Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Elly Marko Macha (3 total)

MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. DKT. ELLY M. MACHA) aliuliza:-
Kufuatia Mpango wa Serikali wa utoaji wa elimu bure kuanzia Elimu ya Msingi hadi Sekondari na kwamba, watu wenye Ulemavu wanakabiliwa na umasikini uliokithiri na hivyo kushindwa kumudu gharama za elimu:-
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa elimu bure kwa wanafunzi wenye ulemavu kwa ngazi ya Kidato cha Tano na Sita?
(b) Je, Serikali inaweza kulihakikishia Bunge hili kwamba itaweka utaratibu mzuri wa usafiri na huduma nyingine muhimu za kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata elimu katika shule wanazopangiwa?
(c) Je, Serikali inaweza kulithibitishia Bunge hili kwamba wanafunzi wenye ulemavu wanaoingia Vyuo Vikuu watapewa kipaumbele katika kupata mikopo bila usumbufu wowote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Elly Marco Macha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia Mpango wa Serikali wa Utoaji Elimu Bure kuanzia Elimu ya Msingi hadi Sekondari na kwamba, watu wenye ulemavu wanakabiliwa na umasikini, Ofisi ya TAMISEMI imeandaa Mpango wa Utoaji wa Elimu ya Msingi bila malipo ili kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014. Sera hiyo inaelekeza kwamba wanafunzi wote wa madarasa ya Awali, Msingi na Kidato cha Kwanza hadi cha Nne wanatakiwa kusoma bila kulipia ada wala michango ya aina yoyote. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania mwenye umri wa kwenda shule, anapata fursa ya kupata elimu. Aidha, Sera ya Elimu Msingi Bila Malipo haijumuishi wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikiingilia kati kwa kutoa misaada kwa watoto wenye mahitaji maalum pale inapojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba jukumu la kuwatunza na kuwalea wanafunzi wenye ulemavu ni la kwetu sote.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Na. 9 iliyoanzisha Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, inatamka bayana kuwa waombaji wanaotakiwa kupewa kipaumbele katika kupewa mikopo ni pamoja na wanafunzi wenye ulemavu. Aidha miongozo ya ukopeshaji ambayo hutolewa na Serikali kila mwaka imeendelea kutamka wazi kuwa wanafunzi wenye ulemavu ni kundi linalotakiwa kupewa kipaumbele katika mikopo.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA aliuliza:-
Elimu kwa watoto wenye ulemavu hupatikana kwa vikwazo na matatizo mengi kiasi kwamba wengi huanza shule katika umri mkubwa ukilinganisha na watoto wasio na ulemavu:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuongeza umri wa kustaafu kwa lazima kuwa miaka 65 kwa watu wenye ulemavu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa upendeleo maalum wa ajira kwa watu wenye ulemavu katika Wizara na Taasisi zake pale ambapo mtu mwenye ulemavu atakuwa na sifa stahiki wakati wa zoezi la ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu kuhusiana na mambo mbalimbali kama vile upatikanaji wa elimu na ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba elimu na ajira ni baadhi ya mambo muhimu kabisa yenye uwezo wa kumtoa mtu mwenye ulemavu kutoka katika hali ya unyonge na utegemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, napenda kujibu swali namba199 lenye sehemu (a) na (b) lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Elly Macha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002, umri wa kustaafu kwa lazima kwa mtumishi ni miaka 60. Hata hivyo, suala la kuongeza umri wa kustaafu kwa watumishi wenye ulemavu litategemea mabadiliko ya sera na hasa kwa kuzingatia maoni ya wadau na ushauri mwingine utakaotolewa kulingana na uhalisia wa suala hilo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa upendeleo maalum wa ajira kwa watu wenye ulemavu katika Wizara, Taasisi zake na Mashirika yasiyo ya Kiserikali pale ambapo mtu mwenye ulemavu anakuwa na sifa stahiki za ajira wakati wa zoezi la ajira. Kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010, kifungu cha 31(2) kinaeleza wazi kwamba kila taasisi au sekta binafsi yenye watumishi wapatao 20 basi asilimia tatu wawe ni watu wenye ulemavu.
Aidha, kifungu cha 32 cha Sheria hii kinaeleza kuwa kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda ajira ya watu wenye ulemavu, kila mwajiri anatakiwa kufanya bidii ya kuendeleza ajira ya watu wenye ulemavu katika eneo lake la kazi. Serikali itaendelea na inaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria hii ili ajira za watu wenye ulemavu ziweze kupatikana kwa kuzingatia sheria na taratibu za ajira nchini.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA aliuliza:-
Katika miaka ya 60 na 90, Serikali yetu kwa ufadhili wa nchi rafiki kama Norway na Sweden ilijenga vyuo vya ufundi vilivyotoa mafunzo mbalimbali kwa watu wenye ulemavu hapa nchini kama vile Yombo - Dar es Salaam, Singida, Mtapika – Masasi, Masiwani – Tanga, Mbeya, Ruanzari – Tabora na Mwirongo-Mwanza; hivi sasa kati ya vyuo saba ni vyuo viwili tu vya Yombo na Singida ndiyo vinafanya kazi tena kwa kusuasua:-
(a) Je, ni sababu zipi zilizosababisha vyuo hivyo vitano vifungwe wakati kuna mahitaji makubwa ya watu wenye ulemavu kupata mafunzo ya ufundi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua haraka vyuo hivyo vilivyofungwa ili viendelee kutoa mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu?
(c) Ili kutoa fursa zaidi za mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu, je, Serikali ina mkakati gani wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye vyuo vyake vya VETA na FDC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Elly Marco Macha, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zilizosababisha vyuo hivi kufungwa ni pamoja na uchakavu wa majengo na miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu; upungufu wa watumishi ambapo baadhi yao wameshastaafu na wengine wamefariki.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu nchini wanapata mafunzo siyo tu ya ufundi, bali ya aina nyingine yatakayokidhi mahitaji ya ajira na kuondoa utegemezi kwa watu wenye ulemavu. Aidha, Serikali imewasilisha maombi maalum Hazina, kuomba fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo fedha hizo zitatumika kufanya ukarabati na kuboresha miundombinu ya vyuo mbalimbali nchini. Vilevile, Wizara imewasilisha ikama ya watumishi ili utaratibu wa kuajiri watumishi ufanyike mapema kuziba nafasi zilizo wazi.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika Vyuo vya VETA na FDC ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuwa na walimu wenye mbinu za kufundisha watu wenye ulemavu. Katika kozi ya ualimu MVTTC ipo moduli inayohusu mbinu za kufundisha watu wenye ulemavu.
(ii) Ukarabati wa miundombinu ya njia za kutembelea na ukarabati wa majengo ili kuwapa fursa watu wenye ulemavu kushiriki katika mafunzo ya ufundi pasipo kikwazo chochote.
(iii) Kuwashirikisha wakufunzi wenye ujuzi wa lugha ya alama kupitia Chuo cha Watu Wenye Ulemavu – Yombo katika kutoa mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu hasa katika kozi fupi fupi.