Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Anastazia James Wambura (9 total)

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kusimama na kuzungumza mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchukuwa nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ushindi wa kishindo alioupata katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Vilevile namshukuru kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na imani yake kwangu, naahidi kutekeleza majukumu yangu kwa weledi na juhudi kubwa ili kumsaidia Mheshimiwa Waziri katika kutekeleza majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Zanzibar katika kipindi kingine cha miaka mitano. Natumia fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile nawapongeza Mawaziri wote walioteuliwa kuongoza Wizara mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda kumpongeza Spika, Mheshimiwa Job Ndugai; Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, wewe mwenyewe pamoja na Wenyeviti wote kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru sana Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, kwa kunielekeza na kuniongoza katika kufanya maamuzi sahihi yanayohusu utekelezaji wa shughuli zinazohusu sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa, nawashukuru wanawake wa UWT Mkoa wa Mtwara kwa kunichagua kwa kipindi cha tatu kuwa Mbunge wao kupitia tiketi ya Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa nimetenda haki pasipo kuishukuru familia yangu, hasa mume wangu mpenzi, Bwana Laurent Werema Paul na watoto wangu kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa na kunitia moyo katika kutekeleza majukumu yangu ya kazi za kila siku za Wizara ninazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ya Yanga katika historia ya nchi yetu imeweka rekodi kwa mara nyingine baada ya rekodi ya mwisho iliyowekwa na timu ya Simba mwaka 2003. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza sana timu ya Yanga kwa kuwa Bingwa wa Soka Tanzania Bara, lakini pili kushiriki Kombe la Washindi Bara la Afrika; na ni matarajio yetu kwamba wataingia hatua ya makundi baada ya mechi yao na timu ya Angola na hasa kutokana na ushindi walioupata katika mechi ya kwanza katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja ya Wizara yetu na baada ya kusema hayo, naomba sasa kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya kwanza ambayo inahusu kutokuwepo viwanja vya michezo katika ngazi za Mkoa, Halmashauri na shule. Hoja hii imetoka kwa Waheshimiwa wafuatao; Mheshimiwa Kasuku Bilago, Mheshimiwa Lucy Owenya, Mheshimiwa Stanslaus na Waheshimiwa Wabunge wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kila Halmashauri, nadhani tunatambua kabisa kwamba kuna Kamati za Mipango Miji na vilevile kuna Baraza la Madiwani na Wabunge sisi ni miongoni mwa Baraza la Madiwani. Sasa Wizara tunasisitiza kabisa kwamba Halmashauri kupitia Baraza la Madiwani na Kamati ya Mipango Miji watenge maeneo katika kila shule. Watakapokuwa wanatenga maeneo ya shule tunawaomba Halmashauri wakumbuke kuacha maeneo ya kutosha kwa ajili ya viwanja vya michezo ili hata watakapokuwa wakiongeza majengo, lazima yabaki maeneo kwa ajili ya michezo. Vilevile katika ramani za makazi, tunaomba Halmashauri wahakikishe kwamba wanaacha viwanja vya michezo katika makazi ili wananchi waweze kufanya mazoezi na kucheza michezo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge wasimamie zoezi hili na wahakikishe kwamba wanafanya ukaguzi katika maeneo ambayo yametengwa ili kuona kama viwanja vya michezo vipo. Kuhusu ubora, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) litakuwa likikagua ili kuangalia ubora wa viwanja hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya pili ambayo inahusiana na kutokuwepo watumishi wa sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo katika baadhi ya Halmashauri. Waliochangia wameonyesha kwamba pia hata zile Halmashauri ambazo zina watumishi hawa, bado kuna matatizo kwamba wanakosa vitendea kazi. Sasa sisi kama Wizara tumeshaongea na Wizara ya TAMISEMI ili ianzishwe Idara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kila Halmashauri. Hii tunaamini kabisa itasaidia Idara hii kuwa na fungu lao la bajeti ili waweze kuwa wanapata vitendea kazi na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kubwa ni kuendeleza sekta hizi za habari, utamaduni na michezo kuanzia ngazi za chini na tunataka Wizara iwafikie wananchi vijijini kupitia Idara hii. Lengo lingine ni kwamba tunataka Wizara iwe na mfumo mzuri wa upatikanaji wa taarifa kupitia Idara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili tuweze kupanga vizuri shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine ya tatu ambayo imetolewa na Mheshimiwa Martha Mlata na Wabunge wengine, ni kutaka wasanii wapatiwe ardhi lakini vilevile kuwepo kituo kwa ajili ya sanaa za aina mbalimbali. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara tumeshaongea na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya suala hili na upatikanaji wa ardhi utakuwepo kwa sababu Wizara ya Ardhi imeshaanza kulishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Kituo cha Sanaa na Utamaduni, Wizara tayari tumeshapata eneo la ekari 25 katika eneo la Kiromo, kule Bagamoyo na taratibu za ujenzi zitafuata, lakini vilevile kwa wale watu binafsi ambao wanapenda kuingia, sekta binafsi ambazo zitapenda kuingia ubia ili kuweza kuharakisha ujenzi tunawakaribisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya nne ambayo imegusiwa pia na wachangiaji wengi, ni kutokuwepo usikivu wa redio ya TBC katika baadhi ya Wilaya za nchi yetu.
Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara tayari imeshatenga fedha za maendeleo katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017 kwa ajili ya Mkoa wa Kigoma ambayo itaongeza usikivu katika Wilaya za Kasulu na Kakonko, Mkoa wa Mara Wilaya ya Tarime, usikivu katika Mkoa wa Ruvuma Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Tanga Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Arusha Wilaya za Longido na Ngorongoro, Mkoa wa Kilimanajro Wilaya ya Rombo na Mkoa wa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wakubali kupitisha bajeti yetu ili tuweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutupa fursa hii ya kuweza kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya nchi yetu kwa muktadha wa uendelezaji wa Sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Watanzania wenzangu wote kutoa pole kwa msiba huu uliotupata na Mungu atupe faraja kama wazazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kusimamia vizuri Serikali na hasa kwa upande wa mapato na matumizi hadi kupelekea Wizara yetu kuongezewa bajeti kwa asilimia 19 kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Pia nimpongeze Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti kwa kuliongoza Bunge kwa weledi, lakini pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa umoja na ushirikiano walionao katika kuwatetea wananchi na kuboresha bajeti ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wangu, kwa hotuba nzuri ya Bajeti ya Wizara aliyoitoa tarehe 5 Mei, 2017 ambayo utekelezaji wake utaleta matokeo na mageuzi makubwa katika kuimarisha sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri wangu kwa ukarimu wake mkubwa kwangu, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Idara na Taasisi pamoja na watumishi wa Wizara yangu kwa ushirikiano wanaonipa katika kazi zangu za Naibu Waziri. Niwashukuru wanawake wote wa UWT wa Mkoa wa Mtwara kwa kuendelea kushirikiana na mimi na kuniombea pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nasema ahsante kwa familia yangu inayoongozwa na mume wangu mpenzi Laurent Werema, kwa kunivumilia, kunitia moyo na kuniombea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, naomba na mimi nichangie kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianzie na sekta ya habari. Katika sekta hii tuna kundi la kwanza ambalo ni TBC ambapo Kamati iliitaka Serikali kulipa shirika uwezo wa kujiendesha. Wizara na TBC tayari zimelifanyia kazi suala la tozo ya visimbuzi (ving’amuzi) na andiko kuhusu tozo hii mpya linafanyiwa kazi na Wizara ya Fedha na liko katika hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la Kamati ni kwamba TBC ijenge studio ya kisasa Makao Makuu Dodoma. Fedha za kuboresha studio za TBC Dodoma zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018. Tukiangalia ukurasa wa 79 katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri fedha hizi zinaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pamoja na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameitaka Serikali kuimarisha usikivu wa TBC na utendaji, lakini pia kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Ni kweli kwamba TBC inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa mitambo lakini hata hivyo Serikali imeanza kuchukua hatua zifuatazo katika kutatua kwa awamu changamoto za shirika. Katika mwaka ujao wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha za matumizi ya kawaida na bajeti ya maendeleo kutoka shilingi za Kitanzania bilioni moja hadi shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni moja kwa mwaka 2016/2017 imeshapatikana na hii ni kwa ajili ya kuboresha usikivu katika maeneo matano ya mipakani na moja ni Kakonko (Kibondo), Mheshimiwa Kasuku kama yupo amelipigia sana kelele suala hili kwa hiyo awaambie watu wake wakae mkao wa kula. Pia katika Wilaya za Nyasa, Longido, Rombo, Tarime na leo pia nimesikia Mheshimiwa Ngonyani akilipigia kelele, kwa hiyo, wananchi wa Nyasa nao wakae tayari kwa ajili ya usikivu wa TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Kamati pia ambalo linaitaka Wizara ihamishe mashine ya zamani ya TSN ya kuchapia magazeti ifungwe Dodoma ili kurahisisha upatikanaji wa magazeti. Wizara itafunga mtambo mpya Dodoma na hii ni kwa sababu kitaalam mtambo wa zamani ukifunguliwa na kuhamishiwa Dodoma unaweza kuharibika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utamaduni; Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Serikali kukuza utalii wa kiutamaduni na majibu yake ni kwamba Serikali imeendelea kuratibu, kusimamia na kutangaza bidhaa za utamaduni na kufanya maonesho na matamasha ya fani mbalimbali za utamaduni ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuvutia utalii na kuingiza mapato.

Mheshimiwa Spika, kuna mchangiaji mmoja pia alipendekeza kwamba kila mkoa kuwe na makumbusho lakini hili ni suala la Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Kitengo cha Malikale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kudhibiti mmomonyoko wa maadili ambalo limechangiwa na Wabunge kadhaa. Maadili ni mwenendo unaokubalika na wengi katika utendaji kazi au uendeshaji wa maisha. Kwa hiyo, suala hili ni la watu wote na inatakiwa lianzie katika familia hadi katika taasisi. Hata hivyo, Wizara inaendelea kutoa elimu kuhusu uzingatiaji wa maadili ya Mtanzania na kuchukua hatua mbalimbali za kisheria pale panapotokea ukiukwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maendeleo ya sekta ya sanaa, Kamati imeitaka Wizara iendelee kupambana na wizi wa kazi za wasanii. Wizara inaishukuru Kamati kwa kuunga mkono jitihada za Wizara na pia kwa kutoa msimamo wake kwa kuwataka wote wanaohusika na uharamia wa kazi hizo kuacha mara moja. Aidha, Wizara inakubaliana na ushauri wa Kamati kuhusu uboreshaji wa kazi hizo na itaendelea kushirikiana na wadau kuwajengea uwezo ili kuboresha kazi zao ili waweze kuendana na maendeleo ya teknolojia na kushindana katika soko la ndani na la nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Kamati imehimiza uboreshaji wa filamu za ndani na wananchi pia kununua kazi za ndani. Ushauri huo wa Kamati umepokelewa na utafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Kambi ya Upinzani katika sekta ya sanaa kwamba matumizi ya stempu za TRA kutofanya kazi vizuri kutokana na teknolojia ya mtandao. Stempu hizo hutumika kubandikwa katika DVD na CD ambazo kwa sasa ndiyo mfumo unaotumika kusambaza kazi hizi hapa nchini. Kutokana na ukuaji wa teknolojia tayari taratibu za kutengeneza stempu katika nakala laini zinaendelea na stempu hizi toka zimeanza kutumika zimefanikisha kubaini na kukamata kazi zisizo halali zenye thamani ya shilingi bilioni 5.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani pia ilionesha kwamba kuzuia kazi za nje ya nchi sio kinga ya wizi wa kazi za filamu na muziki. Serikali haijazuia filamu za nje bali inazitaka kufuata sheria, kanuni na taratibu. Kwa hiyo, dhana hii kwamba tunazuia kazi za nje si kweli, tunataka utaratibu ufuatwe na sheria vilevile zizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Wizara ni kulinda mila na desturi zetu na kulinda kazi za wasanii na hatutakubali ukiukwaji wa utamaduni wetu na hatutakubali pia kazi za nje ziingie katika nchi yetu bila kufuata utaratibu. Wizara yangu iliwasilisha barua TAMISEMI kuwaomba wawasiliane na mikoa yote ili kuona namna bora ya kuondokana na filamu zisizofuata utaratibu. Kwa hiyo, utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni kwa nchi nzima. Kwa hiyo, tusichukulie kwamba kwa kuwa yeye ametekeleza kwamba ni uamuzi wake.

Mheshimiwa Spika, nimeshasema kwamba Wizara iliandika barua TAMISEMI na kuomba wawasiliane na mikoa yote ili kuona namna bora ya kuondokana na filamu zisizofuata utaratibu, kwa hiyo, mikoa yote inatakiwa kufuata na kuzingatia agizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la upatikanaji wa Vazi la Taifa ambalo nalo limechangiwa na Wabunge kadhaa. Suala hili lilifikia katika ngazi ya Baraza la Mawaziri na uamuzi ulikuwa kwamba Vazi la Taifa litokane na kuamuliwa na wananchi wenyewe. Nikitoa mifano tu ni kwamba hata kipindi cha zamani ilikuwa inatokea mama zetu tulikuwa tukiwasikia wanasema leo tuvae Kitaifa, lakini hapa katikati pia lilizuka vazi fulani ambalo linatokana na kitambaa cha kitenge (makenzi) likaenda mpaka kutaka kuwa kama Vazi la Taifa. Kwa hiyo, ni vyema wananchi wakaamua sasa tuvae vazi gani kama ndiyo Vazi la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuboresha soko la ndani la tasnia ya filamu na kusimamia mapato ambapo tayari wapo watayarishaji wa filamu ambao wameendelea kutengeneza filamu nzuri zilizoweza kuingia kwenye soko la ushindani la ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, hoja ya uwepo wa filamu za nje zisizofuata taratibu zimefanya soko la ndani kukumbwa na ushindani mkubwa na Serikali na wadau husika kukosa mapato. Serikali katika kuboresha soko la ndani imeendelea kuwajengea uwezo watayarishaji na wazalishaji wa filamu ili kufanya kazi zao kwa weledi na kwa ubora wa hali ya juu kama inavyoelekezwa kwa kina katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uboreshaji wa tasnia ya ulimwende ambalo limechangiwa na wachangiaji kama wawili hivi. Tasnia ya ulimwende imeendelea kuendeshwa nchini kutoka mwaka 1994 na imeendelea kuwa na mafanikio makubwa hasa katika kuitangaza nchi na vivutio vyake ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na waandaaji kurekebisha dosari mbalimbali zilizojitokeza na kuwa na mfumo bora na uwazi wa uendeshaji wa mashindano mbalimbali ya ulimwende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Miss Tanzania, Wizara katika kulinda hadhi ya shindano hilo imetoa maagizo yafuatayo kwa waandaaji wa shindano hilo (Lino International Agency). Lino International Agency ihakikishe kwamba Kamati ya Miss Tanzania inatoa zawadi ya gari kwa mshindi wa Miss Tanzania 2016 na washiriki wengine wote wanaodai zawadi zao ndani ya mwaka huu kabla ya Juni, 2017 na endapo wakikaidi ama wakishindwa kutoa zawadi katika muda huo watakuwa wamejitoa wenyewe kwenye biashara hii na sheria itachukua mkondo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuitaka Serikali ikamilishe utungwaji wa Sera ya Filamu. Tayari maandalizi ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Filamu yamefikia hatua ya kupata rasimu ya sera. Wadau mbalimbali wametoa maoni na rasimu hiyo itawasilishwa katika ngazi za maamuzi mwishoni mwa mwezi Juni, 2017. Rasimu hiyo ya sera imezingatia pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuanzishwa kwa shule ya filamu (film school).

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya michezo. Katika sekta ya maendeleo ya michezo kuna hoja iliyojitokeza ya CCM kurejesha viwanja vyake Serikalini. Hili suala limetolewa ufafanuzi mara kadhaa hapa Bungeni lakini hata hivyo niendelee kusema tu tena kwamba viwanja hivi ni vya CCM kwa sababu hatimiliki ni ya CCM. Niseme tu tena kwamba haipo hati ambayo inaonesha kwamba kuna kiwanja kilikuwa cha mmiliki mmoja kikahamishiwa kwa CCM, kwa hiyo tuelewe wazi kwamba hivi viwanja ni vya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameitaka Serikali ijenge na kulinda viwanja na maeneo ya wazi. Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995 inaelekeza kuwa jukumu la ujenzi wa viwanja linashirikisha wadau wote ikiwemo Serikali na wadau wengine. Serikali katika juhudi zake za kuboresha miundombinu ya michezo inashirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje kujenga miundombinu kwa ajili ya matumizi ya michezo.

Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha azma hiyo, Serikali imejenga Viwanja vya Taifa na Uhuru na sasa inajiandaa kujenga Uwanja wa Dodoma. Aidha, mamlaka mbalimbali na wadau nchini wanahamasishwa kushiriki kama walivyoanza baadhi kama vile Azam, Halmashauri ya Bukoba Mjini, Liwale, Lindi na kadhalika na taasisi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa wadau mbalimbali wa michezo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kuwa halmashauri zao zinatenga maeneo na bajeti kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya michezo. Aidha, natoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa viwanja vyote vilivyovamiwa katika maeneo yao vinarejeshwa ili viweze kutumika kwa shughuli za michezo na burudani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba yupo mdau mmoja muhimu sana katika kuendeleza viwanja vya michezo ambaye ni TFF. Kwa taarifa ni kwamba kwa sasa ule Uwanja wa Tanga uko mbioni kuanza kujengwa mwaka huu, wanasubiri tu bajeti ipitishwe ili waweze kuujenga. Vilevile kama nilivyosema hapo awali, viwanja vya Lindi na Memorial Moshi viko kwenye list ya ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme tena naunga mkono hoja, ahsanteni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Pongezi nyingi kwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri na kwa kazi nzuri hasa ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Kwanza naomba Wizara yako ifuatilie tozo wanayotozwa wavuvi wa Mtwara, shilingi mia tano arobaini na saba kwa kilo ya samaki. Je, ni tozo ya watu binafsi? Kimsingi tozo hii imeathiri uchumi wa wavuvi wa Mtwara na naomba Mheshimiwa Waziri atembelee Mkoa wa Mtwara kama alivyofanya kwa jamii za wakulima na wafugaji.
Pili, napongeza jinsi Wizara ilivyoongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji katika nchi yetu. Umwagiliaji huu kwa kiasi kikubwa ni kwa mazao ya chakula cha wanga. Ushauri wangu kwa Wizara ni kuongeza uzalishaji wa mbogamboga na matunda kwa kuwezesha umwagiliaji wa matone (Drip Irrigation).
Hoja yangu inatokana na hali halisi ya upatikanaji wa mboga na matunda kwa msimu fulani ambapo wakati mwingine bidhaa hizi huadimika na kupelekea bei kupanda kwa kiasi kikubwa. Athari za hali hii zinaweza kuonekana katika lishe ya jamii kuwa duni. Hivyo, naomba wataalam wa Wizara wajitahidi kuwaandaa wananchi pale watakapopata mikopo ya milioni hamsini wengine wawekeze kwenye kilimo cha mbogamboga na matunda kwa (Drip irrigation).
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. „Kama mnataka mali mtaipata shambani‟
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri Mahiga, Naibu Waziri Kolimba na timu yote ya Watendaji kwa kuandaa vizuri hotuba ya bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri katika maeneo mawili. Kwanza, nashauri Wizara iwekeze katika viwanja vilivyoko nje ili kupata fedha za kuendesha balozi zetu. Kwa mfano, kiwanja tulichopewa na Serikali ya Msumbiji tukakiacha, mwisho wake tunaweza kunyang‟anywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Maafisa wa Korea Kusini waliwahi kuja kuongea na Kamati yetu ya Mambo ya Nje na kuialika iende nchini humo ili kuona uwezekano wa kuanzisha Ofisi ya Ubalozi Korea Kusini. Ni ushauri wangu kwamba Wizara ilifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja yetu hii ya Azimio la Mkataba wa Kudhibiti Matumizi ya Dawa na Mbinu Haramu katika Michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kukupongeza kwa kazi nzuri ambayo unaifanya, kwa kuliendesha Bunge kwa kutumia Kanuni vizuri. Vilevile niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika hoja yetu hii na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi alivyowasilisha hoja kwa umahiri mkubwa. Hongera sana Mheshimiwa Waziri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na faida kubwa ambazo ziko katika mkataba huu tunaona hakuna vipengele vyovyote ambavyo hatuhitaji kuviridhia, kwamba hakuna reservations. Kwa hiyo ni mkataba mzuri, hii inaonesha wazi kabisa huu ni mkataba mzuri na ndiyo maana hakuna reservations zozote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie tu na hili la kijana wetu huyu aliyepatwa na dalili, hakukutwa moja kwa moja na madawa lakini kulikuwepo na dalili ambazo zinaashiria kwamba kulikuwa na dawa za kuongeza nguvu kule Brazil, akafungiwa kwa miaka miwili. Sasa kutokana na hilo inaonekana kwamba mwaka 2015/2016 zimechukuliwa sample 14 na kupelekwa katika Maabara za Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri tunashukuru sana Wizara inafurahi na ina faraja kwamba sampuli zote hizi 14 hakuna hata moja ambayo ilikutwa na dalili za kuwepo na matumizi ya dawa au mbinu za kuongeza nguvu michezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu una manufaa makubwa, mojawapo ni lile la kutoa elimu pamoja na mafunzo kwa vijana wanamichezo wetu pamoja na watalaam wengine, lakini pia inatoa fursa kubwa sana za utafiti. Nami nichukue fursa hii sasa kutoa wito kuwaomba watafiti wetu wajiandae, pale ambapo mkataba huu utakapokuwa umeanza kufanyakazi kuna maeneo mengi sana ya kufanyia utafiti na yanaelezwa katika vifungu mbalimbali vya mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, wanaweza wakafanya utafiti katika maeneo ya saikolojia, maeneo ya utu wa wanamichezo, physiology, wanaweza wakafanya pia utafiti katika sayansi ya michezo, wanaweza pia wakafanya utafiti katika vitu mbalimbali ambavyo vinajitokeza kulingana na maendeleo ya kiteknolojia, kuna vitu vipya ambavyo vinaweza vikajitokeza kama matumizi au dawa za kuongeza nguvu. Kwa hiyo watafiti wetu wajiandae kufanya kazi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja moja ambayo imejitokeza kutoka kwa Mheshimiwa Hafidh Ali alipokuwa akichangia kwamba ni vizuri sasa tukafanya maandalizi. Nafurahi kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara imeshaanza kufanya maandalizi machache. Kwa mfano, kuna wataalam ambao tayari wameshaanza kupewa elimu ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeshaandaa eneo pale katika uwanja wa Taifa kwa ajili ya ofisi ya National Anti-doping Agency. Kwa hiyo, maandalizi kama hayo yamefanyika. Pia yanatakiwa maandalizi ya kisera, kisheria na kanuni ambavyo napenda kulitaarifu Bunge lako kwamba Wizara yetu imejipanga vizuri kabisa kwa ajili ya hili, kuandaa, kurekebisha sera na kufanya marekebisho, kuipitia upya pia sheria yetu ya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hafidh Ali pia katika mchango wake aligusia jambo ambalo naona pia ni muhimu sasa watafiti tutawaomba wajiandae kulifanyia kazi, kwamba kuna watu ambao unaona kabisa umri umepita lakini wanacheza vizuri tu mpira na amekuwa na mashaka kwamba labda kuna vitu wanavyotumia. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo pia watafiti wanaweza wakalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine ambayo inahusiana na matumizi ya bangi na pombe katika michezo. Suala la pombe lipo limezuiliwa na liko katika kundi la alcohol, lakini kuzuiwa kwake ni wakati wa mashindano tu. Kwa hiyo hili nalo tutaliangalia, wakati wa kutunga sheria nitaomba Bunge lako pia liangalie kama kweli izuiliwe kwa wanamichezo wakati wa mashindano tu au sasa watazuiwa moja kwa moja sijui, lakini bangi inazuiwa na iko katika kundi la cannabinoids. Bangi inazuiwa kabisa, hairuhusiwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine ambayo ameichangia Dkt. Ndugulile kwamba, hata zile dawa ambazo ni za tiba zinazuiliwa. Naomba kumtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kipo Kifungu cha 34 katika Mkataba huu na hiki Kifungu kinaruhusu sasa ile World Anti-Doping Agency, kufanya Amendments kwa ile list ambayo ni prohibited list ili therapeutic use exemptions. Kwa hiyo utaona kwamba, hii WADA ikifanya amendments masuala ya dawa kwa ajili ya matumizi ya kiafya yanaweza yakaruhusiwa kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. Ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Maghembe na Naibu wake Engineer Ramo pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika Wizara ya Maliasili.

Mheshimiwa Mwenyekiti mchango wangu uko katika maeneo mawili, kwanza ni kuhusu utalii wa utamaduni, lakini pili nimalizie kuhusu suala la Vazi la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukiri kabisa kwamba tuna vivutio vingi vya utalii wa utamaduni katika nchi yetu kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wenzangu, lakini Wizara yetu ina kazi kubwa, iko katika mchakato wa kutekeleza Mkataba wa UNESCO wa mwaka 2003 ambao unahusu Urithi wa Utamaduni Usioshikika na ule mkataba wa mwaka 2005 wa Kulindwa na Kukuzwa kwa Uanuai wa Kujieleza Kiutamaduni.

Sasa tunachofanya sisi Wizara ni kukusanya taarifa na tafiti kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo Halmashauri, na taarifa hizi zinahusu maeneo ya kihistoria, kimila, kidesturi na vivutio vya utalii wa kiutamaduni.

Mheshimiwa Mwenyekiti katika zoezi hili tunashirikiana kwa karibu kabisa na Wizara ya Maliasili, Kitengo cha Malikale pamoja na TAMISEMI na zoezi hili ni endelevu na uendelevu wake utaona kwamba kuanzia mwezi Agosti, 2016 hadi sasa tumeshapata vivutio vipya kutoka Halmashauri 35 na Mikoa 19. Lengo kumbwa ni kuzitumia taarifa hizi katika kuwasaidia wananchi kuweza kutumia utalii wa kiutamaduni kuongeza kipato. Kwa hiyo, nitoe wito kwamba Halmashauri zote ziendelee na zoezi hili na tuna dhamira kubwa ya kutumia baadhi ya mila na desturi zetu katika kuzipeleka kwenye orodha wa Urithi wa Utamaduni wa Dunia. Kwa mfano, mila na desturi ya jando na unyago ambayo iko katika Mikoa ya Kusini na Mikoa ya Ukanda wa Pwani kama vile Wamakonde; na ile mila ya Wamasai ya kurithisha ngazi ya rika ya kipengele cha Engpaata Yunoto na Olng’esher. Kwa hiyo, vivutio hivi vikiingia katika Orodha ya Urithi wa Dunia vitasaidia sana kuwa vivutio vya utalii wa utamaduni katika yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi binafsi nikiri kwamba nimeshawahi kutembelea baadhi ya vivutio na niseme tu kwamba bado Halmashauri zetu zina kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba zinaboresha mazingira katika maeneo yale ya vivutio. Kwa mfano, Halmshauri hizi zihakikishe kwamba kunakuwepo na vyoo, barabara nzuri, maeneo ya kulia chakula kwa sababu vivutio vingine vingi viko katika maeno ya maporini, lakini ni vizuri sana. Kwa mfano nilishawahi kufika katika kichuguu ambacho kinacheza kule Babati, kunahitajika maboresho ili kusudi watalii wengi waweze kufika. Nishauri tu Halmashauri zione umuhimu wa kutenga bajeti ili kusudi kuweza kuboresha maeneo hayo Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande mwingine nizishauri halmashauri pia ziwatumie wacheza filamu pamoja na waigizaji katika maeneo yao kwa kuwapa mikopo ili kusudi waweze kucheza filamu za…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana kwake Mheshimiwa Waziri Charles Tizeba na Naibu Waziri Mheshimiwa William Olenasha kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na timu yao, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara. Hotuba yao ni nzuri na imejitosheleza kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji lishe bora kwa wananchi wote wa Tanzania. Ni muhimu tuwahakikishie upatikanaji wa mboga na matunda kwa mwaka mzima kwa bei nafuu. Wizara ianzishe Drip Irrigation kila Wilaya kwa kutumia visima virefu. Kilimo hiki pamoja na kuboresha lishe ya jamii kitasadia kuongeza kipato hasa kwa makundi ya wanawake na vijana. Pia kitaongeza ukuaji wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zitembelewe na ukaguzi ufanyike kuhusiana na tozo kubwa wanazotozwa wavuvi. Yapo malalamiko ya kwamba wavuvi kule Mtwara wanalipa dola 500 kwa kila kilo moja ya samaki wanaovuliwa kutoka Msumbiji na hivyo kupelekea hasara kwani bei ya kuuzia huwa ni ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana kwa usimamizi mzuri wa zao la korosho. Kwa msimu huu umakini uongezeke katika ugawaji wa pembejeo kwa wakati na udhibiti wa kangomba. Kutokana na bei nzuri ya korosho ya mwaka uliopita wakulima wengi sasa wanaomba mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao mengine kama mbaazi. Wizara iangalie uwezekano wa kuanzisha mfumo huu kwa mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ninaitakia Wizara kila la heri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, hongera sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kuandaa vizuri hotuba ya Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia majedwali katika kitabu cha hotuba jedwali namba 13 la orodha ya visima vilivyochimbwa hadi mwezi Machi, 2017, sehemu inayoonesha uwezo wa kisima kuna maeneo yameachwa wazi na maeneo mengine yameachwa wazi kwa uzembe. Kwa mfano, kisima namba 204 cha Msijute kilichofadhiliwa na ESRF na kuchimbwa na Wakala wa Visima wa Serikali kuna uzembe mkubwa umefanyika. Baada ya kuchimba kisima waliletwa watu wa kupima uwezo wake wakatoa taarifa kwamba hakuna maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa ESRF wamehitaji wapate taarifa itakayowaelekeza nini kifanyike ili maji yapatikane lakini miezi imepita bila mafanikio, binafsi wakala waliniambia niongeze shilingi milioni tatu ili wachimbe kisima kingine na baadae mwezi wa nne nikaambiwa niongeze shilingi milioni sita ili nichimbiwe kisima kingine. Ajabu ni kwamba watu wa bonde walipokuja wamepima na kuona kwamba maji yapo kwa asilimia 30 ya mita 150 zilizochimba, wamesema kwamba wale waliojaribu kupima uwezo wa kisima walitumia pump kubwa ambayo ilikausha maji kwa muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yao ni kwamba zingetumika pump zenye uwezo tofauti na pia ilibidi wa-flash kisima, ushauri wangu kisima kile ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Msijute ambao walimuamini Wakala wa Visima wa Serikali. Ni vema iandikwe taarifa ya ukweli na uwazi kwa ESRF ili aweze kuchukua hatua za ziada kuwasaidia wananchi wa kijiji cha Msijute wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, chunguzeni visima vyote ambavyo havioneshi uwezo wake mjue sababu na taarifa itolewe kuepusha ubabaishaji wa baadhi ya wachimbaji visima. Fikeni katika maeneo husika mkutane na wachimbaji na Mamlaka za Mabonde na wafadhili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote. Nichukue pia nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Nape Moses Nnauye kwa hotuba yake nzuri ambayo ameitoa, lakini vilevile kwa ujasiri na kazi kubwa ambayo ameifanya hadi kufikia hatma ya kufikisha Muswada huu Bungeni; hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuishukuru Kamati ya Bunge kwa ushirikiano wao na kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kutengeneza vizuri Muswada huu. Vilevile niwashukuru watendaji wa Wizara kwa ushirikiano ambao wametupa hadi kufikia dakika hii tunayozungumzia Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumshukuru mume wangu mpenzi Lawrent Paul pamoja na familia yangu kwa kuniombea kila wakati. Kwa namna ya pekee kabisa naomba nichukue nafasi hii pia kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri sana na ya kujenga ambayo naamini kabisa baada ya hapa Muswada huu unakwenda kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Nina masuala machache sana, matatu tu ambayo nitayazungumzia. Suala la kwanza ni ushirikishwaji wa wadau. Nizungumzie ushirikishwaji wa wadau na hasa pale ambapo liliibuka suala kwamba wadau walihitaji wapate miezi miwili zaidi na kikubwa ambacho baadaye kimezungumziwa baada ya kuwa ufafanuzi wote wa kina umetolewa na Mheshimiwa Waziri na Kamati, lakini baadaye ikaibuka kwamba kulikuwa na hitaji la kufika mikoani ili kusudi wadau waweze kuongea na press clubs kule mikoani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kusema kwamba sisi Wizara tulikuwa tunajua kwamba tuna Muswada huu na tuligawana kazi na Mheshimiwa Waziri. Katika kazi zetu za Wizara tulikwenda mikoani na tulipokwenda mikoani moja ya kazi ambayo tuliifanya ni kukutana na press clubs.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba walitupa ushirikiano mzuri sana; walikuwa wazi kutoa changamoto zao wakajieleza vizuri, lakini kati ya hizo changamoto ambazo tuliziona ni za muhimu kuletwa na kuingizwa katika Muswada wa Huduma za Habari ni mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza ilikuwa ni masharti magumu ya kupata press cards na changamoto ya pili ilikuwa ni kutokuwa na bima katika kazi zao, lakini pia kulikuwa na uhitaji wa kuwekwa katika Mfuko wa Hifadhi za Jamii. Haya yote tumeyaingiza katika kifungu cha 12(a) kinachoeleza kwamba Bodi ya Ithibati itakuwa ikitoa ithibati lakini pia itakuwa ikitoa press cards. Nashukuru kwamba hata Waheshimiwa Wabunge akiwemo Msemaji wa Kambi ya Upinzani wameliunga mkono na wamelipongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bima pia linaonekana katika kifungu cha 58; na hiki pia tumepongezwa kwamba ni jambo zuri ambalo limefanyika. Kwa hiyo, kimsingi suala la kuwashirikisha wadau na hasa pale ambapo tunatakiwa tuongeze muda mpaka mwezi wa Pili ili kusudi wale press clubs waweze kutoa mawazo yao, tayari tulikwishalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la pili ambalo limejitokeza na nataka kulizungumzia ambapo inaonekana katika michango yetu tumekuwa tukichanganya kati ya leseni, ithibati pamoja na vitambulisho. Sasa naomba nitoe ufafanuzi tu kidogo hapa kwamba, masuala ya leseni; leseni zinatolewa kwa vyombo vya habari hasa machapisho na hili linaonekana kwa mujibu wa kifungu cha 8(1), ila masuala ya hawa waandishi wa habari wao hawapatiwi leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, wasiogope kwamba watachukua mlolongo mrefu au watanyimwa uhuru wa kufanya kazi zao kwamba ni hadi wapate leseni, hao hawahusiki kabisa na leseni, wao wanachotakiwa kupata ni ithibati pamoja na vitambulisho. Kwa hiyo, wasiwe na wasiwasi kwamba kuna masuala ya leseni. Msuala ya leseni ni vyombo vya habari na kwa mujibu wa Sheria ya TCRA leseni ni kwa redio na televisheni, lakini kwa mujibu wa sheria hii inatolewa leseni kwa machapisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kifungu cha 7(1)(b)(iv) ambacho pia imeonekana kama kuna tatizo. Wengi wamekuwa wakitetea kwamba kwa ule wajibu wa vyombo vya habari unaosema kwamba vyombo vya habari vitatangaza au kuchapisha habari au masuala ambayo ni muhimu kwa Taifa kwa kadri Serikali itakavyoelekeza. Kwa hiyo, imeonekana kwamba kwa sababu wao ni wafanyabiashara hawatahitajika kuagizwa na Serikali kutoa taarifa za masuala muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mushashu kwa ufafanuzi mzuri ambao ameutoa jana, amelieleza vizuri sana jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee tu, kwa mfano, kuna nchi moja ya China, mwezi wa kumi kulitokea watabiri wa hali ya hewa, walitabiri kwamba kutatokea upepo mkali katika baadhi ya Majimbo kule China, lakini kwa kushirikisha vyombo vya habari waliweza kutangaza kwa wananchi kwamba upepo huu unatokea wapi na una speed gani. Vilevile, vyombo vya habari vikawatangazia wananchi wanunue chakula cha kutosha wiki nzima na wakaambiwa wakae ndani, wasitoke nje mpaka pale watakapotangaziwa kwamba hali imeshakuwa shwari na waliweza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo, hayakuweza kutokea madhara makubwa kwa binadamu na badala yake yalitokea madhara madogo madogo ambapo ilikuwa magari yaliyokuwa yame-park nje miti ikawa imeangukia, lakini siyo kwa binadamu. Pia yalitokea madhara machache kwa wale ambao walikaidi na pengine wale wanaoendesha pikipiki, upepo ule kwa sababu ulikuwa ni mkali uliweza kuwazoa. Vinginevyo visingekuwa vyombo vya habari kushirikiana na Serikali, ina maana kwamba sasa hivi yangekuwepo madhara makubwa katika nchi ya China.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuunge mkono muswada huu kwa sababu una umuhimu mkubwa sana kwa wanahabari, kwa vyombo vya habari, lakini pia kwa kila mmoja wetu ambaye yuko hapa na kwa wananchi wote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudia kusema tena, naunga mkono hoja, ahsanteni sana.