Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni nchi ya kilimo. Asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania wanategemea kilimo. Ili kupunguza umasikini na kuondoa utegemezi wa nchi wahisani, ni lazima tuwekeze kwa kiasi kikubwa katika kilimo na tuwe na mikakati thabiti ya kukiboresha kilimo chetu. Hivyo basi, hatuna budi kilimo chetu sasa kijielekeze katika kuongeza uzalishaji kwa ekari moja na kuachana kabisa na ukulima wa jembe la mkono. Kwa mfano, nchi kama China wamefanikiwa sana katika kilimo cha uzalishaji kwa ekari moja. Ukilinganisha ukulima wao na wetu, wakulima wetu wanalima ekari tatu mpaka nne lakini wanapata mazao ya ekari moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida kijiografia ni mkoa wenye hali ya ukame ambao unapata mvua kwa msimu mmoja na unakabiliwa na changamoto nyingi katika Sekta ya Kilimo. Kwa hiyo, kuna haja ya Serikali kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Singida waweze kulima na kunufaika na kilimo cha matone kwenye maeneo yenye chemchemi na maeneo ambayo hayana chemchemi, basi Serikali iwasaidie kuchimba mabwawa ya maji ili waweze kulima na kuvuna kwa misimu yote ya mwaka. Maeneo ambayo yamenufaika na kilimo cha matone Mkoani Singida ni Isana, Mkiwa, Uhamaka na Kisasida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida pia unakabiliwa na uhaba wa Maafisa Ugani pamoja na mashamba darasa. Naomba Serikali iunge mkono jitihada za uanzishwaji wa mashamba darasa kwani yana mchango mkubwa wa maendeleo ya kilimo, siyo tu kwa kuwafundisha wakulima kwa niaba ya Maafisa Ugani, bali pia husaidia kutoa utaalam wa kuzalisha mbegu bora za daraja linalokubaliwa, yaani QDS.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni mkoa unaosifika kwa kilimo cha alizeti, mahindi, mtama, uwele, karanga na vitunguu, lakini bado wakulima wake hawajanufaika na ukulima huo na hii ni kutokana na ukosefu wa soko la kudumu au vituo maalum vya kuuzia mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ya Awamu ya Tano kuona umuhimu wa kujenga soko kubwa la kisasa la mazao kwenye Manispaa ya Singida, kwani uwepo wake utatoa nafasi kwa wakulima wengi kunufaika na bei za mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida unakabiliwa pia na ukosefu wa vituo vya utafiti ikiwemo maabara ya matumizi ya udongo na hii hupelekea wakulima wengi wasiweze kujua hali ya ardhi yao na hivyo kusababisha uzalishaji duni. Naomba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kulitazama kwa kina na kuona ni namna gani wataweza kuwasaidia wakulima wetu katika kutambua matumizi bora ya ardhi ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mifugo, Singida ni hodari wa ufugaji wa ng‟ombe, mbuzi na kondoo lakini bado zipo changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya mifugo Mkoani Singida. Changamoto hizo ni uhaba wa majosho, uhaba wa maeneo ya malisho na magonjwa ambayo kwa asilimia 70 yanachangiwa na mdudu kupe. Hivyo basi, naiomba Serikali yangu sikivu kuongeza majosho ya kutosha, kutenga maeneo ya malisho na maji na kuleta dawa za chanjo na dawa hizo zifike kwa wakati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu katika bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, mwingi wa neema ambaye ameniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliongoza Taifa hili.
Vilevile nampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Baraza la Mawaziri kwa namna ambavyo wanajituma kuhakikisha kero za Watanzania zinapungua au zinakwisha kabisa. Ninapenda kuwatia moyo waendelee kukaza buti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Singida hususan wanawake na vijana kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi za ndio napenda kuwahakikishia kwa heshima hii kubwa waliyonipa sitawaungusha na wala sitaanguka katika kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo najielekeza moja kwa moja katika kuchangia. Mwanafalsa mmoja John Dew aliwahi kusema education is not preparation for life, education is life itself, akimaanisha kuwa elimu siyo maandalizi ya maisha, elimu ni maisha yenyewe, hivyo basi, elimu ndiyo msingi mkuu katika kuyamudu maisha ya kila siku na ndiyo mkombozi wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inatajwa kuwa na elimu ya kiwango cha chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, hii ni kutokana na ukweli kwamba elimu inayotolewa haikidhi viwango vya ubora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu inayotolewa katika vyuo na shule zetu za Serikali haimuandai kijana kujiamini, kuwa mbunifu, kuwa ni mwenye uwezo wa kubembua mambo, kuwa na communication skills, kuweza kujiajiri au kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kijana aliyemaliza elimu ya kidato cha nne kutoka nchini Kenya au Uganda akija Tanzania anapata ajira bila wasiwasi wowote, hii ni kwa sababu elimu aliyopata ni bora, inamwezesha kujiamini, inamwezesha kujielezea kwa ufasaha kwa lugha ya kiingereza ambayo hapa nchini kwetu ni lugha ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo sababu kadhaa ambazo zinachangia kushuka kwa kiwango cha elimu katika shule zetu za Serikali. Sababu hizi nitazitaja kama ifuatavyo:-
Kwanza, ni utayarishaji wa mitaala ambayo haiendani na wakati na mazingira ya sasa. Mitaala ambayo inakosa skills ambazo zingeweza kumsaidia mwanafunzi kujiamini au kujitegemea baada ya kumaliza elimu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zimeonyesha kwamba kuna changamoto za utayarishaji na utekelezaji wa mitaala bila kufanyiwa majaribio jambo linalopelekea walimu wengi kukosa stadi za maisha, kukosa maarifa ya kufundishia. Mfano katika Taifa la Netherland mtaala wake unasisitiza kufundisha elimu ya ujasiriamali kuanzia shule za sekondari. Hivyo basi, ningeishauri Serikali kutizama upya mitaala ambayo itazingatia uchambuzi wa kina wa kumwezesha kijana kuweza kujitegemea na kujiamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili inayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu, ni uhaba wa vitendea kazi na teaching methodology ambazo kimsingi hazimjengi mwanafunzi kujitegemea au kujiamini. Shule zetu nyingi za Serikali zinafundisha kwa nadharia zaidi kuliko vitendo. Wenzetu wa dunia ya kwanza wanasema practice makes perfect. Unapomfundisha mwanafunzi kwa nadharia na vitendo unamwezesha mwanafunzi huyo kulielewa somo hilo vizuri zaidi. Hivyo kuna haja ya msingi ya kurudisha elimu ya vitendo katika shule zetu za msingi na sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, ukimfundisha mwanafunzi mapishi ya keki kwa nadhari na baadaye ukaweza kumuonyesha namna ya keki hiyo inavyopikwa ataelewa zaidi. Kusoma kwa nadharia tu ni sawa na kuwa-feed wanafunzi kitu ambacho hawana reference nacho. Hivyo basi, ningeomba sana elimu ya vitendo ilirudishwe kama zamani ilivyokuwa ikifundishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linachangia elimu yetu kuendelea kuwa duni ni kukosekana kwa uwiano kati ya mwalimu na wanafunzi darasani katika shule zetu wanafunzi katika darasa moja wanaweza kufikia idadi ya wanafunzi 35 mpaka 50, idadi hii inamuwia mwalimu ugumu kuweza kufanya assessment kwa kila mwanafunzi. Matokeo yake anaangalia tatizo la mwanafunzi mmoja na kulitolea suluhu kwa wanafunzi wote darasani. Tofauti ya darasa lenye wanafunzi kumi mpaka kumi tano, ni rahisi mwalimu assessment ya kila mwanafunzi na kujua wana tatizo gani pindi atakapomaliza kufundisha na kuona namna gani ya kuwasaidia hao wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutomuandaa mwalimu vema ili afundishe kuendana na wakati wa sasa nayo ni sababu inayochangia kuporomoka kwa elimu yetu. Ajira ya ualimu imewekwa katika kundi la kitu ambacho hakina thamani. Leo hii wanaochukuliwa kujiunga na ajira hii ni wahitimu waliopata daraja la nne katika kidato cha nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine maslahi ya walimu ni duni. Mwalimu kwa kweli hawamjali mwalimu, mwalimu huyu hana nyumba ya kuishi, anaishi katika mazingira duni, mshahara wake ni mdogo na wala haumkidhi mahitaji yake na wakati mwingine haufiki kwa wakati. Ningeiomba Serikali yangu kuwaangalia walimu na kuangalia maslahi yao upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unategemea nini kwa mwalimu kama huyo na atakuwa kweli na morali ya kufundisha si ata-beep tu kutimiza wajibu wake na kuondoka zake. Ndiyo maana kiwango cha elimu kimeendelea kushuka kutoka asilimia 22.3 mwaka 1985 na kufikia asilimia 49.6 mwaka 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali kuja na mpango utakaowawezesha walimu kupata training za mara kwa mara na semina zinazolenga mahitaji ya sasa ili kuwawezesha kufundisha kwa ufanisi na ufasaha katika dhama hizi za sayansi na teknolojia. Lakini pia vilevile walimu watakaokuwa wamejiendeleza wapewe incentives kulingana na madaraja yao, hii itasaidia sana kupunguza madai ya uhamisho ya mara kwa mara na kuwafanya walimu watulie katika maeneo yao ya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba katika shule zetu za Serikali hatuna programu za kuhamasisha watoto wapende kusoma vitabu, wanafunzi wetu hawana tabia ya kujisomea vitabu, lakini pia vitabu vyenyewe hakuna vya kutosha. Serikali ione umuhimu wa kuanzisha programu au iwena slogan maalum ambayo itawahamasisha wanafunzi wetu na katika kila mkoa uwe na e-library ambayo wanafunzi watapata ku-access vitabu mbalimbali zikiwemo story books ambazo zitaweza kuwasaidia katika ku-improve english language ambayo ni medium of instruction in secondary schools.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa yenye changamoto nyingi katika sekta ya elimu. Mkoa wa Singida una jumla ya shule 542, kwa wastani kwa mwaka watoto 25,000 humaliza shule ya msingi ukilinganisha na ufaulisha watoto 13,383 kwa mkoa mzima. Ukilinganisha idadi hii ya wananfunzi waliomaliza shule za msingi hailingani kabisa na wale wanaondelea na masomo ya shule za sekondari. Zaidi ya vijana 10,000 wanakaa mitaani…
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala ulioko mbele yako sasa. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, mwingi wa neema kwa kunijalia uzima na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania wote, familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba uliotufika wa kuondokewa na Spika Mstaafu, Marehemu Mzee Samuel Sitta. Enzi za uhai wake aliweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo katika Taifa hili hivyo basi hatuna budi kumuunga mkono na kumuenzi kwa vitendo vyake vizuri. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa Halmashauri katika kuleta maendeleo ya Taifa hili bado kuna ubadhirifu mkubwa wa watendaji wa Halmashauri katika usimamizi na utekelezaji wa miradi na hii husababisha miradi kutokukamilika kwa wakati na mingine kuvunjika kinyume cha mikataba. Ukitazama kitabu hiki cha taarifa yetu, ukurasa wa 8 utaweza kuona baadhi ya mifano ya miradi ambayo haijakamilika au kutekelezeka. Mfano, mradi wa maji katika Kijiji cha Kayenze Jijini Mwanza wenye thamani ya shilingi milioni 618.7, mradi huu haukutekelezwa. Mradi wa maendeleo wa shule ya sekondari wa ujenzi wa bweni wenye thamani ya shilingi milioni 94.2 katika Kijiji cha Ndogosi na shilingi milioni 100.13 katika Kijiji cha Ruanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambao haujakamilika na mifano mingine inajionesha hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe katika Kamati ya LAAC. Katika utekelezaji wa majukumu yetu, tumebaini mambo mengi hayako sawa katika Halmashauri zetu kwani kuna ubadhirifu mkubwa wa rasilimali za umma pamoja na matumizi mabaya ya fedha ambayo yanakinzana na sheria na kanuni za fedha za Serikali za Mitaa. Hapa naishauri Serikali kuweka sheria kali na kuzisimamia kwa uwazi ili watendaji ambao wanakwenda kinyume na matarajio ya Watanzania na kinyume na dhamira safi ya Mheshimiwa Rais wetu ambaye anataka kuona nidhamu katika rasilimali za umma washughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara kwa mara tunakaa hapa tukiwajadili watendaji wabadhirifu wa mali za umma wakati sheria zipo kwani hawa watendaji wana pembe? Kwa nini wasishughulikiwe kikamilifu? Nini commitment ya Serikali juu ya jambo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati mwingine Serikali inahusika kwenye udhaifu huu kwa kuwaacha watendaji wa Halmashauri kwenye kituo kimoja kwa muda mrefu. Hii humfanya mtendaji kujisahau au kufanya kazi kwa mazoea na wakati mwingine watendaji wengine kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu. Kama wana uwezo kwa nini wasithibitishwe? Kama hawana uwezo kwa nini wasiondolewe katika nafasi hizo ili tuweze kuwabana vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumebaini Halmashauri nyingi hazizingatii Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, aidha, kwa makusudi au kwa matakwa yao binafsi. Tulibaini baadhi ya Halmashauri zinafanya manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya bajeti husika wakati kanuni zinazitaka kufanya manunuzi kulingana na bajeti zilizoidhinishwa. Katika Halmashauri nyingine hakukuwa na kamati za manunuzi hivyo kutokudhibiti ubora na idadi ya bidhaa kulingana na thamani ya pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tulibaini baadhi ya watendaji hutoa zabuni kwa wazabuni ambao hawana sifa wala vigezo vya kupewa zabuni hizo na kusababisha mikataba mingi kuvunjika kabla ya utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iendelee kuwabana watendaji ambao hawazingatii kikamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ambao mara nyingi wamekuwa wakiitia hasara Serikali na kusababisha upotevu wa fedha za umma. Kwa upande mwingine naiomba Serikali kupeleka pesa za miradi ya maendeleo kwa wakati kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuondoa mianya ya kupanda gharama za miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto nilizozitaja hapa juu naongea kwa masikitiko makubwa juu ya jambo hili, Halmashauri zetu nyingi zimekuwa hazipeleki 10% kwenye Mfuko wa Wanawake na Vijana na hii imesababisha vijana kutokupata fursa za kujiajiri au kufanya miradi ya maendeleo. Fedha hizi zingekuwa zinapelekwa kwa wakati zingeweza kusaidia vijana kujiajiri au kujikwamua kiuchumi. Mbali na watendaji kushindwa kupeleka 10% kwa vijana na wanawake lakini pia wameshindwa kupeleka 20% za fedha zinazotoka Serikali Kuu kwa vijiji kana kwamba pesa hizo ni za hisani na siyo lazima. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa kuwa hakuna sheria za kuwabana watendaji kupeleka kwa wakati 10% kwa vijana na wanawake na 20% kwa vijiji itunge sheria ili kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kwa wakati na kwa mtiririko unaofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumzia mengi, kwa haya machache naomba niishie hapa. Ahsante kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.