Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zainab Athman Katimba (7 total)

MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ilifanya ongezeko la fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu kwa shilingi 1,000 kutoka shilingi 7,500 mpaka shilingi 8,500 katika mwaka wa fedha 2015/16 ongezeko ambalo haliendani na kasi ya mfumuko wa bei uliorekodiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoka aslimia 4.2 Februari, 2015 mpaka kufikia asilimia 5.6 Februari, 2016:-
Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha hizo kufikia shilingi 10,000 kwa siku ili kuendana na kupanda kwa gharama za maisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya utafiti juu ya gharama halisi za maisha ya wanafunzi ambazo hujumuisha gharama za chakula na malazi. Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilifanya utafiti katika vyuo vyote nchini ili kujua gharama halisi ya chakula na malazi. Utafiti huo ulionesha kuwa gharama hizo zilikuwa kati ya shilingi 8,000 mpaka 8,500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utafiti huo hufanyika kila baada ya miaka miwili, Wizara yangu itafanya utafiti mwingine, ili kubainisha gharama halisi za chakula na malazi. Matokeo ya utafiti huo yatatumika kupanga viwango vya fedha atakazolipwa mwanafunzi kwa kuzingatia gharama halisi pamoja na upatikanaji wa fedha.
MHE.PETER J. SERUKAMBA (K.n.y MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-
Mwaka 1993 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana (Youth Development Fund – YDF) ili kutoa mikopo kwa vijana nchini. Mwaka 2013/2014 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 6.1 na mpaka mwezi Machi, 2014 jumla ya shilingi bilioni mbili zilitolewa na Serikali.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuwaeleza vijana nchi nzima kuwa ni vijana wangapi na wa maeneo gani ambao wamenufaika?
(b) Je, maisha ya vijana waliopewa fedha hizo yamebadilika kwa kiasi gani ili tuweze kupima haja ya mfumo huo na usimamizi wake?
(c) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuangalia upya mfumo uendeshaji wa mfuko huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum na kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali. Kupitia utaratibu huu, vijana huwezeshwa kujitegemea, kupunguza umaskini wa kipato na kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vikundi vya vijana 309 kutoka Hamlashauri mbalimbali nchini vilifaidika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kupata mikopo yenye jumla ya shilingi 1,867,899,520 ambako mpaka sasa tayari SACCOS za vijana kutoka katika Halmashauri 94 zimepatiwa mkopo huu.
Vijana hawa pia hupatiwa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa miradi, utunzaji wa fedha na utafutaji masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za mkopo zitokanazo na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umekuwa msingi mzuri katika kuandaa vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Kupitia fedha hizo, vikundi vingi vya vijana vimefanikiwa kukuza vipato vyao kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, usindikaji wa mazao na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo. Aidha, shughuli hizo zimefanya vijana waachane na utegemezi na badala yake kutumia muda wao mwingi katika uzalishaji na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vikundi vya mfano ambavyo kupitia mfuko huu vimekuwa kielelezo cha dhati katika kubadili mtazamo wa vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi kujiajiri wenyewe na kukuza vipato vyao. Vikundi hivyo ni pamoja na THYROID Group kutoka Halmashauri ya Chunya kinachosambaza taa za solar vijijini, MIRANACO Group kinachomiliki duka kubwa la dawa za binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi, Maswa family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu Milk kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha uendeshaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathmini mbalimbali mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kubaini changamoto za kiutendaji zinazojitokeza. Katika mwaka huu wa fedha, Serikali inapitia upya muongozo wa utoaji fedha kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana wa mwaka 2013 ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kuanzisha viwanda vidogo katika kuendana na sera ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
MHE. PETER J. SERUKAMBA (K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-
Shule za Sekondari za Umma zimeendelea kufanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne na sita, ambapo kwa mwaka 2015 katika matokeo ya kidato cha nne watahiniwa waliopata daraja la nne ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 na waliopata daraja la sifuri ni 113,489 sawa na asilimia 32.09:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika Shule za Umma za Sekondari nchini ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya madarasa, mabweni na maabara?
(b) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifuta
kazi Bodi ya Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuiunda upya kutokana na kushindwa kusimamia ubora wa elimu nchini ambayo ni moja ya jukumu lake?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifufua zilizokuwa shule za vipaji maalum za Ilboru, Kilakala, Mzumbe na Kibaha zilizowahi kufanya vizuri miaka ya 1990?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II) Serikali imekamilisha uboreshaji wa Shule za Sekondari 792 kwa kukarabati miundombinu na kuweka samani; shule 264 ziliboreshwa katika awamu ya kwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 56; na shule 540 katika awamu ya pili kwa gharama ya shilingi bilioni 67.8 na zote zimekamilika. Ukamilishaji wa ujenzi wa shule hizo, umesaidia katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia katika Shule za Sekondari za Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ubora wa elimu linajumuisha mambo mengi ambayo yanahusisha kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia jambo ambalo linatekelezwa kupitia mipango na bajeti kila mwaka. Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inasimamia udhibiti wa ubora wa elimu ikishirikiana na taasisi nyingine zinazotekeleza Sera ya Elimu Tanzania. Kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha elimu nchini, hatuoni sababu ya kuvunja Bodi hiyo, badala yake tutaendelea kuiwezesha kutekeleza majukumu yake vizuri zaidi kwa kushirikiana na taasisi nyingine.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea
na ukarabati wa shule kongwe zote 89 nchini zikiwemo Ilboru, Kilakala, Mzumbe na Kibaha. Mwaka wa fedha 2013/2014 Serikali ilitoa shilingi bilioni 12.8 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule kongwe na shilingi bilioni 3.5 zilitolewa na kutumika kukarabati shule saba za ufundi za Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma, Bwiru Boys na Ifunda. Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) itakarabati shule kongwe 11 zikiwemo za vipaji maalum za Mzumbe, Ilboru, Kilakala, Tabora Boys, Tabora Girls, Pugu, Nganza, Mwenge, Same na Msalato.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
(i) Je, Serikali ina mkakati gani mahususi katika kuboresha mazingira ya kujifunza katika shule za umma za sekondari nchi nzima ikiwa ni pamoja na ukarabati wa majengo, madarasa, mabweni na maabara?
(ii) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifuta kazi Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuiunda upya kwa sababu imeshindwa kusimamia ubora wa elimu nchini?
(iii) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifufua shule zilizokuwa za watoto wenye vipaji maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), refu sana, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule za umma za sekondari nchini. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II) ulianza kutekelezwa mwaka 2004 hadi mwezi Disemba 2016, jumla ya shule za sekondari 792 zimejengwa na kukarabatiwa miundombinu yake na kuwa shule kamili kwa gharama za shilingi bilioni 123.8.
Aidha, katika kipindi hicho jumla ya maabara 6,287 sawa na asilimia 60.52 ya lengo zimekamilika kati ya maabara 10,387 zilizohitajika. Kupitia Mpango wa Lipa kwa Matokeo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 21.9 zimeidhinishwa kwa ajili ya upanuzi wa shule 85 za sekondari na shule 19 za msingi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya vyumba vya madarasa 320, mabweni 155 yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila moja na matundu ya vyoo 829 yatajengwa.
(b) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Elimu Tanzania huchangia katika kukuza ubora wa elimu nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi chuo kikuu. Changamoto iliyopo ni upatikanaji wa fedha za kutosha kuwezesha kutekeleza miradi mingi zaidi kama inavyotarajiwa na wananchi katika maeneo mengi nchini.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuzikarabati shule kongwe 89 zikiwemo shule nane za wanafunzi wenye vipaji maalum kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). Mradi huu utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni 89 hadi kukamilika unatekelezwa kwa awamu. Hadi kufikia Julai, 2017 jumla ya shule kongwe 43 zimekarabatiwa na shule 20 zitakarabatiwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kupiga marufuku uingizwaji wa nyama kutoka nchi za nje ili kuruhusu ukuaji wa viwanda vya nyama nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika baada ya Ethiopia. Aidha kumekuwepo na uingizaji wa nyama ya ng’ombe, nguruwe na kondoo kwa wastani wa tani 2,000 kwa mwaka kuanzia mwaka 2013 hadi 2015. Hata hivyo kiasi hicho kimepungua kuanzia mwaka 2016 tani 1,182.79 na mwaka 2017/2018 tani 1,225 kutokana na kuwepo kwa machinjio na viwanda 23 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 44,820.6 za nyama na bidhaa zake kwa mwaka zenye ubora linganifu na nyama inayotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2016/2017 jumla ya nyama tani 2,608.93 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 5,679,217.28 iliuzwa katika nchi za Oman, China, Hong Kong, Dubai na Vietnam. Vilevile idadi ya machinjio nchini kwa sasa ni 1,632 na yana uwezo wa kuchinja nyama kiasi cha tani 625,992 kwa mwaka.
Pia masoko ya nyama inayozalishwa ndani ya nchi yameongezeka ambapo inauzwa katika hoteli za kitalii, maduka maalum (super markets) na migodi yote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inafanya tathmini ya kina kuhusu biashara ya mifugo na mazao yake ili kujua kwa uhakika kiasi cha nyama kinachoingizwa nchini, masoko na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha nyama na mazao yenye ubora na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha, kuchakata na kusindika nyama na bidhaa zake zenye viwango na ubora unaokubalika. Pia, imeweka mapendekezo ya kuongeza tozo ya uingizaji wa nyama na bidhaa zake ili kuleta ushindani wa haki katika soko la ndani utakaowezesha kukua kwa viwanda vya ndani, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa uingizaji wa nyama kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba wizara inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kuufanyia kazi na kwa kuzingatia matokeo ya tathmini tunayoendelea hivi sasa.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunikumbusha, naomba isomeke dola za kimarekani 5,679,217.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Charles Kitwanga alikaririwa na vyombo vya habari mwezi Desemba, 2015, akiliagiza Jeshi la Polisi kumkabidhi majina ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ambazo ongezeko lake nchini lina athari hasi dhidi ya vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa:-
(a) Je, ni hatua gani zimechukuliwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani katika kuwabaini, kuwachunguza na hatimaye kuwafikisha Mahakamani wale wote waliobainika kujihusisha na mtandao wa biashara za dawa za kulevya?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wanaojiingiza kwenye dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya nchini?
(c) Je, ni vijana wangapi kwa nchi nzima ambao kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita wamepatiwa tiba kusaidiwa kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athumani Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kati ya Oktoba, 2015 hadi Aprili, 2017 Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 9,140 wa dawa za kulevya ambapo watuhumiwa 14,410 kesi zao zinaendelea Mahakamani na zipo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 2,401 walikutwa na hatia, watuhumiwa 615 waliachiwa huru na watuhumiwa wengine 13,071 kesi zao ziko chini ya upelelezi.
(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kupitia Programu ya kuzuia uhalifu limeendelea kutoa huduma ya urekebishaji kwa waaathirika wa dawa za kulevya. Kwa kutumia vikundi mbalimbali vya michezo chini ya miradi ya kuzuia uhalifu kama vile familia yangu haina mhalifu na klabu ya usalama wetu kwanza.
(c) Mheshimiwa Spika, vijana 3,000 walipatiwa tiba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa kushirikiana na wadau.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Vijana wengi wanakosa sifa za kuajiriwa kwa kukosa uzoefu kazini.
Je, Serikali haioni haja ya kutungwa kwa Sera ya Mafunzo kwa Vitendo Kazini kwa wahitimu wa elimu ya juu na vyuo vya ufundi (Internship Policy for Higher Learning Institutions and Technical Colleges Graduates) ili vijana waweze kupata ujuzi utakaoendana na mahitaji ya soko la ajira?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha pengo la ujuzi (skills mismatch) kati ya ujuzi walinao wahitimu na ule unaohitajika katika soko la ajira unazibwa. Ni kweli Serikali imeona kuna haja ya kuwa na miongozo ya kisera kama alivyoshauri Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba ambapo kupitia ofisi yangu tumeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu (National Internship Guidelines). Mwongozo huu unasaidia wadau kuandaa, kutekeleza, kusimamia na kuratibu mafunzo ya uzoefu kazini kwa wahitimu. Mwongozo huu ulizinduliwa mwezi Septemba, 2017 na kuanza kutumika rasmi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 zaidi ya nafasi 750 zimetolea na waajiri mbalimbali kuwezesha wahitimu kufanya mafunzo kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, kufanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili kuendana na mahitaji ya sasa. Sera mpya pamoja na mkakati wa utekelezaji wake ipo katika hatua za mwisho ambapo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2018. Miongoni mwa matamko mahsusi ya sera hii ni pamoja na kusisitiza kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu wa vyuo. Baada ya kupitishwa sera hii, suala la mafunzo ya vitendo kazini kwa wahitimu litawekwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa programu ya mafunzo kazini kwa wahitimu kwa kutoa fursa kwa vijana wahitimu kujifunza katika maeneo yao ya kazi.