Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ummy Ally Mwalimu (1 total)

MHE. UMMY A. MWALIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, kata 10 kati ya kata 27 za Halmashauri ya Jiji la Tanga zina mitaa yenye sifa za vijiji, kama vijiji vya Muheza, Handeni, Mkinga, Pangani na Korogwe Vijijini. Kwa nini mitaa hii yote isiingizwe katika utaratibu wa wananchi kupata umeme wa REA wa shilingi 27,000?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa, Wakuu wa Nchi wamepitisha Azimio la Nishati Safi la Dar es Salaam chini ya uenyeji wa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa nini Serikali isianzishe programu maalum ya kuwawezesha wananchi kuunganisha umeme wa mkopo halafu walipe kidogo kidogo, kupitia matumizi ya kila siku ya umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kuhusiana na Mitaa ya Tanga Mjini ambayo Mheshimiwa amesema iunganishwe na REA kwa sababu, ina sifa za vijiji. Ndiyo maana Serikali tunatekeleza miradi ya Peri-Urban kwenye maeneo haya, ili kurahisisha kuwafikia wateja wengi zaidi kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwa sasa hivi ndiyo maana tumepeleka umeme katika vitongoji 15, lakini miradi ya Peri-Urban inaendelea, ili wananchi waweze kuunganisha umeme kwa gharama nafuu. Jambo la kuendelea kuwasisitiza, ni kwamba, wakati miradi inaendelea, basi wananchi waweze kuunganisha umeme, ili kuepuka kadhia pale ambapo miradi inaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili la wananchi kuunganisha umeme na kulipa kidogo kidogo. Ninapokea wazo la Mheshimiwa Mbunge na tutaendelea kulichakata ili kuona namna ya kulifanyia kazi kwa sababu, huko nyuma tayari TANESCO walijaribu kufanya hivyo, baadaye wakawapatia Akiba Commercial Bank kufanya hivyo, lakini marejesho hayakuwa mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuchakata kuona namna ambayo tunaendelea kulifanyia kazi ili wananchi waendelee kupata huduma. Kwa hiyo, ni wazo zuri, tutaendelea kulichakata. Ahsante.