Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Anna Richard Lupembe (9 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, wale watu ambao walikuwa hawalipi kodi, lakini Mheshimiwa Rais wetu amethubutu kufanya kazi hiyo na matokeo yameonekana na kodi sasa zimeonekana mpaka hatimaye sasa watoto wetu wameweza kwenda kusoma bure
kwa sababu ya mambo mazuri ambayo Rais wetu alituahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ni kazi, mimi nitaendelea. Kuna kazi ambayo tunatakiwa tuifanye na Serikali inatakiwa iangalie kwa makini kuhusu Halmashauri zetu upande wa Wakurugenzi pamoja na Watendaji. Kuna sehemu nyingine watendaji
wanakaimu na kama Mkurugenzi mara nyingi anakaimu siyo Mkurugenzi kamili inakuwa kazi kufanya kazi ya maendeleo katika maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta sehemu nyingi kuna miradi mbalimbali ambayo Serikali iliainisha ili iweze kufanyika. Katika maeneo mengi miradi hiyo haikuweza kukamilika kutokana na utendaji. Ukienda pale anasema mimi Kaimu, Mkurugenzi kasafiri siwezi kufanya
jambo lolote. Hilo limekwamisha sana miradi yetu tuliyokuwa nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kazi inaendelea, kuna Wakurugenzi wengi wamesimamishwa kutokana na majipu, lakini bado kuna maeneo mengi ambayo uaminifu ni mdogo. Naomba kazi hiyo iendelee, tuweze kusafisha ili fedha za maendeleo tukipanga bajeti
ziweze kufikia malengo yale tunayoyatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende upande wa wakulima na wafugaji. Kifike kipindi sasa Serikali, iainishe maeneo ya wakulima na wahainishe maeneo ya wafugaji.
Limekuwa tatizo kubwa sana kiasi ambacho sasa hivi kuna vitu ambavyo vinaashiria siyo vizuri, wanapigana, wanauana na sisi nchi yetu ni nchi ya amani na utulivu. Naomba Serikali yetu ijipange vizuri kwa ajili ya eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Waziri wa Ardhi, ametuandikia barua Wabunge wengi tuainishe migogoro ya ardhi. Naomba nikupongeze sana Waziri wa Ardhi kwa kuliona hilo, tuweze kukusaidia na tuainishe maeneo yote yenye migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye reli, watu wengi wamezungumza kuhusu masuala ya reli. Kwangu Mpanda ni kitu muhimu sana kutokana na na hali halisi ya sasa hivi barabara zote hazifai, wananchi wa Mpanda wako hewani, mambo yao hayaendi vizuri.
Namwomba Mheshimiwa Waziri reli hii ya Mpanda hata kesho treni ianze kwenda kwa sababu wananchi wa Mpanda wanapata shida, taabu kwa ajili ya mahitaji yao binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye masuala ya uchumi, uchumi hauwezi kukua bila miundombinu. Maeneo ya Tabora, Kigoma, Mpanda ni maeneo ambayo yana uchumi mkubwa, wanalima sana, wana mazao mengi, ambayo yanatakiwa yatoke kwa ajili ya
Watanzania wote, lakini kutokana na miundombinu mibaya, barabara hazifai. Mtu anatoka Tabora kwenda Mpanda anatumia siku tatu, analala njiani, kusema kweli tunasikitika sisi Wabunge tunaotoka maeneo hayo kuwa tumesahaulika muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, mtuangalie kwa jicho la huruma wale wananchi ni Watanzania kama Watanzania wengine, wanahitaji mahitaji muhimu. Shughuli zao za kilimo, basi waweze kutoa mazao yao ili waweze kupata mahitaji yao binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja upande wa polisi, nawapongeza sana polisi wetu, wamefanya kazi nzuri, lakini kuna maeneo mengi nyeti hakuna vituo vya polisi, wananchi usalama wao unakuwa mdogo, maeneo mengi utakuta wana mazao mengi, lakini usalama
wao haupo kutokana na kukosekana kwa kituo cha polisi katika maeneo hayo. Tunaomba Serikali ijipange basi kupeleka vituo vya polisi katika maeneo hayo ili wananchi waweze kupata usalama wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye mapato tena. Zamani kulikuwa kuna Shirika lilikuwa linaitwa NASACO, Shirika la NASACO lilikuwa linakusanya mapato bandarini, ile mizigo yote inayotoka kwenye meli, lile shirika sasa hivi halipo. Sasa naomba kama kuna
uwezekano Serikalini, lile lilikuwa linasaidia sana mapato yalikuwa hayawezi kupotea ndani ya bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi Serikali ijipangwe vizuri, kuona ni jinsi gani ya kuweza kupitisha makontena ndani ya bandari zetu, maana kuna maeneo mengine hakuna usalama mzuri, watu wanaingiza mizigo bila kulipa ushuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia Tanga, bandari bubu nyingi, lakini na Mpanda, Kalema kuna bandari, mpaka leo hatuwezi kujua hatima yake itaisha vipi. Kuna sehemu nyingi muhimu, nyeti ambazo zinaweza kuliletea Taifa hili mapato, lakini tumeliacha wazi. Tunaomba
basi na sisi bandari ile ya Kalema ifanyiwe kazi, ina miaka sijui sita sasa hivi, majengo yalianza, Mkandarasi sijui ka-disappear wapi hatufahamu. Tunaomba basi ili uchumi uweze kukua, bandari, reli na barabara ziweze kutengenezwa vizuri kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali ijipange, mnapoteza hela nyingi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha, tafadhali naomba ukae
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANNA L. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetulinda, ametuleta tena mara nyingine hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja, naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Wizara yao ni kubwa sana lakini wanajitahidi sana, wana majukumu mazito, naomba mpambane Mungu atawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi sasa hivi una miaka kama minne inaelekea mitano, hatuna Hospitali ya Mkoa. Tumeambiwa tumetengewa pesa tujengewe Hospitali ya Mkoa wa Katavi lakini mpaka leo hatuoni jitihada ya aina yoyote. Sasa hivi Mkoa wa Katavi una watu wengi, ukishasema mkoa ina maana umepanua wigo mkubwa kwa hiyo, shughuli mbalimbali zinafanywa ndani ya Mkoa wa Katavi lakini hatuna Hospitali ya Mkoa, tumebaki na Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambayo ndiyo imebeba majukumu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ni ndogo na wafanyakazi ni wachache, nashukuru na wao wenyewe wamejionea. Wameainisha hapa kwenye hotuba ndani ya Mkoa wetu wa Katavi ukiangalia Wilaya ya Mpanda Vijijini, Mpanda Mjini na Wilaya mpya ya Mlele kuna sehemu wamesema asilimia 100 hakuna wahudumu. Sasa sijui wananchi wa Mkoa wetu wa Katavi wanaoumwa wanafanyaje. Naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie kwa makini sana suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamekukaribisha uende kwenye Mikoa yao, naomba Mheshimiwa Waziri uje Katavi ujionee mwenyewe hali halisi ya Mkoa wetu na jinsi wananchi wanavyopata shida ya matibabu. Hospitali ile ya Wilaya, manesi pamoja na madaktari saa nyingine wanachoka, wakichoka sasa lugha zinakuwa tofauti. Wagonjwa wakienda pale kauli zinakuwa tofauti, zinakuwa mbaya kwa sababu si wao, wamechoka. Naomba Mheshimiwa Waziri muangalie kutupatia Hospitali ya Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mlele ina hospitali ambayo imejengwa na Serikali. Naomba niipongeze Serikali imejenga hospitali nzuri sana Inyonga lakini mpaka leo ni kituo cha afya. Mmeweka vifaa vingi na vizuri lakini kasoro yake ni ndogo sana, ni choo tu hakuna ndiyo imefanya hamtaki kuipandisha iwe Hospitali ya Wilaya ina maana Wilaya ya Mlele hakuna Hospitali ya Wilaya. Mheshimiwa Waziri tunaomba tupandishie hii hospitali na tuletee wafanyakazi. Vile vifaa mlivyoleta vimekaa sasa vimeanza kuharibika kwa sababu hakuna wataalam wa kuvitumia. Sasa inakuwa tunachezea hela za Serikali kututangulizia vitu wakati wahudumu na wataalam hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hospitali ambayo iko Inyonga imejengwa vizuri sana lakini tatizo lake ni choo tu. Mmejenga majengo makubwa, mazuri, lakini sijui ilikuwaje huyo mkandarasi aliyewekwa hakuweka choo mpaka leo hii tunashangaa ilikuwaje. Kila mtu anashangaa kwa sababu tunaomba muipandishe hadhi inashindikana, ukiuliza tatizo unaambiwa hamna choo. Sasa sijui katika utaalam ilikuwaje, mmejenga majengo mazuri, mmeleta vifaa vikubwa na vizuri halafu choo hakipo halafu hamtaki kutoa kibali ili iwe Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa naomba mtusaidie kwani wananchi kule wanapata shida, jiografia yetu ya Mkoa wa Katavi jamani ni ngumu, naomba chonde chonde mtusaidie. Ukienda kule Mheshimwa Waziri utasikitika wananchi wanavyohangaika huduma hamna. Naomba Mheshimiwa Waziri ile hospitali hata kama haina vyoo tupandishieni iwe na hadhi ya Hospitali ya Wilaya ili wananchi wa Wilaya ya Mlele wapate huduma safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa Chuo chetu cha Msaginya. Tuna chuo pale kinaitwa Msaginya, Chuo cha Maendeleo lakini hakifanyi kazi yoyote. Chuo kile ni kizuri, mnakitolea pesa kila mwaka, lakini kwa nini hamna mipango mizuri mkapeleka watu wakajifunza pale? Kuna vijana wengi ambao wamekaa bure hawana kitu chochote cha kufanya wangeenda huko. Vyuo mmevijenga vizuri, wataalam mmewaweka kwa nini vijana wasiende pale wakajifunza useremala na akina mama wakaenda pale wakajifunza ujasiriamali? Vile vyuo majengo yanaharibika na mnapoteza hela nyingi.
Naomba hivi Vyuo vya Maendelo ya Jamii viwekewe mikakati mikali ili vijana wengi wajifunze ujasiriamali kupitia Vyuo hivi vya Maendeleo ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa Benki ya Wanawake. Kwanza, naomba nimpongeze Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake, Mama Chacha, amefanya kazi nzuri lakini bado hajatufikia sisi akina mama kwenye Mikoa, Wilaya na Vijiji vyetu, ameishia Dar es Salaam na asilimia kubwa ya akina mama wako vijijini. Najua watu wengi wamesema hii benki haiwezekani lakini wanawake wote wana haki ya kupata benki hii kila mkoa kwa sababu hela iliyochukuliwa kuianzisha ni Serikali. Kwa hiyo, kila mkoa tunahitaji Benki ya Wanawake ili wanawake wa Tanzania hii wajivunie benki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuzungumzia Bima ya Afya, hii mimi naisemea kila siku. Bima ya Afya dawa hakuna! Tunaomba sasa Bohari Kuu waende moja kwa moja viwandani kuchukua dawa. Kama dawa ziko huko Ujerumani, India waende moja kwa moja wakachukue dawa huko ili waje kuwahudumia Watanzania. Hizi dawa wanazochukua kwa wafanyabiashara hazikidhi mahitaji.
Tunaomba sasa Serikali iwape fungu kubwa Bohari Kuu ya Dawa ili sasa wananchi wote waweze kupata huduma safi na salama wajivunie Serikali yao kupitia Bima ya Afya. Sisi tuko tayari kufanya hamasa, wananchi wote waingie kwenye Mfuko wa Bima ya Afya lakini tunaomba mtuwekee dawa ili wananchi wapate huduma safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye aliyetuumba, ametupa uzima na uhai, siku hii ya leo ametutunza na tuko Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba niunge mkono asilimia mia kwa mia bajeti hii iliyopo mbele yetu.
Ninaomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwapa imani Watanzania, kwa elimu bure, Watanzania wameona matunda yake, vilevile Watanzania wote wanampongeza jinsi anavyofanya kazi nzuri ya kutumbua majipu, Watanzania wanaona, wanafurahi na jinsi ya kubana matumizi. Zile pesa zinawaendea wenyewe kwa ajili ya matatizo yao na kuwapa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wa haki na uhuru. Jana nilikuwa Zanzibar, kuna amani tosha. Nimepata marashi ya karafuu murua kwa ajili ya Watanzania jinsi tunavyoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mawaziri wote wanavyofanya kazi vizuri na yaliyokuwa mbele yetu kwa ajili ya Taifa letu, kwa ajili ya kutimiza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Endeleeni, kazeni buti, mnafanya kazi nzuri ambayo sasa hivi kila mtu anaona jitihada zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende upande wa Halmashauri kupitia elimu. Shule zetu zimezeeka sana ambazo ziko upande wa kijijini, zina nyufa, chini sakafu hakuna, ninaomba basi miundombinu hiyo itengenezwe na Halmashauri zetu sasa zifanye mikakati mikubwa na mipango mizuri ya kuboresha shule zetu kila mwaka waweze kujenga madarasa manne au mawili kwa ajili ya uboreshaji wa shule zetu za primary, pamoja na kuanza kujenga kwa kasi kubwa…
TAARIFA...
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siikubali taarifa yake kwa sababu mimi nilikuwa Zanzibar, nimekaa siku nne, kuna amani na utulivu, na uchaguzi umefanyika kwa haki. Kama kuna mabomu yeye anafanya nini humu ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar ni tulivu kabisa, hakuna mabomu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo maana yeye yuko humu ndani, anakula upepo, ina maana kama uchaguzi usingefanyika wa haki yeye asingekuwepo hapa. Demokrasia imechukua mkondo wake, Wazanzibari wamefanya kazi yao nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Precision Air inaanza kwenda Pemba, safari ya Dar es Salaam, Unguja - Pemba, naomba nimpe taarifa hiyo, kwa sababu ya amani na utulivu wa nchi hii.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji vingine havina shule kabisa ya primary, ninaomba Serikali iangalie kupitia Halmashauri zake, vile vijiji ambavyo havina shule za msingi ziweze kujengwa. Pia shule za sekondari, zipo shule za sekondari ambazo hazikujengwa kwa kiwango leo hii ukienda zina ufa, ninaomba zichukuliwe hatua ambazo zitaboresha shule zile pamoja na nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la afya. Tuna Bima ya Afya ambayo tumewahamasisha wananchi wetu ambao Wabunge wengi wamezungumzia. Ninaomba Bima ya Afya ni matatizo makubwa sana kwa wananchi wetu. Wakienda hospitali kwenda kuchukua dawa wanaambiwa dawa hakuna waende kununua dawa. Tunaomba mikakati mizuri ya Bima ya Afya iwekwe vizuri ili wananchi wetu waweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya hasa Wilaya ya Mpanda vimekaa vibaya. Ukienda Kituo cha Afya Kalema, Mwese na Mishamo ni distance ndefu mno, hatuna gari hata moja. Ndiyo maana tumepata matatizo makubwa sana, asilimia ya vifo vya wanawake wajawazato mwezi wa nane na mwezi wa tisa, kila mwezi tulikuwa tunapoteza akina mama 40 wanaokufa kutokana na vifo. Tunaomba sana mtuangalie kwa jicho la huruma, mtupe ambulance za kuweza kusaidia akina mama Wilaya ya Mpanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye zahanati unakuta muuguzi mmoja tu, hakuna msaidizi, matokeo yake muuguzi yule akiondoka, maana muuguzi huyo ndiye daktari, ndiye nesi, ndiye mhudumu. Ina maana akitoka akina mama wakienda pale au mgonjwa akiwa serious hatapata huduma kutokana na muuguzi kuchoka, hayupo, amekwenda kunywa chai, matokeo yake tunapata matatizo mengi makubwa ya vifo ambavyo hatukuweza kuvitegemea. Ninaomba tuweke mikakati mizuri, tutengeneze kila Mkoa, tuwe na vyuo ambavyo ni vya kuwa na wahudumu wetu pamoja na manesi, tuibue manesi kila Mkoa ili waweze kusaidia vituo vyetu vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda zahanati nyingi, watu wengi wamesema, zahanati nyingi, shule nyingi hazina maji safi na salama ni shida. Tunaomba Serikali ijiwekee mikakati mizuri kwa ajili ya maeneo ya zahanati na shule zetu za msingi na shule zetu za sekondari kuwe na maji safi na salama kwa ajili ya watoto wetu. Unakwenda unakuta vyoo hakuna, vyoo vingi vimechakaa, vyoo vingi vimeshaanza kutitia. Tunaomba uboreshaji kwenye shule zetu za primary na sekondari vyoo vijengwe upya ili watoto wetu waweze kuishi kwenye mazingira mazuri na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mazingira. Upande wetu wa Mpanda eneo kubwa ni misitu. Misitu ile imevamiwa na watu, wameingia wanakata miti kama mchwa, mazingira yanaharibika. Tunaomba mikakati mizuri ya Serikali kutunza mazingira kwa ajili ya afya zetu za mvua ili tuweze kupata mahitaji muhimu ndani ya jamii yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja upande wa bibi maendeleo. Hatuna mabibi maendeleo ndani ya Wilaya zetu na Kata zetu. Akina mama wanapata shida sana jinsi ya kuweza kufundishwa ujasiriamali na jinsi ya maendeleo kutokana na kutokuwa na mabibi maendeleo, hatuna mabwana shamba kila kata. Tunao mabwana shamba wachache sana. Sasa unakuta akina mama wanaohitaji kufundishwa jinsi gani ya kulima kilimo bora hakuna watalaam ambao wanaweza kuwafundisha. Tunaomba jitihada za Serikali tuongeze mabibi afya, tuongeze mabibi maendeleo, tuongeze mabwanashamba kwa ajili ya huduma nzuri ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji. Ndani ya vitongoji vyetu na vijiji vyetu akina mama wanapata shida sana ya maji. Maji wanafuata maeneo ya mbali ambapo wakati mwingine maeneo mengine akina mama wanaamka usiku sana, saa nane za usiku, saa tisa za usiku kwenda kutafuta maji. Ninaomba mikakati ya maji iwe mikubwa na mipana zaidi kwa ajili ya akina mama ambao wanapata shida ya kutafuta maji. Maji yenyewe wanapoenda kuyatafuta ni maji machafu, siyo maji salama. Ninaomba Serikali yangu sikivu iweze kupanga mikakati mizuri ili iweze kupata maji salama kwa ajili ya wananchi wetu waweze kupata manufaa ya sera yetu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ninaomba niunge mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuongea machache kuhusu bajeti iliyokuwa mbele yetu. Naomba niingie moja kwa moja kwenye hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanategemea reli hususani mkoa wangu wa Katavi na Wilaya ya Mpanda. Alikuwepo Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Arfi, alikuwa anatetea sana reli ya kutoka Tabora - Mpanda. Mimi kila siku najiuliza Wabunge humu ndani wanazungumza kuhusu reli, lakini utekelezaji wake haupo. Mheshimiwa Arfi alivyokuwepo humu ndani alikuwa anazungumza kila siku, reli ya Mpanda - Tabora siyo salama. Mpaka leo reli ya Mpanda - Tabora ina pounds 40 na reli hiyo inabeba mizigo mingi, inailetea pesa nyingi Serikali na wananchi wa Mpanda wanategemea reli lakini mpaka leo reli ile wala haijashughulikiwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unasikia kuna sehemu reli zinang‟olewa zinapachikwa pound nyingine. Sasa najiuliza zile pound zinatoka zinakwenda wapi? Hivi karibuni walizing‟oa pound 60 Tura, sasa zile zilipelekwa wapi? Badala ya kutolewa pale na kupelekwa sehemu ambapo kuna pound ndogo ili reli yake iweze kuimarishawa lakini ndugu zangu hakuna kitu kama hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku wananchi wa Mpanda tunalalamika kuwa hatuna barabara, tunategemea reli na ndiyo maana Wabunge wengi wanasema RAHCO na TRL waunganishwe hili shirika lingine life kwa sababu hawana faida. Kuna pound zingine wameziacha pale makao makuu, pound 80 zimekaa hawajui kama wananchi wengine wanahitaji hizo pound, sasa wana maana gani? Hii RAHCO tunaomba Serikali sheria ilikuja Bungeni na ikaunganisha RAHCO na TRL, sasa sheria hiyo ije tena tutenganisha Shirika la RAHCO pamoja na TRL, sheria hiyo ije tena tupangue tuunganishe hili shirika liwe moja. Kwanza ukiangalia wanapewa hela nyingi halafu vitu vyake havieleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka mnasikia Godegode kuna matatizo, treni inaanzia Dodoma, ina maana Serikali mpaka leo haina ufumbuzi wa tatizo la pale Godegode? Kila siku Godegode treni imeishia Dodoma, Godegode treni imeishia Dar es Salaam, Godegode kuna mafuriko. Mnajua kabisa Godegode tatizo, kwa nini msichukue hatua za kurekebisha kwa sababu treni inayotoka Dar es Salaam – Mwanza – Kigoma - Mpanda inabeba abiria wengi sana na wananchi wengi maskini wanategemea reli, kwa nini hapo Godegode hapashughulikiwi, kila siku Godegode shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwanza Kaimu Mkurugenzi mpya, nashangaa kwa nini hawampi ukurugenzi, amethubutu safari hii, wananchi wamekwama njiani na treni amechukua chakula yeye kama yeye kuwapelekea wananchi. Tunaomba hawa Wakurugenzi ambao wanao uthubutu wapewe ukurugenzi. Kitu cha kushangaza, mimi naomba niseme, leo hii mashirika yote makubwa, bandari Mkurugenzi Kaimu, uwanja wa ndege Mkurugenzi Kaimu, TRL Mkurugenzi Kaimu, wapeni ukurugenzi kamili ili waweze kufanya kazi nzuri, wameweza kuthubutu hawa wapeni basi ukurugenzi waweze kufanya kazi vizuri. Mnavyowaacha na ukaimu wanafanya kazi kwa wasiwasi, wapeni mamlaka ili waweze kutekeleza yale mliyowakabidhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri akija hapa aniambie kabla ya standard gauge haijaanza maana haya ni majaliwa, Mbunge ametoka hapa kusema hayo ni majaliwa, tunaomba kujua reli ya kutoka Tabora - Mpanda mtatubadilishia lini zile pound 40 iwe angalau tu 60 ili ile reli iweze kuwa stable. Kwa sababu wananchi wa Mpanda wapo rehani huku barabara ikiziba huku treni wasiwasi. Kabla standard gauge haijaanza tunaomba uimarishaji wa reli ya kutoka Tabora - Mpanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaenda kwenye standard gauge na tumesema inafika mpaka Karema, Karema tunategemea bandari, lakini hatujaona mwamko wowote wa bandari Karema. Naomba hii mikakati ianze ili wale wananchi wa Karema waone kama na wenyewe wapo Tanzania kwa hii bandari inayopelekwa huko kwa ajili ya standard gauge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja darala la Kavuu; kuhusiana na barabara ya kutoka Inyonga – Majimoto, hii ni Wilaya mpya. Wananchi kutoka Mpimbwe huko Majimoto, Kibaoni, Usevya, Kasansa mpaka wafike makao makuu yao ya Wilaya Inyonga wanatembea siku mbili. Mtu anatoka Kasansa aje Mpanda alale kesho yake aondoke aende Inyonga, hiyo ni Wilaya au kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge wengine hapa wamesema kuhusu masuala ya barabara, hili daraja la Kavuu limechukua miaka saba. Hebu jamani mtuangalie watu wa mkoa wa Katavi, kila siku tunazungumza, tunaomba hili daraja liishe ili wananchi wa upande wa Kibaoni, Usevya, Kasansa waweze kufika kwenye makao makuu yao ya Wilaya siku moja. Tunaomba chonde Waziri akija hapo atuambie daraja la Kavuu litaisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza ile barabara ya kutoka Stalike - Mpanda na nikasema pale Mpanda kuna shimo, lile shimo linaisha lini? Ni kero kwa wananchi wa Mpanda, kila siku ajali zinatokea. Nilizungumza Januari lakini mpaka leo hakuna mkandarasi, hakuna kitu chochote, kila kitu kipo vilevile. Tunazungumza mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niunge mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti. Kwanza kabisa, naomba niipongeze bajeti yetu, bajeti nzuri, naomba niiunge mkono kabla sijaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali yangu sikivu kwa kututengenezea barabara ambayo ilikuwa inasumbua sana wananchi wa Mpanda; Mpanda – Tabora kwenye Daraja la Ipole. Lile daraja sasa hivi limekwisha. Nomba tu Serikali yangu basi itoe kauli hilo daraja liweze kufunguliwa ili wananchi wa Mpanda sasa waweze kupata maisha mazuri, waweze kufanya biashara zao na kufanya shughuli zao kwa amani kwa sababu daraja lile la Ipole lilikuwa ni kikwazo, walikuwa hawawezi kusafiri, walikuwa wanazunguka mwendo mrefu. Naomba Kauli ya Serikali kwa ajili ya daraja hilo, kwa kuwa limekwisha ili tuweze kupata manufaa ndani ya maisha ya wananchi wa Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kuchangia bajeti hii kwa upande wa akinamama. Kwa kuwa mimi ni Mbunge wa akinamama, nianze na akinamama. Asilimia tano ya akinamama mara nyingi tunaitenga lakini akinamama hawaipati kutokana na Halmashauri zetu kwamba hazina uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ukiangalia, makusanyo mengi yameingia Serikali Kuu, ina maana TRA ndiyo watakusanya. Ina maana Halmashauri watakuwa hawana kipato cha kuwapa akinamama pamoja na vijana zile asilimia tano. Sasa sijui Serikali itafanyaje kwa sababu akinamama wengi sasa hivi wameshapata mwamko, ni wajasiriamali. Nanyi wenyewe mnaona sasa hivi hata mkienda vijijini mnakuta akinamama wengi ni wajasiriamali kutokana na juhudi nzuri za Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sasa tunaomba hii asilimia tano iliyowekwa na hivi vigezo ambavyo viliwekwa, hela nyingi zimechukuliwa Halmashauri, akinamama hawa wajasiriamali watapataje mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata sasa hivi kupata hiyo asilimia tano kwenye Halmashauri zetu ni shida. Sasa naomba Serikali yangu sikivu kwa bajeti hii ione ni jinsi gani ya kuweza kutenga au kutafuta ili hawa akinamama waweze kupata asilimia tano ili waweze kufaidika na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye upande wa maji. Hakuna kitu kigumu na shida katika maeneo yetu kama maji. Nikiangalia, Wilaya yangu ya Mpanda kuna vyanzo ambavyo Serikali ilifanya jitihada kubwa, lakini unakuta miradi ile haiishi na ile bajeti inayopangwa haiendi kwa wakati ile miradi ikaisha.
Sasa sijui bajeti hii ambayo imekuja mbele yetu, itaweza kukamilisha miradi ile ya maji na wananchi waweze kupata kwa urahisi na wepesi zaidi. Hususan Wilaya ya Mpanda, kuna mradi wa Ikorongo One; bajeti ya mwaka 2015 mkatupangia kuwa mtatupatia shilingi bilioni nne, lakini zile pesa hazikuweza kupatikana. Matokeo Wilaya ya Mpanda Mjini, Manispaa, maeneo mengi maji ni shida. Yaani maji yale yakipatikana leo, kesho hawapati; au wanaweza wakakaa siku tatu ndiyo wanapata maji. Maeneo mengine kama Makanyagio, Ilembo, hakuna maji kabisa, ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi, hii bajeti ya safari hii, miradi ambayo inaelekezwa, iweze kukamilika ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. Nafikiri na Waziri alivyotusomea bajeti yake, alisema sasa ni kipindi cha akinamama kufurahi; anawatua ndoo. Sasa naomba basi akinamama hususan wa Mpanda Vijijini, kuna vijiji havina maji kabisa wala havina miradi kabisa. Akinamama wanapata shida sana. Naomba bajeti hii iweze kutimiza yale malengo waliyoyataja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya ardhi ni mikubwa mno. Ukiangalia kama Wilaya yangu ya Mpanda, Kata ya Ilembo ni shida. Naiomba Serikali sasa kupitia bajeti hii, migogoro hii ya ardhi iweze kwisha. Tunaomba bajeti hii ambayo leo tunaisema hapa ifanye kazi kama mlivyoileta mbele yetu, kwa sababu, migogoro ya ardhi haiishi. Kwa nini haiishi? Mimi nashangaa kila siku, kwa nini haiishi? Lazima sasa bajeti hii ambayo tunaichangia hapa, tunaomba migogoro ya ardhi kupitia bajeti hii, iishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijijini mwetu wanavijiji wanavaa mitumba na ndiyo nguo rahisi walizozizoea, ndiyo maana ukienda sasa hivi vijijini unawakuta akinamama wengi ni wasafi kutokana na mitumba. Leo sisi bado viwanda vya kutengeneza malighafi ya nguo havijafika, lakini leo tumeipandishia mitumba ushuru mkubwa, ina maana wale wananchi wa vijijini washindwe kuvaa kabisa?
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kuhusu mitumba iangalie upya, watoe ushuru wa mitumba kwa sababu wananchi wetu ndiyo mavazi yao wanayayategemea kuliko kitu kingine chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii. Katika nchi yetu kuna miradi mingi ambayo tuliiandaa na sera yetu inasema kuhusu Zahanati na Vituo vya Afya, lakini tukiangalia sehemu nyingi Vituo vya Afya, havijakamilika, unakuta sehemu nyingine kuna jengo zuri sana Serikali imejenga, lakini vifaa vya mle ndani havijakamilika. Naomba kupitia bajeti hii Serikali ijitahidi sana, miradi yote ya vituo vya afya pamoja na zahanati walizojenga wananchi ziweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna vifaa kama dawa, vifaa tiba; katika sehemu nyingi, zahanati nyingi hazina vifaa tiba, wananchi wanapata taabu. Kwa mfano, sisi pale Mkoa wetu wa Katavi, Wilaya ya Mpanda, ile hospitali ni ya Wilaya lakini tunasema ni kama Hospitali ya Mkoa. Hakuna kabisa vifaa, wananchi wa Wilaya ya Mpanda wanapata shida, ina maana kama ni ya Mkoa, maana yake ndiyo Makao Makuu ya Mkoa, lakini hawana vifaa kabisa. Naomba kupitia bajeti hii, Serikali ijitahidi kufikisha vifaa ili wananchi wetu waweze kupata matibabu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa akina mama, kuna tatizo la maji vijijini. Tunasema maji vijijini kwa sababu sisi akina mama tunahitaji maji na utakuta maeneo mengi vijijini akina mama wanapata shida, wanaenda kutafuta maji sehemu za mbali, anaamka saa 8.00 za usiku, saa 9.00 za usiku anaacha familia yake. Naomba kupitia bajeti hii tunaomba sana Serikali itufikishie maji vijijini. Kwa sababu tutakuwa tumewakomboa sana wananchi kupitia maji hususan akina mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kupitia bajeti hii ambayo tumesema kuhusu shilingi milioni 50 za kila kijiji, napendekeza kupitia bajeti hii, fedha hizo ziende kila kijiji. Vile vijiji ndiyo vinawajua wananchi katika maeneo yao husika, maana kuna vijiji halafu kuna Mitaa. Mijini wanatumia mitaa; kwenye maeneo ya vijijini, kuna vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba zile fedha, kwa sababu kama mtaa ndiyo unawafahamu watu, Mwenyekiti wa Mtaa na ile Kamati yake ndio anawajua watu wa mtaani kwake. Sasa fedha zile shilingi milioni 50 zikifika pale wale watajuana ni jinsi gani watagawana zile fedha na kukopeshana ili waweze kupata faida ya Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi mazuri ambayo yanayofanywa Serikali, tunaomba Serikali kupitia vile vile michezo, mara nyingi bajeti hii imekumbuka michezo, sanaa lakini bado mfumo wetu wa michezo haujakaa vizuri, hususan vijana wetu wa vijijini wako vijana wachezaji mpira wazuri ambao wanaweza kulikomboa Taifa hili, lakini bado hatujawafikia na bajeti zetu haziwafikii kule wakatambulika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wako wasanii wazuri ambao wanajua mambo ya usanii huko vijijini, lakini kutokana na uwezo, hawawezi kufika mijini au hawawezi kufika sehemu ambayo anaweza akajulikana au akafahamika. Basi tunaomba kupitia bajeti hii sasa, Serikali ikatambue wale watoto walioko vijijini, ambao wanaweza kuja kulipatia faida Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi yanayotakiwa yafanyike ndani ya nchi yetu, kupitia bajeti hii. Pia kuna haya mashirika makubwa hususan bandari na viwanja vya ndege. Wao wanapata mapato ndani ya shirika kama vile bandari, lakini unakuta kuna mfuko wa Serikali na tumesema safari hii fedha yote iingie Serikalini, lakini vilevile kuna mambo wao kama shirika, wanatakiwa waboreshe ili waweze kupata faida zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba kupitia bajeti hii, kama bandari kuna fedha ambazo wanaingiza katika Mfuko wa Hazina, tunaomba yale mahitaji wanayoyataka wenyewe kuboresha bandari ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi, wapewe zile fedha haraka ili waweze kuinua uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika viwanja vya ndege, tunajua kuna miinuko ambayo inaruka ndege, kuna faida kubwa ndani ya viwanja vyetu, lakini wana mahitaji ambayo wanataka kuweka labda taa, na kadhalika, naomba basi Serikali iwape zile fedha haraka kwa ajili ya mahitaji yanayoweza kuleta faida katika viwanja vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi yanayofanyika katika mashirika ambapo sasa hivi pesa nyingi zitakuja kwenye Mfuko wa Hazina. Maana yake sasa hivi fedha zinazotoka katika mashirika mengi tumesema kupitia bajeti hii zitaingia kwenye mfuko maalum. Naomba Serikali, pindi watakapohitaji fedha zile wafanye jambo fulani, naomba wapewe ili waweze kuongeza ufanisi ndani ya kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali yetu kwa mpango mzuri kwamba kwa kupitia bajeti hii tumepanga kununua ndege tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba nchi yetu hapo katikati usafiri ulikuwa ni shida. Sisi tumefarijika sana kupitia bajeti hii kuona sasa Serikali yetu imekumbuka kununua ndege tatu, kusema kweli tumefarijika sana. Tunaomba sasa mikakati na utaratibu kuhusu Shirika la Ndege la ATCL, mikakati yake ipangwe vizuri tusije tukaharibu kama tulivyoharibu mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua shirika letu hili lina madeni mengi, lakini najua Serikali imeamua kufanya kitu ambacho safari hii hatuwezi kuharibika tena, kwa sababu madeni yale najua kuna bajeti ambayo mtaipanga, tulipe yale madeni, halafu shirika sasa lisimame kama shirika na sisi Tanzania sasa tuwe na Shirika la Ndege. Tutafurahi kwa sababu kama mimi Mkoa wangu wa Katavi, nashukuru Serikali naomba niipongeze, mlitujengea uwanja mzuri sana, lakini hakuna ndege hata moja inayotua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hili sasa, hizi ndege tatu, nami najua sasa Mkoa wa Katavi, ndege itatua. Naomba niwapongeze kwa hilo, basi tununue hizo ndege ili sehemu nyingi ambazo ndege zilikuwa hazifiki, sasa ziweze kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukurru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuongea kengele ya pili isinigongee. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili kuweza kuzungumzia mpango wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetulinda ametuleta tena kwa mara nyingine mahali hapa, tunaendelea kuomba neema yake na rehema yake atulinde mpaka tumalize Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya kwa ajili ya kupigania nchi yetu na maslahi ya Taifa zima. Naomba nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambazo kwa muda mfupi kwa muda wa mwaka mmoja wameweza kuzifanya.
Leo hii naomba nimpongeze Rais wangu kwa kazi nzuri na maamuzi magumu ambayo ameyafanya kuhamia Dodoma, leo hii Serikali inahamia Dodoma ni mafanikio makubwa kwa sababu ilikuwa inazungumzwa kwa muda mrefu na miaka mingi leo Awamu ya Tano imeweza kufanya leo hii Serikali imehamia Dodoma.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba niipongeze Serikali, ingawa bado pesa hizi hazijatoka za kwenda kila kijiji shilingi bilioni 59.5, tuna mategemeo Serikali hii ya Awamu hii ya Tano hizo hela zitafika kwa wananchi wetu kwa ajili ya uchumi wa Tanzania hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kununua ndege mbili mpya. Leo hii tunajivunia Serikali ina ndege, alama yetu ya twiga ipo ilikuwa haipo lakini leo sasa ipo kutokana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano yameendelea kuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite sana kwenye masuala ya dawa. Ninaomba sasa Waziri wetu aweke mpango mkakati wa ujumla ili wananchi wetu waweze kupata dawa. Dawa ni kitu muhimu sana kwa wananchi wetu wa Tanzania. Ninaomba mikakati mikubwa ichukuliwe sasa hivi, ufanywe mkakati maalum kwa ajili ya dawa ili hospitali zote zipate dawa. Ninajua Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu, mipango inayopanga sasa iweke mikakati ili tuweze kupata dawa kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; lazima sasa tufanye mikakati ya kujenga vituo vya afya kila Kata ili wananchi wetu waweze kupata huduma za ukaribu. Tukiweka mipango mizuri na mikakati mizuri kila Kata iwe na kituo cha afya akina mama wengi wataende kufanyiwa operation ndani ya kata zetu na maeneo yetu husika, hiyo mipango iweze kupangwa. Mimi najua Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, mipango yote tunayomweleza Waziri wetu ataifanya na ataitenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji; bado maji hatujawafikia wananchi vizuri husasan maji mijini bado kuna maeneo ambayo maji hayajawafikia wananchi vilevile maeneo ya vijijini, lazima sasa hivi tuamue kuweka mipango mikakati.
Kuna Mbunge hapa amezungumza kama sisi tunapakana na maziwa, mfano Ziwa Tanganyika li-supply Mkoa wa Katavi inawezekana, kwa sababu kuna mipango iliyopangwa nyuma. Leo hii Mwanza, Shinyanga wanapata maji kutoka Ziwa Victoria, tunaomba na sisi tunaokaa Katavi, Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine kama Kigoma yale maziwa yetu yaweze kunufaisha maeneo husika, vijijini pamoja na mijini, mpango ukikaa vizuri nafikiri tutaweza kufanikiwa vizuri sana upande wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu; ninaomba mipango mizuri ifanyike kwenye elimu. Tunajua Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi nzuri ya kutafuta madawati, leo hii tuna madawati mengi. Vilevile kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano imefanya elimu imekuwa bure, kutokana na elimu bure sasa hivi wanafunzi tumekuwa nao wengi ndani ya shule zetu. Sasa tunaomba Serikali ipange mpango makakati wa kujenga madarasa ili watoto wote waweze kuenea ndani ya madarasa. Kwa sababu madawati, mpango umekwenda vizuri hakuna sehemu sasa hivi watu wanalalamika kuwa mtoto anakaa chini, tunaomba bajeti hii inayokuja tuweke mikakati ya kujenga madarasa nchi nzima ili watoto wetu wote waweze kukaa madarasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa ardhi; leo hii tunawaleta wawekezaji, lakini kuna matatizo kidogo ndani ya maeneo yetu husika. Leo hii migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi imekuwa mikubwa mno. Ninaomba Serikali sasa kwa sababu tuna lengo zuri la kuweka mikakati mizuri ya wawekezaji nchini na vilevile tunaendelea kuwaleta wawekezaji ndani ya nchi yetu, kwenye upande wa ardhi tujipange vizuri na Watanzania tumeongezeka, lazima sasa hivi Serikali ipange mikakati ya kuongeza ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingine tumeweka mipaka, mipaka ile tuipanue ili wananchi sasa pamoja na wawekezaji wakae sehemu nzuri. Wawekezaji wengine wanatukimbia kutokana na migongano kati yao na wananchi. Ninaomba Serikali iweke mipango mizuri, mikakati mizuri ili wananchi na wawekezaji waweze kukaa vizuri na waweze kujenga viwanda vyao ndani ya nchi yetu ili vijana wetu wapate ajira, mama lishe zetu wale wanaohangaika waweze kupata ajira kwa ajili ya mipango mizuri ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mikopo ya akina mama. Akina mama wengi bado hatujawafikia kwa elimu. Tunapenda akina mama wapate mikopo, tunapenda akina mama waweze kuinuka, lakini bado hatujawafikia ili waweze kupata elimu nzuri waweze kutumia hayo mabenki tunayoyasemea leo hii mambo yamekuwa siyo mazuri, akina mama tukiwafikia tukiwapa elimu nzuri wakiweza kujikomboa wao kama wao, tukiwawekea mikakati mizuri ninafikiri Taifa hili ukimwezesha mwanamke, tumewezesha jamii nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kilimo; bado Watanzania tunalima asilimia 80 ni wakulima, asilimia 20 ni wafanyakazi. Mpaka leo hapa tulipo wananchi kule hawajapata mbolea na hili lazima tuliwekee mikakati mikubwa na mipana ili kipindi cha mvua kabla hakijafika wananchi hawa waweze kupata mbolea kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katikati tulikuwa tuna mawakala, leo hii hiyo mipango ya mawakala tumeitoa na wale mawakala ambao tuliowatoa bado hatujawalipa wanatudai na mpaka sasa hivi hatuna mawakala wala hatuna nini, wananchi wameilewa. Hatujui hiyo mbolea itauzwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ichukue jukumu ambalo sasa kupanga mikakati mizuri na mipango mizuri ili wananchi waweze kupata manufaa kupitia Serikali yao kwa ajili ya kilimo kwa sababu upande wa kilimo ndiyo uwekezaji upo mkubwa sana kuliko upande mwingine, ninaomba Serikali hii sikivu mipango hiyo iweze kupangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepanga mipango mingi, tunaongea mipango mingi, lakini kuna watu ambao ni muhimu sana ambao tukiwajengea uwezo na tukiwafanyia mipango mizuri, mikakati mizuri wanaweza wakakaa vizuri zaidi. Hapa mara nyingi tunawasahau sana askari wetu na sehemu nyingi ukienda unakuta askari hawana sehemu ya kuishi, lazima sasa Serikali ichukue jukumu la kuweka mpango mkakati wa kuwajengea askari nchi nzima ili hawa askari wanaotulinda wananchi wawe na sehemu nzuri za kukaa ili nchi yetu iweze kuwa na amani na utulivu kama tulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima sasa tuwawekee mikakati mizuri na mipana ili kila sehemu nchi nzima, nyumba za askari, nyumba za manesi, nyumba za walimu ziweze kuwekewa mikakati mikubwa na mipana zaidi ili sasa nchi yetu iweze kutulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utalii, kwetu Mpanda nilishasema kipindi kilichopita tumejengewa uwanja mzuri. Naomba nirudie kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo ilifanyika kununua ndege mbili. Ninajua sasa uchumi wa Tanzania na uchumi wa Mkoa wangu wa Katavi utazidi kuongezeka, ninajua sasa ndege itatua Mpanda, Katavi kwa ajili ya kuleta watalii ili uchumi wa Katavi uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaomba niunge mkono asilimia mia kwa ajili ya mpango huu mzuri.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa ninaomba niunge mkono hoja za ripoti za Kamati zote tatu ambazo zimewasilishwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Kamati. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye nyumba za askari wetu. Askari wetu wanaishi kwenye mazingira magumu sana katika nchi yetu ya Tanzania, unaweza ukasema labda Mkoa wa Katavi wanaishi labda vibaya, hawana nyumba, hawana nini, lakini ukitoka ukienda sehemu nyingine unasema loh, afadhali kwangu kuliko sehemu nyingine. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali hizi bajeti tunazipanga ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaomba zifike kwa wakati ili askari wetu waweze kujengewa nyumba au hata kuboreshewa nyumba wanazoishi, kwa sababu askari wetu ndiyo wanaotuweka sisi kwenye mazingira ya amani na upendo katika maeneo yetu husika. Tunaomba Serikali ijipange kuangalia hao askari. Tunawapa majukumu mengi makubwa ambayo wanatakiwa watekeleze lakini mazingira yao ambayo wanaishi sio mazingira rafiki. Tunaiomba Serikali hizi bajeti tunazopitisha safari hii Serikali ijipange kujenga nyumba angalau nyumba za askari. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeona at least Jeshi la Kujenga Taifa wamejengewa maghorofa sehemu mbalimbali, hapo tunaweza tukawapongeza kwa sababu wamejitahidi kwa upande mwingine, lakini kwa upande wa askari polisi bado hatujawatendea haki, wanaishi kwenye mazingira magumu sana. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende upande wa bodaboda. Bodaboda ni vijana wetu ambao wanajitafutia tuseme maisha yao na maisha haya wanajitafutia kutoka vyombo hivi ambavyo vimekuja kuwarahisishia maisha yao, lakini unakuta sasa ndani ya maeneo yetu kuna baadhi ya maaskari wanawanyanyasa sana bodaboda. Ninaomba basi Serikali, tunajua wale ni watoto wetu tumewapa ajira, wamejitafutia ajira kupitia bodaboda, tupange mikakati ya kuwafundisha usalama barabarani kwa sababu tunaona labda wanafanya vitendo vibaya, wanakwenda vibaya, wanaumia, wanapata ajali usiku na mchana, tufanye mikakati ya kuweza kuwapa semina ili waweze kujua jinsi gani watakavyotumia zile bodaboda. Ninaomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itekeleze hayo.(Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda upande wa magereza. Magereza zetu zimejaa sana; sasa mimi najiuliza, kuna wengine wamekaa kule magerezani miaka kumi, kesi zao haziishi, uchunguzi bado unachunguzwa. Tunaomba Serikali sasa hivi ifanye mikakati ya kuwatoa wale watu wenye kesi zao za muda mrefu waweze kutoka mule ndani kwa sabaabu wanakula bure, wamekaa kama vile mahabusu wengine mpaka leo wamekaa miaka sita, saba, nane hawajahukumiwa sasa wanajaza magereza na chakula kila siku tunasema kinapotea, tunaendelea kuwaweka watu ambao wanatakiwa waweze kuondoka ili magereza ile iweze kupungua. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, mahakama ndani ya nchi yetu. Mahakama bado, kama sisi kwetu Katavi mahakama hatuna ya Mkoa, hatuna hata Mahakama ya Wilaya huwezi ukasema kama tuna mMahakama. Tunaomba basi Serikali ijitahidi kujenga mahakama ndani ya nchi yetu ili tuweze kupata urahisi katika huduma mbalimbali za kimahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwenye Balozi zetu. Balozi zetu Wabunge wengi wamesema pesa haziendi kwa wakati. Wako nchi za nje huko wanaishi kwenye mazingira magumu sana. Tazameni Balozi zetu kuzipelekea pesa, unakuta sehemu nyingine balozi nyingine mazingira wanayoishi na lile jumba walilonalo utafikiri ni gofu. Hampeleki pesa za kutengeneza majengo ambayo yako maeneo hayo. Tunaomba Serikali, jitahidini jamani bajeti tunazopitisha, tafuteni pesa za kupeleka maeneo hayo ili mazingira yawe rafiki kwa wale watu tunaowapeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.