MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kumekuwa na matukio ya uhalifu katika maeneo ya mipakani na ni kutokana na mwingiliano wa wageni kutoka nchi jirani. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na kuimarishwa na kudhibiti hali ya usalama katika mipaka yote nchini hususan katika maeneo ya Mkoa wa Kigoma ambako kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya uhalifu ambayo yanahusisha matumizi ya silaha za moto?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katimba, Mbunge wa vijana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ulinzi na usalama nchini ni jukumu letu sote, suala la ulinzi na usalama nchini napenda kuwahakikishia Watanzania na wote ambao wanakuja nchini Tanzania kwamba, ulinzi na hali ya amani na utulivu nchini inaendelea vizuri kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi vinaendelea kufanya kazi katika maeneo yote na kuhakikisha kwamba Tanzania inabaki kuwa salama.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge amezungumzia wasiwasi wake wa hali ya ulinzi na usalama kwenye mipaka na ameeleza hasa Mkoani Kigoma ambako natambua yeye pia anatoka Mkoani Kigoma. Nimefanya ziara Mkoani Kigoma, yako matukio kadhaa yameripotiwa, lakini hasa matukio haya ni kutokana na mchanganyiko tulionao na hasa kwenye mikoa yote iliyoko pembezoni.
Mheshimiwa Spika, nimeenda Kigoma, Kagera na Mkoani Kilimanjaro nimeona dalili hizo na taarifa za Jeshi la Polisi, lakini sehemu kubwa ni salama. Nini tahadhari ya maeneo haya, ni kutokana na mwingiliano wa nafasi ambazo tunazo na nchi jirani ambazo zinazunguka kwenye maeneo haya, tahadhari kubwa imechukuliwa. Nataka pia nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania hasa wale tulioko mipakani kushiriki kikamilifu katika kulinda mipaka yetu na kubaini vyanzo vyote vinavyoashiria kuleta uvunjifu wa amani nchini tukishirikiana na vyombo vya dola ambavyo vyenyewe vina nafasi ya moja kwa moja kwenye ulinzi wa usalama hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya ni nini kwenye mipaka? Kwanza, tumeimarisha mipaka hiyo kwa kuweka maeneo maalum ya wanaoingia nchini ili kuweza kuwatambua wote wanaoingia na kukagua wamengia na zana gani kwa lengo la kudhibiti uingiaji wa silaha ambazo haziruhusiwi kuingia hapa nchini. Pia vyombo vyetu vya ulinzi vimeweka tahadhari kubwa sana na nchi jirani ambazo sasa tunashuhudia huko kuwa na migogoro mingi ya ndani, kwamba migogoro hiyo kwenye nchi hizo jirani isihamie kwenye nchi yetu.
Kwa hiyo, Majeshi yetu na vyombo vyote vya dola vinaendelea na umakini huo ikiwemo na Mkoa wa Kigoma ambako tunapakana na nchi jirani zisizopungua mbili, tatu, nne ambazo na zenyewe pia tunaendelea kujenga mahusiano ya kiulinzi kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine anaweza kuhamishia migogoro nchi nyingine ili kufanya nchi hizi kuendelea kuishi kwa umoja, mshikamano pia kuwa na ulinzi wa pamoja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nataka niwahakikishie wananchi wote wanaoishi maeneo ya pembezoni matukio yote madogo yanayoripotiwa yanachukuliwa hatua lakini udhibiti wa mipaka hiyo unaendelea kuimarishwa lakini nitoe wito sasa kwa Watanzania wenyewe tushirikiane, tushikamane katika kubaini viashiria vyote vinavyoleta uvunjifu wa amani nchini kwa lengo ya kuifanya Tanzania kuendelea kuwa salama, kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa ni kimbilio la wale wote wanaopenda amani, kwa lengo la kuwafanya Watanzania wenyewe kufanya shughuli zao za maendeleo wakiwa na uhakika wa maisha yao, wakiwa na uhakika wa shughuli zao.
Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba vyombo vya usalama vinalinda maeneo yote ili kuhakikisha kwamba nchi inabaki salama. Ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika ahsante, zao la chikichi ni zao ambalo linaweza kuleta ukombozi mkubwa kwa Taifa katika kujitosheleza katika uzalishaji wa mafuta ya kula nchini, hasa ukizingatia kwamba kujitosheleza katika uzalishaji wa mafuta ya kula nchini kutasaidia kupunguza changamoto ya nakisi ya urari wa malipo inayotokana na uagizaji wa bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi.
Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kunakuwa na programu endelevu ya kukuza zao la chikichi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya nchi ambapo zao la chikichi linastawi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia zao la mchikichi, ni kweli kwamba Serikali yetu tulishaanza mkakati wa kulirudisha zao hili kwa wakulima kwa kulima kisasa na kupata mbegu bora ili tuongeze uzalishaji ukilinganisha na uzalishaji tuliokuwanao awali ambao ulikuwa unatumia mbegu ambazo hazizalishi na kutoa mafuta mengi, lakini pia hata hamasa ya kilimo cha chikichi ilipungua sana.
Mheshimiwa Spika, tulipokuwa tunaanza kurudisha zao hili liwe kwenye mpango wetu wa kiserikali, inatokana na mahitaji makubwa ya mafuta hapa nchini. Kwa hiyo, mkakati wa kupata mafuta ya kula hapa nchini unatokana na mkakati wa ndani kwa mazao hayo ya chikichi na mazao mengine kama vile alizeti na mazao yote yanayotoa mafuta.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali katika kulipanua zao hili, kwanza tumeimarisha kuwa na kituo cha utafiti, na kule Kigoma tumejenga kituo cha utafiti na ndicho ambacho kimeleta mafanikio makubwa kwa kupata mbegu yetu wenyewe Watanzania kutoka kwenye vituo vyetu. Ndiyo hiyo ambayo tumeipanda na sasa inaendelea vizuri na tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara na tumethibitisha kwamba mbegu yetu inafanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, pia utafiti huu unakwenda sambamba na kutafiti udongo unaoweza kumea mchikichi na kupata matunda, siyo tu kwa ukanda wa Ziwa Tanganyika bali na maeneo mengine yote nchini ili tulipande zao hili, liwe pana, na watu wanaoshughulika na kilimo waweze kuingia kwenye sekta hiyo wakiwa na uhakika kwamba wanapanda mchikichi kwenye ardhi ambayo inaweza kuzalisha zaidi. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, pili, tumeanza kampeni ya zao hili na sasa imeanza kuleta matunda. Tunaona pia Mkoa wa Tabora wanalima, tumeona Mikoa ya Pwani, Mkoa wa Pwani wenyewe, Dar es Salaam, ndiyo twende Lindi, Mtwara, tunaona maeneo yote yanayopanda zao la minazi pia tunaambiwa yanaweza kustawisha zao la mchikichi. Huu ni mpango wa kupanua zao hili ili tupate mazao mengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunapoanza na mkakati huu kupitia kituo chetu cha utafiti na kuzalisha mbegu nyingi, tumeanza kutoa mbegu inayozalishwa bure kwa wakulima katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja ili kupanua wigo wa watu ambao wanaanzisha kilimo hiki ili waweze kupanda zao hili la mchikichi, huku pia tukiimarisha uwekaji wa viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya wachakataji, kwa sababu baada ya kuwa tumezalisha, tunahitaji sasa tuone matokeo. Hii itasaidia watu wengi kuingia kwenye kilimo na kuwezesha kulima zao hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mkakati huu wa kukuza zao hili tunausimamia toka tulipoanza kulima zao hili Kigoma, na Mkoa wa Kigoma ni watu ambao wameanza mara moja kulilima zao hili na mafanikio tunayaona na tunaona mikoa mingine nao pia wanachukua miche na upandaji tunaona maendeleo yake. Kwa hiyo, tunataka tuhakikishe kwamba zao la chikichi sasa linaanza kuchangia upatikanaji wa mafuta ndani ya nchi na mazao yake mengine na kunufaisha yeyote ambaye anaingia kwenye kilimo cha chikichi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wakulima wa zao la chikichi kwamba Serikali itaendelea kusimamia maendeleo ya zao hili na hapo baadaye litakapokuwa kubwa tunaweza tukaliundia chombo chake cha usimamizi wa zao hili ili pia liweze kusimamiwa kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, malengo yetu ni kwamba tunatoa fursa kwa Watanzania wanaotaka kulima kilimo wawekeze kwenye mashamba makubwa, wanaotaka kujenga viwanda na tumehusisha pia na taasisi za umma na taasisi binafsi kulima zao hili. Kule Kigoma tuna Magereza, Magereza zote zinalima chikichi, shule za msingi nyingi zimekuwa na mashamba yao, wanalima chikichi, pia Jeshi la Kujenga Taifa, JKT Bulombora nao wana shamba kubwa zaidi ya ekari 4,000 na tunaendelea kuhamasisha taasisi zote zilime zao hili lilete manufaa makubwa.
Mheshimiwa Spika, niwahamasishe Watanzania kulima mchikichi kwa faida yao. Tulime mchikichi kwa ajili ya kupata mafuta mengi, tulime mchikichi kwa sababu na yenyewe inatoa sabuni na bidhaa nyingine ambazo pia zinaleta faida kwenye zao hili.
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mkakati wa Serikali wa kupanua zao hili. (Makofi)