Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ummy Ally Mwalimu (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru, lakini nianze na kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi na Wanawake wa UWT wa Mkoa wa Tanga kwa kunipa heshima hii ya kurudi tena katika Bunge hili.
Pia kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa sana kwangu, namwahidi tutachapa kazi, kama kauli mbiu ya Serikali inavyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikiliza michango, maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na tunawashukuru wote ambao wamechangia katika eneo hili. Lengo ni kutaka kuboresha utoaji wa huduma za afya, lakini pia kuhakikisha tunajenga jamii ya Watanzania inayojali na kuheshimu usawa wa jinsia, haki za wanawake, haki za watoto na haki za wazee. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na niwathibitishie katika hatua hii kwamba tutafanyia kazi maoni yenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, nitajikita katika masuala makuu mawili ambayo yameongelewa sana na Waheshimiwa Wabunge wote. Kama walivyosema wenzangu, wakati wa kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mpango wa Maendeleo wa 2016/2017 tutatoa mwelekeo wa vipaumbele vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa ambalo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge, lakini pia limejitokeza kwa sauti kubwa wakati wa Hotuba ya Mheshimiwa Rais ni suala la upatikanaji wa dawa katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya katika Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba tumedhamiria kuhakikisha tunapunguza tatizo la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu. Tayari tumeshaanza kuchukua hatua na kwa sasa hivi uwezo wetu wa kutoa dawa ni asilimia 70 na tunakusudia tufikie asilimia 95. Hii tutawezaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza dawa ambazo zinafika kwa wananchi, nyingi zinapotea mtaani katika mikono ambayo siyo salama. Kwa hiyo, kubwa ambalo tumelifanya na tutaendelea kulifanya ni kudhibiti upotevu wa dawa za Serikali na vifaa tiba. Sasa hivi tumeshaweka nembo katika dawa zote za Serikali ambazo ni muhimu. Asilimia 80 ya dawa za Serikali sasa hivi tayari zina nembo.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuhamasisha wananchi wetu, watakapoona dawa ya Serikali ambayo ipo katika duka la dawa ambalo halistahili, watujulishe na wachukue hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo tumelifanya ni kuimarisha mfumo wa usambazaji, ununuzi na uhifadhi wa dawa. Hili ambalo tumelifanya tumeshaagiza MSD kuhakikisha dawa hazishushwi katika kituo chohote cha afya cha Umma bila kuwepo kwa Kamati ya Afya ya Kituo husika.
Waheshimiwa Wabunge, sisi sote ni Madiwani, tuhakikishe Kamati za Afya za Zahanati, za Vitua vya Afya za Wilaya zinatimiza wajibu wao wa kuhakikisha tunadhibiti dawa na vifaa tiba vya Serikali.
Jambo lingine ambalo ningependa kulisisitiza, mpango wetu wa muda mrefu ni kuhakikisha tunanunua dawa kutoka kwa wazalishaji, badala ya kununua dawa kutoka kwa wafanyabiashara na hili linawezekana sana. Kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kwamba tunabana matumizi. Kwa hiyo, tunaamini tutakaponunua dawa kutoka kwa wazalishaji, tutaweza kupata dawa nyingi, lakini pia kwa bei nafuu na hivyo kuweza kutatua tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, tutaongeza bajeti ya kununua dawa, vifaa na vifaa tiba. Waheshimiwa Wabunge, wameongelea suala la ukosefu wa X-Ray, Ultra-Sound, CT-Scan na MRI. Tayari tumeshachukua hatua, sasa hivi Muhimbili hamna shida tena katika vifaa hivyo vikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mpango pale Wizarani wa kuhakikisha katika kila Hospitali ya Rufaa ya Mkoa tunaiwezesha katika eneo zima la uchunguzi, maana yake, ni vifaa vyote ambavyo vinahitajika katika kufanya uchunguzi. Tayari tumeshapeleka mapendekezo yetu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuone ni jinsi gani tutaweza kusonga mbele.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, duh!
Meshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la miundombinu. Nikuhakikishie kwamba tutafanya kazi na wenzetu wa TAMISEMI kuhakikisha kwamba tunajenga zahanati katika kila kijiji, vituo vya afya katika kila Kata na Hospitali za Wilaya. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hili kwa kweli, sisi la kwetu itakuwa tu ni kuweka vibali. Kwa hiyo, wale Wabunge wote ambao wamejenga vituo vya afya...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ummy, tafadhali weka nukta!
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema, kama mwanamke, afya ya mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano. Tutahakikisha tunapunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano. Hilo ni la kipaumbele, tutaongea kwenye Mpango wa Maendeleo. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa, lakini kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuleta hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri. Katika hatua hii napenda kusema kuwa tumepokea maoni yenu na ushauri wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya, masuala makubwa ambayo yamejitokeza katika michango na maoni ya Waheshimiwa Wabunge, kwanza ni suala la miundombinu ya utoaji wa huduma za afya na ni suala linalohusu ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa kwa mikoa ile mitano mipya, lakini pia na hospitali za kanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwepo na suala la rasilimali watu na hili linahusika kwa kiasi fulani na uhaba wa madaktari, wahudumu, wauguzi na wafanyakazi wengine katika sekta ya afya. Lilikuwepo pia suala la upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na kwa upande wa sekta ya maendeleo jamii, jinsia na watoto, masuala makubwa matatu ambayo yamejitokeza katika mjadala huu ni suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi. Pia suala la elimu kwa watoto wa kike na suala la mainstream gender katika mipango yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge wote kwamba katika suala la miundombinu ya huduma ya afya, tutajenga zahanati katika kila kijiji kama tulivyoahidi, tutaonesha katika bajeti yetu, ni zahanati ngapi tutajenga katika mwaka wa fedha 2016/2017; tutaonyesha ni vituo vya afya vingapi vitajengwa na Hospitali za Wilaya ngapi zitajengwa. Tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kuhakikisha kwamba 2020 tunaporudi kuomba kura, Watanzania watatupa kura kwa sababu ya ahadi ya kuboresha miundombinu ya vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la rasilimali watu juzi niliongea. Tunao uhaba wa wafanyakazi especially madaktari katika vituo vyetu vya afya kuanzia ngazi zote, uhaba ni karibu 52%. Kwa hiyo, bajeti inayokuja ya mwaka 2016/2017, tutajikita katika kuajiri watumishi wapya wa sekta ya afya, Mmadaktari, wauguzi na wakunga lakini pia tutaweka kipaumbele katika ile Mikoa tisa kama nilivyosema ambayo ina uhaba mkubwa ikiwemo Katavi, Geita, Simiyu, Tabora na Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tutalipa kipaumbele ni kuhakikisha kwamba tunatoa motisha kwa Madaktari kukubali kufanya kazi vijijini. Kwa hiyo, tutahakikisha tunajenga nyumba za madaktari, lakini pia tunataka sasa hivi daktari yeyote ambaye anataka kuongeza ujuzi kwa kutumia fedha za Serikali tutampa mkataba, ata-sign mkataba kwamba atakaporudi atakwenda kufanya kazi Katavi kwa miaka mitatu kabla hajaamua kuondoka katika Serikali, hili linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la vifo vya akinamama wajawazito. Mimi ni mwanamke na nimepewa jukumu hili, nakubali ni changamoto kuona wanawake karibu 7,900 wanafariki kila mwaka kwa sababu tu wanatimiza haki yao ya uzazi. Kila saa moja tulilokaa hapa mwanamke mmoja wa Tanzania anafariki kwa sababu tu anatimiza haki yake ya msingi ya kuzaa. Nimedhamiria, tumedhamiria Wizarani hili suala tutalipa kipaumbele kuhakikisha vituo vya afya vyote vinakuwa na vifaa vya kufanyia upasuaji mdogo, maana wanawake wengi wanakufa kwa sababu wanakosa upasuaji, lakini suala la damu salama, suala pia la kuhakikisha kuna ambulance ili wanawake waweze kukimbizwa pale ambapo watapata matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala moja ambalo kwa kweli Mheshimiwa Edward Mwalongo amelizungumzia, vikwazo vya mtoto wa kike katika kupata elimu. Kwa mamlaka niliyopewa namtangaza Mheshimiwa Edward Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini kuwa shujaa, champion wa haki ya mtoto wa kike kupata elimu kwa mwaka 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutampa tuzo rasmi ya Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii. Kwa mara ya kwanza katika Bunge hili, mwanaume anasimama, anatetea haki ya zana za kujistiri kwa mtoto wa kike. Hili jambo tumelisema, lakini limesemwa na mwanaume kwa kweli tumepata nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Elimu mwanamke, Mheshimiwa Waziri anayehusika na Utumishi ni mwanamke, Mheshimiwa Jenista na mimi, tutalipigania kuhakikisha watoto wa kike wanapata taulo ili waweze kupata haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia afya njema. Pili, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, kwa maoni yao na ushauri mzuri kwa Wizara katika kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini, pia katika kujenga jamii ya Watanzania inayojali na kuheshimu haki za wanawake, haki za wazee na haki za watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Dkt. Godwin Mollel kwa hotuba yake nzuri na niwashukuru Wabunge wote waliochangia hoja ambayo tumeianza toka jana. Jumla ya Wabunge 123 wamechangia hoja hii. Wabunge 63 wamechangia kwa maneno kwa kuzungumza na Wabunge 60 wamechangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda na kwa mujibu wa Kanuni za Bunge nitashindwa kuwataja majina mmoja baada ya mmoja, lakini naomba Bunge tu litambue kwamba tunatambua michango yao, tunatambua ushauri wao na tupo tayari kusikiliza na kutekeleza ushauri mzuri waliotupatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza kwa makini taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, nimesikiliza kwa makini taarifa ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na nimesikiliza kwa makini michango ya Wabunge waliyoitoa toka jana. Naomba nitoe maneno ya utangulizi matatu. Kwanza nilichojifunza kutokana na mijadala iliyokuwepo hapa toka jana ni kwamba afya haina itikadi, afya haina vyama, afya haina rangi, afya haina kabila. Tumepata michango mizuri sana, watu wameweka ushabiki wa vyama pembeni, wamejikita kuchangia kwenye hoja ambayo iko hapa mezani, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, tunathamini sana michango yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kulianza la jumla ni kwamba, kutokana na mijadala toka jana, jambo ambalo limejitokeza wazi hakuna viwanda bila afya, hakuna ulinzi bila afya, hakuna kilimo bila afya, hakuna elimu bila afya na Mheshimiwa Mwigulu rafiki yangu anasema ukitaka mali utaipata shambani, lakini lazima tu-qualify huo msemo ukitaka mali utaipata shambani endapo utakuwa na afya bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu la jumla ambalo nataka kulisema hapa mbele ya Bunge lako Tukufu ni kwamba, tunatambua jukumu kubwa ambalo mimi na wenzangu tumekabidhiwa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini. Jukumu hili ni kubwa lakini nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, uwezo, dhamira na nguvu ya kupambana, kuhakikisha tunaboresha huduma za afya nchini tunao, pia katika kuhakikisha tunajenga jamii ya Kitanzania, inayowajali na kuwaheshimu wasichana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo ya utangulizi, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutoa ufafanuzi na Waheshimiwa Mawaziri pacha wangu Angellah Kairuki pia Naibu Waziri wa TAMISEMI na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba nijikite kwenye hoja kubwa ambazo zimetolewa na Kamati na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Naomba nisijikite kwenye hoja moja moja za Wabunge maana nina page takribani 175, nikisema namjibu kila Mbunge mmoja kwa kweli nitashindwa kumaliza. Nitajikita katika mambo makubwa matano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo limeongelewa ni suala la upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya sekta ya afya, Mheshimiwa Naibu Waziri amesaidia kufafanua, lakini nataka kujikita katika rasilimali fedha ambazo zinatoka katika chanzo cha Serikali Kikuu ambacho ni Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inatoa kipaumbele kwa sekta ya afya kwa sababu tukiangalia mwenendo wa mapato wa fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya sekta ya afya kwa Wizara yangu Fungu 52 na kwa ajili ya TAMISEMi utaona kwamba kumekuwa na ongezeko la bajeti ya fedha kwa ajili ya sekta ya afya. Kuanzia mwaka 2008 mpaka 2009, bajeti ilikuwa bilioni 769, mwaka 2014/2015, bajeti ya sekta ya afya ilikuwa trilioni 1.5 na kwa mwaka 2015/2016 bajeti ya sekta ya afya ilikuwa trilioni 1.8, mwaka huu wa fedha sekta ya afya imepatiwa maombi au imetengewa na Hazina bajeti ya shilingi trilioni 1.9. Kwa hiyo, kaka yangu Mheshimiwa Zitto nataka kuliweka wazi, ukichukua bajeti yote ya Serikali ya trilioni 29 na ukigawanya kwa 1.9, sekta ya afya siyo chini ya asilimia nne tuko kwenye asilimia saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kwa kweli tunatambua kwamba hatutaweza ku-finance hii sekta kwa asilimia mia moja kutoka Hazina. Naibu Waziri amelieleza vizuri, tunajikita katika kutafuta vyanzo vingine vya ku-finance na kuweza kusimamia sekta hii ya afya. Kubwa ambalo tunategemea kwamba tutapata fedha ni kwa kupitia huduma kwa kupanua wigo wa Mfuko wa Bima ya Afya lazima tuhakikishe Watanzania wengi wanakuwa wanachama wa Bima ya Afya kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri. Mwezi wa Septemba nitakuja mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Muswada ambao utawataka Watanzania wote kuwa na Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kuhusu utegemezi wa bajeti ya afya kwa wadau wa maendeleo, kwamba fedha za nje zimepungua nataka kuwathibitishia dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha tunatumia fedha zetu za ndani kwa ajili ya kutatua changamoto zetu. Hili nataka kulionesha kwamba kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutumia fedha zetu za ndani badala ya kutegemea wafadhili wa nchi za nje, tumeongeza bajeti ya vyanzo vya ndani kutoka bilioni 66 mwaka 2015/2016, sasa hivi tuna bilioni 320. Ni fedha zetu wenyewe Watanzania ambazo tutaweza kutumia kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika suala la pili ambalo limetolewa maoni na Waheshimiwa Wabunge wengi nalo ni suala la upatikanaji wa dawa. Nikiri kwamba tunazo changamoto katika upatikanaji wa dawa, lakini binafsi nauona mwanga baada ya kutoka katika shimo kubwa. Nauona mwanga kwa sababu bajeti ya kwanza ya dawa ya Serikali ya Awamu ya Tano imeongezeka kama tulivyoonesha, kutoka shilingi bilioni 66 lakini sasa hivi bajeti yetu ni shilingi bilioni 251 na hii 251 tumeiweka kwamba tutalipa deni la MSD ambalo ni takribani shilingi bilioni 85 na hela zinazobaki tutazitumia kwa ajili ya kununua dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiniuliza bajeti yangu ya kwanza ya afya, kipaumbele chake ni nini? Nitajibu mbele ya Bunge lako Tukufu na napenda kuwathibitishia Watanzania kwamba, bajeti hii ni bajeti ya dawa kwa sababu tutaweza kulipa deni la MSD zaidi ya bilioni 85.2, pia tumeweka fedha kwa ajili ya kununua dawa. Tumefanya haya makisio ni shilingi ngapi tunahitaji kwa ajili ya kununua dawa kwa mwezi? Kwa mwezi tunahitaji takribani bilioni 21, kwa hiyo kwa mwaka tunahitaji bilioni 252 na Mheshimiwa Rais ametupa maombi yetu kwa asilimia mia moja yamepitishwa, ndiyo tutalipa deni, lakini ndiyo fedha ya dawa, kwa hiyo tutaweza kulipa deni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Watanzania wajue kwamba, maneno ya Rais kwamba, tutatatua changamoto ya upatikanaji wa dawa hayakuwa maneno ya kuomba kura, yalikuwa ni maneno ya dhati na ndiyo maana dhamira yake hii ameionesha katika bajeti yake ya kwanza ya dawa. Ongezeko la dawa ni asilimia 810 ukilinganisha na bajeti ya dawa ya mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimesemwa changamoto mbalimbali kuhusu usambazaji na uhifadhi wa dawa. Changamoto zipo lakini tutaboresha mfumo mzima wa usambazaji ikiwemo ununuzi wa dawa kuhakikisha kwamba dawa zinafika katika vituo vyetu vyote vya afya kupitia bohari ya dawa. Tumeshatoa maelekezo pia kuhakikisha kwamba dawa lazima zifike, tatizo kubwa dawa zilikuwa zinachelewa kwa sababu MSD ilikuwa haina mtaji, lakini kama tutaweza sasa kupata hii fedha, tukawalipa deni, MSD wakawa na fedha ya ziada ya kununua dawa naamini dawa zitafika kwa Watanzania, dawa zitafika katika zahanati zetu na zitafika katika vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe angalizo kwa sababu Waheshimiwa Wabunge ni Madiwani, ni lazima na sisi tuzihimize Halmashauri zetu kuleta mapema maoteo yao ya dawa badala tu ya kushtukiza muda umefika ndiyo wanaleta maoteo yao ya dawa. Pili hatuwezi kutegemea fedha hizi za dawa za kutoka Serikali Kuu. Tutaendelea kuhimiza na kuhamasisha Halmashauri zitumie mapato yao ya ndani kwa ajili ya kununua dawa, vifaa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa mfano wa baadhi ya hospitali kabla ya kudhibiti mifumo ya ukusanyaji mapato walikuwa wanapata fedha ndogo, kwa mfano hospitali ya rufaa ya Kanda ya Mbeya walikuwa wanakusanya milioni 50 mpaka milioni 60 kwa mwezi, sasa hivi wanakusanya zaidi ya milioni 500. Kwa hiyo, kadri kituo cha afya kinavyokusanya fedha za mapato ya Bima ya Afya au ya papo kwa papo maana yake pia wataweza kujenga uwezo wao wa ndani wa kuhakikisha kwamba wananunua dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kwenda eneo la tatu nimezungumza suala la MSD kufungua maduka ya dawa. Tunataka kusema kwamba kwa sasa hivi tunataka kujikita katika hospitali za Rufaa za Kanda, hospitali kuu hizi za Kitaifa na hospitali za Rufaa za Mikoa. Nimeyasikia maombi ya akina Mheshimiwa Shabiby, Mheshimiwa William Ngeleja na Mheshimiwa Anna Lupembe kwamba twende sasa katika ngazi ya Wilaya na Wabunge wote ambao sikuweza kuwataja. Kwa hiyo, tunaomba sasa hivi kwa mwaka huu wa fedha mtuache kwanza tuishie katika ngazi ya hospitali za Rufaa za Mikoa, lakini lengo letu ni kuhakikisha kwa kweli tunapunguza changamoto zinazojitokeza katika upatikanaji wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja katika eneo hili ni kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya maamuzi magumu kwamba dawa karibu zote sasa hivi tutanunua kutoka kwa wazalishaji badala ya kununua kutoka kwa wafanyabiashara Dar es Salaam. Tunapingwa sana na wafanyabiashara. Kwa hiyo, hii itatusaidia kuhakikisha kwamba tunanunua dawa moja kwa moja na tayari tumeshapeleka mapendekezo kwa Waziri wa Fedha kuhakikisha kwamba Sheria ya Manunuzi pia inaondoa dawa katika bidhaa ambayo itafuata taratibu zile ambazo kidogo ni ndefu za kununua dawa na vifaa na vifaa tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo kubwa ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge takribani wote ni vifo vya mama na mtoto na mimi ni mama wa mabinti warembo wawili na mume wangu leo yuko hapa. Kwa hiyo, kama mwanamke naguswa na suala la vifo vitokanavyo na uzazi, lakini niweke wazi kwamba kwanza sitaki kubishana na Bunge lako Tukufu kwamba vifo hivi ni 42 kwa siku au ni vifo 22 kwa siku. Ninachotaka kusema ni msimamo wetu Serikali, msimamo wa Wizara, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa ambayo imetolewa mwaka 2015 na ambayo ndiyo tunaitumia, kwa mujibu wa taarifa hii vifo ni 22 kwa siku na siyo vifo 42 kwa siku. Hii haitupi sisi sababu ya kutochukua hatua, haitupi sisi sababu ya kuhakikisha hawa wanawake 42 na wenyewe tunawahakikishia usalama wao na usalama wa vichanga vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya utafiti na kugundua sababu zinazopelekea vifo vya akinamama wajawazito. Sababu ya kwanza ni kutokwa na damu nyingi ambapo ni takriban asilimia 19, pia kuna kifafa cha mimba, kuna masuala ya uzazi pingamizi lakini kuna uambukizi na sababu nyingine ikiwemo ukosefu wa damu, malaria na maambuzi ya VVU- UKIMWI. Kwa hiyo, Bunge lako Tukufu pamoja na Kamati wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wametaka kujua tumejipangaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo tutalifanya ni kuhakikisha tunapandisha hadhi vituo vya afya ili viweze pia kufanya upasuaji wa kutoa mtoto. Tukifanya hivi maana yake tutapunguza vifo kwa takribani asilimia11 na la pili ambalo tutalifanya ni kuhakikisha kwamba tunahakikisha upatikanaji wa damu salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hili nipongeze vyama vyote, chama changu Chama cha Mapinduzi kupitia Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wamejitolea kukusanya damu lakini pia tumeona wenzetu wa Chama cha CHADEMA na wenyewe wakijitolea kukusanya damu. Ndiyo maana tunasema afya haina itikadi, afya haina vyama. Niko tayari kuambatana na kushirikiana na vyama vyote endapo tu tutaweza kupata damu salama ili tuweze kuokoa akinamama wajawazito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutahakikisha pia tunaanzisha benki za damu salama katika mikoa na kanda mbalimbali na tayari nimeshatoa maelekezo na naomba nitoe maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya, kuhakikisha angalau kila mwezi wanakuwa na mpango wa kuchangia damu salama kwa wiki. Tukifanya hivi tutaweza kuhakikisha tunaokoa maisha ya akinamama wajawazito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tutalifanya ni kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya wanawake wajawazito ambao wanahudhuria kliniki na kujifungua katika vituo vya afya. Ukiangalia takwimu sasa hivi ni takriban wanawake asilimia 51 ndiyo wanajifungua katika vituo vya afya. Tutaendelea kufanya mikakati na programu mbalimbali za kuhamasisha wanawake kujifungua katika vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe, Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mheshimiwa Abdallah Mtulia na Mheshimiwa Zuberi Kuchauka wameongelea kwa uchungu suala la vifaa vya kujifungulia wanawake, tena kaka yangu Mheshimiwa Zuberi ndiyo ametoa mfano mbaya. Mwanamke anakwenda na beseni utasema anakwenda kufunga harusi! Kwa sababu na mimi nimepita labour mara mbili, nimeshafanya maamuzi katika bajeti hii, tutatoa vifaa bure vya kujifungulia kwa wanawake wajawazito na tutaanza na wanawake laki tano. Tutagawa kutokana na uwiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Liwale wanazalisha kwa mwaka wanawake 80, kwa hiyo tutakupa asilimia 25 ya wanawake hawa, lakini lengo letu ni wanawake wote wanaokwenda kujifungua wapate vifaa hivi bure, badala ya kufikiria pamba, mkasi au gloves, tunataka wanawake wafikirie jambo moja tu, la kusukuma kutoa mtoto, hili linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutahakikisha pia tunahamasisha wanawake kutumia njia za uzazi wa mpango, pia kuongeza ushiriki wa jamii katika masuala haya ya uzazi salama. Jana nilitoa mfano wa Kijiji cha Uturo ambacho tangu mwaka 1998 hawana vifo vitokanavyo na uzazi kwa sababu tu wao jamii imeamua kushirikiana nao na wameweza kupunguza vifo hivi na kwa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambapo tunawaita Community Health Workers. Katika bajeti hii tutaajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kuhamasisha na kutoa elimu ya afya ile ya awali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezungumzwa suala la upatikanaji wa ambulance nalo linasaidia kwa kiasi fulani kuokoa vifo vya akinamama wajawazito. Nataka niseme bajeti hii haijapanga kununua ambulance hata moja kwa hiyo amesema vizuri Mheshimiwa Jaffo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, hili ni jukumu la Halmashauri husika. Natoa changamoto kwa Wabunge Wanawake na Madiwani Wanawake wa Tanzania, hivi mko wapi wakati Halmashauri inapanga vipaumbele, hawapangi vipaumbele vya uzazi salama? Lazima hili tulibebe, Wabunge wanawake tuungane, Madiwani wote wanawake lazima washike hatamu katika kuhakikisha kwamba Halmashauri zinaweka vipaumbele katika uzazi salama ikiwemo kujenga vituo vya afya, ikiwemo pia kununua haya magari ya wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru Waheshimiwa Wabunge. Najua Wabunge wengi wamenunua magari ya wagonjwa (ambulance), Wabunge wengi wamenunua mashuka, vifaa na vitanda vya kujifungulia. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na nasema mnawatendea haki wapiga kura wenu kwa sababu asilimia 51 ya wapiga kura wenu ni wanawake. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kuona Mfuko wa Jimbo ukielekezwa kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zinazowakabili wanawake ikiwemo suala la uzazi salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Wabunge wanawake pia naelewa kwa nini wanaomba na wenyewe wapewe Mfuko wa Jimbo ili wakaweze kutatua changamoto zinazowakabili wanawake katika Majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nizungumzie suala la huduma za uzazi wa mpango, ni kweli tunakubali kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi yenye ongezeko kubwa la watu takriban kwa asilimia 3.1 kwa mwaka. Ili kuonesha kwamba Awamu ya Tano imedhamiria kutatua changamoto hii. Tumeweza kubajeti fedha ingawa siyo fedha kubwa, lakini kwa mara ya kwanza tumeweka bilioni tano za ndani kwa ajili ya kufanyia kazi ya kutatua changamoto zinazohusika na huduma za uzazi wa mpango. Tulikuwa tunategemea wafadhili wa nje lakini ili kuonesha dhamira yetu ya wazi tumeamua kutenga fedha za ndani kwa ajili ya uzazi wa mpango, of course na wadau wetu wa maendeleo wametutengea bilioni 12.8 kwa ajili ya uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba wanawake wengi wanataka kutumia huduma za uzazi wa mpango na hatujaweza kuwafikia kwa sababu sasa hivi kwa mujibu wa TDHS ya mwaka 2010, takriban wanawake asilimia 20 tu ndiyo wanatumia matumizi haya ya njia za kisasa za uzazi wa mpango, lengo letu ni kuhakikisha tunapokwenda mwaka 2020 tufikie wanawake asilimia 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda pia naomba nimalize kwa kusema katika suala la vifo vya akinamama wajawazito ni eneo la kipaumbele changu, hivyo ni kipaumbele cha Wizara na kipaumbele cha Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Tunaamini kwamba wanawake wenzetu hatutawaangusha na tutaleta mabadiliko makubwa katika kuboresha huduma ya afya ya uzazi na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala la matibabu kwa wazee, ninayo Sera ya Afya ya mwaka 2007. Kwa mujibu wa Sera ya Afya ambapo mimi nimepewa dhamana ya kuisimamia, bado wazee kuanzia miaka 60 wanatakiwa kupata matibabu bure, wajawazito wanatakiwa kupata matibabu bure na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanatakiwa kupata matibabu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuongea na wenzangu na kaka yangu Mheshimiwa Bashe ali-propose kwamba tuwakatie Bima ya Afya wanawake wajawazito ambapo kwa mujibu wa takwimu zetu deliveries kwa mwaka ni kama milioni 1.2 mpaka milioni 1.5. Tumepiga mahesabu, milioni 1.5 ukizidisha mara 50,400 ni takriban bilioni 76, sitaki kudanganya Wabunge, sitaki kudanganya Bunge lako kwamba tutakuwa nazo bilioni 76, lakini tutakachofanya ni kuona ni jinsi gani Mfuko wa Bima ya Afya na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inachukua hatua, inaongeza jitihada katika kuhakikisha sera za Serikali zinatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wazee tutahakikisha kwamba madirisha haya ya wazee katika hospitali zetu yanafanya kazi na kwa mujibu wa sera ni kwamba mzee anatakiwa kupata huduma za ushauri wa Daktari (consultation) iwe ni bure. Vipimo mzee anatakiwa kuwa bure, pale ambapo labda dawa hakuna ndipo mzee ataambiwa akanunue dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie Bunge hili kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa wote, Waganga Wakuu wa Wilaya wote na Wakuu wa hospitali za umma wote, kuhakikisha kwamba wanatoa huduma za matibabu bure kwa wazee na tutahakikisha kwamba hiyo changamoto ya dawa kwa wazee tunaitatua. Nimeshamuagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali kwamba katika kila ile bajeti ya dawa, basi tutenge asilimia ya fedha kwa ajili ya kununua dawa kama nne au tatu muhimu kwa ajili ya matibabu ya wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, jambo hili wenzangu wamelikubali, kwa hiyo, tutaelekeza kwamba kwa mfano Halmashauri inanunua dozi laki moja za antibiotic, wazee ni asilimia 5.6, sioni ni kwa nini tushindwe kuwahudumia wazee wetu. Katika kila Watanzania 100 maana yake utakuwa na wazee sita. Hili jambo linawezekana kabisa. Kwa hiyo, tutahakikisha katika kila dawa tunatenga dawa kama tatu au nne ambazo zinagusa magonjwa ya wazee mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu, wao hawajatenga tu dirisha kwa ajili ya wazee, lakini wameweka sehemu maalum kwa ajii ya kutoa matibabu kwa wazee. Mzee akienda pale anapata vipimo, anapata dawa, anamwona Daktari! Kwa hiyo, nitoe changamoto kwa Waheshimiwa Wabunge, wazee ni hazina na kama kampeni yetu inavyosema, “mzee alikuwa kama wewe na wewe utakuwa kama yeye, tutoe kipaumbele cha huduma kwa wazee”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize suala la upatikanaji wa huduma za afya. Waheshimiwa Wabunge wameongea, tangu jana. Nashukuru sana Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu) kidogo alitusaidia, kwa sababu Wabunge tangu jana wameongea kuhusu zahanati, wameongea kuhusu vituo vya afya, wameongea kuhusu hospitali za Wilaya. Hatukatai kwamba Sera ya Afya iko chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya, lakini anayetakiwa kuweka hii miundombinu ni wenzetu wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimeona upatikanaji wa huduma za afya katika ngazi ya chini unahusiana moja kwa moja na kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto, tumeshakaa na mwenzangu Mheshimiwa George Simbachawene na kuona kwamba, ni lazima baada ya bajeti yangu, kesho, wataalam wangu watatu watakaa pamoja na wataalam watatu wa Mheshimiwa Simbachawene na watu wa Fedha, tuoneshe ni jinsi gani sasa tutajenga vituo vya afya, tutajenga hospitali za wilaya na hospitali za mikoa katika mikoa ambayo haina huduma hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge. Wizara ya Afya kazi kubwa ambayo ilifanya ni kuhakikisha ujenzi wa miundombinu umeingia katika Mpango wa Maendeleo wa Pili wa mwaka 2016 - 2021 na pesa zimetengwa. Kwa hiyo, tutaonesha katika kila mwaka tutajenga vituo vya afya vingapi na tutajenga hospitali za Wilaya ngapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge, naamini kwa boss wangu Mheshimiwa Rais, Dkt, John Pombe Magufuli ambaye anataka kuona mambo tangible, tutaweza kujenga vituo vya afya katika kata zetu, katika wilaya zetu. Nataka kuwathibitishia, maneno yaliyokuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi yatasimama na tutaonesha matokeo yake. Mwaka 2020 tutakapokuja kwa Watanzania tuwaeleze tumejenga vituo vya afya vingapi na hospitali za wilaya ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui nina muda kiasi gani niende kwenye eneo la jinsia. Sitawatendea haki wanawake wenzangu, watoto kama sitagusa suala la usawa wa jinsia na uwezeshwaji wa wanawake. Nataka kujikita katika mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza ambalo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi akiwemo dada yangu Mheshimiwa Faida Bakar, Mheshimiwa Aida Khenani na Mheshimiwa Anna Lupembe kwamba Benki ya Wanawake tunataka kuiona ikienda katika mikoa, katika wilaya na katika kata mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwathibitishia kwamba katika mwaka huu wa fedha tutafungua vituo vitatu vya Benki ya Wanawake katika mikoa mitatu. Pia nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kati ya riba ya asilimia 10 mpaka asilimia 12 ili Benki ya Wanawake iweze kukidhi matarajio ya kuanzishwa kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo pia tutalifanya kupitia Benki hii ya Wanawake ni kutoa mikopo midogo ya kuanzia laki mbili mpaka milioni moja bila kuwataka wanawake watoe dhamana ya hati ya kiwanja, hati ya nyumba au wengine wanatoa fenicha, wengine wanaambiwa walete sijui mikufu yao, hatutafanya hivyo. Tunataka kuonesha ni kiasi gani tumedhamiria kuwakomboa wanawake wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kuhusu haki za mtoto na hapa niwapongeze wadogo zangu watatu, Mheshimiwa Upendo Peneza, Mheshimiwa Halima Bulembo na Mheshimiwa Maria Kangoye, wameonesha ni jinsi gani wanaguswa na tatizo na changamoto zinazowakumba wasichana wenzao. Pia Mwalimu Kasuku S. Bilago na Mheshimiwa Mama Margaret Sitta wamegusia kwa kiasi fulani haki ya mtoto wa kike kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwathibitishia Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano inaamini kwamba, maendeleo ya kweli na endelevu ya Tanzania hayataweza kupatikana iwapo asilimia kubwa ya wanawake hawatakuwa na elimu. Mimi ni muumini, mbeleko ya kweli ya mwanamke na mtoto wa kike ni elimu, habebwi na kitu kingine chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo takwimu ambazo zinaonesha kwamba, kwa kila mwaka mmoja ambao mtoto wa kike anapata elimu, unamkinga na maambuzi ya UKIMWI mara saba, lakini katika kila mwaka mmoja ambao mtoto wa kike anapata elimu unamuepusha na vifo vya uzazi. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba tunatatua changamoto zinazomkabili mtoto wa kike katika kupata elimu ikiwemo kupata zana za kujisitiri ili kuhakikisha kwamba watoto wetu wanasoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha, lakini katika suala la ukeketaji, ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na wanaume pia, dawati letu lile linaitwa Dawati la Jinsia, haliitwi dawati la wanawake, kwa hiyo wanaume ambao mnapata vipigo ndugu zangu msione aibu, nendeni mkaripoti kwenye Dawati la Jinsia ili muweze kupata haki zenu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la mwisho la maendeleo ya jamii, Waheshimiwa Wabunge wamependekeza kwamba Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi tuvihamishe viende VETA. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tayari Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa, amehamisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kwenda Wizara ya Elimu ili viweze kutoa mafunzo ya VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kuniamini, pia nakishukuru sana chama changu Chama cha Mapinduzi na wanawake wa Mkoa wa Tanga kwa kunirudisha Bungeni. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Watendaji wote wa Wizara, Katibu Mkuu Dkt. Mpoki, Katibu Mkuu Mama Sihaba Mkinga na Waheshimiwa Mawaziri wote, hasa Mheshimiwa Angellah Kairuki na Mheshimiwa George Simbachawene ambao wananipa ushirikiano mkubwa katika utendaji wa kazi zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tena, jana nilimshukuru mume wangu lakini hakuwepo, namshukuru sana, sana kwa uvumilivu wake na kwa moyo wake wa kunishauri na kunitetea. Nakushukuru sana Mume wangu Paschal, Mwenyezi Mungu akubariki, Mwenyezi Mungu akuzidishie heri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami jianze kwa kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Taarifa yao, lakini nawashukuru kwa ushauri na maoni ambayo wamekuwa wakitupatia mara kwa mara katika kuboresha utendaji wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua hii niseme kwamba Wizara yangu inapokea maoni na ushauri wa Kamati kama walivyoyawasilisha hapa na ninaahidi kwamba tutayafanyia kazi masuala yote waliyoyabainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, napenda kutoa ufafanuzi katika masuala makuu matatu kama muda utatosha na suala la kwanza ni kuhusu hali ya upatikanaji wa dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa nchini ilikuwa inasababishwa na upatikanaji wa fedha, lakini hivi ninavyosema tumetoka katika kutaja bajeti ya Afya ya shilingi bilioni 251 na kusema pesa ambazo Wizara ya Afya imepokea; mpaka sasa hivi tumepokea shilingi bilioni 91 kwa ajili ya kununua dawa, vifaa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia mwaka 2016 MSD ilipokea shilingi bilioni 24 tu kwa mwaka mzima kwa ajili ya kununua dawa. Sasa hivi kila mwezi Wizara ya Fedha inatuletea shilingi bilioni 20. Tumetoka kwenye kupokea shilingi bilioni mbili kila mwezi tunapokea shilingi bilioni 20 kila mwezi kwa ajili ya dawa. Kwa hiyo, baada ya kuwa tunapata fedha, hali ya dawa kwa kiasi kikubwa inazidi kuimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tunapimaje upatikanaji wa dawa? Tunaangalia upatikanaji wa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa. Hivi sasa MSD ana aina za dawa 105 kati ya dawa 135 muhimu za kuokoa maisha. Hii ni sawa na 78%. Nakiri kwamba sasa hivi kazi inayoendelea ni kuhakikisha dawa hizi sasa zinashuka katika zahanati zetu na vituo vya afya.
Waheshimiwa Wabunge, nimewaandikia barua na kesho mtaipata kuainisha mchanganuo wa kila fedha ya dawa ambayo tumebajeti katika Halmashauri yako ili uweze kupima. Kubwa tunawaomba msimamie matumizi ya fedha za dawa na matumizi ya dawa. Hali ya upatikanaji wa dawa kama wote hatutaimarisha Kamati za Vituo, basi hatutaweza kuwa na upatikanaji wa dawa hasa katika ngazi za chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitoe angalizo, hatuwezi kuwa na upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100 kwa sababu ya ongezeko la watu kila siku, ongezeko la magonjwa na vituo. Kwa hiyo, kubwa ambalo Wizara ya Afya tunalifanya sasa hivi ni kujikita kwenye kinga badala ya tiba. Maana inakuwa ni Taifa la kujikita kwenye tiba badala ya kinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo tumeibaini ni MSD anabajeti fedha ya kununua dawa kutoka kwenye Fungu 52 - Wizara ya Afya, lakini kuna fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya, kuna vyanzo vya makusanyo tumeomba wenzetu wa TAMISEMI, maana MSD ananunua dawa za wateja za shilingi bilioni 70, lakini wateja wake wana fedha za kununua dawa za shilingi bilioni 300. Kwa hiyo, haiwezekani MSD kuweza kutosheleza soko lake. Nawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutafanyia kazi suala hili la kuhakikisha dawa zinafika kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwamba MSD ipewe fungu, tulipokea ushauri wa Kamati na tukamwandikia Waziri anayehusika na masuala ya Utumishi na Utawala Bora kwa sababu wao ndio wanatoa Vote. Wakatushauri tuombe line item. Sasa hivi tuna line item katika Bajeti ya Wizara ya Afya kwa ajili ya MSD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Halmashauri ambazo zinadaiwa fedha na MSD ziruhusiwe zilipe kidogo kidogo; tumepokea pia ushauri wa Kamati. Sasa hivi katika ile fedha ambayo tunaingiza katika bajeti ya Halmshauri, tunakata asilimia 25 tu, asilimia 75 tunawapa kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu deni la MSD, mpaka sasa hivi tumelipa shilingi bilioni 11, lakini tumeona chanzo kinachofanya deni hili likawa kubwa ni tozo. Kwa hiyo, tayari tumewaelekeza tupitie tozo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Kamati inashauri kwamba i-cover magonjwa yote. Nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia mwezi Septemba tumeingiza kitita cha huduma za upasuaji wa moyo na matibabu mengine ya hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NHIF kusimamia kuweza kutumika Bima zao mpaka nchi za Afrika Mashariki, sheria iliyoanzisha NHIF inaruhusu NHIF kufanya kazi ndani ya nchi. Tumepokea ushauri na tutaleta. Waheshimiwa Wabunge ni mapendekezo yenu, tutayaleta hapa ili NHIF itumike ndani ya nchi za Afrika Mashariki, nasi tuko tayari na ninaamini kwamba Muswada huu mtaweza kuupitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize neno moja tu. Kuhusu uzazi wa mpango, nakubaliana na ushauri wa Kamati kwamba ni changamoto kubwa, Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono. Ni asilimia 32 tu ya wanawake wanaotumia uzazi wa mpango. Lengo letu ni kuhakikisha huduma hizi zinapatikana mitaani badala tu ya kwenye vituo vya afya na hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uzazi salama ni kipaumbele chetu. Nawathibitishia Waheshimiwa Wabunge, nikiwa Waziri mwanamke na mama wa watoto wawili, tutasaidiana kupunguza vifo vya akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa jinsi ambavyo wameandika ripoti yao vizuri na ushirikiano wanaotupa katika kufanya na kutimiza majukumu yetu. Niwahakikishie kwamba mapendekezo yao mazuri sana waliyoyatoa kwenye ripoti yao tutayafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Mheshimiwa Kadutu kuwapongeza sana Serengeti Boys kwa mafanikio makubwa waliyoyapata na kuipa heshima nchi yetu kwa kufanikiwa kwenda kwenye fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba hata kufika pale walipofika kuna mkono mkubwa sana wa Serikali. Wakati mwingine siyo kila jambo unalisema hadharani, lakini ni hakika kwamba mkono wa Serikali umesaidia wao kucheza na kufika pale walipofika, lakini pia kusukuma rufaa yao mpaka wakapata kushinda na kwenda kwenye fainali za mashindano haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Watanzania kwa pamoja, bila kujali tofauti zetu tuungane kwa pamoja, tuwatie moyo vijana hawa na kuwasaidia. Tunaamini watafanya vizuri kwenye mashindano haya na bila shaka tunaweza tukarudi na kombe. Wakifika nusu fainali, basi tuna uhakika wa kwenda kwenye Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo mazuri ya Kamati na wameainisha humu changamoto ambazo zinaikabili sekta ya michezo, niseme tu moja ya eneo kubwa ambalo linatusumbua sana ni namna ya ku-finance michezo katika nchi yetu. Niahidi katika Bunge hili kwamba tutaleta hapa Bungeni mpango mahsusi wa ku-finance michezo katika nchi yetu na hili litakuwa jibu la tatizo hili la kuendelea kwa michezo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitia Sera ya Michezo kama walivyoeleza katika taarifa yao na baada ya muda sera hii itakamilika, iko katika michakato ya mwisho. Ikikamilika, tutaleta sheria na kanuni zake hapa na bila shaka itasaidia sana katika ukuaji wa sekta ya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la mwisho ambalo nilipenda nilizungumzie ni suala la usikivu na utendaji kazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa. Ni kweli kama ilivyooneshwa kwenye ripoti ya Kamati, Wilaya 81 za nchi yetu TBC haisikiki kabisa. Waheshimiwa Wabunge, tukumbuke wakati fulani TBC ilikuwa inasikika nchi nzima wakati tukitumia teknolojia ya zamani. Bahati mbaya wakati wa mabadiliko haya ya teknolojia mpya, vifaa vingi vile vya zamani sasa havifanyi kazi tena na uwekezaji ulikuwa haujafanyika wa kutosha na ndiyo maana ukweli ni huo kwamba nusu ya nchi yetu inasikika na nusu ya nchi yetu haisikiki. Sasa kwa Shirika la Utangazaji la Taifa kusikika nusu ya nchi, nadhani ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie Bunge lako kwamba bajeti ijayo nadhani tutafanikiwa kuleta hapa mpango wa kupata fedha za kutosha wa ku-finance TBC. Uwekezaji mkubwa unahitajika ili kusaidia katika teknolojia, lakini pia kuboresha studio zao na vipindi vyao. Nina hakika Bunge hili likituunga mkono tutakapoleta mapendekezo hayo tutapata pesa za kutosha na tutaliondoa Shirika letu la Utangazaji pale lilipo na ndoto zetu kwamba liwe shirika bora kabisa katika nchi yetu. Inahitajika uwekezaji mkubwa, naamini Bunge litatuunga mkono wakati utakapofika na tutakapoleta hapa wakituunga mkono, tunaamini Watanzania watafurahia huduma nzuri na kazi nzuri ya Shirika la Utangazaji la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuunga mkono mapendekezo mengi yaliyoletwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge. Nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Ahsante sana.