Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Cecilia Daniel Paresso (12 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyoko mezani. Nianze kwa kusema Serikali nyingi duniani huongozwa kwa Katiba iliyojiwekea, Sheria zilizopo, Kanuni zilizopo, Taratibu zilizopo au Dira
ambayo imejiwekea kama nchi, lakini katika Serikali ya Awamu ya Tano tunaona mnaongozwa
kwa kauli mbiu ya hapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtanielewa tu! Nasema mnaongozwa kwa hapa kazi, bila kufuata Sheria zilizopo, Kanuni zilizopo, utaratibu uliopo na Katiba mliyojiwekea. Nasema haya kwa mifano nitakayoitoa; Rais anafukuza watumishi wa umma! Ni kweli kwamba kuna baadhi ya watumishi wa umma sio waaminifu na wana upungufu. Pia, ni kweli kwamba kuna baadhi ya watumishi wako kwenye mamlaka ya Rais, wale aliowateuwa anaweza kuwaondoa, lakini kuna wale ambao wameajiriwa, ni sharti taratibu na sheria za kiutumishi zifuatwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine; mmesema mnatoa elimu bure, mtapeleka takribani shilingi bilioni 18 kwa Halmashauri! Mnapeleka kwa bajeti ipi ambayo hatujapitisha ndani ya Bunge? Bunge la Kumi, tulipitisha Bajeti, ni lini mmeleta Supplementary Budget ndani
ya Bunge, ili mtekeleze hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine, Rais alifuta sherehe za Uhuru! Ni kweli kwamba katika Bunge la Kumi kati ya mambo ambayo Upinzani tulikuwa tunapigia kelele, ni kufuta sherehe mbalimbali ambazo hazina tija, ni jambo jema. Amefuta sherehe za Uhuru akatoa agizo fedha zipelekwe kwenye ujenzi wa barabara ya Morocco; amefanya fedha hizo zimekwenda, taratibu za manunuzi, kutangaza tender, Sheria mliyojiwekea ya Manunuzi, mmefuata au mnasema tu hapa kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kupitia vyombo vya habari, jana au juzi, Afisa mmoja wa Serikali amesema watapeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji! Nawauliza kwa Bajeti ipi? Kwa Sheria ipi? Kwa Supplemantary Budget ipi mliyojiwekea? Au mnaongozwa tu kwa hapa
kazi, bila kufuata sheria zilizopo? Mtakuwa ni Serikali ya ajabu duniani kuongozwa na kauli mbiu badala ya sheria mlizojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hotuba ya Rais ameelezea kwa upana suala la amani na utulivu na mmekuwa mkijivunia amani na utulivu. Mnawaambia Watanzania kuna amani na utulivu, wakati hakuna demokrasia ndani ya nchi hii, demokrasia zinaminywa zinakanyagwa.
Kuna migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, halafu mnasema amani na utulivu! Hakuna ajira kwa vijana, halafu mnasema amani na utulivu! Mahakama hazitoi haki kwa wakati, halafu mnasema amani na utulivu! Hospitalini hakuna dawa, kinamama wakienda kupata huduma
zipo mbali au wakati mwingine hazipatikani, mnasema amani na utulivu! Tumeona utumiaji wa nguvu za kidola wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi, halafu mnasema amani na utulivu!
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itafika mahali Watanzania hawatathubutu tena kuvumilia amani na utulivu wakati wana shida lukuki! Hakuna haki, watu wanakandamizwa, watu wananyanyaswa, halafu mnang‟ang‟ania kusema amani na utulivu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie machache kwa kusema katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ameelezea hali ya kisiasa Zanzibar. Hili tunamwambia nalo ni jipu alitumbue, alifanyie kazi! Mshindi atangazwe! Si mmesema ninyi hapa kazi! Fuateni basi Sheria, Katiba na Taratibu mlizojiwekea. Mtangazeni mshindi wa Zanzibar, kwa nini mnaogopa? Mkiambiwa hili mnaogopaogopa na mnaanza kupiga-piga kelele, kuna nini kimejificha hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka suala la mgogoro wa kisiasa, kama amesema yeye atakuwa ni Rais wa kutumbua majibu basi atumbue na hili, Wazanzibari wapate haki yao waliyemchagua aweze kutangazwa. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora na Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba ni ukweli usiopingika hali za Halmashauri zetu nchini kwa ujumla wake ni mbaya sana. Halmashauri hizi zina hali mbaya kwa sababu nyingi zimekuwa tegemezi na kwa asilimia kubwa zinategemea fedha kutoka Serikali Kuu. Halmashauri zetu hizi pia vyanzo vile muhimu ambavyo vingewezesha mapato ya Halmashauri zetu kuongezeka, kwa kiwango kikubwa vimechukuliwa pia na Serikali Kuu. Kwa hiyo, tumeziacha Serikali zetu za Mitaa katika hali ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kuna uhaba mkubwa wa watumishi katika Serikali za Mitaa kwa maana ya rasilimali watu. Takwimu zinaonesha tuna uhaba wa watumishi 43,560 katika idara 470 za Halmashauri zetu nchini, huu ni upungufu mkubwa sana. Kama kuna upungufu huu mwisho wa siku hata ufanisi wa fedha zinazopelekwa unakuwa hauonekani au haupo kabisa au ufanisi unakuwa kwa kiwango kidogo sana.
Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikaangalia ni namna gani wanakwenda kupunguza uhaba wa watumishi walioko katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine unapoongelea suala la Serikali za Mitaa huwezi kuwaacha Madiwani pembeni. Ni kwa muda mrefu Serikali mmewatelekeza Madiwani si kwenye maslahi, si kwenye kujengewa uwezo, Madiwani maslahi yao yanaboreshwa kwa kiwango kidogo sana. Ukiangalia sisi Wabunge hatuna utofauti sana na Madiwani lakini tunawaacha Madiwani na sisi tukiwa Bungeni muda mrefu wanaotufanyia kazi kwa kiwango kikubwa na kutusaidia ni Madiwani. Ni muhimu sana Serikali ikaangalia namna gani maslahi ya Madiwani yanaboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si maslahi tu, wakati wa awamu iliyopita walifuta mafunzo (capacity building) kwa Madiwani. Hivi unampeleka Diwani akamsimamie Mkurugenzi na watendaji wake ambao wao ni wataalam wa mambo fulani fulani halafu Madiwani wetu wamechaguliwa tu kwa kigezo cha kusoma na kuandika, hana ujuzi wowote, baadhi lakini wako wengine ambao wana ujuzi lakini walio wengi hawana ujuzi huo, hivi kwa nini Serikali isiirudishe ile programu ya kuwajengea uwezo Madiwani kwa kuwapatia mafunzo. Mimi nilikuwa Diwani, nakumbuka kulikuwa kuna programu ya kuboresha Serikali za Mitaa, tulikuwa tunapelekwa mafunzo ya miezi sita lakini inakwenda kwa awamu, ilitusaidia kutujenga na kusimamia zile fedha zinazopelekwa. Kwa hiyo, ni muhimu pia mkalitazama hili muone namna gani Madiwani wanarudishiwa hizo programu za kujengewa uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia kuhusu TAMISEMI ni udhaifu mkubwa ulioko katika usimamiaji wa Bajeti na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa. Kuna udhaifu mkubwa sana, udhaifu huu unaendana na bajeti zilizoidhinishwa kutokufuatwa na hizi bajeti wakati mwingine hazifuatwi kwa sababu ya matamko ya viongozi mlioko ngazi za juu na mlioko katika Serikali Kuu. Mfano, Halmashauri 34 zimetumia kiasi cha shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Hakuna mtu anayepinga au anakataa umuhimu wa maabara, umuhimu wa maabara unajulikana lakini ujenzi huu na fedha hizi zimetokana na tamko lililotolewa na Rais bila kuangalia wakati huo anatoa tamko kwenye bajeti za Halmashauri za Wilaya fedha hizi zipo? Kwa hiyo, inaonesha kuna shilingi bilioni 33 zimetumika kinyume na bajeti eti kujenga maabara katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, kuna takriban upotevu wa shilingi bilioni nane kwa ajili ya malipo yaliyofanywa na Serikali za Mitaa bila kuwepo na nyaraka za malipo. Pia kuna Halmashauri 62 zimefanya malipo ya shilingi bilioni 1.4 kinyume na vifungu vilivyopitishwa katika bajeti. Sasa kama Serikali hizi za Mitaa hazifuati bajeti ambayo imejiwekea hakuna sababu ya kupitisha bajeti au kama kuna matamko yanayotolewa bila kuangalia uhalisia wa Serikali zetu za Mitaa hakuna sababu ya kuwa na Serikali za Mitaa kama hatutambui na kuthamini yale ambayo yanayopitishwa katika bajeti zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti ya CAG anasema watekelezaji wa miradi 76 walifanya matumizi nje ya bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 4.6. Yote ni kukiuka bajeti waliyojiwekea, yote ni kukiuka Sheria ya Fedha ambayo ipo. Wanasema matumizi mengine yalifanywa nje ya bajeti na yameongezeka, CAG anasema matumizi nje ya bajeti yameongezeka kwa asilimia 224. Kwa hiyo, haya ni mambo ya kuyaangalia na kuyasimamia kuona yanaondoka katika Serikali zetu za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo lingine la elimu bure. Mmesema mnatoa elimu bure, lakini nilidhani mngepaswa kujiridhisha na kuangalia hivi ni kweli mnaweza kutoa elimu bure au mlikurupuka tu mkachukua Ilani yetu na yenyewe mkaweka kwenye Ilani yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, kuna watu wamefanya tafiti, wanasema ili uweze kutekeleza elimu bure unahitaji takriban shilingi bilioni 715 kwa mwaka mmoja wa fedha. Ili uweze kutekeleza elimu bure maana yake unahitaji mambo makuu manne; jambo la kwanza ni kutoa ile ruzuku ambayo ilikuwa inatolewa ya shilingi 10,000 kwa shule za msingi na shilingi 25,000 kwa shule za sekondari. Kama ile ruzuku mmeamua kuitoa kwa sababu mnasema ni elimu bure maana yake Serikali inahitaji karibia shilingi bilioni 130 kwa shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kama mnaondoa ada ya shilingi 20,000 kwa watoto wa sekondari, Serikali inahitaji kuwa na shilingi bilioni 31.5 ili kufidia ada hiyo. Hivi hizi fedha hizi mnazo? Si huwa mnasema kasungura kadogo? Safari hii kamenenepa? Nadhani mnapaswa kuangalia haya mliyoyasema ya elimu bure hivi mnakwenda kutekeleza? Halafu mmetoa Waraka mwingine Na. 5 wa elimu mnasema kama wanataka wapate kibali kwa Mkuu wa Mkoa, sasa kwa nini hizi contradiction, si mmesema elimu bure? Basi acheni bure mbebe huo mzigo, mtafute fedha hizi mwende kutekeleza elimu bure ambayo mnataka kuitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa haraka ni kuhusu Mfuko wa Vijana na Wanawake. Waheshimiwa Wabunge wengi tunachangia kwamba tuhakikishe Serikali za Mitaa zinatenga ile 10 percent kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake lakini lazima kidogo twende mbali ya hapa. Mifuko hii ukiangalia mwongozo wake na mwongozo huu ulipitishwa na Bunge hili mwaka 1991, ni mwongozo wa zamani ambao hauendani na uhalisia wa leo.
Katika Bunge la Kumi niliuliza Swali Na. 379 kuitaka Serikali i-review ule mwongozo wa kuanzisha Mifuko ya Vijana na Wanawake, ni mwongozo wa zamani sana kwa sababu unasema kikundi cha watu watano watapewa mkopo wa shilingi 500,000. Hivi unawapa mkopo wa shilingi 500,000 kwa watu watano, shilingi laki moja moja inasaidia nini, haisaidii kitu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni vizuri mkaangalia tena kwa upya namna gani ya kuu-review mfuko huu uendane na hali halisi iliyoko katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, kuna Mfuko wa TASAF. Mfuko wa TASAF ni mkopo kutoka World Bank ambao ni dola za Kimarekani milioni 200 lakini fedha hizi zinakwenda kupewa watu kwenye kaya, wanasema kaya maskini na kwenye kaya maskini wanaangalia vigezo mbalimbali kama kuna wategemezi na vitu kama hivyo na kwenye kila kaya range ya fedha hizi ni kati shilingi 20,000 mpaka shilingi 62,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuwakwamua watu wetu kutoka kwenye hali mbaya ya umaskini hivi ni kuwapa fedha mkononi? Kwa sababu ukimpa fedha mkononi itamsaidia nini? Kwa sababu hizo hizo Kaya maskini wakati mwingine hata mlo kwa siku ni taabu, ukimpa shilingi 20,000/= unamwendelezaje aondokane na huo umaskini? Kwa hiyo, ni muhimu mkaangalia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na mifuko mingi ambayo mwisho wa siku hatuoni manufaa yake.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha hotuba yake nzuri inayoonesha mwelekeo mzuri wa kuletea maendeleo Taifa letu. Pia nimpe changamoto kwamba ajitahidi kwa sababu Wizara hii ndiyo Wizara ambayo iko kwenye kioo cha kila mtu. Kwa hiyo, akifanya kweli ataonekana na asipofanya ataonekana hata kabla ya kuja hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia kuhusu hali ya anga la Tanzania. Kwa uono wangu kimataifa tunajulikana Tanzania tuna anga la Tanzania, hakuna anga la Zanzibar wala anga la Tanzania Bara. Hivyo basi, ni muhimu tunavyotoa huduma za anga tuzijenge kulenga kufanikisha kwa sifa ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na mawasiliano ya muda mrefu kati ya TCAA na Mamlaka ya Kiwanja cha Ndege cha Zanzibar. Kiwanja hiki kwa muda mrefu hakijafungwa kifaa cha Instrument Landing System (ILS) ambacho kilikuwa kifungwe kipindi cha miaka minne, mitano iliyopita, kila siku ahadi inakuwa kitakufungwa. Kweli huduma za ndege zinaendelea lakini hiki ni kifaa muhimu kinachowasaidia marubani kutua wakati wa usiku, mawingu na mvua kwa uhakika na usalama zaidi.
Niombe basi Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie kama hili jukumu si la TCAA, ni bora watoe kauli dhahiri inayosema kwamba hiki kifaa hawatakifunga na hakiwahusu ili sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iweze kuchukua jukumu la kutafuta hicho kifaa na kukifunga kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri vitu kama hivi vikawa vinatupwa kama mpira. Ni bora kuambizana ukweli ili kila mtu afahamu jukumu lake, lakini litekelezwe ili kuleta ufanisi wa kazi tunazozifanya za kila siku. Tukipata sifa ya anga, nasema mara ya pili, ni sifa ya Tanzania na likitokea tatizo bado mamlaka hizi zitahusika na kutakiwa kujibu maswali ambayo kwa kweli nahisi hayatakuwa muhimu na ya msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nichangie hilo lakini nimkumbushe Mheshimiwa Waziri akisaidie kiwanja hiki cha ndege cha Zanzibar. Nakumbuka lilitolewa jibu lakini nimsisitize tu awasaidie kulipwa lile deni lao la shilingi milioni 230 na ATC. Tunasikia au tumeambiwa madeni yatahamishiwa Hazina, lakini nimuombe tu alipe uzito ili kuwasaidia wenzetu hawa kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba dakika tano na nahisi zimenitosha kwa kuchangia jambo hili muhimu sana. Na mimi naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini kuna mabonde yenye mchanga ambapo siku za awali (nyuma) umiliki huo ulikuwa chini ya vijiji husika na kuwezesha vijiji hivyo kupata mapato.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, Wizara ya Nishati na Madini imebadili utaratibu huo na kukabidhi mabonde hayo kwa mawakala mbalimbali ambao wamekuwa wakitoza tozo tofauti kwa kila eneo na wakati mwingine mawakala hawa hutoza tozo hizi katika barabara kuu kwa kuweka road blocks kwa kushirikiana na askari wa barabarani. Kwa kuwa utaratibu wa tozo hizo ni chanzo cha mapato ya Halmashauri za Vijiji na wameweka katika by laws zao; na kwa kuwa utaratibu huo mpya haujawashirikisha vijiji husika, je, Serikali haioni upo umuhimu wa kupitia upya utaratibu huu kwa manufaa ya Serikali za Vijiji hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Karatu ni mji wa utalii kwa kuwa ni lango kuu la kuingilia Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro. Tukitambua mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika nchi yetu lakini baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Karatu havina umeme. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Buger, Gongali, Endamanghang, Kansay na baadhi ya vijiji katika Mji wa Karatu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, Wizara imeeleza kwamba inafanyia mapitio ya Sera ya Ardhi ya mwaka 1995. Mapitio haya yatakuwa hayana maana kama Wizara haitajikita kuimarisha mfumo wa utendaji wa vyombo vya usimamizi wa ardhi katika nchi hii. Hapa tunaongelea Serikali za Vijiji, pamoja na mabaraza yake ya ardhi maana yake hata kama ukiwa na sera lakini hujaviwezesha vyombo hivi ukavipa rasilimali fedha, ukavipa rasilimali watu, sera yao wanayokwenda kurekebisha itakuwa haina maana.
mamlaka hizi za usimamizi wa ardhi katika nchi yetu na kuimarisha mfumo mzima wa utendaji wa Wizara katika maeneo mbalimbali. Pamoja na marekebisho hayo ni muhimu tukaangalia masuala mazima ya wawekezaji au baadhi ya wawekezaji na viongozi na wanasiasa kuhodhi maeneo makubwa kinyume na taratibu au kuihodhi kwa kufuata utaratibu lakini wameya-damp na hawayaendelezi ni muhimu sana hili likatazamwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wawekezaji wengi baadhi yao wana-forge muhtasari wanalaghai Serikali zetu za Vijiji, wanahodhi maeneo na wanayatumia maeneo hayo kwenda kukopea benki na kudanganya au kudanganya kwamba wana mitaji lakini hawana mitaji, wanatumia ardhi hiyo kwenda kukopa benki wanafanya biashara nyingine wanatelekeza zile ardhi. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara ikatazama kwa ujumla wake suala zima la hawa wawekezaji, baadhi yao wamekuwa ni wadanganyifu wakubwa wakitumia ardhi zetu vibaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna baadhi ya wawekezaji wanabadilisha matumizi ya ardhi kinyume na hati miliki zao zinavyoeleza, kuna wawekezaji wanapewa kwa ajili ya kilimo, anakwenda kubadilisha. Nimpe mfano Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Karatu, kwa taarifa ambayo tumeletewa kwenye Baraza la Madiwani kuna mashamba ambayo yanamilikiwa na wawekezaji, yametembelewa mashamba 18 ambayo yana jumla ya hekari 13,985 wengi wao mashamba haya wamepewa kwa ajili ya kilimo cha kahawa, lakini wako baadhi wamebadilisha matumizi wamejenga hoteli kubwa za kitalii, hatuna uhakika kama wamefuata taratibu za sheria za kuomba kubadili matumizi ya ardhi ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya ardhi ile inaonekana ni kilimo, lakini wako wengine wamejenga hoteli za kitalii maana yake ni nini? Maana yake ni pia wanaikosesha Serikali mapato, anakwenda kulipa tu kwa sababu inaonekana hati yake ni ya kilimo lakini amejenga hoteli kubwa ya kitalii analaza wageni, anapata fedha za kutosha. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara ikafanya uhakiki kutembelea mashamba, ambayo jumla yako mashamba 32 ndani ya Wilaya ya Karatu yakabaini ni watu gani ambao wamekiuka taratibu za kisheria katika umiliki wao wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika hao wawekezaji wenye mashamba 32, wako wengine wameyatelekeza mashamba, wako wengine wameyaacha, wamehifadhi halafu kuna wananchi wengi pembezoni pale hawana hata maeneo ya kuzika. Mheshimiwa Waziri ningetamani aje karatu aone. Yako mashamba yanamilikiwa na Wahindi, wananyanyasa watu, wanadiriki kuwaambia hata kaya zinazokaa pale, ni marufuku kuzaana eti kwa sababu wataongeza idadi, huu ni unyanyasaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana Mheshimiwa Waziri afike, aone jinsi gani wananchi hawa, hawana hata maeneo ya kuzikana sasa wananchi wanakuwa watumwa katika nchi yao, haiwezekani! Hatuwezi kuthamini wawekezaji, hatuwezi kuthamini watu hao tukawapuuza wananchi wetu ambao ni damu zetu. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, suala hili liondoke na wananchi hawa wapate haki yao, wapate maeneo angalau hata kuweza kuzikana katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka niongelee ni kuhusu migogoro ya ardhi. Migogoro hii ya ardhi imekuwepo kwa muda mrefu na migogoro hii mara nyingi ni kati ya wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi, vijiji na vijiji na kadha wa kadha kama ambavyo imeoneshwa katika hotuba yetu ya Kambi ya Upinzani. Pamoja na kwamba bado tuna migogoro lakini imepungua sana, lakini inawezekana ikaendelea kuibuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii pamoja na sheria tulizonazo, lakini ni lazima Serikali ijikite katika kuimarisha vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi na lazima Serikali iangalie namna bora ya kumaliza migogoro hii ya ardhi kwa njia shirikishi na kutumia mila na desturi za maeneo mbalimbali. Hatuwezi tu kusema wakati mwingine tunafuata sheria kama ilivyo, kwa sababu mkisema mnafuata sheria kama ilivyo, ndiyo mnaua watu, mnajeruhi watu, mnafukuza watu, wakati mwingine busara itumike kwa kutumia mbinu shirikishi ya kuondoa migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano migogoro ya wakulima na wafugaji inaweza wakati mwingine kusuluhishwa kwa kutumia, mila na desturi na njia shirikishi siyo unakwenda kusuluhisha migogoro hii kwa kuchimba sijui mitaro, sijui kwa kusema wasivuke huku, haiwezekani ni lazima mtumie njia shirikishi ambayo itaweza kuondoa migogoro ya ardhi katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala moja la umiliki wa ardhi. Wapo Watanzania wengi ambao hawana hati miliki na wako wachache ambao wana hati miliki. Sababu ambazo zinapelekea hili, wakati mwingine ni urasimu na mlolongo mzima wa kupata hati hizi, kuanzia kwenye Halmashauri zetu mpaka hizo Ofisi za Kanda ambazo zinatoa hati miliki. Pia, wakati mwingine kuna rushwa kwenye halmashauri zetu, Halmashauri kule kuna shida sana kwa hao Maafisa Ardhi. Hizi rushwa zinawanyima wananchi haki ya kupata ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali muandae programu maalum ya kuhakikisha mnakopesha wananchi, yaani kuliko mwananchi atafute fedha ya kuingia gharama ya hatua hizi mpaka apate hati, mnaonaje mkiwa na programu maalum, Serikali ikagharamia, mkawakopesha wananchi wakawa na hati zao, wakalipa kidogo kidogo mpaka akamilishe deni lile, ili tuhakikishe wananchi walio wengi wanapata hati, maana yake hati hizi wakipata mwisho wa siku wanalipa mapato, inakuwa ni sehemu ya mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jambo la mwisho, kuhusu ulipaji wa fidia pale ardhi inapotwaliwa. Jambo hili mmeeleza kwamba mmeanzisha Mfuko huu wa kutoa fidia ambayo itaanzia na bilioni tano. Ni muhimu sana Serikali ikawalipa wananchi fidia kwa wakati, ikawashirikisha wananchi katika…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mchango wangu wa kwanza utajikita katika suala zima la misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kushuhudia misitu yetu ikizidi kutoweka kwa kasi kubwa sana na hatujaona mikakati ya dhati ya Serikali kuhakikisha kunakuwa na misitu endelevu. Kuna takwimu ambazo zinaonesha national annual deforestation ni kati ya 0.8% mpaka 1.1%. Kwa kiwango kikubwa misitu hii inatoweka kwa shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za kilimo, uvunaji wa miti, moto na pia biashara kubwa ya mkaa. Ni vizuri Serikali ikatambua misitu hii leo tunaipoteza miaka 20, 30 ijayo nchi hii inaenda kuwa jangwa na hatujaona mkakati wa dhati kabisa wa Serikali kuhakikisha tunakuwa na misitu endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba tuna hiyo TFS ambapo jukumu lake kubwa ni kuhakikisha inasimamia na kutunza hiyo misitu ya asili. Hata hivyo, hii TFS imejikita katika kukusanya mapato zaidi bila kuwa na mipango endelevu ya misitu hii. Mheshimiwa Mbunge mmoja jana alichangia hapa akahoji hata mapato yenyewe yanakusanywaje na haya mapato yanayokusanywa kweli yana uhalisia? Ukichukua mfano, kuna tafiti zimefanywa, kwa Mkoa wa Tabora peke yake kwa mwaka wanazalisha magunia ya mkaa 2,244,050 wanapata shilingi bilioni karibu 21 kwa mwaka kwa shughuli za mkaa peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa za TFS wao wanasema makusanyo ya mkaa tu kwa mwaka ni shilingi bilioni saba, lakini Mkoa tu wa Tabora ni bilioni 21, kitaifa wanasema ni shilingi bilioni saba. Kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri anapaswa ku-deal na hawa watu wa TFS, kuna tatizo hapa. Kuna watafiti wamefanya utafiti wanaonesha hizi takwimu mkoa mmoja wanaingiza fedha nyingi, lakini Kitaifa TFS wanasema ni shilingi bilioni saba tu. Wizara inatakiwa kuhakikisha wanaitazama vizuri hiyo TFS kwa sababu wao nadhani ama ni rushwa ama kuna watendaji ambao si sahihi wanakwamisha shughuli hizi za kukusanya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishauri Serikali kwamba pia wasiitazame TFS katika kuhakikisha inawaletea mapato tu au kutoa vibali vya misitu na vitu kama hivyo. Ni muhimu TFS ikatekeleza majukumu yake kama dhamira ya uanzishwaji wa TFS ilivyokuwa katika taratibu zake za uanzishwaji. Ni muhimu sana Serikali mkatazama hawa TFS wanapotoa leseni, watoe leseni lakini hao wanaopewa leseni walete mpango mbadala au mkakati mbadala wa kuendeleza misitu yetu ili tuweze kuondokana na kutoweka kwa misitu kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la migogoro ya mifugo inayoingia hifadhini. Waheshimiwa Wabunge sisi kama viongozi pia wakati mwingine ni lazima tuangalie kauli zetu zisije zikalibomoa Taifa. Ni kweli kwamba tunawahitaji wafugaji, ni kweli tunawahitaji wakulima, ni kweli kwamba tunahitaji hifadhi au misitu. Ni muhimu tukafahamu kuwa mifugo inaongezeka na mahitaji ya kilimo kwa maana ya wakulima wanaendelea kuhitaji ardhi lakini ardhi ni ile ile tu haiongezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana Serikali wakakaa na Wizara zote ambazo zinaingiliana katika masuala haya ya mifugo, kilimo na wa maliasili kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo yao, wanatengewa kabisa, hifadhi nayo inakuwa na maeneo yasiingiliwe na wafugaji, vivyo hivyo kwa wakulima pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema pia wakati mwingine unaruhusu moja kwa moja mifugo inaingia hifadhini lakini kama hawa watu wangetengewa maeneo yao hakika tusingekuwa na hii migogoro ambayo inaendelea. Serikali lazima ipime, ukipima kati ya suala la maliasili na utalii na kati ya sekta ya mifugo utaona kwa takwimu kwa sasa kwamba maliasili inaiingizia Serikali pato zaidi kuliko mifugo. Inawezekana pia mifugo ingeweza kuliingizia Taifa pato zaidi kuliko maliasili lakini kama wangekuwa na ufugaji wa kisasa, wakapangiwa maeneo yao, wasiingiliane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali wakayapima haya, wakahakikisha migogoro hii ya wakulima na wafugaji inakwisha. Niwasihi Waheshimiwa viongozi wenzangu Wabunge, ni muhimu sana tukachunga kauli zetu, tuangalie tunawahitaji watu wote. Tunawahitaji wakulima, tunawahitaji wafugaji, tunahitaji pia na misitu yetu na uhifadhi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la utalii. Wizara imetoa takwimu hapa kwamba kwa mwaka nchi yetu inaingiza watalii karibu 1,200,000 na kuna Mheshimiwa Mbunge wa Arusha jana alichangia vizuri sana akafanya comparison na nchi nyingine ambazo zinakuwa na idadi kubwa ya watalii. Nchi yetu mtalii kuja hapa anakumbana na tozo kibao. Anaanzia kwanza kwenye viza, akienda kama ni Ngorongoro getini kuna fees, akilala kwenye hoteli kitanda kina fees, kila mahali Mzungu huyu au mtani huyu anatozwa tozo na hizi tozo zimekuwa ni fixed mwaka mzima na watalii ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali kwa nini msiwe na promotion package kwa kipindi fulani ili muongeze idadi ya watalii halafu baadaye mkifika kwenye pick fulani mtaendelea na hizi tozo zenu ambazo ziko fixed ili tuhakikishe tunaongeza idadi ya watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni muhimu sana pia wakahakikisha wanakuza utalii wa ndani. Kuna baadhi ya maeneo, mimi natoka Wilaya ya Karatu, Wilaya ya Karatu ina hoteli za kitalii 54, wako Watanzania ambao hawajui. Mtanzania yuko Dar es Salaam anafikiria kwenda kupumzika South Africa lakini kumbe angekuja kupumzika Karatu kuna hoteli nzuri, zile ambazo wanazifuata nje ya nchi pia ziko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti,una hoteli nzuri sana ambazo wageni wengi wanapenda kulala pale halafu wanakwenda kutembea Ngorongoro. Wilaya kama hizi ambazo ziko pembezoni mwa Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni sehemu ya lango la kuingilia Ngorongoro tayari kuna hizi hoteli za wawekezaji na wazawa pia wamejitahidi kujenga hoteli za standard mbalimbali, unakuta kuna hoteli ya mpaka kulala siku moja ni karibu dola 700, hoteli yenye standard na quality ya juu kuliko labda hizo mnazofuata South Africa na kwingine, ziko Karatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu pia Wizara wakaangalia Wilaya kama hizi ambazo tayari kuna hoteli kama hizi wakazitangaza, wakafanya utalii wa ndani pia wakawa na target ya kukuza utalii wa ndani na si tu kuangalia target ya kukuza utalii wa wageni kutoka nje. Kwa hiyo, ni muhimu sana wakalitazama hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu TANAPA. TANAPA ina jukumu la msingi la kusimamia hifadhi za Taifa, uhifadhi wa wanyamapori na shughuli za utalii. Leo TANAPA mapato yake yote yanapelekwa kwenya pool moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, lakini hawa baadaye wakitaka kutekeleza shughuli zao maana yake waje tena waombe huko, kwa maana ya Hazina au Mfuko Mkuu wa Serikali waweze kwenda kutekeleza majukumu yale. Mfano, leo pale Ziwa Manyara liko chini ya hifadhi ya TANAPA linapotea kwa sababu limejaa tope hakuna kinachofanyika. TANAPA wanakusanya fedha badala nyingine zirudi kwenda kutekeleza zile shughuli zinapelekwa Mfuko Mkuu wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanaipa TANAPA kazi ya kutengeneza madawati nchi nzima halafu Waheshimiwa Wabunge wanapongeza wakati TANAPA ina kazi ya kudhibiti ujangili, ina kazi ya kudhibiti na kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu, ina kazi ya kuhakikisha mfano Ziwa Manyara linaendelea kuwepo? Mheshimiwa Waziri baada ya miaka 10 au 20 Ziwa Manyara linapotea kwa sababu limejaa tope maji yale yanakuwepo tu msimu wa masika baada ya muda ni tope linajaa pale. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara wakaangalia shughuli za TANAPA zisiweze kusimama. Haiwezekani wao wanakusanya fedha wanawapelekea halafu mwisho wa siku yale majukumu yao ambayo wanapaswa kuyafanya hawawezi kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu Operesheni Tokomeza. Kwa kuwa kulikuwa na Azimio la Bunge kwa wananchi walioathirika na Operesheni Tokomeza ni muhimu sana Serikali ikahakikisha inalipa fidia kwa wakati kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu leseni ya biashara ya Nyara, kuna baadhi ya kampuni zilizopewa leseni hizo na baada ya muda leseni zikafutwa na tayari kampuni hizo zilishakuwa na nyara hizo na baada ya muda wahusika kukamatwa ilhali wakati wanatekeleza jukumu hilo walikuwa na leseni halali. Serikali itueleze kwa nini kumekuwa na mkanganyiko huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Wilaya ya Karatu inapakana na TANAPA (upande mmoja) na Hifadhi ya Ngorongoro (kwa upande mwingine). Wilaya imekuwa haina makubaliano ya kimkataba wa namna gani Wilaya hiyo inafaidika na utalii ili kujenga ujirani mwema. Misaada hiyo imekuwa inatolewa bila ya kuwa na uhakika wa kuipata (hisani). Ni kwa nini mamlaka hizi zisiingie makubaliano rasmi ya kimkataba ili Halmashauri iwe na uhakika kwa mwaka ni miradi ipi, kwa gharama ipi itatekelezwa na mamlaka hizo? Ni muhimu mambo haya yakawekwa wazi ili kujenga ujirani mwema.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Naomba nitoe mchango wangu mfupi hasa kuhusiana na suala zima la hali ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa ya tathmini ya MDG kwa nchi yetu kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, taarifa inaonyesha kwamba uchumi wetu umekua kwa asilimia saba kwa kipindi cha miaka 15. Lakini taarifa hiyo inaonesha kwamba kama uchumi utakuwa mfululizo kwa asilimia saba kwa miaka 15 maana yake inategemewa suala la umaskini utapungua kwa kiwango cha asilimia 50. Lakini taarifa hiyo inaonyesha kwa Tanzania imepungua kwa asilimia kumi tu, kwamba bado tuna safari ndefu ya kufikia hicho kinachoitwa uchumi wa kati ambayo ni dira ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema suala la ukuaji wa uchumi lazima pia tuangalie sekta zingine ambazo zinaweza kuchochea suala zima la ukuaji wa uchumi, bado tuna safari ndefu. Ukiangalia kwenye sekta tu ya kilimo uchumi unakua kwa asilimia mbili tu na tunajua kabisa suala la kilimo ni tegemeo kwa Watanzania wengi, wanategemea ili kuondokana na umaskini.
Lakini sekta hiyo imekua kwa asilimia mbili tu kama ambavyo taarifa hiyo inaonyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la ukuaji wa uchumi Serikali mkija hapa na figures na kujigamba mkisema kwa ujumla wake inakuwa kwa asilimia saba bila shaka mtakuwa mna wahadaa wananchi lakini kwa uhalisia ukienda kwenye sekta moja moja ambazo zinachochea uchumi huo bado tupo nyuma na tuna hali ngumu. kwa hiyo, ni vizuri sana mnaposema suala hili la uchumi muangalie uhalisia wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema pia suala la uchumi tukiangalia hali ilivyo sasa kuna mdororo mkubwa wa uchumi, hakuna mzunguko wa fedha, hakuna fedha katika hata bajeti tuliyopitisha ukiangalia sasa tunaingia kwenye quarter ya pili hata asilimia 26 ya utekelezaji wa bajeti bado hamjafikia na kama mmefikia ni hiyo asilimia 26 tu. Kwenye Serikali za Mitaa hakuna fedha, kwenye taasisi za umma hakuna fedha, Wizarani tumeona taarifa mbalimbali Wizara zikiwasilisha kwenye Kamati hakuna fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya, hakuna fedha, nini kipaumbele? Mna mpango gani wa kufikia hiyo bajeti ambayo tumeipitisha kwa shilingi trilioni 29 katika mwaka huu. Lakini mnafanya projection ya bajeti ya shilingi trilioni 33 kwenye bajeti ijayo. Napata mashaka sana kama hii tu ya sasa utekelezaji wake tunaingia kwenye quarter ya pili bado hali ni mbaya halafu unafanya projection ya shilingi trilioni 33 kwenye bajeti ijayo tafsiri yake ni kwamba mnajifurahisha ninyi kama Serikali kwa namba hizi kubwa kubwa, lakini mnawaongezea wananchi mzigo wa kuendelea kulipa kodi.
Kwa hiyo, unaona kabisa ni bajeti ambayo kwa kweli mwisho wa siku haitaweza kutekelezeka ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeeleza katika mpango huu kumekuwa na changamoto mbalimbali za kuweza kufikia mipango hiyo. Mojawapo mmesema ushiriki mdogo wa sekta binafsi lakini pia kuna suala la upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji. Hivi hizi sekta binafsi kama hazijatengenezewa mazingira rafiki, kama hizi sekta binafsi hazijawa na imani na Serikali iliyopo madarakani kwa sababu tumeona wakati mwingine mna ndimi mbili mbili sekta binafsi ataogopa ku-invest hela zake kwasababu hajui Serikali kesho inatamka nini? Inafanya nini? Kesho inakuja na kodi gani? Kama msipoweka haya mazingira mazuri hakuna sekta binafsi atakayeweza kuja kuwekeza katika nchi hii kama ambavyo nyie wenyewe mmekiri hapa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado tunahitaji kuwepo na sera na mazingira rafiki ya kuweza kuhakikisha hizi sekta binafsi kwa kweli zinakuwa na wao ni sehemu ya uchumi wa nchi hii. Mmeeleza pia changamoto nyingine ni upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji, hili pia ni changamoto kweli kwa sababu kama sasa hivi mabenki hali ni mbaya, mabenki mengine yameshakua chini ya usimamizi wa BOT, mabenki hayana mzunguko wa fedha, fedha ambazo zilikuwa za Serikali kwenye commercial banks zote zimehamishiwa BOT, obviously hakuna uwekezaji unaweza kufanyika. Kwa hiyo, bado tuna changamoto kubwa sana ambayo kwa kweli itakuwa ni ngumu sana kuweza kufikia hicho kinachoitwa uchumi wa kati ambayo ni dira ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hali ilivyo sasa hivi, lakini wakati mwingine unajiuliza hivi kuna haja gani ya kujadili pia mpango au kujiwekea mpango wakati mpango wenyewe ukienda kwenye utekelezaji hauwezi kufanyiwa tathmini na kuona matokeo. Lakini kuna vitu vingine ambavyo vinaenda kutekelezwa ambayo hayapo kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao tunaumalizia 2016/2017 suala la kuhamia Dodoma halikuwepo lakini Rais amelitamka limetekelezeka, halikuwepo kwenye mpango na kuhama Dodoma sio kazi ndogo, inahitaji fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini angalau sasa hivi mmeiweka kwenye mpango unaokuja; sasa unaona wakati mwingine kama tunaendeshwa kwa matamko ya namna hii ambayo hayapo kwenye mipango maana yake unaenda kuharibu bajeti ambayo imepitishwa hapo. Kwa hiyo, pia wakati mwingine ni lazima haya ambayo mnayatamka ni lazima yaendane na bajeti ambayo tumeipitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Waziri wa Fedha na anisaidie majibu atakapohitimisha. TRA wamesema wanakusanya 1.3 trillion kila mwezi, hiyo ni projection. Mishahara inayolipwa nchi hii ni shilingi bilioni 540, madeni ya ndani ama ya nje inalipwa shilingi bilioni 900, ukifanya hapo mahesabu ni kama one point four trillion na makusanyo ni 1.3 trillion kila mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza hizo ndege zilizonunuliwa kwa fedha cash hii hela mliipata wapi? Wakati mnachokikusanya TRA kila mwezi ni 1.3 trillion, ukilipa madeni, ukilipa mishahara ni 1.4 trillion; fedha za kununua ndege kwa hela cash mmeipata wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri unijibu ama ni hizo fedha zilizopo BOT ambazo zimekusanywa na taasisi zikawekwa kule mkaenda mkazichukua mkanunua ndege cash? Naomba nipate majibu ya suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala lingine ni kuhusu suala zima la elimu. Wakati nimechangia kwenye bajeti ya elimu hapa mnajivunia leo suala la elimu bure, lakini elimu bure hii ni bure tu kwa sababu hawalipi kile ambacho kinatakiwa. Ukienda kwenye uhalisia wa shule zetu hali ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi mmesema mwanzoni wakati wa awamu ya JK mliagiza kujengwe maabara nchi nzima; wananchi wakajichanga, mkaita wadau mbalimbali wakachanga maabara ikajengwa, yamebaki majengo yameachwa. Mmeyaacha yale majengo hayana vifaa, maabara hayafanyi kazi ni majengo tu yaliyosimama mkahamia kwenye madawati mmetangaza madawati nchi nzima watu wametengeneza madawati mengine hayana standard, hayana quality inayotakiwa leo mnataka kukimbilia kujenga madarasa kwa mfumo ule ule wa kulipuka. Kule mmeshasahau maabara, madawati mengine hayana kiwango, leo mnakurupuka mnaenda kujenga…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema muache kukurupuka, mkianzisha jambo moja likamilike, liwe na manufaa, lianze kufanya kazi muende kwenye jambo lingine, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi taarifa zilizowasilishwa mbele yetu, taarifa ya Kamati ya PAC na LAAC. Mchango wangu wa kwanza utajielekeza katika suala zima la Deni la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Juni, 2016 Deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 9.76 maana yake linakimbilia shilingi trilioni 40. Madeni haya kwa mujibu wa taarifa ya CAG ameeleza kabisa hakuna mkakati wa namna gani yanaweza kwenda kulipika. Kulikuwa kuna rasimu ya mkakati huu ya mwaka 2002, ikatengenezwa rasimu nyingine ya mwaka 2004, ikatengenezwa nyingine ya 2014 lakini zote ni rasimu bado haijakamilika kuwa mkakati wa kuona namna tuta-control Deni la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoangalia, itafikia mahali fedha zote za makusanyo ya nchi hii zinaenda kulipa madeni. Kama ambavyo ilivyo leo kila kinachokusanywa karibu shilingi bilioni 900 inaenda kulipa madeni. Kwa hiyo, ni lazima Serikali ifike mahali iandee mkakati. Ripoti ya CAG imesema kabisa hii rasimu ambayo ipo tena imeandaliwa kizamani haiendani na hali halisi ya uchumi wa nchi. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaona umuhimu wa kuwa na mkakati huu ambao utaendana na hali halisi ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Tuna Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo kwa kiwango kikubwa fedha zake zinakopwa na zinaenda kuwekezwa katika miradi mikubwa. Hatukatai kufanyia shughuli hizo, lakini unapoenda kukopa halafu hurejeshi inakuwa ni tatizo. Mfuko mmojawapo tu kwa mujibu wa taarifa ya CAG ni PSPF una hali mbaya ambapo unakaribia kufilisika kabisa kwa sababu Serikali hairejeshi fedha ilizozikopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima ifike mahali muache kabisa kukopa hizi fedha za wanachama. Ni fedha za wanachama wanaweka kule wakijua wanajiwekea akiba lakini Serikali mnaenda kuzichukua na ku-invest kwenye miradi mikubwa ambayo tunaona kabisa siyo rahisi muweze kurudisha kwa sababu mmejaa madeni, mnadaiwa ndani na nje, mnakopa tena kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, mnadaiwa kila kona, mwisho wa siku mtaenda kuua hii akiba ya wafanyakazi ambao wanatarajia waipate siku wakistaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaongelea sana suala la kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tumesema sana kwenye Bunge la Kumi. Leo mnajiita wazee wa hapa kazi tu, wazee wa kubana matumizi, si ndivyo mnavyojiita? Kama kweli mnataka kubana matumizi ni lazima muangalie suala la kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iko takribani tano au sita yote ina Wakurugenzi, ofisi, inaendeshwa kwa gharama na kwa fedha za wanachama. Kama mnasema mnabana matumizi muende muunganishe hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwepo na ama mifuko miwili au mitatu ili hicho mnachokiita cha kubana matumizi mkifanye kwa vitendo siyo mnatuambia tu halafu hakuna mnachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya mwisho nitajielekeza katika Serikali za Mitaa. Katika Awamu hii ya Tano mnaenda kuua kabisa Serikali za Mitaa. Mnaenda kuzimaliza wakati Serikali za Mitaa zipo kwa mjibu wa Katiba ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uteuzi tu mliofanya, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa hawa ma-DC, ma-DED, ma-DAS, kwa kweli ni watu ambao hawajapitia kwenye mifumo ya local government, wengine wametolewa mnakojua, wamepewa nafasi ambazo hawana experience hata nukta moja. Hivi wanaendaje kufanya kazi? Ma-DED wengine hawajui hata vote ni nini, anauliza vote ni nini? Wanauliza hawajui. Hivi mnategemea kutakuwa na ufanisi? Ndiyo maana tunawaambia mnaenda kuua Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali miaka yote imeonesha suala la Serikali Kuu kutokupeleka fedha za maendeleo katika Halmashauri za Wilaya. Hivi tunavyoongea leo, fedha zilizoenda katika local government ni fedha za mishahara tu. Mfano mzuri ni Halmashauri yangu ya Karatu. Fedha kidogo tu iliyoenda ni ya barabara shilingi milioni 50 lakini hakuna fedha za miradi ya maendeleo zilizoenda yaani mpaka leo tunaingia robo ya pili ya bajeti ya Serikali fedha hazijaenda katika Serikali za Mitaa. Mnatarajia nini si mnaenda kuziua Serikali za Mitaa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na namshukuru Mheshimiwa Mwakajoka kwa kunipa dakika tano. Nami nianze kuchangia kwenye suala zima la mamlaka makubwa ambayo nafikiri RC na DC na DAS wanazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi sana kuona leo kwa sababu mwaka jana hapa wakati sisi Wabunge wa Kambi ya Upinzani tunajaribu kuonesha matatizo na changamoto na udhaifu ambao baadhi ya RC na DC wanayo katika maeneo yetu, tulibezwa hapa, hatukusikilizwa lakini leo humu baadhi ya Wabunge wa CCM nao wameona hiyo shida na wameanza kusema. Nafikiri huu utakuwa ni mwanzo mzuri ili tuendelee kuelewana sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba hawa RC na DC wamekuwa Miungu watu, wameona kwamba wana mamlaka makubwa kuliko mtu yeyote, hawatambui nafasi za Wabunge, wanaweza ku-revoke maamuzi ya Baraza na kuyaingilia, hata pale ambapo hayastahili. Ifike mahali hizo semina elekezi ambazo mlizisema zimefutwa nadhani iko haja ya kurudisha na kukaa na hao watu na kuwaambia. Siyo semina tu, hata akili nyingine tu ya kawaida ya busara ya RC au DC kujua mipaka yake, kujua namna ya kushirikisha hawa watu hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima muangalie mfumo mwingine, sijui wateuliwe wengine au wafanye nini hawa wameshindwa kazi, wamekuwa Miungu watu. RC anakaa kwenye kikao anaongea anasema, nadhani mnaelewa hapa kuna Waziri naweza kuwa na maamuzi makubwa kuliko Waziri hata Waziri mwenyewe anaelewa, anasema kwenye kikao na Waziri yupo, huyu ni RC. Sasa kama wanasema vitu kama hivi mbele ya Mawaziri unategemea nini kwa Wabunge?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, RC anakuja kwenye eneo lako, Wabunge mnaomba kuonana nae hana muda na Wabunge. Haya ni masikitiko, lakini sasa angalau tunaanza kuelewana humu ndani na angalau haya machungu na ninyi Wabunge wa CCM mmeanza kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utawala wa sheria; sioni sasa kama kuna utawala wa sheria. Kuna Mbunge mmoja ameongelea kuhusu mlundikano wa kesi au mlundikano wa wafungwa Magerezani, lakini leo kama kuna kesi ya uchochezi ya mwana CHADEMA haichukui miezi mitatu hukumu tayari na inasikilizwa haraka sana, lakini kuna watu wamekaa gerezani kwa kesi ama za kusingiziwa au ambazo siyo za kisingiziwa miaka tisa, miaka 10, miaka mitano, miaka miwili wanasema upelelezi bado, lakini mwana-CHADEMA akisema jambo tena anaambiwa mchochezi na hii tafsiri ya uchochezi itabidi mtuambie uchochezi ni nini maana yake neno uchochezi linatumika vibaya, anaambiwa ni mchochezi, anapelekwa Mahakamani haraka hukumu miezi sita, miezi nane, miezi mitatu jela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama kuna utawala wa sheria, ni lazima mjitafakari upya, muangalie kama tuna Katiba, kama tuna sheria, kama kweli kuna kutenda haki kwa nini haki inatendeka kwa watu wachache na watu wengine wananyanyaswa kwa sababu ni washabiki wa upande fulani au wa Chama fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la mwisho kuhusu Madiwani; Madiwani wamekuwa ni Wasaidizi wetu hata sisi Wabunge kwa maana kama tukiwa hapa Bungeni kwenye vipindi virefu vya Vikao vya Bunge, wao ndiyo wamekuwa wakikaa na wananchi na wakiwasikiliza kero zao, lakini Madiwani wamesahaulika. Madiwani leo wanapewa posho ya sh. 350,000 basi na hizo posho za vikao, tena wako Wakuu wa Wilaya wengine wanafuta posho za Madiwani ambazo zingine ziko kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wakuu wa Wilaya wengine wanasema posho hii haitakiwi, hii haitakiwi, kweli kuna zile ambazo haziko kwa mujibu wa taratibu, lakini zile zilizoko kwa mujibu wa taratibu DC wanaingilia, wanazifuta. Tumewasahau Madiwani, hatufikirii kuwaongezea posho zao, tumewaacha Madiwani hawapewi mafunzo, capacity building haipo tena, angalau kwenye awamu zilizopita walikuwa wanapewa. Sasa unampeleka Diwani asimamie mradi wa mabilioni, yuko kwenye Kamati ya Fedha lakini hajajengewa uwezo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, usikilizaji wa mashauri mahakamani; pamoja na Serikali kueleza 80% ya mashauri yameweza kusikilizwa, kasi hii bado inahitaji kuwekewa nguvu zaidi ili kuendelea kupunguza mrundikano wa kesi zilizopo mahakamani. Serikali lazima itie nguvu na mkazo katika Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya kwani huko ndiko kwenye mrundikano wa kesi nyingi, jambo ambalo linawafanya wananchi wenye kesi mbalimbali kuendelea kutumia muda mwingi mahakamani. Hata hivyo, haki inayocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa. Nashauri Serikali iendelee kujipanga kuhakikisha mrundikano wa kesi katika mahakama za chini zinakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo; pamoja na umuhimu wa Taasisi hii ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, ipo haja ya kuongeza chuo hiki katika kanda nyingine za nchi hii. Ni ukweli kuwa nchi hii ni kubwa na wanafunzi wanaohitaji kupata mafunzo haya ni wengi. Hivyo basi, ni muhimu kwa Serikali kuongeza vituo vya mafunzo hayo kwa angalau Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kusini na Magharibi. Kwa kuongeza vituo hivyo itasaidia wanafunzi kumudu gharama za mafunzo na hivyo kuongeza wanafunzi zaidi.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Miswada iliyoko mbele yetu, mchango wangu utajikita katika Muswada wa kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni takriban asilimia 73 ya Watanzania hutegemea kilimo na ni muhimu sana ili kilimo hiki kimnufaishe Mtanzania au Watanzania hawa wa asilimia 73 ni lazima hiki kilimo kiwe na manufaa, kiwe na tija lakini ni lazima kiwe ni kilimo ambacho tafiti zitafanywa zitaweza kuwasaidia kuboresha kilimo chao ili kiweze kuwasaidia kwa maana ya uchumi, mahitaji ya familia na mahitaji ya nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumekuwa tukianzisha hizi taasisi. Hii ni moja tu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo lakini tunakuwa na taasisi nyingi na Muswada huu unapendekeza kuanzisha taasisi hii ambayo itakuwa ina Bodi, Menejimenti na Itakuwa na Baraza la Taifa la Utafiti. Kikwazo kikubwa ambacho mara nyingi tunakiona ni uwezeshwaji wa hizi Taasisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna changamoto kubwa sana, Taasisi zinaundwa, zinaachwa, fedha inapewa „kiduchu‟, inapewa OC, zile za other charges lakini fedha kwa ajili ya maendeleo na fedha kwa ajili ya shughuli maalum hasa ya utafiti inakuwa ni mtihani na mara nyingi hili tumeliona. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Wizara na Serikali kwa ujumla kwamba ni muhimu sana mtakapokamilisha mchakato huu kuhakikisha hii taasisi inapatiwa fedha ya kutosha kuhakikisha inaendesha shughuli zake, inafanya utafiti ili iweze kuwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na fedha, wanahitaji pia kupata fedha au wanahitaji kupata fedha za uwezeshwaji wa kununua hivyo vitu ambavyo watafanyia utafiti au ambavyo vitaendana na teknolojia ya kisasa zaidi ili kuwasaidia na kurahisisha ufanyaji wao wa kazi. Kwa hiyo, ni muhimu sana, pamoja na kwamba tunapitisha hii Miswada, tunaunda hizi Taasisi ambazo ziko nyingi lakini bila kuwezeshwa kwa bajeti ya uhakika ya maendeleo mwisho wa siku hizi taasisi zitabaki tu kwenye makaratasi itakuwa hakuna kazi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi hii itakuwa ina kazi ya kuratibu utafiti, ufuatiliaji na tathmini, kwa hiyo, ni muhimu sana inapofanya tathmini yake, inapofanya tafiti yake, haya matokeo yanayopatikana ni lazima yawe-shared yaweze kushirikisha na mrejesho uweze kuwafikia wadau husika kwa maana ya wakulima au wale wote ambao wananufaika kwa namna moja ama nyingine. Kwa hiyo, haya ni masuala ya msingi sana kuyazingatia kuona tathmini hii inayofanyika ni lazima wadau washirikishwe, ni lazima wadau waweze kunufaika nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii taasisi sasa ni lazima iangalie namna ambavyo itaungana au itaunganisha nguvu za pamoja na vyuo vyetu vikuu ambavyo vimekuwa vikifanya tafiti mbalimbali. Kwa hiyo, tusiwaache pembeni pia wataalam wetu, kwamba leo tunaanzisha hii Taasisi lazima pia tuangalie namna gani tutaendelea kushirikisha na kuunganisha nguvu za pamoja na hivi vyuo vikuu ambavyo vimekuwa vikifanya tafiti miaka yote kabla ya kuanzisha chombo hiki. Kwa hiyo, haya ni mambo ya msingi ya kuzingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kuanzisha Taasisi hii, tunatarajia kwamba ni lazima Serikali sasa itumie takwimu hizi, itumie matokeo ya tafiti hizi katika upangaji wa mipango yake, katika upangaji wa bajeti, katika kukifanya kilimo kiwe na tija kwa wakulima. Kwa hiyo, ni lazima hili likazingatiwa kuona tunaanzisha taasisi inakuwa na matokeo fulani, inakuwa na mitazamo fulani, inakuwa ina ushauri fulani kuhusiana na masuala haya ya kilimo, ni vyema Serikali ikayafuata, ikayachukua, ikawa ni dira yake ya kupangia bajeti na mipango mbalimbali ya sekta ya kilimo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie sasa kwa kuchambua kidogo Muswada na kutoa mapendekezo. Ukisoma Muswada huu wa Kiswahili, kwenye heading pale inahitaji kufanyiwa marekebishao kwa sababu kule juu inasomeka Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, lakini content zote ni Taasisi ya Kilimo na mwanzo kabisa wa heading hapa kwenye Kiswahili, ya Kiingereza iko sawa, lakini kwenye Kiswahili imeanza, ukurasa wa kwanza iko sawa, kwamba ni Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, lakini ukiendelea page ya pili mpaka ya mwisho inasomeka Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na siyo Mifugo. Kwa hiyo, nadhani inahitaji kufanyiwa marekebisho ili iweze kuleta maana sahihi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kifungu cha 5(2)(a) kinasema, Mwenyekiti wa Bodi atateuliwa na Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 8(1) pia kinaeleza, Mkurugenzi atateuliwa na Rais. Kama ambavyo Kambi ya Upinzani imependekeza ni lazima tuondoke kwenye huu mfumo wa uteuzi, tuingie kwenye mfumo wa ushindani, tushindanishe watu wenye sifa, tutangaze hizi kazi, ni kazi ambazo kwa kweli zinahitaji utaalam na watu ambao wako tayari. Kwa hiyo, ni lazima tuondokane na huu mfumo wa uteuzi ambao umekuwa ni mwingi mno wa kubebana. Ni lazima tutoke huku tushindanishe hizi kazi, watu wenye sifa waombe, wachujwe kwa vigezo ili mwisho wa siku waweze kupata hizi nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda Kifungu cha 8(2)(d) wanasema katika uteuzi wa huyu Mkurugenzi anasema awe mbunifu, najiuliza hivi utapimaje ubunifu wake wakati ndiyo uko kwenye uteuzi? Sina hakika kama unaweza ukapimika ubunifu wa mtu kabla hujampa task fulani aifanye. Kwa hiyo, nadhani hapa inahitaji kurekebishwa labda ibaki tu yale maneno mengine kwamba awe na uzoefu na uadilifu, lakini ubunifu sina uhakika kutakuwa na kigezo gani cha kumpima ubunifu wake. Kwa hiyo, nadhani inahitaji kufanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kifungu cha 21(1)(c) kinazungumzia kuanzisha Kamati ya Kitaifa za kuratibu tafiti za mazao. Mwanzoni kwenye vifungu vingine inaeleza mfumo wa taasisi, kutakuwa kuna Bodi, kutakuwa kuna Menejimenti, kutakuwa kuna Baraza la Ushauri la Utafiti la Kitaifa, lakini huku tena mnasema kutakuwa kuna Kamati za Kitaifa za kuratibu utafiti wa mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tunaweza tukawa na Kamati na Mabaraza mengi ambayo mwisho wa siku ukiyapima au pamoja kuyapima yatakuwa na gharama kubwa za uendeshaji lakini ukipima hata matokeo yake yanaweza mengine yanaingiliana kazi zake au majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani ama Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi wakati anahitimisha ama hili liweze kufanyiwa marekebisho na kuona namna gani linaondolewa ili kupunguza hizi Kamati na haya Mabaraza ambayo yamekuwa mengi, mwisho wa siku inagharimu fedha nyingi ikiwa na matokeo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie tu kwa kusema kwamba ni lazima Serikali iangalie umuhimu wa kuwezesha hizi taasisi ambazo zimekuwa zikianzishwa, siyo tu kuwapa fedha za mishahara, fedha nyingine za OC, lakini fedha za maendeleo hamuwapi. Kwa hiyo, ni lazima Serikali muwajibike kuwapa fedha ili hiki kinachokusudiwa katika Muswada huu na kuwalenga Watanzania asilimia 73 ambao wao wanategemea kilimo, basi kiweze kuwa na tija na manufaa, kwao binafsi, jamii zao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.