Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Cecilia Daniel Paresso (135 total)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika ahsante, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, Waziri amekiri hapa kwamba kati ya mwaka 2011/2014 waliandaa mpango wa majaribio wa kuwaondoa watoto hawa wanaoishi katika mazingira hatarishi, na suala la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi linaeleweka, na ni kubwa ndani ya nchi hii. Ni kwa nini Serikali hii ya CCM mnafanya mipango ya majaribio ambayo inatumia muda mrefu, fedha nyingi na yenye matokeo machache au matokeo kidogo?

Swali la pili, umekiri katika majibu yako kwamba meaandaa Mpango Kazi wa kuweza kuwaondoa watoto hao wanaoishi katika mazingira hatarishi. Ni kwa kiasi gani Mpango Kazi huu umekuwa shirikishi kwenye Serikali zetu za Mitaa kwa maana ya Halmashauri, ili na wao waziweke katika bajeti yao, ili kwa pamoja waweze kuona watoto hawo wanaondoka katika mazingira hatarishi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Asante, nakushukuru Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii, na ninakushukuru Mheshimiwa Paresso kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwamba ni kwa nini Serikali inaandaa mpango wa majaribio ni kwa sababu za kitaalamu. Hauwezi ku-embark kwenye mradi mkubwa utakaolihusisha Taifa zima kwenye Mpango Mkakati wa kuwaondoa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu bila kufanya pilot study. Labda kiswahili tu kinaweza kikawa kinasumbua lakini kwa namna yoyote ile kwenye operational research na kwenye programming huwa tunaanza kwa kufanya pilot study ambayo ikifanikiwa tutakuwa tumejifunza changamoto zilizopo na baada ya hapo sasa tunaweza tuka scale up kwenye eneo kubwa zaidi. Kwa hiyo, kuanza na pilot study ni taratibu za kawaida tu kwenye programming.

Swali la pili, ni kwa namna gani mpango huu umekuwa shirikishi, majibu ni kwamba wakati unafanya pilot study jambo la kwanza ambalo unalolifanya ni kufanya table research. Ni kufanya utafiti wa mezani, unasoma tafiti mbalimbali, unaangalia nyaraka mbalimbali lakini baada ya hapo unatengeneza dodoso ambalo unawashirikisha wadau mbalimbali, na mwanzoni sasa unafanya formative assessment maana yake unawakusanya wadau, unawashirikisha kwenye utafiti wako wa awali ambao umeufanya kwa kutumia nyaraka mbalimbali na baada ya hapo sasa wale wadau waliopo watakupa, mawazo utajifunza changamoto kutoka kwao, utaziona fursa kutoka kwao, utaweza kupanga mbinu kwa pamoja na wao na kwa maana hiyo wanakuwa sehemu ya mradi husika.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Wilaya ya Arumeru Mashariki kwa kiasi kikubwa ardhi yake inamilikiwa na wawekezaji na ni ukweli mara nyingi kumetokea migogoro kutokana na wananchi kuwa na mahitaji makubwa ya ardhi, na kwa kuwa mpaka sasa mnasema ni ekari 80 tu imerudi katika Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, je, Serikali haioni sasa uko umuhimu wa kupitia mashamba hayo na kufanya tathmini upya ili wananchi hawa ambao wanahitaji ardhi waweze kupata ardhi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa mzima wa Arusha maeneo mengi pia ardhi yao imemilikiwa na wawekezaji ikiwemo Wilaya ya Karatu ninayotoka na kumekuwa na mgogoro mkubwa sana wa wananchi kuhitaji ardhi kwa sababu ardhi nyingi imemilikiwa na wawekezaji mfano Shamba la Tembo Tembo liloko Karatu. Je, Serikali sasa iko tayari kufika Wilaya ya Karatu na kufanya tathmini ya kuwatambua wawekezaji ili wananchi waweze kupata ardhi yao?
NAIBU WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ametaka kujua Serikali ina mpango gani katika kuyatambua mashamba yote haya na kufanya tathmini ili yaweze kugawiwa kwa wananchi. Naomba niseme kwamba mpaka sasa Waziri alishapeleka barua katika Mikoa yote ikiwataka kwanza wao wayatambue kwa sababu wanayafahamu, lakini mpaka sasa Wizara yangu imeshabaini mashamba 22 katika Mkoa wa Arusha ambayo tayari yameshabatilishwa kwa minajili ya kuja kuwagawia wananchi wenye shida ya maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili anazungumzia habari ya mgogoro na uhitaji wa ardhi katika eneo la Karatu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi mwenyewe nilifika Karatu na migogoro hiyo niliambiwa na wakati huo nilikuwa nashughulikia masuala ya Mabaraza ya Ardhi. Hata hivyo, kwa sababu Wizara imeweka mpango mzuri kwa ajili ya kuweza kuyafikia maeneo yote kwa wakati, tunajaribu kukusanya migogoro yote na ndiyo maana tuliomba tuweze kuipata na tuko tayari kurudi tena Karatu kwa ajili ya kutatua mgogoro huo ambao anauzungumzia. Kabla ya Bajeti ya Wizara kuisha, Wabunge wote watakuwa wamegawiwa vitabu na wataweza kubaini migogoro ambayo tumeiainisha ambayo tunatarajia kuanza kuitembelea baada ya Bunge hili kumalizika. Kwa sababu migogoro ya ardhi ni suala mtambuka na Wizara zingine zitahusika. Kwa hiyo, kila Mbunge ataona katika Mkoa au Wilaya yake ni migogoro ipi ambayo Wizara imeiainisha kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu umegharimu shilingi bilioni tano kwa hospitali ya Bombo, Tanga, Mwananyamala na kitengo cha MOI. Je, Serikali ilifanya utafiti wa gharama halisi za mifumo hii kutoka kwenye taasisi zingine ambazo zimefunga mfumo huu kwa gharama nafuu sana mfano hospitali ya Haydom imefunga kwa gharama ya shilingi milioni 150, Hospitali ya Seliani imefunga kwa gharama ya shilingi milioni 120. Je, mlifanya utafiti?
Swali la pili; kuna tafiti zimefanyika katika kufunga mfumo huu kwenye hospitali za Wilaya inagharimu kati ya shilingi milioni 28 mpaka 35 na hospitali za Rufaa inagharimu kati ya shilingi milioni 75 mpaka milioni 200. Nataka kupata taarifa ya Serikali, hapa hakuna harufu ya ufisadi kwa Hospitali 5 kufunga mfumo kwa shilingi bilioni 5 na hapo hapo, Hopsitali ya Bombo ya Tanga ilishakuwa funded na Wajerumani kufunga mfumo huu lakini kupitia NHIF tena wamepewa fedha katika hii bilioni 5.
Je, mko tayari kufanya utafiti? Kufanya Special audit? Kuleta taarifa hapa na wahusika wawajibishwe?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa maswali yake ya nyongeza. Pili nimpe taarifa tu kwamba kuna tofauti ya mifumo inayofungwa kwenye hospitali za Wilaya na mfumo huu ambao umefungwa kwa ufadhili wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Katika hospitali za Wilaya, tunafunga Electronic Payment Systems tu! Hatufungi Comprehensive, Health Management Information System, ambayo yenyewe inaunganisha hadi na taarifa za Bima ya Afya na taarifa za Vizazi na Vifo lakini pia taarifa za claims – Online Claims System ambayo inawafanya hospitali husika waweze ku-submit maombi ya madai yao ya Bima ya Afya kwa Bima ya Afya kwa njia ya mtandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo mifumo tunayofunga ni tofauti sana kati ya hii inayofungwa kwenye Hospitali za Wilaya, Hospitali za Mikoa na huu mfumo mahsusi ambao umefungwa katika hizi hospitali 5 kwa majaribio na taasisi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), labda nimwambie tu kwamba kwa kufanya huu utaratibu wa kufunga mifumo ya kielektroniki, Serikali imeweza kufanya mapinduzi makubwa katika makusanyo ya fedha zinazopatikana kwa kutoa huduma za afya kwa wananchi nchini. Mimi hapa ninayezungumza nimekuwa pioneer wa wazo hili ndani ya Serikali, hivyo ninafahamu mifumo hii na ninaelewa tunachokifanya ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba mfumo uliofungwa kwa ufadhili huu wa NHIF umekuja pamoja na source codes, kitaalam ndiyo mfumo halisi, ndiyo ile Architecture halisi ya mfumo huo. Kwa hiyo, kazi iliyobaki sasa ni kwa taasisi ya NHIF kuchukua hizi source codes na kuwekeza kwenye switch zile za mtandao kuwekeza kwenye computer, kwa ajili ya kutanua mfumo huu kwenye hospitali nyingine mbalimbali. Kwa hivyo, kwa kuwa, tuna source codes zetu wenyewe sasa tuna uwezo wa kufunga mfumo huo kwa gharama ya chini zaidi kwenye hospitali nyingine zote nchini na huko ndiko tunakoelekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza hapa, mwezi wa sita taasisi ya Bill & Melinda Gates imeamua kumtuma mke wa Bill Gates, Melinda Gate, kwa ajili ya kuja kuzungumza na Naibu Waziri wa Wizara hii, tayari kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye mifumo ya taarifa za afya nchini. Haya ni mafanikio ambayo yanakuja kutokana na initiative tuliyoifanya ndani ya Serikali ya kuwekeza kwenye mifumo ya ki-electronic.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa inatekeleza mradi wa program ya maji kwa vijiji kumi kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na kuna baadhi ya Halmashauri hawakufanikiwa kupata hata anagalau vijiji vitano. Je, Serikali iko tayari sasa kutuletea taarifa ya kina ikionesha Halmashauri moja baada ya nyingine na taarifa hiyo ikionesha ni miradi mingapi imefanikiwa kwa kila Halmashauri ili tuweze kujua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, tulianza Programu ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji mwaka 2006 na tumemaliza Awamu ya Kwanza mwaka 2015. Sasa hivi tumeanza Programu ya Pili ambayo imeanza mwezi Januari, 2015, kwa hiyo tunaendelea.
Mheshimiwa Spika, iko miradi ambayo hatukuikamilisha kwenye Programu ya Kwanza. Bajeti ambayo tumeitenga mwaka 2016/2017, itaanza kwanza kukamilisha ile miradi ambayo ilikuwa inaendelea, haijakamilika, lakini pili itaendelea na ile miradi ambayo imekuwa earmarked kwenye Programu ya Kwanza. Kwa hiyo, tutaingia mikataba na kuikamilisha, hiyo ndiyo Sera yetu tunaendelea namna hiyo, ikiwa ni pamoja na Jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Pamoja na hilo ni kwamba tunayo orodha ya Wilaya zote, kwa hiyo, kama utahitaji upatiwe tutakapokuwa tumesoma bajeti Mheshimiwa Mbunge tutakupatia hiyo orodha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa sera zinaelekeza kwamba barabara zinazounganisha mikoa zitajengwa kwa kiwango cha lami na kuna barabara inayotoka Mbulu kuja Karatu kwa maana inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, ni barabara ya siku nyingi; ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera zetu nimezieleza wazi, sera hizo zinatafsiriwa vizuri katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Na Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema itawafikia wananchi wote hasa kuunganisha hii mikoa. Kama eneo hili linaunganisha Mkoa kwa Mkoa, Waziri wa Miundombinu akifika katika hotuba yake hapa nadhani atatuelezea mchanganuo wa mambo mengi zaidi. Kikubwa zaidi ni kwamba katika utekelezaji wa Ilani, maeneo yote yaliyoainishwa kwamba yatafikiwa, kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, jambo hilo litafanyika.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kesho tuna bajeti yetu, na barabara zote ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami tutaeleza kwa kina kesho. Naomba Waheshimiwa Wabunge muwe wavumilivu mpaka kesho mtasikia mambo yote. Ahsanteni.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Mgogoro huu kati ya wananchi na Hifadhi ya Ziwa Manyara umedumu kwa muda mrefu na chanzo cha mgogoro ni ardhi ya wananchi kuchukuliwa na Hifadhi bila ridhaa yao.
Huko nyuma waliwaruhusu waweze kutumia angalau umbali wa mita 100 kwa ajili ya kuchungia mifugo yao na baadaye hifadhi ikanyang‟anya tena.
Je, Serikali haioni suluhisho la kuondoa mgogoro huu ni kuwaachia hizo mita 100 tu ili mgogoro uishe kabisa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Waziri alipokuja alitoa ahadi kwa wananchi kwamba, kuna fedha shilingi milioni 160 zitapelekwa; shilingi milioni 100 kwa ajili ya madarasa na shilingi milioni 60 kwa ajili ya soko la akinamama, lakini mpaka leo fedha hizo hazijatolewa! Ni lini fedha hizi zitatolewa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu kuwaachia wananchi eneo linalozungumziwa. Swali la msingi lilikuwa ni nini matokeo ya Kamati. Sehemu yake ya pili, ni lini wananchi watapewa Taarifa ya Kamati hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya kikamilifu ya swali hili yamo katika Taarifa tunayoizungumzia. Kwa hiyo, kwa kuwa, Taarifa tayari ipo na tumemwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba Taarifa hiyo itakuwa tayari kuwasilishwa mbele ya wananchi ndani ya muda wa miezi mitatu. Nikisema ndani ya muda wa miezi mitatu, inaweza kuwa wiki moja, itakuwa ni vema tukasubiri wakati utakapofika tujue wale waliofanya utafiti wa kitaalam na wakaandaa taarifa wamesema nini, kuliko jibu ambalo linaweza kuwa la haraka haraka tu hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya fedha halikadhalika kwa sababu waliofanya utafiti wameangalia mgogoro kwa ujumla wake na upana wake na muundo wa Kamati yenyewe iliyofanya uchunguzi ulijumuisha wananchi pia, nina hakika kama hili ni mojawapo ya mambo yaliyozungumziwa, litakuwemo ndani ya ripoti hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba Mheshimiwa Mbunge, akubaliane na mimi tu kwamba kwa kuwa, nimesema ndani ya miezi mitatu na nimesema ndani ya miezi mitatu inaweza kuwa wiki moja, akavumilia tu Wizara itakapokuja kuwasilisha taarifa hii mbele ya wananchi na mambo yote yatakayojitokeza yatakuwa yameamuliwa wakati huo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hospitali zetu mbalimbali nchini zina upungufu mkubwa wa dawa, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha dawa za uhakika zinapatikana katika hospitali zetu nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili, kwa kuwa MSD pia inaidai Serikali fedha nyingi, je, ni lini Serikali itahakikisha inalipa deni la MSD?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoeleza hapa katika vipindi tofauti, jukumu kubwa la Serikali ni kuhakikisha tunaondoa upungufu wa dawa na vifaa tiba. Katika swali la kwanza linalosema Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana, ni kama tulivyoeleza hapo awali kwamba jukumu letu kubwa hivi sasa ni kuhakikisha kwanza tunajielekeza zaidi katika ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipindi tofauti nimesema kwamba ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ni kuongeza ukusanyaji wa fedha katika hospitali, zahanati na vituo vyetu vya afya. Tutakapofanya hili kwa upana wake maana yake ni kwamba vituo vya afya vitakuwa na dawa za kutosha kwa sababu mwongozo unasema jinsi gani pesa zinazopatikana zitaenda kwenye ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la deni la MSD Waziri wa Afya alipokuwa aki-table bajeti yake na katika mijadala mipana iliyojitokeza imejielekeza kuhakikisha deni la MSD linalipwa lengo likiwa ni MSD kuwa na uwezo wake wa kusambaza dawa. Waziri wa Afya alielezea suala hili kwa upana sana na Wizara ya Fedha ilichukua commitment ya kuhakikisha kwamba MSD deni lake linalipwa ili mwisho wa siku MSD iweze kusambaza dawa katika hospitali, zahanati hali kadhalika vituo vya afya na hospitali za mkoa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Huko nyuma takribani kama miaka sita sasa kumewahi kutolewa ahadi ya kujengwa baadhi ya barabara katika Mji wa Karatu kwa kiwango cha lami na ahadi hii imekuwa ni ya muda mrefu na mara nyingi tumeuliza hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ituambie ahadi ile ilikuwa tu ni kuwahadaa wananchi ili watoe kura au mmeshindwa kutekeleza? Tunaomba jibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi zote za Serikali zinaonyesha dhamira ya dhati ya viongozi wote wanaotoa ahadi ya kutaka kujenga hizo barabara. Kinachotukwamisha zaidi ni uwezo wa kifedha na naomba nichukue fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hicho kipande chake kitashughulikiwa kama ambavyo viongozi wetu waliahidi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mahitaji ya Sekta ya Afya hapa nchini yapo, yalikuwepo na yataendelea kuwepo, ni kwanini Serikali mlikubali kuingia mkataba huu au makubaliano haya ya fedha hizo asilimia 33 zinaenda tu kwenye ununuzi wa dawa na asilimia 67 inaenda kwenye fedha hizo zinaenda kwenye masuala ya usimamizi na ufuatiliaji kwa maana ya administrative cost, ni kwanini mliingia makubaliano haya amabyo hayana manufaa kwa Sekta ya Afya hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali imesaini Abuja Declaration ya kutaka asilimia 15 ya bajeti yake iende katika sekta ya afya. Ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya afya hapa nchini kwenye zahanati zetu, vituo vya afya, hospitali za wilaya ina changamoto kubwa sana ikiwemo ukosefu wa dawa, lakini leo hatujui kipaumbele cha Serikali ni nini. Serikali leo inang‟ang‟ana kuhamia Dodoma wakati kwenye hospitali zetu hakuna dawa hata kidogo. Ni kwanini hamuwi na vipaumbele vya afya ya Watanzania kwanza kuliko haya mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwamba kwanza ni kwanini Serikali iliingia makubaliano haya? Jibu ni rahisi tu, kwamba fedha za Health Basket Fund ni fedha za ziada za nyongeza ambazo tunapewa na wafadhili wetu. Sasa haiwezi kutokea mtu akaja akasema nakuongezea kitu kutatua changamoto inayokukabili halafu ukakataa. Kwa hivyo kulikuwa hakuna sababu ya Serikali kusema eti ijiulize maswali mara mbili mbili wakati imepata wafadhili na wafadhili wanakuja kuongeza tija kwenye kutoa huduma za afya kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ya hapo, fedha hizi kutengwa, kwamba asilimia 33 iingie kwenye dawa na asilimia 67 iende kutumika kwa ajili ya ku-administrate mfumo mzima wa afya kwamba sio jambo la muhimu; pengine Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso ungejifunza kwa ukaribu zaidi namna ya ku-administrate mambo ya mfumo wa afya. Mfumo wa afya ni katika mifumo complex ambayo unaweza ukaikuta hapa duniani, na si kazi rahisi ku-administrate utoaji wa huduma za afya. Wewe unapokwenda hospitali unaona ni kitu kirahisi tu unapoonwa na daktari na ukapewa dawa, lakini nyuma ya hiyo visit yako moja ambayo unaenda kuipata kwa daktari ukae ukijua kuna mchakato mrefu sana wa ku-administer mfumo mzima mpaka kufikia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa afya unaendana na mambo kama ufuatiliaji, tathmini, tafiti, surveillance za muda mrefu pamoja na kukusanya takwimu. Haya ni mambo mhimu sana ambayo Serikali yetu kwa kweli haikuwa ikiwekeza kabla ya kupata hizi pesa za Health Basket Fund.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzipata wafadhili wakasema kwamba ni lazima watusaidie katika eneo hili kwa kiasi kikubwa. Lakini hata hivyo kwenye jibu langu la msingi nimesema tunaangalia uwezekano kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wakati akisoma hotuba yake ya bajeti hapa katika mwaka wa fedha unaokuja tufanye mapitio ili sehemu kubwa zaidi ya fedha hizi ziweze kuwekezwa kwenye dawa kama ambavyo tumefanya mabadiliko kwenye pesa zinazotokana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu Abuja Declaration. Abuja declaration kweli ni commitment ambayo nchi yetu iliingia kwenye miaka ya mwanzo ya 2000, kwamba tutatenga asilimia 15 ya bajeti yote kubwa kwenye sekta ya afya. Serikali yetu kwa nyakati mbalimbali imekuwa ikifanya jitihada hizo za kuongeza bajeti kwenye sekta hii, lakini bahati mbaya sana ukuaji wa uchumi haukuweza kuendana na kasi ya mahitaji yetu makubwa ya kuwahudumia Watanzaia kwenye sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ifahamike hapa kwamba huduma za afya ni katika huduma zenye gharama kubwa sana kwenye taifa lolote lile; na kwa maana hiyo kusema uchumi wetu huu mdogo unaweza ukakidhi mahitaji yote si jambo la rahisi na si jambo la kusema linaweza likafikiwa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano kupitia maelekezo yaliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM tumejikita kwenye kuitafsiri Ilani ile kwa kuhakikisha tunaanzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambao utamlazimisha kila Mtanzania kuwa kadi ya Bima ya Afya ili wananchi washiriki kwenye kuchangia huduma kabla ya kuzitumia, tukiamini kwamba kama kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya maana yake atakuwa na uhakika wa kupata huduma hizo pale ambapo anazihitaji bila kupata changamoto ya kifedha, na hii ni njia mojawapo ya kukusanya pesa kwa watu wengi zaidi ambayo kwa kiasi kikubwa inaendana na misingi ya Sera ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo sisi wa Chama Cha Mapinduzi tunaisimamia.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitoa taarifa za makusanyo kila mwezi na imekuwa ikijisifia kwamba makusanyo yameongezeka kwa kiasi kukubwa. Lakini ni ukweli kwamba katika Halmashauri zetu fedha hazifiki na hazipo kabisa.
Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa hizo fedha ambazo mmekuwa mkisema mkizikusanya kwa wingi zikafika kwenye Halmashauri zetu nchini kwa sababu kule ndiko kwenye watu, ndiko ambako huduma inatakiwa kutolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme wazi kwamba Serikali imekuwa na tumekuwa tukitoa taarifa kila mwezi kwamba kwa kipindi cha sasa Serikali katika makusanyo yake imejitahidi kwa kiwango kikubwa sana kukusanya fedha na makusanyo hayo ya fedha lengo lake mnakumbuka mwaka huu tuna bajeti takribani ya shilingi trilioni 29.54 na hii maana yake lazima fedha zikusanywe ili kwamba miradi iweze kutekelezeka.
Kwa hiyo, hayo makusanyo ya fedha yanayoendelea hivi sasa, imani yangu kubwa sasa hivi Serikali inajipanga kuna vipaumbele vingi ndiyo maana katika suala zima la awali kuna ile miradi ya maji ilikuwa inaendelea na wakandarasi wali-mobilise vifaa kutoka site na ndiyo maana kwamba katika eneo la kwanza la kipaumbele ukiangalia miradi mingi ya maji ambayo ilikuwa inaendelea, hivi sasa mingi inatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda katika sekta ya miundombinu ya barabara, ninyi mnafahamu ni mashahidi, wale wanaotoka kule maeneo ya Tunduru wanakuta barabara kutoka Songea mpaka kule Mtwara kwenda Masasi pale, zamani mitambo ili-stuck pale ilikuwa haifanyi kazi, lakini Serikali imepeleka pesa hizi. Sisi watu wa Dodoma na watu wa Manyara wanafahamu, barabara kutoka Dodoma kwenda Manyara pale, hapa katikati kipindi kilichopita, Wabunge walikuwa wanalalamika, kazi ilikuwa imesimama, sasa hivi ukiangalia karibuni zote zinaenda. Serikali inakusanya hizi nguvu na nina amini miradi yote iliyopangwa katika mwaka wa fedha mwaka huu tutahakikisha inatekelezeka kwa sababu ni commitment ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi hiki cha bajeti.(Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa makubalinao hayo yalifikiwa mwaka 2011 na sasa ni miaka sita, na tatizo hili limeendelea kuwepo; je, ni lini sasa kwa uhakika kabisa Serikali itaenda kumaliza huu mgogoro uliopo kati ya wananchi na eneo hilo la Jeshi?
Swali la pili, kwa kuwa migogoro hii ya mipaka ya Jeshi na maeneo ya wananchi haipo tu Monduli, iko katika maeneo mbalimbali kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, nafahamu kumekuwa na mgogoro huu katika maeneo mengi ambapo Jeshi ina kambi zao. Sasa ni lini kwa uhakika Serikali itatuletea taarifa hapa Bungeni kwamba ina mkakati huu wa kwenda kumaliza matatizo hayo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mgogoro huu ni wa siku nyingi na kwamba sasa hivi wakati umefika upatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Spika, nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya Wizara yangu ilitenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya shughuli za uthamini, upimaji na ulipaji wa fidia katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, tukianza kupata fedha hizo hususan tatizo dogo kama hili la kuhuisha tu mipaka litashughulikiwa mara moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la kwamba migogoro hii iko mingi na lini taarifa italetwa, nataka nikiri kwamba sehemu nyingi za nchi yetu migogoro baina ya vijiji na Kambi za Jeshi ipo na kama nilivyosema awali tatizo ni fedha za kufanya uthamini kwa yale maeneo ambayo hayajathaminiwa, fedha za kufanya upimaji kwa maeneo yanayohitaji kupimwa na fedha za kulipa fidia kwa maeneo ambayo Jeshi linatakiwa kufidia.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe pia kwamba kuna maeneo mengi ambayo wananchi ndiyo wameingia katika maeneo ya Jeshi. Kwa hiyo, inabidi waelekezwe, waelimishwe wasiwe wanavamia maeneo ya Jeshi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tutakapoanza tu kupokea hizi fedha, kazi zote hizi nilizozitaja zitaanza kufanywa ili tuondoe migogoro hii inayokabili Jeshi letu na wananchi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, umuhimu wa kiwanda hiki cha matairi unajulikana na uwepo wa kiwanda hiki kufufuliwa katika Mkoa wa Arusha utaongeza ajira, lakini katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 60, mpaka tunapoongea imetolewa shilingi bilioni mbili tu. Je, kwa Serikali hii ambayo imefilisika kuna dhamira ya kweli kufufua kiwanda hiki?
Swali la pili; kuna wafanyakazi ambao bado wanakidai kiwanda hiki na madai yao wameshayafikisha Hazina, lakini mpaka leo hawajalipwa. Je, ni lini sasa madai haya ya wafanyakazi yatalipwa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na lile gumu la madai ya wafanyakazi. Mheshimiwa Mbunge naomba nakala ya madai iliyopelekwa kwa Treasury Registrar, nipewe nakala hiyo, mimi nitafuatilia. Naomba Mheshimiwa Mbunge anifuatilie mimi na mimi nimfuatilie Treasury Registrar.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza juu ya dhamira ya kweli, Serikali hii ina dhamira ya kweli na nitumie fursa hii, kwamba Tanzania kuna soko la matairi siyo habari mpya, kwamba sisi ni sehemu ya Afrika Mashariki, it is not the news, kwamba sisi tuko SADC siyo tatizo, tumeelekezwa katika Ilani ya Chama chetu na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano General Tyre ifufuke.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kama kuna mtu yeyote ana mwekezaji, anataka kujenga kiwanda mimi nitahakikisha nitajenga kiwanda, Mheshimiwa Rajab Adadi na Mheshimiwa Stephen Ngonyani (Majimarefu) wamekuwa wakinifuatilia, fursa ipo, sisi kazi yetu ni kuweka mazingira wezeshi, kupiga sound ili kusudi wawekezaji waje wawekeze, Serikali haitajenga kiwanda inatengeneza mazingira wezeshi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, kuna majengo ambayo yalikua yanatumika na Halmashauri ya Karatu, na sasa Halmashauri imehamia kwenye majengo mapya na huku nyuma kulishakuwa na azimio la Baraza la Madiwani kwamba majengo yale yatumike kama Chuo cha VETA.
Je, Serikali iko tayari sasa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kutumia yale majengo ya zamani ili kuweza kufungua chuo cha ufundi VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, nilipokuwa najibu swali la Mheshimiwa Keissy nilijibu kwa confidence kwa sababu majengo hayo ninayafahamu, nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na mimi mwenyewe pia nilishiriki kuona kwamba yangefaa kutumika hivyo. Sasa katika hili ambalo umenifahamisha kuhusu majengo ya Karatu, naomba tuweze kuyaangalia kwanza kabla sijatoa majibu. Kwa hiyo, tutafanya utaratibu wa kuja kuyaona.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sekta ya Utalii ni sekta ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa na sekta hii ili iweze kuwa endelevu ni lazima pawepo na uhakika wa usafiri ikiwemo viwanja vya ndege. Kuna Kiwanja cha Ndege kilichopo Karatu kwa maana ya Kiwanja cha Ndege cha Manyara; kimetelekezwa na hakiendelezwi. Je, ni lini Serikali itahakikisha inaendeleza kiwanja hicho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitawasiliana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Bodi yao tuone nini kinaweza kufanyika katika kiwanja hiki na mipango yao ikoje katika kuvifufua viwanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na hiki.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Wilaya ya Longido imeanzishwa mwaka 2007, takribani miaka tisa mpaka leo Wilaya ile haina hospitali ya Wilaya, matokeo yake wagonjwa wakipewa rufaa, wanapelekwa, Mount Meru - Arusha, kiasi cha kilometa 94 na Serikali imekuwa ikiahidi itajenga Hospitali ya Wilaya. Tunataka majibu ya uhakika, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Longido?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Longido haina Hospitali ya Wilaya kama zilivyo Wilaya nyingine nyingi tu hapa nchini. Niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba miradi ya Halmashauri, inaanzia kwenye mipango ya Halmashauri na baadaye bajeti ya Halmashauri. Kwa hiyo, niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge kwamba kule kwenye mipango ya Halmashauri ndiko vitu hivyo vionekane ili baadaye vikija huku Bungeni tuweze kuvitengea bajeti kwa mujibu wa taratibu za kibajeti.
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kawaida mimi kupata wageni wanaoomba vitu nje ya bajeti. Uwezo huo sina na hata Waziri wa Fedha, nadhani hana. Bajeti ikishapitishwa ndicho kitakachofanyika. Hivyo, Wilaya ipange mipango yake, mipango hiyo iwemo kwenye bajeti za Halmashuari zao. Jambo kubwa litakalobakia sasa ni kwa Wabunge ku-demand utekelezaji wa bajeti ili tufikie yale malengo hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwasihi Waheshimiwa Wabunge, kwamba kwa sera ya Serikali ni kuweka kituo cha afya kila kata, lakini Serikali tumeamua na tumepanga na Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba kila Halmashauri basi angalau ijenge kituo kimoja. Katika Halmashauri 185 tulizonazo, tukifanya tutapata vituo karibu zaidi ya 400, wakati toka uhuru tuna vituo kama 600 tu.
Mheshimiwa Spika, nadhani hii itatusaidia sana, wa-dedicate maeneo, indication kulingana na maeneo ambako kuna problem kubwa. Jambo lingine ni kwamba kwenye zahanati wananiomba ramani, ramani ile iliyotolewa na Wizara ya Afya tumekubaliana na Waziri wa Afya kwamba ni kubwa mno kwa zahanati kila kijiji na haitekelezeki kwa sababu ya gharama kubwa karibu ya 1.8 billion ili iweze kutekeleza ule mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumekubaliana ku-review ile bajeti, kwa sababu tuna zahanati ambazo zilijengwa wakati tulipopata uhuru tu, zilitosha kutuhudumia mpaka leo tupo. Kwa hiyo, tunadhani zisiwe kubwa kiasi cha kushindwa ku-manage uchumi wa kijiji kwa sababu sehemu kubwa ni michango ya wananchi itatumika pamoja na kwamba Serikali itaweka mkono wake, lakini lazima ramani iwe ya kawaida inayoweza kuwa manageable.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilijigamba kwamba itatoa elimu bure na utekelezaji wa elimu bure kwa mujibu wa watafiti wa haki elimu inahitaji takribani shilingi bilioni 700 kwa mwaka mmoja wa fedha. Na hali ilivyo sasa hivi, fedha mnazopeleka ni kidogo tu za fidia ya ada.
Je, mko tayari sasa kuwaambia Watanzania mmeshindwa kutekeleza elimu bure ili Watanzania wachangie suala la elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Watanzania wanafahamu. Wakati hatuna programu ya elimu bure, vijana wengi walikuwa wanakosa hata hii elimu ya msingi, wengine walikuwa wanatishwa vitumbua kwenda kuuza barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi juzi nilipita kule katika Mkoa wa Kagera, nilipofika pale Nyakanazi, shule ambayo mwaka huu ime-register wanafunzi wengi zaidi ya wanafunzi 800 wa shule ya msingi peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kutoa elimu bure hii kusaidia mitihani, gharama za ada, hata suala zima la posho, ni jambo kubwa sana. Mimi naamini ndio maana kwa rekodi mwaka huu inatuonesha vijana wengi sasa hivi wanaripoti shule za seondari ukilinganisha na kipindi cha mwanzo, kwa sababu mwanzo wazazi walikuwa wanashindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kikubwa zaidi naomba tuamini kwamba Serikali katika jambo hili imeleta ukombozi mkubwa. Na hili niseme kwa vile Serikali tumejipanga na hili nimelisema sehemu mbalimbali, changamoto yetu inatufanya tunataka tuseme lazima private schools sasa si muda mrefu zitatakiwa zijipange vizuri, kwa sababu tunaenda kwa kasi kubwa ya ajabu. Huku tunakokwenda tutakwenda kupata mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu Watanzania wote tutaungana pamoja, hii nchi yote ni ya kwetu, Watanzania wote ni wa kwetu na watoto ni wa kwetu tusaidiane kuhakikisha Tanzania inafika mahali salama katika suala zima la utoaji wa elimu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wamekuwa wakikumbwa na changamoto kubwa sana kwa sababu wanaishi katika eneo la hifadhi. Hata hivyo kumekuwa na ahadi nyingi za Serikali
za kumaliza hiyo changamoto lakini hakuna mafanikio na mpaka leo wananchi wale wanaishi tu kwa matumaini. Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba wamekataza mifugo isiingie crater lakini kuna changamoto ya upatikanaji wa maji. Kumeshawahi kutengwa takribani shilingi bilioni tano na zimetumika, wamejenga ranchi kwa ajili ya kuhifadhi mifugo isiingie crater na haitumiki. Je, ni kwa nini ranchi imejengwa kwa gharama kubwa halafu haitumiki mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, changamoto za Hifadhi ya Ngorongoro ni kubwa na nyingi. Hata hivyo, napenda ieleweke kwamba katika kusimamia uhifadhi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro jambo hili sisi wote kwa pamoja tunatakiwa tuzingatie ukweli kwamba maslahi ya mtu mmoja mmoja yatazingatiwa, maslahi ya makundi yatazingatiwa lakini mwisho wa siku maslahi ya Taifa yanayotokana na kuhifadhi eneo lile ndiyo
yatakayopewa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, ni kweli, hapa na pale katika
kipindi chote cha uwepo wa sheria hii tunayoizungumzia ya mwaka 1959 mengi yametokea. Yako yale ambayo Serikali ilisema itatekeleza, tumetekeleza kikamilifu, yako yale ambayo bado Serikali inaendelea kuyatekeleza, lakini tumesema msingi wa kuweza kushughulikia tatizo hili vizuri na kikamilifu ni kufanya marekebisho ya sheria. Kwa sababu kufanya kitu chochote kile nje ya sheria kwa ajili tu ya kutaka
kujibu hoja za makundi au za mtu mmoja mmoja ni jambo ambalo halitaweza kutufanya tukafanikiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Mbunge na wadau wengine wote na Taifa kwa ujumla tufanye subira. Tusubiri mabadiliko ya sheria ambayo yataweka misingi sasa ya kuweza kutatua changamoto hizi
kwa namna ambayo itakuwa ni endelevu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kama ambavyo Wilaya ya Serengeti inazungukwa na mbuga ya wanyama, vivyo hivyo Wilaya ya Ngorongoro ina changamoto kubwa sana ya kijiografia kutoka tarafa moja kwenda tarafa nyingine ni kilometa nyingi ikiwemo kutoka Tarafa ya Ngorongoro kwenda Tarafa ya Loliondo ambapo kuna takribani kilometa mia na zaidi, na Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika umejionea mazingira ya Ngorongoro. Je, Serikali iko tayari sasa, kulingana na ugumu wa jiografia ya Ngorongoro, kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi hao inapatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifika Ngorongoro takribani wiki tatu na nusu zilizopita, na ni kweli jiografia ukitoka hapa Karatu wakati unatoka getini pale
mpaka unafika kule Loliondo ni mbali sana na sio hivyo tu, nilifanya jiografia pana sana nikazunguka lile Jimbo la Ngorongoro nikapita mpaka katika Ziwa Natron pale, kweli changamoto ya maji ni kubwa na kama nilivyokuwa kule site niliahidi kwa wananchi kwamba tutafanya kila liwezekanalo kushirikiana na Halmashauri ile ya Ngorongoro kuangalia jinsi gani tutafanya kuhakikisha kwamba tunapata ujenzi wa maji kule kama ni borehole au vyovyote.
Kwa mfano ile Shule ya Sekondari ya Ziwa Natron pale, watoto wako pale lakini na maji yapo pale ila isipokuwa jinsi gani kuyasambaza kufika shuleni. Kwa hiyo, vyote nimeenda kule nimeweza kufanya needs assessment ya eneo lile na naomba nikuhakikishie kwamba kama Serikali na matakwa
yetu ya Kiserikali tutafanya kila liwezekanalo kuwasaidia wananchi wa Ngorongoro.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Katika Mkoa wa Arusha kuna majimbo saba na katika majimbo hayo majimbo mawili yana jiografia ngumu sana
ikiwemo Jimbo la Longido na Jimbo la Ngorongoro. Je, Serikali iko tayari sasa katika bajeti tunayoiendea kutazama majimbo haya kwa mujibu wa jiografia yao ili wananchi wanaoishi
katika maeneo hayo waweze kupata huduma za afya kwa urahisi na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Serikali inapeleka nguvu kubwa sana katika eneo hilo, na ndiyo maana juzi juzi nilikuwa katika Wilaya hizo zote mbili;
Wilaya ya Longido pamoja na Wilaya ya Ngorongoro, katika Wilaya ya Ngorongoro siyo muda mrefu sana Mungu akijaalia katika kipindi hiki cha katikati tutakwenda kuwekeza nguvu
kubwa sana kwa kupeleka takribani milioni 700. Lengo kubwa ni kwamba maeneo yale yana jiografia tata sana wananchi waweze kupata huduma kujua kwamba Serikali yao ipo
vitani katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma hiyo inayokusudiwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha Madiwani nchini kutokupata nyongeza ya
posho kwa muda mrefu. Ni ukweli usiopingika kwamba Madiwani hawa wamekuwa wakifanya kazi kubwa hasa
kutusaidia sisi Wabunge tukiwa huku Bungeni muda mrefu, lakini Madiwani hawa wamekuwa wanasimamia fedha
nyingi sana zinazopelekwa katika Halmashauri zetu, lakini wameachwa hawana mafunzo, hawana vitendea kazi na
posho zao haziongezeki.
Je, Serikali sasa iko tayari kumaliza kilio cha Madiwani cha muda mrefu katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli
anavyosema Mheshimiwa Paresso na tukifanya reference ya mwaka 2002 kulikuwa na Tume iliyokuwa inaitwa Tume ya Lubeleje ambaye ni Mbunge senior yuko hapa. Tume hiyo iliundwa na iliweza kubaini mambo hayo. Bahati nzuri katika mikitano yetu ya ALART miwili tuliyofanyia hapa Dodoma na Musoma, jambo hilo vilevile lilijitokeza. Serikali hivi hatuwezi kutoa kauli hapa haraka haraka kwa sababu mchakato huu wa bajeti tutakuja ku-table bajeti na mambo mengine tutajadili kwa pamoja hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kazi ya Madiwani ni kubwa na Serikali inaona hilo, lakini tutajadiliana kwa upana
katika mchakato wa bajeti tuone ni nini tunafanya, way forward katika suala zima la Madiwani wetu katika Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sera ya masuala ya ujenzi ni kuunganisha barabara ya mkoa mmoja na mwingine kwa kiwango cha lami, na kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Njiapanda - Karatu - Mang’ola mpaka Lalago, ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu, je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Paresso asubiri, ni keshokutwa tu bajeti yetu inakuja, na ramani yote ya shughuli za ujenzi wa barabara zote itakuwa imeanikwa wazi. Nisinge penda kwenda kwa undani kwa sababu ni sehemu ambayo Waziri wangu ataishughulikia keshokutwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Ubaguzi huu wa Wabunge kati ya Wabunge wa Viti Maalum na Wabunge wa Majimbo pamoja na kutokupewa Mifuko ya Jimbo, lakini pia hatuingii katika Kamati za Fedha kwenye Halmashauri zetu na jambo hili tumeshalisema muda mrefu, kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi kuruhusu Wabunge wa Viti Maalum katika Halmashauri tulizowapa tusiingie katika Kamati ya Fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum ni hofu tu, tutawang’oa Majimboni. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba kujibu swali ambalo nadhani litakuwa swali maarufu la mwaka na limeulizwa kwa staili ambayo haijawahi kufanyika, ninakupongeza Mwenyekiti kwa utaalamu wa kujua Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili linahusu Mfuko wa Jimbo na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Ester Mmasi, Mheshimiwa Munde Abdallah na wengine wengi Wabunge wa Viti Maalum wanataka na wao wapate mgao wa fedha za Mfuko wa Jimbo. Swali hili siyo kwamba linaulizwa kwa mara ya mwanzo leo, limekuwa likiulizwa na mara nyingi tumekuwa tukitoa majawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu maarufu ambayo tumeyatoa kwamba tutakwenda kushughulikia tuone utaratibu wake, lakini kila tunaposhughulikia tunapata ugumu kwa sababu mfuko huu umezaliwa kwa mujibu wa sheria, sheria yenyewe inaitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfuko wenyewe unaitwa Mfuko wa Jimbo na kwa hiyo, kuupa jina linguine lolote lile ni kazi ngumu kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani kuna Wabunge
wa Majimbo, kuna Wabunge wa Viti Maalum, kuna Wabunge wa Mikoa, kuna Wabunge wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais. Bunge hili likitambua kwamba Wabunge wa aina hizi zote wapo, lilitunga Sheria ya Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye instrument yangu kwa mujibu wa sheria nilizopewa kuzisimamia nina sheria inayosema nitasimamia Mfuko wa Jimbo, haisemi vinginevyo. Ndiyo maana kwenye jibu letu la msingi nimesema kama Bunge litaona vinginevyo suala hilo linakuja kwa utaratibu mwingine, lakini kwa sasa mimi ninasimamia Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale Wabunge waliokuwa wanadai sana mfuko huu, waliokuwa wa Viti Maalum, walipopata majimbo na wenyewe msimamo wao umebadilika, ni kwa sababu ya majukumu anayoyapata Mbunge wa Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mengine yameulizwa na Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim ambaye ameuliza suala la fedha kuchelewa Zanzibar, hili tumelichukua, tunawasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais tuone utaratibu bora zaidi wa kuweza kufanya fedha hizo ziwafikie Wabunge wa Zanzibar, hasa tunatambua yapo mapendekezo ya kwamba bora zikapita katika Ofisi ya Bunge Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine dogo limeulizwa na Mheshimiwa Paresso kwamba Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Kamati za Fedha. Kamati za Fedha zinatambua uwepo wa Madiwani na Mbunge unapoingia kwenye Halmashauri huwi Mbunge unakuwa Diwani, kule kwenye Kamati ya Fedha wanaoteuliwa kuingia kwenye Kamati ya Fedha huwa ni Madiwani. Sasa nadhani ni utaratibu wa Halmashauri zenu, kama wewe Mbunge kuteuliwa kuna baadhi ya Wabunge ambao wanaingia kwenye Kamati ya Fedha, lakini kule wameingia kwa tiketi ya Udiwani wao kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napata shida hapa
kwa sababu la kwanza, kwamba kwa Majimbo ambayo yana Wabunge wengi wa Viti Maalum, na mfahamu kikao kile kina utaratibu wa gharama zake na mambo mengine. Ingawa gharama siyo hoja kubwa, lakini kwa Jimbo ambalo lina Wabunge wa Viti Maalum nane, 10, sijui hali itakuwaje kwa sababu gharama za uendeshaji wa Halmashauri zitakuwa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ingelikuwa Wabunge labda ni mmoja au wawili pengine unaweza kuichukulia hili jambo likawezekana, lakini kwa hali ilivyo kuna tatizo kubwa sana na ninadhani ni vema hili jambo likabaki kama ilivyo na ndio utaratibu ulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tiketi ya Udiwani, Mbunge anaweza akateuliwa na Mwenyekiti kwa utaratibu ule akawa Mjumbe wa Kamati ya Fedha.(Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante,kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekuwa ikihaidi kwamba itarejesha kodi hii ya majengo kwenye halmashauri zetu na ni ukweli kwamba mmekuwa hamrudishi; kwa mfano Halmashauri ya Kinondoni kabla haijagawanyika mliahidi mtarejesha bilioni 10 ikiwa ni sehemu ya makisio ya halmashauri husika, lakini mpaka leo hamjarudisha; je, Serikali hamwoni kwamba jambo hili hamliwezi sasa mtamke rasmi kwamba mtabakiwa na hizo kodi? (Makofi)
Mheshiiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano katika kila mwaka wa fedha imekuwa ikiendelea kuzinyang’anya halmashauri zetu vyanzo vingi vya mapato kiasi kwamba halmashauri nyingi sasa hivi zinaelekea kushindwa kujiendesha kwa sababu Serikali Kuu inachukua fedha zote; je, Serikali haioni umuhimu sasa mlete mabadiliko ya Katiba hapa Bungeni mzifute rasmi Serikali za Mitaa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa si kwamba hatuwezi jambo hili, hilo nakanusha. Nimesema hapa ufanisi halisi tukilinganisha kati ya halmashauri pamoja na TRA. Katika hili naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba sote sisi ni Watanzania na zote tumeona tarehe za mwisho wa mwezi wa Sita wananchi walivyotoka kwa wingi kwenda kulipia kodi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kusema Serikali tumeshindwa si sahihi kabisa na ndiyo maana Serikali kwa kuangalia wananchi wetu jinsi ambavyo wamelipokea jambo hili kwa matokeo mazuri kabisa tumeongeza wiki mbili na naomba mtupime Serikali baada ya hizi wiki mbili ni ambacho tutakuwa tumekifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kubadilisha Katiba ya Nchi naomba nimwambie Mheshimiwa Cecilia kwamba kwenye jibu langu la msingi nimesema kwamba mamlaka yenye mamlaka halisi ya kukusanya mapato ya nchi yetu ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ndicho ambacho kwa mujibu wa Sheria Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekifanya na tunaendelea kufanya hatujafanya kitu chochote ambacho kiko kinyume na katiba kinachotupelekea kuleta Mabadiliko ya katika Katiba katika Bunge lako. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na tishio kubwa la ugonjwa wa sukari hapa nchini ambao umekuwa ukiwakumba watu wa rika mbalimbali na hatuna wataalam wa kutosha katika hospitali zetu. Vilevile hata dawa wanazopewa ikifikia hatua mgongwa wa sukari anatakiwa apate insulin dawa hizo zimekuwa zikiuzwa ghali, watu hawawezi ku-afford. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na tatizo hili?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso kuhusu upatikanaji wa dawa za kisukari na ongezeko la wagonjwa wa kisukari nchini. Ni kweli sasa hivi tunashuhudia ongezeko la wagonjwa wa kisukari lakini kwa sababu kwanza ya mfumo wa maisha ambao watu wanaishi, watu hawafanyi mazoezi, wanakula vyakula bila kuzingatia lishe lakini bila ku-check afya zao mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kubwa badala ya kujikita kwenye kutibu tumejikita kwenye kuzuia Watanzania wengi wasipate maradhi ya ugonjwa wa kisukari. Pale ambapo Mtanzania ana ugonjwa wa kisukari kwa mujibu wa Sera ya Afya dawa ya mgonjwa wa kisukari inatakiwa kupatikana kwa bei nafuu. Kwa hiyo, tunawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapoandaa maoteo ya dawa basi wahakikishe pia wana-order dawa za kutosha kwa ajili ya wagonjwa wa kisukari. Kama hawawezi ku-order za kutosha sisi hatuwezi kuwapelekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili la uhaba wa Madaktari wa Meno, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri na hata wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Utumishi alitoa maelezo kwamba Mheshimiwa Rais ameridhia kuajiri watumishi wa Serikali takriban 52,000 na kati ya hao tunategemea kupata watumishi wa sekta ya afya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Savelina Mwijage tutakapopata kibali tutawapanga pia kwa ajili ya hospitali za Mkoa za Kagera. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, asante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna kampuni ya OBC ambayo inamirikiwa
na mwarabu na imekuwa ikiwepo Loliondo kwa muda mrefu na wamekuwa wakifanya uwindaji, wamekuwa wakiangalia maslahi yao zaidi bila kuangalia maslahi mapana ya uhifadhi wa Bonde Tengefu la Loliondo. Ni kwa nini Serikali inamshirikiali au inamaslahi gani na huyu mwarabu amekaa huko kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ulipata mashaka, lakini na mimi nilikuwa na mwelekeo huo huo, lakini hata hivyo kwa ajili tu ya kuweza kuboresha, niseme tu kwa kifupi kwamba kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kamati iliyoundwa ile ya kitaalam ilihusisha makundi yote, wataalam lakini pia wawekezaji na wananchi. Unapohusisha makundi yote, basi kila jambo ambalo ni changamoto linajadiliwa kwa mapana na marefu wakati kamati ikiwa inafanya kazi. Ninaamini ndani ya taarifa ambayo iko kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo yote ambayo yanahusiana hasa na wawekezaji, na napenda hapa tutumie lugha sahihi ya kuwa-address wawekezaji, na nafikiri jambo la msingi ni kwamba hawa ni wawekezaji wana haki zao nchini wa mujibu wa sheria, lakini kama yapo yale ambayo ni changamoto na yanatakiwa kufanyiwa kazi, basi hiyo ndiyo kazi ambayo kamati imefanya. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, asante kwa kunipa nafasi, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali inakiri kwamba baada ya TRA kupokea jukumu hili mapato yameongezeka ukilinganisha na Halmashauri za Wilaya; na kwa kuwa Serikali mnapaswa kurudisha fedha hizo katika Halmashauri kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 Serikali imefuta vyanzo vingi vya Halmashauri ambavyo vilikuwemo kwenye bajeti ikiwemo ushuru wa mabango, makanyagio, ushuru wa mazao chini ya tani moja, farm gate price kutoka asilimia tano mpaka asilimia tatu na kwa kiwango kikubwa uendeshaji wa Halmashauri zetu unategemea fedha za ndani (mapato ya ndani).
Je, Serikali sasa baada ya kufuta vyanzo hivi vingi ambavyo kwa kiwango kikubwa inaharibu utekelezaji wa bajeti zetu katika Halmashauri. Ni lini mtahakikisha fidia ya vyanzo hivi inatolewa na Serikali Kuu ili Halmashauri zetu ziendelee kufanya kazi kwa ufanisi? (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nafuta na nauliza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekuwa ikichelewesha fedha mmekuwa mnasema mnakusanya TRA na baadaye fedha zitarudishwa kwenye Halmashauri. Kwa kuwa mmekuwa mkichelewesha. Sasa ni lini mtaacha kuchelewesha ili fedha hizi ziende kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwanza kwa kurekebisha Kiswahili kile lakini sio kosa lake ni kosa la watani zangu hawa wa Manyara, lakini nashukuru umerekebisha sasa imekaa vizuri.
Mheshimiwa Spika, nianze kusema kwamba kwanza Serikali haipendi kuchelewesha fedha hizi kupeleka katika Halmashauri zetu. Tunachofanya Wizara ya Fedha tunasimamia mpango wa cash budget, tunakusanya na tunapokusanya tunahakikisha Halmashauri zetu zinapatiwa fedha kulingana na bajeti zao ambazo zimetenga.
Mheshimiwa Spika, hii inakwenda katika swali lake la pili alilosema tumefuta vyanzo vingi, lengo letu kama Wizara, kama Serikali, ni kuhakikisha tunapeleka unafuu wa maisha kwa wananchi wetu. Usumbufu wa kodi mbalimbali na ushuru ambao walikuwa wakisumbuliwa ndiyo ambao Mheshimiwa Rais wetu aliahidi kufuta na sisi kama Wizara tumesimamia na tumefuta.
Mheshimiwa Spika, kama Wizara niseme hatujawahi kuacha kupeleka bajeti kwa halmashauri zetu pale ambapo fedha yetu imekuwa inatosha. Tunapeleka na tunaahidi kuendelea kuzipelekea halmashauri zetu bajeti zao kama ambavyo zimepitishwa na Bunge lako tukufu, na nimhakikishie Mheshimiwa Cecilia kwamba halmashauri zote zitapata bajeti zao kama ambao zimepitishwa. Na hii ni dhamira yetu na tumeanza utekelezaji, na yeye ni shahidi kule kwenye halmashauri yake anaona jinsi ambavyo tunapeleka fedha hizi kwa sasa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali ndogo la nyongeza.
Kwa kuwa hicho kinachoitwa kifuta jasho au kifuta machozi kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori, imekuwa hailipwi kwa wakati pale ambapo wananchi wakipata uharibu wa mazao yao hasa katika maeneo ambayo yanapakana na hifadhi:-
Je, ni kwa nini Serikali sasa isifikirie kuanzisha mfuko wa fidia ambao utachangiwa na hizi mamlaka zote kama TANAPA, Ngorongoro ili wananchi wawe wanaweza kutapata fidia yao kwa wakati bila kucheleweshwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna changamoto kubwa sana kuhusiana na malipo ya vifuta jacho na vifuta machozi. Ukweli ambao ni wa kudumu, hakuna namna ambayo tunaweza tukalifanya zoezi hili kwa namna endelevu kwamba madai yote yanahusiana na vifuta jasho na vifuta machozi yakalipwa kwa kile kinachoitwa kwa wakati hata kama tukianzisha mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili namna pekee ya kuweza kuliweka vizuri, namna bora zaidi ni kuzuia zaidi kuweka kinga na kupunguza matukio ambayo yanasabisha ulipaji wa vifuta jasho na vifuta machozi. Ndiyo maana pale awali wakati najibu swali la nyongeza nilisema wazo la kushirikisha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi ni wazo la msingi zaidi. Ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza kufanya uhifadhi kwa namna ambayo tunaweza kupunguza matokeo yanayolazimisha sasa Serikali ilipe vifuta jasho na vifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima twende kwa utaratibu wa kuweka ushirikishi zaidi na kuanza kuangalia kwamba wananchi hawakai kwenye maeneo ambayo ni ya mapito ya wanyama hawakai kwenye maeneo ambayo ni ya mtawanyiko wa wanyama na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji kwenye maeneo yale. Pale inapotokea kwamba wanyama wanahama kutoka kwenye maeneo yao, maeneo ambayo siyo yale ya mtawanyiko ya yale ya njia za mpito, basi tutakuwa tumepunguza kwa kiwango kikubwa matukio hayo, lakini pia tutaweka mbinu mbadala za kuweza kuzuia wanyama kuweza kuleta uharibifu kwenye mazao lakini pia kudhuru wananchi wanaozunguka maeneo hayo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Majimbo ya Longido na Ngorongoro ni majimbo ambayo yapo kwenye mazingira magumu sana na upatikanaji wa huduma za afya si wa uhakika. Wilaya ya Ngorongoro haina hospitali ya wilaya, Wilaya ya Longido imetengwa kwenye bajeti lakini utekelezaji bado. Je, ni lini Serikali itaweka mkazo kwenye majimbo haya ambayo kwa kweli yana mazingira magumu ya kijiografia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema mwenyewe kwamba Majimbo ya Longido na Ngorongoro yapo katika mazingira magumu na Wilaya ya Longido hakuna hospitali na Wilaya ya Ngorongoro tayari iko katika bajeti. Naomba ushirikiano wake mara fedha ambazo zipo kwenye bajeti zitakapopelekwa, ashiriki kikamilifu katika kusimamia ili matumizi ya fedha zile yawe mazuri kama ambavyo ilikusudiwa. Mwaka ujao wa fedha tushirikiane naye kuhakikisha kwamba Longido nao tunawawekea bajeti. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa hapa nchini wamekuwa wakiwasimamisha hovyo watumishi wa Serikali za Mitaa bila kufuata taratibu na sheria zilizopo. Je, nini kauli na msimamo wa Serikali katika suala hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kukanusha, hakuna sehemu yoyote ambayo Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa amesimamisha watu kazi hovyo, hakuna! Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba usimamishaji wowote wa kazi unafuata masharti ya taratibu za kazi na sheria zinazomwongoza anayetoa amri hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Arusha una majimbo ambayo kijiografia yana mazingira magumu sana, hasa Jimbo la Ngorongoro na mara nyingi Mawaziri mmekuwa mkifika pale mmeona mazingira yale na kumekuwa na tatizo kubwa sana la upatikanaji wa maji kwenye vijiji vilivyoko katika Jimbo la Ngorongoro.
Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha Jimbo la Ngorongoro linatizamwa kwa upekee na wananchi wake wanaweza kupata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali ambalo limeelekezwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Ngorongoro kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Januari, tumesaini mkataba wa milioni 270 kwa ajili ya mradi wa maji katika Halmashauri ya Mji wa Ngorongoro, sasa hivi tunafanya design ambapo tunatarajia mwezi Aprili, tutasaini mkataba mkubwa ambapo tutapeleka maji zaidi ya vijiji tisa likiwemo eneo la Mageli. Kwa hiyo, suala la maji upande wa Ngorongoro linashughulikiwa na tutahakikisha kwamba asilimia 85 itakapofika 2020 inafikiwa pia katika Halmashauri ya Ngorongoro. (Makofi)
MHE. CECILIA DANIEL PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kumekuwa na Mamlaka nyingi za usimamizi na uwezeshaji katika mipango ya Serikali hasa katika suala hili la la viwanda.
(a) Je, Serikali kupitia SIDO ina mkakati gani wa kuunganisha mipango hii na hiyo mipango ikaunganishwa na rasilimali watu wanaozalishwa katika vyuo vyetu vya Ufundi hapa nchini?
(b) Sera na usimamizi wa kodi ni mambo muhimu sana katika kufanikisha suala la viwanda. Je, ulipwaji na utozwaji wa kodi unaofanywa na mamlaka husika hapa nchini, umezingatia vipi suala hili ili kutokuhathiri sekta hii changa ambayo inakua?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, niseme tu kwamba katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ni kwamba suala hili ni mtambuka na linafanywa na wadau mbalimbali na sekta nyingi na hivyo hata usimamizi ulikuwa umepangwa zaidi kulingana na uhalisia wa eneo ambao usimamizi wake unahitajika ufanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwenye suala la madawa na vyakula, tunazungumzia masuala ya kiafya. Kwa hiyo, unaangalia kwamba kulikuwa na kuangalia mamlaka hiyo ya usimamizi itakuwa imeweza kufanya kazi zake vizuri na kuondoa vikwazo kwa kiasi gani kama itakuwa imekaa katika eneo hilo. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikiendelea kufanyia kazi suala hilo ili kuona namna bora zaidi ya hizi mamlaka za usimamizi zinavyoweza kuunganishwa ili kuweza kuleta tija zaidi katika uchumi huu wa maendeleo ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, kwa suala ambalo ni la SIDO kuwa yeye sasa kama muunganishaji. Kimsingi SIDO haifanyi kazi peke yake, mfano tu kwamba kwa mfano katika Mkoa wako wa Manyara ukiangalia katika suala la uendelezaji wa zao la vitunguu swaumu, pale tayari kuna wadau wengi ambao wamehusika MIVAP ambao kulikuwa na jengo pale lakini pia katika chain ya kuongeza thamani, ukienda Magugu kuna SNV wanaoshirikiana na SIDO katika uongezaji thamani katika eneo la mpunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika na katika eneo la Hanang, vilevile kuna suala la kuangalia menejimenti ya kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna. Kwa hiyo, kimsingi ni kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wadau wote wanaunganika pamoja na kila mtu kuweka intervention katika eneo linalohusika ili kuweza kupata tija katika uendelezaji wa wajasiriamali na viwanda kwa ujumla.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa upandishaji hadhi wa vituo vya afya nchini umekuwa na urasimu sana kwa sababu vibali lazima vitolewe na Serikali Kuu: Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna umuhimu wa upandishaji hadhi wa vituo tu vya afya ukarudi kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuliko kusubiri iende Serikali Kuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuna jambo moja hapa, kwa sababu katika mchakato wa upandishaji wa vituo vya afya, siyo Serikali tu inaamua. Jukumu kubwa ni kuhakikisha kwamba kuna vikao halali ambavyo vinakaa na mwisho wa siku yale maamuzi yote yaliyopitishwa mpaka katika Baraza la Madiwani yanakwenda Wizara ya Afya. Baadaye wakaguzi wanakuja kuangalia na mwisho kile kituo kinapandishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima kurudisha katika Serikali za Mikoa; katika Mikoa kwa mujibu wa sera za afya, tuna Wakaguzi wa Kanda za Afya. Ni kwa nini zinafika mpaka Wizarani? Lengo ni kupata wataalam ambao watahakikisha quality control inafanyika na kituo kile kinakidhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mawazo mazuri, huko mbele au siku za usoni tutaangalia ni jinsi gani tutafanya, ikiwezekana katika ku-decentralize, tukaweka timu za kufaa katika ngazi za mikoa ambapo wakati mwingine tunaweza tukafanya jambo hilo likaendeshwa katika huko, lakini kwa sasa hivi huo ndiyo utaratibu, lakini wazo ni zuri, huko siku za usoni inawezekana tukalifanyia kazi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Mkoa wa Arusha una kiwanda hicho ambacho kinafahamika zaidi cha General Tyre lakini ni ukweli kwamba Mkoa wa Arusha pia una viwanda vingine vingi ambavyo vimebinafsishwa ikiwemo Kiwanda cha Maziwa, Kiwanda cha Phillips, Kiwanda kilichokuwa cha Nguo. Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda vyote vilivyopo katika Mkoa wa Arusha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso. Napenda niseme ukweli, sipo hapa kudanganya watu. Sina kumbukumbu kwamba Kiwanda cha Phillips kilikuwa cha Serikali lakini hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni kuona Arusha inapata viwanda.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anawahisha shughuli, nimekuwa Arusha mara tano tangu niwe Waziri, nimeupendelea Mkoa wa Arusha. Napenda kusema kwamba viwanda vitaanzishwa na vitaanzishwa kwa Watanzania kuhamasishwa kushiriki katika viwanda.
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Maziwa ni kiwanda kidogo na tunao mkakati wa kuanzisha Viwanda vya Maziwa, Viwanda vya Ngozi na Viwanda vya Viatu. Kwa hiyo, wakati utakapofika kila mkoa utapata dozi yake na viwanda vitaanzishwa kiuchumi. Bahati mbaya kuna watu hawataki viwanda, hatutapeleka viwanda pale wasipovitaka.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. CECILIA. D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Katika Awamu ya Nne Mheshimiwa Rais aliyepita aliwahi kutoa ahadi ya kujenga kiasi cha kilometa takriban mbili hadi nne za lami katika Mji wa Karatu na hasa ukizingatia Mji wa Karatu ni mji wa kiutalii kwa sababu ni lango la kuelekea Ngorongoro. Je, ni lini ahadi hii itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nisingependa sana kumaliza utamu wa hotuba ya Waziri wangu ambayo inakuja Jumanne wiki ijayo. Ningeomba Mheshimiwa Mbunge asubiri hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo itakuwa inajibu kiu yake hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu pekee ambacho naweza kumhakikishia ni kwamba ahadi zote zilizoko katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo Serikali hii inaitekeleza, ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akiomba kura sehemu mbalimbali za nchi, ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na ahadi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, tutaziangalia na kuhakikisha kwamba zinatekelezwa kwa sababu zote kwa pamoja ni ahadi za Chama cha Mapinduzi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi ni Mheshimiwa Paresso, kwa niaba ya Mheshimiwa Magereli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ni ukweli kwamba hakuna aliye juu ya sheria lakini wakati mwingine wanajeshi wetu baadhi wamekuwa wakijiona kwamba wao ni superior kuliko watu wengine; je, Wizara ina mkakati gani wa kuendelea kutoa elimu ili wanajeshi hao wafuate sheria na kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na jeshi?
Swali la pili, pia kumekuwa na mahusiano hafifu kati ya jeshi na wananchi hasa katika yale maeneo ambao yana migogoro ya ardhi. Je, Wizara sasa ipo tayari kuhakikisha migogoro hii inaisha kwa wakati ili mahusiano haya yaendelee kuimarika?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kutoa elimu upo. Wanajeshi mara zote wamekuwa wakikumbushwa kuishi vizuri na raia hususan wale wanaowazunguka katika makambi yao. Mara kwa mara zimekuwa zikichukuliwa hatua za kinidhamu ndani ya vikosi vyetu vya jeshi pale wanapokiuka utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tueleze vilevile kwamba sheria za nchi hii zinataka mtu anapohisi amevunjiwa haki yake, basi ana haki ya kwenda kushtaki. Kwa kuwa wanajeshi hawako juu ya sheria, sheria hufuata mkondo wake. Kwa hiyo, hilo lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mahusiano hafifu kwenye migogoro ya ardhi, hili napenda niliseme, kama tulivyoeleza wakati tunatoa bajeti yetu hapa, kwamba juhudi zote zinafanyika ili migogoro ya ardhi inayohusisha Kambi za Jeshi iweze kuisha. Yapo maeneo ambayo wananchi wamevamia maeneo ya jeshi, kwa hiyo, ni vizuri wananchi nao wakapewa elimu hiyo hiyo ili wasiweze kuvamia maeneo ya jeshi. Kwa yale maeneo ambayo jeshi imechukua haijalipa fidia, juhudi zinafanyika ili tuweze kulipa fidia. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa ni ukweli kwamba wakandarasi hapa nchini pamoja na wazabuni mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa Serikali, wamekuwa wakiidai Serikali fedha nyingi na Serikali imekuwa hailipi kwa wakati.
Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba wakandarasi hao wakimaliza kazi na wazabuni wakimaliza huduma wanazotoa waweze kulipwa kwa wakati bila kuhatarisha kazi ambazo wanafanya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakati tunaingia tulirithi deni la shilingi trilioni 1.215 la makandarasi. Nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara ya Fedha wametuwezesha kati ya hizo tumeshalipa shilingi bilioni zaidi ya 790, sasa hivi tumebakiza deni dogo sana katika yale madeni ya nyuma makubwa. Ingawa kwa kulipa madeni hayo, makandarasi wameendeleza kuongeza nguvu ya kuongeza kazi na wameongeza tena madeni mengine, lakini hayo madeni mengine walau sasa hivi yanashughulikiwa kwa namna ambayo hayazalishi tena idle time ambayo ni fedha ambazo tunalazimika kuzilipa wakati kazi haifanyiki kwa sababu tu ya kuchelewa kulipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwamba sasa suala hilo halipo tena na kwa kweli tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi hii, naomba mtupongeze na tutaendelea kukamilisha deni lililobakia ili hatimaye wakandarasi hawa wasiwe tena na madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine miradi yote ya wakandarasi wazalendo tumekuwa tukilipa kikamilifu kabisa, huwa haichelewi kwa sababu tunajua uwezo wao ni mdogo na kwa kulipa mara deni linapo-accrue lengo ni kuwawezesha hawa wakandarasi wa kizalendo waweze kukua zaidi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua mfumo wa kodi ya majengo kukusanywa na TRA, lakini kumekuwa na sintofahamu kubwa kwa wananchi wetu kwamba ni majengo yapi hasa ambayo yanatakiwa kulipiwa kodi katika Halmashauri zetu maana hata nyumba za tembe na udongo nazo zinachangiwa kodi. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli mwaka 2015 kupitia Sheria ya Fedha tulifanya marekebisho ya sheria na katika kifungu cha 25(2)(b) tulieleza kwamba chanzo hiki badala ya kuwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mijini kiende hata kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa zilizo Vijijini yaani District Councils. Hata hivyo, tafsiri ya mabadiliko haya haijatafsiriwa vizuri na mamlaka zenyewe kwa sababu mazingara haya yalikuwa ni mahsusi kwa maeneo kama yafuatayo; kwa mfano, Ngurdoto pamoja na establishment yote kubwa ya hoteli, facilities na kumbi za mikutano unaikuta iko vijijini, huwezi ukaacha kukusanya pale property rate au Bagamoyo yako maeneo mengi sana ya hoteli ambazo zipo vijijini, yalikuwa ni maeneo maalum kama hayo.
Mheshimiwa Spika, ili uweze kukusanya chanzo hicho ni lazima itugwe Sheria Ndogo kutoka kwenye Halmashauri husika na sheria hiyo inatungwa Waheshimiwa Wabunge mkiwa wajumbe. Unakuta inatungwa Sheria ya Ndogo ambayo kabisa inakiuka tafsiri nzuri ya sheria iliyotungwa na Bunge.
Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kueleza tu kwamba tafsiri ya kwamba ukusanyaji wa property rate sasa unakwenda mpaka kwenye vijiji kwenye nyumba za tope na udongo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, usahihi ni kwamba kwa mazingira maalum ya uwekezaji ambayo uko vijijini lakini unauona ni uwekezaji wa kimjini huko ndiko zinatakiwa kukusanywa. Si kwa nyumba ya mwananchi wa kawaida ambayo haiingizi kipato chochote, hajapangisha mtu yeyote, yeye anaishi tu, hatujafikia hatua hiyo kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuziagiza Mamlaka zote za Serikali za Mitaa ambazo zinafanya hivyo kukusanya kutoka kwenye nyumba za tope, nyumba za bati au nyumba zozote lakini ambazo haziingizi mapato, si za kibiashara na ziko vijijini, hapana, haitakiwi kukusanya na Serikali ya CCM haijaamua uamuzi huo bado. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza nilitaka niongezee tu kwamba kwa mwaka huu ambao tunamalizia, TRA ilikusanya kodi ya majengo kwa Halmashauri 30 tu, Halmashauri nyingine zilitakiwa kuendelea na utaratibu wa kawaida wa kukusanya mapato hayo yanayotokana na kodi ya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisisitize nchi yetu hii ili tuende ni lazima tuendelee kujenga utaratibu wa wananchi wetu kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Nitatoa ufafanuzi mchana kuhusu kodi hii ya majengo na nimwombe sana Mheshimiwa Cecilia Paresso avumilie tu kidogo mpaka ile hotuba itakayowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali mchana tutafafanua zaidi kuhusu kodi hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa kuwa Serikali inakiri kwamba kuna baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wamekuwa wakiitumia sheria hii vibaya.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuleta mabadiliko ya Sheria hii hapa Bungeni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wamewasimamisha baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ambao wamechaguliwa kihalali kwa muda mrefu na kukaimisha nafasi hizo kwa watu wengine, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na sheria, kanuni na taratibu bora za uendeshaji wa Serikali za Mitaa. Je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, hivi sasa sheria hii inajitosheleza. Changamoto kubwa ni matumizi ya ile sheria. Ndiyo maana tumesema kwamba ofisi yetu na kupitia Waziri wangu hapa, aliitisha kikao maalum cha kupeana maelekezo ya jinsi ya kutekeleza vizuri sheria hii. Lengo kubwa ni kwamba makusudio ya sheria hii yaweze kufikiwa kama vilivyo.
Kwa hiyo ukiangalia, muktadha wa sheria yenyewe haina matatizo isipokuwa katika implementation ya sheria. Ndiyo maana tumesema kwamba maelekezo maalum yametolewa na sasa hivi hatutarajii kwamba kama kutakuwa na mapungufu yoyote mara baada ya maelekezo hayo ambapo ofisi yetu imefanya kazi kubwa sana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Wenyeviti wa Vijiji kusimamishwa na baadhi ya Wakuu wa Wilaya, naomba ikiwezekana tupate taarifa ya eneo specific, liko wapi, halafu tuangalie kesi gani ambayo imejitokeza katika eneo husika tuweze kuangalia tatizo gani limesababisha kusimamishwa. Hata hivyo tuna imani kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kwamba utaratibu wote unasimamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na wakati mwingine inawezekana baadhi ya vijiji kuna baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji huenda wameuza ardhi ya kijiji au kufanya jambo lingine ambalo lilikuwa tofauti na utaratibu, ndiyo maana utakuta Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anafanya taratibu za kisheria. Lakini kama kuna jambo ambalo limekiukwa basi naomba ofisi yetu tupate taarifa hizo tuweze kulifanyia kazi kwa misingi ya kisheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Sheria hii ya Mikoa inatoa mamlaka kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuweza kumkamata mtu katika mazingira ambayo wanaamini kwamba mtu huyo ama anatenda kosa la jinai, ama kwa ufahamu wao ametenda kosa la jina, ama anafanya kitendo chochote kinachovunja amani na utulivu, ama anaona mtu huyu anatarajia kutenda au kuhatarisha amani, hivyo ndio tafsiri ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu hili wamepewa hawa kwa sababu ya ku-maintain law and order. Utaiona leo hii inapokuwa ipo kinyume na wewe kama mbaya, lakini ikiwa inakusaidi katika wakati ambapo amani yako, haki yako au jinai dhidi yako inataka kutokea, mkuu huyu anapochukua zile hatua ndipo utakapoona msingi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama, mamlaka haya yanatokana na nguvu kubwa waliyonayo katika msingi wa Katiba. Halikadhalika, mtu yoyote anayo haki ya kuomba mtu mwingine ambae anaweza kutenda kosa la jinai dhidi ya mtu fulani au ya watu fulani kuomba wakamatwe.
Kwa hiyo haki hii sio tu wamepewa hawa peke yao, ukisoma vizuri sheria nyingine tulizonazo pia zinakupa wewe nguvu ya kusema wewe hapana, Simbachawene mimi naona huyu anatarajia au anahatarisha amani au anataka kutenda kosa, akakamatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa cha msingi ni pale tu ambapo inapaswa kutumika kwa kuzingatia sheria. Mtu huyo awe ana mtarajio ya kupelekwa mahakamani immediately baada ya kukamatwa na baada ya muda ule kupita. Isikamatwe kwa ajili ya show off tu, asikamatwe mtu kwa ajili ya ku-show, asikamatwe kwa ajili tu ya kuonesha kwamba wewe una madaraka. Lazima akamatwe mtu huyo kama kweli kitendo chake kinahatarisha amani na utulivu. Hapa ndipo ninapotaka nisisitize kwamba Wakuu wetu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa kutumia sheria hii, wawe makini na kuhakikisha kwamba wanaitumia kama vile sheria inavyotaka. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri zilizo nyingi zinashindwa kutenga hii asilimia kumi kwenye Mfuko wa Vijana na Wanawake na hii inathibitishwa na ripoti mbalimbali za CAG, na ni ukweli kwamba tuna Mifuko karibu 19 ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kupunguza Mifuko hii angalau kati ya miwili mpaka mitano ikiwemo hii iunganishwe kuwe Mfuko mmoja ili kuwe na ufanisi na iwafikie kweli wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ku- harmonize hii Mifuko tuwe na Mfuko mmoja nadhani ni suala la kuzungumzika, tutafanya tathmini ya kina. Hata hivyo katika Mfuko wa asilimia kumi kuna maelekezo sasa hivi tunayatoa. Sasa hivi zile fedha katika ten percent zinaingia katika deposit account kama unaingiza katika dust bin mwishowe hata assessment hatuwezi kufanya vizuri; ndiyo maana sasa hivi tunaangalia jinsi gani tutafanya; kama ikiwezekana tuwe na akaunti maalum ya Mfuko katika Halmashauri ili tuweze kui-monitor vizuri; ili zikiingia zinazorudi kutoka kwa watakaokopa tuweze kuisimamia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wazo zuri tutaendelea kuchukua yote haya ili hatimaye tuboreshe Mifuko hii iweze kuwasaidia vijana na akinamama na hatimaye tutatengeneza ajira kwa wananchi wetu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, vifungashio vya mazao haya ya vitunguu katika Tarafa ya Eyasi hufanyika kwa aina mbili. Kuna kifungashio cha Mkenya maarufu wanaita net ambapo net hii ikijazwa net tatu inakuwa sawa na debe kumi; na kuna kifungashio kingine kinaitwa kifungashio cha Mganda ambapo kifungashio hiki cha Mganda kinachukua kati ya debe nane mpaka tisa jambo ambalo kwa kweli linawaumiza wakulima.
Je, ni kwanini Serikali isihakikishe kunakuwa kuna standard ya vifungashio kwa wakulima hawa ili tusiweze kuwaumiza?
Swali la pili, tatizo la ujazo kupita kiasi maarufu kama lumbesa bado ni changamoto kwa wakulima hawa katika maeneo mbalimbali na zao hili linapofika sokoni wanunuzi wanachukua yale ambayo yamejazwa kwa maana ya lumbesa kuliko yale ambayo yana ujazo wa kawaida. Mfano, labda ujazo huu unatokea Singida, unatokea Kilimanjaro, unatokea Mang’ola wale ambao wana ujazo zaidi ndiyo itanunuliwa zaidi na wale ambao wana ujazo wa kawaida ambao ni standard inakuwa hainunuliwi.
Je, ni kwa nini sasa Serikali isiendelee kutia msisitizo ili jambo hili lisimamiwe katika maeneo yote kwa ukamilifu wake ili kuwepo na ujazo ambao unafanana?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Kwanza, nisisitize tu kama ambavyo swali limejibiwa kwamba kipimo sahihi cha uzito wa aina ya bidhaa kama vitunguu ni kilogram, kwa hiyo tunachosema ni kwamba whether hicho kifurishi kitawekwa kwenye net, kitawekwa kwenye debe, kitawekwa kwenye kitu chochote kile ilimradi baada ya kuwekwa humo basi kipimwe kwenye uzito sahihi ambao ni kilogram ndivyo inavyostahili.
Pili, ulivyouliza kuhusu suala la lumbesa ni hivyo hivyo kwamba kwa mfano, unavyofungasha kwenye gunia likaitwa hili ni gunia la kilo 50 wakati ndani yake kumbe kuna kilogramu zaidi ya 50 inasababisha kwamba kwanza mkulima mwenyewe ananyonywa, lakini vilevile hata Halmashauri inaweza ikakosa mapato kutokana na kuwa na uzito ambao haustahili kutokana na kwenye kile kitu ambacho kimefungashiwa. Ijulikane kwamba siyo kwamba bidhaa zote zinakuwa na ujazo unaofanana. Kwa mfano, ujazo wa pamba kwenye kiroba ni tofauti na ujazo huo huo ukiwa ni wa viazi na ndiyo maana tunasisitiza kilogramu ambayo ndiyo kipimo sahihi ambacho kinastahili katika kupimia.
Mheshimiwa Spika, hivyo ninawaomba sana wananchi wote pamoja na wafanyabiashara kuhakikisha kwamba tunakuwa na mizani katika maeneo yetu ya kibiashara na hilo ndiyo linalosisitizwa sasa kuwa na masoko ya pamoja ili kuweza kuwafanya hawa wananchi wanaolima mazao kama hayo, kuweza kuwa na ushirikiano katika kudhibiti hali kama hiyo ya kuwa na vipimo ambavyo haviruhusiwi kisheria.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa vitunguu katika Tarafa ya Eyasi wanayo miundombinu ya umwagiliaji ambayo imejengwa na World Vision na fedha za DADPs na Shirika na Maendeleo la Jimbo Katoliki la Mbulu na Waziri Mkuu alikuja kuzindua. Tatizo kubwa si miundombinu kama ambavyo imeelezwa na Mbunge mmoja hapa, suala ni uhifadhi wa chanzo ambao wakulima wale wanatumia kumwagilia vitunguu vyao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhifadhi chanzo kile ili wananchi waweze kulima zao hilo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Eyasi linatumia chanzo cha maji ya mbubujiko kutoka chini ya ardhi eneo la Mang’ola. Nilikwenda kule na tayari tumeshaweka mipaka ili kuzuia wananchi wasifanye shughuli za kibinadamu karibu na vile vyanzo. Mipaka hiyo inaendelea kuwekwa na Mheshimwa Mbunge tuendelee kushirikiana, na kama utaona kwamba kuna kitu ambacho hakiendi vizuri, tuwasiliane. Lengo ni kuboresha ili yale maji yaendelee kutoka kila wakati.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Sekta za Elimu na Afya ni sekta ambazo zinaongoza kwa upungufu wa watumishi hapa nchini na tunaelewa Sekta ya Elimu inaandaa rasilimali watu wa Taifa na Sekta ya Afya inaenda kuhudumia hii rasilimali watu ili Taifa liweze kusonga mbele. Hata hivyo, upungufu umekuwa mkubwa sana kwenye hizi sekta mbili hasa. Nini mkakati wa Serikali wa muda mfupi na wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba sekta hizi angalau kwa asilimia 60 mpaka 70 zinapata watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, nadhani nimepatia sasa maana huwa ninakosea kosea sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii najibu kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kwa niaba ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, ambaye ni baba yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hadi sasa imetoa kibali cha kuajiri watumishi 52,000. Katika hao watumishi 52,000 kipaumbele kikubwa kimeelekezwa kwenye sekta hizi mbili, Sekta ya Elimu na Sekta ya Afya ambazo kwa pamoja zitakuwa na waajiriwa wapya wapatao 33,000 ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya waajiriwa wote ambao wataajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Paresso na Waheshimiwa Wabunge wote wa-support huu mchakato unaoendelea ambao utapunguza sana mahitaji au upungufu wa watumishi katika sekta hizi mbili ambazo ni muhimu sana katika nchi yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii inachangia takribani 17% ya pato la Taifa na wamiliki wa hoteli hizi za kitalii wamekuwa wakitozwa kodi nyingi au tozo nyingi sana takribani 46 na wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu. Je, ni kwa nini Serikali isifikirie utaratibu mwingine wa kuwarahisishia hao wawekezaji kwenye hoteli za kitalii ulipaji wa tozo hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na kodi na tozo nyingi ambazo zimekuwepo katika baadhi ya hoteli, lakini jitihada zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha hizi kodi zote zinahuishwa zinabaki chache. Mwaka jana, kama mtakumbuka, kuna baadhi ya kodi ziliondolewa na mwaka huu hivi sasa kuna kazi inaendelea kwa ajili ya kuhuisha kuangalia hizi kodi ziunganishwe kwa pamoja ili kurahisisha walipaji hao kusudi wasiwe na kodi za hapa na pale. Kwa hiyo, jitihada hizo zinafanyika na Mheshimiwa awe na subira, pale tutakaposoma bajeti yetu atasikia ni hatua gani ambazo tunakusudia kuzichukua.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Ujenzi inaelekeza kuunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami na kumekuwa na kilio cha muda mrefu na ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa kiwango cha lami ya barabara ya kutoka Njiapanda – Karatu – Mang’ola - Lalago. Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli ni sera ya Serikali kuunganisha mikoa na mikoa. Kwa hiyo, tunaanza kuunganisha mikoa na mikoa, tunaungamisha mikoa pamoja na nchi za jirani na hizi harakati zinaendelea, zipo barabara chache sana ambazo zimebakia kuunganishwa kwa maana ya mikoa kwa mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa barabara kubwa ambazo zimebakia ni chache ikiwemo barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja ikiwa inatokea kule Simiyu – Lalago – Sibiti – Mbulu – Karatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba ukitoka Sibiti yako matawi mawili ya barabara, iko barabara ambayo inapita kandokando ya Mto Eyasi kwenda Karatu na hii barabara ambayo inapita Haydom – Dongobesh - Mbulu Mjini lakini itaunganika na barabara inayotoka Mbuyu wa Mjerumani - Mbulu Mjini - Karatu.
Kwa hiyo, hizi barabara zote ziko katika hatua mbalimbali. Barabara inayopita Eyasi tayari michoro yake imeshakamilika tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi na katika bajeti hii iliyopitishwa na Bunge lako tumetenga fedha za kuanza ujenzi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, lakini kizuri pia nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo ya Lalago kuja upande huu wa Manyara na Arusha kwamba pale Sibiti tulikuwa na tatizo kubwa sasa ujenzi wa lile daraja unakamilika, vile vyuma ambavyo tulivisubiri kwa muda mrefu vilishafika na baada ya mvua kupungua tutapandisha vile vyuma hata kabla ya harakati za kukamilisha lami basi wananchi wataweza kupita kutoka Lalago kuja katika mikoa hii pamoja na kuja Singida. Tutapunguza kilometa karibu 400 kwa mtu anayetoka Mwanza na Simiyu kwenda Karatu kama atapita pale Sibiti akipitia Eyasi kwenda Karatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge vuta subira, sisi tumejipanga vizuri na Serikali inaendelea kutoa huduma na kuunganisha mikoa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na Mifuko mingi ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, mingine iko Ofisi ya Waziri Mkuu na mingine iko TAMISEMI; na kwa kuwa sheria/ takwa hili la kutaka kutengwe asilimia 10 kwenye Serikali za Mitaa, muda mwingi katika ripoti za CAG imeonekana ufanisi ni hafifu, kama kweli mna lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi, kwa nini msifikirie kuunganisha mifuko hii uwe mfuko mmoja ili kuwepo na ufanisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba nitoe majibu ya nyongeza kwenye swali la msingi sana aliloliuliza Mheshimiwa Paresso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa ndani ya Serikali tumeanza kutafakari na kuona ni kwa kiasi gani tunaweza kuitazama kwa kina mifuko hii yote takriban kama 16 ama 19 hivi tuliyonayo, tukaiunganisha na kuipunguza ikajenga nguvu kubwa zaidi na ikawa na impact kubwa zaidi kwa Watanzania wengi na hasa wale ambao wako vijijini. Kwa hiyo, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi hii imeshaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu inaishughulikia vizuri na baada ya muda mfupi nadhani tunaweza tukaja na sheria ya kuunganisha baadhi ya mifuko na kuibakiza michache ambayo itakuwa na impact kubwa kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, fedha hizi za TASAF tunafahamu ni mkopo kutoka World Bank na fedha hizi zimekuwa zikitolewa kwa kaya maskini na fedha hizi hazijawahi kuonesha matokeo ya moja kwa moja kwa wale wananchi wanaopewa. Je, Serikali sasa iko tayari kufanya uchunguzi wa kina na tathimini na kuleta taarifa hapa Bungeni yenye kuonesha matokeo ya moja kwa moja kwa kaya hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni ukweli usiopingika kwamba fedha hizi za TASAF zimekuwa zikitolewa kisiasa kwa wana CCM na fedha hizi wakati panapotokea chaguzi ndogo zimekuwa zikitumika sana kushawishi kama sehemu ya rushwa kwa wana CCM ili CCM iweze kuchaguliwa. Nini kauli ya Serikali ikizingatia kwamba fedha hizi ni mkopo na zitarudishwa na Watanzania wote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi naomba nianze kumpongeza muuliza swali Mheshimiwa Msabaha kwa swali lake zuri, lakini pia nataka niwapongeze walengwa wa TASAF Unguja na Pemba. Katika nchi yetu mikoa inayoongoza kwa kufanya vizuri miradi ya TASAF ni mikoa ya Unguja na Pemba na kwa maana hiyo nataka nimpongeze Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed anayesimamia TASAF kule Pemba na Zanzibar ambaye anamsaidia Makamu wa Rais ambaye ndio Waziri mwenye dhamana ya TASAF Zanzibar. (Makofi)
Baada ya pongezi hizo naomba nitoe majibu ya maswali niliyoulizwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba TASAF haijaonesha matokeo; mimi ninanomba tusichanganye mambo, hoja kwamba mnaomba taarifa ya utekelezaji wa TASAF ikoje ni hoja ya msingi na inaweza ikaletwa. Mheshimiwa Mao Tse Tung anasema no research no right to speak. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndio Waziri wa TASAF na juzi nimetoka Kilimanjaro nimeona jinsi walengwa kule na wengi ni wakina mama walivyopambana na umaskini kwa kutumia TASAF wameanza biashara ndogo ndogo mwingine amenunua ng’ombe, wengine wamejenga majumba mimi ninamuomba ndugu yangu, ng’ombe ananunuliwa baada ya kudunduliza. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba muuliza swali akubali ombi lake la mwanzo kwamba tupewa taarifa ya utekelezaji wa TASAF lakini kwa uhakika Kamati husika ya Bunge inapewa taarifa ya utekelezaji wa TASAF kila baada ya muda. Mheshimiwa Spika akisema taarifa ya TASAF anataka ailete humu ndani italetwa pasipo na mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba zinatolewa kisiasa, zinatumika chaguzi ndogo ndogo nini kauli ya Serikali jamaa zangu ndio yale niliyosema jambo hujalifanyaia utafiti usiliseme. Walengwa wote wa TASAF wanapendekezwa na wana vijiji wenyewe, wana vijiji wanaambiwa andika jina la mtu unayemuona kijijini kwako hapo anastahili kupata msaada wa TASAF, wakishafanyiwa hivyo sasa ndiyo Watendaji wa TASAF wanazunguka kwenda kuthibitisha kwamba je, huyu yuko na katika kuthibitisha hivyo wengine tumewafuta kwa kuona hawastahili kupata.
Mimi nataka niwaambieni hakuna mtu anayechanganya siasa katika TASAF wala hakuna ushahidi kwamba hela ya TASAF inatumika katika uchaguzi, mimi ningeweze kumuomba Spika kwamba Mheshimiwa athibitishe kauli yake, tusifike huko mimi nimekusamehe. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, panapotokea migogoro hiyo basi wananchi wengi wanakimbilia kupata suluhu katika Mabaraza yetu ya Ardhi ya Kata, lakini uwezeshwaji ili kuwepo na ufanisi wa Mabaraza hayo umekuwa ukisuasua. Mabaraza haya yanategemea faini za wateja wake ili yaweze kujiendesha na halmashauri imekuwa haisaidii. Je, ni lini sasa Serikali itatia mkazo wa kuwezesha Mabaraza haya ili ufanisi uweze kupatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Paresso, nilitaka kusema Gekul maana wakati mwingine wanafanana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba uanzishwaji wa Mabaraza ya Ardhi ilikuwa ni kwa ajili ya kusaidia wananchi na hasa katika maeno ambayo wale wajumbe wanayafahamu vizuri kulikoni kwenda kwenye mambo ya kisheria. Tunachotarajia kwanza ni wao kwenda kubaini na kuweza kusuluhisha.
Mheshimiwa Spika, pia ni ukweli usiopingika kwamba baadhi ya Mabaraza wamekuwa wakitumia zile tozo ambazo wanatoza wananchi kama chanzo na wakati mwingine kumekuwa mpaka hata haki kutotendeka. Ni vizuri tukalitizama kwa ujumla wake, maeneo mengine wanafanya vizuri, katika maeneo ambayo hawafanyi vizuri na hasa kwa kuanzia wale wajumbe ambao wanachaguliwa kuwa katika lile Baraza, katika maeneo ambayo haki imetendeka wamekuwa wakifanya vizuri sana lakini maeneo mengine lazima tukubaliane kwamba kumekuwa na shida ni vizuri tukalitizama kwa ujumla wake ili tukafanya revision namna nzuri ya kuweza kuenenda na suala hili.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali ndogo la nyongeza. Ahadi hizi ambazo zimetolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ziko nyingi nchi nzima na kwa kweli zipo ambazo hazijatekelezwa kabisa, ikiwemo ujenzi wa kilomita mbili za lami katika Mji wa Karatu. Ahadi hiyo ilitiliwa msisitizo na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano akasema ataongeza kilomita nane jumla ziwe kilomita 10, lakini mpaka leo utekelezaji haujafanyika. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba kuna ahadi ambazo zimetolewa na Marais waliotangulia na katika utaratibu wa kawaida ni kupokezana kijiti, pale ambapo mwenzako ametekeleza yale ambayo hakuyamaliza wewe unahakikisha unayachukua na wewe unaongeza ahadi za kwako ili kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Paresso ni azma ya Serikali ndani ya kipindi cha miaka mitano ambayo ndiyo mkataba wa Mheshimiwa Rais na wapiga kura wake, barabara yake hiyo itaweza kutekelezwa kama ambavyo ahadi ya Mheshimiwa Rais ilivyoahidiwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ambayo yamewasilishwa hapa Bungeni na Serikali muda huu yanaeleza kwamba Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatengeneza kanuni za kulazimisha halmashauri iweze kutenga hizo fedha kwa ajili ya mfuko huu. Suala si kuwa na kanuni na sheria kali, suala ni kwamba vyanzo vingi vya halmashauri vimechukuliwa na Serikali Kuu hivyo halmashauri inashindwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwapa mikopo wanawake na vijana. Ni kwa nini Serikali sasa, kwanza iache kutengeneza kanuni hizo lakini itenge fedha hizo kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa sababu mapato yote imeyachukua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Paresso na Bunge lako Tukufu kwamba agizo la kutenga asilimia 10 linahusu makusanyo ya ndani. Kama wamekusanya Sh.100 basi asilimia 10 ya Sh.100 watenge hiyo hiyo. Hatujasema kwamba mtu amekusanya Sh.100 atenge Sh.200, hapana. Amekusanya Sh.100 basi atoe asilimia 10 ya hiyo Sh.100 ili kusudi aweze kutoa mikopo kwa vikundi vya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ambayo imekusanya Sh.100,000,000 inatakiwa itoe Sh.10,000,000 kwa ajili ya vikundi vya vijana na wanawake. Kwa hiyo, kama kuna changamoto nyingine, taratibu za mawasiliano ndani ya Serikali Wakurugenzi wa Halmashauri wanazifahamu sana. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wabeba mizigo kwenye milima yetu ambao wanatembeza Wazungu wamekuwa hawapewi mafunzo na wanafanya kazi hii kwa uzoefu Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanapatiwa mafunzo haya lakini na maslahi yao kwa ujumla yanatazamwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso ambalo kwa kweli anataka kujua kwamba ni mpango gani tulionao katika kutoa mafunzo kwa hawa wanaobeba mizigo. Naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejiandaa vya kutosha katika mwaka huu wa fedha unaoanza Julai mwaka 2018, tunategemea kutoa mafunzo mafupi kwa hao watu wote pamoja na wale wanaongoza utalii katika eneo la Mlima Kilimanjaro ili kusudi waweze kutoa zile huduma ambayo wateja wetu wanazitarajia. Kwa hiyo, awe na subira, baada ya mwaka kuanza ataona matunda na mabadiliko makubwa yatakayojitokeza.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Changamoto ambazo zinakabili vijiji hapa nchini vinavyopakana na hifadhi za wanyama zimekuwa ni changamoto za muda mrefu kwamba, wanyama wanaingia na kuharibu mazao na kuuwa watu, lakini ukiangalia nchi mbalimbali zilizoendelea duniani wanaweka electrical fence, ili kudhibiti moja kwa moja tatizo hili. Je, Serikali kwa nini isianze kwa awamu kutekeleza na kuweka hizo electrical fence, ili angalau kukomesha kabisa tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, dada yangu ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu sana matukio mbalimbali na amekuwa alifanya kazi nzuri sana, hongera sana.
Mheshimiwa Spika, sasa kuhusu electrical fence kuwekwa katika hifadhi zetu zote ni suala zuri, lakini uwezo wa kifedha ndiyo changamoto. Ukiangalia ukubwa wa hifadhi tulizonazo kwamba, zote tutaweka electrical fence kwa kweli, inaweza ikachukua muda mrefu sana. Sitaki kutoa commitment ya Serikali, lakini tutaendelea kulifanyia kazi ili tuone kwamba, kama litawezekana, kama pale ambapo bajeti itaruhusu basi tunaweza kulitekeleza.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza ninasikitika hiyo kauli aliyotoa Mheshimiwa Waziri hapo na wale wazee ambao, maana yake mzee anaanzia kijana, mtoto ambaye inawezekana mazingira yake yote alikuwa ni yatima. Sasa huyu pia unamfanyaje, maana yake Serikali mnakwepa wajibu. Swali langu ni kwamba Serikali ya Awamu ya Nne iliahidi kutoa pensheni kwa wazee na tafiti zilishafanyika, kauli ikatolewa hapa Bungeni. Je, ni lini Serikali itatoa pensheni kwa wazee wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize majibu ambayo amesema Mheshimiwa Waziri, kwa mujibu wa Sera yetu ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo inatamka kwamba majukumu ya kwanza ya kumtunza mzee ni familia, ndugu na jamii husika kabla Serikali haijabeba majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea tunahudumia wazee zaidi 500 ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo bado tunaendelea kusisitiza kwamba majukumu ya awali ya msingi yawe katika ngazi ya familia na jamii kabla ya Serikali haijachukua majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake ambalo anauliza kwamba ni lini na tumefikia wapi katika pensheni hii ya wazee, bado Serikali inaendelea kulitafakari jambo hili, kuangalia utaratibu mzuri zaidi wa kuweza kulitekeleza. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa malengo ya kuanzishwa kwa kituo hicho ilikuwa ni maamuzi ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya jinsia na wanawake; na kwa kuwa malengo haya yalijikita katika kuhakikisha kunakuwa na kituo ambacho kitasaidia uwezeshwaji wa ufanyaji wa tafiti na kuhifadhi machapisho hayo ya utafiti na kuwashauri watunga sera kuhusiana na masuala mazima ya maendeleo ya wanawake na jinsia; ni ukweli kwamba pamoja na kuzindua kituo hiki lakini Serikali haijweka msisitizo wa kukiwezesha kituo hiki kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Je, Serikali sasa iko tayari kufufua mchakato huu wa kukianzisha kituo hiki ili kiweze kutimiza malengo ya uanzishwaji wa kituo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutenga eneo kama ambavyo wameeleza katika Chuo cha Tengeru ni jambo moja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali watu na rasilimali fedha ni jambo lingine. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha inakipatia fedha kituo hiki ili malengo ya uanzishwaji wake yaweze kutimia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Paresso amesema kwamba je, Serikali ina mkakati gani wa kukifufua. Niseme tu kwamba kituo hiki kipo na nilipata fursa ya kutembelea Chuo cha Tengeru na kukitembelea hiki kituo. Kipo na kinafanya kazi. Kwa hiyo kaika hoja kusema kwamba tunahitaji kukifufua hili halipo kwa sababu ni kituo ambacho kinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kuongeza rasilimali watu na rasilimali fedha kituo hiki pamoja na kwamba lilikuwa ni azimio, sisi kama Serikali kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii tunaendelea kukihudumia kituo hiki kuhakikisha kwamba kinafanya kazi na kadri rasilimaliwatu itakapokuwa inaongezeka na sisi tutaongeza watumishi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeenda mbali zaidi; kwa sababu ya majukumu ya kituo hiki katika kutoa elimu na uelewa katika masuala ya jinsia tumeendelea kuwasiliana na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu na taasisi mbalimbali ambazo zinafanya tafiti katika masuala ya jinsia ili nao watusaidie kutupatia yale machapisho yao na kuyahifadhi katika maktaba zetu hizi kwa lengo la kupanua wigo kwa kupata machapisho mbalimbali yanayohusiana na masuala ya jinsia.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa waraka wa kusitisha taratibu wa upandishwaji wa baadhi ya zahanati kwenda vituo vituo vya afya ikitaka vituo vya afya vijengwe kwenye kila kata, lakini kwamba Halmashauri zetu hazina fedha za uhakika za kujenga lakini hata wananchi wenyewe hali ya uchumi ni ngumu kuweza kujenga vituo hivyo vya afya.
Je, Serikali kwa nini msifikirie kwa upya kubatilisha uamuzi huo na kuangalia zile zahanati ambazo kwa kweli zinakidhi haja ziweze kupandishwa kuwa vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya suala zima la kupandisha zahanati kuwa vituo vya afya, kwanza naomba tukubaliane, zahanati zina ramani zake na vituo vya afya vina ramani zake. Hoja ya msingi ni kwamba tungependa wananchi wapate huduma ya afya jirani sana, naomba kwa sababu mpaka sasa hivi tulikuwa tunaongelea tuna asilimia 12 tu ya vituo vya afya na bado na uhitaji wa zahanati bado uhitaji ni mkubwa.
Naomba azma hiyo ya Serikali yakuhakikisha kwamba kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila Kata kunakuwa na kituo cha afya bado ndio msimamo wa Serikali na wananchi waendelee kushiriki ili tuhakikishe kwamba huduma hii ina inawasogelea wananchi kwa karibu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa, kila mwaka wananchi wa Monduli wamekuwa wakipoteza mali lakini pia kupoteza maisha kutokana na uharibifu huu; na Mheshimiwa Naibu Waziri kutokana na takwimu ulizoziwasilisha hapa si kweli kwamba ni vijiji vyote vimelipwa. Kuna vijiji vya Moita, Naiti, Mswakini, Makuyuni na Isilalei wananchi hawa hawajalipwa fidia kwa mwaka 2014/2015, 2015/2016, 2016/2017. Je, ni lini sasa Serikali mtawalipa wananchi hao ambao wamepata uharibifu mkubwa na wamesubiri kwa muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kanuni hii ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi ambayo imekuwa ikitumika kwa wananchi ambao kwa namna moja ama nyingine mazao yao au mali zao zimeharibiwa na wanyamapori katika nchi hii imepitwa na wakati na kwa kweli imewaletea wananchi usumbufu mkubwa sana kwa sababu wananchi hao mali zao zinaharibika kwa kiwango kikubwa na wanachokuja kulipwa hakilingani na uhalisia. Je, Serikali sasa haioni ni wakati mwafaka kuendana na hali ya sasa na thamani ya fedha ya sasa kubadili kanuni hii ili kulipa uhalisia wa uharibifu unaofanywa na wanyamapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba si vijiji vyote ambavyo vimeshalipwa fidia. Hivi sasa naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba madai ambayo yamepokelewa kutoka katika wilaya mbalimbali hapa nchini yalifika takribani 15,370 na madai ambayo yameshalipwa tayari ni 6,185. Kwa hiyo, utaona kwamba kuna madai karibu 9,562 ambayo bado hayajahakikiwa na bado hayajalipwa, hivi sasa zaidi ya shilingi milioni 828 zinadaiwa. Kwa hiyo, baada ya zoezi la uhakiki kukamilika vijiji vyote hivyo vitapata fidia na kifuta machozi hicho ambacho tumekisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba hivi sasa tunafanya mapitio ya Kanuni za Kifuta jasho na Kifuta Machozi za Mwaka 2011. Mara tu zitakapokamilika kupitiwa na kuidhinishwa, basi haya masuala yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema yataangaliwa. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mazao haya ya pareto na vitunguu saumu na hata vitunguu maji ambavyo vinalimwa katika maeneo ya Mbulu na Karatu, wakulima wamekuwa wakiuza kwa vipimo vya debe badala ya kilo, na sheria ya vipimo inataka mazao haya yauzwe kwa kilo. Je, kwa nini Serikali isihakikishe kwamba mazao haya yanauzwa kwa kilo badala ya madebe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa pia kuna changamoto ya wafanyabiashara kufuata mazao haya shambani jambo ambalo linamfanya mkulima ananyonywa na asipate faida ya kile anachokilima, hasa mazao ya vitunguu maji ambayo yanalimwa sana kwenye Tarafa ya Eyasi, Wilayani Karatu, lakini pia maeneo ya Mbulu.
Je, Serikali sasa mna mkakati gani wa kuhakikisha kunakuwa na centeres za uuzaji wa mazao haya ili mkulima aweze kufaidika na mazao anayoyalima? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia ujazo na uzito katika kupima mazao, marekebisho ya Sheria ya Vipimo Namba. 340 iko mezani kwangu na nimekataa kuisaini ilivyoletwa nikitaka twende kwa uzito, tupime kwa uzito. Nakubaliana na wewe na sitasaini mpaka wataalam wangu wakubaliane twende kwa uzito. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu vituo vya kuuzia mazao, napenda nimueleze Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote, wakulima wetu tuwahimize warudi kwenye ushirika, washikamane kuwadhibiti wale wanaokuja kunyemelea mazao. Local Government (TAMISEMI), wameshaanza zoezi la kuwa na centers ambako tutaweka mizani, lakini tukiwa na ushirika hao wanaonyemelea ambao wakulima tutaweza kuwadhibiti. Kwa hiyo, ni jukumu letu muisaidie Serikali sisi ndio Serikali twende pamoja tutaweza kuwasaidia wakulima wetu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza; kwa kuwa Serikali inakiri kwamba zoezi hili litaanza siku za hivi karibuni na ni ukweli kwamba tumebakiza muda mchache kuelekea uchaguzi mkuu na kwa kuzingatia tumekuwa na utaratibu wa kuandikisha kupata vitambulisho vya Taifa kupitia NIDA, kumekuwa na changamoto nyingi na watu wengi kukosa na vitu kama hivyo.

Kwa muda huu mchache uliobaki na kwa ukubwa na jiografia ya nchi hii na kwakweli kuna uhitaji wa watu wengi kuandikishwa ili wapate fursa ya kupiga kura, je, Serikali kweli inania ya dhati ya kuanzisha zoezi hili na kuhakikisha watu wote wenye vigezo na sifa wanapata fursa hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara ya mwisho tulivyofanya maboresho haya ya Daftari ya kupiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kulikuwa na changamoto nyingi za ubovu au uhafifu wa vifaa vya uandikishaji, mfano zile mashine za finger printzilikuwa wakati fulani hazifanyi kazi kwa ufanisi na kamera zilikuwa hazifanyi kazi kwa ufanisi.

Je, Serikali ipo tayari sasa kupitia changamoto zilizotokea huko nyuma kuwa na vifaa vya uhakika na vya kisasa kuhakikisha kwamba changamoto zilizojitokeza haziwezi kutokea tena ili kila Mtanzania mwenye fursa aweze kupata fursa hiyo ya kuingia kwenye maboresho ya Daftari ya kupiga kura na kuingia kwenye uchaguzi mkuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, nikianza na swali lake la kwanza la hofu yake juu ya ukubwa na jiografia ya nchi yetu na muda uliopo, kwa mujibu wa Sheria kifungu cha 15(5) kinazungumza kwamba Tume ya taifa ya uchaguzi itafanya maboresho ya Daftari mara mbili kabla uchaguzi mwingine kwa maana kwamba kabla ya nomination day.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo nataka lieleweke kwa Mheshimiwa Mbunge kwanza kabisa, ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kushiriki kwenye uchaguzi na kama Serikali tutahakikisha kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ya kushiriki kwenye uchaguzi anashiriki kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu hofu ya kwamba watu ni wengi sana, tumefanya hivi kwa sababu ya changamoto zilizotokea wakati uliopita, tuliona ni vyema kwanza tukaboresha miundombinu na mifumo ya ndani ili changamoto zilizojitokeza wakati uliopita, hivi sasa tuweze kuzitatua na moja wapo ilikuwa ni kuanzisha kanzidata maalum ambayo itatupa nafasi ya kuweza kuwafikia watu kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili pia si kwamba tutakwenda kuwaandikisha watu upya tunakwenda kuboresha wale ambao wanasifa kwa wakati huo. Kwahiyo, tunategemea kwa mwaka 2019 huo kuandikisha zaidi ya wapiga kura milioni nne wapya wenye sifa na wale ambao wanapata changamoto kwa wakati uliopita na pia mapema mwakani mwaka 2020 tutafanya marejeo tena kwa kwa ajili ya kuwapa watu wenye sifa.

Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu vifaa, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, Serikali inafahamu kwamba ni lazima kila mtu mwenye sifa ya kushiriki uchaguzi ashiriki uchaguzi. Kwa hiyo, moja kati ya maandalizi ambayo tunayafanya ni kuhakikisha kwamba tutakuwa na vifaa bora na vya kisasa ili kila Mtanzania aweze kushiriki haki yake ya kimsingi na yakikatiba.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, kuna ujenzi wa kiwango cha lami unaendelea kutoka Kisolya, Jimbo la Mwibara inapita Bunda Mjini na kuishia Nyamswa, Jimbo la Bunda Vijijini; na kwa kuwa, katika Jimbo la Bunda Mjini barabara hiyo imeingia kwenye makazi ya wananchi na wananchi hao wamewekewa alama ya X, maana yake wanapaswa kulipwa fidia. Je, ni lini na kwa uhakika Serikali itawalipa Wananchi hao fidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ya Awamu ya Nne ilitoa ahadi ya ujenzi wa kilometa nane katika Mji wa Bunda zijengwe kwa kiwango cha lami lakini mpaka leo ahadi hiyo haijatekelezwa na barabara hizo hazijaanza kujengwa. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi wa ujenzi wa barabara ya lami unaoendelea sasa ni kati ya Bulamba na Kisolya, lakini nimfahamishe pia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuko kwenye hatua ya manunuzi ya kujenga barabara kutoka Bulamba kupita Bunda kwenda Nyamswa, kilometa 56 na wakati wowote mkandarasi atapatikana barabara hii itaanza kujengwa, lakini Mheshimiwa Mbunge afahamu pia kwamba, harakati za ujenzi wa barabara zitaanza pindi ambapo wananchi watalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wawe na subira kwamba, sasa mkakati wa kujenga barabara hii kilometa 56 utaanza na hii itakuwa kwa kweli, ni neema kwa wananchi wa Bunda na Musoma kwa ujumla kwa sababu, itaungana na barabara inatoka Makutano kwenda hadi Mugumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu swali lake la pili kuhusu ahadi za kilometa nane, ahadi za viongozi wakuu; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi tumejipanga kuhakikisha kwamba, tunatekeleza ahadi zote za viongozi. Kwa hiyo, wananchi wavute subira, kama wanavyoona sasa tunajenga barabara hii kubwa kupita katika mji wa Bunda, kwa hiyo, sina mashaka pia kilometa nane hizi zitajengwa na wananchi wataendelea kunufaika na barabara.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Madai ya wananchi ya kudai fidia kutokana na miradi ya ujenzi nchini yapo kila siku, ni mengi na ni makubwa. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanawalipa wananchi hawa kwa uhakika na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu tumeendelea kufanya malipo ya fidia miradi inapotekeleza nchi kote katika maeneo mbalimbali. Pia niseme tu shughuli za miundombinu zinaendelea, kwa hiyo tutaendelea kuwalipa wananchi fidia na kadri miradi itakavyoendelea tutaendelea kufanya malipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge tusiwe na wasiwasi tumejipanga vizuri, kwa mwaka wa fedha mmetupitishia fedha zakufanya usanifu kilomita 3,856. Sasa tuone kwamba hitaji la kufanya maboresho ya miundombinu litaendelea na kulipa fidia kwa wananchi tutaendelea kulipa kulingana na sheria na taratibu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kwa kuwa Sera ya Elimu ni kuwa na VETA katika kila Wilaya na kwa kuwa Wilaya ya Karatu tumeshaonesha mfano huo wa kuwa na VETA kupitia Wafadhili wetu na ni ukweli kwamba kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri siyo rahisi kukiendesha Chuo hiki Je, Serikali sasa iko tayari kukichukua Chuo hiki na kukiendesha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Wafadhili hao mpaka sasa wanaendelea kutoa fedha za uendeshaji na wanaendelea kujenga baadhi ya miundombinu, na kwa kuwa wanaweza kukoma wakati wowote Je, Serikali sasa kupitia Wizara iko tayari katika Bajeti ya mwaka unaokuja 2020/2021 kutenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Chuo hiki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba inawezekana kabisa kwamba katika mazingira ambayo halmashauri au basi Mamlaka ya Serikali za Mitaa inashindwa kuendesha VETA kuna uwezekano mkubwa wa halmashauri hiyo kuweza kuipa VETA na VETA ikaweza ikabeba majukumu yote ya uendeshaji pamoja na gharama zote ambazo zinahusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba kama Halmashauri ya Karatu inaona kwamba kwa sasa haiwezi kuendesha Chuo hiko kikamilifu na kutimiza malengo yake kinaweza kikaomba VETA iweze kuimiliki na hivyo kuiendesha moja kwa moja na kuondoa changamoto ambazo wanazipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu kwamba kama inawezekana fedha zikatengwa katika Bajeti inayokuja kwa ajili ya Chuo hiko baada ya wafadhili kuanza kushindwa kumalizia. Ushauri wangu ni kwamba ni vigumu kwa sasa VETA au Wizara kuipangia fedha kwa sababu inachukuliwa kwamba bado ni Chuo cha Serikali za Mitaa katika maana kwamba bado ni Chuo cha halmashauri kwa hiyo wakitaka fedha zitengwe na Serikali Kuu ni lazima kwanza waanze utaratibu ule wa kuipeleka VETA.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni kweli siyo Mwanamichezo, lakini nawakilisha wanamichezo. Watanzania wote leo tunamshangilia na kumfurahia Samatta kwa kusajiliwa na hiyo timu ya Uingereza. (Kicheko)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wanataka kujua tu ni timu gani hiyo. Inaitwaje hiyo? (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, Aston Villa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, amesajiliwa kwa sababu ya jitihada zake mwenyewe, sasa inatuambia Watanzania kwamba tunaweza kuwa na Samatta wengi kwa kadri inayowezekana kama Serikali ikiwezekeza vya kutosha kwenye michezo. Sasa kwa nini Serikali isianzishe Sports Arena kwenye Majiji Makuu kama ambavyo wanafanya Nchi ya Rwanda ili kuwatoa Samatta wengi?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana ya michezo. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kutokana na juhudi za Serikali pamoja na wananchi wenyewe, tuna wachezaji 22 wanacheza nje ya nchi yetu, wanacheza Kimataifa siyo Samatta peke yake na hii inatokana na uelewa tulioupata Watanzania kwamba vipaji hivi havipatikani ukubwani unaanzia huku chini ndiyo maana Serikali inaingia gharama kila mwaka kuendesha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA kwa shule za Msingi na shule za Sekondari.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema, sasa hivi wito wetu wa kushiriki kila mtu kujenga viwanja, miundombinu siyo tu Kinondoni imeitikia hata vilabu binafsi kama Simba Sports Club wamejenga viwanja viwili Dar es salaam vya nyasi bandia pamoja na nyasi za kawaida, viwanja vizuri nimeenda kuvitembelea. Siyo hivyo tu, Mkoa wa Arusha unaongozwa unastahili pongezi, Halmashauri ya Jiji la Arusha sasa hivi imejenga Ngarenaro kiwanja changamani kizuri ambacho kina Netball, Basketball pia Soccer lakini vilevile katika Kata nafikiri ya Sinoni kuna Mtanzania ambaye anaishi Marekani anajenga kiwanja kizuri sana kimefikia asilimia 90. Nitoe wito kwa vijana wetu pia wanaoishi Ulaya, nje ya nchi waige huo mfano, wasishinde tu kwenye mitandao ya kijamii. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuulizwa swali dogo la nyongeza. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri hapa kwamba mnafanya mapitio ya Sera ya Mbolea kwa ujumla, lakini kumekuwa na changamoto ya usambazaji wa mbolea na kutokufika kwa wakati kwenye maeneo husika na uhitaji wa uhalisia wa eneo husika.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha usambazaji unafanyika kwa wakati na kwa mahitaji ya maeneo husika ili basi hizi ardhi zetu ambazo zimekosa rutuba ziweze kupata rutuba?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba kuna upungufu katika baadhi ya maeneo katika suala la uasmbazaji wa mbolea na Wizara sasa hivi inachukua hatua ya kufanya reform katika Taasisi yetu ya TFC ili tuweze kuondokana na hili tatizo pale ambapo tunafanya bulk procurement kupitia TFC ili matatizo ya namna hiyo yasiweze kujirudia. Lakini yapo maeneo ambayo kuna wazalishaji wa ndani kama Minjingu ambao tumeamua kama Serikali kuwapa priority ili maeneo ya karibu ambayo kiwanda hichi kinafanya kazi na mbolea yake inaweza kutumika iweze kutumika kwa haraka, lakini sisi kama Wizara tunapitia mfumo mzima wa usambazaji wa pembejeo za mazao ili kuondoa mambo makubwa mawili:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ucheleweshaji, mbili wizi unaoendelea katika usambazaji wa pembejeo ambao siku ya mwisho anaenda kubeba mkulima. Kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge kwamba mchakato huu unaendelea na tunaaamini kwamba msimu huu wa kilimo mambo mengi yatabadilika katika usambazaji wa pmebejeo. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo huu wa Mto wa Mbu ni sawasawa na Mji Mdogo wa Karatu; kwa maana ni miji ambayo watalii wanapita kuingia katika Hifadhi ya Manyara na Hifadhi ya Ngorongoro.

Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu wa kuwa na mpango mkakati wa kuendeleza miji hii kwa sababu ni kitovu cha kuingia katika Hifadhi zetu za Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mbunge ameongelea Mji Mdogo wa Mto wa Mbu na Mji wa Karatu; ni kweli ni miji ambayo ni ya pekee kwa sababu ni lango katika watalii wanapoenda kutembelea mbuga zetu. Kama ambavyo Serikali imekuwa na mpango kupitia TSSP tumekuwa tukiendeleza miji kwa kujenga barabara za kiwango ambacho ni kiwango kizuri. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuridhika na Serikali yetu hatua kwa hatua tunamaliza hiyo miji ambayo tulianzanayo nina hakika, katika mji ambao ameutaja kwa sababu ni jicho la kipekee kwa watalii nao hakika hatutauacha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na mwongozo huo ambao Serikali imeutaja lakini ni ukweli kwamba bado tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya afya na hivyo vifo vinaendelea kuongezeka. Je, Serikali haioni umuhimu bado wa kuwatumia hawa wakunga kwa kuwapa mafunzo ili waweze kusaidia uzalishaji ili tuendelee kupunguza vifo hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sasa upungufu katika sekta ya afya kwa maana ya watumishi wataalam ni asilimia 50, kiwango ambacho ni kikubwa sana na watu wetu wanaendelea kupata taabu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tunapunguza upungufu huu kwa kuongeza ajira katika sekta ya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, kutokana na kuwa na vifo vingi vya akina mama na watoto sisi kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapunguza sana vifo hivi kwa kuwekeza katika miundombinu ambapo zaidi ya Hospitali za Wilaya 352 zimeboreshwa lakini kuhakikisha akina mama wanakwenda kliniki. Sasa hivi tumepiga hatua kubwa sana idadi ya akina mama ambao wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka asilimia 51 mpaka asilimia zaidi ya 63.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna-encourage kabisa akina mama wajifungulie katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya. Hawa wakunga wa jadi tunaendelea kushirikiana nao kwa sababu nao wana mchango kwenye jamii lakini katika lengo la kuhamasisha akina mama kwenda kliniki na kujifungulia katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ili kupata huduma sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili lilikuwa kuhusiana na ajira, ni kweli tuna changamoto ya rasilimali watu lakini tumeendelea kuajiri watumishi wa afya kadri vibali vya Serikali vinavyopatikana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tukitaka kufanya mapinduzi ya kilimo, hakika kilimo cha umwagiliaji ndicho ambacho kinaweza kumsaidia mkulima wa Tanzania. Katika Bonde la Eyasi Wilayani Karatu, wananchi wale wanatumia kilimo cha umwagiliaji lakini hakuna miundombinu ya uhakika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inawejengea miundombinu ya uhakika ili umwagiliaji wao uwe endelevu na kilimo chao kiweze kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli bonde hili la Eyasi ambalo mimi mwenyewe nilifika, ni bonde muhimu sana kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na ni chanzo kikubwa cha uchumi kwa watu wa Tarafa ile hasa kwenye zao la vitunguu.

Mheshimiwa Spika, katika bonde hili mikakati tuliyokuwa nayo kama Serikali, kwanza kama nilivyosema ni kwamba hatuwezi kusubiri pesa za kibajeti miaka yote hii. Kwa hiyo, sasa hivi kupitia Sheria ile ya PPP tumekuja na mpango kabambe kwa ajili ya kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza miundombinu hii kwa utaratibu ule niliosema kwenye jibu la msingi la jenga, endesha na kabidhi baada ya yule mdau anayeendesha ule mradi kurudisha gharama zake.

Mheshimiwa Spika, pili, kupitia Serikai ya Halmashauri, ukizingatia Halmashauri hii ya Karatu zaidi ya 33% mapato yake yanatoka kwenye bonde hili. Kwa hiyo, tukasema zaidi ya mapato hayo ya ndani 20% warudushe kuwekeza katika bonde lile ili liweze kurudisha maendeleo kwa wananchi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya vikwazo ambavyo wanakutana navyo wawekezaji wengi hapa nchini ni urasimu na mchakato mrefu unaochukua muda mrefu wa kupata vibali vya kuwekeza katika maeneo mbalimbali; na mara nyingi Serikali imekuwa ikisema kwamba, inaendelea kuona namna gani inapunguza urasimu huo. Je, ni hatua gani imefikiwa kupunguza urasimu huu ili wawekezaji wanapokuja wasikutane na hivyo vikwazo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali ni dhahiri. Kwanza Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Wizara mahususi kwa ajili ya kushughulikia suala la uwekezaji kulikoni ilivyokuwa zamani, ilikuwa haijulikani hasa suala hili liko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzisha Wizara ambayo inashughulikia uwekezaji na maelekezo na miongozo ambayo imekuwa ikitolewa na yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais na Viongozi wengine Wakuu wa Kitaifa kwamba, tupunguze urasimu ili tuweze kuvutia uwekezaji, naamini itatuondoa katika hali ya urasimu uliokuwepo na uwekezaji utachukua tija kwa muda mfupi zaidi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza kabisa napenda tu kusema kwamba anayoyasema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, lakini pia ninachosema ni kwamba tumebadilika sana ndani ya Serikali, lakini pia katika mamlaka zetu za Serikali za Mitaa. Moja, ambalo tunalifanya hivi sasa, kwanza ni kufanya mabadiliko na mapitio ya Sera yetu ya Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tayari kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara mbalimbali na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunavyoongea hivi sasa tayari timu iko kazini, inafanya marekebisho ya maeneo mbalimbali ambayo yamekuwa yakionekana ni vikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, tunashukuru sana Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI yenyewe, tayari tumeshaanza kuanzisha ofisi za kusaidia wawekezaji kupitia Regional Investiment Facilitation. Tayari Arusha wako katika hatua hiyo, tayari Iringa wameshaanza na tunaendelea kufanya hivyo katika mikoa mingine. Pia tunaandaa mwongozo ili mikoa yetu na mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kuwahudumia vizuri zaidi wawekezaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tunaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na tunaamini vikwazo vyote na mifumo mbalimbali ya udhibiti kupitia mamlaka zetu itaondolewa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante wka kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Sera ya Wizara hii ni kuunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami na kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa barabara ya kutoka NJiapanda - Mang’ola - Karatu mpaka Lalago ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu na kumekuwa kuna ukarabati mdogo mdogo unafanyika mara kwa mara ambao unagharimu fedha nyingi.

Sasa kwa nini Wizara isifikirie angalau kuanza kilometa chache chache kwa kiwango cha lami mpaka itakapokamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naona Mheshimiwa Mbunge anatabasamu anafahamu kwamba Serikali inayo nia thabiti ya kufanya maboresho ya barabara katika maeneo haya na ndiyo maana kuna usanifu umefanyika wa barabara hii, hii bypass hii kutoka Karatu kupita eneo la Mang’ola kwenda Sibiti halafu kuunganisha katika Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza. Unafahamu kinachoendelea na nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge hivi wiki iliyopita Mameneja wa TANROADS pamoja na wenzetu ambao pia walikuwa wanasanifu eneo hili wamekuwa na kikao madhubuti kwa maana ya kuliangalia eneo hili kwasababu usanifu ulishakamilika kwa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara hii tunaitazama sambamba na barabara ya kutoka Karatu- KIlimapunda kuja Mbulu Mjini, kuja Dongobeshi kwenda Haidom, kwenda Sibiti tunakwenda kuungana na hiyo barabara uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Zote hizi barabara tunaziangalia kwasababu eneo la Mang’ola ni eneo muhimu na lina historia, Wahadzabe wako maeneo haya, lakini pia kuna kilimo cha vitunguu kikubwa katika maeneo haya kwahiyo Serikali imeliona eneo hili kwa maana ya kuwasaidia wananchi maeneo haya ili uchumi uweze kupanda kwa maana hiyo vuta tu subira tumejipanga vizuri, tunazitazama hizi barabara zote ili sasa eneo hili tuweze kulifungua na tuweze kutoa huduma muhimu hii ya barabara. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika kata husika nilizozitaja katika swali langu la msingi kuna baadhi ya mashamba wawekezaji wamehifadhi mapori ambayo hawayaendelezi. Mapori hayo yanahifadhi pia wanyama ambao ni hatarishi kwa wakati katika maeneo hayo.

Je, Serikali sasa wako tayari kwa kushirikiana na halmashauri kwa sababu, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuhakikisha wanayatambua haya maeneo na kufanya partial revocation na yale maeneo yarudi kwa wananchi ili wananchi wanaozunguka maeneo hayo pamoja na wanafunzi wanaoenda shule waishi katika maeneo salama bila kuathiriwa na maisha yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika mashamba hayo hayo niliyoyataja, kuna shamba mojawapo linaitwa Shamba la Benduu, mwekezaji alishafariki, nitamwandikia Mheshimiwa vizuri kwa karatasi; mwekezaji alishafariki, lile shamba wafanyakazi wake hawajalipwa takribani miezi nane na hawaruhusiwi kwenda kufanya kibarua kwenye mashamba mengine, hawajui hatima ya haya maslahi yao na hawajui hatima ya nini wafanye kwa sababu, wakitoka kwenda kufanya kazi kwenye shamba lingine anafukuzwa asirudi kwenye lile shamba. Je, sasa Serikali wako tayari kwenda kutatua mgogoro uliopo katika shamba hilo, ili wananchi wanaofanya kazi na vibarua wanaofanya kazi katika eneo hilo wapate haki zao na pia waruhusiwe kufanya kazi katika maeneo mengine, ili waendelee kujipatia kipato? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameongelea kwamba, baadhi ya mashamba yamefanywa mapori na yanafuga wanyama kule ambao pengine ni hatarishi kwa watu na anaomba pengine yaweze kufanyiwa partial revocation kwa maana ya kwamba, ile sehemu ambayo pengine haitumiki basi iweze kuondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kutoa jibu la moja kwa moja kwa sababu, ni mpaka anachokisema hicho kiwe na uhakika kwa sababu, unapopewa shamba kuna muda wake wa kuweza kuliendeleza, ndani ya miaka mitano unatakiwa kuwa umeendeleza angalau moja ya nane ya hilo shamba. Sasa kama mashamba hayo hayajaendelezwa kwa kiwango hicho kwa sababu, tumeshasema uhakiki unaendelea kufanyika basi, tutapita pia kuona hilo shamba likoje, lakini kama nilivyosema mwanzo mashamba yote 25 ya Wilaya ya Karatu yamefanyiwa uhakiki na kwa sehemu kubwa yameendelezwa zaidi ya asilimia 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anaongelea Shamba la Benduu, nadhani atanipa karatasi, kwamba, mwekezaji alikwishafariki na watumishi wale wanadai hawana malipo. Nadhani hili ni suala la kisheria zaidi kwa sababu, kama mtu amefariki kuna mtu ambaye anatakiwa kuwa administrator wa mali ya yule aliyefariki. Kama atakuwa ameteuliwa msimamizi wa mirathi katika eneo lile basi, huyo atabeba dhamana pia ya kuweza kulipa wafanyakazi ambao wanadai, wanayemdai alishafariki na tayari kuna mtu ambaye anasimamia mirathi ile atashughulikanao katika suala zima la kuweza kupata haki zao.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana lakini kwenye tablets zetu hatuna Order Paper.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kumekuwa na utamaduni wa fedha nyingi zilizopangwa kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya barabara kucheleweshwa hivyo ufanisi wa kile kinachokusudiwa hakifikiwi. Je, Serikali sasa mko tayari kuhakikisha kama fedha zinatengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara yoyote zinatoka kwa wakati ili barabara hizo zitengenezwe?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Karatu inatoka Njia Panda – Mang’ola - Lalago ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. Barabara hii imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami hasa kipindi cha uchaguzi ahadi inakuwa ni tamu kweli masikioni mwa wananchi lakini baada ya hapo barabara hiyo haijengwi kiwango cha lami. Serikali mtuambie ni lini kwa hakika barabara hiyo itajengwa kwa sababu Sera ya Wizara ya Ujenzi inasema kuunganisha barabara za Mikoa na Mikoa kwa kiwango cha Lami na barabara ile inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu fedha za miradi mbalimbali ya barabara kuchelewa kupelekwa katika miradi hiyo, utaratibu wa fedha kupelekwa katika miradi mbalimbali unazingatia upatikanaji wa fedha ambazo zimetengwa kwenye bajeti husika. Hivyo, kutokana na kutegemea mapato ya ndani kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo, mara nyingi kumekuwa na ucheleweshwaji na miradi hiyo kwa sababu ya upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, Serikali imeendelea kuongeza jitihada kuhakikisha kwamba mapato yanakusanywa kwa wakati na fedha za miradi hiyo zinawasilishwa kwenye miradi husika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha mpaka sasa takribani asilimia 48 ya fedha ya miradi ya barabara tayari imekwishawasilishwa katika mamlaka ya Serikali za Mitaa na kazi za utekelezaji wa miradi hiyo zinaendelea. Suala hili litaendelea kufanyiwa kazi kwa karibu zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na barabara ya Arusha Simiyu inayotokea Karatu, ni kweli hii ni barabara muhimu sana na inaunganisha mikoa hii miwili. Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba barabara hizi kuu ambazo zinaunganisha mikoa zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na za kijamii.

Mheshimiwa Spika, kama alivyouliza kwamba Serikali imekuwa ikitoa ahadi, ni kweli na ahadi ya Serikali hakika itatekelezwa. Nimhakikishie tu kwamba mara fedha zikipatikana barabara hiyo itajengwa ili wananchi waweze kupata huduma zilizokusudiwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Wizara ya Ujenzi inataka kuunganisha barabara za mikoa kwa kiwango cha lami na kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuzi- upgrade barabara zetu kuwa kwa kiwango cha lami kwa sababu itasaidia wananchi kusafirisha mazao, lakini wananchi wataweza kupata huduma bora za kupita kwenye barabara inayopitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya kuunganisha barabara katika Mkoa wa Arusha ambayo inatoka Karatu kuunganisha Simiyu na inayotoka Karatu kwenda Mbulu kwa maana inaunganisha Arusha na Manyara.

Je, ni lini barabara hizi zitajengwa kwa kiwango cha lami kama ahadi inavyoeleza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja za Karatu – Simiyu – Mbulu – Manyara ni barabara muhimu na ni barabara za Mkoa na ni kipaumbele cha WIizara na Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zimeshawekwa kwenye mpango kwa sababu zinatakiwa zijengwe, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kujenga hizi barabara kunahitaji fedha na tunapopata fedha ndiyo tunapoanza ujenzi.

Kwa hiyo, kwa kuwa zipo kwenye Mpango na fedha hizi zinategemea pia na mapato ambayo Serikali inapata ili iweze kuzijenga kwa hiyo kwa kuwa stadi zimeshafanyika, mara fedha itakapopatikana na tunavyotambua ni kipaumbele chetu barabara zote ni mpango wa Serikali zote zinazounganisha mkoa na mkoa, wilaya na wilaya ziwe kwa mpango wa lami, lakini hatutazijenga zote kwa wakati mmoja. Lazima tutaanza na barabara chache, tunafuata zingine mpaka tutakamilisha. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi ya ukarabati katika hospitali mbalimbali kongwe hapa nchini lakini bado kumekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mapungufu hayo yanakidhi haja iliyopo kwa maana ya idadi ya watumishi wanaotakiwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ujenzi wa hospitali au ukarabati wa zahanati, vituo vya afya na hizo hospitali ni pamoja na kuhakikisha mambo muhimu ya madawa, vitendanishi vinapatikana katika hospitali zetu. Je, Serikali inahakikisha vipi kwamba upatikanaji wa madawa yote muhimu yanapatikana katika hospitali zetu na katika vituo vya afya na zahanati zetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa kuwajali na kuthamini sana afya za wananchi imeendelea kujenga vituo vya afya kote nchini na kwa kweli kuna upungufu wa watumishi kwa takribani asilimia 45. Serikali imeweka mipango thabiti ya kuhakikisha tunaendelea kuajiri watumishi katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za Halmashauri na ndiyo maana mwezi wa Tano hadi wa Sita tulikuwa na ajira za watumishi wa afya 6,324 na watumishi hao wamekwisha ajiriwa tayari wamepelekwa kwenye vituo vya huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, zoezi hili la kuendelea kuajiri watumishi ni endelevu, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua na itaendelea kuhakikisha kwamba inaajiri watumishi kwa awamu ili kupunguza uhaba wa watumishi katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, pili; ni kweli kwa sababu ya ongezeko la vituo vya huduma za afya kumekuwa na upungufu wa baadhi ya dawa muhimu katika vituo vyetu na Serikali imeendelea kupeleka fedha Bohari Kuu ya Dawa mpaka Juni tarehe 30 mwaka huu, jumla ya bilioni 120 zilikuwa zimepelekwa Bohari Kuu ya Dawa kwa ajili ya kununua dawa kupeleka katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2021/ 2022 fedha zimetengwa zaidi ya bilioni 280 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba dawa zinapelekwa katika vituo vyetu. Kwa hivyo, nimhakikishie kwamba suala hilo litaendelea kutekelezwa kwa ufanisi unaotakiwa ili dawa zipatikane katika vituo vyetu. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa katika majibu ya Serikali wanaonesha kabisa kwamba mbadala wa wanyama hawa kutokuingia kwenye maeneo ya wananchi ni kutumia mbinu zilizoainishwa hapa, lakini mbinu hizi zinahitaji wananchi waelimishwe na wawezeshwe kwa sababu unapomwambia afuge nyuki na kadhalika, mwananchi huyu hana huo uwezo. Sasa je, Serikali inafanya nini kuwawezesha wananchi hawa kama kweli wana uhakika hili ndiyo litakuwa suluhisho ya kuondoa kero hii ya muda mrefu ya wanyama kuingia kwenye maeneo ya wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wanapoingia kwenye maeneo wakaribu mazao, fidia inayolipwa hailingani na uharibifu uliotokea, lakini hata fidia hiyo inayolipwa inachukua miaka na miaka mwananchi kupata fidia hiyo. Je, ni lini sasa Serikali italeta sheria hapa Bungeni tuifanyie marekebisho ili wananchi waweze kupata haki yao kwa jinsi ambavyo wanastahili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekiri kwamba kumekuwa na changamoto ya hawa wanyama wakali wakiwemo tembo kuendelea kuvamia mashamba ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii tumeendelea kuiongelea hata katika Bunge lako hili Tukufu kwamba kwa kuwa wananchi wameendelea kusogea kwenye maeneo ya hifadhi na asilimia kubwa ya maeneo ambayo shughuli za kilimo zinafanyika ni ushoroba wa wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni changamoto kwa sababu wanyama hao sasa badala ya kupita yale maeneo wakaenda kwenye shughuli zao zingine zikiwemo pamoja na kutafuta madini pamoja na dawa asili wanazotumia ambazo sisi wanadamu hatuwezi kuzitambua, lakini wao kama nilivyokuwa nikiendelea kusema, wana Serikali yao, basi yale maeneo sasa wanapokutana na mazao wanafanya vurugu ambayo sio ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuhamasisha wananchi kama wataweza waachane na mazao yanayohamasisha tembo kupita katika maeneo ya mashamba yao. Kama itashindikana sana basi kwenye jibu langu lile la msingi nimeelezea mbinu mbadala ya kuweza kusaidia ili angalau kuepuka hili tatizo linaloendelea kujitokeza kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kutoa elimu kwenye maeneo husika na kupitia vyombo vya habari na hata hapa naendelea kutoa rai kwa wananchi kwenye maeneo ambayo mashamba yao yanavamiwa na tembo, wafuate haya tunayoelekeza ili wasaidie. Wapande pilipili, waweke hiyo mizinga ya nyuki, lakini pia waendelee kutoa taarifa kwa Serikali kwa sababu Serikali iko kwa ajili yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu fidia. Lengo la Serikali si ku-compensate mpaka mwananchi afurahi. Tukisema kila mwananchi apate kile ambacho anakusudia, basi hii Wizara haina haja ya kuwepo kazini kwa sababu uhifadhi ni gharama kubwa sana, lakini pia hata tunapotekeleza tunahakikisha kwamba tunahifadhi ili kuendelea kuiongezea Serikali mapato kupitia utalii, lakini kwa wakati huo huo tunaendelea ku-compensate wananchi wanaoathirika na hao wanyama. Kwa hiyo niombe rai kwa wananchi…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge, ameelewa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Loliondo – Wasu - Mto wa Mbu ni ahadi ya muda mrefu kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami. Natambua kuna kipande cha Waso - Sale kilometa 49 sasa hivi kinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami ila kuna eneo korofi sana la Sale – Ngaraesero, je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako nimuagize Meneja wa TANROADS Mkoa aweze kwenda kwenye barabara hii ya Sale - Ngaraesero ili aweze kufanya tathmini na aone kama tunaweza tukajenga kipande; imekuwa ni kawaida sehemu ambayo tunaona ni korofi yenye vilima ama yenye miteremko mikali ama yenye utelezi aende akafanye tathmini na kuleta bajeti ili tuone namna ambavyo tunaweza tukafanya ili tusikwamishe wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa awe na amani na ikiwezekana baada ya kikao hiki tuweze kukutana ili aweze kunipa taarifa kamili ya eneo hilo ili tuweze kulifanyia kazi. Ahsante.
MHE.CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba idadi ya watu nchini inaongezeka, lakini ardhi tuliyonayo haiongezeki na yapo mapori kama hayo na mengine ambayo kwa namna moja ama nyingine hayana tija kwa Taifa.

Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kufanyia tathmini mapori mengine kuyagawa kwa wananchi ili waweze kuyatumia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliaisli na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea mawazo hayo na hata sasa kwa sababu kuna changamoto na migogoro mingi kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, Serikali inaendelea kufanya tathmini na yale maeneo ambayo yanaonekana sio ya faida sana, Serikali itaangalia na italeta mapendekezo kwenye Baraza la Mawaziri na mwisho Mheshimiwa Rais atatoa maelekezo, ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba bado bei ya bidhaa sokoni ni kubwa na haijashuka hasa kwenye vifaa vya ujenzi. Je, Serikali inasema nini juu ya suala hili?

Mheshimiwa Spika, ni takribani miaka kama mitano au kumi hatujawahi kupata utulivu wa uhakika wa bei ya mafuta ya kula, sukari na unga wa ngano ambayo ni mahitaji muhimu kwa wananchi kila siku. Serikali inasema nini juu ya suala hili? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Cecilia ni mfuatiliaji sana wa masuala haya ya mfumuko wa bei, nakumbuka hata kwenye michango yake ya hotuba mbalimbali nimewahi kujibu swali linalohusiana na mfumuko.

Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei (inflation) sio bei kama ambavyo amesema bei za bidhaa fulani bado zipo juu. Mfumuko wa bei ni ile kasi ya bei kubadilika, tofauti na bei zenyewe kama bidhaa ipo katika bei hii hauwezi ukai-judge hapa Bungeni kama ipo juu au chini kwa sababu itategemeana tu na bidhaa zenyewe zimepatikana kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Spika, sisi tunachoongelea na tunachoshughulika nacho ni ile kasi ya bei zenyewe kubadilika na katika Tanzania utakumbuka kwa takribani karibu miaka zaidi ya 10 tumefanikiwa kushusha mfumuko wa bei na tumefanikiwa kuuweka ucheze kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0 ambacho ni viwango vya Afrika Mashariki. Na hilo ndio lengo kubwa la kuweza kuhakikisha kwamba bei zetu hazibadilikibadiliki kwa kiwango ambacho kinasababisha vitu visitabirike katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ambalo ametaja bidhaa mahususi, kuna mikakati ambayo ni mahususi kwenye mazao hayo aliyoyataja ikiwemo mafuta ya kula pamoja na masuala kama ya sukari. Utakumbuka hotuba ya Waziri wa Viwanda ilielezea vizuri jinsi Serikali ambavyo imejikita kwenye kuongeza uzalishaji wa sukari ambapo kutakuwepo na upanuzi wa mashamba pamoja na uzalishaji wa sukari ambao sasa utaenda kutoa jibu la uhakika na la kudumu kuhusu hizo bei zinazokuwa zinapandapanda na kubadilikabadilika kwenye masuala ya sukari.

Mheshimiwa Spika, na hii ilikuwa inatokea kwa sababu, kwenye masuala ya sukari kuna vipindi ambavyo viwanda vinakuwa havizalishi. Tulikuwa tunalazimika kutafuta sukari kutoka maeneo mengine kuziba pengo la aina hiyo, lakini kwa mkakati ambao umewekwa wa kuziba pengo hilo la sukari kwa uzal;ishaji wa ndani, utaenda kutoa jibu la kudumu la mabadiliko ya harakaharaka ya bei za sukari.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mafuta ya chakula utaona jinsi ambavyo Waziri Mkuu kila wakati utamuona yuko katika maeneo mahususi ambayo yanashughulika na masuala ya uzalishaji, kuhamasisha uzalishaji wa mazao haya ambayo yatatupatia mafuta ya chakula, ili kupata jawabu la kudumu la upungufu wa mafuta ya chakula ambao ndio unasababisha kupanda kwa bei. Umeona jinsi anavyofanya kazi Kigoma, anavyofanya kazi Singida pamoja na maeneo mengine ambayo anashughulikia masuala ya aina hiyo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi.

Katika Mkoa wa Arusha, Jimbo ambalo lina jiografia ngumu sana, ni Jimbo la Ngorongoro; na ukisema uweke tu Hospitali ya Wilaya pale Loliondo Mjini, Kata nyingine zenye umbali mkubwa hawawezi kupata hii huduma:-

Je, Serikali inalitizamaje Jimbo hili ili wale wananchi waweze kupata huduma nzuri za afya na zinazotakiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ni kweli kwamba Jimbo la Ngorongoro ni kubwa na jiografia yake ina changamoto, lakini Serikali imeweka mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba kwanza kupitia Sera ya Mpango wa Maendeleo ya Afya Msingi kila Kijiji kinakuwa na zahanati, lakini pia kila Kata inakuwa na kituo cha afya na Halmashauri kuwa na Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia mpango huo ambao utakwenda kujenga zahanati katika kila Kijiji, lakini pia kujenga vituo vya afya katika kila Kata, tutakwenda kutatua changamoto ya ukubwa na jiografia ya Jimbo la Ngorongoro na hivyo tutahakikisha kwamba huduma za afya zinawafikia ipasavyo wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba katika Wilaya ya Karatu, Tarafa ya Eyasi kuna Shule ya Msingi Endamaghan ambayo ni maalum kwa ajili ya hawa watoto wa kifugaji kwa maana ya Wahadzabe ambao wanatoka kwenye hii Tarafa ya Eyasi, lakini wapo wengine wanatoka Wilaya ya Mbulu, lakini shule hiyo ni ya muda mrefu inahitaji marekebisho kimiundombinu ili hawa wanafunzi waweze kupata hiyo huduma muhimu ya elimu. Je. Serikali sasa ipo tayari kutazama shule hiyo na kuipatia fedha kwa ajili ya maboresho hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua jambo hilo na tutafanya marekebisho na tutaboresha hiyo shule. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya kujenga barabara katika Mji Mdogo wa Karatu kwa kiwango cha lami toka Serikali ya Awamu ya Nne na Awamu ya Tano.

Je, ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa kujenga kilometa 10 za lami katika mji dogo wa Karatu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Mjini Karatu zitajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha kadri Serikali itakavyopata fedha. Kwa hiyo, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu ya Ujenzi na Uchukuzi ikisaidiana na Wizara ya TAMISEMI tutahakikisha kwamba barabara hizi ambazo ni ahadi za viongozi na zipo kwenye Ilani zinajengwa kwa kiwango cha lami kama zilivyoahidiwa. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna ahadi ya muda mrefu ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Karatu – Kilimapunda – Mbulu, ahadi hii imekuwa ni ya muda mrefu sana.

Je, ni lini sasa Serikali mtatekeleza ahadi hiyo kwa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara aliyoitaja ya kuanzia Karatu kuja Mbulu ni ahadi ya muda mrefu, lakini nataka nimhakikishie kwamba katika bajeti ijayo lakini hata mwaka huu barabara hii itatangazwa mara moja kuanzia kipande cha Mbulu kwenda Haydom ambayo ni sehemu ya barabara hiyo. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kutekeleza hiyo ahadi. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Kwanza nisikitike kwa majibu yasiyoridhisha au niseme labda ya sitaki kutumia kauli kama ya uongo dhidi ya matukio haya ambayo yametolewa na Serikali, na imekuwa ni rahisi sana askari wa TANAPA kujichukulia sheria mkononi kuliko majeshi mengine yoyote, na hii inafanyika maeneo mbalimbali nchini.

Sasa swali langu la kwanza; tarehe 29 Desemba, 2020 wananchi saba waliingia hifadhilini ikisadikika wanakwenda kuchimba madini, wananchi wanne mpaka leo hawajulikani walipo na inasemekana wamechomwa moto hadi kufa na askari wa TANAPA.

Je, hao nao waliamua wenyewe kujichoma au askari wa TANAPA waliwachoma wananchi hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tarehe 22 Oktoba, 2020 siku ya kupiga kura askari wa TANAPA waliwapiga risasi ng’ombe kumi wa mama mjane kwenye eneo hili mpaka leo mama huyu hajafidiwa wale ng’ombe sasa hawa ng’ombe nao walijipiga risasi wenyewe au askari wa TANAPA waliwapiga risasi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba maelezo yote niliyosema hapa ni kweli na akihitaji ushahidi tutautoa kama Serikali. Askari wetu ni wengi sana wanauawa na tumekuwa tukishambulia zaidi askari, lakini haya matukio yanatokea pande zote mbili kwamba askari wanakuwa kwenye sheria na kukabiliana na maeneo yao ya hifadhi kwa maana ya kuyalinda yale maeneo lakini inapotokea sasa wananchi kutotii sheria basi huu mtafaruku unatokea.

Mheshimiwas Spika, lakini kwenye hili analoliongelea kwamba waliingia na kuchomwa moto, mimi hilo siwezi kuliongelea hapa kwa sababu taarifa zake tulishawahi kuziongelea hapa kwamba ziko kwenye uchunguzi na DNA ilishapelekwa kwenye maeneo yetu ya uchunguzi na taarifa hizi ni za kiusalama zaidi, kwa hiyo, tamko la Serikal litakuja kutolewa baada ya uchunguzi kufanyika.

Mheshimiwa Spika, na hili la risasi kwamba kuna ng’ombe walipigwa risasi pengine labda nimuombe Mheshimiwa atuletee uthibitisho kwamba wakati ng’ombe hawa wanauawa kama alikuwepo basi tuweze kulishughulikia, lakini vinginevyo ninaomba sana na nimuombe kama anavithibitisho vyovyote ambavyo askari walienda kupiga hao ng’ombe atuletee na Serikali itachukua hatua, ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimwa Spika, ahsante, kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimwa Spika, kwa kuwa fursa kama hizi mfano Ujenzi wa Mradi wa Bomba la Gesi ni fursa nzuri sana kiuchumi katika nchi na kwa kuwa Serikali imesema italipa fidia kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo wa Tanga, lakini je, Serikali haioni ipo haja ya dharura hata kutafuta mkopo wa dharura ili fursa hii ya ujenzi wa bomba la gesi uendane na ukarabati wa uwanja huo wa Tanga?

Mheshimwa Spika, swali la pili, kuna mchakato pia wa upanuzi wa uwanja wa Lake Manyara, Karatu ambao ni uwanja muhimu sana kwa utalii katika Kanda ya Ngorongoro – Serengeti, wananchi wale hawajalipwa fidia muda mrefu.

Je, ni lini sasa Serikali italipa fidia wananchi hawa wa Lake Manyara pale Karatu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza naamini anakusudia kusema bomba la mafuta na si bomba la gesi; kama hivyo ndivyo Serikali inatambua umuhimu wa bomba hili na ndio maana tunapoongea hivi tayari kuna watu wanafanya tathimini kwa ajili ya watu watakaopisha upanuzi wa kiwanja hiki ili uwanja huu uendane na kasi ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta la kutoka Tanga kwenda Uganda. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali inalitambua hivyo na ndio maana iko kasi kuhakikisha kwamba uwanja huu unajengwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kama amesikiliza kwenye jibu langu la msingi nimetaja viwanja 11 ambavyo viko katika mpango huu na katika kitabu chetu cha bajeti ambayo imepitishwa kiwanja cha Lake Manyara ni kati ya viwanja hivyo 11 ambavyo pia vinafanyika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unafanyika hili kuweza kuhakikisha kwamba ndege sasa zinatua uwanja huu wa Lake Manyara kwa ajili ya kuongeza shughuli za utalii eneo hili la Mkoa wa Manyara na Karatu kwa ujumla wake, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki hii ya Kilimo ipo Dar es Salaam lakini wakulima walio wengi wapo katika mikoa mbalimbali kwa maana ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Kaskazini na kwingineko. Je, ni lini sasa huduma hizo zitapanuka ili wakulima wote waweze kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Cecilia Paresso amezungumza hoja ya msingi, nimhakikishie kwamba kwa kipindi hiki ambacho TADB haijawa na matawi katika maeneo yote nchini imekuwa ikifanya kazi zake kwa utaratibu mzuri wa kuwasaidia wakulima kwa kuweka utaratibu maalumu wa kuratibu kupitia Idara Maalumu ambayo inajihusisha na masuala ya wakulima wadogo wadogo katika benki hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa wazo hili ni jambo jema, nimhakikishie kwamba tumelipokea na tutalifanyia kazi. Pale ambapo hali itaruhusu tutaweza kusambaza huduma ya TADB katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna changamoto kubwa sana katika maeneo ya wafugaji; na kwa sababu wana utamaduni wa kuhama; na changamoto hii iko katika baadhi ya Kata katika Wilaya ya Karatu na Mbulu Vijijini katika eneo linaitwa Yaeda Chini; je, Serikali sasa iko tayari kutazama maeneo haya na kuhakikisha wanajenga mabweni kuanzia Shule za Awali, Msingi na hadi Sekondari ili kuhakikisha kwamba jamii hii ya kifugaji na wenyewe watoto wao wanapata haki ya kupata elimu kama ambavyo walivyo katika maeneo mengine nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaomba kwamba tuendelee kuyazingatia maeneo ya wafugaji na ameainisha hapa eneo la Yaeda Chini na anataka commitment ya Serikali ikiwemo kujenga shule kuanzia awali, msingi na sekondari ili tuweze kuwasaidia maeneo hayo. Nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikizingatia kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, katika eneo ambalo anatokea Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, kwamba Serikali ilijenga kule shule. Kwa hiyo, hata maeneo yote ya wafugaji tutaendelea kuyazingatia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuyaweka kwenye mpango kwa kadri fedha inapopatikana na kuhakikisha kwamba tunahudumia wananchi wote ili wapate huduma ya msingi ya elimu ikiwemo hayo maeneo ambayo ameainisha. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia korongo lililopo katika Wilaya ya Mbulu Mji ambalo linaenda mpaka Wilaya ya Karatu na katika Tarafa ya Yasi ambako kuna wakulima wa vitunguu katika maeneo hayo. Sasa je, Serikali haioni ipo haja ya kuikutanisha TANROADS Mkoa wa Arusha kwa maana ya Wilaya ya Karatu na TANROADS Mkoa wa Manyara ili kwa pamoja kuwe na nguvu ya kuhakikisha haya madaraja ambayo yanaathiri wilaya mbili yanapatiwa ufumbuzi ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kama inavyotakiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nikubali na nipokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwa sababu Serikali ni moja na tunafanya kazi kama wamoja, basi kwa kutumia hadhara hii niahidi tu kwamba tutakaa pamoja na watu wa ujenzi kuhakikisha, hao TANROADS Arusha na Manyara wanakutana na kufanya tathmini katika maeneo hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha. Kwa hiyo tumepokea ushauri wake na tutaufanyia kazi. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Utafiti kama huo ambao umefanyika Ziwa Tanganyika umewahi kufanyika pia katika Ziwa Eyasi katika Jimbo la Karatu kuhusu upatikanaji wa mafuta katika ziwa hilo. Je, utafiti huo umekamilika au bado na je, matumaini ya kupata mafuta yapo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunalo bonde linaitwa Bonde la Eyasi Wembere ambalo linatoka Singida, linapita Tabora, linapita Simiyu na kipande cha Manyara pia kipo. Utafiti katika bonde hilo unafanywa na Shirika letu la TPDC na kwenye Bonde la Eyasi-Wembere bado tunaendelea na utafutaji wa awali wa kujua maeneo ambayo tunaweza tukapata mafuta au gesi katika maeneo hayo. kwa hiyo, utafutaji bado unaendelea na utakapokuwa umekamilika, basi utapata matunda ya kuweza kuvuna gesi na mafuta.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto iliyoko Arumeru ya mashamba ambayo hayajaendelezwa iko pia katika Wilaya ya Karatu kwa baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo kutokuyaendeleza na hivyo kufanya mapori ambayo yanahifadhi Wanyama ambao wanajeruhi Watoto na wananchi kwa ujumla.

Je, ni lini Wizara itasimamia hili ili mashamba ambayo hayajaendelezwa yaweze kutwaliwa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa utoaji wa maeneo umeelekezwa kisheria katika Sheria ya Ardhi Na. 4 na Na. 5 na Kanuni zake nyinginezo. Nataka nimwelekeze Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili kama nilivyoeleza katika majibu mengine ya msingi kwamba hili ni jambo la mchakato, anzisheni mchakato katika maeneo yenu na hatua za kufuatwa juu ya maeneo hayo zitafanyika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo nyongeza. Tuna Mifuko mingi sana ya uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi na mifuko hiyo imekuwa kwenye Wizara mbalimbali ndani ya Serikali: -

Kwa nini Serikali sasa isifikirie angalau kuwa na mifuko miwili ambayo itatosheleza mahitaji ya walengwa kwa maana ya wanawake na vijana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Paresso kwa sababu anauliza swali la msingi sana kuona namna ambavyo tunaweza kupunguza wingi wa Mifuko hii ambayo inahudumia wananchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, tunalipokea wazo hili na Serikali ipo kwenye michakato kuona namna gani ya kuunganisha mifuko inayotoa huduma zinazofanana ili kuweza kuifanya iwe na tija kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ikiwemo akina mama, vijana na walemavu. Kwa hiyo, tunachukua mawazo yake, nasi tunaendelea kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali na majarida mbalimbali yanaonyesha bado vifo vinavyotokana na uzazi vinazidi kuongezeka. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inapunguza vifo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vifo vinavyotokana na wazazi vipo lakini vinapungua kwa kila wakati. Suala zima la mkakati wa kuendelea kupunguza zaidi ndiyo maana umeona Rais wetu ameelekeza tutumie shilingi bilioni 23 kujenga wodi maalum kwa ajili ya watoto njiti, kwa sababu vifo vya watoto wachanga vinachangiwa asilimia 48 na watoto njiti wanaozaliwa.

Vilevile kwenye suala la akinamama ukiona tunasogeza vituo sana, kumekuwepo na tozo kwa ajili ya kuchangisha kuhakikisha tunajenga vituo kule sehemu ambazo hakuna vituo vya afya ni kuhakikisha wale akinamama ambao wanashindwa kujifungua, basi vituo vinavyoweza kufanya huduma ya dharura na kuokoa maisha ya akinamama vinapatikana hivyo ukiona hela nyingi zinaelekezwa kwenye vituo vya afya, zahanati lakini kwenye kuboresha huduma za afya dawa, ndiyo hatua ambazo zinatumika kuhakikisha tunapunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwenye nchi yetu vifo vya akinamama na watoto vinaendelea kupungua. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Hapa siku za karibuni tumesikia taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba uhifadhi wa samaki hapa nchini kwenye baadhi ya maeneo, samaki wanahifadhiwa kwa kutumia dawa za kuhifadhia maiti, jambo ambalo linaleta taharuki kwa wananchi na wananchi hawajui nini cha kufanya ili wasipate hao samaki waliohifadhiwa kwa namna hiyo.

Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha samaki hao hawahifadhiwi kwa vitu hivyo ambavyo vinasababisha kansa kwa Watanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili alilolisema Mheshimiwa Paresso ni hypothesis halina hakika hadi sasa hivi. Ni kwamba watu wanahisia kuwa kiko kitu cha namna hiyo na ndiyo maana Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuwa Jijini Mwanza aliagiza Wizara ya Afya ifanye utafiti ili kama ni kweli kinafanyika kitu cha namna hiyo basi kizuiwe mara moja. Naomba niwatoe hofu Watanzania hakuna jambo linalohusu tuchukue samaki kutoka Mwanza tulete Dodoma au tupeleke Dar es Salaam kwa kuhifadhi na maji ya maiti, halipo jambo la namna hiyo! Naomba wawe na uhakika ya kwamba samaki wanaovuliwa na wavuvi wetu na wanaokwenda katika masoko mbalimbali wako salama hawana shaka yoyote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni lini sasa taarifa hiyo ya tume itawekwa wazi kwa wadau na wananchi wote kuifahamu na kuijua?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, migongano na migogoro hii imesababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi, na je, Serikali haioni haja ya kuja na mkakati wa pamoja kama Serikali mkakati wa haraka kuhakikisha namna gani tunakabiliana na hii changamoto ya watu kujichukulia sheria mkononi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama ambavyo tumesema katika jibu letu la msingi kwamba kufuatia kuongezeka kwa matukio haya tayari Serikali imeunda tume ama timu maalum kwa ajili ya kuchunguza na kuweza kuleta majibu.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kweli timu iliundwa na taarifa zimekuja, majibu yamekuja lakini bado Serikali tunaangalia kama kutakuwa kuna haja ya namna ya kuweza kutoa hizi taarifa kwa jamii basi zitatolewa. Kama hatuna namna basi tutaona namna nyingine ya busara zaidi ya kuwafikishia majibu wananchi ya tume hii iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza hayo matukio.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusiana na mkakati, ama bila ya shaka kuna haja ya kuwa na mkakati na mkakati upo, na mkakati wa kwanza katika hili ni kuendelea kuwaelimisha watu. Moja kuhusiana na masuala haya ya kishirikiana, kwamba si kila ambaye anakuwa na sababu hizo maana yake auliwe. Lakini kingine ni kushurutisha sheria kwamba watu lazima wafuate sheria na wasijichukulie sheria ama hatua mikononi mwao. Nashukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango ambayo Serikali imeainisha hapa ya ujenzi ya vituo vya afya lakini hakuna mpango wa wazi wa kuonesha namna gani sasa tunajenga vituo vya afya lakini tunaajiri watumishi wa sekta ya afya tukizingatia kwamba tuna upungufu wa takribani asilimia 50 ya watumishi wa afya kwenye sekta zetu za afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inajenga na moja ya mkakati tulionao ni kuajiri na hata katika mwaka huu wa fedha nafikiri kama wiki ijayo Mheshimiwa Waziri wa Nchi atatangaza nafasi za ajira ambazo tutakwenda kuajiri katika maeneo haya ya afya pamoja na elimu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali imejipanga kuajiri na Waziri wa Nchi atatangaza hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja na soko kutokuwa na uhakika, kumeibuka utamaduni wa wanunuzi kufika mpaka mashambani, wao ndio wanapanga bei na aina ya vifungashio ambapo kwa kiwango kikubwa inamuumiza mkulima.

Je, Serikali inasema nini kuhusiana na hili?

Swali la pili, je, Wizara ipo tayari sasa kwenda kukaa na wakulima hawa kusikiliza changamoto zao lukuki walizonazo ili waweze kupata ahueni na kuondokana na changamoto hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Paresso kwa kufuatilia hili la mazao hasa kwenye zao la vitunguu. Ni kweli kumekuwa na changamoto hiyo ya wanunuzi wengi na wakati mwingine hata wa nje kufika kwa wakulima kule vijijini. Tumeshatoa maelekezo mara nyingi hasa kwa wenzetu wa halmashauri tuendelee kushirikiana kuhakikisha tunaendelea kujenga collection centers, yaani maeneo ya kuuzia kama masoko. Maeneo hayo ndiyo maalum kwa wakulima ili waweze kuuza kwa tija na kwa vipimo.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kusema kwamba Wakala wa Vipimo ambao wako chini yetu waendelee na waende eneo hili maalum wakaone changamoto hii iliyopo ili kukomesha ufungashaji wa mazao yetu kwa njia ambayo siyo sahihi. Maana tumeelekeza mazao yote yauzwe kwa vipimo, siyo kwa vifungashio. Pia kulikuwa na hii habari ya lumbesa, naamini tulishasema na ninarudia tena, kuhakikisha wanauza kwa vipimo na tuhamasishe halmashauri waweke collection centers ili wakulima wapate bei yenye tija kwa mazao yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda kukagua; nitaenda, na niagize WMA waende kwanza, nasi tutaenda kuona changamoto hasa katika eneo hili Bonde la Eyasi ili tuweze kutatua changamoto hii ambayo nadhani ni sehemu zote nchini na tunaendelea kufanyia kazi hilo. Nakushukuru sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya Taifa limechukua muda mrefu sana na imekuwa na sintofahamu. Kuna Watanzania ambao takribani miaka mitatu mpaka minne wana namba tu hawana kadi.

Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hili? Kama mmeshindwa muwaambie Watanzania kwamba mmeshindwa na haiwezekani zoezi hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hili jambo lilikuwa limekwama kidogo, lakini tulikuwa tuna changamoto na sababu ya kwamba hivi vitambulisho vichelewe kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba bado Serikali haijashindwa kuwapatia wananchi vitambulisho, hivi ninavyokuambia vitambulisho vimeshazalishwa na tayari huko Wilayani vimeshasambazwa. Kikubwa ni kwamba kama Wilaya ambavyo vitambulisho havijafika basi tuelezane tujue namna ya kufanya lakini vitambulisho tayari vimeshapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, even if vinazalishwa kwa speed siyo ile ya kawaida lakini kwa ufupi ni kwamba vitambulisho vinazalishwa na vitawafikia wananchi ili waweze kupata hiyo huduma ya vitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Stendi iliyopo katika Wilaya ya Karatu haikidhi vigezo na hasa wakati wa masika inakuwa na changamoto kubwa. Je ni lini Serikali itajenga stendi ya kisasa tukizingatia karatu ni mji mdogo wa kitalii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uhitaji wa stendi katika Halmashauri ya Karatu ni muhimu na ni kweli kwamba kuna uhitaji huo, lakini tumekwishamwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kufanya tathmini ya gharama, lakini kama gharama ni kubwa juu ya uwezo wa halmashauri, walete kama mradi wa kimkakati, lakini tunasisitiza halamashauri kutenga fedha za mapato ya ndani kuanza kukarabati stendi hii ya karatu, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Katika Miji Midogo iliyoko nchini sasa hivi kumekuwa kuna sintofahamu kati ya Mamlaka ya Miji Midogo na Halmashauri kuhusu nani hasa akusanye mapato yapi? Je, Serikali sasa iko tayari kutoa mwongozo unaoeleweka ili mamlaka zote mbili zijue mipaka yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi tuna mamlaka za Miji Midogo 71 kote nchini inawajibika katika Halmashauri Mama na inatekeleza majukumu yake chini ya usimamizi wa Halmashauri Mama. Kwa hiyo, haina mamlaka ya moja kwa moja mpaka pale itakapopata sifa ya kuwa Halmashauri ya Mji. Kwa hiyo, ikiwa Mamlaka ya Mji mdogo bado haina mamlaka ya moja kwa moja na wao siyo Accounting Officers, kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba kwanza tunawawezesha kwa kuwajengea uwezo lakini ku-harmonize mahusiano kati ya Halmashauri Mama lakini na Mamlaka za Mji Mdogo. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Karatu – Njiapanda - Mang’ola - Lalago kwa kiwango cha lami. Je, ni lini ahadi hii itatekelezwa ili barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ahadi hiyo ipo ya kujenga hiyo barabara ya Karatu hadi Lalago kwa kiwango cha lami. Serikali bado haijaufuta mpango huo, inaendelea kutafuta fedha na fedha zikipatikana basi barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, siku za karibuni kupitia vyombo vya habari tumeshuhudia mama mmoja ambaye alifika Zanzibar akiwa na ndizi na alipigwa faini, akatakiwa arudi na bidhaa hiyo upande wa Bara. Lakini wote tunaelewa kwamba Tanzania ni nchi moja.

Ni nini kinasababisha kwamba bidhaa kama hizo zikienda upande wa pili zinarudishwa na nini kauli ya Serikali kwenye hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nishukuru kwa busara yako njema ya kuongoza Bunge letu hili tukufu.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dada Paresso alizungumza suala zima la kuzuiliwa kwa ndizi za mama mmoja wiki iliyopita ambapo Watanzania walishuhudia jambo lile likitokea katika mitandao ya kijamii. Na kweli mimi mara baada ya kuona jambo lile kwa sababu ninahusika na dhamana ya Muungano wetu, lakini nikifahamu kwamba Muungano wetu katika mambo tunafanya vizuri katika upande wa Muungano maeneo yote mawili. Ililazimu ofisi yangu kwa haraka sana kuwasiliana na ofisi ya mwenzangu, Mheshimiwa Hamza, Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili Zanzibar, kumuuliza kulikoni ninachokiona katika mitandao?

Mheshimiwa Spika, Waziri mwenzangu alinijibu ya kwamba jambo hilo ni kweli limetokea, lakini ni kwa sababu kufuatia Tangazo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambalo limetolewa kwa mujibu wa Sheria Namba 9 ya mwaka 1997, Sheria ya Uhifadhi wa Mimea, na tangazo hilo limetokana na hivi karibuni imebainika kuna ugonjwa wa mnyauko wa migomba ambao unaitwa Banana Xanthomonas Campestris.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kutoa tangazo maalum la kuzuia mazao yote ya migomba ikiwemo ndizi, mimea na majani kwa lengo la kuepusha ugonjwa huo usisambae katika maeneo mbalimbali, lakini wakatoa maelekezo katika maeneo yote ya kuingilia vyombo mbalimbali kuzuia mimea hiyo isiweze kuingia.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa mujibu wa Sheria hiyo Namba 9 ya mwaka 1997; endapo kosa hilo litabainika kuna adhabu zake tatu, jambo la kwanza aliyehusika kuingiza mimea hiyo anapaswa kuiteketeza kwa gharama zake mwenyewe; ahabu ya pili ni kwamba anaweza akapewa fine ya 50,000 kulipa ama zaidi ya hapo na adhabu ya tatu, anaweza akaelekezwa ya kwamba adhabu yake ni kifungo cha miezi sita kwenda gerezani miezi sita ama adhabu zile mbili kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa Sheria Namba 9 ya mwaka 1997.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tangazo hili lilikuwa limetoka na kuwekwa katika maeneo yote ya kuingilia kwa mipaka ile. Tunafahamu kwamba kila nchi duniani ina utaratibu au kila maeneo mamlaka zina taratibu zake za kulinda.

Kwa hiyo, hili lilikuwa ni suala zima la udhibiti, lakini kwa bahati mbaya mama yule alikuwa hafahamu kwamba kuna lile tangazo lilitoka kabla. Kwa hiyo, ndio maana tulipofuatilia tulipata majibu hayo kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ni kweli tangazo lile lilitoka kwa kuziia suala zima la ugonjwa wa mnyauko wa migomba usiingie katika upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, sisi katika hilo tukaona basi ni vyema tangazo lile likatolewa kwa uwazi zaidi. Lengo kubwa ni kwamba watu wasiofahamu kwamba kuna zuio la kuingiza mazao ya migomba basi kila Mtanzania aweze kulipata kwa ajili ya kuchukua tahadhari hizo.

Mheshimiwa Spika, na hicho ndicho kilichojiri kule Zanzibar. Kwa hiyo, mpaka hivi sasa tangazo lile ni tangazo halali la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, limewekwa kwa ajili ya kuzuwia mimea hasa mazao ya migomba, ndizi zake, migomba na majani yasiingie kwa ajili ya kuzuia suala zima la uambukizaji wa ugonjwa wa mimea hii ya ndizi.

Mheshimiwa Spika, huu ndio mustakabali wa jambo hili. Kwa hiyo, hili wenzetu wameli-treat hivyo, lakini ni kwa mujibu wa Sheria ya Quarantine kule utaratibu wa kuhifadhi mimea katika eneo hilo. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na ahadi ya muda mrefu sana ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka njia panda Oldiani-Mangola mpaka Matala Lalago ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu.

Je, ni lini Serikali angalau hata kwa vipande itaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii itaanza kujengwa kwa vipande, lakini barabara itakayoanza kujengwa ni ya Babati kuja Mbulu - Hydom kwenda Sibiti kwa kiwango cha lami na tutaanza sehemu ya Mbulu kuja Hydom na hiyo aliyoitaja tutaanza baada ya muda kwa sababu ni barabara ambayo zinaenda parallel. Kwa hiyo tumeamua tuanze kwanza hii ya Babati – Mbulu - Hydom kwenda Sibiti halafu barabara aliyoitaja itafuata. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Wakulima wengi ambao wanatumia hivi viuatilifu wanahatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kansa, mtindio wa ubongo na mengine kutokana na kutokutumia ipasavyo viuatilifu hivi. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inawalinda wakulima kiafya katika matumizi haya ya viuatilifu? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli viuatilifu vikitumika vibaya vinakuwa na madhara kama jambo lolote lile, hata chakula watu wakila vibaya kunakuwa na madhara.

Kwa hiyo tunachokifanya kama Serikali ni kwamba tunatoa mafundisho kupitia Tanzania Plant Health Authority iliyokuwa TPRI huko zamani na baadhi ya mazao sasa hivi tumeanza utaratibu wa ku-train vikundi vya vijana ambavyo vinapewa mafunzo maalum na TPRI na kupewa leseni kwa ajili ya kufanya kazi za kupulizia viuatilifu.

Mheshimiwa Spika, vile vile tumeanza kuwataka wasambazaji wa viuatilifu wanapotengeneza vifungashio watumie lugha ya Kiswahili kutoa maelezo ambayo namna ya mkulima kuchanganya ili iwe rahisi mkulima anaponunua kile kiuatilifu kuweza kufanya kazi ile yeye mwenyewe na kupata mwongozo badala ya kutumia lugha ya Kiingereza ambapo inakuwa ni vigumu kuongoza. Kwa hiyo huo ndiyo utaratibu tumeanza na viuatilifu vyote kuanza sasa vinavyosajiliwa TPRI hata vilivyokwisha sajiliwa na nipitie Bunge lako hili kumwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Plant Health Authority atekeleze maagizo ya Serikali kwamba viuatilifu vyote vifungashio viandikwe kwa lugha kwa Kiswahili ili mkulima aweze kusoma na kuelewa. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa matukio haya ya kuungua masoko yamekuwa yakitokea kwa masoko haya ambayo hayajajengwa kisasa kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu hiyo ya uzimaji wa moto na kwa kuwa Serikali wamekuwa wakichukua kodi au tozo katika haya masoko kwa sababu kuna wafanyabiashara humo.

Je, sasa Serikali haioni ni muhimu kufikiria namna ya kuwalipa fidia wale wananchi ambao waliumizwa na matukio haya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa hayo masoko ya zamani hayana miundombinu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa-train vijana miongoni mwao wanaofanya biashara na kuwawezesha wawe na vifaa vyote ili inapotokea majanga haya basi iwe ni raihisi wao wenyewe waweze…

SPIKA: Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo: -

Mhehimiwa Spika, kuhusu suala la kulipa fidia hili ni suala la kisheria kwa mujibu wa sheria tulizonazo, sasa hatuwezi kusema lolote kwa sababu Bunge lako halijatoa utaratibu kama huo. Hata hivyo, nadhani lililo la umuhimu ni elimu ya kinga dhidi ya majanga haya ili yasitokee kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la mafunzo hilo ni jambo jema na tumeanza kutoa kupitia kwa Scout, lakini vilevile na mifumo yetu ya Serikali za Mitaa ili kuwawezesha watu hawa kujikinga na majanga ya moto au kuzima yanapotokea katika hatua za awali. Nashukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Wizara hii inaelekeza kuunganisha barabara ya Mkoa mmoja na Mkoa mwingine kwa kiwango cha lami. Tuna barabara mbili kutoka Karatu kwenda Mbulu ambapo ni Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Arusha; na kuna barabara inayotoka Karatu – Njiapanda – Mang’ola – Lalago ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu, zote hizi hazijajengwa kwa kiwango cha lami: Je, lini Serikali mtakamilisha barabara hizi au mtajenga barabara hizi kwa kiwango cha lami ikiwa sera yenu inaelekeza hivyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sera ni kuunganisha barabara kwa kiwango cha lami Mkoa na Mkoa, lakini kipaumbele pia ni kuhakikisha kwamba, kama barabara ambazo zinakwenda parallel tutaanza na moja halafu itafuata nyingine kulingana na upatikanaji wa fedha. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara ya Oldeani – Mang’ola kwenda Matala - Sibiti inakwenda kama parallel, yaani sambamba na barabara ya Karatu –
Mbulu – Hydom – Kidarafa hadi Sibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo barabara ambayo tunaita Serengere Southern Bypass imeingizwa kwenye mpango wa kuijenga kwa EPC + F, lakini Serikali inafikiria kuijenga barabara kuanzia Oldeani hadi Mang’ola kwa kiwango cha lami kabla ya kupita Mang’ola kwenda Sibiti, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Tuna walinzi katika shule zetu za msingi, sekondari, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya lakini hakuna…

SPIKA: Swali.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, je, kada hizi zinalipwa na Mamlaka ipi hasa kwa sababu kuna mkanganyiko mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, juu ya ajira hizi za walinzi na kada mbalimbali kama ulivozitaja walipaji ni halmashauri kutokana na ikama ambayo wamejipangia.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kumekuwa kuna changamoto kwa wakulima hasa wa zao la mahindi msimu huu, mahindi yamevamiwa na wadudu lakini mkulima anatumia dawa nne, sita mpaka nane, anazichanganya lakini bado hazi-react kwa wadudu hao na elimu kwa wananchi wetu bado ni ndogo: Nini mkakakti wa Serikali kuhakikisha kwamba dawa sahihi kulingana na wadudu husika ambao wamevamia mazao inapata tiba kwa wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na viuatilifu (TPHPA) Serikali imekuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba viuatilifu vyote vinavyoingizwa nchini ni vile ambavyo vinakidhi mahitaji na matakwa ya changamoto ambazo zinawakabili wakulima wetu. Hivyo ambacho tutakifanya zaidi, ni kuendelea pia kutoa elimu kwa wakulima wetu juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu hivi ili viweze kuleta matokeo chanya na viweze kumsaidia mkulima katika kupambana na uhalibifu wa mazao.

Mheshimiwa, Mwenyekiti, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Serikali inatambua changamoto zilizojitokeza na kuendelea na ukaguzi ili tukibaini kwamba kuna changamoto kama hiyo katika baadhi ya maeneo, tutaweza kuchukua hatua stahiki na tuweze kufuta mpaka usajili katika wale ambao wanahusika. Sambamba na hili, uhakika tu ni kwamba tutahakikisha kwamba mkulima wetu anapata viuatilifu ambavyo ni sahihi kwa wadudu sahihi.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Endapo ikitokea mwananchi ameua tembo au gari limegonga tembo au mnyama yoyote faini anayotozwa ni kubwa sana, lakini ikitokea vinginevyo kwamba mnyama amemuua mwananchi au ameharibu mazao yake, sheria haimpi haki mwananchi. Je, nini kauli ya Serikali ku-balance haya mambo ili kuhakikisha kwamba Mtanzania anapata haki yake ndani ya nchi yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tutambue kwamba hawa wanyama ambao tunao katika nchi yetu ni rasilimali za Taifa na wanalindwa kisheria kama ambavyo tunawalinda wanadamu na tutambue kwamba changamoto hii ya wanyamapori wakali na waharibifu imeanza hivi karibuni. Miaka ya nyuma wanyama hao walikuwa wanaishi kwa uhuru na salama kabisa na hatukuwahi kuwa na changamoto hizi. Kwa hiyo ukiangalia mahitaji ya ardhi, ongezeko la watu tumeendelea kusogea katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema leo hii changamoto hii tuielekeze kwenye faini, mzigo ni mkubwa sana kwa Serikali hautaweza kugharamia hasara ambayo itaweza kujitokeza. Kwa hiyo tunaendelea kuhamasisha wananchi kwamba tusiendelee kuyasogelea maeneo haya na ndio maana kanuni hii ilitungwa kwa wale ambao Wanyama wamewafata basi tunawashika mkono ili kuhakikisha kwamba Serikali inaonesha kwamba iko nao.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Je, ni lini mifumo ya malipo ya TANAPA, TAWA, Ngorongoro pamoja na ile ya Wizara itaunganishwa na kuwa mfumo mmoja wa malipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itaruhusu uhai wa leseni za TALA uwe kwa mwaka ambao leseni imekatwa tofauti na sasa hivi ambavyo leseni inakuwa ni kalenda ya mwaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo ya malipo katika taasisi zetu tayari imeshaanza kutumika. Baadhi ya taasisi kama Ngorongoro na TANAPA utekelezaji wake unaendelea, lakini baadi ya taasisi tayari tulishaunganisha. Kwenye upande wa leseni; sasa hivi leseni inatoka kwa mfumo mmoja tu ambapo imeunganishwa mifumo yote. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye suala la leseni wadau wote wanafaidika na mfumo huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili lingine la TALA, tumeshaanza kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali hususan wadau wa masuala ya utalii na tunaangalia tupitie kanuni upya tuone kama zitaleta tija katika marekebisho ya utoaji wa leseni. Nawakumbusha tu wadau hawa kwamba Serikali ina calenda year ambapo ndiyo huwa inakusanya mapato yake na imejiwekea mipango yake. Kwa hiyo, kama tutaona kuna haja ya kurekebisha kanuni hizi, basi tutawashirikisha kwa kuchukua maoni yao, lakini kwa kuangalia pia Serikali katika ukusanyaji wa mapato, ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Tumeshuhudia mvua kubwa zinazoendelea nchi nzima na kufanya mawasiliano katika baadhi ya maeneo kukatika na hivyo kuchukua muda mrefu kuzitengeneza kwa wakati ili wananchi waweze kuendelea na usafiri na usafirishaji, lakini kuokoa uhai wa watu kwa wale ambao labda wanahitaji huduma hizo kwenda hospitali na vinginevyo: -

Nini mkakati wa Serikali wa haraka endapo inatokea changamoto ya namna hiyo, inafanyika kwa haraka na mawasiliano yanarudi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunategemea tutaoa taarifa, kama alivyoongea hata juzi Mheshimiwa Kunambi. Barabara nyingi ambazo tunazo Tanzania, ni Kilometa kama 36,000 ambazo tunazihudumia. Kati ya hizo, ni kilometa 12,000 tu ambazo zina lami. Kwa hiyo, barabara hizi zenye urefu wa kilometa kama 24, nyingi ni za changarawe na nyingine zipo mabondeni ambazo tumeshatoa taarifa kwa wakuu wa barabara kwa maana ya Meneja wa TANROADS kuhakikisha kwamba barabara zote ambazo zinakuwa na changamoto wanazi-attend kwa muda.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambapo ni kwenye madaraja, tuna madaraja ya muda ya chuma ambayo kama ni daraja linaweza lakini bahati mbaya unakuta siyo tu daraja limeondoka, lakini ni tuta pengine la kilometa moja mpaka mbili limeondoka na wakati mvua inanyesha inakuwa ni ngumu kuweza kufanya hiyo kazi wakati pana maji, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya tarehe 22 Jumatatu, kumetokea vurugu na sintofahamu kubwa sana kati ya wananchi wa Kijiji cha Jangwani Eneo la Mto wa Mbu na Askari wa Uhifadhi wa Eneo la Ziwa Manyara na kusababisha mwananchi mmoja kufariki na wananchi kadhaa kujeruhiwa kwa risasi za moto: Je, ni kwa nini askari hawa wa uhifadhi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kukabiliana na hii migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi kiasi kwamba, wananchi wanapoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa? Kwa nini kusiwe na njia nyingine mbadala kukabiliana na changamoto hizi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nifafanue kidogo kwa ridhaa yako. Kwa kawaida wahifadhi wanakuwa kwenye maeneo yao ya kutekeleza majukumu yao ya kawaida ya kila siku. Mgogoro huu ulijitokeza katika ziwa Manyara ambapo askari walikuwa katika shughuli zao za doria na waliweza kukamata wahalifu watatu ambao walikuwa wamevamia katika hifadhi hiyo. Baada ya wahalifu hawa kukamatwa ili wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo, wavuvi zaidi ya 30 walijiunga kwa pamoja na wakaenda kuwavamia wale wahifadhi ambapo walikuwa katika maeneo yao ya doria ya kawaida. Kwa bahati nzuri walikuwa tayari wameshawafunga pingu wale wahalifu watatu, lakini wananchi walienda kuwashambulia hao askari. Katika kujiokoa, waliweza kuwaachia hao wahalifu wakakimbia na pingu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichotaka kusema hapa ni kwamba, suala linapofika kwenye vyombo vya sheria ama wahalifu wanapokutwa na hatia, basi tuache sheria ichukue mkondo wake; lakini inapofika wananchi wanaungana pamoja, wanalishambulia jeshi, jeshi lenyewe sasa linakuwa linaonekana halina nguvu. Kizuri zaidi na kwa kuwa, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri yameshaelekeza kwamba tusitumie nguvu, hawa askari waliweza kukimbia na hawakuweza kufanya vurugu yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maandamano hayo, ilisababisha askari kujumuika na wahifadhi ili kuwatawanya watu. Watu walikuwa wengi sana kwa sababu waliungana, ni wanavijiji wa maeneo yale waliwazingira na kufanya maandamano, na walikuwa wanavunja magari, wakikutana na gari wanafanya uhalifu. Kwa hiyo, katika vurugu zile ndiyo zilisababisha sasa huyo mwananchi kufikwa na maafa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba sana wananchi wajitahidi sana kuheshimu vyombo vya Dola vilivyopo kwa sababu, viko kisheria na vinatekeleza majukumu yaliyokasimiwa. Kizuri zaidi, hawa tumewakasimisha madaraka kulinda rasilimali za nchi. Kwa hiyo, tunapowashambulia, tunawapunguzia nguvu ya kulinda rasilimali zilizopo hapa nchini.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza niseme siridhiki na majibu ya Serikali kwa sababu hizo jitihada zimefanywa na wananchi na takribani watu 24 ndani ya miaka mitatu wakiwemo Watoto wameuawa na fisi. Sasa swali langu;

a) Je, ni lini na kwa uhakika hilo jeshi la uhifadhi litafika katika eneo hilo na kuwavuna fisi hao ili wananchi waendelee kukaa kwa amani?

b) Je, ni lini, Serikali itakuja na mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi ili yanapotokea majanga kama hiyo waweze kujihami na kukabiliana na Wanyama wa namna hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye swali lake la nyongeza linalohusiana na lini Jeshi la Uhifadhi litaenda kuwasaka, naomba tu niendelee kuelekeza kuanzia sasa kwamba Jeshi la Uhifadhi Kanda ya Kaskazini waelekee Karatu, wakaamnze kufanya msako wa fisi hao ili wananchi waweze kuona umuhimu wa uhifadhi lakini pia fisi hao waweze kurudishwa hifadhini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala hili la elimu. Kwa sasa hivi tumeanza programu za kufundisha au kuelimisha wananchi namna ya kujikinga na wanyama wakali na uharibifu. Kwa hiyo naendelea kuelekeza kwenye upande wa Kanda ya Kaskazini kwamba, pamoja na msako huo utakaofanyika pia watoe elimu kwa wananchi ili tuweze kuwa na mashirikiano ya pamoja.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuulizwa swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ya Wilaya ya Karatu pia ina mpango wa kujenga stendi ya kisasa, na kwenye bajeti ijayo, halmashauri umetenga fedha kidogo, tunajua haitaweza kutosheleza.

Je, Serikali kuu iko tayari sasa ku top-up hicho kidogo kilichotengwa na halmashauri ili malengo yaweze kufikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso la Stendi ya Karatu. Kwanza ni pongeze jitihada za halmashauri ya Karatu kwa kutenga fedha zao kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa stendi hii. Ni dhamira ya Serikali hasa hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha inawezesha halmashauri zetu zote nchini kuwa na uwezo wa kupata mapato, kama nilivyosema awali, ambayo ni sustainable kwa ajili ya uendeshaji wa halmashauri hizi. Hivyo tutakapo pokea andiko kutoka Halmashuri ya Karatu juu ya ujenzi wa stendi hii basi tutaangalia tutachakata andiko hilo na kuliwasilisha Wizara ya Fedha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa dawa ya kisukari kwa wagonjwa wa sukari imekuwa ni changamoto sna kwenye vituo hivi vya afya mpakla waende Wilayani. Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa ku-review utaratibu huu ili kwenye level za Vituo vya Afya pia waweze kupata?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo lilikuwa linaleta malalamiko mengi hasa kwenye zahanati na vituo vya afya hasa kwa wazee wetu wagonjwa wa kisukari na presha ni eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amesema. Ukiona hapa tumeongeza dawa kwa kiasi hiki ni moja wapo ya dawa hizi za sukari na presha kuhakikisha sasa hiyo shida iliyokuwepo huko nyuma haitatokea tena.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Bonyokwa Jimbo la Segerea. Je, ni lini changamoto hii itakwisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge Viti Maalum kuwa maeneo ya Segerea, Bonyokwa tuna miradi ambayo iko mwishoni kabisa kukamilika, tunatarajia mapema mwaka wa fedha ujao maeneo haya yote yanakwenda kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kuna Mamlaka za Miji Midogo hapa nchini imekaa kwenye wadhifa huo kwa muda mrefu na sasa vinakidhi kwenda kwenye hatua nyingine. Je, ni lini Serikali sasa itazipandisha ikiwemo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kuna mamlaka nyingi ambazo zinahitaji kupanda hadhi, moja ya jukumu kubwa la Serikali sasa hivi ni kuhakikisha kwanza tunaboresha miundombinu katika Halmashauri ambazo bado hazijakamilika. Lakini pili, kulingana na mahitaji tutapandisha hadhi, na sisi tutapendekeza kulingana na vilevile mahitaji ya wakati husika. Kwa hiyo, hilo ndiyo jibu la Serikali kwa sasa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini dhamira au msukumo wa Serikali wa kufikiria kuanzisha taasisi moja badala ya kuimarisha taasisi zilizopo na hususan hii taasisi ya KAVIWASU kwa sababu imekuwa ikifanya vizuri zaidi kulinganisha na ile taasisi ya Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; utozaji wa bei kati ya taasisi hizi mbili hutofautiana na ni ukweli kwamba hiyo taasisi ya Serikali inapata unafuu na bei yake inakuwa nafuu kwa sababu, inapata ruzuku kutoka Serikalini, ilhali ile taasisi iliyoanzishwa na wananchi haipati unafuu wowote na gharama zinabaki palepale. Serikali kwa mara nyingine mpo tayari kuipa ruzuku taasisi hii ya wananchi ili kuunga mkono jitihada za wananchi katika kupata maji katika Mji Mdogo wa Karatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, lini tutaweka hizi taasisi kuwa moja; mara baada ya taratibu zote za Kiserikali kukamilika tutahakikisha tunafanya hizi taasisi mbili inakuwa moja kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utozaji wa bei unatofautiana, chombo ambacho kinasimamiwa na Serikali kinapewa ruzuku na kile cha wananchi hakipewi ruzuku; kitakachofanyika ni kitakuwa chombo kimoja kwa hiyo, ruzuku ya Serikali itaingia na lengo la Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama mpendwa anayetaka akinamama tuwatue ndoo kichwani, tuhakikishe huduma zinakuwa chini, tutahakikisha bei zinakuwa rafiki kwa wananchi na ruzuku pale inapobidi itakuwa inafika kwa wakati.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mchakato wa upandishaji hadhi wa zahanati zetu kwenda vituo vya afya unafanywa na Wizara; je, Wizara haioni sasa mchakato huu mkaziachia Sekretarieti za Mikoa ifanye kazi hiyo kwa vigezo vilevile ili kupunguza huo urasimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilai Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, upandishaji hadhi wa zahanti kuwa vituo vya afya au kuwa hospitali za Halmashauri unafanya na Wizara kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo Halmashauri wanafanya tathmini kulingana na vigezo, wanawasilisha mikoani kwa RAS na wanawasilisha Wizara ya Afya, lakini pia Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utaratibu huu ni shirikishi haifanyi Wizara pekee yake ni ngazi zote zinahusika na tutaendelea kufanya hivyo kwa sababu ndiyo maana ya D by D. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Pamoja na uhaba wa watumishi/wataalam wa hivyo vifaa tiba lakini pia ma-engineer au mafundi wa kutengeneza hivyo vifaa tiba pindi inapoharibika inakuwa ni changamoto kubwa sana.

Je, katika ajira zilizoko mnazingatia pia na wataalam hawa ili inapopata breakdown yoyote basi inatengenezwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Ni kweli kwamba tumekuwa na changamoto ya upungufu wa wataalam wa vipimo kwa maana diagnostic issues ikiwemo X-ray na ultrasound, lakini Serikali kwanza tumeweka mpango mkakati wa kuwafanyia mafunzo kazini wataalam zaidi ya 300 ambao watakwenda ku-cover mapengo kwenye vituo vya afya na hospitali ambazo zinajengwa ili yale majengo yaliyojengwa na vifaa tiba ambavyo vinakwenda vianze kutumika mapema iwezekanavyo.

Lakini pili tuna wataalam wa ufundi kwa maana ya biomedical engineers katika halmashauri zetu na katika ajira hizi pia wataajiri wataalam hao, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mchakato wa uvunjwaji wa Bodi hii haukishirisha wananchi na hapa mmekiri mlienda kwenye Mamlaka ya Serikali, kwa wawakilishi wa wananchi lakini hamkufika kwa wananchi. Je, ni lini mtafika kwa wananchi na kuwapa sababu za kwa nini mlivunja mradi huu? (Makofi)

Swali la pili, mmeeleza kwamba baada ya chombo hiki kuundwa kuna ufanisi wa maji, naomba niwaambie Wizara hakuna ufanisi wowote matokeo yake tumerudi kwenye adha kubwa ya ukosefu wa maji katika Mji wa Karatu. Ni lini na kwa haraka mtarekebisha tatizo hili ili wananchi waweze kupata maji kwa uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie tena Mheshimiwa Waziri yeye mweyewe, Jumaa Hamidu Aweso na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo walishirikiana na Waheshimiwa Madiwani waliweza kushirikisha wananchi. Kama wananchi hawakupata taarifa wote basi kuendelea kutoa elimu ni moja ya jukumu la Wizara, kwa hiyo tutaendelea kutoa elimu kwa sababu dhamira ya Wizara ni njema kabisa, lengo la kuunganisha hivi vyombo ni kupunguza mzigo wa gharama za bei kwa wananchi na kabla ya kuviunganisha mwananchi aliweza kulipia unit ya maji shilingi 2,000 na baada ya kuviunganisha tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri alihakikisha bei zimeshuka na sasa hivi ni shilingi 1,300.

Mheshimiwa Spika, kuonesha ufanisi mkubwa wa mradi wa huduma ya maji, tayari Wizara, Karatu tumeiangalia kwa jicho la kipekee kabisa na tayari kazi zinaendelea, tutahakikisha huduma ya maji Karatu wataendelea kuboreshewa lengo ni kupata maji safi na salama bombani yakiwa ya kutosha.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri ahsante sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni, sasa aulize swali lake.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri zetu mbalimbali hapa nchini kuna nguvu za wananchi zimetumika kujenga shule kwenye level ya shule za msingi na shule za sekondari, zimebaki kama maboma kwa muda mrefu bila ukamilishaji.

Je, Serikali sasa kwanini isizitake Halmashauri, izitambue na kuwapa timeframe wa ukamilishaji wa majengo hayo ambayo ni nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa nia njema ya kuhakikisha kwamba maeneo yetu yote yanakuwa na shule za msingi kwa maana ya vijiji lakini na shule za sekondari kwenye Kata, ilihamasisha nguvu kazi za wananchi lakini Serikali inachangia nguvu zile kukamilisha maboma ya madarasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kazi kubwa sana, sote ni mashahidi kwamba fedha nyingi sana zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha madarasa hayo katika miaka yote ya fedha ukiwepo mwaka huu, kupitia EP4R, kupitia SEQUIP lakini tunakwenda na mpango wa BOOST.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu kwamba tungependa kuweka deadline kukamilisha maboma hayo kwa Halmashauri, lakini pia bado kuna changamoto za uwezo wa mapato ya ndani kukamilisha kwa pamoja kutoka na wingi wa majengo ambayo yamejengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba safari ni hatua, tumekwenda kwa kiasi kikubwa sana na tutakwenda kukamilisha maboma yaliyokamilika, kwa sababu mpango umewekwa vizuri kwa ajili ya shughuli hiyo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tunatambua kwamba kuna mwongozo ambao umetolewa na Wizara ya fedha ku-regulate riba kwenye microfinace hapa nchini, lakini mwongozo huo haufuatwi na hizo taasisi za kutoa fedha wakati mwingine zinachukua hadi kadi za ATM za watumishi wanaokwenda kukopa pale, Serikali inasema nini juu ya hili ili miongozo hiyo iweze kufuatwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali siku zote inafuata miongozo na taratibu ambazo zimewekwa, kama zipo changamoto ambazo ameziona acha tuzichukue twende tukajadili, tuangalie, tukijiridhisha basi tutazifanyia kazi. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Upandishaji hadhi wa baadhi ya zahanati hapa nchini kuwa vituo vya afya unafanywa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na huwa ni mchakato mrefu sana. Je, ni kwa nini Serikali isifikirie kukaimisha madaraka hayo kwenye Sekretarieti za Mikoa kwa kutumia vigezo vilevile baada ya kufanya tathmini ili kufupisha mlolongo huu mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hakuna mlolongo mrefu wa kupandisha hadhi zahanati kuwa vituo vya afya kwa sababu, wanaohusika ni Mganga Mkuu wa Halmashauri kupitia CHMT na Mkurugenzi. Wanafanya tathmini, wanawasilisha kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kupitia RAS na baadaye wanawasilisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi ambayo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inaifanya ni kutoa idhini, lakini mchakato wote unafanyika katika ngazi ya halmashauri. Tutaendelea kuboresha mchakato huo ili vituo ambavyo vinakidhi haja viweze kupandishwa hadhi kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sensa iliyopita, wanufaika wameongezeka katika kijiji hicho na wananchi wamekuwa wanatarajia mradi huu ukamilike kwa wakati kwa sababu umekuwa ni mradi wa muda mrefu sana

Je, ni lini kwa uhakika, kwa sababu kilichopo site na unachokisema kina tofauti kidogo, ni lini kwa uhakika wananchi hawa watarajie kupata mradi huu wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna wananchi wa vijiji vya jirani ikiwemo Rhotia Juu pamoja na Kilimatembo Juu, ni lini na wananchi hawa wataweza kupata maji kwa sababu vijiji hivyo havina maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli natambua na Serikali inatambua uwepo wa changamoto hii katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea na ni kiu ya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji. Ni kweli mradi huu umechukua muda mrefu, ni kweli kabisa kwa sababu ya hatua mbalimbali ambazo zilikuwa zinachukuliwa na Serikali ikiwemo utafutaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kwa mujibu wa majibu yangu ya msingi, mradi huu unaenda kukamilika Juni, 2024. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika eneo la Kilimatembo pamoja na Rhotia, kuna mradi ambao unaendelea pale, lakini Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kupanua miundombinu ili tufikishe huduma ya maji katika maeneo yanayozunguka katika mradi ule na Kijiji cha Kilimatembo pamoja na Rhotia wataweza kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa jinsi ambavyo mtiririko wa bajeti unaendelea kila mwaka na kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya ujenzi wa VETA, na kwa kuwa kuna baadhi ya Wilaya hapa nchini, kuna taasisi za dini zina vyuo vya ufundi. Je, Serikali sasa hamuoni upo umuhimu wa kuingia kwenye mfumo wa PPP na hizo taasisi ili wananchi wetu ambao wanahitaji ujuzi huo waweze kwenda VETA?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa mapendekezo au mawazo haya muhimu. Kimsingi utaratibu huu kwa hivi sasa Serikalini haupo au hatuna, kwa vile ni mapendekezo tunaomba tuchukue mawazo haya, tuende tukayafanyie kazi, tufanye tathmini ya kina, tuweze vilevile kukaa na wakuu hawa wa taasisi hizi, tuweze kuangalia namna gani tunaweza tukaendelesha vyuo hivi labda kwa mwendo ule wa PPP.

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Fidia imekuwa ikicheleweshwa sana kwa muda mrefu kwa hawa wanaopisha upanuzi wa viwanja na mmekuwa mkiahidi mtalipa riba, mfano pale Uwanja wa Manyara - Karatu. Je, ni lini mtalipa hizo riba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya fidia katika viwanja vyote nchini ikiwemo Kiwanja cha Manyara yatalipwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za ulipaji fidia Serikalini.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 40 ya vifo hapa nchini inatokana na magonjwa yasiyoambukiza, haya magonjwa yasiyoambukiza yana gharama kubwa pia kwenye matibabu yakiwemo moyo, kansa, figo na kadhalika. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba haya magonjwa yasiyoambukiza wananchi wanapewa elimu ya namna ya kuishi ili kuepukana na hiyo gharama kubwa ya matibatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni mkakati wetu wa siku zote wa Elimu ya Afya kwa Umma. Ni kweli kwamba ni gharama kubwa sana matibatu ya moyo na vitu vingine. Kwa mfano, ukizungumzia moyo ni kwa sababu ya teknolojia inayotumika, Serikali inaingia gharama kubwa sana kwenye kununua teknolojia yenyewe kama teknolojia inayosaidia kwa mfano umeme wa moyo unakuta ni teknolojia ya hali ya juu, kwa hiyo, suluhisho letu ni bima ya afya kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nimuombe Mheshimiwa Mbunge yeye ni mdau na Bunge zima tuendelee pamoja kuhamasisha masuala ya afya na masuala ya magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu Wizara ya Afya wakati wote imekuwa ikilijengea Bunge uwezo na lengo letu ni kufikisha huduma kule chini.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Barabara ya Karatu – Kilimapunda – Mbulu ujenzi wake utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge itajengwa kama tulivyopanga kwenye kitabu chetu cha bajeti.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini wananchi wanaopisha upanuzi wa Uwanja wa Manyara watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hatua tuliyopo ni uandaaji wa taarifa ya uthamini, mara tutakapokamilisha, tutawalipa fidia.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza. Benki zetu bado riba ni kubwa sana. Je, Serikali haina mpango wa kufikiria kupunguza riba ili angalau wananchi walio wengi waweze kukopa katika benki zetu?
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko kwenye mpango huo na jambo hilo linalohusisha riba ni jambo mtambuka, lina hatua nyingi mpaka kufikia kwenye hatua hiyo. Moja ya hatua ambayo Serikali imefanya, umeona kwenye masuala ya sensa na makazi, masuala ya vitambulisho vya Taifa, hayo yote ni ya kuwezesha wananchi watambulike ili kupunguza risk na risk zikipungua, definitely tutakuwa tunaenda kwenye uelekeo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea pia kuongea na Benki Kuu pamoja na benki zingine, kuweza kuona utekelezaji wake ili uweze kufanyika bila kuathiri sekta ya fedha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, vitongoji 115 vilivyosalia ni vingi kwa idadi na wananchi wanahitaji umeme, je, ni lini kwa uhakika wananchi hao watapelekewa huduma hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkandarasi aliyepewa kazi ya ujazilishi bado anatusuasua kutekeleza mradi huo, nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vitongoji 115 kwa sasa REA inakamilisha hatua za mwisho za kumpata mkadarasi, ni imani yetu ni kwamba ndani ya wiki moja ijayo mkandarasi huyu atakuwa amesaini mkataba. Aidha, kazi hiyo inatarajiwa kuanza katikati ya mwezi ujao.

Mheshimiwa Spika, kwa lile swali lake lingine, ninaielekeza REA wamsimamie kwa ukaribu mkandarasi yule aweze kutimiza wajibu wake.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, ahadi ya ujenzi wa Barabara hii kwa kiwango cha lami ni ya muda mrefu sana na maneno haya ya upembuzi yakinifu tumeyasikia muda mrefu bila matokeo. Je, kwa nini sasa Serikali isifikirie kuanza tu angalau eneo ambalo linatumika sana la Karatu – Mang’ola lenye urefu wa kilomita takribani 54 kwa kiwango cha lami kwanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii Barabara ya Karatu – Kilimapunda hadi Mbulu, nafahamu mlishasaini mikataba na wakandarasi na ilikuwa ujenzi wa kiwango cha lami uanze katika mwaka huu wa fedha, lakini mpaka leo hakuna kilichoanza. Ni lini barabara hii nayo itaanza kwa kiwango cha lami kwa sababu, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Manyara na Arusha?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba usanifu wa barabara hii ya Karatu – Mang’ola umeshakamilika, tunachofanya ni kutafuta fedha kuijenga. Pia, sisi kama Serikali tunajua kwamba eneo muhimu sana ni Karatu hadi Mang’ola na tumekuwa tukijibu kwamba Serikali inatafuta fedha hizo lakini pia Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kulikuwa na daraja ambalo lilikuwa linasumbua sana Kona ya ‘S’ ambapo tuliona ilikuwa inakwamisha magari mengi. Sasa hivi tunaijenga ili tuhakikishe kwamba at least kwa mwaka mzima barabara hii inapitika hadi eneo la Mang’ola.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara ya Karatu - Kilimapunda kwenda Mbulu tayari tushasaini mikataba; tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi kuona lini mkandarasi ataanza na utaratibu ambao kama alivyosema anaufahamu ni EPC+F ambapo tuko kwenye hatua za mwisho za kuongea na hawa wakandarasi, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Zahanati zetu nchini, nyingi sana hazina vifaa vya maabara. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha zahanati zetu zinakuwa na vifaa vya maabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imepeleka zaidi ya shilingi bilioni 250 katika Sekta ya Afya ya Msingi, kwa ajili ya kununua vifaa tiba na hivi leo halmashauri zote 184 zimepokea kati ya shilingi milioni 700 hadi shilingi bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba, bado kuna mahitaji ya vifaa tiba kwenye baadhi ya zahanati. Hii imetokana na kasi ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na hospitali mpya zimekuwa nyingi, lakini namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwenye bajeti ya mwaka huu imetengwa zaidi ya shilingi bilioni 55, kwa ajili ya vifaa tiba na tutahakikisha zahanati zote, vituo vyote na hospitali za halmashauri zenye upungufu wa vifaa tiba zinapewa kipaumbele kupewa fedha hiyo. Ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Miongoni mwa wanaoidai Serikali kwa muda mrefu ni pamoja na wakandarasi wanaotengeneza barabara hapa nchini, na wako wengi wana madai ya muda mrefu. Ikumbukwe watu hawa wanapochukua hizi kazi wengine wanaenda kukopa benki. Wakati wanapotakiwa kufanya marejesho, Serikali haijawalipa. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na hawa wakandarasi wanaodai, na wapo wengine wanafilisiwa na benki husika kwa sababu walienda kukopa? Nini kauli ya uhakika ya Serikali kuwapa matumaini watu hawa na ikiwezekana walipwe?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba madeni yote yanaendelea kuhakikiwa na Serikali. Uhakiki utakapokamilika na upatikanaji wa mapato, wazabuni wote pamoja na wakandarasi watalipwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za kusafisha figo kwenye Hospitali Binafsi na Hospitali za Serikali ina utofauti mkubwa wa bei. Hospitali Binafsi zina unafuu ukilinganisha na Hospitali za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri ni kwamba ukienda kusafisha figo kwenye Hospitali za Serikali ni ghali zaidi kuliko Hospitali Binafsi; ni nini kauli ya Serikali kupunguza zaidi gharama hizi ili waathirika wa jambo hili waweze kupata unafuu na kupata matibabu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kwa kweli kwenye eneo hili amekuwa akifuatilia karibu sana, lakini amekuwa akifuatilia sana wananchi wa kule Arusha kwa ukaribu sana hususani Karatu na amekuwa akinilitea wagonjwa wa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba inategemea unazungumzia Hospitali Binafsi kwa level gani? Maana yake ukiwa na Hospitali Binafsi ambayo let say ni Polyclinic na unazungumzia Muhimbili, bado bei haisababishi kuwa kubwa na vile vifaa na tiba yenyewe, maana yake kuna mambo mengi yanayozingatiwa kulingana na level ya hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge, nikimaliza kujibu swali tukae mimi na wewe unioneshe maeneo specifically ili nijue, tuangalie tatizo tulitatue kwa pamoja kwa sababu kwa kweli Hospitali za Serikali ndiyo inatakiwa iwe bei rahisi kuliko za private. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka kujua specifically ni nini, ili tuweze kushughulikia kwa pamoja. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri aliahidi kutoa kiasi cha shilingi bilioni nne, kwa ajili ya Mradi wa Maji katika Wilaya ya Karatu. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, jiandae Mheshimiwa Kilave.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, naomba nipate maswali.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Paresso rudia swali lako.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri, kwa maana ya Serikali, alitoa ahadi ya kutoa kiasi cha shilingi bilioni nne, kwa ajili ya mradi wa maji katika Wilaya ya Karatu. Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa sababu, lengo ni wananchi wapate maji. Namwahidi kwamba, hili nalipokea na nakwenda kulishughulikia ili kujua ahadi hiyo imefikia katika hatua gani ili kuhakikisha kwamba miradi inaendelea.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Karatu tumepata Hospitali mpya ya Wilaya lakini bado kuna upungufu wa vifaa na rasilimali watu. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha hospitali hiyo inapata mahitaji hayo ili kuwepo na ufanisi katika utoaji wa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imejenga Hospitali mpya ya Halmashauri ya Karatu na Serikali inatambua kwamba kweli kuna upungufu wa watumishi na vifaatiba. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwanza tumeshapeleka fedha zaidi ya shilingi milioni 800 katika Halmashauri ya Karatu kwa ajili ya kununua vifaatiba na vituo vingine vya afya na zahanati pia tutaendelea kupeleka fedha hiyo katika mwaka wa fedha huu na mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na watumishi tayari Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali cha ajira ya watumishi zaidi ya 46,000. Watumishi wa Sekta ya Afya ni miongoni mwa watumishi watakaoajiriwa, tutahakikisha tunatoa kipaumbele kwa Hospitali ya Halmashauri ya Karatu ili itoe huduma bora zaidi kwa wananchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sensa iliyopita, wanufaika wameongezeka katika kijiji hicho na wananchi wamekuwa wanatarajia mradi huu ukamilike kwa wakati kwa sababu umekuwa ni mradi wa muda mrefu sana

Je, ni lini kwa uhakika, kwa sababu kilichopo site na unachokisema kina tofauti kidogo, ni lini kwa uhakika wananchi hawa watarajie kupata mradi huu wa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna wananchi wa vijiji vya jirani ikiwemo Rhotia Juu pamoja na Kilimatembo Juu, ni lini na wananchi hawa wataweza kupata maji kwa sababu vijiji hivyo havina maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli natambua na Serikali inatambua uwepo wa changamoto hii katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analiongelea na ni kiu ya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji. Ni kweli mradi huu umechukua muda mrefu, ni kweli kabisa kwa sababu ya hatua mbalimbali ambazo zilikuwa zinachukuliwa na Serikali ikiwemo utafutaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kwa mujibu wa majibu yangu ya msingi, mradi huu unaenda kukamilika Juni, 2024. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika eneo la Kilimatembo pamoja na Rhotia, kuna mradi ambao unaendelea pale, lakini Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kupanua miundombinu ili tufikishe huduma ya maji katika maeneo yanayozunguka katika mradi ule na Kijiji cha Kilimatembo pamoja na Rhotia wataweza kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Nini mkakati wa Serikali wa kuimarisha barabara zilizoko ndani ya hifadhi zetu, kwa mfano, Barabara ya kutoka Ngorongoro kuelekea Serengeti ambayo ni mbovu sana?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inafanya kazi ya kuboresha kilometa 400 zilizoko ndani ya hifadhi zetu. Nimhakikishie kwamba, barabara aliyoitaja tunaipa kipaumbele kwa sababu, ni barabara muhimu sana kwa ukuaji wa utalii wa nchi yetu.