Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (71 total)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Warizi kwa majibu mazuri. Napenda nimwulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ya Naibu Waziri yanaonyesha dhamira ya Serikali ya kupunguza kodi ya Pay As You Earn kwa wafanyakazi wa kima cha chini, napenda kujua sasa kama Serikali ina mpango wowote kwa wafanyakazi ambao wana makato ya kiwango cha juu cha asilimia 30.
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amesisitiza ukusanyaji wa mapato katika kila source ambayo inatakiwa kulipa kodi, je, hatuoni wakati umefika sasa kuwapunguzia kodi hawa wafanyakazi wenye kiwango cha juu? Ahsante.
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la kwanza kwenye kuangalia kama Serikali ina mpango gani wa kupunguza kodi hii ya mapato kwa watumishi ambao wanapata zaidi ya hii shilingi 500,000/= ambapo wanatozwa asilimia 30; niseme tu kwamba kwa upande wa Serikali na kupitia Ofisi ya Rais (Utumishi) tayari tumekwishawasilisha mapendekezo katika Kamati ya Tax Workforce ambayo inaifanyia kazi. Katika Kamati hii wako Wajumbe kutoka Hazina na Wajumbe kutoka TRA.
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba tutakapokutana na sasa ana Baraza Kuu la majadiliano katika Utumishi wa Umma mwaka huu baadaye, tutaweza kuweza kutoa feedback ni kwa kiasi gani suala hili limeweza kuzingatiwa. Aidha, Serikali inaona kwa kweli ni suala la msingi, ikizingatiwa kwamba na wenyewe wanatozwa kodi ya mapato iliyo kubwa.
Mheshimiwa Spika, nadhani nimeshajibu yote, nimeunganisha. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Katika azma ya kuboresha maslahi ya walimu, katika sherehe ya siku za walimu duniani katika awamu iliyopita, Rais mstaafu aliwaahidi walimu kuwapatia posho ya kufundishia yaani teaching allowance, lakini hadi leo posho ya kufundishia (teaching allowance) hawajapatiwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba ahadi ambayo aliitoa Rais inatekelezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kumekuwa na tabia ya kutolipa madeni ya walimu kwa wakati unaostahili na mara nyingi madeni ya walimu hulipwa hasa wakati wa kukaribia uchaguzi, hii ni tabia mbaya. Ni lini na Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba walimu wanalipwa madeni yao kwa wakati unaostahili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na posho ya kufundishia niseme tu kwamba ni kweli kwamba Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati huo alipokwenda katika sherehe za walimu alielezea kwamba suala hili litafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba sisi kupitia Baraza Kuu la majadiliano katika utumishi wa umma tutaliangalia na kila mwaka tunakaa mara moja. Kwa hiyo, tusubiri tutakapokaa na vyama hivyo vya wafanyakazi katika Baraza hili Kuu la Majadiliano tuone tutasemaje. Tunaweza tukapanga viwango lakini tukajikuta vinakuwa ni viwango ambavyo Baraza Kuu kupitia Vyama vya Wafanyakazi wakawa hawajaviridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madeni ya walimu, kwa upande wa Serikali inaweka mkazo mkubwa sana kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao, lakini si kwa walimu tu na kwa watumishi wote mbalimbali wa umma. Ukiangalia katika mwaka huu peke yake, tumeshalipa takribani bilioni 3.7, lakini vilevile kwa mwaka jana tu peke yake tulilipa takribani shilingi bilioni 27.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya hivi sasa tunahakikisha tunakamilisha kulipa na kuhakiki, maana huwezi ukalipa tu. Wapo wengine vilevile wanafanya madai ambayo si ya kweli. Kwa hiyo, niseme tu kwamba sisi kama Serikali tupate nafasi tuendelee na uhakiki lakini wakati huo huo tukiendelea kulipa kwa kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Walimu wamekuwa wakinyanyasika sana katika suala la upandishwaji wa madaraja na hata wanapokuwa wamepandishwa hayo madaraja, bado malipo yao kulingana na madaraja waliyopewa hawapewi kwa wakati, inawachukua muda mrefu kulipwa kulingana na madaraja waliyopewa. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya jambo hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwamba tumekuwa tukilipa malipo haya na ni kweli mengi yamekuwa hayalipwi kwa wakati, lakini kuna sababu zake. Hata hivyo, pia ukiangalia uwezo wa Kiserikali wa bajeti, tumekuwa tukijitahidi, tunafanya uhakiki na mara tunapothibitisha kwamba kweli madai hayo ni ya halali, tumekuwa tukijitahidi kufanya jitihada za ziada kuweza kuyalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyomjibu Mheshimiwa Masoud Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha madeni haya inakuwa ni historia.
Vilevile tunachokifanya pamekuwa na tatizo kubwa katika mfumo ambao tunautumia wa human capital, ukiangalia namna ambavyo wanakokotoa, kuna namna inakokotoa kupitia automatic system, lakini vile vile wale ambao unakuta wameajiriwa baada ya tarehe kumi na tano, unafanyaje? Inabidi waje wasubiri mpaka mwezi unaofuata. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa madeni haya yataendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya sasa ni kuangalia ni kwa namna gani tutaweza kuufanyia mapitio mfumo wetu wa malipo na taarifa za kumbukumbu za watumishi ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaondokana na malimbikizo haya.
Vilevile kuhusiana na wanaopandishwa madaraja, niseme tu kwamba majukumu ya kupandisha watumishi especially walimu ni Kamati mbalimbali za Ajira kupitia Wilaya zao na kama ambavyo nilijibu juzi kupitia swali la Mwalimu Kasuku, nilieleza changamoto ambayo walikuwa nayo Idara ya Walimu walikuwa na changamoto ya watumishi, lakini pia walikuwa na changamoto ya kibajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini suala hili litakuwa historia baada ya Tume ya Utumishi ya Walimu itakapoanza kazi rasmi mwaka huu, mwezi Julai. Niseme tu kwamba kwa upande wa walimu hawa, ukiangalia katika quarter tu ya kwanza ya Julai mpaka Oktoba mwaka huu takriban walimu 10,716 tayari walikuwa wameshapandishwa vyeo vyao. Vilevile tulikuwa tunasubiri kupata taarifa mbalimbali kupitia Kamati hizi za Ajira na mamlaka mbalimbali za ajira katika Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mary Chatanda, sasa hivi tunafanya kila jitihada kupitia TAMISEMI na tunatarajia kumalizia Wilaya 90 zilizobaki pamoja na Mikoa 12 ili kuweza kuwapandisha Walimu hao madaraja yao.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa imeonekana taasisi nyingi hazifuati mfumo huu wakati Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 iliweka ni lazima kwa kila mtumishi kujaza hizo fomu na kutekeleza mfumo huu. Je, ni hatua gani ambazo Serikali imekusudia kuchukua kwa taasisi na watumishi ambao hawafuati huu mfumo ambao ni wa lazima kwa mujibu wa sheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kutangaza hadharani taasisi ambazo zimefanya vizuri katika kutekeleza mfumo huu kungesaidia sana kuwapa motisha wafanyakazi wanaofanya kazi katika taasisi hizo. Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba umefika wakati sasa taasisi zinazofanya vizuri na zile ambazo zinafanya vibaya zitangazwe moja kwa moja hadharani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza, kuhusiana na hatua gani ambazo Serikali inakusudia kuchukua kwa watumishi ambao hawazingatii mfumo huu, nipende tu kumwambia kwamba, kuanzia mwaka 2012, Katibu Mkuu Utumishi alitoa Waraka na ilielekeza kwamba kuanzia kipindi hicho hakuna mtumishi wa umma atakayepandishwa cheo endapo hajaweza kujaza fomu ya OPRAS. Vile vile tunakusudia kuweka tozo maalum kama adhabu kwa ajili ya watumishi ambao hawatazingatia sharti hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili alitaka kufahamu endapo Serikali iko tayari kutangaza hadharani taasisi zinazofanya vizuri. Nipende tu kusema kwamba, tunafikiria pia kuweka tuzo, lakini tunapokea ushauri na tutaangalia ni kwa namna gani suala hili linaweza kutekelezwa kwa kutangaza hadharani.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili.
Kwanza, kwa kuwa mipango hii ya bajeti tunayoijadili sasa hivi katika Bunge letu inahitaji sana kada hizi za Watendaji na kwa kuwa nafasi nyingi katika kada hizi ziko wazi, je, ni kwa nini Serikali isione umuhimu mkubwa wa kutoa nafasi kwa wale vijana waliomaliza Vyuo vya Serikali za Mitaa na Vyuo vya Utawala, wakaanza kujitolea katika kipindi hiki cha mpito kutegemeana na makubaliano yao katika Serikali za Mitaa hususan kwenye maeneo yao, ili baadaye waweze kuingia katika mfumo wa ajira?
Pili, ni kwa nini sasa Serikali isione inapaswa kutenga fedha za kutosha katika kuwezesha ofisi za Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa sababu fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika ngazi za chini zinatumika kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uendeshaji katika ofisi hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issaay ambapo katika suala lake la kwanza alitaka kujua kwamba ni kwa nini Serikali isitoe fursa au nafasi kwa hawa WEO na VEO ambao wanajitolea katika kipindi hiki cha mpito.
Mheshimiwa Naibu Spika suala zima la kujitolea au la liko mikononi mwao katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Kwa hiyo, nitoe tu rai kwa Mheshimiwa Mbunge, mipango hiyo wanaweza wakaifanya na kuitekeleza huko chini kabisa katika Mamlaka zao za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika kama ambavyo nimesisitiza, ni kutokana tu na ufinyu wa nafasi na wigo wa kibajeti, katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo nilieleza tumepanga kuajiri ajira mpya, nafasi 71,496 na katika nafasi hizo kwa ujumla wake katika WEO na VEO na nafasi zinginezo kwa upande wa Mbulu watapata nafasi 466, vile vile tutawapandisha vyeo katika promotion nafasi 1066. Kwa hiyo, nimwombe tu waendelee kuwa wavumilivu kipindi hiki na kama nilivyoeleza mwezi huu wa Tano ajira hizo zitaanza kutekelezwa na ni imani yangu watatekeleza kwa wakati, ili nafasi hizo ziweze kuzibwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kwa nini sasa Serikali isiweze kutenga fedha za kutosha kuziwezesha Kata hizi ziweze kufanya kwa ukamilifu niseme tu kwamba, mipango ya kibajeti kutokana na uwezo tulionao, Halmashauri zenyewe zinashirikishwa katika mpango mzima wa maandalizi ya bajeti. Kwa hiyo, niwaombe tu wahakikishe kwamba wanapokuwa wanapanga mipango yao wanaweka vipaumbele katika kuziwezesha Kata hizi kuwa na fedha ambazo zitaweza kufanya majukumu yao ya msingi, lakini kwa sasa inawezekana zisitoshe kabisa na ni kutokana na wigo wa bajeti.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, vilevile niwashukuru sana ndugu Thadei Mushi kwa naMheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza; kwa kuwa Serikali inafahamu baada ya kuwa imempandisha daraja Mwalimu na kumrekebishia mshahara inachukua muda mrefu sana. Utumishi hawaoni kuwa nao imefika wakati wachukue ile model wanayochukua watu wa Nishati na Madini ijulikane kabisa kwamba ukipandishwa daraja kwa kipindi fulani mshahara wako utakuwa umerekebishwa ili watumishi hawa wawe na uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa malimbikizo ya mshahara baada ya kurekebishwa mshahara yanachukua muda mrefu, Serikali inawaambia nini watumishi wa umma hususan Walimu kwamba watalipwa lini, kwa uharaka zaidi malimbikizo ya mshahara haya ambayo yanachukua miaka mingi sana kabla ya kulipa?mna wanavyotupa ushirikiano.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nimshukuru kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia sana masuala mazima ya ustawi na maslahi ya utumishi wa umma hususan Walimu. Natambua ametokana na Chama cha Waalimu Tanzania, nakupongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Biteko alitaka kufahamu endapo Serikali labda kwa nini isifikirie mtumishi anapopandishwa daraja moja kwa moja aweze kuwa amefanyiwa marekebisho yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilieleza kinachofanyika kupitia Mfumo huu wa Taarifa za Kiutumishi na nashukuru kwamba ameweza kumpongeza Afisa Utumishi aliyeko katika Wilaya ya Bukombe kwa kazi nzuri anayoifanya, wanapokuwa Kamati ya Ajira imeshampatia barua ya kupandishwa cheo, kinachofanyika wana-post katika mfumo huu wa Lawson wa taarifa za kiutumishi na mishahara, lakini ni jukumu sasa la Utumishi kuhakikisha kwamba, mtumishi huyu aliyepandishwa cheo kwanza taarifa zake za tathmini kwa uwazi kwenye OPRAS zipo, kuhakikisha kwamba katika muundo wa utumishi kweli anastahili kupanda katika ngazi hiyo na kutokana na sifa na uzoefu ambao umeainishwa katika muundo wa maendeleo ya utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhakikisha kwamba ni kweli ana utendaji mzuri pamoja na uadilifu. Bado naendelea kuhimiza niwaombe sana waajiri pamoja na Maafisa Utumishi ambao wanasimamia suala zima la mfumo huu, kuhakikisha kwamba wanapandisha kwa wakati vilevile wanafanya marekebisho kwa wakati kwa kuzingatia maelekezo mbalimbali ambayo tumewapatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa madeni ya Walimu napenda tu kusema kwamba kwa kiasi kikubwa madeni haya yamelipwa, zaidi ya Walimu 13,000 tayari malimbikizo yao wameshalipwa ya mishahara, vilevile kwa upande wa Hazina madeni mbalimbali yamekuwa yakilipwa. Bado naendelea kusisitiza tena kuhakikisha kwamba, waajiri wanalipa kwa wakati malipo haya na kuhakikisha kwamba wanayatengea bajeti katika mwaka husika, vile vile wapandishe watumishi kwa kuzingatia muundo na kwa kuzingatia kwamba wana Ikama hiyo na bajeti kwa sababu wasipofanya hivyo ndiyo maana wanasababisha malimbikizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile changamoto nyingine ambayo tumekuwa tikiipata, unakuta mfumo wetu wa Lawson una-calculate automatic arrears, wakati huo huo unakuta Mwajiri mwingine naye analeta manual arrears, kwa hiyo tusipokuwa makini kufanya uhakiki unaweza ukajikuta umemlipa mtumishi mmoja malipo ambayo hayastahiki. Bado naendelea kusisitiza kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa watumishi na itakuwa ikiendelea kulipa kila mara kwa kadri ambavyo uwezo umekuwa ukiruhusu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, naitwa Mwalimu Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika huu mpango wa Serikali wa kutoa elimu bure, napenda kufahamu Serikali ina mpango gani sasa kuboresha maslahi ya walimu kwa mpango utakaoitwa elimu bure na maslahi bora kwa walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa ualimu, lakini vilevile tunatambua umuhimu wa watumishi wote wa umma. Lakini kwa kutambua umuhimu huo wa walimu kama Serikali, kwa miaka takribani nane tumeshapandisha takribani asilimia 160 ya mshahara wa walimu. Ukiangalia hivi sasa mwalimu wa chini kabisa anapata shilingi 419,000/=, na wa juu anapata shilingi 719,000/=. Tunatambua bado mazingira ya kuishi gharama ni kubwa na wanahitaji kuongezewa kipato na tutafanya hivyo kwa kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiruhusu.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, asante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Waziri mwenyewe amekiri katika majibu yake ya swali la msingi kwamba ajira ya walimu imekasimiwa kwenye mamlaka zingine, na mamlaka zilizokasimiwa ajira za walimu ndizo zimesababisha matatizo makubwa ya walimu, walimu kutopanda madaraja kwa wakati, walimu kutolipwa mishahara mizuri na walimu kutolipwa madai yao kwa muda mrefu sana.
Je, Waziri yuko tayari hii Tume iliyoundwa namba 25 ya mwaka 2015 iwe na mamlaka kamili ya kuwaajiri na kulipa mishahara bila kukasimiwa kwenye mlolongo wa vyombo vingine?
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyosababishwa ya walimu nchini yametokana na mfumo kwa kukasimu mamlaka ya ajira ya walimu kwa vyombo vingine vingi kuanzia Katibu Kata, Mratibu, TSD, Utumishi, Hazina na kadhalika, vyote vinavyoleta usumbufu kwa ajira ya mwalimu na maslahi yake kupotea.
Je, Serikali iko tayari kuwahudumia walimu kwa dharura kabisa kulipa madai yao yanazidi shilingi bilioni 20 kwa dharura ya haraka ili walimu hao waweze kufanyakazi kwa moyo? Asante
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwalimu Bilago ametaka kujua kama Serikali iko tayari kuipa Tume ya Utumishi ya Ualimu mamlaka kamili ya kulipa mishahara. Niseme tu kwamba ukiangalia katika kifungu cha 5 kinachoanzisha Tume hii ya Utumishi wa Walimu, Mamlaka kwa Tume hii ni Mamlaka ya ajira. Bado suala zima la kulipa mishahara kama ilivyo Kanuni ya Utumishi wa Umma na kama wanavyolipwa watumishi wote wa umma itabaki katika Serikali. Lakini ukiangalia kama Mamlaka ya Usimamizi kwenye Serikali za Mitaa, ambao ndio wanaendesha na wenye shule uko chini, wao wanachokifanya ni kulipa tu mishahara kwa kuwa wao ndiyo mamlaka ya usimamizi, kwa hiyo tutaendelea hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba pamekuwa na changanmoto ambazo tunazitambua kwa kuanzisha Tume hii tunaamini sasa kwa kuwa ni Tume ambayo inajitegemea, maana ukiaangalia huko awali Idara ya Walimu ilikuwa chini ya Utumishi wa Umma, lakini Tume hii mpya ambayo tunayoianzisha itakuwa ni Tume inayojitegemea na tunaamini sisi kama Serikali kwa kuwa tumejipanga kuiwezesha kwa rasilimali fedha, kuiwezesha kwa rasilimali watu na vitendeakazi mbalimbali tunaamini changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza basi zitaweza kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge aweze kuwa na imani, tuweze kuanza Tume hii halafu tuone mambo yatakavyojitokeza lakini sisi kama Serikali tuko tayari kuiwezesha Tume hii kwa hali na mali. Ukiangalia katika mahitaji ya kibajeti yaliyobainishwa ni takribani shilingi bilioni 75, wakati ukiangalia ni ilipokuwa ni Idara ya Utumishi wa Walimu walikuwa wanategemea bajeti yao kutoka katika Tume ya Utumishi wa Walimu, ndiyo maana changamoto mbalimbali za kupandishiwa mishahara, changamoto za kupandishwa madaraja na mambo mengine yalikuwa zinajitokeza. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aiamini Serikali, tuipe nafasi Tume iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kuhusiana na madeni ya walimu, kama nilivyoeleza jana. Ni kweli madeni ya walimu yako katika kiwango cha juu, takribani shilingi bilioni 42, lakini hivi sasa tunachokifanya ni kuhakiki madeni haya. Nilitoa angalizo, yako madeni au madai yanayowasilishwa ambayo unajikuta yana mapugufu fulani, yako ambayo unajikuta hayana nyaraka mbalimbali za kiutumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunalipa madeni haya haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa kupitia Bunge lako Tukufu, kwa kuwa mfumo wetu wa Human Capital Management System uko katika Halmashauri mbalimbali, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao nao ni Madiwani katika Halmashauri husika waweze kufuatilia madeni haya, yako kiasi gani kwa mwezi husika, mwezi unaofuata unatarajiwa kulipa kiasi gani, lakini vilevile endapo kuna madai ambayo yamerudishwa changamoto ni nini, waweze kutusaidia.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza swali, jibu lililotolewa kwenye swali namba (b) siyo kweli kwamba Wilaya ya Kaliua imepewa asilimia 70; Wilaya ya Kaliua ina vijiji 101, vilivyopewa ni 54 tu. Kwa hiyo, ni chini ya asilimia 70 kama asilimia 55. Kwa hiyo, kama lengo ni asilimia 70, Kaliua haijapata asilimia 70 kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali namba moja, mchakato mzima alioeleza Mheshimiwa Waziri, kuhusiana na namna ya kuweza kupata hizi kaya maskini ni kinadharia zaidi kuliko hali halisi kule kwenye vijiji. Kama ilikuwa inafuatwa kama ilivyoandikwa hapa, isingewezekana kwamba leo hii baadhi ya Watendaji familia zao zimewekwa kwenye mpango, wenye uwezo mzuri wamewekwa kwenye mpango, maskini kabisa wameachwa.
Kwa hiyo, naomba kujua Serikali kwa kuwa hapa imeandika vizuri, imeweka utaratibu gani basi, mpango mzuri kuhakikisha haya yaliyoandikwa kwenye suala namba „A‟ yanakwenda mpaka chini kwenye ground ili wale walengwa waweze kunufaika na mradi huu wa TASAF III. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; TASAF III inalenga zaidi kutoa fedha kuliko kuweka mfumo ambao utakuwa endelevu; na kwa kuwa mpango wowote kwa kuwa ni mradi, una muda wake; naomba kujua Serikali imejiandaa vipi baada ya Mradi wa TASAF III, zile familia ambazo zinapewa fedha cash haziwekewi utaratibu wa kuweza kujiendeleza, ziweze kuwa endelevu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Magdalena Sakaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na kipengele (b) kwamba wamenufaika na vijiji 54 wakati wana vijiji 101. Kwa mujibu ya taarifa za Mratibu na barua ninayo ya Machi, 2015, alieleza vimesalia vijiji 17 na nitaomba tu-share pamoja kukupa orodha hiyo na baadaye tufuatilie kwa nini visiwe ni vijiji 47 na yeye alete vijiji 17?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza kwamba katika mchakato au hatua ambazo nimeelezea za upatikanaji wa fedha za TASAF, kwamba ni wa kinadharia zaidi kuliko uhalisia; ni kweli changamoto zipo, nami naomba kupitia Bunge lako Tukufu, ukiangalia mchakato mzima wa Mpango huu wa TASAF III na awamu nyingine ambazo zilitangulia unabuniwa na jamii yenyewe. Wanachokifanya TASAF kupitia uwezeshaji wa Kitaifa wanaenda tu pale kusaidia katika kutoa elimu, kuwasaidia wananchi wa eneo husika waweze kujua ni namna gani wanaibua miradi yao.
Mheshimiwa Maibu Spika, tatizo kubwa tumegundua linajitokeza katika vijana wetu ambao siyo waaminifu ambao wanapita katika kila kaya kufanya madodoso; kwa hiyo, naomba tushirikiane, mtakapoona kuna udanganyifu wowote, ziko taratibu za malalamiko. Iko fomu Na. HU1 ya malalamiko na madai. Basi wakati wowote wanakijiji wahudhurie mikutano hii inapoitishwa, lakini vile vile wanapoona kuna kaya ambayo imeorodheshwa na siyo kaya masikini sana, basi pale pale wao kupitia Mkutano wa Kijiji waweze kuchukua hatua na mtu huyo aweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile inapokuwa orodha hii imefikishwa TASAF Makao Makuu, wanapoanza kufanya uchambuzi kupitia kompyuta, ni uchambuzi ambao unaangalia vigezo vya umaskini kwa mujibu wa Household Survey ambayo inatolewa na National Bureau of Statistics. Wakati mwingine unakuta kaya zinazofanyiwa dodoso majumbani, hawaelezi ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mara nyingi kaya ambazo zinastahili kufuatwa ni zile kaya ambazo unakuta hazina hata mlo mmoja kwa siku; ni zile kaya ambazo haziwezi kumudu gharama za matibabu; ni zile kaya ambazo haziwezi kumudu huduma mbalimbali za kijamii, lakini vilevile zina watoto wengi na zinashindwa kuwapeleka shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kupitia Bunge hili tuelimishe wananchi wetu, lakini na sisi kama TASAF, tutaendelea kuto elimu hii. Wananchi wetu kwenye zile kaya wanapofanyiwa madodoso, basi waweze kutoa taarifa zenye ukweli ili waweze kunufaika. Vilevile kupitia uongozi wa vijiji, katika mikutano ile, wanapoona mara moja kuna mtu ambaye hastahili kuingizwa, basi mara moja waweze kumtoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu tulizonazo, unajikuta katika mikutano mingine wale viongozi wa vijiji wote wanawaogopa, wanajikuta hawawezi kubainisha upungufu uliopo. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane kwenye hili, wakati wowote nitakuwa tayari na sisi tutafanya uhakiki na kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaanza kuchukua hatua. Mfano, kwa upande wa Karagwe tulichukua hatua katika Kijiji cha Kibondo lakini vile vile kwa Wilaya ya Kalambo na kwenyewe tulichukua hatua dhidi ya watumishi ambao wamefanya ubadhirifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba tumejiandaa vipi kuhakikisha sasa fedha hizi zinakuwa endelevu? Ukiangalia programu hii imeanza mwaka 2000 na hii ni awamu ya tatu; mara nyingi wale wanufaika au walengwa wanatakiwa wapate huduma hii kwa miaka mitatu. Baada ya miaka mitatu tunafanya tathmini kuangalia kama wameweza kuondokana na hali ya umaskini. Kwa kweli kwa msingi mkubwa wengi takribani asilimia 52 ambao wamekuwa wakinufaika, wameweza kunufaika na kuondokana na umasikini.
Kwa hiyo, tujitahidi tuendelee kuelimisha, waweze kunifaika, maana wako wengine wamekuwa wakitisha watu kwamba fedha hizi ni za Freemason, fedha hizi sijui ni za kitu gani; na unakuta wanufaika wengine wamekuwa hawajitokezi kunufaika nazo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Angellah, nilikuwa napenda niulize swali fupi la nyongeza.
Je, kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo kwamba fedha hizi zinatumika vibaya na wahusika wanatoa majina hewa, na inasemekana Waziri aliyekuwa ana-deal na TASAF, alitumia fedha hizo vibaya kwa ajili ya kutafuta nafasi ya Urais. Uko tayari kuchunguza hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba malalamiko yoyote tukatakayoyapokea, tutafanya uchunguzi. Nimekuwa nikisema suala hili kuna uwazi mkubwa katika vikao mbalimbali vya vijiji na wakati wowote mtakapoona kuna matatizo, basi msisite kututaarifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami mwenyewe nimejipanga, kutokana na malalamiko mengi ambayo nimeyasikia, kwa kweli hayo majipu tutayatumbua. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa pamoja na mishahara ya watumishi hawa wa sekta ya afya, Serikali ilikuwa ikitoa motisha mbalimbali ikiwemo on call allowance kwa wauguzi wetu; lakini hadi hivi tunavyoongea Serikali haipeleki pesa hizi kwa wakati; na nitoe mfano kwa Hospitali yangu ya Mrara katika Jimbo la Babati Mjini, tangu mwezi wa pili wauguzi wale katika hospitali ile tangu mwezi wa pili hawajalipwa fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu, ni kwa nini Serikali haipeleki fedha hizi kwa wakati kama ilivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika bajeti iliyopita OC katika Halmashauri zetu na katika hospitali zetu zilipunguzwa kwa zaidi ya asilimia 60; nitoe mfano wa hospitali yangu ya Mrara, ilikuwa inapokea OC ya shilingi milioni 154 lakini ikapunguzwa hadi shilingi milioni 46 kwa mwaka na hizi fedha sasa zilipe likizo za watumishi, maji na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu kauli ya Serikali, ni kwa nini fedha hizi zimepunguzwa ilhali mambo haya sasa yamekwama? Mfano sisi, zaidi ya shilingi milioni 10 hospitali inadaiwa, imeshindwa kulipa BAWASA bili ya maji. Serikali iko tayari kufikiria kuhusu uamuzi huu wa kupunguza OC katika hospitali zetu za Wilaya ili waweze kuziendesha hospitali hizi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Eeh, unisamehe Mheshimiwa Pauline Gekul, ni Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, ulitokea Viti Maalum, uniwie radhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la kwanza kwamba ni kwa nini Serikali haipeleki kwa wakati posho mbalimbali hususan ya on call allowance, nimejaribu kufanya ziara katika maeneo mbalimbali, ni kweli posho hii imekuwa ikichelewa, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba itaendelea kutolewa kwa wakati kwa kadri hali ya uchumi itakavyoendelea kuimarika kwa sababu fedha hizo tayari zilishapangwa katika bajeti, kwa hiyo, zitatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na OC kupunguzwa, haijapunguzwa kwenye OC za Hospitali ya Mrara peke yake, ukiangalia nchi nzima fedha za matumizi mengineyo zilipunguzwa na wote tunajua kabisa, tulikuwa na malengo ya aina gani kama nchi, asilimia zaidi ya 40 imepelekwa katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba watumishi waendelee kuvuta subira, tutakapoenda katika mid year review, siwezi kulisemea hili kwa Wizara ya Fedha, tunajua kabisa kila mwaka mwezi Januari au Februari huwa kuna mid term year review. Kwa hiyo, hilo niwaachie wao, naamini itakapofika wakati huo, wataona ni maeneo gani yanayoweza kufanyiwa maboresho ili kuweza kuendana na wakati. Nakushukuru.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, niulize maswali madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa kila mwaka mwezi Julai kunakuwa na ongezeko la mshahara, kupanda vyeo ama madaraja kwa watumishi, lakini mpaka sasa Serikali haijafanya chochote.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi katika kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mlundikano tena wa madai kwa kupandisha mishahara ya watumishi?
Pili, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha madai haya hayatakuwepo tena? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie tu kwamba tunaendelea kulipa madeni haya kwa kadri yanavyojitokeza na kwa kweli ukiangalia tangu mwaka 2013 tulipoanza kutumia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, madai haya yamekuwa yakiendelea kupungua kwa nyakati mbalimbali.
Vilevile kwa upande wa madeni yanayotokana na kupandisha mishahara na kwa madeni yanayotokana na upandishwaji wa vyeo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishatoa maelekezo kwamba ni lazima madai haya yalipwe kupitia mfumo pindi watu hawa wanapopandishwa vyeo pamoja na madai haya yanapokuwa yamejitokeza ili kuhakikisha kwamba hatuleti milundikano ya madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunakikisha tunakuwa na mkakati endelevu, yapo madai mengine yanatokana na watumishi kuhama, tumeshaelekeza tuhakikishe kwamba mtumishi hahamishiwi kama hakuna fedha za uhamisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa wingi ni masuala au madai ya posho ya kukaimu. Tumeshaelekeza pia na yenyewe, pindi barua ya kukaimishwa na marekebisho ya mshahara yanapotoka, basi mtumishi aingiziwe marekebisho hayo mapema na marekebisho ya mshahara yaweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya waajiri wamekuwa hawatengi fedha kwa ajili ya matibabu, likizo na posho zao nyingine, matokeo yake imekuwa inasababisha sasa pindi mtu anapotakiwa kwenda likizo, inaleta madeni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaagiza waajiri wote, wanapokuwa wanapanga bajeti zao za kila mwaka, wahakikishe stahili za msingi na za kisheria na za kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma zinatengwa ili kuhakikisha kwamba hawasababishi madeni, lakini vilevile kuhakikisha tunazingatia haki za msingi za watumishi hao. Nakushukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo yanamhusu Mbunge wa mwendokasi aliyetoka, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wizara ya Utumishi, imeshindwa kutoa vibali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo inatugharimu takribani milioni 28 kuhudumia watumishi 58. Je, ni lini Wizara hii itatoa kibali kwa Halmashari ya Wilaya ya Lushoto?
Swali la pili, kwa kuwa pesa hizi ambazo Halmashauri ya Lushoto inazitumia, kulipa mishahara zilikuwa ziende kwenye makundi maalum hasa ya vijana na akinamama, zile asilimia tano. Je, Wizara haioni kwamba pesa hizi kutumika kulipa watumishi inakinzana na dhana nzima ya utawala bora?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba maswali haya naona yametoka nje kabisa na swali hili la msingi. Kuhusiana na lini sasa Ofisi ya Rais, Utumishi itatoa kibali kwa Halmashauri ya Lushoto, kwa ajili ya kibali cha ajira, niseme tu kwamba kwa sasa Serikali bado inaendelea na mchakato na pindi vibali hivyo vitakapokuwa tayari, basi taasisi husika zitaweza kufahamishwa na wataendelea na michakato hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba kutokana na vibali hivi kuchelewa, imepelekea Halmashauri ya Wilaya yake kuweza kutumia mapato yake ya ndani au own source kwa ajili ya kulipa mishahara. Niseme tu kwamba kila mwaka na Halmashauri zote na mamlaka za ajira wanafahamu mchakato wa ajira, kila mwaka mamlaka ya ajira inatakiwa iwasilishe ikama yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia huwa wanawasilisha ikama, ikama inaidhinishwa na baadaye Halmashauri inaenda kinyume kabisa na kuwaajiri watu wake kwa kupitia fedha zao za ndani. Niseme
tu kwamba kwa kweli suala hili limekuwa likileta changamoto na tuombe sana Halmashauri zijikite zaidi katika ikama ambazo zinaidhinishwa na Serikali kwa kutumia mishahara ya Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ningependa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo zinafanya kazi zinazofanana na hii inasababisha kwamba bado gharama ziendelee kubaki kuwa kubwa. Serikali ina mpango gani wa kupitia upya taasisi zake zote ili kuhakikisha kwamba zile zinazofanana zinaunganishwa, kusudi kuweza kupunguza matumizi zaidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme tu kwamba, kama alisikiliza vizuri jibu langu la msingi, hiyo ndiyo azma na mwelekeo wa Serikali. Hata hivyo, nimpongeze na kumshukuru sana, kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia masuala mazima ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba tayari Katibu Mkuu Kiongozi, kupitia Ofisi ya Rais, alishatoa maelekezo kwa Wakuu wote wa Taasisi za Umma na tayari Taasisi zote, Wizara zote zimekwishawasilisha mapendekezo katika Ofisi ya Rais, kuhusiana miundo na mgawanyo wa majukumu ambayo wao wangeipendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hivi sasa tayari Ofisi ya Rais tumeishaunda timu ya wataalam na wameanza kupitia ili kuangalia endapo majukumu yaliyopo kwa taasisi fulani fulani, kama yanaweza kuhalalisha uwepo wake. Lakini vile vile kuangalia ni majukumu gani, nitolee tu mfano ziko Wizara unakuta zimeunganishwa Wizara mbili, Wizara moja ilikuwa tayari ina kitengo chake cha mawasiliano, ina kitengo chake cha mambo ya teknohama, lakini na Wizara nyingine vile vile, ilikuwa na kitengo kama hicho na idara zingine zinazofanana na mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba ni lazima itabidi kufanyia mapitio idara moja tu ndiyo iwepo. Vile vile watumishi hao wengine itabidi waangaliwe sasa ni wapi watapelekwa, katika sehemu zingine ili waweze kuleta tija zaidi na kupunguza gharama kwa Serikali.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa ongezeko la ajira kwa watoto wadogo ni kubwa sana hapa nchini; na kwa kuwa tatizo hilo kuchangiwa na kuvunjika kwa ndoa kwa kutokuwa na msingi na kuachiwa akina mama kulea hao watoto. Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka kuleta mabadiliko ya sheria ya mwaka 1971 ili wanawake na watoto hawa waweze kupata haki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa TASAF III imeonesha mpango mzuri sana na mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu kwenye mashamba makubwa watoto hao wapo wengi na wanaonekana kama vile kwenye mashamba ya tumbaku, kahawa, chai, pamba na kadhalika, je, Waziri yuko tayari kuwakusanya hawa watoto na kuwapa elimu ya kutosha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa swali lake la kwanza kuhusiana na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, bahati nzuri suala hili limekuwa likizungumzwa katika nyakati mbalimbali na hata katika Bunge hili na Mkutano huu wa Tatu, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria amelisemea sana, lakini vilevile Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto pia ameweza kulizungumzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kurudia kwa mara nyingine tena, ni kweli sheria hii ilionekana kuna upungufu. Ukiangalia viko baadhi ya vifungu vinavyoruhusu masuala mazima ya ndoa za utotoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kutambua kwamba katika masuala haya ya ndoa kuna mkanganyiko wa masuala ya kimila na kidini, ikaonekana kwamba ni vema suala hili likapatiwa suluhu kwa kupata maoni ya wananchi wengi zaidi kupitia mchakato wa White Paper. Mwanzo wakati zoezi hili Wizara ya Katiba na Sheria ilipotaka kulianza, taratibu zote karibia zilikuwa zimeshakamilika, lakini ikawa imeingiliana na mchakato wa Mabadiliko ya Katiba. Ikaonekana itakuwa si wakati mzuri kuwachanganya wananchi, huku wanatakiwa watoe maoni kuhusiana na Katiba Mpya lakini wakati huo huo unawapelekea zoezi lingine kuhusiana na marekebisho ya Sheria ya Ndoa. Vilevile ilionekana kwamba huenda wakati ule kwenye kukusanya maoni ya Mabadiliko ya Katiba wananchi wangeweza kulisemea jambo hili lakini kwa kiasi kikubwa halikusemewa sana. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria bado wanasubiria wakati mzuri zaidi wa kuweza kulipeleka lakini ni lazima liende kupitia Waraka wa Maoni kupitia White Paper.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba je, Serikali iko tayari kutoa elimu kwa watoto ambao wamekuwa wakifanya ajira mbalimbali za utotoni, niseme tu kwamba kupitia Wizara ya Kazi kwa Mheshimiwa Jenista, wamekuwa wakifanya kazi hii na wanaendelea kufanya kazi hii kuhakikisha kwamba watoto hawa ambao wako katika ajira za utotoni wanaelimishwa, lakini zaidi kuhakikisha kwamba wazazi wao wanapewa elimu hii. Ndiyo maana kupitia TASAF kama nilivyoeleza, nichukulie tu kwa upande wa Zanzibar, zaidi ya watoto laki moja na mbili wamekuwa wakinufaika na ruzuku hii ili kuwawezesha kwenda shule.
Kwa hiyo, ni imani yangu bado kupitia Serikali kwa ujumla wake na mipango mbalimbali na TASAF ikiwemo tutahakikisha tunatoa elimu hii, lakini vilevile kuona ni kwa namna gani watoto wengi zaidi wanaweza kunufaika nayo. Nakushukuru.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa TASAF III imekuwa ikihamasisha sana hizi kaya maskini kujiunga na Mfuko wa Bima za Jamii (CHF). Je, mpaka sasa ni kaya ngapi zimeweza kujiunga na huu Mfuko huu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tu niombe uniruhusu niweze kutoa maelezo ya utangulizi kidogo kabla sijajibu hoja yake. Kumekuwa na hoja na watu wengi wamekuwa wakitoa ushauri kwamba katika hizi kaya ambazo zinanufaika na ruzuku hii ya uhawilishaji, walazimishwe kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii.
Kwanza kabisa niseme duniani kote katika taratibu za uendeshaji wa mipango ya uhawilishaji wa fedha katika jamii huwa ni hiari. Kwa hiyo, tunachokifanya sisi kama TASAF ni kuhakikisha kwamba katika kila siku wanapoenda kupokea malipo tunawaelimisha kuhusiana na umuhimu wa kuweza kujiunga na Mfuko huu wa Bima ya Afya. Hadi sasa kaya 54,924 kutoka katika Halmashauri 28 zimeweza kujiunga na Mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato ambayo zaidi ya 90% ya walengwa wake wameshajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya. Nitoe pia pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ambapo 60% ya walengwa wake tayari wameshajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.
Vilevile nitoe pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Halmashauri au Manispaa ya Mtwara pamoja na Kibaha lakini na nyingine nyingi. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge na ninyi pia mtusaidie kuendelea na uhamasishaji ili kuhakikisha kwamba walengwa hawa wanaweza kujiunga ili waweze kupata huduma ya matibabu ya afya pale wanapohitaji. Nakushukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Askari Magereza wapo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa kuwa Askari Magereza na wenyewe wanajiendeleza, wanapata shahada, wanapata elimu ya juu zaidi, lakini mishahara yao imekuwa ikibaki kuwa ile ile ambayo haitofautiani na askari wa kawaida aliye na cheti cha form four. Ukiangalia Jeshi la Polisi mtu mwenye shahada anapata sh. 860,000 lakini pia anapata posho ya ujuzi asilimia 15, kwa Askari Magereza wanalipwa sh. 400,000 wakikatwa inabaki 335,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwalipa Askari Magereza kulingana na ujuzi wao maana imekuwa ikiwaahidi kwamba itawaongezea mshahara kulingana na ujuzi wao, lakini mpaka leo bado. Ni lini sasa itakwenda kuwalipa Askari Magereza kulingana na ujuzi wao ili kuwapa motisha kama askari wengine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko hususan katika masuala mazima ya kupanga mishahara ya Askari Magereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua katika kada mbalimbali si wote ambao wanapata mishahara ambayo inaendana na kazi zao. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Esther Matiko, tayari tumeshaanza zoezi la tathmini ya kazi na hata ninavyoongea hapa watu wangu wa Bodi ya Mishahara wako hapa Bunge, wameshaongea na Tume ya Huduma za Bunge, lakini vilevile wameshazunguka nchi nzima kuongea na kada mbalimbali. Ifikapo mwezi wa Pili zoezi hili litakuwa limekamilika na baada ya hapo tukae sasa kupanga uwiano wa kazi pamoja na uzito wa majukumu kwa kada moja baada ya nyingine tukitambua ugumu wao wa kazi pamoja na majukumu yao. Vile vile tutaweza kupanga pia miundo yao pamoja na madaraja yao katika ngazi za mshahara. Kwa hiyo, nimhakikishie zoezi hili litaweza kufanyika kwa Askari Magereza, lakini vilevile kwa watumishi wote wa umma kwa ujumla wake.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa wanavyojitahidi na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kuhusiana na kadhia hii au suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Katika uhakiki unaondelea kuchukuliwa hadi tarehe aliyoitaja Mheshimiwa Waziri ni hasara kiasi gani Serikali imepata hadi kufikia tarehe hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pamoja na mikakati ambayo Serikali imekuwa ikichukua kuhusiana na watumishi pamoja na maafisa waliohusika na swala hili. Serikali itambue kwamba kuna udhoroteshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa inakwama pamoja na ukosefu wa madawa pamoja na ufinyu wa bajeti uliokuwa unajitokeza.
Je, Serikali inaweza kukubaliana na mimi kwamba pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kwa watumishi kwamba iwepo adhabu ya kurudisha fedha ambazo walizipoteza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mara nyingi tumekuwa tukitoa takwimu mwezi hadi mwezi endapo watumishi hao hewa wasingeondolewa kwa mwezi husika wangeisababishia hasara kiasi gani? Niseme tu kwamba hadi sasa tumeshaondoa watumishi hewa 19,629 ambao endapo wangeendelea kubaki katika orodha ya malipo ya mshahara kwa mwezi husika mmoja wangeisababishia Serikali hasara ya shilingi 19,749,737,180, hiyo ni kama wangebaki kwa mwezi mmoja husika bila kuondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nitoe labda takwimu ya Halmashauri mojawapo. Ningeweza kutaja kwa ujumla wake maana yake tuliomba takwimu lakini sijapiga mahesabu kwa jumla kwa haraka. Nikianzia na Kinondoni tangu ambavyo wameondoa watumishi hewa waliondoa watumishi hewa 107 na kwa kiasi cha fedha ambacho walilipwa watumishi hao ni shilingi bilioni 1.279. Nikija kuchukua kwa Halmashauri ya Kishapu watumishi 73 wamelipwa shilingi milioni 543. Kwa hiyo, ambacho naweza kusema ni kwamba endapo wangeendelea kubaki kwa kweli ni gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ni mikakati gani ambayo Serikali inachukua kuhakikisha kwamba pamoja na watumishi hawa hewa kuondolewa basi wanarejesha fedha. Nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyotoa takwimu kwa wale ambao tayari mashauri yao yamefikishwa mahakamani wametakiwa pia aidha kulipa faini lakini pamoja kurejesha fedha na endapo watashindwa kufanya vyote viwili basi watapata kifungo jela. Na kesi mbalimbali zimekuwa zikiendelea; tayari kesi 38 zilishamalizika mahakamani, tayari kuna majalada mengine ya uchunguzi 126 yanaendelea, lakini vilevile bado tunaendelea kuhakikisha kwamba tunakamilisha na wote walioshiriki basi wanafikishwa katika vyombo vya kisheria.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba eneo hili ni eneo muhimu sana katika utendaji wa Halmashauri zetu na ndiyo maana kumekuwa na Wakuu wa Idara wenye taaluma mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri anisaidie kitendo cha uteuzi wa Wakurugenzi kutoka nje ya wale Wakuu wa Idara na wakati mwingine watu ambao hawana taaluma kabisa ya kuendesha Halmashauri kuteuliwa kuwa Wakurugenzi katika maeneo haya na hata Waandishi wa Habari na maeneo mengine waliteuliwa ikaonekana kwamba ni form four na wakawa disqualified wakaondoka katika maeneo hayo na wengine wakaogopa kwenda kwenye maeneo waliyoteuliwa ……
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kitendo hicho cha kutoteuliwa wale Wakuu wa Idara kama sehemu ya promotion ni kuwavunja moyo katika utendaji wao wa kila siku?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafurahi kwamba yeye mwenyewe amesema ni promotion na hili ni suala la uteuzi. Teuzi hata siku moja haziombwi, mwenye mamlaka ndiye anayeamua amteue nani. Vilevile, kwa mujibu wa Ibara ya 36, Mheshimiwa Rais anayo mamlaka ya kumteua mtu yeyote ambaye anaona anafaa. Kwa hiyo, ni sahihi kabisa na naamini Mheshimiwa Rais ametenda haki kwa kufuata taratibu.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa viongozi, wapo wanaokiuka taratibu za kuanzisha mashtaka katika utumishi wa umma, ikiwemo taratibu za uendeshaji wa mashauri ya nidhamu. Je, Waziri anatoa kauli gani kwa viongozi hao wasiotimiza wajibu wao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati ambaye ametaka kusikia kauli ya Serikali tunasema nini kuhusiana na viongozi ambao wanakiuka taratibu katika uendeshaji wa masuala mbalimbali ya kinidhamu na uchukuaji wa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulie kusema kwamba kumekuwa kuna kauli nyingi kwamba watumishi wa umma wanakatishwa tamaa, watumishi wa umma wanakosa kujiamini na mambo mengine kutokana na hatua mbalimbali za kinidhamu zinazochukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba pamoja na malengo mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano, lengo mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunarejesha nidhamu katika utumishi wa umma, ikiwemo pia kuchukua hatua kwa watumishi wa umma ambao watakiuka sheria, kanuni na taratibu. Endapo mtumishi wa umma yuko katika mstari anatekeleza wajibu wake ipasavyo, sioni ni kwa nini kuwe na hisia au hofu. Niwahakikishie tu kwamba, Serikali yao iko pamoja nao na hakuna ambaye ataonewa bila kufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema mambo yafuatayo:-
Taratibu nzima za kinidhamu zinasimamiwa na Sheria yenyewe ya Utumishi wa Umma, Kifungu cha 23(2), lakini kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kwa mujibu wa Kanuni ya 42, 47 na Kanuni nyinginezo, napenda kusema utaratibu mdogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hatua yoyote ya nidhamu haijachukuliwa ni lazima kuwe na hati ya mashtaka, ambapo mtuhumiwa au mtumishi huyo wa umma atapewa nafasi lakini vilevile katika hati hiyo atakuwa ameelezewa shutuma zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni lazima mtumishi wa umma huyo anayetuhumiwa apate haki au fursa ya kuweza kujibu hati hiyo ya mashtaka ambayo amepatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni lazima iundwe Kamati huru ya uchunguzi ambayo itampa fursa pia mtuhumiwa aweze kujibu au kukanusha tuhuma zilizoko chini yake. Vilevile kwa mujibu wa Kanuni ya 47 Mtumishi huyu wa Umma anayetuhumiwa atakuwa na haki ya kusikilizwa kikamilifu, atakuwa na haki ya kuweza kumhoji mwajiri, atakuwa na haki ya kuweza kuona vielelezo mbalimbali vilivyotumiwa katika kumshtaki. Pia Kamati hii sasa ya Uchunguzi, ziko ambazo zimekuwa zikikiuka taratibu, ni lazima ndani ya siku 30 baada ya kutoa uamuzi wake iweze kuwasilisha ripoti katika mamlaka ya nidhamu na ajira. Baada ya siku 30 tangu ambapo Kamati ya Uchunguzi imewasilisha ripoti yake ni lazima mamlaka ya ajira iweze kumjulisha mtuhumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mtuhumiwa atakuwa hajaarifiwa ndani ya siku husika, basi italazimika kuondolewa mashtaka na atakuwa huru kwa mujibu wa kifungu cha 48(9) cha Sheria ya Utumishi wa Umma. Nazitaka mamlaka mbalimbali za nidhamu kuhakikisha wanatimiza matakwa ya sheria hizi ili wasije wakawasababishia usumbufu watumishi wa umma vilevile wasije wakaisababishia Serikali hasara baadaye.
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema hapa kwamba shida ni watu ambao wamewasababishia wafanyakazi hawa ambao wanafanya kazi zao kwa nia ya dhati ya kuitumikia nchi yao. Naomba Waziri atoe commitment ni lini wafanyakazi wote hasa wa Idara ya Uhamiaji ambao wameanza kazi zaidi ya miezi mitano sasa, hawajalipwa mshahara hata mwezi mmoja, , watalipwa malimbikizo yao ya mishahara mara moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba commitment ya Serikali. Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niunge mkono majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Sasa hivi inapotokea ajira mpya siyo kwamba hawajalipwa kwa miezi minne.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoeleza; kulikuwa na ajira mpya za Maafisa Uhamiaji 297, Maafisa wa Utumishi wa Idara ya Uhamiaji ni lazima wafanye higher action katika mfumo wetu wa taarifa za kiutumishi na mishahara, walikuwa hawajafanya. Kwa hiyo, ingekuwa ni vigumu wao kuweza kulipwa. Kwa mwezi huu tayari tunaendelea vizuri watakuwa wameshalipwa. Pia kuhusiana na masuala ya malimbikizo mara tu Maafisa Utumishi wa Uhamiaji watakapokuwa wamefanya hizo higher action na pending salaries arrears automatically katika mfumo wataweza kulipwa mara moja.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kuna watumishi ambao walipandishwa daraja kama alivyosema muuliza swali wa kwanza, na kupokea mshahara mpya mwaka jana; na kisha hiyo mishahara ikasitishwa na sasa hivi watumishi hawa ambao ni walimu na watumishi wa afya kuna baadhi yao wameshastaafu, na wengine wanatarajia kustaafu miezi ijayo hii.
Je, Serikali itatumia hesabu gani katika ku-calculate, itatumia mshahara upi? Ule wa zamani au mshahara mpya katika kukokotoa kile kiinua mgongo cha mwisho? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa watumishi ambao walikuwa wameingia katika utumishi wa umma, halafu baadaye wakaambiwa warudi nyumbani, tumeshawarudisha watumishi 421 na kwa sasa tayari wameshalipwa takribani watumishi 379, 42 tumewarudishia waajiri wao ili waweze kukamilisha baadhi ya taratibu za ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja yake ya pili kwamba unakuta wengine wameshastaafu, lakini ni kiwango gani kitatumika katika kukokotoa mafao yao? Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wote wanaosikiliza, kwa wale ambao wanastaafu wanapewa kipaumbele miezi miwili kabla ya tarehe ya kustaafu mishahara yao inarekebishwa na watakuwa wamepata katika cheo stahiki ili waweze kutokuathirika na mafao.
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Waziri, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na utaraibu wa wastaafu kuongezewa mikataba ya kufanya kazi. Je, Serikali haioni kwamba hii ni sababu mojawapo ya ukosefu wa ajira kwa vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kati ya Wilaya saba za Mkoa wa Mwanza, Wilaya sita ambazo ni Sengarema, Ilemela, Nyamagana, Misungwi na Magu, pamoja na Ukerewe, zinategemea asilimia kubwa ya mapato yake kutoka kwenye sekta ya uvuvi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri vijana wenye taaluma ya uvuvi ili kuweza kukidhi haja ya elimu ya kilimo cha samaki pembezoni mwa Ziwa Victoria? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusiana na Serikali kuongezea muda wastaafu au kuwapa mkataba wa ajira, nipende kusema yafuatayo; kwanza kabisa tunao waraka ambao ndio mwongozo unaotoa taswira au mwongozo ni watu gani au kada zipi ambazo zinastahili kuweza kuongezewa mkataba wa ajira.
Nipende tu kusema kwamba kwa sasa kipaumbele kipo kwa marubani, kipaumbele kipo kwa wahadhiri wa vyuo vikuu na hao ndio wanaopewa mikataba. Lakini ni lazima wao pia wanapoomba kuongezewa mkataba wa ajira baada ya kustaafu, ni lazima waweze kuwasilisha mpango wao wa kurithishana madaraka, lakini vilevile ni lazima na wenyewe waweze kutoa wamefanya jitihada gani za kuhakikisha kwamba wanawawezesha watumishi wengine walioko chini yao kuhakikisha kwamba wanaweza ku-take over baada ya wao kuondoka katika nafasi hizo walizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili hasa katika ajira za vijana na ameongelea zaidi katika ajira za uvuvi; kwanza nipende tu kusema kwamba Mkoa wa Mwanza katika takribani Wilaya zake nne tunatambua ndizo ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi ikiongozwa na Wilaya ya Buchosa, Wilaya ya Kwimba pamoja na Wilaya ya Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika ikama ya mwaka huu 2016/2017 nitolee tu mfano katika Wilaya ya Ukerewe, wavuvi wasaidizi takribani watano wamepangiwa na hizo ni katika nafasi chache ambazo zimewekwa katika utaratibu wa ikama ya mwaka 2016/2017. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kada ambazo zina upungufu mkubwa katika Halmashauri hizo tutazipa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba, wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi na kwa uweledi mkubwa.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumza ni Februari tunaelekea Juni, mwaka wa fedha unaishia na Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa ambayo ina tatizo kubwa la watumishi na hasa wa sekta ya afya. Nilitaka kufahamu ni lini hicho kibali kitatolewa na ajira hizo zitaajiriwa? Kwa sababu ninavyo vituo viwili vya afya vyenye vyumba vya upasuaji, lakini hakuna upasuaji unaofanyika kwa sababu hakuna watumishi na Wilaya nyingine zote za Mkoa wa Mtwara hali ni hiyo hiyo, ni lini kibali kitatolewa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia masuala mazima ya utumishi na tunatambua pia, na yeye alishakuwa Waziri wa Utumishi na alifanya kazi kubwa na nzuri sana hapo alipokuwa na sisi tumeweza kuvaa viatu vyake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sasa, kama nilivyoeleza, tumeanza na watumshi wa sekta ya elimu pamoja na mafundi sanifu wa maabara na tunatarajia ifikapo mwezi wa tatu wataweza kuingia katika ajira. Kwa upande wa watumishi wa sekta ya afya, muda si mrefu tutaanza pia awamu yao na ninadhani kati ya mwezi wa tatu mpaka wa nne watakuwa wameshaingia katika utumishi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba kuna changamoto nyingi kwa watumishi wa umma, ni pungufu kwa uwezo mdogo wa Serikali kuajiri na wengine wametumbuliwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nijue ni nini kauli ya Waziri wa Utumishi kwa watumishi wale ambao wanashushwa vyeo, wanadhalilishwa na kutukanwa na viongozi, hasa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa na ukizingatia matokeo ya form four yametoka, wameanza kutumbuliwa. Sasa nini kauli ya Serikali kuwatia moyo waliopo kazini na kuwatia moyo ambao watapata ajira, ili wajue wataenda mahali salama wakafanye kazi nzuri kutumikia Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata majibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme tu kwamba masuala mazima ya nidhamu, ajira pamoja na upandishwaji wa vyeo na kushushwa vyeo yanaongozwa na kanuni, sheria na taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema tu ni kwamba, kama kuna ambaye anaona kanuni hazikufuatwa, basi tuweze kupata taarifa ili tuweze kufuatilia. Lakini tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali kwa viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji kuhakikisha kwamba, wanazingatia Sheria ya Utumishi wa Umma, wanazingatia Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba kama kuna mtumishi ambaye naona yeye hakutendewa haki basi asisite kuwasilisha malalamiko yake.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Waziri Mheshimiwa Kairuki, napenda niongezee tu kwenye swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kumekuwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutokana na watumishi wazembe. Na mtambue kwamba katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tulisema kwamba kwa watumishi wazembe hatutakubali kuendelea nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii kusema kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamegawiwa maeneo yao ya utawala na wanasimamia masuala yote, lakini wanasimamia yote kwa mujibu wa sheria. Haiwezekani unapewa pesa ya basket fund, wewe ni DMO halafu huzitumii na watu wanakosa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya utafiti katika mikoa minne, ziko hela nyingi kwenye Halmashauri hazitumiki, wanataka kuzifanyia nini? Mnasema tusichukue hatua, haiwezekani. Haiwezekani unapewa shule una walimu zaidi ya 15 pamoja na changamoto zilizopo ambazo ni haki yao kuzidai, lakini si sababu ya wao kutokutimiza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba Wakuu wa Mikoa wanayo haki ya kisheria kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote awe ni Mkuu wa Shule, kwa mfano uteuzi wa Mkuu wa Shule unateuliwa na RAS ambaye ndio Katibu Mkuu wa Mkoa. Kwa hiyo, Mkuu wa Mkoa akichukua ile hatua, nimekuwa nikiulizwa na Wabunge wengi hapa kwamba mbona wanaingilia mambo mengine. Jamani, mkumbuke mlikuwa mnasema watumishi wetu ni wazembe. Ngonjeni kidogo tubanane ili twende kwenye ufanisi na Watanzania wanangojea hayo mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwasihi tu Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane. Wenzetu nao wale ni binadamu katika namna moja au nyingine wanaweza wakafanya makosa, tuwasiliane, turekebishane, ndio maana ya administration and leadership. Si kwamba wao hawakosei, wanaweza wakakosea kwa namna moja ama nyingine, lakini na mazingira yale tuyaangalie, lakini huku nikitambua kwamba watumishi nao wana haki yao, lakini na wao pia watekeleze majukumu tuliyowapa.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka kuongezea tu kwenye jibu linalohusu mkakati wetu wa kupeleka huduma za upasuaji kwenye vituo vya afya nchini wakati hakuna watumishi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishakutoa maelekezo kama Serikali kwa Makatibu Tawala wote wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kufanya redistribution ya watumishi ndani ya maeneo yao, kuwatoa kwenye maeneo ambapo wapo wengi na kuwapeleka kwenye vituo hivyo ambavyo tunataka vitoe huduma za upasuaji. Huu ni mkakati wa muda tukisubiri mkakati wa kudumu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 Serikali kupitia Ofisi ya Rais - Utumishi ilikipa Chuo cha Utumishi wa Umma kikishirikiana na chuo kimoja cha Macintosh cha Canada kuandaa framework ya kuwandaa viongozi ambayo ilijulikana kama Leadership Competence Framework. Na katika framework hiyo ilikuja na sifa 24 yaani leadership competencies 24. Sasa, je, ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kuziingiza hizo competencies katika mafunzo ambayo tayari yameandaliwa na Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika utaratibu wa majeshi yetu kuna utaratibu kwamba mtu hawezi kupata cheo chochote mpaka kwanza apate mafunzo fulani. Sasa kwa kuwa Serikali imesema inaandaa utaratibu wa kozi ambazo zitakuwa ni lazima kwa watumishi wa umma waandamizi. Je, ni lini sasa tamko la Serikali hizo kozi zitaanza ili watumishi hawa wawe wanafundishwa na wanaandaliwa ili wawe mahiri kabla hawajapata uteuzi wa madaraka ya aina yoyote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hasunga, alikuwa ni mtumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kwa hiyo, anaifahamu sekta hii vizuri sana na anakifahamu chuo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuingiza zile sifa 24 za uongozi katika mafunzo yake; nisema tu kwamba sasa tunaandaa utaratibu katika hayo mafunzo ya lazima, utakapokamilika na zile sifa zote 24 katika leadership competence zitaweza kuingizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, ni lini sasa katika mafunzo ya in-service, kabla watu hawajapandishwa cheo yataweza kuwekewa utaratibu, nipende tu kusema kwamba pamoja na haya tumeandaa pia, utaratibu wa kuwa na assessment centre ambao tutaweza kuweka kuwa na pool ya watu mbalimbali ambao wana-managerial positions ambazo wakati wowote wanaweza wakateuliwa. Watakuwa tested, lakini pamoja na hayo pia, kutakuwa na yale mafunzo ya lazima ambayo niliyaeleza awali yatakapokamilika basi wataweza kupatiwa na tutakuwa hatuwezi kupandisha cheo mtu kabla hajapata mafunzo hayo.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Tatizo la viongozi kukosa semina elekezi juu ya masuala ya uongozi yamekuwa yakionekana kuanzia ngazi za juu, kwa mfano mdogo tu hapa katika swali lililopita unakuta Mawaziri wamejibu, Naibu Waziri naye anajibu kwa hiyo, protocol inakuwa inaonekana pale haijafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala langu ninalotaka kujua ni kwamba taratibu kama hizi, viongozi ambao wanakosa semina za mafunzo elekezi na contradiction inaonekana ndani ya Bunge lako Tukufu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka nijue makosa kama haya yataendelea mpaka lini kwa viongozi ambao hawana semina kama Mawaziri? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na semina elekezi au mafunzo elekezi kabla watu hawajaingia katika madaraka nimeshaeleza awali.
Lakini pili, kwa mwaka huu wa fedha peke yake Taasisi ya Uongozi imetoa mafunzo kwa viongozi 544, lakini pia tumekuwa tukitoa mafunzo kwa Mawaziri, tumekuwa tukitoa mafunzo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na nafasi nyinginezo na tutaendelea kufanya hivyo kila wakati itakapobidi.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru Wizara ya Kilimo, vilevile kumshukuru Rais. Nimemweleza hili, nimeona cheche kidogo. Niseme, kwa kuwa tumeshamkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Siha na amewekwa ndani kwa muda kwa ajilii ya tuhuma kama hizi za ufisadi, lakini sh. 1,600,000/= ambazo zimeshushwa siyo za kweli. Amesharudisha ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Charles Mlingwa na risiti tunazo. Tulimtafuta tukamkamate, lakini tukakuta amezungukwa na Jeshi la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kuwa Mkuu Mkoa wa Kilimanjaro Meck Sadiq amemtishia Meneja wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kilimanjaro, kwamba hizi tuhuma anazozichunguza ni za uongo, swali langu la kwanza ni kwamba. Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha watuhumiwa wote wa ufisadi ndani ya ushirika na KNCU Mkoa wa Kilimanjaro, wamefikishwa mbele ya sheria; na kutuhakikishia watamlindaje Mkuu wa TAKUKURU anayezuiliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufanya kazi zake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali inatupa commitment gani kwamba Charles Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, vilevile Meck Sadiq ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, bado wanastahili kupeperusha bendera ya Tanzania na vilevile kupigiwa saluti na majeshi yetu ya Tanzania kama Wakuu wa Mikoa na kumwakilisha Rais baada ya vitendo hivi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na swali lake la kwanza, kwamba Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha kwamba watuhumiwa wanafikishwa Mahakamani au wanafunguliwa mashtaka? Nimhakikishie kwamba tunaendelea na chunguzi mbalimbali na pindi chunguzi hizo zitakapokamilika na itakapothibitika pasipo shaka kwamba wanayo hatia au wana hoja ya kujibu Mahakamani, basi kwa hakika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili kwamba Afisa wa TAKUKURU wa Mkoa anaingiliwa ama anazuiwa kufanya kazi zake na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, niseme kwamba siyo kweli. Ukiangalia kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, TAKUKURU kama chombo, kinao uhuru wa kufanya kazi zake bila kuingiliwa na imekuwa ikifanya hivyo. Hata katika jibu la msingi nilieleza, tayari kulikuwa kuna mkutano wa wanaushirika, tena Mheshimiwa Meck Sadiq huyo huyo aliitisha na waliweza kusomewa taarifa ya TAKUKURU pale na aliweza kuridhika na ndiyo maana mpaka leo kunakuwa na utulivu na uhimilivu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, endapo ataona ana malalamiko dhidi ya Wakuu wa Mikoa hao, basi asisite kuwasilisha malalamiko stahiki na aweze kuchukuliwa hatua.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo ya vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya ya Siha, yanafanana sana na matatizo ya Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Wilaya ya Hai; na kwa sababu Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro vimehodhi maeneo makubwa sana ya ardhi, ambayo kimsingi kwa Mkoa wa Kilimanjaro ndiyo backbone ya economy ya Mkoa ule kwenye upande wa kilimo; na kwa kuwa kumekuwa na shutuma nyingi za muda mrefu ambazo pengine zimelindwa kwa kiwango kikubwa na sheria yenyewe ya ushirika, ambayo inatoa limited power kwa mtu mwingine yeyote kuingilia vitendo na kazi za ushirika:-
Je, Serikali haioni sasa kwa sababu ya matatizo haya ya muda mrefu yaliyokithiri, ni wakati muafaka wa ku-review Sheria ya Ushirika; na kabla ya kui-review Sheria ya Ushirika, kuangalia kwa kina matatizo ya Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kuweza sasa kuweka mapendekezo sahihi ya kurekebisha sheria ile?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kuhusiana na kufanya mapitio katika Sheria ya Ushirika, Wizara ya Kilimo bahati nzuri wapo. Niseme tu kama Serikali tumekuwa tukifanya hivyo kwa sheria mbalimbali siyo hii tu ya ushirika; na naamini Wizara husika itaweza kulichukua na nina uhakika watakuwa wameshaanza mapitio kwa sababu ni suala endelevu kila mara kungalia sheria inakidhi mahitaji ya wakati husika.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Serikali kuviangalia Vyama hivi vya Ushirika kama vina matatizo, napenda tu kusema kwamba katika Mkoa wa Kilimanjaro hata hivi sasa tunavyoongea tayari Vyama vya Ushirika vinne vimefanyiwa uchunguzi na tayari vyama vitatu uchunguzi umeshakamilika, kimebakia kimoja. Naamini matokeo ya uchunguzi hayo yataweza kutangazwa huko baadaye ili kuona ni hatua gani iweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, vile vile tumeshafanya uchunguzi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha KNCU na tumefanya uchunguzi katika Chama cha Tanganyika Coffee Curing CompanyLimited na siyo kwa Vyama hivi vya Ushirika peke yake. Tumefanya pia uchunguzi katika SACCOS nne na tayari mbili zimeshafikishwa Mahakamani na mbili zinaendelea na uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbowe, kwa kutambua umuhimu wa Vyama hivi vya Ushirika kwa wakulima, tutakapoona kuna harufu au chochote kinachoashiria vitendo vya rushwa au vitendo vingine vya ubadhirifu wa mali za umma, tutahakikisha kwamba hatua stahiki zinachukuliwa.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika ahsante kwa kunipa nafasi. Nashukuru kwa majibu mazuri
ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Pamoja na Mahakama hiyo lakini liko tatizo kubwa sana la Mabaraza ya Kata. Mabaraza ya Kata yamekuwa ni
mwiba mchungu sana kwa wananchi katika maeneo mbalimbali na hasa hasa katika Jimbo la Njombe. Kinachosababisha, moja; ni kukosa weledi. Je, Serikali sasa ipo tayari kuajiri mtaalam mmoja mmoja katika Mabaraza ya Kata ili asaidiane na wale wananchi wanaokuwa wajumbe wa Mabaraza haya ili kupunguza matatizo
yanayojitokeza kwa kukosa utaalam?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali ipo tayari kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Mabaraza haya ya Kata ili
kusudi wanapofanya kazi zao za kusuluhisha migogoro mbalimbali kwa wananchi wawe na uelewa? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuhusiana na kuongeza idadi ya watumishi katika mabaraza ya kata. Nimhakikishie tu kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikifanya kazi nzuri katika kuyasimamia mabaraza haya na lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba Mabaraza haya ya Kata pamoja na Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya pamoja na mahakama zetu zote zinasogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kuwa na miundombinu, vitendea kazi, lakini pia kuwa na watumishi wa kutosha kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tunalipokea, tutalifanyia kazi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, kwamba, endapo Serikali tupo tayari kutoa mafunzo kwa watendaji
hawa katika Mabaraza ya Kata; nimhakikishie ndiyo na Ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikifanya hivyo kila mara ili
kuhakikisha kwamba wanaenda na wakati, wanafahamu sheria na masuala mengine wanayosimamia.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo lililopo Njombe linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Kata ya Mtae Jimbo la Mlalo Wilayani Lushoto. Je, ni lini Serikali itayakarabati majengo yale machakavu ya Mahakama ile ya mwanzo Mtae?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nimhakikishie tu kwamba, azma ya Serikali kupitia Mahakama ni kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi. Ukiangalia tu katika mwaka huu wa fedha ambao tunaumaliza Serikali ilitenga zaidi ya Shilingi bilioni 46.5 na hata katika mwaka huu wa fedha ambayo bajeti yake tunaanza nayo zaidi ya Shilingi bilioni 18.1 pia zimetengwa kwa ajili ya kujenga mahakama mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaliona suala hili, tutakwenda kuliangalia; lakini katika mahakama ambazo ziko katika utaratibu kwa mwaka huu tunaomalizana nao ni ujenzi wa Mahakama Kuu, Tanga ambako na yeye pia anatoka, tunakamilisha ukarabati huo. Vile vile tunakamilisha ukarabati katika
Mahakama Kuu, Dar es Salaam lakini pia tunaanza ujenzi katika Mahakama Kuu, Mara pamoja na Kigoma na vile vile tunakamilisha ujenzi wa Mahakama za Wilaya Bagamoyo, Kigamboni na Mkuranga.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama za Mwanzo tunakamilisha ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo
Kawe pamoja na Kinyerezi, vile vile katika mwaka huu wa fedha, zaidi ya Mahakama za Mwanzo 10 zitaweza kujengwa na kukarabatiwa.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nakubaliana naye kwamba kwa mujibu wa Sheria na Katiba yetu, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho na ndiye Mwajiri Mkuu.
Swali la msingi limeulizwa kwamba kumekuwa na practice ya kuanzia Rais mwenyewe na ma-DC na RCs kutumbua au kuwasimamisha watu kwa njia ya mnada, kupigia kura atumbuliwe au asitumbuliwe, kwa hiyo, swali la msingi linaulizwa hapa, ni kwa nini Serikali isifuate utaratibu na kanuni na sheria ambazo sisi wenyewe tumeziweka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa ma-RC na ma-DC ni kada ya kisiasa kama sisi Wabunge tulivyo, hawana weledi na ndiyo maana Baba wa Taifa alisema tuliweka sheria ngumu sana ili mtu asizuke tu na kufukuza watu ovyo ovyo. Kwa kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alithamini sana kada ya watendaji wa umma; je, Serikali itatoa tamko sasa kwamba ma-RC na ma-DC wasikurupuke tu kuwafukuzisha watu bila kufuata taratibu na kanuni za nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na kwa nini Serikali isifuate utaratibu, napenda kuendelea kusisitiza kwamba Serikali inafuata uratatibu na kwamba kwa wateule ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais, hatua zao za kinidhamu huchukuliwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa mujibu wa kifungu cha 4(3)(d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema katika Ibara ya 36(4), Mheshimiwa Rais pamoja na kukasimu bado anayo mamlaka ya mwisho na hakatazwi kutumia mamlaka yake. Kwa watumishi wengine wa umma, kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Mamlaka za Nidhamu zimepewa mamlaka yao ya mwisho kabisa ya kuweza kuchukua hatua kwa watumishi wengine ambao sio wateule wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuendelea kusisitiza kwamba jambo la msingi katika mamlaka za kinidhamu zinapochukua hatua, wanatakiwa wazingatie hatua tatu zifuatazo:-
Kwanza kabisa waweze kutoa hati ya nashtaka; pili, watoe fursa ya kujitetea kwa yule mtuhumiwa au mtumishi; na mwisho, tatu, uchunguzi wa kina uweze kufanyika ili kuthibitisha tuhuma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kusema, utaratibu mzima wa kina na mwongozo umefafanuliwa katika kanuni ya 46 na 47 za Kanuni za Utumishi wa Umma. Endapo kuna mtumishi wa umma anaona hajaridhika na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa, anayo fursa kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Utumishi wa Umma kuweza kukata rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili kwamba Serikali inatoa tamko gani katika hatua ambazo zimechukuliwa na ma-RC na ma-DC? Naendelea kusisitiza kwamba kifungu cha 6(1)(b) na kifungu cha 4(3)(d) kimeelekeza Mamlaka za Nidhamu ni zipi? Ndicho ambacho
Serikali imekuwa ikifuata.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwenye majibu ya Mheshiwa Waziri amesema, endapo mtumishi hajaridhika na hatua za kinidhamu alizochukuliwa, akate rufaa. Sasa endapo mtumishi huyo ametumbuliwa na Mheshimiwa Rais na hajaridhika na hayo matokeo, wapi achukue hatua za kuja kukata rufaa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza Mheshimiwa Silinde ameuliza swali zuri sana; na kama atakuwa amefuatilia hata katika hotuba yangu ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi), ziko kesi mbalimbali ambazo hata Ofisi ya Rais (Utumishi) pia tunashitakiwa. Wako ambao wanafungua kupinga maamuzi ya Mheshimiwa Rais, wako ambao wanafungua kesi kupinga maamuzi ya Katibu Mkuu Kiongozi, lakini pia
katika Tume yetu ya Utumishi wa Umma ambayo ni mamlaka yenye Mamlaka ya Urekebu wamepokea kesi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, katika mwaka huu wa fedha tu peke yake, zaidi ya watumishi wa umma 76 wameweza kukata rufaa katika Tume ya Utumishi wa Umma na endapo hawataridhika, bado tunacho Kitengo cha Rufaa chini ya Mheshimiwa Rais pia (Public Service Appeals) wanaweza pia wakakata rufaa nyingine. Kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zipo na zinafuatwa na ziko wazi kabisa na wako ambao hata wanajikuta walikata rufaa dhidi ya Mheshimiwa Rais na wakaja kushinda endapo kama kuna taratibu inaonekana hazikufuatwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Utumishi kwa majibu mazuri sana. Nilitaka kuongezea, kuna moja ambalo limewataja Wakuu wa Mikoa
na Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua za kuwasimamisha au kuwafukuza kazi watumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kifungu cha (5) cha Sheria ya Tawala za Mikoa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wawakilishi wa Serikali Kuu kwenye maeneo yao. Ukisoma pia kifungu cha 87 cha Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, kinawataja hawa na kwa ajili ya usahihi wa nukuu, napenda nisome kwa sababu wakati mwingine tunauliza swali lile lile kila siku. Bahati mbaya imeandikwa kwa Kiingereza, inasema hivi; “In relation to the exercise of the powers and performance of the functions of the Local Government Authorities confered by this Act, the role of the Regional Commissioner and the District Commissioner shall be to investigate the legality when questioned of the actions and decisions of the Local Government Authorities within their areas of jurisdiction and to inform the Minister to take such other appropriate action as may be required.”

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukisoma kifungu hiki unaona kabisa kwamba wao kuchukua hatua zozote zile, ziwe za kiutumishi ni sahihi, isipokuwa utaratibu aliouzungumza Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ndiyo unaotakiwa.
Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa anaposema wewe hufai, umefanya makosa haya, akasema publicly, siyo ndiyo kafanya tendo hilo la kumsimamisha au kumuadhibu yule mtumishi, anachofanya pale, baada ya tamko lile, sasa Mamlaka ya Nidhamu ya mtumishi husika ndiyo inachukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika level ya Halmashauri, sasa Mkurugenzi atamwandikia barua kama ni ya kumsimamisha au kumtaka atoe maelezo fulani kulingana na maagizo ya Mkuu wa Wilaya, au Mkuu wa Mkoa atafanya hivyo. Kwa ngazi ya Mkoa, RAS ndio Mamlaka ya Utumishi, naye anaweza kuagizwa na kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kutamka tu kwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, ndiyo tayari basi yule amemchukulia hatua za kinidhamu.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Wizara ya Utumishi ina watumishi wanaofanya kazi vizuri, hawajatumbuliwa, Serikali kwa maana ya Chuo cha Ualimu, kutokana na swali langu namba 81 ambalo nilijibiwa kwamba suala la upandishaji madaraja na likizo za Watumishi wamelipwa kwa kiasi kile ambacho walikuwa wamekitaja.
Je, watakuwa tayari sasa kutoa orodha ile ya wale waliokwishalipwa kwa Chuo kile cha Korogwe cha
Ualimu ili kusudi Walimu waweze kujitambua kwa sababu huwa kama wanawalipa, wanaingiza moja kwa moja kwenye mishahara, watakuwa tayari kuitoa hiyo orodha ili iende kwa Mkuu wa Chuo kila mtu aweze kutambua kile alichoweza kulipwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chatanda. Nimelifuatilia swali hili, nadhani wiki iliyopita lilijibiwa na Mheshimiwa Stella Manyanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema kwamba nitafuatilia na Wizara ya Elimu kwa karibu ili kuona waliolipwa ni akina nani na orodha iweze kutolewa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyoko huko Buchosa yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko Itigi katika Halmashauri mpya ya Itigi. Wakati Halmashauri hii inaanzishwa ilipata watumishi kutoka Halmashauri mama ya Manyoni ambayo hata nayo ilikuwa na watumishi wachache na hivi tunavyozungumza Halmashauri ya Itigi pia imekutana na janga hili la vyeti fake, kuna baadhi ya watumishi ambao wameondoka, je, Serikali iko tayari sasa itakapotoa ajira kutuletea watumishi wa kutosheleza katika Halmashauri mpya ya Itigi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massare kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua upo upungufu na kama ambavyo tumekuwa tukieleza humu ndani, mwaka kesho tunatarajia kuajiri zaidi ya watumishi wapya 52,436. Jana tu pia tayari Mheshimiwa Rais alishaagiza, tumetoa kibali cha watumishi wapya 15,000 kwa ajili ya kwenda kuziba pengo la watumishi ambao wamekutwa na vyeti vya kughushi, lakini vilevile kuweza kuziba ikama na tutaendelea kufanya hivyo kila mara itakapobidi.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye Jimbo langu la Serengeti katika process za kuongeza vijiji, vitongoji na kata, kuna baadhi ya maeneo ambayo utaratibu haukufuatwa, baada uchaguzi kuna Serikali za Vijiji walijiuzuru. Kwa hiyo, kimsingi kuna migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji na mpaka ninavyoongea hakuna uongozi kwenye vijiji hivyo. Nini tamko la Wizara kuhusu maeneo ambayo yana migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba iko migogoro mbalimbali lakini migogoro inatofautiana, iko mipaka ya kijiji kwa kijiji, kata kwa kata, iko ya aina nyingi na kwenye orodha tumeorodhesha zaidi ya 250 kwa nchi nzima.
Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mazingira ya migogoro hii inatofautiana kutoka mgogoro mmoja hadi mwingine hatuwezi kuwa na tamko la pamoja kwa hiyo atuletee ili tuweze kuona hiyo scenario ikoje ili tuweze kutatua mgogoro husika ikiwa ni pamoja na mamlaka za uongozi wa maeneo husika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, yapo pamoja na majibu ya Serikali ambayo kimsingi hayajatatua tatizo lengo lilikuwa ni Serikali itutue huu mzigo. Kama utakumbuka ni kwamba mapato ya ndani yanatakiwa yaende kwenye makundi maalum ikiwepo wanawake na vijana zile asilimia 10. Sasa Halmashauri inapotumia pesa zote hizi kwa ajili ya kulipa watumishi ambao ni jukumu la Serikali, je, Serikali haioni kwamba hili linaendana na kinyume na dhana nzima ya utawala bora?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa uhitaji huu
wa kutumia own source kulipa watumishi wa ndani bado unaonekana mahitaji yapo kwa sababu Serikali Kuu haiajiri na kwa sasa wakati wa zoezi zima hili la uhakiki wa vyeti Halmashauri ya Lushoto imepoteza zaidi ya watumishi 115. Serikali inatoa tamko gani la kufidia hili pengo ambalo wafanyakazi hawa wametoka?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, pamoja kwamba anasema kwa upande mmoja alikuwa hajaridhika, nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia suala zima la ajira hizi zinazofanyika kwa kutumia mapato ya ndani.
Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kusema yafuatayo; kama Serikali hatu-entertain sana ajira hizi kwa kutumia mapato ya Halmashauri. Tunatambua kwamba mapato haya ya Halmashauri au own source yanatakiwa kwenda katika vipaumbele vingi na ndiyo maana tuaendelea kusisitiza ni vema Halmashauri zetu kupitia kwa waajiri ambalimbali na Maafisa Utumishi wahakikishe wanaweka mapendekezo yao na makisio yao ya Ikama ili kipindi ambapo tunaajiri basi waweze kupata mgao wa ajira kwa wakati sahihi bila kuathiri uwezo wao Halmashauri katika kulipa.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukipata changamoto nyingine, wako ambao walikuwa wakiajiri kupitia hizi own source lakini unakuta hawafuati taratibu. Nipende kuweka angalizo kupitia Bunge lako, mchakato wa ajira hizi za own source unatakiwa usitofautiane na mchakato wa ajira zingine kama zinazofanyika katika Serikali Kuu na kulipiwa na Serikali Kuu, lakini vilevile hata katika sifa na miundo ya kiutumishi inatakiwa pia isiwe compromised, sifa zile zile kwa mujibu wa miundo ya maendeleo ya kiutumishi. Kwa hiyo, nimeona niseme hayo kwanza kabla sijajibu swali lake kwa undani.
Mheshimiwa Spika, nipende kumtoa hofu Mheshimiwa Shangazi, wao walipoleta haya mahitaji walionekana wanauweza kulipa, lakini nimuhakikishie tu katika mwaka huu ujao wa fedha 2017/2018 kwa Halmashauri ya Lushoto tumewatengea ajira nafasi 252 ambapo kati ya hizo kwa kada za afya tumewatengea nafasi 54, kwa upande wa elimu nafasi 132 kilimo nafasi 10, mifugo nafasi tano na nafasi nyinginezo 51.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa watumishi walioathirika katika zoezi la vyeti fake, kama nilivyosema katika siku nne zilizopita, tayari tumeshatenga nafasi 15,000 kwa ajili ya kuzibia zile nafasi 9,932 pamoja na nafasi zingine za ziada zaidi ya 5,000 katika maeneo mbali mbali yenye upungufu mkubwa na mahitaji.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Niseme tu majibu ya Serikali yamekuwa ni yale ya ought to be, rather than what is the real situation. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, je, Serikali inasema nini pale ambapo watendaji maalum kama DED, DAS, RAS na walimu wanapohamishwa kila baada ya muda mfupi katika Wilaya husika? Na mfano ni Wilaya Mafia ambapo katika miezi michache ma-DED walihamishwa na tukapata wapya kama watatu na hii ilitokana zaidi na jinsi walivyoendesha uchaguzi na kuusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ufanisi sio tu kutunga sheria za kusimamia, hivi Serikali haioni kwamba masuala kama ya kuhakikisha watumishi wanapata makazi bora, wanalipwa stahiki zao ipasavyo na vilevile wana uhakika wa kuwa na periodic training za ku-upgrade zile nafasi zao ni namna za kujenga ufanisi katika utendaji kazi?Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kuzungumzia alipokuwa anasema kwamba tumejibu tu namna inavyotakiwa kuwa na siyo uhalisia. Sisi tunasimamia Menejimenti nzima ya Utumishi wa Umma na ndiyo maana tunatoa miongozo na taratibu mbalimbali na kuifuatilia. Ndiyo maana nimemueleza utaratibu kwa sababu yeye ameuliza utaratibu na vigezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba ni kwa nini unakuta watumishi wengine wanahamishwa bila kufuata taratibu. Tumekuwa tukitoa nyaraka mbalimbali za kiutumishi, tumetoa Waraka kwa TAMISEMI mwaka 2006, tumetoa pia Waraka mwaka 2007 kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kueleza ni namna gani na masuala gani yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wanapohamisha watumishi. Pia katika jibu langu la msingi nimemueleza muuliza swali, lengo kubwa ni kuangalia manufaa ya umma, kuangalia uwiano katika Halmashauri zetu na katika sehemu zetu za kazi na si kwa kumkomesha mtu wala kwa lengo lolote, lakini kubwa zaidi ni kuhakiksha kwamba ikama na bajeti ya fedha imetengwa ili kuhakikisha kwamba mtumishi wa umma hapati usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumuongezea Mheshimiwa Mngwali, hata Mheshimiwa Rais ameweza kutoa msisitizo zaidi tarehe 1 Mei, 2017 wakati wa siku ya wafanyakazi. Maelekezo yamekuwa yakitoka lakini ameweka mkazo kwamba kuanzia sasa hakuna kumhamisha mtumishi yeyote wa umma kama gharama zake za uhamisho hazijatengwa na pia kama hakuna manufaa katika uhamisho huo na hakuna ufanisi wowote ambao unaenda kuongezeka katika kuboresha ikama hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la makazi pamoja na umuhimu wa mafunzo, niseme tu katika Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma pamoja na Sera ya Mafunzo, tunatambua umuhimu wa kuwa na mafunzo na watumishi wetu wa umma kuwa na makazi bora. Ndiyo maana kama Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania, Watumishi Housing, Shirika la Nyumba la Taifa, TBA na mashirika mengine tumekuwa tukiweka msisitizo na kuhakikisha kwamba nyumba zinajengwa kwa ajili ya watumishi wetu wa umma.
Vilevile katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wamekuwa mwaka hadi mwaka wakitenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi wetu. Lengo kubwa likiwa ni kuwaboreshea watumishi wetu wa umma makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi ya yote nitoe rai kwa waajiri wetu kuona ni namna gani wanaweza kuweka vivutio mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wanavutia watumishi waweze kufanya kazi katika maeneo yao ya kazi. Zaidi katika mafunzo pia ni vema waajiri wakahakikisha kwamba kila mwaka wanatenga bajeti kwa ajili ya kuwapatia mafunzo watumishi wao na kuwaendeleza.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali kuhusu uhamisho wa watumishi, Halmashauri mbalimbali ikiwemo Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara wameendelea kufanya uhamisho huo bila kulipa stahiki za uhamisho za watumishi hao na hivyo kuzalisha madeni. Je, Serikali inachukua hatua gani juu ya watendaji hawa ambao hawazingatii maelekezo wala mwongozo wa Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza tumekuwa tukitoa maelekezo katika nyakati mbalimbali lakini nimefanya reference ya maelekezo ya mwisho ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 1 Mei, 2017. Tumekuwa tukichukua hatua na mifano ya karibuni tu ni katika Halmashauri ya Kilombero na Bagamoyo ambapo wale ambao hawakuzingatia taratibu hizi waliweza kuchukuliwa hatua mbalimbali za kiutumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuwaeleza Wakurugenzi wetu na Mamlaka za Ajira wazingatie maelekezo haya. Ni lazima pindi wanapofanya uhamisho wawe wametenga fedha katika ikama, lakini vilevile wahakikishe kwamba lengo la uhamisho huo lina manufaa kwa umma na ni katika kuboresha ikama katika Halmashauri zetu.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kutokupandisha madaraja kwa wakati, kutolipa na stahili za wafanyakazi kwa wakati na kufuta posho mbalimbali kumefanya ufanisi wa wafanyakazi kushuka. Je, Serikali ina mpango gani katika hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 13 Juni, 2016, tulitoa Waraka wa Utumishi kupitia kwa Katibu Mkuu tukitoa maelekezo mbalimbali. Lengo kubwa la Waraka huo tulikuwa na mazoezi mawili; zoezi la kwanza ni kupitia upya muundo wetu wa Serikali pamoja taasisi zetu kuhakikisha kwamba tuna muundo wenye ufanisi lakini zaidi kuhakikisha kwamba tuna muundo ambao unahimilika. Kama mnavyofahamu tumepunguza idadi ya Wizara kutoka 26 mpaka sasa tunazo 18 au 19.
Kwa hiyo, ni lazima pia na ni dhahiri kwamba baadhi ya taasisi ambazo zitakuwa na muingiliano wa majukumu nyingine itabidi ziweze kuunganishwa, lakini vilevile baadhi ya Idara na baadhi ya Vitengo vingine pia itabidi viweze kuunganishwa kuhakikisha kuwa tunaenda na wakati na tunaendana na mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kutokana na Waraka huo huo tuliahirisha zoezi la kupandisha madaraja pamoja na kupandisha watu vyeo. Napenda kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kuanzia mwaka ujao wa fedha tutapandisha madaraja zaidi ya watumishi 193,166 na hakuna atakayepoteza haki yake.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na vigezo ambavyo vimetolewa vya upangaji na uhamishaji watumishi wa umma, je, Serikali haioni kuwa ulemavu nao uwe ni miongoni mwa vigezo ambavyo vimetolewa ili mtu mwenye ulemavu awe comfortable na hatimaye aweze kutimiza wajibu wake ipasavyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru kwa swali zuri au kwa ushauri. Hili ni eneo ambalo tutakwenda kuliangalia, tumekuwa tukiangalia sababu za kiafya, wengine kuwafuata wenzi wao, niseme na lenyewe tutalifanyia kazi ili kuona ni namna gani na hii pia inaweza kuwa ni moja ya kigezo.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini nimpe taarifa tu kwamba mahitaji ya walimu kwenye Wilaya ya Bukombe sasa yameshaongezeka mpaka mahitaji tuliyonayo sasa ni walimu 914 na siyo walimu 400 kama ambayo imeripotiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nijue, huu mpango wa kuhamisha walimu walipo sekondari wa masomo ya sanaa ambao ni wa ziada, kuwarudisha shule za msingi umesemwa kuwa muda mrefu sana na inakaribia sasa mwaka unapita; namuomba Mheshimiwa Naibu Waziri aseme specifically baada ya muda gani? Kwa sababu hali ya mahitaji ya walimu kule siyo nzuri. Ukiwapata wale walimu wanaweza kusaidia kuziba hilo pengo. Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie kwamba walimu hawa wa shule ya msingi wapo na bahati nzuri tayari tumeshapitisha na kama nilivyoeleza awali, kibali kilishatoka. Sasa hivi tunaendelea tu na hatua ya awali ili wahusika waweze kutuletea majina yao wafanyiwe uhakiki na hatimaye TAMISEMI waweze kuwapangia vituo.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu pamoja na Halmashauri nyingine na Halmashauri ya Bukombe nayo itaweza kupatiwa walimu wa kutosha.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Tatizo la walimu ni kubwa na ndiyo maana linasababisha hata matokeo ya wanafunzi yanakuwa hafifu. Kwa mfano, Jimbo la Vunjo lina upungufu wa walimu 207, sasa mchakato huu ni lini utamalizika kwa sababu mitihani iko karibuni na hali inazidi kuwa mbaya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimweleze tu kwamba tunatambua upungufu uliopo katika Wilaya ya Vunjo na nimhakikishie tu kwamba by tarehe 15 Julai, 2017 tunaamini tutakuwa tumefika katika sehemu nzuri. Ahsante.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Suala la Teaching Allowance huwa halieleweki vizuri ndiyo maana linachanganywa na kada zingine. Teaching Allowance lengo lake ni ku-offset zile saa nyingi ambazo mwalimu anatumia kusahihisha madaftari au kazi za wanafunzi mpaka nyumbani kazi ambayo haifanywi na sekta zingine. Hakuna Bwana Kilimo anakwenda kusimamia…
Najenga hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali lazima iangalie Teaching Allowance kwa walimu kama kitu pekee kabisa. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mkakati rasmi wa kuwasaidia walimu hawa kupata hiyo Teaching Allowance? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wazir wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bilago, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimueleze tu Mheshimiwa Bilago kwamba kama Serikali tunatambua umuhimu na thamani ya mwalimu na uzito na ugumu wa kazi wanayofanya na ndiyo maana ukiangalia katika kada za utumishi wa umma walimu wamepewa kipaumbele cha hali ya juu na bado hatutasita kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika,nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, tumeanza zoezi la tathmini ya kazi, tunaangalia uzito, majukumu na aina za kazi kwa ujumla wake katika Utumishi wa Umma na posho zipi zitatakiwa kuwepo katika kada gani.
Nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira, zoezi hilo la tathmini ya kazi litakamilika katika mwaka huu wa fedha na baada ya hapo tutaweza kuainisha na kupitia na kuhuisha miundo mbalimbali ya kiutumishi vilevile kuangalia ni posho zipi ambazo zinahitajika kuwepo ikiwemo na hiyo ya Teaching Allowance kwa mapana yake. (Makofi)
MHE. SUSANNE P. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Ni lini sasa Serikali itaondoa hii dhana ambayo imeanza kujengeka kwamba Serikali haiwezi kuajiri kwa sababu haina fedha na kwamba Mheshimiwa Rais ndiye amekuwa akiajiri kwa utashi wake bila kufuata sheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali inajigamba kwamba imekusanya mapato mengi na imeondoa Wafanyakazi hewa, lakini ni kwa nini haijapandisha mshahara wala kupandisha watu madaraja? Serikali iwaambie Watumishi, ni kwanini haifanyi hivyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa napenda kusema hakuna dhana kwamba Serikali haina uwezo wa kuajri. Wote mnafahamu katika mwaka wa 2015/2016 mazoezi yaliyokuwa yakiendelea katika uhakiki, lengo letu kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na idadi ya rasilimali watu ambayo tuna uhakika nayo, pia kujiriddhisha fedha ambayo tunalipa kama kweli ni thamani ya fedha kulingana na rasilimali ambayo ipo kazini.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa kufanya hivyo, tumeweza kuondoa zaidi ya watumishi hewa 19,708 ambao endapo wangeendelea kubaki katika orodha ya malipo ya mshahara, wangeisababishia Serikali hasara kila mwezi ya zaidi ya shilingi bilioni 19.8 fedha ambazo zingeweza kwenda kutumika katika miradi mingine ya maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia tu katika mwaka huu wa fedha, tayari katika bajeti yetu tuliji-commit kama Serikali kwamba tutatoa ajira katika mwaka huu wa fedha 2017/ 2018 zaidi ya ajira 52,436. Pia tumeshaanza, ukiangalia katika mwaka huu wa fedha ambao tulikuwa tunaumalizia mpaka Julai, tayari tumeshatoa zaidi ya vibali vya ajira 10,184 na zaidi ya vibali vingine 4,816 pia viko katika taratibu za kutolewa kwa ajili ya kuziba mapengo yaliyojitokeza kutokana na suala zima la vyeti vya kughushi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la kupandisha mishahara pamoja na vyeo au madaraja; katika suala la mishahara, mwaka huu kilichofanyika na nimekuwa nikilisema mara nyingi, ni kweli hatujapandisha mishahara. Hatujapandisha mishahara kwa sababu bado tunaendelea kuangalia hali ilivyo, pia na hali ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya kwa mwaka huu ni nyongeza ya miashahara ya mwaka ambayo ni annual increment na wakati wowote kuanzia sasa nyongeza hiyo ya mishahara ya mwaka itaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madaraja, tayari fedha ilishatengwa. Kuna zaidi ya shilingi bilioni 660 zimeongezeka katika bajeti ya mwaka huu ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2016 iliyokuwa shilingi trilioni 6.6. Mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi trilioni 7.205 na hii itasaidia kulipa maadeni ya watumishi, itasaidia pia kupandisha watumishi zaidi ya 193,166 na tunaamini wakati wowote stahiki hizo watumishi wataweza kuzipata.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maelezo ya Serikali na hakuna dhana iliyojengeka kwamba hatuwezi kuajiri wala kupandisha mishahara. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ametueleza kwamba waliondoa watumishi hewa 19,708. Ni dhahiri kwamba kuondolewa kwa wafanyakazi wenye vyeti fake kumeathiri zaidi maeneo ya elimu na afya. Napenda kujua statistically ni vipi Serikali, maana yake ametuambia wataajiri; mpaka sasa hivi Serikali imeajiri walimu wangapi na wafanyakazi wa sekta ya afya? Maana yake kuna zahanati nyingine hazina kabisa watumishi.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine unakuta shule zina walimu watatu tu, tunaweza kuona ni madhara gani watoto wetu watapata. Sasa kama walikuwa na hili zoezi la vyeti fake, walijiandaa vipi ku-replace hawa wafanyakazi kwenye sekta ya elimu na afya? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa kama nilivyoeleza, tumeshatoa vibali hivyo 10,184 na sasa hivi kwa upande wa elimu, tayari Wizara ya Elimu imeanza zoezi la kuchambua, wanatuma vyeti wale ambao walikuwa ni wahitimu na wanaostahiki kuingia, baada ya hapo watahakikiwa na kuweza kuingia katika ajira.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika walimu kwa ujumla wake, katika ku-replace watumishi ambao wameondoka kwa walimu, ni zaidi ya walimu 3,012 wataweza kuajiriwa katika zoezi hili. Pia katika suala zima la sekta ya afya, tutaajiri zaidi ya watumishi 3,152. Hili ni katika kuziba pengo la walioghushi vyeti feki. Baada ya hapo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 ajira bado ziko pale pale 52,436 na ni kutokana na hali ya uwezo wa kibajeti.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimwa Naibu Spika, pamoja na maelezo ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, nataka tupate tamko la Serikali lini wataanza kulipa malimbikizo hayo ya likizo za wafanyakazi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri haki zao hizo za msingi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni mwaka wa
pili sasa hakuna increment yoyote kwa walimu wala kupandishwa madaraja. Nataka kauli ya Serikali ni lini wataanza kupandisha madaraja na kuongeza increment hasa za walimu ambao morali zao zimeanza kushuka katika maeneo yao ya kazi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende tu kusema kwamba Serikali imekuwa ikijitahidi kulipa malimbikizo mbalimbali ya mishahara pamoja na madai mengine yasiyokuwa na mishahara kwa watumishi wa umma na itaendelea kufanya hivyo kila mara. Nipende tu kusema kwamba katika mwaka huu wa fedha kupitia bajeti za OC mbalimbali za waajiri wetu wametenga ulipaji wa madeni, lakini vilevile kupitia Serikali kwa ujumla wake tumetenga fedha zaidi ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi pamoja na madeni ya wazabuni wengine mbal imbali waliotoa huduma katika Serikali. Kwa hiyo, wakati wowote tu kuanzia sasa pindi tu madeni hayo yatakapokuwa yameshahakikiwa basi watumishi wataweza kuona madeni hayo yakilipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na increment na kupanda madaraja, nilipokuwa nikijibu swali hapa Jumatatu au Jumanne nilieleza kuhusiana na suala hili. Tayari taratibu zimeanza na hivi sasa tunakamilisha tu taratibu za mwisho ili kuweza kuanza kulipa nyongeza hiyo ya mwaka ya mishahara kwa watumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa upandishwaji wa madaraja, nilishasema fedha zimeshatengwa na niwahahakishie tu watumishi wote wa umma wenye stahili za kupanda madaraja hakuna ambaye ataachwa. Niendelee tu kuomba waajiri wahakikishe kila ambaye anastahili kupanda daraja basi ameingizwa katika orodha, lakini bila kuacha kuzingatia seniority list ili watumishi wenye stahili waweze kupatiwa madaraja hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kurudia kusema tena tumeshatenga fedha kwa ajili ya watumishi 193,166 ambao watapanda madaraja mwaka huu. Niendelee kuwatoa hofu watumishi wa umma hakuna ambaye atakakosa daraja lake analostahili katika mwaka huu.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naitwa Nuru Awadh Bafadhili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kuna baadhi ya walimu mfano katika Halmashauri ya Jiji la Arusha katika Shule ya Msingi Olkerian, Kata ya Olkerian mpaka leo wanasumbuliwa kulipwa fedha zao za likizo na wakati huo huo tayari walishatumia fedha zao. Wanapouliza wanaambiwa andikeni barua ili muweze kulipwa pesa zenu. Je, Waziru anatuambiaje kuhusu suala hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze kwa kurudi tena Bungeni, alikuwa ni Mbunge kipindi cha mwaka 2005-2010, hongera sana na karibu tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua yako madeni mbalimbali ya watumishi wanaodai fedha zao za likizo. Nipende tu kusisitiza kwa waajiri kila mwaka pindi wanapoandaa mapendekezo ya bajeti za mwaka wahakikishe wanatenga fedha kwa ajili ya nauli za likizo katika bajeti ya matumizi ya kawaida au bajeti za OC. Vilevile nipende kusema kwamba kwa yeyote ambaye hakulipwa fedha hizo hilo ni deni na kama Serikali tunalitambua na tunalichukua na tutaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatiwa malipo yao. Niombe tu anisaidie huko baadaye taarifa kamili ili tuweze kushirikiana katika ufuatiliaji, lakini ni haki ya msingi ya mtumishi na ni lazima walipwe.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mpango wa kupandisha watumishi madaraja wale wanaostahili lakini kuna changamoto ya wale watumishi ambao wanapandishwa madaraja mishahara huwa inachelewa ku-reflect lile daraja ambalo amepandishwa. Je, ni nini maelezo ya Serikali kuhusu suala hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba ni kweli wako baadhi ya Maafisa Utumishi ambao wamekuwa hawatekelezi wajibu wao kama inavyopaswa na wamekuwa wakichelewesha kurekebisha mishahara katika mfumo wetu wa ulipaji wa malipo ya mshahara wa LAWSON. Nipende kutoa tamko hapa na maelekezo kwa mara nyingine tena, tulishachukua hatua katika Halmashauri ya Bagamoyo, Kilombero, Temeke na nyingine nyingi, hatutamvumilia Afisa Utumishi yeyote au mhusika yeyote katika mamlaka ya ajira ambaye atachelewesha kurekebisha malipo ya mshahara baada ya mtumishi kupandishwa daraja.
Nipende kusema sasa hivi tumeenda mbali itafika wakati tutaanza kuwafungia hata Wakurugenzi wa Halmashauri mishahara yao ili na wenyewe waweze kuona uchungu wa kuchelewesha upandishwaji wa madaraja wa watumishi hao.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Upungufu mkubwa wa Ikama na zoezi la uhakiki wa vyeti limepelekea shida kubwa ya watumishi katika maeneo ya afya, elimu, Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata katika Manispaa yetu ya Katavi, kiasi cha kwamba mtumishi mmoja anafanya kazi zaidi ya moja.
Ni lini Serikali itaajiri katika maeneo hayo niliyoyazungumza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tunakiri ni kweli kuna upungufumkubwa wa watumishi katika baadhi ya maeneo. Niendelee tu kusisitiza kwamba lengo letu kubwa kama Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunaenda kwa kuzingatia maeneo yenye vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tutahakikisha kwamba tunaimarisha maeneo yenye upungufu mkubwa. Nimweleze tu kwamba katika kada alizozitaja zitakuwa ni miongoni mwa kada ambazo pia tutazipa ajira katika mwaka ujao wa fedha. Vilevile labda nimtoe tu hofu kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi; katika mwaka ujao wa fedha tutatoa ajira 52,436 na labda tu niseme kwa mchanganuo ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Elimu tutatoa ajira 16,516 kwa upande wa Sekta ya Afya 14,102, Kilimo 1,487, Mifugo 1,171, Uvuvi 320, Polisi 2,566, Magereza nafasi 750, Jeshi la Zimamoto 1,177, Uhamiaji nafasi 1,500, hospitali za mashirika ya kidini na hiari kwa kuwa nazo tunatoa ruzuku, nafasi 174 pamoja na nafasi nyinginezo 12,673 ambazo zitahusu Sekta zote na jumla kuu ni 52,436.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe Mheshimiwa Kapufi hofu, ikama zote na mapendekezo kutoka kwa waajiri tumezipokea na tutaangalia katika kuimarisha maeneo hayo.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ulituahidi kwamba unaajiri walimu wa hesabu katika shule zetu, lakini ajira iliyotoka mwezi wa nne kwa upande wa walimu ni walimu wa biology na chemistry, ulituletea katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimesema katika Bunge hili kwamba, katika shule zangu kumi za Babati Mjini za sekondari hakuna shule yenye mwalimu wa hesabu. Sasa naomba nifahamu ni kwa nini msituambie kwamba walimu wa hesabu ninyi hamna na hamna mpango wa kutuletea badala ya kutuahidi kila siku kwamba mtatuletea walimu? Watoto wetu hawasomi hesabu. Naomba kauli ya Serikali. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Bahati nzuri ninayo orodha ya nafasi 3,081 za walimu wa hesabu na sayansi ambao tumewapangia vituo katika mwezi Aprili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Babati Mjini naweza kuangalia kwa haraka haraka, lakini nitoe tu mfano kwa Tarime DC, tumepeleka walimu wa hesabu, Musoma DC tumepeleka walimu wa hesabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tutaliangalia na kama katika Manispaa yake hajapata kabisa, tutaweza kulifanyia kazi ili naye aweze kupata walimu hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kumtoa hofu Mheshimiwa Gekul kwamba tulitoa kibali cha walimu wa sayansi na hesabu 4,129 na hizi ni kwa ajira za mwaka 2015. Tayari ukiangalia tumepata tu Walimu 3,081, bado kuna nafasi zaidi ya 1,000 na zaidi katika kibali hicho ambacho tumekitoa, bado hawajajitokeza. Tunashirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) tuweze kupokea maombi hayo, tumeanza kuyachambua. Watakaopatikana naamini ikitokea na walimu wa hesabu wako katika kundi hilo, basi kwa hakika kabla ya mwaka wa fedha na wewe utakuwa umepata walimu hao wa hesabu.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali ni sahihi yanaendana na lengo la 16 la Malengo Endelevu ya Dunia ya leo. Kwa kuwa Wabunge majukumu yao ni kuwa na uelewa mkubwa na ni sehemu ya viongozi katika jamii, Waziri haoni umuhimu wa kutoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge ambapo watapata uelewa wa kutumia muda wao itakiwavyo kwa maslahi ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa Serikali imelitambua hili na inaonekana Waheshimwia Wabunge hawaijui vizuri hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na kwa kuwa zipo sheria vile vile zinazoambatana na Katiba ambapo Wabunge tukipata uelewa na hasa majukumu manne ya Mbunge; la kwanza likiwa kwa Taifa lake; la pili, kwa Jimbo lake la uchaguzi; la tatu, kwa chake cha siasa; na la nne, kwa dhamira yake binafsi ili tuweze kupata uelewa wa hali ya juu namna hiyo na Bunge liweze kujenga maslahi kwa Taifa?
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kujibu swali moja kama ambavyo umeeleza, ingawa yeye ameweka kama maswali mawili lakini naomba nijikite kwenye swali moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na umuhimu wa kutoa semina kwa masuala mbalimbali ya namna ya kutumia muda kuweza kuuliza maswali kama haya, Mheshimiwa Mbunge anayo fursa na anayo haki ya kuweza kuuliza swali lolote. Ndiyo maana sisi kama Serikali tunaona ni fursa muhimu kuweza kutumia Bunge lako Tukufu kujibu maswali kama haya kuweka kuelimisha. Siyo Bunge tu, lakini vile vile Umma mzima wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, suala la namna ya kuelimisha kuhusiana na uelewa wa Katiba, ni jukumu la kila Mheshimiwa Mbunge lakini vile vile na wananchi wote kwa ujumla kuweza kuhakikisha kwamba wanayo elimu ya masuala mbalimbali ya siasa na elimu ya uraia ikiwemo uelewa wa Katiba.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri sana ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, hili tatizo siyo la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza peke yake, ni tatizo la nchi nzima, kwamba kumekuwa na tatizo kubwa la kushindwa Sasa swali kwa Mheshimiwa Waziri; ili tuweza kujenga Taifa moja lenye kuheshimu kwamba vyama vingi vya siasa ni takwa la kikatiba kwa mujibu wa Ibara Na. 3 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba nchi yetu ni ya vyama vingi vya siasa; hatuoni kama kuna sababu za msingi za Serikali kukemea watumishi wa Serikali ambao wanafikiri wana haki ya kutenda haki kwa chama kinachotawala lakini kutokutenda haki kwa vyama vingine ambavyo ni tofauti na Chama cha Mapinduzi? (Makofi)kutofautisha majukumu ya Chama cha Mapinduzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo la baadhi ya watumishi katika Serikali kufikiria wao ni sehemu ya Chama Tawala, limekuwa ni tatizo kubwa ambalo linapekea kutokutenda haki katika maeneo mengi sana ya Taifa letu. Swali la Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba linajenga tu misingi ya kibaguzi, linajenga misingi ya kichochezi kwamba nihaini kuwa kwenye chama kingine tofauti na Chama cha Mapinduzi; na jambo hili liko katika ngazi mbalimbali za utawala katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba swali hili sisi binafsi kwa upande wa Serikali hatujaliona kama ni la uchochezi na ndiyo maana tumeweza kulijibu na ninaamini upande wa pili wameweza kufurahia majibu ambayo tumeyajibu kwa sababu tumetenda haki kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kwamba watumishi wengine wamekua labda hawatendi haki kwa vyama vingine, kwa kweli sidhani kama ni sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Watumishi wa Umma wanatakiwa watekeleze sera za Serikali; wanatambua kwamba kuna Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa, lakini vilevile wanatambua kwamba ipo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho Chama kinatawala katika wakati husika. Kwa hiyo, hawana jinsi, wanatumikia kwa kufuata Ilani ya chama kilichopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa wao, pamoja na kwamba wanatumikia chama kilichopo madarakani, yapo makatazo. Hawatakiwi kujionyesha dhahiri kwamba wanahusika katika masuala ya kisiasa. Ndiyo maana ukiangalia katika sehemu (f) ya Kanuni zetu za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 imeeleza ni kada gani ambazo hazitakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwa kawaida viongozi wa kisiasa hawapati pensheni bali sisi kama Wabunge tunapata gratuity. Isipokuwa viongozi wetu hawa wakuu ambao muuliza swali amewazungumzia kwamba wao wanapewa pensheni wakiamini kwamba wameshamaliza kazi na wanatulia na wanapewa pensheni ili wasitapetape na kuhangaika kwenda hapa na pale kuhemea.
Je, huoni sasa ni wakati wa kuirekebisha sheria kwamba pensheni hiyo itolewe pale tu ambapo tumeshajiaminisha kwamba kiongozi huyu sasa ameshastaafu kweli, anastahili pensheni na kwamba hatatapatapa tena mpaka kufikia hatua ya kukataa kwamba hajafanya kazi yoyote? (Makofi)
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, ukiangalia stahili mbalimbali ikiwemo na pensheni au pensheni ya mwaka, iko kwa mujibu wa sheria; Sheria Na. 3 ya mwaka 1999 lakini vilevile iko kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria Na.11 ya mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza, bado mtu anayo haki. Nami nitoe tu rai kwamba kwa wale Viongozi Wakuu Wastaafu ambao wanahudumiwa kwa mujibu wa sheria hii ambayo niliitaja ya mwaka 1999 pamoja na mwaka 2005, wajitahidi kuenenda na misingi ya Kifungu Na. 6(j) aya ya tatu, imeweka masharti kwa Viongozi wa Umma, ni masuala gani wanatakiwa wayafuate.
Mheshimiwa Spika, hawatakiwi kutoa siri za Serikali walizozipata wakati wakitumikia; hawatakiwi kutoa masuala mbalimbali ambayo waliyapata wakati wakitumikia kama viongozi wa umma; hawakatazwi kujiunga na masuala mengine kwa sababu Sheria haijakataza.
Mheshimiwa Spika, mimi naomba kwa wale viongozi wa umma wa kisiasa, basi wajikite katika misingi ya kifungu Na. 6(j)(3) cha Sheria ya Maadili; Sheria Na. 13 ya mwaka 1995. (Makofi)
MHE. ALI HAFIDH TAHIR: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kuniona na ninawashukuru wale wote ambao walinisaidia katika kuuliza maswali ya ngongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza nataka niweke indhari kwamba wale watumishi wa Serikali ambao tuliambiwa labda hawataweza kuingia katika mambo ya siasa, humu ndani ya Bunge hivi sasa kuna mwenzetu mmoja alishawahi kuwa Katibu Mkuu; na hivi sasa yumo ndani ya Bunge hili kwa upande upinzani. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, nilichokuwa nazungumzia katika swali langu ni ulafi wa madaraka. Ndicho nilichokuwa nazungumza! Nimesema mtu anapomaliza Uwaziri Mkuu kwa kupitia Chama cha Mapinduzi au chama kingine chochote, iweje tena aitumie nafasi ile ambayo aliipata katika Chama cha Mapinduzi kwenda katika chama kingine kudai nafasi ya uongozi? Hicho ndicho nilichokuwa nakiulizia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mifano miwili hai hivi sasa, tuna Mawaziri… (Kelele)
MHE. ALI HAFIDH TAHIR: Mheshimiwa Spika, kuna Mawaziri Wakuu wawili ambao hivi sasa, mmoja kati ya hao ameshawahi kugombea urais akakosa; swali langu liko pale pale, pensheni hizi zinakwendaje? Kwa mfano, angeshinda Urais ingekuaje? Ndiyo swali langu kubwa muhimu hilo. Ulafi wa madaraka! (Makofi)
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la kwanza kwenye makatazo, tunatoa elimu kwa umma. Hayanipi taabu!
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la kwanza kwenye makatazo ya viongozi wa utumishi umma ambao wamekua wakikatazwa kugombea nafasi za siasa na ametolewa mfano wa Mbunge, Mheshimiwa Ruth Mollel, ambaye alikuwa ni Katibu Mkuu katika Wizara mbalimbali; kwa faida ya hadhira hii, ukiangalia katika sehemu (f) kama nilivyoeleza mwanzoni ya kanuni za kudumu, inaeleza kwamba watumishi walioajiriwa katika Taasisi zifuatazo; Jeshi la Wananchi na Jeshi la Kujenga Taifa, Usalama wa Taifa…
MHE. ANGELLAH JASMINE KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Nimepewa nafasi, naomba tupeane fursa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa watumishi ambao wanakatazwa kujiunga au kushiriki katika masuala ya kisiasa ni watumishi walioko katika Jeshi la Wananchi na Jeshi la Kujenga Taifa, watumishi walioko katika Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto, Mgambo, TAKUKURU, Ofisi ya Bunge, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mawakili wa Serikali, Majaji na Mahakimu.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Katibu Mkuu huyu kama ambavyo nimeeleza, itaonekana ni dhahiri kwamba hajawekewa katazo.
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, alitaka kujua iweje sasa Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Lowassa aweze kutumia tena nafasi hii kuomba nafasi nyingine? Kama nilivyoeleza kupitia Ibara ya 20, haijaweka katazo, kwa hiyo, unaona ni dhahiri anayo haki hiyo. Pia alitaka kujua endapo angeshinda Urais ingekuaje? Mimi nadhani tungevuka daraja wakati huo tumelifikia. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Waziri kwa majibu yake lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ingie madarakani annual increment zimesimama na hata kwa bajeti hii ya mwaka huu, ya Waziri wa Fedha aliyoitoa juzi hakuna mahali popote tunaona kuna increment yoyote kwa ajili ya Watumishi wa Umma. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mishahara ya watumshi inaboreshwa ili waweze kupambana na hali ya uchumi na hali ya maisha ambayo imepanda?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, vile vile tangu Awamu ya Tano imeingia madarakani training ilikuwa imesimamishwa na training ni sehemu moja ya kuwapa watumishi motisha na kuwawezesha kupata weledi. Je, Serikali itaanza lini kutekeleza mpango wa mafunzo ambao upo na haujatekelezwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la annual increment nadhani kama atakuwa alifuatilia vizuri hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa Mei Mosi ilielezwa kabisa bayana kwa Vyama vya Wafanyakazi annual increment mwaka huu itakuwepo.
Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia katika bajeti ya mshahara maana yake yeye amesema kwamba hajaiona, obviously kwenye bajeti ya mshahara huwezi kusema sasa hapa hii ndio itakuwa nyongeza ya mwaka. Bajeti ya mwaka jana ilikuwa ni trioni 6.6, bajeti ya mwaka huu ni nadhani trioni 7.25.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, asubiri aone katika mwaka wa fedha utakapoanza endapo annual increment hiyo itakuwepo au la! Nadhani tusichanganye na kima cha chini cha mshahara, nadhani atakuwa ameelewa kwa sababu yeye amekaa Utumishi anafahamu, lakini nimtoe hofu nimweleze tu kwamba Mheshimiwa Rais alishaahidi kupitia siku ya Mei Mosi kwamba nyongeza ya mwaka itakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kupandisha Watumishi mishahara Serikali imekuwa ikifanya hivyo kila mara hali ya kiuchumi inapoimarika na tumekuwa tukijitahidi na tutakuwa tukifanya hivyo kila mara kwa mujibu wa takwimu, lakini vilevile kwa kuangalia mfumuko wa bei pamoja na takwimu nyinginezo zinazotolewa na shirika letu la NBS.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mafunzo; mafunzo hayajawahi kusitishwa, mafunzo yanaendelea na hata kama mkiangalia katika bajeti mbalimbali za Mawizara zilizopitishwa, kupitia kwa waajiri wao na Maafisa Masuuli wamekuwa wakitenga bajeti zao. Niendelee kusisitiza kupitia Bunge lako Tukufu waajiri waendelee kuweka mipango yao ya mafunzo ya kila mwaka, wajitahidi kufuatilia mipango hiyo lakini zaidi waweze kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza na kutoa weledi kwa ajili ya watumishi wao.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali. Kwanza niipongeze Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiifanya katika nchi hii. Hivi karibuni kulikuwepo na zoezi la uhakiki wa vyeti feki na katika uhakiki huo kuligundulika kwamba kuna vyeti feki katika taasisi nyingi na kusababisha sasa kuwepo na upungufu mkubwa sana katika taasisi mbalimbali na hasa katika hospitali zetu na Halmashauri zetu. Sasa napenda kujua je, ni lini sasa zoezi la kuziba zile nafasi ambazo wale wenye vyeti feki wameondolewa zitaweza kuzibwa ili kusaidia wale wafanyakazi waliopo wasifanye kazi kwenye mazingira magumu sana? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia ustawi wa watumishi lakini pia kwa namna ambavyo anafuatilia upungufu huu uliojitokeza wa watumishi kutokana na zoezi lililoendeshwa la wenye vyeti feki.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba, tumekuwa tukieleza humu ndani tayari kibali kimeshatolewa cha ajira 15,000. Tulikuwa tunafanya mashauriano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, wameshatuletea orodha maana yake ilikuwa ni lazima tujue katika kila kituo ni nafasi ipi ambayo iko wazi.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba katika maeneo ambayo yameathirika sana ni sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya kwa zaidi ya asilimia 70 na zaidi kidogo. Pia kwa sekta ya afya tu peke yake zaidi ya watumishi 3,360 wamekumbwa katika zoezi hili. Nimweleze tu kwamba tayari tumeshaanza mchakato huo na muda si mrefu nafasi hizo zitazibwa.
MHE. MICHAEL J. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inakiri kwamba Ukerewe ni moja kati ya maeneo ambayo watumishi wake wanafanyakazi katika mazingira magumu na kwa kuwa huduma za elimu na afya visiwani Ukerewe hususan kwenye Visiwa vya Ilugwa, Ukara, Bwilo na kwingineko zinaadhirika sana na changamoto zinazowakabili watumishi kwenye maeneo haya.
Je, Serikali iko tayari kutoa fedha na kuwezesha sera hii ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma kuanza kutekelezwa ili kuokoa maisha na mazingira ya wakazi wa visiwa hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwanzoni mwa mwaka huu Serikali ilisambaza walimu kwenye Halmashauri zetu hasa walimu wa sayansi lakini kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa walimu hawa kuishi katika mazingira magumu sana kwa sababu ya kutolipwa stahiki zao. Je, nini kauli ya Serikali juu ya tatizo hili? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NAUTWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli ukiangalia si tu kwamba wananchi wa Ukerewe wanaadhirika kutokana na ukosefu wa huduma za elimu na afya, lakini hata watumishi wenyewe walio katika mazingira magumu pia huduma ya elimu katika eneo lile na afya inapokuwa si nzuri inawafanya pia na wenyewe wasivutiwe kufanya kazi katika maeneo hayo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiona changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kwa ujumla wake mwongozo huu haujaanza kutekelezwa lakini kupitia Bajeti ya Serikali na kupitia bajeti za Halmashauri ambazo zimepitishwa wameshaanza kutekeleza maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu pamoja na afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba tutaendelea kulifanyia kazi kama Serikali kutoa msisitizo ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanayokabiliwa na changamoto hizi basi yanaweza kutengewa fedha za bajeti za kutosha ili kuweza kutekeleza sera hii.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na walimu wa sayansi na hesabu walipangiwa vituo mwaka huu, kwamba hawajalipwa stahiki zao. Kwa kweli ni jambo ambalo limetusikitisha, na haswa ukizingatia katika Halmashauri moja unakuta mtu amepangiwa walimu 12 tu, inakuwaje Halmashauri inashindwa kuwahudumia kwa watumishi wake wapya waliopangiwa katika kituo kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, niseme kupitia hadhara hii natoa tamko au agizo kwa Halmashauri zote zilizopokea walimu wapya wa sayansi na hesabu lakini pia zilizopokea wataalam wa maabara za sayansi zihakikishe ndani ya siku saba zimewalipa watumishi hao stahiki zao zote. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hamasa kubwa kwa vijana waajiriwa katika shule zetu hasa za maeneo ya pembezoni pamoja na vituo vya afya na zahanati, ni kule kuwepo kwa mitandao ya simu na umeme wa uhakika, kwa kuwa vijana wetu kwa kweli wanapenda kutumia simu za mikononi katika mitandao hiyo kwa uhakika; na kwa kuwa maeneo yetu ya vijijini hasa katika Mkoa wetu wa Manyara na kwingineko maeneo ya pembezoni, huduma hiyo ya umeme na mitandao ya simu haipo.
Je, Serikali hasa Wizara ya Utumishi ina mikakati gani mahususi ya kuwa na mawasiliano ya karibu kuhakikisha kwamba katika maeneo ya pembezoni katika shule hasa za sekondari na vituo vya afya kunakuwepo na umeme ili kutia hamasa ya waajiriwa waendelee kuishi maeneo hayo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba kwa utafiti uliofanywa na bodi yetu ya mishahara katika utumishi wa umma mwaka 2014/ 2015, moja ya changamoto ambazo zilibainika, kwanza katika mazingira haya magumu inategemeana na sekta kwa sekta maeneo mengine jiografia, hali ya miundombinu, huduma za kijamii zilizopo; lakini pia nafurahi kwamba ametaja suala zima la mitandao ya simu pamoja na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kumuhakikishia tu kwamba kupitia ripoti ile ya utafiti tulitoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini pia tumewasilisha katika Wizara husika ikiwemo Wizara ya Nishati na nyinginezo kuhakikisha kwamba wanapopanga mipango yao ya maendeleo basi wanatoa vipaumbele katika maeneo haya yenye mazingira magumu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa kigezo cha kutoa asilimia 0.3 kwenye Halmashauri ambazo kuna kazi za uchimbaji unaofanywa na migodi inatokana na athari ambazo wananchi wa maeneo hayo wanapata. Katika Mji wa Tunduma kuna forodha ambayo inahudumia nchi karibu nane Kusini na Kati mwa Afrika na kumekuwa na madhara mengi sana kwenye mpaka wa Tunduma ambayo yanafanana kabisa na maeneo wanayochimba migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna magonjwa ya UKIMWI lakini kuna miongamano mkubwa sana wa magari na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wangu ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni muda muafaka kuona na sisi kama Halmashauri ya Tunduma tunaweza kupata asilimia 0.3 ya ruzuku kama ambavyo wanapata katika maeneo ambayo wanachimba migodi? Ahsante.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na nipende kujibu swali la Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kama ambavyo kifungu cha 6(1)(u) cha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa kinavyoeleza, fedha hii ya ushuru wa huduma si kwa ajili ya madhara ni kwa ajili ya wao kupata stahiki ya huduma mbalimbali na mapato yaliyotokana na shughuli za uchimbaji. Kama ambavyo tumeeleza, kwa upande wa Tunduma bado hakuna leseni ya uchimbaji madini ambayo ilitolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa ufuatiliaji tumekuwa makini kufuatilia kutaka kujua kwa nini Mheshimiwa Mbunge amekuwa akitaka kuulizia suala hili. Tumefuatilia katika eneo la Mkombozi na Chapwa ambapo katika eneo la Chapwa kulikuwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi ya kifusi, lakini yalikuwa yakichimbwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara. Kwa sasa tunachokifanya tumeanza kurasimisha ili leseni ziweze kutolewa kwa wale ambao waliokuwa wakichimba kwa kificho basi waweze kuingia katika shughuli hizo za uchimbaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na waweze kugaiwa leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asubiri tu, leseni zitakaporasimishwa kwa wachimbaji wale katika eneo la Chapwa pamoja eneo la Mkombozi basi wataweza kupata ushuru huu wa huduma au service levy.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Chakula Duniani (FAO) ni moja kati ya wafadhili wa miradi hii ya kilimo kwenye nchi yetu na wanao mkataba maalum kwa wataalam wao wanaostaafu kuendelea kufanya kazi kati ya umri wa miaka 60 mpaka 70 na labda ni-declare interest tu kwamba mimi ni mstaafu, lakini nauliza swali hili kwa maslahi mapana ya nchi.
Je, kwa nini Serikali mpaka sasa haijasaini mkataba wa utumiaji wa wataalam (national experts) na Shirika la FAO wakati kuna nchi zaidi ya 67 wanachama wa FAO wameshasaini?
WAZIRI WA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA):
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa niaba ya Serikali nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha utumishi wetu wa umma, lakini zaidi kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia maslahi na mustakabali wa wastaafu wetu. Nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwa takwimu za mwaka 1995 mwezi Machi, ndipo ambapo Tanzania ilikuwa bado haijaweza kusaini mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwaka 1998 Tanzania ilikuwa imeshasaini na kwa sasa hivi tunayo Technical Cooperation among Developing Countries pamoja na Countries in Transition na ninaamini Serikali itaweza kunufaika, lakini pia na wataalam wetu katika sekta mbalimbali, lakini nimshukuru kwa kuleta hoja hii na tutaendelea pia, kufuatilia na mikataba mingine ya kimataifa ili watu wetu waweze kunufaika.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, zalio la vyeti feki ni Chama cha Mapinduzi na Serikali yake, Mheshimiwa Rais akiwa ni sehemu ya CCM kwa kipindi chote hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Walimu ama Watumishi wengi walianza na cheti cha mtu wakaenda wakasomea taaluma, wakafaulu taaluma zao, wakaenda kulitumikia Taifa hili kwa miaka mingi sana. Serikali ya watu ni Serikali yenye ubinadamu. Sasa nauliza, hivi ni kweli Serikali ya CCM inadhani ni sahihi kwa watu ambao wametumikia hili Taifa kwa miaka 20, wengine mpaka miaka 40 wengine miaka 30, waondoke hivi hivi bila hata kupata kifuta jasho, wanadhani ni sahihi?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri dada yangu ama mdogo wangu naye ni Mwanasheria. You cannot benefit from your own wrong, suala hili lilikuwa ni jinai, huwezi ukanufaika hata kama uliweza ku-penetrate katika mfumo ikafikia hapo na ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliweza kutoa amnesty na amnesty hii haikuweza kutoka bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Halima aweze kuelewa suala hili halijazalishwa tu hivi na Serikali ya CCM ni Criminal Offence na ilikuwa ni lazima kufanya hivyo. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Uwekezaji kwa majibu mazuri na ya kina. Pamoja na majibu haya nina maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza; kwa kuwa Watanzania wana hamu kubwa sana ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda kama ambavyo kauli ya Mheshimiwa Rais ambayo siku zote amekuwa akiisema na kwa kuwa Wizara hii iko chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini kauli ya Serikali ya kuleta mabadiliko ya haraka na ghafla yaani radical change yatakayowezesha kutekeleza mapendekezo ya Blueprint ambayo amezungumza hapa na mikakati mingine ya kuharakisha uwekezaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wako baadhi ya wawekezaji wa ndani na nje ambao wamekuwa wakizunguka ofisi baada ya ofisi nyingine wakitafuta vibali mbalimbali vya uwekezaji, kitu ambacho kimekuwa kikichafua sana nchi hii kwa sababu wanaposhindwa kupata vibali hivi kwa muda wanahama kwenda nchi zingine na hii inakuwa haileti dalili njema kwa nchi yetu. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kipindi hiki cha Bunge la Bajeti awaite wawekezaji wote ambao wana kero mbalimbali, akutane nao pamoja na Mawaziri wengine wote ili kuhakikisha kwamba matatizo yao yanatatuliwa mara moja? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chegeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na tunatoa kauli gani ya kuleta mabadiliko ya haraka au kama alivyoeleza mwenyewe radical change, nipende kusema kwamba ni kweli ili tuhakikishe kwamba tunapata faida ya uwekezaji na biashara nchini, ni lazima mabadiliko ya kina yaweze kufanyika. Tayari kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi Serikali imeanza kuchukua hatua kupitia maboresho mbalimbali na kama alivyoeleza mwenyewe mpango mzuri wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, tumeandaa pia mpango jumuishi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi huu wa kuboresha mazingira ya biashara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huu utatekelezwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mpango kazi huo jumuishi tumeeleza kabisa ni masuala gani ambayo yanatakiwa kufayiwa kazi na Wizara ipi pamoja na taasisi zipi za kisekta na tutaendelea kuwafuatilia pia kwa mujibu wa road map ya utekelezaji wa mpango huo kwa namna tulivyojipangia. Pia tutaleta mpango huo kazi tutakapokuwa tayari ili na Waheshimiwa Wabunge waweze kuuona na kuweza kufuatilia na kuweza kujua ni hatua gani tumefikia katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kama nitakuwa tayari kufanya kikao katika kipindi hiki cha Bunge kuwaita wawekezaji wote wenye kero mbalimbali. Kwanza nipende kusema ni ushauri mzuri, lakini la pili tayari tumeanza, nimejigawia vipaumbele, moja tumeanza na mikoa mbalimbali na tunaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa.

Pili, kwa kushirikiana na Mawaziri mbalimbali wa kisekta tutaendelea kufanya vikao mbalimbali vya kisekta kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili kuhakikisha kwamba tunatatua kero zao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Mbunge ni shuhuda tulipoenda Rungwe kupitia kampuni ile ya Rungwe Avocado pamoja na bwana Robert Clowes ambaye tulienda kuangalia na kutatua mgogoro ule kwenye sekta ile ya kilimo cha maparachichi.

Nimshukuru sana kwa ushirikiano ambao aliutoa kipindi hicho na naamini mgogoro ule sasa utafika sehemu nzuri na utaweza kumalizika. Pia nimhakikishie na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na naomba pia ushirikiano wao wa dhati, endapo kuna mgogoro maalum kwa mwekezaji ambaye anamfahamu au katika Jimbo lake analoliongoza au mkoa wake, basi wasisite kunipa taarifa kwa sababu nimeteuliwa kwa kazi hiyo maalum na niko tayari kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pamoja na mikoa, pamoja na sekta mbalimbali, ili kuweza kuhakikisha kwamba taswira yetu kama nchi katika uwekezaji tunaendelea kuikuza, wiki ijayo kuanzia tarehe 17 nitakuwa na kikao na wawekezaji wote wa kichina na tutaendelea kufanya hivyo na wawekezaji wa Uturuki, wa Marekani, Uingereza na nchi zingine kwa mujibu wa viwango vile vya nchi 10 zinazoongoza katika kuvutia mitaji nchini kwetu, lakini tutahakikisha pia na nchi zingine tutazingatia. Kwa hiyo nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, lakini nitaomba ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge wa dhati. Ahsante.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu yaliyotolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kwamba kutokana na utafiti uliofanyika kuangalia uwepo wa jasi katika Kata ya Bendera na Makanya umechukua muda mrefu, je, Serikali haioni umuhimu kusaidiana na Wizara ya Madini ili watume wataalamu wakafanye utafiti wa kina kujua kuna-deposit kiasi gani ili hata TIC wakiwa na nyaraka hizo iwe rahisi kwa mwekezaji kujua kwamba kuna potential ya kuwekeza katika eneo hili? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, awali yote kwanza nichukue nafasi hii kupongeza sana uongozi wa Wilaya ya Same kama nilivyoeleza awali kwa kuweza kutenga eneo hili la uwekezaji zaidi ya ekari 4000

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niweze kujibu swali dogo nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ukiangalia kwa takwimu za uzalishaji za hivi sasa kwa Makanya peke yake uzalishaji ni zaidi ya takriban tani 145,000 na kwa upande wa Bendera ni takriban tani 25,200. Vilevile ukiangalia kwa takwimu tulizonazo kwa TIC nchi nzima tumeweza kusajili zaidi ya miradi 78 ambayo inahusika na uzalishaji wa cement na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na jasi. Kwa hiyo, ukiangalia inathibitisha kabisa kwamba kweli Wilaya ya Same inahitaji mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hitaji la kufanya utafiti, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini kuweza kuona ni kwa namna gani tunaweza kuharakisha kufanya utafiti ili kuweza kujua rasilimali iliyoko pale kwa kujua tani ni ngapi ili kuweza kuwa na uhakika hata mwekezaji anapokuja basi ijulikane ataweza kuzalisha kiasi gani lakini vilevile uhai wa migodi ile pia ni kwa miaka mingapi. Nishukuru sana kwa kufuatilia na nishukuru kwa namna ambavyo mmekuwa mkishirikiana pia na Mheshimiwa Kilango na uongozi mzima wa Wilaya ya Same.
MHE. DKT. MARY M NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali hili muhimu. Ukija Wilaya ya Hanang katika ukuta wa Bonde la Ufa malighafi zote za kutengeneza cement zimejaa na naambiwa kwamba hakuna mahali ambapo malighafi zote zimekuwepo isipokuwa kwenye eneo lile. Je, Mheshimiwa Waziri atatuletea wawekezaji ili na Wilaya yetu ya Hanang iwe na kiwanda kikubwa cha cement?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimwa Dkt. Mary Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ukiangalia kwa Tanzania katika maeneo ambayo imethibitika kuwa na jasi ni pamoja na Pwani, Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara, Lindi, Singida na Manyara. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kufuatilia na kuona ni kwa namna tunaweza pia na kwa upande wa Manyara kuona wanaweza kupata mwekezaji. Kwa sasa kiko kiwanda kikubwa kabisa cha China cha Huashan ambapo wameonesha nia ya kuja kuwekeza. Tunachokifanya sasa ni kuwapeleka katika maeneo mbalimbali ili watakapoona deposit ile kama inawaridhisha basi iwe ni rahisi kuweza kufanya uwekezaji. Vilevile wajenzi wa Stigler’s Gorge na wenyewe wameonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda kikubwa kabisa cha kuzalisha cement hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kubwa ambalo limekuwa likileta changamoto, wengi wamekuwa wakitaka wapewe eneo ambako kunakuwa kuna chokaa au limestone ambayo inakuwa ni rahisi zaidi na ni rasilimali muhimu au malighafi muhimu katika uzalishaji wa cement.

Kwa hiyo, bado tunaendelea kushawishi na naamini watakapokuja katika maeneo pia ya Manyara watakapoona kiasi kinathibitika na endapo wataridhika basi naamini inaweza ikawa ni rahisi wao kuwekeza.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata jibu kwamba Serikali inashughulikia suala hili lakini naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Tanzania ni nchi mojawapo katika nchi 4 za Afrika ambazo zinalima pamba ambayo ni organic. Naomba Serikali iniambie ina mikakati gani ya kuwaalika wawekezaji katika zao hili la pamba nchini ili wafungue viwanda hapa nchini kuliko ambavyo tunauza pamba ghafi ambapo tunapata hasara sana? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akisimama imara katika kuhakikisha kwamba zao letu la pamba linaongezewa thamani ili badala ya kuuza zaidi ya asilimia 70 ya pamba yetu ghafi basi kwa kiasi kikubwa tunaweza kuiongezea thamani hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama Serikali tunayo mikakati ya muda mfupi, wa kati pamoja na muda mrefu. Mfano ukiangalia katika nchi zingine kama Bangladesh na Ethiopia kwa upande wa Afrika ambazo zimefanikiwa unaangalia kuna mnyororo wa thamani, wapo ambao wameanzia katika utengenezaji wa nyuzi, mfano kama Bangladesh na Ethiopia wao wameanzia katika mnyororo wa mwisho kabisa wa kutengeneza mavazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika masuala ya mtaji, mfano mwekezaji mmoja tu ambaye anatengeneza mavazi anaweza akaajiri mpaka watu 20,000 lakini wakati huohuo mtaji wake anaoutumia inaweza ikawa ni dola milioni 3 mpaka milioni 4. Wakati ukianzia katika ngazi labda ya nyuzi pamoja na vitambaa inaweza ikakugharimu zaidi ya dola milioni 10 au zaidi na wakati huohuo ajira pia inakuwa sio nyingi sana. Kwa hiyo, kama Serikali tunatambua umuhimu wa mnyororo mzima wa thamani, tunachokifanya kwa sasa ni kuangalia sasa twende vipi, twende na hatua zote kwa upande huo wa mnyororo au tujikite zaidi kama ambavyo wenzetu wa Ethiopia wamefanya na ukizingatia kwamba hata hawazalishi pamba nyingi zaidi hai kama ambavyo tunafanya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisema tu kwamba kwanza naendelea kuwapongeza wakulima wote wa pamba na naendelea kutoa rai kubwa waone ni kwa namna gani wanaboresha ubora wa pamba yenyewe wanayoizalisha kupitia kilimo. Ukiangalia katika uzalishaji wenyewe wa mavazi pamoja na nguo zetu kwa kiasi kikubwa zinahitaji kuwa na consistency katika mnyororo mzima. Haiwezekani leo ukawa na ubora wa aina hii halafu kesho una ubora mwingine. Kwa hiyo, niendelee kutoa rai kwa Maafisa wetu wa Ugani waendelee kutoa elimu kwa wakulima wetu wa pamba kuhakikisha kwamba katika uzalishaji wa pamba wanayoizalisha basi kuona kwamba inaendelea kuwa na ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukiangalia hata katika viwanda vyetu, pamba inayozalishwa ni takribani tani 300,000 mpaka 400,000 kwa mwaka. Katika msimu wa mwaka huu kwa makadirio ya Wizara ya Kilimo ni kuweza kupata takribani tani 450,000 lakini ukiangalia uwezo wa viwanda vyetu takribani 54 ni kuweza kuzalisha zaidi ya tani 786,000. Kwa hiyo, bado tuna upungufu ni lazima yote haya uzalishaji pamoja na kuboresha uwekezaji viweze kwenda sambamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni suala zima la mitaji. Ukiangalia katika sekta nzima ya uzalishaji wa nguo na mavazi, viwanda vinahitaji mitaji mikubwa sana. Si hilo tu, wapo ambao wamefanikiwa kama kina Jambo Spinning lakini wamejikuta wameshindwa kuendelea na uzalishaji. Hii ni kutokana na sababu kwanza mtaji ni mkubwa lakini akifanikiwa kuweka mtaji bado mazingira siyo wezeshi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachokifanya kama Serikali sasa hivi ni kuangalia sekta ndogo hii ya nguo na mavazi kupitia Mkakati wetu ule wa Nguo na Mavazi wa mwaka 2016 – 2020 kuweza kuona ni kwa namna gani sasa tutaweza kuweka vivutio maalum. Kwenye hili siwezi kusema tutaweka vivutio vya aina gani kwa kuwa tutatunga sheria pamoja, Mungu akijaalia nadhani muda si mrefu tutakuja na Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ili tuweze kuangalia katika zile sekta ndogo mbalimbali, ni sekta zipi ndogo ambazo kama nchi tunaziwekea kipaumbele tukitambua kwamba ndizo zinaajiri watu wengi lakini tukitambua kwamba inakuwa na mnyororo mkubwa wa thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Kilango na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamekuwa wakifuatilia sana uzalishaji wa pamba lakini zaidi uongezaji wa pamba na matumizi yake. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuuliza swali langu kwanza kwa ruhusa yako napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake kwa kutuletea ndege mpya aina ya Dreamliner Na.787 ambayo imefanya ndege zetu sasa kuwa saba (7). Sambamba na hilo, pia uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, sasa naomba niulize swali langu la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali imejipanga vipi katika kuhakikisha inaleta wawekezaji wengi na kuendeleza miradi mingi ya uwekezaji kwenye Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Kigamboni ambayo yana ardhi ya kutosha, Ilala maeneo ya Chanika lakini pia Kinondoni katika maeneo ya Mabwepande? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba tunashukuru kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kwa pongezi alizozitoa kwa jitihada ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya mpaka sasa katika kuhakikisha kwamba tunaongeza miundombinu ya usafirishaji lakini vilevile miundombinu mingine kama vile ya mawasiliano pamoja na ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maeneo ya uwekezaji nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba kupitia Wizara Ardhi tayari maeneo ya uwekezaji yameshatengwa kwa Dar es Salaam Kigamboni na tutaendelea kufanya hivyo katika maeneo mengine ya Mkoa wa Dar es Salaam na tutaona ni kwa namna gani tunaendelea kuhakikisha kwamba tunapeleka Wawekezaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwa Kigamboni tulishapata Wawekezaji hao wanaojenga Mradi huu wa Nyerere Hydro, wamekuwa wana nia ya kujenga Industrial packs pamoja na vyuo vya kiufundi na tayari tumeshawapeleka Kigamboni waweze kuangalia na endapo wataridhika na maeneo hayo, basi kwa hakika wataweza kuwekeza kwa upande wa Kigamboni.

Pia niendelee kumuhakikishia pia Mheshimiwa Mbunge wapo Wawekezaji wengine katika viwanda vya nguo kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara watakuja tarehe 8 Novemba, kutoka Italy na kwenyewe pia tutafanya hivyo kuona ni kwa namna gani tunawapeleka wakaangalie na kuendelea kuwashawishi ili waweze kuwekeza katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niendee kutoa rai kwa Wizara ya Ardhi pamoja na Mamlaka zetu za Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya uwekezaji ambayo yana miundombinu wezeshi ili na sisi iwe kazi rahisi kuvutia uwekezaji, lakini wanapokuja basi wapate maeneo ambayo ni tayari ambayo watatumia muda mfupi katika kuanzisha uwekezaji wao, nakushukuru.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mafupi ya nyongeza. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo inafanywa kwa ajili ya mambo ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa kuwa alipokuwepo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, alikuwa ameandaa na alishawatayarisha wawekezaji kutoka nchini China ambao walikuwa tayari kuwekeza katika Kiwanda cha Tumbaku, kwa bahati mbaya waliishia Dar es Salaam na kulikuwa na matatizo ya Uhamiaji: Je, Waziri yuko tayari sasa kuwafuatilia hawa wawekezaji wa Kichina ambao walikuwa tayari kabisa na maeneo yalitengwa ili waweze kuja kuwekeza kwenye zao la tumbaku?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, amefanya jitihada kubwa na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwa kuboresha maeneo katika mkoa mzima na Wilaya zote: Sasa je, Waziri yupo tayari sasa kuwaleta wataalamu rasmi ili kuweza kuainisha hayo maeneo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme tunashukuru kwa pongezi na nikuhakikishie tutaendelea kufanya kazi nawe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine pamoja na mikoa yetu katika kuhakikisha kwamba tunachochea na kuvutia uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kweli nimefahamishwa kwamba alikuwepo mwekezaji kutoka China ambaye alikuwa na nia ya kuwekeza Kiwanda cha Tumbaku Tabora. Mpaka sasa tumeendelea kumfuatilia, lakini bado hajaonyesha nia.

Napenda kusema kwamba tutaendelea kumhamasisha yeye zaidi na kutafuta wawekezaji wengine zaidi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Viwanda pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili katika swali lake la pili kuhusiana kuleta wataalam, kwanza napenda kuwapongeza Mkoa wa Tabora kwa kutenga ardhi hiyo ya zaidi ya ekari 42, lakini kipekee napenda kusema tu kwamba ni takribani asilimia tano ndiyo tayari inakidhi vigezo. Imewekwa ardhi kubwa, mfano ukiangalia Kaliuwa, wana zaidi ya ekari 37,201, lakini ni asilimia tano tu ya Mkoa mzima wa Tabora katika maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa, ndiyo ambayo tayari yalimewekewa miundombinu wezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi pamoja na Mkoa husika wa Tabora kwanza kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanawekewa miundombinu wezeshi lakini pia kuhakikisha Halmashauri nazo zinaendelea kutenga fedha ili miundombinu iweze kutengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza sana kipekee Halmashauri ya Nzega ambao tayari kwenye bajeti yao wameweka zaidi ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya suala zima ya upimaji. Kwa hiyo, natoa rai kwa Halmashauri nyingine saba zilizobakia na nyingine nchini, basi wajitahidi kutenga fedha katika bajeti yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la kuleta wataalam, nimhakikishie kwamba tuko tayari kuleta wataalamu, lakini zaidi niwapongeze Halmashauri zile nane, kila moja imekuja na mradi wake wa kimkakati; wako ambao wana mradi wa machinjio, wako ambao wana mradi wa mashamba ya mifugo, kuweka kiwanda cha usindikaji na utengenezaji wa vyakula vya mifugo pamoja na sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza mikoa yote na Halmashauri zote ambazo tayari wameweza kubuni miradi ya mikakati. Nawaomba waendelee kufuatilia, washirikiane na Wizara ya Kilimo pamoja na Benki yatu ya Kilimo na benki nyingine za kimaendeleo ili kuweza kupata mitaji ya kuweza kuwekeza. Nakushukuru.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Napenda tu kuuliza Serikali, tuna mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya niobium katika milima ya Panda Hill Songwe; na kwa bahati nzuri ile miradi ita-attract direct investment ya karibu dola milioni 200 na wawekezaji wapo tayari; na katika ziara ya Mheshimiwa Rais alipofanya ziara kule Mbeya…

MWENYEKITI: Swali, swali!

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu: Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuwaruhusu hao wawekezaji waanze kuchimba haya madini ya niobium ili vile vile wajenge na kiwanda cha kuchakata hayo madini ambacho ni cha kwanza Afrika na cha nne duniani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kusema kwamba tunatambua kuhusiana na mradi huu wa Niobium ambao utafanyika katika milima ya Panda Hill na bahati nzuri nami nilipata bahati ya kukaa katika Wizara ya Madini, niliweza kuwaona wawekezaji hawa; na ni madini ambayo kwa kweli ni ya muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tulishaanza kuwashughulikia, pia tumekuwa na mashauriano na Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Viwanda kupitia EPZ. Tutakutana pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Viwanda ili kuweza kuona ni kwa namna gani tunakwamua mradi huu muhimu.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake kwamba asilimia zilizokuwa zikikopeshwa kwenye Halmashauri zipitie benki: -

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa wanawake na vijana watakuwa wanakopeshwa kupitia benki: Je, ni kwa nini sasa Serikali isiamue vikundi ambavyo ni vya wanawake na vijana vilivyounda SACCOS navyo viunganishwe katika kukopeshwa kupitia benki? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Genzabuke na pia nimpongeze sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Dugange kwa majibu mazuri yenye umakini mkubwa sana; na niwashukuru kwa maswali yote yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge wote; Mheshimiwa Shally Raymond pamoja na Mheshimiwa Halima Mdee.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tayari Mheshimiwa Rais ameshaelekeza kwamba tutakuwa na mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hii ya asilimia 10, napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba tumeshaanza kuandaa utaratibu na pindi utakapokuwa tayari, tutawajulisha na tutaweza kujua katika benki tutakuwa kwa mfumo wa aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kupokea maoni yoyote yatakayoboresha namna gani katika benki pia mfumo huu uweze kutumika na tunawashukuru. Kikubwa tunawaomba, kwa zile ambazo tayari zilishatolewa na zilishakopeshwa, tulishaanza kuingia mikataba na walionufaika na mikopo hii na ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo zilitolewa tangu mikopo hii kuanza kutolewa zinarudishwa na ndiyo moja ya fedha hizo hizo pia tutakazozitumia katika kupeleka katika benki zetu na kuzikopesha kwa ajili ya utaratibu mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kuwasisitiza na kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa wanaingia Mabaraza ya Madiwani, kuhakikisha kwamba fedha zote zilizokopeshwa nyuma zinarudi, na pia bado tunaendelea kupokea ushauri kwamba ni namna gani tunaweza tukatekeleza vyema katika huo mfumo mpya utakaotolewa katika benki zetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Tarafa ya Mlalo yenye kata nne inahitaji kituo kimoja cha kimkakati ambacho kitahudumia Kata ya Lukozi, Malindi, Manolo na Shume.

Je, Serikali ina mpango gani kujenga kituo hiki kwa haraka kwa sababu pia ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Kata ya Lukozi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nipende kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru kwa namna ambavyo ameendelea kufuatilia maendeleo ya jimbo lake lakini kwa namna ambavyo ameendelea kufatilia utekelezaji wa ahadi za viongozi wetu. Nipende tu kumwakikishia kwamba tunatambua umuhimu na namna ambavyo Kata hii ya Lukozi iko kimkakati. Tunajua kituo hichi endapo kitajengwa kitaweza kuhudumia zaidi ya kata nne ikiwemo Manolo, Malindi, Lukozi yenyewe na nimpe tu uhakika. Kwamba tutakijenga katika mwaka ujao wa fedha 2023/2024 kama ambavyo tutaweza kupanua Kituo cha Afya cha Mlalo vilevile katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa Mheshimiwa Shekilindi tutaweza pia nako kujenga kituo cha afya kwa upande Gare, nikushukuru.