Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Zainab Athuman Katimba (260 total)

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza nashukuru Serikali kwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya kumalizia bwalo hili la Shule ya Malagarasi, hata hivyo, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; shule hii imeanza mwaka 1995 baada ya wananchi kujenga madarasa sita, madarasa haya hayajawahi kufanyiwa ukarabati. Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kukarabati madarasa ya shule hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; shule hii ina zaidi ya wanafunzi 1,240 ikiwa ni kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita na wanafunzi takribani 418 wa kidato cha sita hawana mabweni. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni angalau mawili kwa ajili ya mabinti wetu katika shule hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyowapambania wananchi wake. Swali lake la kwanza, kuhusu ukarabati wa madarasa chakavu, napenda Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba Serikali inatambua uwepo wa shule chakavu za msingi na sekondari na ndio maana Serikali tayari imeshaanza ukarabati wa shule hizo kupitia miradi ya EP4R, SEQUIP na BOOST. Serikali kwa kutambua uhitaji na kwa kadri fedha zitakapokuwa zikipatikana, Serikali inakusudia kuja kufanya marekebisho katika shule yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, ambapo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuhusu ujenzi wa mabweni na hasa kwa wasichana. Mheshimiwa Mbunge naomba ufahamu Serikali inatambua kwamba kuna umuhimu wa kupata mabweni na hasa kwa watoto wa kike na ndio maana Serikali ilianza ujenzi wa shule za sekondari za bweni za wasichana katika kila mkoa kupitia Mradi wa SEQUIP. Kwa hiyo, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na mabweni na hasa kwa watoto wa kike Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja fupi. Shule ya Msingi Igumila madarasa yake mawili yamebomoka na Naibu Waziri Utumishi alipopita pale alituahidi kutupa madarasa mawili. Je, ni lini fedha hizo zitapelekwa ili turejeshe hayo madarasa mawili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge kutambua uhitaji wa madarasa katika Shule ya Msingi Igumila, Serikali inaendelea kuangalia vipaumbele na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itafanya jitahada kwa kadri fedha zinavyopatikana iweze kujenga madarasa haya. Ahsante
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; shule hii ilitembelewa na Mheshimiwa Rais wakati akiwa Makamu wa Rais na kuahidi kuipandisha hadhi mbele ya wadau na wadau hao tayari wameshakamilisha ujenzi wa madarasa. Je, Serikali wakati inaendelea kutafuta fedha haioni sababu ya kuwaomba wadau hao hao kukamilisha ujenzi wa mabweni ili shule hiyo iweze kuanza kwa sababu wako wadau ambao tayari wamejenga madarasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Shule ya Sekondari Ilula iliyotajwa kama yenye kidato cha tano na sita, mabweni yake yametitia kutokana na mvua na kuwa hatarishi kwa watoto wanaosoma pale. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea hali hiyo na kuchukua hatua za dharura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa natambua jitihada anazozifanya Mheshimiwa Mbunge kuwapigania wananchi wake. Kuhusu swali lake la kwanza ambapo anasema Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ujenzi wa mabweni basi na yeye ameweza kutoa maoni kwamba Serikali itazame namna ya kushirikiana na wadau katika kukamilisha mabweni hayo. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge mawazo yake ni mazuri na Serikali imeyapokea na tutayachakata na kufanya mawasiliano na wadau ili tuone kwamba kwa pamoja Serikali na wadau tunaweza kujenga mabweni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu bweni kuzama na nipo tayari kuambatana naye kwenda kuona hali halisi na kuchukua hatua za dharura. Nakubali Mheshimiwa Mbunge kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, ahsante
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Lukoto iliyoko katika Wilaya ya Rungwe ukizingatia sekondari hiyo imezungukwa na kata ambazo na zenyewe zina uhitaji wa shule hiyo na kata zenyewe ni Kata ya Ikuti, Kimo, Masukuru, Bagamoyo, Suma na Sheli ya Masukuru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rungwe aweze kwenda kufanya tathmini katika shule aliyoitaja Mbunge ili kutazama miundombinu na kuweza kuona kama miundombinu inakidhi vigezo vya kupata usajili wa kidato cha tano na sita. Baada ya kukamilisha tathmini hiyo waweze kuwasilisha maombi katika Wizara ya Elimu kwa ajili ya taratibu za kupata usajili wa kidato cha tano na sita. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwanza kabisa nipongeze majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na taulo za kike. Pamoja na kwamba Serikali zinatenga hizo fedha halmashauri, lakini bado kuna malalamiko makubwa sana katika shule zetu. Je, utaratibu gani unatumika kuhakikisha kwamba hizi fedha zinatengwa na hizi taulo zinawafikia wadau wanaotakiwa kupatiwa fedha hizi kwa sababu siku zote ukienda katika shule zote huoni kabisa taulo za kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuhusiana na swali la Mheshimiwa Mbunge, nataka kumhakikishia kwamba, fedha hizi zinatoka. Nachukua nafasi hii kuwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri kusimamia kwa umakini zoezi hili, ili fedha hizi zinazotengwa kwa ajili ya kupata taulo za kike ziweze kusimamiwa kwa ufanisi na kuleta tija. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ni nini mkakati wa Serikali wa kupunguza kodi kwa malighafi ambazo zinatumika kutengeneza taulo za kike, ili taulo hizi sasa ziweze kutengenezwa shuleni kwa kupitia somo la maarifa ya jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea mawazo mazuri ya Mheshimiwa Mbunge na tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuangalia masuala haya ya kikodi na kuona kinachoweza kufanyika. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la kwanza; kwenye Wilaya ya Mbogwe kuna hizo barabara alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna madaraja ambayo hayapitiki kabisa sasa hivi pamoja na kwamba nashukuru kwa majibu ya Serikali. Je, Serikali ina mpango gani wa kulitengeneza na Daraja la Ikalanga – Ilangale kwa sababu sasa hivi haipitiki na wakulima wamelima mazao mengi ambayo yanatarajiwa kutoka huko?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mpango wa Serikali wa kuunganisha kwa kiwango cha lami wilaya na mkoa. Je, ni lini sasa Serikali itaitimiza ahadi hii ili kuunganisha Wilaya ya Mbogwe na Geita kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge, naomba nitumie nafasi hii kumwagiza Meneja wa TARURA katika Wilaya ya Mbogwe ili aweze kwenda kufanya tathmini na kubaini kwamba barabara hiyo inahitaji kupatiwa fedha za dharura kwa ajili ya kuirekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kuunganisha wilaya na mkoa, tutaendelea kufanya tathmini na kuzingatia uhitaji na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Mwakibete, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha hizo kwa ajili ya kujenga daraja hili, lakini kutenga ni jambo lingine, kuanza ujenzi ni jambo lingine. Je, lini ujenzi utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga kuna daraja kama hilo kutoka upande wa Isupilo kwenda Itimbo kufupisha njia ya watu wanaokwenda Iringa na kusafirisha mazao ya misitu. Je, Serikali iko tayari wakati ujao kututengea fedha ili na sisi tujenge daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza ni kwamba, fedha imetengwa na dhamira ya Serikali ni kutekeleza miradi kwa kadiri bajeti inavyokuwa imetengwa. Kwa hiyo kwa kadiri fedha itakapokuwa inapatikana daraja hili litajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kuhusiana na daraja katika jimbo lake. Nimwambie pia kazi kubwa ya TARURA ni kufuatilia na kuangalia sehemu zenye mahitaji na kupanga vipaumbele. Kwa hiyo kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na kwa kuzingatia vipaumbele daraja hilo litajengwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa daraja linalounganisha Kata ya Nkilizya na Kata ya Bukongo Jimboni Ukerewe limekuwa ni kilio cha muda mrefu na limekuwa linaathiri sana uchumi wa wananchi wa maeneo haya. Je, ni lini sasa daraja hili litajengwa kupitia Kijiji cha Msozi na Nkilizya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu hii na kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha Serikali itajenga miundombinu hii kwenye jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Nashukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri Daraja hili la Kiteputepu ni daraja ambalo linatumia mbao, linacheza na maji ni mengi sana. Wamesema kwamba wametenga na wataweka bajeti ili waweze kulifanyia kazi. Tunaomba Serikali ifanyie kazi haraka kwa maana wanawake wengi wanazama katika daraja hili pale Ntaba.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napokea maombi ya Mheshimiwa Mbunge, tutayachakata na nitarudisha mrejesho kwake Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali sasa haioni kuwa kuna haja ya kutumia wahitimu waliohitimu ufundi katika Miradi ya Force Account?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali haioni kuwa, kuna haja ya kushirikiana na taasisi za ufundi ili kusimamia miradi ya force account badala ya kutumia watumishi ambao hawana fani hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea mawazo ya Mheshimiwa Mbunge, tutachakata maoni yake na tuone tunaweza vipi kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa miradi hii.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina upungufu wa walimu wa sayansi na hesabu wapatao 83,000 lakini pia ina walimu wa sayansi na hesabu ambao wanajitolea 44 ambao ni takribani 53% ambao wamehakikiwa. Kwa sababu Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 na ukichukua sample ya Tarime Mji ina maana Tanzania nzima wana average zaidi ya walimu hao wanaojitolea ni zaidi ya 50%, sasa kwa nini Serikali katika hizo ajira 12,000 isitenge 50% kwa ajili ya walimu hao wanaojitolea ili kuendelea kutoa motisha zaidi kwa walimu wengi kuweza kujitolea na kupunguza uhaba wa walimu wa sayansi na hesabu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Shule ya Msingi Magufuli yenye wanafunzi wenye uhitaji maalum iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo ni kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili, ulemavu wa kuona na kusikia, ina upungufu wa walimu 13 ambao ni takribani 53%. Kwa nini Serikali isitoe kipaumbele kwa shule zote maalumu nchini kwa kuwa wote tunatambua ugumu uliopo wa kufundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, kuona na akili? Serikali iweze kutoa kipaumbele na kupeleka walimu toshelezi katika shule hizi (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la walimu wanaojitolea kupewa kipaumbele katika ajira zilizotangazwa za walimu, maoni haya ya Mheshimiwa Mbunge tunayachukua na tutaona namna ya kuyachakata tulishirikiana na wenzetu wa Utumishi ili tuweze kuona ni namna gani nzuri tunazingatia miongozo na taratibu za kiutumishi katika kuajiri walimu hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo amezungumzia uhitaji wa kuajiri walimu wenye uhitaji maalumu, kwa mujibu wa taratibu katika kila ajira zinazokuwa zimetangazwa za walimu angalau asilimia tatu, ni lazima wawe ni walimu wanaofundisha wanafunzi wenye uhitaji maalumu. Mwaka 2023 Mei, ajira za mwisho za walimu tayari waliajiriwa walimu kwa 2.7% kwa sababu kwa kawaida wanaojitokeza huwa hata asilimia tatu hawafiki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watakaojitokeza, walimu watakaoomba nafasi hizo ambao wanakidhi vigezo vya kuwa walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu kwa mujibu wa taratibu watachukuliwa. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo kubwa la walimu, takwimu zilizopo, walimu wa sayansi ni walimu wa somo la physics. Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuhakikisha inaajiri walimu wa somo hilo ukizingatia tunaenda kwenye mafunzo ya amali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na walimu na hasa wanaofundisha masomo ya sayansi na kwa kila ajira zinapotangazwa, Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba inaajiri walimu wa sayansi. Kama tunavyofahamu, tayari zimetangazwa ajira za walimu 12,000. Kwa hiyo, Serikali itazingatia katika kuajiri walimu hao 12,000 wapatikane walimu wa sayansi na hasa wa somo la fizikia kama aliyotaja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Simiyu kuna upungufu wa walimu zaidi ya 6,000 katika shule za sekondari na za msingi: Je, ni lini Serikali italeta walimu wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutetea wananchi wake na kutetea na wanafunzi waliopo katika eneo lake la utawala. Aidha, Serikali tayari imeshatangaza ajira 12,000 kwa sababu inatambua upungufu wa walimu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi za walimu 12,000 jimbo lake la lenyewe litatizamwa kwa kipaumbele. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ipo tayari kuainisha aina ya michango hiyo ambayo imeruhusiwa kuombewa kibali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule kuwaruhusu wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuchangia michango hiyo kwa wakati? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 umeeleza na umeweka utaratibu wa kuzingatiwa ili kuweza kupata kibali kwa ajili ya kuwepo kwa michango katika shule za msingi lakini katika shule za sekondari iwapo kuna uhitaji na katika waraka huo ni lazima kupata kibali cha Mkuu wa Wilaya, lakini michango hii ambayo tunaizungumzia hapa inaweza ikawa ni ile michango ambayo wazazi wenyewe kupitia mikutano ya wazazi na kamati za shule wanakubaliana, kwa mfano wanaweza wakasema wanataka wanafunzi wawe wanavipindi vya ziada, kwa hiyo wanakubaliana kutoa michango ya aina fulani, lakini michango mingine ni hii ambayo inafahamika ambayo ni michango ya uendeshaji wa shule ambayo kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi ukomo umewekwa kwa shule za bweni kidato cha tano ni shilingi 80,000 na kwa shule za kutwa ni shilingi 50,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba niendelee kusisitiza maagizo ambayo yametolewa huko awali kwamba Maafisa Elimu wa Mikoa, wa Wilaya, wa Kata, Wakuu wa Shule hawaruhusiwi kukataa kuwapokea wanafunzi kwa sababu tu wamekosa pesa za michango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nisisitize hilo kwa sababu ni maelekezo ambayo tayari yalishatolewa, mwanafunzi asikataliwe kupokelewa shuleni kwa sababu amekosa pesa ya michango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue nafasi hii kutoa wito kwa wazazi wa wanafunzi wa kidato cha tano wale waliyochaguliwa kuingia kidato cha tano waweze kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao shule hata kama hawajakamilisha michango au kuwa na sare, ni muhimu sana watoto wanapochaguliwa kwenda kidato cha tano waweze kwenda shuleni kuripoti. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa madarasa mengi na nyumba za walimu nyingi zilizopo sasa hivi zilijengwa wakati wa mpango huu mkubwa wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na kwa kuwa kiasi kinachotengwa sasa hivi kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya ukarabati na ukamilishaji wa maboma ni kidogo; je, Serikali haioni haja ya kutafuta fedha nyingi ili madarasa haya ambayo yamechakaa yaweze kukarabatiwa kwa kiasi kikubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mpango huu wa MMEM ulihusisha na uboreshaji na uendeshaji wa vituo vya walimu (TRCs). Je, Serikali inampango gani wa kuendeleza vituo hivi ili walimu waweze kupata mafunzo kazini wakiwa katika maeneo yao ya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifanya kazi kubwa sana ya kufuatilia maslahi ya wananchi wake na hususani kwenye masuala pia ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ambayo katika mwaka wa fedha 2022/2023 – 2023/2024 Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 70.39 kwa ajili ya ukarabati wa shule 793 lakini kupitia miradi ya elimu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI miradi kutoka Wizarani, Serikali inatenga na imekuwa ikitoa fedha nyingi sana kwa ajili ya ukarabati wa shule zetu hizi kongwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya shule hizi au ujenzi wa madarasa mapya unalenga kupunguza umbali wa wanafunzi kusafiri ili kufika mashuleni, lakini pia unalenga kupunguza msongamano.

Kwa hiyo, Serikali inaendelea kupitia mradi wa BOOST kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaendelea kukarabati shule kongwe, lakini kujenga madarasa mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu vituo vya walimu naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia mradi wa GPETSP, mradi huu ambao upo kwenye awamu ya tatu umepanga kujenga vituo vya walimu 300 lakini mpaka hivi tunavyozungumza tayari kuna vituo vya walimu 252. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kutekeleza mradi huu na kuendelea kujenga vituo hivi muhimu vya walimu. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Sekondari Ngonga iliyopo Wilayani Kyela imejengwa tangu mwaka 2007 mpaka sasa haina nyumba hata moja ya walimu; sasa je, Serikali ni lini itajenga nyumba za walimu kwenye shule hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mradi wa GPETSP nilioutaja hivi punde, mradi huu pia unalenga katika kujenga nyumba za walimu, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina mkakati na imetengeneza mipango ya kuhakikisha inaendelea kujenga nyumba za walimu katika maeneo mbalimbali nchini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itakuja kufika ijenge nyumba za walimu katika shule aliyoitaja ya Ngonga. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ipo tayari kuweka wazi mpango mkakati wa ukarabati shule kongwe zilizochakaa sana kwenye Wilaya ya Moshi Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imepanga kufanya ukarabati wa shule kongwe 50, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaweka katika kipaumbele ombi lake la kurekebishiwa au kufanyiwa marekebisho katika shule kongwe aliyoitaja katika jimbo lake.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kutambua changamoto za kijiografia ambazo zimekuwa zinaathiri utendaji na kupata wakandarasi bora kwenye maeneo ya pembezoni kama Ukerewe, mwaka jana Serikali iliniahidi kutupatia vifaa vya ujenzi kama magreda na kadhalika kwa ajili ya kuondoa changamoto hiyo. Nataka kujua na Wakerewe wanataka kujua hatua ipi imefikiwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa pesa za mafuta kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji kwa TARURA zinapelekwa mkoani jambo ambalo limekuwa linaathiri wahandisi wilayani kufuatilia hasa inapotokea dharura. Ni upi sasa mkakati wa Serikali kufanya marekebisho ya utaratibu huu? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilitoa ahadi ya kupeleka magreda na vifaa mbalimbali vya ujenzi wa miundombinu ya barabara na ahadi hii mpaka sasa bado haijatekelezwa. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa vifaa hivi katika jimbo lake na inafanya taratibu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kununua vifaa hivyo ili viweze kupelekwa. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itatekeleza ahadi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua changamoto aliyoiainisha Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na upatikanaji wa fedha kwa wakati kwa ajili ya TARURA kuweza kutoa huduma zake kwa dharura. Kwa muktadha wa suala hili analozungumza Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa fedha za TARURA kutoka Serikali Kuu lakini kutoka katika Serikali ya Mkoa zinapatikana kwa wakati ili kuweza kutimiza mahitaji ya ujenzi wa barabara kwa dharura. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni kuongeza milioni 500 kuwa bilioni moja katika Barabara za TARURA, je, ni lini fedha hizo zitatoka?

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa barabara nyingi zimekatika kutokana na athari za mvua ikiwemo Chiwale, Masasi Mkoani Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani kupitia TARURA wa kuhakikisha barabara hizo zinapitika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kweli kuongeza bajeti kutoka shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni 1.5 na Serikali ina nia ya kutekeleza ahadi hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itaweza kutimiza ahadi hii na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitalifuatilia suala hili. Tukitoka hapa tunaweza tukakutana tukazungumza ili kujua mustakabali wa masuala ya wananchi wa Geita Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, Serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha na hivi sasa bajeti ya TARURA imetoka shilingi bilioni 272 na imeongezwa mpaka shilingi bilioni 710. Ni ongezeko kubwa, lakini tunatambua kwamba bado kuna mahitaji zaidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri pesa zinavyopatikana Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi za TARURA na hasa kwa sababu zinagusa ustawi wa wananchi lakini pia zinagusa ustawi wa uchumi. Kwa hiyo, kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana Serikali ina nia ya kuhakikisha barabara hizi zinajengwa na zinafanyiwa ukarabati. Ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; hii Kata ya Ngima wananchi kwa kushirikiana na mimi Mbunge tumejenga tayari madarasa manne. Je, Serikali iko tayari kutenga fedha japo kidogo kukamilisha madarasa haya ili yaweze kutumika mwakani Januari?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wa Kata ya Matiri pamoja na Kata ya Nguzo nao wamejenga Shule ya Sekondari Nguzo pamoja na Benaya Sekondari hazina miundombinu ya kutosha. Je, Serikali iko tayari kupeleka fedha kukamilisha miundombinu ya shule hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali ina nia ya kuendelea kuboresha miundombinu ya shule na hivyo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha Serikali itaweza kujenga madarasa hayo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, Serikali inatambua jitihada ambazo zimefanywa na wananchi wa Mbinga DC za kujenga Shule ya Sekondari ya Benaya na Nguzo na shule hizo tayari zimeshasajiliwa na zina wanafunzi mpaka kidato cha pili. Kwa kuzingatia miundombinu ambayo bado haijakamilika katika shule hizo, Serikali kupitia bajeti ya halmashauri ya 2024/2025 imepanga kutumia shilingi milioni 62.5 kwa ajili ya shule hizo. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya ukamilishwaji wa miundombinu ya shule hizo ili kuongeza fedha kulingana na upatikanaji wake kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule hizo unakamilishwa na kuunga mkono jitihada za wananchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni lini Serikali itapeleka gari la usimamizi wa huduma katika Halmashauri ya Uyui ambayo ina majimbo mawili Tabora Kaskazini na Igalula?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na jiografia kati ya vituo hivi vya afya, mfumo wa kutumia gari moja la Kaskedi hautofanya kazi vizuri, je, ni lini Serikali itapanga kupeleka magari mawili katika Kituo cha Afya cha Upuge na Kituo cha Afya cha Mabamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, magari 70 yaliyokuwa yamebaki ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za afya tayari yameingia nchini na Serikali inaendelea na utaratibu wa kuyatoa magari haya bandarini na hatua nyingine za usajili wa haya magari. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba magari haya yakitoka, Halmashauri ya Uyui na yenyewe itapata gari moja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba kama Serikali ilivyotenga pesa kununua magari ya kusafirishia wagonjwa na kuweza kuyaleta katika jimbo lake. Nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza magari ya wagonjwa kwa ajili ya kuhudumia katika Vituo vya Afya vya Upuge na Mabamba kama alivyoomba. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Serikali tayari imejenga vituo vitatu vya afya katika Tarafa zilizopo Mbulu Mjini. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia gari la wagonjwa vituo hivi vyote vitatu vya Jimbo la Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu awali kwamba Serikali itahakikisha inatafuta pesa ili iweze kupata magari ya kuhudumia wagonjwa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kadiri fedha itakavyokuwa inapatika na magari haya kununuliwa, basi yanaweza yakaja kuletwa kwenye vituo vya afya ulivyoomba.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, suala la magari linaendana na watumishi wanaohusika kwenye hospitali. Sasa je, ni lini Serikali itapeleka madaktari kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chunya maana hospitali nzima ina madakari wawili na mahitaji ni madkatari nane? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikitoa vibali vya ajira kwa ajili ya ya kuajiri watumishi katika kada ya afya na kila mwaka imekuwa ikiajiri watumishi hawa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa katika mwaka huu wataajiriwa na katika mwaka ujao wa fedha wataendelea kuajiriwa ili waweze kuhudumia katika vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya ya msingi.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuipatia Hospitali ya Wilaya ya Tunduru gari la utawala, je, ni lini Serikali itaipatia gari la wagonjwa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutafuta fedha za kuhakikisha inanunua magari ya kuwahudumia wagonjwa na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ya afya msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba magari haya yakipatikana na yeye ataangaliwa kwa jicho la kipaumbele kwenye jimbo lake.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Kitomanga ni miongoni mwa kituo cha afya ambacho hakina magari. Je, kati ya magari hayo 70 Kitomanga itakuwa ni miongoni mwake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi kwamba magari 70 ndiyo yaliyokuwa yamebaki na tayari mpaka muda huu yamefika na yapo bandarini yanaendelea na taratibu za kutolewa na kufanyiwa usajili. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba na wao watapata gari hili la usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za afya. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mtwango ni kituo cha afya kikubwa sana ambacho kinahudumia Kata ya Kichiwa, Igongolo, Ikuna na Mpakaninga lakini hawana gari la ambulance kwa ajili ya wagonjwa. Ni upi mpango wa Serikali wa kupeleka ambulance Mtwango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya kununua ambulance. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri fedha zitakavyopatikana na magari haya ya kuhudumia wagonjwa yatakaponunuliwa nimhakikishie kwamba Kituo cha Afya cha Mtwango na chenyewe kitapewa mgao wa magari haya.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya ujenzi huo wa ofisi.

Swali la nyongeza, kwa kuwa Serikali ilitoa fedha nyingi sana kwenye ujenzi huo na majibu ambayo nimeyapata ni mazuri, lakini niiombe Serikali kwa sasa bado hali haijawa nzuri kwenye miundombinu ambayo imebakia.

Je, ni lini Serikali mtaikamilisha ile miundombinu kwa sababu kituo kile tayari kimekwishaanza kutumika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeamua kuleta huduma kule chini kwa wananchi, tunayo Kata moja ya Chikongola ambayo ina Kata moja ya Magomeni katika Jimbo la Mtwara mjini ina watu zaidi 29000.

Ni lini Serikali itatuletea kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imefanya tathmini na kubaini kwamba zinahitajika shilingi milioni 883.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la utawala, lakini inahitaji milioni 176 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la hospitali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetengeneza mikakati na ukamilishaji wa majengo hayo yapo katika mpango wa Serikali na Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha inakamilisha majengo haya muhimu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge linahusu uhitaji wa kituo cha afya kuhudumia idadi kubwa ya wananchi 29,000 nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake hili la Mtwara Mjini tayari Serikali imepokea maombi ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati na Mheshimiwa Mbunge na yeye ameleta eneo lake mahsusi ambalo anaona kwamba linahitaji ujenzi wa kituo cha afya na bila shaka eneo hilo kwa kauli ya Mheshimiwa Mbunge ndio hili aliloliombea hapa fedha.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mipango ya upatikanaji wa fedha wa kujenga vituo vya afya vya kimkakati tutazingatia maombi yake ili kituo cha afya kiweze kujengwa.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Bariadi Somanda ni ya kwanza kabisa kujengwa katika Mkoa wa Simiyu lakini haina jengo la ICU, ni lini Serikali itatuletea fedha tujenge jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama vile Serikali ilivyoanza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine katika hospitali hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imetenga fedha katika mwaka wa bajeti 2024/2025 kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi viporo ya hospitali za halmashauri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge fedha itakuja kwa ajili ya kuendelea kukamilisha na ujenzi wa jengo hilo la ICU.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika haina fence kwenye majengo yake. Ni lini Serikali itapeleka fedha kukamilisha ujenzi wa fence ya hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu mkubwa sana wa miundombinu aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia Serikali Kuu, lakini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kunajengwa uzio huo katika hospitali aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ina nyumba moja tu ya daktari, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza nyumba za madaktari ili watumishi hawa wakae karibu na hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa sana wa nyumba za watumishi na hasa katika kada ya afya, Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia Serikali Kuu, lakini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya mapato ya ndani ya halmashauri kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za watumishi ili waweze kuwa karibu na vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi na kuweza kuwahudumia wananchi kwa ukaribu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Myula, Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kuhakikisha vituo vya afya vyote ambavyo Waheshimiwa Wabunge waliorodhesha kwamba ni vituo vya kimkakati vinaweza kujengwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na kama kituo alichokitaja ni kituo cha kimkakati katika eneo analotoka nimhakikishie Serikali itahakikisha inapata fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ahsante ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Vituo vya Afya vya Kharumwa na Nyang’hwale vina uhitaji mkubwa, je, uko tayari kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ili atenge fedha kupitia mapato ya ndani kuweza kujega majengo ya x-ray machine hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, lini Serikali itapeleka mashine ya x-ray katika Manispaa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu D by D yaani ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa inazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa na zenyewe kutafuta mapato na kuweza kuweka katika mipango na bajeti zake kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali na ujenzi wa miundombinu muhimu. Kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na chumba au jengo mahsusi kwa ajili ya matumizi ya mashine hizi za x-ray.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mkurugenzi aweze kuweka katika mipango ya kibajeti na waweze kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga majengo haya ili mashine hizi za x-ray ziweze kuanza kuwanufaisha wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, nimhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 66.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaweka ombi lako katika kipaumbele ili na wewe kituo chako kiweze kupata mashine ya x-ray.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya x-ray katika Vituo vya Afya vya Hirbadau, Mogitu pamoja na Bassotu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 66.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wewe vituo vyako hivi vya afya vitakuwa katika mgao wa manunuzi ya vifaa tiba. Kwa hiyo, utapata mashine hii ya x-ray.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Arusha DC katika Jimbo la Arumeru Magharibi tumeomba x-ray kwa maandishi kupitia Wizara. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka x-ray kwenye hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali imeshatenga bajeti ya vifaa tiba shilingi bilioni 66.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025 nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge maombi yake yamepokelewa na yatachakatwa, na yeye atakuwa kwenye mgao wa manunuzi ya vifaa tiba hivi ikiwemo hiyo x-ray machine.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, vituo vyote sita vya afya katika Wilaya ya Kilwa havina mashine za x-ray. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka mashine za x-ray katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kadiri ya fedha itakapokuwa imepatikana na kwa kuzingatia bajeti iliyopangwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itaanza kununua vifaa tiba mbalimbali ikiwemo mashine za x-ray. Kwa hiyo, wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaangalia na itaona vipaumbele, lakini itaweza kununua vifaa tiba na yeye atakuwa kwenye mgao.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, ni lini Serikali itapeleka x-ray machine katika Kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA, RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali tayari imeshatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kwa kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 itanunua vifaa tiba, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumepokea maombi yake kwa ajili ya kuona ni namna gani tunaweza tukanunua vifaa tiba ikiwemo hiyo x-ray machine aliyoiomba.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wana utaalamu wa kuanzisha vikundi na kuvisimamia kwa nini wasibaki huko kwenye kusimamia vikundi tu?

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna Maafisa Masoko na Biashara ambao wako kwenye halmashauri na wana utaalamu wa mikopo kwa nini hawa wasisimamie mikopo na kutoa mikopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, vikundi vyetu hivi vinavyoundwa katika halmashauri vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu havijishughulishi na biashara peke yake, lakini vinajishughulisha na shughuli nyingine za miradi kama ya kilimo, ufugaji, utoaji wa huduma za afya, habari na teknolojia. Kwa hiyo hawa maafisa maendeleo ya jamii kazi yao kimsingi ni uratibu na wanashirikiana na wataalamu katika kila sekta wakiwemo hao maafisa biashara, wakiwemo maafisa kilimo, maafisa mifugo, wataalamu wa afya na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii ni maafisa mahususi kabisa kwa ajili ya kufanya hii kazi, lakini zaidi ya hapo pia umuhimu wa kuwatumia hawa maafisa maendeleo ya jamii ni kwa sababu wapo pia katika kila kata yaani muundo wao wapo katika kila kata na hivi vikundi vinavyoundwa vipo katika ngazi ya kata na vijiji, lakini ukiangalia maafisa biashara wenyewe muundo wao unaanzia katika ngazi ya halmashauri. Kwa hiyo, tafsiri yake hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wanakuwa ni maafisa bora zaidi na mahsusi kwa ajili ya kufanya uratibu kwa kushirikiana na wataalamu kwa ajili ya kufanya kazi ya vikundi hivi.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi hasa kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo pembezoni, je, lini Serikali itatuongeza watumishi ili kuweza kupunguza kero hii ya watumishi iliyopo sasa hivi katika vituo vyetu na zahanati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sera ya afya imeweka wazi kwamba kila kijiji lazima kiwe na zahanati na kila kata lazima kuwe na kituo cha afya. Mimi pamoja na wananchi wangu wa Mvomero tumeshajenga maboma zaidi ya kumi, je, lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya kumalizia haya maboma ambayo tumejenga wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa watumishi wa kada ya afya katika kuhakikisha huduma bora inawafikia wananchi katika vituo vya kutoa huduma ya afya msingi, tayari Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuajiri watumishi wa kada ya afya na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali iliajiri watumishi wa kada ya afya 33, mwaka 2022/2023 Serikali iliajiri watumishi wa kada ya afya 36 na mwaka 2023/2024 Serikali imeajiri watumishi wa kada ya afya 48 katika Jimbo la Mvomero.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaajiri na kunakuwa na watumishi wa kada ya afya ili waweze kutoa huduma zilizo bora katika vituo vyetu vya kutolea afya msingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo anaeleza kwamba ameweza kuwashirikisha wanchi wake katika kujenga maboma ya zahanati, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali inatambua jitihada kubwa ambayo imefanyika katika ujenzi wa maboma haya na tayari Serikali imefanya tathmini na kubaini kwamba kuna maboma ya zahanati 1,265 ambayo yatahitaji jumla ya shilingi bilioni 75.9 kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeweka mikakati ya kutafuta na kupata fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za wananchi. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali ipo kazini na itahakikisha inatafute fedha ili kujenga maboma hayo uliyoyataja ambayo yako katika jimbo lako.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Kata ya Ilangu ni kata ya kimkakati, je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Ilangu Wilayani Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kutumia mwongozo na maoni ya Waheshimiwa Wabunge Serikali tayari ilishaainisha vituo vya afya vya kimkakati vya kujenga katika kila jimbo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kituo hiki alichokitaja katika Kata ya Ilangu ni miongoni mwa vile vituo vya afya vilivyoainishwa vya kimkakati nimhakikishie Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaenga vituo vya afya hivyo vya kimkakati.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni lini Serikali itamalizia majengo ya zahanati katika Kijiji cha Iyayi, Uhominyi Nyawegete, Kitoho na Winome ambayo tayari yameshapauliwa na yako katika hatua za umaliziaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu sana wa huduma ya afya msingi na imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inajenga miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma hii ya afya msingi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutafuta fedha ili iweze kukamilisha miradi ambayo tayari imeanza ikiwemo mradi alioutaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kabwe kimekuwa kinatolewa kauli tofautitofauti juu ya umaliziaji wake, leo nataka kusikia kwa mara ya mwisho, ni lini mtakamilisha kituo hiki ili kianze kufanya kazi?

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani kinaitwa nini ili siku nyingine ukiuliza tukukumbushe ulisema leo ni mara ya mwisho.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kabwe, leo ni mara ya kumi nauliza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ilishakusanya vituo vya afya vya kimkakati vya kujengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 bila shaka Mheshimiwa Mbunge ulileta kituo hiki kukiombea fedha kujengwa katika mwaka wa fedha huu. Nikuhakikishie Serikali inatafuta fedha kuhakikisha kwamba vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo yote vinajengwa na kama hiki kituo ni kituo ambacho wewe ulikileta kwamba ni kituo cha kimkakati nikuhakikishie Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona, Kituo cha Afya cha Mji Mdogo wa Makongolosi kimekamilika na kimeanza kutoa huduma, lakini hakina nyumba za madaktari. Chama Cha Mapinduzi Kata ya Bwawani Makongolosi wameanzisha ujenzi wa nyumba za madaktari.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili nyumba hizi za madaktari ziweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuwapongeza wananchi kwa kushirikiana pamoja kuhakikisha kwamba wanaunga mkono jitihada za maendeleo na kwa kuanza ujenzi wa miundombinu hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama vile ambavyo Serikali imekuwa ikiunga mkono jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu na hasa katika sekta ya afya na kuunga mkono tafsiri yake ni kupitia miradi kutoka Serikali Kuu, lakini pia kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, nikuhakikishie Serikali kwa utaratibu huo huo itaendelea kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana kwa ajili ya kuunga mkono miradi ambayo inaenda kugusa miundombinu muhimu ya afya.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Halmashauri hii ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa kweli ina changamoto kubwa sana. Mfano, hapa ninapozungumza kuna baadhi ya shule ina mwalimu mmoja tu wa chemistry, kuna baadhi ya shule ina mwalimu mmoja tu wa physics...

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba wakati umefika, katika huu mgao wa walimu, Halmashauri hii ya Mtwara Mikindani ikapewa kipaumbele zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nakwenda kwenye Halmashauri yangu ya Nanyumbu. Katika halmashauri hii, hali ndiyo mbaya zaidi ya huko. Hapa ninapozungumza, hata ufaulu wa wanafunzi ni mbaya. Mfano katika mitihani iliyopita kati ya wanafunzi 998 ni wanafunzi 19% tu ndiyo waliofaulu masomo ya sayansi. Je, Serikali haioni haja sasa kwa hii Mikoa ya Kusini ikapewa kipaumbele kupatiwa walimu wa sayansi ili vijana nao wapate haki ya kusoma masomo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu mkubwa wa walimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, mwaka huu Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000. Sasa katika mgao huo, Serikali itaweka jicho la kipekee katika jimbo hili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba walimu hao wanaweza kupatikana ili kupunguza upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa kuwa na walimu na hasa walimu wa masomo ya sayansi na kwa sababu Serikali tayari inaajiri walimu 12,000, kwa hiyo, itaangalia jimbo lako kwa jicho la pekee ili kuona kwamba walimu wanapatikana ili kupunguza ukali wa upungufu kwenye jimbo lako. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Zipo halmashauri ambazo zina uwezo wa mapato na zina uwezo wa kuajiri walimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kugatua suala la ajira ya walimu liende kwenye halmashauri ambazo wanaweza wakaajiri na wakaweza kuwalipa walimu badala ya kusubiri mgao wa kitaifa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na mambo mengine inasimamia suala la ugatuzi kwa maana ya D by D na inapenda sana kuona halmashauri zinaweza kuwa na uwezo na ubunifu wa kutengeneza mapato makubwa ya ndani na kuweza kujiendesha zenyewe. Kwa hiyo, mawazo ya Mheshimiwa Mbunge ni mawazo mazuri, tunayachukua sisi kama Serikali, tutayachakata na tunaamini kwamba yataweza kutekelezeka.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Jina langu ni Kikoyo siyo Chikoyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kikoyo.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza. Wilaya ya Muleba tumejenga zaidi ya shule 30 mpya, lakini walimu wamebaki wale wale. Serikali ina mpango gani mahususi kwa Wilaya ya Muleba kutupatia walimu wa ziada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kumekuwa na shule nyingi mpya ambazo zimejengwa ambazo zina uhitaji mkubwa wa walimu. Tayari Serikali imeanza mikakati mbalimbali ikiwemo kufanya msawazo wa walimu kutoka kwenye shule zile za zamani kuwahamishia kwenye shule hizi mpya. Pia Serikali inatumia njia ya kuajiri walimu ili kufidia upungufu katika maeneo ya shule hizi mpya na hata zile shule za zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali itaendelea na mikakati hii ili kuhakikisha shule zote zinazojengwa zinaweza kupata walimu ili wanafunzi waweze kupata elimu iliyo bora.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hii fursa. Shule ya Sekondari Indoombo ina walimu watano tu. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha ili kukidhi uwiano unaokubalika kitaifa na kimataifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu mwaka huu tuna ajira mpya za walimu, kwa hiyo, katika mgao ule tutaangalia kipekee pia kwenye jimbo lake naye aweze kupata mgao wa walimu hao.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imeanza kupeleka maabara za kompyuta kwenye shule zetu za sekondari nchini: Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa wale walimu wanajengewa uwezo ili kompyuta hizi ziweze kufanya vizuri zaidi na wanafunzi waweze kupata uelewa wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba pamoja na ujenzi wa miundombinu na kupatikana kwa vifaa mbalimbali muhimu katika elimu, pia itawajengea uwezo walimu wake ambao wote wanatoa huduma kwa wanafunzi. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha hilo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa masomo ya sayansi katika Mkoa wa Rukwa hususan Shule ya Sekondari ya Mazwi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Serikali katika mwaka huu wa fedha itaajiri walimu 12,000, kwa hiyo katika mgao wa walimu hawa Serikali itaweka jicho la kipaumbele na la kipekee kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo katika shule zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo wa kuweka zege kwenye barabara za milimani kwa sababu wanapoweka vifusi pindi mvua inaponyesha barabara zile zinazolewa na tunatia hasara Serikali na wananchi wanashindwa kupita, hata hivyo na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Barabara za Msanga – Chome – Ikokoa – Makanya – Tae – Suji na Barabara ya Kisiwani hadi Msindo zina maeneo makorofi mengi sana, je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutenga bajeti ya kutosha kusudi barabara hizi zitengenezwe kwa kiwango cha zege ili tuweze ku-save hela za Serikali zinazotokana kumwaga vifusi ambavyo vinazolewa na mvua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini yuko tayari kutembelea Jimbo hili na kuziona hizi Barabara za Chome, Barabara za Makanya – Tae pamoja na Kisiwani – Msindo ili aweze kuona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutetea wananchi wake. Kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ameuliza baadhi ya barabara Serikali ina mkakati gani wa kuzijenga kwa tabaka la zege na hasa kwenye maeneo korofi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Msanga – Chome – Ikokoa katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 zimetengwa shilingi milioni 267.15 kwa ajili ya kujenga meta 100 kwa kiwango cha zege kwenye eneo korofi, lakini pia kwenye eneo hatarishi la Mlima wa Chome imejengwa strip concrete ya meta 350, lakini katika mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 74.9 kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha zege meta 180 kwenye eneo hatarishi la Mlima Ikokoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu Barabara ya Makanya – Tae – Suji Serikali imetenga katika mwaka wa fedha 2024/2025 milioni 161.18 kwa ajili ya kujenga kwa tabaka la zege urefu wa meta 100 kwenye eneo la Mgwasi – Tae, lakini pia ujenzi wa driffs nne za meta 32 na kwenye Barabara ya Kisiwani – Msindo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitumia shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga meta 500 za strip concrete. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga kwa kiwango cha zege kwenye maeneo hatarishi, kwenye barabara zake hizi ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa mimi na yeye tutazungumza, tutapanga ratiba vizuri nipo tayari kutembelea Jimboni kwake kuangalia miundombinu hii ya barabara ili tuweze kuona umuhimu wa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuzikarabati na kuzijenga vizuri. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea kufungua barabara za mitaa kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale pale Kharumwa kwa kiwango cha udongo. Je, Serikali ina mpango gani kuziwekea mpango wa kuweka changarawe na baadaye lami hizo barabara za mitaa Kharumwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweza kuzihudumia barabara za wilaya kwa kiwango cha lami, lakini kama wote tunavyofahamu tunaanza. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kuhudumia barabara hizi kwa viwango tofauti ikiwemo viwango vya changarawe, lakini mwisho wa siku hatimaye tunataka barabara zetu zote hizi za wilaya ziwe kwa kiwango cha lami ambacho kitafanya barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu na ziweze kupitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya na hususan pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, changamoto za barabara za Mlimani kule Same Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Meru na nimeishalisema hapa mara nyingi. Kwa hiyo, sasa niulize Serikali inatoa tamko gani kuhusu barabara za milimani kule Arumeru Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipambania sana suala la Ujenzi wa barabara kwa viwango vitakavyodumu hasa katika Jimbo lake ambalo lina milima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari tumeshazungumza na suala tayari lipo kwenye michakato na fedha tayari zimeshatengwa, nikuhakikishie Serikali itakuja kujenga barabara, itatenga fedha kila mwaka kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara hizi na hasa katika jimbo lako ambalo ni la milima. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Luagara kwenda Liponde kilometa 1.5 ilishafanyiwa feasibility study na watu wa TARURA na walishaweka kwenye bajeti miaka miwili nyuma, ni lini sasa Serikali itakwenda kuweka lami kipande kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii tayari imeshafanyiwa usanifu na tayari ipo kwenye bajeti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia kwa karibu hata baada ya kutoka kwenye maswali hapa tutakaa tutafuatilia kwa karibu ili tuhakikishe kwamba mwaka huu kwa sababu fedha tayari imeishatengwa ili iweze kujengwa barabara hii.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, okay kwa kuwa sasa ujenzi wa shule umefikia 85%, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi huo pamoja na nyumba za watumishi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mbunge kwa swali hili zuri sana kwa maslahi ya watoto wote wa kike ambao watasoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha mwaka 2023/2024 Serikali itapeleka shilingi bilioni 1.1 katika shule zote zile 16 za wasichana ambazo zilipelekewa shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa kumi, lakini chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu na mabweni manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itapeleka fedha hii kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza kuzitumia.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba unipe fursa nimpongeze sana Rais wa Nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliona hili kwa ajili ya wasichana. (Makofi)

Naomba kuuliza swali je, katika shule hizo zinazoenda kujengwa ambazo ni za sayansi, wamezingatia kutupatia lab technicians? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa hizi shule kama nilivyotangulia kusema awali ukiacha majengo tu ya madarasa, lakini kutakuwa kuna chumba cha TEHAMA, kutakuwa na maktaba, nyumba za walimu na mabweni. Kwa hiyo, chumba cha TEHAMA kitakuwepo na kwa sababu msingi ni kuhakikisha kwamba shule hizi zinatoa elimu iliyobora kwa watoto wa kike, wakati wa kutoa watumishi yaani wakati wa kuajiri na kupanga watumishi kwa ajili ya kuhudumia shule hizi lazima Serikali tutazingatia ili hiki chumba cha TEHAMA kipate matumizi kiwe kina lab technicians.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Rungwe tuna shule nzuri sana ya wavulana. Tunashukuru Serikali kwa kuikarabati ni lini mtatujengea shule ya wasichana katika wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi shule hizi zipo 26 ziko kwenye Mradi wa SEQUIP na kila mkoa inapata shule moja ya wasichana, ya bweni na ni ya sayansi. Kwa hiyo, Mkoa wa Mbeya tayari una shule moja kwa hiyo hatutojenga katika kila kata, ni shule maalum Mheshimiwa Rais amehakikisha ametenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kila mkoa unapata shule hii ya bweni ya wasichana ya sayansi. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliona hili na kujenga na kutupatia hizo shule 26 katika nchi yetu ya Tanzania na mkoani kwetu Lindi hasa kwenye Jimbo langu kuwa ni miongoni mwa zile shule za kwanza ambazo zimejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kike wanahitaji ulinzi, je, ni lini mtatupatia pesa kwa ajili ya uzio kwa ajili kuwalinda watoto hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akitetea sana, sana, sana maslahi ya watoto wa kike kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kama nilivyotangulia kujibu katika swali la nyongeza hapo awali Serikali italeta na itapeleka shilingi bilioni 1.1 kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha kuisha, mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu yote ya msingi katika shule hizo ambazo zilipewa fedha katika awamu ya kwanza, kwa sasbabu shule hizi 16 ikiwemo shule ambayo imejengwa Mkoa wa Lindi zilipokea shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza na sasa zitapokea mwaka huu shilingi bilioni 1.1 awamu ya pili kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu yote ya msingi.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili yenye kifungu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilishawahi kutengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili la kivuko hiki, lakini haijatekelezwa. Leo majibu ya msingi yanaonesha kwamba wanaendelea au wamekamilisha tathmini na gharama wamezipata upya, sasa wanatafuta fedha. Nini commitment ya Serikali kujenga daraja hili ili kuokoa vifo vya watoto ambapo hata jana tu mtoto mmoja amekufa kwenye kivuko hiki?

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mpiji wenyewe na Mto Mbezi ambapo kuna vivuko vingi sana hatarishi kwa watoto wetu na watu wanaotumia. Je, ni ipi ahadi ya Serikali kuleta fedha maalum kujenga vivuko hivi ili tuokoe maisha ya watu wetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali imefanya tathmini na imebaini kwamba zinahitajika shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini na ndiyo maana kuna ongezeko kubwa la bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka muda huu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia imeridhia kuongeza bajeti maalum ya shilingi bilioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea na itaweka kipaumbele kikubwa sana kuhakikisha kwamba inaanza ujenzi wa miundombinu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, vivyo hivyo nirejee maelezo yangu ya awali kwamba Serikali inaona umuhimu mkubwa sana wa miundombinu hii muhimu kwa maslahi ya wananchi, na tayari bajeti ya dharura ya TARURA imeongezeka. Vile vile kuna bajeti maalum kwa ajili ya ukarabati na marekebisho na ujenzi wa miundombinu hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukulia suala hili la ujenzi wa miundombinu hii kwa umakini mkubwa na itakuja kujenga miundombinu hii.
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwenye Wilaya ya Kilindi kipo Kijiji cha Mgera ambacho kina daraja limekatika takribani miaka mitatu sasa na Serikali haijarekebisha hali hiyo na upande wa pili ndipo ambapo taasisi zote za Serikali zipo huko. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA kwenda kurekebisha daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele vya TARURA ni pamoja na kuhakikisha kwamba inahakikisha miundombinu ya barabara hizi haikatiki kimawasiliano. Kwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tukutane, tukae, tuweze kufanya mawasiliano na kama ni kweli eneo hili limekata mawasiliano, kuna umuhimu na kipaumbele kikubwa sana ambacho inabidi kitolewe kwa ajili ya kuhakikisha tunarudisha mawasiliano katika eneo hili.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Mpendo na Kijiji cha Amia kinatenganishwa na mto mkubwa ambao unaitwa Mto Bubu. Ni lini sasa Serikali itajenga daraja ili kuunganisha vijiji hivi viwili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyotangulia kusema kwamba ni muhimu sana kuwe kuna mawasiliano na ndiyo kipaumbele katika mipango kazi au utekelezaji wa majukumu ya TARURA kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadiri alivyoleta maombi yake na kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha, Serikali itamsaidia kwenda kurekebisha miundombinu hii.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini kuna madaraja mawili ambayo yana changamoto kubwa. Moja lipo katikati ya mji ambalo vivuko vyake vimekatika pembeni, watoto wanapata ajali ya kuanguka; daraja lingine la Kitifu, limekatika kabisa, hakuna mawasiliano kati ya kata mbili; Kata ya Mgombezi pamoja na Mtonga: Je, Waziri haoni sababu ya kuwaelekeza TARURA kurekebisha madaraja hayo mawili muhimu kwenye Jimbo la Korogwe Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya mawasiliano na Meneja wa TARURA ili kufahamu changamoto iliyopo katika eneo hilo na kama ni dhahiri kwamba mawasiliano yamekatika, basi kama ulivyo utaratibu wa TARURA ni kuweka kipaumbele katika kuhakikisha inaunganisha na kuna mawasiliano katika barabara zetu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tumelipokea na tutalifanyia kazi.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutenga shilingi milioni 947.2 kujenga kilometa 31. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Katika majibu ya Serikali ni kwamba, kilometa mbili zitajengwa kwa kiwango cha lami kupitia Mradi wa TACTIC. Nataka nifahamu, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni lini Serikali itajenga Barabara ya Mbinga – Kikolo – Kihungu na barabara ya Mbinga – Kitanda hadi Miembeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari hatua zote za muhimu zimekamilika kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi huu sasa utaanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo ya lami ya kilomita mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ambalo ameuliza juu ya ujenzi wa Barabara ya Mbinga Mjini – Kikolo mpaka Kihungu yenye urefu wa kilometa 30, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka wa fedha 2024/2025 zimetengwa shilingi milioni 60 kwa ajili ya kufanya marekebisho ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kitanda ambayo yenyewe ina kilometa 28, kwenye mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ilitenga kwenye bajeti shilingi milioni 80, lakini katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga shilingi milioni 47.18 kwa ajili ya marekebisho. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imelichukua suala hili la ujenzi wa barabara hizi kwa umakini mkubwa na itaendelea kutekeleza ujenzi huo.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kimenye ina walimu wawili tu wa kike, je, Serikali iko tayari kupeleka walimu wengine wa kike ili kuweza kuwasaidia watoto wa kike wanaosoma katika shule hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kupambania haki ya watoto kupata elimu, lakini kuwapambania watoto wa kike waweze kupata walimu wa kike kwa ajili ya malezi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu katika majibu ya msingi kwamba Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa walimu wa kike katika malezi ya wanafunzi. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kutazama mahitaji ya uhitaji wa walimu ikiwemo walimu wa kike kwa ajili ya kuwapeleka katika shule zetu hizi waweze pamoja na kufundisha, lakini kuwa walezi kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itatizama na katika vipaumbele na sifa za kuajiri walimu na kuwapeleka katika shule na kwa kuzingatia mahitaji itaendelea kupeleka walimu kwa sifa mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wanaenda kuwa walezi pia kwa watoto wa kike. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo la walimu wa kike hasa kwenye shule za vijijini ni kubwa mno na inafikia wakati ambapo kuna shule zinakosa mwalimu hata mmoja wa kike jambo ambalo wanafunzi wa kike wanakosa matron kwenye shule.

Je, Serikali haioni upo umuhimu sasa wa kuangalia mgawanyo wa walimu wa kike katika nchi hii ili kuhakikisha kwamba walimu wa kike wanaongezwa zaidi katika shule za vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taratibu, waajiri wa walimu kimsingi unazingatia taaluma. Kwa hiyo, ajira zile za walimu zinazingatia professionalism, lakini hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni hoja ya msingi sana na sisi kama Serikali tumeipokea kwa ajili ya kuichakata na kuangalia namna nzuri ya kuweza kufanya utekelezaji kwa maana ya kuzingatia uhitaji wa walimu wa kike katika shule zetu. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, swali la kwanza ni kwamba ni kweli kuna utaratibu wa shule za SEQUIP kujengwa na mojawapo ikiwa ni katika Jimbo la Mheshimiwa Kasalali, je, ni lini kwa mwaka huu wa fedha shule hizo zitaanza kujengwa kwenye jimbo hili na majimbo mengine? (Makofi)

Swali la pili, kuna shule za SEQUIP za awamu ya kwanza ambazo hazikuwa zimekamilika, je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha shule hizo kwenye majimbo yote ikiwemo Jimbo la Sumve na Jimbo la Kilolo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitafuta fedha na akapata fedha jumla ya shilingi trilioni 1.2 katika mradi tunaouita Mradi wa SEQUIP ambao lengo lake ni kuongeza shule zetu za sekondari kwenye kata na kuhakikisha zinafika, tunaongeza idadi ya shule kwa ajili ya kupunguza kwanza umbali wa wanafunzi kusafiri ili kufika kwenye shule, lakini pia kupunguza msongamano katika baadhi ya maeneo ambayo kuna msongamano kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa lengo la Serikali na lengo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anaboresha sekta ya elimu na hasa elimu hii ya shule za sekondari na shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba ni lini awamu hii au mwaka huu fedha zitatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule hizi katika mwaka huu wa fedha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeshafanya uhakiki wa maeneo yote yaliyoainishwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizi za kata katika mwaka huu na ninamhakikishia, wakati wowote fedha zitatolewa kwa ajili ya kuhakikisha tunatekeleza mradi huu kwa kadiri vile tulivyokuwa tumepanga kwa maana ya awamu ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu kwamba zile shule za awamu ya nyuma ambazo hazikukamilika, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha inakamilisha shule hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali ilishaanza kutoa fedha na itahakikisha inapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu ya shule hizi za kata ili wanafunzi waweze kuanza kuzitumia. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nina swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga Barabara ya Kizumbi – Lupata hadi Msamba kwani kuna shule mpya ya sekondari imejengwa na ni eneo la kiuchumi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu ya msingi, Serikali tayari imeshaanza kufanya ujenzi wa barabara mbalimbali katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhudumia barabara katika jimbo lako, pia ikiwemo barabara hii ya Kizumbi mpaka kufika Msumba. Nakuhakikishia barabara hiyo itajengwa na Serikali italeta fedha kwa ajili hiyo. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Negezi ambacho kimeanza kufanya kazi sasa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Kituo cha Afya cha Mwanhakanga, Kituo cha Afya cha Mwamigumbi na Kituo cha Afya cha Dulisi, ni vituo vya afya ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi na michango iliyotokana na mapato ya halmashauri.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inakamilisha miundombinu iliyosalia ikiwemo wodi za akinamama, akinababa na watoto, walkways, fence na mambo mengine yanayoendana na sifa za vituo vya afya ili mradi vituo vile vianze kufanya kazi kikamilifu na ipasavyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Zahanati ya Lagana ni moja kati ya zahanati ambazo zinahudumia kata tatu zinazozunguka katika maeneo hayo na moja kati ya mambo ambayo tulielekezwa na Serikali kama Waheshimiwa Wabunge ni kutoa mapendekezo ya kuhakikisha maeneo ambayo ni ya kimkakati na yaliyopembezoni yaweze kupewa kipaumbele cha kuwekewa vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha zahanati hii inapandishwa hadhi kuwa health center ili kiweze kuhudumia maeneo haya yanayozunguka kata jirani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ya kuwatetea wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu kuhusu Kituo cha Afya cha Mwanhakanga, Kituo cha Afya cha Dulisi na Mwagimbi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Mwanhakanga tayari kimekamilika na kimeanza kutoa huduma, lakini Kituo cha Afya cha Dulisi na Kituo cha Afya cha Mwagimbi ni vituo vya afya ambavyo pia vimejengwa kwa nguvu za wananchi na vina majengo ya OPD pekee. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya miradi viporo ya hospitali, lakini mahsusi pia kwa ajili ya miradi viporo ya vituo vya afya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali itakuja kukamilisha ujenzi wa vituo vyake hivi muhimu vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu Zahanati hii ya Lagana, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanya jitihada ya kupata fedha ili Zahanati hii ya Lagana iweze kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya kutokana na umuhimu wake na kutokana na hoja ya msingi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza kuhusiana na kupatikana kwa kituo cha afya kwenye eneo alilolitaja. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Binza ni Kata kubwa sana na ina wakazi 9,787 lakini haina kituo cha afya, je, lini Serikali itajenga kituo cha afya katika kata hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alishazungumza na Waheshimiwa Wabunge na akawa amewataka waweze kuainisha vituo vya afya vya kimkakati vya kujengwa katika maeneo yao. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kama Kata ya Binza ni miongoni mwa kata zinazohitaji vituo vya afya vilivyoainishwa kimkakati kwenye maombi yale yaliyoelekezwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, ninamhakikishia kwamba Serikali inatafuta fedha ili kukakikisha vituo hivyo vya afya vinajengwa. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Kata ya Didia iliyopo katika Jimbo la Solwa ni kata ambayo ina watu wengi zaidi ya 60,000.

Je, nini mpango wa Serikali kuwapatia kituo cha afya katika ksata hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha inaimarisha huduma za afya msingi na katika kufanya hivyo imekuwa ikiboresha miundombinu ya hospitali za wilaya, vituo vya afya mpaka zahanati na namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha inapata fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma ya afya msingi. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kutafuta fedha ili ije iweze kufikia ujenzi wa kituo cha afya katika Kata hii ya Didia kama ulivyosema ina wananchi wengi na wanahitaji huduma iliyo bora ya afya. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, mwaka 2020 tulivyokuwa tunafanya kampeni, Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha OPD Himo kuwa kituo cha afya na kutuahidi kwamba wangetupa majengo ya maabara, wodi moja pamoja na mortuary. Mpaka leo hii hakuna kilichofanyika lakini kituo kinaendelea kutoa huduma kama kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Serikali sasa iseme kwamba ni lini itatoa fedha kwa ajili ya majengo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hoja hii muhimu ya Mheshimiwa Mbunge naomba tukae baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu ili tutazame mkwamo upo eneo gani. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba huduma za afya msingi zinaimarika na zinakuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa misingi ya alichokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tuna kituo ambacho kinatoa huduma ya kituo cha afya, lakini haina miundombinu ya msingi ya kuweza kutosheleza kutoa huduma ya kituo cha afya, nadhani kuna hoja ya msingi. Kwa hiyo, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuona changamoto ipo wapi ili Serikali iweze kupeleka fedha kwa ajili ya kuleta miundombinu muhimu katika kituo hicho cha afya.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo Serikali ilitenga shilingi bilioni nane kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya takribani 20 ambavyo havitoi huduma kama vituo vya afya kamili na miongoni mwa vituo hivyo Wilaya ya Biharamulo tulitengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kukarabati Vituo vya Afya vya Nyabusozi na Kalenge, lakini mpaka sasa pesa hiyo haijatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali kwa sababu mwaka wa fedha unaisha na sijaona pesa hiyo ikiwa imepelekwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu awali, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha huduma za afya msingi. Kwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie kwamba Serikali ipo kazini na ndiyo maana kwanza ilianza kutenga bajeti. Kwa hiyo mimi na yeye tutakaa na tutazungumza tuone mkwamo upo sehemu gani.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, Kata ya Jaila tunayo zahanati ambayo ina sifa zote za kuwa kituo cha afya, lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya majengo hayajakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari kutuletea kiasi cha fedha kumalizia majengo hayo na kuwa kituo cha afya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha huduma za afya msingi. Katika jitihada hizo imekuwa ikipandisha hadhi zahanati kuweza kutoa huduma za vituo vya afya kwenye maeneo ambayo yanauhitaji, lakini yana mazingira ambayo yanawezesha kuanzishwa kwa kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaja eneo hili la Zahanati ya Jaila ambayo imepandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatafuta fedha kuhakikisha hizi zahanati zote ambazo zimepandishwa hadhi kuwa kituo cha afya zinapatiwa fedha ili kuimarishwa ili huduma zitakazotolewa ziendane na huduma zinazotakiwa kutolewa katika vituo vya afya. Kwa hiyo, nikutoe shaka Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inalifanyia kazi suala hili.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Chunya wanaishukuru sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo imefanyika mpaka sasa, lakini wana maswali.

Je, sasa hizi pesa ambazo zimetengwa ni kweli zitawahi ili zipelekwe na hospitali hiyo kuanza kufanya kazi kwa haraka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hospitali mojawapo katika Mkoa wa Mbeya ambayo ni kongwe sana ni Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Je, ni lini ukarabati wa hospitali hiyo kwa viwango vya kimataifa utaanza kufanyiwa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga shilingi milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya. Kama vile ambavyo tayari katika miaka ya nyuma Serikali ilikuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuboresha na kukamilisha miundobinu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya hivyo hivyo katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetenga fedha na fedha zitafika kwa wakati kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, Hospitali ya Halmashauri ya Mbulu imeanza kujengwa na karibu inamalizika lakini haitoi huduma kwa sababu shilingi milioni 500 za mwisho ilikuwa zipelekwe na mpaka sasa hazijapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, lini mtapeleka ile fedha shilingi milioni 500 ili hospitali ile ikaisha na wananchi wakapewa huduma ambayo wanastahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha ujao Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi viporo ya hospitali za halmashauri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hospitali ya kwao ya Halmashauri ya Mbulu na yenyewe itakuwa miongoni mwa hospitali zitakazohudumiwa kwa maana ya kukamilisha miundombinu ya hospitali ile iliyokuwa imebakia kwa sababu fedha imetengwa katika mwaka ujao wa bajeti.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, Kijiji cha Kisana tunajenga zahanati ambayo imetumia zaidi ya miaka 10 haijakamilika. Ni lini Serikali itatoa hela ya kumalizia hilo boma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inakamilisha miundombinu ambayo haijakamika kwenye vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imetenga bajeti, pia itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaendelea kukamilisha miundombinu ambayo haijakamilika kwenye vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya msingi ikiwemo katika zahanati hii katika Kijiji cha Kisana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Hospitali ya Wilaya ya Itilima haina uzio, je, ni lini Serikali itaoa fedha za kujenga uzio ule? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga miundombinu katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya msingi kwa kutumia utaratibu kwa fedha kutoka Serikali Kuu, lakini kwa kutumia fedha kutoka kwenye mapato ya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huo Serikali itaendelea kuhakikisha inaboresha miundombinu ya vituo vyetu hivi vya kutolea huduma ya afya msingi. Kwa muktadha huo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba uzio katika hospitali ya halmashauri aliyoitaja itaendelea kutafutiwa fedha, kutengewa fedha na kujengwa kwa utaratibu wa fedha kutoka Serikali Kuu, lakini kupitia pia mapato ya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupata majibu ya Serikali, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Tarime ina mapato makubwa ya ndani na chanzo cha mapato hayo ni wananchi wenyewe: Je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kwa Halmashauri ya Tarime iweze kuondoa changamoto za matundu ya vyoo, viti, meza na madawati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Same inafahamu vema kwamba nimefanya jitihada kubwa kutengeneza madawati kwenye shule za msingi zaidi ya madawati 500: Je, Serikali hamwezi kuwaelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Same ikachukua hatua nayo ya kutengeneza madawati sasa hasa katika shule za Kata za Lugulu, Mtii, Vuje na Bombo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, ukweli ni kwamba shule ni mali ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na shule zipo chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia wajibu wa kutunza na kusimamia shule hizi uko chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, tafsiri yake ni kwamba, ununuzi wa madawati, viti, ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine ni wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia bajeti za maendeleo. Huo ndiyo msingi wa D by D.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya Serikali Kuu kimsingi ni miradi ya nyongeza kwa maana ni complimentary. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kukumbushia maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kwamba, wahakikishe wanafanya tathmini ya miundombinu na samani na kutenga kwenye bajeti za maendeleo kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maelekezo hayo ya Mheshimiwa Waziri yanaenda pia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada binafsi za kuhakikisha kwamba ananunua madawati haya kwa ajili ya kupeleka kwenye shule zake. Jitihada hizi ni nzuri na zinafaa kuigwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukumbushia maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizopo nchini kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kwenye mapato yao ya ndani, kwenye bajeti ya maendeleo kuhakikisha kwamba wanatumia fedha hizi kwenda kununua madawati haya na pia kuendeleza miundombinu mingine kama kujenga vyoo. Hilo ni jukumu lao kwa mujibu wa D by D. Kwa hiyo, naomba nikumbushie hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mashariki. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza kabisa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa kwa manufaa ya wananchi wa Kilombero na Kilolo kufungua barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, barabara hiyo inaishia Kijiji cha Itonya, je, Serikali itakuwa tayari sasa kuunganisha mtandao wa barabara hiyo katika Kijiji cha Itonya - Kimara mpaka Idete ambapo inapita barabara ya TANROADS ili kufungua uchumi na pia kuunganisha na reli ya TAZARA ili kusafirisha mazao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa barabara nyingi sana sasa hivi katika Mkoa wetu wa Iringa zimeharibika sana kutokana na mvua kubwa; na kwa kuwa, kuna barabara ya Boma la Ng’ombe Masisiwe wananchi wameanza kuchangishana ili kuondoa sehemu korofi magari yaweze kupita kwa urahisi: Je, Serikali inawasaidiaje wananchi hao ili kuweza kutengeneza sehemu zote korofi waweze kupitisha mazao yao, akina mama wajazito na wazee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la kwanza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuunganisha barabara za Kitaifa na Wilaya kwa maana ya barabara za TANROADS na TARURA. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali siyo tu iko tayari kuunganisha mtandao wa barabara ya Kijiji cha Itonya na Kimara, lakini ndiyo mpango wa Serikali uliopo wa kuunganisha barabara zote nchini, kwa maana ya barabara zote za vijiji ikiwemo vijiji hivi vya Itonya, Kimara na Idete, vitaunganishwa na barabara za Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, awali ya yote nawapongeza wananchi wa Boma la Ng’ombe ambao kwa jitihada binafsi wameweza kuchangia fedha kuboresha barabara iliyopo katika eneo lao. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari kuunga mkono jitihada hizi za wananchi ili kuboresha barabara hii ya Boma la Ng’ombe - Masisiwe. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaifikia barabara hii.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza ujenzi wa lami kwa ajili ya kuchochea viwanda barabara ya Themi - Viwandani kwa kujenga kilometa 1.4, lakini bado kuna maeneo ya viwanda vya Lodhia, Dash, Mount Meru pamoja na Coca Cola hadi kwenda kwenye World Vision bado havina lami mpaka sasa. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ili kuendelea kuchochea maendeleo ya viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inazingatia sana na inatambua umuhimu wa kujenga miundombinu ambayo itachochea uchumi katika nchi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambazo zitaunganisha wananchi kutoka kwenye mashamba yao kwenda kwenye viwanda. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya uboreshaji wa barabara hizo kwa ajili ya kuchochea uchumi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa sasa Kata nne za Jimbo la Kilolo hazipitiki kabisa kutokana na madhara ya mvua. Kata hizo ni Masisiwe, Ukwega, Kimara na Idete. Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha upelekaji wa fedha za dharura ili Kata hizi ziweze kuunganishwa na barabara na huduma ziweze kuendelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameeleza barabara hizi hazipitiki, namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki cha Maswali na Majibu tukae ili tuweze kufuatilia kujua mustakabali mzima wa kuleta fedha kwa ajili ya kurekebisha barabara hizi.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Mheshimiwa Rais alipokuja Mkoa wa Tabora tulimpelekea ombi maalumu la kuanzisha Halmashauri mpya ya Kizengi na akatoa maelekezo kwa mkoa na wilaya kuandika maombi hayo na kuyapeleka Wizarani na mkoa ulishafanya hivyo na maombi yale yameshawasilishwa kwa Katibu Mkuu, TAMISEMI. Nataka Waziri aniambie, je, hiyo barua imefika kwao au bado?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Uyui, hasa Jimbo la Igalula katika Kata za Loya, Tula Miswati, Mbale wanapata adha sana ya kupata huduma katika Halmashauri yetu kutoka kilometa nyingi wanatembea kufuata huduma. Hamuoni haja kama Wizara kumshauri Mheshimiwa Rais ili aweze kuitangaza Halmashauri ya Kizengi ili kuongeza huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora maombi hayo aliyoyazungumza Mheshimiwa Mbunge na inaendelea kuyafanyia uchambuzi kulingana na vigezo vilivyopo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barua hiyo ilishafika Serikalini Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu kwa mujibu wa Ibara ya 9(a) (4) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi wa Mwaka 2020 ni kuimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kutimiza wajibu wao. Kwa mantiki hiyo Serikali kwa wakati huu imejikita katika kuimarisha maeneo ya utawala yaliyopo kwa maana ya kuajiri watumishi katika maeneo ambayo yenye upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Serikali itatengeneza au kuweka miundombinu muhimu kama majengo ya ofisi, kupeleka shule, huduma za afya, maji, barabara na umeme. Kwa hiyo, kwa wakati huu Serikali imejielekeza katika kuboresha mamlaka zilizopo tofauti na kuanzisha mamlaka mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kuendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi katika maeneo waliyonayo ili huduma ziweze kuwafikia wananchi wote karibu na maeneo yao ili kuongeza ufanisi na huduma bora zaidi kwa wananchi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake. Naomba Barabara hii iweze kupitika kwa sababu hali yake ni mbaya sana. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Barabara ya Ilula – Image - Ibumu ni ahadi ya Serikali ya muda mrefu sana, lakini kwa sasa hivi hali yake ni mbaya sana, haipitiki na wananchi wamekuwa wakipata shida sana. Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake? Kwa sababu hii barabara ikijengwa ni pamoja na kumuenzi Eng. Patrick Mfugale ambaye anaishi katika hilo eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Barabara ya Kitowo – Kihesa - Mgagao – Mwatasi - Masisiwe ambayo inakwenda mpaka Idete ni barabara ya kiuchumi, lakini ina hali mbaya sana na haipitiki. Je, Serikali iko tayari angalau kujenga zile sehemu korofi tu ili iweze kupitika wakati huu kwa sababu mabasi hayapiti? Wananchi wanapata shida sana hata wanaokwenda kujifungua, wagonjwa na wazee. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuja katika Mkoa wetu wa Iringa ajionee hali mbaya ya barabara jinsi ili aweze kusaidia wananchi, nao waweze kufaidika na Serikali yao na uchumi uweze kujengeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa sana ya kuwatetea wananchi wake. Mara kwa mara tumekuwa tukiwasiliana akinieleza changamoto za miundombinu katika eneo lake la uwakilishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali lake la kwanza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Ilula – Image – Ibumu tayari imeanza kujengwa baada ya kupokea fedha jumla ya shilingi milioni 150 za dharura. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hizi tayari zimeshatolewa na ujenzi wa barabara hii umeshaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Barabara hii ya Kitowo – Masisiwe – Mwatasi imetengewa bajeti ya shilingi milioni 36.8 katika Mwaka wa Bajeti 2023/2024 kwa ajili ya kuchonga kilomita nane za barabara na kuweka kifusi kwa kilomita mbili kwenye maeneo korofi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi kwa Uchumi, lakini pia kwa ustawi wa wananchi na inafanyia kazi kwa kadri fedha inavyopatikana kwa kufanya marekebisho na kujenga katika maeneo ya barabara ambazo zina changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, nikitoka hapa nikikaa kwenye kiti changu tutazungumza ili tupange ratiba nzuri ya mimi kufika katika eneo lake ili kuona changamoto za wananchi na kuzitafutia suluhu. (Makofi)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Bajeti ya TARURA katika Wilaya ya Ikungi ni ndogo na kwa kuwa muunganiko wa eneo na eneo umekuwa ni changamoto kwa haya madaraja. Je, ni upi mpango wa Serikali katika kujenga madaraja haya ili kuunganisha vijiji, kata pamoja na wilaya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Mtaturu kashawasilisha bajeti ya Madaraja matano ambayo ni Matongo – Mpetu, Misughaa – Ntutu, Misughaa – Kikio, Kimbwi na Lighwa na kwa umuhimu wake na udharura wake na kwa sababu bajeti tayari ipo mezani, tunataka kujua, je, ni lini Serikali itafanya uharaka wa kujenga hayo madaraja ili kuunganisha vijiji na kata hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tukiwasiliana na Mheshimiwa Mtaturu mara kwa mara akinieleza changamoto hizi za miundombinu kwenye jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijibu swali lake la kwanza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba inajenga na inaboresha miundombinu katika maeneo yote nchi nzima. Barabara hizi za wilaya zina jumla ya urefu wa kilometa 144,429 na ni mtandao mkubwa ambao unahitaji bajeti kubwa. Mpaka muda huu tayari Mheshimiwa Rais amehakikisha Bajeti ya TARURA inaongezeka kutoka bajeti ya awali ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 275 mpaka sasa tunavyoongea bajeti ya TARURA ni shilingi bilioni 710.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pale inapotokea dharura, Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki kwa wananchi, kwa maana ya barabara hizi zenye umuhimu na ambazo zinahitajika kujengwa ili ziunganishe kijiji na kijiji na kata na kata. Nimhakikishie pia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafanyia kazi ujenzi wa madaraja na miundombinu yote ambayo ni muhimu kwa ajili ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusu madaraja matatu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema bajeti ya dharura imeongezwa kutoka shilingi bilioni 21.2 mpaka sasa imefika shilingi bilioni 52.6, yote hii ni kwa sababu Serikali inataka pale inapotokea dharura, basi inapeleka fedha kwa ajili kushughulikia udharura huo.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye kutia matumaini. Sitakuwa na swali la nyongeza ila naipongeza Serikali kwa kuliona hilo na niwaombe sasa wakajenge hiyo hospitali kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Muleba. Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametoa pongezi kwa Serikali kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu hii muhimu na sisi kama Serikali tunapokea pongezi hizo.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayojengwa kule Mabogini katika Jimbo la Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hospitali yake hii ya halmashauri itajengwa kwa sababu katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi bilioni 43.84 kwa ajili ya kukamilisha miradi viporo ya hospitali za halmashauri. Kwa hiyo nimhakikishie Serikali inakuja kujenga hospitali hiyo. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Iringa Vijijini ina majimbo mawili, hospitali ya wilaya ilijengwa katika Jimbo la Ismani ambayo wananchi wa Kalenga hawaitumii kwa sababu ipo mbali sana. Je, ni lini Serikali itajenga hospitali katika Jimbo la Kalenga? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakusudia kusogeza huduma za afya msingi karibu na wananchi na ndiyo maana kila mwaka inatenga fedha kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi ya hospitali hizi za halmashauri. Kwa hiyo nimhakikishie Serikali ipo kazini na itahakikisha inasogeza huduma ya afya msingi kwa wananchi kwa kuendelea kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizi za halmashauri.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022, Serikali ilitupatia shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Makete, baada ya hapo hatujapata fedha nyingine yoyote. Je, ni ipi commitment ya Serikali kutuongezea fedha ili Hospitali ya Wilaya ya Makete irudi kwenye hadhi yake ambayo wananchi wa Makete wanaitegemea na ni ahadi ya Serikali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu hapo awali katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 43.84 kwa ajili ya kuhakikisha inaendelea kuboresha miundombinu katika hospitali zetu hizi, kwa sababu tayari Serikali imekuwa ikitenga fedha kuhakikisha ujenzi wa hospitali hizi unaendelea. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali italeta fedha kwa ajili ya kuboresha na kukamilisha miundombinu katika hospitali yako.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Rais Samia mwaka juzi Wilayani Bunda aliagiza hospitali ya halmashauri ijengwe katika Jimbo la Mwibara. Je, ni lini hospitali hiyo itajengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Viongozi Wakuu wa Nchi ikiwemo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kipaumbele kikubwa sana katika utekelezaji wa miradi hii ya Serikali. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itakuja kuhakikisha kwamba inatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetwaa eneo la KIA kwa ajili ya Uwanja wa Ndege na Zahanati ya Tindigani imechukuliwa kwenye eneo hilo. Je, ni lini sasa Serikali itajenga zahanati nyingine kufidia hii ya Tindigani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa afya msingi na kadri ya upatikanaji wa fedha itaangalia vipaumbele muhimu kama alichokitaja Mheshimiwa Mbunge ili kuhakikisha kwamba inaboresha na kujenga miundombinu hii muhimu kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya msingi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa shilingi bilioni tatu laki tano mia sita hamsini elfu kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, lakini mpaka leo ni miaka minne hospitali hiyo haijamalizika. Je, ni lini Serikali itamalizia hospitali hiyo ili iweze kufanya kazi kwa Halmashauri ya Bunda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali imetenga shilingi bilioni 43.84 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa ajili ya kukamilisha miradi viporo ya hospitali za halmashauri. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba, Serikali italeta fedha ili kuhakikisha inakamilisha mradi wa hospitali hiyo.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mradi huu uliombewa toka Mwaka wa Fedha 2023/2024 na mpaka sasa haujaanza kwa sababu hizo nzuri ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mwantona mara baada ya Bunge hili kwenda kuwahakikishia wananchi wa Kata ya Kiwira ambao wana imani sana na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya ujenzi wa soko hili kama alivyoeleza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni Jimbo langu la Mwanga, je, ni lini Serikali itajenga Soko la Kisasa katika Halmashauri ya Mwanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, nikipata nafasi kwa sababu Mheshimiwa Mbunge hayupo leo, lakini tutazungumza naye ili tuweze kukubaliana ratiba ya kwenda kwenye jimbo lake; kwenda kukagua eneo la mradi huu na kukutana na wananchi wake kama alivyoleta maombi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kwenye halmashauri kupitia mapato ya ndani zinaweza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa masoko. Pia, kuna njia nyingine ambayo ni ya kuomba mradi wa kimkakati. Kwa hiyo nichukue nafasi hii kuendelea kumkumbusha mkurugenzi aweze kuona katika nafasi hizo mbili; ya kwanza kutenga mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa soko, lakini kuna njia nyingine ya kuandika andiko maalum kwa ajili ya kuomba mradi wa kimkakati wa ujenzi wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa njia hizo mbili Mheshimiwa Mbunge anaweza kuleta maombi, lakini kutenga fedha kwenye mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa soko au kuleta maombi kwa ajili ya kupatiwa fedha ya kujenga mradi wa kimkakati wa soko katika jimbo la Mbunge.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itajenga mapaa kwenye Masoko kongwe ya Mwika, Marangu, Kisambo, Lyamombi na Himo kwenye Jimbo la Vunjo ambapo wanawake hususan wanaofanya biashara huku wananyeshewa na mvua na kupigwa na jua kali mwaka mzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa umuhimu wa miundombinu hii ya maghala, Serikali kwa kadri ya upatikanaji wa fedha itaona jinsi gani inaweza kukamilisha ujenzi wa majengo haya muhimu.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Lamadi la kimkakati ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2022?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, ahadi za viongozi wakuu wa nchi ni kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge bila shaka tayari andiko hili lilishafika na limepita katika ngazi zote, kwa hiyo Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuja kutekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kwa muda mrefu sana wananchi wa Mto wa Mbu Wilayani Monduli Mkoa wa Arusha waliahidiwa soko la kisasa lakini hadi leo ahadi hiyo haijatekelezwa. Lini Serikali itatekeleza ahadi hii kwa wananchi wa Mto wa Mbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia mapato ya ndani waweze kutenga fedha kwa ajili ya kujenga soko hili. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali kupitia mapato ya ndani itahakikisha kwamba inafanya tathmini na kuweka katika mipango ya kibajeti kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa soko hili.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina uzalishaji mkubwa sana wa mahindi, lakini hatuna soko la kisasa ambalo lingeweza kusaidia mapato kwa ajili ya Wilaya ya Kilindi. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuendelea kumkumbusha mkurugenzi anaweza akafanya tathmini, wakaandika andiko la kuonesha uhitaji, lakini kuonesha kwamba soko hili linaweza likawa lina tija kwa wananchi kama Mheshimiwa Mbunge alivyozungumza, apitishe katika michakato yote na ikikidhi vigezo kwa kweli Serikali italeta fedha kwa ajili ya kuhakikisha soko hili muhimu linajengwa kwa maslahi mapana ya wananchi. Sifa mojawapo muhimu sana katika mchakato huu ni kwamba ni lazima halmashauri iwe ilipata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwa hiyo andiko hili likikidhi vigezo hivi vyote, basi namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hili.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, majina ya kilugha yana shida sana, Shekilindi siyo Shelukindo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na kuharibika kwa miundombinu ya barabara hasa maeneo ya Malibwi, Kwekanga hadi Makole na Mbelei, Baga hadi Mgwashi pamoja na Migambo hadi Kifungilo. Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kutengeneza barabara hizo ili kuwaondolea adha wanaoendelea kuipata wananchi wangu hadi sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa kuona ni kuamini, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana na mimi ili akaone mazao ya wananchi yanavyoharibika mashambani kwa sababu ya ubovu wa barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi za Wilaya na ndiyo maana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongeza bajeti ya barabara za Wilaya, kwa maana bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni mia mbili sabini na tano mpaka sasa shilingi bilioni mia saba na kumi, yote hii ni kuhakikisha kwamba miundombinu ya barabara hizi za Wilaya inakuwa mizuri kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaweza kuifikia huduma lakini pia inawajenga kiuchumi kwa kufanya shughuli zao za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, barabara yake aliyoitaja ya Mbelei – Baga – Mgwashi ya kilometa 42, katika mwaka wa fedha 2023/2024 tayari imepokea shilingi 30,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa kalvati mistari nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mwaka wa fedha 2024/2025, imetengwa shilingi milioni 207.5 kwa ajili ya kuendelea kuboresha barabara hiyo. Kwa mfano, barabara yake ya Mabwi – Kwekwanga – Ngwelo ya kilometa 16.8 na yenyewe katika mwaka wa fedha 2024/2025, imetengewa jumla ya shilingi milioni 295. Kwa hiyo namuhakikishia Mheshimiwa Mbunge Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa hizi barabara za Wilaya ikiwemo barabara ambazo zipo katika Jimbo lako na itaendelea kuhakikisha inaleta fedha kwa ajili ya kuziboresha na kuzijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ambalo ameuliza kama nipo tayari kuambatana na yeye kwende Jimboni kwake kujionea mazingira haya, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu, tutakutana pembeni tutakubaliana ratiba ili niweze kufika katika Jimbo lake. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara ya kutoka Ihemi ambayo ni Jimbo la Kalenga kwenda mpaka Ihimbo ambayo itapita Mgama imekuwa ni mbovu na inasumbua wananchi kwa sababu wanalima mazao mengi na imeharibika wakati wa mvua.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatengeneza barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, Serikali inaweka kipaumbele kikubwa sana kuhakikisha kwamba barabara zetu hizi za Wilaya zinapitika ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za uzalishaji lakini kuweza kufikia huduma muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuleta fedha kuhakikisha kwamba inaifikia barabara hii uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ili wananchi waweze kupata huduma nzuri ya barabara nzuri na waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo na za uzalishaji mali. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mvua kubwa zilizonyesha Tanzania nzima pamoja na Chemba, zimeharibu kabisa miundombinu ya barabara. Baadhi ya barabara hizo ambazo kwa sasa hazipitiki ni Barabara ya Kwa Mtoro – Sanzawa – Mpendo, Soya – Chandama, Soya – Magasa na maeneo mengine mengi. Tumeomba fedha za dharura lakini mpaka leo hatujapewa fedha kabisa. Naomba kujua ni ipi commitment ya Serikali kuhakikisha miundombinu inarudi ili watu waendelee na kazi zao kama kawaida? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi za Wilaya. Kwa wakati huu Serikali pia inatambua kwamba barabara zetu hizi nyingi zimeharibika kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha na ndiyo maana fedha ya dharura Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan ameongeza bajeti kutoka bajeti ya shilingi bilioni 21 mpaka shilingi bilioni 13, kwa ajili ya kuhudumia Barabara ambazo zinapata uharibifu mkubwa kama huu ili ziweze kutengenezwa kwa udharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua changamoto ya miundombinu katika Jimbo la Mbunge na itahakikisha kwamba inaleta fedha kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu inaimarika katika Jimbo lake.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, barabara nyingi zimekuwa zikiharibika na kuifanya Serikali iwe na matengenezo ya mara kwa mara. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kutumia rasilimali ya mawe tuliyonayo hasa katika maeneo ya miji ili kuwa na barabara imara ambazo hazitasumbua wakati wa mvua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni hoja ya msingi sana, kwa kutambua hilo, Serikali tayari imeshaanza kutumia teknolojia mbadala katika ujenzi wa barabara zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeanza kutumia teknolojia ya barabara ambazo tunaziita eco roads ambazo zenyewe zina gharama nafuu katika ujenzi lakini pia zina life span kubwa zaidi, zinakaa kwa muda mrefu haziharibiki kama hizi barabara zetu zingine za kawaida. Pia teknolojia aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ya kutumia mawe, kwa hiyo Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa kutumia teknolojia hizi mbadala na tayari imeshaanza majaribio kwenye baadhi ya maeneo ili kuona ufanisi na ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuthibitika, baada ya hicho kipindi cha majaribio, Serikali inaona umuhimu mkubwa sana wa kujenga barabara hizi ambazo zitakuwa na gharama nafuu lakini zitaweza kuishi kwa muda mrefu zaidi na kupunguza adha ya wananchi kuharibikiwa na barabara na kupata changamoto kutokana na barabara zetu hizi kuharibika na hasa kipindi cha mvua. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nimeuliza maswali kuhusu uzio wa shule za mabweni za wasichana. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa majengo, madarasa pamoja na mabweni ili ziende sambamba na uzio wa shule hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mwaka 2023 Shule ya Sekondari ya Uyungu, Kidato cha Sita walivamiwa na vibaka. Je, hawaoni sababu ya kuweka uzio katika shule hizo ambazo ni Shule ya Margaret Simwanza Sitta pamoja na Shule ya Sekondari ya Urambo Day?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa ni mtetezi mkubwa sana wa mazingira ya wanafunzi kwa kuhakikisha wanasoma katika mazingira yaliyo mazuri, bora na yenye usalama zaidi. Naomba nijibu maswali yake yote mawili kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu ikiwemo hiyo ya uzio. Kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba Serikali imeweka kipaumbele zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya msingi ambayo inawawezesha wanafunzi wote kupata fursa ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa uzio katika shule zetu hizi, naomba nimkumbushe Mkurugenzi wa Halmashauri afanye tathmini na kuweka katika mipango ya kibajeti katika halmashauri inayotokana na mapato ya ndani ili kuona kwa kadiri fedha zitakapokuwa zinapatikana waweze kujenga uzio huo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itajenga uzio kwenye Sekondari ya Mlongwema, Ubiri pamoja na Shambalai?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee majibu yangu ya awali kwamba, miradi ya Serikali Kuu ni miradi ambayo ni complimentary, lakini halmashauri zenyewe zina wajibu wa kuhakikisha kwamba na zenyewe zinakuwa ni sehemu ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hii muhimu. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumkumbusha Mkurugenzi aweze kufanya tathmini na kuweka katika mipango ya kibajeti ili fedha kadiri zitakapokuwa zinapatikana waweze kujenga uzio katika shule aliyoitaja.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kawe lina mashina zaidi ya 1,000 na takribani kila shina lina barabara sita na huu ni mzigo mkubwa. Serikali ikitumia utaratibu wa kawaida inaweza isiweze kumaliza mzigo wa barabara hizi.

Je, Serikali ina mpango gani wa ziada wa kumaliza Barabara hizi ambazo ni karibu elfu sita na kitu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli tunamwona jinsi gani anavyotembelea maeneo mbalimbali kutazama na kuleta msukumo katika kuhakikisha wananchi wake wanapata barabara zilizo bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kwamba Serikali inatenga fedha katika Manispaa ya Kinondoni shilingi bilioni saba kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia barabara hizi za TARURA, lakini pia Manispaa ya Kinondoni ipo katika Mradi wa DMDP II ambao ni mradi wa jumla ya USD milioni 438. Mradi huu utaenda kusaidia sana katika kurekebisha barabara katika jimbo lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa sababu ninyi mkiwa kama sehemu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni mmeweza kununua mitambo kupitia mapato ya ndani; mmenunua wheel loader, grader na excavator ambazo sasa hivi zipo katika hatua ya clearance na wiki ijayo mitambo hii itakuwa imetoka. (Makofi)

Sasa ninawapongeza kwanza, lakini ninachukua nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwagiza Mkurugenzi, mara tu mitambo hii itakapotoka iingie site, ifike katika Jimbo la Kawe, ianze kuchonga barabara ili wananchi waweze kupata barabara nzuri kabisa. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zinazolikuta Jimbo la Kawe zinafanana kabisa na zile za Jimbo la Kigamboni, maeneo ya Kisarawe II, maeneo ya Kigogo ya Viwandani, Mwasonga, Tundwi Songani, Kimbiji na Mkundi katika Kata ya Pemba Mnazi, maeneo haya barabara zimeharibika kabisa na mvua.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kurekebisha barabara hizo ili zikae vizuri na wananchi wa maeneo hayo waweze kupita vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kupaza sauti yake ili kuhakikisha wananchi wanaweza kutengenezewa barabara hizi ambazo ni muhimu sana kiuchumi, lakini kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kila mwaka wa bajeti inatenga fedha kwa ajili ya kuhudumia barabara hizi za TARURA ikiwemo katika Jimbo la Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nafasi ya Mkurugenzi kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha na yeye anaweza kusimamia katika kurekebisha barabara hizi. Mheshimiwa Mbunge ule Mradi wa DMDP II ambao ni mradi wa jumla ya USD milioni 438 na wenyewe unaenda kunufaisha Manispaa ya Kigamboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua hii tayari kazi zilishatangazwa na tayari wakandarasi wameshapatikana, ipo katika hatua za mwisho kabisa za ununuzi na mikataba itasainiwa ili wakandarasi waingie site waanze sasa kurekebisha barabara. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa halmashauri nyingi sasa zimeonesha uwezo wa kununua mitambo kwa ajili ya kuchonga barabara, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vitengo maalumu vya maintenance katika halmashauri hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni mawazo mazuri sana ya Mheshimiwa Mbunge, tumeyapokea, tutayachakata na tutayafanyia kazi. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa TAMISEMI alifanya ziara katika Jimbo la Tarime Vijiji, Makao Makuu ya Halmashauri Nyamwaga na aliahidi ujenzi wa kilometa mbili pale Makao Makuu, ninapenda kujua kama ile ahadi bado ipo au imeyeyuka? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nipokee alichokisema Mheshimiwa Mbunge na baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tutafanya ufuatiliaji ili kujua imefikia hatua gani, utekelezaji wa ujenzi wa hizi kilometa mbili zilizoahidiwa na Mheshimiwa Waziri.
MHE. DKT. JOHN J. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya barabara za vumbi iliyoko kule Jimboni Kawe inafanana sana na hali ilivyo jimboni kwangu ambapo barabara nyingi zinapanda mlimani, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuongeza bajeti ili kuondoa hiyo changamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akisemea sana mazingira ya jimbo lake na hasa kwa sababu ya mazingira ya kuwa katika milima. Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari tumekuwa tukiwasiliana mimi na wewe. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha tunatengeneza msukumo ili kuweza kupatikana bajeti ya kutosha ambayo itakuja uhudumia barabara katika jimbo lako. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule hii iko barabarani kabisa, njia kuu ya kutoka Kahama kwenda Rwanda na watoto wanakuwa kwenye risk kubwa sana, je, pamoja na kujenga miundombinu ya madarasa, hamuoni kuwa uzio nacho ni kipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kumekuwa na matukio mengi ya watoto kuvamiwa na kuibiwa mali zao na wazazi kuwa na wasiwasi na usalama wa watoto wao, je, hamwoni kuwa kuna umuhimu sasa wa kutafuta fedha za dharura ili uzio uweze kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge yote mawili kwa pamoja; kwanza nianze kwa kumpongeza sana kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba watoto wanasoma katika mazingira yaliyo salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu kwa sasa kipaumbele chake ni kuhakikisha kwamba inajenga miundombinu ya msingi ambayo itawezesha kupokea na kuongeza udahili wa wanafunzi, lakini masuala ya usalama wa wanafunzi wanapokuwa shuleni pia ni ya muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi, afanye tathmini katika shule aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuona mazingira na aweke katika mipango ya mapato ya ndani ya halmashauri na kutenga bajeti kwa ajili ya kwenda kuweka uzio katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tumejengewa shule ya wasichana ya mkoa inaitwa Solya Girls Secondary School na tayari tuna udahili wa watoto 288 wa kidato cha kwanza na kidato cha tano lakini shule ile haina uzio.

Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba ili kuwalinda watoto wa kike wanajenga uzio? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anazungumzia maslahi mapana kabisa na hasa ya usalama kwa wanafunzi wetu katika shule hii mahsusi kabisa ya wasichana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali Kuu imeshatoa fedha shilingi 50,500,000 katika shule zote hizi za mikoa za wasichana za sayansi kwa ajili ya kujenga uzio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaomba niendelee kutoa msisitizo kwa Wakurugenzi kupitia mapato ya ndani ya halmashauri na wenyewe waweze kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za kuboresha miundombinu na kuimarisha usalama wa Watoto, hasa katika shule hizi. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi tunayo shule ya wasichana inaitwa Kilindi Girls na ni kwamba eneo hilo ambalo ipo hii shule ni eneo ambalo linazungukwa at least na msitu. Sasa kwa usalama wa wasichana ni jambo muhimu sana, je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kulipokea hili na kulifanyia kazi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuzungumzia masuala ya kuimarisha usalama wa wanafunzi wetu wanapokuwa shuleni. Ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hili tumelipokea na tutafanya jitihada kwa sababu Serikali imeanza kujenga miundombinu hii kwa awamu. Awamu ya kwanza miundombinu hii ya shule imepatikana na ndiyo maana watoto wameweza kuanza kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila awamu Serikali itakuwa inaleta fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha miundombinu iliyobakia. Kwa hiyo, nimelichukua jambo lako hili Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kulifanyia kazi.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, wakati tunasubiri mpango wa Serikali wa hizi barabara nyingine kujengwa, je, hamuoni ipo sababu ya kurudisha mawasiliano katika barabara ya Tinyango kwa sababu kuna uharibifu mkubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Mama Kibonge katika Kata ya Buza Jimboni Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana yenye lengo la kutetea wananchi, lakini kuhusiana na swali lake la kwanza naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ya Tinyango itajengwa kwa kutumia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke pamoja na Meneja wa TARURA wa Temeke kuhakikisha kwamba wanatangaza kazi zote zile zilizobakia ambazo ni za matengenezo na zinatokana na fedha ya mapato ya ndani katika halmashauri wazitangaze haraka iwezekanavyo ili wakandarasi wapatikane waanze kuzijenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, barabara hii ya Tinyango ni miongoni mwa barabara moja ambayo ipo katika utaratibu huo na kwa wakati huu naomba niendelee kusisitiza kwamba wananchi waweze kutumia njia mbadala ambazo zimewekwa. Kuna njia mbili; kuna njia ile ya Mbande - Kisiwani, lakini kuna ile ya Uvikiuta – Tinyango. Kwa hiyo, mpaka ile barabara ya Tinyango itakaporudishiwa mawasiliano wananchi waweze kutumia barabara hii. Namwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke aharakishe utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kuhakikisha inafanya matengenezo na kuboresha barabara zetu hizi za wilaya. Nimhakikishie kwamba barabara yake hii ambayo ipo Buza na yenyewe ipo katika utaratibu wa kufanyiwa matengenezo katika mwaka huu wa fedha. Namwahidi itatengenezwa, itarekebishwa na wananchi wake wataweza kuitumia kwa manufaa mapana ya kiuchumi na ya kijamii.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali na kuishukuru sana kwa kutupa kiasi hicho cha fedha ambacho kwa kweli kwa kiasi kikubwa kimeweza kusaidia miundombinu katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja tu. Hizi shule zote ambazo nimezitaja hapa ni shule za Kidato cha Tano na cha Sita lakini zina uhitaji mkubwa sana sana hususan shule ya Sekondari ya Mkindi na Shule ya Sekondari Vungwe. Hizi shule tuna wanafunzi na kila shule ina wanafunzi 600 na hawana bwalo la kulia chakula. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuiona hii kama ni dharura ili kuweza kurahisisha kupata huduma kwa wanafunzi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli amekuwa akifuatilia sana maslahi mazuri na mapana ya wanafunzi katika jimbo lake kwa kuhakikisha anaendeleza miundombinu hii katika shule hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari Serikali imeshaanza na kila mwaka inatenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii. Naomba nimtoe hofu kwamba Serikali inalichukua hili na tutalifanyia kazi kwa ukaribu. Tutazungumza mimi na wewe tuone ni namna gani tunaweza kuhakikisha miundombinu hii muhimu inapatikana kwa ajili ya wanafunzi wetu hawa katika shule hizi alizozitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Sekondari ya Kata ya Bulamatamu haina mabweni na kuna mazingira magumu sana. Ni lini Serikali itapeleka mabweni kwenye shule ya sekondari hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kuwasemea wananchi wake ili kuhakikisha wanapata miundombinu bora kabisa katika shule hizi na hasa hii ya sekondari aliyoitaja ambayo iko Kata ya Bulamata.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali kila mwaka inatenga fedha kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri na kupitia Serikali Kuu kwa ajili ya kuendeleza muindombinu katika shule zetu hizi. Pia, Serikali imekuwa ikiendeleza hii miundombinu kwa awamu. Kwa awamu ya kwanza, tayari majengo yamejengwa ambayo yamewezesha udahili wa wanafunzi na wameanza kuyatumia majengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa awamu inayofuata tutaendelea kwa kadiri fedha zinavyokuwa zinapatikana na zinavyotengwa kwenye bajeti, tutazileta kwa ajili ya kuhakikisha tunakamilisha miundombinu mingine iliyobakia, hususan hii uliyoitaja katika Shule hii ya Bulamata. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Sekondari Maili Sita watoto wanatembea umbali mrefu sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga bweni na bwalo? Tayari tumeshaandaa eneo la kutosha na wananchi wako tayari kushirikiana na Serikali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kuwasemea wananchi wake ili kuhakikisha wanapata miundombinu iliyo bora kabisa katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tayari ilianza; imejenga shule mpaka kwa ngazi iliyofikia. Namhakikishia kwa kadiri tutakavyokuwa tunapata fedha, awamu inayofuata tutaangalia ni namna gani nzuri ya kuleta fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hii ya bweni na bwalo kwa kushirikiana na Halmashauri, kwa maana ya mapato ya ndani na kwa kutumia fedha kutoka katika Mfuko wa Serikali Kuu. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Serikali ya Isongole haina mabweni kabisa kwa form five na form six ukizingatia shule hiyo inafanya vizuri sana. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni kwenye shule hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele kikubwa sana kujenga mabweni kwa ajili ya kuruhusu udahili na kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa awamu. Kwa hiyo, Serikali itaendelea na utaratibu huo Shule hii ya Isongole iweze kupata mabweni, ili iweze kupandishwa hadhi kuwa Kidato cha Tano na cha Sita, wanafunzi wetu wapate sehemu nzuri ya kusomea na walimu wapete sehemu nzuri ya kufundishia. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli kabisa, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema, kumekuwa na drop out au ku-miss kuhudhuria masomo kwa wanafunzi kati ya siku tatu mpaka tano na wakati mwingine inaenda mpaka siku saba. Je, ni kwa nini sasa Serikali isiweke mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba, inagawa hizi sanitary pads kwa shule zote kwa usawa ili watoto ambao wamefikia umri wa kuingia kwenye siku zao waweze kuhudhuria masomo bila kukatisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa Serikali imeelekeza kwamba, wana mkakati wa kujenga chumba maalum, lakini pia, kumekuwa hakuna usiri, kwani watoto wanachanganyika, wengine ni wa umri mkubwa na wengine umri ndogo. Kwa hiyo, wanavyoenda kufanya changes kule inakuwa ni kama vile inaleta embarrassment. Ni kwa nini Serikali isiweke mkakati madhubuti sasa hivi wa kuhakikisha kwamba, wanarekebisha vyoo vyote vinakuwa na chumba maalum, kwa ajili ya watoto wetu kwenda kubadilishia pads wakiwa katika siku zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, yote kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ana hoja ya msingi. Kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, Serikali inatambua uhitaji wa vifaa vya kujisitiri watoto hawa na ndiyo maana imevunja ukimya na imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba jamii inatambua umuhimu wa hedhi salama na kusaidia kupatikana kwa vifaa vya hedhi kwa wasichana.

Kwa hiyo, Serikali tayari imekuwa inatoa vifaa hivi kwa ajili ya watoto kuvitumia pindi wanapokuwa kwenye hedhi, lakini imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika jitihada hizi ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri kwa watoto wetu kujihifadhi kipindi wanapokuwa kwenye hedhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la chumba maalum. Kama nilivyojibu hapo mwanzo kwamba, Serikali imetoa Mwongozo na mpaka wakati huu katika ujenzi wa miundombinu ya shule, ramani zinazingatia kuwepo kwa chumba maalum kwa ajili ya watoto kujisitiri pindi wanapokuwa kwenye hedhi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inaendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha watoto wetu hawakosi kwenda shule kwa sababu wako kwenye hedhi. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali iliondoa tozo katika taulo za kike na baadaye ikairudisha. Ni lini tutakaa tena na kuweza kuondoa tozo hizo ili kusaidia watoto wa kike kuzipata kwa bei ya chini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, suala hilo ni la kikodi. Ni hoja ambayo wenzetu wa Wizara ya Fedha nadhani watakuwa wameisikia.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, wewe lichukue. Ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, pia, mimi nalichukua kwa niaba yao. Nitalifikisha.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na napenda kuuliza swali moja tu la nyongeza. Kwanza nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni moja tu. Je, ni lini sasa shule hii ya watoto wenye mahitaji maalumu itajengwa katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuona umuhimu wa kuwasemea watoto wenye mahitaji maalumu ili waweze kupata maeneo au miundombinu mizuri kwa ajili ya kupata elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi nimesema sasa hivi Serikali inaweka kipaumbele kikubwa na msisitizo mkubwa wa kuhakikisha kwamba shule zetu hizi tunazojenga zinakuwa jumuishi kwa maana zinaweza kupokea wanafunzi wa kawaida, lakini na wale wanafunzi wenye mahitaji maalumu na Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba kwenye hizi shule inapeleka vifaa visaidizi, lakini inapeleka walimu wa elimu maalumu, lakini fedha ya chakula kwa ajili ya watoto wote wenye mahitaji maalumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule hizi ambazo ni mahususi kabisa kwa ajili watoto wenye mahitaji maalumu zipo, kuna shule moja ipo Arusha, Shule ya Sekondari Patandi ambayo inapokea watoto wenye mahitaji maalumu na inawahudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha huu 2024/2025 kuna shule ya watoto wenye mahitaji maalumu inatarajiwa kujengwa katika Halmashauri ya Bahi, lakini msisitizo mkubwa ni kuhakikisha kwamba shule zetu zinakuwa na miundombinu ambayo itawezesha ziwe jumuishi kwa ajili ya kuwahudumia pia watoto wenye mahitaji maalumu.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba ufahamu hivyo tunataka watoto wetu wasome kwa pamoja. Wale wenye mahitaji maalumu na hawa wengine washirikiane kwa pamoja ili wote kwa pamoja waweze kupata elimu, lakini wengine hao wenye mahitaji wanakuwa wanasaidiwa. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ilikamilisha taratibu zote na taarifa za RCC ninaimani iko katika Ofisi ya TAMISEMI. Sasa kwa vile katika hatua hizo, Kijiji cha Mbalizi ambacho hakipakani na Vijiji vingine vya Kata za Utengule Usongwe, kimezungukwa na Kata za Nsalala ambayo ni tofauti na Kata ya Iwindi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha mipaka ya Kijiji cha Mbalizi na kwa vile kina watu zaidi ya 40,000 ili kigawanywe kupata Kata mpya ya Mbalizi, Mtakuja Pipeline na Utengule Usongwe?

Swali la pili, kwa vile mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini tuna vitongoji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambavyo vina wakazi wengi sana kikiwemo Kitongoji cha Nzunya katika Kata ya Tembela.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipandisha hadhi hivi vitongoji ili viendane na sheria za nchi na ziweze kushiriki vizuri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa uwakilishi mzuri wa wapigakura wake, lakini naomba maswali yake yote mawili niyajibu kwa pamoja:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Ofisi ya Rais-TAMISEMI imepokea maombi haya na tathmini inaendelea, kwa ajili ya kubaini uhitaji. Ila sasa, kwa wakati huu kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha na kwa kuzingatia kwamba, pia, Ibara ya 9 (a) (4) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha inaimarisha Serikali za Mitaa, ili ziweze kutimiza wajibu wake. Kwa mantiki hiyo, kwa sasa Serikali inahakikisha kwamba, inaajiri watumishi kwenye maeneo ambayo yana upungufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Serikali inajielekeza zaidi katika kuweka miundombinu muhimu kama vile ofisi, lakini kama vile huduma za afya, shule, miundombinu ya barabara, umeme na maji. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kumuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba, waendelee kushirikiana na Serikali kwa maana ya kutizama katika kipaumbele cha kuhakikisha huduma za kijamii na za kiuchumi zinaweza kuwafikia wananchi na wakati ukifika Serikali itafanyia kazi maombi haya ya kuanzisha mamlaka au maeneo mapya ya utawala, lakini kwa wakati huu kipaumbele ni kuhakikisha maeneo ya utawala yaliyopo yanaimarishwa zaidi.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Mgogoro wa mpaka kati ya Mkoa wa Singida na Mkoa wa Tabora ni wa muda mrefu sana, lakini uliisha Mwaka 2019. Kilichobaki ni Serikali, kwa maana ya Wizara ya TAMISEMI na Ardhi, kwenda kuweka beacon kwenye mpaka ambao ulikubalika. Je, Wizara inasema nini kuhusu hatua hiyo? Kwa nini imechelewa na tunakwenda kwenye uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilichukue suala hili. Tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi ambao ndio wenye mamlaka kimsingi, ili tuone hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa, kugawanyika kwa mipaka hii ni mahitaji ya wananchi ambayo yanasababisha wao kupata changamoto. Kwenye Kata ya Chilulumo na Kata ya Mkulwe vinatokea Vijiji vya Sanja, Kaonga pamoja na Chuo ambavyo vinaonekana kwamba, vinapaswa kupata Kata mpya na ni mahitaji makubwa ya wananchi hao na tumeshaanza taratibu kwa ngazi ya chini. Je, kama taarifa hizi zitawafikia au zimekwisha kuwafikia, mnatuhakikishia kwamba, mtatusaidia kupitisha, ili kupata Kata mpya katika vijiji hivyo na viweze kushiriki uchaguzi mwakani, Mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kujibu katika jibu la msingi. Serikali kwa wakati huu inazingatia Ibara ya 9(a)(4) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 ambayo inataka kuimarishwa kwa Serikali za Mitaa, ili ziweze kutimiza wajibu wao. Kwa hiyo, kama nilivyosema hapo awali, kwa wakati huu kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha inaboresha maeneo ya utawala yaliyopo na siyo kuanzisha maeneo mapya ya utawala, lakini wakati ukifika, Mheshimiwa Mbunge, tathmini itafanywa, ili kubaini uhitaji na uhitaji ukibainika bila shaka maeneo hayo mapya ya utawala yataanzishwa.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Wakati Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipotembelea Wilaya ya Nanyumbu mapema Mwezi wa Tisa, mwaka jana, Waziri mwenye dhamana aliahidi, mbele ya Mheshimiwa Rais, kuipatia Halmashauri hii ya Nayumbu magari matatu muhimu, kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mtambaswala ambacho kiko kilomita 70 kutoka Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Nanyumbu ambacho kiko kilomita 45 kutoka Makao Makuu ya Wilaya na Kituo cha Afya cha Michiga ambacho kiko kilomita 30 kutoka Makao Makuu ya Wilaya, Mheshimiwa Rais alihakikishiwa na Mheshimiwa Waziri kwamba, magari haya yatapatikana mara baada ya kurudi. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza agizo lake ambalo Mheshimiwa Waziri alilitoa mbele ya Mheshimiwa Rais kwa wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya uwakilishi kwa wananchi wake, lakini kuhusu swali lake hili la msingi ni kweli, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI alitoa ahadi ya kuongeza gari la kubebea wagonjwa katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge magari kwa wakati huu tayari yameshafika bandarini na kinachoendelea ni taratibu tu za kuyatoa na kufanya usajili, kwa kadiri Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI alivyoahidi. Basi, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge utapata magari hayo.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Waziri wa TAMISEMI alivyotembelea Hanang aliahidi magari mawili na sasa hivi tumepata gari moja tu. Je hilo gari la pili tutalipata lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tutakaa, ili tuweze kufuatilia ahadi hiyo ni ya lini na tutazame utekelezaji wake.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kituo cha Afya cha Soya ni cha muda na hakina gari la wagonjwa. Ni lini sasa Serikali itapeleka gari la wagonjwa katika kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu mkubwa sana wa kuwa na magari ya kusafirishia wagonjwa katika vituo vyetu vya kutoa huduma za afya ya msingi imekuwa ikifanya utaratibu wa kununua na kupeleka magari haya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa kadiri ya upatikanaji wa haya magari na kwa kuzingatia vipaumbele vya uhitaji, basi gari hili litafikishwa katika jimbo lako, kwa ajili ya kuhudumia kituo ulichokitaja.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itanunua magari, kwa ajili ya vituo vya afya vya Mabama na Upuge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itaendelea kuagiza magari haya ya kusafirishia wagonjwa (ambulance), kwa ajili ya kusambaza katika maeneo tofauti-tofauti katika vituo hivi vya kutolea huduma ya afya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha Serikali italeta magari haya katika vituo ulivyovitaja.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Kata ya Makonde ambacho kiko ziwani kinategemewa na kata tano na mawimbi yakitokea ziwani usafiri kwenye maji hauwezekani. Je, ni lini Serikali itapeleka gari, kwa ajili ya kusafirishia wagonjwa wa Kata hizi tano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikinunua magari haya ya kusafirishia wagonjwa, kwa ajili ya kuyasambaza katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya ya msingi. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa kadiri ya fedha zinavyopatikana na magari haya yanavyonunuliwa na kwa kuzingatia vipaumbele, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ataletewa magari haya, kwa ajili ya kutoa huduma.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri ya Serikali katika kuendelea kuajiri walimu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira ya kazi na motisha kwa walimu, hususan wale wanaoishi na kufanya kazi vijijini? Hili ni muhimu, ili kuzuia walimu wengi wanaokimbilia mijini na kusababisha upungufu wa walimu vijijini. Ahsante.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni hoja ya msingi na Serikali inatambua umuhimu wa motisha kwa walimu, hasa wale wanaofanya kazi vijijini, ili waweze kufanya kazi kwa hamasa. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali katika eneo hili kwanza ni kujenga nyumba za kuishi kwa walimu, ili kuboresha mazingira yao ya kazi wanapokuwa wanafanya kazi katika maeneo yao ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imekwishajenga nyumba 253 ambazo zinabeba familia mbili. Kwa hiyo, hii ni sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya walimu wanaofanya kazi vijijini.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, walimu wanalipwa malimbikizo yao na stahiki zao kwa wakati. Katika Mwaka 2022/2023 Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 22.73 za madeni ya walimu yasiyokuwa ya mishahara. Kwa hiyo, hii ndiyo mikakati ambayo Serikali inaendelea kufanya, ili kuhakikisha walimu wanaofanya kazi vijijini wanafanya kazi kwa hamasa.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali kwa majibu yake mazuri. Pomoja na majibu hayo, je, Serikali haioni ipo sababu ya kuleta pesa kwa haraka, kwa ajili ya mabinti hawa 500 ambao wanakula hovyo-hovyo bila kuwa na bwalo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Shida iliyopo Mkugwa Sekondari, ipo pia Usagara na Kumgogo. Je, Serikali haioni ipo sababu ya kutenga pesa kwa haraka kwa hizi shule za kidato cha tano na sita, ili kunusuru maisha ya Watoto hawa mashuleni?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Tayari nimekwishakutana na Mheshimiwa Mbunge na tumezungumza kwa kina kuhusiana na changamoto hizi za miundombinu katika shule zake alizozitaja. Kwa hiyo, naendelea kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama tulivyoongea, suala hili linafanyiwa kazi na kupitia mapato ya Halmashauri, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga bwalo katika Shule hiyo ya Mkugwa Sekondari.

Mheshimiwa Spika, pia, kuhusu swali lake la pili la kujenga miundombinu katika Shule ya Kidato cha tano na sita pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaliwekea kipaumbele suala hili, ili fedha ziweze kutengwa na kujenga miundombinu hii muhimu kwa ajili ya wanafunzi katika shule hizi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali madogo mawili. Kwanza, napongeza majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Je, walimu kuandaa vifaa vya maabara hamuoni kama mnapunguza muda wa mwalimu kuandaa masomo yake?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Kutunza Maabara ni fani inayotambulika; je, kwa kufanywa na mtu ambaye hana utaalamu hamuwezi kusababisha madhara ya kiutendaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nijibu maswali yake yote mawili kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuhusu upungufu wa wataalamu wa maabara lakini Serikali inaendelea na jitihada ya kuhakikisha kwamba inaajiri wataalamu hao wa maabara. Kwa wakati huu Serikali inatumia walimu hawa wa sayansi ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaendelea na masomo yao. Sasa sababu ya msingi pia ya kuwatumia walimu wa sayansi ni kwamba walimu wa sayansi na wataalamu wa maabara fani zao zinaingiliana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika mafunzo mwalimu wa sayansi anaweza kufanya kazi ile ambayo mtaalamu wa maabara anaifanya. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada hizi ni za makusudi kabisa ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaendelea kupata elimu na hasa katika masomo ya sayansi. Serikali inaendelea na utaratibu wa kuajiri hawa wataalamu wa maabara na wakishaajiriwa wale walimu wa sayansi wataendelea na kazi zao nao wataalamu wa maabara wataendelea na kazi zao za kitaalamu.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, lakini bado kuna tatizo kubwa sana la watoto wetu kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu kutokana na kwamba kuna upungufu mkubwa sana wa mabweni. Sasa, Serikali ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha kwamba inatenga fedha kwa ajili ya kumalizia mabweni ambayo yalianzishwa na nguvu za wananchi, lakini mabweni ambayo Serikali ilitenga pesa lakini bado hayajakamilika na mabweni hayo yameanza kupoteza ubora wake kutokana na miundombinu hiyo kuharibika kutokana na mvua zinazonyesha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; napenda kuelewa, upi mkakati wa Serikali wa kuwaajiri patrons na matrons katika mabweni ambayo tayari yamekamilika kwa ajili ya malezi ya watoto wetu shuleni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwatetea wanafunzi wa mkoa wake. Nataka kusema kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na mabweni na hasa katika shule za sekondari. Kwa hiyo nachukua nafasi hii kuzielekeza halmashauri zote ikiwemo Halmashauri kutoka katika Mkoa wa Katavi, ziweze kushirikiana na wananchi katika kujenga hosteli hizi na kuweza kuzihudumia kutokana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema katika majibu yangu ya msingi, kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha inajenga mabweni kwa ajili ya kidato cha tano ili kuhakikisha wanafunzi watakaofaulu kidato cha nne wengi au wote wanapata nafasi ya kuingia kidato cha tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na kupata walezi katika mabweni, naomba nichukue nafasi hii pia kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa halmashauri kuhakikisha kwamba wanasimamia kila shule iweze kuwa na walimu ambao ni walezi katika mabweni kwa sababu ni muhimu sana katika malezi ya wanafunzi. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imefanya jitihada kubwa sana na kuhamasisha wananchi kujenga mabweni na yamejengwa mabweni kwenye maeneo ya Shule ya Sekondari ya Ilangu, Shule ya Sekondari Majalila na Shule ya Sekondari Bulamata. Je, ni lini wataenda kupeleka fedha ili hayo mabweni yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi yaweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa mabweni kwa wanafunzi hawa, naomba pia nichukue nafasi hii kuendelea kusisitiza maelekezo na maagizo, kwamba halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Tanganyika kufanya tathmini ya maboma hayo ambayo wananchi wametumia nguvu yao kubwa sana kuwekeza katika ujenzi ili waweze kuweka katika mipango ya bajeti za halmashauri kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni hayo.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wananchi wa Kata ya Lumuli, Jimbo la Kalenga wameweza kujenga maboma kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Lumuli ambayo ni kwa ajili ya wasichana lakini hayajakamilika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanakamilisha mabweni hayo ili wanafunzi waweze kutumia kwa sababu halmashauri imekuwa na mzigo mkubwa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nichukue nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri katika Jimbo hilo la Kalenga, atume timu waende wakafanye tathmini ya kuona majengo hayo ili iweze kuwekwa mikakati ya kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni hayo. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nitauliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, mwezi wa Pili nilisimama kwenye Bunge lako Tukufu nikauliza juu ya barabara inayotokea Mawela kuelekea Kituo cha Walemavu mpaka Kituo cha Afya cha Uru Kusini nikajibiwa kwamba barabara hiyo itatengewa bajeti 2024/2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwenye takwimu za Mheshimiwa Waziri, barabara hiyo haipo. Ni lini sasa barabara hiyo itajengwa ili kunusuru maisha ya wananchi wa Moshi Vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wakati TARURA wanaingiza barabara nyingi kwenye mfumo, barabara nyingi za Moshi Vijijini ziliachwa nje ya mfumo kwa kusahaulika. Ni lini sasa Serikali itaainisha barabara hiyo na kuzitengea bajeti ili ziweze kutengenezwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kupaza sauti kuhakikisha kwamba wananchi wanapata barabara nzuri. Kuhusu swali lake la kwanza, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 Barabara hii ya Mawela Kanisani kwenda Zahanati ya Mawela itafanyiwa matengenezo ili iweze kupitika na iweze kutoa huduma iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ambalo amezungumza kuhusiana na kuweka katika mtandao, kuingiza katika mfumo au mtandao wa barabara zinazosimamiwa na TARURA, barabara katika jimbo alilolitaja, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kusajili barabara hizi za Wilaya kuziingiza katika mtandao unaosimamiwa na kuhudumiwa na TARURA, mchakato huo unaanza kwenye Halmashauri kupeleka katika Road Board (Bodi ya Barabara) ya Mkoa na baada ya hapo inawasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ili waweze kupitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tayari vikao hivyo vimeshaketi, Tarehe 13/11/2023 Kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa kilikaa na kupitisha barabara zenye urefu wa kilomita 413. Haya ni maombi kabisa kwa ajili ya kupitishwa ili yaweze kuingia katika mtandao utakaohudumiwa na TARURA. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika swali lake alilouliza, Serikali inachukua hatua. Barabara hizi tayari zimeshapitishwa katika utaratibu, bado tu kuthibitishwa ili zianze kuhudumiwa na TARURA.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi ni Diwani katika Halmashauri ya Moshi DC. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini ni lini hasa barabara hiyo ya kutoka Mawela kwenda Shule ya Okaseni kupitia kambini ikiunganisha na hicho Kituo cha Walemavu pamoja na hiyo dispensary nayo itatajwa katika barabara ambazo zimewekewa bajeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake lenye tija kubwa sana kwa wananchi wa Moshi DC. Kama nilivyotangulia kujibu ni kwamba, Serikali inafanya jitihada na tayari imeshafanya mchakato wa kuingiza na kutambua barabara katika Halmashauri ya Moshi, katika Wilaya ya Moshi DC ambazo zitaingia na kuanza kuhudumiwa na TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejibu kwamba, katika mwaka huu wa fedha barabara hii ya Mawela Kanisani kwenda zahanati ya Mawela zitafanyiwa ukarabati ili ziweze kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mchakato upo, yaani unaendelea. Barabara hii itaingizwa rasmi katika barabara zinazotambulika na kuhudumiwa na TARURA, lakini katika mwaka wa fedha huu tayari kuna mchakato wa kuhakikisha kwamba hii barabara inakarabatiwa na inaweza kuhudumia watu.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Magunga, Kata ya Maboga, kwenda Wasa imeharibika sana.

Je, ni lini sasa Serikali itaitengeneza hiyo barabara kwa kiwango cha changarawe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba inahudumia barabara, hasa hizi za TARURA ambazo zinabeba umuhimu mkubwa sana kuwahudumia wananchi kiuchumi na kijamii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama vile ambavyo Serikali tayari imeanza kuhudumia barabara hizi, barabara yake hii na yenyewe itahudumiwa ili iweze kuwa katika hadhi nzuri na iweze kuwahudumia wananchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Barabara ya Ikola kwenda Kata ya Isengule, Vijiji vya Isengule, Shukura na Kasangatongwe ni barabara ambayo imeharibika kwa kiwango kikubwa sana baada ya mvua zilizonyesha na kuwafanya wanafunzi kushindwa kusoma kwa sababu ya kuvunjika kwa daraja. Ni lini Serikali itaenda kuikarabati hiyo barabara ili wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara hizi, hasa kiuchumi na kijamii; na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii na daraja hili ambalo lipo linawezesha watoto kwenda shule, basi naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo kazini na itahakikisha inafika na inaihudumia barabara hii ya Ikola – Isengule na hasa katika eneo hili la daraja ambalo linawasaidia wanafunzi kuweza kufika katika shule.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa vipande vya barabara kutoka Sangisi – Akeli hadi Ndoobo na Sangisi – Chuo cha Jeshi Duluti hadi Nelson Mandela? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikikarabati na kujenga barabara zetu hizi za TARURA kwa awamu. Mheshimiwa Mbunge katika jimbo lake barabara hizi za Wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA zimekuwa zikiendelea kutengewa fedha kila mwaka wa bajeti. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itahakikisha barabara hizi alizozitaja katika jimbo lake zinaweza kukarabatiwa na kujengwa.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kuuliza maswali ya nyongeza. Swali langu la kwanza, wananchi wa Kata ya Shilela kwa kushirikiana na Mbunge wao Iddi Kassim Iddi tuliweza kushirikiana na kuanzisha ujenzi wa bweni ambapo wananchi walitoa nguvu zao na Mheshimiwa Mbunge alitoa milioni 20. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwenda kumalizia bweni hilo linalopatikana kwenye Shule ya Sekondari Shilela?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kutambua umuhimu wa watoto wenye mahitaji maalum kuweza kupata haki yao ya msingi ya elimu tuliamua kuanzisha ujenzi wa mabweni mawili la wasichana na wavulana ili kuweza kuwapatia haki watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu. Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili iweze kumalizia mabweni hayo ambayo tangu mwaka juzi bado hayajakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali yake yote mawili kwa pamoja. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada hizi za makusudi za kuweza kuboresha elimu kwa wananchi wake. Nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala kwenda kufanya tathmini katika majengo hayo na kuweka katika mipango ya kibajeti ya halmashauri kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu hiyo muhimu sana katika sekta ya elimu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Ushetu ina shule moja tu ya kidato cha tano na sita, lakini tuna Shule Kongwe ya Tarafa ya Mweli ambayo ina vigezo vyote. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuipandisha shule hii ili iweze kukidhi vigezo vya kidato cha tano na sita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, sawa, namwelekeza mkurugenzi atume watu waende wakafanye tathmini kwenye hiyo shule waone kama kuna miundombinu hitajika ili waweze kutuma maombi Wizara ya Elimu ili waweze kuja kuipandisha hadhi shule hiyo kama inakidhi vigezo. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni dhahiri kwamba drop out nyingi ni kwa sababu ya sekondari za kata ambazo ziko umbali mrefu na solution yake ni kujenga mabweni. Hapa Serikali wanaonesha kipaumbele ni kujenga mabweni kwenye kidato cha tano na cha sita. Tusipowekeza kidato cha nne au cha tatu na cha pili hatutoweza kuwapata wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Je, kwa nini Serikali isibebe vipaumbele vyote viwili, kidato cha tano na kuangalia zile shule zenye umbali mrefu ziweze kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na mabweni katika shule za o-level, lakini pia kwenye shule za kidato cha tano na cha sita, ndiyo maana nimetoa hapa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote kushirikiana na wananchi katika kujenga hostel katika zile shule ambazo ni za kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne. Nimesema kwamba Serikali kwa wakati huu imeweka kipaumbele katika ujenzi wa mabweni katika shule za kidato cha tano na cha sita, kwa hiyo zinaenda kwa pamoja. Halmashauri zitenge fedha katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga mabweni katika shule za sekondari, lakini kwa wakati huo huo Serikali Kuu nayo inaunga mkono jitihada kwa kuhakikisha kuwa, kuna ujenzi wa mabweni katika kidato cha tano na cha sita.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ni kweli aliyoyasema Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini shule ile ina uhitaji mkubwa wa hiyo fence. Naomba basi commitment ya Serikali kwa kuwa fensi hii ina umuhimu mkubwa; je, ni lini wanaweza wakaanza kufanya mpango wa kujenga fence hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nakubaliana na kabisa na Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze sana kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba wanafunzi katika shule hii ya wasichana wanaweza kupata usalama au wanaweza kupata ulinzi mzuri wanapokuwa katika mazingira ya shule. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kupitia mapato ya ndani katika mwaka wa fedha huu ujenzi wa fensi au uzio kwa hadhi ya matofali utaanza. Kwa hiyo, nimhakikishie Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuimarisha usalama katika shule hii na itafanya jitihada kuhakikisha fence inakamilika.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka pesa za kujenga uzio katika Sekondari ya Ubiri – Mlongwema na Shambalai ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa ulinzi na usalama wa wanafunzi wetu wanapokuwa shuleni na Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi sana kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi ambayo itawezesha udahili wa wanafunzi ili waweze kuanza kusoma katika shule hizi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari Serikali imeanza awamu ya kwanza kuhakikisha inaweka majengo ya msingi. Serikali itatafuta na kutenga fedha ili kuhakikisha inaendelea kuimarisha miundombinu mingine ikiwemo ya uzio.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Ahsante sana, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nishukuru kwa ajili ya ujenzi wa hizi shule ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja na bado nyingine za sekondari zimepatikana pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukiangalia rekodi ya Sensa ya Mwaka 2022 Jimbo la Biharamulo ndiyo linayoongoza kwa idadi ya watu kwa Mkoa wa Kagera that means tuna watoto wengi sana ambao bado wanahitaji huduma. Kwa hiyo, ni nini mpango wa Serikali kwenye kutuletea vyumba vya madarasa vingine kwa ajili ya maeneo mengine ambayo bado yana watoto wengi wasiyoipata hiyo huduma kwa Shule za Msingi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia watoto hawa wanapofaulu kwenda Sekondari kwa sababu ni wengi bado wana uhaba wa vyumba vya madarasa na pia wanapoelekea Sekondari. Kwa sababu ni Wizara hii hii na ni jambo hili la vyumba vya madarasa naomba kusikia pia kauli ya Serikali juu ya watoto wanaofaulu kwenda Sekondari Wilaya ya Biharamulo waweze kuongezewa vyumba vya madarasa ili wapate accommodation nzuri wanapoenda sekondari. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ya uwakilishi anayoifanya. Lakini kuhusiana na swali lake la kwanza napenda nianze kukumbushia msingi mzima wa ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi ni kuhakikisha kwamba Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinakuwa na fees code centralization, yaani zinaweza zenyewe kujitegemea kwa maana kutafuta mapato na kuweza kuendeleza miundombinu ya msingi. Kwa sababu jukumu la msingi la kutengeneza miundombinu mbalimbali liko kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lakini tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Miradi ya BOOST kwa ajili ya Shule za Misingi na Mradi SEQUIP ameleta fedha nyingi sana kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na ndiyo maana kila mwaka Serikali imekuwa ikituma fedha katika huu Mradi wa BOOST kwa ajili ya kwenda kuongeza madarasa katika shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika muktadha wa swali lake yeye kwa maana ya Shule za Sekondari. Sasa kwenye swali lake la pili katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 kupitia Mradi wa SEQUIP Serikali imeleta jumla ya shilingi milioni 584.2 kwa ajili ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Lusahunga, lakini pia imeleta jumla ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya nyumba za walimu. Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikileta fedha kila mwaka wa fedha kuhakikisha kwamba inaongeza nguvu pale ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa tayari zimeanza na zenyewe kuunga mkono au kujenga miundombinu hii muhimu katika Sekta ya Elimu. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kuhakikisha inaboresha miundombinu ya Sekta ya Eilimu na pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu wa shule za sekondari zaidi ya 11,300 ikiwa ni pamoja na walimu 205 ambao walihama, lakini nafasi zao bado hazijajazwa. Je, Serikali itajaza lini nafasi za walimu hawa ambao walihama kwa muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ukiangalia idadi ya walimu wa shule za msingi na sekondari ambao tutaletewa bado haitatosha ukizingatia upungufu ambao upo na kikubwa ambacho sisi tunahitaji ni kwamba, pale walimu wanapokuwa wamehama, basi angalau Serikali ijitahidi kujaza zile nafasi kwa wakati. Swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inakuwa ikijaza nafasi hizi za walimu wanaohama kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri sana. Kuhusu swali lake la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, katika ajira mpya zilizotangazwa za walimu Mkoa wa Mtwara atapata walimu 502.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ilishatoa mwongozo wa utaratibu wa uhamisho wa walimu kwamba, uhamisho wa walimu unafanywa kwa kuzingatia kubadilishana, kwa hiyo, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutaendelea kusimamia utaratibu huo ili kuondoa upungufu wa walimu kwenye eneo moja kutokana na uhamisho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutazingatia ili wale walimu wanapohama kwenye kituo kimoja, basi apatikane mwalimu mwingine wa kuja kuziba ile nafasi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tumezingatia sana ombi na mwongozo wako na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutazingatia utaratibu huo.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Mbogwe ina upungufu wa walimu wengi kwenye...

SPIKA: Nenda moja kwa moja kwenye swali la upungufu; watu wote humu ndani tunao huo upungufu, nenda maalum la kwako wewe.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itatoa walimu upande wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Mbogwe kwa maana zina upungufu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ilishatangaza ajira za walimu kuwa katika mwaka huu kutakuwa na ajira za walimu 11,015. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mgao wa walimu hawa, naye katika Wilaya ya Mbogwe atapata walimu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Naibu Waziri amekiri kwamba, ili uhamisho uweze kufanyika lazima kuwe na programu ya kubadilishana, lakini recently katika Wilaya ya Biharamulo tumekuwa tunapokea barua za uhamisho wa watumishi kutoka TAMISEMI bila hata halmashauri kuhusika na chochote.

SPIKA: Mheshimiwa swali, swali, swali.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, sasa uko tayari kutoa kauli ya kusimamisha uhamisho wowote ambao umetokea TAMISEMI moja kwa moja kuja Biharamulo bila programu ya kubadilishana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mimi na yeye tutakaa na tutafanya ufatiliaji kuona tatizo alilolisema katika jimbo lake ili tuweze kuchukua hatua stahiki, lakini msimamo wa Serikali ndiyo huo kwamba, uhamisho unapofanyika, mwalimu anapotoka katika kituo kimoja lazima awe amepatikana mwalimu mwingine wa kuja kuziba pengo lake. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza changamoto ya upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuendelea kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari Serikali imeshatangaza ajira za walimu wapya 11,015 na katika jimbo lako, Mheshimiwa Mbunge, utapata mgao wa walimu hawa wa shule za msingi na sekondari. Tunaendelea kuwasisitiza Wakurugenzi kutumia utaratibu wa kupata walimu wa kujitolea ambao watalipwa posho, pamoja na kuajiri walimu kwa mikataba ili waweze kutosheleza na waweze kuongeza nguvu kuwafundisha wanafunzi wetu.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Je, Serikali itakuwa imewazingatia wale walimu waliojitolea kwa muda mrefu katika ajira hii mliyotoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tayari ilishatoa utaratibu na kwa sababu ajira hizi ziko katika ofisi hii walitoa utaratibu wa kwamba watu waombe, lakini watazingatiwa pia kwa uzoefu na kujitolea kwao katika maeneo ambayo wanafanya kazi kwa maana ya kwamba, kama anazungumzia suala la walimu, basi ni wale walimu ambao wanajitolea. Kwa hiyo, nadhani suala hilo linazingatiwa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, walimu wangu wa Salma Rashid Kikwete Secondary, Kilolambwani pamoja na Kilangala wanakidhi vigezo. Je, ni lini watapata ajira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tayari ilishatoa tangazo la ajira na tayari wameomba. Kwa hiyo, naomba tuache utaratibu wa kufanya mchakato nina imani kwamba, walimu au waliojitolea katika shule alizozitaja Mheshimiwa Mbunge na wenyewe watakuwa na sifa ambazo zinahitajika, kwa ajili ya kuajiriwa kwenye nafasi hizi. Nadhani basi utaratibu utafatwa ili waweze kupata ajira hizi.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, kuna upungufu mkubwa wa walimu wa shule za sekondari na primary katika Mkoa wa Simiyu. Je, ni lini Serikali itatuletea walimu wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika ajira 11,015 za walimu ambazo tayari zimetangazwa na yeye katika mkoa na katika jimbo analotokea atapata mgao wa walimu hawa wa shule za sekondari na shule za msingi.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Shule za Msingi za Itema, Tumbi, Itonjanda pamoja na shule nyingine za Kata ya Kabila zina upungufu mkubwa sana katika Manispaa ya Tabora.

SPIKA: Mheshimiwa swali.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, lini Serikali itapeleka walimu katika shule hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu tayari Serikali imetangaza ajira za walimu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, naye atapata mgao wa walimu hawa katika jimbo lake. Naomba niendelee kutumia fursa hii kuwasisitiza Wakurugenzi na wenyewe waweze kutumia utaratibu wa walimu wa kujitolea na pia, waweze kuajiri walimu kwa mikataba ili kuendelea kupunguza ukali wa upungufu wa walimu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, kwa hakika uhaba wa walimu kwenye shule za sekondari na msingi kwa Mkoa wa Lindi ni mkubwa sana, lakini wimbi la kuhama nalo ni kubwa sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia uhamaji huu mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili la walimu kuhama (uhamisho), Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatia mkazo zaidi ili kuhakikisha changamoto aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge inaweza kudhibitiwa ili walimu wasihame na kuleta upungufu mkubwa katika Jimbo lake. Kwa hiyo, utaratibu utazingatiwa. Pale mwalimu anapohama awe amepatikana mwalimu mwingine wa kuja kuziba pengo.

Mheshimiwa Mbunge, mwaka huu katika ajira hizi 11,015 zilizotangazwa, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge nawe utapata mgao wa walimu wa shule za msingi na shule za sekondari.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeshajenga shule ya vipaji maalum ya wasichana pale jimboni kwangu, je, ni lini sasa italeta walimu ili waanze kutoa huduma ya ufundishaji ulio bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, katika walimu wanaoajiriwa mwaka huu, zile ajira za walimu 11,015, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaleta walimu katika Jimbo lake ambao wataenda kuhudumu katika shule aliyoitaja.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, katika ajira mpya, tungependa kujua kwa Jimbo la Bunda Mjini tutapata mgao hasa katika walimu wa sayansi na hesabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Jimbo la Bunda naye atapata mgao wa walimu wa shule za sekondari na shule za msingi. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa una upungufu mkubwa sana wa walimu, hususan Wilaya ya Kalambo. Je, katika mgao ambao utafanyika, Serikali itahakikisha inapeleka walimu wengi Kalambo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali imetangaza ajira 11,015 za walimu katika mwaka huu. Naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mgao wa walimu hawa 11,015 Mkoa wa Rukwa na wenyewe utapata walimu wa shule za msingi na shule za sekondari. Kwa hiyo, katika Jimbo lake atapata mgao wa walimu hao. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, shukrani sana. Naomba nimwulize Naibu Waziri, hivi Serikali inayo kanzidata inayoonyesha ni walimu wangapi na madaktari wangapi wanaojitolea katika nchi hii kwa madhumuni ya marejeo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari imeanza kutengeneza utaratibu mzuri wa kutunza kumbukumbu na rekodi za watumishi wote wanaojitolea. Pia, kwa sababu tumesema tunajipanga kwenda katika utaratibu wa kuhakikisha wale wanaojitolea wanakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuweza kuajiriwa na kuwa considered kupata ajira hizi, kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ina utaratibu wa kutunza taarifa za hawa watumishi wanaojitolea.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itajenga Barabara ya Kata ya Kilakala ambayo ni reli kwa reli ambayo inakwenda kutokea Kata nyingine ya Vituka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli amekuwa akisemea sana wananchi katika Jimbo lake ili waweze kujengewa barabara zilizo imara na bora. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kuhakikisha kwamba inaendeleza ujenzi na ukarabati wa barabara zetu hizi za TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mbunge, Serikali itaendelea na utaratibu huo kuleta fedha ili hii barabara uliyoitaja ya kutoka kwenye Kata hii ya Kilakala kwenda Vituka na yenyewe iweze kujengwa iwe kwenye hadhi nzuri, wananchi waweze kuitumia.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; sasa, kwa kuwa Serikali iko kwenye mkakati wa kufanya uchambuzi wa kujua gharama, je, imefanya mawasiliano na mkandarasi wa ujenzi wa eneo hilo ili wasifunge barabara ili wananchi waweze kuendelea kulitumia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati wa ujenzi wa Reli ya SGR, limejengwa daraja pale kwenye Mto Ruvu ambalo limepitisha reli tu na hapakuzingatiwa eneo la kupita watu waendao kwa miguu na kwa magari. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja sasa la matumizi ya waendao kwa miguu na magari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri kabisa haya kwa lengo la kuwasemea wapiga kura wake. Kuhusiana na swali lake la kwanza, ninaomba niendelee kumwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba tuendelee kuwafahamisha na wananchi kwamba kufungwa kwa barabara hii ambayo ipo kando ya reli yaani kwa maana ya SGR ni takwa la kisheria. Ni takwa la kisheria kwa tafsiri ya kuimarisha usalama wa wananchi, watumiaji wa reli lakini pia kulinda ile miundombinu ya reli. Kwa hiyo naomba tuendelee kuwaelimisha wananchi ili waweze kufahamu kwamba hili ni suala ambalo linahusu usalama wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, naomba niendelee kumueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua hoja uliyoisema na ni ya msingi. Kwa wakati huu Serikali itafanya jitihada kuhakikisha inaimarisha miundombinu katika eneo hili la Ruvu ambalo mwisho wa siku litakuja kufanyiwa ujenzi kwa maana ya tafsiri tayari SGR inapita katika eneo hili. Tutaimarisha na tutatengeneza mazingira mazuri ili kuweza kutengeneza njia ya wananchi kupita, lakini pia magari kupita na kutengeneza suluhisho la kudumu. Kwa hiyo, hoja yako Mheshimiwa Mbunge tumeipokea na tunaifanyia kazi. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutujibu vizuri na naishukuru Serikali kwa kutupa matumaini kupitia majibu ya swali hili. Maswali yangu ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa, barabara hii ya Mingoi – Kiembeni ya kilometa sita inatumika na wakazi wengi takribani 17,000 wa mitaa kwa mfano Kiharaka, Kiembeni yenyewe, Mingoi, Tungutungu na kadhalika; na kwa kuwa wananchi wa maeneo haya wameunda mpaka Kamati ya Barabara chini ya uongozi wa Ndugu Mapunda ambayo imekuwa ikijichangisha mara kwa mara kutengeneza barabara hii. Sasa, ninamuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, je, yupo tayari kutembelea maeneo haya ili aone athari za mvua hizo za El-Nino na aone kama kiwango hiki kilichotengwa kwenye bajeti hii kama kitatosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa barabara hii linajengwa daraja kubwa la Mpiji Chini, chini ya TANROADS na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Bashungwa alitembelea pale na kutoa ahadi kwamba kuna uwezekano wa kuipandisha hadhi barabara hii kwa kuwa ni kiungo kati ya Bagamoyo na Kinondoni. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari kuisimamia TARURA ili ikamilishe mchakato wa vigezo ili barabara hii iende TANROADS na ile ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami iweze kutimia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika Mheshimiwa Mbunge amekuwa akisemea sana Barabara hii ya Mingoi – Kiembeni na hasa kwa sababu ina wakazi wengi, kwa maana wakazi zaidi ya 17,000. Wengi ni wanawake na watoto wapo humo kwa hiyo amekuwa akisemea sana barabara hii ili kulinda maslahi ya makundi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kama nipo tayari kuambatana na yeye kwenda kujionea hali halisi katika eneo hili ili kuona kama bajeti inatosheleza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya kutoka katika kujibu maswali haya, tutakaa, tutazungumza na tutapanga ratiba ili niweze kufika. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hata kwenye swali lake la pili, nikija kwenye ziara hiyo, nina imani hata suala hili la kuharakisha mchakato wa kuitoa barabara hii ya eneo la Mpiji Chini kwenye daraja hili linalojengwa na TANROADS kupandisha hadhi barabara hizi ili ziweze kutoka TARURA zihamie TANROADS, ninaamini tunaweza kulisimamia nikiwa nimefika kwenye eneo husika. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba nipo tayari na tutafanya kazi bega kwa bega kwa maslahi mapana ya watu wa Bagamoyo. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Wakati wa mvua za El-Nino barabara nyingi sana katka Jimbo la Ngara ziliharibika, ikiwemo Barabara ya Kibirizi kwenda Keza ambapo daraja liliondolewa kabisa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kwenda kujenga barabara hizi ili kurudisha miundombinu iliyoharibika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusiana na Barabara hii katika eneo hili la Kibirizi – Keza na hasa kwa sababu mawasiliano hapa yamekatika. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipaumbele namba moja katika kuhudumia miundombinu hii ya barabara ni kuunganisha mawasiliano. Maeneo yote ambayo mawasiliano yamekatika yanapewa kipaumbele namba moja katika kuhakikisha kwamba Serikali inarudisha mawasiliano hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya mawasiliano na Meneja wa TARURA, ananisikia kwa wakati huu, ili kuona ni namna gani tunaharakisha kurudisha mawasiliano katika eneo hili ambalo amelitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mwaka wa 2024 ulikuwa ni mwaka wa mvua nyingi za El-Nino na bahati mbaya sana zimeathiri barabara nyingi na madaraja mengi yamevunjika; zaidi ya kilomita 50 zimeathirika katika Wilaya ya Kishapu na Serikali imefanya tathmini na kugundua kwamba zaidi ya bilioni 2.7 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo. Je, ni lini Serikali itatekeleza uletaji wa fedha wa haraka na wa dharura ilimradi urudishaji wa miundombinu hiyo uweze kufanyika haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba mvua zilizonyesha, mvua za El-Nino, zimefanya uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara zetu na hasa hizi barabara za wilaya zinazosimamiwa na TARURA. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka wa bajeti ili kuhakikisha kwamba inafanya matengenezo ya barabara hizi ambazo zimeharibika. Nimhakikishie kwamba katika jimbo lake pia Serikali itaendelea kupeleka fedha kuhakikisha tunaziweka hizi barabara katika hadhi nzuri.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwenye eneo langu katika Jimbo la Kilindi kuna Kata inaitwa Kata ya Kilwa barabara inayoanzia Kata ya Kwediboma – Kilwa hadi Kwadundwa mvua za El-Nino za mwaka jana zimeharibu miundombinu na kata hiyo sasa hivi haifiki kabisa. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha kwamba na eneo hilo linapitika kwa sababu lina uzalishaji mkubwa wa bidhaa nyingi sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa barabara zetu hizi za TARURA hasa kiuchumi lakini pia kijamii; na inatambua kuwa mvua zilizonyesha za El-Nino zimefanya uharibifu mkubwa. Kwa hiyo, Serikali imekua ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kuhakikisha kwamba inafanya matengenezo na inajenga barabara mpya hizi za TARURA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kupeleka fedha katika Jimbo lake kwa ajili ya kuhudumia barabara zake ikiwemo hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya kutoka Kigorogoro Kata ya Kibale kwenda Kishanda na pia kwenda Rulama katika Wilaya ya Kyerwa imeharibika sana. Je, ni ni lini hizi barabara zitatengenezwa kwa sababu hazifai kabisa? Ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatenga fedha kila mwaka wa bajeti; na sote ni mashahidi tunaona Bajeti ya TARURA imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka bilioni 275 mpaka bilioni 710 kwa mwaka. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaifikia barabara hii na kuijenga ili iwe katika hadhi nzuri na wananchi waweze kupata huduma.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Makete ni moja kati ya majimbo ambayo yana changamoto ya mvua za muda mrefu; barabara nyingi ni za TARURA na sisi ndio tunaoongoza kwa uzalishaji wa vyakula ambavyo vinatumika mijini. Je. Serikali ina mkakati gani wa kurudisha miundombinu ya Barabara iliyoharibika kwenye Jimbo la Makete hususan maeneo ya Matamba – Kikondo na maeneo ya Lupila? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amekuwa akisemea sana barabara hizi alizozitaja hasa katika maeneo hayo ya Lupila na maeneo ya Matamba. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kwa ajili ya kuhudumia barabara zikiwemo barabara katika jimbo lake. Hata katika mwaka huu wa bajeti 2024/2025, Serikali imetenga fedha na itafikia barabara katika jimbo lake ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata barabara zilizo bora kwa ajili ya shughuli za uchumi na za kijamii. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Baada ya mvua kubwa za El-Nino kuharibu barabara nyingi za Mjini Liwale; kwanza tunashukuru tuliletewa fedha kipindi kile, lakini ipo haja kwa Serikali kutuletea fedha kufungua Barabara za Mpigamiti – Liwale, Kikuyungu - Liwale, barabara ambazo bado mpaka sasa hivi hazipitiki kirahisi. Je, ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya barabara hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara hizi za TARURA zinakuwa katika mazingira ya kupitika mwaka mzima. Tunafahamu kwamba mvua kubwa za El-Nino zimeleta uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara hizi. Kila mwaka wa bajeti Serikali inatenga fedha kuhakikisha kwamba inafanya ukarabati pamoja na kufanya ujenzi katika barabara hizi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata Mwaka huu wa Bajeti wa 2024/2025, Serikali italeta fedha kwa ajili ya kuhakikisha inahudumia barabara katika jimbo lake. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Barabara ya International School Kibosho - KNCU hadi Kwa Raphael ujenzi wake unakwenda taratibu sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilichukue swali hili. Nitafanya mawasiliano na Meneja wa TARURA wa Wilaya ili kufahamu changamoto iliyopo ambayo inapunguza kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hii inayotoka International School kwenda Kwa Raphael. (Makofi)
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ni kweli aliyoyasema Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini shule ile ina uhitaji mkubwa wa hiyo fence. Naomba basi commitment ya Serikali kwa kuwa fensi hii ina umuhimu mkubwa; je, ni lini wanaweza wakaanza kufanya mpango wa kujenga fence hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nakubaliana na kabisa na Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze sana kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba wanafunzi katika shule hii ya wasichana wanaweza kupata usalama au wanaweza kupata ulinzi mzuri wanapokuwa katika mazingira ya shule. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kupitia mapato ya ndani katika mwaka wa fedha huu ujenzi wa fensi au uzio kwa hadhi ya matofali utaanza. Kwa hiyo, nimhakikishie Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuimarisha usalama katika shule hii na itafanya jitihada kuhakikisha fence inakamilika.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka pesa za kujenga uzio katika Sekondari ya Ubiri – Mlongwema na Shambalai ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa ulinzi na usalama wa wanafunzi wetu wanapokuwa shuleni na Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi sana kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi ambayo itawezesha udahili wa wanafunzi ili waweze kuanza kusoma katika shule hizi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari Serikali imeanza awamu ya kwanza kuhakikisha inaweka majengo ya msingi. Serikali itatafuta na kutenga fedha ili kuhakikisha inaendelea kuimarisha miundombinu mingine ikiwemo ya uzio.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba katika hao walimu 12,000 watakaoajiriwa watapewa kipaumbele maeneo ya pembezoni kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambako walimu wengi wanahama sana kuliko kuhamia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inaendelea kuajiri walimu kila mwaka, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza motisha na kuboresha mazingira ya maeneo ya pembezoni ili kuvutia walimu na kubaki katika maeneo ya pembezoni na kupunguza walimu kuhama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la msingi kabisa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi za walimu 12,000, walimu hawa wanatarajiwa kuajiriwa kwa kuzingatia idadi yao, lakini pia kuzingatia uwiano na uhaitaji. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwa sababu Serikali mpango wake ni kuhakikisha kila eneo, mkoa, jimbo na kila shule yenye uhitaji inapata mgao, basi nikuhakikishie na wewe Mheshimiwa Mbunge katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru shule zako zenye uhitaji na zenyewe zitapata walimu hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana kuhakikisha inaboresha mazingira ya kufundishia katika maeneo ya vijijini. Kupitia miradi ya BOOST, SEQUIP, GPE, TSP na EP4R, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa sana ya kujenga nyumba za walimu ili kuboresha mazingira hayo ya kufanyia kazi, lakini pia imekuwa ikihakikisha huduma zinapatikana kwa mfano umeme unapatikana kupitia REA (Umeme wa Vijijini); huduma za maji kupitia RUWASA na imekuwa ikihakikisha barabara za TARURA na zenyewe zinajengwa, lakini huduma za msingi kama afya zinapatikana kwenye maeneo ya vijijini. Yote hiyo ni kutengeneza mazingira mazuri ili walimu wanaopangwa kufundisha katika maeneo ya vijijini waweze kufanya kazi katika mazingira bora zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuendelea kuzisisitiza halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinafanya msawazo wa walimu ili wale walimu wanaokuwa wamejazana katika shule za mijini waweze kusawazishwa na kuweza kuhamishwa kwenye maeneo ya shule zilizopo vijijini ambazo mara nyingi zinakuwa na upungufu mkubwa.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri, lakini nina maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, daraja hili ni muhimu sana kwa wananchi wa Kata ya Itenka. Mashamba na shughuli zao zote za kijamii ziko ng’ambo ya mto na kipindi cha masika hakuna watoto wala wananchi wanaokwenda kufanya shughuli zao za kijamii. Je, ni lini Serikali itajenga daraja hili ili wananchi wa Itenka waweze kupata maisha mazuri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri, je, yuko tayari Bunge hili likiisha twende naye Itenka ili akaone uhalisia na shida ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maana anapigania maslahi mapana ya wananchi wake. Naomba nimhakikishie kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa daraja hili kuichumi na kijamii. Ndiyo maana Serikali imechukua hatua ya kufanya mapitio ya usanifu ili daraja litakapojengwa liwe la kudumu na liwe lina ubora ambao utakuwa ni wa muda mrefu zaidi na utawasaidia wananchi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mara baada ya mapitio ya usanifu kukamilika, Mwezi wa Tisa, taratibu za ujenzi zitaanza. Kwa hiyo, katika mwaka huu wa fedha, daraja hili litajengwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge. Tayari tulishanong’ona na ameshaniomba niweze kwenda kutembelea katika jimbo lake, niweze kwenda kujionea uhalisia katika eneo hili la Kata ya Itenka. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nipo tayari, tutakaa na tutakubaliana ratiba ili niweze kufika katika eneo hili.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Kigogwe katika Kata ya Munzeze? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu mkubwa sana wa madaraja haya na hasa kwa maslahi mapana ya wananchi kiuchumi na kijamii, Serikali tayari imeshaanza jitihada mbalimbali za kuhakikisha inajenga madaraja haya ili wananchi waweze kuyatumia. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kuleta fedha ili kuhakikisha daraja hili ulilolitaja katika Kata ya Munzeze liweze kujengwa. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Daraja linalounganisha Barabara ya Mwamanyili na Mwamkala litakamilika? (Makofi
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka wa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombimu na hasa ya barabara zetu katika ngazi za Wilaya, yaani kwa maana barabara zinazosimamiwa na TARURA. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuleta fedha, kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hii ikiwemo daraja hili alilolitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; fedha inayotengwa kumlisha mwanafunzi kwa siku ambayo ni shilingi 1,500 na zaidi kidogo haitoshi kuweza kumpa milo mitatu, kwa maana ya mlo kamili (balanced diet). Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza hicho kiasi ili kusudi kiweze kulingana na hali halisi ya maisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kiasi ambacho kilishalipwa, lakini madeni ya wazabuni wa vyakula mashuleni bado ni makubwa na mengine bado yako kwenye halmashauri, hayajafika hata Wizarani. Je, Serikali mna mpango gani wa kuhakikisha kwamba, sasa wanaweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, hayo madeni yanalipwa kila mwezi ili yasiendelee kurundikana kule? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge ambaye ameuliza maswali mazuri kabisa haya kwamba, kiwango cha fedha, kwa ajili ya kununua chakula cha wanafunzi katika shule kimepandishwa, kimeboreshwa kutoka shilingi 1,500 kwa mwanafunzi mmoja mpaka shilingi 2,000. Kwa hiyo, Serikali itakuwa inahakikisha inafanya mapitio ya gharama hii ili kuweza kuiboresha zaidi kwa kadri muda unavyozidi kwenda na kwa kadri bajeti inavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, pia, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha kwamba, fedha zote zile ambazo zinakuwa zimetengwa zinatolewa zote kulingana na idadi ya wanafunzi wa bweni walioko katika shule zetu hizi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imefanya mapitio ya gharama hizo na itaendelea kufanya mapitio zaidi, ili kuendelea kuboresha kiwango.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba, inalipa wazabuni. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 mpaka 2022/2023, Serikali tayari imelipa wazabuni wa chakula shuleni kiasi cha shilingi bilioni 26.3. Kwa muktadha wa swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba nichukue nafasi hii, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kutoa maagizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote ambazo zina shule za bweni wafanye uhakiki wa madeni yote ya wazabuni wa chakula na waweze kuyawasilisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuweze kuyawasilisha Wizara ya Fedha, kwa ajili ya taratibu za malipo.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Shule nyingi za Sekondari Mkoani Tanga zina maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo ambayo yangesaidia kupata chakula cha mchana kwa wanafunzi. Je, ni lini Serikali itatoa waraka maalum kwa walimu wa Mkoani Tanga, ili maeneo hayo yatumike vizuri, kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, nani anayepaswa kulima kati ya wanafunzi na walimu ili niwe nimeelewa swali lako vizuri?

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, swali la msingi la kwenye hili swali Namba 43 linazungumzia chakula ambacho...

SPIKA: Hilo limeeleweka, yaani muktadha wa swali lako, umesema walimu waelekezwe ili yale maeneo yatumike vizuri; kwa maana ya kutafuta wakulima wa kulima? Ama yale maeneo walime walimu ama walime wanafunzi?

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, vyovyote iwavyo, lakini maeneo yatumike vizuri. Yanakuwa ni kama vile sehemu ya elimu ya kujitegemea, lakini pia, shule ziwe na miradi ili kuepusha huu mzigo wa Serikali kuwalipa wazabuni. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa lishe na hasa katika ustawi wa wanafunzi wetu. Kwa hiyo, kwa muktadha wa swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba nichukue nafasi hii kuendelea kuwahamasisha Wakuu wa Shule waweze kuwa wabunifu, kuanzisha vibustani vidogo vya matunda, mbogamboga na mazao madogo ili waweze kuchangia katika lishe za wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Mbunge dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, shule zetu hizi na zenyewe kwenye maeneo yao wanaweza kuwa wabunifu na kuanzisha vimiradi vidogo ambavyo vitasaidia katika lishe za watoto ambazo ni muhimu sana katika makuzi yao katika kupata afya ambayo itawawezesha kupokea masomo vizuri.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kwamba uwiano wa walimu nchini upo chini ya kiwango kinachostahili, je, Serikali sasa ipo tayari kuchukua suala hili kuwa kipaumbele maalum cha Taifa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa yapo maeneo ambapo shule zetu za sekondari hazina kabisa walimu wa kike, je, Serikali ipo tayari sasa kuweka kipaumbele katika ajira za walimu kwa wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua upungufu wa walimu na imekuwa ikifanya jitihada za kuajiri walimu kila mwaka. Mathalani mwaka huu kuna ajira tayari zimetangazwa 11,015 za walimu na Serikali inachukua jitihada mbalimbali ikiwemo pia matumizi ya TEHAMA katika kufundishia kwa maana kutumia smart classes. Pia kutumia walimu wa kujitolea pamoja na kuwatumia walimu wale ambao wapo kwenye mafunzo kazini (wale wanaofanya internship) ambao mwaka wao mmoja wa masomo wanatakiwa wafanye mafunzo, sasa waanze kuingia katika shule wakifanya mafunzo kwa vitendo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu mkubwa na inaweka kipaumbele katika kuhakikisha inapata walimu na inapunguza ukali wa upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge naomba nichukue nafasi hii kuwahamasisha waombaji wa ajira hizi za ualimu ambao ni wanawake wajitokeze kwa wingi waombe ajira hizi kwa sababu ajira za walimu ni kwa ajili ya wanawake lakini wanaume. Kwa hiyo wanawake wajitokeze na waombe nafasi hizi za ualimu ili tuweze kupata wanawake wengi zaidi katika nafasi za walimu pia. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nadhani tukiendelea kuwahamasisha wanawake wakajitokeza kwa wingi wakaomba nafasi tutaweza kuongeza idadi ya walimu wanawake ambao tunawahitaji pia.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto ya uhaba mkubwa wa walimu katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali tayari imeshatangaza ajira mpya za walimu katika mwaka huu ajira 11,015, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mgawo wa walimu hawa na yeye atapata walimu hawa katika jimbo lake. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu Wilaya ya Nyasa imekuwa na matokeo mabaya sana ya kidato cha nne katika yale masuala ya upimaji na changamoto kubwa ni walimu wengi wanahama kuliko ambao wanabakia kwenye maeneo. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti wa kina kwenye hizi wilaya za vijijini ili kupata mkakati maalum wa kuhakikisha watoto wa maeneo hayo nao wananufaika na elimu ya Tanzania kuliko hali ilivyo sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza Ofisi ya Rais, Utumishi imeshatoa mwongozo kwamba mtumishi anapopangiwa kituo cha kazi haruhusiwi kuhama kwenye kituo hicho cha kazi mpaka awe ametimiza angalau miaka mitatu. Kwa hiyo hiyo ni jitihada moja ambayo inafanywa na Serikali kuhakikisha maeneo ya pembezoni hayapati changamoto kubwa ya walimu au watumishi kuhama.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea kuchukua jitihada ya kuboresha mazingira ya kufundishia na hasa katika maeneo ya pembezoni ili kupunguza ile changamoto ya watumishi kuhama na kwa muktadha wa swali lako yaani walimu kuhama katika maeneo ya pembezoni kwenda kutafuta mazingira bora zaidi ya kufanya kazi. Kwa hiyo Serikali inatambua changamoto ya ukosefu au kuhama kwa watumishi na hasa walimu kutoka katika maeneo ya pembezoni na tayari Serikali inachukua jitihada mbalimbali ili kuhakikisha maeneo hayo hayapati upungufu huo kwa kutengeneza mazingira ambayo watumishi na walimu wataweza kuendelea kubaki kuwafundisha watoto wetu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maeneo ya vijijini au pembezoni hali ni mbaya zaidi ambapo unakuta mwalimu mmoja ana uwiano wa wanafunzi 90 mpaka 120 kinyume na Sera ya Elimu ambao inasema wanafunzi 40 kwa mwalimu mmoja na maeneo ya mjini uwiano walau ni mzuri kidogo; na kwa kuwa Serikali ina program ya TEHAMA, je, ni kwa nini sasa isichukue walimu kutoka mijini iwapeleke vijijini maeneo ya pembezoni ili kuweza ku-balance kuhakikisha watoto wote wanapata elimu sawa kwa sababu huku mjini wanaweza wakatumia TEHAMA kuweza kufundisha wanafunzi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu katika jibu la msingi ni kwamba Serikali inafanya jitihada kuhakikisha inapunguza upungufu wa walimu na inatumia jitihada tofauti tofauti kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge kwamba pia kuna matumizi ya TEHAMA. Tayari tumeshaanza kufanya majaribio katika baadhi ya maeneo Mkoa wa Dodoma kwa hiyo tutaendelea kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia kama hizi yaani smart classes.

Mheshimiwa Spika, kwa wakati huu pia tunaendelea kuzikumbusha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweza pia kutumia namna ya kuchukua walimu wale wa kujitolea ambao wanapewa posho kidogo kwa hiyo wanaweza kuwafundisha wanafunzi wetu na kupunguza kwa kweli ukali wa upungufu wa walimu. Pia nimesema tunatumia njia nyingine ya walimu ambao wapo katika mafunzo kwa vitendo (internship).

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua upungufu na hasa katika maeneo haya ya pembezoni na inachukua hatua hizi mbalimbali. Kwa hiyo nimhakikishie hata katika maeneo yake ya utawala anapowakilisha katika mkoa wake tutaendelea kuwafikia kwa awamu. Ahsante.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niishukuru Serikali kwa majibu yake, naomba kuuliza kwamba ahadi ilikuwa ya kilometa 15 lakini mpaka leo miaka inakwisha ni kilometa 1.6 ndiyo imekamilika.

Je, ni lini hizo kilometa 12 zitakamilika kwa uhakika badala ya kwenda nusu nusu?

Swali la pili, tarehe 30 Januari, 2024 Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kilometa 12 katika Manispaa ya Ilemela, mpaka leo hakuna kilometa hata moja ambayo imeanza.

Je, ni lini kilometa hizo zitajengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali mazuri yenye lengo la kuboresha miundombinu ya barabara kwa ajili ya wananchi na hasa wale anaowawakilisha, lakini ambao Mheshimiwa Mbunge Tabasam anawawakilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, ile ahadi iliyotolewa ya kilometa 15 ni ahadi ambayo tunaiweka katika kipaumbele namba moja katika utekelezaji wa miradi hii ya ujenzi wa barabara. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa barabara hii haiwezi kujengwa kwa wakati mmoja kilometa zote ndiyo maana Serikali kila mwaka wa fedha inatenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hii kwa vipande. Kwa hiyo, nimhakikishie hata katika mwaka huu wa fedha, fedha zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara inaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili ambayo ni ahadi katika Jimbo la Ilemela, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara kwa maana ina maslahi makubwa kwa wananchi kiuchumi, lakini kijamii. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kutafuta fedha ipate fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni lini Serikali itaanza uboreshaji wa miundombinu ya barabara za Mji Mdogo wa Katoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akipambania maendeleo katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba Serikali kila mwaka wa bajeti inatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara. Mathalani katika Serikali ya Awamu ya Sita, bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka bilioni 275 mpaka kufikia bilioni 710.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo ni dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba inafikia mtandao mkubwa zaidi wa barabara hizi kwa kuwa zina manufaa makubwa kwa wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kila mwaka wa fedha itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inazifikia barabara nyingi zaidi ikiwemo barabara katika Mji wa Katoro.(Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Ndala kwenda Mwawaza, Manispaa ya Shinyanga ambako kuna Hospitali ya Rufaa, iko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi lakini Makamu wa Rais alikuja Shinyanga akatoa ahadi.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya uwakilishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii aliyoitaja iko kwenye mpango na fedha ikipatikana nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge dhamira ya Serikali ni kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kuwanufaisha wananchi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni lini barabara ya kutoka Vwawa – Londoni - Msiya hadi Isarawo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi kwa wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inafikia barabara nyingi iwezekanavyo, kupanua mtandao wa barabara hizi za Wilaya ziwe zina hadhi nzuri na ziweze kupitika katika kipindi cha mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga fedha kila mwaka na barabara hii ipo kwenye mpango, hivyo nimhakikishie kwamba barabara hii itajengwa. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Ludewa kwenda Ibumi ilikuwa imefunga kutokana na mvua zilizozidi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilituma wataalamu kuikagua hiyo pamoja na nyingine tatu na kuahidi zitapewa fedha kutoka World Bank.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha hizo ili kabla ya mvua ziweze kufanyiwa matengenezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akizisemea sana hizi barabara kwa kuwa anatambua na ana matamanio wananchi wake waweze kupata barabara nzuri zenye hadhi nzuri ambazo zitawezesha shughuli za kiuchumi na kijamii katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hizi kwa ajili ya dharura zimepatikana shilingi bilioni 170 na nimhakikishie kwamba hatua ambayo ipo sasa ni ya manunuzi, kupata wakandarasi ili waweze kuingia site. Nimhakikishie baada ya muda mfupi kutoka sasa tutawaona wakandarasi wako site kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hizi.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais ya barabara ya KCMC, YMCA ambayo ina taasisi zaidi ya kumi na msongamano mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa tayari mimi na yeye tumeshazungumza kuhusiana na barabara hii na tayari tumeiweka katika vipaumbele kabisa iko kwenye mpango, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi fedha zitakapopatikana barabara hii inakuja kujengwa.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, barabara ya kutoka Kwamtoro - Sanzawa - Mpendo yenye kilometa 54 imeharibika sana kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha, hata hivyo, tumeleta maombi maalum.

Je, ni lini sasa Serikali italeta fedha ili tuweze kufanya ukarabati wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa maombi yake haya sisi tuliyapokea na tunayafanyia kazi ili tuweze kuhakikisha kwamba dhamira ya Rais inatimia ya kuhakikisha Watanzania wanapata barabara zilizo bora ambazo zinapitika katika misimu yote katika mwaka mzima.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunafanyia kazi maoni haya mahsusi kabisa na pindi fedha zitakapopatikana tunakuja kuhakikisha kwamba tunajenga barabara hizi. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba amesema katika kilometa 15 tunatengenezewa kilometa moja na nusu, sasa hiyo ni ahadi ya Rais wakati wa uchaguzi mwaka 2020.

Je, ni lini sasa TAMISEMI wataheshimu ahadi za Rais wanazozitoa katika kampeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya. Nilipata nafasi ya kutembelea Jimboni kwake na kwa kweli baadhi ya changamoto hizi aliziwasilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi na yeye tayari tulishazungumza na nimemfahamisha kwamba suala lake hili la barabara na hasa hizi za ahadi ya Rais, ahadi za viongozi wakuu kwa kweli ni kipaumbele namba moja katika utekelezaji wa majukumu yetu sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama tulivyozungumza, tunaweka msukumo kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga barabara hii kwa awamu kila mwaka tutakuwa tunatenga fedha ili mwisho wa siku ahadi ile iweze kutimia.(Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo anatujibu kwa kujali maswali ya wananchi wa majimbo yetu, naomba niulize swali moja dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati amekuja Mheshimiwa Makamu wa Rais, Wilaya ya Nyasa, wananchi walikuwa wamempa kilio cha Daraja la Mto Likwilu ambalo lilibomolewa na maji miaka kama mitatu iliyopita, wale wananchi wanateseka sana na tumeandika maombi maalumu kuleta katika Wizara yako. Je, ni lini ombi hilo litatekelezwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpa pongezi kubwa sana Mheshimiwa Mbunge, hakika mara kwa mara amekuwa akipaza sauti yake kwa ajili ya kuwaombea wananchi wake maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maombi haya ni kweli yamepokelewa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi na yeye kwa pamoja tutaendelea kufuatilia ili mwisho wa siku tuweze kuhakikisha ahadi hii imetekelezwa kwa sababu ahadi za viongozi wakuu hakika ni kipaumbele katika utekelezaji na mipango tunayoweka kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba maombi yake tumeyapokea na kwa kweli tunayapa uzito unaotakiwa na nimhakikishie kwamba fedha zikipatikana kwa kweli Daraja la Likwilu litaenda kujengwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwenye Kata ya Chiwale ulianza kwa kutumia fedha za Jimbo pamoja na fedha za tozo ambazo ziko ring-fenced. Hata hivyo, wakandarasi wengi wameji-mobilize wameondoka maeneo yao ya kazi kwa sababu hawajapewa fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kufahamu, ni kwa nini fedha hizi haziwafikii wakandarasi, nani anazishikilia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi yake nzuri anayoifanya ya uwakilishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili mahsusi kabisa naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu mimi na yeye tuweze kukaa ili tuweze kufanya ufuatiliaji wa wakandarasi hawa ambao wame-raise certificate na bado hawajapata malipo yao, kwa sababu malengo ya kutaka wazawa waweze kushiriki katika zabuni kama hizi hasa za ujenzi wa miundombinu muhimu kama ya barabara, dhamira ni kuwawezesha wazawa. Kwa hiyo, hatuko tayari kuona kwamba wanaangamia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tutafanya ufuatiliaji ili tuweze kupata muafaka wa wakandarasi hao.
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara ya kutoka Buguma kwenda Mchigondo kimeliwa na maji. Sehemu hiyo imekuwa ni karaha kubwa sana kwa akina mama, watoto na wazee kupita. Nataka Mheshimiwa Waziri aniambie, ni lini tutaongozana naye aende pale, aone tu jinsi akina mama wanavyopita pale wakivuka? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi wa wananchi wake. Kuhusiana na ombi lake mimi na yeye tutakaa tutajadili na tutapanga kwa ajili ya utekelezaji.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa eneo la Kata ya Kurasini ndani ya Jimbo la Temeke ni eneo la uwekezaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga zile barabara za ndani ambazo kontena nyingi zinapita kwa kiwango cha zege?

Swali la pili, je, mko tayari kutengeneza barabara inayoitwa Kilima cha Nyani ndani ya Kata ya Vituka katika Jimbo la Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Mara kadhaa amekuwa akifanya ufuatiliaji wa karibu sana kuhusiana na masuala ya miundombinu ya barabara katika Jimbo lake na mimi na yeye tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu. Kwa hiyo, naomba niendelee kumhakikishia kwamba katika eneo hili la Kurasini ambalo ni eneo la uwekezaji, Serikali inaweka kipaumbele kikubwa sana na tayari ujenzi wa barabara hizi kwa kiwango cha zege upo kwenye mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna fedha nyingi ambazo tayari zimepatikana kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo katika Jimbo lake, nimhakikishie tumeanza na maeneo mengine, lakini tutakuja kufika katika barabara hizi kwa umuhimu wake, kutokana na msingi mzima wa kuwa eneo la uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na barabara hii ya Kilima cha Nyani nimhakikishie kwamba barabara hii iko kwenye mpango na itajengwa, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hii nafasi. Ninatumia pia nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuweza kujenga kwa kiwango cha zege kipande cha barabara eneo Ndoombo ikiwa ni sehemu ya barabara ndani ya barabara inayoanzia Sangisi - Akheri hadi Ndoombo.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka wa kuendelea na zoezi hilo la kujenga kwa zege barabara zote ambazo zinapanda milimani kule Meru, tukianza na eneo la Ulong’a - Kata Nkoanrua, eneo la Sela - Kata ya Seela Sing’isi, Sura - Kata ya Poli na Songoro - Kata ya Songoro? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, hakika mimi na yeye tumekuwa tukizungumza mara kwa mara kuhusiana na ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya barabara katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na barabara hizi za milimani ambazo kwa kweli amekuwa akizizungumzia mara nyingi sana hapa Bungeni, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumekwishaanza. Hii ni hatua ya kwanza na kila mwaka tutakuwa tunatenga fedha ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kuziboresha barabara hizi ili ziwe katika hadhi ya zege ambayo ina uimara zaidi na inayostahimili mazingira ya milimani.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha zege Barabara ya Tinyango kuunganisha na Machimbo katika Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ya uwakilishi anayofanya na ya kuwasemea wananchi wake na hasa kwenye masuala ya miundombinu ya barabara. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na barabara hii ya Tinyango anayoitaka ijengwe kwa kiwango cha zege kwamba barabara hii ipo kwenye mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka fedha zinatengwa kwa ajili ya kuendeleza barabara zetu hizi za wilaya na nimhakikishie kwamba ni kwa kadiri ya fedha zitakavyokuwa zinapatikana. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inafikia barabara zote ikiwemo barabara hii aliyoitaja ya eneo la Tinyango. Kwa hiyo, tutalifikia Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Maretadu – Dongobesh – Haydom kwa kiwango cha zege kwa sababu barabara hii imekuwa ikichakaa kila mwaka na haipitiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya uwakilishi anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala lake la barabara zake kujengwa kwa kiwango cha zege hatua ya kwanza itakuwa ni kufanya usanifu na kubaini ni kiwango gani cha bajeti kinachohitajika kwa ajili ya kuziendeleza barabara hizi. Baada ya hatua hizo kukamilika, hatua zinazofuata zitachukuliwa ili hatimaye fedha ziweze kupatikana na kuhakikisha kwamba barabara zinaweza kuboreshwa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, napenda kutoa taarifa kwamba taratibu zote zimefuatwa kwa muda mrefu na siyo zaidi ya mara moja. Kwa majibu haya, nilikuwa naomba Serikali iniambie ni lini itapeleka hizo huduma za kipaumbele kama shule ya sekondari na kituo cha afya kwenye Kata hii ya Mwangeza ambayo kutoka mwanzo wa kata mpaka mwisho wa kata ni zaidi ya kilometa 70 na Watanzania wanapata tabu sana kwenda kufuata huduma hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imesema itaboresha huduma, naomba Serikalii iniambie leo, kituo cha afya na sekondari vitapelekwa lini katika kata hii ili kuondoa adha kubwa ya wananchi wa Mwangeza wanayoipata katika Jimbo langu la Mkalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya uwakilishi katika jimbo lake. Kama nilivyotangulia kusema kwamba kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuimarisha Serikali za Mitaa zilizokuwepo kwa kuhakikisha inasogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha kwamba inajenga miundombinu ya msingi kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikifanya hivyo kupitia miradi tofauti tofauti. Mathalan, kwenye Sekta ya Elimu, Serikali inajenga shule za sekondari kupitia Mradi wa SEQIP. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ombi lake la kituo cha afya, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba inaimarisha huduma za Afya Msingi, na kila mwaka Serikali inatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu, na kununua vifaa na vifaatiba kwa ajili ya kutoa huduma za afya msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha, 2023/2024 kwa kadiri alivyoainisha kipaumbele cha kituo cha afya, atapatiwa fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya katika jimbo lake.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa vituo 898 hadi Septemba, 2024. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya kwenye Kata ya Nyakagomba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye Kata ya Lwamgasa na Magenge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akifuatilia sana kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inafika katika jimbo lake na inanufaisha wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba niyajibu maswali yake yote mawili kwa pamoja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya uwekezaji mkubwa sana katika kuimarisha huduma za afya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shilingi trilioni 1.18 zimetumika katika kuhakikisha kunajengwa miundombinu mizuri kwa ajili ya kutoa huduma ya afya msingi, lakini pia kununua vifaa na vifaatiba. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika Kituo hiki cha Afya cha Nyakagomba ambacho ameomba na ninaamini ni kipaumbele kabisa katika jimbo lake, basi katika mwaka huu wa fedha zitatoka fedha kwa ajili ya kuja kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kuwatangazia Wabunge wote kwamba, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu na uhitaji wa kuimarisha huduma za afya msingi, basi na kwa kusikia vilio vya Waheshimiwa Wabunge vya uhitaji wa vituo vya afya katika majimbo yao, katika huu mwaka wa fedha naomba mfahamu na mpokee taarifa kwamba nyote mtapata fedha kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali iliahidi kutujengea kituo cha afya cha kimkakati kwenye Kata ya Busolwa na Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mwaka huu fedha zitapelekwa, je, anatuhakikishia na sisi tupo kwenye hiyo fedha itakayopelekwa kwa mwaka huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akifanya ufuatiliaji mkubwa sana kuhakikisha kwamba kituo cha afya cha mkakati kinajengwa katika jimbo lake. Naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha kituo cha afya kinajengwa katika kila jimbo. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika jimbo lake atapata fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha mkakati.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Ndanto ina wakazi zaidi ya 17,984, na pia Kata ya Kiwila kwa Sensa iliyopita ina wakazi 36,000, Serikali haioni sasa ni wakati wa kujenga vituo vya afya katika hatua hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala mbalimbali ya maendeleo kwa watu wake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufanya uwekezaji katika eneo la kuimarisha afya ya msingi na katika mwaka huu wa fedha kila jimbo majimbo 214, kila jimbo litapata fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini na itawafikia kwa ajili ya kuanza kujenga kituo hicho cha afya cha kimkakati katika eneo analoliwakilisha.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama Naibu Waziri alivyoeleza kwamba fedha zitatoka kwenye kila jimbo, sasa nataka nijue, ni lini sasa fedha hizo zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Utili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya uwakilishi katika jimbo lake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge akae kwa mkao wa kupokea wakati wowote katika mwaka huu wa fedha, fedha zitateremshwa kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya katika majimbo 2,114. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa na kwenye jimbo lake naye atapata fedha hizi kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Geita lina vituo vya afya vinne vilivyokamilika kikiwemo Kituo cha Ibisabageni, Bugarama, Kasota, Kakubiro na vituo vyote hivi havijapata vifaatiba. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kulitembelea jimbo langu ili aweze kujionea baadaye atuletee fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika anafanya kazi kubwa sana ya uwakilishi katika jimbo lake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa siyo tu kwamba niko tayari kuambatana naye kwenda kuangalia mazingira katika vituo vya afya alivyovitaja, lakini naomba nimhakikishie kwamba katika mwaka huu wa fedha zimetengwa fedha mahususi kabisa kwa ajili ya kuhakikisha vituo vya afya na zahanati zote zinaweza kupatiwa fedha kwa ajili ya kununua vifaa na vifaatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zitakuja kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya msingi zinaboreshwa katika jimbo lake, kwa kuhakikisha vifaa na vifaatiba vinapatikana katika vituo vya afya alivyovitaja.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Sisi kule Songwe vituo viwili wananchi wameshajitolea; Kata za Namkukwe na Kanga wameshajenga maboma yameisha. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema mwaka huu Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya kuunga mkono kila kituo cha afya kwenye majimbo yetu, lakini kule Songwe tayari vituo viwili vimekamilika na bado kuletewa fedha tu. Naomba anihakikishie kwamba nasi tutapata fedha katika vituo hivyo viwili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi wake, lakini niendelee kutoa msisitizo katika majibu niliyoyatoa awali kwamba katika mwaka huu wa fedha kila jimbo, majimbo 214 yatapatiwa fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge naye kwenye jimbo lake atapata fedha hizo kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati pamoja na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma ya afya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga fedha mahususi kwa ajili ya kununua vifaa na vifaatiba ili vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya viweze kuwa na vifaa vya kisasa na viweze kutoa huduma iliyo bora. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha katika mwaka huu wa fedha zipo na zinasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya msingi vinapata vifaa na vifaatiba.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Kata ya Ibumu watapatiwa kituo cha afya kwa sababu kata ya jirani ya Image pia hawana kituo cha afya, pamoja na kuwa wananchi wamekuwa wakijichangisha ili kituo cha afya kijengwe na wamekuwa wakitembea umbali mrefu sana kwenda mpaka Ilula kufuata matibabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya uwakilishi, lakini naomba niendelee kusisitiza na kukumbusha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kufanya uwekezaji katika huduma ya afya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zimetengwa katika mwaka huu kuhakikisha kwamba kila jimbo linapatiwa fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kituo cha afya cha kimkakati lakini katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita zaidi ya shilingi trilioni 1.186 zimetoka kwa ajili ya kuhakikisha inajenga miundombinu ya kutolea huduma ya afya msingi na kununua vifaa na vifaatiba. Kwa hiyo, Serikali itaendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha inaimarisha utoaji wa huduma ya afya msingi katika maeneo aliyoyataja.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha afya cha Gonyaza kilichopo Kata ya Suji - Same Mashariki ni kituo ambacho kinahudumia watu wengi sana na kutokana na jiografia yake ya milima, wananchi wanapata shida sana, lakini kituo hicho kinasuasua katika ujenzi wake. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya uwakilishi anayoifanya. Naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaimarisha utoaji wa huduma ya afya msingi na inafanya hivyo kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ikiwemo ya ujenzi wa vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya msingi kama hospitali, zahanati pamoja na vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kituo cha afya alichokitaja Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie kwamba Serikali itahakikisha kituo hiki kinakamilika na kinaweza kupatiwa vifaa na vifaatiba pamoja na watumishi wa kada ya afya ili kiweze sasa kuanza kutoa huduma za afya.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Songambele Wilayani Kyerwa ni miongoni mwa kata ambazo tulizileta kama kata za kimkakati. Mheshimiwa Naibu Waziri ananihakikishiaje kwa sababu ya umuhimu wa kata hii? Yuko tayari kupelekea fedha ili kituo cha afya kianze kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi, lakini naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuimarisha utoaji wa huduma ya afya msingi; na kwa sababu Mheshimiwa Mbunge amekuwa akipaza sauti kuomba kupatiwa kituo cha afya katika Kata ya Songambele, na kwa kuwa katika mwaka huu wa fedha zitatoka fedha kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo 214, na kwa kuwa Kituo cha Afya cha Kata ya Songambele kitakuwa kinakidhi vigezo vinavyohitajika, nimhakikishie kwamba nacho kitapatiwa fedha katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru na kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Samia kwa namna ilivyotutendea haki kwenye miundombinu ya barabara chini ya TARURA; nimebaki na deni Rutoro na Bumbile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mawili ya nyongeza ni kwamba mkandarasi aliyejenga kilomita 13 za Kata ya Ngenge kuelekea Rutoro anadai pesa zaidi ya shilingi milioni 500, na hiyo kilomita 13 karavati zimeachwa wazi, yaani watu hawawezi kupita kwa sababu kijana amefulia, ni mjasiliamali, alikuwa ameanza, sasa amefulia. Naomba Serikali mumpatie uwezo angalau wa kufukia karavati ili liweze kupitika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Eneo la Kata ya Rutoro ambalo nina imani Serikali itatekeleza ahadi yake, walipata matatizo makubwa ya El-Nino, barabara zinazopitika hizo za panya zikapata makorongo. Ombi langu, naomba Serikali mtutengenezee karavati, msipige greda, mtutengenezee karavati kwenye yale maeneo makorofi ili tukae tukisubiri kuja kupata hiyo ahadi kubwa ya bajeti ya mwaka ujao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akipaza sauti yake kuhakikisha kwamba maendeleo yanapelekwa katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali yake yote mawili, kwanza haya ni maombi, nimeyapokea, nasi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tutayafanyia kazi ili tuweze kufanya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuhusiana na hili swali kwamba mkandarasi ana madai ya shilingi milioni 500, hili kwa upekee kabisa naomba Mheshimiwa Mbunge tukae kwa pamoja tufanye ufuatiliaji ili wakandarasi wetu waweze kuwezeshwa kufanya kazi hizi ambazo wanazifanya za kuboresha miundombinu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na fedha hizi za kuchonga na kutengeneza makaravati katika barabara hii ya Rutoro, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nimelibeba suala hili kwa uzito mkubwa sana na kwa sababu yeye binafsi amekuwa akilizungumzia mara nyingi, tunalifanyia kazi na litapata majawabu kwa sababu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka kuboresha miundombinu ya barabara kwa kutambua umuhimu wake kiuchumi na kijamii.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia leo imetimia miezi 11 Kata za Kibata na Kata ya Tandawale hazina mawasiliano kabisa ya Barabara na Makao Makuu ya Tarafa ya Kipatimu. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa haraka ili kuhakikisha kwamba shughuli za kiuchumi na kijamii katika kata hizo mbili muhimu zinaendelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi wake. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza kwa kiwango kikubwa bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 275 mpaka sasa kila mwaka inatengwa shilingi bilioni 710.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa katika mwaka uliopita kumekuwa na madhara makubwa katika barabara zetu hizi hasa hizi barabara zinazosimamiwa na TARURA kutokana na El-Nino, basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetambua mahitaji ya kuongezeka kwa bajeti na ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameongeza bajeti ya dharura kutoka ya shilingi bilioni 21 kwa mwaka mpaka kufikia shilingi bilioni 254.3 katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha na inarekebisha miundombinu ambayo imeharibika ili wananchi waweze kupata miundombinu iliyo bora, iweze kuwanufaisha kijamii na kiuchumi.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wilaya ya Makete ni moja kati ya Wilaya ambazo zimepata changamoto ya kuharibika kwa Barabara, tunaishukuru Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kujenga Barabara ya Itundu, Barabara ya Mang’oto, Barabara ya Ibaga, Barabara ya Kinyika, lakini kumekuwepo na changamoto ya wakandarasi wamesaini mikataba, site hawajaja. Mheshimiwa Waziri ipi ni kauli yako kwa wakandarasi wote ambao hawajaja kujenga Barabara ya Makate wakati Serikali imewapatia fedha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya uwakilishi katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la Mheshimiwa Mbunge naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelea kusisitiza mameneja wote wa TARURA wa ngazi ya mkoa, na wilaya kuhakikisha wanafanya usimamizi wa miradi hii ya barabara. Wakandarasi wanapokuwa wamepatikana, na fedha zikiwa zimetoka, wajibu wa msingi ni kusimamia kuhakikisha kwa uharaka kabisa miradi hii inatekelezwa na wananchi wanaweza kupata barabara zilizobora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumsisitiza Meneja wa TARURA wa mkoa huu aweze kuhakikisha kwamba anaenda kusimamia miradi yote ya ujenzi wa barabara ambazo fedha zake zimetoka na wakandarasi wamepatikana ili waweze kujenga barabara hizi kwa wakati ikiwemo Makete. Kwa hiyo, Meneja wa TARURA wa Makete pia ujumbe huu unamhusu, asimamie kwa ukamilifu kuanza utekelezaji wa miradi pamoja na kuikamilisha kwa wakati.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itajenga barabara kutoka Rau kuelekea Materuni ambako kuna maporomoko na watalii wengi wanafika kule, lakini wanashindwa kufika kwa wakati kutokana na barabara mbovu na hivyo Serikali kukosa mapato? Ni lini sasa Serikali itajenga barabara hii ya kimkakati? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa uwakilishi wake mzuri, lakini kuhusiana na swali lake naomba niendelee kukumbusha kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaimarisha barabara zetu hizi hasa zinazosimamiwa na TARURA ambazo ni barabara zetu za wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kwamba bajeti ya TARURA imeongezeka kutoka shilingi bilioni 275 mpaka shilingi bilioni 710 kila mwaka. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufikia barabara nyingi zaidi na kuziweka katika hali iliyo nzuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba haikwamishi miradi mbalimbali na shughuli mbalimbali za kiuchumi na za kijamii. Kwa hiyo, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ninayo maswali mawili. Swali la kwanza; ziko barabara ambazo zimekatika kata tatu ambazo nimekuwa nikizitaja hapa mara kwa mara. Barabara ya Kimala – Msonza – Masisiwe - Boma la Ng’ombe na Barabara ya Ukwega - Lulindi. Barabara hizi hazipitiki na zimesababisha changamoto kubwa. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za dharura kwa haraka ili matengenezo yaweze kufanyika wananchi wapate mawasiliano?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara ya kutoka Mngeta - Idete ilijibiwa swali ni barabara inayounganisha na Mlimba, Mkoa wa Morogoro na ni barabara muhimu, imetengewa shilingi milioni 100 na haziwezi kutosha. Je, kwenye mipango ya bajeti ijayo ni kiasi gani cha fedha kimetengwa ili barabara hii iweze kukamilika na wananchi waendelee kupita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja Mheshimiwa Mbunge katika kata tatu Barabara ya Boma la Ng’ombe - Masisiwe barabara hii imeombewa fedha za dharura na nimhakikishie barabara hii itajengwa. Barabara ya Msonza - Kimala yenyewe imetengewa milioni 51.3 katika bajeti ya mwaka huu wa fedha na tayari mkandarasi amepatikana, baada tu ya mvua kukatika kazi ya ujenzi wa barabara hii itaanza. Barabara yake ya Idete - Mngeta na yenyewe ni sehemu ya Barabara ya Mhanga - Mngeta ambayo imeidhinishiwa milioni 100 na ujenzi utaanza wiki ijayo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara zake hizi alizozitaja na amekuwa akizizungumzia mara kwa mara, lakini hata mimi na yeye tulikaa kuzijadili, nimhakikishie barabara zake hizi zitajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusiana na hii Barabara ya Idete - Mngeta ambayo imetengewa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi anasema kwamba fedha hii anaona haitoshelezi. Nimhakikishie tayari Serikali imeanza kwa awamu hii tumetenga milioni 100, katika mwaka mwingine wa fedha tutatenga fedha zaidi ili kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa viwango na inaweza kuwasaidia wananchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Ikola kwenda Kata ya Isengule imekatika na madaraja yamesombwa na mawasiliano hayapo kwa sasa. Je, ni lini Serikali itaenda kukarabati barabara hiyo ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki. Kwa hiyo kwenye maeneo yote ambayo miundombinu imekatika na wananchi wanakosa mawasiliano, basi Serikali inaweka kipaumbele na inachukua ujenzi wa miundombinu hiyo kama dharura. Kwa hiyo nimhakikishie tukitoka kwenye kipindi hiki cha maswali na majibu mimi na yeye tutazungumza ili kuhakikisha katika mipango ya dharura ya ujenzi wa barabara hizi na barabara hii aliyoitaja iweze kujengwa.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Juzi tulipokuwa kwenye kikao cha mabalozi pale Mafinga walilalamikia kwamba barabara ya kwenda Kituo cha Afya cha Ifingo mkandarasi amerundika tu kifusi hajaendelea na kazi. Je, ni lini watafanya msukumo ili amalize kazi ile ya muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu hii inajengwa kuhakikisha kwamba huduma za kijamii zinaweza kuwafikia wananchi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tutazungumza baada ya kutoka hapa ili tuweze kufuatilia ni kitu gani kinakwamisha utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu katika barabara aliyoitaja.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Akheri kuanzia Sing’isi hadi Ndoombo ambayo ujenzi wake unakwenda kwa kusuasua sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameshawahi kunieleza kuhusiana na umuhimu wa barabara hii na nirejee makubaliano tuliyozungumza kati ya mimi na yeye kumhakikishia kwamba, barabara hii itajengwa ili iweze kuwanufaisha wananchi wake.
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali itatengeneza lini Barabara ya kutoka Mashariki inayopitia Nasomba hadi Lukala, Kata ya Mchesi ili iweze kupitika muda wote?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara yenye sehemu korofi kwa urefu wa kilometa 16 kutoka Milunde kwa Chami hadi Kalulu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye maswali yake yote mawili, naomba niyajibu kwa pamoja. Serikali itahakikisha inajenga barabara hizi muhimu na Serikali ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya barabara za TARURA, barabara za wilaya kutoka bilioni 275 mpaka sasa ni bilioni 710. Yote hiyo ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kuhudumia barabara zetu hizi za wilaya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana, tutahakikisha barabara hizi zinajengwa ili wananchi waweze kuzitumia na uchumi uweze kukua kwa maana barabara hizi zinachochea uchumi kwa wananchi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa Barabara ya kutoka Mkuyuni kwenda Tambuka Reli – Butimba - Nyangulugulu mpaka Mahina upembuzi wake na usanifu umeshakamilika kwa 100%, kinachosubiriwa ni kuanza kwa ujenzi wa kiwango cha lami na fedha ilishatengwa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaotumia barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, baada ya mvua kukatika, wakandarasi wataingia uwandani na barabara hiyo itaanza kujengwa. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wako, watapata barabara hii kwa kiwango cha lami hivi karibuni baada tu ya mvua kukatika kwa kuwa wakandarasi wataingia site.
MHE. FESTO D. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya kutoka Iwawa- Isaplano hadi Nkenja ni barabara ya kiuchumi na Serikali kupitia TARURA iliitenga kama sehemu ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami ya kisasa ya majaribio, taarifa tulizonazo ni kwamba imeondoka. Je, ni ipi kauli ya Serikali kwa wananchi wa Makete kuhusu barabara hii kujengwa kwenye kiwango cha lami kama ambavyo waliahidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Iwawa – Isaplano - Nkenja ni miongoni mwa barabara ambazo zipo katika majaribio ya ujenzi wa barabara kwa kutumia teknolojia ya kisasa yaani Eco-roads. Kwa hiyo, ni kweli barabara hii ilitengewa fedha kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha teknolojia mpya ya lami kwa kilometa 12. Baada ya kufanya testing ya udongo ikabainika kwamba teknolojia ile haiendani na udongo wa Makete, lakini sasa hivi Serikali ipo katika mpango wa kuhakikisha inapatikana teknolojia inayoendana na udongo wa Makete ili barabara hii iweze kujengwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge barabara yake ya kilometa 12 ya Iwawa-Isaplano - Nkenja itajengwa kwa kutumia teknolojia mpya ya ujenzi wa barabara kwa maana ya Eco-roads.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itaanza kurekebisha barabara zilizopata athari ya mvua hizi katika Jimbo la Mbagala na ukizingatia mvua sasa zimeisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa Serikali inatambua madhara makubwa ambayo yamejitokeza kwenye barabara zetu hizi kutokana na mvua. Nikupe taarifa bajeti maalum ya bilioni 350 imepatikana kwa ajili ya kuhudumia barabara hizi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge, baada ya mvua kuisha katika mwaka mpya wa fedha, tayari ataanza kuona wakandarasi wanaingia site kwa ajili ya kuanza kufanya marekebisho ya barabara hizo, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami katika Mji mdogo wa Laela. Ni lini Serikali itatimiza ahadi hii? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama vile Serikali iivyoahidi ujenzi wa barabara hizo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itahakikisha inakuja kujenga barabara hizo katika jimbo lake.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningependa kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; Serikali iko tayari kutuunga mkono kwenye ujenzi wa Bwalo kwenye Shule ya Sekondari ya Sululu ambayo tayari wananchi wameshajenga mabweni mawili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tumejenga shule kwenye kila kata, kuna changamoto nyingi sana za watoto wa kike kupata ujauzito, pia na watoto kutopata ufaulu uliotosheleza. Je, Serikali haioni haja ya kuanza kujenga mabweni kwenye shule zetu hizi za sekondari ili watoto waweze kunufaika na ukaaji mabwenini na kukuza taaluma zao pamoja na nidhamu? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeshafanya tathmini ya kuona maboma yanayohitaji kukamilishwa ambayo yapo kwenye sekta ya elimu. Tathmini hiyo imeonesha wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 300 kinahitajika, kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inahakikisha inapata fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma haya ambayo wananchi wameyaanza kwa kutumia nguvu zao kuunga mkono jitihada za Serikali. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge boma hili la bweni alilolitaja litajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa ujenzi wa mabweni, kwa ajili ya wanafunzi wetu wa kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, nimesema kwamba, Serikali itaendelea na jitihada za kuhamasisha wananchi, kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha hostel zinaendelea kujengwa kwa ajili ya shule hizi za kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazikumbusha pia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba, wanatenga fedha katika bajeti zao, kwa maana ya katika mapato yao ya ndani ili kujenga miundombinu hii muhimu kwa kuzingatia kuwa huo ndiyo msingi wa ugatuzi kwa maana ya D by D.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali ilitoa shilingi milioni 80 kujenga Mabweni ya Sekondari ya Nyamang’uta na Sekondari ya Mihingo, lakini mpaka sasa ni miaka mitano mabweni hayo hayajamalizika. Je, ni lini Serikali itamalizia mabweni hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, lengo la Serikali ni kuhakikisha miundombinu muhimu ya mabweni inakamilika na wanafunzi wanaweza kutumia mabweni hayo. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itahakikisha mabweni hayo aliyoyataja yanakamilika ili wanafunzi waanze kuyatumia.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Serikali ilitoa fedha, kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi ambao walikuwa wamejenga mabweni mawili katika Sekondari ya Iseke na Sekondari ya Kintinku, lakini fedha zile hazikutosha. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha mabweni hayo ili yawasaidie watoto wa kike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu hii ya mabweni katika shule zetu. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali itaendelea kutafuta fedha na itahakikisha inapata fedha kwa ajili ya kukamilisha mabweni haya ili wanafunzi waweze kuyatumia na wapate mazingira mazuri zaidi ya kusomea.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kutokana na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa Shule ya Sekondari ya Igunga, ipo mjini na bajeti ya uzio huo ni shilingi milioni 276. Halmashauri imetenga shilingi milioni 55.

Je, Serikali sasa haioni kuna haja kutoa fedha Serikali Kuu na ku-support uzio huu ili uweze kukamilika kwa ajili ya usalama wa watoto hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, ni lini Serikali sasa itaweza kutenga fedha kwa pamoja za majengo ya madarasa pamoja na uzio ili viende sambamba? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana masuala ya elimu na hasa kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, sisi sote ni mashahidi kwamba kutokana na utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi wa shule za msingi, lakini sekondari. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata udahili kuingia katika shule za msingi na sekondari, Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi kwa maana ya madarasa, lakini pia maabara za sayansi na mabweni. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa ujenzi wa uzio katika shule zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha kuna kuwa na miundombinu ya kutosha ya madarasa ili wanafunzi wote waweze kupata udahili kuingia katika shule zetu hizi za msingi, lakini shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, la Mheshimiwa Mbunge ambalo anataka Serikali Kuu iweze kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio, lakini kwa misingi ile ile ya ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Serikali za Mitaa zina jukumu la msingi la kutafuta bajeti, kupata mapato, lakini kuhakikisha inajenga miundombinu ya msingi ikiwepo miundombinu katika sekta ya elimu kwa maana ya madarasa mabweni na uzio.

Kwa hiyo, nichukue nafasi hii, kwanza kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga kwa kutenga fedha hii shilingi milioni 55 kwa ajili ya kuanza kujenga uzio huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa wito kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa, kuendelea kutenga fedha katika mipango na bajeti zao kwa ajili ya kujenga miundombinu muhimu kama hii ya uzio kutegemeana na hali ya eneo husika.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali tayari imeanza kujenga uzio kupitia fedha zilizotengwa katika mapato ya ndani na Mkurugenzi huyu na Serikali itahakikisha inaendelea kutenga fedha kwa utaratibu huo ili uzio uweze kujengwa kwa maslahi mapana ya wanafunzi wetu. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa hatua inazochukua na majibu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hatuwezi kuweka uzio kwenye shule zote nchini kwa wakati mmoja shule za A level na shule nyingine zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wakiwepo wale walinzi na walezi katika shule zetu. Kwa kuwa gharama ya uwekaji wa huu uzio ni mkubwa Serikali haitakiwi kufanya tathmini ya kina ili kuja na mpango mkakati wa ulinzi thabiti kwa wanafunzi wetu katika shule zetu hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kwanza, Mheshimiwa Mbunge, kwa kuendelea kufuatilia na kufuatilia hasa masuala ya ulinzi wa wanafunzi wetu na maeneo ya shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya halmashauri zetu hizi kupitia mapato ya ndani zina nafasi ya kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha zinasimamia masuala ya msingi ikiwemo haya unayoyazungumza Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie kwa sababu yote ni Serikali, tutaendelea na sisi kufanya tathmini na kutengeneza msukumo na kutengeneza mwongozo mzuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kwenye shule zetu kuna kuwa na ulinzi na wanafunzi wanaweza kusoma katika mazingira yenye amani na utulivu. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Amandus Chinguile ipo Nachingwea Mjini na imezungukwa na makazi ya watu, je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga uzio katika shule hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa msingi wa kutafuta fedha, kutafuta mapato na kutenga kwenye bajeti zake fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya muhimu ikiwemo ujenzi wa uzio katika shule zetu. Kwa hiyo, niendelee kumkumbusha Mkurugenzi aweze kuweka katika mipango ya kibajeti katika halmashauri yake ili aweze kutenga fedha kwa kadiri ya vipaumbele na kwa kadiri ya mahitaji kwa ajili ya ujenzi wa fence katika shule hii ya Amandus Chinguile. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Missenyi, Serikali imejenga hosteli katika shule za sekondari na shule hizo zimejengwa pembezoni mwa makazi ya watu ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya vijana wetu kusoma.

Je, ni lini sasa Serikali itatujengea uzio katika Shule za Sekondari za Ruzinga, Bwabuki, Bunazi na Minziro ili wanafunzi wawe katika hali ya usalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza kwanza jukumu lake la msingi la kutenga bajeti kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya msingi katika sekta elimu. Kwa hiyo, niendelee kumkumbusha Mkurugenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi aweze kutathmini, lakini aweze kutengeneza mipango na kutenga bajeti kwa kadiri ya vipaumbele kwa ajili ya kuendeleza miundombinu muhimu hii katika sekta ya elimu. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari ya Endasak, Nangwa, Mulbadaw na Balangdalalu ni za kidato cha tano na sita na zote hazina uzio.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka msukumo kwenye ujenzi wa uzio kwa sababu ya usalama wa watoto wanaosoma kwenye shule hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwemo umuhimu wa ujenzi wa uzio. Niendelee kumhakikishia Serikali inatambua umuhimu mkubwa na itaendelea kutenga fedha kupita Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini kupitia miradi ya Serikali Kuu kwa ajili ya kuhakiksiha inaboresha miundombinu katika shule zetu hizi za kidato cha tano na cha sita kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, shilingi milioni 399 ambazo anasema zimekwenda mwaka 2022/2023 kujenga mifereji kwa ajili ya kupunguza mafuriko hazijaonekana kufanya kazi hiyo kikamilifu kwa sababu wananchi wetu wameendelea kupata mafuriko mwaka hadi mwaka pindi mvua zinaponyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaweza kuniambia ni mifereji ipi ambayo imetumia fedha hizo kujengwa mitaro hiyo ili tuweze kujua ni mitaro gani ambayo imejengwa kwa ajili ya kusaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri unaonaje tukimaliza Bunge hili mwezi Julai tuongozane ili tuweze kwenda kuona hali halisi jinsi ilivyo katika Manispaa ya Tabora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kupambania wananchi kuhakikisha kwamba wanapata miundombinu bora ya mifereji hii ili kuzuia mafuriko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua shilingi milioni 399.12 katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilienda kujenga mifereji katika eneo gani? Kumjibu hilo fedha hii ilienda kujenga kilometa 2.2 katika Barabara ya Kombomasai - Kata ya Malolo, Navimajo - Kata ya Mpera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kwamba nipo tayari baaada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kutembelea na kukagua eneo hilo na ujenzi wa miundombinu hii. Nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge mimi sitasubiri mpaka mwezi Julai, mwisho wa Bunge, Jumamosi hii ninatarajia kuwa Tabora na nikuhakikishie nitaenda kukagua eneo hili kujionea hali halisi na kuona kwamba fedha hii imeenda kuwanufaisha wananchi na tutaenda pamoja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zilizojengwa na TARURA kwenye Wilaya ya Tanganyika zimeharibika baada ya mvua nyingi kuvunja madaraja na mifereji ikiwemo Barabara ya Ikaka - Mnyagala, Ikaka - Kamsanga. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kutokana na mvua nyingi zinazonyesha miundombinu ya barabara maeneo tofauti tofauti imekuwa ikipata changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba inaenda kufanya ujenzi wa dharura kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika ili kuhakikisha mawasiliano yanarudi, yanaunganika na yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, amenitajia barabara zake hizi, mara baada ya kutoka katika kipindi hiki cha maswali na majibu nitakaa nay echini ili aweze kuniainishia haya maeneo husika na tutayachukua sisi kama Serikali ili kuona hatua gani za dharura zinaweza kuchukuliwa ili kuhakikisha tunaunganisha mawasiliano katika maeneo aliyoyataja.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Kata ya Nkwenda, Kijiji cha Nkwenda ambako kunafanyika soko linalowaleta pamoja wafanyabiashara wa Kyerwa na Karagwe kuna mtaro mkubwa sana umeelekezewa kwenye hilo soko la Nkwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua mkakati wa kujengea huo mtaro ili uweze kuwa salama kwa wafanyabiashara kuepusha mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara nyingi na kufanya soko au biashara ishindikane kufanyika kwenye eneo hilo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu ya barabara, mifereji na hasa katika kuchochea uchumi kwa maana ya kuwezesha shughuli za uchumi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itahakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kuhakikisha inajenga mitaro katika eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge ili kuboresha mazingira na kuwawezesha wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji mali kwa utulivu na kwa urahisi zaidi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, mvua za El-Nino zimenyesha kwa kiwango kikubwa katika Halmashauri ya Itigi, Barabara ya Itigi – Damweru haipitiki kabisa, ilikuwa imejaa maji na sasa maji yameanza kukauka, lakini Barabara ya Kalangali kwenda Tulieni imeharibika kabisa haipitiki.
Je, Serikali iko tayari kutuongezea pesa za kutosha kurudisha miundombinu hii ili watu wafanye maisha yao ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi na hasa za wilaya na kama nilivyotangulia kusema kipaumbele cha Serikali katika kipindi hiki ni kuhakikisha inaunganisha mawasiliano ya barabara kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itatafuta fedha na itatumia taratibu za dharura kuhakikisha inaunganisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo yameathirika sana na mvua na mawasiliano yamekatika katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa uendelevu Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii ili iweze kuwa miundombinu imara ambayo inapitika kwa misimu yote na mwaka mzima.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu ya Serikali Wananchi wa Jimbo la Manonga wamekuwa wakijitolea miradi mbalimbali na wanafunzi wanaokwenda kusoma katika shule za kidato cha tano na sita katika Jimbo la Manonga wanatoka Tanzania nzima.

Je, Serikali hamuoni haja sasa kwa kuwa mna upungufu wa shule za kidato cha tano na sita mkaziongezea miundombinu shule hizo za Manonga ili wanafunzi waweze kupata elimu nzuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; matatizo yaliyoko katika Jimbo la Manonga ndivyo ilivyo Jimbo la Igalula katika Shule ya Sekondari Tura. Miundombinu ya mabweni iko safi watoto wanasoma vizuri tunapokea wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali, lakini kuna chgangamoto ya bwalo la chakula. Ikifika mwezi wa 11 wakati wa masika watoto wanakosa sehemu ya kupatia chakula. Je, lini Serikali mtapeleka bwalo la chakula kwenye Sekondari ya Tura ambayo ina kidato cha tano na sita sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Kuhusiana na swali lake la kwanza naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba jukumu kimsingi la kujenga miundombinu ya shule za primary na za sekondari ni jukumu la Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi ya Serikali Kuu ni kuongeza nguvu tu ili kuziunga mkono Halmashauri pale zinapokuwa zimeonyesha jitihada ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue fursa hii kuendelea kusisitiza na kumkumbusha Mkurugenzi lakini na Mbunge wote washirikiane ili Halmashauri iweze kutenga fedha katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu hii inayohitajika inajengwa na shule hizi zinaweza kuombewa kupanda hadhi kuwa shule za kidato cha tano na cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi Serikali imeelekeza nguvu kubwa sana katika kuimarisha miundombinu ya shule ambazo zimeshapangiwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita ambacho katika Jimbo la Manonga Shule ya Ziba na Shule ya Choma zimetengewa na zinapelekewa shilingi milioni 692 kwa ajili ya kujenga mabweni madarasa na vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na bwalo la chakula, naomba niendelee kusisitiza kwamba Halmashauri ziweze kufanya jitihada za kutenga bajeti kutoka kwenye mapato ya ndani ili kuweza kukamilisha miundombinu hii. Pia Serikali Kuu pale kunapokuwa na uhitaji mkubwa na yenyewe itaendelea kuunga mkono jitihada hizi zinazokuwa tayari zimeanza kufanywa na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia utaratibu huo huo, jitihada za Serikali Kuu na jitihada pia za Mamlaka za Serikali za Mitaa tutashirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba bwalo hili la chakula katika shule uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge linajengwa ili wanafunzi wetu waweze kupata miundombinu mizuri katika shule hiyo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mlalo tunazo sekondari 31 na sekondari za Mkundi, Mtumbi pamoja na Mtaya zote hizi miundombinu yake inaruhusu uanzishwaji wa madarasa ya kidato cha tano na sita. Je, Serikali iko tyari kuzifanyia kazi shule hizi ili ziweze kuwa na kidato cha tano na sita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mbunge amekuwa ni mahiri sana katika kuhakikisha anapambania changamoto za wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali hili. Kama shule hizi alizozitaja za Mkundi, Mtumbi na Mtale zina miundombinu hitajika basi hatua inayofuata ni Mkurugenzi kuweza kupeleka maombi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuomba kupandishwa hadhi kwa shule hizi kwa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo naomba nichukue fursa hii kumwelekeza Mkurugenzi aweze kufanya tathmini katika shule hizi ili kuona kama zina miundombinu hitajika aweze kupeleka maombi ya kupandisha hadhi shule hizi ili ziweze kuwa shule za kidato cha tano na cha sita.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuwapa wananchi wa Kilimanjaro pole kwa kuondokewa na Katibu Tawala wetu. Nilikuwa nauliza swali, Shule ya Sekondari Ng’uni imekuwa na majengo chakavu sana na wananchi wamejitahidi kuanza ujenzi wa maabara pale shuleni. Je ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya kumalizia majengo haya lakini pia na mabweni ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Ng’uni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yenye tija kabisa kwa ajili ya wananchi wake. Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia miundombinu chakavu na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea na utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la ujenzi wa mabweni. Kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu ya awali nimesema kwamba Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza kujenga miundombinu muhimu katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa utaratibu huohuo naomba nichukue nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba Mkurugenzi mshirikiane pamoja ili kuhakikisha kwamba mnatenga fedha katika mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hii muhimu. Pia, kama nilivyotangulia kusema, Serikali Kuu itaongeza nguvu kwa ajili ya kuhakikisha pale jitihada zinapokuwa tayari zimeanzishwa Serikali iweze kuunga mkono ili kuhakikisha miundombinu hii muhimu inakamilishwa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge toa shaka Serikali itahakikisha ushirikiano na utaratibu huo mabweni haya yanajengwa. (Makofi)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa kijana wangu aliyepata ajali katika Waitara Cup kule Sirari na namshukuru Mungu kwamba wahuni wote na shetani wameshindwa na Mungu ameshinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Serikali; swali la kwanza. Serikali ipo tayari kuleta takwimu za maboma ya nyumba za walimu msingi na sekondari nchi nzima kwenye majimbo yote ambayo wananchi wameweka nguvu zao kuyajenga na yameishia kwenye lenta na kuonyesha mkakati namna ambayo watakamilisha maboma hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Halmashauri yangu ya Tarime DC ina mapato makubwa. Serikali ipo tayari kutoa maelekeza mahususi kukamilisha maboma yote ambayo wananchi wangu wamechangia nguvukazi ili wapate nguvu kuendelea kuchangia maboma mengine baada ya kukamilisha yale ambayo wameshiriki kuyajenga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake haya yenye tija. Kuhusiana na swali lake la kwanza, Serikali tayari imeshafanya tathmini ya kubaini ni maboma mangapi kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi na tayari tathmini imekamilika na Serikali inafanya taratibu za kuhakikisha fedha inapatikana ili kuweza kuunga mkono jitihada zile za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la takwimu Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukawasiliana nikakupatia lakini tayari Serikali ilishafanya tathmini kubaini idadi ya mabama na kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili; Halmashauri anayotoka yeye anasema ina mapato makubwa na kwamba tayari kuna maboma ambayo wananchi walianza kuyajenga. Nitumie nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba pale kunapokuwa na juhudi za wananchi Halmashauri na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinakuwa na uwezo na ni lazima ziweze kutenga fedha na kuzingatia vipaumbele kuweza kuunga mkono jitihada za kuendeleza miundombinu na hasa hii muhimu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue nafasi hii kuendelea kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri kutoka anapotokea Mheshimiwa Mbunge ili waweze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuendelea kuendeleza miundombinu hii muhimu katika sekta ya elimu.

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je ni lini sasa Serikali itajenga shule ya sekondari ndani ya Jimbo la Temeke kwenye Kata ya Makangarawe kwa sababu tulikuwa hatuna eneo lakini sasa hivi tumepata eneo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia programu ya SEQUIP imekuwa ikijenga miundombinu ya shule zetu hizi katika kata. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge bila shaka shule hii uliyoitaja ya sekondari itajengwa kupitia program hii ya SEQUIP. Kwa hiyo Serikali itaendelea kufanya tathmini na kuweka vipaumbele na shule shule hii Serikali itakuja kujenga. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa. Ni lini Serikali itajenga nyumba za walimu katika shule za Sekondari za Jimbo la Newala Vijijini ili kuwapunguzia umbali walimu ambao wanakaa mbali na shule? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga nyumba za walimu kupitia taratibu mbalimbali na kupitia utaratibu wa program. Kwa mfano programu ya GPE, TSP na kupitia mradi wa SEQUIP Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba inatenga fedha mahususi kabisa kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatambua kwamba jukumu lote la kujenga nyumba za walimu haliwezi kutekelezwa na Serikali kuu peke yake. Ndiyo maana tunasisitiza na Halmashauri zenyewe ziweze kutenga fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani na Wakurugenzi waweze kufanya tathmini sahihi ya kujua uhitaji wa nyumba hizi za walimu ili kwa pamoja kupitia miradi hii inayotoka Serikali Kuu na kupitia mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa pamoja tuweze kushirikiana kuhakikisha kwamba walimu wanajengewa nyumba za kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa muktadha huo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu Tanzania nzima lakini pia hususan katika Mkoa na Jimbo analotoka Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa halmashauri zilizo na uhaba mkubwa sana wa walimu hasa katika Kata ya Ilangu, Ipwaga, Mnyagala na Isengule kwenye shule za sekondari.

Je, ni lini wataleta walimu ili waweze kufanya kazi kwenye maeneo ya kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mbunge, swali lake ni la msingi na kama nilivyotangulia kujibu hapo awali, Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 mwaka huu. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na yeye kwenye jimbo lake atapata mgao wa walimu hawa 12,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza mbinu na mikakati mbalimbali ambayo pia inatumiwa na Serikali kupunguza ukali wa upungufu wa walimu. Mkakati mmojawapo ni kuhakikisha kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa na zenyewe zinajipanga kutenga bajeti kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuweza kuajiri walimu kwa mikataba ili waweze kupunguza ukali wa uhitaji wa walimu.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwa njia hizi Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inaleta walimu shuleni katika jimbo lako lakini pia inatumia mbinu tofauti tofauti za kupunguza ukali wa upungufu wa walimu.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbogwe ina changamoto ya upungufu wa walimu, je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri walimu wanaojitolea kwenye Halmashauri ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu awali kwamba Serikali itaendelea kuajiri walimu na katika mgao wa walimu hawa 12,000 wanaotarajiwa kuajiriwa, Mheshimiwa Mbunge na wewe utapata mgao wa walimu kwenye shule zilizopo katika jimbo lako, lakini kupitia mapato ya ndani ya halmashauri pia mnaweza mkatenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuhakikisha mnaweza kuajiri kwa mikataba pia kuwalipa posho walimu wanaojitolea.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo wa kuweka zege kwenye barabara za milimani kwa sababu wanapoweka vifusi pindi mvua inaponyesha barabara zile zinazolewa na tunatia hasara Serikali na wananchi wanashindwa kupita, hata hivyo na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Barabara za Msanga – Chome – Ikokoa – Makanya – Tae – Suji na Barabara ya Kisiwani hadi Msindo zina maeneo makorofi mengi sana, je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutenga bajeti ya kutosha kusudi barabara hizi zitengenezwe kwa kiwango cha zege ili tuweze ku-save hela za Serikali zinazotokana kumwaga vifusi ambavyo vinazolewa na mvua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini yuko tayari kutembelea Jimbo hili na kuziona hizi Barabara za Chome, Barabara za Makanya – Tae pamoja na Kisiwani – Msindo ili aweze kuona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutetea wananchi wake. Kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ameuliza baadhi ya barabara Serikali ina mkakati gani wa kuzijenga kwa tabaka la zege na hasa kwenye maeneo korofi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Msanga – Chome – Ikokoa katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 zimetengwa shilingi milioni 267.15 kwa ajili ya kujenga meta 100 kwa kiwango cha zege kwenye eneo korofi, lakini pia kwenye eneo hatarishi la Mlima wa Chome imejengwa strip concrete ya meta 350, lakini katika mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 74.9 kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha zege meta 180 kwenye eneo hatarishi la Mlima Ikokoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu Barabara ya Makanya – Tae – Suji Serikali imetenga katika mwaka wa fedha 2024/2025 milioni 161.18 kwa ajili ya kujenga kwa tabaka la zege urefu wa meta 100 kwenye eneo la Mgwasi – Tae, lakini pia ujenzi wa driffs nne za meta 32 na kwenye Barabara ya Kisiwani – Msindo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitumia shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga meta 500 za strip concrete. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga kwa kiwango cha zege kwenye maeneo hatarishi, kwenye barabara zake hizi ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa mimi na yeye tutazungumza, tutapanga ratiba vizuri nipo tayari kutembelea Jimboni kwake kuangalia miundombinu hii ya barabara ili tuweze kuona umuhimu wa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuzikarabati na kuzijenga vizuri. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea kufungua barabara za mitaa kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale pale Kharumwa kwa kiwango cha udongo. Je, Serikali ina mpango gani kuziwekea mpango wa kuweka changarawe na baadaye lami hizo barabara za mitaa Kharumwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweza kuzihudumia barabara za wilaya kwa kiwango cha lami, lakini kama wote tunavyofahamu tunaanza. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kuhudumia barabara hizi kwa viwango tofauti ikiwemo viwango vya changarawe, lakini mwisho wa siku hatimaye tunataka barabara zetu zote hizi za wilaya ziwe kwa kiwango cha lami ambacho kitafanya barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu na ziweze kupitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya na hususan pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, changamoto za barabara za Mlimani kule Same Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Meru na nimeishalisema hapa mara nyingi. Kwa hiyo, sasa niulize Serikali inatoa tamko gani kuhusu barabara za milimani kule Arumeru Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipambania sana suala la Ujenzi wa barabara kwa viwango vitakavyodumu hasa katika Jimbo lake ambalo lina milima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari tumeshazungumza na suala tayari lipo kwenye michakato na fedha tayari zimeshatengwa, nikuhakikishie Serikali itakuja kujenga barabara, itatenga fedha kila mwaka kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara hizi na hasa katika jimbo lako ambalo ni la milima. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Luagara kwenda Liponde kilometa 1.5 ilishafanyiwa feasibility study na watu wa TARURA na walishaweka kwenye bajeti miaka miwili nyuma, ni lini sasa Serikali itakwenda kuweka lami kipande kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii tayari imeshafanyiwa usanifu na tayari ipo kwenye bajeti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia kwa karibu hata baada ya kutoka kwenye maswali hapa tutakaa tutafuatilia kwa karibu ili tuhakikishe kwamba mwaka huu kwa sababu fedha tayari imeishatengwa ili iweze kujengwa barabara hii.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naishukuru Serikali kwa juhudi za kutenga fedha za kujenga mitaro hiyo, lakini kwa kuwa tatizo hili ni kubwa sana na ni la siku nyingi na ni endelevu, naomba kufahamu, je, Serikali imeshafanya usanifu kwenye maeneo gani ya kuleta suluhisho la kudumu katika maeneo yote hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo hili liko Mkoa wote wa Kilimanjaro katika majimbo yote tisa, kuanzia Jimbo la Siha, Hai, Moshi Vijijini, Vunjo, Rombo, Mwanga, Jiimbo la Same Mashariki hadi Same Magharibi na hata Manispaa ya Moshi huwa inaathirika na tatizo hili. (Makofi)

Sasa swali langu, kwa kuwa maji hayo yakitoka kwenye milima yanatirirka hovyo barabarani, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabwawa ya kukinga maji hayo ili yatumike kwenye kilimo au mifugo na tatizo hili kuisha kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake haya muhimu sana na yenye tija. Naomba nimjibu maswali yake yote mawili kwa pamoja kuwa tafiti tayari zilifanyika mwaka 2014 katika Wilaya ya Siha na Serikali ilibaini kwamba ujenzi wa barabara za zege una tija sana, lakini ikabaini pia kutua paving blocks na strip concretes na ujenzi wa majaribio ulifanyika katika barabara ya Lawate – Kibong’oto na kimsingi majaribio yalionesha ufanisi mkubwa.

Kwa hiyo, kwa hivi sasa baada ya kufanya performance evaluation, majaribio na kuonesha ufanisi sasa mkoa unatekeleza ujenzi wa miundombinu hii katika maeneo mengine ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala lake ni la muhimu sana na Serikali tayari imeshakuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inajenga miundombinu iliyobora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mapendekezo, mawazo na ushauri wako wa ujenzi wa mabwawa ya kupokea maji hayo kwa ajili ya matumizi ya kilimo, ni maoni na mawazo mazuri na sisi kama Serikali tunayapokea, kuyachakata na kuona namna nzuri ya kufanya utekelezaji wake.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha zege barabara zilizopo kwenye miinuko katika Milima ya Matumbi inayoanzia Pungutini kupitia Mwengei kwenda Kibata hadi Kipatimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiboresha kufanya ujenzi na marekebisho ya miundombinu ya barabara kwa kuzingatia pia topografia ya eneo husika na kama nilivyotangulia kutolea mfano katika maeneo ya Kilimanjaro ambayo yana miinuko. Serikali imekuwa ikitumia teknolojia ya kuweka zege ambayo inakuwa na ubora zaidi na inaweza kuhimili changamoto mbalimbali za kimazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika utaratibu huo huo Serikali itaendelea kuhakikisha inatafuta fedha kuhakikisha kwamba miundombinu bora hii ya zege na hasa katika maeneo ya miinuko katika jimbo lake yanaweza kujengwa ili nao waweze kupata barabara zilizobora zitakazopitika katika mwaka mzima na zitakazoweza kuhimili misukosuko ya kimazingira.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, okay kwa kuwa sasa ujenzi wa shule umefikia 85%, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi huo pamoja na nyumba za watumishi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mbunge kwa swali hili zuri sana kwa maslahi ya watoto wote wa kike ambao watasoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha mwaka 2023/2024 Serikali itapeleka shilingi bilioni 1.1 katika shule zote zile 16 za wasichana ambazo zilipelekewa shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa kumi, lakini chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu na mabweni manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itapeleka fedha hii kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza kuzitumia.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sayansi zinaenda sambamba na kuwa na laboratories na laboratories hizo zinataka lab technicians, lakini naomba kumwuliza Naibu Waziri, je, mmezingatia kutoa au kutuma lab technicians wa kutosha kwenye shule hizo mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa hizi shule kama nilivyotangulia kusema awali ukiacha majengo tu ya madarasa, lakini kutakuwa kuna chumba cha TEHAMA, kutakuwa na maktaba, nyumba za walimu na mabweni. Kwa hiyo, chumba cha TEHAMA kitakuwepo na kwa sababu msingi ni kuhakikisha kwamba shule hizi zinatoa elimu iliyobora kwa watoto wa kike, wakati wa kutoa watumishi yaani wakati wa kuajiri na kupanga watumishi kwa ajili ya kuhudumia shule hizi lazima Serikali tutazingatia ili hiki chumba cha TEHAMA kipate matumizi kiwe kina lab technicians.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Rungwe tuna shule nzuri sana ya wavulana. Tunashukuru Serikali kwa kuikarabati ni lini mtatujengea shule ya wasichana katika wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi shule hizi zipo 26 ziko kwenye Mradi wa SEQUIP na kila mkoa inapata shule moja ya wasichana, ya bweni na ni ya sayansi. Kwa hiyo, Mkoa wa Mbeya tayari una shule moja kwa hiyo hatutojenga katika kila kata, ni shule maalum Mheshimiwa Rais amehakikisha ametenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kila mkoa unapata shule hii ya bweni ya wasichana ya sayansi. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliona hili na kujenga na kutupatia hizo shule 26 katika nchi yetu ya Tanzania na mkoani kwetu Lindi hasa kwenye Jimbo langu kuwa ni miongoni mwa zile shule za kwanza ambazo zimejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kike wanahitaji ulinzi, je, ni lini mtatupatia pesa kwa ajili ya uzio kwa ajili kuwalinda watoto hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akitetea sana, sana, sana maslahi ya watoto wa kike kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kama nilivyotangulia kujibu katika swali la nyongeza hapo awali Serikali italeta na itapeleka shilingi bilioni 1.1 kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha kuisha, mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu yote ya msingi katika shule hizo ambazo zilipewa fedha katika awamu ya kwanza, kwa sasbabu shule hizi 16 ikiwemo shule ambayo imejengwa Mkoa wa Lindi zilipokea shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza na sasa zitapokea mwaka huu shilingi bilioni 1.1 awamu ya pili kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu yote ya msingi.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara inayotoka Miembeni – Dampo ambayo iko Moshi Vijijini, Kata ya Babogini, wananchi wanatoa takataka kupitisha katikati ya mashamba ya miwa badala ya kupitisha barabarani kwa sababu barabara ni mbovu. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii?

Swali la pili, kuna barabara ya Rau – Wami – Mrawi inayoelekea Mnambe Water Falls ambako kuna kivutio cha watalii, barabara hii ikijengwa itavutia watalii na kuongeza Pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja katika Jimbo la Moshi Vijijini. Je, ni lini barabara hii itajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na maswali yake yote mawili naomba niyajibu kwa pamoja kuwa barabara hizi alizozitaja za Miembeni – Dampo na Barabara ya Rau – Wami, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa sana ya kuongeza bajeti katika ujenzi wa miundombinu ya barabara zetu hizi za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimfahamishe katika Mkoa wa Kilimanjaro pekee katika kipindi cha miaka mitatu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji wa jumla ya shilingi bilioni 153 kwa ajili ya kuhakikisha anaboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya hii ya Moshi Vijijini katika mwaka wa fedha 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 8.3 kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara. Pia kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imetengwa shilingi milioni mbili katika mwaka huu wa bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inazifikia barabara katika Wilaya hii ya Moshi Vijijini, kuhakikisha kwamba miundombinu ya barabara inatekelezwa.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa dhamira ya Serikali ni kufikia barabara hizi, kuhakikisha kwamba zinajengwa, zinakuwa katika hali nzuri na zinaweza kuwanufaisha wananchi wa Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitambue kwamba Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, naye amekuwa akisemea sana, amekuwa akipaza sauti, kwa kweli mmekuwa mkishirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba wananchi wa Moshi Vijijini wanapata barabara zilizo nzuri. Hiyo ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha inawapelekea Watanzania barabara nzuri kwa ajili ya kuimarisha uchumi na kuhakikisha wanapata huduma nzuri za kijamii. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, naomba niongeze maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Igalako – Mwatenga – Mapala na Barabara ya Ipwani – Limsemi ziko katika hali mbaya kutokana na mvua zilizopita. Ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha mnakwendwa kututengenezea barabara hizo kabla ya msimu wa mvua unaokuja?

Swali langu la pili, kutokana na mvua kubwa zilizopita tumekuwa na madaraja mengi ambayo hayapitiki, ni lini sasa mtaanza ujenzi wa Daraja la Mambi na Daraja la Mloo, Wilayani Mbarali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana ya uwakilishi kwenye Jimbo lake la Mbarali. Naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha inajenga, inaendeleza, inafanya ukarabati wa barabara zetu hizi za Wilaya ambazo zina umuhimu mkubwa sana kiuchumi na kijamii kwa wananchi, ihakikishe kwamba inazijenga hizi barabara ili ziweze kuwanufaisha wananchi.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itazifikia barabara hizi ulizozitaja, lakini itafikia madaraja haya uliyoyataja na kuhakikisha yanajengwa, yanakuwa kwenye hali nzuri ili wananchi waweze kuzitumia barabara na madaraja haya. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, barabara ya kutoka Boma la Ng’ombe – Masisiwe – Idegenda iliharibiwa na mvua na haipitiki mpaka sasa; je, Serikali ina neno gani la matumaini kwa wananchi wa maeneo hayo kwa sababu mawasiliano hayakurudi tangu ilivyoharibiwa na mvua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Justin Nyamoga kwa kuendelea kuwapambania wananchi wake kuhakikisha wanapata miundombinu bora ya barabara katika jimbo lake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipaza sauti kuhusiana na barabara hii na nimhakikishie kwamba Serikali itaifikia barabara hii ili iweze kuhakikisha mawasiliano yanapatikana, iweze kuwanufaisha wananchi wake kiuchumi na kijamii.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Wilaya ya Meru inalisha karibu 60% ya wananchi wa Arusha, lakini barabara ambazo zinasafirisha mazao haya ni mbovu sana; je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati barabara hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila mwaka Serikali inatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha na inafanya ukarabati wa miundombinu ya barabara zetu hizi za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafika katika eneo hili la Meru kuhakikisha inaboresha miundombinu hii ya barabara ili iweze kuwanufaisha wananchi na hasa kutokana na umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwenye eneo la kilimo kama alivyoainisha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kapanga – Bujombe hadi Kalya inayounganisha Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Uvinza na Wilaya ya Tanganyika iliahidiwa na Serikali kutolewa shilingi bilioni 1.5; je, ni lini fedha hizo zitapelekwa kwenye hiyo barabara ili iweze kuwasaidia wananchi hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Kakoso kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi wa wananchi wake na naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba mara baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu, naomba mimi na yeye tukae na tuzungumze ili tuweze kufuatilia utekelezaji wa ahadi hii ya shilingi bilioni 1.5 kwa maslahi mapana ya wananchi.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, siku tatu zilizopita Mji wa Geita ulikumbwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na tatizo linajulikana kwamba kuna mitaro miwili mikubwa ambayo inatakiwa kujengwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi wa wananchi wake. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi na yeye tayari tulishazungumza kuhusiana na changamoto wanayoipitia katika Jimbo la Geita Mjini na hasa katika changamoto hii ya mitaro inayosababisha mafuriko. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linafanyiwa kazi ili kuleta muafaka na kuboresha mazingira ya miundombinu ya barabara katika Jimbo lake.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itajenga barabara ya kuanzia Kilosa – Mkata - Merela Junction ili iweze kupitika kwa mwaka mzima kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Ishengoma kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwaka inatenga bajeti kwa ajili ya kufanya ukarabati na ujenzi wa hizi barabara zetu za Wilaya. Kwa hiyo, hata barabara hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, Serikali itahakikisha inaifikia na inaifanyia ujenzi kwa kiwango cha lami ili wananchi waweze kunufaika nayo.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali haioni kuna haja ya kuharakisha huo usanifu ili badala ya kutumia miezi nane na miezi mitatu ya mkandarasi tukatumie miezi michache zaidi ili tuweze kuanza mradi mapema?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kutekeleza ahadi za viongozi wakuu ambako Masasi tuliahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014ujenzi wa kilometa 2.7 za lami ndani ya Mji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya katika jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya wiki mbili tayari consultant atafika kwa ajili ya kuanza kazi hii ya usanifu wa kina. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya miezi hii nane japokuwa yeye anasema ni miezi mingi, lakini kwa mujibu wa taratibu baada ya miezi nane kazi hii ya usanifu itakuwa imekamilika, atatafutwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge huu ndiyo utaratibu na utazingatiwa na cha muhimu ni kuhakikisha wakati wa utekelezaji wa mradi atakapopatikana mkandarasi aweze kukamilisha utekelezaji wa mradi ndani ya muda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mradi huu wa TACTIC tayari kuna component moja muhimu ya barabara ya lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wakuu ni kipaumbele namba moja katika mipango na katika utekelezaji wa shughuli za Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kama vile ilivyoahidiwa. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa miji 45 ambayo ilikuwa ijengwe ya TACTIC, Makambako ni mojawapo ambako tunatakiwa tujengewe soko, stendi na barabara za lami pamoja na garden. Ni lini sasa Makambako, tupo awamu ya ngapi ili kuweza kujengewa hii ambayo tulishaahidiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ilivyokuwa imepangwa kwenye ratiba ni kweli miradi hii ya TACTIC imegawanywa kwa makundi. Kuna kundi la kwanza, kundi la pili na kundi la tatu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imepangwa na yeye Makambako watakuja kutekelezewa mradi huu wa TACTIC ili miradi aliyoiainisha iweze kutekelezwa.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni moja ya halmashauri zile 45 ambazo zinatakiwa zijengewe miradi ya TACTIC. Katika miradi hiyo kuna ujenzi wa barabara, ujenzi wa soko na ujenzi wa stendi mpya. Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba mradi huo unatekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya. Ninaomba nimhakikishie kwamba miradi hii inayotekelezwa katika miji 45, miradi ya TACTIC ipo inatekelezwa kwa mujibu wa ratiba. Nimhakikishie mpaka muda huu ratiba bado inaendelea kuzingatiwa na kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa sababu fedha ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba awataarifu wananchi wake wa Mbinga wakae mkao wa kupokea mradi huu muhimu ambao utaenda kujenga barabara, utaenda kujenga soko na stendi kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Kwa kuwa Mji wa Njombe na wenyewe upo kwenye mradi huo, lakini ni kundi la pili, ni lini ujenzi wa miradi ya lami TACTIC kundi la pili inaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi na nimhakikishie kwamba katika mwaka huu wa bajeti mradi huu utaanza kutekelezwa katika Jimbo lake.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, Halmashauri ya Mji Nanyamba ni miongoni mwa halmashauri ambazo zinatekeleza miradi ya TACTIC na kuna ujenzi wa soko, stendi na barabara; je, ni lini utekelezaji huu utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi kwenye Jimbo lake. Nimhakikishie kwamba taratibu za utekelezaji wa miradi hii ya TACTIC unaendelea kwa kuzingatia kundi husika na nimhakikishie kwamba wao wapo kwenye kundi la tatu ambapo mchakato unaoendelea sasa hivi ni mchakato wa kupata consultant kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina ili inapofika mwakani mwezi wa saba utekelezaji wa mradi uweze kuanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wananchi wake wataweza kupata manufaa makubwa sana ya mradi huu kwa ujenzi wa soko, stendi pamoja na lami. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa mara ya kwanza naomba nikiri wazi kwamba Serikali imejibu maswali kwa ufasaha sana, swali hili limejibiwa kwa ufasaha na hali ndivyo ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna ambavyo amekuwa akiendelea kujibu kwa ufasaha maswali ya Wabunge hapa Bungeni, namuombea Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki na fahamu zake zizidi kukua kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza. Barabara hii imekuwa ni mkombozi mkubwa haswa hivi karibuni tulipata mvua ambazo zilifunga barabara kubwa ya TANROADS, barabara hii ikawa ndiyo mkombozi. Lakini zipo kona kali ambazo magari makubwa kuanzia tani nne na kuendelea yanashindwa kupita kwa ufasaha.

Je, Serikali ipo tayari kurekebisha hizi kona takribani tatu ili barabara hii iweze kuwa na ufanisi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kupokea pongezi za Mheshimiwa Mbunge pia na mimi nimpongeze kwa utumishi wake uliotukuka kwa wananchi wake na hasa kwa sababu amekuwa akifuatilia sana masuala ya miundombinu ya barabara kwenye Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la nyongeza alilouliza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge TARURA inatambua uwepo wa hizo kona kali tano, ambazo kimsingi zinazuia magari yenye zaidi ya tani nne kuweza kupita. Katika mwaka 2024/2025 Serikali imetenga milioni 328 kwa ajili ya kuanza kurekebisha kona mbili kati ya hizo kona tano ambazo zimebainika ni kali sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Serikali itatumia hizi fedha milioni 328 kupasua miamba na kuweka tabaka la zege ili magari yaweze yenye ukubwa wa kuanzia tani nne hadi 10 yaweze kupita. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itahakikisha inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu na hasa katika barabara uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.(Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2022/2023 tulipokea milioni 500 kwa ajili ya kujenga barabara ya kiwango cha lami kutoka Manyinga kwenda Madizini yenye urefu wa kilomita moja, lakini jambo la kushangaza barabara hii imejengwa mita 500. Kipindi kifupi cha miezi sita barabara hii ikawa imeharibika.

Je, Serikali ipo tayari kufanya ukaguzi maalum wa kujiridhisha na matumizi ya hizi fedha milioni 500? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba inajenga na inakarabati barabara kwa viwango vinavyokubalika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala alilolitaja kuhusuana na hii barabara yake ya Manyinga, tumelichukua na tutaliweka katika vipaumbele kuhakikisha fedha zinatengwa na barabara zinarekebishwa na kujengwa kwa viwango vinavyokubalika, kwa sababu hiyo ndiyo dhamira ya Serikali.
MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninashukuru sana Serikali kwa kuwa tayari kujenga daraja hilo, lakini ili daraja liwe na tija zaidi ni lazima kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kutoboa ili kuunganisha kati ya barabara ya Wilaya ya Liwale pamoja na Ulanga inayopita katikati ya Mbuga ya Mwalimu Nyerere. Sasa ni lini Serikali itakuwa tayari kufungua barabara hiyo ili kuunganisha Mikoa ya Kusini pamoja na Morogoro?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni lini Serikali itaunganisha barabara ya kutoka Makanga – Mafinji ili kuunganisha Wilaya ya Ulanga na Malinyi na kurahisisha usafiri, kwa sababu sasa hivi wananchi wanazunguka kilomita 80 ili kufika Wilaya ya Malinyi? Ila barabara hiyo ikiisha itakuwa inapitika kwa kilomita 30 peke yake. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kumalizia barabara hiyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli amekuwa akifanya ufuatiliaji mkubwa sana katika masuala haya ya kupata barabara katika jimbo lake, lakini pia katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, katika swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, ametaka kujua ni lini na mkakati wa Serikali ni upi katika kuhakikisha kwamba inajenga barabara ile ambayo itaunganisha Wilaya ya Liwale pamoja na Wilaya hii ya Ulanga ambayo kimsingi ni Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu ambazo zinahitajika hapa ni kuhakikisha kwamba barabara hii inapandishwa hadhi, ili sasa iweze kuwa barabara ya mkoa ambayo inaunganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia Road Board, waanzishe mchakato huu ili barabara hii iweze kupandishwa hadhi, lakini pia iweze kufanyiwa upembuzi yakinifu, kwa sababu barabara itapita katika eneo la Hifadhi ya Selous. Kwa hiyo, inahitajika upembuzi yakinifu kwenye upande wa mazingira. Baada ya kukamilisha taratibu hizo barabara hii itajengwa ili iweze kuwa na tija kubwa kwa ajili ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge anauliza kuhusiana na ujenzi wa Barabara ya Makanga na Mafinji ambayo kimsingi ina kilometa 35 tofauti na barabara inayotumika sasa hivi ile njia ya Lupilo ambayo ina urefu wa kilometa 80. Ninaomba kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kwa kilometa 30 tayari imeshafunguliwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2023/2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.061.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi 200,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa ma-culvert makubwa mawili. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge mchakato wa manunuzi unaendelea na pindi utakapokamilika, barabara hii itajengewa ma-culvert hayo makubwa mawili.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kilometa tano zile zinazobakia katika kilometa hizi 35, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, tumeweka katika Mpango ujenzi wa ma-culvert 15, lakini pia itatengewa fedha shilingi 900,000,000 kwa ajili ya kukamilishwa. Kwa hiyo ninakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini kuhakikisha kwamba katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge, wanapata miundombinu ya barabara iliyo bora.