Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ritta Enespher Kabati (51 total)

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ilipata kuwa hadhi ya Wilaya toka mwaka 2002 lakini majengo mengi katika Wilaya bado hayajakamilika, kama Hospitali ya Wilaya bado wanatumia Hopitali ya Mission, Makao Makuu ya Polisi bado hayajajengwa kwenye Wilaya yake na vilevile Mahakama bado hakuna…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naomba uulize swali!
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, huwa vigezo gani vinatumika katika kuweka mipango kujenga hizi Wilaya? Kwa sababu Wilaya za zamani bado hazijatimiziwa majengo yote na zinaanzishwa Wilaya mpya, nilitaka nijue vigezo gani vinatumika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba miundombinu ya Wilaya ya Kilolo bado haijakamilika, siyo Wilaya ya Kilolo peke yake isipokuwa ni Wilaya mbalimbali, vipaumbele vinavyotumika kwanza mazoezi yote yanaanza katika mchakato wa bajeti, na ndiyo maana mwaka huu ukiangalia tuna karibu Wilaya zipatazo 44, hizi ni Halmashauri na Wilaya mpya mbalimbali ambazo tumezipa fedha.
Hali kadhalika tunaangalia upungufu katika maeneo mbalimbali. Imani yangu kubwa ni kwamba suala la Kilolo limesikika na kwa sababu tuna Wilaya mpya na Halmashauri nyingine tunaendelea katika ujenzi wa miundombinu, tukifika katika mafungu yetu ya Mikoa utakuja kubainisha kwamba jinsi gani kila Mkoa katika mafungu yake yameweza kuelekezwa. Ile sehemu ambapo miundombinu haijakamilika lakini Wilaya ambazo ni mpya tunaanza kuziasisi tena upya, jinsi gani tume-allocate funds katika mwaka huu wa fedha ili tuweke hali halisi ya kuhakikisha kwamba wafanyakazi katika maeneo hayo waweze kufanyakazi katika mazingira rafiki.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA(MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Naibu Waziri Jafo, nilitaka tuelewane kwenye jambo hili la uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni gumu na sote hapa tunafahamu kwamba maombi haya ya kuanzisha haya maeneo yanatokana na mahitaji ya wananchi. Lakini ni sisi wenyewe kwenye maeneo yetu ndiyo huwa tunaanzisha haya. Kwa kuwa maombi haya yanakuja mengi na wakati mwingine Serikali siyo rahisi sana kupata fedha kwa mara moja kujenga mahitaji yote ya Makao Makuu ya Halmashauri au Wilaya ni lazima tuvumiliane. Ni lazima tuvumiliane twende kidogo kidogo na ndiyo maana Serikali imekuwa ikitenga milioni 500, tunaamini tukifanya hivyo kwa miaka mitano, miaka minne, tunaweza tukakamilisha majengo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuvumiliane kwa sababu Wabunge wengi wanakuja kuniona wakiwa na maombi mapya ya maeneo mengine ya utawala, sasa tukianza kuulizwa maswali kama kwa nini tunakuwa hatujajipanga na tunayaanzisha, kuna wengine hapa mmeahidi huko mlikotoka kwamba sisi tutahakikisha hapa panakuwa Mji Mdogo, sisi tutahakikisha tunakuwa na Halmashauri, sisi tutahakikisha tunakuwa na Wilaya.
Sasa tuvumiliane na tuende pamoja na tuamini kwamba kadri Serikali itakapopata uwezo tutakuwa tunafanya, lakini jambo hili ni gumu.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa wanawake wengi sana wanaoishi vijijini hasa katika Mkoa wetu wa Iringa, wamekuwa wakipata shida sana wanapotafuta msaada wa kisheria; na kwa kuwa mashirika haya mengi yako mijini.
Je, Serikali inawasaidiaje wananchi ambao wanakaa mbali na miji ili angalau hata kupeleka mobile elimu ili waweze kufikiwa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wanawake wengi walioko vijijini wanakabiliwa na changamoto ya kupata msaada wa Sheria, lakini nataka nimthibitishie kwamba kwa sasa hivi Waziri wa Katiba na Sheria tayari ameshaleta mapendekezo ya Kutunga Sheria ya Msaada wa Kisheria ambapo itahakikisha msaada wa kisheria unapatikana kwa wananchi wote wenye mkahitaji, wakiwemo wanawake walio vijijini. Kwa hiyo, ni suala ambalo tayari Serikali ya Awamu ya Tano inalifanyia kazi na tunataka kumuahidi kwamba ndani ya siku chache tutakuwa na sheria, hivyo wanawake wataweza kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili; tayari tunazo NGOs mbalimbali ambazo zinafanya kazi ya kutoa Msaada wa Sheria kwa wanawake, ikiwemo Chama cha Wanasheria Wanawake na Chama cha Wanawake Wanahabari. Kwa hiyo, tunazo taasisi mbalimbali ambazo zinatoa msaada wa sheria kwa wanawake.
RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili.
Kwa kuwa Wilaya ya Kilolo imezungukwa na mito ya Ruaha, Mto Rukosi; ni kwa nini Serikali isivute maji kutoka katika mito hiyo kuliko kuchimba visima ambavyo vimekuwa vikichimbwa, lakini havitoi maji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa visima…
SPIKA: Hilo, swali la kwanza ulilouliza ni kwa niaba ya kaka au? (Kicheko)
Mheshimiwa endelea!
MHE. RITTA E. KABATI: Swali la pili, kwa kuwa visima virefu huwa havina uhakika sana wa kutoa maji na mara nyingi vimekuwa vikiharibika! Ni kwa nini Serikali isielekeze nguvu kwenye kuchimba mabwawa badala ya kutumia fedha nyingi sana katika kuchimba hivi visima ambavyo mara nyingi vimekuwa havina uhakika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKAL ZA MITAA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza lilikuwa ni kwa nini sasa tusitumie fursa za mito ambayo inapita katika Jimbo la Kilolo badala ya kwenda kuchimba visima virefu. Katika utekelezaji wa miradi ya maji, kwanza wataalam wanaangalia au wanafanya analysis, ni chanzo gani cha maji ambacho kitaweza kusaidia, lakini utafiti huo vilevile unaendana na bajeti.
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo mbalimbali ambayo yamebainika kwamba kumeenda kuchimbwa visima virefu, lakini sehemu zingine kuna fursa za maji. Hili naomba nikiri hapa wazi kwamba, watu wengi mbalimbali hasa wa kutoka maeneo mbalimbali ambayo kuna mito mirefu au maziwa, kama watu wa Kanda ya Ziwa wanasema kwa nini tuchimbiwe visima badala ya kutumia vyanzo vilivyopo. Naamini katika Programu ya Maji ya Awamu ya Pili ambayo sasa inaanza, Watalaam wetu, wataangalia katika sehemu ambayo kuna fursa ya vyanzo vikubwa vya maji hasa mito viweze kutumika vizuri kutokana na bajeti iliyopo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mbunge kwamba katika Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji, watalaam wetu wataenda mbali zaidi kuangalia fursa. Ndiyo maana tulisema pale awali kwamba maeneo yote yanayozungukwa na vyanzo vikubwa vya maji, basi watalaam itabidi wajielekeze huko kuona jinsi gani ya kufanya ilimradi kupata maji ya uhakika na kuhakikisha fedha inatumika vizuri.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kwa nini sasa kuchimba visima virefu badala ya kuchimba mabwawa. Mara nyingi sana watalaam wanazungumza kwamba maji ya kisima kirefu, kitaaluma au kitalaam, ukiyatoa yanakuwa maji safi na bora, kwa sababu yanakuwa hayana contamination, lakini maji ya bwawa maana yake yanataka ufanye treatment.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, imeonekana wazi, sehemu zingine visima virefu kweli vimechimbwa, lakini hatukupata maji. Kwa sababu uhitaji wa maji ni mkubwa na sehemu zingine water table inasumbua sana, naamini sasa, ndiyo maana katika mkutano wetu wa pili tuliofanya tathmini pale Dar es Salaam, tulielekeza kila Halmashauri, ikiwezekana kila mwaka twende katika uelekeo wa mabwawa kwa sababu maeneo mengi mbalimbali tuliyochimba visima virefu ni kweli wakati mwingine tulikosa maji na wakati mwingine miradi hii inaharibika. Vitu hivi vyote vitakwenda sambamba kwa pamoja kuangalia engineering specifications ya maji inasemaje kwa ajili ya kuelekeza wananchi wapate maji bora na salama.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize Sali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa njia mojawapo ya kupunguza hivi vifo vya mama na mtoto ni pamoja na kuboresha mfumo wa referral, yaani kutoka kwenye Vituo vya Afya, ama kwenye Hospitali za Wilaya kwenda kwenye Hospitali ya Mkoa; na kwa kuwa vituo vyetu vingi sana katika Mkoa wetu wa Iringa havina magari ya kubebea wagonjwa na vipo katika miundombinu mibaya sana ya barabara: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kila Kituo cha Afya kinapatiwa gari ili kupunguza hivi vifo vya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba taarifa hizi zimfikie Mheshimiwa Ritta Kabati na Wabunge wote ambao wangependa kupata magari ya ambulance kwenye Halmashauri zao, kwamba kwanza jukumu la kununua magari haya lipo kwenye Halmashauri zenyewe. Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa ni sehemu ya Halmashauri hizi, kwenye mipango yao ya bajeti tayari tutakapomaliza Bunge hili utaratibu wa mchakato mzima wa bajeti utaanza, basi Wabunge wahudhurie vikao hivyo na waweke ambulance kama kipaumbele cha kwanza kwenye bajeti zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hivyo, sisi Wizara ya Afya, tutaendelea kuwaomba na kuwashirikisha wadau wa maendeleo watupe ufadhili. Kama tutafanikiwa kupata ambulance, basi tutazigawa kwenye hospitali zetu nchini.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuunganisha barabara za mikoa na za wilaya kwa lami lakini katika Mkoa wetu wa Iringa, Wilaya ya Kilolo ni wilaya ambayo toka mwaka 2002 imepata hadhi ya kuwa wilaya mpaka leo hii haijaweza kuunganishwa kwa lami kutoka yalipo makao makuu. Ni lini sasa Serikali itaunganisha wilaya hii na makao makuu kwa lami ili hii sera iweze kutimia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Wilaya ya Kilolo haijaunganishwa na barabara ya lami kama ambavyo Mbunge wa Kilolo na Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Ritta Kabati wamekuwa wakifuatilia suala hili ofisini kwetu na nyakati zote tumekuwa tukiwaahidi kwamba tutafuatilia. Kwanza Mheshimiwa Rais alipopita lile eneo hiyo pia ilikuwa ni sehemu ya ahadi yake licha ya kwamba hii ni ahadi ya kiujumla kwa wilaya zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie maadam dhamira yetu ni kuhakikisha miundombinu inajengwa na ahadi zote za viongozi wetu tunazitekeleza atupe muda ili tutakapopata ratiba kamili ya suala hili tutatekeleza. Mnafahamu tumeanza kwa kiwango fulani, ni kiwango ambacho hakitoshelezi nakubali kama ambavyo Mheshimiwa Mwamoto amekuwa akinisukuma kila wakati kuhusu hilo suala. Niwahakikishie wote Mheshimiwa Mwamoto na Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba ahadi hiyo tutaitekeleza kama ambavyo tumeongea nao tukiwa maofisini.
MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza swali fupi tu. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuanzisha Kitengo cha Matibabu ya Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa hapa Dodoma. Hata hivyo, nimeona Hospitali ya Muhimbili pia ina kitengo kinashughulikia matibabu ya figo. Ni kwa nini Serikali isiweke eneo moja, kwa mfano hapa Dodoma washughulikie tu mambo ya figo na kule Muhimbili washughulikie tu mambo ya moyo? Pia nimeona tengeo katika bajeti, sasa hapa ni kama kuharibu rasilimali, naomba jibu.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ni kwamba, tayari Serikali ndicho inachokifanya, hospitali ya kisasa kabisa ya Benjamin Mkapa Ultra-Modern Hospital itabobea zaidi kwenye kutoa tiba mahsusi ya magonjwa ya figo. Tutaanzia kwenye hizi tiba ambazo sasa hivi tunazo kwenye hospitali nyingine za dialysis kwa maana ya kusafisha figo na tunakwenda mbele zaidi hadi kuanza kufanya huduma za kupandikiza figo (transplant) na hayo yatafanyika kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa hapa Dodoma.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nina maswali tu madogo mawili ya nyongeza.
Pamoja na askari wa Iringa kuishi kwenye mazingira magumu sana, lakini zaidi ya nusu ya askari wanaishi nje ya makambi yao yaani uraiani. Pia katika Mkoa huo wa Iringa, Wilaya ya Kilolo Serikali haijaweza hata kujenga jengo lolote la ofisi wala makazi ya askari na katika majibu yake Serikali imesema kwamba itakuwa inajenga kadri itakavyokuwa inapata fedha.
Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa kipaumbele kwa Mkoa wetu wa Iringa ili askari wetu waweze kuishi kwenye mazingira bora yajengwe mapema sana? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa askari wa Mkoa wa Iringa wanadai posho na stahiki zao kiasi kikubwa sana cha pesa na Serikali imesema kwamba bado wanafanya uhakiki. Je, ni lini sasa uhakiki utakamilika ili askari wetu wa Mkoa wa Iringa waweze kupata stahiki zao na posho kwa sababu familia zoa zimekuwa zikiishi kwa shida sana na hasa watoto na wake za askari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, wakati tunakamilisha mchakato wa ujenzi wa nyumba za askari ule ambao nimekuwa nikiuzungumza hapa Bungeni kila siku ambao pia utahusisha na Mkoa wa Iringa tunajipanga kutumia rasilimali za ndani pamoja na rasilimali zilizopo katika maeneo husika pamoja na rasilimali watu ili kupunguza tatizo au changamoto za makazi kwa askari wetu na vituo vya polisi.
Mheshimiwa Spika, nataka nichukue fursa hii kwanza kabisa na kwa dhati nimpongeze Mheshimiwa Ritta Kabati kwa jitihada zake kubwa sana ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Polisi Iringa, ambapo sasa hivi nguvu zake anazielekeza maeneo ya Kilolo, lakini kwa kutambua kwamba Mheshimiwa Mbunge amefanya kazi kubwa sana pale Iringa ya ujenzi wa kituo nataka nimhakikishie kwamba tutakuwa pamoja na yeye tutashirikiana naye ili tuweze kuona kwa haraka sana tutatumia mpango huu wa matumizi ya rasilimali katika eneo husika ili kupunguza changamoto ya makazi pamoja na vituo vya polisi.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha Bunge tukae kwa pamoja tushauriane tuone iko vipi kwa haraka sana mpango huu ambao tumeubuni hivi karibuni tunaanza kutekekeleza kwa Kilolo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na lini ukaguzi utamalizika. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba tunakamilisha ukaguzi haraka iwezekanavyo ili malipo haya yaweze kulipwa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu na nimpongeze sana niongezee tu kwa kumpa assurance Mheshimiwa Mbunge ambaye jambo hili amekuwa akilifuatilia kwa umakini sana la maisha ya polisi na vitendea kazi vyao kwamba tarehe 9 Septemba, 2016 wale wenzetu ambao tulikuwa tunaongea nao kuhusu mkataba wa ujenzi wa nyumba za askari kiongozi wao mkubwa atakuja na atakutana na IGP pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara na baada ya hapo tutabakiza mawasiliano ya ndani ya Serikali kwa ajili ya kwenda kwenye utekelezaji wa jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, la pili Wizara tumeamua kwenda na jambo hili sambamba kwamba jitihada zitakazofanyika za kibajeti tuzioanishe na jitihada za rasilimali tulizonazo ndani ya taasisi zetu hizi na nimeelekeza mikoa yote wafanye tathmini ya kila mkoa tuna wafungwa wangapi wanaoweza kufanya kazi za kufyatua tofali na wafanye tathmini ya vitendea kazi vinavyoweza kutumika kufyatulia tofali hizo na aina ya tofali ambazo zinatakiwa, lakini pia na kutumia bajeti kidogo zilizopo kwa ajili ya vitendea kazi vingine ambavyo vitatakiwa kama cement ama nondo kwa ajili ya kuanza miradi hiyo katika maeneo ambayo kazi hiyo si kubwa sana kwa ajili ya kupunguza tatizo hili sambamba na jitihada za kibajeti ambazo tunazifanya.
Kwa hiyo, Serikali inatambua ukubwa wa tatizo hili na inaweka uzito unaostahili na Mheshimiwa Rais tayari alishatuelekeza wasaidizi wake na sisi tunatembea kwenye nyayo zake kuhakikisha tunamaliza tatizo hilo la manung‟uniko ya askari.
Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo kwenye upande wa madai yao nimeelekeza kila ambaye anatunza kumbukumbu za askari waweze kuhakikisha kwamba wanaorodhesha vizuri kuwarahisishia wale wanaokagua, wanaofanya ukaguzi ili madai hayo ya askari yasikae muda mrefu sawasawa na maeneo mengine ambayo yana uficho ama yana tatizo la kuweza kufanya ukaguzi kwa sababu askari anapokuwa kazini huku anadai inampunguzia morali ya kazi na inampunguzia uwezo wake wa kufanya kazi.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa ujenzi wa daraja la Igumbilo ambalo leo hii wakimbiza mwenge wanalizindua pale katika Jimbo la Iringa Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kuhusiana na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Dodoma - Mtera - Iringa ambao umekamilika lakini sasa kuna malori makubwa sana yanakatiza katikati ya mji na kusababisha msongamano na barabara hii kuharibika katikati ya mji. Ni lini sasa ule mchepuko ambao ulikuwa umetengwa, ambao unatokea kwenye Chuo cha Tumaini kwenda kwenye barabara kuu utakamilika kwa sababu sasa hivi magari mengi sana yanapita kwenye ile barabara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa mzito wa Iringa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mchepuo wa Iringa upo katika mipango yetu. Naomba nimhakikishie kwamba kile ambacho wao kwa maana ya RCC walikileta kwetu na sisi tumekichukua, tutakifuatilia kuhakikisha kwamba tunakitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini? Naomba tu Mheshimiwa Mbunge anipe nafasi kwa sababu siyo sahihi sana kutamka tarehe hapa, lakini naomba aangalie dhamira yetu kwamba ni ya dhati na tutatekeleza mradi huo wa ujenzi wa mchepuo wa barabara pale Mjini Iringa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa muda mrefu sana Serikali iliahidi kujenga barabara inayokwenda kwenye hifadhi la Ruaha National Park na nakumbuka nilishawahi kuleta swali hapa Bungeni na Mheshimiwa ambaye sasa hivi ni Rais alikuwa Waziri alijibu kwamba, kuna pesa zinatoka Marekani kwa ajili ya ujenzi wa hiyo barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa anijibu ni kwa nini, kwa sababu barabara hii ni muhimu sana kwenye Mkoa wetu wa Iringa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba anijibu kwa sababu katika tengeo la bajeti ya safari hii sijaielewa vizuri, sasa atuambie ni lini barabara ile itajengwa inayokwenda kwenye Ruaha National Park?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, barabara hiyo hatujaiweka katika mwaka huu wa fedha unaoanza Julai, lakini namhakikishia ahadi hii kama ambavyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais na viongozi wengine itatekelezwa kama ilivyoahidiwa kabla ya kipindi hiki tulichopewa cha uongozi kwisha.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa kuwa hili ni ombi, basi tunalichukua, halafu mimi na yeye tutakaa, tunajuana ma-comrade, tuweze kuona uwezekano wa kulitimza hilo.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza.
Kumekuwepo na wimbi kubwa sana la ujambazi ambalo linafanywa na hawa vijana wanaojulikana kama panya road ambao wamekuwa wakileta utata sana katika miji mikubwa na sasa hivi mpaka Iringa wameshatokea, Serikali ina mpango gani ama mkakati gani wa kuondoa ujambazi, hawa panya road kwa sababu ni vijana ambao nasikia wanafahamika kwenye mitaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la panya road, ni kweli kulikuwa na kundi la vijana ambalo lilikuwa linafanya uhalifu. Lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Kabati kwamba Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri kudhibiti kundi la vijana hawa na nadhani Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba kwa kipindi fulani sasa matukio hayo hayajitokezi na vijana hao wamedhibitiwa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo tu mawili ya nyongeza.
Kwanza nikushukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yako, ningependa kujua tofauti kati ya hizi Mahakama za kawaida na Mahakama za Coroner?
Swali la pili, kwa kuwa hata katika Mkoa wetu wa Iringa, vipo vifo ambavyo huwa vinatokea vyenye utata; je, ni vifo vingapi ambavyo vilipelekea kuundwa hii Mahakama ya Coroner?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ipo tofauti kati ya Mahakama ya Coroner na Mahakama za kawaida za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya.
Kwanza kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Mahakama ya Coroner kazi yake kubwa ni kupata chanzo cha kifo ambacho kimetokea na kina utata, kujua chanzo chake ni nini. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kazi kubwa Mahakama ya Uchunguzi inafanywa ikiongozwa na Coroner na ndipo hapo unakuta atatumia madaktari, ma-pathologist, forensic experts, criminologist waweze kumsaidia kujua chanzo cha hicho kifo ni nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya, wao wanakwenda mbele zaidi, wakishapata tukio kwamba limetokea wao sasa wanaangalia vilevile dhamira ya yule aliyetenda hilo kosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe ni Mwanasheria na kwa Waheshimiwa Wabunge ambao ni Wanasheria pia wataelewa lakini naomba nieleze tu kwamba Mahakama za Hakimu Mkazi, wao wanaongozwa na Kanuni ya Sheria inayosema tendo pekee halitoshi kuweza kumhukumu mtu, lazima liendane na dhamira ovu ya yule aliyetenda, yaani the act alone haitoshi it must be accompanied by blameworthy state of mind na kwa kilatini mnakumbuka mliosoma sheria „actus non facit reum nisi mens sit rea; kitendo pekee hakitoshi. Kwa hiyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi kazi yake ni kuangalia kitendo kiendane vievile na dhamira ovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kuhusu swali la pili la matukio yaliyotokea na kwa nini iliundwa hiyo Mahakama. Mheshimiwa naomba tu nikiri kwamba naliona tatizo la elimu kwa umma hapa, kwamba haijatosha na ndiyo maana pengine huduma hii ya Coroner naona Watanzania wengi hawajaielewa sana. Hili naliona ni tatizo ambalo Wizara yangu sasa nafikiri tutalikazania sana katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba mashauri yanayopelekwa kwa Coroner au kwenye Mahakama hizi yapo, nakumbuka shauri moja ambalo mimi mwenyewe nilihusika ni Shauri Na. 152 la mwaka 2003, lilitokea Mbeya ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi ilikaa chini ya Coroner ya kuweza kupata ufumbuzi wa kitu kilichotokea katika Kituo cha Polisi na matokeo yake yalikuwa mazuri. Ndiyo maana nimesema kwa kweli ni wajibu wa Wizara hii sasa kuuelewesha umma vizuri zaidi kuhusu huduma hii ambayo ipo na hata muuliza swali wa kwanza alidhani kwamba hii mahakama haipo ni huduma ambayo tunafikiria kuianzisha.
MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Kwa kuwa ugonjwa huu wa fistula umeleta athari sana kwa wanawake wakiwemo hata wanawake wa Iringa pamoja na Njombe, kutokana hasa na ukosefu wa vifaa vya kujifungulia na miundombinu migumu sana ambayo wanawake wamekuwa hawavifikii hata vituo vya afya wala zahanati.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanawake kwanza hawajifungulii majumbani na vifaa kuwepo katika zahanati na vituo vya afya hasa vilivyopo katika vijiji vyetu huko ndani kabisa?
Swali la pili, je, Serikali imebaini ni kwa kiasi gani wanawake wameathirika kutokana na ugonjwa huu wa fistula?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu kwanza niseme jambo moja kwa ufupi kwamba ugonjwa wa fistula ni ugonjwa ambao unasababisha kuwepo kwa tundu lisilo la kawaida kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya kutolea haja kubwa.
Jambo la pili ambalo ningependa kulifafanua ni kwamba, ugonjwa huu hausababishwi na laana, kurogwa au mwanamke kutembea na wanaume wengi wakati wa ujauzito. Nimeona niliseme hili kwa sababu wanawake wengi wamekuwa ni wahanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali yake mawili ya nyongeza; kwamba tuna mikakati gani sasa ya kuhakikisha wanawake wanajifungulia katika vituo vya afya. Tulieleza wakati tunawasilisha bajeti yetu hapa, la kwanza ni kwamba tutaendelea kutoa elimu kwa wanawake wajawazito kuhakikisha wanahudhuria kliniki wakati wanapokuwa wajawazito na especially tutahamasisha wale wanawake wa kuanzia miezi miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo tutalifanya ni kuhakikisha kwamba tunaweka huduma za upasuaji wa dharura katika vituo vya afya. Nimesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala huu ambao unaendelea wa bajeti ya Serikali hasa Wabunge wa chama changu, wanawake wa Chama cha Mapinduzi, wameongea kwa sauti kubwa sana kuhusu umuhimu wa kuboresha huduma za upasuaji wa dharura.
Kwa hiyo, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba bajeti ya Wizara ya Afya inayokuja itahakikisha tunaweka vichocheo vya kuwafanya wanawake wahudhurie kliniki na nilishasema, tutatoa vifaa vya kujifungulia kwa wanawake 500,000 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, madhara ya ugonjwa huu wa fistula. Yapo madhara ya kiafya, madhara ya kiuchumi na kijamii. Ya kiafya kama nilivyosema, mwanamke anatokwa na mkojo bila kujizuia, lakini pia haja kubwa inatoka katika njia ya uke. Kwa hiyo, hayo ni madhara ya kiafya na asilimia 85 ya wanawake ambao wanapata fistula wanapoteza watoto.
Mhehimiwa Naibu Spika, madhara makubwa ni ya kiuchumi na kijamii. Wanawake wengi wanaachwa na wanaume wao kwa sababu tu wamepata ugonjwa huo wa fistula, lakini wanawake hawa hawawezi kufanya shughuli za kujiletea maendeleo yao kwa sababu wana harufu, hawezi hata kufungua duka la maandazi au kigenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ambalo nataka kuwathibitishia wanawake, ugonjwa wa fistula unatibika na matibabu yake yanapatikana katika hospitali zetu. Lengo la Wizara ya Afya ni kuhakikisha wanawake hawapati fistula, lakini kama wakipata basi wapate matibabu. Kwa hiyo, katika Hospitali zetu zote za Rufaa za Mikoa tutahakikisha huduma za upasuaji wa matibabu ya fistula zinapatikana. Nakushukuru.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa TASAF III imekuwa ikihamasisha sana hizi kaya maskini kujiunga na Mfuko wa Bima za Jamii (CHF). Je, mpaka sasa ni kaya ngapi zimeweza kujiunga na huu Mfuko huu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa tu niombe uniruhusu niweze kutoa maelezo ya utangulizi kidogo kabla sijajibu hoja yake. Kumekuwa na hoja na watu wengi wamekuwa wakitoa ushauri kwamba katika hizi kaya ambazo zinanufaika na ruzuku hii ya uhawilishaji, walazimishwe kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii.
Kwanza kabisa niseme duniani kote katika taratibu za uendeshaji wa mipango ya uhawilishaji wa fedha katika jamii huwa ni hiari. Kwa hiyo, tunachokifanya sisi kama TASAF ni kuhakikisha kwamba katika kila siku wanapoenda kupokea malipo tunawaelimisha kuhusiana na umuhimu wa kuweza kujiunga na Mfuko huu wa Bima ya Afya. Hadi sasa kaya 54,924 kutoka katika Halmashauri 28 zimeweza kujiunga na Mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato ambayo zaidi ya 90% ya walengwa wake wameshajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya. Nitoe pia pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ambapo 60% ya walengwa wake tayari wameshajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.
Vilevile nitoe pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Halmashauri au Manispaa ya Mtwara pamoja na Kibaha lakini na nyingine nyingi. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge na ninyi pia mtusaidie kuendelea na uhamasishaji ili kuhakikisha kwamba walengwa hawa wanaweza kujiunga ili waweze kupata huduma ya matibabu ya afya pale wanapohitaji. Nakushukuru.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naomba niulize maswali mawili tu ya nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Iringa hasa katika Wilaya za Kilolo, Iringa Vijijini, Isimani, Kalenga na Mufindi, miradi mingi sana ya maji imekuwa haikamiliki kwa wakati na kusababisha wanawake wengi sana hata ndoa zao zimekuwa hatiani kwa sababu ya baridi; wamekuwa wakiamka asubuhi sana kwenda kutafuta maji. Je, ni lini sasa miradi ile iliyopo katika Mkoa wetu wa Iringa, Serikali itafanya kwa uharaka zaidi, pamoja na kuponya ndoa za wanawake wa Iringa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wakandarasi wengi sana wamekuwa wakikamilisha miradi, lakini Serikali imekuwa haiwalipi madai yao kwa wakati. Je, ni mkakati gani umewekwa na Serikali kuhakikisha Wakandarasi hawa wanalipwa kwa wakati ili hii miradi iweze kukamilika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kutoa pole sana kwa wale ambao ndoa zao zimeingia hatiani, mashakani kwa hiyo changamoto ya maji. Naomba niwasihi akinababa kwamba hawa akinamama msiwahukumu katika hilo kwa sababu wanachokifanya ni kuwatafutia maji watoto na ninyi akinababa wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza ni kwamba lini miradi hii itakamilika? Katika vipindi mbalimbali nimeelezea hapa, ni kweli miradi mingi ya maji imechelewa kukamilika kwa muda na watu mnafahamu ile miradi ya World Bank hasa tuliyokuwa tukiitekeleza katika kipindi kilichopita ambayo mpaka sasa tunaendelea nayo, ni kwamba miradi mingi Wakandarasi waliweza kutoa vifaa kutoka site, ni kwa sababu Wakandarasi wengi sana wali-raise certificate lakini walikuwa hawajalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa kama nilivyosema awali, ni kwamba, kwa sababu mwaka uliopita ulikuwa ni wenye changamoto kubwa sana, kwani fedha za miradi hazikwenda vizuri. Kama nilivyosema, katika Serikali hii ya Awamu ya Tano jukumu lake kubwa lilikuwa ni kukusanya kodi na mnafahamu kwamba tokea mwezi wa 12 mpaka hivi sasa, makusanyo ya kodi kila mwezi tumevunja rekodi ukilinganisha na kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana certificate zote zilizokwenda katika Wizara ya Maji, zimelipwa na hata Naibu Waziri wa Maji juzi juzi hapa alikuwa anasema kwamba Mkandarasi yeyote mwenye certificate ambaye anatakiwa alipwe, afikishe haraka Wizara ya Maji pesa hizo zitalipwa. Ndiyo maana wale Wakandarasi wote waliokuwa hawajalipwa mwanzo, sasa hivi wote wamelipwa. Imani yetu kubwa ni kwamba sasa miradi hiyo itakwisha kwa sababu Wakandarasi wote wako site.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madai yao kwamba ni lini yatalipwa? Ndicho nilichokisema hapa katika majibu yangu ya awali, kwamba sasa pesa zote za Wakandarasi wote zimeshapelekwa katika Halmashauri. Tunachohitaji ni kwamba zile certificate ambazo Wakandarasi wamelipa, Wakurugenzi wa Halmashauri wafanye haraka waweze kulipwa pesa zao ilimradi kwamba ile miradi iweze kukamilika na wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua elimu shirikishi kuhusiana na wanafunzi wenye uhitaji maalum, kwa sababu shule yetu ya Lugalo iliyopo katika Mkoa wa Iringa ina wanafunzi ambao wana uhitaji maalum, lakini utakuta hawa wanafunzi hawana vifaa vya kujifunzia wala Walimu hawana vifaa vya kuwafundishia. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na hilo?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na elimu shirikishi na changamoto za elimu maalum, nadhani nimeeleza wazi dhamira ya Serikali ya kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Ritta Kabati pengine anaona mikakati ambayo tumeiweka kwenye bajeti haitaweza kuondoa changamoto mahususi, ambazo ziko kwenye shule katika eneo lake, nimhakikishie kwamba, niko tayari kuongozana naye ili nione matatizo halisi ili tuweze kuyatatua, kwa sababu hiyo ndiyo dhamira ya Serikali.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali yetu ya Manispaa ya Iringa ilifunguliwa ili kupunguza msongamano mkubwa sana uliopo katika Hospitali ya Mkoa, lakini mpaka leo hii Hopsitali hii haina mashine ya X-Ray wala Ultra Sound. Pia hospitali hii imekuwa ikihudumia mpaka wagonjwa wanaotoka Kilolo kwa sababu Kilolo pia Hospitali yao ya Wilaya imekaa vibaya kiasi kwamba wagonjwa wanaotoka kule Kilolo wanakuja kuhudumiwa katika hospitali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba, kama mashine hizi zingekuwepo zingeweza pia kuingiza pesa ili kuzisaidia ziweze kujiendesha. Je, Serikali sasa inaisaidiaje hospitali hii iweze kupata hizi mashine ili iweze kuhudumia wananchi waliopo katika Manispaa ya Iringa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nasema ngoja nilichukue hili kwa sababu katika kuangalia kwa haraka haraka sikuweza kufahamu kwamba mpaka hivi vifaa vya X-Ray bado vina changamoto kubwa, lakini naomba tulichukue hili kwa ajili ya kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea kule Kilolo, nilijua kwamba watu wa Kilolo wote wanakuja kupata huduma pale na nilijua kwamba vifaa vyote vimekamilika. Jambo hili tutalifanyia kazi kwa pamoja ili Hospitali hii ya Manispaa iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wote kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niseme kwamba tutashirikiana kwa pamoja na Mheshimiwa Ritta Kabati pamoja na Wabunge wengine wa huko ili hospitali ile ambayo ni centre kubwa sana ya magari makubwa yanayopita kutoka nchi za jirani kuja Tanzania iwe na uwezo wa kuwahudumia watu kwa kiwango kikubwa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa viongozi, wapo wanaokiuka taratibu za kuanzisha mashtaka katika utumishi wa umma, ikiwemo taratibu za uendeshaji wa mashauri ya nidhamu. Je, Waziri anatoa kauli gani kwa viongozi hao wasiotimiza wajibu wao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati ambaye ametaka kusikia kauli ya Serikali tunasema nini kuhusiana na viongozi ambao wanakiuka taratibu katika uendeshaji wa masuala mbalimbali ya kinidhamu na uchukuaji wa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulie kusema kwamba kumekuwa kuna kauli nyingi kwamba watumishi wa umma wanakatishwa tamaa, watumishi wa umma wanakosa kujiamini na mambo mengine kutokana na hatua mbalimbali za kinidhamu zinazochukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba pamoja na malengo mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano, lengo mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunarejesha nidhamu katika utumishi wa umma, ikiwemo pia kuchukua hatua kwa watumishi wa umma ambao watakiuka sheria, kanuni na taratibu. Endapo mtumishi wa umma yuko katika mstari anatekeleza wajibu wake ipasavyo, sioni ni kwa nini kuwe na hisia au hofu. Niwahakikishie tu kwamba, Serikali yao iko pamoja nao na hakuna ambaye ataonewa bila kufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema mambo yafuatayo:-
Taratibu nzima za kinidhamu zinasimamiwa na Sheria yenyewe ya Utumishi wa Umma, Kifungu cha 23(2), lakini kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kwa mujibu wa Kanuni ya 42, 47 na Kanuni nyinginezo, napenda kusema utaratibu mdogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hatua yoyote ya nidhamu haijachukuliwa ni lazima kuwe na hati ya mashtaka, ambapo mtuhumiwa au mtumishi huyo wa umma atapewa nafasi lakini vilevile katika hati hiyo atakuwa ameelezewa shutuma zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni lazima mtumishi wa umma huyo anayetuhumiwa apate haki au fursa ya kuweza kujibu hati hiyo ya mashtaka ambayo amepatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni lazima iundwe Kamati huru ya uchunguzi ambayo itampa fursa pia mtuhumiwa aweze kujibu au kukanusha tuhuma zilizoko chini yake. Vilevile kwa mujibu wa Kanuni ya 47 Mtumishi huyu wa Umma anayetuhumiwa atakuwa na haki ya kusikilizwa kikamilifu, atakuwa na haki ya kuweza kumhoji mwajiri, atakuwa na haki ya kuweza kuona vielelezo mbalimbali vilivyotumiwa katika kumshtaki. Pia Kamati hii sasa ya Uchunguzi, ziko ambazo zimekuwa zikikiuka taratibu, ni lazima ndani ya siku 30 baada ya kutoa uamuzi wake iweze kuwasilisha ripoti katika mamlaka ya nidhamu na ajira. Baada ya siku 30 tangu ambapo Kamati ya Uchunguzi imewasilisha ripoti yake ni lazima mamlaka ya ajira iweze kumjulisha mtuhumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mtuhumiwa atakuwa hajaarifiwa ndani ya siku husika, basi italazimika kuondolewa mashtaka na atakuwa huru kwa mujibu wa kifungu cha 48(9) cha Sheria ya Utumishi wa Umma. Nazitaka mamlaka mbalimbali za nidhamu kuhakikisha wanatimiza matakwa ya sheria hizi ili wasije wakawasababishia usumbufu watumishi wa umma vilevile wasije wakaisababishia Serikali hasara baadaye.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli katika Mkoa wetu wa Iringa tatizo hili limekuwa kubwa sana. Kwa mwaka 2016 tu zimeripotiwa karibu kesi 221 na kesi zilizopo Mahakamani zilizofikishwa ni 37 tu. Kwa kuwa kumekuwa na ukiritimba mkubwa sana wa kushughulikia hizi kesi, sasa kutokana na ukubwa wa tatizo hilo ni kwa nini Serikali isianzishe Mahakama Maalum ya kushughulikia kesi hizi yaani Sexual Offence Court kama wenzetu South Africa?
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu kama ilivyo Mahakama ya Mafisadi, Mahakama ya Ardhi. Kama jambo hili ni gumu ni kwa nini kesi hizi zisipewe kipaumbele kama kesi za watu wenye ualbino? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa, hili tatizo kwa kweli limekuwa likiwaathiri sana watoto wanaobakwa, wazazi, hata sisi viongozi. Na kesi hizi zimekuwa zikichukua muda mrefu sana na kuathiri ushahidi mzima na mbaya zaidi hawa wenzetu wabakaji wamekuwa wakitumia wanasheria wanapopelekwa mahakamani, lakini hawa wenzetu ambao wamekuwa wakipata hizi kesi wamekuwa hawana uwezo, wengi hawana uwezo wa kuwatumia wanasheria.
Ni kwa nini, Serikali isiweke utaratibu wa kuwapatia msaada wa kisheria waathirika wa tatizo hili, badala ya kutegemea NGO ambazo nyingi haziko huko vijijini?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikiri kabisa kwamba kuna tatizo kubwa siyo tu Iringa, lakini na sehemu zingine za Tanzania. Jana na juzi nilikuwa Mkoani Iringa kujiridhisha mimi mwenyewe kuhusu hali hiyo, nimefika mpaka magerezani.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa takwimu Kitaifa kwa miaka miwili mitatu iliyopita ni kwamba, kila siku ya Mungu kuna matukio 19 ya kubaka na kulawiti hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la matendo haya kwa upande wa Iringa ni kwamba yanatokea katika familia na ndugu, lakini familia hizo tunapopeleka kesi mahakamani ama tunapochunguza wanalindana, hawatoi ushirikiano kwa vyombo vyetu vya upelelezi ndiyo maana kesi nyingi zinachelewa. Hata tukianzisha mahakama hiyo ya Sexual Offences Court or whatever, bado hiyo mahakama itakwama kwa sababu wananchi hawajapata uelewa kwamba, wanavyolindana ndivyo wanazidi kuchochea hayo makosa.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kutoka Mkoa wa Iringa akiwemo Mheshimiwa Msigwa na wengine, naomba tuendeshe kampeni kwa pamoja kuwaomba wananchi wetu, wapiga kura wetu, waachane na mchezo huu wa kulindana katika makosa haya. Otherwise Iringa baada ya muda si mrefu tutakuwa na idadi kubwa ya vijana waliokwishaharibika.
Mheshimiwa Spika, suala la kutoa msaada kwa waathirika hilo liko wazi na leo hii akisoma Mheshimiwa Mbunge Order Paper, nawasilisha hapa Muswada wa Msaada wa Kisheria. Sheria hiyo, nawahakikishia wananchi utawasaidia sana Watanzania, siyo tu waathirika wa vitendo hivi, lakini vilevile wajane, wanawake wanaonyanyaswa wakati wa mirathi, katika ndoa, katika talaka na kadhalika ili tuweze kukidhi matakwa ya Ibara ya 13 ya Katiba ya usawa kwa kila mtu mbele ya sheria. Ahsante.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. Kwa kuwa barabara inayokwenda katika mbuga za wanyama katika Mkoa wetu wa Iringa ni barabara ya kiuchumi pia na Serikali kwa mara ya mwisho nilipouliza swali hilo iliniambia kwamba inafanya upembuzi yakinifu.
Je, ni lini sasa Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo kwa sababu hii barabara tunategemea kwamba kama itakuwa imemalizika, uchumi wa Iringa kutumia utalii utaongezeka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Ritta Kabati pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, walimchukua Waziri wangu wakaenda kuikagua barabara hii na nafahamu aliyowaahidi alipokuwa kule site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuhakikishie, yale ambayo Waziri wangu aliwaelezeni kule site ni lazima tutayatekeleza.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko kwenye Kamati ya Miundombinu; kwa kuwa uwanja huo huo wa Nduli tayari kuna pesa zimetengwa kwa ajili ya ukarabati huo lakini pia mradi huu umeshakubaliwa na wananchi kwa sababu
Serikali tayari ilishakaa na wananchi waliopo katika eneo lile. Sasa naomba jibu kutoka kwa Serikali, kwa sababu kuna wananchi ambao wamekuwa wakiendeleza maeneo ambayo yataguswa sasa ni lini itaweka alama na ili
wasiyaendeleze maeneo yale ili wakati wa kulipa fidia pesa iwe kidogo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ritta Kabati amekuwa akihoji haya masuala ndani ya Kamati ya Miundombimu na mimi niendelee kumpongeza kwa namna anavyochukua hatua kuwatetea wananchi na kuhakikisha kwamba maslahi yao yanazingatiwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kama
ambavyo nimekuwa nikimhakikishia mara nyingi katika Vikao vya Kamati, kwamba kazi hii ya kuweka alama tutaifanya hivi karibuni. Naongelea si zaidi ya miezi mitatu, minne ijayo kazi hii itakuwa imekamilika ili kuhakikisha kwamba wananchi wa pale wanajua mipaka ya maeneo tutakayotumia katika kukarabati na kupanua ule uwanja wa Nduli.
MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa huu udhalilishaji ambao umekuwa ukifanyika na hao wawekezaji siyo katika migodi tu, upo hata katika viwanda vyetu. Nimeshuhudia mara nyingi sana Mheshimiwa Naibu Waziri akienda kusuluhisha migogoro hasa ikihusiana na unyanyasaji wa wafanyakazi. Je, ni adhabu gani kubwa kabisa ambao wamekuwa wakipatiwa hawa waajiri au wawekezaji ambao wamekuwa wakiwanyanyasa hawa wafanyakazi. Kwa sababu nimeona jambo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI,VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwekezaji anayekuja kuwekeza hapa nchini hasa wale ambao wanapitia TIC na wale ambao wamejisajili katika Vyama vya Waajiri. Wamekuwa wakipewa sheria za nchi hii na utaratibu ambao unapaswa kufuatwa na jambo lolote linalojitokeza kinyume chake hapo sisi kama Serikali tumeendelea kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto kubwa sana kwa wawekezaji raia wa China ambao wengi wamekuwa wakiingia nchini na taratibu za kisheria zimekuwa hazifuatwi, lakini wale ambao wamesajiliwa wako chini ya ATE. ATE wamefanya kazi kubwa ya tafsiri sheria za kazi za nchi yetu kwenda katika lugha ya Kichina. Maana mwanzoni wao walikuwa wanatumia excuse ya kutofahamu sheria, ingawa katika principle zile za sheria katika ile maxim inayosema ignorantia juris non excusat, ambayo inasema muhimu kabisa kwamba hakuna excuse kwa mtu ambaye hafahamu sheria. Kwa hiyo walichokifanya hawa waajiri wametafsiri sheria zile, lakini bado kuna watu ambao wanakiuka taratibu hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tamko tu mbele ya Bunge hili kwamba wale waajiri wote hasa wawekezaji ambao wanafahamu sheria za nchi zetu, wanapaswa kufuata utaratibu ambao wanaendelea na unyanyasaji, tutaendelea kuwachukulia hatua stahiki ili kuhakikisha kwamba, tunaondoa dhana hii ya udhalilishaji na unyanyasaji wa wafanyakazi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia adhabu kubwa ambayo tumekuwa tukiichukua ni kwamba, tumekuwa tukiwandoa nchini mara moja wale wote ambao tunawabaini ni wageni wanawadhalilisha Watanzania katika nchi yetu ili tutengeneze kitu kinaitwa deterrence, mtu mwingine yeyote asiweze kurudia kosa hilo.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali moja tu dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, Mkoa wetu wa Iringa una mito kama Ruaha, Mto Lukosi na kadhalika, lakini wananchi wamekuwa wakipata shida sana kwa suala la maji hasa vijijini ikiwepo Kilolo na Mufindi. Ni kwa nini Serikali sasa isitumie mito hii kuondoa huu upungufu ambao upo katika Mkoa wetu wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Iringa una utajiri mkubwa sana wa mito ikiwepo Ruaha Mkuu, lakini bado kuna Ruaha Mdogo, kuna Mto Lukosi ambao unatokea maeneo ya Kilolo. Kutokana na utajiri huo wa kuwa na mito mingi, kwanza kabisa Mto Ruaha Iringa Mjini tumeutumia, maji yanapatikana kwa asilimia 100 katika Mji wa Iringa. Sasa hivi tunaanza kusambaza maji kuyapeleka nje ya Mji wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia Mto Lukosi, nimeenda kule Kilolo, sasa hivi tunafanya utaratibu wa kuhakikisha tunasanifu mradi ili tuweze kutoa maji Mto Lukosi kuyapeleka maeneo yanayopitiwa na huo mto kuhakikisha kwamba maeneo mengi ya Iringa yanakuwa na maji ya kutosha ambayo ni safi na salama.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali tu madogo ya nyongeza. Kwa kuwa tumekuwa tukikaa katika vikao vya Bodi za Barabara mara nyingi sana hasa katika Mkoa wetu wa Iringa, barabara nyingi sana za Halmashauri zetu tunakuwa tukipeleka lakini hazipandishwi daraja. Je, ni vigezo gani sasa vinatumika maana utakuta sehemu nyingine barabara zinapandishwa lakini sehemu nyingine barabara nyingi hazipandishwi madaraja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza pesa kwenye Halmashauri kwa sababu Halmashauri nyingi barabara zake ni mbovu sana ili Halmashauri hizi ziweze kutengeneza barabara zake kwa kiwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vya kupandisha hadhi barabara vimeainishwa katika Sheria ya Barabara pamoja na Kanuni zake kama ambavyo nilisema katika jibu langu la swali la msingi. Vigezo hivyo havijabadilika na kama tutataka kubadilisha tutakuja Bungeni kuvibadilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza fedha; fedha nazo tumekubaliana kwamba Mfuko wa Barabara unagawa asilimia thelathini zinaenda kwenye Halmashauri na asilimia 70 zinaenda kuhudumia barabara za trunk road za mikoa. Sasa kama tunadhani kwamba formular hii kwa sasa labda haitufai bado ni suala la kuamua sisi Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge hili Tukufu ili tuweze kubadilisha zile sheria ambazo tulikubaliana wenyewe.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri alipokuwa anajibu majibu yake alisema kwamba, kwenye miji mikubwa kuna hiyo huduma inatolewa, lakini ukija kwenye miji midogo kwa mfano Iringa kuna vijana wengi sana wameathirika. Lakini tumshukuru sana Dkt. Ngala pale Iringa, ameweza kuhamasisha wananchi wamefungua vituo kama hivi, lakini sasa wananchi wanashindwa gharama imekuwa kubwa sana kwenda kwenye vituo.
Sasa je, Serikali iko tayari kutoa ruzuku kwa watu ambao wamenzisha vituo hivi ili viweze kusaidia kwenye miji midogo kama Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu maswali haya mawili, Mheshimiwa Waziri wa Nchi atamalizia kwa ujumla yanayohusu supply reduction.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kwanza la Mheshimiwa Amina Mollel, kwanza nimpongeze siku ya jana aliniletea wageni kutoka Chama cha Wananchi ambao wanajihusisha na Afya ya Akili Nchini na katika mazungumzo tuliyoyafanya ni pamoja na hili suala la Madaktari Bingwa wa Afya ya Akili kwenye Mikoa nchini. Mkakati tulionao na ndio taarifa niliyowapa wale wananchi wenzetu ni kwamba Serikali ina-scale up huu mkakati wa kuwa na hizi kliniki kama iliyopo Muhimbili, Temeke na Mwananyamala kwa mwaka huu kwenye mikoa kumi ya Tanzania Bara na kwa mwaka ujao tutaongeza mikoa mingine kumi, tunakwenda kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, kila tutakapoanzisha hii kliniki ya methadone ni lazima awepo Daktari Bingwa anayehusika na ku-administrate hiyo dawa kwa sababu methadone inalindwa kwa taratibu maalum za kuitunza na kuitoa kwa wagonjwa. Kwa hiyo, ni lazima awepo Daktari Bingwa anayeweza kufanya hivyo kwa hivyo, kwa mwaka huu nimhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel kwamba tutakuwa na Madaktari Bingwa kwenye mikoa kumi ncjini, pindi kliniki za methadone zitakapoanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni la Mheshimia Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kuhusu hizi kliniki na rehabilitation centres kwenye Mikoa; kwa sasa kweli, tuko Dar es Salaam peke yake, lakini kwenye mkakati wetu tunakwenda kwenye mikoa kumi kama nilivyosema. Na kwenye kila kanda tunakwenda kuanzisha rehabilitation centre ambapo tutakuwanazo nne sasa katika nchji nzima. Kwa hivyo, hii ni mikakati ambayo tunayo katika siku za usoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ruzuku, Serikali haina utaratibu wa kutoa ruzuku kwenye taasisi mbalimbali za binafsi, kwa sababu wao wanafanya kwa hiyari na tunawaomba na kuwatia moyo waendelee kufanya hivyohivyo kwa hiyari, lakini sisi kama Serikali tuna mikakati yetu ya kuwasaidia wenzetu ambao wameathirika na dawa za kulevya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba nijibu maswali ya nyongeza yaliyoulizwa kwa umoja wake, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, kwa majibu mazuri aliyokwishakuyatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tena kwa kulipongeza Bunge letu Tukufu kwa sababu mwaka 2015, ndilo lililosababisha kufanyika kwa mageuzi makubwa ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa kutungwa kwa sheria mpya ambayo imeunda hiyo mamlaka sasa ambayo tumemuona Kamishna Jenerali akifanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na makamishna wenzake kuhakikisha kwamba tunapambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niliarifu Bunge
lako Tukufu Kamishna Jenerali baada ya kuteuliwa na mamlaka kuanza kazi rasmi, ameshahakikisha ametengeneza Mpango Mkakati Maalum wa Taifa wa kuhakikisha kwamba tatizo hili la dawa za kulevya nchini linaondoka. Na mpango mkakati huo unashirikisha pande zote mbili za Muungano, upande wa Zanzibar na upande wa huku Bara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Khatib wala usiwe na wasiwasi, tunafanya kazi hizi kwa pamoja, vyombo hivi vyote viwili vinafanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumegundua kwamba, wenzetu wa private sector wanafanya kazi nzuri sana kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini. Na hivyo nichukue nafasi hii kwanza niwapongeze wale wote ambao wameamua kujitolea kusaidiana na Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania, tunawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mwaka huu wa bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu imeamua kuweka bajeti kidogo ambayo itasaidia kushirikiana na hao wenzetu ambao wameonesha kwamba, wana nia ama ya kuanzisha sobber houses kwa ajili ya kuwasaidia hawa walioathirika na dawa za kulevya, lakini vilevile kufanya kampeni na kuleta uhamasishaji mkubwa wa kuwasaidia vijana wetu kuwaondoa kwenye tatizo hili.
Kwa hiyo, tuko pamoja tunafanya kazi hii kwa pamoja, mapambano yanaendelea na tunataka kuona kwamba tunaondoa tatizo hili katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza na nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake. Pamoja na Serikali kukiri kuwa zao la mbao linachangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa nchini, lakini barabara zinazoingia katika maeneo ya misitu ni mbovu sana na hazipitiki hasa wakati wa mvua. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka lami katika maeneo hayo ambako mbao hizo zinavunwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa serikali imekuwa ikimuuzia mwekezaji wa nje (MPM Mgololo) nusu bei ya magogo, je, iko tayari sasa kuwauzia wajasiliamali wetu bei sawa na hiyo ili kuitikia wito wa uchumi wa viwanda. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Ritta kwanza kwa kuonesha nia na dhamira ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuendeleza viwanda nchini na hasa viwanda vinavyopata malighafi yake kupitia misitu; lakini pia nijibu maswali yake ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza la uboreshaji wa miundombinu ya barabara. Kwanza ni jambo ambalo hata upande wa Serikali ni la interest, kwamba maeneo ya mashamba yaweze kupitika kirahisi kwa ajili ya kuweza kuyahudumia mashamba yenyewe. Hata hivyo kuhusiana na suala la barabara zainazokwenda kwenye mashamba yenyewe ambazo zipo kimsingi chini ya Halmashauri ya Wilaya, barabara za makundi haya mawili zinashughulikiwa kwa namna tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi barabara ambazo zipo chini ya Halmashauri; katika Halmashauri ambazo zina mashamba Serikali inachokifanya ni kuweza kuchangia nguvu na uwezo wa kuweza kuhudumia barabara hizo kupitia uazimishaji wa mitambo mbalimbali ya ujenzi wa barabara. Mahali ambapo Serikali za Halmashauri zenyewe huweka mafuta kwenye mitambo hiyo na kuwezesha ujenzi wa barabara hizo. Serikali itaendelea kutumia njia hiyo ili kuweza kuhakikisha kwamba barabara hizo zinaendelea kuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa barabara za ndani, tutaendelea kuziboresha kama ambavyo tunaendelea kufanya. Nimshauri tu Mheshimiwa Ritta kwamba haiwezekani kufanya barabara hizo zikafikia kiwango cha lami kwa sasa kwa sababu ya majukumu mengine ya Serikali ya uendelezaji wa miundombinu katika maeneo mengine, hizi za mashambani zitakuwa bora lakini katika kiwango hicho hicho cha barabara za udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la mwekezaji wa Kiwanda cha Karatasi pale Mgololo (MPM); suala hili ni pana, kubwa na la kina na Serikali mara kwa mara imekuwa ikitoa maelezo kuhusu suala hili la mwekezaji huyu ambaye historia yake ni ndefu inaanzia wakati wa Sera ya Ubinafsishaji ya Taifa huko miaka ya nyuma. Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa maelezo ninayoweza kuyatoa hapa kwa sasa hivi ni kwamba kwanza ieleweke kwamba miti ambayo ilikuwa inauzwa au ambayo inauzwa kwa mwekezaji ni magogo yanayotokana na miti ambayo ni ya umri mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, umri wa uvunaji wa miti
kwa ajili ya bidhaa ya mbao ni miaka 25 na zaidi, lakini magogo haya ambayo yanauzwa kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa ambayo inakwenda kuwa malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa karatasi inayoitwa pulp ni miaka kuanzia 14.
Kwa hiyo, si magogo yale yale ambayo anauziwa mwekezaji huyu ambayo wanauziwa wazalishaji wa mbao katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ninachoweza kusema ni kwamba, kwa sababu ya kina cha maelezo katika suala hili, Mheshimiwa Waziri ameandaa maelezo ya kutosha kwa kirefu kuhusiana na suala hili kwa sababu ya kupokea hoja mbalimbali kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo hayo na Mheshimiwa Ritta Kabati kwa kuwa ameungana na wananchi wa maeneo hayo kutaka kujua ni namna gani wananchi wananufaika zaidi na Taifa linanufaika zaidi basi muipe fursa Serikali tuweze kupata nafasi Mheshimiwa Waziri atakuja kutoa maelezo ya kina zaidi katika wakati ambao ataweza kutoa maelekezo.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukurru sana. Naomba tu nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze na kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuhakikisha kwamba kaya maskini angalau zinaweza kunufaika na huu mpango wa TASAF na kwa kweli katika mkoa wetu kaya nyingi zimeweza kunufaika na mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Manispaa yetu ya Iringa ambayo ipo Jimbo la Iringa Mjini tuna mitaa 192 na mitaa 98 tu ndiyo ambayo imeweza kunufaika na mpango huu na kuna mitaa 84 ambayo bado haijaweza kufikiwa kabisa na mpango huu wa TASAF; kwa mfano kwenye Kata ya Nduli kuna mitaa ya Kisoeyo, Mikoba, Kilimahewa, Mgongo na Njiapanda na kwenye Kata ya Kituli kuna mtaa wa Hoho; Kata ya Mkwawa kuna mtaa wa Mosi. Je, ni lini Serikali sasa itazifikia kaya hizi maana hali ya kaya katika mitaa hii ni mbaya kuliko hata zile ambazo zimeweza kufikiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nina swali lingine la pili. Kwa kuwa zipo kaya ambazo ni maskini na pia zina watoto wenye ulemavu. Kwa mfano katika Mkoa wetu wa Iringa kwenye Jimbo la Kilolo, Kijiji cha Lulanzi, kuna kaya ambayo ina watoto wanne, wote wana ulemavu na baba yao amepooza, mama yao sasa hivi amevunjika mguu. Je, katika mpango huu Serikali inawasaidiaje watu ambao tayari ni maskini na hawawezi kufanya kitu chochote katika kuwasaidia ili waweze kupata miradi? Kwa mfano labda kujengewa/kuwekewa mradi wa kisima ambao wanaweza wakauza maji wakiwa pale pale au wakapewa bajaji ili kuweza kunusuru kaya ambazo ni walemavu halafu ni maskini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niseme Serikali inakubali kwamba ni kweli si vijiji vyote, mitaa, kata na shehia nchini mwetu zimeweza kufikiwa na mpango huu wa TASAF. Ni takriban asilimia 70 tu kama nilivyoeleza ya vijiji, kata, shehia 9,989 ndiyo imefikiwa.
Napenda tu kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa tumeanza taratibu, tunasubiri tu fedha zitakapotoka tuweze kuendelea na zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha walengwa liweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sasa hivi tuko katika mpango tuliokuwa tunamalizia kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAf ambayo itamalizika mwaka 2018 kuelekea 2019; na sasa hivi tumeanza kusanifu awamu nyingine na tunaamini pia katika zoezi hilo nalo pia tutaendelea kufanya utambuzi na kujua program itakuwaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi tu fedha zitakapopatikana tutaweza kuendelea na zoezi la utambuzi wa walengwa na kuweza kuwaandikisha. Vile vile tutakapoendelea katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF tunaamini walengwa wataweza kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumzia kaya za watu ambao ni maskini ambao unakuta ni watu wenye ulemavu. Nipende tu kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati program hii ya TASAF awamu ya tatu inasanifiwa, suala zima la ulemavu halikuwa kigezo, kigezo kilikuwa ni umaskini lakini pia walikuwa wanaangalia umaskini wa kaya nzima kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika aina za ruzuku ambazo zinatolewa, ruzuku ya kwanza kabisa ambayo inatolewa bila hata masharti ya kuangalia kama familia ina watoto ilikuwa inatolewa kwa kaya nzima. Hata hivyo, nipende kusema, endapo kaya hiyo ina watu wenye ulemavu ambao wako chini ya miaka minane walikuwa wanakuwa treated au wanahesabiwa kama watoto wengine katika familia hiyo kwa mujibu wa ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa familia ambazo tumezikuta zina ulemavu wamekuwa wakishirikishwa katika miradi mbalimbali ya ajira ya muda. Hata hivyo, bado kama alivyoeleza yeye tulipata changamoto, ziko familia ambazo unakuta zina watu ambao wamezidi miaka 18, hata wakipewa ajira ya muda wengine ni mpaka wabebwe na hawawezi kufikia katika hiyo miradi mbalimbali. Niseme tu, tumelipokea na sasa hivi tunaposanifu awamu ya tatu ya mradi huu tutaendelea kuliangalia; kwamba katika awamu nyingine ni nini kifanyike kwa ajili ya watu wenye ulemavu lakini pia kwa sasa tunaangalia tunaweza tukawasaidiaje. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, naomba kuuliza maswali tu madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa jibu katika swali langu la msingi linakiri kuwa kumbukumbu na hukumu katika Mahakama za Wilaya hadi Mahakama ya Rufani ni kwa Kiingereza. Je, Serikali haioni kuwa kumbukumbu na hukumu katika lugha ya kigeni yaani Kiingereza ni kikwazo kikubwa kwa mwananchi anayetaka kukata rufaa kwa kupata haki yake?
Swali la pili, kwa kuwa kauli mbiu ya Serikali ni haki sawa kwa wote na kwa wakati, lakini tumekuwa tukishuhudia Mahakama zikijitahidi kumaliza kesi zake, lakini hukumu zinakuwa zinapatikana kwa kuchelewa sana, hali inayopelekea wengine kutokukata rufaa kwa wakati na walioko gerezani kuendelea kuteseka gerezani.
Je, Serikali inatoa kauli gani? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kukubaliana na Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba ana hoja ya msingi, lakini nikumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tuliamua mwaka 1964 kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa, vilevile Kiingereza kuwa lugha ambayo tunaitumia katika shughuli za Serikali. Ni kama Mheshimiwa Baba wa Taifa alivyosema kwamba Kiingereza ndiyo Kiswahili cha dunia.
Kutoka 1964 mpaka sasa tumeweza kufanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha kwamba tunakiingiza Kiswahili katika mfumo wa Mahakama bila kupotosha utoaji haki.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni suala la utumiaji wa Kiswahili kwa kumbukumbu, kwa hukumu, kwa uendeshaji katika Mahakama za Mwanzo ambao umefanikiwa sana. Hatujaona kabisa miscarriage of justice pale.
Mheshimiwa Spika, pili Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ambayo mwanzoni ilikuwa inaitwa TUKI (Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili) chini ya Profesa Mlacha, iliweza kushirikisha Baraza la Kiswahili la Tanzania pamoja na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa Sheria, nilikuwepo mimi pamoja na Marehemu Profesa Joan Mwaikyusa, Mungu aiweke roho yake pema, peponi, tukaweza kutoa Kamusi ya kwanza ya Kiswahili ya Kisheria, yote haya ni maandalizi.
Mheshimiwa Spika, tatu, kila Muswada wa Sheria leo hii ukiletwa hapa Bungeni na sheria zenyewe, lazima ije kwa Kiingereza na Kiswahili na hilo wewe mwenyewe umekuwa ukisisitiza sana.
Mwisho BAKITA imeshakusanya sasa hivi Istilahi zaidi ya 200 za kisheria ambazo zinasubiri tu kusanifishwa (standardize). Kwa msingi huo, Mahakama yetu ambayo ni chombo huru katika Katiba yetu ni Muhimili unaojitegemea, una msingi sawa wa kutosha tuweze kupanua wigo wa matumizi ya Kiswahili katika kumbukumbu na hata kutoa hukumu hata kwenda Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi kwa kuanzia.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Kabati kwamba tunachoepusha hapa ni kukurupuka tu kuingia na kutumia Kiswahili ilikuwa tu ni kuepusha utata katika nyaraka zetu, ambiguities na kuwa equivocal, kuwa na utata katika utafsiri nyaraka za Kimahakama, ndiyo maana tumekwenda polepole sana.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, nakubaliana naye kwa kweli haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa, lakini ni kweli vilevile kuwa haki iliyowahishwa sana mara nyingi hukosa umakini. Kesi nyingi zinachelewa hasa za jinai kumalizika si kwa sababu ya Mahakama lakini kutokana na mchakato mzima wa utoaji haki. Kwa mfano, suala la upelelezi huchukua muda mrefu sana, na inachukua muda mrefu si kwa sababu vyombo vyetu vya dola havifanyi kazi, lakini kuna tatizo la kutopata ushirikiano mzuri kwa mashahidi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Iringa anakotoka Mheshimiwa Kabati, tuna kesi nyingi sana, sana za makosa ya kujamiiana na yanatokea ndani ya familia, kupata ushahidi mle ndani ni kazi kubwa kweli na ndiyo maana tunatoa wito kwa wananchi wote kushirikiana na vyombo vya dola pale inapotokea kosa, kusaidia katika ushahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kwamba, uthibitisho wa makosa mengine unahitaji Mkemia Mkuu achunguze na atoe jibu, inachukua muda mrefu, Mkemia Mkuu anaweza kuwa na mafaili 3000 ya uchunguzi na yote yanahitaji kwenda Mahakamani, kwa hiyo kazi ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la mwisho ni uhitaji wa kisheria kwamba kila kosa lazima lithibitishwe beyond reasonable doubt yaani pasipo na wasiwasi wowote. Sasa hiyo hatuwezi kulikwepa ili kuweza kulinda haki za kila mtu.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la msingi linafanana kabisa na tatizo tulilonalo katika Hospitali yetu ya Mkoa, karibu asilimia 85 ya Madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa wanaishi nje kabisa ya hospitali ile na kusababisha wagonjwa kupata matatizo makubwa wanapokuja usiku kwa ajili ya matibabu. Tatizo kubwa lililoko katika Hospitali ya Mkoa kuna mwingiliano wa Magereza na Hospitali. Tulishauri mara nyingi kwamba Waziri wetu wa Afya pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani waweze kukaa pamoja waone kwamba lile gereza liweze kutoka ili madaktari wengi waweze kukaa karibu na Hospitali ile ya Mkoa ili kusaidia wagonjwa wanaofika hata usiku.
Je, ni lini sasa ombi hilo la Mkoa litaweza kutekelezeka ili wananchi wa Iringa waweze kupata haki ya kupata madaktari wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Kabati kwa sababu wiki mbili zilizopita tulikuwa pale Iringa tukaenda mpaka Kilolo na miongoni mwa mambo tuliyopitia katika sekta ya afya kipindi cha nyuma tulifika mpaka Hospitali ya Frelimo kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma. Kwa jambo hili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu Waziri wa Afya na Waziri wa Mambo ya Ndani wameshakaa tayari ku-discuss jambo hilo, usihofu kila kitu kitaenda vizuri lengo kubwa ni tuweze kuwapatia huduma wananchi wetu vizuri. Kwa hiyo, hilo jambo ondoa hofu kila kitu kitaenda vizuri Serikali itashughulikia.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo tu la nyongeza.
Kwa kuwa uhaba wa Maafisa Ugani uko sawasawa kabisa na uhaba wa wataalam wa mifugo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Mifugo wa kutosha ili wananchi wasaidiwe haki katika Halmashauri zetu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itashughulikia tatizo la uhaba wa Maafisa Ugani sambamba na tatizo la Maafisa wa Mifugo.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili na nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake.
Je, Serikali inasaidiaje kufuatilia wafanyakazi wahamiaji nchi za Uarabuni na kwingineko ambako wanateseka bila kuridhia mkataba huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitafutiwa kazi kupitia hizi wakala za ajira (Employment Agency), lakini kumekuwa na malalamiko ya kupunjwa haki zao.
Je, Serikali inachukua hatua gani ili kulinda haki za wafanyakazi ambao wanapata ajira zao kupitia wakala hawa, pamoja na madalali ambao wamekuwa wakiwatafutia wafanyakazi wa majumbani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya kwamba tuendelee kuangalia mazingira bora ya namna ya ku-ratify mkataba huu hasa pale ambapo kama nchi tutakuwa tumejiridhisha kwamba, mazingira ni rafiki na hivyo kuusaini mkataba huo ambao utasaidia sana katika kulinda haki za wafanyakazi wa ndani, lakini vilevile ambao wanatoka nje ya nchi, kwa maana ya Watanzania.
Mhweshimiwa Mwenyekiti, la pili la kuhusu Wakala wa Ajira; kama nilivyokuwa nikijibu katika maswali mengine ambayo yamewahi kuulizwa katika eneo hili, ni kwamba pale katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira, ipo taasisi ambayo inashughulikia masuala ya ajira kwa maana ya wakala wa ajira ambaye anaitwa TaESA. Na rai yetu ilikuwa ni kwamba, wafanyakazi wote wa kitanzania ambao wanakwenda kufanya kazi nje ya nchi ni lazima wapitie TaESA, ili tuwatambue tujue na katika nchi ambazo wanakwenda. Tumefanya hivyo kwa sababu wakienda katika njia ambazo si sahihi, sisi kama Wizara si rahisi sana kuweza kufahamu akina nani wako wapi na ndio maana tunawataka kwamba wote wapitie katika ofisi zetu na sisi huwa tunaongea na Balozi husika, ili waweze kushughulikiwa matatizo pale wanapopatwa na matatizo nje ya nchi, ikiwemo ukosefu wa mikataba na haki nyingine.
MHE. RITTA A. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna baadhi ya wazazi au walezi hasa katika Majiji kwa mfano Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakiwatumia watoto wadogo kuomba omba hata kule kwenye magari, tumekuwa tukishuhudia na nimeona katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wazazi kama hao wanatakiwa wachukuliwe sheria/ hatua, kwa sababu watoto hawa wanakosa haki yao ya msingi na wakati elimu ni bila malipo.
Je, ni nani sasa anawachukulia hatua wale wazazi au walezi ambao wanawatumia watoto katika kuomba omba kwenye magari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2008 mtoto hana haki zake kama tano. Mtoto ana haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushirikishwa na pia mtoto hana haki ya kutobaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba mtoto kama nilivyoainisha katika haki zake za msingi, ni jukumu la kwetu sisi wazazi, walezi, jamii na Serikali katika ngazi ya Mitaa na Serikali Kuu kuhakikisha kwamba mtoto anapata haki zake zote hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kabati alikuwa ameelekeza swali lake katika Mkoa wa Dar es Salaam, tuna mikakati mbalimbali ambayo tunaendelea nayo kuhakikisha kwamba watoto wale wa mitaani wanapata haki zao stahili pamoja na kuondolewa katika mitaa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza kabisa nianze kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa mapokezi makubwa kabisa ya ndege ya Bombadier ambayo jana ilitua na Mheshimiwa Rais akiwa anaongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili pia niipongeze Serikali kwa kuanza sasa kujenga kiwanja chetu cha Nduli kwa sababu nina imani kabisa sasa hata utalii utafunguka katika Mkoa wetu wa Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ndege ya Bombadier ina uwezo wa kutua katika kiwanja chenye urefu wa kilometa 1.2 na kiwanja chetu cha Nduli kina urefu wa kilometa 1.6, tatizo ni kipande tu kidogo cha mita kama 100 ambacho ni kibovu sana ambacho hakiwezi ndege kubwa kutua na hata zile ndege ndogo ambazo zinatua, zinatua kwa matatizo makubwa sana na mpaka sasa hivi kiwanja chetu kina abiria karibu 20,886,000. Je, Serikali sasa haioni umuhimu sasa wa kujenga hicho kipande kidogo cha mita 100 ili tuweze kupata ndege kubwa na hizo ndogo zipate kutua vizuri wakati tunasubiri huo ujenzi wa kiwanja hicho, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; nimesikia tayari zoezi la uthamini wa mali limeshaanza katika kiwanja chetu cha Nduli. Hofu yangu kubwa ni kwamba zoezi hili huwa linafanyika mapema kabisa lakini huwa linachukua muda mrefu sana kwa wananchi kulipwa mali zao, nina mfano halisi kabisa wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho toka mwaka 2010 karibu miaka nane bado hawajalipwa na vilevile hata barabara yetu ile ya mchepuo ilichukua karibu miaka sita mpaka wananchi kuanza kulipwa. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa wananchi hawa ambao wanapisha hiki kiwanja wanalipwa mapema zaidi? Mheshimiwa Naibu Sika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nizipokee pongezi nyingi ambazo amezitoa kwa kupokea ndege ambayo jana Mheshimiwa Rais ameipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia uboreshaji wa kiwanja hiki, amekuwa akifuatilia na mimi binafsi nilifika kuona hali ya uwanja. Suala la kwanza ambalo amelizungumzia juu ya kuongeza urefu wa kiwanja. Ilikuwa imetengwa shilingi bilioni 47 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja hiki lakini kwa bahati nzuri tumepata fedha kwa udhamini wa Benki ya Dunia tutakwenda kujenga kwa thamani ya shilingi bilioni 94.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha kwamba huduma nyingi katika uwanja huu zitakuwa zimeongezeka. Hii ni pamoja na kuweka taa za kuongozea ndege, kuongeza urefu wa uwanja na sasa huu uwanja pamoja na taa zitakapowekwa utakuwa na urefu wa mita 2,500 kwa maana utaweza kumudu kiwango hiki ambacho Mheshimiwa Mbunge anaomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge, wananchi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla tuvute subira, tunaenda kuboresha huu uwanja utakwenda kuwa wa kisasa pamoja na kuweka majengo, jengo la abiria pamoja na jengo la wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni ushahidi tosha kwamba sasa hivi compensation hazichelewi kulipwa. Viko viwanja ambavyo vinaendelea kujengwa kule Shinyanga, compensation imelipwa lakini uthamini umeshakamilika, tunaendelea kuhakiki wenzetu wa Wizara ya Fedha wanahakiki umethaminishwa kama Sh.3,043,626,000 kwa ajili ya kulipa compensation. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge uvute subira, uhakiki unafanyika na mara uhakiki ukikamilika fedha hizi zitalipwa kwa wananchi. Kwa hiyo, wananchi wasubiri kulipwa compensation yao. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwamba hii Awamu ya Tano imeagiza kwamba hii mifuko ya hifadhi ya jamii iweze kuwekeza katika viwanda na katika hivi vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wetu, alipokuja Mkoani Iringa katika ziara yake, alitembelea kile kinu chetu cha National Milling na aliahidi kwamba NSSF ingeweza kutoa mtaji ili kiweze kufanya kazi vizuri, pamoja na kutoa ajira nyingi kwa wananchi wa Iringa. Sasa nataka tu kujua: Je, agizo lake lile limeshafanyiaka? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi anavyojibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge vizuri sana ndani ya Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba nchi yetu inaingia katika uchumi wa viwanda na hivyo basi Serikali kwa makusudi mazima imeiagiza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ianze sasa kuhakikisha na yenyewe inaunga mkono nguvu za Serikali na mpango wa maendeleo wa Serikali wa kuingiza nchi yetu kwenye uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha wanafufua baadhi ya viwanda ambavyo vilikuwa vimekufa na kuanzisha viwanda vingine vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Rita Kabati, kwa karibu sana amefanya kazi na Serikali kwa kupitia Mfuko wa NSSF kuhakikisha kinu cha National Milling pale Iringa kinafufuliwa na kinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Dada Ritta Kabati kwamba NSSF kwa kushirikiana na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wameshafikia hatua nzuri ya ununuzi wa mashine na vifaa vinavyotakiwa katika kufufua kinu chetu cha Iringa. Baada ya muda siyo mrefu, uzalishaji utaanza kwa nguvu sana na ajira zitaongezeka na hivyo basi, wananchi wa Mkoa wa Iringa na Mji wa Iringa wajue kwamba Mbunge wao amefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kushirikiana na Serikali na Mfuko wetu wa NSSF na Mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii, tuna mpango wa kufungua viwanda visivyopungua 25 na kuongeza idadi ya ajira zisizopungua 200,000 katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali. Kwanza niipongeze Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiifanya katika nchi hii. Hivi karibuni kulikuwepo na zoezi la uhakiki wa vyeti feki na katika uhakiki huo kuligundulika kwamba kuna vyeti feki katika taasisi nyingi na kusababisha sasa kuwepo na upungufu mkubwa sana katika taasisi mbalimbali na hasa katika hospitali zetu na Halmashauri zetu. Sasa napenda kujua je, ni lini sasa zoezi la kuziba zile nafasi ambazo wale wenye vyeti feki wameondolewa zitaweza kuzibwa ili kusaidia wale wafanyakazi waliopo wasifanye kazi kwenye mazingira magumu sana? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia ustawi wa watumishi lakini pia kwa namna ambavyo anafuatilia upungufu huu uliojitokeza wa watumishi kutokana na zoezi lililoendeshwa la wenye vyeti feki.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba, tumekuwa tukieleza humu ndani tayari kibali kimeshatolewa cha ajira 15,000. Tulikuwa tunafanya mashauriano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, wameshatuletea orodha maana yake ilikuwa ni lazima tujue katika kila kituo ni nafasi ipi ambayo iko wazi.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba katika maeneo ambayo yameathirika sana ni sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya kwa zaidi ya asilimia 70 na zaidi kidogo. Pia kwa sekta ya afya tu peke yake zaidi ya watumishi 3,360 wamekumbwa katika zoezi hili. Nimweleze tu kwamba tayari tumeshaanza mchakato huo na muda si mrefu nafasi hizo zitazibwa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo tu la nyongeza japokuwa kidogo linafanana na muuliza swali aliyepita. Ili kurahisisha ukusanyaji na ulipaji kodi ni kwa nini TRA isiweke vituo katika kila Halmashauri ya Wilaya ili kupunguza usumbufu mkubwa wanaopata walipa kodi? Kwa mfano, ukichukulia Mkoa wetu wa Iringa, jiografia yake ni mbaya sana inawasabisha hata watu wengine kukwepa kodi kwa sababu tu vituo vya TRA viko mbali sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi na hakuna Taifa lolote linaweza kuendelea bila kukusanya mapato, tunafahamu kabisa hilo kama Wizara yenye mamlaka ya ukusanyaji wa mapato Tanzania. Hili la kuanzisha ofisi kila Halmashauri, nilishawahi kujibu ndani ya Bunge lako Tukufu kwamba kuanzishwa kwa ofisi huwa kuna tathmini ambayo huwa inafanyika kuangalia cost and benefit analysis ya kuanzisha ofisi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mbunge, tutafanya uhakiki na tathmini hiyo kujua kama kuna uhitaji mkubwa wa kuweka ofisi hizi katika kila Halmashauri ndani ya Mkoa wa Iringa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mwuliza swali alikuwa anauliza kuhusu ukarabati wa kituo, lakini kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ni ya siku nyingi sana na haijawahi kujengewa Makao Makuu ya OCD yalipo Makao Makuu ya Wilaya toka imeanzishwa, na kufanya OCD kukaa mbali na DC. (Makofi)
Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kujenga Makao Makuu ya Polisi yalipo Makao Makuu ya Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni sahihi kabisa, Kilolo hatuna Kituo cha Polisi cha Wilaya na hii ni moja ya vituo 65 vya wilaya nchini ambavyo hatunavyo na ambavyo vipo katika mpango wa Serikali wa kuvijenga. Kwa hiyo, Kilolo ni kimojawapo.
Mheshimiwa Spika, wakati jitihada hizi za Serikali za kuweza kuona jinsi gani tunafanya kujenga vituo 65 zinaendelea, basi nataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya ziara katika Mkoa wa Iringa hivi karibuni ili tushirikiane tuangalie namna gani nyingine ambayo tunaweza tukafanya ili kuweza kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali yetu ya Wilaya iliyopo katika Manispaa ya Iringa ilifunguliwa ili kupunguza msongamano mkubwa uliyopo katika hospitali ya mkoa, lakini hospitali ile mpaka sasa hivi haina jengo la vipimo, haina wodi za wagonjwa wengine ina wodi za wazazi na hospitali ile imekuwa ikisaidia wagonjwa wanaotoka katika Wilaya ya Kilolo, Iringa DC na kwingineko; na Mheshimiwa Jafo tunamshukuru alifika; je, Serikali sasa inasaidiaje pamoja na kuwa imetoa pesa kwa ajili ya kujenga hospitali za wilaya nyingine wakati bado hazijajengwa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba ukienda Manispaa ya Iringa na kwa kuanzia hospitali ya mkoa ina wagonjwa wengi sana, ndiyo maana Serikali katika kuhakikisha kwamba tunapunguza mlundikano wa wananchi kwenda kutibiwa katika hospitali ya mkoa, ikawa ni wajibu kuhakikisha kwamba inajengwa hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama anavyotoa maelezo kwamba ile hospitali ya wilaya haijakamilika kwa kiwango ambacho kilitarajiwa, naomba nimhakikishie, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba hospitali zote za wilaya ambazo zinajengwa zinakuwa katika kiwango ambacho tunakitarajia ili mwananchi akipata rufaa kutoka kituo cha afya akienda kutibiwa kwenye hospitali ya wilaya apate matumaini kwamba nimefika katika hospitali ambayo hakika kwa majengo na huduma ataweza kupona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie, kwa kadri bajeti itakavyokuwa imeruhusu tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba suala la afya ni kipaumbele kama Serikali ilivyoelekeza.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza nianze kumshukuru Waziri kwa majibu yake, lakini naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huu mradi ni muhimu sana na una tija sana katika manispaa yetu na ni mradi ambao kwa kweli toka mwaka 2008 umeanzishwa na ni chanzo kizuri sana cha mapato kama ambavyo amesema kwenye jibu lake. Pia tulikuwa tunategemea kwamba kama ungekamilika, ungeweza kutoa ajira zaidi ya 200 katika Manispaa na katika Mkoa mzima wa Iringa. Katika majibu yake, Serikali bado haijatoa commitment ya mradi huu kwa sababu tulikuwa tunategemea kwamba kama mradi huu ungekamilika kwa wakati…
Je, hiyo pesa ambayo inahitajika katika mradi huu Serikali inaji-commit vipi maana ni mradi ambao tunategemea kwamba utaweza kusaidia hata miradi mingine katika manispaa yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kwanza nimpongeze Balozi wa Comoro, Mheshimiwa Mabumba kwa sababu aliweza kuwaalika wafugaji wanaotoka Tanzania kwenda kuona fursa zilizoko katika nchi ya Comoro na kwa kweli tuliona kuna soko kubwa sana la nyama, ng’ombe na la mbuzi. Je, Serikali sasa inawasaidiaje wafugaji kuunganishwa na masoko hayo katika nchi hiyo ya Comoro au nchi nyingine ili iweze kuleta tija katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza amezungumzia juu ya commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba mradi huu wa machinjio ya Manispaa ya Iringa unaweza kupata pesa na hatimaye unakuwa ni chanzo cha mapato cha Halmashauri na kuzalisha ajira. Nimpongeze sana Mheshimiwa Ritta Kabati kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya watu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yeye mwenyewe Mheshimiwa Ritta Kabati unafuatilia vizuri ataona kwamba hivi sasa Serikali imekuwa ikifanya miradi ya kielelezo ya kusaidia Halmashauri zetu ziweze kujizalishia kipato chao wao wenyewe. Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyokwishaianza kwa ajili ya Maispaa za Mkoa wa Dar es Salaam na kwingineko katika Taifa letu. Zimetolewa pesa nyingi kwa ajili ya miradi ya kielelezo ikiwemo ya machinjio kama machinjio ya Vingunguti imepata pesa nyingi ili iweze kufanya vizuri na kuwa na tija. Nina imani kwamba baada ya kumaliza Dar es Salaam vilevile Serikali inaweza ikafanya kazi ya kuelekea katika maeneo mengine ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza juu ya namna sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tulivyojipanga katika kuhakikisha wafugaji wetu wanapata masoko. Kama Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine watakuwa wafuatiliaji wazuri wataona kazi kubwa tunayoifanya. Katika kuhakikisha tunatangaza mifugo yetu na tunapata soko nje sisi katika Wizara tuna Idara inayoitwa Idara ya Huduma za Mifugo na Masoko na tunayo Bodi ya Nyama ambayo kazi yake ni kutafuta masoko nje ya nchi na kuitangaza nyama yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunatoa ushauri na kuangalia ubora wa nyama yetu ili iweze kupata masoko nje. Kusema ukweli hivi sasa tumekuwa tukipata masoko makubwa sana. Katika mwaka wa 2004 tulikuwa tunauza tani zisizozidi tatu, mwaka wa 2016/2017 tumeuza zaidi ya tani 1,000 za nyama nje ya nchi kutoka Tanzania. Mkakati wetu ni kuhakikisha tusiingize nyama ndani ya Taifa letu, badala yake sisi tuwe na uwezo wa kutoa nyama nje ya nchi. Kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge, watuunge mkono kuhakikisha jambo hili kama Wizara tunaendelea nalo na tunaweza kufanikisha ajenda yetu ya Tanzania ya Viwanda hasa ile inayohusu mazao yetu ya nyama na samaki.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika Mkoa wetu wa Iringa kuna magari ambayo huwa yanaharibika tu kidogo yanawekwa katika vituo lakini tumekuta kuna mlundikano mkubwa sana wa magari mabovu. Ni kwa nini Serikali sasa aidha itengeneze au iyauze haraka sana ili yaweze kusaidia upungufu mkubwa ulipo katika Mkoa wetu wa Iringa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Ritta kwa wazo alilotoa. Niseme tu kama Serikali tunapokea ushauri huo, tutayatengeneza yale yanayotengenezeka na tutafanya utaratibu wa kuyauza yale yasiyoweza kutengenezeka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu maoni yako upande wa pikipiki nilishatoa maelekezo kwamba vijana wa bodaboda wanaokamatwa kwa makosa madogo madogo wafanyanyiwe utaratibu wa kuandikisha na kuruhusiwa waendelee na kazi zao ili waweze kulipia kama kuna faini ambazo walitakiwa kulipa kuliko kuzirundika pikipiki hizo na zingine kuweza kuharibika wakati wangeweza kulipia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, juzi sikukuona pale Uwanja wa Taifa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kwenda pale kwa sababu kwa kweli kwa matokeo yale kama Rais asingekuwepo viti visingebaki salama. (Makofi/ Kicheko)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza, lakini kabla sijauliza nilikuwa naomba nisahihishe jina langu, naitwa Ritta Enespher Kabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na mpango wao kabambe wa umwagiliaji, naomba nimwulize maswali mawili.
Kwa kuwa mradi huu wa Mkoga umekuwa ni mradi wa muda mrefu sana toka umeanzishwa katika Manispaa yetu. Tulikuwa tunategemea kama mradi huu ungekamilika, ungeweza kunufaisha zaidi ya wananchi 400 wakiwemo akina mama na vijana kuweza kujiajiri katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie katika mwaka wa fedha 2019/2020 kama Serikali itaweza kutoa pesa ili kuweza kuukamilisha huu mradi ambao umekuwa wa muda mrefu sana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nilikuwa nataka kuuliza kwamba kwa kuwa katika Manispaa yetu hii ya Iringa bado tunao mradi mwingine wa Kitwiri Irrigation mradi ambao pia toka umeanzishwa haujawahi kupatiwa fedha, je, ni lini utapatiwa fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile namwomba Mheshimiwa Waziri kama yuko tayari kuja sasa katika mkoa wetu wa Iringa ili aitembelee hii miradi yote miwili na vilevile atembelee hata miradi mingine ya mkoa wetu wa Iringa ili iweze kukamilika na iweze kunufaisha wananchi wa mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Mheshimiwa Ritta Kabati, ni mmoja ya wamama shupavu sana katika kuhakikisha wanatetea matatizo ya wananchi wao katika Mkoa wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu, tumekuwa na miradi mingi sana katika umwagiliaji zaidi ya 2000 lakini ni miradi 960 tu ndiyo iliyoendelezwa, zaidi ya miradi 1,967 haijaendelezwa. Sisi kama Wizara ya Maji, tukitambua kabisa umwagiliaji ndiyo kilimo mbadala ambao kinaweza kuchangia uchumi wa nchi yetu, tumeona haja sasa ya kuunda Tume ambayo itapitia mpango kabambe wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili tuwe na miradi michache ambayo itakuwa na tija kubwa sana katika nchi yetu kwa sababu tumekuwa na miradi mingine haina hata chanzo cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la umwagiliaji, maana yake ni kilimo cha mbadala. Tunajua kabisa nchi yetu wakulima wengi wanalima kwa kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu mpaka mvua inyeshe. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie, katika mpango huu kabambe tutakaoupitia katika mradi huu wa Mkoga, tutaupa kipaumbele katika kuhakikisha tunaukamilisha ili wananchi wake wa Iringa waweze kunufaika na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu mimi kwenda Iringa, nataka nimwambie mwenda kwao haogopi kiza. Nitakwenda Iringa katika kuhakikisha naenda kuzungumza na wananchi wa Iringa ahsante sana. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali ya nyongeza. Kwanza kabisa nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amenipatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefungua mradi wa REGROW ambao utafanya kazi ya kukuza utalii wa ukanda wa Kusini ukiwemo Mkoa wa Iringa; je, Serikali ina mkakati gani wa kujengea uwezo wananchi waliopo katika mkoa wetu ili watumie vizuri fursa hiyo kujiajiri na kuweza kujipatia kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nje ya maeneo ya utalii kuna historia kubwa za machifu akiwemo Mtwa Mkwawa, lakini kuna Kituo cha Kalenga, eneo la Mlambati ambapo Mwalimu Nyerere aliweka jiwe la msingi mwaka 1998 kama ukumbusho wa miaka mia moja.
Je, ni lini Serikali itachukua ya kuyaboresha kwa ajili ya kuvutia watalii na kuhakikisha kwamba pesa inayopatikana katika maeneo hayo, inawasaidia wananchi wanaozunguka eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kabla sijajibu haya maswali nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza kwa jinsi ambavyo amesimama imara katika kuupigania Mkoa wa Iringa, lakini pia alipigania sana kuhakikisha kwamba Kituo cha Utalii kinajengwa pale Kihesa, Kilolo. Kwa kweli nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ameuliza; je, tuna utaratibu gani wa kuhakikisha tunawajengea uwezo? Naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba katika mradi mkubwa ambao tunaenda kuutekeleza Mikoa ya Kusini unaohusu hifadhi nne yaani Udzungwa, Mikumi, Ruaha pamoja na Selous ya Kaskazini, tuna utaratibu wa kuimarisha miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi wa Mkoa wa Iringa waweze kufaidika na huu mradi, ni lazima wajengewe uwezo ili waelewe umuhimu wa kuuendeleza utalii na wawe tayari kuwakarimu watalii watakaokuwa wanatembelea katika Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivi sasa tuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba, kwanza tunawaelimisha namna ya kuanzisha makampuni ya kitalii ya kuongoza watalii, lakini pili, namna watakavyowakarimu pamoja na kuwaonyesha mambo mbalimbali ambayo yapo katika Mkoa wa Iringa ukiwemo utamaduni wa Iringa na tatu, ni pamoja na kuwapokea na kuwakarimu katika hoteli mbalimbali. Kwa hiyo, hii mipango yote tutaitekeleza katika mwaka wa fedha huu unaoanza Julai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kile Kituo cha Kalenga, kama alivyosema kweli kabisa miundombinu bado haitoshelezi. Hivi sasa tuna mpango kabambe wa kuhakikisha barabara ya lami inajengwa kutoka Iringa hadi kwenye lango kuu la Ruaha. Wakati tutakapokuwa tunajenga ile barabara, tutaangalia uwezekano wa kuimarisha ile miundombinu, kuchepusha pale kupeleka katika hiki Kituo cha Kalenga kwa sababu ni karibu ili tuhakikishe kwamba nako panafikika kiurahisi. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa swali dogo la nyongeza. Nimpongeze kwanza Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuja katika Mkoa wetu wa Iringa na kujionea jinsi ambavyo Mji wetu wa Iringa ulivyokua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kuuliza swali dogo; kwa kuwa Mji wa Iringa unakua kwa kasi kubwa sana, kuna baadhi ya maeneo ambayo hayapati maji kama kule Tagamenda, Isakalilo na Kigonzile. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea pesa ili kuongeza ule mtambo wa kusambaza maji pamoja na kuwa sasa hivi tunapata asilimia 96, lakini maji yetu tunaweza tukapata asilimia 100?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi wakati inajenga mtambo wa kutibu maji Iringa iliweka matoleo ili population itakapoongezeka basi tuweze kupanua ili maji yaweze kuongezeka. Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga bajeti kwa ajili ya kuanza kupanua mtambo wa kutibu maji ili maji yaweze kuenea katika kata zote.
MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika Manispaa yetu ya Iringa kuna Daraja la Igumbiro, daraja ambalo limekuwa likileta maafa kila mwaka na ambalo limechukua muda mrefu sana kumalizika. Je, ni lini sasa Serikali itatoa pesa ili Daraja lile la Tagamenda liweze kukamilika?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo tunafanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ni pamoja na Manispaa ya Iringa. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuboresha miundombinu katika Manispaa hiyo ya Iringa na hivi sasa tumekamilisha barabara kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba wataalam wangu wataenda kufanya tathmini katika eneo hilo ambalo limebakia linaonekana lina changamoto. Lengo letu kubwa ni ili tuhakikishe kama hiyo kazi ina upungufu wa aina yoyote tuweze kuurekebisha ili wananchi wa Iringa wawe katika mazingira mazuri ya kuweza kusafiri.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.
Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa anakwenda Mbeya alipitia katika hospitali yetu ya Iringa na akajionea changamoto kubwa kabisa ambazo ziko katika mkoa wetu. Kwanza kabisa ni udogo wa eneo la hospitali ambayo iko katika mkoa wetu ambayo kwa kweli pia kuna muingiliano wa Magereza. Tatizo kubwa Madaktari Bingwa hawana kabisa maeneo ya kuishi kwenye lile eneo na wagonjwa wanapata shida sana wanapokuja kutibiwa usiku na vilevile alielezwa kuhusiana na eneo ambalo mkoa umeutafuta ili kuwepo na alternative mbili aidha magereza itoke au walipie lile eneo ili madaktari wetu waweze kuwasaidia wagonjwa usiku.
Je, sasa Serikali inatuambiaje maana yake hili ni tatizo la muda mrefu ili wananchi wa Mkoa wa Iringa waweze kutatua hiyo changamoto? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ritta Kabati kwa sababu jambo hili amekuwa akilifuatilia sana na hii inaonyesha ni jinsi gani anavyojali masuala ya ustawi wa wananchi wa Iringa Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani imelitafakari sana jambo hili na kuona kwamba kilicho rahisi kuhama ni Magereza kwa sababu kwanza eneo lipo na lipo ndani ya Manispaa na kiusalama liko vizuri zaidi kuliko pale ambapo wagonjwa au ndugu wanaoenda kuwaona wagonjwa hulazimika kupita mbele ya geti kubwa la gereza ambacho kiulinzi inaleta matatizo. Kwa maana hiyo sisi kama Wizara tunaendelea tu kuangalia logistic za kibajeti ili tuweze kuanza utaratibu huo wa kuhamisha gereza ili kutoa fursa nzuri ya wananchi kuweza kupata matibabu na expansion ya Hospitali ya Mkoa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vijana wetu kutumia madawa ya kulevya na kwa kuwa sober nyingi sana zinamilikiwa na watu binafsi na kwa kweli zimekuwa zikifanya vizuri, lakini gharama za kuziendesha tunaona ni kubwa kiasi kwamba vijana wengi wanashindwa kumudu gharama zake. Je, ni kwa nini sasa Serikali isitoe ruzuku kwa hizi sober house za watu binafsi au kuanzisha za kwake ili kusaidia vijana wetu kurudi katika hali zao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakiri kwamba kumekuwa na tatizo la dawa ya kulevya na Serikali imechukua juhudi
na hatua ya kuhakikisha kwamba tunadhibiti uingizaji wa dawa za kulevya na kwa kiasi kikubwa kwamba tumepunguza sana matumizi ya madawa za kulevya hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunatambua vilevile kwamba kuna wahanga ambao walikuwa wanatumia hizi dawa za kulevya, sisi Serikali tumeendelea tukishirikiana na wadau binafsi. Kwa upande wa Serikali tumeanzisha vituo mbalimbali vya matibabu katika hospitali zetu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na hivi karibuni tumezindua hapa Itega Dodoma, lakini tunatambua mchango mkubwa wa sober houses na sisi kama Serikali tumetoa mwongozo wa usimamizi wa hizi sober houses, lakini sasa hivi bado ni mapema sana kusema kwamba Serikali itakuwa inachangia Ruzuku kwa uendeshaji wa hizi sober houses.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali madogo tu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba niipongeze Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa tamko lake ambalo limehakikisha kwamba wazabuni wote wanalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna baadhi ya wazabuni wakiwemo hata wa Mkoa wangu wa Iringa wameshafanyiwa uhakiki zaidi ya mara moja, lakini wanadaiwa na mabenki, wanadaiwa na TRA na wanatishiwa mpaka kuuziwa mali zao:-

Je, Serikali inawasaidiaje wasifilisiwe? Maana wengi wao tayari wameshapata maradhi na kufa na wengine wameshafilisika kabisa kwa ajili ya madeni ambayo wanaidai Serikali.

Swali langu la pili; je, ni vigezo gani sasa vinatumika kwenye malipo ya madeni ya wazabuni hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza kuhusu msaada wa Serikali ili wananchi wetu wasifilisiwe, naomba kumwambia Mheshimiwa Rita na kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tunalipa madai pale yanapokuwa yamehakikiwa. Wananchi wetu hawa wa Mkoa wa Iringa, kama wapo ambao madeni yao yamehakikiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Ndani wa Serikali, basi tumekuwa tukiwasaidia mmoja baada ya mwingine wanapofika na kuwasilisha nyaraka zao kuonyesha kwamba wamehakikiwa na sisi kujiridhisha kwamba wapo kwenye orodha ya kulipwa ndani ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Ritta na nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kuwatetea wananchi wa Iringa. Ameshakuja siyo mara moja wala mara mbili ofisini kwangu, naomba tuendelee kushirikiana ili tuwasaidie wananchi wetu ili wasifilisiwe na ili wasiendelee kupata maradhi kama wapo kweli waliopata maradhi. Tuendelee kushirikiana tuwasaidie wananchi hawa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ameuliza ni vigezo gani vinavyotumika kulipa madai haya ya wazabuni pamoja na wakandarasi wengine? Kwanza kabisa ni kuhakikisha deni limehakikiwa na limekidhi vigezo vya kuwa deni halali. Hicho ni kigezo cha kwanza kwamba deni hilo linalipwa.

Mheshimiwa Spika, sababu ya pili au kigezo cha pili ambacho kinapelekea kulipwa, tunaangalia deni lile kama hali-attract riba kwa Serikali, lakini pia kwa yule ambaye anaidai Serikali. Kama deni hili lina-attract riba tunayapa kipaumbele ili Serikali isiendelee kuumia na ili tusiendelee kuwaumiza wananchi wetu ambao wanaidai Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, kigezo cha tatu ni kuhakikisha kwamba ukubwa wa deni lenyewe, kwa wale ambao wana madeni ambayo siyo makubwa na ambao ndio wengi tumekuwa tukiwapa kipaumbele kuhakikisha kwamba tunawalipa madeni yao kwanza ili kuweza kuchachua uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mwaka 2017/2018 Bunge lako Tukufu lilitupitishia bajeti ya shilingi trilioni moja kwa ajili ya kulipa madeni haya na Serikali ililipa zaidi ya shilingi trilioni 1.096 kwa sababu dhamira ya Serikali yetu ni njema kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Spika, kigezo cha nne, ni umri wa deni. Madeni yale ambayo yamekaa kwa muda mrefu na tayari yamehakikiwa, tumekuwa tukiyapa kipaumbele na kuhakikisha yote yanalipwa ili kuwawezesha wananchi wetu kuendelea kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Magufuli kwa uzinduzi wa barabara ya kutoka Makambako mpaka Mufindi jana. Naomba niulize swali moja. Katika ujenzi wa barabara ya kutoka Dodoma - Mtera mpaka Iringa, pale katika kona za Nyang’holo huwa kunakuwa na maporomoko makubwa sana ambayo huwa yanajitokeza hasa wakati wa mvua:-

Je, Serikali inatusaidiaje? Maana kutakuja kutokea ajali kubwa sana, hata jana nimepita pale. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tayari ameshafika ofisini zaidi ya mara tatu akifuatilia kipande cha barabara hii ya kutoka Mtera - Iringa hasa kwenye kona zile za Nyang’holo ambazo ni korofi kabisa. Tunakiri na bahati nzuri nimeshamwelekeza Meneja wa TANROAD Mkoa kufuatilia eneo hilo ili tuanze tararibu za kulirekebisha kwa ajili ya usalama wa Watanzania.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Muungano umetuletea faida nyingi sana katika nchi yetu na ndiyo maana viongozi wetu, waasisi na sisi wenyewe tumekuwa tukiuenzi na kuulinda kwa nguvu zote na kwa kuwa sasa huko vijijini vijana wetu wengi wamekuwa hawana uwelewa sana wa kutosha kuhusiana na huu Muungano. Je, ni ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wakati wa sherehe hizi elimu itolewe kwa ajili ya vijana wetu na wananchi walioko vijijini kuliko kufanya sherehe kitaifa zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati kwa niaba yake ambapo swali la msingi lilikuwa la Mheshimiwa Martha Moses Mlata. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mlata kwa swali hili ambalo litatoa ufahamu mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kutoa rai, siku ya tarehe 26 nafahamu itakuwa siku ya Ijumaa mwezi wa Nne kwamba Taasisi zote za Elimu zitumie fursa hii ya kutoa elimu kuhakikisha kwamba wanakuwa na makongamano na mijadala mbalimbali juu ya historia ya Muungano wetu. Ahsante.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kukubaliana kwamba kuna unyanyasaji mkubwa sana kwa wanawake na watoto lakini upo unyanyasaji mkubwa sana kwa kina baba, wapo ambao wamekuwa wakipigwa na wengine kunyanyasika. Kuna maandamano ambayo tuliona katika mitandao katika nchi ya jirani ya Kenya akina baba wakiandamana kudai haki zao za msingi kwa akina mama. Je, ni lini sasa sheria pia itajengwa kuwalinda akina baba ambao wamekuwa wakinyanyasika kila wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Iringa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inapoongelea ukatili wa kijinsia haimaanishi tunaongelea ukatili wa akina mama na watoto, jinsia ina cut-across na akina baba. Bahati mbaya sana matukio ya ukatili wa kijinsia ya akina baba siyo mengi yanakuwa reported. Nitumie fursa hii kuwaomba wale akina baba ambao nao wanapigwa, wanafanyiwa ukatili wa kingono, wanaonyanyaswa kisaikolojia nao waweze kujitokeza ili madawati yetu ya jinsia yaweze kuyafanyia kazi.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na tatizo kubwa wananchi kubambikizwa kesi hasa kwenye hizi kamera, mtu unapigwa kamera ukienda kuhoji wanasema kwamba imekosewa namba ya gari kwa hiyo wananchi wengi wamekuwa wanabambikiziwa makosa ambayo si ya kwao. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na kamera ambazo zimekuwa zinawabambikia wananchi makosa ambayo siyo ya kwao.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi haya ya teknolojia tumeanzia na kamera, tuna mfumo VTS na tuna mambo mengine mengi ambayo tunaelekea nayo huko, yote haya yana dhamira ya kupunguza hizo dhana dhidi ya askari wetu kuhusiana na kubambikia watu makosa.

Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba matumizi ya tochi yamekuwa yakitusaidia sana. Hata hivyo, ikiwa kuna changamoto upungufu wa kimaadili wa baadhi ya askari wetu na hilo hatuwezi kulikataa kwa sababu askari nao ni binadamu huwezi kuwa na askari wote hawa wakose wawili watatu ambao watakuwa na upungufu wa kimaadili, tumekuwa tukiendelea kuchukua hatua pale ambapo tunapata taarifa na uthibitisho juu ya kubambikia wananchi makosa ambao hawahusiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumsisitiza Mheshimiwa Mbunge kwamba tusaidiane kwa pamoja kufichua wale askari wachache ambao watakuwa wanatuhumiwa ama wanajihusisha na tabia kama hizo zilizokuwa kinyume na maadili ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya maji unategemea na mpango wa fedha, natambua kuna baadhi ya Wakandarasi bado hawajalipwa fedha zao: Je, ni lini sasa Mkandarasi ambaye anatekeleza mradi wa Mji Mdogo wa Ilula katika Jimbo la Kilolo atapatiwa malipo yake ili wananchi wa Ilula waache kupatiwa migao ya maji mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapigania akina mama na Watanzania hususan katika suala zima la maji. Kikubwa, utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Kama unavyoona, gari haliwezi kwenda bila mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulikuwa tunadaiwa takribani zaidi ya shilingi bilioni 88 na Wakandarasi, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Wizara ya Fedha, wametupatia fedha zote shilingi bilioni 88 ambazo tulikuwa tunadaiwa na Wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mradi wake ule wa Ilula kwa Mheshimiwa Mwamoto, Kilolo pale, tumeshamlipa zaidi ya shilingi bilioni moja. Tunataka zile fedha tulizomlipa sasa awekeze pale katika kuhakikisha anakamilisha mradi na wananchi wa Ilula waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatolesheleza.