Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Angelina Adam Malembeka (6 total)

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba wenzangu wa upande wa pili wawe watulivu na hizo microphone wasiwe wanawasha kwa sababu sisi huwa hatuwashi. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na timu yake yote. Pia nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Kiaina nimpongeze aliyetengeneza kitabu hiki kwa kumwonesha komandoo akiwa kwenye mavazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu kwenye Wizara hii kwanza naunga mkono kwa asilimia mia moja. Nichangie kwenye nyumba za askari. Nimeona juhudi za Wizara katika kujenga nyumba za askari. Naomba Serikali yangu tulivu iendelee kuwajengea nyumba askari hawa ili waweze kuishi vizuri na kufanya kazi zao kwa umakini zaidi. Nimeona maeneo mbalimbali ambapo nyumba zimejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe Serikali yangu tulivu iendelee kuboresha maslahi ya askari wetu ikiwepo mishahara na vyombo ya usafiri. Niombe pia Wizara hii kwa nguvu za dhati ihakikishe mafunzo kwa askari wapya yanafanyika yakiwa yamelenga kada tofauti. Nimesikitishwa hapa na mwasilishaji wa Kambi ya Upinzani akishangaa Askari mstaafu kuwa mganga wa kienyeji. Mimi naamini kabisa kule kwenye uaskari siyo kwamba wana fani moja tu ya kushika bunduki na kucheza gwaride. Najua kabisa kule tunao Askari ambao ni wajasiriamali, wana ujuzi wa teknolojia mpya, wanahabari, wanamichezo, madaktari, madereva, marubani, walimu, mafundi umeme na waokoaji. Kwa hiyo, huyo Askari aliyeenda kuwa mganga wa kienyeji ndiyo fani yake usimlaumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia zaidi katika ajira. Naomba jeshi hili hasa Jeshi la Wananchi liangalie uwiano wa mikoa yote. Kuna baadhi ya maeneo imeonekana kama vile kuna kabila moja tu ndiyo jeshi hilo kazi yake mpaka inafika kipindi mitaani huko ukiwauliza JWTZ ni nini, wanakwambia ni Jeshi la Wakurya Toka Zamani.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba ajira zile ziangalie mikoa mbalimbali angalau ukikuta Wachaga kumi basi na Wamasai, Waluguru na Wapare wapo isiwe kabila moja ndio linafanya kazi ya jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia Wizara hii iangalie ubunifu wa vijana wetu. Tunao vijana wengi ambao katika utundu wao wameweza kubuni redio, TV, simu mpaka helikopta. Ni vizuri jeshi hili likawachukua vijana wale na kuwapa mafunzo halafu baadaye wapate ajira. Nategemea kwa kufanya hivyo tutaendelea kuwa na vijana ambao watakuwa askari bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia katika kambi za jeshi. Najua wakati zinaanza zilikuwa nje ya mji lakini baadaye mji jinsi ulivyokua imeonekana kama vile vimeingiliana. Katika kuepuka madhara zaidi ya mabomu kama yale ya Gongo la Mboto na Mbagala au kuepuka migogoro ya ardhi kati Wanajeshi na raia lakini pia kuepuka migororo ambayo mingine inaingilia mipaka ya kimapenzi kati ya Askari na raia, ni vizuri basi tuangalie uwezekano wa kubadilisha makazi hayo. Mapori bado tunayo mengi, wahame kidogo waende kule ili wananchi waweze kukaa katika maeneo hayo kwa utulivu. Yapo maeneo ambayo hayawezekani kuhamishwa kutokana na hali halisi ilivyo basi wale ambao wanazunguka eneo lile wahamishwe kwa utaratibu unaofaa ili waweze kupisha jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii itasaidia katika kujenga heshima ya jeshi. Imefika sehemu heshima ya jeshi inaanza kupungua kwa sababu wanajichanganya sana na raia. Katika kujichanganya na raia unakuta kuna mambo mengine ambayo Wanajeshi wanafanya unashangaa. Hata katika foleni za magari unakuta kwenye mchepuko na yeye anaingia, unatazama unaona ni Askari na ana kofia. Napenda zaidi Askari waoneshe wao wako makini na ni watii wa sheria, siyo wote wanaofanya hivyo ni baadhi. Wapo ambao pia wanakuwa wasumbufu katika maeneo ya watu yaani hata jirani yake anaogopa kukaa jirani na mjeshi. Naomba wale wachache wenye tabia kama hizo wabadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kuhusu baadhi ya shule ambazo zinasimamiwa na jeshi zikiwepo shule binafsi nikitolea mfano Mgulani na Lugalo.
Kuna shule ambazo zimeendeshwa vizuri wanafunzi wa pale wanakuwa na maadili mazuri. Ni vizuri shule kama zile ziendelezwe na kupewa ushirikiano ili tuendelee kupata wanafunzi wenye nidhamu na wenye uchungu na nchi yao ambao hata kesho wakija huku Bungeni wataongea kwa kuitetea nchi yao siyo kuzomeazomea.
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa na vyuo vya ualimu ambavyo vilikuwa vinasimamiwa na jeshi nikitolea mfano ya Monduli, Morogoro TC na Tabora Boys. Vyuo vile vilikuwa vinatoa walimu wenye nidhamu nzuri na wenye uchungu na nchi yao. Kama kuna uwezekano utaratibu ule urudishwe ili tuendelee kupata Wanajeshi ambao wanakuwa na fani tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kunyamaza kimya bila kusemea suala la uchaguzi wa Zanzibar. Tunakubali wote kwamba Amiri Jeshi Mkuu alisema, tena matangazo yalitoka kwenye televisheni, redio na magazeti kwamba yeye kama Amiri Jeshi Mkuu ana wajibu wa kulinda usalama Tanzania hii katika mkoa wowote siyo Dar es Salaam, Pemba au Mwanza na alimalizia kwa kusema atakayefanya fyokofyoko nitamshughulikia. Ukiona mtu analalamika kama alifanya fyokofyoko anashughulikiwa. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuonesha, kama angesema halafu wakanyamaza wangedharau wakasema amesema mbona hajafanya lolote, amesema na hawajathubutu kufanya fyokofyoko ndiyo maana wamenyamaza na kama watafanya fyokofyoko, Amiri Jeshi Mkuu aendelee kufanya kazi yake, ndiyo tutaendelea kuheshimiana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee zaidi katika suala zima la mafunzo ya kijeshi kwa vyama vya kisiasa. Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya vyama vya kisiasa kutengeneza makundi ya kijeshi kwa kujifanya kwamba wanalinda wakati wa kampeni au kulinda kura zao. Naomba jeshi lifanye kazi ya ziada, Mheshimiwa Waziri alisimamie, yapo makundi yanayojiita mazombe, wenyewe wanayajua huko ndiyo maana kila saa wanayataja, kuna makundi yanajiita blue guard yapo huko, yanafanya vituko kusingizia vyama vya siasa. Naomba Mheshimiwa Waziri yale…
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Green guard umetaja wewe sijataja mimi. Kwa hiyo, ninachoomba yale makundi yote yanayoendesha mafunzo ya kijeshi kwa kusingizia vyama wayadhibiti kwa sababu hayo ndiyo yanayotuletea fujo katika nchi yetu na kusababisha makundi ya wahalifu katika mitaa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 na wale waliobana sasa wameachia. Ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malembeka wakati ukichangia, kuna tuhuma hapa umezitoa kuhusu ukabila jeshini. Kwa mujibu wa Kanuni ya 72(1) na Kanuni ya 64(1)(a), naomba ufute hayo maneno halafu tuendelee. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitolea mfano na nafuta kauli hizo.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, na mimi naungana na wenzangu kumpongeza Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya. Nampongeza kwa dhati kwa sababu najua hii Wizara aliyoipata ambayo anaifanyia kazi mara nyingi amekuwa anaifanyia kwa vitendo. Nimemshuhudia mwenyewe Mheshimiwa Nape akipiga gitaa, nimemshuhudia mwenyewe Mheshimiwa Nape akiimba, nimemshuhudia mwenyewe Mheshimiwa Nape akicheza kiduku, nimemshuhudia Mheshimiwa Nape akicheza sindimba, nimemshuhudia Mheshimiwa Nape akicheza mayonjo, ina maana yuko kwenye fani. Nakupongeza sana Mheshimiwa Nape pamoja na Naibu Waziri wako. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utaenda kwa vifungu, kwanza nianze kidogo kwa mkwara tuliopigwa kwamba tukienda kucheza kwa King Kiki tutakuwa tumekula rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Afya wakati anawasilisha Bajeti yake alikuja na wanakijiji hapa akatuambia kijiji kile kina miaka mitano hakuna mama aliyefariki kutokana na uzazi, tukapiga makofi. Alipokuja Waziri wa Muungano na Mazingira alikuja na Waasisi wa Muungano akatuonesha tukapiga makofi, lakini pia, akatuonesha mwanafunzi Getrude Clement ambaye alituwakilisha Marekani kwenye masuala ya mazingira, tukapiga makofi. (Makofi)
Lakini pia alipokuja Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji alituambia pale nje kuna wafanyabiashara wa magari wanaotaka kwenda kununua yako pale, tukapiga makofi. Pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati anawasilisha mada yake hapo tuliwaona maafande wamejaa huku tele wa kila Idara tukapiga makofi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuko Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Waziri anaonesha wadau wake, tunaambiwa tukienda kucheza kwa King Kiki tunakula rushwa, hiyo haki kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi King Kiki nimemjua nikisoma shule ya msingi, nikasoma sekondari, nikaolewa, nikacheza muziki kwa raha yangu, nimeingia Bungeni King Kiki yupo na akipiga ninaingia. Kwa sababu hiyo imeonesha jinsi gani wanamuziki wakongwe waliokaa hapa nchini na kufanya kazi zao bila kutetereka, sasa kama mtu amefanya shughuli ya muziki kwa kipindi kirefu, leo anakuja hapa kuonesha ujuzi wake na kuwafurahisha Wabunge, mnasema ni rushwa. Hivi mambo mangapi yanayofanyika humu ndani, mbona hamyasemi? Mmeona tu ya King Kiki kuja hapa kuwaburudisha Wabunge ndiyo imekuwa nongwa? Tubadilike! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuzungumzia sekta ya habari. Kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wamiliki wote wa vyombo vya habari hapa nchini bila kuwasahau wenzetu wa Gazeti la Uhuru na Mzalendo, pamoja na redio Uhuru. Pamoja na pongezi hizo kwa wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari nizungumzie maslahi ya wanahabari.
Mheshimiwa Mwenyekiit, wanahabari wengi mapato yao yako chini, wanahabari wanaweza wakapewa sehemu wakafuatilie kazi bila usafiri. Lakini wanahabari hawa pia bado tuna matatizo nao kwamba wana utaalamu wa kuandika pia habari potofu. Unaweza ukakuta taarifa ile ile kwenye gazeti hili unaambiwa sita wamekufa, hili saba wamekufa, lingine 10 wamekufa, na lingine watatu wamekufa, ajali ni ile ile moja, hilo pia ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo la kutoa habari kwa upendeleo. tatizo hili tumeliona hasa kipindi cha uchaguzi na kipindi cha kampeni. Ni vizuri basi, zile taasisi za habari zijielekeze moja kwa moja kwamba tuko hivi, kama walivyofanya redio Uhuru na magazeti ya Uhuru kwamba, ukienda kule unajua wewe ni Chama cha Mapinduzi, vingine vimekaa kimya huku vinatoa habari kwa upendeleo. Tumeviona, tunavijua na tutavifanyia kazi maana Serikali ni yetu, Mheshimiwa Nape ni wetu na tutapambana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kabisa kama Mbunge utakaa ndani ya Bunge kwa miaka mitano, toka asubuhi mpaka jioni wanakuona kwenye tv kwenye Jimbo lako utapata maji, utapata zahanati, utapata shule, utapata barabara, utapata umeme hiyo siamini! Ninachoamini ni kwamba utakapokuja kwenye Bunge na kutoa hoja zako na kurudi kwenye Jimbo lako kwenda kutekeleza yale ya wananchi waliyokutuma ndipo utakapopata maendeleo na ndipo watakapokuchagua. Hawakuchagui kwa kuangaliwa kwenye tv. Ingekuwa kuangaliwa kwenye tv tunachaguliwa tusingeenda Majimboni kuomba kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu gani kinachong‟ang‟ania sana tu kwenda kwenye tv. Mmemzomea Rais hapa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tumenyamaza, mkatuona wajinga. Mkaendelea akaja Waziri Mkuu hapa mkakataa kusikiliza hotuba yake wala kuichambua, tukanyamaza kimya mkasusa mkatoka hatujawasemesha, lakini pia uchaguzi wa Zanzibar mmenuna, sisi tumepiga kura tumemalizika.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, siku zote ninyi mkinuna wenzenu wanakula. Kununa mnanuna wenyewe halafu mnalalamika! Hakuna kitu chochote ambacho hakina mwanzo. Tuliingia kwenye Bunge vizuri, tulikuwa tunaonekana kwenye televisheni na kila mtu alikuwa anaona raha kuonekana kwenye televisheni, lakini haya mmeyataka ninyi wenzetu. Televisheni mmefanya ndiyo kituo cha kutukania viongozi wakubwa Serikalini, kutukania Marais, kukashifia Serikali iliyoko madarakani, hatuwezi kukubali. Kuna watu hawapendi ugomvi, kuna watu wameamua kujiweka sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameamua kujiweka sawa kwa maana kwamba, kitu kingine kama mtu hataki…
MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba utulivu jamani tumsikilize Mbunge. Naomba nidhamu ndani ya Bunge, upande huu nimewasikia.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Kama mtu hataki siyo lazima apambane na wewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usiwe na wasiwasi mimi nilishasema daktari aje apime watu akili. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi waache wazomee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu toka asubuhi anatoka nyumbani anamuaga mke wake anakuja hapa kwa kazi ya kuzomea. Halafu analalamikia tv! Tv ya nini?
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mimi nitakubali kweli mzazi wangu anatukanwa humu halafu nakubali. Hicho kitu hakiwezi kukubalika. Binafsi kama Mheshimiwa Malembeka siwezi kukubali kiongozi wangu anatukanwa humu televisheni na wote wanamuangalia, siwezi kukubali. Kwa sababu hata mzazi wako kama anatukanwa, ukihadithiwa tu unataka kupigana sembuse kuangalia. Hicho hatuwezi kukubali.
Taarifa....
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa kwa sababu zifuatazo; Kwanza nina uhakika humu ndani kuna watu wameoana bila taratibu, wake zao nyumbani hawajui lakini hapa wanajifanya mke na mume, hilo la kwanza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo ninaikataa kwa sababu mimi ninajua ndoa ya mkristo ni moja, siyo mbili wala tatu, lakini kuna watu humu wana wake, ambao wake zao hawajui, mbona hawaoneshi kwenye televisheni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea, wasinipotezee muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudi kuhusu suala la michezo. Kwanza nizungumzie suala la vifaa vya michezo, ninaomba bei zipungunzwe kwa sababu sasa hivi vijana wengi wamejikita kwenye michezo lakini vifaa bei iko juu. Ndiyo maana utakuta wakati mwingine wanacheza mpira bila viatu, kwa hiyo ni vizuri bei ya vifaa vya michezo zipunguzwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nizungumzie Kijiji cha Michezo kilichopo Mvuti katika Kata ya Msongola, eneo lile limetengwa heka 10 kwa ajili viwanja vya michezo…
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naungana na wenzangu kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Makamu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wenzangu kuzungumzia nyumba za bei nafuu ambazo siyo nafuu. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri mwenyewe wakati anazungumza katika vipindi mbalimbali akizungumzia bei ya nyumba zinazoitwa nyumba nafuu, lakini siyo bei nafuu. Mimi naona kwa kuwa, yeye ameligundua hilo naomba alisimamie! Haiwezekani nyumba ya vyumba viwili ikauzwa milioni 70 halafu unasema ni nyumba ya bei nafuu! Hilo naomba alisimamie ili wananchi wetu wenye kipato kidogo waweze kufaidika na nyumba hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, nizungumzie mradi wa viwanja eneo la Mvuti katika Manispaa ya Ilala. Tulihamasishwa, kwanza napenda ku-declare interest kwamba, nilishakuwa Diwani wa Kata ya Msongola, lakini pia, nimekuwa Diwani wa Kata ya Chanika kwa miaka 10 mfululizo ambako katika Kata hizo pia, imeweza kutoka Kata ya Majohe, Kata ya Buyuni na Kata ya Zingiziwa, kwa hiyo, nina uzoefu karibu katika Kata tano katika Jimbo la Ukonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Mvuti tulihamasisha wananchi na wananchi walikubali kuingia katika mradi wa upimaji viwanja katika Mitaa ya Kidole, Sangara, Mkera na Luhanga, lakini tangu mradi ule wananchi walivyokubali hakieleweki nini kinachoendelea kwa sababu, wamekatazwa kulima na hawajengi, lakini mradi hauendelei!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa wengi wameanza kukata mazao yao ikiwepo michungwa na miembe wakichoma mkaa wakitegemea kwamba, nyumba wakati wowote zinakuja, ili nao waishi kimjinimjini, lakini hali inakwenda taratibu. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja niweze kujua mradi wa viwanja katika Kata ya Msongola katika maeneo hayo niliyoyataja umefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, napenda kujua taarifa kuhusiana na nyumba za Buyuni katika mradi wa viwanja elfu 20 vya Buyuni. Katika eneo hilo imehusisha mitaa ya Kigezi, Mbondole, Zavala na Vikongolo, kuna nyumba zaidi ya 2000 hazijulikani mwenyewe ni nani! Wengine wanasema Shibat wengine wanasema za Mchina! Katika nyumba hizo wanaoishi pale ni karibu watu 20 tu maeneo yaliyobaki yamerudi tena kuwa pori! Sasa zile nyumba sasa hivi zimeshakuwa zina mgogoro kwa maana kwamba, zinawapa matatizo wananchi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yale watu wanabakwa, maeneo yale wezi wanakwenda kujificha, lakini maeneo yale tena yameshakuwa, mtu huwezi kupita jioni kwa sababu, nyumba ziko nyingi wanaoishi ni wachache, mapori yamerudi tena na nyumba zile hazijulikani mwenyewe nani na kwa nini watu hawakai, lakini kwa uchunguzi wa haraka tumeambiwa kwamba, zile nyumba pamoja na kwamba, zimekamilika bei ni kubwa sana ndiyo maana wananchi hawakai! Sasa majengo yamejengwa yako tupu yanaendelea kuharibika! Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze nyumba zile ni za nani na kwa nini hawahamii mpaka sasa hivi wakati zimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala la Kazimzumbwi. Kazimzumbwi inagusana na Mitaa ya Kigogo, Kimwani, Nyeburu, Nzasa na Ngobeje. Hapa naomba niongee kwa kina. Suala la mgogoro wa ardhi wa Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Kata ya Chanika haujaanza jana wala juzi, ni wa muda mrefu, lakini niseme wanasiasa tunazidisha sana mgogoro ule kuufanya usimalizike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshiriki vikao mbalimbali vya kutatua mgogoro ule, lakini utakuta wakati wa uchaguzi ukifika wagombea wa vyama mbalimbali wanaenda kuwashawishi wananchi msikubali, msifanye hivi. Kwa hiyo, kunakuwa na vurugu, zile Kamati hazifiki mwisho, uchaguzi ukiisha yanakwisha, uchaguzi ukikaribia vurugu zinaanza tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa sasa hivi uchaguzi umekwisha, hatuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hatuna uchaguzi wa Mbunge, aende kule akafanye kazi ili wale wananchi wawe na jibu la uhakika badala ya kuwa na majibu ya kisiasasiasa. Huyu anakuja asubuhi anasema nendeni, huyu anakuja anasema toeni. Naomba kwa kipindi hiki akafanye kazi tuje na jibu kuhusiana na Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Kata ya Chanika na mitaa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tena suala la mashamba pori. Mara nyingi limekuwa linazungumziwa kwamba mashamba pori yachukuliwe lakini bado haujatolewa mwongozo wananchi wanayachukua kwa utaratibu gani? Kuna wananchi wakishasikia huku Bungeni mmesema mashamba pori marufuku, wanavamia mashamba, wanakamatwa, wengine wanapigwa na wengine wanapelekwa mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wanapotoa mwongozo kwamba yale mashamba makubwa yachukuliwe, watoe na ufafanuzi wanachukua kwa utaratibu gani ili wananchi wasipate matatizo. Wakati huohuo kuna mashamba makubwa ambapo wamiliki wana hati zao na wameyanunua kwa ajili ya kujenga shule, zahanati au hosteli kwa siku zijazo. Kwa hiyo, ni vizuri basi masuala haya yawe yanatolewa ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kumaliza kuongea kabla sijazungumzia viwanja vya CCM. Kuna watu hapa wakikaa wanazungumzia CCM ina viwanja, ni vyetu. Utaratibu wa Chama cha Mapinduzi huwezi kujenga tawi kama huna kiwanja ambacho ni halali. Kwa hiyo, kila tawi lazima lihakikishe uhalali wa kiwanja chake ndipo linaitwa tawi Ukiona tawi ina maana lina wanachama si chini ya 50. Unapoona Tawi la Mjumbe wa Shina ina maana si chini ya wanachama 10.
Sasa mtu anakuja anakaa mwenyewe anazunguka tu viwanja vyote vya CCM, viwanja vyote ni vya CCM, ni vya kwetu, ni vya halali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, wale wote kupitia Chama cha Mapinduzi watakaoleta maombi ya kupata hati ya viwanja vyao alifanyie kazi ili Chama cha Mapinduzi viwanja vyake viweze kuwa na hati.
Maana kuna watu wana uchu yaani mtu anasimamisha bendera moja….
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na uendelea kunilindia muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba mara zote anayeanza kusema anaonekana mwema wa mwisho anamalizia. Nasema viwanja vya Chama cha Mapinduzi visiwatie presha ni vyetu! Kama mnataka viwanja vingi njooni ndani ya Chama cha Mapinduzi mtapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena bahati nzuri au bahati mbaya ndani ya Chama cha Mapinduzi ukiona Mjumbe wa Shina kaweka bendera moja ina maana ana watu 10, ukiona tawi lina bendera moja lina watu zaidi ya 50, tofauti na vyama vingine yaani mtu mmoja anapata uongozi bendera 200 zinamwagwa.
Naomba muelewe kwamba Chama cha Mapinduzi viwanja vyake ni vya halali hatujaiba. Kama kuna mtu ana uhakika tumeiba aende mahakamani, tutapambana naye. Namwomba kwa mara nyingne Mheshimiwa Lukuvi, maombi yote ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya hati za viwanja vya Chama cha Mapinduzi ayasimamie kama kawaida kwa sababu wale maombi yao ni halali siyo kwa wizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwa sababu wale Mawaziri ambao wako kwenye Wizara hii wanajiamini wanaweza kufanya kazi na wana uwezo wa kutoa maamuzi, siyo watu wa kuyumbayumba. Akisema bomoa, bomoa, jenga, jenga na huo ndiyo msimamo wa kiongozi, lazima uwe unaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanazozifanya na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kukupongeza wewe kwani katika filamu inayoendelea ndani ya ukumbi huu, wewe ndio nyota wa mchezo. Nikuhakikishie siku zote sterling huwa hauwawi, akiuawa ujue picha imekwisha. Kwa hiyo, naendelea kukupa moyo, endelea kufanya kazi mpaka tarehe 1 Julai na wewe ndiyo kipepeo wa jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza bajeti hii kwa sababu imeweka vipaumbele katika afya, elimu, maji na miundombinu na wenzangu wamechangia vizuri na mimi naomba niongeze nyama katika yale waliochangia wenzangu.
Kwanza niishauri Serikali yangu sikivu kwamba bajeti hii ilivyopangwa naomba fedha hizo zipelekwe kwa muda muafaka. Kumekuwa na tabia ya kupanga vitu tunashangilia halafu hela haziendi kwenye maeneo husika na zikienda zinaenda zikiwa zimechelewa na wakati mwingine zinafika kidogo. Sasa ili kutekeleza yale ambayo tumeyapanga hapa, ni vizuri fedha hizo zikapelekwa kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuikumbuke ile miradi kiporo. Iko miradi ambayo sasa hivi imekuwa magofu na kila anayesimama anataja kwenye Jimbo lake, kwenye Wilaya yake. Naona ni vizuri sasa viporo hivyo tuvikamilishe ili hadithi ile ya kuhadithia tena, iwe imekamilika na isiadithiwe tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi ambayo imeanzishwa kwa nguvu au michango ya wananchi. Tumehamasisha wananchi wamajitolea na wamejenga hadi walipofikia lakini Serikali bado haijapeleka hizo fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo. Naomba Serikali ipeleke hizo fedha ili kuwatia nguvu wananchi ambao wamejitolea kwa namna mbalimbali kuikubali miradi ile na kuichangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ukusanyaji wa mapato kupitia kodi za majengo. Katika hili, naomba tathmini ifanyike upya kwa baadhi ya maeneo. Mfano kuna nyumba yangu moja iko Chanika ndani ya plot moja lakini nimeletewa karatasi tatu. Nyumba yenyewe ina karatasi yake, banda la kuweka gari lina karatasi yake na choo cha nje kina karatasi yake. Sasa najiuliza hapa nikalipe nini, kuna nyumba isiyokuwa na choo nje au nikalipe choo tu nyumba niache, au nilipe banda la gari nyumba niache au nikalipe banda la kuku nyumba niache? Siyo hiyo peke yake, nimeona katika nyumba yangu ya Mvuti jiko la nje nalo nimepewa karatasi yake, sasa najiuliza hiyo tathmini ilifanywaje, kwa kuangalia sura ya mtu au kwa majina?
Naomba katika maeneo kama hayo tathmini ifanyike upya, wananchi wako tayari kulipa kodi ya majengo na sisi viongozi tuko tayari kulipa kodi ya majengo lakini iende kihalali. Yapo maeneo ambayo kuna nyumba ya vyumba viwili havijapigwa plasta lakini anaambiwa alipe shilingi 36,000 wakati mwingine ana vyumba vinne vina tiles, bati la South Africa anaambiwa alipe shilingi 21,000, hivi tathmini hiyo inapigwaje? Ni vizuri tujipange upya ili kutekeleza suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hilo hilo la ukusanyaji wa kodi ya majengo na mimi naungana na wenzangu kuomba Halmashauri ziachiwe kukusanya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba yapo mambo ambayo tumekubaliana kwamba mambo haya yatafanywa na Halmashauri, tutakapochukua kodi ya majengo, tutakuwa tunaziua zile Halmashauri na yale ambayo tumewapangia wafanye watashindwa kuyafanya. Kama tumekubaliana kuwapa mamlaka basi tuwape na madaraka ili waweze kufaya kazi vizuri. Halmashauri zimejipanga na zimeishafanya utafiti wa kutosha na wako tayari kwa ajili ya kukusanya fedha hizo za majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kwenye suala la vivuko. Yapo majimbo mengi ambayo yamelalamikia vivuko na yakitaja viongozi mbalimbali wa zamani kwamba waliahidi kuvikamilisha lakini havijakamilika. Yapo maeneo ya Mafia, Bukoba, Ukerewe katika Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika lakini pia bila kusahau Visiwa vya Unguja na Pemba. Wenzetu hawa suala la boat au meli ndiyo chombo kikubwa cha usafiri kwao. Kwa hiyo, yapo mambo ya kusubiri, lakini mengine inabidi tuyafanyie kazi mapema ili wenzetu twende nao pamoja. Kila nikifikiria mimi msiba wa MV Bukoba na MV Spice, bado najiuliza kwa nini mpaka leo hii meli nyingine hazijanunuliwa, naomba hilo tulifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la michezo. Imefika sehemu hizi timu zinakuja kuonekana kama ni za mtu binafsi wakati zinawakilisha nchi. Inafika sehemu timu ya ngumi, netball, riadha, mpira wa miguu, kuogelea, unaambiwa imeshindwa kwenda kambini au imeshindwa kusafiri kwenda kuiwakilisha nchi kwa sababu hakuna pesa, sasa sijui tunajipangaje? Ndiyo maana wale wanaojitolea wachache kusafirisha timu wanajifanya wao maarufu sana na wanajifanya wao ndiyo wanazijua sana hizi timu kuliko Serikali, naomba Serikali zile safari za nje iwe inazigharamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba pia nichangie kuhusiana na ahadi za viongozi. Kuna ahadi za viongozi ambazo wamezitoa katika kampeni, zinavyojirudia mara tatu, mara nne, mara tano kwa awamu tofauti, ile tu siyo aibu kwa Serikali lakini pia ni aibu kwa chama chetu ambacho kimeongoza kwa kipindi chote. Naomba katika awamu hii zile ahadi zote zilizoahidiwa na viongozi waliopita zifanyiwe kazi ili tuendelee kuwapa imani wananchi na pia kuwahakikishia kuwa Chama cha Mapinduzi hakidanganyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ili nisipoteze muda, napenda kuzungumzia suala la kukata kodi ya kiinua mgongo kwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo waliotetea majimbo, mimi ni Mbunge wa Viti Maalum nawakilisha Mkoa mzima, misiba huko mkoani tunaijua, mipira ya huko mikoani tunaijua, michango ya huko mikoani tunaijua, tuna matatizo chungu mzima. Kama kukatwa kodi tulishakatwa kwenye mishahara na ipo michango mbalimbali ambayo Wabunge tunatakiwa tuitoe na huwa tunaitoa. Mpaka tunapofika dakika ya mwisho tunajipanga kwa ajili ya uchaguzi mwingine, naweza nisiwe mimi lakini akaja mtu mwingine, mnapokuja kumkwangua Mbunge moja kwa moja atasaidiaje yule mgombea wa chama chake ili aweze kuingia? Hakuna uchaguzi usiokuwa na gharama, chaguzi zote zina gharama, ndiyo maana hata Serikali huwa inajipanga.
Sasa mimi niombe, suala la kukata kiinua mgogo kodi ya Wabunge litafakariwe upya na tuangalie jinsi gani ya kulifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili niweze kutoa nafasi kwa wengine tena, naendelea kukupongeza kwamba wewe ndiyo nyota wa mchezo, ahsante kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuingia katika kikao hiki cha bajeti kwa awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja za Mawaziri wote wawili kwa asilimia mia moja. Nachukua pia nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wote wawili pamoja na Naibu na team zao zote wanazofanya nazo kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, michango yangu itakuwa michache na nitajaribu kuitoa kwa ufupi sana. Nianzie na mpango wa MKURABITA. Nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Nimepita miradi mbalimbali ya MKURABITA na nimeona jinsi gani wananchi walivyohamasika na jinsi walivyokubaliana na shughuli ya MKURABITA na hivyo kuweza
kumiliki ardhi na kuwa na hati ambazo zinawezesha kupata mikopo katika taasisi za fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali yangu kwa kuwa wananchi wameridhia ni vyema kabisa kwamba kwa sasa hivi shughuli hii iende moja kwa moja nchi nzima kwa kuangalia Majimbo ili kila Jimbo angalau tuwe na mfano mmojawapo wa kufanyia hii kazi. Nimeona
akinamama jinsi walivyopata hati za kumiliki ardhi pamoja na vijana, kwa hiyo, nashukuru na naiomba iendelee kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la TASAF, nimepita katika miradi mbalimbali nimeangalia, nimeona TASAF jinsi ilivyofanya kazi vizuri na kuwezesha watu wenye kipato kidogo kuweza kujenga nyumba, kupeleka watoto wao shule na kuwanunulia uniform, lakini pia na kubuni miradi mbalimbali ambayo imewawezesha kuongeza kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, kwa wale Watendaji wachache ambao hawakuwa wema, wakaamua kuvuruga utaratibu huu, nafahamu kwamba wamechukuliwa hatua, lakini ni vyema Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atuambie wale watendaji ambao kwa
makusudi wameamua kuvuruga utaratibu huu wamechukuliwa hatua gani? Badala ya kuwalazimisha wananchi walipe pesa ambazo hawakuziomba. Wale waliowajazia ndio walikuwa na matatizo. Kwa hiyo, tuwanusuru wale ambao wanalipishwa fedha ambazo hawana uwezo wa kulipa, tuwashughulikie wale waliowaandikisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika Mfuko wa Rais wa Uwezeshaji. Mfuko huu umefanya kazi vizuri sana, nampongeza Mheshimiwa Waziri na team yake yote, kwa sababu vikundi vya vijana ambavyo vimewezeshwa na Mfuko huu vimefanya kazi vizuri, lakini fedha zile zinazotolewa
zimekuwa chache. Ni vizuri tuangalie uwezekano wa kuwaongezea ili waweze kufanya kazi na kujiajiri wenyewe. Kwa sababu katika vikundi nilivyopitia, nimekuja kugundua kwamba siyo wote ambao elimu yao ni ndogo, wapo ambao wana elimu kubwa, wamejiunga na
wamewachukua wenye elimu ndogo na kufanya mradi wa pamoja hivyo kuweza kuajiriana wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, nawapongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la TAKUKURU. TAKUKURU imefanya kazi nzuri, japo watu wanabeza. Kwa sasa hivi suala la rushwa limepungua, kwa kiasi kikubwa na kama Mheshimiwa Waziri alivyoelezea, wameweza kuokoa mamilioni kadhaa kutokana na mchakato uliofanywa katika kukagua na kutenda kazi zao. Ninachoshauri, fedha zile mmeeleza zimeenda Serikalini, lakini hatujaambiwa zimeenda kufanya nini? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie fedha hizo walizookoa zimeenda kufanya nini? Kwa sababu bado tuna matatizo kwa wananchi, fedha hizo zinaweza zikatumika kwa ajili ya kazi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la Usalama wa Taifa. Suala la Usalama wa Taifa ni suala nyeti na kama ni suala nyeti, naona kuna watu wanalifanyia uzembe uzembe tu. Mtu anaamka asubuhi, anatuma message, nimetekwa nyara. Hivi kutekwa nyara mchezo!
Mnatania suala la kutekwa nyara! Yaani mtu anatuma message, “nabadilisha nguo, naenda Polisi, nimetekwa nyara. Huko kutekwa nyara, mbona mnaifanyia utani taasisi hii!
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu ananyanyuka, anasema Wabunge 11 watatekwa nyara; yeye alikaa nao vikao akawajua hao Wabunge 11! Naomba Usalama wa Taifa kwanza wawanyanyue wale waliosema kuna Wabunge 11 humu watatekwa nyara, watutajie ni akina nani? Walikaa
wapi? Wanatekwa nyara kwa kosa gani? Kwa sababu Usalama wa Taifa, mimi nategemea mpaka tumekaa hapa, ni kwamba wako kazini na wanafanya kazi vizuri. Ni vizuri basi wakaongezewa fedha katika idara yao, wapate mbinu mpya za kufanya kazi, waongezewe vifaa tuweze kupata usalama zaidi. Mtu kutwa, anaamka asubuhi anatuma message kwa rafiki yake, “nimetekwa nyara.” Hebu waulizeni waliotekwa
nyara, hiyo simu unaipata wapi ya kutuma hiyo message? Kutekwa nyara mchezo! Hebu waulizeni wanaotekwa nyara, watakwambieni ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mchezo wale wanaojifanya usalama fake, naomba Mheshimiwa Waziri unayehusika washughulikie. Kwa sababu sasa hivi mtu akishakata panki lake, akavaa kaunda suti yake, anatoa kitambulisho; mimi Usalama wa Taifa. Usalama wa Taifa
mchezo! Mtu amejizungusha zungusha tu huko, anawatisha watu mtaani, anasema Usalama wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wale ambao wanajifanya Usalama wa Taifa na kuwahenyesha watu mtaani, washughulikiwe. Wale wanaojifanya Usalama wa Taifa, kutoa data za uongo, washughulikiwe; sambamba na data za uongo za kwenye mitandao. Tumechoka! Nchi iko juu juu; watu tuko juu juu tunahangaika! Usalama wa Taifa wapo, mnawanyanyapaa; hebu fanyeni kweli; na tuanzie humu humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anasema hapa ushahidi ninao, usalama wa Taifa upo, hamjamchukua mpaka leo kuja kukwambieni Mbunge gani aliyetekwa nyara; mnamwacha tu, kwa nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie suala la utawala bora nikienda sambamba na maadili ya viongozi. Tumekaa muda mrefu tukizungumzia Ma-DC, Ma-RC tunajisahau sisi humu ndani. Maadili tuanze nayo sisi wenyewe na uongozi tuanze nao sisi wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukaa humu ndani miaka 30 au miaka mitano; kama toka mwanzo wamekuja na mpango wako wa kutukana, utafikiria utaratibu wa huku ni wa kutukana. Naomba semina hizi zianze pia na kwa Wabunge ili tuweze kuwasimamia wenzetu. Kama semina
hizi watu watapata, kila mtu atajua wajibu wake ni nini, mamlaka yake na madaraka yake yanaishia wapi? Hatutazozana na DC, RC na wala wao hawatazozana na Wabunge. Isipokuwa kwa sababu semina hizi hazipo, ndiyo maana kila mtu anajiona yeye kubwa kuliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Ma-RC, Ma- DC wazuri sana, wanafanya kazi vizuri sana; lakini wale baadhi ambao wanakosea ni sawasawa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walioko humu wanaofanya kusudi. Kuna wakati nilisema tupimwe akili, watu wakacheka, lakini
tunakoelekea itafika wakati watu watapimwa akili humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu yanayofanyika huku unajiuliza kweli huyu kiongozi, wanafikiria kujaza zile form za maadili ndiyo maana yake umemaliza maadili ya viongozi kumbe ni pamoja na matendo tunayoyafanya.
Taarifa....
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba unitunzie muda wangu. Pili nataka kumwambia anayeongea, hiyo taarifa yake siipokei. Kwanza naona kazuka tu! Kwa sababu suala la Usalama wa Taifa, imeitwa Taifa; haijaambiwa wa chama wala wa idara fulani. Ina maana hapa tulipo wenyewe wapo na wanafanya hiyo mambo yake halafu asijadiliwe, ndiyo maana mnaitwa mnahojiwa. Ingekuwa hivi hivi, humu ndani kusingekuwa salama. Iko siku humu ndani mtu angetoka vichwa vingebaki humu; lakini kwa sababu watu wapo na wanatulinda, ndiyo maana mnaona amani ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba, suala la Usalama wa Taifa wasilichukulie mchezo, mchezo. Watu wana-support tu; wakisikia fulani katekwa nyara, hata kwa message wanakubali. Ninachosema ni kwamba, tunaomba amani iwepo na ninaendelea kusisitiza wale Wabunge waliosema wanawajua 11 wapo, watutaje; inawezekana labda na mimi nimo, nijue ni jinsi gani ninavyojilinda. Hawawezi kusema halafu wakaachwa na wamesema wanao ushahidi. Mmeona!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kabisa, asubuhi tunaingia hapa tunaomba dua, tunawaombea na viongozi wetu na Rais tunamwombea; baada ya dakika kumi, wanamtukana halafu wanasema hashauriki. Sasa hata ungekuwa wewe, huyo mtu anakudharau, anakutukana,
unamwita akushauri nini? Kwa sababu kinachotakiwa hapa Wabunge tumepewa nafasi ya kuishauri Serikali na kuisimamia. Muda tunaopewa kuishauri Serikali na kuisemea, hatufanyi hivyo, tunaikashifu na kuitukana, halafu mkihojiwa mnasema kuna kanuni. Kuna haja ya kuja kubadilisha hizi kanuni ili watu tuheshimiane vizuri humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwamba kama suala la kuheshimiana, tunavyoapa hapa, tunajaza form, tuendelee kuheshimiana na tumheshimu kila mtu kwa nafasi yake. Mheshimiwa Rais sio mtu wa kumtukana; asubuhi huwezi ukamwombea dua, mchana unamtukana, wajirekebishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema siku moja kwamba nyoka wa kijani huwa haumi, siku akiuma hana dawa. Sasa yule nyoka kaanza kufanya kazi; wakiitwa kuhojiwa wanasema wametekwa nyara. Hatuteki nyara mtu! Mnatakiwa mkatoe maelezo kwa nini mnatukana? Ujiulize,
kwa nini kila siku unahojiwa wewe? Jiulize, kwa nini kila siku unaitwa wewe Polisi? Ukishapata jibu utanyamaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema kwamba naungana na wenzangu wote wanaotetea Madiwani posho zao ziongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.