Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zainab Athman Katimba (4 total)

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nitambue kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii katika utekelezaji wa majukumu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mfumo wa uhakiki wa vigezo vinavyotumika kutoa mikopo kwa wanafunzi, ili kuhakikisha wanaopata mikopo ni wenye sifa na uhitaji na sio wale ambao wanafanya udanganyifu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mfumo huu wa utoaji mikopo utaendelea kuwa himilivu na endapo idadi ya wanafunzi itaendelea kuongezeka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Bodi inatakiwa kuhakikisha kuwa kumbukumbu za wote wanaoomba mikopo zinakuwa kamilifu kwa kushirikiana na vyuo ambavyo vina wanafunzi wanaopewa mikopo hiyo. Kila chuo kinatakiwakuwa na dawati maalum ambalo linashughulikia mikopo, lakini pia katika kutoa mikopo ni lazima kuzingatia vigezo na sifa ambazo zimewekwa. Hivi karibuni Wizara imepitia vigezo hivyo na vigezo vinazingatia hasa uhitaji, uraia, lakini pia uombaji lazima upitie kwenye mtandao na vilevile kwa kuzingatia mahitaji ya nchi, yaani kipaumbele katika taaluma ambazo zinahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kuona kwamba, mikopo hiyo inakuwa endelevu ni kwamba, Wizara baada ya kuangalia matatizo yaliyokuwa yakijitokeza katika ulipaji wa mikopo, imeangalia upya Sheria ya Bodi ya Mikopo na hivyo tuko katika kutaka kuileta Bungeni, ili kuona kwamba, inarekebishwa kuweka mikopo kuwa ni deni la kipaumbele kwa mwombaji ambaye ameshamaliza chuo. Lakini vilevile kuhakikisha kuwa waajiri wanahusika nao moja kwa moja katika kuhakikisha mikopo hiyo inalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika sambamba na hiyo tunaangalia namna ya kuboresha upya mifumo mizima ili kuona mfumo huo unaweza kuongea na taasisi nyingine zinazohudumia raia, ikiwemo ya Vitambulisho vya Taifa. Ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA:Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Serikali ina mpango kabambe wa kupima na kurasimisha ardhi nchi nzima na imekuwa ikishirikisha sekta binafsi katika kufanya hivyo. Aidha, kumekuwa na gharama kubwa sana katika upimaji na urasimishaji huo wa ardhi. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya gharama hizo ili kuweza kuwapunguzia wananchi mzigo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zainab anazungumzia habari ya gharama kubwa katika suala zima la upimaji. Lakini naomba nimkumbushe tu bajeti ya mwaka jana ilivyosomwa gharama zile zilishuka kutoka shilingi 800,000 kwa heka mpaka shilingi 300,000 kitu ambacho ilipunguza sana gharama zinaongezeka kulingana na ukubwa wa eneo ambalo linaenda kupimwa. Kwa mwaka huu pia katika bajeti yetu nadhani kuna maeneo ambayo Serikali imeyafanyia kazi mtayasikia wakati tunatoa bajeti.
Kwa hiyo, niseme kwamba gharama tunaziangalia
na namna bora ya kuweza kumuwezesha mwananchi wa kawaida aweze kupima ardhi yake na kuweza kumiliki ili kumletea maendeleo katika shughuli zake.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii niulize swali la nyongeza.
Kwa niaba ya vijana wote wa Tanzania ambao wanaweza kuwa wanufaika wakubwa sana wa michezo naomba kuuliza swali la nyongeza lifuatalo:
Je, Serikali haioni umuhimu wa kwamba ni wakati muafaka wa kuwa na shule maalum kwa ajili ya kukuza vipaji katika michezo kama sports academy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninampongeza kwa kuwatetea vijana kimichenzo, kama alisikiliza vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ni kwamba tumedhamiria. Serikali sasa hivi imekwishatenga shule takribani 55 ambazo ziko katika Mikoa yote ya Tanzania, hizi ndizo ambazo tutazichukulia kama ndizo academy zetu. Vilevile michezo ya UMISETA, michezo ya UMITASHUMTA itasaidia sana kuibua vipaji, hata hivyo tunashirikiana sana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba michezo inafundishwa katika ngazi zote za elimu tangu awali, sekondari na vyuoni. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na niseme ninatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha elimu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, Serikali ina mkakati gani katika mabweni haya 155 ambayo inatarajia kuyajenga katika mwaka wa fedha 2017/2018 kuhakikisha kwamba, inazingatia kipaumbele katika ujenzi wa mabweni katika shule zetu za kata?
La pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Mamlaka ya Elimu ya Juu Tanzania ambayo inaonekana inapata changamoto kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha, inatengewa fedha za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kujenga mabweni kwa kushirikiana na Halmashuri na wananchi, kama ambavyo tumekuwa tukifanya na hivi natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kule kwenye maeneo yao ambako kuna ujenzi wa mabweni, basi wasaidie kuwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu kwenye mkakati huu, lengo ni kuhakikisha kwamba, tunakamilisha ifikapo mwezi Juni mwakani, kama ambavyo tumejipanga.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tutaweka fungu maalum kwenye bajeti kwa ajili ya kuisaidia taasisi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja pamoja na taasisi nyingine ambazo zinasaidia maendeleo ya elimu nchini. Ahsante sana.