Primary Questions from Hon. Cecilia Daniel Paresso (29 total)
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Katika Bunge la Kumi aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii aliunda Kamati Ndogo ya kushughulikia mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kata ya Buger na Hifadhi ya Taifa ya Manyara:-
(a) Je, ni nini matokeo ya Kamati Ndogo iliyoundwa?
(b) Je, ni lini wananchi watapewa taarifa ya Kamati Ndogo iliyokuwa inashughulikia mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alifanya ziara katika Wilaya ya Karatu tarehe 2 Juni, 2015 na kuteua Tume iliyopewa Hadidu za Rejea kuhusu kutatua mgogoro baina ya wananchi wa Kata ya Buger na Hifadhi ya Taifa ya Manyara.
Tume ilifanya mahojiano na makundi mbalimbali na kupitia taarifa zote zilizotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Taarifa ya awali imeandaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa ya Tume imebaini kuwa kwa ujumla chanzo kikubwa cha migogoro baina ya wananchi na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ni idadi kubwa ya mifugo na kukosekana eneo la kuchungia katika Kijiji cha Buger. Tume imependekeza hatua za kuchukuliwa ambazo ni pamoja na hizi zifuatazo:-
(a) Kufanya sensa ya mifugo kwa vijiji vilivyopo katika Kata ya Buger ili kubaini idadi ya mifugo iliyopo dhidi ya ukubwa wa ardhi waliyonayo;
(b) Vijiji kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi;
(c) Kutoa elimu ya uhifadhi na Sheria katika vijiji vinavyozunguka hifadhi, hasa Msitu wa Marang;
(d) Kuanzisha Kamati za Mazingira za Vijiji na kuimarisha zilizopo ili kutekeleza vema majukumu yake; na
(e) TANAPA kuweka nguvu katika kuchangia miradi ya maendeleo ya jamii kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaandaa kikao cha wadau ndani ya miezi mitatu ili kuwasilisha mapendekezo ya Kamati na kujadili utekelezaji wake.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Serikali kupitia mfumo wa Bima ya Taifa ilitoa tenda kwa kampuni moja binafsi kwa ajili ya kufunga mfumo wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za wagonjwa na taarifa za Bima:-
(a) Je, ni fedha kiasi gani ilitumika kwa hospitali hizo kufunga mfumo huo?
(b) Je, ni kwa kiasi gani Serikali ilizingatia thamani halisi ya fedha (value for money) ukilinganisha na mahitaji makubwa katika sekta ya afya kama madawa, vifaatiba na watumishi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwaniaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Zabuni hii ilitangazwa Kimataifa ambapo kampuni za ndani na za nje ziliruhusiwa kushiriki. Na jumla ya kampuni 17 ziliwasilisha zabuni zao. Baada ya mchakato wa uhakiki, kampuni ya Maxcom Africa Limited ya hapa nchini ikishirikiana na kampuni ya Sevenhills E-Health PVT LTD ya nchini India zilishinda zabuni hii. Thamani ya zabuni hiyo ni shilingi 5,887,079,539 ikijumuisha kodi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini zabuni hii ilizingatia thamani halisi ya fedha kutokana na uzoefu ambao Wizara yangu imeupata kwa kuimarisha mifumo ya habari na mawasiliano, ambao ni pamoja na vituo kuongeza mapato ambayo yamepelekea kuongezeka kwa ari na tija katika vituo vyetu. Vile vile, zabuni imewezesha upatikanaji wa taarifa na takwimu za uhakika kuhusu huduma za afya nchini. Taarifa hizi zinasaidia katika mipango mbalimbali na utoaji taarifa mbalimbali kwa wadau wa sekta ya afya pamoja na tafiti mbalimbali zinazohusu sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani ya Wizara yangu kuwa, kwa kuwa na mifumo madhubuti ya kielektroniki katika taasisi hii, tutaweza kuongeza tija katika utoaji huduma za afya kwa wananchi wetu hasa tunapoelekea kuwa na Bima ya Afya ya lazima kwa kila mwananchi. Aidha, kwa kupitia zabuni hii sasa Taasisi yetu ya NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya) imeweza kupata mfumo halisi (source code) inayoumiliki na kuwezesha mfumo huu kuwekwa katika vituo vingine nchini katika siku za usoni.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Mwongozo wa fedha za wafadhili wanaochangia katika Sekta ya Afya (Health Basket Fund) katika Halmashauri zetu unaelekeza asilimia 33 ya fedha hizo zitumike kwa manunuzi ya dawa na asilimia 67 zitumike katika shughuli za utawala, uaimamizi na ufuatiliaji;
(a) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kubadili mongozo huu?
(b) Je, ni lini Serikali taacha kutegemea fedha za wafadhili na hasa katika Sekta ya Afya.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsate. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso Mbunge wa Viti maalum lenye sehemu A na B kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haiwezi kubadili mwongozo wa mgao huo kwasababu unalindwa na makubaliano baina yake na wadau wa mfuko wa pamoja wa Afya (Health Basket Fund). Hata hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa Serikali inaangalia uwezekano wa kufanya mapitio ya makubaliano hayo na wadau wa Health Basket Fund.
(b) Mheshimwa MWenyekiti, Serikali haitegemei fedha za wafadhili kuendesha huduma za Afya kwa asilimia 100. Wafadhili wanachangia tu gharama za baadhi ya huduma. Uchumi wa nchi yetu utakaporuhusu utegemezi utapungua kama siyo kwisha kabisa. Hata hivyo, katika kuelekea kujitegemea, Serikali imetengeneza mkakati wa ugharamiaji huduma za afya na imeandaa mapendekezo ya Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambayo yatawasilishwa hapa Bungeni pindi mchakato wa ndani ya Serikali utakapokamilika. Mheshimiwa Mwenyekiti, inatarajiwa Sheria hii kama itapitishwa na Bunge lako tukufu kila Mtanzania atapata huduma za Afya kwa kadi yake bila kiwazo cha kifedha.
MHE. QAMBALO W. QULWI (K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO) aliuliza:- Wilaya ya Karatu inapakana na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro ambapo watalii wengi hutembelea hifadhi na kufanya Wilaya hii kupata fursa ya kujengwa hoteli za kitalii, pamoja na hoteli hizo kujengwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya, Halmashauri hiyo hainufaiki na uwekezaji huo. (a) Je, Halmashauri hiyo hairuhusiwi kutoza hotel levy? (b) Je, nini mkakati wa Serikali kuitangaza Wilaya hii kutokana na uwekezaji wa hoteli nyingi, nzuri na za kisasa zilizopo katika Wilaya hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Hoteli Halmashauri hairuhusiwi kukusanya kodi katika hoteli za kitalii, hata hivyo Halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa kifungu cha 26(3) cha sheria hiyo kukusanya ushuru wa hoteli katika nyumba za kulala wageni (guest houses) zilizopo ndani ya Halmashauri. Vilevile Halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura Na. 290 kifungu cha 6(u) kukusanya ushuru wa huduma (service levy) katika hoteli za kitalii zinazoendesha shughuli zake ndani ya Halmashauri kwa kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya taasisi husika. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ipo katika hatua za mwisho za utengenezaji wa tovuti (website) yake ili kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutangaza vivutio vyote vilivyopo vya kitalii hapa nchini kupitia makongamano na shughuli mbalimbali za Kitaifa yakiwemo maadhimisho ya Nanenae na Sabasaba ambayo hufanyika mara kwa mara kila mwaka ili kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kufahamu fursa za uwekezaji zilizopo huko Karatu.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali ilitangaza kuzinyang’anya halmashauri uwezo wa kukusanya mapato ya kodi majengo (property tax) na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kupewa jukumu hilo.
(a) Baada ya TRA kupewa jukumu hilo je, ufanisi umefikiwa kwa kiasi gani ikilinganishwa na mapato yaliyokuwa yakikusanywa na halmashauri?
(b) Kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za miji, manispaa na majiji na majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi hayajapunguzwa; Je, Serikali imejipangaje kufidia vyanzo hivyo vilivyopotea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimia Cecilia Daniel Paresso, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali haijazinyang’anya Halmashauri uwezo wa kukusanya mapato yake hususan kodi ya majengo na badala yake imebadilisha na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo. Mamlaka ya Mapato Tanzania ndiyo yenye jukumu kuu kisheria la kukusanya mapato ya Serikali. Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura 399 kifungu cha 5(1), Waziri wa Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kuikabidhi TRA jukumu lolote linalohusu ukusanyaji wa mapato yoyote kama atakavyoona inafaa kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA ilianza rasmi kukusanya kodi ya majengo kwa halmashauri 30 kati ya 183 kuanzia Oktoba, 2016 baada ya tangazo la Serikali Na. 276 kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali tarehe 30 Septemba, 2016. Katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2016, Halmashauri zote zilielekezwa kuendelea kukusanya kodi ya majengo wakati TRA ikikamilisha taratibu za kisheria na kimfumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho cha Julai, hadi Septemba, 2016, halmashauri 30 ziliweza kukusanya shilingi milioni 3,399 ikiwa ni sawa na asilimia 24 ya lengo la kukusanya milioni 14,502. Ufanisi huu ni sawa na na wastani a shilingi milioni 1,133 kwa mwezi. Aidha, katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2016 hadi Aprili, 2017 jumla ya Shilingi milioni 10,652.6 zilikusanya sawa na ufanisi wa asilimia 22 ya lengo la kukusanya shilingi milioni 48,340.2 katika kipindi husika. Ufanisi huu ni sawa na wastani wa makusanyo ya shilingi milioni 1,521.8 kwa mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu hizi ni wazi kwamba TRA imekusanya kodi ya majengo kwa ufanisi zaidi ikilinganishwa na halmashauri. Ufanisi wa TRA unatarajiwa kuongezeka kwa makusanyo ya mwezi Mei na Juni, 2017 baada ya mifumo yote kukamilika ikiwa ni pamoja na wananchi wengi kupata elimu na kuitikia wito wa kulipa kodi ya majengo kwa hiari kwa tarehe za mwisho wa mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna fidia inayotolewa au itakayotolea na Serikali Kuu badala yake halmashauri zitarejeshewa makusanyo ya kodi ya majengo kulingana na nakisi ya bajeti ya halmahsauri husika. Kwa mantiki hiyo, kodi ya majengo itaendelea kuwa ni chanzo cha mapato ya halmashauri na Serikali kwa ujumla kwa mujibu wa sheria na kwamba chanzo hicho hakijapotea bali mfumo wa ukusanyaji umebadilishwa na kuboreshwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitangaza kuzinyang’anya Halmashauri uwezo wa kukusanya mapato ya kodi ya majengo (property tax) na kuagiza kodi hiyo kukusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).
(i) Je, baada ya Mamlaka ya Mapato kupewa jukumu hilo, ufanisi umefanikiwa kwa kiasi gani ikilinganishwa na mapato yaliyokuwa yakikusanywa na Halmashauri zenyewe?
(ii) Kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji na majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi hayajapunguzwa. Je, Serikali imejipanga vipi kufidia vyanzo hivyo vilivyopotea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa (The Local Government Finance Act, Cap. 290) kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 na kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania jukumu la kukusanya kodi ya umiliki wa majengo yaani (property tax) kwa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30. Ufanisi wa Mamlaka ya Mapato ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, makusanyo yatokanayo na kodi za majengo kutoka Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji 30 yaliyokuwa yakisimamiwa na TRA yameongezeka kutoka shilingi bilioni 28.28 kwa mwaka 2015/2016 zilizokusanywa na Serikali za Mitaa hadi shilingi bilioni 34. 09 kwa mwaka 2016/2017 kipindi ambacho TRA ilianza kukusanya kodi hii. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 20.6 ya makusanyo ya Halmashauri husika kabla ya kodi hii kuhamishiwa TRA.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma za jamii. Hata hivyo, hatua ya Serikali ya kuhamishia jukumu hilo la ukusanyaji wa kodi za majengo TRA haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali kuimarisha ukusanyaji wake. Takwimu nilizotoa hapo juu zinadhihirisha kuwa TRA imefanya vema katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu wa kibajeti ambao unaziwezesha Halmashauri kupata fedha za makusanyo ya kodi ya majengo iliyokusanywa na TRA ili kuziwezesha kutimiza majukumu yao. Utaratibu uliopo ni kwamba Halmashauri zinatakiwa kuomba fedha hizo kutoka Serikali kuu kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao. Kwa mantiki hiyo, Halmashauri zinashauriwa kuzingatia utaraibu huo ili ziweze kupata fedha hizo.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kama Serikali ya viwanda na kuna Shirika la Serikali lililoanzishwa kwa ajili ya kuanzisha na kuimarisha Viwanda Vidogo Vidogo vya SIDO .
(a) Je, kwa kiasi gani Serikali imeliwezesha Shirika hilo katika kufikia malengo yake na malengo ya Serikali kwa Tanzania ya viwanda?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Shirika hilo linakuwa na matawi katika kila Wilaya tofauti na sasa kuwa na Ofisi katika ngazi za Mikoa tu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuliwezesha Shirika la SIDO kutoa huduma za kujenga uwezo kwa wajasiriamali kupitia programu za mafunzo, ushauri, teknolojia, masoko na utoaji wa mitaji. Katika kufanikisha hilo Serikali imekuwa ikiimarisha bajeti za SIDO kila mwaka na kwa mwaka wa fedha 2018/2018 SIDO ilitengewa shilingi bilioni 14.2 kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya viwanda na kuongeza mtaji kwenye mfuko wa NEDF. Kati ya fedha hizo Serikali imekwishatoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Ofisi na Industrial Sheds katika mikoa ya Simiyu, Geita, Kagera kwa hatua ya kwanza na utaratibu unakamilika kwa hatua ya pili katika mikoa ya Mtwara, Manyara, Dodoma na Katavi.
Pia Serikali kwa kushirikiana na wabia na maendeleo ikiwemo Serikali ya Japan kupitia JICA, Serikali ya Canada kupitia CESO na Serikali ya India zimeendelea kuipatia SIDO uwezo ikiwemo kuanzisha vituo vya viatamizi vya kuonyesha na kufundishia teknolojia mbalimbali, kuendesha makongano ya wanaviwanda vidogo nchini na kushirikiana na SIDO kutambua mahitaji halisi ya wajasiriamali na kuwasaidia kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira yetu kuwa karibu na wananchi katika dhama hizi za kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda kwani viwanda vidogo na vya kati ni muhimu katika kujenga uchumi ulio jumuishi. Kutokana na ufinyu wa bajeti kwa sasa tunahudumia ngazi ya kata mpaka Wilaya kwa kupitia Halmashauri za Wilaya.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inawapa mamlaka ya kipolisi Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwatia nguvuni watu wa muda wa saa 48, lakini sheria hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kutoa amri za kukamata Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na hata watumishi wa umma wakiwemo madaktari.
• Je, Serikali inawachukulia hatua gani Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaotumia vibaya madaraka na sheria hiyo?
• Je, ni lini Serikali itaifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuwaondolea Wakuu wa Mikoa na Wilaya mamlaka ya kuwaweka watu ndani kwa kuwa ni kandamizi, inakiuka haki za binadamu na inatumika vibaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kisheria ni wasimamizi wa shughuli zote za Serikali katika maeneo yao ya utawala. Hivyo, ni jukumu lao kuchukua hatua pale sheria za nchi zinapokiukwa ili kuhakikisha kunakuwepo amani na usalama kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa jumla. Hata hivyo, wapo baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao wanatumia vibaya mamlaka yao, tayari Serikali imetoa maelekezo mahususi kuzingatia mipaka yao ya kazi katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa Wakuu wa Mkoa na Wilaya wamepewa madaraka ya kuwa mlinzi wa amani na usalama (peace and security). Kifungu cha 7 na 15 vya Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura, 97 Vinawapa Mamlaka viongozi hao kumweka ndani mtu yeyote kwa muda wa saa 48 ikiwa itathibitika kuna hatari ya uvunjifu wa amani na usalama au mtu huyo ametenda kosa la jinai. Tumetoa maelekezo yanayofafanua matumizi mazuri ya sheria hii kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote pamoja na mafunzo kuhusu mipaka na majukumu ya kazi zao, hivyo kwa sasa sheria inajitosheleza, ila tutaendelea kusisitiza matumizi sahihi ya sheria husika.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Wananchi wengi wa Tarafa ya Eyasi katika Wilaya ya Karatu wanajishughulisha na kilimo cha vitunguu maji, hata hivyo mavuno yanayotokana na kilimo hicho hupimwa kwa debe yanapouzwa badala ya kilo.
Je, ni kwa nini Serikali isihakikishe na kusimamia uuzwaji wa mazao haya kwa kutumia kilo badala ya vipimo vya debe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Namba 340 ya mwaka 2002 na mapitio yake ya mwaka 2016, vipimo sahihi ni kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo na siyo vinginevyo ambapo kipimo chake ni kilo kwa bidhaa za aina hii yaani vitunguu vikiwa ni mojawapo vinavyostahili kupimwa kwa kilo.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa njia ya redio, luninga, makala za magazeti na kwa kushiriki katika maonesho mbalimbali. Vilevile Wakala wa Vipimo wametoa elimu kwa wadau wa biashara hiyo ya vitunguu huko Mang’ola Tarafa ya Eyasi wakiwemo wakulima, viongozi wa vijiji, kata, tarafa, halmashauri ya wilaya kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya vipimo vinavyoruhusiwa kisheria.
Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Vipimo ilipitiwa na Bunge lako Tukufu mwezi Novemba, 2016 ili kuruhusu Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na Sheria Ndogo (by-laws) za kuwawezesha kuanzisha vituo vya ununuzi wa mazao na bidhaa katika eneo la mamlaka husika vitakavyokuwa na mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo. Hali kadhalika, Serikali inaendelea kuhamasisha ujenzi wa vituo maalum vya ununuzi wa mazao (buying centres) vyenye nafasi ya maghala ya kuhifadhia mazao, ambapo kwa Tarafa ya Eyasi, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kwa kushirikina na wadau wa maendeleo tayari imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kituo katika kijiji cha Mang’ola chenye maghala matatu kwa ajili ya kuhifadhi vitunguu. Kituo hiki kinatarajia kuanza kutumika katika msimu wa mwaka huu wa ununuzi wa vitunguu. Vituo vya aina hii vitasaidia wakulima kuwa na nguvu ya pamoja kujadiliana na wanunuzi na kutumia vipimo sahihi ili kupata bei yenye ushindani na haki katika soko.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu ninapenda kuwatahadharisha wakulima na wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara ya vitunguu na mazao mengine yote kuhakikisha kuwa wanatumia vipimo sahihi. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia kuchukua hatua za kisheria pale inapobidi kufanya hivyo kwa wanaokiuka sheria hiyo.
MHE. CECILIA D. PARESO aliuliza:-
Serikali ilihusika kikamilifu katika uanzishwaji wa kituo kijulikanacho kama International Graet Lakes Woman Research Centre ambapo kwa Tanzania kituo hicho kuliazimiwa kiwe Tengeru Arusha:-
i. Je, mpaka sasa utekelezaji wake umefikia wapi?
ii. Je, ni mafanikio gani yamepatikana tangu kituo hicho kianzishwe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Pareso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Great Lake Woman Recherch and Documentation Centre kilianzishwa mwaka 2009 ikiwa ni utekelezaji wa maazimio kikao cha Mawaziri, wanaosimamia masuala ya wanawake kutoka nchi za Maziwa Makuu kilichofanyika mwezi Julai, 2008 Kinshasa, Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nchini kituo hicho kilianzishwa chini ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii, Tengeru kwa malengo ya kufanya utafiti kuhusu masuala ya maendeleo ya jinsia na wanawake hapa nchini, kuhifadhi matokeo ya tafiti hizo ili kuwasaidia watunga sera na wafanya maamuzi kukusanya taarifa na takwimu mbalimbali zinazohusiana na jinsia na wanawake pamoja na kusambaza taarifa hizo kwa njia mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zilizofikiwa katika kuanzisha Kituo hicho, ni pamoja na kutenga eneo maalum ndani ya taasisi linalotumika kwa ajili ya kituo; kukipatia Kituo hicho rasilimali watu ikiwemo Mratibu wa Kituo pamoja na Mkutubi kwa ajili ya kuendesha na kusimamia shughuli za kituo; Kukipatia kituo vifaa ikiwemo computer ishirini na nne, mashine ya fax na simu; kuanzisha tovuti ya kituo inayopatikana kwa anuani ya www.wrdc. or.tz kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kuanzishwa kwa kituo hicho baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kwa wanawake na wanaume ili kuwajengea uwezo wa kuendesha shughuli zao na kujiongezea kipato kwa ufanisi na hivyo kupunguza umasikini kwenye jamii. Aidha, chuo kimetoa mafunzo kwa wanafunzi mia mbili wa shule za sekondari ili kuwajengea uelewa wa masuala ya ukatili wa jinsia na madhara yake katika kujenga uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kituo kimewahudumia zaidi ya watu mia tatu ishirini kati ya hao wanawake mia mbili thelathini na moja na wanaume sabini na tisa; na kuwawezesha kupata taarifa walizozihitaji zenye kuelimisha kuhusiana na masuala ya haki za umiliki wa ardhi kwa wanawake, ukatili wa kijinsia na elimu ya ujasiriamali kupitia tovuti na machapisho mbalimbali yaliyopo kwenye Kituo.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Kwa kuwa tumebakiza mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020 na ili Watanzania waliokidhi vigezo wapate haki ya kupiga kura, uboreshaji wa daftari la kupiga kura ni jambo lisiloepukika:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha mchakato wa kuboresha daftari la wapiga kura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura ulianza mwezi Agosti, 2018 kwa kufanya maandalizi yafuatayo:-
(i) Kuhuisha kanzidata ya Daftari la Kudumu la Wapiga kura; na
(ii) Kuboresha mifumo ya uandikishaji na utunzaji wa kumbukumbu za Daftari
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchuguzi ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mara ya kwanza na uandikishaji wa majaribio kwa baadhi ya mikoa ili kuona ufanisi au changamoto zinazoweza kujitokeza unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Wilaya ya Karatu ilipata mfadhili wa kujenga Chuo cha VETA na ujenzi umekamilika toka mwaka 2017 na tayari majengo yote yamekabidhiwa kwa Halmashauri.
Je, ni lini sasa Serikali itakipa Chuo hicho usajili wa kudumu pamoja na mahitaji mengine kama ilivyo katika vyuo vingine?
NAIBU WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi nchini husajiliwa kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Utaratibu wa kuomba usajili huhusisha kujaza fomu inayopatikana katika tovuti ya VETA na kwenye Ofisi zote za Kanda za VETA. Ofisi za kanda hukagua vyuo vilivyoomba na kupewa usajili wa awali (Preliminary Registration). Hii ni hatua ya mwanzo kuelekea kupata usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, usajili kamili hutolewa baada ya kufanyiwa tathmini ambayo inahusisha kutimiza vigezo ambavyo ni chuo kuwa na mfumo wa uendeshaji unaosimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi au ya Wadhamini pamoja na menejimenti yenye sifa stahiki za kitaaluma. Chuo kuwa na miundombinu stahiki kwa mujibu wa viwango na vigezo vilivyowekwa. Chuo kuwa na vifaa na mitambo ya kufundishia kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na chuo kuwa na Walimu wenye sifa stahiki za kitaaluma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarehe 26 Novemba mwaka 2019, Chuo cha VETA Karatu kilipewa fomu ya kujitathmini ili kijaze na kuwasilisha ofisi za VETA Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi wa mwisho ili kipate Usajili Kamili yaani Full Registration kwa mujibu wa taratibu za usajili. Hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu haijarejesha fomu hii, ili iweze kupatiwa usajili wa kudumu na kuanza kudahili wanafunzi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO) aliuliza:-
Mfumo wa Vehicle Tracking System umefungwa katika mabasi yote nchini ili kudhibiti mwendokasi kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani:-
(a) Je, mfumo umegharimu fedha kiasi gani?
(b) Je, mzabuni wa kazi hii kwa nini hakupatikana kwa ushindani kwa kufuata Sheria ya Manunuzi?
(c) Je, mfumo huu unaendeshwa na kusimamiwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kuhusiana na mfumo wa Kuratibu Mwenendo wa Mabasi (Vehicle Tracking System), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa VTS ni mfumo unaowezesha upatikanaji wa taarifa mbalimbali za basi likiwa safarini. Taarifa hizo ni pamoja na mwendokasi, mahali basi lilipo, matukio ya ajali, jina la dereva na kadhalika. Taarifa hizi hupatikana baada ya basi kufungwa kifaa maalum cha mawasiliano kinachochukua matukio na kuyarusha kupitia mfumo wa satelaiti na teknolojia ya Global Postioning System
- GPS pia kupitia mitandao ya simu yenye teknolojia za Global Pocket Radio System - GPRS na hivyo kutoa taarifa za basi husika kwa wakati (real time). Lengo la kuweka mfumo huo pamoja na mambo mengine ni kudhibiti matukio ya ajali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa VTS uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.4 ambazo zilitokana na mapato ya Serikali kupitia SUMATRA.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mzabuni aliyefanya kazi hii ni Kampuni ya BSMART Technologies ya Malaysia akishirikiana na Kampuni ya Computer Center ya hapa nchini na alipatikana kwa njia ya ushindani kwa mujibu wa kifungu cha 150 cha Kanuni ya Sheria ya Manunuzi, Tangazo la Serikali No.446 la mwaka 2013. Zabuni hiyo ilitangazwa kupitia zabuni ya kimataifa Na.AE/025/2015-2016/HQ/G/22 katika gazeti la Daily News la tarehe 14 Januari, 2016 pia kupitia PPRA Tender Portal, Tanzania Procurement Journal Toleo No. ISS:1821 VOL IX-No.3 pia zabuni ilitangazwa kwenye tovuti ya SUMATRA.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu unasimamiwa na kuendeshwa na SUMATRA kupitia kituo maalum kilichoko Mikocheni Jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, SUMATRA imeingia mkataba na Kampuni ya TERA Technologies and Engineering Company kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo kwenye magari. Kampuni hiyo ilipatikana kwa ushindani kupitia zabuni (Invitation for Tenders Na.AE/025/2016- 2017/HQ/G/39 ya tarehe 25 Oktoba, 2017 ambayo pia ilitangazwa kupitia PPRA Tender Portal, Tanzania Procurement Journal na kwenye tovuti ya SUMATRA.
MHE. CECILIA D. PARESSO Aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuyagawa kwa wananchi mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji katika Kata za Daa na Oldeani, Wilayani Karatu ambayo hayaendelezwi huku wananchi wakikosa ardhi kwa ajili ya makazi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kusimama toka Bunge la Kumi na Mbili limeanza, naomba unipe fursa na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema, lakini nimshukuru sana Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini tena katika kipindi hiki cha pili, kunipa dhamana ya kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, niwashukuru Wanailemela wote walionipa fursa hii ya kuweza kuwatumikia kwa miaka mingine mitano na kwa leo nitoe pole kwa msiba mkubwa wa Mkuu wa Shule ya Bwiru, shule ya ufundi, Ndugu Elias Kuboja ambaye amefariki dunia. Nawapa pole Wanailemela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshinia Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya kazi ya uhakiki na ukaguzi wa mashamba makubwa nchini ili kubaini uzingatiwaji wa masharti ya umiliki yaliyotolewa. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kubatilisha milki za mashamba ambayo wamiliki wamekiuka masharti ya uendelezaji. Katika kipindi cha miaka mitano (2015 – 2020) jumla ya mashamba 45 yenye jumla ya ekari 121,032.243 yalibatilishwa kutokana na waliokuwa wamiliki kushindwa kutekeleza masharti ya umiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata za Daa na Oldeani Wilaya ya Karatu, kuna mashamba 25 ambayo yalimilikishwa kwa wawekezaji kwa ajili ya shughuli mbalimbali hususan kilimo na ufugaji. Taarifa za awali za uhakiki zinaonesha kuwa mashamba hayo yameendelezwa kwa viwango tofauti ambapo mashamba tisa yameendelezwa kwa wastani wa asilimia 50. Sehemu nyingine ya mashamba hayo imejengwa miundombinu ya barabara na huduma za jamii kama vile shule, nyumba za kulala wageni, viwanda, vituo vya watalii na kadhalika. Kwa sasa Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa kina wa mashamba yote na kuchukua hatua kwa wamiliki ambao wameshindwa kutimiza masharti ya umiliki.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Wananchi wanaoishi jirani na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Wilayani Karatu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha kubwa ya wanyama kuingia na kuvamia mashamba yao na wakati mwingine kujeruhi wananchi:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo na ufugaji kwenye shoroba za wanyama, maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na maeneo ya kinga ya Hifadhi ya Ngorongoro, kumekuwepo na changamoto ya wanyamapori kuingia kwenye mashamba yaliyopo pembezoni mwa hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto hii, Wizara inatoa rai kwa wananchi kutumia mbinu mbadala za kuepuka wanyamapori wakali na waharibifu kuingia kwenye maeneo yao. Mbinu hizo ni pamoja na kwanza, ni kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki kwenye mipaka ya Hifadhi zilizo karibu na maeneo ya vijiji ili kuhakikisha kuwa wanyamapori hawavuki kwenda kwenye mashamba hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu nyingine ni wananchi wanahamasishwa kulima zao la pilipili kandokando ya mashamba yao, kwani zao hili limeonekana kuwa ni tishio kwa wanyama wakali na waharibifu kama tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu nyingine ni wananchi wanashauriwa kutopanda mazao yanayovutia tembo kusogea katika mashamba yao kama vile mazao yanayohusiana na katani, miwa, ndizi na matikiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wananchi kuendelea kutumia oil chafu iliyochanganywa na pilipili na majivu ili kuzuia wanyama kama tembo kusogea kwenye maeneo ya mashamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni wananchi wanashauriwa sasa kutoa taarifa haraka pindi wanyama hao wanapoonekana kukaribia kwenye maeneo ya mashamba.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za kuongezeka kwa matukio mbalimbali ya wanyama wakali wakiwemo tembo, Wizara imeongeza idadi ya vituo vya muda na vya kudumu vya askari katika maeneo yaliyohifadhiwa likiwemo eneo la Ngorongoro (Wilaya ya Karatu) na kuendelea na doria za usiku kuhakikisha wanyamapori waharibifu wanarudishwa hifadhini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa ulioanza tangu Desemba, 2020 ambao umefanya gharama za maisha kupanda?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei ulipanda kutoka asimilia 3.2 mwezi Desemba 2020 hadi asilimia 3.5 mwezi Januari 2021. Hii ilitokana na upungufu wa baadhi ya bidhaa sokoni ambao hutokea mara kadhaa katika vipindi vya mwanzo wa mwaka kama hivyo.
Aidha, mfumuko wa bei ulishuka na kufikia asilimia 3.3 mwezi Februari 2021 ikiashiria kuwa bidhaa na huduma zilianza kupatikana kwa bei nafuu kulinganisha na mwezi Januari mwaka uliopita.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unaendelea kubaki ndani ya wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0. Lengo hili linaweza kufikiwa kutokana na mikakati mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha usambazaji wa chakula kutoka maeneo ya uzalishaji hadi katika maeneo ya walaji, kuimarisha usimamizi wa Sera ya Fedha na bajeti na kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi katika masoko.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na baadhi ya askari wa TANAPA wanaolinda Hifadhi ya Msitu wa Marang inayopakana na Kata ya Buger Wilayani Karatu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wananchi wanaoingia kwenye hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, baadhi ya wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Msitu wa Marang, hasa wafugaji wanapoingiza mifugo yao hifadhini na kukamatwa na askari wa hifadhi, hukataa kutii sheria bila shuruti na kupiga yowe maalum ijulikanayo kama HAYODAA ikiwa ni kiashiria cha hatari kwa kabila la Wairaki. Hivyo, wananchi wengi hujitokeza wakiwa na silaha za jadi zikiwemo fimbo, mishale, mapanga na mikuki ili kuwadhuru askari wa hifadhi na kupinga ukamataji huo wa mifugo na kuchukua mifugo yao kwa kutumia nguvu.
Mheshimiwa Spika, yamefanyika matukio mengi ya askari kunyang’anywa silaha au mifugo iliyokamatwa hifadhini na wananchi ambapo husababisha kutokuelewana kati ya askari wa hifadhi na wananchi. Kati ya mwaka 2013 hadi 2020 jumla ya matukio saba yalitokea ambayo yalihusisha wananchi kuwashambulia askari wa hifadhi, kuwajeruhi na wengine kupoteza maisha.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau pamoja na wananchi wa maeneo hayo imeandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ambapo kwa sasa hati zinaandaliwa na baada ya uhakiki wananchi watakabidhiwa hati hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, nini kauli ya Serikali katika kutatua changamoto ya wimbi kubwa la mauaji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge Wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimwa Spika, ni kweli kumekuwa na ongezeko la matukio ya mauaji hapa nchini. Matukio mengi yanasababishwa na wananchi kwanza kujichukulia sheria mikononi mwao, lakini pili ni wivu wa mapenzi, lakini zaidi migogoro ya ardhi, ulevi na imani za kishirikina.
Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti wimbi hili tuliunda tume maalum ya kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua, pamoja na kuchukua hatua za kisheria kama zilivyopendekewa na tume tuliyoiunda, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwashirikisha viongozi wa siasa, dini, wazee wa mila na watu wanaoheshimika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, katika kutatua migogoro na migongano katika jamii. Nashukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, nini kauli ya Serikali kwa wakulima wa vitunguu maji katika Bonde la Eyasi juu ya upatikanaji wa masoko pamoja na bei ya zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanapata soko la uhakika, na kuwa mkulima anapata bei nzuri na kunufaika.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Idara ya Maendeleo ya Biashara na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya zao la vitunguu maji vinavyolimwa hapa nchini, ikiwa ni pamoja na vitunguu kutoka Bonde la Eyasi ili kupata bei nzuri itakayo wanufaisha wakulima wa zao hilo hapa nchini. Nakushukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya matukio ya moto katika Masoko kwenye maeneo mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu: -
Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na matukio ya moto katika baadhi ya masoko nchini. Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine umebaini sababu mbalimbali za matukio hayo. Sababu hizo ni pamoja na uunganishwaji holela wa mifumo ya umeme, kutokuzingatia tahadhari za moto kwa mama lishe na baba lishe na shughuli za uchomeleaji holela wa vyuma katika masoko.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vyanzo vya matukio hayo umefanyika ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo ya matumizi ya vifaa vya awali vya kuzima moto katika masoko nchini. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inashirikiana na Halmashauri zote kuboresha miundombinu ya kuzima moto katika masoko na kuhakikisha ramani za masoko mapya zinakaguliwa na zinakidhi vigezo vya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusisitiza uwepo wa vifaa vya awali vya uzimaji moto, uwepo wa ulinzi wa masoko kwa saa 24 na kuzingatia utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa maalum za kaguzi zinazotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Nashukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha mifumo ya utoaji leseni katika Sekta ya Utalii ili kurahisisha upatikanaji wa leseni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeshaunganisha mfumo wa utoaji wa leseni katika sekta ya utalii kupitia mfumo wa kieletroniki wa MNRT – Portal. Hatua hiyo imeongeza tija katika utoaji huduma ikiwemo kurahisisha mchakato wa utoaji wa leseni za biashara za utalii na hivyo kupunguza gharama, muda na kuongeza wigo wa ushiriki wa wananchi na wawekezaji mbalimbali katika biashara hizo.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuvuna fisi wanaovamia makazi ya Wananchi, kujeruhi na kuua Watu katika Kata ya Endamarariek?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto ya fisi kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi hususan kwenye Kata ya Endamarariek Wilayani Karatu, Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imekuwa ikifanya msako wa fisi katika maeneo husika ambapo tangu mwaka 2019 hadi sasa jumla ya fisi saba wamevunwa. Aidha, mapango/makazi ya fisi 11 yameharibiwa katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fisi wanaishi katika makundi, Wizara inaendelea kufanya soroveya ili kuyabaini makundi ya fisi yaliyosalia na kuyavunja ikiwa ni pamoja na kuharibu makazi yao.
MHE. GRACE V. TENDEGA K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia msaada wa kisaikolojia watu waliopitia ukatili wa kijinsia?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha vituo 22 vya huduma ya mkono kwa mkono (One Stop Centres) kwa ajili ya hospitali za mikoa 13 ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Arusha, Tabora, Morogoro, Kigoma, Dodoma na Simiyu kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Vituo hivyo hutoa huduma za kipolisi, ushauri nasaha na huduma za afya. Lengo la Serikali ni kuwa na kituo angalau kimoja kwa kila Mkoa. Vilevile kuna nyumba salama 11 nchini na Madawati ya Jinsia katika vituo vyote vya polisi na magereza. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaipatia ruzuku Bodi ya Maji ya KAVIWASU kwa kuwa imekuwa ikiendeshwa kwa gharama za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Maji Namba 5 ya mwaka 2019 ya Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira kupitia kifungu cha 13(1)(b) vyombo vya watumia maji vinaruhusiwa kutoa huduma za maji kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ambapo chombo cha watumia maji cha KAVIWASU kinatoa huduma kwenye baadhi ya maeneo ya mji wa Karatu. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha hakuna changamoto katika utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa mji wa Karatu unapata huduma ya maji inayotolewa na kusimamiwa na taasisi mbili za KARUWASU na KAVIWASU. Hivyo, Serikali inao mpango wa kuanzisha taasisi moja na imara itakayotoa huduma ya maji kwa ufanisi kwa eneo lote la mji wa Karatu. Taasisi hiyo itapata ruzuku kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali ilivunja Mradi wa Maji wa KAVIWASU katika Mji wa Karatu bila kuwashirikisha wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Maji Namba 5 ya mwaka 2019 ya Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira kupitia kifungu Na. 13(1)(b) vyombo vya watumia maji vinaruhusiwa kutoa huduma za maji kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ambapo chombo cha watumia maji cha KAVIWASU kilikuwa kinatoa huduma kwenye baadhi ya maeneo ya Mji wa Karatu.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma ya maji kwenye Mji wa Karatu, Serikali iliunganisha vyombo viwili vya kutoa huduma ya maji vya KARUWASU na KAVIWASU kuwa chombo kimoja ambacho mpaka sasa kimeendelea kutoa huduma ya maji kwa ufanisi katika eneo lote la Mji wa Karatu. Uundaji wa chombo hicho ulishirikisha wananchi ambapo Wizara ilifanya majadiliano ya kina na Mamlaka za Serikali, Wawakilishi wa Wananchi wa Karatu na wadau wa maji na kufikia maamuzi ya kuviunganisha vyombo hivyo viwili ili kiwepo chombo kimoja madhubuti kitakachosimamia utoaji wa huduma endelevu na kuondoa mkanganyiko wa bei za huduma.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji katika Kijiji cha Chemchem – Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Chemchem unaohusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 135,000 kwenye mnara wa meta sita, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 16.5, ujenzi wa vituo 14 vya kuchotea maji, ujenzi wa ofisi ya CBWSO, ujenzi wa nyumba ya kuendeshea mitambo (pump house), kufunga mfumo wa umeme jua (solar system) pamoja na ujenzi wa mbauti ya kunyweshea mifugo (cattle trough).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 85% na umeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo; Shule ya Msingi Chemchem, Shule ya Sekondari Chemchem na Zahanati ya Chemchem. Utekelezaji wa mradi huo unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2024 na kunufaisha wananchi wapatao 6,010 wa Kijiji cha Chemchem, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji uliokwama kwa muda mrefu katika Kijiji cha Mang’ola Juu Wilayani Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Kijiji cha Mang’ola Juu Wilayani Karatu. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matenki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita 270,000, ulazaji wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 30, ujenzi wa vituo 25 vya kuchotea maji, ujenzi wa Ofisi ya CBWSO, ujenzi wa nyumba ya kuendeshea mitambo (pump house) na ujenzi wa mbauti tatu za kunyweshea mifugo (cattle trough).
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 30% ambapo umeanza kutoa huduma kwenye baadhi ya maeneo kupitia vituo saba vilivyokamilika wakati utekelezaji ukiendelea. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 na kunufaisha wananchi 5,616 waishio kwenye vijiji cha Mang’ola Juu, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha miradi ya Umeme katika Vitongoji na Vijiji ambavyo havijafikiwa na miradi hiyo Wilayani Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Karatu ina jumla vijiji 57 ambapo vijiji vyote vimeshapatiwa umeme. Aidha, Jimbo hilo lina vitongoji 265 na kati ya hivyo, 125 vina umeme na 140 havina umeme. Kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji ambavyo havina umeme inaendelea ambapo Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 10 kupitia mradi wa ujazilizi 2B na vitongoji 15 kupitia Mradi wa Vitongoji 15 kwa kila Jimbo katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, hivyo, vitongoji 115 ndivyo vilivyosalia ambapo kazi ya kuvipelekea umeme itaendelea kuratibiwa na Wakala Nishati Vijijini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya kutoka Karatu – Mang’ola – Matala hadi Lalago kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Karatu – Mang’ola – Matala – Lalago yenye urefu wa kilomita 229 umekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha, kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Karatu – Mang’ola – Matala hadi Sibiti yenye urefu wa kilomita 156. Ahsante.