Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ester Amos Bulaya (30 total)

MHE. ESHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao wanazungukwa na hifadhi kwa Mkoa wa Mara, Tarime, Serengeti, Bunda Mjini na Bunda, wamekuwa wavumilivu sana. Hivi tunavyozungumza hakuna mwaka ambao tembo hawatoki kwenye hifadhi na kuja kwenye vijiji, nazungumzia kwenye Jimbo langu, Kijiji cha Serengeti, Tamau, Kunzugu, Bukole, Mihale, Nyamatoke na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tulienda na Mheshimiwa Jenista, akajionea mwenyewe tembo wanavyoharibu mazao ya wananchi, lakini bado fidia ni ndogo, shilingi 100,000/= mtu anaandaa shamba kwa milioni 10. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Utalii na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…..

MHE. ESTER A. BULAYA: Komeni basi, kelele niongee!

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jenista wamepeleka magari mawili na askari sita kuhakikisha yale mazao ya wananchi yanalimwa. Tunaposema ni lini Serikali mtatafuta ufumbuzi wa kudumu ili hao wananchi waepukane na njaa wakati wana uwezo wa kulima na lini ufumbuzi wa kudumu utapatikana badala ya kupeleka magari na askari kwa ajili tu ya kulinda mazao ambayo yako shambani?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya ziada ya kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alikuwa kule na alitoa ahadi, alijionea mwenyewe na kutoa ahadi kwamba Serikali itafanya juhudi ya kupeleka magari na askari wa ziada ili kuhahakikisha kwamba tembo hawaharibu mazao ya wananchi. Ni wiki moja na nusu sasa magari yale yako kule yanafanya kazi na tunaamini kabisa kwamba hii ni hatua ya kwanza ya Serikali kulishughulikia jambo hili kwa hatua za kudumu.

Mheshimiwa Spika, tumeanza pia kutumia ndege ambazo hazina rubani, tumeanza majaribio katika Wilaya ya Serengeti na Wilaya ya Bunda ili kuzitumia ndege hizi kuwatisha tembo na kuwaondoa katika maeneo ambayo wako karibu na mashamba ya watu na tunategemea kwamba jambo hili litatatuliwa kwa kudumu kwa kutumia utaratibu huo wa teknolojia.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo la maji la Makambako kwa asilimia kubwa linafanana na Jimbo la Bunda Mjini. Natambua Serikali ya Awamu ya Nne ilianza mradi mkubwa wa maji tangu mwaka 2006 ni wa muda mrefu sana na ulikuwa ukamilike, lakini mpaka sasa hivi haujakamilika.
Mheshimiwa Naibu spika, mradi ule unaanzia Kata ya Guta lakini hauna vituo na kama mradi ule wa kupeleka maji katika Mji wa Bunda ukiwa na vituo, vile vijiji jirani Kinyambwiga, Tairo, Guta A, Guta B, Gwishugwamala, vyote vitanufaika na mradi wa maji. Sasa je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kuweka vituo ili vijiji hivyo vinavyopita mradi kwenda Mji wa Bunda vinufaike na mradi huo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna mradi ambao tumetekeleza katika Mji wa Bunda tumeweza kujenga bomba kubwa kutoka Ziwa Victoria, tumeweza kujenga matanki, hiyo ni awamu ya kwanza. Sasa awamu ya pili tutakwenda kusambaza katika maeneo yale ambayo bomba hilo limepita. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba, kazi hiyo tutakwenda kuifanya kwa manufaa ya wananchi wa Bunda. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Angellah, nilikuwa napenda niulize swali fupi la nyongeza.
Je, kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo kwamba fedha hizi zinatumika vibaya na wahusika wanatoa majina hewa, na inasemekana Waziri aliyekuwa ana-deal na TASAF, alitumia fedha hizo vibaya kwa ajili ya kutafuta nafasi ya Urais. Uko tayari kuchunguza hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba malalamiko yoyote tukatakayoyapokea, tutafanya uchunguzi. Nimekuwa nikisema suala hili kuna uwazi mkubwa katika vikao mbalimbali vya vijiji na wakati wowote mtakapoona kuna matatizo, basi msisite kututaarifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami mwenyewe nimejipanga, kutokana na malalamiko mengi ambayo nimeyasikia, kwa kweli hayo majipu tutayatumbua. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ukarabati wa barabara pia unaendana na utanuzi wa barabara. Serikali ilikuwa inatanua barabara kuu ya kutoka Mwanza kwenda Musoma na ilifuata nyumba za wananchi na wakawafanyia tathmini, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo hawajalipwa na kuna wazee wangu kule wanapata taabu sana, nyumba zao hazijalipwa na wanaishi kwa taabu. Miongoni mwa wazee wangu ni pamoja na baba yangu Mzee Wasira, naye nyumba yake imefanyiwa tathmini katika kijiji chetu cha Manyamanyama.
Je, ni lini mtawalipa wananchi wa Bunda kwa sababu mmeshawafanyia tathmini miaka mitatu iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
MWENYEKITI: Lini mtawalipa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Fedha zitakapopatikana tutawalipa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali kuamua kufanya tathmini kwenye Mabaraza ya Watoto ni kwamba kuna changamoto ambazo zipo na kuyafanya Mabaraza hayo yasitetee haki za msingi za watoto hasa za watoto yatima.
Je, tunatambua kwamba kuna center za watu binafsi ambazo zinahudumia watoto yatima na zinafanya kazi kwenye mazingira magumu sana nchi nzima ikiwepo na Jimboni kwangu Bunda. Serikali ina mkakati gani wa kusaidia center hizi ili kusaidia watoto yatima waweze kulelewa vizuri na kupata huduma sahihi hasa za elimu kama wanavyopata wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mmesema Rais aliweka sahihi tarehe 22 Mei, 2015 na kwamba mpaka sasa hivi hamjakamilisha taratibu za kanuni. Ni jambo gani linawakwamisha, hamuoni kwamba kuna haja ya kukamilisha hizi kanuni mapema na mwaka huu wa fedha tutenge bajeti ili Baraza ili lianze na vijana wawe na chombo chao cha kuibana Serikali na kutetea vijana wao katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza muuliza swali Mheshimiwa Ester Amos Bulaya na aliyeuliza swali la msingi Mheshimiwa John John Mnyika kwa kuendelea kufuatilia haki na maslahi ya vijana wa nchi yetu. Pamoja na pongezi hizo naomba kujibu maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwamba kuna changamoto zinazowakabili watu wenye taasisi ama vituo binafsi vinavyolea watoto yatima na kwamba Serikali inawasaidiaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina majukumu ya kutengeneza mfumo wa kisheria ambao utaziwezesha taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na za watu binafsi kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa sheria hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo mfumo huo sasa upo na tunatengeneza Mabaraza haya kwa malengo ya kutoa ushauri kwa Serikali juu ya namna bora ya kuendesha taasisi mbalimbali za binafsi ama za Serikali zinazotoa huduma kwa watoto yatima ama watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwamba tumechelewa kuunda kanuni. Ni miezi takriban sita tu toka sheria ile imesainiwa na Mheshimiwa Rais na sidhani kama tumechelewa. Imani yangu ni kwamba, kanuni zitatengenezwa haraka na zitaanza kufanya kazi kwa sababu mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu na watu wengi walikuwa busy na kwa kipindi kirefu, hivyo Mawaziri wasingeweza kufanya kazi ya kutunga kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ipo kazini, naomba atuamini, tutatunga kanuni hizo haraka na tutawashirikisha wadau wote ili mawazo yao yaweze kuwemo humo ndani na mwisho wa siku tutunge kanuni zilizo bora ambazo zitaweza kuleta ustawi wa vijana wa nchi yetu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tunajua kuna Halmashauri nyingi mpya na kutangaza Halmashauri mpya ina maana kama Halmashauri ilikuwa moja kuna mgawanyo wa vyanzo vya mapato na kadhalika. Hizi Halmashauri mpya nyingi vyanzo vyake vya mapato ni vidogo ikiwepo Halmashauri ya Mji wa Bunda na huko ambako wewe pia una interest nako barabara nyingi hazipitiki.
Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanapeleka fedha za kutosha kwenye Halmashauri hizi mpya kupitia TANROADS Mikoa ili waweze kuhakikisha barabara zinapitika ikiweko na barabara yangu kutoka Rwahabu – Kinyabwiga na barabara ya kutoka Tairo – Gushingwamara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza huko nyuma kwamba TANROADS Mkoa siyo wa TANROARD Taifa na wale Wahandisi wa Halmashauri wote sasa nchi nzima, wakae na kuhakikisha zile barabara ambazo zimekatika sasa tunazirudishia, hii ni pamoja na Mfuko wa Barabara ambako fedha zinatoka. Tunajua hizi barabara zingine ni za Halmashauri, zingine za Mkoa na zingine za Kitaifa lakini hii ni dharura, kwa hiyo wote tunashirikiana kwa pamoja ili tuweze kufungua mawasiliano pale ambapo yamekatika.
MHE. ESTER N. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Naibu Waziri wa Fedha kwa makini, kwa jinsi alivyojibu ametutajia figure kubwa sana ambazo zimeenda katika sekta ya kilimo, lakini ni wazi na Waheshimiwa Wabunge wanajua bado wakulima wetu kilimo chao ni cha kusuasua na wanalima katika mazingira magumu. Hata wale ambao wanajitokeza katika kilimo cha umwagiliaji wakiwemo watu wangu wa Tamau, Nyatwali na maeneo mengine wanakosa vifaa. Mna mkakati gani wa kuhakikisha hizi figure zinaendana na hali halisi ya mkulima mmoja mmoja?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru kwa kuelewa kwamba kiasi hiki nilichokitaja ndicho ambacho kimetoka Benki ya TIB (Tanzania Investment Bank) kwenda katika miradi ya kilimo na miradi mingine niliyoitaja. Mimi kama Naibu Waziri wa Fedha na Mipango jukumu langu ni kuhakikisha pesa hizi zinafika kwa wale wanaomba pesa hizi. Kwa hiyo, naamini tutafanya kazi kwa ushirikiano mzuri mimi na Waziri wa Kilimo, mtani wangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ili tuhakikishe sasa pesa hizi zinawanufaisha walengwa na zinaweza kukidhi mahitaji yale waliyoomba.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Bunda Mjini tangu nikiwa Mbunge wa Viti Maalum nilikuwa nazungumzia mradi wa maji wa kutoka Nyabeu kuja Bunda Mjini. Huo mradi una miaka nane, sasa niulize hivi ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mradi ule, wananchi wa Bunda ambao hawajawahi kupata maji safi na salama tangu uhuru waone na wenyewe ni wananchi wa Tanzania na ndiyo liwe swali la mwisho kuuliza katika Bunge hili Tukufu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nikiri wazi kwamba Mheshimiwa Ester toka tukiwa katika timu moja alikuwa akiuliza swali hili, naomba niseme.
Mheshimiwa Spika, lakini najua kabisa katika mpango wa maji ambao nadhani Wizara ya Maji watakapokuja ku-table bajeti yao hapa watazungumzia jinsi gani wana programu kuhakikisha maeneo haya miradi yote ya maji inaenda kukamilika. Ukiangalia jinsi gani watazungumza katika bajeti yao ya Wizara ya Maji, sitaki kuwazungumzia sasa. Lakini nikijua kwamba Wizara ya Maji na TAMISEMI ni Wizara pacha, tunahusiana Wizara ya Maji, TAMISEMI, Kilimo halikadhalika na Wizara ya Afya. Mambo yetu yanaingiliana yote kwa pamoja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Ninajua kabisa katika mpango wa maji wa sekta ya maji namba mbili imeweka mipango ya kumalizia miradi yote ya muda mrefu. Mimi ninaamini wananchi wa Bunda kipindi hiki sasa ule mradi wa maji kama Serikali ilivyokusudia utaweza kukamilika katika kipindi hiki.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka mwezi Machi, REA walikuwa wamepata karibia asilimia 40 tu ya fedha za kwenda kumalizia katika REA ya Awamu ya Pili. Nilitaka kujua, mpaka sasa hivi Wizara yako imepokea kiasi gani ili vijiji vyangu ambavyo vilikuwa viporo kabla ya hii REA ya Awamu ya Tatu, kama Kunzugu, Mihale, Nyamatoke, Bukole, Kamkenga, Kangetutya, Rwagu na maeneo mengine yapate umeme katika ule ule mpango wa REA ya Pili na huu wa REA ya Tatu?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba tulikuwa asilimia 40, lakini kwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 75, kwa hiyo jinsi ambavyo tunakusanya fedha na ndivyo jinsi ambavyo Hazina inatupatia fedha. Kwa hiyo, kwa mipangilio inavyokwenda na wakandarasi tumewaambia huu mwezi Mei tutafanya tena tathmini kwa kila mkandarasi amefanya kazi kiasi gani, nadhani hadi kufikia mwezi Mei tutakuwa tumefika karibu asilimia 80. Mheshimiwa Mbunge nataka kukuhakikishia na ndiyo maana tumekubaliana na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kama miradi yako ya REA Awamu ya Pili haikukamilika ni lazima itapewa kipaumbele kwenye REA Awamu ya Tatu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kwa baadhi ya majibu ya uongo ambao Mheshimiwa Naibu Waziri ameyajibu. Mimi ndio
Mbunge wa Jimbo husika na kuna mwananchi wangu nimemhudumia katika Hospitali ya DDH. Aliyekupa hizo taarifa kamwulize vizuri, amekuongopea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda sasa kwenye swali. Sheria ya Kazi Na. 6, mtu anapokufa kazini, analipwa fidia shilingi milioni 10. Hawa wananchi wangu walikuwa kazini, mbali na kwamba wamejiajiri wenyewe, mwalipe fidia, siyo kifutajasho cha laki moja moja. (Makofi)
Swali la pili; Mheshimiwa Waziri, tatizo la mamba katika vijiji nilivyokwambia ni kubwa sana, hata kwa kaka yangu kule Mheshimiwa Kangi, wananchi wanavua kienyeji kwa kutumia kuku. Lini Wizara yako itapeleka wataalam mwavue? Wananchi wangu wanakufa kila siku wanakuwa vilema halafu unatoa majibu mepesi hapa!
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba umesema swali la kwanza pengine lingejibiwa na Waziri wa Sheria lakini napenda kutoa sehemu ya majibu.
Mhehimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya kazi zake kwa kutumia mfumo wake. Kwa hiyo, taarifa ambazo zimo katika majibu niliyoyatoa zimetoka kwenye Halmashauri ya Bunda na vyombo vya Serikali vilivyopo kule. Kwa hiyo, kwa kuwa Mheshimiwa Ester Bulaya ni Mjumbe wa Halmashauri ya Bunda, anaweza kwenda kuwahoji waliotoa taarifa hizi ambao ni Halmashauri inayohusika kwamba kwa nini wameleta majibu ya uongo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia kwamba Serikali inalipa kifuta jasho au kifuta machozi na siyo fidia; na Mheshimiwa Mbunge angependa badala yake tulipe fidia, kwa sababu kiwango cha shilingi laki moja ni kidogo; nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Hakuna namna yoyote ambayo unaweza kuendesha nchi bila kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi ni utaratibu uliopitishwa kwa mujibu wa sheria ambayo imepitishwa na Bunge hili. Iwapo itaonekana kwamba utaratibu huo haufai kwa namna yoyote ile, ni wajibu wa Waheshimiwa Wabunge kwa niaba ya wananchi, Mheshimiwa Ester Bulaya akiwa mmoja wao kuleta mapendekezo ya kufanya mapitio upya ya Sheria hii na kama itafaa, pengine Serikali inaweza ikaanzisha utaratibu mwingine badala ya huu.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuongezea jibu zuri ambalo limetolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza napenda niseme kwamba Wizara itafuatilia kuona kama kuna taarifa zaidi ya zile ambazo tunazo ili tuweze kuzishughulikia kama ambavyo tumeshughulikia sheria hizo nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mimi sio Mwanasheria, lakini najua kwa sababu nilifanya kazi kwenye Wizara ya Kazi, kwamba hakuna Sheria ya Kazi ambayo inafidia raia wakati yuko kwenye shughuli zake. Sheria ile ya Kazi ni ya wafanyakazi kama ambavyo inajulikana kwenye sheria ile.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi yetu ni migogoro ya ardhi na eneo ambalo inasemekana kumekuwa na migogoro ya ardhi ni pamoja na eneo la Kibada Kigamboni ambapo kuna viwanja vilipimwa na Serikali na wananchi wakapewa na Wizara husika. Sasa, nataka kujua nini status ya eneo hilo wakati Wizara imepima, imewapa wananchi lakini leo imetokea kwamba eneo ambalo amepewa mtu mmoja tayari amejitokeza mtu mwingine amesema hilo eneo ni la kwake wakati Wizara ndio wametoa hati; nini status ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka sote hapa Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi akiwa hapa Bungeni alitamka kwamba migogoro yote ya ardhi ambayo Waheshimiwa Wabunge mliwasilisha humu Bungeni na migogoro mingine ambayo inahusisha taarifa mbalimbali ambazo zimeshafanyiwa uchunguzi, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliunda Tume ya kupitia taarifa hizi za uchunguzi zilizofanyika, lakini na migogoro ambayo Waheshimiwa Wabunge tayari waliiwasilisha kipindi cha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekit, nataka kuwaambia kwamba, timu hiyo ya wataalam iko kazini na Mheshimiwa Bulaya avumilie, asubiri, taarifa hiyo ya wataalam itakapokamilika tutawaletea hapa Bungeni ili kila mmoja ajue status ya kila eneo la mgogoro ambavyo limeshughulikiwa na Serikali.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi Mheshimiwa Waziri alivyojibu swali lake, kwamba bado hawajagundua nani ambaye amesababisha tatizo, lakini Serikali iliji-commit kulipa fidia. Sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa suala la pamba limekuwa ni issue kubwa sana.
Je, Mheshimiwa Waziri, tatizo la pamba likijitokeza tena, uko tayari kujiuzulu kwa sababu majibu yako tayari unajikanganya hapa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri kama ofisi inawezekana anavyosema Mheshimiwa Mbunge alitoa majibu ya kusema Serikali italipa fidia. Lakini hizo fedha ni fedha ya umma ambayo haiwezi ikalipwa tu bila kujiridhisha kwa kweli kwamba anayelipwa anastahili na kwamba Serikali inayo liability katika hilo jambo. Kwa hiyo, ni lazima kuwa na uhakika kwamba kwanza kweli Serikali inayo liability katika hilo jambo, lakini pili anayelipwa anastahili kulipwa hizo fedha na ndiyo maana hatua hizi zinafanyika. Kama nilivyosema kwenye suala la viuatilifu, tumekwisha jiridhisha beyond doubt nani wamehusika na hilo kosa la kusababisha dawa zisiwe na effect katika kuua wadudu kama ilivyotarajiwa na kwa hiyo hawa watachukuliwa hatua kama sheria inavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata kwenye mbegu, tutakapajiridhisha exactly ni nani muhusika kwanza hawa watachukuliwa hatua na kama ni Serikali, itakuwa na wajibu wa kulipa tutafanya namna hiyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Dhamira ya Benki ya Kilimo ni kuwasaidia wakulima wadogowadogo, lakini kwa muda mrefu wanaokopa katika benki hii wengi ni wakulima wakubwa ambao pia wanakopesheka katika mabenki mengine.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itahakikisha benki hii inawanufaisha wakulima wadogowadogo ambao wengi wako vijijini na si wale wakulima wakubwa ambao wanaweza kukopesheka katika mabenki mengine?
ambao wanasemwa ni wakubwa ambao wanakopeshwa na Benki ya Kilimo, benki hii imewakopesha wakulima wadogowadogo katika mikoa ambayo nimeitaja katika vikundi. Mpaka sasa katika hiyo mikoa niliyotaja, vimekopeshwa vikundi 89 ambavyo vina wakulima wadogowadogo 21,526 na hawa wanaokopeshwa wanakopeshwa mikopo midogomidogo kutegemea, wengine wanapata mikopo miaka miwili, wengine miwili mpaka mitano na wengine mitano mpaka 15. Kwa hiyo, si kweli kwamba benki hii imekuwa inakopesha wakulima wakubwa tu. Tunawakopesha pia vikundi vya wakulima wadogowadogo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nasikitika kwamba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara wamemuongopea kabisa. Kwa sababu suala la EPZ nilianza ku-deal nalo tangu nikiwa Mbunge wa Viti Malaam na mpaka Mbunge wa Jimbo, hiyo Kata ndiyo Kata yenye wapiga kura wengi na ndiyo waliyonipa kura nyingi kwa sababu ya hiki kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pesa zilizotumika kulipa EPZ ni shilingi 1, 240, 000, 000, hakuna ukaguzi wowote ambao umefanyika, wala uchunguzi wowote mpaka hivi sasa tunavyoongea. Kilichotokea, Mkaguzi wa Ndani alitoa ripoti kwa Mkuu wa Mkoa ambaye naye katumbuliwa kuhusiana na hili na Mkuu wa Wilaya aliyeshiriki na ubadhirifu huu ametumbuliwa kwa ajili ya udanganyifu wa suala hili.
Swali la kwanza, je, uko tayari sasa kuagiza TAKUKURU na CAG kufanya uchunguzi ili watu waliokuwa wakilindwa na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wiliya washughulikiwe?
Swali la pili, nini hatma ya wananchi wa eneo hili ambao waliahidiwa watapelekwa katika eneo mbadala ili kupisha mradi wa EPZ na wala hawana tatizo nalo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya.
Mheshimiwa Spika, taarifa nilizopewa na watendaji wangu wanasema wamelipa bilioni 2.3, yeye alizopata ni bilioni moja, hapa kuna tatizo na hili ni tatizo la kipolisi. Mimi pamoja na CAG pamoja na TAKUKURU, nitamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi anisaidie. Hili siyo suala la TAKUKURU siyo suala la Polisi, tofauti ya bilioni moja ni pesa kubwa sana wala haihitaji uchuguzi, ni kupiga foleni watu, aliyelipwa akae huku, ambaye hakulipwa akae huku watu wanakwenda selo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niko tayari na nitaomba Mheshimiwa Mwigulu anisaidie na Mheshimiwa Simbachawene, kwa sababu wanaotuhumiwa ni watu wa TAMISEMI. Hili siyo langu, hivi siyo viwanda hivi, hili siyo eneo langu ni la Mheshimiwa Simbachawene na Mheshimiwa Mwigulu. Wizi siyo viwanda.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Bulaya nashukuru, Serikali itakwenda kulishughulikia tunapokwenda Mawaziri watatu kukamata panya hao, tutahakikisha wananchi wanapewa maeneo mazuri. Zaidi niwaambie watu wa Mara, jambo la muhimu linaloniuma ni kuhakikisha watu Mara tunatafuta wawekezaji ili EPZA iweze kutengeneza sehemu ya uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya ukanda ule.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimesikia na tutalishughulikia!
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mbali na changamoto ambayo inakikabili Chuo cha Maendeleo ya Jamii - Kisangwa kuhusiana na kutopata fedha za uendeshaji, karakana na kadhalika lakini chuo hicho pia hakina gari. Hivi tunavyozungumza aliyekuwa Mkuu wa Chuo alijiuzia VX kwa Sh. 600,000/= na kufanya Mkuu wa Chuo wa sasa hivi asiwe na gari na kusababisha shughuli za chuo zisiende. Je, Serikali iko tayari kushughulikia ufisadi huu kwa sababu hakuna VX inayouzwa Sh. 600,000/= na kupeleka gari ili chuo hicho kiendeshe shughuli zake vizuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali kutoka kwa rafiki yangu Mheshimiwa Ester Amos Bulaya kuhusu kile anachopenda kukiita ufisadi. Majibu ya Serikali ni kwamba kwenye kuuza mali za umma ambazo zimemaliza muda wake na ama zimekuwa classified kama ni dilapidated ama mali zilizochoka unajulikana na umeandikwa. Kwa hivyo, kama Mheshimiwa Mbunge ana ushahidi kwamba utaratibu huu ambao umeandikwa kwenye sheria mbalimbali za kuuza mali za Serikali zilizochakaa haukufuatwa, naomba anikabidhi nyaraka alizonazo ili niweze kufuatilia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wakandarasi kujenga barabara chini ya kiwango au kukarabati barabara
chini ya kiwango si jambo geni na Mheshimiwa Spika, na wewe ni shahidi barabara ya kutoka Morogoro kuja hapa
Dodoma sasa hivi tayari imeshavimba, Wabunge wote mnajua. Lakini hiyo barabara ninayoitaja pia inapita Jimboni
kwako, nadhani shahidi tayari sasahivi imeshaanza kuvimba, nimeona tu nikuulizie bosi wangu.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pia mashahidi, ukarabati unaofanywa hata kwenye barabara
za hapa Dodoma, Area D, Area C pia uko chini ya kiwango, unaigharimu sana Serikali kuwa tunakarabati barabara mara kwa mara pindi Waheshimiwa Wabunge wanapokuja Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kingine, barabara ya kutoka Musoma – Bunda na yenyewe pia, ilishaharibika kabla hata
ya kukabidhiwa.
Swali langu, je, mna mkakati gani katika barabara mpya ya kutoka Kisorya - Bunda Mjini - Nyamswa, ambayo
bado haijajengwa, inajengwa kwa kiwango cha lami, ili barabara hiyo isiigharimu Serikali fedha za kutosha na iwe ya kiwango? Naomba jibu zuri na ujue unamjibu Waziri Kivuli na Mjumbe wa Kamati Kuu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nimechanganyikiwa kwa sababu swali ninalotakiwa nilijibu ni moja, sijui ni jibu lile la Mbande, niache lile la Kisorya au nijibu la Kisorya niache haya ya Mbande?
SPIKA: Nimekuachia kama Engineer nikajua tu utapata moja la kujibu hapo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka
Morogoro hadi Dodoma na viunga vya Dodoma huwa zinajengwa kwa kufuata mikataba. Katika ile mikataba kuna
viwango ambavyo vinawekwa kwa mkataba na kutokana na kiwango cha fedha. Kwa hiyo, mimi nimhakikishie
Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba barabara hizi za kutoka Morogoro hadi Dodoma, pamoja na Dodoma Mjini,
tunahakikisha kwamba kile kiwango cha mkataba kinafikiwa. Nichukue nafasi hiyo kuwapongeza watu wa
TANROADS kwa kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa kiwango kikubwa na pale inapotokea mkandarasi
aliyetengeneza hajafikia kiwango, hatua bhuwa zinachukuliwa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwenyekiti wangu wa zamani wa vijana.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwenye majibu yake, anasema moja ya mikakati ni kuhakikisha wanafanya doria imara; ni jambo zuri kabisa. Sasa huwezi kufanya doria imara kama huna magari mazuri.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Bunda kuna magari mawili na mabovu na ndiyo ambayo yanatakiwa yafanye doria kwenye Jimbo la Kangi na Jimbo la Boni. Sasa uhalifu unazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, maswali yangu, katika kuhakikisha
hiyo doria imara kama Mheshimiwa Waziri amejibu, je, Serikali iko tayari sasa kutupatia gari jipya ili kupunguza vitendo vya uhalifu kwa kufanya hiyo doria imara? (Makofi)
Swali la pili, ili kuweza kukabiliana na hizi changamoto, moja ya vituo ambavyo vipo hohehahe ni Kituo cha Polisi cha Bunda. Sasa wameanza mradi wa ujenzi wa jengo la upelelezi kupitia michango ya polisi, ya wadau, nami Mbunge wa Jimbo kupitia Mfuko wa Jimbo nimewachangia. Serikali mpo tayari kuungana na jitihada zetu kukamilisha jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la magari, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea changamoto yake ya magari. Wakati ambapo magari yatapatikana tutatoa kipaumbele kwa Jimbo lake ili tumpatie gari la ziada ili aweze kuongeza nguvu ya yale magari machache yaliyopo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni suala la ujenzi
wa kituo cha upelelezi. Kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuamua kutoa fedha za Mfuko wake wa Jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi. Natambua kwamba Mfuko wa Jimbo una fedha kidogo na Majimbo yetu yanachangamoto nyingi. Kwa hiyo, kitendo cha Mheshimiwa Mbunge kuamua kwamba sehemu ya fedha hizo ziende kwenye ujenzi wa vituo vya polisi ambavyo vina changamoto kubwa ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Ester kwamba jitihada zake pamoja na za wananchi zimezaa matunda, kituo hicho kimekamilika, tunatarajia wakati wowote mwaka huu tutakizindua. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda niulize swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri shemeji yangu. Hivi tunavyoongea mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Bunda unakaribia miaka 10 bila wananchi wa Bunda kupata maji safi na salama, yaani kama mihula ya Mheshimiwa Rais ni mihula miwili. Tatizo kubwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni mkandarasi, mkandarasi yule ni mwizi, ana madeni, kila pesa mnayoiweka Serikalini kwa ajili ya kukamilika mradi ule ili wananchi wa Bunda wapate maji safi na salama…
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 tumetenga bilioni 1.6 kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kutengeneza chanzo cha maji. Tumeendelea na shughuli ya kufanya ununuzi wa makandarasi, tukapata makandarasi wabaya, kwa hiyo tumetangaza tena. Hata hivyo, kuhusu hao wakandarasi hao wanaoendelea Mheshimiwa Bulaya nimuahidi kwamba nitaenda huko niende nikawaone. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wanyama waharibifu ni kubwa sana katika Jimbo langu la Bunda Mjini na Jimbo la kaka yangu Boni. Sisi wananchi wa Mkoa wa Mara hatuhitaji kuomba chakula na mwaka jana Mheshimiwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, Mheshimiwa Jenista alikuja akaliona tatizo hilo na Mheshimiwa Waziri mwenyewe anajua, tatizo la tembo kuharibu mazao ya wananchi, kuua wananchi pamoja na mali zao. Sasa nataka kujua, ni lini Serikali mtahakikisha mnakuwa na mkakati wa kudumu wa kumaliza tatizo hili katika vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika Mkoa wa Mara na hasa Wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na Wilaya za maeneo yale kuna kadhia kubwa sana ya wanyama waharibifu wanaotoka hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuingia katika mashamba na wakati huu ambapo mavuno yanakaribia ndiyo kadhia hii inaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi, mwaka tutachukua hatua ya kuongeza askari na magari ya patrol ili kuhakikisha kwamba kama mwaka jana tunawaokoa wananchi na tatizo hili.
Pili, tunazungumza na washirika wetu wa maendeleo kuona ni namna gani tunaweza kuweka fensi ya kilometa 140 ili kuangalia kwa majaribio kama itakuwa ni suluhisho la tatizo hili.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi napenda niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini na Halmashauri ya Mji ya Bunda Mjini wanataka Hospitali ya Manyamanyama iwe Hospitali ya Wilaya na tayari vikao vya Halmashauri vilishakaa. Tatizo hawana jengo la mortuary na tayari kupitia wadau wameshaanza ujenzi. Je, Serikali haioni kwamba inapaswa kuisaidia Halmashauri ya Mji wa Bunda na hasa ukizingatia Halmashauri ile ni changa kumaliza jengo lile ili sasa ile dhamira ya Hospitali ya Manyamanyama kuwa hospitali ya Wilaya ifanikiwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata manufaa na faida ya kwenda kutembelea Halmashauri ya Bunda nikiwa na ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa bahati mbaya Mheshimiwa Mbunge hakuwepo, angekuwepo tungeenda Manyamanyama tukapata fursa ya kujua nini hasa ambacho kinatakiwa kifanywe ili tuweze kushirikiana. Naomba kwa wakati mwingine tuungane tuone namna nzuri ya kuweza kusaidia ili wananchi waweze kupata huduma.
MHE. ESTER A. BULAYA: Ahsante Mwenyekiti na Mtemi wa Wanyantuzu kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa dhamira ya Serikali ya kuanzisha benki ya kilimo, ni kwa ajili ya kuinua sekta ya kilimo na kuwasaidia wakulima kwa ujumla ambao ndiyo sekta hiyo ndiyo inayochangia katika ajira pamoja na pato la Taifa. Tunajua, Benki ya Kilimo ….
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo naenda Benki ya Kilimo ina mtaji wa Bilioni 60, ili kufikia malengo ya kuwasaidia wakulima ilikuwa inapaswa kuwa na Bilioni 800, Serikali mkaji-commit kwa kila mwaka kwa miaka minane kupeleka bilioni 100, 100 lakini mpaka hivi tunavyoongea hamjapeleka.
Je, ni lini Serikali sasa mtapeleka fedha hizo kwenye Benki ya Kilimo, ili wakulima wanufaike na benki hiyo na kuhakikisha wanachanigia zaidi katika pato la Taifa na Sekta ya Kilimo kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jana tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha alisema vizuri sana kuhusu Benki ya Kilimo. Kwa hiyo, na Mheshimiwa Ester alikuwepo naamini anakumbuka na Bunge lako Tukufu linakumbuka kwamba dhamira ya Serikali yetu ni kuhakikisha kwanza tunaimarisha ufanisi wa utendaji kazi wa Benki ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba nikope maneno yako uliyoyasema jana; “Kwamba tayari tuko mchakato unaelekea mwisho wa kuhakikisha menejimenti inakaa vizuri ili pesa ya Serikali inayoingizwa kwenye benki hiyo iweze kufanya kazi vizuri na waweze kuwafikia wakulima wetu.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikumbushe Bunge lako Tukufu, nimekuwa nikisema benki hii sasa pamoja na ukakasi uliopo kwenye menejimenti lakini tayari walishaanza mchakato wa kufungua matawi kwenye kanda sita ndani ya Tanzania, hii ikiwa ni dhamira ile ya dhati ya Serikali yetu yakuhakikisha benki hii inawafikia wakulima kule walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira yetu ni ya dhati na ndiyo maana tumechukua pesa kutoka African Development Bank na kuzipeleka benki ya Kilimo. Kwa hiyo, hii bilioni moja, moja kwa miaka nane inayosemwa mbona hatuongelei hizi pesa za African Development Bank. Hizi ni pesa za Serikali pia na ndiyo maana tumepeleka ili kuiwezesha benki yetu iweze kuhudumia wananchi wetu. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza ninachoweza kusema Mheshimiwa Waziri katika mgawanyo takwimu wamekuongopea, Halmashauri yangu imepata walimu ambao hawafiki hata 60; ni 58 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kusema, hao wanane Bunda sisi hawatutoshi. Hisabati mahitaji ni 55 waliopo 20 peke yake, fizikia mahitaji 27 waliopo 10 peke yake, biology mahitaji 32 waliopo 15 chemistry kidogo
ndio mmejitahidi mahitaji 29 waliopo 21 bado wanane. Ukiangalia yaani hao tuliogawanywa na mahitaji kwa ujumla wake ni 68. Ni lini Serikali mtatupa Bunda walimu wa sayansi? Tumechoka Bunda kuwa miongoni mwa Wilaya zinazofanya vibaya katika masomo, swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunajia TEA ina- deal na masuala ya infrastructure. Hivi kwa nini Serikali msitenge fedha za kutosha, mkawapa TEA wakajenga pia na nyumba za walimu mbali na kwamba kuna changamoto kwenye shule za walimu ili pia walimu wawepo shuleni kuepuka usumbufu ambao unajitokeza na kusababisha watoto kufeli halafu hatimaye tunalaumiana mnaanza kuwafukuza wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu uliopo katika shule za Jimbo lake; ni kweli kwamba kuna upungufu wa walimu wa sayansi nchi nzima na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza mikakati iliyopo ya kuhakikisha kwamba, tunaondokana na upungufu huo.
Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu kwamba tunafahamu kwamba kuna upungufu na si kwake tu. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba, upungufu huo unafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kujiingiza zaidi katika kujenga shule za walimu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutegemeana na bajeti ambayo TEA wanatengewa ambayo kimsingi kwa miaka mitatu sasa mfululizo wanatengewa shilingi bilioni 10, itaendelea kujenga nyumba za walimu, lakini ikumbukwe kwamba jukumu hasa la TEA ni suala la kuongeza ubora, lakini vilevile kuhakikisha kwamba kuna upatikanaji wa elimu na suala la usawa yaani access, equity na quality.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, TEA haikuundwa ili ichukue majukumu yote ya miundombinu za shule katika Halmashauri zetu. Jukumu la kujenga miundombinu katika shule ambazo ziko chini ya Serikali za Mitaa litabakia kuwa jukumu la Serikali za Mitaa.
Kwa hiyo, nimuombe Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu sisi wenyewe ni Madiwani tuendelee kuwahamasisha wananchi washirikiane na Serikali kujenga miundombinu kwa ajili ya shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini TEA vilevile na hasa nyie Waheshimiwa Wabunge mkiwaongezea bajeti kwa sababu nyie ndiyo hasa mnaongeza bajeti itaendelea kufanya hayo kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa, ubora lakini yale maeneo ambayo yatakuwa na upungufu yaweze kupatiwa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze utaratibu kwamba ukiacha mbali la Halmashauri yenyewe kuomba TEA waweze kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi lakini vilevile Wizara kwa kushirikia na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunakusanya takwimu, kwa hiyo, tunajenga miundombinu kulingana na takwimu ambazo tumepata za nchi nzima. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Mkutano wa World Heritage ambao ulifanyika nchini Qatar, Pori la Akiba la Selou na lenyewe lilitangazwa kama urithi wa dunia na nchi mbalimbali zilikubaliana kuisaidia Tanzania takribani dola milioni mbili kwa ajili ya kupambana na ujangili wa tembo. Nataka kujua status ya hali ya ujangili wa tembo katika Pori la Akiba la Selous?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa sasa hivi hali kidogo ni nzuri, hakuna tena ujangili kama ambavyo umekuwepo na ndiyo maana matukio mbalimbali yale ambayo tulikuwa tunapotelewa na tembo na maeneo mengine yamepungua kwa kiwango kikubwa sana katika hili eneo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Kati ya wakulima wanaopata taabu kwa kulaliwa bei na watu ambao hawana soko la uhakika ni wakulima wa pamba. Kwa sababu wanunuzi wengi wanalangua na wanapanga bei wanayoitaka wao na mwisho wa siku wakulima wanapata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, ni lini Serikali itawatafutia wakulima wa pamba soko la uhakika ili na wenyewe waweze kunufaika na kilimo cha pamba? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nitofautiane kidogo sana na Mheshimiwa Bulaya kuhusu uhakika wa soko. Soko la pamba ni la uhakika na hatujawahi kuwa na tatizo la kuuza pamba nchini. Pamba ni bidhaa inayouzwa na nchi nyingi duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, soko la Tanzania haliwezi kuwa tofauti na Soko la Dunia la Pamba. Majadiliano yanapofanyika kati ya wadau na wauzaji, ni zao pekee ambalo kwa msingi wadau wanajadiliana na wanunuzi, wanafikia muafaka wa bei. Hii inakuwa pegged kwenye bei ya pamba katika Soko la Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bei inayopatikana siyo kwamba inawalalia wakulima, lakini pia inawapa faida wafanyabiashara na wakulima wanapata haki yao kutegemea na soko la dunia lilivyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi kwamba hakuna mtu anayeunga mkono uvuvi haramu na sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa tumekua kutokana na samaki. Kitu ambacho tunahoji ni namna gani hii operesheni watu wasiowatakia mema wananchi wetu wanavyoiendesha.
Mheshimiwa Spika, nilimwambia Waziri Jimboni kwa Mheshimiwa Kangi watu walienda kuvunja mafriji (fridges) ma-frizer (freezers) na kuwakamata wale watu na kuchukua pesa zao kinyume na utaratibu. Hivi navyoongea jimboni kwangu juzi Polisi wamewavamia akina mama na kuwapiga mabomu wakishirikiana na Mkuu wa Wilaya. Swali langu, hivi ni kweli operesheni yenu inalenga kunyanyasa watu na mnatoa tamko gani kwa watu ambao wanafanya vitu vya namna hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza natoa shukrani kubwa sana kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuwa Bunge zima limetuunga mkono juu ya suala linalohusu uvuvi haramu, kwa sababu uvuvi haramu ni uharibifu wa maliasili za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, swali lake linahusu ni kwa nini watu wanaotekeleza jukumu hili la operesheni dhidi ya uvuvi haramu wananyanyasa wananchi. Kwa heshima kubwa na taadhima nataka niseme kwamba tunachokifanya tunakiita kwa kifupi Operesheni Uvuvi Haramu, lakini sisi tunakwenda mbele zaidi na kupambana na biashara haramu ya mazao yanayotokana na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, kesi anayoisema Mheshimiwa Ester Bulaya ni maalum, kwamba kuna tatizo la wananchi katika jimbo lake au jimbo la Mheshimiwa Kangi Lugola wamenyanyaswa katika mafriji yao. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali ipo kuanzia katika ngazi za Wilaya, sisi tuko tayari kupokea malalamiko yote yanayohusu specific cases na kuyashughulikia.
Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie tumewatuma kufanya kazi ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi na siyo kuwanyanyasa watu. Kwa hivyo, kama ipo kesi maalumu inayohusu mtendaji wetu amenyanyasa mtu, sisi tuko tayari kupokea kesi hiyo, kuichukulia hatua na hata kumchukulia hatua Mtendaji yeyote atakayethibitika kwamba amefanya vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kuwaonea Watanzania.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niwapongeze vijana wote wa JKT wanaoendelea kujitolea. Kumekuwa na malalamiko ya kubaguliwa katika upande mzima wa suala la kupewa ajira kwa vijana wanaomaliza JKT hasa ajira ambazo zimetokea kwenye Jeshi la Polisi na hasa katika Operesheni ya Jakaya Kikwete.
Sasa swali langu, nini tamko la Serikali kuhusiana na tabia hii ya kibaguzi, na wapo vijana wa jimboni kwangu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuamua kwa makusudi kujiunga na Mfunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa akiwa hapa Bungeni, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la malalamiko ya ubaguzi wakati wa ajira, nataka nimfahamishe kwamba mara zote kuna kuwa kuna uhaba wa idadi ya vijana wanaoajiriwa ukilinganisha na wale walioko kwenye kambi. Kwa mfano katika kipindi kilichopita jeshi la Ulinzi liliajiri vijana 2,000 kati ya vijana 9,000 waliokuwepo kule; bila shaka wale 7,000 wataona kwamba wamepaguliwa, lakini ukweli ni kwamba nafasi zinakuwa chache wakati wao wako wengi. Ni kweli hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa ajira, lakini vile vile idadi ya vijana walioajiriwa ni chache sana ukilinganisha na vijana waliokuwepo katika Kambi za JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati mwingine vigezo vya ajira vinaweza vikafanana lakini kwa sababu ya idadi imekuwa ndogo basi kuna wengine bilashaka wataachwa ndiyo hayo yanasababisha malalamiko.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kuna mgogoro unataka kufukuta katika Jimbo langu kwenye Kata ya Nyatwali inayojumuisha wakazi zaidi ya 11,000. Lile sio Pori la Akiba ni maeneo yao ambayo wanaishi, inasemekana Serikali inataka kuwahamisha haijawashirikisha, hawajui wanaenda wapi na wanalipwa nini. Nini tamko la Serikali kuondoa hili tatizo kwa sababu mna migogoro mingi msitengeneze migogoro mingine na Bunda hatutakubali.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampongeza kwa jinsi ambavyo anawateea wananchi wake. Niseme tu kwamba mpaka sasa hivi hatuna taarifa rasmi kwamba tunataka kuihamisha hiyo Kata ya Nyatwali. Kwa hiyo, kama kuna fununu za namna hiyo lazima zitazingatia taratibu na sheria zote zilizopo kuhakikisha kwamba wananchi wanashirikishwa kikamilifu na viongozi wote wanashirikishwa ndipo hapo wananchi wanaweza kuhamishwa. Kama wananchi watakuwa waliingia kinyume na taratibu hapo ndiyo lazima nguvu zitatumika lakini kama siyo hivyo nikuhakikishie tu kwamba wananchi watashirikishwa vizuri kabisa ili kuhakikisha kwamba sheria inazingatiwa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Waziri katika majibu yake wataalam wanajibu kana kwamba bado Halmashauri ni moja lakini tuna Halmashauri mbili; Halmashauri ya Wilaya ina majimbo mawili ya Mwibara kwa Mheshimiwa Kangi na Bunda kwa Mheshimiwa Boniphace; Halmashauri ya Mji ina Jimbo moja tu la Ester Bulaya, Bunda Mjini. Sasa haya majibu waliyompa ni ya enzi zile za babu, za Wasira, sio kipindi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza maswali yangu mawili ya nyongeza. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara kwenye Jimbo langu la Bunda alitembelea Kikundi cha Igebesabo kilichopo Kata ya Nyatwali ambacho kina mradi mkubwa wa umwagiliaji uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 700. Pale wana changamoto ya mashine kubwa ya kusukuma maji ambayo yanatoka Ziwa Viktoria aliwaahidi atawasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini ahadi hii itatekelezwa kwa sababu pia katika hicho kikundi kuna vijana kama wewe Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Idara ya Umwagiliaji ina changamoto nyingi ikiwepo ya bajeti na vitu vingine, lakini kwa sasa hivi hawana gari la kuweza kufanya patrol katika miradi mbalimbali ya umwagiliaji katika Wilaya nzima ya Bunda. Ni lini sasa watawapatiwa gari ili sasa kilimo cha umwagiliaji Bunda kiweze kushamiri na vijana wengi graduates sasa hivi wamejiajiri wenyewe kwenye shughuli za umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa maswali mazuri lakini kubwa ambalo nataka nimhakikishie, ahadi ni deni. Kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha tunaitimiza kwa wakati ili wananchi wake, kwa maana ya kile kikundi, waweze kupata mashine hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala zima la gari, ili mradi uwe bora na wenye tija kwa wananchi lazima kuwe na usimamizi na ufuatiliaji wa karibu. Kwa hiyo suala la gari ni jambo la muhimu sana. Niagize wataalam wetu wa Bunda kufuatilia kitendea kazi hiki na sisi kama Wizara ya Maji tutatoa ushirikiano wa dhati kabisa katika kuhakikisha kinapatikana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto katika utekelezaji wa mradi wa REA pia ni upatikanaji wa nguzo. Katika Jimbo la Bunda Mjini ni lini sasa nguzo zitafika katika maeneo ya Bunda Store, Nyamswa, ambapo katika Kitongoji cha Zanzibar pamoja na Nyabeu Sazila ili wananchi wahakikishiwe kupata umeme wa uhakika kwa sababu tatizo kubwa la maeneo hayo ni nguzo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini, Mheshimiwa Esther Bulaya, juu ya masuala ya upatikanaji wa nguzo katika maeneo ambayo ameainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme Mkandarasi DEM yuko site anaendelea na kazi. Kama changamoto ilikuwa ufunguaji wa Letter of Credit kwa ajili ya kuagiza vifaa kwa wingi, tumeshawafungulia Wakandarasi wote; na kwa kuwa pia viwanda vya kuzalisha nguzo ambavyo viko ndani ya nchi, tumekutana navyo na nguzo zipo. Kwa mfano, hapo Kuwaya Iringa, Saw Mill Iringa na tumefanya uhakiki kwamba nguzo za kutosha zipo. Rai yangu kwa wakandarasi wote, waagize hivyo vifaa kwa wakati ili kusiwe na visingizio. Nakushukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri mambo mengi wamekuongopea humu, siyo Wilaya wala Halmashauri ya Mji ambayo imewahi kunufaika na chochote kutokana na Mbuga ya Serengeti. The way walivyokujibu kama Bunda, kuna Halmashauri moja. Hivi vijiji vyote viko kwenye Halmashauri ya Mji na asubuhi nimetoka kuongea na Mkurugenzi na Mhasibu hatujawahi kupata hata shilingi moja. Ni lini sasa tutapata hii asilimia 25 ya tozo za uwindaji? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wanaozunguka Mbuga ya Serengeti katika Jimbo langu wamekuwa wakipata tatizo kubwa sana la tembo kuharibu mali zao na Mheshimiwa Jenista ameshajionea uharibifu huu. Takribani wananchi 880…
...kati ya hao waliolipwa ni 330 tu, bado watu 550 hawajalipwa kifuta jacho japo kidogo. Ni lini sasa watalipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba ni kweli kabisa Wilaya ya Bunda ina Halmashauri mbili na haya majibu sisi tunayoyatoa tunatoa katika Wilaya, siyo katika Halmashauri. Tunatoa katika Wilaya nzima, tunazungumzia Wilaya. Kama ingekuwa kwamba labda inatakiwa tuangalie kwenye Halmashauri, basi majibu hayo yengefanana. Hayo majibu niliyoyasema na hizo fedha ambazo nimezisema ni zile zilizoletwa katika Wilaya nzima ya Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu maswali yake kama ifuatavyo; kwa asilimia 25 na kwa kuwa Halmashauri yake ya Mji ina vijiji vinavyopakana na haya Mapori ya Akiba na hizi fedha nilizosema zimeshapelekwa, kama bahati mbaya Halmashauri yake haijapata mgao, basi tukitoka hapa nitafuatilia kuhakikisha ule mgawanyo unakwenda katika vijiji vyote vinavyohusika. Kwa hiyo, hilo nitalifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba nirekebishe kidogo takwimu, kwa takwimu sisi tulizonazo Mheshimiwa Mbunge, katika Wilaya ya Bunda, kifuta jasho kilicholipwa ni kwa wahanga 1,127 ambao jumla ya shilingi 186,333,350 zimelipwa kama kifuta jasho. Shilingi milioni moja zililipwa kama pole kwa mhanga mmoja ambaye alipoteza maisha.
Kwa hiyo, suala la kusema kwamba hazijatolewa, zimetolewa na katika list niliyonayo mpaka sasa hivi nimeangalia kama Bunda kuna wahanga ambao wanadai, bado sinayo. Kwa hiyo, kama wapo ambao bado wanadai, naomba hiyo list tuipate ili tuweze kuifanyia kazi kusudi waweze kulipwa mara moja. (Makofi)