Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (33 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine waliochangia hoja hii. Napenda kuchukua fursa hii kuchangia machache yaliyojitokeza katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, lakini vile vile kwa michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wameitoa kupitia hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa ufinyu wa muda, nitajaribu kujibu masuala machache na nitajikita zaidi katika suala la kupambana na rushwa, lakini vilevile katika masuala mazima ya Utumishi, hususan madeni mbalimbali ya watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia TAKUKURU kwa namna ambavyo ameweza kuonesha utashi na kuonesha njia yake katika kupambana na tatizo la rushwa. Kupitia TAKUKURU, nimhakikishie Mheshimiwa Rais na wananchi wote wa Tanzania kwamba tutaunga mkono azma yake hii, tayari ameshatuonesha njia, kwa kweli ameipa TAKUKURU silaha iliyo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa sisi TAKUKURU tutahakikisha hatutaacha jiwe lolote ambalo halitageuzwa. Yeyote atakayejishughulisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma atachukuliwa hatua stahiki. Hatutaona haya, hatutamwonea aibu mtu yeyote atakaye jikita na vitendo hivi, hatutaangalia cheo cha mtumishi yeyote wa umma alichonacho Serikalini, ili mradi amejikita katika vitendo hivi viovu, basi atapata malipo yake stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuliunga hili mkono, tumejaribu kushauriana na wenzetu wa TAMISEMI, kuangalia ni kwa namna gani sasa tunaweza kuziba mianya mbalimbali ya ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri. Katika miaka mitano iliyopita, tayari tumeshachukua hatua na kesi mbalimbali zimefika Mahakamani. Watumishi takribani 6,794 wamefikishwa Mahakamani na wengine wamekuwa katika hatua mbalimbali za mashauri hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tumepeleka Waratibu mbalimbali wa Kanda wa TAKUKURU ambao watakagua kila Mradi wa Maendeleo ili kihakikisha kwamba fedha inayokwenda katika miradi, basi ni fedha ile ambayo kweli imepangiwa matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa 2014/2015 kupitia Waratibu hawa wa Kanda wa TAKUKURU, tumeweza kuiokolea Serikali fedha takriban Shilingi bilioni saba. Kwa mwaka huu wa fedha tutajitahidi kuongoza kasi zaidi ili tuweze kuokoa fedha nyingi zaidi za miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu Waheshimiwa Wabunge na vilevile wananchi mbalimbali kwa ujumla wenye miradi ya maendeleo katika Halmashauri, waweze kutoa ushirikiano wa dhati kabisa kwa Waratibu hawa wa TAKUKURU wa Kanda, lakini pia kwa Ofisi nzima za TAKUKURU katika maeneo hayo ili tuweze kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite sasa katika suala zima la Utumishi, hususan suala zima la madeni ya watumishi katika malimbikizo ya mishahara.
Tunatambua deni ni kubwa, lakini sisi kama Ofisi ya Rais Utumisi wa Umma tumejitahidi, tumeshalipa takriban shilingi bilioni 27.9 kwa walimu mbalimbali. Vilevile kwa mwaka huu wa fedha peke yake tumeshalipa takriban shilingi bilioni 7.9 ambayo ni malimbikizo ya mishahara kwa watumishi mbalimbali takriban 8,793.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelewa mzigo walionao watumishi wa umma na niwahakikishie kwamba, mimi kama Waziri ninayesimamia masuala ya watumishi, lakini vile vile Mbunge wa Wafanyakazi, kwa kweli nitaangalia kwa kadri inavyowezekana kwa kushirikiana na Serikali yangu, kuona ni kwa namna gani sasa madeni haya yanapungua kama siyo kumalizika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kwa wenzangu watumishi, nyaraka mbalimbali za madai wanazowasilisha, basi ziwe ni nyaraka ambazo ni za kweli, nyaraka ambazo tutakapofanya uhakiki zisipoteze muda. Wapo watumishi ambao wamekuwa sio waaminifu. Unakuta kuna madai makubwa, baadaye tukifanya uhakiki, gharama inakuja kupungua. Vilevile kwa kufanya hivyo, unamcheleweshea yule ambaye anastahiki kulipwa malipo yake kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana ushirikiano wa watumishi wenzangu wa umma, tujitahidi tupeleke madai hayo kwa wakati, lakini vilevile kwa Halmashauri zetu, madai ambayo yanatakiwa kulipwa na Halmashauri zile, basi wayalipe kwa wakati na wasisababishe mzigo kwa watumishi wetu wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilijitokeza hoja mbalimbali kwa upungufu wa watumishi, niseme tu kwamba nakubaliana nao; lakini changamoto kubwa ambayo tunaipata kupitia Serikali, yako mahitaji makubwa kweli ya watumishi wa umma katika sekta mbalimbali, lakini ukiangalia hivi sasa wage bill yetu au malipo ambayo tunalipa kwenye mishahara ya watumishi wa umma ni takriban asilimia 51.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa watumishi wa afya mwaka huu, 2016 tutaajiliri takribani watumishi 10,873, vile vile tutaajiri walimu 28,975 na watumishi kwa ujumla wa sekta ya umma watakuwa 71,496.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, mengine tutaongea wakati wa kuchangia Mpango. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo walizichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kipekee nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuweza kujibu hoja hizo kama nilivyoeleza awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kipekee kuchukua nafasi hii kumshukuru sana kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake ya mara kwa mara na ushauri ambao amekuwa akinipatia katika utekelezaji wa majukumu ya kusimamia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, eneo ambalo sote tutakubali kwamba ni eneo mtambuka katika utawala wa nchi yetu na katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelekezo na ushauri ambao wananipatia katika kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini. Napenda pia kumshukuru sana Spika na Naibu Spika pamoja na Uongozi wote wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa ambao mnaipatia ofisi hii ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za pekee ziende kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote ambao walitoa maoni ya ushauri ambao tunaamini kabisa utaweza kusaidia sana kuboresha utekelezaji wa majukumu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ipo kwa awamu mbalimbali za Serikali zilizotutangulia, Serikali hii ya Awamu ya Tano inaendelea kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaendelea kutekeleza sera na Mipango ya Kitaifa ya muda mrefu ambayo wote tunafahamu ilibuniwa kwa ajili ya kuwaondolea wananchi wa Taifa letu umaskini lakini vilevile kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia sera na mikakati hiyo, lakini vilevile kupitia dira yetu ya Taifa ya Maendeleo pamoja na MKUKUTA na MKUZA, pamoja na Mpango wetu wa Maendeleo wa muda mrefu, tunaamini kabisa mipango hii itakapotekelezeka, basi lengo letu ni kujenga uchumi wa viwanda pamoja na maendeleo ya watu. Wote mtakubaliana nami kwamba ili kutekeleza sera hizi, tunahitaji Utumishi wa Umma ulio imara na makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwetu sisi katika Utumishi wa Umma, sekta ambayo naiongoza, nia yetu ni kuendelea kuboresha Sekta ya Utumishi wa Umma, kuhimiza misingi ya weledi, kuweka mifumo ya Menejimenti inayowezesha watumishi wa umma kuwajibika na kuwa na maadili ili waweze kutoa huduma kwa wananchi na wadau wengine na hivyo kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini endapo Watumishi wa Umma watazingatia sifa nilizozitaja awali, tutakuwa na utendaji mzuri katika utendaji wetu, utendaji ambao utakuwa na matokeo, lakini vilevile utendaji ambao utatuwezesha kuwa na tija zaidi, kuwa na mapato zaidi na hatimaye kuboresha zaidi maslahi ya Watumishi wa Umma; na wote mnafahamu hilo ndilo lengo letu la mageuzi kupitia Sekta ya Umma ambayo tunaendelea kuyafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Utumishi wa Umma ni sehemu muhimu sana katika utendaji wa Serikali, ni utumishi ambao unahitaji kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ya Serikali iliyopo madarakani. Wote tunaamini ili Utumishi wa Umma uweze kutekeleza sera na mikakati ya Serikali iliyo madarakani ni lazima kuzingatia misingi ifuatayo:-
· Ni lazima kuwa na dira na dhima inayoashiria matakwa ya jamii ya kuleta maendeleo na siyo kwa maslahi binafsi;
· Kuwa na msingi ambao itaonekana Serikali inaungwa mkono na wananchi kwa kuwa jitihada zake zinaleta faida kwa wananchi wake; na
· Kuwa na mfumo wa kiutawala, Menejimenti na Kisheria inayoelekewa na kuheshimiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Utumishi wa Umma uongozwe na kusimamiwa ili kuhakikisha kwamba hauendi kinyume na misingi hiyo mitatu ambayo nimeieleza. Ili kuweza kulinda misingi hiyo niliyoieleza awali, Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko katika usimamizi wa Utumishi wa Umma; imekuwa ikifanya mabadiliko haya katika usimamizi wa Utumishi wa Umma mara kwa mara ili kuenenda na misingi niliyoitaja awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii imejidhihirisha wazi kupitia mageuzi ambayo tumeyafanya tangu uhuru, lakini vilevile kupitia program ya kuleta mabadiliko ya utendaji katika Utumishi wa Umma au Public Service Reform Program ambayo ilitekelezwa kuanzia mwaka 2000 mpaka 2014. Kama ilivyo katika Awamu mbalimbali za Serikali zilizotangulia, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuboresha Utumishi wa Umma ili uendelee kuwa na manufaa kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatua mahsusi za kusimamia Sera na mifumo ya Menejimenti; matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano; nidhamu; mapambano dhidi ya rushwa; uadilifu na uwajibikaji; zimeendelea kuchukuliwa. Tunaamini kwamba kwa kuzingatia mambo haya, Watumishi wa Umma watafanya kazi kwa weledi na bidii, lakini vilevile bila kusahau maslahi yao kulingana na hali ya uchumi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tutaendelea kuimarisha vita dhidi ya rushwa kama hatua ya kuimarisha uadilifu, tutaendelea kuhakikisha kwamba viongozi na Watumishi wa Umma wanatoa Viapo vya Uadilifu. Vile vile pamoja na viapo hivi vya uadilifu, tutahakikisha kwamba Watumishi wa Umma wanakwenda kwa kuzingatia viapo vyao, wanawajibika kutokana na matokeo ya maamuzi ya kazi wanazozifanya ili kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutumia ofisi na nyezo kwa manufaa binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hizi, Serikali vilevile itaendelea kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unazingatiwa katika Utumishi wa Umma, lakini vilevile mifumo ya Kimenejimenti inayojumuisha matumizi zaidi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, nayo pia inaimarishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi yangu inachukua hatua thabiti za kukomesha watumishi hewa kwa kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taarifa za kiutumishi na mishahara wa Lawson na kuufanya uweze kuzungumza na mifumo mingine kwa kuongeza uwajibikaji kwa Wakuu wa Taasisi katika ulipaji wa mishahara na maslahi; kufanya ukaguzi wa kushtukiza wa mara kwa mara kwenye orodha ya malipo na mishahara; lakini vilevile kufanya ukaguzi dhidi ya mfumo wenyewe; na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kijinai watumishi wote watakaobainika kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa takwimu za haraka haraka, ukianzia tarehe 1 Machi, 2016 hadi tarehe 24 Aprili, 2016 watumishi 8,236 waliweza kuondolewa katika mfumo huu wa mishahara na utumishi. Mgawanyo wa watumishi hao kupitia Serikali Kuu ni watumishi 1,614 na katika Serikali za Mitaa ni watumishi 6,622. Ukiangalia hili ni ongezeko la watumishi 2,731 ukilinganisha na uchambuzi ambao uliwasilishwa tarehe 11 Aprili na Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika fedha ambazo zingepotea endapo watumishi hawa 8,236 wasingeondolewa katika mfumo kwa miezi hiyo, ingeligharimu Taifa letu takribani Shilingi bilioni 15.4. Kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, nitaendelea kutoa taarifa kwa kadiri itakavyokuwa ikiwezekana, lakini vile vile viongozi mbalimbali wa Taifa letu nao pia wataendelea kutoa taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kumekuwa na tabia ya Watumishi wa Umma ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mfumo na wamekuwa wakiuhujumu mfumo huu na kwa muda mfupi tu tayari tumeshawafungia Maafisa Utumishi 56, lakini vilevile hivi sasa tunafanya uchambuzi wa kujua masuala yote ambayo wameyafanya kinyume na taratibu, lakini vilevile kuhakikisha wanarejesha fedha zote ambazo wamelisababishia hasara Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaishia kwenye kurudisha fedha peke yake, ni lazima mkondo wa sheria uchukue hatua yake na hatutasita! Tumefundisha Maafisa Utumishi 1,500 ambao wanaweza wakasimamia mfumo huu. Hatutasita hata ikibidi kuwafukuza wote! Kwa hiyo, napenda tu kutoa tahadhari kwa Maafisa Utumishi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mfumo huu kuhakikisha wanausimamia kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yangu imechangiwa na takriban Waheshimiwa Wabunge 85, wakiongozwa na Mheshimiwa Jasson Rweikiza, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, lakini vile vile Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na nitambue pia na kumshukuru Mheshimiwa Ruth Mollel, Waziri Kivuli wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa maoni na michango yao mizuri ambayo naamini kabisa itatusaidia katika kuboresha Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile muda uliopo hautoshi kujibu hoja zote kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge walivyowasilisha humu Bungeni, nitajitahidi kujibu hoja kwa kadri muda utakavyoruhusu. Napenda kuwahakishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zote zitajibiwa kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge wataweza kupata majibu hayo kabla ya kumalizika kwa Mkutano huu wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa baada ya kusema hayo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao nitakuwa sijataja majibu ya hoja zao waridhike, tutawapatia kwa maandishi pamoja na Wabunge wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikielezea utenguaji wa uteuzi wa Makatibu Wakuu ambao walitenguliwa uteuzi wao tarehe 8 Aprili na alitoa ushauri kwamba ni vema Serikali iwalipe kifuta jasho (golden handshake) kwa kutumia uzoefu wa miaka ambayo wameitumikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Makatibu Wakuu hao ambao wametenguliwa, wameshaandikiwa barua za kujulishwa hatima zao; vile vile wako ambao tayari tumewashuhudia wameteuliwa katika nyadhifa nyingine; mfano, wako ambao wameteuliwa kuwa Makatibu Tawala wa Mikoa. Pia kwa wale ambao utumishi wao tayari umeshakoma, Serikali itawalipa mafao yao kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya kwamba Serikali ihakikishe inazingatia sheria na kanuni wakati inapokuwa inachukua hatua dhidi ya Watendaji mbalimbali na kwamba kwa watakaokutwa na hatia za ufisadi na rushwa, wachukuliwe hatua za kinidhamu na kufilisiwa mali zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, uchukuaji wa hatua katika masuala mbalimbali, yaani kinidhamu kwa Watumishi wa Umma, umekuwa ukifanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ambazo ziko katika Utumishi wa Umma. Napenda tu kutaja vifungu vichache; ukiangalia kwa mujibu wa kifungu cha 34, 38 na 40 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 kuhusiana na suala zima la kufilisi mali zilizopatikana kwa njia ambayo siyo halali; mali ambazo zimepatikana kwa njia hizo ambazo hazifai, zinatakiwa zitaifishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema tu kwamba utaifishwaji huu unafanyika tu pale ambapo ushahidi unakuwa umethibitika na unakuwa umekusanywa na baada ya watuhumiwa kupatikana na hatia Mahakamani. Nilihakikishie tu Bunge lako kwamba Serikali hii itaendelea kuzingatia misingi ya utawala bora katika usimamizi mzima wa Utumishi wa Umma. Vilevile tutahakikisha kwamba nidhamu katika Utumishi wa Umma inakuwa ya hali ya juu na inaimarishwa, pia fedha zote na mali za umma zitalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Felister Bura, Mheshimiwa Mama Genzabuke na Mheshimiwa Mama Sara kuhusiana na madeni ya Watumishi wa Umma especially wa kada za chini; Walimu, Wauguzi, Polisi na alitoa ushauri kwamba ni vema yakahakikiwa ili kuhakikisha kwamba madeni haya ya watumishi yanaondolewa na hayatakuwepo tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kulithibitishia Bunge lako kwamba, tayari madai mbalimbali ya Watumishi wa Umma yamekuwa yakilipwa kwa nyakati mbalimbali. Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ameweza kuelezea namna ambavyo madai mbalimbali yasiyo ya mishahara jinsi ambavyo yamelipwa. Nalihakikishia tena Bunge lako Tukufu kwamba, tutaendelea kulipa kwa kadiri hali ya kiuchumi inavyoruhusu; na tunatambua kwamba madai hayo ni muhimu lakini lazima tuzingatie suala zima la uhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa malimbikizo ya mishahara, kwa madeni ambayo tayari yameshahakikiwa na yanayosubiri kulipwa watumishi 1,622 yenye thamani ya takriban Shilingi bilioni 2.1, tayari yamekuwa yakiendelea kuhakikiwa na pindi yatakapokamilika basi yataweza kulipwa kwa utaratibu unaofaa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka huu wa fedha peke yake tayari Serikali imelipa takriban Shilingi bilioni 26.9 kwa watumishi 28,787 kama madeni mbalimbali yanayohusiana na malimbikizo ya mishahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo tumekuwa tukiipata katika madeni haya ni hasa katika suala la mfumo wetu kukokotoa automatic arrears. Kwa wale watumishi ambao taarifa zao au madai yao yanaingizwa katika mfumo baada ya tarehe 15, mfumo wetu kwa namna ambavyo umekuwa set, payroll inakuwa imefungwa. Kwa hiyo, inakuwa ni vigumu kuweza kuingiza taarifa hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba tumeona hili ni tatizo na limekuwa likileta usumbufu mkubwa na hivi sasa tunalifanyia kazi ili kuona ni kwa namna gani suala hili linaweza kurekebishwa ili hata kama Mtumishi atakuwa ameingizwa katika mfumo, baada ya payroll kufungwa, basi ukokotoaji uweze kufanyika bila ya kumsababishia mtumishi usumbufu wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo tumekuwa tukiipata, unakuta mfumo unakokotoa automatic arrears, lakini vile vile unakuta katika Watendaji wetu au Waajiri na wenyewe wanaleta madai mengine manually kupitia karatasi. Sasa kwa kufanya hivyo, kunasabisha marudio katika gharama na kufanya hivyo ni lazima sasa ili tuwe na uhakika, tufanye uhakiki, tusije tukajikuta tunalipa gharama mara mbili na kuisababishia Serikali hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na uhamisho kwa Watumishi wa Umma na kwamba uende sambamba na ulipaji wa fedha za uhamisho. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, tayari Serikali ilishatoa Waraka wa Utumishi Na.1 wa mwaka 2009 kuhusiana na udhibiti wa ongezeko la madeni ya Serikali kwa Watumshi wa Umma. Napenda kusisitiza kwa mara nyingine tena, waajiri wetu wahakikishe hawafanyi uhamisho kama hawajatenga fedha, kwa sababu wakifanya hivyo watajikuta wamekiuka suala zima la usimamizi wa Watumishi wa Umma na watakuwa wamewanyima haki watumishi ambao wamehamishwa bila kupata fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine ya Mheshimiwa Makilagi, Mheshimiwa Mwakajoka pamoja na Waheshimiwa wengine kuhusiana na suala zima la uboreshaji wa misharahara ya watumishi, lakini vile vile kuweka uwiano mzuri wa mishahara ya Watumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali inatambua sana umuhimu wa kuboresha mishahara pamoja na maslahi kwa watumishi wake, lakini vile vile kuweza kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ili kuweza kuwavutia watumishi wengi zaidi waweze kuingia katika Utumishi wa Umma na kuhakikisha kwamba wanapenda kubaki katika Utumishi huu wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, kupitia Tume ya Mheshimiwa Ntukamazina wakati huo, iliandaa mapendekezo kwa Mheshimiwa Rais ya kuanzisha Bodi ya Mishahara na Maslahi. Ni Bodi ambayo tayari ipo na imeshaanzishwa na majukumu yake makubwa ni kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusiana na suala zima la uboreshaji wa mishahara na maslahi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vile vile kueleza kwamba, tayari Bodi hii imekuwa ikifanya kazi nzuri na tayari imeshaanza suala zima la tathmini ya kazi pamoja na uhuishaji wa madaraja. Ni imani yetu kwamba itakapofika mwezi Februari, mwaka 2017 tathmini hii itakapokamilika, basi tutaweza kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kujua ni kwa namna gani sasa tunaoanisha pamoja na kuwianisha mishahara pamoja na kuangalia ngazi mbalimbali za mishahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tulishafanya utafiti kupitia Bodi hii kuangalia watumishi ambao wanafanya kazi katika maeneo yenye mazingira magumu, ni kwa namna gani sasa wanaweza wakapata motisha. Rasimu ya mwongozo huo iko tayari na hivi sasa inakamilishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi Serikalini na itakapokuwa tayari ni imani yetu kwamba tutaiwasilisha pia kwenu ili muweze kuifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi pia imeandaa rasimu ya mwongozo wa kupendekeza mishahara. Ukiangalia kuna sheria mbalimbali zinazoanzisha mamlaka na taasisi mbalimbali. Kila taasisi unakuta imejiwekea wajibu kupitia Bodi yake kupanga mishahara mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko taasisi ukiangalia kati ya Kiongozi Mkuu wa taasisi husika mpaka yule wa chini anayepata kima cha chini, uwiano unatofautiana sana. Wengine wana uwiano wa 1:63. Yeye anapata mshahara mmoja mwenzake ni mpaka akae miezi 63 ndipo aweze kumfikia. Pia utakuta taasisi nyingine ni uwiano 1:23, wengine ni uwiano wa 1:50. Kwa hiyo, ni lazima sana, wako ambao wamesema kama shirika husika linajitengenezea faida, linatengeneza fedha zake lenyewe, kwa nini lisiweze kujilipa gharama kubwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili kwa kweli tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuhakikisha kwamba mshahara hautazidi Shilingi milioni 15. Kwenye hili kwa kweli hatutarudi nyuma na tayari hatua zimeshaanza kufanyiwa maandalizi na wakati wowote utekelezaji utaweza kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na suala zima la upandishwaji wa vyeo kwamba uendane na ulipwaji wa mishahara. Changamoto ambayo tumekuwa tukiipata; upandishwaji wa vyeo unapofanyika, ni lazima Mwajiri aweze kutuma taarifa mbalimbali za maamuzi ya Kamati ya Ajira ya Taasisi husika; lakini wanapotuma kwa ajili ya uidhinishaji Utumishi, wengine unakuta taarifa zao zinakuwa na makosa, wengine unakuta waliwapandisha bila kuzingatia miundo ya maendeleo ya Utumishi, wengine unakuta waliwapandisha bila kuweka bajeti katika mwaka huo wa fedha, lakini vile vile unakuta katika suala zima la ikama hawakuweza kulizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kuwataka Waajiri waweze kuzingatia maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi (Chief Secretary) pamoja na Katibu Mkuu Utumishi katika suala zima la upandishaji vyeo watumishi na waweze kujitahidi; wazingatie vigezo vilivyoelezwa na waweze kuchukua hatua kwa wakati ili wasisababishe madeni na malalamiko ya watumishi yasiyokuwa ya lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la upungufu wa watumishi katika sekta mbalimbali. Napenda tu kuliarifu Bunge lako na kusisitiza kama ambavyo nimeeleza katika hotuba yangu, katika mwaka huu wa fedha tutaajiri watumishi 71,496. Wako waliosema ni mchakato; ni mchakato, ni lazima ili kuweza kuandaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapofanya maandalizi ni lazima pia kuweza kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara. Bajeti ya mishahara inategemea mapato ya ndani. Sasa inapofikia umezidi zaidi ya asilimia 51, tungependa sana kwa kiasi kikubwa bajeti yetu ya mishahara iwe kubwa, lakini inakuwa ni ngumu. Vipo vigezo vya Kimataifa tunafungwa navyo na ni lazima tuweze kuhakikisha tunavizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Sekta ya Elimu katika mwaka huu wa fedha, tutatoa ajira mpya za watumishi 28,957, kwa upande wa afya, ajira 10,870; kwa upande wa kilimo ajira 1,791; mifugo ajira 1,130; uvuvi ajira 400; Polisi ajira 3,174; Magereza ajira 1,000; Zimamoto ajira 850 na ajira nyinginezo 23,324. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizo ajira nyinginezo 23,324 ziko pia nafasi 1,349 kwa ajili ya Watendaji wa Vijiji na nafasi 648 kwa ajili Watendaji wa Kata ambazo zitatumika kujaza nafasi za ajira kwa kada hizi katika Halmashauri mbalimbali nchini. Nipende tu kueleza ajira hizi zitaanza mwezi Mei, 2016. Kwa hiyo, nitaomba kwa kweli muweze kutupa ushirikiano wa dhati katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ikulu pamoja na Utawala Bora kulikuwa na hoja kuhusiana na Fungu 30 la Ofisi ya Rais, kwamba ilikuwaje mwaka wa 2015 walikuwa na Shilingi bilioni 310.3 zilizoidhinishwa lakini kwa mwaka huu wana Shilingi bilioni 354.6. Napenda tu kueleza kwamba, kiasi kilichoongezeka ni Shilingi bilioni 52.3 na kinatokana na nyongeza ya mishahara ya taasisi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu baada ya mishahara kupanda mwezi Julai mwaka 2015 na mishahara hiyo ndiyo inayolipwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Msigwa alitaka kufahamu, au alibeza kwamba nimepata wapi uhalali wa kuwasilisha bajeti hii Bungeni wakati utawala bora unakanyagwa? Napenda tu kusema kwa mara nyingine tena kwamba, utawala bora haukanyagwi. Kama ambavyo alieleza misingi mbalimbali 22 ya utawala bora, tutaendelea kusimamia utekelezaji wake, tutaendelea kuhakikisha kwamba hatukiuki Katiba. Vile vile nimhakikishie kwamba kupitia Ibara ya 55 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri ana mamlaka kamili ya kuwasilisha bajeti Bungeni. Vile vile wasilisho hili ambalo nimelifanya, limezingatia misingi ya utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia na hoja ya Mheshimiwa Mwakajoka kwamba Kiongozi wa Kitaifa, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akishindwa kutambulisha Vingozi wa Vyama vya Upinzani wakati wa ufunguzi wa miradi mbalimbali mikubwa. Napenda kupingana na hoja hii, kwa sababu nikichukua takwimu za haraka haraka, tukiangalia katika ufunguzi wa flyover ya TAZARA; ufunguzi wa Daraja la Kigamboni; kwa Kigamboni mimi mwenyewe nilikuwepo. Meya wa Jiji alitambulishwa. Kwa nini hamwelezi hapa kwamba walitambulishwa? Pia walitambulishwa kupitia ufunguzi wa Mradi wa flyover.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa AG kwa ufafanuzi ambao ameutoa kuhusiana na TAKUKURU kupewa nafasi au mamlaka ya kupeleka kesi za rushwa Mahakamani. Kwa kweli ameeleza vizuri sana, lakini bado niendelee kusisitiza, ni maamuzi mazuri kuhusiana na suala zima la checks and balances.
Vile vile ukiangalia kwa DPP kupitia Ibara ya 59 ya Katiba yetu, imeeleza atakuwa na mamlaka ya kuendesha mashtaka. Kwa makosa yale ambayo Mheshimiwa AG ameyaeleza, yanayoangukia katika Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya 2007 ndiyo ambayo yamekuwa na mamlaka kwa TAKUKURU kuweza kushtaki bila kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, tunachukua ushauri na tutaendelea kuufanyia kazi kuona faida na hasara zake, endapo tutaamua kubadili mfumo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Grace Kiwelu alitoa kwamba kuna Shilingi milioni 90 ziliibiwa katika Basket Fund. Napenda nishukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametupatia taarifa mbalimbali kuhusiana na upotevu wa fedha. Nawahakikishia kwamba tutazifanyia kazi kwa kina na hatua stahiki zitachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Manispaa ya Moshi, tayari watuhumiwa wameweza kurejesha fedha ambazo walikuwa wamezifuja, lakini hii ni hatua ya awali tu. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakapokamilisha tathmini ya ushahidi na majalada haya yatakapopelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, yatakapopata kibali tutaweza kuyawasilisha Mahakamani na hatua stahiki zitachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa AG kuhusiana na majibu ya hoja ya hati fungani ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Kabwe Zitto; vile vile kulikuwa kuna hoja kuhusiana na IPTL na Tegeta Escrow ambapo shauri liko Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja ya hati fungani, kwamba ni kwa nini Serikali ya Tanzania au TAKUKURU haijaishtaki Benki ya Standard Bank. Napenda tu kueleza kwamba, suala hili linahusisha uchunguzi unaoendelea na vile vile suala hilo sote tunafahamu iko kesi nyingine Mahakamani. Tutakapokamilisha mashauriano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi na endapo ushahidi utathibitisha tuhuma ambazo zimeelezwa, bila kusita Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya mtu au taasisi yoyote ya ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia kwamba Maafisa wa TAKUKURU wasikae sehemu moja zaidi ya miaka mitatu. Tayari upo utaratibu, kwa mpango ambao TAKUKURU wamejipangia, wao ni miaka mitano mitano. Tutahakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha tunaouanza tutaanza kuhamisha watumishi 90 ambao wameshakaa kwa zaidi ya miaka mitano. Inakuwa ni miaka mitano kwa sababu, wakati TAKUKURU imeundwa upya mwaka 2007 waliajiriwa watumishi wengi zaidi.
Kwa hiyo, tukienda kwa miaka mitatu mitatu tutajikuta pia tunawavunja nguvu na matokeo yake wanaweza wakajikuta wana upungufu wa watumishi. Vile vile tunazingatia pia suala zima la gharama katika uhamisho huo ambao umekuwa ukifanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia kuna hoja ya Mheshimiwa Kakunda kwamba, wako watumishi ambao wanajikuta wameshtakiwa, wana mashtaka ya rushwa halafu wamekuwa wakitumia fedha za Serikali kwenda katika kesi zao Mahakamani; wamekuwa wakijilipa per-diems. Napenda kukemea, wako Wakurugenzi mbalimbali wa Halmashauri wamekuwa wakifanya hivyo. Tunaendelea kuwachunguza na itakapothibitika, watatakiwa kurudisha fedha zote ambazo walikuwa wakizitumia kwa ajili ya kwenda Mahakamani, lakini vile vile gharama zote ambazo walizitumia kwa ajili ya kuendesha magari na mafuta na kuwalipa madereva kuwapeleka Mahakamani kusikiliza kesi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni lazima likome na liwe fundisho kwa watendaji wengine wote mbalimbali watakaokuwa na mashauri mbalimbali ya kiutendaji na ya kuhusiana na rushwa Mahakamani kutumia gharama za Serikali kwa ajili ya kesi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja kwamba wako watumishi wana kesi mbalimbali za jinai, lakini bado wanaendelea na Utumishi wa Umma. Niseme tu kwamba kupitia kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 imetoa discretion kwa Mwajiri aidha, mtumishi aendelee na kazi au asimamishwe mpaka hapo shauri lake litakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika Kanuni ya 30 (2) ya Standing Order, lakini vile vile kanuni ya 50(a) zimetoa discretion hii. Mara zote ambapo wamekuwa wakithibitika, hatua stahiki za disciplinary procedures za kusimamishwa pamoja na kuhitimishwa katika kazi zimekuwa zikichukuliwa. Niseme suala hili tunalitambua na kwa kweli kidogo na sisi limekuwa likitupa concern. Tumeshaanza sasa hivi kufanya mapitio ya Standing Orders mbalimbali, lakini tutayapeleka kwa wadau, watakachopendekeza tutaweza kuona ni nini kiweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mtuka ambaye alieleza kwamba suala la bajeti ya TAKUKURU kwa kweli imekuwa ni ndogo. Niseme tu kwamba tunamshukuru kwa ushauri wake na Serikali tutaendelea kuchukua hatua kuiwezesha TAKUKURU kwa kadiri uwezo wetu wa kifedha utakavyokuwa ukiruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kisangi aliendelea kupongeza suala zima la uanzishwaji wa clubs za wapinga rushwa na nimhakikishie kwamba tutaendelea kufanya hivyo kila mwaka itakapobidi na tunaomba ushirikiano wao wa dhati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwenye suala zima la upungufu na ukosefu wa majengo kwa ajili ya Sekretarieti ya Maadili. Napenda tu kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, tayari kwa jengo la Kusini Mtwara limeshakamilika na tayari wameshahamia, tunasubiri tu kukamilisha hatua chache zilizobaki kwa ajili ya kuhitimisha jengo hili liweze kukamilika kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika bajeti ya mwaka huu kama ambavyo mtaona, tumetenga bajeti katika fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Kanda ya Kati Dodoma. Tumeanza maandalizi, tutafanya usanifu wa jengo la Ofisi ya Sekretarieti, Makao Makuu au Maadili House na tunaendelea pia kufanya mashauriano na Wakala wa Majengo (TBA) ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kupata mbia wa ajili ya kuliendeleza jengo hili la Makao Makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja kutoka kwenye Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikiitaka Serikali ihakikishe kwamba inafungua Ofisi katika kila Mkoa kwa ajili ya Sekretarieti za Maadili. Ushauri huu tunaupokea na lengo letu kama Sekretarieti ni kuhakikisha kwamba, tunasogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kwa hivi sasa tumeshafungua ofisi saba na tutaendelea kufanya hivyo kwa kadiri hali itakavyokuwa ikiruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba mali na madeni ya viongozi zitangazwe kwa uwazi wakati viongozi wanapoingia madarakani na wakati wanapohitimisha uongozi wao. Ukiangalia katika Kifungu cha 20 kikisomwa pamoja na Kifungu cha saba (7) cha Kanuni za Maadili za Viongozi wa Umma, mwananchi anayo fursa ya kuweza kukagua daftari la tamko la mali na madeni atakapokuwa amelipia sh. 1,000, lakini haipaswi kutangaza mali zile hadharani. Unatakiwa uzitumie tu kwa sababu zilizokupelekea kufanya ukaguzi huo. Kwa hiyo, napenda tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 20 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, lakini vile vile matakwa ya kanuni ya saba (7) ya Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma za mwaka 1996.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia kuna hoja kutoka kwa Kamati ya Mheshimiwa Lubeleje pamoja na Waheshimwa wengine, kwamba TASAF iendelee kutoa elimu kuhusiana na TASAF Three. Nipende tu kuhakikisha kwamba tayari TASAF imekuwa ikitoa elimu kuhusiana na mpango huu na imekuwa pia ikieleza kuhusiana na taratibu mbalimbali na kero mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza zimekuwa zikijibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukitumia Redio mbalimbali za kijamii ambazo ziko katika Halmashauri zetu kuweza kujibu hoja mbalimbali ambazo zimejitokeza katika jamii kuhusiana na mpango huu wa TASAF awamu ya tatu. Niendelee tu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa wako karibu zaidi na wananchi na wenyewe pia waendelee kutusaidia kuuelezea mpango huu ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba, wako watu ambao wamekuwa hawafanyi uadilifu katika fedha hizi za TASAF! Napenda tu kuliarifu Bunge lako Tukufu, kuanzia mwezi Aprili tumeshaanza uhakiki kuangalia walengwa wote ambao wananufaika na mpango huu ambao hawastahili na tayari tumeshaondoa kaya 6,708, lakini vilevile tunaendelea kuchukuwa hatua stahiki za kinidhamu pamoja na za kijinai kwa wale ambao walisababisha majina haya kuingizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba asilimia 70 peke yake ya Vijiji ndiyo ambavyo vimefikiwa na mpango huu. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, katika mwaka huu wa fedha asilimia 30 ya Vijiji ambavyo vimebaki, Shehia na Mitaa mbalimbali itaweza kufanyiwa utambuzi pamoja na uandikishaji na baadaye malipo yatakuja kuanza katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kulikuwa kuna hoja nzuri sana kwamba, walengwa hawa wanaopatiwa ruzuku hii ya uhawilishaji, ikiwezekana waweze kuunganishwa na Mfuko wa Afya ya Jamii au CHF. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tayari Halmashauri 27 zikiwemo Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Singida pamoja na Mtwara, wamekuwa wakifanya vizuri na kaya takribani 52,980 zimeshajiunga na Mfuko huu wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa rai kwa wananchi wengine mbalimbali, tutakapokuwa tukiwahamasisha na kuendelea kuwaelimisha kuhusiana na umuhimu wa fedha hizi na Mfuko huu, basi wajitahidi kujiunga kwa sababu tunaamini itaweza kuwapunguzia gharama kubwa. Kama tunavyofahamu, ruzuku hii imepeleka pia masharti katika suala zima la elimu, lishe pamoja na afya. Kwa hiyo, tunaamini kwa gharama ile ya Sh. 10,000/= kwa mwaka mzima, itaweza kuwasaidia pia katika suala zima la afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja ilitolewa kwamba ufanyike ukaguzi maalum kuhusiana na ufanisi wa Mfuko, lakini vilevile kuangalia kama suala zima la kugawa fedha litaweza kuwa na tija. Napenda tu kusema kwamba tulishaagiza kwa CAG kufanya ukaguzi maalum kujiridhisha tu kama mambo yote yanaenda vizuri. Pia napenda tu kusema kwamba tija ipo. Ukiangalia katika Mfuko huu unaotolewa katika ruzuku hii ya uhawilishaji imekuwa ikienda sambamba na suala zima la kuelimisha wananchi pia katika suala zima la uchumi na umuhimu wa kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu imeunganisha na mpango wa kuweza kulipa ujira, wanakuwa wanapewa fedha kidogo, ruzuku ya uhawilishaji, lakini hapo hapo kwa siku 14 kwa wakati ambao wanapata ukata wa hali ya juu, wamekuwa wakiweza kufanya kazi mbalimbali za kijamii na kulipwa. Tumejionea pia kwa wale ambao wametumia fedha hizi vizuri, wameweza kwa kweli kujikomboa na wengi wao ndani ya miaka mitatu wameweza kuondokana na mfumo huu na kutoa nafasi kwa wananchi wengine kujiunga na mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kuhusu miradi ambayo haikukamilika katika TASAF awamu ya pili. Tayari tumeshafanya tathmini, iko miradi 137 ambayo haikuweza kukamilika katika TASAF awamu ya pili, lakini tayari tumekwishaingia makubaliano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tayari tumeshaelekeza kwamba Halmashauri ambazo hazijakamilisha, basi zijitahidi kuendelea kuhakikisha kwamba zinakamilisha mapema na pindi zitakapokamilisha miradi hiyo iliyobakia 137 TASAF itaweza kutoa Hati kuhusiana na ukamilishaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kuhusiana na MKURABITA. Wengi wameweza kuchangia sana kuhusiana na suala zima la mpango wa matumizi bora ya ardhi. Wote tunafahamu, katika nchi yetu ni asilimia 10 pekee ndiyo imeandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Vijiji vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kushirikiana na MKURABITA pamoja na Wizara ya Ardhi imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kwamba Vijiji vyote vinaandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kwa kutambua kwamba fedha inayotoka ni kidogo kidogo na hatuwezi kukamilisha asilimia yote 90 kwa mwaka mmoja, Serikali imeanzisha Mfuko endelevu wa Halmashauri mbalimbali kwa ajili ya urasimishaji wa ardhi katika ngazi za Wilaya na tayari katika mwaka huu wa fedha kuanzia tarehe 1 Mei, urasimishaji wa majaribio utaanza katika Mkoa wa Iringa; Iringa Mjini pamoja na Morogoro Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa waunge mkono na ni imani yangu Mheshimiwa Mchungaji Msigwa hutachukulia na kulipeleka kisiasa suala hili na utaweza kuliunga mkono. Tutahakikisha kwamba fedha zile zitakazotolewa; MKURABITA watatoa milioni 100 kwa kila Wilaya, kwa kuanzia na Wilaya hizi za majaribio.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Halmashauri zitaweza kukopeshwa na Benki ya CRDB ili kuweza kuhakikisha kwamba suala zima la upimaji na suala zima la uuzaji wa viwanja linafanyika ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaingia katika mfumo rasmi wa umiliki wa ardhi. Wote tunatambua; unapokuwa na ardhi ambayo imerasimishwa itaweza kukusaidia pia kuweza kuitumia kama dhamana kwa ajili ya kujipatia mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia kwamba, baadhi ya Benki hazitambui hati mbalimbali za kimila. Napenda kutoa rai kwa Benki mbalimbali, hati hizi zinayo thamani sawa kabisa na waweze kuhakikisha kwamba wanaziunga mkono na kuweza kutoa mikopo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitimisha kwa kuomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu muweze kuiunga mkono hoja hii ili kutuwezesha kutekeleza vema majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Taasisi zake kwa ufanisi katika mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kuchangia hoja hii ya Taarifa ya Shughuli ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa mwaka huu wa fedha. Kwanza kabisa, niseme naunga mkono hoja hii ya Kamati na niipongeze sana Kamati chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Rweikiza na Makamu Mwenyekiti pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote kwa namna ambavyo wamekuwa wakitushauri na kutusimamia kama Serikali katika majukumu mbalimbali tunayoyatekeleza. Kipekee zaidi niwashukuru kwa ziara mbalimbali walizozifanya katika maeneo yetu tunayoyasimamia na zaidi katika kutembelea miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba, yote yaliyowasilishwa na Kamati tutayafanyia kazi na tutaleta utekelezaji katika Kamati kuona ni kwa namna gani tumeweza kuyatekeleza. Vilevile nipende kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia taarifa hii kwa ushauri wao na kwa changamoto ambazo wamezibainisha na niwahakikishie kwamba tutazifanyia kazi na kuzitekeleza na naamini wataweza kuona mrejesho wake namna ambavyo tutazitekeleza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuna hoja kubwa katika suala zima la utaratibu wa hatua za kinidhamu katika utumishi wa umma. Ni jambo ambalo nimeliona limesemewa sana na Kamati lakini Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kiasi kikubwa wamelisema suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa nidhamu na ajira katika utumishi wa umma unatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu lakini zaidi ya yote sheria yetu mama ambayo ni Katiba ya nchi yetu. Vilevile kama Wizara ya Utumishi wa Umma tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali ambayo inasimamia utumishi wa umma na kuongoza viongozi wote ambao wanatekeleza masuala ya nidhamu pamoja na ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo mamlaka mbalimbali za ajira na nidhamu. Ukiangalia katika kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na Kanuni ya 35 ya Kanuni za Utumishi wa Umma zimeeleza bayana ni namna gani mamlaka za nidhamu zitaweza kutekeleza majukumu yake katika kuchukua hatua za kinidhamu. Hata itakapotokea Wakuu wa Mikoa au Wakuu wa Wilaya au kiongozi mwingine yeyote wa Serikali anapochukua hatua stahiki za kinidhamu ni lazima mamlaka ile ya ajira na nidhamu ndiyo itekeleze jukumu hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba ieleweke bayana na napenda kuwatangazia wote tuzingatie misingi ya kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Umma pamoja na Kanuni ya 35 ya Kanuni zetu za Utumishi wa Umma. Hata katika makundi mengine ya utumishi, tunao watumishi wa Bunge, tunao watumishi wa Mahakama, tunao wanataaluma wengine, tunao watumishi wengine katika vyombo vya ulinzi na usalama, nao pia ni makundi ya utumishi wa umma lakini ipo miongozo ya mamlaka zao pia za ajira na kinidhamu. Kwa hiyo, niombe sana viongozi wetu wengine wa kisiasa pamoja na viongozi mbalimbali na mamlaka za ajira na nidhamu waweze kuhakikisha kwamba wanatekeleza misingi hii kama ilivyoanishwa katika sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nisisitize mahusiano. Jambo kubwa ukiangalia sehemu zingine unakuta mahusiano ni tatizo. Kila mmoja aone ana wajibu wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na mahusiano mazuri na viongozi wa Serikali vilevile pamoja na viongozi wa kisiasa. Naamini tukiwa na mahusiano na mawasiliano mazuri kwa kiasi kikubwa migongano ambayo ipo itaweza kuondoka kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetolewa pia hoja kuhusiana na semina elekezi. Nipende tu kusema kama Serikali na asubuhi nilikuwa na swali nimejibu, tumekuwa tukitoa mafunzo ya aina hii na hatutasita kuendelea kutoa mafunzo kama haya tena. Hata Utumishi mwezi huu tumepanga tena mafunzo ya siku saba kwa viongozi hawa kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiutumishi, masuala ya maadili ya utumishi wa umma nao kama viongozi vilevile masuala mengine ya rushwa, nidhamu pamoja na masuala ya fedha. Niwaombe sana viongozi hawa wote wanaohusika waweze kuhakikisha kwamba wanazingatia sheria, kanuni na utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia kwa Waheshimiwa Wajumbe wote waliochangia kuhusiana na hoja za TASAF na nashukuru kwamba mmeweza kuona ina manufaa. Niwahakikishie kwamba tutaendelea kufuatilia ili kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazojitokeza na upungufu wote uliopo basi unaweza kuchukuliwa hatua. Tumeanza kuchukua hatua ya kuboresha usimamizi zaidi pia tunaangalia suala zima la mfumo wa utambuzi, ni namna gani kaya hizi maskini zinazostahili kuingizwa kwenye mfumo zinaweza kutambuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote wameeleza hapa, wapo ambao walikuwa hawahudhurii katika mikutano ya hadhara ya wananchi ya kuibua kaya hizo, wako ambao wengine walikuwa wanasema hela hizi ni za freemason matokeo yake zimekuja kuingizwa zingine ambazo hazistahili na zile zinazostahili zimekuwa zikiachwa nyuma. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tutayafanyia kazi, tumeanza kuondoa kaya 55,692 lakini zaidi tutaangalia control mechanisms. Pia nilimsikia Mheshimiwa Bashe tutaenda kuangalia kwa kina ili kuona tuje na mfumo gani mzuri zaidi ambao utaweza kutusaidia katika kutekeleza mfumo huu wa maendeleo ya jamii bila kuleta matatizo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia kuna mtu anasema kuna kaya zimechukua hizi fedha ambazo hazistahili kwamba iweje leo hii waambiwe warudishe. Nipende tu kusisitiza kwamba kila fedha iliyochukuliwa kwa kaya ambayo haistahili ni lazima itarudi whether ni kaya maskini au ni tajiri lazima itarudi kwa sababu kama angekuwa ni maskini angekuwa kwenye mpango kihalali. Yule ambaye ameondolewa hastahili kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na ofisi yetu ya Takwimu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya suala zima la ajira, niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tayari tumeshaanza kufungulia ajira. Tulishaajiri nafasi 5,074 na tayari wamesharipoti na kwa sasa tuko katika hatua ya kuajiri watumishi wengine wa sekta ya elimu pamoja na maabara watumishi 4,348. Baada ya hapo tutaingia katika sekta ya afya pamoja na sekta zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge walioeleza upungufu katika sekta ya afya, ni kweli tuna upungufu wa takribani asilimia 51.3 ambao ni sawa na watumishi 54,459. Tunachokifanya sasa tunaangalia pia uwezo wetu wa kibajeti, tungependa kuajiri watumishi wengi sana. Kwa ujumla kwenye Serikali tuna upungufu wa watumishi 160,172,000 lakini kwa sasa tunajitahidi kwenye maeneo yenye vipaumbele na kwenye Halmashauri zenye upungufu mkubwa kuona ni kwa namna gani tunawapatia watumishi hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja pia kuhusiana na uhakiki wa matamko ya fomu za maadili. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameshawasilisha matamko yao. Kweli kwa kipindi hiki tumeweza kuvuka lengo ukiangalia waliowasilisha tarehe 31 walikuwa ni zaidi ya asilimia 87, ni namba ambayo kwa kweli ilikuwa haijawahi kufikiwa huko nyuma. Kwa hiyo, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Zaidi niwahakikishie pia tutaendelea na uhakiki, tumeshafanya uhakiki kwa viongozi wa umma 116 na lengo letu kabla ya kufika mwezi Juni tutakuwa tumefanya uhakiki wa viongozi 500. Kwa hiyo, tunaomba tu Waheshimiwa viongozi wa umma waweze kutoa ushirikiano watakapofuatwa kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki wa mali zao na madeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja pia ya maabara ya uchunguzi au forensic laboratory, tunazo maabara za aina mbili. Kuna moja yenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kieletroniki na nyingine ina uwezo wa kufanya uchunguzi wa kimaandishi. Ile ya uchunguzi wa kieletroniki imeshaanza kazi. Tunawashukuru Kamati kwa kuifuatilia na tayari wameshachunguza majalada takribani 109. Kwa upande wa document forensic au uchunguzi wa maandishi, kwa sasa kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ni Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ndiyo ambaye anaruhusiwa kuwaruhusu TAKUKURU kuweza kuwa na maabara hii ya kuweza kufanya uchunguzi wa kimaandishi. Tayari tumeshawasilisha na tunaendelea vizuri na tunaamini ataweza kukubali maombi haya ili TAKUKURU maabara yake iweze kufanya kazi kwa ajili ya kuharakisha uchunguzi na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa kesi zetu mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia watu wanasema uhakiki hauishi. Tumekuwa tukifanya uhakiki kwa umakini mkubwa sana na niseme uhakiki kwa watumishi hewa tumeshamaliza, lakini mwisho wa siku bado utakuwa endelevu pindi tutakapokuwa tunaona kuna watu ambao wameingia hawastahili watakuwa wakihakikiwa na watakuwa wakiendelea kuondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tunachokifanya ni uhakiki wa vyeti vya kitaaluma na nipende kusema kupitia Bunge hili tumeshatangaza kwa mtumishi wa umma ambaye aliombwa awasilishe cheti chake cha taaluma cha form four, six na cheti cha ualimu au taaluma nyingine akashindwa kuwasilisha lakini bado tukatoa fursa aweze kuwasilisha index namba na bado akashindwa, basi itakapofika tarehe 1 Machi tunaanza mchakato wa kuanza kufukuza kazi mtumishi wa aina hiyo. Kwa hiyo, niombe kupitia Bunge hili iweze kusikika vizuri kabisa na waweze kuzingatia suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema uhakiki hauishi hapana, huu ni uhakiki mwingine kabisa. Ni lazima tuwe na watumishi wa umma ambao kweli wamebobea na kweli wameenda shule. Wako watu wengine wana vyeti vya ualimu hata kwenye chuo cha ualimu chenyewe hakuwahi kufika kabisa, unategemea nini? Tunalaumu hapa kwamba ni masuala ya elimu bure fedha inaenda kidogo, kuna mambo mengine ni kama haya ndiyo ambayo yanachangia. Kwa hiyo, tunaomba mtupe fursa tujitahidi kuweka mambo sawa kuhakikisha kwamba tuna watumishi wa umma wale tu ambao kweli walisomea, kweli vyeti vyao ni vya halali na hawajaingia katika ajira kwa sifa ambazo hawastahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja nyingine kuhusiana na hatua za kinidhamu ambazo zimechukuliwa dhidi ya watumishi wa umma au viongozi waliobainika kusababisha watumishi hewa. Nipende tu kusema kwamba hadi sasa Serikali imeshawachukulia hatua watumishi wa umma 1,595 kwa mujibu wa Sheria zetu za Utumishi wa Umma na taratibu zao za nidhamu ziko katika hatua mbalimbali. Kati ya watumishi hao 1,595 watumishi 16 wanatoka katika Wizara sita, watumishi tisa wanatoka katika Sekretarieti za Mikoa na 1,564 wanatoka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Tutaendelea kusimamia na kuhimiza utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyopo katika utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja kuhusiana na Wakala wa Serikali Mtandao kwamba inawezekanaje mpaka sasa bado wana ukosefu wa sheria inayoanzisha Wakala huu. Nipende tu kusema kwamba tunashukuru na tunapokea ushauri wa Kamati na tayari tumeanza kuufanyia kazi, tuko katika hatua nzuri ya kuandaa Waraka kwa ajili ya kuanzisha Wakala huu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchukua fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa namna ambavyo amekuwa akiniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya kusimamia Menejimenti ya Utumishi wa Umma pamoja na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee pia nimshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwani wao pia wamekuwa wakituongoza vyema na wamekuwa wakitoa msaada mno na ushauri ambao umenisaidia sana katika kutekeleza majukumu ya ofisi yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Bunge, Katibu wa Bunge pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati yangu kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanikisha majukumu ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Utekelezaji wa Sera, Mikakati mbalimbali Pamoja na Mipango. Wote tunafahamu namna ambavyo inahitaji kuwa na watumishi wa umma wenye weledi, uadilifu na walio makini kwa kuwa wote tunajua utumishi wa umma ndiyo nguzo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Nia ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni kuendelea kuiboresha Sekta yetu ya Utumishi wa Umma, kuhimiza katika misingi ya weledi, kuendelea kuweka mifumo ya menejimenti inayowezesha watumishi kuwajibika vyema, kuwa na maadili ili waweze kutoa huduma iliyo bora na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma endapo watazingatia sifa hizo nilizozitaja basi kwa hakika tutaweza kujionea utendaji mzuri zaidi wenye matokeo na hii itatuwezesha kuwa na tija zaidi, kuwa na mapato makubwa zaidi na hatimaye kuweza kuboresha zaidi maslahi ya watumishi wetu wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunaendelea kuhakikisha kwamba utumishi wa umma unaongozwa na kusimamiwa ili kuhakikisha kwamba hauendi kinyume na misingi hiyo niliyoitaja awali. Ili kuhakikisha kwamba tunalinda misingi hiyo, kama Serikali tumekuwa tukifanya mabadiliko na maboresho mbalimbali katika Sekta yetu ya Utumishi wa Umma, lakini vile vile katika sekta mbalimbali tumeshuhudia maboresho katika utendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia programu yetu ya Maboresho katika Utumishi wa Umma hadi mwaka 2014, lakini vile vile tumeanza kuchukua hatua kwa kushirikiana na DFID pamoja na World Bank kuona ni kwa namna gani tunaweza kuweka utaratibu mwingine na kubuni maboresho yatakayoendeleza mipango ya matokeo makubwa katika utoaji wa huduma kwa kuondoa vikwazo katika utumishi wetu wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano, tumekuwa tukichukua hatua mahsusi za kusimamia Sera na mifumo ya kimenejimenti, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, masuala mazima ya nidhamu, mapambano dhidi ya rushwa, uadilifu na uwajibikaji navyo pia tumekuwa tukiendelea kuweka mkazo. Sisi tunaamini kwamba tutakapozingatia haya, basi watumishi wa umma watafanya kazi kwa weledi na kwa bidii kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, niwaahidi tu kwamba kama Serikali tutaendelea kuimarisha vita dhidi ya rushwa ambapo kama hatua ya uadilifu, tutaendelea pia kuhakikisha kwamba viongozi na watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo vya taaluma zao, viapo vya uadilifu na pia kuhakikisha kwamba wanawajibika kwa matokeo ya kazi na maamuzi yao ili kuhakikisha kwamba tunaondokana na maamuzi na matumizi mabaya ya madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba yangu. Niwashukuru sana Wabunge 47 walioweza kuzungumza, niwashukuru pia Wabunge 27 ambao waliweza kuchangia kwa maandishi. Nawashukuru Wabunge hawa kwa kuongozwa na Mheshimiwa Rweikiza Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Makamu wake mwanamama machachari Mheshimiwa Mwanne Nchemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimtambue na kumshukuru Mheshimiwa Ruth Mollel Waziri kivuli wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa maoni na michango yao ambayo naamini kabisa itaweza kutusaidia kuboresha utumishi wa umma na utawala bora nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda hautoshi kuweza kujibu hoja zote, nitajitahidi kadri nitakavyoweza, lakini niwahakikishie tu kwamba katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la 11 Wabunge wote mtaweza kupata majibu yetu kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na hoja chache zilizojitokeza katika Utumishi wa Umma. Kulikuwa kuna hoja ya Kamati yetu ya Bunge, kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma ni vyema kikawezeshwa ili kiweze kumiliki majengo yake katika campus zake na hususan walitolea mfano wa campus ya Mbeya ambayo wamekuwa wakitumia gharama kubwa sana kwa aili ya kulipia pango. Niseme tu kwamba nawashukuru Kamati kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia utendaji wa Chuo hiki. Waliweza kufika katika campus ya Chuo chetu cha Mbeya, waliweza kujionea na kuweza kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, tayari tumeshawasilisha maombi kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wanaliangalia jambo hili kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ili kuona ni namna gani sasa Chuo cha Utumishi wa Umma tunaweza tukamilikishwa majengo haya kwa taratibu ambazo tutaweza kupangiwa na kuelewana kwa pamoja. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunasubiri maamuzi ya TAMISEMI na tunaenda vizuri, tunaamini tunaweza tukafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja pia ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo pia Mheshimiwa Sannda aliitolea maelezo pamoja na Mheshimiwa Bobali. Hii ni kuhusiana na umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wetu wa umma, lakini wao walienda mbali kwamba tupanue wigo sasa, katika mafunzo haya basi tuangalie pia ndani ya nchi lakini twende pia na nje ya nchi ili kuhakikisha kwamba watumishi wanakuwa exposed zaidi katika kupata mafunzo. Niwashukuru wote kwa hoja hii. Hakuna anayebisha hata kidogo umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu kwamba tunayo Sera yetu ya mafunzo kama Serikali lakini vile vile tunayo Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 1999 ambayo ilirekebishwa mwaka 2004. Kimsingi Sera hii pia inasisitiza katika umuhimu wa waajiri kuweka kipaumbele katika kuandaa mipango ya mafunzo ambayo itazingatia mahitaji yao halisi lakini pia kuhakikisha kwamba wanaongeza ufanisi katika sehemu zao za kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema tu kwamba kupitia ofisi yangu pia katika Idara ya Uendelezaji wa Rasilimali watu tumekuwa tukitafuta fursa mbalimbali za mafunzo ili kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wengi zaidi wanaweza kujiendeleza na kuweza kupata ujuzi. Nikichukua tu katika mwaka 2015/2016 zaidi ya watumishi wa umma 395 waliweza kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu nje ya nchi. Pia katika Mwaka huu wa Fedha zaidi ya watumishi wa umma 654 nao pia waliweza kupata mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba ni eneo ambalo tunalipa kipaumbele. Nipende kutoa rai kwa waajiri wetu mbalimbali, kama ambavyo wanatenga fedha kwa kuzingatia masuala mbalimbali ya kuzuia virusi vya UKIMWI pamoja na masuala mengine yanayowekewa mipango katika MTF, ni vyema sasa first priority katika bajeti zao wahakikishe kwamba kipaumbele kinawekwa katika mafunzo. Tusitafute visingizio na sababu kwamba hakuna fedha. Humo humo katika kidogo, tuone namna gani tunawajengea uwezo watumishi wetu.

Mheshimiwa Mweyekiti, kulikuwa na hoja ya utumbuaji wa watumishi na kwamba utumbuaji huo uchukuaji wa maamuzi ya kinidhamu ulikuwa hauzingatii sheria na umekuwa ukifanywa kwa ukiukwaji na hata umepingwa na Tume ya Haki za Binadamu. Nipende tu kusema kwamba waliotoa hoja hii hususan Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wanajua kabisa taratibu nzima za maamuzi ya kinidhamu, Sheria Namba 8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 imeeleza kabisa bayana taratibu. Zaidi ya hapo tunazo Kanuni za Utumishi wa Umma. Ukiangalia katika Kanuni ya 46 na 47 imeeleza bayana ni masuala gani na hatua zipi za kuzingatiwa pindi mamlaka ya ajira na nidhamu inapotaka kuchukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, hatua hizi za kutengua teuzi, kusimamisha mtu kazi na kuwafukuza kazi zimeelezwa bayana. Ni yule tu mwenye mamlaka ya nidhamu ndiyo anatakiwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, niombe sana watu waendelee kufuata taratibu hizo na zaidi ya yote nisingependa kusikia sehemu zingine inaelezwa mchakato mzima usizidi siku 120 katika hatua za kinidhamu, lakini unashangaa kuna mwingine zaidi ya miezi minne tangu amepewa hati ya mashtaka shauri hilo halijahitimishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana na tunaendelea kuwafuatilia na kwa mwajiri yeyote tutakayembaini amekiuka taratibu, amekiuka masharti ya Kanuni ya Utumishi wa Umma katika kuchukua nidhamu tutahakikisha tunamchukulia hatua na ajira yake pia itakuwa mashakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuendelea kusisitiza, hakuna mamlaka yoyote ya nidhamu inayoruhusiwa au inayopata ruksa ya kukiuka haki za watumishi kwa namna yoyote ile. Kwa hiyo, ni vyema tu waajiri wahakikishe kwamba wanazingatia Sheria, wanazingatia Kanuni, Miongozo pamoja na Taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine kuhusiana na upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta ya utumishi wa umma, mifano iliyotolewa ni kada ya afya pamoja na elimu. Waheshimiwa Wabunge walitaka kufahamu Serikali itaajiri lini watumishi wa kada hizo. Hoja hii ilitolewa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani lakini vile vile Mheshimiwa Rashid Chuachua, Mheshimiwa Bura, Mheshimiwa Atashasta na wengine wengi walilisemea hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kaka yangu Simbachawene ameanza kuliwekea utangulizi kidogo na niseme tu kwamba kama Serikali tunatambua umuhimu wa kuwa na rasilimali watu inayotosheleza kuweza kuhudumia wananchi wetu kwa utoshelevu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema, kama nilivyoeleza katika maelezo ya hotuba yabgu, tayari tulishatoa vibali zaidi ya 9,700 na wameshaingia kazini. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais pia, kwa kuona umuhimu wa Madaktari zaidi ya 258 na tayari Jumatatu wanaingia kazini. Nipende tu kusema huo si mwisho, tunaendelea pia na watumishi wengine katika kada zingine ili kuhakikisha kwamba kweli tunakuwa na utumishi wa umma wenye watumishi wa kutosha. Niwahakikishie tu kwamba kabla ya mwaka wa fedha haujakwisha mtakuwa mkisikia na kushuhudia watumishi katika sekta mbalimbali wakiendelea kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili kuweza kutoa neno lingine la kutia moyo, katika mwaka ujao tena wa fedha wa 2017/2018 tutaajiri tena kwa nyongeza watumishi wengine 52,436. Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba kama Serikali tunaliona na tunaendelea kuajiri kwa awamu kwa kuhakikisha kwamba haturudii makosa yale ya wakati ule ya kuwekwa wale watumishi hewa, kurudia makosa ya kuwa na watumishi ambao hawana sifa na weledi unaohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja kwamba Serikali hii imekuwa ni ya kuhakiki tu. Kwa kweli ni hoja ambayo imenishangaza sana mimi. Duniani kote, kama kweli unataka kuwa na utumishi wa umma uliotukuka hutaacha kufanya uhakiki wa rasilimali watu wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukakaa tukawa na watumishi wa umma zaidi ya laki tano na arobaini na mbili elfu na mia moja na sabini na sita bila kujua kila mmoja ana sifa na weledi, bila kujua kama kweli work load analysis kwa kila sehemu kila mtu ana kazi inayomtosheleza, bila kujua kama kila mmoja anatekeleza majukumu yake inavyotakiwa, bila kujua kama kweli ana sifa na weledi unaotakiwa katika utumishi wa umma, lakini pia bila kujua kama kweli yuko kazini au hayuko kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba kwa sasa zoezi la jumla la uhakiki ni kama limeisha lakini uhakiki ni endelevu. Mkija mkisikia uhakiki mwingine unaendelea wala msishangae, tutaendelea kufanya hivyo na wala hatutafanya hivyo kwa kuwa tunaogopa mtu yoyote au kusikiliza maneno kwamba tunatishwa tusifanye uhakiki kwa kuwa Serikali hii itaonekana ni Serikali ya kufanya uhakiki kila kukicha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako ambao walitaka kufahamu uhakiki huu matokeo yake yamekuwaje. Nipende tu kusema kwamba kama mlivyofahamu, zaidi ya watumishi hewa 19,708 waliweza kubainika katika orodha yetu ya malipo ya mishahara na waliondolewa. Endapo tungewaacha hawa katika ajira ingeigharimu Serikali kila mwezi Shilingi bilioni 19.8, hivi ni fedha ndogo hizo? Si fedha ndogo hata kidogo! Ziko baadhi ya Wizara zingine ndiyo bajeti yake ya mwaka mzima huo. Kwa hiyo nipende tu kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge watuelewe, tunapofanya haya tunafanya kwa nia njema kuhakikisha kwamba hakuna mianya hata kidogo na kuhakikisha kwamba fedha za Serikali zinatumika kwa matumizi sahihi ili walipa kodi waweze kujionea manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hiyo tu, tumewaeleza hapa ajira mpya tutakazozitoa zaidi 52,000 katika mwaka ujao wa fedha. Tunapoendelea pia kutoa watumishi hawa hewa, pia inatengeneza fursa zingine kwa ajili ya watu wengine wahitimu ambao wako nje wanasubiri ajira. Hivi tusingewatoa hawa 19,000 si tungeendelea kuziba ajira? Tunaendelea kila mwezi kulipa zaidi ya bilioni 19.8. Kwa hiyo, nipende tu kuwahakikishia Wabunge pia hiyo ni fursa nyingine kwamba wahitimu wetu wataendelea pia kupata fursa hizo za ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu walitaka kufahamu pia kwamba mpaka sasa katika watumishi hawa hewa 19,700 waliondolewa, wale maafisa walioshiriki katika kuhakikisha kwamba watumishi hao hewa wamekuwepo wamechukuliwa hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba katika zoezi zima la kuondoa, tumehakikisha pia kwamba kwa yeyote aliyeshiriki na mpaka sasa tumeshawabaini zaidi wa watumishi 1,595 wa madaraka mbalimbali au ngazi mbalimbali ambao wamehusika katika uwepo wa watumishi hewa katika orodha ya malipo na mishahara na tayari tumeshawachukulia hatua mbalimbali. Wako ambao tayari wana kesi mahakamani, wengine wamechukua hatua nyingine za kisheria na wako ambao wamefukuzwa kazi, lakini zaidi ya yote, zaidi ya bilioni 9.3 zimesharejeshwa Hazina na tunaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kila fedha iliyochukuliwa basi fedha hiyo itarudi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine ya Walimu ambao walipandishwa vyeo na hii inaendana pia na watumishi wengine wa umma, lakini baadaye mshahara wao ukarudi kwenye mshahara wa zamani na watu walitaka kufahamu mishahara hiyo itarekebishwa lini na hiyo ni pamoja na watumishi wa umma waliopandishwa madaraja wakarekebishiwa mishahara yao kwa wakati ni nini kitafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema, kwanza kabisa wapo ambao walisema miaka mitatu mtu automatic ana sifa ya kupanda cheo. Nipende kutofautiana nao, mtumishi anapanda cheo kwa kuzingatia muundo wake wa maendeleo ya utumishi, mtumishi atapanda cheo kwa kuwa ameshatimiza sifa si chini ya miaka mitatu, siyo fixed kwamba ni lazima miaka mitatu unapanda.

Pili, ni lazima bajeti hiyo ya wewe kupandishwa cheo iwe imekasimiwa na mwajiri, lakini tatu uwe na utendaji uliotukuka katika kipindi chote hicho na uwe umejaziwa tathmini ya form ya OPRAS kwa zaidi ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba tutaendelea kufuatilia na kuhakikisha kwamba watumishi wanapanda kwa kuzingatia sifa na kwa kuzingatia utendaji uliotukuka. Kwa hiyo, kupanda cheo si automatic, tutaangalia vigezo hivyo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wako kweli ambao walipandishwa hadi kufikia mwezi Juni, 2016. Wako ambao walishapata mshahara uliorekebishwa mwezi mmoja, wako waliopata mishahara iliyorekebishwa miezi miwili, wakarudishwa katika mishahara ya zamani. Nipende tu kusema kwamba, Serikali ilifanya hili kwa nia njema na lengo lilikuwa ni kuwapa fursa Serikali kuweza kuupitia muundo wake upya ili pia kuhakikisha kwamba tunaondoa watumishi wale hewa, lakini pia kutoa nafasi ya kuendelea kuhakiki vyeti vya kidato cha nne, kidato cha sita na vya vyuo vya ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba, tayari zoezi hili limekamilika. Kwa upande wa uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne tunategemea mwezi huu litakamilika na matokeo yake naamini mmeshaanza kumsikia Mheshimiwa Rais na tusubiri baada ya hapo ni nini kitakachofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema, kwa wale waliopandishwa wote ndani ya mwaka huu wa fedha, wataweza kupandishwa na kurudi katika madaraja yao sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja kuhusiana na TASAF. Wako ambao, especially Kamati, ilisema kuwa kwamba kuna kasoro katika usimamizi, katika utambuzi na katika uandikishaji wa kaya za walengwa wetu wa mpango wa kunusuru kaya maskini. Pia wako Waheshimiwa Wabunge wengi kina Mheshimiwa Nditiye, Mheshimiwa Sikudhani, Mheshimiwa Ikupa na wengine wengi, walieleza hisia zao kwa namna ambavyo waliona zoezi hili kwa namna moja au nyingine utambuzi haukwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao walitoa maoni zaidi, katika suala zima la kuondoa kaya ambazo zilikuwa hazistahili na hasa walikuwa wanaamini kwamba wako wengine waliondolewa bado ni maskini, lakini mbaya zaidi wametakiwa warejeshe fedha. Nipende tu kusema kwamba, uhakiki huu ulifanyika kwa nia njema na tayari tumeshatoa miongozo katika halmashauri zote nchini pamoja na halmashauri zote za Zanzibar kusitisha kuwaondoa walengwa ambao ni kaya maskini, ambazo ziliingizwa katika mpango kwa kufuata taratibu zote ambazo zilitakiwa na tayari kaya hizo zimeshaanza kurejeshwa kwenye mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote, tatizo kubwa lililojitokeza unakuta wengine walikofanyiwa uhakiki walipoonekana hali zao zimeboreka wakaondolewa. Kwa hiyo, tumetoa maelekezo kwamba mtu ataingia kwenye graduation strategy baada ya kuwa tathmini imeshafanyika ili kuhakikisha kwamba kweli hali yake imeboreka na hataweza kurudi katika umaskini. Kwa hiyo, niwape tu comfort kwamba wameshaanza kurudishwa na hakuna atakayedaiwa fedha hizo kama kweli mtu huyo ni maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaotaka kuhangaika nao ni wale ambao waliingizwa kama ni kaya zisizo na sifa, ni wale ambao waliingizwa ni watumishi wa umma, ni wafanyabiashara na wenye kipato na wameingizwa na kuonesha kwamba hawana uwezo wakati uwezo huo wanao. Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba hili litafanyika vizuri na hakuna atakayeonewa lakini zaidi niwashukuru kwa namna ambavyo mmelisemea kwa hisia kubwa na kwa namna ambavyo mmekuwa mkilifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wabunge wengi pia wamekuwa wakilisemea hili, kuhusiana na asilimia 30 ya vijiji vya walengwa wa TASAF ambavyo bado havijafikiwa, sasa hivi tumefikia asilimia 70. Kamati ya Bunge imelieleza hili, Mheshimiwa Bobali amelieleza, vile vile Mheshimiwa Rhoda Kunchela naye pia ameweza kulisemea. Nipende tu kusema, mpaka sasa hatujafikia mitaa, vijiji na shehia 5,690.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu ilikuwa ni mwaka huu tufanye utambuzi pamoja na uandikishaji lakini bahati mbaya kutokana na ufinyu wa bajeti, zoezi hilo la utambuzi halikuweza kufanyika. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge, katika awamu hii ya kwanza itakapomalizika Serikali imetuhakikishia kwamba itatenga fedha kupitia mchango wake wa ndani ili kukamilisha zoezi la utambuzi pamoja na uandikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya hatua gani zimechukuliwa dhidi ya waliovuruga utaratibu na kuingiza walengwa wa TASAF ambao hawastahili. Mheshimiwa Lubeleje, Mheshimiwa Malembeka, Mheshimiwa Maige na wengi tu pamoja na kamati wamelieleza vizuri sana. Kwanza niwashukuru kwa namna ambavyo mmekuwa mkifuatilia, lakini niwaombe pia, kwa kuwa na ninyi ni Madiwani na tumewagawia orodha pia muweze kufuatilia katika orodha ya ruzuku iliyofika katika maeneo yenu, kujiridhisha kama kweli pia ruzuku hiyo katika mizunguko yote hiyo imefika au haijafika ili muweze kuwa pia jicho na sikio letu kwa niaba ya Serikali huko katika maeneo yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshachukua hatua, zaidi ya waratibu wa mpango 84 walioko katika halmashauri wameshachukuliwa hatua na wamesimamishwa na sasa hawawezi kushughulikia au kuratibu shughuli za TASAF. Vilevile Watendaji wa Vijiji pamoja na Kata na Mitaa 156 nchi nzima wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi lakini si hiyo tu hata TASAF kwenyewe Makao Makuu kwa sababu nako pia wamehusika katika usimamizi. Zaidi ya watumishi 106 walisimamishwa kazi na hatimaye wameweza kuchukuliwa hatua na wengine wamepewa onyo ili kuhakikisha kwamba upungufu kama huu hauwezi kujirudia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, watumishi saba waliokuwa makao makuu ambao mikataba yao imekwisha na walionekana pia utendaji wao ulikuwa haujaridhisha nao pia mikataba yao haijaweza kuhuishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya Mfuko wa Rais kujitegemea kuweza kuwezeshwa kifedha. Nipende tu kusema kwamba, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mama Kilango, Mheshimiwa Ritta Kabati na wengine wote ambao wameweza kuusemea Mfuko huu wa Rais wa Kujitegemea. Ni kweli ni Mfuko ambao ni wa muhimu sana, ni Mfuko ambao una historia ya muda mrefu, tangu hayati Sokoine mwaka 1984 ambaye alidiriki hata kuchangia sehemu ya mshahara wake, kuweza kuanzisha Mfuko huu. Niwashukuru sana lakini nipende tu kusema kwamba katika mwaka huu tumeutengea Shilingi milioni 500 na tunaamini itaweza kusaidia katika kutimiza malengo yake na Serikali itakuwa ikiongezea fedha kila mara itakapokuwa na uwezo ulioboreka katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Mama Kilango, kwamba ni lini Mfuko huu wa PTF utaanza kutoa huduma zake Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mama Kilango kwamba katika mwaka 2018/2019, PTF imejiwekea mipango ya kwenda Kilimanjaro pamoja na Tabora pamoja na mikoa mingine tutakuja kuitangaza huko baadaye. Kwa mwaka huu tutaenda Dodoma, Iringa pamoja na Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kulikuwa kuna hoja Mfuko huu unaonekana ni wa Muungano, kwa nini haufanyi shughuli zake Zanzibar? Ni hoja nzuri sana. Nipende tu kusema kwamba, Zanzibar upo Mfuko wa Rais wa Kujitegemea pia kupitia SMZ ambao unafanya kazi nzuri, ambacho tunakifanya sasa ni Mifuko hii miwili kuwa na ushirikiano na kuweza kufanya kazi pamoja lakini hoja hii tumeisikia tutaona ni namna gani pia inaweza ikafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Kishoa kwamba Serikali hii imekosa utawala bora, kiasi kwamba haipati mikopo, kiasi kwamba haipati misaada. Kwa kweli nipende tu kusema ni hoja ambayo kidogo imenishangaza na inasikitisha. Kwa takwimu zilizopo Waziri wetu wa Fedha amekuwa akifanya majadiliano mengi tu na amekuwa akisaini mikataba mingi tu na mikataba hii imekuwa ikiwa na mafanikio makubwa. Nitoe tu mfano, ukiangalia hadi sasa kupitia Kuwait Fund na Serikali wameingia mkataba na zaidi ya dola milioni 51 tayari kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahuwa umepitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa EU na Tanzania Rais amehakikishiwa fedha zitatoka; lakini nisiende mbali nikienda kwenye TASAF tu peke yake, DFID imetoa zaidi ya dola milioni 170, ndogo? Benki ya Dunia imetoa zaidi ya dola milioni 420, Irish Aid imeahidi kutoa zaidi ya dola milioni 11, USAID inatoa dola zaidi milioni 10 hapo sijaenda mbali kwenye Wizara zingine, niangalie tu zinazonihusu kwa harakaharaka. Sijaangalia TAKUKURU, sijaangalia Maadili na kwingineko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipende tu kusema kwa kweli, hebu tusiupotoshe umma kuonekana kwamba ni Serikali ambayo haina utawala bora. Utawala bora upo, fedha zimetoka, Abu Dhabi fund wametuahidi, barabara zinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huko Iramba kwa Mheshimiwa Kishoa naamini mafanikio yako mengi tu na wananchi wako wanakusikia unaposema uongo, watakapokuja kuona hizo fedha hazipo tutakuja na tutafanya ziara huko Iramba pia kuweza kusema kama ni uongo au ni kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kuhusiana na semina elekezi kwa viongozi walioteuliwa. Tumekuwa tukifanya hivyo, tukitoa mafunzo kwa kutambua umuhimu wa viongozi wenye uwezo wa kitaalam, lakini ambao wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utawala bora. Kila mara tulipoona inahitajika tumekuwa tukitoa semina hizo na mafunzo kuhakikisha kwamba wateule wetu na watumishi wetu wanapata mafunzo kuhusiana na namna Serikali inavyofanya kazi, wanapata mafunzo kuhusiana na namna Serikali ilivyo na utamaduni wake, kupata mafunzo ya namna ya kuwa mtumishi bora wa umma pamoja na wao kuelewa majukumu yao mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipende tu kuhakikisha kwamba, tutaendelea kufanya hivyo na hata katika mwaka huu wa fedha tunaoumaliza mpaka Juni zaidi ya viongozi 80 watapata mafunzo na mpaka ikifika Desemba viongozi wote watakuwa wamepatiwa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya madai ya malimbikizo na namshukuru kaka yangu Simbachawene ameeleza. Katika madai yasiyo ya mishahara, zaidi ya bilioni 33 zimeshalipwa na imekuwa ikifanya hivyo kila mara. Niwahakikishie tu watumishi wa umma, Serikali yenu inawajali, Serikali yenu inawathamini, tunatambua mchango wenu na kila mara tutaendelea kuangalia maslahi ya umma na kuyaboresha kwa kadri uwezo na bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tu katika haya madai mbalimbali, wako baadhi ya watumishi wamekuwa wakiwasilisha madai ambayo si sahihi na ndiyo maana tunasema uhakiki unachukua muda mrefu. Unachukua muda mefu kwa sababu huwezi ukalipa, hii ni fedha ya walipa kodi, ni lazima ujiridhishe kila hela unayoilipa ni hela ile ambayo kweli ndilo deni ambalo ni sahihi na ambalo limepitia katika michakato mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kulikuwa kuna hoja kwamba tuna Makatibu Tawala zaidi ya mmoja katika mkoa, tuna Wakurugenzi Watendaji zaidi ya mmoja...... hilo na tayari kila mmoja kwa nafasi yake ........na wale wengine wamepangiwa majukumu katika ofisi zao zinazowahusu.
(Hapa maneno mengine hayakusikika kutokana na hitilafu ya mtambo)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na niombe kwa wale ambao sijawataja waweze kuridhika na tutahakikisha kwamba majibu hayo mnayapata kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuhitimisha kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge mWendelee kuunga mkono hoja hii, ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora na taasisi zake kwa ufanisi katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nipende tu kusema kwamba naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja. Kipekee tu napenda kumpongeza sana yeye Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa Hotuba nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kama msimamizi wa Sekta ya Madini nipende tu kutoa shukrani sana kwa Serikali kupitia kwake Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kukubali kuweza kufuta tozo zilizokuwa zikitozwa katika chumvi, tozo takribani 10 kati ya 16 ambazo kimsingi zilikuwa zimesababisha sana gharama za uzalishaji wa chumvi kuwa kubwa na pia kumsababishia mchimbaji wetu mdogo wa chumvi kutokuweza kupata faida.

Mheshimiwa Spika, ilikuwa kwa takribani gunia la kilo 50 walikuwa wanapata faida ya Sh.150 tu ilikuwa ni faida ndogo. Pia walikuwa wanashindwa kushindana kisoko na matokeo yake ilikuwa chumvi ya kutoka nchi za jirani ilikuwa inaingia kwa wingi zaidi na hatimaye sisi ambao tuna chumvi nyingi humu kutoweza kufanya biashara au kuwa na ushindani. Kwa hiyo nipende tu kusema kwa niaba ya Sekta ya Madini na Wizara tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Musukuma kuhusiana na tozo au kiwango kikubwa cha kodi kinachotozwa katika madini ya dhahabu au kwa wachimbaji wetu wadogo wa dhahabu na alikuwa ameeleza kwamba kuna tozo ya asilimia takribani kumi na nne (14%).

Mheshimiwa Spika, nipende tu kumweleza Mheshimiwa Musukuma kwamba kwa mujibu wa Sheria yetu ya Madini Sura namba 123, wachimbaji wadogo wanatozwa takribani asilimia 12.3 ya kodi ambayo inajumuisha mrabaha wa asilimia sita, inajumuisha kodi ya zuio ya asilimia tano, ada ya ukaguzi wa uzalishaji wa madini asilimia moja, pamoja na ushuru wa huduma au service levy kwa halmashauri kwa asilimia 0.3 ambayo jumla yake ni asilimia 12.3 na kwa upande wa wachimbaji wakubwa na wa kati wao wanatozwa mkokotoo wa asilimia 37.3.

Mheshimiwa Spika, alipendekeza kodi kwa wachimbaji wadogo ziondolewe; nipende tu kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekuwa tukiliona na kwa kuwa Serikali yetu ni sikivu kama ambavyo tumefanya katika chumvi. Niendelee tu kuwaomba shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo (FEMATA) tukae, tuweze kulizungumza suala hili na kuliona ni kodi zipi au ni tozo zipi ambazo zinaweza zikafikiriwa kuzingatiwa katika punguzo hilo au kuweza kuondolewa.

Mheshimiwa Spika, lengo letu kubwa kama Serikali nikuhakikisha kwamba tunakuwa na uchimbaji mdogo, uchimbaji mdogo ambao utakuwa na faida kwa wachimbaji wetu. Lakini pia sisi kama Serikali bado tunaendelea kuona ni namna gani tunawasaidia kwa upande wa teknolojia,
masuala mazima ya mtaji, mafunzo, kupata masoko lakini zaidi kuwapa teknolojia mpya na waweze pia kujifunza teknolojia ya kisasa katika uchimbaji.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia kupitia Serikali kupitia bajeti yetu ya Wizara ya Madini katika mwaka ujao wa fedha tutajenga vituo vya mifano vitano katika maeneo ya Chunya, Bukombe, Rwamgasa, Tanga pamoja na Kilwa. Pia tutajenga vituo saba vya umahiri Mpanda, Handeni, Musoma, Songea, Bariadi, Bukoba na kwingineko.

Mheshimiwa Spika, lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunawafundisha kwa mfano ili waweze kuchimba kwa teknolojia ya kisasa kupitia vituo hivyo ambavyo tumeviweka kwa gharama nafuu sana, lakini hatimaye lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawarasimisha ili waweze kuingia katika mfumo rasmi wa kibiashara pamoja na kikodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho nipende tu kuoa rai kwa Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, kuhakikisha kwamba wanazingatia viwango vya tozo za kodi vilivyoanishwa katika Sheria. Wako wengine unakuta wameenda katika maduara ya uchimbaji wa Madini, unakuta wanaambiwa wakivuna mifuko 10, mifuko labda mitano inaenda kwenye Halmashauri. Niombe sana tuzingatie viwango ambavyo vimeainishwa kisheria ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wetu hawa wadogo hatimaye wanaweza kukua.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Sera yetu ya Wizara ya Madini na Serikali kwa ujumla wachimbaji hawa hadhi yao hii si ya kudumu wanatakiwa tu watumie hadhi ya uchimbaji mdogo kama daraja hatimaye waweze kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye pia kuwa wachimbaji wakubwa kama ambavyo wengine kama wakina Busolwa Mining pamoja na akina Mzee wangu Marwa wameweza kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja pia ya zuio la usafirishaji wa carbon, hoja hii nadhani leo nitakuwa nasimama kwa mara ya tatu kuweza kuielezea. Kaka yangu Mheshimiwa Musukuma ameweza kuieleza lakini nipende tu kurudia maelezo ya Serikali kwamba zuio letu la usafirishaji wa carbon liko palepale kama nilivyotoa maelezo yangu tarehe Mosi Juni, kama nilivyotoa maelezo yangu pia tarehe 14 Juni.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kwa kweli kuwapongeza sana wamiliki wa Illusion Plants takribani watano kwa Kahama tayari wameshaanza kujenga Illusion Plants hizo. Nipende pia kuwapongeza wawekezaji takribani watatu ambao wameshaanza kuonesha nia ya kuwekeza Shinyanga, vile vile pia niwapongeze sana wawekezaji wengine watatu ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo ya Tabora.

Mheshimiwa Spika, zaidi niwapongeze sana Kampuni ya GEMAAfrica ambao tayari wameshakamilisha kujenga mtambo wa Illusion Plants Wilaya ya Geita. Nipende kuwapongeza Kampuni ya Transco Gold pamoja na Nyamigogo, Nang’ana Group pamoja na Busamu Company ambao nao wameshakamilisha ujenzi wa Illusion Plants katika Wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Spika, kipekee pia niwapongeze Framal Investment ambao tayari nao wameshakamilisha ujenzi wa mitambo yao katika Wilaya ya Musoma pamoja na Deep Mine Service ambayo kwa sasa na wenyewe wanatafuta eneo la kujenga mitambo husika ya Illusion Plants katika Wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Geita na Tarime bado watu wengi wamekuwa wakionesha nia. Nipende tu kuwakaribisha sana wawekezaji na Watanzania wengine kuona ni namna gani wanatumia fursa hii kuwekeza katika ujenzi wa Illusion Plants katika sehemu ambazo bado wawekezaji hawajenda lakini pia huduma zao zinahitajika. Hata hivyo, nipende kusema kwamba agizo la Serikali bado linasimama palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kuhusiana na Mheshimiwa Ole Millya alieleza kwa kina sana kwamba mapendekezo ya Kamati Maalum ya Mheshimiwa Spika iliyochunguza mnyororo mzima wa biashara ya uchimbaji wa Tanzanite kwamba hayajatekelezwa. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu hata siku moja hatuwezi kudharau mapendekezo au maazimio ya Kamati Maalum ya Spika ambayo tunaamini ni mapendekezo ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, vilevile nipende tu kueleza tu kwamba kama ambavyo tulieleza tarehe Mosi, Juni, 2018 katika hotuba yangu ukurasa wa 46, tulieleza namna kabisa masuala mazima ya majadiliano kupitia ubia wa Kampuni ya Tanzanite One pamoja na STAMICO yanavyoendelea na tulieleza katika hotuba yangu ukurasa wa 46 kwa wale ambao watakuwa nayo wanaweza kufuatilia.

Mheshimiwa Spika, tumeotoa maelekezo kwa Kampuni ya Tanzanite One pamoja na STAMICO kurudisha leseni ya uchimbaji ili iweze kuandaliwa utaratibu mpya ambao utaiwezesha Serikali na Taifa kwa ujumla kuweza kunufaika zaidi katika uchimbaji na biashara nzima ya Tanzanite kwa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura namba 123.

Mheshimiwa Spika, hayo mengine ya kusema yamegawia, sijui imekuwaje mara imehuishwa, nipende tu kusema kwamba niwaombe Waheshimiwa Wabunge wajikite zaidi katika maelezo ya Mheshimiwa Kabudi aliyoyatoa tarehe Mosi, Juni lakini pia wajikite katika kufanya reference katika hotuba yangu niliyoitoa ya bajeti katika ukurasa ule wa 46. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nipende tu kusema kwamba katika makubaliano yale ambayo Kamati ya Majadiliano ya Taifa kupitia kwa Kiongozi Mheshimiwa Kabudi, makubaliano yaliyoingiwa tarehe 15 Aprili na Kampuni ya Tanzanite One tayari wameshaanza kulipa mkupuo wa kwanza wa fidia ambayo walikuwa wameelekezwa na obviously fidia hii inaingia kwa Taifa na kuna taratibu zake kwa mujibu wa Wizara ya Fedha kwa malipo kama hayo yanalipwa kwa taratibu gani.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru na napenda kusema tu kwamba, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii kipekee kabisa kukushukuru kwa kunipa fursa hii kuweza kuhitimisha hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote takribani 65 ambao waliweza kuchangia, kwa kuongea walikuwa 26 na kati yao 39 waliweza kuchangia kwa maandishi. Kwa hakika kwa niaba ya Wizara ya Madini tunawashukuru sana kwa michango hiyo mizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kipekee kuchukua nafasi hii kumshukuru kwa mara nyingine tena Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuendelea kuniamini na kwa kunipa nafasi hii ambayo kwa hakika ni heshima kwetu. Niendelee tu kumhakikishia mimi pamoja na Naibu Waziri wangu; Mheshimiwa Nyongo pamoja na Mheshimiwa Biteko kwamba hatutamwangusha na tutahakikisha kwamba tunatekeleza majukumu yetu kwa weledi na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Biteko. Kwa hakika kama nilivyosema wakati nawasilisha hoja hii wamekuwa ni watu wa msaada sana kwangu. Nilieleza kwa takribani miezi mitatu sikuwepo, wamefanya kazi kubwa lakini pia wanaendelea kufanya kazi kubwa, kwa kweli ninajivunia kuwa nao kama Naibu Mawaziri wangu. Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki na niwahakikishie kwamba nitakuwa wazi kwao, tutaendelea kushirikiana wakati wowote watakapohitaji mwongozo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Prof. Kabudi, tumekuwa tukishirikiana sana katika suala hili la usimamizi wa sekta hii ya madini hususani katika suala zima la majadiliano ya mikataba. Napenda kumshukuru pia Mheshimiwa Dkt. Kilangi kwa namna ambavyo anaendelea kutushauri kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kutupatia Miongozo mbalimbali na tafsiri na fafanuzi katika masuala ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wahenga walisema tunahitaji mikono, jicho na mdomo wa kila mwanakijiji kuweza kumlea mtoto mmoja kwa mafanikio. Kwa hakika hivi ndivyo ilivyo kwa Wizara hii mpya ya Madini. Katika upya wetu tunahitaji sana mchango wa maoni, mapendekezo, ushauri wenu kukosolewa na kila Mheshimiwa Mbunge pale ambapo mtakapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Sisi tunaamini kwa kufanya hivyo, hiyo hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kuimarisha Wizara yetu hii mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mwaka jana upande wa sekta ya madini wachangiaji hawakuwa wengi sana lakini nilikuwa nafurahi sana kila ambavyo nilikuwa naona Mbunge anasema mpaka tumefikisha Waheshimiwa 65 kwa maandishi na mdomo, tunawashukuru sana sana. Napenda kipekee kuwashukuru wote walioweza kuchangia hoja hizi, mmetuimarisha sana na napenda kutoa shukrani za dhati kwa michango mizuri ambayo mmetupatia. Niwahakikishie kwamba tumeipokea, tumefaidika sana na niwaahidi tu kwamba tutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajibu hoja chache lakini kwa zile ambazo nitaweza kuzijibu niwahakikishie kabla ya Bunge letu hili halijaweza kuhitimishwa tarehe 30 Juni tutaweza kuwasilisha majibu yote kwa maandishi kwa kila Mheshimiwa Mbunge kwa namna alivyochangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ambacho kinanipa faraja mimi na wenzangu ni kwamba sisi na Waheshimiwa Wabunge wote tunazungumza lugha moja na sote tunavuta katika upande mmoja wa kutetea maslahi ya Watanzania wenzetu. Sote tunaamini kwamba sekta ya madini itakaposimamiwa vizuri, tutaweza kuvuna zaidi ya kiasi cha madini tunachokivuna hivisasa. Zaidi kwa ujumla wetu tunao, muafaka sote kwamba wananchi wetu ndiyo wenye kustahili kufaidika zaidi na rasilimali ya madini waliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Pia tunakubaliana kimsingi kwamba wakati ndioyo sasa na sisi ndiyo wale historia imetukabidhi jukumu na wajibu wa kuliwezesha hili. Naamini, madamu tunakubaliana katika haya ya msingi basi hakuna kwa hakika litakaloharibika. Kwa lugha ya leo tunaweza kusema yajayo yanafurahisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano iko bega kwa bega na Bunge lako Tukufu katika kusimamia rasilimali ya madini ya nchi yetu. Ni kwa msingi huo Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini ambayo Waheshimiwa Wabunge mliweza kuipitisha pamoja na Kanuni mpya nilizozitunga mwaka huu wa 2018. Niwahakikishie tena Waheshimiwa Wabunge tangu mabadiliko ya Sheria yalipofanyika, kampuni mbalimbali za madini za ndani na nje ya nchi zimeonyesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kufuatia kuundwa kwa Tume mpya ya Madini tunatarajia kwamba maombi ya leseni kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya madini yatashughulikiwa mapema ipasavyo. Vilevile kama Serikali tumeanza kutekeleza mpango wa kujenga uwezo wetu wa kuhakiki mitaji inayowekezwa na shughuli zinazofanywa na kampuni za madini. Nia yetu kubwa ni kuwa na uwezo wa kuhakiki taarifa za kampuni kuhusu uwekezaji wao na shughuli zao. Napenda kuwahakikishia kwamba sisi kwa upande wetu kama Wizara hatutalala, tutakuwa macho na tutaendelea kuchukua hatua kila mara itakapobidi. Nachoomba Waheshimiwa Wabunge kutoka kwenu ni mambo mawili. La kwanza, ni imani na ushirikiao wenu katika kutekeleza wajibu wetu huu mkubwa. Pili, niendelee kuwaomba kwa heshima na unyenyekevu mkubwa mtupitishie bajeti hii ambayo kwa hakika ndiyo itakayokuwa nyenzo muhimu kwetu ya kutuwezesha kutekeleza azma yetu hii. Haya yote mawili kwa hakika yamo ndani ya uwezo wenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi, niruhusuni sasa nianze kujibu baadhi ya hoja kama zilivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwepo hoja ya Mheshimiwa Kanyasu kuhusiana na Mzee wangu Felix Ngowi na wenzake ambao wana mgogoro na mgodi wa GGM. Kwa kweli ameeleza kwa hisia kubwa na mimi nimesikitika. Hukumu takribani sita zimeweza kutolewa kuhusiana na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Kanyasu pamoja na Mheshimiwa Musukuma na Wabunge wote wa Geita na wengine wote wenye mapenzi na wanyonge wetu katika Taifa hili kwamba suala hili nitalichukua kwa uzito wa pekee. Kwa kuwa na mimi mwenyewe ni mwanasheria, nitakaa na Mheshimiwa Jaji Mkuu kuweza kuliangalia suala hili limekaaje ili kuweza kulipatia ufumbuzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia kuhusiana na GGM, wanapokuwa wanatoa mipango mbalimbali ya uwajibikaji katika jamii au CSR kwamba bei kubwa za vifaa zinakuwa inflated. Tulielezwa hapa, lori moja la mchanga mpaka takribani Sh.350,000. Napenda kusema tu kwamba hili halikubaliki, niendelee tu kuwaomba Waheshimiwa Madiwani wetu, kupitia kifungu cha 105(1)(2) na (4) cha Sheria yetu ya Madini ya 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017, kabla hawajaridhia mpango wa mwaka wa uwajibikaji kwa jamii wahakikishe kwamba wamejiridhisha kile kinachoahidiwa katika mpango huo wa mwaka basi kweli kinaendana na thamani halisi ya fedha. Napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, tutafanya ukaguzi maalum kupitia Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuiangalia migodi yote mikubwa katika CSR zao ambazo wamekuwa wakizitoa katika jamii zao na kuona kwamba kweli zinaendana na kiasi halisi cha fedha inayoelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kuhusiana na ruzuku, wapo wachimbaji wadogo ambao waliweza kunufaika lakini kwa bahati mbaya wapo takribani wanufaika tisa ambao hawakuweza kuwa waaminifu na walizitumia fedha zile vibaya kwa kukiuka mkataba. Napenda tu kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge suala hili tumelipaleka TAKUKURU na tayari uchunguzi wake umefanyika na tunaamini wataweza kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine kuhusiana na suala zima la madini ya bati kwa upande wa Kyerwa. Wote tunafahamu tunao Mkataba wa ICGLR ambapo kupitia mkataba huo, hatuwezi kuuza madini yetu nje ya mipaka yetu bila kusaini Itifaki ile ya Illegal Exploitation pamoja na mkataba ule wa ICGLR kuhusuiana na usalama na ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Bilakwate ameeleza suala hili kwa uchungu mkubwa, tunaona hoja hii kwa msingi wake. Kama Serikali tumeshaanza kulifanyiakazi na tuko katika hatua ya mwisho ili kuhakikisha kwamba tunaleta mkataba huu Bungeni ili uweze kuridhiwa na kuruhusu biashara ya bati kuuzwa katika soko la kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kuhusiana na mgodi wetu wa Buckreef, kwa muda mrefu wabia wetu au wabia wenza wa STAMICO wamekuwa wakishikilia mgodi ule lakini wamekuwa hawatimizi kama ambavyo mikataba imewataka. Napenda kuwahakikishia tayari tumeshafikisha suala hili katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tunaamini tutaweza kupata tafsiri na miongozo ya namna gani ya kuweza kuachana na mikataba huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine kuhusiana na kukamilisha ujenzi wa smelter; Mheshimiwa Mama Nagu, Mheshimiwa mama Mbene, Mheshimiwa Kapufi na wengine wengi wameweza kulizungumzia hili kwa uzito mkubwa. Kama nilivyowaeleza awali, niwahakikishie kwamba tayari tumeshapata waombaji takribani 27 na tunachokifanya hivi sasa ni kuhakikisha kwamba tunayachambua na kuweza kufanya uchunguzi au due dilligence ili kuhakikisha kwamba tunampata mwekezaji ambaye kweli anavyo vigezo na ni mahiri katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja za Mheshimiwa Catherine Magige kuhusiana na utoroshwaji wa madini ya tanzanite lakini zaidi alitupa ushauri tuweze kuimarisha mipaka yetu ya Namanga, Horohoro pamoja na mipaka mingine. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufuatilia mnyororo mzima wa uchimbaji, uendeshaji wa biashara hii ya tanzanite pamoja na mauzo nje ili kudhibiti utoroshaji. Pia napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kama Wizara hivi sasa tunaandaa utaratibu imara wa kuweza kuwapatia motisha wananchi watakaoweza kutoa taarifa au whistleblowers juu ya watoroshaji wa madini ya tanzanite pamoja na madini mengine. Pia tunaandaa simu maalum au hotline maalum ambayo tutaitumia katika kupokelea taarifa kuhusiana na masuala ya utoroshaji na biashara nzima hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja za Mheshimiwa Ndassa ambaye kimsingi aliweza kutushauri tuweze kuonyesha ni namna gani tunaweza kuwasomesha wathamini wetu wa madini ambao hivi sasa tunao wathamini wachache. Napenda kumshukuru kaka yangu Mheshimiwa Ndassa na nimhakikishie tu kwamba tunalipa suala hili la uthamini wa madini uzito wa kipekee. Tayari tumeshaainisha au tumeshawatambua watumishi 10 ambao tutawapeleka kwenye mafunzo katika nchi ya Thailand pamoja na India ili waweze kupata mafunzo maalum ya gemology kwa ajili ya kuweza kutambua madini ili waweze kutambua na kufanya uthamini ili tusiweze kuibiwa na kuweza kupata fedha stahiki au mirabaha stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kuhusiana na kufunga security system katika ukuta wetu wa Mererani. Nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Bulembo kwa kuweza kuona umuhimu wa suala hili. Nimhakikishie kwamba ni suala ambalo kwa kweli tunalipa upekee mzito. Ameeleza hapa masuala ya mitobozano na masuala mengine. Nisingependa kueleza masuala mengi ya kiusalama lakini nimhakikishie kwamba hoja na ushauri wake utazingatiwa na tutahakikisha kwamba tutakuwa na mfumo wa ulinzi ambao kwa kweli hapatakuwa na utoroshaji hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Bobali kuhusiana na tozo nyingi katika chumvi pamoja na masuala mengine lakini pia Mheshimiwa Hamida, Mheshimiwa Ngombale na Waheshimiwa wengine, niwashukuru kwa hoja hii. Kipekee kabisa napenda kuwaeleza kwamba nilipata hoja hii kutoka kwa Taasisi yetu ya TASPA ya wazalishaji wa chumvi. Nasi kama Wizara kwa kweli tuliliona kwa uzito mkubwa. Ukiangalia gharama inayotumika katika uzalishaji wa chumvi wanapata faida kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni takribani Sh.150 peke yake katika kilo 50, Sh.3 kwa kila kilo ni fedha ndogo sana. Hii inatokana na tozo zilizopo katika biashara nzima, wana tozo zaidi ya 16. Tayari kama Serikali, tumeanza mashauriano, tumewasilisha Wizara ya Fedha, kwa upande wetu kama Wizara ya Madini na Wizara ya Viwanda kuona ni namna gani suala hili linaweza likaangaliwa kwa mapana yake ili kuweza kuhamasisha uzalishaji wa chumvi ya Tanzania. Maana yake hivi sasa Tanzania tunayo chumvi nyingi na ukiangalia sekta hii ya chumvi imekuwa ikiajiri akina mama wengi sana lakini tumegeuzwa kuwa soko la nchi nyingine, tunanunua chumvi ya nchi zingine kwa sababu tu gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa. Napenda tu kusema kwamba tunaomba muweze kutuvumilia katika suala hili, Serikali yetu sikivu, tunaamini suala hili litaweza kupatiwa ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na pendekezo la Mheshimiwa Bilakwate kuhusiana na suala zima la uongozi wa STAMICO. Napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tumeanza kufanya mageuzi kwa ajili ya uongozi wa Shirika hili la STAMICO. Tayari tumeshambadilisha Mkurugenzi Mtendaji, tumeshaanza kubadilisha baadhi ya Wakurugenzi na tutafanya hivyo kila mara itakapoonekana inahitajika. Hoja hiyo pia ilielezwa na kaka yangu Mheshimiwa Bobali pamoja na Waheshimiwa wa Bunge wengine. (Makofi)

Mheshimiwa n aibu Spika, ilijitokeza pia hoja ya Mheshimiwa Rashid Shangazi kuhusiana na madini ya bauxite kule Lushoto lakini pia alinialika niweze kutembelea eneo hilo. Nimueleze kwamba mimi natoka Same na anajua Same ni jirani na Lushoto, kwa hiyo, kwa hakika kila nikitembelea Same nitahakikisha pia nakwenda Lushoto ili kuweza kujionea maeneo yale ya Makanya, Magamba, Soni pamoja na Malindi lakini zaidi kuwaunganisha wananchi wa Lushoto wale ambao wanayo reserve ya bauxite na wawekezaji ambao watakuwa tayari kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ya Ndugu yangu Mheshimiwa Issaay ambaye naye aliweza kutualika. Pia alitoa ushauri wa kuendelea kutoa ruzuku kwa wachimbaji wetu wadogo. Nimhakikishie tu kwamba suala hili tunaliangalia ili kuweza kupata utaratibu mzuri ambao utaweza kuwanufaisha wachimbaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine ambapo Waheshimiwa Wabunge walishauri STAMICO iachie maeneo ambayo haiendelezi. Napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, tayari kwa upande ule wa mgodi wa Buckreef tumeshaainisha mgodi ule au eneo la Lwamgasa South II pamoja na Nyamalimbe II na Lwamgasa West na hayo tutaendelea kuyatambua na kuweza kuwatengea wachimbaji wetu wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia ya Mheshimiwa Ngalawa ambaye alipendekeza GST wajengewe uwezo iliwaweze kufanya utafiti zaidi katika suala hili la uchimbaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia kuna hoja ya Mheshimiwa Mussa Mbarouk kuhusiana na Chuo cha Madini kuongeza idadi ya wanafunzi ili kuweza kupata wataalam zaidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mussa Mbarouk kwa mwaka huu wa fedha tumepata wanafunzi 542 lakini kuanzia Julai tutakuwa na wanafunzi 850 na lengo letu ni kuhakikisha kwamba ifikapo 2019/2020 tunakuwa na wanafunzi 1,350.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi tumeanza mashauriano na Bodi yetu ya Mikopo ili kuona ni namna gani sasa wanafunzi wale wanaosomea cheti na diploma katika sekta ya madini katika Chuo chetu cha Madini na wenyewe waweze kunufaika na mkopo huu wa elimu hiyo. Naenda kuwaalika Waheshimiwa Wabunge, ndugu zenu lakini zaidi wapiga kura wenu waweze kukaribia katika Chuo chetu cha Madini ili kuweza kujifunza katika sekta hii ya madini ikiwemo jiolojia na masuala mengine ya uhandisi na uchenjuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kuhusiana na usimamizi wa ufuatiliaji wa walipa kodi katika sekta ya madini. Napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tutafanya hivyo na tutashirikiana na taasisi zingine ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata kodi zake stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Alhaj Bulembo pia aliweza kutupa ushauri kwa Tume yetu mpya ya Madini ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu na zaidi itahitaji ushirikiano mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Seif Gulamali kuhusiana na usafirishaji wa carbon kutoka Geita ambapo yeye alitolea mfano carbon ambayo ilikuwa ikienda Mwanza. Nitaomba Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo hili mnisikilize kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya uchenjuaji katika miaka ya 2000, wachimbaji na wachenjuaji wadogo wengi nchini wamekuwa wakitumia kemikali ya cyanate kwa ajili ya kuchenjua madini ya dhahabu. Ni kwa kutumia teknolojia hii ya kemikali hii ya cyanate waliweza kuchenjua madini ya dhahabu ambayo imekuwa ikihusisha utumiaji wa vat leaching pamoja na activated carbon.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi nisingependa kwenda kwenye utaratibu mzima wa namna ambavyo vat leaching hii na carbon inafyonza dhahabu lakini napenda tu kusema kwamba, katika suala zima la usafirishaji wa carbon kutoka katika maeneo mbalimbali hususani Geita, Singida pamoja na maeneo mengine wamekuwa wakienda katika mkoa jirani au katika mkoa mwingine wa pili kwa ajili ya kufanya uchenjuaji. Napenda tu kusema, kuanzia leo tarehe 1 Juni, 2018 itakuwa ni kosa kwa mtu yeyote kusafirisha carbon kutoka katika mkoa ambapo mchanga au carbon inazalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona katika televisheni wale wenye viwanda vya uchenjuaji Mwanza na sehemu zingine wakieleza na mpaka humu ndani wameandika barua yao kwamba suala hili litawakosesha ajira. Kama Serikali napenda kusema kwamba Sheria ya Madini iko wazi na kuanzia leo niombe vyombo vya ulinzi na usalama yeyote atakayekutwa anasafirisha carbon kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine achukuliwe hatua kazi za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa suala la ajira, nitolee mfano wa eneo la Geita, miundombinu ipo, barabara zipo, umeme upo na kila kitu kipo, haingii akilini nini kishindikane wachenjuaji wale wenye viwanda vya uchenjuaji kuweka viwanda vyao vya uchenjuaji Geita, Singida, Tanga na maeneo mengine? Ni marufuku kuanzia leo tarehe 1 Juni, 2018, yeyote atakayekamatwa anasafirisha carbon hiyo kutoka katika eneo moja kwenda lingine hasa mkoa mmoja kwenda mwingine itakuwa ni kosa la jinai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nisisitize hili, lengo hapa ni kuhakikisha tunalinda ajira katika mkoa husika unaozalisha carbon ile pamoja na mchanga ule wa madini hususani madini ya dhahabu na mengineyo. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza mzunguko wa fedha na tunadhibiti utoroshwaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wamekuwa wakitoa dhahabu Geita, Singida kwenda Mwanza na maeneo mengine lakini unashangaa katika record zetu Wizara ya Madini huoni record za mauzo yale ya madini, huoni record za vibali tunavyovitoa vya mauzo ya madini yale nje, huoni record ya malipo ya mirabaha na kwa kweli tumekuwa tukipoteza fedha nyingi katika eneo hili. Niombe sana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vihakikishe vinalisimamia suala hili ili kupiga marufuku na kuhakikisha suala hili linafika mwisho na ni imani yangu tutapeana ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi niwaombe TRA pamoja na Ofisi zetu za Madini kufanya ukaguzi wa kina na forensic audit kwa wote ambao walikuwa wakifanya uchenjuaji au walikuwa wana viwanda hivyo vya uchenjuaji na kufuatilia minyororo mizima ya biashara yao hiyo katika viwanda vya uchenjuaji ili kuhakikisha kwamba Serikali inapata fedha na malipo yake stahiki. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunachochea ukuaji wa uchumi katika maeneo husika ambako michanga hiyo na carbon zinazalishwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tuone mabenki katika maeneo hayo, huduma zingine zipo, malazi yapo, bidhaa zipo sasa unajiuliza, iweje mtu atoe carbon Geita aipeleke Mwanza, iweje mtu atoe carbon Tanga aipeleke Mwanza? Kwa nini asiichenjue pale au kwa nini asiwezekeze pale? Endapo atashindwa kuwekeza wako wengine ambao wako tayari kuwekeza na wameonyesha nia hiyo. Kwa hiyo, napenda sana kusisitiza eneo hili na ni imani yangu Ofisi zetu za Madini pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vitalisimamia agizo hili kikamilifu ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuona tija na ufanisi katika susla zima la uchenjuaji na sekta hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwahamasisha wachimbaji wote na wawekezaji watakaoguswa na agizo hili, waweze kujenga mitambo na miundombinu ya uchenjuaji katika mikoa ambayo wanazalisha hiyo carbon pamoja na michanga ili kuweza kutekeleza agizo hili ipasavyo. Pia nizitake Ofisi za Madini zishirikishe kikamilifu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili kuweza kusimamia shughuli za uzalishaji wa madini kwenye maeneo husika. Nipige marufuku kuanzia leo kwa Ofisi zetu za Madini kutoa kibali cha usafirishaji wa carbon pamoja na michanga hiyo kutoka katika mkoa mmoja kwenda katika mkoa mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja hapa kuhusiana na ruzuku katika awamu yetu ya I na ya II ya SMMRP. Wapo ambao walitaka kujua ni Mikoa mingapi imeweza kunufaika na mikopo hiyo. Napenda tu kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge, ni mikoa takribani 24 yenye wanufaika takribani 115 ndiyo walioweza kunufaika na mkopo wetu wa SMMRP.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mwambalaswa kwa ushauri wake mzuri ambao ameendelea kutupatia kuhusiana na namna ya kusimamia sekta yetu ya madini katika Wilaya yake ya Chunya na katika eneo lake la Itumbi. Kipekee tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa mapendekezo yao mazuri pamoja na ushauri. Niwahakikishie mimi pamoja na wenzangu tutayafanyia kazi na wakati wote tutaweza kutii maelekezo yenu na ushauri na tutakapoona tuna changamoto tutaweza kurudi kwenu na tutaomba basi muweze kutuwezesha ili kufanikisha yale tunayoyahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona kwa leo nieweze kuyasema hayo. Kwa wale ambao tutakuwa hatujaweza kuwajibu vizuri, tutaomba tuweze kuwajibu kwa maandishi kwa siku za usoni. Kwa kipekee kabisa tuwaombe waweze kutupitishia bajeti yetu hii ili tuweze kuwa na nguvu kuweza kutekeleza na kusimamia sekta hii nzito ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kipekee kabisa, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nipende tu kusema kwamba naunga mkono hoja hii ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na nipende kipekee kuwapongeza sana Kamati yetu hii ya Bunge kwa ripoti hii nzuri na niwahakikishie tu kwamba nitafanya nao kazi kwa karibu. Niwashukuru kwa mchango wao na ushauri mzuri walioutoa na yote walioyatoa tutayazingatia. Zaidi pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameweza kuchangia hoja hii hususan katika masuala yanayohusu sekta ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipende tu kuanza kwa kuwapa comfort Waheshimiwa Wabunge, kwamba katika sekta ya uwekezaji Tanzania tumekuwa tukiendelea kufanya vizuri, hususan katika suala zima la kuvutia wawekezaji. Hata ukiangalia katika ripoti ya World Investment Report ya mwaka 2018 ambayo ilitolewa na UNCTAD imeonesha pia kwamba Tanzania katika nchi za Afrika Mashariki tumeongeza katika kuvutia uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka jana tu peke yake takribani dollar za Kimarekani bilioni 1.18 zimetufanya tumekuwa wa kwanza tukifuatiwa na Uganda na Kenya imekuwa ni nchi ya tatu. Kwa hiyo nipende tu kusema kwamba ni vyema tusibeze jitihada mbalimbali zinazofanyika, muhimu tu kwamba tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba tunaimarisha uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende sasa kipekee kujibu hoja mbalimbali ambazo zimetolewa na Kamati lakini pia na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ilikuwa ni kuhusiana na changamoto mbalimbali katika mazingira ya ufanyaji wa biashara. Ukiangalia kwa kiasi kikubwa katika ripoti ya Kamati yetu ya Bunge, lakini pia Waheshimwa Wabunge wengi wamejikita sana katika masuala mazima ya changamoto zinazojitokeza, utitiri wa kodi, mifumo ya udhibiti, kuwa na regulatory authorities nyingi ambapo nyingine unakuta zimekuwa zikikwamisha jitihada mbalimbali. Nipende tu kusema kwamba tayari kupitia Serikali mwaka 2016, ilifanya utafiti na ikafanya uchambuzi wa kuangalia changamoto mbalimbali na kero ambazo zinajitokeza katika mazingira ya kufanya biashara nchini, lakini pia katika masuala mazima ya uwekezaji. Ndiyo maana ukiangalia mwaka 2018, mwezi Mei Baraza letu la Mawaziri kupitia Serikali liliweza kupitisha Blue Print (Mpango) wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara. Vile vile tunayo Programme ya Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji na tayari tumeshaanza kuandaa road map pamoja na Mpango Kazi Jumuishi (Comprehensive Action Plan) ya miaka mitatu ambayo tayari tunashirikiana na ESRF katika kuhakikisha kwamba hili linaenda kutekelezwa. Tunaamini wiki ijayo tutaweza kukaa na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mpango kazi huu jumuishi unafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuwatoa hofu tena Kamati kama ambavyo wamekuwa wakitushauri, lakini pia katika maelekezo yao ambayo wametoa katika taarifa hii, kwamba ni vyema sasa wapate taarifa ya utekelezaji, lakini pia waweze kupata namna ambavyo changamoto hizi zimeweza kutatuliwa. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati yetu kwamba suala hili litakapoendelea kufanyiwa kazi tutawaletea taarifa ya utekelezaji ya mpango wetu huu jumuishi wa kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja nyingine ya sheria za kodi. Kimsingi Kamati imekuwa ikifanya ulinganisho na kodi mbalimbali zinazotozwa hususan katika kodi za forodha katika nchi zingine za Afrika Mashariki na nyinginezo na kwamba vyema sasa katika utozaji wa kodi tukaangalia mazingira yetu tuliyonayo, lakini pia kuangalia wakati tulionao kwa sasa. Nipende tu kusema kwamba Serikali imekuwa sikivu na ndiyo maana kupitia Wizara ya Fedha tumemsikia Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameunda Kamati ya Mapitio ya Kodi au task force kwenye reforms za kodi lakini pia ametoa mpaka tarehe 10 Februari, yeyote ambaye ana mapendekezo kuhusiana na mapitio ya kodi na maboresho basi wanaweza kuwasilisha huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya tatu ilikuwa ni kuboresha au kufanya mapitio ya Sera yetu ya Uwekezaji, pamoja na Sheria ya Uwekezaji. Nipende tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hili ni eneo ambalo nitahakikisha katika mwaka huu ujao wa fedha suala hili linakuwa limetekelezwa. Niombe tu ushirikiano tutakapoleta Muswada huu Bungeni, basi tuweze kuupitisha kwa kutambua kwamba utakuwa umeondoa changamoto nyingi. Maana ukiangalia hivi sasa katika Sheria yetu ya Uwekezaji kwa mujibu wa kifungu cha 20, unakuta tunao wawekezaji wa miradi maalum (strategic investors), wanavyo pia vivutio mbalimbali vya kodi na vingine visivyo vya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo unakuta upande mmoja vivutio vyao vimetajwa katika Sheria ya Uwekezaji; lakini upande mwingine bado tunazo Sheria zingine za Fedha na Kodi ambazo unakuta zinakwamisha kuweza kuwapatia vivutio kama ambavyo wamepewa mikataba kwa mujibu wa performance contracts. Suala hili nalo pia ni eneo ambalo tutalizingatia tutakapofanya mapitio yetu ya Sera ya Uwekezaji pamoja na Sheria yetu ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja pia ya kuboresha vituo vyetu vya One Stop Center au vituo vya kutolea huduma za pamoja. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeendelea kuboresha huduma za One Stop Center na hivi sasa tumeongeza Taasisi nyingine takribani tano na kuongeza TFDA, tumeongeza NIDA, NBS, NEMC pamoja na OSHA na wenyewe pia sasa hivi wako under one stop shop ya TIC. Vile vile tunaendelea kuongeza idadi ya Watumishi walioko katika Idara yetu ya Kazi, katika One Stop Center ya TIC, lakini pia tumeshaunda mfumo wa kielektoniki wa Tanzania Investment Window ambao unawasaidia wawekezaji wetu wanaotaka kuchakata au kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya kupata cheti cha uwekezaji na maombi ya vibali mbalimbali vya kazi. Kwa hiyo, tunawakaribisha wakati wowote, mifumo hiyo ya kielektoniki ipo lakini pia kwa wale watakaotaka kufanya kwa mifumo (manual) huduma hizo pia zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia ni suala zima la upatikanaji wa ardhi. Kumekuwa na changamoto hususan katika kubadilisha ardhi kutoka katika ardhi ya kijiji kwenda kwenye ardhi ya jumla, lakini pia imekuwa ikichukua muda mrefu na wakati mwingine wamesema miaka miwili, mpaka miaka mitatu. Napenda tu kusema kwamba ni maeneo ambayo tunaendelea kuyafanyia kazi na Wizara ya Ardhi; na kwa kweli wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa kuhakikisha kwamba kila mara wawekezaji wetu wanapokuja, basi wanaweza kupata ardhi zao kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la zaidi tu, Mheshimiwa Waziri Mkuu pia alishatoa maelekezo kwa Halmashauri zetu, kuhakikisha kwamba wanatenga maeneo maalum ya uwekezaji, lakini siyo kutenga tu maeneo. Katika eneo hili naomba sana Halmashauri zetu, tuweze kusikilizana vizuri. Wako ambao wamekuwa wakitenga maeneo ya uwekezaji, lakini uhakiki unapoenda kufanyika, idadi ya ekari zinazotajwa unakuta ni tofauti na idadi ya ekari hizo ambazo wao wamesema wamezitenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi tunataka maeneo maalum ya uwekezaji ambayo tayari yameshalipiwa fidia, hakuna mgogoro wa ardhi, lakini yameshapimwa na yameshaandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia TIC pamoja na EPZA wameendelea kutoa ushirikiano kwa Halmashauri zetu kuhakikisha kwamba maeneo haya yanatengwa na yanakuwa ni maeneo ambayo yametengwa kwa kufuata Sheria zetu za Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni matamko ya viongozi mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ni eneo ambalo pia Kamati nashukuru na wenyewe wameweza kulizungumzia. Napenda tu kusema kwamba kazi kubwa inafanyika katika kuvutia wawekezaji. Hatuwezi kufikia katika kiwango hicho cha kupata FDI’s za zaidi ya bilioni 1.18 ya Dola za Kimarekani kama hatupeani ushikiano; kama Taasisi mbalimbali za udhibiti na mamlaka nyingine zinazohusika katika kuwezesha uwekezaji, hazitoi ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mamlaka za Serikali za Mitaa, tunajua kwamba wao ndio kioo kwetu kule katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri zao, basi tujitahidi kuzingatia Sheria na tujitahidi zaidi kuweka mazingira wezeshi ili kuweza kuwavutia wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda ilishaandaa mwongozo wa namna ya kujenga uchumi wa viwanda, nasi pia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, tutakaa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI WA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: …kuhakikisha kwamba tunatoa mwongozo wa kuona namna gani Mamlaka za Serikali za Mitaa kweli zitaweza kuchukua nafasi yao kule waliko katika kuwezesha uchumi lakini zaidi kuhakikisha kwamba tunavutia uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi, lakini kwa sasa napenda tu kusema kwamba tutakuja kueleza mengi kadiri siku zinavyozidi kuendelea. Zaidi, naomba sana ushirikiano na Waheshimiwa Wabunge, lakini pia kupata brief profile za maeneo yenu ya uwekezaji ili tuweze kuvutia uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia mapendekezo haya. Niupongeze uongozi mzima wa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote. Mpango huo au mapendekezo haya yaliyowasilishwa kwetu kwa kweli ni mazuri, kwa vigezo vyote, lakini zaidi, ukiangalia katika masuala matatu.
Mapendekezo haya ya Mpango, yamejengwa katika mafanikio ya Mpango wa Maendeleo wa Kwanza. Pili, mapendekezo haya yamezingatia Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi, inayotekelezeka, iliyo bora, lakini vilevile ni ilani ambayo inapimika, lakini tatu, ukiangalia umezingatia, mabadiliko yaliyopo katika Serikali ya Awamu ya Tano, katika utendaji wake kazi na kupitia dhana nzima ya hapa kazi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na masuala ya Utawala Bora, katika Mpango huu, utaona kabisa suala zima la utawala bora limewekwa kama kipaumbele muhimu sana. Ukiangalia ili tuweze kupata mafanikio yoyote, ili tuweze kufanikiwa katika uchumi huu wa viwanda, ni lazima tuweze kuwa na mafanikio makubwa katika utawala bora.
Kwa upande wetu tutahakikisha kwamba, tunaimarisha taasisi zetu mbalimbali zinazotekeleza masuala ya utawala bora ikiwemo TAKUKURU, ikiwemo Sekretarieti ya Maadili, lakini vilevile kwa upande wa Mahakama na taasisi nyingine za utoaji haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu ambao walisema hakuna utaratibu wa kuandaa viongozi. Niseme tu kwamba katika Serikali utaratibu huo upo na hivi sasa wameandaliwa viongozi wengi, wamepatiwa mafunzo na wengi wao wapo katika kanzidata ambapo itkapojitokeza tuna mahitaji, basi wanaweza kuchukuliwa na kuweza kupewa nafasi mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza. Tunayo assessment center methodology, ambayo kimsingi imeweka watumishi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tu kurudia na kusisitiza kwa watumishi wenzangu wa umma. Tuombe sana sana, waweze kuzingatia nidhamu ya hali ya juu. Waweze kuwa wabunifu, waweze kuzingatia maadili, kwa sababu bila ya kuwa na watumishi wa umma wenye sifa na wenye kutekeleza majukumu yao kwa kujituma na kuwa na uwajibikaji, Mpango huu utakuwa ni ndoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali, tutaendelea kufuatilia na kuchukua hatua, dhidi ya mtumishi yoyote wa umma ambaye atakiuka utumishi wake. Vilevile kama mnavyofahamu, kupitia utumishi wa umma, viongozi mbalimbali wamesaini, wamekula kiapo, kupitia ahadi ya uadilifu. Niwaombe tu watumishi hawa wa umma waendelee kuishi, kupitia viapo vile walivyokula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba tumeyapokea yote mengi mazuri, ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyapendekeza hapa na tutayatekeleza. Pia niseme kwamba, kupitia TAKUKURU tutaendelea kuijengea uwezo. Ukiangalia hivi sasa, wanazo ofisi 52 tu nchi nzima, majengo 52. Ukiangalia katika kila Wilaya mahitaji ni zaidi ya watumishi sita mpaka saba ili uweze kuwa na ufanisi. Hivi sasa wapo watumishi watatu tu na kupitia Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, tutahakikisha tunawapa idadi kubwa ya watumishi wasiopungua 400 katika mwaka ujao wa fedha, ili basi kila Wilaya iweze kuwa na ufanisi katika suala zima la ufuatiliaji kwa watu wanaokiuka masuala mbalimbali ya uadilifu, lakini vilevile wanaochukua rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa inaathiri masuala ya haki za binadamu, rushwa inaongeza tofauti kubwa iliyopo kati ya walionacho na wasionacho, rushwa kwa kiasi kikubwa, imekuwa ikiathiri sana utoaji wa huduma. Kama ambavyo nilisisitiza wakati ule nikiwa nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, tutaendelea kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhakikisha kwamba fedha zile zinazotengwa, basi zinakuwa na ufanisi na zitatumika kama zilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uongozi, tutaendelea kutoa programu mbalimbali za mafunzo, lakini vilevile kwa upande wa sekta ya umma tunaamini, ni lazima tuhakikishe tunaboresha huduma tunazozitoa. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanaendelea kuongezeka, kwa kadri ya mahitaji na kadri uchumi utakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunafahamu kwamba watumishi hawa hawawezi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, bila ya kuangalia maslahi mbalimbali ya watumishi wa umma. Niwatoe hofu, watumishi wa umma wenzangu, tutayaangalia kwa kina na wataweza kupata maslahi ambayo wanastahili baada ya kuwa tumefanya tathimini ya kazi, itakapokamilika baada ya miezi 15. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana Wizara iongeze wigo wa utalii kwani sekta hii ni sekta muhimu yenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Makumbusho ya Taifa, taasisi hii ikiendelezwa na kusimamiwa vizuri ikaboreshwa zaidi inaweza nayo ikatoa mchango wake. Pale katika Kijiji cha Makumbusho (Millennium Towers) eneo ni kubwa, lingeweza kutengenezwa na kuendelezwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa namna tao la Mashariki (milima) inavyolindwa. Ombi langu endeleeni kuangalia milima hiyo ikiwemo Msitu wa Shengena. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nami nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Makamu wa Rais; Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na uongozi wao makini na mahiri na kwa namna ambavyo wanaliongoza Taifa letu ili liweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, napenda pia kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa ambayo bado anayo kwangu kwa kuniteua hivi karibuni kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya uwekezaji. Itakumbukwa kwamba Mheshimiwa Rais alipofanya mabadiliko haya ilimpendeza kuweka jukumu la kuratibu, kuhamasisha, kuvutia na kusimamia suala zima la maendeleo ya uwekezaji nchini chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kimsingi uamuzi ule ulikuwa na mambo ya msingi matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kwa namna ambavyo yameonesha yeye mwenyewe na Serikali yake inavyotambua umuhimu na mchango mkubwa ambao uwekezaji unao katika ujenzi wa Taifa letu.

Pili, ni imani kubwa ambayo Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe anayo kwa sekta binafsi nchini lakini kwa wawekezaji kwa ujumla wake. Tatu, ni usikivu wa Mheshimiwa Rais wetu juu ya kilio cha sekta binafsi na uwekezaji ambacho Mheshimiwa Rais kupitia uteuzi huu ameamua kukisikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uamuzi huo, Mheshimiwa Rais amethibitisha kwa vitendo kwamba anajali sekta binafsi na wawekezaji. Itoshe tu kusema kwamba utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Taasisi za Udhibiti kupitia Blueprint; Mpango Jumuishi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara ya Uwekezaji nchini na tatu kuteua Waziri mahsusi wa Uwekezaji pamoja na kuhamishia jukumu hili la uratibu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni sehemu tu ya mambo mengi ambayo yanaonesha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwa sekta binafsi na uwekezaji. Hakika mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee pia napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake mahiri kabisa ambayo imeweka msingi na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambayo baadhi yake kama ambavyo mlisikiliza hotuba ile mwanana kabisa iligusa masuala ya uwekezaji. Pili, napenda sana kumpongeza pacha wangu na dada yangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa; Makatibu wetu Wakuu, mama Tarishi, mama Mwaluko pamoja na Bwana Massawe na watumishi wote kwa ushirikiano mkubwa ambao wanatupatia katika ofisi hii ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nichukue nafasi hii kuishukuru sana Kamati yetu ya Bunge ya Kudumu ya Sheria na Katiba kupitia kwa Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mchengerwa, Mheshimiwa Najma pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa ushirikiano mkubwa walionipatia na kwa mchango na ushauri wao mkubwa ambao tunaamini utatuletea ufanisi katika majukumu yetu. Mwisho kabisa, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote kwa umahiri wao katika kusimamia shughuli za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na si kwa umuhimu na nitakuwa sijatenda haki nisipowashukuru sekta binafsi kwa ujumla na wawekezaji wote kwa namna ambavyo wamewekeza mitaji yao katika kuhakikisha kwamba wanakuza uchumi wetu wa Taifa. Pia kuwapongeza sana TNBC, niwashukuru kipekee TIC ambayo iko chini ya Ofisi yangu, EPZA, TPSF, TCCIA, Balozi zetu za Tanzania nje ya nchi pamoja na CEO Roundtable lakini na Wakuu wa Mikoa wote, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wetu wa Halmashauri na viongozi mbalimbali na wananchi ambao wameona na kutambua umuhimu wa uwekezaji katika uchumi wa Taifa letu. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, nitaendelea kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara ili kuweza kusikiliza kero na changamoto zao mbalimbali kwa lengo la kuzitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipeke kabisa nimshukuru sana mume wangu mpenzi Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na watoto wangu. Zaidi pia viongozi wote na wanachama wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa kwa namna ambavyo wamekuwa wakinipa ushirikiano pia kunivumilia wakati ninapotekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, kabla sijajibu hoja za Waheshimiwa Wabunge nianze na maelezo ya jumla kwa kuelezea umuhimu wa uwekezaji ambao upo katika maendeleo ya Taifa lolote ulimwenguni. Kwa hakika wote tunatambua mchango mkubwa wa wawekezaji katika kuongeza ajira, uzalishaji na tija pia kwa namna ambavyo unashiriki katika kuongeza Pato la Taifa, kuleta teknolojia mbalimbali na kuwezesha wananchi na kupunguza umaskini. Ni kutokana na umuhimu huo ndiyo maana Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba uwekezaji wa ndani na nje unakua kwa kasi sambamba na kuhakikisha kwamba wananchi wetu nao pia wanaweza kunufaika na uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka 10 nikitolea tu takwimu za mwaka 2008 - 2018, TIC iliweza kusajili miradi takriban 6,596. Napenda kusema kwamba hii si miradi yote ya uwekezaji, iko miradi mingi ya uwekezaji ambayo imeingia nchini na mitaji yake lakini unakuta mingine bado haijasajiliwa TIC. Ni miradi yenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 79.4 ambapo si kiwango kidogo na umeajiri zaidi ya wafanyakazi 788,547. Tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaendelea kuongeza mitaji zaidi kutoka nje lakini zaidi pia kuhakikisha kwamba wawekezaji wetu wa ndani na wenyewe wanashiriki katika uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tutaendelea kuhakikisha kwamba tunasonga mbele katika tasnia ya uwekezaji kama ambavyo tumetambuliwa na ripoti mbalimbali za Kimataifa za uwekezaji tumepiga hatua, tunaongoza katika nchi za Afrika Mashariki lakini pia katika nchi ambazo zinapendekezwa kuwekeza Afrika Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zimependekezwa katika uwekezaji. Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wote kwa pamoja tuongeze jitihada ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kuvutia wawekezaji zaidi kutoka nje ili waweze kuiona Tanzania kama kituo au nchi bora kwa ajili ya kuweka uwekezaji wao. Hili ni jukumu letu sote Waheshimiwa Wabunge ambao tuna wananchi nyuma yetu, mna Halmashauri ambazo ziko chini yenu mnazoziongoza, tuendelee kuwa mfano na tutoe ushirikiano ili kuhakikisha kwamba wawekezaji wetu wanapokuja basi waweze kuwekeza mitaji yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhamasisha wawekezaji wa ndani, tunaendelea na mikakati yetu mbalimbali kama Serikali kuhakikisha kwamba tunafanya makongamano ya ndani na nje ya nchi. Pia tunatoa elimu ya uwekezaji kuwawezesha wawekezaji wetu wadogo wadogo nao waweze kupata mitaji ya kuwekeza kutoka katika taasisi za fedha ikiwemo katika Benki ya Kilimo kama ambavyo Waziri wa Mifugo ameeleza lakini pia tutaendelea na mikakati mingine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia katika takwimu mbalimbali ukilinganisha na mwaka 2005 ambapo wawekezaji wa ndani walikuwa ni takriban asilimia 25 tu lakini nafurahi kusema kwa sasa wawekezaji wa ndani ni zaidi ya asilimia 72. Tutaendelea kuhamasisha ili kiwango hiki kiweze kukua zaidi ili Watanzania nao waweze kuona manufaa ya uwekezaji na waweze kupata pato kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia malengo yetu kiuchumi kama Serikali, tumeweka vipaumbele au mipango katika kuvutia miradi ya uwekezaji katika sekta ambazo zina tija na zina mchango mkubwa kiuchumi na kwa wananchi. Lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba tunaimarisha minyororo ya thamani katika mazao ya kilimo, mazao ya uvuvi pamoja na mifugo lakini pia katika masuala ya madawa ya binadamu, kemikali na bidhaa kwa ujumla ambazo zinatumika kwa wingi nchini lakini pia ambazo zinaajiri wananchi wengi na ambazo zinatumia malighafi zinazozalishwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaje vipaumbele vichache ni pamoja na uzalishaji wa mafuta ya kula kwa kutumia mbegu zinazozalishwa. Hili limeelezwa vizuri sana na Waheshimiwa Wabunge wengi sana na ukiangalia tuna upungufu wa zaidi ya tani 320,000. Kwa hiyo, napenda kuwatangazia Watanzania hii ni fursa kubwa ambayo naamini kila moja akijipanga kwa namna ya uwezo wake wa kimtaji tunaweza tukatumia soko hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, uzalishaji wa mbegu. Ukiangalia kwa sasa mbegu zinazozalishwa nchini ni tani 51,000 tu lakini mahitaji ambayo yanaagizwa kutoka nje ni tani zaidi ya 16,000 na mahitaji kwa ujumla wake ni tani zaidi ya 370,000. Kwa hiyo, hapa napo jamani ndugu zangu ni fursa, hebu tuwekeze katika uzalishaji wa mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni suala la sukari. Ukiangalia mahitaji ni zaidi ya tani 670,000 kwa sukari ya viwandani pamoja na ya majumbani na tumekuwa tukiagiza kwa kiasi kikubwa nje ya nchi ukilinganisha na kiwango ambacho kinazalishwa hapa. Hapa napo tunaweka mkazo ili tuhakikishe kwamba tunajitosheleza kwa mujibu wa uwekezaji wetu uzalishaji wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni uzalishaji wa dawa za binadamu na nafurahi na kushukuru sana kwa namna ambavyo tumeshirikiana na Mheshimiwa Waziri wa Afya katika kuhakikisha kwamba tunachochea, kuhamasisha na kuvutia wawekezaji katika sekta hii ya dawa. Tumeona pale Zegereni viko viwanda vingi ambavyo vimejengwa na wakati wowote vitaanza kuzalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya uvuvi wa kisasa pamoja na kuchakata viwanda vya samaki. Vilevile tuna masuala ya vifungashio, ni fursa kubwa na katika korosho tuna tani zaidi ya 230,000 ambazo lazima ziweze kuongezewa thamani kwa kuchakatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau hoja ya Mheshimiwa mama Kilango, Mheshimiwa Njalu na Waheshimiwa wengi sana ambao walionyesha umuhimu wa kuwekeza katika viwanda vya nguo. Napenda kuwashukuru wote walioongelea suala hili ikiwemo na viwanda vya ngozi, viatu, maziwa, pembejeo pamoja na mbolea tunaiona hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa sasa ambacho Serikali imekifanya kupitia mazao sita ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali imeyatamka kama mazao ya kimkakati na pamba ikiwemo ni kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji ili wanapokuja wawekezaji katika sekta hii basi waweze kuwa na uzalishaji ambapo watakuwa na uhakika wa malighafi kwa siku 260. Kwa mujibu wa ufanisi wa viwanda unatakiwa uwe na malighafi mfululizo kwa siku takriban 260.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachokifanya hivi sasa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Wizara zingine za kisekta ni kuhakikisha kwamba tunaongeza malighafi ili tuwe na malighafi ambazo zitaweza kujitosheleza.

Nawashukuru, tutaendelea kukaa na wadau kuhakikisha kwamba tunaweza kuzitambua kwa kina changamoto ambazo zinawakabili ili kuhakikisha kwamba watakuwa na viwanda ambavyo wamewekeza kwa tija na kuweza kupata faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea, pamoja na changamoto zote hizo nilizozieleza, wako wengine ambao malighafi zinawatosheleza lakini bado wana changamoto. Tutahakikisha tunaweka vivutio maalum kwa ajili ya wale watakaowekeza katika sekta hizi ambazo nimezieleza ni za vipaumbele ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuendesha viwanda vyao kwa tija na kuweza kutupatia pato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala kama zipu, vifungo na materials mbalimbali ambazo unakuta zinatumika katika viwanda vya nguo ambavyo kimsingi usipoviondolea kodi inakuwa ni ngumu wao kuzalisha kwa faida. Kama tulivyoelezwa hapa yuko Mheshimiwa nadhani ni Salum Mbuzi mwenye kiwanda cha Jambo Spinning ambaye alituelezea changamoto zake na nimhakikishie kwamba ni maeneo ambayo tunayafanyia kazi ili tuweze kupata suluhu katika suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau hoja za uwekezaji katika hoteli, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla amezieleza vizuri. Tutaenda kuangalia masuala ya utalii katika Selous Game Reserve, Kilwa Kivinje, Mafia pamoja na sehemu zingine. Yako maeneo mengi kwa sasa niishie kwenye vipengele hivyo tu na mengi nitaeleza nitakapokuwa najibu hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo ya utangulizi, niungane na wote walionitangulia lakini zaidi kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika suala zima la uwekezaji. Nawashukuru sana kwani natambua nia yenu kama Waheshimiwa Wabunge ni kuona kwamba tunakuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji nchini lakini kuhakikisha kwamba mazingira haya yanaboreshwa na kila siku kuhakikisha kwamba taasisi na Wizara zetu zinaweza kubadilika, kwenda na wakati ili kuhakikisha kwamba kodi, ajira na bidhaa zinaweza kupatikana kupitia uwekezaji tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kujibu hoja hizi, nihitimishe kwa kutoa rai kwa mamlaka mbalimbali zihakikishe kwamba zinakuwa wabunifu na kuona namna gani wanaweka mikakati ya kufanikisha uwekezaji nchini kwa kuwa uwekezaji ni suala mtambuka. Ni muhimu wakaonesha kwa vitendo kila Afisa wa Serikali aone ni kwa namna gani anaweza kujenga taswira na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini. Kwa kitendo kimoja tu inaweza ikatuondolea wawekezaji wengi sana ambao kuwarudisha itakuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa niwahakikishie katika suala zima la wepesi wa kufanya biashara. Ni suala ambalo kwa kweli nitajikita nalo sana kupitia viashiria vile 11. Niitakaa na Mawaziri wa sekta kwa sekta na menejimenti zao na kuhakikisha kwamba yale yote yaliyoelezwa katika viashiria vya Tathmini ya Benki ya Dunia ambapo kwa mwaka huu tumekuwa nafasi ya 144 kati ya nafasi 190, hii ni nafasi ambayo tulikuwa 2016, 2017 tulishapiga hatua nzuri tukawa 132, hatuwezi kurudi nyuma. Ukiangalia malengo yetu mwaka 2025 ni kufikia nafasi ya 95 katika wepesi wa kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana sekta zote mkae mkao mzuri, tutakuja kuketi. Bahati nzuri nimeshawapata wale wathamini wenyewe Benki ya Dunia wako Chile na nina mpango wa kufanya nao video conference wiki hii ambapo wamepanga kunipitisha katika kila kiashiria ni nini hasa wanakiangalia ili kuhakikisha kwamba tunapiga hatua katika wepesi wa kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho kinaturudisha nyuma, katika kujaribu kupitia ripoti za wepesi wa biashara wa nchi mbalimbali, unaangalia Rwanda, unaangalia Uganda, wanatupita katika rank hiyo. Kwenye uwekezaji tunawashinda, iweje kwenye wepesi wa kufanya biashara hawa watushinde?

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo nimeligundua, ukiangalia katika improvements za reforms ambazo nchi nyingine wamehesabika wamefanya vizuri, moja au mbili tu, inaonekana yako mengi mazuri ambayo tumeyafanya lakini unajikuta wale wanaohojiwa hawayaelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hili naomba sana, wako Wanasheria wa Kampuni binafsi za kisheria na wako watoa huduma wengine mbalimbali ambao wanapata huduma pia kwenye taasisi zetu, yale mazuri yanayofanywa na Serikali, basi wasisite kueleza maboresho ambayo yamefanywa. Kwa sababu kwa kufanya hivyo, mwekezaji anaangalia pia ranking ambayo nchi inayo katika wepesi wa kufanya biashara, ndipo anaamua pia kwenda kuwekeza. Kwa hiyo, kwenye hili nitaomba sana ushirikiano na ni imani yangu kila mmoja ataweza kubadilika na kutoa ushirikiano kwenye hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijibu sasa hoja ambazo zimeelezwa. La kwanza ambalo lilikuwa ni kubwa ni kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa ajili ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ili kuweza kuongeza fursa za ajira na biashara na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba kama Serikali tunapokea ushauri huu na niendelee kuwahakikishia kwamba, lengo la Serikali ni kuhakiksiha kwamba tunaimarisha mazingira ya biashara ya uwekezaji, kama nilivyoeleza awali ili kurahisisha uanzishaji na zaidi ukuaji wa biashara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuongeza maeneo mbalimbali ya kiuchumi (special economic zones) na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa ardhi na kuwa na miundombinu wezeshi ambayo itaweza kuwasaidia wawekezaji wetu kuweza kuwekeza. Pia tutaendelea kufanya vikao vya mashauriano na wawekezaji wetu na wafanyabishara kupitia ngazi mbalimbali za kisekta mikoa na wilaya ili kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakizibainisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya Msemaji wa Kambi Rasmi Bungeni, ambapo yeye alikuwa haamini kama Serikali au kupitia TIC tumeweza kuvutia zaidi ya miradi 145 mpaka sasa. Napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbowe, nimtajie tu chache, kuna Alpha Pharmaceuticals ya Dar es Salaam, ambayo watawekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 20 na ajira zaidi ya 40. Tunayo Bio-Sustain Limited ya Singida ambao hawa watakuwa wakichakata mafuta ya alizeti na watawekeza zaidi ya Dola milioni 11 za Kimarekani; tunayo GBRI Business Solution ya Shinyanga; tunayo Kilimanjaro Bio-Chemical Limited ambao watakuwa wanazalisha Ethanol; tunayo KOM Food ya Shinyanga ambao nao wataweza kuchakata alizeti na watawekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 20; tunayo pia MW Rice Millers ambao nao pia watawekeza zaidi ya dola milioni 17. Siyo maneno na akiitaka orodha hii kwa kina; na anaweza kwenda kuwatafuta wawekezaji hao ambao wamesajili miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbowe pia alitaka kujua mgawanyo wa hizi dola bilioni 1.18. Napenda kumwambia kwamba kwa wawekezaji wa ndani, tunatarajia kwamba watawekeza mitaji ya dola milioni 401.66, lakini kwa upande wa wawekezaji wa nje, watawekeza mitaji ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 127; na kwa upande wa miradi yenye ubia kati ya wawekezaji wa ndani na nje, watawekeza Dola za Kimarekani milioni 423.75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba sana wawe na imani. Tunachoki-present hapa ni takwimu na taarifa ambazo ni thabiti na zina ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kulikuwa kuna hoja nadhani ya Mheshimiwa Anna Kilango, kulikuwa na Mheshimiwa Mashimba na wengine wengi; ni kwa namna gani tunaendelea kuwalinda wazalishaji wa ndani? Niendelee kuwahakikishia tu kwamba, kupitia mfano wa hatua za kikodi, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018, iliongezwa kodi kwa wale wanaoagiza mafuta mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Kwa yale ambayo ni ghafi, kuna kodi ambayo ilianzishwa ya takriban asilimia 25 na kwa mafuta ambayo yamechakatwa ilianzishwa kodi ya zaidi ya asilimia 35.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeendelea kudhibiti uingiaji wa mafuta ya kula kutoka mipakani. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunalinda viwanda vyetu vya ndani na tutaendelea kufanya hivyo na kuhakikisha kwamba tunakuja na hatua nyingine za kikodi ili kulinda viwanda vyetu vya ndani pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na mifugo, kuona ni kwa namna gani tunaweka vivutio vya kodi kama nilivyoeleza kule mwanzo. Kwenyewe pia kupitia Sheria ya Fedha, waliweza kupunguziwa kodi ya makampuni na hili lilifanyika kupitia viwanda vya ngozi, pamoja na viwanda vya madawa vipya. Badala ya kulipa Corporate Tax ya asilimia 30, wao kwa sasa wanalipa Corporate Tax ya asilimia 20 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye kodi ya ongezeko la thamani kwa upande wa mitambo na vifaa vya viwanda hivyo na kwenyewe pia kodi hizi ziliondolewa. Tunaweza kuona kwa kiasi kikubwa Serikali inaweza kuweka jitihada katika kuhakikisha kwamba viwanda vinalindwa, lakini kuweza kuwapa nafuu wawekezaji waliowekeza katika sekta hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kuendelea kuhakikisha kwamba tunafanyia maboresho sera yetu pamoja na sheria. Niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, tayari tumeshafanya tathmini ya mazingira ya uwekezaji na tumeshabainisha maeneo ambayo ni muhimu yanayohitaji kufanyiwa mapitio ili kuboresha mazingira haya ya uwekezaji. Kufuatia tathmini hiyo, tutakuja sasa na Sera mpya ya Uwekezaji ambayo sasa hivi imeanza kufanyiwa mapitio, tayari tumeshaanza mchakato wa kupata timu ya watalamu ambao wataendesha zoezi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Sheria ya Uwekezaji na yenyewe kwa kiasi kikubwa tutaifanyia marekebisho ili kuhakikisha tunaondoa vikwazo vilivyopo, ikiwemo na kuwa na vivutio vipya katika sekta mbalimbali maalum kama nilivyozieleza huko awali. Pia kuona ni kwa namna gani suala zima la upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wawekezaji, suala zima la miundombinu wezeshi kwa ajili ya wawekezaji na kuondoa changamoto mbalimbali za kitaasisi ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na mazingira ambayo ni shindani kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshafanya tathmini na kuandaa blueprint kama nilivyoeleza kule mwanzo na masuala yote muhimu ambayo yamekuwa yakikwamisha uwekezaji yalishabainishwa na hata wahusika ambao wanatakiwa kutatua changamoto hizo wanajulikana. Ni suala ambalo kupitia mpango kazi ule jumuishi ambao niliusema, pindi tu utakapokuwa tayari, basi hili nalo litaweza kuondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, pamoja na kwamba mpango kazi jumuishi unaandaliwa, lakini tayari yako maeneo ambayo yameshaanza kufanyiwa kazi. Kama ambavyo tumemsikia Mheshimiwa Mavunde ambavyo ameeleza, pia sasa hivi wanapita sheria ile namba moja ya mwaka 2015, kuweza kuona wanaweza kuleta ufanisi kiasi gani katika masuala mazima ya vibali vya ajira pamoja na taratibu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia katika masuala ya tozo, kwenye sekta tu pekee ya kilimo; nawapongeza sana Wizara ya Kilimo, kwa kuwa tayari, kuweza kuondoa zaidi ya tozo 114, siyo jambo dogo. Kwa hiyo, naomba tu Wizara nyingine, badala ya kuona wanataka maduhuli makubwa, hebu tuangalie kikapu kikubwa zaidi. Tutakapochangia katika Mfuko Mkuu wa Hazina, naamini mengi yataweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kuwaomba Mawaziri wenzangu, kila mmoja aweze kupitia tozo ambazo zinaweza zikapunguwa; nampongeza Mheshimiwa Ummy naye pia anajiandaa kupunguza tozo mbalimbali kupitia TFDA. Nampongeza Mheshimiwa Jenista kupita OSHA zaidi ya tozo tano wameweza kufuta; lakini pia Wizara ya Madini, waliokuwa wenzangu tukiwa nao zaidi ya tozo tisa ziliweza kuondolewa katika uzalishaji wa chumvi. Naamini Serikali itaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa kumalizia hoja chache, napenda tu kusema kwamba kwa upande wa zao la chikichi, ukiangalia tumeweka kipaumbele pia katika zao hili. Tayari kupitia TIC zaidi ya hekta 13,000 zimetengwa katika Mkoa wa Kigoma kwa kutambua kwamba zao hili ni la muhimu na la kipaumbele na kuhakikisha kwamba tunakuwa na mafuta ya kupikia ya kutosha na hii ni malighafi muhimu sana kama nilivyoeleza katika maelezo yangu ya utangulizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja za Mheshimiwa Shangazi kuhusiana na namna ya kulinda mazao ya wakulima, hususan katika kuondoa parking fees, landing fees pamoja na kuondoa tozo mbalimbali katika cold-rooms. Ni hoja nzuri na ninaamini kwa kuwa tulitembelea Rungwe pamoja na Hai na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, naamini kupitia Task Force ile ni eneo ambalo atakuwa ameliangalia ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kulinda mazao au bidhaa ambazo zinaweza kuharibika kama nyanya, matunda na mbogamboga kupitia regime ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza pamoja na maandishi. Niwahakikishie hoja zote, endapo kuna nyingine ambazo hatujazijibu, tumezipikea, tutazinakili na tutaweza kuwawasilishia majibu, kila mmoja ataweza kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi, kwa kuwa nina mwezi mmoja tu katika ofisi hii, niendelee kuwaomba sana ushirikiano wa dhati kabisa na tutakuja katika maeneo yenu ili kuweza kutembelea uwekezaji katika sekta mbalimbali. Tunaomba mtupatie ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nami niendelee pale ambapo wameishia wenzangu, kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake shupavu unaotufikisha katika hatua hii kwa kishindo na kwa mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo mara kadhaa alikutana na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na amekuwa akitoa maelekezo kwetu wasaidizi wake na watendaji kuhakikisha kwamba changamoto za wawekezaji zinatatuliwa ili kuharakisha maendeleo ya nchi yetu. Nampongeza pia kwa uamuzi wake mzuri na makini wa kuliweka jukumu la kusimamia uwekezaji chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo ambalo limewezesha kupata mafanikio makubwa katika kusimamia uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza kipekee Makamu wa Rais pamoja na Rais wa Zanzibar kwa maelekezo mbalimbali ambayo wamekuwa wakitupatia kwa namna ambavyo tunatekeleza majukumu tuliyokabidhiwa na Mheshimiwa Rais. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu kwa hotuba yake mahiri ambayo imeweka msingi na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021. Kwa hakika hotuba hii pamoja na mambo mengine tumeshuhudia namna ambavyo imegusa masuala ya uwekezaji ambayo ninayasimamia chini ya uongozi wake madhubuti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana dada yangu, pacha wangu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista kwa namna ambavyo tumeshirikiana kwa pamoja katika ofisi hii katika masuala mazima ambapo ametusaidia katika uratibu wa shughuli za kiserikali lakini masuala ya uwekezaji. Pia namshukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde pamoja na Mheshimiwa Ikupa kwa namna ambavyo tumefanya kazi kwa karibu. Nimshukuru sana Katibu Mkuu Mama Mwaluko, Katibu Mkuu Nzunda na Bwana Masawe pamoja na watumishi wote Wakuu wa Taasisi na Wakurugenzi kwa namna ambavyo wameweza kutoa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu tuliyonayo katika Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa sijatenda haki nisipochukua nafasi hii kukushuru sana wewe binafsi kwa namna ambavyo umetulea na kutuongoza. Vilevile namshukuru Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge kwa namna ambavyo mmekuwa na usimamizi mzuri na uwezeshaji wa shughuli za Bunge lakini kwa kuanzisha huduma za Serikali mtandao. Kwa hakika na Serikali naamini haitatuchukua muda mrefu kwani itatusaidia pia na sisi katika kutoa huduma kwa wawekezaji kupunguza urasimu na gharama kwa wawekezaji wetu. Tunaamini pia kuwa mfano ambao umeuonyesha itakuwa ni chachu kubwa kwa matumizi ya Serikali mtandao pia kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nishukuru sana Kamati yetu ya Bunge ya Katiba na Sheria kupitia kwa Mheshimiwa Mchengerwa (Mwenyekiti), Mheshimiwa Najma Giga (Makamu Mwenyekiti) na wajumbe wote kwa namna ambavyo wametupa ushirikiano mkubwa lakini kwa ushauri wao mzuri ambao kwa hakika umetuwezesha sana kuongeza ufanisi katika uhamasishaji, usimamizi na kufanikisha uwekezaji nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana TNBC TIC, TPSF, TCCIA, CTI, Jumuiya wa Wafanyabiashara Tanzania na CEO Roundtable. Pia sitasahau Balozi zetu za Tanzania nje ya nchi ambazo kwa hakika wamekuwa na mchango mkubwa wa kufanikisha uwekezaji na biashara nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na shukrani zangu kwa sekta binafsi, napenda kutoa salamu za pole kwa msiba wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Ndugu Shamte uliotokea hivi karibuni. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi, amen.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua pia uwekezaji unafanyika katika wilaya na mikoa, sina budi kutambua na kuwashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote, Wakuu wa Wilaya na Wenyeviti wetu wa Halmashauri, Madiwani na viongozi mbalimbali kwa namna ambavyo wamefanya kazi yangu ya kuhamasisha uwekezaji kuwa nyepesi na rahisi na kwa namna ambavyo tumeshirikiana nao. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tutaendelea kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara ili kuweza kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa pekee kabisa nimshukuru sana sana mume wangu kipenzi, Mheshimiwa Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na watoto wangu Kemilembe, Kokubelwa pamoja na Mwesigwa kwa mapenzi yao na kwa uvumilivu wao kwangu wakati wote na kwa kunipa egemeo muhimu linaloniwezesha kuhimili majukumu yangu niliyokabidhiwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru UWT, Mkoa wa Dar es Salaam, UWT - Baraza Kuu Taifa pamoja na TUCTA kwa ushirikiano mzuri waliyonipatia napotekeleza majukumu yangu. Kwa hakika sina cha kuwalipa zaidi ya kuwahakikisha kwamba sitowaangusha. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Same.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, naambiwa nishukuru na Same hapa, Same nakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kipekee nielezee machache kuhusiana na wepesi wa kufanya biashara Tanzania.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wote ambao wamechukua wajibu wao katika kuhakikisha kwamba tunapanda nafasi tatu katika Tathmini ya Wepesi wa Kufanya Biashara. Nishukuru Wizara zote zinazosimamia yale maeneo 11 ambayo tunapimwa kwa mchango wao mzuri ambao kwa hakika ndiyo umepelekea kupata mafanikio haya.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwahakikishia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara mbalimbali 11 zinazosimamia maboresho, tutaweza kufanya vizuri zaidi mwaka huu mwezi wa 10 lakini na katika miaka mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa melengo yetu kwa mwaka 2025 ni kuhakikisha kwamba tunafikia nafasi ya digit 2. Mwaka huu tulikuwa na nafasi ya 141 na tunaamini kwamba ndani ya miaka hiyo mitano ijayo tutaweza kufikia malengo hayo.

Mheshimiwa Spika, nitaje maeneo matatu ambayo tayari tumeshaweza kufikia nafasi ya tarakimu 2 ikiwemo suala la upatikanaji wa mikopo. Namshukuru sana Waziri wa Fedha na BoT tumefikia nafasi ya 67 kati ya 190. Nimshukuru sana Mheshimiwa Mahiga pamoja na Jaji Mkuu kwa upande wa usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na kulinda mikataba.

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni suala la upatikanaji wa umeme kupitia kwa Mheshimiwa Kalemani ambapo tumefikia nafasi ya 85 kati ya 190. Naamini kupitia Mawaziri hawa, tunayo nafasi ya kufanya vizuri zaidi na nitoe rai kwa Mawaziri wengine na kwa Makatibu Wakuu kwenye maeneo yale mengine nane yaliyobakia kuona namna gani tutafanya maboresho ili kuwa nafasi nzuri zaidi kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru sana sekta binafsi kwa uamuzi wao wa kuwekeza nchini na kwa namna ambavyo wanaendelea kuwekeza mitaji. Nawaomba waendelee kuwa na imani wakitambua kwamba nafasi ya Tanzania katika biashara na uwekezaji itaendelea kuimarika zaidi, waendelee kutuamini wakitambua kwamba tutatekeleza majukumu yetu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kutekeleza mpango wetu wa blueprint, kuhuisha mpango wa kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuanzisha utaratibu wa kuwapa Ubalozi wa Heshima katika masuala ya uwekezaji; kuimarisha Kituo chetu cha Uwekezaji Tanzania na kuimarisha mfumo wa kupokea na kutatua changamoto za wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, vilevile tutaboresha sera na sheria ya uwekezaji, kuimarisha miundombinu ya kiuchumi kama vile nishati ya umeme, maji, mawasiliano na miundombinu, kuimarisha huduma za kifedha ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji wa ndani na kuimarisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwa kuendelea kuzihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga maeneo ya uwekezaji. Pia tutalinda wawekezaji wa ndani dhidi ya ushindani usio na haki unaotokana na uingizaji wa bidhaa za magendo.

Mheshimiwa Spika, sitaweza kujibu hoja zote lakini nishukuru sana kwa michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia. Tunatambua nia yenu ni kuweza kuona kwamba nchi yetu inakuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji. Ni imani yangu watumishi mbalimbali katika Wizara zetu na taasisi za Serikali wataendelea kubadilika kwenda na wakati kulea wawekezaji na kufanikisha uwekezaji ili kuhakikisha kwamba uwekezaji Tanzania unaendelea kukua, kuimarika na kuchangia zaidi katika pato la taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na niwahakikishie kwamba majibu yao watayapata kwa maandishi na tutaendelea kutekeleza yale yote waliyoshauri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi, ninakupongeza kwa namna ambavyo umeendesha mjadala huu, pia ninakupongeza kwa kazi nzuri ambayo unaifanya.

Mheshimiwa Spika, kipekee pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaendelea kuliongoza Taifa letu, vilevile Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na viongozi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kuwashukuru Kamati, hususan ya LAAC pamoja na PAC kwa taarifa zao, zaidi kwa michango, maelekezo na ushauri mbalimbali ambao pia wameweza kuutoa, bila kuwasahau Waheshimiwa Wabunge wote walioweza kuchangia hoja hizi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba, kunakuwa na thamani halisi ya matumizi ya fedha kwa hiyo, kipekee tunawashukuru sana kwa ushauri mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika kuchangia hoja hizi, ninaomba niweze kuanza na hoja ya kwanza kwa upande wa LAAC na baadae muda ukiruhusu nitaenda hoja za PAC. Kwa upande wa LAAC kulikuwa kuna hoja za aina mbalimbali za hati za ukaguzi ambazo zimekuwa zikitolewa, ninapenda tu kushukuru kwa namna ambavyo wameeleza mitiririko mbalimbali, lakini na mimi nipende kusema kwamba, ukiangalia mwenendo mzima wa ukaguzi na hati mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa za ukaguzi utaona namna ambavyo kumekuwa na kuimarika katika nidhamu, hususan nidhamu ya mapato, matumizi, pia namna ambavyo uandaaji sasa wa taarifa zetu mbalimbali za hesabu za mwaka ambavyo zimekuwa zikiendelea kuboreshwa.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia nikiainisha miaka miwili ya fedha iliyopita, huko nyuma ukienda na mwaka 2021 katika hati ambazo zilikuwa zinaridhisha, ukiangalia katika mwaka 2019/2020 tulikuwa tuna hati 124 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 67. Halmashauri 124 ndiyo zilipata hati safi, lakini ukiangalia kwa mwaka 2020/21 takribani Halmashauri 178 ambayo ni sawa na asilimia 96, unaona namba inazidi kuongezeka, ni kweli bado zipo Halmashauri ambazo zina hati zisizoridhisha, lakini walao unaona namna ambavyo Serikali inachukua hatua katika kuimarisha nidhamu ya mapato. Tunaendelea kuahidi Bunge lako Tukufu tutaendelea kusimamia kwa umakini kuhakikisha kwamba, kunakuwa na matumizi sahihi, kuhakikisha kwamba taarifa zetu zinazingatia vigezo vinavyohitajika na kwamba, tunakuwa na hati zinazoridhisha.

Mheshimiwa Spika, vilevile ukiangalia kwa mwaka 2019/2020 kwa hati zenye mashaka. 2029/2020 tulikuwa na Hati zenye Mashaka 53 ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 29, kwa mwaka 2020/2021 utaona zimepungua hadi kufikia hati Sita ambayo ni sawa na asilimia Tatu. Kwa hiyo, utaona kutoka Halmashauri 53 kwenda kwenye Halmashauri Sita, hata hizo Sita hatutaki ziwepo, lakini walau utaona kuna maboresho ambayo Serikali imeendelea kuyafanya na hatua zimechukuliwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile Halmashauri zenye Hati Mbaya. Ukiangalia katika mwaka 2019/2020 ilikuwa ni takribani Halmashauri Nane zilikuwa na Hati Mbaya, lakini kwa mwaka 2021 ni Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambayo Mheshimiwa Getere ameisemea kwa umakini na ninaamini huko mbele ataendelea kusimamia kwa umakini na yeye kwa kuwa anaingia katika Kamati ya Fedha ili kuhakikisha kwamba, tunapokuja katika miaka mingine tumetoka Nane, tuko Moja na ikiwezekana miaka ijayo basi iwe ni Halmashauri 0 kabisa na ninaamini hili linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapenda kusema kwamba kwa kweli mengi ya haya yametokana na kazi nzuri mnayoifanya LAAC pamoja na Kamati zingine. Tunaendelea kuwashukuru kwa mara nyingine tena, tunaahidi kuendelea kusimamia maelekezo yenu, pia ushauri mbalimbali na maelekezo ya CAG kama ambavyo yanabainishwa katika hoja mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, ningependa pia kujielekeza katika hoja ya matumizi yasiyofaa, hususan katika Akaunti ya Amana ambayo imesemwa sana hapa. Kimsingi ninapenda kusema kwamba, akaunti hii ya amana katika Halmashauri mara nyingi inawekwa kwa ajili ya fedha maalum. Unakuta zinawekwa fedha nyingine kwa ajili ya kulipia labda Wakandarasi au kunakuwa kuna shughuli maalum hela zimehifadhiwa hapo. Upo mwongozo tayari umeshatolewa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuhusiana na matumizi na usimamizi wa akaunti hii. Kipekee tutaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kwamba, watu wote wanaosimamia akaunti hii wanasimamia ipasavyo na watakapokuwa wametumia fedha katika akaunti hii ya amana kinyume na utaratibu na miongozo basi hatua stahiki zitaweza kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili suluhu ya yote tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuona ni kwa namna gani sasa fedha zote zilizoko humu ndani zinakuwa ring fenced na zisiweze kutolewa bila utaratibu ili kuhakikisha kwamba kweli zinatolewa kwa madhumuni yale tu yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya Tatu kuhusiana na ruzuku ya miradi ya maendeleo kutolewa tofauti na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Katika hili tutaendelea kukaa na Wizara ya Fedha kuona ni namna gani bora ya kuweza kutekeleza ushauri ambao Kamati yetu ya LAAC imeweza kuutoa.

Mheshimiwa Spika, hoja ya Nne ya udhauifu katika usimamizi wa manunuzi, hasa pamoja na mikataba. Tunapenda kusema kwamba, tumeshachukua hatua mbalimbali. Ukiangalia mpaka ilipofikia Agosti mwaka huu, tuliweza kuchukua hatua kwa watumishi 116 kama awamu ya kwanza na tumezielekeza ofisi zetu za Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kwamba, inapofika tarehe 15 Novemba, wanaleta hatua ya pili ya utekelezaji wa ni namna gani wameweza kuchukua hatua kwa wote ambao wameonesha udhaifu katika usimamizi wa mikataba, vilevile katika usimamizi wa manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa mchanganuo, ukiangalia tayari tunao watumishi zaidi ya 22 wameshafikishwa Mahakamani, tunao watumishi zaidi ya 23 wameshafikishwa Polisi na TAKUKURU. Tunao watumishi Watatu wamefukuzwa kazi, watumishi 20 tayari vilevile wamesimamishwa kazi, tunao watumishi takribani 47 ambao kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi wamepewa barua ya onyo, vilevile tunae mtumishi Mmoja ambaye ameshushwa cheo.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka kutoa taarifa kwa mchangiaji kwamba, huko tunakoelekea sasa kwa maeneo anayozungumzia kumekuwa na tabia ya Watumishi wa Serikali kutoka TAMISEMI wanapokuwa wamekwapua maeneo mbalimbali, dakika mbili amepata barua ya kuhamishwa, ikiwepo Bunda sasa hivi wameagiza magari ya sensa, sensa imeisha magari hayajaja, tayari aliyekuwa anashughulika na sensa ana barua anapishana na Madiwani.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, huo ulikuwa tu ni mfano wa hizo changamoto, lakini unaweza kuwa huna taarifa nayo hapo. Kwa hiyo, endelea na mchango wako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, labda nikijielekeza hapohapo tayari ukiangalia katika Manispaa ya Ubungo, Rorya, Mwanza, wako watumishi ambao walihamishiwa Makao Makuu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na tumewarudisha katika Halmashauri hizo kuweza kujibu hoja zao. Tukifuatilia pia kwa Halmashauri ya Bunda kama na yenyewe ikithibitika hatutasita pia kuwarudisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuweza kujibu hoja zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tumevua vyeo zaidi ya watumishi 57. Wako Waweka Hazina zaidi ya 15 vilevile tumeweza kuwavua vyeo, Wakuu wa Idara ya Utawala na Utumishi zaidi ya 14, Maafisa Mipango Watatu, Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi Watatu. Vilevile kwa watumishi takribani 384 ambao wamekaa kwa muda mrefu hasa Wakuu wa Idara wa DHRO, DPMUs, watu wa Internal Auditor na wengine na wenyewe pia tumewahamisha katika maeneo mbalimbali. Sasa hivi tunaandaa fedha kuhakikisha kwamba, watumishi waliokaa kwenye kituo kimoja zaidi ya miaka Saba wanahamishwa ili kuhakikisha tunaweza kuchukua hatua stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya Tano kuhusiana na udhaifu katika uwekezaji wa mitaji ya umma na katika miradi ya Halmashauri. Kwenye eneo hili kulikuwa kuna malalamiko kwamba, kumekuwa na uwekezaji ambao mwingine ulikuwa ukifanyika bila kuwa na upembuzi yakinifu, lakini bila kuwa na maandiko ya miradi. Ni kweli baadhi ya Halmashauri umekuta wengine pia wakiiga aina ya miradi hasa ya stendi na masoko, vilevile wengine wamekuwa wakipeleka hela katika uwekezaji katika benki ambazo hazina utendaji unaoridhisha na bila kufanya upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Spika, ninapenda tu kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kwa sasa tumeshaandaa muongozo wa namna ya uandishi wa miradi mbalimbali ya uwekezaji katika Halmashauri zetu, vilevile tumeshirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNCDF, tayari tunayo Kamati ya Kitaifa yenye wajumbe au wataalam takribani 44, wameshapatiwa mafunzo wa kutoka TAMISEMI, Wizara ya Fedha pamoja na mamlaka zingine mbalimbali kuhakikisha kwamba, tunakuwa na mwongozo sahihi na tunaendelea kuwafundisha wataalam wa Halmashauri ili wanapoandaa miradi ya uwekezaji na mingi ni katika miundombinu, kuhakikisha kwamba wanakuwa na ubobezi na wametimiza vigezo vinavyohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuanzia Julai 2022 tunashukuru Mheshimiwa Rais aliweza kuidhinisha muundo wa kiutumishi wa Halmashauri zetu au Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na muundo huu umeshaanza kutumika na kwa sasa tunayo Idara na Section mpya ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Lengo kubwa la kuanzisha Idara hii ni kuhakikisha kwamba, kabla Halmashauri hazijaja au hazijaanza kutekeleza miradi ya uwekezaji katika Halmashauri zao basi mapendekezo hayo au maandiko yanapitishwa katika Idara hiyo ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuweza kupitiwa, wanapojiridhisha pia hawatamaliza wenyewe kule, wataleta TAMISEMI nasi pia kwa wataalam wabobezi waliopo, watapitia na kujiridhisha endapo kweli miradi hiyo inayopendekezwa ya uwekezaji inakidhi vigezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye eneo hilo pia, eneo la tatu…

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, kuna taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nasi tungekuwa tunawasimamisha hivyo kila dakika nadhani tusingefika hapa.

MBUNGE FULANI: Aah!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Ni haki yake ya msingi Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Charles Kajege, taarifa. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka nimpe taarifa msemaji, anaonesha kutaka ku-deal na tatizo kwa kumfukuza nani huyu… kuwafukuza watumishi na kuhamisha watumishi wa ngazi ndogondogo badala ya ku-deal na tatizo kubwa ambalo tunaliona kwamba, liko Makao Makuu, Mheshimiwa Waziri atuambie kuhusu hapo?

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, sipokei taarifa hiyo. Naomba tupeane nafasi kidogo ili tuweze kumaliza hoja hizi.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunakamilisha mwongozo wa kusimamia miradi baada ya kukamilika hasa katika kuanzisha special purpose vehicle katika miradi yote ya uwekezaji. Kama ambavyo imebainishwa katika changamoto mbalimbali na Kamati, tunapenda tu kusema kwamba, tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunazifanyia kazi kwa ukamilifu na tunaamini maboresho mbalimbali tuliyoyaeleza hapa kupitia masuala ya SPV, kupitia uanzishwaji wa Kitengo cha Biashara, Viwanda na Uwekezaji pamoja na mambo mengine basi tunaamini hili litaweza kutekelezwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya usimamizi na utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Yapo mapendekezo mbalimbali ambayo tunayapokea, kulikuwa na mapendekezo ya kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya fedha zitakazotolewa na kurejeshwa ziwekwe katika kumbukumbu za vikundi vinavyokopa.

Mheshimiwa Spika, ninapenda tu kuliarifu Bunge lako Tukufu, tayari hili limeshatekelezwa. Kuanzia mwaka 2021/2022 Julai, tayari kuna akaunti mbili za Halmashauri katika masuala ya mikopo. Akaunti ya kwanza iko Benki Kuu na akaunti hii inatumiwa na Halmashauri kuweza kuchangia asilimia 10 ya mapato ya ndani, vilevile ni akaunti ambayo inatumika kwa ajili ya utoaji wa mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili au akaunti ya pili ni akaunti ambayo tumeifungua katika akaunti za kibiashara katika Benki ya NMB pamoja na CRDB ambayo ndiyo tunaitumia kwa ajili ya kupokea marejesho ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, la pili, marekebisho mengine ambayo tumeyafanya, kwa sasa tunao Mfumo wa Kielektroniki wa Ten Percent Loan Management Information System. Na kupitia mfumo huu ambao tumeshaanza kuutumia tangu Mei, 2022, tumeshaanza kuona mabadiliko katika suala zima la hali ya utoaji wa mikopo pamoja na urejeshaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, kuna mikopo ya nyuma (mikopo chechefu), tumeshakaa na halmashauri zetu pamoja na maafisa ustawi wa jamii kuweza kupata tathmini tangu mpango huu ulipoanzishwa mpaka sasa ni kiasi gani cha fedha zimetolewa, kiasi gani kimerejeshwa na kiasi gani bado hakijarejeshwa mpaka sasa. Tumewaomba taarifa za mpaka Juni, 2022 na tumewapa muda mpaka tarehe 30, Novemba, 2022 waweze kuwa wamewasilisha taarifa hizo za backlog ya mikopo.

Mheshimiwa Spika, tunaamini baada ya kupata taarifa hizo na baada ya kusafisha data (kufanya data cleaning), basi tutaweza kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha kwamba mikopo yote iliyotolewa inaweza kurejeshwa.

Mheshimiwa Spika, pia tumefanya marekebisho katika Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2019. Marekebisho haya yalifanyika mwaka 2021 ambapo kwa sasa halmashauri zimeruhusiwa kuweza kutenga fedha kati ya shilingi milioni sita hadi 60 kwa mwaka ili kuzitumia fedha hizo kutoa mafunzo ya kiungozi, kiutawala, usimamizi wa fedha, uendeshaji wa miradi na utoaji wa taarifa kwa vikundi vyetu.

Mheshimiwa Spika, fedha hizo pia – kati ya milioni sita mpaka 60 kwa halmashauri – zitaweza pia kutumika kufanya ufuatiliaji wa mikopo na tathmini ya namna ambavyo vikundi vinavyopata mikopo hiyo vinaendelea.

Mheshimiwa Spika, tunaona mabadiliko, tumeona hoja kwamba fedha nyingi zinatoka, na hata ukiangalia mwaka huu zaidi ya bilioni 75, na kwa kweli ni lazima fedha zote zilizotolewa ziweze kurejeshwa. Tupende tu kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba ukiangalia kuanzia mwaka 2019/2020 na 2020/2021 utaona namna kiwango cha mikopo kinachotolewa. Huko nyuma ilikuwa inaanza kutoka kwa asilimia 65, lakini kwa sasa, mwaka 2021/2022, takribani asilimia 90 ya mikopo imeweza kutolewa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa marejesho, mwaka 2019/2020 marejesho yalikuwa kwa asilimia 72 na mwaka 2021/2022 marejesho sasa yamefikia asilimia 84 na tunaendelea kuimarisha suala hili. Tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wameliongea kwa hisia kali. Kwa kweli hizi fedha si msaada, zinatakiwa kweli kuwa ni mikopo na ni mikopo ambayo imetolewa kwa masharti nafuu. Kwa hiyo na sisi tunapokea hoja hiyo na tutaendelea kuimarisha mifumo kuhakikisha kwamba tunakwenda kwenye utoaji wa asilimia mia na hatimaye pia urejeshaji uwe kwa kiwango kikubwa kinachoridhisha.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya baadhi ya stahiki za watumishi kutolipwa ipasavyo, wengine michango yao ya hifadhi ya jamii imekuwa haipelekwi kwa wakati, hali ambayo imewaathiri wakati wanapostaafu, posho za likizo, gharama za uhamisho, gharama za masomo pamoja na posho nyingine nazo pia zimekuwa hazitolewi.

Mheshimiwa Spika, nikienda katika hoja ile ya watumishi waliostaafu katika halmashauri. Unakuta wengine wamestaafu lakini wameshindwa kulipwa mafao yao kutokana na baadhi ya halmashauri kutopeleka na nyingine ni shilingi laki mbili au tatu tu.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu tarehe 01, Novemba ilituita na tuliweza kufanya kikao pamoja na makatibu tawala wa mikoa na tumeshakubaliana kuweza kuhakikisha kwamba tunahakiki madai yote na kuhakikisha kwamba wanakuja na mpango kazi wa namna watakavyolipa madai yao hayo kwa ajili ya watumishi wetu hawa wa halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho tumekubaliana na mifuko yetu ya hifadhi ya jamii, kwa kiasi kikubwa kwa madai ambayo yamesababishwa na halmashauri mbalimbali kutopeleka michango, basi waweze kulipwa fedha hizo bila ya kuleta usumbufu kwa mtumishi aliyestaafu.

Mheshimiwa Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja, malizia mchango wako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nije kwenye hoja ile ya uthamini wa DART. Nipende tu kusema kwamba kwa wale wananchi wa eneo la Gerezani kulikuwa na maombi hapa au maelekezo ya Kamati kuhakikisha kwamba taarifa ya tathmini inaangaliwa upya na kwamba walioshiriki basi wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba PAC ilielekeza nyaraka mbalimbali ziwasilishwe kwa CAG na sisi tutafanya hivyo na kuhakikisha kwamba CAG anapata nyaraka hizo ili apitie kwenye valuation report kuona kama kweli kilicholipwa kupitia yale malipo ya usumbufu na malipo ya uthamini ndicho ambacho kilistahili kulipwa au kuna malipo ya ziada au kama kuna mapungufu basi taarifa hiyo ndiyo itakayoelekeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja ya kuungua kwa Majengo ya Shirika la Masoko Kariakoo, na kwamba alipokwenda CAG kuna hati mbalimbali za takribani shilingi bilioni 3.5 hazikuweza kupatikana, na kwamba hii ilitokea baada ya CAG kubaini tu baadaye soko likaungua.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwanza, mwezi Aprili, 2021, tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliunda timu; kabla hata haya hayajajitokeza, kwa ajili ya kuangalia ubadhirifu mbalimbali; na tayari kuna hatua nyingine zinaendelea kuchukuliwa. Lakini kwenye hili la kufanya forensic audit tunakubaliana na Kamati na tutafanya mawasiliano na mamlaka zenye dhamana ya kufanya forensic audit ili iweze kufanyika. Na endapo kuna jinai yoyote basi iweze kuthibitika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami napenda kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Elimu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Naibu Waziri wake, lakini vile vile na Uongozi mzima wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu hoja chache zinazohusiana na masuala ambayo yako chini ya Utumishi ili kuweza kutoa ufafanuzi kidogo. Hoja ya kwanza ambayo ni kuhusiana na madeni mbalimbali ya malimbikizo ya mishahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imekuwa ikiwalipa watumishi mbalimbali wakiwemo Walimu na Watumishi wengine ambao sio Walimu, madai yao mbalimbali ya malimbikizo ya mishahara. Kwa mwaka huu wa fedha kuanzia Julai, 2015 hadi 25 Mei, mwaka huu wa 2016, Serikali imeshalipa madai ya Watumishi 24,677 yenye thamani ya shilingi bilioni 22.9. Kati ya madai haya ya shilingi bilioni 22.9 Walimu 14,366 waliokuwa wakidai takribani shilingi bilioni 10.7, wameshalipwa madeni hayo ya malimbikizo ya mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tumeshapokea madai mbalimbali ambayo yalipokelewa manually na mengine ambayo yalikokotolewa kwa mfumo wa ni automatic, tunaendelea kuhakiki madeni yenye thamani ya shilingi bilioni 11.5 na yatakapothibitika kwamba kweli madai hayo ni halisi, basi yataweza kulipwa bila shaka yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile yapo madeni ya takriban shilingi bilioni 2.3 tayari yameshahakikiwa ya Walimu zaidi ya 1984 na wakati wowote yanasubiriwa kulipwa. Kwa hiyo, ni imani yangu yataweza kulipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu, kwamba tangu tuliposimika mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara au Lawson mwezi Mei mwaka 2012, tumekuwa tukitekeleza ulipaji wa madai mbalimbali. Changamoto kubwa ambayo tulikuwa tukiipata, kwanza ukiangalia katika mfumo ulikuwa unakokotoa madai haya automatically, yaani kupitia mfumo. Wakati huo huo watumishi mbalimbali wenye madai au Walimu wakiwemo, wengine walikuwa wakileta pia taarifa zao manually kwa madeni yale yale na mengine unakuta yalikuwa yanaenda tofauti na madeni ambayo yalikuwa ni automatic arrears.
Kwa hiyo, hii ilikuwa inatupa taabu, unajikuta umepokea deni huku na huku pia umepokea. Kwa hiyo, ilikuwa ni lazima tuendelee na uhakiki. Nawaomba tu Walimu na Watumishi wengine wawe na subira lakini wajitahidi kuhakikisha kwamba wana-submit madai ambayo ni ya kweli na halisi. Aidha, nawaomba zaidi waajiri wazingatie hili kwa sababu hatuta- entertain manual arrears, tuna-entertain zaidi automatic arrears claims tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo imekuwa ikitupata kama Serikali na ambayo imekuwa ikisababisha madai haya ya malimbikizo ya mishahara, mfumo huu tulionao wa taarifa za malipo ya mishahara, hauwezi kukokotoa madai au malimbikizo ya mishahara ambayo yanawasilishwa, watu wanaingia kwenye payroll kuanzia tarehe 15. Bado ulikuwa haujajengewa uwezo wa kuweza kukokotoa madai ya siku kwa siku. Mtu anayeingizwa baada ya tarehe 15, labda amekaa siku 14 tu, lakini kwa sasa tunaendelea kulifanyia kazi na ni imani yangu ndani ya muda mfupi suala hili litaweza kuwa limekwisha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ilikuwepo hoja kwamba baadhi ya Walimu na watumishi wengine wamekuwa hawaingizwi katika orodha ya malipo ya mishahara kwa wakati. Kwa takwimu nilizonazo za mwaka 2014 na 2015, tulikuwa na ajira mpya 56,816 na kati ya hizo ajira 57,036 zilishaingizwa katika mfumo wa human capital management information system na kati ya ajira hizo, ni ajira mpya 2020 peke yake ndizo tuliwarudishia waajiri ili waweze kufanya marekebisho mbali mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda tu kusema kwamba tayari ajira zaidi ya 57,036 zimeingizwa katika mfumo. Vile vile, nitumie nafasi hii kuwakumbusha waajiri kuhakikishia wanawaingiza waajiriwa wapya mapema katika mfumo huu wa payroll pindi wanapokuwa wamepangiwa katika maeneo yao ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilitolewa ni kuhusu kuweka posho ya kufundishia au kuirudisha pamoja na posho ya mazingira magumu. Serikali inatambua ugumu wa kazi ambao wanaipata Walimu, lakini vile vile inatambua umuhimu wa kada hii muhimu. Kwa kutambua hilo, tunayo nia ya kuboresha maslahi mbalimbali ya watumishi ikiwemo Walimu na kuhakikisha kwamba tunawapa mishahara ambayo kwa kweli itakuwa imeboreshwa. Lengo letu ni kwamba badala ya kulipa posho zaidi, tutahakikisha kwamba tunaboresha mishahara. Tumeshaanza zoezi la tathmini ya kazi pamoja na upangaji wa madaraja au job evaluation na kama ambavyo nilieleza katika bajeti yetu, zoezi hili litakamilika ifikapo mwezi Februari, mwaka kesho 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itakuwa siyo kwa ajili ya kada ya Walimu tu, bali Serikali nzima kwa ujumla wake kwenye watumishi wa Umma. Tutaoanisha na kuwiainisha mishahara pamoja na posho mbalimbali au marupurupu mbalimbali ambayo wanayapata. Tutaangalia pia aina ya kazi; kama ambavyo nilieleza, siyo kwa Walimu tu, tunatambua umuhimu lakini na wenyewe pia wataangaliwa kuona namna gani wataboreshewa. Unakuta kuna Mtumishi X, mwenye sifa sawa, elimu sawa, uzoefu sawa kazini labda mmoja ni Mwanasheria EWURA, mwingine ni Mwanasheria kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini unajikuta wanapishana mishahara wengine mara tano mpaka hata mara kumi. Tukasema hili haliwezekani. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tuvute subira, eneo hili tunalipa kipaumbele kikubwa na Walimu tutawazingatia katika uboreshaji wa mishahara yao na maslahi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limesemewa sana na Waheshimiwa Wabunge ni suala zima la upandishaji wa madaraja kwa Walimu. Serikali imeshawapandisha Walimu 85,533 madaraja yao katika mwaka huu tu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia idadi hii ni takriban asilimia 28.5 ya Walimu wote waliopo katika Utumishi wa Umma. Vile vile, tumekuwa tukiendelea kuboresha maslahi ya Walimu, lakini vile vile kwa kupitia Muundo wa Utumishi wa Walimu wa mwaka 2014 tuliweza kufungulia ukomo wa kupanda vyeo kwa Walimu na Halmashauri mbalimbali zimekuwa zikianza kuwapandisha madaraja waliofikia ukomo na wale ambao walikuwa hawajafikia ukomo. Natambua Halmashauri mbalimbali wanaendelea na vikao kuona ni kwa namna gani basi wanaweza kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanaweza kupandishwa madaraja yao kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imekuwa ikisumbua sana na ambayo inaendana na upandishwaji wa madaraja, unakuta watumishi wengine na Walimu wanapandishwa madaraja lakini mishahara yao wanakuwa hawajarekebishiwa kupata mishahara mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha ambao tunaumalizia, tumeweza kurekebisha mishahara ya Walimu 57,898 ambao walipandishwa madaraja katika mwaka huu wa fedha. Aidha, katika idadi hiyo kama nilivyoeleza Walimu 4,927 tumekuwa tukihakiki taarifa zao na wakati wowote kuanzia sasa wataweza kurekebishiwa mishahara yao. Vile vile, kwa ambao walipandishwa madaraja, lakini vielelezo vyao vimekuwa havijitoshelezi ni Walimu 23,314.
Kwa hiyo, naomba waajiri mbalimbali waendelee kufuatilia kuhakikisha kwamba Walimu hawa wanaweza kurekebishiwa mishahara yao kwa wakati kwa sababu sisi kama Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, tulishakasimu mamlaka kule kule chini kwa waajiri kwa ajili ya kuboresha huduma na kuisogeza huduma karibu zaidi na watumishi hawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami nachukua fursa hii kwanza kabisa kuunga mkono hoja hii ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya, lakini nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake pamoja na uongozi mzima wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama tu hapa kutoa assurance, nimesikia katika michango mingi, kwa kweli kwa kiasi kikubwa Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana tatizo la uhaba wa watumishi katika Sekta hii ya Afya. Napenda tu kusema na kurudia kwamba katika mwaka huu wa fedha unaomalizika 2015/2016, katika Sekta ya Afya wataajiriwa wataalam 10,870. Muda wowote kuanzia sasa ndani ya mwezi huu kibali cha ajira kitaweza kutoka na Wizara ya Afya wataweza kuendelea kuwapangia vituo vya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mgao huo wa watumishi 10,870, watumishi 3,147 ni wa kada mbalimbali 10 zinazohusiana na masuala mbalimbali ya utabibu. Vilevile ukiangalia katika wauguzi, ni wauguzi 3,985. Pia ziko kada nyingine kama za mama cheza au wataalam wa viungo pamoja na Wafamasia na wengineo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika miaka mitano tu, kuonesha ni kwa namna gani Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika upatikanaji wa wataalam wa afya, kwa upande wa utumishi, tumetoa vibali 52,937 na kati ya vibali hivyo walioweza kuajiriwa ni wataalam 38,087 na ambao hawakuweza kuripoti ni 14,860. Asilimia 71.93 ndiyo ambao waliweza kuripoti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini? inawezekana mkaona siyo jambo la kweli; ukiangalia katika sekta binafsi katika ushindani na wenyewe pia wanang‟ang‟ania wataalam hao hao, lakini mwisho wa siku ukiangalia pia katika vyuo vyetu vya umma pamoja na vyuo binafsi mahitaji yanayohitajika pamoja na output inayotolewa bado haitoshelezi. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tuwe katika mkakati wa kuangalia ni kwa namna gani sasa katika vyuo vyetu wataweza kutoka wataalam wengi zaidi ili waweze kuajiriwa na kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwaka jana tu, mwaka 2014/2015 pamoja na kwamba ikama zimejazwa na Halmashauri zetu. Ziko kada zaidi ya 12 zenye wataalam 335 hawakuweza hata kupata watu kabisa, ukiangalia ni kada ambazo hata mafunzo yake hapa nchini hayatolewi. Nitolee tu mfano biomedical engineers pamoja na wengine wengi, tunaelewa umuhimu na tunaendelea kujitahidi kuongeza idadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia 2014/2015 tulitoa kibali cha watumishi 8,345 lakini mwisho wa siku ukiangalia katika soko la ajira kulikuwa na ukosefu wa wataalam katika soko la ajira 4,467, tungependa kuweka idadi kubwa na hata hii idadi yenyewe tunayowaambia ya 10,870 tunaangalia kwa mujibu wa wahitimu wanaotoka katika kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wahitimu waliopo katika mwaka 2015/2016 ni wataalam 10,000 na sisi tunatoa kibali cha 10,870. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tunaona umuhimu wa sekta hii na tutaendelea kwa karibu kabisa kama Serikali na kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuona ni kwa namna gani sasa idadi hii itaweza kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika mwaka 2010/2011 tulianza na wataalam 7,903, lakini ukiangalia katika mwaka huu wa fedha tutakwenda katika wataalam 10,870. Kwa hiyo itoshe, tu kusema kwamba, kama Serikali tutaangalia katika namna ambavyo wanapangwa sasa. Tutazingatia yale maeneo ambayo yana upungufu mkubwa uliokithiri wa wataalam, vilevile kuangalia sasa ni kwa namna gani tunaweza kuhuisha mfumo wetu katika mchakato wa ajira au upangaji wa vituo, uweze kuwa ni centrally katika sehemu moja ili kuona ni kwa namna gani sasa katika vituo vyetu tunaweza kupata wataalam wa kujitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niseme hayo, niwahakikishie sana Waheshimiwa Wabunge kila mwaka kwa kadri bajeti itakavyokuwa ikiruhusu, tutakuwa tukijitahidi, sekta hii ni sekta ya pili ambayo tunaipa kipaumbele. Katika Sekta ya Elimu wataalam 20,857 na katika Sekta hii ya Afya wataalam 10,870 lakini bado tunazingatia kwamba ni muhimu vyuo vyetu viweze kuwa na output zaidi ili tuweze kupata wataalam wa kuweza kuwaajiri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wengine wote wa Wizara hii muhimu kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao na kuiongoza Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi kwa sekta ya utalii kutoa ajira ya watu 500,000 za moja kwa moja. Ni vema hata hivyo Wizara ikaongeza nguvu katika ukuzaji wa utalii na matangazo katika nchi ambazo zina watalii wengi tena wenye uwezo wa kuja Tanzania kutalii kama China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni muhimu tukaendelea kuhamasisha uwekezaji zaidi katika ujenzi wa hoteli ya kisasa ya nyota kuanzia nne, tano, sita ili kuongeza idadi ya vyumba kwa ajili ya malazi yenye viwango na ubora wa wageni, watalii wa nje na wa ndani. Hii inapaswa kwenda sambamba na kuwa na wafanyakazi wenye uwezo na viwango bora katika kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niungane na Wabunge wengine wote ambao wamepongeza Kamati hizi mbili na kipekee nipongeze Kamati yangu ya Utawala na Serikali za Mitaa kupitia kwa Mwenyekiti Mheshimiwa Chaurembo na Wabunge wote kwa taarifa hii nzuri, ya kina, ambayo kwa kweli maudhui yake yatatusaidia sana pamoja na ushauri na maoni mbalimbali ambayo wameweza kuyatoa.

Mheshimiwa Spika, nikienda katika mapendekezo yaliyosomwa na Mwenyekiti, lile la kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na suala zima la migogoro ya ardhi lile lililoko katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Nipende kusema kwamba tunapokea mapendekezo haya, tutayatekeleza na vile vile tutazingatia wakati wa kufanya uchunguzi huu wa kina, kuhakikisha kwamba watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hawahusiki katika timu itakayofanya uchunguzi. Hata hivyo tumewasikia hapa Wabunge lakini pia Kamati ikieleza kwa kirefu kuhusiana na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa TARURA, tunashukuru kwa namna ambavyo maoni na mapendekezo yaliyojitokeza na hasa kutokana na suala zima la ufinyu wa bajeti. Nipende kusema kwamba suala hili tumelipokea, tumekuwa tukiendelea kuwasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tunalifanyia kazi ili kuendelea kuona ni kwa namna gani TARURA itaweza kuongezewa fedha nyingi zaidi ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuwa na bajeti inayowatosheleza. Kwani kwa sasa tuna bajeti ya shilingi bilioni 838 na mahitaji bado ni makubwa. Ukiangalia bado tuna vikwazo vingi katika wilaya zetu na bado tunahitaji fedha nyingi kwa ajili ya kufungua na kuondoa vikwazo hivyo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati. Kwanza ningependa kusema, hakuna upendeleo katika utekelezaji wa miradi hii na pili, nadhani kuna mkanganyiko kidogo, wako ambao walikuwa wanasema kwamba miradi hii haiangalii halmashauri ambazo ni ndogo ndogo. Nipende tu kusema kwamba miradi hii ya kimkakati inatekelezwa kwa vigezo mbalimbali. Tumekuwa tukishirikiana na Wizara ya Fedha katika kuhakikisha kwamba miradi inayoibuliwa na halmashauri ile ambayo inakidhi vigezo basi ndiyo miradi ile ambayo inaweza kuzingatiwa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo changamoto kubwa ambayo tuliiona, unajikuta katika baadhi ya halmashauri walikuwa Maafisa Mipango wengine hawana uwezo mkubwa sana wa kuandaa maandiko ya miradi hii mikubwa ya kimkakati na ndio maana pale nilisikia hoja ya nadhani Mheshimiwa Kwagilwa, akisema kwamba nyie hamna uwezo wa kuandaa sijui moja, mbili, tatu, sijui mpaka muandaliwe mwongozo.

Mheshimiwa Spika, siyo kwamba tumeandaliwa mwongozo, ni pamoja na kutoa mafunzo kwa Maafisa Mipango wetu wa Halmashauri ili waweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuandaa maandiko zana, kufanya upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wenyewe pamoja na masuala mengine kadha wa kadha. Hii ni kuhakikisha kwamba miradi itakayopelekwa Wizara ya Fedha ili iweze kuzingatiwa, basi kweli iwe ni miradi ambayo itakuja kuleta thamani halisi ya fedha badala ya kuwa tu na miradi yoyote kama ambayo walikuwa wanakopiana zaidi kama miradi ya stendi na miradi ya masoko.

Mhesimiwa Spika, unakuta Halmashauri kama ya Ukerewe kumbe huenda wangeweza kuja na mradi mkakati wa kuweza kutengeneza chakula cha Samaki, mradi wa kutotolesha vifaranga vya Samaki, nyavu za kuvulia samaki na vitu vingine kadha wa kadha. Kwa hiyo, siyo kwamba tumekuwa tukipendelea au kutafuta watu ambao hawahitajiki.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, huu mwongozo tunaandaa pia na suala zima la special purpose vehicle. Nitoe tu mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, pale wana Kiwanda cha Chaki pamoja na Halmashauri nyingine. Sasa je, wanapokuwa wamefungua kampuni, au wanapotekeleza mradi wa aina hiyo, wautekeleze kwa mfumo gani?

Mheshimiwa Spika, na lenyewe hilo ukiangalia dhana nzima ya suala la special purpose vehicle suala jipya kidogo kwetu. Kwa hiyo, ni vema pia na lenyewe tupate maelekezo ya kina kupitia mwongozo ambao Halmashauri zetu zitaweza kuuelewa na kuweza kujua ni kwa namna gani wanaweza kutekeleza. Kwa hiyo, kwenye hili tutaendelea nalo na siyo kwamba watu hawana uwezo wa kuweza kufanya hilo, lakini tunataka tujenge uwezo mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba Mungu niweze kupata muda wa kutosha kwa suala la upungufu wa Walimu. Wabunge wamelieleza kwa uzito mkubwa. Ukiangalia tuna upungufu wa walimu zaidi ya 238,000. Tunashukuru kwamba kupitia jitihada za Mheshimiwa Rais, ndani ya muda mfupi sana tangu ameingia, utaona alipoingia tu tuliweza kupata kibali cha kuajiri walimu 9,800. Siyo hilo tu, tunaendelea na jitihada hizo na kuhakikisha kwamba tunaendelea kujairi kwa mujibu wa mahitaji na kwa kuzingatia uwezo wa kifedha wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mkenda ataongea kwa kina kuhusiana na Mwongozo wa Walimu wanaojitolea. Tumefurahi kuona kwamba Wabunge pia wameona hili litakuwa na mvuto na litaweza kusaidia sana katika kupunguza changamoto ya Walimu wetu. Pia wamejitokeza wadau wengi ambao wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuona ni kwa namna gani tutakapoanza sasa kuendelea kuweka mfumo sahihi namna gani Walimu wanaojitolea waweze kujitolea, wako tayari kuweza kutuunga mkono. Kwenye hili, tayari tumeshaanza mashauriano na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na UNICEF na wengine pia ambao wamekuwa tayari kuunga mkono jitihada hizi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya DMDP II na kwamba mradi umechelewa. Napenda tu kumweleza Mheshimiwa Bonnah, Wabunge wa Dar es Salaam na wengine ambao wanaufuatilia mradi huu, tayari concept note tulishaiandika, tumeshaiwasilisha Benki ya Dunia, na kwa sasa tunaendelea na majadiliano na na Benki ya Dunia kupitia Wizara yetu ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mradi wa TACTIC, na yenyewe pia ilijitokeza kwamba ni miji ile ile inayopewa miradi ya mikakati, na wenyewe tena wanapewa mradi huo wa uboreshaji wa miundombinu ya miji ya kimkakati ile 45. Napenda kusema kwamba miradi hii iliibuliwa kwa kufuata vigezo na hasa vigezo vya kupata wanufaika hivi vilitokana na taarifa ya idadi ya watu, na pia ongezeko la ukuaji wa idadi ya watu kwa mujibu wa taarifa ya Tume yetu ya Takwimu ya NBS na tumeweza kuzingatia hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwa nini mradi umechelewa? Kulikuwa kuna majadiliano mbalimbali na Benki ya Dunia. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, na leo hii Mheshimiwa Naibu Waziri Silinde ameweza kujibu maswali hapa kwamba kuanzia mwaka huu wa fedha tutaanza na wale waliopangiwa katika awamu ya kwanza miji 12, awamu ya pili tuna miji 15 na awamu ya tatu tutakuwa na miji 18. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote, ifikapo 2025 mradi huu wa TACTIC kwa miji hiyo 45 yote itakuwa imeshatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu kwa wale ambao wako katika makundi ya mwisho. Anayecheka mwisho ndiye anayecheka sana. Kwa hiyo, kama kuna hofu nyinginezo huko, wale ambao mko mwishoni mwishoni pia naamini mtaweza kucheka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa kulikuwa kuna ile hoja ya madarasa 8,000 kuhamishwa, nadhani ilikuwa hoja ya Mheshimiwa Kunti. Napenda kutoa ufafanuzi kidogo kwenye hili. Katika yale madarasa 8,000 tulikuwa tunahangaika na changamoto ya wanafunzi 1,076,037 ambao wameanza Kidato cha Kwanza tarehe 9 mwezi Januari. Tulikuwa tuna siku 75 tu za kuweza kutekeleza mradi. Sasa kweli watu walituletea shule nyingine mpya, kwa nini badala ya madarasa haya manne, na haya manne kwa shule hii tunisiyaunganishe nipate madarasa nane nikajenge shule mpya moja? Kwa nini limeshindikana?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, tulipata mapendekezo ya shule 465, na ili shule iwe kamili inatakiwa iwe na walimu siyo chini ya 11. Kwa hiyo, tulitakiwa tuwe na Walimu wapya zaidi ya 5,115 ndani ya miezi miwili. Wote tunajua taratibu za ajira na masuala mengine, kwa muda huo isingeweza kupatikana, lakini vilevile miundombinu mingine siyo madarasa tu, kuna maktaba, maabara, pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu kwamba kupitia mradi wetu wa SEQUIP Februari hii mpaka June tutajenga shule 184 na tutaendelea kujenga shule nyingine zote za kata mpaka tufikishe idadi ya shule 1,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii ya Kamati na mapendekezo yote yaliyopendekezwa tutayatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetuwezesha sote kuweza kufikia hatua hii ambako hatimaye naweza kuhitimisha hoja hii ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, kipekee ninashukuru na ninakupongeza sana wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri ambao umetuwezesha na umewezesha Bunge lako Tukufu kuweza kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa weledi mkubwa sana. Aidha, nichukue nafasi hii kuweza kuwapongeza na kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote walioweza kuchangia hoja hii, takribani Wabunge 96 wameweza kupata nafasi ya kuweza kuchangia hoja hii, kwa kweli tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hakika maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge utatusaidia sana kuweza kupata mwelekeo wa kuweza kusimamia vizuri zaidi utekelezaji wa mpango wetu na bajeti kwa mafungu yetu yote 28 ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatimaye kuweza kuimarisha utoaji wa huduma zetu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa sijatenda haki na nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitaweza kuishukuru Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi pamoja na Makamu Mwenyekiti wake Mheshimiwa Nyamoga Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati kwa umahiri wao, kwa weledi wao na namna ambavyo wameendelea kushiriki katika kupendekeza na kutushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee napenda pia kuwashukuru Mawaziri wote ambao wameweza kuwa nami pamoja na wenzangu katika kuhakikisha kwamba tunaweza pia kuhitimisha hoja hii vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kipekee pia napenda kuwashukuru Wabunge wote, lakini zaidi pongezi. Pongezi mlizozitoa, naomba sana zimrejee Mheshimiwa Rais Wetu Mpendwa, ambaye ndiye ametuwezesha sisi kwa maelekezo yake na msukumo wake kuweza kuyafikia yote haya tuliyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi nashukuru kwa pongezi kwake mlizozitoa na kwa namna ambavyo nanyi pia katika mafanikio yote haya hayawezi kupatikana bila ninyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani, Watendaji mbalimbali katika ngazi zote za msingi, lakini bila kuwasahau Waheshimiwa sana Wakuu wetu wa Mikoa, Wakuu wetu wa Wilaya, Wakurugenzi wetu wote wa Halmashauri, Makatibu Tawala wetu wote wa Mikoa na wa Wilaya. Kipekee nawashukuru sana Wenyeviti wetu wote wa Halmashauri pamoja na Mameya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nitakuwa sijatenda haki endapo nitashindwa kuwashukuru Manaibu Waziri wangu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Wameweza kuonesha uwezo na umahiri Mkubwa. Nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Dugange kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiendelea kuifanya ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji. Vile vile nampongeza na kumkaribisha tena Mheshimiwa Ndejembi, hata kwa leo mmeona kwa muda mfupi tu aliokaa Wizarani, namna ambavyo yuko mahiri na ana weledi mkubwa sana. Kwa kweli nawashukuru, na bila ya wao kwa hakika nisingeweza kuwasilisha hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nitakuwa sijatenda haki nisipomshukuru Katibu Mkuu Ndg. Adolf Nduguru pamoja na Manaibu Katibu Wakuu wote, Dkt. Msonde, Dkt. Mahela pamoja na Dkt. Mtwale; Makamishina wote, Wenyeviti wote wa Bodi za taasisi zetu, na vile vile Watendaji Wakuu wa taasisi zilizoko chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wakurugenzi wote, na wafanyakazi wote walioko chini ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI)na taasisi zetu. Kwa kweli nawashukuru sana kwa kazi kubwa. Kwa hakika nadhani wenyewe wamejionea maandalizi waliyoyafanya na wameweza kuona matokeo.

Mheshimiwa Spika, zaidi tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Endapo kuna sehemu tutakuwa tumewakwaza, tunawaomba radhi, haikuwa nia yetu, na tutaendelea mwaka hadi mwaka kuweza kuboresha ili kufikia viwango na matarajio ambayo mnayo katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, naomba nisitaje majina moja moja, maana yake nikisema yote 96 niweze kutaja, nitakuwa sijatendea haki muda wako. Napenda tu kufanya muhtasari kwa hoja takribani 16 za aina mbalimbali zilizojitokeza. Ipo hoja ya Uboreshaji wa huduma ya elimu Msingi na Sekondari; kulikuwa kuna hoja kuhusiana na kukamilishaji wa maboma ya elimu na utoaji wa huduma za afya msingi; miundombinu chakavu ya shule za msingi na uhaba wa matundu ya vyoo na madawati; uhaba wa nyumba za watumishi katika ngazi ya elimu msingi na afya msingi; uimarishaji na ubora wa huduma ya afya ngazi ya msingi; maoni mbalimbali kuhusu kuanzishwa kwa daraja jipya au kundi jipya ambapo Halmashauri 56 wamo kuhusiana na wao kuchangia kiwango cha asilimia 20 katika miradi ya maendelo kutoka mapato ya ndani yasiyolindwa; na uhitaji wa watumishi na utaratibu wa ajira.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilihusu watumishi wanaojitolea; nyongeza ya posho ya Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa; hitaji la ongezeko la bajeti kwa ajili ya wakala wetu wa wa TARURA; wingi wa miradi isiyokamilika na ubadhirifu wa fedha; kuongeza bajeti kwa ajili ya uendelezaji ya miundombinu ya barabara; utekelezaji wa ahadi za viongozi; uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani; uimarishaji wa ukaguzi wa ndani; na ufuatiliaji wa tathmini ya miradi ya maendeleo na ufuatiliaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hayo maeneo niliyoyabainisha, kwa uchache, napenda sasa kuchukua nafasi hii kuweza kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali kama ambavyo zimetolewa na Kamati, na Waheshimiwa Wabunge katika kujadili Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya Kamati kupitia Mheshimiwa Londo ambapo walituelekeza kuona ni namna gani tunaweka vipaumbele na hasa katika matumizi ya fedha hizi za uwajibikaji wa makampuni yenye leseni katika HakiMadini au CSR. Vile vile kabla ya kupokea kwa fedha hizo, alishauri tuangalie vipaumbele, na kuona ni kwa namna gani fedha hizi zinaweza kutumika na kufanya tathmini kuhusu maeneo yote ambayo yamenufaika na fedha hizi; na pia kuwa na mwongozo mzuri wa matumizi ya fedha hizi za CSR.

Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema tunapokea ushauri na tunashukuru. Kwa kweli ni hoja ambayo wamekuwa wakiisemea kwa uzito wa kipekee na kwa kweli tumewaelewa na tunaiona hoja yao.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa utoaji wa fedha hizi za uwajibikaji wa Makampuni ya Madini katika jamii, unaongozwa na sheria kupitia kifungu cha 105 cha Sheria yetu ya Madini na hasa kifungu kile kidogo cha (2) ambacho kinaelekeza kabisa, kampuni ambayo itakuwa na HakiMadini inatakiwa iandae Mpango wa Mwaka wa Uwajibikaji wa Kampuni katika Jamii. Pia inatakiwa iandae kwa pamoja na Halmashauri husika ambako shughuli zile za madini zinafanyika. Baada ya hapo, wanatakiwa wawasilishe kwa kushauriana na Waziri anayesimamia masuala ya TAMISEMI pamoja na Waziri wa Fedha na hatimaye kwa baadaye inaweza kuidhinishwa kwa utaribu mahususi.

Mheshimiwa Spika, napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tunaendelea, na wiki mbili zilizopita tumepokea Mpango wa Mwaka kwa upande wa GGM kwa Halmashauri ya Geita Mji na Geita yenyewe. Tunaendelea kusimamia hilo kwa karibu, na niwahakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Wizara ya Madini tutaendelea kulisimamia suala hili kwa karibu sana.

Mheshimiwa Spika, tayari Wizara ya Madini imeanza kuandaa kanuni zinazosimamia suala zima la CSR, na vilevile sisi kama TAMISEMI tunaandaa Mwongozo mahususi utakaosimamia utekelezejai huu na lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza tija katika miradi inayotekelezwa tukitambua kwamba CSR hii haitakuwepo milele, na kwamba shughuli za madini hazitakuwepo pale milele. Kwa hiyo, ni lazima pia miradi inayoibuliwa kama vipaumbele na Halmashauri husika iwe kweli ni miradi mizito na miradi yenye tija ambayo kweli itaweza kuacha alama na itakayokuwa na manufaa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine ya Kamati katika upande wa mradi wetu wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP). Kwenye eneo hili tumekuwa tukitoa Shilingi milioni 470 kwa kuanzia kama awamu ya kwanza na awamu ya pili tunatoa Shilingi milioni 130 na tayari tumeshafanya ujenzi wa shule hizi katika maeneo mbalimbali na Majimbo yote mmeweza kupata, na tumeweza kujenga takribani Shule 231.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumeelekezwa na Kamati kuona ni kwa namna gani tunaweza kutafuta fedha zitakazoweza kuongezea kukamilisha majengo ambayo yatakuwa yalijengwa na hayajakamilika. Napenda tu kuwahakikishia Kamati na Waheshimiwa Wabunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaendelea kukamilisha tathmini ya kina ya gharama halisi zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa shule hizo na pia kuweza kutafuta fedha zitakazoweza kukamilisha ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja pia ya gharama za vifaa vya ujenzi au gharama elekezi. Tumeanza. Tulianza na darasa moja kwa Shilingi milioni 20. Maeneo mengine ilikuwa katika ujenzi wa vyoo ni Shilingi milionI 1.1, tumeiboresha sasa hivi ni Shilingi milioni 2.1. Katika madarasa, tumeboresha kikanda. Katika kanda saba tumefanya mapitio. Ukiangalia kuna maeneo mengine kutoka Shilingi milioni 20 tumepeleka Shilingi milioni 22 mpaka Shilingi milioni 26.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa hoja ya Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, lakini pia maeneo mengine kama ya Mafia, visiwa vya Goziba, Muleba na kwingineko.

Inawezekana pia bado kwenye moja, kwa mfano, Dar es Salaam ni kanda kweli ya Pwani, lakini ukiangalia Dar es Salaam na Pwani yenyewe inaweza ikatofautiana gharama. Pwani yenyewe pia, ukiangali Kibaha, Bagamoyo haiwezi pia kufanana na Mafia wala Rufiji kwa upande wa Delta. Kwa hiyo, pia na Ukerewe tunaipokea na tutaendelea kuifanyia kazi vizuri, lakini walau tumetoka katika hiyo 20 tunakwenda katika hiyo 22 mpaka 26 katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, yote hii ni michango yenu Waheshimiwa Wabunge, ndiyo imetuwezesha pia kuweza kufanya mapitio na marejeo ya gharama hizi. Tunawashukuru.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine ya suala zima la umuhimu wa upembuzi yakinifu. Tunaliona na hasa hufanywa kabla ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Ni kweli Kamati ilienda Mwanza kuangalia soko. Ukiangalia katika aina ya udongo ni lazima ufanye due technical investigations, tunaona na tunambua na tunashukuru kwa maoni yale. Vile vile tunaendelea kuweka umuhimu wa kuwa na hitaji la kufanya upembuzi yakinifu kabla ya kuweza kutekeleza miradi hii ili kuhakikisha kwamba miradi inavyotekelezwa inakuwa ni miradi ambayo haina changamoto mbalimbali na inakuwa kweli imezingatia maeneo husika lakini pia imeweza kuzingatia vigezo vyote vya kiutalaamu na kuhakikisha kwamba kweli tunawajengea timu zetu za Halmashauri uwezo na utaalamu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya matumizi au uwepo wa fedha ya bakaa. Mwaka wa fedha unaisha, lakini bado unajikuta miradi haijakamilika na fedha nyingine hazijatumika. Kwa mujibu wa Waraka Namba (1) wa Hazina, ukiangalia katika kipengele cha 4.3 kimeelekeza vizuri zaidi ni namna gani mwaka wa fedha unapoanza, mara tu baada ya bajeti kukamilika, inatakiwa wale ambao wamenufaika au wameelekezewa fedha za miradi wanatakiwa waziombe.

Mheshimiwa Spika, fedha za miradi ya maendeleo haziji tu. Baada ya kupitisha hapa kwenye Bunge. Mamlaka zote za Serikali za Mitaa hazitakiwi kukaa, zinatakiwa zipeleke maombi. Mikoa yetu haitakiwi kukaa, inatakiwa ipeleke maombi, na vile vile Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama walivyo wanufaika wengine wa bajeti, hawatikiwi kukaa, ni lazima waziombe Hazina. Hazina hawawezi kukuletea fedha bila wewe kuziomba.

Mheshimiwa Spika, sasa tumezielekeza Ofisi zetu za Mikoa kuhakikisha wanaunganisha maombi yote kutoka katika Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kupitia kila Halmashauri. Tunapoanza Julai mosi, tunaziwasilisha kwa Katibu Tawala wa Mkoa ambaye atapeleka kwa Wizara yetu ya Fedha akiwa na maombi na mchanganuo wote wa fedha wa Mkoa husika na Halmashauri zake ili kuhakikisha kwamba Hazina wanapata nafasi ya kufanya uchambuzi wa kina na makini. Lengo ni kuhakikisha kwamba Hazina wanatuletea fedha mapema na kwa wakati, na ziweze kutoa muda wa kutosha pia na nafasi, ili kuwa na utekelezaji mzuri na wenye ubora wa miradi yetu. Badala ya kuletewa fedha mwezi wa Nne, mwezi wa Tano, na hapo una mradi wa maendeleo, mwingine ni wa ujenzi, kwa hakika ni lazima hela itabaki na utakuwa na bakaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuanzia Julai mosi, na niliwambia mikoani tutaendelea kuwapima na hiki kitakuwa ni kigezo, nani amewasilisha, nani hajawasilisha? Ulipata lini? Endapo ulipata mapema na hujaweza kukamilisha mradi kwa wakati, kwa hakika ni lazima watakwenda na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia kuna hoja ya kufanyia maboresho Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma ambazo kwa mfumo na muundo na hasa katika majukumu ya Serikali za Mitaa ni lazima Sheria hii ya Fedha iangalie kwa majukumu yake. Serikali kuu namna ambavyo wanatumia fedha na muundo wake hauwezi kufanana na Serikali zetu za Mitaa. Kwa hiyo, na yenyewe pia tutawasilisha Wizara ya Fedha. Tunapokea ushauri huu mzuri ili kuweza kuona ni kwa namna gani suala hili pia linaweza kutatuliwa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kumalizia maboma yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ili kuondoa hasara inayoweza kupatika. Kwa kweli kwenye hili nawashukuru sana wananchi wa maeneo mbalimbali kwa namna ambavyo wamejitolea. Zaidi nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge kupitia Mifuko yenu ya Majimbo, mmeweza kuunga mkono na kuweza kupeleka fedha kuhakikisha kwamba majengo haya yanamalizika na kuwa na ubora. Siyo hivyo tu, mmetoa hata fedha zenu binafsi na wadau wengine mbalimbali. Kwa hakika kwa niaba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nawashukuru wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha uliopita, miaka miwli 2020/2021 na 2021/2022 tuliweza kutenga kama Serikali takribani Shilingi bilioni 280.35 ambazo zimetumika kumalizia maboma ya madarasa, mabweni, mabwalo na vituo vya afya kama 52 pamoja na zahanati zaidi ya 1,419. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwa mwaka huu wa 2023/2024 tumeweza pia kutengewa fedha takribani Shilingi bilioni 20.56 ambapo tutaweza kukamilisha maboma ya zahanati zaidi ya 376, mabweni 10 pamoja na miundombinu mingine mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na mikoa yetu na Halmashauri tumefanya tathmini ya mahitaji halisi ya maboma ambayo hayajakamilishwa pamoja na yale yanayoendelea kujengwa kwa upande wa afya na elimu ili kuweza kuyawekea mkakati wa kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna hoja ya Kamati pia kuona kuna umuhimu wa watendaji wetu wa kata kuweza kupata mafunzo ya awali kuhusiana na utumishi wa umma, masuala ya usalama, masuala ya huduma za kijamii ni namna gani wanatakiwa waenende na wawe taswira katika jamii zetu ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na uwajibikaji mzuri zaidi katika ngazi zetu za vijiji na kata. Napenda kuihakikishia Kamati na Waheshimiwa Wabunge kwamba katika Bajeti hii 2022/2023 inayomalizika Juni, tumetenga fedha na tutahakikisha kwa kuanzia, tutaanza na mafunzo kwa Watendaji wa Kata 1,936 na tutaendelea kutoa mafunzo hayo pia kwa awamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna hoja kuhusiana na mradi wa KKK wa Kupima, Kupanga na Kumilikisha ambapo Halmashauri zetu zilitengewa takribani Shilingi bilioni 49.47.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, napenda tu kuwaambia kwamba fedha nyingi zilielekezwa katika kupima viwanja na tuliweza kufanikisha upimaji kwa takribani ya asilimia 91.37. Hadi kufikia mwezi Februari mwaka 2023 tumeweza kurejesha takribani shilingi bilioni 16.75, kati ya fedha iliyotolewa ambayo ni asilimia 33.85. Pia tumetoa ukomo kwamba ifikapo tarehe 31/10/2023 ni lazima fedha hizi zote ziwe zimerejeshwa Serikalini, na vile vile kuhakikisha kwamba zinazopatikana basi haziwi sehemu ya mapato ya ndani ya Halmashauri na badala yake ziwe ni sehemu ya fedha za mradi unaojitegemea, na zirejeshwe katika utekelezaji na uendelezaji wa mradi huo wa Kupima, Kupanga na Kumilikisha.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja pia ya kuendelea kuzijengea uwezo Halmashauri zetu katika kuandaa maandiko ya miradi ya kimkakati ya kuona ni kwa namna gani tunafanya tathmini ya marejeo ya mapitio ya mwongozo wa miradi ya kimkakati ili kuona sasa katika mwongozo tulionao sasa tunautatua vipi?

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako kwamba tumeendelea kufanya zoezi hili, tunashirikiana na Wizara yetu ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi ya UNCDF na tayari tunayo tume au timu ya kitaalamu ya kitaifa kwa ajili ya kujenga uwezo wa Mikoa yetu na Halmashauri na hasa katika suala zima la uandishi wa miradi ya kimkakati. Tayari tumeanza kutoa mafunzo katika timu zetu za kitaifa, ambayo yameshirikisha watendaji wa Mikoa na Halmashauri, na tayari takribani Mafisa zaidi ya 281 wameshapatiwa mafunzio hayo katika Mikoa na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, wakiwemo Makatibu Tawala Wasaidizi wa sehemu ya Mipango na Uratibu katika mikoa yote 26.

Mheshimiwa Spika, vile vile, tunaendelea kutekeleza maelekezo ya Kamati ya kufanya marejeo ya vigezo vya Mwongozo wa Miradi ya Kimkakati ili kuona ni kwa namna gani tunahuisha vigezo hivyo na kuziwezesha pia Halmashauri zetu nyingi zaidi kuweza kukidhi vigezo hivyo kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Kimkakati.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya TARURA kutokuwa na ofisi za kutosha. Ni kweli; tayari wameshaanza mkakati wa kujiandaa kuendelea kupata viwanja katika Halmashauri zetu, na vile vile mkakati wa ujenzi kuhakikisha kwamba Ofisi zote za TARURA zinamilikiwa na TARURA yenyewe.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya upungufu au changamoto ya ukosefu wa magari. Mpaka sasa TARURA ina magari takribani 282 na kati ya hayo tumeendelea kununua 245 tayari tumeshayapokea na mengine tumeshaanza kuyagawa. Hadi sasa upungu wa magari tulionao ni takribani magari 177. Kama Serikali tumeendelea kuyapangia bajeti. Nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi, TARURA Wilaya ya Lushoto itapewa kipaumbele katika magari ambayo tunayasubiri, lakini vile vile tutaangalia na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya kaka yangu Mheshimiwa Deo Sanga Mzee wa Mabii na Matrilioni. Kwa upande wa soko lao la Kituo cha Mabasi ya Makambako, nimhakikishie kwamba Halmashauri yetu ya Makambako ni moja ya Halmashauri ambazo zitanufaika na Mradi wa TACTIC ambao unanufaisha Miji, Majiji na Manispaa 45. Kwa upande wetu wa Makambako, tumeitenga katika awamu ya tatu ya TEA III lakini kubwa niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge wote, kabla ya 2025 mradi huu utakuwa umekwishaanza kwa hatua mbalimbali kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Spika, nami pia ni mwanasiasa ndugu zangu, siwezi kukubali suala hili likapita kipindi hicho ukikaribia uchaguzi, halafu miradi hii haijaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kubwa niwatoe hofu, lazima hili litaanza. Iwe iwe mvua, iwe jua, iwe nini tutahakikisha hili inatekelezeka. Lakini pia Mheshimiwa Rais amenielekeza kulisimamia suala hili kwa karibu zaidi, na tarehe 15 mei tunaanza kutangaza kuna baadhi ya zabuni kwa ajili ya usanifu zitaanza kufanyika, na tunaamini ndani ya muda mfupi sana mtaweza kuona mambo mengi zaidi yakifanyika kwenye mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Rashid Shangazi na wengine, kwamba fedha zinazotolewa na Mfuko wa Barabara zinachelewa kutolewa na matokeo yake imesababisha baadhi ya wakandarasi kutoomba zabuni za utekelezaji wa barabara. Nipende tu kumwambia Mheshimiwa Shangazi na Waheshimiwa wengine, kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI tunapokea ushauri na tutafuatilia ili kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatolewa mapema zaidi na kwa wakati. Wizara ya Fedha imekuwa ikijitahidi kuweza kuzitoa mapema. Tutaendelea kuona ni kwa namna gani wataongeza kasi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya DMDP; Mheshimiwa Bonnah Mheshimiwa Chaurembo Mheshimiwa Jerry Silaa na wengine wote wa Dar es Salaam. Ni kweli tunatambua Dar es salaam bado kwa kiasi kikubwa ina miundombinu mibovu, lakini nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wenzake, kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunatarajia kuanza utekelezaji wa BMDP awamu ya pili, na halmashauri zote tutaanza Dar es salaam zitanufaika na mradi huo ambao utajumlisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, mifereji mikubwa ya barabara, ya maji ya mvua, madaraja na miundombinu ya usimamizi wa taka ngumu. Hadi sasa mradi uko katika hatua za mwisho za kupata wataalamu washauri wa usanifu wa miundombinu ya kipaumbele; lakini pia kuweza kuandaa nyaraka muhimu zikiwepo za masuala ya kijamii, mazingira pamoja na mengine.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kufanya mashauriano na majadiliano ya mwisho na Benki ya Dunia, lakini hiyo haizuii hatua zingine kuendela. Kama tulivyoeleza zaidi ya asilimia 36 ya miradi ambayo imekusudiwa usanifu wake unaanza na tayari tunakusudia gharama yake itahusisha kama takribani kilomita 174 katika utekelezaji wa mradi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Chaurembo ya kuunganisha barabara nyingi za Dar es salaam kutoka eneo moja na lingine ili kuona ni kwa namna gani tunapunguza msongamano. Nimshukuru kwa hoja hiyo na nimhakikishie kwamba tunapokea ushauri na tutatumia vyanzo mbalimbali vya fedha ili kujenga barabara za kuunganisha sehemu mbalimbali za mkoa wa Dar es salaam na kupunguza msongamano. Tumefanya hivi kupitia mradi wa DMDP wa awamu ya kwanza na tuatafanya hivyo na DMDP wa awamu ya pili na DART katika halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaam na katika miradi ya ujenzi wa barabara zinazotumia fedha za ndani.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Chumi kuhusuiana na kuona ni namna gagi tunasaidia haswa wakandarasi wa ndani kwa kuwajengea uwezo au pia hata kuona namna au umuhimu wa kuwapa udhamini ili waweze kupata mikopo ya mitambo; lakini pia kuona ni kwa namna gani TARURA kila kanda itakuwa na mitambo yake ambayo itakuwa inakodishwa kwa wakandarasi na baadaye wakandarasi wetu hawa wazawa waweze kukatwa kutokana na malipo. Nipende kusema tu kwamba tunapokea ushauri huu, Serikali itafanya tathmini ya pendekezo hili kabla ya kuanza kulitekeleza.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya hospitali kongwe katika mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na kwamba zimechakaa, sana na zinahitaji kufanyiwa ukarabati. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tayari kwa mwaka huu tnaoumalizia tulitenga zaidi ya shilingi bilioni 16.65 na tumeweza kukarabati zaidi ya hospitali 19. Lakini katika mwaka ujao wa fedha tutakarabati takribani hospitali kongwe 31, na tumeshazitengea takribani shilingi bilioni 27.9.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya magari ya wagonjwa. Niwape habari njema Waheshimiwa Wabunge wetu; tuliagiza magari 527; na nipende kusema ilikuwa yawe ni magari 407 lakini kwa uzarendo na kwa kushirikiana na Wizara yetu ya Afya na UNICEF, badala ya kupata magari 407 kwa mbinu tulizozitumia tutapata magari 528. Kwa hiyo tumeokoa zaidi ya magari 121 ambayo endapo tusingetumia utaratibu huu hayo magari yasingepatikana. Kwenye hili Waheshimiwa Wabunge kila halmashauri itapata magari mawili ya kubebea wagonjwa na itapata gari moja kwa ajili ya suala zima la usimamizi na uratibu wa miradi ya afya katika halmashauri zao. Kwa hiyo kwenye hili naulizwa na Mheshimiwa Hawa Mwaifunga hapa ni lini; nimpe habari njema nafuatilia kwenye simu bill of lobing tangu tarehe saba magari yameshafika bandarini. Yako yaliyofika tarehe 14 na yako yanayoingia tarehe 21, na vivyo hivyo mpaka tumalize magari 528. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa yaliyo katika ukomboaji ni magari 55, hardtop kadhaa taktiban 30 na ambulance 25 tayari zimeshaanza kukombolewa; lakini kubwa kuliko yote kila mmoja atapata kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya suala la hospitali mbalimbali; kwa Muleba, Mbulu na kwingineko. Niwahakikishie Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Massay na wengine wote, kwa zile fedha za vituo vya afya ambazo zilikuwa hazijapelekwa tutahakikisha fedha hizo zinapelekwa kwa wakati ili kuendeleza miradi iliyoanza lakini vilevile kwa ile ambayo ilikuwa haijaanza; yote tuliyoahidi fedha hizo zitapelekwa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya shule za msingi kuchakaa hali ambayo hata imepelekea mdondoko wa wanafunzi wetu na kupunguza ufaulu. Nipende kuwahakikishia kuwa tayari kupitia mradi wetu wa kuimarisha elimu ya awali na msingi kupitia BOOST tumetenga shilingi bilioni 230 kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kati ya sasa, Aprili na Juni bilioni 230, hapo vipi? Na mmeona wenyewe barua, si maneno, na tayari wiki hii fedha hizo tutaziwasilisha katika halmashauri zenu. Kubwa ninalowaomba Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine, nawaomba; kwa kuwa mradi huu wa bust ni wa lipa kwa matokeo, itakapofika tarehe 30 juni ni lazima fedha hizo bilini 30 kila mmoja kwenye jimbo kadri alivyopangiwa basi ni lazima ziwe zimekamilika na ujenzi uwe umekemilika na matokeo yaweze kuonekana. Tukija mwezi julai baada ya kufanya mapitio na tathmini kadri utakavyokuwa ume-deliver fedha nyingine zaidi zitaweza kujitokeza katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya walimu waliomaliza vyuo wapewe mwaka mmoja wa kujitolea kabla ya kuajiriwa, tunapokea ushauri. Serikali inaendelea kufanyia kazi suala hili ili kuweza kupata mwongozo wa utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Mussa Sima lakini vilevile illikuwa ni hoja ya Ndugu yangu Mheshimiwa Sekiboko, na nitaomba kidogo hii niisemee. Jukumu la Wizara ya Elimu ni pamoja na kutengeneza Sera ya Elimu Mitaala, Sheria ya Elimu na mitaala yetu iweje pamoja na Mihutasari jukumu la Ofisi ya Rais TAMISEMI kama mtekelezaji ni kusimamia utekelezaji ili umahiri wa watoto wanotarajiaa waupate waweze kuupata. Lengo letu ni kumtengeneza mwanafunzi awe na ile sura kama ambavyo wizara ya imetuelekeza.

Mheshimiwa Spika, na Sera yetu ya Ugatuaji wa Madaraka iko wazi kabisa; Wizara ya Elimu inafanya nini mpaka wapi, Ofisi ya Rais TAMISEMI inafanya nini mpaka wapi hatuwezi kuwa na shule tukazisimamia halafu tukasema sisi tuna majengo tukaacha, hilo halitawezekana na liko wazi kabisa. Kwa hiyo nipende kusema tu kwa lugha nyepesi sana Wizara ya Elimu ni msanifu halafu Ofisi ya Rais TAMISEMI sisi sasa tunajenga kile tulichoelekezwa kusanifu mtoto wa Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja katika mkataba wa utendaji kazi au performance contract, kwamba zimewasumbua walimu na mambo mengine kadhaa wa kadhaa. Nipende kusema, kwamba tulijipangia makataba wa kuboresha elimu nchini ambao umepitishwa mwezi wa nane mwaka jana ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu; na Katibu Mkuu Naibu Katibu Mkuu wa Elimu ambaye kwa sasa ndio Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu pia alishiriki kama Mgeni Rasmi katika hatua moja wapo wakati mkutano huu.

Mheshimiwa Spika, tulichokifanya katika mkataba wa utendaji kazi ni kutafsiri ule mkakati wetu wa kuboresha elimu Tanzania. Kwamba tunataka elimu ya aina gani katika msingi na sekondari. Yako majukumu ambayo tumewapatia walimu wetu. Mwalimu ana jukumu la kujenga umahiri na stadi mbalimbali kwa ajili ya watoto wetu, hawezi akaachwa hivi hivi, kwa hiyo hakuna kipya kilichofanyika. Tumeangalia mdondoko wa ufaulu, tumeutafsiri, ni lazima na sisi kama Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu tuje na mkakati; na ndio maana tukaja na ule mkakati.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili mtaona maafisa wetu wa elimu wilaya na mkoa pia hawakai ofisini, wanatoka huku na ule kuhakikisha kwamba kila wiki wanaenda kukagua katika shule zetu ili kujiridhisha na kile ambacho kinafundishwa katika shule zetu. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na uimara katika stadi ambazo tunataka kweli wanafunzi wetu wapate; na kubwa tuliangalia zile changamoto, tuliangalia dosari mbalimbali zilizopo nza kuhakikisha kwamba tunaqweza kuzirekebisha.

Mheshimiwa Spika, moja ya mafanikio ya haya, huku nyuma kulikuwa kuna changamoto pia hata katika kiwango cha uandikishwaji, lakini kwa sasa kupitia mkataba huohuo wa utendaji kazi unaosemwa na mkakati wa uboreshaji wa elimu walau katika elimu ya awali tumeweza kufikia uandikishwaji wa awali asilimia 109, na hata tumeweza kuvuka hata lengo lilokuwa limepangwa.

Mheshimiwa Spika, kwa darasa la kwanza uandikishwaji ni asilimia 108 na kwa upande wa kidato cha kwanza tumeweza kufikia asilimia 93. Mkakati huu pamoja na mkataba huo wa utendaji kazi ndio umetewesha kuweza kufikia mafanikio hayo ndani ya muda mfupi sana. Kwa hiyo nipende tu kusema kwamba hakuna kikubwa katika mkataba huo wa utendaji kazi. Wadau wote wa elimu wana majukumu; kama wazizi wana majukumu yao kama wanafunzi wana majukumu yao, walimu wana majukumu yao, jamii ina majukumu yake; lakini na mwalimu naye jukumu lake kubwa ni kujenga umahiri katika mazingira ya watoto wetu. Kwenye eneo hilo niliona niliwekee mkazo kidogo ili kuonesha kwamba kwanza hakuna kitu kipya. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha tu kwamba tunaborsha kiwango chetu cha elimu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya ajira watendaji wa vijiji, kwamba haitoshi. Nipende tu kuwakikishia Wabunge wetu kwamba tutaendela kuajiri. Kwa sasa tuna upungufu wa watendaji wa kata 262, kwa upande wa mtaa tuna upungufu wa watendaji wa mtaa 2,864, lakini vilevile kwa upande wa vijiji nako kuna upungufu wa watendaji wa vijiji 1,773. Kama Serikali tutaendelea kuajiri watendaji wa kata vijiji na mtaa kulingana na namna Serikali itakavyoendelea kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya halmashauri nyingi kukosa wahandisi ambao wamekuwa hawapo kwa ajili ya kusimamia miradi. Nipende kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari Mheshimiwa Rais ameshaelekeza tupate kibali cha watumishi takribani 250 wahandisi 100 wakadiriaji majengo 100 na vilevile maafisa manunuzi 50. Lengo letu kubwa ni kuona ni namna gani watumushi hawa wapya wataweza kusimamia shughuli za ujenzi wa miradi inayotekelezwa ili kuimairisha tawala zetu za mikoa lakini pia kuhakikisha tunakuwa miradi ya maendeleo ambayo ina kidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ambayo ilikuwa ina wachangiaji wengi sana, kuhusiana na walimu wanaojitolea wapewe kipaumbele katika ajira. Kwenye hili naomba unilinde kidogo endapo dakika zitakata basi walau kuna hoja kama mbili na nyingine moja ikikupendeza basi walau kidogo kunipa upendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja hii kwanza niwashukuru Wabunge kwa kulileta, lakini la pili niseme kwamba tunatambua uwepo wa walimu wanaojitolea kufundisha katika shule za msingi na sekondari katika mamlaka zetu za Serikali za mitaa. Uwepo wa walimu hawa umesaidia sana kuweza kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu katika baadhi ya shule za msingi na sekondari nchini.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kuwatahadharisha au kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba hadi sasa hatuna mfumo ulio rasmi unaotumika kuwatambua na kuwa na taarifa za walimu wanaojitolea. Hivyo basi kwa sababu hii baadhi ya walimu na hata kwa upande wa sekta ya afya wamekuwa wakipata nafsi ya kujitolea kweli lakini wapo wengine ambao walitamani wazipate pia lakini hawajawahi kuzipata nafasi hizi. Wamekuwa wakikosa nafasi katika shule lakini vilevile katika vituo vya kutolea huduma za afya ambako kuna mahitaji hayo. Kukosekana kwa mfumo au utaratibu huo ulio rasmi na uliowazi bado unaweka ombwe kati ya walimu na watumishi wengine wa sekta ya afya waliohitajika kujitolea kupitia uongozi wa shule au kupitia uongozi wa kituo cha kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi tunaandaa utaratibu mahususi na maalumu wa kuweza kutumia mifumo yetu ya kielektroniki kupitia Wizara yetu ya Afya, tunashirikiana pia na Wizara ya Elimu; tuone ni namna gani, kwa mfano upande wa sekta ya elimu; hivi waombaji wataomba vipi, kanzidata itakuwa vipi, hawa walimu wanaojitolea katika shule zetu watakuwa na utendaji wa aina gani na watafuatiliwaje, na taratibu zingine kadhaa wa kadhaa. Nipende tu kusema baadhi ya mnaeneo unaweza ukaangalia, labda Kinondoni, waombaji ambao wameomba katika sekta ya afya 150 lakini unakuta wengine pia haukuwa wazi labda wamepata 50 tu au 100.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kwamba katika mchakato huu tulionao sasa kwanza tutaanza na ajira za 2015 waliomaliza shule mwaka 2015; na tunaangalia maeneo matatu tu vigezo vyetu vikubwa. Kwanza mwaka wa kuhitimu, la pili kwa elimu ni masomo, na kwenye hili labda niliweke wazi ni masomo ya aina gani inawezekana wengine hawayajui, ni masomo ya sayansi, ukiangalia fizikia, chemistry, biology lugha ya kiingereza lakini pia English in literature na wale wataalamu wetu wa ufundi katika maabara zetu za sayansi.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hilo tutaanza kwanza na mwaka wa kuhitimu. Na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, na kwenye hili kwa kweli niwaondolee lawama zote Waheshimiwa Wabunge, wala wananchi wenu wasiwahukumu kwamba labda hukumsaidia mtu au lolote. Mimi niwape comfort, binafsi hata katika vigezo vyote mpaka kufika hapa tulipofika na mimi mwenyewe na Manaibu wangu na uongozi mzima wa wizara tumekuwa karibu hatua kwa hatua. Lakini sisi pia ni viongozi, hatutataka kuharibu au kuchafua majina yetu; tutahakikisha kwa nguvu zetu zote tunasimamia kuhakikisha kwamba zoezi hili linafanyika kwa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtakubaliana na mimi hata wengine wakinitumia zingine meseji hata sizijibu. Wako hata viongozi ambao wamenipigia simu na nimesema siangaliii kiongozi siangalii nani ni nani, tunatenda haki. Kwa sababu tusipofanya hivyo ndugu zangu mtu asiyemjua mtu tutajenga taifa ambalo huko mbele tutapata shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe binafsi nami ni mwanasisasa yako maeneo ninakotoka wako wengine ni ndugu zangu nimewaambia nenda kwenye mfumo na wala sihitaji hata kupata cheti chako; nenda kwenye mfumo. Kwa hiyo nataka kutoa comfort leo hii jioni tarehe 18 haki itatendeka. Na hata juzi na jana nimerejea tena kwa watendaji Ofisi ya Rais TAMISEMI, kama hata kulikuwa kuna chembe ya aina yoyote ya kutoaminika kwa mtu kwenye eneo hili kuna watu watakwenda na maji, kwenye eneo hili kuna watu watapata mashtaka ya jinai, na ndiyo maana kila hatua unavyoona nikitangaza matangazo nawaambia jamani watu wasitapeliwe watu, wasiahidiwe fedha kwa sababu atakayestahili ndiye atakayepata lipo jopo linalopitia na hata mimi mwenyewe nimewaambia tunafunga matangazo tarehe 25, tarehe 27 baada tu ya muungano mimi mwenyewe nitaenda pia kwenye mfumo kuona mchakato ulivyofanyika na jina kwa jina.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungmzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri dakika mbili malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwenye hili nimeona nieleze kwa kina na ni vivyo hivyo kwa watendaji wengine wa afya katika suala zima la ajira hizi.

Mheshimiwa Spika, kwa dakika nikuombe kwenye ile hoja ya makundi ya zile halmashauri 56 ambazo zimewekwa katika halmashauri kundi la asilimia 20. Walikuwa wanatakiwa kutoa asilimia 40 ya mapato ya ndani yasiyolindwa lakini sasa wamewekwa katika asilimia 20.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru Wabunge waliochangia hoja hii na wamechangia kwa hoja nzito. Ninipende kuwatoa hofu, lengo la Serikali limekuwa ni zuri. Tuliwaweka kwenye asilimia 20 kutokana kwamba uwezo wa halmashauri haulingani. Ziko halmashauri ambazo zingine hazikuweza kupeleka hata yale mapato ya mikopo ya asilimia 10, wamepeleka asilimia saba, hawakufikia asilimia kumi. Wako ambao katika miradi ya maendeleo badala ya asilimia 40 wamepeleka asilimia 33 na hata pungufu.

Mheshimiwa Spika, pia wako ambao hata walipelekea kuto kulipa stahiki sahihi za madiwani. Lakini si hilo tu wakati wa hitimisho la kazi na Waheshimiwa Madiwani kwa mwaka 2020 ziko halmashauri zaidi ya 20 bado kuna deni la shilingi bilioni 3.05 ambazo madiwani walikopa walikuwa wnatakiwa kukatwa na halmashauri lakini halmashauri hazikuweza kuwakata zingine kwa sababu ya madeni mbalimbali na hatimaye sasa hivi tunajikuta TAMISEMI na Serikali tunaubeba mzigo huu, na tumeshindwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lengo letu ilikuwa ni kuwapunguzia mzigo halmashauri zile 56 ili walau waweze kuapata unafuu lakini tumewasikia wamelisema kwa hisia za kipekee suala hili. Sisi tuwaombe wabaki kwenye hiyo 20 lakini endapo bado wanaona kuna haja basi tutaendelea kushauriana ndani ya Serikali na Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla wake. Ili kuweza kuona sasa ni nini kifanyike warudi tena kwenye asilimia 40 au wawekwe katika kundi la asilimia ngapi.

Mheshimiwa Spika, lengo letu lilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunawapunguzia mzigo ili shughuli mbalimbali za kuendesha halmashauri ziweze kwenda vizuri. Stahiki mbalimbali za viongozi wa kisiasa katika halmashauri zao na watumishi wa umma ziweze kwenda vizuri lakini na wao pia waweze kutekeleza majukumu mengine kama ambavyo wamekasimiwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru kwa nafasi lakini zaidi niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna walivyochangia hoja yetu na kwa kuzingatia maeneo hayo, niwashukuru sana na nipende kuseme naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nianze kwa kuunga mkono mapendekezo haya ya Bajeti Kuu ya Serikali lakini kipekee nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais lakini vilevile kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu Waziri na uongozi mzima wa Wizara ya Fedha kwa kuona umuhimu wa kuja na mapendekezo haya, mapendekezo ya kimapinduzi, mapendekezo ya kimaendeleo lakini vilevile mapendekezo ya Bajeti ambayo yameangalia makundi mbalimbali pamoja na sekta zote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Bajeti hii ni Bajeti ambayo inataka tuelekee zaidi katika kujitegemea. Ukiangalia zaidi ya takribani shilingi trilioni 31.38 zitatokana na mapato ya ndani. Kwa kweli ni hatua kubwa sana na nitoe pongezi sana kwa Wizara nzima ya Fedha chini ya Mheshimiwa Waziri kwa kuja na mapinduzi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nishukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hii na ambao wameweza kugusa katika maeneo ambayo Ofisi ya Rais TAMISEMI tunayasimamia katika utekelezaji. Kulikuwa kuna hoja ambayo ilijitokeza huu mchango kuhusiana na utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo ya 10% katika halmashauri zetu kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuhakikisha kwamba mfumo huo mpya unaopendekezwa basi uwe ni mfumo rafiki kwa walengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tayari kikosi cha wataalamu kinaendelea kufanya uchambuzi na mapendekezo na kimeweza kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kweza kupata maoni zaidi na pindi utaratibu mpya utakapokamilika basi tutaweza kuutangaza na utoaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo utaweza kuendelea. Niwahakikishie kwamba azma yetu ni kuhakikisha kwa kiasi kikubwa inakuwa ni mfumo ambao utakuwa na ufanisi lakini mfumo ambao utakuwa rafiki ambao utaweza kuwasaidia vijana wetu, wanawake na watu wenye ulemavu kuweza kuendeleza shughuli zao mbalimbali za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mchango kuhusiana na TARURA kuweza kuongezewa fedha. Kwanza nipende kumshukuru sana Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa mapendekezo ya nyongeza ya takribani shilingi bilioni 350. Mtakumbuka mwezi wa nne Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipowasilisha Bajeti yake hapa tuliweza kuwasilisha Bajeti ya takribani shilingi bilioni 855.37 kwa ajili ya TARURA na ukiangalia tangu miaka miwili Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alipoingia madarakani tulianza na Bajeti ya shilingi bilioni 275.03. Mwaka huu tumeweza kuwasilisha hapa Bajeti ya shilingi bilioni 855.37. Utaona ndani ya miaka miwili tu peke yake takribani mara tatu mpaka mara nne Bajeti imeongezeka lakini hiyo haikutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais bado akaweza kumuelekeza Waziri wa Fedha na wataalamu wake wakafanya uchambuzi na wametuletea mapendekezo ya nyongeza ya shilingi bilioni zingine 350 ambayo endapo Waheshimiwa Wabunge mtapitisha Bajeti hii basi TARURA kwa Mwaka huu wa Fedha wa 2023/2024 itakuwa ina Bajeti ya shilingi trilioni 1.235. Sasa hebu angalia kwa miaka miwili nyuma ilikuwa na Bajeti ya shilingi bilioni 275, nani kama Mheshimiwa Rais Samia? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hakuna.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kwa kweli nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa usikivu wake lakini zaidi kwa ushirikiano na kuweza kutambua umuhimu wa barabara katika maeneo yetu lakini namna ambavyo tutaweza kufungua maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa na vikwazo. Tutajenga madaraja ya kutosha, tutaweka vivuko lakini vilevile tutahakikisha kwamba tunakuwa na barabara ambazo zinapitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika nyongeza hiyo tutajitahidi kwa kiasi kikubwa kuweza kuweka nyongeza katika fedha ile ya Jimbo ambayo kila Mbunge alikuwa akipata. Tutaongeza shilingi milioni 500 nyingine ya ziada ili kuhakikisha kwamba maeneo yenu mengi zaidi yanaweza kupitika na kuweza kufunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia pia mapendekezo kwa kiasi kikubwa Waheshimiwa Wabunge wakihoji ahadi mbalimbali za Viongozi wa Kitaifa. Tumeweka pia walau fedha za kutosha katika eneo hilo kupitia nyongeza hii ya Bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri Fedha amependekeza ya shilingi bilioni 350. Kwa hiyo, niendelee kuweka msisitizo tunaomba Waheshimiwa Wabunge waweze kuiunga Bajeti hii mkono na yote haya yametokana kwa kweli na mapendekezo yao kwa namna mbalimbali na vipaumbele vyao kwa kweli niwahakikishie tumekuwa tukivipokea na tutaweza kuvifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kweli nikushukuru sana sana sana na timu yako. Umeturahisishia kazi yetu kubwa na ninaamini haitaishia hapa na ninaamini na mwaka kesho pia mtaendelea kutuangalia katika nyongeza ya Bajeti ili walau sasa TARURA tuendelee kufikika zaidi kwa wananchi, TAMISEMI ya wananchi lakini zaidi wananchi wetu kule na sisi tutakuhakikishia Mheshimiwa Waziri tutakuonyesha kwa vitendo. Barabara hizi tutazielekeza katika maeneo ya uwekezaji, katika maeneo ya kiuchumi, katika maeneo ya uzalishaji ili kuhakikisha kwamba na ule mfuko pale ulipo punguza basi tuweze kukuongezea fedha nyingi zaidi na tuweze kuonyesha matokeo chanya kupitia Bajeti hii na nyongeza mliyotupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kuongeza idadi ya shule za kidato cha tano na cha sita. Nipende kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tumeendelea kupokea mapendekezo mbalimbali na kwenye hili pia tena niweze kuwashukuru sana Wizara ya Fedha kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo tumeona fedha nyingi zimeendelea kutolewa. Tutakuwa na takribani zaidi ya shilingi bilioni 248.5 ambazo tutazielekeza katika kuongeza miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na shule nyingi za kutosha za kidato cha tano na cha sita. Kwenye hili pia nimshukuru Waziri wa Elimu kupitia Kamishna wa Elimu ambao walipopata mapendekezo mbalimbali ya kupandisha hadhi shule ambazo unakuta zilikuwa hazijafikia vigezo baada ya kuweka miundombinu basi wamekuwa tayari kuweza kupandisha hadhi shule hizo tunashukuru pia nao sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Asenga. Alitaka kuweza kuona Serikali inatoa tamko na haswa katika usafirishaji wa mazao yaliyo chini ya uzito wa tani moja. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kupitia jedwali la kwanza la Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa sura ya 290 imeweka zuio la kutokutoza ushuru wa mazao kwa mzigo wenye chini ya tani moja unaosafirishwa kutoka halmashauri moja kwenda nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kusisitiza tu katika halmashauri zote ziweze kufuata masharti ya jedwali hili la kwanza la Sheria hii ya Fedha ya Serikali za Mitaa na tusije tukaleta usumbufu kwa wananchi wetu mbalimbali ambao wanasafirisha idadi hiyo ndogo ya mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa kuhitimisha niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wote tumesikia hoja mbalimbali kuhusu hitaji la watumishi. Tuendelee kuwahakikishia kwamba tutaendelea kupeleka watumishi kwa kadiri Bajeti ya Serikali itakavyokuwa ikiendelea kuruhusu na niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tayari tumeshapeleka takribani watumishi wa afya 5,319 na tunakamilisha mchakato wa ajira zingine 2,751 na pindi watumishi hawa watakapopatikana pia tutaweza kuwasambaza katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya katika halmashauri zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vifaa vya afya na vifaatiba. Nimewasikia Waheshimiwa Wabunge tumetenga katika mwaka ujao wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 116.92 ambazo tutaweza kuzisambaza katika hospitali zaidi ya 31, katika vituo vya afya 278 pamoja na zahanati mbalimbali 367 nchini na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mikoa yote mtaweza kuguswa na usambazaji huo wa vifaa na vifaatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia na hoja kwa upande wa magari ya wagonjwa na kwenye hili pia niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tumeendelea kuyapokea tunaamini muda siyo mrefu tutaweza kukabidhi magari mawili mawili katika kila halmashauri lakini vilevile gari moja kwa ajili ya usimamizi wa huduma mbalimbali za afya na uratibu katika maeneo yenu katika halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia na hoja ya mfumo wetu wa TAUSI. Niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tumeendelea kuuimarisha na sasa tunatoa leseni zote za kibiashara na leseni nyingine mbalimbali katika mfumo wa kidijitali. Tuendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kusaidia kuwahamasisha wananchi wetu watoe ushirikiano na kuweza kutumia mfumo huu wa TAUSI kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato lakini vilevile katika kupata huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia nafasi na nipende kusema ninaunga mkono hoja hii kwa 100%. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kabisa kwa kusema kwamba, naunga mkono hoja ya Muswada huu uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaingia kwenye Muswada nianze kuzungumzia maoni ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Kwanza kabisa, tumemsikia na nashukuru Mheshimiwa Nape amelieleza vizuri sana kwamba Rais amekuwa akiteua viongozi mbalimbali bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Ibara ya 37(1 na (2) zimeeleza bayana kabisa utaratibu na mamlaka ya Rais katika utendaji na utekelezaji wa shughuli zake. Rais ndiye anayeteua viongozi wakuu, Rais ndiye anayeteua viongozi wanaosimamia na kutekeleza sera, lakini vilevile Wakurugenzi hawa wanaotajwa ndiyo watekelezaji wakuu au moja ya makundi ya watekelezaji wa sera, kwa hiyo, Rais wala hajakiuka chochote hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, The Ministers‟ Discharge of Duties Act na katika GN ya 144 ya Aprili 2016, imeeleza kabisa majukumu ya Wizara moja baada ya nyingine. Ukiangalia katika Ofisi ya Rais (the Presidency) imeweka kabisa majukumu na mojawapo likiwemo la Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, yeye mwenyewe ndiye Waziri, lakini vilevile ana mamlaka ya kuweza kuteua. Niseme tu kwamba delegation does not mean application na hamna chochote ambacho kimekiukwa, lakini hata wale wateule wa Rais wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu pamoja na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kujikita sasa katika suala zima la Sheria hii ya Utumishi wa Umma. Nimesikia hapa wako wanaosema kuna ILO Convention imekiukwa. Wako wanaosema kwamba haijazingatia masuala mbalimbali ya Vyama vya Wafanyakazi na wako wanaosema kwamba tunatengeneza bomu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Bilago anajua kwanza Muswada huu ulitangazwa na ukasomwa kwa Mara ya Kwanza ili watu wajiandae wausome watoe maoni. Hata hivyo, Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge ilialika wadau mbalimbali kuja kutoa maoni kuhusiana na Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba tunayo Sera ya Malipo na Mishahara na Motisha ya mwaka 2010. Kwa mujibu wa sera hii na imeelezwa bayana kabisa dhumuni la kuoanisha na kuwianisha mishahara na maslahi mbalimbali katika utumishi wa umma. Nimemsikia hapa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani akisema watu walikuwa wakifanya mikutano Dubai, akisema hapa watu walikuwa wanajilipa mishahara mikubwa, hivi kweli anataka au tunataka tubaki katika hali hiyo? Hivi kweli tunataka kuwa na tofauti ya mishahara wengine wana milioni zaidi ya 40 kweli katika utumishi huu huu wa umma? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma tulikuwa na Shirika/Taasisi yetu ya SCOP si kitu cha ajabu hata kidogo, ilikuwa ikioanisha na ilikuwa ikiwianisha mishahara yetu. Baada ya kugundua tatizo hili, Tume ya Ntukamazina ilikuja na hoja na ndiyo maana tarehe 3 Juni, 2011 iliundwa Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma. Hivi ninavyoongea hapa kiko chombo kwa ajili ya kazi hiyo na kazi yake ni kumshauri Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu Utumishi wa Umma, lakini vilevile kumshauri Mheshimiwa Rais kutokana na tafiti mbalimbali inazozifanya kuhusiana na motisha, maslahi na mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapa ni kutaka tu kuchanganya watu. Nimeona katika mitandao mbalimbali, nimeona distortion kubwa ambayo imekuwa ikifanyika kwamba posho zote zinafutwa, si kweli ndugu zangu! Labda tuoneshwe kifungu kimoja tu kinachosema kuna posho fulani itafutwa! Tunachokisema hapa, tunamwongezea mamlaka Katibu Mkuu Utumishi kwa mujibu wa kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na majukumu yake mengine basi aweze kuoanisha na kuwianisha mishahara, motisha, marupurupu na maslahi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepunguza mishahara ya baadhi ya wakuu wa taasisi kuanzia Julai hakuna anayepata zaidi ya shilingi milioni 15. Tumeshuhudia wakuu wa taasisi wengine baadhi ya posho za nyumba wanajilipa mshahara mzima!
Anajikuta anapata mshahara wa milioni 30 na posho yake ya nyumba ni equivalent kwa mshahara wake wa mwezi mmoja! Haiwezekani! Wako ambao wana magari zaidi ya matatu, ana gari lake, la mke wake na lingine liko nyumbani kwa ajili ya pool! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumwogope Mwenyezi Mungu. Tumekuja kwa nia njema na mapendekezo haya na si nchi ya kwanza kufanya hili na sisi pia tulishapita huko. Kenya wanafanya hivyo, wanayo Salary and Remuneration Commission. Ireland, South African na nchi nyingine pia wamekuwa wakifanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwarejeshe Waheshimiwa Wabunge katika kifungu cha 8(3)(e), Katibu Mkuu kupitia kwa Bodi ya Mishahara wanayo mamlaka ya kufanya tathmini ya kazi kwa ajili ya kupanga upya madaraja mbalimbali ya mishahara na miundo. Zoezi hilo tumeshaanza kupitia Bodi ya Mishahara na linakwenda vizuri, lakini kwa sasa hakuna posho yoyote inayofutwa ila itakapofikia kuna maombi mbalimbali ni lazima tuangalie uwezo wetu wa kibajeti na miundo yetu ya kiutumishi ilivyokaa na mambo mengine kadha wa kadha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niliweke hilo bayana ili kuweka rekodi sawa na lengo hasa la kuleta Muswada huu. Ukiangalia katika sheria mbalimbali katika miaka ya 1990 na 2000 wakala mbalimbali zimekuwa zikitunga sheria zikizipa bodi zao mamlaka za kutoa kibali cha kupandisha mishahara, haiwezekani! Ukiangalia Ofisi ya Rais, Utumishi ndiyo wana mamlaka ya kuangalia payroll management nzima, ni lazima waweze kujua, je, uwezo huo tunao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako ambao wanasema bodi zao zinazalisha fedha za kutosha lakini tukumbuke fedha hizi ni za umma. Hata kama shirika lako limezalisha ziada ni lazima zirudi katika chungu kikuu, ni lazima upendekeze kwa utaratibu wa kawaida na ndipo baadaye utaweza kuidhinishiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Bunge, Bunge haliidhinishi mishahara yake peke yake. Bunge linapendekeza na hatimaye Rais ndiyo anayeidhinisha na ndicho tunachokifanya hapa. Bodi hazikatazwi kupendekeza, taasisi hazikatazwi kupendekeza nyongeza ya mishahara na mambo mengine, lakini mwisho wa siku tunataka tuwe na mamlaka moja itakayopitia, itakayokuwa na kumbukumbu sahihi ili kuhakikisha kwamba hatuendi nje ya mstari na bajeti yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wanaosema kwamba tunakiuka dhana ya ugatuaji wa madaraka. Hakuna popote tunapokiuka dhana hii, lakini tuseme ni lazima kuwa na uwiano wa kipato. Nitashangaa kama kuna Serikali yoyote ambayo haiangalii uwiano wa kipato baina ya watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika suala la mashauri ya nidhamu katika kifungu cha 26 na yenyewe imezungumziwa sana. Ukiangalia katika utaratibu wa sasa liko wazi kabisa. Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma imeainisha mamlaka za nidhamu na ajira katika utumishi wa umma. Inajulikana kabisa katika masuala ya kuthibitishwa kazini, kupandishwa cheo, kuthibitishwa ajira, kufukuzwa kazi na mengine, mtu anaanzia katika mamlaka ya ajira, anaweza kukata rufaa katika mamlaka ya kwanza katika Tume ya Utumishi wa Umma na hatimaye kufikia kwa Mheshimiwa Rais. Hizi ni taratibu administratively lakini bado haizuii mtu atakapokuwa ame-exhaust administrative measures na administrative organs baada ya hapo kwenda Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaleta mapendekezo haya kwa sababu tumekuwa tukishuhudia wako watu katika utumishi wa umma mara tu wanapokuwa charged kwenye mamlaka ya ajira au katika Tume, akishafikishwa Tume tu anaenda kufungua shauri katika Baraza la Usuluhishi, haiwezekani! Ni lazima aweze kutumia nafuu zote zilizoko katika utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mwingine ameenda Tume, rufaa yake ikishakataliwa badala ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais yeye tayari ameshakwenda Mahakamani au katika Baraza la Usuluhishi, tunasema hii hapana! Ni lazima tuweke consistency, ni lazima tufuate sheria kama ilivyoainishwa ili kuhakikisha kwamba tunakwenda sawa. Hatumkatazi mtu kwenda Mahakamani lakini ni baada ya kuwa ameshapitia nafuu na taratibu zilizopo katika utumishi wa umma anaweza akaenda kupitia judicial review katika Mahakama zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Serikali Mtandao wa Mwaka 2019
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kipekee napenda kukushukuru wewe binafsi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa jinsi walivyoeleza masuala haya kuhusiana na Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma. Kipekee niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusiana na Muswada huu ambao wamezungumza lakini pia wengine ambao wameweza kuchangia kwa maandishi kuhusiana na Muswada huu muhimu kwa ajili ya maendeleo na maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba michango na maoni yote iliyotolewa tunatambua kwamba imetolewa kwa lengo la kuboresha na napenda tu kusema kwamba tumeipokea. Kama ambavyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati na Wabunge wengi waliochangia wamesema kwamba Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kweli kwa kiasi kikubwa ni kama tumepokea na tumetekeleza maoni yote mliyoyatoa. Kwa hiyo, hatutaweza kushindwa kutekeleza ushauri mwingine ambao mmeutoa hapa wakati mlipokuwa mkichangia na kuboresha Muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba masuala ya Serikali Mtandao wote mnafahamu yamekuwa yakifanyika Serikalini tangu mwaka 2004 pia haya yalifanyika baada ya kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri lilipofanyika kipindi hicho cha kuanzisha Wakala wa Serikali Mtandao. Ni kwa kutambua umuhimu huo wa kuwa na uratibu na usimamizi ulio bora wa masuala ya Serikali Mtandao ndipo mwaka 2012 kama nilivyoeleza Serikali iliamua kuanzisha Wakala wa Serikali Mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtatambua kwamba ni takribani miaka 15 sasa imeweza kupita tangu Serikali ilipofanya uamuzi wa kuweza kuanzisha huduma hii ya Serikali Mtandao. Tulikuwa tunasikia hapa wengine wakisema kwamba Muswada huu ni njiti na kwamba bado haujakomaa na bahati nzuri au mbaya mimi mwenyewe nilizaliwa njiti, kwa kweli nisingependa mtumie maneno kama hayo, kwa kweli ni maneno ya kashfa ambayo hamtakiwi kabisa kuyasema kwa Serikali na hasa Serikali yenye nia njema kama hii ya sasa kwa kuja na Muswada huu ambao lengo lake kubwa ni kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuhakikisha kwamba huduma mbalimbali za Serikali zinawafikia wananchi tena wananchi wa matabaka ya aina yote na haswa wale wa vijijini na wengine ambao ni wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine walisema kwamba ni secondary tulitakiwa tuanze na primary issues, napenda kusema kwamba hapa ndio primary issues, tumekuja tumeanza, tunatekeleza na si mara ya kwanza kwa Serikali Mtandao kutoa huduma hizi hapa tu tunaongeza nguvu kwa ajili ya huduma za Serikali Mtandao badala ya kufanywa na Wakala wa Serikali Mtandao ziweze kutolewa na Mamlaka kamili itakayokuwa na nguvu kama ambavyo imeelezwa katika Muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa Serikali Mtandao wote mnatambua kumekuwa na changamoto nyingi ambazo kimsingi ndizo zimepelekea kuletwa kwa Muswada huu na kama nilivyoeleza sababu mbalimbali katika hotuba yangu asubuhi lakini pia kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameweza kufafanua na sina haja ya kwenda ndani zaidi. Kubwa zaidi ni manufaa ambayo Serikali na wananchi watapata kwa kuweza kuwa na Mamlaka hii lakini zaidi usimamizi, uratibu na urekebu wa masuala mbalimbali ya huduma ya Serikali Mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, ukiangalia hata Muswada huu kubwa zaidi ni kutekeleza ajenda ya Mheshimiwa Rais ambapo ni mwendelezo wa ajenda yake muhimu katika usimamizi wa masuala mbalimbali ya kimenejimenti. Wote tumekuwa tukimshuhudia mara zote Mheshimiwa Rais namna ambavyo amekuwa akisisitiza kuhakikisha kwamba kunakuwa na utumishi wa umma ambao unakuwa na ufanisi na tija. Pia tumekuwa tukiona mara zote akisisitiza kuwa na Serikali ambayo inatoa huduma kibiashara zaidi ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na tija na hili ndiyo tunafanya kama mwendelezo wa ajenda hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nitakuwa sijatenda haki endapo sitawapongeza Wakala au Mamlaka ambayo inayokusudiwa ya Serikali Mtandao kwa huduma nzuri ambazo inazitoa. Nimpongeze sana Dkt. Bakari pamoja watendaji wote lakini zaidi Ofisi ya Rais yenyewe Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa namna ambavyo wamekuwa wakisimamia na kuhakikisha kwamba huduma za Serikali Mtandao zinatolewa kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nikisikia nadhani ilikuwa ni Mheshimiwa Riziki Lulida, tunashukuru sana kwa maangalizo kuhusu kufanyika kwa vetting na imekuwa ikifanyika kwa kutambua kwamba watu hawa wanakuwa wameshikilia usalama wa taarifa nyingi muhimu lakini zaidi usalama wa taarifa hizo lakini usalama wa huduma na kuhakikisha kwamba hata mara moja huduma hizi hazikwami. Watumishi hawa wamekuwa wakifanya hivyo kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele, wakihakikisha kwamba kunakuwa na uzalendo. Bahati nzuri kwa kuwa na mimi nilishakaa Wizara hii, natambua na sina shaka na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mara zote wamekuwa wakitanguliza uzalendo lakini kuhakikisha wanaokoa fedha za umma ili fedha hizo zingine ziweze kupelekwa katika huduma nyingine mbalimbali za kiserikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, napenda kusema kwamba maoni yote yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni ushahidi kwamba suala la Serikali Mtandao ni muhimu sana katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na wote tunaamini kwamba suala hili limekuja katika wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda katika majibu ya hoja, nianze na ile hoja ya kwanza ya OGP. Katika Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni walikuwa wakishangaa kwa nini tumejiondoa OGP lakini pia tunaanzishaje Mamlaka ya Serikali Mtandao wakati hatupo katika OGP. Napenda tena kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge, tarehe 13 Novemba, 2017, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Mkuchika alijibu hapa Bungeni swali la Mheshimiwa Zitto Kabwe kuhusiana na uanachama wetu katika mpango huu wa OGP.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu wa OGP ulikuwa ni wa hiari haukuwa ni wa lazima na takribani nchi 70 zilikuwa zimejiunga lakini pia ziko nchi nyingi ambazo zimejiondoa katika mpango huu ikiwemo Hungary na Russia. Kama nilivyoeleza ni mpango ambao Serikali zinaingia kwa hiari kwa ajili ya kuweza kujitathmini lakini kubadilishana uzoefu kuhusiana na namna ambavyo Serikali mbalimbali zinatenda shughuli zake kwa uwazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza, ni mpango ambao Serikali zinaingia kwa hiyari kwa ajili ya kuweza kujitathmini, lakini kubadilishana uzoefu kuhusiana na namna ambavyo Serikali mbalimbali zinatenda shughuli zake kwa uwazi. Napenda kusema kwamba, tayari tuna uwazi na tumekuwa tukipimwa katika mifumo mbalimbali; tumekuwa tukipimwa katika African Peer Review, katika Shirikisho la Taasisi za Kupambana na Rushwa, tumekuwa tukipimwa pia kupitia Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa (UNCAC) pamoja na mipango mingine mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kulihakikishia Bunge lako kwamba, kujitoa kwa Tanzania katika Mpango huu wa Kimataifa wa OGP, tayari tunayo mipango mingi ambayo tunaitekeleza ndani ya nchi kama nilivyoeleza na tunaamini kwamba ni mipango ambayo inajitosheleza na tutaendeleza na kuimarisha misingi ya uwazi, lakini pia uwajibikaji pamoja na mapambano dhidi ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja kwamba mwananchi wa kawaida atanufaika vipi kwa kupitishwa kwa Muswada huu, iko wazi kabisa. Kwa upande wangu tu ambaye nasimamia wepesi wa kufanya biashara na mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, napenda tu kusema kwamba hii yenyewe kupitia mifumo mbalimbali ya utoaji wa leseni, mifumo ya ulipaji wa kodi pamoja na mifumo mingine mbalimbali katika mazingira haya kwa hakika wawekezaji wenyewe hawawezi kuja bila kuwa na mifumo ya uwazi ambayo ina mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivi, tunakuwa tumechangia pia katika kuboresha, lakini kuhakikisha kwamba kunakuwa na wepesi wa kufanya biashara. Hii itawanufaisha pia hata na wafanyabiashara wa kawaida, lakini pia watu wanaokuja, wananchi wa kawaida kupata huduma mbalimbali za Kiserikali pamoja na huduma nyingine za Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumesikia, bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri amelijibia vizuri kuhusiana na manufaa ambayo yatapatikana, lakini pia hata vijijini. Kupitia ile *152*00 hata mwenye simu ya tochi bado ana uwezo wa kupata huduma mbalimbali za kimtandao (e-services) kupitia namba hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba, ni vyema kuheshimu sheria na uendeshaji wa kampuni binafsi ili kuhakikisha kwamba, kunakuwa na faragha kwa wateja. Napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, faragha inazingatiwa sana kupitia sheria mbalimbali; kupitia Sheria ya Electronic Transactions, kupitia Sheria hii ya Kuanzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao, lakini pia kupitia Sheria ya Cyber Crimes pamoja na sheria nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sheria inatoa fursa kwa makampuni binafsi kuweza kufanya kazi na Serikali. Napenda tu kusema kwamba, kupitia sheria hii tunayoipendekeza, haitoi mwanya hata kidogo kwa Serikali kuweza kuingilia taratibu za kampuni binafsi wala kuingilia faragha za wateja wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na mifumo mbalimbali. Napenda tu kuwapongeza tena EGA kwa mara nyingine tena, kwa kweli mwendelee kubuni mifumo mbalimbali ya kimtandao. Mmebuni mfumo wa e-office, mmebuni mfumo wa e-permit ambao sasa hivi tunashuhudia wataalam na watumishi wa Serikali wakiomba vibali kupitia mtandao, lakini pia kupitia e-office yenyewe. Tumeshuhudia sasa hivi, mimi naweza nikawa Dar es Salaam au Ruvuma na bado ninaweza kupata access ya kuweza kushughulikia file ambalo liko mezani kwangu kupitia mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunamsikia hapa Mheshimiwa Msigwa akikebehi. Napenda kusema kwamba toka tumehamia Dodoma, mfumo wa e-office pamoja na mfumo wa e-files umekuwa wa msaada mkubwa na yote haya ni matokeo ya Serikali Mtandao ambayo tumeona yamefanywa na Taasisi yetu ya EGA.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, tumeshuhudia mfumo wa Ofisi Mtandao ambao mpaka sasa unatumiwa na taasisi 60. Napenda tu kutoa rai kwa taasisi nyingine ambazo bado hazijajiunganayo kuweza kuona kwamba, wanajiunga na mfumo huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia mfumo wa Barua Pepe Serikalini, tumeona tayari umeshaundwa. Mfumo wa malipo ya kiserikalini wa kielektroniki wa GDG ambao wengi wameusifia na umekuwa na manufaa makubwa. Kupitia ile hoja ya control number kwa nini zinabadilika, napenda tu kusema kwamba, Mheshimiwa Lulida tunaichukua tutaenda kuangalia, lakini naamini watakuwa wana sababu kwa nini zinabadilika, lakini naamini litaweza kuangaliwa na kama kutakuwa kuna sababu, basi litaweza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Mtandao wa Govnet, pia na wenyewe umekuwa wa msaada mkubwa kwa taasisi mbalimbali katika Serikali za Mtaa, lakini pia na Wizara nyingine ambazo tayari zimeshaunganishwa, lakini pia wameweza kuunda kituo cha kuhifadhi mifumo pamoja na data (Government Data Centre) ambacho mpaka sasa kimeweza kutumiwa na taasisi takribani 53, pamoja na kuweza kuhifadhi takribani tovuti 230 za taasisi za Umma na wameweza kuzihifadhi kwa usalama mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile wameweza kusimamia masafa ya internet Serikalini ambazo mpaka sasa tumeweza kushuhudia takribani taasisi za Umma 175 ambazo zimeendelea kusimamia mfumo huu. Sambamba na hayo tumeweza kushuhudia namna ambavyo mifumo mbalimbali ya kuboresha utendaji kazi imefanyika kupitia TAKUKURU. Tumeona TBA, EWURA, Engineers Registration Board, lakini pia na taasisi nyingine za Kiserikali ambazo wameweza kuboresha mifumo yao mbalimbali ya utendaji Serikalini kupitia huduma na mifumo iliyobuniwa na eGA.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tulisikia hoja ya Mheshimiwa Mwakibete, ambapo alipongeza sana Open University kuhusiana na suala la e-lerning. Napenda tu kusema kwamba, tutaendelea kufanya hivyo na Wizara ya Elimu imekuwa ikiwa champion mkubwa sana wa masuala ya e- education pamoja na e-learning na ninaamini watafanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawapongeza sana Wizara ya Afya kwa namna ambavyo wameendelea kusimamia masuala ya telemedicine na kwa sasa Wizara ya Kilimo wanaelekea katika e-agriculture; na kwa upande wa e-commerce kwa sasa Wizara ya Viwanda kupitia TANTRADE pamoja na e-Government pia wanaendelea kuangalia masuala haya kuona ni kwa namna gani platform hii ya electronic itaweza kubuniwa ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kufanya biashara zaidi kupitia mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza taasisi zote na wadau binafsi ambao wameweza kuanzisha platform zao wenyewe ambazo zimewezesha hivi sasa kuweza kufanya biashara kupitia mtandao. Tumeona kina Junior Food pamoja n taasisi nyingine, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa umuhimu wa usalama niseme kwamba hatuwezi tukasema zaidi, lakini tunazingatia usalama kutokana na maslahi ya Taifa. Niendelee kuwahakikishia kwamba, hatuwezi ku- compromise na suala zima la usalama wa taarifa pamoja na usalama wa mitandao na tutaendelea kuhakikisha kwamba taarifa zinaweza kulindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wako Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa na hofu ya ulinzi wa taarifa. Tayari Wizara ya Mawasiliano inalifanyia kazi na wako mbioni watakuja na Sheria ya Data Protection ili kuhakikisha kwamba data mbalimbali za wateja pamoja na watu wengine zinaweza kulindwa kitaarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya kutoa elimu kwa watumiaji ya Mheshimiwa Aida. Napenda tu kusema kwamba, EGA wanaendelea kutoa elimu kwa watumiaji, lakini pia tutahakikisha kwamba Muswada huu utakapopitishwa, itakapokuwa sheria, basi tutaendelea kuongeza kasi zaidi ya kuhakikisha kwamba tunatoa elimu zaidi kwa ajili ya watoa huduma, lakini pia na taasisi za Umma ambazo zimeanzisha huduma mbalimbali za kimtandao, tunaendelea kutoa rai pia nao waendelee kutoa elimu kwa Umma ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma hizo wanazozitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Haonga kuhusiana na OGP pamoja na Mamlaka hii ya Serikali Mtandao. Kama nilivyoeleza awali, kwanza hivi ni vitu viwili tofauti. Mamlaka ya Serikali Mtandao yenyewe inahusika na utoaji wa huduma mbalimbali za kimtandao kupitia taasisi za Umma na Serikali na OGP kama nilivyoeleza mwanzo yenyewe ilikuwa ni huduma ya hiyari au mpango wa kihiyari ambapo nchi takribani 70 ziliweza kuingia ili kuweza kuona ni kwa namna gani wanaweza kutangaza kazi zao na huduma mbalimbali wanazozitoa kwa uwazi zaidi kupitia mitandao mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine ya kuanzisha Bodi ambayo itasimamia wataalam wa masuala ya TEHAMA Tanzania. Nadhani ilikuwa ni hoja ya Mheshimiwa Zainab Mndolwa. Napenda tu kusema kwamba, tunayo tayari Tume ya TEHAMA ambayo ndio ina jukumu la kusimamia masuala ya TEHAMA yote Serikalini. Kwa upande wa EGA au Mamlaka hii ya Serikali Mtandao, yenyewe itasimamia tu masuala ya huduma ya Serikali Mtandao kwa Serikali pamoja na taasisi za Umma na hii ndiyo tofauti ambayo ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa kwa mara nyingine tena napenda kusema kwamba tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na niwahakikishie kwamba sasa tunaelekea katika kukimbia. Wako wengi walikuwa wakitolea mifano ya Rwanda, lakini kama Tanzania tumekuwa tukipigiwa mfano sana katika makongamano mbalimbali ya utumishi wa Umma na makongamano mbalimbali yanayojadili masuala ya Serikali Mtandao na tumekuwa tukifanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kama Serikali hatujaridhika na ndiyo maana tumeangalia changamoto, tumeona sasa ili kuweza kujibu changamoto hizi na ili kuweza kwenda haraka zaidi, basi tuweze kuipa nguvu zaidi mamlaka yetu hii ya Serikali Mtandao ili iweze kujengewa uwezo mkubwa zaidi na kuweza kuchukua hatua kama ambavyo tumeshuhudia katika vifungu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna ushauri kutoka kwa Mheshimiwa Bobali kuhusiana na kuongeza kasi zaidi katika huduma zetu kimtandao. Ndiyo maana mnaona huduma mbalimbali zimekuwa zikitolewa na taasisi yetu hii ya EGA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kuwa na system zinazofanana, ndiyo maana ukiangalia katika Kifungu cha 5 na cha 6 cha Muswada huu utaweza kuona mamlaka ambayo EGA imepewa kuhakikisha kwamba inasimamia na kufanya ICT Audit pamoja na compliance ya systems mbalimbali ili kuhakikisha kwamba hakuna udurufu wa systems na inakuwa ni mifumo ambayo imekidhi viwango kama ambavyo vimekusudiwa katika miongozo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee napenda tu kuwahakikishia tena usalama wa taarifa, kwamba sheria hii itakapopitishwa kwa mujibu wa kifungu cha 60, 61 na kwa mujibu wa kifungu cha 27 tutahakikisha kwamba, miongozo mbalimbali inatolewa, lakini pia kanuni zitatungwa ambazo zitaweza kufafanua masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya usimamizi wa miamala mbalimbali ya kifedha. Hili limezingatiwa katika kifungu cha 27(2) na (3) ambapo masuala haya yatasimamiwa kupitia kanuni. Imeeleza kabisa na imempa mamlaka Waziri mhusika kuweza kusimamia masuala haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni makosa, ukiangalia katika kifungu cha 57 imeeleza kabisa makosa gani ambayo yakifanywa, basi kutaweza kuwa kuna adhabu kali. Hii ni pamoja na watu kutokuzingatia miongozo hii. Ninatoa rai sana kwa wataalam wote wa masuala ya TEHAMA walioko Serikalini kuhakikisha kwamba baada ya sheria hii kupitishwa wanaisoma kwa kina pamoja na miongozo yote ambayo itatolewa na Serikali ili kuhakikisha kwamba hawakiuki hata kifungu kimoja kwa sababu kuna makosa ambayo yameainishwa, lakini pia kutakuwa na adhabu inayoambatana na makosa hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia kifungu cha 61 kuhusiana na kanuni za Maadili, pia zimeelezwa pale. Waziri mwenye dhamana ya Utumishi na Utawala Bora amepewa mamlaka, ataweza kutunga kanuni mbalimbali za maadili ya watumishi wataalam wa masuala ya TEHAMA Serikalini ili kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi zao kwa kufuatilia uadilifu na kwa kuzingatia miongozo pamoja na sheria hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kipekee nawashukuru tena sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii muhimu. Tunawashukuru na tuwahakikishie kwamba ushauri wenu ni wa muhimu sana, tunauchukua kwa thamani na tunaamini tutaendelea kushirikiana tena na tutaweza kuyatekeleza haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA – MHE ANGELLAH J. KAIRUKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Bajeti hii Kuu ya Serikali.
Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu kwa maandalizi mazuri ya bajeti na kwa kweli ukiangalia sura ya bajeti hii unaona kabisa ni kwa namna gani Serikali imejipanga katika kumkwamua Mtanzania wa kawaida ili aweze kuona nafuu katika maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza zaidi kwa namna ambavyo Wizara imeandaa Sera ya Matumizi katika kuhakikisha kwamba tunabana matumizi yasiyokuwa na tija na kuhakikisha kwamba Serikali itakuwa na matumizi yale tu ambayo kwa kweli, yataweza kuwa na tija kwa wananchi wake.
Mheshiumiwa Naibu Spika, napongeza zaidi kwa jitihada za Wizara ya Fedha za kuamua kuja na marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma na kwa hakika kupitia Sheria hii pindi itakapopitishwa itaweza kuwa na manufaa makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie sasa katika hoja ambazo zimegusa Ofisi yangu na katika hoja ya kwanza ilikuwa ni katika suala zima la watumishi hewa. Kulikuwa na hoja, baadhi ya Wabunge walitaka kufahamu ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya Maafisa Masuuli, dhidi ya Wakuu wa Idara pamoja na vitengo mbalimbali vya Uhasibu ambao kimsingi wao wameamini kwamba wanaweza kuwa walishiriki katika masuala haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, kimsingi watumishi hewa wanatokana na kwamba, unakuta wakati mwingine labda mtu amefariki, wengine unakuta ni watoro, lakini wanatakiwa wawe wameondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara au Payroll, lakini wale waliokasimiwa mamlaka wanakuwa hawajatimiza wajibu wao ipasavyo. Wako watumishi wengine wanakaa katika Payroll na walitakiwa waondoke, hadi inafikia hata miezi 10 na zaidi!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, kama Serikali, ili kukabiliana na tatizo hili tumekuwa tukiendelea kuchukua hatua na tunaendelea kumshukuru sana pia, Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake na kwa msukumo ambao ameupatia katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie tu kwamba, kwa sasa ambacho tumkifanya, kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba tunawaondoa watumishi wote ambao tumewabaini mpaka sasa; na tumeshabaini watumishi hewa 12,246 ambao endapo wangeendelea kuwepo katika orodha ya malipo ya mishahara, takriban shilingi bilioni 25.091 ingeendelea kulipwa kila mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, ukiangalia, hii ni kuanzia Mwezi Machi tu, tarehe 1; mpaka tarehe 30 Aprili, ambapo Mheshimiwa Rais alitangaza, walibainika watumishi hewa 10,295 na mpaka tarehe 30 Mei ndiyo hii watumishi 12,246!
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichokifanya hivi sasa tumezielekeza Mamlaka zote za ajira kuhakikisha kwamba wanachukua hatua za kinidhamu na za Kisheria. Hatutaki tu tutangaze kwamba tumeshaokoa kiasi kadhaa na kuondoa watumishi hawa hewa. Tunachokitaka hivi sasa; na ninapongeza sana mamlaka mbalimbali za ajira katika Mkoa wa Singida, mamlaka mbalimbali za ajira Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara na mikoa mingine yote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kuhakikisha kwamba watu wote walioshiriki katika kusababisha watumishi hewa kuwepo, wameweza kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuhakikisha kwamba mashitaka yote ambayo yatakuwa yamefunguliwa dhidi ya wale ambao walikuwa wakitafuna fedha za Serikali ambazo hazikuwa zinapaswa kulipwa kwao, lakini vilevile kuhakikisha kwamba, Maafisa Utumishi ambao kimsingi ndio tiumewaidhinishia matumizi ya mfumo huu, tumefundisha Maafisa Utumishi 1,500.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa tayari wakati wowote hata ikibidi kuwasimamisha Maafisa Utumishi hao wote 1,500 ili tuweze kuanza upya, tuwe na Maafisa Utumishi wenye uadilifu, wenye uzalendo na ambao wana hofu ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, naendelea kuomba mamlaka za ajira wahakikishe kwamba, wanachukua hatua za kinidhamu pamoja na za Kisheria na wahakikishe mashitaka yote yanafikishwa katika mamlaka zinazohusika. Kwa wale ambao watashindwa kuweza kuchukua hatua stahiki kwa zile mamlaka za ajira kwa Maafisa Masuuli na wengineo tutawachukulia hatua kali za Kisheria kwa mujibu wa Sheria, Kanuni pamoja na taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine iliyouliza, endapo kuna umuhimu wa kuwa na PDB au la!
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu Ofisi ya Rais ya kusimamia ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi. Ofisi hii ilianzishwa mwaka 2013 na niseme tu kwamba, ni ofisi ambayo kwa kweli ni ya muhimu sana. Ukiangalia katika manufaa mbalimbali ambayo yameshapatikana hadi hivi sasa, sekta takriban 13 za kipaumbele zimeweza kuutumia mfumo huu na zimeweza kufuatilia na kutekeleza miradi yake mbalimbali kwa kweli kwa mafanikio makubwa na tumeshuhudia mafanikio ya takribani asilimia 71.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia katika ushirikiano ambao PDB imekuwanao na Pemandu ya Malaysia, ni mfumo ambao ukiangalia Uingereza wameutumia, Rwanda wameutumia, Malaysia wameutumia na kwa kweli, wameona mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, pamoja na kwamba, sekta ambazo ziko katika mfumo huu ni 13, lakini hivi sasa Mahakama haikuwepo katika mfumo huu, lakini wenyewe walishaanza kutekeleza mapendekezo ya mfumo huu na wamefanya vizuri sana nawapongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalipongeza pia Jeshi la Polisi na ninapenda pia kupongeza mamlaka mbalimbali za maji Mijini kwa namna ambavyo wameimarisha utekelezaji wa majukumu yao, lakini vilevile namna ambavyo wamekuwa na mafanikio katika kupanga na kufuatilia matokeo ya miradi yao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia ofisi hii itakuwa ya muhimu zaidi hasa katika mwaka huu ambapo tumekuwa na mapinduzi katika maandalizi ya bajeti. Takribani asilimia 40 ya bajeti yote ya Serikali itaenda katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Usipokuwa na ufuatiliaji mzuri na tathmini, ni namna gani fedha zako zimeenda huko? Ni vipaumbele gani ulikuwanavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuwa na ripoti mbalimbali za kila wiki ili kuweza kujua namna miradi mbalimbali inavyotekelezwa. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, naendelea kuomba mamlaka mbalimbali ambazo ziko katika mfumo huu, lakini na nyingine ambazo bado hazijajiunga na Mfumo wa BRN basi wajitahidi kuona ni kwa namna gani wanaweza wakajiunganao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono Bajeti hii Kuu ya Serikali.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA – MHE ANGELLAH J. KAIRUKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Bajeti hii Kuu ya Serikali.
Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu kwa maandalizi mazuri ya bajeti na kwa kweli ukiangalia sura ya bajeti hii unaona kabisa ni kwa namna gani Serikali imejipanga katika kumkwamua Mtanzania wa kawaida ili aweze kuona nafuu katika maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza zaidi kwa namna ambavyo Wizara imeandaa Sera ya Matumizi katika kuhakikisha kwamba tunabana matumizi yasiyokuwa na tija na kuhakikisha kwamba Serikali itakuwa na matumizi yale tu ambayo kwa kweli, yataweza kuwa na tija kwa wananchi wake.
Mheshiumiwa Naibu Spika, napongeza zaidi kwa jitihada za Wizara ya Fedha za kuamua kuja na marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma na kwa hakika kupitia Sheria hii pindi itakapopitishwa itaweza kuwa na manufaa makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie sasa katika hoja ambazo zimegusa Ofisi yangu na katika hoja ya kwanza ilikuwa ni katika suala zima la watumishi hewa. Kulikuwa na hoja, baadhi ya Wabunge walitaka kufahamu ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya Maafisa Masuuli, dhidi ya Wakuu wa Idara pamoja na vitengo mbalimbali vya Uhasibu ambao kimsingi wao wameamini kwamba wanaweza kuwa walishiriki katika masuala haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, kimsingi watumishi hewa wanatokana na kwamba, unakuta wakati mwingine labda mtu amefariki, wengine unakuta ni watoro, lakini wanatakiwa wawe wameondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara au Payroll, lakini wale waliokasimiwa mamlaka wanakuwa hawajatimiza wajibu wao ipasavyo. Wako watumishi wengine wanakaa katika Payroll na walitakiwa waondoke, hadi inafikia hata miezi 10 na zaidi!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, kama Serikali, ili kukabiliana na tatizo hili tumekuwa tukiendelea kuchukua hatua na tunaendelea kumshukuru sana pia, Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake na kwa msukumo ambao ameupatia katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie tu kwamba, kwa sasa ambacho tumkifanya, kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba tunawaondoa watumishi wote ambao tumewabaini mpaka sasa; na tumeshabaini watumishi hewa 12,246 ambao endapo wangeendelea kuwepo katika orodha ya malipo ya mishahara, takriban shilingi bilioni 25.091 ingeendelea kulipwa kila mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, ukiangalia, hii ni kuanzia Mwezi Machi tu, tarehe 1; mpaka tarehe 30 Aprili, ambapo Mheshimiwa Rais alitangaza, walibainika watumishi hewa 10,295 na mpaka tarehe 30 Mei ndiyo hii watumishi 12,246!
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichokifanya hivi sasa tumezielekeza Mamlaka zote za ajira kuhakikisha kwamba wanachukua hatua za kinidhamu na za Kisheria. Hatutaki tu tutangaze kwamba tumeshaokoa kiasi kadhaa na kuondoa watumishi hawa hewa. Tunachokitaka hivi sasa; na ninapongeza sana mamlaka mbalimbali za ajira katika Mkoa wa Singida, mamlaka mbalimbali za ajira Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara na mikoa mingine yote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kuhakikisha kwamba watu wote walioshiriki katika kusababisha watumishi hewa kuwepo, wameweza kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuhakikisha kwamba mashitaka yote ambayo yatakuwa yamefunguliwa dhidi ya wale ambao walikuwa wakitafuna fedha za Serikali ambazo hazikuwa zinapaswa kulipwa kwao, lakini vilevile kuhakikisha kwamba, Maafisa Utumishi ambao kimsingi ndio tiumewaidhinishia matumizi ya mfumo huu, tumefundisha Maafisa Utumishi 1,500.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa tayari wakati wowote hata ikibidi kuwasimamisha Maafisa Utumishi hao wote 1,500 ili tuweze kuanza upya, tuwe na Maafisa Utumishi wenye uadilifu, wenye uzalendo na ambao wana hofu ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, naendelea kuomba mamlaka za ajira wahakikishe kwamba, wanachukua hatua za kinidhamu pamoja na za Kisheria na wahakikishe mashitaka yote yanafikishwa katika mamlaka zinazohusika. Kwa wale ambao watashindwa kuweza kuchukua hatua stahiki kwa zile mamlaka za ajira kwa Maafisa Masuuli na wengineo tutawachukulia hatua kali za Kisheria kwa mujibu wa Sheria, Kanuni pamoja na taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine iliyouliza, endapo kuna umuhimu wa kuwa na PDB au la!
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu Ofisi ya Rais ya kusimamia ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi. Ofisi hii ilianzishwa mwaka 2013 na niseme tu kwamba, ni ofisi ambayo kwa kweli ni ya muhimu sana. Ukiangalia katika manufaa mbalimbali ambayo yameshapatikana hadi hivi sasa, sekta takriban 13 za kipaumbele zimeweza kuutumia mfumo huu na zimeweza kufuatilia na kutekeleza miradi yake mbalimbali kwa kweli kwa mafanikio makubwa na tumeshuhudia mafanikio ya takribani asilimia 71.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia katika ushirikiano ambao PDB imekuwanao na Pemandu ya Malaysia, ni mfumo ambao ukiangalia Uingereza wameutumia, Rwanda wameutumia, Malaysia wameutumia na kwa kweli, wameona mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, pamoja na kwamba, sekta ambazo ziko katika mfumo huu ni 13, lakini hivi sasa Mahakama haikuwepo katika mfumo huu, lakini wenyewe walishaanza kutekeleza mapendekezo ya mfumo huu na wamefanya vizuri sana nawapongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalipongeza pia Jeshi la Polisi na ninapenda pia kupongeza mamlaka mbalimbali za maji Mijini kwa namna ambavyo wameimarisha utekelezaji wa majukumu yao, lakini vilevile namna ambavyo wamekuwa na mafanikio katika kupanga na kufuatilia matokeo ya miradi yao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia ofisi hii itakuwa ya muhimu zaidi hasa katika mwaka huu ambapo tumekuwa na mapinduzi katika maandalizi ya bajeti. Takribani asilimia 40 ya bajeti yote ya Serikali itaenda katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Usipokuwa na ufuatiliaji mzuri na tathmini, ni namna gani fedha zako zimeenda huko? Ni vipaumbele gani ulikuwanavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuwa na ripoti mbalimbali za kila wiki ili kuweza kujua namna miradi mbalimbali inavyotekelezwa. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, naendelea kuomba mamlaka mbalimbali ambazo ziko katika mfumo huu, lakini na nyingine ambazo bado hazijajiunga na Mfumo wa BRN basi wajitahidi kuona ni kwa namna gani wanaweza wakajiunganao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono Bajeti hii Kuu ya Serikali.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa niseme tu kwamba na mimi naunga hoja kuhusiana na mpango huu. Lakini pili, nichukue nafasi hii kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kwa kufikisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani. Lakini zaidi pia mwaka mmoja ambao umejaa mafanikio makubwa katika kuiongoza nchi yetu. Utendaji wake kwa hakika umetukuka, umeiletea sifa kubwa nchi yetu ndani na nje ya mipaka yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa niweze kujibu hoja chache kwa haraka. Hoja ya kwanza nisuala zima la usitishaji au ucheleweshwaji wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba sababu kubwa ambazo zilipelekea au zimepelekea kutotoa ajira mpaka hivi sasa; ya kwanza ni suala zima la uwepo wa watumishi hewa kama ambavyo tulikuwa tukisema, na idadi imekuwa ikiendelea kupanda, mpaka sasa hivi tumeshaondoa watumishi 19,629 hewa ambao kwa kweli wangeendelea kubaki katika orodha ya malipo wangeendelea kusababisha hasara kubwa takribani shilingi bilioni 19.7 kwa kila mwezi.
Mheshimiwa mwenyekiti, sababu ya pili, baada ya kuwa tunaendelea kuhakiki watumishi hewa tulibaini pia uwepo wa vyeti vingi vya kughushi, tukaona hapana ni lazima tuhakikishe kwamba tunakuwa na ajira mpya baada ya kuwa tumehakikisha kwamba katika mfumo wetu wa ajira basi wale walioko katika ajira ni wale tu wenye sifa zinazostahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya tatu ni uwepo wa miundo mkubwa katika Serikali na taasisi zetu. Tulipopunguza Wizara bado katika taasisi mbalimbali miundo ilikuwa haijafanyiwa tathmini, tumeshaanza huo mchakato na mchakato unaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwa sasa tumeanza kuimarisha mifumo ya utambulisho na ninawapongeza sana NIDA pamoja na wote walioshiriki katia zoezi, tumeongeza alama za utambulisho. Mwanzoni ilikuwa tu ni jina na check number, lakini hivi sasa walau tunaweza tukapata picha ya mtumishi wa umma, tunaweza tukapata alama za vidole pamoja na namba ya utambulisho wa Taifa katika kuhakikisha kwamba hakuna alama ambayo inaweza ikagushiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana pia na suala la muundo tumekuwa tukiangalia pia kuhakikisha kwamba tunakuwa na muundo wenye tija na muundo ambao unahimilika. Lakini vilevile tutaendelea kuhakikisha tunafanya uhakiki ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na watumishi wale tu ambao wana sifa. Lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wanaotusikiliza wakati wowote sasa hivi hatua tumefika pazuri tutatangaza ajira muda sio mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kulikuwa kuna hoja ilitolewa na Mheshimiwa Zitto Kabwe kwamba ni nani anasema ukweli kati yangu na Waziri wa Fedha. Nimwambie tu kwamba Serikali ni moja, Waziri wa Fedha anasema ukweli na mimi pia ninasema ukweli. Kigezo cha kusema kwamba watumishi hewa; naomba tusikilizane ili muweze kuipata hoja vizuri halafu mtakuja kupinga mnavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hewa wameondoka 19,629, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataeleza kwa kina sana. Lakini ipo michakato mingine wage bill maana yake ni nini, ni lazima Mheshimiwa Zitto Kabwe afahamu. Bajeti ya mishahara ina include vitu vingi sana, kuna masuala mazima ya upandishwaji vyeo, kuna masuala mazima ya upandishwaji wa madaraja, huwezi kuwa kuna mtu anastaafu usimrekebishie mshahara wake akajikuta anaathirika katika malipo ya pensheni.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Zitto Kabwe, mimi na Mheshimiwa Mpango wote tupo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili alisema pia kwamba tumesema tunaokoa shilingi bilioni 17 kila mwezi, hatujasema hivyo, tunachokisema kwamba endapo watumishi hewa 19,000 kwa mfululizo kuanzia mwezi Machi mpaka sasa hivi wasingeondolewa kwa mkupuo (cummulative), basi katika mwezi husika wa mshahara wangeisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 19.7. Lakini hakuna popote tuliposema kwamba kila mwezi Serikali inaokoa shilingi bilioni 17. Lakini maelezo ya kina Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataeleza vizuri sana na nini kimefanyika na niliomba rekodi hiyo iweze kuwekwa sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kipekee kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kutekeleza Mradi wa Same – Mwanga – Korogwe. Mradi huu ni vema ukakamilishwa mapema kwa mujibu wa mpango kazi ili wananchi waweze kunufaika. Aidha, ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kuhakikisha dola milioni 97.6 zinapatikana ili Vijiji vya Hedaru, Mabilioni, Gavao, Makanya, Mgwasi, Bangalala, Mwembe, Njoro, Ishinde, Ruvu, Bendera na vinginevyo vipate uhakika wa maji kwa wananchi 264,793 wa Wilaya ya Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa uboreshaji unaoendelea katika Jiji la Dar es Salaam katika sekta ya maji. Wizara ione haja ya kuharakisha utafutaji wa fedha ili kuanza ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kidunda na Kisima cha Kimbiji na Mpera. Aidha, natoa rai Serikali ikamilishe ujenzi wa Tanki jipya la Changanyikeni na Kituo cha Kusukuma Maji Makongo katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa Serikali kuona umuhimu wa kuweka mfumo mpya wa kusambaza maji katika maeneo yasiyokuwa na mtandao wa mabomba. Ni vema basi mkandarasi apatikane na fedha za ujenzi wa mifumo hii mipya zitafutwe mapema ili wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo waweze kusambaziwa maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya, ili kuweza kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji, ni muhimu visima vingi zaidi vikachimbwa ili wananchi ambao hawapati maji waweze kupata. Aidha, maeneo kama ya Kigamboni na mengineyo yaangaliwe ili nayo yaweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni muhimu pia Kijiji cha Suji – Malindi -Kitunda (Same, Kilimanjaro) waweze kusambaziwa mfumo wa mabomba ili waweze kupata maji ya kutosha na waweze pia kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji maana mfumo uliopo sasa ni wa zamani sana na uliwekwa wakati eneo hili lilikuwa na wananchi wachache. Aidha, maji kupitia Msitu wa Shengena yapo, ni suala tu la kutandaza mabomba yenye uwezo mkubwa ili nao wapate maji ya kutosha. Eneo hili ni la mlimani, hawajanufaika na Mradi wa Same – Mwanga – Korogwe, hivyo, ni vema na maeneo ya milimani nayo yaangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais. Nampongeza kwa hotuba yake nzuri ambayo kwa kweli imeeleza masuala mengi kwa kina na mafanikio mbalimbali ambayo wameyapata katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe ufafanuzi au maelezo katika hoja ya ajira katika Taasisi za Muungano pamoja na mgawo au utaratibu wa mgawo wa nafasi hizo za ajira katika Taasisi za Muungano. Iko hoja iliyotolewa hapa kwamba, suala hili halijarasimishwa, suala hili haliko kisheria, suala hili watendaji wanaweza wakaharibu wasieleze ukweli katika mgawo huu na mambo mengine. Napenda tu kusema mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa utaratibu huu haukuwepo huko nyuma. Ni jitihada katika kuondoa changamoto katika Muungano ikaonekana kuwe na utaratibu mahsusi kabisa kwa ajili ya mgawo wa nafasi za ajira katika taasisi za Muungano. Utaratibu huu pia ni wa muda katika kuhangaikia suluhisho la kudumu ambalo litasaidia kuweka nafasi hizi na utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nafasi za vyombo vya ulinzi na usalama haziko katika mgawo huu wa asilimia 21 Zanzibar na asilimia 79 katika SMT. Ukiangalia katika mwaka 2013/2014 na 2014/2015, katika nafasi zilizotolewa katika Wizara ya Mambo ya Nje asilimia 25 zilichukuliwa na SMZ na asilimia 75 ndiyo zilichukuliwa na SMT. Kwa hiyo, hata hapo utaweza kuona pia, hata ule mgawo wa asilimia 21 ulizidi mpaka asilimia 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda katika Taasisi za NIDA, ukienda katika Ofisi ya Makamu wa Rais yenyewe, Zanzibar walipata mgawo katika ajira za 2013/2014 asilimia
33. Imezidi hata ile asilimia 21 ambayo ilikuwa imewekwa katika utaratibu wa mgawo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Taasisi nyingine nia ni njema. Nyingine ajira zake zilifanyika kabla ya waraka huu haujatungwa mwaka 2013/2014, lakini bado kama Serikali pande zote mbili tumekuwa tukilifanyia kazi pamoja na Waziri wa Utumishi kutoka SMZ, SMT na Ofisi ya Makamu wa Rais, tumekuwa tukiliangalia suala hili kwa kina na Mheshimiwa Makamu wa Rais amekuwa pia akilifuatilia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa inayokuja katika maombi ya ajira, kwanza wengine unakuta hawajitokezi, hawaziombi. Pili, lazima tuangalie pia na sifa. Huwezi tu pia ukagawa nafasi bila kuangalia sifa na vigezo. Tumekuwa tukiendelea kuhamasisha Wazanzibari waendelee kujitokeza pamoja na Bara ili kuhakikisha kwamba asilimia 79 na asilimia 21 inaweza kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, changamoto nyingine ambayo tunaipata katika kupata taarifa sahihi, unakuta wapo wanaotoka upande wa Zanzibar wamekuwa pia wakiomba nafasi, lakini unakuta wengine wamekuwa wakitumia anuani za kutoka Tanzania Bara. Kwa hiyo, unajikuta kuweza ku-compute namba kamili imekuwa kidogo ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ziko taasisi mbalimbali za kiuhasibu, nafasi nyingine katika sekta ya elimu, nafasi nyingine katika sekta ya afya, ambazo hata siyo taasisi za Muungano, Wazanzibari wamekuwa wakipata fursa na wamekuwa wakiomba, hawakatazwi. Fursa iko wazi kwa sababu, wote ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunaendelea kufanya jitihada kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Tumeshafungua ofisi eneo la Shangani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaratibu ajira zote za Taasisi za Muungano pamoja na kurahisisha na kuendesha majukumu yake wakiwa Mjini Zanzibar ili kurahisisha zaidi kwa waombaji kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuwa tukiendelea kutangaza nafasi za ajira pia kwa kutumia Vyombo vya Habari vikiwemo vya Zanzibar ili kuwahamasisha Wazanzibari kuhakikisha kwamba nafasi zinazotangazwa waweze kuomba. Nia ni njema na tutaendelea kufanya hivyo kila mara inapobidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Afya. Kipekee nipende kumpongeza sana pacha wangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya katika kuboresha utoaji wa huduma ya afya, masuala ya maendeleo ya jamii, ulinzi kwa mtoto pamoja na masuala mengine ambayo yako chini ya usimamizi wa Wizara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu kuongelea suala kubwa kuhusiana na ajira. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kwa hisia kubwa, lakini lengo kubwa ikiwa ni kupaza sauti kwenye suala zima la umuhimu wa kuwa na watumishi katika sekta ya afya wanaotosheleza kwa ajili ya kutoa huduma ya afya iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka 2015, Ofisi yangu imetoa vibali vya ajira 52,947 kwa ajili ya kada mbalimbali katika sekta ya afya. Ukiangalia katika mwaka huo huo miaka hiyo mitano takribani watumishi 14,860 hawakuripoti katika vituo walivyopangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa, mahitaji ni makubwa lakini udahili katika vyuo vyetu pia haujajitosheleza na tumeshaanza kuchukua hatua ya kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na vyuo vikuu vinavyotoa taaluma hizo ili kuona ni kwa namna gani wanaweza kuongeza udahili ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na wataalam wa kutosha watakaotosheleza soko letu la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza kuchukua hatua, kama ambavyo mmeshasikia tumeshaanza kuajiri watumishi wa sekta ya afya, Madaktari 258 na tayari wameshapangiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, Kibong’oto pamoja na Mirembe. Vile vile kwa upande wa TAMISEMI wamewapangia pia katika Halmashauri mbalimbali za Wilaya pamoja na Halmashauri nyingine za miji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza jana na leo pia nilieleza; kwa kutambua zoezi letu lililokuwa likiendelea, baada ya matokeo ya uhakiki wa vyeti; tunatambua ni kweli katika hospitali nyingi, katika vituo vingi vya afya na zahanati kumekuwa na upungufu mkubwa baada ya baadhi ya watumishi nao kuwa wamekumbwa na kadhia hiyo. Tumechukua hatua za haraka na za makusudi, tumeshatoa kibali cha ajira kwa ajili ya watumishi 15,000 na tutaweza kuwapangia. Tumeanza mashauriano na TAMISEMI ili kuweza kujua ikama ikae vipi, eneo gani lina upungufu mkubwa; na tunaamini kwa wiki ijayo zoezi hili litaweza kufika katika sehemu nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, hii ni kati ya sasa na mwezi Juni, lakini kwa kiasi kikubwa watumishi wengi pia watakuwa katika sekta ya afya. Kwa hiyo, niwatoe hofu sana Waheshimiwa Wabunge, tutajitahidi kucheza na namba hizo 15,000 na tunaamini zitaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza upungufu mkubwa wa wataalam wetu uliopo katika sekta hii ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika mwaka ujao wa fedha kuanzia mwezi Julai tutatoa pia tena ajira nyingine 52,436 na kwa kiasi kikubwa ajira nyingi zitakwenda katika sekta ya afya, elimu pamoja na Sekta nyingine. Kwa hiyo niwatoe tu hofu Waheshimiwa Wabunge, nimewasikiliza vizuri na tutaangalia kwa kweli ikama imekaa vipi kuhakikisha kwamba yale maeneo ya pembezoni, maeneo yenye upungufu mkubwa na kada zile za kipaumbele basi zitaweza kutendewa haki kama ambavyo inahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda nizungumzie suala zima la telemedicine. Nilimsikia Mheshimiwa Mbunge mmoja wa Mbeya akielezea umuhimu wa kuweza kutoa matibabu au rufani kwa njia ya telemedicine. Bahati nzuri kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi yangu Wakala wa Serikali Mtandao tunahimiza masuala ya matumizi ya TEHAMA katika huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kupitia mradi wa RCAP ambao tunafadhiliwa na Benki ya Dunia na kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tumeshaweza kujenga mfumo huu wa telemedicine na mfumo umekamilika, lakini vile vile tumeshafunga vifaa mbalimbali na tumesimika mfumo katika vituo vyote isipokuwa Mafia ambako kulikuwa kuna changamoto kidogo ya mawasiliano lakini tunaendelea kuifanyia kazi na naamini suluhisho litaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshatoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huu wa telemedicine, lakini vile vile tutaanza majaribio kuanzia tarehe 15 Mei mwaka huu hadi tarehe 15 Juni na tunaamini majaribio haya tutayafanya katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Hospitali ya Wilaya ya Nyangao Lindi Vijijini, Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, Hospitali ya Rufaa Morogoro, Hospitali ya Wilaya Turiani, Hospitali ya Wilaya Kilosa pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Baada ya majaribio hayo tunaamini sasa tutakuwa katika nafasi nzuri zaidi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kwenda katika hospitali zote kama nilivyoeleza awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni suala zima la maslahi kwa watumishi wa sekta ya afya. Waheshimiwa Wabunge wameeleza kwa hisia kubwa na ni kweli tunatambua risk mbalimbali ambazo wataalam hawa wanakutana nazo wanapokuwa wanatenda kazi zao. Vile vile tumejitahidi kuweka aina mbalimbali za maslahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kubwa na rai kwa waajiri, wanapopanga bajeti zao wahakikishe wanazingatia stahiki mbalimbali za watumishi wakiwemo watumishi wa sekta ya afya. Waangalie masuala mazima ya on-call allowances. Wameeleza Waheshimiwa Wabunge masuala ya upungufu wa uniforms na wamefanya mpaka comparison kwa nini sekta nyingine wananunuliwa na sekta nyingine hazinunuliwi. Tuombe sana kwa masuala ya muhimu kama haya ni vema mwajiri katika first charge ya vipaumbele vyake akaweka masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niseme naunga mkono hoja hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapende kipekee kumpongeza sana Mheshimiwa dada yangu, Profesa Ndalichako pamoja na Mheshimiwa Injinia Manyanya, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na utendaji mzima wa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya katika usimamizi wa sekta yetu ya elimu, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda tu kutoa ufafanuzi katika hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa na tunashukuru sana kwa hoja hizo; la kwanza ni kuhusiana na ulipaji wa madai ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madai ya malimbikizo ya mishahara vilevile yapo madeni ambayo yanahusiana na masuala mengine kama uhamisho, nauli na mengineyo ambayo siyo ya mishahara. Ukiangalia katika mwaka 2015/2016, tulilipa walimu 18,702 malimbikizo ya mishahara ya zaidi ya shilingi bilioni 13.9. Vilevile katika mwaka huu wa fedha katika kipindi cha Julai mpaka sasa tulipofikia, tumeweza kulipa madai ya walimu 12,037 yenye jumla ya takribani shilingi bilioni 12.6, vilevile tunaendelea kuhakiki madai yao, pia tumeendelea kuhakiki madai ya malimbikizo ya mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia tumeendelea kuhakiki madai ya malimbikizo ya walimu 8,155 yenye jumla ya shilingi bilioni 9.7.

Ninashukuru sana kwa Wizara ya Elimu kupitia mradi wa P for R wameweza kulipa zaidi ya shilingi bilioni 10.5 na Serikali tumeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 42.3 kwa watumishi mbalimbali ambao wana madai yasiyokuwa ya mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo mengine ya malimbikizo tunaendelea kuyafanya wakati wowote uhakiki utakapokamilika basi yataweza kulipwa. Kulikuwa kuna hoja kwamba wako ambao walipandishwa cheo au vyeo lakini walikuwa hawajarekebishiwa mishahara yao na Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii walitaka kufahamu ni kwa nini suala hili limejitokeza. Kama Wabunge watakumbuka tulipotoa uamuzi wa kuahirisha ajira mpya tarehe 13 Juni, masuala yote haya ya kimaendeleo ya kiutumishi nayo pia yalisimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapoingia katika mwaka ujao wa fedha, watumishi ambao walikuwa wanastahili kupata vyeo vyao wataweza kurekebishiwa na kupata vyeo sahihi vya kimuundo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge katika suala zima la upandishwaji wa vyeo, katika mwaka ujao wa fedha 2017/ 2018, tumetenga au tumekasimiwa kupandisha vyeo watumishi wa umma 193,166, kwa hiyo tunaamini tutakuwa tuko vizuri na wote wanaostahili kupata vyeo vyao kwa mujibu wa sifa zinazohitajika na vigezo basi wataweza kupandishwa vyeo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya hospitali ya Mloganzila kwamba inashindwa kufaya kazi kutokana na upungufu wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kusema kwamba tumeshapeleka watumishi 50 na katika ajira mpya ambazo tumetoa kibali cha Wizara ya Afya na TAMISEMI 258 tumewapelekea tena watumishi wengine kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo walikuwa na nafasi wazi 213, kitu ambapo tunachokifanya sasa tumewapa kibali na kuwahamisha kutoka kwa watumishi wengine walioko ndani ya Serikali na tayari kati ya idadi hiyo 213, watumishi 109 wamesharipoti na tunasubiri hao 104 wengine tunaendelea kujaza nafasi zao kwa njia ya uhamisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea pia na tunatarajia kabla hatujamaliza mwaka huu wa fedha, tutatoa pia kibali cha ajira mpya kwa Mloganzila 105 mpaka tutakapomaliza mwaka huu wa fedha mwezi Juni, watakuwa wamepata watumishi wapya 378 na tutaendelea kufanya hivyo mwaka hadi mwaka kuhakikisha kwamba wanapata Ikama ambayo wanaweza wakafanya nayo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya upungufu wa walimu pamoja na wataalam wa maabara. Tayari tulishatoa kibali na tumeanza na Walimu wa Sayansi 4,129 na tayari ofisi ya TAMISEMI imeshawapangia vituo wameshaanza kazi. Vilevile tumetoa kibali cha Wataalam wa Maabara 219 na tayari 137 hadi sasa wameshapatikana na tutaendelea kufanya hivyo.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi naanza moja kwa moja kwa kuunga mkono hoja hii, na kipekee namshukuru sana Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake, Makatibu Wakuu na uongozi mzima wa wizara kwa kuja au kwa kuandaa bajeti hii nzuri sana ya Serikali kwa mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi niungane na wasemaji waliotangulia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia rasilimali zetu, maliasili na madini katika kuhakikisha kwamba zinatumika kwa manufaa ya taifa letu. Waheshimiwa Wabunge kama tutakumbuka mwaka 2015 wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa akizindua Bunge hili, alieleza vipaumbele kadhaa na nipende tu kupongeza sana bajeti hii ya Serikali kwa kiasi kikubwa imeweza kutimiza vipaumbele vile au imeanza kufanyia kazi vipaumbele hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alieleza namna ambavyo atahakikisha kwamba anakuza uchumi, alielezea namna ambavyo ataziba mianya ya mapato ya Serikali; na kwa kweli nipongeze sana Wizara ya Fedha, tumeweza kuona e- government payment system namna ilivyoanza, tumejionea mifumo ya kielektroniki katika Serikali za Mitaa, lakini pia tumejionea namna TRA pamoja na ZRB namna ambavyo wameboresha mifumo yao ya malipo. Ni kwa kufanya hivi ndipo tutapata bakaa ya kuweza kupata fedha na kuboresha huduma nyingine za Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia aliahidi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali. Tumeweza kujionea namna ambavyo hata sasa safari za nje ya nchi ni zile tu ambazo ni za lazima. Hata kwa wale ambao wanaenda, ukiangalia ujumbe wao (delegation) kidogo kwa kiasi kikubwa imepungua na kwa kweli imekuwa ikileta tija na kutusaidia kupata fedha kwa ajili ya huduma zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi tumeona namna utawala bora unavyoendelea kudumishwa, tumeona namna ambavyo mapambano dhidi ya rushwa yanavyoendelea, na mmeona katika wiki kadhaa kesi zinazidi kwenda mahakamani. Nipende tu kusema kwamba kupitia TAKUKURU na Serikali nzima kwa ujumla hatutafumbia macho mtu yeyote ambaye atataka kuchezea rasilimali, ambaye atafanya ubadhirifu wa mali za umma akifikiri tu kwamba ataweza kuchezea kwa kuwa Serikali haipo macho.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba TAKUKURU iko macho, itaendelea kufanya hivyo na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafuatilia miradi yote ya maendeleo na tunaomba tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi watupatie ushirikiano ili kuhakikisha kwamba haya yanafanyika.

Mheshimiwa Spika, moja ya vipaumbele vingine ilikuwa ni kufanya mabadiliko makubwa ya utendaji Serikalini. Wote mtashuhudia sasa hivi mkienda katika taasisi mbalimbali za umma kwa kiasi kikubwa huduma imeboreka sana. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi muendelee kutupatia ushirikiano, itakapotokea unaenda kupata huduma unaombwa rushwa tafadhali toa ripoti katika namba 113 ili tuweze kuchukua hatua dhidi ya yeyote ambaye anataka kukupatia haki yako mpaka uwe umefanya malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sasa nielekee katika hoja chache ambazo zilijitokeza kuhusiana na ofisi yangu au masuala ya kiutumishi. Ilikuwepo hoja kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2017/2018 nyongeza ya mshahara haijaonekana katika bajeti. Nipende tu kusema kwamba ukiangalia bajeti ya mwaka 2016/2017 ilikuwa ni ya shilingi trilioni 6.6; bajeti ya mwaka huu 2017/2018 ni shilingi trilioni 7.205, kuna nyongeza hapo ya zaidi ya shilingi bilioni 605 ambayo ni sawa na asilimia 9.18. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha hizi tumepanga sasa zitatumika kwa ajili ya kulipia mishahara ya watumishi mbalimbali, lakini pia fedha hizi zitatumika katika kulipia malimbikizo ya maslahi mbalimbali ambayo watumishi wanadai, pia tutatumia katika ajira mpya. Kama nilivyoeleza tumepanga kuajiri watumishi 52,436. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo ambao wamekuwa wakisema kwamba uhakiki umekuwa ukiendelea muda mrefu. Nipende tu kusema kwamba kama una Serikali makini ni lazima pia uweze kufanya uhakiki ili kujiridhisha kwamba unalipa watumishi wale tu ambao kweli ndio umewakusudia; tumeondoa zaidi ya watumishi hewa 19,708. Endapo watumishi hawa wangeendelea kuwepo katika orodha ya malipo ya Serikali au payroll, kila mwezi Serikali ingepoteza takribani shilingi bilioni 20, si fedha ndogo. Sasa hivi tunatumia shilingi bilioni 18.8 kila mwezi kulipia elimu katika shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wewe ujiulize kama mafanikio yote haya yanapatikana kwa fedha hizo halafu upande mwingine kulikuwa kuna zaidi ya shilingi bilioni 20 kila mwezi zilikuwa zinaondoka kwa ajili ya watumishi hewa. Kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba watasema tunaendelea na uhakiki, tunaonekana tumekuwa maarufu kwa uhakiki, naomba bora niwe hivyo na nitaendelea kuwa Waziri wa uhakiki ikibidi ili kuhakikisha kwamba hakuna hata fedha moja ya Serikali ambayo inapotea; na kwa kufanya hivi ndipo tunapata walau ahueni ya fedha nyingine ya kuweza kuboresha maslahi ya watumishi pamoja na huduma nyingine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo ambao wanasema ajira hazijatoka, sio kweli. Tumeshaajiri ajira zaidi ya 9,000. Katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama watumishi mbalimbali wameajiriwa, wapo ambao walisema hawajaona ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama; wameshaajiriwa wote waliotoka katika mafunzo ya depo wameshaajiriwa, labda aseme kama kuna wengine ambao wako katika mafunzo ambao bado hawajaajiriwa.

Mheshimiwa Spika, tumeshaajiri walimu wa sayansi na hesabu, wataalam wa maabara na tutaendelea kufanya hivyo kwa kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu. Niwatoe tu hofu wahitimu wetu kwamba ajira wakati wowote zitaendelea kutolewa kwa awamu kwa mujibu wa sekta husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwamba katika sekta ya elimu zaidi ya watumishi 16,516 tutawaajiri mwaka huu, lakini pia katika sekta ya afya zaidi ya watumishi 14,102 tutaweza pia kuwaajiri na hii pia ni pamoja na kuongeza na nyongeza nyingine ya ku-replace wale ambao waliondoka kwa mujibu wa zoezi la uhakiki wa vyeti fake ambalo lilikuwa likiendeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine, nadhani ni ya Mheshimiwa Nsanzugwanko; kwamba Serikali baada ya kumaliza uhakiki wa vyeti feki ifanye performance audit. Nipende tu kumueleza kwamba ufanisi katika utoaji wa huduma unapimwa kwa kutumia vigezo vingi ikiwemo uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo, usahihi na uadilifu lakini vile vile kuangalia viwango na ubora wa huduma hiyo inayotolewa kwa mujibu wa fedha inayotolewa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: ...nipende tu kumwambia mifumo ipo, tunayo mifumo ya tathmini ya uwazi kabisa ya OPRAS, na kuanzia mwezi Julai, tutaanza kupima utendaji wa Taasisi zote za umma, tutawaanzishia performance contract watendaji wote wa taasisi za umma katika kuhakikisha kwamba wanaenenda kwa mujibu wa viashiria na kuona kwamba kunakuwa na utendaji mzuri.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru na niseme na mimi kwa ufupi naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi naanza moja kwa moja kwa kuunga mkono hoja hii, na kipekee namshukuru sana Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake, Makatibu Wakuu na uongozi mzima wa wizara kwa kuja au kwa kuandaa bajeti hii nzuri sana ya Serikali kwa mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi niungane na wasemaji waliotangulia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia rasilimali zetu, maliasili na madini katika kuhakikisha kwamba zinatumika kwa manufaa ya taifa letu. Waheshimiwa Wabunge kama tutakumbuka mwaka 2015 wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa akizindua Bunge hili, alieleza vipaumbele kadhaa na nipende tu kupongeza sana bajeti hii ya Serikali kwa kiasi kikubwa imeweza kutimiza vipaumbele vile au imeanza kufanyia kazi vipaumbele hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alieleza namna ambavyo atahakikisha kwamba anakuza uchumi, alielezea namna ambavyo ataziba mianya ya mapato ya Serikali; na kwa kweli nipongeze sana Wizara ya Fedha, tumeweza kuona e- government payment system namna ilivyoanza, tumejionea mifumo ya kielektroniki katika Serikali za Mitaa, lakini pia tumejionea namna TRA pamoja na ZRB namna ambavyo wameboresha mifumo yao ya malipo. Ni kwa kufanya hivi ndipo tutapata bakaa ya kuweza kupata fedha na kuboresha huduma nyingine za Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia aliahidi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali. Tumeweza kujionea namna ambavyo hata sasa safari za nje ya nchi ni zile tu ambazo ni za lazima. Hata kwa wale ambao wanaenda, ukiangalia ujumbe wao (delegation) kidogo kwa kiasi kikubwa imepungua na kwa kweli imekuwa ikileta tija na kutusaidia kupata fedha kwa ajili ya huduma zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi tumeona namna utawala bora unavyoendelea kudumishwa, tumeona namna ambavyo mapambano dhidi ya rushwa yanavyoendelea, na mmeona katika wiki kadhaa kesi zinazidi kwenda mahakamani. Nipende tu kusema kwamba kupitia TAKUKURU na Serikali nzima kwa ujumla hatutafumbia macho mtu yeyote ambaye atataka kuchezea rasilimali, ambaye atafanya ubadhirifu wa mali za umma akifikiri tu kwamba ataweza kuchezea kwa kuwa Serikali haipo macho.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba TAKUKURU iko macho, itaendelea kufanya hivyo na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafuatilia miradi yote ya maendeleo na tunaomba tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi watupatie ushirikiano ili kuhakikisha kwamba haya yanafanyika.

Mheshimiwa Spika, moja ya vipaumbele vingine ilikuwa ni kufanya mabadiliko makubwa ya utendaji Serikalini. Wote mtashuhudia sasa hivi mkienda katika taasisi mbalimbali za umma kwa kiasi kikubwa huduma imeboreka sana. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi muendelee kutupatia ushirikiano, itakapotokea unaenda kupata huduma unaombwa rushwa tafadhali toa ripoti katika namba 113 ili tuweze kuchukua hatua dhidi ya yeyote ambaye anataka kukupatia haki yako mpaka uwe umefanya malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sasa nielekee katika hoja chache ambazo zilijitokeza kuhusiana na ofisi yangu au masuala ya kiutumishi. Ilikuwepo hoja kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2017/2018 nyongeza ya mshahara haijaonekana katika bajeti. Nipende tu kusema kwamba ukiangalia bajeti ya mwaka 2016/2017 ilikuwa ni ya shilingi trilioni 6.6; bajeti ya mwaka huu 2017/2018 ni shilingi trilioni 7.205, kuna nyongeza hapo ya zaidi ya shilingi bilioni 605 ambayo ni sawa na asilimia 9.18. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha hizi tumepanga sasa zitatumika kwa ajili ya kulipia mishahara ya watumishi mbalimbali, lakini pia fedha hizi zitatumika katika kulipia malimbikizo ya maslahi mbalimbali ambayo watumishi wanadai, pia tutatumia katika ajira mpya. Kama nilivyoeleza tumepanga kuajiri watumishi 52,436. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo ambao wamekuwa wakisema kwamba uhakiki umekuwa ukiendelea muda mrefu. Nipende tu kusema kwamba kama una Serikali makini ni lazima pia uweze kufanya uhakiki ili kujiridhisha kwamba unalipa watumishi wale tu ambao kweli ndio umewakusudia; tumeondoa zaidi ya watumishi hewa 19,708. Endapo watumishi hawa wangeendelea kuwepo katika orodha ya malipo ya Serikali au payroll, kila mwezi Serikali ingepoteza takribani shilingi bilioni 20, si fedha ndogo. Sasa hivi tunatumia shilingi bilioni 18.8 kila mwezi kulipia elimu katika shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wewe ujiulize kama mafanikio yote haya yanapatikana kwa fedha hizo halafu upande mwingine kulikuwa kuna zaidi ya shilingi bilioni 20 kila mwezi zilikuwa zinaondoka kwa ajili ya watumishi hewa. Kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba watasema tunaendelea na uhakiki, tunaonekana tumekuwa maarufu kwa uhakiki, naomba bora niwe hivyo na nitaendelea kuwa Waziri wa uhakiki ikibidi ili kuhakikisha kwamba hakuna hata fedha moja ya Serikali ambayo inapotea; na kwa kufanya hivi ndipo tunapata walau ahueni ya fedha nyingine ya kuweza kuboresha maslahi ya watumishi pamoja na huduma nyingine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo ambao wanasema ajira hazijatoka, sio kweli. Tumeshaajiri ajira zaidi ya 9,000. Katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama watumishi mbalimbali wameajiriwa, wapo ambao walisema hawajaona ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama; wameshaajiriwa wote waliotoka katika mafunzo ya depo wameshaajiriwa, labda aseme kama kuna wengine ambao wako katika mafunzo ambao bado hawajaajiriwa.

Mheshimiwa Spika, tumeshaajiri walimu wa sayansi na hesabu, wataalam wa maabara na tutaendelea kufanya hivyo kwa kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu. Niwatoe tu hofu wahitimu wetu kwamba ajira wakati wowote zitaendelea kutolewa kwa awamu kwa mujibu wa sekta husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwamba katika sekta ya elimu zaidi ya watumishi 16,516 tutawaajiri mwaka huu, lakini pia katika sekta ya afya zaidi ya watumishi 14,102 tutaweza pia kuwaajiri na hii pia ni pamoja na kuongeza na nyongeza nyingine ya ku-replace wale ambao waliondoka kwa mujibu wa zoezi la uhakiki wa vyeti fake ambalo lilikuwa likiendeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine, nadhani ni ya Mheshimiwa Nsanzugwanko; kwamba Serikali baada ya kumaliza uhakiki wa vyeti feki ifanye performance audit. Nipende tu kumueleza kwamba ufanisi katika utoaji wa huduma unapimwa kwa kutumia vigezo vingi ikiwemo uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo, usahihi na uadilifu lakini vile vile kuangalia viwango na ubora wa huduma hiyo inayotolewa kwa mujibu wa fedha inayotolewa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: ...nipende tu kumwambia mifumo ipo, tunayo mifumo ya tathmini ya uwazi kabisa ya OPRAS, na kuanzia mwezi Julai, tutaanza kupima utendaji wa Taasisi zote za umma, tutawaanzishia performance contract watendaji wote wa taasisi za umma katika kuhakikisha kwamba wanaenenda kwa mujibu wa viashiria na kuona kwamba kunakuwa na utendaji mzuri.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru na niseme na mimi kwa ufupi naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Niungane na wenzangu kwa kuwapongeza sana Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri pamoja na Makatibu Wakuu na wengine wote katika Wizara hii, kwanza kwa namna ambavyo wanachochea uwekezaji katika viwanda lakini pia kwa namna ambavyo wanasimamia kuhakikisha kwamba biashara zinashamiri tukitambua kwamba biashara na sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zimejitokeza hoja mbalimbali, ntajitahidi kwa ufinyu wa muda kujibu baadhi, hususani nipende kuingia katika hoja ya wingi wa taasisi za udhibiti nikiunganisha pamoja na mazingira bora ya uwekezaji na biashara. Kama ambavyo tumekuwa tukisema, lakini pia hata katika hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara imejitokeza, Serikali katika nyakati mbalimbali kuanzia wakati wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara wakati wa BEST Programme mwaka 2003 lakini pia mwaka 2010 ulipoundwa Mpango Kazi au Mwelekeo wa Roadmap, pia mwaka 2017/2018 ambapo Serikali ilikuja na mpango wa kuangalia mifumo mbalimbali ya taasisi za kiudhibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari kama Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara imekuwa ikiliangalia suala hili kwa kina na hasa kuangalia changamoto ambazo zimekuwa ndiyo vikwazo katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwekezaji mkubwa lakini pia biashara kuweza kukua. Napenda tu kusema kwamba tayari Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara nyingine katika sekta mbalimbali, tumeshachukua hatua kupitia mapendekezo yote ambayo yametolewa katika roadmap pamoja na blueprint, tumeendelea kuandaa mpangokazi wa blueprint pamoja na ile comprehensive action plan.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hilo tu, Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenyewe kwa kutambua kwamba yeye ndiye mratibu na msimamizi wa shughuli mbalimbali za Serikali, tayari alishaitisha kikao tarehe 17 Aprili, lakini pia tarehe 18 Jumamosi hii tena tutakua na kikao na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Wizara mbalimbali ili kuweza kupitia kwa kina changamoto na vikwazo vyote ambavyo vimekuwa vikichangia kutokua kwa biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba tayari Serikali inaendelea kuyafanyia kazi. Kwa kutambua hili, tayari ziko tozo ambazo zimependekezwa kuondolewa. Naamini kwa kuwa tumeshaziwasilisha Wizara ya Fedha kupitia ile Task Force ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ya kuangalia maboresho ya kodi, katika Muswada wa Fedha ambao utaletwa mwezi Juni nyingi mtaweza kujionea mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo tozo ambazo Mheshimiwa Waziri wa Afya amezipendekeza kupitia TFDA, zipo ambazo zitafutwa kabisa, lakini tunaamini zipo ambazo zitapunguzwa. Pia katika Bodi yetu ya Maziwa, Bodi yetu ya Nyama pamoja na taasisi nyingine za Kiserikali, TBS na nyinginezo, yapo mapendekezo mengi tu ambayo Wizara mbalimbali zimeweza kuyawasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba suala zima la mifumo ya udhibiti tunaliangalia ili kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu pamoja na wawekezaji wanafanya biashara zao na wanakuwa na uwekezaji ambao unashamiri bila kuwa na vikwazo vya aina yoyote. Naamini tutaweza kujionea mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Lucy Mayenga ya kuleta mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji. Kwanza, nimshukuru kwa kuleta hoja hii, ni hoja ambayo pia kama Serikali tumeiona tukitambua kwamba Sheria yetu ya Uwekezaji ni ya muda mrefu, ni takribani miaka 22 na ukiangalia mambo ambayo yaliasisiwa na kuakisiwa wakati huo, mwaka 1997, inawezekana kabisa hayaendani na mazingira ya sasa ya mwaka 2019 na baadaye. Pia kuangalia suala zima la ushindani baina yetu na nchi nyingine Afrika pamoja na nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijahitimisha endapo muda utaniruhusu, wapo wengi sana ambao wamezungumzia masuala ya kuomba viwanda Muheza, wengine wamezungumzia masuala ya kuwa na viwanda mbalimbali katika uchakataji wa mifugo, kilimo, uvuvi na mengineyo. Napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba katika azma yetu ya uwekezaji suala zima la kilimo, mifugo na uvuvi ni eneo ambalo limepewa kipaumbele kikubwa na ni moja ya vipaumbele namba moja katika kuvutia uwekezaji. Tunafanya hivi kwa kutambua kwamba zaidi ya asilimia 65.5 ya Watanzania wameajiriwa katika kilimo na tunafanya hivi kwa kutambua kwamba unapowekeza katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa kiasi kikubwa, tija yake ni kubwa na wananchi wanapata athari kubwa katika uwekezaji wa aina hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho tumekifanya hivi sasa kwa kushirikiana na Mheshimiwa Jenista na Mawaziri wengine ambao wanasimamia kilimo, mifugo na uvuvi; tunaandaa programu maalum ya uwekezaji mahsusi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuangalia vikwazo zaidi ni nini kupitia Mradi wetu wa ASDP II.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaanza mashauriano na Taasisi Isiyokuwa ya Kiserikali au Mdau wa Maendeleo AGRA ili kuja na programu jumuishi kabisa ambayo itasaidia kuangalia sekta binafsi katika kilimo, mifugo na uvuvi ni nini hasa imekuwa ni kikwazo, tunafanyaje kuwekeza katika mbegu, tunafanyaje katika masuala mazima ya trekta, teknolojia, pembejeo, mitaji na mambo mengine kwa ujumla wake ili tuangalie mnyororo mzima wa uzalishaji na uchumi katika sekta nzima ya kilimo, mifugo na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kwa kufanya hivi tutaweza kupiga hatua kubwa na na Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wataweza kujionea mabadiliko makubwa. Hatufanyi tu katika kilimo, mifugo na uvuvi, tutaendelea pia kuangalia sekta zingine ambazo tunaamini zitaweza kuwa na tija na athari kubwa katika uchumi na uwekezaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine waliounga mkono hoja hii kipekee nipongeze sana Kamati yetu ya Katiba na Sheria kwa kazi nzuri waliyoifanya lakini kwa taarifa nzuri waliyoiandaa nishukuru kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana nasi pamoja na Mheshimiwa Waziri mwenzangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista kwa kweli wamekuwa wakitupa ushirikiano mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia masuala machache la kwanza kuendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba kwa upande wa uhamasishaji na kuvutia mitaji ya uwekezaji tunaendelea kufanya jukumu hilo na wawekezaji wamekuwa wanakuja kwa wingi na kwa mwaka uliopita tumeweza kupata takribani uwekezaji wenye mtaji wa zaidi ya Dola Bilioni 2.8 na tunaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja nadhani ya Mheshimiwa Jitu ilijitokeza kwamba tuone namna gani tunaendelea kujenga wawekezaji wazawa zaidi jukumu hilo tunaendelea kulifanya na ukiangalia katika Usajili wa Miradi ile ambayo imesajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania zaidi ya asilimia 48 ilikuwa ni Miradi ya wazawa na tunaendelea kuhamasisha na tunatoa rai wazawa wengi zaidi ikiwezekana waweze kusajili Miradi yao TIC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kutokuwa na uratibu au kutokuwa na ushirikiano baina ya Wizara na Taasisi nipende tu kusema kwamba tunaendelea kushirikiana vizuri na tutaendelea kuboresha namna ambavyo tunaendelea kuratibu lakini vilevile kushughulikia masuala mbalimbali ya Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya ucheleweshwaji wa huduma na Kamati imeweza kutoa ushauri mzuri sana ya kuweza kutumia zaidi huduma za kielektroniki nipende kusema tu kwamba tumeanza na kwa kuanzia kwa sasa walau katika Idara yetu ya kazi wameunganishwa katika Mfumo wetu wa Kituo cha kazi kupitia Mifumo ya Vibali vya Kazi na kwa sasa vingi vinatolewa pia kwa mfumo wa elektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sasa pia tumeandaa mfumo kwa ajili ya kuweza kutoa mrejesho kutoka kwa wawekezaji na wafanyabiashara lakini vilevile kwa Wafanyabiashara wetu na wawekezaji kuweza kutoa malalamiko yao kupitia mfumo wa kielektroniki na ni jukumu ambalo tunashirikiana Ofisi ya Waziri ya Mkuu, CPSF pamoja na Baraza letu la Biashara la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya suala zima la utelekezaji wa blueprint nipende tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ndiyo wamepewa jukumu hili, Wizara ya Viwanda na Biashara tayari wameshaandaa mapendekezo na tunaamini mchakato ndani ya Serikali utakapokamilika basi mapendekezo hayo kwa ajili ya kutunga Sheria ya Uwezeshaji wa Biashara au business facilitation Act yatawasilishwa Bungeni mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa Sheria yetu ya Uwekezaji ambayo kimsingi tutaupitia upya muundo wa TIC lakini kuangalia masuala mbalimbali ya kitaasisi na namna ambavyo tunashirikiana na Taasisi nyingine. Vilevile mipaka ya Taasisi moja na Taasisi nyingine katika kuvutia na kuhamasisha uwekezaji na masuala mazima ya uratibu wa Uwekezaji nayo ni masuala ambayo tunakusudia kuyaingiza katika Sheria hiyo ambayo itakuja humu bungeni muda si mrefu na tutaomba ushirikiano wenu Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja pia la ukosefu wa miundombinu wezeshi na ya msingi kwa ajili ya uwekezaji ni jambo ambalo tumeliona na ni kweli na tayari tunashukuru Ofisi ya Waziri ya Mkuu kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumeendelea kuzihamasisha halmashauri zetu kutenga maeneo ambayo yatakuwa na miundombinu ambayo inakidhi lakini vilevile miundombinu ya umeme, maji na Mawasiliano maeneo ambayo yatakuwa yamelipiwa fidia hayana mgogoro lakini yaliyopimwa na yaliyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili pia ilijitokeza hoja ya ucheleweshwaji wa suala zima la uhavilishaji kutoka katika ardhi ya Kijiji kwenda katika ardhi ya jumla ni eneo ambalo ni kweli limekuwa ni changamoto wakati mwingine Mwekezaji amekuwa akitumia miaka mitatu mpaka miaka minne kwa sababu ya mlolongo ambao unahitajika katika uhavilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hatua ambazo kutokana na mfumo wetu kama Tanzania wa Umiliki wa ardhi, ardhi ya Kijiji ukomo wake kuweza kuiuza ni eka hamsini tu. Kwa hiyo, kwenye hili hatuwezi kuliepuka lakini tunashukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweza kutoa maelekezo kwa halmashauri zote kuweza kuona ni kwa namna gani wataandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili waweze kuainisha maeneo yanayohitajika kwa uwekezaji na tunaamini halmashauri zetu na vijiji zitakapofanya hivyo basi wataweza kupunguza muda wa uhavilishaji lakini vilevile itatuhakikishia kuwa na uhakika wa ardhi ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuwatoa hofu Wana Vijiji ukiangalia kwa kila Kijiji kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa takwimu kama nitakuwa sijakosea haizidi kati ya milioni sita mpaka milioni nane. Kwa hiyo, ni muhimu waweze kuona umuhimu wa kutenga fedha kupitia mapato mbalimbali ambayo wanayapata ili kutekeleza jukumu hili ambalo ni la muhimu sana kwa ajili ya kuwa na uhakika wa utatuzi wa Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa kuna hoja ya mwingiliano wa majukumu ya Kitaasisi kama nilivyoeleza kupitia Sheria ile ya Uwezeshaji wa Biashara au business facilitation tunaamini suala hili pia kwa kiasi kikubwa litaweza kuondoka vilevile kwa sasa Serikali inaendelea kupitia majukumu ya baadhi ya Taasisi ili kuona ni kwa namna gani tutaweza kuondoa mwingiliano katika usimamizi vilevile kuona ni kwa namna gani tutaweza kupunguza muda na gharama kwa ajili ya uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaanza kwa TBS pamoja na TMDA tutaendelea vilevile kufanya kwa Taasisi nyingine za Serikali. Kulikuwa kuna hoja nyingine kuhusiana na kupunguza tozo tayari ndani ya miaka miwili Wizara ya Fedha na Mipango tuliona hapa kupitia Sheria ya Fedha imeleta zaidi ya tozo 163 kwa mwaka 2017/2018 tozo zaidi 109 ziliweza kufutwa lakini kwa 2018/2019 tozo zaidi ya 54 zimeweza kufutwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatua nzuri na tunaamini kadri tunavyoendelea na Bajeti ya Serikali basi Wizara ya Fedha na Mipango itakuwa ikiendelea kufanya hatua hiyo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa kuna hoja ya halmashauri zetu za wilaya pamoja na mikoa kuweza kutumia na kuutekeleza muongozo uliotolewa TNDC katika kufanya majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi tunashukuru bahati nzuri nimefanya Mikutano kwa kushirikiana na Mawaziri wengine wa kisekta zaidi ya Mikoa saba na tumekuwa tukipata ushirikiano mzuri sana kutoka TNDC vilevile kutoka katika mikoa na halmashauri zetu na wamekuwa wakisisitizwa kuona ni kwa namna gani wanaweza kutekeleza mwongozo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru lakini niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kuvutia na kuhamasisha Uwekezaji muhimu tu kwa halmashauri zetu Wabunge na wananchi kwa ujumla waweze kutambua manufaa ya Uwekezaji kwa ajili ya Taifa letu nakushukuru. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kujibu au kuchangia hoja hizi zilizoko mezani, na hasa hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa au LAAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na hoja ya kwanza, kuhusiana na kutokupeleka taarifa ya utekelezaji wa maazimio ambayo yalitolewa tarehe 04 Novemba, mwaka jana; nipende tu kusema kwamba, tayari tulishapeleka na tumewasilisha Ofisi ya Bunge na tunaamini itaweza kuwasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa mujibu wa taratibu. Kwa hiyo, kwenye hilo tulishawasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kumekuwa na hoja, na hususan changamoto ya nidhamu katika ukusanyaji na utumiaji wa mapato ya Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwenye hili nikubali, ni kweli changamoto hii ipo. Tumekuwa tukiendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba tunafuatilia, lakini vilevile kuhakikisha kwamba fedha hizi zote zilizoko katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, zilizokusanywa, zinatumika kama ambavyo inatakiwa kwa mujibu wa kanuni na sheria zetu za matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kuimarisha udhibiti tumeendelea kuboresha pia ofisi za wakuu wa mikoa na hasa kupitia sekretarieti za mikoa yetu kwa kupitia na kuuangalia upya muundo wa sekretarieti zetu za mikoa. Kwenye eneo hili tumeendelea kuhakikisha kwamba, tunaanzisha section ya usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi ambayo pamoja na mambo mengine watakuwa pia na jukumu la kuweza kusimamia, kufuatilia, lakini pia kukagua shughuli mbalimbali ambazo zinatekelezwa katika mikoa, lakini pia katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizoko chini ya mikoa yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa wakuu wa sections katika mikoa 22 tayari wameshapatikana, lakini vilevile tunaendelea na taratibu za kujaza wakuu wa sections katika mikoa minne katika sekretarieti za mikoa, ili kuhakikisha kwamba zinakuwa zimekamilika na wanatimiza majukumu yao ipasavyo. Si hilo tu, tumeendelea pia kuongeza fedha za matumizi mengineyo katika sekretarieti za mikoa kutoka bilioni
57.44 hadi kufikia bilioni 79.09. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunaziwezesha sekretarieti za mikoa na wataalam wetu katika sections hizo kuhakikisha kwamba wanaweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo likiwemo jukumu kubwa na la msingi la ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli mbalimbali za Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya kaguzi mbalimbali ambazo zimefanyika kupitia kwa Mkaguzi wetu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Ameweza kufanya kaguzi nyingi na nitagusia tu chache kama ambavyo na wenyewe kwenye Kamati wamegusia, hasa kuhusiana na ile kaguzi maalum ya Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Ubungo, Kigamboni, Iringa, na nikipata muda nitaweza kugusia au kujibia chache: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kusema kwamba baadhi ya maeneo kweli tunakubaliananayo na tunaendelea kuchukua hatua kwa kujibia hoja hizo za ukaguzi. Nipende tu kukuhakikishia Mheshimiwa Naibu Spika na Bunge lako, kwamba tayari kama Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali, lakini vilevile tumeiweka Manispaa ya Ilemela kwenye uangalizi wa karibu sana. Tunaendelea kuziangalia Manispaa na Halmashauri mbalimbali ikiwemo Bunda, Ilemela, Kigamboni, vilevile Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Morogoro pamoja na nyinginezo vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba, hatua hazichukuliwi. Watu wamekuwa wakiishia tu kuhamishwa. Nipende kukuhakikishia kwamba tunaendelea na hatua mbalimbali za kinidhamu, lakini vilevile za kijinai. Kwa yale ambayo yanatakiwa kuchukuliwa hatua mbalimbali za kiutumishi tayari tumeshatoa maelekezo katika sekretarieti zetu za mikoa kupitia makatibu tawala wa mikoa kuweza kuchukua hatua. Vilevile tayari kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU hatua mbalimbali pia zimeendelea kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumepata mrejesho kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU. Takribani watumishi nna wazabuni 672 wameshafanyiwa uchunguzi, lakini vilevile watumishi na wazabuni 46 kati ya hao uchunguzi wao tayari umeshakamilika kutokana na kutothibitika kwa tuhuma dhidi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile watumishi na wazabuni 53 majalada yao yako katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, kwa sababu ndio utaratibu, kwa ajili ya kuwaombea kibali cha kuweza kuwafikisha Mahakamani kwa ajili ya mshitaka ya jinai. Pia tayari watumishi na wazabuni 51 mashauri yao yako Mahakamani tunavyoendelea hivi sasa, lakini vilevile yako mashauri yanayowahusisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nipende kusema naunga mkono hoja na yote yaliyopendekezwa hapa tutayatekeleza na kuhakikisha kwamba hatua stahiki zinachukuliwa. Hatutamfumbia macho yeyote atakayetumia fedha kwa kukiuka taratibu. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipatia nafasi. Nianze na mimi kwanza kwa kuanza kuunga mkono hoja hii ya Bajeti ya Wizara yetu ya Ardhi na nimpe pongezi nyingi sana Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi na uongozi mzima wa Wizara hii kwa kuja na bajeti hii. Naamini itakuwa ni bajeti ya kihistoria, bajeti ambayo itaweza kutusaidia na kuweza kutoka, lakini zaidi kutatua migogoro mbalimbali na kuweza kuhakikisha kwamba tunakuwa na ardhi ambayo imepangwa, imepimwa lakini vile vile imeweza kumilikishwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze mpango walionao katika suala zima la usimamizi wa ardhi nikiamini katika fedha zile za mikopo, zitaweza kusaidia pia wanawake wengi zaidi kuweza kuwa na milki ya ardhi ambayo pia itaweza kuwasaidia wanawake wetu na vijana katika suala zima la uwezeshaji pia wananchi kiuchumi, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nitajikita zaidi katika suala zima la utatuzi wa migogoro. Tumeweza kuwasikia Waheshimiwa Wabunge na mna hoja ambazo ni za msingi tumezipokea. Hakuna hoja hata moja ambayo hatutaitilia maanani, tutaendelea kulifanyia kazi suala hili na kuhakikisha kwamba tunaendelea kushirikiana na wananchi lakini pia nanyi kama viongozi wao na wawakilishi katika suala zima la utatuzi wa migogoro hii yetu ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili tutaendelea pia kusimamia suala zima la utatuzi wa migogoro ya mipaka katika vijiji na vijiji, kata na kata, wilaya na wilaya lakini pia na mikoa, mmoja na mwingine kuhakikisha kwamba kila mmoja anajua mipaka yake sahihi na wananchi wetu wanajua pia wanaangukia katika eneo gani la mipaka, lakini kubwa zaidi kuweza kutatua migogoro ambayo kimsingi siyo ya lazima na ninaamini hili linawezekana kama ambavyo tumekuwa tukiendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea pia kuweka mkazo katika suala zima la mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kushirikiana na Tume yetu ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi tumeendelea kufanya hivyo. Ukiangalia mfano katika Wilaya ya Ifakara tumeweza pia kupima muda siyo mrefu. Mwaka jana tu vijiji zaidi ya 30 lakini vilevile kwa upande wa Serengeti zaidi ya vijiji 33 na tunaendelea pia kutenga fedha na hata Ikungi muda siyo mrefu pia tumeendelea kushirikiana na halmashauri na wadau mbalimbali ikiwemo UN Women katika kuhakikisha kwamba tunaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi, lakini kubwa tunaendelea kutenga fedha na tumezielekeza halmashauri zetu ziweze kutenga fedha katika suala zima la Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ili kuwa na matumizi sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kujikita pia katika eneo la Kamati za Mipango Miji; tunaendelea kusimamia Kamati zetu za Mipango Miji kuhakikisha kwamba kwanza zinafanya kazi kwa uadilifu, lakini vilevile kwa weledi unaokusudiwa kuhakikisha kwamba tunaenenda kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ambayo ipo na kwa kamati zile ambazo zitaonekana pia hazitimizi wajibu wao ipasavyo hatutaendelea kusita kuzivunja na kuweza kuunda zingine. Lengo tu ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na kamati ambazo kweli zina weledi, zina uadilifu lakini pia zinafanya kazi kwa ufanisi kuhakikisha kwamba hatuleti migongano na migogoro ambayo haina msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia tu kulihakikishia Bunge lako tukufu, tunaweka mkazo katika suala zima la kupanga, kupima na kumilikisha kama mamlaka za upangaji kupitia halmashauri zetu na tushukuru sana Serikali yetu. Tumeweza kupata zaidi ya shilingi bilioni 42.3 ambazo tumeshazikopesha kwa halmashauri takribani 54 na mwelekeo ni kuhakikisha kwamba fedha hizi tunaweza kuzikopesha, lakini pia zimetengewa mfuko maalum, hazichanganyiki na fedha zingine za halmashauri ili ziweze kuwa na mzunguko na kuweza kupanga miji yetu vizuri zaidi, kuweza kumilikisha, lakini pia wananchi wetu waweze kupata hati au kupata milki ambazo zitakuwa salama na ambazo zimeweza kupimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa kushirikiana na Wizara yetu ya Ardhi tutaendelea kusimamia suala zima la usimamizi wa sekta yetu hii sekta ambayo ni muhimu sana katika uchumi, lakini vilevile katika suala zima la maendeleo ya jamii, lakini pia maendeleo ya kiusalama na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema naunga mkono hoja na ninashukuru kwa kupata nafasi hii. (Makofi)