Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Subira Khamis Mgalu (8 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa jioni hii kuchangia. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kusimama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nawashukuru Wapigakura wa Mkoa wa Pwani kwa kukiwezesha Chama chetu kushinda Majimbo yote ya Mkoa wa Pwani, iliyopelekea kutuingiza Wabunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tano pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Naona ameanza kazi vizuri na anasema Serikali yake siyo Serikali iliyochoka; Serikali makini ambayo inakusanya trilioni 1.4; Serikali ambayo inatumbua majibu kadiri inavyoweza; Serikali ambayo imechaguliwa na watu takriban milioni nane; Serikali ambayo ndani ya Bunge hili ina 74% ya Wabunge.
Mhesimiwa Mwenyekiti, Serikali hiyo haijachoka na Chama hicho kinaaminiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye Mwelekeo wa Mpango 2016/2017. Wakati najielekeza, naomba ninukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge hili, ukurasa wa 22 aliposema: “Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umasikini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Mwelekeo wa Mpango 2016/2017 kwa kuwa umejielekeza kwenye miradi ya maji; Mradi wa Maji wa Ruvu Juu, Mradi wa Maji wa Ruvu Chini, Mradi wa Maji wa Chalinze, Mradi wa Maji wa Visima Virefu vya Kimbiji na Mpera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono nikiwa na matumaini kwamba miradi hii itakapokamilika; Mradi wa Maji wa Ruvu Juu umekamilika kwa 97%, nina imani maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Mlandizi, Kisarawe na Mkuranga yanaenda kupatiwa maji kutokana na kukamilika kwa miradi hii ambayo nimeitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mwelekeo wa Mpango huu wa 2016/2017 kwa sababu, suala la elimu; na naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako kwa kuanza mpango wa utoaji wa elimu bure. Natambua wapo baadhi ya Wapigakura wangu wa Mkoa wa Pwani walikuwa wanashindwa kulipa ada ya mitihani ya Baraza la Mitihani; walikuwa wanashindwa kulipa ada ya Sh. 20,000/= mpaka Sh. 70,000/= kwa Shule za Sekondari; walikuwa wanashindwa kugharamia baadhi ya gharama ambazo Serikali imezibeba kupitia capitation. (Makofi)
Kwa hiyo, nasema mwanzo wa safari ni moja. Tumeanza vizuri. Naipongeza Serikali, lakini natambua Serikali ipo sasa, inaangalia changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza awamu hii ya elimu bure. Naiomba Serikali iangalie sana kwenye baadhi ya maeneo, hasa suala zima la uandaaji wa mitihani, suala zima la gharama, umeme, mlinzi katika shule zetu; nina imani mambo yatakuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika suala hili la elimu, natambua Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Bunge hili, tulipitisha Sheria ya Kuanzisha Tume ya Walimu. Naiomba Serikali ya Awamu ya Tano iharakishe uandaaji wa Kanuni ili hii Tume iweze kuwatendea haki Walimu, mishahara yao, kupanda kwa madaraja, lakini pia Serikali iendelee na mpango wa kuzipa Halmashauri zetu kila mwaka milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Vile vile Serikali ikiangalie sana Kitengo cha Ukaguzi wa Elimu. Kitengo hiki mara nyingi hakitengewi fedha na tunakitegemea sana katika kukagua ubora wa elimu. Kwa hiyo, hayo yakifanyika, ninaamini utoaji wa elimu bure utaenda sambamba na elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu pia umejielekeza kwenye afya vijijini. Kama ambavyo Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ilivyoahidi, kila Mkoa kuwa na Hospitali ya Rufaa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati, naomba Serikali itakapokuja na Mpango ujieleze kinagaubaga, awamu hii itaongeza zahanati ngapi katika vijiji vyetu? Itaongeza Vituo vya Afya vingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali hii ijielekeze zaidi kwa watoa huduma kwenye Zahanati hizo na Vituo vya Afya. Yapo maeneo katika Mkoa wetu wa Pwani, hasa maeneo kwenye Jimbo la Kibiti, Kiongoroni, Kiechuu, Maparoni; maeneo haya ni maeneo pekee ambayo yanahitaji uangalizi maalum, kwani zipo Zahanati mpaka sasa hazina watoa huduma, hazina Madaktari wala nyumba. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie maeneo yale maalum hasa yale yanayozungukwa na maji, ikiwemo Wilaya ya Rufiji, hususan Jimbo la Kibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Sera za Serikali za kubana matumizi na katika Sera za Mapato. Hapa najielekeza kwenye utaratibu wa retention. Naipongeza Serikali kwa kuamua ku-retain fedha zake na Sheria ya Fedha (Public Finance Act) ya mwaka 2001, ilisema kinagaubaga, fedha zote zitaingia kwenye Mfuko Mkuu (Consolidated Fund).
Kwa hiyo, hapa nampongeza Dkt. Mpango kwa kuja na hili suala kwamba yapo mashirika ya EWURA, TICRA, walikuwa na pesa nyingi zaidi. Yapo mashirika, hata hizi tunazosema zinasimamia mbuga zetu, lakini tulijionea Taasisi ya Ngorongoro, TANAPA; kuna wakati fedha zilitumika kwa kulingana, siyo na bajeti, lakini matakwa ya viongozi wa wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini fedha hizi zikikusanywa kwenye Mfuko Mkuu, lakini naiomba Serikali ijielekeze kuuondoa urasimu. Hazina mjipange kupunguza urasimu na kuzileta pesa hizi kwa mashirika haya kwa wakati uliokusudiwa. Ila ombi langu, Halmashauri zetu tuendelee kukusanya kwa sababu tunayo Mabaraza ya Madiwani yatasimamia, tutafuata Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Halmashauri, tukusanye na tuweze kufanya maendeleo ambayo yanakusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, najielekeza kwenye suala la kilimo. Tulikuwa na utaratibu wa Kilimo Kwanza, lakini pia tulikuwa na utaratibu wa SAGCOT; vile vile kipindi cha BRN kuna baadhi ya maeneo yalichaguliwa kuongeza uzalishaji wa sukari, mpunga na mahindi. Nina imani kabisa, kupitia Mpango huu, naomba kipaumbele pia kiwekwe kwenye kilimo na mipango iliyowekwa hii, BRN, bado ina nafasi ya kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna maeneo ambayo yalitengwa, kwa mfano Wilaya ya Bagamoyo lilitengwa eneo, watu wapo ECHO Energy, wanataka kufanya kazi kwa haraka, tuzalishe sukari nyingi tupunguze pesa tunazozitumia kwa ajili ya uagizaji wa sukari zifanye shughuli ambazo ni za kutoa huduma ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika ujenzi wa viwanda; Wilaya ya Kisarawe tumetenga eneo la viwanda. Tunalo, tunategemea miundombinu ya maji na miundombinu ya umeme ili eneo lile wadau mbalimbali wanaojitokeza waweze kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nina imani sana na Serikali. Serikali inaweza! Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ina uthubutu. Serikali hii, amani ipo. Waliokuwa na nia ya kuvuruga amani ni waliokwenda kwenye Vituo vya Television na kujitangazia ushindi wamepata kura milioni kumi; hawana fomu za matokeo na walikuwa na Mawakala nchi nzima, wanajitangazia kura wakiwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuliokuwa site, tuna uhakika, kura tulizihesabu vituoni, tunajua Wagombea Urais walipata kura ngapi, hakukuwa na utata. Matokeo yaliyotangazwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli alishinda, hatukuwaona mlete ushahidi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani Serikali haijachoka, itafanya kazi. Hata hivi karibuni Serikali kupitia utaratibu wa utumbuaji wa majibu, napongeza ilivyotumbua jipu la Hati Fungani. Vipo Vyama vinajidai vinapinga ufisadi, lakini hatukuwaona kwenye majukwaa wakisema kupinga ufisadi. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alijipambanua, alitoa ahadi kwamba yeye atapambana na ufisadi. Wengine hatukuwasikieni! Mlisemea wapi? Leo mkija ndani ya Bunge, mnasema ninyi ndiyo mnapambana na ufisadi, lakini naomba mtoe boriti zilizopo kwenye macho yenu kisha mtazame Vyama vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, napongeza na Bunge hili, wananchi wa Tanzania msibabaishwe na miongozo na kanuni, zimejaa Kanuni nyingi; lakini ukiangalia hata Taarifa yao hiyo waliyoandaa, Mpango huu umeandaliwa kwenye karatasi mbili tu. Zote hizi wameandaa maoni ya Mpango wa Miaka Mitano ambao haujadiliwi sasa! Maoni ya Mpango huu ni kurasa mbili tu. Kuonekana, mmesituka! Hongereni Watanzania. Ahsanteni sana. (Kicheko/Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Pia namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa kunipigia kura na kunifanya kuwa Mbunge katika Bunge lako. Niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano kwa kuanza kazi vizuri, nina kila sababu ya kumpongeza kwa matukio yafuatayo machache:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa usimamizi mzuri wa makusanyo ya mapato ambayo naamini yatatekeleza mpango wa maendeleo unaokuja na bajeti hizi ambazo zinaendelea. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa fly over na naipongeza Serikali ya Japan ilikuwepo, napongeza kwa uzinduzi wa mradi wa Kinyerezi I pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi kinyerezi II. Pia nampongeza sana Rais Museven kwa kukubali bomba la mafuta kupitia Bandari ya Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nayapongeza haya nikiamini kabisa viongozi wa Mataifa mbalimbali ya nje yana imani na Mheshimiwa Rais wetu, hawana tatizo na kuona kwamba mpaka sasa instruments hazijatoka, kwa sababu wanaamini wao ni kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia napongeza fursa ambayo Serikali ya China imeonesha kutaka kutu-support katika ujenzi wa reli ya standard gauge. Naipongeza kwa sababu China wanataka kutoa hela nyingi lakini hawajapata kuuliza instrument ya Waziri wa Mawasiliano wala ya Waziri wa Ujenzi, naamini wao wanaamini hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na pongezi hizo, naomba nijielekeze kwenye bajeti. Nampongeza Waziri wa TAMISEMI, pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora na Naibu Waziri wameanza kazi vizuri, wanashughulikia masuala ya mishahara hewa vizuri na wanapambana. Nikipitia hotuba ya Waziri wa TAMISEMI pamoja na mikakati ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, naomba nijielekeze zaidi kwenye sekta ya afya. Katika kujielekeza sekta ya afya nimeona kupitia bajeti hii mkakati wa Serikali wa ujenzi wa vituo vipya vya afya, ujenzi wa zahanati, ukarabati wa hospitali za wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali iangalie sera, Wizara ya Afya nadhani ingekuwa vizuri kama ingepewa jukumu pia la usimamizi wa vituo hivi kwa sababu wao wanasimamia sera. Inapokuwa TAMISEMI na wao wana mambo mengi, lakini changamoto kubwa zipo kwenye maeneo ya vituo vya afya, ziko kwenye maeneo ya hospitali za wilaya na ziko kwenye zahanati. Kwa kuwa TAMISEMI wanaendelea kusimamia, lakini kwa kuwa haihusiani na masuala ya sera, usimamizi kidogo unakuwa hafifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijielekeza zaidi katika ujenzi huo wa zahanati na ukarabati nimeona bajeti ya mwaka 2014/2015 takribani bilioni 263 zilitumika, lakini mwaka 2016/2017 zimetengwa bilioni 27. Naona hiki kiwango ni kidogo nikiangalia changamoto ambazo zinatukabili na nazielekezea changamoto hizo kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Mkuranga ambayo haina X-Ray; kituo chetu cha afya cha Kibiti katika Wilaya mpya hakifanyiwa upanuzi wa jengo la wazazi; kwenye kituo chetu cha afya Mkoani Kibaha changamoto kubwa ni jengo la upasuaji, pia hata kituo cha afya Maneromango, vifaa vya upasuaji vipo, lakini jengo halipo. Nashauri katika kifungu hiki angalau kingeongezwa zaidi ili tuweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona wakati nikipitia hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani katika ukurasa wa tatu, nanukuu:
“Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka Wabunge wa CCM waache kufanya ushabiki Bungeni”.
Pia katika ukurasa huo huo nanukuu kwamba:
“Vyombo vya Habari vya Umma na Binafsi virushe moja kwa moja mijadala ili wananchi wajue fedha zao zinavyogawanywa katika Halmashauri zao na wajue ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 89 imeipa Bunge wajibu wa kutunga Kanuni za Uendeshaji wa Bunge hili, Kanuni za Kudumu za Bunge, Kifungu 116 zimempa mamlaka Spika kuunda Kamati, pia zimeipa mamlaka Kamati zenyewe kuchagua Wenyeviti wao wa Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Usimamizi wa pesa za Halmashauri (LAAC) na Kamati ya Hesabu ya Serikali (PAC), kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ambazo zinatokana na Katiba zinatakiwa ziongozwe na Wapinzani. Leo wanapoituhumu Serikali kuvunja Katiba, kuvunja taratibu mbalimbali, wao hawajitazami mpaka leo Wenyeviti wa Kamati hizo hawajachaguliwa, leo wanaposema Bunge lioneshwe live lakini wao hawajatimiza wajibu wao zaidi ya miezi minne, Kamati hazijapata Viongozi kutoka Kambi ya Upinzani na mamlaka hiyo ni ya Spika.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekeni Kiongozi unajipangia utaratibu kuteua Wajumbe wa Kamati hukupewa mamlaka hiyo! Ni mamlaka ya Spika kuwapanga Wabunge kwenye Kamati zao kwa vigezo vyao na Kanuni tumetunga wenyewe za Bunge hili. Nilidhani wangetoa ushauri kwamba Kamati zinazoongozwa zipewe mamlaka zenyewe. (Makofi)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Taarifa!
Taarifa....
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa siipokei, kwa kuwa hakujielekeza kwenye Kanuni yoyote na mimi nimesema kama ana ushahidi wa Party Caucus kukutana ili kuchagua viongozi, walichaguliwa ndani ya Kamati husika, hiyo taarifa yake siyo sahihi naomba watimize wajibu wao kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG (Controller and Accounting General) amewasilisha ripoti yake, lakini najua kwa nini hawajachagua mpaka sasa hivi, wamepima maji wameona yana kina kirefu. Mheshimiwa Aeshi endelea na kazi, chapa kazi PAC, umegundua mambo, LAAC nayo endeleeni, chagueni Makamu Mwenyekiti aendelee na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze pia kwenye ukurasa wa mwisho wa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wanaelezea masuala ya vifungu vya Sheria ya Bajeti, kwa kuwa kitabu hiki kinatumika na Wabunge wote na ni upotoshaji, sasa nataka nijielekeze kwenye Public Finance Act hiyo, Kifungu 19 naomba wanavyo-quote Sheria za Fedha wamalizie wasi-quote nusunusu. Kifungu cha 19 kinasema; “If at the close of account for any financial year it is found that moneys have been expended:-
(a) on any expenditure vote in excess of the amount appropriated for it by an Appropriation Act;
(b) for a purpose for which no moneys have been voted and approaprated.
(c) the amount of excess expended or not appropriated as the case may be shall be included in a statement of expenditure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mwaka wa fedha wa Serikali haujakwisha msiwahishe shughuli, mnapo-quote Sheria mbalimbali za Fedha mmalizie, mme-quote Public Finance Act 18 (a) na 14, kwa nini hamku-quote 19 ambayo ndiyo imetoa mamlaka mwisho wa mwaka wa fedha kama kuna pesa zimetumika za ziada ambazo hazikutengwa ziwasilishwe ndani ya Bunge katika taarifa maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha haujakwisha lakini kama pia pesa zilitumika zaidi na naomba kwenye masuala ya barabara, nimeona kwenye kitabu cha TAMISEMI mpango wa ujenzi wa barabara, namwomba tu Waziri wa Fedha mwaka wa fedha wa Serikali ukiisha awasilishe statement, tuipitishe kwa sababu yamefanyika mambo ya heri na mamlaka hiyo anayo, kwa hiyo hakuna uvunjaji wowote wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niwazungumzie Wabunge Wanawake namna ambavyo hawashiriki vikao vya Kamati vya Fedha Halmashauri za Wilaya. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, Ibara ya 66, imetaja aina za Wabunge wakiwemo Wabunge Wanawake. Wabunge wote wana haki sawa, inashangaza kwamba Wizara ya TAMISEMI Katibu Mkuu anatoa mwongozo wa kuwatoa Wabunge Wanawake ambao wanasimamia maslahi ya wanawake, maslahi mapana na changamoto mbalimbali katika Kamati za Fedha, kama leo wanapoleta milioni hizo hamsini, asilimia 10 ya Vijana na Wanawake, mambo ya sekta ya afya, mambo ya kilimo, Mbunge Mwanamke na yeye ana mchango mkubwa kwenye Kamati ya Fedha ambayo inakutana kila mwezi, Wabunge wana uwezo wa kuchangia hoja na kujenga hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya TAMISEMI tumelisemea kila siku, huu ni mwongozo tu, mtoe mwongozo kuwa Wabunge Wanawake na Madiwani Wanawake, tusibaguliwe na wala tusinyanyaswe, kwa sababu pia Katiba imekataza sheria yoyote inayoonesha ubaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Bajeti na naunga mkono kwamba hakuna uvunjaji wowote wa Kanuni wala wa Katiba, wanaposhutumu na wao wajitazame, wajisahihishe, kidole kimoja kinawatazama. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa afya njema inayoniwezesha kutoa mchango katika sekta zinazosimamiwa na Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba na Naibu wake pamoja na Makatibu Wakuu na wafanyakazi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuendeleza Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kujielekeza kwenye tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa sehemu ya bajeti ya maendeleo ambapo hadi tarehe 30, Aprili, 2016 kiasi cha shilingi 5,192,797,589/= tu zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ikiwa ni asilimia 15.9 ya fedha zilizoidhinishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ya kutopeleka kwa wakati fedha za maendeleo zinaweza kufifisha jitihada ya kuleta mapinduzi ya kilimo itakayopelekea uzalishaji wa malighafi zitakazotumika kwenye viwanda, ambacho ndiyo kipaumbele cha Serikali hii ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali nashauri ijitahidi kupeleka kiasi kilichosalia kwenye Fungu hili la maendeleo la Wizara hii ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kupongeza Wizara, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bodi ya Korosho, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Pwani na wadau wengine wa korosho kwa kuwezesha mfumo wa Stakabadhi Ghalani kuanza kutumika tena katika Mkoa wetu wa Pwani. Mfumo huu wa stakabadhi ghalani kwa mwaka huu umepelekea wakulima wa korosho wa Wilaya za Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Bagamoyo na Kibaha kupata bei nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza sana Serikali kwa kuwezesha Vyama Vikuu na Vyama vya Ushirika vyenye madeni ya zamani katika Benki za CRDB na NMB kushiriki katika msimu huu wa korosho na kuweka utaratibu wa kurejesha madeni hayo ya Vyama vya Msingi bila kuathiri hela za wakulima. Naipongeza sana Benki Kuu ya Tanzania kwa kukubali kuwa msuluhishi/mpendekezaji wa utaratibu wa ulipaji wa madeni ya vyama hivyo bila kuathiri utaratibu wa Stakabadhi Ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara kuhakikisha pembejeo za zao la korosho (dawa) zinapatikana kwa wakati ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa korosho na hivyo kuipelekea nchi kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa asubuhi ya leo kuweza kuchangia bajeti ya Wizara yetu hii ya Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi. Nianze moja kwa moja, kwanza kuwapongeza Walimu wote nchini Tanzania kwa kazi kubwa wanayofanya. Kipekee niwashukuru Walimu hao kuanzia Shule ya Msingi, Sekondari Mtwara Girls na Ndanda High School, Chuoni IFM, Mzumbe University na Walimu wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kwa namna ambavyo wamenisaidia, nimepata fursa ya kusimama ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba leo, kabla hata sijachangia niliwasiliana na wanafunzi niliosoma nao ambao pia ni Walimu ambapo, changamoto nitakazozichangia hapa na ni maombi yao, ni maombi yaliyotokana na Walimu wenyewe baada ya kuwasiliana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi vizuri; hatua alizochukua dhidi ya Bodi ya Mikopo, hatua alizozichukua dhidi ya TCU, binafsi naziunga mkono. Pia, nampa pole sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufiwa na mama yake mzazi, Mwenyezi Mungu ampe subira na wepesi katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nina matumaini sana ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuwa, naamini inaongozwa na Rais wetu aliyepata kuwa Mwalimu, Waziri Mkuu aliyepata kuwa Mwalimu, First Lady aliyepata kuwa Mwalimu, Walimu wana matumaini makubwa sana katika Awamu hii kwamba, jitihada zilizoanzishwa katika Awamu mbalimbali changamoto zao nyingi zitapata fursa ya kutatuliwa katika Awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nipongeze kwa utekelezaji wa suala zima la Waraka Namba Tano (5) wa Elimu Bure ambao umeanza mwaka jana Disemba, 2015 mpaka sasa. Nipongeze dhamira ya Serikali ya kutenga kiasi cha bilioni 18 kila mwezi kukabiliana na majukumu mazima ya kutoa elimu kwa Shule za Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Pwani suala hili limetusaidia, ongezeko la uandikishaji kwa ngazi ya mkoa limefikia 150%. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile 50% ya watoto walioongezeka katika Elimu ya Awali na Msingi ni wazi kuwa kuna wazazi ambao ilikuwa inashindikana kabisa kupeleka watoto wao kutokana na changamoto mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwanzo wa hesabu moja. Natambua Roma haikujengwa kwa siku moja. Katika utaratibu mzima wa utoaji wa elimu bure, naiomba Wizara iangalie, isije ikawa utekelezaji wa elimu bure imewapa Walimu Wakuu mzigo mkubwa na Walimu wenyewe bado wanalalamika mishahara bado ni midogo na marupurupu yao mengine; kwa nini nasema hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji huu wa elimu bure, kuna kipengele cha utawala. Utakuta shule inawezekana ina wanafunzi wachache, lakini gharama za utawala ni moja; kama ni bei ya shajara ni moja, masuala ya mitihani ni mamoja, lakini utakuta ile 10% hasa kwa shule ambazo zina mazingira magumu, mfano shule za Kata ya Kibindu Wilaya ya Bagamoyo, Shule za Delta, Kiongoroni, Mbuchi, Msala, Maparoni Wilaya ya Rufiji! Shule za Wilaya ya Kisarawe zilizopo Vikumburu, Dololo, Kimaramisale, Mafia, Visiwa vya Jibondo, Chole, Mkuranga, Visiwa vya Kwale, Koma, mazingira yao ni magumu kiasi kwa mfano Visiwa vya Rufiji, kuja Makao Makuu ya Wilaya Utete, Mwalimu anatumia 50,000/= nauli. Zilikuwepo boti kwa ajili ya kuwasaidia walimu hawa, lakini zile boti zimeharibika, lakini anaenda kufuatilia cheque kwa ajili ya masuala ya utawala. Kwa mfano kuna shule iko Msala na inapokea 40,000/= asilimia 10 ni 4,000/=, lakini afuatilie hiyo hela mpaka Utete ni 40,000!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iangalie mazingira haya magumu na iwatendee haki Walimu, wamelalamika! Walimu sasa wanatumia pesa zao mifukoni kwa ajili ya uendeshaji wa shule. Vile vile suala hili limeathiri masuala ya mitihani; kifungu cha mitihani hakitoshelezi, kwa hiyo, baadhi ya mitihani imepunguzwa! Labda shule zilipanga utaratibu mock ya Kikata, mock ya Wilaya, mitihani ya kila mwezi, ya kila wiki na mitihani hii ilikuwa inasaidia ufaulu. Kwa hiyo, nadhani Wizara iangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Walimu niliowasiliana nao wameomba hiki Chama cha Walimu Tanzania, wamesema chama hiki kimeshasimama, kina miliki jengo, kinafungua benki! Masuala ya kuwakata asilimia ya mishahara yao kwa ajili ya kuchangia chama ambacho kimeshasimama, kina uwezo, naomba Wizara mfuatilie, Walimu wanalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini chama hiki hakipo wazi! Sisi tumekaa Wilayani, hatuoni msaada mkubwa kwa Walimu wetu, lakini mara nyingi utakuta kwenye masuala ya michakato ya kisiasa kiko mbele, lakini siyo katika kuwasaidia Walimu! Nadhani michango waliyochangia Walimu ingewezekana Chama cha Walimu kingethubutu, sasa hivi kinamiliki benki, kinamiliki jengo kubwa Dar-es-Salaam, kingethubutu hata kuwapunguzia makali ya maisha walimu ambao ni wanachama wao. Kwa hiyo, hilo nalo walimu waliniomba, lakini wamesema sasa hivi chama kimesimama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Walimu wameiomba jitihada za kuimarisha miundombinu. Bajeti ya miaka iliyopita, hususan mwaka jana, kulikuwa na kifungu waziwazi cha ujenzi wa nyumba zao kama 500 kila mwaka.
Nimejaribu sana kuangalia kwenye bajeti ya mwaka huu sioni vizuri, hakionekani waziwazi, lakini bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Walimu wameniomba, kuna Walimu waliajiriwa Juni, 2015 mpaka leo bado hawajalipwa pesa zao za kujikimu na pesa zao za nauli, inawakatisha tamaa. Walimu pia, wameniomba Serikali iendelee na jitihada za kulipa madeni yao; wanatambua hata mwaka jana mwezi wa 10 baadhi ya madeni yao yamelipwa, lakini kwa kuwa yanajilimbikiza kwa muda mrefu, Walimu wameomba pia suala hili litekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu pia wameniomba niwasilishe, utekelezaji wa Waraka wa Posho za Viongozi, sijaliona waziwazi kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri! Walimu Waratibu wa Elimu Kata walipangiwa sh. 250,000/=, Wakuu wa Shule walipangiwa sh. 200,000/=, hizi zinaweza zikawasaidia, naomba hilo nalo litazamwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Pwani tunalo tatizo, baadhi ya shule zetu zina Walimu mmoja mmoja. Mfano Shule ya Gundumu Kata ya Talawanda, Shule ya Kwa Ikonji, Pera, Kata ya Kibindu ina Mwalimu mmoja, lakini shule hizi zina madarasa kuanzia la kwanza mpaka la saba. Kwa mfano kwenye Shule ya Gundumu kuna Walimu wawili wanajitolea kwa sh. 50,000/= lakini tangu Disemba hawajalipwa! Kwa hiyo, mimi binafsi kama Mbunge wao nimeona niwasaidie, nilichukue jukumu hilo ili niweze kuona jinsi Serikali itakavyotusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la Bodi ya Elimu. Kwanza nakubaliana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya TCU, lakini pia nasikitika hela zaidi ya milioni 700 zilizotumika kwa vijana wale na mimi binafsi siyo Mwalimu, lakini nikiangalia maelezo ya Mheshimiwa Waziri na vigezo walivyovitumia kuwadahili wale na nikirejea maelezo ya Kamati yetu ya Huduma za Jamii, ukurasa wa 11 kwamba, Kamati imebaini kuwa, vijana wengi wenye alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya elimu ya juu wameshindwa kuendelea kutokana na hela hizi za mikopo kuwa si nyingi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kama wapo vijana wenye elimu, wenye vigezo, wako mitaani wanakosa fursa ya mikopo, tufike hatua ya kuwadahili wanafunzi wenye Arts kusoma masomo ya sayansi kwa ajili ya kuja kutufundishia watoto wetu! Kwenye suala hili kwa kweli, naunga mkono. Nimesema mimi siyo Mwalimu, lakini naamini Profesa Ndalichako amejiridhisha, naamini na Tume aliyoiunda itafanya kazi nzuri, lakini hatua lazima zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nimalizie kwa kuomba huu ujenzi wa miundombinu, hasa kwenye shule ambazo, kwa mfano tuna Shule ya Mlegele Kisarawe, tuna Shule ya Kidugalo, Tondoroni, Sofu na Kola; shule hizi zina vyumba viwili viwili vya madarasa, lakini zina madarasa kuanzia la kwanza mpaka la saba! Kwa hiyo, utakuta changamoto katika miundombinu ya elimu, bado ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niiombe Serikali, maoni ya Kamati yetu ya Huduma za Jamii ni mazuri sana, hasa uwekezaji kwenye Sekta ya Elimu. Tunapoliandaa Taifa letu kuwa Taifa la kipato cha kati na Taifa la viwanda, tunatarajia kufufua Viwanda vya Nguo, Viwanda vya Kusindika Korosho, tusipoandaa wataalam na tukawekeza zaidi katika Wizara hii, hasa miundombinu yake. Tunaweza tukawa na kila kitu, lakini Taifa litakalokosa wafanyakazi wenye elimu inawezekana hata hii azma nzima tusiitimize. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniamsha salama na kusimama ndani ya Bunge lako na naanza kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na jambo la msingi lililozungumzwa na Waheshimiwa wachache waliopita juu ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011. Najielekeza kwenye Sheria ya Manunuzi ya Umma kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais kupitia hotuba yake ndani ya Bunge hili lakini kutokana pia na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo asilimia 40 inatarajiwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunatambua wakati ule ilipokuwa chini ya asilimia 40, kwenye asilimia 22 na kuendelea tuliona changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, udhaifu wa taasisi mbalimbali katika usimamizi wa matumizi ya pesa za maendeleo na za kawaida. Leo tulipopokea taarifa ya miscellaneous amendment zinazotarajiwa kuwasilishwa Bungeni kutoonekana kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma imetufanya baadhi ya Wabunge tupate mashaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mashaka hayo nikaenda kuchukua taarifa ya PPRA ya mwaka 2014/2015; nikajaribu kupitia kwa kina upungufu uliobainishwa na taarifa hiyo. Pamoja na kwamba taarifa inaonesha masuala ya manunuzi ya umma katika taasisi mbalimbali za kiserikali level of compliance iko juu lakini ukaguzi wa mashirika haya, kwa mfano mwaka 2014/2015 wamekagua jumla ya taasisi za manunuzi 80 kati ya hizo 39 ni za Halmashauri, lakini tunazo Halmashauri 168. Kufanya maamuzi ya kuchelea kuleta marekebisho ya sheria kwa ripoti kwamba labda mambo siyo mabaya si sahihi kwa sababu hata ukaguzi unafanyika kwa taasisi chache.
Kwa hiyo, niombe Serikali iwasilishe Muswada huo tufanye marekebisho kwenye baadhi ya vipengele ili asilimia 40 ya fedha za maendeleo zilete tija na value for money na matumizi hayo yaonekane ili Watanzania wenzetu waweze kufaidika katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo naungana na Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa mimi ni Mbunge wa Viti Maalum na kundi kubwa naloliwakilisha hapa ni wanawake na vijana; na wanawake na Watanzania wengi walikipigia kura chetu kwa matumaini ya ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Tunaamini ahadi hii ikitekeleza itakuwa chachu katika uibuaji wa miradi mbalimbali na pia itakuwa chachu ya mzunguko wa fedha katika maeneo yaliyokusudiwa. Naungana na maoni ya Kamati yangu, Serikali pamoja na changamoto iliyopo, lakini dhima ya kuinua uchumi wa watu wachache au kupitia vikundi vya SACCOS ni muhimu kwa sababu mwisho wa siku watalipa kodi kutokana na shughuli watakazozifanya na itaongeza mapato ya Serikali, huu ni mzungunguko tu.
Kwa hiyo, niombe Serikali iongeze kwani asilimia sita haitoshi na wengine tumeshafanya ziara katika maeneo mbalimbali, wanawake wa Kibaha, Mafia, Mkuranga, Rufiji, Bagamoyo na Kisarawe pamoja na vijana na makundi mengine mbalimbali yanayohusiana na masuala haya ya asilimia 20 wako tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nijielekeze kwenye suala zima la utekelezaji wa bajeti ya mifuko kwa 2015/2016. Tunaweza tukawa na bajeti nzuri, tunaweza tukatenga pesa nzuri kwa maendeleo na matumizi mengineyo lakini kama mifuko hii kwa mfano Mfuko wa NAOT mpaka mpaka Machi, 2016 una asilimia 45 tu. Ofisi hii Kikatiba imepewa dhima ya kukagua matumizi na mapato ya fedha za Serikali. Kwa dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kupambana na ufisadi, kupambana na ubadhirifu, kupambana na maovu mbalimbali na tumeona kasi yake, mchango mkubwa atasaidiwa na Ofisi ya Ukaguzi wa Serikali (National Audit Office). Kwanza niiombe Wizara ijitahidi kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha iweze kuwawasilishia fedha ambazo hawajasilisha mpaka sasa, asilimia 45 mpaka Machi ni kiasi kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna Mifuko ya Mahakama pia asilimia 61, Mfuko wa Bunge asilimia 49 pamoja na interest. Nataka kusema dhima ya mifuko hii ina nafasi kuchangia katika ukuzaji wa uchumi. Kwa hiyo, napenda kusisitiza Serikali ilione hili kwa sababu kama Mfuko wa Ukaguzi utakuwa haufanyi kazi iliyokusudiwa hata uwepo wa Bunge hili katika kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali ambapo msaidizi wetu mkubwa ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inawezekana tukapata tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nizungumzie Wizara zingine, kwa mfano mpaka mwezi Machi Wizara ya Kilimo ilikuwa haijapelekewa fedha ya maendeleo. Kama kweli tunataka kuongeza mapato ambapo tunategemea kilimo ndicho kitachangia katika mchango wa Taifa, Wizara hii mpaka Machi kuwa haijapelekewa fedha za ndani ni tatizo. Pia tunayo Wizara ya Afya asilimia 11 tu, hata Wizara yenyewe ya Fedha naomba niisemee pia asilimia sifuri. Wizara hii ina mchango mkubwa katika kusimamia uchumi wa Taifa letu kama ambavyo Wajumbe wengine wamesema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye masuala ya mishahara hewa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ametoa maelekezo na kwa namna ambavyo kazi imefanyika vizuri na kwa namna ambavyo Serikali imeweza kubaini zaidi ya watumishi hewa 10,000. Hata hivyo, inawezekana kabisa tatizo kubwa ni mfumo. Kwa hiyo, naungana na maoni ya Kamati kwamba Serikali izidi kuangalia mifumo yake hasa LAWSON ambao unatumika katika mishahara, lakini pia EPICA, kuweza kuiunganisha kati ya EPICA9 na LAWSON na isisitize matumizi ya Mkongo wa Taifa. Nadhani kupitia Mkongo wa Taifa masuala ya TEHAMA itaweza kuziunganisha Halmashauri na Serikali Kuu katika mawasiliano ya namna ya kudhibiti watumishi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tungependa kuona hatua za haraka zimechukuliwa kwa watu waliosababisha kuwa na watumishi hewa. Maana kama tumeshapata idadi ya watumishi hewa 10,000, kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa mwaka kilikuwa kinatumika, tunatakiwa tuwajue kinagaubaga na waliohusika wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa niiopongeze Wizara ya Fedha, niendelee kuwaomba…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa jioni ya leo kuchangia Bajeti hii ya Serikali, na nianze kusema naunga mkono hoja. Pia niungane na Waheshimiwa Wabunge wengi kukupongeza wewe binafsi na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha walioandaa bajeti hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kujielekeza kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa saba. Hotuba hii alinukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akifungua Bunge. Naomba ninukuu, kwenye ukurasa wa nane Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilijielekeza katika kusema kwamba huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa maji, elimu bora na afya ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Nimejielekeza kwenye hotuba yake, naunga mkono wazo la maombi ya kuongeza tozo ya Sh. 50 kwenye bei ya mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunamalizia bajeti ya mwaka ambao Bunge lilipendekeza tozo ya Sh. 50 kwenye lita moja ya mafuta, bei ya mafuta ilikuwa sh. 2,100 mpaka 2,400. Hapa katikati bei ya mafuta imeshuka lakini hatukuona athari yoyote, hazikushuka bei za usafiri, hazikushuka bei za vyakula, hazikushuka bei za aina yoyote, lakini mpaka sasa bei ya mafuta ni 1,700 hadi 1,900 bado Watanzania wana uwezo wa kuhimili ongezeko la Sh. 50. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini naomba niunge mkono pendekezo hilo ambalo limetokana na Kamati yetu? Ni kutokana na hotuba hii ambayo Awamu ya Tano inajielekeza kutatua kero hizi kubwa za Watanzania. Ukiangalia hotuba yetu kero kubwa ya Watanzania ukiacha maji inayofuatia ni upungufu wa zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka mmoja takribani akina mama 15,000 wanapoteza maisha, akina mama 42 wanapoteza maisha kwa siku, lakini sababu kubwa inayochangiwa kupoteza maisha kwa akinamama hawa ambao ni nguvu kazi ni uhaba wa vituo vya afya, uhaba wa zahanati na uhaba wa vifaa tiba. Pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri, bajeti hii ninavyoiona hakuna kifungu cha moja kwa moja kinachoonesha ujenzi wa zahanati, ukarabati au kumalizia majengo yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika kwa nini nasema hivyo? Tuliwasilishiwa mkeka na Wizara ya TAMISEMI ambayo ilikuwa inaonesha takribani bilioni 32 zimetengwa na Halmashauri zetu, lakini ukiangalia vyanzo vya Halmashauri zetu ni own source, Local Government capital grant ambavyo vyote havina uhakika. Ndiyo kusema hata huu mkeka unaoonesha kwamba kuna vituo vya afya vitakarabatiwa, kuna zahanati zitajengwa, kuna wodi zitaongezeka, hauna uhakika kwa sababu chanzo chake hakina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sisi wote Wawakilishi wa wananchi ndio tunaowasemea wananchi wetu kama walikubali tozo ya Sh. 50 wakati bei iko 2,100 hebu tuwaongezee tozo na kiasi kikubwa itahimiliwa na sisi wenyewe ili tuweze kutenga kiasi cha pesa kuziongezea hizi bilioni 32 ili hali ya vituo vya afya na zahanati zetu iboreke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa viwanda unategemea afya bora ya Mtanzania, lakini wanawake wakiwa ni moja ya nguvu kazi; tunategemea kuanzisha viwanda vya nguo, viwanda vya kubangua korosho; asilimia kubwa ya wafanyakazi ni wanawake, ambao wanahitaji kupata afya bora wakafanye kazi kwenye viwanda hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana na nasema hivyo naunga mkono hoja kwa sababu hata nikiangalia kwenye Mkoa wa Pwani kwenye orodha hii ya mkeka ulioletwa ni wilaya mbili tu; Kisarawe na Mafia. Wakati ninaposimama namkumbuka Daktari wa Zahanati ya Kijiji cha Kitomondo Kibaha Vijijini analala kwenye gari ndogo, hana nyumba na tulimwombea milioni 25 kumalizia nyumba. Tunapochangia Wabunge wanawake sekta ya afya inatuuma, inatugusa. Naomba Serikali ilitazame hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kama nilivyosema kwa sababu hata sasa tuna vituo vya afya 716 kati ya Kata 3,800 ni asilimia 18 tu, maendeleo ni mchakato lakini kama shilingi bilioni 30 katika shilingi bilioni 250 ambazo zitaongezwa kwenye miradi ya maji kwenda kwenye sekta ya afya, kupanga ni kuchagua. Naomba Bunge lako Tukufu kupitia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tupange mipango hii vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningeomba kujielekeza ni suala zima linalohusu mfuko wa CAG, na mimi naomba niingie kwenye rekodi na naomba kwa sababu naamini Hansard itatumika vizazi vijavyo na ninawapongeza Wabunge wote waliochangia kuomba Serikali itazame jicho la huruma ofisi hii ni wazalendo, tunaliomba hilo kwa sababu tunaamini ni mmojawapo ya nguvu itakayomsaidia Mheshimiwa Rais wetu ambaye amejipambanua wazi wazi kwenye hotuba yake atapambana na ubadhilifu, atapambana na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ina shilingi trilioni 29, matumizi ya kawaida shilingi trilioni 17, matumizi ya maendeleo shilingi trilioni 11, Ofisi ya CAG kufuatilia hizo hela, shilingi bilioni 18, kwenye matumizi mengineyo. Tuna Halmashauri 168 na mimi nayasema hayo kwa sababu nilishawahi kuwa Mkaguzi miaka kumi, najua adha ya ukaguzi! Najua utaratibu na kukagua unakagua kutokana na Tanzania Auditing Standards na International Auditing Standards, zipo taratibu. Leo tunapopeleka hela mpaka kwenye kijiji CAG anafikaje? Tunapopeleka hela kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, CAG anafikaje? Tunapopeleka hela kwenye pembejeo? (Makofi)
Kwa kuwa kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, ushauri inategemea, lakini kazi yetu kubwa ni kuisimamia na tunaisimamia kupitia oversight committee. Nikuombe kwa kulinda hadhi ya Bunge lako na kwa kuwa kuisimamia Serikali ni kupitia oversight committee isije tunakuja Bunge lijalo Kamati zako PAC na LAAC zinakosa kazi ya kufanya. Hela hizi nyingi. Naomba sana itazame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema ataangalia, ameji-commit lakini mwezi wa 12 mapitio ya bajeti CAG anatakiwa amalize kazi zake, tunaende kwenye kufunga mwaka wa fedha za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona na mimi niingie kwenye Hansard kwamba nimeisemea ofisi hii ili vizazi vijavyo viweze kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimeona nia njema ya Serikali ya kuleta usawa kwenye masuala ya pensheni, nami naunga mkono. Lakini naomba usawa huu ubainishwe kinagaubaga ni makundi gani? Kwa sababu tunayo Sheria ya Retirement Benefits za Viongozi wa Kisiasa walitajwa pale! Lakini ieleweke wazi hata Wabunge wanalipa kodi shilingi 1,200,000 kwa mwezi; kwa mwaka shilingi milioni 15, kwa miaka mitano ni shilingi milioni 75. Wabunge hawa pia wanachangia shughuli mbalimbali za maendeleo. Hata kuzika, madawati tumeunga mkono, vituo vya afya tunaunga mkono, lakini isionekane Watanzania msikubali kuamini kwamba Wabunge eti ni kundi linalojipendelea, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ingekuwa mimi ningewaombea pia wafanyakazi wa Tanzania msamaha kwenye kiinua mgongo chao. Mfanyakazi anafanya miaka 40, miaka 30, anavyostaafu kwanini asipewe kiinua mgongo chake? Kwa kuwa kundi la wafanyakazi, kundi la wanasiasa ni kundi ambalo liko loyal kulipa kodi, kwa nini nisiwatetee? Kwa nini isifike wakati nao wasamehewe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono. Najua kuwa kweli kuna changamoto katika misamaha ya kodi, zimetajwa taasisi…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha jioni ya leo kuchangia mapendekezo ya mpango yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha.
Awali ya yote nampongeza Waziri wa Fedha, sisi kama Kamati ya Bajeti tulishirikiana nae vizuri katika kujadili mapendekezo haya. Na naenda moja kwa moja kwenye mchango wangu katika suala zima la kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wake wa kutoa elimu bure, nikiwaona mamia ya wanafunzi walioongezeka kwenye shule za msingi, sekondari, waliokuwa wanapoteza fursa kutokana na ada na michango mbalimbali na nikiona utayari wa wazazi kuchangia huduma ambazo pengine Serikali haijachangia kwenye ule mchango wa kila mwezi kwa kweli nafarijika. Ndio maana baadhi ya maeneo sisi tumejipanga tunafyatua matofali kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya shule, ujenzi wa madarasa mapya na ndio maana baadhi ya maeneo tumejipanga, tumetengeneza wenyewe madawati pamoja na Waheshimiwa Wabunge acha yale ya kupewa na Bunge. Lakini yapo maeneo tumechangia madawati, tumejenga nyumba za kuhifadhi hayo madawati. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye masuala ya kufungamanisha maendeleo ya viwanda na afya. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali pia kwa jitihada mbalimbali za uboreshaji wa afya husasan katika tukio la mkutano wa wafadhili wa Kimataifa juu ya afya ya mama na mtoto. Nampongeza sana Mheshimiwa Ummy pamoja na Wizara yake kwa kufanikishwa kufanikisha kupatikana kwa zaidi ya dola milioni 30 kwa ukarabati wa vituo vya afya mia moja. Ukarabati huo utahusu ujenzi wa theatre, maabara ya kuhifadhi damu, wodi ya wazazi, nyumba moja ya mtumishi. Ninaamini itakuwa ni ukombozi mkubwa na Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa imeaanza vizuri. Kwa kuwa tuna vituo 489, vituo 113 ndiyo vyenye fursa hizo ukivijumlisha na vituo hivi mia moja vinabaki vituo 376. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali, natarajia mapendekezo ya mpango huu utakapokuja kuwa kamili na tutakapo kaa Kamati ya Mipango mwezi wa pili, nadhani watakuja na mapango utakaoainisha vituo vilivyosalia namna ya ukarabati na uboreshaji, lakini pia ujenzi wa zahanati mpya kwa ajili ya kupunguza vifo vya akina mama, wajawazito na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimewasilishwa taarifa mbalimbali; mpango nimeuchangia kwenye Kamati, taarifa zilizowasilishwa kuna taarifa ya Waziri, lakini kuna taarifa ya Waziri Kivuli. Naomba kwa kuwa taarifa zote ni za Bunge na zinajadiliwa na ninapojadili hapa, kambi nyingine huwa wakiona Wabunge wanachingia wanasema anataka Uwaziri. Najua Wizara ile imejaa, Mawaziri wapo wanatosha lakini nachangia ili kuweka sahihi kumbukumbu na kuuacha upotoshaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo ukurasa wa 19, tumeambiwa tulipitisha bajeti hewa na katika ukurasa wa 19, katika maelezo ya Waziri Kivuli anaeleza kwamba, sisi tulipitisha shilingi trilioni 23 kama matumizi. Nataka nimfahamishe kwa kuwa Waziri wetu Kivuli ni mgeni katika Wizara hiyo, alikuwa anahudumu Wizara ya Ardhi, mambo bado hajayajua. Lakini nataka nimfahamishe kuna vitabu Volume III, aliruka fedha za maendeleo kwa Mikoa bilioni 4.3. Pia aliruka fedha za maendeleo kwa ajili ya Halmashauri trilioni 1.3 na trilioni nne, hakuna, hakuna! Kwa kuwa hotuba hii ilichapwa kwenye magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako endapo zinawasilishwa hotuba zenye nia ya kupotosha na watu waliondoka wenyewe ndani ya Bunge. Napenda niwataarifu Watanzania hatukupitisha bajeti hewa na hili nimelisemea kwa sababu Mheshimiwa Waziri Kivuli huyu hawezi kuendana sawa na Dkt. Mpango wala Dkt. Ashatu na watendaji wa Wizara ya Fedha waliopoteza muda mwingi kuandaa makaburasha haya, kila kitu kiko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niweke record sawa na kwa kuwa iligusa pia Kamati; anapozunguza masuala ya bajeti wa kuwasilisha pia maoni ni Kamati. Sasa nashangaa mwenzetu, lakini ninaomba pia wakati mwingine upangaji wa Wizara ziangalie na taaluma pia, nilishangaa Mwanasheria kuwa Waziri wa Fedha, nilishangaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mapendekezo ya mpango walifanya tathimini ya sekta ya fedha na hapa naomba nijielekeze ni kweli katika taarifa aliyowasilishwa Waziri kunaonyesha mikopo ya kibiashara na shughuli za uchumi kwa quarter iliyoanza Julai zimeshuka na sababu zinazopelekea ni kupungua kwa shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ikae na mabenki, ikae na sekta za fedha kwa sababu sekta hii inachangia kwenye ukuaji wa uchumi kwa mwaka ambao miezi sita imechangia zaidi ya asilimia 13 inawezekana kupungua kwa fedha katika mabenki hayo inasababishwa na shughuli mbalimbali au maendeleo ya teknolojia ya simu ambazo watu wengi wanatumia miamala ya fedha au masuala ya microfinance. Kwa kuwa inachangia ningeomba sana Serikali isikilizane na sekta hii ya fedha, lakini sekta ya fedha nayo iweke mazingira wezeshi itafute wateja katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho, muda umeisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho lilizungumzwa, ukiangalia umbile la…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Subira, muda umekwisha.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Eeh! Ahsante!
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, asubuhi ya leo na mimi niweze kuchangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Serikali kwa marekebisho haya, lakini nampongeza kwa kuwa marekebisho mengi yaliyowasilishwa yamelenga kuimarisha ustawi wa wanawake na watoto, kwa hiyo ninampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, name nianzie kwenye Marekebisho ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353. Napongeza Serikali kwa hatua hizi ambazo zimewasilishwa, hatua kali ambazo zimelengwa kuchukuliwa kwenye makosa ya kumpa ujauzito mwanafunzi, kuoa au kuolewa na mwanafunzi na pia kwa wale ambao wanaficha, wana-facilitate matendo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na adhabu hizi ambazo zimelenga kutekeleza Sera ya Elimu ya Msingi kwa lazima, na pia baada ya Serikali kuamua kabisa kugharamia elimu ya msingi mpaka sekondari, kuna tatizo la msingi kubwa la mdondoko wa wanafunzi. Ukiangalia miaka ya karibuni tatizo la ujauzito kwa wanafunzi siyo kubwa sana mimba zimepungua, lakini tatizo lililopo ni wanafunzi wanaoanza elimu ya msingi wanapofika elimu ya msingi wanapofika darasa la saba wanaomaliza ni wachache sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninatakwimu chache, kwa mfano katika Wilaya yetu ya Rufiji watoto walioanza shule mwaka 2009 ambao walimaliza shule mwaka 2015 walianza shule ya msingi takribani 8,555; lakini waliomaliza ni 4,433 ambao ni sawa na asilimia 52. Kwa hiyo inaonesha zaidi ya asilimia 48 hawakumaliza shule. Inawezekana ni ndoa, inawezekana ni mimba, lakini nashauri Serikali, baada ya marekebisho ya sheria hii, ijielekeze zaidi kutambua chanzo cha mdondoko ambalo tatizo ni kubwa zaidi, wanafunzi wanaoanza siyo wanaomaliza, nusu yake wanaishia njiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani tuangalie pengine nayo itasaidia kuweka adhabu kali hata wale ambao hawahudhurii madarasani, hajaolewa, hana mimba, lakini wapo majumbani. Tumeona hilo zoezi wakati wa kufuatilia mdondoko wa wanafunzi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninaliunga mkono ni katika Sheria hiyo ya Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Watoto ambayo inalenga kumwokoa mtoto wa kike katika suala zima la ukeketaji. Kutokana na madhara mkubwa ya ukeketaji, naunga mkono adhabu ambazo zimeainishwa, ninaamini kitendo hiki sasa hivi itapunguza idadi kubwa ya watoto wa kike ambao wanakeketwa na wengine siyo kwa hiyari yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naunga mkono marekebisho yanayopendekezwa juu ya suala zima la kuongeza thamani ya kesi za mirathi katika Mahakama za Wilaya Sheria Na. 352. Mirathi imekuwa tatizo kwa wanawake wengi wanakosa haki zao, na kwa kuwa Mahakama Kuu haziko katika ngazi Wilaya na kwa kuwa, kwenda ngazi ya Mahakama Kuu kwa hii sheria ya zamani ilikuwa inawakwaza wanawake wengi pamoja na watoto wao. Kwa hiyo, kuongeza kiwango cha kutoka milioni 10 mpaka milioni 100 kusikilizwa ngazi ya Wilaya ninaona ni ukombozi mkubwa sana kwa wanawake wengi na ninaamini wengi wanatumia fursa hii kufungua kesi ili haki ipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimeona mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya Misitu 323; adhabu mbalimbali zimependekezwa kuongezeka kwa namna ambavyo mtu yoyote atakayekutwa na mazao ya misitu isivyo kihalali. Naunga mkono mapendekezo haya kwa sababu hali ya uharibifu wa misitu yetu tatizo limekuwa kubwa sana, na kwa kuwa uharibifu wa misitu unachangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabia nchi, tunapata mvua chache, lakini pia tunaigeuza nchi yetu kuwa jangwa, kwa hiyo sheria hii imefika wakati muafaka kabisa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili pia nikumbushie Serikali tulilalamika hapa namna ambavyo mojawapo ya zao la misitu kitanda, kimeongezwa bei kutoka shilingi 8,000 mpaka shilingi 120,000; kwa hiyo naikumbusha katika hilo isiwe adhabu hizi zikatumika pia kuwakomoa wale wanaofanya kihalali na kufanya vijana wengi wanaoshughulika na biashara hizi kihalali wakakosa haki zao.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pia naunga mkono Marekebisho ya Sheria yanayohusiana na Migogoro ya Ardhi, migogoro hii hasa wanaoathirika wengi ni wanawake, namna ambavyo zile siku za kukata rufaa zimetamkwa sasa kinaga ubaga ili kupata haki kutoka Mabaraza ya Ardhi na Mahakama za Wilaya kwenda Mahakama Kuu, kuna matatizo ya kimsingi sana kwenye Mabaraza haya na watu wengi wanakosa haki zao, kwa kuwa sheria sasa imeainisha ni siku ngapi ambazo anaruhusiwa kukata rufaa katika Mahakama Kuu ili haki ipatikane.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua kabisa wanawake wengi hasa maeneo ambayo tuna migogoro ya ardhi, maeneo ya Mkwapani, Bagamoyo wana migogoro mingi ya ardhi, Kisarawe, Rufiji, Kibiti, Mafia, Mkuranga na Kibaha. Wanawake wanapofika kwenye Mabaraza ya Wilaya, hukumu inapotoka na kwa kuwa, kunakuwa na mkanganyiko na kwa kuwa, wanawake wengi wanaofika Mahakama zile uwezo wao unakuwa mdogo, inachukua muda mrefu kukata rufaa na anapokuwa nje ya kipindi kile haki yake anaikosa. Kwa hiyo ninaunga mkono kabisa kwamba, siku zilizowekwa hizi zitaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuunga mkono pia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria inayohusu Masuala ya Makosa ya Jinai, kutambua ushahidi wa mtoto, ili kama una-credibility ili uaminiwe na haki iweze kutendeka. Tumeona makosa mengi ya jinai wako watoto wanatoa ushahidi, lakini wakati mwingine kwa kuwa sheria haikuweka wazi, sasa kifungu hiki kimewekwa, ninaamini pia watoto watalindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaunga mkono mapendekezo ya namna ambavyo wenzetu wa Ustawi wa Jamii wanaweza wakatoa maoni kwa ajili ya kesi mbalimbali zinazohusu watoto. Pia ninaunga mkono namna ambavyo mtoto amelindwa na namna ambavyo adhabu zinazotakiwa kutolewa zihusiane na Sheria ya Mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa name pia ninaungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kukamilisha safu ya Wakuu wa Wilaya na wote walioteuliwa nawapongeza sana, hata wale walioachwa nawapongeza sana kwa kazi nzuri waliyoifanya katika maeneo mbalimbali, kwa kipindi cha utumishi na Mwenyezi Mungu pia atawajalia mengine na nawatakia kheri katika maisha ya mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono Muswada huu.