Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Boniphace Mwita Getere (13 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Bunda na kwa bahati nzuri nina Kata saba, kwa hiyo, niwashukuru wapiga kura wa Nyamang’uta, Nyamswa, Salama, Mihingo, Mgeta na Hunyali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Wabunge wote nikiwemo mimi mwenyewe, hatua ya kufika hapa ni ndefu sana. Kwa kweli, Mwenyezi Mungu ametusaidia tumefika hapa wote, jambo la kwanza naomba tupendane, hii habari ya kushabikia vyama na kunyoosheana vidole itakuwepo, lakini iwe kwa wastani, kwa sababu wote tunaishi kama binadamu na tukifa au tukifiwa tunaenda kupeana pole, kwa hiyo tunapokuwa humu ndani naomba tupendane.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Wabunge wa CCM wajue kwamba, nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumekabidhiwa sisi, hawa jamaa zetu wapo tu kwa kupinga na kupiga kelele. Kwa hiyo, tunatakiwa tufanye kila la maana kuwatendea haki Watanzania ili tunapofika 2020 hawa watakwenda kuuliza, tuliwaambia CCM hamuwezi sasa mnaona mmefanya nini? Kwa hiyo, tufanye kila la maana ili nchi yetu iweze kupata maendeleo ikifika 2020 tuwaoneshe kwamba tumefanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, sijui huwa najiuliza mara mbili mbili hivi kuna nini? Kwa sababu kabla ya mambo yote tunasema nchi inaliwa, nchi mbovu, hali mbaya, tunalia kila mahali, leo tumepata jembe, tingatinga anapiga kila upande bado watu wananung’unika nini? Hivi nchi hii tusipopata Rais nje ya Magufuli tunapata Rais wa aina gani? Kilichobaki ni kusahihishana tu pale na hapa mambo yanakwenda sawa, lakini Rais anafanya kazi nzuri sana.nn(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye utawala bora. Katika utawala bora naangalia mafunzo ya Halmashauri za Vijiji, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata. Tumekuwa na tabia ya kuchagua viongozi halafu hatuwapi mafunzo, hata humu ndani Wabunge tumo tu, hatukupata mafunzo bora, juzi nilikuwa namuuliza mwenzangu hapa, hivi maana ya mshahara wa Waziri ni nini? Ananiambia na mimi sijui! Unashika mshahara wa Waziri, mshahara uko benki wewe unaushikaje? Anasema sijui. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulitakiwa kuelezwa kwamba hivi vitu vinakwendaje, kuna Vote, kuna sub-vote, kuna program tulitakiwa tupewe mafunzo. Mafunzo kwa Watendaji wa Vijiji ni jambo la msingi sana, lakini imezungumzwa hapa habari ya Wenyeviti wa Vijiji kulipwa mshahara au kupewa posho. Serikali za Halmashauri au Halmashauri za Wilaya haziwezi kutoa posho, hilo tukubaliane!
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote tumetokea maeneo hayo, tumetoka kwenye vijiji, tumetoka kwenye Kata tunakuwaje hatuwatetei watu hawa wapate posho nzuri? Tunapaswa kufanya kila namna Watendaji wa Halmashauri za Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji wapate posho nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo nizungumzie habari ya migogoro ya mipaka. Kuna migogoro ya mipaka ya Wilaya na Wilaya, kuna migogoro ya mipaka kati ya Kata na Kata, kuna migogoro ya mipaka kati ya Vijiji na Vijiji na ni mingi sana, kwenye Jimbo langu ipo katika kila eneo. Tunaomba Wizara zinazohusika na maeneo hayo, TAMISEMI na Ardhi washirikiane kumaliza migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Shule za Msingi, jambo ambalo Bunge la Kumi na Moja tutafanya na tutapata heshima ni kupata madawati ya watoto, madawati ya wananfunzi katika shule za msingi. Ukienda shule ya msingi ukiingia darasani watoto wanaamka wanakusalimia shikamoo mzazi, unasema marahaba, halafu unawaambia kaeni chini au unafanyaje? Wanakaa kwenye vumbi! Huwa najiuliza, naomba Waziri Mkuu afanye kazi mmoja, tufanye kazi moja au kazi mbili tu na nitoe njia. Kwanza, tukubaliane kwamba Bunge hili Bajeti yoyote kutoka Wizara mbalimbali ikatwe tupate bilioni 150 za kuweka madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga hesabu hapa yamepungua madawati 1,500,000 kama milioni nne, kwa hiyo, tukipata bilioni 160 au 170 maana yake madawati nchi nzima yanakuwepo. Waheshimiwa Wabunge tukitoka hapa tutakwenda kupambana na tatizo la madawati hamtakwepa, saa hizi kuna meseji zinazotoka kwa DED ooh! Mheshimiwa Mbunge hela yako ya Mfuko natengenezea madawati, nani kakutuma utengeneze madawati mimi sijafika huko?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tukubaliane kwamba madawati ni jambo la kwanza katika Bunge hili. Tutoke humu tujue kwamba tunakwenda kupata madawati nchi nzima, tukisema hii ya Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa tumetofautiana kipato katika Mikoa. Dar es salaam watatengeneza, Arusha watatengeneza, Bunda je, ambayo ni Wilaya ya maskini? hawawezi kutengeneza madawati! Kwa hiyo, nafikiri kwamba jambo la msingi sana kufanya mambo kama haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kama hatuwezi kuweka bajeti bilioni 160 kutoka Wizara mbalimbali, tukubaliane na Waziri Mkuu aunde Kamati ihusishe Kambi zote, Kamati itafanya kazi moja ya kujua idadi ya madawati nchi nzima, lakini kujua mashirika mbalimbali. Kwa mfano, tukasema hivi ukiweka shilingi tano katika Makampuni ya Simu, ukiweka shilingi tano kwa Makampuni ya Mafuta, ukiweka taasisi mbalimbali tulizonazo, hatuwezi kupata bilioni 160? Inawezekana! Waziri Mkuu aunde Kamati ili tuweze kupata watu, wafanye tathmini, watuletee hapa, wote tuchange.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Bunge letu limechanga, tumechanga bilioni sita au uwongo jamani?
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumechanga bilioni sita kutokea Bungeni humu ndani, tunataka Mashirika mengine yote na Taasisi zingine zichange.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu kwa leo yalikuwa hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani zangu za awali kwa wote walioandaa hotuba hii ya Wizara ya Elimu na hasa Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Naibu Waziri.
Matatizo ya Jimbo langu la Bunda Vijijini; moja ni kutoa kibali cha ufunguzi wa sekondari ya (High School) ya Makongoro (Makongoro High School). Tunahitaji msaada wa Wizara, wananchi wamejenga vyumba vya madarasa, mabweni na jengo la utawala, tunahitaji shilingi 72,000,000 ili kumaliza ujenzi wa high school hii. Tunaomba msaada ili kupunguza makali ya michango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili ni upungufu wa walimu wa sayansi, (kemia, fizikia, biolojia na hesabu). Zaidi ya sekondari 30 wanahitajika walimu 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni matatizo ya mazingira ya vyoo. Zaidi ya shule za msingi 40, zina matatizo ya vyoo vibovu vya shule na tatizo la maji shuleni, hivyo naomba Wizara ya Elimu kupitia mashirika yake ya kutoa huduma za msingi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tatizo la vyoo magonjwa ya watoto shuleni yameongezeka sana, (typhoid, kuhara, U.T.I). Naomba msaada wa suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba nne, matatizo ya maabara, madarasa na nyumba za walimu. Wizara iangalie namna ya kusaidia Jimbo hili jipya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii kwa maeneo yanayohusu Jimbo langu la Bunda Vijijini. Jimbo la Bunda lina Vijiji 39. Matatizo ya umeme ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, REA I vijiji vilivyopata umeme ni Kyandege, Migeta, Mariwanda, Salama „A‟ na Hunyuri Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo umeme wa REA Phase I uliwekwa katika maeneo ya center (Barabara kuu). Aidha, maeneo yote ya Taasisi; Mashuleni, Hospitali, Ofisi) hakuna umeme. Aidha, katika Vijiji vya Mariwanda, Hunyari, umeme uliwekwa katika volt ndogo (muhimu). TANESCO Bunda wanajua.
REA II: Vijiji vilivyopata umeme ni Kiloreli, Kambubu, Nyamuswa, Marambeka, Salama Kati, Kurusanga, Mikomariro na Mibingo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo vijiji vya REA II nilivyovitaja kuanzia cha 1 – 6 umeme umewaka katika maeneo ya center tu. Taasisi zote za Umma hakuna umeme. Wizara imetoa agizo kupitia Mheshimiwa Muhongo (Waziri) kuwa Taasisi zote za Umma zipate umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA III; vijiji ambavyo vinahitaji umeme ni Manchimaro, Tingirima, Nyangiranga, Rakana, Tiringati, Bigegu, Nyaburundu, Mahanga, Mmagunga, Nyariswori, Sarakwa, Majengo, Nyangere, Nyabuzame, Mmuruwaro, Nyang‟ombe, Nyanungu, Rubimaha na Bukoba,
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kuwa maeneo yote hayo yatapewa umeme wa REA Phase III kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni.
N.B. Vijiji vya Bukoba na Samata vimewekewa transformer, tunahitaji umeme uwake. Mungu ibariki Wizara, Mungu ibariki Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitangulize shukrani zangu za dhati kwa Serikali yangu ya CCM. Nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Fedha na Sekretarieti yake kwa kuthubutu kutoa mapendekezo yao kwa Mpango huu wa Maendeleo wa Mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya ni mazuri kwa sehemu kubwa. Mchango wangu katika mapendekezo yangu upo katika sehemu tatu:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni Elimu ya Bure Shule za Msingi na Sekondari. Kwa maoni yangu, fedha hizi zinazotolewa mashuleni na hasa shule za msingi, hazifanyi kazi iliyokusudiwa. Mfano, Shule ya Msingi „A‟ kwa mwezi itapata shilingi 230,000/=. Fedha hizi hugawanywa kwa asilimia ishirini ishirini. Kwa maoni yangu, fedha hizi hazitoshi hata kununua mpira.
Kwa mahitaji makubwa ya shule ni chaki, mitihani na utawala. Kwa nini Serikali isifungue akaunti maalum kila Halmashauri na fedha hizi zikawa katika akaunti hii na kila shule ikapewa mahitaji muhimu ya wanafunzi na utawala. Napendekeza style iliyokuwa inatumika enzi za Mwalimu, kila mwanafunzi alikuwa anapewa vitabu, madaftari, chaki na vitu vingine muhimu kuliko fungu la fedha hizi ambazo sehemu kubwa hazifanyi kazi. Fanyeni utafiti.
(b) Nashauri Serikali itenge fidia ya wakulima kwa mazao yaliyoharibiwa na wanyama waharibifu (ndovu) Jimboni kwangu. Wakulima wanadai zaidi ya shilingi milioni 400. Serikali ihakikishe fidia kwa wakulima, inalipwa.
(c) Malambo kwa wafugaji. Maeneo mengi ya hifadhi ya Taifa hayana maji kwa mifugo. Serikali iwe na mpango maalum wa kuchimba malambo Jimbo la Bunda.
(d) Vile vile Serikali iwe na mpango maalum wa kujenga vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu kwa shule za msingi na sekondari. Mfano, Jimbo langu la Bunda lina upungufu wa vyumba vya madarasa 586 vyenye thamani ya shilingi milioni 687. Serikali iwe na mkakati maalum wa kujenga/kutatua kero hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushuru kwa kunipa nafasi hii, namshukuru Ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi; Mheshimiwa Mabula ambaye ni jirani yetu Kanda ya Ziwa. Tumshukuru Rais kwa kuwapa nafasi hiyo, mnafaa kupewa nafasi hiyo na Mungu awasaidie muweze kutongoza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nimeangalia taarifa hizi za Kamati ya Ardhi na Kambi Rasmi ya Upinzani wamesema vizuri sana. Wametofautiana kitu kimoja tu, hawa waCCM wameunga mkono, wale wa upinzani wameunga mkono kwa kushauri kwamba Serikali ikae pamoja itatue migogoro, jambo zuri sana.
Namshukuru rafiki yangu wa Bukoba Town na leo ni mnada, kwa hiyo, tutajua namna ya kufanya huko. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye mambo muhimu na naomba niulize maswali ambayo natakiwa wakati unakuja hapa ku-wind up uweze kuyatolea ufafanuzi. Ni nani anapima mipaka kati ya vijiji na hifadhi za wanyamapori? Kama ni Wizara ya Ardhi inapima, inakuwaje mpaka huo buffer zone moja iwe na kilometa kadhaa na buffer zone nyingine au kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa binadamu ni nusu kilometa; lakini kutoka mpaka wa wananchi kwenda porini ni zero. Nani anapima mipaka hiyo na kwa upendeleo gani wa aina hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanapima wataalamu wa wanyamapori, kweli wanaweza kutenda haki? Mipaka ya Jimbo langu la Rubana, kwa Mto Rubana, ukiingia mtoni, ukivuka tu, umekamatwa. Ukivuka mto tu, umekematwa; lakini wao kutoka mpakani, mita 500 ambayo ni nusu kilometa. Kwa hiyo, ina maana mita 500 hizo kama kuna mazao yakiliwa na wanyamapori, hakuna kulipwa. Hakuna malipo! Hawa jamaa wamejiwekea sheria, unalipa kutoka kilometa moja mpaka kilometa tano ndiyo unalipwa na unalipwa kwa heka moja shilingi 100,000. Kwa hiyo, kama tembo amekula mazao heka 20, unalipwa heka tano, heka 15 ni sadaka ya Serikali. Nani alifanya maneno ya namna hii? Tunataka kujua nani anapima hii mipaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nani anatatua migogoro kati ya hifadhi ya wanyamapori na wananchi? Maana yake wamelalamika mika nenda-rudi, hakuna mtu anaenda. Tuna eneo moja linaitwa Kawanga; mpaka uchaguzi wa mwaka 1995 ulimtoa Waziri Mkuu, hiyo Kawanga. Aliuliza swali, nani atatatua mgogoro wa Kawanga? Akasema hii ni sheria, tutakwenda kufanya. Wakasema hapana, sisi tumeshachoka. Mpaka leo mgogoro upo, Mawaziri wameenda watano, sita, wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Mawaziri wengine mlioko humu ndani, hebu tuambieni, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Waziri wa Ardhi, wametamka humu Bungeni kwamba watakaa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii watatue migogoro ya wakulima, wafugaji na Hifadhi za Taifa, mtakaa mtatue. Uchaguzi tumetoka juzi! Mheshimiwa Rais wetu mtiifu amesema wafugaji sitawangusha. Tumetoka juzi tu, lakini operation zinaendelea kukamata watu. Hii maana yake nini hasa? Migogoro haijatatuliwa, watu wanakamatwa, watu wanatolewa; nani sasa amesema wewe uko sahihi kutoa watu? Tupo tu tunaangalia. Mheshimiwa Lukuvi, nafasi yako naitaka, ikifika miaka miwili na nusu miaka ijayo kama migogoro haijaisha angalau hata robo, wewe toka tu mimi niingie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mgogoro wa Jimbo la Bunda, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, ameandika vizuri sana hapa. Mgogoro wa Bunda kati ya Wilaya tatu; kuna Serengeti, Bunda na Musoma Vijijini. Mgogoro wa mwaka 1941 mpaka leo haujaisha. Watu wanapigana, wanauana mgogoro upo tu. Mheshimiwa Mabula, wewe ulikuwepo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, unaujua mgogoro. Mara uko TAMISEMI, mara uko Ardhi, mara uko wapi, toka miaka hiyo mpaka leo. Mimi sitaunga mkono hoja hii kama kweli mgogoro huu hautaniambia unaisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la Kyandege na wameliandika vizuri hapa. Sasa haya ni mambo ya ajabu. Wakati fulani hawa wenzetu wakisema maneno hapa, ingawaje sisi hatuna mpango wa kutoka madarakani, lakini wana maneno yao mazuri. Hivi inakuwaje? Kwa mfano, inakuwaje GN ya kijiji imetoka; na imetoka Makao Makuu ya Ardhi, imekwenda kijijini; imeandika mpaka kati ya kijiji ni kaskazini na kusini, lakini anayekwenda kukata mipaka kutoka Halmashauri au sijui kutoka wapi, anaenda anakata Magharibi Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamelalamika toka 2007 mpaka leo; eneo hilo tu moja, Muliyanchoka kweli hii? Hapana, hii hapana! Kwa hiyo, naomba kujua hili tatizo litaisha lini? Kwa kweli kusema kweli yapo mambo ya msingi ya kufanya, lakini vinginevyo nakushukuru sana unajitahidi kufanya. Tatizo tulilokuwa nalo, Waziri ulielewe na Mawaziri wote mlielewe, mnafanya kazi sana ya kutumikia watu lakini watumishi wenu wakati fulani wanasema ninyi wanasiasa tu. Watumishi wenu wanawaangusha sana ninyi. Kila ukisema maneno wanakwambia huyu ni mwanasiasa tu. Sasa muangalie, hao wanaosema wanasiasa waondoeni kwanza mbaki ninyi ambao mnafanya kazi. Nashukuru sana.
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nianze kwa kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Bunda, kwa kunipa nafasi ya kuja hapa Bungeni na mimi nijumuike na wenzangu katika kuwatetea Watanzania wenye matatizo mengi. Nianze kwa migogoro ya moja kwa moja, migogoro ya wafugaji na hifadhi za wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa, lakini kwenye Jimbo langu la Bunda kuna eneo maarufu linaitwa Kawanga, na mimi niombe kwa kusema wazi tu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, ng‟ombe ana laana, toka mmetunga Sharia hii ya wanyama pori ya kukamata ng‟ombe mnamfanya kama nyara, mnamkamata porini hachungi na mnampiga risasi, Mawaziri zaidi ya tisa wamesha toka humu ndani; ng‟ombe ana laana. Kwa hiyo, yeyote anayeshughulika na ng‟ombe vibaya ajue mambo yake yatakwenda vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu eneo la Kawanga. Eneo hili mwaka 1974 alikuja Mwalimu Nyerere pale kama kijiji cha ujamaa, akawashauri wananchi wa maeneo yale kwamba jamani acheni maeneo ya malisho. Wakavuka Mto Lubana wakaacha eneo la Kawanga, wakawa wamechimba malambo mawili makubwa ya Chifu Makongoro, wananywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 ukaja ujanja ujanja eneo hili likachukuliwa kama game reserve, Ikolongo Game Reserve na Grumeti Game Reserve, pori la akiba.
Mheshimiwa Mwwenyekiti, kwanza huwa najiuliza hivi pori la akiba maana yake ni nini? Mwalimu alisema hivi vitu vya akiba viwepo pale ambapo wananchi wana shida wapewe nafasi.
Sasa inavyoonekana mapori ya akiba yote ni ya wanyama pori, ikija kwa binadamu nongwa. Leo ikitokea operation ya kuzuia tembo asiende kwenye mashamba ya watu na operation ya kwenda kuzuia ng‟ombe wasiende porini, operation ya ng‟ombe inachukua nafasi. Kwa sababu ng‟ombe wanakuwa na faida ukiwatoa kwenye operation unawakamata unawatoza, wanatoa hongo na mnawauza sijui hela za ng‟ombe zinazouzwa zinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Kawanga wakahama watu, mkalifanya Pori la Gruneti, malambo mawili yako upande ule, mpaka wetu ni mto, na mto ule maana yake ng‟ombe akivuka tu, amekamatwa ndivyo mpaka ulivyo. Lakini kutoka kwenye mpaka wa Mto Rubana kwenda kwenye watu, unatembea nusu kilometa kwenda pale mbele, ndiyo buffer zone yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza kama wananchi wa maeneo yale tembo wanakula mazao yao, ngo‟mbe hawavuki kwenye Mto Rubana, malambo yao mmechukua na hamkufidia halafu mnasemaje tuna mahusiano mabaya na ninyi? Profesa Maghembe mimi naomba nikuambie hivi, pengine kule Mwanga ninyi Ubunge wenu wakati fulani akisema fulani mnapata. Sisi Ubunge wetu ni wa kazi, kuna maeneo mengine Ubunge akisema mkubwa fulani watu wanapewa, lakini sisi Ubunge wetu mpaka utoe jasho ndipo upate. Sasa naomba uje Kawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina ugonvi na wewe, na mimi nikuambie wazi wala huna ugonvi na Wabunge, tatizo lako ni kwamba una-attack ng‟ombe, kwa nini una- attack ng‟ombe sisi tunaolea ng‟ombe. Mimi mke wangu ametoka ng‟ombe namuita Nyabulembo, sasa wewe una-attack ng‟ombe mara kwa mara kwa nini? Tunataka ng‟ombe kweli watoke porini sawa, lakini watoke kwa mpango maalum. Hivi kwa nini majangili wamewashinda porini mnang‟ang‟ana na ng‟ombe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa kwenye ripoti ya wapinzani hapa, anasema kwamba ujangili ni mfupa uliowashinda CCM. Na kila siku asubuhi, hata leo asubuhi nimesikia, kwamba kiongozi mmoja mhifadhi wa wanyama pori sijui amekamatwa na pembe za ndovu. Sasa kwa nini msishughulike na hawa mnashughulika na ng‟ombe? Profesa achana na mambo ya ng‟ombe watakulaani hapa. Naomba uje Kawanga uangalie mpaka ulivyo ni mbovu. Lakini ndugu zangu Wabunge tunaotoka kwenye maeneo ya wafugaji, naomba niwaambie wazi, hizi kanuni na sheria za wanyama pori zitaua watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zitaua humu ndani, sheria hii imeandika ng‟ombe ni kama nyara, akikamatwa anapelekwa mahakamani, akionekana ameingia porini auzwe. Ng‟ombe wa Usukumani, ng‟ombe wa Jimbo la Bunda, ng‟ombe wa Tarime na maeneo mengine ana tofauti gani na ng‟ombe wa Ngorongoro? Ng‟ombe wa Ngorongoro anachunga na wanyama, kwani ile sheria ya Ngorongoro imekuwa ni sheria ya Mungu haibadiliki? Sheria ya Ngorongoro ambayo ng‟ombe wanachunga na wanyama haibadiliki imekuwa ni sheria ya Mungu? It’s too rigid haiwezi kubadilika. Tuone maeneo mengine ambayo yanahitaji uhitaji wa Ngorongoro wapelekewe hiyo sheria. Profesa nakuomba uje Bunda, uangalie eneo la Kawanga tuone ni namna gani tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo. Nakupongeza kwa maana ya kwamba msimu mdogo uliopita umenisaidia sana, tembo kidogo, watu wamevuna. Lakini ndugu zangu Wabunge na ndugu zangu Watanzania, mnyama tembo, mama mmoja tulienda kwenye mkutano akatuuliza hivi, hivi hao tembo hawana uzazi wa mpango? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana kama wamezidi tuwafanyie uzazi wa mpango, tembo siku hizi wanakwenda kwenye maghala, wanaangusha maghala wanakula mazao. Maeneo ya Bunda, Unyari, Kiumbu, Mariwanda na kwa Mheshimiwa Ester Bulaya pale Bukore na Mihale wanakula mazao asubuhi na mchana na Profesa upo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipiga kelele hapa mnasema tumekuwa wabaya, watu hawa wanaozunguka wanyama pori hawa, mazao yao yanaliwa fidia haipo. Tunadai fidia zaidi ya milioni 400 hamjalipa kutoka mwaka 2012 mpaka leo, na wanakula mazao kila siku na magari mnayo, watu mnao, mkiambiwa mnasema kwamba Halmashauri ndiyo ilinde wale wanyama. Halmashauri ina askari pori mmoja na gari bovu halipo na Halmashauri hazina own source. Halmashauri hazina hela unawaambia walinde tembo watalinda saa ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mbaya zaidi Halmashauri alinde tembo, asipolinda tembo anakula mazao, wakila mazao mnalipa nyie hivi kwa nini mpo hasara sasa? Kwa hiyo nilikuwa nafikiri kwamba ni vizuri ukaangalia. Lakini mambo mengine niseme mapambano ya kuzuia ujangili yaendelee kuwepo, kuimalisha misitu yetu muendelee kuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze kidogo juu ya TFS. Hao TFS ulionao nikushukuru kwanza umewashughulikia, ni jipu. Haiwezekani kwenye makusanyo yao, kila mwaka asilimia 100, asilimia 200, asilimia 150 uliona wapi? Yaani kila makusanyo ya TFS asilimia 100, asilimia 250, asilimia 300 uliona wapi? Angalieni makusanyo yao asilimia walizokusanya kila mwaka, asilimia 120, asilimia 110, asilimia116 kila mwaka, wao makadirio yao yanakuwaje mpaka wapate hizo asilimia? Kwa hiyo, mliangalie hili nalo hao watu inawezekana wakawa jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya shilingi milioni 400 watu wa Bunda unawalipa lini? Hii fidia sijaiona kwenye bajeti yako. Profesa ukija hapa uniambie kwamba hii kitu unalipa lini. Lakini naomba kuanzia leo na kwenda muda unaokwisha, kwa muda wa mwezi mmoja na nusu naomba mtusaidie kupata magari ili watu wale wapate mavuno yao. Wamebakiza mwezi mmoja tu, tembo leo wanaenda usiku na mchana na kama hamuwezi, Profesa ngoja nikuambie, Marekani ni wanjanja sana lakini wanaishi na Mexico. Waliona haiwezekani kuishi na Mexico maskini na wao wakiwa matajiri, ikabidi wawafadhili wao wapate hela. Hamuwezi mkafanya wananchi wanaozunguka maeneo ya pori, mkasema eti mtakuwa marafiki wakati ninyi mnawanyonya haiwekani, lazima muwafadhili ili waweze kuishi na wanyama vizuri. Na ninyi niwaambie huku Serikalini… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia uhaba wa chakula. Kwanza niwashukuru watoa hoja wote, Kamati ya Ardhi na Kamati ya Kilimo, wamezungumza vizuri kwenye vitabu hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua tu kwa Mawaziri wanaohusika na Wizara hizi au wa Serikali sijawahi kuona kwamba kwa nini kila siku tunazungumza hivi vitu vinavyohusu mifugo, vinavyohusu ardhi kutopimwa na sina hakika kwamba hivi muda huu toka Wabunge wamekuja toka mwaka 1961, haya mambo ya kupima ardhi yalikuwa hayajazungumzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba kwa Wabunge wenzangu mkitaka Bunge hili tulitendee haki tuondoeni maneno yanayohusu U-CHADEMA na U-CCM. Mkiondoa haya maneno haya mtajenga Bunge ambalo ni imara na litasimamia Serikali. Tukifika humu tumebaki kubishana tu, tunabishana upande huu mara mwingine azushie Magufuli maneno, mara sijui Rais amefanya nini hatutafika hiyo. Tuzungumze mambo yanayohusu wananchi tuwaulize Serikali kwa nini kila siku tunazungumza migogoro ya mifugo na haitatuliki. Kama hakuna majibu tuseme sasa itakuaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila siku tunakuja hapa maneno tu kama ngonjera tu, tukubaliane kwamba kama sisi ni wasimamizi wa Serikali, tuiulize Serikali kwa nini sasa mipango hii ya ardhi ambayo wakulima na wafugaji wanauana, kwa nini haifiki mwisho? Tutapata majibu siku hiyo. Kama haifiki mwisho hatuendi kwenye bajeti, tutapata majibu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kwenye eneo langu la Bunda. Amekuja Waziri Mhagama, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ndugu yangu hapa Ramo Makani, amekuja Naibu Waziri Kilimo, Mheshimiwa Ole-Nasha wamejionea hali halisi ya uharibufu ya wanyama tembo katika maeneo yangu, kata saba na Bunda Mjini. Wameona hali ilivyo, ikaahidiwa kwamba watapeleka chakula hakijaenda. Sasa nimeona humu wanaandika tupeleke mbegu bora, unaipanda wapi? Unapanda mbegu bora lakini tembo anaishi pale kila siku, wale Wazanzibar wanaita ndovu, anaishi pale pale kwenye shamba, tunapeleka mbegu bora ya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hao tembo au ndovu hawawezi kutoka kwenye Jimbo lile watu watalima lini? Nawashukuru siku hizi wanajitahidi wapeleke na magari, lakini tembo au ndovu zimewashinda kutoa. Wanaishi pale pale kila siku, wamepeleka tochi imeshindikana. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri Serikali ituambie kama mpango wa eneo langu, vijiji vya Unyali, Maliwanda, Kihumbu, Nyamang’unta, Tingirima, Mgeta na kule kwa neighbour wangu Mheshimiwa Ester Bulaya, vijiji vya Nyamatoke na Mihale, watuambie kama maeneo haya hayawezi kulimwa basi Serikali ijiandae kwenda kuwapa chakula cha bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo sasa hivi wamefika wakati sasa wanavunja maghala, wanachukua chakula wanakula, hawana uwezo sasa wakulima pale, ngombe hawaendi porini wanakamatwa, sasa tunafanyaje? Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika hili kuwa wepesi wa kupeleka chakula cha msaada au chakula cha bei nafuu wapeleke katika Kata Saba za Jimbo langu. Hali ni mbaya na Kata Tatu za Jimbo la Bunda Mjini. Hali ni mbaya sana kwenye maeneo haya, njaa ni shida.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimpa rafiki yangu, jirani yangu anaitwa Ryoba dakika tano uwe unanichunga kama zikizidi itakuwa mbaya zaidi. Kwa hiyo, niseme tu kitu kimoja…
MWENYEKITI: Mheshimiwa zimekwisha dakika tano zako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo yangu yote ya Ofisini kwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu yazingatiwe.
(i) Kukasimu barabara ya Mugeta – Misingo – Mekomariro (Bunda) hadi Sirorisimba (Butiama) na Serengeti.
(ii) Kutangaza mkandarasi wa barabara ya Nyamuswa – Bunda (ahadi ya Mheshimiwa Waziri 31/12/2016) aliposimama Kata ya Nyamuswa na kuahidi kutangaza mkandarasi ifikapo Februari, 2017.
(iii) Kutangaza mkandarasi kipande cha Sanzate hadi Nata. Nasikitika kuona kipande hiki kimerukwa badala yake Wizara ilitangaza barabara ya Nata. Kwangu naona kama sikutendewa haki na hasa ikizingatiwa hii Lot ilitakiwa kwisha kabla ya kutangaza huku. Naomba haki itendeke.
(iv) Uwanja wa Ndege Musoma, Mheshimiwa Waziri alishasema anatafuta shilingi bilioni 10 za ukarabati wa uwanja huu mapema 2016/2017. Nasikitika kuona bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni tatu badala ya shilingi bilioni 10. Naomba suala hili lizingatiwe.
(v) Reli ya Arusha – Musoma. Reli hii toka mwaka 1975 inapewa ahadi hadi leo. Tunaomba kwa miaka mitano watu wa Musoma waone jitihada ya Serikali katika kujenga reli hii.
(vi) Bandari ya Musoma ilikuwa ikipokea meli ya MV Victoria, MV Butiama na MV Umoja. Nimeona juhudi za Wizara za kutengeneza meli hizo, tunaomba meli hizo zikitengenezwa zifike Musoma. Matengenezo ya Bandari ni kidogo sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwnyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwashukuru Waziri na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Niendelee kutoa pongezi kwa Jemedari wetu, Rais wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya, sina mashaka na yeye. Wasiwasi wangu ni kwamba akimaliza miaka yake kumi atakuja mtu mzuri kama yeye au vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Hospitali ya Mkoa wa Mara. Sijajua kwa Mkoa wetu wa Mara ni kitu gani kinatokea kwa sababu vitu vingi haviendi vizuri. Hospitali hii imechangiwa karibu miaka 32 na haijaisha. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kongwa, imekuwa ikitengewa fedha kidogo kila mwaka na mpaka leo haijulikani itaisha lini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atueleza kwa mwaka huu wa fedha imetengewa kiasi gani na ni lini hospitali inaweza kwisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, nadhani ukurasa wa 149, anazungumzia habari ya kupeleka fedha za vijana na akina mama katika vikundi. Katika Wilaya ya Bunda wameandika kwamba imepeleka shilingi milioni 106, nikashangaa! Sasa nataka kujiuliza haya maandishi humu ni ya kweli au mtu ameyabandika tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nimempigia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kumuuliza hii hela mmepeleka ninyi? Anasema sisi tumepeleka shilingi milioni 20 tu. Maana Bunda yenyewe kukusanya shilingi milioni 100 ni kesi. Sasa nataka kujiuliza hizi fedha zimetoka Wizarani za muda mrefu au za namna gani? Kwa hiyo, kama ni za Wizarani ni sawa lakini kama ni za kutoka kwenye Halmashauri na ni own source, hizi fedha hazijatoka. Kwa hiyo, nataka kuuliza suala hili limekaaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nizungumzie habari ya watumishi katika Jimbo langu la Bunda. Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ametembelea katika Jimbo langu la Bunda ameona katika kila kituo nurse ni mmoja-mmoja tena wale wa daraja la chini na akaahidi mtakapopata nafasi mtatuletea watumishi katika Jimbo la Bunda. Zahanati zote zina nurse mmoja-mmoja na Naibu Waziri ameshuhudia mwenyewe. Kwa hiyo, naomba katika nafasi zitakazopatikana mnisaidie kupata watumishi wa maeneo hayo. (Makofi)

Lakini pia mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii. Tumetembelea Muhimbili, Ocean Road na maeneo mengine mengi, fedha haziendi kwenye vituo vyote vikuu. Tunaiomba Serikali katika bajeti inazotenga fedha ziende kwenye maeneo muhimu ambayo imezitengea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona Mloganzila, tumeambiwa kile Kituo cha Ufundishaji cha Tiba kimeisha lakini hakina watumishi. Kinahitaji fedha kiasi cha shilingi bilioni nne ili kianze kazi. Tunaomba Serikali ipeleke pale madaktari na kituo kile kiweze kuanza kazi mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa iko hapa, tunaomba watumishi waende maeneo hayo ili waweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna Hospitali ya Nyamuswa, ni kituo ambacho tumekijenga kiko kwenye hali nzuri. Tunaomba pale mtakapopata x-ray na nimesikia Waziri anasema mtapata x-ray basi mtupelekee kwenye Kituo cya Nyamuswa ili watu waweze kupata huduma katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika haya mambo ya vijana mimi nadhani sasa kuwepo na mkakati maalum kupitia hii Wizara na Wizara ya Kazi tujue sasa hizi fedha za taasisi za kijamii zinazoenda kwa ajili ya kuwakopesha akina mama na vijana zina mfumo mzuri ambao unaeleweka. Maana inaonekana kwamba kuna maeneo mengine yanapata fedha kutoka makao makuu na wengine wanapata kutoka own source sasa haijulikani ni wapi wanapata manufaa. Nashauri tuweke mfuko mmoja wa hizi fedha zijulikane kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kabla sijatoa hoja yangu ya kuunga mkono niwape pole wakazi wa Jimbo langu la Bunda kwa taabu kubwa waliyonayo ya upungufu mkubwa wa chakula na niwahakikishie kwamba Serikali kwa maelekezo yake hivi karibuni inaweza kuwasaidia kupunguza tatizo walilonalo.

Suala la pili, niwape pole wanavijiji wa barabara ya Bukama, Salamakati, Mihingo na Mgeta ambayo imevunjika daraja zake kwasababu ya mvua na mkandarasi wiki ijayo au wiki mbili zijazo atakuwa kwenye site, kwa hiyo wategemee watapata huduma, kwamba Serikali inawasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu kwamba humu ndani pamoja na kwamba tupo Wabunge wengine wa miaka mingi lakini pia kuna wazee humu ndani, hili suala la bajeti ya maji tumelisema sana, watu wameonyesha njia, lakini iko hoja ya msingi kwamba sasa litakwenda kwenye Kamati ya Bajeti ambayo itakaa na kulitazama upya. Sasa kama hiyo ndiyo hoja basi hakuna haja ya kulipinga ni kuliunga mkono tu kwamba pengine katika ongezeko litakalokuja litatusaidia kufanya mambo.

Kwa hiyo, mimi nitaiunga mkono hii bajeti mkono kwa sababu itakwenda na itarudisha majibu ambayo yataleta neema. Mambo mengine haya ya kuota kwamba CCM itakufa lini, unaweza ukakaa miaka mingi tu hujapata jambo hilo kwa sababu CCM pia ni nembo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja ya msingi ya Jimbo langu la Bunda. Haihitaji kusoma sana kujua kwmana asilimia 72.6 ya huduma ya maji inayopatikana vijijini haihitaji kwenda darasa la saba wala la ngapi. Hivi kwa mfano, kama asilimia 72.6 ndiyo huduma ya maji vijijini, kwa lugha nyingine ni kwamba kama una watu milioni moja maana yake watu 726,000 wanapata maji vijijini. Yaani kama tuna vijiji 1,000 ina maana vijiji 726 tu vinapata maji sasa jamani hivi ni kweli? Maana yake ni kwamba vijiji 274 ndivyo havipati huduma ya maji. Hivi Waziri, wazee wangu hawa mmetoka sijui engineer sijui nini inahitaji hilo kutuuliza? Hivi takwimu hizi tunazipata wapi? Waheshimiwa Wabunge sisi wote tuko humu ndani, kwanini usituambie kila Mbunge atuletee vijiji vyenye huduma ya maji na wewe ukaviona kwenye asilimia? Msikariri bajeti hizi kwa mambo ya kukariri kwenye vitabu jamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wangu nyie ndiyo mnamalizia hivi, mkishatoka hapa na uwaziri unaacha. Kwa hiyo naomba mjikite kutusaidia sisi. Mbona Waziri wa Nishati na Madini ametuambia leteni vijiji ambavyo havina umeme, tumempa na ameviona vijiji vinaonekana, ninyi kwa nini hamfanyi hivyo? Mnakariri bajeti sio wataalam? Mimi ninawaambia kumekucha hali si nzuri sana. Kwenye Jimbo la Bunda amezungumza mwenzangu hapo, lakini niseme tu nimeandika barua tarehe 26/10/2016, utata wa miradi ya Jimbo la Bunda nikataja mradi wa maji Mgeta-Nyangaranga. Nashukuru kwa sasa hivi mkandarasi yupo lakini bado anasuasua tu, anaweka leo bomba moja kesho haweki, hakuna kinachoendelea pale, mradi una miaka sita unahangaika tu, haiendi vizuri. Barua hii haikujibiwa; hata sikujibiwa mimi kama Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupewa nilichoandika jamani ni sawa? Mheshjimiwa Waziri nimekuja kwako, Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuja kwako, kwa Katibu nimeenda, sasa mnataka tuende wapi? Wazee wangu mnataka tuende wapi tuseme? Mradi wa Maji Mgeta matatizo, Mradi wa Nyamswa Salama Kati mmetenga shilingi 367,291,127, wanasema mradi umetengenezwa kwa asilimia 55 umekufa una miaka mitatu; mnataka twende wapi? Nimezungumza mkasema mtarekebisha miradi ya zamani iendelee, lakini hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mradi wa Kilolei shilingi milioni 400, vijiji vya Nyabuzume, Kiloleni na Kambugu shilingi milioni 400, ile mnasema visima kumi. Nimewaambia ofisini hakuna kinachoendelea, mnasema tuseme nini sasa kwenye hili? Ameandika Mhandisi wa Wilaya ya Bunda tarehe 1 Juni, 2016 miradi ya viporo vya madeni ya wakandarasi wa mradi wa maji Wilaya ya Bunda; mmeleta shilingi bilioni tano. Miradi karibu asilimia sabini na kitu asilimia haifanyi kazi, ninyi mkija kwenye asilimia hapa mnaandika maji yanapatikana Bunda, hayapo, hayapo Bunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu wamekuja watu wa JICA tumewapa taabu kubwa sana, tumewaambia watusaidie kwa sababu kwenye Jimbo langu la Bunda lina ukame mkubwa, wametuambia tufanye bajeti tumewapelekea bajeti ya dola 63,879 ya ukarabati ya marambo yaliyoingiliwa na magugu maji.

Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mliwahi kujibu hapa Bungeni kwamba mwaka huu mtafanya ukarabati wa malambo sita, iko wapi mzee wangu? Sasa mnafikiria sisi Wabunge tufanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, JICA hawa hawa wamesema tutengeneze malambo, tumewapa bajeti ya dola 255,237.17 tusaidieni basi, tusaidieni kwenye JICA hawa ambao wametuona kwenye tatizo mtusaidie kutusemea watusaidie. Jimbo la Bunda lina ukame wa kutisha, Jimbo hilo hilo ndio lina tembo wanaokula mazao ya watu kila siku, lina watu wana taabu zao kule; tunaomba mtusaidie kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mradi wa umwagiliaji Bunda. Mradi wa umwagiliaji maji wa Nyatwali hauko Jimbo la Bunda, haupo Wilaya ya Bunda uko Bunda Mjini. Bunda DC kuna mradi wa umwagiliaji wa Maji unaoitwa Mariwanda pamoja na mradi wa Kasugutwa wa Buramba, haiku kwenye bajeti yanu; na kwenye takwimu zenu mnaonesha kwamba Mradi upo Bunda DC lakini upo Bunda Mjini. Kwa hiyo, naomba mlirekebishe hili na mradi wetu wa Mariwanda muufanyike kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu hebu tusaidieni, kama mmepewa hiyo Wizara na hali ndio hii inaenda miaka miwili sasa inaenda miaka mitatu na ninyi wazee ma-engineer mpo hapo, watu wazima ambao tunawategemea mtusaidie na hamna plan mpya ya kukomboa mambo ya maji, tunakaa na ninyi humu kufanya biashara gani? Maana sasa lazima tuwaambie kwamba miaka mitatu ijayo mtuambie mmeingia humu ndani mmekomboa nini au ndiyo zile asilimia mnazoimba tu asilimia 72 wakati hazipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimeandika kwenu, nimewaleta, kwenye Jimbo langu mnasema kwamba miradi ya zamani iendelee kuwepo; na kwangu miradi ya zamani ipo, endeleeni kunisadia au mnampango wa kuniondoa huko ndani? Mniambie sasa mapema nijue.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze tu kwa kuipongeza Wizara, Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe; Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo na watendaji wote wakiongozwa na Katibu, Mkuu Meja Jenerali Milanzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa nchi yetu kwa kuwateua hawa lakini kwa kulinda maliasili ya nchi yetu na kuonesha kwamba ana nia nzuri ya kuendeleza utalii kwa kununua ndege ambazo zitakuwa zinatoa watalii maeneo mbalimbali na kuwaleta hapa kwa ajili ya kuongeza mapato ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze leo kwa kutumia hotuba zote hizi mbili ya Waziri na Kamati, yote ambayo tulitegemea kusema humu ndani hasa mimi naona wamezungumzia maeneo mengi. Nianze kwa kuangalia kitabu cha hotuba ya Waziri, ukurasa wa 17, ibara 36 wanasema:-
“Dhana ya ushirikishwaji jamii katika uhifadhi wa wanyamapori ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanashiriki katika uhifadhi na kunufaika kwa mujibu wa Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maeneo yangu ya Bunda na kwa bahati mbaya lugha inakuwa tofauti nikisema tembo inakuwa kosa basi niseme ndovu. Nimshukuru Waziri katika msimu wa kilimo wa mwaka jana na mwaka huu wametusaidia kuleta magari na askari ili kuzuia ndovu wasije kwenye maeneo ya makazi ya watu na kula mazao yao. Nina ombi maalum kwa Waziri kwamba kwa sasa wakulima wale wamelima sana na mazao yao yako kwenye hatua nzuri, kwa mwezi wa Tano, Sita na Saba watusaidie kupeleka magari na askari wa wanyamapori ili wananchi waweze kuvuna kwa msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu hiki cha hotuba ukurasa wa 19, ibara ya 39 inasema, jumla ya shilingi milioni 567.5 zimelipwa kwa wananchi ambapo shilingi milioni 504 ni kifuta jasho. Miongoni mwa Wilaya zilizolipwa hizo hela ni Bunda, nikushukuru Waziri kwa sababu amewakumbuka watu wa Bunda kwa Vijiji vya Unyari na Kiumbu. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Kijiji cha Maliwanda ambacho kimeathiriwa sana na wanyamapori lakini kwa bahati mbaya katika malipo haya hawakupata na Kijiji cha Sarakwa. Nilishaenda Ofisi kwao wakaniahidi kwamba watafanya marekebisho na hawa watu watapata malipo yao ya kifuta jasho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo nizungumzie hili la kifuta jasho. Mwaka jana katika hotuba hii ya bajeti tumezungumzia marekebisho ya kanuni za wanyamapori kuhusu kifuta jasho. Wanasema kutoka kwenye mpaka, mpaka kwenye eneo ambalo ni kilomita tano kutoka kwenye mpaka ambao wananchi na wanyamapori wanaishi, mwananchi atakayeliwa mazao yake zaidi ya kilomita tano analipwa shilingi laki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuseme ndovu amekula mazao kilomita arobaini kutoka eneo la mpaka analipwa shilingi laki moja kwa heka moja. Iko sheria pale kwamba kama umelima heka arobani halafu ndovu wamekuja kwenye shamba lako wamekula heka arobaini unalipwa heka tano tu kwa shilingi laki moja. Kwa lugha nyingine unalipwa shilingi laki tano, kwa heka 40 unalipwa heka tano tu heka 35 inakuwa sadaka. Sasa ni vizuri tukaangalia namna gani ya kurekebisha sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwenye kitabu hiki namna gani watu wanaozunguka wanyamapori wananufaikana nao. Katika eneo langu la Unyari miaka mitatu iliyopita ndovu walivunja jengo la watoto na akina mama wajawazito. Tukajitahidi kujenga jengo hilo na Serikali ikaahidi kwamba itaezeka na kufanya finishing. Niishukuru Wizara imetoa shilingi milioni 50 jengo lile linaendelea vizuri lakini alipokuja Waziri wa Afya amesema jengo lile kwa sababu tumelijenga vizuri liwe kituo cha afya. Kwa sababu ya sera yetu, nafikiri Mheshimiwa Waziri ni vizuri sasa akatusaidia hela nyingine kwa sababu inahitajika pale shilingi milioni 50 nyingine ili kubadilisha maeneo yale yote yawe kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba tutasaidiana katika jengo hili ili kiwe kituo cha afya na ikiwezekana hata kama litaitwa Profesa Maghembe siyo mbaya ili mradi tu umetutengenezea eneo limekuwa zuri zaidi kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya mipaka kati ya vijiji kumi na tano na Pori la Akiba la Grumeti. Mgogoro huu ni wa muda mrefu, tumesema sana na tunafikiri ile Kamati iliyoundwa ya Wizara tatu itafika kwenye eneo letu na kuweza kuangalia mipaka hii. Ipo hoja kwamba mwaka 1994 wakati eneo hilo linachukuliwa kutoka open area kuwa game reserve (pori la akiba), wananchi hawakushirikishwa. Kwa hiyo, tunafikiri kuwa sasa ni muda muafaka kuangalia mipaka hiyo na Kamati imesema ili tuweze kujua ukweli uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba wakati hilo pori la akiba linachukuliwa ambalo maarufu kule kwenye maeneo yangu kama Kawanga kulikuwepo na malambo mawili yaliyochimbwa na wananchi kwa ajili ya kunywesha mifugo. Yale malambo mawili sasa wanyamapori ndiyo wanakunywa maji lakini sisi huku chini hatuna maji ya kunywa. Mheshimiwa Waziri anajua mpaka wetu ni Mto Rubana, sasa watu wakienda katika maji yale wanafukuzwa kwa sababu wakivuka Mto Rubana tu wameenda porini. Kwa hiyo, tulifikiri ni muhimu sana Serikali kuja kuangalia namna ya kuchimba malambo upande wa pili ili ng’ombe wawe wanapata maji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kero ya mipaka ambayo ni ya muda mrefu lakini kuna vijiji vya Mgeta, Tingirima, Kandege na vyenyewe havikupata huu mgao wa kifuta jasho. Ni vizuri sasa tukaona ni namna gani wanaweza kuzingatiwa, lakini Maliwanda ni kijiji cha kwanza kuzingatiwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilitaka nichangie hayo, ahsante sana.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami nitoe mchango wangu. Kwanza, nampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutuletea hii miswada mizuri sana; inaonekana wamefanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikutie moyo na wewe Mama Mchapakazi; inavyoonekana ni kwamba kuna watu hawaelewi. Kuna mambo mawili duniani yanapatikana tu kwa kufanya kazi, kwamba busara na umaarufu, hakuna chuo cha busara wala umaarufu. Kwa hiyo, umaarufu wako na busara yako ni kushinda matatizo. Kwa hiyo, nawe unaelekea kushinda matatizo, tunakupongeza kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, nilikuwa naangalia hizi sheria, sasa najiuliza, kwanza nimeangalia mambo hapa. Kuna watu tunazunguza mambo hapa bila kujali tunapoelekea. Nchi yetu hii tuna watoto wa mitaani au watoto kwa mfano tunaita mayaya sijui, wale wanaofanya kazi nyumbani wanaitwaje? Wamejaa hata kwenye nyumba za Wabunge humu ndani, lakini sasa tunaangalia tu jambo hili, jambo hili; la pili hatuangalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukiangalia hapa ni kitu kimoja, ninachoomba ni Serikali itafute vipimo vya DNA, vitapakae kwa kila Halmashauri na kila vituo vya afya ili tuweze kujua nani kampa mtoto huyu mimba? Maana watoto wa mitaani hata tunaowaona Dar es Salaam, wengine ni wa watu wakubwa tu. Tumeona kesi kubwa kabisa inaendeshwa na watu, viongozi wakubwa tu wana watoto. Sasa nataka tujue, Mwanasheria aniambie, hivi vipimo vya DNA vinapima muda gani? Kabla au baada? Tujue maana yake! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mimi nimempa mtu mimba halafu kwa ushahidi wa mazingira, ukanifunga miaka 30. Waziri wa Sheria uko hapa, nikapigwa miaka 30, nikarudi baada ya miaka 30, nikafanya utafiti mtoto aliyezaliwa DNA ikaonesha siyo wangu na wamenipiga miaka 30 inakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba hivi vitu tuviangalie inavyokuwa. Vile vile sheria hii ukiisoma vizuri hapa kwa Mwanasheria alivyotuletea hapa, inamzungumzia mwanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari, ndiyo inavyozungumza. Sheria kuu inasema, anayepewa mimba ni mtoto wa chini ya miaka 18. Sasa kwa elimu yetu kuna watoto wanasoma kwa mfano Sekondari, kuna mwanafunzi ana miaka 18, akipigwa mimba inakuaje? Anahukumiwa kwa uanafunzi au kwa umri wake? Maana nataka kuliona hili nalo limekaaje hapa ili tuweze kujua wanahukumu kwa umri au utoto? Kwa sababu inaonekana hapa tunazungumzia wanafunzi wa Primary na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninachokiona ni ile adhabu tunayotaka kuitoa. Tunatoa adhabu ya miaka 30, sasa najiuliza, hii adhabu tunamwadhibu mhalifu au tunaiadhibu Serikali? Kwa mfano, unamfunga mtoto wa Chuo Kikuu, inawezekana akampa mtoto wa Primary au wa Sekondari mimba, tukampiga miaka 30, lakini miaka 30 hiyo Serikali inatoa chakula, inamhudumia Gerezani. Sasa tunaimpa adhabu Serikali au mhalifu? Kwa sababu mhalifu atakwenda atasoma, atafanya ufundi na kadhalika. Tuangalie na hii miaka ambayo tunaitoa.
Mheshimiwa naibu Spika, kingine ambacho nataka kukizungumza hapa ni wale wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi; na wakati fulani sasa tunamwacha mzazi miaka 18. Halafu tumesema kwamba atakayesaidia mtoto kupata mimba huyu naye tumshitaki. Sasa tunajiuliza, ni nani anayesaidia? Kwa mfano, chini ya miaka 18, wale wanaomaliza Darasa la Saba wako wa miaka 7, 8, au 9; Je, akitoroka yeye amekwenda mjini, wako wanaokwenda kusalimia mjini, sijui wanaenda kusalimia shangazi wapi, wakitoroka huko, halafu unamkamata mzazi wake? Una maana gani? Unamwonea. Wanaosaidia ni akina nani hawa? Pengine nafikiri wanaosaidia ni wale ambao kwa mfano, Serikalini wamekwenda wamefanya mkataba wa mtoto kuolewa. Amepita kwa Mwenyekiti wa Kitongoji amekubali, amepita kwa Mtendaji wa Kijiji amekubali au Mzazi wake amechukua mahari, hapo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kama mtoto ametoroka, halafu unasema mzazi wake amemwoza Dar es Salaam, anajuaje? Tutaonea watu hapa. Lazima tuangalie ni namna gani tunafanya katika kutetea haya mambo. Vinginevyo kikubwa ninachokiona mimi ni DNA. Serikali ilete DNA itapakae kila mahali, tuipeleke kwenye Vituo vya Afya ikae pale halafu tulete wataalam ili mtu ahukumiwa kwa ukweli. Kama amempa mtu mimba, ioneshe kwamba hii mimba ni ya mtoto kabla hajazaliwa ili mtu akahukumiwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. BONIFACE M GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nipate kuchangia katika miswada hii miwili. I declare interest kwamba ni member wa Kamati hii sasa kwa bahati mbaya unasema Kiswahili lakini lugha yenyewe ya chemistry na yenyewe inahusu Kiingereza sana. Sasa ndio maana…
NAIBU SPIKA: Kwa mfano neno member ni mjumbe huna haja ya kusema member unasema mimi ni Mjumbe wa Kamati, sio? (Kicheko)
MHE. BONIFACE M GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kuleta miswada hii mzuri sana. Waziri na Naibu Waziri wake tunawashukuru sana, Kamati na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kwa ujumla sisi tumepitia sana hii miswada yote miwili lakini kwangu leo mimi nitajikita kwenye Muswada huu wa Government Laboratory Authority Act 2016 ambao ukija hapa utachukua page namba 16 mpaka 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu nizungumze mambo yanayohusu Wabunge kwa ujumla, mjue hali halisi ilivyo kwenye maisha yetu Watanzania. Kunazungumzwa mambo ya sample au sampuli. Kuna sampuli za aina mbili, kuna zile signal ambazo zinachukuliwa na polisi wakati mtu akihisiwa kwamba amekunywa sumu au ameuawa kwa sumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo sasa hapa ni namna gani hiyo sample au hivyo vipimo vya mtu aliyefariki inachukuliwa na polisi kutoka kijiji A mpaka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Kuna matatizo makubwa sana ya kufanya hiyo postmoterm anapokwenda kuchukua daktari, anapokwenda polisi. Polisi mwenyewe kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali mpaka alipwe na analipwa na mtu ambaye amefiwa. Sasa imagine kwa mfano mtu huyu ni maskini anafanyaje, inakuwa ni shida na Mkemia Mkuu wa Serikali ukipeleka lazima uwalipe. Sasa hii naishauri Serikali kwamba katika hivi vipimo ruzuku zitolewe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali katika maabara hii ili pale ambapo watu hawana uwezo wa kupima vipimo hivyo waweze kupimiwa bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna zile sample zinapochukuliwa kutoka kwenye viwanda, environmental pollution, yale maji machafu yanatoka kwenye viwanda wanakwenda kupima, mathalani ni kijiji A kimepata athari, wamepiga kelele amekuja mtaalam wa NEMC amechukua vipimo amepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu wa Serikali anataka hela, mtu wa NEMC wa kupeleka hiyo sample anataka hela na vipimo kutoka kwenye viwanda kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali unalipa milioni tatu mpaka milioni saba.
Sasa ni lini wanakijiji watapata haki hiyo? na anayelipa hizo hela milioni tatu, milioni saba ni mwenye kiwanda. Ambaye anatuhumiwa ndiye mlipaji wa hizo hela. Kwa hiyo, hapa tunafikiri kwamba Serikali iweze kutoa hela nyingi kwenye maabara hii ili tuweze kupimiwa, kwa mfano wanavijiji ambao hawana uwezo waweze kupimiwa bure ili waweze kupata haki yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho mimi nakizungumzia hapa ni suala la DNA. Nimezungumza kwenye kipindi kilichopita kwamba wakati fulani hiki kitu usipopima vizuri watu wataozea magerezani. Mathalani unapelekwa kufungwa kwa hisia tu kwamba mimi nimempa mtoto mimba, mtoto wa shule miaka 10, 20, unaenda unafungwa miaka 20 au 30. Siku unatoka kwa sababu kipimo chenyewe kinasema mpaka mtoto apatikane, sasa miezi tisa imepita, mtoto amepatikana amekwenda kufanya utaalam wakasema mimi siye niliyeweka hiyo mimba na mimi nimeshaozea magerezani, sasa haya ni maneno gani haya? (Makofi)
Kwa hiyo nafikiri kwamba wataalam nao wajikite zaidi kujua vipimo hivi kabla mtoto hajazaliwa ili mtu aweze kuokoka kwa kujua kama mtoto si wake. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vingine katika hii DNA ni suala la kuangalia, wamezungumza wengi, Kambi ya Upinzani imezungumza sisi kamati tumezungumza. Hivi hawa watu wakemia hawa! Kwa mfano mimi nahisi mtoto si wangu, nimekwenda kusoma Marekani nimerudi, sura nikiangalia mpaka kidole sio changu sasa naanza kujihisi, hapa kuna nini? Sasa napeleka kutafuta DNA, sasa huyu mtu ana nafasi kubwa sana ya kusema mtoto huyu ni wako. Wakienda wakakubaliana na mke wangu kwenye mambo fulani hivi akasema ni wako sasa halafu mimi nikagundua si wangu namfungia wapi? Tunawapa nafasi kubwa sana hawa, tutafute vifungu vya kuwabana ili waweze kuona kwamba namna gani itaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mimi nimefurahi sana jana. Jana tumepitisha muswada mzuri hapa, nimshukuru Mheshimiwa Halima Mdee na Mheshimiwa Mama Profesa pale, wametuletea vifungu, huu ni muswada unahitaji vifungu, sasa maneno ya kebehi ya nini hayana maana humu ndani. Kwa hiyo, nafikiri kwamba muswada wa jana ulikuwa mzuri sana na huu unaokuja tukubaliane kwamba hali ndivyo ilivyo. Kwa mfano leo tunasema Waziri asiteue, lakini Mawaziri wote wanateua. Sasa kama tunataka Waziri asiteue Baraza basi tulete sasa muswada humu ndani au maombi rasmi ya kuondoa Mawaziri wote wasiteue Mabaraza. Sasa huyu Mheshimiwa Ummy Mwalimu tutakuwa tunamuonea sisi hapa. Kwa hiyo, tumruhusu kwamba hii kazi ni ya kwake lakini naye aweze kukaa na management yake huko tunakokwenda mbele tufanye mabadiliko kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Ndugulile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo niishukuru Serikali, niwashukuru na Wabunge wote, tufanye mambo kama ya jana, tuonekane Bunge liko vizuri tusizomeane, sisi sote ni ndugu, unanizomea mimi ndugu yako!
Mheshimiwa Katekista Selasini, unanizomea wakati tunasali wote? Mimi ndugu yako! Sasa unanizomeaje? Kusema kweli mimi nilifikiri kwamba iko siku kama haya mambo yataendelea mturuhusu tuingie humu na rungu basi tupigane halafu tuendelee kushindana humu ndani. Naunga mkono hoja.