Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Elly Marko Macha (3 total)

MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja dogo la nyongeza, je, Waziri anaweza kulihakikishia Bunge hili kwamba katika hii bajeti ya 2016/2017, kutatengwa bajeti kwa ajili ya kuliwezesha Baraza la Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu kuanza kazi na programu zake kuwafikia watu wenye ulemavu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa uwakilishi wake mahiri na hasa katika kundi hili la walemavu katika nchi yetu ya Tanzania na swali lake ni swali lenye msingi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba pamoja na utungaji wa Sheria namba 9 ya mwaka 2010 ambayo imetoa maelekezo ya namna gani kundi hili muhimu katika nchi yetu ya Tanzania litaweza kuzingatiwa katika nyanja zote za maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Ofisi ya Waziri Mkuu inathamini na kuona umuhimu wa kundi hili maalum na hakika katika bajeti ya mwaka huu unaokuja wa fedha itazingatia kuona Baraza la Watu Wenye Ulemavu linatengewa fedha na linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria iliyotungwa, Sheria namba 9 ya mwaka 2010.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sikuridhika sana na jibu lililotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri hasa katika kipengele (a). Kwa ajili hiyo basi, naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni lini basi mchakato wa mabadiliko ya sheria utafanyika ili kuhakikisha kwamba sheria inawapigania watu wenye ulemavu kwa kuwaongezea umri wa kustaafu kwa kuwa umri wao wa kuanza shule unakua umechelewa ili waweze kupata nafasi ya kufanya kazi zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni mechanism gani ambayo Serikali imeweka katika kuhakikisha kwamba taasisi zake pamoja na sekta binafsi zinatenga asilimia tatu katika kila waajiriwa 20? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Elly Macha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la ni lini, lazima niseme kwamba siwezi nikatoa specific date kwa sababu ili kubadilisha umri wa kustaafu kuna watu wengine wanahusika kama waajiri, taasisi zinazohusiana na hifadhi za jamii na watu wenye ulemavu wenyewe. Tayari assignment ya kwanza kuifanya baada ya kushika nafasi hii ilikuwa ni kukutana na watu wenye ulemavu na moja ya mambo ambayo tulikubaliana ni kwamba walete maoni yao yote ambayo yatapelekea kubadilishwa kwa Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ili kuboresha baadhi ya mambo yakiwemo masuala yanayohusiana na ajira kwa watu wenye ulemavu kwa sababu tunaamini katika ile principle inayosema nothing for us without us ambayo ni muhimu sana kwa watu wenye ulemavu. Kwa sababu maoni yao yanafanyiwa kazi siwezi nikatangulia kabla ya kupata maoni yao kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu natambua kwamba wako baadhi ya watu wengine walianza kufanya hivyo mwaka 2003 nchini Kenya, umri wa kustaafu wakati huo ulikuwa ni miaka 55 kwa lazima kwa watu wenye ulemavu ilikuwa ni miaka 60 lakini mwaka 2009 ikabadilishwa. Serikali ya Kenya ilivyosema umri wa kustaafu kwa lazima ni miaka 60, mwaka 2013 ilipelekwa Bill ya kutaka kuongeza umri wa kustaafu kwa watumishi wenye ulemavu Kenya kufikia miaka 65 lakini mpaka navyozungumza Bill hii bado haijafanyiwa mabadiliko kutokana na sababu mbalimbali za kitaalamu zinazosababisha review ya sheria hiyo kuwa ngumu kidogo. Hata hivyo, hilo ni wazo zuri na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu mkakati uliowekwa, sheria imeonyesha wazi na tayari tumeshatoa maelekezo kwamba waajiri wote ni lazima watekeleze hili na Maafisa Kazi wanapokwenda kusimamia utekelezaji wa sheria baadhi ya mambo ambayo wanapaswa kuuliza ni utekelezwaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ikiwemo percentage na mambo mengine kama reasonable accommodation. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Elly Macha kwamba Serikali inafuatilia kwa makini usimamizi wa sheria hii kwa hiyo asiwe na wasiwasi wowote ule.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana ambayo ameyaweka mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulihakikishia Bunge lako kwamba wakati tunatunga sheria hii kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata haki sawa katika nchi yetu, kifungu cha 12(1)(a) cha sheria hiyo kinalipa nguvu na mamlaka Baraza hili la Watu Wenye Ulemavu kuangalia matatizo na mambo mengine yote ambayo yamekuwa yakiwakumba watu wenye ulemavu nchini na kutoa mapendekezo na kuishauri Serikali nini cha kufanya. Kwa sababu tumeendelea kutenga fedha za kulifanya Baraza hili liwe linakutana, ningeshauri sana tufanye kazi kwa karibu na Baraza na yale ambayo wanayaona ni mambo ambayo yanatakiwa yafanyiwe mabadiliko ya kisheria, ya kikanuni na vitu vingine, basi wanaweza kulitumia lile Baraza tukashauriana na Serikali na tukaona lini na namna gani tunaweza tuka-consider hayo mambo ambayo ni ya msingi sana katika kuweka welfare ya walemavu nchini.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kusema tu kwamba sikuridhika kabisa na nina hakika watu wenye ulemavu hawakuridhika kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ameyatoa. Ina maana kwamba kwa kutokuwa na miundombinu au kutokuwa na watumishi ni sababu ya kutosha ya kusababisha vyuo vifungwe kwa miaka mingi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atupe concrete sababu kwa nini vyuo vimefungwa na vitafunguliwa lini, atupatie time frame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa watumishi ambao anasema wanatayarishwa, tunahitaji muda gani kuwatayarisha hawa watumishi kwa sababu watu wenye ulemavu wamekuwepo na vyuo vimekuwepo miaka mingi lakini vimefungwa kwa miaka mingi na inaonekana kama ni business as usual but it is not business as usual. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kimsingi, pamoja na kufungwa kwa vyuo hivyo jambo ambalo tayari limeshatolewa ufafanuzi namna gani litafanyika, kupitia mfumo wa elimu jumuishi sasa hivi vyuo vyote vya ufundi ikiwemo VETA, FDC lakini hata shule zinazotoa mafunzo ya ufundi tunahakikisha kwamba tunazingatia namna tunavyoweka miundombinu na namna ya kufundisha kwamba watu wenye ulemavu wanazingatiwa. Hao nawazungumzia hasa wale vijana wenye umri wa kuweza kuingia katika vyuo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba, kwa hali ya sasa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini pia kupitia ngazi zetu za juu kama tulivyoona Ofisi ya Waziri Mkuu, tunahakikisha kwamba walemavu wanapewa kipaumbele cha hali ya juu na yeye atakuwa shahidi hata sasa tunapotoa kwa mfano karatasi zetu humu Bungeni au taarifa zozote lazima tuzi-print kwa nukta nundu na mambo mengine. Kwa hiyo, walemavu wanapewa fursa nyingi na tunawajali kupita kiasi katika kila ngazi. Naomba atuvumilie aone namna ambavyo tutaweza kuendelea katika kuhakikisha tunarekebisha hali ambazo zipo.