Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Boniphace Mwita Getere (9 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita na kupata fursa ya kujiunga na vyuo mara tu wamalizapo masomo yao, huruhusiwa kutumia National Examination Results Slip kwa ajili ya taratibu za kujiunga na chuo.
Je, kwa nini wanafunzi wanaomaliza stashahada katika vyuo mbalimbali na kutaka kujiunga na elimu ya juu wasiruhusiwe kutumia academic transcripts badala ya kutakiwa kuwasilisha vyeti halisi ambavyo huchukua muda mrefu kutolewa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kiujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua kuwa vyeti vya kuhitimu stashahada huchelewa kutolewa, wanafunzi wanaomaliza stashahada katika vyuo mbalimbali na kutaka kujiunga na elimu ya juu wanaruhusiwa kutumia hati ya matokeo yaani academic transcripts ili kupata usajili wa muda yaani provisional registration mpaka hapo wanapopata vyeti vyao ili kupatiwa usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa udahili wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu hufanyika kupitia mfumo wa udahili wa pamoja yaani central admission system.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu unaratibiwa kwa pamoja kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu na hutumia matokeo ya mitihani ya ngazi ya stashahada yaliyohifadhiwa kwenye Hazina data ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi. Hivyo, waombaji udahili hawatumii vyeti kuomba udahili kwa kuwa baadhi ya taasisi zinazotoa mafunzo ya Stashahada huchukua muda mrefu kutoa vyeti hivyo katika jitihada za kudhibiti udanganyifu wa vyeti.
Kwa hiyo, wanafunzi hawa wanapo-report vyuoni hupewa usajili wa muda na baada ya kupata cheti ndipo huwasilisha taarifa hizo na kupata usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wanafunzi wanaopata tatizo la kutumia hati ya matokeo kusajiliwa vyuoni watoe taarifa ili Wizara yangu iweze kufanyia kazi ipasavyo suala hili.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Zao kuu la biashara katika Wilaya ya Bunda ni pamba lakini viwanda vya kusindika pamba vya Ushashi Ginnery na Kibara Ginnery vilivyokuwa vinamilikiwa na MCU (1984) havifanyi kazi tangu mwaka 1990:-
(a) Je, ni lini Serikali itafufua viwanda hivyo ili wakulima wa pamba wapate bei nzuri?
(b) Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika pamba ili kuongeza thamani ya zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphance Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba viwanda vya kuchambua pamba vya Ushashi na Kibara havifanyi kazi tangu mwaka 1990. Viwanda hivi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge vinamilikiwa na kilichokuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Musoma (MCU) ambacho kwa sasa kipo kwenye utaratibu wa mufilisi ulianza mwaka 1997. Utaratibu wa mufilisi umechukua muda mrefu kutokana na baadhi ya wanachama wa MCU kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu kutaka viwanda hivi visifilisiwe na badala yake ikiwezekana viendeshwe kwa ubia kati ya sekta binafsi, wanaushirika na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya ushirika imeanza kushughulikia suala la mali za MCU ikiwemo viwanda hivyo ili vitafutiwe utaratibu wa kufufuliwa kwa ubia na vianze kazi ili kuwezesha ulipaji wa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bunda ina ginnery tatu zinazofanya kazi ya kuchambua pamba inayopatikana katika wilaya hiyo. Hivyo wakulima wa Bunda wanapata huduma za uchambuzi wa pamba kupitia ginneries hizo. Aidha, taarifa zilizopo zinaonesha kuwa ginneries zilizopo katika Wilaya ya Bunda bado hazipati pamba ya kutosha na hivyo kufanya kazi chini uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inahamasisha sekta binafsi na wadau wengine kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo vya kusindika pamba ili kuongeza thamani ya zao la pamba na wakulima wapate faida zaidi. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wakulima wanajengewa uwezo wa kumiliki vinu vidogo vidogo vya kuchambulia pamba katika vikundi vya wakulima na Vyama vya Ushirika. Kwa kuwa tayari Serikali inasambaza umeme vijijini kwa nguvu kubwa kinachofuata sasa ni kujenga mazingira ya kuwawezesha wakulima kumiliki viwanda vya kusindika mazao yao ikiwepo pamba. Hii ndiyo nia na namna ya bora ya kuleta mapinduzi ya viwanda nchini katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inawashauri wamiliki wa vinu vikubwa vya kuchambua pamba wafikirie kuwekeza kwenye hatua zinazofuata za mnyonyoro wa thamani kama kusokota nyuzi katika maana ya spinning, kufuma vitambaa, weaving na kutengeneza nguo (textile).
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Malambo ya Kijiji cha Mikomahiro, Salamakati, Salama „A‟, Sanzati, Mgeta, Kihumu/Hunyari na Nyang‟aranga yamekuwa hayatumiki ipasavyo kutokana na magugu maji na hivyo kujaa matope:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha malambo haya ili yatoe huduma nzuri kwa watumiaji?
(b) Malambo haya yalichimbwa miaka ya nyuma na watumiaji kwa sasa wameongezeka; je, Serikali ina mpango wa kuyapanua malambo hayo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa malambo umewekwa katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Halmashauri kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo tathmini iliyofanyika imebaini kuwa zinahitajika shilingi milioni 90 kwa kazi ya kuondoa magugu maji na matope. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kipaumbele kimewekwa katika ujenzi wa masoko mawili na mnada wa Mgeta kwa gharama za shilingi milioni 60. Aidha, malambo mengine matano ya kunyweshea mifugo yatajengwa katika Vijiji vya Hunyari, Manchimweru, Kyandege, Salama Kati na Kaloleni ambayo yatagharimu shilingi milioni 200 hadi kukamilika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, mpango wa Serikali ni kukarabati malambo sita na kujenga mengine matano ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Aidha, mabirika ya kunyweshea mifugo yatajengwa katika Vijiji vya Hunyari, Kihumbu, Igundu, Salama Kati, Kaloleni, Mekomariro II, Manchimweru, Kyandege Nyang‟aranga, ambapo tathmini ilionesha zinahitajika shilingi 110 kukamilisha kazi hiyo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Eneo la Buhemba Holding Ground Farm (KABIMITA) linalomilikiwa na vijiji vitatu vya Magunga, Milwa (Wilaya ya Butiama) na Mekomarino (Wilaya ya Bunda) kwa ajili ya kilimo na ufugaji ambalo lilitolewa na Serikali tangu miaka 1970 na 1980 kama kituo cha kukusanyia mifugo (ng‟ombe) na kuwatibu kabla ya kupelekwa kwenye mnada wa ng‟ombe Bukoba; na sasa ni miaka 33 eneo hili linatumiwa na wakazi wa vijiji hivyo kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwamba eneo hilo ni mali ya vijiji hivyo kisheria ili kuondoa dhana ya kuwa eneo hili ni mali ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Buhemba Holding Ground chenye ukubwa wa hekta 2,446 kilijengwa mwaka 1949 na Serikali ya kikoloni kwa ajili ya kukagua, kukarantini na kunenepesha ng‟ombe, mbuzi na kondoo waliokuwa wanauzwa nchi za jirani. Baada ya uhuru kituo hiki kilikabidhiwa kwa Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya mifugo hadi mwaka 1975 kilipokabidhiwa kwa Kampuni ya Biashara ya Mifugo Tanzania (KABIMITA) ili kitumike kwa karantini na kunenepesha mifugo kwa ajili ya kuchinjwa katika viwanda vilivyokuwa vinamilikiwa na Tanganyika Packers Limited vya Arusha na Kawe, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1982, kampuni ya KABIMITA ilikitumia kituo husika kukarantini mitamba ya ng‟ombe wa asili kwa ajili ya maandalizi ya kuisafirisha kwenda Uganda kupitia sehemu ya kupakilia mifugo ya Kituo cha Bweri Holding Ground cha Musoma Mjini. Mwaka 1984 Kampuni ya KABIMITA ilifutwa na kituo hicho kilihamishiwa kwenye Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1993, Wizara kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ilianzisha mradi wa uendelezaji wa miundombinu ya masoko ya mifugo ya Tanzania (Tanzania Livestock Marketing Project). Mradi huo uliendeleza kituo hicho kwa kuweka alama za kudumu kwenye mipaka, kujenga ofisi za nyumba na nyumba ya Meneja wa Kituo, kukarabati nyumba za watumishi na kununua vitendea kazi kwa gharama ya shilingi milioni 104.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya karantini na Holding Ground nchini yanalindwa kwa mujibu wa Sheria Namba 17 ya Kuzuia Magonjwa ya Mifugo ya mwaka 2003 na Sheria ya Nyama Na. 10 ya mwaka 2006. Maeneo haya ni kwa ajili ya matumizi ya mifugo ya biashara ambayo ni lazima iwekwe chini ya karantini ili kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kabla ya kuchinja kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeruhusu wananchi kutumia eneo hilo kwa shughuli mbalimbali huku ikiendelea kuwa chini ya umiliki wa Wizara. Hata hivyo, Serikali inatoa rai kwa wananchi kutopanda mazao ya kudumu na kujenga makazi katika eneo hilo pamoja na vituo vingine vya karantini na Holding Ground nchini.
Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge muwaelimishe wananchi juu ya umuhimu wa maeneo haya katika ukuaji wa tasnia ya nyama nchini ili mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kukubalika katika masoko yenye ushindani kikanda na Kimataifa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kunusuru Taifa na janga la mabadiliko ya tabianchi?
(b) Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba Ofisi za Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri zinakuwa na Idara ya Usafi na Mazingira inayojitegemea kuliko kuitegemea Taasisi ya NEMC ambayo inaonekana kuzidiwa na majukumu ya kudhibiti na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi?
(c) Je, Serikali ilipata ushauri gani kuiondoa Idara ya Mazingira kutoka kwenye Kamati ya awali ya Mazingira, Ardhi, Maliasili na Utalii na badala yake kupelekwa kwa Viwanda na Mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012. Mkakati huo umeainisha vipaumbele vya kisekta na hatua za kuchukua ili kunusuru Taifa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya hatua hizo ni ambazo Wizara za sekta zimekuwa zikitekeleza ni pamoja na kuhimiza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya misimu ya mvua, ufugaji endelevu, kuhifadhi vyanzo vya maji na misitu, ujenzi wa mabwawa ya maji, upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala, ujenzi wa miundombinu imara ya barabara, madaraja na mifereji ili kuhimili mafuriko na matumizi ya teknolojia rafiki wa mazingira viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu unazingatia Wizara zote za kisekta na Serikali za Mitaa kuhuisha suala la mabadiliko ya tabianchi katika mipango yao.
Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile ujenzi wa kuta kwenye kingo za bahari, upandaji wa mikoko na kujenga uwezo wa wataalam kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI ilishatoa mwongozo wa uanzishwaji wa Idara ya Usafi na Mazingira katika Halmashauri zote nchini na Halmashauri nyingine zimeshaanzisha idara hiyo. Aidha, kutokana na changamoto za utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa mapendekezo ya kuboresha muundo huo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge ni jukumu la Ofisi ya Spika wa Bunge na Wizara haihusiki katika uandaaji wa miundo ya Kamati.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Zao la pamba ndilo zao kuu katika Wilaya ya Bunda:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia zao mbadala wakulima wa zao la pamba, baada ya zao hili kuelekea kutokomea kutokana na matatizo ya bei ndogo isiyokidhi mahitaji ya uzalishaji wake?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba hasa ikizingatiwa kuwa Wilaya ya Bunda yenye majimbo matatu inategemea viwanda vya pamba katika mapato na ajira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali bado inaona kuwa kuna tija katika zao la pamba kwa wakulima wa Bunda na maeneo mengine yanayolima pamba nchini kuliko mazao mengine kwa manufaa ya wakulima wenyewe na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, wakulima wanaweza kulima pamba
sambamba na mazao mengine kama vile mazao ya bustani ili kujiongezea kipato. Aidha, kuyumba kwa uzalishaji wa pamba hapa nchini kunasababishwa na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya mara kwa mara ya bei katika soko la dunia, kukosekana kwa mbegu bora, upatikanaji na matumizi sahihi ya viuatilifu na mbolea.
Mheshimiwa Spika, hali hii imefanya wakulima wengi wa pamba nchini kuzalisha wastani wa kilo 300 kwa ekari tofauti na kilo 800 zinazopaswa kuzalishwa kwa ekari. Ili mkulima aweze kuona faida ya kilimo cha pamba anayouza kulingana na bei inayopangwa na wadau wakiwemo wakulima, mkulima anatakiwa azalishe zaidi ya kilo 800 kwa ekari ya pamba nyuzi yenye ubora unaotakiwa na soko.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeandaa mpango maalum wa kuhakikisha kuwa kufikia msimu wa 2018/2019 wakulima wa pamba kote nchini wanatumia mbegu bora za pamba aina ya UKM08 zenye tija kubwa badala ya mbegu aina ya UK91 ambayo imepoteza ubora wake. Mbegu hiyo ya UKM08 inazalishwa katika maeneo ya Meatu, Nzega na Igunga ambayo hayana ugonjwa wa mnyauko. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia upatikanaji wa viuatilifu bora na matumizi sahihi ili kuhakikisha wakulima wanatumia na kupata pamba iliyo bora na kukidhi mahitaji ya soko.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa Cotton To Clothing 2016 – 2020 wenye lengo la kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la pamba ambao utaondoa utegemezi wa bei ya soko la kimataifa kwa kuwekeza katika viwanda vitakavyonunua pamba ya wakulima na hivyo kupunguza uuzaji wa pamba ghafi nje ya nchi. Hatua hii inakwenda sambamba na malengo ya Kitaifa ya kuwa nchi ya viwanda.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Miradi ya maji ya Mugeta/Nyang’aranga na Nyamuswa ambayo inadhaminiwa na Benki ya Dunia imeshindwa kumalizika tangu mwaka 2013 hadi leo.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi hii kwa ufanisi na kukabidhi kwa watumiaji?
(b) Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya ahadi ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Makala akiwa Bungeni ya ukaguzi wa miradi hii hususan mradi wa Mugeta ambao una bajeti mbili kwa mradi mmoja?
NAIBU WA WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza miradi ya maji chini ya Programu ya Maendeleo ya Maji (WSDP) ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inatekeleza Miradi kwenye Vijiji 10 vikiwemo Vijiji vya Mugeta/Nyang’aranga na Nyamuswa. Jumla ya miradi mitano ya Karukekere, Mumagunga, Kung’ombe, Mugeta na Ligamba imekamilika. Miradi ya Nyamuswa, Nyamatoke, Kibara, Bulamba na Kinyambwiga ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mugeta umekamilika na hivi sasa wananchi wanapata huduma ya maji isipokuwa Kitongoji kimoja cha Manyangale ambacho kitapata maji kutoka chanzo kingine baada ya kufanyiwa usanifu mwezi Agosti, 2016. Ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Nyang’aranga umekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa kuwa mradi huu ulikuwa unatumia bajeti mbili, tayari Mkoa wa Mara umechukua hatua kwa kuunda timu ya wataalam kukagua na kuchunguza jambo hilo. Pindi ripoti hiyo itakapotufikia, basi hatua stahiki zitachukuliwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kukarabati malambo ya Vijiji vya Makomariro 2, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Kihumbu, Kisangwa, Sanzete, Salama A, Salama Kati na Nyangaranga ambayo yamejaa magugu maji na mengine kina chake kimepungua?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilichimba malambo katika Vijiji vya Makomariro 2, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Kihumbu, Kisangwa, Sanzete, Salama A, Salama Kati na Nyangaranga kwa ajili ya kutatua matatizo ya ukosefu wa maji ya kunyweshea mifugo na kwa matumizi ya binadamu. Ni kweli malambo hayo kwa sasa yamejaa magugu maji na tope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi wa vijiji husika kuyaweka malambo hayo katika mipango yao ya bajeti na kuiwasilisha Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ili yawekwe na kutengewa fedha kwenye mpango wa bajeti ya mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa malambo hayo, Halmashauri ya Bunda ilifanya tathmini ili kujua gharama halisi ya ukarabati unaohitajika kwa ajili ya kuweka kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019. Ukarabati huo utagharimu jumla ya Sh.36,825,600 kwa mchanganuo ufuatao: Lambo la Kyandege litahitaji Sh.25,618,350, Mugeta Sh.97,870,400, Sanzete Sh.36,286,000, Salama A Sh.25,926,000, Salama Kati Sh.46,315,850, Makomariro Sh.25,926,000, na Kihumbu Sh.108,883,000. Ukarabati wa malambo haya umepangwa kufanywa katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili malambo yaliyochimbwa au kukarabatiwa yaweze kuwa endelevu, Serikali inatoa ushauri kwa vijiji husika kuunda Kamati za Uendelezaji wa Malambo ambazo zitahusika na utungaji wa Sheria ndogondogo za utunzaji wa malambo hayo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuza:-
Je, ni kwa nini mikakati ya dhati ya Serikali katika kunusuru na kuzuia uchafuzi wa mazingira ya Mto Rubana ambao unaingiza maji yake katika Ziwa Victoria na ni chanzo kikubwa cha maji katika Vijiji vya Tingirima, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Sarakwa, Kihumbu na Hunyari katika Jimbo la Bunda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Rubana ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni chanzo muhimu cha maji kwa wananchi wa vijiji vilivyoko maeneo unakopita mto na pia kwa shughuli za uhifadhi. Maji ya mto huu hutumiwa na wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kunyweshea mifugo, kilimo na uvuvi. Aidha, maji ya Mto Rubana hutumiwa na wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la akiba la Grumeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa Mto Rubana kama chanzo cha maji na shughuli za uhifadhi, Serikali imechukua hatu zifuatazo ili kunusuru na kuzuia uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika mto huo:-
(i) Kuziagiza Halmashauri za Serengeti, Bunda na Bunda Mjini kuzingatia na kutekeleza kikamilifu Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006 na Mkakati wa Hatua za Haraka za kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa wa mwaka 2008 katika maeneo yao ili kuzuia uharibifu wa Mto Rubana.
(ii) Kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa viongozi wa Halmashauri za vijiji na wananchi wote wa Kata za Hunyari, na Mugeta kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 inayozuia ukataji miti ovyo na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009.
(iii) Kufanya doria za mara kwa mara na kukamata wanaokaidi na kukiuka sheria na kusababisha uharibifu wa mazingira ya mto kwa kukata miti ovyo na uchomaji wa mkaa.
(iv) Kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kunyweshea mifugo ili kuzuia wananchi kunyweshea mifugo kwenye mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wadau wote ikiwemo viongozi katika ngazi ya Halmashauri, Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa Kata na Vijiji na wananchi wote katika maeneo hayo kushirikiana katika kutekeleza mikakati ya Serikali ili jitihada za kunusuru Mto Rubana na kuzuia uchafuzi zifanikiwe kikamilifu.