Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Taska Restituta Mbogo (46 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza nasimama mbele ya Bunge hili Tukufu, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na leo hii mimi Taska Restuta Mbogo nimesimama hapa nachangia hoja. Napenda kuwashukuru wananchi wangu wa Mkoa wa Katavi hususan akinamama walionichagua na kuniwezesha mimi kuwa Mbunge wa Viti Maalum ndani ya Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote wa vyama vyote mliomo humu ndani, mliofanikiwa kuja ndani ya Bunge hili Tukufu. Napenda nimpongeze Rais Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na napenda nikipongeze Chama cha Mapinduzi kwa kupata ushindi mkubwa na kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwa hotuba yake nzuri, lakini ninayo machache ya kuchangia kuhusu hotuba yake. Kwanza kabisa, napenda nichangie suala la viwanda. Tunaposema kwamba tunakwenda kwenye nchi ya viwanda tunatakiwa tuwe na maji ya kutosha, tuwe na miundombinu bora kama barabara, reli ambazo zinapitika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano mdogo tu, kule kwetu Katavi hatuna miundombinu ya barabara mizuri, reli yenyewe ni ya kusuasua, siyo reli ambayo inaweza ikabeba mzigo mkubwa wa kiwanda. Kwa maana hiyo ni kwamba, hata kama kiwanda kinajengwa kule, bado tutakabiliwa na miundombinu mibovu ambayo iko katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katavi inaunganika na Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Kigoma, lakini huwezi kusafirisha mazao kutoka Mkoa wa Katavi kuyapeleka Mkoa wa Kigoma kwa barabara kwa sababu barabara hiyo haipitiki, ni barabara ya vumbi.
Pia huwezi ukasafirisha mazao ukayatoa pale Mkoa wa Katavi ukayapeleka Mkoa wa Rukwa kwa sababu barabara ile ni ya vumbi ina vipisi vipisi tu vya lami ambavyo havijakamilika. Kwa hiyo, kama tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, nchi yetu ya Tanzania tunapaswa pia tuangalie miundombinu hiyo iwe bora, maji yawepo ya kutosha. Kule Katavi ni pale Mjini tu ambako ndiyo kuna maji, lakini sehemu nyingine wananchi wanatumia bado maji ya visima. Kwa hiyo, naomba suala hili la maji pamoja na barabara liangaliwe kabla ya hivyo viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mkoa wetu wa Katavi ni Mkoa ambao hauna kiwanda hata kimoja; na tangu nchi hii imeumbwa hakujawahi kujengwa kiwanda hata kimoja, hata kiwanda cha kiberiti hakuna, wala cha sindano. Kwa hiyo, napenda Mheshimiwa Waziri anapokuja kutoa ufafanuzi, labda atuambie kwamba kule Katavi ataanza kutujengea kiwanda cha kutengeneza nini? Kwa sababu Katavi tunazo fursa nyingi; sisi ule Mkoa tunayo asali ya kumwaga, naweza nikatumia neno “ya kumwaga.” Tunazo karanga nyingi sana; tunayo tumbaku; tunao mpunga unalimwa. Ina maana mchele kule kilo ni shilingi 1,200/=, tunayo mahindi ambayo mpaka yananyeshewa na mvua nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie utaratibu wa kujenga viwanda vinavyohusiana na hayo mazao. Kwa Mfano, Serikali ikijenga Kiwanda cha Kuchakata Asali, asali itapakiwa vizuri, itapelekwa nje. Asali inaleta pia nta; ile nta ni zao zuri sana ambalo likipelekwa nje ya nchi linaweza likaleta mapato kwa nchi yetu ya Tanzania. Nta inatumika kwa mambo mengi; inatumika kutengeneza mabegi, viatu; ina manufaa mengi ambayo ni pamoja na gundi zinazotumika maofisini. Mazao hayo yangeweza kuongeza kipato cha mwananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye suala la tumbaku; inalimwa kule Katavi, Tabora lakini Kiwanda cha Tumbaku kipo Morogoro. Sasa inamkatisha tamaa mwananchi kulima tumbaku. Tumbaku yenyewe ina grade 72. Yule classifier anapofika pale anai-grade ile tumbaku, anaweza akamwambia mtu kwamba hii tumbaku yako nanunua kilo moja kwa sh. 500/=, lakini kama Kiwanda cha Tumbaku kingekuwa karibu, kwa mfano, kingejengwa Tabora au hapo Katavi, kingeweza kuwanufaisha wananchi wote ambao wanalima hilo zao la tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Mheshimiwa Waziri angefikiria suala la kuleta kiwanda cha kutengeneza mafuta kama ya alizeti. Tunalima alizeti sana kule, pia tunalima karanga nyingi, tusingeweza kuagiza mafuta ya nje hayo ambayo yanakuja yamechakachuliwa hujui hata kama ni mafuta yametengenezwa na nini, unaambiwa tu ni vegetable oil. Tungeweza kutumia mafuta ya alizeti, tukatumia mafuta ya karanga na wananchi wakapunguza cholesterol mwilini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mikoa yetu ya Katavi, Tabora na Rukwa ni Mikoa ambayo ina ardhi safi sana, ambayo kuna sehemu nyingine ardhi ile tangu imeumbwa na Mwenyezi Mungu hamna binadamu ambaye ameweza kukaa. Naomba Mheshimiwa Waziri wawekezaji wanapokuja, jaribuni kuwapeleka pia mikoa ya pembezoni. Najua mnatuambia kwamba ile ni mikoa ni ya pembezoni ya mwisho wa dunia, lakini ni mikoa ambayo inazalisha mazao mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wanapokuja kutaka kuwekeza Tanzania msiwape tu ramani za kusema kwamba wawekeze Dar es Salaam au wawekeze Arusha, wapelekeni pia na mikoa ya pembezoni. Mikoa ya pembezoni kwa mfano kule Katavi, hiyo ardhi mwekezaji anapokuja, akichukua akalima mahindi yake akatengeneza unga na pia hayo mahindi akatengeneza mafuta ya mahindi ambayo ni mazuri sana kwa kupikia chakula, ambapo pia mwekezaji angeweza kuongeza pato na kuweza kuajiri vijana na kupunguza matatizo ya vijana ambao hawana kazi kwa sababu kiwanda kitakuwa pale, kitaajiri wale vijana ambao watafanya kazi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi pia unazo mbao nyingi. Hili tatizo la Madawati ambalo sasa hivi Serikali inakabiliana nalo, lingeweza kutatuliwa. Kwa mfano, kama Serikali ingekuwa imewekeza ikaleta Mwekezaji mmoja akajenga Kiwanda cha Mbao kule Katavi ambapo kunapatikana mbao nzuri sana ya mninga ambayo hata mdudu anaogopa kuitoboa, ina maana madawati yangetengenezwa kwa wingi kwa sababu mbao zinapatikana nyingi sana, tungeweza kuondoa tatizo la madawati ambalo linawakabili wanafunzi na watoto Tanzania hii yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbao ni nyingi sana kule Katavi, Tabora na Rukwa; pia asali ni nyingi sana maeneo hayo. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja na majumuisho atuambie ni lini atatuletea hivyo viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumwambia Mheshimiwa Waziri kwamba hao Maafisa Biashara ambao wameajiriwa kwenye Ofisi za Halmashauri, wajaribu kuwa wanaenda kutoa elimu ya biashara kwa wananchi, kwa sababu muda mwingi wanautumia ofisini na kutumia computer. Wanatakiwa Waonane na wananchi wawape elimu ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wao wanakuwa wana-chat kwenye computer, wanataka kufanya kazi kwa mtandao, lakini mwananchi wa kawaida hayuko kwenye computer, anataka asikilize ile elimu ya biashara na hiyo elimu iweze kumsaidia yeye na kuweza kujiinua kwenye biashara yao. Kwa sababu pia wao wanalipwa mshahara kwa ajili ya kuwa Maafisa Biashara wa Halmashauri, lakini huwa siwaoni wakitoa hiyo elimu ya biashara kwa wananchi, wanatumia muda mwingi kukaa ofisini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Awamu ya Tano ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mungu kwa kunipa uhai na leo nachangia hoja kwa mara ya kwanza kwa hii bajeti ya Serikali mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais mwenyewe kwa kazi nzuri anazozifanya na juhudi anazozionesha kwa kunyanyua maisha ya Watanzania. Napenda nikupongeze wewe mwenyewe kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Philip Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Ashatu kwa kazi nzuri wanazozifanya. Napenda niwaambie Wabunge wenzangu kwamba, Jimbo la Mheshimiwa Philip Mpango ni Tanzania nzima si kwamba Mheshimiwa Philip Mpango hana Jimbo, Jimbo lake ni mipaka ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwapongeze akinamama wenzangu, Wabunge wa Viti Maalum na niwaambie kwamba ninyi akinamama Wabunge wa Viti Maalum Majimbo yenu ni makubwa kuliko Wabunge wa Jimbo kwa sababu mipaka yenu ni mkoa mzima, kwa mfano wewe unatoka Mkoa wa Kigoma, ina maana wewe ni Mbunge wa Jimbo la Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda kuchangia bajeti hii ya Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwenye elimu. Nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano imetenga pesa nzuri kuboresha elimu mpaka tunaweza kupata elimu bure ambayo itashughulikia vitabu bure mashuleni, chakula bure, gharama zote za mitihani zitakuwa zinashughulikiwa na Wizara ya Elimu. Napenda niipongeze sana Serikali kwa hilo. Hata hivyo, napenda kutoa angalizo kwa maneno machache kuhusu elimu ambayo wanafunzi wanaipata ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Elimu ingeangalia utaratibu wa kujenga shule za kindergarten kwenye shule zetu za primary ili watoto kabla hawajaingia darasa la kwanza waweze kujifundisha, kwa sababu unakuta uelewa wa mtoto Mtanzania ambaye ana miaka mitatu ni wa chini ukilinganisha na mtoto wa miaka mitatu wa kindergarten kutoka nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba shule zetu za primary zijengewe darasa kwa ajili ya kindergarten ili watoto wawe wanapita pale kindergarten kabla hawajaingia kwenye elimu ya primary school.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba kuchangia juu ya tatizo la wasichana wadogo wa umri wa miaka 15 mpaka 19, ambapo imeainishwa kwenye kitabu ukurasa wa 10 kwamba, kuna ongezeko, kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2015; ambapo watoto wenye umri mdogo wa miaka 15 mpaka 19 wamekuwa wakipata mimba za utotoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iliangalie hili suala kwa makini kwa sababu baada ya miaka mitano tutajikuta tuna watoto wengi sana, Serikali itakuwa na mzigo wa kuhudumia hawa watoto, pia Serikali inakuwa na mzigo wa kuwasomesha kwa sababu watoto wengi wa aina hii wanaishia mitaani na Serikali yenyewe na nchi yetu yenyewe kama tunavyojua hatuna nyumba nyingi za kulelea hawa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo natoa ushauri kwamba, Serikali ingezifuatilia shule za sekondari ambazo zinajengwa, hasa shule za watu binafsi, iangalie kwamba, zile shule ziwe na mabweni ya kulala wasichana. Kwa sababu unakuta shule nyingine inajengwa haina mabweni, matokeo yake wasichana wanapanga kwenye nyumba za watu binafsi, hii inapelekea kupata matatizo ya upataji mimba za utotoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda Serikali iangalie suala la kubadilisha sheria ili hawa watu ambao huwa wanakatisha masomo ya watoto waweze kupewa adhabu kali. Pia naomba Serikali ingeangalia suala la kurekebisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inamruhusu mtoto kuolewa akiwa na umri wa miaka 15; kwa sababu vyote hivyo ni vitu ambavyo vinamfanya yule mtoto aone kwamba yuko tayari kuingia katika majukumu hayo kwa sababu hata sheria za nchi zinamruhusu kwa upande mmoja aolewe na miaka 15 na upande mwingine zinamwita mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ijaribu kuzileta zile sheria zijadiliwe na wadau na kubadilishwa hasa sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kwa sababu hatuwezi tukawa na sheria mbili ambazo zinakimbizana; sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na sheria ya ndoa ya mwaka 1971. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niende kwenye suala la Mkoa wangu wa Katavi. Katika Mkoa wangu wa Katavi tunayo matatizo kwa sababu mkoa ni mpya na Halmashauri nyingi ndiyo zinaanza kujengwa na Wilaya zile ambazo zimepitishwa kuwa Wilaya kwa mfano kama Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda hawajatengewa fedha kujenga zile ofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Serikali ijaribu kuangalia utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga ofisi za Halmashauri ili ziweze kujiendesha. Kwa sasa mkoa una Halmashauri mpya za Wilaya tatu. Awali mkoa ulikuwa na Halmashauri mbili na sasa hivi una Halmashauri tatu mpya ambazo hazina ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Katavi tunao wageni (waliokuwa wakimbizi) ambao sasa hivi ni Watanzania wenzetu, wako kule mishamo na Katumba. Wageni hawa walijengewa shule na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo zile shule hazitoshi kwa sababu wale tangu walipokuja wakiwa wakimbizi ni siku nyingi na kwamba sasa wameongezeka kwa idadi yao, hivyo, unakuta wengine wanasomea chini. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie utaratibu wa kuangalia suala hilo na kuweza kuongeza shule kwenye Mkoa wangu wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mitumba. Nchi yetu ya Tanzania hatujawa na viwanda vingi vya nguo, naomba hiyo mitumba iachwe kwa sababu ndiyo nguo ambazo zinatumika kule vijijini kwetu na nyingine zilizopo ni za ghali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la kukatwa kodi kwa kiinua mgongo cha Wabunge. Naomba kuzungumzia hili suala kwa sababu Mbunge ndiye kiunganishi cha Serikali na wananchi. Mwananchi wa kawaida anapopata matatizo anampigia simu Mbunge, hawezi kumpigia simu Waziri wala hawezi kuipigia simu Serikali. Kwa hiyo, naomba suala hili liangaliwe kwa sababu mishahara yetu inakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba suala la kiinua mgongo cha Mbunge lijaribu kuangaliwa ili ile kodi isikatwe kwa sababu Mbunge mshahara wake au kitu chake anachokipata si kitu ambacho anatumia peke yake, mshahara wake anatumia na watu wengi na kusaidia wananchi na yeye ndiyo kiunganishi cha Serikali pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwananchi anapomwomba Mbunge kitu chochote amsaidie, Mbunge kama hajamsaidia anachukulia kwamba, Serikali ndiyo haijamsaidia. Naomba suala hili liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwatetea watu wa bodaboda, kwamba kodi hiyo kutoka 45,000 kwenda 90,000 ni kubwa sana. Ukiangalia vijana wengi hawana kazi, wamemaliza shule na vijana wengi wanajihusisha na biashara ya bodaboda kuwapa tozo la sh. 90,000 kulipa kodi ni hela kwa kijana na unaweza kukuta ile bodaboda amekopeshwa anatakiwa arudishe zile pesa kwa mwenye bodaboda. Sasa si sawa kumwambia alipe 90,000 akasajili ile bodaboda, na pesa yenyewe amechukua kwa mkopo na hiyo pesa ni kubwa sana naomba tuangalie vyanzo vingine vya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri; kwa mfano Mkoa wetu wa Katavi tunao utalii mzuri, tunaye twiga mweupe ambaye hapatikani mahali popote. Naomba Waziri wa utalii amtangaze huyo twiga ili watalii waje kumwangalia yule twiga kule na waweze kuleta mapato nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watalii wanakuja kuangalia vivutio vyetu vingi, lakini kama tutazidisha kodi watalii wanaweza wakakimbia wakaenda Kenya. Pia naomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ijaribu kuutangaza sana Mlima Kilimanjaro kwa sababu mara nyingi unakuta Mlima Kilimanjaro unatangazwa kwamba upo Kenya. Kwa hiyo, watalii wengi wanapokuja wanashuka Kenya na wanapakizwa kwenye mabasi kupitia Namanga kuja Tanzania...
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kuchangia mambo yafuatayo zaidi ya yale niliyochangia;
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara itoe elimu ya biashara kwa wananchi kwa kupitia Maafisa Biashara wa Wilaya na Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara ijitangaze kwenye internet kwa maana ya kutangaza fursa zilizopo Tanzania ili wawekezaji waweze kuona fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya SIDO vijengwe mpaka Wilayani ili viweze kutoa elimu kwa vijana kwa sababu viwanda vingi viko Mikoani sehemu nyingi Wilayani hakuna viwanda vya SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamiliki wa viwanda waangalie afya za wafanyakazi kwa sababu kuna viwanda vingine vinazalisha sumu kama maji ya sumu na unakuta wafanyakazi hawapewi Boot za kufanyia kazi au vitendea kazi. Nashauri Wizara iwe na Wakaguzi watakaokuwa wanakagua viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri katika hotuba yake, ukurasa wa 13 anasema kuna viwanda 37 vimefungwa, nashauri Waziri aje na plan kuonesha kwamba atafufua vipi viwanda vilivyobinafsishwa, ambapo tulikuwa na viwanda takribani 474. Pia atueleze mikakati ya hivyo viwanda 37 ikoje. Je, inaweza kuvunjwa kwa sababu katika kubinafsisha kiwanda kuna mkataba umesainiwa, je mikataba ya viwanda hivyo ikoje? Inaweza kuvunjwa bila madhara kwa Serikali kulazimika kulipa fedha nyingi kwa ajili ya kuvunjwa mkataba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri aje na Plan, atuambie ataanza kujenga viwanda vya aina gani, vya kilimo nikiwa na maana, viwanda vya mbolea au viwanda vya nguo au viwanda vya chuma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara iwasiliane na Halmashauri ili ziwe zinatenga maeneo makubwa ya kujenga masoko na Mikoani ili wananchi waweze kuuza biashara zao. Mara nyingi unakuta Halmashauri inatenga maeneo madogo ya masoko tena mengine hayana hata Parking, matokeo yake wananchi wanapanga bidhaa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu kama barabara, reli iboreshwe ili wawekezaji waweze kuvutiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni wa shida, Mkoa wa Katavi hauna umeme wa Grid wanatumia umeme wa jenereta. Kwa hiyo ili kuwezesha Katavi kuwa Mkoa wa viwanda inatakiwa Mkoa upate umeme wa grid.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji bado ni tatizo nchi nzima, viwanda haviwezi kijengwa bila maji, maana viwanda vingi vinahitaji matumizi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijengwe viwanda vya kuchakata mazao ya asili kama pamba, mahindi, karanga, alizeti, ngozi, na tumbaku katika maeneo yanayozalisha hayo mazao bila kusahau mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itumie ardhi kama mtaji kwa wananchi.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nichangie Azimio la Kuridhia Mkataba wa Mabaharia nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niipongeze Serikali kuleta hili Azimio kwa sababu limekuja wakati muafaka, tumekuwa tukiona vijana wa Kitanzania wamekuwa wakipata shida huko nchi za nje wanapokwenda kufanya kazi za ubaharia. Pia wamekuwa wakipoteza mali zao kwa sababu Tanzania ilikuwa haijaridhia hii mikataba ambayo ni mikataba takribani 37 ambayo Tanzania ilishindwa kuridhia kwa muda wa miaka hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuunganisha Mikataba hii 37 kuleta mkataba huu itawawezesha vijana wetu wa Kitanzania kupata ajira kirahisi kwenye meli za nje, itawezesha pia Tanzania nchi yetu kusaidia kwenye ajira za kazi kwa



sababu tuna ukosefu wa ajira vijana wetu wataweza kuajiriwa nje na Serikali itaweza kupata manufaa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninalo angalizo dogo kuhusu sheria ambazo zitatumika kwa sasa hivi tunazo sheria za SUMATRA, pia tunazo sheria za Zanzibar kwa sababu tunakwenda kuingia Mkataba wa Kimataifa itabidi Serikali ilete hizi sheria izirekebishe maana yake flag country itakuwa ni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar wanasajili meli wanaye Agent anayesajili hizi meli kule Dubai, lakini SUMATRA hawana. Ningeomba Serikali ijaribu kuliangalia hili suala kwa sababu mkataba huu hautaonesha kwamba hii meli imesajiliwa na Zanzibar na hii imesajiliwa Tanzania Bara, inabidi sheria hizi ziunganishwe kwa pamoja za ZMA na SUMATRA kwa sababu mkataba ni wa Kimataifa, kitakachokuwa kinaeleweka hapa ni sovereignity of the state ambayo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haitakuwa busara kwamba sasa hivi hii meli imesajiliwa na Zanzibar, kwa hiyo ikipata pale matatizo tutasema kwamba hii meli ilisajiliwa na ZMA au hii ilisajiliwa Tanzania Bara, ningeomba uoanisho wa hizi sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Azimio hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Angeline Mabula kwa kazi yao nzuri sana waliyoifanya, kwenye Wizara ya Ardhi na kwa kweli wananchi wanawashukuru na mimi binafsi nawashukuru. Pia nawashukuru watendaji wote wa Wizara ya Ardhi, namshukuru Kamishna Mary Makondo na Naibu wake Nicholas Mkapa na watendaji wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kwenye Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kuchangia kuhusu ardhi yetu yetu ya Tanzania. Ardhi ya Tanzania iliyopimwa ni asilimia 25, ardhi nyingine iliyobaki haijapimwa. Ardhi ni mali, lakini ardhi hii pia ikipimwa mwananchi wa kawaida inamsaidia kupata mkopo benki. Pia ardhi hii ikipimwa inamsaidia huyo huyo mwananchi wa kawaida kwenda kulima mazao yake ya biashara, lakini pia na mazao ya chakula. Sasa basi ardhi yetu ya Tanzania na ukubwa wa eneo letu la nchi ni asilimia 25 tu ndio imepimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, iongeze nguvu kwenye kupima ardhi ili mwananchi wa kawaida aweze kufaidika na ardhi hii lakini pia ili Serikali yenyewe iweze kupata mapato. Kwa sababu ardhi inapopimwa mwananchi atapata hati anapopata ile hati anailipia kila mwaka na kuna mzunguko wa kulipia zile hati kila mwaka kwa maana hiyo Serikali itaingiza pesa, lakini pia huyu mwananchi atakuwa na uhakika wa eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, naomba kwenye bajeti ijayo Serikali kupitia Wizara ya Ardhi iongeze pesa ili maeneo mengi yaweze kupimwa nchini kwetu Tanzania. Liko tatizo ambalo ningependa kulizungumzia tatizo lenyewe ni kuhusu upungufu wa wataalam wa ardhi kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri nyingi nchini kwetu zina upungufu wa wataalam wa ardhi na wataalam hawa ni kuanzia Wapimaji, Wathamini na Warasimishaji. Hivyo basi inasababisha ucheleweshaji wa upimaji wa ardhi kwenye halmashauri zetu. Naomba tuweze kuwatumia wanafunzi wanaomaliza Chuo cha Ardhi cha Dar es salaam, wanafunzi wanaomaliza Chuo cha Mipango hapa Dodoma lakini pia wanafunzi wanaomaliza kile Chuo cha Morogoro pamoja na Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote hawa wanajua kupima hizi ardhi na wote wamesoma haya masomo ya kuthamini hizi ardhi, tungeweza kuwa-comodate hawa wanafunzi na kuwatumia ili waweze kupima ardhi yetu. Pia Serikali inawasomesha kwa mikopo, kwa hiyo wanapomaliza shule nafikiri Serikali ingewatumia hawa wanafunzi ili waweze kutusaidia tuweze kutatua hili tatizo la kutokupima ardhi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda pia halmashauri nchini kwetu Tanzania zijitambue kwamba zenyewe ndio zenye mamlaka ya kupima ardhi kwenye halmashauri zao. Hata hivyo, niliona bajeti ya halmashauri hapa wakati inapitishwa, halmashauri nyingi zilikuwa hazijatenga fedha za kupima kwenye maeneo yao. Niombe basi hizi halmashauri ziweze kujitambua na kupima maeneo yao ili wananchi waweze kufaidika na hayo maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kupima hayo maeneo niweze kutoa rai kwa halmashauri zetu kumekuwa na watendaji wengi ambao wanafanya kazi let say, mtu anafanya kazi pale kwenye Halmashauri ya Mji wa Mpanda anaweza akapima yale maeneo lakini hafikirii miaka mia ijayo hayo maeneo yatakuwaje. Naomba watendaji wa wataalam wetu wa kupima ardhi wanapopima ardhi waipime kwa kuangalia kwamba leo tupo na kesho tupo lakini tuangalie miaka 100 ile ardhi itatumikaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoharibu mji kwa sasa hivi unapima barabara ndogo, lakini labda hujaweka eneo la kuchezea watoto au eneo la kupumzika, matokeo yake tunakuwa na miji ambayo haina maeneo ya kupumzikia, lakini haina parking na wala haina maeneo ya kucheza Watoto. Tunakuwa na congested town na kurekebisha ni vigumu kwa sababu unakuta mji umeshapimwa huwezi kubomoa zile nyumba. Niombe sana wataalam wanapopima miji waliangalie hilo wasi-focus kuangalia sasa hivi waangalie hundred years to come huu mji utakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la vile vijiji ambavyo vinakua kwenda mji. Unakuta kata inaanza kukua, kuna majumba mazuri yamejengwa pale, unakuta kuna umeme na maji yamewekwa, lakini unakuta lile eneo halijapimwa, matokeo yake tunajaza squatter kwenye miji squatter nyingi na tunapokuja kuzirasimisha kunakuwa na matatizo ya upungufu wa pesa, lakini pia uthamini utakuta mtu amejenga nyumba yake nzuri lakini inathaminiwa kwa pesa ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba zile vijiji ambavyo vinaanza kukua kwenda kuwa miji hizi halmashauri ziwe zinaviangalia na kuvipima ili kupunguza ukaaji holela na kupunguza migogoro ya ardhi kwenye maeneo yetu na kwenye hiyo miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumizia hapa ni suala la hizi halmashauri ambazo zilikopeshwa pesa lakini hazijarudisha. Kwa sababu tunataka halmashauri nyingine zipate zile pesa ili ziweze kupima ardhi zao, tunaziomba zile halmashauri ambazo zilipewa pesa na Ofisi ya Ardhi ziweze kurudisha hizo pesa ili halmashauri nyingine ziweze kupewa hizo pesa na hizo halmashauri ziweze kupima maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuupongeza sana Mkoa wa Mbeya kwa sababu wao walipewa pesa, wamezitumia vizuri, wamepima na wamerejesha na walipata faida. Nawapongeza sana, lakini sipongezi mikoa kama ya Iringa na mingine ambayo Mheshimiwa Waziri aliiorodhesha hapo. Kwa hiyo niombe tu zile halmashauri zilizingatie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kutoa ushauri wa jumla kwa akinamama wa Tanzania. Napenda kutoa ushauri kwamba akinamama wa Tanzania, waume zetu wanapokwenda kununua ardhi basi tuhakikishe na sisi majina yetu yanakuwepo pale pembeni. Natoa ushauri huu kwa sababu akinamama wengi wamekuwa wakidhulumiwa nyumba, lakini wakidhulumiwa pia mashamba, lakini unakuta huyu mama aliolewa na huyu mtu akiwa kijana, wakaanza Maisha, wakanunua kiwanja kwa pamoja, lakini sisi kina mama kwa sababu huwa tunakuwa na tabia ile ya uvuvi wa kutaka kuweka majina yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nitoe wito, mume wako kama anataka kwenda kununua kiwanja basi mwambie na yeye aweke jina lako pale ili iondoe matatizo pale mmoja wenu anapoondoka duniani ili usiweze kufukuzwa. Naomba nitoe wito kwa akinamama wa kule Mkoani kwangu Katavi lakini pia kwa akinamama wa Tanzania na pia tusiwe wavivu wa kwenda kutafuta ardhi kwa sababu sheria haimkatazi mwanamke kununua ardhi wala kununua kiwanja, tusipende sana kuwatumatuma akinababa kaninunulie kiwanja halafu akifika pale haweki jina lako, matokeo yake unakaa pale after 40 years unaonekana kama wewe ni mpangaji kwenye nyumba ambayo mmejenga pamoja.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Sofia Mwakagenda.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa taarifa kwa mzungumzaji kwamba ni kweli anachosema kwamba sisi akinamama tujitahidi kuwaambia waume zetu watuandike majina. Hata hivyo, waume hawa Mheshimiwa Taska Mbogo wanapoenda kununua viwanja hawatuagi na wakati mwingine wananunua akiwa bahati mbaya amefariki unashangaa kumbe mko sita wakati wewe unajua uko peke yako. (Makofi/ Kicheko)

NAIBU SPIKA: Sasa Waheshimiwa Wabunge huu mchango, hakuna akinamama wanaotumwa na waume zao kwenda kununua ardhi. Mheshimiwa Taska Mbogo sekunde kumi kwa sababu kengele ya pili ilikuwa imeshagonga.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda nipende kusema tu kwamba naupokea vizuri sana mchango wa Mheshimiwa Mwakagenda, ni mchango wenye tija lakini na mimi pia niendelee kutoa wito kwa akinababa ili kuondoa matatizo unapotoka duniani na mke wako kupata shida kutoka kwa ndugu zako kumfukuza kwenye nyumba basi muweke mke wako kwenye hati ya nyumba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia, wito wangu kwa akina mama ni huu.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mulamula - Waziri wa Mambo ya Nje kwa taarifa yake nzuri aliyoiwasilisha hapa Bungeni nawapongeza watendaji wote, lakini pia nawapongeza mabalozi wote pamoja na UN agencies zilizokuja leo hapa asubuhi kuungana nasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuzungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki na muda ukiruhusu nitazungumza mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilianza toka mwaka 1967 lakini ika-collapse mwaka 1977, ikaanza tena rasmi mwaka 2000. Watanzania wengi ukiwauliza hata kule vijijini hawajui hii Jumuiya ya East Africa inafanyaje kazi, hawajui tumeungana nini na hawajui hata ile treaty/ule mkataba ambao Tanzania imesainiana na nchi nyingine ambazo ni Rwanda, Burundi, South Sudan, Kenya na Uganda hawajui kimeandikwa nini. Hivyo basi niiombe ofisi ya Mheshimiwa Waziri iweze kueleza ni kitu gani ambacho tumeungana kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa ningependa pia hizi nchi ambazo tumeungana ziweze kwenda kwenye treaty. Tuliona hapa juzi juzi kulipotokea na ugonjwa wa Covid kila nchi ilikuwa na mwelekeo wake, tuliona madereva wengi walikuwa wakikwama mpakani, lakini tuliona pia mahindi yakikwamba pale mipakani, tunamshukuru Mheshimiwa Rais alivyoenda haya mambo yalinyooka, lakini wananchi walikuwa tayari wameshapata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni nini; hoja yangu ni kwamba kama nchi nyingine ina mahindi mengi basi ile nchi inunue yale mahindi. Haiwezekani Tanzania tukawa tunaagiza sukari toka nje wakati labda Kenya kuna sukari na Uganda kuna sukari. Kwa hiyo, hoja yangu ni kwamba hizi nchi zilizoko kwenye Jumuiya zishirikiane kiuchumi, lakini pia ili kuleta nafuu kwa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikuwa naomba wale wawakilishi wetu ambao wanatuwakilisha huko tunao Wabunge wa East Africa ambao kwa kweli sielewi uwajibikaji wao huwa ukoje, yale wanayoyapitisha kule wangekuwa wanajaribu kutuletea hapa tukaona kumepitishwa nini. Nalisema hilo kwa sababu tunawachagua hapa, lakini tungepata mrejesho kule wamefanya kazi gani kwenye Bunge lile la Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuzungumza suala ambalo limezungumzwa na wachangiaji wengi waliopita hapa. Napenda kuzungumzia suala la uraia pacha. Kama walivyozungumza wachangiaji waliopita ipo haja sasa ya kuangalia sheria yetu hasa ile Citizen Act kuangalia jinsi gani tutaweza kuwa-accommodate hawa Watanzania wanaoishi nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi walioenda nje ya nchi walikwenda kutafuta kazi, lakini wengine walikwenda kusoma, baada ya kusoma walipoona wamekosa kazi huku wakaajiriwa kule. Hivyo basi zile sababu ambazo zilikuwepo zamani labda za kusema kwamba hatuwezi tukawa na uraia pacha wakati ule dunia ndiyo ilikuwa bado haijawa kijiji, kwa sasa hivi dunia ilivyo kijiji ipo haja ya kuwa na uraia pacha. Lakini tunapokuwa na uraia pacha maana yake nini; tunapokuwa na uraia pacha kwanza tunamwezesha yule Mtanzania aliyeko kule nje ya nchi ambaye alikwenda kwa ajili ya kutafuta maslahi na pia kusaidia ndugu zake aweze pia kuwa na ule moyo mkunjufu wa kujiona kwamba na mimi bado ni Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wale watu wako kule wameoa na wamezaa na wengine mpaka wana wajukuu kuwaacha kukaa kule moja kwa moja kwa sababu wamechukua uraia wa nchi nyingine ni kama vile tunakipoteza kizazi cha Watanzania ugenini. (Makofi)

Hoja yangu nilikuwa nataka niishauri Serikali inaweza ikawa-accommodate huu uraia pacha, lakini ikawawekea masharti ya wale Watanzania na huu uraia pacha hauji kwa wageni kwa maana kwamba ya foreigners, uraia pacha uwe kwa Watanzania ambao wamezaliwa humu nchini Tanzania, lakini wameenda kule nje kwa ajili ya masomo na hii katika nchi nyingi za Afrika zinaendelea ku-accommodate hili suala kuna nchi karibu 24 zimesharuhusu uraia pacha. Kwa hiyo, na sisi tujaribu kuangalia sheria zetu na tuwawekee sheria ambazo zitaweza ku-accommodate.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo faida ya kuwa na uraia pacha kuliko kutokuwa na uraia pacha kwa sababu ya uwekezaji kiuchumi pamoja na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni suala la mabalozi walioko...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba jambo analolizungumzia la uraia pacha yaani yako mambo ya kufikiria sana, kwa mfano Mtanzania anakwenda kusoma MarekaniM ameenda kwa ajili ya masomo atazaa huko huko Marekani na kwa sheria za Marekani ukizalia Marekani anakuwa na uraia wa Marekani. Sasa kama huyu mtoto naye hatapata uraia wa Kitanzania tutakuwa tunapoteza watoto wanaenda Ulaya na mama anarudi nyumbani au baba anarudi nyumbani au baba anarudi nyumbani. Kwa kweli hili jambo ni la kufikiria sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo unapokea taarifa hiyo?

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hiyo taarifa, ni taarifa ambayo ni sahihi, ni kweli kizazi cha Watanzania kinapotea kule ughaibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumzia suala la mabalozi, hawa mabalozi ambao wapo kwenye nchi zile zilizopo ambazo sisi tuna ofisi zetu za balozi kule nilikuwa naomba waitangaze nchi yetu, wanaitangaza vipi. Nilikuwa naomba iwasiliane na Wizara ya Maliasili na Utalii wachukue zile brochures ambazo zinatangaza vivutio ambavyo viko nchini kwetu Tanzania ili waweke kwenye zile ofisi za mabalozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia waweze kuchukua bidhaa ambazo tunazo huku nchini kwetu Tanzania waziweke kwenye ofisi za mabalozi. Nimeona kwenye ofisi nyingine za balozi nchini kule nje ya nchi unakuta kuna bidhaa, kuna kahawa, kuna majani ya chai, kuna nini, kila kitu wame-advertise/wanatangaza zile bidhaa ambazo zinatoka kwenye nchi zao.

Kwa hiyo. nilikuwa naomba hawa mabalozi waweze kufanya hiyo kazi. Lakini zaidi ya hapo wawe na mikutano ya kuangalia kwa mfano mtu yuko Ethiopia ajaribu kuita wale matajiri wa pale Ethiopia labda wenye viwanda vya ngozi au viwanda vya nguo aongee nao jinsi gani wanaweza wakaja nchini kwetu kununua ngozi zilizopo hapa. Ngozi za Tanzania zinatupwa tu, lakini kule Ethiopia wana viwanda wanatengeneza majaketi, wanatengeneza vitu vizuri sana vya ngozi mpaka viatu, lakini sisi ngozi zetu zinatupwa hata ukienda hapa Dodoma zinatupwa, ukienda Dar es Salaam zimetupwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe wale walioko kwenye hizo nchi waweze kuwasiliana na wale wafanyabiashara na wale wenye viwanda ili waweze kuja kuchukua malighafi zinazotokana huku nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuongelea ni suala la Sera ya Mambo ya Nje, haiwezekani tunakaa tunazungumza kumbe Wizara ya Mambo ya Nje haina sera, niiombe kwanza Serikali ilete Sera ya Mambo ya Nje ili pia wale Watanzania waliopo nje waelewe kwamba sera ya mambo ya nje ni ipi nah ii itawasaidia sana wale Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri alisema kwamba ameagiza Balozi ziwaorodheshe, kuwaorodhesha sawa waorodheshwe, lakini je, baada ya kuwaorodhesha Sera ya Mambo ya Nje inasema nini kuhusu watu wanaoishi nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii Watanzania wako kama nilivyosema mwanzo wako zaidi ya milioni moja, lakini hawana fursa pia ya kupiga kura, hatujaweka system kwenye balozi zetu za kuwaruhusu hawa Watanzania kupiga kura. Sasa inapofika wakati wa uchaguzi wale Watanzania walioko nje ya nchi hawapigi kura. Lakini kama mzungumzaji aliyepita alisema kunapokuwa na maoni ya kitu chochote cha Serikali huwa wanaulizwa yale maoni kwa sababu bado ni Watanzania na bado ni kizazi chetu tuweze kuwa-accommodate ili sera hiyo ikitoka nafikiri itajumuisha na hayo mambo mengine wataweza kupata haki zao za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda pia kuzungumzia suala lingine ambalo litakuwa ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai leo hii tunachangia masuala ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu za kwanza napenda nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya kuboresha elimu nchini kwetu Tanzania, hususan kwa kujenga shule za sekondari kila Mkoa kwa ajili ya watoto wetu wa kike ili waweze kusoma masomo ya sayansi. Nampongeza pia, kwa kujenga shule za VETA 63 ambazo zitaenda kujengwa kwenye Wilaya ambazo hazina shule za VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia kwa ujenzi wa shule za sekondari zinazoendelea nchini Tanzania na nampongeza Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa madarasa kwenye shule zetu za primary kwa kutumia mradi wa Boost. Baada ya pongezi hizo napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Mkenda na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine ziende kwa watendaji wote wanaofanya kazi Wizara ya Elimu na walioandaa mabadiliko ya sera ambayo tutakwenda kuitumia nchini kwetu Tanzania ikiwa ni mwongozo wa nchi yetu kwa miaka inayokuja. Nawapongeza kwa kuja na hiyo sera, lakini ninayo mambo mawili ya kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu inaleta sera, mtekelezaji wa sera ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Sasa bado tunayo matatizo kwenye shule zetu, matatizo ya madawati, matatizo ya upungufu wa vyoo, lakini pia na matatizo ya madarasa. Tunaomba huyu mtekelezaji wa hii Sera ya elimu aweze kuwezeshwa, lakini asimamiwe katika kutekeleza hayo, hususan kwenye suala la madawati, lakini pia kwenye suala la ujenzi wa vyoo, lakini pia kwenye suala la kukarabati zile shule kongwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shule zile kongwe utazionea huruma. Ziko shule kule Mpanda ambazo hususan kama mimi niliondoka pale miaka mingi, ile rangi niliyoiacha bado ipo mpaka leo, mfano Shule ya Kashaulili Mpanda. Pia zipo shule nilizitaja mara ya mwisho nilipokuwa nachangia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, watoto kutoka darasa la kwanza mpaka la nne wanakaa chini, Shule ya Msakila, Shule ya Shanwe, Shule ya Nyegere, Shule ya Mkapa. Shule hizo watoto kutoka darasa la kwanza mpaka la nne wanakaa chini, hawana madawati, ukienda kwenye shule hizo pia vyoo havitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuja na haya mabadiliko ya sera, naomba Wizara inaposimamia hii sera ili ikatekelezwe ihakikishe kwamba, hivyo vitu vipo vinatekelezwa. Madawati yapo na watoto wanakaa kwenye madawati, sio kukaa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichangie kwenye suala la Walimu. Hapo zamani miaka ya nyuma kwa wale tuliozaliwa mbele kidogo kulikuja mfumo kwamba, mtu akimaliza darasa la saba anaweza akafundisha shule za primary, elimu ikayumba. Naomba tunapokuja kutekeleza hii sera Wizara ya Elimu ihakikishe kwamba, inafundisha Walimu watakaoenda kutekeleza hii sera ambayo tunakwenda kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kutakuwa na program. Tuna matatizo ya watoto wetu kufeli, lakini tuna matatizo pia ya watoto wetu kutokuwa na competence. Hivyo basi, tunaomba hii competence ya watoto ipelekwe kwanza kwa Walimu wafundishwe ili waweze kwenda kufundisha vizuri. Haiwezekani wewe umepata division four ukaenda kumfundisha mtu apate division one, kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Chaya. Kwa hiyo, naomba hilo liwekewe mkazo. Walimu wapelekwe training ili waje wafundishe hizi shule ambazo Waziri ameziita amali, zamani tuliziita ufundi na sijui kwa nini amezibadilisha jina? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo ningependa kulichangia hapa, napenda niunge mkono hoja ya Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Waziri katika Wizara yake ameruhusu Halmashauri zijenge shule za english medium, ameruhusu Halmashauri zichukue walimu ambao wanalipwa na Serikali wakafundishe shule za english medium. Halmashauri inakusanya kodi kutoka kwa wananchi, ina maana mimi kama nauza nyanya, nauza mitumba, nauza ndizi, nina duka, unakusanya kodi kwangu, ukishakusanya zile kodi kwenye halmashauri yangu unakwenda unanijengea shule ya english medium, halafu unarudi unaniambia kama nataka mtoto wangu asome pale nikulipe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliona hili ni tatizo na linaenda kugawa Watanzania. Sasa hivi kuna halmashauri ambazo zimejenga shule za english medium na hili ni tatizo nimeona niliseme hapa na liko ni hoja ya Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, iliwasilishwa hapa Bungeni, lakini nimeona nichangie kwenye Wizara kwa sababu nafahamu hawa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hawawezi wakajenga hii shule kama hawajapata kibali kutoka kwenye Wizara ya Elimu ambayo Waziri ni msimamizi wa sera hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anawezaje kumtumia Mwalimu ambaye analipwa na Serikali akafundishe shule ya english medium, halafu utatumia yale mapato ambayo wewe umekusanya kodi kwa wale wananchi walioko kwenye hilo eneo? Hii si sahihi, tunakwenda kujenga matabaka na hatutaki matabaka nchini Tanzania kwa sababu, watakaosoma hapa watakuwa ni wale watoto wenye uwezo na wale watoto wa wafanyakazi. Yule mtu ambaye ulichukua kodi yake ya shilingi 200, anayechoma mahindi, anayeuza mitumba, anayeendesha bodaboda, hawezi akamleta mtoto wake pale kwenye ile shule ya English Medium. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja nyingine nakaa nikijifikiria, kama Waziri alisema kwamba, anakuja na hoja humu Bungeni kwamba, Kiswahili si ndio lugha yetu, masomo yafundishwe kwa Kiswahili, kwa nini anaruhusu Halmashauri zijenge shule za english medium? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni hivyo, basi Kiingereza kifundishwe kwenye shule zote za Serikali kutoka darasa la kwanza, ili twende na usawa na ili tusiwe na matabaka. Suala la halmashauri kuanzisha hizi shule si sahihi, tuachie shule binafsi kwa sababu, wanakwenda kutumia resources zilezile za Serikali, lakini wanakwenda kutengeneza mapato, lakini ukiangalia chanzo chake ni hicho nilichokisema. Naona siyo sawa, na sioni sababu. Kama ni hoja kufundisha english medium basi namwomba Mheshimiwa Waziri hii english ifundishwe kutoka darasa la kwanza kwenye shule zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, tumesema lugha ni biashara, lugha ni uchumi, kama wachangiaji wengine waliopita walivyosema, lakini pia tunakwenda kwenye teknolijia ya kisasa. Unaposema nchi yetu ya Tanzania iendelee kukikumbatia Kiswahili, tuendelee kuwafundisha watoto Kiswahili hayo mambo yalitakiwa yafanyike 1961 tulipopata Uhuru, siyo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, 1961 tulipopata Uhuru ungesema basi tunakwenda na mfumo wa kufundisha watoto Kiswahili kitupu, lakini Kiswahili pamoja na Kiingereza ni official languages, ni lugha za Taifa, Kiingereza ni Lugha ya Taifa na Kiswahili ni Lugha ya Taifa. Sasa unapokuja kutoa lugha moja unasema ifundishwe kwa mtindo huu, ili nyingine ifundishwe kwa mtindo mwingine, mimi ninaona siyo sahihi. Ninataka Kiingereza kifundhishwe kutoka darasa la kwanza kwa watoto wote, kwa shule zote ili kila mtoto awe na competence, anapokwenda ku-compete huko nje kwenye interview, mtoto unakuta anajua kitu lakini kwa sababu hakuandaliwa na hakusomeshwa ana-feel uncomfortable, kwa sababu anashindwa kujieleza. Na matokeo yetu tumekuwa tukidai nchi za jirani watu wake wanafanya kazi nje, wanafanya kazi nje kwa sababu wanajua lugha, wanaongea Kiingereza, wanaongea Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, utaendaje kufundisha Kiswahili Marekani, Ujerumani, Sweden kama hujui Kiingereza? Ni lazima ujue Kiingereza ili ukafundishe kile Kiswahili, ili uweze kutafsiri. Mheshimiwa Waziri ninaomba hili ulichukulie uzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mengine nitaandika. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mwaka huu 2024 leo ndiyo siku ninachangia mara ya kwanza; namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai. Napenda nichukue nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambazo anazifanya za kuwatumikia Watanzania. Watanzania wote wameona kazi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyofanyika kuanzia kijijini mpaka mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, napenda kuunga mkono Maazimio yote ya Kamati yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Timotheo Mnzava.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulikuwa hapa, Bunge likatoa maagizo na maazimio yakapitishwa. Kati ya maazimio hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa na maazimio 10. Maazimio manne yametekelezwa, mawili yanaendelea kufanyiwa kazi lakini manne hayajatekelezwa. Naomba niyasome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maazimio ya mwaka 2023 tuliyokuwa tumeazimia yameshindwa kutekelezwa:-

(a) Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Wanyamapori TAWA.

(b) Kushindwa kutekeleza mchakato wa kupandisha hifadhi ya misitu Tanzania TFS.

(c) Kushindwa kuanzisha mchakato wa sera zilizopitwa na wakati.

(d) Kushindwa kuchukua hatua za haraka kwa wawekezaji wa hoteli na lodge ambao walikiuka masharti ya mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maazimio hayo tuliyoyatoa mwaka 2023 hapa Bungeni na hayajatekelezwa. Sasa ninaanza pale kwenye kushindwa kuchukua hatua madhubuti kwenye hoteli zilizoshindwa kutekeleza mikataba yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliazimia na tukatoa maazimio ndani ya Bunge hili ambayo ni maazimio ya Bunge, kwamba Serikali irudishe zile hoteli ambazo watu walibinafishiwa lakini hawakuweza kuendeleza. Nini maana yake? Kuna hoteli ambazo toka zimebinafisishwa hazijawahi kufanya kazi. vilevile, kuna hoteli ambazo zimebinafisishwa lakini zina-operate kwa kiwango cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Nyerere, alijenga hoteli kila mkoa. Kulikuwa na Mbeya Hotel, Tabora Hotel, Dodoma Hotel, Musoma Hotel. Hoteli hizi zote zina-operate kwa kiwango cha chini. Ni bora zilivyokuwa kabla hazijabinafisishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitia azimio kwamba, Serikali irudishe hoteli hizo kwa sababu waliopewa wamevunja mkataba na hawakuweza kutimiza masharti ya mikataba. Hata hivyo, azimio hilo halijatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hotel kama Embassy Hotel, Kunduchi Beach Hotel, Mikumi na Lodge nyingi kule Manyara, zote hizo zipo na zilikuwa za Serikali, zilibinafisishwa na zinafanya kazi kwa kiwango cha chni sana. Embassy imefungwa na ninafikiri takribani miaka 14 sasa pana uzio pale na iko katikati ya Dar es salaam. Vile vile, kuna Agip Hotel pale ziko nyingi. Hivyo, ninaomba Bunge hili labda lije na utaratibu wa kuunda Kamati ambayo itakwenda kufuatilia Mazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa ni kusisitiza kwamba, katika hizo hoteli tulimwita TR wa wakati huo kabla ya huyu wa sasa alikuja kwenye Kamati na tukampa maagizo ya kulifanyia kazi hilo suala. Tunamuomba TR wa sasa alifanyie kazi suala la hoteli ambazo zilibinafsishwa na hazifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni suala la miundombinu mibovu iliyopo kwenye mbuga zetu za wanyama. Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, amezungumza hapa lakini na mimi napenda nizungumzie hapo. Mbunga zetu za wanyama zinatuingizia pato la Taifa kama alivyosema Mwenyekiti hapa takribani asilimia 25. Hata hivyo, mbunga hizo za wanyama barabara zake ni mbovu. Nachelea kusema kwamba ni mbovu. Katika mvua hizi za masika tumeona magari yakizama kule Serengeti na watalii wakishuka na kusukuma magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaraja yaliyopo kwenye mbunga zetu za wananyama, kama derava hajui kuendesha vizuri gari linatumbukia kwenye maji. Niombe basi, hii Wizara ya Maliasili na Utalii washirikiane na Wizara ya Ujenzi ili waweze kuweka miundombinu mizuri kwenye Hifadhi zetu za Taifa. Tukianzia na hiyo Serengeti ambayo inafahamika duniani kote, lakini pia Ngorongoro na hifadhi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo madaraja ya Serengeti siyo kwamba ninazungumza kwa kusoma kwenye karatasi tu, tulikwenda Serengeti na nilishuhudia jinsi magari yalivyokuwa yanazama. Ni kitu ambacho nilikiona na ninaweza kuchelea kusema kwamba, vilevile, vidaraja ni vidogo na havifai kuwa kwenye hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara ishirikiane na iangalie itatoa wapi pesa au itafanyaje ili iweze kujenga barabara zetu zilizoko kule kwenye hifadhi zetu, na ukiangalia kwamba Pato la Taifa asilimia 25 linatokana na wageni wanaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi hapo hapo kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Mheshimiwa Rais alitusaidia kuitangaza nchi hii kwa filamu yake ya Royal Tour. Sasa hivi wageni wanaokuja kwenda kwenye hifadhi wanakosa vitanda, nikiwa na maana kwamba hoteli hazitoshi. Ndiyo maana natoa msisitizo kwamba, hoteli ambazo zimeshindwa kutekeleza masharti ya mkataba Serikali izichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni utangazaji wa hifadhi zetu. Hifadhi zetu za Tanzania zinapaswa zipewe uwiano mzuri wa kutangazwa. Nikiwa namaanisha kwamba, tusitangaze Ngorongoro kila siku, Serengeti kila siku, ziko na hifadhi nyingine. Nitoe mfano hifadhi ya kule kwetu Katavi nayo pia inahitaji kutangazwa. Hii ni kwa sababu nayo ni hifadhi nzuri lakini pia ina Wanyama wazuri; ina twiga mpaka mweupe ambaye hapatikani kwenye hifadhi nyingine yoyote. Sasa iwenje unapofungua ile channel ya Tanzania ambayo inatangaza unakuta inarudia hifadhi Serengeti, Serengeti shall never die, Ngorongoro hiyo hiyo, wakati kuna hifadhi nyingine. Tuweke uwiano kama ni mwezi mzima unatangaza Serengeti, mwezi ujao tangaza Katavi National Park mwezi mwingine tangaza Saadani, mwezi mwingine tangaza Gombe ili kuwe na uwiano. Nafikiri hawa waratibu wa haya matangazo wamenisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni suala la kuweka mazingira rafiki kati ya wale wageni wanaokuja na hoteli zilizopo kwenye mbuga zetu. Kuna hoteli katika mbuga zetu ambazo charge usiku mmoja ni takribani dola 1400 kwa siku. Ina maana mtalii analala kwa dola 1400. Hivyo basi, muone kama mtu binafsi anaweza kujenga hotel akatengeneza dola 1400 kwa siku ni kwa nini Serikali isitengeneze hoteli ya aina hiyo hiyo ikatengeneza dola 1400 kwa siku? Zipo hoteli kama Four Seasons kule Serengeti na nyingine nyingi. Kwa hiyo, kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ninapenda kulisisitizia hilo na lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye Wizara ya Ardhi. Kwenye Wizara ya Ardhi nitakuwa na machache ya kusisitiza, hususani suala la zile fedha, dola bilioni 150 sawa na takribani bilioni 346 ya hela za Kitanzania. Kati ya fedha hizo kuna suala la ujenzi wa ofisi za ardhi katika kila mkoa. Niombe basi, wakati watakapokuwa wanatoa hizi pesa za kujenga hizo Ofisi, basi kwanza ningeomba ile ramani ya jengo ifanane, kwa sababu katika ripoti yao walisema watajenga ofisi za ardhi katika mikoa 25. Niombe, ili kuwe na uwiano wa pesa na ili ile pesa iweze kutumika vizuri na isionekane kuna upendeleo kwa fulani na fulani; kwanza ramani iwe moja ambayo itajengwa hiyo ofisi ya ardhi kwenye kila mkoa. Pili, yale matumizi ya pesa, kama Mkoa wa Tabora utapewa bilioni kadhaa, labda let say bilioni 80, basi na Mkoa wa Katavi upewe bilioni hiyo hiyo na ramani iwe moja ili isije ikaonekana Mkoa mwingine kwamba umeongezewa pesa kwa sababu ramani yake ni kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye Wizara ya Ardhi, naomba nirudi kwenye Wizara ya Maliasili niende niizungumzie TAWIRI, TAWIRI ni taasisi ya Serikali. Hii TAWIRI ni Tanzania Wildlife Research Institute ambayo inafanya Research kwa ajili ya wanayama wetu nchini Tanzania, kuangalia kama kuna magonjwa Wanyama wamepata lakini pia kuangalia mambo yote ya wanyamapori nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi hii ilianzishwa tangu mwaka 1980, lakini cha kushangaza ndiyo taasisi ambayo inafanya research kwa wanayama wote, sijui kiboko, sijui tembo ameugua, sijui pundamilia wamekufa, sijui nini, wote hao ndiyo wanafanya research kuangalia ni kwa nini wamekufa. Maana yake ni scientific research lakini cha kushangaza taasisi hii haina jengo tangu mwaka 1980. Taasisi hii inapewa bajeti ndogo. Pia, niliona jengo la research kule Serengeti ni kama vinyumba nyumba fulani hivi vimekaa pale ambavyo vimeachwa kwa muda mrefu bila kupakwa rangi. Halafu eti unategemea taasisi kama hii ije na research ambayo itaweza kuboresha mambo ya wanayamapori nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuboresha mambo ya wanayamapori na kupata research nzuri kutoka kwenye hii taasisi ya Tanzania Research institute (TAWIRI) ambayo ipo Arusha tuna wajibu wa kuwapa bajeti ya kutosha, kujenga makao makuu ya taasisi hii pamoja na kwenda kurekebisha yale majengo yaliyopo Serengeti ambayo kwa kweli nachelea kusema ni majengo ambayo yako kwenye kiwango cha chini kabisa; nimeyaona kwa macho yangu. Hivyo, basi nilikuwa naiomba Serikali itilie mkazo suala hili la hii research ya TAWIRI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuboresha taasisi hii, tutajua ni jinsi gani tunakwenda kupandisha utalii wetu nchini Tanzania kwa faida yetu sisi lakini pia kwa faida ya kizazi kinachokuja. Haiwezekani taasisi mwaka 1980 mpaka sasa ni almost 40 years taasisi haina jengo eti tunasubiri kupata results nzuri kutoka kwenye taasisi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba tu niseme kwamba ninaunga mkono hoja zote za Kamati na Maazimio yote yaliyotolewa na Kamati na ninaomba maazimio ya mwaka jana na maazimio ya mwaka huu Serikali isipoyatekeleza mwakani tutayaleta, na hata mwaka 2030 tutayaleta tena. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nikutakie mwenyewe kheri ya mwaka mpya, Mawaziri wote, Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kufanikisha kuingia mwaka 2017. Tunapenda kumshukuru Mungu kwa pamoja kwa kutupa uhai.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie hoja ya Muswada wa Sheria wa Legal Aids. Muswada huu Waheshimiwa Wabunge umekuja wakati muafaka na ni Muswada muhimu sana kwa wananchi wote wa Tanzania ambao utasaidia kuwawezesha kupata haki zao muhimu kuanzia akinamama, watoto, vijana, walemavu na watu wote wa Tanzania, Muswada huu umekuja wakati muafaka kwa sababu watu wengi wamekuwa wakikosa haki zao za msingi kwa sababu tu hawajui watazipata wapi au hawana uelewa wa kutafuta hizo haki zao. Sasa kuleta Muswada huu kwa wananchi wa Tanzania ni muhimu na utawasaidia wengi kupata haki zao za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko haki zao za msingi za wananchi wa Tanzania ambao wamekuwa wakizikosa kila siku. Mfano mdogo tu, mtu anaweza akakamatwa na polisi asipelekwe Mahakamani kwa muda wa siku tatu wakati Sheria inasema kwamba mtuhumiwa anapokamatwa na polisi anatakiwa ndani ya masaa 24 awe amepelekwa mahakamani. Hata hivyo, kwa sababu mtu anakuwa hajui kwamba ana haki ya kudai kwamba kwa nini sijapelekwa mahakamani na nimeshakaa hapa kituo cha polisi kwa muda wa siku tatu; kwa sababu anakuwa hajui jinsi sheria inavyosema, anafikiria kwamba ni haki kwa polisi kumshika mtuhumiwa na kumweka pale kituo cha polisi kwa siku tatu bila kumpeleka mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa na Muswada huu, watu wengi watapata elimu. Ukija pia upande wa akinamama, akinamama wengi wamekuwa wanakosa haki zao za msingi kwa sababu tu hawazielewi na hawajui jinsi ya kuzitafuta. Kwa kuwa na Muswada huu, akinamama wengi wataamka, watafahamu haa! Kumbe hata mimi nina haki hii! Mfano mdogo tu; mama anaweza akafiwa na mume wake lakini unakuta kwamba kikao cha familia kinakaa, kina-control ile mali ambayo imeachwa na mume wake wakati mama huyo ana haki na ile mali na wakati sheria inasema kwamba sio lazima mama awe anafanya kazi na mume anafanya kazi ndiyo aweze kupata zile haki za msingi. Kitendo tu cha mama kuchemsha maji ya moto na kumchemshia bwana chai asubuhi kina-contribute kumfanya yule bwana aende kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea kwamba yule bwana amefariki unakuta vikao vinakaa na kudai kwamba yule mama haku-contribute kitu na kwamba yule mama si sehemu ya ile mali. Kwa kuleta Muswada huu, akinamama wengi wataelimika, wataelimishwa. Kwa sababu inakwenda mpaka vijijini unakuta kule vijijini akinamama wamekuwa wakidhulumiwa. Unaweza ukakuta mume wake alikuwa anamiliki shamba lakini anapofariki kikao cha ukoo kinakaa na kinadai kwamba mwanamke huwa harithi ardhi. Hii ni ardhi ya ukoo, kwa hiyo, mwanamke haruhusiwi kuitumia. Lakini kwa kuwa na Sheria hii, akinamama wengi wataamka, wataelewa jinsi ya kwenda kudai hizo haki zao za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija pia kwa upande wa watoto. Watoto wengi wamekuwa wanadhulumiwa. Utamkuta baba anazaa mtoto wa nje, anapomzaa yule mtoto wa nje anamtelekeza; kwa kuwa na sheria hii, wale watoto wataelimishwa jinsi ya kudai haki zao kwa sababu mtoto wa nje mara nyingi anaambiwa kwamba yule mzazi akifa hawezi kurithi mali. Ukija kwenye sheria zote, Sheria za Serikali na Sheria za dini zetu zinamhesabu kwamba ni mtoto wa nje. Hata kama akiwa Muislamu ataelimishwa kwamba “wewe mwambie baba yako akuandikie urithi” kwamba atakapokufa utarithi kitu fulani ili uweze kupata haki yako. Pia yule mtoto ataelimishwa kwamba mwambie baba yako akutambue kisheria kwamba wewe ni mtoto wake ili atakapokufa uweze kudai haki yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija pia kwa upande wa walemavu, utakuta majengo mengi humu nchini kwetu yanajengwa hayana miundombinu ya kuwawezesha wale walemavu kufika kwenye zile ofisi, lakini kama sheria zetu zitakaa vizuri na wale watafundishwa zile sheria jinsi ya kuzidai, wataifanya Serikali iweke sheria muafaka kwamba mtu anapojenga jengo kama ni hoteli lazima aweke miundombinu ya walemavu. Haki hii pia itakwenda pia kwenye magereza. Tumekuja kuona kwamba watu wengi ndani ya magereza wanafungwa na wanashindwa hata jinsi ya kuandika appeal, akija kwenda kuomba kwamba nataka ku-appeal kesi yako anaambiwa kwamba muda umekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kupitisha Sheria hii, hawa ma-legal aids watakwenda kule magereza, watakuwa wanatoa elimu, wale wafungwa walioko kule magereza wataweza kujua kwamba “natakiwa nifuate procedure gani ili niweze ku-appeal kesi yangu”. Hata wale pia watakaokuwa kituo cha polisi watafahamu kwamba hii kesi yangu natakiwa nifuate njia gani ili niweze ku-appeal kwenye hii kesi yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu Muswada ndugu zangu, Wabunge wenzangu na Watanzania wote naomba tuunge mkono, umekuja wakati muafaka, wakati wa zama za utandawazi. yako mambo mengi, yako mambo ya ugaidi yanayoendelea duniani, naombeni tuunge Muswada huu mkono ili uweze kupita ili mwananchi wa kawaida aweze kusaidiwa kupata haki yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nauunga mkono Muswada huu, naunga hoja hii, nauunga Muswada huu naona umekuja wakati muafaka. Naomba na wenzangu muunge mkono Muswada huu ili wananchi wetu na watu wetu mpaka wa hali ya chini, vijijini mpaka huko kwenye Kata zetu waweze kupata ile elimu. Yako mambo mengi ambayo kwa mfano kwa mwanamke ziko sheria nyingi, Sheria za mpango wa uzazi, ukija kwenye mikataba ya kimataifa ambayo nchi yetu imeingia; mikataba ya wanawake kuna vitu vingi ambavyo wanawake hawavifahamu lakini ujio wa Muswada huu utawafanya wale waliosomea mambo ya wanawake na hizi Taasisi za Legal Aids ambazo sasa hivi tunazo kama hizo TAWLA, ambazo zinatoa msaada kwa sasa hivi, itazifanya ziende mpaka vijijini kuwaelimisha wanawake ili waweze kujua ile mikataba ya kimataifa inasemaje juu ya mwanamke.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo tu, mwanamke anayo haki ya kupanga uzazi, sio lazima apite kwenye Wizara ya Afya akapange uzazi. Ziko Sheria za Kimataifa na protocol zake ambazo zinampa mamlaka mwanamke kupanga uzazi kwamba anahitaji watoto wangapi. Ziko Sheria nyingine za Kimataifa zinampa mamlaka mwanamke anapoolewa hahitaji kubadili jina lake kutumia jina la mume wake. Kwa hiyo, vitu kama hivyo wanawake wanatakiwa waelimishwe na kuja kwa Muswada huu kutawafanya wale ambao wanazijuia hizo sheria waweze kwenda kule vijijini kuwaelimisha hao akinamama ili waweze kupata hiyo elimu ambayo itakuwa inatolewa. Sijajua zimebaki dakika ngapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kuzungumzia suala la wazee. Zipo Sheria za wazee ambazo zimepitishwa na Bunge hili Tukufu ambazo wazee kule vijijini hawazifahamu na wengine wala hawajui kwamba kuna Sheria ambazo sisi tumezipitisha. Kwa mfano tu suala la kwamba wazee wapate matibabu bure. Wazee wengi kule vijijini; kwanza unakuta zile hospitali zenyewe ambazo zina-offer hayo matibabu bure hazipo. Unaweza ukakuta mara nyingi ni zahanati za watu binafsi, kwa hiyo mzee anapokwenda pale inabidi alipe. Kwa ujio wa Muswada huu hawa watoa msaada wa kisheria wataweza kwenda mpaka vijijini ambako wataweza kuwaelimisha hawa wazee kwamba tazama zipo sheria ambazo zimepitishwa na Bunge ambazo mzee unatakiwa utibiwe bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wale wazee itawasaidia wao kudai haki zao za msingi, kudai watibiwe bure na kuidai Serikali yao. Tukiangalia tu kwa mfano mdogo, nikija kwenye suala la watoto; tukiangalia kwamba nchi yetu ya Tanzania inao uhaba wa magereza za watoto. Watoto wanapofungwa, natoa mfano mdogo wa kule Arusha; iko nyumba imekodiwa ya mtu ambayo watoto huwa wakifungwa wanawekwa pale sasa inahesabiwa kwamba pale ni magereza. Nchi nzima hii ya Tanzania ina magereza matatu tu ya watoto wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii legal aids ikipitishwa, wale wanaofahamu mikataba ya kimataifa ya watoto wataweza kuwasaidia hawa watoto kudai mambo yao ya msingi na kuelewa kwamba ziko Sheria za Kimataifa ambazo zinam-guide mtoto na zinamlinda mtoto ili aweze kupata haki zake za msingi. Watakwenda mpaka kule vijijini tunawaona watoto wengi wanakosa kwenda shule, wanakosa chakula, wanakuwa wanatembea tembea tu mtaani, lakini ikipita hii Legal Aids wale watoa huduma wataweza kwenda kule vijijini watawaelimisha, wataweza kujua haki zao za msingi. Wataweza kujua kwamba hata kama sina mzazi natakiwa nidai haki zangu za msingi Serikalini na wataweza kupata haki zao za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la wanafunzi; wanafunzi pia watafundishwa huu Muswada wa Legal Aids, wataelewa haki zao za msingi. Tunazo education grants na tunayo Mikataba ya Kimataifa ambayo inalinda pia inamlinda mwanafunzi, Walimu ambazo hawa legal aids ambao ni wataalam katika hayo masuala wataweza pia kuwafundisha hao watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hao legal aids, siwezi kuzungumzia tu suala la wanawake upande mmoja, wataweza pia kuwaelimisha wanaume ili waweze kutoa haki zao za msingi kwa watoto wao, wazee wao na kwa akinamama. Hawa legal aids wataweza pia kuwaelimisha zile sheria kandamizi ambazo zinamkandamiza mwanamke kama vile vipengele fulani fulani vilivyoko kwenye Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, Ibara ya 13, 14 na 15 inaonesha kumuengua mtoto wa kike kumtofautisha na mtoto wa kiume. Ujio wa Sheria hii ya Legal Aids itawafanya wale legal aids waweze kuwafundisha wasichana waweze kuelewa na waweze labda kudai marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili isiweze kuweka tofauti kati ya mtoto wa kiume na mtoto wa kike.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana tumeona mifano mingi. Mara nyingi hata kwenye shule, watoto wa kike wanapopata mimba wao ndiyo huwa wanafukuzwa shule; yule mtoto wa kiume anabaki shuleni anaendelea. Hata kama wanasoma shule moja unakuta kwamba yule mtoto wa kike ndiyo anayeharibikiwa, anafukuzwa shule lakini yule mtoto wa kiume yeye anabaki anaendelea na shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ujio wa Sheria hii utawafanya wale watakaokuwa wanatoa somo la hii legal aids na misaada hii ya Sheria kuwaelimisha watoto wa shule angalau sheria zikabadilishwa kama basi watoto wanasoma shule moja na imetokea matatizo, mmoja amekuwa mjamzito, basi wahusika wote wakae nje ya shule sio anakaa mtoto mmoja wa kike, wa kiume yule anabaki anaendelea na shule yule wa kike anakuwa ameharibikiwa na maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisemee suala la watoto wa mitaani ambao pia nao wataweza kudai haki zao za msingi kwa sababu watakuwa wamepata elimu. Nimesemea suala la vijana, watadai haki zao za msingi. Watakuwa wamepata elimu, watasaidiwa. Mambo pia ya mifugo, mashamba, mkulima atadai haki zake, mfugaji atadai haki zake za msingi. Serikali itakuwa na sheria nzuri ambayo itaweza kutenganisha maeneo ya wafugaji na maeneo ya wakulima kwa sababu wakulima watapata elimu kutoka kwa hawa legal aids…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kuleta mabadiliko ya sheria hii, naomba nimpongeze Jenista Mhagama na Mawaziri wote waliokuja kwenye Kamati yetu, tuliita Serikali na kwa kweli kwa mara ya kwanza tulishuhudia Mawaziri wanne walikuja kwenye Kamati yetu na kila mtu alikuwa anajibu hoja ambazo Kamati iliziuliza. Tulikuwa na Waziri wa Maji, mwanangu Mheshimiwa Aweso; tulikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Kwandikwa, tulikuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tulikuwa na mwandishi Mkuu wa Sheria za Bunge (CPD), wote walikuja kwenye Kamati yetu na wote waliweza kutuelekeza yale ambayo tuliyouliza kwenye Kamati na majibu tuliyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye muswada huu mimi nakwenda kwenye page ya 14 na nitachangia kile kifungu ambacho kimeongeza adhabu ya mtu anachezesha game ambaye atamshawishi mtoto mdogo kuingia kwenye hiyo michezo na kuangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kifungu kilikuwa kimewekwa adhabu ndogo ambayo ilikuwa inaishia shilingi 500,000; lakini kwa kuongeza adhabu kuanzia shilingi milioni moja mpaka shilingi milioni tano kitawafanya wale wanaochezesha hii michezo ya kuigiza na wale ambao huwa wanapenda kuwashawishi watoto kwenda casino wataweza kuogopa, maana yake tabia nyingi za watoto/ watoto wengi wanaharibika baada ya kuangalia movie zile ambazo anaangalia, anapata ushawishi ambao unamfanya na yeye anasema na yeye ebu nijaribu na mimi nijaribu hiki kitu. Kwa hiyo, kwa kuweka kifungu hiki, wale wote ambao wanachezesha hii michezo hata kule vijijini, mikoani na wilayani wataogopa kuwaingiza watoto wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ningependa kukichangia kwenye muswada huu ningependa kuipongeza Serikali kwa kuleta katazo la upigaji picha mtu aliyekufa na maiti kwenye kile kifungu cha 162, lakini hata pia ningeiomba Serikali iongeze wigo kwa sababu mtu unaweza ukawa unasafiri ukakuta basi limeanguka labda limeanguka kwenye mtaro na watu wamekufa ukataka uchukue zile picha kwa ajili ya kuhabarisha umma au kwa ajili ya kuzipeleka polisi ili ziwe ushahidi.

Mheshimiwa Spika, sasa maeneo mengi kama unavyojuwa nchi yetu, hatujafikia kile kiwango cha kuwa na kamera kwenye barabara zetu, kwa wenzetu wa Magharibi wao wanakamera kwenye barabara zao kila mahali, kwa hiyo, hata kama ukikataza upigwaji wa picha unakuta kwamba ni sahihi, lakini kwetu sisi hatujawa na kamera kwenye barabara zetu ambazo zinaweza zikapiga picha ajali inapotokea mahali popote hata kama ni porini.

Kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali ijaribu kuangalia kwa katika circumstance ambazo zinatokea mtu amekuta watu wamekufa pale anataka kutumia hiyo picha kama ushahidi basi aweze kupiga na kuhabarisha umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kipengele hicho lakini niseme naipongeza kwa kuja na hiyo sheria kwa sababu watu wengine walikuwa wanaitumia vibaya kupiga miili ya watu kwa mfano mzuri ilikuwa ni ajali ya Morogoro iliyotokea hapa juzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele kingine ambacho ningependa kukizungumzia ni kile kipengele cha 54(2) chenye interpretation act cap. 1; kipengele hiki kimeandikwa katika lugha pana, ingependeza zaidi kama sheria ingeainisha ni maeneo gani mahususi ambayo Katibu Mkuu atayafanya, lakini kwa kuiacha tu ndani ya wigo kwamba Katibu Mkuu anaweza akafanya mambo fulani wakati ile bodi haipo na haiainishi yale mambo ambayo Katibu Mkuu anatakiwa afanye naona kipengele hiki kitampa mwanya mkubwa Katibu Mkuu kiasi kwamba kama ni mtu ambaye anataka ku-misuse power zake akatumia hiki kipengele cha 54(2) ningeomba Serikali ijaribu kukiangalia na kukiandika vizuri zaidi ili kikidhi hitaji ambalo linahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kufuta ule Mfuko wa SSRA. Naipongeza Serikali kwa sababu imeangalia ikaona kwamba ilikuwa inatumia pesa nyingi kuwa na huo mfuko, kwa hiyo imeondoa yale majukumu ya ule mfuko inayapeleka kwenye Wizara ya Mheshimiwa Jenista, lakini niiombe Serikali hiyo division itachukuwa majukumu ya ile mifuko yote ijaribu kuihudumia Ile mifuko ambayo inaidumia kama jinsi ambavyo SSRA ilivyokuwa inafanya kazi zake, isiwe tu kwamba tumevunja kwa sababu leo kwa kipengele namba 72 ina maana tunaivunja rasmi SSRA hapa Bungeni, ila tunaendelea kutumia sheria zake ambazo zimeainishwa kwenye kipengele 72 nafikiri kila mtu ana muswada huu anaweza akaenda akaangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naipongeza Serikali na naiomba Serikali kama inaona vitu vingine ambavyo ilivianzisha, lakini imeshaona kwamba haiwezi ikaendelea kutumia pesa nyingi kuwa na mifuko ya aina hiyo inaweza ikaleta tu pia nayo tukabadilisha kwa sababu hata nyumbani ukiona umefanya kitu lakini unaona hakiendi unabadilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sioni vibaya kwa Serikali kuvunja huo mfuko na kupeleka haya majukumu kwenye Wizara kwa sababu kuna kitengo kitaanzishwa pale, kuna idara itaanzishwa pale ambayo itakuwa inashughulikia majukumu hayo, lakini niseme tu kamba na kamba kuna taasisi nyingine ambazo zimeazishwa ambazo Serikali inaona kwamba ni mzigo mkubwa kuziudumia basi ilete zile sheria na niwaombe Wabunge humu Bungeni tuzibadilishe na tusione ubaya wa Serikali kuivunja SSRA na kubaki tunatumia zile sheria zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kuzungumzia suala la adhabu ya kulipa interest ambayo imeshazungumzwa na Wabunge wengi kwa mtu ambaye ameshapewa adhabu na amekabiliwa lakini anapochelewa kulipa inabidi alipe interest.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijatoa kikokotoo cha interest na tulivyoiuliza Serikali kwenye Kamati yetu ilisema italeta kwenye regulations. Kwa hiyo niombe tu Serikali itakavyoleta regulations hizo za kikokotoa hizo interest ilete kikokotoo kizuru isimuumizi yule mtu ambaye amepewa adhabu kwa sababu mtu anaweza akawa amepewa adhabu ya kulipa milioni 100, lakini sasa interest ikawa unaambiwa kila mwezi ulipe shilingi milioni 20 by the time miezi sita inaisha unakuta yule mtu anadaiwa milioni 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe kikokotoa hicho kitakacholetwa kiwe ni kikokotoa ambacho kitakuwa rafiki, ambacho yule mdaiwa anaweza akakilipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni bond ambayo imeshazungumzwa na Wajumbe waliopita, niipongeze Serikali kwa kuleta utaratibu wa kuweka security bond kwa hawa wanaochezesha michezo siku hizi kwa sababu ni wengi wameibuka, wanachezesha hiyo michezo, kwa hiyo, kwa kuweka security bond ina maana mtu atakapo win kama asipolipa ile pesa yake ile security bond ya yule aliyechezesha mchezo inaweza ikatumika kumlipa yule mchezeshaji, kwa hapa niombe kuipongeza sana Serikali kuja na sheria hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwa kutumia floor hii, Serikali ijaribu kuangalia sheria nyingine zote ambazo zimepitwa na wakati izilete ili tuweze kuzibadilisha hapa Bungeni kwa sababu tunazo sheria nyingi sana. Nitoe tu mfano, kuna sheria za traffic zimepitwa na wakati, anamgonga mtu amekufa, amevunjika mkono, lakini akienda mahakamani akikubali lile kosa anaishia kulipa 50,000 na Sheria nyingi tu ambazo zimepitwa na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kwa sababu inayo Tume ya Kubadilisha Sheria nchini, basi Tume hii ya Kubadilisha sheria nchini itumike vizuri katika kipindi cha mwaka mmoja tuone ile tume imefanya kazi kubadilisha sheria zipi. Tunazo sheria nyingi sana ambazo zimekaa, zingine ni za toka mwaka 1963, lakini bado zinatumika humu nchini. Ukiziangalia hata kwenye sheria nyingine ambazo si nzuri kwa wanawake kama mtu kupewa matunzo ya shilingi 100 kwa mwezi, zote hizi ambazo ziko kwenye Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 bado niiombe Serikali kama jinsi inavyoweza kubadilisha sheria hizi basi ichukue tena umuhimu wa kubadilisha hizo sheria nyingine ambazo zimepitwa na wakati ili ziweze kukidhi hitaji la Watanzania wote wanawake na wanaume.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwenye huu Muswada kwa sababu nilikuwa Mjumbe wa Kamati na tumeuchambua kwa undani, nikiendelea kusema mambo mengi ambayo hatukuchambua kwenye Kamati nitakuwa ninasema uongo. Naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante!

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Finance Bill. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mpango na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya siku zote hizi kuhakikisha kwamba hii bill inakuja vizuri na Watanzania waweze kupata nafuu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia ushuru wa bidhaa. Napenda sana kuipongeza Serikali kwa kuondoa ushuru wa bidhaa za mvinyo wa mazao yanayosindikwa nchini Tanzania. Hii itatusaidia sana kuwakaribisha wawekezaji kuja kufungua viwanda nchini kwetu Tanzania na ukiangalia kwamba tunayo matunda mengi sana nchini kwetu Tanzania. Matunda kama maembe, mapapai, mapera, mananasi, machungwa ambayo yanalimwa kwa wingi Tanzania lakini tulikuwa tunakosa wawekezaji kuja kufungua viwanda nchini kwetu kwa sababu ya kodi ambayo ilikuwa imewekwa. Kwa kuviondolea kodi viwanda hivi vitakavyofunguliwa nchini kwetu, itatusaidia sana kupata wawekezaji wengi na ukiangalia kwamba nchi yetu ni ya amani, kila mtu yuko huru, mtu yeyote anaweza akaingia hapa akafungua kiwanda chake, akaajiri watu haina masharti ambayo yanamkatisha tama mtu kufungua kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo, amani yenyewe ninayoisema ni kwamba niitolee mfano kidogo tu siwezi kuitaja nchi ninayotaka kuisema. Kuna nchi nyingine huwezi kutembea baada ya saa nne, ukitembea mita 100 unaulizwa kipande cha kodi. Kwa hiyo amani hii tuliyonayo ni nzuri kwa wawekezaji na kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa hiyo nipongeze sana hilo la kuondoa ushuru wa bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulipongeza na kulizungumza ni kuondoa ushuru wa kodi ya mapato katika Income Tax Act Section 9, imeondoa ule usumbufu wa kufanya mahesabu kwa wafanyabiashara wa milioni 20. Ukiangalia kwa dunia ya sasa mtaji wa milioni 20 kwa wafanyabiashara wakubwa wakubwa ilikuwa ni mtaji mdogo lakini ulikuwa na usumbufu mkubwa sana wa kumtafuta mhasibu aje kukufanyia hesabu halafu akishatoa zile hesabu ndiyo uende ukakabidhiwe mapato yako. Zaidi ya hapo ilikuwa inaongeza gharama kwa sababu yule mtu wa kuja kukufanyia hesabu inabidi umlipe tena fedha ili aje afanye hesabu yako. Sasa kwa kuweka kiwango hiki cha kutoka milioni 20 mpaka milioni 100, kwa kweli naipongeza sana Serikali, hapa imepiga hatua na imewafanyia vizuri wafanyabiashara wetu nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu haya marekebisho yote pamoja na ile ya wafanyabiashara wa chini ya milioni 4,000,000 kupunguziwa kodi. Kwa pamoja niombe haya marekebisho yaandikwe vizuri na yawekwe kwenye mbao za matangazo ikiwezekana kwenye halmashauri ili wananchi waweze kusoma kwa sababu yakiachwa hivi hivi bado kuna watumishi ambao siyo waaminifu watawazungukia tena wale wafanyabiashara na kuwadai kodi. Kwa sababu ukiangalia pia kuna kodi nyingi ambazo Serikali ilizifuta hata mwaka jana, lakini bado wale watumishi ambao siyo waaminifu huwa wanarudi kwa mgongo wa nyuma kuwadai wafanyabiashara kodi. Niombe TRA iandae zile kodi zote ambazo zimefutwa na Serikali zibandikwe kwenye matangazo ili Watanzania wote wazione. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuleta vile vitambulisho vya 20,000. Ila naomba kutoa angalizo kwenye hivi vitambulisho vya 20,000, niiombe Serikali iweze kuweka picha ya mtumia kitambulisho ili mtu aeleweke ni nani anayefanya biashara katika lile eneo. Kwa sababu kwa kuiacha wazi mimi leo naweza nikaamua nikanunua kile kitambulisho nikakaa Kisasa nikauza biashara yangu na kesho nikahama nikaenda Majengo nikauza biashara yangu kwa sababu kile kitambulisho hakina picha. Labda kama kingeweza kuwekewa kwamba na eneo la makazi ni wapi, lakini idea ni nzuri kwa sababu ukiangali wananchi walikuwa wanateseka sana kwa kupitia hawa watoza ushuru ambao walikuwa wanadai mia mbili, mia mbili kila siku, walikuwa wanawanyanyasa wakiwakuta wanawamwagi vitu vyao, wanawaambia huruhusiwi kuuza mpaka umelipa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuleta hiki kitambulisho ina maana mfanyabiashara atakuwa huru kuuza biashara yake mahali popote, ili mradi tu hiki kitambulisho kiboreshwe na pia utoaji wake yule mwananchi wa kawaida unaweza ukaiona 20,000 ni ndogo, lakini kwa mfanyabiashara wa kawaida kama mama anayeuza njugu au anayeuza vitu vyake vidogo vidogo kama mchicha kupata hiyo 20,000 kununua kile kitambulisho inakuwa ni shida. Kwa hiyo utaratibu uwekwe kama vile mtu anaweza akalipa kidogo kidogo labda kwa awamu nne elfu tano tano mpaka anatimiza ile 20,000 itakuwa imemsaidia zaidi huyu mama wa chini anayeuza karanga na huyu kijana wa chini ambaye anatafuta maisha labda na yeye pia kwa kuuza njugu, kwa kuuza mchicha, kwa kuuza matunda kwa kitu chochote ili aweze kuweka ile fedha yake. Akiuza aweke kidogo kidogo ikifika 5,000 alipe mpaka atimize hicho kitambulisho cha 20,000, ukiiacha kuitoa 20,000 kwa mara moja wengine kama huko tunakotoka kuweka 20,000 inakuwa shida kidogo. Niiombe tu Serikali ijaribu kuangalia hapo jinsi ya kuwasaidia hao wafanyabiashara wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala lingine, ni kodi ambazo zimepunguzwa kama za visima vya maji. Niipongeze Serikali ni nzuri kwa sababu zilikuwa zinasaidia kwenye maeneo ambayo maji hayatoki, watu walikuwa wanachimba vile visima wanawasaidia wananchi. Ukiangalia maeneo mengi nchini kwetu Tanzania hayana maji, kwa hiyo walikuwa wanawasaidia wananchi wa eneo lile kupata maji. Sasa kwa kuwawekea kodi tulikuwa kama vile wanataka kuvunjwa moyo wa kutaka kusaidia wananchi wa eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sehemu nyingi wananchi bado wanatumia maji ya visima na bado maji ya bomba hayajaenea kwenye vijiji vyetu, ndiyo kwanza tunahangaika kutafuta maji ya bomba. Tumeanzisha miradi ambayo tunataka tuchimbe maji ya bomba na Watanzania wote waweze kutumia maji ya bomba. Kwa kifupi ni kwamba maji ya bomba hayajafika vijijini, kwa hiyo kwa kuondoa hii kodi, hii tozo ya kwenye visima vya maji ni sahihi kabisa. Naipongeza Serikali itasaidia sana, itawafanya wafanyabiashara wengine wenye uwezo waweze kuchimba maji na kuwasaidia wananchi wa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningeweza kulizungumzia, nawashangaa sana wanaume wanasimama humu ndani wanachangia mambo ya nywele, mimi nafikiri wangechangia mambo yanayowahusu wao. Hivi vitu ni personal issue za wanawake, mwanamke anahitaji yeye mwenyewe anajiangalia leo afanye nini; asuke nywele ya rasta, aweke hilo wigi, anyoe kipara au afanyeje. Sasa mwanaume anasimama humu anasema mimi nampenda mke wangu akisuka kipilipili, so what! Kila mtu ana interest yake, kuna mwanaume mwingine anampenda mwanamke aliyenyoa kipara, mwanaume mwingine anampenda mwanamke aliyevaa wigi, mwingine anampenda mwanamke…

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska kuna taarifa huku, Mheshimiwa Selasini.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, kwa kiasi kikubwa hayo mawigi tunanunua sisi kwa ajili yao.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska una dakika moja malizia mchango wako.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Mheshimiwa Selasini siwezi kuipokea kwa sababu akinamama sasa hivi wameamka wanashika uchumi. Akinamama wanafanya biashara za kila aina, wanauza maduka, wanapika mama ntilie, wana hoteli, wanaendesha mpaka magari na bajaji. Kwa hiyo, suala la kuwaambia kwamba wanaume wanawanunulia nywele si sahihi, si sahihi kabisa, taarifa yake hiyo siipokei. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, akinababa wanapenda sana kutelekeza watoto, hizo nywele utaweza kununua!

Tukihesabu watoto wa mitaani wanaotembea ni wale watoto ambao wamekimbiwa na baba zao, sembuse hiyo nywele kununua.

MBUNGE FULANI: Sema!

MHE. TASKA R. MBOGO: Wanaume huwa hawawezi kumnunulia mwanamke nguo wala kitu, mwanamke huwa anajiremba mwenyewe. Kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba akinamama wasife moyo, wanaovaa wigi wavae wigi, wanaotaka kusuka wasuke, wanaotaka kusuka rasta wasuke na hizo nywele hata kama zimepanda kodi sisi tutazinunua tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze wewe mwenyewe kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda nimpongeze Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais akiwa ni mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961. Napenda niwapongeze Mawaziri wote mliochaguliwa katika nafasi zenu na pia nimpongeze Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Afya Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy, ukiwa kama mama kwa kuchaguliwa kuiongoza Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza hayo, ninayo machache ya kuzungumza. Katika Mkoa wetu wa Katavi tunacho Chuo cha Afya ambacho kilianza kukarabatiwa mwaka 2010 na kikasimama, lakini mwaka jana kimeanza kukarabatiwa kwa kasi. Naomba kasi hiyo iendelee na chuo hicho kiweze kufunguliwa ili kiweze kusaidia huo Mkoa wa Katavi na kiweze ku-train wanafunzi ambao watausaidia mkoa, kwa sababu mkoa upo pembezoni na watu wengi huwa wanasuasua kwenda kufanya kazi huko. Kwa hilo, naomba niishukuru Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, napenda niongelee pesa za Basket Fund. Naomba pesa hizo ziwe zinawahi kupelekwa kwenye mkoa wetu zinatakiwa zipelekwe mwezi Julai mpaka Septemba, lakini zile pesa huwa zinapelekwa mwezi wa kwanza au zinapelekwa Disemba zikiwa zimeunganishwa na pesa za Oktoba mpaka Disemba. Matokeo yake katika Mkoa wetu wazee wanashindwa kupata matibabu, wanaishia kuandikiwa cheti ili waende kununua dawa, vifaa tiba vinakosekana hospitali, pia watoto wanakosa chanjo, vitanda vinashindwa kununuliwa mahospitali kwa sababu hizo pesa zinachelewa takribani miezi sita ndiyo zinapelekwa kwa pamoja. Kwa maana hiyo, kwa muda wote huo wa miezi sita kunakuwa hakuna vifaa. Kwa hiyo, nashauri zile pesa ziwe zinaharakishwa kupelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizungumzie suala la MSD. Napenda Serikali iwe inapeleka pesa Wizara ya Afya ili pesa hizo ziweze kupelekwa kimkoa na ili dawa ziweze kununuliwa kwenye zahanati na kwenye vituo vya afya. Kwa mfano, kule kwenye Mkoa wetu wa Katavi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina vijiji 54. Katika hivyo vijiji kuna vituo vya afya 14 tu, vijiji 40 havina vituo vya afya na katika vijiji hivyo 54 tunazo kata 16, katika hizo kata vituo vya afya vipo vitatu, kwa maana kwamba Kata 13 hazina vituo vya afya. Kulikuwa na ule mpango wa MMAM. Mpango huo kadri ya rekodi za Wizara ya Afya unakwisha mwaka 2017 na kule kwetu Katavi hivyo vijiji bado havijajengewa zahanati na hivyo vituo vya afya 13 havijajengwa. Sijui ni muujiza gani ambao utatokea kwa muda wa mwaka mmoja hivyo vijiji 40 viwe vimepata zahanati na hizo kata 13 ziwe zimepata vituo vya afya.
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri akija kwa sababu mpango wenyewe wa MMAM bado upo na unakwisha mwaka 2017 labda atatuonea huruma sisi wa mkoa wa pembezoni tuweze kupata hizo zahanati pamoja na hivyo vituo vya afya.
Naomba niishukuru sana Wizara kwa kututengea shilingi milioni 300 kwenye Mkoa wetu wa Katavi, lakini naomba muwaambie MSD wafungue duka la dawa katika Mkoa wa Katavi kwa sababu duka ambalo tunalitegemea kwa sasa hivi lipo Mkoa wa Mbeya na umbali wa kutoka Katavi kufika Mkoa wa Mbeya ni kilometa 600, kwa hiyo, naomba muangalie utaratibu wa kuweza kufungua duka la dawa kupitia MSD katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine nashukuru sana kwa watendaji ambao mmewapeleka katika Mkoa wa Katavi, lakini naomba watumishi mnaowaleta katika Mkoa wa Katavi wawe ni trained, msituletee medical attendant, kwa maana ya kwamba kuna vifaa vingine ambavyo wanaweza wakawa wanashindwa kuvitumia, maana yake rekodi inaonesha kwamba, mikoa ya pembezoni huwa inapenda kusukumiwa medical attendant. Naomba mtuletee watumishi ambao ni trained.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nitume ujumbe kutoka kwa Wazee wa Mkoa wa Katavi, wanaomba bima ya afya iweze kutumika na mikoa mingine kwa sababu wanaposafiri wakitoka Mkoa wa Katavi, wakiingia Mkoa wa Tabora ile bima inakuwa haifanyi kazi tena. Wanaomba bima ya afya iwe kama ATM ya benki ambayo hata wakiwa Dar es Salaam waweze kutumia hiyo bima ya afya na waweze kupata matibabu yao.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze suala la afya. Katika suala la afya naomba Wizara yako ya Afya ijaribu kuwa na mawasiliano na wale Maafisa Afya walioajiriwa ambao wako kwenye Halmashauri za Wilaya. Wale Maafisa Afya mara nyingi wanakuwepo pale, lakini unakuta miji ni michafu, unakwenda stand unakuta vyoo ni vichafu, unaenda sokoni, unakuta vyoo ni vichafu. Pia hili suala la kubinafsisha vyoo mpaka stand je, mwananchi ambaye hana pesa atatumia nini?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba haya masuala ya uchafu, kwa mfano kama sasa hivi tunakabiliwa na masuala ya kipindupindu katika nchi hii ya Tanzania. Kama hawa Maafisa Afya wangekuwa wanatoa elimu ya kipindupindu kwamba, watu waweze kunawa mikono yao michafu, wasiweke uchafu, kusiwe na maji ya kutiririka nadhani hili suala la kipindupindu lingekuwa halipo.
Mheshimiwa Spika, pia naomba Wizara ya Afya itoe elimu ya homa ya bonde la ufa, elimu ya ugonjwa zika kwa wananchi kwa sababu kuna mbu anayeeneza huo ugonjwa na wananchi wengi hawajajua athari yake. Hivyo, ikiwezekana basi tuwe kama nchi nyingine ambazo zinapita kuua yale mazalia ya mbu, kwa sababu mfano mzuri, kuna nchi nyingine kama Zambia wanaua mazalia ya mbu ambayo matokeo yake yanapunguza malaria na hayo magonjwa ya zika yanaweza pia kupungua.
Mheshimiwa Spika, naomba pia liangaliwe suala la usafi wa barabara ambazo mifereji unakuta imeziba na yale maji hayatembei na ndiyo yanayosababisha matatizo yote ya magonjwa ya milipuko ambayo yanaathiri sana nchi yetu ya Tanzania na yanaathiri watu wanakwenda kuugua magonjwa hayo ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Mheshimiwa Spika, naomba vilevile akinamama wapewe elimu ya kutojifungulia nyumbani, wawe wana-attend kliniki ili kupunguza vifo vya akinamama ambavyo katika kitabu chako umeeleza ni vifo ambavyo vinatisha. Siwezi nikasema idadi hapa, lakini kila mtu amesoma, kwa hiyo, akinamama wangepewa elimu, wasiwe wanajifungulia nyumbani, wanapokuwa wajawazito waweze kwenda kliniki ili waweze kupata matibabu na kuelekezwa jinsi ya kufanya.
Mheshimiwa Spika, kinachotokea sasa hivi ni kwamba, akinamama wale wanakosa elimu na kwa sababu kwa mfano kwenye Mkoa wetu wa Katavi hakuna hizo zahanati kama nilivyosema mwanzo, kwa hiyo, matokeo yake mama anatafuta njia nyingine ili aweze kujifungua atamtumia mkunga wa jadi, kwa sababu katika eneo lake hakuna zahanati na miundombinu ni mibovu, hivyo hawezi akatoka kijijini kule akaenda kufuata hospitali ambayo unakuta hospitali iko kilometa kama 200. Kwa hiyo, naomba hilo lizangatiwe.
Mheshimiwa Spika, naomba kama huo mpango wa MMAM upo Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho aje atueleze kama anaweza akatupatia zahanati na hivyo vituo vya afya kwenye Mkoa wetu wa Katavi ili tuweze kupunguza vifo vya akinamama ambavyo vimekuwa vinaathiri sana Mkoa wetu na vinaathiri Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia kuzungumzia suala la dawa na huo Mfuko wa NHIF ambao watu wengi wamejiunga na hiyo bima ya afya lakini wanapokwenda hospitali matatizo yanakuwa ni hayo ya ukosefu wa dawa, lakini kwenye hiyo mikoa yetu mingine inakuwa ni tatizo la hizo funds ambazo zinakuwa zimechelewa kufika ndio zinasababisha...
NAIBU SPIKA: Tayari dada muda, haupo upande wako.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Afya.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nami naomba niongelee suala la ripoti yetu ya Kamati ya Katiba na Sheria, na-declare interest mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie ufinyu wa bajeti. Kamati yetu ya Katiba na Sheria tulishindwa kukagua miradi ambayo iko nje ya Dar-es-Salaam kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Kamati imepewa milioni 20, milioni 10 kwa safari za ndani, milioni 10 kwa safari za nje. Kamati ina Wajumbe 25 sasa kama ni safari ya nje watakata tiketi ni shilingi ngapi hiyo? Milioni 10 si itakuwa imekwisha? Kwa hiyo, matokeo yake Kamati hii ilishindwa kabisa kwenda kujifunza jinsi Kamati nyingine za Katiba na Sheria zinavyofanya kazi zake nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye Kamati yetu tuliletewa Muswada wa Legal Aid ambao tumetoka kuupitisha ndani ya wiki hii. Ilipaswa sisi kama Kamati tusafiri twende nchi jirani, Kenya walishapitisha huo Muswada, South Africa walishapitisha huo Muswada au Uganda, tukajifundishe, je, tunahitaji kuboresha kitu gani kwenye ule Muswada?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hii ya Katiba na Sheria haikupata hiyo nafasi ya kwenda kujifunza kwa nchi za wenzetu wa jirani ile Miswada inasemaje. Matokeo yake tukaletewa huo Muswada, tukajadili kwenye Kamati yetu, tukawa tuna-struggle sisi wenyewe mpaka tukaweza kufanikisha kuleta huo Muswada humu Bungeni. Hilo naona ni tatizo na naomba kwenye bajeti ijayo Serikali ijaribu kufikiria na ijaribu kutuongezea bajeti na kuziongezea bajeti Kamati nyingine ili zisiwe zinapitisha vitu bila kuangalia nchi nyingine wanafanyaje, kwa sababu siku zote mtu unaangalia je, nyumba ya jirani wanafanyaje ili uweze kufananisha na kile kitu ambacho ninyi mmeandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona kuna hitilafu siyo vibaya mtu uka-copy kutoka kwa jirani yako au ukajifundisha kutoka kwa jirani yako. Kwa hiyo, naomba suala la Bajeti za Kamati Serikali itakapokuja na bajeti ya mwezi wa Julai ijaribu kufikiria kuongeza bajeti ya hizi Kamati zetu, hasa Kamati yetu ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine Kamati yetu ilishindwa kwenda kukagua maafa kule Kigoma wakati kile Kitengo cha Maafa kiko chini ya Kamati yetu ya Katiba na Sheria. Samahani siyo Kigoma ni Kagera! Kagera walivyopata maafa sisi Kamati ya Katiba na Sheria tulipaswa twende kule tukakague yale maafa yameathiri kiasi gani, lakini hatukuweza kwenda kwa sababu ya ufinyu wa bajeti wakati lile fungu la Kitengo cha Maafa, fungu lake liko kwenye Kamati yetu, lakini hatukuweza kwenda kule Kagera kukagua huo mradi kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Kwa hiyo, naomba suala hili kwa kweli Serikali mwezi wa Julai itufikirie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba Kamati ya Katiba na Sheria tunapoagiza maagizo, kwa mfano, tuliwaagiza NSSF watuletee mkataba wao walioingia na wale waliojenga zile nyumba za Kigamboni, zinaitwa Dege Eco Village, tuliagiza kwenye Kamati kwamba, watuletee ule mkataba kwa sababu NSSF huwa sera zao zinapitia kwenye Kamati yetu, tuliwahi kwenda kukagua zile nyumba pamoja na lile daraja la Kigamboni ilitushirikisha, lakini tulipoagiza kwenye Kamati tuletewe ule mkataba walioingia kati ya NSSF na lile shirika lililojenga hizo nyumba za Dege Eco Village, huo mkataba hatujaletewa mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashangaa Kamati na mimi nikiwa mmoja wa Wajumbe kwenye ile Kamati, kama Kamati inaagiza Mkataba kwa nini hao NSSF wasilete huo mkataba wakati sisi tulihitaji na nafikiri ni jukumu letu kwa sababu tunasimamia sera zao tuuone ule mkataba, lakini ule mkataba haukuweza kuletwa kwenye Kamati yetu. Kwa hiyo, naomba nalo hilo lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa maagizo, tulienda kukagua Ofisi ya Makamu wa Rais tukakuta lile jumba limejengwa kwa nusu ya kiwango. Tumeingia pale Ofisi ya Makamu wa Rais ina muda sijui wa mwezi mmoja, lakini tulikuta mipasuko, finishing ilikuwa chini ya grade, siyo standard! Tukaagiza kwamba tuletewe ripoti ya fedha zilizotumika kwenye hilo jengo na tukaagiza marekebisho yafanywe, lakini ripoti ile hatujaletewa mpaka leo! Ni mwaka mzima tangu tulivyopita kwenye Jengo la Makamu wa Rais. Tulishindwa kwenda kutembelea Jengo la Makamu wa Rais lililoko Zanzibar kwa ufinyu wa bajeti, lakini Jengo la Makamu wa Rais la hapa Dar-es-Salaam tulilitembelea na kuna makosa tuliyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo tulikuta jengo halina mlango wa kutokea unapotokea moto. Jengo limejengwa chini ya kiwango! Tulikuwa tumetoa hizo tuhuma na tukawaambia kwamba, watuletee wamefikia wapi, lakini hawakuwahi kuleta mpaka leo ni mwaka mzima. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba tunapotoa maagizo kama Kamati yatekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka kuongea kuhusu mambo ya mamlaka ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Nafikiri kila professional watu waheshimiane, mtu mwingine aheshimu professional ya mwenzie, kama ni Daktari aheshimike kama ni Mwalimu aheshimike. Kama ni Mkuu wa Wilaya afanye kazi zake za Ukuu wa Wilaya, lakini asimuingilie kwa mfano Daktari! Daktari ni professional, yuko professional, Mwalimu yuko professional, Injinia wa Mkoa yuko professional au wa Wilaya yuko professional, kwa nini aingiliwe katika utendaji wake wa kazi? Kila mtu aheshimu profession ya mwenzie. Tukiheshimiana hivyo kila mtu atatimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitawezekana kwamba, mtu anakuwa ni Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anaenda kutoa maagizo ya mambo ya Engineering wakati yeye siyo Engineer, anajuaje standards za engineering? Mtu ni Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anaenda kutoa maagizo ya Daktari, yeye hajasomea udaktari, hana profession ya udaktari! Anatoaje maagizo kama hayo? Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anaenda kutoa maagizo ya Afisa Kilimo, yeye hajasomea kilimo! Anajuaje mambo ya kilimo? Mkuu wa Mkoa siyo Mwalimu. Kila profession iheshimiwe! Mkuu wa Wilaya afanye kazi zake, Mkuu wa Mkoa afanye kazi zake tuheshimiane katika profession zetu ili tuweze kujenga hii nchi kwa sababu, usitoe maagizo ambayo hujasomea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hilo liweze kufikiriwa na watu waweze kuwajibika kwenye nafasi zao ili wasiogope kwa sababu, hili litazua utendaji mbaya wa kazi maana mtu atashindwa kutimiza wajibu wake kwa sababu atasema kwamba, nikifanya hivi Mkuu wa Wilaya atanifokea! Nikifanya hivi Mkuu wa Mkoa atanifokea! Matokeo yake ni yule mwananchi wa chini ambaye anahitaji zile huduma za Engineer au huduma za Daktari ndiye anayeathirika, Mkuu wa Wilaya hawezi kuathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niongelee suala la Halmashauri. Kwa mfano mdogo tu kule kwetu, ile Halmashauri ya Mpanda haina gari la kuzolea taka na hizi Ofisi za Wizara hii ya TAMISEMI imeziachia majukumu hayo Manispaa. Manispaa nyingine ni maskini siyo tajiri na hazina uwezo wa kununua hayo magari ya kuzolea taka, matokeo yake taka zinarundikana barabarani na kusababisha kipindupindu unasikia hakiishi(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo tu kule Kalema kuna kipindupindu na pale Mpanda taka zinaweza zikakaa wiki moja hazijazolewa kwa sababu hawana gari la taka na hawana uwezo.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nirekebishe jina siitwi Raphael Mbogo naitwa Taska Restituta Mbogo.
MWENYEKITI: Ahsante Restituta Mbogo.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nikushukuru kwanza wewe kwa kunipa nafasi hii kuchangia hoja hii ya Wizara ya Afya ambayo ni Wizara muhimu kwa sisi akina mama na ni Wizara muhimu kwa nchi yetu.

Napenda kwanza kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi yake ya hapa kazi. Ninasema hivi kwa sababu katika Mkoa wetu wa Katavi tulikuwa hatuna duka la dawa tangu labda niseme tangu Wilaya ile ianzishwe mwaka 1945.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata Mkoa hapa juzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea kule akatuahidi duka la dawa na ndani ya miezi sita duka la dawa la MSD lilikuwa limejengwa na tukaenda kulizindua, naipongeza sana Serikali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kazi nzuri, kwa sababu baada ya uzinduzi tuliweza kupata pia vitanda, hivyo naishukuru sana Serikali hii kwa kasi yake ya ufanyaji kazi maana yake ndani ya miezi sita duka la dawa lilijengwa. Hongera Serikali yote, hongera kwa Mawaziri wote na hongera sana kwa Mheshimiwa Rais wetu na tunakupongeza sana endelea na kazi na hekima zako unazozitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niende moja kwa moja kwenye hoja ya Wizara ya Afya. Ninampongeza Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, naomba nitoe ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sihoji uwezo wao wa Watendaji wanafanya kazi vizuri sana akiwepo mwenyewe Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, lakini naona Wizara hii ni kubwa, naona kama vile upande wa maendeleo ya jamii, wazee, unasahaulika. Naomba kutoa ushauri kwa Serikali iweze kuigawa Wizara hii, Wizara ya Afya ibaki peke yake, Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wazee itenganishwe na hii Wizara, huu ni ushauri tu nautoa maana Wizara ya Afya ina mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye dawa hospitalini Waziri na Naibu wake washughulikie, zahanati, vituo vya afya, hela za mgao kwenda kwenye Mikoa yote mpaka Wilaya, vifaatiba kuangalia japokuwa ndiyo tunasema viko TAMISEMI, lakini Waziri pia anatupia jicho, yote hayo yanamkabili Waziri wa Afya na Naibu wake, naona kama vile kazi inakuwa kubwa mno. Natoa ushauri tu kuomba Wizara ya Afya ingeachwa peke yake ili iweze kutoa huduma vizuri kwa sababu kila Mtanzania bila kuwa na afya njema sidhani kama kuna kitu ambacho mtu anaweza akafanya. Hata hapa tunakaa kwa sababu tuna afya, ukiwa na afya iliyotetereka sidhani kama utaingia humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niongelee sakata la vyeti fake. Ninavyoongea hapa kule Mkoani kwangu Katavi kuna Halmashauri Tano, ndani ya hizo Halmashauri tano wafanyakazi 60 wa Wizara ya Afya walikuwa na vyeti ambavyo vinasemekana kwamba havijakaa vizuri au ni vyeti fake. Sasa tuna uhaba wa wafanyakazi 60 ghafla kwenye Mkoa wetu wa Katavi, tunaomba replacement. Uajiri wafanyakazi kama wafanyakazi wapya madaktari pamoja na wauguzi, hili limewakumba madaktari pamoja na wauguzi. Mkoa mzima kupoteza wafanyakazi wa sekta ya afya 60 ni wengi mno, utaangalia mwenyewe jinsi gani vituo vya afya, zahanati na hospitali zetu zitakavyokosa huduma na jinsi gani wananchi wa Mkoa wa Katavi watakavyokosa huduma. Naomba ajira iharakishwe ya hawa madaktari, Serikali jinsi ambavyo imezungumzia suala la vyeti fake basi wakamilishe huo utaratibu na ajira mpya za wale madaktari pamoja na wauguzi wenye vyeti ambavyo ni genuine iweze kutangazwa mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala la Kituo cha Afya cha Mkoani Katavi. Mheshimiwa Waziri kile kituo cha afya ambacho mwaka jana tulisimama hapa tukaomba kirekebishwe na kifanyiwe ukarabati, napenda kushukuru Serikali kituo cha afya kimefanyiwa ukarabati kimekwisha, tatizo hakijafunguliwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho yake atuambie kile kituo cha afya cha Mkoa wa Katavi ambacho kimekwisha kitafunguliwa lini?

Naomba pia kile chuo cha afya kiweze pia ku-train wauguzi wasaidizi ili tuweze kuwa na ma-nurse wengi na hawa Medical Assistants wengi ambao watakuwa wamekuwa trained Mkoani Katavi, kwa sababu ukiangalia jiografia kule kwetu ni Mikoa ambayo iko pembezoni lakini kama mtu atakuja atasoma kule ile miaka miwili atazoea mazingira kiasi kwamba hata kama atapangiwa kufanya kazi katika Mkoa wa Katavi atakaa. Ukimtoa mtu Mikoa ya mbali ukamleta kule anaweza akaona jiografia ni mbaya na hiyo kazi yenyewe asiipende kwa hiyo naomba kile chuo pia kiweze kuwa-train wauguzi wasaidizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la ndoa za utotoni. Sheria zetu tulizojipangia wenyewe katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaweza ukasema kwa upande mwingine zinachangia ndoa za utotoni. Tunazo sheria ambazo zinakinzana, tunayo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo ibara ya kwanza inasema kwamba mtu yeyote ambaye yuko chini ya umri wa miaka 18 ni mtoto. Ibara ya kwanza hiyo ambayo ni ya Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inasomeka hivyo. Ukienda kwenye Sheria za Kimataifa ambazo tumeziridhia tunayo Sheria ya Kimataifa ya Mwanamke ambayo inatoa tafsiri ya umri wa mtoto na tunayo mikataba ambayo imeonesha umri wa mtoto ni miaka mingapi. Ukichukua zile sheria ambazo tumezisaini na tuliziridhia ambazo tunatakiwa tuzifuate zinakuja zinakinzana na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1970 ambayo inamruhusu mtoto wa kiume kuoa akiwa na miaka 18 na mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa unakuta kwamba kunakuwa na discrimination, ukishaweka ile tofauti ya age, moja kwa moja umeweka utofauti wa mtu mmoja kuwa supreme na mwingine kuwa chini yake kwa ajili ya jinsia. Kama unataka kuwaweka watoto wote kuwa sawa, unatakiwa ule umri usiweke ile tofauti kati ya mtoto wa kike na mtoto wa kiume. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia hoja hii. Kwanza nianze kwa kutoa pole nyingi sana kwa wananchi Mkoa wa Arusha, kwa Watanzania wote, kwa walimu wote wa shule ya Lucky Vincent, mmiliki wa shule, wazazi waliopoteza watoto wetu wapendwa, nawaombea Mungu awape ujasiri wa kukabiliana na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie Wizara hii kwa mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nilikuwa naomba kuelewa kwenye Halmashauri zetu kuna Afisa Michezo na Afisa Utamaduni. Sasa nilikuwa naomba kujua hawa watu huwa wanawajibika kwa nani? Mwajiri wao anakuwa ni Wizara ya Utamaduni au anakuwa ameajiriwa pale Halmashauri? Kazi zao zinakuwa ni zipi, kwa sababu ukiangalia kwenye michezo; michezo ndiyo hiyo imedorora mashuleni. Ukingalia pia kwenye utamaduni, utamaduni ni huo nao umedorora mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka miaka ya nyuma wakati sisi tunasoma, sisi tuliosoma zamani, kulikuwa na mashindano ya michezo. Unakuta zinakusanywa shule za primary za Wilaya hiyo zinashindanishwa na shule moja inaibuka inakuwa mshindi, inapewa zawadi ya kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye suala la utamaduni, kulikuwa na mashindano; shule za primary zinashindana ngoma za utamaduni na shule moja inaibuka mshindi wa utamaduni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika kuimba kulikuwa na mashindano. Kwenye utamaduni walikuwa wanaweka mashindano ya nyimbo, ngoma, wanaimba ngoma za makabila tofauti na nyimbo zinatungwa zenye maudhui ya nchi hii ambazo zingekuwa na mafundisho. Wakati ule sisi ilikuwa ni mambo ya siasa za ujamaa, kwa hiyo, wanaimba nyimbo za ujamaa ambayo pia zilisaidia kuwajenga watoto mashuleni na kutujenga sisi pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vitu kama hivyo sasa hivi sivioni. Kwa hiyo, huwa inaniwia vigumu, halafu unapoenda kwenye Wilaya unashindwa kujua kazi za Afisa Utamaduni na Afisa Michezo aliyeko Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, wengi mtakumbuka, michezo imeibuliwa kule mashuleni, mimi ninao mfano wa watu ambao waliiwakilisha nchi hii nje ya Tanzania na wakailetea medali. Mwinga Mwanjala ni mchezaji ambaye aliibuliwa toka primary school na akaenda akaiwakilisha nchi hii, akaleta medali. Nzaeli Kyomo aliibuliwa toka secondary school, akina Gania Mboma wote hao waliibuliwa toka mashuleni na wakaweza kuiletea medali nchi hii na wakailetea heshima nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo nilikuwa naomba na niungane na wenzangu waliotangulia, michezo irudishwe mashuleni. Wizara ya Elimu irudishe mashuleni michezo iwe kama kipindi, kama ambavyo zamani tulikuwa tuna vipindi vile vya michezo. Pia viwanja vya michezo vijengwe vingi kwenye mashule. Shule inapoanzishwa wahakikishe kwamba ina kiwanja cha michezo; aidha iwe ni Shule ya secondary, primary kwa Shule za binafsi au Serikali viwanja vya michezo viwepo pale; iwe ni condition moja ya kuanzisha hiyo shule ili kuibua hivyo vipaji. Kwa sababu naona wachangiaji mnasema kwamba hatuna wawakilishi, mnaongea mambo ya mpira ya miguu kwamba Tanzania inakosa kwenda kucheza michezo ya kuiwakilisha nchi labda kwenye Kombe la Dunia au Kombe la Afrika, lakini ni kwa sababu tumeshindwa kuibua vipaji vya watoto ambavyo vinapatikana kwenye shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye utamaduni. Naomba nizungumzie suala la utamaduni; katika kitu ambacho mtu unaweza ukapoteza heshima yako ni kukosa utamaduni wa nchi yako au kabila lako.

Mheshimjiwa Spika, naomba hizi nyumba za makumbusho ambazo zimejengwa kule Dar es Salaam na moja iko kule Arusha, labda na Mwanza wanayo, naomba Wizara hii izingatie, hizi nyumba za makumbusho zijengwe kila Mkoa. Ninaamini kwamba kila Mkoa una utamaduni wake na kila Mkoa una makabila ambayo yalikuwepo kwenye huo Mkoa tangu wakati huo, ambao wana mila zao na vitu vyao vya zamani ambavyo walivitumia. Hivyo vitu vingeweza kuhifadhiwa kwenye nyumba za makumbusho za kila Mkoa ili iwe faida kwa kizazi kilichopo na kizazi kinachokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kama sisi tutakuwa tumepotea, lakini pale mkoani watoto wataweza kwenda kutembelea kwenye zile nyumba za makumbusho na kuona vitu ambayo vilitumika zamani na wazazi wao. Kwa sababu mimi naamini kwamba mkataa kwao ni mtumwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Uingereza wameweza ku- maintain vitu vyao vya asili na sehemu zao za asili ambazo zilikuwa zinatumika tangu enzi za King George. Unakuta yale maeneo yao ya asili yapo mpaka leo yanatumika kama makumbusho na wanakwenda ku-visit.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hayo maeneo, kila Mkoa utenge sehemu ambayo watajenga nyumba ya makumbusho ambayo watahifadhi vitu vya makabila ya Mkoa huo kwenye nyumba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la mchaka mchaka. Nilikuwa naomba Wizara ya Elimu ishirikiane na Wizara ya Michezo mchaka mchaka urudi mashuleni. Sisi wakati tunasoma, tulikuwa tunakimbia mchaka mchaka asubuhi. Ni kiasi kwamba watoto wanapofika pale shuleni kabla hawajaingia darasani, wakimbie mchaka mchaka, wazunguke hata eneo la shule ili wawe wakakamavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoona, Mheshimiwa Makamu wa Rais amesema kwamba watu wafanye mazoezi. Sasa kwa nini hayo mazoezi yasianzie kwenye shule zetu? Maana yake tunahimiza watu wazima wafanye mazoezi kama anavyosema Makamu wa Rais, basi na pia na mashuleni tuwahimize watoto wakimbie kabla hawajaingia madarasani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nilikuwa naomba kuwe na paredi mashuleni, watoto wafundishwe kuimba Wimbo wa Taifa. Ni aibu unamkuta mtoto anamaliza Darasa la Saba hajui kuimba Wimbo wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, sisi zamani tulikuwa tunaimba Wimbo wa Taifa kabla hatujaingia darasani. Siku hizi sijui kama vitu hivyo vinatekelezwa. Ingewekwa tu kama policy kwamba watoto kabla hawajaingia darasani, waimbe Wimbo wa Taifa. Hii ni kwa faida yao, pia ni kwa faida ya nchi yetu. Sisi zamani mbona tulikuwa tunaimba Wimbo wa Taifa kabla hatujaingia darasani. Kuwe na paredi na mchaka mchaka, nilikuwa naomba nisisitizie hilo kwenye mashule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itawapa ukakamavu na pia itawajenga kutokufikiria vitu vingine, kwa sababu mtu anakuwa amekimbia, mwili umechangamka, anapofika mle darasani ana-concetrate na shule, Ndivyo sisi tulivyolelewa. Vitu ambavyo tulilelewa ambavyo vilitusaidia sisi tunapaswa tuvipeleke kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni kuhusu wasanii hizi kazi za wasanii waweze kupata haki zao, lakini pia usajili wa kazi za wasanii nilikuwa naomba labda wangeweka mpaka mikoani. Kwa mfano, kule kwetu Katavi, mtu atatokaje Katavi aende mpaka Dar es Salaam kwenda kusajili hiyo kazi yake? Kwanza kuna nauli, halafu kuna hizo kodi ambazo atatumia, pesa zenyewe za usajili nimesikia hapa mnachangia, sio mtalaam sana kwenye mambo ya usanii, lakini mnasema sijui shilingi 300,000 kodi sijui ya nini.

Mheshimiwa Spika, kwa kijana ambaye anaanza maisha, hiyo inakuwa ni hela ngumu sana kupata ili aweze kusajili kazi yake. Kwa hiyo, naomba ili kuwawekea unafuu, hizo ofisi za usajili za kazi za wasanii ziweze kupelekwa mpaka mikoani ili na wananchi hata na wale wasanii wangu wa kule Katavi waweze kusajili kazi zao kwa wepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nilikuwa naomba vitu vya zamani virudishwe. Kwa mfano, kulikuwa na zile sikukuu ambapo ilikuwa zinaweza kukutana ngoma za Mkoa huo zikashindanishwa na zikapewa zawadi. Zawadi siyo lazima iwe kubwa, lakini hii inatufanya tusipoteze utamaduni. Ndiyo maana unakuta mara nyingi mnawalaumu vijana wa sasa hivi wakitunga miziki sijui wanaimba miziki ya hip pop na nini, ile miziki wanayoiga kule ilitumiwa zamani na Waafrika weusi ambao walikuwa wanadai uhuru, ndiyo ikaja hii mambo watoto wakiimba wana-rap. Sisi tunayo miziki yetu ya asili ambayo inatutambulisha sisi kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, napata utata sasa hivi ninapoona kwamba hivi Mtanzania anaweza akasimama hapa akasema muziki wake wa asili ni upi? Kwa sababu naona miziki yote imechanganywa na utamaduni… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Utamaduni.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nichangie hoja zilizoletwa na Kamati yangu ya Katiba na Sheria na Sheria Ndogo. Naomba nianze na Kamati yangu ya Katiba na Sheria naomba nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa jinsi alivyoshirikiana na sisi kwenye Kamati yetu na kuweza kutuwezesha sisi kufanya kazi yetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila ninayo maoni machache ambayo ningeomba kuyachangia. Nilikuwa naomba Kitengo cha Maafa kilichoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Serikali ijaribu kukiongezea fungu ili kiweze kuwafundisha wataalam mbalimbali wa maafa mbalimbali kama vile kuogelea (divers). Tunayo mifano mingi sipendi kukumbushia mambo ya zamani lakini tuliwahi kupata matatizo huko nyuma meli ya MV Bukoba ilipozama ilikaa chini kule muda kama wa wiki moja nafikiri kama tungekuwa na divers wazuri wale watu wangeweza kuokolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba kitengo hiki kiongezewe nguvu na ikiwezekana zile sehemu zenye maziwa kama vile Ziwa Victoria, Nyasa, Tanganyika hao divers wawe based kule na pia kingeweza kufundisha wataalam wa zimamoto. Hilo ndio lilikuwa ni ombi langu kwenye Kitengo cha Maafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda niende ukurasa wa 14 wa wasilisho la Kamati ya Katiba na Sheria. Niipongeze Bodi mpya ya NSSF kwanza kwa kulichukulia suala na kuwasimamisha kazi wale wote waliofanya ubadhirifu pale NSSF. Lakini sasa niombe hatua zaidi zichukuliwe kwa sababu kumsimamisha mtu kazi tu haitoshi na kwa sababu pia tunayo Mahakama ya Wahujumu Uchumi, Mahakama ya Mafisadi ambayo imeanzishwa lakini haina kesi, itakuwa ni vizuri kama watu hawa wakapelekwa kwenye hiyo mahakama ili iweze kujulikana kama kwamba walifanya huo ubadhirifu au hawakufanya. Na ukiangalia Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipengele namba 107 kinatuambia kwamba mahakama ndio mamlaka ya mwisho ya utoaji haki. Kwa hiyo, kwa kuwapeleka mahakamani haki itatendeka itajulikana kama walifanya ubadhirifu au hawakufanya huo ubadhirifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuongelea suala la The Law Reform Commission ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kamishna hii ipo lakini cha kushangaza zipo sheria nyingi nyingi ambazo zina matatizo hazibadilishwi kwa mfano Sheria ya Traffic, hii sheria bado ina faini za miaka ya nyuma sana ambayo iliachwa na wakoloni wetu watawala wetu. Kwa mfano, sheria hiyo ya traffic unaweza ukakuta mtu anagonga gari lakini anapokwenda mahakamani pale akikiri kosa faini ya mwisho ni shilingi 50,000.

Mimi nadhani hii kamisheni ingefanya kazi yake ili iweze kuzichukua zile sheria zote ambazo zina matatizo iweze kuzirekebisha kwa sababu inawezekana wakati wanazitunga zilikuwa zinafaa wakati huo kuwa na faini ya aina hiyo lakini sasa miaka mingi ilikwishapita na nchi zimeendelea na mambo yamekuja mengi. Sasa huwezi ukakaa na faini ambayo imetungwa toka mwaka 1963 bado unatoza faini hiyo hiyo. Nilikuwa naomba hiyo sheria iweze kurekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine hii kamisheni nilikuwa naomba ijaribu kurekebisha sheria…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tizeba, Waziri wa Kilimo na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendeleza kilimo nchini Tanzania. Niende moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi ni mkoa ambao unazalisha mazao ya chakula na biashara. Sisi Katavi ni miongoni mwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayolisha Tanzania, the big six ambayo ni Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Ruvuma. Katavi hatuna njaa, tunalima mazao ya kilimo cha biashara na chakula. Mazao hayo ni mahindi, mpunga, alizeti, karanga, pamba, korosho na nyuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi tumekuwa tukilima zao la biashara la tumbaku kwa muda mrefu sana, ni zao linalotegemewa kwa biashara, lakini zao hilo limekuwa likiwaumiza sana wakulima, afya zao zinaharibika maana tumbaku inashuruba sana kuanzia ulimaji wake, kukausha, mpaka kuuza, kote kuna kazi ya kutumia nguvu. Mkulima anapokuwa amevuna anakuwa ameumia sana. Pia katika uuzaji wa zao la tumbaku kuna shida maana kuna utaratibu wa kupangiwa kilo za tumbaku za kuuza na kila mwaka kilo wanazopangiwa kuuza zinapungua. Hii inawapa shida wakulima, wanapata hasara maana wanachopangiwa kinapungua kila mwaka hivyo basi lipo hitaji la kuongeza zao la biashara Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilo za tumbaku walizopewa ni kama ifuatavyo:-

(i) Season 2014/2015 walipewa kilo 11,910,459.

(ii) Season 2015/2016 walipewa kilo 8,445,786.

(iii) Season 2016/2017 walipewa kilo 12,099,742. Tumbaku iliyozidi imevunwa ni kilo 2,711,709.

(iv) Season 2017/2018 ambayo inakaribia kununuliwa, makadirio ni kilo 7,452,562.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Mkoa wa Katavi ni kama ifuatavyo:-

(i) Tunaomba mtuongezee Maafisa Ugani kwa sababu Mkoa wa Katavi asilimia 80 ya mkoa mzima hakuna maafisa hawa. Hivyo, tunaomba tumepewa Maafisa Ugani kila kijiji.

(ii) Maafisa Ugani waliopo ambao ni wachache wapewe mafunzo kuhusu mazao mapya ya pamba na korosho ambayo yameletwa Mkoani Katavi. Kwa sasa hivi Maafisa Ugani waliopo hawana ujuzi wa zao la pamba na korosho.

(iii) Mfumo wa soko wa zao la pamba haujawekwa vizuri maana wakulima wanatakiwa wawauzie vyama vya ushirika. Pia wakulima wa Katavi hawana uelewa wa zao hili la pamba.

(iv) Serikali iruhusu mapema kuuza mahindi nje, sio wasubiri mpaka mahindi yaharibike.

(v) Mkoa wa Katavi tunaomba mbegu za korosho kwa wingi ili wakulima waweze kulima kwa wingi.

(vi) Tunaomba Bodi ya Korosho ituletee mbegu ya korosho Mkoani Katavi.

(vii) Miundombinu ya biashara ni mibovu inafanya wafanyabiashara wanunue mazao kwa wakulima kwa bei ndogo sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na rehema kwa kutupa uhai, sisi wote hapa Bungeni ni wazima na tunasikiliza Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda kumpongeza Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa kazi nzuri wanayoifanya. Napenda kuwapongeza Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kutumikia Taifa hili. Napenda kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya za kuwanyanyua wanyonge na kuleta heshima ya kazi ndani ya Taifa hili. Zamani kazi ya Serikali ilikuwa inadharaulika na Manesi hawa walikuwa na lugha mbaya lakini sasa hivi wana lugha nzuri, Mheshimiwa John Pombe Magufuli usi-change gear ongeza gear nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda niende kwenye Mkoa wangu wa Katavi, napenda nishukuru kwa pesa tulizopata kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mkoa, naomba muuangalie kwa jicho la pekee mkoa huu kwa sababu mkoa huu ni mpya, naomba mtuongezee pesa kwa sababu sisi ndiyo tunaanza kujenga hospitali. Mkoa huo ni mpya, miundombinu ni mibovu, kwa hiyo, watu wote wa Mkoa wa Katavi wanasubiri Hospitali ya Mkoa iweze kuisha ili iweze kuwasaidia maana yake Hospitali ya Rufaa iko mbali Mkoa wa Mbeya ni kilometa 500 kutoka Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo hitaji lingine la Mkoa wa Katavi tunaomba gari la chanjo kwa Manispaa ya Mpanda. Manispaa ya Mpanda haina gari la chanjo, Halmashauri zingine zipo, kwa hiyo, inawafanya watoto pale wadogo wale wanaozaliwa kwenye Manispaa ya Mpanda waweze kukosa huduma ya chanjo. Namuomba Mheshimiwa Waziri utupatie gari hilo la chanjo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine ni kile kituo cha afya ambacho kilikuwa kinafanyiwa marekebisho pale kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kiweze kufunguliwa, ninazo taarifa kwamba Mheshimiwa Ndugulile ulikwenda Kakuni ukakagua ile shule ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo amejenga pale Kakuni, ametupatia sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi ifunguliwe iwe kituo cha afya.

Nimuombe basi Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa sababu ulikwenda pale Kakuni na ukaiona hiyo shule, ufanye uharaka wa kukamilisha hili jambo ili kituo hicho cha afya kiweze kufunguliwa na kile kituo cha afya cha zamani kiweze kutumika kwa akina mama wa Mpanda pamoja na watoto kwa maana ya kuwa kliniki ya watoto. Naomba hilo Mheshimiwa Ndugulile kwa sababu jambo hili unalifahamu na Kakuni ulifika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu kwa kutupatia hiyo shule ambayo alikuwa ameijenga kijijini kwake, ahsante sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine la wananchi wa Mkoa wa Katavi kuhusu afya, tunaomba ile Hospitali ya Inyonga bado haijapewa hati ya kuwa Hospitali ya Wilaya, tunaomba ipewe hati ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wa Mlele.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine kwa sababu dakika ni tano naenda u upesi, ombi lingine la wananchi wa Mkoa wa Katavi wazee wa Mkoa wa Katavi wanaomba sana wapewe bima ya afya. Sasa hivi wale wazee huwa wanapigwa picha wanapewa vitambulisho wanakwenda kutibiwa kwenye dirisha la wazee lakini wanapokosa zile dawa pale hospitali hawawezi kuzipata zile dawa kwa sababu hawana bima ya afya. Nimeangalia pale Manispaa ya Mpanda mmewapatia shilingi milioni saba, kwa ajili ya wazee wa Manispaa ya Mpanda na wao waliomba shilingi milioni 17, lakini mimi nasemea wazee wote wa Mkoa wa Katavi muwaangalie kwa jicho la pekee. Mkoa ni mpya ndiyo unaanza, una mahitaji mengi na wale wazee wa kule hawajafaidika na hii bima ya afya, nawaombea wazee wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuiomba Wizara ya Afya ninaomba Mkoa wa Katavi mtupatie wadau wa afya. Tunaye mdau mmoja anaitwa Water Rid yeye ndio yuko Mkoa wa Katavi anatusaidia saidia tunamshukuru sana, tunaomba mnapopata wadau wa afya wengine huko Wizara ya Afya muwalete Mkoani kwetu Katavi ili waweze kutusaidia kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya pia nizungumze suala dogo kuhusu usafi ambalo limezungumziwa pia na mwenzangu aliyepita Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja hundred percent.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nichangie Wizara ya Maji. Kwanza kabisa napenda kumpa pongezi Waziri wa Maji, Mheshimiwa Isack Kamwelwe kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwenye Wizara hii. Pia napenda nimpongeze Naibu wake, Mheshimiwa Aweso, wote kwa pamoja mnajitahidi kufanya kazi ya kutatua matatizo ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niungane na Wabunge wenzangu waliochangia kuhusu kuongeza shilingi 50 kwenye petroli na dizeli ili iweze kusaidia bajeti ya maji kwa kupata chanzo kikubwa cha kuendeleza miradi ya maji. Naungana na Wabunge wenzangu waliounga mkono hoja ya kuongeza shilingi 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Maji. Bajeti ya Wizara ya hii ni ndogo ukilinganisha na mahitaji ya maji nchini Tanzania na mikoani kote. Kila mahali unapoenda iwe ni vijijini, wilayani na city center ni kilio cha maji. Niiombe Serikali iongeze bajeti ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naenda moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Mkoani kwangu Katavi, Wilaya ya Mpanda tunalo Bwawa linaloitwa Milala. Bwawa hili limechimbwa miaka mingi tangu enzi za ukoloni, enzi za Mpeluki kwa wale wanaotoka Katavi wanafahamu lilikuwepo toka kabla ya uhuru. Bwawa hili lilikuwa linatumika ku-supply maji pale Mpanda Mjini kwa matumizi ya wananchi wote wa Manispaa ya Mpanda. Sasa hivi bwawa hilo haliwezi kutumika tena kwa sababu lina viboko wengi wamezaliana pale, wanakula mazao ya wananchi, mipunga, mahindi, wanachafua maji kiasi kwamba yale maji ya bwawa hilo hayawezi kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara ya Maji na Umwagiliaji ishirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii iwatoe hawa viboko ili yale maji yaweze kutumika. Manispaa ya Mpanda, kata nyingi hazina maji, Kata za Mpanda Hoteli, Ilembo, Magamba na Shanwe, zote hizo hazina maji. Kwa kusafisha haya maji yaliyoko kwenye Bwawa la Milala litafanya kata hizi ziweze kupata maji. Nimeshawahi kupeleka hili swali ili lije hapa Bungeni niliulize, lakini nashangaa limechukua miaka miwili halijaletwa hapa kuhusu kuhamishwa viboko hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukichukulia kwamba hilo bwawa liko mjini pale Mpanda, zamani lilikuwa ni nje ya mji lakini sasa hivi limezungukwa. Kwa hiyo, kuwa na viboko ni hatari na kuna shule ya sekondari ya Mwangaza iko karibu na hilo bwawa, watoto wa shule wanakwenda pale kuchota maji na viboko wenyewe huwa wanatembea kutoka kwenye bwawa hilo wanakuja mpaka Mpanda Mjini. Niiombe sana Serikali na Waziri Mheshimiwa Kamwelwe iweze kututatulia hilo tatizo la viboko Mpanda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala la viboko, niende moja kwa moja kwenye suala la maji ya visima. Kwanza Mpanda tunashukuru kwa visima vya maji lakini niombe sana vile visima ambavyo vinatumia mkono muangalie uwezekano wa kuweka solar ili wale akina mama wa vijijini na hasa wazee waweze kuchota maji yale. Muweke pump inayotumia umeme na tape ili akina mama wale waweze kuchota maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, visima vingi vimechimbwa kule lakini havijakwisha na vingi ni vya ku-pump na akina mama vijijini ambao hawana nguvu wanashindwa ku-pump yale maji. Mnaweza mkatumia umeme wa solar kwa sababu umeme wa REA haujapita kwenye vijiji vyote vya Mpanda na ukizingatia kwamba Mkoani kwetu Katavi hakuna umeme wa gridi. Niombe basi uweze kutumia umeme wa solar ili akina mama wa Mkoa wa Katavi waweze kufaidika na maji haya ya visima ambavyo vinaendelea kuchimbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napende kuzungumzia miradi iliyoko Mkoani Katavi; tunao mradi wa Ikorongo II ambao utaleta maji kwenye vijiji vya Magamba. Nafahamu Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba lipo tank la Mwanamsenga kule Ilembo ambalo halifanyi kazi limechoka. Niombe likarabatiwe ili vijiji vile vya Magamba viweze kufaidika na maji hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba vile visima vinajengwa kule Mkoani kwetu Katavi ni temporary. Nimwombe Mheshimiwa aharakishe kuleta mradi mkubwa Mkoani Katavi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika ili yaweze kusambazwa Mkoa mzima wa Katavi. Maji ya visima ni temporary measure, utakapoletwa mradi mkubwa wa kutoka Ziwa Tanganyika utaweza ku-supply vijiji vingi vya Mkoa wa Katavi na Waziri anafahamu miundombinu ya mkoa wetu si rafiki. Kwa kupata maji haya inaweza ikawarahisishia akina mama shughuli nyingine za biashara ambazo wanaweza wakafanya kutokana na haya maji yatakayotoka Ziwa Tanganyika. Maji haya pia yataweza kusaidia mikoa ya jirani kama Mkoa wa Rukwa, mkoa wetu wa zamani ambao tulikuwa pamoja, haya maji yanaweza yakafika pale kwa kupitia Jimbo la Kavuu mpaka Sumbawanga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la umwagiliaji. Kule mkoani kwetu Katavi miradi ya umwagiliaji iko nyuma sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri miradi ambayo ilikuwa imeanzishwa Mkoani kwetu Katavi ifuatiliwe ili iweze kuendelea. Miradi ilianzishwa lakini mimi kama mimi sijaiona ile miradi kwamba imekwisha na hatuelewi ilifikia wapi na taarifa kama vile Wabunge wengine wamekuwa wanazungumza inatakiwa ieleweke ile miradi huwa inakuwa chini ya nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa umwagiliaji Kata ya Ugala lakini jinsi ulivyoisha sielewi uliishaje na sielewi ulikuwa chini ya usimamizi wa nani na maelezo yake hayaeleweki. Niiombe Wizara ya Maji ijaribu sana kuwa inafuatilia kwa ukaribu miradi yote ya maji ambayo inaanzishwa humu nchini ili kuona kwamba mradi huu umegharimu shilingi ngapi na zimebakia shilingi ngapi na wamelipwa shilingi ngapi. Kama mradi umetolewa pesa na haujakamilika basi wale watu wanaohusika na hiyo miradi waweze kuwajibika. Tunaona tu kwenye makaratasi kwamba kuna mradi huu wa maji lakini miradi inakuwa haijaisha na pesa hazijulikani zimekwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie suala hili la maji. Napenda sana kumshukuru Rais kwa hatua aliyoichukua jana pale Morogoro kumpigia simu Katibu Mkuu wa Maji lakini nafikiri hili suala lilikuwa ndani ya Waziri mwenyewe wa Maji na Naibu wake kufuatilia ile miradi ya maji. Basi niombe wawe wanaifuatilia kwa karibu ili suala la maji lisilete tatizo sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu maji taka kwenye Mkoa wetu wa Katavi. Miundombinu ya maji taka ya Mkoa wa Katavi bado, nimwombe Wazir Kitengo cha Majitaka kiweze kufuatiliwa kwa sababu ule mkoa ni mpya lakini suala la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ametujalia afya njema na uhai tuko hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze kwanza Kamati ya Sheria Ndogo, ambayo ni Kamati yangu kwa kazi nzuri inayoifanya chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Mtemi Chenge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wajumbe wa Kamati hii kwa sababu moja Kamati ya Sheria Ndogo mtu mwingine/mwananchi au Mbunge anaweza akasema kwamba Kamati ya Sheria Ndogo ni ndogo. Lakini niwaambie wananchi wa Tanzania pamoja na Wabunge mliomo humu ndani, Kamati ya Sheria Ndogo siyo ndogo kwa namna hiyo, kwanza ilipaswa iitwe Kamati ya Sheria Kubwa kwa sababu Kamati hiyo inapitia kanuni zote za Halmashauri zote nchini ambazo zinakwenda kumuathiri mwananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maana kwamba kanuni zote zinazotungwa na Halmashauri nchini Tanzania zinapita kwenye Kamati ya Sheria Ndogo na kanuni hizo zinakwenda kumuathiri mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, unaweza ukaenda miji mingine unakuta Halmashauri imetunga sheria kwamba ukitupa hata gamba la big G chini unalipa shilingi 50,000; ni nani anaathirika, si mwananchi wa kawaida? Ndiyo maana nikasema hizi kanuni zinamuathiri na zinatumika na mwananchi wa kawaida, anaishi nazo kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda nichangie mawili/matatu kuhusu kanuni ambazi zinaletwa kwenye Kamati yetu. Kanuni zinaletwa kwenye Kamati yetu wakati ambapo zinakuwa zimeshakuwa gazetted kwenye Gazeti la Serikali na zinakuwa zimeshaanza kutumika na wananchi moja kwa moja wanakuwa wameshaathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zinapokuja pia kurekebishwa, tunapokuja kukaa sisi pale kwenye Kamati tunazirekebisha, zinapokwenda tena kuchapwa na kwenda kutumika tena lakini utakuta damage inakuwa ni kubwa mwananchi wa kawaida anakuwa ameshakuwa damaged.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyochangia wachangiaji waliopita, niombe tu utaratibu utumike kwamba inapotungwa sheria, zile kanuni zinapotungwa zije kwanza kwenye Kamati ya Sheria Ndogo tuzipitie, tuzirekebishe kabla hazijakwenda kuwa gazetted kwenye Gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao ninapenda kuutoa ambao naona kwamba kanuni na sheria ndogo zinamuathiri mwananchi wa kawaida, ni matamko ya viongozi. Kwa mfano tamko la Waziri, tamko la Mkuu wa Mkoa, tamko la Mkuu wa Wilaya, moja kwa moja linamuathiri mwananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Mkuu wa Wilaya anaweza akatamka kwamba kila Jumamosi ni siku ya usafi maduka yasifunguliwe mpaka itakapofika saa nne asubuhi, anayeathirika hapa ni mwananchi wa kawaida. Kwa maana hiyo ni kwamba kwa mfano mwananchi akifungua lile duka au hoteli yake kabla ya ile saa nne asubuhi, atalipa faini labda ya shilingi 500,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi niombe tu yale matamko tunapoyatamka sisi viongozi, awe ni Waziri, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, tuyaangalie yasiwe na athari kwa mwananchi wa chini ambaye anakwenda kuishi na yale matamko yetu kwa maisha yake ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutoa pendekezo lingine kwa Serikali, niombe hizo kanuni ziwe zimepita kwenye Kamati ya Sheria Ndogo tuzirekebishe, lakini pia niombe wale watendaji wanapotunga zile kanuni ambazo zinakwenda kutumika kwa wananchi waziangalie zile kanuni ziwe zinaendana na sheria mama. Kwa mfano kanuni haiwezi ikazidi sheria mama, zile kanuni zinatakiwa ziwe chini ya sheria mama au zifuate ile sheria mama inasemaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotunga kanuni ambayo inakuwa ni kinyume na ile sheria mama ina maana unakwenda nje ya ile sheria, ina maana wewe hapo unatunga sheria nyingine. Kwa hiyo, basi niombe tu wale watendaji wa Serikali wawe wanazisoma vizuri zile sheria na watunge kanuni ambazo zinaendana na ile sheria mama iliyopo ambayo imewafanya watunge kanuni hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulitoa kama ombi, Halmashauri zetu nchini Tanzania zinapotunga zile sheria ndogo zijaribu kuzichapa na kuweka kwenye notice board ili wananchi wanapopita waangalie kwamba katika mji wetu kuna sheria fulani ambayo tunatakiwa tusiifuate. Ukitunga kanuni ukazikalia ofisini ukaweka kwenye draw hizo kanuni zinakuwa hazina faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tu niseme unaweza ukawa umetunga kanuni kwamba parking eneo hili hairuhusiwi, lakini hujaweka notice board na hujaweka kwenye mbao za matangazo kwamba hilo eneo halitakiwi mtu ku-park gari, mtu anapokuja ku-park unampiga faini ina maana hapo inakuwa si sahihi. Niombe Halmashauri kanuni zao ziwe zinawekwa kwenye mbao za matangazo na pia matamko ya Mawaziri yawe na limit, kwa mfano akitoa tamko liwe na duration period kama ni tamko la mwezi mmoja au mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwaombe sisi Wabunge tujaribu kununua yale magazeti yanayokuwa gazetted, zile kanuni zinapotolewa kwenye Gazeti la Serikali sisi Wabunge tunatakiwa tununue tuzisome na tukawaeleze wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja na mambo yote yaliyoandikwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia kwa kutujalia uhai mpaka leo tumeweza kuwa humu ndani ya Bunge tunachangia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia napenda kuwaambia Watanzania wote kwamba tuilinde amani tuliyonayo na tuilinde kwa bidii kwa sababu amani ikipotea haina cha Mkristu, Mpagani, Muislam wala mtu wa aina yoyote, wote tutazama kwenye hiyo bahari. Amani ikipotea ina maana Watanzania wote tutazama kwenye hiyo bahari. Naomba Watanzania wasisikilize maneno, waendelee kuilinda amani tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kuchangia mjadala ulio mbele yetu. Napenda kumpongeza kwanza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Napenda vile vile kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote kwa nafasi zao tofauti na Wizara zao tofauti kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mwigulu na Naibu wake Mheshimiwa Masauni kwa kazi nzuri wanayoifanya. Napenda pia kupongeza Jeshi la Polisi kwa kulinda raia na mali zao au zetu kwa ujumla. Napenda vile vile kulipongeza Jeshi la Magereza kwa kuwalea wafungwa Magerezani na kuwafundisha tabia njema wanapotoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kulinda mipaka yetu ya Tanzania na kulinda wahamiaji wanaoingia ndani ya nchi yetu. Pia napenda kupongeza Jeshi la Zimamoto kwa kusaidia maafa ya moto yanapotokea nchini mwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niende moja kwa moja kwenye kuchambua hoja moja moja za Idara hii. Nianze na Idara ya Uhamiaji. Naomba Idara ya Uhamiaji ifanye kazi kwa weledi. Ihakikishe nchi yetu ya Tanzania haiingiliwi na wahamiaji haramu, iwadhibiti wahamiaji haramu wote waaoingia ndani ya nchi hii. Ihakikishe nchi yetu ya Tanzania siyo kisiwa cha kupokea maharamia na Alkaida wanaotoka nchi nyingine. Ihakikishe nchi yetu ya Tanzania siyo kisiwa cha kupokea dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, Idara ya Uhamiaji wafanye kazi kwa weledi kwa kuangalia mipaka yote na nawaomba wasifanye kazi kwa computer, waende field. Wasifanye kazi kwa kuingia ofisini na kucheki computer unaona kwamba kuna usalama. Waende field wakakague mipaka yetu. Wachukue ramani ya Tanzania na waangalie mipaka ya Tanzania yote imekaaje? Waitembelee kwa kuiona visible siyo kwa kukaa kuiangalia kwenye computer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mkurugenzi wa Uhamiaji kwa sababu ni mama tumeona mabadiliko anayoyafanya, atendee haki kiti chake; atembelee mipaka ya nchi yake ya Tanzania aijue, asifanye kazi kwa computer pamoja na timu yake yote ili nchi yetu iweze kuendelea kuwa na amani hii Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, haiingii akilini; juzi juzi hapa kuna wananchi walishikwa pale Dar es Salaam wako kwenye nyumba, ina maana hawa Immigration na Polisi kulikuwa na uzembe fulani ndiyo maana hawa watu waliweza kupenyeza mpaka kuwa kwenye nyumba ya mtu, walishikwa wakiwa wanagombania chakula, ndiyo maana wakafahamika kwamba wako pale, ina maana hapa Jeshi la Polisi na Uhamiaji halikufanya kazi yake vizuri. Kwa hiyo, haiingii akilini kuona wahamiaji haramu wanashikwa Dar es Salaam. Wamepitaje Tanga, wamepitaje Moshi mpaka wanakwenda kufika Dar es Salaam? Naomba warekebishe hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nichangie suala la Polisi. Polisi wanafanya kazi yao vizuri, lakini naomba wajirekebishe wawe rafiki na raia. Naomba nichangie hasa upande wa traffic. Traffic wamekuwa wakiwa-harass sana hawa vijana wa bodaboda kiasi kwamba wanawakimbia mpaka wanaenda sehemu nyingine na kuweza kusababisha ajali. Vijana wale wanatafuta maisha, kwa hiyo, wanahitaji tu kupewa semina ili waweze kufanya kazi zao vizuri za bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kuhusu traffic, unaposhika gari njiani, mimi mwenyewe nimewahi kukamatwa, tumelipa fine ya Sh.30,000/= lakini hatukupewa receipt, tumepewa notification. Sasa tunajuaje hiyo hela kama imefika Wizara ya Mambo ya Ndani? Naomba Mheshimiwa Mwigulu wale traffic ambao wanakamata magari njiani, wapewe mashine wanapokamata magari watoe receipt. Wasitoe ile karatasi ya notification. Notification siyo receipt. Unapodai receipt wanakwambia kwamba receipts utaipata mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikamatwa hapa kutoka Chemba tukaambiwa tutakuta receipt Chemba, tumefika pale Chemba wala gari la Polisi lilikuwa halipo. Kama vitendea kazi hamna, naomba Mheshimiwa Mwigulu hawa traffic wasikamate magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na leo tuko hapa Bungeni tunachangia hoja za Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, napenda kutoa pongezi kwa wafuatao. Pongezi za kwanza napenda ziende kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuwatumikia Watanzania na kwa moyo wake thabiti ambao umeonesha kubadilisha maisha ya Watanzania na dunia imeona na imekubali kwamba sasa tunaye Rais ambaye atakwenda kubadilisha nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Prof. Ndalichako na Makamu wake Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi nzuri ya kubadilisha elimu yetu nchini kwa kufuatilia mambo mengi ambayo yalikuwa hayaendi vizuri katika Wizara ya Elimu. Nawapongeza sana na ninawaombea Mungu mwendelee kufanya kazi kwa ajili ya maslahi ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kuchangia mawili, matatu kuhusu Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa, Wizara hii ya Elimu imekuwa ikijitahidi sana katika kuboresha elimu, lakini lipo tatizo kubwa ambalo limekuwa tunaenda nalo sasa kwa muda wa miaka mingi. Tatizo hilo ni tatizo la wanafunzi kumaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika. Wengine kwa sababu siku hizi ni multiple choice, wanafikia kwenda sekondari lakini hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili limekuwa ni sugu, linahitaji tulifanyie upembuzi na labda iundwe Tume ambayo itashughulikia tatizo hili. Kama mtakumbuka, hapo nyuma hata Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, alisema iko haja ya kukaa mezani kuangalia matatizo ya elimu nchini Tanzania. Kwa maana hiyo, ni kwamba wale watoto ina maana wanakuwa wamemaliza miaka saba wakitembea pale shuleni lakini hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaweza tukaangalia jinsi ya kutatua hili tatizo. Kwanza, elimu ya watu wazima iboreshwe ili waweze kwenda kule wakajifunze kusoma na kuandika. Zaidi ya kuboresha, vijijini kwetu kuna wananchi wengi sana Watanzania ambao hawajui kusoma na kuandika. Hata unapokwenda kwenye vijiji vya wafugaji, kule mkoani kwangu Katavi kuna wafugaji, kwa hiyo, wale wana tabia ya kuhama hama na majority yao hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kile Kitengo cha Elimu ya Watu Wazima ambacho najua kwamba kipo lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 nimeona hakijaelezea sana. Naomba uangaliwe utaratibu wa kuboresha namna ya wananchi ambao hawajui kusoma na kuandika ili waweze kujiunga na hii elimu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati tunakua, miaka ya 1970 mpaka 1980. Elimu hiyo ilikuwa na mkazo na watu wengi walijua kusoma na kuandika kupitia elimu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la kuboresha maslahi ya walimu. Kwa mfano, kule mkoani kwangu Katavi, Jiografia ya Makao Makuu ya Wilaya ni mbali. Unakuta kuna kilometa kama 150 kutoka kwenye kijiji kwenda kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Mwalimu huyu anapanda basi au bajaji ama kitu chochote, anakuja Makao Makuu ya Wilaya ambayo yapo kilometa 150. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Elimu iangalie utaratibu ambao inaweza ikaboresha maslahi au ikawapa marupurupu walimu wanaofundisha vijijini ili wawe na interest ya kwenda kufundisha vijijini. Tukichukulia tu kwamba mwalimu anayefundisha mjini anapata maslahi sawa na mwalimu anayefundisha vijijini, kwa kweli naona kwamba hii ina-demoralize katika kufundisha. Nafikiri kwamba si vizuri, tujaribu kuangalia tunaongeza marupurupu gani kwa walimu wanaofundisha vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika kuboresha elimu, maana nimesema kwamba wanafunzi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika; hii ni kwa sababu wanajaa darasani. Darasa moja lina watoto 200. Naomba Wizara ya Elimu iangalie ni utaratibu gani tutaufanya kuongeza ujenzi wa madarasa? Kwa sababu kipindi cha kufundisha darasani ni dakika 40. Mwalimu mmoja hawezi akafundisha watoto 200 kwa dakika 40. Ina maana wale ambao ni cream ndio watakaojua kusoma na kuandika, wale wenzangu mie watabaki nyuma, watakuwa wanasindikiza darasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuboreshe pia kwa kuongeza maslahi ya walimu na kwa kujenga madarasa mengine mapya, lakini nguvu hii pia tuwashirikishe wazazi pamoja na TAMISEMI kwa pamoja tunaweza kujenga madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni maabara zilizojengwa. Wananchi walitumia nguvu yao kubwa, walichanga michango mingi, karibuni kila shule imejenga maabara, lakini hizo maabara hazina vifaa. Niiombe Wizara ya Elimu iangalie, hili tatizo italiondoaje? Shule nyingi zina maabara, hata kule Katavi kuna shule zina maabara lakini hazina vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo tulikuwa tunavitumia sisi, unaenda kwenye chumba cha sayansi unakuta kuna Bunsen burner, na kadhalika. Hivyo vifaa ni vigumu kwa shule kuvinunua na kuviweka kwenye maabara. Naomba Serikali iangalie ni jinsi gani itasaidia. Majengo mengi sana yamejengwa kwenye shule, maabara zimejengwa lakini hazina vifaa. Naomba Wizara ya Elimu iingilie kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu shule za ufundi. Naomba ili kutatua suala la ajira nchini, tuongeze shule za ufundi. Pia, kuna zile shule ambazo zilikuwa ni shule za wazazi. Kwa sababu zile shule za wazazi ziko karibu kila mkoa, zingeweza kugeuzwa zikawa Shule za Ufundi ili watoto wetu waweze kujifunza na waweze kutoka wakiwa wameelewa kitu chochote kama ni kujenga, kushona na kadhalika ili waweze kujiajiri kwa sababu Serikali kama ilivyo hatuwezi tukaajiri wanafunzi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la ajira nchini. Tuangalie ni mbinu gani tutazitumia ili kutoa tatizo la ajira nchini kwa kuzitumia shule za wazazi ambazo nafikiri ziko katika kila Mkoa. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho anaweza akaniambia ni shule ngapi za wazazi ambazo ziko. Ninaamini kwamba kila Mkoa una shule za wazazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni watoto wa kike, ambapo kiutaratibu Wizara huwa inapeleka pesa kule za kujikimu watoto. Hizi pesa kwa sababu watoto wa kike wana matatizo yao ya maumbile ya kibaiolojia, naomba sana Mheshimiwa Waziri, lile fungu lisigawiwe sawa na mtoto wa kiume kwa sababu mtoto wa kike… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa muda huu ili kuchangia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai leo hii na uzima. Napenda niungane na Watanzania wote kutoa pole kwa kifo cha Mheshimiwa Dkt. Mengi ambaye amesaidia sana makundi mbalimbali ya jamii, natoa pole kwa wananchi wote wa Tanzania, familia yake na wote walioguswa na msiba huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri Ummy na Makamu wake, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuboresha afya za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nitoe pongezi kwa Madaktari wote wa nchi hii ya Tanzania kwa huduma wanazotupatia za kuboresha afya za Watanzania wote, ndiyo maana tunaweza kuja humu Bungeni na tunaweza kufanya kazi zetu kwa sababu ya Madaktari.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu muda ni mdogo, niende moja kwa moja kwenye changamoto. Mkoa wetu wa Katavi baada ya ile changamoto ya kuwatoa Madaktari na Manesi feki, tumekumbwa na tatizo la uhaba wa watumishi. Nimwombe Mheshimiwa Ummy aweze kutupatia Madaktari kule Mkoani kwetu Katavi, atupatie Madaktari Bingwa; hatuna Gynecologist, hatuna Madaktari wa Macho, hatuna Madaktari wa Mifupa, kiasi kwamba mtu akivunjika mguu kule Katavi inabidi asafiri kutoka Katavi mpaka Muhimbili kwenda kufanyiwa matibabu ya mguu. Kwa hiyo niombe sana watakapokuwa wanaajiri Madaktari auangalie Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho napenda kukiomba Mkoani kwetu Katavi, naomba kukiombea Kituo cha Afya cha Mamba, naomba akipatie ambulance, kituo hiki kipo umbali wa kilometa 150 kutoka pale Mpanda Mjini na hakina ambulance. Pia nimwombe Mheshimiwa Waziri, kuna kituo cha afya kilikuwa kinajengwa cha Mwamapuli katika Jimbo la Kavuu, naomba akipatie pesa ili kiweze kwisha kwa sababu anafahamu jiografia ya Mkoa wetu wa Katavi, Jimbo la Kavuu liko kiasi cha kilometa 150 kutoka Mpanda kwenda Makao Makuu ya Wilaya, kwa hiyo naomba akiangalie kituo hiki cha afya. Niombe pia vitendeakazi kama x-ray na ultra sound kwa vituo vya afya vyote vya Mkoani kwetu Katavi kwa sababu viko mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya, umbali wa kilometa 150. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho napenda kuzungumzia, nimwombe Mheshimiwa Ummy, iko Sera ya Wazee ambayo Serikali ilipitisha toka mwaka 2003, niombe sasa alete Sheria ya Wazee kwa sababu Sera ya Wazee imekaa umri wa miaka 15, lakini hakuna Sheria ya Wazee, sasa sera ikikaa hivihivi kama sera inaweza siku nyingine Serikali ikaamua tu kwamba inafuta ile Sera ya Wazee lakini ikiwa ndani ya sheria wazee watakuwa protected zaidi. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ninakiomba ni kuhusu kuajiri hii Sekta ya Afya upande wa Community Health Service. Hawa watu ni muhimu sana kwa sababu wao wanakwenda deep kwenye kaya, ina maana wana uwezo wa kwenda nyumba kwa nyumba kwenda kufundisha mambo ya afya. Ukiangalia kwamba mara nyingi nchi yetu huwa tunapata matatizo ya kipindipindu, ni kwa sababu tuna uhaba wa hawa Maafisa Afya Jamii. Hawa ni muhimu sana kwa sababu wao wanakwenda kwenye kijiji, wanaweza kufundisha umuhimu wa kutumia vyoo, umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kula, hii yote itasaidia wananchi wa Tanzania wasiweze kupata magojwa ambukizi. Kwa hiyo, niombe waweze kuajiri hawa Maafisa Afya Jamii kwa manufaa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia, Mheshimiwa Ummy katika Sekta ya Afya amefanya vizuri sana upande wa madawa, upande wa kujenga hospitali, upande wa kujenga vituo vya afya, lakini upande wa wanawake nimwombe kabla hajaondoka aweke legacy kwa wanawake, aangalie sheria ambazo zinamkandamiza mwanamke, zije humu Bungeni zibadilishwe. Nafikiri hiki ndicho kitakachomfanya aweke historia kwa wanawake, Sheria kama ya Ndoa ya Mwaka 1971, kipengele cha 13 ambacho kimekuwa kigugumizi katika nchi hii kubadilisha umri wa mtoto wa kike kuolewa na mtoto wa kiume kuoa, aweke legacy kwa kubadilisha sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sheria nyingine pia ambazo ni kandamizi kwa wanawake. Kwa mfano, ipo GN ya mwaka 1963 ambayo ina vipengele vingi sana vinamkandamiza mwanamke. GN hii bado inatumika na nashangaa sana hata kuna kesi ambayo ilishatolewa kwamba GN hii ifutwe, lakini bado nimeona kwamba ni kigugumizi sana kufuta GN hii. Haiwezekani utumie GN ya mwaka 1963 kwa wanawake wa Tanzania ambayo inawabagua sana katika mambo ya mirathi, inawabagua sana katika kutumia ardhi mume wako akifa na pia ina kipengele ambacho kinasema kwamba mwanamke akifiwa na mume wake arithiwe na mdogo wake na akikataa atoke katika ukoo huo. Nimuombe sana afuatilie hizi sheria zote azilete hapa na atakuwa ameweka legacy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, GN hiyohiyo pia inamtambua mtoto wa kiume kwamba ndio mrithi halali, wanamwita principal heir, lakini haimtambui mtoto wa kike kwamba ni mrithi wa mali za baba yake. Nimwombe Mheshimiwa Waziri basi aweke legacy kwa kubadilisha sheria hizi ambazo ni mbovu, zinamnyanyasa mtoto wa kike ili tutakapoondoka katika Bunge hili, basi akinamama waseme tulikuwa na Waziri mwanamke ambaye pia alishughulikia masuala ya wanawake. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia taarifa ya Kamati yangu ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai, baada ya hapo napenda kuishukuru Kamati ya Sheria Ndogo ikiongozwa na Mtemi Chenge kwa kazi kubwa ambayo inafanya kila siku ya kuchambua Kanuni zote za Wizara zote zilizopo nchini Tanzania, Kamati hii imekuwa ikipitia Kanuni zote ambazo zinatumika kwenye Wizara zote ambazo zilizopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzirekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Makatibu wa Kamati hii nawapongeza sana na ninapenda niseme ndani ya Bunge hili Makatibu wa Kamati ya Sheria Ndogo wamekuwa na kazi kubwa sana kupitia Kanuni ambazo huwa zinaletwa kwenye Kamati yetu ambazo zimeandikwa zimekosewa, naomba nitoe wito kwa Waandishi wa Sheria ambao wanaandika Kanuni hizi ambao wapo kwenye Wizara tofauti tofauti wawe makini wanapoandika hizi sheria, zinapoletwa kwenye Kamati, kila siku Makatibu wanakesha kuzichambua kuzioanisha kutoka kwenye Kanuni kupeleka kwenye Sheria Mama, mfano sheria labda ni ya Wizara ya Ardhi inatunga kanuni ya Wizara ya Ardhi unakuta kifungu hakiendani na Sheria Mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu kinasema vingine Kanuni inasema vingine, hii inaleta matatizo kwa wananchi kwa sababu hizi sheria mnaisema kwamba ni sheria ndogo hizi sheria siyo ndogo ndiyo sheria ambazo mwananchi wa kawaida anaishi nazo na anaziishi kila siku, kila siku anaishi kwa zile Kanuni, mwananchi wa kawaida haishi kwa kufuata zile Sheria Mama, Sheria Mama inapotungiwa Kanuni zile Kanuni ndiyo zinambana mwananchi wa kawaida.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali najua kuwasomesha Waandishi wa Sheria ni gharama lakini naomba niishauri Serikali itumie pesa kusomesha waandishi wa sheria kwa sababu waandishi wengi wa sheria wamestaafu wameshafika miaka 60 wamestaafu mfano mzuri hata huyu Mwandishi mzuri hata huyu Mwandishi aliyekuwepo hapa Bungeni Mama Kibagana sijui nimekosea jina lakini kuna Mama ambaye alikuwa anaandika sheria hapa Bungeni amestaafu mwaka jana, kwa hiyo tuna CPD mpya yuko hapa, lakini wengi waliokuwa trained miaka ya nyumba wanakwenda miaka 60 kama hana miaka 60 na 58 kwa hiyo atastaafu hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itumie pesa kusomesha Waandishi wa Sheria ili sheria zetu zinapotungwa zitungwe vizuri na kwa sababu nchi kama nchi inaishi na sheria na inatunga sheria kila siku, sasa sheria zinapokosewa zinaletwa pale sisi tunaanza kuchambua tena kwa kweli inaleta shida, niombe sana Serikali izingatie hili tutumie pesa tupate waandishi wazuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ningeweza kusema ni kwamba Kanuni ambazo zinatungwa kwenye Wizara kila Wizara inapotunga zile kanuni iangalie zile kanuni zisiwe kandamizi kwa wananchi kwa sababu zile kanuni ndiyo wanazoenda kuzitumia mtaani, sasa unapoweka kanuni ambayo inambana sana mwananchi wa kawaida unamuongezea matatizo. Kanuni ziangalie wananchi watakapoenda kutumia hii kanuni itakuwa ni friendly na wataishi nayo, siyo kanuni ambayo unatunga leo, inambana mwananchi anashindwa hata kuishi kwa sababu ya hiyo kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ningependa kuchangia hayo machache kwenye Kamati yetu kwa sababu kanuni zote zililetwa hapa na tulizipitia tumejaribu kuzirekebisha lakini niombe tu labda wale Waandishi wa Sheria wanapoandika wajaribu kuwasiliana na yule Mpiga Chapa wa Serikali ili wanapochapa wasiweze kubadilisha vile vifungu kwa sababu mara nyingi unakuta kama ni kifungu ni 53 lakini kanuni imeshuka huku chini alafu imekosewa, labda Mpiga Chapa pia anaweza akawa ana matatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu na kumpongeza Waziri Hasunga na Manaibu wake Mheshimiwa Mgumba na Mheshimiwa Bashungwa kwa jitihada zenu za kubadilisha kilimo nchi Tanzania.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Mkoa wangu wa Katavi sisi asili yetu ni wakulima. Mkoa wa Katavi una Squire mita 47,586 ambapo asilimia 58.6 ni misitu pamoja na Mbuga za wanyama na asilimia 44 tunatumia kwa kilimo.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wangu huu wa katavi una mapungufu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, pungufu la kwanza hatuna Maafisa Ugani. Mkoa unahitaji Maafisa Ugani 248; kwa sasa una Maafisa Ugani 164. Tuna upungufu wa Maafisa Ugani 16 Mleleji DC, 42 Mpanda DC, 34 Mpanda DC, 41 Nsimbo DC na 31 Mpimbwe DC; jumla tuna upungufu ya Maafisa Ugani 164. Ninaomba Wizara ya Kilimo mtuletee maafisa ugani.

Mheshimiwa Spika, mkoa wetu una changamoto za miundombinu; tukipata maafisa ugani wataweza kwenda vijijini; na mkoa wetu pia vijiji vyake havipo karibu; umbali wa kutoka kijiji kimoja kwenye kijiji kingine ni umbali kama wa kilometa 10 mpaka kilometa 20 ndipo unakuta kijiji kingine. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utupatie Maafisa Ugani ili waweze kuusaidia mkoa wetu wa katavi.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ninalotaka kuomba pia; kwa sababu mkoa ni mpya naomba Wizara ya Kilimo muutupie jicho la huruma, muwapatie Maafisa Ugani hawa vitendea kazi ili waweze kusafiri; angalau pikipiki au hata baiskeli; ukilinganisha na umbali kati ya kijiji na kijiji.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kwamba Mkoa wetu wa Katavi hauna Maafisa Kilimo, tunauhitaji wa Maafisa Kilimo kama 4, lakini Mkoa wa Katavi una Afisa Kilimo mmoja. Hii yote inasababisha afisa kilimo mmoja hawezi akazunguka mkoa mzima kwenda kuangalia shughuli za kilimo. Niombe Wizara iuangalie mkoa huu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia; mwaka jana wakulima wa Mkoa wa Katavi walipata hasara sana ya mazao yao. Walipotaka kuyauza waliambiwa mahindi yao hayanya ubora. NFRA walipofika kule katavi waliangalia yale mahindi wakawaambia hayana ubora. Hii yote ilisababishwa na ukosefu wa Maafisa Ugani ambao hawakuwafundisha mahindi yenye ubora ni mahindi ya namna gani, kwa hiyo wakulima waliishia kula yale mahindi bila kuyauza.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la hawa Maafisa Ugani wa Mkoa wa katavi. Kuna mazao mapya yameenda kule Katavi, zao la pamba na korosho. Maafisa Ugani waliopo Mkoani wa Katavi hawana uzoefu na haya masuala. Ningeomba kupitia bodi za korosho na bodi za pamba haya maafisa ugani wapewe elimu ya pamba na korosho ili waweze kuwafundisha wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa manufaa ya zao hili na manufaa ya wananchi wa mkoa huo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia mwaka jana Serikali ilitoa tozo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Taska malizia unga mkono hoja.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja nilitaka kusema kwamba Serikali ilitoa tozo la asilimia tano kwenda asilimia tatu kwa mazao ya biashara na asilimia tatu kwenda asilimia mbili kwa mazao ya chakula, lakini wakulima hawajanufaika, nataka kuuliza swali, aliyenufaika hapa ni mfanya biashara au mkulima?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge letu Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai, afya njema na leo tuko hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi Taifa na Mkoa wangu wa Katavi kwa kuniamini na kunituma tena kuja hapa Bungeni. Napenda kuwashukuru sana akina mama wa Mkoa wa Katavi kwa kuniamini tena kunipa nafasi kwa kipindi cha pili, leo hii tena nimekuja Bungeni kuwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kuwatumikia Watanzania na kwa kuwapa moyo wa kufanya kazi mpaka nchi yetu imetoka kwenye lile group la nchi maskini na imeingia kwenye group la nchi ambazo zina uchumi wa kati. Ni wajibu wetu sote sisi Watanzania kushirikiana na Mheshimiwa Rais lakini na kumpongeza kwa bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri Mkuu na Mawaziri wote. Nawapongeza Wabunge wote mliorudi kwenye Bunge la Kumi na Mbili; hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, nimeisoma hotuba yake aliyokuja kutufungulia Bunge letu la Kumi na Mbili, lakini pia aliyofunga kwenye Bunge la Kumi na Moja. Mimi nakwenda kwenye page ya 16 pale mahali ambapo Mheshimiwa Rais ameongelea jinsi ya kuleta nidhamu ya kazi maofisini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema wazi, katika umri wangu huu ina maana nilisoma katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, nikafanya kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Pili, ya Tatu na ya Nne na hii ya Tano nikaingia Bungeni. Niliona mmomonyoko wa maadili katika maofisi kwa awamu zote hizo tano. Kwa hiyo, bila kuuma maneno napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kurudisha nidhamu kazini. Awamu ya Tano oyee, nidhamu kazini ilikuwa imeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano kwenye sekta ya afya. Mama anakwenda kujifungua unakuta wale manesi wanashona vitambaa. Mtu anaweza akawa anaumwa uchungu anaita nesi njoo nisaidie anaambiwa mtapike mtoto. Hizo zilikuwa ni lugha za zamani, siku hizi hazipo, sasa hivi nidhamu imerudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho napenda kukizungumzia hapa ni suala la amani. Suala la amani katika nchi yetu hii tunatakiwa sisi Wabunge tuliomo humu ndani tulihubiri, tuilinde hii amani ili watoto wetu wanaokuja waje waikute amani hii. Ni wajibu wetu kuitunza, kuilinda na kuiendeleza amani kwa faida yetu na kwa faida ya wajukuu zetu. Sisi tumekuta nchi hii ikiwa na amani, lugha zetu ziwe za kuendeleza na kudumisha amani, zisiwe za kubomoa, ziwe za kujenga kwa sababu sisi sote ni Watanzania, Tanzania ni moja lakini ina Tanzania Visiwani na Tanzania Bara.

Naomba Wizara ya Muungano itoe elimu ya Utanzania kwenye redio. Mtu ukiwa Zanzibar jisikie kwamba wewe ni Mtanzania, ukiwa Tanzania Bara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Ukiwa Tanzania Bara jisikie kwamba wewe ni Mtanzania. Tanzania ni moja, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. RESTITUTA T. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, nakushukuru. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai leo tupo hapa Bungeni tunachangia mada kwenye Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia mambo mawili matatu, lakini napenda kwanza nianze na suala la sheria ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu, zimetungwa muda mrefu, lakini nafikiri zilipokuwa zinatungwa kwa wakati ule zilikuwa zinahitajika kwa namna hiyo lakini sasa zinahitaji mabadiliko. Labda sababu ilizofanya zitungwe kwa wakati ule zilihitajika zitungwe kwa namna ile, lakini kwa sasa hivi zinahitaji mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971. Ilipotungwa mwaka 1971 sheria hiyo ilikidhi mahitaji ya mwaka 1971 kwa kuonyesha kwamba mtoto wa kike anaweza akaolewa na miaka 15. Kwa sasa hivi watoto hawa wa kike wanasoma, wanakwenda shule, wanakwenda kozi mbalimbali na pia Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga mashule mengi mpaka vijijini.

Kwa hiyo basi, mahitaji ya wakati ule wa mwaka 1971 siyo mahitaji ya sasa hivi ya kuwepo na sheria hiyo ambayo ina kipengele hicho ambacho kinaweka tofauti ya mtoto wa kiume na mtoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha 13 cha Sheria ya mwaka 1971 na Kipengele cha 17 kinatoa ile tofauti ya mtoto wa kike kuolewa na mtoto wa kiume. Sasa ili twende na usawa na kwa sababu tulimsikia pia Mheshimiwa Rais pale alisema kwamba akili za mtoto wa kike na wa kiume ni sawa, naomba kipengele hiki kibadilishwe umri wa kuoelewa wa mtoto wa kike uwe sawa na umri wa kuoa wa mtoto wa kiume. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni Sheria ya Mirathi ambayo kwa wakati ule mila zilikuwa zimeshamiri na zilikuwa zinafuatwa sana nchini kwetu Tanzania. Miaka ya 1963 wakati wa Uhuru, tulihitaji sana kufuata mila. Maamuzi mengi ya Mahakama yalikuwa yanafuata mila za eneo lile au mila za kabila ile, ndiyo maana kukaja na hiyo customary Law, sheria zikaletwa wale watawala wetu wakaona watahukumu zile sheria kufuatana na mila na desturi za eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hiyo Sheria ya Kimila ina section ambayo ina ubaguzi wa hali ya juu kwa mwanamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano nikichukua Section ya 27 ambayo inaelezea kwamba, mwanamke anaweza akatumia zile mali za familia, lakini hawezi kurithi mali za familia. Ijapokuwa Mheshimiwa aliyechangia aliyepita, alijaribu kuzielezea, lakini naomba nidadavue kidogo. Sheria hiyo inamfanya kwanza, mwanamke aji-feel ni inferior kwa mwanaume kwa sababu, katika ubongo wake anakuwa anaelewa kwamba mali hii anahitajika kuitumia tu, lakini sio kuirithi. Pia, sheria hii imekuwa ikiendeleza ule ubaguzi wa jinsia ya kike na ya kiume. Tunayo Tume ya Kurekebisha Sheria lakini haijachukulia ule mkazo thabiti wa kubadilisha sheria hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu, nimekuwepo hapa Bungeni miaka mitano iliyopita, niliona sheria ambazo zililetwa na tukazibadilisha humu Bungeni, lakini kwa sheria hizi mbili kumekuwa na kigugumizi cha aina fulani kuchelewa kuletwa kuja kubadilishwa. Kwa hiyo, niombe kwa sababu, hiyo Tume ya Kurekebisha Sheria ipo izifuatilie hizo sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, zipo pia sheria nyingine nyingi tu ambazo siwezi nikazitaja humu Bungeni lakini pia, either zinawanyima haki wananchi au vile vile labda zinatengeneza mazingira magumu kwa wananchi ambao wanakuwa hawawezi kupata haki zao vizuri. Kwa mfano, Sheria ya Usalama Barabarani nayo pia ina vipengele ambavyo mwananchi anakosa haki pale anapogongwa na gari au ajali inapotokea barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia suala la Wanasheria wa Serikali. Wanasheria wa Serikali wanafanya kazi ngumu sana kuhakikisha kwamba, wanaitetea Serikali mahakamani. Naomba miundombinu yao iboreshwe, Wanasheria hawa wa Serikali wanakwenda mahakamani kutetea kesi za pesa nyingi, lakini unakuta anapotoka pale anakwenda kukaa kwenye nyumba ya kupanga na unakuta hata usafiri hana. Naomba waboreshewe makazi yao, lakini pia waboreshewe mishahara yao. Hawa watu wanatetea Serikali, lakini wanatetea kesi kubwa za madawa ya kulevya, za ugaidi hivyo wanahitaji kuwa na ulinzi na wanahitaji wafahamike wanakaa wapi ili angalau hata inapotokea jambo waweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye mahakama zetu. Kama alivyosema hata Mwenyekiti wa Bajeti hapa, mahakama nyingi hasa zile Mahakama za Mwanzo zimechoka. Wizara ya Katiba na Sheria ichukue jukumu la kuziboresha hizi mahakama either kubomoa zile mahakama ambazo zilijengwa na watawala wetu na zijengwe mahakama ambazo tutasema sisi tumejenga. Litengwe fungu zijengwe mahakama, zinazohitajika kuboreshwa ziboreshwe. Vile vile miundombinu ya mahakama iboreshwe, kwa mfano, niliuliza swali hapa Bungeni Hakimu na Jaji anachukua jukumu la kusikiliza kesi, kukusanya ushahidi na pia anakuja kuandika ile hukumu yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini isianzishwe division ya stenographer ili wawe pale mahakamani waweze kuandika yale mambo ambayo yanazungumzwa pale mahakamani. Hii itasaidia sana wananchi kupata hukumu zao mapema, sasa hivi kumekuwa na usumbufu kesi inahukumiwa leo tarehe 28, lakini hukumu mpaka iandikwe ni baada ya mwezi mmoja. Mwananchi anatembea anakanyaga kwenda kule mahakamani kufuatilia hukumu hii. Hii inaweza ikatengeneza mazingira ya rushwa kwa sababu, unaweza kusema kwamba, naomba uniandikie hukumu yangu ili niweze kwenda kufuatilia. Labda una kesi ya madai, sasa itabidi ufatilie ile hukumu, upate ile hukumu ili uweze ukatekeleze ile kesi yako ya madai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba sana hiyo division wangejaribu kufikiria hii Wizara ya Katiba na Sheria ili kuwarahisishia kazi hawa Majaji na Mahakimu, wanafanya kazi kubwa sana. Mishahara yao iboreshwe, wanahukumu kesi nzito na wanafanya kazi ngumu sana pale mahakamani, vile vile wanakuwa na jukumu la kukaa kuanza kuandika ile hukumu ili kumpa mwananchi. Ukiangalia na sasa hivi tunakwenda kutafsiri hizi sheria kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili, basi jukumu lao la kazi litakuwa ni kubwa mno wanahitaji kuwa na hiyo division. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza leo, ningependa kuwaambia wananchi lakini pia kujiambia sisi wenyewe kwamba, tuishi kwa kutii sheria. Tukiishi kwa kutii sheria nchi yetu itaendelea kuwa na amani lakini pia, sisi wenyewe tunakuwa na uhuru zaidi. Naamini kwamba, Polisi au mtu hawezi akapelekwa mahakamani na akawekwa rumande kwa muda mrefu kama hana kosa. Kwa hiyo, naomba tunapokwenda kusema kwamba, sheria kwa nini imefanya hivi, tujaribu pia na sisi kujielekeza kwamba, tuishi kwa kutii sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana kwamba, tusiishi kwa kufanya makosa ili tukitegemea kutafuta upenyo wa kutolewa kwenye lile kosa. Ukivunja sheria, sheria itakushughulikia, lakini pia sheria ndio inayoweza kudumisha amani nchini kwetu, vinginevyo humu barabarani Mwenyezi Mungu asingeweka sheria sisi tusingepita barabarani, wewe ungepita barabarani yaani mtu angekutemea mate, mtu angekugonga, kwa hiyo, sisi wenyewe tufuate sheria na tuziheshimu sheria zetu ili tusiweze kuvunja sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda nimpongeza Mheshimiwa Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri sana aliyoifanya kwenye Wizara hii ya Elimu. Mchango wangu unaenda moja kwa moja kwenye lugha ya kufundishia, siamini kwamba watoto wakifundishwa Kiswahili wataelewa Zaidi, kwa sababu hata mimi nilijifundishwa kwa lugha ya Kiswahili, nimesoma masomo kutoka darasa la kwanza mpka darasa la saba kwa Kiswahili. Nikaenda Sekondari ya Loleza nikapambana na Kiingereza. Nikasoma geography kwa Kiingereza, history kwa Kiingereza, hesabu kwa Kiingereza, chemistry kwa Kiingereza, biology kwa Kiingereza na masomo mengine yote kwa Kiingereza na tuliweza kufanya hivyo tukaweza kufaulu mitihani. Hoja yangu ni kwamba tuangalie tatizo ni nini, lugha sio tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba tusije tukawandanganya Watanzania tukasema kwamba wakifundishwa kwa Kiswahili ndio wataelewa wakati watoto wetu tunawasomesha kwenye english medium, hiyo itakuwa ni dhambi kubwa sana tumeifanya. Naamini Wabunge humu ndani watoto wao wanasoma kwenye zile shule zilizoanzishwa sasa hivi za English medium, sasa tukianza kujenga hoja hapa kwamba watoto wafundishwe kwa Kiswahili tutakuwa tunawakosea sana Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hoja muhimu ni kuangalia tatizo nini, kwa nini wanafunzi hawelewi darasani, lakini tatizo sio lugha. Je, utakuwa unajenga Taifa gani ambalo litakuwa linafundisha lugha moja ya Kiswahili, naamini kwamba lugha ni biashara, lugha ni mtaji na lugha ni elimu. Nasema lugha ni mtaji kwa nini, lugha ni mtaji kwa sababu unapojua lugha nyingi unajua Kifaransa, Kispaniola na Kiingereza, ina maana una-command lugha, hata unapoitwa kwenye interview utakuwa unaenda kujieleza vizuri. Kwa maana kwamba unaweza ukaenda kwenye zile nchi, ukafanya kazi, lakini kama wewe umekaa na lugha moja ina maana huna exposure, huwezi kwenda kufanya kazi hizo nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mawazo yangu, ningependa kwanza Mheshimiwa Ndalichako aongeze lugha; lugha nyingi zifundishwe mashuleni kama Kifaransa, Kispaniora na Kiingereza kiwekewe mkazo ili watoto wawe na confidence wanapoitwa kwenye International Organizations, wasiingiwe na ile inferiority complex, wanaanza can you explain yourself, anaanza ho ho ho badala ya kueleza my name is so and so.

Mheshimiwa Naibu Spika, lugha pia ni biashara, mfano unakwenda china unajua Kichina, ina maana wewe uta-bargain biashara za kule China. Kwa hiyo hoja yangu ni kwamba shule ziongezewe lugha za kufundishia, lugha ziwe nyingi, sio lugha moja tu ya Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo ningependa kulizungumza leo ni vitendea kazi kwenye shule zetu za msingi pamoja na sekondari, lakini hasa za msingi. Ningeomba Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Waziri wa Elimu awasiliane na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kuna misitu mingi sana hasa kule kwenye Bwawa la Nyerere ambako kunajengwa umeme kule Stigler’s Gorge, ile miti inayokata wanatengeneza mbao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri awasiliane nao, apate zile mbao ili ziweze kutengeneza madawati kwa sababu wanasafisha pale kwenye lile bwawa, kwa hiyo ile miti wanatengeneza mbao lakini zile mbao wanaziuza. Namwomba awasiliane na Wizara ya Maliasili ili mbao ziweze kupatikana madawati yaweze kutengeneza kwa wingi na watoto wetu wasiweze kukaa chini na hapo tutakuwa tumeienzi falsafa ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya elimu bure kwa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nafasi bado ipo nilipenda kuzungumzia pia mfumo wa elimu. Mheshimiwa Ndalichako itakuwa ni vizuri sana kwa sababu amesema anakwenda kurekebisha mfumo, tunaomba kwa sababu kulikuwa na kujichanganya hapa katikakati 2015 to 2020, alikuwa amesema watoto watasoma kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la 12 ndio watakuwa wamehitimu, lakini baadaye akaja akarudisha kwenye ile sera zamani tuliyosoma sisi la kwanza mpaka la saba, halafu kwenda sekondari, itakuwa ni vizuri sana aki-review hii sera ya elimu ili tujue Tanzania sera yake elimu ni ipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la mwisho ambalo ningependa kuzungumzia kama muda upo…

Mheshimiwa Naibu Spika, basi nimeona umewasha kipaza sauti, hivyo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara nyeti, Wizara ya Ulinzi. (Makofi)

Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Kwandikwa kwa hotuba yake nzuri sana aliyeitowa leo napenda niwapongeze wanajeshi wote nchini Tanzania kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya kutulinda sisi wananchi, lakini pia kulinda mali zetu na kulinda nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu wa leo kabla sijaenda kwenye hoja ya Mheshimiwa Kwandikwa, napenda nizungumzie Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye Mkoa wangu wa Katavi pale Mpanda Mjini mwaka 1984 kuna mnara uliwekwa pale maeneo ya Kampuni, lakini mwaka 1993 Jeshi liliondoa huo mnara, badaye mwaka 2020 ule mnara ulirudishwa pale na mwaka 2021 waliweza kufunga hiyo radar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni nini yale maeneo yanazungukwa na kata tatu, Kata ya Ilembo, Kata ya Mpanda Hotel, na Kata ya Msukumilo na hoja iliyopo Jeshi lilipokuja mwaka 1984 lilikuwa na hekari 100, liliporudi mwaka 2020 liliongeza yale maeneo na kuwa na hekari 2,200. Sasa katika maeneo yale walioongeza kuna shughuli za kijamii zinaendelea pale, kuna watu wanalima wanafuga, lakini pia kuna nyumba za watu ambazo zilikuwemo katika eneo hilo. Ombi langu kwa Wizara ya Ulinzi na kwa Mheshimiwa Waziri ni kwenda kutatua ule mgogoro ili wananchi pamoja na wanajeshi waweze kukaa kwa amani, kwa sababu kwa sasa hivi kinachoendelea wale wananchi wanapokatiza lile eneo la Jeshi kwenda kuangalia shughuli zao wanajeshi wanawapiga, lakini pia wanachoma nyumba zao na kuwanyang’anyia mali zao kama mabati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, ili kuwe na amani na ili Jeshi kwa sababu ni Jeshi la wananchi, nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri atafute muda ili aende Mkoani Katavi pale kwenye Wilaya ya Mpanda Mjini akaangalie hilo tatizo na aweze kulimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri; Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ameeleza changamoto ambazo anazikabili kwenye ukurasa wake wa 19; aya ya 78, 79 mpaka aya 80.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba tatizo analokabiliana nalo ni ukomo wa bajeti, ili nchi iweze kufanya mambo mengine, ili nchi iweze kutatua tatizo la maji, tatizo la umeme, tatizo la barabara, lakini pia ili wananchi waweze kufanya kazi kwa amani lakini pia wanajeshi wale wanatakiwa waongezewe marupurupu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiona bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi inaukomo sasa bajeti ikiwa na ukomo na Mheshimiwa Waziri katika hizi aya nilizozitaja ameeleza kwamba ameshindwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi, ameshindwa kuwapeleka kusoma, kununua vifaa, lakini pia ameshindwa hata kutoa yale mahitaji muhimu yanayohitajika pale Jeshini kwa sababu ya ukomo wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali bajeti ya Ulinzi, isiwekewe ukomo wa bajeti na hii itatusaidia sana sisi wananchi wa Tanzania ili tuweze kuishi kwa amani, lakini pia ili tuendeleze amani yetu iliyopo sasa hivi. Suala hili ni muhimu, nimeliona nilizungumze hapa la ukomo wa bajeti ili tuweze kuangalia tunalifanyia vipi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kulizungumza leo ni mipaka ya nchi yetu. Mipaka ya nchi yetu mingi hakuna barabara na ndiyo maana tuna wahamiaji haramu wengi wanaingia nchini kwetu, utaweza ukajiuliza uko pale Mbeya au uko Dodoma mhamiaji haramu ameingiaingia vipi mpaka akafika hapa Dodoma na ameingilia wapi? Jibu unaweza ukajijibu mwenyewe kwamba ameingilia kwenye uchochoro wa mpakani kwa sababu hakuna barabara. (Makofi)

Kwa hiyo niiombe Serikali na nimuombe Waziri awasiliane na Waziri wa Ujenzi waangalie ni jinsi gani wataweza kuitengeneza barabara zinazozunguka nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni muhimu kwa sababu nchi yetu inapakana nan chi nyingi, inapakana na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Msumbiji, lakini na nyingine nyingi. Sasa ili tuwe na uimara wa mipaka yetu na hili wale walinzi wa mipakani ambao ni wanajeshi wetu waweze kuwagundua kwa mapema wale wahamiaji haramu ni muhimu barabara zikawepo. Kwa sababu ukosefu wa barabara, mlinzi atakuwa amesimama hapa kwenye lindo, lakini yule mhamiaji haramu anapata upenyo wa kupita eneo lingine kwa sababu hakuna barabara inayonyooka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba suala la barabara za mipakani lizingatiwe, lakini pia mipaka yetu ioneshwe, sisi tupo lakini kuna siku tutaondoka katika dunia hii, tunatakiwa kizazi kitakachokuja kikute mipaka ya nchi yetu ikiwa inafahamika vizuri. (Makofi)

Suala la mipaka nchi nyingi zimeweza kugombana kwa ajili ya mpaka wa hatua moja au mbili. Mheshimiwa manyanya alizungumza leo asubuhi kuhusu mpaka ulioko Ziwa Nyasa ndiyo utaangalia jinsi gani umuhimu wa kuweka mipaka yetu sasa hivi ili kizazi kinachokuja kikute mipaka yetu iko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala ambalo wengine wamelizungumza hapa kuhusu nyumba za wanajeshi wetu na kukaa uraiani. Ili kuweka ile dhana ya kusema huyu sasa ni mwanajeshi turudi kama jeshi lilivyokuwa zamani wale wanajeshi wakae katika kambi zao, wasikae uraiani, kwa sababu hii kwanza kikanuni inaweza ikapunguza ile sijui nitumie neno gani? Hali ambayo mwananchi anamuona kwamba huyu mwanajeshi ni mlinzi wa amani ya kwangu na ni mlinzi wa nchi, sasa inakuwa kwamba yule mwanajeshi anakaa nyumba moja na mwananchi wanatumia geti moja, labda wanatumia bafu moja, naona kama inapunguza kitu cha namna fulani, nimeshindwa kuweka maneno gani mazuri hapa, lakini maana yangu ilikuwa ni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba tulilirudishie jeshi letu heshima yake ya toka mwanzo kama jinsi lilivyoanzishwa. Nafahamu yapo mapungufu lakini kama tunaweza kutatua hili tatizo la makazi ya wanajeshi litatusaidia sana, majeshi yakae mahali pao, polisi wakae mahali pao japokuwa siyo bajeti yao hii, lakini nilitaka tu kusema hivi wale watu ambao kwa sababu wanajeshi wenyewe uwezi kumkuta mwanajeshi ameingia baa au polisi ujuwe huyo siyo mwanajeshi halali. Sasa kama huko kuna miiko basi na ukaaji vilevile wasichanganyike na rai ndiyo suala ambazo nilipenda kulizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nilitaka kusema ni suala la la vile viwanda ambavyo vimeanzishwa na Jeshi letu la wananchi, kulikuwa wanajeshi waliwahi kutengeneza gari inaitwa Nyumbu, lakini sijui gari hiyo iliishia wapi.

Kwa hiyo wangekuwa wamewezeshwa na wale wataalamu waliokuwa waliotengeneza hiyo gari nafikiri sasa hivi wangeshatengeneza magari mengi, lakini pia Jeshi lina kiwanda cha kutengeneza uniform, kwa hiyo sioni hoja ile ya kusema mwanajeshi anakosa uniform wakati kuna kiwanda cha kutengeneza uniform na nilivyosoma kwenye hii taarifa ya Mheshimiwa Waziri kile kiwanda kina uwezo wa kutengeneza uniform 400 kwa siku. Sasa kama kina uwezo wa kutengeneza 400 kwa nini mwanajeshi akose uniform, ni kwamba sisi tumekosa kuwapa zile fedha/mitaji ya kununua zile material ili waweze kutengeneza hizo uniform. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ombi langu kwa Serikali ni kuangalia hivi vitu ambavyo viko viwanda na tunafahamu wanaviwanda wanamambo ya kilimo ambayo yameanzishwa na wanajeshi na ambayo kwa kweli yanawasaidia sana kujitegemea wao wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sisi tuweke input tuporeshe kama ni hivyo viwanda Serikali iweke pesa hizo uniform zitengenezwe hakuna haja ya kusimama hapa na kusema kwamba wanajeshi hawana uniform wakati wanakiwanda cha kutengeneza uniform zao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi niungane na wengine kukupongeza, Kiti kimekuenea. Napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ndumbaro na Makamu wake Mheshimiwa Mary Masanja. Nampongeza Katibu Mkuu Allan Kijazi na watendaji wote wa Serikali. Napenda pia kumpongeza Profesa Silayo kwa kazi nzuri aliyoifanya nchini kwa kulinda misitu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 17 ya pato la Tanzania linatokana na utalii na asilimia 25 ya pesa za kigeni zinatokana na utalii nchini kwetu Tanzania. Nichelee kusema kwamba barabara zinazokwenda kwenye hifadhi za Taifa za nchini kwetu hazifai. Sasa kama barabara haifai, hili pato la Taifa litapanda vipi? Tulikwenda Ruaha National Park barabara kutoka Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park, ukimpeleka mgeni pale, the moment anafika pale Ruaha National Park akirudi the business is finished there! Hatarudi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, Wizara hii ishirikiane na Wizara ya Ujenzi waweze kujenga barabara zote zinazokwenda kwenye Hifadhi ili utalii uweze kukua nchini kwetu Tanzania. Kama tunavyojua, wageni wanapokuja wanataka kuona vitu mbalimbali. Hivyo basi, ninaishauri Wizara ya Maliasili na Utalii, isijikite kwenye utalii wa wanyamapori peke yake. Hebu fungukeni, nendeni kwenye utalii mwingine, nendeni kwenye utalii wa fukwe (Marine tourism); nendeni kwenye utalii wa nyuki (Api-tourism); nendeni kwenye utalii wa misitu (forest tourism); nendeni kwenye utalii wa malikale (traditional tourism); msijikite tu kung’ang’ania kuangalia tembo, faru na simba. Fungueni milango mingine ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niyaseme hayo kwa sababu nimeona kila kitu ni wanyamapori, wanyamapori. Utalii mwingine, hautangazwi. Naomba mtangaze na utalii mwingine ambao unapatikana nchini mwetu kama nilioutaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala la uhifadhi wa malikale. Uhifadhi wa malikale nchini Tanzania haupo. Tunazo malikale nyingi nchini Tanzania, lakini hazijahifadhiwa vizuri na hatujaziweka kama ni kivutio cha watalii kuja nchini kwetu Tanzania. Labda kuzisema tu kwa uchache, tunayo mapango ya Amboni Tanga, tunayo Laitoni footprint ambayo iko kule Ngorongoro, tunayo magofu ya Kilwa, tunacho kimondo pale Mbozi, tunayo michoro iliyochorwa kule Kondoa Irangi; lakini pia UNESCO walizitambua hifadhi za Ngorongoro kama ni urithi wa dunia; walitambua pia magofu ya Kilwa kama ni urithi wa dunia; walitambua pia hifadhi ya Taifa ya Selous kama urithi wa dunia; walitambua pia hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro kama ni urithi wa dunia; walitambua Mji Mkongwe wa Jiji la Zanzibar kama urithi wa dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hivi vitu, Wizara ya Maliasili na Utalii ivizingatie na iviweke viwe kama ni vivutio vya utalii nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia hapa ni suala la wanyama wanaovunwa. Kuna mito ambayo ina mamba mengi na kuna maziwa ambayo yana mamba wengi kama Rukwa, lakini pia kule Mpanda kuna bwawa moja la Milala ambalo lina viboko wamejaa pale mpaka siku hizi hatutumii yale maji ambayo zamani tulikuwa tunatumia. Naomba Wizara hii ya Utalii iangalie wale wanyama waharibifu kama mamba wavunwe na kama viboko wavunwe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Taska Mbogo.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja, maana yangu ni kwamba hatuwezi ku-compromise maisha ya binadamu na wanyama ambao tumepewa tuwatunze. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai. Vile vile napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, jemedari wetu, mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi tukiwa kama wanawake nchini Tanzania tunatembea kifua mbele kwa ajili yake na tunamuunga mkono na tutaendelea kumpambania hata kule katika majimbo yetu kwa kuyaeleza yale mazuri yote anayowafanyia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa yafuatayo: Kwanza kabisa, ameweza kuongea na wazee pale Jijini Dar es Salaam, aliweza kuongea na viongozi wa dini, aliongea na sisi akina mama hapa Dodoma na pia aliongea na vijana pale Mwanza na kukubaliana na maombi ya vijana kwamba wataunda Baraza lao la Vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuja na bajeti nzuri ambayo imekwenda kuwapunguzia kodi wafugaji, wakulima pamoja na wale wenye NGOs zao. Pia ni kodi ambayo imeangalia mpaka yule mtu wa hali ya chini, bodaboda kwamba kipato chake ni cha chini na kuweza kumpunguzia kodi ya adhabu kutoka shilingi 30,000 kwenda shilingi 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi za Mheshimiwa Rais, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake, Mheshimiwa Engineer Masauni kwa bajeti yao nzuri sana ya mwaka 2021/2022. Nawapongeza sana watendaji wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Katibu Mkuu pamoja na Gavana wa Fedha, Mheshimiwa Luoga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu wake kwa kuja na wazo la kukusanya Property Tax kutoka kwenye Luku. Pia nawapongeza sana kwa sababu area hii ya ukusanyaji wa kodi ilikuwa imeleta shida, Halmashauri zilishindwa kukusanya, lakini TRA pia walivyopewa walishindwa kukusanya. Kwa hiyo, kwa kuja na wazo hilo, nawapongeza sana. Naomba mawazo hayo wayapeleke pia kwenye land rent, waweze kutafuta utaratibu ambao viwanja ambavyo vimepimwa nchini kwetu Tanzania vitaweza kukusanywa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nawapongeza pia kwa suala la kuja na kodi ya miamala ya kwenye simu na tozo zile kwenye vocha tutakazokuwa tunaweka kwenye simu. Hii inamfanya hata Mtanzania wa hali ya chini aweze kuchangia kodi ya nchi yake. Kuchangia kodi ya nchi, ndiyo utaratibu wa nchi zote duniani. Hii itamwezesha mwananchi kuiuliza Serikali ni kwa nini haijajenga barabara? Ni kwa nini haijaleta maji kwenye eneo? Kwa nini haijajenga kituo cha afya; zahanati pamoja na kuhudumia wananchi kwa ujumla? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia Mkoa wangu wa Katavi. Sisi katika bajeti iliyopita tuliahidiwa kujengewa reli kutoka pale Mpanda Mjini kwenda sehemu moja inaitwa Karema ambako kuna bandari ambayo itakuwa inapokea mizigo kutoka Kongo. Naomba tu hili zoezi la ujenzi wa hiyo reli lisiishie kwenye karatasi, litekelezwe ili wananchi wale wa Mkoa wa Katavi waweze kufanya biashara kwenda Kongo na pia Taifa letu la Tanzania liweze kupata kipato kutokana na ushuru utakaotokana na wale wafanyabiashara ambao watapitisha mizigo yao. Maana yake hiyo reli ikiisha, mzigo utakuwa unatoka Dar es Salaam unapita Tabora - Mpanda mpaka kwenye Bandari ya Karema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuliahidiwa barabara ya lami kutoka pale Mpanda Mjini kwenda kwenye hiyo Bandari ya Karema. Naomba pia Waziri wa Fedha asije akatusahau. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii pia kupongeza miradi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, kama Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge. Ni umeme ambao utauzwa mpaka nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na dunia kwa kutupa uhai kuuona mwaka 2023. Kabla sijaendelea na mchango wangu napenda kuunga mkono hoja za Kamati yangu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, hoja zote za msingi ambazo zilisomwa na Mwenyekiti wa Kamati, naunga mkono kwa asilimia mia moja, naunga mkono pia hoja za Kamati ya Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia changamoto ambazo zinawakabili wananchi lakini ambazo ziko nchini kwetu jinsi wanyama waharibifu ambavyo wanaweza wakaathiri wananchi. Zipo changamoto ambazo zinaikabili Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali. Wizara hii ina upungufu wa hifadhi 1,680 ambao wanatakiwa ili kuepusha wananchi wasije wakadhurika na wanyama wakali, lakini bado wanahitaji vitendea kazi kama pikipiki, helikopta kwa ajili ya movements za kule kwenye hifadhi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya matatizo, matokeo yake imekuwa mara nyingi wananchi wameweza kuumizwa na hao wanyama wanaotoka kwenye hifadhi. Pia tumekosa ufanisi zaidi wa kuangalia hizi hifadhi tunazidhibiti vipi, ningependa kujua kwamba kwanza, je, lile suala la buffer zones la mita mia tano kutoka kwenye hifadhi bado lipo na linazingatiwa kwenye hii Wizara ya Maliasili na Utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nipende tu kuzungumzia kwamba mwananchi anapopata matatizo kwa mfano ameumizwa na hawa wanyama wakali, fidia zake haziridhishi kama jinsi Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu alivyozungumza wakati anawasilisha hapo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea mwananchi ameumizwa na hawa wanyama kwa bahati mbaya kwa mfano akiwa ameuawa, mwananchi huyu analipwa kifuta machozi cha shilingi 1,000, akiwa amepata ulemavu analipwa kifuta machozi cha shilingi 500, akiwa ameumizwa kidogo anapata kifuta machozi cha shilingi 500,000.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Ruhoro.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba kifuta machozi anachokisema inapotekea mwananchi ameuliwa na mnyama mkali siyo shilingi 1,000 ni shilingi 1,000,000. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taska.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nililigundua hilo kosa nikawa nimesahihisha labda msikilizaji hakusikia. Nilisema kwamba inapotokea mwananchi amefariki kifuta machozi anapata Sh.1,000,000, anapokuwa amepata ulemavu wa kudumu anapata Sh.500,000 na anapopata majeraha madogo madogo anapata Sh.200,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ukienda kwenye matangazo ya hifadhi zetu unakuta kuna hifadhi imebandikwa pale kwamba ukimgonga nyati unalipa Dola 1,900, ukimgonga twiga kwa bahati mbaya unalipa Dola 15,000, ukigonga tembo pia unalipa Dola 15,000 na wanyama wengine wameorodheshwa hapo, utakuta wamebandika hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati alivyowasilisha asubuhi, Kanuni za mwaka 2011 za Malipo ya Kifuta Jasho zinatakiwa zibadilishwe kwa sababu haziendani kabisa na hali halisi ya sasa hivi. Sisemi kwamba mwananchi akifariki alipwe labda dola 15,000, nafahamu uhai hata kama mtu kama angelipwa dola 100,000, siyo sawa na uhai lakini angalau basi kile kifuta jasho kiweze hata kufanikisha mazishi yake lakini pia kiweze kusaidia hata familia yake iliyobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifuta jasho cha shilingi 1,000,000 kwa mtu ambaye amepoteza uhai ni kifuta jasho kidogo sana na ukilinganishwa na compensation ambayo mtu analipa akiwa amegonga twiga, tembo au nyati, hivyo basi niombe haya yarekebishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitu kingine ambacho ningependa kukizungumzia ni suala la malipo ya fidia kwa hao hao wanyama. Kifuta jasho cha mtu mwenye shamba lake likiwa ndani ya mita mia tano halipwi kitu, lakini shamba likiwa umbali wa mita 500 mpaka kilomita moja analipwa shilingi 25,000, lakini analipwa kwa hekari tano tu. Kwa hiyo hapa hata kama mtu shamba lake limeliwa la ekari 100, atalipwa ekari tano tu kadiri ya sheria inavyosema. Niombe sheria hizi zibadilishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa nilizungumzie hapa ni suala la utalii. Utalii unaenda vizuri, tunampongeza Mheshimiwa Waziri wa Utalii lakini pia tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour, wageni wengi wamekuja nchini lakini tuna matatizo makubwa ya mahoteli, mahali pa kulala wageni wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo Serikali ilikuwa inamiliki hoteli 23. Hoteli hizi Serikali ilizibinafsisha, lakini katika ubinafsishaji kuna watu ambao walibinafsishiwa hizo hoteli ambazo hazifanyi kazi mpaka leo na wengine walizozichukua zinafanya kazi kwa kiwango cha chini ambacho siyo standard.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna uhitaji wa hoteli nafikiri hoteli hizo kama zisingeuzwa zingeweza kutusaidia. Naunga mkono hoja ya Kamati ya kusema kwamba hoteli zote ambazo hazifanyi kazi, zimefanya vibaya, zichukuliwe na Serikali ziweze kutafutiwa wawekezaji wapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Hoteli ya Embassy, tangu ilivyobinafsishwa ina takribani miaka 14 haijawahi kufanya kazi na kule ndani kila kitu kimeharibika, lakini pia zipo Hoteli za Kunduchi Beach na Mikumi Lodge hazifanyi kazi na mwekezaji aliyepewa hoteli hizo ni mwekezaji mmoja, ambaye amepewa Hoteli za Embassy, Kunduchi Beach pamoja na Mikumi ameshindwa kuzikarabati hizi hoteli kwa takribani miaka 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi mtu kama huyu ni mtu ambaye tayari automatically amevunja ule mkataba wa ubinafsishaji. Sioni sababu ya Serikali kuanza kumbembeleza kumwandikia barua ya kuja kwenye meza ya maridhiano, kwa sababu automatically huyo mtu ameshavunja mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wageni wengi wanakuja. Niseme tu, Sera ya Ubinafsishaji wa Hoteli kwa wakati ule labda ilikuwa nzuri, lakini haikuleta tija kwa Taifa letu. Hivyo basi, naomba kama Mwenyeketi wa Kamati alivyosema, tunataka action, hatutaki majadiliano, tunataka hoteli hizo zirudi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu Wizara ya Ardhi. Waliozungumza mbele yangu nawaunga mkono kwa hoja walizozizungumza, lakini napenda kuzungumzia suala la fidia. Kuna hizi kampuni ambazo zinapita zikipima. Wanapomkuta mtu ana shamba lake, kwa mfano shamba la ekari 100, hana hela ya kupima, wana tabia ya kusema kwamba tutakupimia bure halafu utatupa sehemu ya viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Ardhi ilete utaratibu, ijulikane kabisa kampuni kama inapima bure italipwa viwanja vingapi? Kuliko kama ilivyo sasa hivi, makampuni yanakwenda kule, yanafanya negotiation, matokeo yake wanawadhulumu wananchi. Unakuta mwananchi ana shamba lake la ekari 100 anapimiwa viwanja, anaonekana kwamba yule aliyepima kachukua viwanja 30 akagawanya sawa kwa sawa na mtu mwenye ardhi yake. Hiyo siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na kanuni ambayo itatoa mwongozo kwamba iwapo mwananchi ana shamba lake, anataka kupimiwa, basi kanuni inasema kwamba labda ni asilimia 100 ya viwanja; kama amepima viwanja 10, labda hiyo kampuni ichukue kiwanja kimoja. Siyo kampuni ipime viwanja 10 ichukue viwanja saba au sita, inagawana sawa na mwenye mali, naona siyo sahihi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umeisha.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Dunia kwa kutujalia uhai, leo hii tuko hapa Bungeni tunachangia hoja ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya kuwatumikia Watanzania. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Angellah Kairuki na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Festo Dugange na Naibu wake Mheshimiwa Deo Ndejembi. Wote kwa pamoja nawapongeza kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuzungumzia kazi alizozifanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miaka miwili katika upande wa TAMISEMI. Mheshimiwa Rais kwa upande wa TAMISEMI ameshughulikia sana masuala ya afya ya binadamu kwa maana anawapenda Watanzania. Mheshimiwa Rais amehakikisha zahanati 1,066 zinajegwa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha Hospitali za Wilaya 135 zinajengwa nchini Tanzania. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha vituo vya afya 713 vinajengwa. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha majengo ya dharura (EMD) 80 yanajengwa nchini Tanzania. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha vyumba vya dharura (ICU) 28 vinajengwa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hakuishia hapo, ameweza kuhakikisha kwamba nyumba za watumishi 450 zinajengwa nchini Tanzania. Mheshimiwa Rais kwenye suala la afya hajaishia hapo, ameweza kutoa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi bilioni 250. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha kuna ajira 10,324 nchini Tanzania. Makofi kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo imefanya jumla ya Shilingi bilioni 600 kutumika kwenye masuala ya afya nchini Tanzania. Hili ni jambo kubwa, Mheshimiwa Rais amejali afya za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu vitu hizi Mheshimiwa Rais amevifanya kwa muda wa miaka miwili tu tangu alipoingia madarakani. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, kwenye suala la elimu nchini Tanzania amehakikisha kwamba zinajengwa Shule maalum mpya za Sekondari za wasichana kwenye mikoa yote, na kila mkoa umepewa shilingi bilioni nne na shilingi bilioni 10 zimeshatolewa, na shule nyingine zinaendelea kupata fedha hizo, kwa maana ya kwamba, kila mkoa utapata shilingi bilioni nne kujenga shule hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, kumekuwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa 23,000 nchini Tanzania. Hili ni jambo la kumpongeza Mheshimiwa Rais. Pia kumekuwa na ujenzi wa shule za sekondari na msingi ambazo zinaendelea nchini Tanzania chini ya juhudi za Mheshimiwa Rais. Ni obvious lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kasi hii ya miaka miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, kwenye suala la miundombinu tumeona barabara za vijijini zikijengwa na zikiimarishwa kwa maana kwamba tumeona TARURA wakipewa pesa kuimarisha barabara za vijijini na mijini. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba akina mama kutoka vijijini wataweza kufika mjini kupata huduma zao za afya au kama wana mahitaji zaidi.

Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, sasa naomba niende kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye suala la elimu, naiomba Serikali… (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Restituta, mimi ni Mwenyekiti sio Makamu Mwenyekiti.

MHE. TASKA R. MBOGO: Samahani Mwenyekiti. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la elimu kwa Mkoa wangu wa Katavi tunaipongeza Serikali, madarasa yanaendelea kujengwa. Nina ombi kwa Serikali. Ombi langu ni moja, ninaiomba Serikali iangalie suala la madawati. Nitoe mfano, pale Mpanda Mjini tuna Shule ya Msakila, ina upungufu wa madawati 400. Watoto wa darasa la kwanza wanakaa chini, chekechea wanakaa chini, darasa la tatu wanakaa chini na darasa la nne wanakaa chini. Pia wana Mwalimu wao Mkuu; Mwalimu Didas anajitahidi kuwafundisha watoto hawa, mpaka hii shule ni miongoni mwa shule bora kwenye Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Shule ya Shanwe ina upungufu wa madawati 447. Naiomba Serikali, inapotupatia vyumba vya madarasa iangalie utaratibu wa kuziambia Halmashauri ziweze kuchonga madawati. Napenda kusema kwamba, niliwahi kumwuliza Makamu Katibu Mkuu Mheshimiwa Musonda, alisema kwamba suala la madawati ni suala la Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba basi Halmashauri zipewe Waraka ziweze kuchonga hayo madawati kwa sababu ukichukua mfano Shule ya Shanwe ni shule ya miaka mingi, imeanza toka mwaka 1961 lakini ina miundombinu mibovu, madawati hamna, na ina vyumba vitano. Ina uhitaji wa vyumba 12 vya madarasa, lakini sasa hivi ina vyumba vitano tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia pia, ni suala la matundu ya vyoo. Shule zetu nichukulie mfano, Shule hii ya Msakila, ambayo ni shule nzuri sana pale Mpanda Mjini, ina wanafunzi 2,300, lakini shule hii ina matundu ya vyoo 10 tu. Unaweza ukafikiria mwenyewe uhitaji wa wanafunzi 2,300 kwenda kwenye matundu ya vyoo 10, hali inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wakati tunakwenda kupata majengo mazuri ambayo tunajengewa sasa hivi, na Mheshimiwa Rais wetu amejitahidi kupata fedha za kujenga majengo hayo, tunaomba pia miundombinu ya vyoo izingatiwe. Darasa linapokwisha, madarasa yanapoongezeka, tunaomba pia masuala ya vyoo, maana ndio afya ya msingi ya shule, yazingatiwe. Pia masuala ya madawati yazingatiwe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umeisha Mhehsimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Afya kwanza kabisa napenda kupongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake nzuri anayoijali kwa kujali Afya ya Watanzania. Mama mjali afya ya Tanzania hiki hakina ubishi kila mtu ameona nchini Tanzania jinsi gani Mheshimiwa Rais alivyoweka pesa nyingi kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Molel wote kwa pamoja wanafanya kazi nzuri sana kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe Watanzania kazi ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya kwenye Wizara ya Afya. Mheshimiwa Rais amehakikisha kwamba Nchini Tanzania kumejengwa zahanati 1,066 kila sehemu katika kipindi cha miaka miwili Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha kuna vituo vya afya vimejengwa 234 kwa kipindi tu hiki cha miaka miwili. Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha kuna majengo ya ICU yamejengwa takribani 28 nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha kwamba kuna majengo ya dharula maana yake kuna magonjwa yale dharula yamejengwa takribani majengo 80 nchini Tanzania. Huyu Rais anayejali afya za watanzania, huyu Rais anaejali kizazi kinachokuja kwa sababu anataka watanzania wawe na afya njema ili waweze kufanya kazi vizuri na waweze kuendeleza nchi yetu ya Tanzania pongezi ngingi sana kwa Mheshimiwa Rais makofi kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hayo tu leo asubuhi Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha taarifa yake amekuja hapa na madaktari ambao watapita kwenye hospitali zetu kwenda kuwafundisha wale madakta kwenye kila wilaya hili ni jambo ambalo linatendeka kwa mara ya kwanza nchini kwetu Tanzania. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako ni jambo jema wale watakapopita watakwenda kuboresha afya za watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia kwa jinsi hospitali yetu ya Benjamini Mkapa inavyofanyakazi wagonjwa wengi wanakuja pale wanatibiwa. Pia kwa lile jambo ambalo Mheshimiwa Ummy alituelezea hapa kuhusu kuweza kuwashughulikia wagonjwa wa Selemundo hilo ni tatizo kwa watanzania wengi. Watanzania wengi wanaumwa huu ugonjwa wa sickle cell na watoto wengi wameweza kupoteza maisha kwa ajili ya ugonjwa huu. Kwa hiyo, kuwepo kwa tiba hii nawapongeza sana sana Wizara ya Afya pamoja na watendaji wenu, lakini tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuyatekeleza yote haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona jinsi gani wilaya na mikoa zimepewa ambulance, hili halina ubishi. Katika kipindi cha miaka miwili ambulance nyingi zimepelekwa kwenye hospitali zetu, hata kwenye Mkoa wangu wa Katavi, ambulance zilipelekwa. Ninapenda kushukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa ajili ya ambulance hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi ninayo machache ya kuzungumzia kuhusu Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye Mkoa wangu wa Katavi tunayo matatizo ya upungufu wa madaktari takribani 17 (MD). Tuna upungufu wa wauguzi 33, pia tuna upungufu wa wataalamu wa maabara takribani 13, tuna upungufu wa wataalamu wa meno. Vilevile tuna upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi. Katika hospitali zetu za wilaya pale tuna upungufu wa vifaa tiba ambavyo vinatakiwa viwepo pale kwenye hospitali yetu ya wilaya. Tuna upungufu mpaka wa vitanda na magodoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hapa ili muweze kusaidia pale tuweze kupata magodoro pamoja na vitanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Katavi ina madaktari bingwa sita tu, ambapo tuna matatizo katika magonjwa mengine kwenye Mkoa wetu wa Katavi; na mgonjwa anapokuwa na hilo tatizo inabidi apelekwe kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambayo ni mbali. Kwa sababu kutoka Mkoani kwangu Katavi mpaka kufika Mbeya kule pana umbali. Kwa hiyo kama inapotokea kuna mgonjwa wa figo anatakiwa kuchujwa damu inabidi apelekwe Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba tuweze kupatiwa hivyo vifaa. Lakini kwenye Mkoa wangu pia wa Katavi tunayo matatizo ya Madaktari Bingwa. Mgonjwa anapoumia, kwa mfano anapovunjika mkono inabidi aende rufaa kama nilivyosema Mbeya au apelekwe Bugando. Lakini tatizo ambalo nimeliona kwenye Mkoa wangu wa Katavi kuna tatizo la kuchangia mafuta kwenye ambulance, lakini

kuna tatizo pia la kuchangia fedha ya yule nesi anayemsindikiza mgonjwa. Pia kunakuwa pia na tatizo la kumchangia pesa ya kujikimu…

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumuongezea taarifa mama yangu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalumu kutoka kule Katavi. Jambo hili la kuwataka wagonjwa wachangie mafuta kwenye ambulance lipo pia na kwenye Mkoa wetu wa Songwe hususan kwenye Jimbo la Momba. Watu wakiumwa wanataka wachangie mafuta kwenye ambulance, sasa, watu wa vijijini wanapata wapi hela ya kuweka mafuta kwenye ambulance zaidi ya lita 50? Mheshimiwa Waziri jambo hili anapaswa kulitambua kwenye ngazi za zahanati na vituo vya afya.

NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo unampa aliyezungumza.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Nampa taarifa mama yangu wakati yeye anamwambia Mheshimiwa Waziri…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska.

MHE. TASKA R MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo kwa sababu ndilo suala ambalo nilikuwa ninalizungumzia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia ule umbali wa kutoka pale kwetu Katavi mpaka kufika kule Mbeya kwenye hospitali ya rufaa unamwambia mgonjwa aweke mafuta hiyo ambulance. Kuna familia moja kule kwetu mkoani Katavi ilibidi wauze nyumba ili waweze kumpeleka hiyo mgonjwa kule rufaa Mbeya; lakini wameenda kule wameuza bill kubwa lakini pia mgonjwa yule alifariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa ninaomba ufafanuzi; zile ambulance ni nani anatakiwa aweke mafuta kwenye ile ambulance? Lakini pia yule nesi anakuwa yuko kazini, dereva anakuwa yuko kazini kwa sababu anaendesha ile ambulance ambayo ni ya hospitali, sasa inakuwaje anatakiwa alipwe posho zake na mtu ambaye anamuuguza mgonjwa wake? Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wako najua nyinyi ni wachapakazi wazuri ninaamini kwamba suala hili mmelisikia na mtalishughulikia kwa sababu linafanya mpaka wagonjwa wengine kutoka kwenye ule Mkoa wangu wa Katavi washindwe kwenda kwenye hospitali za rufaa kwa sababu wanakuwa hawana ule uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, tuna mapungufu ya madaktari bingwa, wagonjwa wa ndani, watoto, macho wagonjwa wa akili, mionzi pamoja na mapungufu ya vifaa tiba ni suala ambalo linaukabili Mkoa wetu wa Katavi kwenye vituo vya afya pamoja na zahanati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara ya Ardhi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai tunachangia hii Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kwa jinsi alivyoanza kushughulikia matatizo ya Wizara ya Ardhi, kwanza kwa kuunda ile Kamati ya Mawaziri Nane ili waende kushughulikia migogoro ya ardhi, lakini pili hapa juzi juzi aliweza kutoa msamaha wa riba kwenye pango la ardhi ili wananchi waweze kulipa pango lao la ardhi. Napenda pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa hilo, lakini niombe ikiwezekana atuongezee muda, awaongezee wananchi ili waendelee kulipa pango la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Angelina Mabula na Naibu wake kwa kutuletea watendaji wa Wizara ya Ardhi hapa Bungeni na sasa tunaweza kushughulikia masuala yetu ya ardhi kwa wepesi zaidi. Napenda niwapongeze watendaji wote wa Wizara ya Ardhi na hususan nitaanza na Kamishna wao Mheshimiwa Mathew kwa uwajibikaji wake wa kupokea simu haraka na kujibu message. Nampongeza pia, Mkurugenzi wa National Housing Mheshimiwa Hamad Abdallah kwa kasi mpya aliyokujanayo kwenye sekta ya national housing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizo pongezi ninayo masuala ya kuchangia kwenye Wizara hii. Kwanza kabisa naunga mkono hoja ya Kamati ya Ardhi, nikiwa kama Mjumbe naunga mkono mambo yote yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati yetu. Sisi kama kamati tuliona kwamba, Wizara ya Ardhi ina wajibu wa kupima ardhi na kusimamia ardhi ya Tanzania inapimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Tume ya Mipango ya Ardhi. Tume ya Mipango ya Ardhi imekuwa ikipewa pesa ndogo sana za kupima ardhi na matokeo yake imekuwa ikishindwa kutimiza wajibu wake wa kupima ardhi na hatima yake ni uzalishaji wa migogoro kwenye masuala ya ardhi kwa wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wakati tunapitisha bajeti hapa tuliomba tume iongezewe pesa shilingi bilioni nne, lakini suala hilo limechelewa kutekelezwa mpaka tumekuja kuingia kwenye bajeti nyingine. Tukiwa kama wajumbe wa Kamati tunaona kwamba, hii inaidhoofisha Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi kuweza kutimiza wajibu wake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiona migogoro ya mipaka ikiendelea, lakini pia tumeona wakulima hawajui mipaka yao ni eneo gani la kulima, pia tumekuwa tukiona wafugaji hawajui maeneo yao ya ufugaji na hii kusababisha migongano kati ya wakulima na wafugaji. Ombi langu kwenye Wizara ya Ardhi ni kuiongezea Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi Nchini ili iweze kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ninaomba kuzungumzia suala la pesa za mkopo ambazo Serikali yetu ya Tanzania imekopa mkopo huu ambao unaitwa Land Tenure Improvement Program. Pesa hizi ni dola 150, sawa na shilingi bilioni 350 za Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tuliona kwamba, fedha hizi zingeelekezwa zaidi kwenye upimaji wa ardhi. Kwa maana kwamba, tukiwa kama Kamati tulipendekeza zaidi pesa hizi ingepewa Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi ili iweze kwenda kutekeleza wajibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi ina uwezo wa kupima vijiji 826 kwa mwaka, lakini mradi huu unakwenda kupima vijiji 500 kwa muda wa miaka mitano. Ukiangalia uwiano ni kwamba, kutakuwa na uwiano wa vijiji 100 kupimwa kwa mwaka mmoja. Kitu ambacho tunaona kwamba, kwa mfano kama hii fedha Tume ya Mipango ingepewa ingeweza kupima vijiji 826 kwa mwaka, na matokeo yake kwa muda wa miaka mitano ingeweza kupima zaidi ya vijiji 4,131. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia unakuta kwamba, uwiano wa vijiji 500 kwa miaka mitano ni tofauti kubwa na uwiano wa vijiji 4,131 ambavyo vingeweza kupimwa na Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi nchini Tanzania. Ombi langu kwa Serikali, ninaomba fedha hizi waweze kufanya utaratibu; Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi ipewe fedha hizo ili iweze kupima hivi vijiji na ili iweze kuendana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imesema kwamba, kwa muda wa miaka mitano tungeweza kupima vijiji zaidi ya 4,131. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa kwenye huo huo mradi; tunaomba ile mikoa ambayo inakwenda kujenga hizi ofisi kutokana na hizi fedha, kwanza tungeomba ofisi zijengwe kwa uwiano wa kufanana. Yaani kwamba, mikoa yote gharama ya ujenzi ilingane; kwa maana ya kwamba, hata kule Katavi waweze kupata ofisi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia hap ani suala la mipaka yetu ya nchi yetu ya Tanzania. Suala la mipaka ni tata kwa sababu gani, tumeona sehemu nyingine hazijawekewa mipaka, lakini pia sehemu ambazo zimewekewa mipaka ni wanajenga vi-box vidogo sana ambavyo ni kama mita moja. Mfano, tulikwenda pale Tunduma tukakuta mpaka, ni kitu kimetoka chini urefu wa mita moja mpaka hapa, ndio unaitwa mpaka wa Tanzania na zamabia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuboresha mipaka ya nchini kwetu Tanzania ninaomba Serikali iweke utaratibu, hususan Wizara ya Ardhi ambayo inaratibu hili jambo, ijenge mipaka ya kuonekana ambayo itakuwepo sasa na miaka 100 ijayo. Ujenzi wa mipaka ambao unaendelea sasahivi, mipaka ile ni midogo na sehemu nyingine hazionekani, haijulikani mpaka uko wapi, umeishia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya ujenzi wa mipaka ya nchi yetu ya Tanzania ni fedha chache. Hii inasababisha kwamba, huko baadaye sisi tutaishi na tutapotea, lakini tunataka kizazi kinachokuja kikute mipaka ya nchi yetu imeratibiwa vizuri na inaonekana. Kwa maana kwamba, kama unajenga urefu wa mita moja kutoka chini na unasema kwamba, huu ndio mpaka ina maana unahitaji baada ya muda labda miaka kama 20 utahitaji kujenga tena, kurudia zoezi lilelile la kujenga mipaka upya, kitu ambacho naona kwamba ni utumiaji wa fedha mara mbili. Kama tunaboresha mipaka yetu basi tungeboresha mipaka yetu vizuri na tujenge mpaka wa kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia, wananchi wengi wanakaa kwenye vijiji hawaelewi kwamba wanapaswa kupima ardhi zao. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake mwekezaji anafika pale anachukua ile ardhi kwa sababu, yeye amewekeza na yule mwananchi ambaye amekaa pale kwa takribani muda wa miaka mingi anaondoka pale kwa sababu tu, alikuwa ahajapima ile ardhi na kwa sababu alikuwa hana hati. Ombi langu kwa Serikali, ninaomba Wizara ya Ardhi iwaelimishe wananchi waweze kupima ardhi zao kama ni shamba, ni kitu chochote waweze kukipima, ili kutoa huu usumbufu wa kunyang’anywa ardhi zao ambazo wanakuwa wamekaa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu anakaa mahali takribani zaidi ya miaka 50 halafu unakuja kumwambia kwamba, hapa si nyumbani kwako kwa sababu huna hati. Kwa hiyo naomba wananchi waelimishwe waweze kupima ardhi zao, lakini pia waweze kutumia hizo hati zao kwa ajili ya kupata mkopo benki na sehemu nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia hoja ya Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Dunia kwa kutujalia uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa kiongozi namba moja kuitangaza nchi yetu ya Tanzania kwenye Filamu ya Royal Tour ambayo imeiweka Tanzania katika ramani ya dunia. Napenda pia nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mary Masanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza Wakurugenzi wote; Mkurugenzi wa Misitu, Profesa Silayo; Mkurugenzi wa TANAPA, Mheshimiwa Mwakilema, na Katibu Mkuu Mheshimiwa Dkt. Abbasi, lakini nawapongeza pia watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya bila kumsahau Mkurugenzi wa TAWA na watendaji wengine wa Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu utajikita sana kwenye migogoro ya wananchi na wafugaji lakini kwenye mambo ya malikale pia kwenye sheria ambazo zimepitwa na wakati ambazo bado zinatumika. Kwa nianze na migogoro ya wananchi kati ya wananchi na wahifadhi. Migogoro hii ukiiangalia kwa undani imesababishwa na sababu ya Wizara yenyewe kutokuweka mipaka yake. Hivi karibuni ndiyo kumekuwa na uwekaji wa mipaka hiyo. Hifadhi nyingi mipaka yake haijulikani na hili lilisababisha wananchi wengi kwenda kujenga kwenye maeneo ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ushauri wangu kwa Wizara hii ya Maliasili na Utalii ishirikiane na Wizara ya Ardhi iweze kutambua maeneo yake kwa sababu kinachojitokea sasa hivi ambacho Wizara inakuja inasema hapa ni ushoroba wa wanyama, hapa hawa wananchi wamevamia, na vijiji vingine, kwa mfano, tulikwenda kule Kilosa, tulikuta vijiji vya Ng’ombo viko katikati ya hifadhi, lakini kuna zahanati na shule, vitu ambavyo vimewekwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, unakuta kwamba hakuna ule uelewano kati ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Maliasili. Kwa sababu kijiji kinapoanzishwa kinasajiliwa na Serikali inakitambua kama ni Kijiji, inakiwekea shule, lakini kinakuwa ndani ya hifadhi. Hivyo basi, ili twende pamoja na tuache kulaumu kwamba wananchi wanavamia maeneo ya hifadhi, ni bora Wizara ya Maliasili na Utalii ikatambua hifadhi zake iweke mipaka yake kwa kujenga barabara kuzungushia hifadhi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye ushoroba. Utasema kwamba wananchi wamejenga kwenye ushoroba, wananchi hawaanzishi kijiji kwa siku moja. Kijiji hakioti kama uyoga, au mji hauanzi kwa siku moja ukasema kwamba hawa wananchi wamejenga kwenye ushoroba. Kijiji huwa kinaanza kidogo kidogo na miji pia inaanza kidogo kidogo kwa nyumba moja na ya pili: Ni kwa nini wahifadhi au Idara ya Maliasili unapoona kwamba kuna kijiji kinaanzishwa kwenye eneo la maliasili wasiwakataze wale wananchi, waambiwe kwamba hapa ni shoroba? Unangoja mwananchi amejenga nyumba yake ya thamani unakuja kubomoa kwamba hapa ni Shoroba na malipo yake yanakuwa ni kidogo? Kwa hili naomba nisiwaunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa, pia ni ile Kamati ya Mawaziri Nane. Kamati ya Mawaziri Nane ilipita, ikaainisha kwamba yale mamlaka ya kuendelea na ile kazi ibaki kwa Wakuu wa Mikoa. Niwaombe Kamati ya Mawaziri Nane mweze kurudi kwenye mikoa mliyopita mkatatue matatizo ya ardhi yaliyoko. Kuna wengine wanaambiwa mmejenga maeneo yasiyostahili, mmejenga kwenye hifadhi, au mmejenga kwenye vyanzo vya maji. Kwa hiyo, nawaomba, mlipita mkiwa mnaenda maeneo ya mjini, nawaomba mtakaporudi sasa muende site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze tu Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa kwa kwenda Tarime na kwenda Mbarali na nikuombe usiache kufanya hivyo. Usifanye kazi ya kukaka kwenye kompyuta ofisini, fanya kazi ya kwenda site ili uone maeneo yako yakoje? Ukikaa kuangalia kwenye kompyuta pori hili lina ukubwa gani, hii kazi itakuwa ngumu kwako mwanangu. Ni ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa ni kuhusu kutangaza utalii mwingine. Tunaona TV kila siku zikimtangaza tembo, zinatangaza sijui nini, tunaomba pia mtangaze utalii mwingine kama wa fukwe, utalii wa malikale na pia mweze kuangalia vivutio vingine viko wapi? Hasa hapa sasa naomba nizungumzie watu wa malikale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa malikale ni wazembe, hawafatilii malikale zilizopo kwenye mikoa. Katika yetu kuna sehemu nyingi sana ambazo ni vivutio kwa wananchi na ambavyo ambavyo pia vinaweza vikaleta pesa kwa Serikali yetu ya Tanzania, lakini wao malikale wamejikita sehemu moja. Kila mkoa una historia yake, kuna mambo ya machifu na mengine mengi. Unakuta kuna mikoa ambayo ina historia ya biashara ya utumwa, kuna maeneo ambayo wakoloni (labda niseme wageni walivyokuja kwa mara ya kwanza waliingilia pale), kuna wavumbuzi wa kwanza ambao walikwenda maeneo yale. Sehemu kama hizo, hawa watu wa malikale wanatakiwa waifatilie. Tulikwenda pale Arusha…

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MWENYEKITI: Mchangiaji, endelea kuchangia.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, amenikoroga kidogo huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Nilikuwa nazungumzia malikale, kwamba malikale wafanye utaratibu wa kuainisha maeneo yao, washilikiane na watu wa TAMISEMI waainishe maeneo yao. Maeneo yao mengi hawana happy, maeneo yao mengi yamevamiwa kwa sababu wameyaacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la malikale limeanza tangu tulivyopata Uhuru wa nchi hii. Lakini malikale wamekuwa mambo yao hayaendi, huoni kwamba kuna msukumo hapa wa malikale lakini nafikiri sijui ni bajeti ndogo au ni kitu. Tungeomba hawa malikale waweze kuongezewa. Kuna vitu vingi kama kule Mkwawa kuna Kinjekitile, kuna mambo ya Machifu wa zamani wanatakiwa kuwa kwenye historia ya nchi hii ili sisi tutakapokwenda watoto wetu wawezi kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taska Mbogo, ahsante sana kwa mchango wako. (Makofi)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nusu dakika, robo dakika. Ninaomba TANAPA iongezewe bajeti, tulikuwa na hifadhi 16 zikaongezwa hifadhi sasa hivi ziko hifadhi 22, fedha ni kidogo. TAWA pia waongezewe, kwa sababu mapoli yaliongezwa lakini pesa hazikuongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Maazimio mawili yaliyoletwa hapa na Kamati yangu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai mpaka sasa tumekaa hapa miezi mitatu tupo hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia suala la Azimio la Bunge la kuridhia kufutwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi na kuruhusu kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi. Napenda nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa na Naibu wake, Mheshimiwa Masanja lakini na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri waliyoifanya mpaka tumefikia leo hapa tupo kwenye majadiliano ya Azimio hili.

Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kufutwa Hifadhi ya Kigosi na kuanzisha Hifadhi ya Msitu wa Kigosi. Ninazo sababu za kumpongeza, kwa sababu inapokuwa hifadhi wananchi hawaruhusiwi kuingia ndani ya hifadhi, lakini inapokuwa hifadhi ya misitu wananchi wa eneo hilo wataweza kupata fursa za kuingia kwenye hifadhi na wataweza kwenda kufanya shughuli zao za kijamii kama kutundika mizinga, kuvua samaki lakini pia na kufanya mambo yao ya asili kama matambiko.

Mheshimiwa Spika, eneo hili ni kubwa ni kilometa za mraba takribani elfu saba mia nne na kitu. Ni eneo kubwa ambalo wananchi wanaozunguka maeneo hayo watafaidika nalo. Pia eneo hili linakwenda kuifungua nchi kiuchumi kwa sababu tunaweza kupata wawekezaji wakawekeza hata kwenye mambo ya hewa ya ukaa. Mbali na hapo kutakuwa na viwanda, viko kule viwanda vitano ambavyo vinachakata mazao ya asali kama nta, lakini asali pia inapouzwa nje ya nchi inaleta pesa za kigeni na wananchi wanapata manufaa kutokana na mazao hayo.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita na nalipongeza azimio hili na naunga mkono kuwepo kwa azimio hili na naomba Wabunge wenzangu waliunge mkono kwa faida ya wananchi na faida ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kupongeza Azimio la Ruaha kwa sababu linakwenda kutatua matatizo yaliyopo pale Ruaha, lakini pia ni faida kwa wananchi kwa sababu maji yanayotokana hapo yanakwenda kujaza Ziwa la Kidatu na pia yanakwenda mpaka Ziwa la Mwalimu Nyerere ambako Serikali imewekeza mradi mkubwa kwa ajili ya kufua umeme.

Mheshimiwa Spika, eneo hili ni eneo ambalo maji yanayokwenda kwenye Ziwa la Mwalimu Nyerere yanatokea sehemu hiyo. Hivyo basi, kupitishwa kwa azimio hilo kutasababisha yale maji yaweze kuwepo kwa wingi na kwenda kwenye Ziwa hili ambalo litatengeneza umeme mwingi ambao tutaweza pia kuuza hata kwenye nchi za jirani.

Mheshimiwa Spika, kwenye Azimio hili la Ruaha, niombe sana wale watendaji ambao watakuwa wanakwenda kutekeleza ile mipaka wawe marafiki na wananchi wa maeneo hayo. Vilevile niombe Wizara ya Maliasili na utalii, sisi kama Kamati tulikuwa tumeomba sehemu ya eneo ambalo liko karibu na yule mwekezaji mkubwa Kapinga One, wananchi wapewe hilo eneo ili na wao waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo kwa sababu hili eneo limeleta mgogoro maana yake wapo wananchi wanaolalamika kwamba kwa nini yule mwekezaji ameachwa pale. Tuliomba na yeye eneo lake la juu, tulikubaliana kwamba waweze kwenda kupima lile eneo la Kapinga one wananchi waweze kugawiwa ili nao waweze kufanya shughuli zao za kilimo.

Mheshimiwa Spika, viko vitongoji ambavyo vimechukuliwa vitakuwa ndani ya hifadhi kwa maana kwamba vile vijiji vitano vinaenda kufa kama vijiji. Ombi langu kwa Wizara ni hili, wale wananchi walioko kwenye hivyo vijiji na vitongoji vinavyoenda kufa, wafanyiwe uthamini wa mali zao waweze kulipwa haraka iwezekanavyo. Pia kama Serikali itaona jicho la huruma, iweze kuwaonesha sehemu nyingine ili wananchi hawa waweze kwenda kujenga nyumba zao kwa sababu vile vijiji na vitongoji vinakufa. Viko vijiji vitano vinaenda kufa kabisa kwa sababu vitakuwa ndani ya hifadhi, lakini pia vipo vitongoji vingine ambavyo vinaenda kufa.

Mheshimiwa Spika, tuombe malipo yao yaharakishwe na sio Sheria ipite hapa Bungeni halafu inapofika wakati wa malipo ije iwe shida. Jambo hili litaleta mgogoro kwa wananchi kwa sababu kama umechukua eneo, basi ni wajibu wa Serikali kufanya uharaka wa kulipa hayo maeneo ambayo watakuwa wameyachukua, lakini kuwaangalia wananchi kwa jicho la huruma waweze kuwasaidia kupata maeneo mengine ya kuishi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la vibali. Niombe sana hawa Idara ya Misitu ambao wanakwenda kuangalia hii Hifadhi ya Misitu ya Kigosi waangalie jinsi ya kutoa vibali. Vibali visigeuke kuwa manyanyaso kwa wananchi, wanapokwenda kuomba vibali kwenda kutundika mizinga au wanapokwenda kuomba vibali vya kwenda kuvua samaki, basi wale wafanyakazi wawe rafiki kwa wananchi ili kutoa migogoro ambayo inaweza kutokea kati ya wale wahifadhi wanaolinda hiyo misitu, watu wa TFS pamoja na wananchi.

Mheshimiwa Spika, hapa Azimio linaweza likapita kwamba ni azimio rafiki ambalo Mheshimiwa Rais amelileta linalokwenda kuwafaidisha wananchi, lakini pia linaweza likageuka likawa kitega uchumi kwa yule Mhifadhi ambaye atakuwa analinda ule msitu. Kwa hiyo ombi langu ni kwamba, wale wahifadhi ambao watakuwa wamepewa jukumu la kutoa hivyo vibali wawe rafiki kwa wananchi ili hivyo vibali visije vikageuka tena vikawa ni kitega uchumi cha Mhifadhi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la mwisho kabisa ambalo nataka kulizungumza hapo, niombe wale wataalam wetu wanapokwenda kwenye maeneo haya yote ya Hifadhi ya Kigosi lakini pamoja na kule Ruaha wakawe marafiki na wananchi, waitishe mikutano, sio mwananchi anaamka asubuhi anakuta mpaka umewekwa, ni bora mikutano wakashirikisha Wenyeviti wa Vijiji pamoja na wananchi kwa kuitisha mikutano ya hadhara na wananchi waone ile mipaka inavyowekwa.

Mheshimiwa Spika, naona umewasha taa, naomba kuunga mkono hoja suala la Azimio la Hifadhi ya Kigosi pamoja na Azimio la Ruaha. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Dunia kwa kutujaalia uhai na leo hii tuko hapa Bungeni, tunachangia Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Angeline Mabula na Mheshimiwa Ridhiwan Kikwete, mwanangu kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pia nawapongeza watendaji wote wa Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kufanya kuiweka Wizara hii vizuri na kufanya Watanzania waweze kufurahia ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu pamoja na hizo pongezi kuna mambo ambayo ningependa kuyazungumza kwenye Wizara hii. Kwanza kabisa napenda kuzungumza kuhusu Tume ya Taifa ya Mipango ya Ardhi kama walivyoweza kuzungumza watangulizi wengine. Kazi za Tume hii ni kuipima ardhi ya Tanzania, lakini Tume hii haina meno ya kupima ardhi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ardhi ya Tanzania ikipimwa itajulikana maeneo ya wafugaji yako wapi, maeneo ya wakulima yako wapi na itajulikana maeneo ya mambo ya jamii yako wapi; kama shule na Hospitali. Hii itapunguza sana mwingiliano na vurugu zilizopo kati ya wakulima na wafugaji. Kazi hii inashindwa kutekelezeka kwa sababu Tume ya Mpango wa Ardhi inapewa fedha ndogo. Haieleweki akilini, Tume ambayo inapima ardhi ya Tanzania inapewa Shilingi bilioni 1.4 na hata mwaka 2021 ilipewa Shilingi bilioni 1.9. Naiomba Serikali, kama kweli inataka kuondoa matatizo ya wafugaji na wakulima nchini Tanzania, iipe Tume hii fedha za kutosha. Migogoro mingi iliyopo ni kwa sababu ardhi ya Tanzania haioneshi mipaka ya mfugaji iko wapi, mipaka ya mkulima iko wapi; na mipaka ya mashamba ya mwananchi wa kawaida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Tume pia ina Bodi ambayo siyo ya Utendaji. Tume hii ina Bodi ya Ushauri. Ili Bodi hii iweze kufanya kazi, inatakiwa iwe Executive Board, lakini hii ni Advisory Board. Naomba Serikali ibadilishe sheria ili Tume hii iweze kuwa na Bodi ambayo itakuwa ni Bodi ya Wakurugenzi, ambayo itakuwa na meno na pia itaweza kutoa ushauri mzuri kwenye Tume na Tume iweze kufanya kazi zake vizuri. Pia Tume hii itakapokuwa imepata mambo hayo, itaweza kuwa na bajeti yake. Sasa hivi Tume hii haiwezi kupanga mambo yake ya Bajeti kwa sababu haina Bodi yenye meno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusisitiza, kama jinsi wachangiaji wengine walivyosema, Tanzania tuna Vijiji 12,319 lakini Tume hii tangu imeanzishwa imeweza kupima vijiji 2,565. Ukienda kwenye Ilani ya CCM kama wengine walivyosema, inasema mpaka kufikia 2025 angalau vijiji 80,000 nchini Tanzania viwe vimepimwa, lakini kwenye mpango wa matumizi wa 2020 mpaka 2025 wenyewe umesema angalau asilimia 50 ya vijiji viwe vimewekewa mpango wa matumizi. Kutokana na hilo, naiomba Serikali iangalie ni jinsi itaweza kuipa nguvu hii Tume ya Taifa ya Mpango wa Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuzungumzia hapo hapo kwenye Tume suala la uhaba wa wafanyakazi. Tume hii ina wafanyakazi 79 tu nchini Tanzania. Ina uhitaji wa wafanyakazi 179, kwa hiyo, kuna upungufu wa wafanyakazi 100 kwenye Tume hii. Ili Tume iweze kufanya kazi mikoani vizuri, inatakiwa iongezewe wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Rais; Kamati ya Mawaziri nane ambayo ilipita kuzungumzia migogoro ya ardhi. Kwanza kabisa, napenda kuishukuru Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kuunda hiyo Kamati ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini Tanzania. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini pamoja na hizo pongezi, nimpongeze tu kwa Tuzo aliyoipata ya kuwa Kiongozi bora duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Kamati ya Mawaziri nane kwa sababu Mawaziri walipita kukagua masuala ya ardhi na matokeo yake Serikali ilitoa vijiji 975. Katika vijiji 975, vijiji 925 Serikali iliwapa wananchi. Katika Mkoani kwangu Katavi vijiji 60 tulipewa. Sasa basi katika hivi vijiji 60 vya Mkoani kwangu Katavi, havijapewa GN namba. Pia kuna matatizo makubwa katika utekelezaji, kwamba kuna maeneo ambayo vile vijiji vimepewa lakini bado kuna mamlaka zinakwenda kuwafukuza wananchi na kuwachomea nyumba. Nitoe mfano Kijiji cha Kaseganyama Wilaya ya Tanganyika, eneo la visima viwili, wananchi wale wamechomewa nyumba, na mazao yao na kufukuzwa wakati walikuwa wameruhusiwa kukaa pale.

Mheshimiwa Spika, nimetoa mfano Kijiji cha Kaseganyama Wilaya ya Tanganyika, eneo la Visima Viwili, wananchi wale wamechomewa nyumba lakini pia wamechomewa mazao yao na kufukuzwa wakati walikuwa wameruhusiwa kukaa pale. Pia vipo Vijiji kwa mfano vya Kapalala, Sempanda, operation ya kuwafukuza inaendelea.

Mheshimiwa Spika, siyo Kapalala tu, zipo Kata za Ilunde na kule Inyonga bado kuna operation kama hizo za kuwafukuza zinaendelea. Vile vile Kata ya Kamsisi kule Inyonga nako pia wananchi wamechomewa nyumba pa wamefukuzwa kwenye maeneo ambayo tena kuweka hali kuwa mbaya, Serikali ya Kijiji cha Kamsisi iliwauzia wananchi yale maeneo na ikapata fedha ambazo iliweza kujenga zahanati, lakini leo hii watu wa TAWA wameingia pale wanawafukuza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe mamlaka hizi zisiwe zinaingiliana, kama Serikali iliweza kutoa vile vijiji 920 ili wananchi wavitumie, tunashukuru sana na Mkoa wangu wa Katavi ukapata vijiji 60. Sasa kwa nini kunakuwa na mwingiliano wa mamlaka, kwa nini mamlaka nyingine ije kuwafukuza wananchi wakati walikuwa wameruhusiwa; na Kamati ya Mawaziri Nane ilipita na kuwakagua na kupewa ile ardhi. Sasa naona kuna mwingiliano wa mamlaka katika utendaji, haiwezekani, Serikali hiyo iwape wananchi vile vijiji kwamba wakae halafu Serikali hiyohiyo irudi kesho yake mamlaka nyingine iwaondoe na kuwachomea nyumba. Ningeomba sana Serikali ilirekebishe hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo ningependa kulizungumzia ni maeneo ya malipo kwa wananchi ambao Serikali inachukua ardhi yao. Kule Mpanda Mkoani Katavi kuna maeneo ambayo yana mgogoro mkubwa wa ardhi, maeneo ya Kampuni, Ilembo, Misukumilo, Mpanda Hotel, wananchi wametoka katika ile ardhi lakini wengine hawajalipwa malipo yao mpaka leo. Ningeomba Serikali inapowahamisha wananchi kwa ajili ya kujenga mambo ya maendeleo ya nchi yetu kama shule au zahanati, basi iwe inaandaa malipo kwa wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu kumekuwa na mgogoro mkubwa katika maeneo hayo niliyoyataja ambayo yapo pale Mpanda Mjini. Wananchi waliachia ile ardhi na Serikali imeanza kujenga taasisi zake nyingi, imejenga kama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ipo kwenye maeneo ambayo wananchi bado wanadai ile ardhi; lakini mahakama imejengwa kule, vituo vya polisi na ofisi za Walimu, lakini unashangaa ni kwa nini maeneo hayo bado yana mgogoro wananchi hawajalipwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda w Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ilikuwa imelia dakika moja nyuma.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa pili na kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na pia na afya njema.

Napenda kumpongeza Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Mulamula, Naibu wake Mheshimiwa Mbarouk kwa kazi nzuri ambazo amezifanya na kwa kuonyesha kwamba wamefanyakazi nzuri leo hii tunao mabalozi ndani ya nyumba hii ambao wamekuja kusikiliza bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje nafikiri kwa mara ya kwanza ukumbi umejaa mabalozi na wawakilishi wa konseli mbalimbali tunakushukuru sana na tunaomba muendelee na moyo huo wa ushirikiano kwa nchi za jirani zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuifungua nchi yetu ya Tanzania na kidhibiti cha mambo haya ni pamoja na Balozi ambazo ziko hapa leo, lakini pamoja na mambo ambayo Serikali ya Tanzania imeyapata kutokana na Mheshimiwa Rais kufungua nchi yetu. Tumeona matokeo mengi sana kwa ziara za Mheshimiwa Rais tumeona ushirikiano jinsi gani Mheshimiwa Rais anashirikiana na Marais wengine lakini pia tumeona ni jinsi gani anakwenda kutafuta pesa za kuweza kuleta kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi sisi kama Wabunge tunatakiwa tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuifungua nchi yetu ya Tanzania, lakini pia tunampongeza kwa tuzo ambazo ameendelea kuzipata hususani tuzo ambayo ameipata hivi karibuni aliyopewa na Benki ya Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo napenda sasa kutoa mchango wangu mbalimbali kuhusu Wizara ya Mambo ya Nje. Kwanza kabisa napenda nizungumzie suala la viwanja vilivyopo kwenye Balozi zetu. Katika ripoti ambayo ameisoma Mheshimiwa Waziri nimeifuatilia na nimeisikiliza na kuisoma ameeleza ni jinsi gani Serikali ya Tanzania imeweza kupoteza viwanja vyake ambavyo vipo nje ya nchi, hususani kile kiwanja cha Ethiopia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia Ethiopia kwa sababu nafahamu Serikali ya Tanzania ilikuwa na kiwanja pale na niliishi pale kwa hiyo naelewa yale mazingira ya pale Ethiopia kiwanja hicho kilikuwepo siku nyingi tangu miaka ya 2000 lakini nafikiri hatukuweza kuwekea mkazo kukijenga. Hivyo basi niombe Serikali ya Tanzania lakini kupitia Wizara hii ya Mambo ya Nje zile mali ambazo zipo nje ya nchi, hususani viwanja Serikali ijitahidi kujenga yale majengo ili watumishi wanaofanya kazi nje ya nchi waweze kukaa kwenye hizo nyumba ni gharama sana Serikali kupanga nyumba nje ya nchi, lakini tukiwa na jengo letu tutaweza kuokoa fedha zile ambazo zinalipwa kwa ajili ya pango la nyumba za wafanyakazi wanaofanya kazi Wizara hiyo. Niombe basi katika bajeti inayokuja Serikali ijaribu kutoa fedha ili majengo hayo yajengwe, (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niombe kutoa msisitizo kwa mabalozi ambao wanateuliwa na Mheshimiwa Rais wanapokuwa nje ya nchi yetu ya Tanzania, wao ndio wawakilishi wa Watanzania wote, lakini pia wao ndio wawakilishi wa Mheshimiwa Rais. Niwaombe wanapokuwa kule kwenye zile nchi za nje waweze kutumia nafasi yao kukuza hii diplomasia ya uchumi ambayo Mheshimiwa Rais anapambana nayo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kumuachia Mheshimiwa Rais peke yake kwenda kuongea na wadau nje ya nchi wakati kuna Balozi zipo kule ni suala pia ambalo Balozi anatakiwa alifanye, Balozi ni mwakilishi pale kwenye nchi ile, lakini Balozi anauwezo wa kukutana na wadau mbalimbali Wachumi akakutana na wawekezaji. Kwa hiyo Balozi anapokuwa kule kwenye nchi za nje azingatie kukuza diplomasia ya uchumi ambao Mheshimiwa Rais ameianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la diaspora, katika suala la diaspora nilikuwa naomba Serikali ijaribu kuangalia ni jinsi gani itaweza kuwa-accommodate Watanzania ambao wanakaa nje ya nchi. Mara ya mwisho niliweza kuchangia hapa na katika bajeti iliyopita mwaka jana nilizungumza kwamba Serikali inaweza ikawapa uraia pacha wale watanzania wanaokaa nje ya nchi, lakini ikawawekea condition ya kutokugombea nafasi za uongozi na hii itasaidia sana kuwawekea ile limit ya kuingia Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiacha kizazi cha Watanzania kukaa nje ya nchi bila kuwapa uraia pacha naona kama tunapoteza kizazi chetu ambacho kinakaa ughaibuni. Ukienda kwenye baadhi ya nchi unakuta kuna Watanzania kule wameoa wana watoto wana wajukuu yaani wanafamilia, yaani wana kizazi ambacho unakuta wanakwambia kwamba kizazi hiki asili yake ni Tanzania, wengi wao unakuta wamepoteza ule uraia wa Tanzania kwa sababu nchi yetu …

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa mzungumzaji taarifa kwamba Serikali tayari inajipanga kutoa hadhi maalum na kupitia hadhi hii maalum Watanzania diaspora wataweza kupata haki zote kasoro tu kushiriki kwenye masuala ya kiasiasa pamoja na kufanya kazi kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbogo, Taarifa hiyo.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nafikiri kwa sababu Mheshimiwa Waziri atakuja ku-wind up atalielezea vizuri suala ambalo Mheshimiwa Neema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili, ahsante.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika naunga mkono hoja Wizara ya Mambo ya Nje. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia, aliyetujalia uhai na leo tuko hapa tunachangia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambazo anazifanya kwa Watanzania, kuanzia ujenzi wa vituo vya afya, shule na kila kitu. Kweli, ameonesha ni mama anayejali, kama jinsi mama anavyowajali watoto wake nyumbani na yeye anawajali Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa na Manaibu wake. Mwanangu Mheshimiwa Zainab Katimba, hongera sana, nafasi imekuenea mwanangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo napenda kutoa mchango wangu kwa mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni halmashauri pamoja na manispaa nchini Tanzania zimezua tabia ya kujenga shule zenye mkondo wa Kiingereza, kwa maana ya English Medium. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapitisha Bajeti ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lakini linapopitisha hii ndani yake huwa kunakuwa na pesa ambayo inapaswa kwenda kuhudumia shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapopitisha bajeti hii ina maana linataka elimu bora kwa Watanzania wote, kwa watoto wote wa Kitanzania. Sasa uanzishwaji wa shule hizi zenye mkondo wa usomaji wa Kiingereza, tunaziita English Medium, wananchi wanaambiwa walipie, lakini siyo wananchi wote wenye uwezo wa kulipia hizo shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza, Sera ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu elimu ni Elimu Bila Malipo, sasa, je, Ofisi hii ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inataka kuniambia kwamba, sasa hivi Serikali inafanya biashara kwa kufungua shule zenye mkondo wa Kiingereza? Kwa sababu shule hizo zinalipiwa na siyo wananchi wote wenye uwezo wa kulipia, kama kuna haja ya kufundisha Kiingereza, ni kwa nini basi hiki Kiingereza kisifundishwe kwenye shule zote? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo, shule hizi zinatumia walimu ambao wanalipwa mshahara na Serikali. Sasa iweje walimu wale walipwe mshahara na Serikali halafu halmashauri au manispaa ziseme kwamba, zimetengeneza kitega uchumi wakati walimu wanaofundisha pale ni walimu ambao wanalipwa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo wanachukua wale walimu bora, mawazo yangu ni kwamba, wale walimu wangetawanywa kwenye shule zote nchini ili waweze kuwafundisha wanafunzi wote. Naona shule hizi zinakwenda kujenga matabaka nchini Tanzania. Hapa tulipo tutajenga matabaka ya watoto wa walionacho na watoto wa wasiokuwanacho na ina maana haya matabaka tutakuwa tumeyatengeneza sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Sera ya Serikali ni Elimu Bila Malipo, basi sioni sababu ya halmashauri au manispaa kujenga shule ambazo zinahitaji kulipiwa ada. Mwaka jana nilimuuliza Waziri wa Elimu atoe ufafanuzi, akasema shule hizo hata kama zimejengwa watoto watasoma bure. Naomba Hansard irejewe, hayo yalikuwa ni majibu ya Waziri wa Elimu. Kwa suala hili, naomba halmashauri zilizoanzisha shule hizo ziweze kuzibinafsisha kwa watu binafsi ili waweze kuziendesha kwa sababu, Serikali huwa haifanyi biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naenda kwenye Wilaya ya Mpanda katika Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye Mkoa wangu wa Katavi nime-sample research ya shule zilizoko kwenye Wilaya ya Mpanda pale Mpanda Mjini. Shule hizi ni chakavu, nikianza na Shule ya Shanwe, shule hii ilianzishwa mwaka 1959, ina wanafunzi 1,588, lakini ina walimu 18 tu wanaowafundisha hao wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Shanwe ina madarasa 11 tu. Vilevile shule hii ina uhitaji wa matundu ya vyoo kwani yaliyopo kwa sasa ni matundu 11 tu kwa ajili ya wasichana na matundu mengine 11 yanayotumiwa na wavulana. Shule inahitaji madawati 316, watoto kuanzia darasa la tatu, la nne wanakaa chini. Ina maana watoto wanaokaa kwenye madawati ni watoto wanaoanza darasa la tano, la sita na la saba. Watoto hao wanakaa chini, hii ni Shule ya Shanwe inayopatikana pale Mpanda Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nyingine, Shule ya Nsemulwa imeanzishwa mwaka 1974 ina wanafunzi 1,582, ina walimu 16 tu na madarasa nane. Shule ina upungufu wa madawati 568, shule ina matundu ya vyoo 12 tu, sita kwa wasichana, sita kwa wavulana. Huu ni upungufu wa hali ya juu na hizi shule zote zinapatikana pale Mpanda Mjini ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule ambayo utashangaa ni shule ya Misukumilo. Shule hii ina wanafunzi 3,082, lakini ina walimu 19 tu ambao wanafundisha hao wanafunzi 3,082. Shule hii yenye wanafunzi 3,082 ina upungufu wa madawati 500, ina maana watoto wanakaa chini lakini ina matundu ya vyoo 13 kwa wavulana na 13 kwa wasichana, shule yenye watoto 3,082… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tunaomba utulivu ndani ya Bunge.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, shule hii yenye watoto 3,082 ina walimu 19 tu ambao wanafundisha hao watoto, huu ni upungufu wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nyingine pale pale Mpanda Mjini, Shule ya Msakila ina wanafunzi 2,370, lakini ina upungufu wa vyoo, ina upungufu wa madawati na ina upungufu wa walimu. Kuna shule nyingine, Shule ya Nyerere ipo pale Mpanda Mjini ina wanafunzi elfu moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, lakini naomba Serikali iangalie kutupatia walimu pamoja na vitendea kazi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutujalia uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha elimu kwa Watanzania. Napenda pia kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Elimu Mheshimiwa Profesa Mkenda na Naibu wake Mheshimiwa Kipanga pamoja na watendaji wote wa Wizara hii. Pia, natumia fursa hii kuwapongeza walimu wote wa shule za msingi, shule za sekondari, shule za awali pamoja na wa vyuo vikuu nchini Tanzania, wanafanya kazi kubwa sana ya kuwaelimisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nakwenda kuchangia kadiri ya wasilisho la Mheshimiwa Waziri. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali kwa kuja na mtaala mpya. Mtaala mpya ni mzuri na wazo ni zuri, lakini una mapungufu. Mapungufu hayo napenda kuyataja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala tumeupokea, lakini katika upokeaji wa mtaala, hatukuwa tumejiandaa. Kwa nini nasema hatukuwa tumejiandaa? Nasema hivi kwa sababu, walimu wanaokwenda kufundisha ule mtaala, hawajaandaliwa. Wizara ya Elimu inasema imeandaa walimu, lakini walimu iliowaandaa ni imechukua walimu wawili kutoka kwenye shule; nafanya kama sampling, kwa mfano, Shule ya Nsemulwa, Mpanda, wamechukua walimu wawili wakaenda kufundishwa, lakini zipo shule nyingi ambazo wamechukuliwa walimu wawili wamefundishwa ili na wao wakawafundishe walimu wenzao. Nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walimu wawili waliochukuliwa kwenda kufundisha walimu wenzao, ina maana kama hawajaelewa kile kitu, basi na wao watakwenda kukifundisha vilevile. Hilo naona ni pungufu. Ni nini ushauri wangu? Ushauri wangu ni kwamba, ni kwa nini wasifundishe wakufunzi, wakawaita let say wakaenda pale Wilaya ya Mpanda, wakawaita walimu wote wakawafanyia hayo mafunzo? Suala la kuchukua walimu wawili kwenye kila shule na kwenda kuwafundisha, kuwafanya ndiyo wakufunzi, naona kama bado hapo kuna tatizo kwa sababu, wale ni walimu, hawawezi wakaenda kuwa wakufunzi, japokuwa wamewafundisha. Pia, wale walimu wengine wangependa wafundishwe kwa utaratibu unaofaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pungufu lingine ni vitabu na vitendeakazi. Kweli, mtaala umekuja, lakini vitendeakazi hakuna. Unakuta shule ina kitabu kimoja wanaambiwa watoe photocopy, lakini ukiangalia maisha ya vijijini hizo photocopy hakuna. Je, hizi shule za vijijini zitatoaje photocopy kwa ajili ya mtaala huu? Naona hilo nalo ni pungufu kwenye kutekeleza mtaala huu vizuri. Suala ambalo naliona hapa ni tulitakiwa twende taratibu, ili kutekeleza huu mtaala uweze kuwa vizuri. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu huwezi kufanya test kwa wanafunzi. Unafanya majaribio ya mtaala wakati hujaandaa vifaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo siyo sahihi. Ilitakiwa vifaa, kwa maana ya vitabu na kila kitu viandaliwe na walimu waandaliwe ili mtaala uanze. Hakuna mtu ambaye anakataza mtaala usianze, yote haya tunayapongeza ni juhudi nzuri, lakini tatizo ni ule utekelezaji, tulitakiwa twende taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumza hapa ni hizi shule za amali. Shule za amali hakuna kilichobadilika ni zile shule za ufundi za zamani ni kwamba, zimebadilishwa jina tu. Hizi shule za ufundi zilikuwepo na vitendeakazi vilikuwepo. Je, tumejiuliza kitu kilichoua zile shule za amali ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kilichoua zile shule za amali ambazo sisi tulisoma zamani ilikuwa ukifika, ukienda darasa la needle work, unakuta vyerehani vimekaa pale, ukienda darasa la cookery room unakuta majiko yamekaa pale, majiko ya gesi; kule mnafundishwa kupika, mnafundishwa usafi. Je, mnapoanzisha hizi shule za amali ni kitu gani kimebadilika? Vitendeakazi vimenunuliwa kwenye hizi shule za amali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo shida ninayoiona hapa kwa sababu, hizo shule zipo ni jina tu limebadilika, badala ya kuita shule za ufundi zimeitwa shule za amali. Tukienda kwenye shule za technical college, tulikuwa na shule nyingi za technical college, kuna Moshi Technical, kuna Mkwawa, nyingi tu, lakini kitu kilichofanya zile shule zikafifia, ni vitendeakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ninalojiuliza ni tumeanza mtaala huu tangu Januari, je, hivi vitendeakazi vimeshafika hukou kwenye hizi shule? Jibu litakuja ni hapana. Hili naona kama ni suala ambalo tunakwenda kufanya test, kuwa-test watoto wakati tayari tukiwa tumeanza mtaala tangu Januari. Napenda Wizara ya Elimu kama ingelichukua hili jambo taratibu, liende taratibu, ifundishe walimu na pia iandae hivyo vifaa ili mtaala huu uweze kukamilika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia hapa ni lugha ya kufundishia. Wazungumzaji waliopita hapa wamezungumza suala la lugha kwamba, huwezi kuachanisha Kiingereza na Kiswahili, ni lazima viende sambamba. Ili mwanafunzi au mtu aende kufundisha Kiswahili Marekani ni wajibu wake ajue Kiingereza, ili aende kufundisha Kiswahili China, sijui Japan, Australia, ni lazima ajue Kingereza. Sisi tuna matatizo ya walimu wa Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, sijui hili umejipanga vipi ili kutoa hili tatizo la elimu kwa watoto wetu, hasa kwenye hizi lugha mbili, Kiswahili na Kiingereza kwa sababu, ndiyo lugha international ambazo zinaenda kwa pamoja. Hizo lugha nyingine ndiyo zipo, lakini tunaangalia Kiingereza kinazungumzwa kwenye nchi ngapi? Kinazungumzwa almost duniani kote kwa sababu, Kiingereza ndiyo lugha ya dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watoto wetu wengi wamekuwa wakienda kwenye interview, siyo kwamba watoto hawana akili, wanaelewa hayo mambo, lakini wanavyoenda ku-compete kwa sababu, hatujawaandaa vizuri, tunaonekana kwamba hatuna vijana wengi ambao wanafanya kazi kwenye hizo international organizations sababu ya lugha. Ningeomba Mheshimiwa Waziri suala la walimu wanaoenda kufundisha Kiingereza lichukuliwe kwa umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni marupurupu na stahiki za walimu. Walimu hawa ndio tunawategemea, kuna mwalimu unakuta anafundisha zaidi ya masomo matatu, lakini mwalimu huyu mshahara ni ule ule, anavunjika moyo wa kufundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie madai ya walimu walipwe, lakini tuangalie ni jinsi gani tunawaongezea incentives wale walimu ambao wanafundisha zaidi ya masomo matatu. Kwa sababu haiwezekani mwalimu anachukua masomo matatu au manne, lakini bado mshahara ni ule ule, hamna anachoongezewa, anavunjika moyo. Nilitaka hili Wizara ya Elimu iliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Wizara ya Elimu ndiyo msimamizi wa Sera ya Elimu hapa nchini Tanzania. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, leo wakati anakuja kuhitimisha hoja yake ya Wizara ya Elimu, atupe msimamo wake juu ya hawa walimu ambao wanalipwa na Serikali halafu wanakwenda kufundisha shule za private ambazo zimejengwa na Halmashauri zetu nchini, kwenye baadhi ya halmashauri na manispaa, ili tuelewe tunaendaje? Je, ni sahihi huyu mwalimu ambaye analipwa na Serikali kwenda kutumika kwenye shule ya private halafu ionekane kwamba mapato yametengenezwa na halmashauri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara ya Ardhi. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alitilia mkazo kwenye masuala ya ardhi nchini Tanzania. Vilevile napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa na Naibu wake Mheshimiwa Geophrey Pinda na watendaji wote wa Wizara ya Ardhi kwa kliniki ya ardhi waliyoianzisha, kitu ambacho awali hakikuwepo, hongereni sana. Tumeona jinsi ambavyo mnatatua matatizo ya wananchi wa Tanzania, matatizo ambayo mengi yanayohusiana na ardhi; migongano ya ardhi, double allocation na mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kuchangia kama jinsi ripoti ya Kamati yetu ilivyosomwa hapa Bungeni. Mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati tumekuwa tukiwasiliana na Wizara ya Ardhi, lakini tuna mapendekezo yetu ambayo tuliweka kama Kamati. Mapendekezo na ushauri wa Kamati uliosomwa leo hapa umeonyesha Mradi wa LTIP kwamba unasuasua, ina maana hauna kasi, hautekelezwi kama inavyopaswa kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa LTIP ni mradi wa uboreshaji wa usalama wa milki za ardhi nchini. Mradi huu ni ule ambao una mkopo wa dola bilioni 150, sawa na fedha za Kitanzania shilingi bilioni 345. Fedha hizi ni za mkopo, hivyo Wizara ya Ardhi inatakiwa kwanza izitumie vizuri, lakini zaidi ya kuzitumia vizuri, mipango yake ya matumizi ijulikane, kwamba zimefanya kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri aliyoisoma na kuiwasilisha hapa leo ameongelea Mradi wa LTIP, lakini hakuongelea kwa upana. Amesema unakwenda kuboresha hati za miliki nchini Tanzania, lakini kwenye ripoti yake ukurasa wa 60 ameelezea kuwa amepima vijiji 843.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 wakati Bajeti ya Ardhi ilipopitishwa hapa tulitoa mapendekezo. Mradi huu ulikuwa unapima vijiji 250 kwa muda wa miaka mitano, Bunge likapendekeza, na kwenye mapendekezo ya Kamati tukapendekeza kuwa vijiji viongezwe. Hii ilikuwa ni mwaka 2023. Sasa kitu ambacho ninajiuliza, tangu mwaka 2023 mpaka sasa hivi, ni kama miezi kumi imepita. Leo kwenye ripoti Mheshimiwa Waziri ameandika kwamba tayari wameshapima vijiji 843.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tukiwa kama Kamati, tumetembelea Wilaya ya Ruangwa katika Kijiji cha Nkatila, na huko tukashuhudia utoaji wa hatimiliki kwa kile Kijiji. Pia tulitembelea Maswa. Hivi vijiji vingine 843 hatujavitembelea. Pia ningependa kujua kama hivi vijiji tayari vimeshapewa hati na Tume ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi, kwa sababu naona inakuwa ni ndoto ya ajabu kwa muda wa mwaka mmoja vijiji 843 viwe vimepimwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi inahitaji kama shilingi bilioni 30 ili iweze kupima vijiji, lakini Tume hii imekuwa ikipewa fedha kidogo kwa ajili ya kupima vijiji hivyo. Matokeo yake ni kuwepo kwa migogoro ya ardhi ambayo haiishi Tanzania. Migogoro hii inatokana na sababu kwamba Watanzania wanakuwa hawajui maeneo wakalime wapi au wakafuge wapi. Vijiji vimepimwa lakini havijapangiwa matumizi ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo namwomba Waziri angaalie utaratibu wa kuweka kasi kwenye mradi huu wa LTIP. Katika hotuba yako umeeleza pia kuna ujenzi wa ofisi 25 za mikoa, lakini kwenye Ripoti ya Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba ndiyo kwanza mchakato unaendelea. Mheshimiwa Waziri, huu mradi ni wa miaka mitano, hizi ofisi utazijenga lini kwenye mikoa kwa muda mfupi? Sasa hivi huu mradi una kama miaka mitatu. Mradi umeanza toka mwaka 2022, hii ni 2024 ofisi hazijajengwa, bado zipo kwenye mchakato, mradi wa miaka mitano. Je, kuna uhakika wa kumaliza hizi Ofisi za Ardhi za Mikoa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja, atuambie. Pia Mheshimiwa Waziri kwenye ripoti yake hajaweza hata kueleza huu mradi ambao mpaka sasa una miaka mitatu umetumia fedha kiasi gani? Tunashukuru kwa kliniki, ni za huo mradi, lakini tungependa kupata ufafanuzi, fedha za mradi zimetumika kiasi gani mpaka sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni suala la wale Wafanyakazi wa Mabaraza ambao wamefanya kazi kwenye Ofisi za Ardhi na walishastaafu, lakini hawalipwi fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wafanyakazi sio wengi, lakini wamekuwa wakidai malipo yao kwa muda mrefu sana. Wizara ya Ardhi haiwalipi na hawa watu walifanya kazi kwenye Ofisi za Ardhi kwenye Mabaraza. Ina maana waliisaidia Wizara ya Ardhi, lakini hawalipwi fedha zao. Wamekuwa wakipigwa danadana, leo wameenda huku, kesho nenda huku, tutawatumia cheque, lakini Wizara ya Ardhi haijawekea umuhimu wa kuwalipa wafanyakazi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu walisaidia na walifanya kazi Wizara ya Ardhi, wangewekewa kipaumbele walipwe fedha zao, kwa sababu inaonekana kwamba watu wamefanya kazi wametumika, lakini kwa kuwa hawapo tena kwenye sekta ya ardhi, wanaonekana hawajafanya kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni zile halmashauri ambazo zilikopeshwa fedha kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Zipo halmashauri mbazo zilipewa hizo fedha, zimesharudisha, tunazipongeza sana. Pia zipo halmashauri nyingine zenyewe zimerudisha fedha nusu, bado zinadaiwa na nyingine hazijarudisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba zile halmashauri ambazo hazijarudisha zile fedha ziweze kurudisha ili halmashauri nyingine ziweze kukopeshwa na ziweze kuendelea na utaratibu wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi inapopangwa inaondoa matatizo mengi, lakini fedha hizi halmashauri zilikuwa zimekopeshwa toka mwaka 2021 mpaka leo halmashauri hizo zinaendelea kukaa na mkopo huo na halmashauri nyingine zinashindwa kukopeswa kwa sababu fedha hazijarudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la Wizara ya Ardhi kuweka mfumo unaoeleweka kwa ajili ya bili za ardhi. Kama ilivyo kwenye Wizara ya Maji, mtu anapata bili yake mkononi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha, muda umeisha.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali na kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta Amendment za Sheria ambazo amezitaja leo hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia amendment za Education Act Cap. 353. Napenda nichangie hili kutokana na mambo yafuatayo ambayo yamekuwa yakitokea katika nchi yetu. Kwanza kabisa, kumekuwa na ongezeko la watoto wa mitaani ambapo watoto hawa wanasababishwa na vijana wetu kupata ujauzito kabla ya wakati na wale baba zao wanakimbia, matokeo yake yule binti ambaye amepata huo ujauzito anashindwa kumlea yule mtoto na yule mtoto anaishia mitaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake ni kwamba utakuta miji mingi ya Tanzania kuna watoto, ukienda stendi utakuta kuna watoto wako mitaani; sisi wenyewe tunawaita majina ambayo hayafai kama ombaomba, lakini ni watoto ambao wana baba zao ambao wamewaacha hawakuwalea.
Aidha, unakuta ni baba ambaye alikuwa ni mume wa mtu, amempa ujauzito binti wa shule na anakimbia responsibility za kulea yule mtoto. Kwa hiyo, basi yule baba anakuwa amelinda nyumba yake na amelinda ndoa yake lakini yule binti anakuwa ameharibikiwa na maisha yake moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake binti anapozaa nyumbani, kwanza anakuwa psychologically affected. Ni tatizo kubwa mno ambalo limewa-affect wasichana wengi, wapo wasichana wengi ambao wangeliweza kuendelea na shule mpaka level ya Chuo Kikuu; na wengine labda wangekuwa Wabunge, mpaka Mawaziri lakini waliishia mitaani kwa sababu ya kupata ujauzito wakiwa Form One, Form Two, Form Three au Form Four.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hizo sababu nilizozitaja, naipongeza Serikali kwa kuja na adhabu kali ya miaka 30 jela, labda tu angeniongezea na viboko wakati anaingia na wakati anatoka. Ili kuondoa hili tatizo, mtu atakuwa anafikiria mara ishirini kwenda kuomba urafiki na mtoto wa shule. Itabidi ajishauri sana kuomba urafiki na mtoto wa shule na atamwogopa mtoto wa shule na hii itasaidia sana nchi yetu kuondoa matatizo kwanza ya kuwa na watoto wa mitaani na pili kuwa na hawa watoto ambao tunawapa majina mabaya kwamba ni ombaomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale watoto siyo ombaomba, ni kwa sababu wamekosa malezi nyumbani, wamekosa chakula nyumbani kwa sababu ya kuachwa na baba zao; na wale baba zao utakuta wana nyadhifa na wanazo fedha lakini kwa sababu wanaona aibu kile kitendo cha kuonekana kwamba nilizaa na mwanafunzi, kwa hiyo, wanaamua kukimbia hiyo responsibility.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo, Tanzania imeridhia mikataba ya Kimataifa kama vile The African Charter, The Charter of United Nations; tumeridhia mikataba kama The Convention on Elimination of All Form of Discrimination Against Women, ambayo sisi tumeiridhia pamoja na protocol yake. Kwa hiyo, lazima tuende na hiyo mikataba ya Kimataifa ili na sisi nchi yetu itoe haya matatizo ambayo yanawakabili watoto sasa hivi. Kwa hilo, naunga mkono hoja Serikali miaka 30, hundred percent. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la usafirishaji. Watu wanaosafirisha binadamu, naomba pale kwenye adhabu ya shilingi milioni 20 iongezwe, kwa sababu tumekuwa tunaona matatizo mengi, watu wanasafiri kutoka nchi nyingine wanakuja wanakwama humu nchini, wengine wanakufa, unakuta wanatelekezwa humo njiani, wanakufa na njaa, wanaishia hapo, hawafiki kwenye nchi zile walizokuwa wanataka kwenda.
Kwa hiyo, matokeo yake unakuta kwamba Tanzania imepokea wahamiaji wamefia humu Tanzania, Serikali inaingia gharama la kuwazika na kutafuta kujua walitokea nchi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naona hii faini ya shilingi milioni 20 ni ndogo sana. Labda mtu alikuwa amewaambia atawasafirisha wale watu atalipwa shilingi milioni 100, ukimwambia alipe shilingi milioni 20 atashindwa nini? Atailipa tu. Naomba hii faini ya shilingi milioni 20 iongezwe atleast hata kama ingekuwa shilingi milioni 50 au shilingi milioni 100 ili mtu apate uchungu kwamba nikishikwa nasafirisha binadamu, nitapata adhabu kali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa pia nizungumzie suala la Anti-terrorism, naomba niunge mkono hoja ya Serikali ya Anti-terrorism Act kwa sababu zifuatazo: sasa hivi huku duniani kumekuwa na mambo ya ugaidi yanayoendelea, watu wanaamua kujitoa mhanga, kujilipua na kupoteza maisha ya innocent people ambao hawana makosa yoyote. Mtu anaweza akaamua akajilipua kwenye treni, stendi, super market na anaua watu ambao hawana hatia.
Kwa hiyo, hii amendment ya Anti-terrorism Act ambayo imeletwa sasa hivi, kwa kutoa hiki kifungu, naomba kuunga mkono hoja hicho kifungu ili hata wale watu ambao watakuwa wanahifadhi hao magaidi ambao wamo humu nchini watakuwa wanajifikiria mara mbili kwamba nikishikwa nitapata adhabu hii kulikoni na kinyume kwamba hapa zamani ilikuwa haioneshi kwamba mtu akishikwa amehifadhi gaidi anatakiwa afungwe miaka mingapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa na hii Sheria watu watoogopa kuhifadhi magaidi. Maana mtu hata kama ndugu yake ni gaidi, itabidi amkimbie asimhifadhi na wala asimsaidie kwa chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sheria na ndiyo mambo yanayoendelea duniani kote, kupinga ugaidi na kama tunavyojua, nchi ziliambiwa zitoe msimamo aidha zinapinga ugaidi au hazipingi ugaidi. Nasi Tanzania tuna-support kupinga ugaidi duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya…
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Muswada huu.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nitoe pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake thabiti wa kulileta suala hili kwa wananchi wa Tanzania na kuangalia vipengele ambavyo viko kwenye Sheria ya Madini ambavyo havimnufaishi Mtanzania kuvileta hapa Bungeni ili tuweze kuvitungia sheria mpya. Nampa pongezi za pekee yake kwa sababu ni Rais aliyethubu kuweka wazi suala la Sheria ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichukue nafasi kumpongeza Waziri wa Katiba na Sheria na timu yake yote kwa kazi waliyofanya mpaka kufanikisha Sheria hii ya Madini sasa hivi tunaweza kuijadili humu Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie mawili matatu kuhusu Muswada huu. Muswada huu ni mzuri sana kwani unaenda kuondoa zile sheria zote mbovu ambazo zilikuwa hazimnufaishi Mtanzania na kuleta sheria mpya zitakazomnufaisha Mtanzania. Pia Muswada huu unakwenda kuweka umiliki wa madini ambao utakuwa chini ya ungaalizi wa Mheshimiwa Rais. Ukienda section 5(1) utaona kwamba madini yatakuwa chini ya trust ya Mheshimiwa Rais. Ukienda kwenye kipengele cha 5(a) utakuta kwamba kuna udhibiti wa maeneo ya madini. Hapo zamani wachimbaji wa madini maeneo yao yalikuwa hayadhibitiwi lakini sasa hivi yale maeneo ya madini yatakuwa na ulinzi wa Serikali. Naomba nipongeze kwa kuweka kipengele hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kipengele cha 20, utakuta kuna Kamishna wa Madini. Pia kwenye kipengele cha 21 cha Muswada hii utakuta itanzishwa commission ambayo itakuwa na Katibu Mkuu kutoka Hazina, Katibu Mkuu kutoka Ardhi, Katibu Mkuu kutoka Ulinzi, Katibu Mkuu kutoka Serikali za Mitaa, Katibu wa Chamber of Minerals and Energy, Naibu Mwanasheria Mkuu na watu wawili mashuhuri ambao Rais atawateua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sisi kwenye Kamati yetu tulitoa hoja kwamba wachimbaji wadogo wawe mwakilishi kwenye commission hii. Hiyo italeta faida sana kwa wachimbaji wadogo ambao mara nyingi huwa wanavumbua maeneo yao baadaye yanachukuliwa na wachimbaji wakubwa. Wale wachimbaji wadogo kwa kuwa na mwakilishi kwenye commission hii wataweza kutetea maslahi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze pia kuleta kipengele ambacho kinalazimisha yale makampuni kutumia bidhaa za Tanzania. Pia kunufaisha vijana wetu ambao watakuwa wanapata training kwenye hayo makampuni. Hii itasaidia vijana wetu waweze kuajiriwa kwenye makampuni hayo kwa sababu watakuwa wamepata uzoefu wa kufanya kazi kwenye makampuni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuletwa Muswada huu kwa dharura, napenda kusema kwamba dharura ndiyo inamfanya mtu aweze kubadilisha kitu kama huna dharura huwezi ukabadilisha kitu. Kwa hiyo, kwa dharura iliyokuwepo ndiyo imefanya Muswada huu uje tuubadilishe sasa hivi ni sahihi kabisa kwa sababu kusingekuwa na tatizo kusingekuwepo dharura ya kuja kubadilisha Muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda nitoe ushauri kuhusu haya makampuni yanapokuja kuchimba madini. Naomba umiliki ule wa leseni, hisa za kampuni zianzie kwenye leseni ina maana ile kampuni ya kigeni inapokuja nchini kuchimba madini ishirikiane na Serikali ianzishwe kampuni ambayo ita-regulate zile hisa za Serikali na zile hisa za makampuni. Mfano mdogo ni kuangalia kampuni ya Acacia inachimba madini kule Buzwagi, Bulyankulu na North Mara lakini…

(Hapa kengelee ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Muswada huu. Napenda kuipongeza Serikali kwa kuja na marekebisho ya sheria hizi. Ningeomba tu Serikali iendelee kuboresha Muswada huu kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili uweze kukaa vizuri zaidi. Hii ni kwa sababu kanuni ya kushirikisha wadau ni kanuni ya 84 na Ibara ya Katiba ya 8 na 21 inatuambia kwamba tunapotunga sheria lazima tushirikishe wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu sheria hizi zinakwenda kutumika kwa wananchi wote wa Tanzania. Sisi tukiwa kama wawakilishi wao tunakuja tu kuleta mawazo ya wananchi wanasemaje, lakini tunapowaleta wadau kuja kutoa maoni yao kuhusu sheria fulani inasaidia kuelewa zaidi undani wa sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niipongeze Serikali kwa kubadilisha umri wa kustaafu kwa Maprofesa na Madaktari, kutoka umri wa miaka 55 mpaka 60 kwenda umri wa miaka 60 mpaka 65. Naipongeza Serikali kwa sababu hizi profession za udaktari na uprofesa unaweza ukasema ni rare professions kwa sababu si kila mtu anaweza kufika level ya uprofesa na sio kila mtu anaweza akafika level ya kuwa daktari bingwa. Kwa hiyo ili tuweze kuwatumia hawa madaktari bingwa vizuri na tuweze kuwatumia maprofesa wetu vizuri, naipongeza Serikali kwa kubadilisha huo umri kutoka miaka 60 mpaka miaka 65.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata kule UN sasa hivi wanastaafu wakiwa na miaka 65 na voluntary retirement ni miaka 62. Kwa hiyo, kwa kuleta Muswada huu ni muafaka, sisi tungebaki peke yetu kufika kwenye miaka kustaafu na miaka 55. Kwa kuja na wazo la miaka 60 mpaka 65 kwa maprofesa na madaktari ni wazo jema. Tena nafikiri kwa profesa na daktari kwa sababu mtu akishajifunza kitu kinakaa kichwani maisha na hakibadiliki labda Serikali ingefikiria kutoka 65 kupeleka 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu unamkuta profesa ana miaka 72 lakini bado ana nguvu zake, anastaafu Serikalini na anakwenda kufanya kazi kwenye private institution. Tunavyo vyuo vya private unakuta profesa ametoka pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini unamkuta amekwenda pale Tumaini University anafundisha au amekwenda university nyingine kama za Makumira kule Arusha anafundisha pale. Sisi kama Wabunge tunatakiwa tulifikirie hili na tu-support Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Serikali inaweza siku nyingine ikaja na miaka 65 kwenda 70 kwa maprofesa na madaktari. Hii ni kwa sababu ujuzi wanakuwa nao kichwani na ujuzi wa mtu unakaa lifetime, si kwamba mtu anazeeka anatoa ujuzi, mtu anapokuwa mzee nafikiri ule ujuzi ndio unazidi kushamiri vizuri pale kichwani kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali kwa kuja na marekebisho ya ibara ya 120 na naipongeza Serikali kwa kuwa haijafanya marekebisho kwenye zile hati za kimila ila ningeomba baadaye Serikali ifikirie pia kuweka sheria, kuzijumuisha zile hati za kimila ili wazawa wa Tanzania na wananchi wa vijijini waweze kutumia zile hati zao za kimila kupata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu katika Muswada huu hati za kimila hazipo, hazihusiki kwenye Muswada huu, lakini kwa baadaye kadri Serikali itakavyoona, kwa sababu wananchi wengi walio na mashamba makubwa wengi wameyarithi kutoka kwa wazazi wao. Shamba unakuta lilikuwa la babu yake ndio pale ambapo kila kitu kipo, makaburi ya babu zake yapo pale, ni mashamba ambayo wamegawana pale kiukoo na wana hati ya kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa baadaye Serikali iangalie jinsi gani ya kujumuisha hizi hati za kimila ziweze kutumika ili wananchi wa vijijini nao waweze kutumia hati zao za kimila kupata mikopo benki na kuweza kupata mitaji ya kufanyia biashara kubwa. Pia wananchi wa vijijini wapate opportunity ya kuweza kuwekeza nje ya nchi kwa kutumia hati zao za kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kufuata maoni ya Kamati ya Katiba na sheria kwa kuondoa kifungu namba 25B ambacho kilikuwa kinampa mamlaka Waziri kutoa maoni yake kwamba mtu anapotaka kustaafu kilikuwa kinampa power Waziri ya kuweza ku-determine umri wa mtumishi kustaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu ulipokuja kwenye Kamati yetu, tulipendekeza kwamba kifungu hiki namba 25B kiondolewe kwa sababu Waziri mhusika anaweza akakitumia vibaya, anaweza akawa hampendi profesa fulani au hampendi mwajiriwa fulani akakitumia vibaya kwa sababu ana mamlaka ya kuongea na Rais akapendekeza kwamba yule mtu astaafishwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hiki kilipokuja kwenye Kamati yetu tulipendekeza kwamba kiondolewe kwa sababu tuliona kwamba kwanza kina ubaguzi halafu kinampa Waziri excess power ambayo anaweza akaitumia vibaya. Nashukuru katika marekebisho yaliyowekwa hapa kwenye jedwali, Serikali imekuwa sikivu na imekiondoa kifungu hiki. Sababu zilizofanya tukiondoe zilikuwa ni sababu hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali hapo baadaye iendelee kuongea na wadau wa benki, nikimaanisha kwamba benki tofauti, iendelee kujadiliana nao kuhusu suala la wakopaji. Katika Muswada huu tumeona kwamba benki wanao wajibu wa kupeleka ripoti Serikalini kuhusu pesa ambazo wanamkopesha huyo mtu aliyeenda kukopa pesa na kuweka dhamana ya shamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifano mingi ambayo tumeona, yapo mashamba mengi ambayo watu wanazo hati za hayo mashamba na wameweza kwenda benki na wakachukua pesa nyingi benki na baadaye tumeona kwamba wale watu ambao wapo nje ya Tanzania wamekuwa ni mabilionea kwa kutumia ardhi ya Tanzania kupata huo ubilionea. Wameweza kutumia haya haya mashamba yetu yalipo humu nchini, wamepewa yale mashamba, walipewa hizo hati miliki na wakazipeleka benki wakachukua pesa. Baada ya hapo wameenda nje wanafanya biashara nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe sasa Serikali kwa kutumia Muswada huu na kwa kutumia sheria hii itakapopita iweze kuwafuatilia wale wote ambao walichukua mashamba humu nchini Tanzania na wakachukua hizo hati wakaenda benki wakazoa mamilioni ya pesa na sasa hivi ni mabilionea nje ya nchi hii ya Tanzania; wawafuatilie ili waweze kurudisha hizo pesa zetu. Nafikiri sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria hii baada ya kupita tunaiomba Serikali ichukue jukumu la kurudisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja a hundred percent.
Muswada wa Sheria ya Usuluhishi wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Kamati yangu ya Sheria Ndogo kwa kushughulikia huu Muswada kwa muda wa siku kumi mpaka hapa ulipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta Muswada huu wakati muafaka, wakati tunauhitaji kwa sababu Sheria ya Arbitration iliyokuwa inatumika ilikuwa ni sheria ya muda mrefu ambayo ilitungwa na Wakoloni, yaani watawala wetu toka mwaka 1931. Sasa kwa kuleta sheria hii, kubadilisha hii sura ya 15 kwa kuleta Sheria ya Usuluhishi inaifungua nchi yetu ili kushirikiana na nchi nyingine katika kutatua migogoro ambayo itajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria iliyokuwepo mwanzo ilikuwa haitekelezi yale matakwa ya usuluhishi wa Kimataifa. Kwa kuja na sheria hii wawekezaji wengi watashawishika kuja nchini Tanzania kuwekeza kwa sababu tumefungua uwigo wa kusuluhisha matatizo yetu nje ya Tanzania na ndani ya Tanzania kwa kutumia sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia niipongeze Serikali kwa kuja na wazo la kufungua Arbitration Centre katika Ibara ya 77. Kama nilivyosema hii Arbitration Centre itatusaidia sana kuleta wawekezaji wengine kwa sababu walikuwa wanaogopa kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa sababu tulikuwa hatuna Arbitration Centre ambayo inapotokea matatizo yoyote wanashindwa waende wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika kuanzisha hii Arbitration Centre, naiomba Serikali ijaribu kutunga sheria ambayo zitai-guide hii Arbitration Centre kama zilivyo Sheria za TIC lakini pia itunge rules ambazo zitaendana na hii Arbitration Centre. Zaidi ya hapo naiomba Serikali ije na Sera ya Usuluhishi kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali ya Tanzania haina Sera ya Usuluhishi wa Migogoro. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijitahidi ije na hiyo sera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Serikali isomeshe vijana wetu kwa kiwango cha juu ili wanapokwenda kuitetea nchi yetu kwenye migogoro ya Kimataifa waweze kwenda kutuwakilisha vyema kwa maana ya kwamba Serikali itumie rasilimali zake kuwasomesha vijana suala la kusuluhisha migogoro ya Kimataifa. Tumeona mambo mengi yametokea, vijana wanapokwenda ku-defend case zetu huko nje, wakati mwingine zipo case ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishindwa kwa sababu tu ilikuwa vijana wetu hatujawapeleka kwenye hilo eneo sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda napenda nizungumzie Ibara ya 13 ya Muswada huu, Ibara hii inazungumzia consequence ambapo kuna marekebisho ya sheria kama criminal procedure pamoja na civil procedure. Katika ile Ibara ya 93 ukienda nayo ukiisoma moja kwa moja mpaka ile subsection ya pili nafikiri wajumbe mnazo unakuta kuna mahali ambapo imetoa room kwa migogoro ambayo inatokea ya domestic violence kusuluhishwa nje ya Mahakama. Ninaona kuweka room ya kusuluhisha migogoro ya domestic violence nje ya Mahakama tutakuwa tunarudisha nyuma mambo ya gender ya wanawake ambayo tumekuwa tukiyapigania siku zote mpaka tukaweka ile sheria ya sexual violence. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kumewekwa room kwamba ile domestic violence inaweza ikatumika vibaya, maana yake mtu anaweza akampiga mke wake hata akamvunja mguu lakini akaruhusiwa kutoa ile case Mahakamani. Naomba Serikali ijaribu kuainisha hizo domestic violence ambazo inataka kuzitoa kwenye kusuluhishiwa nje ya Mahakama ni domestic violence za aina gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Ibara ya 107 ya Katiba ya Sheria ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania inaruhusu ule usuluhishi, inaruhusu haki kuipata Mahakamani. Sasa tungeomba Serikali inapotuambia kwamba domestic violence zinaweza zikasuluhishwa nje za Mahakama, ni domestic violence za aina gani? Je, mtu hata akivunjwa mkono, basi aombwe msamaha aitoe ile case Mahakamani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)