Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Cecilia Daniel Paresso (1 total)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, sekta ya afya ni muhimu kwa Watanzania na kwa kuwa tunatambua kuna jitihada zinazoendelea za kuhakikisha kwamba sekta hii inaboreshwa, ikiwemo kudhibiti magonjwa mbalimbali yayoambukiza na yasiyoambakiza mfano malaria na mengineyo. Kutokana na mazingira yetu mengi katika maeneo mbalimbali, kuna madimbwi mengi yamejaa maji, lakini na mrundikano mwingi wa uchafu katika maeneo mbalimbali unaosababisha mazalia mengi ya mbu.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba mazalia haya yanamalizwa na mapambano dhidi ya malaria yanaendelea? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Paresso, Mbunge kutoka Mkoa wa Arusha, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazalia ya mbu na kusababisha malaria, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote wanajua kwamba Serikali yetu ina miradi maalumu ya uthibiti wa magonjwa ya malaria. Serikali inaendesha kampeni kwenye maeneo yetu yote mpaka vijijini ya usafi na usafi huu pia unagusa maeneo yote yenye mazalia ya mbu ili kuzuia kabisa na ikiwezekana kuondoa tatizo la malaria hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na utoaji wa net kwa matumizi ya watoto, mama na mtoto kwenye maeneo hayo kwa lengo la kujikinga na malaria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kampeni hii ya kufanya usafi, pia ikilenga kuondoa maeneo yote yenye mazalia ya mbu ambao wanasababisha malaria, inaenda sambamba na hamasa ya Serikali kwa wawekezaji kujenga viwanda vya kutengeneza dawa mbalimbali zinazosaidia kutibu ugonjwa wenyewe wa malaria, lakini pia kuua hata hayo mazalia ya vijidudu. Kwa sasa hivi wote mnajua kwamba pale Kibaha, Mkoani Pwani tuna kiwanda kikubwa sana kinachotengeneza dawa za kunyunyuzia maeneo haya yenye mazalia ya mbu ili kuua vijidudu hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara kadhaa nimefanya ziara pia kwenye eneo lile na kutoa wito kwa halmashauri zetu za wilaya pamoja na kampeni ya usafi bado wanapaswa kutenga fedha kwenye bajeti zao ili wakanunue zile dawa pale Kibaha, waweze kunyunyiza kwenye maeneo yote ambayo yana mazalia ya mbu ili kuua kabisa hawa mbu. Tukiwa tunaendelea na kampeni hii, tutaendelea kuimarisha bajeti zetu kwenye halmashauri kununua hizo dawa, lakini pia ujenzi wa viwanda na uwekezaji. Tumeendelea kukaribisha wawekezaji wote wanaoweza kujenga viwanda vya kutengeneza dawa mbalimbali, mbali ya malaria lakini na dawa nyingine kwa lengo la kujaribu kupunguza kabisa kiwango cha magonjwa ili kuweza kulifanya Taifa hili kuendelea kuwa salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa nakamilisha kutoa maelezo ya jibu hili niwahakikishie Watanzania kwamba kampeni yetu ambayo inaendelea kwa sasa nchini kote, itaendelea kuimarishwa mpaka ngazi ya vijiji. Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, lakini pia Wakurugenzi kwenye halmashauri zao chini ya Maafisa Waganga wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanafanya tathmini kwenye maeneo yote na kubaini maeneo yenye tatizo la ugonjwa wa malaria, chanzo cha ugonjwa huo na kuanza kufanya kampeni ya usafi angalau kila wiki na kampeni hii ambayo pia tunaendelea nayo kwenye maeneo ya wazi, kwenye masoko, shule, vituo vya mabasi itasaidia sana kupunguza kiwango cha uzalishaji wa wadudu ambao wanasabisha ugonjwa wa malaria, ahsante sana. (Makofi)