Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile (208 total)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa, Serikali imeona umuhimu wa kufufua na kurejesha majengo ya maendeleo ya jamii. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata wataalam wa kutosha ili kuhudumu katika majengo hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, hali ya maisha imebadilika sana na wananchi wengi wana msongo wa mawazo na matatizo mbalimbali, mfano, masuala ya ukatili, hivyo wanahitaji wataalam wa unasihi na nasaha. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka muda maalum ili kuharakisha Halmashauri zote nchini zifufue majengo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi katika Sekta nzima ya Maendeleo ya Jamii na hivi sasa tuna upungufu wa asilimia takribani 61. Hata hivyo, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili katika mafunzo ya watumishi katika sekta hii, mpaka sasa hivi tumeongeza udahili kwa kiasi kikubwa sana. Lengo ni kuhakikisha kwamba sasa huu upungufu tulionao tunaweza tukapata watumishi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba, kutokana na kuonekana kuna wananchi wengi sasa hivi wamekuwa na msongo wa mawazo, tunapokea ushauri huu nasi katika sekta ya afya tutaangalia njia nzuri zaidi ya kuweza kulifanyia kazi jambo hilo.(Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize swali dogo tu kuhusiana na idara hii ya maendeleo ya jamii.
Kwa kuwa, idara hii ya maendeleo ya jamii ni muhimu sana katika Vijiji, Kata na Halmashauri zetu kwa ujumla, lakini unakuta idara hii haijaimarishwa na kwa muda mrefu Maafisa Maendeleo wamekaa katika sehemu moja kwa miaka mingi na bila nyenzo za kufanyia kazi. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuimarisha kitengo hiki na kuwasaidia Maafisa Maendeleo ya Jamii ili wafanye kazi yao ambayo sasa hivi tunavyoingia katika viwanda ndio watasaidia sana kuhamasisha wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mchango mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii hususan katika kuhamasisha na kufua hali ya wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya hapo awali ni kwamba Serikali inatambua suala hili na kupitia Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1997, tumesisitiza kwanza kuweka msisitizo katika masuala mazima ya udahili; pili. kuweka msukumo sasa katika kupitia Serikali kuu na katika Halmashauri zetu kuweka msisitizo katika kuhakikisha kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapata kipaumbele na wanaajiriwa ili waweze kwenda kuhudumu katika Halmashauri zetu. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nami niulize swali la nyongeza kuhusiana na masuala ya matumizi ya Maafisa Maendeleo ya Jamii na nipendekeze kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, vilevile kuna kundi zima la vijana wengi wanaomaliza shule kuanzia Darasa la Saba, Kidato cha Pili, Kidato cha Nne mpaka Kidato cha Sita. Je, kuna uwezekano wa kuwatumia hawa kuwapa mafunzo ili watumike katika Vijiji vyao kama Maafisa Maendeleo ya Jamii hata kama ni Para Community Development Officers wa kufanya uraghibishi wa aina mbalimbali ili waweze kusaidia katika nguvu ya maendeleo ya jamii yaliyopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Janeth Mbene ametoa ushauri kwa Serikali kwamba kwa sababu sasa hivi tunaelekea Tanzania ya viwanda na tuna changamoto kubwa sana ya vijana ambao hawana ajira; mawazo yake tunayapokea, tutaenda kuyafanyia kazi na kuangalia jinsi gani ya kuweza kuwashirikisha vijana katika kuleta maendeleo. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa sababu kampeni ilizinduliwa tangu mwaka 2016 mpaka leo ni mikoa mitano tu na maeneo mengi yaliyofikiwa yana hospitali kubwa kama Muhimbili, KCMC, sasa ni lini kampeni hiyo itafika katika Mkoa kama wa Singida, Wilaya ya Mkalama na mikoa mingine maeneo ya vijijini kwa sababu vifo vinaendelea kutokea kwa kasi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali itawathibitishia vipi Watanzania, wakiwemo wananchi wa Mkalama, kwamba Serikali inagharamia matibabu kufuatia jibu la Waziri, kwa sababu mimi ni mhanga, mwananchi…
Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itawathibitishia wananchi kugharamia matibabu ya kansa? Mkalama kuna mwananchi amepoteza maisha kwa kukosa dawa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tumetengeneza ratiba. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, muda utakapofika kwa Mkoa wa Singida nimwombe atoe ushirikiano ili zoezi hili liwe la mafanikio.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili ambalo lilikuwa linauliza Serikali imejipangaje kuhusiana na masuala ya upatikanaji wa dawa; napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali katika mwaka huu wa fedha imeongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni 30 mpaka zaidi ya bilioni 260.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia, hadi hivi sasa, hali ya upatikanaji wa dawa za kansa ni zaidi ya asilimia 80 na vilevile, hospitali kama ya Ocean Road imefungua dirisha la dawa ambapo dawa nyingine ambazo hazipatikani pale zinapatikana kwa gharama nafuu kuliko katika maduka mengine ya dawa.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tatizo la Iramba Mashariki linafanana kabisa na matatizo ambayo yako katika Mkoa wa Katavi. Uhaba wa Madaktari Bingwa katika Mkoa wa Katavi umekuwa ni changamoto kubwa sana, kwa mfano katika Kata za Mishamo, Chamalendi, Kakese pamoja na Mwamkulu, ni maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za Madaktari na wanapopewa rufaa kwenda katika Mikoa ya Mbeya pamoja na Dar es Salaam inawagharimu gharama kubwa za kuishi pamoja na za madawa. Sasa nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanaharakisha tunapata Madaktari Bingwa katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nakiri kwamba tumekuwa na changamoto kidogo katika upatikanaji wa Madaktari Bingwa, lakini hivi karibuni tumepata kibali cha kuajiri wataalam wapya wa afya na Mkoa wa Katavi ni mmoja k atika mikoa ambayo imepata Madaktari hao.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika kipindi cha mpito, tumeongeza udahili katika fani za Madaktari Bingwa, lakini vilevile tumekuwa tunaendesha mobile clinics kwa ajili ya kuwapeleka wale wataalam wachache katika mikoa iliyo pembezoni kwa ajili ya kupata huduma hizo.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo yanaridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wako wafanyabiashara wanaendelea kuingiza na kufanyabiashara ya vipodozi hivi ndani ya nchi na vipodozi hivi vinawapatia madhara wananchi wetu kwa kiwango kikubwa sana, wanapata maradhi makubwa kutokana na vipodozi hivyo. Je, Serikali yako inatoa kauli gani iliyokuwa kali kuhakikisha hawa wafanyabiashara hawatoingiza wala hawafanyi tena biashara ya vipodozi hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina mkakati gani wa kuwasidia wale watumiaji ambao wametumia vipodozi hivi bila kuvitambua kurudi katika hali yao ya kawaida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo. Niendelee tu kusisitiza kwamba Serikali inaendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vyake kama nilivyoainisha hapo awali, tunaendelea kuboresha maabara zetu, lakini vilevile sasa hivi nimezungumzia kifungu cha adhabu tunafikiria kukiboresha zaidi ili kutoa adhabu kali kwa wale ambao wanaingiza vipodozi haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili lilikuwa linauliza je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wahanga wa vipodozi vilivyo chini ya viwango. Kwa sasa hivi Serikali hatuna mkakati wowote wa kuwasidia wale wahanga, lakini tunachokifanya ni kutoa elimu ya kutotumia vipodozi ambavyo havijasajiliwa nchini. Vilevile tunashirikiana na mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na TFDA, Polisi na Halmashauri kubaini vipodozi ambavyo vimeingia nchini kinyume cha taratibu na kuvikamata na kuchukua hatua stahiki kwa wale ambao wanahusika.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sambamba na vipodozi hivyo, pia kumekuwepo na wimbi la baadhi ya akina dada na akina mama kutumia sindano za kuongeza sehemu za maumbile yao kama vile makalio na maziwa. Je, nyongeza hizi za maumbile yao zina athari yoyote kiafya na kama zinayo Serikali inatoa tamko gani? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu alituumba kila mtu kwa aina yake, kwa rangi yake na maumbile yake. Nyongeza hizi kitaalam zina madhara kama vilivyo vipodozi haramu. Ngozi ina matumizi yake, Mwenyezi Mungu hakuiweka pale kwa makosa, inatusaidia sisi kwanza kujikinga na mionzi na magonjwa. Kwa hiyo, matumizi ya vipodozi moja, yanaleta madhara katika ngozi lakini pili yanaweza kupelekea mtu kupata saratani sambamba na hizi sindano na dawa nyingine za kuongeza maumbile zina madhara makubwa kwenye mwili. Kauli yangu kwa wananchi, tuache kutumia vipodozi na madawa haya, Mwenyezi Mungu alituumba na makusudio yake tuendelee kuishi kwa maumbile na rangi zetu. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mashaka na madhila yatokanayo na matumizi ya vipodozi hatarishi yanazidi kuwaathiri wananchi wetu waliokuwa wengi, japokuwa Mheshimiwa Waziri umegusia kama mtatoa elimu, lakini nataka kujua kuna mkakati gani madhubuti kwa elimu hii ya umma ili wananchi hawa wafahamu na wasiweze kutumia vipodozi hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali iwe na mkakati wa kuwawajibisha na kuwalazimisha kulipa gharama za tiba kwa maradhi yanayosababishwa na matumizi ya vipodozi hivi kwa vile kila siku tunaambiwa tusitumie na wao hawasikii. Kwa hiyo, sehemu ile ya tiba walipe wale kwa sababu Serikali ina maradhi mengi sana ya kushughulikia, lakini bado…
inashughulikia maradhi ya makusudi ya kutafuta weupe. Kwa hivyo, Serikali ina kauli juu ya hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Asha Mshua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza mkakati wa kutoa taarifa na elimu katika vyombo vya habari, mihadhara, matangazo ya redio, mafunzo kwa njia ya mada, maonyesho pamoja na huduma kwa wateja.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 tumeweza kutoa elimu kwa wanafuzi 73,323 katika vyuo saba na shule za sekondari 170 katika mikoa yote 21 nchini. Nitaendelea kusisitiza kwamba tunapokea ushauri wako Bi. Mshua na tutajaribu kuzingatia wakati tunafikiria kuongeza adhabu zinazohusiana na uingizaji na matumizi ya vipodozi haramu.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia sugu ya wazazi hasa wababa kutelekeza watoto na kuwaachia akina mama walee watoto hao peke yao.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudumu wa kuyapa nguvu Madawati ya Jinsia na Mabaraza ya Usuluhishi katika kata zetu ili waweze kuweka sheria ngumu ambayo itawafanya wababa hawa wasiweze kutelekeza watoto wao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kuzileta Bungeni Sheria za Ustawi wa Jamii ili tuweze kuzibadilisha kama siyo kuziondoa zile za zamani ili ziweze kuendana na hali ya maisha ya sasa? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga kwa maswali yake mazuri, lakini vilevile kuwa mtetezi mzuri wa haki za watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali imeandaa na kuzindua Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Jinsia dhidi ya akina Mama na Watoto wa mwaka 2017/2018 na utaisha mwaka 2020/2021. Sambamba na hilo, utekelezaji wake umeshaanza kwani hivi tunavyoongea sasa hivi tumezindua madawati 417 katika vituo vyetu vyote vya polisi ambavyo vinasimamia masuala yote yanayohusiana na ukatili wa kijinsia kwa akina mama na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, sasa tunakwenda mbali zaidi na kwamba tunaanzisha Kamati za Ulinzi wa wanawake na watoto ambapo Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Wajumbe wa Mabaraza watakuwa ni sehemu ya mkakati huo, kuwajengea uwezo, kuwapa elimu kusimamia haki za wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri katika swali lako la pili kwamba viwango vya sasa haviendani na hali halisi, sasa hivi tu katika mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Ustawi wa Jamii ambayo itazingatia hali ya sasa.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa hakuna shaka yoyote chanzo kikuu cha ongezeko la watoto hawa ni kutokana na wanaume wanaoshindwa kutimiza wajibu wao na kuwaachia ulezi wanawake peke yao. Katika Bunge lililopita nilishuhudia binafsi hapa Bungeni wanawake wakileta watoto waliotelekezwa na Waheshimiwa Wabunge. (Kicheko/ Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kupitia Waziri wa Afya, yuko tayari kutoa wito kwa wanawake wote waliotelekezewa watoto na Waheshimiwa Wabunge wawalete hapa na wakabidhiwe majukumu yao? (Kicheko/ Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, shida siyo kuzaa, shida ni matunzo na kulea na mimi nitoe rai kwa wanaume wote pamoja na sisi Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba tunashiriki kikamilifu katika matunzo na malezi ya watoto. Hata hivyo, nataka tujielekeze zaidi katika mfumo wa sheria na kutengeneza mfumo endelevu. Sheria yetu inatutaka twende katika Ofisi za Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zetu badala ya kuwaleta watoto hawa wote hapa Bungeni. (Kicheko)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi nipate kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na tatizo la watoto wa mitaani hasa kwenye miji mikubwa kwa mfano, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na kadhalika na watoto hawa wamekuwa wakitumiwa kwenye masuala ya uhalifu kama madawa ya kulevya na kadhalika. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha watoto hawa wanarudi shuleni na kupata angalau malezi bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tunakiri tumekuwa na tatizo hilo na moja ya jambo ambalo tumelifanya kwanza ni kubaini idadi ya watoto katika hii miji mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika takwimu tulizokuwa nazo sasa hivi katika Mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Dodoma na Arusha tuliweza kubaini watoto 7,748 ambapo 6,365 walibainika kwamba wanashinda mitaani na kurudi nyumbani na watoto 1,383 hushinda na kulala mitaani. Pamoja na juhudi hizo, Serikali kati ya mwezi Julai, 2017 mpaka Novemba, 2017 tuliweza kuwaunganisha watoto 952 na kuwarejesha katika familia zao.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Septemba, 2016 niliuliza swali kama hili na nikatoa utafiti nikampa Naibu Waziri ambao ulionesha Serikali ya Tanzania haijui tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Baada ya kusikiliza majibu ya Serikali, nalazimika kusema kwamba bado Serikali haijalijua kwa undani suala la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Je, ni lini sasa Serikali itaamua kufanya utafiti na kuja kutupa namba sahihi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema kwamba Serikali haijui takwimu sahihi na hapa katika majibu yangu ya swali la nyongeza ambalo lilikuwa limeulizwa na Mheshimiwa Maryam Msabaha nimetoa takwimu naomba nizirudie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mikoa sita ambayo tumefanya ukaguzi kwa maana ya Mkoa wa Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Dodoma na Arusha tumebaini watoto 7,748 kati yao 6,365 walikuwa wanashinda mitaani na kurudi majumbani na watoto wengine 1,383 hushinda na kulala mitaani.
Katika hawa watoto Mheshimiwa Halima Bulembo 952 tumeweza kuwarudisha na kuwaunganisha na familia zao. Kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kusema kwamba Serikali inatambua tatizo hilo na imeshachukua hatua.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya ukatili na unyanyasaji mkubwa wa watoto wa kike ni wa kuwanyima fursa ya kurudi shuleni pale ambapo wanapata ujauzito kwa kuzingatia mazingira mbalimbali ambayo yanapelekea watoto wetu wa kike kupata mimba wakiwa watoto wadogo. Sasa ninatambua kwamba kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na cabinet yake, kuna initiative mbalimbali walizozifanya hali iliyopelekea kuanza utekelezaji wa re-entry policy, kwamba mtoto anapata mimba, anapata fursa ya kurudi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka tu Serikali iniambie, kwa kuzingatia kwamba kama viongozi, tuna wajibu wa kujali mustakabali wa mtoto wa kike; na kwa kuzingatia kwamba katika nchi yetu kuna mazingira mengi ambayo nikiyataja hapa siwezi kuyamaliza, yanayopelekea mtoto huyu kushindwa kusoma na kushindwa kuzuia hivyo vishawishi ama kushindwa kukabiliana na nguvu kubwa za nje ambazo zinamzidi uwezo wake wa akili; ni lini sasa Serikali itafanya utekelezaji wa ile kazi kubwa ambayo mlifanya katika kipindi cha miaka 10 iliyopita mpaka kipindi cha awamu ya Mheshimiwa Jakaya kilipoisha? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji kujua utekelezaji tu.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na maandalizi ya re-entry policy lakini utekelezaji wake sasa umepitwa na wakati kutokana na maagizo ambayo yametolewa na Serikali kwamba mtoto ambaye amepata ujauzito hataruhusiwa kurudi tena katika shule ambayo alikuwa anasoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maagizo haya hayajamzuia mtoto wa kike ambaye amepata ujauzito kutoendelea na masomo. Naomba tuelewane vizuri, imezuia mtoto wa kike kurudi shule ambayo alikuwa anasoma, lakini haijazuia mtoto wa kike kuendelea na masomo. Kwa hiyo, ndani ya Serikali tunajaribu njia mbadala ya kuhakikisha kwamba watoto hawa ambao wamepata ujauzito wanaendelea na masomo.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maelezo yake mazuri kuhusiana na suala la watoto ambao wanapata ujauzito kurudi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kwamba Serikali imekwishaeleza kwamba mwanafunzi anayepata ujauzito hawezi kurudi shuleni, lakini mwanafunzi huyo anaweza akaendelea na masomo kwa kupitia njia mbadala ambazo tuna vituo vya elimu, zipo Taasisi zetu za Elimu ya Watu Wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, msimamo wa Serikali ni kwamba mwanafunzi hawezi kurudi shuleni lakini anaweza akapata masomo kupitia njia mbalimbali ambazo Serikali inazitoa. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la kutelekezwa kwa watoto ni jambo ambalo wanawake/ Wabunge hatuwezi kulifumbia macho; ili kupata uhakika na ukweli kuhusu watoto wanaotelekezwa na Waheshimiwa Wabunge wanaume, kwa nini tusifungue Kituo cha Ustawi wa Jamii hapa ili kuweka mambo sawa? Ahsante. (Kicheko/ Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana suala la utelekezaji wa watoto hapa Bungeni ni changamoto kubwa sana. Naomba nirudie majibu yangu ya msingi kwamba sheria ya mtoto imeweka utaratibu mzuri tu wa kushughulikia mashauri ambayo yanahusu utelekezwaji ama watoto kutopata matunzo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza kwamba madawati yetu ya Halmashauri katika ngazi ya Halmashauri yatumike katika masuala haya.
MHE. RITTA A. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna baadhi ya wazazi au walezi hasa katika Majiji kwa mfano Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakiwatumia watoto wadogo kuomba omba hata kule kwenye magari, tumekuwa tukishuhudia na nimeona katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wazazi kama hao wanatakiwa wachukuliwe sheria/ hatua, kwa sababu watoto hawa wanakosa haki yao ya msingi na wakati elimu ni bila malipo.
Je, ni nani sasa anawachukulia hatua wale wazazi au walezi ambao wanawatumia watoto katika kuomba omba kwenye magari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2008 mtoto hana haki zake kama tano. Mtoto ana haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushirikishwa na pia mtoto hana haki ya kutobaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba mtoto kama nilivyoainisha katika haki zake za msingi, ni jukumu la kwetu sisi wazazi, walezi, jamii na Serikali katika ngazi ya Mitaa na Serikali Kuu kuhakikisha kwamba mtoto anapata haki zake zote hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kabati alikuwa ameelekeza swali lake katika Mkoa wa Dar es Salaam, tuna mikakati mbalimbali ambayo tunaendelea nayo kuhakikisha kwamba watoto wale wa mitaani wanapata haki zao stahili pamoja na kuondolewa katika mitaa.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilitaka kufahamu kutokana na maswali yaliyokuwa yanaulizwa, Mheshimiwa Mbunge aliyeketi muda siyo mrefu ameongea kuhusu Waheshimiwa Wabunge kutelekeza watoto. Sasa nilitaka kuuliza, Waheshimiwa Wabunge hawa wanatelekeza watoto kwa Waheshimiwa Wabunge wenzao ama nje ya Wabunge? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana suala la kutelekeza watoto katika Bunge limekuwa ni kubwa sana. Hili nalirudisha katika kiti chako sasa uweze kuangalia utaratibu mzuri wa kuweza kulishighulikia. (Kicheko)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ingawa hakuwa na takwimu kabisa kwenye eneo la madaktari maana yake amekili upungufu uliopo nilioutaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Geita inahudumia takribani wagonjwa 400 kila siku. Na mwaka jana wakati Waziri wa Afya amefanya ziara kwenye Hospitali hiyo aligundua kwamba mpaka wakati tunatoka kwenye bajeti tulikuawa bado tunaichukulia Hospitali ya Geita kama Hospitali ya Wilaya, haikuwa kwenye Hospitali za Mkoa na ndiyo sababu mpaka leo pale tuna specialist mmoja ambaye ni surgeon hatuna kabisa Physiotherapy Doctor, hatuna mtu wa mionzi, hatuna gynaecologist, hatuna mtu wa usingizi kwa sababu ilikuwa inachukuliwa kama Hospitali ya Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu kwa kuwa tumeongeza vituo vingine vya Nyamkumbu na Kasamba tumejenga theater kwa ajili ya upasuaji na kuna wataalam wengi wamezagaa ambao wanaomba ajira. Ni lini Wizara italeta wataalamu wanaoweza kukudhi kiwango cha Hospitali ya Mkoa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Geita ambapo nimesema hatuna wataalam tuna ujenzi wa Hospitali ya Mkoa baada ya kuchukua Hospitali ya Wilaya ambayo tulifanya kuwa Hospitali ya Mkoa, tunajenga Hospitali y Mkoa, lakini speed ni ndogo. Nini kauli ya Serikali ili kuifanya ile Hospitali ya Halmashauri irudi kwa wananchi na huduma ziweze kupungua gharama yake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ilikuwa ni kuhusiana na idadi ya wataalam. Ni kweli lazima nikiri katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kuna changamoto kubwa sana ya Madaktari Bingwa na hilo sisi tumeliona kama nilivyojibu katika swali langu la msingi. Ni kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba tunafanya training ya kutosha Madaktari Bingwa na pale watakapopatikana basi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tutaipa kipaumbele kuongeza idadi ya Madaktari Bingwa ili waweze kutoa huduma pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake lingine la pili lilikuwa lina husiana na kwa nini sasa Serikali isiongeze mkono wake katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na ile iliyokuwepo pale iweze kurudi kuwa Hospitali ya Wilaya.
Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge ni kwamba mwishoni mwa mwaka jana Serikali ilifanya maamuzi ya kuziondoa Hospitali za Rufaa za Mkoa kutoka ngazi za Serikali za Mitaa na kuzipeleka Serikali Kuu. Jukumu hilo sasa na sisi tumelipokea, tumekabidhiwa rasmi na mimi nimuhaidi tu Mheshimiwa Mbunge sasa na sisi tutajielekeza nguvu zetu kuhakikisha kwamba tunazijenga na kuziboresha Hospitali za Rufaa za Mkoa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba sasa hivi Tanzania kuna dawa hizi ambazo zinaitwa tressa medicines ambazo zinatolewa kwenye Hospitali za Rufaa ama Hospitali za Mikoa tu na kwamba kule vijijini kwenye Zahanati na Vituo vya Afya hizi dawa hazitolewi za magonjwa kama BP, magonjwa HIV, Kifua Kikuu sasa swali langu; nilikuwa naomba kujua kwa sababu wananchi wanapata tabu sana kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta dawa hizi kwenye Hospitali za Mikoa na Hospitali za Rufaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufundisha wale Medical Assistant’s kule vijijini ili dawa hizi ziweze kutolewa kule vijijini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kutoa ufafanuzi, tumapoongelea suala la tressa medicines tuna maanisha kwamba ni dawa zile muhimu na ambazo sisi zina tusaidia katika sekta ya afya kubaini na kuangalia kwamba zile dawa muhimu zipo. Tressa medicines sio dawa ambazo unasemasijui kwa lugha ya kitaalam mnasemaje kwamba ni dawa ambazo ni muhimu ambazo zilikuwa zinatakiwa kutotolewa katika sehemu fulani tressa medicine ni general term ambayo sisi tunaitumia kuhakikisha kwamba tunazibaini na kuzipatia zile dawa muhimu kule ambapo tunazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa labda niendelee kwa kusema kwamba sasa hivi ndani ya Serikali na mwanzoni mwa mwezi huu tumetoa mwongozo wa utoaji wa dawa katika ngazi mbalimbali. Mwongozo huu kwa jina la kitaalam tunaitwa standard treatment guedline hapo siku za nyuma kila ngazi ilikuwa inajitolea dawa holela na kadri walivyokuwa wanaiona. Na hii changamoto tulikuwa tunaipata sana katika Hospitali kubwa makampuni ya dawa yana kuja yanamwambia mtoa huduma andika dawa hii wakiwa wanampa na yeye motisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sisi Serikali tunaagiza dawa nyingi kwa pamoja unakuta sasa mgonjwa anaandikiwa dawa anaambiwa dawa hazipo. Serikali imeongeza sana bajeti ya dawa kutoka bilioni 30 mwaka 2015/2016 kufikia bilioni takribani 270 katika mwaka wa 2017/ 2018 ni zaidi ya mara tisa ndani ya miaka miwili. Kwa hiyo, hali ya upatikanaji wadawa sasa hivi nchini ni nzuri sana pamoja na hizi tressa medicines.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lako lingine la nyongeza ilikuwa sasa kutokana na mwongozo huu, umeweka utaratibu dawa gani kwa ugonjwa gani zitakuwa zinapatikana na kwamba hivyo vituo vya afya vitatakiwa kuzingitia dawa gani na kutoa matibabu kwa kulingana na ule mwongozo wa utoaji dawa ambao kama na sisi Serikali tumetoa. Tunatambua kwamba baadhi ya maeneo ambayo tunachangamoto ya watumishi tunaendelea kutoa mafunzo ili na wale watumishi waweze kutoa tiba kwa wale wagonjwa wanaofika pale ambapo hamna madaktari kwa kuzingatia miongozo ambayo na sisi tutakuwa tumewapa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu haya mfuko huu unatambua tu viongozi na watumishi wa umma, lakini watumishi wa sekta za kisiasa kama Wabunge na viongozi wengine hawapo katika mfumo huu. Je, Serikali sasa iko tayari kuwaingiza watumishi wa kisiasa wakiwemo Wabunge katika utaratibu huu ambao unafikia miaka 55 au 60 waweze kupatiwa kadi za afya na wawe ni wanachama?
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama Serikali inakubali, je, ni lini utaratibu huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge ndio wanatunga sheria na nataka nimuombe sana Mheshimiwa Massare, kama jambo hili kwa umuhimu wake alipitishe katika Tume ya Utumishi wa Bunge lijadiliwe halafu sasa lifikishwe Serikalini kwa taratibu nyingine kufuatwa. (Makofi)
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Je, Serikali inaweza kutuambia ni kwa nini wazee kama baba na mama wa Mbunge hawakuwekwa miongoni mwa wategemezi katika bima ya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taratibu wa Sheria ya Bima ya Afya, inatambua yule mwenye kadi, mwenza wake na watoto wake, wategemezi wengine; baba, mama, walezi, wale wako nje ya utaratibu huo. Kwa hiyo, niendelee kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge kwamba changamoto hii na sisi tumeiona, tunaendelea kuitafakari kuangalia jinsi bora zaidi ya kuweza kulifanyia kazi ili hawa nao waweze kunufaika.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri, tunafahamu kwamba sekta zisizo rasmi zinachangia sana Pato la Taifa na wengi wao wako kwenye hatari ya kupata ajali na magonjwa kama watu wa bodaboda. Serikali ina mpango gani wa kurasimisha na kuwaweka katika mpango wa bima ya afya sekta isiyo rasmi, hasa vijana wetu wa bodaboda? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunatambua kwamba sekta isiyo rasmi nayo ina mchango mkubwa sana katika ukuaji na kuchangia katika uchumi wa nchi yetu, lakini sisi kupitia bima ya NHIF na CHF tunatambua makundi haya na kwa kupitia vikundi vyao kuna mfumo wa bima ambao wanao ambao wanaweza kukata kwa kupitia vikundi vyao. Lakini hata hivyo, kwa mtu mmoja mmoja sasa hivi tunakuja na utaratibu wa CHF iliyoboreshwa ambayo nayo itakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutoa huduma kwa mtu mmojammoja ambaye atakuwa anahitaji.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi ni kwa muda mrefu sasa Sera ya Matibabu Bure kwa mama wajawazito ya mwaka 2007 imeendelea kuwabagua akina mama wanaopata miscarriage kwa kuwatoza gharama za kusafishwa.
Je, Serikali haioni kwamba hii ni ajali kama ajali nyingine, hivyo basi akinamama hawa ambao walikuwa wana kiu ya kupata watoto wanastahili kufarijiwa kwa kusafishwa bila malipo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni ipi sasa kauli ya Serikali juu ya mabadiliko ya kisera ili ianze kuwa- include akina mama wanaopata miscarriage na wale ambao mimba inatunga nje ya kizazi kuanza kupata matibabu bure na sio kuwaweka kwenye group (orodha) ya magonjwa ya akina mama ambayo kimsingi yanalipiwa kwa asilimia 100? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza lilikuwa limejielekeza kwa nini akina mama ambao mimba zao zinaharibika ama kwa lugha ya kitaalam miscarriage, kwa nini nao wasipate matibabu bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu langu la msingi nilisema kwamba huduma za akinamama wajawazito kuanzia mwanzo wa mimba mpaka mwisho ni bure, hii inakwenda sambamba na tiba ambayo inaambatana na mimba kuharibika. Ninaomba tu niseme kwamba huduma hii ni bure kwa mujibu wa sera yetu lakini kama suala hili halitekelezeki kama inavyotakiwa katika sera niseme tu kwamba tutalichukua na kutoa maelekezo katika mamlaka husika ili sasa hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, sasa hivi Serikali tunafanya mapitio ya Sera ya Afya, tutaweka utaratibu mzuri wa kuweza kulisimamia jambo hili.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, akina mama wengi wajawazito wanapata madhara na kufariki hasa wanapokuwa na referral kutoka zahanati kwenda vituo vya afya na hospitali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma ya ambulance ili hawa akina mama wanapopata matatizo vijijini waweza kufikishwa haraka kwenye vituo vya afya na zahanati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua kwamba kumekuwa na changamoto ya kuwasafirisha akina mama wajawazito kwenda katika sehemu za kupata huduma, na kwa kiasi kikubwa kwa kweli kumekuwa na muitikio mkubwa sana wa akinamama kujifungulia katika vituo vya afya, hivi tunavyoongea sasa hivi ni zaidi ya asilimia 60 ya akina mama wajawazito wanajifungulia katika vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuboresha vituo vya afya na fedha kama alivyosema Naibu Waziri TAMISEMI, zaidi ya vituo 205 vimefanyiwa maboresho kwa kujenga theater, wodi ya akina mama kujifungulia ili hizi huduma za kujifungulia ziweze kuwa karibu zaidi. Lakini sambamba na hilo, Serikali imeendelea kutoa magari (ambulance) katika vituo vya afya na hospitali za wilaya, na kadri muda unavyokwenda tutakuwa tunaziongeza ili tuweze kufikia vituo vyote.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, tatizo la akina mama kujifungua mara nyingi wakati mwingine linaletwa pia na matatizo ya baadhi ya ma-nurse ambao huwa wanawanyanyapaa akina mama wenzao wanapotaka kujifungua.
Sasa sijui Serikali ina mpango gani au huwa inachukua hatua gani kuwadhibiti hawa akinamama ambao wana tabia za kuwanyanyasa akina mama wenzao wanapotaka kujifungua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na tatizo la baadhi ya watoa huduma kutoa lugha zisizokuwa sahihi kwa wagonjwa ambao wanafika katika hospitali, na hili ni jambo ambalo ni kinyume kabisa na maadili na taaluma za afya ikiwa ni pamoja na ma-nurse.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kuimarisha mabaraza yetu na hivi karibuni, wiki iliyopita tu, Mheshimiwa Waziri alitoa kauli ya kuhakikisha kwamba watoa huduma wote, ikiwa ni pamoja na madaktari na ma-nurse, wanakuwa wanatoa huduma nzuri ambayo inazingatia maadili na miiko ya kazi ambayo wanayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naendelea kulisisitiza hilo, na tumeendelea kuimarisha mabaraza yetu na tumeanza kuchukua hatua kwa wale ambao wanakiuka taratibu hizo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkanganyiko katika utaratibu wa upatikanaji wa vitambulisho kwa wazee ili waweze kupata huduma za afya ambapo baadhi ya maeneo wazee hawa wamekuwa wanatakiwa kuchangia baadhi ya gharama.
Sasa Serikali inaweza kutoa kauli ni upi wajibu wa halmashauri na upi wajibu wa wazee hawa ili waweze kupata vitambulisho ili wapate huduma za afya bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni agizo la Serikali kwamba Halmashauri zitoe vitambulisho vya wazee ili waweze kutambulika kirahisi wanapokwenda kutafuta matibabu ya afya. Na hii inaendana na Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasema kwamba wazee watapata matibabu bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho hivi vinapaswa vitolewe bure kwa sababu halmshauri zinagharamia. Inawezekana kwamba zile gharama ndogondogo kama upigaji wa picha ambazo wanatakiwa wazee nao wazigharamie ambayo sio gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapenda kusema tu kwamba gharama ya kitambulisho ni bure na Halmashauri zinatakiwa zigharamie hilo.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na rai aliyoitoa kwa wahusika. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa tatizo hili linaonekana kuongezeka nchini; je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Hospitali Maalum ya wagonjwa wa akili nchini yaani hospitali ya Mirembe inawezeshwa kiutaalam na vifaa ili kuweza kukabili tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuwahakikisha kwamba hospitali zote za Wilaya pamoja na za Mikoa zinapatiwa angalau Daktari mmoja ambaye ni mtaalam wa mambo ya akili ili kuweza kutoa huduma ya karibu kwa wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuifanyia maboresho Hospitali ya Rufaa ya Mirembe. Hivi tunavyoongea tunakamilisha ukarabati ambao umetugharimu zaidi ya milioni 976 na itaongeza kupanua wigo sana kuiboresha hospitali yetu ili kutoa huduma nzuri na za ziada. Sambamba na hilo tumeendelea kuongeza Wataalam na kutoa mafunzo kwa wataalam walioko ili waweze kutoa huduma bora na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili alitaka kujua, je, tuna mkakati gani wa kupeleka wataalam katika ngazi za mikoa na wilaya. Katika utaratibu wetu wa sasa ngazi ya rufaa katika masuala ya afya ya akili ni ngazi ya mikoa hili tunalifahamu na tuko katika mchakato wa kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo Madaktari ili tuweze kupata Madaktari Bingwa wa Afya ya Akili kuweza kutoa huduma hizo katika ngazi ya rufaa ya Mikoa.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo wagonjwa wote wa akili wanaranda mitaani hata miongoni mwetu tunaweza kuwa wapo wagonjwa wa akili. Kwenye nchi za wenzetu wamefanya utafiti wa wagonjwa wa akili nchi kama Marekani, Uingereza na Australia, tafiti zao zinasema katika kila watu wanne kuna mgonjwa mmoja mwenye tatizo la akili. Je, ni lini sasa nchi yetu itamua kufanya utafiti kama huu ili kubaini tuna wagonjwa wangapi wa akili nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Halima Bulembo kwamba, siyo wagonjwa wote wa akili wanarandaranda mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tafsiri ya afya ya Shirika la Afya Duniani inasema kwamba being health is not just merely absence of disease is mental, physical and social well-being. Sasa siyo kwamba tu unapokuwa na mwili umeathirika ndiyo unaweza ukasema kwamba wewe umeathirika. Kwa hiyo, katika suala la afya ya akili, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba si kila mtu anayerandaranda mitaani ndiyo mwenye ugonjwa wa akili, hata sisi inawezekana kama nilivyokuwa nimesema, katika swali langu la msingi, tunakadiria kwamba asilimia moja ya Watanzania wana matatizo ya akili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya akili naomba niendelee kutoa maelezo tuna matatizo mengi sana ya akili. Kuna sonona ambayo ni depression, kuna schizophrenia, kuna mania, obsessive complusive disorder, kuna mlolongo mkubwa sana ambao ni mpana sana na ambao kwa kweli hatuwezi tukafanya utafiti wa moja kwa moja kuweza kubaini katika jamii, ila tunaweza tukalifanya kwa wale ambao wanafika katika vituo vyetu vya afya na wale ambao tunaweza kuwabaini katika jamii. (Makofi)
MHE. SUSAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri, amekiri kwamba sasa hivi kuna magonjwa mengi ya akili na sasa hivi linaongezeka hili la vyuma kukaza watu wamekuwa na stress sana. Pamoja na kwamba Hospitali ya Mirembe ndiyo Hospitali ya Kuu na inafanyiwa maboresho na tunakubaliana kwamba magonjwa haya yamekuwa mengi na kwa maana hiyo jamii nzima ina haya magonjwa. Je, wana utaratibu gani kuhakikisha kwamba kwenye vituo huko mikoani, wilayani, wanaviboresha ili kuweza kuwasaidia hawa watu wenye matatizo ya magonjwa ya afya ya akili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Magonjwa ya akili yanasababishwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na kurithi kijenetiki lakini vilevile matumizi ya vilevi mbalimbali, changamoto na stress za maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambazo Serikali inazifanya; moja ni kama tulivyosema tumeboresha huduma katika hospitali yetu ya Rufaa ya Mirembe. Sambamba na hilo tumeendelea kujenga uwezo katika hospitali zetu za Rufaa za Kanda na tumesema tutakwenda mbali zaidi na kwenda kuboresha katika hospitali zetu za Rufaa za Mikoa, sambamba na hilo kuweka mifumo mizuri ya Rufaa kutokea ngazi ya dispensari hadi katika hospitali yetu ya Mirembe. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Benki hii imekuwa ikikiuka taratibu za kibenki kwa muda mrefu sana jambo ambalo limepelekea BOT kuwapa karipio kali. Je, Serikali imejiridhisha vipi kwamba ubadilishwaji wa Menejimenti ndiyo dawa au suluhisho pekee la uendeleaji mzuri wa benki hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama alivyosema katika maelezo yake ya awali Mheshimiwa Waziri, ni kwamba baada ya kufanya mapitio ndani ya Benki yetu tukaona kwamba kulikuwa kuna upungufu, hatua ambazo tulizichukua moja ni kufanya mabadiliko ya Menejimenti na kuanzia mwezi Mei, tumeweka Mkurugenzi mpya, tumepitia mfumo wa utendaji na uongozi katika benki ile na kuajiri watumishi wapya ambao ni waadilifu, sasa hivi hatua ambazo zimechukuliwa kwa haraka na imetusaidia kuhakikisha kwamba hata ule mtaji wetu umezidi kukua na hasara kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa ndani ya muda mfupi, ndani ya mwaka huu tutakuwa tumepiga hatua nzuri na benki itarudi kwenye mstari. (Makofi)
MHE. SUZAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini tutambue kwamba sisi sote ni Wazee watarajiwa na kwa maana hiyo tunapaswa kuweka miundombinu imara ya kuweza kusaidia wazee hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hapa umesema kwamba Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha na ukaelezea Ilani ya CCM, ninavyoelewa hii ni Ilani ya Kumi na Mbili ya CCM toka tumepata Uhuru au Ilani ya Nane kuanzia mwaka 1977 lakini bado tuna tatizo kubwa sana la masuala ya wazee; Ni miujiza gani Awamu hii ya Tano ya Hapa Kazi Tu mtafanya kuhakikisha kwamba hawa wazee wanaboreshewa maslahi yao na mahitaji yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa toka mwaka 1999 Serikali iliamua kwa dhati kuwa na Sera ya Wazee, Sera ambayo ilitengenezwa mwaka 2003. Mpaka leo hakuna sheria iliyoletwa, hawajaleta Muswada hapa Bungeni na Mheshimiwa Waziri wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Ummy, aliahidi na ameendelea kuahidi akaja Kigwangalla akaahidi na leo sasa Mheshimiwa Naibu Waziri Ndungulile, wanaiambia nini nchi hii. Je, ni kwa nini hawaleti Muswada ambao utatatua matatizo yote ya wazee katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO; Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Tano sasa hivi takribani inaingia mwaka wa tatu na nimeainisha katika jibu langu la msingi hatua ambazo tayari tumeanza kuzichukua katika kuboresha makazi ya wazee, sambamba na hilo kuhakikisha kwamba Wazee wale wanapata huduma ya chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tutenga bilioni mia nne tisini na tisa. Mpaka sasa hivi tumeshaweza kutoa milioni mia tatu hamsini na tatu elfu kwa ajili ya vyakula katika kambi hizi 17 za Wazee. Changamoto ambayo ipo na niendelee kusisitiza ni kwamba jukumu la kwanza la kutunza wazee ni la familia, baada ya hapo inafika ndugu na baada hapo ni jamii. Serikali inakuja mwishoni. Kwa hiyo, nataka niliwekee msisitizo hili ili nasi kama wanajamii tuweze kulitambua hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameulizia ni lini Serikali italeta sheria, Sera ambayo ameiongelea Mheshimiwa Mbunge ni ya mwaka 2003 imepitwa na wakati. Sasa hivi tuko katika mapitio mapya ya sera ili sasa tuhuishe mahitaji ya wazee kwa sasa na baada ya hapo tutaelekea kutunga sheria. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa ni Sera ya Serikali kwa Wazee kupata matibabu bure, Kambi ya Funga Funga ya Mjini Morogoro, ambayo inahudumia wazee wengi hivi sasa wanakosa huduma ya matibabu kutokana na hospitali ya Mkoa wa Morogoro kukosa madawa ya kutosha, hivi sasa wazee wale wakifika hospitali wanapewa panado na madawa mengine wanaambiwa wakanunue kwenye pharmacy za nje ya hospitali. Nataka kujua, je, Sera hii ya matibabu bure kwa Wazee inatekelezeka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 imetamka wazi kwamba matibabu kwa Wazee wasiojiweza itakuwa bure na hili tunalitekeleza kwa kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hatuna uhaba wa dawa sasa hivi, bajeti ya dawa imeongezeka sana kutoka bilioni 30 kufikia takribani bilioni 270, dawa zote za muhimu zinapatikana. Kama kuna suala mahsusi kuhusiana na Kambi hii Mheshimiwa Devotha Minja ningependa kupata maelezo ya ziada ili tuweze kuchukua hatua stahiki. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini pia nishukuru kwa majibu ya kitaalam ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sababu za kimaumbile pamoja na mabo mengine kama alivyotaja katika jawabu lake la msingi Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bado kuna mila potofu za ukeketaji wa wasichana kwa kutumia zana za kienyeji, zana moja kwa watu wengi. Lakini pia kuna mila potofu ya kurithi wajane, kuna mila ambazo mjane anarithiwa baada ya mume kufa bila ya kupima au kujulikana amekufa kwa sababu zipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, bado Virusi vya UKIMWI au UKIMWI katika nchi yetu ni tatizo na maambuzi kila siku yanazidi kuliko kupungua, na ziko njia nyingi ambazo zinasababisha maambukizi kama vile ngono na Serikali inajua kuna vishawishi vingi na kuna biashara ya ngono hasa katika maeneo ya mjini.
Je, Serikali ina mpango gani hasa hasa maalum ambao watautumia katika kuzuia biashara hizi za madangulo, biashara hizi zinafanyika na hatuwezi kuwalaumu…
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba kumekuwa na mila potofu za ukeketaji na kurithi wajane ambazo kwa njia moja au nyingine nazo zinachangia kwa kiasi katika maambukizi dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Serikali tunaendelea kuchukua jitihada za kuelimisha jamii kuhusiana na madhara haya ya masuala ya ukeketaji na ya kurithi wajane. Moja ya shughuli ambayo na mimi nitaifanya baada ya Bunge hili kukamilika ni kwenda katika Wilaya ya Kilindi katika Mkoa wa Tanga kwenda kushiriki pamoja na jamii wale wakeketaji ambao walikuwa wanafanya shughuli hizi za kuiacha shughuli hiyo na sasa kuanza sasa kuhakikisha kwamba taratibu za kawaida zinaweza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali inaendelea kuchukua juhudi ya kutoa elimu lakini vilevile kuamasisha jamii kuachana na mila potofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na suala la biashara ya ngono. Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwenye jamii kuhusiana na biashara hii ya ngono na kuchukua taratibu za kisheria pale tunapobaini kwamba kuna madangulo katika maeneo husika.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la wingi wa wagonjwa katika Hospitali ya Morogoro inafanana na wingi wa wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Songea ambao unasababishwa na kukosekana kwa Hospitali ya Wilaya ya Songea. Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya Songea?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali imetukabidhi hospitali za rufaa za mikoa na tunaendelea na maboresho; lakini kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuna fedha ambazo wamezitenga kwa lengo la kuhakikisha kwamba baadhi ya Wilaya ambazo hazina Hospitali za Wilaya ziweze kujenga. Lengo ni kuhakikisha kwamba ule mtiririko wa huduma kutoka katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mkoa, hospitali za kanda mpaka hospitali maalum za kitaifa unazingatiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, naomba kuongezea kidogo katika majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kutambua umuhimu wa kuwepo na hospitali za wilaya za kutosha, katika bajeti ya mwaka 2018/2019 tunaenda kujenga Hospitali za Wilaya 67. Sina uhakika na naomba Mungu iwe katika hizo Wilaya 67 na Songea ikawepo, ni vizuri tukatizama katika orodha ili tukaona nao kama wapo, nashukuru. (Makofi)
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Lushoto inatumia x-ray ya zamani na pia ni ndogo haina uwezo. Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray ya kisasa (digital x- ray) ili kuondoa adha wanayoipata wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuboresha huduma za x-ray. Kama alivyokuwa amesema katika swali lake la msingi, ni kweli tulikuwa na x- ray pale lakini katika mkataba huu ambao tunao na Philips lengo letu sasa ni kuziondoa zile x-ray za zamani na kuweka x-ray mpya; na tutalizingatia hilo kwamba mgao huu mpya utakapokuja basi na Hospitali ya Lushoto nayo iweze kuwa katika sehemu zile ambazo zitapata.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa swali lako la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina mkataba wa utoaji wa huduma za x-ray nchi nzima kwa kupitia kampuni hii ya Philips.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu haya, maana kwa siku nyingi sana tulikuwa tumeahidiwa na majibu yalikuwa hivi hivi, lakini haya mpaka tumepewa date kwamba Juni tutapata hiyo x-ray digital tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kuuliza maswali ya nyongeza kwamba; kwa kweli pamoja na kupata hiyo digital x-ray lakini bado kuna huduma nyingine ya mashine za kisasa ambazo zitasaidia hawa majeruhi kuweza kuchunguzwa zaidi. Kwa mfano tumeshuhudia hivi majuzi Waheshimiwa wenzetu Wabunge walivyopata ajali ilibidi wakimbizwe haraka sana kwenda Muhimbili kule kwa ajili ya uchunguzi zaidi, lakini kama tungekuwa na mashine hizi tungesaidia hata wagonjwa kuokoa usumbufu na maisha yao na gharama; mashine hizo ni MRI na CT-Scan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba kuuliza, je, Wizara ni lini sasa mtatuletea pia katika Hospitali hii ya Mkoa wa Morogoro mashine za MRI na CT-SCAN ili kupunguza hata rufaa kule Muhimbili na kupunguza msongamano lakini pia kuokoa maisha ya wagonjwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pale Morogoro kama tunavyoona ile hospitali inapokea wagonjwa wengi sana wa ndani ya mkoa lakini pia na mikoa mingine. Sasa bado kuna huu usumbufu ambao unapata wagonjwa kwamba operating theatre ya mifupa haipo wanatumia theatre moja, je, ni lini sasa pia Serikali itatenga fedha za kujenga theatre hii ili kuokoa maisha ya wagonjwa na kuondoa usumbufu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tisekwa ambaye leo anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa, nimpongeze kwa hilo, lakini nimpongeze vilevile kwa maswali yake mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunaendelea kujipanga; tunatambua kwamba Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Mkoa wa Pwani pamoja na Dar es Salam ziko katika highway na kumekuwa na ajali nyingi ikiwa ni pamoja na ambayo imetokea kwa Waheshimiwa Wabunge wiki iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tuna mradi ambao tunashirikiana na wenzetu wa Benki ya Dunia kuweka huduma za dharura na ajali na tumejaribu sana kulenga katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ambapo huduma mbalimbali za dharura zitawekwa ikiwa ni pamoja na ambulance na kuangalia sasa uwezekano wa kuweka hizo huduma za CT-Scan na MRI katika hospitali hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo Serikali imetukabidhi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hospitali zote za rufaa za mikoa. Tumezifanyia tathmini za kina na katika bajeti ya 2018/2019 katika moja ya maeneo ambayo tutaenda kuboresha ni pamoja na kuongeza vyumba vya upasuaji. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono bajeti yetu ya Wizara ya Afya itakapofika.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa vitendo hivi vinapotokea mara nyingi ushahidi wa awali haupatikani. Je, Serikali imejipanga vipi kutoa taaluma kwa wananchi nini kifanyike mara tu linapotokea jambo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inachukua hatua za kutosha dhidi ya udhalilishaji huu lakini bado vitendo hivi vinaendelea kwa kasi kubwa katika jamii zetu. Je, Serikali haioni kwamba adhabu inayotolewa ni ndogo hivyo basi ilete sheria hapa Bungeni tuipitishe yeyote atakayepatikana na hatia ya kubaka mtoto mdogo ahasiwe? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio mengi ya udhalilishaji sasa hivi yanakuwa reported na hii inaonesha kwamba mwamko wa jamii nao umeongezeka. Tumepanua wigo sana kupitia Idara zetu za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii pamoja na Jeshi la Polisi kwa kuanzisha Madawati ya kuweza kutoa taarifa kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini matukio mengi ya udhalilishaji dhidi ya watoto yamedhihirisha kwamba yanafanywa na watu wa karibu wa familia. Naendelea kutoa rai kwa wanajamii na familia kuyatolea taarifa punde yale matukio yanapotokea na sisi ndani ya Wizara ya Afya pamoja na Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri kuyashughulikia kwa uharaka zaidi pindi yanapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi kwa mujibu wa sheria udhalilishaji wa mtoto adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano na kifungo kisichozidi miezi sita ama vyote kufanyika kwa wakati mmoja. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutafakari kwa kadri inavyoona inafaa kama kuna umuhimu wa kuongeza adhabu kutokana na matukio kama hayo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hili tatizo la udhalilishaji wa watoto sasa hivi limekuwa ni sugu ama ni donda ndugu yaani ni zaidi ya kila kitu na sisi wazazi inatuuma sana. Unaweza ukamuona mtoto anatoka mafunza mwanamume anamdhalilisha mtoto mchanga, hii iko sana kule kwetu Zanzibar, inauma sana maana hata wazazi wenyewe wengine wanawaingilia watoto wao. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu kama hao wanaofanya udhalilishaji wa watoto wetu hasa ikizingatiwa kwamba wakifanyiwa tatizo hilo wanaficha na wanamalizana wenyewe kule nyumbani hawapeleki taarifa kunakohusika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Faida Bakar ambalo amelielezea kwa hisia kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, mtoto ana haki zake tano na naomba nizinukuu kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge. Mtoto ana haki ya kuishi; kulindwa; kuendelezwa; kushirikishwa na kutobaguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo, Serikali inakemea sana udhalilishaji wowote wa kijinsia dhidi ya mtoto. Ndiyo maana tumesema kwamba tumeweka mkakati wa kiserikali wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2020/2021 na lengo na kusudio ni kuhakikisha kwamba tunatokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimetoka kusema kwamba udhalilishaji mwingi unafanyika katika ngazi ya familia. Naomba nitoe rai kwetu sisi Wabunge wote na jamii yote ambayo inaendelea kutusikiliza, tusiyafumbie macho matukio na udhalilishaji wowote dhidi ya wanawake na watoto na sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na jamii kuchukua hatua za haraka kwa wote wanaofanya matukio kama haya.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Udhalilishwaji wa watoto ni pamoja na watoto wa kike kutopata mahali pa kujisitiri katika shule zetu za msingi na sekondari. Serikali ilishatoa kauli kwamba shule zetu ziwe na vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa mashuleni lakini vyumba hivyo mpaka sasa havijakamilika. Ni kwa nini Serikali imeshindwa kusimamia kauli yake yenyewe wakati watoto wa kike wamekuwa wakidhalilika katika mazingira yao ya masomo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba watoto wa kike ambao wako shule wanahitaji sehemu ya kujisitiri wakati wakiwa katika siku zao. Niseme tu kwamba hili tumeshaanza kulifanyia kazi kwa kushirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Elimu. Katika vyoo ambavyo sasa hivi tumeanza kuvijenga kwenye baadhi ya shule tumeshaweka utaratibu huo wa kuwa na vyumba na vyoo maalum kwa ajili ya watoto wa kike.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuwaadhibu wale wote wanaofanya vitendo vya udhalilishaji, lakini watoto hawa wanaofanyiwa udhalilishaji wanapata madhara ikiwemo kuambukizwa magonjwa na kupewa mimba. Je, Serikali ina jitihada gani za kuhakikisha watoto hawa ambao wamepata maradhi au wamepata mimba wanasaidiwa ili kutimiza ndoto zao za maisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua ambazo nimetoka kuzieleza na ambazo Waheshimiwa Mawaziri wametoka kuzisema za kuchukua hatua kuhusiana na wahusika ambao wanafanya matendo hayo ya udhalilishaji, nami niendelee kutoa rai tu, changamoto ya kuyafikisha mashauri haya Mahakamani mojawapo ni kwamba ndugu na wazazi wa watoto wale wanakubaliana na mtuhumiwa kuyamaliza mashauri yao nje ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba udhalilishaji wowote wa mwanamke na mtoto masuala haya yasimaliziwe mtaani, badala yake yaweze kufikishwa katika vyombo vya dola. Sisi kama Wizara na Serikali tutaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba matibabu kwa wale ambao watakutwa wameathirika na virusi vya UKIMWI, kwa sababu huduma za tiba ya UKIMWI zinatolewa bure na Serikali na pale itakapothibitika kwamba binti yule ameweza kupata ujauzito basi huduma za afya kwa wajawazito ni bure kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa swali la msingi linazungumzia kuhusu kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto na kwa kuwa takwimu zinaonesha kwamba kila watoto sita wanaozaliwa watoto wanne sio wa baba mhusika. Je, Serikali inaonaje kuhusu udhalilishaji wa akinababa kwa kubambikiziwa watoto ambao siyo wa kwao ki-genetic? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke kumbukumbu sahihi ili hii dhana ili isizidi kuenea. Si kweli kwamba watoto sita katika watoto wetu tuliokuwa nao wote si wa baba ama wazazi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke vizuri jambo hili. Takwimu ile ilikuwa inatokana na wale waliopeleka vipimo vyao kwa ajili ya vinasaba kutambua uhalali wa mzazi. (Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)
Naomba Waheshimiwa Wabunge mnisikilize, nataka tuelewane vizuri. Ni sawasawa unaenda katika wodi ya TB unataka kujua maambukizi ya wagonjwa wa TB katika wodi ya TB. Wale wote waliopeleka sample maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni wale ambao tayari wana wasiwasi kuhusiana na uzazi wa wale watoto na ndiyo maana hicho kiwango kilichopatikana kikawa hicho, lakini siyo kwamba kwa ujumla wetu Tanzania nzima watoto wengi hususan kwa akina baba siyo watoto wao, siyo kweli!
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiweke hiyo taarifa wazi ili sasa Wabunge na especially wanaume tusianze kukimbia majukumu yetu ya msingi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu mapema Januari, 2017 baada ya kuona maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, kwanza hakuridhishwa na bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 38 ya kujenga Hospitali ya Mkoa. Hivyo, akasema hospitali hiyo ijengwe kwa shilingi bilioni 10 na kwamba akatoa ahadi zitolewe shilingi bilioni 10 ili mwaka 2019 aje kuzindua hospitali hiyo. Mpaka sasa ni jengo la OPD tu ndilo lililokamilika na 2017 mpaka leo hakuna fedha yoyote iliyoletwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba commitment ya Serikali kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, swali langu dogo la pili; tunayo Hospitali Teule ya Somanda, hospitali hiyo ina changamoto. Madaktari wanaohitajika ni 22, waliopo ni wanane, lakini hao wanane hawana examination room, hamna Mganga wa Usingizi wala hakuna casuality room.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha hospitali hiyo teule ya mkoa ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu wasihangaike kwenda Mkoani Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Leah Komanya; na nimpongeze kwa kufuatilia afya na maendeleo ya wananchi wa Simiyu.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba, Mheshimiwa Rais mwishoni mwa mwaka 2017 alikabidhi hospitali zote za rufaa za mikoa ambazo zilikuwa zinasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuja katika Wizara ya Afya. Na sisi ndani ya Wizara ya Afya tumeshajipanga kuhakikisha kwamba hospitali hizi tunazihudumia na kuzisimamia kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kama nilivyosema katika jibu langu la awali.
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema tu kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni commitment, nasi ndani ya Wizara tutaendelea kuisimamia kuhakikisha kwamba fedha hizo zinapatikana kwa malengo ambayo yamekusudiwa, baada ya kufanya tathmini ya kina kuangalia mahitaji halisi ya Hospitali hii ya Simiyu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na watumishi. Katika mwaka wa fedha uliopita, Serikali iliajiri watumishi 3,152 ambao tuliwagawa katika mikoa mbalimbali. Tunatambua bado tuna changamoto kubwa sana ya watumishi na tunatarajia kwamba Serikali itatoa kibali hivi karibuni na Mkoa wa Simiyu utazingatiwa katika mahitaji yake.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, sipingani na mpango huu wa Serikali katika kuzichukua moja kwa moja hospitali hizi, hasa ukizingatia Halmashauri zetu sasa hivi zina hali mbaya kichumi kutokana na vyanzo mbalimbali kuondolewa. Nataka kujua sasa, mfumo wa utumishi baada ya kuzichukua hizi hospitali utakuweje kwa maana za mamlaka za kinidhamu kwa watumishi waliokuwa wakifanya kazi kwenye hizi hospitali? Hilo moja.
Mheshimiwa Spika, la pili, wakati Wizara inapanga namna gani ya kuzihudumia hizi hospitali, huwa inaangalia idadi ya watu katika eneo husika, mfano kwa Hospitali ya Temeke mnaangalia idadi ya watu katika Wilaya ya Temeke, lakini ukweli ni kwamba Hospitali ya Temeke haihudumii tu watu wa Temeke, inahudumia na maeneo jirani kwa sababu ya jiografia yake ilivyo, maeneo kama ya Kigamboni, Mkuranga na sehemu nyingine kama Kibiti na Rufiji.
Je, Wizara mmelizingatiaje hili, ili kuhakikisha sasa huduma mtakazozitoa katika Hospitali ya Temeke zitaenda sambamba na idadi kubwa ya watu wanaopata huduma katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, sisi ndani ya Wizara baada ya kukabidhiwa hospitali hizi tumefanya tathmini ya kina kuangalia mahitaji ya miundombinu ya kiutumishi ya hospitali hii. Niseme tu kwamba kuna maboresho makubwa ambayo tumeyafanya ndani ya Wizara kwanza; kwanza, kuanzisha section maalum ambayo itakuwa inasimamia Hospitali za Rufaa na za Mikoa katika Idara ya Tiba.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika Idara Kuu ya Utumishi tumefanya mabadiliko, tutakuwa na Mkurugenzi Msaidizi ambaye naye atakuwa anasimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tumefanya maboresho vilevile katika Hospitali za Rufaa za Mikoa baada ya kuitwa Waganga Wafawidhi. Matarajio yetu ni kwamba sasa wasimamizi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa watakuwa wanaitwa Wakurugenzi kamili na watapata hadhi hiyo na taratibu zote hizo tumeshazikamilisha.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Nidhamu bado yako chini ya Mabaraza ya Taaluma ambayo nayo yako chini ya Ofisi ya Mganga Mkuu. Kwa hiyo, Mamlaka za Nidhamu zitaendelea kufanya kazi kwa mujibu ule ule, hata pale wakati zikiwa TAMISEMI, mamlaka ya nidhamu yalikuwa bado chini ya Wizara ya Afya chini ya mabaraza, chini ya Mganga Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mtolea, ni kweli Wilaya ya Temeke ina watu takribani milioni 1.6 na Hospitali ya Temeke imekuwa ikiwahudumia wananchi wengi pamoja na Wilaya nyingine za jirani. Serikali inatambua hilo, tutazingatia hilo, lakini sambamba na hilo tunaboresha mnyororo wa utoaji huduma kwa maana ya kuboresha vituo vya afya, kujenga Hospitali za Wilaya na zahanati ili sasa ule mnyororo wa rufaa uweze kuwa kamili na kuhakikisha kwamba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inafanya kazi ya rufaa ya mkoa.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa takwimu zinaonesha Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni na moja ya sababu ni kutokuimarishwa kwa elimu ya uzazi wa mpango.
Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuanzisha kampeni ya kitaifa ili kuwawezesha wanafunzi na hasa wa kike kuanzia shule za msingi hadi sekondari kuweza kujitambua na kuepukana na mimba za utotoni? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa hospitali za Mkoa wa Singida pamoja na vituo vya afya vina uhaba mkubwa wa wataalam na vifaatiba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hospitali na vituo vya afya vya Mkoa wa Singida vinapatiwa wataalam na vifaatiba vya kutosha ili kuziwezesha hospitali hizo kufanya kazi kwa ufanisi na kuokoa vifo vya akinamama wajawazito na watoto? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aisharose Matembe kwa kuwa mpiganaji mkubwa sana wa masuala ya afya ya akina mama na watoto katika Mkoa wa Singida na kwa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba tuna changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni na takwimu ambazo tunazo zinaonyesha kwamba wastani wa asilimia 27 ya vijana ambao wapo kati ya miaka 15 mpaka 19 aidha, wameshapata watoto au ni wajawazito, hii idadi ni kubwa sana na baadhi ya Mikoa inakaribia asilimia 50. Kwa kutambua hilo, Serikali imeweka mkakati na Wizara tumeanzisha kampeni inayoitwa “Mimi ni Msichana, Najitambua, Elimu Ndio Mpango Mzima.” Hii kampeni tayari tumeshaizindua na inaendelea kusambaa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ndani ya Wizara sasa hivi tunakamilisha kuandaa mkakati wa afya ya uzazi kwa vijana, ambao itatoa dira na mwelekeo wa nini tunahitaji kufanya hususan katika yale maeneo ambayo mimba za utotoni zimeshamiri. Sambamba na hilo, tumeanzisha club katika maeneo mbalimbali hususan katika shule za sekondari kuwajengea uwezo vijana wetu hususan mabinti wa kike kujitambua na kuhakikisha kwamba wanapata elimu ya kutosha kuhusiana na elimu ya uzazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, tafiti zimethibitisha kwamba tunapomnyanyua mwanamke kiuchumi vilevile tunazuia uwezekano wa wale mabinti kupata mimba za utotoni, sambamba na hili kuna miradi ambayo tunaifanyia upembuzi yakinifu sasa hivi ambayo itatoa fedha kidogo kuwajengea uwezo wale mabinti especially wale ambao wapo nje ya mfumo wa shule kuweza kujikimu kimapato na hii ni moja ya mkakati ambao tumeuona umekuwa na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeweza kuongeza bajeti ya mpango wa afya ya uzazi kutoka shilingi bilioni tano mpaka shilingi bilioni 18. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza nini mkakati wa Serikali kuongeza wataalam na vifaatiba. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaatiba ni bilioni 269 na nimeongelea hapa bajeti ambayo tumeiweka katika family planning kutoka bilioni tano mpaka bilioni 18. Tatizo siyo fedha, tatizo niwaombe Waheshimiwa Wabunge watusaidie ni kuwahimiza waganga wetu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanaagiza vifaa na dawa ambazo zinahusiana na masuala ya uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni tabia ya baadhi ya watoa kutoagiza vifaa hivi kwa sababu wanaona kwamba havina tija au havitoki haraka katika hospitali zao, lakini ni sehemu ya tiba muhimu na dawa muhimu sana hususan katika upande wa uzazi wa mpango, lakini Serikali itaendelea kutoa elimu hiyo na kuhamasisha watoa huduma kuhakikisha kwamba wanaagiza dawa hizo na sisi kama bohari ya dawa tunazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kweli tumekuwa na changamoto ya uhaba wa watumishi na tunaamini kwamba kadri vibali vinapopatikana tutakuwa tunaongeza wigo wa watoa huduma katika hospitali hizi. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hospitali za Mikoa ya Dar es Salaam, kwenye wodi za akina mama kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa mama wajawazito, wengine wanalala wawili na wengine wanalala chini.
Je, Serikali ina jitihada gani za maksudi kuhakikisha hizi wodi za akina mama zinakuwa na mpangilio maalum, mama mjamzito anavyofikishwa hospitalini apate kitanda cha peke yake, kwa sababu wako wawili na kulala watu wawili pia inachangia kuambukiza maradhi? Je, Serikali ina mkakati gani…
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaboresha mnyororo wa utoaji wa huduma za afya kwa kuboresha mifumo ya rufaa na moja ya mikakati ni hii ambayo tumeendelea kuisema na nimeigusia hapa kuboresha vituo vya afya, hospitali za Wilaya na hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma za uzazi salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema jana, kwangu siyo faraja sana kusikia kwamba wakina mama 100 wamezaa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Tunachotaka kuona pale Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ni case zile ambazo zipo complicated, kesi nyingine zote sasa hivi tumejenga uwezo katika vituo vyetu vya afya, hospitali zetu za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma. Nitoe rai kwa wananchi kuzitumia hospitali zetu hizi. (Makofi)
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia wanawake wengi wakati wanapojifungua wanapata maradhi ya fistula, je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha wanawake hawa wanaojifungua wanaepukana na maradhi haya ya fistula?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa swali zuri ambalo ameuliza Mheshimiwa Munira.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke kupata fistula maana yake ni kwamba hakupata huduma nzuri wakati alipokuwa anakaribia kujifungua na hiyo ndiyo tafsiri yake kubwa ya msingi, kwa sababu fistula haipaswi kutokea kama mwanamke alipata uangalizi mzuri wakati anajifungua. Katika changamoto hiyo tumeiona, tunaendelea kuboresha utoaji wa huduma, kutoa elimu kwa watoa huduma wa afya, vilevile kuhakikisha kwamba tunazisogeza huduma za dharura za kumtoa mtoto tumboni karibu zaidi na wananchi ili hali ile ambayo inatokana na mwanamke kukaa labor kwa muda mrefu tuondokane nayo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameonesha kwamba huduma hizi sasa zinaanza kutolewa kuanzia Hospitali ya Wilaya, na ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wetu wengi wapo vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha huduma hizi katika vituo vya afya ili kupunguza adha ya wananchi wetu kutembea kwenda Hospitali ya Wilaya?
Swali la pili, miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na kisukari, hivi sasa kuna ujenzi unaoendelea wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kule Mtwara, amesema kwamba hospitali za rufaa za kanda zitatoa vilevile huduma hii katika ngazi ya kanda.
Je, Serikali imejiandaaje sasa itakapofunguliwa Hospitali ya Kanda ya Kusini ambayo inajengwa Mtwara, kwamba huduma ya saratani pia itatolewa katika hospitali hiyo ili kuwapunguzia adha Wanamtwara kwenda Hospitali ya Ocean Road iliyopo Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Abdallah Chikota kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya na kwa kuwapigania wananchi wake wa Jimbo lake na Mkoa wa Mtwara katika masuala yote yanayohusiana na afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukizwa, siyo tu kisukari, lakini hata vilevile kiharusi, masuala ya pressure, magonjwa ya figo. Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga uwezo katika mnyororo wake wa utoaji wa huduma, sasa hivi tuko katika ngazi ya Wilaya lakini tunaendelea kuboresha kushuka katika ngazi ya vituo vya afya na mwisho tutashuka mpaka katika dispensaries.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba huduma za awali kwa magonjwa kama haya ya upimaji wa sukari, upimaji wa pressure, yote yanafanyika katika ngazi zote za mnyororo, lakini dawa kwa mfano, insulin ambazo zinahitaji utaalam zaidi zinapatikana katika ngazi ya Wilaya. Lakini tutaendelea kuboresha utaratibu huu kadri tutakapokuwa tunajenga uwezo katika mnyororo wetu wa utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza, je, Serikali itakuwa tayari kuanzisha huduma za saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ambayo inajengwa Mtwara. Kwa mujibu wa taratibu katika ngazi hiyo ya Rufaa ya Kanda, moja ya huduma ni pamoja na upatikanaji wa huduma za saratani. Kwa hiyo, pindi hospitali hii itakapokuwa tayari huduma hiyo nayo tutaiweka. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu linakabiliwa na tatizo kubwa ambalo kimsingi ni janga la utapiamlo na lishe iliyopitiliza, hii lishe iliyopitiliza ndiyo chimbuko sasa la magonjwa kama kisukari na magonjwa ya moyo.
Je, Serikali ipo tayari kwa maksudi kabisa kuandaa semina kwa Bunge zima ili Wabunge hawa wakielimika iwe chachu ya kutoa elimu kwa jamii nchini?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kitandula ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge, Masuala ya Lishe, kwa kusimamia vizuri masuala ya lishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya utapiamlo pamoja na suala la lishe iliyopitiliza ambayo kwa lugha ya kitaalam tunaita viribatumbo (obesity) na sisi kama Serikali tumeweka mkakati ambao ni jumuishi na ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana, ambao unashirikisha sekta zote kuhakikisha kwamba tunajenga Tanzania yenye lishe. Wizara tupo tayari kutoa semina kwa Wabunge ili kuwajengea uwezo na uelewa na wao kwenda kusemea masuala ya lishe na viribatumbo katika jamii wanazotoka.(Makofi)
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni kubwa, nzuri na ya kisasa ambayo inatumika kuwahudumia wananchi wa Dodoma, wanafunzi wa UDOM pamoja na sisi Wabunge, lakini ina tatizo kubwa sana la Madaktari pamoja na watumishi wengine. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Madaktari ni kidogo sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo ndiyo mamlaka ya kusimamia Hospitali ya Benjamin Mkapa, inatambua kwamba tuna changamoto ya Madaktari Bingwa.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeweka mikakati ya kuainisha mahitaji ya Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na Hospitali zote za Rufaa za Mikoa na tutafanya mgawanyo kwa kuangalia yale maeneo ambayo yana Madaktari wa ziada na kuwapeleka katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa, ikiwa pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, katika mwaka huu wa fedha tumefadhili masomo ya Madaktari Bingwa 125 katika fani ambazo hatuna katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa. Pindi Madaktari hao watakapomaliza watakuwa posted katika hospitali hizi.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Licha ya majibu mazuri, nina maswali mawili mafupi ya kumuuliza.
Kwa kuwa mpaka sasa hivi tafiti zinaendelea hapa duniani kuhusu ugonjwa wa kisukari, lakini mpaka sasa hivi azijazaa matunda, napenda kujua; je, tafiti hizi zimehusishaje tiba mbadala au tiba asilia kuhusu kutibu ugonjwa huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ugonwja huu umeenea sana na unaleta vifo na inaonekana kuwa inawashambulia pia watoto wadogo na wajawazito na njia mojawapo inahusisha mambo ya lishe; je, kuna mkakati gani wa kutoa elimu kwa watu wote na hasa tukianza na Waheshimiwa Wabunge humu ndani kuhusu ugonjwa huu wa kisukari na hasa na mambo ya lishe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sisi kama Serikali, tunatambua kwamba sasa hivi hatuna tiba dhidi ya ugonjwa wa kisukari, lakini Serikali vilevile inatambua umuhimu wa tiba asili na tiba mbadala, ndiyo maana ndani ya Wizara ya Afya tuna Kitengo Maalum ambacho kinasimamia tiba asili na tiba mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia taasisi zetu za Utafiti za Magonjwa ya Binadamu (National Institute of Medical Research) na Taasisi ya Tiba Asili ambayo iko Muhimbili, tumekuwa tunaendelea kufanya utafiti wa tiba mbalimbali ambazo zinapunguza kiwango cha sukari mwilini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, hatujapata tiba mbadala, lakini mtu yeyote ambaye amekuja na dawa ambayo anadhani inaweza kusaidia kupunguza makali ya ugonjwa wa kisukari, tumekuwa tunazifanyia utafiti na kuziangalia ili ziweze kutumika kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameuliza kuhusiana na masuala ya lishe. Serikali mwezi Julai, 2017 imezindua mkakati wa Kitaifa wa masuala ya lishe na uzinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na lengo ni kuhakikisha sasa tunaongeza nguvu na kuongeza juhudi kuhusiana na magonjwa ya kuambukiza. Magonjwa ya kuambukiza yanazidi kuongezeka. Tunakadiria kwamba wastani wa asilimia 13 za Watanzania wana ugonjwa wa kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasi tunaendelea kuhamasisha wananchi pamoja na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea hapa Bungeni, wenzetu wa Bima ya Afya tumeleta Madaktari Bingwa wa magonjwa yote pamoja na kisukari na mimi nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, twende pale kliniki tupime afya zetu; siyo suala tu la Kisukari lakini magonwja yote pamoja na Saratani huduma hizi zinapatikana Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishie kwa kutoa rai kwa wananchi wa Tanzania, magonjwa yasiyoambukizwa ikiwa ni pamoja na kisukari na shinikizo la damu, yanatokana kwa kutozingatia masuala ya lishe, kutofanya mazoezi na matumizi yaliyopindukia ya vilevi na sigara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwasisitiza Watanzania kuzingatia msingi ya afya bora. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kama alivyokiri Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mgonjwa wa kisukari ili aweze kuishi ni lazima apate dawa za kisukari kila siku. Sasa kule Jimboni Bagamoyo kwenye Hospitali ya Wilaya kuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa dawa hizi kwa wagonjwa wa kisukari. Pia hata vipimia vya kiwango cha sukari navyo havipatikani hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba dawa hizi na vipimo vinapatikana kwa urahisi ili wananchi wetu wa Tanzania waweze kuendelea kuishi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na vilevile majibu ya nyongeza ni kwamba tunatambua sasa hivi ongezeko kubwa sana la wagonwja wa kisukari, na sisi kama Serikali tumeelekeza nguvu zetu katika bajeti ambayo tumeitenga ya fedha kwa ajili ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi, bajeti ya ugonjwa wa kisukari nayo imo ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuongeza wigo wa utoaji wa huduma hii kwa kushirikiana na wadau, kusambaza vifaa vya upimaji, vilevile kusambaza dawa za insulin pamoja na vidonge vyake na katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kununua matumizi ya insulin.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba hili suala la Bagamoyo tutajaribu kulifuatilia kuhakikisha kwamba sasa huduma hizo za dawa pamoja na vipimo vinapatikana.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la maradhi ya kisukari mpaka kuna baadhi ya watoto wachanga wanazaliwa wakiwa na maradhi haya; je, Serikali inaweza kutuambia nini chanzo kinachosababisha watoto wadogo kuzaliwa wakiwa na kisukari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nilisema kuna aina tatu za kisukari. Aina ya kwanza ni kisukari ambacho kinawapata watu katika umri mdogo na changamoto ya aina hii ni kwamba mtoto anazaliwa zile cell zake za kongosho ambazo kwa lugha ya kitaalam tunaita pancreas mwili wake wenyewe unaanza kuishambulia ikiona kwamba kile ni kitu ambacho ni kigeni ndani ya mwili. Kwa hiyo, hiyo ni aina moja ya kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya pili ya ni kisukari ambacho kinawapata watu katika umri mkubwa; na hiyo ndiyo hali ambayo ilikuwepo kutokana na jinsi tunavyokula, masuala ya uzito, matumizi ya vilevi na kutofanya mazoezi. Sasa hivi hali imeendelea kubadilika, hata watoto wadogo kwa sababu ya lishe. Mara nyingi ukiona mtoto anakuwa na uzito mkubwa na sisi kama wazazi tunaona kwamba ni faraja. Uzito uliopitiliza wa aina yoyote hauna tija na ni moja ya kitu ambacho kinapelekea sasa hivi watoto wetu kuanza kupata kisukari wakiwa na umri mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya tatu ni kisukari ambacho kinatokana na ujauzito. Mama anapokuwa mjamzito kuna baadhi wanapata kisukari na mara nyingi kinaisha baada ya yule mtoto kuzaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu na kwa kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim, ni kwamba ni lazima sisi kama wazazi tuzingatie misingi ya lishe kwa watoto wetu, tusiwalishe chakula kilichopitiliza na watoto wetu wakawa wazito na uzito mkubwa kwa sababu nayo ina mchango mkubwa sana katika kupata kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kikundi kidogo ambacho miili yao tangu wamezaliwa zile cells zao za kongosho sinashindwa kufanya vizuri, hazizalishi insulin ama kwa kuwa na deformity ama kwa kuwa haikuumbwa vizuri zaidi au zikawa zimeshambuliwa; hawa wako wachache na wao watakuwa wanahitaji insulin tangu wakiwa na umri mdogo. Kubwa la msingi ni kuzingatia suala la lishe hususan kwa watoto hawa wasiwe na uzito mkubwa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza.
Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba wamekuwa na teknolojia mpya ya upimaji na ugunduzi wa vimelea vya TB kwamba sasa ndani ya masaa mawili badala ya siku tatu.
Napenda kujua nini hasa mkakati wa Serikali wenye kutoa kampeni maalum ya elimu ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo ya migodi, viwanja vya michezo, mikusanyiko ya wavuvi pamoja na mikusanyiko ya wasafiri?
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, inaonekana kwamba mkakati wa kukabiliana na tatizo hili ni kwamba ndani ya taratibu hizi za kibajeti, fedha hizi wameachiwa wahisani ambao ni Wazungu. Matatizo ni ya Watanzania, ugonjwa ni wa Watanzania, lakini matibabu ni kwa wahisani wafadhili, Wazungu.
Napenda kujua, kwa nini Serikali imetenga shilingi bilioni 33.3 na ni fedha za nje, hakuna hata senti tano ambayo ni fedha za ndani ambapo fedha hizi za nje huwa hazitolewi kwa wakati na wakati mwingine hazitolewi kabisa. Kwa nini Serikali isipange mkakati wake wa kuweka fedha za ndani badala ya kutegemea fedha za wahisani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Masoud kwa kuwa amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa masuala ya afya, TB pamoja na masuala ya UKIMWI. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo umeendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza katika maswali yake ya msingi, ni kwamba sasa hivi Serikali baada ya kuona kwamba tumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo wengi wamekuwa wanaathirika kama nilivyoyataja katika majibu yangu ya msingi, tumeelekeza juhudi mahususi katika masuala ya makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakumbuka, mara nyingi ugonjwa huu wa UKIMWI umekuwa ni ugonjwa pacha vilevile wa ugonjwa wa UKIMWI. Sasa hivi mikakati ambayo tunayo, kwanza tumejielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali kwa vyombo vya habari pamoja na mitandao ya jamii. Vilevile sasa hvi tuna mkakati mahususi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi. Sambasamba na hilo, katika mikakati yetu tumetengeneza mikakati jumuishi kati ya ugonjwa wa UKIMWI na ugonjwa wa TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza kijielekeza mahali pengi ambapo tunaweza tukapata wengi kwa pamoja na hususan wanaume. Tumeelekeza nguvu kwenye migodi, tumeelekeza nguvu kwenye kambi za uvuvi na sasa hivi tunataka twende mbali sana katika upande huu wa UKIMWI, hata kule ambapo wanaume wanakuwa katika bar, msishangae na sisi tukiwa tunapita kule tunawaomba kufanya upimaji wa masuala ya UKIMWI pamoja na masuala ya TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali lake la pili alilielekeza katika suala la fedha akihoji kwa nini Serikali na katika kitabu pale inaonesha kwamba kuna fedha za nje na kwa nini sisi kama Serikali hatujaweka fedha za ndani. Naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 kufikia shilingi bilioni 269 katika mwaka wa fedha 2017/2018 na katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge mmetupitishia hapa juzi, bajeti ya dawa imeongezeka mpaka shilingi bilioni 270. Katika hiyo bajeti, ni kwa ajili ya dawa, vitendanishi na vifaatiba na ndani ya hiyo tumetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya ugonjwa wa TB. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama Mheshimiwa Waziri alivyosema ni kwa kweli hospitali hizi zinafanya kazi kubwa sana, lakini hali ilivyo sasa tangu Septemba, 2013, hospitali hizi hazijapewa ruhusa ya kufanya ajira mpya wala ajira mbadala na watumishi wapo pungufu zaidi ya asilimia 50. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuangalia hospitali hizi hasa Hospitali ya Huruma, Kilema, Machame mpaka kule Karatu ambazo zina upungufu wa watumishi kwa zaidi ya asilimia 50?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mkataba kati ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC na Bugando tangu Septemba, 2017 haujakamilika au haujafanyiwa kazi ambapo hospitali hizi haziendeshwi vizuri inavyotakiwa na ni hospitali za rufaa. Je, ni lini Serikali itakamilisha utaratibu huu wa mkataba kati ya Serikali na Mashirika haya ya Dini hasa Hospitali ya Bugando na KCMC?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba baadhi ya hospitali ambazo zimetajwa zimekuwa na changamoto ya rasilimali watu na kadri tunapopata uwezo tumekuwa tunapeleka watumishi. Tunatarajia baada ya Bunge hili la Bajeti tutapata watumishi wa ziada ambapo katika hospitali hizi za DDH na sisi tutapeleka watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili ameongelea suala la mikataba. Ni kweli Serikali imekuwa inapeleka rasilimali watu na fedha, lakini tumekuwa tunapata changamoto katika baadhi ya hizi hospitali katika usimamizi wa fedha na rasilimali watu ambao tumepeleka. Sasa hivi Serikali inafanya mapitio na pale mapitio haya yatakapokuwa yamekamilika, basi tutaingia mkataba ili tuweze kusimamia vizuri rasilimali fedha za Serikali na watumishi ambao tunawapeleka.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali inatoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa vijana wetu wenye umri wa miaka tisa mpaka 14. Je, baada ya kupatiwa kinga hizo vijana wetu wasichana iwapo watakuwa wanafanya ngono zembe, kinga hiyo itaendelea kumkinga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imezindua chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi na tumejielekeza kwanza kwa mabinti wote wa miaka 14 na baada ya hapo tutakuja mabinti wa miaka tisa mpaka 13 na baada ya hapo tutakuja mabinti wa miaka tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zimejionyesha kwamba vijana wengi wanaanza kujamiiana wakiwa na umri mdogo, chanjo hii itawakinga mabinti dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi, haitawakinga mabinti dhidi ya magonjwa mengine ya kuambukiza kama vile magonjwa ya kaswende, kisonono pamoja na UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote wanaotusikiliza, chanjo hii ni salama na lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaondokana kabisa na saratani ya shingo ya kizazi ambayo inawaathiri wanawake walio wengi.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa maijibu mazuri, ametupa faraja watu wa Kigoma. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Hospitali hii ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni ni hospitali kubwa ukizingatia Kigoma tuko mpakani, inahudumia wananchi zaidi ya milioni mbili, lakini mpaka sasa hatuna vifaa muhimu kama CT-scan na vile vya kupimia saratani ya kizazi kwa wanawake. Naomba majibu ya Waziri, ni lini mtatuletea vifaa hivi katika hospitali hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Kigoma umekuwa ukikumbwa na changamoto nyingi za magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hasa katika Wilaya yangu ya Kigoma Vijijini. Nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha wanamaliza tatizo la kipindupindu ndani ya Mkoa wa Kigoma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, S wali lake la kwanza ameuliza ni lini Serikali itapeleka mashine ya CT-scan na vipimo vya kupima saratani. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa mpango wa Serikali na aina ya huduma ambazo zinatolewa, sasa hivi katika ngazi za Hospitali za Rufaa za Mikoa, hatuna mpango wa kuweka CT-scan kwa sababu, moja, mashine hizi kwanza ni za gharama kubwa lakini pili zinahitaji utaalam ambao kwa sasa hivi katika ngazi za rufaa za mikoa hatuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi katika mikakati yetu ni kwamba mashine za aina ya CT-scan upatikanaji wake unaanzia katika Hospitali za Rufaa za Kanda. Hata hivyo, vipimo kwa ajili ya dalili za awali za saratani ya shingo ya uzazi vyote vinapatikana hadi katika ngazi ya vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi ambao wanatusikiliza kwamba huduma hizi zinapatikana. Kwa wale wanawake ambao hatujawagusa katika chanjo hizi, huduma hizi tumezisogeza, zaidi ya vituo 1,000 ndani ya nchi hii vifaa hivi vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili limehusiana na suala la kipindupindu. Ugonjwa wa kipindupindu ni mtambuka na sisi kama Wizara ya Afya ambao tunasimamia masuala yote ya afya, tunaendelea kushirikiana na mamlaka katika ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha kwamba mikakati yote ambayo sisi tumeiweka ya kutokomeza ugonjwa huu inatekelezwa kwa maana ya kutoa dawa, vipimo, kutibu maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa wa kipindupindu.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ipo katikati ya barabara za Iringa, Mbeya, Dodoma na ajali nyingi zinatokea lakini mpaka leo kuna matatizo ya X-ray machine. Je, ni lini Serikali itaipatia uwezo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro X-ray machine kwa sababu ajali nyingi huwa zinatokea katika barabara hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ni moja kati ya hospitali 10 ambazo tutazipatia mashine ya X-ray. Tunatarajia ifikapo mwezi Juni mwaka huu mashine hii itapatikana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Kigoma kunaakisi hali halisi ilivyo katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambayo inafanya kazi kama hospitali ya mkoa. Je, ni lini Serikali itatusaidia Madaktari na wataalam wengine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze amekuwa anafuatilia sana masuala kuhusiana na afya katika eneo lake la Mpanda. Pia nimhakikishie tu kwamba kadri Serikali itakapokuwa tunapata watumishi na tunatarajia mwezi Julai mwaka huu tutapata watumishi wengine wa ziada, Hospitali ya Mpanda ambayo na mimi nimeshaitembelea na natambua changamoto zake itakuwa ni moja ya hospitali zitakazopata watumishi. Sambasamba na hilo, Serikali imejielekeza sasa katika ujenzi wa hospitali mpya kubwa ya rufaa katika Mkoa wake wa Katavi.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wizara ya Afya haijaanza jana wala juzi. Nimesikitika sana kusikia Mheshimiwa Waziri akisema sasa ndiyo wanafanya tathmini ya kujua Madaktari Bingwa ni wangapi ili waweze kuwapanga. Swali langu, hawaoni huu ni uzembe mkubwa kwamba walipaswa kuwa na kanzidata au database ya Madaktari Bingwa ili kusiwe na tatizo hili kwa sababu kila siku tunauliza na tunaambiwa kuna tatizo? Hawaoni huo ni uzembe kwamba walipaswa kuwa nayo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambao nao wanasimamia sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maana ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhiwa hospitali hizi za rufaa za mikoa mwishoni mwa mwaka jana wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mloganzila. Tunatambua idadi ya Madaktari tuliokuwa nao na tunakuwa na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wa afya wa kutosha. Kwa hiyo, si uzembe, kila kitu ni mikakati ambayo Serikali tumeendelea kujiwekea na tutaendelea kuzihudumia na kuwapatia watumishi wa kutosha kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyojitosheleza. Pia naishukuru Serikali yangu kwa kutenga hizo shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Itilima na Busega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza; kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu jengo la OPD lipo tayari na maelezo ya mkandarasi ambaye ni TBA amesema jengo hilo litakabidhiwa tarehe 28 Mei, 2018 kwa Katibu Tawala wa Mkoa. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuweza kutujengea wodi ya wazazi, watoto, wanawake na wanaume ili hospitali hiyo ianze kazi haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Hospitali Teule ya Mkoa haina kabisa gari la kubebea wagonjwa kupeleka Hospitali ya Rufaa Bugando, gari lililopo wanatumia hardtop almaarufu chai maharage; je, ni lini Serikali itatuletea gari la kubebea wagonjwa kupeleka katika Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya Wizara ya Afya ambayo tumeipitisha hivi karibuni, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikao ya Katavi, Njombe, Simiyu, Songwe na Mara. Kwa hiyo, Hospitali ya Simiyu ni sehemu ya hospitali ambazo zitaendelezwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba ya hilo, Serikali imeagiza ambulances na zitakapofika Mkoa wa Simiyu utakuwa ni mmoja ya mkoa ambao tutaufikiria kupata ambulance. (Makofi)
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa umahiri wake wa kijibu swali, siyo hili tu, hata mengine ambayo nimeshuhudia akiwa anayajibu. Naipongeza pia Wizara kwa ujumla kwa jinsi na namna ambavyo inachapa kazi kwa ufasaha na ufanisi. Pia kwa Serikali nzima ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Afya nikipita kwenye mitandao huko kote kwa kweli nataka kuipigia chapuo Serikali kwa performance hiyo. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inatekeleza mpango mkakati iliyoutaja kwa mwaka 2016 mpaka 2020 na kwa kuwa katika utekelezaji wa mpango huo Serikali imezingatia maeneo matatu na moja ya maeneo hayo ni huduma wakati wa kujifungua na kwa kuwa katika huduma za wakati wa kujifungua mojawapo ya mahitaji muhimu ni chumba cha upasuaji na kwa kuwa ndani ya chumba cha upasuaji mojawapo ya vitu muhimu ni vitanda vya upasuaji ambavyo vinaitwa operation beds au operation tables; na kwa kuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru hospitali pekee katika Wilaya ambayo ina vijiji karibu 160 hali ya chumba hicho ni mbaya kwa maana ya miundombinu ya jengo lenyewe lakini pia na vifaa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kurekebisha chumba hiki cha upasuaji ili kiweze kuwa bora kabisa cha kuweza kutoa huduma kama sera inavyoelekeza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwanza naipongeza Serikali kwa kuboresha vituo vya afya hivi vichache ambavyo tunavyo. Isipokuwa vituo vyetu vya afya viko mbali sana kutoka kwenye Hospitali ya Wilaya na kwa hiyo, ili uweze kutoa huduma bora zaidi ya uzazi wa mpango au kutoa huduma vizuri zaidi kwa mpango wa uzazi na mtoto unahitaji kufikisha wagonjwa kwa wakati kwenye Hospitali ya Wilaya, lakini hatuna magari ya wagonjwa hata moja. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiomba Serikalini tuweze kupatiwa angalau...
Mheshimiwa Naibu Spika, swali sasa. Ni lini Serikali itaweza kuipatia Wilaya ya Tunduru gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwahudumia akina mama wajawazito pamoja watoto kwa ajili ya huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE, NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa kwa kufuatilia sana masuala ya afya na hususan afya ya uzazi katika Wilaya yake ya Tunduru. Takwimu zinaonyesha kwamba akina mama wa Tunduru wanafanya vizuri sana kwa kujifungulia katika Vituo vya Afya kwa zaidi ya asilimia 81 lakini vilevile katika matumizi ya uzazi wa mpango. Nawapongeza sana kwa kazi kubwa na nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na maswali yake ya msingi ambapo ameuliza kwamba, jengo pamoja na chumba cha upasuaji na upatikanaji wa kitanda cha upasuaji ni changamoto katika hospitali ya Wilaya, naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali zetu hizi pamoja na hii hospitali ya Tunduru ambayo ni hospitali ya Wilaya zina vyanzo mbalimbali. Kwanza, kupitia Serikali Kuu tumekuwa tunapeleka fedha za dawa. Naomba Waheshimiwa Wabunge, tunaposema fedha ni za dawa, haimaanishi ni dawa peke yake. Ni fedha za dawa, vitendanishi na vifaatiba. Meza ya upasuaji ni moja ya kifaatiba. Kwa hiyo, kuna vyanzo viwili ambavyo hospitali hii inaweza ikatumia ili kuweza kupata ile operating table na moja ya chanzo ni fedha zile tunazozipelekea katika hospitali yetu na katika mgao huu wa fedha mpaka sasa hivi Wilaya ya Tunduru tumeshapeleka shilingi milioni 268.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo kingine ambacho wanaweza wakakitumia ni makusanyo yao ya ndani pamoja na makusanyo kupitia mfuko wa NHIF. Kwa hiyo, niendelee kumshauri Mheshimiwa Mbunge wakae katika ngazi yao ya Halmashauri na kupanga matumizi mazuri ya fedha ambazo wanazipata na wanazozizalisha katika hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, ameulizia kwamba ni lini Serikali itaipatia huduma ya Ambulance Hospitali ya Tunduru. Mimi niseme tu kwamba Serikali imeagiza magari na yatakapofika, tutaangalia vigezo vya uhitaji kulingaa na umbali na idadi ya vifo vya akina mama na watoto na Wilaya ya Tunduru itakuwa ni moja ya Wilaya ambazo tutazifikiria. (Makofi)
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana na yenye msingi, nampongeza sana. Hata hivyo, nina maswali yangu mawili ya nyongeza hapa. Swali la kwanza, kwa kuwa ubakaji umekithiri hapa nchini na hasa wanaume ndio chanzo kikuu cha masuala hayo; je, Serikali itachukua hatua gani za kimkakati ili wananchi watokwe na hofu na suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali ina mpango gani wa kutunga sheria kali ili kudhibiti ubakaji na udhalilishaji? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeeleza mikakati ambayo Serikali inaifanya kuhakikisha kwamba tunapunguza sana matukio haya ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto na mikakati naomba niirudie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuuhakikisha kwamba mpango mkakati ule ambao tumeuandaa tunausimamia vizuri; Pili, tumeendelea kushirikiana na vyombo vya dola na kuanzisha madawati mbalimbali; Tatu, kuanzisha one stop centre; Nne, ni kutoa elimu kwenye jamii. Tunatambua kwamba matukio mengi ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yanafanya karibu sana na wanafamilia. Niendelee kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba tusifumbie macho matukio kama haya na tusimalizane nayo katika ngazi ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, linahusiana na kwa nini tusitunge sheria kali; sheria tulizokuwa nazo za mwenendo wa adhabu na Sheria ya Mtoto na Sheria ya Masuala ya Kujamiiana zinajitosheleza kabisa na hatua zilizokuwepo pale zinatosha kabisa kuchukua hatua kwa wale wote ambao wanafanya matukio kama haya.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Watanzania wanawake watatu kati ya kumi na mwanaume mmoja kati ya kumi wamekuwa waki-experience hii kunyanyaswa kijinsia, kikatili (sexual abuse). Idadi hii inaweza ikawa kubwa zaidi kwa sababu moja, watu wengi hawatoi taarifa, sasa Serikali imekuja na mikakati mbalimbali ya kurekebisha hili, lakini tatizo sugu ni kwamba taarifa hazifiki kwenye mamlaka husika. Sasa Serikali itakuja lini na mkakati mahususi wa kuhakikisha kwamba taarifa zinapelekwa kwenye mamlaka husika ili tatizo hili lipate ufumbuzi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiangalia kabla hatujazindua mpango mkakati tulikuwa tuna changamoto ya utoaji wa taarifa. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, matukio kama haya yalikuwa yanafanywa na watu wako karibu sana na familia. Sasa ukiangalia takwimu zetu kuanzia baada ya kuzindua mpango mkakati wetu, utoaji wa taarifa wa matukio umezidi kuongezeka. Hili linaweza likamaanisha mambo mawili; moja, matukio yanaongezeka, lakini pili, linaweza likawa linamaanisha kwamba utoaji wa taarifa umeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutoa rai kwa jamii kwamba vyombo vya dola viko imara na tunashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi. Pia nitoe rai kwa wananchi kwamba badala ya kumalizana na masuala haya ya udhalilishaji wa kijinsia majumbani, twende kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yanayoelimisha umma juu ya ugonjwa wa Ini, ugonjwa ambao ni hatari kama alivyoeleza mwenyewe Naibu Waziri kwamba, ugonjwa huu unaweza ukaambukizwa kwa kujamiiana, kwa mama kumuambukiza mtoto wake mchanga, kudungwa au kujidunga sindano na mama kumwambukiza mtoto anapojifungua. Ni ugonjwa hatari sana ambao wananchi wengi hawaujui na hawajui namna ya kujikinga. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kutoa elimu kama inavyotoa juu ya ugonjwa wa malaria, kifua kikuu na maradhi mengine ili wananchi wajiepushe na wawe na elimu juu ya ugonjwa huu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua wigo kwa zahanati na vituo vya afya kuwa na uwezo wa kupima ugonjwa wa Ini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Moja, ametaka kujua Serikali tunafanya nini katika kuelimisha jamii. Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii kupitia vitengo vyake vya elimu kwa umma imekuwa inaandaa majarida na machapisho mbalimbali ambayo tumekuwa tunayatoa kwa umma na kwa kupitia katika Vyombo vya Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumekuwa tunatoa elimu hii katika kliniki mbalimbali lakini kutokana na umuhimu wa ugonjwa huu, tutajaribu kuongeza juhudi zaidi kuhakikisha kwamba wigo wa elimu hii unapanuka na kuweza kuwafikia Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alitaka kujua wigo wa upimaji. Kwa sasa upimaji wa ugonjwa huu unafanyika katika ngazi ya Wilaya kwenda juu kwa aina ya vipimo ambavyo tulikuwa navyo, lakini kwa sababu teknolojia imekua sasa hivi na vipimo vya haraka (rapid test) zimeweza kupatikana, Serikali inatafakari sasa upatikanaji wa vipimo hivi katika ngazi nyingine za chini ili upimaji wa ugonjwa huu uweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nitoe rai kwamba maambukizi ya Hepatitis B yanafanana na maambukizi ya UKIMWI na nawaomba sana wananchi tuwe tunajenga tabia ya kupima ili tuweze kutunza maini yetu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwamba kuna aina tofauti za maradhi ya ini lakini amesema kuna (A), (B) na (C) lakini ukipata aina ya A, B na C zinaathiri vipi ili tuweze kujielewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba nipate ufafanuzi huo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba tunapozungumzia virusi vya ugonjwa wa Hepatitis maana yake ni kwamba ni virusi ambavyo vinashambulia Ini. Katika jibu langu la msingi nilisema kwamba kuna makundi matano, kinachotofautiana pale ni jinsi gani ya virusi hivi vinaambukizwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, virusi vya type B, C na D maambukizi yake yanafanana na yanafanaa vilevile kama mtu ambaye anaambukizwa virusi vya UKIMWI kwa maana kuongezewa damu, kujitoga ama kwa kujamiiana. Virusi vya type A na E uambukizwaji wake mara nyingi ni kwa njia ya maji, mtu anapokunywa maji yasiyo safi na salama anaweza kuambukizwa virusi hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu virusi hivi vyote type A, B, C, D na E vinashambulia ini dalili zake zote huwa zinafanana kwa maana mgonjwa kuwa na macho na ngozi kuwa manjano, mkojo kuwa mweusi, kupata homa, kuumwa tumbo na wengine kuweza kuhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwa Hepatitis B tuna chanjo ambayo sasa hivi tunaitoa kwa watoto lakini Hepatitis C hii haina chanjo mpaka sasa, hizi nyingine kwa mfano Hepatitis A na E ni magonjwa ambayo athari zake sio kubwa sana kama zilivyo za Hepatitis B.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda tu sasa kufahamu na niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa kuwa vifaa hivi vya uchunguzi ni muhimu sana kwenye Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa na Kanda, Serikali imeonekana kuwa inachukua muda mrefu sana bila kutekeleza ahadi za kupeleka vifaa hivi kwa wakati na izingatiwa kwamba suala la afya ni muhimu sana. Mheshimiwa Waziri atuambie kwa kuwa wanategemea mradi wa ORIO ambao muda siyo mrefu watapata vifaa hivyo, ni lini Hospitali ya Bugando itapata kipata kifaa cha MRI kwa sababu ya wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa kupata huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunayo hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure, vifaa hivi kama CT Scan kwenye hospitali ya Mkoa ni muhimu sana. Ni lini sasa Wizara kwa mpango ule watahakikisha walau kifaa kimoja, CT Scan kwenye Hosptali ya Rufaa ya Sekou Toure kinapatikana na kusaidia wananchi wengi zaidi? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa ufuatiliaji wa karibu katika masuala ya afya katika Mkoa nzima wa Mwanza vilevile katika Jimbo lake la Nyamagana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mabula ameuliza ni lini mashine ya MRI itapatikana. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi nilisema kwamba Serikali inaendelea na maandalizi na tuko katika majadiliano na Serikali ya Netherlands kupitia mradi wa ORIO na awamu ya kwanza ya mashine ya kwanza ya X-Ray, vilevile na upatikanaji wa CT Scan na MRI kwa baadhi ya hospitali ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando tunatarajia kabla ya mwisho wa mwaka huu itaweza kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza ni lini sasa tutapeleka mashine ya CT Scan ama MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure. Kulingana na mwongozo wetu tulio nao sasa huduma ya CT Scan na MRI zinapatikana kuanzia ngazi ya Rufaa ya Kanda, lakini tumeona kwamba mahitaji yamezidi kuongezeka, idadi ya watu imezidi kuongezeka na mfumo wa uendeshaji hospitali za rufaa umebadilika, kwa hiyo, sasa hivi Wizara inafanya mapitio ya miongozo yake ikiwa ni pamoja na kuangalia mahitaji ya huduma kama ya CT Scan katika ngazi ya Rufaa za Mikoa. Tutakapokamilisha taratibu hizo basi huduma hizi CT Scan tutazishusha katika ngazi ya Rufaa ya Mkoa.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, stadi zinaonesha lipo jaribio linalohusisha utolewaji ama utumiaji wa ARV kwa watu wasio kuwa na maambukizi ya VVU ama UKIMWI ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia maambukizi mapya endapo mtu huyu aliyetumia ARV pasipo kujamiana na mtu ambaye tayari ana maambuki ya VVU ama UKIMWI.
Ningependa kusikia kauli ya Serikali hali ipoje nchini Tanzania juu ya matumizi hayo ya ARV kwa mtu ambaye hana maambukizi ili kumzuia asiambukizwe endapo atajaamiana na mtu mwenye maambukizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kufuatia mikakati inayofanywa na Serikali ambayo mengi wameainisha kwenye majibu yao ningependa kujua jambo moja mahususi. Je, Serikali inashughulikiaje swala zima la ongezeko la watoro ambao tayari wako kwenye kujiunga na utumiaji wa matibabu ya HIV and AIDS? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sayansi katika matibabu ya ugonjwa wa UKIMWI yameonesha kwamba mtu asiyekuwa na maambukizi ya UKIMWI anaweza akapatiwa dawa ambazo zinaweza kumsadia kumkinga dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa lugha ya kitaalamu inaitwa pre-exposure prophylaxis.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuweke msisitizo hadi hivi sasa hatuna tiba ya ugonjwa wa UKIMWI, tunachokifanya hichi ni dawa kinga, na sisi kama Tanzania tunalitambua hilo na tumeshaanza katika ngazi ya majaribio na lengo letu ni kwamba baada ya majaribio haya tuweze roll out nchi nzima na tunalenga makundi mahususi ambayo ni pamoja na wanaofanya biashara ya ukahaba, kwa wale ambao wanajidunga madawa ya kulevya na wale ambao wanajamiiana kwa jinsia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize kwamba kinga hii inaendana sambamba na kutumia njia nyingine za kujikinga na wala sio suluhu ya kutopata maambuzi ya UKIMWI, nilitaka niliweke msisitizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana wale ambao wanaacha dawa.
Sasa hivi Serikali tumeanza mchakato wa kuwabaini na changamoto ambayo tumeiona ni kwamba siyo kwamba wengi wanaacha ni mtu amekuwa eneo moja anachukua dawa baada ya hapo anahamia katika nyingine na kule anaenda kujisajili kama mteja mpya na sisi tumekuwa hatuna kumbukumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi tuna kitu ambacho tunachokifanya ni kuweka utaratibu wa kutumia mifumo wa biometric kwamba mtu akipata matibabu sehemu moja akienda tena sehemu nyingine atatambulika kama ni mtu ambaye tayari tunaye kwenye database na hili tunalifanyia kazi na hivi karibuni tutali-introduce. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kinipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya njia ya kupunguza maambukizi ya UKIMWI ni kuhakikisha kwamba vituo vya utoaji wa huduma vinakuwa jirani na wananchi. Kwenye maeneo ya vijijini vituo vya afya vipo mbali na zahanati maeneo mengi hazitoi huduma hizi za kupima,lakini pia utoaji wa dawa.
Je, ni lini Serikali itaagiza au itaweka utaratibu rasmi kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati zote zinatoa huduma ya upimaji, lakini pia zinatoa huduma za ARV? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la Mheshimiwa Hongoli. Sisi kama Serikali mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba ifikapo 2030 tumeweza kufikia asilimia 90 ya Watanzania tunaowapima, asilimia 90 ya wale ambao tumewapima tunawaanzishia dawa na asilimia 90 ya wale ambao tumewaanzishia dawa tuweze kufubaza virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ambayo tumekuja nayo tumeendelea kupanua wigo wa vituo vyetu vya kutolea huduma hizi za ugonjwa wa UKIMWI. Lakini tumeanzisha mkakati wa kuwa na kitu kinaitwa outreach, watoa huduma wetu wa afya kwenda kule katika maeneo ambapo hakuna huduma za kuweza kuweza kutoa huduma hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaendelea kuhamasisha Watanzania kwa utaratibu ambao tunaenda nao sasa badala ya kutoa dawa za mwezi mmoja mmoja tumeongeza sasa tu kwa wale wagonjwa ambao wako stable sasa hivi tunatoa dawa za miezi mitatu mitatu na yote haya ni mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma hizi zinawafikia wananchi wengi iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Kama alivyoeleza kwamba ugonjwa huu hapa kwetu upo, pamoja na kwamba anasema wanaoathirika zaidi ni Marekani, lakini hapa kwetu tayari umeingia na mazingira yake tumeona kwamba wanawake waathirika zaidi lakini na umri ni miaka 15 mpaka 45.
Je, Serikali haioni haja ya kuelimisha juu ya ugonjwa huu kwa sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kama ilivyo katika magonjwa mengine, wajibu wetu Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa mbalimbali, vyanzo vyake, dalili zake na matibabu yaliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuhamasisha jamii kupata uelewa wa kina katika jambo hili, Serikali kupitia Kitengo chake cha Elimu ya Afya kwa Umma, tutaweka utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii ili wananchi nao waweze kupata uelewa vizuri wa ugonjwa huu.
Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, siyo ugonjwa ambao unabainika kirahisi, wala chanzo chake kinajulikana kirahisi na wala matitabu yake siyo rahisi kama nilivyogusia katika jibu langu la msingi. Kwa hiyo, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutazingatia katika mpango wetu wa elimu ya afya kwa umma.
MHE. RICHARD M. NDASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Magonjwa yako mengi kama alivyosema huu ugonjwa wa Lupa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa Ebola ni hatari sana. Ugonjwa huu umejitokeza nchini DRC Congo (Kivu Kaskazini) na umeshaua zaidi ya watu 77 na watu 116 wamegundulika wana ugonjwa huu na kwa sababu sisi Congo, Kivu Kaskazini inapakana na Rwanda, Burundi na Uganda: Je, Serikali kwa sababu ugonjwa huu ni hatari sana, tunamwomba Mwenyezi Mungu apishie mbali ugonjwa huu usije kwetu nchini; Serikali imejipangaje kukabiliana na ugonjwa huu hatari na mbaya sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Ebola ni ugonjwa hatari na unaambukiza kwa haraka sana na mara nyingi ugonjwa huu hauna tiba na wale wanaopata ugonjwa huu zaidi ya asilimia 50 hawaponi, huishia kufariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwa takwimu ambazo amezitoa Mheshimiwa Mbunge kwamba wenzetu katika nchi ya DRC limejitokeza balaa hili la ugonjwa wa Ebola na mpaka sasa hivi zaidi ya watu 76 wamefariki na zaidi ya 100 wameugua ugonjwa huu. Sisi kama Tanzania tumechukua hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumeimarisha mifumo yetu ya ufuatiliaji wa wagonjwa katika mipaka yetu yote kwa kuhakikisha kwamba watu wote wanaoingia nchini katika maeneo ambayo tunayahisi yanaweza yakawa ugonjwa huu, tumeimarisha mfumo wa ufuatiliaji; tumeweka thermo scanner, tumeweka maeneo mahususi kwa wale watakaoingia nchini ambao tunawahisi wana dalili, tunawatenga, tumeweka hizo isolation center.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumetoa elimu ya kutosha katika mikoa yetu ambayo ipo mipakani kwa viongozi wote wa Serikali pamoja na watoa huduma wetu wa afya ili endapo mgonjwa ataingia nchini, waweze kuchukua hatua kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesambaza vifaa vya kujikinga (personal protection equipment) katika maeneo yote ambayo yapo pembezoni ili watoa huduma wetu na wale ambao wataingia, watakutana na wale wagonjwa waweze kujikinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeimarisha mifumo yetu ya maabara, endapo tutapata mgonjwa ambaye atahitaji kuchukuliwa sampuli, tumenunua vifaa, tunavyo na maabara tumeziandaa.
Mwisho kabisa, tumeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na gonjwa hili kuu, kwamba endapo mtu atamwona mtu ambaye ametoka katika nchi za jirani ana dalili za homa, ana maumivu ya viungo ama kutoka damu sehemu mbalimbali za mwili, wananchi waweze kutoa taarifa kwa haraka katika mamlaka na kuchukua tahadhari ya kutomshika mtu yule ambaye ana dalili zile ambazo nimezigusia. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli Serikali imetoa elimu kwa wananchi wanaoishi mikoani juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, lakini kituo cha kuhudumia wagonjwa wa Ebola endapo watapatikana kipo pale Temeke. Sasa kwa nini Serikali haioni haja ya kutoa elimu hiyo ya uelewa kwa wananchi wa Temeke pia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo cha Isolation Center kwa magonjwa haya hatarishi kipo pale Temeke, watoa huduma wetu katika Hospital ya Temeke wameshapewa Elimu hiyo na tutaendelea kutoa elimu kwa ujumla kwa wananchi wote ikiwa ni pamoja na wananchi wa Temeke kuhusiana na athari za ugonjwa huo.
MHE. HASNA S. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Jimbo la Kigoma Kusini tunapakana na nchi ya Congo kwenye vijiji 27 na niliona juzi/hivi karibuni wakati Mheshimiwa Waziri anatoa tamko la kupata ugonjwa huu, ukawa unaweza kuingia nchini, tuliona Kigoma kuna mtu mmoja tu ambaye alioneshwa kwenye tv kwamba yupo peke yake na kifaa anachotumia ni kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangaliza kwa mazingira ya Mkoa wa Kigoma, Jimbo hili la Kigoma Kusini ndilo ambalo lina vijiji vingi vinavyopakana na nchi ya Congo kwa maana ya ukanda wote wa Kalemi. Hadi leo nilikuwa nawasiliana na DMO, hakuna kituo hata kimoja ambacho kimewekewa mashine ya kuwapima Wakongo wanaotumia maboti kuingia nchini kwetu.
Je, Wizara imejipangaje kuisaidia Halmashauri ya Uvinza, wananchi wake wasiathirike na huu na ilhali wameingiliana kwa kiwango kikubwa sana na nchi ya Congo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kusisitiza kwamba sisi kama Serikali tumeendelea kujipanga, siyo tu katika sekta za afya, tunashirikiana na mamlaka nyingine za Kamati za Ulinzi na Usalama na zimepewa elimu hii kuhakikisha kwamba katika maeneo ambayo tuna mipaka, tunaweka ufuatiliaji wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, timu yetu ya Wizara kupitia Mganga Mkuu wa Serikali, hivi tu juzi ametoka tena Kigoma kwenda kukaa na kufuatilia kuhakikisha haya tunayoyasema wakiwa pamoja na Shirika la Afya Duniani kwenda kuangalia jitihada na juhudi ambazo tunaendelea kuvifanya. Niseme tu kwamba mipaka yetu iko salama, tutaendelea kuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja yake nyingine ambayo ameisema Mheshimiwa Mbunge, kuhusiana na kuweka huduma za ufuatiliaji wa wagonjwa katika Vituo vyetu na Zahanati, hatuwezi tukaweka katika maeneo yale. Ugonjwa huu ndugu zangu ni hatari sana. Sio kila mtu anayeruhusiwa kumgusa wala kumtibu mgonjwa huyo. Pale anapobainika, watoa huduma wetu wamepewa maelekezo jinsi gani ya kum-handle na kum-isolate yule mgonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ambazo zina uwezo zaidi ambazo ni zile Isolation Centers zetu na maabara zile ambazo tumezitenga, ndiyo ziweze kuchukua majukumu ya kumtibu yule mgonjwa. Sio kila mtu ana uwezo wa kuwatibu wagonjwa hao. Kwa hiyo, nilitaka nimhakikishie tu kwamba mipaka yetu iko salama, na sisi kama Serikali, tumejipanga vizuri.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba, bado asilimia ni ndogo sana ya watumizi wa mfuko huu. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwaelimisha Wananchi, ili aweze kujiunga na mfuko huu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba bado idadi kubwa sana ya Watanzania hawajafikiwa na huduma ya bima ya afya, lakini tunatambua vilevile gharama za matibabu zinazidi kuongezeka. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea kupanua wigo wa vifurushi vyetu ili kuhakikisha kwamba tunaweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi, lakini sambamba na hilo tunaendelea kuboresha vifurushi, lakini tunaboresha vilevile utaratibu wa wananchi kuweza kuchangia na moja ya mkakati tunaoufikiria ndani ya Serikali ni utaratibu wa jipimie, ambapo mwananchi atakuwa anachangia kadiri kipato chake kinavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati wa muda mrefu ambao tunaendelea kuufanyia kazi, dunia ya sasa imeelekea katika Mpango wa Bima ya Afya kwa wananchi wote na sisi kama Tanzania tumeridhia azimio hilo la kidunia na sasa hivi tuko katika mchakato wa kuandaa muswada wa sheria ambao utafanya bima ya afya kuwa ni kwa lazima kwa Watanzania wote.
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kuniona na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na ya ufasaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa upande wa Zanzibar majimbo mengi tulijikusanya na tukawa tumewalipia bima ya afya watu mbalimbali, lakini baadae Mfuko huu wa NHIF ukasitisha kile kifurushi. Na sasa hivi nadhani karibu miaka miwili tunaambiwa assessment inaendelea ili kuona kwamba tunapata alternative ya ile bima ya afya ambayo ilikuwa imesitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mpaka lini au lini sasa hii assessment itakamilika ili tuje na mpango mpya tuweze kuwahudumia wananchi wetu katika majimbo yetu ambao wanahitaji hii huduma ya afya kupitia Bima ya Afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa kuna utaratibu wa kutoa bima ya afya kupitia vikundi, lakini kusudio lile naomba labda nianze kutoa maelezo ya awali ili Waheshimiwa Wabunge nanyi mnielewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tunapokuwa tunazungumzia suala la bima tunwataka watu wanaojiunga ni wale ambao hawana magonjwa pale wanapokuwa wanaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawasawa unataka kukata bima wakati gari lako limepata ajali. Sasa baadhi ya watu kilichotokea ni kwamba kuna vikundi vilikuwa vinajikusanya ambavyo tayari wana magonjwa makubwa na ya muda mrefu wanatengeneza vikundi, wanalipa hela ndogo shilingi 70,000 halafu wanaenda sasa hospitalini wanapata huduma kubwa, kwa utaratibu huo tungeweza tukaufilisi mfuko.
Kwa hiyo, baada ya kubaini kwamba, kulikuwa na changamoto hiyo, tulisitisha hilo fao, ili kuweza kupitia taratibu nzuri za kutengeneza vile vikundi na vigezo vya kuzingatia kwa hiyo, bado hiyo kazi inaendelea kufanyika na tutakapokamilisha tutautangaza upya utaratibu mpya wa kujiunga na vikundi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suluhu ya kudumu, sisi kama Serikali tuko katika hatua ya mwisho ya kuandaa muswada na utakapokamilika ndani ya Serikali tutauleta hapa Bungeni na mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika muswada huo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na niseme wazi nimeyaelewa sana majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na majibu hayo mazuri na ufafanuzi huo, wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro wamehamasika sana kwenye SACCOS na sio vikundi vya ambao wameshapata maradhi tayari, bali ni vikundi vya akinamama ambao wanafundishana mambo mengi ikiwemo ujasiriamali, scheme za elimu pamoja hiyo kujiunga na NHIF. Ni muda mrefu sasa toka mwaka jana wameandikiwa barua kusitisha zoezi hilo, lakini kwao imekuwa ni usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri haoni kwamba itakuwa sasa ni usumbufu wale akinamama kurudi kuanza upya, badala ya kuweka muendelezo kwamba walikuwepo kwenye NHIF na waendelee?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sina maelezezo kamili kuhusiana na hivi vikundi vya Mkoa wa Kilimanjaro ambavyo Mheshimiwa Mbunge anaviongelea, mimi nimuombe sana Mama Shally Raymond baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu tuonane anipe maelezo na mimi nimtume Meneja wangu wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro aende akavitembelee na kuvikagua vikundi, kwa sababu tunapozungumzia vikundi vya washirika na vikundi hivi vya SACCOS ni vikundi ambavyo na sisi tumekuwa tunavihamasisha vijiunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichotaka tuweze kupata maelezo kidogo tuweze kubaini changamoto zilizopo na tuweze kuchukua hatua kwa haraka zaidi.
MHE. NURU AWADHI BAFADHIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa wananchi wengi wamehamasika katika kujiunga na bima ya afya, wananchi hawa wanapofika hospitalini daktari anaweza akamuandikia dawa moja paracetamol nyingine anaambiwa akanunue. Je, Serikali inatwambiaje kuhusu hawa Wananchi wanaoambiwa wakanunue wakati wao wamejiunga na Bima ya Afya, ili waepuke makali ya maisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 30 hadi shilingi bilioni 270 katika bajeti ambayo tumeipitisha mwezi Julai mwaka huu; hali ya upatikanaji wa dawa nchini sasa hivi ni zaidi ya 90%; lakini sambamba na hilo mwezi Februari tulitoa mwongozo wa utoaji huduma za afya na aina za dawa ambazo zitatumika katika kila ngazi kwa aina ya ugonjwa na orodha hii tumejaribu kuihuisha pamoja na wenzetu wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo tumeanzisha utaratibu wa maduka ya dawa muhimu ambazo haziko katika orodha yetu ya dawa zile muhimu ambazo ni 167 ili yale maduka yaweze kutoa dawa zile ambazo ziko nje ya utaratibu wetu wa hizi standard treatment guideline lakini zinahitajika katika utaratibu wa bima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na nimhakikishie Mbunge kuwa tunaendelea kuboresha mfumo huu kuhakikisha kwamba dawa zote ikiwa na zile ambazo zilikuwa zinahitajika kwa wagonjwa wa bima zinapatikana katika hospitali zetu za umma.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa nitapenda nikuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Rais John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kabisa kutoa elimu bure kwa watoto wote; na kwa kuwa, wazazi wengi wa jamii ya kifugaji hawajajitokeza kuwaandikisha watoto wao badala yake wanaamua kuanzisha shule zao ama kufungua shule zao na kuwapeleka watoto wao. Napenda kujua sasa je, Serikali mna taarifa na uwepo wa shule hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, kama Serikali inafahamu uwepo wa hizo shule ni nini sasa mkakati wa kuhakikisha mnazisaidia shule hizo, ili ziweze kufanya vizuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilikuja na mpango wa elimu bure. Lengo ni kuhakikiksha kwamba kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya kuendelezwa kwa mujibu wa sheria kupitia nyanja ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la msingi ambalo aliuliza kwamba, je, tuna ufahamu wa hizi shule bubu, ambazo naziita shule bubu;-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge kama ana taarifa ya hizi shule basi na sisi atujulishe kwa sababu shule zetu zote za msingi ni shule ambazo zinatambuliwa Kiserikali na zimesajiliwa na Serikali na zinapata ruzuku na sisi tunapeleka walimu. Kama kunakuwa na shule bubu napata shida kuelewa kwamba hizo shule zimesajiliwa wapi? Hao walimu wanawapata wapi na aina ya elimu ambayo wanaitoa ni elimu ya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge kama ana taarifa ya hizi shule, basi atujulishe Serikali, ili tuweze kuzitambua. Na kama tukiona kwamba, zina mazingira ambayo na sisi kama Serikali tunaweza kuzichukua, basi tutaweka utaratibu wa kuzirasimisha rasmi.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kuchukua hatua kali za kuzuia ukeketaji jamii zinazojishughulisha na ukeketaji zimekuja na njia mpya za kuwakeketa watoto wakiwa bado wachanga. Je, Serikali inalifahamu hili na kama inalifahamu ni hatua gani zimechachukuliwa mpaka sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa sita nilipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika pale Arusha liliibuliwa suala la ukeketaji wa watoto wachanga. Baada ya Serikali kubana na kutoa elimu ya kutosha na kwa watoto kujitambua mara nyingi watoto hawa ambao wana umri mkubwa wamekuwa wanatoa taarifa na sisi tumekuwa tunachukua hatua. Sasa kuna baadhi ya wazazi ambao wameendelea na sasa hivi wamehama kutoka kukeketa mabinti ambao umri umekuwa wamehamia katika kukeketa watoto wachanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunalitambua hilo na tumeshatoa maelekezo katika wizara yangu ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto idara kuu ya maendeleo ya jamii kushirikiana na idara kuu ya afya kuweka utaratibu mahususi ambao tutaanza kubaini watoto wote ambao wanakeketwa wakiwa na umri mdogo hususani pale watoto wanapokuwa wanaenda kliniki. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina amini swali la msingi lilikuwa linahusu watoto kunyimwa haki yao ya kwenda shule kutokana na mila na destruri. Pamoja na mila na desturi sasa hivi au kwa muda mrefu kumezuka tabia ya wazazi hususani wanawake wakitembea na watoto yaani wakiwa na watoto wao wadogo au watoto wa kukodi kwa ajili ya kuombaomba, hali inayopelekea watoto hawa wasiende shule kwa sababu wakiwa na wale watoto maana yake wananchi watawahurumia na kuwapa msaada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inajua kwamba kuna hili jambo na kama inajua ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wazazi hao hawatumii watoto wao kama chambo cha kupata misaada na watoto hawa waweze kwenda shule kwa sababu bila hivyo watoto hawa wataendelea kuwa nyumbani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Susan Lyimo ameuliza swali zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haki za msingi za mtoto ni pamoja na kuendelezwa, kulindwa, kutunzwa na kutotumikishwa kazi nzito. Swali hili ambalo ameliuliza katika maudhuhi yake yote haya haki zote hizi za msingi za mtoto zinavunjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwaombe na tumeshatoa maelekezo kwa wataalam wetu ndani ya Wizara, kwanza tumefanya katika haya majiji makubwa sensa ya kubaini watoto wote ambao wanaishi katika mazingira hatarishi na tumebaini kama watoto karibu 7,000. Mpaka sasa hivi tumeweza tuwarudisha watoto zaidi ya 1,000 majumbani kwao kutegemea na nature ya matatizo ambayo tumekutana nao, lakini tunajua database ya watoto ambao tunao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuwasisitiza Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii hususani katika haya majiji makubwa kuhakikisha kwamba hawa wakina mama ambao wana tabia kama hizo ambao watoto hawaendi shule na watoto wanatumikishwa kazi nzito tunaweza kuwabaini na kuchukua hatua za msingi ili kukomesha kabisa matatizo kama haya. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza mswali ya nyongeza, nina maswali mawili ya nyongeza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa Wizara haidhibiti kope bandia na kucha bandia lakini bado zina madhara makubwa sana kwa watumiaji hasa wanawake.
Je, Serikali haioni umefikia wakati kupitia Wizara ya Afya na TFDA kufanya utafiti ili kubaini ukubwa wa tatizo?(Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kuwa wagonjwa takribani 700 hupelekwa Muhimbili kutokana na athari za kujibadili rangi.
Je, Serikali haioni umefikia wakati kuwa na mpango kabambe wa kuihabarisha jamii na hasa wanawake kubaki na rangi zao za asili na kuepuka kutumia vipodozi vyenye madhara na hasa wanaume wawe ndiyo waelimishaji? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kufanya tafiti na kubaini madhara ya kucha na kope bandia na baada ya hapo sasa tutaanza kuwa na mfumo wa kuwa na takwimu mbalimbali kuhusiana na madhara haya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza je, Serikali hatuoni umuhimu wa kuhabarisha jamii kuhusiana na vipodozi ambavyo vinabadilisha rangi ya mwili. Naomba nitumie fursa hii kutoa elimu kidogo kwa Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, Mwenyezi Mungu alituumba na hizi ngozi zetu hizi kwa makusudi yake mahsusi. Kwanza ngozi hizi ni moja ya kinga ya mionzi ya ultraviolets ambayo ngozi inatukinga dhidi yake, lakini pili, ngozi hii ni sehemu ya kinga za mwili ama kizuizi cha kinga ya mwili pale wadudu ama bakteria ama vijidudu vya aina yoyote vinapotaka kuingia katika miili yetu vinazuiliwa na ngozi zetu. Tunapokuwa tunajichubua ngozi zetu tunaziondoa kinga hizi na tunaondoa kinga hii dhidi ya miale hi ya ultraviolet, lakini tunaondoa kinga hii dhidi ya vimelea vya wadudu hatari.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mtu ambaye anafanya kujichubua ngozi anaingia katika madhara ya magonjwa ya ngozi, madhara ya kupata saratani ambayo inatokana na vimelea vilevile miale ya jua. Kwa hiyo, mimi naomba kutoa rai tu kwa Watanzania wote ambao wanatusikiliza na Waheshimiwa Wabunge ngozi zetu za asili ni urembo uliotosha, kama Wabunge tulizingatie hilo na wanaume tushiriki, rangi ya asili... naishia hapo (Makofi/Kicheko)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru na ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu.
Mheshimiwa Spika, Jiji la Mwanza ni moja kati ya majiji yanayokuwa kwa kasi sana hapa nchini na hasa kwa ongezeko la watu na kasi ya ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi inaendelea kuwa kubwa sana.
Sasa ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kasi ya idadi ya uundaji wa kamati hizi za ulinzi na usalama; kamati 11 kwenye mitaa11 peke yake kati ya mtaa 175, anadhani kasi hii inatosheleza kukabiliana na changamoto hii ambayo ipo katika Jiji la Mwanza na maeneo mengine?
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, tunafahamu kwamba pamoja na tafiti nyingi ambazo zimefanywa moja ya jambo kubwa ni hao wazazi kuwatumikisha watoto walioko kwenye mazingira yanayoonekana ni hatarishi. Nini sasa mkakati wa Serikali madhubuti kwa ajili ya wazazi wanaowatumikisha watoto na mifano ipo. Ukienda pale Dar es Salaam ukiwa unapita barabara ya Ali Hassan Mwinyi, barabara ya Nyerere pale Mwanza na Kenyatta wako wazazi wana kaa kando ya barabara wanatuma watoto kwenda kuomba magari yanaposimama na watoto wanapopewa wanapeleka kwa wazazi wao. Nini mkakati wa Serikali kukomesha masuala yote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kasi hii ya uanzishaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto bado inasuasua.
Naomba nitumie fursa hii kuwahimiza na kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanatekeleza agizo la Serikali la kuanzisha kamati za ulinzi kwa wanawake na watoto ambayo iko katika mpango wa mkakati wetu wa kitaifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Tungependa kuona kabla ya mwaka huu kuisha kamati hizi zimeanzishwa katika ngazi zote kuanzia ngazi ya taifa mpaka katika ngazi ya vitongoji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mabula lilikuwa linauliza kuhusiana na wazazi kuwatumikisha watoto, kwa maana ya omba omba. Watoto wana haki zao za msingi ambazo zimebainishwa kisheria katika sheria hii ya mtoto ya mwaka 2009. Baadhi ya haki hizi za mtoto ni pamoja na haki ya kutunzwa, haki ya kulindwa, na haki ya kutokutumikishwa kazi nzito.
Sasa Mheshimiwa Mbunge ametuuliza nini sisi kama Serikali tunafanya. Nimeeleza kwamba tumetengeneza mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na moja ya mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba ukatili huu na kutumikishwa huku kwa watoto kunadhibitiwa kupitia mpango mkakati huu.
Vilevile kwa kupitia hizi kamati za ulinzi wa wanawake na watoto tunatarajia kwamba zikiweza kufanya kazi vizuri hii ni moja ya changamoto ambayo inaweza ikatatuliwa kwa kupitia kamati hizi.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kutokana na mazingira halisi ya watoto hawa chances za kupata maambukizi ya UKIMWI ni kubwa sana. Serikali sasa haioni umuhimu wa kuangalia afya za watoto hao kabla ya kuwapatia settlement ili kuepusha maambukizi mapya katika jamii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba watoto ambao wanaishi katika mazingira hatarishi wako katika risk kubwa zaidi ya kupata ya kupata maambukizi ya magojwa mbalimbali za zinaa ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa UKIMWI. Sisi kama Serikali mkakati wa kwanza ni kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata malezi mazuri ya familia zao na pale inaposhindikana jamii inahusika kabla ya sisi kama Serikali kuja kuchukua majukumu ya malezi haya.
Mheshimiwa Spika, vilevile mimi niendelee kuwaomba, kwa sababu watoto hawa wengi wako kule mitaani na wako katika jamii zetu, tuombe tu kwamba sisi kama jamii tushirikiane na Serikali katika kuhakikisha watoto hawa wanapata malezi stahiki. Kama Serikali tuna mpango mkakati mbalimbali ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI.
Kwa mujibu wa takwimu za hali ya viashiria hali ya UKIMWI ya mwaka 2017 imeonesha kwamba vijana nao wamekuwa katika risk kubwa sana ya kupata maambukizi ya UKIMWI. Hilo tumelitambua tumeweka mipango mikakati mbalimbali ya kuwafikia na kufanya upimaji, lakini vile vile tumeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba sasa hata ile dawa kinga ya pre exposure for prophylaxis tunaweza kuwapatia kwa baadhi ya makundi ikiwa ni pamoja na vijana.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hapa nitoe ombi kwamba ni vizuri akatuletea takwimu hizi kwa maandishi kwa sababu tatizo la kutelekeza watoto ni kubwa sana katika nchi yetu, na mfano ni pale Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama alipofanya zoezi la kuwatambua watoto waliotelekezwa. Nilikuwa naomba hapa atuletee kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa viwango vilivyowekwa vya kutunza watoto waliotelekezwa ni vidogo, lakini hata nilipopitia hii sheria haioneshi kwamba mzazi anayeacha watoto wake anatakiwa apeleke kiasi gani kwa mwezi au kiasi gani kwa mwaka badala yake ni busara ya Mabibi Maendeleo ya Jamii, badala yake ni mahakama zinatumia busara wanalipisha kiwango cha shilingi 2,000 kwa mwezi kiwango ambacho hakitoshi kabisa kutunza watoto.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka utaratibu wa kisheria utakaowafanya wazazi wanaotelekeza watoto waweze kubanwa kisheria na waweze kutunza watoto?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu baadhi ya wazazi walio wengi katika jamii yetu wanatekeleza watoto kwa kisingizio kwamba si watoto wao, na kwa sababu katika vituo vyetu vya afya na katika zahanati zetu hapa nchini hakuna vipimo vya kupima DNA.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa Serikali ina mkakati gani ili kupeleka vifaa hivi na kuweza kuwabana wazazi wote wanaokwepa kulea watoto wao kwa visingizio kwamba si watoto wao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, mwitikio wa swali hili unaonesha kwamba suala hili la utelekezaji wa watoto ni changamoto kubwa hata ndani ya nyumba yako. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Amina Makilagi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taratibu tulizonazo ni kwamba, kiwango na gharama za matunzo ambazo zinatolewa yanapatikana baada ya kufanya assessment ya yule mhusika kuona hali yake ya kipato na hali ya maisha na umri wa yule mtoto na pale ndipo mahakama inaweka utaratibu wa kiwango ambacho kinatolewa. Mimi niseme tu kwamba katika suala hili sisi kama Wizara tunaendelea kufanya mapitio ya sera zetu na vilevile kuja na sheria ambayo itajaribu sasa kufanya mapitio ya yote haya kuangalia sasa ni utaratibu gani mzuri tunaweza tukaweka kuhakikisha kwamba wale wote wanaotelekeza watoto basi wanabanwa vizuri zaidi na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Makilagi ameuliza kuhusiana na kupanua huduma za upimaji wa DNA. Niseme tu kwamba upimaji wa DNA unafanywa na ofisi au taasisi ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Upimaji huu si upimaji ambao holela mtu anaweza akanyanyuka akaenda na sampuli yake pale anapojisikia kwenda kufanya upimaji. Kuna taratibu ambazo zimewekwa kwamba ni mamlaka ikiwa ni pamoja na Mahakama, Maafisa Ustawi wa Jamii au Polisi ambao wanaweza wakaagiza na si kila mtu ambaye ukiwa na sampuli yako unafikiri kwamba mtoto si wako unaweza ukaenda pale ukafanya, hatufanyi upimaji, request zote zinapatikana kupitia mamlaka husika.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kadri ya swali namba 65 linaelezea zaidi kuhusu kutelekeza watoto na familia zao, kwa maana ya matunzo na hili jambo linakwenda sambamba kabisa na masuala ya uzazi wa mpango. Jana tulishuhudia Mheshimiwa Rais kwenye mkutano wake akisema kwamba Watanzania ambao tumeshiba tunaweza tukazaa kadri tunavyotaka bila kuwa na mipaka.
Sasa swali langu ni kwamba je, Serikali imeamua kubadilisha sera yake ya uzazi wa mpango kutokana na kauli iliyotolewa jana na Mheshimiwa Rais? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali ina Sera ya Uzazi wa Mpango na Sera yetu inasema kwamba hatujaweka kikomo cha idadi ya watoto ambayo familia inapaswa kuzaa. Sera yetu inasema mtu apate idadi ya watoto ambao anamudu kuwatunza na kuwapa nafasi kati ya mtoto mmoja mpaka mwingine. Huo ndio mwelekeo wetu wa sera na Mheshimiwa Rais hajatoka sana katika nje ya sera. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa takwimu zinaonesha ni takribani asilimia 30 tu ya akina mama wajawazito ndio wanaohudhuria kliniki.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa akina mama wajawazito ili wahudhurie kliniki na waweze kuepuka matatizo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; umbali kutoka mahali ambapo akina mama wajawazito wanapata huduma ni moja kati ya sababu zinazosababisha matatizo hayo. Kwa mfano, kwenye Jimbo la Ukerewe ambalo linaundwa na visiwa vingi, Visiwa kama Zeru, Kamasi, Bulubi, Gana vyote vile vinatumia zahanati moja.
Sasa kama Serikali ilivyofanya kwa Kituo cha Bwisya, tunashukuru, je, Serikali iko tayari kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Afya ili ama kituo hiki cha Kamasi kiweze kupandishwa na kupata pesa za kutengeneza miundombinu kuweza kutoa huduma zilizo bora kwa kina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu za hali ya utoaji huduma za afya mwaka 2015 akina mama ambao wanakwenda kliniki angalau mara moja tuko asilimia 90, lakini tunataraji kina mama waende kliniki angalau mara nne katika kipindi chao cha ujauzito, na sasa hivi tuko kwenye zaidi ya asilimia 60 katika kiwango cha kitaifa. Kwa hiyo, rai yangu bado naendelea kutoa kwa wanawake wote wajawazito katika nchi yetu kuhakikisha kwamba wanapokuwa wajawazito angalau kufika katika vituo vyetu vya kutolea (Anti-Natal Clinic) angalau mara nne ili iweze kuwasaidia kupata ushauri na jinsi gani bora ya kuweza kuhudumia ujauzito waliokuwa nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameongelea suala la umbali. Serikali inatambua hilo na tumekuwa tunaendelea kuboresha huduma za afya na hivi vituo 208 ambavyo tumeviboresha hivi karibuni na kuweza kutoa huduma nzuri za ujauzito na upasuaji pamoja na kujifungulia ni moja ya mkakati wa Serikali. Kuna mkakati wa kuongeza Hospitali za Rufaa za Wilaya, tuna mkakati wa kuongeza Hospitali za Rufaa za Mikoa na kadri tutakapokuwa tunaona mahitaji katika hivyo visiwa vingine vya Ukerewe ambavyo umevisema hatutasita kukaa na wenzetu wa TAMISEMI na kuangalia jinsi gani ya kuboresha huduma katika maeneo hayo husika.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, na mimi nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja kumbe, haya. (Kicheko)..... Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ziko sababu kadhaa ambazo nyingine hazizuiliki zinazosababisha watoto hawa kuzaliwa mapema, je, Serikali ina utaratibu gani wa kuziimarisha na kuziboresha hizi special care intensive nurseries zilizopo na zipo ngapi katika mikoa yetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi huduma kwa mtoto yeyote ambaye anatarajiwa kuzaliwa inaanza katika mahudhurio ya kliniki. Ninaendelea kusisitiza na kutoa rai kwamba wanawake wajawazito na baada ya kubaini wameshapata ujauzito ni muhimu sana kwenda kliniki mara nne, kwa sababu katika mahudhurio haya ya kliniki ndipo hapo ambapo tunaweza tukabaini changamoto kama hizo na uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa njiti. Sambamba na hilo nimesema kwamba tumetoa elimu kwa watoa huduma wetu wote katika ngazi zote kuhusiana na jinsi gani wanaweza wakawahudumia watoto njiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali sasa hivi katika bajeti ambayo mmetupitishia katika moja ya kipaumbele ambacho tumesema tutaweza kuweka katika hospitali za rufaa za mikoa ni pamoja na huduma za Neonatal ICU. (Makofi)
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, naomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) Wanawake wengi ndani ya Mkoa wa Kigoma hawana elimu ya kutosha kuhusu uzazi wa mpango na hata wale ambao ni wajawazito bado hawaelewi ni hatua zipi waweze kuziona na wakimbie katika vituo vya afya. Serikali mmejipangaje katika kuwapatia elimu wananchi wa Kigoma?
(b) Wilaya ya Kigoma Vijijini katika Vijiji vya Zashe, Mtanga, Kalalangabo, vijiji hivi vinakabiliwa na ukosefu wa wauguzi; hospitali ina muuguzi mmoja. Nini kauli ya Serikali katika kusaidia vijiji hivi viweze kupata wauguzi wa kutosha kwa haraka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wastani wa taifa wa matumizi ya njia za uzazi salama ni asilimia 38; asilimia 32 kwa njia za kisasa na asilimia sita kwa njia za asili, bado tuko nyuma sana, lengo letu lilikuwa tuifikie asilimia 45. Kwa hiyo, na sisi kama Serikali tumeliona hilo, tunaendelea kuweka afua mbalimbali za kutoa elimu kwa jamii, na mimi niendelee kusisitiza jamii kwamba njia za uzazi bora ni salama na tuachane na imani potofu na zitatusaidia sana kuhakikisha kwamba tunazaa, tunapata watoto kwa idadi na kwa wakati ambao na sisi tunawahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na hali ya watumishi. Tunatambua baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi. Katika mwaka huu wa fedha Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi wa afya 8,000; watumishi 6,200 kati ya hao katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na 1,800 katika Wizara ya Afya. Kwa hiyo zoezi hili litakapokamilika maeneo ambayo niliyoyataja yatakuwa ni sehemu ambayo yatapata watumishi.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, natambua kazi kubwa wanayofanya Waziri wa Afya na Naibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri waliyompelekea haya majibu wamemdanganya, kwa sababu mimi ni tomaso, naomba niambatane naye, nikapapase mwenyewe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyoko kwenye hiki kituo ni matatizo makubwa sana. Kama kuna kitu ambacho Wizara haifahamu katika kile kituo kuna wazee 52 na katika hao 52 kuna wazee wanne ni kati ya wazee waliyopigania Vita vya Pili vya Dunia.
Mheshimiwa Spika, tuna matatizo makubwa ya Watumishi wa Afya tuna Watumishi wawili tu, mmoja anakaa Babati Mjini na mwingine anakaa kilometa moja na nusu kutoka kwenye kituo, maana yake usiku kukitokea dharura wale wazee hawapati huduma za haraka. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea nyumba wale watumishi wapate kuishi karibu na wale wazee?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nchi nzima idadi ya wazee inajulikana na kwa kuwa umri mkubwa wa uzee ndiyo unaopatikana na magonjwa makubwa nyemelezi pamoja na kuwa Serikali imesema huduma ya wazee ni bure. Je, Serikali iko tayari kuwapatia bima wazee wote nchi nzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, labda nianze kwa kusema kwamba kuwepo na idadi kubwa ya wazee ambao sasa hivi wanafikia milioni 2.7 ni ishara kwamba kumekuwa na maboresho makubwa sana katika huduma ambazo tumekuwa tunazitoa katika ngazi ya afya, vilevile hali ya lishe na matunzo ambayo tumekuwa tunayatoa kwenye jamii yetu, kwa hiyo ni kitu ambacho najivunia. Sasa hivi umri wa kuishi wa Mtanzania umefikia miaka 65 wastani, kwa hiyo, ni jambo jema ambalo tunapaswa kujivunia.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali ambayo ameuliza Mheshimiwa Anna Gidarya ni kweli tunatambua kwamba Serikali tumeendelea kuwa tunaboresha makambi haya ya wazee kadri uwezo unavyoongezeka. Pia hili ombi la kuhakikisha kwamba tunakuwa na nyumba katika kituo hichi cha Magugu, tutalifanyia kazi katika bajeti kama nilivyokuwa nimesema kwamba tuna fedha ambazo tumezitenga katika bajeti hii ambayo ipo.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, sasa hivi Serikali ipo katika mapitio ya sera ya afya. Katika sera ambayo tunaenda nayo sasa hivi ya mwaka 2017/2018 ambayo tunayo sasa hivi, tumekuwa tunasema kwamba matibabu kwa wazee yatakuwa ni bure, lakini sasa hivi Serikali tunaelekea katika mfumo wa kuwa bima ya afya kwa wote na masuala ya haki ya wazee yatazingatiwa katika sera hii mpya.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema tu kwamba kuhusiana na ombi lake la ziara kwenda kupapasa niko tayari kufanya Jumapili. (Kicheko)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza ninasikitika hiyo kauli aliyotoa Mheshimiwa Waziri hapo na wale wazee ambao, maana yake mzee anaanzia kijana, mtoto ambaye inawezekana mazingira yake yote alikuwa ni yatima. Sasa huyu pia unamfanyaje, maana yake Serikali mnakwepa wajibu. Swali langu ni kwamba Serikali ya Awamu ya Nne iliahidi kutoa pensheni kwa wazee na tafiti zilishafanyika, kauli ikatolewa hapa Bungeni. Je, ni lini Serikali itatoa pensheni kwa wazee wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize majibu ambayo amesema Mheshimiwa Waziri, kwa mujibu wa Sera yetu ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo inatamka kwamba majukumu ya kwanza ya kumtunza mzee ni familia, ndugu na jamii husika kabla Serikali haijabeba majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea tunahudumia wazee zaidi 500 ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo bado tunaendelea kusisitiza kwamba majukumu ya awali ya msingi yawe katika ngazi ya familia na jamii kabla ya Serikali haijachukua majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake ambalo anauliza kwamba ni lini na tumefikia wapi katika pensheni hii ya wazee, bado Serikali inaendelea kulitafakari jambo hili, kuangalia utaratibu mzuri zaidi wa kuweza kulitekeleza. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa malengo ya kuanzishwa kwa kituo hicho ilikuwa ni maamuzi ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya jinsia na wanawake; na kwa kuwa malengo haya yalijikita katika kuhakikisha kunakuwa na kituo ambacho kitasaidia uwezeshwaji wa ufanyaji wa tafiti na kuhifadhi machapisho hayo ya utafiti na kuwashauri watunga sera kuhusiana na masuala mazima ya maendeleo ya wanawake na jinsia; ni ukweli kwamba pamoja na kuzindua kituo hiki lakini Serikali haijweka msisitizo wa kukiwezesha kituo hiki kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Je, Serikali sasa iko tayari kufufua mchakato huu wa kukianzisha kituo hiki ili kiweze kutimiza malengo ya uanzishwaji wa kituo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutenga eneo kama ambavyo wameeleza katika Chuo cha Tengeru ni jambo moja na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali watu na rasilimali fedha ni jambo lingine. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha inakipatia fedha kituo hiki ili malengo ya uanzishwaji wake yaweze kutimia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Paresso amesema kwamba je, Serikali ina mkakati gani wa kukifufua. Niseme tu kwamba kituo hiki kipo na nilipata fursa ya kutembelea Chuo cha Tengeru na kukitembelea hiki kituo. Kipo na kinafanya kazi. Kwa hiyo kaika hoja kusema kwamba tunahitaji kukifufua hili halipo kwa sababu ni kituo ambacho kinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kuongeza rasilimali watu na rasilimali fedha kituo hiki pamoja na kwamba lilikuwa ni azimio, sisi kama Serikali kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii tunaendelea kukihudumia kituo hiki kuhakikisha kwamba kinafanya kazi na kadri rasilimaliwatu itakapokuwa inaongezeka na sisi tutaongeza watumishi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeenda mbali zaidi; kwa sababu ya majukumu ya kituo hiki katika kutoa elimu na uelewa katika masuala ya jinsia tumeendelea kuwasiliana na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu na taasisi mbalimbali ambazo zinafanya tafiti katika masuala ya jinsia ili nao watusaidie kutupatia yale machapisho yao na kuyahifadhi katika maktaba zetu hizi kwa lengo la kupanua wigo kwa kupata machapisho mbalimbali yanayohusiana na masuala ya jinsia.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, kwa kuwa maradhi ya figo ni hatari sana. Je, Mheshimiwa Waziri atawasaidia vipi wananchi wanaoishi vijijini ili kujitambua mapema kwamba tayari wameshaambukizwa na maradhi hayo na wakati huo baadhi yetu hatupendi ku-check afya zetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna baadhi watoto wachanga huzaliwa na maradhi ya figo wakati wazazi wao hawatambui watoto kuwa na maradhi hayo na kupelekea mtoto kusononeka. Je, Wizara inatoa elimu gani kwa wazazi baada ya kuzaa ili kuwa na hofu ya maradhi hayo kwa watoto wao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli magonjwa ya figo yanazidi kuongezeka na hoja yake ya msingi ilikuwa, je, wale watu ambao wako vijijini wanawezaje kutambua magonjwa haya. Niendelee kusisitiza kwamba magonjwa haya ya figo visababishi vikubwa sana kwanza ni ugonjwa wa kisukari lakini la pili ni ugonjwa wa shinikizo la damu. Tunaweza tukazuia magonjwa haya tukizingatia mambo makubwa matatu. La kwanza ni kuhakikisha kwamba tunapata lishe bora badala ya bora lishe. Pili, kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi lakini la tatu ni kuhakikisha tunakuwa na matumizi sahihi na yasiyopitiliza kiwango ya pombe na sigara. Kwa hiyo, niendelee kuhamasisha kwamba tuendelee na utamaduni wa kufanya check-up ya miili yetu mara kwa mara na iwapo tutafanya hivi, tunaweza tukayagundua magonjwa haya mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia kwa watoto wachanga. Watoto wachanga nao wanaweza wakapata magonjwa ya figo kwa sababu ya maumbile ya figo zao kumekuwa na changamoto wanaweza wakazaliwa na tatizo la figo. Dalili gani ambazo mtu anaweza akazigundua kama mtoto anaweza kuwa na tatizo la figo? Mara nyingi mtoto anakuwa anavimba macho, sura, tumbo, miguu na sehemu mbalimbali za mwili. Mara nyingi unakuta hata ile haja ndogo haipati kwa kiwango kinachostahili. Niendelee kusisitiza kwamba iwapo mtu ataona mtoto ana dalili kama hizo afike katika vituo vya afya aweze kupata ushauri sahihi.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wagonjwa wa figo wako pia kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini. Kwa vile wanapokuwa na matatizo hayo wanatakiwa waende hospitali ya wilaya ili waweze kupata referral ya kwenda Hospitali ya Muhimbili. Je, ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Jimbo la Kigoma Kusini ili wagonjwa wangu wa vijijini wenye ugonjwa wa figo waweze kupata eneo la kutibiwa na kupata referral ya kwenda Muhimbili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunaendelea kuboresha mifumo yetu ya rufaa na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na za magonjwa haya ya figo. Sasa hivi huduma hizi kwa kiasi kikubwa sana tumeweza kuzisambaza sehemu mbalimbali za nchi, tunazijengea uwezo hospitali zetu za rufaa za mikoa vilevile tunazijengea uwezo hospitali zetu za wilaya kuweza kutambua dalili za awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, magonjwa haya ya figo yanasababishwa sana na magonjwa makubwa mawili ya kisukari na shinikizo la damu ambayo kama hatutaweza kuyadhibiti vizuri na kupata matibabu yaliyo sahihi yanapelekea mtu kupata ugonjwa wa figo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba swali la msingi la Mheshimiwa Hasna Mwilima alikuwa anaulizia ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya katika Jimbo lake la Kigoma Kusini ili wananchi wake waweze kupata huduma hii. Katika bajeti hii ya mwaka huu Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za wilaya. Naamini hospitali ya wilaya hii itakuwa ni moja kati ya hospitali hizo zitakazojengwa.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri amesema na mimi najua kwamba ugonjwa wa kisukari ndiyo unaoongoza katika magonjwa yasiyoambukiza na mimi mwenyewe ni muathirika. Wataalam wanasema ugonjwa huu hauna dawa hasa Diabetic 1 lakini wataalam wengine hasa wa tiba mbadala wamekuwa wakidai kwamba ugonjwa huu unatibika. Ndiyo maana wengi wamekuwa wakienda huko ama wanatibiwa kweli au hawatibiwi. Naomba kujua Serikali inasema nini kuhusiana na hizi tiba asilia ambazo kimsingi naona kama zinapotosha. Nilikuwa naomba kauli ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeza kwa kuwa ni mfuatiliaji mzuri sana masuala ya magonjwa yasiyoambukiza hususan ugonjwa huu wa kisukari. Hoja yake ya msingi amegusia suala la tiba asili ya magonjwa ya kisukari. Naomba nitoe kauli kwamba hadi hivi sasa hatuna dawa yoyote ya tiba asili ambayo sisi kama Serikali tumeithibitisha kwamba inatibu ugonjwa wa kisukari. Nitumie nafasi hii kuwaambia watoa tiba za asili kwamba tunawahitaji na tunawataka wajisajili kama watoa huduma lakini kama kuna mtu ambaye anadhani ana tiba/dawa inayoweza kusaidia katika magonjwa yoyote yale kuna utaratibu wa kuhakikisha dawa hiyo inafanyiwa utafiti na inasajiliwa kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba mpaka sasa hatuna dawa ambayo inatibu ugonjwa wa kisukari.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri hayaendani na hali halisi iliyopo Amani kule taasisi kwenyewe (NIMR) ambapo majengo hayo yapo. Mheshimiwa Waziri wa Afya alifika kule na aliyaona majengo yale na baada ya kuongea na wananchi aliahidi kwamba angeweza kuleta shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba chuo kikuu kile kinaanza kujengwa au majengo yale yanaanza kufanyiwa ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, NIMR ya Tanzania ina sifa kubwa sana duniani kutokana na utafiti inaoufanya. Kwa sababu majengo yale yamekaa muda mrefu na kugeuka kuwa magofu, kuna mpango gani wa haraka wa kuweza kuyanusuru?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, hata kama sheria hairuhusu kuanzisha chuo kikuu lakini inaweza kubadilishwa kwani majengo yale yana facilities zote za kuanzisha hicho chuo kikuu. Kwa kuanzia ni lini mtaanza kutoa hayo mafunzo ya vyeti pamoja na diploma ili kuweza kuokoa hali ya pale ilivyo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana amekuwa akifuatilia suala hili la vituo vyetu vya utafiti vya Amani pale Muheza. Niseme kwamba Mheshimiwa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto alipita pale na hilo tunalikiri na aliahidi kwamba majengo yale yatafanyiwa ukarabati. Niendelee kusisitiza kwamba ahadi hiyo bado ipo na sisi kama Serikali tunaendelea kujipanga kutafuta fedha ili kuyafanyia ukarabati majengo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi taasisi yetu hii ya NIMR tunaendelea kuijengea uwezo. Tulipokuwa tumeianzisha mwanzoni makusudio yalikuwa ni kuelekeza nguvu zaidi katika magonjwa ya kuambukiza lakini sasa hivi kumekuwa na mabadiliko makubwa sana katika magonjwa yasiyoambukiza na tumeanza kuona tunakuwa na magonjwa haya. Kwa hiyo, tumewaelekeza NIMR vilevile kuanza kujikita katika kufanya utafiti katika magonjwa yasiyoambukizwa. Kwa hiyo, tutapokuwa tumefanya ukarabati huo tutajaribu sasa kuhakikisha kwamba pamoja na hizi tafiti ambazo tumekuwa tunazifanya katika magonjwa ya kuambukiza vilevile tunaanzisha utaratibu wa utafiti kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Sheria ya NIMR hairuhusu sisi kuanzisha chuo kikuu lakini haituzuii kufanya kazi na baadhi ya vyuo vikuu kwa kujenga ushirikiano wa kufanya tafiti (reseach). Katika swali lake ameuliza ni lini tutaanza sasa kutoa yale mafunzo ya muda mfupi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kujipanga na katika mwaka wa fedha ujao tunatarajia kwamba tutaanza kutoa mafunzo mafupi mafupi katika kada mbalimbali za afya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri umekiri kwamba katika Mkoa wa Rukwa hakuna Hospitali ya Wilaya hata moja na nia ya sisi wawakilishi na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha sio kuepusha au kupunguza vifo vya wanawake na watoto ila ni kuhakikisha suala hilo linapotea kabisa linakwisha kwa ya kuwasaidia wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la kuepusha vifo hivyo sio kuandaa tu vitanda ila ni kuhakikisha tunatengeneza mazingira rafiki ya mama anayejifungua pamoja na mkunga. Kwa maana hiyo kunahitajika vitanda ambavyo vitakuwa na instrument kwa ajili ya kuepusha masuala hayo. Ni lini sasa Serikali itapeleka vitanda ambavyo vitakuwa rafiki kwa wauguzi pamoja na wanawake wanaweza kujifungua?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri wa Afya alipokuja Sumbawanga Mjini katika maadhimisho ya siku ya wanawake aliahidi kuleta magari mawili ambayo yataendana na mazingira yaliyopo katika Mkoa wa Rukwa ambayo yataweza kuwasaidia wanawake kutoka kwenye mazingira walionayo kuna umbali mrefu kufika kwenye Hospitali ya Rufaa. Ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kuhusiana na suala la vitanda, Serikali hii ya Awamu ya Tano katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 269 na bajeti hii imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hatuna uhaba wa fedha, tatizo lililopo ni kwamba Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa, Vituo vyetu vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya hazijaagiza vitanda hivyo. Kwa hiyo, niendelee kumwomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na hospitali yake ambapo ina upungufu wa viwanda ili hospitali hiyo husika kwa kutumia fedha ambazo Serikali inazitoa waweze kuagiza vitanda hivyo. Vitanda vipo katika Bohari yetu ya Madawa ya MSD.
Swali lake la pili, ameuliza ni lini magari ambayo Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya kuweza kuyapata. Sasa hivi Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza magari na yatakapopatikana ahadi hiyo itatekelezwa.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini nina maswali yangu mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wengi hawafahamu waende wapi pale matatizo wanapohitaji unasihi na hii imejidhihirisha hivi karibuni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza wanawake waliotelekezwa waende kwake, wamejitokeza wengi sana, sambamba na hilo na wanaume pia walijitokeza. Sasa nilitaka kufahamu je, Serikali haioni imefikia wakati wa kuhabarisha jamii kwamba huduma hizi zinatolewa ili waweze kupata huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii wako katika ngazi mbalimbali, je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga siku maalum walau siku mbili kwa wiki na kutenga maeneo maalum ili wananchi waweze kwenda kupata ushauri wa unasihi badala ya kusubiri kwenda kipindi cha muda wa kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kuhusiana na suala la uelewa wa wananchi, tunapokea ushauri wake na tutaufanyia kazi kwa lengo la kujengea uelewa na nitoe rai tu kwa wananchi kwamba huduma za ustawi wa jamii zipo katika Halmashauri zote na katika baadhi ya maeneo hadi katika ngazi ya kata. Wanapokuwa na changamoto zinahusiana na masuala ya migogoro ya familia masuala ya ustawi, watoto yatima, waende katika ofisi za Halmashauri ama za ngazi ya kata kuweza kupata huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili katika swali lake la nyongeza ameulizia kwamba kwa nini Serikali isitenge siku maalum na maeneo maalum ili huduma hii iweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Maafisa Ustawi wa Jamii ni waajiriwa wa Serikali na wapo muda wote kuweza kutoa huduma hizi kwa hiyo, huduma hizi zinatolewa siku zote za kazi katika muda wa masaa ya kazi katika maeneo husika ngazi ya Halmashauri, kata na mitaa ambapo Maafisa Ustawi wa Jamii wapo.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini niseme tu suala la tathmini linachukua muda mrefu na tathmini hii haijulikani itakwisha lini. Narudi palepale kuuliza swali langu la nyongeza, ni lini Serikali italeta Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tatizo la upungufu wa watumishi katika sekta ya afya limekuwa ni tatizo kubwa hata katika vituo vyetu vya afya na zahanati. Je, Serikali inajipanga vipi kuhakikisha upungufu tulionao katika vituo vya afya na zahanati unakwenda kumalizika kabisa ama kupungua kwa kiasi kikubwa? Nakushuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba bado tuna changamoto kubwa sana ya watumishi katika sekta ya afya, watumishi tuliokuwa nao ni takribani asilimia 52 tu ya idadi ya watumishi ambao hatunao. Katika mkakati wetu wa kwanza ameuliza ni lini tutapeleka Madaktari Bingwa, Serikali inaendelea kufanya jitihada kama nilivyosema tumeshakamilisha zoezi la tathmini tunajaribu sasa kuhakikisha kwamba wale wachache tuliokuwa nao baada ya kupata taratibu za kiutumishi tutawahamisha, lakini sambamba na hilo tunatarajia kupata kibali kipya cha ajira ambao wale watumishi watasambazwa katika maeneo mbalimbali ya kwenye uhitaji ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, Hospitali za Wilaya, Vituo vya afya na Zahanati kulingana na mahitaji. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi hii na nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuweza kuniwezesha kunipa fedha za Kituo cha Afya cha Mwese na fedha za Kituo cha Afya cha Mishamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali dogo la nyongeza ambalo nilitaka kujua, Mkoa wa Katavi kwa ujumla na Wilaya ya Tanganyika ambako kuna Kituo cha Afya cha Mwese, Kituo cha Afya cha Kalema, Kituo cha Afya cha Mishamo, sambamba na zahanati zilizomo kwenye Wilaya ya Tanganyika na Mkoa kwa ujumla wa Katavi kuna uhaba mkubwa sana wa madaktari kwenye sekta hiyo ya afya. Ni lini Serikali ina dhamira ya dhati kutoa tatizo la uhaba wa watumishi wa sekta ya afya katika Mkoa wa Katavi hasa Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya swali la msingi nimeelezea kwamba bado ni kweli tuna changamoto kubwa sana ya rasilimali watu katika sekta ya afya. Katika mwaka huu wa fedha Serikali ilitoa kibali cha ajira cha watumishi 3,152 ambao walisambazwa katika mikoa mbalimbali, lakini vilevile nimesema katika jibu langu la msingi tunatarajia kupata kibali kipya cha kuajiri watumishi katika Serikali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Mheshimiwa Mbunge pindi kibali hicho kitakapotoka Mkoa wa Katavi utakuwa ni mmoja wa mikoa ambayo tutazingatia.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga linafanana kabisa na tatizo lililopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Kwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inatakiwa kupokea wagonjwa 50 kwa siku, lakini inapokea wagonjwa zaidi ya 200; na hospitali hii ina uhaba mkubwa sana wa Madaktari Bingwa, vifaatiba kama kama CT-SCAN, MRI, pamoja na gari la kubebea wagonjwa. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha lakini na Madaktari Bingwa pamoja na gari la kubebea wagonjwa ili wananchi wake waweze kupata huduma bora za afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inakiri kwamba kuna uhaba wa Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kama nilivyowaeleza katika majibu yangu ya msingi changamoto hiyo tunaitambua, tumeweza kupeleka madaktari wachache, lakini tunatambua kwamba bado hawatoshi. Katika kibali kipya ambacho tutakachokipata mahitaji ya Mkoa wa Singida yatazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika hili ni ameulizia suala la vifaa, niendelee kumuomba Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Singida kama nilivyosema sasa hivi fedha kwa ajili ya bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaatiba tunavyo vya kutosha, hospitali zinatakiwa ziainishe vifaa ambavyo wanavyovihitaji ili kuweza kuvipata. Tahadhari yangu ni kwamba teknolojia nyingine ambayo wanaiulizia ya kwamba kuwa na CT-SCAN na MRI katika ngazi hizi kwa sasa bado hatuna uwezo na wataalam wa kuweza kuzisimamia na kuvihudumu. CT-SCAN na MRI tumeanza katika miongozo yetu zinaanza kutumika katika ngazi za Hospitali za Kanda. Kadri tutakavyokuwa tunajenga uwezo basi tutazishusha chini katika ngazi ya rufaa Hospitali za Rufaa za Mikoa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla sijauliza swali la nyongeza kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mawaziri wote wanaohusika kuona wahudumu kwenye wizara hii kwa kunipunguzia tatizo la wafanyakazi, baada ya kunipatia wafanyakazi sita kwenye kada hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya shida iliyopo wale wafanyakazi sita imekuwa kama tone la damu kwenye bahari. Kwa hiyo, shida iliyopo katika hospitali yetu ya Wilaya ya Liwale ni kubwa sana kiasi kwamba wauguzi wawili wanahudumia wodi tano kwa wakati mmoja, jambo hili ni baya sana vilevile linapunguza ufanisi wa kazi.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuniongezea wafanyakazi kwenye kada hii ya wauguzi ili kuongeza ufanisi kwenye hospitali ile ya wilaya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba tunajua na tunatambua mahitaji ya watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na Manesi katika hospitali za Liwale. Pindi tutakapopata watumishi basi Wilaya ya Liwale ni moja ya wilaya ambayo na sisi tutaizingatia.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme Kigoma ni wingi wa umeme na bahati mbaya sana Kigoma bado haijaunganishwa na Gridi ya Taifa na hata mpango ambao ulisainiwa kwa msaada wa Serikali ya Korea ambao Waziri wa Fedha alisaini takribani mwaka na nusu uliopita bado kabisa kuanza kutekelezwa. Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Mto Malagarasi, Igamba III ambao ndio jawabu la kudumu la umeme katika Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe sahihisho kidogo sio Malagarasi Igamba III; ni Malagarasi Igamba II. Baada ya kusema hayo sasa ni kweli kabisa mradi wa Malagarasi ilikuwa kwanza utekelezwe wakati wa mradi wa MCC mwaka 2008, lakini ikaonekana kwamba kulikuwa kuna matatizo ya REA species.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe taarifa katika Bunge lako tukufu ni kweli kabisa mradi huu sasa utaanza kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha na tumeshatenga fedha na juzi Mheshimiwa Zitto nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge tulikuwa nao wakati tunakamilisha majadiliano ya Benki ya Maendeleo ya Dunia kwa ajili ya kufadhili mradi huo na zinahitaji dola milioni 149.5 kwa ajili ya kuutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Mbunge mradi huu unakwenda kutekelezwa kwenye mwaka huu wa fedha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, hivi majuzi tu ulizinduliwa upimaji wa VVU unaofadhiliwa na USAID, Shirika la Kimarekani, nataka kufahamu nini mkakati wa Serikali kumaliza tatizo hili hasa kitakwimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na tatizo hili la VVU hasa kwa waathirika wengi ambao kwa namna moja au nyingine dawa zimekuwa pia ni tatizo. Wapo wanaotumia kikamilifu lakini kwa wengine upatikanaji wake ni changamoto lakini pia upatikanaji wa dawa unapaswa uendane na lishe. Nini sasa mkakati katika kusaidia wananchi wale ambao kipato chao ni cha chini lakini wana maradhi haya na kutokana na ukosefu huo wa lishe wanasababisha vifo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amina Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameelekeza katika suala la changamoto za takwimu. Niendelee kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu zetu za masuala ya UKIMWI ziko vizuri. Serikali kupitia Taasisi ya TACAIDS pamoja na Wizara ya Afya, Kitengo cha UKIMWI ndio wanaoratibu takwimu zote za masuala ya UKIMWI na nimthibitishie katika malengo haya ya 90-90-90 takwimu zetu kama nchi ziko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amezungumzia suala la upatikanaji wa dawa. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba upatikanaji wa dawa za UKIMWI ni asilimia 100 na tunazisambaza nchini kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amegusia kidogo suala la lishe, ni kweli tunatambua kwamba kumekuwa na changamoto ya lishe katika baadhi ya makundi lakini sisi mkakati wetu tunajaribu sana kutoa elimu katika jamii na kwa wale ambao kabisa wanaonekana wana changamoto ya lishe basi kwa wale wachache kuna utaratibu maalum wa kuweza kuwasaidia. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika Mkoa wangu wa Arusha, Wilaya mbalimbali kama Longido, Monduli na nyinginezo na upanuzi mkubwa wa vituo vya afya ukiendelea, nataka kufahamu; Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha wanaleta wataalam wa kutosha hasa wa dawa za usingizi ili wananchi wa Arusha wapate huduma, hasa ya mama na mtoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza katika uboreshaji wa vituo vya afya takribani zaidi ya 300 nchi nzima. Hata hivyo tunatambua kwamba uboreshaji huu unaendana sambamba na kuongeza huduma za upasuaji. Sisi kama Serikali sasa hivi tumeshapeleka watumishi zaidi ya 200 kwenda kusomea masuala ya usingizi. Tunatumaini ndani ya muda mfupi huu watumishi wale watakuwa wamekamilisha mafunzo hayo na tutawasambaza katika vituo vya kutolea huduma.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. imeuliza kuhusu Hospitali ya Kibena; nimepewa majibu kidogo sana juu ya Hospitali ya Kibena lakini zaidi majibu yamejikita kwenye hospitali mpya ya mkoa inayojengwa. Hospitali ile ya Kibena ni hospitali chakavu, ina wodi moja tu ya akinababa. Wanaopata ajali na wanaougua maradhi mbalimbali wote wanalazwa katika wodi moja. Hospitali hii haina fence tangu wakati imerithiwa kutoka Kampuni ya TANWART. Naomba sasa commitment ya Serikali, ni lini Serikali itatusaidia kuboresha hospitali ya Kibena kwa maana ya wodi ya wagonjwa na fence?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imetusaidia tumepewa fedha kujenga Kituo cha Afya Ihalula, lakini hata sisi katika halmashauri yetu kwa kushirikiana na wananchi katika Kata ya Makoa wamejenga kituo cha afya, Kata ya Kifanya wanaendelea na ujenzi wa kituo cha afya, ndiyo wanakamilisha. Naomba pia commitment ya Serikali, je, ni lini itatusaidia sasa vifaa kwa ajili ya vituo hivi vya afya ambapo viwili vimekaribia kukamilika na kimoja kinakaribia kukamilika?.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi nimeeleza kwamba na bahati nzuri nimepata fursa ya kutembelea hospitali zote mbili, hii ambayo ni Hospitali ya Kibena pamoja na hospitali mpya ya rufaa ambayo tunaendelea kujenga. Sisi kama Wizara, msukumo wetu sasa hivi ni kuweka nguvu kwa kuhakikisha kwamba ile Hospitali mpya ya Rufaa ya Njombe inakamilika.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto na mimi binafsi nimeona katika Hospitali ile ya Kibena na ndiyo maana sasa hivi maboresho makubwa ambayo tunayafanya ni kupanua ule wigo wa utoaji huduma. Kwa hiyo nataka nimhakikishie tu kwamba sisi kama Serikali tunataka tukamilishe ile hospitali kubwa na ya kisasa ili huduma za msingi kwa wananchi wa Njombe Mjini ziweze kupatikana pamoja na Mkoa mzima wa Njombe.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vifaa kwa vituo vipya vya afya ambavyo tunaendelea kuviboresha, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inaendelea kununua vifaa hivyo na kadri inavyofika kutoka kwa Washitiri tutakuwa tunavisambaza, ikiwa ni pamoja na vituo hivi ambavyo viko Njombe Mjini.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ili kuondoa ile dhana kwamba hatupongezi kila kitu, naomba niseme kwamba naipongeza Wizara na hasa Katibu Mkuu aliyepita Dkt. Mpoki, kwa kutoa ushirikiano kwa Mbunge katika hili mpaka hapo tulipofika na jengo kukamilika na CT-Scan kupatikana. Swali la kwanza, ningependa kujua sasa, hiyo MRI chini ya huo Mradi wa ORIO itafika lini ili jengo lile lianze kazi? Kwa sababu tunalifuatilia na kwa taarifa tulizonazo ndani ya wiki mbili litaanza kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, vipi kuhusu wataalam (specialists), maana tunafanikiwa kwenye majengo ila mara nyingi tunakuwa na uhaba mkubwa wa specialists. Binafsi, kama ningeweza kumshauri Mheshimiwa Rais, ningemshauri huyu Dkt. Mpoki aliyekuwa Katibu Mkuu kuliko kupelekwa Ubalozini angeletwa hata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa sababu ule utaalam wake ni muhimu sana kwa Taifa na wako Madaktari wachache sana wenye utaalam ule. Kwa hiyo, kumpeleka mbali, ni kupeleka huduma mbali kutoka kwa Taifa. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa kwa kuipongeza Serikali, nami nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu katika suala hili la ujenzi wa jengo la radiolojia katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ni lini Serikali itapeleka mashine ya MRI; kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni kwamba sasa hivi Serikali kupitia Mradi wa ORIO ambao tunashirikiana na Serikali ya Uholanzi, ina kusudio la kupeleka mashine za radiolojia kwa maana ya X-Ray, Digital X-Ray, mashine za fluoroscopy, CT-Scan pamoja na MRI. Kwa hiyo, mchakato huo unaendelea. Tunategemea katikati au mwishoni mwa mwaka huu, utaratibu huo utakuwa umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, Madaktari bingwa katika eneo hili; mkakati ambao tunakwenda nao sisi kama Wizara kwa sasa hususan katika wataalam wa Sekta ya Radiolojia, tumeamua kwamba tutumie ubunifu na teknolojia ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea, huko duniani X-Rays zinazopigwa mathalan katika nchi ya Marekani, nyingine hazisomwi Marekani, zinasomwa katika nchi nyingine kwa kutumia teknolojia. Hizi mashine za Digital X-Ray ambazo tunazifunga sasa hivi, sisi kama Wizara tumeamua kuweka kituo chetu pale katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo tutaunganisha na mtandao wa fibre- optic, kutakuwa na screen pale ili picha ambazo zitakuwa zinapigwa Tanzania nzima kwa teknolojia hii, ndani ya dakika tano picha umepata. Tunaweza tukatuma kwa njia ya mtandao, zitasomwa Dar es Salaam na majibu ndani ya dakika 15 kurudishwa katika eneo husika. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri sana katika eneo hilo.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Hospitali ya Bombo katika Jiji la Tanga ndiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa; na kwa kuwa hospitali hiyo haina lift kiasi kwamba wanawake wazazi wanatengenezewa theater kule kule kwa ajili ya kuwasaidia wasipate taabu ya kubebwa na mabaunsa: Je, ni lini Hospitali ya Bombo itapatiwa lift?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nuru kuhusiana na suala la Hospitali ya Bombo. Nikiri ni kweli Hospitali ya Bombo, jengo la akina mama na watoto halina lift. Nami bahati nzuri nilipata fursa ya kwenda kulitembelea, nimeiona hiyo adha, nasi kama Serikali tumeingiza katika mipango yetu ya bajeti ili tuweze kukarabati hiyo lift.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa takwimu zinaonesha miji mikubwa nchini inaongoza kwa idadi kubwa ya kuwa na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kampeni ya Kitaifa ili kuwalinda watoto hawa na kuhakikisha wako katika mazingira salama?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa chanzo kikuu cha watoto wanaoishi mitaani ni njaa katika familia na kukosekana kwa maadili mazuri katika jamii: Je, Serikali ina mpango gani wa kukazia sheria zetu na kuhakikisha kwamba wazazi na walezi wanawajibika katika malezi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo amekuwa anafuatilia kuhakikisha kwamba watoto wa Tanzania wanapata haki na ustawi ndani ya nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, sisi kama Wizara tulianza katika hatua ya awali kwa kufanya tathmini ya ukubwa wa tatizo ndani ya nchi yetu na kwa kupitia mpango mkakati ambao nimeuelezea wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, tumeanza sasa kazi ya kwenda hatua ya pili ya kuanza kuwaunganisha wale watoto ambao tuliweza kuwabaini wanaishi mtaani na baadhi ya familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumekuwa tunaendeleza kampeni ndani ya mikoa mbalimbali ya kuweza kuwatambua watoto hawa na kuwarudisha katika maeneo yao ya makazi, lakini vilevile kuendelea kutoa elimu kwenye jamii kuhusiana na masuala ya matunzo ya watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kukazia sheria; tuna Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria hii imeweka msisitizo wa haki za msingi za watoto ambazo ningependa Bunge lako Tukufu nalo lizifahamu. Watoto wana haki takribani tano ambazo zimeainishwa kisheria; mtoto ana haki ya kuishi, mtoto ana haki ya kutunzwa, ana haki ya kuendelezwa, ana haki ya kushirikishwa katika maamuzi yanayomhusu na mtoto ana haki ya kutobaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria hii, haki za mtoto zimeainishwa vizuri sana. Kikubwa ambacho sisi kama Wizara tunaendelea kusisitiza ni kuweka misingi ya kuwasisitiza wazazi kuhakikisha kwamba wanazingatia misingi hii ya haki za watoto na kuimarisha misingi ya familia.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili ya nyongeza.
Katika majibu ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wanaandaa kampeni mbalimbali kwa ajili ya kuamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU na Serikali inasema inautaratibu wa wananchi kujipima wenyewe kwa kutumia mate yaani HIV self-testing. Napenda kujuwa mkakati huu wa Serikali wa kuwaruhusu wananchi kujipima wenyewe kwa kutumia mate umefikia hatua gani hadi sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, waathirika wakubwa wa VVU ni vijana wa rika balehe kuanzia 15 hadi 24 ambayo baadhi yao wapo katika shule za sekondari na kwenye vyuo, ningependa kujua mkakati wa ziada wa kuwafikia vijana hawa hasa walio shule ya sekondari na kwenye vyuo ili kujuwa hali zao katika mkakati wa kufikia 90, 90, 90?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeingia imeridhia malengo ya kidunia ya 90, 90, 90 na moja ya mkakati ni kuakikisha kwamba sasa tunapanua wigo wa upimaji na hususani kulenga yale makundi ya wanaume ambayo imekuwa ni changamoto kidogo. Kwa hiyo, Serikali inataka kuja na mkakati wa self-testing kama mtu kujipima mwenyewe kwa kutumia sampuli ya kina na hatua ambayo tumefikia sasa hivi mchakato ndani ya Serikali tumeshaazisha na sasa hivi ipo kwenye hatua za mwisho za maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Masoud aliongelea kwamba rika balee umri kati ya miaka 15 mpaka 24. Ni kweli kwa mujibu wa takwimu za hali na viashiria vya UKIMWI vya Mwaka 2017 imeonyesha wazi kwamba maambukizi katika kundi la vijana kati ya miaka 15 mpaka 24 yanazidi kuongezeka ndani ya nchi na hususani kwa mabinti wa kike. Baada ya sisi kulibaini hilo tumekuja na afua mbalimbali moja ni kuweka msisitizo katika suala la elimu, lakini la pili tunataka tufanye mabadiliko ya sheria kwa sababu ni wazi na dhahiri kabisa kwamba takwimu zinaonyesha mabinti wetu wanaanza kujamiana wakiwa na umri mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka tufanye mabadiliko ya sheria kushusha umri wa kuweza kutoa ridhaa ya kupima kwa sababu kwa sasa kwa mujibu wa sheria ya sasa, Sheria inasema mtu atapimwa ni mtu mzima mwenye miaka 18 na atapima kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na mtoa huduma katika sehemu za afya. Kwa hiyo, katika mabadiliko haya ya sheria tunataka sasa kushusha age of consent ili sasa hao mabinti ambao wameanza kujiamiana katika umri mkubwa na maambukizi yamekuwa ni makubwa waweze kupata ridhaa ya kuweza kupima.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri na vilevile nitambue na kupongeza jitihada za Serikali katika kusaidia makundi maalum hasa watu wenye ulemavu. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kweli Serikali imeanza utaratibu huo, lakini usambazaji wa mafuta haya hasa kwa maeneo ya vijijini bado ni tatizo. Albino wengi wanaangamia kutokana na saratani. Napenda tu kufahamu jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wanafika vijijini ili kuweza kuwanusuru watoto hawa. Nini mpango mkakati wao kuhakikisha kwamba wanawafikia? Hilo ni swali namba moja.
Swali la pili, albino wengi wanaoishi vijijini, tayari wameshaathirika na ugonjwa wa saratani; na hali za maisha kama tunavyofahamu hasa wa vijijini ni duni sana, kupata shilingi 10,000/= ni shida. Nini mpango mkakati wa Serikali kuwasaidia na kunusuru maisha ya watu wenye albinism hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, utaratibu ambao Serikali tunatumia sasa hivi katika usambazaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ni utaratibu ambao unaitwa pool system. Miaka ya nyuma tulikuwa tunatumia push system. Push system maana yake nini? Ni kwamba sisi Serikali tulikuwa tunanunua dawa, vitendanishi na vifaa tiba tunavipeleka katika vituo vya kutolea huduma ya afya pasipo kuzingatia mahitaji halisi ambayo yako kule. Kwa hiyo, hukuta baadhi ya vifaa, dawa na vitendanishi vinachina kwa sababu uhitaji haukuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ambao tunautumia sasa hivi ni wa pool system. Wao kama Vituo vya Afya wanajua mahitaji mbalimbali ya huduma na dawa, vitendanishi na vifaa tiba na wao kuingiza katika mipango yao na kuagiza kutoka MSD. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, dawa hizi na mafuta haya kwa ajili ya kundi hili la walemavu wa ngozi tunavyo ndani ya MSD, ni wajibu sasa wa Halmashauri mbalimbali na hospitali za mikoa kuziagiza kulingana na mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Amina amegusia suala la walemavu wa ngozi kwamba wamekuwa wanaathirika na ugonjwa wa kansa. Hili ni kweli, tunakiri. Ni kwa sababu jua hili ambalo ni mionzi yetu ya jua lina ultraviolet rays ambazo zinaathiri ngozi za wenzetu hawa ambao wana ulemavu wa ngozi kwa kiasi kikubwa kulinganisha na wengine ambao wasiokuwa walemavu wa ngozi na tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba wenzetu ambao wana ulemavu wa ngozi wanajikinga dhidi ya miale ya jua kwa kuvaa kofia na nguo ambazo zinakinga sehemu kubwa ya miili yao, lakini vilevile kutumia mafuta ambayo yanawakinga dhidi ya hii miale ya jua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, huduma za matibabu ya kansa ni bure ndani ya nchi yetu. Nami nawaomba sana, mtu yoyote ambaye anaona kuna mabadiliko katika ngozi yake, basi aweze kufika katika vituo vya kutolea huduma ya afya aweze kupata huduma kwa haraka.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea kidogo kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya pamoja na majibu yake mazuri; ni kwamba naomba tu niendelee kutoa msisitizo kwamba Wakurugenzi katika Halmashauri mbalimbali wajitahidi kwamba wanakuwa na idadi kamili ya haya mahitaji kwa maana ya watu wenye mahitaji, watu wenye ualbino. Kwa sababu wasipokuwa na orodha kamili ya mahitaji, inakuwa ni ngumu upatikanaji wa hizi dawa kutoka MSD. Hili limekuwa ni tatizo ambalo katika ziara ambazo nimewahi kuzifanya imeonekana kwamba mahitaji haya hayapatikani kulingana na uhalisia wa watu waliopo. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hospitali yetu ya Mpanda Manispaa ndiyo ina-act kama hospitali ya Mkoa; na ndani ya ku-act kwake hatujawahi kupata mafunzo hata siku moja; na Serikali ilitutengea kachumba kadogo sana ambako ndiko kanatunza watoto njiti, lakini hatuna kabisa Muuguzi ambaye anayefanya kazi hiyo; nasi ukiangalia ndani ya Wilaya yetu ya Mpanda, Hospitali ile Wauguzi wako wachache sana, ndiyo maana watoto njiti wanafariki kutokana na huduma inakuwa siyo nzuri; ukizingatia vifaa vyake vile vya kutunzia wale watoto hatuna: Je, ni lini sasa Serikali itatuletea hawa Wakufunzi waje waweze kutufundishia Wauguzi wetu pale katika Hospitali yetu ya Mpanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika wodi ya wazazi, ndiko kulitengwa hicho kichumba kidogo, napo kuna vitanda vitatu tu; watu wazima wanakaa mle ndani, hakuna usalama kabisa: Je, ni lini Serikali itatujengea wodi maalum kwa ajili ya watoto njiti?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge, nini maana ya watoto njiti? Watoto njiti ni wale watoto ambao wanazaliwa kabla ya mimba kufikisha umri wa miezi tisa au wanazaliwa na uzito pungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hawa wanakuwa na athari zaidi kwa sababu viungo vyao vinakuwa havijakamilika vizuri, ama havijakomaa vizuri na uwezekano wa wao kupoteza maisha kwa shida za kupumua na kupata magonjwa mbalimbali ni mkubwa sana. Sisi kama Serikali, moja ya mkakati wetu ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na tumejikita kuhakikisha katika mwaka huu wa fedha na baada ya Serikali kutukabidhi Hospitali za Rufaa za Mikoa, vipaumbele vyetu sisi kama Wizara, ni kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za magonjwa ya dharura, ujenzi wa theatre, uwepo wa ICU, lakini tumeweka msisitizo katika huduma ya mama na mtoto, vilevile kuhakikisha kwamba kuna huduma za ICU za Neonatal. Huo ndiyo mpango mkakati wetu katika ile bajeti ambayo mmetupitishia mwezi Julai, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maswali haya ambayo Mheshimiwa Amina Lupembe ameuliza, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, elimu hii tunaendelea kuitoa kwa awamu na nina uhakika kwamba Mkoa wa Katavi nako tutawafikia. Bahati nzuri nami nimefika katika ile hospitali, nimeliona hilo jengo la mama na mtoto liko katika hali ambayo siyo nzuri sana. Kama nilivyosema katika jibu letu la msingi, tunaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vyetu vya kutolea huduma, hususan Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa na kuzipatia vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke msisitizo vilevile, pamoja na hii elimu ambayo tuna upatikanaji wa vifaa, kuna utaalam wa gharama nafuu ambao tumeendelea kuwajengea uwezo wataalam wetu wa huduma za afya na jamii kwa ujumla matumizi ya kangaroo method.
Mheshimiwa Naibu Spika, kangaroo method maana yake ni nini? Ni yule mtoto njiti au yule premature baby mama anatakiwa akae nae atoe joto la ngozi kwa ngozi na imeonekana kwamba utaratibu huu wa kangaroo method umekuwa na manufaa makubwa sana katika kuhakikisha uhai wa watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ujenzi wa wodi ya watoto kama nilivyosema katika jibu langu la msingi hili tutaendelea kulijenga kwa awamu na hivi ninavyoongea kwamba wataalam wetu wa Wizara wameshapita Hospitali zote ikiwa ni pamoja na hii Hospitali ya Rufaa ya Mpanda kuangalia mahitaji ya nini kinachohitajika pale na taratibu zitakapokamilika tutajenga wodi hiyo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri naomba tu kuuliza tu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kumekuwepo malalamiko sehemu nyingi za Shinyanga na hata Kahama kwa baadhi ya wazee kutokukamilishiwa utaratibu wa kupata vitambulisho ili wapate huduma za tiba bure kama Serikali ilivyowaelekeza. Je, Serikali inachukua hatua gani kuweka maelekezo maalum kwa Watendaji wa Serikali wa Kata na hata Vijiji ili kukamilisha zoezi hili wazee wapate tiba baila usumbufu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili wananchi pamoja na Serikali hasa katika maeneo ya Msalala wamefanya kazi kubwa ya kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na hivi sasa kwa mfano Msalala tuna vituo vya afya vipya viwili, kituo cha Bugalama na Chela. Lakini vituo hivi havina vifaa tiba wala madawa ya kutosha pamoja na watumishi. Je, Serikali inachukua hatua gani kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na watumishi kwenye kituo cha afya cha Chela pamoja na Bugalama ambavyo ni vituo vya afya vipya nashukuru?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kwa lengo la kutoa vitambulisho ambavyo vitawatambua wazee zaidi ya miaka 60 ili waweze kupata matibabu kwa mujibu wa sera tunatambua kwamba baadhi ya Halmashauri hazijatekeleza hilo na nitumie fursa hii kuzikumbusha hizo halmashauri kuzingatia hili agizo la Serikali kuhakikisha kwamba wazee wote ambao wako zaidi ya miaka 60 wanapata vitambulisho.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alifanya uzinduzi wa mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wazee na Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwamba Wizara iharakishe zoezi la kufanya mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003. Lakini vilevile kuanzisha na sheria ya wazee ili sasa haya mahitaji ya wazee yawe kwa mujibu wa sheria na sisi kama Wizara tumeshaanza utekelezaji wa hilo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kuhusiana na vituo vya afya ambavyo vimeboreshwa nimthibitishie tu kwamba Mheshimiwa Mbunge kwamba baada kazi ya kukamilika ya ujenzi wa maboma ya vituo vya afya. Serikali inaendelea na utaratibu wa kupata vifaa kwa ajili ya vituo vyote vya afya ambavyo vimeboreshwa, baadhi ya vifaa vimeshafika na vingine viko njiani vinakuja.
Nimthibitishie tu kwamba Mheshimiwa Mbunge vifaa hivyo vinakuja na tutaendelea kupatia watumishi wa kutosha kadri ya uwezo na Serikali itakapokuwa inaajiri. Lakini nimuhakikishie kwamba dawa tunazo za kutosha zaidi ya silimia 90 kwa hiyo, mgao wa dawa tutauongeza kulingana na mahitaji.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya kwa sababu ni miongoni mwa Mawaziri ambao wana ushirikiano mkubwa sana katika Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Waziri amekiri kwamba Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya utaletwa Bungeni na kwa kuwa wananchi wengi waishio vijijini na mijini hawana uelewa mkubwa kuhusiana na huduma hii ya bima ya afya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha, ili waweze kujiunga na bima ya afya na kuweza kupata huduma nzuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli, sasa hivi tuna takribani asilimia 34 ya Watanzania ambao wapo katika mfumo wa bima na tunatambua kwamba Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya na huduma zimezidi kuboreshwa, lakini uwezo wa wananchi kugharamia matibabu umekuwa ni moja ya changamoto. Sisi kama Wizara tumeendelea kujikita kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma na tumeendelea kufanya uhamasishaji na tunajaribu kuja na vifurushi vipya ambavyo vinaweza vikajibu baadhi ya hizi changamoto za uwezo wa wananchi kuweza kugharamia matibabu.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alikuwa katika mikoa ya Kusini katika kuhamasisha fao jipya la washirika ili hawa wakulima ambao wako katika mazao ya mkakati basi na wao waweze kupata cover ya bima hii ya afya. Sisi kama Wizara tutaendelea kufanya hivyo kuhakikisha kwamba jamii nzima ya Watanzania wanakuwa katika mfumo wa bima ya afya.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wananchi wengi hasa wa Ulanga wamekuwa na muamko mkubwa wa kujiunga na CHF liyoboreshwa, lakini wamekuwa wakilipa hela wanapoenda hospitali huduma zimekuwa haziridhishi, na hii inatokana na usimamizi mbovu wa CHF iliyoboreshwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali mwezi Aprili, 2018 imetoa mwongozo kuwa mtumishi atakayepangiwa kuwa CHF Manager asiwe na majukumu mengine yoyote, lakini huu mwongozo umekuwa haifuatwi. Je, kauli ya Serikali ni ipi kwa watumishi hawa wanaopangiwa kuwa Mameneja wa CHF, lakini wanapangiwa na majukumu mengine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunakiri kwamba, mfumo huu wa CHF umekuwa na changamoto na sisi kama Serikali tumeiboresha, kuongeza mafao, zamani CHF ilikuwa unapata huduma katika kituo kilekile ambacho ulikatia, lakini sasa hivi unaweza kwenda mpaka katika ngazi ya mkoa. Hili tunalipokea, hii changamoto ambayo Mheshimiwa Goodluck Mlinga ameitoa kwenda kuboresha mfumo wa usimamizi wa CHF iliyoboreshwa ili iwe na matarajio na makusudio ambayo yamelenga.
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo sasa hivi mwelekeo wa Serikali ni kwenda katika One National Health Insurance Scheme kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunakuwa na bima moja ya afya kwa wananchi wote. mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tutakapoleta muswada huo Bungeni, basi mtusaidie kuunga mkono.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda Serikali isikwepe wajibu wake wa kuhudumia watu wasiojiweza. Natambua kabisa kuwa kuna walemavu wenye uwezo lakini watu wengi wenye ulemavu wana matatizo mengi; kuna wale ambao ni yatima, kuna wengine ambao wametelekezwa na kuna wengine ambao kaya zao ni maskini sana. Ni kwa nini Serikali isiwajibike kuwahudumia watu hawa wenye ulemavu hasa kwa kuwatambua na pili kuwapatia bima ya afya bure? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema wagonjwa kuna wagonjwa wengi sana wa msamaha ambao wako katika hospitali zetu. Sawa wako wagonjwa wengi lakini ni lini Serikali sasa itatekeleza wajibu wake wa kutoa ruzuku katika hospitali zetu za mikoa au hospitali zetu za rufaa kwa sababu hawa wagonjwa ambapo wengine ni watu wenye ulemavu, watoto umri chini ya miaka mitano na wazee wanakwenda katika hospitali hizi kutibiwa na hizi hospitali zinakuwa na watu wengi ambao wanatakiwa kupata vifaatiba na vitendanishi? Ni lini Serikali itatoa ruzuku katika hospitali zetu ili ziweze kujikimu na kutoa huduma bora? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kutoa huduma za afya na haijawahi kusitisha kutoa huduma ya afya kutokana na sababu eti kwamba mtu anashindwa kugharamia matibabu. Hilo lipo vizuri ndani ya Sera yetu ya Afya na kuna makundi ambayo tumeyaainisha katika sera ambapo watu wanapata matibabu bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la walemavu kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, si kila mlemavu hana uwezo wa kupata matibabu, nataka niweke msisitizo. Ndiyo maana nimesema katika Sera hii Mpya tutaweka utaratibu mzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya sasa kati ya asilimia 60 - 70 ya wagonjwa ambao wanafika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya wanapata matibabu bure. Sasa hivi tunataka tuweke mfumo mzuri na kuhuisha na mifumo mingine kama ile ya TASAF kuhakikisha kwamba tunawatambua tu wale ambao kweli hawana uwezo na wanahitaji kupata matibabu. Tutakapokuja na huu utaratibu wa bima ya afya kwa wananchi wote tutakuwa na kundi dogo sana ambalo limebaki ambalo litakuwa linagharamiwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini Serikali haipeleki ruzuku. Nimthibitishie Mheshimiwa
Mbunge na bahati nzuri naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na analijua na hivi karibuni tumetoa taarifa ya utekelezaji ya nusu mwaka, Serikali inapelekea mishahara hatujashindwa kupeleka mishahara, dawa na hela ya uendeshaji. Hakuna hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo haijapata huduma zote hizo ambazo nimezitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuna vyanzo vingi vya mapato ndani ya hospitali. Pamoja na ruzuku ya Serikali tuna fedha za papo kwa papo, fedha za bima na nyingine zinapata basket fund. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nikiri kwamba sisi watu wa Mkoa wa Njombe hospitali zetu na vituo vyetu vya afya tunapata pesa za dawa zaidi ya asilimia 90, lakini bado Mheshimiwa Naibu Waziri kuna changamoto. Tuna changamoto ya dawa za afya ya akili pamoja na chanjo ya kichaa cha mbwa ambazo inatulazimu vifaa vya afya kwenda kununua kwa wa zabuni kwa bei kubwa sana. Sasa je, ni lini MSD itatatua changamoto hii kuhakikisha kwamba, inapeleka dawa za afya ya akili na chanjo ya kichaa cha mbwa katika vituo vya afya na hospitali za Mkoa wa Njombe?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, pesa za Basket Fund zimekuwa zikichelewa sana katika vituo vyetu vya afya na hospitali zetu za Wilaya ndani ya Mkoa wa Njombe. Hivi sasa ninavyozungumza Hospitali ya Wilaya ya Ludewa, Hospitali ya Wilaya ya Makete, wamepata pesa za Basket Fund kwa quarter ya kwanza tu ilihali sasa hivi tuko quarter ya tatu. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa hizi za Basket Fund kwa wakati ili hospitali hizi ziweze kununua dawa kwa sababu bila kuwa na pesa hata waki-place order kule MSD, MSD hawakubali kuwapatia dawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mgaya kwa kuwa mfuatiliaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya na kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kule Njombe katika kuwahudumia akinamama na watoto. Sasa naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao tunautumia sasa hivi Serikali ni utaratibu unaitwa pull system, hapo awali tulikuwa tunapeleka dawa pasipo kuzingatia mahitaji na uhalisia ambao ulikuwepo katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya. Sasa hivi utaratibu ni kwamba hospitali zinaagiza kulingana na mahitaji yake na nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, chanjo tunazo zote asilimia mia moja na hizi tunazisambaza kulingana na mahitaji ya mikoa.
Mheshimiwa Spika, la pili, chanjo za kichaa cha mbwa na dawa za afya ya akili; dawa hizi tunazo katika bohari yetu ya madawa na katika stoo zetu za kanda pale Iringa. Niombe tu Mheshimiwa Mbunge atusaidie kuwaomba mamlaka kule kuagiza kwa sababu zile dawa zina mahitaji mahususi, huwezi ukazipeleka tu kwa sababu wagonjwa wa afya ya akili pamoja na wagonjwa ambao wameumwa na mbwa si wengi kiasi hicho. Hata hivyo, sisi kama Serikali kupitia bohari ya dawa, tunazo dawa hizo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli tunakiri kwamba pesa za Basket Fund zinakuwa zinachelewa na hii kwa sababu fedha hizi nazo zina mkono wa wafadhili, wanapochelewa kutufikishia na sisi mchakato mzima unachelewa kuzifikisha kule. Hata hivyo, niseme tu kwamba fedha za Basket siyo chanzo pekee cha fedha ambazo zinatumika katika dawa, tuna fedha za ruzuku za dawa ambazo tunazipeleka, tuna fedha papo kwa papo na tuna fedha za bima ya afya ambazo zote kwa kiasi kikubwa nazo zinapelekwa katika manunuzi ya dawa. Kwa hiyo kutokuwepo kwa pesa ya Basket Fund, siyo kigezo na wala siyo sababu ya kukosekana dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. (Makofi)
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, niMshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Kama utafiti wa UNICEF - Tanzania ni sahihi kwamba akina mama 24 na watoto 144 wanafariki kwa siku na kwa mwezi kufanya idadi ya 5,040 na Serikali iliingia makubaliano mbalimbali ya Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha kwamba wanaboresha huduma za afya kutoka asilimia 28 hadi asilimia 60 ili kuokoa watoto 102,000,000 na wanawake 16,000,000, je, ni kwa nini sasa Serikali imeshindwa kufikia makubaliano haya ya asilimia 60 ya huduma ya afya ili kuokoa maisha ya watoto na akina mama hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali kwa sababu imeshindwa kufikia asilimia 60 ya huduma ya afya, ina mikakati gani ya makusudi kuweza kuimarisha ili kuondokana na vifo hivi vya watoto na akina mama?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijashindwa kufikia hayo makubaliano na haya niliyokuwa nayasema ni mlolongo wa utekelezaji wa maazimio hayo. Katika takwimu zangu nimeonyesha kwamba tunaendelea kupata mafanikio. Moja ni kwamba sasa hivi tumeongeza idadi ya akina mama ambao wanajifungulia kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya kutoka asilimia 50 – 73, haya ni mafanikio, akina mama wengi wanaenda kujifungulia katika vituo vyetu vyakutolea huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesema kwamba akina mama wanaohudumiwa na wataalam wa afya wameongezeka kutoka asilimia 40 – 72. Sambamba na hilo, tumeendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya ili viweze kutoa huduma za dharura na uzazi na vituo zaidi ya 300 vimeboreshwa na kuwekewa vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumezindua Mpango wa Tujiongeze Tuwavushe Salama ambapo Makamu wa Rais alizindua ukishirikisha Wakuu wa Mikoa na kila Mkuu wa Mkoa amepewa majukumu yake na kila Mkuu wa Mkoa ameenda kusimamia haya katika wilaya zake. Kama Wizara tumeanza kuchukua takwimu ambazo siyo rasmi lakini mwelekeo wetu unaonyesha kwamba vifo vya akina mama vimepungua sana ndani ya nchi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kwa niaba ya akina mama wote wa Tanzania, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze waziwazi, nafahamu wazi kabisa huduma ya bure iliyokuwa inatolewa kwa mama na mtoto kupitia Huduma ya Tumaini la Mama imefutwa na kwamba hakuna mzazi yeyote anayeandikishwa sasa hivi kuanzia tarehe 31 Desemba.
MWENYEKITI: Swali.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, ni nini tamko la Serikali kutokana na jambo hili kwa sababu hailijatangaza waziwazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Cecil Mwambe kwa swali nzuri kwa niaba ya wanawake wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunakiri kwamba huu utaratibu wa Tumaini la Mama ulikuwa na mchango mkubwa sana katika afya ya uzazi katika Mikoa ya Kusini. Mkataba ule umekwisha na sisi ndani ya Serikali bado tunaendelea kuufanyia kazi pamoja na Wizara ya Fedha. Taratibu zitakapokamilika tutatoa taarifa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 14 inasema kila mtu anayo haki ya kuishi. Mwanamke na mtoto hawatakiwi kufa hasa mama wakati analeta kiumbe kingine dunia. Tunaona vifo ni 556 kati ya vizazi hai 100,000 na kule kwa watoto 21 kati ya vizazi hai 1,000 na tunaambiwa tufikapo 2020 tufikie 10 kati ya vizazi hai 1,000. Je, Dira hii ifikapo 2020 au 2025 tunaweza kuifikia ili kunusuru maisha ya hawa wazazi pamoja na watoto wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Salima Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali na Serikali hii ya Awamu ya Tano imedhamiria kabisa kuhakikisha kwamba tunapunguza vifo vya akina mama na watoto. Nikiri kauli ambayo ameisema Mheshimiwa Salma Kikwete kwamba ujauzito haujawahi kuwa ni ugonjwa na mama mjamzito hapaswi kufariki kutokana na uzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe tu comfort Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imewekeza nguvu sana na kipaumbele chetu kikubwa sana ndani Wizara ni kuhakikisha tunapunguza vifo vya akinamama na watoto. Tumeongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba katika masuala ya uzazi; tumeboresha vituo vya afya; tumeendelea kutoa mafunzo kwa wataalam wetu wa afya na tumeendelea kuweka mifumo mbalimbali na kuhakikisha kwamba tunatoa hamasa katika jamii na viongozi wote katika ngazi zote kuwajibika. Mimi niseme tu in a very an official way kwamba tutakapofanya utafiti mwakani nina uhakika tutapata takwimu nzuri zaidi.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyotuelimisha, lakini kama alivyokiri mwenye pamoja sheria zilizopo bado dawa za makundi yote matatu zinauzwa holela. Swali la kwanza, je, Serikali inatathimini yoyote inayoonesha madhara gani yanatokea kwa matumizi haya ya hovyo ya dawa za maumivu na antibiotic na dawa zote alizozitaja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jem haoni sasa kuna haja ya kuhamisha hizi dawa ambazo ni restricted kwa maduka ya MSD yaliyoenezwa nchi nzima ili pharmacy zingine ambazo zitatoa dawa hizi ziwe rahisi kufuatilia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Janeth Mbene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze kwa maelezo ya awali, tunakiri kwamba pamoja na kwamba dawa hizi zipo katika makundi haya bado kuna changamoto ya matumizi ya dawa pasipo na cheti cha daktari. Wimbi la tatizo hii limeanza kuwa kubwa na nitumie fursa hii kutoa elimu kwenye jamii, baada ya Serikali kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya, tumeanza kuona matumizi ya madawa ambayo kwa lugha ya kigeni tunaita prescription drugs zimeanza kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote ambao wanaendelea kutusikiliza, matumizi ya dawa hizi za hospitali na matumizi ya vileo na tumeanza kuona kwamba kuna tatizo kubwa sana ya prescription drugs pamoja na vileo ambavyo vinapelekea athari kubwa sana kwa wananchi. Matumizi ya pombe yana athari katika ubongo wa mtumiaji na prescription drugs zina athari katika mapafu na katika maini ya watumiaji. Kwa hiyo, mtu ambaye anatumia dawa hizi kwa pamoja na pombe yuko katika hatari kubwa zaidi ya kuweza kupoteza maisha kwa sababu hivi vyote vinafanya kazi za aina moja yaani dawa hizi zinaongeza kasi ya zile athari za pombe na zile dawa zinapokuwepo mwilini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumeliona hili na tumelibaini tatizo na tumeanza ndani ya Wizara kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba hizi dawa ambazo zipo control tumeweka mfumo mzuri toka zinaingizwa nchini mpaka pale ambako zinakwenda kutumika na mtumiaji wa mwisho. Hili ni jambo ambalo tunaendelea kulifanyia kazi ndani ya Wizara.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Watumiaji wa madawa ya kulevya hivi sasa Serikali kutokana na jitihada kubwa na nzuri za mapambano dhidi ya madawa sasa hivi wamegeuza kibao wameanza kutumia dawa kama pethidine, benzodiazepine dawa hizi zimekuwa zikisabisha kwamba watu ambao wanatumia madawa kulevya madawa hakuna wanatumia dawa hizi. Je, Serikali iko tayari sasa kuleta sheria ambazo zitakuwa kali sana ili kuweza kudhibiti usambazaji na manunuzi ya dawa hizi ili zifanane na jitihada kubwa na nzuri zinazofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya awali tumeanza kuona ongezeko
la madawa ya hospitali ama prescription drugs zikianza kutumika ndivyo sivyo kama mbadala wa madawa haya ya kulevya. Sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua na ni mambo ambayo tunaendelea kuyafanya kama ndani ya Serikali. Kuanza kutoa elimu kama ambayo nimeitoa hapa kwamba hizi dawa zinatakiwa zitumike kwa malengo ambayo yamekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili tumeanza sasa kuweka utaratibu mzuri wa kufanya udhibiti wa hizi dawa kuhakikisha pale tangu zinapoingia mpaka kwa mtumiaji wa mwisho. Niseme kwamba uratibu huu tumeshauanza ndani ya Wizara na tutaendelea nao. Sheria tulizonazo za matumizi ya madawa ya kulevya zinaongelea vilevile hizi dawa za prescription drugs na sheria ni nzuri tu zinajitosheleza kwa adhabu.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vijana wetu kutumia madawa ya kulevya na kwa kuwa sober nyingi sana zinamilikiwa na watu binafsi na kwa kweli zimekuwa zikifanya vizuri, lakini gharama za kuziendesha tunaona ni kubwa kiasi kwamba vijana wengi wanashindwa kumudu gharama zake. Je, ni kwa nini sasa Serikali isitoe ruzuku kwa hizi sober house za watu binafsi au kuanzisha za kwake ili kusaidia vijana wetu kurudi katika hali zao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakiri kwamba kumekuwa na tatizo la dawa ya kulevya na Serikali imechukua juhudi
na hatua ya kuhakikisha kwamba tunadhibiti uingizaji wa dawa za kulevya na kwa kiasi kikubwa kwamba tumepunguza sana matumizi ya madawa za kulevya hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunatambua vilevile kwamba kuna wahanga ambao walikuwa wanatumia hizi dawa za kulevya, sisi Serikali tumeendelea tukishirikiana na wadau binafsi. Kwa upande wa Serikali tumeanzisha vituo mbalimbali vya matibabu katika hospitali zetu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na hivi karibuni tumezindua hapa Itega Dodoma, lakini tunatambua mchango mkubwa wa sober houses na sisi kama Serikali tumetoa mwongozo wa usimamizi wa hizi sober houses, lakini sasa hivi bado ni mapema sana kusema kwamba Serikali itakuwa inachangia Ruzuku kwa uendeshaji wa hizi sober houses.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa watoto hawa wadogo hawatumiki katika kubeba mizigo tu, lakini kuna wengine ambao hutumika kuwaongoza baadhi ya wazazi au walezi na watu wazima katika kwenda kuombaomba.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwanusuru watoto hawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Toufiq kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tumefanya sensa ya kubaini watoto ambao wanaishi mitaani au wanaoishi katika mazingira hatarishi katika baadhi ya Majiji na tumebaini idadi na wale ambao tuliwabaini na vyanzo vyao ambavyo vimewasababisha wao kuwa mitaani wengine tumeweza kuwaunganisha na wazazi wao, lakini vile vile, tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba wale ambao tunawabaini hawana wazazi kabisa, tunawatunza katika nyumba zetu za kuwalelea watoto.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na aliyejibu swali sasa hivi, Jiji ambalo lina watoto wengi kuliko hili, moja ya nane ya Dodoma ni Jiji la Dar es Salaam. Hao wa Dar es Salaam ambao sasa limeitwa Jiji la Utalii, lina wageni wengi na ni wengi, yaani ni wengi kuliko; hatua zipi za makusudi zinachukuliwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuondoa ombaomba ili hawa watalii wanaonyang’anywa, wanaoibiwa waweze kuwa na raha katika Jiji la Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, sina takwimu za papo kwa papo, lakini kwa ujumla najua katika sensa yetu tuliyofanya, tulibaini kama watoto zaidi 6,000, lakini nahitaji nifanye uhakiki kujua katika Majiji haya ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma na maeneo mengine ni wapi ambapo takwimu zipo nyingi.
Mheshimiwa Spika, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo taarifa tutampatia. Sisi kama Wizara, tumeendelea kulifanyia kazi suala hili, lakini kama alivyosema katika jibu la msingi la Mheshimiwa Kandege ni kwamba jukumu la malezi ya mtoto ni la familia. Pale inaposhindikana ni jamii ambayo inaizunguka na mwisho pale inapoonekana kabisa hakuna wa kuwasaidia wale watoto, sisi kama Serikali tunachukua majukumu hayo.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba tunatimiza majukumu yetu ya msingi ya kuwalea watoto kama ilivyoainishwa katika sheria.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru Serikali kwa kukubali na kuelewa kwamba suala hili linatambulika na lipo.
Mheshimiwa Spika, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nataka ieleweke kwamba suala hili kama ilivyo ushoga yaani Lesbianism ni masuala ya usiri sana, kwa hiyo, kuyajua kwake siyo rahisi sana. Kwa hiyo, kwanza ningeomba Serikali isicheleweshe jambo hili la utafiti ili tuweze kujua kiwango cha athari hizo.
Mheshimiwa Spika, pia nataka ieleweke na itambulike kwamba kunyamaza kwetu kimya sasa hivi na kuogopa mambo haya miaka 50 ijayo ndani ya Bunge hili badala ya kujadili maandeleo na maadili mema ya Kitanzania watakuja kujadili namna gani ya kupitisha ndoa ya jinsia moja.
Mheshimiwa Spika, sasa narudi kwenye maswali yangu ya nyongeza. Swali la kwanza, nashukuru Serikali imeona umuhimu wa kutoa elimu pamoja na kwamba kuna sheria ambazo zinadhibiti suala hilo na baada ya utafiti wamesema pia watafanya marekebisho ya sheria. Swali langu lipo hapa, je, wakati tunaendelea kufanya utafiti huo, kwa nini sasa Serikali isishirikiane Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya kuona namna gani bora wanaweka mitaala katika shule zetu na kuonyesha madhara na athari ya mambo haya ambayo ni kinyume cha maadili ya Tanzania ili wanafunzi wetu ambao wanasoma waanze kujengeka na misingi ya maadali na kuachana na mambo haya popote watakapoyaona?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba tuna wanazuoni wengi sana katika Taifa hili wa dini mbalimbali, kwa nini Serikali sasa hakai nao na ikawataka watoe mahubiri ya kukataza masuala hayo ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza badala ya mambo mengine ambapo haya hawajayatilia mkazo? Maswali yangu ni hayo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Najma Giga ambaye ameongea kwa uchungu sana.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameuliza kwa nini Wizara ya Afya isikae pamoja na Wizara ya Elimu kuangalia mitaala ili masuala haya ya maadili yaweze kufundishwa katika shule mbalimbali. Tunapokea ushauri wake na sisi kama Serikali tutaenda kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini tusiwatake wanazuoni nao wakatoa mahubiri kuhusiana na suala hili. Moja ya taasisi ambayo imekuwa inatujenga katika maadili mema ni pamoja na taasisi zetu za kidini. Kwa hiyo, naamini nao wanatusikiliza kupitia Bunge lako hili Tukufu na wao tuwaombe wachukue majukumu yao ya msingi kuhakikisha kwamba wanahubiri maadili mema ya kitaifa vilevile wanawajenga waumini wao katika maadili mema yanayozingatia misingi yetu ya maadili ya kitaifa. Kwa hiyo, sisi kama Serikali hatuwezi kusema taasisi za dini zifanye lakini taasisi za kidini nazo zina wajibu kuhakikisha kwamba zinajenga waumini wao na Watanzania katika msingi ya maadili mema.
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; Serikali wamesema wameweka mikakati, nataka kujua ni mikakati ipi ambayo wameweka ili kupunguza ama kumaliza tatizo hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba; kwa kuwa tatizo hili ni kubwa sana na kesi mbalimbali zinapelekwa mahakamani na baadhi ya kesi watuhumiwa wanashinda kutokana na kwamba kuna vitu ambavyo vinakosekana kama vile shahawa ama majimaji ambayo yanalingana na yule mwanaume ambaye amembaka au kumnajisi mtoto, je, Wizara ya Afya imeshusha mwongozo gani kuwashushia Madaktari ili kuwaongoza waweze kupima vitu kama hivyo ili wananchi wasikate tamaa kupeleka kesi zao mahakamani na kushindwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kubaini ukubwa wa tatizo na nianze kwa kutoa takwimu tu kwamba kati ya Januari mpaka Desemba, 2017 tulikuwa na matukio 41 ya ukatili wa kijinsia na kati ya hayo, 13,000 yalikuwa ni masuala ya ukatili dhidi ya watoto. Sisi kama Serikali tumeandaa mpango mkakati wa kuzuia ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na watoto ambao unaitwa MTAKUWA wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha mwaka 2021/2022. Katika mkakati huu tumejielekeza katika maeneo makubwa yafuatayo:-
Moja, kuanzisha Kamati za Ulinzi na Usalama wa Wanawake na watoto ambapo mpaka sasa hivi kuna kamati zaidi ya 10,000 tumezianzisha katika ngazi mbalimbali kuanzia Taifa, Mikoa, Wilaya na katika ngazi ya Halmashauri hadi katika Kata; kuanzisha madawati ya jinsia ndani ya Jeshi la Polisi zaidi ya madawati 400 tumeshaanzisha. Sambamba na hilo, kumekuwa na kuanzishwa na mahakama maalum za watoto ili mashauri ya watoto yaweze kukaa na kusikilizwa. Tunaendelea kushauriana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba kunakwa na Walimu walezi ambao wanaweza wakatoa ushauri nasaha na kupokea baadhi ya mashauri kwa watoto ule ukatili ambao wanafanyiwa wakiwa majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kama nilivyoeleza katika jibu la msingi ni kwamba mashauri mengi tunashindwa kuyafikisha mwisho kwa sababu wanaofanya ukatili huu ni watu ambao wako ndani ya familia. Kwa hiyo, nami nitoe rai kwa jamii kwamba tusiyamalize mashauri haya kifamilia na badala yake turuhusu mkondo wa kisheria uweze kuchukua nafasi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ameelezea kwamba kushindwa kwa baadhi ya kesi kwa sababu ya ushahidi wa kitaalam kutoka kwa wataalam wetu wa afya. Hili tumeshalitolea maelekezo kwa wataalam wetu wote wa afya na tumeweka msisitizo mkubwa sana kwamba mtu yeyote katika Sekta ya Afya ambaye amepewa jukumu la kuthibitisha vipimo ambaye atakwenda kinyume na misingi na miiko ya maadili ya taaluma hatutasita kumfungia na kumfutia leseni ya Udaktari.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tatizo la ubakaji na ulawiti kwa watoto bado ni changamoto kubwa sana, hasa kwa Mkoa wetu wa Iringa. Sasa wenzetu wa Chuo cha Mkwawa na RUCO walifanya utafiti na walibaini kuwa wazazi na walezi wamekuwa wanaachwa na mzigo mkubwa sana kugharamia matibabu ya watoto hao.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa kuweka utaratibu maalum kwa matibabu, ukizingatia hawa watoto huwa wanaachwa na physical damage na psychological damage kubwa ili waweze kuwalea watoto hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Rose Tweve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tulishalitolea tamko suala hili kwamba wahanga wote wa ukatili wa kijinsia Serikali itatoa matibabu bure.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza; nataka tu kujua katika ile Hospitali ya Mkoa ya Ligula kuna Madaktari Bingwa wangapi na wanatibu magonjwa gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa hospitali ile ni ya mkoa, maana yake inahudumia mkoa mzima na ni ya rufaa na sisi hatuna hospitali ya kanda, Kanda ya Kusini, bado haijaanza kufanya kazi.
Katika jibu lake la msingi amesema Madaktari wa kufanya upasuaji wa kawaida na mifupa bado wapo masomoni wanasoma na ukizingatia kuna ajali nyingi zinazotokea, anawaambia nini vijana, wananchi wa Mtwara ambao wanapata matatizo, wanataka tiba ya upasuaji wa kawaida na mifupa; wasubiri mpaka mwaka 2021?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mtwara, Ligula tuna Daktari Bingwa mmoja katika Magonjwa ya Akinamama, lakini tunatambua kwamba tunahitaji huduma za Madaktari Bingwa katika hospitali zetu za rufaa za mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tulitangaza nafasi hizi Madaktari hawa hawako mtaani na ndiyo maana sisi kama Serikali tumewekeza katika kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo kwa Madaktari Bingwa wengi iwezekanavyo na tumeendelea sasa hata kufanya mabadiliko ya mifumo ya kufundisha Madaktari ili tuweze kupata Madaktari Bingwa wengi kwa utaratibu wa fellowship ambao na sisi ndani ya Wizara tunakwenda nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa lengo la kutibu changamoto ambazo tunazo Serikali imekuwa inafanya kambi mbalimbali za kutoa Madaktari Bingwa kutoka sehemu moja kwenda kwenye sehemu mbalimbali na hii tumekuwa tunafanya kwa kushirikiana na Bima ya Afya na kwenda katika kambi katika mikoa mbalimbali kuhakikisha kwamba zile huduma za dharura ambazo zinahitaji upasuaji nazo zinaweza zikafanyiwa kazi wakati tunasubiria kujenga uwezo wa kuwa na Madaktari Bingwa wengi zaidi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tunashukuru Serikali kwa kujenga Kituo cha Afya cha Kaloleni katika Jiji la Arusha pamoja na kutujengea jengo la mionzi lakini kituo hiki hakina mashine ya X-ray. Je, ni lini Serikali itatuletea mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya cha Kaloleni katika Jiji la Arusha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali iko katika maandalizi ya mpango wa kufanya uboreshaji wa huduma za mionzi nchini na tumeanza kwanza katika Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na baadhi ya Wilaya. Tutakapomaliza hapo tutakuja sasa kuangalia vituo vya afya ambavyo vina uwezo kuweza kupata hizo huduma na wataalamu ambao wanaweza kutoa hizo huduma.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mhehimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa tatizo hili sasa ni kubwa na linafahamika kwa muda mrefu hususani Mkoa wa Iringa.
Je, Waziri atakuwa tayari kuja Iringa kuona hali ambayo inaendelea kwa sababu hali ni mbaya hiyo elimu ambayo ilitakiwa itolewe haitolewi kwa muda na watu wanazidi kuathirika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa shule nyingi wanakunywa uji, je, sasa haoni ni wakati muafaka sasa wa kuchanganya chakula lishe kwenye uji wao ili iwe rahisi zaidi watoto wote wakapata kwa sababu ndio wanaoathirika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza kwa kuwa ni mdau wa masuala ya lishe, lakini nipongeze vilevile Bunge lako Tukufu kwa sababu wana Chama cha Waheshimiwa Wabunge ambao wanasimamia masuala ya lishe ambacho kinaongozwa na Mheshimiwa Dunstan Kitandula, yote hii inaonesha kwamba na nyinyi kama Bunge mnalisimamia suala hili kikamilifu.
Pia kwa njia ya kipekee vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuzindua mpango mkakati wa masuala ya lishe nchini na kutoa maagizo kwa Wakuu wote wa Mikoa na kuwapa malengo ambayo ya kusimamia katika masuala haya ya lishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niko tayari muda wowote kwenda Iringa kwenda kuwahamasisha masuala ya lishe katika mkoa huu. Vilevile ninachotaka kukisema ni kwamba hali ya udumavu tunaiona katika mikoa inazalisha chakula kwa wingi Rukwa, Katavi pamoja na Iringa ni mikoa ambayo kwa kiasi kikubwa sana inazalisha chakula kwa wingi, lakini kuna udumavu mkubwa sana kuliko mikoa mingine ambayo haizalishi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, yote hii inaonesha kwamba elimu ya lishe bado ni changamoto kubwa sana na hili sisi kama Wizara tuko tayari kwenda kule kushirikiana na timu zetu za mikoa kuhakikisha kwamba tunalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii sasa hivi kama Taifa tunaona hali ya udumavu inazidi kupungua, lakini tumeanza kuona vilevile lishe iliyopitiliza imeanza kuongezeka, asilimia 10 ya Watanzania wana lishe ambayo imepitiliza, maana yake ni nini? Ni kwamba wote hapa wengi hatuzingatii misingi ya lishe, tunakula bora chakula kuliko chakula kilicho bora.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inahudumia zaidi ya wagonjwa 300 kwa siku na inatoa huduma katika maeneo mawili tofauti, ipo hospitali ya zamani, ambayo ipo katika Kata ya Ipembe na hospitali mpya ya Rufaa iliyopo katika Kata ya Mandewa. Je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha inapeleka fedha za kutosha ili kumaliza ujenzi katika hospitali mpya ya Rufaa ya Mandewa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hospitali hii inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Madaktari Bingwa wakiwemo wa wanawake na watoto pia ina uhaba wa vifaa tiba kama Oxygen Concentrator, baby warmer na phototherapy machine. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mahitaji haya muhimu katika hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aisharose Ndoghoi Matembe, amekuwa ni mfuatiliaji mkubwa sana wa maendeleo ya hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na amekuwa ni mdau mkubwa sana kwetu sisi Wizara ya Afya kufuatilia masuala mbalimbali, nataka kumpa pongezi hizo. Naomba sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aisharose Matembe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumezipokea hizo hospitali za Rufaa za Mikoa na kusudio letu ni kuhakikisha kwamba tunaziboresha ili ziweze kutoa huduma za kibingwa kama zilivyokusudiwa na ni kweli kwa sasa Mkoa wa Singida una hospitali ya zamani ambayo inatumika kama hospitali ya Rufaa ya Mkoa, lakini kuna ujenzi wa hospitali mpya ambao unaendelea pale Mandawe na nilishaitembelea na kusudio la Serikali ni kuhakikisha kwamba sasa tunaikamilisha ile hospitali. Baada ya hapo ile hospitali ya zamani tuirudishe katika ngazi ya halmashauri iweze kutumika kama hospitali ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, tutaendelea kuboresha na kuongeza Madaktari kadri tutakavyokuwa tunaendelea kuzalisha. Mwaka jana tumesomesha Madaktari takriban 125, mwaka huu tena tumeshasomesha Madaktari Bingwa zaidi ya 100. Kwa hiyo, kadri wanapokuwa wanamaliza na sisi tutakuwa tunawapangia katika hospitali zetu za Rufaa za Mikoa. Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba zile huduma za msingi za magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto, magonjwa ya mifupa, magonjwa ya akinamama, wataalam wa radiolojia, wataalam wa magonjwa ya dharura, kila hospitali ya Rufaa za Mkoa iweze kuwa nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na masuala ya vifaa tutaendelea kuongeza vifaa hivi kadri tutakavyoweza lakini nitoe msisitizo kwa waganga Wakuu wote wa hospitali za Rufaa wote wa hospitali za mikoa, masuala mengine wala siyo kuhitaji kusubiri Serikali, fedha wanazo waweze kuagiza vile vifaa ambavyo wanaviona ni muhimu katika utoaji wa huduma zao za afya.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru matatizo yaliyoko Singida ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Geita DC, Hospitali ya Wilaya ya Geita imepandishwa hadhi takriban miezi sita na tunaishukuru sana Serikali kwa sababu imetuletea vifaa vingi x-ray machine, Ultra sound, machine za meno, vitu vya theatre, lakini vitu hivi vyote viko store kwa sababu hatuna wataalam na hospitali ile inaendeshwa na AMO na Madaktari wetu wengi bado wako Geita Mjini wamekaa tu ofisini. Je, ni nini kauli ya Serikali kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa apeleke watu wenye hadhi ya kuendesha Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Joseph Musukuma kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kufuatilia Hospitali hii ya Nzela katika Wilaya ya Geita na nilipata fursa ya kutembelea hospitali hii na ni hospitali kubwa na iliyojengwa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelekezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhambi kubwa sana kama hospitali imekamilika na vifaa vipo na haitoi huduma zile zilizokusudiwa wakati sisi kama Serikali tulishapeleka wataalam. Nitumie fursa hii kumkumbusha Mganga Mkuu na kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba wale wataalam wote ambao Serikali imewapatia na wapo mjini hawako katika kituo cha kazi kuhakikisha kwamba mara moja wanafika kule na wanatoa huduma kwa wananchi.
MHE. JAPHARY R. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Singida halitofautiani sana na tatizo la hospitali ya Mawenzi ya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo hospitali ile imezidiwa sana na wagonjwa.
Sasa swali langu kwa Serikali, wako tayari kusaidia kuongeza Madaktari katika hospitali ile ya Mawenzi ili iweze kutoa huduma inayoridhisha kwa wagonjwa katika hospitali ile?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Japhary Michael, Mbunge wa Moshi, kama ifuatavyo:-
Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ni hospitali ya Mkoa katika Mkoa wa Kilimanjaro na bahati nzuri nimepata fursa ya kutembelea ile hospitali. Kwa maana ya kuwa na Madaktari tunao Madaktari wa kutosha, changamoto ambayo tunayo pale ni Madaktari Bingwa na hili tumeshaliona Mheshimiwa Mbunge. Juhudi ambazo tunazifanya sasa hivi ni kusomesha Madaktari wengi zaidi na kuanza kuwapanga katika idara mbalimbali ambazo nimezisema katika swali la msingi, kuhakikisha kwamba sasa zile huduma za kibingwa zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaboresha mnyororo wa rufaa kwa maana ya kuboresha vituo vya afya na ujenzi wa hospitali za wilaya mbili ambazo zinaendelea katika Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha sasa ule mzigo ambao ulikuwa unakwenda pale katika hospitali ya mkoa, uweze sasa kuchukuliwa na hivi vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tatizo la wagonjwa wa akili wanaorandaranda limekuwa sasa ni tishio kwenye jamii. Kwa mfano, wiki iliyopita tu mama mmoja Wilaya ya Nzega ameua watoto sita na amejeruhi watoto wengine wanne lakini katika jitihada za kumdhibiti na yeye mwenyewe ameuawa. Tunaona tena pia wagonjwa hawa wa akili wakiwa wamebeba mizigo na madudu chungu nzima na wanatishia usalama wa watu wengine.
Je, Serikali iko tayari sasa kuwaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Franz Mwalongo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tunaendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na masuala haya ya magonjwa ya afya ya akili. Tunachokifanya sasa hivi tumeweka Waratibu katika ngazi za Mikoa na Halmashauri zote. Kwa hiyo, katika masuala yanayohusiana na masuala ya afya ya akili, majukumu ya msingi yapo kwa Waratibu wa Afya ya Akili ngazi ya Mkoa na Halmashauri na tutaendelea kuwahimiza na kuwasimamia kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao huo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa akili una sababu nyingi kama kurithi, matumizi ya madawa ya kulevya lakini vilevile mifadhaiko. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, zamani kulikuwa na vituo vya couseling kwenye shule, vyuo vikuu, taasisi ambazo zinajumuisha watu wengi kama hata hapa Bunge ambapo watu walikuwa wanakwenda wanapewa ushauri nasaha. Je, Serikali iko tayari kufufua vituo hivyo ili kusaidia kukabiliana na ugonjwa huu wakati unapoanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Selasini, nichangie kidogo katika suala hili ambalo umelisema, siyo kwamba wagonjwa wengi wa akili wako Dodoma, la hasha. Tulianzisha taasisi hii kubwa ya Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Mirembe Dodoma kwa sababu tu ya nature, pale tuna Gereza la Isanga na wengi wa wafungwa wanaopelekwa katika gereza lile ni wenye kesi kubwa hususani za mauaji, kwa hiyo, lengo ilikuwa ni kujihakikishia kama afya yao ya akili iko vizuri. Kwa hiyo, Mirembe ipo Dodoma siyo kwa sababu Mkoa wa Dodoma una wagonjwa wengi wa ugonjwa wa afya ya akili.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nirejee katika swali la msingi la Mheshimiwa Joseph Selasini, ni kweli visababishi vya afya ya akili ni pamoja na kurithi. Kuna watu ambao ndani ya familia yao wanapata magonjwa haya ya akili kutoka kwa baba na mama kwenda kwa watoto. Visababishi vingine ni matumizi ya madawa ya kulevya, vileo mbalimbali lakini hali ya maisha na stress ambazo watu wanazipata nazo zinapelekea watu kupata afya ya akili.
Mheshimiwa Spika, ugonjwa mkubwa ambao unasumbua sana sasa hivi ni ugonjwa wa sonona (depression). Ugonjwa huu kidogo ni mgumu sana kuweza kutambulika, mtu huwa anaanza kujitenga, anajiona kwamba hana thamani katika jamii, anaona hathaminiwi na wengi wanaishia kwenda kujiua. Ni kweli hili jambo na sisi tumeliona kwa sababu tumeona matukio mengi ya aidha mtu kujidhuru yeye mwenyewe ama kudhuru familia yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hili tumeliona na tunaendelea kuimarisha huduma za msingi ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha lakini vilevile naendelea kutoa rai jamii kuanza kubaini zile dalili za awali na kumpatia mtu huduma za afya ambazo anazihitaji. Magonjwa mengine haya si rahisi sana kuyabaini katika hatua za mwanzo lakini mtu anapoanza kuona mabadiliko ya kitabia kwa mtu ambaye yuko karibu naye ni vizuri basi mtu yule apate ushauri na nasaha au aende katika hospitali kupata huduma za afya.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ugonjwa wa kifafa una mahusiano makubwa sana na ugonjwa wa akili, kwa sababu mgonjwa wa kifafa akikosa zile dawa zake anakuwa amechanganyikiwa na anakuwa mkorofi na kibaya zaidi mgonjwa wa kifafa huwa anaanguka, kwa hiyo, anaweza kuangukia kwenye moto ama kwenye maji.
Mheshimiwa Spika, Ulanga ni miongoni mwa maeneo kinara duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kifafa na Serikali kwa uzito huo ikaamua kutoa dawa hizo bure kwa nchi nzima, lakini mgao tunaoupata Ulanga haukidhi mahitaji na Serikali inalitambua hilo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipa Ulanga kipaumbele kwa upatikanaji wa dawa hizi za kifafa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mikoa ndani ya nchi yetu ambayo inaonekana kuna wagonjwa wengi wa kifafa ni pamoja na Ulanga. Nasi kama wataalaam wa afya tunajaribu kufanya utafiti kubaini chanzo, kwa nini Mkoa huu wa Morogoro na hususan katika Wilaya hii ya Ulanga kumekuwa na wagonjwa wengi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dawa za wagonjwa wa kifafa pamoja na wagonjwa akili tunazo za kutosha, tutafuatilia katika Wilaya hii ya Ulanga kwa nini hizi dawa hazifiki ili kuhakikisha kwamba wale wote ambao wana ugonjwa huu wa kifafa katika Wilaya ya Ulanga wanapata tiba sahihi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Wauguzi wanaofanya kazi katika Wodi za Wagonjwa wa Akili, wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi sana kwa sababu wagonjwa hao mara nyingi wako hyper:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwakatia Wauguzi hao bima ya maisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, matibabu ya afya ya akili ni taaluma na wataalam wetu hawa wamepata mafunzo mazuri tu ya jinsi gani ya kuweza kuwatibu wagonjwa hawa wenye matatizo ya afya ya akili katika hatua zile za awali ambazo sisi mara nyingi katika lugha ya kitaalaam tunaita acute phase, lakini vilevile katika hatua ya mwendelezo wa yale matibabu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba wataalam wetu wako vizuri na ndiyo maana hujawahi kusikia kwamba kuna muuguzi wala daktari amefariki au amepata kipigo kikubwa kutokana na kuhudumia wagonjwa hawa wa afya ya akili. Kwa hiyo, kwa sasa hatuna evidence ya kutosha ya kusema kwamba sasa watu wote ambao wanatoa huduma za afya kwa wagonjwa wa akili tuweze kuwakatia bima ya maisha.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ninapozungumza watoto njiti nina maana wanazaliwa kabla ya miezi tisa haijatimia:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; dawa ya kusaidia mtoto ili aheme vizuri inayoitwa surfactant inauzwa shilingi laki sita kwa dozi moja na inategemea hali ya mtoto ambayo amezaliwanayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama una mtoto mmoja shilingi laki sita, kama umejifungua watoto wawili ni shilingi 1,200,000/=. Na watoto walio wengi wanatoka katika familia zenye hali duni na kipato cha hali ya chini, kama wanashindwa tu kwenda nao kliniki itakuwa na hii shilingi laki sita. Je, sasa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, dawa hizi zinatolewa bure, ili kunusuru maisha ya watoto hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba, likizo ni siku 84 kwa mtoto mmoja na siku 100 kwa watoto mapacha, lakini hawa ni watoto njiti. Kama amejifungua kabla ya miezi tisa tusema miezi saba ina maana kuna miezi miwili ambayo iko kabla ya miezi ile tisa. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, wazazi wote wawili, baba na mama, wanapata likizo yenye malipo kwa miezi hiyo iliyopo kabla ili waweze kutunza hawa watoto njiti? Asante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Grace tendega kwa swali lake zuri. Na nianze kwa kutoa tafsiri ya mtoto njiti, watoto njiti wako katika makundi mawili; kuna wale ambao wamezaliwa kabla ya wiki 37 na kuna wale ambao wanazaliwa na uzito mdogo kuliko ule ambao tunatarajia, kwa maana ya kilo 2.5 kwa hiyo, wote hawa tunawaweka katika group hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, watoto ambao wanazaliwa njiti mara nyingi wanazaliwa na changamoto mbalimbali, hususan wale ambao wamezaliwa kabla ya umri wa wiki 37. Na moja ya changamoto ambayo wanayo ni matatizo ya kupumua, mapafu yanakuwa hayajakomaa na wanahitaji dawa ambayo ni surfactant kukomaza yale mapafu. Na nikiri kweli, gharama za surfactant ni kubwa na sisi kama Seriakali tumeliona hilo, tunajaribu kuliangalia utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, tunatoa afua kwa akinamama ambao wamezaa watoto njiti. Hatutaweza kuitoa bure, lakini tutaweka utaratibu ambao unaweza ukapunguza gharama katika utaratibu ambao tunao sasa hivi wa kuagiza dawa moja kwa moja kutoka viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linahusiana na kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wazazi ambao wana watoto njiti:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, watoto njiti wanazaliwa wakiwa na changamoto nyingi pamoja na matatizo ya kupumua, wengine wanazaliwa na viungo bado havijakomaa, ikiwa ni pamoja na ubongo na wengine wanaweza wakapata matatizo mengine endapo hawatapata matunzo ya karibu. Lakini jiwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, sasa hivi kwa mujibu wa teknolojia watoto ambao wanazaliwa hata akiwa na wiki 22 kwa maana ya miezi mitano, wana uwezo mzuri sana wa kuweza kukua na kuishi vizuri. Na mtoto ambaye ameweza kuzaliwa na…
MWENYEKITI: Muda, muda.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalotaka kulisema kwa kifupi tu kwamba, Serikali inaweza ikaliangalia suala hili kwa maana ya kuwa, pale kama mtoto ana matatizo mzazi anaweza akawa anapewa ruhusa kwa mujibu wa kanuni na taratibu ambazo tunazo.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa, rate ya mama wanaojifungua watoto njiti imekuwa ikiongezeka nchini. Serikali ina mipango gani ya ziada kuweza kuwasaidia wamama wajawazito kuepukana na tatizo hilo, lakini pia ni sababu gani zinazowasababisha wamama wajawazito kujifungua watoto njiti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sisi kama Serikali tunasisitiza sana, mama anapopata ujauzito kuhakikisha kwamba, anaenda kliniki na sisi katika kliniki tunaweza tukabaini visababishi ambavyo vinaweza vikasababisha mama kuzaa mtoto njiti na kuweza kuvitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kifupi tu visababishi ni vingi, moja ni uzito wa mama mwenyewe; ikiwa mama ana uzito mdogo au uzito mkubwa inaweza ikasababisha kuzaa mtoto njiti, maambukizi ambayo mama anaweza akayapata, matumizi ya vileo, stress ambazo anaweza akawanazo mama wakati wa ujauzito ni sehemu ya visababishi ambavyo vinaweza vikasabaisha mtoto kuzaliwa njiti.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kutokana na changamoto ya kuzaliwa kwa watoto njiti kuwa ni changamoto kubwa sana, hususan, katika maeneo ya vijijini. Na kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza kwa kutueleza baadhi ya sababu ambazo zinasababisha miscarriage au kuzaliwa kwa mtoto njiti ni dhahiri kwamba, zipo ambazo zinazuilika na ziko ambazo hazizuiliki.
MWENYEKITI: Swali, swali.
MHE. MBONI M. MHITA:Je, Serikali ina mpango gani madhubuti, hususan, maeneo ya vijijini, ili kuweza kutoa elimu ambayo itaweza kuwasaidia akinamama kuweza kuepuka kupata kuzaa watoto ambao ni njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, visababishi vingi na viashiria vya ujauzito ambavyo vinaweza vikaleta shida, mara nyingi tunavibaini pale akinamama wanapokwenda kliniki. Na ndio maana sisi kama Serikali, tunahimiza sana akinamama kwenda kliniki angalau mara nne katika kipindi chao cha ujauzito. Lakini vilevile unapokwenda kliniki wanaweza wakawapa elimu kuhusiana na visababishi mbalimbali ambavyo nimevitaja, ili waweze kuviepuka na kuweza kuzaa watoto ambao wamefika wiki 37.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, lengo la kujenga vituo vya afya na zahanati ni kupunguza vifo vya akinamama wajawazito pamoja na watoto, lakini kwa kuwa, tatizo la upungufu wa madaktari ni kubwa sana. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri unasemaje kuhusu hilo, kuongeza madaktari katika vituo vya afya na hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakiri kwamba, tuna changamoto ya rasilimali watu, lakini Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba, tunakabiliana na changamoto hii. Na katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19 Serikali iliajiri watumishi wa afya takribani 11000 na tunaendelea sasa hivi mkakati tuliokuwanao ni kuziba mapengo ya hawa ambao wamestaafu, waliofariki na katika kipindi cha mpito. Lakini Serikali inaendelea kuweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba, katika vibali vya ajira mpya na watumishi wa afya wanakuwemo.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe, Kibena, ina kituo cha watoto njiti, lakini kituo kile kina mazingira duni sana na kinahudumia mkoa mzima. Na sasa hali ya hewa inakwenda kuwa ya baridi sana kuanzia mwezi wa tano. Je, Serikali iko tayari kutusaidia Wananchi wa Njombe kupata huduma haraka iwezekanavyo katika kituo cha watoto njiti cha Kibena Hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali na kupitia hospitali zetu za rufaa za mikoa kwa sasa, moja ya msisitizo mkubwa ambao tumeuweka ni pamoja na kuboresha huduma za watoto wachanga, ikiwa ni pamoja na njiti. Sijajua, hususan, jambo gani ambalo analiongelea pale, lakini katika Mkoa huu wa Njombe sasa hivi tuko katika hatua za mwisho kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa na lengo letu ni kwamba, baada ya hapo ile Hospitali ya Kibena tuirudishe katika ngazi ya halmashauri. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mikakati yetu ambayo tunayo kama Wizara ni kuhakikisha kwamba, huduma za watoto wachanga, ikiwa ni pamoja na njiti katika Mkoa wa Njombe itapewa kipaumbele.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Hapa Tanzania takriban watoto 213000 njiti huzaliwa kila mwaka na kati ya hao zaidi ya 9000 huwa wanafariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa natambua kwamba, tarehe 17 Novemba, kila mwaka ni siku ya watoto njiti duniani. Nilitaka Waziri atuambie kwa hapa Tanzania wanaadhimishaje siku hiyo kwa sababu, nadhani hata Wabunge hatuna taarifa; mnaadhimishaje siku hiyo kuhakikisha kwamba, tatizo hili sasa linapungua na wananchi wanalielewa vizuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge Viti Maalum, kwa ufuatiliaji mkubwa na kuwa mdau wa masuala haya. Niseme tu kwamba, siku hii ya tarehe 17 Novemba, ni fursa kwetu kama Wizara kutoa elimu kwa jamii kwa njia mbalimbali kuhakikisha kwamba, na mara nyingi tunakuwa na kauli mbiu mbalimbali kuhusiana na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na suala hili, visababishi vyake ni nini, huduma zake ni zipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kama Serikali sasa hivi tunahimiza sana hili suala la Kangaroo Motherhood. Kinamama kuwalea watoto wao njiti kwa kupitia kupeana joto la mwili kwa mwili, ili kuhakikisha kwamba, wale watoto ambao mara nyingi wanakuwa na matatizo ya mapafu na kutunza joto basi waweze kupata joto pasipokutumia incubators.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Kitete ina wodi ambayo inalea watoto njiti, lakini wodi hiyo ni finyu na vifaa vilivyopo ni duni. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha wodi ile na vifaa kuongeza, ili kuweza kuendana na kasi iliyopo pale?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya awali moja ya mkakati ambao tunao Serikali baada ya kukabidhiwa hospitali za rufaa za mikoa tumejielekeza katika maeneo makubwa matano;
(i) Kuhakikisha tunaboresha huduma za dharura;
(ii) Huduma za upasuaji; na
(iii) Masuala ya theatre, vilevile tunataka tuboreshe huduma za mama na mtoto ikiwa ni pamoja na huduma za ICU pamoja na ICS za watoto.
Kwa hiyo, tumeshafanya tathmini za kina hospitali zote, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Kitete na tumeshaweka Mpango Kazi wa kuboresha huduma hiyo katika Hospitali ya Kitete.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa majibu ya Waziri anasema kuna mkakati wa kuanzisha vyumba maalum vya matunzo ya watoto na matibabu, yaani neonatal care units kwa maana hiyo, hivi vyumba havipo. Anawaambiaje Watanzania kwa muda huu atawasaidia vipi akinamama wanaopata matatizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kwamba, huduma za neonatal care hazitolewi. Ni baadhi kwamba, kuna baadhi ya hospitali zina vyumba maalum vya neonatal care units na baadhi ya hospitali hazina, watoto wanawekwa katika wodi moja. Kwa hiyo, katika mkakati ambao tunao sasa hivi ni kuhakikisha kwamba, kila hospitali ya rufaa ya mkoa inakuwa na chumba mahususi kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga, lakini si kwamba, huduma hizi hazitolewi kwa sasa.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali hili karibu kwa ufasaha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri alikiri kuwa dawa hizi ni ghali na zina gharama kubwa na Serikali isiogope gharama kwa wananchi wake, wananchi ndio Serikali na Serikali ndio Wananchi na Mheshimiwa Lyimo alizungumza karibu watoto 9000 wanakufa kwa mwaka. Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itajaribu kuiga lini formular kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya utawala wa Dkt. Ali Mohamed Shein, kutoa dawa zote Unguja na Pemba bure? Na Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeiga mambo mengi kutoka Zanzibar, dawa…
MWENYEKITI: Swali moja, swali moja tu Mheshimiwa Jaku.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Je, ni lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano itafuata nyayo za Mheshimiwa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein kutoa dawa bure kutoa dawa bure kwa wananchi na sio kwa mdomo, dawa zipo Unguja na Pemba.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kwamba, Serikali itatoa dawa bure kwa Watanzania wote milioni 55 haitawezekana. Kwa hiyo, sasa hivi sisi kama Serikali kuleta nafuu kwa wananchi kuweza kumudu gharama za matibabu tunajielekeza katika mpango wa bima ya afya kwa wananchi wote, ili wananchi waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Hospitali ya rufaa ya Temeke haina mashine ya kufulia nguo, hadi kupelekea mashuka ya wagonjwa kupelekwa katika Hospitali ya Muhimbili ili kuweza kufuliwa. Je, Serikali itapeleka lini mashine ya kufulia nguo katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na Hospitali ya Rufaa ya Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyojua Hospitali yetu ya Rufaa ya Temeke inamashine ya kufulia, inawezekana katika kipindi hiki cha karibuni imeharibika na niombe tu baada ya kikao hiki cha Bunge nitafuatilia. Vile vile tumekuwa na utaratibu mbadala katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Muhimbili ina mashine kubwa za kuweza kufulia na mara nyingi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa katika Mkoa wa Dar es Salaam wanapopata tatizo basi huwa tunatumia Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kama mbadala. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya kikao nitafuatilia kuhakikisha mashine hiyo inafanya kazi.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri na kazi nzuri inayofanywa na Serikali katika kuhakikisha inatokomeza ukatili wa watoto na wanawake, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo lakini ni ukweli usiopingika masuala ya ukatili wa wanawake na watoto bado ni ya kiwango kikubwa sana. Tumeshuhudia watoto wanafanyiwa ukatili na Mheshimiwa Waziri Mkuu juzi alikuwa anazindua tuliona hata zile takwimu wanawake wajane wananyang’anywa mali zao hasa viwanja na mali nyingine lakini watoto yatima na wanawake majumbani na hata kwenye familia zao bado wanafanyiwa ukatili…
MBUNGE FULANI: Kubakwa.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Ndiyo, kubakwa na halikadhalika na hata kufanyiwa ulawiti.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Serikali imefanya kazi nzuri ya kutunga sheria inayotoa fursa kwa watu wanaofanyiwa ukatili kwenda kupata haki yao bila kujali anacho au hana, kazi hii imekuwa ikifanywa na mashirika yasiyo ya Kiserikali. Napenda kujua Serikali imejiandaaje kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza mpango huu ili kutuachia peke yake mashirika yasiyo ya Serikali ambayo na yenyewe yanategea misahada kutoka nje? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, napenda kujua ni mkakati gani sasa umewekwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wa kuratibu na kuona hao wanawake na watoto wanaopata msaada wa kisheria ni matokeo gani yamepatikana na changamoto zilizopo na Serikali inajiandaaje na kukabiliana na changamoto hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kufuatilia masuala mbalimbali yanayohusiana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba suala hili sisi kama Serikali tunalichukulia kwa kipaumbele kikubwa sana na ndiyo maana tumeanzisha Mpango Mkakati wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.
Mheshimiwa Spika, kupitia mkakati wetu huu imetusaidia sana maana matukio haya yanakuwa reported kwa kiasi kikubwa sana, kwetu sisi kama Serikali inatupa faraja kubwa sana. Kati ya Januari na Desemba, 2017 matukio 41,000 yaliripotiwa ndani ya nchi yetu na kati ya hayo 13,000 yalikuwa ni ukatili ya kijinsia dhidi ya watoto. Kwa hiyo, mwamko katika jamii umekuwa mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba Serikali imepitisha Sheria ya Usaidizi wa Kisheria, Namba 1 ya mwaka 2017 na kwa kiasi kikubwa sasa hivi usaidizi huu wa kisheria umekuwa unapitia katika taasisi zisizo za kiserikali, Serikali imeliona hilo na iko katika hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunaanzisha Legal Aid Fund ambapo sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili sasa ya usaidizi wa kisheria pale mashauri haya yatakapokuwa yanajitokeza.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali imeendelea na hatua mbalimbali na iko katika hatua za mwisho za kuandaa Sera ya Ardhi, umilikiwa ardhi ulikuwa ni changamoto kubwa sana kwa wanawake. Sasa hivi Sera hii ya Ardhi inaenda kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba wanawake nao wanakuwa na sauti katika masuala ya umiliki wa ardhi ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Wizara tunaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sera hii ya Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto. Kwa kiasi kikubwa mwamko umezidi kuwa mkubwa lakini niendelee kutoa rai tu kwa jamii kueleza kwamba masuala mengi ya ukatili wa kijinsia yanafanywa na watu ambao wapo karibu na familia. Tuendelee kutoa taarifa na niombe sana masuala haya tusiyamalize ndani ya familia badala yeke tuhakikishe kwamba vyombo vya dola vinapewa fursa ya kuweza kuyashughulikia badala ya familia kuyamaliza ndani ya familia.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kukubaliana kwamba kuna unyanyasaji mkubwa sana kwa wanawake na watoto lakini upo unyanyasaji mkubwa sana kwa kina baba, wapo ambao wamekuwa wakipigwa na wengine kunyanyasika. Kuna maandamano ambayo tuliona katika mitandao katika nchi ya jirani ya Kenya akina baba wakiandamana kudai haki zao za msingi kwa akina mama. Je, ni lini sasa sheria pia itajengwa kuwalinda akina baba ambao wamekuwa wakinyanyasika kila wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Iringa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inapoongelea ukatili wa kijinsia haimaanishi tunaongelea ukatili wa akina mama na watoto, jinsia ina cut-across na akina baba. Bahati mbaya sana matukio ya ukatili wa kijinsia ya akina baba siyo mengi yanakuwa reported. Nitumie fursa hii kuwaomba wale akina baba ambao nao wanapigwa, wanafanyiwa ukatili wa kingono, wanaonyanyaswa kisaikolojia nao waweze kujitokeza ili madawati yetu ya jinsia yaweze kuyafanyia kazi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika ripoti ya hivi karibuni ya Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria imeonesha kwamba kuna ongezeko kubwa la unyanyasaji wa wanaume unaofanywa na wanawake hasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba. Nilikuwa nataka kujua ni lini sasa Serikali itaanza kuzuia ongezeko hili ili kusimama na ile kauli ya Mwenyezi Mungu ya Arrijalu qawwamuna ala-Nnisai.
SPIKA: Hivi hawa wanaume wananyanyaswaje mbona Spika haelewi.
Maswali mengine nashindwa hata kuyaruhusu, labda Mheshimiwa Naibu Waziri unaelewa tafadhali, nasikia wanaume wa Dar es Salaam wanaonewa sana, majibu tafadhali.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Wanaonewaje?
SPIKA: Anataka ufafanuzi wanaonewaje, Mheshimiwa Yussuf.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, katika ile ripoti walisema wanaume wananyanyaswa na wake zao, wanafanyishwa kazi ndani, wanapigwa, wananyimwa haki zao na wengine mpaka wanafikia kulazwa hospitali kwa vipigo wanavyovipata kutoka kwa wanawake.
WABUNGE FULANI: Aaaaa.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, ni ripoti ambayo imetolewa na Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria, si ripoti yangu.
SPIKA: Kumbe jambo kubwa hili, inasemekana hata Wanyamwezi wanapata shida hiyo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Waziri, yanatakiwa majibu ya uhakika hapa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunakiri kwamba yapo baadhi ya matukio ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa wanaume. Hata hivyo, kwa sasa hatuna takwimu za Mikoa ambayo ameitaja zinazoonesha matukio haya ni makubwa kiasi gani. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tutaendelea kufuatilia ili kubaini suala hilo.
Mheshimiwa Spika, pia amegusia ripoti ambayo sisi hatujaiona, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha Bunge basi aweze kutupatia taarifa hiyo ili na sisi tuweze kufuatilia. Niendelee kusisitiza tu kwamba matukio haya ya ukatili wa kijinsia ni makubwa zaidi dhidi ya wanawake na watoto kuliko wanaume.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa Serikali imekiri kwamba imetenga bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa na nafikiri na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwangu itakuwepo. Na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna ufinyu wa majengo katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora kupelekea hata vitanda kukosa sehemu ya kuweka na hivyo kupelekea msongamano wa wagonjwa na kudumaza utoaji wa huduma ya afya kwa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua sasa kati ya hizi bilioni 12 ni kiasi gani cha fedha kimetengwa specifically kwa ajili ya Hospitali hii ya Mkoa wa Tabora ili sasa kuondoa ufinyu wa majengo na kuweza kuondoa msongamano na vitanda viweze kupata mahala pa kuweka na wananchi wa Tabora waweze kupata huduma stahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni dhahiri kabisa inatambulika kwamba tuna uhaba wa wauguzi kwa maana ya madaktari, manesi na madawa katika hospitali zetu nyingi nchini. Na tunatambua kwamba uhaba huu umepelekewa na sababu mbalimbali ikiwepo zoezi la vyeti feki ambalo Serikali ya Awamu ya Tano iliendesha, vifo na kustaafu. Hospitali yangu ya Mji wa Tarime ina ukosefu wa daktari ni wengi lakini specifically daktari wa meno ambaye amefariki kuanzia mwaka jana na nimekuwa nikiongea hapa. Ningetaka kujua sasa ni lini Serikali itaweza kutuletea daktari wa meno ili wananchi wa Tarime waendelee kupata huduma hii ya meno?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza specifically kiasi gani ambacho tumekitenga katika Hospitali ya Rufaa ya Mko wa Tabora hususan katika kuboresha miundombinu ile. Hiyo data sinazo hapa kwa hiyo nitamwomba tu Mheshimiwa Mbunge tukishamaliza kikao hichi tuongee na watendaji wetu ili waweze kutupatia hizo taarifa na niweze kumpatia taarifa ambayo kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili ameulizia kuhusiana na daktari wa meno ni kweli Serikali imekuwa inaendelea na jitihada za kuziba mapengo wa vyeti feki na zile ajira nyingine. Na katika awamu ya kwanza tuliajiri takribani watumishi 3152 kuziba pengo la watumishi feki na Serikali baadaye ikaongeza watumishi takribani 8000 na sasa hivi tuko katika hatua za mwisho kuangalia hawa ambao walistaafu, wamefariki ili nao nafasi zao ziweze kuzibwa na tuko katika hatua za mwisho kabisa kuweza kuziba haya mapengo ya wale ambao wamefariki na wamestaafu ili sasa nafasi zao ziweze kujazwa. Na nikuhakikishie kwamba Tarime huyo daktari ambaye wamemwitaji wa meno naye atapatikana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi hii. Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo ni miongoni mwa hospitali kongwe hapa nchini na inahudumia zaidi ya halmashauri 11 pia inahudumia kisiwa kizima cha Pemba. Miundombinu yake imechakaa sana kiasi kwamba sasa hivi hata sio rafiki kwa wagonjwa lakini pia kwa wenzetu wenye ulemavu kwa sababu hakuna lifti katika wodi za wagonjwa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya hospitali hii kongwe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tunakiri miundombinu ya hospitali ya Bombo ni hospitali moja kongwe sana ndani ya nchi na nimepata fursa ya kuitembelea hospitali hii na kuona hizo changamoto hususani klatika jengo la wazazi ambapo wagonjwa hakuna lifti pale na imekuwa inaleta adha kidogo kwa wagonjwa kuweza kufika kule juu gorophani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumeliona hilo na kama nilivyosema katika jibu langu la msingi Serikali tumekabidhiwa hospitali hizi za rufaa za mikoa, makusudio yetu ni kuziboresha hospitali zetu zote hizi za rufaa kwa kuanza tunataka tujielekeze katika huduma za dharura, huduma za ICU, huduma za theatre, na majengo ya akina mama na watoto. Kwa hiyo tathmini tumeshafanya na kadri fedha zitakapopatikana tutaendelea kufanya maboresho haya na kuhakikisha kwamba hospitali hizi za rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Bombo zinafanyiwa marekebisho yanayostahiki.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo kubwa la misongamano katika hospitali zetu ni tabia ya Serikali kupandisha hadhi vituo vya afya kwenda hospitali ya wilaya, hospitali ya wilaya kuwa hospitali ya mkoa, hospitali ya mkoa kuwa hospitali ya rufaa. Kwa mfano Hospitali ya Mwananyamala ilianza kama clinic lakini leo ni hospitali ya rufaa kwa hiyo wale watu waliokuwa wanatibia pale wanaenda wapi? Kwa hiyo, nilitaka kujua ni lini Serikali itaacha tabia hii mbaya ya kupandisha vituo kuwa hospitali badala yake kama wanataka kujenga hospitali wajenge hospitali na vituo vya afya vibaki kama vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kutoa ufafanuzi Serikali haina tabia mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba idadi ya watu inazidi kuongezeka miji inazidi kukuwa na ndio maana na huduma zinazidi kuhitajika kwa wingi zaidi. Inawezekana tulianza kama zahanati ikaja kituo cha afya, hospitali za wilaya na zitakwenda mpaka ngazi ya rufaa. Lakini sisi kama Serikali tumeliona hilo na bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge tulikuwa naye na ni mjumbe wa kamati yetu anajua kuna maboresho makubwa sana hata lile jengo ambalo tulikuwa limesuasua la jengo la uzazi hilo Serikali imeshapata fedha na tuko katika hatua sasa hivi za kutaka kulikamilisha lile jengo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma katika hospitali ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo Serikali imeendelea kuweka mikakati moja ya changamoto ambayo inaleta misongamano katika hospitali hizi nyingi za rufaa za mikoa especially pale katika Jiji la Dar es Salaam ni mfumo mzima wa rufaa. Kwa hiyo, uboreshaji wa hivi vituo vya afya ambavyo tunavyovijenga ujenzi wa hospitali hizi za wilaya naami nazo zitasaidia sana kupunguza ule mzigo mkubwa ambao unaonekana katika hospitali zetu nyingi za rufaa za mikoa. Kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi Mheshimiwa Mbunge hili tumeliona na tumelifanyia kazi kwa kuimarisha sasa mifumo ya afya ya msingi ili sasa hospitali za rufaa za mikoa ziweze kutoa huduma zake za msingi kama hospitali za rufaa za mikoa.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na jitihada kubwa za Serikali ambazo zinafanyika lakini bado tatizo la utapiamlo katika mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi bado linaendelea kukua. Sasa je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kuajiri watoa huduma za lishe katika vijiji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiangalia mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi nchini ndio mikoa ambayo nayo inaoongoza sana kwa utapiamlo. Na siku zote nimeendelea kusema bado tuna changamoto watanzania kula bora chakula kuliko kula chakula kilicho bora. Na hii tunaiona katika mtiririko mzima kwa maana ya udumavu vilevile tuna tatizo la Tanzania kuwa na lishe iliyopitiliza zaidi ya asilimia 10 ya watanzania wana lishe ambayo imepitiliza kwa maana ya wanaviriba tumbo, kina mama wana vitambi na kina baba wote wana vitambi, vyote hivyo nayo inaonyesha kwamba ni lishe ambayo siyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Serikali tumeliona hilo na ndio maana tulifanya uzinduzi wa mpango mkakati wa masuala haya ya lishe na mpango mkakati huo ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka juzi hapa Dodoma na lengo ni kuweka msisitizo katika masuala haya ya lishe na katika sekta zote. Na mpango mkakati huu unaratibiwa pale chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na sisi kama Wizara tuna nafasi yetu kubwa katika maeneo haya kuhakikisha kwamba tunapunguza udumavu kwa watoto wadogo lakini tunaanza kupambana na lishe iliyopitiliza kwa sababu nayo ina mahusiano ya karibu sana na magonjwa yasiyo ambukizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee tu kumsisitiza kwamba kuhusiana na suala ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliuliza kwamba tunaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali katika mikoa ile kuhakikisha kwamba watu katika mikoa ile wanapata elimu sahihi kuhusiana na masuala ya lishe. Sambamba na hilo tutaendelea kuajiri watumishi, maafisa lishe kadri uwezo wa Serikali utakapokuwa unaruhusu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, miaka minne ya makuzi ya mtoto ni ya muhimu sana kwa maisha yake yote tuko tulivyo kwa sababu ya malezi ya miaka minne ya mwanzo. Sasa zamani katika MSH pamoja na kuwapima uzito watoto pamoja na chanjo nakadhalika manesi na wataalam wa afya walikuwa wanafundisha akinamama namna ya kuwalea hawa watoto na MSH nyingine zilikuwa na vichezeo nakadhalika, sasa siku hizi hilo halipo.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba malezi ya hawa watoto katika hii miaka minne yanazingatiwa ili tuweze kuwa na kizazi ambacho ni bora siku zijazo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba katika misingi ya afya siku muhimu katika uhai wa mtoto ni siku 1000 na siku hizi 1000 tunaanza kuzihesabu tangia mimba inatungwa mpaka pale mtoto atakapokuwa anatizimiza miaka miwili. Katika kipindi hichi ndio tunapojenga msingi wa afya na ukuaji wa mtoto katika maisha yake yote, ukikosea pale unaanza na msingi mbovu kwa maana ya afya na ustawi wa yule mtoto. Ndio maana tunasisitiza kwamba utunzaji sahihi wa ujauzito, lakini unyonyeshaji wa mtoto kwa miezi sita na baada ya pale na mtoto anyonyeshwe mpaka miaka miwili akipewa na vyakula vingine ambavyo vinaweza vikamjenga mtoto sahihi katika afya sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili sisi kama Serikali tunaendelea kulisisitiza na ndio maana katika moja ya maagizo ambayo tumeyafanya tumepiga marufuku matumizi ya vyombo vyetu vya habari kwa maana ya television kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kuonyesha mpira, tamthilia na muziki badala yake tuwe tunatoa jumbe ambazo zinaweza zikawasaidia akina mama wanapokuja pale clinic kwa ajili ya chanjo ama huduma nyingine za afya basi waweze kupata elimu iliyokuwa sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeanza kuwekeza katika watoa huduma katika jamii ili kuweza kutoa elimu sahihi kule kwenye jamii jinsi gani ya utunzaji wa ujauzito lakini kuhakikisha kwamba wazazi wanapewa elimu sahihi kuhusiana na maandalizi ya chakula sahihi ili watoto waweze kupata afya bora na katika ustawi bora ambao unatakiwa.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka tu kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwenye Jimbo langu la Serengeti Kata ya Busawe, Kijiji cha Busawe, wananchi wamejenga kituo cha afya wameweka mpaka na vifaa vinavyostahili kwa ajili ya kituo cha afya, lakini ni muda mrefu sasa tangu waombe usajili wa kituo chao cha afya. Maombi yamekaa Wizarani muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inawaambia nini wananchi wa Kata ya Busawe na Kijiji cha Busawe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza sana Mheshimiwa Ryoba, Mbunge wa Serengeti na wananchi kwa kujenga kituo chao cha afya. Sisi kama Serikali tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunaungana na nguvu za wananchi pale ambapo wao wenyewe wametoa nguvu zao na wamejenga kituo chao cha afya. Ni wajibu wetu kama wataalam kwenda kukagua na kuhakikisha kwamba kinakidhi vile vigezo na kuweza kutoa huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu suala hili ndiyo nalisikia hapa kwa mara ya kwanza; na Mheshimiwa Ryoba ni rafiki yangu, siku zote tunakaa tunaongea, namwomba baada ya kipindi cha maswali na majibu awasiliane nami tujue tatizo ni nini na nimhakikishie ndani ya muda mfupi kituo chake kitapata usajili.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa bahati ni siku ya watoto, yamekuja maswali mawili mfululizo na yakilenga juu ya suala la kudumaa, suala la makovu ya kuona mambo mabaya na ukuaji kiakili; lakini haya yote kama alivyosema Mheshimiwa Selasini yanaweza kwenda katika kitu kinaitwa All Childhood Development.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina fursa ya kukopa kwa mkopo nafuu kutoka World Bank dola milioni 200 kwa miaka mitatu sasa; na Serikali haijafanya hivyo ili iweze kutekeleza hiyo program ya All Childhood Development. Je, Serikali ni lini itawasiliana, ita-finalize na World Bank ili mkopo huo uweze kupatikana na uweze kutumika kwa ajili ya All Childhood Development tupate watu wenye akili zaidi katika Taifa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunafanya kazi kwa karibu sana na World Bank na katika programu mbalimbali za maendeleo ya awali ya watoto, moja ya maeneo ambayo tumejikita katika hizi huduma za afya, ama huduma za msingi katika hizi siku 1,000 za mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa hili analoniambia Mheshimiwa Mbunge kwangu linaonekana kwamba ni jipya, basi namwomba anipe maelezo zaidi katika suala hili ili tuweze kufuatalia, lakini World Bank tunafanya kazi nao kwa karibu sana na tunashirikiana sana katika masuala ya ustawi na maendeleo ya watoto.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na ukizingatia leo ni siku ya kwanza kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nawatakia kheri wale wote ambao wamejaaliwa kufunga na wasiojaaliwa Mungu awape tahfifu waweze kufunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua, Serikali ina mpango gani au ina mkakati gani kwa wale watoto ambao wamehukumiwa na kupelekwa magerezani ikiwa ni gereza la pale Upanga au kwa jina lingine Kisutu? Nini wanapewa katika masuala ya kujiendeleza kielimu ya kawaida au elimu ya ufundi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipate majibu katika maswali haya.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria, watoto chini ya miaka 18 hawapaswi kufungwa magereza ya watu wazima. Kwa hiyo, kuna utaratibu wa Serikali kuwa na mahabusu za watoto, lakini vilevile kuna maeneo ambayo tunaita Gereza la Watoto, ambapo wale watoto wanatuhumiwa kwa mujibu wa sheria wamehukumiwa kifungo gerezani, basi wanapelekwa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuwarekebisha kitabia, siyo kuwaadhibu wale watoto, la hasha, Serikali ina lengo la kuhakikisha kwamba tunawarekebisha kitabia. Kwa hiyo, kule wanapata huduma zote za matunzo, lakini wanapata huduma za elimu na huduma za kuweza kuwasaidia kuwarekebisha kitabia ili hata baadaye wakitoka basi wawe ni sehemu ya raia wema katika jamii hii.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambayo inahudumia wagonjwa 500 kwa siku, hospitali hii kwa miezi minne hivi sasa haina kipimo cha full blood picture, hospitali hii kwa miezi minne haina oxygen, hospitali hii kwa miezi minne haina film, wagonjwa wakienda kupima x-ray wanapewa CD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu Serikali ina mpango gani wa haraka wa kusaidia hospitali hii iweze kutoa huduma kwa wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Minja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina taarifa ya hili ambalo analolisema sasa hivi, lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki tuweze kulifuatilia na kuhakikisha kwamba, hiyo huduma ambayo ni ya msingi kwa wagonjwa iweze kupatikana katika Hospitali hii ya Rufaa ya Morogoro.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa jitihada inazozichukua katika kulipoteza hili suala baya katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza, mwaka jana nilizungumza hapa kwamba iwapo elimu tosha itatolewa basi ripoti hizi zitazidi. Kweli Mheshimiwa Waziri amethibitisha, hivyo nawapongeza sana kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kujua hii idadi kubwa ambayo imeongezeka baada ya wananchi kuhamasika na kutoa ripoti, je, ni wangapi kati ya hao wameweza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na wangapi wametiwa hatiani na kuchukuliwa hatua zinazostahiki? Siyo lazima mnijibu sasa hivi lakini majibu nayataka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunajua kabisa vitendo hivi vinafanywa miongoni mwa jamii tunazoishi, ni miongoni mwa wanaume tunaoishi nao wakiwemo babu zetu, baba zetu, waume zetu, wajomba zetu na wengine wanaofanana na hao. Kwa nini Serikali haiji na mpango mbadala wa kutoa ruhusa kwenye jamii ili kuwatambua hawa watu ambao wanajulikana wana vitendo hivi kama ambavyo wanatambuliwa wabakaji, wezi, wavuta unga na wavuta bangi; ili jamii yetu sasa iweze kuwajua na wazazi pamoja na watoto wetu waweze kujitenga na watu hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio haya ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa yanafanywa na watu ambao wako karibu na familia na mara nyingi inakuwa ndani ya familia. Sisi kama Wizara tumeendelea kuelimisha jamii na tunawashukuru sana wenzetu wa Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Mahakama, wamekuwa wanatoa ushirikiano mkubwa sana. Matukio mengi yanashindwa kufika mbali kwa sababu ushirikiano umekuwa ni mdogo ndani ya familia kwenda kutoa ushahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hapa sina takwimu ambazo zinaonesha matukio ni mangapi na kiasi gani yamehukumiwa, lakini kwa taarifa chache ambazo ninazo, ni matuko machache sana ambayo yanafika mwisho kwa sababu tu familia zimekuwa hazitoi ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na Idara ya Mahakama ili matukio haya yaweze kufika mwisho. Kwa hiyo, nitoe rai kwa jamii kutomalizana na haya matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto majumbani na badala yake waruhusu mkondo wa sheria uweze kufika mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili, katika nchi ambazo zimeendelea, kuna kitu kinaitwa Sexual Offender Register. Wale watu ambao wamehukumiwa kutokana na makosa haya ya ukatili wa kijinsia wanatambulika wapi wanakaa, wapi wanafanya kazi na akihamia sehemu mpya watu wote wanaweza wakamfahamu. Kwa hiyo, kwa sasa Serikali hatuna utaratibu huo, lakini ni wazo ambalo tunaweza tukalipokea na kuweza kuliangalia ni jinsi gani ya kulifanyia kazi.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekiri changamoto kubwaya utekelezaji wa Sera hii ya kutoa huduma bure kwa makundi haya maalum ikiwemo wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee wanaozidi umri wa miaka 60 ambao hawana uwezo lakini pia makundi ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii makundi haya yanateseka sana kupata huduma maeneo mbalimbali na wengi kiukweli wanapoteza maisha. Leo maeneo ya vijijini, Wilayani huko wanaandikiwa barua kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya watembee mitaani wanaomba misaada ili waweze kutibiwa kwahiyo Serikali ione changamoto kubwa hii iliyopo.
Mheshimiwa Spika, napenda kujua, Serikali imekuja na mkakati wa kuweza kuwepo hii huduma ya kuweza kutoa bima kwa wote sasa hawajasema specific ni lini itakamilika. Wanasema mpaka mchakato wa Serikali kutoa maamuzi. Hebu muone umuhimu ni lini sasa, naomba commitment hapa Bungeni ni lini mchakato huu utakamilika ili mfuko huu uweze kuwa na fedha ya kutosha makundi haya yatibiwe yaweze kupona kwa kuwa wengi wanapoteza maisha?
Mheshimiwa Spika, lakini tangu Serikali imetoa agizo kwenye Halmashauri zetu ni miaka zita sasa na Mheshimiwa Waziri kwenye majibu yake ni asilimia 40 tu wametekeleza, kwa hiyo bado wazee wengi hawajapewa vitambulisho, hawapati huduma za fya kwenye madirisha maalum.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali, siyo kutoa tu rai, Serikali sasa naiomba leo iweze kutoa tamko hapa Bungeni, itoe deadline ni lini ambapo vitambulisho hivi vikamilike na wale Halmashauri ambazo hazijakamilika kwa wakati waweze kupewa adhabu ili wazee hawa ambao wametumikia Taifa hili wapate huduma za afya bure waweze kuishi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Magdalena Sakaya alitaka commitment ya Serikali kwamba ni lini utaratibu au mchakato huu wa Bima ya Afya kwa wananchi wote utakamilika; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ifikapo Bunge la Septemba Serikali tutaleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wananchi wote ndani ya Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, lakini ameuliza swlai la pili kuhusiana na wazee na lini mchakato huu tuweze kutoa tamko; mimi naomba niseme tu kama ifuatavyo; nchi yetu sasa hivi inaendelea kupata neema na wastani wa Matanzania sasa hivi kuishi ni iaka 64 kwamba tunategemea kwamba na tunatarajia kama kila mtu atatunza afya yake vizuri tunatarajia tu kwamba atafika miaka 64, kwa hiyo umri huu unazidi kuongezeka na iddai ya watu hawa wanazidi kuongezeka ambao wanazidi miaka 60. Kwa hiyo, hatuwezi tukasema wkamba tutatoa ukomo kwamba ifikapo kesho wazee wote wa miaka 60 wawe wamepata vitambulisho.
Kwa hiyo mimi niendelee kusisitiza tu kwamba Serikali imeshatoa maagizo kwa Halmashauri zote na hili ni agizo la Serikali wanatakiwa waendelee kuwatambua wazee na waendelee kuwapatia vitambulisho wale wazee ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli suala hili la matibabu bure limekuwa na changamoto kubwa sana mpaka kuna baadhi ya vituo na hospitali wakina Mama wajawazito wanambiwa waende na mabeseni, pamba na hata mikasi.
Je, ni lini Serikali sasa itaona umuhimu wa kuweka angalau fedha kidogo za kuchangia akina mama wajawazito ili waweze kupata huduma bora? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma kwa ajili ya akina mama wajawazito ni bure na sisi kama Seriakli tumekuwa tunaendelea kuwekeza sasa hivi takribani akina mama milioni mbili wanajifugua kwa mwaka ndani ya nchi yetu na sisi kama Serikali kupitia Bajeti hii ya dawa, vifaatiba na vitendanishi tumejaribu sana kuhakikisha vifaa vya kujifungulia vinakuwepo, tumehakikisha kwamba chanjo kwa ajili ya watoto tunakuwa nazo, dawa zote za muhimu kwa maana dawa za kupunguza upungufu wa damu kwa akina mama yale madini ya iron pamoja na phera sulfate pamoja na folic acid tunakuwa nazo, dawa za kuongeza uchungu oxytocin tunakuwa nazo na dawa za kupunguza kifafa cha mimba tunakuwa nazo. Kwa hiyo, ni sehemu chache sana ambazo tunapata malalamiko kama hayo na mimi kama Naibu Waziri nimetembelea sehemu mengi sana basi ni sehemu nyingi vifaa vya kujifungulia tunavyo na sisi kama Serikali tunavyo kupitia Bohari yetu ya madawa.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Same Mashariki lina tatizo kubwa sana la huduma za afya. Kituo kilichokuwa kimeitwa Kituo cha Afya Vunta kwenye Tarafa ya Mamba Vunta ilikuwa ni ghala la mazao kikapandishwa hadhi lakini hakina hadhi hata ya kuwa dispensary, Tarafa ya Gonja haina hata zahanati wala kituo cha afya cha serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kuiomba Serikali kwamba kwa muda mrefu nimeenda kuongea na Serikali kuhusu kuboresha angalau basi Hospitali ya Gonja Bombo ambayo Serikali kupitia KKKT wanasaidia watu wa Tarafa hii ya Gonja na ya Mamba Vunta kupata huduma katika hospitali hii.
Je, ni lini Serikali itapeleka angalau Madaktari basi wakasaidie kuboresha huduma hii ili akina mama wajawazito wasife wakitembea umbali mkubwa zaidi ya kilometa 15 mpaka 30 kufuata huduma katika Tarafa ya Ndungu ambayo kituo kipo bondeni na Tarafa hizi zote kubwa ziko milimani ambapo hata barabara zetu ni mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za wananchi pale ambapo wanaanzisha ujenzi wa maboma ya zahanati Serikali kupitia Halmashauri imekuwa ikichangia kukamilisha yale maboma lakini sambamba na hilo tumefanya maboresho makubwa sana ya vituo vya afya takribani kati ya vituo zaidi ya 500 ndani ya nchi yetu, zaidi ya 300 na tumeweza kuvifanyia maboresho kuweza kutoa huduma za dharura za kumtoa mtoto tumboni.
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, Serikali katika mwaka huu wa fedha mabao unakwisha tumejielekeza nguvu katika kujenga hospitali za Wilaya 67 na lengo ni kusogeza hizi huduma za fya karibu zaidi na wananchi.
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, katika maeneo ambapo hatuna Hospitali za Wilaya tumekuwa tunafanyakazi kwa karibu sana na hizi hospitali ambazo ziko katika taasisi za kidini ambazo kwa jina zimekuwa zinaitwa DDH na tumekuwa tunawapatia rasilimali fedha kwa ajili ya dawa pamoja na watumishi. Kwa hiyo, sisi tuko tayari kama Serikali tukipata maombi mahususi kuhusiana na hii Hospitali ya DDH ambayo nimekuwa nimeiongelea kama kuha hitaji la rasilimali watu tuko tayari kuweza kushirikiana nao kwa ajili ya lengo la kutoa huduma kwa wananchi wa Same Mashairiki.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, suala alilosema Naibu Waziri ni suala zuri sana wala halina mjadala, lakini sasa Serikali haioni ni wakati sasa wa kufanya matibabu yakawa bure nchini hasa kwa wale waliokuwa hawana bima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri ametoa rai kwamba watu waende kwenye mazoezi, kuhusu suala la mlo na mambo mengine, ni kweli lakini napenda kuishauri Serikali, je, ni kwa nini haitoi elimu kwa jamii namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizika hasa haya ya pressure, sukari na shinikizo la damu? Ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Je, Serikali haioni sasa kuwaondolea matibabu yakawa bure nchini hasa kwa wale wasio na bima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri ametoa rahi hapa kwamba watu waende kwenye mazoezi, kuhusu suala la mlo na mambo mengine, ni kweli lakini napenda kuishauri Serikali. Serikali haitoi elimu kwa jamii namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa hasa haya ya pressure, sukari na shinikizo la damu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwantumu Dau kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nianze kumpa tu maelezo ya awali kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ameliongelea. Magonjwa haya yasiyoambukizwa ni magonjwa ambayo yana gharama sana na ni magonjwa ya kudumu. Naomba nitoe mfano, mgonjwa wa tatizo la figo ili kusafisha damu kwa wiki anahitaji kati ya laki saba na nusu mpaka milioni moja; na upandikizaji wa figo kwa sasa nchini tunafanya kwa takribani milioni 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mgonjwa wa kisukari anahitaji kati ya shilingi 50,000 mpaka 100,000 kutokana na idadi ya dawa; vivyo hivyo kwa mgonjwa ambaye ana shinikizo la damu. Kwa hiyo tumekuwa tunaona ongezeko kubwa sana na ndiyo maana utaona kwamba sisi kama Serikali tumeweka msisitizo mkubwa sana na tunataka kuanzisha program ya kitaifa; lengo ni kuanza kupambana kwasababu mwanzoni tulikuwa tunapambana na magonjwa ya kuambukiza. Unapomtibu malaria mtu leo hatorudi tena katika kituo chetu cha huduma za afya labda baada ya mwaka mmoja. Lakini mgonjwa ambaye anatatizo la kisukari, pressure na saratani, huyu anaingia katika mfumo wetu wa kudumu wa kupata huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo gharama za matibabu haya ni kubwa, na sisi kama Serikali ili kutoa nafuu kwa wananchi ndiyo sasa tunataka tuelekee katika mfumo wa bima ya wananchi wote na mwezi Septemba tunataka tulete Muswada huo ambao utaweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mwananchi anakuwa na bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kipindi hiki cha awali msisitizo mkubwa ambao tunaendelea nao ni kutoa elimu. Tunatoa elimu kupitia Wizara, na ndiyo maana tuliona hata tumepiga marufuku matumizi ya tv zetu katika vituo vya afya ili viweze kutoa elimu kwa umma. Tunaongea na wenzetu wa SUMATRA ili hata katika vyombo vya usafiri elimu ya afya kwa umma.
Mheshimiwa Mwneyekiti, na mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, magonjwa haya ya kuambukiza yanazidi kukua; nitoe rai ya kuhakikisha kwamba tunatunza afya zetu na kutunza afya zetu ni kuhakikisha kwamba tunakula mlo sahihi tunafanya mazoezi na tuhakikishe kwamba tunakuwa na matumizi ya wastani ya vileo ikiwa ni pamoja na pombe na sigara.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana hususan katika haya magonjwa yasiyoambukizwa kama saratani. Kuna shida kubwa sana ya kutambua magonjwa haya mpaka zinakuwa dalili au zile hatua za mwisho sana. Sasa Serikali haioni imefika wakati wa kuja na mkakati mahususi kwa kutoa elimu kujua hizo symptoms na kuboresha huduma katika vituo vyetu vya afya ili kuweza kutoa diagnosis inayotakiwa mapema? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Sware kama lifuatavyo; na ameuliza swali moja zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyektii, ni kweli kansa nyingi ambazo tunaziona katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya zinakuja katika hatua za mwisho sana, na hili yote ni suala tu la elimu na hususan saratani ya shingo ya uzazi ambayo inawaathiri wanawake wengi sana. Wengi wanakuja katika hatua ya tatu na ya nne ambazo ni hatua za mwisho sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Serikali tumeendelea kutoa elimu katika masuala haya magonjwa ya saratani, na tumeendelea vilevile kuhakikisha kwamba huduma za msingi za utambuzi tunazitoa na tunazitoa bure. Katika vituo vyetu vya afya utambuzi wa sarakani ya shingo ya uzazi tunazitoa hizi huduma bure, na mashine za Clio therapy tumeziwekeza sana kwa ajili ya matibabu ya awali ya saratani za shingo za kizazi, zipo.
Mheshimiwa mwenyekiti, na tumekwenda mbali, sasa hivi tunatoa chanjo ya kukinga saratani dhidi ya shingo ya kizazi. Kusudio letu ni kwamba takriban watoto mabinti 650,000 walio kati ya miaka tisa mpaka 14 tuweze kuwafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tumeendelea kuboresha huduma zetu za matibabu ya saratani. Pale ocean road tumefunga linear accelerator ambayo inaifanya Hospitali yetu ya Ocean Road kuwa hospitali ya kisasa kabisa katika matibabu ya mgonjwa wa kionzi. Vilevile tutafunga mashine ya PET scan ambayo itaifanya sasa Taasisi yetu iwe ni taasisi ya kisasa sana katika matibabu ya kansa ndani ya dunia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaendelea kuboresha huduma hizi za matibabu ya saratani kule Bugando, wanatoa dawa lakini vile vile watatoa huduma za mionzi. Pia tunaendelea kuboresha kule KCMC ili waweze kutoa huduma za dawa na vile vile matibabu ya mionzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mikakati ya Serikali ipo na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kufika katika vituo vya afya na kufanya uchunguzi na utambuzi wa ugonjwa wa kansa mapema iwezekanavyo.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ugonjwa wa dengue ni ugonjwa hatari sana na umekuwa ukiwa kwa kasi sana katika nchi yetu, lakini ugonjwa huu ni mgonjwa wa mlipuko kama magonjwa ya kipindupindu na magonjwa mengine, na Serikali imekuwa na utamaduni wa aidha wa kutibu bure au kwa gharama ya chini za matibabu.
Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kutibu ugonjwa huu bure kwa wananchi ili waweze kupambana nao na usisambae katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna mlipuko wa ugonjwa wa dengue ndani ya nchi yetu na hadi kufikia wiki hii tuna cases 1901 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Kilimanjaro pamoja na Singida ambayo imetambuliwa; na hawa mikoa mengine wengi walikuwa ni wagonjwa ambao wamepitia mkoa huu wa Dar es Salaam. Sisi kama Serikali tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba tunaudhibiti ugonjwa huu wa dengue
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama nilivyosema hapo awali na katika taarifa zetu, ugonjwa huu hauna tiba, tunachokifanya ni kutibu zile dalili ambazo mgonjwa anakuja nazo ikiwa ni pamoja na matibabu ya homa, maumivu pamoja na upungufu wa maji ambao anakuwa nao. Changamoto kubwa ilikuwa katika katika upatikanaji wa vipimo. Sasa hivi niwahakikishie kwamba katika vituo vyetu vya umma vipimo vimepatikana na tumevisambaza katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na hapa Dodoma. Kusudio letu ndani ya wiki moja ijayo tutapata vipimo tena ambavyo tutataka sasa tuvisambaze nchi nzima ili kuhakikisha kwamba tunaweza kubaini hizi cases za ugonjwa huu wa dengue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hoja kubwa katika maswali mengi ambayo tumekuwa tunayapata ni ugharamiaji ugonjwa huu wa dengue na husasan kwa wale wagonjwa wa bima. Niseme tu kwamba wagonjwa wa ugonjwa huu wa dengue wanapata matibabu kwasababu huu ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine, na wanatibiwa na pale lilikuwa ni suala sasa la vipimo. Kwa wale wagonjwa ambao ni wagonjwa wa dengue ambao wanakadi ya bima za afya wanapokwenda katika vituo vya umma huduma ile ya vipimo wataipata bure. Tutazitoa hizi huduma za vipimo katika hospitali zetu za umma na kwasababu tumeshasambaza vipimo katika hospitali zetu za Umma.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza na pia kwa Mheshimiwa alivyonijivu kidogo inaleta afueni kwa wazee wetu lakini bado haijawa ya kuridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wazee bado wanaendelea kuteseka kupata matibabu yaliyo bora.
Je, Wizara imefanya tathmini gani ya kuona kwamba wazee hawa wanaendelea kutunzwa na kwamba hawawezi kupata shida?
Swali la pili, kwa kuwa wazee wanahaki ya kutunzwa na kulelewa lakini hakuna sheria iliyotungwa ilhali Sera imetungwa tangu mwaka 2007 lakini sheria hadi hii leo haijatungwa; unategemea nini, kwamba Sera yako hii itaweza kufanyakazi na wazee hawa waweze kutunzwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake ameuliza kwamba tumefanya tathmini na changamoto ni zipi. Changamoto kama nilivyosema, ni kwamba kwanza ni utambuzi wa wazee. Taifa letu limepata bahati, sasa hivi kadri tunavyoboresha sekta yetu ya afya umri wa wazee nao kuishi unazidi kuongezeka. Sasa hivi wastani wa Mtanzania kuishi ni miaka 64 na wengi miaka 64 bado wana afya njema, na kundi hili linazidi kukua kwasababu ya maboresho haya ambayo tumeyafanya katika sekta yetu ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo moja ya changamoto ambayo tunayo ni utambuzi wa hawa wazee. Ndiyo maana tumetoa rai kuhakikisha kwamba halmashauri zinaendelea kuwatambua na kuwapatia vitambulisho. Wizara tumetoa maelekezo ya kuwa na madirisha maalum kwa ajili ya kuwahudumia wazee, na hili tumeendelea kulifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto nyingine ambayo tumeibaini na ambayo sasa nayo tunataka kuitibu ni magonjwa ambayo yanawaathiri wazee ni magonjwa mahususi sana; na katika jibu langu la msingi kwa swali lililopita nilijibu kwamba sasa tunataka kwenda katika National program ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo itakwenda mpaka chini kuhakikisha kwamba sasa wazee wale ambao magonjwa yao mengi ni yale magonjwa sugu basi waweze kupata huduma zao kule kule katika ngazi za kata na zahanati ambazo wanazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, changamoto nyingine ambayo tumeibaini na ambayo sasa tunataka kuitibu ni ugharamiaji wa matibabu kwa wazee ambapo sasa tunataka mwezi Septemba tuje na muswada wa sheria ambao utakuwa na bima ya wananchi wote ambao sasa utaweza kufanya ugharamiaji wa matibabu haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili linauliza ni lini Serikali italeta sheria ya wazee. Sera ambayo tunayo sasa hivi sisi kama Serikali tumeona imepitwa na wakati na sasa tuko katika hatua ya kufanya mapitio ya Sera hii ya Wazee ili iweze kuendana na mazingira ya kwetu ya sasa na baada ya hapo sasa Serikali itatafakari kama kuna umuhimu wa kuja na sheria mpya ya wazee.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Pamoja na huduma bure kwa wazee bado tuna ule mkakati pia au huduma ambayo inatolewa kwa mama na mtoto hasa akina mama wanaokwenda kujifungua. Ni kweli inatakiwa iwe bure lakini ukweli on the ground akina mama hawa wanatakiwa kwenda na kits, na ninaushahidi wa ndugu yangu ambaye amejifungua watoto watatu juzi japokuwa hawakuwa riziki; alikwenda na kila kitu kwenda kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa changamoto hii ambayo bado watu wanakwenda na vifaa, ni kwa nini Serikali isipate taasisi zetu au REPOA au ESRF waweze kufanya utafiti kuona ni kwanini kits zinakuweko na kwanini wahusika hawapewi? maana yake mkienda nyinyi Mawaziri hamtapata ukweli lazima tupate mtu wa pembeni atakayefanya utafiti.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Mollel Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunagharamia ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kujifungulia akina mama. Ninachokiona hapa ni changamoto ya uelewa kwa watoa huduma wetu wa afya. Mama anapokwenda kliniki anaambiwa ajiandae ili atakapopata dharura kabla hajafika katika kituo cha kutoa huduma ya afya endapo atapata dharura basi awe na vifaa ambavyo vinavyomsaidia. Hata hivyo vifaa hivi si mbadala wa vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya kuwa na vifaa vya kujifungulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaipokea hii changamoto na sisi tutaweza kutoa maelezo vizuri kwa watoa huduma wetu wa afya ili waweze kuzingatia misingi hii; kwasababu sisi kama Serikali tunagharamia vifaa na vifaa hivi tunavyo katika bohari yetu ya madawa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze sana Serikali kwa kupeleka jenereta tena kwa ajili ya kuendeleza huduma katika hospitali ya Mkoa wa Geita, lakini bado kuna changamoto nyingine pia kwamba hospitali ya Mkoa wa Geita pia ina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatikana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo hospitali ya Mkoa wa Geita pia katika vituo vingi vya kutolea huduma kwenye Mkoa wa Geita hakuna nishati ya umeme na hii inasababisha huduma kutolewa lakini pia kupata changamoto hasa kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua usiku;
Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinapatiwa huduma ya umeme maeneo yote katika Mkoa wa Geita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakiri kwamba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tuna changamoto ya rasilimali watu, watumishi waliokuwepo pale ni takriban asilimia 50 ya watumishi wote ambao wanahitajika. Serikali imeliona hilo na inaendelea kuongeza watumishi kadri vibali vya ajira vinavyopatikana. Sambamba na hilo, tunaendelea kusomesha wataalam mbalimbali kuhakikisha kwamba zile huduma za kibingwa basi zinapatikana katika Mkoa huu wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia kuhusu suala la umeme katiak vituo vyetu vya kutolea huduma za afya. Wizara ya Afya tumekuwa tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Nishati kupitia mpango wa REA na moja ya mkakati katika mradi huu ni kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma za afya na shule vinapata umeme. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Nishati kupitia mradi wa REA itahakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanapitiwa na mradi wa REA basi nayo yanapata umeme.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, asilimia kubwa ya wananchi wetu kipato chao ni cha chini na wamekuwa wakitegemea hpspitali zetu za Serikali kama msaada mkubwa pindi wanapopata changamoto za afya. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba, hawa madktari bingwa wachache ambao tunao hawapati vishawishi vya kwenda kufanya kazi nje ya nchi ama kwenye private hospitals?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ukiangalia idadi ya madaktari bingwa ambao tunao bado ni chache sana, lakini hospitali nyingi za mikoa hazina madaktari bingwa. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha madaktari hawa wanagawiwa kwa uwiano mzuri, ili kuepusha usumbufu wa Wananchi wengi kutoka mikoani na kufuata huduma Hospitali ya Muhimbili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako kwamba, katika nchi ambazo tumejaliwa kidogo kwamba, madaktari wetu hawatoki sana kwenda nje ya nchi kulinganisha na nchi nyingine katika Bara la Afrika, Tanzania ni mojawapo.
Mheshimiwa Spika, na moja ya mkakati ambao tumeuweka wa kuhamasisha madaktari wetu na wataalam wetu wa afya kuendelea kukaa nchini ni maboresho ambayo tunaendelea kuyafanya katika sekta ya afya; vituo zaidi ya 352 tumeviboresha, hospitali za wilaya 67 tumejenga, sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa hospitali za rufaa tano za mikoa na maboresho mengine makubwa ya kimiundombinu, ya vifaa, ambayo sasa hivi yamesababisha kwamba, hata huduma zile kubwa za kibingwa ambazo zilikuwa zinafanyika nje ya nchi sasa hivi zimeweza kufanyika nchini. Kwa hiyo, hili nalo limesaidia sana kuwafanya wataalam wetu wazalendo kubaki, pamoja na motisha nyingine za ndani ambazo tumeendelea kuwapatia watalaam wetu katika sekta yetu ya afya.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Sonia Magogo ameulizia suala la uwiano; ni kweli tunakiri tumekuwa na changamoto kubwa sana ya uwiano wa upatikanaji wa Madaktari Bingwa katika baadhi ya mikoa. Na hili sisi kama Wizara tumeshaliona na moja ya mkakati ambao tumeufanya sisi kama Wizara ni kuhakikisha kwamba, wataalam ambao tunaenda kuwasomesha kwa fedha ya Serikali tunachukua katika maeneo ambayo yamekuwa na uhaba mkubwa wa wataalam kwa lengo kwamba akimaliza na tumewasainisha kitu kinaitwa bonding kwamba, ukimaliza na iwapo kama umesoma na fedha za Serikali basi tutakurudisha kulekule katika maeneo ambayo ulikuwa umetoka, ili uweze kupata utaalam huo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha mpito ambapo huduma hizi hazijaweza kupatikana katika baadhi ya mikoa ndio tumekuwa tunaendesha kambi; Madaktari Bingwa hawa wachache tulio nao tumekuwa tunawazungusha ndani ya nchi kwa kambi maalum katika baadhi ya mikoa, ili waweze kutoa hizo huduma kwa wale Wananchi, ili angalau katika ile mikoa basi huduma zile ziweze kupatikana.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu haya ya Serikali, pia nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kusaidia mashirika haya ya Kiserikali na kuyawekea utaratibu mzuri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Taasisi Zisizo za Kiserikali, Ofisi za Mrajisi wa Mashirika hayo kati ya Zanzibar na Tanzania Bara wana ushirikiano mzuri na ushirikiano wa pamoja, lakini kuna changamoto moja. Taasisi zisizo za Kiserikali zinapotaka kufungua upande mmoja wa Muungano aidha Bara au Zanzibar taasisi hizo zinalipishwa sawasawa na taasisi za kigeni zinapotaka kufungua Mashirika ya Kiserikali hapa Zanzibar.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hiyo ili mashirika yetu ya kiserikali ya Zanzibar na Bara yasiwe yanalipishwa sawasawa na taasisi ambazo zinatoka nje ya nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, Taasisi Zisizo za Kiserikali zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana katika kuinua mchango wa nchi na uchumi wa wananchi, zimekuwa zikisaidia sana kutatua baadhi ya changamoto mbalimbali za kusaidia jamii na huduma mbalimbali za kijamii. Je, Serikali inatambua vipi mchango huo wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika,
kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu sana wa utendaji wa Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na hususan masuala haya ya NGOs. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa sheria tuliyokuwa nayo sasa hivi ambayo inasimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni sheria ambayo si ya Muungano, kwa maana kwamba Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Serikali Tanzania Bara ni tofauti na yule ambaye yuko kule Zanzibar. Hata hivyo, tunatambua kwamba kuna NGOs nyingi hapa nchini ambazo zinafanya kazi Tanzania Bara na vilevile Tanzania Visiwani.
Mheshimiwa Spika, changamoto ambayo ameeleza Mheshimiwa Mbunge tunakiri kwamba tunayo, lakini sisi kama Serikali tulishaanza kuchukua hatua, Msajili wa Mashirika Yasiyo Serikali Tanzania Bara pamoja na kule Zanzibar wamekuwa wakifanya vikao. Kikao cha kwanza walikifanya mwezi Septemba na Disemba mwaka jana wamekaa tena na kuweza kuweka utaratibu mzuri ambapo Taasisi ama NGOs ambazo zinafanya kazi Tanzania Bara zinaweza zikapata unafuu wa kuweza kufanya kazi Zanzibar na zile za Zanzibar zinaweza zikafanya kazi Tanzania Bara wakati marekebisho ya sheria yakiendelea ili kuweza kuweka utaratibu mzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili ameuliza kuhusiana na mchango wa NGOs. Tulipofanya marekebisho ya Sheria ile ya NGO’s, lengo na mahususi lilikuwa ni hilo, kwa sababu kwanza kulikuwa kuna mkanganyiko mkubwa sana wa usajili wa NGOs, kulikuwa kuna NGOs ambazo zilikuwa zinasajiliwa chini ya Msajili wa NGOs na kulikuwa kuna NGOs ambazo zilikuwa zinasajiliwa BRELA, kulikuwa kuna NGOs ambazo zilikuwa zinasajiliwa kwa Msajili wa Societies. Usimamizi na mchango ilikuwa ni mgumu sana kuuratibu, lakini kwa utaratibu huu mpya sasa hivi ambao umeuhisha usajili wa NGOs, sasa hivi tutaweza kujua mchango wa NGOs zote takribani 10,000 ndani ya nchi na sisi kama Serikali tutakuwa tunautambua na kuuthamini mchango huo katika taarifa zetu mbalimbali za Serikali.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza napenda nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amekiri kwamba watoto wa mitaani wapo.
Mheshimiwa Spika, zipo sababu nyingi zinazosababisha uwepo wa wimbi kubwa la watoto wa mitaani ikiwemo na wazazi na hasa akinababa kutelekeza familia zao.
Je, Serikali inachukua hatua gani pindi inapowabaini wazazi wa aina hiyo, inawachukulia hatua gani katika kuhakikisha wanarudi katika familia zao na familia zinaimarika? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali inatekeleza programu ya kuwaunganisha watoto na familia na kuwapa malezi mbadala na Waziri ameeleza kwamba programu hii inatekelezwa katika Mkoa wa Mwanza, tunayo mikoa 26; ni nini sasa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha programu hii inafika katika mikoa mingine ikiwemo Mkoa wa Ruvuma ili wazazi na watoto waliopo katika maeneo yale wafaidike na programu hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya, lakini kwa ufuatiliaji wa karibu sana kuhusiana na masuala ambayo yanahusiana na haki na ustawi wa watoto Tanzania. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa tumeona ongezeko la watoto ambao wanaishi na kuzurura mitaani na moja ya kisababishi ni hiyo sababu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema, wazazi kutelekeza majukumu yao ya msingi ya kuwasimamia watoto hawa. Na ni kweli kwamba tuna Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ambayo imetoa haki za msingi kwa mtoto. Na sisi Serikali kupitia Ustawi wa Jamii tumeendelea kuyashughulikia mashauri mbalimbali ya wazazi na hususan akinababa kutelekeza watoto na kuyapeleka Mahakamani kukazia hukumu.
Mheshimiwa Spika, tunatambua bado ipo changamoto ya wigo wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo mbalimbali na sisi kama Serikali tunajaribu sana kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo mbalimbali. Lakini vilevile tunaendelea kutafakari kuhusiana na hizi adhabu ambazo tumeziweka, hususan pale ambapo mzazi kuna hukumu ya Mahakama, lakini wazazi wanaendelea kukaidi. Tunaangalia njia bora zaidi ya kuhakikisha kwamba zile adhabu zinawekewa msisitizo.
Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuna hii programu ambayo tumeianzisha ya kuwaunganisha watoto na walezi ama walezi mbadala ama wazazi mbadala. Hii tumeianza katika ngazi ya majaribio tutakapoona mafanikio na matunda ya programu hii, hapo sasa ndio tutakapoanza kwenda katika maeneo mengine ya nchi hususan majiji ambayo tuna changamoto kubwa ya watoto wanaozurura mitaani.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kuweka mpango mzuri kabisa wa elimu kwa watoto wetu kwamba watoto wote wanahakikisha wanapata elimu, lakini bado kuna wazazi ambao kwa mfano pale Dar es Salaam wanakaa pale barabarani wanawatuma watoto kwenda kuomba kwenye magari, sasa wale watoto wanakosa haki kabisa ya msingi ya kusoma.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba watoto wetu wale wanasoma na wale wazazi wanachukuliwa hatua?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya nyongeza kwa Mheshimiwa Chikambo, watoto, labda kwa faida ya Bunge lako tukufu, Tanzania tumeridhia Mkataba wa Kimataifa na sisi tukaanzisha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inatoa haki kwa watoto. Mtoto ana haki ya kutunzwa, mtoto ana haki ya kuendelezwa, mtoto ana haki ya kushirikishwa katika maamuzi yanayomhusu na mtoto ana haki ya kutokutumikishwa kazi nzito.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiangalia katika sheria hii utaona hapa tunagusa katika maeneo makubwa mawili; kwanza haki ya mtoto ya kuendelezwa, lakini haki ya mtoto kutotumikishwa kazi nzito. Serikali tumeendelea kuchukua hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, lakini naomba nitumie fursa hii sasa kuongea na kuziagiza Halmashauri za manispaa na majii kuhakikisha kwamba, wanasimamia kikamilifu sheria hii ya mtoto na ili watoto wale waweze kupata haki yao ya msingi ya kuendelezwa kwa maana ya kusoma, lakini pili kutokutumikishwa kazi na badala yake wale watoto waweze kukaa shuleni na kupata elimu. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, sijui mchakato utakamilika lini, lakini kuna mambo mawili; kunakuwepo mashine na kunakuwepo msomaji. Katika Hospitali hii ya Mkoa wa Mtwara kuna tatizo pia la msomaji wa x-ray, mtu amevunjika mkono sehemu ya nyuma, inaonekana amevunjika mkono sehemu ya mbele. Sasa nataka kujua Serikali imejipanga vipi inapopeleka hiyo mashine tena ya digital na kumpata mtu ambaye ataendana na hiyo mashine katika usomaji wake?
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, katika Hospitali ile ya Mkoa wa Mtwara kumekuwa na tatizo kubwa la madaktari hasa upande wa wanawake. Nataka kujua Serikali imejipanga vipi na ni lini itapeleka madaktari hao ili kutoa kero hii ambayo iko kwa muda mrefu? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tunza Malapo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri na ufuatiliaji ambao anaufanya katika sekta hii ya afya na hususan katika Mkoa huu wa Mtwara. Labda niseme ni hivi kwamba katika hili eneo ambalo ameligusia kuna mambo mawili kuna suala la mpiga picha ambaye ni radiographer, yeye kazi yake ni kupiga picha, lakini tuna radiologist ambaye yeye ni msomaji wa picha. Digital x-ray tutafunga na ni kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, mashine ziko bandarini tunafanya utaratibu wa ugomboaji na tutaenda kuifunga pale Ligula, radiographer tunao.
Mheshimiwa Spika, suala la msomaji tunakuja na utaratibu mpya kwa sababu hii ni digital x-ray sisi kama Serikali na sisi tunaingia katika mfumo unaitwa telemedicine na tutakuja na kitu kinaitwa tele-radiology, kwamba hizi digital x-ray zote ambazo tunazifunga kwa kutumia Mkongo wa Taifa pale Muhimbili na pale MOI sasa hivi tumetengeneza kitu kinaitwa hub. Tutakuwa na centre moja ambayo kutakuwa na screen ambayo imeunganishwa na mtandao, picha zitakazopigwa Tanzania kote iwe ni Mbinga, iwe ni Ligula, iwe katika eneo lolote Tanzania hii zitakuwa zinatumwa, wataalam/madaktari wetu bingwa pale Muhimbili wataisoma ndani ya dakika 15 na lile jibu linarudi tena kulekule ambako linatoka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikutoe mashaka sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba matumizi ya hizi digital x-rays zinaweza zikatumika na wananchi wa Tanzania wananufaika na utaratibu mpya ambao tumeanza nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la Madaktari Bingwa; ni kweli Hospitali ya Mkoa ya Ligula ina changamoto ya Madaktari Bingwa na sasa hivi sisi kama Serikali tunawekeza katika kuhakikisha kwamba hospitali za rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Ligula tunakuwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto, madaktari bingwa wa magonjwa ya mifupa, madaktari bingwa wa magonjwa ya dharura, pamoja na mengine mengi.
Kwa hiyo, sasa hivi wapo Madaktari wapo katika mfumo wa mafunzo na tumesomesha zaidi ya madaktari 100 kwa mwaka pale watakapokamilisha masomo yao tutawapangia katika hospitali zetu ya Iligula na hospitali zingine za RRH. Lengo na kusudio la Serikali wakati tunaboresha vituo vya afya, hospitali za wilaya, tunataka sasa hospitali za rufaa za mikoa zitoe huduma za kibingwa kama ilivyokusudiwa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kwanza kabisa kwa masikitiko makubwa naomba nitoe pole zangu za dhati kwa wananchi waliopatwa na kadhia ya mvua na hasa katika Mkoa wetu wa Lindi kule Kilwa, Liwale pamoja na Lindi Vijijini na hasa katika eneo la Mchinga ambao watu wamepoteza makazi yao, mazao yao na vitu vingi mbalimbali, tunawapa pole sana kwa hilo.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nataka niulize swali langu la nyongeza kutokana na swali la msingi namba tisa kuhusu suala la x-ray, nitauliza suala la mashine ya dialysis. Tunajua na tunatambua kwamba ugonjwa wa kisukari unaongezeka siku hadi siku na kutokana na kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari unapelekea matatizo ya figo na matatizo ya figo yanapelekea watu kufanya dialysis. Dialysis hizi ziko katika maeneo machache hapa nchini kwetu Tanzania. Je, ni lini mashine za dialysis zitapelekwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Viti Maalum/Mbunge wa Taifa lakini anawakilisha Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunaona ongezeko kubwa sana la wagonjwa wa figo ambao wanahitaji huduma za kusafisha damu na ni kweli huduma hizi zimekuwa katika hospitali ngazi ya kanda na katika mikoa mingi huduma hii ilikuwa inakosekana hali ambayo ilikuwa inapelekea watu wengi kusafiri muda mrefu kwenda kupata huduma hii. Aina ya huduma hii inahitaji mtu apate dialysis mara tatu au nne kwa wiki ili aweze kuendelea na maisha yake. Serikali tumeliona hilo na sasa hivi tumepata dialysis machines takribani 45, tunazisambaza katika mikoa nane na mkoa ambao tutaanza nao ni pamoja na Mkoa wa Mtwara, Lindi hatujaiweka katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, kusudio letu ni kwamba kadri tunavyojenga uwezo na upatikanaji wa hizi mashine kwa sababu naomba niseme dialysis machine si kila mtu ambaye anaweza akaifanya, inahitaji utaalam, inahitaji miundombinu tofauti kabisa, inahitaji maji maalum, inahitaji manesi maalum, kwa hiyo tunaendelea kujenga na kwa kuanzia tunaanza na mikoa nane ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Mtwara, tunaamini kwamba huduma hii sasa tutakuwa tumeisogeza karibu zaidi na wananchi wa Mkoa wa Lindi wakati tunaendelea kujenga uwezo na baada ya hapo tutafika mikoa yote ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Lindi. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo inajitahidi kuboresha afya ya Watanzania lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na jitihada za Serikali lakini kuna tatizo kubwa ambalo liko vijijini na mijini, wanawake wengi bado wakiwa wajawazito hawana ile elimu ya kuona kwamba ni muhimu waende clinic. Sasa Serikali mnajitahidi kiasi gani kuhakikisha wanawake wakiwa wajawazito vijijini pamoja na mijini wanakwenda clinic? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tafiti zilizofanywa katika nchi yetu ya Tanzania, bado watoto ambao wana chini ya umri wa mwezi mmoja baada ya kuzaliwa wanakufa kwa wingi na ukweli tafiti zimeonesha kwamba hawajapungua kabisa, wanaendelea kufa. Serikali mnaniambia nini katika hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpa pongezi sana amekuwa ni champion mkubwa sana katika masuala ya afya ya uzazi wa akina mama na mtoto. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze katika maswali mawili mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyauliza. La kwanza ni kuhusiana na akina mama kwenda kliniki. Ni kweli, Serikali imewekeza juhudi kubwa sana katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya. Mwaka 2015 idadi ya akina mama ambao walikuwa wanakwenda clinic ilikuwa ni asilimia 38 kwa mara zote nne katika kipindi cha ujauzito lakini Serikali imeendelea kuweka juhudi, mikakati mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa akina mama, hivi tunavyoongea hadi kufikia Desemba 2019, asilimia 80 ya akina mama wanakwenda kiliniki.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii nayo ni hatua kubwa sana katika kuhakikisha akina mama wanapata elimu, ushauri katika kipindi chao cha ujauzito na hii inaweza kusababisha hata kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Nitoe rai kwa akina mama wote na akina baba kwa sababu masuala haya ya ulezi wa ujauzito ni jukumu la wazazi wote wawili kuhakikisha kwamba kila mama mjamzito anafika kliniki kwa ajili ya kuweza kupata ushauri nasaha na jinsi gani ya kuweza kutunza ujauzito ule.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili vifo vya watoto chini ya mwezi mmoja, ni kweli katika takwimu ambazo hazishuki ni pamoja na hii. Katika mwaka 2015, tulikuwa na watoto wachanga chini ya mwezi mmoja wakifariki 26 kwa vizazi hai 100,000. Sasa hivi tunapoongelea Desemba mwaka jana imeshuka kwa unit moja tu mpaka 25 kwa vizazi hai 100,000.
Mheshimiwa Spika, lakini sisi kama Serikali tunajaribu kuweka hatua, kwanza kuhamasisha akina mama kwenda kliniki; pili kuhakikisha kwamba chanjo zote za msingi za watoto chini ya miaka mitano zinapatikana; kutoa elimu kwa watoa huduma wa afya pamoja na akina mama ikiwa ni pamoja na jinsi ya kutunza watoto njiti. Visababishi vikubwa vya watoto chini ya mwezi mmoja ni zile complication ambazo wanazipata wakati wa kupumua wakati wa kujifungua, maambukizi ya magonjwa ambayo wanayapata wakati wa kujifungua ikiwa ni pamoja na uzito wa chini.
Mheshimiwa Spika, hii ndiyo mikakati ambayo tumejaribu kuifanua kwa kupanua huduma za afya kuhakikisha kwamba akina mama wajawazito ambao wana pingamizi wanapata huduma kwa haraka. Tumepunguza sana maambukizi ya watoto hawa na kuhakikisha wale watoto njiti wanatunza kwa njia ya kangaroo motherhood ambapo kwa kiasi kikubwa tunaamini sasa tutapata matokeo makubwa sana. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Waziri amesema kwamba ugonjwa huu ni tatizo kubwa nchini lakini katika Mkoa wa Tabora hasa Wilaya za Sikonge, Kaliua pamoja na Uyui umekuwa ni mkubwa zaidi hadi kusababisha kila siku watoto 40 kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete. Watoto hawa ni wengi sana na ndiyo hawa ambao wamejitokeza kuja hospitalini, hatujui hawa ambao hawajaja hospitalini. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wazazi kuhusu ugonjwa huu wa mguu kifundo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Daktari aliyepo katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete yupo tayari kufanya kliniki kwenye Wilaya hizi ili angalau kuwafuata wazazi ambao hawana uwezo wa kuwapeleka watoto wao Kitete?
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti kidogo ili Daktari huyu aweze kufika kwenye Wilaya hizi na kuweza kutibu watoto wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge kutoka Mkoa wa Tabora, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba mguu kifundo kwa lugha ya kitaalam tunaita Talipes ni ugonjwa ambao hutokea kwa baadhi ya watoto; mmoja kati ya watoto 1,000. Niseme tu kwamba mtoto akibainika mapema anaweza akapata matibabu na zaidi ya asilimia 80 ya hawa watoto miguu hurejea kuwa katika hali ya kawaida. Nitumie fursa hii kuongea na jamii ya Watanzania kusema kwamba wazazi wote ambao wana watoto ambao wana tatizo hili la mguu kifundo wawafikishe katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya ili waweze kupata huduma za utengamao. Kama nilivyosema hapo awali, ugonjwa huu unaweza ukatibika kwa kutumia utaratibu wa hizi huduma za utengamao.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, sisi kama Wizara hatuna shida kama tuna mtaalam pale katika hospitali yetu ya Kitete kumpa usaidizi ili kuweza kufanya kliniki katika Wilaya zote. Hili Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukakaa tukaangalia utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba hii huduma inaweza ikapatikana katika Wilaya nyingine ambapo si rahisi kufika katika hospitali yetu ya Kitete pale Tabora.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa majengo yanayotumika sasa hivi yana uchakavu mkubwa na ya muda mrefu, je, watakuwa tayari sasa angalau kuwapa fedha waweze kukarabati yale majengo ambayo yanatumika sasa hivi ikiwa ni pamoja na uzio?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, chuo kile kina uhaba wa watumishi wa kada ya ualimu watano pamoja na karani, mpiga chapa na mtu wa IT. Wizara itakuwa tayari kutusaidia angalau kuweza kupatikana hao walimu watano pamoja na hao watumishi wengine niliowataja?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini kwa ufuatiliaji wa karibu sana wa chuo hiki na niliweza kufika katika chuo kile na kuona hali ya majengo. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge hili sisi kama Wizara tunalichukulia kwa kipaumbele cha hali ya juu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi sasa hivi tuko katika zoezi la kufanya uhakiki kuangalia mahitaji, vipaumbele na kitu gani ambacho tunahitaji kukifanya kwa haraka zaidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pindi utaratibu huu utakapokamilika basi chuo hiki nacho tutakipa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo vilevile amegusia suala la uhaba wa watumishi. Hili kama Wizara tumelipokea na tumekuwa tunaendelea kufanya tathmini katika vyuo vyetu hivi vya afya. Kadri tunavyopata vibali vya ajira basi na chuo hiki nacho tutakipa kipaumbele kupata hawa watumishi ambao wamepungua.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vitendo hivi vinasikitisha sana. Huwezi ukakuta ng’ombe dume anapanda ndama, huwezi ukakuta jogoo anapanda kifaranga lakini binadamu aliyepewa utashi anafanya vitu hivyo. Ukiangalia trend ya matukio yanaongezeka kwa kiasi kikubwa. Matukio 13,457 mwaka 2018 yameongezeka kwa 1,000 lakini ukienda Mahakamani hukuti hizi kesi. Je, Wizara ina mkakati gani kuhakikisha haya matukio yote inasimamia upatikanaji wa ushahidi na kuhakikisha yanakwenda Mahakamani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sehemu kubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinasababishwa na mila na desturi potofu. Kwa mfano, katika mila za Kihehe kuna utamaduni unaitwa Nyangusage, katika tamaduni za Kisukuma kuna mila inaitwa Chagulaga na Kigoma kuna Teleza. Wizara ina mkakati gani wa kutoa elimu kuhakikisha mila na tamaduni potofu zinatokomezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matukio haya yamekuwa yanaongezeka na changamoto kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba asilimia zaidi ya 60 ya matukio haya yanafanywa na watu ambao wako karibu na familia na tumekuwa tunapata changamoto kama Serikali kuyafikisha na kuchukua hatua kwa wale wahusika kwa sababu ndugu na jamaa wanakaa vikao vya familia wanaamua kumalizana kwa kutozana faini au kwa kumtorosha yule mwathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba haya mambo hayamalizwi katika mazingira ya nyumbani na badala yake mkondo wa sheria uruhusiwe kuchukua hatua. Kama Serikali ama kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto tunafanya kazi kwa karibu sana na Idara ya Mahakama, tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani na tuna mpango unaitwa MTAKUWA ambao ni mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha 2021/2022. Katika mpango mkakati huu, taasisi zote za kisekta ambazo zinashirikiana kwa pamoja tuna lengo la kuhakikisha kwamba suala hili la ukatili wa kijinsia tunaweza kulidhibiti ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mlinga ameuliza swali lake la pili kuhusiana na mila na desturi potofu. Hili kama Wizara tunaendelea kulifanyia kazi na tumekuwa tunafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa kidini, kimila, wanazuoni na sasa hivi tumeanza hata kufanya kazi na wasanii mbalimbali kuhakikisha kwamba tunafikisha ujumbe huu kwa jamii. Suala lililotokea kule Kigoma la Teleza, lile siyo mila, ni suala la uhalifu, nasi kama Serikali tulichukua hatua na kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa ninavyoongea wako Mahakamani na mkondo wa sheria unachukua hatua zake. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ukiangalia matukio yote haya yanatokana na sababu kwamba wananchi wengi hawajapata elimu. Hapa Mheshimiwa Naibu Waziri anazungumzia suala la mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini sisi kama wadau wakubwa hatujapata hata semina wala hatujui huo mpango. Nataka kujua, Serikali italeta lini mpango huo ili sisi kama Wabunge tuujue na tuweze kuupeleka katika maeneo yetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baada ya kubaini ukubwa wa tatizo hili, tulikuja na mpango unaitwa MTAKUWA ambao ni Mpango Mkakati wa Serikali wa Kutokomeza au Kudhibiti Ukatili wa Kijinsia wa Wanawake na Watoto. Ndani ya Mpango huu kuna mambo mbalimbali mbayo tumeyaainisha, moja ni kuanzisha Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto, kuanzisha huduma za mkono kwa mkono na masuala ya kutoa elimu mbalimbali katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge naye ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Wabunge, wote kwa ujumla tutafanya utaratibu wa kuhakikisha tunatoa elimu kuhusiana na mpango mkakati huu. Tunawaomba sana Waheshimiwa Wabunge nanyi muwe mabalozi wa mpango huu wa MTAKUWA kwenda kukemea masuala haya ya ukatili wa kijinsia katika sehemu ambazo mnatoka.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake japo hayaridhishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Sera ya Afya inazungumzia suala la uchangiaji, lakini vilevile Serikali itakubaliana nami kwamba Tanzania bado watu wengi ni maskini lakini kubwa zaidi maiti inapaswa kupata heshima yake na ndiyo sababu inahifadhiwa na uhalisia unaonesha wazi, kwamba watu wengi wameshindwa kutoa maiti hizo na matokeo yake tumeona hata hivi majuzi pale Muhimbili Mheshimiwa Rais akitoa takribani 5,000,000 kwa yule Mama kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza Mheshimiwa Rais ataenda kila mahali kutoa hizo fedha. Nilitaka kujua sasa Serikali ina utaratibu gani wa muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha kwamba wale wenye matatizo makubwa ambao wanashindwa kabisa wanakabidhiwa maiti zao kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Waziri amesema kweli watu wajiunge kwenye Bima ya Afya nami nakubaliana naye, lakini Serikali hii mpaka leo tunapoongea ni asilimia takribani 33 tu ya watu waliojiunga kwenye Bima ya Afya. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba hiyo asilimia 66 nayo inajiunga kwenye Bima ya Afya ili tuondokane kabisa siyo tu na tatizo la kutoa maiti hospitalini, vilevile wananchi wapate afya kama haki yao ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapokwenda kupata matibabu kuna matokeo mawili anaweza akapona au akapoteza maisha. Nami naomba niseme tu kwamba hakuna maiti ambayo imezuiliwa moja kwa moja au tumezishikilia moja kwa moja kutokana na kwamba mtu ameshindwa kutoa gharama za matibabu. Serikali mimi pamoja na Waziri wangu na Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wanatufuata, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi katika ambao wanapata huduma katika hospitali zetu kubwa na hii tumekuwa tunaipata changamoto katika Hospitali ya Mloganzila, Hospitali ya Muhimbili na maeneo mengine kufika ofisi ya Ustawi wa Jamii katika hospitali husika, pale watapewa malekezo sahihi ya utaratibu wa kufanya na utaratibu wa kulipa, wanaweza wakapewa maelekezo ya kulipa taratibu. Siyo jukumu na nasi kama Serikali hatuzuii ile miili lengo ni kuhakikisha kwamba tunaweka utaratibu mzuri zaidi kuhakikisha kwamba yale madeni yanalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano kwa Mheshimiwa Mbunge hospitali ya Temeke kati ya Juni na Agosti mwaka huu ambao tunakaa tunaongelea wagonjwa wa msamaha kwa mwezi Juni, Temeke yake walikuwa ni wagonjwa 4,949, Julai wagonjwa 4, 816, mwezi Agosti wagonjwa 4, 809, na jumla yote ukikaa ukipigia hesabu ni takribani zaidi ya milioni 500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la kuwa na mgonjwa amefariki haiondoi jukumu la ndugu na jamaa wa yule mgonjwa kuhakikisha kwamba wanalipia zile gharama. Kama nilivyosema utaratibu tumeweka wa Serikali kupitia Idara za Ustawi wa Jamii katika hospitali husika mgonjwa ama ndugu wanapaswa kwenda pale na watapewa utaratibu sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili umeongelea kwamba asilimia 33 tu ya wananchi wako katika Bima ya Afya hii ni kweli tumeliona hilo, kusudio la Serikali ni kuleta Muswada wa Bima ya Afya ndani ya Bunge hili na huu mchakato umefikia hatua nzuri tunategemea kwamba ikifika Bunge la Novemba, Muswada huu tutauleta ndani ya Bunge lako Tukufu. Lakini katika kipindi cha mpito tumeona umuhimu na haja na uhitaji wa wananchi, tunataka sasa tufanye uzinduzi wa vifurushi ambavyo vitakuwa ni rafiki zaidi wananchi wa kawaida wanaweza wakavimudu kwa lengo kuhakikisha kwamba hii changamoto ambayo tunaipata wakati Serikali tumeboresha sana Sekta ya Afya, lakini uwezo wa wananchi kugharamia huduma za afya umekuwa ni changamoto ili wananchi sasa na kwa sababu wananchi tayari wameshahamasika tunaamini tutakapokuja na hivi vifurushi mbadala ambavyo tunategemea tutavizindua hivi karibuni itaongeza wigo mkubwa sana wananchi kuweza kujiunga nje ya wale ambao wamekuwa ni Watumishi wa Umma.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini niiombe Serikali. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa kabisa vitendo hivi vya udhalilishaji hasa vya kijinsia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia nasi kama Serikali tumeliona hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 tuliandaa mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambao unatambulika kama MTAKUWA na katika mpango mkakati huu Serikali imetoa maelekezo ya kuanzishwa Kamati za Ulinzi wanawake na watoto katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya Kitongoji na Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeendelea kutoa elimu katika jamii kuhusiana na masuala haya lakini tumeendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Idara ya Mahakama na Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba tumeanzisha madawati ya jinsia takribani 417 katika Jeshi la Polisi, vilevile tumeendelea kufanya kazi kwa karibu sana na Idara ya Mahakama pamoja na wenzetu wa Katiba na Sheria kuhakikisha kwamba mashauri haya yanapotokea basi hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wale watuhumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa jamii, nitumie fursa hii kusema matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanafanywa na watu ambao wako karibu na ndani ya familia, niiombe sana familia wasimalizane ndani ya familia na badala yake watoe ushirikiano kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. (Makofi)
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea fedha kutoka kwa wafadhili katika kuhudumia waathirika wa gonjwa la UKIMWI fedha ambazo upatikanaji wake umekuwa na changamoto kubwa. Nilitaka kujua tu, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba sasa inatenga fedha za ndani katika kuhudumia kundi hili la wagonjwa wa UKIMWI? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imekuwa inashirikiana na wadau katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI na wadau wakubwa ni pamoja na Global Fund na PEPFA.
Mheshimiwa Spika, katika kuliona hilo na kwa lengo la kuhakikisha kwamba hizi huduma za matibabu au huduma afua za VVU kwa waathirika zinakuwa endelevu, Serikali imeanzisha Mfuko wa Masuala ya UKIMWI ambao unaitwa AIDS Trust Fund ambapo Serikali inaweka fedha pale, inachangia fedha zake kwa lengo la kuhakikisha kwamba baadhi ya afua zinakuwa funded kwa kupitia mfuko huo.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika ahsante sana kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa takwimu zinaonyesha wazi kwamba matatizo ya magonjwa ya akili yanaongezeka yanayotokana na msongo wa mawazo pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya lakini hospitali maalum ya magonjwa hayo ni Milembe pakee. Je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga hospitali kubwa ya magonjwa ya akili katika eneo hilo la Chamazi ili kusaidia wananchi wa Kanda ya Pwani waweze kupata matibabu lakini pia waweze kupata eneo ambalo wataendelea kufanya kazi mbalimbali pale za mifugo ili kujikimu kuliko vile walivyo watoto wetu walioharibiwa na madawa ya kulevya, kwamba hawana ajira na wanahangaika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Halmashauri ya Temeke imekuwa na tatizo kubwa la ardhi, na kwa kuwa idadi ya wagonjwa inaongezeka siku hadi siku katika Hospitali ya Zakiemu. Je, Serikali haioni haja sasa ya kushirikiana na Halmashauri ya Temeke ili kujenga hospitali pale katika eneo la Chamanzi Muhimbili ili iweze kuwasaidia wananchi wanaotoka Mbande, Chamazi, Mbagala, Maji Matitu pia na hata wale wa Wilaya ya Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YAJAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kisangi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli sasa hivi dunia imeweka msisitizo katika afya ya akili, na kwa sababu na sisi kama Serikali na dunia kwa ujumla inaona kwamba tatizo la afya ya akili linazidi kuongezeka kwa kasi sana na linahitaji msukumo na mtazamo wa aina ya pekee kabisa katika kutatua changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna hospitali moja kubwa ya Mirembe; na sisi kama Serikali mtazamo wetu wa mbele ni kuhakikisha kwamba, especially katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili badala ya kuwa na vitengo vidogo vidogo lengo letu sisi ni kwamba kila kitengo kuwa ni taasisi. Tumeanza na taasisi ya magonjwa ya moyo tumekwenda taasisi ya masuala ya mifupa; na lengo letu ni kwamba hata baadaye tuwe na taasisi ya magonjwa ya afya ya akili.
Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake la pili; ameongelea kwa nini Serikali isione umuhimu wa kujenga hospitali ya ziada katika eneo hili la Chamanzi. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zote ni taasisi za umma. Sisi kama Wizara hatujapokea ombi lolote kutoka halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Pindi tutakapopokea ombi hilo tutalijadili na kulifanyia uamuzi kwa sababu tunaamini eneo lote hili ni kwa ajili ya utoaji huduma ya afya, na kwa sababu tuna eneo kubwa hatuoni sababu kwa nini tusiongeze wigo wa utoaji huduma, especially katika eneo la Temeke ambapo kuna changamoto ya ardhi.
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Hospitali yetu ya Mawenzi nayo inayo kitengo cha afya ya wagonjwa wa akili na imejenga eneo katika eneo la Longuo; na kitengo hicho kinahudumia Kanda nzima ya Kaskazini. Hata hivyo katika kitengo kile hakuna uzio pia wahudumu hawako wa kutosha. Sasa nataka nijue, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanakarabati eneo lile na kuweka uzio na kuwepo na wahudumu wa kutosha kwa sababu inahudumia Kanda nzima ya Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Owenya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema katika jibu langu la msingi eneo hili la afya ya akili sasa hivi limeanza kuwekewa msukumo kidunia na sisi kama nchi tumeanza kuliwekea nalo msisitizo. Tunatambua kwamba vitengo vyetu vingi vya afya ya akili vimekuwa na uchakavu na vinahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa watumishi. Watumishi katika kada hii ni wachache sana, na ndiyo maana sasa hivi Serikali imewekeza katika mafunzo ya wataalamu wa afya wa akili ili tuweze kwenda sambamba na changamoto na wimbi kubwa ambalo tunaliona katika jamii kwa wahanga wa afya ya akili.
Mheshimiwa Spika, kadri ya uwezo wa kifedha unapopatikana na sisi kama wizara tutaendelea kufanya ukarabati wa kiuo hichi pamoja na vituo vingine vya afya ya akili nchini.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili ya nyongeza. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake; lakini sambamba na hilo; kwa kuwa vituo vilivyopo katika haya maeneo havitoshelezi, hii imebainishakabisa katika majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, nilipenda kujua, je, serikali ina Mkakati wowote wa kujenga vituo vya nyongeza katika bajeti ya mwaka ujao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa taarifa za ukatili hasa ulawiti kwa watoto wa kiume zimekuwa zikiongezeka, na inawezekana ni kutokana na utandawazi; je, Serikali ina mkakati wowote wa kuzuia hizi picha mbaya au picha za ngono ili kuweza kunusuru kizazi hiki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza sana amekuwa ni mdau mkubwa sana wa kufuatilia masuala mbalimbali yanayohusu afya ya mama na mtoto lakini vilevile masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, nikupongeze sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kusudio la Serikali kuongeza vituo hivi; kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba tumeanza katika mikoa hii 11 na kusudio letu sisi kama Serikali nikufika katika mikoa yote. Ni kweli na ni lazima tukiri kwamba matokeo ya ukatili wa kijinsia yanazidi kuongeza ndani ya nchi yetu. Mwaka 2017 tulikuwa na matukio ya ukatili wa kijinsia takribani 41,000, mwaka 2018 yakawa zaidi ya 45,000 na sasa hivi tunafanya compilation ya matukio ya mwaka 2019. Lakini tunaamini kwamba matukio haya bado yanazidi kuongezeka na ndio maana sisi kama Serikali tumekuja na huu Mpango wa MTAKUWA ili kujaribu kuhakikisha tunadhibiti kabisa matukio haya, ikiwa pia na kwa kwenda sambamba na kuhakikisha kwamba wale wahanga wa ukatili wa kijinsia wanapata huduma stahiki. Kwa hiyo kusudio letu la Serikali ni kwenda katika ngazi zote, katika ngazi ya mkoa na baada ya hapo tutaanza kushuka katika ngazi ya wilaya.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili aliongea matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto hususan watoto wa kiume, na mligusia hili kutokana na masuala ya kiutandawazi. Ni kweli matukio haya tunayapata na sisi kama Serikali, na mara nyingi matukio haya yanafanywa na watu wa karibu ndani ya familia. Katika maelezo ya Mheshimiwa Waziri jana aliliongelea hapa ndani ya Bunge; kusema kwamba tunahitaji kwa kweli kama wazazi kuhakikisha tunakaa karibu zaidi na watoto wetu, tunafatilia maendeleo ya watoto wetu, tunakaa na kuongea na watoto wetu majumbani.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tuna mkakati mwingine wa ziada wa kuhakikisha kwamba katika shule tunaweka madawati ya masuala ya ukatili wa kijinsia; kwa sababu ukatili wa kijinsia mara nyingi unafanywa na watu wa karibu na nyumbani na saa nyingine mtoto anaweza asiseme kwa kuhofia kupata adhabu kwa mtu ambaye amemfanyia ule ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasahivi tunafanya maongezi na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba kuna walimu katika kila shule ambao wamepata mafunzo haya ili watoto waweze kuyasema haya mashuleni na hawa walimu kuweza kusaidia kuchukua hatua. Vilevile tunashirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni na Sanaa kuhakikisha kwamba kunawekwa misingi mzuri ya udhibiti wa mtangazo katika redio, television na vyombo vingine vya habari kwa kuhakikisha kwamba zile content ambazo zipo zinaendana na maadili ya kwetu sisi kama Watanzania.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Kwa kuwa ukatili wa kijinsia huathiri watu mbalimbali kisaikolojia na huathiri; afya ya akili na kwa kuwa ukishaathirika kisaikolojia afya ya akili inaleta kutokuzalisha vizuri kama ni shughuli za kutuletea uchumi au watoto ku-perform darasani kwa hiyo unakuwa na taifa ambalo halipo sawasawa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wale wanaoathirika kisaikolojia au afya ya akili wanakosa kupata huduma stahiki kwa sababu kuna changamoto ya gharama tiba na pia watalamu ambao wanafanya hizi shughuli za counseling wapo wachache nchini; sasa Serikali haioni ni muda muafaka wa kufanya tathmini wa hali hii na jinsi ya kuweza kuwapatia huduma wananchi wake stahiki inavyotakiwa kwa gharama ambayo wanaweza wakaimudu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sware Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli hathari moja wapo ya ukatili wa kijinsia ni kuweka makovu ya kisaikolojia kwa watu wengi na napelekea baadhi ya watu hata kushindwa kufanya vizuri katika masomo, kushindwa kujenga mahusiano na watu wengine, kuwa na tabia ya kuwa na hasira na vitu vingi ambavyo vinamwathiri mtu kisaikolojia. Ni kweli hili tatizo linazidi kukuwa na sisi kama Serikali kupitia mpango wetu wa MTAKUWA tumeainisha baadhi ya mikakati ambayo tunaiweka katika kudhibiti hali hiyo. Tunatambua kwamba ni kweli tuna changamoto hii ya wigo wa ushauri nasaha kwa hawa wahanga na gharama za matibabu kwa hawa wahanga wa ukatili wa kijinsia. Tutafanya hiyo tathmini na kuangalia jinsi gani sasa ya kuweza kutoa huduma nzuri kwa hawa wahanga wa ukatili wa kijinsia.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mtakubaliana nami kwamba kuna mstari mdogo sana kati ya uzima na afya ya akili. Katika nchi ambazo tafiti zimefanyika kwa mfano Marekani inaonyesha katika kila watu wanne mmoja ana tatizo la afya ya akili, Uingereza katika kila watu watano mmoja ana tatizo la afya ya akili, Australia katika watu 6 mmoja ana tatizo la afya ya akili.
Mheshimiwa Spika, nadhani wewe mwenyewe unaweza kuwa shahidi hata humu ndani wakati mwingine unajiuliza tuko salama kiasi gani. Nataka kufahamu je, Serikali yetu imefanya tafiti ya kujua ni idadi gani ya watu ambao wameathirika na ugonjwa wa afya ya akili Tanzania? Na kama tayari tafiti zimefanyika matokeo yake yakoje?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kemilembe Lwota Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mwanza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli changamoto za afya ya akili zinazidi kuongezeka na ndio maana Shirika la Afya Duniani sasa hivi linaweka msukumo mkubwa katika kuliangalia suala la afya ya akili. Takwimu zake ziwezi nikazipinga, ni kweli takribani karibia asilimia moja ya katika jamii yetu ya Tanzania tunaamini kwamba wana tatizo l a afya ya akili.
Kwa hiyo hata hili alilolisema, kwamba hata humu ndani inawezekana na sisi ile asilimia moja tuna changamoto kama hizo. Sisi kama Serikali bado hatujafanya utafiti wa kina wa kuangalia ni uzito wa jambo hili likoje aina gani ya magonjwa ya akili ambayo tunayo ndani ya nchi yetu. Tunalipokea hili Mheshimiwa Mbunge na tutaenda kulifanyia kazi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maelezo yake mazuri ambayo yatasaidia wazazi waliokuwa hai na wanaoweza kuwatumia watoto isivyo kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kuna baadhi ya barabara wanapotembea, pembezoni mwa ile barabara utakuta mzazi na mtoto wake wanaomba ili waweze kujikimu kimaisha: Je, Wizara hii suala hili wanaliona? Kama wanaliona, wanamnusuru vipi yule mtoto ili aweze kuendelea na masomo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna baadhi ya watoto ni wadogo, wakati wa masomo utawakuta mitaani wanatembea na biashara, wengine za maandazi na matunda na wakati wazazi wao wanajulikana na sehemu wanazokaa: Je, Wizara hii itamnusuru vipi yule mtoto ili aweze kwenda shuleni kwa wakati ule wa masomo badala ya kupita mitaani na biashara akitembeza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze kwa kutoa maelezo kuhusu haki za mtoto ni zipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania tuliridhia Mikataba ya Kimataifa na tukatunga Sheria Na. 21 ya mwaka 2009 ambayo inatoa haki za msingi kwa mtoto. Naomba kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge, ni vizuri Wabunge na hata vijana na watoto ambao wako kwenye gallery waweze kuzitambua.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto ana haki ya kuishi, mtoto ana haki ya kuendelezwa, mtoto ana haki ya kushirikishwa na mtoto ana haki ya kutofanyishwa kazi nzito. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sheria hii, Kifungu cha 14 kimeeleza vizuri tu kwamba pale haki hizi zinapokiukwa, Serikali inaweza ikamshtaki mzazi na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na faini isiyozidi shilingi milioni tano na kifungo kisichozidi miezi sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini ambacho sisi kama Serikali tumefanya? Kwanza kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi, tumeanza kufanya tathmini ya kina katika maeneo ya majiji kuweza kuwabaini watoto wale ambao wako mitaani. Ukiangalia tumefanya katika njia mbili; moja, tumefanya mchana hili na kujua idadi yao, lakini vilevile tumefanya hili zoezi usiku. Tulichokibaini ni kwamba, watoto wengi wanakuwa mtaani mchana, lakini usiku wengine wanarudi majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Watoto hawa wanafanyishwa shughuli za ombaomba na nyingine hizi za kufanya biashara. Kwa hiyo, tumekuja na Kampeni inayokwenda kwa jina la “Twende Sawa” ambapo moja ya jambo tutakaloenda kulifanya katika kampeni hii, ni kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Vilevile tumejumuisha na hili suala la watoto ambao wanatumikishwa na kufanyishwa biashara mitaani, kwa lengo la kuanza kutoa elimu katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya Halmashauri kuweza kufanya zoezi hili la kufanya tathmini katika maeneo yao na kuanza kwenda kuchukua hatua kwa wale wazazi ambao wanakaidi na ambao hawasimamii majukumu yao ya msingi na kuwatumikisha watoto kama ombaomba na kufanya biashara mtaani.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mpaka kufikia Desemba, 2019 Serikali mlikuwa mmesajili makao ya kulelea watoto kutoka 13 mpaka 213. Pamoja na mikakati mizuri ambayo meiwekwa, Serikali yetu mpaka sasa hivi ina Kituo kimoja tu cha makao maalum ya watoto na Mheshimiwa Naibu Waziri ameonesha kabisa changamoto ya watoto wa mitaani bado ni kubwa:-
Je, Serikali haioni umuhimu sasa kuanzisha na wao badala ya kuachia Taasisi za Kidini na watu binafsi nayo ikaanzisha vituo maalum kwa ajili ya kulelea watoto hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rose Tweve kwa swali lake zuri. Sisi kama Serikali msimamo wetu ni kwamba watoto walelewe na wazazi, hilo ndiyo jukumu la kwanza. Endapo wazazi wameshindwa kutekeleza yale majukumu, basi jamii inayozunguka wale watoto iweze kuwalea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali kuwachukua watoto na kuanza kuwalea katika makazi ya watoto ni hatua ya mwisho sana. Ni kweli tuna hayo majengo ya kule Kurasini ambacho ni Kituo cha Kulelea Watoto lakini nikupe tu taarifa kwamba na hapa Dodoma kama Makao Makuu ya nchi tunakusudia kuanza ujenzi wa Kituo kingine cha watoto mwaka huu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza; kwa kuwa tatizo hili ni kubwa kwa nchi nzima na kwa kuwa baadhi ya familia ambazo zina watoto hawa ni watu wenye uwezo, wametelekeza kutokana na matatizo mbalimbali ya kifamilia:-
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutafuta namna ya kutafuta msimamizi halisi wa sheria hii kwa ngazi ya Wilaya na Ofisi za Ustawi wa Jamii ili kuweza kuleta tija kwa kundi hili muhimu sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi Serikali ya Tanzania imeridhia Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Mtoto na ndiyo maana tuna Sera ya Mtoto ya Mwaka 2008 na vilevile tuna Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009. Sheria hii imeainisha kwa kina sana haki hizi za mtoto. Niseme tu kwamba sheria ipo na imeainisha adhabu ambazo zinaweza zikatolewa endapo haki za mtoto zitakiukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo inatukabili ni idadi ndogo ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo mbalimbali katika Halmashauri zetu. Nasi kama Serikali tumeliona hilo, tunaendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi Jamii wetu katika Halmashauri ambapo wapo lakini vilevile dhamira ya Serikali ni kuongeza idadi ya Maafisa Ustawi wa Jamii ili waweze kusimamia jukumu hili la kuweza kuhakikisha kwamba haki za watoto zinalindwa.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha karibu shilingi bilioni moja kwa ajili ya Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi inaenda kwa kusuasua sana na Mheshimiwa Waziri alituahidi kutupa fedha karibu shilingi bilioni nne ili ziweze kujenga hospitali hiyo: Je, ni lini Serikali italeta hizo fedha?
Mkoa wa Katavi una Chuo cha Uuguzi ambacho ni cha muda mrefu sana yapata miaka 10 hakijaendelezwa: Je, ni lini Serikali itamalizia hiki Chuo cha Uunguzi ili watu weweze kupata huduma za kimsingi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Serikali imetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.4, tumeshatanguliza shilingi bilioni 1.5 na fedha hizi zipo, kadri Mkandarasi anapokuwa anaendelea na kazi na ana-raise certificate, sisi Serikali tutaendelea kufanya malipo.
Mheshimiwa Spika, lengo na kusudio la Serikali ni kuhakikisha hospitali hii inakamilika na kwamba baada ya hapo, ile Hospitali ya Mpanda ambayo ilianza kama Kituo cha Afya na sasa hivi imekuwa ndiyo Hospitali ya Mkoa, tuweze kuirejesha katika Halmashauri na kuweza kuhudumu kama Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameulizia kuhusiana na Chuo cha Afya cha Uuguzi kilichopo pale. Ni kweli, nami nimewahi kufika pale Mpanda tumekiona. Wizara ilituma timu kwenda kufanya mapitio na kuangalia hali ya majengo na uhitaji. Sasa hivi tupo katika mkakati wa kuangalia matumizi bora ya kile chuo. Pindi taratibu zitakapokamilika tutawapa taarifa Mkoa wa Mpanda, jinsi gani ya kuweza kukitumia kile Chuo kwa malengo ambayo tulikuwa tumekusidia.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake kuonyesha kwamba Serikali inatambua mchango wa wazazi ambao wamehangaika kutulea hadi kufikia hapa tulipo. Tukumbuke kwamba hata vitabu vitakatifu vya Mungu, kwa mfano amri kumi za Mungu ni amri ya nne pekee ambayo inatoa na ahadi kwamba ukiheshimu wazazi utapata baraka na utaishi miaka mingi duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutatunza wazazi, wenzetu ambao wazazi wapo hai ni vizuri, it is a blessing. Tuendelee kuangalia wazazi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina maswali mawili ya nyongeza kwamba Je, Serikali ipo tayari kutunga sheria itakayowabana watoto hawa wanaotelekeza, ili waweze kuwatunza wazazi wao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, wakati tunasubiri hiyo sheria kutungwa, Serikali ipo tayari kuweka Dawati la Wazee ili waweze kusikilizwa katika malalamiko yao, hasa kwa wale ambao wanatelekezwa na watoto wao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Jasmine Tisekwa Bunga. Swali lake la kwanza ameuliza kwamba, je, Serikali iko tayari kutunga sheria ya kubana watoto ambao wanawatelekeza wazee? Niseme tu kwamba kwa sasa hivi hatuna mpango huo kama Serikali. Tunajikita na kujielekeza zaidi katika kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha kwamba wanatambua wajibu wao na kutimiza majukumu yao ya kutunza na kulea wazee.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kwamba, je, tuko tayari kuanzisha Dawati la Wazee? Niseme kwamba tunayo mifumo kupitia Maafisa Ustawi wetu wa Jamii ambao majukumu yao ni pamoja na kuhakikisha kwamba huduma kwa wazee zipo. Kwa hiyo, wale wazee ambao wanaona kwamba matunzo au zile haki za msingi hawazipati, ni vizuri wakafika kwa Maafisa Ustawi wa Jamiii ili kupata msaada wa kuwaunganisha na watoto wao.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tuna nyumba za kuwatunza wazee 17 na tuna wazee takribani kama
500. Nasi Serikali tunachukua tu wale wazee ambao imedhibitika kwamba hawana watoto, hawana ndugu, jamii ile inayowazunguka haiwezi kuwatunza, ndipo pale Serikali inawachukua na kuwatunza.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi. Ilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwamba kwa kuwa Sera ya Wazee ipo toka mwaka 2003, lakini sheria hamna ndiyo maana wazee wanaendelea kunyanyasika. Hata hivyo, kuna Sheria ya Watoto ambapo mzazi asipomlea mtoto au asipompa matunzo, anashtakiwa.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini basi kusiwe na sheria ambayo italazimisha mtoto au kijana, mtu mzima aweze kumlea mzazi wake kwa sababu tunajua kwamba wazee hawa kwa kweli wamefanya kazi kubwa, wamewasomesha watoto, lakini watoto wamewatelekeza. Ni kwa nini kama kuna Sheria ya Watoto, kusiwe na Sheria ya Wazee ambayo itarahisisha sana maisha ya wazee hapa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, changamoto ya wazee tutazidi kuiona ikiongezeka na hii ni kwa sababu ya maendeleo makubwa ambayo tumeyapiga katika huduma zetu za jamii. Sasa hivi wastani wa Mtanzania kuishi miaka 64. Kwa hiyo, tunatengemea tutakuwa na idadi kubwa sana ya watu ambao wanaitwa wazee, kwa sababu vifo vimepungua na hali ya afya nayo imeboreka sana.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera ya Afya ni ya mwaka 2003 na sasa hivi tumeiona kwamba imepitwa na wakati. Tupo katika marejeo ya kuipitia hii Sera mpya ya Afya. Tukapoikamilisha, tuangalia sasa uwezekano kwa kuja na sheria mpya ambayo sasa itakuwa inaweka haki za wazee katika msingi mizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, hili ambalo analisema Mheshimiwa Susan Lyimo ni moja ya jambo ambalo tunaweza tukalizingatia.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na mwongozo huo ambao Serikali imeutaja lakini ni ukweli kwamba bado tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya afya na hivyo vifo vinaendelea kuongezeka. Je, Serikali haioni umuhimu bado wa kuwatumia hawa wakunga kwa kuwapa mafunzo ili waweze kusaidia uzalishaji ili tuendelee kupunguza vifo hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sasa upungufu katika sekta ya afya kwa maana ya watumishi wataalam ni asilimia 50, kiwango ambacho ni kikubwa sana na watu wetu wanaendelea kupata taabu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tunapunguza upungufu huu kwa kuongeza ajira katika sekta ya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, kutokana na kuwa na vifo vingi vya akina mama na watoto sisi kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapunguza sana vifo hivi kwa kuwekeza katika miundombinu ambapo zaidi ya Hospitali za Wilaya 352 zimeboreshwa lakini kuhakikisha akina mama wanakwenda kliniki. Sasa hivi tumepiga hatua kubwa sana idadi ya akina mama ambao wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka asilimia 51 mpaka asilimia zaidi ya 63.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna-encourage kabisa akina mama wajifungulie katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya. Hawa wakunga wa jadi tunaendelea kushirikiana nao kwa sababu nao wana mchango kwenye jamii lakini katika lengo la kuhamasisha akina mama kwenda kliniki na kujifungulia katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ili kupata huduma sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili lilikuwa kuhusiana na ajira, ni kweli tuna changamoto ya rasilimali watu lakini tumeendelea kuajiri watumishi wa afya kadri vibali vya Serikali vinavyopatikana. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali duniani zinaonesha kwamba mwanaume mmoja ana uwezo wa kuwapa ujauzito wanawake tisa (9) kwa siku moja wakati mwanamke mmoja ana uwezo wa kushika mimba moja (1) kwa miezi tisa (9). Je, Serikali haioni sasa kuendelea na programu za uzazi wa mpango kwa wanawake ni uharibifu wa rasilimali na badala yake programu za uzazi wa mpango zielekezwe sasa kwa akina baba? Ahsante. (Makofi/ Vigelegele)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Khadija Nassir, kama ifatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhana potofu kudhani kwamba suala la uzazi wa mpango ni la wanawake peke yake. Suala la uzazi wa mpango linawahusu wanaume vilevile. Sisi kama Serikali tuna-encourage akina baba na akina mama wote kushiriki katika suala zima la mpango wa uzazi salama.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kuweza kuendelea kuwahudumia wananchi wake wawapo kazini na wale ambao wamestaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kuna mabadiliko ya utaratibu wa uchangiaji kutoka miaka 10 hadi
15 lakini bado baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiendelea kuchangia miaka 20 na kuendelea lakini wazazi wao hawajatambuliwa kuwa wafaidika wa mfuko huo na ukiangalia wamechangia fedha nyingi na muda wanaopata matatizo ni mdogo. Vilevile kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawana watoto, mume wala mke. Je, Serikali inaweka utaratibu gani wa kisheria kuweza kuwatambua Waheshimiwa Wabunge katika kufaidika na Mfuko huo watakapokuwa wamestaafu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Maida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, amegusia kuhusiana na Wabunge ambao wamekua wanachangia Mfuko huu na kwa nini Serikali isifanye mabadiliko ya sheria. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge ndiyo tunatunga sheria na hii sheria ambayo inahusu mafao yetu ni sisi wenyewe tunahusika. Pili, ni sisi wenyewe Wabunge ambao tunatengeneza Kanuni zetu za Uendeshaji wa Bunge letu. Kwa hiyo, hili suala wala siyo suala la Serikali ni la Bunge lenyewe kukaa na kuamua kupitia Kanuni zao na Tume ya Utumishi wa Bunge kuweka utaratibu wa mafao na haki stahiki katika masuala ya bima ya afya kwa Waheshimiwa Wabunge.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuja na majibu mazuri sana yenye faraja kwa wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa wakilazwa katika Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala sasa mashine za kufulia zinapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nampongeza sana kwa majibu hayo mazuri, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mashine za kufulia katika hospitali hizo zinakosa pia mashine nyinginezo za vipimo zikiwemo mashine za MRI, mashine za kupima ubongo na mashine nyingine hali ambayo inawalazimu wagonjwa kufuata huduma hiyo ya vipimo katika Hospitali ya Muhimbili. Wanapofika katika Hospitali ya Muhimbili, vipimo hivyo hupewa kwa gharama mara mbili ya ile bei ya kawaida ya Hospitali ya wagonjwa waliopo Muhimbili. Je, Serikali kwa nini inatoa gharama tofauti wakati hospitali hizi zote ni za Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwanza naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza Ilani yake ya Chama kwa kujenga Hospitali za Wilaya 67 na zimepewa fedha karibia bilioni 1.5 na milioni 500 wameongezewa ikiwemo Kigamboni katika Jiji la Dar es salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuhakikisha hizo hospitali 67 ambazo zitajengwa kuwa na mashine na vipimo vyote vinavyostahili katika kila hospitali.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es salaam amekuwa ni Mbunge wa mfano katika Wabunge wa Viti Maalum katika ufuatiliaji wa mambo mbalimbali yanayotokea katika Mkoa wa Dar es salaam na sisi kama mmoja wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam nampongeza sana Mheshimiwa Mariam Kisangi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba sasa hivi Serikali inafanya maboresho makubwa katika Sekta ya Afya na tumeona kwamba kuna uhitaji wa kuboresha na kupanua wigo wa utoaji wa huduma za afya hususan vile vipimo mahsusi kama uwepo wa MRI, CT Scan na vipimo vingine mahsusi ambavyo hapo awali vilikuwa vinapatikana katika Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivyo, kupitia mpango wetu wa sasa hivi wa kuboresha huduma na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa Serikali imedhamiria kupanua wigo kuhakikisha kwamba vipimo kama CT Scan na MRI zitaanza kupatikana katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ameuliza kwa nini baadhi ya vipimo vinachajiwa mara mbili zaidi ya zile gharama halisi ambazo zipo pale. katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tumeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba rufaa inazingatiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni Hospitali ya Taifa, maana yake ni kwamba unapokwenda pale unahakikisha kwamba umetoka katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya, Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, umekwenda Hospitali ya Kanda Mloganzila wameshindwa pale sasa unakwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na baadhi ya watu ambao katika magonjwa ya kawaida ambayo yangeweza kutibiwa katika maeneo mengine wanakwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Ili sasa kuweka mfumo wa rufaa ukae vizuri, mtu ambaye amekwenda kwa mfumo wa rufaa gharama zake zinakuwa chini, yule ambaye amekwenda kwa mfumo nje ya rufaa, yule anahesabika kwamba ni mgonjwa amekwenda kama mgonjwa binafsi na gharama zake mara nyingi zinakuwa zipo juu. Lengo ni kuhakikisha kwamba mfumo wa rufaa umezingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza ni nini mkakati wa Serikali kuelekea katika ujenzi huu ambao tumejenga hospitali za Rufaa za Wilaya 67 tuna mpango gani wa kuhakikisha kwamba inakuwa na vifaa vya kutosha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kusudio la Serikali ni kwamba pale miundombinu ya hospitali hizi za Wilaya zitakapokuwa zinakamilika na sisi kama Wizara pamoja na kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI tumeshaanza maandalizi ya kuhakikisha kwamba hospitali hizi zitakapokamilika vifaa vitapatikana ikiwa ni pamoja na rasilimali watu. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Changamoto iliyopo Temeke na Mwananyamala inafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Ngara, Hospitali ya Nyamiaga haina mashine ya kufulia nguo. Je, ni lini Serikali itatuletea mashine ya kufulia nguo ili kutatua changamoto hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Oliver Semguruka, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa ambayo naye anaifanya katika kufuatilia masuala mbalimbali ya afya katika Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo Serikali tunayafanya lakini vilevile kuna mambo ambayo hivi vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya nayo inapaswa kuvifanya. Wanafanya makusanyo ya fedha na sisi Serikali tunawapelekea bajeti, ni wajibu wa Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali ile na Mganga Mkuu wa Wilaya kuweka ununuzi wa mashine za kufulia ndani ya mipango yao. Gharama za mashine za kufulia sio gharama kubwa, ni vitu ambavyo Hospitali hii ya Nyamiaga wanaweza wakafanya kwa kupitia bajeti zake za ndani. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama ilivyo katika mikoa mingine, Wilaya ya Rungwe tunayo shida kubwa sana ya mashine za kuchomea taka na kuzivunjavunja ikiwemo pamoja na ukosefu wa vifaatiba ambavyo vinatakiwa kupatikana katika hospitali ile. Je, Serikali inajipangaje kutusaidia wananchi wa Wilaya ya Rungwe tuweze kupata mashine hiyo ikiwepo na mashine za X-ray za kusaidia wanawake katika Wilaya ya Rungwe, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mbeya na nimpongeze kwa swali lake hilo ambalo ameuliza kuhusiana na masuala ya kuchomea taka na upatikanaji wa huduma za X-ray. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za uchomaji taka katika hospitali mbalimbali na sisi kama Wizara tumetoa mwongozo huo katika vituo vyetu vyote vya kutolea huduma za afya na tunaendelea kufanya tafiti za teknolojia rahisi ambazo zinaweza zikatumika katika kutengeneza vichomea taka kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na niiombe tu Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI na hata kupitia kwetu Wizara ya Afya tupo tayari kushirikiana nao kuwapa ushauri na huo utaalam ili sasa waweze kujenga hicho kichomea taka kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa huduma ya X-ray, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tumeendelea kufanya tathmini ya uhitaji wa huduma za X-ray katika hospitali mbalimbali za Wilaya ndani ya nchi na tumetengeneza orodha ya Hospitali zote za Wilaya ambazo zinahitaji huduma hii na tumeshaanza mkakati wa uagizaji wa mashine mpya za kisasa za digital X-ray. Nimhakikishie kwamba pindi X-ray hizo zitakapofika basi na Wilaya ya Rungwe nayo tutaifikiria. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na vilevile naipongeza Serikali kwa kweli kwa kuboresha huduma za afya pamoja na kwamba kazi ni kubwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nauliza kwamba tulikuwa na ICHF au CHF katika Wilaya zingine kama ilivyo Hanang’ na ilikuwa inafaidisha sana wananchi sasa nasikia kuna utaratibu wa kubadilisha utaratibu na wananchi wanateseka sasa hivi kama hawawezi kutumia CHF au ICHF, Serikali inasemaje kwa hili? Ni kweli kuna utaratibu? Na kama kuna utaratibu sasa hivi katika transition au katika muda wa mpito wananchi wanafanya nini na wananchi wa Hanang’ kwa kweli wamelalamikia hilo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali tulikuwa na utaratibu unaitwa CHF na katika utaratibu ule wa awali, mtu alikuwa anakata kadi anapata huduma za afya katika eneo tu ambalo ametoka, kama ni zahanati basi anapata pale kwenye ile zahanati peke yake sasa katika kile kituo ambacho yeye alikuwa amekatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumekuja na kitu kinaitwa CHF iliyoboreshwa, katika CHF boreshwa inampatia wigo wa huduma mpaka katika ngazi ya Mkoa, yanaanzia katika ngazi ya zahanati, anakwenda katika kituo cha afya, anakwenda Hospitali ya Wilaya mpaka katika ngazi ya Mkoa, haitoki nje ya pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na huu utaratibu wa CHF iliyoboreshwa unatupa gharama ya shilingi 30,000 kwa maeneo ya Vijijini na gharama ya 150,000 katika maeneo ya mjini mtu na mwenza wake na wategemezi 4 wanapata huduma zote za afya kwa gharama hiyo ambayo nilikuwa nimeisema. Kwa hiyo, utaratibu huu ndio ambao unakuwa unaendelea na mimi nipo tayari kukaa na wewe Mheshimiwa Mary Nagu kuweza kubaini changamoto zilizopo katika Wilaya ya Hanang ili tuweze kuzitatua kwa haraka. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa ugonjwa wa sickle cell unatokana na mtoto kurithi cells kutoka kwa baba na mama yake, wazazi wake wote wawili wanakuwa na cells ambazo ziko half. Sasa mtoto anapozaliwa anakuwa amerithi zile cells ndiyo maana anazaliwa na huo ugonjwa.
Je, ili kuzuia hili tatizo Serikali ina mkakati gani wa kuwapima watoto wanapozaliwa kwenye vituo vya afya na katika hospitalini mara tu wanapozaliwa iwapime ili wagundulike kwamba wana ugonjwa wa sickle cell ili kuepusha vifo vya watoto kwa sababu mara nyingi wanapogundulika wanakuwa wameshakuwa watu wazima na wengi huwa wanapoteza maisha, hasa vijijini?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa commitment kwamba Serikali inaandaa mwongozo wa kutoa msamaha wa matibabu bure kwa familia ambazo hazijiwezi kupitia kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, sasa basi, yako magonjwa kama UKIMWI na TB watu hawahakikiwi, wanapata matibabu bure.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa bure matibabu ya sickle cell bila kuhakikiwa kama ilivyo magonjwa ya UKIMWI na TB?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Restituta Mbogo kwa kuwa ni mfuatiliaji wa karibu wa magonjwa haya yasiyoambukiza na hususani ugonjwa huu wa seli mundu.
Mheshimiwa Spika, hoja yake inahusiana na suala la upimaji wa watoto wanapozaliwa. Ni kweli ugonjwa huu huja kwa njia ya pale wazazi wanapokuwa na vinasaba ambavyo vinahamishwa katika kipindi cha ujauzito kuja kwa watoto pale wazazi wanapokuwa na vinasaba hivi vya ugonjwa huu wa seli mundu, genetic transfer. Kwa hiyo, katika nchi ambazo zimeendelea, watoto ambao wana Ugonjwa huu wa seli mundu wanaweza wakabainika kwa njia mbili; njia ya kwanza ni kupima ujauzito wakati mtoto akiwa bado tumboni kwa kupitia katika maji yaliyopo katika mfuko wa uzazi, unaweza ukabaini kwamba mtoto anaweza akazaliwa na ugonjwa wa seli mundu. Lakini njia ya pili, baada ya mtoto kuzaliwa akipimwa anaweza akabainika kama ana ugonjwa huu wa seli mundu.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi; Tanzania na nchi nyingi za Afrika ugonjwa huu ni mkubwa na wako wagonjwa wengi na sisi kama Serikali, pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika pale Hospitali ya Muhimbili kupitia programu ile ambayo inaongozwa na madaktari mahiri ya Profesa Julie Makani, wamekuwa wanatoa msaada mkubwa sana kwa wagonjwa hawa wa seli mundu. Sasa sisi kama Serikali tumeamua sasa tunataka tuje na mpango wa kitaifa ambao utasimamia matibabu haya ya seli mundu na ndiyo maana tumesema kwamba ifikapo Novemba programu hii tutakuwa tumeianzisha rasmi na mkakati wa upimaji unaweza ukawa ni moja ya mkakati huo ambao tutaweza kuufanya kuhakikisha kwamba tunaubaini ugonjwa huu katika hatua za awali na kuweza kuwatibu hawa wagonjwa vizuri zaidi na kwa ufasaha zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusiana na suala la uhakiki wa wagonjwa. Ili uweze kumbaini mgonjwa wa seli mundu ni lazima kwanza apimwe na kuthibitishwa. Katika utaratibu ambao tunao sasa hivi hizo njia ambazo nimezisema hapo awali hatuzifanyi, kwa hiyo, mara nyingi unakuta mgonjwa anakwenda akiwa na tatizo la upungufu wa damu au akiwa na zile crisses, maumivu makali ambayo anayapata kutokana na ugonjwa huu, na akishathibitika kwamba ni mgonjwa wa sickle cell anapata matibabu.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa hatuna mfumo wa matibabu bure kwa wagonjwa wa seli mundu na hili niseme tu kwamba pale anapobainika mgonjwa kwamba hawezi kugharamia matibabu, kwa utaratibu wa sasa tuna utaratibu wa misamaha na utaratibu ni ule ambao nimeusema katika jibu langu la msingi, wanatakiwa kupita katika Serikali zao za Mtaa au Serikali za Vijiji kupata barua, wakija kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya hospitali watapata matibabu bure. Lakini katika mpango ambao tunataka kuanzisha mwezi Novemba tutaweka utaratibu mzuri zaidi wa matibabu kwa wagonjwa hawa wa seli mundu.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ninaridhika nayo na ninaipongeza Serikali kwa kupandisha hadhi Hospitali hizo za Ilala, Amana, Mwananyamala na Temeke, kwa kweli hosptali hizo zimekuwa msahada mkubwa na tumepunguza sana route za kwenda Muhimbili na Mloganzila.
Swali langu sasa kwa kuwa katika hospitali hizo za Mkoa hazina hizo mashine za MRI jambo ambalo linasababisha msongamano mkubwa wa kupata huduma hiyo katika Hospitali ya Muhimbili. Je, Serikali inautaratibu gani wa kupunguza foleni ya kupata kipimo hicho katika Hospitali ya Muhimbili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una Wilaya mpya za Kigamboni na Ubungo ambazo Wilaya ya Kigamboni wanatumia Hospitali ya Vijibweni kama Hospitali ya Wilaya na Wilaya ya Ubungo wanatumia Hospitali ya Sinza Palestina kama Hospitali ya Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo hizo za mashine za x-ray na mashine nyingine katika hospitali hizo ambazo zinawasaidia wananchi wa Kigamboni na wananchi wa Wilaya ya Ubungo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mhemiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, amekuwa ni chachu ya kufuatilia mambo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam ni mfano wa kuigwa Wabunge wa Viti Maalum kwa sababu amekuwa ametupa ushirikiano mkubwa sana sisi Wabunge wa Majimbo ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi tuliona mahitaji ya huduma ya CT-Scan na MRI yanazidi kukua kutokana na hali ya mabadiliko ya wagonjwa na nitoe tu historia kwa sababu miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto ya magonjwa ya kuambiza, sasa hivi tuna matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo huduma hizi za CT-Scan na MRI zinahitajika sana. Na kwa mwanzo tulikuwa tumeanza katika Hosptali za Rufaa za Taifa na Kanda, lakini kutokana umuhimu wa huduma hizi za CT- Scan na MRI ndiyo maana sisi kama Serikali tumesema sasa tunataka tuziweke katika ngazi ya Rufaa ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kupunguza tatizo la foleni la huduma ya CT-Scan pale Muhimbili ndiyo maana sasa sisi tumekusudia kuhakikisha kwamba huduma hizi zinapatikana katika Hospitali za Rufaa za Amana, Mwananyamala pamoja na Temeke na hilo ndilo kusudio letu na mchakato tumeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swala lake la pili ameuliza jinsi gani tunaweza tukapanua wigo wa huduma hizi katika hospitali nyingine hususani katika zile za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii naomba niliseme kwamba tunajenga Hospitali hizi za Wilaya moja pale Kigamboni, vilevile kule katika Wilaya ya Ilala. Lakini na mimi niombe niseme kwa sababu moja ya hoja ambayo umeigusia hapa ni katika Jimbo langu ambalo na mimi ni mwakilishi wa wananchi na niseme hivi tunavyoongea leo tunazindua huduma za x-ray katika Hospitali ya Vijibweni na nitoe rai kwa wananchi wa Kigamboni kwenda katika Hospitali ya Vijibweni huduma ya x-ray sasa inaanza kupatikana kuanzia leo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, napongeza viongozi wa Wizara hii; Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wamekuwa wakifanya safari nyingi kuja Mtwara ili kukabiliana na changamoto za hospitali hii. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa imeonekana hali ni tete kwa sababu hospitali yetu ya Rufaa ina Daktari Bingwa mmoja tu, sasa ningependa kujua kwamba: Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi kuhakikisha kwamba tunapata angalau Madaktari Bingwa watatu kwa kipindi hiki ambacho tunasubiri hao ambao wameenda vyuoni wahitimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri kama alivyojionea alivyotembelea hivi karibuni Ligula kwamba majengo mengi yamechakaa yanahitaji ukarabati: Je, Wizara ina mpango gani kuyakarabati majengo hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Abdallah Chikota, Mbunge ambaye naye anatoka Mtwara kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya, lakini katika ufuatiliaji wa karibu katika masuala mbalimbali ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora za afya katika mikoa yote nchini na ndiyo maana Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kuhamisha Hospitali za Rufaa za Mikoa kuja chini ya Wizara ya ili ziweze kupata usimamizi wa karibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweza kujibu swali lake la kwanza, ni mikakati gani ambayo tunayo ya muda mfupi kuhakikisha kwamba tunapata hizi huduma za kibingwa, nimeeleza katika jibu langu la msingi kwamba katika hiki kipindi cha mpito, Wizara kwa kushirikiana na Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wamekuwa wanaendesha kambi mbalimbali za huduma za udaktari bingwa katika baadhi ya mikoa na tumekuwa na mizunguko hiyo ili kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo hayana huduma hizo kwa sasa zinaweza kufikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wale madaktari ambao wanamaliza sasa hivi,tumeweka utaratibu wa kuwafanyia kitu kinaitwa borning kwamba daktari ambaye amesoma kwa fedha za Serikali, atapangwa pale ambapo Serikali itamhitaji kwa kuwa ametumia fedha za Serikali na kwa chini ya utaratibu huo, madaktari ambao tunawapanga sasa hivi kwa sababu tumefanya tathmini ya Ikama, basi tutawapeleka katika maeneo ambayo wanahitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumefanya tathmini ya kina ya miundombinu ya uchakavu wa majengo katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa na sasa hivi tumeanza kujielekeza kama Wizara katupitishia fedha ambazo ziko kwenye bajeti kufanya ukarabati mkubwa, nami nilikuwa pale Ligula tunafanya ukarabati wa jengo la bima, tumefanya ukarabati wa corridor, tunataka tukamilishe ile wodi ya grade one na vile vile tunataka sasa kuhamisha ile majengo ya theatre ili wananchi wa Mkoa wa Mtwara waweze kupata huduma nzuri na yenye ubora.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa ambalo tunataka tulifanye sasa Mtwara ili kufuta kilio cha wananchi wa Mtwara cha muda mrefu, kusudio la Serikali ni kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza majibu ya Serikali na nilitarajia kwa kuwa Serikali hii inakusanya kodi basi ingetilia mkazo katika ujenzi wa nyumba hizi za wazee ambazo nyingi ni chakavu na nyingi zimegeuka kuwa magofu walau wazee hawa nao wajisikie kuwa ni sehemu katika Taifa hili. Swali la kwanza, je, ni upi mkakati thabiti wa Serikali kuhakikisha kuwa nyumba hizi za wazee zinakarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali imekuwa ikitoa maagizo kuwa wazee wote watapata huduma za matibabu bure lakini hali ilivyo hivi sasa wazee wengi hawapati matibabu kama inavyopaswa katika hospitali za Serikali na hata katika vituo vya afya. Je, ni lini Serikali italeta sheria hapa Bungeni ambayo itasimamia matibabu na maslahi ya wazee hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Devotha Minja kwa maswali yake mazuri na kwa kufuatilia kwa karibu masuala ya wazee hususan katika kambi hii ya Fungafunga pale Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na naomba nitoe maelezo ya awali kwamba Serikali tuna kambi 17 za kuhudumia wazee. Hata hivyo, kwa mujibu wa sera yetu Serikali inachukua wazee pale inapoonekana yule mzee hana watoto wa kumtunza, ndugu na watu katika jamii ambao wanaweza wakamtunza. Mpaka sasa hivi tuna wazee takribani 500 ambao tunawahudumia sisi kama Serikali ambapo katika vigezo hivyo vitatu ambavyo nimevisema pale awali wametimiza na ndiyo maana tunawachukua na sisi kama Serikali tunawatunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa hii miundombinu ya vituo vyetu 17 umeshaanza na vituo ambavyo tumeshavifanyia ukarabati ni pamoja na Bukumbi, Mwanzage na Magugu. Aidha, tumejenga tena nyumba mpya pale Kolandoto na tumefanya ukarabati wa bweni pale Kilima. Ndiyo maana nasema tunakwenda awamu kwa awamu kuhakikisha kwamba hizi kambi zote tunaweza kuzifikia na kuzifanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na matibabu kwa wazee, Serikali ilitoa agizo kwamba wazee wote ambao wamefika umri wa zaidi ya miaka 60 wapate vitambulisho ili waweze kupata matibabu bure. Kumekuwa na changamoto kidogo ya kusuasua katika utekelezaji kwenye baadhi ya Halmashauri kutoa vitambulisho. Nitumie fursa hii kuzikumbusha Halmashauri kuzingatia agizo hili la Serikali la kutoa vitambulisho kwa wazee ambao wamefika miaka 60 na vilevile kutenga madirisha mahsusi kwa ajili ya wazee.
Mheshimiwa Naibu Spika, suluhu ya kudumu ya jambo hili ni hili jambo ambalo tunataka kulifanya kama Serikali kuhakikisha kwamba kila mtu anaingia katika mfumo wa Bima ya Afya ya Wote. Mwezi Septemba tunataka tulete Muswada ambapo utaratibu wa kuwa na bima utawekwa ili kuhakikisha wanapata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunatambua kwamba kuna magonjwa mahsusi ya wazee na sisi wataalam tuna kitu kinaitwa geriatric medicine. Ndani ya Wizara, tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba haya magonjwa ambayo ni mahsusi kwa wazee nayo tunayawekea utaratibu ili wazee waweze kupata matibabu kulingana na magonjwa waliyonayo.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri lakini bado kundi hili ni kubwa mno. Ukienda masokoni watoto wanabeba mizigo, bandarini watoto wanapara samaki na wengine wanatumiwa kuuza madawa ya kulevya, kwa hiyo, bado Serikali inatakiwa kufanya kazi na ina mkakati gani wa makusudi kuliondosha kabisa tatizo hili ili watoto wetu warudi katika malezi mazuri na wapate elimu? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, vilevile kuna wanawake ambao wanajihusisha na udhalilishaji wa watoto, wanawatoa vijijini na kuwapeleka mjini na kuwafanyisha biashara ya ukahaba na ni kundi kubwa tu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuunda Kamati Maalum kuwafuatilia wanawake hawa na wanatakapopatikana wapewe adhabu ya kutosha ili iwe ni fundisho kwa wengine ili suala hili la kudhalilisha watoto liondoke kabisa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, ambaye naye amekuwa anafuatilia sana masuala ya ustawi na maendeleo ya watoto, nimpongeze sana kwa hilo.
Mheshimiwa Spika, nianze kujibu maswali yake mawili. Tuna Sera ya Maendeleo ya Mtoto lakini tuna Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ambazo zimeainisha haki za msingi za motto. Mtoto ana haki ya kutunzwa, kuendelezwa na kutofanyishwa kazi nzito. Kwa hiyo, hizi sheria zipo na ziko wazi na pale mzazi au mlezi anapokiuka basi hatua za kisheria zinachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe tu jamii na sisi kama Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuyasemea haya. Sisis kama Wizara tutaendelea kuchukua hatua pale tunapobaini na mashauri yale yanapofika katika ngazi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hili ameongelea suala la watoto kufanyishwa kazi za kingono na baadhi ya walezi. Niseme tu katika Mpango Mkakati wa Serikali wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha mwaka 2021/2022, tumeelekeza kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto. Kamati hizi zimeanzishwa katika ngazi ya taifa mpaka katika ngazi ya kijiji na tunaendelea kuziimarisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pale tunapopata taarifa kwamba kuna matukio kama haya zile Kamati zina wajibu wa kuyafuatilia matukio hayo na sisi kama Serikali tunafuatilia na kuchukua hatua stahiki.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Uwepo wa kundi kubwa la watoto wazururaji kunasababishwa na wazazi kutofuata njia bora ya uzazi wa mpango. Njia bora kabisa ya uzazi wa mpango isiyo na madhara yoyote ni matumizi ya mipira ya kike na ya kiume.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa katika jamii yetu kumekuwa na tatizo kubwa la watu kutotumia mipira ya kike na ya kiume licha ya watengenezaji kuweka vionjo mbalimbali katika dhana hii kwa mfano strawberry, ndizi, chocolate na hivyo kusababisha siyo tu kuwa na watoto wa mitaani bali ongezeko kubwa la magonjwa ya zinaa na HIV. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu inayoendana na wakati ya watu kutumia mipira hii ya kiume ili kuondokana na changamoto hii ya watoto wa mitaani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, moja ya kisababishi ambacho kinapelekea kuwepo na watoto wa mitaani, ni wazazi kutojiandaa kupata watoto na labda na lingine ni moja ni kwamba watu kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo pasipokuwa na uwezo wa kulea.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tumekuwa tunahimiza sana suala la uzazi wa mpango na katika suala hili la uzazi wa mpango kuna njia mbili, kuna matumizi ya dawa, lakini hata hii mipira ya kiume kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema.
Mheshimiwa Spika, kKwa hiyo rai yangu kwa jamii ni kwamba kabla hatujaanza kuingia katika suala la kupata watoto ni muhimu ni vizuri tukajitafakari katika masuala mazima ya malezi na matunzo ya watoto. Suala siyo kuzaa tu ila ni kuhakikisha kwamba watoto wale tunaweza tukawalea na kuwapa matunzo ambayo yanastahiki na njia zote hizi tunazo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa kondomu tunazo za kutosha ndani ya nchi.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Waziri naomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, afya ni jambo la msingi sana, Serikali ilikuwa imeshauri kwamba kila halmashauri iweze kutenga asilimia nne, wanawake; nne, vijana; na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu ili waweze angalau kujimudu kiuchumi, lakini halmashauri nyingi zimeshindwa kutenga fedha hizo kwa sababu vyanzo vingi vya mapato vimekwenda Serikali Kuu ikiwemo halmashauri yangu ninayotoka mimi ya Iringa DC. Swali la kwanza, je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hawa watu wenye ulemavu wanapata matibabu bila vikwazo ikiwemo wale wenye bima unakuta hata wakiwa katika bima vifaa tiba kama sun screen lotion inakuwa ni shida, haipatikani?
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini sasa Serikali italeta huo Muswada wa Bima ya Afya kwa Watu Wote (Universal Health Coverage) ili tuupitishe na watu hawa wenye ulemavu waweze kupata huduma hii ya afya bila matatizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali tuliweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya vijana, wanawake na asilimia mbili kwa ajili ya walemavu na hili ni takwa kwa kila halmashauri ambalo wanapaswa wazingatie na kuhakikisha kwamba hii mikopo inafika na inapatikana pasipo kuwa na riba.
Mheshimiwa Spika, nikiongelea suala la matibabu, hakuna mwananchi ambaye anahitaji matibabu atayakosa kwa sababu ya hali yake ya maumbile. Kwa hiyo hilo nataka niliweke wazi na sisi kama Serikali tutaendelea kutoa matibabu kwa walemavu ambao wanastahili kwa mujibu wa taratibu ambazo tunazo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameongelea ni lini Serikali italeta Muswada wa mabadiliko ya sheria ama sheria inayohusiana na bima ya afya kwa wananchi wote, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge mpango wetu sisi Serikali ni kuleta katika Bunge la Septemba.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini pia niendelee kumshukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Iringa, Dkt. Mwakalebela kwa kazi nzuri sana ambayo amekuwa akiifanya katika hospitali yetu kutokana na changamoto nyingi zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mkoa wetu wa Iringa unakabiliwa na ajali nyingi sana lakini kipindi kirefu hatuna daktari bingwa wa mifupa pia hatujawahi kupatiwa daktari bingwa wa watoto toka hospitali ile imeanzishwa. Tuna wodi kubwa sana katika hospitali yetu ya Mkoa kuliko hospitali zote za Nyanda za Juu Kusini.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa anatupa ahadi gani wananchi wa Mkoa wa Iringa kutokana na changamoto hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba niipongeze Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika nchi yetu. Mkoa wetu una upungufu mkubwa sana wa watumishi takriban asilimia 70 inawafanya wauguzi na madaktari kufanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Je, nini mpango wa Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ritta Kabati, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Ritta Kabati amekuwa anafanya kazi nzuri sana ya kufuatilia masuala mbalimbali ya afya katika Mkoa wa Iringa. Kwa kweli amekuwa anatufuatilia sana sisi ndani ya Wizara na tunashukuru kuona kwamba ni mdau mkubwa sana katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linahusiana na kwamba kuna upungufu wa madaktari wa upasuaji wa mifupa pamoja na madaktari wa watoto. Hilo kama Serikali nakiri lakini sasa hivi Serikali inafanya mkakati wa kufanya mafunzo ya madaktari bingwa takribani 100 mwaka jana tumesomesha, mwaka huu tunasomesha madaktari wengine zaidi ya 100. Wwale watakaomaliza mafunzo na tumeweka utaratibu kwamba madaktari bingwa ambao wanasomeshwa kwa fedha za Serikali baada ya kuhitimu masomo yao, sisi Serikali tutawapangia wapi wanatakiwa kwenda kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi madaktari hawa watakapomaliza masomo yao basi Mkoa wa Irinnga utakuwa ni moja ya mikoa ambayo tutawapa kipaumbele. Hawa madaktari ambao amewaongelea ni madaktari wa kipaumbele ambao na sisi tumeweka msisitizo kuhakikisha kwamba tunawapa mafunzo na hospitali zote za Rufaa za Mikoa zinakuwa na madaktari bingwa hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaongeza rasilimali watu. Ni kweli hili jambo tunalo na katika mwaka huu ambao unaisha sasa, Serikali imeajiri watumishi zaidi ya 11,000 kuziba mapengo mbalimbali ambayo yamekuwepo na ajira mpya. Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) pamoja na Ofisi ya Rais (Utumishi), tunaendelea kufuatilia vibali kuhakikisha kwamba tunapata wataalam wa afya kwa ajili ya maboresho makubwa ambayo tumeyafanya kwenye vituo vya afya na ujenzi wa hospitali za Wilaya ambazo tunaendelea kuzijenga kwa sasa kote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto hii ya watumishi, kwa kweli watumishi wetu wa afya wanafanya kazi kubwa sana na nzuri katika kuwahudumia Watanzania. Rai yangu katika mikoa yote ikiwa ni pamoja na Mkoa huu wa Iringa ni kuhakikisha kwamba viongozi wa Serikali na viongozi wa vyama wanatengeneza mazingira wezeshi kuhakikisha kwamba watumishi ambao tunawapeleka kule basi wanatengenezewa mazingira wezeshi ya kuweza kufanya kazi zao vizuri.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, maswali yangu ni haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, idadi ya wananchi 13,234 waliofikiwa pamoja na wadau wengine ni ndogo sana kulingana na idadi ya watu tuliopo katika nchi hii. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa ziada wa kuwafikia wananchi ili kampeni hii iweze kufika katika eneo kubwa zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naipongeza sana Serikali kwa kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili pamoja na ndoa za utotoni. Hata hivyo, Mpango Kazi huu haufahamiki katika maeneo mengi na pia hata baadhi ya Wabunge hawaufahamu. Je, Serikali haioni umefikia wakati sasa kuishirikisha jamii katika kampeni hii ili kuwanusru watoto wetu wa kike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fatma Toufiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze amekuwa ni mdau mkubwa sana ambaye amekuwa anafuatilia haki mbalimbali na ustawi wa watoto wa kike pamoja na wanawake katika Mkoa wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla. Nikupongeze sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na maswali yake mawili, la kwanza ni kuhusu idadi ndogo ambayo tumeweza kuifikia. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, tulianza katika mikoa sita na tulijaribu kulenga maeneo ambayo tumekuwa na changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni. Takwimu zetu za Kitaifa zinaonesha kwamba asilimia 27 ya mabinti kati ya miaka 15-19 aidha wana ujauzito au wameshazaa na Mkoa wa Katavi ndiyo unaongoza kwa takriban asilimia kama 49 na mikoa mingine ambayo tumekwenda kule katika kampeni yetu inaonesha kwamba ni ile mikoa ambayo kwa kweli ina mzigo mkubwa sana katika tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejaribu sana kushirikisha makundi mbalimbali katika hili zoezi, siyo tu kwenda kuongea na jamii lakini tumejaribu kuangalia makundi gani ambayo yanaweza yakatusaidia kuweza kufikisha ujumbe. Tumeongea na viongozi wa kimila, kidini, Serikali, watu wa bodaboda, walimu na jamii kwa ujumla, lengo ni kuhakikisha kwamba ujumbe huu unafika vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumekuwa tunatumia vyombo vya habari kwa kutumia televisheni, magazeti na majarida. Pia sasa hivi jambo lingine ambalo tumeanza kufanya ni matumizi ya sanaa katika kuhakikisha kwamba tunafikisha ujumbe. Tumeanza kufanya maongezi na wasanii mbalimbali ili na wao watusaidie kufikisha sauti zao kwa njia zao kwa makundi ambayo nao wanaongea nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili ambalo ameliulizia ni huu Mpango Kazi wa Serikali wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto na mimba za utotoni. Sisi kama Serikali tumeshaanza mkakati wa kuhakikisha kwamba hizi Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya vijiji zinatengenezwa na zinafanya kazi. Mpaka sasa hivi tuna Kamati takriban 10,000, tunaendelea kuziimarisha na kuzijengea uwezo ili nazo ziweze kwenda kusimamia majukumu haya ya kuhakikisha kwamba ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na mimba za utotoni unaondoka katika jamii yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, tafiti zinaonesha kadri tunavyoendelea kuboresha elimu ndiyo hvivyo hivyo mabinti wanachelewa kupata ujauzito. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) tutaendelea kuboresha mkakati wa kuonesha kwamba wasichana wote wanaendelea kukua shuleni ili kuanza kupunguza hili suala la ndoa na mimba za utotoni.