Primary Questions from Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo (14 total)
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru mauaji ya vikongwe nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeweka mikakati mbalimbali ya kunusuru mauaji ya vikongwe nchini ikiwa ni pamoja na:-
(i) Kufanya operesheni na misako ya mara kwa mara kubaini waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi na wasiofuata sheria;
(ii) Kutoa elimu kupitia Polisi Jamii, wadau mbalimbali wa ulinzi na usalama, madhehebu ya dini na mashirika na taasisi binafsi, lengo likiwa ni kuwaelimisha wananchi madhara ya kujichukulia sheria mkononi; na
(iii) Kuanzishwa kwa vikosi kazi ili kuweza kufuatilia na kutafuta taarifa mbalimbali za watuhumiwa wanaotenda matukio hayo maarufu kama wakata mapanga, kabla na baada ya kufanyika kwa tukio.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kwenye Bunge lako Tukufu kutoa rai kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vinavyosababisha mauaji kwa nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR (K.n.y MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOSS NYIMBO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka uzio kwenye vituo vikubwa vya Polisi vilivyopo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Galloss, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango wa kujenga uzio katika Vituo na Makambi yote ya Polisi Tanzania. Aidha, Jeshi la Polisi kwa kutumia rasilimali zilizopo eneo husika, limekuwa likijenga uzio wa muda au wa kudumu katika maeneo mbalimbali na litaendelea kujenga uzio katika vituo zaidi hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar, Serikali imeanza kujenga uzio kwa baadhi ya maeneo ya Kambi ya Ziwani Zanzibar, mathalani eneo la Chuo Ujenzi umeanza kwa kutumia fedha zilizotokana na mapato ya ndani. Aidha, kwa upande wa mbele ujenzi unafanyika sambamba na kujenga maduka ambayo yatasaidia kuendesha shughuli za Polisi na kujiingizia mapato.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS aliuliza:-
(a) Je, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imepeleka wanafunzi wangapi kusoma nje ya nchi?
(b) Je, kada gani ambazo zilipewa kipaumbele?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Galoss, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa masomo 2015/2016, Serikali ilipeleka jumla ya wanafunzi 159 katika nchi za China 84, Algeria 57, Urusi wanne (4), Misri wawili (2) na Uingereza kupitia Jumuiya ya Madola 12.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapeleka wanafunzi nje ya nchi kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa ambavyo ni masomo ya sayansi, teknolojia na TEHAMA. Hivyo wanafunzi wanaopelekwa nje ya nchi husoma shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu katika fani za nishati na madini; mfano masuala ya gesi na mafuta, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, uhandisi, afya na sayansi shirikishi, usanifu majengo, elimu, uchumi na mawasiliano.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na wachongaji wa vinyago hasa pale wanunuzi wa vinyago hivyo kutoka nje wanaponyang’anywa bidhaa hiyo wafikapo airport kwa madai mbalimbali ikiwemo kutolipa kodi.
(a) Je, vinyago hivyo ambavyo ni biashara ya wanyonge baada ya kuzuiliwa hupelekwa wapi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kufanya hivyo kunawapotezea wateja na soko kwa wanaofanya ujasiriamali wa aina hiyo lakini pia kuwaingizia hasara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, vinyago sio miongoni mwa bidhaa zinazotozwa kodi au ushuru kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi. Ikiwa vinyago vilizuiliwa uwanja wa ndege au mpakani, sio kwa sababu ya kutolipiwa kodi au ushuru wa forodha. Utaratibu unaotumika kimataifa ikiwemo nchi yetu katika kushughulikia bidhaa zozote zinazokamatwa kwenye sehemu za kuingia au kutokea nje ya nchi kama viwanja vya ndege na mipakani ni wa aina mbili:-
Moja, kuziharibu au kuziteketeza bidhaa hizo au kuzipiga mnada. Bidhaa zinazoharibiwa au kuteketezwa ni zile ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi au kwa afya ya binadamu, kwa mfano, silaha, vyakula au kemikali zilizobainika kuwa si rafiki kwa matumizi ya binadamu na mazingira. Bidhaa nyingine ambazo haziangukii kwenye kundi hilo, ikiwa ni pamoja na vinyago hupigwa mnada na baada ya kuondoa gharama zozote za uhifadhi, mapato yake huingizwa Serikalini. Kwa kuwa swali la Mheshimiwa Tauhida halijabainisha ni lini na ni wapi vinyago hivyo vilikamatwa, idadi yake au taasisi au mamlaka ipi ilikamata vinyago hivyo ni vigumu kueleza vinyango hivyo vilipelekwa wapi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia vinyago au bidhaa nyingine yoyote inaposafirishwa nje ya nchi, hufanyika tu baada ya kubainika kuwa kuna ukiukwaji wa sheria na kanuni. Kwa hiyo, lengo la kufanya hivyo ni kujiridhisha kuwa wadau wote wa biashara au bidhaa hiyo wanafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili asiwepo yeyote mwenye kupoteza mapato yanayotokana na biashara au bidhaa hiyo ikiwemo Serikali yetu.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO aliuliza:-
Kuna taarifa zilizotolewa na Wizara ya Nishati na Madini za kugunduliwa kwa gesi ya Hellium yenye ujazo wa takribani futi bilioni 54 za ujazo nchini.
Je, Serikali imejiandaaje kimkakati kuhusu ugunduzi huo na uchimbaji wa gesi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa mataifa makubwa kama Marekani yalishatangaza kukosekana kwa gesi hiyo ifikapo 2030?
NAIBU WAZIRI WA MADINI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos Nyimbo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Kampuni ya Hellium One Ltd. imegundua kiasi cha gesi ya Hellium yenye ujazo wa cubic feet 54 billions katika maeneo ya Ziwa Rukwa. Ugunduzi huo ulitokana na uchunguzi wa sampuli tazo za Mavujia yaani gas seeps ya gesi ya Hellium katika maeneo hayo kiasi ambacho kinakadiriwa kuwa kikubwa zaidi ya mara sita ya mahitaji ya dunia kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Hellium One Ltd. imegundua madini ya hellium kupitia Kampuni zake tanzu za Gogota Tanzania Ltd., Njozi Tanzania Ltd. na Stahamili Tanzania Ltd. zinazomiliki leseni z utafutaji wa gesi ya hellium katika Mkoa wa Rukwa ikiwemo maeneo ya Ziwa Rukwa. Kampuni hizi zilipewa leseni za utafutaji wa hellium katika maeneo mbalimbali kuanzia mwaka 2015. Shughuli za utafutaji wa kina wa gesi ya helium unaendelea kwa kukusanya taarifa zaidi za kijiolojia, kijiokemia, kijiofizikia na 2D Seismic Survey ili zitumike kwa ajili ya uchorongaji wa visima vya utafiti yaani exploratoty wells. Kazi ya uchorongaji ikikamilika itawezesha kuhakiki kiasi halisi cha gesi ya hellium kilichopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa gesi ya hellium utaanza mara baada ya kazi ya utafiti wa kina, upembuzi yakinifu na tathmini ya athari za mazingira, kukamilika kwa leseni ya uchumbaji wa gesi hiyo kutolewa. Matokeo ya gesi hizo ndiyo yatakayoonyesha kama kiasi cha gesi kilichopo kinaweza kuchimbwa kibiashara kwa kipindi gani na taifa litanufaikaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufundisha wataalam stahiki yaani wajiolojia, wahandisi wa migodi na wachumi wa madini kusudi wawe na ujuzi wa kutosha na hadi sasa Serikali ina jumla ya wataalam 454 wenye fani za mafuta na gesi katika viwango mbalimbali na elimu. Pia kuna wanafunzi 137 walipo katika mafunzo ya mafuta na gesi katika ngazi za shahada za uzamivu katika vyuo mbalimbali nje ya nchi na wanafunzi 455 katika ngazi ya diploma na shahada ya kwanza ndani ya nchi.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani juu ya raia wa kigeni wanaopewa vibali vya kuja kufanya kazi hapa nchini kwa muda na kuwazalisha watoto na wadogo zetu na inapofika muda wa kuondoka huwakimbia na kuwaacha watoto hao wakiishi maisha yao yote bila baba kitu ambacho huwasababishia unyonge katika maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Magharibi, kama Ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji inatoa vibali vya ukaazi nchi kwa wageni baada ya Wizara ya Kazi kutoa vibali vya kazi kwa wageni hao.
Mheshimiwa Spika, mikakati ambayo Serikali inachukua ni kuelimisha raia wa Tanzania kuwa wasidhani kila mgeni anayekuja kufanya kazi Tanzania ni mtu mwema au ana uwezo wa kifedha na kutegemea kuwa atasaidiwa na mtoto wake kwenye malezi, hivyo kuwa waangalifu ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na kujiingiza kwao katika mahusiano ya kimapenzi na watu wasiowafahamu vema ikiwemo mimba na maradhi yanayosababishwa na ngono.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS) aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kufunga Kamera ndani ya Vituo vya Polisi sasa ili kupunguza malalamiko kwa baadhi ya wananchi wanapohudumiwa kwa kumwezesha Mkuu wa Kituo kufuatilia mwenendo wa shughuli za Kituo akiwa Ofisini au kwa kutunza kumbukumbu za matukio yanayotokea kwenye vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la matumizi ya CCTV Camera katika vituo vyetu ni la umuhimu mkubwa katika kuhakikisha huduma ya Polisi kwa wananchi zinatolewa kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi lina nia ya kufanya maboresho yakiwemo matumizi ya TEHAMA kwa kufunga kamera katika vituo vyake ili kuwapa nafasi Viongozi wa Kamandi kufuatilia matukio mbalimbali yanayotokea vituoni ikiwemo namna Askari wa chini wanavyohudumia wananchi.
Aidha, kutokana na ufinyu wa bajeti unaochangiwa na wingi wa changamoto, Jeshi la Polisi kwa sasa halina bajeti hiyo. Hata hivyo, limeruhusu wadau katika maeneo mbalimbali kuwezesha ufungaji wa kamera za ufuatiliaji kwa nia ya kuboresha na kufuatilia utendaji wa Askari.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kushirikisha wadau katika maeneo yao kuchangia upatikanaji na ufungaji wa CCTV Camera vituoni ili kupunguza malalamiko ya huduma isiyo na weledi ya Askari kwa wananchi.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO Aliuliza:-
Je, Serikali ina maelezo gani juu ya viongozi kutoka nje ya nchi wanaokuja Tanzania na kutembelea baadhi ya maeneo na kisha wanapokuta miradi ya wananchi huahidi kusaidia na baadae kushindwa kutimiza ahadi zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imekuwa ikipokea viongozi wageni kutoka nje ya nchi na makundi aina mbili yaani wa Kiserikali na wasio wa Kiserikali. Viongozi hao hutembelea Tanzania kwa ziara za kikazi na binafsi ambapo hupata fursa ya kuona miradi ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ina jukumu la kuratibu na kusimamia ziara za kikazi za viongozi wa Serikali kutoka mataifa ya kigeni ikiwa ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zinazotolewa na viongozi hao kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na taasisi za Kiserikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ambazo hutolewa na baadaye kushindwa kutimizwa, Wizara huratibu vikao vya majadiliano vinavyoshirikisha wahusika pamoja na Wizara za kisekta na taasisi za Kiserikali ili kupata mwafaka juu ya suala husika.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA (K.n.y. MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS) aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa muda mrefu kati ya kituo cha polisi Bububu na soko dogo la wananchi lililopo karibu na kituo hicho?
(b) Je, kiutaratibu umbali kati ya kituo cha polisi na makazi ya wananchi ni hatua ngapi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Galoss, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, si kweli kuwa kuna mgogoro wa kiwanja kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika eneo la kituo cha polisi Bububu. Ndiyo sababu wakazi wa eneo hilo ikiwemo wafanyabiashara wa soko hilo dogo hupata huduma za kiusalama katika kituo cha Bububu bila shaka yeyote. Aidha, kiwanja kilipojengwa kituo cha polisi Bububu na majengo mengine ya kituo yanamilikiwa kihalali na Jeshi la Polisi ingawa kuna kibanda cha kuuza samaki karibu na kituo hicho cha polisi kinachoitwa soko dogo la wananchi. Kibanda hicho kipo kati ya kituo cha Polisi Bububu na majengo mengine ya kituo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli upo utaratibu wa kuwepo kwa umbali kati vituo vya polisi, kambi za makazi ya askari ya wananchi. Hii ni kutokana na sababu za kiusalama kwa miundo mbinu ya Jeshi la Polisi. Aidha, kutokana na changamoto za makazi na ujenzi holela mijini. Uvamizi wa maeneo sehemu mbalimbali na kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu zisizo rasmi imesababisha maeneo mengi ya vituo vya polisi kuingiliwa na kusogeleana na makazi ya wananchi.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti ongezeko la uhalifu nchini?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea na mikakati yake ya kudhibiti vitendo vya uhalifu hapa nchini kwa kuimarisha doria, kufanya misako na operesheni mbalimbali dhidi ya uhalifu na wahalifu, pamoja kutoa elimu kwa jamii kutokujihusisha na vitendo vya uhalifu na kufuata sheria za nchi. Kushirikisha jamii kwenye ulinzi wa maeneo yao kupitia dhana ya ulinzi shirikishi. Pia Serikali imewapeleka wakaguzi wa polisi kwenye kata na shehia ili kushughulikia uhalifu kwa kushirikiana na wananchi.
ASYA SHARIF OMAR K.n.y. MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kulinda miundombinu ya maji nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Gallos Nyimbo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha miundombinu ya maji inayojengwa inatunzwa na kulindwa ili kutoa huduma endelevu. Katika kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, Serikali ilitunga Sheria Na.5 ya Mwaka 2019 ambayo inakataza kuharibu, kuvamia au kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yenye miundombinu ya maji. Kupitia sheria hiyo ni kosa la jinai kuharibu miundombinu ya maji. Aidha, Serikali inaendelea kujenga uzio kwenye miundombinu ya maji ikiwemo matanki ya kuhifadhia maji na mitambo ya kutibu maji. Vilevile, elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji nchini inaendelea kutolewa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA K.n.y. MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kukusanya madeni ya TANESCO katika taasisi kubwa ili shirika hilo liweze kujiendesha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kufikia mwezi Machi, 2023, TANESCO inadai jumla ya shilingi bilioni 244 kutoka kwa wateja wake mbalimbali wakiwemo wateja wa umma na wateja binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuzuia ukuaji na kuwezesha ukusanyaji wa deni, kwa upande wa Serikali, Serikali inahakikisha inatenga na kuweka fungu la fedha za kulipia huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO imeweka mikakati ya kukusanya na kuzuia madeni kwa kuweka mita za LUKU, kuhamasisha na kufuatilia madeni na inapobidi basi kukata huduma ya umeme kwa mteja mwenye deni kubwa na sugu ili liweze kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. AMINA ALI MZEE K.n.y. MHE. TAUHIDA C. GALLOS aliuliza:-
Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha Sera ya Wazee kupata matibabu bure inatekelezwa katika kila Kituo cha Afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, wazee wasio na uwezo wa kugharamia huduma za afya wameendelea kupatiwa huduma hizo kwa utaratibu wa msamaha. Hata hivyo, ni kweli kuna changamoto kwenye baadhi ya maeneo. Kuanza kwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote itakuwa suluhu ya kudumu katika kutatua tatizo hilo.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS aliuliza:-
Je, kuna mpango gani kuhakikisha wasanii wanafanya kazi zao kwa uhuru pasipo kuvunja sheria, kanuni na maadili ya Kitanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yetu kupitia Baraza la Sanaa la Taifa iliandaa Mwongozo wa Uzingatiaji wa Maadili katika Uzalishaji wa Kazi za Sanaa, ambao ulizinduliwa rasmi tarehe 3 Novemba, 2023. Kwa sasa tunaendelea na maboresho ya Kanuni za BASATA za Mwaka 2018 na pia mwongozo wa uendeshaji matukio ya sanaa ili kuweka misingi thabiti ya usimamizi wa matukio hayo.
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la maboresho haya ni kulinda maadili katika uzalishaji wa kazi za sanaa na kuwafanya wasanii wajitathmini wenyewe kabla hawajazalisha na kuzitoa kazi hizo kwa walaji. Aidha, BASATA inaendelea kutoa elimu kwa waandaaji wa kazi za sanaa kuzingatia miongozo iliyotolewa kabla ya kuzalisha kazi yoyote iwe ya sauti (muziki) ama ya kutengeneza maudhui mtandaoni.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa, BASATA inaendelea kuwaelimisha wasanii ili kuwajengea uelewa wa kulinda maadili ya Mtanzania katika uzalishaji wa kazi zao.