Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Zainab Athuman Katimba (36 total)

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Bwalo katika Sekondari ya Malagarasi - Muhambwe lililosimama tangu mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali ilitoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Bwalo la Chakula katika Shule ya Sekondari Malagarasi. Fedha hiyo ilitumika kukamilisha kazi za ujenzi wa bwalo na hadi sasa lipo katika hatua za umaliziaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa baadhi ya miundombinu ya bwalo hilo haijakamilika kujengwa. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga bajeti ya shilingi milioni 187 kwa ajili ya kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa Bwalo katika Shule ya Sekondari Malagarasi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapandisha hadhi shule ya Sekondari Kilolo kuwa ya Kidato cha Tano na Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Wilaya ya Kilolo ina tarafa tatu ambazo ni Kilolo, Mazombe na Mahenge ambazo zote zina Shule za Kidato cha Tano na Sita. Shule hizo ni: Udzungwa Sekondari (Kilolo); Ilula Sekondari (Mazombe) na Lukosi Sekondari (Mahenge) ambayo imepandishwa hadhi mwaka huu 2024 na inatarajiwa kuanza Julai, 2024, baada ya Serikali kupeleka shilingi milioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uwepo wa shule hizo, Serikali itaendelea na mpango wake wa kupandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Kilolo kuwa na kidato cha tano na sita kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali kutenga Bajeti kwa ajili ya Taulo za kike shuleni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa taulo za kike kupitia fedha zinazotokana na ruzuku ya uendeshaji (Capitation Grants), wadau pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, shilingi bilioni 3.16 zilitumika kugharamia taulo za kike. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.97 zilitoka katika ruzuku ya uendeshaji, shilingi milioni 539 zilitoka katika mapato ya ndani ya halmashauri na shilingi milioni 655 zilitoka kwa wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali ilitenga shilingi bilioni 2.64 kwa ajili ya kugharamia taulo za kike. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.06 ni za ruzuku ya uendeshaji na shilingi bilioni 1.58 ni fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri. Hadi Machi, 2024 shilingi bilioni 2.2 zimetumika. Pia, wadau mbalimbali walichangia jumla ya shilingi bilioni 1.5 na Miradi ya Shule ya Elimu ya Kujitegemea ilichangia shilingi milioni 119.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuzisisitiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya upatikanaji wa taulo za kike shuleni.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza:-

Je, lini barabara za lami zinazofadhiliwa na Benki ya Dunia zitaanza kujengwa Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa RISE katika Wilaya ya Mbogwe zina jumla ya urefu wa kilometa 102. Barabara zitakazojengwa kwenye Mradi huo ni Masumbwe – Iponya - Nyashimba (kilometa 20), Lulembela – Kiseke – Isebya (kilometa 17), Mkweni – Nhomolwa - Nyanhwiga (kilometa 21), Ishigamva – Busabaga – Ilolangulu (kilometa 14) na Ivumwa – Ushirika - Shibutwe (kilometa 30).

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Barabara za Masumbwe – Iponya – Nyashimba (kilometa 20), Lulembela – Kiseke – Isebya (kilometa 17), Ishigamva – Busabaga – Ilolangulu (kilometa 14) na Mkweni – Nhomolwa – Nyanhwiga (kilometa 21). Aidha, kazi za usanifu wa barabara za awamu ya kwanza zilianza Januari, 2024 na zinatarajiwa kukamilika Agosti, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kazi ya usanifu wa barabara kukamilika Serikali kupitia TARURA itatangaza zabuni na kumpata mkandarasi wa kujenga barabara za awamu ya kwanza kwa kiwango cha lami.
MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Nsanga – Kiteputepu katika Kata ya Ntaba – Busokelo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Nsanga linaunganisha Kata ya Ntaba upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo na Kata ya Ipinda upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Daraja hilo hutumiwa na wakulima wa mpunga na kokoa kutoka mashambani kwenda kwenye masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali kupitia TARURA imetenga shillingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu la zege katika sehemu hiyo ambapo kwa sasa kuna kivuko cha waenda kwa miguu ambacho kinatumika.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutumia wataalam wa ujenzi kwenye Miradi ya Force Account hata ikiwa kwa mikataba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inazingatia miongozo iliyopo kwenye kutekeleza kazi za ujenzi wa miradi kwa kutumia njia ya force account ili miradi hiyo iweze kutekelezwa kwa ubora na ufanisi mkubwa. Aidha, Serikali imekua ikiwatumia wataalamu wa ujenzi kwa mikataba na waajiriwa wa halmashauri ili kuhakikisha miradi inayojengwa kwa force account inakua bora na imara.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, kuna upungufu wa walimu kiasi gani kwa shule za msingi na sekondari kwa masomo ya sayansi na hesabu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa upungufu wa walimu wa masomo ya Hisabati na Sayansi katika shule za sekondari nchini. Kwa sasa mahitaji ya walimu wa sayansi na hisabati ni walimu 71,027, waliopo ni walimu 31,417, na upungufu ni walimu 39,610, sawa na 55.8%.

Mheshimiwa Spika, kufuatia upungufu huo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa masomo mbalimbali wakiwemo wa masomo ya sayansi na hisabati. Katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2022/2023 Serikali iliajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati 10,853. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Serikali inategemea kuajiri walimu 12,000 wakiwemo wa masomo ya hisabati na sayansi.
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta unafuu wa gharama za michango ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza na cha tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 ambalo pamoja na mambo megine inatamka kuwa Serikali itahakikisha kuwa elimu ya awali, msingi na sekondari inatolewa bila ada katika mfumo wa umma. Aidha, Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa Elimu Msingi Bila Malipo, unabainisha majukumu ya wadau wote ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kuzingatia ili kupata kibali cha mchango wa aina yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuleta unafuu wa gharama za michango, Serikali imetoa maelekezo ya kujiunga na kidato cha tano katika shule zote za sekondari za Serikali Tanzania ambapo ukomo wa michango hiyo umebainisha kuwa shilingi 80,000 kwa shule za bweni na shilingi 50,000 kwa shule za kutwa. Aidha, wanafunzi wa kidato cha kwanza wanapokelewa kwa kuzingatia Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 wa Elimu Msingi bila Ada ambapo wanafunzi hawatakiwi kutoa mchango wowote bila kibali cha Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kukarabati majengo yaliyojengwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu Msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2022/2023 Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilifanya tathimini ya mahitaji na hali ya miundombinu ya shule zote za msingi zikiwemo shule zenye majengo yaliyojengwa chini ya mpango wa maendeleo ya elimu msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2023/2024 Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ukarabati ambapo shilingi bilioni 70.39 zimetolewa kwa ajili ya ukarabati wa shule 793.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za ukarabati wa shule chakavu zikiwemo shule zenye majengo yaliyojengwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu Msingi kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Je, Halmashauri ngapi zimetekeleza agizo la Waziri Mkuu kununua dawa za viuadudu kutoka Kiwanda cha Kibaha ili kutokomeza mazalia ya mbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa afua ya unyunyuziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu yaliyotambuliwa katika halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuzielekeza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kununua dawa za viuadudu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya halmashauri 126 zimetenga shilingi milioni 775.89 kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, kwa nini ujenzi wa Barabara ya Bukiko hadi Bwisya kupitia Katende inayosimamiwa na TARURA haukamiliki kwa zaidi ya miaka miwili sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo ndio siku ya kwanza nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nichukue dakika moja kutoa maneno ya utangulizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na siha njema mpaka wakati huu. Kipekeee naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniteua katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Namuahidi Mheshimiwa Rais nitafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu mkubwa ili kumsaidia majukumu yake na kutimiza maono yake kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kukushukuru wewe kama mlezi wetu sisi Wabunge, kwa nasaha zako, kwa mafunzo yako ambayo yamenijenga mimi kiuongozi, lakini pia katika maisha yangu binafsi, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mkubwa ambao wamenionesha. Kwa heshima kubwa na unyenyekevu niwaombe ushirikiano zaidi sasa ili kwa pamoja tuweze kushirikiana kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutimiza maono yake kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii adhimu pia kuwashukuru akinamama wote na wapigakura wangu wa Mkoa wa Kigoma kwa kuendelea kunipa ushirikiano mkubwa unaonipa utulivu katika kazi zangu. Baada ya kusema maneno hayo ya utangulizi, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini ilifanya matengenezo ya kufungua upya Barabara ya Bukiko hadi Bwisya kupitia Katende kilometa 7.54 kwa gharama ya shilingi milioni 141.2. Fedha hizo zilitekeleza kazi za ufunguzi wa barabara na kuunda tuta la barabara kilometa 7.54, ujenzi wa madaraja madogo matatu na ujenzi wa mistari minne ya madaraja madogo. Kazi zote zilikamilika kwa mujibu wa mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imeweka katika mipango yake ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, kufanya matengenezo ya kawaida na kujenga madaraja madogo mawili kwa gharama ya shilingi milioni 30.16 ili barabara iweze kupitika wakati wote. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO K.n.y. MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-

Je, upi mpango wa Serikali wa kujenga barabara na mitaro Geita Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024, Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 77.94 na ujenzi wa mitaro yenye jumla ya kilometa 6.395. Aidha, Geita ni miongoni mwa miji 45 inayotekeleza Mradi wa Kuboresha Miundombinu Shindanishi katika Miji Tanzania (TACTIC) ambapo mradi utajenga kilometa 17 za barabara kwa kiwango cha lami na kilometa 25 za mitaro kwa gharama ya shilingi bilioni 22.23.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Shule za Sekondari katika Kata za Ngima, Mhongozi na Muungano - Halmashauri ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ina Kata tatu za Muungano, Ngima na Mhongozi ambazo hazina shule za sekondari. Aidha, Kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), halmashauri itaendelea kujenga Shule ya Kata ya Muungano (SEQUIP), awamu ya tatu ambapo ilitengewa shilingi milioni 560 katika bajeti ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2024/2025, Kata ya Mhongozi imetengewa shilingi milioni 560 kwa ajili ya kujenga shule katika kata hiyo kupitia mpango wa kuboresha elimu ya sekondari awamu ya nne. Aidha, Kata ya Ngima itatengewa fedha katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ili kukamilisha ujenzi wa shule za kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Wilaya ya Uyui gari la wagonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepeleka magari mawili ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mwezi Februari, 2024. Magari hayo yamepangwa katika Hospitali ya Wilaya Uyui na Kituo cha Afya Igalula.

Mheshimiwa Spika, magari hayo yanatumika kutoa huduma kwa mfumo wa Kaskedi ambapo Vituo vya Afya vya Loya, Tura, Upuge na Mabama pamoja na zahanati ambazo hazina magari ya kubebea wagonjwa vitahudumiwa.
MHE. HASSAN S. MTENGA K.n.y. MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza : -

Je, Serikali inaridhishwa na ujenzi unaoendelea wa Ofisi ya Halmashauri ya Masasi DC na hospitali yake na juhudi gani zinafanyika kuinusuru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ni moja kati ya Hospitali 67 zilizoanza kujengwa katika awamu ya kwanza mwaka 2019/2020. Hospitali hiyo mpaka sasa imepokea fedha za ruzuku ya Serikali shilingi bilioni 3.49 ambayo imejenga majengo 15. Aidha, majengo 11 yamekamilika na yanatumika na majengo manne ambayo ni wodi mbili za upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la upasuaji (theatre) yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, katika miaka mitatu (2020/2021, 2021/2022 na 2023/2024) Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 2.8 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya halmashauri. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2024 ujenzi wa jengo hilo umefikia 86%. Aidha, miundombinu iliyosalia inategemewa kukamilishwa ifikapo mwezi Septemba, 2024.

Mheshimiwa Spika, jengo la Halmashauri ya Masasi na Hospitali ya Wilaya yameanza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, majengo yaliyochelewa kukamilika na kuanza kutoa huduma Serikali itaongeza kasi ya ukamilishaji wa majengo hayo.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-

Je, ni lini Vituo vya Afya Kharumwa na Nyang’hwale vitapatiwa X–Ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2023/2024 jumla ya mashine 280 za kidijitali za x-ray na mashine za ultrasound 322 zimenunuliwa na kusimikwa katika vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ilipokea mashine mbili za x-ray ambazo zimefungwa katika Hospitali ya Wilaya mwezi novemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za mionzi katika vituo vya kutolea huduma za afya vikiwemo Vituo vya Afya vya Kharumwa na Nyang’hwale.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaajiri wataalamu wa kuendesha mikopo ya halmashauri ya 10% badala ya kufanywa na Maafisa Maendeleo ya Jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kusimamia na kuratibu utoaji wa mikopo ya halmashauri ya 10% kwa sababu ya utaalamu wao katika shughuli za maendeleo ya jamii. Aidha, wataalamu hawa wamekuwa wakihusika katika kuunda na kusimamia vikundi mbalimbali vya kijamii hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali kwa sasa ni kuendelea kuwaajiri na kuwajengea uwezo zaidi Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na kuwawezesha kwa kuwapatia rasilimali mbalimbali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi zaidi.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Boma, Kijiji cha Doma, Wilayani Mvomero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu;-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Doma kipo Kata ya Doma, Kijiji cha Doma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Ujenzi wa kituo hiki ulianza mwaka 2021/2022 kwa wananchi kuanza ujenzi wa jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD) ambalo limefikia hatua ya kupandisha kuta.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imetenga shilingi milioni 40 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya cha Doma.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza Walimu wa Masomo ya Sayansi kwa Shule za Sekondari Mtwara Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa masomo mbalimbali wakiwemo wa masomo ya Sayansi. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 hadi mwaka 2022/2023, Serikali iliajiri walimu wa masomo ya Sayansi 8,425 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ilipata walimu 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 wa masomo mbalimbali wakiwemo wa sayansi ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuweka zege kwenye barabara za mlimani Jimbo la Same Magharibi ili kuokoa gharama za kuweka vifusi mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiweka zege kwenye barabara mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo katika mwaka 2023/2024 Barabara za Makanya – Suji – Mweteni, Saweni – Gavao – Bwambo na Msanga – Chome – Ikokoa zimetengewa shilingi milioni 416.35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za zege zenye urefu wa kilometa 1.6 kwenye maeneo korofi na kazi inaendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2022/2023 TARURA Wilaya ya Same imefanya matengenezo ya barabara kwa kiwango cha zege kwenye Jimbo la Same Magharibi yenye urefu wa kilometa 3.55 kwenye maeneo korofi ya barabara za milimani kwa gharama ya shilingi milioni 671.16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha za matengenezo ya barabara kwa kiwango cha zege hasa ukanda wa milimani kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI K.n.y. MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Shule ya Wasichana Arusha ambayo ilipangwa kujengwa katika Kata ya Enkikret – Longido?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari ilipanga kujenga shule 26 za bweni za wasichana za kitaifa katika mikoa yote nchini. Lengo la shule hizi ni kuongeza fursa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha kukatisha masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa shule hizi umefanyika katika mikoa yote kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilianza kwa mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Songwe, Lindi, Dar es Salaam, Njombe na Ruvuma. Aidha, awamu ya pili imefanyika katika mikoa iliyobaki na kufanya mikoa yote kuwa imepokea fedha za ujenzi wa shule za bweni za wasichana za mikoa ikiwemo Mkoa wa Arusha ambapo ujenzi unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido na umefikia 85%. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. SILYVESTRY F. KOKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mpiji ili kuunganisha Kibaha na Kibwegere Wilaya ya Ubungo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa Daraja la Mto Mpiji linalounganisha Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Kibwegere katika Wilaya ya Ubungo. TARURA kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri Smarcon imefanya usanifu wa kina (detailed design) wa daraja hilo lenye urefu wa mita 60. Kazi hiyo imekamilika na inakadiriwa gharama za ujenzi kuwa ni shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo, na pindi zitakapopatikana, ujenzi utaanza mara moja.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Mbinga Mpepai hadi Mtua kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mbinga Mpepai – Mtua ambayo inatambulika kwa jina la Mbinga – Liparamba yenye urefu wa kilometa 41.87 ipo kwenye utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024, na wakandarasi wapo eneo la kazi. Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi milioni 947.2 ambazo zitatumika kutengeneza kilometa 31 kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa TACTIC itatekeleza ujenzi wa barabara hii kilomita mbili kwa kiwango cha tabaka la lami. Serikali itaendelea kuhudumia mtandao wa barabara katika Mji wa Mbinga ikiwemo barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la uhaba wa walimu wa kike katika shule za msingi na walimu wa sayansi katika shule za sekondari Mkoani Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe una shule za msingi za Serikali 481 na walimu wa shule za msingi 4,211, kati yao walimu 1,932 ni wa kike na 2,279 ni wa kiume. Kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2022/2023 Mkoa wa Songwe ulipangiwa walimu 570 kati yao 272 wa shule za msingi na 298 wa shule za sekondari. Aidha, kati ya walimu 298 wa sekondari, walimu 86 ni wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa walimu wa kike katika malezi ya wanafunzi pamoja na uhitaji wa walimu wa masomo ya sayansi. Katika kutatua changamoto hizo, katika mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 wa kike na wa kiume wa masomo yote yakiwemo ya sayansi ambao watapangiwa vituo mbalimbali ikiwemo na Mkoa wa Songwe.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Shule ya Sekondari Kata ya Malya, Kitongoji cha Mwashilibwa ili kuongeza huduma Vijiji vya Mwitemba, Talaga na Kitunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) inaendelea na ujenzi wa shule za sekondari kwenye maeneo ya kata yasiyo na shule na maeneo yenye msongamano wa wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa shule ya sekondari ya mikondo miwili kupitia Mradi wa SEQUIP awamu ya tatu katika Jimbo la Sumve unatekelezwa katika Kata ya Malya, Kijiji cha Kitunga. Serikali itaendelea kujenga shule katika maeneo yasiyo na shule ili kuwarahisishia wanafunzi kupata elimu katika mazingira ya karibu na nyumbani kwao. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasawazisha vilima vilivyopo kwenye Barabara ya Ninde, Kala na Wampembe ambavyo vimekuwa vyanzo vya ajali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, vilima vilivyopo katika barabara ya Namanyere – Kakoma – Ninde vimeanza kufanyiwa kazi kwa kupunguza miinuko mikali na kuweka tabaka la zege lenye urefu wa meta 150 kwa gharama ya shilingi milioni 84.75 katika mwaka 2022/2023. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Serikali imetenga shilingi milioni 550 kwa ajili ya kupunguza vilima na kujenga tabaka la zege lenye urefu wa meta 700 katika Barabara ya Kitosi - Wampembe ili kuondoa maeneo yote korofi ambapo mkandarasi ameanza kazi.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2024/2025 shilingi milioni 475 imetengwa kupitia Mfuko wa Jimbo kwa lengo la kuvisawazisha vilima vilivyopo katika Barabara ya Nkana – Kala. Aidha, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 180 katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya kupunguza miinuko mikali iliyobaki kwa kujenga tabaka la zege lenye urefu wa meta 200 hivyo kumaliza kabisa tatizo lililopo kwenye vilima vya Barabara ya Namanyere – Kakoma – Ninde.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Tarafa ya Negezi ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwani tarafa hiyo ina kituo kimoja tu cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Negezi ina kata nane ambapo kata mbili kati ya hizo zina vituo vya afya. Vituo hivyo ni Kituo cha Afya Negezi kilichopo Kata ya Negezi ambacho kilipokea shilingi milioni 500 mwaka 2021/2022 na Kituo cha Afya Nhobola kilichopo Kata ya Talaga ambacho ni cha muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati kote nchini zikiwemo kata zitakazokidhi vigezo katika Tarafa ya Negezi.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-
Je, ni lini ahadi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya itaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya unaendelea katika eneo la hospitali ilipo kwa kuiongezea miundombinu muhimu iliyokuwa imepungua. Serikali katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2023/2024 imepeleka shilingi bilioni 2.5 ambapo majengo 13 yamejengwa yakijumuisha jengo la OPD, jengo la kuhudumia wagonjwa wa dharura (EMD), jengo la maabara, jengo la kliniki ya mama na mtoto, jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, jengo la stoo ya kutunzia dawa, wodi nne za kulaza wagonjwa, jengo la mama ngojea, jengo la kufulia na njia za kutembelea wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo yote haya yamekamilika na yanatumika. Katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga shilingi milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
MHE. ANNE K. MALECELA K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza tatizo la matundu ya vyoo, viti, meza na madawati katika Halmashauri zote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024/2025 shilingi bilioni 54 imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 25,825, shilingi bilioni nne kwa ajili ya kununua seti za viti na meza 40,585 na shilingi bilioni 4.28 kwa ajili ya kununua madawati 47,192. Aidha, kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024, ujenzi wa matundu ya vyoo 22,418 kwa shule za msingi na 16,795 kwa shule za sekondari unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali wa kumaliza upungufu wa matundu ya vyoo, viti, meza na madawati katika Halmashauri zote nchini ni kuhakikisha kuwa kila darasa jipya linalojengwa linawekewa madawati 15; dawati moja wanafunzi watatu kwa shule za msingi na viti 50 na meza 50 kwa shule za sekondari. Vilevile ujenzi wa madarasa mapya unaenda sambamba na ujenzi wa matundu ya vyoo kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya madarasa yanayojengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia Serikali Kuu na mapato ya ndani kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa barabara ya Mhanga hadi Mgeta - Kilolo utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Barabara ya Mhanga - Mgeta yenye kilometa 17.0 inayounganisha maeneo ya uzalishaji katika Wilaya za Kilolo - Iringa na Kilombero - Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeanza ujenzi wa barabara hii kwa kutenga fedha kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023, imetoa kiasi cha shilingi 282,500,000 kujenga kilometa 13. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuchimba mifereji urefu wa meta 2,000, kalvati midomo sita pamoja na kuumba tuta la barabara kilometa 13. Kwa sasa mchakato wa kumpata Mkandarasi unaendelea na matarajio ni kuanza ujenzi mwezi huu wa Mei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Mhanga - Mgeta kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuifanya barabara hii kupitika kwa maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Kilolo na maeneo jirani.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, lini Halmashauri ya Wilaya ya Uyui itagawanywa na kutoa Halmashauri mpya ya Kizengi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala huzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Mamlaka za Wilaya Sura 287 na Mamlaka za Miji Sura 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaishauri Menejimenti ya Halmashauri ya Uyui na Mkoa wa Tabora kuendelea na taratibu za maombi na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa hatua zaidi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, lini Barabara ya Mtandika hadi Nyanzwa - Kilolo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mwaka wa Fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi milioni 61 kwa kazi za kuchonga barabara kilomita tano na kuweka changarawe kwenye sehemu korofi katika barabara hii. Pia, kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 imeweka katika mipango kiasi cha shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuchonga barabara kilomita saba na kuweka changarawe sehemu korofi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA imepanga kufanya usanifu wa kina wa barabara hii katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ili kujua kiasi cha fedha kitakachohitajika na kisha kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. MARTHA N. GWAU K.n.y. MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga madaraja kwenye Barabara za Misughaa hadi Kikio na Matongo hadi Mpetu – Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa vivuko na madaraja katika Jimbo la Singida Mashariki. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya shilingi milioni 435 zimetumika katika ujenzi wa madaraja katika Barabara ya Mpetu – Matongo - Misughaa – Msule - Sambaru, Mungaa – Ntuntu - Mang’onyi na Lighwa – Ujaire. Utekelezaji wake umefikia asilimia 90. Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imeweka katika mpango wake kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya shilingi bilioni 1.11 kwa ajili ujenzi wa madaraja katika Wilaya ya Ikungi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Barabara za Misughaa - Kikio na Matongo - Mpetu kuna uhitaji wa jumla ya madaraja matatu ambayo ni Daraja la Mto Matongo lenye urefu wa mita 65, Daraja la Mto Isanja lenye urefu wa mita 45 na Daraja la Mto Siuyu lenye urefu wa mita 30. Kutokana na ukubwa wa madaraja haya usanifu wa kina unahitajika kufanywa. TARURA imeanza kutekeleza kazi ya usanifu wa madaraja haya kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi wake.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Muleba imetengewa shilingi 1,825,662,000 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya hospitali hiyo mpaka itakapokamilika.
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa katika Kata ya Kiwira-Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Soko la Kisasa la Kiwira kwa wananchi wa Wilaya ya Rungwe. Kwa kutambua hilo hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali kuwezesha ujenzi wa soko hilo ambapo upembuzi yakinifu na michoro ya kihandisi imekamilika, upimaji wa udongo wa eneo la ujenzi umefanyika na andiko la mradi huo limeandaliwa. Aidha, andiko la mradi huo limeshapita katika hatua za awali za uchambuzi na hatua inayoendelea ni tathmini ya athari za mazingira na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo ukikidhi vigezo utatengewa fedha kupitia utaratibu wa miradi ya kimkakati. Aidha, mradi huo utakapokamilika utakuwa na eneo la soko, mgahawa, maduka ya kibiashara, kiwanda kidogo cha kuchakata zao la ndizi, jengo la taasisi za kifedha na ghala baridi (cold room).
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, TARURA ina mpango gani wa kujenga barabara kwenye kona kali na milimani kwa kutumia zege katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya uwepo wa kona na miinuko mikali katika baadhi ya barabara za Jimbo la Lushoto. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo, Serikali imekuwa ikitenga fedha na kujenga vipande vya matabaka ya zege katika maeneo yenye milima mikali na kona ili kuondoa changamoto ya upitaji kwa vyombo vya usafiri kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2023/2024, TARURA inajenga tabaka la zege lenye urefu wa meta 900 katika Barabara ya Halmashauri ya zamani – Kwembago - Irente kwa gharama ya shilingi milioni 512.74. Aidha, katika mwaka 2024/2025, shilingi milioni 181.75 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa maeneo yenye kona kali na miinuko katika Barabara ya Dochi - Gare kwa kujenga kwa tabaka la zege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti zijazo ili kuondoa changamoto hizi kwenye maeneo yenye milima na kona kali kulingana na upatikanaji wa fedha.