Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asha Mshimba Jecha (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ufanyaji kazi ya utumbuaji majipu na nchi yetu kuwa ni mahali salama na wananchi wetu kukabiliana na maisha yao bila ya vikwazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kazi nzuri anazozifanya. Naamini kwa muda mfupi ujao maendeleo ya wananchi wetu yataboreka. Aidha, nawapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa utendaji kazi kwa kuwa karibu na wananchi, kubaini changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Watanzania wameridhika na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuwabaini wafanyakazi hewa na kuchukuliwa hatua zinazostahili. Kundi hili ni kubwa lina mtandao mrefu na usiri wa hali ya juu, lakini kila mmoja akichukua wajibu wake vita hii tutashinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kazi wanazofanya kuangalia na kusimamia maadili ya Viongozi wa Umma. Nashauri Tume hii kuangalia na njia nyingine kwa kuwafikia wananchi ambao siyo Viongozi wa Umma katika utaratibu unaoeleweka, lakini wamekuwa viongozi katika mfumo usio rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri inayofanyika, nakubaliana na Wizara kuona ipo haja kufanya utafiti kwa waajiri na wadau mbalimbali ili kubaini changamoto ambazo zimekuwa zinalalamikiwa mfano, baadhi yao walipofuatilia Utumishi walijibiwa na mhusika kwamba bado haja-prove na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Kujitegemea (PTF) ni wa muda mrefu na umeweza kuwafikia watu wengi hasa wanawake. Tunashauri Mfuko huu utangazwe zaidi ili wananchi wetu waweze kufaidika nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Naipongeza Wizara hii kupitia Waziri, Naibu na Watendaji wote kwa kazi ngumu mnayokabiliana nayo katika Wizara hii, kwani kazi ya kusimamia na kuiendeleza taaluma kwa kiwango cha ubora ina changamoto nyingi, lakini penye nia pana njia, msivunjike moyo tuko pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimba kwa wanafunzi wa kike. Umefikia wakati sasa kwa wanafunzi wa kike wanaopata mimba baada ya kujifungua waruhusiwe kuendelea na masomo kama kuna Sheria kandamizi ziletwe Bungeni tuzibadilishe.
Bodi ya Mikopo. Pamoja na jitihada kubwa za Serikali kuwapatia mikopo baadhi ya wanafunzi wanaostahili, lakini kumekuwa na changamoto na kama Wizara/Bodi ya Mikopo haikuzifanyia uchunguzi maalum, basi ile dhana ya kuwapa mikopo wanaostahili haitafikiwa kwa usahihi na mikopo iliyoiva kushindwa kurejeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migomo na maandamano kwa wanafunzi/wanavyuo. Kero ya maandamano na migomo kwa wanafunzi inazorotesha elimu kwani huharibu mazingira na vifaa na wakati mwingine husababisha maafa na hasara kubwa na hata shule kufungwa na wanafunzi kukosa masomo na kurudi majumbani. Wizara ina mkakati gani wa kuzuia changamoto ya maandamano na migomo, hasa kwa yale ambayo yamo ndani ya uwezo wao kwani tumeshuhudia baadhi ya wakati mara tu wanapogoma au kuandamana, kile wanafunzi wanacholalamikia Wizara inawapatia haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dira na Dhima ya Wizara ni nzuri na kama tutaitafsiri kwa vitendo na kuwashirikisha wadau mbalimbali na kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake hakuna lisilowezekana. Hivyo, tunaiomba Wizara iandae mipango mikakati ya muda wa kati na muda mrefu ili kubaini ushiriki mpana na wa wazi katika kufikia Dira ya Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Elimu ya Juu ni suala la Muungano, hivyo pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara kwa kushirikiana na upande wa Zanzibar (Wizara ya Elimu), ipo haja sasa kukaa pamoja wadau wa elimu wa pande hizi mbili za Muungano ili kubaini changamoto na kuzitafutia njia muafaka za utatuzi, hasa ukizingatia tumo katika mchakato wa ushirikiano wa Afrika Mashariki na nchi yetu pia, inakabiliwa na utandawazi. Ni muhimu tujiandae sasa, wakati hautusubiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendeleza maliasili zetu na watalii wanaoingia nchini mwetu wanaongezeka siku hadi siku. Ni jambo jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama tutajipanga vizuri kwa kuutangaza utalii na vivutio tulivyonavyo, mapato yetu yanayotokana na utalii yataongezeka zaidi. Mfano, utalii wa viungo; tuwahamasishe wananchi wetu kupitia mtu mmoja mmoja au vikundi kuanzisha mashamba ya viungo (spices) mbalimbali na watalii wataona kitu kingine badala ya wanyama pekee na wananchi wataongeza vipato vyao moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuwaandaa wananchi kuvutia watalii kwa utamaduni wetu wa asili, mfano ngoma zetu za asili, mila na desturi zetu za asili, mavazi, chakula, lugha, malezi na kadhalika. Kwa utalii wa historia utahusu watawala waliopita na kutawala.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ASHA M. JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Naipongeza Wizara kupitia Mheshimiwa Waziri, Naibu, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote kwa juhudi kubwa wanazofanya kushughulika na afya za Watanzania na kuboresha maendeleo ya jamii. Sambamba na hilo ni weledi wao ulioifanya Wizara hii kusonga mbele na kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kuwahudumia Watanzania popote walipo mjini na vijijini. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wanawake kiuchumi. Naipongeza Wizara kwa mipango mizuri ya kuwainua wanawake kiuchumi. Hata hivyo, bado juhudi zaidi zinatakiwa kuchukuliwa kwani bado wapo wanawake wengi wajasiriamali hawajawezeshwa kiuchumi, wanajitahidi wenyewe lakini kutokana na mtaji kuwa mdogo wanashindwa kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya wanawake, iko mbali na wanawake walioko vijijini. Je, ni lini Wizara itaielekeza benki hiyo kufungua angalau dirisha katika maeneo ya vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hisa katika Benki ya Wanawake, wapo baadhi ya Wabunge tumeshiriki kununua hisa kwa ajili ya uanzishwaji wa benki hii. Je, ni lini tutaarifiwa juu ya kinachoendelea na hatma yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu unyanyasaji wa wanawake na watoto. Naipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inazochukua katika kukabiliana na tatizo hili lakini bado juhudi zaidi zinahitajika kwa kuungana pamoja kupiga vita hali hii isiendelee. Wazee/wazazi waache tabia ya kuwatumia watoto wadogo kama kitega uchumi kwa kuwaingiza katika ajira za watoto hasa kuwatumikisha majumbani na kuwakosesha haki zao za elimu na matunzo ya karibu ya wazazi. Kwa nini Wizara isielekeze ajira za majumbani zifanywe na watu wazima badala ya kuwatumia watoto wadogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kuitangaza elimu kuwa bure na tumeshuhudia wingi wa wanafunzi wakitumia fursa hiyo. Mwenyenzi Mungu atakulipa kwa upendo wako kwa Watanzania na kujali utu na kutoa haki ya elimu kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ongezeko la wanafunzi mashuleni limekuwa kubwa, nashauri Wizara kuwa na programu maalum ya ajira kwa walimu kwa mkataba kwa kuwatumia walimu wastaafu kwa muda mfupi na wa kati, ili kujiandaa na ajira mpya kwa wale walimu watakaomaliza mafunzo, kuwezesha kuziba pengo la ukosefu wa walimu kutokana na wingi wa wanafunzi.

Kuhusu ujauzito kwa wanafunzi wa kike, tunaiomba Wizara kukamilisha mchakato wa sheria ya kuendelea na masomo kwa wanafunzi wanaopata mimba mara tu akishajifungua. Utafiti unaonesha kwamba wale waliopata mimba mara baada ya kujifungua, wakakubali kurudi shule kwa hiari wamefanya vizuri katika masomo yao na wamefaulu na kuendelea na masomo ya juu. Mifano hiyo ya wanafunzi hao iko Zanzibar ambapo tayari tumepitisha sheria ya watoto wa kike wapatapo mimba shuleni kurudi shule mara baada ya kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo elimu zaidi itolewe kwa wanafunzi wote kujitambua kutokana na mabadiliko ya miili yao ili wawe na ufahamu wa jinsi ya kujilinda na unyanyasaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili, je, Wizara ina mipango gani wa lugha ya kiswahili kuikuza na kuzungumzwa kwa usahihi hasa ukizingatia kuwa lugha hii sasa inazungumzwa na nchi nyingi za Afrika na Tanzania ndiyo lugha yetu. Hadi sasa Tanzania imetoa wataalam wangapi wa lugha ya kiswahili kufundisha nje ya nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Naipongeza Wizara kupitia wanajeshi wetu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuilinda nchi yetu na kubaki katika hali ya utulivu na amani. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vijana wanaojiunga na JKT mara wamalizapo mafunzo ya kujitolea (kujitegemea), baadhi yao huajiriwa na vikosi vyetu vya ulinzi, lakini baadhi hurudi katika maeneo yetu na kuzurura bila kazi maalum ya kufanya. Je, Serikali haioni sasa wakati umefika kwa vijana hawa wanaopitia JKT kuwa na mfuko maalum wa kuwasaidia vijana hawa mara tu wamalizapo mafunzo, kupewa na kuanzisha miradi na kujiajiri wenyewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wakati wakiwa JKT wapewe mafunzo ya ujasiriamali ili wakitoka wawe tayari kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Maji ni uhai, kila chenye uhai kinahitaji maji. Hivyo napongeza juhudi kubwa inayochukuliwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Wizara hii kwa jitihada ya kuwafikishia huduma hii wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mahitaji ya maji ni makubwa katika nchi yetu na tunashuhudia wakati huu wa mvua za masika maji mengi yanavyopotea, tunaiomba Wizara ya Maji iandae program mahususi ya kuvuna maji ya mvua ambayo kwa sasa yanapotea bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mwingine ni kuwaelimisha wananchi au taasisi, mfano shule, vituo vya afya na kadhalika, wavune maji kupitia mapaa ya nyumba na kuyahifadhi. Kwa wafugaji wenye mifugo mingi waelimishwe kujiandalia mazingira yatayowezesha kuhifadhi maji hasa wakati wa mvua ambapo maji mengi hupotea bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama kwa asilimia kubwa ndio wanaosumbuka na watoto wao kutafuta maji. Nashauri kuvitumia vikundi vya akinamama katika program mbalimbali za kuvuna maji na kuyahifadhi kwa matumizi endelevu. Tutumie na vikundi vya vijana kubuni njia nafuu za kuvuna maji kwa matumizi ya kilimo na mifugo katika kipindi hiki cha mvua, kwani maeneo mengi mvua zimefika kwa wingi na maji yanapotea bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa kuongezea tozo kwenye mafuta ili kuongeza Mfuko wa Maji.