Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anatropia Lwehikila Theonest (10 total)

changamoto kubwa ya zahanati hizi katika Jimbo la Segerea na Manispaa ya Ilala ni maeneo lakini wapo watu wanaoishi jirani na maeneo hayo, wapo tayari kutoa maeneo yao kwa ajili upanuzi wa maeneo ya zahanati hizi.
Je, Serikali ipo tayari kusaidiana na Halmashauri ya Ilala kulipa fidia kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa maeneo ili kupata zahanati na vituo vikubwa vya afya katika maeneo ya Jimbo la Segerea na Manispaa ya Ilala kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema katika jibu letu la awali, mahitaji ya afya hapa yamekuwa ni changamoto kubwa sana, nilipofanya reference tulipokuwa na Mbunge wa Segerea kipindi kilichopita, alipokuwa na timu iliyoenda eneo la Vingunguti katika machinjio yale, vilevile akaja katika ofisi yangu kuona jinsi gani tutafanya, licha ya suala la machinjio lakini wananchi wana changamoto ya afya.
Mheshimiwa Spika, mimi naamini hayo mawazo ni mazuri, tutakaa vizuri kubadilishana mawazo ili tuone ni jinsi gani tutafanya ujenzi wa zahanati au kituo cha afya maeneo yaweze kupatikana. Lengo kubwa ni kwamba kina mama na watoto wa maeneo yale waweze kupata huduma kama wengine.
Mheshimiwa Spika, ajenda yetu kubwa ni kuhakikisha kwamba hospitali zetu za rufaa sasa tupunguze idadi ya wagonjwa siyo mtu anaumwa mguu mpaka aende Muhimibili au Amana haiwezekani hata kidogo. Lazima tuhakikishe mfumo mzuri unatengenezwa katika sekta ya afya katika ngazi za chini kusaidia sekta za juu ziweze kufanya huduma kubwa zinazohitajika.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, swali la Kigoma Kaskazini linafanana kabisa na swali la wananchi wa Segerea na Ukonga. Wananchi wa Kipunguni A, Kipunguni Mashariki, Kipawa na Kigilagila waliambiwa wapishe maeneo yao kwa ajili ya ujenzi au upanuzi wa uwanja wa ndege. Wanachi hawa wamefanyiwa tathmini tangu mwaka 2007, imekuwa ni danadana, sasa Waziri atuambie ni lini wannachi hawa watalipwa fidia baada ya kuwa wanapewa pesa kidogo wanaambiwa watalipwa na siku zinakwenda na wanashindwa kuendeleza maeneo yao.
Je, ni lini, fidia hizo zitalipwa na hawa wananchi waweze kupata maeneo mengine ya kujisitiri? Wananchi hao wanamsikia. Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Segerea anafahamu kwamba tulikaa kikao…

Naomba nipewe fursa ya kujibu swali.
Mheshimiwa Mbunge wa Segerea alishafanya kikao na mimi mwenyewe kuniita, katika kikao hicho nilikutana na wahusika wote wanaotakiwa kulipwa fidia katika eneo la Kipunguni. Kwa hiyo, namshukuru sana, kwanza Mheshimiwa Anatropia kwa kumuunga mkono Mbunge mhusika katika eneo hili na Mbunge mhusika katika eneo hili anafahamu kwamba nimeshatoa ahadi ya kuhakikisha suala la kulipa fidia eneo la Kipunguni kwa ajili ya kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege nitalishughulikia na litafikia mwisho katika kipindi hiki cha miaka mitano na anafahamu sababu yake.
Mheshimiwa Spika, sababu yake ni kwamba kuna fedha ilishatolewa, lakini kuna uwezekano fedha zilizotolewa zote hazikuwafikia walengwa. Kwa hiyo, tumeunda Tume inafanya uchunguzi wa suala hili kuhakikisha zile fedha zilizotakiwa kuwafikia walengwa tujue zimeenda wapi na tutafunua kila palipofunikwa kuhakikisha fedha zile zilizokusudia kulipa wahanga wale zinapatikana na hatimaye wahanga walipwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilimhakikishia Mbunge mhusika wa hilo eneo na sasa naomba nimhakikishie Mheshimiwa Anatropia, suala hili tumelichukua kwa nguvu na tutalishughulikia, tutafukua kila aina ya kaburi kuhakikisha kwamba wahusika wanalipwa fidia iliyostahili. Nilitoa katika mkutano ule wa wadau kwamba ni katika kipindi hiki cha miaka mitano.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia leseni za kufanya biashara katika Manisapa mbalimbali zinatolewa baada ya kupatikana kwa tax clearance, lakini ukweli ni kwamba sio biashara zote hasa biashara ndogo zinahitaji wakati mwingine tax clearance, haioni ni wakati muafaka kuweka categories za biashara ambazo wanaweza kupewa leseni bila hata tax clearance badala ya kinachofanyika sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hili ni swali la kutoa leseni ambalo ni swali jipya ambalo tumeondoka katika riba, kwa hiyo naomba niseme tu tuna viwango ili kuweza kutoa leseni katika biashara zote zinazoendeshwa ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, kama hawajafikia ndani ya kiwango kile kinachohitajika mfanyabiashara huyo wala hatozwi na wala hapewi leseni lakini akishavuka yale malengo ya biashara yake tayari anatakiwa apewe leseni na tunasimamia kama moja ya njia za kukusanya mapato yetu.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa taarifa zinaeleza kwamba, vyeti vimekuwa vikizalishwa nje ya nchi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzalisha vyeti hapa nchini ili zoezi la kuvitoa liwe rahisi zaidi? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizonazo mimi vyeti vinatengenezwa hapa hapa nchini, tuna vifaa vya kisasa, Baraza la Mitihani lina vifaa vya kisasa sana na ni taasisi ambayo kwa ufanisi wake nchi nyingi sasa hivi zimeanza kuja kujifunza namna tunavyofanya. Kama Mbunge ana taarifa tofauti na hizi naomba tuonane baada ya Bunge hili ili nijue kwa nini yeye ana taarifa ambazo si sahihi.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo changamoto kubwa sana ya barabara kutokana na mitandao ya maji na hasa katika kata mbalimbali za Jimbo la Segerea ikiwemo Kata ya Vingunguti; je, ni kutokana na ubovu wa mabomba ndiyo maana tunazidi kuona maji yanazidi kutiririka hovyo katika maeneo haya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, changamoto hiyo ipo. Kama tunavyokumbuka, wakati nilipotembelea barabara ya Kwa Mnyamani kutoka hapa Buguruni barabara ya Kwa Mnyamani kwenda Vingunguti, barabara ile muda mwingi sana maji yamejaa barabarani’ Tatizo kubwa ni kwamba yale mabomba yanapasuka kwa hiyo yanajaa barabarani na barabara inaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana nilitoa agizo pale kwamba Manispaa yetu ya Ilala, TARURA pamoja na DAWASCO waweze kukaa pamoja kuangalia ile miundombinu yote ambayo iko barabarani iwekwe vizuri. Bahati nzuri zoezi hilo limekamilika, hivi sasa linaendelea vizuri, niwashukuru sana DAWASCO, pia niwashukuru Manispaa ya Ilala kwa kazi kubwa waliyofanya, na hivi sasa hata ile barabara tunaiboresha, sasa itakuwa kwa kiwango cha lami yote kuanzia hapa Buguruni tunapoingilia mpaka unafika Vingunguti.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limefanyika shirikishi, kwamba maeneo hayo sasa yawe yanapitika vizuri, vilevile na mitandao ile ya maji ambayo inachanganyana sana wataalam nimewaagiza waiweke vizuri kuhakikisha kwamba tunalinda barabara zetu hizi. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Majibu ya Naibu Waziri tumeyasikia wakati wote. Mradi wa mfereji anaousema wa DMDP ni mradi ambao tumeambiwa utatekelezwa tangu mwaka 2014 na wakazi wa kata zinazopitiwa na mradi huo waliambiwa wasiendeleze maeneo yao tangu 2014 wakiendelea kuhangaika na mafuriko kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna changamoto ya madaraja na barabara Kata ya Bonyokwa, Kata ya Kinyerezi, Kata ya Segerea, Kata ya Liwiti na kubwa kuliko ni Kata ya Tabata katika barabara ya kwenda Mwananchi, kalvati limebomoka na kwa sasa ninavyoongea…

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali; je, ni lini mradi huo mkubwa wa DMDP utajengwa na barabara au Daraja la Kisiwani? Swali la kwanza.
Swali la pili, uanzishwaji wa TARURA umeondoa uwajibikaji wa Halmashauri sambamba na Madiwani moja kwa moja katika ujenzi wa barabara za mitaa. Je, Wizara ina mkakati gani kuhuisha kazi za TARURA ili waweze kutoa report katika Baraza la Madiwani ambalo moja kwa moja ndiyo wanawajibika kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujua kero zao za moja kwa moja za barabara? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Theonest amesema imekuwa ni muda mrefu hadithi imekuwa ikisemwa, lakini utakubaliana nami kwamba katika majibu yangu kwenye swali la msingi, nimemwambia kwamba kandarasi tunatarajia itatangazwa mwezi Mei na mwezi Mei siyo mbali sana, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumeahidi tutatekeleza katika hili ambalo nimelisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameongelea juu ya suala zima la uanzishwaji wa chombo hiki cha TARURA na anachoomba ni namna gani TARURA watahuisha ili wananchi waweze kupata ushiriki wao kwa kupitia Waheshimiwa Madiwani na Wabunge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ina wajibu wa kuhakikisha kwamba taarifa zake zinapelekwa DCC na DCC Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe, lakini Mwenyekiti au Meya ni Wajumbe na Wakurugenzi ni Wajumbe. Kwa hiyo, taarifa itakuwa inatolewa hapo na tutapata fursa ya kuweza kuwahoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, pia kwenye chombo cha RCC ambapo sisi Waheshimiwa wote ni Wajumbe, naomba tushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijaribu kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla ya kuanzishwa kwa TARURA kila Mbunge na hasa kila Diwani alikuwa anaomba apate angalau hata kilomita moja ya kipande cha barabara au kalavati litengenezwe upande wake kiasi kwamba ule ufanisi (value for money) ilikuwa haionekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukienzi chombo hiki, bado ni mapema kabisa. Maeneo mengine ambayo TARURA imeanza kufanya kazi, wanapongeza. Naomba tukiunge mkono. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nadhani waliomwandikia Mheshimiwa Naibu Waziri hawakunielewa vizuri. Swali langu nimeuliza hivi, ni kwa kiwango gani barabara za mitaa ina maana kutoka barabara ya Segerea kwenda Mandela road tutaweza kupunguza foleni. Kwa maana tutafungua vipi barabara za mtaa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameainisha kwamba wametenga fedha ya ujenzi wa barabara kutoka Barakuda
- Chang’ombe, sasa ukitoka Barakuda - Chang’ombe bado hawajapunguza foleni. Wangesema kutoka Barakuda - Chang’ombe - Kimanga ili wananchi wapite Kisiwani wasiingie Mandela road. Vivyo hivyo kutoka Kinyerezi - Kimara watu waingie Morogoro road wasirudi barabara ya Segerea, tuna changamoto sana ya foleni. Vivyo hivyo …
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ni lini barabara ya Segerea itapunguziwa foleni kwa kuboresha barabara za mitaa zinazotoka na siyo kurudi barabara kwenye moja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wamesema wametenga fedha kwa ujenzi wa daraja wa Tabata Kisiwani. Namwomba Naibu Waziri aje tumuonyesha daraja hilo kwa sababu lina changamoto kubwa. Matajiri wamevamia eneo, daraja haliwezekani kwa sababu mkondo ni mdogo. Ni lini atakuja kuona changamoto ili kuwaondoa wale watu tuweze kujenga daraja pale? Vinginevyo ni kupoteza fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeeleza barabara ambazo zinatengenezwa na tafsiri yake ni nini? Mwananchi ambaye alikuwa anataka kwenda Segerea ana-option ya kutumia barabara ya zingine na ambacho kimekuwa kikitokea ni kwamba hizi barabara zikiwa mbovu sana hata ambaye angeweza kupita kwa Mnyamani hawezi kupita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kadri barabara hizi zingine zinavyotengenezwa inampa nafuu mwananchi wa maeneo hayo. Si kwamba gari zote ambazo zinazopita huko wanataka ni kwa sababu barabara za mtaani zinakuwa siyo nzuri. Aidha, kwa Jiji la Dar es Salaam kuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba tunali-decongest, mpango uko vizuri, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira hilo liko mbioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na daraja ambalo analizungumzia na kuuliza nitakwenda lini, weekend iliyopita nilienda nikafika mpaka Mnyamani bahati mbaya tu Mheshimiwa Mbunge hakuwa na taarifa. Mimi niko tayari kwenda kwa kadri nafasi itakavyoruhusu ili tukatizame site kuona nini kilichopo ili tuweze kushauri vile ambavyo inatakiwa.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niweke rekodi sahihi; swali langu halijajibiwa, nimeuliza kilometa tano za lami zilizoahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika Kata ya Kyerwa. Hii ni kata ya mjini, ina wafanyabiashara wengi, ina shughuli nyingi za kibiashara lakini watu wanateseka na adha ya vumbi inayosababisha ajali mbalimbali za mabasi, boda boda na magari mengine.
Swali ni lini kilometa tano alizoahidi Mheshimiwa Rais katika Kata ya Nkwenda – kata ya kibiashara – zitajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tumeshuhudia taharuki na bomoa bomoa katika Kata hii ya Nkwenda ambayo hatuoni kama imetengewa bajeti lakini bomoa bomoa na X zinaendelea. Swali, wale wanaowekewa X na kubomolewa nyumba zao watapewa fidia kwa kuwa hakukuwa na ramani ya mpangomji na ramani sasa inawafuata watu wakiwepo pale; watapewa fidia katika maeneo yao ambayo yanakwenda kupitiwa na bomoa bomoa ya ujenzi wa barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi, unapoanza kujenga kilometa tano ukaanza na kilometa moja tayari ulishaanza ujenzi kuelekea kilometa tano ambazo Mheshimiwa Rais ilikuwa ahadi yake. Kwa hiyo, nimemhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo wajibu wake ni kutekelezwa ndani ya miaka mitano na kuhakikisha kwamba ahadi hizo zinatekelezwa ndiyo maana tunaanza na kilometa moja. Ukijenga kilometa moja katika tano zinakuwa zimebaki kilometa nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia anauliza juu ya wananchi kulipwa fidia. Sheria iko wazi, kwa wale wananchi ambao wameifuata barabara ambayo; hatuwezi wakati huo huo tukataka maendeleo na wakati huo huo tukataka tubaki katika hali ile kabla ya maendeleo. Kwa hiyo, kwa wale ambao wameifuata barabara hawatalipwa na wale ambao barabara imewafuata watalipwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa ukataji wa leseni unaenda sambamba na uwasilishaji wa tax clearence katika Halmashauri zetu na uwasilishaji wa tax clearance unaamaanisha kwamba watu wamelipa kodi, kwa maana hiyo watu wanalazimika kulipa kodi kabla hata ya kufanya biashara. Je, hatuoni kwamba ni muhimu kuondoa kigezo cha tax clearance katika baadhi ya biashara ili watu waweze kukata leseni na kuanza biashara kabla ya kulipa kodi na kabla ya biashara zenyewe kuanza? (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake linalenga kujaribu kutetea wafanyabiashara wale wanaoanza na utetezi wa aina hiyo siyo mbaya, ni mzuri. Hata hivyo, kwa sababu kuna kanuni, sheria na taratibu ambazo zimewekwa, nalichukulia swali lake kama mchango wa maoni ambao unahitaji kufanyiwa kazi baadaye lakini kwa leo hatuwezi kutoa tamko kwamba sasa tunafuta taratibu hizo. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru swali la nyongeza la kwanza, ni ukweli kwamba idadi ya akinamama wanaoendelea kujifungua kulingana na takwimu inaendelea kuongezeka, lile jengo kusema ukweli bado ni finyu sana kiasi cha kupelekea akinababa kushindwa kuandama na wenza wao, kinyume na alivyosema Naibu Waziri. Sasa swali langu sio kweli kwamba jengo lile haliwezi kubadilishwa, jengo linaweza likaondolewa likajengwa ghorofa angalau moja au likajengwa ghorofa moja sehemu nyingine Serikali ipo tayari kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga eneo angalau la ghorofa moja kuweza kuwa-accommodate watu hawa ambao wanabanana kwenye corridor?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kujifungua ni tendo la faragha sana, wote mtajua Madaktari akinamama wanavyoenda kwenye hicho kitendo wengine wanaweza kutoka vinyesi, wengine wanapata kifafa cha mimba, wengine wanatokwa na maneno ya ajabu na shida nyingine kama hizo ambao wamepitia uzazi wanajua, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza vyumba ambavyo concrete au ku-separate vile vitanda na concrete au kujenga partition ambazo mwanamke mmoja na mwingine hawawezi kuonana tofauti na ilivyo leo kwamba mmeweka pazia ambazo kiukweli wanaonana na inadhalilisha utu wao. Naomba sasa Serikali ituambie ni lini ipo tayari kutengeneza partition kwa ajili ya kustiri utu wa mwanamke pale anapokwenda kujifungua.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Anatropia. Kwanza suala kwa nini tusiongeze jengo lingine Muhimbili Mheshimiwa Mbunge alitakiwa kutushukuru kwa sababu lile ni jengo la ziada, baada ya Mheshimiwa Rais mara tu baada ya kuapishwa alikuta mrundikano wa wangojwa akatunyang’anya ofisi Wizara ya Afya na jengo lile tukaliboresha na kuwa ni jengo la Wazazi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru umenipa fursa ya kujibu hili swali. Muhimbili National Hospital, tumefuta kliniki za mama na mtoto katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Muhimbili. Pale tunapeleka wajawazito ambao wana matatizo ya kujifungua. Kwa hiyo hata ule mrundikano wa wagonjwa wataenda Mwananyamala, wataenda Amana, wataenda kwenye vituo vya afya 350 ambavyo Serikali imeviboresha ili kuviwezesha kutoa huduma. Nitoe wito kwa wanawake, Muhimbili ni National Hospital sio mtu yoyote unaenda tu kwa ajili ya chek up.

Mheshimiwa Spika, suala la pili anataka partition, Mheshimiwa Mbunge angetembelea vituo vya afya tunavyojenga, asingeuliza hili swali, tunajenga kwa kuhakikisha tumeweka partition kwa vituo vya afya vyote. Lengo letu sisi anachosema ufaragha, tunafikiria iliwezekana hata baba amsindikize mama anapotaka kwenda kujifungua. Kwa hiyo tumeliona kama Wizara na tumeweka partition zenye staha katika vituo vya afya.