Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ester Amos Bulaya (10 total)

MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Kumekuwepo na matukio ya mara kwa mara ya wananchi wa Vijiji vya Guta, Tairo, Nyamtwali na Njabeu kukamatwa na kuliwa na mamba; hadi swali hili linaandikwa, jumla ya watu watatu wameliwa na wengine kumi wamejeruhiwa.
Je, Serikali inajipangaje ili kuokoa maisha ya wananchi kutokana na hatari kubwa ya mamba hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vilivyotajwa na Mheshimiwa Mbunge vinapakana na Ziwa Victoria. Mazingira hayo yanasababisha kuwepo mwingiliano wa shughuli za kibinadamu na makazi ya wanyamapori kama vile mamba na viboko ambayo yanaweza kusababisha matukio ya wananchi kuuawa na kujeruhiwa na wanayama hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imepokea taarifa zilizowasillishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambazo zinaendelea kuhakikiwa, kwamba katika Kijiji cha Guta jumla ya wananchi wanne waliuawa na wengine tisa walijeruhiwa na mamba katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015. Katika kipindi hicho, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na kupokelewa kuhusu matukio katika Vijiji vya Tairo, Nyamtwali na Njabeu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 69 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, kimempa mamlaka Mkurugenzi wa Wanyamapori kukasimu majukumu ya kushughulikia masuala ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa Afisa aliyeidhinishwa. Aidha, Sheria imeainisha utaratibu wa kutoa taarifa za matukio kuanzia kwa Mtendaji wa Kijiji, Maafisa Wanyamapori walio karibu hadi Wizarani kwa hatua zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuokoa maisha ya wananchi kutokana na hatari ya mamba na viboko katika vijiji vilivyotajwa, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itafanya tathmini ya ongezeko la mamba na iwapo itadhihirika kuwa idadi yao ni kubwa kuliko viwango vinavyokubalika, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwavuna wanyama hao. Utaratibu huu utatumika katika maeneo yote yenye uhatarishi wa mamba na viboko. Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi, jinsi ya kujilinda na kujiepusha na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo mamba pamoja na taratibu za kuwasilisha madai ya malipo ya kifuta jasho na machozi kwa wale watakaoathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali, Wizara inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika maeneo hatarishi hususan ambayo yamebainika kuwa na mamba au viboko na kuwasilisha taarifa za matukio haraka kwa Viongozi wa Vijiji husika na Maafisa Wanyamapori walio karibu ili kumbukumbu za matukio na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Wananchi wengi katika Kijiji cha Guta na Tairo walitoa ardhi yao kwa ajili ya mradi wa EPZA, sasa ni takribani miaka saba tangu kufanyiwa tathmini, pia wananchi hao hawaruhusiwi kuendeleza maeneo hayo.
Je, ni lini wananchi wa vijiji hivyo watalipwa fidia halisi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 Kifungu cha 3(1)(g)?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, taratibu za kutwaa eneo la EPZ/SEZ Mara zilianza mwaka 2007 kwa kutambua mipaka ya eneo. Eneo lililopendekezwa ni la Kijiji cha Tairo kilichopo Kata ya Guta, Wilayani Bunda na lilikuwa na ukubwa wa hekta 2,200 likijumisha vitongoji vya Kirumi, Mabatini A & B na Bushigwamala. Uthamini wa eneo la mradi ulikamilika mwezi Julai, 2009 na taarifa yake kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali mwezi Septemba, 2009. Kwa mujibu wa uthamini, fidia iliyotakiwa kulipwa kwa eneo lote ni shilingi bilioni 3.477.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, Mamlaka ya EPZ iliamua kupunguza ukubwa wa eneo na hivyo kuendelea na utwaaji wa eneo la kitongoji kimoja cha Kirumi. Aidha, fidia iliyohitajika kufidia eneo hilo ilikuwa ni shilingi bilioni 2.143 zilizopaswa kulipwa ndani ya miezi sita bila riba. Tayari Mamlaka ya EPZ ilikwishapeleka jumla ya shilingi bilioni 2.358 kwa ajili ya malipo ya fidia ikijumuisha riba ya ucheleweshaji. Fedha hizo zililipwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2009 na 2012 kwa wadai wote, isipokuwa wananchi watatu ambao Ndugu Chacha M. Marwa, Ndugu Gati M. Marwa na Ndugu Juma W. Mgoba, ambao bado wanadai jumla ya shilingi milioni 21.943 licha ya EPZ kupeleka fedha zote kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuchelewa kwa malipo hayo, tarehe 20 Mei, 2016 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara aliagiza TAKUKURU na CAG wafanye uchunguzi wa matumizi ya fedha zilizotolewa na EPZA. Taarifa hiyo inasubiriwa ikamilike na pindi itakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watumishi waliohusika na ubadhilifu wa fedha hizo.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha ndani ya Mji wa Bunda na wahanga wa matukio hayo ni wafanyabiashara wadogo wadogo.
Je, ni hatua zipi za kiusalama zimechukuliwa ili kukabiliana na wimbi la ujambazi na unyang’anyi katika Mji wa Bunda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa hivi karibuni kulikuwa na wimbi la uhalifu kwa Mkoa wa Mara na mikoa mingineyo. Jeshi la Polisi limeendelea kubuni na kutekeleza mikakakati mbalimbali ya kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu, kadri uchambuzi wa uhalifu unavyoonesha mwenendo na mwelekeo wa uhalifu nchini ukitumika kama zana ya kutabiri uhalifu wa baadaye.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kuwajengea uwezo Maafisa Wakaguzi na Askari kwa kuyatambua na kuyaundia mikakati ya utekelezaji mambo yafuatayo:-
(i) Kutabiri mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za uhalifu pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo korofi, wahalifu wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na uhalifu huo.
(ii) Kuyatambua maeneo nyeti yenye vivutio vya uhalifu na kuyapangia ulinzi pamoja na misako na doria.
(iii) Kuendelea kufanya misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchini.
(iv) Kushirikiana na wadau wote wa ulinzi na usalama kubadilishana taarifa za Kiintelijensia pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya zamani.
Mheshimiwa Spika, kwa nafasi hii nitoe rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwabaini, kuwafichua na kuwakamata ili mkondo wa sheria uchukue nafasi yake kwani hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivi viovu nchini.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa Serikali imekuwa na mipango mahsusi ya kuhakikisha kwamba tatizo la walimu wa sayansi linapungua au kumalizika kabisa.
• Je, ni kwa kiwango gani mipango hii imesaidia kupunguza tatizo husika?
• Katika utekelezaji wa mpango tajwa hapo juu, Jimbo la Bunda Mjini na Halmashauri ya Mji wa Bunda imenufaika vipi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kama ifuatavyo:-
(a) Imetenga Vyuo vya Ualimu 10 mahsusi kwa ajili ya kuandaa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati.
(b) Kuongeza udahili wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika vyuo vikuu vya Serikali ambavyo hapo awali vilikuwa havitoi kozi za ualimu, kama Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu Mzumbe.
(c) Kutoa kipaumbele cha udahili katika mafunzo ya ualimu wa stashahada na shahada kwa wahitimu wa kidato cha sita wa masomo ya sayansi na hisabati.
(d) Kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu, sayansi na hisabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianzisha pia kozi maalum ya stashahada ya ualimu kwa masomo ya sayansi na hisabati ambapo wahitimu wa kundi la kwanza wapatao 1,799 watamaliza mafunzo yao ifikapo Mei, 2018 na kundi la pili la wahitimu wapatao 5,441 watamaliza Mei, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha ufundishaji na kuvutia wanafunzi wengi kusoma masomo ya sayansi na hisabati na hatimaye kupata wahitimu wengi wa masomo hayo, Serikali imeendelea kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa vya maabara na kemikali katika shule za sekondari na kutoa mafunzo kazini kwa walimu wa sayansi na hisabati. Mkakati huo unalenga kupata wahitimu wengi zaidi watakaojiunga na mafunzo ya ualimu wa sayansi na fani nyingine zinazohitaji masomo hayo na hivyo kuendelea kukabiliana na upungufu wa wataalam wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Bunda ilianzishwa mwaka 2015/2016 baada ya kugawanywa iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Kabla ya kugawanywa Wilaya hii ilikuwa na jumla ya walimu 144 wa masomo ya sayansi na hisabati. Katika taratibu za kugawana rasilimaliwatu katika Wilaya hiyo, Halmashauri ya Mji wa Bunda ilipewa walimu 69 wa masomo ya sayansi na hisabati.
Aidha, walimu wa sayansi na hisabati walioajiriwa mwaka 2016/2017 waliopangwa katika Halmashauri ya Bunda Mji ni wanane ambao wamepangwa katika shule za sekondari za Kunzugu, Rubana, Bunda, Wariku, Sazira, Sizaki, Nyendo na Daktari Nchimbi. Serikali itaendelea kuajiri na kupanga walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika Halmashauri hiyo, kadiri watakavyopatikana.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Kilimo cha umwagiliaji katika Mji wa Bunda kimekuwa kikitengewa fedha kidogo sana kiasi cha kutokidhi mahitaji kazi husika.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha Ofisi ya Umwagiliaji ya Wilaya ili kufanya kilimo kuwa cha kisasa, endelevu na chenye kuleta tija kwa wananchi wa Bunda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amosi Bulaya, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya miradi ya umwagiliaji ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP I), Serikali ilijenga mabwawa mawili ya Maliwanda na Kisagwa na kujenga skimu tatu za umwagiliaji zenye hekta 220,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa skimu katika Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Bunda. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendelea kuboresha kilimo cha umwagiliaji ili kiweze kuleta tija na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na malighafi kwa ajili ya viwanda.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Vijiji vya Tamau, Nyantwali, Serengeti, Mcharo, Kanzugu, Bukore na Mihale Wilaya ya Bunda vinapakana na Hifadhi ya Serengeti lakini havinufaiki na chochote kutoka katika hifadhi husika.
Je, ni utaratibu gani umeandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori ili kusaidia vijana wanaozunguka hifadhi kupatiwa ajira ili kunufaika na hifadhi husika kama njia mojawapo ya kudumisha ujirani mwema?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inapakana na Wilaya nane ambazo ni Ngorongoro, Meatu, Itilima, Bariadi, Busega, Tarime, Bunda na Serengeti. Aidha, Wilaya ya Bunda ina vijiji sita vinavyopakana moja kwa moja na hifadhi ambavyo ni Serengeti, Nyatwali, Tamau, Balili, Kuzungu na Bukore. Aidha, vijiji vya Mihale na Bukore vinapakana na pori la Akiba la Ikorongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 hifadhi imetenga jumla ya shilingi 32,233,180 kuchangia ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Bunyunyi, Kijiji cha Hunywari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inaendelea kukusanya tozo za huduma yaani hotel levy kwenye hoteli na lodges katika hifadhi zilizopo kwenye eneo la utawala la Wilaya hiyo. Mchango wa hifadhi katika Wilaya ya Bunda kutoka mwaka 2004/2005 hadi mwaka 2017/2018 ni shilingi 276,720,630 ambazo zimetumika kutekeleza jumla ya miradi tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi ya ujirani mwema, Wizara imekuwa ikichangia katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 25 ya mapato yanayotokana na ada ya shughuli za uwindaji wa kitalii zinazofanyika katika mapori ya Akiba ya Ikorongo na Gurumeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2004/2005 hadi 2014/2015 Halmashauri wa Wilaya ya Bunda ilipokea jumla ya shilingi 156,200,125.87. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 na 2017/2018 yaani kuanzia juni mwaka 2017 hadi Januari 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imepokea jumla ya shilingi 77,559,441.84.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. ESTHER A. BULAYA) aliuliza:-

Wananchi wa Vijiji vya Manyamanyama, Nyasura, Bunda Mjini na Balili, mwezi Julai, 2003 walivunjiwa nyumba zao kupisha hifadhi ya barabara baada ya TANROADS kuongeza umiliki wa hifadhi toka mita 16 hadi mita 22.5:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa wananchi hao fidia na ni lini itafanya hivyo?

(b) Je, ni tathmini ipi itatumika kuwalipa kwani kumekuwepo na mserereko mkubwa wa thamani ya shilingi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, lenye Sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Jedwali la Kwanza la Sheria ya Barabara ya Mwaka 1932 pamoja na Marekebisho yake, yaani The Highways Ordinance ya Mwaka 1932 Barabara ya Mwanza – Bunda – Tarime – Kenya Border, yaani Sirari, imeainishwa kama barabara kuu yaani Territorial Main Road. Kwa mujibu wa kanuni zilizotungwa chini ya sheria hiyo upana wa hifadhi ya barabara kuu ikiwemo sehemu ya Balili – Bunda – Manyamanyama yenye urefu wa kilometa 9.8 zilikuwa futi 75 kila upande kutoka katikati ya barabara ambayo ni sawa na mita 22.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1932 barabara hii ilipoainishwa kuwa barabara kuu imeendelea kuwa na hadhi hiyo hadi mwaka 2007. Upana wa hifadhi ya barabara hiyo ulibadilika kutoka mita 22.5 kuwa mita 30 kila upande kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya Mwaka 2007 na sio mita 16 kwenda mita 30, kama alivyodai Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maelezo hayo, Serikali itawalipa fidia wananchi waliokuwa nje ya hifadhi ya barabara ya mita 22.5 wakati eneo hilo litakapohitajika kutokana na mabadiliko ya Sheria Namba 13 ya Barabara ya Mwaka 2007 kwa vile wamefuatwa na barabara. Aidha, ulipaji wa fidia utazingatia Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 2001 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 2001 na Kanuni zake.
MHE. ESTHER N. MATIKO (K.n.y. MHE. ESTER A. BULAYA) aliuliza:-

TANESCO Mkoa wa Mara katika zoezi la kupeleka umeme vijijini walipitisha nguzo za umeme kwenye maeneo ya watu katika Kijiji cha Nyabeu, Kata ya Guta na uthamini ulifanyika na iliahidi malipo kufanyika lakini hadi leo hawajalipwa na badala yake wanaambiwa maeneo hayo ni ya TANESCO:-

(a) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi hao fidia stahiki?

(b) Je, ni kwa nini TANESCO inamiliki maeneo kabla ya kulipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miradi ya kupeleka umeme katika Wilaya za Serengeti, Bunda na Ukerewe ilitekelezwa kati ya mwaka 2003 na 2006 chini ya ufadhili za Serikali za Sweden na Hispania kupitia Mashirika yake ya Kimataifa ya Maendeleo SIDA na Spanish Funding Agency pamoja na Serikali ya Tanzania. Kazi ya tathmini ya mali za wananchi waliopisha mradi ilifanywa na Mtathmini Mkuu wa Serikali na malipo yalifanyika mwaka 2009. Ulipaji wa fidia hiyo ulifanyika kwa kuwashirikisha Watendaji wa Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa kuridhia orodha ya wananchi waliostahili kulipwa fidia hiyo. Jumla ya Sh.135,820,993 zililipwa kwa wananchi waliopisha mradi huo ikiwa ni pamoja na wananchi wa Kijiji cha Nyabeu.

Mheshimiwa Spika, TANESCO huchukua maeneo baada ya kufanya tathmini kupitia Mthamini Mkuu wa Serikali na kuwalipa wananchi wanaopisha ujenzi wa mradi.
MHE. ESTHER A. BULAYA aliuliza:-

Jimbo la Bunda Mjini limekuwa likikumbwa na adha ya ukosefu wa maji safi na salama na Serikali imekuwa ikikwamisha mradi wa maji safi na salama Bunda kwa muda sasa kushindwa kutoa fedha za utekelezaji:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha, ili mkandarasi aweze kukamilisha mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Amosa Bulaya, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Mji wa Bunda ni miongoni mwa maeneo ambayo yana shida kubwa ya maji. mahitaji ya maji kwa Wananchi wa Bunda mjini ni mita za ujazo 9,857 kwa siku wakati uzalishaji wa maji kwa sasa ni mita za ujazo 4,464 kwa siku. Hii inatokana na kutokukamilika kwa ujenzi wa miundombinu wa usambazaji maji baada ya mkandarasi kuondoka eneo la utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha mradi huo unakamilika na wananchi kuanza kunufaika na huduma ya maji, Serikali imechukua hatua kuainisha kazi zote ambazo hazijatekelezwa katika mradi huo, zinazogharimu kiasi cha shilingi milioni 375. Fedha hizo zinapelekwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma, ili ziweze kusimamia utekelezaji wa mradi huo na kuukamilisha, hivyo kuanza kuhudumia Wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini. Ni dhahiri kukamilika kwa mradi huu pamoja na ujenzi wa chujio jipya la maji kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo la maji katika mji wa Bunda.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani juu ya ufufuaji wa kiwanda cha USHASHI GINNERY kilichopo Bunda ili kukabiliana na changamoto ya ajira hasa kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Ushashi kwa sasa kinafanyiwa tathmini ili kubaini hali ya uchakavu na kuona namna bora ya kukifufua. Aidha, Mpango wa Serikali ni kuhamasisha na kuwezesha kiwanda hicho kisichofanya kazi kianze kufanya kazi baada ya kukarabatiwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wizara ya Kilimo na Benki ya Kilimo kwa kushirikiana na kuhakikisha viwanda vilivyokuwa vinamilikiwa na Mara Cooperative Union (1984) Ltd vinafufuliwa na kufanya kazi hivyo kuongeza fursa za ajira.