Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Taska Restituta Mbogo (32 total)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mradi wa maji wa Ikorongo umeshindwa kutosheleza mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Mpanda; Kuna vijiji 20 vilivyoko Wilaya ya Nsimbo havina maji; kuna vijiji 13 na vitongoji viwili vilivyoko pale Mpanda Mjini havina maji; kuna vijiji tisa vilivyoko Wilaya ya Tanganyika, havina maji. Je, Serikali ni lini itachimba visima kwenye vijiji hivi na Kata hizi ili imtue ndoo mwanamke wa Mkoa wa Katavi?
Swali la pili; Mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika ni programu ya muda mrefu ambayo haiwezi ikatekelezwa leo au kesho na wananchi na akinamama wa Mkoa wa Katavi wanaendelea kuteseka: Je, Waziri anaweza akatueleza hiyo programu ya kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika itaanza lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwamba mradi wa Ikorongo haujitoshelezi, ni kweli. Mradi wa Ikorongo unatoa lita milioni 3.5 kwa siku wakati mahitaji ya Mji wa Mpanda pekee ni lita milioni 11 kwa siku. Kwa hiyo, kuna upungufu mkubwa. Wakati tunasubiri huu mpango wa muda mrefu, tumeendelea na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya vijiji ambavyo amevitaja. Kwa mfano, tayari tumeshachimba visima katika Halmashauri ya Nsimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaendelea kuchimba visima katika Halmashauri ya Mpimbwe na tayari tumechimba visima katika Halmashauri ya Mlele na Halmashauri ya Tanganyika, sasa hivi tunaendelea kufanya mazungumzo nao ili tuweze kupeleka fedha kwa ajili ya kuchimba visima ikiwa ni hatua ya muda mfupi.
Swali la pili; Mpango huu wa muda mrefu unaanza lini? Mpango huu unaanza katika mwaka wa fedha 2017/2018. Tumeshapokea maandiko tayari, kwa hiyo, katika bajeti inayokuja, tuombe tu Mheshimiwa Mbunge na wewe upitishe hiyo bajeti ili tuweze kuweka Mhandisi mshauri aweze kusanifu ili kuandaa Makabrasha ya Zabuni ya kutoa maji kutoka Karema katika Ziwa Tanganyika kuleta Mji wa Mpanda na kutoa maji upande wa Sumbawanga kuleta Mji wa Sumbawanga kutoka kule Kasanga.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya mahusiano ya ujirani mwema TANAPA Mkoani Katavi wamejitolea kuchimba visima kwenye vijiji vitatu ambavyo ni Kijiji cha Matandarani, Igongwe na Stalike lakini condition yao ni wanakijiji wachangie 30%. Gharama ya hivyo visima ni milioni 21, asilimia 30 itakuwa kama kwenye shilingi milioni saba, wanakijiji watatakiwa wachangie ili waweze kuchimbiwa hivyo visima vitatu. Je, TANAPA ili kudumisha mahusiano mema na Mkoa wa Katavi na ukizingatia kwamba kule mkoani kwetu vipato viko chini, wananchi hawana uwezo wa kuchangia hiyo shilingi milioni saba, inaonaje ikachukua hiyo gharama ikachimba bila kuwachangisha wananchi?Hilo swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, ni lini TANAPA itajenga hoteli ya nyota tatu katika Mkoa wangu wa Katavi ili tuweze kupata watalii kutoka nje na ndani ya nchi? Nauliza hivyo kwa sababu mkoa hauna hoteli ya nyota tatu ambayo inaweza kuwawezesha wageni kutoka nje kuja kutalii mkoa wetu na kuangalia huyo twiga mweupe ambaye hapatikani duniani kokote isipokuwa Mkoa wa Katavi?Ukizingatia kwamba sasa hivi uwanja wetu ni mzuri…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza la uchangiaji kwenye utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema na nafikiri niweke vizuri tu hapa kwamba, TANAPA hawajitolei bali wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwamba pale ambapo kuna wananchi wanaishi jirani na maeneo ya hifadhi, mahali ambako utalii unafanyika tunao wajibu wa kuweza kutekeleza miradi mbalimbali chini ya utaratibu wa ujirani mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango tulioweka wa kuchangia unawafanya wananchi waweze kwanza kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uhifadhi lakini pia kujisikia kwamba na wenyewe ni sehemu ya uhifadhi lakini sehemu pia ya kufanya shughuli za maendeleo. Kwa hiyo, kwa kuwa utaratibu huu uko kwa mujibu wa kanuni, ikiwa Mheshimiwa Mbunge ana maoni bora zaidi ya haya aliyotuambia au ana namna bora zaidi ya kueleza kwa kirefu maoni hayo, basi anaweza kuyaleta Wizarani tukapitia utaratibu mzima wa utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, je, ni lini TANAPA itajenga hoteli ya nyota tatu Mkoani Katavi na kwa kweli anauliza kwamba kwa nini TANAPA wasijenge hoteli ya nyota tatu ili kuweza kuboresha shughuli za utalii Mkoani Katavi. Kwa ufupi tu ni kwamba, Serikali haijengi hoteli kwa ajili ya matumizi ya watalii au kwa ajili ya matumizi mengine yoyote kwenye sekta ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wawekezaji ambao wanatoka private sector kuweza kuwekeza kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge aungane na Serikali kuwashawishi wadau kutoka mahali popote pale waweze kuja kwenye Mkoa wa Katavi kuwekeza na kujenga hoteli si ya nyota tatu tu, hata kama wanaweza ya nyota nne, nyota tano, ili mradi kuwe na mazingira ambayo yatawawezesha watalii kuvutiwa na kuja kutalii wakiwa katika hali ambayo ni bora zaidi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa ajili ya usalama wa nchi kwa kawaida viwanja vya ndege vinatakiwa viendeshwe na Agency za Serikali ambazo ni TCAA na TAA pamoja na Taasisi ya Meteorological . Taasisi hii ya KADCO ni kampuni, sasa swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, Kampuni ya KADCO itaunganishwaje na TAA kama alivyoeleza kwenye majibu yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini ndege za Bombardier zitashuka Wilayani Mpanda, Mkoani Katavi maana tunazihitaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika jibu langu la msingi nimeeleza tu kwamba, KADCO ni Shirika la Umma ambalo linamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, siyo kitu cha ajabu kuunganisha KADCO na TAA kwa sababu zote zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, zote ni taasisi za Serikali na zikiunganishwa tutapata uongozi wa aina moja na bodi ya aina moja ambayo itarahisisha sana menejimenti ya viwanja vya ndege kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, tuko kwenye harakati za kupanua uwanja wa ndege wa eneo hilo. Kwa hiyo, tutakapopanua uwanja wa ndege wa eneo hilo Mheshimiwa Mbunge, ndege za Bombardier zitaanza kushuka. Tuna lengo la kuhakikisha kwamba viwanja vyetu vyote vya ndege vinaongezwa ubora wake na ukubwa ili ndege zote ambazo zina ukubwa wa kutosha ziweze kutua kwa ajili ya kuhudumia Watanzania. Ahsante.
MHE. TASKA R MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo ya Mkoa wa Geita yanafanana na matizo ya Mkoa wa Katavi. Mkoa wetu wa Katavi hauna Hospitali ya Mkoa na hauna pia Hospitali ya Rufaa.
Je, ni lini sasa Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi na kuleta Madaktari Bingwa wa magonjwa mbalimbali kama upasuaji wa macho, meno kwa sababu siku nyingine watu wanavimba ufizi wanashindwa kupasua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mkoa wa Katavi nimeutembelea ikiwa ni sehemu ya Mikoa 12 ambayo nimetembelea ndani ya miezi minne tangu nimeteuliwa kuwa Naibu Waziri. Nimeiona changamoto hiyo katika Mkoa wa Katavi, lakini kama nilivyojibu katika swala langu la msingi ni kwamba sasa hivi Serikali imechukua majukumu ya kuendesha Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachokuomba Mheshimiwa Taska Mbogo na Wabunge wengine wa Mkoa wa Katavi ni kuendelea kuihimiza Serikali yetu ya Mkoa kuhakikisha kwamba wanatenga eneo na kuanza maandalizi ya awali na sisi kama Serikali tutaendelea kujipanga kuhakikisha kwamba tunajenga Hospitali ya Rufaa ya Katavi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme wa gridi mpaka kufika Mkoa wa Katavi utachukua muda mrefu; na kwa kuwa umeme hautoshi Mkoani Katavi, lakini pia napenda kuishukuru Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi kwa ujenzi wa jenereta mbili na jenereta hizo zimeanza kufanya kazi kutoka tarehe 27 Mei, 2017 , lakini jenereta hizo hazitoshi.
Mheshimiwa Spika, umeme unaotakiwa Mkoa wa Katavi ni megawati tano, jenereta zinazalisha megawati 2.2. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza jenereta nyingine mbili kwa Mkoa wa Katavi? Kwa sababu mahali pa kuzifunga jenereta hizo tayaripameshajengwa, maana eneo la hizo jenereta limejengwa sehemu za kufunga jenereta nne, lakini Serikali pamoja na Serikali ya Uholanzi imefunga jenereta mbili, eneo hilo lipo. (Makofi)
Meshimiwa Spika, je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza jenereta mbili?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa jenereta hizi zinatumia mafuta ya dizeli na ni gharama zaidi, je, Serikali haioni kwamba matumizi ya jenereta kwa Mkoa wa Katavi ni gharama zaidi kuliko kufunga umeme wa gridi? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, maswali yake ni mazuri na kwa faida ya Mkoa wa Katavi ambao na mimi mwenyewe natoka kule siwezi kuahidi lakini niseme kwamba nitalifikisha hili ili waweze kuongeza jenereta nyingine mpya kuongeza umeme. Lakini pia haya masuala ni ya kiuchumi. Ipo historia kwamba matumizi ya umeme katika mkoa wetu, hasa katika masuala ya viwanda bado hatujawa na viwanda vingi, kwa hiyo umeme sehemu kubwa unatumika majumbani tu na taarifa iliyopo ni kwamba TANESCO imekuwa inatoa gharama kubwa zaidi kuliko makusanyo yanayofanywa kutokana na matumizi ya umeme, lakini suala hili tutalifikisha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili linalozungumzia dizeli. Ni kweli kabisa kwamba kutumia dizeli ni gharama kubwa kabisa na ndiyo maana sasa hivi Serikali nzima inataka kwenda kwa kutumia umeme ama wa gesi au wa maji, na ndiyo maana sasa Serikali imeshalitambua hili, inaleta umeme wa msongo mkubwa ambao sehemu kubwa utatumia uzalishaji kwa kutumia maji badala ya kutumia dizeli. Kwa hiyo, mawazo yako Mheshimiwa Mbunge ni mazuri na tayari Serikali imeshaanza kuyatekeleza.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum ni Wabunge sawa na Wabunge wa Majimbo, hivyo basi, Serikali haioni kwamba kuwanyima Wabunge wa Viti Maalum kuhudhuria kwenye Kamati za Fedha inawasababisha wasielewe mipango ya fedha kwenye Halmashauri zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini basi hii sheria isiletwe humu Bungeni ikabadilishwa ili kuweka usawa na kuondoa ubaguzi wa jinsia kwa sababu kutomruhusu Mbunge wa Viti Maalum kuingia kwenye Kamati za Fedha ni ubaguzi wa jinsia ya mwanamke na mwanaume ambayo inaanzia kwenye sheria zetu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, ni kweli kama alivyosema ni vigumu sana kujua kwa kina yale ambayo yamejadiliwa na kikao husika kama wewe siyo Mjumbe. Hiyo ni kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu kwa nini Serikali isilete Bungeni marekebisho ya sheria ili kusudi Wabunge wa Viti Maalum wawe Wajumbe, naomba tu nilipokee hili sasa kwa niaba ya Serikali ili tukalizungumze ndani ya Serikali kwa kuwa Vyama vya Siasa ambavyo viliwateua Wabunge wa Viti Maalum na kila Mbunge wa Viti Maalum amepangiwa Halmashauri fulani ya kuhudhuria vikao na kupiga kura. Basi nadhani hiyo inaweza ikawa ni mwanzo mzuri wa kuangalia ni namna gani tuweze kuleta marekebisho ya hiyo sheria. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa wapo watoto ambao wanamaliza elimu ya msingi hawajui kuandika wala kusoma. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kila mtoto wa Tanzania anapomaliza elimu ya msingi ambayo ni darasa la saba anajua kusoma na kuandika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa wapo watu wazima wenye umri na wazee labda umri kama wangu pia hawajui kusoma kutokana na mazingira labda waliyokuwa labda maeneo yao yalikuwa hayana shule. Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha elimu ya watu wazima iliyokuwepo hapo zamani miaka 1973 ili watu hawa waweze kusoma na kuandika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbogo kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize tu kwamba Serikali imeendelea kutoa hamasa na kuwafuatilia walimu, lakini vilevile kuhakikisha kuwa watoto waweze kusoma na kuandika pale wanapokuwa hasa elimu ya msingi na hivyo kwa sasa mtoto inapofikia darasa la tatu ikigundulika hajui kusoma na kuandika imekuwa akipewa mpango maalum wa kumsaidia na kumuwezesha kuweza kumudu masomo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya watu wazima nikubaliane naye kwamba kweli Tanzania bado tunalo kundi kubwa takribani 20% ambao hawajui kusoma na kuandika. Kuna programu mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendelea kupitia elimu ya watu wazima ambapo wanapewa baadhi ya mafunzo ya kujitegemea, lakini vilevile nipende kusisitiza kwamba kila Mtanzania ambaye hajui kusoma na kuandika awe na kiu ya kuweza kujifunza kusoma na kuandika kwa sababu sasa elimu imeshakuwa karibu kila mahali hasa katika maeneo yetu tunayoishi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mila na desturi za makabila yetu ya Tanzania zinaendelea kupotea kwa kasi kubwa; na kwa kuwa vijana wetu wameingia kwenye utandawazi wa kuiga mila za kigeni mpaka wanaiga mambo ambayo sio utamaduni wetu. Kwa mfano, kumekuwa na wimbi la vijana wa Tanzania kutaka mabadiliko ya ndoa za jinsia moja, mwanaume kwa mwanaume au mwanamke kwa mwanamke ambazo siyo desturi na mila zetu za Tanzania kama jinsi tunavyoishi na makabila yetu yalivyo. Je, ni lini Serikali itawatambua rasmi Machifu na Watemi ili waweze kutoa mchango wao kwenye jamii kurekebisha na kufundisha mila na desturi zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mikoa mingi ya Tanzania haina nyumba za makumbusho za kuhifadhi hizo kanzidata za mila na desturi za makabila tofauti. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za makumbusho kwenye mikoa yote ya Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Restituta Mbogo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ametaka kujua ni lini Serikali itawatambua rasmi Machifu pamoja na Watemi. Niseme kwamba si kwamba Serikali haiwatambui Machifu pamoja na Watemi ambao tunao na ndiyo maana katika shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali watu hawa wameendelea kualikwa ikiwepo shughuli ya Mwenge. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali inawatambua na itazidi kuwatambua Machifu na Watemi kwa sababu ni njia mojawapo ya kuendelea kuenzi na kudumisha mila pamoja na tamaduni zetu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kujua kwamba ni lini Serikali itajenga maeneo ya makumbusho kwa ajili ya kuhifadhi mila na tamaduni. Kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba sisi kama Serikali ni waratibu pamoja na wasimamizi wa sera na sheria zinazohusiana na masuala mazima ya utamaduni, wamiliki wakubwa wa utamaduni ni jamii kwa maana ya wananchi. Kwa hiyo, ni jukumu letu sisi sote kuhakikisha kwamba tunashirikiana pamoja na Serikali kujenga na kudumisha mila na tamaduni za Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pia kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, nitoe wito kwa mashirika yote ya umma na ya kiserikali na watu binafsi kuhakikisha kwamba tunashirikiana kwa pamoja kudumisha mila pamoja na tamaduni ikiwepo suala ambalo ni muhimu sana la kujenga makumbusho kwa ajili ya kuhifadhi mila pamoja tamaduni zetu. Ahsante.

WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda tu niongeze kwamba wiki iliyopita nilipata bahati kubwa ya kuhudhuria Maadhimisho ya Kituo cha Kumbukumbu ya Utamaduni wa Kabila la Wasukuma huko Bujora, Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilichonifurahisha sana ni ushiriki mkubwa wa Machifu wa Kisukuma, wote walikusanyika pale. Wana Umoja wao unaitwa Bubobatemi-Babusukuma. Waliweza hata kunipa cheo pale kuwa Manji Mkuu wa ngoma moja pale na ni cheo kikubwa sana hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tu kusisitiza kwamba nafasi ya Machifu katika kudumisha utamaduni wa Tanzania tunaiona. Nadhani hili suala tutaendelea kuliangalia kwa umakini na kulileta lipate mjadala mpana tuweze kuiona nafasi yao kabisa ambayo itaweza kujikita hata kisheria.
Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge wametoa mchango mkubwa sana katika hili eneo hasa tukizingatia ukuzaji wa utamaduni Mkoa wa Songea, Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, Tamasha la Utalii Nyasa; Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, Majimaji Selebuka; Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye kila mwaka naye anaazimisha ngoma za kiutamaduni Mkoa wa Mbeya. Ningeoomba Waheshimiwa Wabunge wote tuingie katika kuhamasisha utamaduni katika maeneo yetu. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, ninayo maswali maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa pamoja unatumika tu kwa mbolea za DAP na UREA. Je, ni kwa nini sasa Serikali isitumie mfumo huu kwa kuagiza mbolea nyingine za NPK, CAN, SA na pembejeo nyingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi ni umbali wa kama kilimita 1,500 kutoka Dar es Salaam, kwa hiyo, mbolea inaposafirishwa na magari inakuwa na bei juu zaidi.

Ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kusafirisha mbolea hiyo kwa njia ya treni ili mkulima wa Mkoa wa Katavi apate bei nafuu ya mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Taska Mbogo alitaka kujua kwa nini Serikali tusitumie Mfumo huu wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) kwa mbolea zingine kama NPK, CAN na SA. Kwanza, mfumo huu tumeanza kuutumia mwaka jana na umeonyesha matokeo mazuri. Tusingeweza kuingiza mbolea zote kwa wakati mmoja lakini baada ya mafanikio tuliyoyaona katika mfumo huu, mwaka huu tumeshaanza kuutumia mfumo huu kwa ajili ya mbolea ya NPK kwa wakulima wa tumbaku na sasa tutaendelea na utaratibu ili kuingiza mbolea tajwa, viuatilifu na pembejeo zingine katika mfumo wa BPS ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea kwa haraka na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anasema kwa sababu Mkoa wa Katavi uko mbali na Dar es Salaam, ni vizuri tungesafirisha mbolea hizi kwa njia ya treni ili kupunguza gharama za usafiri. Tunachukua mawazo haya na tulishayafanyia kazi, tangu mwaka jana kama nilivyosema hii mbolea ya NPK tuliisafirisha kwa kutumia treni na gharama za usafiri zilishuka na mbolea hii kufika kwa wakulima kwa wakati. Mawazo yake tunayachukua ili tuyahamishie katika mazao mengine. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tayari tumeshalielekeza Shirika letu la Reli Tanzania ili kutoa kipaumbele kwenye kusafirisha bidhaa ya mbolea ili kushusha gharama za usafiri.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba wapo Watanzania zaidi ya milioni moja wanaishi nje ya Tanzania kama diaspora. Sheria ya Citizenship ya Tanzania inakataza uraia pacha. Je, ni lini Serikali ya Tanzania itabadilisha sheria hiyo na kuruhusu uraia pacha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2014 Serikali ya Tanzania ilitoa uraia kwa wageni waliokuwa wanaishi kama wakimbizi 150,000 nchini Tanzania. Je, Serikali haioni kwamba kutoruhusu uraia pacha tunawanyima haki Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuja kushiriki na kujenga nchi yao na kukaa na ndugu zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo kwa swali lake zuri la msingi lakini na maswali yake mazuri mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu kubadilisha sheria ili kuruhusu uraia pacha. Suala la uraia pacha ni la Kikatiba, kwa hiyo kabla hatujaongelea sheria tunapaswa kwanza tukaongelee Katiba. Mchakato wa kubadilisha Katiba bado unaendelea, pale Katiba itakapobadilika na kuruhusu uraia pacha ndipo tutakwenda kurekebisha Sheria ya Uraia Na.6 ya mwaka 1995 ili kuongeza kipengele cha kuruhusu uraia pacha.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anasema kwamba hatuoni kwamba kuzuia uraia pacha tunanyima haki. Watanzania hawa ambao wako nje tunaowaita diaspora, bado wanaendelea kufurahia haki nyingine ambazo zimetolewa hapa Tanzania ikiwemo haki ya kuwekeza kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 na haki nyingine ambazo wangeweza kuzipata.

Kwa hiyo, tunashauri kwamba Watanzania hawa kwa hivi sasa na ambao wamefanya kazi nzuri sana kama ambavyo nimeeleza, ikiwemo kuleta misaada mingi sana katika huduma za afya na baadhi ya Majimbo kama Chakechake, Kondoa, Makunduchi, Kivungwe pamoja na Namanyere yamefaidika, bado tunaendelea kushirikiana nao na wanaendelea kufurahia haki zao kama diaspora.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili y nyongeza, swali la kwanza natambua juhudi za Serikali zinazofanywa kuitangaza Kiswahili ili kiweze kutumika duniani mpaka kufikia kwamba Kiswahili sasa ni lugha rasmi inayotumiwa SADC, hatua hizo zinazofanya Serikali ni nzuri lakini ninalo swali moja.

Je, kwa kipindi hiki TBC kama TBC ina mkakati gani wa kuwa na translate kwenye vipindi vyake anaye translate Kiswahili kwenda kingereza, na kingerez akwenda Kiswahili wakati anatangaza taarifa zake za habari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni ukweli usiopingika kwamba kuna television na redio za TBC. Je, TBC kama TBC ina mkakati gani wa kukuza lugha hii duniani kwa kuongeza masafa yake nikiwa na maana frequency ziweze kusikika kwenye nchin mbalimbali duniani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa maswali mazuri ya nyongeza, lakini nikianza na swali lake la kwanza ametaka kujua kwamba TBC tuna mkakati gani kwa kuwa na mtafusiri kutoka kwenye lugha ya Kiswahili kwenda kwenye lugha ya kingereza. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu kangu la msingi kwamba kwa sasa hivi tunavyo vipindi mbalimbali ambavyo vinatangazwa kwa lugha. Kwa hiyo, naamini kwamba kupitia hivyo vipindi watu wa mataifa mengine kwa maana ya nchi za nje wanaweza kupata kila kitu ambacho kinaendelea ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija pia kwenye swali lake la pili anataka kujua kwamba tuna mkakati gani wa kukuza lugha ya ksiwahili duniani. Mimi niseme kwamba Mheshimiwa Taska Mbogo anatambua namna gani ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa mstari wa mbele katika kukuza Kiswahili, vilevile tunamshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ndiye ambaye amewezesha sasa hivi kiswahili kinatumika kwenye mikutano ya SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba sisi kama Shirika la Utangazaji la Taifa mkakati wetu kuhakikisha ya kwamba tunakuza kiswahili na ndiyo maana tumekipa kiswahili kipaumbele katika vipindi vyetu, vilevile tumetengeneza apps mbalimbali ambazo zinapatikana ndani pamoja na nje ya nchi. Kwa hiyo, vipindi vyote ambavyo vinatangazwa ndani ya Tanzania, vilevile kwa kupitia app mbalimbali kwa maana ya mtandao wanapata taarifa mbalimbali ambazo zinatokea katika nchi yetu ya Tanzania, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa ugonjwa wa sickle cell unatokana na mtoto kurithi cells kutoka kwa baba na mama yake, wazazi wake wote wawili wanakuwa na cells ambazo ziko half. Sasa mtoto anapozaliwa anakuwa amerithi zile cells ndiyo maana anazaliwa na huo ugonjwa.

Je, ili kuzuia hili tatizo Serikali ina mkakati gani wa kuwapima watoto wanapozaliwa kwenye vituo vya afya na katika hospitalini mara tu wanapozaliwa iwapime ili wagundulike kwamba wana ugonjwa wa sickle cell ili kuepusha vifo vya watoto kwa sababu mara nyingi wanapogundulika wanakuwa wameshakuwa watu wazima na wengi huwa wanapoteza maisha, hasa vijijini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa commitment kwamba Serikali inaandaa mwongozo wa kutoa msamaha wa matibabu bure kwa familia ambazo hazijiwezi kupitia kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, sasa basi, yako magonjwa kama UKIMWI na TB watu hawahakikiwi, wanapata matibabu bure.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa bure matibabu ya sickle cell bila kuhakikiwa kama ilivyo magonjwa ya UKIMWI na TB?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Restituta Mbogo kwa kuwa ni mfuatiliaji wa karibu wa magonjwa haya yasiyoambukiza na hususani ugonjwa huu wa seli mundu.

Mheshimiwa Spika, hoja yake inahusiana na suala la upimaji wa watoto wanapozaliwa. Ni kweli ugonjwa huu huja kwa njia ya pale wazazi wanapokuwa na vinasaba ambavyo vinahamishwa katika kipindi cha ujauzito kuja kwa watoto pale wazazi wanapokuwa na vinasaba hivi vya ugonjwa huu wa seli mundu, genetic transfer. Kwa hiyo, katika nchi ambazo zimeendelea, watoto ambao wana Ugonjwa huu wa seli mundu wanaweza wakabainika kwa njia mbili; njia ya kwanza ni kupima ujauzito wakati mtoto akiwa bado tumboni kwa kupitia katika maji yaliyopo katika mfuko wa uzazi, unaweza ukabaini kwamba mtoto anaweza akazaliwa na ugonjwa wa seli mundu. Lakini njia ya pili, baada ya mtoto kuzaliwa akipimwa anaweza akabainika kama ana ugonjwa huu wa seli mundu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi; Tanzania na nchi nyingi za Afrika ugonjwa huu ni mkubwa na wako wagonjwa wengi na sisi kama Serikali, pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika pale Hospitali ya Muhimbili kupitia programu ile ambayo inaongozwa na madaktari mahiri ya Profesa Julie Makani, wamekuwa wanatoa msaada mkubwa sana kwa wagonjwa hawa wa seli mundu. Sasa sisi kama Serikali tumeamua sasa tunataka tuje na mpango wa kitaifa ambao utasimamia matibabu haya ya seli mundu na ndiyo maana tumesema kwamba ifikapo Novemba programu hii tutakuwa tumeianzisha rasmi na mkakati wa upimaji unaweza ukawa ni moja ya mkakati huo ambao tutaweza kuufanya kuhakikisha kwamba tunaubaini ugonjwa huu katika hatua za awali na kuweza kuwatibu hawa wagonjwa vizuri zaidi na kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusiana na suala la uhakiki wa wagonjwa. Ili uweze kumbaini mgonjwa wa seli mundu ni lazima kwanza apimwe na kuthibitishwa. Katika utaratibu ambao tunao sasa hivi hizo njia ambazo nimezisema hapo awali hatuzifanyi, kwa hiyo, mara nyingi unakuta mgonjwa anakwenda akiwa na tatizo la upungufu wa damu au akiwa na zile crisses, maumivu makali ambayo anayapata kutokana na ugonjwa huu, na akishathibitika kwamba ni mgonjwa wa sickle cell anapata matibabu.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa hatuna mfumo wa matibabu bure kwa wagonjwa wa seli mundu na hili niseme tu kwamba pale anapobainika mgonjwa kwamba hawezi kugharamia matibabu, kwa utaratibu wa sasa tuna utaratibu wa misamaha na utaratibu ni ule ambao nimeusema katika jibu langu la msingi, wanatakiwa kupita katika Serikali zao za Mtaa au Serikali za Vijiji kupata barua, wakija kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya hospitali watapata matibabu bure. Lakini katika mpango ambao tunataka kuanzisha mwezi Novemba tutaweka utaratibu mzuri zaidi wa matibabu kwa wagonjwa hawa wa seli mundu.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mkoa wa Katavi unaongoza kwa vifo vya watoto wachanga. Takwimu tu za mwaka 2018 zinaonesha kwamba Mkoa wa Katavi ulipoteza watoto wachanga 581. Hii ilisababishwa na ukosefu wa vifaa bora wakati akina mama wakijifungua lakini hata vifaa hivyo vikiwepo kwenye vituo hivyo vya afya haviwezi kufanya kazi kwa sababu havina umeme. Je, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini pamoja na WIzara ya Afya ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba vituo vile vya afya ambavyo havina umeme Mkoani Katavi vinapata umeme ili viweze kutumia vifaa vya kisasa kuokoa vifo vya mama na motto? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wauguzi wengi Mkoani Katavi hawana mafunzo, Serikali kupitia Wizara ya Afya ina mkakati gani wa kutafuta wadau wa afya ya mama na mtoto ili tuweze kutokomeza vifo hivi Mkoani Katavi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya katika majibu ya swali lake la msingi. Pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali kuhusu upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mkoa wa Katavi baadhi ya vijiji havijaanza kufikiwa na mkandarasi. Nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ambayo ameyauliza Mheshimiwa Mbunge mkandarasi ameshaanza kwenda site. Katika Mkoa wa Katavi kuna vijiji 149 vitapelekewa umeme. Sasa hivi mkandarasi ameshawasha Mchakamchaka lakini anaendelea na Kaparara na katika vijiji vingine saba atawasha kuanzia wiki inayokuja. Kwa hiyo, wananchi wa Katavi wategemee kupata umeme katika maeneo yote. Kesho kutwa watawasha kwenye Mgodi wa Society kwa Mheshimiwa Kapufi. Kwa hiyo, mkandarasi yuko site vijiji vyote vitapatiwa umeme kwenye kipindi hiki cha Julai mpaka Desemba mwaka huu. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ambapo sehemu ya swali la kwanza ameshalijibu Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Niendelee na kipengele kingine ambacho kilikuwa kimebaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba idadi ya vifo vya watoto katika Mkoa wa Katavi ni vingi sana na hili ni kweli lakini halitokani na ukosefu wa huduma za afya kwa watoto wachanga. Mkoa wa Katavi una changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni. Wastani wa Kitaifa sasa hivi tuna asilimia 27 ya watoto kati ya miaka 15 mpaka 19 aidha wana watoto au wana mimba. Katika mikoa ambayo inaongoza ndani ya nchi yetu ni pamoja na Katavi, umri wa kupata ujauzito bado ni mdogo sana na kwa kuwa bado hawajafikia ukomavu uliotosha, hili nalo linachangia sana katika vifo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na masuala ya mafunzo, Serikali inaendelea kujipanga na imekuwa inaweka utaratibu wa mafunzo endelevu kwa watoa huduma wake wa afya katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa ajili ya huduma ya mama na motto. Katika Mkoa wa Katavi, Serikali imekuwa inashirikiana kwa karibu sana na wadau.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Serikali haina mpango wa kusomesha Stenographer nchini Tanzania; na kwa kuwa kazi hizi zimekuwa zikifanywa na Majaji na Mahakimu wenyewe; swali langu kwa Serikali: Je, Serikali haioni kwamba inawaongezea mzigo Majaji na Mahakimu wasome, watoe hukumu na pia wanachukua jukumu la kuandika? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi sana nchini Tanzania kwamba baada ya hukumu unakuta mwananchi inamchukua muda, hata mwezi mmoja kupata ile hukumu yake; hii yote ni kwa sababu hatuna stenographer mle Mahakamani: Je, Serikali haioni kwamba inawakosesha wananchi haki yao ya kupata hukumu zao mara tu kesi inapohukumiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa anasema Waheshimiwa Mahakimu na Majaji wanakuwa na mzigo mkubwa sana wakati wanasikiliza kesi na wakati huo huo wanachukua uandishi, ni kweli lakini katika mazingira ya kawaida Serikali kama nilivyoeleza mwanzo kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba hawa watu hawajaingizwa kwenye mfumo wa utumishi wa Mahakama. Kwa maana hiyo, Serikali inapitia utaratibu mzuri utakaowezesha hawa watu, kwa sababu itakuja kama idara mpya kama zilivyo idara nyingine za kiutendaji kwenye Serikali hii. Utaratibu wa kuanzisha idara mpya una milolongo yake katika kuangalia masuala mbalimbali. Tunajua wazi kwamba ni mzigo, ni kweli, ndiyo maana Serikali imeendelea kuupitia mchakato wa kuanzisha section hii Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, kuchelewa kwa hukumu siyo kwa sababu tu hatuna hawa watu, hili ni jambo ambalo lina mambo mbalimbali ambayo yanajitokeza pale Mahakamani. Nikuhakikishie tu kwamba mpaka sasa hukumu hazichelewi zaidi ya mwezi mmoja. Tumeendelea kukaa na Mahakimu na kuona uharakishaji wa utoaji wa hukumu zao.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa sasa hivi tunaelekea kwenye Mahakama ya Kiswahili, kwa hiyo, vitu vingi vitarahisishwa baada ya muda siyo mrefu na mambo yote yatakaa sawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, napenda kuishukuru Serikali kwa ujenzi na swali langu la nyongeza ni kwamba, kwa kuwa ujenzi huu umechukua muda mrefu na kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Katavi bado wanaisubiri kwa hamu sana hiyo Hospitali ya Mkoa. Je, Serikali inatoa commitment gani kutoa pesa zilizobaki bilioni 5.8 kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa hii hospitali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Mkoa wa Katavi tumejenga vituo vingi sana vya afya, lakini pia tunazo hospitali tatu tumejenga kwenye Wilaya zetu tatu za Mkoa wa Katavi pamoja na zahanati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutuletea vifaa tiba kama vile vifaa vya upasuaji, ultrasound na kadhalika kwa ajili wananchi wakati wakiwa wanasubiri hiyo hospitali iishe waweze kuhudumiwa kwenye vituo vya afya pamoja na hizo hospitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze Wabunge wote wa Mkoa wa Katavi, kwa kweli wamekuwa wakifuatilia suala la afya kwenye mkoa wao kwa kina sana na nawaelewa sana kwa sababu ni mojawapo ya mikoa ambayo ni migumu kufikika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kwamba ni lini sasa Serikali kwenye hospitali ambazo zimejengwa itapeleka vifaa tiba. Kama ambavyo Wabunge wanajua Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa bilioni 80 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba. Kwenye hizo bilioni 80 mojawapo ya vipaumbele ambavyo tayari tumeviweka ni hospitali ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja hapa. Kwa hiyo, kwa uhakika kabisa tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Stephen Byabato, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa mradi. Swali la kwanza; Kata za Kasansa, Mamba, Maji Moto, Mbede Mwamapuli, Chamalendi, Usevya na Kibaoni zinatumia umeme wa kutoka nchi ya jirani ya Zambia, umeme ambao hautoshi ni kilowatt 100. Tuliomba kupata umeme wenye kilowatt 500. Je ni lini Serikali itatuletea transformer zenye kilowatt 500?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye Mji ya Nyonga ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Mlele umeme hautoshi kwa sababu umeme uliopo wakati unawekwa ulikuwa umewekwa kwa mahitaji madogo, mji umeongezeka, wananchi wanafanya biashara, wamefungua miradi ya ujasiriamali, ambayo ni mashine za kusaga na vitu vingine. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutuongezea umeme wenye megawatt zaidi ya nne?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kwa kutambua juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba gridi ya Taifa inafika katika Mkoa wetu wa Katavi. Mkoa wa Katavi haujafikiwa na gridi lakini unapata umeme kutoka katika vyanzo viwili, Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Mpanda Mjini wanatumia generator mbili ambazo ziko pale Mpanda mjini na mpaka sasa zinazalisha megawatt kama 5.87 hivi na umeme ule unatosha maeneo yale kwa sababu matumizi ya Mkoa wa Katavi kwa sasa kwenye yale maeneo ya mjini ni megawatt kama 5.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini chanzo cha pili cha umeme kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni umeme ule unaotoka Zambia unapita Sumbawanga unapita Namanyere unakuja kuingia sehemu ya karibu na Mpanda Mjini unakuja kuingia kwenye Wilaya ya Mlele kwenye hayo maeneo ya Mwamapuli, Maeneo ya Majimoto, Maeneo ya Kibaoni aliyoyataja ambayo sasa ndio umeme unaingia pale kutokea Sumbawanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachokifanya kwa sasa cha kwanza kabisa inahakikisha kufikia 2023 imefikisha gridi ya Taifa katika Mkoa wetu wa Mpanda kutokea Tabora. Jambo la pili ambalo inalifanya ni kuhakikisha kwamba inaongeza uwezo wa hizo transformer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita transformer yenye uwezo wa kilowatt 400 imeongezwa katika Wilaya ya Mlele ili kuongeza nguvu kwenye hayo maeneo ya Kata za Mlele ambazo amezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge afanye mawasiliano, atataarifiwa kwamba sasa hali ya umeme imetulia na sasa Katavi inaweza kuendelea vizuri wakati tukiwa tunahakikisha kwamba gridi inafika kwenye Mkoa wetu wa Katavi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika ahsante, kwa kunipa nafasi kwa kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu umeme ninayo maswali mawili ya nyongeza kwa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza wananchi wa Mkoa wa Katavi wanahitaji umeme wa gridi kwa haraka ili waweze kujenga viwanda, lakini pia ili waweze kufanya biashara zao mbali mbali zinazotumia umeme. Kumekuwepo na kusuasua kwa mradi huu wa umeme wa gridi na ujenzi wake unakwenda taratibu kwa sababu ya ufinyu wa pesa zainazotolewa Serikalini kwenda TANESCO: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza bajeti ya TANESCO ili waweze kujenga miundombinu ya umeme kwa Mkoani Katavi? (Makofi)

Swali la pili; umeme uliopo sasa hivi Mkoa wa Katavi hautoshelezi kwa sababu kumeuwa na usambazaji wa umeme wa REA, hivyo watumiaji wa umeme ni wengi mkoani Katavi. Swali langu na ombi langu kwa Serikali: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutupunguzia muda wa ukamilishaji wa ujenzi wa umeme wa gridi badala ya kuwa 2023 uwe 2022? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi ambayo imeianzisha na ile ambayo imeikuta ikiwa inaendelea, nasi tuna uhakika kwamba fedha iliyopo TANESCO itaendelea kutosha na pale ambapo watapungukiwa Serikali itaongeza. Katika bajeti ambayo Bunge lako limepitisha jusi, takribani shilingi bilioni 35 zilitengwa kwa ajili ya kuendelea na hii kazi ya ujenzi wa hiyo njia ya msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora kwenda Mpanda.

Mheshimiwa Spika, tunaamini fedha hizo zitatosha na kwa kadri itakavyohitajika kutoka kwa wataalamu basi Serikali itaongeza pesa hizo kwa sababu inazo.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, kwa kuwa wenzetu wa Katavi hawajafikiwa na gridi; na gridi kwa mujibu wa ratiba ya TANESCO iliyowekwa kwa mchanganuo ule wa kitaalamu wa kwamba tuanze kupembua njia ya kupitisha umeme tulipe fidia, tujenge majengo tuchukue na hatua nyengine; naomba Bunge lako Tukufu, liruhusu na kuielekeza Wizara iende ikakae na kuona kama muda huu unaweza ukaminywa kwa kuzingatia matakwa ya kitaalamu na bajeti tuliyojipangia ili wenzetu wa Katavi waweze kupata gridi hii kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, niongeze kwamba Mkoa wa Katavi unatumia umeme karibia Megawati 1 na kilowati kama 200, tutaenda kuona namna ambavyo tunaweza tukaongeza mashine na mitambo ya kuweza kufua umeme zaidi katika eneo hilo katika kipindi hiki ambacho bado tunaendelea na utengenezaji wa miundombinu yetu ya kufikisha gridi katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa barabara ya kutoka Mpanda kwenda Karema upembuzi yakinifu unakamilika mwezi wa Aprili na kwa kuwa barabara hiyo ni muhimu, inakwenda kwenye Bandari ya Karema ambako Serikali imewekeza shilingi bilioni 47 na kwa kuwa asilimia 81 ya ujenzi wa bandari imekamilika; na kwa kuwa bandari hiyo...

SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo uliza swali.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bandari hiyo inakwenda kupokea mzigo kutoka nchi za SADC. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa na kukamilika kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara iliyopo sasa hivi ina changamoto kwenye maeneo ya Kaseganyama, Kandilankulukulu na Nkungwi haipitiki kipindi cha masika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza bajeti ili barabara hiyo ipitike kipindi cha masika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum Katavi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema na kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kutokana na umuhimu wa barabara hii ambavyo kama alivyosema, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 47 kukamilisha bandari ambayo ipo asilimia 79; ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba hii barabara itakapokamilika kufanyiwa usanifu mwezi Aprili zitatafutwa fedha haraka ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami tukitambua kwamba ndio litakuwa lango kubwa la bidhaa zetu kwenda DRC. Ahsante. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, watoto hawa wa mitaani ndio watoto ambao wanazalisha makundi kama panya road, damu chafu na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Serikali inazo nyumba za kulelea hawa Watoto. Ningeomba kujua Serikali ina vituo vingaapi vya kulelea watoto wa mitaani.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Nchi yetu ya Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu Watoto. Kwa mfano The UN Convention on the Right of the Child na mkataba wa Afrika wa The African Charter on the Right of the Child. Swali langu; je, Serikali inamkakati gani wa kuhakikisha kwamba watoto wa Tanzania ambao wako mitaani wanapata elimu ambayo ni haki yao pamoja na kujua haki zao za msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inavituo viwili vya kulea Watoto ambavyo inavimiliki. Vituo hivyo ni Kurasini ambacho kipo Dar es Salaam na Kikombo ambacho kipo Dodoma. Vituo hivyo vina idadi ya Watoto 142 ambapo 88 wakiwa ni wakiume na 54 ni wa kike.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, watoto wote ambao wanalelewa katika vituo vya watoto ambavyo vinamilikiwa na Serikali wanapata haki zote za msingi ikiwemo elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu na elimu ya ufundi (VETA). Wanapomaliza wanapewa vifaa maalum vya kujiendeleza ili waweze kujiajiri wenyewe. Ahsante sana.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa kumekuwa na matatizo mengi yanayoikabili elimu nchini Tanzania tumeona watoto wengi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma na kuandika, lakini pia idara nyingi za udhibiti wa elimu nchini Tanzania hazina vitendea kazi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwanunulia vitendea kazi hususani magari Idara ya Udhibiti Ubora wa Elimu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, kuna mwongozo wowote ambao umetolewa na Wizara ya Elimu katika kudhibiti hivi vyuo vya watu binafsi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anazungumzia suala la vitendea kazi; kwanza nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeshafanya mambo makubwa sana kwenye udhibiti wa ubora wa elimu nchini hasa kwenye upande wa vitendea kazi.

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali imeshajenga ofisi karibu katika halmashauri zote za wilaya nchini kwa ajili ya maeneo ya ndugu zetu hawa au watumishi wetu kuweza kupata mazingira mazuri na salama ya kutendea kazi zao. Lakini vilevile mwaka uliopita wa fedha Serikali ilinunua magari zaidi ya 184 na kuyasambaza kwenye halmashauri au kwenye ofisi hizi za wadhibiti ubora katika halmashauri zote nchini, lakini juzi juzi hapa baada ya zoezi la Sensa kukamilika tumepeleka vishikwambi katika ofisi hizi kwa ajili ya watumishi hawa katika ngazi hii ya udhibiti ubora.

Kwa hiyo, kwa msingi wa vitendea kazi tayari Serikali tumeshafanya kazi kubwa sana na hivi sasa tupo katika programu za kuwaongezea uwezo kwa maana ya kuweza kuweka programu mbalimbali za mafunzo kwa watumishi hawa ili kuweza kutenda kazi yao sawasawa. Niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari Serikali imefanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la miongozo katika utendaji kazi kwenye udhibiti ubora tunakwenda na kanuni pamoja na miongozo mbalimbali ya elimu, ndio wanayozingatia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku. Kwa hiyo miongozo kimsingi ipo kuhakikisha kwamba kazi hizi zinakwenda sawasawa, nakushukuru sana.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa eneo la kutoka Sikonge kwenda Inyonga lenye kilometa 161 halina mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kunakuwepo na usalama kwenye eneo hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri katika majibu yake amesema kwamba wamiliki wa mabasi wanaweza kuomba kuondoka, kuanza safari zao pale Dar es Salaam muda wa saa tisa usiku au saa kumi. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kutoa tamko hapa Bungeni kwamba mabasi hayo yanaweza kuanza safari muda wa saa tisa au saa kumi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mkakati ambao tunao katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama. Kwanza nikupongeze wewe binafsi kwa kuweza kutupatia changamoto ya kufikiria kuanza usafirishaji wa mabasi ya abiria usiku.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kutekeleza maagizo Mheshimiwa Spika na maombi ya Waheshimiwa Wabunge tumeshaanza kulifanyia kazi suala hilo.

Mheshimiwa Spika, tumekaa na Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi ambao ndiyo wadau wakubwa kuangalia jinsi ya kuweza kufanya na tumeamua kulipa majukumu Baraza la Usalama Barabarani la Taifa ambalo limesheheni wajumbe ama wadau kutoka taasisi muhimu ikiwemo Jeshi la Polisi, LATRA, TANROADS na kadhalika ili wataalam hawa waweze kutushauri namna bora ambayo itaweza kusaidia kuruhusu magari haya kuweza kutembea usiku ikiwemo hili eneo ambalo umeliruhusu.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo ambayo tunategemea kutoka kwa wataalamu hawa ni jinsi ya kuweza kudhibiti changamoto zilizopelekea maamuzi ya Serikali mwaka 1990 kuzuia ambayo ilikuwa ni mambo mawili makubwa.

Mheshimiwa Spika, moja; ilikuwa ni kutokana na changamoto ya ujambazi na utekaji kipindi hicho; pili; ilikuwa ni ajali ambazo zilikuwa zikitokea usiku na kuharibu maisha ya Watanzania wengi.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi; tunataka kuhakikisha kwamba wakati ambapo tunalitafakari jambo hili tutakaporuhusu tuweze kuhakikisha kwamba mabasi haya yanaruhusiwa kusafiri lakini wananchi wetu wanaendelea kubakia salama. Hivyo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba jitihada hizi za kuhakikisha kwamba eneo hilo na maeneo mengine nchi nzima yanakuwa salama kuruhusu usafiri wa usiku yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu tamko; kama ambavyo nimezungumza kwamba tunaomba nitoe tamko kwamba wale ambao wanaona kuna haja ya kuanza safari zao mapema basi walete maombi na tamko ni kwamba tutaridhia maombi hayo kwa wale ambao watakuwa na haja ya kuanza safari hizo wakati tunaendelea na jitihada hizo za kutafutia ufumbuzi wa kudumu suala hili.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri maombi anakuwa analeta nani, mmiliki wa chombo cha usafiri au unaleta mkoa husika au nani analeta hayo maombi?

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, maombi yawasilishwe na wenye vyombo vya usafiri ama wamiliki wa mabasi hayo ambayo yanahitaji kusafiri kwa nyakati hizo.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza napenda kuishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa hii barabara kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa Serikali imewekeza ujenzi wa bandari pale Karema, ujenzi ambao ni mkubwa sana: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba barabara ya kutoka Kagwila kwenda Karema inafanyiwa ukarabati, kwani kwa sasa hivi imeharibika sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kumekuwa na matatizo watu wanapopisha ujenzi wa barabara, Serikali imekuwa na tabia ya kuchelewesha kuwalipa: Je, Serikali imejipanga vipi kuwalipa wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami toka Kagwila kwenda Karema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipokee shukurani kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, kwa sababu shukurani hizo ni zake, ndiye anayetoa hizo fedha kujenga hiyo miundombinu. Kwa maswali yake mawili, nakubali kwamba barabara ya Kagwila kwenda Karema kilomita 112 inayoenda kwenye Bandari ya Karema ilikuwa na changamoto, lakini Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba Mkoa kupitia Meneja, waliomba fedha za ziadam Shilingi milioni 500 tulishatoa, na wako wanakarabati maeneo yale ambayo yalikuwa hayawezi kupitika hasa maeneo ambayo wanalima mpunga karibu na barabara. Kwa hiyo, kwa sasa tunavyoongea, Mheshimiwa Mbunge barabara ile inapitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, tayari tumeshakamilisha tathmini na wananchi wote ambao watalipwa kwa mujibu wa sheria zetu kwa barabara ya Kagwila hadi Karema, tayari wameshatambuliwa na tayari wameshajulishwa kila mtu atalipwa kiasi gani. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itawalipa wote watakaopisha barabara kwa mujibu wa sheria, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili bandari iweze kufanya kazi vizuri, inahitaji kuwa na barabara ya lami kutoka bandarini, lakini pia inahitaji kuwa na reli kwa ajili ya kubeba mizigo. Kwa kuwa barabara ya lami kutoka Karema kwenda Mpanda bado haijakamilika, na kwa kuwa Serikali bado haijajenga reli kutoka Karema kwenda Mpanda;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kujenga reli pamoja na barabara ya lami ili kuwezesha kubeba mizigo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuwa na bandari ambayo haifanyi kazi, ambayo haina meli, ni sawa na kuwa na nyumba ambayo haikaliwi na mtu. Ziwa Tanganyika halina meli inayofanya kazi sasa hivi, MV. Liemba haifanyi kazi na MV. Mwongozo haifanyi kazi;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inajenga meli ili ziweze kubeba mizigo kutoka Kongo na nchi za jirani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Bandari yetu ya Karema inatakiwa ifungamanishwe na barabara kwa kiwango cha lami pamoja na reli. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka wa fedha ambao tunauanza wa 2023/2024, kati ya kilometa 112 zote zimekwisha tangazwa na itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuifungua bandari hii ya Karema – Ikola mpaka Kagwira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anataka kujua meli katika Ziwa Tanganyika. Kama ambavyo tuliweza kuwasilisha bajeti yetu siku ya Jumatatu na Jumanne, tuliweza kutoa commitment kwamba kati ya Ziwa Tanganyika, meli tatu tunaendelea kuzikarabati, hususan Meli ya MT. Sangara inayobeba mafuta ambayo iko asilimi 90, pia kuna Meli ya MV. Liemba ambayo tayari mkataba wake tutasaini mwezi Juni, na MV. Mwongozo tumepata mkandarasi mshauri atakayeweza kuishauri Serikali namna gani ya kuifanya hii meli i-balance maana ilikuwa na shida ya stability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo pia tumetenga fedha kwa kutengeneza meli kubwa mbili, moja ya mizigo itakayobeba tani 3,500 na nyingine ni ya kubeba abiria 600 pamoja na tani 400 ambayo kwa ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma, mlisema ikiwezekana ziwe mbili, na sisi Serikali tukasema tunakwenda kulifanyia kazi hili. Kwa hiyo hii ni mipango na tunakwenda kufanya katika mwaka wa fedha ujao, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO : Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza serikali kwa kutufikiria kujenga Mkongo wa Taifa kutoka Sikonge mpaka Inyonga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Sikonge, Ipole, Inyonga mpaka Mpanda hakuna mawasiliano, Mkongo wa Taifa unaoenda kujengwa unatoka Inyonga kwenda Majimoto mpaka Kizi. Kutoka Inyonga kwenda Mpanda kuna kilomita 130, hapana mawasiliano na ni hifadhi ya Taifa;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Mkongo wa Taifa katika eneo hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwenye Mkoa wangu wa Katavi kuna vijiji ambavyo mawasiliano ni duni. Kwa mfano Kijiji cha Bujombe Wilaya ya Tanganyika na Kijiji cha Mapili kata ya Ilela. Kuna ahadi yako Mheshimiwa Waziri ulisema utaweka Mkonga wa Vodacom;

Je, ni lini utatimiza ahadi yako?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Restituta Mboga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kutoka Sikonge kufauta ile barabra ya lami, sehemu kubwa ya eneo lile halina huduma ya mawasiliano. Serikali kupitia TTCL tumefanya tathmini na tumekusudia kuweka minara mitatu mpaka minne kwenye hilo, eneo ili hilo eneo lipate mawasiliano. Tunajua lipo tatizo kubwa la watu kusafiri hasa wakati wa usiku kwa sababu ya kukosa mawasiliano. Tumeshaweka utaratibu na tumefanya tathmini. Wakati tunajenga huu Mkongo na nguzo za mawasiliano zitawekwa kwenye haya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule alikokutaja kwenye kijiji tunafanya tathmni upo mnara karibu na hiki kijiji tuone kama ukiongezwa nguvu tuone kama unaweza kuhudumia eneo hili. Lakini lile eneo ambalo nilitoa hadi kwmba tutaweka mnara Vodacom kwenye ile minara 758 kuna mnara mmoja ambao unakwenda kujengwa kwenye hili eneo. Hatua za awali za manunuzi zimekamilika vifaa vipo njiani vinakuja na ujenzi utaanza mara moja kwa ajili ya kutoa huduma kwenye eneo husika.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa meli mbili kwenye Ziwa Tanganyika, lakini mwaka 2022 Serikali ilitenga fedha, na mwaka huu Serikali imetenga fedha, lakini majadiliano bado yanaendelea: Je, nini mkakati wa Serikali wa kuharakisha ujenzi wa meli hizi mbili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa wananchi wa Mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa wanategemea meli za MV Liemba na MV Mwongozo: Je, lini Serikali itamaliza ukarabati wa meli hizi ili ziweze kufanya kazi kwenye Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka tunavyoongea hivi tuko kwenye hatua za mwisho kabisa, na wakandarasi wa kuanza kujenga hizo meli kubwa mbili katika Ziwa Tanganyika walishapatikana. Kwa hiyo, wananchi wawe na imani, na ndiyo maana tunategemea kwamba tunaweza hata tukasaini kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha ili tuanze ujenzi wa hizo meli. Mkataba wa ujenzi, tunategemea watajenga kwa muda wa miaka miwili hizo meli mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, tunatambua kwamba kwa sasa hakuna meli ambayo inafanya kazi katika Ziwa Tanganyika. MV Liemba tunavyoongea imeshapata mkandarasi na mkataba ni kwamba ukarabati huo utachukua miezi minane na meli hiyo itakuwa imerudishwa majini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Meli ya Mwongozo, meli hii ina historia yake. Kilichokuwa kimesimamisha hiyo meli isifanye kazi, siyo kwa sababu ya ubovu, ila Serikali ilitaka ijiridhishe kuhusu stability ya hiyo meli. Tunavyoongea, tayari Serikali ilishamu-engage Mhandisi Mshauri ambaye ni Chuo chetu cha DMI kufanya tathmini, na kama kuna marekebisho, yafanyike. Yakishafanyika, hiyo meli pia itarudi majini muda siyo mrefu. Kwa hiyo, tunategemea katika kipindi cha karibuni meli mbili; MV Liemba na MV Mwongozo zitarudi majini kuanza kufanya kazi katika Ziwa Tanganyika kwa muda wa karibuni sana ahsante. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inatuongezea pesa na wakandarasi zaidi ya mmoja, wawe watatu ili Barabara ya Mpanda – Kigoma ikamilike ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kufunguka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, mazungumzo hayo na Benki ya Afrika yatakamilika lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika taratibu za kandarasi inategemea na mlivyopanga lots ama vipande na vipande tunavyovijenga hakuna ambacho kwa sasa kinazidi kilometa 50.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika hivyo vipande vitatu vinavyojengwa kila kipande kina mkandarasi lakini tunategemea katika swali lake la pili kama African Development Bank tutakuwa tumekubaliana nao kutumia bakaa iliyobaki kukamilisha hiyo barabara kwa urefu wa kilometa 94 ni wazi kwamba hatutakuwa na mkandarasi mmoja tutakuwa na zaidi ya mkandarasi mmoja ili kukamilisha kazi kwa haraka kati ya Mpanda na Uvinza kwa kilometa 94 ambazo zimebaki, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, wananchi wa Mkoa wa Katavi hususani Wilaya ya Mpanda Kata za Majengo, Kashaulili, Mpanda Hotel wamekuwa na mgao wa maji hawapati maji kila siku, lakini lipo Bwana la Milala ambalo lilikuwa ni chanzo cha maji sasa hivi bwawa hilo halitumiki kwa sababu limechafuka. Je, Serikali ina mkakati gani wa kusafisha bwawa hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Ziwa Tanganyika ndiyo chanzo kikuu cha kutoa matatizo ya maji kwenye Mkoa wa Katavi; Serikali ina mkakati gani wa kuharakisha upembuzi yakinifu ili maji yaweze kutoka Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Mbogo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali yayote napokea pongezi, lakini vilevile napenda kurudi kwenye jibu langu la msingi eneo la Mpanda linakwenda kunufaika hivi punde na ule mradi wetu mzuri ambao tumeusubiri kwa muda mrefu na Mheshimiwa Rais hivi punde anakwenda kufanya yake na maji yanakwenda kuanza kutekelezwa kupitia mradi wa miji 28.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na bwawa kuchafuka, tutaangalia uwezekano wataalamu watakwenda kuangalia uwezekano wa kuona kama bwawa hili litatufaa au litatupotezea fedha, kama litakuwa linahitaji fedha nyingi ambayo haina tija sana kwenye matokeo tutaendelea na mikakati mingine, lakini suala la msingi ni kuhakikisha wananchi wanakwenda kupata maji safi na salama bombani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la matumizi ya Ziwa Tanganyika ni moja ya mikakati ya wizara nimekuwa jibu hili mara kadhaa tutakwenda kutumia Ziwa Tanganyika kwasababu hakuna asiyefahamu kwamba ni chanzo ambacho kitatuletea tija kubwa sana na miradi itabaki kuwa endelevu kwa vizazi na vizazi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Katavi wanapata shida sana, ndugu zao wanapofariki pale kwenye hospitali ya mkoa ambapo inawalazimu wasafirishe maiti kilometa tatu kupeleka hospitali ya rufaa. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi tu wa ile mochwari kwa sababu ujenzi wake ni shilingi milioni 500? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hospitali ya Mkoa wa Katavi haina ambulance, ina ambulance moja na kwa afua za udaktari huwezi kubeba maiti kwenye ambulance…

MWENYEKITI: Swali.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itatupatia ambulance kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anafuatilia masuala mbalimbali ya afya kwenye Mkoa wa Katavi, lakini nimwambie moja kuhusiana na suala la kumalizika mochwari. Nimhakikishie kwamba kabla ya mwezi wa Kumi mwakani, mochwari yao hii itakuwa imekamilika. Kwa sasa tuendelee kutumia mochwari ya hospitali ya wilaya ambayo ilikuwa inatumika kabla ya hospitali ya mkoa wakati tunaendelea kutatua hili la kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shilingi bilioni 12.9 zimeletwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, shilingi milioni 300 ni fedha ndogo sana katika Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la pili linalohusiana na suala la ambulance, ninyi mnajua kwamba Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amenunua ambulance nyingi na Wabunge wengi ni mashahidi kwamba majimbo mengi wakati huu yamepata takribani ambulance mbili mbili. Nataka kumhakikishia pia kwamba hospitali yao itaongezewa ambulance ya pili ili waweze kufanya shughuli kama ambavyo alitamani kufanya.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa bandari. Swali la kwanza; kwa kuwa bandari imeshakamilika na kwa kuwa ujenzi wa reli hii unakwenda kuunganisha Nchi yetu ya Tanzania na Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pia inakwenda kutoa fursa kwa wananchi wa Tanzania hususan wananchi wa Mkoa wa Katavi kufanya biashara na Nchi ya Congo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata fedha kuharakisha ujenzi wa reli hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa upembuzi yakinifu umeshakamilika wa kilometa 321 kutoka Kaliua Mpanda hadi Kalema kwa ajili ya ujenzi wa reli hii, lakini katika ujenzi huo kuna wananchi ambao watapisha ujenzi wa reli hii. Je, ni lini wananchi wanaopisha ujenzi wa reli hii watalipwa fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama utaridhia kabla sijajibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Taska Mbogo, ninaomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa tukio kubwa linaloendelea sasa hivi Nchini China, ambapo yeye pamoja na Marais wenzake, Rais wa China pamoja na Mheshimiwa Rais wa Zambia, wamesaini hati ya makubaliano ya kuboresha reli yetu ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Bungeni mara kadhaa hoja hii imeulizwa kila wakati, ni lini TAZARA itaboreshwa, leo hati maalum ya makubaliano imesainiwa ili kuifumua TAZARA iweze kubeba mzigo na kufungua biashara kati ya nchi yetu na Nchi za Congo na nchi ya Zambia na sote tunafahamu tuna potential ya mzigo wa ten million metric tons Congo pamoja na seven million metric tons upande wa Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwenye swali la Mheshimiwa Taska Mbogo, namba moja anauliza mkakati wa kupata fedha. Serikali ya Tanzania imejitambulisha kwamba ndiyo Serikali inayoongoza Barani Afrika kwa kuwa na agenda maalum kwenye reli, ndiyo maana tunajenga reli ndefu kuliko reli nyingine yoyote katika Bara letu na duniani tukiwa ni nchi ya tano. Ninamwomba Mheshimiwa Mbogo pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine wa mikoa hiyo wavumilie kidogo, tupo kwenye kipande cha saba sasa kwa maana kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza wakandarasi wapo site tayari na kutoka Tabora mpaka Kigoma wapo site tayari na kutoka Kigoma Uvinza kuelekea mpaka Burundi tupo kwenye hatua za kumpata mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbogo avumilie, tukimaliza hapa tutarudi kwenye vipande vingine vinavyoendelea ikiwa ni pamoja na kwake Kaliua - Mpanda, pamoja cha Mtwara Corridor ambacho najua Wabunge wa Mtwara lazima wangeuliza, leo pamoja na kutoka Rusumo kwenda mpaka Kigali na kutoka Tanga, Arusha na Musoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hoja ya pili, Serikali hii inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, inajali wananchi wake. Nimhakikishie pale itakapobainika kunahitaji fidia wananchi hawa kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi yetu watapewa fidia zao. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, swali langu kidogo lilikuwa linafanana na la Mheshimiwa Paresso.

MWENYEKITI: Kwa hiyo limeshaulizwa?

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niliboreshe kidogo; gharama za kusafisha figo pale Muhimbili ambayo ni Hospitali ya Serikali ni shilingi 180,000 kwa section moja, lakini ili mgonjwa wa figo akae vizuri, anatakiwa kusafisha figo mara tatu kwa wiki, hii ni shilingi 540,000 kwa wiki. Kwa Mtanzania wa kawaida ni pesa nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja yangu ilikuwa, ni lini Serikali itapunguza gharama za kusafisha figo kwenye Hospitali za Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mbunge kwa kweli kwenye eneo hili ninajua anazungumzia, kwa sababu physically anajua anavyoniletea wagonjwa wenye matatizo yao, namna ya kusaidiana pamoja. Kwa kweli anafuatilia sana masuala yanayohusu watu kwenye eneo la afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwambia tu tumeanza, ndiyo maana ukienda baadhi ya hospitali sasa katika hospitali zetu za mikoa, hospitali mbili sasa za Mkoa wa Dar es Salaam tumefanikiwa kuhakikisha tunashusha na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri wa Afya sasa ameunda timu, inapitia kuja na itemization zote ili tujue tunapunguza wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu unaweza ukapunguza, badala ya kupunguza ukaua mfumo wenyewe na kuua mfumo wenyewe unaweza ukasababisha watu wakose huduma kabisa. Ni bora wapate huduma kwa ghali, lakini waendelee kuwa hai wakati tunaangalia mambo yanakwendaje. Kwa kweli tunalichukua hilo, tunaenda kulifanyia kazi na timu imeanza kufanya kazi, wiki ijayo wanaleta ripoti watupe way forward ya kupunguza gharama.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Serikali ina mkakati gani kwa wanafunzi wanaohitimu Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ili kuawaajiri kwenda kuleta tija kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nini tofauti kati ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyoanzishwa na Hayati Baba wa Taifa mwaka 1975 kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi kwa maana ya kutoa mafunzo kwa vijana na kwenda kuleta maendeleo kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na mikakati ya kufanya tathmini kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuhakikisha halmashauri zote nchini zinapata Maafisa Maendeleo wa kutosha. Kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024, jumla ya Maafisa Maendeleo ya Jamii 840 wameajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinatoa elimu kwa ngazi ya Cheti na Diploma kwa ufaulu wa kitaalamu. Pia vinatumia Mitaala ya NACTVET na Vyuo vya Maendeleo ya wananchi vinatoa mafunzo ya ujuzi kwa wananchi ili kuweza kujiajiri wenyewe kama vile ususi, kilimo, useremala na ushonaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara itaendelea kusimamia vyuo hivi kuhakikisha wananchi wanapata ujuzi na kupata elimu ambayo itawasaidia kiuchumi na maendeleo katika jamii, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa hospitali, lakini hospitali imechukua muda mrefu takribani miaka saba haijakamilika. Wing B, ni eneo ambalo kuna theatre ya kisasa, kuna jengo la mama na kuna jengo la mtoto na sasa hivi wanatumia lile jengo la ICU. Swali la kwanza; je, ni nini kauli ya Waziri baada ya bajeti kupata hizo shilingi bilioni tano ili jengo hili liweze kukamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wakati Waziri ananijibu swali mara ya mwisho hapa Bungeni, aliniahidi ambulance kwenye Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Je, niwasiliane na uongozi wa Hospitali ya Mkoa, waweze kumtuma dereva aje kuchukua hiyo ambulance? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza, kauli yangu moja ni kumpongeza Mbunge kwa sababu toka zero amekuwa pamoja na sisi na anajua miaka mitano iliyopita walikuwa hawana kabisa Hospitali ya Mkoa. Leo wana Hospitali ya Mkoa ambayo anaizungumzia majengo kumaliziwa na ameona mengine 98% mengine 20%. Nimhakikishie kwamba, litaenda kwisha.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, la ambulance, kuna ambulance 47, ambazo zipo njiani zinakuja. Nimwombe asiwasiliane na hospitali walete, lakini mimi na yeye tukae nimkabidhi kwa mtaalamu anayegawa ambulance ahakikishe yeye mwenyewe kwamba zitakapofika ya Katavi iweze kuwekwa. (Makofi)