenye ulemavu nchini kwa kuzingatia makundi yao kwa asilimia?

(b) Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuwajengea uwezo wa kujitegemea watu wenye ulemavu hasa Vijana, Watoto na Wanawake ili kuondoa utamaduni wa kuendesha maisha yao kwa kuombaomba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni lenye kipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, idadi ya Watu wenye Ulemavu kwa kuzingatia makundi yao na kwa asilimia ni kama ifuatavyo:-

Watu wenye Ualbino ni 16,477 sawa na 0.04%; walemavu wasioona ni 848,530, sawa na 1.93%; walemavu ambao ni viziwi ni 425,322, swan a 0.97%; walemavu wa viungo ni 525,019, sawa na 1.19%; walemavu wa kumbukumbu ni 401,931, sawa na 0.91%; walemavu wa kujihudumia ni 324,725, sawa na 0.74%; na Ulemavu mwingine, yaani kwa ujumla wake ni 99,798, sawa na 0.23%. Kulinganisha na takwimu hizo jumla ya watu wenye ulemavu, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 ni watu 2,641,802.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hivi sasa inakamilisha zoezi la uanzishwaji wa regista ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi ya watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya mijini na vijijini. Faida nyingine ya kuanzisha regista hizi zitatusaidia pia kutambua sababu za kuongezeka kwa ulemavu katika kila eneo na changamoto zinazowakabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha watu wote wenye ulemavu hasa vijana, watoto na wanawake hawaachwi nyuma kiuchumi, Serikali inaendelea kuwajengea uwezo kuhakikisha watoto wote ikiwa ni pamoja na wenye ulemavu wanapata elimu ya msingi na sekondari ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea. Pia inatoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi ya vijana na wanawake wenye ulemavu kupitia vyuo vya watu wenye ulemavu na programu ya kukuza ujizi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanawezeshwa kiuchumi, Serikali inatoa mkopo wa fedha ya asilimia mbili (2%) zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Hata hivyo, mipango yote ya uwezeshaji kiuchumi nchini ni jumuishi ikiwajumuisha pia watu wenye ulemavu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuza:-

Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa wafanyabiasha kupitia Baraza la Uwezeshaji:-

(a) Je, ni vigezo vipi vinatumika katika kutoa mikopo hiyo?

(b) Je, ni wafanyabiashara wangapi ambao wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua tatizo kubwa la mitaji linalowakabili wananchi wa Tanzania na hasa wajasiriamali, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilisaini makubaliano maalum na Benki ya TPB na Taasisi ya UTT Microfinance kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali. Chini ya makubaliano hayo, miongoni mwa vigezo vya msingi vilivyopaswa kuzingatiwa na waombaji ni kama ifuatavyo:-

(i) Wafanyabiashara wanapaswa kujiunga katika vikundi vya VICOBA au SACCOS kwa ajili ya kupeleka maombi yao ya mikopo;

(ii) Kikundi kinapaswa kuwa na usajili, Katiba na Sera za uendeshaji wa kikundi; na

(iii) Kikundi kinapaswa kuwa na Ofisi inayotambulika, uongozi, mfumo mzuri wa utunzaji wa kumbukumbu za kihasibu na akaunti ya benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi yanayokidhi vigezo husika hupelekwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa ajili ya kuombewa dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Agosti, 2016, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lilidhamini mikopo yenye thamani ya Sh.542,844,500 ambapo jumla ya wajasiriamali 729 wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma kupitia Benki ya TPB. Aidha, Baraza lilidhamini pia mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa SACCOS mbalimbali mkoani humo kupitia Benki ya CRDB. Hata hivyo, Baraza limedhamini wajasiriamali katika mikoa mingine pia ndani ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Juni, 2019 kiasi kilichorejeshwa na wajasiriamali waliokopeshwa kwa dhamana kupitia Benki ya TPB ni Sh.430,292,635.60 sawa na asilimia 79.3. Hivyo, natoa wito kwa wakopaji waliosalia, kukamilisha marejesho ya mikopo yao ili Baraza liweze kuwahudumia wafanyabiashara ama wajasiriamali wengine wenye uhitaji.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-

Mwenge wa Uhuru umekuwa ukileta maendeleo makubwa nchini na kuchangia pato la Taifa:-

Je, kwa mwaka mmoja Mwenge wa Taifa unafungua miradi mingapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2015 mpaka mwaka 2018, jumla ya miradi 5,603 ilizinduliwa au kuwekwa mawe ya msingi. Miradi hiyo ilikuwa na thamani ya shilingi trilioni 2.6. Kwa muktadha huo, uwiano wa miradi iliyozinduliwa kwa mwaka na kuwekwa mawe ya msingi ni 1,402 yenye thamani ya shilingi Sh.651,849,585,126.64.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo pia huendana na kauli mbiu mbalimbali, mfano, mwaka wa fedha 2017 kauli mbiu ilikuwa ‘Uwekezaji katika Sekta ya Viwanda’ lakini kwa mwaka wa fedha 2018 kauli mbiu ilikuwa ‘Uwekezaji katika Sekta ya Elimu’ na mwaka wa fedha 2019 kauli mbiu ni ‘Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa’.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kukiri kuwa Mwenge wa Uhuru umekuwa ukileta maendeleo makubwa nchini.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y. MHE. MAKAME MASHAKA FOUM) aliuliza:-

Sheria Na.9 ya mwaka 2010 ya Watu wenye Ulemavu imeainisha haki za msingi za Watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na haki ya ukalimani katika maeneo ya utoaji huduma kama vile hospitali, taarifa ya habari, shuleni nk:-

Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuharakisha utekelezaji wa sheria hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE WALEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Makame Mashaka Foum, Mbunge wa Kijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na.9 ya mwaka 2010, imeweka misingi ya upatikanaji wa haki kwa watu wenye ulemavu ikiwepo haki ya upatikanaji wa habari kwa kundi la viziwi kupitia wakalimani katika sehemu mbalimbali ikiwemo hospitali, shuleni pamoja na vyombo vya habari yaani luninga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuweka mikakati ya kuwa na wakalimani wa kutosha wa lugha ya alama kwa kuanzisha programu ya mafunzo ya lugha ya alama katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Mradi wa LAT (Lugha ya Alama Tanzania). Chuo kimeandaa mwongozo wa mwaka 2019 wa majaribio ya kufundishia na kujifunza Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa kutumia Lugha ya Alama ya Tanzania kwa darasa la awali, la kwanza na la pili. Aidha, imeandaliwa kamusi ya lugha ya alama na machapisho mbalimbali yanayotoa mwongozo wa namna ya kujifunza lugha hiyo kwa lengo la kuongeza wakalimani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendeleza kundi kubwa la wakalimani na watumiaji wa lugha ya alama, Serikali imechukua hatua ya kutumia lugha ya alama kama lugha ya kufundishia na kujifunzia shuleni. Aidha, kufundisha lugha ya alama kama somo mojawapo katika shule na vyuo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kilele cha Wiki ya Viziwi iliyofanyika katika Manispaa ya Iringa alitoa maagizo kwa vyuo vya elimu ya juu na kati kuweka mtaala ambao utawezesha wahitimu kusoma lugha ya alama kama somo la lazima katika masomo yao (compulsory subject). Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza vyombo vyote vya habari kuwa na wakalimani wa lugha ya alama katika vipindi vya luninga zao.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 kinatekelezwa ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hiki kinahusu utoaji wa nafasi ya ajira kwa watu wenye ulemavu waliokidhi vigezo vya msingi vya nafasi zilizo wazi. Sharti hili la sheria ni kwa waajiri wote yaani Serikali na waajiri binafsi. Sharti hili la sheria ni kwa sababu Serikali inatambua kwamba kazi ni muhimu katika maendeleo ya watu wenye ulemavu inayowawezesha kujitegemea na kuondokana na hali ya kuombaomba. Pia inaleta heshima na hali ya kujiamini katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kifungu hiki kinatekelezwa ipasavyo ni kama ifuatvyo:-

i. Serikali imeanzisha kanzidata ya wahitimu wenye ulemavu wenye fani mbalimbali ambao wanazo sifa za kupatiwa ajira kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

ii. Lakini pia tumekuwa tukifanya kaguzi za kazi kupitia Sheria ya Taasisi za Kazi kifungu cha 45A kinachompa fursa Afisa Kazi kutoa adhabu za papo kwa papo.

iii. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kufanya uhamasishaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu kwa njia mbalimbali zikiwemo warsha, mikutano, makongamano, vipindi vya redio pamoja na runinga.

iv. Kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania tumekuwa tukitoa tuzo kwa mwajiri bora ambaye ameajiri watu wenye ulemavu na kuwawekea mazingira wezeshi ya kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

v. Tumekuwa tukitumia programu ya ukuzaji ujuzi kwa kukuza ajira kwa kutoa mafunzo ya kitalu nyumba kwa vijana wakiwemo wenye ulemavu katika Halmashauri mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri wao wenyewe lakini pia kuajiri wenzao na pia kuweza kuajiriwa.

vi. La mwisho tumekuwa tukitoa mafunzo kupitia vyuo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu vya Yombo - Dar es Salaam na Sabasaba -Singida ambavyo mafunzo haya ambayo yamekuwa yanawawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
MHE. MOHAMMED AMOUR MOHAMMED aliuliza:-

Idadi ya watu wenye ulemavu inakaribia asilimia kumi (10%) ya Watanzania na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa sababu mbalimbali.

Je, Serikali imejipanga vipi katika kuzisaidia na kuwezesha taasisi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na Sheria Na.9 ya mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu, Serikali inayo majukumu yafuatayo katika kuhakikisha taasisi inayoshughulikia watu wenye ulemavu zinatoa huduma stahiki. Kwanza ni kuzijengea uwezo taasisi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu kwa kuzipa mafunzo ya namna ya kuwahudumia watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, Taasisi hizo ni vyama vya watu wenye ulemavu ikiwemo Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo, Chama cha Viziwi Tanzania, Chama cha Wasiona Tanzania, Chama cha Wenye Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi, Chama cha Viziwi Wasiona, Chama cha Watu Wenye Ugonjwa wa Akili, Chama cha Walioumia Uti wa Mgongo na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Akili pamoja na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi.

Mheshimiwa Spika, pia tunatoa miongozo kwa jamii na sekta zote kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na Mikataba ya Kimataifa inayohusu watu wenye ulemavu katika kuleta haki na usawa wao. Kuzitambua na kuzitembea na kuzipa ushauri wa kitaalam taasisi nilizozitaja hapo juu namna ya kuwahudumia watu wenye ulemavu kulingana na aina ya ulemavu na mahitaji yao. Vile vile kuziwezesha taasisi mbalimbali za watu wenye ulemavu, upatikanaji wa nyenzo za kujimudu kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye ulemavu pale inapolazimu kufanya hivyo.