Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aida Joseph Khenani (126 total)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, lakini ni aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Majibu hayo ni ya Arumeru na siyo ya Mkoa wa Rukwa. Halafu mnajiita Serikali ya kazi tu, hapa! Swali hili sijaleta jana, lakini kwa sababu madai ya walimu yako nchi nzima, nitauliza maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa madeni kwa wakati walimu ambao wamekuwa wakilia kila siku na ni malalamiko ya kila siku!
Swali la pili, mpaka sasa walimu wanadai fedha walizosahihisha mitihani ya mwaka 2015 ya kidato cha nne, ni lini Serikali itawalipa walimu hawa na kuwatendea haki kama wafanyakazi wengine wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niweke wazi, katika mchakato wa madeni ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI pale ina maswali zaidi ya takriban 15 ambayo yote moja kwa moja yanalenga katika suala zima la madai ya walimu na yote yanafanana fanana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo, kwa concern ya Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba Serikali haiko makini, isipokuwa jambo hili limekuwa ni kilio karibuni kwa Wabunge wote. Kwa hiyo, suala la msingi ni jinsi gani tutafanya kutatua tatizo hili tuweze kulimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati uliopo, nilisema Serikali kwa awamu ya kwanza ilishalipa haya madeni, lakini naomba niwambie, katika madeni haya katika sehemu nyingine ni fake. Tunafahamu sasa hivi hata katika suala zima la mishahara hewa, mmeona jinsi ambavyo kuna matatizo makubwa, wengine wanaingiza ilimradi waweze kupata pesa. Kwa hiyo, Serikali imejipanga na ndiyo maana uhakiki umefanyika. Katika jibu langu la msingi nimesema kwamba kuna madeni yameshaanza kulipwa na ndiyo maana tulichokifanya ni kuelekeza Halmashauri zote zifanye uhakiki kwa haraka ilimradi walimu waweze kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tukiri kwamba madeni haya hata tukilipa lazima yataendelea kwasababu kila siku walimu wanahama na kila siku walimu wanaenda likizo. Jambo la msingi ni kwamba madeni yanapojitokeza, inapaswa sasa watu waweze kulipwa haki zao wanazostahili.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa uwiano kati ya walimu na wafunzi limekuwa tatizo sugu, katika shule zetu hasa kwamadarasa ya awali hususani Mkoa wa Rukwa, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kukamilisha au kuweka uwiano sana ili kuweka ufanisi wa ufundishaji na uelewa wa watoto wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa walimu hawa walipokuwa wakiwafundisha watoto walikuwa wanatumia mikakati mbalimbali ikiwepo nyimbo, michezo pamoja na kuwapatia uji ili wapende elimu. Toka Serikali imetangaza elimu bure mpaka sasa imetoa kiasi gani kuweza kukidhi mambo hayo ili watotowaendele kupenda shule? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kweli uwiano ni tatizo lakini kilichofanyika ni nini? Mwaka jana tumepeleka walimu katika Chuo chetu cha UDOM, lengo kubwa ni kuhakikisha walimu wale ambao wengine walikuwa hawana zile skills za kufundisha watoto wa awali waweze kupata mafunz hayo na hili hivi sasa limefanyika karibuni nchi nzima na hata jana wakati narudi safari yangu nilikuwa pale Chuo cha Tukuyu ambapo tuna takribani walimu 22,995 ambao tunawaka skills za uchopekaji katika ufundishaji.
Lengo kubwa ni kwamba katika yale mafunzo yale ya uchopekaji maana nadhani lugha ngumu hii, walimu wanaifahamu kwamba integration katika masomo haya kwamba sasa itasaidia katika huu mtaala mpya unaoboreshwa walimu wote watakuwa na mbinu kubwa kuhakikisha kwamba suala zima la ufundishaji watoto wanaomaliza darasa la saba wakijua kusoma na kuandika.
Kwa hiyo katika suala hili lote kwamba ni walimu wangapi ni kwamba tumefundisha walimu takriban 22,000 na sasa hivi katika hii dhana mpya tumefundisha 22,995 tegemeo letu ni kwamba walimu wale wakisharudi shuleni kufundisha walimu wenzao vilevile, lakini katika masomo hayo watu wanaimba nyimbo na mambo mbalimbali ndiyo maana nimesema ni dhana mpya ya uchopekaji ambayo ninaomba sana Waheshimiwa Wabunge muanze kujua dhana hiyo mkienda huko site msishangae mtu anasema sasa naenda kuchopeka darasani, hii ni dhana mpya katika ufundishaji lengo ni watoto waweze kuelewa vizuri.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa mradi wa maji unaoendelea Manispaa ya Sumbawanga umechukua muda mrefu na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga mpaka sasa hawajui huo mradi utaisha lini: Je, Serikali inawaambiaje wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga ikiwepo wanawake ambao wanapata athari mpaka sasa na wengine kupata vifo kwa ajili ya kufuata maji kwenye umbali mrefu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ina mradi mkubwa wa maji pale Manispaa ya Sumbawanga. Mradi ule ulikuwa umalizike toka Septemba, 2015, sasa yalitokea matatizo; kwanza, ilikuwa ni kuchimba visima 12; visima sita virefu upande wa kusini na visima sita upande wa kaskazini. Kwa hiyo, ikabidi baada ya kuanza kuchimba tukakosa, visima vyote havikuwa na maji. Kwa hiyo, tukatafua upande wa Kaskazini, ikabidi tuongeze sasa idadi ya visima kutoka sita mpaka 17, hii ikasababisha muda kuongezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie wananchi wa Sumbawanga, kwanza mradi kwa sehemu kubwa umeshakamilika, kilichobaki ni kujenga mtandao. Ikifika mwezi Desemba mwaka huu mradi ule utakuwa umekamilika na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga watakuwa wanapata maji.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa,
tathmini imefanyika toka mwaka 2009 mpaka leo hakuna kitu kinachoendelea.
Wananchi wa Sumbawanga wanataka majibu ya uhakika ni lini watalipwa pesa
zao, kwa sababu ahadi zimekuwa za kila siku?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, nimhakikishie kwamba mara baada ya uhakiki unaofanyika
kukamilika, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuwalipa wananchi hao fidia zao.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa bidhaa nyingi zinazoonekana nchini kuwa ni feki kwa asilimia kubwa zinatoka nchi ya China na kupitia Bandari ya Dar es Salaam; mpaka sasa Serikali imewachukulia hatua gani TBS, FCC, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyosababisha bidhaa hizi kupita na baadaye kuwaathiri wananchi wasiojua chochote kinachoendelea? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano alitangaza kuzima simu ambazo zilionekana ni fake, wakati zinaingia nchini zililipa kodi na zikaonekana ni sahihi mpaka kuingizwa kwenye maduka na baadaye wananchi wakazinunua. Lakini baadae Serikali hii hii ya Chama cha Mapinduzi ikaona hazifai na zikazimwa, badala yake wananchi ndio wakapata gharama ya kuingia tena kununua simu nyingine. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia au kuwalipa gharama wananchi kwa kuwa uzembe huu ulifanyika na Serikali yenyewe ya Chama cha Mapinduzi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida, na nianze na hili la pili ambalo ni rahisi. Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya mambo yanayotusaidia ni Wanasayansi wa Wizara ya Mawasiliano kwa kugundua njia rahisi ya kuweza kugundua kitu feki. Kwa kufanya hivyo wametusaidia kwa sababu simu zile zina madhara. Bidhaa imeingia, umeinunua, umelipa kodi; si busara kukuacha uendelee kuitumia ikuumize kwa sababu ulilipa kodi; nichukue fursa hii kuwashukuru wataalamu wetu waliogundua njia hiyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawasaidiaje; tunalenga kutengeneza kiwanda cha kutengeneza simu ambazo zitawafaa wale wananchi ambao wanashawishika kununua simu za bei rahisi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, namba (a) hatua gani tumechukua kwa TBS na FCC. Mheshimiwa Mwenyekiti, bidhaa bandia zinaingiaje nchini, tuna matatizo. Mipaka yetu ni porous,lakini katika jibu langu la msingi nimesema kuna wananchi wema wanatusaidia. Kwa hiyo, nchi yetu kwa sababu mpaka ni mkubwa na ni porous,kuna wimbi kubwa la bidhaa zinazoingia humu kimagendo na ndiyo maana kikwazo kimojawapo cha kufufua baadhi ya viwanda, hasa vya nguo ni kwa sababu, kuna bidhaa zinaingia kimagendo kutoka nchi jirani na kutoka hizo nchi zijazo. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba bidhaa yote bandia inatika China, sina uhakika wa suala hilo.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa utaratibu wa Serikali wa kuajiri unaeleweka kwa kufuata taratibu mbalimbali na wapo vijana ambao wana sifa hizo, elimu, uzoefu na vitu vingine. Ni lini Serikali itawapa ajira vijana wa Kitanzania ili kuwaepusha kujiingiza kwenye masuala ya ukabaji, wizi na mambo mengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa nafasi za ajira kwa vijana kwa nafasi ambazo zimekuwa zikitangazwa. Pia kupitia Wizara ya Kazi tumeendelea kutoa msisitizo wa kuanza kuwabadilisha mtazamo vijana na kuwaaminisha kwamba si lazima vijana wote waende kufanya kazi za maofisini hii inatokana pia na takwimu iliyofanyika mwaka 2014 (Intergrated Labour Force Survey) iliyotuambia kwamba kundi kubwa la vijana wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka ni kubwa zaidi kuliko nafasi za ajira ambazo zinazalishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali tumekuja na mipango kadhaa kuhakikisha kwamba tunamfanya kijana huyu wa Kitanzania asiendelee kufikiria kuhusu kuajiriwa tu ofisini mojawapo ikiwa ni kumsaidia kupata ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Pia kuwafanya vijana wa nchi hii sasa washiriki kwenye kilimo, ufugaji na biashara ikiwa pia ni sehemu ya ajira.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Pamoja na agizo la Serikali kwenye Halmashauri kuagiza kutenga asilimia kumi kwa vijana na wanawake, kumekuwa na utaratibu wa Halmashauri kugawa pesa hizi kipindi cha Mwenge. Kwa sababu Halmashauri nyingine wanawake wanapata changamoto sana kipindi cha kilimo, Serikali haioni ni hekima au busara kutoa pesa hizi kipindi cha msimu wa kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nilizungumza mara kadhaa hapa, fedha zile hazitoki kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, fedha zile zinakusanywa katika Halmashauri zetu na Kamati ya Fedha inakaa na kufanya maamuzi fedha zile ziende wapi na kwa akina nani?
Kwa hiyo, jambo hili naomba niseme wazi, kama sisi Wabunge na Madiwani wetu tukiwa committed kuwasaidia wananchi wetu, haitaleta shida kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua concern ya Mheshimiwa Mbunge, lakini niwaelekeze sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, twende sasa tukazihakikishe Kamati zetu za Fedha zinapokaa katika ile ajenda ya mapato na matumizi, katika own source, tutenge kabisa pale pale, tuzielekeze kwa vijana na akina mama waweze kujikomboa kwa kadri Serikali ilivyopanga. Huu ndiyo mchakato wa wazi kabisa, kila mtu ataona ni jinsi gani ameshiriki vyema kuhakikisha jamii yake inakwenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mbunge.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa, ni Wizara hiyohiyo ya Uchukuzi, ingawa niliomba swali namba 70.
Kwa kuwa mawasiliano ni haki ya kila Mtanzania, lakini
toka nchi imepata uhuru kuna maeneoa ambayo hayajapata mawasiliano, ikiweko kata ya Kala na Ninde. Ni lini Serikali itatimiza wajibu wake wa kupeleka mawasiliano katika hizo kata, ikizingatia ziko pembezoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapata mawasiliano na ndio sababu kubwa ya kuanzisha huu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Kwa hiyo, mara tutakapopata fedha tutakuja huko ambako Mheshimiwa Aida umekueleza.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia nashukuru kwa ufafanuzi alioutoa Naibu Waziri ambao utaleta mwanga kidogo kwa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wameamua sasa kufuata utaratibu ili wapate hati, shida yao siyo kumiliki tu hati, ziwasaidie kwenye taasisi pia za kifedha, lakini hati zimekuwa zinachelewa sana. Hamuoni kwamba kuendelea kuchelewa kwa hati hizo mnawanyima fursa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa masuala ya maendeleo kwa sababu wanakosa mambo muhimu hasa katika taasisi za fedha?
Swali la pili, Maafisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga wanajitahidi sana kwa jitihada zao kuwafuata wananchi kwenda kupima maeneo, lakini wanakabiliana na changamoto za usafiri, pamoja na vitendea kazi vingine kwenda kupima ardhi.
Je, Serikali hamuoni kuna umuhimu zaidi wa kuwapa kipaumbele ili wale wakafanye kazi kwa mujibu wa sheria ili wasipate malalamiko kama yanayoendelea kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza amezungumzia ucheleweshaji utaratibu wa kupata hizo hati pengine unakuwa ni mrefu na ni kinyume na utaratibu. Pengine Mheshimiwa Aida bado yuko na mawazo yale ya zamani, kwa sababu sasa hivi kama ambavyo tulieleza kwenye bajeti iliyopita ndani ya mwezi mmoja kama umekamilisha malipo yako vizuri, unapata hati yako, hakuna tena usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda zetu zote Nane zinatoa hati hizo tumeishaweka wataalam kule wako wanafanya kazi hiyo. Kama huko kwake bado hilo linafanyika, nadhani siyo sahihi, na mimi siamini kama linafanyika hivyo kwa sababu utendaji wa Wizara kupitia Kanda zake unakwenda kwa utaratibu na mujibu wa sheria ambavyo tumewawekea, hivyo hakuna tena suala la ucheleweshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Maafisa Ardhi kukosa usafiri na vitendea kazi, naomba tu nitumie fursa hii watendaji hawa ambao wako katika Halmashauri ni jukumu la Halmashauri kuweza kuona ni jinsi gani watu hawa watafanya kazi. Wizara tuna-support yale ambayo yako nje ya uwezo wa Halmashauri. Hii ni Idara kama Idara zingine, kama Idara ya Elimu, Idara ya Afya wanakuwa na usafiri, wanawekewa bajeti zao kila mnapopanga. Mnashindwa nini kufanya hilo kwa Idara ya Ardhi, kwa sababu sehemu nyingi kila unapoenda unakuta Idara ya Ardhi ile ni ombaomba, wakitaka kwenda field mpaka wabembeleze gari sijui la Elimu, lakini ni jukumu la Halmashauri husika kui-treat Idara hii sawa na Idara zingine. Kwa sababu ndiyo kwanza wanaofanya zile kazi ambazo inawezesha Idara zingine kuweza kufanya kazi zao kwa ukamilifu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe kwamba mbali na Wizara kusaidia, ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha kwamba tunapoweka bajeti zetu, katika kupanga vitendea kazi pamoja na kwamba vina gharama lakini lazima tukadirie. Wizara pia inakwenda kuweka utaratibu kwenye maeneo ya Kanda zetu kutakuwa na vifaa vya upimaji kule ambavyo vitasaidia katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, tusaidiane Halmashauri na Wizara ili tuwarahisishie kazi hii na wao waweze kufanya kazi zao kwa ukamilifu.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri sana, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge niwape experience kidogo kwa swali la nyongeza hili kwamba hati hazitayarishwi na Wizara, hati zinatayarishwa pale kwenye Halmashauri. Sasa nawaombeni ninyi Waheshimiwa Wabunge mkirudi majumbani kwenye Halmashauri zenu mfanye tu ujanja ambao nimegundua wanafanya.
Meshimiwa Naibu Spika, nimekuta Kibaha pale hati zinaanza kuandaliwa pale Wilayani makaratasi, hata lile jalada la hati linatengenezwa pale sisi tunakuja kusaini tu huku mwisho. Mkienda kwenye Masjala za Hati kwenye Wilaya zenu zote, mtakuta hati zile zimetayarishwa ziko kwenye mafaili haziendi kokote.
Waheshimiwa Wabunge, hebu kila mmoja aende kwenye Masjala ya Ardhi ya Halmashauri yake, utakuta hati zimeshaandikiwa, watu wameshalipa wametengenezewa na yale majalada ya kaki halafu zimewekwa pale miaka miwili mitatu. Hazifiki kwa Makamishna wa Wizara ya Ardhi kusaini kwa nini? Ndiyo kazi tunayoifanya sisi wenzenu kuja kwenye Majimbo yenu kuja kuangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sasa wote muwe ma-auditor muende kwanye masjala za ardhi mkaziondoe zile hati ambazo zimekaa mle, watu wanataka zikae muda mrefu wasahau halafu waweze kubadilisha wampe mtu mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba mtusaidie kwenda kwenye masjala, mfanye ukaguzi watu wote ambao majalada yameshaandikwa yafike kwa Makamishna wapewe hati zao, tunataka mwezi mmoja tangu mtu amelipia apate hati yake. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa ni zaidi ya miaka 53 toka nchi imepata uhuru sehemu yenye hadhi ya mkoa kama Mkoa wa Rukwa hatuna Hospitali ya Wilaya hata moja. Serikali haioni umuhimu sasa wa kuondoa aibu hiyo angalau hata wilaya mbili zipate hospitali ya wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu, Wabunge wote wa Rukwa wakisimama hapa ajenda kubwa ni afya kwa sababu ni kweli siyo jambo la uongo. Ndiyo maana hata nilivyokuwa nikimjibu Mheshimiwa Bupe swali lake lile la msingi la kwanza nilizungumza kwa ujumla wake. Ndiyo maana tumesema mipango ya Serikali katika Halmashauri ya Kalambo sasa hivi kati ya shilingi bilioni 1.4 tuliyoitenga tumepeleka karibu shilingi milioni 340 lakini hili tutalisimamia vizuri katika mwaka huu wa fedha angalau Kalambo ujenzi uende kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika ukiangalia pale Sumbawanga DC hali ni mbaya vilevile, lakini hivi sasa katika Kituo cha Afya cha Mwimbe tumepeleka fedha karibuni shilingi milioni 500 lakini kule Nkasi tumeshaanza kushughulikia matatizo yake. Jukumu hili lote ni la Serikali. Naomba muwe na imani kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano, commitment yake ile mikoa ambayo ina changamoto kubwa sana tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo wanapatiwa huduma.
Kwa hiyo, Mheshimiwa dada yangu naomba nikusihi kwamba Serikali hii iko nanyi Wabunge wa Rukwa wala msiwe na hofu, tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha huduma ya afya inapatikana vizuri zaidi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mkoa wa Rukwa tunalima sana mazao ya chakula na sasa ni msimu wa mavuno… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkoa wa Rukwa tunalima sana mazao ya chakula na sasa ni msimu wa mavuno, lakini wananchi wa Mkoa wa Rukwa mpaka sasa hawajapata soko la uhakika la kuuza mazao yao wala kiwanda hakipo. Ni lini kiwanda kikubwa kitajengwa Mkoa wa Rukwa ili kiwanufaishe wakulima hao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili swali limejirudia. Viwanda anavyovizungumza, Viwanda vya Asali, vya Ulezi, vya Mahindi ni viwanda vidogo, vya kati na viwanda vikubwa. Kiwanda alichokijenga Mheshimiwa Aeshi chenye thamani ya dola milioni za Kimarekani, ni kiwanda kikubwa.
Kwa hiyo, ninachokwambia, tuhamasishane sisi tujenge viwanda. Msitafute mtu kutoka nje aje achume sisi tumeshahangaika. Viwanda hivi vya shilingi milioni 400 au shilingi milioni 500 tunavimudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze, itafika wakati tutaweza kulazimishana mtu asitoe mahindi Rukwa kuyapeleka Dar es Salaam, tengeneza product, zi-brand; regional branding. Brand unga wako kule upeleke mjini chakula, msipeleke ajira mjini. Ndivyo nilivyozungumza kwenye bajeti yangu na tukubaliane tuanze, hatujachelewa.
Mheshimiwa Aida, kiwanda kidogo cha shilingi milioni 500 unakimudu. Kama hujui fursa uliyonayo, njoo nikuelekeze namna ya kuzipata.
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Serikali ya Awamu ya Tano imepunguza wafanyakazi kwenye kada mbalimbali kwa kigezo cha kutokuwa na sifa, ni lini sasa Serikali itatoa ajira kwa kuwapa kipaumbele vijana wa nchi hii ambao kwa sasa ni wengi wamerundikana mtaani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Kwa kuwa mikopo hiyo anayoizungumza Waziri, Halmashauri inatenga asilimia tano ambayo kwa sasa haiwezi kukidhi haja kulingana na idadai au wimbi kubwa la vijana waliopo mtaani. Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuwa na mpango mkakati wa kuwapa mafunzo maalum au kuanzisha vyuo kwenye mikoa yote ili kuwapa ufanisi vijana waweze kujiajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya kutengeneza nafasi nyingi za ajira hasa kwa kundi kubwa hili la vijana, Serikali imekuja na mipango mikakati mbalimbali, si kweli kwamba tunaweza tukawa tuna nafasi za kuwaajiri vijana wote kwenye sekta ya umma, ndiyo maana kupituia program nilizozisema Serikali imeona ni vyema kuendelea kuishirikisha sekta binafsi, lakini vilevile na kwenda na falsafa ya uchumi wetu wa viwanda, lakini vilevile na kuwahimiza vijana kushiriki katika sekta za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara ili kwa pamoja tuwe tumetengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana kuliko kuendelea kuwafanya vijana wengi wa Kitanzania kuamini kwamba nafasi za kazi ni lazima ziwe za maofisini.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Ajira, imezungumza vyema kabisa tafsiri ya neno ajira maana yake ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato. Kwa hiyo, Serikali tunachokifanya ni kuendelea kutengeneza nafasi nyingi zaidi za ajira ili vijana wengi zaidi waweze kupata nafasi ya kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la nyongeza amesema ni lini tutaanzisha mkakati wa kuanzisha vyuo ili kuwajengea vijana hawa uwezo. Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, tunavyo vyuo vya maendeleo ya vijana ambayo lengo lake ni kuwapa vijana mafunzo, kuwajengea ujasiri na kuwasaidia pia katika kuweza kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Mheshimiwa Spika, pia kupitia programu hizi katika Ofisi ya Waziri Mkuu tunao Mpango Maalum wa Ukuzaji Ujuzi nchini ambao lengo lake ni kumfanya kijana wa kitanzania apate ujuzi ambao utamsaidia kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza hivi sasa kupitia mpango huu tayari tunao vijana takribani 2,000 ambao wanapata mafunzo ya kutengeneza nguo na kukata vitambaa katika Kiwanda cha Tooku Garment pale Mabibo, tunao vijana 1,000 ambao wako tayari Mazava Fabrics, Morogoro ambao wanajifunza kutengeneza t-shirts za michezo na wataajiriwa wote.
Mheshimiwa Spika, pia tunao vijana 1,000 ambao wako DIT - Mwanza wanajifunza kutengeneza viatu na bidhaa za ngozi. Tunao vijana 3,445 ambao wako katika sehemu mbalimbali za Don Bosco ambao wao wanapata mafunzo katika TEHAMA, kutengeneza vitanda kwa maana ya carpentry, masonry, ambao wote hao kupitia programu hii tunaamini kabisa watakwenda kusimama na kujitegemea.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata pembejeo za kutosha na wanapata masoko ya uhakika, jambo ambalo Serikali hii imeshindwa kutimiza wajibu wake.
Swali langu, Serikali ina mkakati gani wa kuandaa masoko ya uhakika badala ya taabu ambazo wanazipata wananchi wetu na kupata umaskini unaosababishwa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikanushe kwa herufi kubwa kwamba Serikali imeshindwa kutengeneza mazingira kwa ajili ya watu wetu. Hiyo ni uongo kabisa na ndiyo maana suala la commodity market kama Wizara tunaendelea kulisimamia na limefika hatua nzuri kuhakikisha sasa wakulima wetu, wafanyabishara wetu wanauza mazao yao katika soko ambalo limeandaliwa kwa umakini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme na ndiyo maana hata zao la korosho limenyanyuka na linakimbia, hii ni kwa sababu ya jitihada za Serikali yetu kuhakikisha wakulima wetu na wafanyabiashara wetu wanaweza kufikiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha migogoro hii pia kinatokana na hifadhi ambazo zinatolewa bila utaratibu, tunajua mpaka eneo litangazwe kuwa hifadhi kuna utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa. Hivi karibuni kumekuwa na utaratibu wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kushirikiana na halmashauri kuwaondoa wananchi na kusema maeneo fulani ni hifadhi na wakijua kabisa maeneo hayo hayajatangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Nini tamko la Serikali juu ya Halmashauri ambazo zinaondoa wananchi hao na ikiangalia kabisa hawajafuata taratibu na sheria za nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hifadhi za misitu kuna misitu ambayo inasimamiwa na Serikali Kuu, kuna misitu inayosimamiwa na TAMISEMI na kuna misitu inayosimamiwa na Serikali za Vijiji. Kwa hiyo, kama vijiji vimetenga kwamba maeneo hayo ni ya hifadhi basi mamlaka zinazohusika zina wajibu wa kuhakikisha kwamba wananchi hawavamii katika hayo maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi, mimi naamini kabisa Wakuu wa Wilaya wamechukua hatua kutokana na maamuzi yaliyokuwa yamefanywa na Halmashauri zinazohusika. Kama kuna maeneo ambayo wananchi wameondolewa bila kufuata taratibu basi ntaomba Mheshimiwa Mbunge anipe hayo maeneo ili tuone na tutafakari ni hatua zipi zilistahili kuchukuliwa. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu, anasema ni askari 105 ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Katika matukio ambayo yametokea ambayo hayana shaka, ni matukio ya wazi, ni matukio ambayo yametokea kwa Mheshimiwa Nape Nnauye ya kutolea bastola hadharani lakini pia Mdude Nyangali ambaye amepigwa mpaka sasa hawezi kutembea vizuri, Husna Amri ni kiongozi wetu wa CHADEMA ambaye amefanyiwa hicho kitendo mpaka sasa hivi tuko hospitali. Je, katika hao askari ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu ni miongoni mwa hao 105?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna askari ambao umekiri kwamba wamechukuliwa hatua za kinidhamu na hawa watu wanaoteswa wengine hawawezi tena kuendelea na shughuli zozote, wanapata fidia gani kulingana na madhara ambayo wamekuwa wameyapata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa naibu Spika, swali lake ameuliza kwa kutoa mifano michache ya baadhi ya watu ambao walipata majeraha mbalimbali, lakini naomba nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi kidogo wa majibu ya swali hili, nadhani itasaidia kuweza kutoa uelewa mpana wa utaratibu wa jinsi ambavyo polisi wanafanya shughuli zao wanapokabiliana na changamoto ya uvunjifu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ukamataji nchini unasimamiwa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu namba 11 ambacho kinaeleza kwamba polisi anapaswa atumie njia ya kumshika muhusika (physical contact) pale tu ikiwa yule mtuhumiwa amegoma. Katika hali ya kawaida ni kwamba polisi wanapohitaji kumkamata mtuhumiwa inamueleza na watuhumiwa ambao wanafuata sheria bila shuruti huwa polisi hawana haja ya kuwashika au kuwakamata kwa kutumia mikono yao. Hii inadhihirishwa na hata Waheshimiwa Wabunge huwa ni mashahidi mara nyingi, wakiwemo viongozi ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa mambo mbalimbali wanapelekewa taarifa kwa njia ya simu au hata kwa barua waweze kujisalimisha wenyewe polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia ya pili ni ambayo sheria hii inaainisha ni kwamba endapo mtu huyo atakuwa amebisha, basi polisi wataweza kutumia njia yoyote ambayo ni stahiki kuweza kumkamata mtuhumiwa, kwa kiingereza wanasema; “may use all means necessary to effect the arrest.”
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivi ndivyo ilivyoandikwa katika Sheria yenyewe ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Hata hivyo, hata hii nayo imefafanuliwa katika PGO namba 274 ambayo inaeleza utaratibu wenyewe hata wa kukamata ukoje na unazingatia mambo mengi. Kwa mfano, unaweza ukaangalia aina ya tishio kwamba je, madhumuni ya mtu huyu ni yapi na mazingira ambayo yanahusisha mtuhumiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengine mengi ambayo yanaangaliwa miongoni mwayo wanaangalia vilevile, kwa mfano; wanaangalia resistance ilivyo. Wakati mwingine inawezekana mtu akawa amesimama tu au ameshikilia kitu au wakati mwingine ameshikilia silaha, kwa hiyo vile vile maamuzi ya kumkamata yanategemea aina ya mtuhumiwa mwenyewe mazingira yake aliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia inetegemea aina ya silaha ambazo polisi anazo, inategemea vilevile utafiti ambao polisi wanafanya kabla, mbinu gani watumie. Wanaweza wakahitaji kupata taarifa za kiintelijensia kabla ya kumkamata muhusika. Niliona nitoe ufafanuzi huo ili nieleweke vizuri. Hata matumizi ya nguvu kwa wale ambao ni majambazi au wanaotumia silaha nao kuna utaratibu wake kwa mujibu wa PGO namba 7 na 8.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kujibu specifically suala la watu ambao wanawataja itategemea na mambo yote ambayo nimeeleza, kwamba je, mazingira ambayo mtuhumiwa alikuwepo yalikuwa ni yapi? Sasa kusema sasa hivi kwamba mtu fulani alikuwa amechukuliwa hatua gani kwa maelezo ya hapo moja kwa moja, nadhani cha msingi ni kwamba tunashughulika na kesi kwa kesi kulingana na aina ya mtuhumiwa jinsi ambavyo ametenda lile kosa. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Na mimi niseme tu kwamba mimi ni miongoni mwa Wenyeviti wa Tanzania wa Serikali ya Mtaa wa Vodacom Kata ya Chanji kwa hiyo, ninaloliuliza ninalijua na changamoto zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya Serikali inayotengwa watekelezaji wa kwanza ni Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, kauli hii ya kwamba wataanza kulipwa posho sio mara ya kwanza ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba time frame ni lini sheria italetwa hapa ili Wenyeviti waanze kulipwa posho kwa sababu sio hisani wanafanya kazi kubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Dada yangu, Mheshimiwa Aida, Mbunge wa Viti Maalum, lakini Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, kama walivyokuwa Wenyeviti wengine wa Jimbo la Ukonga kule nikifahamu hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema hapa kwamba kwanza kulikuwa na uzembe. Naomba niseme kwamba hata ile asilimia 20 kama kungekuwa na commitment ya kurudi vizuri katika Halmashauri zetu, maana sasa hivi tunapozungumza kuna Halmashauri nyingine zinafanya vizuri katika hilo. Tuna baadhi ya ushahidi kuna Halmashauri nyingine Wenyeviti wake wa vijiji wanalipwa vizuri kutokana na kwamba wameweka commitment ya asilimia 20 lazima irudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la time frame ni kwa sababu ni suala la sheria ni suala la kimchakato na taratibu zote sheria hii imeshapitia hivi sasa inaenda nadhani katika Baraza la Mawaziri kupitia katika vifungu mbalimbali, ikishakamilika itakuja humu Bungeni. Sasa niwaombe Waheshimiwa Wabunge sheria ikija humu tunawaomba tushiriki wote kwa pamoja vizuri kwa sababu, ina vifungu vingi sana vinazungumzia suala la mapato katika Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kwamba tutajadili kwa kina tuje kuangalia jinsi gani tutafanya marekebisho mazuri ambayo yataenda kuwagusa Wenyeviti wetu wa Serikali za Vijiji kuweza kupata ile posho yao kwa kadiri inavyostahiki. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia ajira kwa vijana, kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya makampuni kuajiri watu kutoka nje, yakiwemo makampuni ya ulinzi na kuwafanya vijana wa Kitanzania kutengwa kuonekana kwamba, wao hawana uwezo.
Je, Serikali haioni kuendelea kuajiri watu kutoka nje ni kuweka nchi yetu hatarini, badala ya kuajiri vijana wa Kitanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, imetungwa Sheria ya Uratibu wa Ajira kwa Wageni ambayo na sisi kama Wizara, tunaisimamia. Nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika utekelezaji wa sheria hii tunahakikisha nafasi nyingi sana zinashikwa na wazawa, ili kuweza kulinda ajira za Watanzania. Kama kuna jambo lolote limetokea kinyume chake hapo, basi tutaelekeza Maafisa wetu wa kazi waende kufanya ukaguzi na wale wote ambao wameingia kinyume cha utaratibu waweze kuchukuliwa hatua ili vijana wetu waweze kupata nafasi za ajira.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, pamoja na Mkoa wa Rukwa kupata mvua nyingi kuwa na Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika wananchi wake bado wanapata adha kubwa ya maji. Serikali haioni umuhimu wa kutumia Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika kuwafikishia maji wananchi hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa, Mji wa Sumbawanga mwaka huu wa fedha tumekamilisha mradi mkubwa ambao unatoa lita milioni 13 kwa siku, kwahiyo wananchi wa Sumbawanga wanapata huduma ya maji safi na salama. Lakini pili, katika mwaka ujao wa fedha tayari Mkoa wa Rukwa wameleta andiko ambalo sasa tutaweka consultant aweze kufanya feasibility study na usanifu wa kina kwa malengo ya kuyatoa maji kutoka Ziwa Tanganyika kupitia vijiji vinavyokuja Sumbawanga mpaka Sumbawanga ili tuwe na chanzo cha uhakika cha maji.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa lengo la Serikali ni kufanya vyanzo vya maji viendelee, lakini wanapowazuia wananchi kutolima kwenye vyanzo vya maji Serikali haiwapi mkakati wala kutengeneza eneo mbadala la kulima vyakula hivyo ikiwemo Mkoa wa Rukwa. Je, ni nini mkakati wa Serikali kabla haijawazuia kuwaandalia eneo mbadala la kuendelea na mazao hayo wanayolima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli nafahamu, Mheshimiwa Aida ametoka Ziwa Rukwa, katika nchi yetu miongoni mwa Maziwa ambayo yapo hatarini kutoweka zaidi ni katika Ziwa letu Rukwa ambalo linaonekana sasa, wataalam wetu wanasema ukifanya tathmini miaka ishirini iliyopita na hivi sasa hali iko tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu. Maana leo hii tunapozungumza wengine ndio wanaenda kuvamia vyanzo vya maji, kwa hiyo mkakati wa kwanza ni kutoa elimu. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tutawaelekeza wataalam wetu hasa jinsi gani wafanye, kuwabainisha wananchi waweze kutafuta fursa nzuri kwa sababu nchi yetu bado kuna maeneo na fursa kubwa katika suala zima la kilimo. Kwa hiyo jambo hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanya, lakini kwanza ni elimu, watu wafahamu nini maana ya chanzo cha maji na nini athari yake chanzo cha maji kinapoharibika.
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, Halmashauri nyingi nchini zinapopelekwa Mahakamani zinashindwa kesi, hali inayoonyesha ni jinsi gani Wanasheria wetu wa Halmashauri wanashindwa kuwashauri vizuri Wakuu wa Idara na kusababisha hasara kwenye Halmashauri zetu. Serikali ina utaratibu gani wa kufuatilia weledi wa Wanasheria wetu kwenye Halmashauri ili kuepusha hasara zinazotokea kwenye Halmashauri zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika kesi za usuluhishi nje ya nchi napenda kufahamu, ni kesi ngapi tumeshinda kama Serikali na zipi tumeshindwa ikiwepo ya DOWANS, IPTL na nyinginezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anauliza namna ambavyo Serikali inaweza kufuatilia weledi wa Mawakili katika Halmashauri ambao wamekuwa wakisababisha hasara kwa Halmashauri kushindwa kesi nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imekuwa ikiingilia katika baadhi ya mambo ambayo maslahi ya Serikali yanakuwa yako hatarini na pia katika ushauri ambao tumeuweka hapa tumeshauri taasisi hizi zikiwa zina kesi kubwa ambazo zinahitaji intervention ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa-consult mapema, ili wapate ushauri ambao unaweza kusaidia kulinda maslahi ya Serikali. Katika swali aliloliuliza sasa, nitoe tu rai kwa Wanasheria wote, hasa wale Mawakili katika Taasisi za Serikali katika kila Halmashauri kuendelea kufanya kazi hizi kwa weledi mkubwa na ufanisi, ili kulinda maslahi ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Mawakili mbalimbali na pia Halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wanasheria wao, ili pindi wanapokwenda kulinda maslahi ya Serikali, basi wafanye kazi hiyo katika weledi na ufanisi mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la kesi ngapi tumeshinda za usuluhishi; Mheshimiwa Mbunge aniruhusu tu nikachukue takwimu na nikishazipata nitampatia ili na yeye aone ni kwa kiwango gani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanya kazi hii ya kulinda maslahi ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Sera ya Afya inazungumzia zahanati kwa kila kijiji, vituo vya afya kwa kila kata na hospitali za wilaya katika wilaya, jambo ambalo sera hii haijakamilika hasa katika Mkoa wetu wa Rukwa ambao hauna Hospitali ya Wilaya hata moja, ni lini sera hii itakamilika kikamilifu hasa katika Mkoa wetu wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetoka kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mary Chatanda na Mheshimiwa Khenani ni shuhuda kwamba miongoni mwa Wilaya 67 ambazo zinaenda kujengewa Hospitali za Wilaya, ni pamoja na Wilaya ya Kalambo, Sumbawanga Vijijini pamoja na Wilaya ya Nkasi. Sasa siyo rahisi kusema lini exactly kwa sababu na ujenzi nao ni process, lakini na yeye mwenyewe ni shuhuda jinsi ambavyo Serikali imeazimia na inatekeleza.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa pamoja na mafunzo ambayo wanapata Watendaji wa Vijiji katika utekelezaji wanakwenda kushirikiana na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji ambao wamekuwa wakilalamikia sana kuhusu maslahi yao. Napenda kujua, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha maslahi ya Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Vitongoji pamoja na kupewa mafunzo kama watakayopewa Watendaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba tunafanya mafunzo mengi kwa ajili ya Watendaji, lakini napenda nimhakikishie kwamba mafunzo ya aina nyingi vilevile, hasa ya uongozi yamekuwa yakitolea kwa Wenyeviti wa Serikali za Vitongoji, Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Madiwani na viongozi wengine wa kuchaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maslahi, suala hilo kwa sababu liko katika maelekezo ya Serikali kwamba walipwe kupitia 20% zile za mapato ya ndani ya halmashauri, napenda kumuahidi kwamba mimi mwenyewe nitaanza ufuatiliaji wa karibu sana kuanzia mwaka ujao wa fedha ili kuhakikisha kwamba Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji wanalipwa.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Lengo la kutenga pesa hii lilikuwa ni kuwainua vijana na wanawake jambo ambalo limekuwa ni kinyume na lengo ambalo lilikusudiwa hasa pale zinapotolewa kipindi cha Mwenge. Serikali haioni kuna umuhimu wa kupeleka pesa hizi kulingana na mahitaji hasa kwa wale ambao wanajishughulisha na kilimo ikatolewa kipindi cha msimu wa kilimo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana kwa maswali yale ya awali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Aida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tumetoa maelekezo maalum kwa fedha hizi na niwasihi Waheshimiwa Wabunge, siku zote tunasema kwamba fedha hizi zinaishia katika halmashauri hata kule Hazina hazifiki. Ni jukumu la Kamati ya Fedha kila mwezi wanapofanya collection wahakikishe kama wamepata shilingi milioni 100, asilimia kumi ya shilingi milioni 100 maana yake ni shilingi milioni kumi zitolewe kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Kamati za Fedha zote, dada yangu Mheshimiwa Aida nimepata concern yako, zihakikishe wanatenga fedha hizi. Ndiyo maana katika Finance Bill ya sasa hivi tunafanya mabadiliko ya sheria katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290 ili kuhakikisha kwamba Waziri mwenye dhamana anasimamia vizuri eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie wazi kwamba mtu yeyote atakaye-temper na fedha hizi ambapo kwa mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 61, kwa kweli hatutakuwa na ajizi ya aina yoyote. Hata hivyo, niwasihi Wabunge tunapokaa katika Kamati ya Fedha tuweze kuzisimamia vizuri fedha hizi kwa sababu ni jukumu letu wananchi wetu hasa vijana na akina mama waweze kupata mikopo hii.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, kulingana na majibu ya Waziri nafikiri anajua kwamba kabla ya mchakato wa kuondoa watu waliokuwa wanajulikana kama wenye vyeti feki au vya kugushi, kulikuwa na upungufu mkubwa wa watumishi kwenye sekta mbalimbali zikiwemo sekta za elimu, kilimo na afya. Sasa kwa kuwa amejibu kwa data nina imani anajua upungufu mkubwa, tungependa alieleze Bunge lako; kwa kuwa kulikuwa na upungufu na wakaongoza tena upungufu ukawa mkubwa zaidi na mmeajiri kiasi hiki alichokisema, tunaomba kujua, mpaka sasa kuna upungufu wa watumishi kiasi gani?
Swali la pili, Rais wa kwanza wa Zanzibar aliwahi kusema tumesoma hatukujua, tumejifunza tumetambua. Serikali ya Tanzania inathamini zaidi vyeti kuliko kuangalia taaluma na kazi ambazo watu wamefanya. Baada ya kutumbua kuna watu walikuwa wamebakiza mwaka mmoja kustaafu. Ninapenda kujua Serikali imejipangaje kwa kuangalia mchango ambao waliutoa, kwa sababu wamefundisha watu wengine ni Wabunge, wengine ni Mawaziri… (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kujua kwamba mna utaratibu gani wa kuweza kuwalipa watumishi wale ambao walitumikia Taifa hili kwa uaminifu mkubwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunapowauliza maswali Mawaziri hatutakiwi kuwataka takwimu maana hatutembei na takwimu kichwani.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, nadhani hili swali humu ndani limeulizwa tena na tena na wanasheria wakafafanua. Maelezo yako hivi, mwajiri alikuajiri wewe akiamini kwamba vyeti ulivyompa ni vyeti sahihi ndiyo maana ukaingia naye mkataba. Kile kitendo tu cha mwajiri kubaini kwamba ulimdanganya umepeleka cheti feki, Waingereza wanasema ina-nullify mkataba wako, mkataba wako unakuwa null and void, unakuwa umejifuta kwa sababu upande mmoja umewasilisha taarifa ambazo sizo.
Kwa hiyo hapa ndani hatujajipanga kumlipa mtu ambaye mkataba wake ni fake.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuzungukwa na Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa lakini bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya maji. Njia zote ambazo Serikali wamekuwa wanatumia wameshindwa kabisa kumaliza changamoto za wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Je, Serikali haioni kwamba ni muda muafaka sasa kutumia Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kuweza kumaliza tatizo hilo la maji kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye mwenyewe anakaa Mkoa wa Rukwa ni shahidi kwa macho sio kuambiwa kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekamilisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji pale mjini Sumbawanga na Mheshimiwa Rais anakwenda kuzindua mwezi huu, huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 100 katika Mji wa Sumbawanga. Pia tunaendelea kutekeleza miradi mingine katika Mkoa wa Rukwa na kwenye Awamu Pili ya Programu ya Sekta ya Maendeleo ya Maji tutahakikisha mkoa mzima unapata huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge, Ziwa Rukwa maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, ziwa linalofaa ni Ziwa Tanganyika na tayari tuna andiko la kuchukua maji kutoka Ziwa Tanganyika kupeleka Mkoa wa Rukwa.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Katika Mkoa wetu wa Rukwa tumejaaliwa kuwa na maporomoko ya Kalambo ambayo kama Mkoa sisi tumejipanga.
Sasa napenda kujua katika Wizara ya Maliasili na Utalii mmejipangaje katika kutengeneza mazingira rafiki ili kuweza kuwavutia watalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika Mkoa wa Rukwa tunalo eneo lile la maporomoko ya Kalambo ambayo ni maporomoko ya aina yake ambayo tena ni urithi wa dunia. Kwa kweli lile eneo ni zuri sana. Baada ya kuona hivyo, mimi mwenyewe nimefika pale kuangalia mazingira yalivyo, tumechukua hatua ya kuanza kujenga ngazi kubwa ambayo inatoka kule juu kushuka kule chini ambayo ni mita karibu 230. Tunatarajia lile daraja litasaidia sana katika kuboresha na kuvutia watalii kuweza kutembelea yale maporomoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili, tumewaagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha kwamba wanawekeza katika lile eneo; wanaweka hoteli ambayo itakuwa ndiyo kivutio kizuri cha kuwavutia watalii katika lile eneo kusudi waweze kutumia muda mrefu wa kukaa katika lile eneo. Ni tofauti na sasa hivi ambapo unakuta kwamba wenzetu wa Zambia wameweka hoteli upande wao, lakini upande wetu huduma hizi zimekuwa hazipo. Hivyo tumekuwa tukikosa watalii. Nina imani baada ya kuchukua hizi hatua, sasa watalii wataongezeka sana kwa upande wa Tanzania kwa sababu ndiyo sehemu pakee unayoweza ukaiona Kalambo vizuri kuliko maeneo mengine.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa tunaamini kwamba wazee ni hazina ya Taifa letu, kama ilivyotengwa kitengo kwa ajili ya vijana, asilimia tano ya vijana na wanawake, Wizara haioni sasa ni busara kutenga pesa kwa ajili ya kuwalipa wazee wetu iwe kama…

Mheshimiwa Spika, nakushuru. Tunaamini kwamba wazee ni busara ya Taifa na ni hazina ya Taifa letu. Kwa kuwa asilimia tano imetengwa kwa ajili ya vijana na wanawake, Wizara sasa haioni ni busara kutenga fedha kwa ajili ya kuwalipa wazee wetu kama baraka katika Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa kuhusu masuala ya wazee. Kama Serikali na kama ilivyosema katika Ilani ya Uchaguzi miundombinu yote ya kuwezesha wazee hawa kuweza kulipwa imekwishaandaliwa. Kama Naibu Waziri alivyosema ni taratibu za ndani zinaendelea na pindi taratibu hizi zikikamilika, basi Serikali itatekeleza azma yake ya kuweza kuwalipa wazee pensheni kama ilivyosema katika Ilani ya Uchaguzi. Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kulikuwa na kiwanda kinachozalisha zana za kilimo kwenye Mkoa wa Mbeya mpaka sasa hatujui nini kinaendelea. Tunaomba kujua kwenye Wizara ya Kilimo nini mkakati wa Wizara kuweza kufufua kiwanda hicho ili kuendeleza zana za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho nilitembelea Kiwanda hiki cha Zana za Kilimo pale Mbeya, ni kweli bado kinaendelea kutengeneza zana za kilimo, lakini pia kimejikita kuanza kutengeneza nguzo za cement za umeme. Kwa hiyo, kimsingi mwekezaji bado anaendelea na kazi na tunazidi kumshauri aendelee kuongeza jitihada.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri umekiri kwamba katika Mkoa wa Rukwa hakuna Hospitali ya Wilaya hata moja na nia ya sisi wawakilishi na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha sio kuepusha au kupunguza vifo vya wanawake na watoto ila ni kuhakikisha suala hilo linapotea kabisa linakwisha kwa ya kuwasaidia wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la kuepusha vifo hivyo sio kuandaa tu vitanda ila ni kuhakikisha tunatengeneza mazingira rafiki ya mama anayejifungua pamoja na mkunga. Kwa maana hiyo kunahitajika vitanda ambavyo vitakuwa na instrument kwa ajili ya kuepusha masuala hayo. Ni lini sasa Serikali itapeleka vitanda ambavyo vitakuwa rafiki kwa wauguzi pamoja na wanawake wanaweza kujifungua?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri wa Afya alipokuja Sumbawanga Mjini katika maadhimisho ya siku ya wanawake aliahidi kuleta magari mawili ambayo yataendana na mazingira yaliyopo katika Mkoa wa Rukwa ambayo yataweza kuwasaidia wanawake kutoka kwenye mazingira walionayo kuna umbali mrefu kufika kwenye Hospitali ya Rufaa. Ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kuhusiana na suala la vitanda, Serikali hii ya Awamu ya Tano katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 269 na bajeti hii imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hatuna uhaba wa fedha, tatizo lililopo ni kwamba Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa, Vituo vyetu vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya hazijaagiza vitanda hivyo. Kwa hiyo, niendelee kumwomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na hospitali yake ambapo ina upungufu wa viwanda ili hospitali hiyo husika kwa kutumia fedha ambazo Serikali inazitoa waweze kuagiza vitanda hivyo. Vitanda vipo katika Bohari yetu ya Madawa ya MSD.
Swali lake la pili, ameuliza ni lini magari ambayo Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya kuweza kuyapata. Sasa hivi Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza magari na yatakapopatikana ahadi hiyo itatekelezwa.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa taarifa tu ni kwamba na mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa hiyo, hiki nilichokuwa nakiuliza nahitaji Wenyeviti wengine wapate ufafanuzi wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali inatenga fedha nyingi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Majibu ya Naibu Waziri amenukuu Katiba, Ibara ya 146, wanasema madhumuni ya kuanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kuharakisha maendeleo ambapo kuchaguliwa huku na sisi Wabunge, Madiwani pamoja na Rais tunachaguliwa hivyohivyo lakini sisi tunalipwa posho na mshahara. Kama Serikali inaweza kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi, kwa nini haitengi fedha kwa ajili ya kuwalipa Wenyeviti hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa na Vijiji kuna Watendaji wa Vijiji na wa Serikali za Mitaa ambao wanalipwa na Serikali, wanaofanya kazi saa tisa lakini Wenyeviti wanaochaguliwa na wananchi wanafanya kazi saa 24 hawalipwi. Serikali haioni sasa kwa kuwa mpaka sasa haijawalipa Wenyeviti wala hakuna sheria yoyote iliyoletwa kwa ajili ya kuwalipa, kwa nini isiufute Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wabaki hawa wanaolipwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimjibu Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, maswali yake ya nyongeza mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuhusu posho za Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Mimi pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kabla ya kuwa Mbunge tangu 2014 mpaka 2017. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba haya ni maswali ya uchonganishi na naomba niwaambie Wenyeviti wa Mitaa kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inawapenda sana na ndiyo maana inataka kuwaeleza ukweli na naomba wanisikilize.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kwenda kugombea kunakuwa na maelezo na kanuni zimetaja sifa za nani anapaswa kuwa Mwenyekiti wa Mtaa. Sifa mojawapo muhimu sana ni kuwa na kipato cha kumfanya aweze ku- sustain maisha yake binafsi. Kwa hiyo, mtu yeyote anapoenda kuchukua fomu na bahati nzuri mwaka huu mwezi Novemba tunafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kila anayetaka kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au Mjumbe wa Serikali ya Mtaa au Kijiji, Kitongoji, anapaswa asome sifa, ajiridhishe ndiyo achukue fomu, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Wenyeviti wa Mitaa kwa mujibu wa maelezo ya Serikali watalipwa kwa viwango mbalimbali kulingana na uwezo wa Halmshauri yao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anapouliza swali ningetaka aseme kwenye Halmashauri yao wamejipangaje kuwalipa posho Wenyeviti wa Halmashauri kwa sababu pesa ziko kule na miradi iko kule wanaisimamia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa uwezekano wa Serikali kulipa posho za Wenyeviti wa Mitaa kwa maelekezo tuliyotoa makusanyo yakipatikana kinachotakiwa kirudishwe kwenye Halmashauri asilimia 20 walipwe. Ni muhimu kuzingatia Mheshimiwa Diwani anapochukua fomu anafahamu mimi sina mshahara nitalipwa posho, anajiridhisha Sh.350,000 kwa mwezi inatosha.

Mheshimiwa Spika, tunaomba watenganishe kati ya kazi na posho. Wafanye kazi kwa weledi lakini wasiache kuwahudumia wananchi kwa sababu hawajalipwa posho, kwa sababu hayo ni makubaliano na wameridhika kabla ya kugombea. Serikali ikipata uwezo wa kutosha itapeleka posho kwa Wenyeviti wa Mitaa, kwa sasa uwezo haujapatikana, tunawaomba waendelee kufanya kazi kwa weledi, wanafanya kazi kubwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ipo pamoja na Wenyeviti wa Mitaa kinyume na hapo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba kwa sababu Wenyeviti wa Mitaa hawalipwi posho na Watendaji wa Mitaa na Vijiji wanalipwa kwa hiyo tufute wabakie wanaolipwa. Hawa Watendaji wa Mitaa, Kata na Vijiji ni watumishi wa Serikali, wanatajwa kwenye orodha ya watumishi wa umma.

Kwa hiyo, huyu ni mtumishi na ndiyo maana anapotaka kupata nafasi hii tunatangaza nafasi kwa uwezo wa Halmashauri na Serikali Kuu, analeta vyeti, anakuwa- vetted, anakaguliwa, anapewa mkataba wa kazi yake na huyu anapaswa kufanya kazi kwa niaba ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwenye ngazi ya Kijiji na Mtaa huyu Mtendaji ndiyo Mkurugenzi wa Halmashauri na kama kuna jambo lolote hawa wanawajibika. Kwa hiyo, naomba tutofautishe huyu ni mtumishi wa Serikali na huyu ni mtumishi wa wananchi kwa kazi ya kujitolea na wote ni watu muhimu sana katika eneo hili. Huyu Mtendaji na watu wengine watapata kile ambacho kinastahiki kwa kadiri ambavyo tumekubaliana. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watuhumiwa wanaoteswa wakiwa mikononi mwa Polisi kwa lengo la kulazimishwa kusema ukweli, hasa ule ambao Polisi wanautaka wakati mtuhumiwa ana haki ya kutoa hoja yake au kuzungumza ukweli akiwa na Wakili au Mahakamani.

Je, Serikali haioni ni muda muafaka wa kufuatilia mateso haya ambayo watuhumiwa wanapewa na Askari ili kuondoa malalamiko haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushahidi ya mwaka 1967, kifungu cha 31, inaeleza kuhusu namna ambavyo Polisi wanaweza kutumia nguvu kiasi katika kumhoji mtuhumiwa ili waweze kupata ushahidi. Pia sheria hiyohiyo inaeleza kwamba ushahidi ambao utapatikana si lazima Mahakama uuzingatie, Mahakama itazingatia ukweli wa jambo husika. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba inapelekea kuwa-discourage Polisi kutumia nguvu katika kupata ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza katika jibu la msingi la swali kwamba tunapogundua kwamba kuna raia ambaye amefanyiwa vitendo ambavyo si kwa kibinadamu na Polisi basi sisi huwa tunachukua hatua. Tunaomba tutoe wito na rai kwa wananchi wote pale itakapotokea wananchi kupata madhara kama hayo basi wachukue hatua stahiki za kutoa taarifa ili tuweze kuchukua hatua. Hatuwezi kuliruhusu au kukubali wananchi wetu wanyanyaswe na baadhi ya skari wetu ambao pengine hawafuati maadili ya kazi zao.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, anakiri kabisa kwamba madini haya ni muhimu katika kujenga uchumi wa taifa. Mheshimiwa Waziri, ningependa kukuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; tumeshuhudia bei ya tanzanite ikiendelea kushuka kila siku. Ningependa kujua mkakati wa Serikali; mna mkakati gani wa ziada wa kuendelea kulinda thamani ya tanzanite?

Swali la pili; katika aina ya tano ya madini umezungumzia madini ya nishati ambayo ni makaa ya mawe pamoja na gesi. Mkoa wetu wa Rukwa tuna aina ya madini ambayo ni helium, tangu imegundulika ni muda mrefu sasa. Kama ulivyosema dhana ni kujenga uchumi, ningependa kujua na Wanarukwa wafahamu; ni lini madini haya yataanza kuchimbwa ili yawasaidia Wanarukwa na uchumi wa taifa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni lile analoulizia madini ya gesi ya helium yataanza kuchimbwa lini. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tulishatoa leseni ya kuchimba madini ya helium katika Ziwa Rukwa. Tatizo tulilonalo pale ni kwamba katika eneo hilo ambalo tumetoa mashapo ya kuchimba helium ipo pia leseni ya kampuni nyingine ya Heritage ambayo inachimba madini ya gesi ambayo ipo inasimamiwa na Sheria ya Mafuta na Gesi.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali tunachofanya ni ku-harmonize hawa watu wa Heritage pamoja na helium ili waweze kukubaliana tuweze kuanza kuchimba. Hata hivyo, tumeshawapa maelekeo watu wa Helium One waanze kuchimba kwenye eneo ambalo halina mgogoro na watu wa Heritage na mashauriano yanaendelea ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, la pili ni hili alilozungumzia, kuhusu madini ya nishati. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tunaendelea kuwasimamia watu waweze kuchimba haya madini ili yaweze kuongeza uchumi wa nchi yetu.
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na kuwa na vyuo vitatu Nyanda za Juu Kusini, lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha kwenye chuo cha utafiti. Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za kutosha ili kuleta tija kwa ajili ya uzalishaji unaoendelea Nyanda za Juu Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kujua mkakati wa Serikali kupeleka fedha; kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga na tunapeleka fedha zaidi ya bilioni 10 kwenye vyuo vyetu vya utafiti na kilimo kwa ajili ya kwenda kuimarisha utafiti katika vyuo hivyo, ili viweze kuwahudumia wakulima.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Serikali imekuwa ikitenga fedha kupeleka katika miradi mbalimbali ya maji. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Mfili ambao uko Wilaya ya Nkasi lakini mradi huo umeshindwa kabisa kumaliza changamoto ya maji. Napenda kujua, Serikali ina mkakati gani wa ziada wa kuweza kumaliza changamoto hizo ili kuendena na kauli ya kumtua mama ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji vijijini, Bunge lako Tukufu limetenga zaidi ya shilingi bilioni 301. Pia, tumepata zaidi ya dola milioni 500 kwa ajili ya kutatua tatizo la maji zaidi ya miji 28. Vilevile tumepata fedha zaidi ya shilingi bilioni 25.9 kwa ajili ya kukarabati vituo (Payment by Result- PbR) katika kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo tutahakikisha tunafuatilia miradi yetu na mingine tutaifanya kwa kutumia wataalam wetu wa ndani ili kukamilisha kwa wakati na wananchi wapate huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. AIDA J.KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na majibu ya Serikali, Serikali yenyewe inakiri kwamba kuna changamoto mbalimbali zinazopelekea mtoto wa kike kupata ujauzito. Lakini inasema ina mpango wa mtoto huyu wa kike aliyepata ujauzito kusoma elimu ya watu wazima ambayo ni nje ya mfumo rasmi. Kuna wanawake ambao wana familia zao wanasoma degree, wanapata Master’s na Ph.d ambao ni mfumo rasmi. Serikali haioni kwa kufanya hivyo ambao tunawaita ni watoto wakasome elimu ya watu wazima ni kuwaongezea adhabu nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali pia imekiri kwamba umbali mrefu nao unachangia watoto wa kike kupata ujauzito. Kwa kuwa Mkoa wa Rukwa nao umekuwa kinara kwa watoto wa kike kupata ujauzito, Mkuu wetu wa Mkoa amekuja na oparesheni ambayo ina kauli mbiu ambayo inasema, Niacha Nisome. Je, Serikali iko tayari kumsaidia fedha kwa ajili ya kujenga hosteli?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na hilo la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali inasaidiana na wananchi kwenye halmashauri zao kujenga hosteli na mabweni kwa ajili ya kuondoa changamoto ya watoto wa kike ambao wanatembea umbali kwenda shuleni. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tuko pamoja na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba azma yake hiyo inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na lile swali lake la kwanza, kwamba kwa maoni yake siyo haki kuwanyima watoto ambao wamepata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za kawaida. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni zuri kwa sababu tunajaribu kumlinda hata mtoto yule anayezaliwa kwa sababu watoto wale ambao wanapata mimba wanakuwa baadaye wanawabeba wenzao. Ukiwapeleka katika shule za kawaida hawatapa mazingira mazuri ya kuweza kuwalea. Kwa hiyo, tunamjali mtoto yule aliyezaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumeweza kujifunza vilevile kwamba hata watoto hao ambao wamepata ujauzito, mara nyingi wakienda kwenye shule za kawaida zile ambazo wametoka wanakuwa wananyanyapaliwa, kwa hiyo tunawawekea mazingira mazuri ambayo yatawasaidia kusoma kwa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, wanapoenda kusoma kwenye Vituo vya Elimu ya Watu Wazima, inawasaidia kusoma katika utaratibu ambao…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri kwa kifupi sana.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie kwamba tutaendelea kuwasaidia na kwa kweli vituo hivyo ambavyo viko 500 nchi nzima vya watu wazima vimewasaidia watoto wengi wa kike kuendelea na masomo katika ngazi zinazofuata.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa Wilaya ambazo ziko Mkoa wa Rukwa na mpakani, zinapakana na nchi ya Kongo na Burundi na kumekuwa na mlipuko wa magonjwa ikiwepo ugonjwa wa Ebola. Nataka kujua mkakati wa Serikali, haioni ni muhimu sasa kuipa Wilaya ya Nkasi kipaumbele cha kujenga Hospitali ya Wilaya ili kuepukana na matatizo ambayo yanaendelea kujitokeza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi ni kwamba kwenye orodha ya Hospitali za Wilaya zinazojengwa ndani ya Mkoa wa Rukwa na Nkasi nimeitaja. Inawezekana Mheshimiwa Mbunge alikuwa haijaingia lakini kama hiyo haitoshi hivi karibuni katika mgao wa gari kwa ajili ya chanjo na ameongelea suala la Ebola na Nkasi nayo ipo katika mgao. Kwa hiyo, ni namna ambavyo Serikali imekuwa ikitilia maanani mahitaji na imekuwa ikitekeleza.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, swali langu la msingi nilisema wahitimu wa vyuo vikuu waliokidhi Vigezo, sikusema waliohitimu tu ndiyo wote wanastahili kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, kila mwaka takribani Wahitimu laki nane, kwa mwaka, na wanaoajiriwa ni elfu arobaini peke yake, kwa hiyo laki saba na sitini wanabaki mtaani. Ningependa kujua Serikali ina Mkakati gani wa ziada, kwa sababu Mkakati uliopo umeshindwa kukidhi vigezo vya kuweza kuwaajiri vijana wengi ambao wamehitimu? Ni Mkakati gani wa ziada ambao Serikali inao kwa ajili ya kuwasaidia Vijana hawa ambao wengi wako mtaani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kumekuwa na vikwazo mbalimbali kwa hawa wahitimu wanapokuwa wanaomba kazi, na kikwazo namba moja, ni kikwazo ambacho wanawaambia kwamba wawe na uzoefu, na wakiamini wametoka chuoni. Ningependa kujua, Serikali haioni ni kuna Mkakati ambao unahitajika wa ziada sana, kuwa na programu maalum ya kuwa andaa Vijana hawa kabla ya hawajakwenda kazini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niseme kabisa kwamba kila Mtanzania ana haki ya kuomba ajira kwenye Utumishi wa Umma. Lakini vilevile, tuangalie kwamba ajira za Serikalini huzingatia sana scheme of service, huzingatia sana ikama, na bajeti iliyopangwa kwa wakati huo, na vilevile kutegemea na vipaumbele vya Taifa wakati huo. Niwahase wahitimu wote nchini waendelee kuomba ajira kupitia sekretarieti yetu ya ajira ambayo tumeboresha sasa hivi inapitia ajira portal kupitia njia ya mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niliambie Bunge lako Tukufu pia kwamba mwaka ule wa fedha 2018/ 2019 Serikali iliweza kuajiri ajira mbadala na ajira mpya zaidi ya elfu arobaini na moja na laki na sita na Kada ya Walimu ilikuwa elfu nne na mia tano. Lakini kwa mwaka huu wa fedha naomba niliambie Bunge lako Tukufu kabisa kwamba Serikali inatarajia kuajiri zaidi ya ajira elfu arobaini na nne na laki na nane, lakini kana kwamba hiyo haitoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano pia imejipanga tumeanzisha Sera ya local content ili private sector zote nchini ziweze kuajiri Watanzania na nichukue fursa hii kuwapongeza sana Mkoa wa Pwani kwa sababu wao wamezingatia sana Sera ya Viwanda na Uchumi na wameweza kuajiri zaidi ya Watanzania elfu hamsini, iwe ni in direct iwe ni direct na naomba nitoe Rai, Mikoa mingine pia iweze kuiga mfano wa Mkoa wa Pwani ambao wanaufanya mpaka sasa hivi, ili Watanzania wengi pia waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, la Mheshimiwa Mbunge Khenani anazungumzia Mikakati ya Serikali ambayo mingine nimeitaja, amezungumzia kuhusu uzoefu na naomba niseme katika Sera yetu mpya ya Utumishi 2004 Serikali imesema kabisa kwamba ajira mpya hazitazingatia uzoefu, uzoefu unakuja kwa wale ambao tayari wako kazini. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nirudi kwenye swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Aida Khenani na hasa eneo lile ambalo vijana wengi wa Kitanzania wamekuwa wakipata shida sana ya kigezo cha uzoefu, katika kutafuta ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na vijana, kweli limekuwa ni tatizo, Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia masuala ya Ustawi wa Vijana, na baada ya kugundua kwamba vijana wengi wamekosa sifa za kuajiriwa kwa sababu ya kigezo cha uzoefu, Ofisi ya Waziri ya Mkuu, iliamua kutengeneza mwongozo mpya, wa internship ili kuhakikisha vijana wanapomaliza masomo yao, waweze kupata maeneo ya kupata uzoefu kwenye private sector na maeneo mbalimbali, na zinapotoka nafasi za ajira kigezo cha uzoefu kiwe tena siyo kikwazo kwa ajili ya ajira zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa program hiyo sasa imekwisha kuanza, na Ofisi ya Waziri Mkuu imeshasimamia makundi ya kutosha ya vijana na kuwapeleka kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya internship programme tayari kwa kuwafanya wawe na uzoefu wa kuajiriwa. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Changamoto ya ununuzi wa tumbaku inafanana sana na changamoto wanayokabiliana nayo wakulima wa zao la mahindi. Hivi sasa ni msimu wa mavuno, ningependa kujua kwa Serikali imejipangaje kwa mwaka huu juu ya ununuzi wa zao hili la mahindi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika msimu uliopita tulikuwa na changamoto ya masoko ya zao la kilimo, lakini kama sote tunavyojua, Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba inatafuta masoko na muda huu tunapoongea tumepata masoko makubwa sana ya mahindi katika nchi za Kusini. Hivi sasa Rwanda wanahitaji zaidi ya tani 100,000; Burundi wanahitaji zaidi ya tani 100,000; lakini nchi ya Zimbabwe wanahitaji tani 800,000 za mahindi na nchi nyingine nyingi zinahitaji mahindi kwa wingi.

Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba sasa hivi soko la mahindi ni kubwa sana, wakulima wote wenye mahindi tunaomba wajitokeze watuambie wana kiasi gani, washirikiane na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuanzia wiki taasisi zetu ikiwemo NFRA pamoja na CPB wanaanza kununua mahindi na kukusanya mahindi kutoka kwa wakulima mbalimbali pamoja na wafanyabiashara, lakini pia taasisi nyingine ambayo tumeipa jukumu la kupeleka mahindi Zimbabwe nayo inaanza kununua mahindi wiki hii.

Kwa hiyo wakulima wakae mkao kila mahali wenye mahindi sasa hivi ni wakati wa kula mkate mzuri, nakushukuru. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunapozungumzia Hospitali ya Wilaya hatuzungumzii majengo bali tunazungumzia huduma inayotolewa kulingana na level ya Wilaya. Ninapenda kujua Serikali ni lini itatuletea watumishi wa kutosha pamoja na vifaatiba katika Hospitali ya Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uboreshaji wa miundombinu na watumishi katika vituo na hospitali zetu za Halmashauri ni kipaumbele cha Serikali na utekelezaji wake unafanyika kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na ndiyo maana katika mipango ya Serikali ya kila mwaka Serikali inatenga fedha, kwanza, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaajiri watumishi ili kuondoa changamoto ya watumishi katika hospitali na vituo vyetu. Lakini pili, tunatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaboresha upatikanaji wa huduma bora za afya katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua sana kwamba majengo ni kitu kingine na huduma bora ni kitu muhimu pia na ndiyo maana tumeendelea kuboresha miundombinu hiyo, lakini upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na watumishi na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunatekeleza suala hilo.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. changamoto za maji ambazo wanakumbana nazo wananchi wa Butiama zinafanana sana na changamoto zinazowakuta wananchi wa Wilaya ya Nkasi. Natambua kwamba, Serikali imekuwa inapeleka fedha katika miradi mbalimbali katika Wilaya ya Nkasi ambayo haijaweza kumaliza changamoto za maji. Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ambacho ni chanzo cha uhakika ili kuweza kumaliza changamoto za maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji tayari tuna mikakati kabambe ya kuweza kutumia mito, maziwa na vyanzo vyote vya maji pamoja na Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, kufikia mwaka ujao wa fedha Serikali tunaendelea kuona namna bora ya kuweza kutumia Ziwa Tanganyika kutatua tatizo la maji eneo la Nkasi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninashukuru majibu ya Naibu Waziri ambao ndiyo uhalisia wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali lilikuwa ni kuwakomboa au kuwasaidia wakulima, na kwenye majibu yako, majibu ya Wizara, unasema kwamba Sekta binafsi zipo ambazo zinatoza riba kubwa. Ningependa kufahamu Wizara imefanya utafiti kiasi gani kujua ni kwanini Sekta Binafsi zinatoa riba kubwa kwenye matrekta? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mfuko wa pembejeo uko ndani ya Serikali pamoja na Benki ya Kilimo ni kwanini sasa Serikali isiweke ruzuku kwenye hizo Sekta Binafsi kama ilivyofanya kwenye taulo za kike ili wananchi waendelee kupata neema kwenye hizo trekta? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kwanini Sekta Binafsi inatoa riba kubwa. Kkama Serikali na kwa muda mrefu tumekuwa na tatizo la model of financing kwenye Sekta ya Kilimo na ukiangalia financing model na mifumo mingi ya kutoa mikopo inakuwa ni mifumo inayofanana kuanzia grocery, kilimo na sekta zingine za uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Wizara hatua tuliyochukua, tumewasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tumewsiliana na Benki Kuu ili kutengeneza mfumo sahihi unaoendana na Sekta ya Kilimo; na sasa tumeanza majaribio katika Sekta ndogo ya pamba. Kwa mara ya kwanza Sekta Ndogo yap amba tumeipatia mkopo kwa riba ya asilimia mbili. Tumetengeza a vehicle kupitia ushirika, na mwaka huu tumegawa dawa na pembejeo na mbegu bure kwa wakulima kwa gharama ya asilimia mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mfumo huo huo tunaufanyia majaribio safari hii kwenye sekta ya korosho. Kwamba wakulima watapata pembejeo zote za kilimo bure na tutarudisha gharama katika mjengeko wa bei lakini gharama ya financing hii itakuwa asilimia mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ameunda timu ya wataalam ikiwahusisha wataalam kutoka Benki Binafsi na Benki Kuu ambayo tutapeleka ushauri Serikalini kupitia Benki Kuu ili tuwe na regulation za namna gani tutapata financing katika Sekta ya Kilimo ili itazamwe tofauti na sekta zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ruzuku kuwa Sekta Binafsi, hili bado tunaliangalia kwa sababu tunaangalia insurance model. Kwa suala la kutoa ruzuku historia inaonesha ruzuku imetumika vibaya hata huko nyuma kwenye pembejeo, kwa hiyo hatuwezi sasahivi kutoa commitment kwamba tutatoa ruzuku katika taasisi binafsi ambazo zinakopesha. Lakini tumeanza kutumia Benki yetu ya Kilimo kwa mara ya kwanza sasahivi imetoa mikopo kwa asilimia 10, na sasahivi tunajadiliana nayo angalau mikopo ya vitendea kazi iweze kwenda kati ya asilimia tano na isizidi asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Waheshimiwa Wabunge, la muhimu zaidi mkulima anahitaji shamba lake lilimwe na trekta, lipandwe na planter, lipate boom sprayer. Si lazima mkulima wah eka moja a-own trekta. Tunachokifanya kama Serikali ni kuhamasisha Sekta Binafsi, na sasa tumepeleka pendekezo kwenye technical team ya kodi ili VAT inayochajiwa kwenye huduma za kilimo iweze kuondoka kupunguza gharama za wakulima kwa ajili ya kuwalimia. Kwa hiyo ni mchakato tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtupe muda tunalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, natambua mchango wa Serikali kwa kupeleka fedha kwenye ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi lakini kilio cha Wanankasi ilikuwa ni kupata huduma kwa level ya Wilaya. Mpaka sasa jengo lipo lakini huduma inayotolewa hailingani na huduma inayotakiwa kutolewa katika Hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba pamoja na madaktari kulingana na level ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika eneo lake kuna jengo ambalo bado kutumika kwasababu ya vifaa tiba. Na hilo nimwambie tu kabisa kwamba mimi kabla sijafika hapa nilikuwa nazungumza na Waziri anayehusika na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na katika bajeti yake ambayo tutakwenda kuipitisha, kuna fungu ambalo tumetenga kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya hospitali zote ambazo majengo yake yako tayari lakini hayajakamilika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukishapitisha bajeti, ninaamini kabisa kwamba mara baada ya Bunge hili na mara baada ya bajeti kupita, basi hivyo vifaa na vifaa tiba vitatengwa na kupelekwa. Suala la watumishi basi tutaendelea kutenga kulingana na vibali vya ajira ambavyo tunapatiwa na Serikali. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Jitihada za kujitolea ambazo wananchi wa Jimbo la Segerea wamezionesha, zinafanana sana na jitihada ambazo wananchi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini wamezionesha katika kata 17 tunavituo vya afya viwili lakini kuna vituo ambavyo tayari vimeanzishwa kwa nguvu za wananchi. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye Kata ya Kabwe ili kuheshimu na kuendelea kuhamasisha wananchi kujitolea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini pamoja na wananchi wa Nkasi Kaskazini kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya kuhakikisha wanachangia nguvu zao katika ujenzi wa miradi ya maendeleo vikiwemo vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua na inathamini sana nguvu za wananchi na tutaendelea kuhakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ambayo wananchi wameanza kuyajenga kwa nguvu zao na mfano mzuri katika bajeti ya mwaka ujao maboma zaidi ya 108 kwa maana ya vituo vya afya vitakwenda kujengwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri na vituo vya afya 18 vitakwenda kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna vile zahanati maboma 578 yatakwenda kujengwa.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba katika mpango huu ujao pia katika Jimbo hili la Nkasi Kaskazini tutakwenda kulipa kipaumbele kuhakikisha kwamba wananchi wanaona matunda ya Serikali yao katika kujali nguvu ambazo wameziweka katika maboma yale.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru changamoto iliyopo Mtwara ya barabara inafanana sana na changamoto Nkasi. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alituahidi wana Nkasi kipande cha barabara kutoka Chala mpaka Mpalamawe, ningependa kupata commitment ya Serikali kwa kuwa ahadi zote zinakua recorded ni lini ahadi hiyo itatekelezwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ametaka kujua tu ni lini ahadi ya Mheshimiwa Hayati Rais ama niseme ahadi zote za viongozi ni kwamba sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ipo katika hatua ya mwisho tunakusanya na kuandaa mpango wa namna ya kutekeleza ahadi zote za viongozi na nikuhakikishie tu kwamba kuanzia mwaka wa fedha ujao tutaanza kutenga pole pole fedha kwa ajili ya kuhakikisha zile ahadi zote ambazo viongozi wakuu walikua wamezitoa zinaanza kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ni Serikali makini na imeshazungumza hadharani kwamba kazi inaendelea yale yote yaliyozungumzwa tutayaendeleza kuhakikisha kwamba tunawahudumia wananchi wetu vizuri. Kwa hiyo, waambie wananchi wa Nkasi Kaskazini kwamba zile ahadi zilizoaidiwa Serikali itazitekeleza kwa vitendo ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anasema wataendelea kujenga barabara kadri wanavyopata fedha, lakini kuna maeneo ambayo yana changamoto kubwa. Napenda kujua, kuna maeneo ambayo hayapitiki kabisa ikiwemo kule kwangu Nkasi, Barabara ya Kasu – Itindi ambayo mpaka sasa wanawake wanajifungulia njiani kutokana na uharibifu wa barabara :-

Je, ni lini Serikali itakuwa na kipaumbele kwa maeneo ambayo yana changamoto kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge amejaribu hapa kuainisha kwamba tutaendelea kujenga kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Katika yale maeneo ambayo kuna shida kubwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI (TARURA) tuna fungu la dharura kwa ajili ya kurekebisha maeneo korofi kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, endapo patakuwa na shida basi tumekuwa tukipeleka timu ya wataalam kufanya tathmini na baada ya hapo tumekuwa tukitoa fedha kama ambavyo tunaendelea katika maeneo mbalimbali nchini hivi sasa. Kwa hiyo, katika hilo eneo ambalo ameliainisha, naiagiza Ofisi ya Raisi, TAMISEMI (TARURA) kwamba waende wakafanye tathmini halafu baada ya tathmini wailete kwetu tuone namna gani tunaweza tukasaidia wananchi wa Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nimeyasikia majibu ya wizara. Kwa kuwa mpango wa Serikali ulijiwekea malengo kufikia mwaka 2025 upatikanaji wa maji vijijini itakuwa ni asilimia 85. Na leo ni mwaka 2021 na umekiri hapa kupitia majibu yako takwimu ambazo umezisoma kwamba upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Nkansi ni asilimia 48 tu. Kwanza takwimu hizi si halisia. Lakini napenda kuwaambia Serikali kwa kuwa mpaka sasa tuna asilimia 48 hamuoni sasa kuna jitihada za ziada za kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ili kuweza kufikia asilimia 85 kama malengo tuliyojiwekea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la Pili, huu mradi wa maji Namanyere wananchi wameanza kuangalia mabomba toka mwaka jana hawapati maji mpaka leo. Ningependa kujua kuna mkakati upi wa ziada wa Serikali wa kuweza kupelekea wananchi wa Namanyere na Kata zote za Jimbo la Nkasi Kaskazini maji ili waendane na kauli mbiu ya Mama Samia ya kumtua mama ndoo kichwani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mpango wa Serikali kufika mwaka 2025 kadri ya ilani ya Chama Tawala inavyotaka vijijini maji yatapatikana kwa asilimia 85 na zaidi ikiwezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nipende kukutoa hofu Mheshimiwa Mbunge na nikupongeze unafuatilia kwa makini sana masuala haya ya wananchi wako na wewe ni mwanamke ndio maana unaongea kwa uchungu kwasababu unafahamu fika kubeba maji kichwani kwa umbali mrefu namna ambavyo ilivyotabu.

Kwa hiyo tutahakikisha tunawatua kina mama ndoo kichwani. Wewe ni Mbunge mahiri mwanamke na mimi ni Naibu Waziri Mwanamke wote tunafahamu adha ya kubeba maji kichwani tutashughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tunafahamu fika RUWASA haikuwepo na kwa mwaka mmoja tu tumeona namna ambavyo RUWASA imefanya kazi kwa bidii. Na kufufua miradi ambayo ikisuasua na sasa hivi maji yanapatikana mabombani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia Ziwa Tanganyika Mheshimiwa Aida, kama ambavyo tumetoka kuongea kwa kirefu hapa majuzi wakati tunapitisha bajeti yetu. Huu ni mpango mkakati wa kutumia vyanzo hivi vya uhakika, kwa hiyo Ziwa Tanganyika nalo lipo kwenye mikakati ya wizara tutahakikisha tunalitumia ili kuona kwamba mabomba yapate kutoa maji na sio kushika kutu. Kwa hiyo, haya yote uliyoyaongea yapo kwenye utekelezaji wa wizara na ifikapo mwaka 2021/2022 mwaka mpya wa fedha Ziwa Tanganyika nalo tayari lipo kwene mpango mkakati wa utekelezaji. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nishukuru majibu ya Naibu Waziri. Waziri Mheshimiwa Mbarawa akiwa Waziri wa Maji alipofika kwenye mradi huu aligundua shida ni mfumo ambao ni umeme wa kutumia jua na kwa sababu huo mradi wa REA bado haujaanza kufanya kazi Kata ya Kabwe, ni lini watashirikiana na Wizara ya Nishati ili wananchi wa Kijiji cha Odachi, Kabwe Camp pamoja na Kabwe Asilia waweze kupata maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kwa namna nzuri anavyojibu maswali. Sisi Mawaziri viongozi wetu wametuelekeza kufanya kazi kwa pamoja na tumeshafanya mawasiliano na Mheshimiwa Waziri wa Nishati kuainisha maeneo yote yenye miradi yenye mfumo wa jua kuhakikisha kwamba tunafanya mageuzi kuweka mfumo wa REA kwa maana ya nishati ya umeme ili kuhakikisha kwamba tunapunguza gharama ya uendeshaji ili wananchi waweze kupata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Aida hili jambo tumeshakaa na tumeshaainisha kwa hiyo wenzetu wa nishati watatupa nguvu kuhakikisha maeneo yote yenye solar tunafanya mabadiliko kuhakikisha kwamba tunaweka nishati ya umeme. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na jitihada ambazo Serikali inafanya juu ya kuajiri walimu lakini kuna changamoto kubwa kwenye maeneo ya vijijini kukosa walimu wa kike.

Ningependa kujua mkakati wa ziada wa Serikali inafikiri nini juu kuondoa hizo changamoto ambazo watoto wa kike wanakutana nazo shuleni.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni swali zuri na mimi kama mama tunahitaji pia kuwa na walimu wanawake katika shule zetu za msingi na sekondari ni moja ya kigezo tutaki- take into consideration katika kutoa ajira mpya lakini pia kufanya reallocation ya walimu katika shule zetu za msingi na sekondari hususani za vijijini.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa mapokeo ya wananchi kupitia matamko mbalimbali ya Serikali na kwenye swali langu nimeuliza elimubure kama ilivyotamkwa mara ya kwanza tofauti na waraka. Mapokeo ya wananchi kulingana na kwamba ni elimubure wamekuwa na uitikio hafifu wa kuchangia michango wakiamini elimu ni bure kama ilivyotamkwa. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kulieleza Bunge lako na wananchi wakajua sasa kwamba kilichobadilika ni elimu bila ada na utaratibu wa michango umebadilishwa tu kwa kwenda kuomba kibali wanapaswa kuchangia maendeleo ya shule?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nia ya Serikali ilikuwa ni kuwapunguzia wazazi mizigo au changamoto ambazo wanazipata na shida ya huko sio ada peke yake, Serikali kwa nia hiyo hiyo njema hawaoni sasa ni muda muafaka wa kurudi kufanya tathmini kwa kuwashirikisha kikamilifu wadau wa elimu wakawaambia changamoto kubwa iliyopo badala ya ada peke yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka Serikali tueleze kwamba, hii sio elimubure ni elimu bila ada. Niseme tu kabisa kwamba Waraka wa Elimu Na.5 wa mwaka 2015 ulishazungumza, kwamba tulichokisema elimumsingi ni elimu bila ada wala sio bila kitu kingine chochote, elimu bila ada, lakini, Serikali ilitoa tena Waraka mwingine Na.3 wa mwaka 2016, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba, katika ule waraka tumeainisha wajibu; kuna wajibu wa Serikali na vilevile wa mwananchi. Wajibu wa mwananchi ni pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo ya Kiserikali ikiwemo kujenga miundombinu kama madarasa, vyoo na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeainisha pale, lakini sasa tuliweka option ya kwamba wale wananchi wasilazimishwe, wachangie kwa hiari yao kwa kushikirikishana na Bodi za Shule. Huo ndio msimamo wa Serikali mpaka sasa hivi kwamba, elimu bila ada bado inaendelea kwa sababu lengo letu ni kuwasaidia watoto wale wa chini ili watoto wote waweze kupata elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Serikali tufanye tathmini upya; tunaendelea kufanya tathmini kila wakati na tunaendelea kuangalia au kuboresha kadri muda unavyokwenda. Kwa hiyo, tumepokea kwa sababu ndio wajibu wa Serikali kuhakikisha kama kuna mahali kuna upungufu, basi tunarekebisha. Hili katika jibu la msingi ni kwamba, nchi nzima sasa hivi tuna watoto wa sekondari zaidi ya milioni 14. Kwa hiyo, ni lazima Serikali tufanye upya tathmini ili kuangalia namna gani tunasaidia Sera ya Elimu na elimu kwa ujumla nchini. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kama alivyoeleza Waraka Na.3 wa mwaka 2016, umeainisha bayana wajibu wa wazazi katika kushiriki kwenye kuchangia maendeleo ya shule. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wazazi kuendelea kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kwa sababu mazingira ya shule yanapokuwa mazuri na watoto wao wanakuwa na uhakika wa kupata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa tunasisitiza kwamba mwanafunzi asifukuzwe shule kwa sababu ya michango. Hilo ndio jambo ambalo lazima katika kutekeleza Waraka huo, wazingatie kwamba ni marufuku kumfukuza mwanafunzi yeyote shuleni kwa sababu ya michango. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuwa Mji Mdogo wa Namanyere tulishakidhi vigezo na taarifa ziko ofisini kwenu; ni lini sasa mtachukua hatua kwa mujibu wa sheria ili na sisi tuweze kupata Halmashauri ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kimsingi taratibu za kupandisha Mamlaka za Miji Midogo kwenda kuwa Halmashauri za Miji zina utaratibu wake, lakini zina sheria yake na hivyo Serikali siku zote inafanya tathimini kuona kama vigezo vimefikiwa na baada ya hapo hatua stahiki zinachukuliwa.

Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwa taarifa aliyoitoa Serikali pia tutakwenda kupitia vigezo vya Halmashauri kwa maana ya Mji Mdogo wa Namanyere na kama umekidhi vigezo Serikali itachukua hatua kwa mujibu wa taratibu. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuuliza maswali, naomba niishukuru Serikali kwa kunipatia injini siku ya leo Kata ya Kabwe, ninawashukuru sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: - (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amenukuu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 43(h), natambua kwamba Ilani hiyo haijasema tukawatie umasikini Watanzania/wavuvi, imeelekeza mkawapatie mitaji na mikopo. Watu wa Nkasi shida yetu sio Ilani ila Ilani isipotekelezwa hapo ndipo maswali yanakuja. Ni lini Ilani Ibara ya 43 itatekelezwa Wilaya ya Nkasi kwa kuwapatia mikopo wavuvi wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kupitia Ilani hiyohiyo, nimesoma mwanzo mpaka mwisho hakuna sehemu Ilani imesema tukawape umasikini Watanzania. Kwa kuwa baada ya operesheni ya uvuvi haramu, Watanzania hasa wavuvi wa Nkasi wamekuwa maskini. Ningependa kujua, nini mkakati wa Serikali kwa kuwapatia vifaa vya kisasa ili kuwaondoa wavuvi hawa katika umasikini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Khenani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza; ninapokea shukrani kwa niaba ya Serikali na Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi uliyoitoa Mheshimiwa Aida Khenani kwa kuwawezesha wavuvi wa Kikundi cha Ushirika cha Kabwe.

Mheshimiwa Spika, lini tutatoa mitaji? Naomba Mheshimiwa Mbunge yeye na wataalam wetu waliopo kule Halmshauri ya Nkasi kwa pamoja tushirikiane katika kuhakikisha kwamba tunaandaa sasa utaratibu wa vikundi hivi kuweza kupata fomu, kuzijaza, waainishe, wapewe elimu kwa kusudio la kuweza kuwaunganisha na Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Aida Khenani, nipo tayari kabisa kuhakikisha kwamba tunasimamia jambo hili katika kutekeleza Ilani makini kabisa ya Chama Cha Mapinduzi ili kusudi wananchi hawa waweze kupata mikopo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; ni kwa namna gani tutawasaidia mara baada ya kufanya operesheni ambayo yeye Mheshimiwa Mbunge anaitamka kwamba imewatia umasikini. Nataka nikuhakikishie kwamba kwanza operesheni ile ilikuwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi na matokeo ya operesheni ile wengi wameyavutika kwa sababu tulipata samaki wengi, wakubwa na wazuri.

Mheshimiwa Spika, na sasa namna ya mpango tulionao wa namna ya kuwasaidia, moja ni hili tulilolifanya leo kwa kukukabidhi mashine itakayokwenda kuwasaidia watu wa kule Kabwe. Na ninakupa hamasa wewe na Wabunge wengine wanaotoka katika kanda ya uvuvi watuletee maombi zaidi ili kusudi Serikali tuweze kusaidiana nao. Na dirisha la Benki ya Kilimo liko wazi, sisi tunacho kitengo maalum cha kuweza kusaidiana na wavuvi kuandika programu zile na kwenda kuomba zile pesa ili waweze kununua zana bora na waweze kufika mahala mbali kunapoweza kuwasaidia kupata mavuno toshelevu na biashara nzuri, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi, nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza, tunafungwa sana na Sheria ya Takwimu, lakini naomba Bunge lako Tukufu, sheria hii isiwe ni kichaka cha kutoa takwimu za uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri anasema upatikanaji wa maji ni asilimia 52, wakati nafika hapa Meneja ananijibu ni asilimia 27. Sijui nani mkweli kati ya hizo taarifa? Nakosa maneno ya kusema kwa sababu ya Sheria ya Takwimu kwa sababu mtaniambia nimefanya research kupitia nini?

Mheshimiwa Spika, na mimi naomba kusema kwa sababu kwa miradi hiyo…

SPIKA: Hapa Bungeni unaruhusiwa, wewe sema tu, mradi usidanganye tu.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Wana- Nkasi wanasikia, akisema asilimia 52, wakati Kata zenye uhakika wa kupata maji hazizidi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kuna miradi miwili ambayo ni miradi kichefukichefu; Mradi wa Isale na Mradi wa Namanyere ambao una zaidi wa miaka mitatu; na miradi hiyo hata ikikamilika haiwezi kabisa kutatua changamoto ya maji Jimbo la Nkasi Kaskazini: Serikali haioni sasa kuna haja ya kuchukua Maji Ziwa Tanganyika ambayo ni kilometa 64 tu kuweza kumaliza changamoto ya maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa Serikali imepata huo mkopo ambao imegawa kwenye Wizara za Kisekta ikiwepo Wizara ya Maji, napenda kujua, Jimbo la Nkasi Kaskazini tunapata kiasi gani ili angalau ikapunguze makali ya changamoto za maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Dada yangu, Mheshimiwa Aida, kwa ufuatiliaji wa suala hili la miradi hii ya maji na nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Aida kwamba miradi hii ambayo umeiita kichefuchefu tayari Wizara tumeipa nguvu na tutaisimamia kwa karibu sana kuona kwamba inakamilika. Kwa sababu lengo la Mheshimiwa Rais ni kumtua ndoo Mama kichwani nasi kama Wizara ya Maji ni wanufaika wakubwa wa fedha kutoka Serikali Kuu, hivyo, nikutoe hofu, nikuhakikishie tutasimamia na miradi hii itakamilika kama ambavyo miradi mingine mingi zaidi ya 200 ilivyoweza kukamilika.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu kuhusu fedha za Covid. Katika Jimbo la Nkasi Kaskazini pia wamekuwa wanufaika wa hizi fedha ambazo Mheshimiwa Rais ameweza kuzipigania. Tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa sababu wananchi wa Nkasi Kaskazini na wao wametengewa milioni 500 kwa lengo la kufanya mradi wa Mpata.

Mheshimiwa Spika, lengo la hizi fedha ni kufanya mradi utakaokamilika ndani ya miezi sita, miezi tisa, uweze kutoa maji na wananchi wanufaike. Hivyo, tumeweza kuweka mradi mfupi ambao ndani ya shilingi milioni 500 utakamilika na wananchi watanufaika moja kwa moja. Kwa miradi hiyo ya Namanyere tayari ipo ina bajeti, kama Namanyere ina bilioni 1.5. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge nitaendelea kukupa ushirikiano kama ambavyo tumekuwa tukiwasiliana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Ziwa Tanganyika linatumika zaidi ya nchi moja kwa maana ya Tanzania kuna Congo, Burundi na nchi nyingine. Lakini dagaa wengi wanapatikana Ziwa Tanganyika upande wa Tanzania na sheria ambazo mlizitunga pamoja na Kanuni, zinawa-guide wavuvi wa Tanzania wavue usiku wakati dagaa wengi wanapatikana mchana. Kwa hiyo, ni muda muafaka sasa wa Wizara ya Uvuvi hawaoni kwamba, kuendelea kutumia hizo sheria ambazo zinawakandamiza wavuvi wa Tanzania na kuwapa faida nchi nyingine waachane nazo? (Makofi)

SPIKA: Kwa hiyo, kule Congo na wapi wanavua mchana?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ndio wanavua mchana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumepokea malalamiko na tumepokea mapendekezo ya wavuvi wote wa Ziwa Tanganyika na hivi sasa, Wizara inafanyia kazi mapendekezo haya yote yaliyotolewa na wavuvi. Lakini naomba kwa ruhusa yako kwa sekunde moja. Dagaa ni aina tofauti katika miongoni mwa aina za samaki tulizonazo, mle katika Ziwa Tanganyika tunao dagaa, tunao migebuka. Lakini Ziwa Tanganyika ni maarufu zaidi kwa samaki wa marembo wanaouzwa duniani kote na tunapata mapato makubwa sana kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa nini usiku? Tunaweka sayansi inayoelekeza tunapovua usiku dagaa tunaweka light attraction, ni dagaa pekeyake ndiye anayeweza kuvutwa na mwanga wa taa. Migebuka havutwi, samaki wa marembo havutwi, sangara havutwi anayevutwa ni dagaa peke yake.

Sasa, tunafanya vile kuwavuta dagaa ambao wanakuja katika mtindo wa makundi kwa maana sculling, ili kuwaepusha kuchukua samaki wa aina nyingine. Sasa hawa wanaovua mchana, nina hakika siwezi kuzungumzia nchi zingine, lakini hapo nimezungumza from scientific point of view.

Mheshimiwa Spika, ni kwa nini msingi wa kwa nini tunasema usiku na dagaa asivuliwe mchana, ukimvua mchana utavua na migebuka, utavua na samaki wengine wasiohitajika. Kwa sababu, kila leseni anayopewa mvuvi anapewa kwa kusudio maalum. Lakini hiyo tumeichukua hoja hii na sisi kama wataalam tupo katika harakati za kuangalia, ili tuweze kuendana na mahitaji ya wavuvi wetu waweze kunufaika na rasilimali hii. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Serikali imewekeza Bandari ya Kabo kwenye Wilaya ya Nkansi lakini changamoto kubwa ambayo inawafanya watu wasitumie bandari ile ni kwa sababu ya kukosa barabara ya kiwango cha lami cha kutoka Lyazumbi mpaka Kabwe na hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ningependa kujua ni lini mtajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imewekeza kujenga Bandari kubwa ya Kabwe ili tuweze kufungua Mkoa wa Rukwa na Tanzania kwa ujumla kufanya biashara na DRC Congo, na ndio maana tumejenga bandari mpya kabisa ya Kabwe. Lakini baada ya kujenga tunajua lazima kuwe na barabara, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ya kwanza barabara ilikuwa ni finyu.

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo kazi ya kwanza ni kuipanua ile barabara madaraja tunayabadilisha yote na barabara tunaipanua na magari yote yaweze kupitika. Na baada ya hapo sasa mpango unaofuata ni kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami lakini awamu ya kwanza ni kuipanua kubadilisha madaraja ili magari makubwa yaweze kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Barabara ya Aliyazumbi Kabwe kama alivyoahidiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu itajengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Changamoto ya skimu zilizopo Jimbo la Kwela kama ulivyomsikia Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya akiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa; Serikali iliwekeza fedha nyingi kwenye miradi miwili; skimu ya Lwafi pamoja na Katongoro lakini yote haifanyi kazi: -

Mheshimiwa Spika, napenda kupata kauli ya Serikali; Serikali iliwekeza zile fedha zipotee au iliwekeza ili ziwasaidie Watanzania wa Wilaya ya Nkasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Aida Khenani Mbunge, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali haijawekeza fedha zile ili zipotee na mapungufu yeye mwenyewe anafahamu, nilikuwa Jimboni kwake na tumeongea kwa kina kuhusu hizi scheme zilizoko katika Jimbo lake, sasa hivi kama Wizara tunafanya hatua za mwisho kupeleka fedha tuliyokuahidi ya Shilingi Milioni 100 ili fedha hizo ziweze kwenda.

Nataka tu nimuahidi kwamba mapungufu yaliyopo katika scheme zilizoko Mkoa wa Rukwa na sehemu nyingi ya nchi ni kwamba nyingi zimejengwa half way, kwa hiyo sasa hivi tunachokifanya ni kuzifanyia tathmini ili tuweze kuzirekebisha ziwe zinachanzo cha maji cha uhakika na mifereji, scheme nyingi zimejengwa mifereji badala ya kuwa na water reserve, kwa hiyo nataka nimuombe yeye pamoja na Waheshimiwa Wabunge, mtupe nafasi ili tuweze ku-rectify haya matatizo yaliyopo. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wizara tayari imeshaanza utaratibu wa kutoa elimu ya huo uvuvi unaoitwa haramu, miongoni mwa wilaya zilizoathirika ni pamoja na Wilaya ya Nkansi ambao walichomewa nyavu zao kwamba wanavua uvuvi haramu, lakini Serikali haijawahi kuwapatia mbadala wa nyavu zinazoitwa halali. Leo wamejikongoja wachache wameendelea na uvuvi, wanavamiwa na watu kutoka Kongo na Burundi. Wajibu wa Wizara ni kuwalinda wavuvi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, mna mkakati gani wa haraka wa kuwasaidia wavuvi hawa ambao wamevamiwa na vifaa vyao bado viko Kongo na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkansi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni jinai na kwa hiyo, litashughulikiwa katika utaratibu wa kijinai. Naomba kwa kuwa ni jambo mahususi, tuweze kushughulika nalo katika utaratibu wake. Hapa umetaja nchi ambazo ni majirani zetu. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba ni jambo mtambuka. Hapa umetaja jambo ambalo linaweza kushughulikiwa pia na Wizara, sisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya na kwa sababu linahusisha nchi nyingine na Wizara ya Mambo ya Nchi na Nje na wengine tunaohusika katika masuala ya ulinzi na usalama wa Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo Mchinga zinafanana sana na Changamoto za Wilaya ya Nkasi katika Kata ya Isunta na Kata ya Namanyele ambako kivuko hicho kimekuwa kikiathiri sana wanafunzi wanaokwenda Mkangale primary pamoja na sekondari ya Mkangale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itajenga kivuko hiki ili kuwasaidia watoto ambao wamekuwa wakipata shida sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, kama nilivyoeleza awali, madaraja yote yakiwemo yaliyo katika jimbo lake tumeshayafanyia tathmini, na mengi tunatarajia kuyaweka katika bajeti hii inayokuja ya mwaka 2022/2023. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatekeleza ahadi hii ambayo Serikali imeahidi. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto ambayo inawakumba watumiaji wa Bandari ya Kabwe ni barabara inayotoka Lyazumbi kwenda Kabwe na ni agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu. Napenda kujua, ni lini agizo hilo litatekelezeka kwa kuanza kujenga hiyo barabara ili tufikie malengo ya bandari yetu waliyowekeza fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara aliyoisema ya Lyazumbi hadi Kabwe inakwenda kwenye bandari ambayo Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa sana kwa ajili ya biashara kati ya Tanzania na DRC Congo. Naomba nimhakikishie Mbunge kwamba ziko jitihada zinafanyika za kuijenga kwa kiwango cha lami, lakini mpango uliopo sasa hivi ni kipanua ile barabara na kujenga madaraja makubwa na kuiweka kwa kiwango cha changarawe ili magari makubwa yaweze kupita wakati Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya mpango wa kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, nimesikiliza majibu ya Serikali.

Mheshimiwa mwenyekiti, swali langu la msingi lilijikita mpakani tukiamini kwamba Wilaya ya Nkasi inapakana na nchi ya Congo na nchi ya Burundi, Kituo cha Polisi ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu anazungumzia Daraja C, Daraja C hilo ambalo unalizungumza katika kata 10 za mwambao unazungumzia kata tano, na hao askari kila kituo ni askari watano, hakuna pikipiki, hakuna gari, hakuna usafiri wa majini wala wa nchi kavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maeneo hayo yamekuwa yanavamiwa mara kwa mara Serikali haioni haja kwa kuwa shida yetu sio majengo ya kituo cha polisi, tunataka vituo vya Polisi vyenye hadhi ya kupambana ikitokea uvamizi kwenye maeneo ya mpaka. Hamuoni haja sasa ya kujenga vituo hivyo kwenye maeneo ya mpakani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika kata 10 za mwambao ambazo ndio zimekuwa zinatumiwa na hao maadui. Kata tano zina vituo; kata tano hazina.

Je, tunaomba kujua Serikali ina mpango gani wa haraka kwa kuwasaidia ulinzi wa wale watu kwa sababu sio ulinzi wa Nkasi ni ulinzi wa nchi nzima, ni lini mtajenga vituo hivyo vya polisi kwenye kata ya Korongwe, Nkinga na kata ya Kala ambayo wanavamiwa kila wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa vituo vya Polisi hasa maeneo yaliyo katika mipaka, na sio uwepo tu wa Jeshi la Polisi lakini kupitia Wizara ya mambo ya ndani Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo hata vyombo vyengine, ili lengo na madhumuni mipaka yetu iendelee kubakia kuwepo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa nimwambie tu kwamba katika mipaka mingi ambayo nimeizunguka wakati ule hasa nilipokuwa nipo katika Wizara ya Mambo ya Nchi, ambao naamini na Waziri huyu ambae sasa hivi ndio Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwepo kule aliizunguka mipaka mingi. Maeneo mengi vituo vya Polisi vipo, lakini vituo hivi vipo distance kidogo na maeneo ya mipaka. baada ya kuona kwamba kwenye ile mipaka yenyewe Polisi na vyombo vyengine wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimawambi tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, Serikali itaendelea kujenga vituo vya Polisi, ili lengo na madhumuni wananchi waweze kuishi kwa amani na uatulivu ikiwa mipakani, ikiwa ndani ya miji, ikiwa pembezoni, ikiwa popote lengo na madhumuni watanzania waishi kwa amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inapeleka vitendea kazi ili lengo na madhumuni zile huduma za doria na mambo mengine yapatikane katika maeneo ya wananchi, ninakushukuru.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi, nami niulize swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkansi ni miongoni mwa wilaya ambazo zinapata umeme kwa muda mfupi sana. Wizara ya Nishati ilisema wanaweza kuondoa tatizo hilo kwa kutuunganisha kwenye gridi ya Taifa kwa hiyo, tunatumia umeme kutoka Zambia.

Nataka kujua kama Wizara bado inaamini mpaka leo kwamba, kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa ndio suluhisho, ni lini mtatuunganisha kwenye gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi miwili kwa pamoja ya kupeleka gridi ya Taifa katika Mkoa wa Katavi na Kigoma kwa pamoja. Na gridi hiyo ya Taifa inatarajiwa kufika maeneo hayo ifikapo Oktoba mwaka huu. Na itakapokuwa imefika Katavi ndio sasa tutakamilisha mpaka maeneo mengine ya Jirani ambayo hayana gridi ya Taifa.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu ya Serikali kwa hatua ya awali ya kutenga fedha, lakini sote tunajua; kutenga ni jambo moja na kutekeleza mpaka ujenzi ukamilike na meli ianze kutumika ni jambo lingine: Nataka kujua ni lini ujenzi wa meli hizo utakamilika na kuanza kutumika kwenye Ziwa Tanganyika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imewekeza fedha kujenga Bandari ya Kasanga, Bandari ya Kabwe, Bandari ya Kipili, Bandari ya Kigoma pamoja na Karema, lakini hatuna usafiri wa uhakika wa Ziwa Tanganyika wa kubeba mizigo pamoja na mazao ambayo yanazalishwa kwenye hii mikoa mitatu. Nataka kujua kwa sababu huu muda ni mrefu wa kutengeneza hizo meli: Mna mpango wowote wa dharura wa kutuletea usafiri ili kuepusha tatizo la kila siku kupoteza maisha ya Watanzania kwa sababu ya kutumia maboti?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala usafiri ndani ya Ziwa Tanganyika. Nami nimeshuhudia nilikwenda kule, kuna changamoto kubwa hiyo. Nataka nimhakikishie Mbunge na Wabunge wote wa mikoa yote mitatu; Mkoa wa Rukwa, Katavi pamoja na Kigoma, suala la kukamilika, kwanza kama ambavyo nimesema kwenye jibu langu la msingi, tumeshatangaza tenda tarehe 19 ya mwezi huu wa Tisa, tunategemea zitafunguliwa tarehe 2 Novemba na tayari Mheshimiwa Waziri wangu, Profesa Mbarawa alishakwenda kule kuonesha hata sehemu ya kujenga chelezo kwa kampuni ambazo zimeonesha kwamba zina nia ya kwenda kutengeneza ama kujenga hizi meli mpya mbili.

Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, kwamba ni namna gani tunaweza kama Serikali tukafanya jambo la dharura kwa ajili ya wananchi wa mikoa hii yote mitatu; kwanza, tumejipanga katika kukarabati meli zote mbili. Kuna meli ya Liemba pamoja na Mv Mwongozo. Tenda ya Mv Liemba, inatangazwa tarehe 26 ya mwezi huu na tunategemea kwamba itachukua muda wa mwaka mmoja. Kwa Mv Mwongozo ambayo inabeba abiria 500 na tani 150 yenyewe itachukua muda wa miezi sita. Kwa hiyo, ni mategemeo yetu kwamba ifikapo mwakani mwezi wa Kumi mwaka 2023 meli hizi za dharura zitakuwa zimeanza kufanya kazi ndani ya Ziwa Tanganyika. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni hizi ambazo zinaandaliwa, Ziwa Tanganyika tuna-share zaidi ya nchi moja, lakini nchi nyingine kwenye ziwa hilo hilo wanavua mchana. Hamuoni kama zuwio hilo linawapa umasikini wavuvi wa nchi yetu na mbadilishe ili waendelee kunufaika na Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Waheshimiwa Wabunge watambue kwamba rasilimali za uvuvi ni rasilimali za muhimu sana ambazo zinahitaji kuwa na uvuvi endelevu. Kwanza Serikali inafanya kuyalinda maeneo haya, kuyasimamia vizuri, lakini pia kuyahifadhi ili kuwepo na uvuvi endelevu. Hivyo tunavyoelekeza namna ya kutumia uvuvi wa kisasa na ni uvuvi endelevu kwa kuyafanya mazalia ya samaki yaendelee kuwa endelevu wananchi wanapaswa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii ina lengo la kuhakikisha kwamba, tunalinda maeneo haya ili tuwe na uvuvi endelevu, tunapoyamaliza haya mazalia ya samaki tutahakikisha uvuvi usiwepo kabisa hapa nchini. Kwa hiyo, tunaendelea kuwaomba wananchi waendelee kufuata sheria zilizopo ili kufanya uvuvi uwe uvuvi endelevu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, Kata ya Korongwe na Kata ya Mkwamba kuna umbali wa kutosha kufika katika hospitali ya wilaya, na hizo kata zote mbili hazina vituo vya afya: Nataka kujua mkakati wa Serikali ili kuwaokoa wanawake ambao wamekuwa wanajifungulia njiani na kupewa penalty, wanalipa Shilingi 50,000?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nkasi ni miongoni mwa Halmashauri ambazo bado zina kata ambazo hazina vituo vya afya, na tayari Mkurugenzi alishawasilisha kata za kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kata hizi mbili ni sehemu ya kata ambazo tutakwenda kutafuta fedha, kwa kushirikiana na Halmashauri, kwa maana ya mapato ya ndani na Serikali Kuu ili kuanza ujenzi wa vituo vya afya hivi kwa awamu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi, mkakati wa kutoa maji Ziwa Tanganyika ni mkakati wa muda mrefu. Nataka kujua mkakati wa muda mfupi wa kuwasaidia zile kata tano za Wilaya ya Nkasi, Kata ya Namanyele, Nkomoro, Majengo pamoja na Isunta kuepusha hiki kipindi ambacho wanakipitia kigumu?
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jumla ya fedha shilingi bilioni 657 zimetengwa na iko miradi 381 mipya. Ninayo imani kwamba katika hii miradi 381, miradi hii ya Nkasi ni miongoni mwao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Aida uendelee kufuatilia katika kuhakikisha kuwa wananchi wa Nkasi na wenyewe wanapata faida hii ya maji safi na salama.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri na Wizara yake kwa namna anavyopambana na changamoto inayoendelea Nkasi.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayotukumba kama Taifa ni kwa sababu ya miradi tunayoitumia ni mabwawa ambayo yanategemea kupata mvua. Inapotokea mabadiliko ya hali hewa, ndiyo changamoto inaonekana kama hivi sasa.

Je, Serikali ni lini mtaanza kutumia Maziwa makuu badala ya hivi ilivyo sasa inapotokea mabadiliko tunapata changamoto? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli sisi Wizara yetu ya Maji Mheshimiwa Rais alishatupatia maelekezo mahususi kwamba yeye ni mama, hataki kusikia wamama wa nchi hii wakiteseka juu ya adha ya maji. Wizara ya Maji itumie rasilimali toshelevu na yeye yupo tayari kutoa fedha kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, ndiyo uwelekeo wa Serikali hii ya Mheshimiwa Rais Samia Hassan kutumia rasilimali toshelevu hususan maziwa na mito mikubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi.

Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Rukwa, Ziwa Tanganyika ndiyo mkombozi kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Miradi ya Maji ya Wilaya ya Nkasi imekuwa ikusuasua sana pamoja na Mradi wa Namenyere ambao Waziri aliahidi ndani ya Bunge kwamba utakamilika mwezi Desemba mwaka jana, mpaka leo mwezi wa Nne mradi huo haujaweza kuwanufaisha watu wa Wilaya ya Nkasi. Je, ni lini Serikali itaondokana na fikra za kutumia mabwawa badala ya kutumia Ziwa Tanganyika ambapo ni kilomita 64 tu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kadiri tutakavyopata fedha tutakwenda kutumia Ziwa Tanganyika kukamilisha miradi ya maji.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri huu ni msimu wa kilimo kwa Mkoa wa Rukwa na Nyanda za Juu Kusini lakini mpaka sasa nazungumza, upatikanaji wa mbolea na mbegu bora Wilaya ya Nkasi na Mkoa mzima wa Rukwa una changamoto.

Ni nini mkakati wa Serikali ili msiwe kikwazo kwa wakulima hawa?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Aida, nadhani jana wakati tunafanya semina aidha hakuwepo tulitoa majibu yote ya kina kuhusu hili eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo lake, Wilaya yake, jana nimeongea na Mkuu wa Wilaya, tumeongea namna gani baadhi ya maeneo ambayo ni Tarafa zinazo wakulima wengi ziweze kufikiwa mbolea, tumeiomba Halmashauri yake iweze kutusaidia kupata usafiri ili sisi tuweze kuwasaidia mafuta waweze kusambaza mbolea maeneo ambayo mawakala hawafiki. Lakini wakala yupo Jimboni kwako na anauza mbolea. Tatizo lililopo ni mbolea kufika vijijini jambo ambalo tunashirikiana na ofisi ya Mkurugenzi na DC kwa ajili ya kufanya hivi baada ya wewe kuleta hili lalamiko kwetu. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa suluhisho pekee la kumaliza changamoto ya maji Wilaya na Nkasi, Mkoa wa Rukwa ni maji kutoka Ziwa Tanganyika. Ningependa kufahamu mchakato huo umefikia wapi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, matumizi ya Ziwa Tanganyika yapo kwenye mkakati wa Wizara na tayari baadhi ya maeneo tumeshaanza kuyatumia maji ya Ziwa Tanganyika. Hivyo kwa maeneo ya Nkasi na maeneo yote ambayo yapo karibu na Ziwa Tanganyika, tunaomba waendelee kuvuta subira tutakwenda na tutahakikisha chanzo hiki cha uhakika tunakitumia.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya kutoka Chala kwenda Mpalamao imekuwa ni ahadi ya viongozi wengi na iliwekwa kwenye ilani lakini mpaka sasa hatuoni kinachoondelea. Ni lini mtatekeleza ahadi hiyo ya barabara ya Chala - Mpalamao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kutoka Chala mpaka Mpalamao ni kweli tumekuwa tukiizungumza mara kwa mara, na nimemwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ipo katika vipaumbele ambavyo tumeviweka. Kwa hiyo, tunatafuta fedha ili ianze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Waziri pamoja na bei elekezi ambazo zimekuwa zinatangazwa kila wakati, lakini bado imekuwa haitekelezeki kutoka kwenye Mkoa mmoja kwenda Mkoa mwingine hasa Mikoa ile ambayo ni big five kwa uzalishaji wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto hiyo ya uzalishaji ambayo ilikumba na nchi nyingine zote lakini kuna nchi ambazo bado zilifanya vizuri. Je, upo tayari kwenda kujifunza kwenye nchi ambazo nazo zilipata hiyo changamoto ya COVID lakini bado bei ya mbolea iliendelea kuwa nzuri au yenye unafuu wa kwa wakulima ikiwemo Ethiopia, Zambia, Uganda na maeneo mengine. Mpo tayari kwenda kujifunza kwa kuwa ni jambo jema. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba wataalam wa Wizara ya Kilimo wamekwenda Rwanda kwenda kuangalia subsidy scheme ya Rwanda inafanya kazi namna gani, wengine wamekwenda Zambia kwenda kuangalia subsidy scheme ya Zambia inafanya namna gani, wengine wamekwenda Malawi wameenda kuangalia subsidy scheme ya nchi hizo inafanya namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge ni kwamba jambo la subsidy kwenye nchi linahitaji mambo mawili, moja political will na ninamshukuru Mheshimiwa Rais ameonesha utashi wa kisiasa kuwepo kwa subsidy lakini la pili ni management ya mfumo wa subsidy. Nchi yetu ilikuwa na mfumo wa subsidy ambayo ulikuwa abused lakini ukiutazama mfumo ule ya subsidy uliokuwepo ambao ulikuwa abused it was ni mfumo ambao abuse ilitokana na systematic system ambayo ilitengenezwa na kuanzia na aliyekuwa anausimamia mpaka aliyekwenda kuutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka niwahakikishie tu kwamba Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tutafanya mfumo wa utoaji wa ruzuku ambao hautoweza kuturudisha kule ambako tumetokea na utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais umeonekana hadharani na tarehe Nne mbele ya Watanzania aliahidi na alitoa agizo. Kwa hiyo, mtuachia tulifanyie kazi tuta- communicate na watanzania na kuwaambia namna gani tunalifanyia kazi hili jambo. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na changamoto ya upungufu wa watumishi nchi nzima, lakini maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Nkasi ina upungufu wa watumishi 1,939. Je, Serikali inampango gani wa haraka wa kusaidia maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha ajira hasa kule pembezoni ambako kuna upungufu wa watumishi, lakini kama unavyofahamu Serikali inaajiri kulingana na uwezo wa bajeti.

Kwa hiyo, kadri tutakavyozidi kukusanya na bajeti yetu kuruhusu ndiyo tutakapozidi vilevile kuajiri watumishi wa kuweza kwenda kuwahudumia Watanzania hasa wale waliokuwa maeneo ya pembezoni.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Nkasi hatuna shida na uwajibikaji wako Mheshimiwa Waziri, changamoto ni kwamba kwa kuwa umetambua kwamba tuna Ziwa Tanganyika lakini bado hatuna maji kwa hiyo hatuna shida na chanzo. Ni lini utaonyesha uthubutu kuepusha fedha ambazo zinatumika kwenye usanifu na bado miradi haijakamilika lini utakamilisha huo mradi wa maji ili na sisi watu wa Nkasi tuweze kupata maji ya uhakika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa Mheshimiwa Waziri mwenyewe alifika Nkasi mwaka jana na akatoa fedha, ukawaambia kwamba mwezi Desemba mradi huo utakamilika wa maji lakini mpaka leo nazungumza hizo Kata Tano za pale Mjini hazina maji. Ni lini sasa mtaachana na hizi fikra za kutumia visima badala ya kuelekeza nguvu zote ili kusaidia sasa Mkoa mzima badala ya Wilaya ya Nkasi peke yake? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Aida, kwa kweli nimefika Nkasi na unafanya kazi kubwa unafanya kazi nzuri. Kubwa Mwenyezi Mungu hawezi kukupa fursa ya Ziwa halafu akakupa fursa ya kuchimba visima. Maeneo mengi ambayo yamekuwa na Maziwa mengi ukichimba visima tunafeli. Kwa hiyo, namna pekee ya kuhakikisha tunatatua tatizo la maji eneo la Rukwa ni kuhakikisha tunatumia Ziwa Tanganyika na kazi hiyo imekwishaanza.

Mheshimiwa Spika, kubwa nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kutupa ushirikiano na Wizara ya Maji hatutomuacha katika Jimbo lake la Nkasi kuhakikisha wananchi wale wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili tulifika katika mradi ule wa Namanyele, Mkandarasi alikuwa anadai kiasi cha fedha na fedha tumeshampa sasa wananchi wanapata huduma ya maji. Kikubwa ni kuongeza sasa usambazaji ili wananchi wa eneo lile waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko tayari na tutashirikiana bega kwa bega katika kuhakikisha wananchi wake katika eneo la Namanyele wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya Namanyere – Kirando – Kipili ni barabara ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya kukuza uchumi wa Wilaya ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla. Ningependa kujua ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara iliyotajwa ya Namanyere – Kirando – Kipili ambayo inakwenda ziwani ni barabara muhimu sana. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulishafanya usanifu na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na hasa uchumi wa wana Rukwa na Jimbo hasa la Nkasi Kaskazini. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na idadi ya Vijiji ambavyo Mheshimiwa Waziri amevitaja, tunapozungumza Vijiji lakini Wakandarasi wamekuwa na tabia moja. Kwenye Kijiji anafika anaweka nyumba Tano au nyumba Nne na hapo anahesabu kwamba ni Kijiji.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuepusha hizi taarifa ambazo zinakuwa na mkanganyiko kwa Watanzania, unaposema Kijiji wakati ni wananchi wachache tu. Unapozungumza hili uwe umamaliza Kijiji chote?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; pamoja na changamoto ambazo Wakandarasi wamekuwa wanashindwa kumaliza miradi yao kwa wakati. Wamekuwa wana sababu ya kutoa kwamba changamoto ni nguzo. Mheshimiwa Waziri tueleze leo, ni kweli Taifa letu lina changamoto ya nguzo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimwia Aida Khenani, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika maeneo haya bahati nzuri Mheshimiwa Anthony Mwantona na Mheshimiwa Mwakibete suala hili katika masuala ya umeme katika Wilaya ya Busokelo na Rungwe wamekuwa wanakuja ofisini na kulizungumza na mimi na ni dhahiri kwamba katika mfumo wa awali ile scope ya kazi ilipelekwa karibu kilomita moja kwenye kila Kijiji.

Mheshimiwa Spika, taarifa njema ni kwamba Serikali imetafuta na kupata fedha karibu Dola Milioni 148 na tutaongeza na kupeleka kilomita mbili katika kila Kijiji. Kwa hiyo, maeneo yatakayopata umeme katika awamu inayokuja kwa kila Kijiji yatakuwa mengi zaidi na wanachi wengi zaidi watafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ni kweli kulikuwa na changamoto ya nguzo lakini imekwisha lakini changamoto kubwa zaidi ya kusuasua kwa miradi ni ile ambayo tumekuwa tunaizungumza ambayo ni kupanda kwa bei kwa gharama za vifaa vinginevyo ikiwemo waya za aluminum na copper bahati nzuri Serikali inalishughulikia jambo hilo kushirikiana na Wakandarasi lakini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Barabara kutoka Mji wa Namanyere – Bandari ya Kipili ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja amekuwa anaulizia mara kwa mara na mwaka huu tuliipangia fedha na tulishawaambia mameneja wa Mkoa watangaze kwa gharama ile ambayo imepangiwa ili ianze kujengwa hata kama itajengwa kilomita moja, mbili lakini wazitangaze. Kwa hiyo, nataka nichukue nafasi hii kumkumbusha meneja wa Mkoa wa Rukwa aweze kufanya kama alivyopokea maagizo ya kuzitangaza hizi barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Sote tunajua kwamba bado kuna changamoto kubwa sana ya madawati hapa nchini na wananchi wamekuwa ni wahifadhi namba moja wa misitu pamoja na miti mingine ambayo inapandwa na Watanzania wenyewe. Serikali ina mpango gani sasa wa kutumia miti mingine ambayo inataka kufanana na mininga ambayo iko maeneo mengi ili kuweza kuondoa changamoto hiyo ya madawati?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka, kwa niaba yake ameuliza Mheshimiwa Aida, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niweze kuifahamisha jamii na Watanzania wote kwamba, Serikali imefanya utafiti wa miti 19 na moja ya utafiti huu ni pamoja na mti wa mtiki. Tunaangalia namna iliyo bora ya kufanya mazungumzo na Wizara ya Fedha kupitia PPRA ili kuwe na mwongozo maalum wa kuhakikisha kwamba miti hii sasa inatumika kwenye furniture. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto ya madawati ambayo imekuwa ikijitokeza katika jamii inaenda kupungua kwa sababu aina ya miti 19 kama itaenda kutengeneza haya madawati, basi kutakuwa na aina mbalimbali ya miti ambayo ni mizuri na bora na imefanyiwa utafiti na wataalam kutoka Maliasili na Utalii. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Pamoja na utekelezaji wa REA III unaoendelea Wilaya ya Nkasi lakini umeme unakatika kupita kawaida: Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua changamoto hii ambayo wananchi wangu wanapata hasara kubwa hasa wanaosindika Samaki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Nkasi wanapata umeme kutoka nje ya nchi, lakini mradi wa Gridi Imara unapeleka Gridi ya Taifa katika Mkoa wa Katavi ambao utafika pia katika Mkoa wa Rukwa na maeneo hayo. Kwa hiyo, ndani ya miezi kama 18 tatizo hili litakwisha kwa sababu tutakuwa tumefikisha umeme wa gridi kwenye maeneo hayo ambao ni umeme wa uhakika na ambao tunaweza tukau- control sisi wenyewe katika maeneo hayo.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimesikia majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, lengo la kuwapelekea hizi fedha lilikuwa ni kuwasaidia tukiamini ni masikini, kwa hiyo hawana uwezo wa kununua simu. Kwenye simu kuna makato na benki kuna makato. Hatuoni kuweka hilo jambo ni kuondoa lile lengo la kuwasaidia hawa wanufaika ambao hawawezi hata kununua simu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mchakato wa kuwapata wanufaika uligubikwa na mambo mengi sana ikiwemo ubaguzi wa kivyama, kwa maana ya vyama vya siasa. Nini kauli ya Serikali kupitia upya tena mchakato huu ili tuwapate wenye sifa wanaostahili kuwa wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nataka nirejee tena maelezo ambayo nimeyatoa katika swali la msingi.

Mheshimiwa Spika, malipo ya pesa hizi yako katika njia kuu tatu, ni choice ya mhusika mwenyewe njia gani aitumie. Kama akiona kwamba njia ya simu ni ngumu kwake kwa sababu hana simu hiyo inayopokea, anaweza kwenda katika njia nyingine ya benki. Kama akiona njia nyingine ya benki ni ngumu kwa sababu benki iko mbali, upo utaratibu wa kulipa fedha taslimu kupitia madirisha yetu. Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge option hizi zote zinawezekana katika maisha ya kawaida ya ubinadamu wetu na Watanzania wetu na mimi na Serikali tunaamini hivyo.

Mheshimiwa Spika, juu ya swali la pili la upatikanaji wa wanufaika. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba baadhi ya maeneo kumetokea changamoto juu ya utambuzi wa wanufaika katika miradi hii ya TASAF, Serikali imekwishayafanyia kazi katika baadhi ya maeneo na tunaendelea kutambua katika yale maeneo yenye changamoto, nataka nikuhakikishie katika Jimbo lako la Nkasi Kaskazini nako pia timu ya TASAF itafanya kazi, nasi tunategemea zaidi ushirikiano kutoka kwako Mheshimiwa Mbunge ili kuweka mambo ya wanufaika vizuri kwa sababu nia ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote au walengwa wote wa TASAF wanafikiwa na kufikia malengo yao. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na fedha ya dharura iliyotoka Wizarani kwako Mheshimiwa Waziri, bado haijamaliza changamoto ya maji Jimbo la Nkasi Kaskazini. Tunapenda kufahamu mchakato wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kusambaza kwenye Mkoa wa Rukwa umefikia wapi?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu Mwenyezi Mungu ameijalia tuna rasilimali za maji juu ya ardhi na chini ya ardhi mita za ujazo bilioni 126, maji yaliyokuwa juu ya ardhi ni zaidi ya mita za ujazo bilioni 105. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha tunatumia rasilimali hizi toshelevu kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mpango mkakati wa Wizara yetu ya Maji na tutawasilisha katika bajeti yetu ya Terehe Kumi Mwezi wa Tano ni kuhakikisha tunatumia Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji Kigoma, Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali ilituahidi kujenga Mahakama ya Mwanzo Tarafa ya Namanyere, ninapenda kujua utaratibu huo umefikia wapi.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024 kwa bajeti yetu ambayo tumepitisha tunakwenda kujenga Mahakama katika Kata ya Namanyere na katika Wilaya ya Nkasi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mamlaka ya Mji Mdogo Namanyere, tumeshafanyiwa tathmini na tumekidhi vigezo: Ni lini sasa tutapandishwa hadhi kuwa mamlaka ya Mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mji Namanyere kupandishwa hadhi itakuwa ni baada ya Serikali kumalizia ujenzi wa miundombinu katika Halmashauri, Mamlaka za Miji na Majiji ambayo yamehama katika maeneo yao ya kiutawala, na sasa Serikali inapeleka fedha nyingi kumalizia maeneo hayo.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Nkasi Kaskazini lina vituo vya afya vitatu na vinavyofanya kazi ni viwili kati ya kata 17. Ni lini Serikali itajenga vituo 13 vilivyobaki katika Jimbo la Nkasi Kaskazini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kuboresha afya za watanzania na tayari Serikali inatenga fedha katika vituo vya afya kwenye kata za kimkakati pote hapa nchini, ikiwemo kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Aida Khenani za kule Nkasi ambayo ina vituo vya afya vitatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutangalia katika mwaka wa fedha huu ambao unakwenda kuanza kuutekeleza mwezi Julai, kuona Nkasi imepangiwa vituo vya afya vingapi kwa ajili ya utekelezaji. Kama bado itakuwa haijapangiwa basi Mheshimiwa Mbunge tutaangalia katika bajeti ya 2024/2025 ili tuweze kuwapangia wana Nkasi kupata huduma bora za afya kupitia vituo vya afya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Sumbawanga – Mpanda imetengenezwa kimebakia kipande kidogo cha kutoka Chala – Mpalamawe.

Je, ni lini hiki kipande kitajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kipande hiki alichokisema cha Chala – Mpalamawe, kimsingi ndiyo barabara kuu, lakini kwa sababu Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi yako nje ya barabara kuu, Serikali iliona ni busara barabara ya lami badala ya kujengwa huko porini ipite Makao Makuu ya Wilaya ambayo ndiyo inaunganisha pale Mpalamawe kwenda Mpanda. Mpango ni kuja kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami ili kukamilisha hiyo barabara kuu pia, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nimesikiliza majibu ya Serikali na kwa takwimu alizozitoa Naibu Waziri ni wazi kabisa kwamba bado atujawa na dhamira ya dhati ya kuwasaidia wavuvi wa Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kufahamu ni mkakati upi wa Serikali kwa sasa kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wa Ziwa Tanganyika kwa sababu na ninyi mmekili kuna changamoto ya zana ya kisasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika wanakabiliana na changamoto nyingi ikiwemo utitiri wa leseni lakini changamoto ya vizimba pamoja na changamoto ya kanuni zilizopo. Mheshimiwa Waziri uko tayari kwenda kukutana na wavuvi uwasikilize ili mtakapo kuja na kauli au na utekelezaji uendane na uhalisia wa Ziwa Tanganyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu spika, ahsante sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwanza niko tayari kuambana pamoja na yeye Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwenda kujionea hizi adha ambazo Mheshimiwa Mbunge anazieleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili; mkakati wa Serikali ni pamoja na kuongeza zana za kisasa najua kwenye suala ya uwiano ndiyo ambalo limeleta changamoto. Lakini mwaka wa fedha ujao tumepanga hivyo hivyo maana yake tutaongeza kulingana na mahitaji ya maeneo husika ikiwemo mikopo, tutaleta vilevile vizimba ili kuongeza sasa wigo mpana wa wavuvi katika ziwa hilo, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya cha Kabwe, lakini mpaka leo kile kituo hakijakamilika kwa sababu fedha hazitoshi. Ni mkakati upi wa Serikali wa kumalizia kituo kile cha afya ili wananchi wa Kabwe wapate huduma pamoja na kata ya jirani ya Korongwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha afya cha Kabwe kilipelekewa fedha na Serikali kwa ajili ya ujenzi na kwa taarifa kwamba hakijakamilika tutakwenda kwanza kujifunza kwa nini fedha iliyopelekwa haijakamilisha majengo. Kama kuna matumizi mabaya ya fedha ya Serikali wanaohusika watakaothibitika tutachukua hatua za kisheria na za kinidhamu. Lakini pia tutatafuta pia fedha kuhakikisha kwamba kituo kinakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali mwaka juzi 2021 ilitenga shilingi milioni 100 kupeleka Skimu ya Lwafi – Katangoro, lakini mpaka sasa hakuna tija yoyote imeonekana kwenye hiyo fedha: Ni upi mkakati wa Serikali wa kuongeza fedha ili kumaliza skimu hiyo na ianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tayari katika mpango wa mwaka wa fedha huu tunaoenda nao, fedha nyingi zimewekwa kwa ajili ya kukamilisha skimu mbalimbali za miradi ambayo ni mipya na inayoendelea. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na imani kwamba sasa huu mradi utaenda kukamilishwa kwa sababu tayari fedha zimetengwa katika mwaka huu wa 2023/2024 ili kutekeleza pamoja na skimu nyingine ikiwemo na hiyo skimu ya kwa Mheshimiwa Aida Khenani, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na changamoto katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, hospitali ina vifaa tiba vya kutosha, haina wataalam; au ina wataalam, haina vifaa tiba: Serikali haioni haja sasa yakupeleka hivyo vikaenda sambamba ili kutumia fedha hizi vizuri za walipa kodi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu anakubaliana kwamba kuna wakati watumishi wamekuwepo lakini kunakuwa nashida ya vifaa tiba na wakati mwengine kunakuwepo na vifaa tiba, lakini hakuna watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, na kama kuna hilo tatizo kwenye jimbo lake la hiyo irregularity, aniletee tuone jinsi ya kulitatua kwa pamoja.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tunakubaliana kwamba semina elekezi ni muhimu mara baada tu ya kuteuliwa. Nina swali moja tu la nyongeza.

Kwa kuwa ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyotolewa hivi karibuni, imezungumzia matumizi mabaya ya waliopewa mamlaka, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, namna wanavyotumia masaa 24 kuwaweka watu ndani bila kufuata taratibu.

Je, ni lini Serikali italeta Mswada hapa Bungeni ili tufanye marekebisho kuwaondolea hayo mamlaka wabaki kuwa wasimamizi wa shughuli za maendeleo na yabaki kwa Jeshi la Polisi pekeyake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni ukweli kuwa kwamba sasa Serikali imekwisha toa tayari taarifa ya kijinai, na kwamba taarifa hiyo imekwisha anza kufanyiwa kazi na wananchi wanashirikishwa katika maeneo mbalilmbali ili kuweza kutoa maoni yao na baada ya hapo taratibu nyingine za mabadiliko ya sheria ziweze kufuatwa.

Mheshimiwa Spika, namuomba mheshimiwa Mbunge na Bunge lako liwe na Subira wakati mchakato wa kuendelea kukusanya maoni ya watu yanaendelea kupatikana ili itakapokuwa tayari sasa tuweze kuleta; na kama kutakuwa na mapendekezo ya mabadiliko ya sheria na kama kutakuwa na miongozo yeyote ile sisi kama Serikali au nchi tuweze kuifanyia kazi, ahsante.
MHE AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kituo cha Afya Kabwe kikikamilika kinategemea kuhudumia zaidi ya kata tatu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili kumalizia kituo hiki kifanye kazi katika hizo kata tatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itapeleka fedha katika Jimbo la Nkasi kwa Mheshimiwa Aida kule kwa ajili ya kujenga kituo cha afya ambacho amekitaja kadri ya upatikanaji wa fedha. Vilevile nitumie nafasi hii kusema tutatuma timu ambayo nimeisema pia itaelekea kule Kalambo kwa sababu ni mkoa mmoja timu hii pia iweze kufika katika kituo hiki cha afya na kufanya tathmini na kuona ni namna gani tunaweza tukatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki cha afya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Namanyere – Kipili Port ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla;

Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema Mbunge barabara hii inakwenda kwenye Bandari ya Kipili. Tumetenga fedha kiasi kwa ajili ya kuifanyia ukarabati mkubwa ili iweze kupitika. Lakini lengo la Serikali ni kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami, hasa tukizingatia umuhimu wenyewe, kwamba inakwenda kwenye bandari ambayo inahusisha biashara kati ya Tanzania na DR Congo. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana na nashukuru pia majibu ya Serikali nimeyasikia. Lakini wananchi wapokata Bima ya Afya wanajua wameweka akiba kwa ajili ya matibabu pale wanapoumwa kumekuwa na utofauti wanapokwenda hospitalini kupata huduma wanaambiwa bima yako daraja lake huwezi kupata dawa hizi, huwezi kupata huduma hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuwapa elimu mapema kabla hawajakata bima ili kujua kwamba bima yake anaweza kupata matibabu gani kwenye eneo lipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa NHIF na Serikali mmekili kwamba bado kuna changamoto na changamoto hizo na CAG naye amezungumza usimamizi mbovu pamoja na taarifa za uongo zinapotolewa. Ni upi mkakati wa Serikali wa kumaliza changamoto hizi ili kurudisha dhana ile kwa Serikali kuliko hivi sasa wananchi wanaamini hatuna maana tena ya kuwa na Bima ya Afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri lakini naomba tu nimwambie kwamba kwenye eneo la NHIF hakuna madaraja labda akiwa amechanganya kati ya NHIF na CHF. Kwenye CHF ndiyo kuna madaraja kwa maana kuna kutibiwa kwenye kunafikia level fulani hutibiwi level fulani na mambo mengine kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tulikuja na mkakati wakati wa kuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa watu wote tulikuja na mkakati thabiti wa kuboresha eneo la CHF pamoja kwamba tunayo Bima ya Afya kwa wote. Lakini tuone kwa uwezo pili hicho kwa sababu hatufuti CHF lakini tukaja na makakati wa kuboresha ili kuondoa madaraja ambayo Mheshimiwa Mbunge anayazungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nataka kukuhakikishia kwamba matatizo watu wako wa Nkasi wanayoyapata kutokana na hayo mambo tukikubaliana pamoja kwamba baada ya muda tutakuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa wote tutaweza kutoa hilo tatizo. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana niliuliza kwamba kwa kuwa na nyinyi Serikali mmekiri kwamba kuna changamoto kwenye aina ya Bima hiyo ya CHF kwamba mkakati wa Serikali ni upi wakumaliza changamoto hizo ili kuondoa hii dhana ambayo wananchi wanayo sasa kuona hakuna haja ya kuwa na Bima ya Afya wanapoenda kwenye huduma. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachosema Mheshimiwa Aida nimekwenda pamoja na yeye kwenye jimbo lake nimeona hilo tatizo na wananchi wamekuwa lalamika. Kwanza nikupongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ulivyo karibu na nilivyopita kule nilikuwa nashangaa ulishindaje kule kwa ile structure? Nikajua hapo sasa hivi kwa kweli wewe ni mwanamke wa shoka kwa ushindi uliyopata pale Nkasi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba, tumesema hapa moja nimeeleza kwa swali alilosema mwenzetu Mbunge pale kwamba kwakweli kwa sasa tunashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ambao wanasimamia eneo hilo kwamba tuone kwa kipindi hiki cha mpito ambao bado Muswada wa Bima ya Afya kwa wote haujaja tunakaaje tuweze kuboresha eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kwa sababu kuna taasisi ambayo ina support eneo hili na Waziri wa Afya ameishawaita tuone tunakaaje waweze kukaa. Fedha wanazotumia kwenye warsha, matangazo na nini wanaweza kuboresha hicho kitita wakati tunangojea Muswada wa Bima ya Afya kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi mwenyewe eneo hilo la CHF sithubutu kulipigania kule jimboni kwangu. Kwa sababu ukipigania halitoi matokeo unayotegemea lakini naamini kwa ushirikiano wetu na TAMISEMI tumeweka mkakati mzuri sana ambao tutaboresha eneo hilo baada ya muda siyo mrefu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri unajua kwamba kumekuwa na changamoto sana ya uvamizi kwa wavuvi kuchukuliwa vifaa vyao ikiwemo injini pamoja na fedha na tunaposema boti tunazungumzia speed boti kwa ajili ya kuendana na wale wahalifu wanaotoka nje za jirani. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuwapa speed boti kwa maana ya fiber askari polisi ili waweze kuwalinda wananchi wetu na kupambana na wale wahalifu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili Askari Polisi wa Nkasi wanapata changamoto kubwa sana kulingana na jiografia. Ni lini mtawapa gari pamoja na mafuta ya kutosha siyo kama hivi wanavyofanya sasa hivi ili waweze kuwajibika katika majukumu yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba wakati mwingine wananchi wetu wanaathiriwa na majambazi hawa wanaopita maeneo ya ziwani kwa sababu wanakuwa na vifaa bora zaidi kuliko walivyokuwanavyo vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwenye maeneo hayo. Kwa kulitambua hilo ndio maana nimeeleza katika boti tutakazonunua ni fiber zinazokwenda mwendokasi ili kukabiliana na hao majambazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijana wetu ambao wanahitaji magari, nimesema yatakapotoka tutawagawia na Wilaya yako ya Nkasi itanufaika na pamoja na Jimbo la mwenzio Nkasi Kusini ambaye ni Mjumbe wa Kamati yetu ya NUU wote tutahakikisha kwamba tunapata magari. Baada ya kupata magari hayo katika mwaka ujao pia tutaongezea vitendea kazi vingine zikiwemo pikipiki ili kuimarisha uwezo wa vijana wetu wa doria kwa magari na madoria kwa pikipiki, nashukuru sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri, barabara ya kutoka Korongo kwenda Utinta imekuwa na changamoto kubwa sana na kuleta hatari kwa wanafunzi: Ni lini mtawaongezea fedha TARURA ili waweze kujenga kipande hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Serikali imeongezea fedha TARURA ukilinganisha mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022, 2022/2023 na hata 2023/2024 tunayoenda kutekeleza, TARURA wameongezewa zaidi ya mara tatu ya bajeti ambayo ilikuwepo hapo awali. Kwa hiyo, ni kukaa na Meneja wa TARURA wa Mkoa kuangalia ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya kukarabati vile vile eneo la Wilaya ya Nkasi anakotoka Mheshimiwa Khenani ambapo wanafunzi wanavuka kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba vile vile Meneja wa Wilaya ya Nkasi awasilane na Mheshimiwa Khenani ili kuona ni namna gani wanaweza wakaanza ukarabati wa barabara hii.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, natambua msamaha ambao umetajwa na Serikali, lakini pamoja na msamaha unaotolewa wa kodi unakuwa sawa kwenye hizi taasisi lakini wanapotoa hizi huduma, wanatoa kwa gharama tofauti tofauti. Serikali ipo tayari kutoa mwongozo sasa katika hizi gharama zinazotelewa kwenye hizi taasisi binafsi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani bado kuna changamoto ya Kodi ya Forodha kwa vifaa tiba pamoja na dawa.

Je, Serikali iko tayari kutoa hizi kodi zote kama ilivyotangaza kwenye magari yanayotumia umeme ili kutoa kipaumbele kwa afya za Watanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa taasisi ambazo zinafanya biashara zinastahiki kutoa kodi inayostahiki kwa mujibu wa sheria, ambazo zinatoa huduma tu zinapata hadhi ya charitable organization na zitapata unafuu wa kodi.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, Serikali inatambua umuhimu uliopo katika elimu na afya, tunaendelea kuboresha miongozo mbalimbali ya kodi ili kila wakati tuweze kufikia malengo ya utoaji huduma bora kwa wananchi wetu, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa vifo vingi vinavyotokea Ziwa Tanganyika vinatokana na wananchi kutumia usafiri ambao sio salama, kwa sababu hatuna usafiri wa uhakika kwa maana ya meli. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka usafiri wa kisasa Ziwa Tanganyika ili kuokoa vifo vya watu vinavyotokea?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khenani, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliyosomwa tarehe 22 na 23, tulifanya Commitment kwamba mwaka wa fedha ujao 2023/2024 tunakwenda kujenga na kununua meli mbili za kisasa. Vilevile, hivi karibuni tulikuwa na vikao na Waheshimiwa Wabunge wote wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Katavi kuhakikisha kwamba haya ambayo Serikali imefanya commitment katika bajeti, tunakwenda kuyafanya na naamini tutayatekeleza, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wa vijijini wanatumia kuni na mkaa kwa sababu ndiyo nishati inayopatikana kwa wepesi kwenye maeneo yao: -

Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala ambayo ni gesi asilia ili iendane na nguvu tunayotumia kupiga marufuku kutumia kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kabisa kwamba watu wengi wa vijijini wanatumia mkaa na kuni katika hasa nishati ya kupikia. Tunalifahamu hilo na tumeliona na Serikali imeanza jitihada za kuanza kupunguza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia kwa namna ambayo imeonekana ni rahisi zaidi kuliko nishati ya gesi ya asili, ni kuwezesha wananchi kupata mitungi ya gesi ya viwandani kwa kuanza kupikia, na ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha ilitengwa mitungu 70,000, tumetenga kwenye bajeti inayokuja mitungi takribani 200,000 ili angalau tutoe mtaji wa mwananchi kuweza kupata kianzio cha kupata gesi halafu baada ya hapo sasa ataanza kununua na kuelekea kwenye kutumia gesi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaboresha na kuona namna tunavyoweza kupunguza gharama za hii mitungi ya gesi ili wananchi walio wengi waweze kui-afford kwenye maeneo yao, Serikali inaweka ruzuku lakini tutaangalia namna nyingine ya kuweza kupunguza gharama hizi ili kila mwananchi aweze kutumia gesi safi ya kupikia.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nimesikia majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ninazungumzia kata 97 za Mkoa wa Rukwa ambazo hazina maji kutoka Ziwa Tanganyika na hapa wanasema wamejiandaa kwa mwaka wa fedha kumwandaa mtaalam mshauri.

Je, ni lini utaratibu wa kumpata huyo mtaalam mshauri na process kuanza mpaka mradi kukamilika kuanza kutoa maji kwa Mkoa wa Rukwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, mwaja jana kata tano za Jimbo la Nkasi Kaskazini, tulinunua maji ndoo moja shilingi 800 mpaka 1,000.

Je, mna mkakati gani wa dharula wa kuweza kupeleka maji kwenye hizo kata wakati tunasubiri mradi mkubwa wa Ziwa Tanganyika ambao ndio suluhisho la jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Aida Khenani, amefuatilia hili suala kwa muda mrefu na sisi kama Wizara tunakupongeza na hatutakuangusha na hatutakuwa kikwazo. Hizi Kata zote tutakuja kuhakikisha zinapata maji safi na salama. Lakini kwenye hizi kata tano za swali lako la pili, mkakati wa Wizara kwenye maeneo ya aina hii ni kutumia vyanzo vya maji rafiki vilivyokaribu, ikibidi kuchimba visima. Na kwa sababu tayari tuna magari basi tutachimba na kuweza kujenga vichotea maji na kuwasambazia wananchi ili kupunguza adha ya maji.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ningependa kufahamu ni lini Serikali mtapeleka fedha kumalizia ujenzi wa soko la Samaki Kata ya Mkinga, toka mmeahidi mwaka jana hakuna kitu kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunatambua kuhusu mahitaji ya Soko la Mkinga na tuliahidi katika bajeti. Changamoto ambayo ilikuwepo ni kwamba fedha zilikuwa hazijatoka lakini jambo hilo liko katika mpango na nafikiri Wizara ya Fedha itakapokuwa imeleta fedha kwa wakati huu, tutazileta kwa wakati na kuhakikisha soko hilo linajengwa.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka 2016 Serikali iliwekeza fedha kwenye mwalo wa Kirando wenye thamani ya shilingi bilioni 1.1. Lakini mwaka 2019 mwalo huo ulizama ikiwepo Kasanga pamoja na maeneo mengine yote ya Ziwa Tanganyika. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa ziada wa kujengwa mwalo mwingine na kuupandisha hadhi kama ulivyosema kwenye Kata ya Kirando?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ili kunufaika na mazao yatokanayo na uvuvi kwenye ushindani wa soko ni lazima Serikali iwekeze kwenye kulinda mazalia ya samaki. Napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa ziada wa kulinda mazalia ya samaki bila kuathiri wavuvi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza Serikali imeshatoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kupendekeza maeneo wanayodhani kuwa yanaweza kufaa sasa mara baada ya maji kuingia katika mwalo ule wa mwanzo, na mara baada ya kupendekeza tutakuja kufanya tathmini ili tujiridhishe na mchakato sasa wa ujenzi uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili juu ya mazalia; mazalia ya samaki nini mkakati wetu ni kwamba Serikali la kwanza kwa kushirikiana na jamii tuko tayari na tunajipanga katika kuyatambua, kuyaainisha na kuyatangaza kwa mujibu wa sheria ili baadae tuweze kuyalinda na naomba niihase jamii ya wavuvi maeneo yote nchini ya kwamba kazi ya kulinda rasilimali hizi hususan maeneo ya mazalia ni kazi ya jamii nzima, Serikali za Vijiji, Serikali za Kata, Serikali mpaka Wilaya na Mikoa ni kazi yetu sote Watanzania.

Mheshimiwa Spika, bila ya kulinda mazalia samaki wetu watakwisha na hatua kali tutaichukua kwa yeyote anayefanya maingilio ya kwenda katika kufanya kazi ya uvuvi kwenye eneo la mazalia. Huo ni uhalifu na hatutamvumilia yeyote ambaye atakwenda kuharibu rasilimali hii ya Watanzania.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wakulima wa mpunga wa Wilaya ya Nkasi pamoja na Bonde la Ziwa Rukwa changamoto yao kubwa ni skimu za umwagiliaji pamoja na soko la uhakika. Nini mkakati wa Serikali kwa kuzingatia msimu wa safari hii mavuno sio mazuri sana ili wapate soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya mikakati ambayo tumeiweka katika kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga ni kuzikamilisha skimu nyingi za umwagiliaji ambazo zinagusa maeneo aliyoyasema Mheshimiwa Mbunge. Bahati nzuri mimi mwenyewe nimekwenda kama kule Mwamapuli na maeneo mengine Kata ya Kilida kuangalia uwezekano pia kuongeza skimu hizi ili kuongeza tija katika zao letu la mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu na kwamba tumejipanga vyema ili kuongeza uzalishaji na ukiangalia mpunga hivi sasa ndiyo unatutangaza vizuri nje ya mipaka ya Tanzania na uzalishaji umeongezeka sana. Kwa hiyo katika maeneo ambayo tutawapa priority ni pamoja pia na skimu za umwagiliaji katika maeneo ambayo wanalima mpunga ikiwemo katika mkoa ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Naibu Waziri barabara ya kutoka Chala - Mpalamawe ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, pia ilikuwepo kwenye Ilani, lakini sasa hamuitamki. Nataka kujua, mna mpango gani wa kuijenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni barabara kuu, lakini ni barabara ambayo kwa sababu barabara nyingine ilikuwa inapita kwenye Makao Makuu ya Wilaya, Serikali iliamua kwanza ijenge barabara kupitia Makao Makuu na hii ifuate. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri Serikali itakavyopata fedha barabara hii pia itajengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Waziri mwaka jana ulikuja Kirando na ukaona kwamba ule mwalo uliokuwa umewekwa na Serikali umezama. Nini mpango wa Serikali wa kujenga soko ambalo nilikuonesha kwamba eneo tayari tumeliandaa pale Kirando? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nilifika Kirando na kweli mwalo ule tuliukarabati na kujenga miundombinu mbalimbali lakini umezama. Lakini ahadi yetu Mheshimiwa Mbunge iko pale pale kwamba tutaujenga upya Mwalo wa Kirando kwa kutumia bajeti ambayo tayari tumetengewa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba ubora tuliokuwa tunautaka utokee kwenye mwalo huo unaendelea kuwepo.

Kwa hiyo, tutaendelea na juhudi kwa mwaka wa fedha ujao kuweza kukarabati miundombinu iliyoko hapo, ili pia kuweza kuwasaidia wavuvi wetu hasa eneo la Kirando ambao wanavua kwa wingi sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Miongoni mwa kanuni ambazo zinalalamikiwa na wadau wa uvuvi ni pamoja na utitiri wa tozo unaotaka mmiliki alipe Dola 55, lakini chombo alipie Dola 55 na mvuvi alipe Dola 10. Ni lini watafanya marekebisho ya kanuni hiyo ambayo inakwenda kuwatesa hao wavuvi ambao ni Watanzania wanalipa kwa dola? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, lini tutarekebisha kanuni inayoonesha kwamba mmiliki wa chombo analipa leseni, mvuvi analipa leseni na chombo kinalipiwa leseni. Ni kweli kwamba, tunao utaratibu wa chombo cha chini ya mita 11 kinalipiwa leseni katika Halmashauri zetu za Wilaya kama ni sehemu ya mapato ya ndani. Kwa upande wa mmliki wa chombo na yeye analipishwa leseni na yule mvuvi analipishwa leseni ili tuweze kupata namba kwa maana ya takwimu ya wavuvi wangapi wanaoshiriki katika shughuli za uvuvi kila siku kwa kuwa na ile leseni. Hata hivyo, kwa maoni tuliyoyapokea kutoka kwa Wabunge tupo katika mchakato wa kuitafakari kanuni hii ili tuweze kuona namna iliyo bora ya kile cha kupata takwimu lakini vilevile ya kuweza kurahisisha shughuli zetu. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii, niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Umwagiliaji wa Luamfi ni mradi muhimu sana kwa wakulima wa Ziwa Tanganyika. Je, ni lini mradi huu utakamilika kwa kuwa umekuwa unasuasua sana?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimwondoe tu shaka Mheshimiwa Mbunge Aida Khenani kwamba, maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji ikiwemo mradi ambao ameutaja wa Luamfi ni kwamba yote tumeweka katika mipango yetu, ambayo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaitekeleza. Nimhakikishie pia kwamba, bahati nzuri Mheshimiwa Rais anatuunga mkono sana na ameweka jitihada kubwa pamoja na fedha kuhakikisha maeneo yote yanayofaa yanafikiwa. Kwa hiyo hata hilo lenyewe tutalikamilisha kwa wakati, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Kabwe wana changamoto ya kijiografia na wanapata shida kubwa sana ya matibabu kuja Hospitali ya Wilaya; na ile ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kujengewa Kituo cha Afya. Ni lini mtapeleka fedha kumalizia kujenga kituo hicho ili wananchi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi zinazotolewa na viongozi wetu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji. Kwa sababu hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na ninakumbuka nilikuwa kwenye ziara yake, nakuhakikishia tayari tumeshaingiza kwenye Mpango Mkakati kwa ajili ya kutafuta fedha na kwenda kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Kabwe, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Kabwe wana changamoto ya kijiografia na wanapata shida kubwa sana ya matibabu kuja Hospitali ya Wilaya; na ile ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kujengewa Kituo cha Afya. Ni lini mtapeleka fedha kumalizia kujenga kituo hicho ili wananchi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi zinazotolewa na viongozi wetu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji. Kwa sababu hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na ninakumbuka nilikuwa kwenye ziara yake, nakuhakikishia tayari tumeshaingiza kwenye Mpango Mkakati kwa ajili ya kutafuta fedha na kwenda kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Kabwe, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; mipaka hii ambayo inazungumzwa leo iliwekwa mwaka 1948. Ukiangalia idadi ya watu ilikuwa ni watu wachache kuliko ilivyo leo. Kwa kuwa hii migogoro imekuwa ya muda mrefu na ilisababisha tamko na maagizo ya Waziri Mkuu hapa Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuja Nkansi kupitia upya mipaka hiyo kwa kushirikiana na TAMISEMI, mpaka leo hamjafika. Ni lini mtatekeleza agizo la Waziri Mkuu alilotoa kupitia Bunge lako tukufu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; pamoja na changamoto ya migogoro iliyopo kwenye hii mipaka, lakini bado tembo wamekuwa wanavuka kutoka kwenye eneo lao la pori tengefu kwenda kwenye makazi ya wananchi na kula mazao na kuvamia makazi na hivi sasa hawana chakula tena.

Ni lini mtawalipa wananchi hawa kwa kuangalia hali halisi ya sasa badala ya kufuata sheria ya wanyamapori ambayo inawaumiza wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkansi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Rwafi ni pori ambalo kabla ya kuanzishwa lilikuwa chini ya Halmashauri. Baada ya Halmashauri kushindwa kulisimamia vizuri lililetwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii na wakati huo huo wananchi walikuwepo ambao walikuwa hawaijui mipaka vizuri na wakahitaji kufafanuliwa mipaka.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninavyoongea zaidi ya kilometa 50 tayari zimeshaanza kuoneshwa kwa maana ya kuwekwa vigingi kwa kushirikisha wananchi. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa zoezi hili linaendelea, wataalamu wataendelea kushirikisha wananchi kuonesha mipaka halisi ya pori hilo ili waweze kutambua maeneo ambayo yamehifadhiwa.

Mheshimiwa Spika, na swali hili la pili kuhusiana na tembo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Nkansi kwamba kwa kuwa Serikali imeendelea kulipa kifuta machozi na kifuta jasho, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Nkansi tutaenda kulipa kifuta machozi kabla ya kuisha mwaka huu wa fedha, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali swali la nyongeza. Ningependa kufahamu Serikali mnamkakati gani wa ziada kumaliza changamoto kwenye zile Kata tano za Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mkakati wa ziadi kuhakikisha zile Kata tano zinapata maji ni kwenda kupeleka miradi ya muda mfupi ya uchimbaji wa visima ili wananchi waendelee kupata maji wakati utaratibu wa kutumia Ziwa Tanganyika unaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto ya upungufu wa walimu nchini. Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina changamoto kubwa hasa walimu wa kike. Serikali mna mpango gani wa haraka ili kuokoa mimba za utotoni ambazo zinaendelea Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani juu ya upungufu wa walimu waliopo Nkasi; katika ajira ambazo zitatangazwa mwishoni mwa mwezi huu wa Februari kwa ajili ya kupata walimu wapya, basi tutaweka kipaumbele vile vile kwa Mkoa wa Rukwa na hasa Wilaya ya Nkasi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka juzi na mwaka jana mmeahidi kupeleka fedha kwenye Skimu ya Ruafi, lakini mwaka huu hali ni mbaya na wakulima hawawezi kuendelea kulima. Je, mna mkakati gani sasa kupeleka pesa kwa haraka na mkarabati ile skimu?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Skimu ya Ruafi na yenyewe ni moja ya skimu ambayo tume yetu imepata taarifa juu ya kinachoendelea kule na sisi Waziri wa Fedha amekutana na Waziri wa Kilimo kuhakikisha wanatupatia bajeti ili yale maeneo yote ambayo yameharibika sasa tuweze kuyarekebisha. Kwa hiyo hili nikuondoe shaka na tunalifanyia kazi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Kata hii ya Chala na Ninde iko Wilaya ya Nkasi na Serikali imekuwa ikitoa kauli mara kwa mara kwamba, hakuna mpango wa kuongeza maeneo ya kiutawala; kuongeza maeneo ya kiutawala ni takwa la kisheria. Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo hili la kisheria kwa maeneo ambayo yamekidhi vigezo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali haijawahi kutamka kwamba haina mpango wa kuongeza maeneo ya utawala. Serikali imetamka kwamba, imeweka vipaumbele, kwanza kukamilisha majengo ya utawala yaliyopo katika mamlaka zilizopo na hatimaye tutakwenda kuanzisha maeneo mapya ya utawala. Kwa hiyo, hakuna sehemu ambayo tumetamka kwamba, hatuanzishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mbunge kwamba, kwanza tunaendelea kukamilisha miundombinu iliyopo na baadaye tutakwenda kutoa kipaumbele kwenye kata aliyoitaja na maeneo mengine ambayo yatakidhi vigezo ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wenye sifa ya kuajiriwa wapo, changamoto ni kuajiri. Wilaya ya Nkasi peke yake tuna changamoto, upungufu wa walimu 855. Ni lini sasa mtawaajiri kwa kuwa wenye sifa wapo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama nilivyojibu katika swali la awali la msingi pamoja na la nyongeza; ni kwamba tunatambua kwamba wapo walimu ambao wana sifa na bado hawajaajiriwa na Serikali inaendelea kuajiri kulingana na kibali tunachokipata utumishi na bajeti. Kwa hiyo hivi vitu vyote vinakwenda sambamba, hatuajiri tu kwa sababu idadi ya walimu wako mtaani. Tunachozingatia ni mahitaji ya msingi na sisi hilo tunaliona. Kwa hiyo, kadiri uchumi utakavyoendelea kuimarika tunaweza tukaajiri wote kwa wakati mmoja, hilo ndio naweza kulijibu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa Serikali inatenga fedha nyingi kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa sababu tunajua umuhimu wa wenyeviti hawa, ni lini tutaona umuhimu wao kwa kuwalipa posho isiwe fedha kama sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba posho za viongozi hao ambao ni Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa siyo fedha. Zipo kwa mujibu wa Mwongozo na Serikali inahakikisha inalipa wenyeviti hao kwa kadri fedha zinavyopatikana. Changamoto iliyopo ni uwezo wa halmashauri zetu kulipa wenyeviti wote kwa wakati, ndiyo maana Serikali inaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuwezesha halmashauri kukusanya zaidi ili ziweze kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwasisitiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kuongeza uwezo wa halmashauri na kuweka kipaumbele katika kuwalipa viongozi hao. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea majibu ya Serikali. Sasa kwa kuwa, kusainiwa mkataba ni jambo moja na ile miundombinu imeharibika sana na uchumi wa Nkansi sisi tunategemea kilimo na uvuvi. Tunatamini kusikia, mkataba huo utaanza lini na kukamilika ili wananchi waendelee kupata hudumu kwenye Skimu hiyo ya Rwanfi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia hekta 3,300, Wilaya ya Nkansi tuna hekta 6,145. Je, ni lini watamalizia eneo lingine lililobaki kwa sababu ndiyo uchumi wetu wa Wilaya ya Nkansi? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, namthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mara baada ya mkandarasi kusaini mkataba anatakiwa aanze kazi mara moja. Matarajio yetu ni, kwa sababu kazi ni process, ndani ya miezi 24 kazi yote iwe imekamilika na mradi uwe na full capacity.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuongeza ukubwa kutoka hekta 3,300 mpaka hekta 6,145. Hili ni lengo la Wizara kwamba, katika hatua ya kwanza tuta-deal na hizi hekta 3,300 na baada ya hapo tutaongeza miundombinu katika hizi hekta nyingine. Kwa hiyo, ni kazi ambayo ipo katika mipango yetu, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi; Mheshimiwa Naibu Waziri upatikanaji wa maji Mamlaka ya Mji Mdogo Namanyere ni 52% na upotevu wa maji ni 47%, tunahitaji shilingi milioni 400 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini watatupatia hizo fedha tuweze kukarabati miundombinu iliyoharibika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwia Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni swali ambalo tayari Serikali tulilijibu hapa Bungeni na tayari Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso alielekeza fedha shilingi milioni 400 zipelekwe kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, mradi huu unakamilika. Mradi huo unapokamilika wananchi wa Namanyere wanapata huduma ya maji safi na salama, lakini vilevile unaenda kusaidia kuhakikisha kwamba, miundombinu yetu inaboreshwa na kuepusha upotevu wa maji ambao ni hasara kubwa kwa Serikali.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, tuendelee kushirikiana na tutahakikisha kwamba, fedha hizo zinafika kwa wakati na mradi uendelee kutekelezwa. Tunakupongeza kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na utekelezaji wa Ilani ya CCM inaendelea kutekelezwa vizuri sana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kabwe kimekuwa kinatolewa kauli tofautitofauti juu ya umaliziaji wake, leo nataka kusikia kwa mara ya mwisho, ni lini mtakamilisha kituo hiki ili kianze kufanya kazi?

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani kinaitwa nini ili siku nyingine ukiuliza tukukumbushe ulisema leo ni mara ya mwisho.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kabwe, leo ni mara ya kumi nauliza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ilishakusanya vituo vya afya vya kimkakati vya kujengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 bila shaka Mheshimiwa Mbunge ulileta kituo hiki kukiombea fedha kujengwa katika mwaka wa fedha huu. Nikuhakikishie Serikali inatafuta fedha kuhakikisha kwamba vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo yote vinajengwa na kama hiki kituo ni kituo ambacho wewe ulikileta kwamba ni kituo cha kimkakati nikuhakikishie Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Nauliza leo kwa mara ya tisa kuhusu Kituo cha Afya Kabwe. Nataka kufahamu, kwa kuwa bajeti yako tayari tumeshamaliza, ni lini mtaenda kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kabwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza kwa mara ya tisa. Inaonesha ni namna gani yuko serious na Kituo cha Afya cha Kabwe. Namhakikishia tu kwamba, Serikali iko serious zaidi kuhakikisha wananchi wa Kata ya Kabwe wanapata huduma bora za afya na tayari tumeshaanza kuweka kwenye bajeti. Kwa hiyo, ni suala la muda tu, tutakwenda kutekeleza kukamilisha kituo kile, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri natambua mikakati inayoendelea ya kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano na kwa sababu mawasiliano ni haki ya wananchi wote, ningependa kufahamu, kuna kata nne ambazo bado hazina mawasiliano. Kata za Mkinga, Kipili, Isale na Mkwamba, ni lini watu hao watapata mawasiliano?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mikakati inayoendelea lengo lake ni kuhakikisha kila Mtanzania popote alipo anapata huduma za mawasiliano na hasa mikoa ya pembezoni. Mimi nimefanya ziara kwenye baadhi ya maeneo ya Rukwa, Sumbawanga, Katavi na kadhalika na ninajua changamoto iliyopo na hasa maeneo haya ya mipakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kata alizozitaja nitakwenda kuangalia kwenye Mradi wa Tanzania ya Kidigitali kama hazimo jambo ambalo siamini, kama hazimo nitahakikisha zinaingia kwenye mradi unaofuata na kama zimo tutasukuma ili mradi huo uanze mapema tuwahudumie wananchi wako. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anajua kwamba Ziwa Tanganyika sisi tunaotoka maeneo yale ndiyo shamba letu na ndiyo duka letu, hivyo unapopumzisha hilo ziwa kwa miezi mitatu, ningependa kufahamu, Serikali mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kuwapatia wavuvi kwa kipindi hicho cha mpito?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki cha miezi mitatu ni kweli, kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kuwa Ziwa Tanganyika kwa asilimia kubwa wanaozunguka eneo hilo, ndiyo shamba lao. Kwa kutambua hilo, Wizara imekuja na mkakati wa kuwakopesha wavuvi hao vizimba. Vizimba hivi vitasaidia kuongeza uzalishaji ambao umekuwa ukifanyika katika hilo Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli wavuvi wa Ziwa Tanganyika wamepokea jambo hili kwa mikono miwili na wapo tayari. Pia tayari tumeshapokea maombi mengi na tarehe 5/5/2024 Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi anakwenda kukabidhi vizimba kwa wale wote walioomba katika eneo la Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo tayari kuendelea kutoa vizimba kwa wale watakaoomba na milango ipo wazi waendelee kuomba. Huu ndiyo utakuwa mbadala pekee wa kuwasaidia wavuvi katika eneo hilo la Ziwa Tanganyika.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Waziri hilo Bwawa la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Namanyere bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni 6.7, fedha iliyoenda ni shilingi milioni 950, leo tunazungumza ni tarehe 12 Juni, tunaenda kumaliza mwaka wa bajeti na mpaka sasa mkataba tu haujasainiwa. Ni upi mkakati wa Serikali ambao upo kuhakikisha hizi fedha zinakwenda na huu mradi unakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto ya bwawa hili na ninatambua kwamba wananchi wake wanasuburi kuona nini kinafanyika na kwa bahati nzuri pia Mheshimiwa Mbunge uliuliza kuhusu hili swali na nikakupa mkakati wa namna gani tunaenda kufanya. Naomba uwe na subira kwa sababu miradi hii inafanyika kwa hatua na mkandarasi akishapewa mkataba maana yake ni kwamba tutaanza kwa kumlipa advance, hatumlipi pesa yote, maana yake ni kwamba pesa nyingine itakayofuatia ni kulingana na ambavyo atakuwa ana raise certificate kulingana na progress ya kazi ambayo atakuwa anaifanya. Kwa hiyo, nakutoa wasiwasi, Serikali inatambua na tunaenda kulifanyia kazi kwa ukamilifu, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimepokea majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika mwaka wa fedha ambao tunaumaliza mwezi ujao, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga Mradi wa Mji wa Namanyere wenye gharama ya bilioni 6.75. Mpaka sasa hapa ninapozungumza bado mwezi mmoja tu na wamepeleka milioni 950. Je, ni lini watapeleka fedha iliyobaki kwa muda huu uliobakia na mkandarasi aende site kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri hapa kwamba upatikanaji wa maji ni 50%, lakini upotevu wa maji ni 47%. Je, Serikali hawaoni kwamba kuna haja sasa ya kupeleka fedha haraka ili tuanze ukarabati, kwa sababu hata kwenye hicho kiasi kidogo kinapotea?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, anafanya kazi kubwa sana kwa wananchi wake wa Nkasi Kaskazini na kwa kweli anaendelea kushirikiana vizuri sana na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba anashiriki katika utekelezaji wa miradi inayopatikana katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba tuna mradi wa bilioni 6.75 na mwisho wa mwezi huu Serikali tunakwenda kusaini mkataba na mkandarasi ili aweze kuingia. Hizo fedha ambazo zilitengwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024 ni fedha ambazo ni kwa ajili ya malipo ya awali. Kwa hiyo, mkandarasi akishasaini mkataba basi fedha hizo atalipwa na ataingia site kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu upotevu wa maji. Ni kweli kabisa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, kwamba upotevu ni 47% ilhali upatikanaji wa maji ni 52.9%. Kikubwa ambacho naweza kukisema hapa ni kwamba, upotevu wa maji unaweza ukatokana na miundombinu, usimamizi na teknolojia tunayoitumia. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo. Tunaondoka kwenye mechanical meters tunakwenda kwenye smart prepaid water meters.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni katika kuhakikisha pia kuwa tuna-reduce upotevu wa maji na vile vile kuhakikisha kwamba tunapeleka. Mwezi Aprili Mheshimiwa Mbunge tumempelekea shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Mji wa Namanyere. Hii ni katika kuhakikisha kwamba ule uharibifu na upotevu ambao ulikuwa unatokea, basi wananchi waweze kurejeshewa huduma na waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Serikali mna mpango gani wa haraka wa kujenga uzio kwenye Kituo cha Afya Nkomolo kinachohudumia zaidi ya Kata tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu katika majibu yangu ya msingi, Serikali iliweka utaratibu wa kujenga vituo hivi vya afya kwa awamu kwa kuanza na ujenzi wa miundombinu ambayo itasaidia kutoa huduma za afya kwa wananchi na baadaye kwenda kwenye hatua za kujenga uzio kwa ajili ya usalama.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua uhitaji wa uzio katika kituo kile cha afya, na kwa sababu tumeshakamilisha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa miundombinu ya huduma, tutakwenda kuanza ujenzi wa uzio huo ili kuongeza usalama wa kituo kile.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nimeulizwa sana Barabara ya kutoka Namanyere - Kipili Port, ningependa kufahamu ni hatua zipi zinaendelea mpaka sasa kuhusu ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja, iko katika bajeti hii, tunaendelea kuifanyia usanifu wa kina, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa kabla hatujasimamisha kutolewa kwa hii mikopo kulikuwa na makundi ambayo yameshaomba na mengine yaliendelea kuomba na tunatumaini kila halmashauri iliendelea kutenga fedha hizi, napenda kufahamu, mikopo hii ikisharuhusiwa, fedha yote yote itatolewa kwa pamoja au tutaanza na wale ambao walikuwa wameshaanza kuomba mikopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, makundi yote ambayo yalishawasilisha maombi kwa ajili ya mikopo hii yaliendelea kufanyiwa tathmini na kuwekwa kwenye orodha ya kupata mikopo. Kwa hiyo, mara tutakapoanza kutoa mikopo hii, kwanza tuta-consider vikundi vilivyoomba mwanzo kama kipaumbele na vikundi ambavyo vimeomba baadaye vitapata mikopo hiyo pia, ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri unajua mikoa inayoongoza kwa uzalishaji ndiyo mikoa inayoongoza kwa udumavu, ni upi mkakati wa Wizara kwa sababu halmashauri mpaka sasa zimeshindwa wa kuweza kutoa elimu ili kuleta matokeo chanya?
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Aida Khenani kwa kweli amezungumza ukweli mikoa ambayo ndiyo wazalishaji wakuu wa chakula ikiwemo Njombe, Rukwa, Katavi, Iringa na Kagera ndiyo pia wana kiwango kikubwa cha utapiamlo hususani kwa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati kama nilivyoisema changamoto siyo upatikanaji wa chakula, changamoto ni wananchi kuandaa chakula lakini pia na kula chakula mchanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba, 2023 kwa mara ya kwanza tumezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Chakula na Ulaji, mwongozo huu unahimiza katika vyakula tunavyokula kuzingatia makundi sita ya vyakula. Kundi la kwanza ni nafaka, lakini pia kundi la pili ni masuala ya vyakula vya asili ya wanyama, kundi la tatu vyakula vya asili ya kunde na mbegu za mafuta, kundi la nne ni mboga mboga, kundi la tano ni matunda, kundi la sita ni mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aida Khenani niseme tumepata fedha kutoka kwa wadau, tumeamua kidogo tusimame tuangalie zinakwenda kufanya kazi gani kwa sababu siyo tu fedha nyingi zinapelekwa, lakini tunataka kuona interventions ambazo zitagusa wananchi. Kwa upande wa Njombe tumeona wanawake pia hawana muda wa kulisha watoto kwa sababu ni wachapakazi wakubwa sana. Kwa hiyo ndiyo maana pia tunataka kuanzisha vituo vya malezi ya awali ya watoto ambapo pia masuala ya lishe yataweza kufanyiwa kazi na kuhimizwa. (Makofi)