Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ritta Enespher Kabati (12 total)

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
(a) Je, ni lini askari wa Iringa watajengewa nyumba?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha wanachodai askari wa Mkoa wa Iringa posho na stahiki zao zingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la ukosefu wa nyumba za askari wa Jeshi la Polisi hapa nchini. Lengo la Serikali ni kujenga nyumba hizo kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi huo. Kwa nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa suala hili na pia amekuwa akijitoa sana katika kuboresha mazingira ya askari katika eneo lake.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua madai ya askari ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kama ilivyo kwa Mikoa mingine hapa nchini. Askari wa Mkoa wa Iringa wanaidai Serikali jumla ya shilingi 431,147,410 na uhakiki wake unaendelea chini ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ili Serikali iweze kulipa baada ya ukaguzi huo.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Tatizo la kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo limekuwa likiongezeka siku hadi siku katika Mkoa wa Iringa.
(a) Je, nini mkakati wa Serikali kunusuru hawa watoto wasiendelee kufanyiwa matendo haya ya kikatili?
(b) Je, ni utaratibu gani unatumika kushughulikia watuhumiwa wa kesi hizi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti vitendo hivi haramu dhidi ya watoto tumetunga sheria zenye adhabu kali kwa watuhumiwa wanaopatikana na hatia ya makosa ya ubakaji na ulawiti. Kifungu cha 136(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kimeweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kubaka na kifungu cha 132(2) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa yeyote anayekutwa na hatia ya kujaribu kubaka. Aidha, kifungu cha 154 kimeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kulawiti. Lengo la kutoa adhabu hizo kali lilikuwa kutoa fundisho na onyo kwa yeyote mwenye dhamira ya kutenda makosa hayo ya jinai.
Mheshimiwa Spika, matukio mengi ya aina hiyo Mkoani Iringa yanahusisha ndugu au jamaa wa familia moja au sehemu moja. Ushahidi wa msingi hufichwa unapohitajika na wahusika wa pande zote mbili huyamaliza masuala husika kwa maelewano kifamilia na hivyo kuchochea matendo hayo ya jinai kushamiri.
Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuvisaidia vyombo vya dola wakati wa upelelezi na uendeshwaji wa mashauri haya mahakamani ili kukomesha kabisa matukio hayo. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge na wenzako Mkoani Iringa kuwa mstari wa mbele katika kampeni hii ya kuomba ushirikiano na wananchi.
Mhesimiwa Spika, aidha, ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi. Pindi, tukio la kubaka au kulawiti linaporipotiwa upelelezi hufanyika na mtuhumiwa hufunguliwa mashitaka mara moja.
(b) Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika kushughulikia watuhumiwa wa kesi za kubaka na kulawiti umefafanuliwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Sheria hizi zimeainisha namna ya kushughulikia makosa hayo kuanzia wakati wa kupokea taarifa ya kutokea kitendo cha ubakaji na ulawiti mpaka hatua ya kutoa adhabu kwa wahusika wa vitendo hivyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na taratibu za kisheria zilizoainishwa katika sheria hizo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa kesi za kubaka na kulawiti zinamalizika mapema na kuwa sheria zinasimamiwa ipasavyo.
Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa mashtaka kwa lengo la kujenga kesi na kuwa na ushahidi usiotia shaka ili kuiwezesha Mahakama kufikia maamuzi ya kuwatia hatiani watuhumiwa wa vitendo hivyo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. RITTA E.
KABATI) aliuliza:-
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 imekuwa ya muda mrefu na hivyo kupitwa na wakati.
Je, ni lini sheria hii itafanyiwa marekebisho ili iendane na mahitaji na kuondoa upungufu uliopo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ni matokeo ya mjadala mpana na shirikishi kupitia Waraka wa Serikali Na.1 ya mwaka 1969. Lengo la mjadala huo lilikuwa kupata muafaka kuhusu maudhui ya sheria hiyo ambayo yaligusa imani, mila na desturi za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miaka zaidi ya 20 kupita tangu Sheria hiyo ya Ndoa itungwe, Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria iliifanyia mapitio sheria hiyo na kubaini maeneo kadhaa yenye udhaifu na hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa mwenyekiti, kutokana na maoni hayo ya tume, mwaka 2008 Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria iliandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya M waka 1971.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mnamo Desemba, 2010 kabla ya waraka huo kujadiliwa na kuridhiwa na Baraza la Mawaziri, mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukaanza na kulilazimu baraza kusitisha kwa muda mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, wananchi wangetoa maoni kuhusu Sheria ya Ndoa pamoja na sheria nyingine zinazofanana na hiyo. Hata hivyo, maoni yaliyotolewa wakati wa mchakato huo kuhusu Sheria ya Ndoa yalikuwa machache sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na muda kupita na mabadiliko kadhaa yaliyotokea kuhusu Sheria ya Ndoa, Wizara yangu imeendelea na mchakato wa ndani wa kuifanyia mapendekezo ya marekebisho sheria hiyo. Wakati muafaka utakapofika, tutawasilisha mapendekezo ya
marekebisho ya sheria hiyo Bungeni ili iweze kuendana na wakati kwa kuondoa upungufu uliopo kwa maslahi mapana ya nchi yetu na kuhuisha na kuimarisha maeneo yaliyo mazuri ndani ya sheria hiyo.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Zao la mbao linachangia pato la Taifa katika nchi yetu na zao hili linazalishwa kwa wingi katika Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa:- Je, zao hili linaingiza fedha kiasi gani kwa mwaka.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mbao ni miongoni mwa mazao yanayochangia pato la Taifa na pia kutoa ajira kwa wananchi. Zao hili linazalishwa kwa wingi katika Wilaya ya Mufindi kutoka katika shamba la miti la Serikali la Sao Hill. Aidha, kiasi cha fedha kinachopatikana kwa mwaka hutegemea kiasi cha meta za ujazo kilichopangwa kuvunwa ambacho nacho kutegemeana na kiasi kinachoruhusiwa kitaalam kuvunwa kwa mwaka kulingana na mpango wa uvunaji wa kila shamba (annual allowable cut).
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mdororo wa uchumi mwanzoni mwa miaka ya 1980, Serikali ilibinafsisha viwanda vyake vikiwemo viwanda vya bidhaa za misitu. Serikali ilibakia na jukumu la kuhifadhi misitu pamoja na kukuza miti katika mashamba yake. Hivyo, Serikali huuza miti iliyosimama kwa wawekezaji binafsi ambao huvuna na kuchakata magogo kwa ajili ya mbao, karatasi, nguzo na mazao mengine; shughuli za uchakataji zinabaki kuwa jukumu la sekta binafsi. Kwa kuwa Serikali haihusiki moja kwa moja na uchakataji, takwimu halisi zilizopo wizarani ni za ujazo wa miti inayouzwa kwa wadau mbalimbali na kiasi cha fedha kilichopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2015/2016, jumla ya meta za ujazo wa miti zipatazo 767,946.46 zilivunwa kutoka kwenye mashamba ya Serikali na kuiingizia Serikali jumla ya Sh.58,312,894,416.20. Aidha, kwa mwaka 2016/2017, mashamba ya Serikali yalivunwa na kuuza miti yenye meta za ujazo 754,931 kwa viwanda vya kuzalisha mbao na kuipatia Serikali fedha zipatazo Sh.55,102,043,000.00 ikiwa ni mrabaha na tozo, ushuru wa Halmashauri za Wilaya (CESS) na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa misitu ya asili, mapato yanayotokana na zao la mbao, ni wastani wa shilingi bilioni 18.3 kwa mwaka.
RITTA E. KABATI aliuliza:-
Mwaka 2000 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini:-
Je, hali ya utekelezaji wa mpango huo wa TASAF ikoje?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mwaka 2000 ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini. Mafanikio makubwa yamepatikana katika awamu zote za utekelezaji kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa awamu ya kwanza ambayo ilitekelezwa mwaka 2000 hadi mwaka 2005 iliwezesha jamii kutekeleza miradi 1,704 yenye thamani ya shilingi bilioni sabini na mbili katika halmashauri 40 za Tanzania bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Miradi hiyo iliibuliwa na wananchi na ilihusisha sekta zote muhimu za afya, elimu, maji pamoja na barabara vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa awamu ya pili, TASAF ilitekelezwa mwaka 2005 hadi mwezi Juni, 2013 ambapo miradi 12,347 yenye thamani ya shilingi bilioni 430 katika halmashauri 126 za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Miradi hii iliongeza upatikanaji wa huduma za maji, elimu, afya, pamoja na barabara vijijini na kuongeza upatikanaji wa chakula
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya tatu ilizinduliwa mwaka 2012 na utekelezaji wake ulianza mwezi Januari, 2013 na unaendelea kutekelezwa hadi mwaka 2022 katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Madhumuni ya TASAF awamu ya tatu ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa pamoja na uwezo wa kuwagharamia mahitaji muhimu. Kazi zilizofanyika katika awamu ya tatu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kaya maskini milioni 1.1 zenye jumla ya watu takribani milioni tano zimeandikishwa katika vijiji, mitaa na shehia 9,986. Hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu kaya hizi masikini zilishapokea ruzuku ya shilingi bilioni 521.9. Kaya hizo pia zimetekeleza miradi ya kutoa ajira za muda kwa kaya za walengwa 354,648 kutoka katika halmashauri 42 za Tanzania Bara pamoja na Tanzania Zanzibar. Hadi kufikia Agosti mwaka huu, jumla ya miradi 3,553 yenye thamani ya shilingi bilioni 51.1 kutoka katika vijiji 2,063, mitaa 329 na shehia 168 imeibuliwa na kutekelezwa. Hadi sasa miradi 2,952 imekamilika; lakini pia miradi 601 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa kukamilishwa katika mwaka huu wa fedha
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Agosti mwaka huu, miradi ya kuendeleza miundombinu ya huduma za jamii 192 yenye thamani ya shilingi bilioni nane imetekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, mpango wa kuhamasisha kaya kuweka akiba na kuwekeza unatekelezwa na umewawezesha walengwa kushiriki katika kuweka akiba katika vikundi na kutekeleza miradi ya ujasiriamali ikiwa ni mkakati endelevu wa kaya kutoka kwenye umaskini. Jumla ya vikundi 5,136 vya kuweka akiba na kuwekeza vyenye wanachama 11,907 vimeundwa katika Halmashauri sita za Tanzania Bara ambazo ni Kibaha, Bagamoyo, Chamwino, Lindi, Mtwara pamoja na Manispaa ya Lindi, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je, ni lini Mahakama zote nchini zitaanza kuendesha kesi kwa lugha ya Kiswahili?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Mahakama Sura ya 11 yaani (Magistrates’ Courts Act CAP 11; S.12), lugha inayotumika kuendesha kesi katika Mahakama zote za Mwanzo ni Kiswahili. Aidha, kifungu hiki kinatamka kwamba kesi katika Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi zitaendeshwa kwa Kiswahili ama Kiingereza, isipokuwa hukumu inaandikwa kwa Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama Kuu, Kanuni za Lugha za Mahakana ukisoma Kanuni ya (2) inasema kuwa Lugha ya Mahakama Kuu itakuwa Kiswahili au Kiingereza, isipokuwa kumbukumbu za maamuzi, ama hukumu itakuwa kwa lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009, ukisoma Kanuni ya (5) lugha inayotumika katika kuendesha mashauri itakuwa ni Kiswahili au Kiingereza kulingana na maelekezo ya Jaji Mkuu au Jaji anayesikiliza shauri husika, isipokuwa hukumu inaandikwa kwa Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, hivyo ninapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba uendeshaji wa mashauri katika Mahakama zote nchini kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo unaruhusu kutumia lugha zote mbili, Kiswahili na Kiingereza na tumekuwa tukizingatia lugha hizo katika uendeshaji wa mashauri.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Serikali ya Tanzania ilisaini Mkataba Namba 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) tangu tarehe 16 Juni, 2011 na Rais Mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alishawahi kutamka kuwa, Tanzania haina tatizo na Mkataba huo.
Je, kuna kikwazo gani kinachokwamisha kuridhia Mkataba huo wa ILO Namba 189 wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani wakati Baraza la Wafanyakazi (LESCO) limeshapendekeza kuridhia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Tanzania kama nchi mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani ilishiriki kikamilifu katika majadiliano na upitishwaji wa Mkataba ya Kimataifa wa ILO wa Wafanyakazi wa Majumbani Namba 189 wa mwaka 2011 ambao unalenga kukuza kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani. Aidha, hadi kufikia tarehe 30/08/2017 mkataba huo umeridhiwa nan chi 24 kati ya nchi wanachama 187 ambapo nchi za Afrika zilizoridhia mkataba huu ni tatu ambazo ni Afrika Kusini, Mauritius na Guinea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha napenda nielezee kuwa Serikali inathamini mchango wa wafanyakazi wa majumbani katika kujenga uchumi wa nchi. Hii ndio maana Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004, ambayo inazitambua haki za wafanyakazi wa majumbani kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine. Vilevile kwa upande wa Zanzibar ipo Sheria ya Ajira, Namba 11 ya mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuridhia mikataba yote ya kimataifa ikiwemo ya Shirika la Kazi Duniani siku zote Serikali imekuwa ikizingatia maslahi mapana ya nchi na ustawi wa wananchi ikiwemo wafanyakazi kwa ujumla. Endapo Serikali itajiridhisha kuwa mazingira na ustawi wa wafanyakazi kwa sheria zilizopo hakuna ustahimilivu, Serikali itafanya maamuzi stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa kwa kushirikiana na wadau wote vikiwemo vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri, Serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi, ili kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani pamoja na kujenga uelewa wa wadau kuhusu matakwa ya mkataba na haki za sheria za wafanyakazi hao.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Kiwanja cha Ndege cha Nduli kipo katika mpango wa Serikali wa Ujenzi wa viwanja 11:-
(a) Je, ni lini kiwanja hicho kitajengwa?
(b) Mpaka sasa hakuna kituo cha kujaza mafuta katika kiwanja hicho; je, ni utaratibu gani unaotumika ili kiwepo kituo cha mafuta katika kiwanja hicho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:
(a) Kiwanja cha Ndege cha Nduli kililichopo Mkoani Iringa ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliomalizika mwezi Mei mwaka 2017. Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali ilitenga fedha za ndani kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwanja hicho ikiwa ni pamoja na kutangaza zabuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kutokana na Benki ya Dunia kuonesha nia ya kufadhili ujenzi wa uwanja huu, Serikali ilisitisha taratibu za ndani za manunuzi ili kusubiri manunuzi kufanyika kwa kuzingatia taratibu za Benki ya Dunia. Hivyo, uwanja huo utaanza kujengwa mara moja baada ya taratibu hizo kukamilika.
(b) Kwa sasa kiwanja hiki hakina ndege za kutosha zinazoweza kuvutia uwekezaji wa kituo cha mafuta. Ni vema ieleweke wazi kwamba sera ya uwekezaji katika viwanja vya ndege inatoa fursa ya kuuza mafuta ya ndege kwa makampuni binafsi yenye leseni ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makampuni yenye leseni hizo na yaliyoingia mikataba ya biashara ya mafuta ya ndege na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania TAA ni Puma, Oilcom, Total na Prime fuels. Kwa hiyo, ni utashi wa makampuni ya mafuta na nguvu ya soko inayosukuma uwekezaji wa biashara ya mafuta katika viwanja vya ndege. Ni matumaini yangu kwamba kiwanja hiki kitakapokamilika kujengwa kitawavutia wawekezaji na hatimaye kumaliza tatizo hili.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara uliopo Manispaa ya Iringa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka umeanza.
Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha ili kumaliza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara unatekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kushirikiana na wadau wengine. Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2008/2009 na ulikadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania 1,900,000,000. Aidha, mpaka sasa kiasi cha shilingi 928,000,000 zimetumika kugharamia mradi huu kupitia Serikali Kuu, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mradi wa ASDP na Shirika la Maendeleo la Viwanda la Umoja wa Mataifa ambalo lilisaidia kuweka vifaa vya machinjio vikiwemo mashine za kuchakata nyama na vyumba viwili vya kuhifadhi ubaridi (cold rooms).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa sehemu kubwa ya miundombinu inayohitajika kwa ajili ya machinjio imekamilika. Aidha, kiasi cha shilingi 1,090,000,000 zinahitajika kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa zizi, mabwawa matatu ya maji machafu na maji safi, uzio wa machinjio, tanuru la kuchomea taka kwa maana ya incinerator, jengo la ofisi za utawala, vyoo, jiko na kisima cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itashirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhakikisha fedha za kukamilisha machinjio ya Ngerewara zinapatikana ili Watanzania wapate ajira na bidhaa abora za mifugo na kuongeza pato la Halmashauri na Taifa kwa ujumla wake.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji wa Mkoga Irrigation Scheme uliopo katika Manispaa ya Iringa Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ernest Kabati, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kutekeleza ujenzi wa scheme mbalimbali hapa nchini. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia mfuko wa Food Aid Counter Party ilitumia kiasi cha shilingi milioni 270 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mashambani na ujenzi wa mfereji mkuu katika scheme ya umwagiliaji ya Mkoga yaani Mkoga Irrigation Scheme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu wa scheme hiyo haujakamilika na bado unahitaji kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji mashambani. Hivyo Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeingiza scheme ya umwagiliaji ya Mkoga kwenye awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango kabambe wa Taifa wa umwagiliaji utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 hadi mwaka 2025/2026.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio vingi vya utalii kama vile Hifadhi za Taifa za Ruaha na Udzungwa, Makumbusho ya Mtwa Mkwawa ya Kalenga, Isimila, Eneo la Zana za Mwanzo za Mawe na Maumbile Asilia na Makumbusho ya Mkoa ambayo inaonesha utamaduni wa asili wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na mpango kabambe wa uendelezaji utalii, Serikali imekuwa ikitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Iringa. Mpango kabambe wa kuendeleza utalii nchini ulioandaliwa mwaka 1996 na kufanyiwa mapitio mwaka 2002 umeainisha Mkoa wa Iringa kama kitovu cha maendeleo ya utalii (tourism hub) kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuainisha vivutio katika Mkoa wa Iringa lilianza kufanyika mwaka 2007 ambapo mpaka sasa takribani maeneo 38 ambayo ni vivutio vya utalii yameainishwa katika Wilaya za Mufindi, Kilolo na Iringa. Kazi inayofuata sasa ni kuendeleza na kutangaza vivutio hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia taasisi zake ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania imeweka mikakati madhubuti ya kutangaza utalii. Mikakati hii ni pamoja na kujenga utambulisho wa Tanzania (Destination Tanzania Brand), kukuza maonesho ya utalii wa Kimataifa yanayofanyika ndani na nje ya nchi kama vile Karibu Kusini, kuanzisha channel ya utalii, kuanzisha Studio ya kutangaza utalii kwa njia ya TEHAMA, kuadhimisha Mwezi wa Urithi (Urithi Festival) na kuimarisha uhamasishaji kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanafunzi. Vivutio vya utalii katika Mkoa wa Iringa vimejumuishwa katika mikakati hii ya kutangaza utalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo hapo juu na ili utalii Mkoani Iringa, Serikali imeendesha mafunzo ya muda mfupi ya utalii na ukarimu kupitia mradi wa SPANEST kwa takribani watu 300, imefungua Ofisi ya Utalii ya Kanda ya Kusini iliyoko Iringa na imezindua mradi wa kukuza utalii Ukanda wa Kusini ujulikanao kama REGROW. Aidha, Iringa ni miongoni mwa mikoa iliyoajiri Maafisa Utalii kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Halmashauri za Wilaya.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Mheshimiwa Rais alitoa tamko kuwa Wazauni wote wanaoidai Serikali walipwe:-

Je, tokea tamko hilo litolewe ni Wazabuni wangapi wameshalipwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Ernespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jumla ya wazabuni 2,048 wamelipwa madai yao tangu kutolewa kwa tamko na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 3 Januari, 2018 Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Kati ya wazabuni 2,048 waliolipwa, wazabuni 1,277 walihudumia sekretarieti za mikoa na 771 walihudumia Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali.

Aidha, jumla ya shilingi 199,064,014,966.64 zimetumika kulipa wazabuni hao, ambapo shilingi 3,729,605,175/= zimetumika kulipa wazabuni waliotoa huduma kwa sekretarieti za Mikoa na shilingi 195,334,409,791.64 zimetumika kulipa wazabuni wa Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali. Aidha, madai haya yalilipwa baada ya uhakiki kufanyika.

Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba, Serikali itaendelea kulipa madai mbalimbali ya wazabuni kulingana na upatikanaji wa fedha sambamba na uhakiki wa madai husika. Aidha, ili kukamilisha zoezi la uhakiki kwa wakati, wazabuni wote wanaombwa kutoa ushirikiano hususan kuwasilisha taarifa na vielelezo sahihi vya madai yao pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.