Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Asha Mshimba Jecha (2 total)

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:-
Kituo cha Polisi Dunga kimechakaa sana kwani kuta zake zimepasuka na baadhi ya vyumba havitumiki kutokana na kuhatarisha usalama wa askari na wananchi wanaofika kwa ajili ya kupata huduma. Je, ni lini Serikali itajenga upya kituo hicho?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Kituo cha Polisi Dunga pamoja na Wilaya zote mpya zilizoanzishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Kwa kutambua umuhimu wa Kituo cha Polisi Dunga, tathmini itafanyika ili gharama halisi ziweze kujulikana. Aidha, ujenzi wa kituo hicho utaanza mara baada ya fedha kupatikana kwa ajili ya kipaumbele cha Serikali na hivi sasa katika kukamilisha miradi ya zamani ya polisi na kuanza miradi mipya ya ujenzi wa vituo hivyo vya polisi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kuimarisha miundombinu ya ulinzi na usalama, tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kushiriki katika ujenzi wa vituo vya polisi ili huduma za ulinzi na usalma ziweze kupatikana kwa karibu.
ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:-
Mradi wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi Vijijini (MIVARF) katika Mkoa wetu wa Kusini Unguja umeweza kuwakomboa wananchi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha mawasiliano ya barabara na kuweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi. Kwa kuwa mradi huu umeonesha mafanikio na wananchi wamehamasika.
Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea mitaji na mafunzo wananchi hao ili waweze kufikia malengo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha inaunga mkono juhudi za wananchi kushiriki katika uchumi wa kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na kuwapatia mafunzo stahiki. Hatua za kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kimtaji zilianza kwa kuvijengea uwezo wa kiutawala na kiutendaji Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uzalishaji ili viweze kuratibu na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya mitaji itakayopatikana kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matayarisho yanaendelea ili kuvipatia vikundi vya wazalishaji ambavyo tayari vimehakikiwa na uwezo wao baada ya ziara ya uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kutembelea Zanzibar mwezi Mei, 2017. Benki hii ni mshiriki mkubwa wa MIVARF, ambayo huendesha mfuko wa dahamana (Guarantee Fund) wa mikopo utakaofanya benki kuwakopesha wakulima kwa masharti nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekit, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wamesaini makubaliano ya uendeshaji wa mfuko wa dhamana tarehe 3 Novemba, mwaka 2017. Kwa kupitia makubaliano hayo, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 22 kwa TADB ili kuanza utekelezaji kwa kushirikisha benki za biashara kufikisha huduma ya mikopo kwa makundi mbalimbali. TADB walishaanza utaratibu huu kwa kutangaza kwenye magazeti ili kupata benki zitakazoshiriki. Nawashauri wananchi wote watumie fursa hii adhimu kujipatia mikopo ili kupanua shughuli zao za maendeleo na kujiongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa kitoa mafunzo mbalimbali kwa wananchi kupitia mradi wa MIVARF ili waweze kuyafikia masoko yenye tija. Mafunzo hayo ni pamoja mbinu bora za kilimo (good agricultural practice), uongezaji thamani mazao na jinsi ya kuyafikisha masoko yenye tija na kukuza na uimarishaji Vikundi vya Akiba na Mikopo (SACCOS). Programu kupitia kwa watoa huduma (Business Coaches) inaendelea kutoa mafunzo haya kwa wananchi hasa katika Nyanja za kuongeza thamani mazao na kuyafikisha masoko.