Contributions by Hon. Zainab Athuman Katimba (30 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia Mpango uliopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nami nikaweza kusimama katika Bunge hili Tukufu kuchangia hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru sana wapigakura wangu, vijana wa Kigoma; nakishukuru Chama changu kupitia Jumuiya yake ya Umoja wa Vijana na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake kwa kunipa ridhaa mpaka leo hii nikaweza kuwa mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchukua fursa hii kumpongeza Rais wetu wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya hasa katika kupunguza matumizi ya Serikali. Sisi kama vijana tunasema tutamuunga mkono, tutakuwa bega kwa bega na yeye kuhakikisha tunatetea maslahi ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kutoa pongeza za dhati kwa Mawaziri wakiongozwa na Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kuwa katika Baraza la Mawaziri kuunda Serikali ya Awamu ya Tano. Sisi kama vijana, tuna imani kwamba mambo makubwa yatafanyika katika Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kumpongeza Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha Mpango huu lakini pia nawapongeza Wabunge kwa michango yao ya kuboresha Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, kwa mujibu wa takwimu za idadi ya watu Tanzania, uwiano unaonyesha kwamba kundi la vijana linachukua asilimia kubwa zaidi. Kwa hiyo, mimi kama mwakilishi kwa vijana ningependa kujikita na kujielekeza kuzungumzia masuala ya vijana na hasa kuishauri Serikali yangu kwamba ili kuleta maendeleo katika Taifa hili, kundi hili maalum ni lazima tujue na Serikali ijue inalifanyia nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza na imeweka msisitizo, kuhakikisha kwamba changamoto kubwa sana ya vijana ambayo ni ukosefu wa ajira inapata utatuzi. Katika kuleta utatuzi wa changamoto hii ya ajira inashindikana kusema kwamba hatuzungumzii ni jinsi gani sekta ya elimu inaboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu ni sekta ambayo Serikali imejitahidi kufanya mambo makubwa sana na tunawapongeza kwa kazi hiyo. Hata katika Mpango wetu katika ukurasa wa 28 wamezungumzia na wameelezea ni jinsi gani Serikali imejipanga kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuishauri Serikali katika mikopo ya wanafunzi waliodahiliwa kusoma katika Vyuo mbali mbali waweze kupatiwa mikopo yao kwa wakati. Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya vijana hawa kukosa mikopo yao kwa wakati. Ukosefu wa mikopo yao kwa wakati unachangia hata kubadilisha mienendo yao na unaathiri hata matokeo yao ya kielimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli Serikali imefanya mambo makubwa katika sekta ya elimu na ninapenda kutoa pongezi za dhati na hasa katika maamuzi yake ya kubadili mfumo wa kupanga ufaulu wa wanafunzi kutoka katika ule mfumo uliokuwa wa GPA na sasa hivi wameweka mfumo wa division. Mfumo huu wa division sisi kama vijana tunaupongeza kwa sababu tunauelewa zaidi na hata wazazi wanaelewa zaidi na wanaweza kupima ufaulu wa vijana wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu pia napenda kuishauri Serikali kuboresha mitaala ya elimu. Kwa sababu tunasema kwamba tunataka kuwasaidia vijana ambao wanapata changamoto kubwa sana ya ajira, kwa hiyo, mitaala yetu ya elimu lazima ioneshe ni kwa jinsi gani inamwandaa huyu kijana kuweza kujiajiri yeye mwenyewe, hasa tukiangalia na tukijua kwamba hamna ajira za kutosha kwenye Serikali na hata taasisi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji kuwa na mitaala ambayo itaweka msisitizo katika taaluma lakini mitaala hiyo iweke msisitizo katika stadi za kazi. Kwa kuzungumzia stadi za kazi, hapa nitazungumzia vile vyuo vya kati ambavyo vinatoa mafunzo kama ya ufundi, vyuo kama Dar es Salaam Institute of Technology na VETA. Vyuo hivi viweze kuongezewa uwezo ili vidahili vijana wengi zaidi ambao watapata mafunzo ambayo yatawawezesha kujiajiri wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya michezo na sanaa ni sekta ambayo inatoa ajira kubwa sana kwa vijana; sio tu vijana lakini kwa Taifa duniani kote. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali yangu iweke msisistizo na kuwezesha michezo na sanaa kuwekwa katika mitaala yetu ya elimu ili kuibua na kuendeleza vipaji ambavyo vijana wetu wanakua navyo. Ina maana vipaji hivi na sanaa hizi zikifundishwa kwa vijana wetu wanaweza kupata fursa ya kujiajiri wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa hili wako akina Diamond wengi wa kutosha; wako akina Mbwana Samatta wa kutosha; lakini ni kuboresha tu mitaala yetu ili katika mitaala ile ya elimu zipangwe ratiba za kufundisha vijana, michezo, lakini pia kuwa na mafunzo ya sanaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la ajira kwa vijana, nitakuwa sijatenda haki kama nisipozungumzia miundombinu wezeshi.
Napenda kuunga mkono michango ya Waheshimiwa waliotangulia waliosisitiza kwamba Serikali itengeneze mpango wa kujenga reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ya Dar es Salaam haiwezi kukamilika pasipo reli ya kati; Bandari ya Kigoma haiwezi kukamilika pasipo reli ya kati. Kimsingi, reli ya kati itapanua sekta nyingi za uchumi na itanufaisha siyo tu Mikoa ya jirani, lakini itaongeza uchumi wa nchi kwa sababu itafungua milango ya biashara na nchi jirani.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi ya kuchangia…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi kubwa zinazoonekana. Napenda tu kutoa wito kwa vijana wenzangu na Watanzania wote tumwombee Rais wetu, lakini tumpe nguvu na tumpe moyo ili aweze kuendelea kufanya kazi anayoifanya ambayo imedhihirika kwa kipindi kifupi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya. Niseme tuna imani nao, waendelee kufanya kazi zao na wamuombe Mungu awasimamie ili waongeze juhudi na wafanikishe yale ambayo Watanzania wanayategemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuzungumzia suala la vijana. Sisi tunafahamu kwamba vijana hawapati fursa za kutosha kuajiriwa katika Serikali au sekta binafsi na wanahitaji na kila siku tunasisitiza kwamba vijana waweze kujiajiri wenyewe. Kweli sasa hivi vijana wanajitahidi sana kujiajiri wenyewe kupitia mifumo ya kufanya biashara. Sasa Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia BRELA imeweza kufanikisha kutengeneza Online Business Registration Platform yaani ni mfumo wa kielektroniki au wa kimtandao wa kusajili biashara na makampuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu umeleta urahisishaji mkubwa sana katika usajili wa biashara na makampuni na umeleta urahisi. Kwa hiyo, tunachoomba ni zile changamoto ambazo mfumo huu umeleta Wizara iweze kuziboresha ili kuleta ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto ni zipi? Naomba Serikali kwanza mzitambue, lakini mtafute njia ya kuzitatua. Changamoto ya kwanza ni kijiografia tu Tanzania yetu hii ni pana na kwa sababu mfumo huu wa Online Business Registration unahitaji matumizi ya mtandao, basi wawasiliane na Wizara husika ili tuweze kuona mtandao unaweza kupatikana hata huko vijijini na katika Tanzania yetu hii yote nzima ili kuweza kuleta manufaa makubwa zaidi ya mfumo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, kwenye Dawati la Huduma kwa Wateja (Help Desk), ninaiomba sana Serikali iweze kuboresha huduma kwa wateja, kwa sababu mfumo wowote wa kimtandao unahitaji monitoring, unahitaji huduma kwa wateja. Katika huduma kwa wateja katika mtandao huu changamoto ambazo vijana wanazipata katika usajili wa biashara na makampuni ni kwamba unaweza ukapiga simu huduma kwa wateja na ile simu isipokelewe au pale pindi simu inapopokelewa bado kunakuwa hakuna utatuzi wa papo kwa hapo kwa changamoto ile ambayo mtu anayetaka kujisajili anakumbana nayo. Kwa hiyo, naomba Serikali itambue kwanza kuna changamoto hiyo, lakini waweze kuifanyia kazi, kuboresha ili tuwe tuna huduma kwa wateja kama vile tunavyoona katika mitandao ya simu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupata leseni ya biashara kumewekwa kigezo cha kuwa na Kitambulisho cha Taifa ili uweze kujisajili katika huu mfumo (Online Business Registration Platform) ambayo ipo BRELA, ni lazima uwe na Kitambulisho cha Taifa. Sasa sisi tunajua siyo vijana wote wana Vitambulisho hivi vya Taifa, siyo Watanzania wote ambao wana Vitambulisho hivi vya Taifa na wanahitaji kusajili biashara zao, na sisi tunahitaji kurasimisha biashara za Watanzania ili tuweze kupata kodi, lakini wanakosa kitambulisho hiki na wanakosa uwezo wa kusajili hizi biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu naomba Serikali kwa wakati huu ione utaratibu wa kuweza kutumia kitambulisho kama cha Mpiga Kura ambacho sifa ya kuwa na Kitambulisho cha Mpiga Kura ni sifa kama ile ile ya kuwa na Kitambulisho cha Taifa, yaani kwa maana ni Mtanzania ili tusiweze kuwakwamisha vijana wetu au wafanyabiashara wetu kuweza kusajili makampuni yao na biashara zao.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Watanzania wafanye biashara kwa kufuata mifumo ya kisheria, kwa sheria zetu ambazo tumezitunga wenyewe hapa Tanzania. Kwa hiyo, tuwawekee mazingira mazuri ili waweze ku-conform. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imeweka sharti, ili uweze kupata leseni ya biashara lazima upate tax clearance, ulipe kodi ile ya TRA. Sasa hili ni jambo jema, lakini sasa changamoto yake inakuja kwa ile startup businesses, yaani kwa wale wanaoanzisha biashara kwa mara ya kwanza. Kwa sababu hata ukiangalia Sheria ya Kodi (Income Tax Act) inataka na inatambua kwamba kodi ya mapato ni ile kodi inayotokana na biashara halisi. Sasa unataka upate leseni uanzishe biashara, kijana anataka kuanzisha biashara yake ajiajiri, unamwambia aanze kwanza kwa kulipa kodi ambayo hajaifanyia biashara akapata faida, hiki ni kikwazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali ifanye utaratibu ili kwenye startup business kusiwe kuna hii requirement ya tax clearance kwa ajili ya kupata business license. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Serikali imekuwa ina ubunifu wa kuwawezesha vijana na wanawake lakini na makundi mengine katika jamii kwa kutumia mifuko mbalimbali kuwawezesha kimtaji. Hili ni jambo jema sana, tumeona vijana na wanawake wengi wananufaika, lakini sisi wote tunatambua kwamba kumekuwa na changamoto ya kusonga mbele yaani kumekuwa na vicious circle. Kwa nini? Kwa sababu wale wanaopewa mikopo, yale makundi ya vijana na wanawake hayajaandaliwa kitaaluma katika uendeshaji wa biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata kwenye hotuba ukurasa wa 142, utaona wameweka lengo la Wizara ambalo wamesema kwamba ni kuhamasisha na kuelimisha wajasiriamali namna ya kuanzisha na kuendeleza biashara. Kwa hiyo, hili ni lengo mojawapo la Wizara katika sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo ndogo. Kwa hiyo, kuna uhitaji wa kuweza kuwapatia mafunzo ya kuanzisha biashara (to start up their own enterprises) kama ni vijana ama ni wanawake au wajasiriamali wowote waanzishe lakini waweze kuendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya yanaweza yakapatikana kwa kutumia ile machinery tuliyokuwa nayo. Hata katika Serikali za Mitaa kuna Maafisa Biashara wa Mikoa, lakini kwenye Halmashauri pia kuna Maafisa Biashara. Wao wanaweza wakatumika, kwa sababu hii sera ni ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Japokuwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ndiyo inafanya utekelezaji, lakini jukumu kubwa ni la Wizara hii kusimamia utekelezaji wa ile sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, waangalie ni namna gani watatumia ile mifumo ili hata hivi vikundi, kwa sababu tunategemea vipate faida na ile mifuko ya kuwasaidia vijana na wanawake iwe ina manufaa, kwa hiyo, wapatiwe haya mafunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, twende mbele, hii Serikali iwasiliane, kwa sababu katika Wizara ya Elimu, Serikali ione namna ya kuweka katika mitaala ya elimu mafunzo (Basic Entrepreneur Skills) kuanzia ngazi ya chini ya elimu, kuanzia primary mpaka secondary. Kwa sababu tusiwaandae vijana wetu for white collar jobs, tuwaandae pia waweze kujiajiri. Kwa hiyo, tuwape mafunzo yale basic ya kuanzisha enterprises zao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kuchukua maoni hayo na kuyafanyia kazi. Vilevile tusisahau kwamba katika uchumi wa viwanda tunahitaji sana ku-invest katika kilimo. Kwa hiyo, Serikali ione ni kwa namna gani inawekeza katika kilimo, kwa sababu hiki kilimo ndiyo kitakuja kulisha viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwetu Kigoma, sisi kumekuwa kuna jitihada za kuanzisha hata viwanda vya mafuta ya mawese ili kusikosekane mafuta. Yaani hatuwezi Tanzania tukasema hatuna mafuta ya kutosha wakati kuna nchi kama Malaysia ambayo ilikuja kuchukua mbegu ya mchikichi Kigoma na leo hii ina-produce mafuta ya mchikichi (palm oil) kwa wingi sana halafu sisi kama Tanzania tukashindwa kuwekeza katika mbegu bora itakayozalisha kwa kiwango kikubwa na ikaweza kulisha viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Wizara hizi ziweze kufanya kazi kwa pamoja kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sababu mwisho wa siku tunahitaji kilimo ili kije kinufaishe viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza jitihada za Serikali katika viwanda, kwa mfano, mradi huu wa Stiegler’s Gorge ambao utazalisha zaidi ya megawati 2100 za umeme ambazo ni jitihada zinazoonekana za kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAINABU A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kwa sababu tunakoelekea kwenye uchumi wa viwanda tunahitaji kuwekeza katika rasilimali watu. Rasilimali watu ya uchumi wa viwanda ni kada ya kati hasa mafundi mchundo. Nashauri wanafunzi wa vyuo vya ufundi wenye uhitaji wawekwe kwenye mpango wa kukopeshwa na Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo Mezani. Kwanza kabisa, napenda kuanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya na siha njema na pia kutujaalia wote afya na siha njema mpaka wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa upekee kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini katika dhamana hii ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Naendelea kumuahidi kwamba nitafanya kazi kwa bidii, kwa weledi na uadilifu. Pia, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kwa ulezi wake na uongozi wake makini na kunipokea katika Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, anayeshughulikia masuala ya afya kwa ushirikiano wake mkubwa sana tangu nimeingia kwenye Wizara hii. Pia, natambua ushirikiano mkubwa sana wa Katibu Mkuu, Manaibu Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nawashukuru sana kwa mapokezi yenu. Nawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mnaonipa ambao kimsingi nashindwa kuusimulia kwa maneno, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Spika na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa malezi yenu na uongozi wenu kwetu sisi Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natambua mchango mkubwa sana wa Kamati ya TAMISEMI ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Dennis Londo. Natambua mchango na ushirikiano mkubwa sana wa Waheshimiwa Wabunge wote ambao mnatoa ushirikiano mkubwa sana kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nachukua pia fursa hii kuwashukuru wanawake wote wa Mkoa wa Kigoma, wapiga kura wangu na wadau mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano wao na dua zao ambazo kimsingi zinanipa utulivu katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja nyingi zinazogusa sekta ya elimu ya msingi na sekondari. Pia, wamezungumzia masuala ya barabara za wilaya, yaani TARURA. Ninachopenda kusema, kwanza tumepokea ushauri na maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge na tunaahidi kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu ukarabati wa shule kongwe na shule chakavu; na Wabunge wengi wametaka kufahamu kwamba kuna mikakati gani ya kuhakikisha kwamba shule hizi zinakarabatiwa kwa sababu zimechakaa sana? Nataka kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kurekebisha shule hizi. Katika kipindi cha mwaka 2022/2023 mpaka mwaka 2023/2024 tayari Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 70.39 kwa ajili ya ukarabati wa shule 793 za msingi na sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kwamba Serikali haijaishia hapo. Kwa hiyo, katika mwaka wa fedha unaokuja Serikali itaendelea kufanya ukarabati katika shule kongwe kurekebisha miundombinu chakavu katika shule 50 za msingi. Kwa hiyo, Serikali inafahamu umuhimu wa kufanya marekebisho na ukarabati wa miundombinu katika shule hizi na itaendelea kufanya hii kazi katika mwaka wa fedha unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu masuala ya ujenzi wa nyumba za watumishi hususan kwenye kada ya elimu. Tayari katika mwaka wa fedha huu unaoenda kwisha, kupitia miradi ya SEQUIP na BOOST, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imeendelea kujenga nyumba 253 kwa thamani ya jumla ya shilingi bilioni 25.26. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kwamba, Serikali haitaishia hapo. Kwa kupitia hii miradi ya SEQUIP na BOOST, katika mwaka wa Fedha 2024/2025 Serikali imepanga kujenga jumla ya nyumba 562 za Walimu wa Sekondari na Msingi ambazo zitachukua familia 1,124. Kwa hiyo, naomba kuwahakikishia kwamba, Mheshimiwa Rais anatambua umuhimu wa kujenga nyumba za watumishi wetu na hususan kwenye kada ya elimu. Ndiyo maana zinapatikana hizi fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa nyumba hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na ujenzi wa mabweni. Waheshimiwa Wabunge wameeleza ni kwa namna gani kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na mabweni katika shule zetu za sekondari na hasa zile za kutwa. Naomba kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba, katika mwaka huu wa fedha unaoisha 2023/2024, tayari Serikali imejenga jumla ya mabweni 519 nchi nzima yenye jumla ya gharama ya shilingi bilioni 67.41.
Mheshimiwa naibu Spika, katika mwaka wa fedha ujao, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha mabweni 310. Katika mabweni hayo 310, mabweni 274 ni ya shule za sekondari na mabweni 36 ni ya shule za msingi. Aidha, Serikali itaendelea kuwashirikisha wananchi kupitia halmashauri kujenga hosteli kwenye shule za kutwa za kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne kwa kadiri ya mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wametaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miundombinu ya shule mpya inayojengwa na kukamilika ili ianze kutumika na kuepusha uchakavu, kwa sababu, shule nyingi pamoja na miundombinu mingi inajengwa katika hizi shule, lakini kwenye baadhi ya maeneo unakuta kuna madarasa hayatumiki na mwisho wake yale majengo yanaanza tena kuharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili, naomba kurejea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, ambaye amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha kuwa wanatumia utaratibu walioelekezwa wa kuhakikisha kwamba, miundombinu ya shule mpya za sekondari na msingi zilizojengwa inatumiwa na wanafunzi kuanzia Januari, 2025. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tayari Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ametoa maelekezo ambayo ni jukumu la halmashauri kuyazingatia ili haya majengo yote ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi kuhakikisha yanajengwa, wanafunzi wetu wayatumie ili yawe na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge wamezungumza na wamechangia sana kuhusiana na suala la upandishaji wa hadhi wa shule zao kuwa kidato cha tano na sita. Kuhusiana na suala hili, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tayari imetoa maelekezo kwamba, halmashauri zifanye tathmini katika miundombinu yote kuangalia kama ni toshelevu na inakidhi mahitaji. Pale itakapothibitika kwamba miundombinu iliyojengwa inakidhi viwango na mahitaji, basi wawasilishe maombi kwenda Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuomba kupandishwa kwa hadhi ya shule zao kuwa za kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kuendelea tu kusisitiza kwamba, utaratibu upo, unafahamika, Wakurugenzi kwenye Halmashauri waweze kufanya utaratibu huo, wakamilishe, wapeleke maombi kwenye Wizara ya Elimu kwa ajili ya kukamilisha hatua za kupandisha hadhi shule kuwa kidato cha tano na sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kuhusiana na kulipwa kwa madeni na stahiki za walimu. Waheshimiwa Wabunge, wamechangia pia kwenye eneo hili. Naomba kutumia nafasi hii kurejea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye ameelekeza kwamba, madai yote ya likizo na uhamisho yanalipwa haraka. Serikali haitamvumilia Mkurugenzi yeyote ambaye hatatekeleza maelekezo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kurejea kwamba, Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilishatoa maelekezo kwamba madai yote ya likizo na uhamisho yalipwe haraka. Serikali haitamvumilia Mkurugenzi yeyote ambaye hatatekeleza maelekezo hayo. Kwa hiyo, pamoja na kuwa Serikali imekuwa ikilipa madeni na stahiki za walimu ambapo hadi Desemba, 2023 jumla ya shilingi bilioni 202.43 zimelipwa ambazo ni madeni ya malimbikizo ya mishahara, bado maelekezo ya Mheshimiwa Waziri yasimamiwe ili Wakurugenzi wote wahakikishe kwamba wanalipa malimbikizo ya madai yote ya likizo na uhamisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingine ya Waheshimiwa Wabunge imeelekezwa kwenye masuala ya barabara zetu za wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA. Waheshimiwa wametaka TARURA iongezewe vitendeakazi kwenye baadhi ya wilaya na hasa magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 tayari TARURA imenunua na kusambaza magari 18 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za barabara. Katika mwaka wa fedha unaokuja, TARURA imepanga kutumia jumla ya shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa magari. Kwa hiyo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge ambao wametoa hoja hii, wafahamu kwamba tayari kuna fedha zimetengwa na bila shaka vifaa vya kazi, hasa magari vitanunuliwa katika mwaka wa fedha unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza kuhusu upungufu wa watumishi TARURA. Serikali inatambua upungufu huu wa watumishi TARURA, na mpaka muda huu tayari Serikali imeajiri watumishi 27 wa kada ya uhandisi katika mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2023/2024.
Mheshimwia Naibu Spika, katika mwaka wa fedha unaokuja, Serikali imeomba kibali cha kuajiri wahandisi 97, lakini kwa hatua za muda mfupi, Wakala wa Barabara (TARURA) wametumia njia ya kutumia wahandisi 98 ambao wanaendelea kupata mafunzo kwa vitendo. Kwa hiyo, TARURA inatumia wahandisi ambao wanaoendelea kupata mafunzo kwa vitendo, lakini pia ajira za mkataba kwa wahandisi 84 zimetolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inatambua changamoto iliyopo na imechukua hatua hii ambayo ni ya dharura ikiwa ni katika kusubiri mpango wa muda mrefu na wa kudumu ambao ni wa kuajiri wahandisi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la TARURA, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamependekeza na kutoa ushauri kwa Serikali kwamba, Sekretarieti za Mikoa zisaidie Halmashauri katika utekelezaji wa miradi ya TACTIC kwa kutoa wataalamu wake. Serikali inatambua uhitaji uliopo katika eneo hili na kwa kuzingatia taratibu, itachukua hatua za haraka. Vilevile Serikali imepokea ushauri uliotolewa na itazishirikisha kikamilifu sekretarieti za mikoa katika kuhakikisha zinasaidia utekelezaji wa miradi ya hii ya TACTIC katika halmashauri zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo lilizungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo la halmashauri kubaki na jukumu lake la msingi la kutoa elimu kwa usawa na kuachana na utoaji wa elimu kupitia shule za English Medium. Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa ushauri, napenda kusema kuwa ushauri umepokelewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Serikali itazingatia mapendekezo mahususi ambayo yametolewa na kamati kuhusiana na uendeshwaji wa shule hizi za English Medium.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imepokea mapendekezo yote ambayo yametolewa na Kamati ya USEMI kuhusiana na namna ya kuzisimamia hizi shule na hasa kwa sababu Waheshimiwa Wabunge mmetoa maoni na kuona kwamba kunakuwa hakuna usawa kati ya shule za kawaida na hizi za English Medium na kwamba Serikali ibaki na jukumu lake la msingi la kutoa elimu ambayo itakuwa ina usawa na iachane na utoaji wa elimu kupitia English Medium. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema kwamba, tumepokea maoni na ushauri wote na tunaahidi kuwa tutaufanyia kazi. Tunatambua kwamba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni Wizara ya wananchi na pia tunatambua kwamba Mheshimiwa Rais kwa nia ya dhati na mapenzi yake kwa Watanzania, ameweza kutafuta fedha nyingi za miradi ya maendeleo na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza na kutoa ushuhuda wa mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayafanya katika majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anagusa mioyo ya Watanzania, hivyo, inahitaji tuendelee kumuunga mkono na kumtia moyo ili aweze kuendelea na kazi kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Kwa muktadha huo, ninaomba sisi wote, kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja alichangia hapa, Mheshimiwa Dkt. Kigwangwalla alisema tuunge mkono kampeni ile ya “Nasimama na Mama Samia.” Naomba tuitangazie dunia kwamba sisi Watanzania tunasimama na Dkt. Mama Samia na hakuna mbadala. Tumtie nguvu Mheshimiwa Rais ambaye tayari anafanya kazi kubwa ili aweze kuendelea kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa kushirikiana na wengine yaani freedom of association. Ibara ya 20(2) inatoa masharti na vigezo na mipaka ya Vyama vya Siasa kutumia nafasi yake kufanya siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, Ibara ya 20(3) imetoa mamlaka kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutunga sheria itakayohakikisha Vyama vya Siasa vinazingatia masharti yaliyowekwa katika Ibara ya 20. Hivyo, napenda kuipongeza kwa dhati Serikali kwa kufanya mchakato wa kuiangalia Sheria hii ya Vyama vya Siasa na kuona haja ya kuleta marekebisho ya yatakayofafanua na kusisitiza masharti yaliyoainishwa katika Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika taratibu za kutunga sheria, tunafahamu kwamba sheria huwa inaanza na Muswada. Muswada siyo sheria ni mapendekezo ya awali ya sheria au maboreshao ya sharia. Muswada ule unasomwa hapa Bungeni kwa Mara ya Kwanza Wabunge wote wa vyama vyote wanapewa Muswada ule wausome, wauangalie waone kuna maeneo gani ambayo wao wanaweza kuja kutoa mapendekezo yao ya maboresho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, kwa mujibu wa Kanuni zetu za Bunge, Kamati husika ambayo kwa muktadha huu ni Kamati ya Katiba na Sheria, inakaa kuujadili, kuusoma, kupendekeza maboresho ya Muswada huo kwa Serikali. Mapendekezo hayo hayaishii hapo Muswada ule unasomwa kwa Mara ya Pili katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge wanapata muda wa kuujadili na kutoa maoni yao kuhusiana na kuboresha Muswada ule ili baada ya kupita katika mchakato huo ukisainiwa uweze kuwa sheria bora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niseme naipongeza sana Kamati ya Katiba na Sheria kwa kazi yake kubwa iliyofanya katika kutoa mapendekezo ya kuboresha Muswada huu. Tutambue kwamba kwenye Kamati hiyo ya Katiba na Sheria, kuna uwakilishi wa Wabunge kutoka vyama vyote, japokuwa Wabunge walio wengi kwenye Kamati hiyo ni Wabunge wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ni vizuri sana kufahamu kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ni vizuri kufahamu Tanzania inaheshimu uhuru wa kutoa maoni. Hiyo imedhihirika kwa mchakato mzima wa Muswada huu kwa kuweza kuchukua maoni kutoka kwa wadau tofauti tofauti lakini hata kuchukua maoni na mapendekezo kutoka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria na ndiyo maana leo hii Serikali imeleta Jedwali la Marekebisho ya Muswada huu na ukiangalia Jedwali hili limezingatia mapendekezo ya Kamati. Kwa hiyo, hii inadhihirisha ni kiasi gani nchi yetu inaheshimu uhuru wa maoni lakini ni nchi ya kidemokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda nitoe mifano michache tu ya maeneo ambayo Kamati ilitoa mapendekezo lakini na Serikali ikayapokea mapendekezo ya maboresho hayo ya Muswada huu. Kwenye clause 7 ambayo imeanzisha kifungu cha 6B katika Sheria ya Vyama vya Siasa, utaona kwamba kifungu hiki kimeweka sifa ya mwanzilishi au sifa ya mtu atakayetaka kuanzisha chama cha siasa. Kwenye Muswada sifa ya mtu huyu ilikuwa imewekwa kwamba awe ni raia wa Tanzania lakini na wazazi wake wote wawili wawe raia wa Tanzania. Hata hivyo, Kamati kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 13(1),(2) na (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatoa mapendekezo ya maboresho ya kifungu hiki na Serikali yetu kwa sababu ni sikivu, Serikali yetu inaheshimu uhuru wa maoni, imepokea maoni yao na ndiyo maana yanaonekana kwenye Jedwali la Marekebisho ya Muswada huu ambalo limeletwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, kuna kifungu ambacho kimeanzishwa cha 6B(d) ambacho kinazungumzia umri wa mwanzilishi wa chama cha siasa. Hapo awali iliwekwa sharti iwe miaka 21 lakini kwa mapendekezo ya wadau mbalimbali ikiwemo na Kamati ya Katiba na Sheria, ikapendekeza kwamba kwa kuzingatia mashari ya kikatiba Ibara ya 5 na 21 ambayo inatoa na kufafanua umri wa mtu kuweza kushiriki katika shughuli za kisiasa ikiwemo kuchaguliwa na kuchagua lakini kujihusisha na shughuli za umma ikiwemo shughuli za kisiasa, basi mapendekezo yakatoka umri ule uzingatie Katiba na uwe miaka 18. Serikali imechukua mapendekezo hayo na ndiyo maana yanaonekana kwenye Jedwali la Marekebisho ya Sheria. Kwa hiyo, nasema na nasisitiza kwamba tutambue kwamba demokrasia ya kweli ipo lakini uhuru wa kutoa maoni upo na mchakato huu mzima umedhihirisha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, clause 31 ambayo imeenda kuanzisha kifungu kipya cha 21E ambacho kilikuwa kinatoa mamlaka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kumfuta uanachama wa Chama cha Siasa au kumuondolea uanachama wake mwanachama wa Chama cha Siasa pale atakapokuwa amevunja Sheria ya Vyama vya Siasa. Kamati ikapendekeza kwamba yafanyike marekebisho ili mipaka ya mamlaka haya ya Msajili wa Vyama vya Siasa iishie kwenye kutoa na kutaka chama husika kimchukulie hatua ya kidhamu mwanachama wake kwanza. Siyo hivyo tu, kama mwanachama huyo au chama kikishindwa kumchukulia hatua mwanachama wake kwa kukinzana na matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa basi Msajili wa Vyama vya Siasa atoe taarifa na mhusika au mtuhumiwa apewe muda wa kujitetea na baada ya muda wa kujitetea ndiyo adhabu ambayo Msajili wa Vyama vya Siasa atatoa iwe ni kumsimamisha asifanye shughuli za kisiasa. Mapendekezo hayo yamepokelewa na Serikali na ndiyo maana yanaonekana katika Jedwali hili la Marekebisho ya Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye clause 11 ambayo imeanzisha Kifungu cha 8E katika Sheria hii ya Vyama vya Siasa. Utaona kwamba kifungu hiki kimetoa katazo la vyama vya siasa kuanzisha vikosi vya kijeshi au vikosi vya ulinzi na usalama. Napenda kurejea sheria mama yaani Sheria ya Vyama vya Siasa (The Political Parties Act) kwenye kifungu cha 3 na naomba nikinukuu, kimetoa tafsiri ya chama cha siasa (political party), kinasema hivi: “political party” means any organized group formed for the purpose of forming a government or a local government authority within the United Republic through elections or for putting up or supporting candidates to such election”.
Mheshimiwa Spika, tafsiri ya chama cha siasa siyo kikosi cha ulinzi na usalama, masuala ya ulinzi na usalama yametolewa katika Ibara ya 147 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na naomba niisome. Ibara ya 147 ya Katiba inasema: “Ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote”. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sitaki kuishia hapo, ukisoma sheria mama, Sheria ya Vyama vya Siasa kifungu cha 11 kinasema kama ifuatavyo: “Every party which has been provisionally or fully registered shall be entitled-
b) to the protection and assistance of the security agencies for the purposes of facilitating peaceful and orderly meetings”.
Mheshimiwa Spika, lakini kifungu hiki chote cha Sheria hii kimetoa haki kwa kila mwanachana na kila chama cha siasa kupatiwa ulinzi na usalama kwa vyombo ambavyo vimeanzishwa kikatiba. Kwa hiyo, naomba kusisitiza sana kifungu hiki ni muhimu na yeyote ambaye anapinga kifungu hiki maana yake anapinga Katiba kwa sababu sheria hii inaenda kufafanua masharti ambayo yamewekwa kikatiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye Ibara ya 20(2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
inasema: “Bila kujali masharti ya Ibara ndogo ya (1) na ya (4), haitakuwa halali kwa chama chochote cha siasa kuandikishwa ambacho kutokana na katiba au sera yake, hakiruhusu uongozi wake kuchaguliwa kwa vipindi na kwa njia za kidemokrasia.” Muswada wa Sheria hii unakuja kukazia katika matakwa ya kikatiba. Ndiyo maana Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa mamlaka ya kusimamia demokrasia ndani ya vyama. Demokrasia ya kweli inaanzia kwenye vyama vyetu sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafahamu kwamba Wabunge wataridhia na wataona umuhimu wa kuzingatia Katiba waunge mkono mapendekezo ya Muswada huo wa kurekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa ili tuweze kupata sheria bora itakayosimamia misingi iliyowekwa kikatiba katika siasa za Tanzania.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2023.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata fursa hii ili niweze kuchangia hoja iliyopo mezani ya Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023. Ni dhahiri kwamba 70% ya Bajeti ya Serikali inaenda kwenye manunuzi na ni dhahiri katika kipindi hiki cha hivi karibuni sisi sote tumekuwa mashahidi, ni kiwango gani cha fedha nyingi zinatafutwa na Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, lakini ni kwa kiasi gani kuna fedha nyingi sana za walipa kodi ambazo zinahitaji zionekane katika maendeleo ya nchi hii. Ni dhahiri ili fedha hizi ziweze kuonesha tija, tunahitaji kuhakikisha kwamba kunakuwa na thamani halisi ya pesa, yaani thamani halisi ya pesa inapatikana (value for money).
Mheshimiwa Spika, Muswada huu umekuja katika kipindi hiki muafaka, kwa nini? Kwa sababu Sheria ile ya mwanzo ilikuwa ina dosari mbalimbali ambazo sasa tunatarajia kwamba Muswada huu au marekebisho haya ya Sheria hii yatakuja kutatua changamoto hizo na kuondoa ule upotevu wa fedha nyingi ambazo zilikuwa zinatokana na changamoto au mapungufu kwenye manunuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukianza kwanza kwenye Ibara ya 72 ya Muswada huu ambayo inatoa sharti la kwamba manunuzi yote yatakuwa yanafanyika kwa njia ya kieletroniki. Ibara hii ni Ibara muhimu sana kwa sababu kwa muda mrefu tumekuwa tunasema tunataka kuondoa ushiriki wa mkono wa binadamu moja kwa moja kwenye masuala ya manunuzi au moja kwa moja kwenye masuala ya fedha. Kwa hiyo, sasa kutumia mifumo ya TEHAMA, kutumia mifumo ya kieletroniki ni namna nzuri zaidi ya kuondoa mianya ya upotevu wa fedha katika manunuzi.
Mheshimiwa Spika, changamoto moja tu ninayoiona kwenye Ibara hii ni kwamba Ibara ndogo ya (2) ya Ibara hii ya 72 kwenye Muswada inasema; “Endapo mfumo haufanyi kazi, Mamlaka itatoa notice ya mwongozo kwa watumiaji wa mfumo na kwa umma.”
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu hapa kwa nini mfumo haufanyi kazi? Kwa sababu hapa tumeona tumeanza kutumia Bunge mtandao, tunaona kwenye mabenki tunatumia mitandao, tunaona kwenye masuala ya aviation, ticketing kwenye masuala ya ndege tunatumia mtandao na hatujawahi kutengeneza mbadala wa hiyo mitandao. Sasa kifungu hiki kisije kikawa ni mwanya wa kuacha kutumia mifumo ya kieletroniki na ikawa ni sehemu ya kutengenezea huo mwongozo wa kufanya manunuzi nje ya mfumo wa kieletroniki.
Mheshimiwa Spika, nadhani msingi hapa ni kwamba, tukazanie mifumo ya kieletroniki ni lazima ifanye kazi. Kwa hiyo naiomba sana Serikali katika Kifungu hiki, sasa kwa sababu tayari kimeshaandikwa hivi, lakini kisije kikatumika kama kichaka cha kutengeneza manunuzi nje ya mfumo ambao wa kieletroniki. Kwa sababu Ibara hii ya 72 inaweka sharti kwamba manunuzi yote yatafanyika kwa njia ya eletroniki, tubakie huko, tujielekee huko, tuweke nguvu ili mifumo iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Ibara ya 63 ya Muswada huu, ambayo inazungumzia upendeleo kwa makundi maalum ya kijamii. Ibara hii ni nzuri sana kwa sababu inatoa sharti la kwamba taasisi nunuzi zitatenga kiwango fulani cha manunuzi yake kila mwaka wa fedha kwa ajili ya upendeleo pekee kwa ajili ya makundi haya maalum. Kifungu hii cha Sheria kilikuwepo kwenye sheria ile ya zamani ya PPRA na hata kutungiwa Kanuni, kulikuwa kuna Kanuni 30(c) ambayo ilitoa sharti la kwamba Maafisa Masuuli wote wa taasisi za umma, watenge 30% ya manunuzi ya taasisi zao kwa ajili ya kuziwezesha au kwa ajili ya kutoa manunuzi haya kwenye makundi maalum.
Mheshimiwa Spika, Kanuni hiyo ikasisitiza pia, taasisi yoyote inayoshindwa kutenga 30% ya fedha hizi za manunuzi na kuziweka kwa ajili ya makundi haya maalum, itatoa maelezo kwamba ni kwa nini imeshindwa kusimamia sharti hili la kutenga 30% ya manunuzi yake kuyatenga kwa ajili mahususi kwa ajili ya makundi maalum. Pia Kanuni hiyo ikaenda mbele kutaka kwamba Maafisa Masuuli wote ambao wameshindwa kutekeleza takwa hili la kikanuni la kutenga 30% ya manunuzi yao wazitenge mahususi kwa ajili ya makundi maalum, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Spika, sasa mpaka leo hii Sheria hiyo ambayo tumekuwa nazo tunaitumia ya manunuzi, nataka kufahamu hivi ni Maafisa Masuuli wangapi wametoa maelezo ya kwa nini hawajatenga hizo fedha kwa ajili ya makundi haya maalum na kwa nini na wangapi katika hawa Maafisa Masuuli wamechukuliwa hatua? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, msingi wa kuuliza maswali hayo ni kwa sababu tunakiona hiki Kifungu kwenye Muswada huu, tunaona kwenye Ibara 63 inaweka huo upendeleo kwa makundi maalum ya kijamii na hiki Kifungu kimeboreshwa kwa sababu sasa katika kutunga Kanuni kwenye Kifungu hiki Waziri atashauriana na Wizara zinazohusiana na masuala ya makundi maalum, lakini tunajuaje kama itaenda kutekelezeka? Kwa sababu tumekuwa tuna Sheria, tumekuwa tuna Kanuni, tumekuwa na miongozo ambayo haijazingatiwa, haijatekelezwa na hamna hatua yoyote iliyochukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tunarudi tena Bungeni tunafanya marekebisho ya Sheria, sasa nataka kufahamu hapa tunatokaje, kwa sababu hizi ni ajira za Watanzania, tunataka tutengeneze ajira kwa ajili ya wananchi wetu na maeneo ya kupata mitaji, kupata kazi za kufanya za kupata ajira ni kwenye maeneo ya upendeleo kama haya. Sasa tunapokuwa hatusimamii utekelezaji tunatokaje? (Makofi)
Mhehimiwa Spika, naomba sana, nina imani kubwa na Mheshimiwa Waziri, nina imani kubwa na Serikali, naomba sana twende tukatekeleze Ibara hii, kifungu hiki cha 63 kwenye hii Sheria ya Ununuzi wa Umma tunapitisha lakini tunataka utekelezaji. Zile changamoto za kutokutekelezwa kwa Sheria na Kanuni tulizoziona nyuma, hatupendi kuziona katika kipindi hiki. Tunaamini tunaanza upya, lengo ni kutengeneza mazingira mazuri katika Sheria zetu na sheria zisimamiwe, kwa sababu nchi hii inaenda kwa utawala wa sheria. Kwa hiyo sheria zizingatiwe na zitekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Ibara ya 21 ya Muswada huu inazungumzia adhabu au mapendekezo ya hatua za kinidhamu, inatoa hatua zinazoweza kuchukuliwa na mamlaka pale kunapokuwa na ukiukwaji, mamlaka kwa maana ya PPRA, kunapokuwa na ukiukwaji wa sheria hii, kanuni na miongozo yake. Sasa kwenye Ibara hii ya 21 ambayo naomba niinukuu, inasomeka hivi; “Endapo kuna ukiukwaji wa mara kwa mara au ukiukwaji mkubwa wa Sheria hii, Kanuni au miongozo iliyotolewa chini ya Sheria hii, mamlaka itapendekeza kwa chombo chenye mamlaka:
(a) kusitishwa utoaji wa fedha kwa taasisi kadha wa kadha.”
Mheshimiwa Spika, sasa changamoto yangu kwenye Ibara hii ni unaposema endapo kuna ukiukwaji wa mara kwa mara au ukiukwaji mkubwa wa sheria hii kanuni au miongozo tafsiri yake inaenda vipi, kwa sababu kama tunafanya marekebisho, nafahamu kuna kifungu kama hichi kilikuwepo kwenye sheria hii ya zamani, lakini sasa kama tunataka kutengeneza na kuziba mianya ya upotevu wa fedha nyingi ambazo zinatokea kwenye manunuzi kwa,nini tunakuwa tuna Kifungu ambacho kinaruhusu ukiukwaji wa mara kwa mara. Sasa mara kwa mara ni mara ngapi? Je, ni mara moja, mara mbili, mara tatu au mara tano au hata mara kumi, mara kwa mara? Au ukiukwaji mkubwa wa sheria, sababu sheria kimsingi inabidi isimamiwe sasa ukiukwaji upi ni mkubwa na upi ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napendekeza kifungu hiki kiweze kuboreshwa ili kuondoa mianya au kichaka cha wale watakaotuingiza sisi Watanzania kwenye hasara, wamepewa dhamana na maamuzi yao yakasababishia Taifa hili hasara, basi wasiwe wana kichaka cha kupotea kwa misingi ya kwamba hawajafanya uvunjifu wa sheria wa mara kwa mara au hawajafanya uvunjifu wa sheria mkubwa. Kwa hiyo naomba sana kwenye kifungu hiki, naamini Serikali watakuwa wana maelezo mazuri kwa sababu nia yetu ni njema, ni kufanya maboresho ya sheria ambayo yatalinufaisha Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine la kusisitiza ni Ibara ya 61 ambayo inazungumzia, inaweka masharti au inazungumzia kuhusu kujenga uwezo wa kampuni za ndani, kwamba hapa Ibara hii ya 61 kifungu hiki kinazungumzia kuhusiana na kuhakikisha kwamba kunakuwa kuna mazingira ya kuwajengea uwezo au kujengea uwezo kampuni za ndani ili ziweze ziweze kushiriki vizuri katika mikataba mbalimbali ya manunuzi. Tumemsikia Mheshimiwa Eric Shigongo amezungumzia masuala ya kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya wazawa ili na sisi wazawa, Watanzania hii ndiyo sehemu ya kupata ajira. Watanzania wapate fursa ya kupata mikataba na kufanya kazi za manunuzi ili waweze kujipatia kipato na tuondokane na umaskini kwa wananchi, kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwenye Ibara hii ambayo itakuwa ni kifungu 61 cha hii sheria mpya kuwe na msisistizo mkubwa, tujielekeze zaidi katika kuwajengea uwezo wazawa wetu, kwa sababu huko nyuma hata sababu mojawapo ya kutokutenga fedha hizi 30% za manunuzi, hawa Maafisa Masuuli utakuta sababu zao wanasema kwamba makampuni hayana uwezo wa kuja kushiriki kwenye tenda, hayana uwezo ya kupata mikataba hii na kuweza kutoa huduma hii.
Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ijengee uwezo makampuni ya ndani, muswada huu umeonesha maeneo mengi ya upendeleo wa kipekee kwa wazawa. Kwa hiyo katika utekelezaji tunahitaji sana kuona ni namna gani wazawa wanapata manufaa ya sheria hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina imani kubwa na Serikali, nina imani kubwa na Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, kwa hiyo nina imani mchango wangu pamoja na michango ya Waheshimiwa Wabunge wengine ambayo inalenga kuwasaidia Watanzania na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha kwenye manunuzi, Serikali itapokea ushauri na yale yote tuliyosema na kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha siku hii ya leo kukutana katika Bunge hili Tukufu kujadili mambo muhimu kwa maslahi ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kupongeza jitihada za Rais wetu wa awamu ya tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha maisha ya Watanzania, lakini za kupambana na rushwa, kujenga nidhamu na uwajibikaji kwa wananchi na watumishi wa umma. (Makofi)
Aidha, kwa muktadha huo ninaishauri Serikali iimarishe Taasisi ya Kupambana na Rushwa ili iweze kufanya majukumu yake vizuri na kwa weledi. Sanjari na hilo, Serikali iweze kuimarisha Taasisi za Kutoa na Kusimamia haki ili kulinda haki za Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kipekee nimpongeze Waziri Mkuu kwa kasi yake katika usimamizi wa Serikali, lakini pia kwa ziara yake aliyoifanya Mkoani Kigoma. Hakika ziara yake imeacha manufaa makubwa sana na hasa katika ulinzi na usalama wa Taifa letu hili. Pia imewaacha Watanzania na wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakiwa na ari na imani kubwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi; Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujielekeza katika ukurasa wa 46 wa hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inazungumzia nishati. Ni dhahiri kwamba katika maendeleo ya viwanda nchini, haitowezekana maendeleo hayo kufanikiwa pasipokuwa na nishati ya umeme na umeme wa kutosha na wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nangependa kuchukua fursa hii kupongeza jitihada za Serikali za kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts 1226.24 katika mwaka 2015 mpaka Megawatts 1,516.24 kwa Januari, 2016, ambalo ni ongezeko la asilimia 24 na ambalo limetokana na maamuzi sahihi ya Serikali ya kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la gesi. Pamoja na mradi wa kufua umeme wa Kinyeresi I ambao unazalisha Megawatts 150. Aidha, napenda kuunga mkono ujenzi wa Kinyerezi II ambayo itazalisha Megawatts 240.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kabisa lile lengo la Serikali la kipindi cha miaka mitano la kuhakikisha kwamba kuna uzalishaji wa umeme wa kufikia kiwango cha Megawatts 4,915 linafikiwa pasipo na shaka. Nami nina imani kabisa kwamba itakapofika mwaka 2020 asilimia 60 ya Watanzania wataweza kupata nishati hii muhimu ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani mafanikio makubwa sana ya mikakati hii ya kuzalisha umeme utafaidisha sana vijana. Utawafaidisha kwa sababu utaweza kukuza uchumi na tutaingia katika uchumi wa viwanda. Uchumi wa viwanda utaweza kuleta ajira kwa vijana, kwa maana wataweza kuajiriwa katika viwanda, lakini wao wenyewe wataweza kutumia nishati hii ya umeme kuanzisha viwanda vidogo. Kwa mfano, kuanzisha mashine za kukoboa, viwanda vidogo vya kukamua juisi, kukamua mafuta ya alizeti, ufyatuzi wa matofali kwa kutumia mashine za umeme. Kwa hakika mipango hii madhubuti sisi kama vijana tunaiunga mkono kwa sababu inatunufaisha sisi vijana moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kupongeza jitihada za kipekee za Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Muhongo, za kupunguza bei ya umeme. Punguzo la umeme linapelekea punguzo katika gharama za uzalishaji na gharama za uzalishaji zinapopungua, zinaleta upatikanaji wa faida; na faida inayopatikana inaweza kukuza uchumi zaidi, lakini kurahisisha na kuhakikisha kwamba ajira za vijana zinaendelea kuwepo, kwa sababu biashara hazitakufa, viwanda vitaendelea kuwepo, lakini na wao wenyewe vijana kwa faida wanazopata katika biashara zao, wataweza kunufaika na kukuza zaidi uchumi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba sana jitihada hizi za Serikali ziendelee na Serikali itambue kwamba sisi vijana tunathamini na kuunga mkono jitihada hizi, maana sisi ni wanufaikaji wa kwanza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana jitihada za Serikali kupanua mradi wa REA awamu ya pili, kufikia katika vijiji 1,669 katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja 2015/2016. Vijana wa Mkoa wa Kigoma Wilaya Kakonko, Buhigwe na Uvinza wananufaika sana na jitihada hizi kwa sababu wamesogezewa nishati ya umeme; na hivyo wao wenyewe wanaweza kufanya shughuli mbalimbali za kijasiriamali, ambazo zinahitaji nishati hii muhimu ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kupongeza jitihada ya Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuanzisha Mfuko wa Shilingi milioni 50 kwa kila Mtaa na kila Kijiji. Napenda kuishauri Serikali kwamba iweke maandalizi mazuri na nafahamu kuna jitihada zinazofanywa na Serikali kuandaa maandalizi mazuri ya Mfuko huu. Napenda kuishauri zaidi Serikali, iboreshe na kuimarisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana (Youth Development Fund). Katika Mfuko huu, tumeona vijana wengi wameweza kufaidika kwa kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao za kijasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kumejitokeza changamoto mbalimbali, hivyo napenda sana Serikali ichukue mfano au itumie uzoefu na changamoto ilizopata katika kuendesha na kusimamia Mfuko huu wa Youth Development Fund ili iweze kutengeneza mfumo bora zaidi utakaosimamia Mfuko huo wa shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji na kila Mtaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kupongeza mipango endelevu ya kukuza uchumi wa viwanda, lakini inabidi tufahamu kwamba katika mipango hii endelevu ya kukuza uchumi wa viwanda, ni lazima mipango hii iende sambamba na uzalishaji wa nguvu kazi yenye weledi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutoa elimu ya bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari. Imani yangu ni kwamba tunapoelekea katika uchumi wa viwanda, inabidi tufanye jitihada zinazoonekana za kuandaa nguvukazi kwa kuwapatia wanafunzi wetu elimu ya kutosha na yenye ubora wa kuwaandaa kupokea na kukabiliana na changamoto na uchumi wa kati na ushindani wa ajira, biashara na taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutegemei hapo haadaye tutakapokuwa na uchumi wa viwanda vijana au ajira ziende kwa watu wa nje. Tunategemea sana kwamba uchumi wa Viwanda utawanufaisha vijana wetu wa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada na mikakati mbalimbali ambayo Serikali imechukua kufufua viwanda na kujenga viwanda vipya nchini bado naona kuna changamoto ambazo ni vema Mheshimiwa Waziri akazifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kwanza kujifunza kwa nini viwanda vya zamani vilikufa?
Ni vema kujifunza wapi tulikosea kama Serikali na kama nchi mpaka viwanda vikafa
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema tukajifunza changamoto zinazokabili viwanda vilivyopo sasa na namna ya kuzitatua. Sambamba na kukaa vikao vya kimkakati na wamiliki wa viwanda waliopo saa hapa nchini na kupata mawazo na ushauri wa uhalisia wa hali ya uendeshaji wa viwanda hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, viwanda vilivyopo vinakabiliwa na changamoto zipi?
Kimasoko ya bidhaa zizalishwapo nchini?
Upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha na uhakika?
Gharama za umeme?
Sheria mbalimbali, rushwa na urasimu na kadhalika
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni lazima Wizara hii ishirikiane kwa karibu sana na sekta za kimkakati kama Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Elimu na ofisi nyingine wezeshi ili kuweza kufanikisha dhamira hii ya Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema kuwa na mpangokazi unaonesha ratiba ya utekelezaji wa kila hatua kuanzia sasa mpaka 2025. Pia ni vema Waziri atupe majibu ya changamoto zilizopo na namna atakavyozitatua na Wabunge tuko tayari kumpa ushirikiano kutafuta ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuongeze bidii ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kupunguza urasimu na vikwazo visivyo vya lazima ili kuhakikisha maendeleo ya uchumi wa viwanda nchini, sekta binafsi kuwa nguzo muhimu katika kufikia lengo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni lazima Serikali isimamie taasisi za kifedha nchini kwa kufunga sera wezeshi ili Watanzania waweze kushiriki kikamilifu kwenye uwekezaji ni lazima kuwe na upatikanaji wa mitaji yenye masharti nafuu toka kwenye benki zetu nchini ikilinganishwa na benki za nje yanayokopesha wawekezaji wa nje ambao wanashindana na wawekezaji wa ndani kwenye soko moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii adhimu ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Nishati na Madini.
Ninapenda kuendelea kupongeza juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo kwa Taifa hili, pia ninapenda kupongeza jitihada za Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sosthenes Muhongo kwa kazi kubwa anayoifanya. Vijana wa Tanzania tuna imani kubwa sana na Waziri huyu wa Nishati na Madini kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunatambua kazi kubwa iliyofanywa na Wizara hii ya Nishati na Madini katika kuongeza kiwango cha uzalishaji wa nishati ya umeme kutoka kiwango cha megawatts 1226.24 mpaka kufika kiwango cha 1491.69 megawatts ndani ya kipindi kifupi cha mwaka mmoja, kutoka Aprili, 2015 mpaka Aprili, 2016 ambayo ni ongezeko la uzalishaji wa umeme kwa kiwango cha asilimia 19. Sasa kama Wizara hii imeweza kuleta ongezeko la asilimia 19 ndani ya mwaka mmoja tu, basi tuna imani mpaka itakapofika kipindi cha miaka mitano watakuwa wameweza kuongeza uzalishaji wa umeme kwa zaidi ya asilimia 95. Kwa hiyo, ningependa kupongeza jitihada hizi, lakini ningependa Watanzania wote waweze kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kupongeza jitihada za Wizara hii za kuongeza kiwango cha usambazaji wa umeme yaani access level kutoka asilimia 36 mpaka asilimia 40. Hili ni ongezeko ambalo limepatikana ndani ya kipindi kifupi tu Machi, 2014 mpaka Machi, 2015. Kwa hiyo, tuna imani kubwa sana na Wizara hii, tuna imani kubwa sana na Waziri Profesa Sosthenes Muhongo, tuna imani ku…
MWENYEKITI: Siyo Sosthenes, ni Sospeter Muhongo!
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani kubwa sana na Waziri Sospeter Muhongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana tunashukuru sana kwa jitihada za Serikali, jitihada za Wizara za kupunguza gharama ya umeme. Kumekuwa na punguzo la umeme kwa asilimia 1.4 mpaka asilimia 2.4 ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wa Wizara hii katika mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwa Serikali kufuta tozo ya service charge ambayo ilikuwa ni shilingi 5,250; pia tunashukuru sana kwa Serikali kupunguza tozo la kuwasilisha maombi ya kuunganishwa umeme (application fee) ambayo ilikuwa ni shilingi 5,000, tunaiomba sana Serikali iweze kuongeza au kupunguza gharama za umeme katika umeme unaotumiwa katika viwanda, kwa sababu imepunguza umeme kwa wateja wa grade T1 na D1 ambayo ni matumizi ya nyumbani. Sasa tunaomba Serikali iweke pia mkakati wa kupunguza gharama ya nishati hii kwa matumizi ya viwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kutoa msisitizo kwamba, nishati ya umeme ni nishati ambayo inategemewa sana katika kukuza uchumi wa Taifa hili, kwa sababu ukizungumzia maendeleo ya viwanda unazungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme, lakini ukizungumzia mawasiliano unazungumzia upatikanaji wa nishati ya umeme! Ukizungumzia sekta nyingi za uchumi, hata ukizungumzia kilimo cha kisasa (mechanized agriculture), unazungumzia upatikanaji muhimu wa nishati hii ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi sekta nyingi za uchumi katika Taifa hili zinategemea nishati muhimu ya umeme. Ukizungumzia pia ajira kwa vijana utazungumzia nishati ya umeme kwa sababu sekta nyingi za uchumi ambazo ndiyo chanzo cha ajira kwa vijana zinategemea nishati ya umeme. Hivyo, tunaiomba sana Serikali iendelee na juhudi kubwa inazozifanya, vijana wa Kitanzania tunatambua jitihada hizi na tunawaunga mkono na tunawaomba wazidi kuziendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Kigoma tunatumia umeme unaozalishwa na mitambo maalum na mitambo hiyo inatumia nishati ya mafuta. Kusema kweli inagharimu Serikali fedha nyingi sana, tunatambua Serikali kupitia mradi wake wa Malagarasi unatengeneza mfumo au utaratibu wa upatikanaji wa umeme wa megawatts 44.8 ambao mradi huo utaweza kuzalisha umeme unaotokana na nguvu ya maji (hydro electric power). Kwa hiyo, tunaomba sana mradi huu wa Malagarasi Igamba II uweze kutekelezwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Serikali ina mpango kwamba, mpaka itakapofika 2019 mradi huu utakuwa umekamilika. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iweke usimamizi mahiri, ili itakapofika 2019 mradi huu uwe umeweza kukamilika kwa sababu, utawanufaisha vijana wa Kigoma. vijana wa Kigoma wanajishughulisha na biashara, wanajishughulisha na uvuvi, vijana wa Kigoma wanajishughulisha na viwanda vidogo vidogo, pia Kigoma tayari tuko katika utekelezaji wa mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha mafuta kwa kutumia michikichi. Tunafahamu kwamba ili mradi huo na kiwanda hicho kiweze kufanikiwa tunahitaji nishati ya umeme, hivyo tungeomba sana Serikali iweze kutekeleza mpango huu ili uweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote ningependa sana kuiomba Serikali katika mkakati wake wa kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme basi, jitihada hizo ziende sanjari na usambazaji wa umeme huu kwa sababu kama kukiwa kuna uzalishaji lakini usipowafikia watumiaji basi ina maana jitihada hizi zinakuwa hazina tija. Ninaomba sana Serikali iweze kuzingatia haya yote ili Watanzania waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema machache hayo napenda kuwapa nguvu sana na kusisitiza kwamba Watanzania, vijana na wanawake wa Tanzania tunatambua mchango wa Wizara hii na tuna imani kwamba itatusaidia kwa sababu, katika kipindi kifupi tumeona mambo makubwa ambayo yamefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii adhimu ya kuweza kuchangia katika hotuba hii. Ningependa kuendelea kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali. Pia ningependa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwakilishi wa vijana sisi vijana tunatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na Shirika la Nyumba la Taifa yaani NHC, lakini tungependa kuiomba Serikali kwa kuzingatia kwamba takwimu zinaonesha uwiano wa jumla ya idadi ya watu, vijana ndio wanaochukua asilimia kubwa; lakini pia kwa kuzingatia asilimia 59 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Basi vijana waweze kutengenezewa utaratibu wa kipaumbele wa kupata nyumba hizi za NHC lakini za bei rahisi. Kwa wale vijana ambao wanaanza kufanya kazi, wanaoajiriwa, wanakuwa na kazi basi na wenyewe watengenezewe utaratibu wapate hizi nyumba za bei nafuu. Hiyo bei nafuu iwe kweli bei nafuu na isiwe bei nafuu kwa kiwango fulani ambacho vijana watashindwa kuzimudu bei zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuishauri Serikali yangu sikivu juu ya umiliki wa ardhi. Sheria namba nne ya ardhi na sheria namba tano ya ardhi zinaeleza kwamba mmiliki wa ardhi ya Tanzania atakuwa ni Mtanzania na sio mgeni na kama mgeni akitaka kumiliki ardhi atamiliki ardhi kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) na kuna utaratibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria namba nne kifungu cha 20(4) kinaeleza bayana kwamba kampuni inayokuwa na shareholders wa kigeni yaani share nyingi kwa mtu ambaye ni mgeni, kampuni hiyo inakuwa ni kampuni ya kigeni na kampuni ya kigeni kwa sheria za Tanzania hairuhusiwi kumiliki ardhi ila pasipokuwa tu kwa kupitia TIC yaani kwa maana ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna utaratibu ambao wageni wanautumia; wageni wanakuja wanashirikiana na wazawa wanasajili kampuni lakini katika share structure ya hiyo kampuni inaonesha kwamba wazawa ndio wana-share nyingi zaidi lakini baadaye, baada ya kumiliki ardhi wanakuja wanabadilisha ile share structure na share structure inaonesha kwamba yule mgeni anakuwa ana share nyingi zaidi, yaani ni majority shareholder. Kwa hiyo, inaifanya ile kampuni inakuwa ni foreign company, yaani kampuni ya kigeni lakini inakuwa bado imemiliki ile ardhi. Kwa hiyo, inakinzana na hii sheria ambayo inasema mgeni na kampuni la kigeni haliruhusiwi kumiliki ardhi Tanzania pasipokuwa kwa utaratibu maalum ambao umewekwa chini ya Kituo cha Uwekezaji (TIC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali itengeneze utaratibu yaani Msajili wa Makampuni BRELA pamoja na Kamishna wa Ardhi kuwe kuna mawasiliano ili kuweza kubaini mabadiliko haya ya share structure ili kuhakikisha kwamba makampuni ya kigeni au wageni wasitumie makampuni haya kwa kuchezesha hizi share structure kutumia kumiliki ardhi ya Kitanzania tofauti na utaratibu na sheria za nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa sana kuishauri Serikali yangu kuhusiana na sheria yetu hii kwa mfano Sheria ya Ardhi namba tano, kifungu cha 18 kinaeleza bayana kwamba, ardhi au haki yaani customary right of occupancy ina hadhi sawa na granted right of occupancy yaani haki miliki ya kimila ina hadhi sawa na hati miliki ya kupewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii ipo kisheria, iko pia kama yaani sera au kama sheria, lakini kiuhalisia hizi hati za kimila hazina haki sawa na hizi hati miliki ya kupewa. Kwa sababu mtu ambaye ana hii customary right of occupancy ambayo ni hati miliki ya kimila hawezi kwenda benki akataka kuikopea au kupata mkopo ku-mortgage kwa sababu atapata kipingamizi, itaonekana haifai, haitoshi, haina kiwango sawa pamoja na hii hati miliki ya kupewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tunajua vijana wetu wengi waliopo hata huko vijijini wana hizi ardhi na wangependa kutumia hii ardhi waliyoletewa na Mwenyezi Mungu katika Taifa hili kwa ajili ya manufaa yao wao wenyewe na kuboresha uchumi wa Taifa. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kuangalia kwamba hii section 18 ya Village Land Act iweze kuwa na uhalisia kwa sababu ipo tu academically lakini kiuhalisia hati miliki ya kimila haina hadhi sawa na hati miliki ya kupewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kushauri kuhusu Mabaraza ya Ardhi; Mabaraza ya Ardhi yalianzishwa ili kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi, lakini kuharakisha hii migogoro ya ardhi iweze kwisha kwa wakati. Tofauti na matarajio kimsingi haya Mabaraza ya Ardhi yanaonekana yameelemewa; kesi zimekuwa nyingi, zinachukua muda mrefu hadi miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu kwa Serikali, kabla sijakwenda nataka nisome Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kabla sijaenda huko nilikuwa napenda ifahamike Mabaraza haya ya Ardhi ya Kata yanasimamiwa na Wizara ya TAMISEMI; lakini Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya yanasimamiwa na Wizara hii ya Ardhi, lakini ukija kwenye mahakama unakuta mahakama inasimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta kwamba kuna Wizara tatu tofauti ambazo zimepewa mamlaka ya kusimamia jambo ambalo ni moja. Ukisoma Katiba, Ibara ya 107(a) utakuta imetamka bayana kwamba mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni mahakama. Sasa haya Mabaraza ya Ardhi yanafanya kazi ya kutoa haki ambacho ni kinyume na Katiba nadiriki kusema. Kwa sababu mahakama ndiyo chombo cha mwisho cha kutoa haki na sisi tunajua haya Mabaraza yanachukua muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama yameshindwa hii kazi na naweza kudiriki kusema naona yameelemewa, basi hii kazi ya kutoa haki irudishwe katika mfumo wa mahakama, kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka kufika mwisho katika mfumo wa mahakama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia Ibara ya 113 ambayo imeelezea majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, inasema, jukumu mojawapo la Tume ya Mahakama ni kuajiri Mahakimu na kusimamia nidhamu yao. Kwa hiyo, katika mfumo wa mahakama hawa Mahakimu wanasimamiwa na sheria na nidhamu zao zinasimamiwa kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, wana mamlaka ya kuwawajibisha lakini hawa viongozi wanaokaa katika Mabaraza ya Kata, ya Wilaya hamna mamlaka ya kushughulikia nidhamu zao. Hakuna bodi ambayo ina-deal na ethics zao, hivyo, ningeomba sana Serikali iweze kuleta Muswada kwa ajili ya kurekebisha hizi sheria zilizoanzisha haya Mabaraza ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba mahakama ina uwezo mkubwa sana wa kuendelea kutekeleza au ku-solve haya matatizo na changamoto za ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba pia Waziri wakati anahitimisha aweze kutoa kauli juu ya uhalali wa kukopesheka kwa hati hizi za kimila kwa sababu vijana sisi tunajua wengi wetu tunazo hizi hati; tunataka ziweze kutumika kwa ajili ya manufaa yetu, sheria inatamka kwamba zina haki sawa pamoja na hizi hati za Kiserikali. Kwa hiyo, tunaomba Waziri atamke ili ifahamike na ziweze kutambulika kwamba zina hadhi sawa katika mabenki ili tuweze kukopa kwa kuzitumia hizi hati za kimila. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii ya kuweza kuchangia katika hoja iliyopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuleta uchumi wa viwanda kuna mambo ya msingi ambayo Serikali inabidi iendelee kuweka msisitizo. Katika uchumi wa viwanda ni lazima Serikali iweze kuangalia kwamba kuna upatikanaji wa malighafi. Tunahitaji malighafi ya kutosha ili kuweza kulisha viwanda vyetu. Katika malighafi tunazungumzia upatikanaji. Kukiwa kuna viwanda lakini hakuna upatikanaji wa malighafi ya kutosha kulisha viwanda vyetu basi mwisho wa siku tunakuja kuona viwanda vyetu vinafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu nitoe mfano, viwanda vyetu vya sukari hapo awali vilikuwa vinafungwa kwa msimu fulani kwa sababu hakukuwa na malighafi ya sukari ambayo ingeweza kuzalisha sukari. Kwa hiyo, Serikali inabidi iweke msisitizo katika upatikanaji wa malighafi hizi. Na hata tukiangalia nchi ambazo ziliendelea na zimeendelea katika uchumi wa viwanda ilianza kwanza agrarian revolution yaani mapinduzi ya kilimo, yalianza yakaweza kuleta industrial revolution ambayo ni mapinduzi ya viwanda. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuendeleza jitihada zake inazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu, tunahitaji malighafi ambazo ni za bei nafuu. Tukiwa tuna viwanda lakini malighafi zinazopatikana nchini ni za bei ya juu na zinatumia cost of production kubwa kuliko zinazotoka nje ya nchi, mwisho wa siku tunaona kwamba hata gharama ya uzalishaji wa mali ambazo zitazalishwa ndani ya nchi zitakuwa zina gharama ya juu zaidi kuliko mali zitakazoletwa kutoka nje ya nchi.
Kwa hiyo, ningependa pia Serikali iendelee na jitihada zake inazofanya kuhakikisha kwamba malighafi zinapatikana kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu, tunahitaji ubora wa malighafi ambao utatokana na ubora tuseme kwa mfano wa mbegu. Kwamfano kama tunazungumzia viwanda vya kutengeneza, tuseme juisi, inahitaji kwamba kuwe kuna ubora wa hata yale matunda yanayopatikana Tanzania. Kwa hiyo je, mbegu zinazotolewa na mbegu zinazotumika zina ubora wa kuzalisha kwa kiwango kizuri cha kuweza kulisha viwanda vyetu? Hilo ni suala lingine ambalo Serikali inabidi iendelee kufanya jitihada zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mbolea, kuna suala zima la teknolojia inayotumika, je, teknolojia inayotumika Tanzania ni ya kizamani au inaendana na wakati, kwa sababu kutumia teknolojia ya zamani kunaleta gharama kubwa zaidi ya uzalishaji na mwisho wa siku hata mali zetu na viwanda vyetu vinakuwa haviendelei vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia katika suala zima la upatikanaji wa mitaji. Upatikanaji wa mitaji au tuseme mikopo lakini upatikanaji wa mitaji hii kwa riba nafuu. Upatikanaji wa mikopo katika taasisi zetu za kibenki tujiulize, je, unaweza kuhimili uchumi wa viwanda? Je, financial institutions zinaweza kutoa mikopo kwa ajili ya wawekezaji wetu wa ndani kuweza kuwekeza katika viwanda vyetu? Na hiyo mikopo inayotoka na hizo fedha zinazotoka kutoka kwenye taasisi zetu riba zake zikoje, kwa sababu kuna taasisi za kifedha ambazo zinatoa mikopo, zinatoa fedha kwa riba hadi asilimia 25, je, huyu mwekezaji ataweza kweli kufanya biashara zake, ataweza kweli kuhimili matakwa ya kuendesha kiwanda chake na kikaweza kufanikiwa.
Kwa hiyo mimi napenda kuiomba Serikali kwamba ikae na wadau mbalimbali, viwanda na biashara na taasisi za kibenki, ili iweze kusaidia mchakato utakaoweza sisi kutunga sheria itakayoweza kuweka ukomo wa viwango hivi vya riba kwenye mikopo katika taasisi za kifedha. Kwa sababu tukisema tu tunaacha hivi ilivyo, taasisi za kifedha zinaweka riba za hali ya juu na mimi kama kijana najua vijana wenzangu wanajishughulisha katika shughuli za ujasiriamali na wanahitaji hizi fedha, wanakwenda kwenye taasisi za kifedha na wanapata fedha kwa riba kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya nishati, Mpango unaonesha mpaka mwaka 2020 uzalishaji wa umeme ufikie zaidi ya Mw 5000 Installed Capacity, kwa sasa ni Mw 1358 na mradi wa Stieglers Gorge utazalisha Mw 2100. Je, Mw 1542 itatokana na mradi upi ili kufikia lengo la Mw 5000 mpaka ifikapo mwaka 2020?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango haujaainisha kama itashirikisha sekta binafsi au itatumia mradi upi kufikia lengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali katika mradi wa Stieglers Gorge itumie teknolojia ya kisasa ya electricity generation by recycling of water ili kuepusha kusuasua kwa uzalishaji wa umeme kutokana na upungufu wa kina cha maji kwenye vyanzo vya maji. Mfano wa teknolojia iliyotumika kwenye The Grand Ethiopian Renaissance Dam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa namba 14 umeonesha projection ya population growth. Tanzania katika miaka michache ijayo itakuwa na idadi kubwa ya watu. Je, tumejiandaa katika mipango yetu kuhakikisha kuwa ongezeko hili la watu sio tegemezi na lisiwe mzigo wa Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Mtanzania. Je, Serikali imeandaa mikakati gani ya kuimarisha mazingira ya Agro Business Tanzania? Kwa mfano, kuna vyombo kama Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambayo ni chombo cha kusaidia wakulima wanapata soko la uhakika wa mazao yao, lakini Bodi hii haijawezeshwa kibajeti kutimiza malengo. Mfano, mwingine ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambayo inachangamoto ya mtaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iweke katika mipango yake namna ya kuwezesha vyombo vilivyo vya kuendeleza kilimo Tanzania. Lakini Serikali iweke mipango ya makusudi ya kuwahakikishia wakulima soko la mazao yao ili kilimo kiweze kuleta tija. Pia itoe kibali kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kupata shilingi bilioni 8.9 loan kutoka NSSF na kibali cha kupata mkopo wa bilioni 6 kutoka Azania Bank ili Bodi ifanye kazi zake kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefikia wapi katika kuleta Muswada wa sheria itakayoanzisha Price Stabilazation Fund, mfuko utakaoweza kuwa suluhisho la kumlinda mkulima pale bei za mazao zinapoanguka, kwa mfano mbaazi mwaka huu?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi kuweza kuchangia taarifa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa the Interpretation of Laws Act, Cap. 1, imeweka masharti maalum ambayo yanalipa Bunge mamlaka ya kuweza kuzisimamia au kufanya udhibiti wa Sheria Ndogo ambazo zinatungwa na Serikali pamoja na taasisi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge linafanya udhibiti huo baada ya sheria zile ndogo kuwa zimetungwa na Serikali na zimetangazwa katika Gazeti la Serikali, lakini pia zimewasilishwa Bungeni. Katika uchambuzi wa sheria ndogo vitu ambavyo tunajiridhisha ni kwamba, kama sheria ndogo hizo zilizotungwa zinaendana na zinakidhi matakwa na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia zinakidhi matakwa na masharti ya sheria mama na sheria nyingine za nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sheria ndogo ya The Mining Local Content Regulation katika kanuni ya 3, kanuni hii inaonekana kwamba ni ultra vires kwa maana ya kwamba, inakwenda kinyume na masharti ya sheria mama, kivipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, ukiangalia kanuni hii yenyewe inatoa tafsiri ya neno kampuni zawa ambayo katika tafsiri yake imeweka kwamba, kampuni zawa itakuwa ni ile kampuni ambayo katika share holders wake au wanahisa 51% ya wenye hisa wawe ni Watanzania. Si hivyo tu, pia 80% katika utendaji wa juu wa kampuni hiyo pia, wawe ni Watanzania. Sasa ukiangalia Sheria ya Makampuni ambayo ndio sheria mahususi kwa masuala ya makampuni kwa Tanzania hii, haijatoa tafsiri hiyo, ambayo imetolewa katika kanuni hii kwa hiyo, maana yake nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kunakuwa na mkanganyiko wa tafsiri na utaratibu wa kutunga kanuni au kutunga sheria ndogo ni lazima sheria mama zizingatiwe. Pale kunapokuwa na mkanganyiko kati ya sheria mama pamoja na kanuni hiyo inaleta changamoto na ninaomba sana marekebisho yaweze kufanywa ili kuondoa mkanganyiko huo kwa sababu ukiangalia kwenye Sheria ya Makampuni yenyewe inatafsiri kampuni zawa ni kampuni ile ambayo imesajiliwa chini ya BRELA. Kwa hiyo matakwa ya shareholding structure hayajawekwa kwenye Sheria ya Makampuni.
Kwa hiyo, ni vizuri Sheria ya Makampuni ifanyiwe mabadiliko ili kuweza kuendana na matakwa ya mabadiliko na kuzuia mkanganyiko wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pia kwenye The Urban Planning (Appeals), Regulations, 2018 ambayo imetungwa chini ya Sheria ya The Urban Planning Act, Sura ya 355, utaona kwamba kanuni hii imeweka sharti kwamba mahakama mara baada ya kutoa uamuzi, kuwasilisha nakala tatu za hukumu kwa Mamlaka ya Mipango Miji zinazoainisha sababu ya kufikia maamuzi yake. Sasa ukiangalia kanuni hii, utaona kwamba utaratibu uliowekwa na kanuni hii si sawa, kwa nini, kwa sababu hamna chombo au taasisi yoyote ya Serikali…
T A A R I F A . . .
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama ni mhimili unaojitegemea na unaoendeshwa chini ya Ibara 107(b) lakini unapoona kwamba kuna kanuni ambayo inatoa sharti ya kuamuru Mahakama tofauti na utaratibu basi hii kanuni inakuwa ni batili na inakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana gani kwamba Mahakama haiwezi kuamuriwa na Serikali au chombo chochote cha Serikali, bali mahakama inaamuriwa na mahakama iliyo juu yake, si tofauti na hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii kanuni ambayo inayotoa masharti kwa Mahakama kuleta maelezo na kuleta nakala tatu za hukumu kwa Mipango Miji na kuainisha sababu ya kufikia maamuzi yake ina changamoto na sio sahihi na kuna haja ya kufanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, ukiangalia kwenye hii The Urban Planning (Appeals), Regulations, 2018 kanuni ya 4(b) kanuni ya ndogo ya pili na ya tatu utaona kwamba inaweka sharti kwa mtu anayekata rufaa dhidi ya maamuzi ya Mamlaka ya Mipango Miji kutoa nyaraka zote pamoja na zile ambazo hakuwa amezitoa katika usikilizaji wa shauri la awali dhidi ya mamlaka hiyo kuzipeleka kwa Mamlaka ya Mipango Miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika utaratibu mtu anayetoa rufaa hatakiwi wala hapaswi kisheria kupeleka nyaraka zozote kwa yule mrufaniwa, tofauti na hapo inabidi tu asubiri mashtaka yaanze na atakabidhi nyaraka kwa Mahakama na si kumpelekea yule ambaye yeye anaenda kukata rufaa dhidi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo tu hata katika ngazi ya rufaa, rufaa haichukui ushahidi mpya, rufaa inafanya uamuzi kutokana na nyaraka zilizokuwepo kuanzia mwanzo katika mashtaka, lakini kusema kwamba kuletwe nyaraka mpya si utarabu sawa na ni kinyume na tofauti na kanuni hizi zinavyoelekeza. Kwa hiyo, kuna haja ya kufanya marekebisho ili kuendana na sheria zilizowekwa ambazo zinaongoza utaratibu wa kimahakama wa kukata rufaa na wa kimashtaka kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kujielekeza kwenye baadhi ya hizi sheria ndogo, naomba sasa kuishauri Serikali kwamba wakati wa utungaji wa sheria ndogo kwanza wawashirikishe wadau mbalimbali ili hizi sheria ndogo zinapokuja kutungwa kusiwe kuna changamoto wakati wa utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, Serikali pia iongeze rasilimali watu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hasa katika vitengo vinavyojihusisha na kupitia sheria ndogo hizi ili kuondoa zile dosari ambazo zinaonekana ambazo hatimaye zinaleta changamoto katika utekelezaji wa sheria husika. Pia wakati wa utunzi wa sheria ndogo mamlaka au Serikali pia ihakikishe kwamba uchambuzi na utunzi wa zile Sheria Ndogo unazingatia misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sheria ndogo na sheria zingine za nchi ili sheria ndogo tunazozitunga zisije zikaleta conflict of Laws na sheria ziwe zinaweza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu za kufua zao la chikichi na kuongeza zao la chikichi katika mazao ya kimkakati nchini. Zao la chikichi litabadilisha uchumi wa Mkoa wa Kigoma na kunufaisha wakulima wa zao hili, lakini pia kufufua zao hili itasaidia kupunguza uingizwaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi na badala yake kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mafuta ya kula (palm oil) ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la chikichi linahitaji uwekezaji wa miaka mitatu tu lakini mkulima akianza kuvuna anaweza kuvuna kwa zaidi ya miaka nane. Zao la chikichi linaweza kuzalisha bidhaa ya mafuta ya kula (palm oil), sabuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani lakini mashudu ya zao la chikichi yanaweza kutumika kwa ajili ya chakula cha mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ataendelea kushukuriwa na Wanakigoma kwa kuchochea maendeleo kwa kuhakikisha zao la chikichi linakuwa na tija. Aidha, tunaomba zoezi la upatikanaji wa mbegu za zao la chikichi litiliwe/liongezewe mkazo ili wakulima wapate mbegu za kutosha na mbegu zenye ubora. Mbegu za chikichi zinauzwa shilingi elfu sita kwa mbegu, gharama hii ni kubwa, tunaomba Serikali iweze kuangalia namna ya kurahisisha na kupunguza gharama za upatikanaji wa mbegu za chikichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma inathamini sana jitihada za Serikali katika kampeni hii muhimu ya kufufua zao la chikichi. Wabunge na wadau mbalimbali tutaendelea kuunga mkono jitihada hizi za Serikali yetu makini.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya baraka zake nyingi sana. Pia nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuendelea kuniamini. Kipekee kabisa niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Kigoma, wapiga kura wangu ambao wameniamini mimi kijana wao niweze kuwa mwakilishi katika Bunge hili Tukufu. Nachowaahidi sitowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote ni mashahidi ya namna gani Serikali ya Awamu ya Tano imefanya jitahada kubwa sana ya kuwawezesha wanawake lakini pia kusimamia masuala ya kijinsia. Hata ukisoma kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, ukurasa namba 4, utaona Mheshimiwa Rais ametoa ahadi na amesema naomba kunukuu: Kwa msingi huo, napenda nitumie fursa hii kuwaahidi kuwa Serikali ninayoiongoza itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Wanawake na kinamama hoyee”. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Hoyeee.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni katika Serikali ya Awamu ya Tano katika historia ya nchi hii Tanzania tumepata Makamu wa Rais wa Kwanza mwanamke, Mheshimiwa mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye pia amefanya kazi vuziri sana na sisi sote ni mashahidi ni namna gani yeye amedhihirisha uongozi wa mwanamke jasiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo tu, kuna mifano mingi ya wanawake wengi ambao wamepewa fursa katika Serikali hii ya Awamu ya Tano ikiwemo wewe mwenyewe Naibu Spika, Mbunge wa Jiji la Mbeya. Tuna Mheshimiwa Jenista Mhagama, aliyekuwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, tuna viongozi wengi pia kwenye Serikali, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Mabalozi na wote wanafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kusisitiza na kuwaambia wanawake wenzangu tunavyopewa nafasi sisi wanawake tufanye kazi kwa weledi ili tuhakikishe tunajenga taswira nzuri ya uongozi wa mwanamke katika jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma kwenye ukurasa wa 17 - 19 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais, utaona ameelezea mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano. Ameelezea ni namna gani sisi kama nchi tumeingia katika uchumi wa kati, tena tumeingia katika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya ule muda tuliotarajia, haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa wa 20 amesisitiza kwamba mipango hii ya kuendeleza na kukuza uchumi wetu itaendelea. Amezungumzia mipango ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, masuala ya kuhakikisha kwamba anatoa kipaumbele kikubwa sana katika sekta binafsi lakini pia kutengeneza ajira milioni 8. Kusema kweli mipango mingi ya Serikali ni mizuri, naomba kusisitiza katika maeneo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza, naomba sana Serikali ihakikishe na isimamie katika hiki kipindi kunakuwa na sera, sheria, miongozo na taratibu ambayo inagusa masuala ya uwekezaji, biashara na uchumi isiwe inabadilika sana ili kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara kuzitambua lakini kufanya biashara kwa utulivu. Pia Serikali isimamie utekelezaji wa blue print, kazi kubwa imefanyika lakini sasa tusimamie utekelezaji wa haraka ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara yameboreshwa na yamekaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kuishauri Serikali katika sekta ya elimu. Katika sekta ya elimu sisi tunajenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo lazima tuhakikishe tunaandaa rasilimali watu ambao wataenda kuhudumia uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, lazima tuwekeze katika kada ya kati kwa sababu ndiyo inayohitajika kwa ajili ya kuhudumia uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, nguvu yetu kubwa tuangalie katika zile kada za kati kwa maana yaani tuangalie wale wanafunzi wanaosoma cheti, mafunzo ya ufundi na stashahada, hawa ndiyo wengi watakaohitajika katika uchumi wa viwanda. Hata Bodi ya Mikopo iwawezeshe hawa wanafunzi wa hii kada ya kati ili kuzalisha rasilimali kubwa ambayo itahijika kwa ajili ya uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba sana tuangalie katika mtaala ya elimu. Katika mitaala yetu ya elimu tuhakikishe katika masomo yote angalau kuwe na mafunzo ya msingi ya namna gani ya kuanzisha na kuendeleza biashara ili mhitimu anapomaliza chuo hata kama amesoma shahada tuseme ya sociology au political science na anashindwa kuajiriwa katika ajira rasmi basi aweze yeye mwenyewe kuwa mawazo ya namna gani yeye mwenyewe anaweza akaanzisha biashara na kuiendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nawaomba sana Watanzania wote kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anatimiza wajibu wake ili ile dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kulijenga Taifa hili iweze kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza nianze kwa kupongeza sana jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara katika kuleta maendeleo katika nchi yetu hii ya Tanzania, lakini kwa upekee kabisa na kwa msisitizo mkubwa sana, niishukuru Serikali kwa kuwa sikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa katika bajeti ya Wizara ya Fedha nilitaka kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa sababu ya hoja ile ya kutaka Serikali iweze kutoa grace period ya miezi 6 kwa wafanyabiashara wanaoanza biashara/wafanyabiashara wapya kabla ya kuanza kulipa ile kodi ya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukifungua katika ukurasa wa 84 wa hotuba utaona kwamba wamesema hapa kwamba Serikali imesema kwamba itatoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa namba ya utambulisho wa mlipa kodi. Kwa hiyo, ina maana Serikali ni sikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa sababu hii ilikuwa ni changamoto kubwa sana ya vijana pamoja na wafanyabiashara wengine lakini ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukiangalia pia msingi wa kodi ya mapato (income tax). Msingi wa income tax upo kwenye faida yaani income tax inapatikana kutoka kwenye faida na siyo mtaji. Na hapo awali tuseme tu labda tuzungumzie vijana walikuwa wanakutana na changamoto gani yaani unakuta kijana anakosa ajira, hawezi kuajiriwa inabidi ajiajiri yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiacha tu kwamba unakuta kijana amesoma miaka 3 Shahada yake ya Sociology, miaka yote anafundishwa theories za Ma- philosopher mbalimbali kina Karl Marx wanasema nini na nini halafu anakosa ajira inabidi aingie kwenye biashara ambayo tukiangalia hata katika mfumo wetu au katika mitaala yetu ya elimu, bado haijatengenezwa kiasi ya kuwatengenezea msingi wa kuanzisha na kuendeleza biashara wahitimu wetu, unakuta kwamba kijana hajui anaanzia wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akipambana na hiyo changamoto, anarudi tena anakutana na changamoto ya kukosa mtaji, akipambana na changamoto ya kukosa mtaji, akipata huo mtaji kwa mkopo bado anakutana na suala kwamba lazima atumie mtaji wake ule kuanza kutoa kodi kabla hajaanza kufanya biashara. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa sababu kwa kutoa nafuu hii ya miezi sita kwa mfanyabiashara mpya kutokulipa hii kodi kwa kweli mmewasaidia vijana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri katika siku hizo za mbele, tuone kama tunaweza ku-extend hii grace period ili iweze kufikia hata mwaka mmoja kwa sababu kama nchini wanakuja wawekezaji ambao wanaweza kupewa grace period/tax holiday hadi ya 5, 3 years. Kwa hiyo, sisi wazawa wenyewe ili ku-encourage watu waweze kuwa na moyo wa kufanya startups na kwa sababu tunajua kujenga msingi wa biashara siyo jambo rahisi. Kuna mtu anaweza akaanzisha biashara mwaka mzima lakini akashindwa kuiimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana Serikali katika hizo siku za mbele tuangalie ni namna gani tutaongeza hiki kipindi ili kiweze kufika mwaka mmoja. Tutawa-encourage watu wawe wana moyo wa kuanzisha biashara, wasiwe na uoga lakini hii itawanufaisha sana vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la taulo za kike tumesikia limezungumzwa sana, imechangiwa na Wabunge mbalimbali lakini mwaka jana tuliona kwamba Serikali ilichukua jitihada ya kuondoa VAT katika bidhaa hii ya taulo za kike. Hata hivyo, tumeona jitihada hii haikuzaa matunda kwa sababu haikuleta punguzo la bei katika bidhaa hii ili kuleta unafuu kwa watoto wetu wa kike hususan wale ambao wako shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme tu kwamba ninaunga mkono maamuzi ya Serikali ya kuirudisha hii VAT kwenye bidhaa hii ya taulo za kike lakini siyo hivyo tu nina ushauri. ushauri wangu ni upi, pamoja na kwamba VAT imerudishwa katika bidhaa hii ya sanitary towels hizi taulo za kike na kwa kuzingatia kwamba raw materials au malighafi zinazotumika kuzalisha bidhaa hii ya taulo za kike ndani ya nchi na zenyewe zimeondolewa ushuru wa forodha lakini naomba Serikali iweze kuondoa VAT katika raw materials zinazotumika kutengeneza hizi sanitary towels. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja inaweza ikawa kwamba ukiondoa VAT kwenye malighafi za kutengeneza taulo za kike ndani ya nchi, hizi malighafi zinaweza kutumika pia kwa matumizi mengine tofauti. Sasa kwa hoja hiyo, Serikali inaweza ikaangalia utaratibu wa kuweza kuwa malighafi hizi zinaagizwa kwa quarter kama vile inavyofanyika sukari za viwandani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii naamini kwamba ikiondolewa hii VAT kwenye hizi malighafi (raw materials) za kutengenezea taulo za kike itasaidia katika kupunguza gharama ya uzalishaji na itapunguza pia bei, lakini itapunguza bei ya taulo za kike kama Serikali itaweza kuweka na kutoa bei elekezi na kuelekeza kwamba bidhaa hii ya taulo za kike iweze kuwekewa price tag yaani kama vile tunavyoona ukinunua kwenye gazeti, gazeti limeandikwa 1,000. Kwa hiyo, hawezi mfanyabiashara akachukua gazeti akaenda kuuza 1,500 kwa sababu bei ya gazeti imeshaandikwa kwenye lile gazeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuona namna gani itaelekeza na ita-regulate ili bidhaa hii ya taulo ya kike kwa sababu tunajua tayari cost of production itakuwa imepunguzwa na faida itakuwa inapatikana, wafanyabiashara wasitumie misamaha hii ya kodi kujinufaisha na kuongeza wigo wa faida yao na badala yake ile intention ya kuondoa hizi kodi iweze kuwa realized. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, ushauri wangu mwingine ninaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuweka au kutolewa kwa hizi sanitary towels katika mfumo wetu wa bima za afya (health insurance) kwa sababu sisi sasa hivi tunaelekea katika utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtanzania anaweza kuwa na bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika mfumo wa bima ya afya, kinachoweza kufanyika sisi tunajua bima za afya zina madaraja na hata kwa mfano leo hii National Health Insurance Fund (NHIF) yenyewe ina kadi ya kijani, nyekundu, njano na kadi za Kibunge, hayo yote ni madaraja ya bima ya afya. Kwa hiyo, sasa yale madaraja kwa sababu tunataka hizi taulo za kike (sanitary towels) ziweze kupatikana kwa wale wenye uhitaji ambao tumeshasema hapa wenye uhitaji ni watoto wetu wa kike ambao wapo shuleni wanakosa hizi taulo za kike na kuna siku wanakosa masomo shuleni kwa kukosa vitu vya kujihifadhia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa muktadha huo huo, hii bima ya afya unaweza kutengenezwa utaratibu ambapo kuna madaraja ya hizi bima za afya ambayo beneficiaries wake ndiyo wanaweza ku-benefit kwa kupewa sanitary towels. Na kwa sababu hizi bima za afya anaweza akakata bima mzazi na beneficiaries wakawa familia nzima au anaweza akawa mnufaikaji mmoja yule aliyekata bima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye ngazi ya familia inajulikana na hata zile kadi za bima, kila muhusika anapewa na particulars zake zinajulikana. Kwa hiyo, ule umri wa kuwa ni mwanafunzi na vielelezo vya kwamba huyu ni mwanafunzi vinaweza vikajulikana na Serikali na hawa wenye sifa wakawa wana utaratibu wa kupewa hizi sanitary towels kwa kila mwezi labda unasema wanapewa piece mbili. Mimi na… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana. Mheshimiwa Rose Kamili Sukum atafuatiwa na Mheshimiwa Benardetha Mushashu, Mheshimiwa Ahmed Ngwali Juma ajiandae.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza na mimi nianze kutoa pongezi kwa kazi kubwa ambayo ni dhahiri ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. Sisi sote ni mashahidi kwa kiasi gani miaka hii mitano imekuwa ni ya utekelezaji wa yale yote yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa mwaka 2015/ 2020. Kwa sababu ni dhahiri hata sisi huwa tukizungumza na marafiki zetu wengine hususan hawa ambao wamekaa upande wetu wa kulia, tukiongea kiurafiki huwa wanakiri jitihada kubwa ambazo zimefanyika katika utekelezaji wa Ilani.
Mheshimiwa Spika, aidha, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini kwa hotuba yake hii ambayo tunachangia leo. Nafahamu kwamba ana wasaidizi wake Waziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Serikali ambao wanafanya kazi hii kubwa, kwa hiyo nipongeze jitihada hizo.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika masuala ya vijana na kabla ya kuchangia katika masuala ya vijana ningependa na mimi nigusie changomoto hii au janga hili la kidunia na hasa katika sekta ya afya, la ugonjwa wa SARS-Cov2 au tuseme COVID 19. Ugonjwa huu kama wote tunavyofahamu ni janga la dunia, janga la kiafya ya kidunia na sisi Tanzania ni nchi mojawapo ambayo imekutwa na ugongwa huu. Nafahamu kuna jitihada kubwa sana na sisi wote ni mashahidi, ambazo zimefanywa na Serikali katika kuhakikisha kwamba tunautokomeza ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, kuna wazo ambalo lipo katika jamii ambalo naona halijatolewa ufafanuzi. Kuna mawazo (misconception) kwamba ugonjwa huu hauathiri watu wenye ngozi nyeusi kama unavyoathiri watu wa mabara mengine, yaani kwamba Bara la Afrika sisi tuna upekee ambao unatupa nafuu katika kudhurika na ugonjwa huu. Mawazo hayo sidhani kama ni mazuri sana kwa sababu pia yanafanya wananchi wanaweza wakazembea katika kujikinga kwa kuamini kwamba wao wakiwa wana ngozi nyeusi watakuwa wana nafasi kubwa zaidi ya kupambana na ugonjwa huu, hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, lakini kitu kingine, tunafahamu kwamba ugonjwa huu unaleta athari za kiuchumi. Bila shaka Serikali itakuwa ina mkakati wa kuona ni namna gani inachukua hatua za kifedha ili kupunguza madhara ya kiuchumi yanayotokana na janga hili. Kwa hiyo, naomba Serikali na yenyewe iangalie kuona kwamba watachukua hatua gani ambayo itasaidia kuokoa sekta zile ambazo zimeathirika kiuchumi na janga hili la ugonjwa huu
Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu wamezungumzia na wametoa maelezo yanayojitosheleza kwa namna gani masuala ya ajira na uwezeshaji yamefanyiwa kazi na mikakati ya kusonga mbele. Mimi nina ushauri katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, ni kuhusiana na mfuko kutengwa kwa asilimia kumi ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa ajili ya kuwezesha makundi maalum ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake na kundi la ulemavu. Tumeona katika kipindi hiki cha miaka mitano kwenye Bunge hili tulifanya marekebisho ya sheria na sasa tumehakikisha kwamba fedha hizi zinatengwa. Ushauri wangu ni kwamba Serikali ione ni namna gani itatengeneza mfumo wa kielektroniki ambao utaweza kusaidia kufanya michakato yote ya uombaji na utoaji mikopo hii.
Mheshimiwa Spika, pia mikopo hii kuwe na formula kwa sababu jinsi ilivyo sasa hivi kila Halmashauri inakaa vikao vyao kuangalia ni kiwango gani cha chini au cha juu kitatolewa kwa ajili ya mikopo. Kwa hiyo, kuna mbinu tofautitofauti zinazotumika katika maeneo tofauti. Kwa hiyo, katika siku za mbele tuone ni namna gani tunakuwa na mfumo wa kielektoniki ambao utasaidia kusimamia na kuratibu mfuko huu kwa ajili ya kuwezesha vijana, wanawake pamoja na kundi la watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, pia tukiangalia kuna Sheria hii ya Manunuzi ya Umma, Sura 410, kwenye kifungu cha 64(2) kimetoa masharti ya kwamba taasisi au tuseme mashiriika ya umma yatenge asilimia 30 ya manunuzi yake kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Naiomba Serikali iweke mkazo na msisitizo kuona kwamba kifungu hiki cha sheria ikiwa ni pamoja na Kanuni zake kinazingatiwa kwa sababu ni eneo pia la vijana wetu, wanawake pamoja makundi ya watu wenye ulemavu kujipatia nafasi ya kutengeneza kipato na kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa maoni yangu kwenye suala zima la elimu. Sisi sote ni mashahidi ni kwa kiasi gani jitihada zinafanyika kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa Tanzania. Tumeona kuna mkakati wa elimu bure, lakini tunaona Bodi ya Mikopo imeongezewa bajeti kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vijana wengi zaidi.
Mheshimiwa Spika, nachoomba, kwa sababu sote tunafahamu tuko katika harakati za kuhahakisha tunatengeneza vizuri uchumi wa viwandana tunajua uchumi wa viwanda unahitaji zaidi kada ya kati, kwa hiyo, kuna kila haja pia tuwekeze kwa hali inayotosheleza katika kada ya kati. Tunaona kuna jitihada tofauti tofauti lakini tujiulize ni kwa kiasi gani hawa wanafunzi tuseme wanaosoma masuala ya ufundi, hawa technicians, wale wenye uhitaji kwa mfano wa kupatiwa mikopo kwa ajili ya kuwezeshwa wao kupata taaluma hizo umewekwa kwenye utaratibu kama vile tunavyoona kwenye Bodi ya Mkopo.
Mheshimiwa Spika, hawa graduates, unaweza ukawa na Mhandisi mmoja akasimamia Mafundi Mchundo 20 au Mafundi Sanifu hata 60 lakini hawa Mafundi Mchundo pamoja na mafundi Sanifu wanahitajika wengi zaidi. Sasa itakuwa vizuri zaidi kama pia tukijielekeza katika kuhakikisha tunatengeneza mazingira wezeshi zaidi kwa ajili ya kada ya kati kwa sababu yenyewe ndiyo itakayohitajika zaidi katika uchumi wa viwanda tofauti na hizi ngazi zingine za elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika suala zima la elimu tufanye maboresho ya mitaala ya elimu ili iweze kumuandaa mhitimu kuweza kuwa na uwezo wa kutengeneza pesa. Nina maana kwamba mitaala yetu ya elimu iwe inampa mhitimu financial literacy, kwamba akishamaliza kusoma, je, ana uwezo wa kutengeneza pesa? Kwa sababu hiyo ndiyo hoja ya msingi. Unaweza ukawa na degree hata nne lakini kama zile degree zako hujaweza kuzibadilisha katika uzalishaji na kujitengenezea kipato ina maana zinakuwa hazijasaidia. Kwa hiyo, tuone ni namna gani tunaboresha mitaala ya elimu ili iweze kuwaandaa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, kuwaandaa wahitimu kuwa na uwezo wa kuzalisha pesa.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika azimio hili na kuridhia itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuiongezea mamlaka Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wote tunavyofahamu, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianzishwa mwaka 2001 Julai, lakini katika kuimarisha utengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi wanachama ziliweza kuanzisha na kuridhia itifaki tatu; Utifaki ya Uanzishwaji wa Umoja wa Forodha mwaka 2004, Itifaki ya Uanzishwaji wa Soko la Pamoja 2010, na Itifaki ya Uanzishwaji wa Umoja wa Sarafu Mwaka 2013. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki chote kunapotokea dosari katika utekelezaji wa itifaki hizi, basi Mahakama za nchi wanachama wa Afrika Mashariki na hasa kwenye nchi ambapo dosari imejitokeza, ndiyo zilikuwa zina mamlaka ya kuweza kusikiliza mashauri hayo. Hata hivyo, kwenye mkataba wa uanzishwaji wa Afrika Mashariki Ibara ya 9 vimeanzishwa vyombo na taasisi mbalimbali za kiutawala kwa ajili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Mahakama hii ya Afrika Mashariki. Mahakama hii pamoja na kuanzishwa kwake, kwenye mkataba wa huu wa uanzishwaji Afrika Mashariki imepewa mamlaka ya kutafsiri ule mkataba wa uanzishwaji wa Afrika Mashariki, yaani The East Africa Community Treaty.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ibara hiyo, au kwenye ule mkataba mama wa uanzishwaji wa Afrika Mashariki, Mahakama hii haiukupewa mamlaka ya kutafsiri itifaki hizi tatu nyingine zilizoanzishwa. Yaani Itifaki ya Kuanzisha Customs Union, Itifaki ya Kuanzisha Soko la Pamoja (common market) na Itifaki ya Uanzishwaji wa Umoja wa Sarafu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Ibara ya 27 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Afrika Mashariki Ibara ndogo ya (2), ibara hii imetoa mamlaka kwa nchi wanachama kuridhia itifaki kwa pamoja ya kutoa mamlaka zaidi kwa Mahakama hii ya Afrika Mashariki kusikiliza mashauri zaidi (extended jurisdiction), kwa kiswahili kidogo inakuwa inachanganya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa Ibara hii ya 27, Ibara ndogo ya (2) ina maana nchi wanachama wa Afrika Mashariki wanaweza kuiongezea Mahakama ile ya Afrika Mashariki. Sasa kwa muhktadha huu, nchi wanachama tarehe 20 Februari, 2015 kwenye Mkutano wa Kawaida wa 16 wa Wakuu wa Nchi, Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliweza kwa pamoja kupitisha azimio la kuiongezea Mahamaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mamlaka ya kushughulikia masuala ya biashara, uwekezaji na sarafu moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mujibu wa taratibu za jumuiya yetu hii ya Afrika Mashariki, nchi zinavyoleta azimo kama hili, ili sasa azimio hili liweze na nguvu na Mahamaka hii iweze kuongezewa mamlaka, ni lazima nchi wanachama na zenyewe ziweze kuridhia itifaki ile ambayo inakusudia kuanzishwa. Ina maana sasa, ndiyo leo hii tunaona Serikali imeweze kuona azimio la itifaki hii ili nasi kama nchi, kama wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tuweze kuunga mkono itifaki hii na mwisho wa siku mamlaka za Mahakama hii ya Afrika Mashariki ziweze kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hatua tuliyofika ni muhimu sana kwa sababu kuridhia kwa itifaki hii kutawezesha kutatua migogoro ya kibiashara na uwekezaji ambayo inajitokeza katika utekelezaji wa itifaki hizi tatu nilizozitaja; Itifaki ya Uanzishwaji Umoja wa Forodha, Itifaki ya Uanzishwaji wa Soko la Pamoja na Itifaki ya Kuanzisha Umoja wa Sarafu. Kwa hiyo, nawaomba sana Wabunge wenzangu waweze kuwa sehemu ya kuridhia na kuunga mkono hoja hii iliyoletwa na Serikali kwa maana ina umuhimu mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tukienda mbali zaidi, jumuku hili au hatua hii tuliyokuwanayo ni sehemu ya kuweza kurahisisha kuongeza utengemano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa maana ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali tunaona kwamba Mahakama za Nchi Wanachama ndizo zilikuwa na mamlaka ya kuweza kusikiliza mashauri yanayotokana na changamoto za itifaki hizi nilizozitaja, lakini sasa hivi tunataka kuipa Mahakama ya Afrika Mashariki jukumu la msingi la kutafsiri siyo tu mkataba wa uanzishwaji wa Afrika Mashariki, bali na zile itifaki tatu. Sasa katika sheria, sisi tunaona hatua hii itasaidia sana katika kuleta maendeleo sawia katika jurisprudensia ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwamba tutakuza jurisprudensia au tutaleta maendeleo zaidi ya jurisprudensia katika ukanda wa Afrika Mashariki, lakini kwa sababu hii Mahamaka itaanzishiwa sub-registries; ina maana kwenye hizo sub-registries, huduma itawafikia wananchi katika Jumuiya yote ya Afrika Mashariki na pia kutakuwa na fursa mbalimbali za ajira, kwa sababu sub-registries zikianzishwa au hii Mahakama ikiwa ina majukumu zaidi, kazi zikiwa zipo nyingi zaidi, ina maana kutakuwa na nafasi nyingi za kuajiri kada mbalimbali ikiwemo kada ya Majaji. Kwa hiyo, hili suala linatunufaisha kwa njia tofauti tofauti ikiwemo katika suala la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia machache hayo, naomba tena niendelee kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge wenzangu waweze kuunga mkono hoja hii iliyopo mbele yetu ili sisi kama nchi, Tanzania tuweze kuwa sehemu ya kupitisha itifaki hii ili Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kuwa na mamlaka zaidi ya kusikiliza mashauri mbalimbali katika Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake yote na wenyewe kwa kazi kubwa wanayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza maono yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo napenda kuchangia ni kuhusiana na masuala ya usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Sisi sote ni mashahidi na tunafahamu kwamba katika vihatarishi vikubwa vya kufikia malengo na utekelezaji wa mpango wa maendeleo ni kukosekana kwa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Sisi wote ni mashahidi wa jitihada kubwa anazozifanya Mheshimiwa Rais katika kutafuta pesa nyingi kwa ajili ya kuchochea maendeleo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunaweza tukaona kwamba kuna fedha zile za TCRP, fedha za UVIKO ambazo zimekuja na zimechochea kwa kiwango kikubwa maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji pamoja na wajasiriamali wadogo na tumeona kwamba kwa mfano Wamachinga wanajengewa masoko. Sasa hizi ni jitihada kubwa sana ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hizi tu, mfano mwingine kuna hizi pesa za ECF (Extended Credit Facility) ambazo na zenyewe zimeelekezwa kwenye sekta za uzalishaji. Kwa mfano sekta za kilimo, nishati, mifugo na uvuvi; hizi zote ni jitihada ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya za makusudi ili kuhakikisha anachochea maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili fedha hizi ziwe na tija kuna haja kubwa sana ya kudhibiti upotevu wa fedha hizi katika utekelezaji wa miradi. Natambua jitihada za Wizara, kwanza katika kusimamia halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, lakini pia katika jitihada za kudhibiti mianya ya kuvuja kwa pesa hizo na kudhibiti matumizi ya fedha hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto ya matumizi ya fedha mbichi kwenye halmashauri zetu. Namna pekee au nzuri ya kukabiliana na changamoto hii ni kutengeneza utaratibu wa kutoa mkono wa binadamu katika ukusanyaji wa mapato na ili kutimiza lengo hilo au katika utekelezaji wa lengo hilo, kutengeneza mifumo thabiti ya TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa sababu imetengeneza mifumo ya TEHAMA, kuna Mfumo wa TAUSI, kuna Mfumo wa MUSE, kuna Mfumo wa POS, yote hii ni mifumo ya TEHAMA ambayo inakwenda kuondoa na ikisimamiwa vizuri itaondoa kabisa changamoto ya upotevu wa makusanyo, upotevu wa rasilimali fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mifumo hii iwe na tija, kwanza lazima kuwe na mtandao (connectivity) kwa sababu matumizi ya TEHAMA yanahitaji mtandao wa uhakika. Sasa kama kukiwa kuna changamoto ya mtandao ina maana mifumo hii haitakuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kama huu Mfumo wa MUSE ambao ni mfumo wa uhasibu Serikalini ambao unawezesha Maafisa Masuuli kukusanya au kufunga mahesabu ya mwaka kwenye mtandao na uzuri wa mfumo huu ni kwamba zile nyaraka za malipo zinakuwa zinaambatishwa au zinawekwa kwenye mfumo, kwa hiyo inaondoa ile changamoto ya upotevu wa nyaraka ambayo mara nyingi ndiyo hoja za ukaguzi. Anapokuja CAG kufanya ukaguzi hoja nyingi zinatokana na upotevu wa nyaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mifumo hii ni mizuri.kwa mfano kuna huu Mfumo wa TAUSI ambao mteja anaweza kujihudumia yeye mwenyewe kwenye mtandao, kwa maana ya kuomba kwa mfano kama vibali vya ujenzi au tuseme kulipia viwanja vile ambavyo vinapimwa na halmashauri au kuomba leseni za biashara. Kwa hiyo ili mifumo hii iweze kuwa na tija na tuweze kudhibiti mianya ya upotevu wa hizi fedha nyingi ambazo zinatafutwa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya maendeleo, ni lazima kuhakikisha kwamba mifumo inakuwa thabiti na kwamba kunakuwa na mtandao wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja amechangia amesema kuangalia mifumo iwe airtight, kusiwe kuna loophole yoyote ya upotevu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kuchangia, ni suala la asilimia kumi ile ya mapato ya ndani ambayo inakwenda kwa ajili ya kuwawezesha kimtaji vijana, wanawake pamoja na watu wenye ulemavu. Napongeza sana Serikali na Wizara kwa sababu walibuni ule mfumo wa TEHAMA ambao unaitwa Ten Percent Loan Management Information System ambao uliwezesha waombaji wa mikopo hii wafanye maombi hayo kupitia mfumo wa TEHAMA na mchakato ufanyike kupitia TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi bado kumekuwa na changamoto kwa sababu vikundi visivyostahili vimeendelea kupewa hii mikopo, lakini urejeshwa wa mikopo bado umeendelea kuwa ni changamoto. Sisi sote tumesikia maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambaye amesema sasa fedha hizi ziende kutolewa kupitia taasisi za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu katika kuboresha au tuseme katika utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais, suala la kwanza, taasisi za fedha ambazo tutazipa kazi ya kusimamia Mfuko huu, Wizara iangalie kwamba zile gharama za usimamizi (management fee) au zile commissions za hizi taasisi zisitokane na Mfuko wenyewe zikaenda kupunguza mtaji kwenye Mfuko ule na Serikali iangalie chanzo kingine cha kulipa hiyo gharama ya management fee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, programu hii ya kuwezesha kimtaji vijana, wanawale na watu wenye ulemavu ni programu nzuri, lakini kuna component moja ambayo ni muhimu sana; kuwajengea uwezo hawa wanufaika wa Mfuko huu ili waweze kuanzisha na kuendeleza biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kufanikiwa mfuko huu ni lazima kutenga fungu au kutengeneza programu maalum kwa ajili ya capacity building, kutoa mafunzo ya msingi ya namna ya kuanzisha na kuendeleza biashara na kutoa pia msaada wa kitaalam (technical assistance).
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, ni kuvilea vikundi hivi kibiashara, kwa sababu kazi kubwa wanayoifanya hawa maafisa wetu wanaokwenda kufuatilia hivi vikundi ni kufuatilia marejesho, lakini hakuna mtu anayekwenda kufanya mentorship kwa hivi vikundi ili viweze kusimama viwe vina biashara endelevu ambazo zitaweza kuajiri vijana, wanawake na watu wengine wengi zaidi, lakini ambavyo vitaweza kuwa na multiplier effect kwenye uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika mpango wa muda mrefu, naomba Serikali yote itengeneze utaratibu mzuri kwenye mitaala ya elimu, wanafunzi wanapokuwa wanasoma wapewe mafunzo ya msingi ya namna ya kuanzisha na kuendeleza biashara.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zainab Katimba.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema machache hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Awali ya yote nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya katika kuhangaika kuwaletea maendeleo wananchi wake. Tuendelee kumuombe afya, umri na uwezo zaidi wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Mkuu na timu yake nzima ya Wizarani kwa kazi kubwa anayofanya katika kumsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza malengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka kuanza kuzungumzia suala muhimu sana ambalo lipo kwenye Sheria ya Manuuzi (Public Procurement Act). Sheria hii ya Manunuzi inataka kwamba Maafisa Masuuli wote watenge asilimia 30 ya Manunuzi ya Taasisi zao wanazozisimamia ziende kwenye makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria haijaishia hapo. Sheria chini ya Kanuni zake, kwenye Kanuni ya 30(c)(2), inasema kwamba, Maafisa Masuuli watakaoshindwa kutekeleza Sheria ya kutenga asilimia 30 watoe maelezo kwa nini wameshindwa kutekeleza? Haiishii hapo, inasema kwamba Maafisa Masuuli ambao hawatasimamia sheria hii watapewa adhabu, yaani watawajibishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze leo hii kwamba utekelezaji wa Sheria hii uko vipi? Maafisa Masuuli wangapi wametoa maelezo na wangapi wamewajibishwa? Tupate ripoti ya utekelezaji wa sheria hii. Kwa sababu sheria zimetungwa na Bunge, inabidi zisimamiwe. Kanuni imeenda kukazia na kuweka msisitizo. Hii ni sehemu ambayo Mheshimiwa Rais anataka kuwasaidia wananchi wake, anatengeneza mazingira ya kuwawezesha, kila siku anazungumza. Sasa fursa kama hizi ambazo zimewekwa vizuri kwenye sheria, kwa nini hatusimamii utekelezaji wa sheria zetu ili tuweze kuwanufaisha wananchi wetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, nataka kuzungumzia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan. Tumemsikia katika majukwaa tofauti tofauti, katika mikutano tofauti tofauti akisisitiza na akiweka mkazo kabisa anataka wananchi waweze kutengenezewa mazingira mazuri ya kufanya biashara ili waweze kujitengenezea kipato. Imefika hatua tulimsikia Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara amesema kwamba Mheshimiwa Rais ametoa ruhusa ya msamaha wa kodi kwa biashara mpya zilizo kuanzia miezi sita mpaka mwaka. Tunataka kufahamu utekelezaji kwenye suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kulipa kodi ya mapato ni kufanya biashara na kupata faida. Ile faida ndiyo inatozwa kodi ya mapato. Sasa mtu anayeanza biashara, kabla tu hajaanza biashara, anapopewa makadirio ya kodi, anaambiwa aanze kulipa kwanza robo ya kwanza ya yale makadirio, kabla hata hajafanya biashara, atumie mtaji wake kulipa kodi, msingi wa hiyo kodi unatokana na nini? Kwa sababu sheria inataka kodi ya mapato itokane na faida. Ndivyo sheria inavyosomeka leo hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anatengeneza mazingira mazuri sana ya kuwawezesha wananchi wake, mbona hatuoni sheria zikiletwa zifanyiwe marekebisho?
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nami naomba nimpe taarifa mchangiaji, Mheshimiwa Zainab Katimba, kwamba siyo tu huyo mfanyabiashara anatakiwa akadiriwe hiyo kodi wakati anaanza, lakini pia atatakiwa kufanyiwa mahesabu na wahasibu, nao anatakiwa awalipe kabla hajaanza hata hiyo biashara.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Katimba.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa taarifa yake, naipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msingi wa hayo maboresho yote ni kwamba tunataka tutengeneze mazingira rafiki na mepesi ya kufanya biashara ili watu wengi waweze kuingia katika mfumo rasmi, warasimishe biashara zao, tuongeze wigo wa walipa kodi, na tuongeze mapato ya Serikali. Kwa hiyo, naomba nisikie kutoka kwa upande wa Waziri kwenye eneo hili, wamejipanga vipi? Kwa sababu hapo tayari ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuchangia ni kuhusiana na Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (Government Asset Management Information System - GoMIS). Kwanza Sheria ya Manunuzi (Public Procurement Act) na Public Finance Act inaeleza bayana kabisa kwamba Mlipaji Mkuu wa Serikali ndiye ambaye amepewa dhamana ya usimamizi wa mali zote za Serikali. Utaratibu mzuri wa usimamizi wa mali za Serikali umewekwa kwenye sheria hizi nilizotaja na pia kwenye mwongozo ule wa Public Asset Management Guideline ya 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo uko vizuri, lakini kwenye eneo moja la kuuza mali chakavu zile za Serikali, mfumo wa kitehama upo, lakini mfumo ule bado haujaweza kusomana na mifumo mingine muhimu. Kwa mfano mfumo wa malipo ya GePG lakini bado mfumo ule kuna Maafisa Masuuli ambao hawajapewa access, hawawezi kuutumia. Kwa hiyo, inapofika wakati wa mali chakavu za Serikali, inabidi ziuzwe, kuna hatua moja ambayo Pay Master General inabidi amwelekeze mhakiki aende akafanye verification ya zile mali kwamba ni chakavu ili utaratibu wa kuziuza zile mali/wa kuzi-dispose uendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye process hiyo ndiyo tayari kuna mkwamo, kwa sababu mfumo huu wa Tehama hauna teknolijia ya kuweza kufanya verification kwa kutumia Tehama. Tumeona hapa, sisi tumeanza hapa Bungeni tukiwa tuko kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo nje, tumeweza kuona Bwawa la Mwalimu Nyerere live, utafikiri tuko huko site. Kwa nini? Kwa sababu tumetumia Tehama, ile teknolojia ya virtual reality.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tehama imefikia katika hatua ambayo kuna vitu vingi vinaweza kufanyika bila kuhitaji mtu kufika yeye mwenyewe site. Kwa hiyo, naomba waboreshe mfumo huu kwanza uweze kusomana na mifumo muhimu na hasa mfumo huu wa GePG, pia waweze kutumia teknolojia hii kama za Tehama ili kuweza kurahisisha utaratibu wa verification wa uhakiki wa zile mali ili kuondoa mlundikano wa mali za Serikali Tanzania nzima ambazo zinasubiri kuuzwa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya mchango huo, naomba kuunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, kama wote tunavyofahamu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo Nchini Ghana kuanzia tarehe 23 Mei, 2022 kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine amehudhuria mdahalo wa Wakuu wa Nchi kujadili fursa zilizomo na changamoto zinazokabili Nchi za Afrika kama vile kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya vyakula na matumizi ya nishati endelevu.
Mheshimiwa Spika, vilevile tumeshuhudia tarehe 25 Mei, 2022 Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akipewa Tuzo ya Mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Ujenzi wa Miundombinu ya usafirishaji ambayo kwa kawaida hutolewa kwa Mkuu wa Nchi iliyofanya vizuri katika sekta hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya kupewa tuzo hiyo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametajwa pia kuwa miongoni mwa Viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa Duniani kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Gazeti maarufu la TIME la tarehe 24 Mei, 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua sifa hiyo kubwa aliyoipata Rais wetu ambayo inailetea nchi yetu taswira nzuri Kitaifa na Kimataifa, naomba kutumia fursa hii kuliomba Bunge hili Tukufu ambalo ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, kuridhia Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Rais kama ifuatavyo.
Azimio la Bunge kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa Viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya Ujenzi wa Miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 24 Mei, 2022 akiwa katika ziara ya Kikazi Nchini Ghana amepokea tuzo kuu ya Mjenzi Mahiri ya Babacar Ndiaye (Africa Road Builders) kwa mwaka 2022 inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), akiwa ni Rais wa 12 kupata Tuzo hiyo tangu ilipoanzishwa Mwaka 2016. (Makofi)
Na kwa kuwa tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wake kama mwanamke mzalendo na Rais wa kwanza wa Tanzania kupata Tuzo hiyo akiwa anaongoza Serikali ya Awamu ya Sita kwa mafanikio makubwa katika kuendeleza sekta ya miundombinu na usafirishaji hususan eneo la barabara;
Na kwa kuwa Watanzania wote tunatambua juhudi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais kuendeleza miundombinu ya usafirishaji ikiwemo kusimamia na kufungua miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara na reli hapa nchini;
Na kwa kuwa kwa hatua nyingine wakati wa tukio la kupewa tuzo hii Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametambuliwa kama miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Gazeti la TIME la tarehe 24 Mei, 2022, jambo ambalo linaendelea kumpatia sifa kubwa Rais wetu na Taifa kwa ujumla;
Kwa hiyo basi, Bunge hili katika mkutano wake wa saba, kikao cha Thelathini na Moja, tarehe 26 Mei, 2022 linaazimia kwa kauli moja: -
Kwanza, kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambuliwa na kupewa Tuzo Kuu ya Mjenzi Mahiri ya Babacar Ndiaye kufuatia mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu nchini Tanzania. (Makofi)
Pili, kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kwa kutambuliwa kama miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani jambo linaloliletea sifa nzuri nchi yetu ya Tanzania. (Makofi/Vigelegele)
Na tatu, kuendelea kumpa moyo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa juhudi mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika kuiletea nchi yetu maendeleo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, azimio hili limechangiwa na Wabunge mbalimbali kwa sababu ya muda sitoweza kuwataja majina yao, lakini Wabunge hawa wote kwa kauli moja wamepongeza sana tuzo hii aliyoipata Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na pia kwa kutambuliwa kwake kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wameenda mbali, si tu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa umahiri wake kwenye kuboresha miundombinu, lakini wameenda zaidi kupongeza umahiri wake katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya, Sekta ya Elimu, Sekta ya Maji na Sekta ya Kilimo ambazo ndio zinaenda kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kasi sana na kuleta maendeleo ya watu na hasahasa wale wa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kielelezo cha uongozi bora, uongozi mahiri, sio tu kwa Tanzania bali kwa dunia nzima. Pia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameonesha umahiri mkubwa sana katika kuboresha miundombinu katika nchi hii, jambo ambalo linaenda kuchochea uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha uthubutu kwenye kuendeleza na kusimamia miradi mikubwa ya miundombinu ambayo inaenda kuibadilisha Tanzania. Miradi hiyo ni miradi ya kuunganisha mkoa kwa mkoa, miradi ya kuunganisha Tanzania na nchi jirani, ambapo ameendeleza miundombinu ya reli ya kisasa yaani Standard Gauge Railway, barabara na madaraja makubwa nchini. Yote haya yanaenda kuleta mageuzi makubwa sana kwenye nchi yetu na kuchochea sekta mbalimbali za uzalishaji ambazo zitaenda kuleta athari chanya kijamii lakini pia kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, Watanzania tuna kila sababu ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan. Watanzania tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa vitendo na vitendo hivyo ni kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake; tufanye kazi kwa bidiii, tutimize wajibu wetu tunaopewa kwenye dhamana tulizokuwa nazo. Viongozi wote wa kila ngazi tuwahudumie wananchi, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa kuwahudumia wananchi. Nchi hii itajengwa na sisi wote. Hapo pia wananchi tuna wajibu wa kutimiza majukumu yetu kama raia wema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuishukuru sana benki ya AfDB (African Development Bank) kwa mchango wake katika mafanikio haya. Naomba sana nichukue nafasi hii kuendelea kuwaomba sana benki ya AfDB iendelee kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kwa sababu dunia nzima imethibitisha kwamba fedha tunazozipata sisi kama Tanzania tunahakikisha zinaenda kwenye maendeleo ya watu. (Makofi/Vigelelegele)
Mheshimiwa Spika, sisi wote ni mashahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan inasimamia matumizi bora ya rasilimali za Taifa, inasimamia na inapinga ufisadi na inasimamia utawala bora. Kwa hiyo tunaomba sana wadau mbalimbali waendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendeleza yale aliyoyaanza kwa kasi kubwa sana na sisi Watanzania tuendelee kuwa na imani naye, tuendelee kumwombea, naamini Mungu ataibariki Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza na mimi nianze kwa kutanguliza pongezi kwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuendelea kuaminiwa katika Wizara hii, lakini niwapongeze pia watendaji wote katika Wizara hii na niwaambie tu waendelee kufanya kazi kwa bidii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nipongeze pia jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais ambazo tumeona kwenye Royal Tour, tumeona Rais ameweza kuifungua Tanzania, kuitangaza, kuweza kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii na haya mambo yote yanaenda kuleta tija kubwa sana katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini mimi ningependa kwanza kuzungumzia migogoro mikubwa ambayo inatokea kati ya maeneo ya Hifadhi pamoja na Vijiji; na ukisikiliza hata katika michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia migogoro hii.
Kwa hiyo, pamoja na mambo mengine mimi ninadhani kwamba kuna haja ya kuangalia sheria zetu zinazungumziaje masuala haya ya changamoto au migogoro ya ardhi ambayo inatokana na hifadhi zetu pamoja na vijiji. Kwa mfano ukiangalia Sheria ya Wildlife Conservation Act ya mwaka 2009, kifungu cha 16(4) ambacho labda naweza nikakisoma, ambacho kinasema; “The Minister shall, within twelve months after coming into to operation of this Act and after consultation with the relevant authorities, review the list of game controlled areas for purposes of ascertaining potentiality justifying continuation of control of any of such area.”
Halafu kifungu kidogo cha (5) ambacho ndio cha msingi hapa kinasema; “For the purposes of subsection (4), the Minister shall ensure that no land falling under the village land is included in the game controlled areas.” (Makofi)
Sasa hapa sheria inatambua maeneo ya mapori tengefu, lakini sheria inasisitiza kwamba Waziri baada ya kuanza kwa hii sheria, baada ya kutungwa hii sheria ikianza kutumika ndani ya miezi 12, Waziri apitie orodha ya mapori haya tengefu na katika mapitio hayo ahakikishe kwamba maeneo ya vijiji hayatowekwa ndani ya mapori tengefu. Kwa hiyo, vijiji viachwe, maeneo ya vijiji yaendelee kuwa vijiji yasiwe ndani ya orodha ya mapori tengefu. Kwa hiyo, ukisimamia sheria hii inaweza ikandoa baadhi ya hii migogoro tuliyokuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hatuishii hapo tu unajua sheria kwa mfano Sheria ya Ardhi ya Vijiji yaani Village Land Act inatambua kwamba kijiji kinaweza kuwa kile ambacho watu wameishi kwenye eneo hilo kwa zaidi ya miaka 12 kabla ya kuanzishwa kwa sheria hii. Kwa hiyo wamekuwa wakiishi kwa miaka kwa tamaduni zao, wameweka makazi na wameishi kwenye eneo hilo linatambulika kama kijiji. Kwa hiyo, leo hii unavyokuja kutengeneza mazingira ya kumfukuza mtu kwenye eneo ambalo ameishi tangu uhai wake unaanza mpaka anafikia umri huu, unamfukuza, yeye anafahamu eneo lile ni nyumbani kwa hiyo ukimtoa kwenye eneo kama hilo kidogo inakuwa ni changamoto. Lakini mwisho wa siku pamoja na kuwepo sheria hizi zote lengo letu pia ni kuzingatia uhifadhi, kwa sababu maliasili zote tulizokuwa nazo hapa Tanzania kuna haja ya kuhakikisha bado zinaendelea kuwepo zirithiwe, tuwarithishe vizazi na vizazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri na ninafahamu haya mambo ni yanaenda kwenye Wizara tofauti tofauti, Wizara ya Ardhi inahusika na Wizara hii inahusika. Kwa hiyo, waangaalie nafahamu kuna timu ambayo inatatua hii migogoro, lakini waharakishe kwa sababu migogoro imeendelea kuwepo kwa muda mrefu sana na inaleta changamoto kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naweza kuishauri Serikali kuhusiana na migogoro hii ambayo inatokana na mwingiliano wa maeneo ya uhifadhi na maeneo ya makazi ya watu kwa maana vijiji ni kuhakikisha kwamba hivi vijiji na maeneo yake mipaka yake inakuwa inatambulika. Kwa sababu mipaka ya vijiji ikijulikana na vijiji hivi vikipimwa vizuri mimi ninaamini kwa kiwango kikubwa ule mwingiliano wa kati ya vijiji na hifadhi utapungua kwa asilimia kubwa. Kwa hiyo, naomba sana Serikali izingatie hayo kwa sababu migogoro hii haina tija kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni kubwa sana na hili litalisisitiza sana nikiwa kama Mbunge kijana, lakini nikiwa kama mama ni uhifadhi. Wananchi inabidi waelimishwe hasa hawa wananchi wanaokuwa wanaishi kwenye vijiji vinavyopakana na maeneo haya ya hifadhi, waelimishwe umuhimu wa wa kuhifadhi maeneo haya ambayo sisi tumeyarithi kutoka kwa mababu zetu, waelewe umuhimu wa utunzaji wa maeneo haya na mchango wake na athari zake katika mazingira kwa ujumla. Kwa sababu wakifahamu na wenyewe watakuwa ni sehemu ya kuhakikisha wanayalinda maeneo haya ya Hifadhi, wanayatunza ili tuweze kuyarithisha kwa vizazi vijavyo. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba sana na hili suala ukiangalia kwenye ukurasa namba 114 wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwenye kifungu cha 69(d) kimezungumzia mambo ya kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wanaopakana na maeneo haya ya hifadhi ili kuwafanya wananchi na wenyewe waelewe kwa upana wake umuhimu wa hifadhi na waweze kulinda maeneo yetu ambayo tunayahifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho lakini siyo kwa umuhimu, kule kwetu Kigoma tuna hifadhi yetu ambayo inaitwa Gombe na Mahale. Gombe na Mahale wewe mwenyewe ni shahidi kwa sababu nafahamu umeshawahi kufika. Ulitembelea kule na Mheshimiwa Assa Makanika, Mbunge wa Jimbo. (Makofi)
Sasa hifadhi ile ni hifadhi ambayo wanapatikana viumbe ambao wana upekee sana, kule kuna sokwe mtu na duniani kote sokwe mtu hawa wamekuwa wana umaarufu mkubwa sana. Lakini sasa kuna uhitaji mkubwa wa kufungua njia kwa ajili ya utalii katika eneo hili. Kwa hiyo, naomba, kwa sababu Serikali ni moja waboreshe miundombinu ya kufika katika hifadhi hii na miundombinu ya kule mikubwa zaidi ni uwanja wa ndege. Sasa kwenye bajeti ya masuala ya uchukuzi kila mwaka huwa inatengwa fedha kwa ajili ya kupanua kiwanja chetu cha ndege cha pale Kigoma, mwaka wa fedha uliopita shilingi bilioni nane, mwaka huu imetengwa shilingi bilioni saba.
Kwa hiyo, tunaomba mboreshe miundombinu kwa sababu na yenyewe itakuwa kuchochea kwenye masuala ya Utalii na kwa sababu Serikali ni moja ndiyo maana nasema hapa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia hoja zilizoko mezani. Kwanza kabisa nadhani sote tutakubaliana kwamba, Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa sana ya kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwa ajili ya kutuletea maendeleo kwenye Taifa hili. Kwa hiyo, kuna kila sababu ya kuhakikisha fedha hizi zinakuwa na tija katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ukurasa wa 11 wa Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) utaona kwamba, wamebaini upotevu wa fedha nyingi ambao unatokana na dosari katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato. Mfano, ukiangalia, katika mwaka 2021/2022, TRA imerekodi nakisi ya bilioni 887.3 katika ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ukurasa wa 10 kwenye Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) utaona kwamba, wametoa taarifa na wameainisha kuwepo kwa mifumo dhaifu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kushindwa kukusanya madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni katika mwaka 2021/2022, kuna upotevu wa bilioni 11.07 zilizokusanywa na mashine za ukusanyaji wa mapato (POS) ambazo hazikuwasilishwa benki. Sasa kwanza, tunataka fedha hizo ziwasilishwe benki, hiyo ndio hatua ya kwanza. Hatua ya pili, tunataka wote waliohusika na ubadhirifu huu wachukuliwe hatua. Watanzania tunataka kuona hatua inachukuliwa, hii ni jinai, huu ni ubadhirifu, tunataka tuwaone wako katika mikono ya sheria wabadhirifu wa fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mbele tutengeneze Suluhu ya kudumu. Tunahitaji kutengeneza na tuendelee kuwekeza katika kutengeneza mifumo imara ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, lakini katika manunuzi ya umma. Nafahamu Serikali imefanya jambo kubwa sana katika eneo hili, lakini tunahitaji kuwekeza zaidi. Hii mifumo iwe inasomana kwa sababu, tukifanikiwa kutoa mkono wa binadamu katika makusanyo ya mapato na katika manunuzi ya umma, basi, tutafanikiwa kwa kiwango kikubwa kusaidia kuondoa au kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa fedha za umma, rushwa, lakini pia, tutakuwa tumeongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 10 cha Sheria ya Public Audit Act kimefafanua majukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Kwa hiyo, pamoja na majukumu yake ana jukumu kubwa la kufanya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa niaba ya Bunge. Kwa hiyo, CAG kimsingi ni jicho la Bunge katika kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi hizi za CAG mara nyingi kazi yake yeye anayoifanya CAG ni post mortem, yaani anakuta ubadhirifu ulishafanyika, fedha zilishapotea, wezi walikwishaiba kwa hiyo, yeye anatoa ripoti anaiwasilisha kwa hiyo, kazi yake inakuwa imeishia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu muhimu sana anaitwa Mkaguzi wa Ndani. Mkaguzi huyu wa Ndani ni mtu muhimu sana, hii Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani ni ofisi muhimu sana ambayo inahitaji kuwezeshwa kwa sababu, Mkaguzi wa Ndani anaweza kuzuia upotevu wa fedha. CAG anakuja kutoa ripoti, kuripoti ubadhirifu wa fedha, matumizi mabaya ya fedha, lakini huyu Mkaguzi wa Ndani ana uwezo wa kuziwia ubadhirifu wa fedha kabla haujatokea au kabla haujafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kila mwaka Ripoti ya CAG inaletwa kwenye Kamati inajadiliwa, inakuja Bungeni, tunatoa maazimio, mwaka unaofuata tunaenda hivyo hivyo, lakini sasa ili kutengeneza suluhu tumwezeshe huyu mkaguzi wa ndani. Niipongeze Serikali katika eneo hili kwa sababu, katika kipindi cha bajeti, Mkaguzi wa Ndani ameweza kuanzishiwa Fungu Na.6 kwa hiyo, amewezeshwa kibajeti. Hapo awali tulikuwa tunaona changamoto, huyu Mkaguzi wa Ndani, kwa mfano, kwenye Halmashauri, alikuwa anategemea fedha ya kufanya kazi zake kutoka kwa Mkurugenzi na Mkurugenzi ndio huyohuyo anayekaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukikuta kwamba, Mkurugenzi na yeye ni sehemu ya ubadhirifu, maana yake anatengeneza mazingira magumu ya Mkaguzi wa Ndani kufanya kazi. Atasema hamna fedha, atasema hamna gari, mara gari halina mafuta, lakini kwa kuanzishwa kwa Fungu Na.6, hili imeweza kusaidia kumuwezesha Mkaguzi wa Ndani kufanya majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende mbali kwa sababu, Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani inaishia kwenye Menejimenti. Sasa Menejimenti yenyewe ndiyo hiyo hiyo mara nyingi ndiyo inayotuhumiwa kwa ubadhirifu. Kwa mfano, katika Halmashauri. Mkaguzi wa Ndani akileta ripoti katika Menejimenti ndio hao hao watuhumiwa wanaokaa kupokea hiyo ripoti. Unategemea nini kitafanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali iende mbali zaidi. Tutengeneze mamlaka ya juu zaidi, tutengeneze mamlaka za kikanda, lakini iende juu ifike mpaka kwa mamlaka za juu ifike hata katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndio msimamizi wa shughuli za Serikali. Pia, tunaweza tukaangalia ikafika hadi kwa Katibu Kiongozi, ili watu wachukuliwe hatua za nidhamu kabla ubadhirifu haujafika mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza fedha nyingi sana kwa kusubiri kwamba, wezi waibe, wahamishwe vituo, ukaguzi ufanyike, fedha zimepotea, tunakuja kujadili hapa kila mwaka, kila mwaka ripoti hizi zinakuja zinajirudia. Kwa hiyo, tutafute suluhu ya kudumu na tuiwezeshe Ofisi hii ya Mkaguzi wa Ndani iweze kuwa imara, ili iweze kutusaidia kuepuka au kukinga ubadhirifu unaofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Ukurasa wa 29 wa Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) utaona kwamba, imeainishwa. Katika hoja za ukaguzi, kuna hoja za ukaguzi ambazo zinatokana na dosari katika usimamizi wa mkataba na athari zake katika matumizi ya fedha za umma. Mfano, utaona kwamba, Serikali imepata hasara ya bilioni 36.8 ambayo imetokana na tozo ya riba kwa TANROADS kwa kuchelewa kulipa wakandarasi na washauri wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bilioni 36.8 ni fedha nyingi sana na fedha hizi ndio zinasababisha miradi itumie gharama kubwa zaidi kuliko ile iliyokuwa imepangwa. Mradi unakuwa umepangiwa kutekelezwa kwa milioni 100, lakini mwisho wa siku unashangaa mradi umetekelezwa kwa milioni 150. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba sana, hizi fedha zinazopotea zingeweza kutumika katika maeneo mengine yenye uhitaji wa rasilimali fedha. tunaomba Serikali itafute suluhu ya kudumu ya kulipa fedha kwa wakati, wakandarasi walipwe fedha zao kwa wakati, washauri wa miradi walipwe fedha zao kwa wakati, ili tusije tukalipa riba ambayo ni hasara kubwa kwa Serikali na hizi fedha zinaweza kutumika katika maeneo mengine kwa maslahi mapana ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba kuunga mkono hoja za Kamati zote tatu. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ya kuchangia kuhusu Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa wa mwaka 2016. Nichukue fursa hii kupongeza Serikali ya Mheshimiwa Rais Magufuli kupitia Wizara hii ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kutambua haki ya Kikatiba ya Watanzania ya kupata taarifa. Jitihada hizi ni udhihirisho na ushahidi tosha wa utekelezaji kwa vitendo dhana ya uwazi, uwajibikaji na demokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutungwa kwa sheria hii ni utekelezaji wa matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayoitaka Serikali kuwajibika kwa wananchi. Uwajibikaji wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa uwazi utakaochochea uwajibikaji na hivyo kuimarisha demokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kunukuu Ibara ya 29(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inasema:-
“Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vilivyotajwa na Katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetoa haki ya raia kupewa taarifa. Hivyo kutungwa kwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa itaweka utaratibu mzuri utakaohakikisha kwamba raia wanapata haki yao ya kupewa taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujielekeza katika ukurasa 28 wa Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ambapo katika kifungu cha 22 kinatamka hivi:-
Mtu yeyote ambaye anabadili, anafuta maandishi yasisomeke, anazuia, anafuta, anaharibu au anaficha kumbukumbu zozote zinazoshikiliwa na mmiliki wa taarifa kwa dhamira ya kuzuia upatikanaji wa taarifa kutoka kwa mmiliki huyo wa taarifa, anatenda kosa na akitiwa hatiani atatozwa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa la kubadilisha, kuharibu, kuzuia au kufuta taarifa ni kosa ambalo linaenda kukinzana na matakwa ya Katiba, haki ya binadamu ambayo imetolewa kwa mujibu wa Ibara ya 18. Hivyo, kwa kuzingatia uzito wa kosa hili, napenda kuishauri Serikali yangu sikivu katika kutoa adhabu kwa kosa la kubadilisha, kuharibu, kuzuia au kufuta taarifa adhabu ya faini iondolewe na badala yake adhabu pekee ibakie kifungo kisichopungua miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madhara makubwa sana yanayotokana na kosa hili la kubadilisha, kuharibu, kuzuia au kufuta taarifa mbalimbali. Tumeshuhudia upotevu wa taarifa mbalimbali umesababisha madhara makubwa siyo tu kwa Serikali lakini hata kwa watu binafsi na hususan katika upatikanaji wa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mara nyingi hata kwenye kesi mbalimbali ambazo zimehusisha Serikali kwa upande mmoja upotevu wa taarifa umesababisha Serikali yetu kuingia katika hasara ya kulipa mamilioni ya fedha. Hivyo, kosa hili kama makosa mengine ya uvunjifu wa haki za binadamu kama vile wizi, ubakaji, mauaji iwekewe adhabu kali na adhabu ya faini itakuwa ni adhabu ambayo haitomtisha mtu kuifanya. Hivyo adhabu ya kifungo cha zaidi ya miaka mitano nadhani itakuwa ni adhabu kali ambayo itachochea na itahakikisha kwamba inazuia kosa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema machache haya, napenda kuunga mkono muswada huu wa sheria na napenda mapendekezo yangu ya marekebisho yaweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza ningependa kutoa pongezi zangu za dhati kwa jitihada za kizalendo zilizofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tena za makusudi kabisa za kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho ya sheria ili kuhakikisha kwamba tunaepukana na wizi wa aina yoyote dhidi ya rasilimali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kuipongeza Serikali katika mchakato wake huu wote, pia ningependa kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kipekee ningependa kumpongeza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Kabudi kwa jitihada hizi zote na kwa kazi ya kuainisha upungufu ambao upo katika sheria zetu na kuuleta hapa ili tuweze kuufanyia marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujielekeza katika mambo machache. Kwanza, ningependa kupongeza jitihada za kuongeza hiki Kifungu cha tano (5) katika Muswada huu ambacho kimetambua na kuweka umiliki wa rasilimali kwa maana ya madini, petroli na gesi asilia kwa wananchi wote lakini zisimamiwe na Rais kwa niaba ya wananchi wa Tanzania. Kipengele hiki na Kifungu hiki kinaenda sanjari na sambamba na Ibara ya 27 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ambayo inaweka wajibu wa kila mwananchi kusimamia rasilimali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kifungu cha 21, Kifungu hiki kimeweza kuondoa yale mamlaka ambayo yalikuwa kwa Waziri (discretionary powers) za Waziri katika masuala ya madini. Imeanzishwa Kamisheni ya Madini ambayo yenyewe sasa ndiyo itakuwa ina jukumu au kazi kubwa na jukumu la kisheria la kusimamia na kuendesha shughuli zote za madini nchini. Hii ni jitihada kubwa sana na itasaidia sana kuondoa zile discretionary powers za Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi kushauri katika kifungu hiki ni kwamba kuna umuhimu wakati wa utekelezaji wa sheria chombo hiki Kamisheni ya Madini iweze kupewa na
itengenezewe mazingira muhimu yote yatakayowezesha kutekeleza majukumu yake. Kwa maana ya wawepo wataalam wa kutosha wenye uzalendo na wasio na matamanio ya rushwa. Kuwepo na bajeti ya kutosha, muhimu zaidi waweze kupewa vifaa vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufasaha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ukienda katika kipengele cha nane (8) katika Muswada huu ambacho kimezungumzia local content, tumeona kwamba kipengele hiki kinataka yale makampuni yanayokuja kuwekeza katika madini yaweze ku-submit au kuwasilisha mpango wa ushiriki wa Watanzania katika kazi hizi za madini yaani local content.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kushauri zaidi katika kipande hiki kwa sababu tunataka wazawa ndio waweze kunufaika na masharti ya kifungu hiki. Kwa hiyo, ni muhimu katika ku-define local companies yaani makampuni wazawa ambayo na wenyewe ni wazawa kimsingi yaweze kuwa defined kwa kuzingatia majority shareholding kwenye kampuni husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina maana kwamba, kigezo kisiwe usajili wa kampuni, kwa sababu kwa mujibu wa Sheria za Makampuni yaani Companies Act, unaona kwamba Local Company imekuwa defined kumaanisha kampuni iliyosajiliwa na BRELA lakini foreigner au makampuni ya nje yanaweza yakaja yakasajili kampuni Tanzania, badala yake local company iwe defined kwa maana ya wazawa katika kampuni husika wawe wana shareholding zaidi ya asilimia 51. Hivyo ndiyo tutakuwa tunahakikisha kwamba wazawa kweli wanaweza kunufaika na kifungu hiki…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Usuluhishi wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ZAINABU A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchngia katika muswada huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu umekuja kufuta Sheria ya Usuluhishi Sura ya 15 na kutunga Sheria mpya ya Usuluhishi ya mwaka 2020. Sheria ile tuliyokuwa nayo mwanzo sura ya 15 ilikuwa ni sheria ambayo tuliiridhi kutoka kwa wakoloni na imepitwa na wakati sana na haiendani na matakwa tuliyokuwa nayo sasa hivi. Kwa hiyo niseme naipongeza sana Serikali kwa kuleta Muswada huu kwa ajili ya kutunga sheria hii. Muswada huu umekuwa ni muhimu na ulikuwa ni wa lazima kutokana na kwamba tumekuwa tukihitaji sheria ambayo itakidhi matakwa ya wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna umuhimu mkubwa sana; sisi tunafahamu kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107 A inatamka bayana kwamba mahakama ndizo zimepewa nguvu kubwa ya kuhakikisha kuwa haki inatendeka ndani ya nchi. Hata hivyo tunafahamu kwamba taratibu za kimahakama zinaweza zikawa zinachukua muda mrefu zaidi lakini kunaweza kukawa na technicalities nyingi zaidi na ndio maana kuna umuhimu sana, na mara nyingi katika mfumo kunapokuwa na migogoro inapendekezwa kwanza zitumike njia mbadala na za kirafiki za kutatua migogoro kabla ya kwenda mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Sheria hii ya Usuluhishi ndiyo inakuja kuweka misingi na masharti yatakayoongoza masuala ya usuluhishi katika nchi yetu, kwa hili ni jambo zuri sana kwa sababu tunafahamu umuhimu wa kutatua migogoro nje ya mahakama kirafiki; kwa sababu inasaidia pia kuondoa mlundikano wa kesi nyingi mahakamani lakini inakuwa ni njia ya kutatua migogoro kwa amani zaidi tofauti na kupambana katika mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nitoe ushauri katika baadhi ya maeneo katika muswada huu. Nijielekeze kwa ujumla kwanza kusema kwamba kuna taratibu tofautitofauti za utatuzi wa migogoro nje ya mahakama yaani alternative dispute resolution methods, zipo nyingi. Muswada huu unaenda kutunga sheria kwa ajili ya usuluhishi (arbitration) lakini hatuna sheria ambazo ziko detailed zinaelezea taratibu za utatuzi wa migogoro kwa kutumia njia nyingine kama mediation, negation hizo zote hamna sheria ambayo inajitosheleza ambayo imechambua na imeweka masharti ya namna gani tunaweza tukatumia njia hizo mbadala kutatua migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, muswada huu unaweka masharti ya kimsingi kwa ajili ya usuluhishi pekee. Kwa hiyo huko mbele tuangalie ni namna gani tutakuwa tuna sera ambayo itatuwezesha kuwa na sheria zitakazotoa masharti ya taratibu zingine za kutatua migogoro nje ya mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukienda kwenye sehemu ya kumi ya muswada huu ambayo imeanzisha kituo cha usuluhishi (arbitration center) mimi nadhani kifungu hichi ni muhimu sana lakini nilikuwa nadhani kuna haja ya kukiongezea nyama. Kwa misingi ya kwamba hii arbitration center ielezewe muundo wake, ielezewe na mambo mengine mengi kama vile tulivyokuwa tuna Tanganyika Law Society (TLS) ambapo tunajua kuwa ni chombo kinatambulika ambacho kinaongoza masuala ya mawakili. Kwa hiyo hii arbitration center ibebe sura hiyo hiyo na iweze kufafanuliwa vizuri, aidha kwenye sheria hii hii au kwenye sheria tofauti ambayo itaweza kuongeza mambo mengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni kwenye sehemu ya kumi na tatu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 6) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo Mezani.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwanza nianze kuunga mkono maoni ya Kamati ya Sheria Ndogo kuhusiana na hoja iliyopo Mezani. Pia niwashawishi Wabunge wenzangu waweze kuunga mkono hoja hii ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nitambue ushirikiano mkubwa ambao umeonyeshwa na Serikali katika mchakato wa uchambuzi wa Muswada huu. Nawapongeza sana Serikali kwa ushirikiano na kazi kubwa ambayo mmekuwa mkifanya katika kipindi chote cha uchambuzi wa Muswada huu. (Makofi)
Mweshimiwa Spika, sasa nikijielekeza katika ukurasa wa 20 wa Muswada ambapo kuna Marekebisho ya Sheria ya Adhabu (The Penal Code). Marekebisho haya yamelenga kwenda kuongeza adhabu ambazo zilikuwa zimeainishwa katika kifungu cha 29 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (The Penal Code) na imeziongeza ili ziweze kuendana na wakati huu tuliokuwa nao. Kwa mfano, kuna maeneo unakuta kwamba adhabu ilikuwa ni shilingi mia moja, sasa marekebisho haya yameenda kubadilisha adhabu ile ya shilingi mia moja kwa sababu haiendani na wakati, kwa hiyo, imeongezwa kufika shilingi elfu hamsini na maeneo mengine imeongezwa kutoka shilingi mia moja kwenda shilingi laki moja na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, hili ni jambo jema kwa sababu sheria inabidi ziende na wakati. Wakati sheria inatungwa shilingi mia moja ilikuwa inaweza kutoa faini kwa kosa fulani lakini kwa wakati huu shilingi mia moja haitoshi na hivyo, marekebisho haya yanaenda kurekebisha matakwa ya nyakati.
Mweshimiwa Spika, hili ni jambo jema ila ushauri wangu, kuna umuhimu sana wa kuangalia ni wakati gani au inachukua muda gani kufanya marekebisho ya sheria ili ziweze kuendana na wakati. Kwa hiyo, kuna mamlaka na kuna vyombo ambavyo vimeundwa kwa mujibu wa sheria ambavyo vimepewa madaraka au kazi ya kuweza kufanya mapitio ya sheria ili kuhakikisha kwamba zinaenda na wakati. Kwa hiyo, vyombo hivi viweze kupewa nguvu ili viweze kufanya kazi ya kufanya marekebisho ya sheria kwa kadri inavyohitajika.
Mweshimiwa Spika, lakini nikijielekeza pia katika ukurasa wa 21 ambapo kuna marekebisho ya Sheria hii hii ya Kanuni ya Adhabu ambayo imeweka katazo la kusambazwa kwa picha, video za maiti au mazingira ambayo ni hatari (gruesome incidents), mazingira ambayo yanaweza kuleta woga au siyo mazuri kuonyesha katika jamii. Marekebisho ya kifungu hiki kwenye sheria ni muhimu sana kwa sababu sisi wenyewe tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari, hata kwenye simu zetu sisi wenyewe, kwenye media outlets mbalimbali unakuta kuna picha zimesambaa za kuonesha dead bodies, maiti, kuonyesha ajali na wahanga wameumia, mazingira ambayo siyo mazuri sana, yanasambazwa.
Mheshimiwa Spika, kuna familia, kuna ndugu wa hata hao marehemu ambao wanasambazwa kwenye picha na video, kitu ambacho siyo kizuri sana, kinasababisha matatizo makubwa sana ya kisaikolojia pia kwa wanafamilia na wananchi kwa ujumla. Kwa hiyo, kitungu hiki kinakuja kutibu na kuweka katazo la kusambaza picha za namna hiyo au video za namna hiyo.
Mheshiiwa Spika, cha msingi cha kufanya pamoja na marekebisho haya mazuri ni kuendelea kuelimisha jamii ili waweze kuelewa madhara ya usambazaji wa picha na video za namna hii. Siyo hivyo tu, hata sisi Wabunge tuna jukumu kubwa sana la kuwaelimisha wapiga kura wetu. Kwa sababu kuna usemi wanasema kwamba ignorance of law is no defense, yaani kutojua sheria siyo utetezi dhidi ya kosa.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu marekebisho ya sheria leo hii yakipita yataenda kuwa na nguvu ya kisheria, kwa hiyo, pale mtu atakaposambaza picha za aina hii ambazo zimewekewa makatazo kwenye kifungu hiki ina maana ataingia kwenye mkondo wa sheria na atahukumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi kama wawakilishi wa wananchi wa Bunge pia tuna jukumu la kuwaelimisha wananchi wetu, wapiga kura wetu wafahamu kwamba kuanzia sasa hivi picha za ovyo ovyo hajitaruhusiwa kusambaa kwenye vyombo vya habari pasipo kufuata utaratibu. Kifungu hiki kimeweka masharti vizuri.
Mheshimiwa Spika, nijielekeze katika ukurasa wa 15 wa Muswada ambapo kuna marekebisho ya Sheria ya Tafsiri ya Sheria (The Interpretation of Laws Act) ambapo Ibara hii katika Muswada imeenda kufanya marekebisho katika Kifungu cha 54 cha sheria ambacho sasa pale kunapokuwa Bodi haijaundwa na kuna matakwa ya sheria ya Bodi kuundwa na haijaundwa au imemaliza wakati wake wa kufanya kazi au imevunjwa; sasa yale majukumu yote yaliyokuwa yanafanywa na Bodi, yaweze kufanywa na Katibu Mkuu wa Wizara husika.
Mheshimiwa Spika, hili ni jambo jema kwa sababu linaondoa rasimu (bureaucracy). Kwa sababu mwisho wa siku Serikali ni moja na hata yale majukumu yanayofanywa na bodi ni majukumu ya Kiserikali ambapo mwisho wa siku Katibu Mkuu ndio Mtendaji Mkuu kwenye Wizara husika ambayo Bodi imeundwa. Kwa hiyo, kipindi ambacho kunakuwa hamna Bodi ili shughuli za Serikali ziweze kuendelea, nimeona ni vizuri sana hiki kifungu kimewekwa ili kuhakikisha kwamba Katibu Mkuu anaendelea na majukumu ya Kiserikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili ni jambo zuri sana na ninawashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu waweze kuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna mabadiliko ya marekebisho ya sheria katika Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (The Social Security Regulatory Authority Act) ambayo yenyewe imeenda kuondoa mamlaka ile ya udhibiti, SSRA imefutwa.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, tukumbuke hapa Bungeni sisi wenyewe tulikuwa sehemu ya kutunga sheria ya kufanya marekebisho ya sheria kuunganisha mifuko ya hifadhi za jamii. Hapo awali kulikuwa na mifuko mingi ya hifadhi za jamii ambapo ilileta hali fulani ya ushindani baina ya hii mifuko.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu sasa hivi tumebakia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya Sekta ya Umma, lakini kuna Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya Sekta Binafsi na pia tuna Mfuko wa Bima za Afya (NHIF) pamoja na CHF, ule shindani ambao ulikuwa unaonekana hapo awali haupo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kimsingi hata ile kazi iliyokuwa inafanywa na mamlaka hii ya udhibiti inakosekana na hivyo ni muhimu sana kama marekebisho yalivyoletwa na Serikali kwamba Mamlaka au majukumu yale yabakie Wizarani kwenye Wizara husika. Mamlaka ilivyofutwa, inaokoa fedha nyingi sana ambazo zilikuwa zinatokana na michango ya ile Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo kimsingi ni pesa za wanachama. Kwa hiyo, fedha hizi ambazo zilizkuwa zinatumika kwa ajili ya bajeti kwenye hii mamlaka sasa hivi zitaenda kuimarisha masuala mengine katika nchi yetu, yataenda kusaidia sekta nyingine za maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitoshi hivyo tu, ukiangalia katika ukurasa …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Zainab, ni kengele ya pili…
MHE. ZAINAB A. KATIMBA:Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja ya Serikali. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 2) Act, 2022
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ili mimi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mezani.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia niipongeze Serikali kwa kuleta muswada huu wa marekebisho ya sheria. Kama ilivyosomwa na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali marekebisho ya sheria yatagusa sheria tatu. Sasa kuna sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu na kwenye marekebisho yamegusa kifungu cha 4, 5, 6, 7 na 8(a) katika Sheria hii ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo yaliyoletwa na Serikali ni kwamba, mnataka makosa haya ya usafirishaji haramu wa binadamu yaongezewe adhabu; na ndicho kilichofanyika. Katika marekebisho katika hivi vifungu tunaona kwamba hapo awali kulikuwa kuna nafasi ya mahakama kuchagua adhabu kati ya kutoa faini au kifungo. Lakini kwa marekebisho haya tunaona sasa kifungo ni adhabu ya msingi kwa makosa yote yanayohusiana na usafirishaji haramu wa binadamu, halafu kunakuwa pia kuna adhabu ya ziada ambayo ni ya kutoa faini.
Mheshimiwa Spika, lakini kwenye marekebisho haya haikutosha kuishia hapo kuna marekebisho ya Kifungu cha 13 ambacho chenyewe kinaenda kuongeza adhabu, yaani kuweka severe penalty. Kwa maana ya kwamba wale watuhumiwa ambao wanakuwa wamerudia makosa haya ya usafirishaji haramu wa binadamu basi faini yao inakuwa ni ya juu zaidi, kwa maana isiyopungua milioni 100 lakini isiozidi milioni 200.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi naunga mkono marekebisho haya na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wengine waunge mkono marekebisho haya kwa sababu yana tija. Kwa sababu ukitizama athari kubwa ya makosa haya ya usafirishaji haramu wa binadamu katika jamii basi kunakuwa kuna umuhimu wa kuweka adhabu kali zaidi ili kuweza kuzuia watu kujihusisha katika tabia hizi za usafirishaji haramu wa binadamu.
Mheshimiwa Spika, muswada huu umeenda pia kufanya marekebisho katika sheria na kanuni ya maadili ya viongozi wa umma. Na yamezungmzwa hapo awali lakini kwa msisitizo tu, kwa sababu mimi ni mjumbe wa Kamati na tulizungumza na Serikali, na wameridhia tunaona wameleta jedwali la marekebisho, na tumeona kwamba wameondoa yale marekebisho waliyokuwa wamependekeza katika kifungu cha 11(2) ambacho kilikuwa kinataka kutamkwa kwa baadhi ya mali kwenye tamko la kiongozi wa umma. Yaani waliweka kuna baadhi ya vitu ambavyo sisi kama kwenye Kamati tumeona ni vigumu sana utekelezaji wake. Yaani unavyomwambia kiongozi wa umma atamke mali binafsi au vyombo vya nyumbani, samani, furniture vitu kama hivyo; tumeona inakuwa ni ugumu katika utekelezaji. Uzuri Serikali ni Sikivu, kwa hiyo imeleta kwenye jedwali la marekebisho na kifungu hicho naona kimefanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa Spika, lakini kwenye Muswada huu pia imeenda kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95. Msingi hasa wa marekebisho hayo pia ni kuwaongezea mamlaka kwa maafisa, ambapo maafisa sasa wa chombo hicho, wa mamlaka hii ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya waweze kuwa na madaraka ya kukamata, kupekua na kuchunguza makosa ya dawa za kulevya. Kama vile tunavyoona kwenye Criminal Procedure Act polisi wamepewa mamlaka hiyo basi na maafisa hawa wa mamlaka hiyo wapewe sasa mamlaka kubwa zaidi kutokana na aina ya makosa haya ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika, muswada pia umingiza vifungu vipya, kifungu kipya cha 32(4), kifungu kipya cha 32(5) ambacho kinaanzisha au kimetoa mamlaka ya kuanzishwa kwa mahabusu. Na kifungu hiki hakijatamka kwamba mahabusu hizi zitaanzishwa katika kila wilaya, hapana. Kifungu hiki jinsi kilivyoandikwa na tafsiri yake kwa upana ni kwamba mamlaka imetolewa ya kuanzisha mahabusu lakini haimaanishi zote zitaanzishwa kwa wakati mmoja lakini zitaanzishwa pale zinapohitajika.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge niwaambie tu, mazingira ya kesi za dawa za kulevya, sisi tunaishi kwenye jamii, tunafahamu, mazingira yake ni tofauti na kesi nyingine mbalimbali. Kesi za dawa za kulevya zinahusisha fedha nyingi, zinahusisha watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na sisi tunajua fedha inaleta ushawishi. Kwa hiyo mimi naomba tuiamini Serikali na tuwezeshe; kwa sababu marekebisho ya sheria pia yanatokana na changamoto za utekelezaji. Lakini pia marekebisho ya sheria yanakuja kuboresha zaidi yale ambayo tayari yanafanyika. Kwa hiyo katika kuboresha mimi ninaamini kwamba kuanzishwa kwa hizi mahabusu kutaweza kuipa mamlaka hii ya kudhibiti dawa za kulevya nguvu zaidi ya kufanya kazi yake kwa ufasaha.
Mheshimiwa Spika, na kwenye sheria kuna doctrine moja ambayo inaitwa The Doctrine of Chain of Custody. Yaani unapokuwa kuna ushahidi ambao unahitaji uchukuliwe na na hatimaye ndio ambao utakuja kutumika katika kesi. Kuna haja kubwa sana ya ule mlolongo mzima wa kuchukua, kuhufadhi, kurekodi kumbukumbu za ushahidi kuna umuhimu sana uende vizuri, uende bila kuwa na mianya yoyote ya upotevu, uende yaani kwa ufasaha.
Mheshimiwa Spika, sasa katika mazingira ya kesi za dawa za kulevya kama walivyozungumza wengine wamesema unakuta kuna wakati mtuhumiwa amemeza dawa za kulevya na atahitaji muda fulani ambapo atapewa dawa za aina fulani ambazo zitawezesha kutoa zile dawa za kulevya ambazo hatimaye ndivyo vinakuwa vidhibiti katika hizi kesi za dawa za kulevya. Kwa hiyo hizo taratibu zote mimi nadhani kwa utaratibu wa kuwatenga watuhumiwa na taratibu zote hizi zikafatwa kwa ufasaha wakiwa wamewekewa na vifaa mahsusi katika hizo mahabusu; mimi ninaamini itasaidia sana kesi za dawa za kulevya ziweze kufanikiwa vizuri na kwa kasi zaidi kuliko ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba tutoe imani kubwa sana kwa Serikali. Tayari tunaona mamlaka inafanya kazi kubwa sana, basi tuiongezee nguvu iweze kufanya kazi hii kwa ufasaha zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini, jambo la msingi ambalo tunalisisitiza ni kwamba, katika kuruhusu kifungu hichi tunaomba sana masuala ya msingi ya kisheria yazingatiwe hasa kwa wale watuhumiwa. Tunataka tuone adherence of human rights; yaani kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinazingatiwa. Pia tunataka tuone ile doctrine ya presumption of innocence; yaani kwamba mtuhumiwa hajahukumiwa kwa hiyo taratibu zote zile za mtuhumiwa ziweze kufuatwa bila kumchukulia mtuhumiwa kama tayari ni mkosaji halisi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya michango hii naomba sana Waheshimiwa Wabunge waunge mkono Muswada huu ili uweze kupita sheria hizi ziwe zina mabadiliko waweze kwenda kufanya kazi. Ninaiomba sana Serikali iangalie utaratibu mzuri sana wa mamlaka hizi za kudhibiti dawa za kulevya, hii ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar ziweze kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi. Kwa sababu tunafahamu changamoto za dawa za kulevya zipo katika pande zote za Muungano, kwa hiyo washirikiane.
Mheshimiwa Spika, cha mwisho kabisa, ninaiomba Serikali; dawa za kulevya zipo kwa aina tofauti tofauti. Lakini kuna dawa za binadamu ambazo zinaweza kutumiwa na wale wenye addiction ya dawa za kulevya wakazitumia sasa kama dawa za kulevya. Kwa hiyo naiomba Serikali itengeneze utaratibu mzuri wa kuweza kusimamia ununuzi wa dawa. Kwa sababu kuna dawa za aina mbili; kuna dawa ambayo wanaita over the counter, kwamba unaweza ukaingia kwenye duka la dawa ukaweza kununua bila kuwa umeandikiwa cheti na daktari. Halafu kuna zile prescription medication ambazo mara nyingi hizo ndiko kuna baadhi ya dawa ambazo watu wenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya wanaweza kutumia. Kwa hiyo Serikali iangalie usimamizi, zile dawa ambazo ni prescription medication lazima mtu aende na cheti kwenye duka la dawa ili aweze kuzinunua. Serikali isimamie ili wananchi wetu waweze kuwa salama.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Marekebisho haya kimsingi yamekuja kuondoa mapungufu ambayo yalijitokeza katika utekelezaji wa Sheria hii ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi. Kimsingi masharti yaliyokuwepo kwenye Sheria ile kwa kiwango kikubwa yaliweza kuathiri ushiriki wa Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa ubiya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye ukurasa wa 13 wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Ibara ya 18(b)(5) inasema kwamba CCM itaielekeza Serikali kuweka sera madhubuti za uchumi ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia mfumo wa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public Private Partnership) (PPP). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kimsingi suala hili ni la kuleta Muswada wa kufanya marekebisho kwenye Sheria hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi watu huwa wanachanganya kati ya ubinafsishaji na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (Privatization na Public Private Partnership) lakini vitu hivi ni viwili tofauti. Kwa mfano tukizungumzia Public Private Partnership yaani ubia huu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, tuseme Serikali ina miradi mingi ya maendeleo ambayo Serikali ikisema itumie fedha zake itatumia muda mrefu sana ama inaweza ikaongeza deni la Serikali kwa maana ya kutegemea mkopo. Kwa hiyo, mkakati mbadala unaofanyika, miradi ile inatangazwa na wawekezaji wanaweza kuja na mitaji yao, uzoefu wao, wanaweza kuja na utaalam, wanaweza kuja kuwekeza kwenye ile miradi mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hiyo inakuwa inaendeshwa na yule mwekezaji, lakini wananchi wanaweza wakawa wanatoa gharama ile ile kwa ajili ya ile huduma ambayo wangetoa kama mradi ule ungekuwa umejengwa na Serikali. Baada ya muda fulani ambapo kwenye mkataba unakuwa umekubaliwa, mradi ule, yule mwekezaji anakuwa amepata faida yake na amerudisha mtaji wake na ule mradi sasa utakabidhiwa kwa Serikali ili uendelee kuendeshwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi hiki chote ule mradi bado unakuwa ni mradi wa umma. Unakuwa hamna hata kipindi kimoja mmiliki wa ule mradi unakuwa umetoka kwenda kwa sekta binafsi. Mradi unakuwa ni mali ya umma kwa hiyo hii ni mbinu nzuri sana ya kupata mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye Sheria ile tuliyokuwa nayo yaani The Public Private Partnership Act tuliyokuwa nayo ambayo sasa hivi tunaifanyia marekebisho kulikuwa na changamoto kadha wa kadha. Kwanza kwenye Sheria hii na ukienda kwenye Ibara ya 12 ya Muswada inazungumzia masuala ya utatuzi wa migogoro. Yaani Ibara ya 12 ya Muswada imeenda kufanya marekebisha kwenye kifungu cha 22 cha Sheria na sasa hapo mwanzo utatuzi wa migogoro ulikuwa haujatengenezewa sharti ya kwamba mnaweza kutumia mahakama za kimataifa lakini kwa marekebisho haya kwenye Ibara hii sasa mwekezaji atakuwa ana uhuru zaidi wa kuweza kuwekeza kwa sababu kwenye utatuzi wa migogoro atakuwa ana haki ya kutumia aidha Sheria za arbitration za Tanzania au Sheria zinazotambulika za arbitration za kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo ambalo wawekezaji wengi walikuwa wanatamani kuliona lipo kwenye masharti ya Sheria hii. Kwa hiyo, ibara hii ya 12 imekwenda kuleta hayo marekebisho ambayo kimsingi yatavutia wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye Muswada huu ukienda Ibara ya 10 ya Muswada imeenda kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 18(a) cha Sheria hii ya PPP ambapo imeanzisha na imeweka sharti la yule mbia anayeshinda zabuni ya utekelezaji wa mradi wa PPP aunde Kampuni mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kifungu hiki au marekebisho haya ni kwamba sasa huyu mwekezaji kwa sababu atakuwa na kampuni yake achanganye mahesabu ya kampuni yake akachanganya na mapato yale yatakayokuwa yanakusanywa kwenye mradi huu wa PPP. Kwa hiyo, kimsingi ni kulinda maslahi ya nchi na kulinda mapato yatakayotokana na mradi huu wa PPP. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukienda tena kwenye Ibara ya 9 ya Muswada ambayo inaenda kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 15 cha Sheria. Kifungu hiki kinafanya marekebisho na kupunguza yale masharti magumnu ya ununuzi wa mbia na hasa kwenye miradi ile ambayo inaibuliwa au inabuniwa na wabia. Kwa sababu miradi kwenye PPP iko miradi ya aina mbili kuna ile solicited ambayo imeibuliwa na Serikali lakini kuna unsolicited ambayo imebuniwa na mbia kutoka kwenye sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa kifungu hiki hapo awali kilikuwa kinaweka sharti kwenye ile miradi ambayo imeibuliwa na mwekezaji, yule mwekezaji lazima atoe asilimia 3 ya jumla ya gharama ya ule mradi anaotaka kutekeleza, aitoe kama down payment kitu ambacho kilikuwa kinapunguza mtaji wa mwekezaji katika kuwekeza katika huo mradi. Kwa hiyo, masharti ya ibara hii ambayo inaenda kurekebisha kifungu cha 15 imeondoa sharti hilo lakini pia imeweka masharti rahisi zaidi katika masuala ya ununuzi wa mbia katika miradi iliyobuniwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya mabadiliko yote kimsingi yanaenda kubadilisha eneo hili la PPP lakini kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza katika miradi Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa Jumla kwa Serikali, pamoja na marekebisho haya mazuri, naiomba sana Serikali iweze kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwenye miradi kwa sababu feasibility study ndio inatengeneza msingi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: …wa wawekezaji kuvutiwa na kuja kuwekeza katika miradi yetu hapa Tanzania, Ahsante. (Makofi)