Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amina Saleh Athuman Mollel (48 total)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa watu wenye ulemavu na hasa wanafunzi, wengi wao wanatoka katika familia duni na changamoto ni nyingi:-
Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kutoa nafasi ya kipekee na ya upendeleo kwa watoto hawa wenye ulemavu, wale wanaobahatika kwenda Kidato cha Tano na cha Sita ili waweze basi kusoma bure kama walivyosoma katika elimu ya Shule ya Msingi na Sekondari?
Swali la pili, pia baadhi ya wazazi, walezi na hasa katika baadhi ya jamii zetu, huwatenga na kuwaficha watoto wenye ulemavu kwa kuwaona kuwa ni mkosi na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu:-
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya wazazi au walezi wenye tabia hizi wanaokosesha watoto kupata elimu kwa sababu tu ya ulemavu walionao? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba ni jukumu la jamii kwa ujumla kwa maana ya Serikali, wananchi wote na wadau, wakiwemo wazazi na walezi wa watoto na mamlaka zao za Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata nafasi ya kipekee ili waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika utaratibu wa sasa, tumeamua kufanya kazi hiyo kwa kusaidia wale wanaoanza kuanzia chekechea, Shule ya Msingi naKkidato cha Kwanza hadi cha Nne. Kwa Kidato cha Tano na cha Sita, utaratibu huu mara nyingi tunatambua huwa unafanywa chini ya Wakuu wa Wilaya ambao hushirikiana na Halmashauri katika kuwabaini wale ambao hawana uwezo na kuweka utaratibu wa kuwasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tufahamu kwamba unapozungumzia dhana ya D by D ni pamoja na kubeba majukumu kama haya ambayo hayana utaratibu wa moja kwa moja wa kimfumo wa kibajeti. Pale kwenye Halmashauri, Mkurugenzi kazi yake siyo tu kuangalia mambo ya jumla ya kila siku ambayo yanafanywa kwa maana ya Idara zile, lakini pia kwenda zaidi na kuona jukumu lla kubeba jamii yote kwa ujumla, wakiwepo hawa wenye ulemavu na watu wengine wenye mahitaji maalumu kuhakikisha kwamba na wao wanapata haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivi, Mkurugenzi huyu anashauriwa na Baraza la Madiwani ambalo lipo kwa ajili la uwakilishi wa wananchi kama hawa. Kwa hiyo, nina hakika hili jambo limekuwa likifanykia na hawa wanafunzi wanaohitaji nafasi ya kupata elimu kwa sababu ya mahitaji maalum na wale tu wasiokuwa na uwezo hata kama siyo walemavu wamekuwa wakisaidiwa na mamlaka hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwamba kumekuwepo na tabia ya baadhi ya jamii kuwatenga watu wenye ulemavu wasipate haki zao za msingi; tulipotunga sheria mwaka 2010, katika kifungu cha 28 cha sheria ya watu wenye ulemavu, tumezungumzia juu ya haki mbalimbali, lakini pia tumeridhia itifaki mbalimbali za Kimataifa juu ya haki mbalimbali za watu wenye ulemavu.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Vilevile, naipongeza Serikali kwa jitihada za kutatua matatizo hasa changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Lugha ya alama ni changamoto kwa watoto viziwi ambao wengi wao huishia elimu ya sekondari na kushindwa kuendelea na elimu ya juu kutokana na Wahadhiri wengi kutokujua lugha ya alama. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa wa kuingiza lugha ya alama katika shule za msingi, sekondari na katika Vyuo vya Ualimu hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni Vyuo vingi hasa vyuo binafsi, mazingira yake sio rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwepo mwongozo utakaoviongoza vyuo vyote kuzingatia mahitaji na hasa miundombinu kuwa rafiki kuwatimizia majukumu yao hasa watoto hawa wenye ulemavu ili waweze kusoma vizuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kabisa lipo hilo tatizo, kutokana na kwamba kama inavyojulikana kwa muda hawa watu wenye ulemavu wamejikuta hawapati elimu za aina mbalimbali kutokana na mahitaji yao. Sasa hivi Wizara inachofanya, kwanza imetambua hayo mahitaji maalum ya aina mbalimbali na kupitia bajeti hii, tumeshatenga fedha kwa ajili ya kuandaa mitaala kwa ajili ya kutoa mafunzo maalum kwa ajili ya Walimu pamoja na wanafunzi wenyewe katika shule husika, vile vile, kwa ajili ya kununua vifaa ambavyo vitatumika katika kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, juu ya miundombinu rafiki, niseme tu kwamba, hilo suala limekuwa likijitokeza. Ninayo mifano mingi ambayo nimeishuhudia mwenyewe kwamba, watu wanapojenga shule au taasisi maalum, wanasahau kabisa kwamba kuna siku wanaweza wakawa na mwanafunzi ambaye ni mlemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta hata mtu anapojenga iwe ni ghorofa, iwe ni choo, haangalii kama atakuja mwanafunzi mwenye wheel chair, atafika vipi huko au angalau kuwashusha wale wanafunzi badala ya kusoma ghorofani waweze kusoma katika madarasa ya chini ili nao waweze kupata hiyo fursa. Kwa hiyo nitoe wito, tujue kwamba, ulemavu siyo jambo la kujitakia bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu katika kuonesha kazi za uumbaji wake. Ni vyema tuwafikirie na kuwajali watu wenye ulemavu.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na kwa kuwa natoka pia katika Mkoa wa Arusha, pamoja na Mkoa huu wa Arusha kuwa na vyanzo vingi vya maji, vinavyotoka katika Mlima Meru, lakini maji haya yameonekana kuwa na madini ya fluoride na madini haya ya fluoride siyo mazuri sana. Je, Serikali inafanya jitihada gani, kuhakikisha kwamba inapunguza madini haya ya fluoride?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mji wa Arusha katika vile visima ambavyo vinatumika kutoa maji katika Mji wa Arusha, kuna visima ambavyo vimeonekana vina kiwango kikubwa cha maji ya fluoride na visima hivyo viko Mianzini viko viwili. Tulipunguza kiwango cha utoaji maji katika hivyo visima na tukachimba visima vingine viwili ili ku-balance ile fluoride isiwe kwa kiwango kikubwa; ni kwamba fluoride inatakiwa katika mwili wa binadamu lakini kiwango kisiwe juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo suala tayari tumeshalifanyia kazi kwa ku-balance, fluoride yake siyo nyingi sana kiasi ambacho ukiichanganya na maji mengine, basi inaingia katika viwango vile vinavyokubalika. Pia naomba kumweleza Mheshimiwa Mbunge Mollel ni kwamba sasa hivi Arusha tuna mradi mkubwa, tunatarajia kuchimba visima 30 ili kuhakikisha kwamba kiwango cha maji katika Mji wa Arusha baada ya miaka miwili kukamilisha huo mradi, ambao tumepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na financial agreement imeshasainiwa, tatizo la maji tutakuwa tumelimaliza kabisa katika Mji wa Arusha.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la afya au linalohusiana na zahanati kwa ujumla linagusa maeneo mengi katika nchi hii ya Tanzania. Mojawapo ni Zahanati ya Nduruma iliyopo katika Kata ya Nduruma, Wilaya ya Arumeru. Zahanati hii imepandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya lakini hakuna jengo la upasuaji, hakuna vifaa na inahudumia vijiji karibia kumi. Je, Waziri anatuambia nini kuhusiana na kituo hiki cha afya ambacho hakina vifaa na wananchi wanalazimika kwenda Hospitali ya Mount Meru iliyoko mkoani Arusha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Mollel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki moja iliyopita Mheshimiwa Amina Mollel aliniambia kuhusu zahanati hiyo ambayo imepandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya na mimi nilimpa ahadi kwamba tutafanya kila liwezekanalo, huenda kabla Bunge hili halijaisha tutafika pale Arusha kuangalia zahanati hii. Pia ameniambia mambo mengine zaidi kwamba wataalam wengine wameondoka na zahanati ile haifanyi kazi. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza safari yetu itakuwa palepale mimi na yeye, tutaenda pale Nduruma kuona changamoto za zahanati ile kwa karibu zaidi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wale kutoka pale kwenda Mount Meru na Arusha ni jiji linalokuwa na population inaongezeka. Ni lazima maeneo ya pembeni tuyaimarishe ili kupunguza ile referral system kwamba siyo kila mtu ugonjwa mdogo aende katika Hospitali ya Wilaya. Serikali kupitia TAMISEMI na tutakapokwenda pamoja tutahakikisha ule upungufu tunaubaini na kupanga mpango mkakati wa jinsi gani tutafanya ili kituo hiki cha afya kiwe na vifaa tiba na wataalam kiweze kutoa huduma katika maeneo hayo na kata zinazokizunguka.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kutokana na mwamko ambao umejitokeza hivi sasa kwa watoto wengi kuhudhuria shule kutokana na elimu bure, lakini vilevile kumekuwepo na changamoto mbalimbali yakiwemo pia malalamiko kutoka kwa wananchi.
Je, Serikali inajipanga vipi kuhakikisha kwamba changamato hizi inaziondoa ili watoto wote waweze kupata elimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, watoto wenye mahitaji maalum bado wao wanakabiliwa na changamoto nyingi; je, Serikali ili kuendana na kasi hii, inajipangaje kuhakikisha watoto wenye ulemavu ambao jamii imekuwa ikiwaficha na wao pia wanapata nafasi ya kupata elimu bure na kuifurahia nchi yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu ya kwanza ni changamoto zinazozikabili shule zetu. Ni kweli mara baada ya mchakato wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano, ilipojielekeza kwamba elimu kuanzia shule ya awali mpaka form four kuwa ya bure, tumegundua kuna mambo mengi sana yamejitokeza.
Jambo la kwanza ni kitendo cha watoto wengi waliokuwa wakibaki mitaani kwa kukosa fursa ya kujiunga na shule, hivi sasa wanaende shule. Baada ya hilo kilichotokea ni kwamba tumekuwa na tatizo kubwa la upungufu wa madawati na mambo mbalimbali. Katika hili ndiyo maana Waziri wangu wa Nchi sambamba na Waziri Mkuu walitoa maelekezo kwamba ikifika 30 Juni, madawati yote yawe yameweza kupatikana maeneo ili kuondoa changamoto ya watoto wanaokaa chini. Hata hivyo, Serikali imejielekeza kuhakikisha kwamba tunajitahidi katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo madarasa lengo likiwa watoto wote wanaofika shuleni waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna swali la pili linalohusu watoto wenye ulemavu. Ni kweli mimi mwenyewe nikiri kwamba nimetembelea shule kadhaa za watoto wenye ulemavu, kule Mufindi hali kadhalika pale Dar es Salaam, maeneo hayo nilioyatembelea ni kweli watoto hao wana changamoto mbalimbali, lakini nimeweza kutoa maelekezo mbalimbali kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, wahakikishe kwanza watoto hao wenye ulemavu wanapewa kipaumbele. Ndiyo maana katika bajeti yetu ya TAMISEMI mwaka huu tumejielekeza wazi jinsi gani tumejipanga katika suala zima la watu wenye ulemavu ili kwamba watoto wote wanaoenda shuleni kutokana na hali zao wote waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Amina Mollel, najua kwamba wewe ni mwakilishi halisi na makini sana wa walemavu, tutahakikisha ombi lako hili linafanyiwa kazi katika Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa nguvu zote.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa zoezi hili limeleta malalamiko na kwa kuwa baadhi ya waliochangia utaratibu huu kwenda vibaya na kuandikisha kaya ambazo hazikustahili kupata mgao huu wa TASAF; je, Serikali inawachukulia hatua gani watumishi ambao wamefanya makosa haya na kuwakosesha haki yao ya msingi wale waliostahili kupata mgawanyo huu wa TASAF?
Swali la pili, kwa kuwa baadhi ya walionufaika wanadai kwamba kiasi hiki ni kidogo; je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuongeza kiasi cha fedha ili kiwanufaishe walengwa? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutambua kwamba kumetokea udanganyifu kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na kwamba takribani kaya 25,446 ni zile ambazo hazikuwa zinakidhi vigezo vilivyoelezwa vya kiwango cha umaskini, lakini wakawekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumechukua hatua mbalimbali za kinidhamu hasa kwa watumishi wale ambao ni wa Halmashauri, kwa sababu kwa kiasi kikubwa zoezi hili linafanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara hii na Wizara ya TAMISEMI kwa maana ya watumishi wa Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa wale viongozi wa kuchaguliwa, tutaona hatua nzuri zinazofaa kwao, kwa sababu udanganyifu huu umefanywa mahali pengine ni kwa makusudi na mahali pengine siyo kwa makusudi, ni kwa kukosa vielelezo vya kutosha juu ya hao wanaotakiwa kunufaika na utaratibu huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kiasi hiki anachodai Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kidogo na je, hatuoni haja ya kuongeza? Msingi wa kiwango hiki ni kwamba lengo letu ni kuzisaidia, not permanently kaya hizi maskini ili ziweze ku-gain mahali ambapo sasa zinaweza zikajiendesha zenyewe. Vigezo vinavyotumika kama nilivyosema, kwanza kabisa unaangalia kama familia hiyo ina watoto, lakini cha pili, ni kwamba je, hata kama ina watoto je, watoto hao wanaenda shule au wanaenda kliniki?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika mpango huu, baadhi ya maeneo wameamua kuzisaidia hizi familia kuwalipia CHF yaani Mfuko wa Afya ya Jamii ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu. Hili tunalitia moyo sana, kwa sababu moja kati ya vitu vinavyoumiza familia masikini ni kutokupata matibabu stahiki. Sasa hili la shule na lishe ni jambo ambalo tumeweka kama vigezo. Sasa kama haya nia yake ni kuikuza familia itoke pale na ifike mahali ambapo itajitegemea, ikiwa ni pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi, basi fedha hizi kwa kiwango tulichopanga, tumezingatia hali ya kutosha kwake na hivyo watajenga uwezo kidogo kidogo na baadaye wataweza kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito tu kwa watu wanaonufaika na mpango huu kuwa na dhamira ya kujenga kujitegemea na siyo kuendelea kusaidiwa ili baada ya programu hii kuisha, wawe wameshajenga huo uwezo.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba zipo shule za ufundi ambazo zipo katika majengo ya shule za msingi na shule za sekondari ambazo zilikuwa zikijulikana kama shule za ufundi na sekondari. Shule hizi katika miaka ya nyuma zilikuwa maarufu sana, lakini katika miaka ya hivi karibuni shule hizi umaarufu wake umepungua. Je, Serikali haioni kuwa ni wakati sasa wa kuboresha shule hizi na vyuo vya ufundi hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda na ili kuwapata vijana wenye ujuzi kukabiliana na ajira zitakazokuwepo katika viwanda hivyo tunavyovitarajia na kwa kuwa vyuo vingi vya watu wenye ulemavu vilisaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa mafunzo watu wenye ulemavu na katika makundi hayo ya ajira tunatarajia pia kwamba kundi la watu wenye ulemavu nao pia watakuwemo katika uchumi huu wa viwanda na biashara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vyuo vya ufundi mfano kama Chuo cha Yombo Dovya na vyuo vingine ili watu wenye ulemavu waweze kujiandaa kukabiliana na ajira tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. La kwanza, ni kweli kwamba kumekuwa na upungufu kidogo katika baadhi ya shule zetu hasa shule za ufundi zikiwemo zile ambazo zimekuwa ni za ufundi primary pamoja na ufundi sekondari. Sisi kama Wizara suala hilo tulishaliona na kupitia bajeti yetu ya mwaka 2016/2017, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha shule zote za ufundi zile za zamani ambazo ni pamoja na Mtwara, Iyunga, Ifunda, Moshi, Bwiru na Musoma, nadhani nimezitaja zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo tunategemea kwamba baada ya hapo na ukarabati utakaoendelea pamoja na kuweka vifaa itasaidia kuboresha. Pia tunazipitia hata zile shule za msingi ambazo zimekuwa zikitoa mafunzo ya ufundi hasa kwa vijana wanaomaliza darasa la saba ili pia waweze kupata stadi ambazo zitawasaidia katika kumudu maisha yao. Kwa hiyo, naamini kwa bajeti ya mwaka huu, kuna marekebisho mengi ambayo yatafanyika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili katika suala linalohusu watu wenye ulemavu, ni kweli ulemavu siyo maana yake kushindwa kufanya kila kitu. Mimi binafsi nilishawahi kutembelea Shule ya Yombo na nikajionea matatizo wakati huo bado sijawa Naibu Waziri. Kimsingi Waziri wangu pia yuko katika msukumo mkubwa sana kuhusiana na shule za ufundi hasa zinazowahusu watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichoamua kukifanya katika Wizara kupitia bajeti yetu ni kuona kwanza mitaala inaboreshwa kuona inakidhi kufundisha watu wenye ulemavu na kuweza kuelewa yale wanayofundishwa kwa kutumia lugha inayoendana na hali yao, lakini vilevile vifaa saidizi vinavyoendana na hali yao. Pia kuhakikisha kwamba tunaweka vifaa ambavyo vitahusika katika mafunzo. Kwa hiyo, kwa kuwa sisi wenyewe pia ni wadau wa watu wenye ulemavu naamini kuna mambo mengi yataboreshwa katika eneo hilo.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru pia kwa majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika Wizara husika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kutokuwepo kwa takwimu sahihi hasa maeneo ya vijijini kumesababisha kutokuwepo na mipango mahsusi yenye kuleta maendeleo na tija kwa watu wenye ulemavu. Je, Serikali ina mpango gani wa kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu zitakazosaidia kuwepo kwa mipango mahsusi itakayowasaidia watu wenye ulemavu hasa maeneo haya ya vijijini?
Swali la pili, uwepo wa Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, pamoja na uwepo wa sheria ambayo Naibu Waziri ameitaja Sheria Namba 9 ya huduma kwa watu wenye ulemavu zimesaidiaje kutatua matatizo ya walemavu na Waziri haoni kwamba mfuko wa watu wenye ulemavu ambao ungesimamia Baraza la Watu Wenye Ulemavu kutokutengewa pesa kutasababisha jitihada na mafanikio kwa watu wenye ulemavu yasiwepo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake, lakini kwa namna ambavyo amekuwa akitetea na kutushauri hasa katika mambo yanayohusu watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lililoulizwa hapa ni Serikali ina mpango gani kupata takwimu halisi za watu wenye ulemavu. Serikali tayari imekwishaanza mchakato na wameshazindua utaratibu wa kuanzisha kanzidata ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi ya watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya mijini na vijijini. Lengo kubwa la kanzidata hii itatusaidia pia kuwatambua watu wenye mahitaji hasa watu wenye ulemavu katika maeneo ya vijijini na kushirikiana na Kamati zile ambazo zimeundwa kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa mpaka Halmashauri ili iwe rahisi kuweza kuwatambua na pia iwe rahisi kuweza kuwasaidia katika kutatua changamoto zao mbalimbali ambazo zinawakabili.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili ameuliza Sera na Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 imesaidiaje kutatua changamoto na kero ambazo zinawakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikiri kwamba uweo wa sheria hii kwanza kabisa imetengeneza msingi na imetengeneza haki za walemavu na sasa sheria hii imekuwa ndiyo sehemu nzuri na platform ya kuweza kusaidia Serikali katika kutimiza matakwa yake mbalimbali ya kusaidia watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika Sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 imezungumza moja ya jambo ambalo Serikali imeshaanza kulifanyia kazi hivi sasa, changamoto kubwa sana ya watu wenye ulemavu ilikuwa ni upatikanaji wa vifaa vyao ambavyo gharama imekuwa kubwa hasa kutokana na kodi ambayo imekuwa ikitozwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia katika hotuba ya Waziri wa Fedha ambayo aliwasilisha hapa Bungeni Hotuba Kuu ya Serikali ukurasa wa 50, Mheshimiwa Waziri ameainisha bayana kabisa kwamba Serikali sasa inaandaa utaratibu wa kuondoa kodi na kuweka msamaha wa ushuru katika vifaa vyote ambavyo vinawahusu watu walemavu lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba huduma hizi zinawafikia kiurahisi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika sheria yetu, Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ukiangalia kifungu namba 30 mpaka kifungu namba 34 kimezungumza wazi namna ambavyo watu wenye ulemavu na wenyewe wanapaswa kupata fursa za ajira katika taasisi za umma na taasisi binafsi. Kwa hiyo, naamini kabisa uwepo wa sheria na sera imechangia sana katika maendeleo ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa ajali nyingi zinasababishwa na baadhi ya madereva walio wazembe na mfano mzuri ni katika Jiji la Dar es Salaam katika utaratibu mpya ulioanzishwa kwa jitihada za Serikali wa mabasi yaendayo kasi; hadi sasa zaidi ya mabasi 30 yamepata ajali na gharama za matengenezo hayo ni zaidi ya shilingi milioni 90. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhakikisha kwamba kama ni sheria, zinawabana madereva wazembe wanaoisababishia Serikali hasara? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba baadhi ya madereva wakiwemo madereva wa pikipiki, bodaboda na magari binafsi na hata magari mengine tu kwa ujumla, bado sharti na sheria inayotaka wasitumie barabara ya mabasi yaendayo kasi inakuwa ngumu sana kwao na hivyo kusababisha ajali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba barabara ile ni kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi na siyo vinginevyo. Kwa hiyo, mtumiaji mwingine yeyote anayetumia barabara zile anakuwa amevunja sheria na hivyo, yeye ndiye amegonga yale mabasi na kusababishia hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli takwimu zinaonesha kwamba ajali ni nyingi, na sisi tunasema tutaendelea kusimamia sheria ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu, lakini pia watambue kwamba kwa kufanya hivyo wanafanya makosa makubwa na kusababisha hasara. Hawaruhusiwi kutumia barabara za mabasi yaendayo kasi zinazotumika sasa kwa Dar es Salaam.
Kwa hiyo, nawaomba sana wakazi na watumiaji wa barabara Dar es Salaam, kuheshimu barabara za mabasi yaendayo kasi ili kuipunguzia Serikali hasara zinazojitokeza.
MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Mkoa wa Arusha kwenda Chuo cha Mandela na hatimaye katika Vijiji vya Mlangarini, Nduruma na mpaka Bwawani Lusi ni barabara ambayo kwa muda mrefu imekuwa na kero. Tangu enzi za Elisa Molell akiwa Mbunge, Hatimaye Goodlucky Ole-Medeye mpaka sasa barabara hii kilio chake bado hakijasikikika. Je, Waziri anawaeleza nini wakazi wa vijiji hivi vya Mlangarini, Nduruma, Bwawani pamoja na Lusi kwamba barabara hii wataifikiria na kuweza kuijenga katika kiwango cha lami na hasa ukizingatia Chuo hiki cha Nelson Mandela ni Chuo cha Kimataifa na kinatarajiwa kupokea wanafunzi wengi kutoka nchi mbalimbali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kwamba tumesikia kilio cha Mheshimiwa Amina Molell na Chama cha Mapinduzi kwa utaratibu wake, Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo tumefanya intervention kubwa sana katika mradi wetu wa CSP Project ambao unafadhiliwa na World Bank. Sasa hivi Mji wa Arusha, Mbeya na baadhi ya miji, tumefanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii anayoizungumza Mheshimiwa Amina Molell, naomba niseme kwamba tumeisikia kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kwa kuwa pale kuna chuo kikubwa sana na vile vile hii ni ahadi yetu kwa wananchi hawa na lengo ni kuhakikisha lazima tunawahudumia. Serikali imesikia kilio hicho.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu haya yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kike wanahitaji faragha na hasa wanapokuwa katika siku zao. Kwa hali hii iliyopo hivi sasa ni tatizo kubwa kwa watoto wa kike. Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura kuhakikisha kwamba angalau tunawapatia unafuu watoto wa kike na hasa ukizingatia kwamba shule nyingi pia hazina maji kwa mtoto huyu wa kike inakuwa ni vigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je uwiano huu wa 52 kwa 54 na 23 kwa 25 kwa shule za sekondari umezingatia kwa kiasi gani hali ya watoto wenye mahitaji maalum, watoto wenye ulemavu ambao wanalazimika kutambaa katika kinyesi cha watoto wenzao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwa sababu ni changamoto kweli hasa watoto wetu wa kike kuna wakati fulani wanataka faragha ya hali ya juu kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki na hili ndiyo maana nimesema kwamba katika yale matundu ambayo tunayajenga 8,991 kwa shule za msingi na yale 1942 kwa shule za Sekondari kipaumbele ni matundu ya vyoo vya kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna mradi wa MMES II ambao katika shule za sekondari tunajenga takriban matundu yasiyopungua 9,345. Katika haya maelekezo yetu ni kuhakikisha hasa katika shule za sekondari tunaweka nguvu kubwa tuweze kuondoa kabisa tatizo hasa la vyoo vya kike, kwa kujua kwamba, hili jambo ni muhimu sana kwa ajili ya utulivu wa watoto wetu hasa wa kike wanapokuwa katika yale mazingira ambapo hakuna namna lazima wapate mazingira yenye staha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika suala la walemavu ni kweli, katika kipindi cha nyuma kilichopita kwa muda mrefu tulikuwa hatuna kipaumbele cha kutosha katika ujenzi wa miundombinu yetu hasa katika maeneo ya walemavu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Amina Molel, katika vyoo vyetu vya sasa vyote vinavyojengwa suala la vyoo kwa watu wenye mahitaji maalum ni kipaumbele chetu cha msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika maeneo mbalimbali tunakopita na jana nilikuwa katika shule moja ya Chang‟ombe „B‟, tunaenda kujenga karibuni vyoo 20 lakini kipaumbele tumesema katika ujenzi ule ramani zote zinaelekeza watu wenye mahitaji maalum hasa walemavu ili kuhakikisha ujenzi wote unaofanyika sasa hivi uweze kuligusa kundi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Amina Molel nimhakikishie kundi ambalo analiwakilisha vema humu Bungeni, tutahakikisha tunalipa nguvu ya kutosha na kuhakikisha kwamba haki zao zinapatikana kwa muda wote katika kipindi cha utawala huu.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto katika suala zima la elimu na hasa elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu ni kutokana na uhaba wa walimu katika vyuo mbalimbali hasa vyuo vikuu hapa nchini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba katika vyuo vyote vikuu hapa nchini vinakuwa na programu mahsusi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha walimu watakaokwenda kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu hapa nchini ili tuondokane na tatizo hili la uhaba wa walimu pamoja na kuhakikisha kwamba ajira zinakuwepo kwa watu wenye ulemavu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ili kufanikisha hilo, kwa mfano ukiangalia katika utoaji wa mikopo safari hii watu wenye ulemavu wote kwa ujumla wake bila kujali fani anayochukua wamepewa mikopo. Pili, tunacho chuo maalum, Chuo cha Patandi - Arusha ambacho ni kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa walimu ambao wanaenda kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu. Hali kadhalika, kwa upande wa vyuo vikuu tunayo maeneo ambayo yanahusika katika kuzingatia ufundishaji wa walimu kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake niseme tu kwamba eneo hili ni pana sana kwa sababu linahitaji walimu wa aina tofauti tofauti kwa ajili ya kufundisha watu wenye ulemavu wa aina tofauti tofauti. Kwa hiyo, ukiwachukua kwa ujumla wake useme kwamba walimu wenye ulemavu labda 200 ukafikiria ni wengi, hawatakuwa wengi kwa sababu mahitaji ya wale wanaoenda kuwafundisha inakuwa wanafunzi ni wachache katika eneo fulani lakini yale maeneo ni mengi sana. Kwa hiyo, juzi tu mimi mwenyewe nimefuatilia pale Patandi na kuona ni jinsi gani tutaweza kurekebisha hasa miundombinu na kuwawezesha walimu wengi zaidi. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona, na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu (UNCRPD), na mkataba ule unazitaka nchi zilizoridhia mkataba huo kutekeleza, kutatua na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Mfuko wa Watu wenye Ulemavu haukutengewa kabisa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anatueleza nini kuhusiana na mfuko huu ambao haukutengewa fedha zozote na kwa sababu hakuna fedha, inazokwamisha pia hili Baraza la Watu wenye Ulemavu kushindwa kutimiza wajibu wake. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Sera ya Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004, vilevile na United
Nations Conventions of Rights of People with Disabilities na yenyewe imesema namna ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hasa katika kundi hili la walemavu katika kuwasaidia kuboresha maisha yao na shughuli zao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hapo katikati hakukuwepo na fedha za kutosha katika mfuko huu kuwezesha kufanya shughuli zake. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, ya kwamba kwa sasa katika bajeti inayokuja ya mwaka 2017/2018, tumeona umuhimu huo na tumeshaanza kuandaa mapendekezo ya kupeleka katika bajeti yetu hiyo ili sasa mfuko huu uwezeshwe na uweze kukidhi mahitaji na utekelezaji wa mfuko huu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuondoe tu hofu ya kwamba tunafahamu changamoto hiyo ya fedha lakini tumejiandaa this time tuitengee fedha ili iweze kufanya kazi yake kikamilifu.
MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Katika vyuo vikuu suala la miundombinu kwa watu wenye ulemavu ni tatizo, na mfano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni moja ya changamoto inayochangia wanafunzi wengi hasa watoto wa kike katika kwenda madarasani na hata katika suala zima la mitihani ni tatizo kwao kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo. Je, Serikali inatoa kauli gani na hasa kwa kuzingatia chuo hiki ni kikongwe, lakini mpaka leo miundombinu bado ni tatizo na ni kikwazo kwa watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa mujibu wa sera kwa ajili ya watu wenye ulemavu, inazungumzia kuwawekea mazingira bora ya kujifunzia na kufundishiwa. Kwa hali ya sasa ni kwamba tunayo majengo ambayo yamejengwa zamani na unakuta kweli yana changamoto ya miundombinu, lakini tunachofanya ni kwamba tunashauri madarasa yale yenye wanafunzi wenye ulemavu wahakikishe yanakuwa ni yale yanayofikika, kwa mfano kama darasa lina mwanafunzi mwenye ulemavu ni vyema likachaguliwa lile ambalo liko katika ground floor ili mwanafunzi yule aweze kufika darasani bila usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majengo yote mapya yanayojengwa tumeagiza kwamba lazima kila jengo liwekewe miundombinu inayomuwezesha mtu mwenye ulemavu kufikia katika eneo lolote analohitaji kuishi au kujifunzia na hivyo imekuwa ikifanyika na ni rai yangu kusema kwamba hata hiyo miundombinu inayowekwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu iwe ni ile inayozingatia viwango vinavyohusika, kwa sabau sasa hivi unakuta kwamba kuna shule zinapokaguliwa ili zionyeshe miundombinu yenye ulemavu zinaweza zikaonesha tu kwamba kuna lile tuta (rump) limewekwa pale lakini unakuta jinsi ambavyo limewekwa lina msimamo mkubwa kiasi kwamba hata huyo mtu mwenye ulemavu anapata shida, kwa hiyo lazima kuzingatia viwango vinavyohusika katika kuweka miundombinu ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuweka lifti. ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa majengo haya ya Arusha International Conference Center (AICC) yalikuwa yakitumiwa na Mahakama ya Kimataifa (ICTR) na kwa hivi sasa Mahakama hii ina majengo yake na imehama katika majengo haya ya AICC. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba heshima iliyokuwepo kwa majengo haya inaendelea kuwepo kwasababu hivi sasa wapangaji wakubwa hao wamekwishahama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel kwa swali lake la nyongeza kwamba Serikali tutahakikisha majengo haya yanasimamiwa vizuri na kuhakikisha hayaharibiki. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama jana Mheshimiwa Amina Mollel ulisikiliza vizuri kwenye taarifa ya Kamati ya Uwekezaji ya Mashirika ya Umma jana kituo kinafanya kila inachoweza kuhakikisha kinapata watu ambao wanaweza kuja kupanga katika ofisi zile na sisi kama Wizara tutahakikisha tunafuatilia hilo ili kuhakikisha majengo hayaharibiki na yanabaki katika kiwango kinachotakiwa.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru na nashukuru pia kwa majibu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa majibu ya
Mheshimiwa Waziri ni kwamba Serikali iko mbioni kufanya marekebisho ya sheria hii. Napenda kufahamu ni lini sasa Serikali itafanya marekebisho haya na kutenga eneo mahsusi
kwa ajili ya wakazi wanaoishi katika eneo hili la Bonde la Ngorongoro ili waweze kujihusisha na kilimo kwa sababu sio mazao yote yanayoharibu mazingira?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa
ukosefu wa maji kwa mifugo hususan msongamano ndani ya eneo dogo na kuharibu mazingira na kwa kuwa hifadhi hii bado ina maeneo ambayo yanaweza kutengwa kwa ajili
ya mifugo iweze kupata maji na Mheshimiwa Waziri Mkuu alishaiagiza Wizara hii kuhakikisha kwamba inatenga maeneo hayo ili wafugaji waweze kupata maeneo hayo kwa ajili ya
kunyweshea mifugo yao. Je, ni lini Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaweka maeneo haya maji na wananchi wanaoishi katika Bonde hili la Hifadhi ya Ngorongoro waweze kunywesha mifugo yao katika maeneo hayo na siyo kwenda kuharibu mazingira kama ambavyo sasa wanavyodaiwa
kufanya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anataka kujua ni lini mabadiliko ya sheria kama ambavyo tumejibu katika swali la msingi yanafanyika? Mchakato wa mabadiliko ya sheria
unatanguliwa na shughuli kadhaa za kitaalam ambapo kutokana na shughuli hizo za kitaalam ndipo mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yanapelekwa katika hatua mbalimbali za Serikali ili hatimaye mabadiliko ya sheria yale yaweze kuwa na tija kwa sababu yatakuwa yana-input ya kitalaam.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, katika
kipindi cha wiki moja kikosi maalum cha watu wanaotakiwa kufanya sensa kama jambo la kwanza kabisa la kulifanya ili kujua ukweli wa hali halisi ya Ngorongoro kitaanza kazi. Kazi ambayo itafanyika kwa muda wiki moja. Hii inatokana na ukweli kwamba mwaka 1959 wakati Ngorongoro inatengwa kama eneo la hifadhi kulikuwa na jumla ya wakazi 8000 ndani ya eneo lile. Kufikia mwaka 2013 tayari kulikuwa na wakazi jumla ya 87,851, hii ni takribani wastani wa ongezeko la wakazi 1500 kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, changamoto hii ni
kubwa na hivyo hata mabadiliko ya sheria yanatakiwayaangalie uhalisia ambao utakuwa ni uhalisia wa kisayansi. Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, ndani ya kipindi cha mwaka wa fedha ujao tutakuwa tumeanza na kukamilisha utaratibu wa mabadiliko ya sheria
inayohusika.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili
anazungumzia juu ya suala la ukosefu wa maji na ambalo lina maagizo mahsusi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ni kweli, kulikuwa na maagizo ambayo yalikuwa yanataka kutatua changamoto ya maji katika kipindi cha mpito wakati ambapo tunasubiri mabadiliko yale ya sheria ambayo yataweka misingi ambayo itakuwa ni ya kudumu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mpito suala la maji kwa ajili ya mifugo linashughulikiwa kwa kujenga mabwawa katika maeneo ambayo yanaonekana kwamba uwepo wa mabwawa katika maeneo hayo utatatua changamoto ya mahitaji ya maji kwa mifugo. Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro imetenga fedha katika bajeti hii na Waheshimiwa Wabunge mkiipitisha, basi tunaweza kutatua tatizo hili kwa namna ambayo itakuwa ni toshelezi. Kwa hiyo,
namuomba Mheshimiwa Mbunge afanye subira, asubiri Bajeti ya Serikali, bajeti ya Wizara hii itakapopita, hasa kwa upande ule wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro tutakuwa tumeweza kuweka tengeo la kuweza kutekeleza agizo
la Mheshimiwa Waziri Mkuu ipasavyo.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa matatizo makubwa yanayowakabili watu wenye ulemavu hasa waishio vijijini ni umaskini uliokithiri kwa jamii hii. Mbali ya Serikali kutoa maagizo kwa
Halmashauri kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri.
Je, Serikali sasa ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inapunguza umaskini kwa kundi hili la watu wenye ulemavu ambalo liko nyuma?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, sababu kubwa kama nilivyoeleza inayopelekea watu wenye ulemavu kuwa na maisha duni ni pamoja na kutozingatiwa kwa mahitaji yao wanayoyapendekeza katika ngazi mbalimbali wakati wa bajeti.
Pamoja na hizo sababu mambo hayo yanapuuzwa, kwa kuwa bajeti ya Serikali bado kusomwa; je, Serikali haioni muhimu sasa wa kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu ambao katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu haukutengewa hata shilingi, sasa tuangalie ni kwa jinsi gani
basi tutatenga fedha ili tuweze kusaidia kundi hili? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 inazitaka Mamlaka za Mikoa kusimamia uanzishaji wa Kamati za Walemavu kwenye Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji na tulishaagiza kama alivyosema kwenye jibu la msingi Naibu Waziri Mheshimiwa Mavunde, lakini nichukue nafasi hii sasa kutaka nitoe agizo kwa Wakuu wa Mikoa wote kuhakikisha kwamba Kamati hizi sasa tuwape deadline ndani ya miezi mitatu kuanzia siku ya leo ziundwe hizi Kamati, Wakuu wa Mikoa wahakikishe Kamati hizi zinaundwa katika Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji na zaidi ya hapo tutachukua hatua kwa sababu maagizo mengine kama haya yana umuhimu mkubwa kwa sababu yanazaa tena mafanikio mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge hapa anauliza katika bajeti hajaona kitu chochote kilichotengwa kwa ajili ya ulemavu, pamoja na kwamba sekta mbalimbali zinashughulika na jambo la walemavu na kwamba suala la ulemavu ni suala mtambuka, lakini sisi kama Mamlaka ya Serikali za Mitaa tunatafakari maombi makubwa yaliyoletwa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara yangu ambapo maoni mengi ikiongozwa na Mheshimiwa Ikupa alisema wanaomba basi angalau asilimia mbili ya own source ya makusanyo ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa iwekwe kwa ajili ya Walemavu na hili ni jambo ambalo tumeliafiki kwa hatua za awali, lakini tutaendelea kulitafakari kuona namna
gani tunalitekeleza. Sasa inawezekana pia likatekelezwa vizuri endapo Kamati hizi sasa zitaundwa katika level hizi zote za Mkoa, Wilaya, Kata, Halmashauri na Vijiji. Zikiwepo hizi Kamati ndiyo rahisi kutekeleza hata huo mgawanyo wa hiyo asilimia mbili ya makusanyo ya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nikubaliane kabisa kwamba Serikali tuko tayari na tutahakikisha kwamba tunalisimamia jambo hili vizuri kabisa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Simbachawene kwa jibu la nyongeza namba moja lililokuwa linahusu Kamati kwa mujibu wa Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 ya Huduma za Walemavu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongeze majibu ya ziada kwa swali la nyongeza namba mbili linalohusu Mfuko wa Walemavu ambao nao unazingatia Sheria Namba 9 ya mwaka 2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa anasoma bajeti yake na kuhitimisha hoja yake hapa ndani, alilieleza Bunge lako Tukufu kupitia utaratibu ambao tumejiwekea wa Vikao vya Baraza la Watu Wenye Ulemavu ambalo sasa limeanza kufanya kazi. Tumeanza pia kufanya kazi ya kufanya mapitio ya kuona ni namna gani Serikali inaweza kushughulikia pia mfuko huo wa watu wenye ulemavu, vilevile kushirikiana na nguvu hizo nyingine ambazo zimesemwa mbele ya Bunge lako Tukufu
ambazo zinaweza zikasaidia watu wenye elemavu wakapata fursa sawa na watu wengine wote katika nchi yetu ya Tanzania, kupitia mifuko mbalimbali ambayo imeanzishwa na mingi ikiwa inasimamiwa na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kuwa suala hili linafanyiwa kazi kwa kina sana na linaratibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndani ya ofisi yake na tutaendelea kulifanyia kazi ya kutosha. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake za kupambana na dawa za kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa mara ya pili tena.
Ni kwamba naipongeza Serikali kwa jitihada zake.
Na vijana hawa wanapoathirika na hizi dawa za kulevya moja kwa moja tayari wanaingia katika kundi letu, kwa maana ya kundi la watu wenye ulemavu. Na kwa sababu wimbi ni kubwa kwa hivi sasa, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inaongeza Madaktari Bingwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hawa walioathirika na dawa za kulevya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu maswali haya mawili, Mheshimiwa Waziri wa Nchi atamalizia kwa ujumla yanayohusu supply reduction.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kwanza la Mheshimiwa Amina Mollel, kwanza nimpongeze siku ya jana aliniletea wageni kutoka Chama cha Wananchi ambao wanajihusisha na Afya ya Akili Nchini na katika mazungumzo tuliyoyafanya ni pamoja na hili suala la Madaktari Bingwa wa Afya ya Akili kwenye Mikoa nchini. Mkakati tulionao na ndio taarifa niliyowapa wale wananchi wenzetu ni kwamba Serikali ina-scale up huu mkakati wa kuwa na hizi kliniki kama iliyopo Muhimbili, Temeke na Mwananyamala kwa mwaka huu kwenye mikoa kumi ya Tanzania Bara na kwa mwaka ujao tutaongeza mikoa mingine kumi, tunakwenda kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, kila tutakapoanzisha hii kliniki ya methadone ni lazima awepo Daktari Bingwa anayehusika na ku-administrate hiyo dawa kwa sababu methadone inalindwa kwa taratibu maalum za kuitunza na kuitoa kwa wagonjwa. Kwa hiyo, ni lazima awepo Daktari Bingwa anayeweza kufanya hivyo kwa hivyo, kwa mwaka huu nimhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel kwamba tutakuwa na Madaktari Bingwa kwenye mikoa kumi ncjini, pindi kliniki za methadone zitakapoanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni la Mheshimia Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kuhusu hizi kliniki na rehabilitation centres kwenye Mikoa; kwa sasa kweli, tuko Dar es Salaam peke yake, lakini kwenye mkakati wetu tunakwenda kwenye mikoa kumi kama nilivyosema. Na kwenye kila kanda tunakwenda kuanzisha rehabilitation centre ambapo tutakuwanazo nne sasa katika nchji nzima. Kwa hivyo, hii ni mikakati ambayo tunayo katika siku za usoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ruzuku, Serikali haina utaratibu wa kutoa ruzuku kwenye taasisi mbalimbali za binafsi, kwa sababu wao wanafanya kwa hiyari na tunawaomba na kuwatia moyo waendelee kufanya hivyohivyo kwa hiyari, lakini sisi kama Serikali tuna mikakati yetu ya kuwasaidia wenzetu ambao wameathirika na dawa za kulevya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba nijibu maswali ya nyongeza yaliyoulizwa kwa umoja wake, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, kwa majibu mazuri aliyokwishakuyatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tena kwa kulipongeza Bunge letu Tukufu kwa sababu mwaka 2015, ndilo lililosababisha kufanyika kwa mageuzi makubwa ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa kutungwa kwa sheria mpya ambayo imeunda hiyo mamlaka sasa ambayo tumemuona Kamishna Jenerali akifanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na makamishna wenzake kuhakikisha kwamba tunapambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niliarifu Bunge
lako Tukufu Kamishna Jenerali baada ya kuteuliwa na mamlaka kuanza kazi rasmi, ameshahakikisha ametengeneza Mpango Mkakati Maalum wa Taifa wa kuhakikisha kwamba tatizo hili la dawa za kulevya nchini linaondoka. Na mpango mkakati huo unashirikisha pande zote mbili za Muungano, upande wa Zanzibar na upande wa huku Bara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Khatib wala usiwe na wasiwasi, tunafanya kazi hizi kwa pamoja, vyombo hivi vyote viwili vinafanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumegundua kwamba, wenzetu wa private sector wanafanya kazi nzuri sana kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini. Na hivyo nichukue nafasi hii kwanza niwapongeze wale wote ambao wameamua kujitolea kusaidiana na Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania, tunawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mwaka huu wa bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu imeamua kuweka bajeti kidogo ambayo itasaidia kushirikiana na hao wenzetu ambao wameonesha kwamba, wana nia ama ya kuanzisha sobber houses kwa ajili ya kuwasaidia hawa walioathirika na dawa za kulevya, lakini vilevile kufanya kampeni na kuleta uhamasishaji mkubwa wa kuwasaidia vijana wetu kuwaondoa kwenye tatizo hili.
Kwa hiyo, tuko pamoja tunafanya kazi hii kwa pamoja, mapambano yanaendelea na tunataka kuona kwamba tunaondoa tatizo hili katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali ya nyongeza ninayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, awali ya yote ninalipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pongezi ziende kwa Spika wa Bunge kwa kuwa tayari wamekwishaanza kutoa huduma hii katika matangazo haya, wakalimani wamekwishaanza kutafsiri na kuwawezesha wenzetu viziwi kupata taarifa.
Kwa kuwa kilio cha haki ya kupata taarifa ni cha muda mrefu katika mjadala pia wa bajeti ya Wizara tulilizungumzia hili. Ningependa kupata commitment ya Serikali; je, ni lini sasa utekelezaji huu utaanza na kwa kuwa TBC ni televisheni ya umma, commitment ya Serikali kwamba Shirika hili litaajiri lini wakalimani wa lugha ya alama ili basi wenzetu viziwi waweze kupata taarifa?
Swali langu la pili, kwa kuwa haki ya kupata habari ni haki ya Kikatiba, je, Serikali inatoa muda gani kwa wamiliki wa vyombo binafsi vya habari ili na wao basi waone umuhimu na kutekeleza haki hii ya Kikatiba ambayo ni ya Ibara ya 18(d)? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi ambazo ametoa na tunazipokea, tunasema ahsante sana. (Makofi)
Katika swali lake la kwanza ambalo anahitaji kujua
sasa ni lini TBC itaajiri, nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi ambavyo amekuwa amepambania haki za walemavu, na kwa kweli nakumbuka kabisa kwamba hata katika mjadala wa bajeti ya Wizara yetu alichangia suala hili na alitaka kujua ni lini hasa vyombo vya utangazaji vitakuwa vikitoa ukalimani wa lugha ya alama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba, katika kikao ambacho kilifanyika wadau wale walijipangia majukumu mbalimbali. Kwa upande wetu Wizara tuliipangia TBC iwe ni chombo cha mfano, ianze mara moja kutoa ukalimani wa lugha ya alama, na kwa kuanzia TBC tayari imeishatuma maombi ya kupata kibali cha kuajiri wakalimani wawili, hivyo wakati wowote kibali kitakapotoka basi TBC itaajiri ili iweze kuwa chombo cha mfano kwa vyombo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni muda gani tumeweka kwa vyombo vya habari. Kama mlivyosikia katika jibu la msingi ni kwamba, TCRA imepewa jukumu la kuchukua kanzi data kutoka TASLI ambayo ni orodha ya wale wakalimani ambao wana uwezo wa kutoa ukalimani katika vyombo vya habari, wakiishachukua taarifa hizi watakuwa wakipeleka kwa vyombo vya habari.
Sasa tatizo ambalo tunalo ni kwamba vyombo vya habari ni vingi, vyombo vya habari vya utangazaji televisheni, ni vingi takribani 32, lakini kwa mujibu wa TASLI wapo wakalimani 70 na kati ya hao wakalimani 15 tu ndiyo ambao wanaonekana kwamba wana ujuzi na uwezo wa kufanya ukalimani katika vyombo vya habari au utangazaji wa televisheni. Ndiyo maana sasa VETA na CHAVITA wamepewa jukumu la kutoa mafunzo kwa hawa wakalimani wengine waliobaki ili na wao waweze kufikia uwezo wa kutangaza katika vituo vya televisheni. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa Mikoa iliyoathirika na tukio hili la uchomaji wa shule za sekondari, waathirika wakubwa ni wanafunzi. Ningependa tu Waziri atufahamishe kwamba ni hatua gani za haraka zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaendelea na masomo badala ya kuziacha shule hizo kwa muda mrefu pasipo kupewa msaada wowote na badala yake ni wananchi ndiyo wanaojitolea na wasamaria wema. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa Mikoa ambayo ilipata janga la moto. Tukumbuke kwamba janga hili liliikumba maeneo mbalimbali. Bahati nzuri unafahamu wewe ni mwenyeji wa Mkoa wa Mbeya, shule yetu ya Iyunga, Mbeya kulikuwa na sintofahamu kubwa sana, lakini ni nini tumekifanya katika maeneo mbalimbali. Tulichokifanya kama Serikali si kwamba Serikali ilikuwa inaangalia hivi na kuacha, hapana. Tumefanya harakati maeneo mbalimbali hasa kutumia Halmashauri husika na ngazi Mikoa na Serikali Kuu. Ndiyo maana wanaofahamu kama mashahidi katika Mkoa wa Mbeya, shule ya Iyunga na mimi nilikuwepo site moto ule ulivyokuwa umewaka pale, tumefanya kazi kubwa sana shule yote ya Iyunga pale imebadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule ya Mpwapwa kwa Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje nimefika pale site hivi sasa bweni tunamaliza kulipaua. Pia maeneo mbalimbali harakati hizi zinaendelea, lakini tunaenda awamu kwa awamu, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel kwamba Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha bahati nzuri wakati moto unawaka Monduli nilikuwepo pale. Nilienda na nilifanya tathmini hiyo, lengo kubwa ni kwamba tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo sehemu yenye mapungufu yote tutashirikiana na jamii husika kuondoa tatizo hili la watoto wetu ili wasikose maeneo ya kukaa.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliitaka mifuko kusitisha fao la wafanyakazi ambao wanataka kuchukua mafao yao mpaka wafikishe miaka 60. Ningependa tu kufahamu kwa sababu kwa hivi sasa sakata la wale wafanyakazi waliopatwa na vyeti fake ni dhahiri kabisa watapenda kuchukua mafao yao ili wajiingize katika shughuli nyingine.
Nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi hao na wale wengine ambao wana ajira fupi wanachukua mafao yao ili waweze kuendelea na shughuli nyingine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kuhusiana na mafao ya waliokumbwa na kadhia ya vyeti vya kughushi, kwa sasa niseme ni suala ambalo hatuwezi kulitolea maelekezo hapa, pindi taratibu zote zitakapokamilika basi taarifa itaweza kutolewa na watajua hatima yao. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kama ilivyoulizwa katika swali la msingi, baadhi ya Madiwani wanaruhusiwa kuingia katika vikao vya Halmashauri husika lakini baadhi ya Wakurugenzi imekuwa vigumu kwao kuwaruhusu, na mfano mzuri ni Mheshimiwa Stella Allex Ikupa ambaye anapaswa kuingia katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ilala, lakini mpaka leo hii imekuwa vigumu kuhudhuria vikao hivyo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri unatoa kauli gani ili aweze kuingia katika Baraza hilo na kuwatendea haki watu wenye ulemavu katika kuhakikisha kwamba masuala yao yanaingizwa katika bajeti husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii nadhani kwamba imeshakwisha, kwa hiyo kama kuna ukakasi wa aina yoyote ofisi yetu italifanyia kazi; lengo kubwa ni kwamba mtu aliyepewa dhamana katika eneo hilo aweze kushiriki vizuri hasa lile kundi analoliwakilisha, kundi la walemavu.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, unapokuwa katika eneo la huyu mwekezaji Loliondo, unaambiwa welcome to etisalat Arabic network kwa maana kwamba unatumia mtandao wa huko Arabuni na tunafahamu nchi yetu kwa hapa Tanzania kuna mitandao mitano ikiwepo Halotel, Zantel, Tigo pamoja na Airtel na Vodacom.
Je, ningependa kufahamu sheria zinasemaje kwa sababu hawa waliopo wanatambulika na kuna kiasi kinachopatikana kwa Serikali kutokana na mapato ya mitandao hii, sasa je, kwa huyu ambaye anakuambia welcome to etisalat Arabic network naomba ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, mtandao huu anaousema umesajiliwa na TCRA na unasimamiwa na TCRA na unalipa ada zote zinazotakiwa zilipwe chini ya TCRA, tofauti yake tu ni kwamba wao hawajapanua mtandao wao ukaenda na maeneo mengine. Kwa hiyo, wao wamechukua masafa na masafa hayo yanafanya kazi katika lile eneo na inaruhusiwa kisheria, ni mtandao ambao unasimamiwa na nchi yetu.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Wakati Tanzania inatoka katika mfumo wa analojia kuingia katika mfumo wa dijitali inaeleweka kwamba Startimes ndio waliopewa jukumu hilo na katika makubaliano ilikuwa kwamba unapolipia kile king’amuzi cha kwa maana ya kwamba hizi channel za hapa nchini ni bure lakini ni tofauti na ilivyo sasa ni kwamba wamekuwa wakiondoa hizi channel za hapa nchini hazionekani tena kama ilivyokuwa awali. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na jitihada hizo, ninaomba kufahamu ni kwa nini Startimes imekiuka mkataba huo na badala yake hivi sasa hakuna tena kituo chochote cha television ambacho unaweza kukiona baada ya malipo tuliyokuwa tunapaswa kulipia kuisha?
NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Amina Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kwa kuuliza swali ambalo limekuwa likiulizwa mara nyingi sana na wateja na watumiaji wa tv.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wakati mwingine utakuta kwamba mteja anapokuwa amelipia kifurushi na kifurushi chake kikawa kimekwisha basi zile channel ambazo tunaziita kwamba ni free to air zinakuwa hazionekani. Sasa tatizo ni kwamba, kama nilivyotangulia kusema TBC1 peke yake ndiyo ambayo inaonekana katika hivi ving’amuzi vya DDT pamoja na DTH bure bila kulipia. Kwa hiyo, TBC1 hailipi chochote kwa hawa transmitters kabisa. Lakini Sheria ya Leseni walizopata hawa transmitters ina masharti kwamba hizi free to air zote wale wamiliki au makampuni ya televisheni wanatakiwa wawe wanalipa ada fulani kila mwezi, sheria inamruhusu yule transmitter kumkatia au kumuondoa pale ambapo atakuwa ameshindwa kulipa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tatizo linatokea kwamba hawa content providers wanapokuwa wameshindwa kulipa basi wanaondolewa na hawa transmitters. Kwa sasa hatua zimeshachukuliwa, TCRA imewaita na kuwataka wajieleze vizuri ni kwa nini hawalipi kwa sababu wao ndiyo wanaosababisha sasa hizi zisionekane na Sheria inawaruhusu wale transmitters waoneshe kama hawatalipa.
Kwa hiyo, kutokana na kutokulipa kwao ndiyo maana unakuta hizi free to air channel hazionekani lakini sio kwamba yule mteja ndiyo anayetakiwa alipe.
Mheshimiwa Spika, mteja ananunua kifurushi kwa ajili ya zile pay channels lakini sio kwa hizi free to air. Kwa hiyo kimsingi anatakiwa aendelee kuziona hata kama hakulipia/hakununua kifurushi. Kwa hiyo, pale itakapoonekana kwamba maelezo yao hayaridhishi watachukuliwa hatua kali. Hivyo nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwataka wamiliki wote wa tv stations walipie mara moja ada zao za mwezi ili kusudi wananchi waweze kufaidi hizi free to air services. Ahsante.(Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa sheria hii imekuwa ikiwazungumzia sana watoto wa kike na tunapozungumzia watoto, wapo watoto wa kike na watoto wa kiume; na watoto wa kiume kwa sasa wanakabiliwa na janga kubwa la ulawiti:-
Je, Serikali inazungumziaje swali hili ili kuhakikisha kwamba inawalinda watoto hawa wa kiume ambao wamekuwa wakipatwa na madhara hayo?
NAIBU WAZIRI AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kinyume cha sheria za nchi yetu kwa mtu yeyote yule kumwingilia kinyume cha maumbile mtu mwingine yeyote yule. Makosa haya yanaelezwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu, Chapter 16 of the Law, nafikiri ni kwenye Kifungu cha 154 na vifungu vinavyofuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo makosa haya yamekuwa criminalized. Mwaka nafikiri 2012 au 2013 hapa Bungeni tuliongeza ukali wa adhabu ya mtu yeyote yule ambaye atabainika kufanya hivyo. Changamoto inayojitokeza kwa kweli, vitendo vya ulawiti kwa kiasi kikubwa sana vinafanyika kwenye familia. Vinapofanyika kwenye familia, ushahidi unakosekana kwa sababu ndugu wanakuwa hawataki kuripoti vitendo vya namna hii kwa kuhofia ndugu mwingine kwenda kufungwa. Kwa hiyo, wanayamaliza mara nyingi kimya kimya kwenye familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali msimamo wetu uko wazi kwamba adhabu kali ya kifungo kisichopungua miaka 30 itampata mtu yeyote yule ambaye atathibitika bila shaka kwamba amefanya kitendo cha ulawiti kwa mtoto yeyote yule awe wa kiume ama wa kike. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania hivi sasa tunaelekea katika uchumi wa viwanda. Na moja ya ajenda/ suala muhimu ambalo linazingatiwa hivi sasa ni ujenzi wa viwanda. Na kwa kuwa viwanda ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira, kwa mfano nchi ya China pamoja na Marekani ni miongoni mwa nchi ambazo hazikukubali kusaini Mkataba wa Kyoto kutokana na viwanda. Sasa ninachotaka kujua tu ni kwamba, Tanzania kwa sababu tunahitaji viwanda.
Je, tunajiandaaje ili kuhakikisha kwamba viwanda vitakavyojengwa hapa nchini haviwi sababu ya uharibifu wa mazingira? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na baadhi ya nchi matajiri ambao walikuwa hawataki kusaini Mkataba wa Kyoto lakini mkutano niliouzungumzia ambao mpaka sasa wanaendelea kule Bonn, Ujerumani. Mkutano huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa sababu makubaliano yaliyofanyika Mjini Paris kila nchi wanatakiwa sasa wasaini mkataba ule wa mabadiliko ya tabianchi. Ka hiyo, hakutakuwa na nchi hasa hizi tajiri ambazo ndizo zinazalisha hewa ya ukaa ambayo inakuja kuathiri nchi zetu maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tanzania ya viwanda ambayo sasa tunakwenda nayo, sheria yetu ya mazingira ambayo niko nayo hapa, Sheria Namba 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira. Sheria hii inavitaka viwanda vyote kuhakikisha kwamba kabla hawajaanza uzalishaji wawe katika ile Environmental Impact Assessment pamoja na Environmental Management Plan zao, namna ambavyo watakwenda ku-manage emissions zote ambazo zinaharibu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana kupitia Baraza la Hifadhi la Taifa la Mazingira (NEMC) tumekuwa tukikagua mara kwa mara kuhakikisha viwanda hivi vina-comply masharti yale ambayo hayaharibu mazingira. Ndio maana viwanda ambavyo vinakaidi tunavipiga fine na vingine tunavifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwahakikishia Watanzania, katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli hakuna wazalishaji wa viwanda wanaoharibu mazingira watakaotumia nguvu za fedha kuhakikisha kwamba wanaendelea kuharibu mazingira halafu na sisi tunawatazama, lazima sheria hii itawashughulikia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza, pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Tatizo la watu wenye albinism na hasa wa vijijini kutokana na uhaba wa mafuta haya wengi wamekuwa wakifa kwa ugonjwa wa saratani. Pamoja na majibu hayo, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuokoa maisha ya watu wenye albinism hasa wale wa vijijini? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi na kama ambavyo nimewaagiza Wakurugenzi wote wahakikishe wanaweka haya mafuta kwenye orodha ya dawa wanazoagiza. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati wa Serikali kwamba itaendelea kuagiza mafuta haya kadiri inavyotakikana. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongza Mheshimiwa Rais kwa utaratibu wa kutoa elimu bure kwani wanufaika wakubwa ni watoto wenye ulemavu ambao siku za nyuma hawakuweza kupata nafasi hiyo. Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, changamoto ndio bado zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala zima la madawati, madawati ni kweli kabisa yametolewa lakini hayakuzingatia uhitaji hasa kwa watoto wenye ulemavu ambao wengine bado wanalazimika kukaa chini kutokana na hali zao haziwawezeshi kukaa katika madawati hayo.
Je, Serikali ina mpango gani ili basi kuzingatia mahitaji ya watoto hao wenye ulemavu ili waweze kufurahia maisha na kusoma vizuri ili waweze kutimiza ndoto za? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia thabiti ya Serikali kuhakikisha kwamba makundi yote yanazingatiwa katika kutengeneza miundombinu, na ndiyo maana katika hizi siku za karibuni nilivyopata fursa ya kutembelea Mkoa wa Arusha, nikafika Kituo cha Afya Muriet, pale unakuta miundombinu kwa ajili ya walemavu nayo imewekwa. Naomba niwatake Wakurugenzi wote wa Halmashauri, jambo lolote kuhusiana na miundombinu inapotengenezwa sasa hivi lazima tuhakikishe hitaji la watu maalum.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu hayo yanayoonesha jitihada za Serikali katika kusaidia watu wenye ulemavu. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua sasa (time frame) ni lini mchakato wa kukusanya maoni ya wadau utakamilika na kwa kuwa ni miaka minne sasa na wenzetu wa Kenya tayari wameshasaini mkataba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kutokusainiwa kwa mkataba huu wa Marrakesh kumesababisha watu wenye ulemavu wasioona kushindwa kwenda na wakati na kuendelea kuwa maskini na hasa kutokana na kukosa fursa mbalimbali za kujiongezea kipato, fursa hizo ambazo zinapatikana kwenye maandishi zinazohusu maendeleo ya nchi lakini pia ulimwengu kwa jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu hayo.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mollel kwa jitihada kubwa anayoifanya lakini pia yeye mwenyewe atakuwa shahidi, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa ni mdau mkuu namba moja katika masuala yanayohusu watu wenye ulemavu na ndiyo maana unaona hata kwenye Baraza tayari kuna watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo jambo hili tunalichukua kwa uzito mkubwa na tutahakikisha kwamba mapema iwezekanavyo baada tu ya kumaliza hili zoezi wanaloendelea nalo lipelekwe kwenye vikao vya wataalam na kikao cha Makatibu Wakuu na hatimaye liende kwenye Baraza la Mawaziri. Mheshimiwa Waziri wangu amekuwa akilifuatilia sana suala hili na najua nadhani umeona hata anakuja kusisitiza kwamba tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili watu wenye ulemavu wapate haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nikijibu swali la pili ni kwamba, tunatambua watakapoweza kupata machapisho ya aina mbalimbali bila vikwazo itawasaidia pia hata wao kuona namna ya kuweza kuondokana na umaskini. Kwa hiyo, naomba sana ajue kwamba suala hili tumelichukua kwa uzito mkubwa ikizingatiwa kwamba wote sisi ni walemavu watarajiwa. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa miundombinu hiyo katika vyoo kwenye shule zetu za msingi na sekondari bado haizingatii mahitaji ya watoto wenye ulemavu; na baadhi ya watoto wenye ulemavu wanalazimika kutambaa katika vyoo hivyo ambavyo wakati mwingine ni vichafu na vinahatarisha afya kwa watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru kwa majibu yake, lakini sijasikia hata yeye mwenyewe kuona kwa jicho la pili uhitaji wa watoto hawa wenye mahitaji maalum katika vyoo hivi. Ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba wanazingatia mahitaji ya watoto wenye ulemavu ili na wao waweze kusoma vizuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa kufuatilia hasa hasa masuala yanayowahusu wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba michoro ya zamani ilikuwa na upungufu wa kutozingatia mahitaji ya watoto au wanafunzi wenye ulemavu. Hata hivyo michoro ambayo ilipitishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka jana yote imezingatia kwamba darasa, choo na bweni na miundombinu mingine ya shule ambayo inatumiwa na wanafunzi lazima izingatie mahitaji ya watoto wenye ulemavu, na ushahidi ni mabweni mapya na madarasa mapya na vyoo vipya ambavyo vimejengwa tangu mwaka jana mwezi wa saba vyote vimezingatia mahitaji hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Amina Mollel kwenda kufanya ukaguzi kwenye maeneo yote ambayo hatimaye tutaelekeza wafanye marekebisho, ahsante sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Arumeru ina Halmashauri mbili kwa maana kwamba Halmashauri ya Meru na Arusha DC. Wilaya hii eneo lake ni kubwa kiasi kwamba hata wakati mwingine huduma kuzifikia jamii inakuwa ni vigumu. Je, ni lini sasa Serikali (kwa sababu tayari ilikwishaanza mchakato siku za nyuma) itaendelea na mchakato huo kuhakikisha kwamba inagawanya wilaya hii inakuwa wilaya mbili ili huduma za kijamii ziweze kuwafikia wananchi kwa haraka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la dada yangu Amina Mollel Mbunge ambaye anawakilisha hasa kundi la walemavu kwa umakini zaidi humu Bungeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Meru ni kubwa sana, ina Arusha DC na Meru. Ukiangalia, bahati mbaya Halmashauri ile iko kama mbalamwezi fulani hivi, kwamba Jiji la Arusha liko katikati halafu ile wilaya imezunguka hivi. Kwa hiyo hata management yake inakuwa ni ngumu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kama nilivyosema katika maeneo mbalimbali, kwanza naamini michakato mbalimbali imeanza huko lakini wakati mwingine inawezekana taarifa zikawa zimekuja lakini vigezo havikukidhi. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Amina Mollel kwamba tutakapopata taarifa za vikao vya RCC kutoka Mkoa wa Arusha na Mkuu wetu wa Arusha akishajipima kule akiona kwamba jambo hilo limeridhia, na likishafika kwetu na sisi tutalifanyia kazi kufanya taratibu zote za kisheria zinazohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikionekana kwamba inafaa sasa kuigawanya zile wilaya mbili, Serikali itaona jinsi gani ya kufanya katika hilo. Kwa hiyo naomba nikuhakikishie, ni kwamba utaratibu ni ule ule wa kisheria tu, kama unavyosema ugawanyaji wote wa maeneo unasemaje. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana wa eneo hilo akiridhia, basi mchakato utakamilika hatimaye mtapata wilaya mpya.
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Serikali za kusambaza vifaa saidizi kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inajenga shule moja ya mfano ambayo itawajumuisha watoto wenye ulemavu pamoja na watoto wengine ambao hawana mahitaji maalum, ili basi shule hiyo iweze kuwasaidia kwa kiwango kikubwa watoto wenye mahitaji maalum?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inakamilisha mapitio ya michoro kwa ajili ya shule maalum ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kujenga shule ya Kisasa ambayo itakuwa ni ya bweni, shule ya msingi na sekondari kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo shule hiyo itajengwa kwenye maeneo ya Chuo cha Ualimu cha Patandi ambacho ni chuo mahususi kwa ajili ya kufundisha walimu wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi huo utaanza mara moja mara baada ya kukamilisha mishoro kwa sababu fedha kwa ajili ya ujenzi zipo.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali ya nyongeza ninayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, awali ya yote ninalipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pongezi ziende kwa Spika wa Bunge kwa kuwa tayari wamekwishaanza kutoa huduma hii katika matangazo haya, wakalimani wamekwishaanza kutafsiri na kuwawezesha wenzetu viziwi kupata taarifa.
Kwa kuwa kilio cha haki ya kupata taarifa ni cha muda mrefu katika mjadala pia wa bajeti ya Wizara tulilizungumzia hili. Ningependa kupata commitment ya Serikali; je, ni lini sasa utekelezaji huu utaanza na kwa kuwa TBC ni televisheni ya umma, commitment ya Serikali kwamba Shirika hili litaajiri lini wakalimani wa lugha ya alama ili basi wenzetu viziwi waweze kupata taarifa?
Swali langu la pili, kwa kuwa haki ya kupata habari ni haki ya Kikatiba, je, Serikali inatoa muda gani kwa wamiliki wa vyombo binafsi vya habari ili na wao basi waone umuhimu na kutekeleza haki hii ya Kikatiba ambayo ni ya Ibara ya 18(d)? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi ambazo ametoa na tunazipokea, tunasema ahsante sana. (Makofi)
Katika swali lake la kwanza ambalo anahitaji kujua sasa ni lini TBC itaajiri, nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi ambavyo amekuwa amepambania haki za walemavu, na kwa kweli nakumbuka kabisa kwamba hata katika mjadala wa bajeti ya Wizara yetu alichangia suala hili na alitaka kujua ni lini hasa vyombo vya utangazaji vitakuwa vikitoa ukalimani wa lugha ya alama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba, katika kikao ambacho kilifanyika wadau wale walijipangia majukumu mbalimbali. Kwa upande wetu Wizara tuliipangia TBC iwe ni chombo cha mfano, ianze mara moja kutoa ukalimani wa lugha ya alama, na kwa kuanzia TBC tayari imeishatuma maombi ya kupata kibali cha kuajiri wakalimani wawili, hivyo wakati wowote kibali kitakapotoka basi TBC itaajiri ili iweze kuwa chombo cha mfano kwa vyombo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni muda gani tumeweka kwa vyombo vya habari. Kama mlivyosikia katika jibu la msingi ni kwamba, TCRA imepewa jukumu la kuchukua kanzi data kutoka TASLI ambayo ni orodha ya wale wakalimani ambao wana uwezo wa kutoa ukalimani katika vyombo vya habari, wakiishachukua taarifa hizi watakuwa wakipeleka kwa vyombo vya habari.
Sasa tatizo ambalo tunalo ni kwamba vyombo vya habari ni vingi, vyombo vya habari vya utangazaji televisheni, ni vingi takribani 32, lakini kwa mujibu wa TASLI wapo wakalimani 70 na kati ya hao wakalimani 15 tu ndiyo ambao wanaonekana kwamba wana ujuzi na uwezo wa kufanya ukalimani katika vyombo vya habari au utangazaji wa televisheni. Ndiyo maana sasa VETA na CHAVITA wamepewa jukumu la kutoa mafunzo kwa hawa wakalimani wengine waliobaki ili na wao waweze kufikia uwezo wa kutangaza katika vituo vya televisheni. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini bado nina swali moja la nyongeza. Kwa wakati uliopo hivi sasa wanawake wengi wanazaa katika umri mkubwa, hasa kutokana na wengi wamekwenda shule au wakati mwingine pia uzazi kwa hivi sasa kwa wanawake wengi imekuwa ni shida, kwa hiyo utakuta wengi wanazaa…
…Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo najenga hoja, tafadhali nakuomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mtu ana miaka 40 ndipo anapata mtoto wa kwanza, mtu huyu anataka azae ndani ya miaka minne tayari awe na watoto wawili kwa sababu umri haumruhusu kwa wakati huo; hatuoni kwamba kwa sasa hivi sheria hii imepitwa na wakati na inabidi iletwe hapa ifanyiwe mabadiliko? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema watu wanaozaa katika umri mkubwa tuwalegezee masharti waende wanavyotaka. Kwanza nataka niseme hii ni sheria, sheria katika nchi hufuatwa na watu wote, lakini pia mimi kwa ufahamu wangu na utu uzima wangu mama anayezaa akiwa mtu mzima ndiye haswa anatakiwa uangalizi mkubwa kuliko yule aliyewahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo miaka 40 anayoitaja kuanzia 40 kwenda juu, kwa ufahamu wangu, ni kipindi ambacho mama akijifungua anahitaji uangalizi wa hali ya juu. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba hii sheria haijapitwa na wakati, hii sheria ni muafaka, inalinda afya ya mtoto na inajali uzazi wa mpango.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa baadhi ya watoto wanaosoma katika kituo hiki au Shule ya Buhangija wengi wao wametelekezwa kabisa na wazazi wao, kwa maana ya kwamba wazazi wakati ule wa mauaji waliwafikisha watoto wao getini katika ile shule na kuwaacha; na hivi sasa wakati wa likizo na muda wote yamekuwa ni makazi yao katika kituo hiki; Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba angalu siku moja basi, watoto hawa wanawapata wazazi wao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu ameeleza idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi waishio kwenye shule ya Buhangija; je, ina mpango gani pia wa kuhahakisha kwamba tunapata idadi kamili ya watu wenye ualbino na hata watu wengine wenye ulemavu ili basi tunapopanga au tunapotunga sera/ sheria kujua kwamba idadi kamili ya watu wenye ulemavu Serikali iweze kupeleka maendeleo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kilikuwa kinafanywa na Serikali baada ya kutokea lile wimbi la mauaji kwa watu wenye ualbino ilikuwa ni kunusuru maisha yao kama nilivyosema, kwa kuweka kwenye vituo mbalimbali, lakini sasa hivi kitu ambacho kimefanyika Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na vitongoji pia na halmashauri ambako wanatoka iliweza kuangalia jinsi gani hawa watu wanaweza wakarudishwa kwenye familia zao kwa kuangalia usalama na kama ile hali inakuwa imeisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa upande wa Kituo cha Buhangija na vituo vingine, Serikali ambacho inafanya sasa hivi ni kutembelea hivi vituo, lakini kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kama itabainika kwamba kuna watoto wako kwenye hivi vituo, basi Serikali itafanya utaratibu wa kuwapata wazazi wao ama walezi wao ama familia zao na kuweza kuwarejesha kwenye familia zao ama wakati wa likizo sasa waweze kurudi kwenye famila zao kama ambavyo ilivyo kwa watoto wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilijibu kwenye swali la Mheshimiwa Khadija Nassir na wakati pia natoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba sensa inafanyika kila baada ya miaka kumi. Ilifanyika mwaka 2012, lakini pia itafanyika mwaka 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu kwa kuona umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za watu wenye ulemavu kwa ujumla wake, wakiwemo watu wenye ualbino, basi inaandaa mpango ambapo yaani inafanya majadiliano ya ndani kwa kuona kwamba ni jinsi gani sasa tunaweza tukapata takwimu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaweka mipango, kwa hiyo, tutawatumia Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji ili kuweza kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniopa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza na vilevile naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini pia nimpongeze Waziri kwa kushughulikia mgogoro wa Loliondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, tunafahamu awali kulikuwa na tatizo baadhi ya watu na zikiwemo baadhi ya hoteli zilikaidi kukusanya makusanyo haya. Nilitaka tu kujua pamoja na majibu haya mazuri, ni hatua zipi zimechukuliwa kwa wale ambao walikaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni hatua zipi zilichukuliwa kwa hoteli ambazo zilikiuka ukusanyaji huu wa kodi hii yaani concession fees?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Amina Mollel kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya, hasa katika kuwatetea watu wenye ulemavu. Amekuwa akifanya kazi hiyo vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakati tunaanza utekelezaji wa tozo hii baadhi ya hoteli zilikuwa bado hazijapata elimu ya kutosha kwa nini tozo hi imeanzishwa. Kutokana na jitihada ambazo Serikali ilichukua kuwaelimisha wamiliki wa hoteli zote hizo kwa nini tumeanzisha tozo hiyo na kwa nini ni muhimu kulipa na kwa nini tumeachana na mtindo wa zamani, basi hoteli zote hivi sasa zimeelimika na zote zinatekeleza. kwa sababu, zote zina-comply na utaratibu huu mpya basi hakuna hatua ambazo zimechukuliwa. Kwa wale ambao watakaidi ndiyo hapo tutachukua hatua lakini kwa hivi sasa zote zinatekeleza.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Miongoni mwa hizo ahadi napenda kusikia katika barabara ya kutoka Redio Habari…
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Redio Habari Maalum Arusha kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Oltrumet katika Halmashauri ya Arusha DC. Tungependa kusikia ni lini sasa mtatimiza ujenzi wa barabara hiyo kama ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Molle, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema tunaendelea na uratibu wa kuona kwamba ahadi hizi zote zinatekelezwa, tumejipanga vizuri. Nimpongeze sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa concern yake ya kuboresha barabara hii inayokwenda katika Hospitali ya Arusha DC maana tumeizungumza mara nyingi. Nami kwa uzito aliouweka Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili nilikuwa nimepanga kwamba nitatembelea Arusha, nilipotembelea safari iliyopita niliangalia barabara zingine hii sikuiona, ili tuweze kushauriana na kuweka msukumo kuhakikisha watu wanaoenda kupata huduma katika hospitali hii wanapita bila usumbufu wowote, kwa hiyo, tutaifanya namna hiyo.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu kutoka kwa pacha wangu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Watu Wenye Ulemavu ni haki na ni wajibu kwa sababu liko katika makubaliano ya utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006, ambao ni matokeo ya Sheria Namba 9 ya mwaka 2010. Hata hivyo tangu Baraza lilivyoteuliwa tayari limeshamaliza muda wake, lakini mpaka hivi sasa bado Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana hawajateua tena na kulitangaza Baraza ili liweze kushughulikia changamoto na tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuweza kuisaidia na kuishauri Serikali, katika suala zima la watu wenye ulemavu.
Ningependa kufahamu ni lini sasa Serikali itaunda hilo Baraza na kulitangaza ili liweze kufanya kazi zake na liweze pia kuishauri Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa maswala ya watu wenye ulemavu sasa tayari yapo kwenye Wizara hii husika katika Ofisi ya Waziri Mkuu na katika vyama hivi vya watu wenye ulemavu na kutokuwepo kwa hilo Baraza, imekuwa ni changamoto pia kwamba Serikali, haivisaidii kwa kiasi kikubwa hivi vyama; kwa mfano, Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo mpaka sasa hakina viongozi na matokeo yake ni kwamba mambo hayaendi kama yalivyo sawa, wameunda Kamati.
Sasa je, ni lini wataona umuhimu wa kuvisaidia hivi vyama kuvipa ruzuku kama ilivyokuwa hapo awali viweze kufanya mambo yao katika utaratibu unaotakiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maswali yake mawili nikianza na hili la kwanza, nikiri wazi kwamba kweli muda wa wajumbe wa Baraza la Ushauri umekwisha na sisi kama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ofisi yenye dhamana na masuala ya watu wenye ulemavu tayari tulishaviandikia vyama mbalimbali vyote. Kwa maana ya kwamba sisi kama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hatuwateui wale wajumbe kutoka hewani, lazima tushirikishe vyama husika na wadau mbalimbali. Kwa hiyo sasa hivi hatua iliyopo, ni kwamba tayari barua tulishasambaza kwa vyama, na vyama tayari vimesha-respond kwa kutuletea majina mbalimbali. Sasa hivi kinachoendelea ni mchakato wa ndani wa ofisi yetu kuhakikisha kwamba sasa tunateuwa watu ambao wateweza kweli kusaidia watu wenye ulemavu, kwa masuala yanayowahusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali lingine ameuliza suala la ruzuku. Nipende kumthibitishia kwamba Serikali yetu ina nia ya dhati kabisa, katika kuhakikishwa kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanatekelezeka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala hili la ruzuku, tukiangalia huu Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu, ambao sasa katika jibu langu la msingi nimeshaliongelea kwamba tuko katika hatua nzuri, kwamba tumekwisha kutenga fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa huu mfuko. Miongoni mwa kazi za huu mfuko ni pamoja na kuhakikisha kwamba hivi vyama ikiwemo pamoja na ruzuku za vyama zinatekelezeka vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi ruzuku zitaendelea kutolewa kwa vyama pindi huu mfuko utakapokaa vizuri, na pindi ambapo zoezi zima la uteuzi wa wajumbe utakapokamilika.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na jitihada nzuri za Serikali ikiwemo Bunge kuchangia utengenezaji wa madawati katika shule zetu za msingi na sekondari lakini madawati haya katika shule nyingi hayakuzingatia mahitaji ya kundi maalum, yaani watoto wenye ulemavu. Napenda tu kufahamu sasa ni mkakati gani unafanya ili tunapotengeneza au tunapofanya kitu chochote kuzingatia kundi hili maalum kwa sababu watoto wengine hawawezi kukaa hata kwenye hayo madawati ya jumla? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Mollel, kwa kumwambia kwamba maoni aliyoyatoa tunachukua kuwa ni ushauri kwa Serikali kwa ajili ya kuufanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Pamoja na majibu mazuri na jitihada za Waziri mwenye dhamana kutatua kero ya maji hapa nchini, naomba majibu ni lini Serikali itatusaidia wananchi wa Halmashauri ya Arusha DC katika Kata za Oldonyosambu na Oldonyowasi ambako wananchi na hasa watoto wameathirika na maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya fluoride?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anawatetea wananchi wa Arusha ambao kuna maeneo ambayo maji chini ya ardhi yana madini ya fluoride. Siyo Arusha tu, madini ya fluoride yapo Shinyanga na juzi nimegundua juzi yapo hata katika Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuona umuhimu na athari hii inayosababishwa na madini ya fluoride ilitengeneza kiwanda na kuna utafiti wa kutengeneza madini kwa kutumia mifupa ya ng’ombe kwa ajili ya kuondoa fluoride na tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Mwaka jana tulitengeneza mitungi zaidi ya 200 na kusambaza kwa wananchi na mwaka ujao wa fedha tunatengeneza zaidi ya mitungi 1,000 kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi ili kuondoa hayo madini ya fluoride.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza kupata mafanikio makubwa. Wazazi walipata madini hayo lakini watoto wanaozaliwa sasa hivi wako vizuri hawana athari ya madini ya fluoride.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Moja ya Malengo ya Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma na katika vyuo vingi hasa vya Ufundi, havizingatii mahitaji ya kundi maalum la watu wenye ulemavu na hivyo wamekuwa wakiachwa nyuma. Ni nini sasa, jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba ili tunaendana sambamba na kauli hizo za Umoja wa Mataifa, watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Amina Mollel, kwa kweli amekuwa ni mtetezi mkubwa sana wa haki za watu wenye mahitaji maalum. Nimhakikishie tu kwamba, Wizara yangu imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba changamoto ambazo zilikuwepo huko nyuma za kutotoa msisitizo mkubwa kwenye mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu, kwa sasa tunahakikisha tunajaribu kutoa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia Wizara ya Elimu ina Kitengo Maalum kinachohusika na elimu ya mahitaji maalum. Vilevile kwa sasa tumetoa maelekezo kwamba katika ujenzi wowote ule utakaofanywa kwa fedha za Serikali ni lazima tuhakikishe kwamba mahitaji na mazingira ya watu wenye mahitaji maalum yanatiliwa maanani.
Mheshimiwa Spika, ukiacha hivyo, Serikali imewekeza sasa vilevile kwenye kutafuta Walimu na Wataalam wengine kwa ajili ya kuendeleza elimu ya watu wenye mahitaji maalum. Ndio maana tumefanya ukarabati mkubwa sana katika Chuo cha Patandi na tunaamini kwamba tunavyoendelea mbele, tutaendelea kuhakikisha kwamba kunakuwa na Walimu na wafanyakazi wengine ambao wana elimu ya kuweza kusaidia wanafunzi na watoto wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba Serikali inayafanyia kazi vizuri sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ninalo. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu hayo ya Serikali lakini mpaka Mheshimiwa Mbunge anaandika swali hili ni kwamba katika Kata hiyo ya Mateves bado kuna wananchi ambao wanadai fidia ya malipo hayo kwamba bado hawajatimiziwa. Je, Waziri yuko tayari kufuatilia na kuhakikisha kwamba wananchi hawa wote wanapata malipo yao kama ilivyokubalika awali? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ningependa tu kupata commitment ya Serikali amesema kwamba atakapopokea fedha hizo. Je, katika msimu huu wa mwaka 2017/2018 au ni mpaka katika bajeti nyingine na pengine tu kwamba Waziri wenyewe yupo tayari kwenda sasa na Mheshimiwa Mbunge ili kwenda kusikiliza hizo kero na malalamiko ya wananchi na kuweza kuwakamilishia fidia yao. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mollel na Mheshimiwa Mbunge Catherine Magige kwa ushirikiano wao namna ambavyo wanafuatilia ili kuhakikisha kwamba wananchi wao katika maeneo haya ya Arusha wanapata haki zao.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kulipa fidia hizi. Ukiangalia kwa ujumla wake kwamba kulikuwa na jumla ya madai ya shilingi bilioni 2.5, lakini mpaka sasa tunavyozungumza bilioni 2.291 zimekwishalipwa ina maana kwamba asilimia 92 ya madai yote imeshalipwa. Hii inaonesha kwa jinsi gani Serikali iko committed kuhakikisha kwamba hawa wananchi wanaodai wanapata haki zao na kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, nimtoe tu wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba hiki kiasi cha shilingi milioni kama 214 kilichobaki ni kiasi ambacho ni kidogo, lakini ni muhimu kilipwe mapema. Kwa hiyo, tunafuatia na niseme tu kwamba ni wakati wowote na niko tayari kuhakikisha kwamba fedha zikipatikana kutoka Hazina hawa wananchi wanalipwa mara moja. Kwa hiyo, wasiwe na wasiwasi, kama tulivyowalipa hawa wengine na wao watalipwa mara moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment ya Serikali , nisema wakati niko committed kama nilivyoahidi hata wiki iliyopita wakati nikijibu swali lako Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafika maeneo haya ili sasa tuweze kuona pia kwamba ni nini kinachotakiwa kufanyika ili mambo yaende sawia. (Makofi) Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Miongoni mwa vijana wapo pia vijana wenye ulemavu na tunaposema kwamba tatizo la ajira kwa vijana, basi vijana wenye ulemavu ndiyo waathirika namba moja. Nataka kufahamu katika mkakati huu wa sasa kwamba Tanzania ya viwanda. Je, ni mikakati gani ya haraka Serikali inaandaa katika kuhakikisha kwamba vijana wenye ulemavu nao wanakuwa ni sehemu ya ajira na hawaachwi nyuma katika kuendeleza gurudumu la maendeleo hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango yote ya Serikali hasa ya ukuzaji ujuzi, yenye lengo la kumfanya kijana wa Kitanzania aweze kusimama kiuchumi na aweze kuwa na sifa za kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba katika kila mpango kundi la watu wenye ulemavu wanajumuishwa ili na wao pia wapate fursa ya kupata ujuzi stahiki ambao watautumia katika uchumi huu wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika progamu iliyoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya ukuzaji ujuzi kwa vijana ambao lengo lake ni kuwafanya vijana hao kuwa na sifa za kwenda kufanya katika viwanda, kundi la watu wenye ulemavu wanajumuishwa na tumetenga asilimia kadhaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kila programu imguse na mtu mwenye ulemavu.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, hivi majuzi tu ulizinduliwa upimaji wa VVU unaofadhiliwa na USAID, Shirika la Kimarekani, nataka kufahamu nini mkakati wa Serikali kumaliza tatizo hili hasa kitakwimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na tatizo hili la VVU hasa kwa waathirika wengi ambao kwa namna moja au nyingine dawa zimekuwa pia ni tatizo. Wapo wanaotumia kikamilifu lakini kwa wengine upatikanaji wake ni changamoto lakini pia upatikanaji wa dawa unapaswa uendane na lishe. Nini sasa mkakati katika kusaidia wananchi wale ambao kipato chao ni cha chini lakini wana maradhi haya na kutokana na ukosefu huo wa lishe wanasababisha vifo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amina Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameelekeza katika suala la changamoto za takwimu. Niendelee kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu zetu za masuala ya UKIMWI ziko vizuri. Serikali kupitia Taasisi ya TACAIDS pamoja na Wizara ya Afya, Kitengo cha UKIMWI ndio wanaoratibu takwimu zote za masuala ya UKIMWI na nimthibitishie katika malengo haya ya 90-90-90 takwimu zetu kama nchi ziko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amezungumzia suala la upatikanaji wa dawa. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba upatikanaji wa dawa za UKIMWI ni asilimia 100 na tunazisambaza nchini kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amegusia kidogo suala la lishe, ni kweli tunatambua kwamba kumekuwa na changamoto ya lishe katika baadhi ya makundi lakini sisi mkakati wetu tunajaribu sana kutoa elimu katika jamii na kwa wale ambao kabisa wanaonekana wana changamoto ya lishe basi kwa wale wachache kuna utaratibu maalum wa kuweza kuwasaidia. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri na vilevile nitambue na kupongeza jitihada za Serikali katika kusaidia makundi maalum hasa watu wenye ulemavu. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kweli Serikali imeanza utaratibu huo, lakini usambazaji wa mafuta haya hasa kwa maeneo ya vijijini bado ni tatizo. Albino wengi wanaangamia kutokana na saratani. Napenda tu kufahamu jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wanafika vijijini ili kuweza kuwanusuru watoto hawa. Nini mpango mkakati wao kuhakikisha kwamba wanawafikia? Hilo ni swali namba moja.

Swali la pili, albino wengi wanaoishi vijijini, tayari wameshaathirika na ugonjwa wa saratani; na hali za maisha kama tunavyofahamu hasa wa vijijini ni duni sana, kupata shilingi 10,000/= ni shida. Nini mpango mkakati wa Serikali kuwasaidia na kunusuru maisha ya watu wenye albinism hapa nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, utaratibu ambao Serikali tunatumia sasa hivi katika usambazaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ni utaratibu ambao unaitwa pool system. Miaka ya nyuma tulikuwa tunatumia push system. Push system maana yake nini? Ni kwamba sisi Serikali tulikuwa tunanunua dawa, vitendanishi na vifaa tiba tunavipeleka katika vituo vya kutolea huduma ya afya pasipo kuzingatia mahitaji halisi ambayo yako kule. Kwa hiyo, hukuta baadhi ya vifaa, dawa na vitendanishi vinachina kwa sababu uhitaji haukuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ambao tunautumia sasa hivi ni wa pool system. Wao kama Vituo vya Afya wanajua mahitaji mbalimbali ya huduma na dawa, vitendanishi na vifaa tiba na wao kuingiza katika mipango yao na kuagiza kutoka MSD. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, dawa hizi na mafuta haya kwa ajili ya kundi hili la walemavu wa ngozi tunavyo ndani ya MSD, ni wajibu sasa wa Halmashauri mbalimbali na hospitali za mikoa kuziagiza kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Amina amegusia suala la walemavu wa ngozi kwamba wamekuwa wanaathirika na ugonjwa wa kansa. Hili ni kweli, tunakiri. Ni kwa sababu jua hili ambalo ni mionzi yetu ya jua lina ultraviolet rays ambazo zinaathiri ngozi za wenzetu hawa ambao wana ulemavu wa ngozi kwa kiasi kikubwa kulinganisha na wengine ambao wasiokuwa walemavu wa ngozi na tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba wenzetu ambao wana ulemavu wa ngozi wanajikinga dhidi ya miale ya jua kwa kuvaa kofia na nguo ambazo zinakinga sehemu kubwa ya miili yao, lakini vilevile kutumia mafuta ambayo yanawakinga dhidi ya hii miale ya jua.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, huduma za matibabu ya kansa ni bure ndani ya nchi yetu. Nami nawaomba sana, mtu yoyote ambaye anaona kuna mabadiliko katika ngozi yake, basi aweze kufika katika vituo vya kutolea huduma ya afya aweze kupata huduma kwa haraka.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea kidogo kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya pamoja na majibu yake mazuri; ni kwamba naomba tu niendelee kutoa msisitizo kwamba Wakurugenzi katika Halmashauri mbalimbali wajitahidi kwamba wanakuwa na idadi kamili ya haya mahitaji kwa maana ya watu wenye mahitaji, watu wenye ualbino. Kwa sababu wasipokuwa na orodha kamili ya mahitaji, inakuwa ni ngumu upatikanaji wa hizi dawa kutoka MSD. Hili limekuwa ni tatizo ambalo katika ziara ambazo nimewahi kuzifanya imeonekana kwamba mahitaji haya hayapatikani kulingana na uhalisia wa watu waliopo. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Kijiji cha Kipangege, Kata ya Soga mradi wa maji tayari umeshakamilika lakini hadi hivi sasa wananchi hawajaanza kutumia maji hayo. Je, lini sasa mradi huu utakamilika na kuanza kutoa maji ili wananchi wa Kata ya Soga waanze kufurahia huduma ya maji safi na salama?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili pia linafanana na tatizo la Wilaya ya Arumeru katika Jimbo la Arumeru Magharibi, Kata ya Bwawani ambapo mradi wa maji tangu enzi za aliyekuwa Mbunge Elisa Mollel na Ole- Medeye ulianza kujengwa mpaka leo hii bado haujakamilika na Serikali imekwishatoa fedha mkandarasi hayupo. Napenda tu kufahamu majibu kutoka kwa Serikali, nisikie kauli yao juu ya mradi huu ili wananchi wa Kata ya Bwawani nao waweze kupata maji na kuondokana na changamoto kubwa iliyopo hivi sasa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma kwa kazi nzuri anayoifanya katika Mkoa wa Pwani. Kikubwa sisi kama Wizara ya maji jukumu letu ni kuhakikisha Wanapwani, kwa maana ya Soga, waweze kupata maji safi na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema katika Kijiji kile cha Kipagenge katika Kata ya Soga kuna mradi lakini wananchi hawapati maji. Nataka nimhakikishie baada ya Bunge nitafanya ziara katika eneo hilo la Soga, niangalie ili mwisho wa siku mradi ule uweze kukamilika na wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia dada yangu Amina Mollel amezungumza kwamba sasa mradi umekuwa wa muda mrefu sana, kwamba Serikali imekwishatoa fedha lakini mkandarasi hayupo site. Nimhakikishie katika maeneo nitakayotembelea basi na Arumeru Mashariki nitafika na kuhakikisha tunaongeza nguvu katika mradi ule ili wananchi waweze kupata maji safi na salama na yenye kutosheleza.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, namshukuru pia Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kwa kuwa Serikali sasa imekiri taarifa hizi, na tunafahamu kwamba siyo kila jambo linalojadiliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki zinakubaliana na tumeshaona kwamba ni tatizo. Je, Serikali inachukua tahadhari gani ili basi jambo hili lisije kutokea kwa sababu litakuwa na madhara makubwa?

Pili, iwapo Serikali ya Kenya itasimama kutekeleza mradi huo; Je, ni madhara gani makubwa ambayo yanatarajiwa hasa kiikolojia na athari zake katika mzunguko wa wanyama, yaani Wild West Movement? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana kwa swali lake zuri sana, kimsingi uhai wa Mto Mara ndiyo uhai wa Hifadhi ya Serengeti, na ikolojia ya Serengeti inaanzia katika hifadhi zilizoko nchini Kenya. Kwa hiyo, uwepo wa Mto Mara na uhai wa uhifadhi wa Serengeti ni kitu ambacho sisi kama Wizara tunakitilia kipaumbele sana, kwa hiyo, nampongeza sana kwa maswali yake mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza; Je, Serikali inachukua tahadhari gani tumewaelekeza TANAPA kuanza kufuatilia kwa karibu mienendo yoyote ile ambayo inaweza ikapelekea utekelezaji wa mpango huu, na kwa kuwa tunaamini kwamba sisi Serengeti ni Mbuga yetu ambayo tunaitegemea, pia tumewaelekeza kuangalia kama inawezekana kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji ili pale utekelezaji wa miradi hii itakapofanyika wanyama wasije wakaathirika kwa ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni madhara gani makubwa yanayotegemewa ni kwamba kimsingi wanyama tunaowaona Serengeti wengi katika msimu wao wa mwaka mzima huwa wanatembea katika nchi hizi mbili. Kwa hiyo, Wild West Movement ambayo huwa inatokea Tanzania, huwa inapita mpaka Maasai Mara. Kwa hiyo, iwapo ikolojia hii itaharibiwa, maana yake ni kwamba wanyama hawa wataacha sasa kuwa wana-cross border kuja Tanzania au ku-cross kwenda Kenya na matokeo yake utalii huu ambao ni urithi wa dunia unaweza ukaathirika.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza dada yangu Mheshimiwa Mary Mwanjelwa kwa majibu mazuri yaliyokwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali iliwafukuza watumishi ambao walighushi vyeti au hawakuwa na vyeti vya kidato cha nne na kati ya hao watumishi ambao walifukuzwa ni kwamba, walikopa katika benki zetu na mpaka sasa hawajui hatima yao na wengine wamekufa na wengine wamekimbia nyumbani kwa sababu, benki zinawafuata mpaka nyumbani. Nataka kujua kwa sababu, wakati wanachukua Serikali ndio ilikuwa guarantor wao. Sasa je, nini Kauli ya Serikali kwa benki ambazo zinawasumbua hawa watumishi na hawana jinsi ya kuweza kurudisha hizo fedha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la mdogo wangu, Mheshimiwa Amina Mollel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali Mei, 2016 ilienda kwenye zoezi la kusitisha upandishwaji wa madaraja na vilevile kusimamia hilo zoezi zima la vyeti feki, lakini sio vyeti feki tu hata watumishi hewa. Tukumbuke kabisa kwamba, wakati najibu hapa swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Tunza Malapo nimesema Serikali inakwenda mbali zaidi katika kuwajali watumishi kwenye motisha hata katika kuwapatia guarantor mbalimbali ikiwemo na mikopo ya benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukumbuke watumishi hawa walikuwa ni halali, walikuwa ni watumishi halali na ndio maana Serikali inakuwa ni guarantor. Sasa kama wewe tayari umeshafukuzwa na hiyo tunasema ni crime kwa maana hiyo, sisi tunazingatia tu kwa yule mtumishi ambaye ni halali, Serikali itamjali, Serikali itakuwa ni guarantor pamoja na mambo mengine ya motisha. Ahsante.