Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Issaay Zacharia Paulo (10 total)

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Ingawa kuna tatizo la ajira Serikalini, lakini inasemekana kuwa ziko nafasi nyingi zilizo wazi katika ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya hata Vijiji:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali inalificha jambo hili na ni lini sasa itajaza nafasi za ajira zilizo wazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu katika sekta za Utawala kama vile VEO, WEO ambapo wananchi huwalipa watumishi wa kukaimu kwa fedha zao wenyewe kinyume na taratibu?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isipandishe mishahara ya kima cha chini kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya sasa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya nafasi za ajira mpya Serikalini hufanyika kwa uwazi kupitia bajeti ya Serikali ambayo huidhinishwa na Bunge hili. Ajira hizi hufanyika baada ya waajiri kuwasilisha maombi yao Serikalini na kuidhinishwa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilitengewa nafasi za kuajiri Watendaji wa Vijiji (VEO) kumi na Watendaji wa Kata (WEO) Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nafasi hizo Serikali itaendelea kujaza nafasi wazi kila mwaka kulingana na uwezo wa kibajeti na vipaumbele vilivyowekwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipandisha kima cha chini cha mshahara kulingana na uwezo wa bajeti au mapato ya ndani na kwa kuzingatia kupanda kwa gharama za maisha. Kutokana na hatua hii, Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo kwa sasa hulipa kima cha chini cha mshahara sawa na asilimia 80 ya kiwango cha gharama za chini za maisha (minimum living wage).
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wake wa umma kulingana na uwezo wake wa kiuchumi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Serikali imekuwa na azma nzuri kujenga zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata nchi nzima:-
(a) Je, ni lini Serikali itapanua Chuo cha MCH Mbulu kinachotoa cheti kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Binadamu kwa kuwa tayari Baraza la Madiwani limekubali kutumia ardhi yake ya akiba?
(b) Je, kwa nini Serikali isitembelee chuo hicho ili kujionea fursa zilizopo?
(c) Je, ni kwa nini pia Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tango FDC kisitumike kama chuo cha VETA kwa sababu kwa sasa hakina taaluma nzuri katika fani mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Uuguzi na Ukunga Mbulu kiliandaliwa kwa ajili ya kukidhi mafunzo kwa ngazi ya cheti kutokana na miundombinu iliyokuwa nayo pamoja na uwezo wa hospitali inayotumika kama sehemu ya mafunzo. Upanuzi wa vyuo kudahili wanafunzi wa kada za juu kwa kawaida huwa unaendeana sambamba na upanuzi wa miundombinu na upatikanaji wa wataalam kwenye hospitali iliyoridhiwa kuwa ni hospitali ya mafunzo. Wizara ya Afya inaishukuru Halmashauri ya Mbulu kwa kuanzisha mchakato wa kukitengea eneo zaidi chuo hiki ili kijipanue zaidi. Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI juu ya upatikanaji wa ardhi hiyo kabla ya kuingiza suala la upanuzi wa chuo hiki katika mipango yetu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikitembelea Chuo cha Mbulu katika taratibu zake za kawaida za kiutendaji. Mwaka 2015/2016, timu za Wizara zimefanya ziara za ufuatiliaji kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya ukusanyaji taarifa na pia katika kukagua miradi ya maendeleo na ukaguzi wa hesabu za mapato na matumizi ya fedha. Kwa mwaka 2016/2017, Wizara itafanya ufuatiliaji kwenye chuo hiki na lengo kuu litakuwa ni kuona utekelezaji wa ahadi hii ya Halmashauri kuhusu upatikanaji wa ardhi.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi – Tango kinatoa mafunzo ya maarifa na stadi katika fani za kilimo na mifugo, ushonaji, useremala, uashi na umeme wa majumbani. Aidha, hutoa pia mafunzo ya udereva kwa muda mfupi wa miezi mitatu. Chuo hiki kina watumishi wapatao 21 na wakufunzi 10. Kwa sasa chuo kina wanachuo 98 ambapo 59 wanachukua mafunzo ya ufundi stadi kwa kufuata mtaala wa Mamlaka ya Ufundi Stadi yaani VETA Level I - III na 39 wanachukua mafunzo ya muda mfupi ya udereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vina makubaliano maalum na VETA yaani MOU (Memorandum of Undestanding) ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na yale ya elimu ya wananchi ambayo yalikuwa yakitolewa tangu awali. Kufuatia makubaliano hayo, vyuo 25 viliboreshwa na kuanza kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na mafunzo ya elimu ya wananchi kuanzia mwezi Januari, 2013. Lengo likiwa ni kuhakikisha Vyuo vyote 55 vya Maendeleo ya Wananchi vinatoa mafunzo kwa mifumo yote miwili yaani mafunzo ya elimu ya wananchi na yale ya ufundi stadi (VETA).
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango kimewekwa katika awamu ya pili ya maboresho hayo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kumekuwa na ahadi za viongozi wa juu hususan Marais za kujenga daraja la Magara pamoja na barabara ya Mbuyu wa Mjerumani kwa kiwango cha lami na usanifu wa daraja na lami ya zege sehemu ya mlimani hasa ikizingatiwa kuwa ukosefu wa daraja na jiografia ya Mlima Magara kuwa hatarishi sana hasa kipindi cha mvua.
(a) Je, ni lini ahadi hiyo ya viongozi wetu wa Kitaifa itatekelezwa?
(b) Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano katika Mji wa Mbulu itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha Mji wa Mbulu na barabara Kuu ya Babati – Arusha katika eneo la Mbuyu wa Mjerumani. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Magara lenye urefu wa mita 84. Taratibu za kumpata mhandisi mshauri wa kusimamia ujenzi wa daraja hili zinaendelea. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inafanya maandalizi ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Magara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja la Magara na shilingi milioni 455 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha zege (rigid pavement) kwenye Mlima Magara katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itaendelea kutekeleza ahadi za viongozi wa Serikali kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwemo ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami katika Mji wa Mbulu yenye urefu wa kilometa tano.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Aliuliza:-
Maziwa Madogo nchini kama vile Ziwa dogo la asili la Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu yanaelekea kukauka kutokana na kuongezeka kwa magugu maji, kadhalika Ziwa Babati na Ziwa Manyara pia yana dalili ya kukauka na Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina uwezo wa kuyaokoa:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyaokoa maziwa hayo muhimu katika ustawi wa nchi yetu na kizazi kijacho?
(b) Je, kwa nini kusiwe na mpango kabambe wa Kitaifa kuyaokoa maziwa hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu mkubwa wa kuokoa Ziwa dogo la Tlawi lililopo Halmashauri ya Mbulu na maziwa mengine kote nchini yanayokabiliwa na tishio la kukauka na magugu maji kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu hususan kilimo na ufugaji usio endelevu, uvuvi haramu na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu huo, mwaka 2008 Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Bahari Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa. Mkakati huu unaelekeza Wizara na sekta na halmashauri zote nchini kuchukua hatua za haraka kuzuia shughuli zote za binadamu kufanyika kandokando ya maziwa, mito na mabwawa ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha kukauka kwa maziwa hayo.
Mheshimiwa Spika, ili kunusuru Ziwa dogo la Tlawi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imechukua hatua zifuatazo:-
1. Mradi wa DADP’s Wilaya ya Mbulu umetenga Shilingi milioni 100 katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa ajili ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Tlawi.
2. Katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imepanga kutenga kiasi cha Shilingi 15,742,000 ili kutekeleza shughuli za kunusuru Ziwa Tlawi pamoja na kuainisha mipaka ya ziwa hilo, uvamizi wa watu katika shughuli za kilimo, kuhimiza
kilimo endelevu pamoja na miinuko inayozunguka ziwa hilo, kutoa elimu kwa wananchi ya kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji, kuimarisha Kamati za Mazingira na ulinzi shirikishi kwa ziwa katika ngazi za kata, vijiji na mitaa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Serikali itafanya tathmini ya kina kubaini chanzo cha ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki za ziada kuhimili athari katika Maziwa ya Tlawi, Babati na Manyara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja kuwa yako kwenye tishio la kukauka.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY aliuliza:-
Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipeleka maombi maalum ya fedha za ujenzi wa daraja la Gunyoda na wakati huo kutokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Mbulu kupata Wilaya mbili, daraja la Gunyoda limebaki kuwa kiungo muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mbulu vijijini.
Serikali Kuu ilitoa kiasi cha Sh.100,000,000/= ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Mbulu kwa maagizo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne fedha hizo zilielekezwa kwenye ujenzi wa maabara za sayansi katika Halmashauri zote nchini na kuacha daraja hilo bila kujengwa kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu haina uwezo wa kulijenga kwa fedha za ndani:
(i) Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kikwazo kikubwa kwa huduma za kijamii katika Halmashauri zote mbili?
(ii) Kwa kuwa mabadiliko ya Tabianchi yamesababisha uwepo wa makorongo makubwa ambayo yako katika Kata za Gonyoda, Silaloda, Gedamara, Bargish, Dandi, Marangw’ na Ayamaami jambo linalosababisha jamii kukosa huduma za jamii, afya na utawala. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta fedha za dharura ili kusaidia janga hilo katika Halmashauri mbalimbali ikiwemo Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Mbulu linalopita kwenye Korongo la Gunyoda lenye urefu wa mita 70.4 na kina cha mita tano lilifanyiwa usanifu wa awali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na kubaini kwamba zinahitajika shilingi milioni mia nane na hamsini kulijenga. Hadi sasa ni muda mrefu umepita, hivyo Serikali kupitia Wataalam wa Halmashauri itafanya usanifu wa kina kujua gharama halisi za kuingiza katika mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza ujenzi.
(ii) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwkaa wa fedha 2017/2018 Serikali inaanza utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao utatekelezwa kwenye halmashauri 15 ili kuandaa mpango wa kuzingatia athari za tabianchi. Serikali itashirikiana kikamilifu na halmashauri ili kuhakikisha fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya matengenezo ya dharura. Natoa wito kwetu sote kwa pamoja tushirikiane kikamilifu katika kutunza mazingira.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kati ya mwezi Juni – Desemba, 2015 wananchi wapatao sita walishambuliwa na kuuawa na wanyamapori na Shirika la Hifadhi Tanzania (TANAPA) halikushiriki mazishi ya watu hawa, wala hakuna fidia yoyote waliyopata ndugu wa marehemu, hali inayoonesha mahusiano mabaya kati ya jamii na Mamlaka ya Hifadhi, zaidi ya hayo wanyama kama tembo, wamesababisha hasara kubwa sana kwa kuharibu mazao katika Tarafa ya Daudi, Kata za Marangwa, Daudi, Bargish na Gehandu.
• Je, ni lini Serikali itawalipa fidia ndugu wa hao watu sita waliouawa na wanyama wakali katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
• Je, ni lini Serikali kupitia TANAPA italipa fidia kwa wale wote walioharibiwa mazao shambani mwaka 2014/ 2015?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaya, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hailipi fidia kwa madhara yanayosababishwa na wanyamapori hatari au waharibifu, badala yake inatoa kifuta jasho au kifuta machozi, kwa mujibu wa kifungu cha 68(1) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Aidha, kifungu cha (3) cha Kanuni za Malipo ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za mwaka 2001 kinaainisha masharti na viwango vya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imepokea madai ya wananchi watano waliouawa, wanne walijeruhiwa na 31 walioharibiwa mazao yao katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analizungumzia. Madai hayo yamefanyiwa kazi kwa mujibu wa kanuni na yatalipwa mara fedha zitakapopatikana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Wilaya ya Mbulu haina barabara ya lami kutokana na kuzungukwa na Bonde la Ufa kuanzia Karatu, Mto wa Mbu, Babati – Hanang hivyo, kufanya magari makubwa kutoka Uganda, Kenya na Dar es Salaam kuzunguka umbali mkubwa ili kufika Mbulu Mjini.
Je, Serikali ina mpngo gani wa kutekeleza ahadi yake ya kuweka lami katika barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom - Mkalama – Lalago Shinyanga ili kurahisisha usafiri katika njia hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Karatu – Mbulu - Hydom – Mkalama – Lalago – Kolandoto, yenye urefu wa kilometa 389 ni kiungo muhimu kwa Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Singida kwa kupitia Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa barabara hii ina umuhimu mkubwa wa kiuchumi na kijamii na ni kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Singida. Maandalizi ya ujenzi kiwango cha lami ya barabara hii yameanza kwa hatua za awali, ambapo Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeingia mkataba na Mhandisi Mshauri aitwaye HP Gauff Ingenieure GmbH & Co. KG – JBG ya Ujerumani ili kufanya kazi ya upembuzi yakinifu ambayo inaendelea hadi sasa. Kazi hii inagharamiwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali itatafuta fedha na kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi; upungufu huo wa watumishi umeathiri utoaji wa huduma wa Hospitali hiyo na Vituo vya Afya vya Tawi na Daudi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi katika Hospitali hiyo?
• Serikali inatekeleza mpango wa upanuzi wa Vituo vya Afya zaidi ya 200 nchini; je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na changamoto za watumishi, fedha na vitendea kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ni 345, watumishi waliopo ni 206 na upungufu ni watumishi 139. Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa afya kadri wanavyohitimu na kupangwa moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri watumishi 2,058 wa kada za afya kwenye Mikoa na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya hao, Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipangiwa watumishi kumi wakiwemo Madaktari wawili, Matatibu wawili; Afisa Muuguzi mmoja; Afisa Afya Mazingira mmoja na Msaidizi wa Afya, Mazingira mmoja; Mteknolojia Msaidizi mmoja na Wauguzi daraja la pili wawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuwaajiri watumishi 91 ili kupunguza upungufu uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inaendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya 208 nchi nzima ili kuboresha huduma ya dharura kwa mama wajawazito. Ujenzi wa vituo hivyo utagharimu shilingi bilioni 132.9 hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi huo, vituo hivyo vimetengewa shilingi bilioni 35.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba ili kuviwezesha kutoa huduma kwa wagonjwa. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeomba kibali cha kuwaajiri watumishi wa kada ya afya wapatao 25,000 ili kuhakikisha kunakuwepo na watumishi wenye sifa stahiki kwenye hospitali, vituo vyote vya afya na zahanati.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Mwaka 2016 Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi aliahidi kuipatia Wilaya ya Mbulu Baraza la Ardhi la Wilaya:-
• Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa na hatimaye Wilaya ya Mbulu kuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya?
• Je, ni kwa nini Serikali isipime ardhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu na kuwapatia hati ili kuondoa migogoro ya ardhi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mwishoni mwa Julai, 2018 Wizara kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za ajira kwa ajili ya kupata Wenyeviti 20 wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Wenyeviti hawa ni kwa ajili ya Mabaraza 17 ambayo hayana Wenyeviti. Vilevile Wenyeviti wawili ni kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye Mabaraza katika Mikoa ambayo imeelemewa na mashauri mengi na ina Mwenyekiti mmoja kama Dar es Salaam na Mwenyekiti mmoja ni kwa ajili ya Baraza la Mbulu ambalo litafunguliwa na kuanza kufanya kazi punde taratibu za kupata watumishi wengine zitakapokamilika. Kwa ushauri wa Mkoa na Wilaya Baraza hili litakuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Mbulu.
(b) Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi nchini kinapimwa. Azma hii inatekelezwa kwa kupeleka huduma zote za sekta ya ardhi ikiwemo huduma za upimaji katika Ofisi za Ardhi za Kanda na Wapima wa Wilaya. Aidha, Wizara imekalimisha taratibu za kupeleka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia zoezi hili la upimaji na TEHAMA katika ngazi za Kanda vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 ambavyo zimekabidhiwa kwa viongozi wa Kanda wiki hii ambavyo vitasaidia sana katika kurahakisha zoezi hili la upimaji katika Wilaya zetu katika Kanda husika.
Mheshimiwa Spika, napenda kukumbusha kuwa jukumu la upimaji ni la Mamlaka ya Upangaji, hivyo, Halmashauri zote zinatakiwa kushirikiana na Wizara kupitia Afisa Ardhi, Ofisi za Ardhi za Kanda, kuhakikisha kuwa azma ya kupima kila kipande cha ardhi nchini inafikiwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Hali ya barabara zinazosimamiwa na halmashauri ni mbaya sana kutokana na fedha zinazotolewa na Mfuko wa Barabara kukaa kwa muda mrefu na hali ya kuongezeka kwa magari binafsi na yale ya biashara ambapo kila tarafa ina zaidi ya magari 20 na hivyo, kufanya barabara hizo kuharibika na kuwa vigumu kupitika nyakati za masika:-
(a) Je, Serikali haioni haja ya kuleta mapendekezo mapya ya mgao wa fedha za barabara?
(b) Barabara nyingi za Halmashauri ya Mji wa Mbulu zimejifunga katika Tarafa za Nambis na Daudi. Je, kwa nini wataalam kutoka Wizarani wasifike kuzikagua na kutoa ushauri stahili?
(c) Je, kwa nini BQ za tenda za barabara ngazi ya mkoa zisiwekwe kwenye kitabu cha RRB, ili Waheshimiwa Wabunge na wananchi wafahamu shughuli zitakazofanywa na makandarasi waliopewa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mtandao wa barabara nchi nzima ili hatimaye utumike kuangalia kwa kina utaratibu mzuri zaidi wa mgawo wa fedha za barabara kati ya TANROADS inayoshughulikia barabara kuu na barabara za mikoa na TARURA inayoshughulikia barabara za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Barabara za Mji wa Mbulu zilitengewa shilingi milioni 814.56. Kati ya hizo shilingi milioni 262.12 zilitengwa kwa ajili ya barabara kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (Periodic Maintenance) Barabara za Ayamaame – Kainam – Hhasama – Mbulu – Endagikot – Tlawi, Tango FDC, Waama – Masieda, Ayayumba – Hhayloto zenye urefu wa kilometa 35.7 katika Tarafa za Daudi na Nambisi na kuweka changarawe katika Barabara za Ayamaami – Kainam – Hhasama, Mbulu – Kuta na Ayayumba - Hhayloto zenye urefu wa kilometa 8.13
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuchonga barabara ya Uhama – Masieda – Hayayumba – Hailoto zenye urefu wa kilometa 31.5 na ujenzi wa kalavati za njia mbili zenye kipenyo cha milimita 900 katika Tarafa ya Daudi. Barabara zilizokuwa zimejifunga kwa kuharibika na mvua sasa zinapitika ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na kazi inaendelea. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 Barabara za tarafa za Nambis na Daudi zimetengewa shilingi milioni 438.8 kwa ajili ya matengenezo.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa na wananchi kupata taarifa za jumla za barabara zilizopangwa kujengwa katika mkoa, ikiwemo gharama za kazi ambazo wajumbe wanaweza kuzipata katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa.