MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuumuliza swali Waziri Mkuu. Kila ifikapo tarehe 15 Mei ni Siku ya Maadhimisho ya Familia Duniani. Kwa sasa jamii inapita katika wakati mgumu sana kutokana na mmonyoko wa maadili na ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto.
Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuitumia siku hii kama sehemu ya kuielimisha jamii na kuhamasisha umuhimu wa malezi bora pamoja na maadili ili kukabiliana na changamoto hiyo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asharose Mattembe, Mbunge wa Mkoa wa Singida kama ifuatanyo: -
Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo na changamoto ya ukiukwaji wa maadili kwenye maeneo mengi kwa watoto wadogo, wanawake wakati mwingine hata wanaume nao wanaonewa; hayao yote ni mmomonyoko wa maadili na Serikali tuko mstari wa mbele kukemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, dunia iliamua kuwa na siku moja maalumu ya kuelimisha umma juu ya kila mmoja kuhakikisha kwamba tunapiga vita mmomonyoko wa maadili lakini pia ukatili wa kijinsia na watoto vilevile, na sisi Tanzania tumejiunga kwenye siku hiyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Serikali tumejipangaje? Na sisi pia tunasheherekea siku hiyo, siku hiyo pia tunakutana, siku hiyo pia tunatoa elimu kwa umma ya namna ya kila mmoja kushiriki katika kuhakikisha kwamba nchi hii mila zetu, desturi zetu utamaduni wetu lakini maadili ya nchi hii yanazingatiwa ili kupata kizazi ambacho kitakuwa endelevu katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwamba tumejipangaje siku hii; tunajua tarehe 15 ni siku tatu nne zijazo, nitoe agizo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia pamoja na TAMISEMI kila mkoa upange mpango thabiti wa kuwaleta pamoja wananchi kwenye siku hiyo ili haya ninayoyasema yaweze kutekelezwa. Kwanza tutoe elimu, tutoe makaripio lakini pia tuonyeshe dira ya nchi ya umuhimu wa kukinga mmomonyoko wa maadili hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo sasa huu ndio mkakati ambao tunaweza kuutumia. Lakini mkakati huo hauishii tarehe 15 tu, hili suala la kukemea kukiukwa kwa maadili na mmomonyoko ni suala endelevu kwa hiyo wakuu wa mikoa nawaagiza tena, wakuu wa wilaya nawaagiza tena. Tunataka ishuke mpaka kule chini maafisa tarafa, watendaji wa kata, vijiji mpaka vitongojini. Ni muhimu sana Taifa hili tulilinde kwa kuwa na maadili mema, tuendeleze utamaduni wetu na mila na desturi zetu ili kujenga kizazi kipya ambacho kitakuwa endelevu kwa nchi hii na wataweza kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, huo ndio mkakati wa Serikali wa namna ya kuitumia vizuri tarehe 15 mwezi wa tano siku hii ya kupinga mmomonyoko wa maadili.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mkuu, kutokuzingatia kwa sheria za barabarani na uzembe wa madereva wa bodaboda inatajwa kuwa ni sababu inayosababisha vifo vingi kwa Watanzania wengi hususan vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.
Je, Serikali ina jitihada gani za makusudi kuhakikisha kwamba vijana wote waliojisajili katika vijiwe wanapata mafunzo sahihi ya usalama barabarani?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba tunao wajasiriamali ambao wanaendesha bodaboda ambao wanasaidia sana katika kuchangia pato la Taifa pale ambapo wanafanya biashara zao, lakini pia wanasaidia sana Watanzania kupata usafiri wa haraka wa maeneo mafupi mafupi. Wafanyabiashara hawa wameratibiwa kwenye maeneo mbalimbali, lakini pia wengine wako kwenye vijiwe.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya ili kuondoa au kupunguza sehemu kubwa ya ajali na kuwafanya wafanye shughuli zao kwa usalama?
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi na Usalama Barabarani wanaendelea kutoa elimu kwenye makundi haya ya bodaboda kwenye makundi ambayo yameratibiwa na yamesajiliwa na kwa miongozo ambayo imetolewa LATRA sasa wamepewa mamlaka ya kusajili vikundi vyote vya vijana wa bodaboda ili kuwezesha kuwafikia na kuwapa elimu ya usalama barabarani, lakini pia kuwasaidia katika kufanya biashara zao kwa usalama zaidi.
Mheshimiwa Spika, pia uko mpango unaoratibiwa na kila halmashauri kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuwaanzishia SACCOS na ushirika wao mdogo kwa ajili ya kuendesha biashara zao kwa usalama zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kuratibu kundi hili la madereva bodaboda kwa lengo la kupeleka elimu zaidi, lakini pia kuwaanzishia ushirika mdogo mdogo ambao utaweza kuwasaidia kuchangia fedha na kuwaonesha maeneo ya kupta mitaji na kupanua wigo wa shughuli zao za kibiashara na za usafirishaji.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe wito kwa madereva wetu wa bodaboda popote walipo, ni vema sasa wakaamua kukaa maeneo ambayo yako rasmi na yameainishwa na halmashauri ili iwe rahisi sasa kwa taasisi yetu ya LATRA kuwafikia na na kuendesha elimu pamoja na kuwapa fursa mbalimbali za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwahakikishia Watanzania kwamba, eneo hili ambalo limeonekana kuwa na ajali nyingi linaendelea kuratibiwa vizuri kama ambavyo nimesema na Wizara ya Mambo ya Ndani, Kitengo cha Usalama Barabarani kwa lengo la kuwafanya waweze kufanya shughuli zao kwa usalama mkubwa zaidi, ahsante. (Makofi)