Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Flatei Gregory Massay (16 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Kutokana na wizi wa mifugo uliokithiri katika Bonde la Yayeda Chini, Serikali ilianzisha kituo cha polisi na sasa kimeondolewa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukirudisha kituo hicho ili wananchi wapate huduma za ulinzi wa mifugo na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kituo cha polisi cha Bonde la Mto Yayeda Chini kilianzishwa kutokana na matukio ya kukithiri kwa matukio ya wizi wa mifugo. Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi lilipeleka gari PT Na. 1008, Landrover kituo cha polisi cha Hydom kinachotoa huduma ya ulinzi wa eneo hilo na kuanzisha doria za mara kwa mara ili kupambana na wimbi la wizi wa mifugo. Kwa hivi sasa, hali ya wizi wa mifugo na uhalifu mwingine katika eneo hilo umepungua.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kituo hicho hakijaondolewa bali taratibu za kutoa huduma za ulinzi zimebadilika; ambapo askari hupangwa kwa kazi za ulinzi wa doria eneo hilo kwa kipindi maalum na kwa awamu. Jeshi la Polisi litaendelea kutathmini na kuzingatia hali ya uhalifu wa eneo hilo katika kutoa huduma stahiki za ulinzi na usalama.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Barabara ya Mbulu – Hydom – Babati – Dongobeshi, imekuwa na miundombinu mibovu na haipitiki muda wote wa mwaka na kumekuwepo ahadi ya kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Je, Serikali itatekeleza lini ahadi hiyo ambayo pia imetolewa na Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbulu – Hydom ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Kilimapunda – Mbulu – Hydom – Kidarafa yenye urefu wa kilometa 114. Aidha, barabara ya Dareda – Dongobesh yenye urefu wa kilometa 60, ni barabara ya Mkoa na inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) na barabara zote hizi mbili ni muhimu sana kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara, na hasa wa Jimbo la Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Mbulu – Hydom – Kidarafa imejumuishwa kwenye mradi wa upembuzi yakinifu wa barabara inayopita kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Seringeti (Southern Bypass) ya Mbulu Route unaojumuisha barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom - Kidarafa hadi Sibiti. Mradi huu upo kwenye hatua ya ununuzi ili kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu na usanifu chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) ambapo kazi ya kuchambua Zabuni inaendelea.
Aidha kuhusu barabara ya Dareda kwa maana ya Babati hadi Dongobeshi yenye urefu wa Kilomita 60, imejumuishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 katika Mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na itaweka katika mpango wa utekelezaji kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa miaka minne mfululizo kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ili kuhakikisha barabara hizo zinapitika kwa muda wote wa mwaka wakati maandalizi ya kuzijengwa kwa kiwango cha lami yanaendelea. Mathalani, fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 zilikuwa ni shilingi milioni 1,254.163; mwaka 2013/2014 zilitengwa shilingi milioni 1,425.163; mwaka 2014/2015 zilitengwa shilingi 1,258.876 na mwaka huu wa 2015/2016 zimetengwa shilingi milioni 1,655.504.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali kupitia Benki ya Dunia ilianzisha mradi wa maji katika Miji ya Haydom, Masieda, Tumati Arri na Bwawa la Dongobesh lakini mpaka sasa mradi huo haujakamilika baada ya fedha kusitishwa:-
Je, Serikali imejipangaje kumaliza miradi hii ili wananchi wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ya Hydom, Masieda, Tumati Arri na Bwawa la Dongobesh ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama ifuatavyo:-
(i) Mradi wa maji wa Hydom umefikia asilimia arobaini na tano. Mradi huu utapokamilika utahudumia wakazi wapatao 16,737.
(ii) Mradi wa Maji wa Masieda umefikia asilimia tisini na tisa na wananchi wapatao 3,137 wanapata huduma ya maji.
(iii) Mradi wa maji wa Mongahay - Tumati umefikia asilimia kumi na sita. Hata hivyo, mkataba umevunjwa kutokana na mkandarasi kushindwa kutekeleza mkataba. Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu inaendelea na taratibu za kupata mkandarasi mwingine. Mradi huu utakapokamilika utahudumia wakazi wapatao 8,679.
(iv) Mradi wa Arri utahudumia wananchi wapatao 17,580. Ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia arobaini na tano.
(v) Ujenzi wa tuta la bwawa la umwagiliaji la Dongobesh umekamilika kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii imechelewa kukamilika kutokana na kukosekana kwa fedha za kuwalipa wakandarasi. Serikali itaendelea kutoa fedha kila zinapopatikana ili kukamilisha miradi hiyo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika maeneo ya Tarafa za Jimbo la Mbulu za Manetadu, Tumatu Arri, Masieda na Yayeda chini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inagharamia utekelezaji wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini (REA), kupitia mpango huu wa REA Vijijini (REF). Mradi huu unatekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Manyara. Mkandarasi, CC International Nigeria Limited, hivi sasa anaendelea na utekelezaji wa mradi huo katika Wilaya za Mkoa wa Manyara ikiwemo Wilaya ya Mbulu Vijijini. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 84, ambapo tayari transformer zimeshafungwa na pia wateja 354 wameunganishiwa umeme katika Mkoa mzima wa Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unategemea pia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu 2016. Lengo kubwa la mradi huu ni kupeleka huduma za umeme kwa wananchi na hivyo kurahisisha shughuli za kiuchumi pamoja na kijamii. Tarafa za Manetatu, Masieda, Tumatiadi na Yaeda Chini zimejumuishwa katika Mpango wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, utakaoanza mara baada ya bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Haydom kwa sasa inatumika kama Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kupitia Tangazo la Serikali namba 828 la tarehe 12 Novemba, 2010. Serikali imeweka utaratibu wa kuipatia hospitali hii ruzuku ya Serikali kwa ajili ya dawa na vifaa tiba kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya, pamoja na kulipa mishahara ya baadhi ya watumishi wanaotoa huduma katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 134.04 kwa ajili ya dawa na uendeshaji wa shughuli za hospitali, kati ya fedha hizo, zilizopokelewa ni shilingi milioni 111.5. Vilevile hospitali hii imetengewa shilingi milioni 570.6 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya kulipa mishahara kwa watumishi wa Serikali wanaofanya kazi katika hospitali hiyo. Kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mkataba wa utoaji huduma ya afya, lengo likiwa ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ambayo inahudumia Mkoa wa Manyara pamoja na Mikoa jirani.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Hospitali ya KKKT Hydom ilipanda hadhi kuwa Hospitali ya Mkoa muda mrefu, sasa inahudumia Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Singida, Arusha na Simiyu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipandisha hadhi ili iwe Hospitali ya Kanda kuiwezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Hospitali ya KKKT Haydom ilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa mwaka 2010. Aidha, hospitali hii haikupandishwa hadhi ili iwe Hospitali ya Mkoa. Mkoa wa Manyara una Hospitali yake ya Rufaa ya Mkoa. Madhumuni ya kuipandisha hadhi Hospitali hiyo yalikuwa ni kuifanya itoe huduma za ngazi ya rufaa ya Mkoa ikisaidiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara. Ili hospitali iwe ya rufaa ngazi ya Kanda, ni lazima iwe na miundombinu bora tofauti na iliyopo sasa, pamoja na watumishi waliopata mafunzo yanayohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Kaskazini tayari kuna hospitali zinazotoa huduma za kibingwa kama KCMC ila kwa vigezo vingine Hospitali hii imeshakaguliwa na imeonekana ina upungufu kadhaa, pale utakapokamilika itatoa huduma hizo. Aidha, hosptiali ya KKKT Hyadom toka awali ilikuwa inahudumia wananchi wa mikoa iliyotajwa. Hali hii inachangiwa na sehemu ya kijiografia iliyopo hospitali hiyo kwani inafikika kirahisi na wananchi wa mikoa hiyo.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Wananchi wa Mji wa Haydom wamekuwa wakiomba Haydom iwe Mamlaka ya Mji Mdogo.
Je, ni lini Serikali itaupa Mji wa Haydom hadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kuwa na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Haydom yamejadiliwa katika vikao vya awali vya Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira tarehe 25/09/2012, Baraza la Madiwani katika kikao cha tarehe 19/10/2012 na Kamati ya Huduma za Uchumi katika kikao cha tarehe 13/06/2014. Kimsingi, vikao vyote hivyo vimekubaliana na wazo la kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Haydom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri mapendekezo hayo sasa yawasilishwe katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili hatimaye yawasilishwe kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kupata kibali. Hivyo, taratibu hizo zikikamilika na kuonekana mamlaka hiyo imekidhi vigezo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, haitasita kuanzisha mamlaka hiyo kisheria.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Wananchi wa Mbulu Vijijini hawana mawasiliano ya simu wala minara katika Kata za Tumati, Yaeda, Ampa, Gidhim na Gorati:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka minara katika Kata hizo ili kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, iliainisha maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Mbulu likiwemo Jimbo la Mbulu Vijijini na kuyaingiza maeneo hayo katika miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa. Kijiji cha Yaeda Ampa kutoka Kata ya Yaeda Ampa kimeingizwa katika zabuni ya mradi wa kufikisha huduma ya mawasiliano kwa maeneo ya mipakani na kanda maalum. Zabuni hii ilifunguliwa tarehe 27, Aprili, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yetu kuwa Kijiji cha Yaeda Ampa kitapata kampuni ya kufikisha huduma ya mawasiliano na kuondoa kabisa tatizo la mawasiliano katika kata hiyo. Aidha, Kata za Tumati, Gidhim na Gorati zimeingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali kupitia Mradi wa Vijijini kumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia iliahidi kupeleka maji Maretadu, Labay, Gidmadoy, Qamtananat, Garbabi, Magana Juu na Qatabela:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri zote nchini. Utekelezaji wa programu hii unafanyika kwa awamu. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji kwa Halmashauri ya Mbulu Vijiji vya Singu, Masieda, Arri-Harsha, Dongobesh, Mongahay, Tumati, Haydom na Moringa vilihusika. Hadi sasa miradi ya maji katika Vijiji vya Singu na Masieda imekamilika na ujenzi unaendelea katika vijiji vilivyobaki. Serikali katika kuhakikisha inakamilisha miradi ya maji na kuanzisha mingine mipya kiasi cha shilingi bilioni 2.09 zimetengwa kwa Wilaya hiyo katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu ya pili ya utekelezaji wa WSDP iliyoanza Julai, 2016, Halmashauri zote nchini ikiwemo ya Mbulu zimewasilisha mipango ya utekelezaji wa miradi kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa maana 2016/2017 - 2020/2021 ambapo miradi mingi ya maji itatekelezwa kulingana na mpango huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu vilivyopo katika mpango huo ni Maretadi, Labay, Didmadoy, Quantananat, Garbabi, Magana Juu na Qutabela. Kwa kuanzia Vijiji vya Meretadu, Labay na Garbabi vimepewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2017/2018 ikiwa ni pamoja na Vijiji vya Genda, Ng’orat na Endahagichan. Vijiji vingine katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu vitaendelea kutekelezwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Hydom umechukua muda mrefu kumalizika na wananchi wanasubiri maji huku muda wa mkataba na mkandarasi ukiwa umeisha.
Je, kwa nini Serikali isimfukuze mkandarasi huyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Mji wa Haydom ulianza kutekelezwa mwaka 2014 lakini kutokana na changamoto ya fedha utekelezaji ulisimama mwaka 2015/2016. Hata hivyo, pamoja na mkataba wa mkandarasi kuisha muda wake, napenda nimsifu na kumshukuru Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Chelestino Mofuga na Mkurugenzi wa Halmashauri Ndugu Hudson Kamoga kwa kufanya kikao kati yao na mkandarasi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Wizara ya maji Profesa Kitila Mkumbo tarehe 2/11/2017, ambapo muafaka wa mkandarasi kuendelea kutekeleza mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2018 ulipatikana. Kwa maana hiyo, wakazi wa vijiji vya Haydom na Ng’wandakw vinavyounda Mji wa Haydom wenye wakazi 17,406 wataanza kupata maji baada ya mradi huo kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza yangu kuhusu taarifa tulizozipata usiku wa leo zinazohusu changamoto za Mkandarasi zinazohitaji utatuzi wa haraka namwomba Mheshimiwa Flatei Massay na mwenzangu Naibu Waziri wa Maji tukutane hapa Bungeni baada ya kipindi cha asubuhi ili tupate utatuzi wa haraka wa mradi huo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali ina mpango gani wa kuwalipa posho au mishahara Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili kurahisisha ufanisi wa shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika maendeleo ya Taifa. Serikali imezingatia na kuweka utaratibu wa kushirikisha viongozi hawa wanaolipwa posho maalum kwa motisha kupitia asilimia 20 ya mapato yanayorejeshwa na Halmashauri kwenye vijiji. Asilimia 17 ya fedha hizo zinatakiwa kutumika kwa shughuli za utawala, ikiwemo kulipa posho ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa na asilimia tatu kwa shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuboresha utaratibu huu kwa kuingiza katika mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ili kuweka utaratibu mzuri wa urejeshaji wa asilimia 20 kwenye vijiji na kuwanufaisha walengwa. Aidha, tumeimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri zote ili kujenga uwezo wa kutenga asilimia 20 kwenda kila kijiji.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya Simu katika Kata za Yayeda, Ampa Arr, Tumati, Gidilim Gorati, Endaagichan na Haydere katika Jimbo la Mbulu Vijijini ili wananchi waweze kuwasiliana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliyaainisha maeneo mbalimbali ya Jimbo la Mbulu vijijini yakiwemo maeneo ya Yaeda, Tumati, Gidilim Gorati, Masieda, Endaagichan, na Hyadere na kuyaingiza katika zabuni ya awamu ya tatu iliyotangazwa tarehe 5 Juni, 2018. Zabuni hii inategemewa kufunguliwa tarehe 23 Julai, 2018. Endapo mzabuni atapatikana, mkataba kwa ajili ya kazi husika unatarajiwa kusainiwa tarehe 29 Agosti, 2018 na ujenzi wa minara unatarajiwa kuchukua miezi tisa tangu kusainiwa kwa mkataba.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Kutokana na sera ya Serikali kujenga vituo vya afya kila kata.
Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivyo katika Kata za Maretadu, Maghangw, Endamilay, Dinamu, Geterer, Masieda na kupandisha hadhi Zahanati ya Hayderer kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imejenga vituo vya afya 210 nchi nzima kwa gharama ya shilingi bilioni 93.5 vikiwemo vituo vya afya saba vilivyoko Mkoa wa Manyara kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Dongobeshi na Halmashauri ya Miji Mbulu ilipewa shilingi bilioni moja kwa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Tlawi na Daudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutimiza azma ya kuwa na kituo cha afya kila kata hapa nchini Serikali imeweka vigezo maalum juu ya ujenzi wa vituo vya afya, lengo mahsusi ni kusogeza huduma za afya ili zipatikane ndani ya umbali wa kilometa tano kama ilivyoelekeza kwenye Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupandishwa hadhi kwa Zahanati ya Hayderer kuwa kituo cha afya miundombinu iliyopo katika zahanati hiyo haikidhi vigezo vya kuhuishwa kutoa huduma kama kituo cha afya. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeendelea kufanya uhamasishaji kwa wananchi kujitolea kujenga vituo vya afya katika kata zilizotajwa za Maretadu, Maghangw, Endamilay, Dinamu, Geterer na Masieda. Hadi sasa wananchi wa Maretadu wametenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi kulingana na upatikanaji wa fedha na rasilimali nyingine kama watumishi na vifaa tiba.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali iliahidi vijiji vingi vya Jimbo la Mbulu Vijijini umeme wa REA III.
Je, ni lini sasa umeme utafika katika vijiji vya Endahargadat, Endahagichani, Qamtananat, Mewadan, Endalat, Gidbiyo na Manghay?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kufikisha umeme katika vijiji vyote Tanzania Bara visivyokuwa na miundombinu ya umeme ifikapo mwezi Juni, 2021. Jimbo la Mbulu vijijini lina vijiji vipatavyo 76, kati ya vijiji hivyo 12 vimepatiwa umeme. Vijiji 13 vya Qaloda, Getesh, Endesh, Labay, Maretadu, Hayderer, Endanachan (Haydom), Muslur, Dirim, Simha, Yaeda Ampa, Endoji na Gidhim vimejumuishwa katika mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza. Mkandarasi Kampuni ya Angelique International Limited kutoka India ameshaanza utekelezaji wa mradi na anatarajia kukamilisha kazi hiyo mwezi Juni, 2019. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilometa 45.87 za njia ya umeme wa msongo wa Kilovolt 33 na kilometa 35 za nja ya umeme wa msongo wa 0.4 kilovolt, ufungaji wa transfoma 16 na uunganishwaji wa wateja wa awali 347. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 2.6. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili utakaoanza kutekelezwa Julai, 2019 hadi mwezi Juni, 2021. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Serikali iliahidi kuanzisha Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu. Aidha, wataalam wa Serikali walifika Mbulu na kukabidhiwa majengo kwa ajili ya Baraza hilo katika Mji wa Dongobesh na Mheshimiwa Mbunge akachangia shilingi milioni tatu za kuongeza miundombinu.

Je, ni lini Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu litaanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi sasa tuna jumla ya Mabaraza 97 ambayo yameundwa, ambapo kati ya hayo Mabaraza 53 yanatoa huduma na Mabaraza 44 likiwemo Baraza la Mbulu hayajaanza kutoa huduma kutokana na changamoto za uhaba wa rasilimali watu. Ili Baraza liweze kuanza kufanya kazi linahitaji kuwa na angalao Mwenyekiti mmoja, Katibu Muhtasi, Msaidizi wa Kumbukumbu, Msaidizi wa Ofisi, Dereva na Mlinzi.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeipatia Wizara Wenyeviti 20 ambao ni wajiriwa wapya. Wenyeviti tisa kati ya hao ni kwa ajili ya kuongeza nguvu katika maeneo hayo yaliyoelemewa kwa wingi wa mashauri katika Wilaya za Mbulu, Sumbawanga, Kibondo, Kigoma, Temeke, Bukoba, Mwanza, Musoma na Ulanga. Wenyeviti 11 kwa ajili ya mabaraza 11 ambayo hayana Wenyeviti katika wilaya za Ukerewe, Maswa, Kilosa, Same, Kyela, Shinyanga, Lindi, Iramba, Nzega, Lushoto na Tunduru. Taratibu za mafunzo ya awali zinafanywa ili Wenyeviti hawa waweze kupangiwa vituo na kuanza kazi katika Mabaraza hayo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba Baraza la Mbulu linaanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo, Wizara imeshatuma barua kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupata mapendekezo ya wananchi wenye sifa, ili Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aweze kufanya uteuzi wa Wazee wa Baraza la Ardhi na Nyumba kwa Wilaya ya Mbulu.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zitakazopata Wenyeviti wapya wa Mabaraza kutuma mapendekezo ya Wajumbe wa Mabaraza kwa wakati, kila wanapotakiwa kufanya hivyo, ili wananchi wasikose huduma kwa kukosekana Wajumbe wa Baraza. Aidha, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanashauriwa kuangalia uwezekano wa kutoa maeneo ya ofisi kwenye majengo yaliyo katika hali nzuri ili kurahisisha uanzishwaji wa Mabaraza katika Wilaya ambazo Mabaraza hayajaanza kazi.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Madiwani nchini wanafanya kazi kubwa sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea posho na mishahara au maslahi yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa wanayofanya Waheshimiwa Madiwani katika kusimamia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao. Kwa kuzingatia ukweli huo, Serikali imekuwa ikipandisha posho na maslahi ya Madiwani kwa kadri mapato ya Halmashauri yanavyoongezeka. Kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali ilipandisha posho ya Madiwani kupitia Waraka wa mwaka 2012 kutoka shilingi 120,000/= hadi 250,000/= kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 108.3. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipandisha tena posho za Madiwani kupitia Waraka wa mwaka 2014 kutoka 250,000 hadi 350,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inalipa pia posho ya madaraka kwa Wenyeviti wa Kamati kiasi cha shilingi 80,000/= kwa mwezi na posho ya kikao kiasi cha shilingi 40,000/= kwa mujibu wa Waraka wa Mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kikubwa kinachotumika kupandisha posho za Madiwani ni uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri husika. Serikali itaendelea kuthamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayotekelezwa na Waheshimiwa Madiwani na kuongeza posho hizo kadri makusanyo ya mapato yanavyoongezeka.