Supplementary Questions from Hon. Anna Richard Lupembe (39 total)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara hii imetumia muda mrefu takribani miaka sita kutoka Sumbawanga mpaka Mpanda haijakamilika na wakandarasi wanaingia na kutoka mpaka hatima yake sasa hivi barabara ile imeharibika kupita kiasi na pale Mpanda Mjini kuna shimo ambalo mkandarasi alilichimba katikati ya Mkoa halieleweki lile shimo litazibikeje.
Je, Serikali ina mikakati gani kwa ajli barabara hii imekaa muda mrefu mno mpaka wananchi wa Katavi wamechoka, itakwisha?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili sasa hivi Mkoa wa Katavi mawasiliano hayapo, barabara ya kutoka Mpanda kuelekea Tabora haipitiki kabisa na wananchi wa Katavi wanategemea kwenda kuchukua bidhaa zao Tabora, Mwanza, maisha ya Mpanda yamekuwa magumu kutokana na hali ya hewa jinsi ilivyo.
Je, Serikali ina mikakati gani ya dharura ili kuwaokoa wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa ajili ya barabara hizo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu barabara hiyo kuchukua muda mrefu ni kweli baadhi ya barabara zimechukua muda mrefu lakini siku kumi zilizopita Serikali imetoa takribani shilingi bilioni 200 kwa ajli ya kuwalipa Wakandarasi mbalimbali hapa nchini. Tunaamini sasa, nachukua fursa hii kuwaagiza Wakanarasi wote kama nilivyowaagiza wataalamu wetu wa TANROADS kwamba sasa hivi waanze kwenda kwenye site ili kazi hizo zianze mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kweli kuna changamoto kubwa huko sehemu ya Katavi, Mkoa wa Katavi kwa sababu barabara zimekatika. Lakini wataalamu wetu wa TANROADS sasa tumewaelekeza huko ili waweze kuzikarabati barabara hizo. Pia sasa hivi tumefungua njia yetu ya reli kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa huko baina ya Katavi, Tabora na Dodoma ili waweze kupata huduma kama kawaida, asante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa akina mama hao wanatoka mbali na wanaamka usiku wa manane na kwa kuwa wanahatarisha ndoa zao kama katika Kijiji cha Mtambo, Kariakoo, Iwimbi na wako karibu na hifadhi na mara nyingi wanakutana na wanyama wakali kama simba, je, Serikali ina mikakati gani ya kuwasaidia hawa akina mama ili waweze kupata maji karibu na makazi yao kwa sababu wanapata shida sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mto Ugala upo karibu sana na Katumba, ni kilometa 20 tu na wananchi wa maeneo hayo wapo takribani 100,000, je, Serikali ina mikakati gani ya kuwasaidia wananchi hao kwa vile wako wengi ili waweze kupata maji kwa urahisi na wepesi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa haraka wa Serikali, nadhani jana Mheshimiwa Waziri wa Maji alitoa ufafanuzi wakati wa mjadala wa hotuba ya Mheshimiwa Rais kwamba ni kweli changamoto ya maji imeonekana kuwa kubwa. Mheshimiwa Mama Anna naomba nikupongeze sana katika hili maana mara ulipoingia katika nafasi yako umeona kipaumbele cha kwanza ni kushughulikia tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, amesema katika Kijiji cha Mtambo wananchi wanapita katika hifadhi kubwa hivyo lazima wapate huduma ya maji ya haraka. Naomba niseme jambo moja, juzijuzi tulikuwa na semina kubwa na tuliambiwa tulikuwa na awamu ya kwanza ya maji sasa tunaingia katika awamu ya pili ambayo inaanza Januari hii. Mheshimiwa Waziri wa Maji jana alisema katika awamu hii tutaangalia jinsi gani tuweze kutatua matatizo kwenye sehemu zile zenye changamoto kubwa sana ya maji. Mheshimiwa Anna naomba nikuambie Waziri atakapokuja kufanya majumuisho ya Mpango katika suala zima la maji atazungumzia kiuwazi sehemu zenye changamoto tutafanyaje ili mradi tuweze kutatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini umezungumzia matumizi ya Mto Ugala, kama Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba tulichukue ili kuweka mpango mkakati hata ikiwezekana kwa kutumia wataalam wa Halmashauri na Wizara ya Maji tukishirikiana na TAMISEMI kufanya upembuzi yakinifu kuangalia ni jinsi gani mto huu unaweza kutumika kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa eneo hilo la Ugala, ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kuna vifo sana vya akina mama wajawazito na kwa kuwa Madaktari wetu pamoja na Manesi ni wachache:
Je, ni lini Serikali itaongeza Madaktari katika Wilaya ya Mpanda ili vifo vya akina mama wajawazito viweze kupungua?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ni kama vile Hospitali ya Mkoa, hatuna Daktari Bingwa wa akina mama: ni lini Serikali itatuletea Daktari bingwa ili akina mama vifo vyao vipungue?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa sasa, hatuna uhakika ni lini tutakamilisha utaratibu wa ndani ya Serikali wa kutoa vibali kwa ajili ya kuajiri watumishi kwenye Sekta ya Afya. Hivyo naomba avute subira mpaka hapo tutakapokuwa tayari kufanya hivyo.
Swali la pili, kuhusu Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama wajawazito na watoto, kwenye Hospitali ya Mpanda, naomba kumshawishi Mheshimiwa Mbunge kwenye vikao vyao vya Halmashauri vya Bajeti kwenye Bunge linalokuja, wajipange kuanzia chini, kwenye Halmashauri yao kuweka kasma ya watumishi wa aina hiyo, lakini pia sambamba na kuweka kasma ya kuajiri Daktari Bingwa, waandae mazingira yatakayovutia Daktari huyo kuja kwenye hospitali hiyo na akifika, basi akae.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itafanya utaratibu wa kupanga watumishi kwenda kwenye hospitali hiyo kadri ambavyo watakavyokuwa wameomba.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ilitumia pesa nyingi sana kwa ajili ya gati na kwa kuwa Serikali ilijenga majengo, mpaka sasa hivi yale majengo yamekuwa magofu na Wananchi wa Karema wamepoteza imani kabisa na Serikali kwa kwasababu walilia sana gati hili na wakalikosa mpaka sasa hivi:-
Je, ni lini sasa Serikali itaweka imani kwa wananchi wa Karema?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa, tulikuwa tuna mpango wa gati na tumetumia pesa nyingi, majengo yale yapo hayana kitu chochote, popo tu wanaingia na sasa tuna mpango wa bandari:-
Je, Serikali inaweka mikakati gani, kwa kuwa inatumia pesa nyingi na kupoteza kujenga bandari hii na wananchi wa Karema wawe na matumaini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ambayo ilishaanza kufanyika wakati tulikuwa tunategemea kujenga gati, siyo kwamba imepotea, hapana. Tunapojenga bandari haina maana ile kazi yote iliyofanyika wakati tunajiandaa kukamilisha ujenzi wa gati inapotea. Hayo majengo bado yatatumika na kwa hiyo, fedha hazijapotea, ila tutakapoikamilisha hii kazi, majengo hayo na mengine ambayo yataongezeka, badala ya kuwa na gati peke yake tutakuwa sasa na bandari. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba hizo fedha hazijapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kama ambavyo ilielezwa katika bajeti yetu, kama utakumbuka katika kitabu chetu cha bajeti katika ukurasa wa 199 utaona kwamba Serikali imetenga shilingi bilioni 24.05 kupitia TPA kwa ajili ya ujenzi wa gati, bandari katika Maziwa Makuu.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika fedha hivi ambazo tayari zimetengwa, tutaangalia ni kiasi gani tukipeleke pale ambapo kilishapangwa toka mwanzo ili kuweka mazingira ya haraka ili wale wananchi waanze kupatumia pale mahali wakati wakisubiri ujenzi wa bandari ambayo ndiyo mambo makubwa na mazuri zaidi.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Mpanda Manispaa nusu ya eneo lake halina ramani kabisa hususan Semulwa, Kichangani, Makanyagio kuelekea Misunkumilo pamoja na majengo ya katikati ya mji; na kwa kuwa, Serikali inasema sasa TRA itachukua kodi kila eneo na hawa wananchi hawana hati wala uhakika wa eneo lao kwa sababu mpaka sasa hivi hakuna upimaji wa aina yoyote na Wilaya ya Mpanda ni Wilaya Kongwe, je, Serikali itapima lini maeneo hayo ili wananchi sasa watambue haki yao ili waweze kupata mikopo kutoka kwenye benki zetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Wilaya ya Mpanda Manispaa Mabwana Ardhi wanachukua mashamba ya wananchi na kugawa viwanja lakini wale wananchi hawawapi viwanja. Je, ni lini Serikali au ni lini tutaenda na Naibu Waziri akajihakikishie hali ilivyokuwa korofi ya migogoro ya ardhi ndani ya Manispaa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze na ufafanuzi wa swali lako. Tunapoongelea maeneo ambayo yako demarcated ni kwamba upimaji wake ulishafanyika kwa maana ya michoro kamili lakini bado haujatenga maeneo kukamilisha upimaji kujua kiwanja kipi kinaishia wapi. Kwa hiyo, ni maeneo ambayo tayari michoro na viwanja vipo lakini bado havijawekewa mipaka yake na kuweza kukamilika kama inavyostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Lupembe ameeleza kwamba karibu nusu ya eneo katika wilaya hiyo bado halijapimwa na ametaja baadhi ya maeneo kama Changani, Kanyageni, Sukuma na majengo ya katikati ya mji na kwamba Wizara inasisitiza habari ya kuchukua kodi, je, ni lini tutapima? Katika jibu la msingi nimesema kwamba tayari kama Wizara tumeshagundua hayo na tumeona matatizo jinsi yalivyo na jinsi ambavyo watu wanakosa haki yao ya msingi ya kuweza kuwa na ule umiliki halali wa ardhi na kuwa na hati zao ambazo zingeweza kuwasaidia pia kufanya shughuli nyingine za maendeleo ikiwa pia ni pamoja na kujipatia fursa za kupata mikopo benki. Ndiyo maana tumetangaza zabuni na tukataka Halmashauri zote ambazo wana hayo maeneo ambayo upimaji wake haujakamilika kufanya upimaji ili tuweze kuwa na uhakika wa maeneo na watu waweze kumilikishwa ili tunapochukua kodi, basi tuchukue ile kodi ambayo ni halali na iko katika maeneo sahihi ambayo tayari yako katika utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Halmashauri nyingi ambazo bado hazijakamilisha upimaji. Ndani ya Wizara tuna viwanja zaidi ya 240,258 ambavyo tayari upimaji wake upo lakini haujakamilika na Kanda ya Mashariki inaongoza kwa kuwa na viwanja karibu 102,000. Kwa hiyo, tunasema kwamba, ukamilishaji huu umetangaziwa zabuni ili uweze kukamilika na tuweze kumilikisha watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema, baadhi ya Maafisa Ardhi wanachukua mashamba na kupima viwanja halafu wenye mashamba hayo hawapewi stahiki zao kwa maana ya pengine ya kupewa viwanja. Naomba nirudie tena kulisema hili, tulilizungumza pia wakati tunahitimisha bajeti ya Wizara, tulishasema ni marufuku kuchukua mashamba ya watu pasipo kukamilisha fidia zao. Kwa sababu unapotaka kupanua mji, tunajua ni miji mingi ambayo imeiva katika kupimwa sasa kuwa miji halali lakini tunawataka sana wananchi wasiwe rahisi sana katika kutoa mashamba yao kwa sababu wanapunjwa sana na Halmashauri zote hazitakiwi kuchukua mashamba ya watu pasipo kukamilisha taratibu za ulipaji fidia katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Lupembe hakuna Afisa Ardhi yeyote anayeruhusiwa kuchukua ardhi ya mtu bila kumpa stahiki zake. Hata kama limeiva katika upimaji, basi taratibu zile za fidia zifanyike ndipo Halmashauri iweze kuchukua eneo hilo.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Kata ya Litapunga, Halmashauri ya Nsimbo, vijiji vingi havina maji. Je, ni lini Serikali itapeleka miradi Kata ya Itapunga, ili akinamama wale waweze kupata unafuu wa maisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Nsimbo maana yake Jimbo liko pana najua na vijiji viko vingi. Na Katika bajeti zetu za TAMISEMI tulielezea baadhi ya miradi ya maji, lakini na wenzetu wa Wizara ya Maji wameelezea mipango yao katika ujenzi wa maji. Na ni kwamba tulikuwa na programu ya maji ya awamu ya kwanza sasa tunaingia katika programu ya maji ya awamu ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika program ya maji ya awamu ya kwanza kuna maeneo mengine maji tulikosa, visima vilichimbwa, lakini maji hayakupatikana! Katika programu ya Awamu ya II tunaenda mbali zaidi, maana yake maeneo ambayo yalikosa maji yaweze kupata maji. Maeneo yaliyokuwa hayana maji maana yake hawana miradi ile ya maji ni lazima kujielekeza kuweka miradi ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na lengo kubwa ni nini? Tulichokipanga katika kipindi hiki lengo kubwa tulikuwa na ile, principal yetu ni kwamba, lazima tumuondoe mama ndoo kichwani. Nikijua kwamba Nsimbo ina changamoto kubwa sana kama ilivyokuwa Korogwe, Kisarawe, Bahi na kama ilivyokuwa maeneo mengine yote, jukumu letu kubwa ni kwamba, sisi tutafanya analysis jinsi gani tutafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo uliyoyazungumza tutaangalia kwa pamoja kwamba kuna miradi gani ambayo imetengwa kwa sasa hivi, lakini ni jijsi gani tutafanya tuyafikie maeneo ya watu mbalimbali kwa sababu lengo letu kubwa ni kumuondoa mama ndoo kichwani, kutumia fursa mbalimbali, kama visima vilikuwa vinachimbwa, na vilikuwa vimepatikana basi tunaangalia alternative way, kama kutumia malambo au kutumia chanzo kingine cha karibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuahidi Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri mnafanya ushirikiano mzuri wewe na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo pale na yeye tulikuwa na kikao mpaka hata kesho tulipanga kuweza kuonanan katika mambo mengine ya ukusanyaji wa mapato. Lakini hayo ni miongoni mwa mambo mengine ambayo tutaenda kuyaangalia; lengo kubwa ni kwamba kuwapatia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maji kwa hiyo, tumelichukua swali lako kwenda kulifanyia kazi.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mlele, Kata ya Ilunde imesahaulika kabisa kwa mawasiliano. Je, Serikalini ni lini watapeleka mawasiliano Kata ya Ilunde?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunakusudia kupeleka mawasiliano vijiji vyote Tanzania nzima. Namhakikishia hicho Kijiji cha Ilunde kitapata mawasiliano. Kumwambia lini, naomba anipe muda zaidi niwasiliane na yule mtu anayehusika kupeleka mawasiliano tupate uhakika, nitakuja kujibu nikishapata majibu sahihi. Namhakikishia mawasiliano yatapatikana katika kata hiyo na nitafuatilia kwa makini. Nakushukuru sana kwa juhudi zako za kufuatilia suala hili.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mlele, Kata ya Ilunde imesahaulika kabisa kwa mawasiliano. Je, Serikalini ni lini watapeleka mawasiliano Kata ya Ilunde?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunakusudia kupeleka mawasiliano vijiji vyote Tanzania nzima. Namhakikishia hicho Kijiji cha Ilunde kitapata mawasiliano. Kumwambia lini, naomba anipe muda zaidi niwasiliane na yule mtu anayehusika kupeleka mawasiliano tupate uhakika, nitakuja kujibu nikishapata majibu sahihi. Namhakikishia mawasiliano yatapatikana katika kata hiyo na nitafuatilia kwa makini. Nakushukuru sana kwa juhudi zako za kufuatilia suala hili.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo bado hayajaridhisha sana kwa sababu maeneo mengi wananchi bado wanajenga kiholela. Wakishajenga kiholela baadaye ndiyo Serikali inajua kuwa hawa wamejenga kiholela wanaanza kuja kuwasumbua, kunakuwa hakuna barabara hata watu wakiugua kwa mfano akinamama wajawazito jinsi ya kutoka maeneo yale kwenda hospitalini inakuwa shida kwa vile usafiri hauingii katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaona jambo hili kuwa wananchi wanajenga kiholela na baadaye inakuwa shida na tabu, lini sasa itaweka mipango mikakati ya kuhakikisha inapima kwanza halafu inawagawia wananchi viwanja ili waweze kupata maeneo mazuri na yenye kupitika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa Manispaa ya Mpanda kuna migogoro mingi sana ya ardhi na nilishamwambia Waziri aje Mpanda kuona jinsi wananchi wanavyopata tabu. Je, ni lini sasa mimi na yeye tutaongozana kwenda Mpanda ili aende akatatue matatizo ya wananchi wa Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameanza kwa maelezo na kusema kwamba Serikali inaacha watu wanajenga holela na baadaye inakuja kuwabomolea, lini itaweka mpango mkakati wa kupima ardhi yote? Kama Wizara tayari tumekwishaanza zoezi hili na tulilitambulisha pia wakati wa bajeti na tumeanza na Mkoa wa Morogoro katika zile Wilaya tatu za Ulanga, Kilombero na Malinyi. Huko ndipo tulipoanzia na uzoefu mzuri utaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii haizuii Halmashauri kufanya mipango yake ya upimaji wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao. Kwa sababu kama itaachiwa Wizara peke yake haiwezi kupima kwa wakati na ikamaliza kwa nchi nzima hii. Ndiyo maana kama Halmashauri tunacho kitengo/idara yetu, mipango miji wako pale ambapo wanatakiwa pia kuangalia namna ya upangaji miji. Ndiyo maana sasa hivi tuna miji zaidi ya 33 ambayo wameandaa mipango yao kabambe ili kuweka miji salama. Vilevile ujenzi unafanyika kule kwenye Halmashauri zetu, kwa hiyo kama Halmashauri tunapaswa pia kulisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai tu kwamba zoezi hili tunapaswa wote kushirikiana kuweza kuangalia watu wanawezaje kuendeleza makazi yao vizuri na kwa kuzingatia sheria kwa sababu tuko nao karibu zaidi katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, tunalichukua kama changamoto, lakini bado tunalirejesha kama changamoto pia kwenye Halmashauri zetu kuweza kusimamia matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao na kama mipango haijapangwa basi iweze kupangwa. Wataalam wa Wizara yangu wapo wanaweza wakasaidia kikanda kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuwaondolea wananchi hawa kero ambayo wanaipata pale ambapo wanabomolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ameongelea migogoro ya Mpanda na alitutaka twende. Nadhani tulizungumza kwamba migogoro iliyopo ni mingi na kama Wizara tumeipokea. Juzi wakati tunajibu swali hapa tumesema tunayo timu maalum inayoandaa tathmini ya ile migogoro. Kwa sababu unapofunga safari huwezi kwenda kufanya kazi ya mgogoro mmoja halafu ukarudi. Tunataka unapokwenda mahali uende ukaipitia migogoro yote iliyopo lakini pia uwe umeshapata ABCs za ile migogoro na chanzo chake, ukifika kule unatoa ufumbuzi wa kudumu na siyo kwenda tena halafu kurudi mara nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, zoezi hili la kwenda kwenye maeneo baada ya muda si mrefu tutawatembelea na tutafika kwa sababu timu inayoandaa tathmini ya ile migogoro na kuweka mapendekezo na kupitia zile taarifa za zamani za tume mbalimbali ili tuweze kuzifanyia kazi, karibu inakamilisha kazi yake na ikikamilika utaona tutafika na niko tayari kufika kwenye eneo lake.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele tayari
imeshatimiza masharti yote ya kujenga maabara, ya kujenga mfumo wa maji safi na taka pamoja na matundu nane ya vyoo; na kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Mlele hususan akina mama wa Tarafa ya Inyonga wanapata shida sana kwa ajili ya matibabu yao kwa sababu kile ni kuwa kituo cha afya lakini Halmashauri yao imefanya juhudi kubwa kwa matengenezo yote waliyoweka vigezo Serikali. Je, ni lini sasa Serikali itatoa kibali ili kile kituo cha afya kiweze kuwa Hospitali ya Wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa yale maeneo ambayo yanajengwa majengo mengine wananchi hawajalipwa fidia zao, wanadai sasa muda mrefu hawajalipwa, ni lini Serikali itawalipa pesa zao ili wananchi wa Wilaya ya Mlele hususan Tarafa ya Inyonga waweze kupata pesa zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na mimi nakumbuka nilitembelea katika Mkoa wetu wa Katavi na
miongoni mwa hospitali nilizokwenda kutembelea ni hiki Kituo cha Afya lakini kipindi kile kilikuwa kinakabiliwa na changamoto kubwa sana ya maji na nilitoa maelekezo pale na nimshukuru sana Mbunge wa Jimbo pale amefanya harakati imepatikana fedha hivi sasa mfumo wa maji
umepatikana. Na bahati nzuri hospitali hii kwa watu wasiofahamu ni kwamba ni kweli miundombinu yote imekamilika, na siku ile nilitoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwamba sasa kwa sababu eneo lile ndiyo
eneo la kimkakati na Makao Makuu ya Wilaya ya Mlele yako pale Iyonga, nikasema kwa sababu vipaumbele vyote vinavyotakiwa na mahitaji yote yameshakamilika basi waanze mchakato kuhakikisha eneo lile sasa linakuwa rasmi, kituo kile kinakuwa rasmi kuwa Hospitali ya Wilaya ilimradi waweze kukidhi vile viwango vya upataji bajeti inayolingana na hospitali ya Wilaya.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Anna Lupembe naomba
nikuhakikishie kwamba haya yalikuwa maelekezo yangu nilipokuwa kule site kutokana na mahitaji ya maeneo hayo yalivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la wakazi waliokuwa pale; ni kweli, ukiangalia kwamba kuna nyumba nyingi sana zimejengwa katika maeneo yale na bahati mbaya sana kuna watu wanaotaka fidia pale na nilitoa maelekezo katika Halmashauri yetu sasa ipange mkakati jinsi
gani wale watu wataweza kulipwa fidia. Kwa sababu eneo lile likishakuwa hospitali ya wilaya lazima tuwe na eneo la kutosha kwamba wananchi katika eneo lile na hospitali ile iwe na hadhi kwamba maeneo yale sio kuingiliwa na watu na nina imani kwamba katika vipaumbele vya bajeti ya Halmashauri mwaka huu itakuwa imetengwa hiyo. Lengo kubwa ni kuifanya hospitali ile sasa iwe rasmi kuwa Hospitali ya Wilaya.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano sasa hivi kwa wananchi ni uchumi. Kwa sababu wananchi sasa hivi wanafanya mawasiliano kwa mambo mengi ya kibiashara ya mawasiliano ya magonjwa na kila kitu na vilevile mawasiliano ninafikiri kama hakuna sehemu hakuna mawasiliano hakuna maendeleo. Katika kata za Sibwesa na Kasekese wameweka minara tayari toka Mei na pesa zimashatumika sasa ni lini Serikali itawasha kwa sababu wananchi wanaona ile minara lakini haina faida katika muono wao?
Swali la pili, wananchi wa Ilunde wameahidiwa kwa muda mrefu sana kuhusu mawasiliano. Na ukiangalia kata ya Ilunde iko katikati ya pori ina maana wananchi wale maisha yao yako hatarishi na wengine wanakwenda kupanda kwenye miti, wengine wanadondoka wanavunjika mikono na miguu kwa ajili ya kutafuta mawasiliano. Ninaomba kauli ya Serikali, ni lini sasa Serikali itawajengea mnara kata ya Ilunde? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na Mheshimwa Mbunge kwamba mawasiliano ni biashara na nakubaliana naye kwamba ni muhimu sana kuwe na mawasiliano maeneo yote na kama nilivyosema katika majibu yangu ya swali la msingi kwamba Serikali nia ya dhati ya kuhakikisha tunapeleka mawasiliano kila sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nikiri kwamba mikoa mitatu hii ya Songwe, Rukwa na Katavi sijaizungukia sawa sawa ili nijue hasa matatizo yake katika sekta zote tatu. Nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kikao hiki cha Bunge la Bajeti nitafika katika mikoa hii mitatu hususan katika kijini hiki cha Ilunde nione na nipate hali halisi. Na mimi nijisikie hali…na hatimaye tupange mipango ya kuondoa matatizo haya.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Mlele haina Mahakama kabisa, ni lini watajenga Mahakama ya Wilaya ya Mlele? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango iliyopo katika Mahakama, Wilaya ya Mlele imepangwa kujengewa Mahakama ya Wilaya mwaka 2017/2018 na nimalizie hapo hapo na Wilaya za Mpanda na Tanganyika mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Kijiji cha Mtisi wanapata shida sana, hawana kabisa eneo la kilimo. Nafikiri umeona kabisa hapa jinsi gani eneo la hifadhi ni kubwa zaidi kuliko eneo la kilimo na kaya zimeonekana hapa. Naishukuru Serikali imepanga kuwapa ardhi Novemba mwishoni lakini wananchi wa Mtisi wanahitaji kulima sasa, sasa hivi ndiyo kipindi cha maandalizi ya kilimo, wanatakiwa waandae mashamba yao. Je, Serikali haioni ni vema kubadilisha hii Novemba mwishoni wafanye Novemba hii mwanzoni ili wananchi wale waweze kupata maeneo ya kilimo waweze kupata chakula ndani ya familia zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ndani ya Kata hii ya Sitalike kwenye Vijiji vya Matandalani na Igongwe kutokana na ardhi ndogo wako ndani ya ramani toka 1972, lakini Serikali ilienda kuwabomolea nyumba zao na mpaka leo hii imekuwa tafrani, wala hawaelewi hatma ya maisha yao. Je, Serikali ina mpango gani na wananchi wa Matandalani na Igongwe? Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kwenda kwenye Kata ya Sitalike kuona adha hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kurejea majibu yangu ya swali la msingi katika kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba ifikapo mwishoni lakini hadi sasa kazi za kuwapatia ardhi wananchi hao zinaendelea. Hadi jana kaya 200 zilikuwa zimeshatambuliwa na zilikuwa zimeshatengewa eneo maalum. Kwa hiyo, bado zoezi hilo linaendelea ile mwishoni mwa Novemba ni kumalizia kazi, kazi itakuwa imekamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema kwamba wananchi wa Kijiji cha Matandalani na Igongwe walibomolewa nyumba ni kwa sababu walikuwa kwenye hifadhi. Natoa wito kwa wananchi ambao wako kwenye maeneo ya hifadhi kwamba wanatakiwa waondoke wenyewe badala ya kusubiri kuondolewa kwa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa shida hiyo iliyopo kule Matandalani na Igongwe na Halmashauri ya Nsimbo kwa ujumla, nilipita juzi lakini niko tayari kwenda tena kama matatizo yataendelea kuzidi kuwepo.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa ajili ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ziwa Tanganyika, Kalema, Ikola pamoja na Kapalamsenga, vijana wale wako duni sana kwa ajili ya uvuvi wa lile Ziwa Tanganyika. Je, Waziri yuko tayari kwenda na mimi ili akaone hali halisi ya vijana wale?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anna Lupembe kwamba niko tayari kwenda Ziwa Tanganyika kuonana na wavuvi wa ziwa hilo wakati wowote baada ya kumaliza shughuli za Bunge hapa.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kazi nzuri na juhudi zinazoendelea kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunashukuru kweli tunajengewa Mahakama ya Mkoa pamoja na Wilaya katika jengo moja. Lile jengo limejengwa vyumba vinne tu na Mahakimu wa Mkoa wanahitajika wawili na Mahakimu wa Wilaya wanahitajika wawili. Jaji akija hana ofisi ya kukaa na hakuna sehemu nyingine ya huduma mbalimbali za kiofisi.
Je, Serikali haioni kwamba hilo jengo ni la muda tu siyo la muda mrefu? Serikali haioni kama itapata hasara kujenga sasa hivi na wakati mwingine wajenge tena. Lini sasa Serikali itaongeza lilelile jengo liwe kubwa na la kutosheleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi Mahakimu ni wachache sana, je, Serikali itaongeza lini Mahakimu ndani ya Mkoa wetu wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anazungumza kuhusu jengo hili kuwa na vyumba ambavyo havitoshi na kama Serikali itaingia hasara kwa sababu baadae tena itahitajika kujenga jengo lingine. Nianze kwa kusema jengo hili la Mahakama ya Mkoa linajengwa katika eneo moja ambalo linaitwa Ilembo, Manispaa ya Mpanda. Tumempeleka mkandarasi ambaye anaitwa Moladi Tanzania yuko pale anafanya kazi hiyo, kilichojitokeza ni kwamba baada ya mvua kubwa kunyesha na udongo wa pale Ilembo ni mfinyanzi mkandarasi na consultant wameshauriana tumebadilisha michoro tena ambayo inachorwa upya na lengo hapa ni kuhakikisha tunajenga jengo lenye ubora wa juu ili shughuli za Mahakama ziendelee katika eneo hilo la Ilembo katika Manispaa ya Mpanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatua ya kwanza ambayo Serikali imefanya. Mheshimiwa Mbunge naomba ukubaliane kwamba ni hatua kubwa sana ya ujenzi wa vyumba hivyo ambavyo vitawaweka Mahakimu wa Mkoa pamoja na Mahakimu wa Wilaya. Yako bado maeneo mengi nchi nzima ambayo yana mahitaji ya Mahakama. Kwa hiyo, kwa kuanza pale Ilembo ni fursa ya kipekee kwa Mkoa na tushukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo msemo mmoja wanasema ndege mmoja wa mkononi ana thamani kuliko wawili wa shambani. Sasa tayari pale Mpanda wameshapata majengo haya, waishukuru Serikali ikitotokea bajeti nyingine tutaona namna ya kufanya lakini mahitaji ni makubwa sana kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumza kuhusu Mahakimu wachache, hii ni changamoto si tu katika Mkoa wa Katavi lakini katika Mikoa mingi sana ndani ya nchi yetu. Pindi pale bajeti itakaporuhusu ya kuwaajiri watumishi wengine, Mkoa wa Katavi pia na wenyewe tutauangalia ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa Mahakimu.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Mlele haina Mahakama kabisa, ni lini watajenga Mahakama ya Wilaya ya Mlele? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango iliyopo katika Mahakama, Wilaya ya Mlele imepangwa kujengewa Mahakama ya Wilaya mwaka 2017/2018 na nimalizie hapo hapo na Wilaya za Mpanda na Tanganyika mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza naomba nimpongeze Mkuu wa Wilaya ya Mlele, tayari ameshaanza kufanya hamasa kwa ajili ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Mlele, lakini kwa kuwa jengo hili la polisi ambalo wanalitumia sasa hivi ni jengo ambalo walijenga wananchi wakati ikiwa Kata ya Inyonga kwa ajili ya usalama wao, sasa hivi imekuwa Wilaya na matukio yamekuwa mengi zaidi kupita nyuma na uhitaji wa usalama unahitajika zaidi kwa sababu sasa hivi ni Wilaya siyo Kata na wananchi wale walivyojenga hili jengo ambalo walilikabidhi Polisi, walijenga Kituo kidogo na chumba cha mahabusu kidogo…
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wananchi walijenga, Serikali inatakiwa ifanye maboresho. Je ni lini Serikali itafanya maboresho ili sasa kile kituo kionekane kama kituo cha Wilaya?
Swali langu la pili, kutokana na chumba kidogo cha mahabusu, kwa sababu sasa hivi mahabusu wale wanachukuliwa wanapelekwa Mpanda Mjini, halafu wanarudishwa Inyonga, gharama kila siku gari limekwenda Mpanda linarudi Inyonga, Serikali haioni ni vyema zile gharama ambazo zitumika kila siku kupeleka gari Mpanda Mjini na kurudisha Inyonga zikatumika kujenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Mlele?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake wa eneo hilo na Mbunge wa Jimbo husika kwa jinsi ambavyo wameweza kufanikiwa kuanza ujenzi wa kituo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikijibu mara kadhaa hapa, siyo kwamba Serikali haina mpango wa kujenga vituo vya polisi hususan katika ngazi za Wilaya, mpango huo upo. Nilizungumza jana kwamba tuna mpango wa kujenga vituo takribani 95 nchi nzima, lakini kwa sasa hivi bado hali ya kibajeti haijakaa sawa. Pale ambapo hali ya kibajeti itakapokaa vizuri, eneo hili ni moja katika vipaumbele vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa tutakapojenga kituo katika eneo hilo, litatatua vilevile changamoto ya udogo ya chumba cha mahabusu. (Kicheko)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanya kusema kweli kwa hiki kituo, kilikuwa ni kituo chakavu sana na kinatumika na watu wengi sana. Tunashukuru sana kwa hizi pesa ambazo mmetuletea na kuanzia sasa hivi ukarabati umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wafanyakazi wa sekta hii ni wachache sana, hatuna kabisa manesi, madaktari wala wahudumu kabisa; je, ni lini Serikali itatuletea watumishi katika kituo hiki ha Mwese? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ndiyo hospitali inayobeba matatizo yote katika Mkoa wetu wa Katavi; je, ni lini Serikali itatuletea Madaktari Bingwa, kwa sababu Hospitali ya Mpanda haina Madaktari Bingwa? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nipokee pongezi zake kwa fedha ambazo tumepeleka Mwese na nimpongeze naye mwenyewe kwa kufanya kazi za Kibunge hasa katika Mkoa wake wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la watumishi katika Kituo cha Mwese, napenda nimhakikishie kwamba kwa sababu kituo hakijakamilika, Serikali itaweka kipaumbele katika kutenga watumishi ambapo kituo hicho mara kitakapokamailika tu tutawapeleka mara moja ili waweze kutoa huduma kwa wananchi. Hao watumishi tutawaajiri mwezi Julai, wataanza kazi, wataripoti, lakini kuna watumishi ambao tutawa-retain kwa ajili tu ya Kituo hiki cha Mwese.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, kwanza nilitembelea hospitali ile mwezi Novemba, 2017 hospitali yenyewe tu kwanza inahitaji uangalizi wa karibu kwa maana ya ukarabati na mambo mengine. Nimhakikishie kwamba katika ajira ambazo tunaendelea nazo sasa hivi, kati yetu sisi tuna ajira 6,000 ambazo tunaendelea kuziratibu na Wizara ya Afya ina ajira kati ya 1,800 mpaka 2,000 ambazo wanaendelea kuziratibu, basi tutaweka kipaumbele cha kupeleka Madaktari Bingwa kupitia ajira hizi.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Mlele inakaa Mahabusu kidogo sana, wanakaa watu takribani kumi, lakini kutokana na uhaba wanakaa watu kuanzia 30 mpaka 40 na wale ni binadamu na sisi binadamu tuna maradhi mengi wanaambukizana, wanakula mle ndani. Kwa nini Serikali wale watu wenye makosa madogo madogo wanaotakiwa kupewa dhamana, wasipewe dhamana ili waende kufanya shughuli zao zingine ili Mahabusu isikose watu kwa sababu mhalifu anajulikana na mhalifu ni Mtanzania anajulikana katika maeneo anayoishi. Je, ni kwa nini wasiwe wanapenda kutoa dhamana ili Mahabusu hizi zisiwe na watu ili msongamano uweze kupotea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Wilaya ya Mlele katika kile Kituo cha Polisi hakuna magari, hakuna magari sasa unakuta Mahabusu wale wanakaa wiki nzima wakibanana mle ndani; je, ni lini Serikali itatununulia magari kwa ajili ya uboreshaji zaidi kwa sababu wanatolewa Mlele wanapelekwa Mpanda? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Richard Lupembe Mbunge wa Viti Maalum ambaye ni Mtumishi wa Mungu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Anna Lupembe ambaye ni Mtumishi wa Mungu kwa namna ambavyo amekuwa akiwahamasisha Watanzania na waumini katika kulinda amani na kufanya doria za kiroho. Kwa hiyo nimpongeze sana kushiriki kwenye ujenzi na ulinzi wa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba pale Mlele kuna tatizo la Gereza na kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba Serikali iko kwenye mchakato wa kuhakikisha hizi Wilaya mpya tunajenga Magereza na Magereza mengine kwenye mikoa mipya. Tatizo ni kwamba ni kitu ambacho hakiwezekani kupangisha Gereza kwamba unaweza ukaenda kwenye nyumba ya mtu ukasema tumekuja tupangishe kwa ajili ya Gereza. Kwa hiyo kwa vyovyote vile lazima sisi kama Serikali tuendelee na mipango yetu ya kuhakikisha kwamba tunajenga Gereza. Ndiyo maana tumeanza kupunguza msongamano kwa kutumia Sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na mawazo yake aliyoyasema ya dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye swali la gari, Wilaya zote tumezipa gari kwa ajili ya kuhakikisha kwamba gari zile zinasaidia kubeba Mahabusu. Kwa kesi ya Mlele Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi nichukue fursa hii kumpongeza ameshaanza juhudi kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya kuhamasisha wananchi na tayari ameshatoa mifuko 200 kwa ajili ya kuanza kujenga Gereza la Mlele na tayari tumeshampatia ramani. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya tutakapokwenda Mlele tutashirikiana pamoja na wananchi. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hospitali yetu ya Mpanda Manispaa ndiyo ina-act kama hospitali ya Mkoa; na ndani ya ku-act kwake hatujawahi kupata mafunzo hata siku moja; na Serikali ilitutengea kachumba kadogo sana ambako ndiko kanatunza watoto njiti, lakini hatuna kabisa Muuguzi ambaye anayefanya kazi hiyo; nasi ukiangalia ndani ya Wilaya yetu ya Mpanda, Hospitali ile Wauguzi wako wachache sana, ndiyo maana watoto njiti wanafariki kutokana na huduma inakuwa siyo nzuri; ukizingatia vifaa vyake vile vya kutunzia wale watoto hatuna: Je, ni lini sasa Serikali itatuletea hawa Wakufunzi waje waweze kutufundishia Wauguzi wetu pale katika Hospitali yetu ya Mpanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika wodi ya wazazi, ndiko kulitengwa hicho kichumba kidogo, napo kuna vitanda vitatu tu; watu wazima wanakaa mle ndani, hakuna usalama kabisa: Je, ni lini Serikali itatujengea wodi maalum kwa ajili ya watoto njiti?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge, nini maana ya watoto njiti? Watoto njiti ni wale watoto ambao wanazaliwa kabla ya mimba kufikisha umri wa miezi tisa au wanazaliwa na uzito pungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hawa wanakuwa na athari zaidi kwa sababu viungo vyao vinakuwa havijakamilika vizuri, ama havijakomaa vizuri na uwezekano wa wao kupoteza maisha kwa shida za kupumua na kupata magonjwa mbalimbali ni mkubwa sana. Sisi kama Serikali, moja ya mkakati wetu ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na tumejikita kuhakikisha katika mwaka huu wa fedha na baada ya Serikali kutukabidhi Hospitali za Rufaa za Mikoa, vipaumbele vyetu sisi kama Wizara, ni kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za magonjwa ya dharura, ujenzi wa theatre, uwepo wa ICU, lakini tumeweka msisitizo katika huduma ya mama na mtoto, vilevile kuhakikisha kwamba kuna huduma za ICU za Neonatal. Huo ndiyo mpango mkakati wetu katika ile bajeti ambayo mmetupitishia mwezi Julai, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maswali haya ambayo Mheshimiwa Amina Lupembe ameuliza, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, elimu hii tunaendelea kuitoa kwa awamu na nina uhakika kwamba Mkoa wa Katavi nako tutawafikia. Bahati nzuri nami nimefika katika ile hospitali, nimeliona hilo jengo la mama na mtoto liko katika hali ambayo siyo nzuri sana. Kama nilivyosema katika jibu letu la msingi, tunaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vyetu vya kutolea huduma, hususan Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa na kuzipatia vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke msisitizo vilevile, pamoja na hii elimu ambayo tuna upatikanaji wa vifaa, kuna utaalam wa gharama nafuu ambao tumeendelea kuwajengea uwezo wataalam wetu wa huduma za afya na jamii kwa ujumla matumizi ya kangaroo method.
Mheshimiwa Naibu Spika, kangaroo method maana yake ni nini? Ni yule mtoto njiti au yule premature baby mama anatakiwa akae nae atoe joto la ngozi kwa ngozi na imeonekana kwamba utaratibu huu wa kangaroo method umekuwa na manufaa makubwa sana katika kuhakikisha uhai wa watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ujenzi wa wodi ya watoto kama nilivyosema katika jibu langu la msingi hili tutaendelea kulijenga kwa awamu na hivi ninavyoongea kwamba wataalam wetu wa Wizara wameshapita Hospitali zote ikiwa ni pamoja na hii Hospitali ya Rufaa ya Mpanda kuangalia mahitaji ya nini kinachohitajika pale na taratibu zitakapokamilika tutajenga wodi hiyo.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Shule hii ni kongwe halafu iko kwenye eneo ambalo ni hatarishi, kuna bwawa ambalo lina wanyama wakali ambao wanaingia katika eneo la shule kwa sababu shule hii haina uzio kabisa; na shule hii ina upungufu mkubwa sana wa madarasa na vilevile ina upungufu wa mabweni; na kwa kuwa Serikali imepanga fedha na imesema hapa kuwa imeji-commit na pesa tayari zipo; sasa naomba commitment, ni lini Serikali itakarabati shule hii kwa sababu wanafunzi wa shule hii wanapata taabu sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, shule hii ina wasichana takribani watoto 888, ni watoto wa kike ambao wanapata shida sana; usiku wakiugua hakuna gari katika shule hii: kwa kuwa hii shule ni kongwe, ni lini Serikali itatuletea gari katika shule hii ya Sekondari ya Mpanda Girls?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba zimetengwa fedha shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kukarabati shule nyingine mwaka huu wa fedha na commitment ya Serikali ni kwamba ukarabati huu unaanza mara tu tutakapoanza kutekeleza bajeti ya mwaka 2019/ 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ametoa hoja ya gari na ni kweli kwamba kwa shule hizi kongwe na kutokana na mazingira ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge, naomba tupokee ombi hili tutalifanyia kazi kwa kadri uwezo wa Serikali utapopatikana.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na jitihada za Serikali kama ilivyoeleza kwenye swali langu la msingi, lakini wafanyabiashara WENGI wanashindwa kufanikisha kutokana na utitiri wa kodi na vikwazo mbalimbali na kuwa siyo rafiki na TRA kutokana na ukusanyaji wa kodi. Je, ni lini sasa Serikali itaweka mikakati kuondoa vikwazo hivi? Maana wanapata vikwazo vingi sana, watu wa TRA wanawasumbua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa masoko hasa ya nje bado ni kikwazo kwa wajasiriamali na wazalishaji wa ndani, ni mkakati gani endelevu wa Serikali kutafuta na kuwaunganisha wazalishaji ambao ni wajasiriamali wetu na masoko ya nje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapo awali ni kwamba Serikali baada ya kutambua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, ndiyo maana tulikuja na suala linaloitwa blue print. Katika mpango huu ambao sasa tuko katika hatua za mwisho za kuandaa mpango wa utekelezaji, ni kwamba taasisi zote za udhitibi ikiwemo TRA, tutaangalia vile vikwazo ambavyo tayari vimeshaainishwa, aidha viweze kuunganishwa na kutozwa na mamlaka moja badala ya kutozwa na mamlaka nyingi nyingi pamoja na kuondoa vikwazo vingine vinavyohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TRA, hivi juzi tu nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Fedha akitangaza kwamba iwe ni marufuku kwa mtu wa TRA kufungia biashara kwa kuweka makufuli, badala yake wazungumze na wafanyabiashara na kuona namna bora ya kulipa kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, katika kutafuta masoko ya nje, napenda tu kuwaambia kwamba kimsingi kupitia taasisi yetu ya TANTRADE, tumekuwa tukifanya maonyesho na kuwashirikisha wafanyabiashara kuwaonesha masoko mbalimbali yaliyopo. Pia na sisi wenyewe tunasaidia kutafuta hayo masoko na kuhakikisha kwamba bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na kiwango na zinafungashwa vizuri ili kuweza kutumika kwa ajili ya soko la nje.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza tunaishukuru sana Serikali wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kutuletea mradi mkubwa sana huu ambao utatusaidia katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu wa Mkoa wa Katavi ni mradi wa mkakati, Mkoa wa Katavi tunataka kujenga bandari na vilevile tunataka standard gauge inafika katika Mkoa wetu wa Katavi. Na mradi huu unaenda kwa kusuasua sana ninavyoongea sasa hivi nilikuwa naongea na Meneja wa TANESCO wa Mkoa wangu wa Katavi mradi unaenda kwa kusuasua, tunaomba tupate majibu mazuri lini mradi huu utaanza na utaisha lini ili kwa manufaa ya wananchi wa Katavi kwa sababu tuna malengo ya kupata viwanda ndani ya Mkoa wa Katavi tumechelewa sana tunataka viwanda ili tuweze kufaidika na Serikali yetu ya Awamu ya Tano? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na vilevile swali langu la pili kwa kuwa Mkoa wa Katavi kuna vijiji vingi sana na umeme wa REA bado haujawafika, ni lini umeme wa REA utatufikia katika vijiji vyetu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika eneo hili napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mradi huu mahususi wa North West Grid. Kwanza ni lini mradi utaanza mradi umeshaanza kupeleka Grid ya Taifa katka maeneo ya Katavi na kwa hatua ya kwanza tumeanza na utekelezaji wa kuutoa umeme wa Grid kutoka Mjini Tabora kama ilivyosoma katika swali la msingi kupitia Ipole, Inyonga na hatimaye Mpanda. Umbali wa takribani kilomita 381 na utekelezaji umeanza na tunatarajia mradi kukamilika kabla ya mwezi Mei mwakani, kwa hiyo wananchi wa Katavi watakuwa wameshapatiwa umeme wa Grid kabla ya mwezi Mei Mwakani huo ni Awamu ya I ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya II, mradi utaanza kutekelezwa kuanzia mwakani mradi ambao unatokea kimsingi Iringa, Mbeya, Sumbawanga na baadaye kutoka Sumbawanga, Mpanda na hatimaye Kigoma umbali wa takribani kilomita 1384 kwa ujumla wake mpaka Nyakanazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu hii eneo hili litaanzwa kutekelezwa kwa maana nyingine mwanzo mwa mwaka lakini utaisha mwaka 2022. Mradi huu ni muhimu sana kwa sababu unaunganisha kati yetu na nchi ya Zambia kwa umeme wa kilovoti 400 na umeme utakapopatikana maeneo ya Katavi wananchi wa Katavi wataweza sasa kufanya shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wa Katavi wavute subira mradi wakati unatekelezwa na utakamilika kama nilivyotaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili kuhusu vijiji ambavyo havijapata umeme katika Mkoa mzima wa Katavi. Mkoa wa Katavi bado vijiji 132 havijapata umeme na vijiji vyote tumeviingiza kwenye mpango wa REA Awamu ya II unaoanza mwezi Februali hata hivyo vile vijiji ambavyo vinatekelezwa na mkandarasi kwa sasa vitakamilishwa vyote ifikapo mwezi Aprili mwaka huu 2020.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mahitaji ya walimu wa sayansi ni makubwa sana na ukizingatia wananchi ambao tunaishi pembezoni unakuta shule moja kama Rungwa Sekondari pale Mpanda ina watoto 1,150, walimu wa sayansi kuanzia Form One mpaka Form Six walimu wako wanne tu. Na ukiangalia sehemu nyingine kama Usevia shule Form One mpaka Form Six walimu wawili.
Je, Serikali itatuletea lini Mkoa wa Katavi walimu kwa sababu tunahitaji sana walimu kutokana na uhitaji wa wanafunzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili,kwa kuwa Serikali ilifanya kazi kubwa ya kuhamasisha kujenga maabara katika shule zote za Kata nchini, na wananchi walihamasika sana wakajenga maabara na maabara zile zimekamilika lakini walimu wa sayansi hakuna kabisa.
Je, lini Serikali itaweka mikakati maalum kama ilivyofanya kuhamasisha kujenga maabara ili tuweze kupata sasa walimu wa sayansi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza ninampongezasana Mheshimiwa Mbunge Anna Lupembe kwa kuendelea kuwasemea watu wake wa Mkoa wa Katavi ili waweze kupata elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tuna changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi na hasa katika masomo ya sayansi na hisabati. Vilevile Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kuongeza juhudi ya kutafuta fedha ili tuweze kuajiri walimu hawa wakasaidie kuondoa changamoto ya walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwataarifa tu mwezi Mei mwaka huu Serikali ilipeleka fedha za EP4R motisha ili moja, zikamalizie maboma ya shule za msingi na sekondari, pili ilikuwa ni ku-balance ikama katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaelekeze Waheshimiwa Wakurugenzi katika Halmashauri zetu na Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya, zile fedha za Serikali ilikuwa ni kuangalia kama kuna shule moja ina upungufu, shule nyingine ina walimu wa ziada, ilikuwa ni kuwahamisha kutoka eneo moja kwenda lingine ili kuweza ku-balance Ikama na kupunguza changamoto ya Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama nilivyosema katika maswali yaliyopita leo asubuhi, tumeshaomba kibali cha kuajiri walimu hawa, zaidi ya 15,000. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na maeneo mengine ya pembezoni, tutakapopata kibali cha kuajiri walimu wa sayansi na hisabati, maeneo ya pembezoni yatakuwa kipaumbele, tutaanza na maeneo ambayo yana upungufu mkubwa wa walimu kwenda pale ambapo pana upungufu ambao siyo mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia maboma ya maabara zetu. Ni kweli, tumekubaliana tunagawana kazi, Waheshimiwa Wabunge, Serikali na wadau mbalimbali wa elimu na maendeleo.Kazi ya kumalizia maboma haya ya maabara ni ya kwetu sote kama nilivyotaja. Serikali tumejipanga, hapa tulipo tupo kwenye manunuzi, wakati wowote kuanzia sasa taratibu za manunuzi zitakamilika tutapeleka vifaa katika maabara zetu. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine tuendelee kuchangia kwa namna mbalimbali tumalizie maboma yetu, vifaa tutapeleka, wataalam tutapeleka na hii changamoto hatimaye itaisha ili watoto wetu waweze kusoma katika mazingira ambayo ni rafiki. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika ni jiografia yake ni ngumu sana na Makao Makuu ya Wilaya yako Majalila, lakini OCD anakaa Mishamo na ukizingatia jiografia ile ni pana sana, watu wa Karema wanashindwa kwenda Mishamo.
Je, Serikali itaweka mikakati gani kuhakikisha basi kile kituo cha polisi hata kama bado fedha hazijapatikanika, lakini kituo kiwekwe center ili watu wote katika Wilaya ile waweze kujua kituo chao cha polisi kiko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na jiografia mbaya ya Wilaya ya Tanganyika, je, ni lini Serikali itatuletea magari ya polisi kwa ajili ya patrol kwa sababu kuna misitu mingi, mikubwa sana katika wilaya ile, sasa majambazi wako wengi na uhalifu unafanyika mara kwa mara. Serikali itatuletea lini magari kwa ajili ya patrol ya Wilaya yetu ya Tanganyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hoja ya Mheshimiwa Lupembe ni ya msingi, na kwa kuzingatia msingi wa hoja yake, sasa tutalifuatilia kwa karibu tuone lile eneo ambalo Halmashauri imekusudia kulitenga kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, liwe Majalila kama ambavyo amependekeza ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya. Sambamba na ule ujenzi wa nyumba nne ambazo mchakato wake unaendelea wa ujenzi katika eneo hilo la Wilaya ya Tanganyika, liende sambamba pamoja na rai ambayo Mheshimiwa Mbunge ametoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusianana na magari nayo, kwa sasa hatuna magari mapya ambayo yameingia, lakini kwa kutambua umuhimu wa jiografia ya Tanganyika kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, basi suala lake tumelichukua na pale ambapo magari yatapatikana basi tutazingatia.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika mimi nasikitika sana, kata hii ina vijiji 16 hakuna mawasiliano kati ya kijiji hiki na kijiji kingine. Madaraja yote yamekwenda na maji, mito na barabara zote zimeunganika. Wananchi wa Kata ya Katumba wanapata shida sana. Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara za wananchi wa Kata ya Katumba? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Naibu Waziri yuko tayari kwenda na mimi tukimaliza tu Bunge tukatembelee Kata ya Katumba yenye vijiji 16 ili aone uhalisia wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna changamoto ya barabara katika Halmashauri ya Nsimbo na katika kata hii husika, lakini Serikali katika bajeti ya Wilaya ya Nsimbo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ya shilingi milioni
556 tayari shilingi milioni 148 sawa na asilimia 27 zimekwishapelekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa ajili ya kutekeleza miundombinu ya barabara ambazo zinaunganisha vijiji husika.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza Serikali inatambua changamoto hiyo na ndio maana imepeleka fedha kiasi hiki kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo na madaraja hayo na nimhakikishie kwamba utaratibu wa kuendelea kupeleka fedha nyingine kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika Halmashauri ya Nsimbo na katika vijiji hivi vya kata hiyo unakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba, niko tayari baada ya shughuli za Bunge kwenda naye katika Halmashauri hiyo kupitia vijiji hivyo ambavyo vinahitaji matengenezo ili tuweze kuongeza nguvu pamoja na kuondoa changamoto za wananchi. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi tena niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Kijiji cha Matandarani hakina kabisa hata kisima kimoja na wananchi wanakunywa maji machafu siku zote; na kwa kuwa, mradi huu mpaka sasa hivi una asilimia 10 tu na mradi huu ni wa muda mrefu ambapo wananchi wanauona, lakini juhudi ambazo zinatakiwa zifanyike hazipo: Je, lini mradi huu utakwisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, vijiji vyote ambavyo amevitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ni kweli havina maji kabisa: Mtisi hakuna maji kabisa, ukienda Kijiji kinachofuata cha Magula hawana maji kabisa; na huu mradi mmesema unaenda mpaka Ibindi, kata jirani, nako hakuna maji kabisa: Je, Serikali ina mkakati gani kupitia hii miradi na kuhakikisha inakwisha kwa haraka kwa sababu, wananchi wanapata taabu sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, amekuwa mfuatiliaji wa karibu sana katika suala hili la tatizo la maji katika maeneo haya ya Vijiji vya Matandarani, Ibindi, Mtisi na Magula.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kupitia jitihada zake, mimi binafsi kama Naibu Waziri ninakuhakikishia mara baada ya hili Bunge tutakwenda pamoja mpaka kwenye mradi huu. Usanifu wa mradi huu unatuonesha utakamilika mwezi Septemba. Hata hivyo, tutajitahidi kwa hali na mali tufanye kazi hii usiku na mchana na kurejesha muda nyuma ili mradi huu sasa usiishe Septemba, basi tujitahidi hata ikiwezekana uishe kabla ya usanifu muda unavyoonekana. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Hii Kata ya Ugalla na huo mradi anaosema umeanza mwezi Machi, lakini hakuna dalili yoyote ya mradi, hakuna kitu chochote; na wananchi katika kata hiyo wamesubiri kwa muda mrefu, ni kata; kuna Kata ya Litapunga na Ugala wana miaka mingi wanaona wenzao wanapata umeme lakini wenyewe hawajawahi kupata umeme wala dalili ya nguzo hamna, lakini hapa ameniambia kuwa mwezi Machi mradi umeanza. Sasa hapo kidogo napata wasiwasi kwa sababu hamna dalili kabisa, hakuna dalili ya umeme. Sasa naomba basi Naibu Waziri aji-commit twende akaone ili ajue hali halisi ya wananchi kwa jinsi wanavyopata tabu.
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; wananchi katika vijiji vingine wanalipia umeme Sh.27,000, lakini wanachukua muda mrefu sana miezi sita, saba mpaka nane hawaingiziwi umeme, basi Waziri atueleze wakilipa inachukua muda gani ili wananchi wanaweza kupata umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Lupembe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa upelekaji umeme wa awamu ya tatu, mzunguko wa pili, ulisainiwa na kuzinduliwa rasmi mwezi Machi na hatua kwa hatua zimekuwa zikianza sehemu moja moja kuendelea. Kwa mfano Mtwara wameendelea, Jumamosi iliyopita Mheshimiwa Waziri alizindua tena Arusha, kwa hiyo kufikia Disemba mwakani ndio maeneo yote yatakuwa yamekamilika. Kuna maeneo mengine yameshaanza, mengine bado yanaendelea, lakini hatua za kupeleka nguzo zimeanza. Kwa hiyo uzinduzi ndio ulikuwa mwezi Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo mengine kama alivyosema kwake, watu wanapolipa umeme zinachukuliwa zile hatua sasa za kupeleka vifaa mbalimbali kwa wale wananchi waliolipia kama nguzo kama waya kwa pamoja ili sasa tuweze kufunga kwa pamoja. Hata hivyo, tunachofanya tunaweka utaratibu angalau tuseme ndani ya mwezi mmoja, kila mtu aliyelipia umeme awe ameupata kulingana na mazingira aliyokuwa nayo. Pengine kwenye three phase inachukua hadi pengine siku 90, lakini tumekuwa tukijitahidi kuhakikisha kwamba kila aliyelipia umeme anaupata na anaupata kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake la msingi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli utelekezaji wa mradi kambambe wa awamu ya tatu, round ya pili umeanza rasmi toka mwezi Machi mwaka huu na wakandarasi wote wameshakwenda site. Kesho tuna mkutano wa wakandarasi wote hapa Dodoma, kuwaarifu watoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani katika maeneo yao. Kwa hiyo inawezekana Mheshimiwa Mbunge kweli hajakutana nao, lakini wameshaanza kazi rasmi na wanakwenda kila eneo kwenye maeneo ambako wamepangiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, nitoe taarifa tu kwa wakandarasi kupitia Bunge lako Tukufu kwamba, wakandarasi wote wakaripoti kwa Waheshimiwa Wabunge wanapoingia katika maeneo yao ili Waheshimiwa Wabunge wapate taarifa hizo. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri, lakini kwa kuwa mtendaji ni mmoja na watendaji wa vijiji wako wawili tu, kata ni kubwa, ina vijiji 16: Ni lini Serikali itaongeza watendaji kwa ajili ya kata hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kutokana na mazingira magumu ya kata hiyo, vijiji 16 na mazingira magumu: Ni lini Mtendaji wa Kata ya Katumba anaweza kupata usafiri kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua kwamba kata hii ni kubwa, ina vijiji 16 na inahitaji nguvu zaidi kwa watendaji wa kata kuhakikisha kwamba wanatoa huduma na pia watendaji wa vijiji. Naomba nilichukue jambo hili, tutalifanyia kazi na nitawasiliana naye kuhakikisha kwamba kata hii inaongezewa nguvu ya watendaji. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Hiki Kijiji cha Kanoge hata kwenye ramani ya REA hakipo, pamoja na vitongoji vyake. Sasa ninaomba uhakika kwa sababu nimetokea huko hata kwenye ramani ya REA, ina maana kijiji hiki ni kijiji cha siku nyingi, kilirukwa sasa naomba commitment ya Wizara. Ni lini kitawekwa kwenye ramani pamoja na vitongoji vyake na wataingia katika mchakato wa kuwekewa umeme?
Mheshimiwa mwenyekiti, la pili, katika Kijiji cha Usense Kata ya Ulwira pamoja na Kijiji cha Nyamasi, Kata ya Ugala mpaka leo miti inaoza hasa naomba commitment ya Wizara;
Je, ni lini vijiji hivyo vitapata umeme, kwa sababu hakuna dalili kabisa ya kupatiwa umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Lupembe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kabla ya mwaka huu kuisha, vijiji hivyo alivyovitaja ambavyo vinaonekana havijafikiwa na huduma ya umeme, vitakuwa vimefikiwa kwa sababu kwenye mkataba wetu tumekubaliana kabla ya Desemba mwaka huu vijiji hivyo viwe vimepata umeme na zile changamoto tulizokuwa nazo tayari tumezitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la kwanza naomba nikitoka hapa nitawasiliana nae kwa sababu sisi taarifa tulizo nazo kutoka site ni hizi. Kwa hiyo tutakaa pamoja ili tuweze kuziweka pamoja. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba baada ya mradi wa REA-3 awamu ya pili kupita hatutarajii kuwepo na kijiji chochote ambacho hakina umeme; na hayo ndio maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo tutahakikisha rekodi zetu zinakaa sawa ili kila kijiji kiweze kuwa kimepata umeme kwa kadri ya mkataba na maelekezo yaliyopo.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunpa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi hawa wamesubiri muda mrefu, wamepisha barabara hii takribani sasa tokea 2012 ina maana sasa hivi takribani miaka 11 mpaka leo hawajapata fidia zao na kuna wengine wamefariki. Je, kupitia hii kero Waziri yuko tayari kuja kuzungumza na wananchi wa Kata ya Sitalike?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hii imekwisha kuwa shida. Je, Serikali inajipangaje sasa kupitia tatizo hili la fidia kuhakikisha kabla hawajawatoa watu wahakikishe wamewalipa kwanza ili isiwe kero kupitia Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo yote kwa pamoja kwa ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la fidia hasa kwa mita 7.5 limekuwa linajitokeza mara kwa mara, na mimi napenda tu nitumie nafasi hii kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba hii ni Sheria ya kuongeza upana wa barabara kutoka Mita 45 kwenda mita 60 ya mwaka 2007. Kufanyika huku kulikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na hifadhi kubwa ya barabara ili tunapotaka kufanya shughuli zozote ikiwa ni pamoja na kuongeza upana wa barabara ama kupitisha mifumo mingine yote iwe ya maji, ya mikongo ya mawasiliano tuweze kuwa na hifadhi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na hifadhi kubwa ya barabara ili tunapotaka kufanya shughuli zozote, ikiwa ni pamoja na kuongeza upanda wa barabara, ama kupitisha mifumo mingine yoyote iwe ya maji, na mikongo ya mawasiliano, tuweze kuwa na hifadhi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tutakuja na taarifa sahihi ya utaratibu ambao tutaufanya kwa sababu ni nchi nzima ambapo tumeongeza huo upana wa barabara, namna bora na sahihi ya kuweza kuchukua hayo maeneo na kuwalipa fidia, ama kama kutakuwa na maelekezo mengine ambayo Serikali itakuja kuyatoa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Anna Lupembe pamoja na Wabunge wengine wote ambao wana changamoto hizo kwenye majimbo yao kwamba, Serikali itakuja na utaratibu mzuri wa namna bora ya kufidia wananchi ambao barabara imewafuata, ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya ucheleweshwaji wa mradi huu masika ikakuta mradi umecheleweshwa na mvua za masika, lakini Mkandarasi alichukua muda mrefu sana kuingia site katika kujenga mradi huu na mradi huu unajengwa na Wizara, haushirikishi Halmashauri ambayo wako katika eneo husika la mradi.
Je, Serikali ina mkakati gani kushirikisha kwa ukamilifu Halmashauri ya Nsimbo ili kuendelea kusimamia mradi huu?
Swali la pili, Serikali inachelewesha malipo ya Mkandarasi, Mkandarasi anashindwa kutekeleza mradi kutokana na kukosa kulipwa pesa. Je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi pesa zake ili aweze kukamilisha mradi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza miradi hii ni miradi ya Serikali, haijalishi mradi unatekelezwa na Wizara ama unatekelezwa na Halmashauri, miradi hii yote ni ya Serikali. Miradi hii inapokuja huku kwenye Halmashauri maana yake mamlaka zote za Serikali zinapaswa kushiriki katika kutekeleza mradi huo, kwa sababu miradi hii haimaanishi kwamba inapojengwa na Wizara ni kwamba Serikali nyingine haihusiki, Hapana! Sasa hii ni dhana ya uelewa katika Halmashauri zetu kwamba miradi inapokuja kwa namna moja au nyingine ni lazima watumishi wa Halmashauri washiriki kwa namna moja ama nyingine katika kusimamia mradi huo ili kuleta tija na ubora wa miradi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua namna ya ucheleweshaji wa malipo. Malipo ya Serikali yoyote yanalipwa kulingana na certificate ya utekelezaji wa mradi alipofikia huyo Mkandarasi. Serikali inalipa fedha kutokana na certificate alizo-raise ambazo zinatokana na kazi aliyoifanya kwa kiwango hicho na huyu mkandarasi mpaka sasa ameshalipwa zaidi ya asilimia 70 ya malipo yake kwa sababu jumla ya shilingi milioni zaidi ya 270 amekwishalipwa kati ya milioni 510.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mkandarasi huyu anakwenda vizuri na ukiona mradi unachelewa ni kwa sababu ya upatikanaj wa fedha lakini ni pamoja na kwamba kazi anayoifanya ndiyo itakayo-determine analipwa fedha kiasi gani, kwa hiyo, huyu analipwa kulingana na kazi anayoifanya. Naomba kuwasilisha.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwakunipa nafasi niulize swali. Naomba niulize swali moja ni lini Skimu ya Usense itakamilika Kata ya Ulurwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba tu nimuhakikishie Mheshimiwa Anna Lupembe kwamba kwa kuwa ujenzi unaendelea. Sisi tutakachohakikisha ni kum-push Mkandarasi aweze kukamilisha kwa wakati mradi huo kama ulivyopanga, ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini mkandarasi huyu ambaye alikuwepo kwenye Skimu ya Usense hakushindwa kujenga skimu ile ila pesa hakuweza kupatiwa kwa wakati na tukakatisha mkataba wake na Sasa hivi tupo kwenye mchakato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzoefu wa skimu zingine kama kwenye Jimbo langu kuna Skimu ya Ughala ilikuwa hivyo hivyo tulipoteza bilioni moja na sasa tumepata hofu kupitia hii skimu; je, kutokana na huo mchakato mpaka sasa hivi umechukua muda mrefu takribani miaka miwili, ni lini utakamilika na lini ujenzi utaanza mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kutokana na wananchi wanahamu ya kulima kupitia skimu hii ambayo mlitupangia takribani milioni 700; je, kutokana na ucheleweshaji Mheshimiwa Waziri yupo tayari kwenda na mimi kuhakikisha na kuona uhalisia wa hizi skimu zote mbili, Skimu ya Usense pamoja na Ughala?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nsimbo kwamba mradi wake kama ambavyo ipo katika mchakato, hii mchakato tuliopo sasa hivi wa upembuzi yakinifu, ninaamini tutaumaliza kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha na mradi huu tutauweka katika mwaka wa fedha unaokuja ili uanze utekelezaji wake ili wananchi wa Jimbo la Nsimbo waweze kupata hiyo faida lakini kwenda na yeye nipo tayari muda wowote tukashuhudie hicho ambacho Mheshimiwa Mbunge amekieleza.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Barabara ya Kawejense – Ugalla mpaka Kaliuwa itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara hii tayari tumeshaanza kuijenga na kwa kipande tumeshaanza kwanza kujenga madaraja kabla hatujalifikia Daraja la Mto Ugalla ambao tuna uhakika hatuwezi tukalifikia mpaka kwanza tujenge madaraja unganishi. Tukishakamilisha tutakamilisha usanifu pia upande wa Tabora ili kuijenga barabara yote.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini zitaletwa fedha awamu ya pili katika Kituo cha Afya cha Itenka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba Kituo cha Afya cha Itenka ambacho kipo katika Jimbo la Nsimbo ni kituo ambacho pia kinahitaji fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshaweka mkakati, baada ya ukamilishaji wa hospitali za halmashauri, tutakwenda kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi, ahsante sana.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa, Kata hii ina vijiji 10 na hakuna mawasiliano kabisa na kwa wakati huu mawasiliano ni biashara na katika shughuli mbalimbali watu wanawasiliana na sasa hivi mkataba umeenda kwenye vijiji viwili. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika vijiji nane vilivyobaki?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa sababu mradi huu wa Vijiji viwili Kaguzi ‘A’ na Kaguzi ‘B’ umechukua muda mrefu, sasa hivi takribani tunaelekea mwaka mzima mradi ule haujakamilika kabisa wala haujajulikana utaanza lini. Je, Waziri yupo tayari kuambatana nami ili aende kuhakikisha na kuona uhalisia wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Anna Lupembe kwa kufuatilia hili na niseme tu kama yeye alivyosema ni mradi ambao sasa hivi umeshaweza kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja na mkataba uliosainiwa ni miezi 24. Kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi huu utatimia ndani ya wakati na nipo tayari kuambatana naye baada ya Bunge hili kwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika vijiji hivi 10 mara baada ya mchakato kukamilika na niwasihi wenzetu wa mamlaka zinazoshughulikia vibali, kuhakikisha suala hili linapata utekelezaji wake kwa haraka ili huu mnara katika vijiji hivi kumi uweze kutekelezeka.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri, lakini nina maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, daraja hili ni muhimu sana kwa wananchi wa Kata ya Itenka. Mashamba na shughuli zao zote za kijamii ziko ng’ambo ya mto na kipindi cha masika hakuna watoto wala wananchi wanaokwenda kufanya shughuli zao za kijamii. Je, ni lini Serikali itajenga daraja hili ili wananchi wa Itenka waweze kupata maisha mazuri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri, je, yuko tayari Bunge hili likiisha twende naye Itenka ili akaone uhalisia na shida ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maana anapigania maslahi mapana ya wananchi wake. Naomba nimhakikishie kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa daraja hili kuichumi na kijamii. Ndiyo maana Serikali imechukua hatua ya kufanya mapitio ya usanifu ili daraja litakapojengwa liwe la kudumu na liwe lina ubora ambao utakuwa ni wa muda mrefu zaidi na utawasaidia wananchi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mara baada ya mapitio ya usanifu kukamilika, Mwezi wa Tisa, taratibu za ujenzi zitaanza. Kwa hiyo, katika mwaka huu wa fedha, daraja hili litajengwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge. Tayari tulishanong’ona na ameshaniomba niweze kwenda kutembelea katika jimbo lake, niweze kwenda kujionea uhalisia katika eneo hili la Kata ya Itenka. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nipo tayari, tutakaa na tutakubaliana ratiba ili niweze kufika katika eneo hili.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa hili swali ambalo limejibiwa.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Itenka sasa hivi kina takribani ya miaka miwili na kila siku tukiuliza kuhusu fedha zilizobaki kwa sababu tuliahidiwa milioni 850, lakini mpaka sasa hivi zimeletwa milioni 480, kiasi ilichobaki ni kingi. Wananchi wa Itenka wanatamani sana ile hospitali iweze kukamilika.
Je,ni lini Serikali itaweza kukamilisha? (Makofi)
Katika Kata ya Ugala kuna Kituo cha Afya, nacho tuliahidiwa milioni 850 mpaka sasa hivi zimekuja milioni 500. Je, ni lini Serikali wataleta fedha za Kituo cha Afya cha Ugala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninampongeza Mheshimiwa Mbunge Mama Anna Richard Lupembe amefuatilia kwa karibu sana kuhusiana na fedha za awamu ya pili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Itenka na Ugala. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati wa ujenzi huo wa vituo hivi vya afya tuliweka mpango wa kujenga vituo hivi kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza tulipeleka milioni 500 kwa vituo vyote kote nchini na imekamilika majengo yale matano ya awamu ya kwanza. Awamu ya pili tutakwenda pia kwa vituo vyote ambavyo vimekamilika awamu ya kwanza kwa ajili ya majengo mengine kama wodi za wanaume, watoto na wanawake kawaida. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, vituo hivi viwili ambavyo vimeshapata fedha za awamu ya kwanza, tutakamilisha kwanza majengo ambayo hayajakamilika ya awamu ya kwanza na baadae tutaingia kwenye awamu ya pili na nimhakikishie kwamba, tutapeleka fedha kwa ajili ya kazi hiyo, ahsante. (Makofi)