Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Boniphace Mwita Getere (22 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Kwa jina naitwa Boniphace Mwita ni Mbunge wa Jimbo la Bunda na ieleweke hivyo, mdogo wangu Ester Bulaya ni Mbunge wa Bunda Mjini.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya Jimbo la Bunda yanafanana na matatizo ya Nkasi, kuna Kata ya Unyari, ambayo ina vitongoji vyake na maeneo yake, ambavyo ni Nyamakumbo, Manangasi, Magunga, na Nyamatutu, na kijiji cha Kihumbu vitongoji vyake na Kihumbu na Mwimwalo vina tatizo lile lile la kutokuwa na mawasiliano, na kwa kuwa maeneo haya yana wakulima wengi na wafugaji wengi, na kwa kuwa wakulima hawa wako kwenye hali hatari ya tembo.
Je, Mheshimiwa Waziri haoni kuna umuhimu sasa wa kupeleka mawasiliano maeneo hayo ili wajiokoe na hali ya ulinzi wake na pia kwa mawasiliano ya kawaida?
Kwa kuwa wananchi hao wamechoka kuahidiwa na leo wamekuja hapa Bungeni kuonana na Waziri kuhusiana na maeneo yao hayo.
Je, Waziri yuko tayari kuonana nao leo? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mbunge kwamba nitakuwa tayari ofisini tuonane tu-discuss masuala yote aliyoyaongelea na tumpe takwimu sahihi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, tatizo la watoto au wanachuo wanaohitimu elimu ya diploma au stashahada ni kubwa mno. Haya mambo hayakuanza leo, toka mwaka 2007 wanafunzi wa Vyuo Vikuu kwa Taasisi ya TAHLISO wanadai hili suala halipo vizuri sana.
Kwanza vyuo vyenyewe vinapomaliza muda wake, muda wa kuhitimu masomo unakwepana na muda wa kusajili. Wanafunzi wanapopata ile wanaita supplimentary, kiswahili sijui; lakini na hawa wanachelewa kufanya mitihani yao kujiunga nao chuo. Sasa kama kweli majibu haya yako sahihi, kwanini bado wanapata matatizo haya?
Swali la pili, tatizo hili la kudahili wanafunzi wa diploma, wanapata shida sana kupata mikopo yao kwa maana vyuo vyao vinachelewa sana kupata vile vyeti na wao watu wa Bodi ya Mikopo hawapokei transcript ya mwanafunzi wa diploma. Sasa tunauliza, kwa kutumia hii Taasisi ya Elimu na kwa umaarufu wa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Ndalichako na kwa kutumia ma-engineer…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Naam!
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi ni kwamba naomba wanafunzi wanaomaliza stashahada wapewe nafasi ya kupata mikopo ya elimu ya juu, nalo ni tatizo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwa siku za nyuma kulikuwa na usumbufu kidogo ambao ulikuwa unajitokeza hususan kwa hawa wanafunzi ambao wanamaliza stashahada. Tatizo ambalo lilikuwa likijitokeza ni kwamba kwa upande wa wale ambao ni wanafunzi kwa mfano form six, wao matokeo yao yanakuwa moja kwa moja yanapitia Baraza la Mitihani ambalo ni moja, lakini kwa upande wa vyuo kumekuwa na utaratibu kati ya chuo na chuo kiasi kwamba baadhi ya vyuo vikuu vimekuwa haviamini kwa uharaka kwamba matokeo tunayoletewa ni sahihi. Kwa hiyo, walikuwa wanatafuta namna ya kufuatilia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukaa pamoja na kuelezana uhalisia na kwa sababu matokeo hayo ya vyuo vilevile yanaenda kuhifadhiwa katika Hazina data za NACTE, kwa misingi hiyo hakuna huo usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, napenda nitoe agizo kwa vyuo vyote kwamba hakuna sababu ya kufanya usumbufu kwa wanafunzi hao ikizingatiwa kwamba matokeo yao yapo na yanaongea moja kwa moja na system ambayo inafanya shughuli ya udahili.
Kwa upande wa suala la udahili wa Stashahada kusababisha wanafunzi kushindwa kuingia katika nafasi za mikopo, kwasababu suala hili linalohusiana na mfumo, ni vyema tulichukue tuendelee kulifanyia kazi na hivyo tutashirikaiana na wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge kupitia Kamati. Ahsante

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu wangu wa Elimu, ningependa kuchangia kidogo tu katika suala hili.
Kwanza napenda kutoa ufafanuzi kwamba mwanafunzi ambaye ana supplementary bado hajamaliza chuo. Mwanafunzi anakuwa amemaliza chuo pale ambapo anakuwa ame-clear mitihani yake. Kwa hiyo, mwanafunzi ambaye ana supplementary hawezi akadahiliwa kwenda katika chuo kwa sababu bado hajakamilisha masharti ya kumaliza elimu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia kuhusiana na mikopo kwa wanafunzi wenye stashahada ya ualimu. Mwanafunzi anapata mkopo kulingana na vigezo vinavyowekwa na hivyo basi, kama mwanafunzi wa stashahada amekidhi matakwa ya kujiunga na elimu ya juu na anakidhi matakwa ya mikopo, hakuna usumbufu wowote unaotokea katika upatikanaji wa mkopo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujua tu ahadi ya ujenzi wa barabara ya kutoka Nyamwiswa – Bunda kwa kiwango cha lami ni ya muda mrefu toka mwaka 2000. Sasa napenda kujua ni lini Mkandarasi wa kujenga barabara hiyo ataanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumbukumbu yangu, hii barabara imeshaanza kujengwa. Tatizo kiwango tunachokijenga ni kidogo, labda ndiyo anachokilalamikia Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie kama kumbukumbu zangu zitakosea atanisamehe, lakini kuanza tumeshaanza. Namwahidi tu kwamba, tutaongeza kasi ili hatimaye barabara hii ikamilike kujengwa katika muda mfupi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba zao la pamba bei yake ni ndogo mno ukilinganisha na uzalishaji wake. Ni lini Serikali itafanya mikakati ya dhati ya kupandisha bei ya pamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hivi viwanda vidogo vidogo ambavyo kwa swali la msingi wamevitaja kwamba vitaanzishwa kwenye Wilaya ya Bunda hasa jimbo langu la Bunda ni lini vitaanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ikilinganishwa na nchi nyingine pamba yetu haipati bei nzuri. Hii inasababishwa pamoja na mambo mengine na ukweli kwamba wakulima wetu wengi wanauza pamba ikiwa ghafi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wakulima katika vikundi vyao wanajengewa uwezo wa kumiliki viwanda vidogo vidogo ili waweze kuchambua pamba kwa sababu faida kubwa kwenye pamba ipo katika hatua nyingine za mnyororo kama kuchambua ambayo wakulima wetu hawashiriki. Hiyo kazi imefanywa na watu wachache. Kwa hiyo, tunataka tuwajengee uwezo waweze wenyewe kumiliki viwanda vidogo vidogo kama vya alizeti ili waweze kufaidika na mazao mengine yanayotokana na pamba kama mafuta pamoja na cotton seed.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile bei ya pamba inashuka kutokana na ukweli kwamba wakulima wetu wanakuwa na gharama kubwa za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kununua pembejeo kwa bei ambayo ni ghali. Ndiyo maana Serikali imechukua maamuzi ya kuangalia namna ya kupunguza tozo na kodi mbalimbali zinazotozwa kwenye pembejeo ili kuondoa gharama kubwa za uzalishaji na hivyo baadaye wakulima wetu waweze kupata bei nzuri wakati wanapouza pamba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, viwanda kama nilivyosema, mkakati wa kujenga viwanda vidogo, nafikiri mlishasikia bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwamba katika Awamu hii ya Tano tunataka kujenga uchumi wa viwanda na hasa viwanda vile vinavyotumia malighafi inayopatikana hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba pamba kama tungekuwa na viwanda vya kutengeneza nguo, kusingekuwa na haja hata ya kuhangaika ya kuuza pamba yetu nje. Kwa hiyo, ni kweli kabisa kwamba kuna mkakati mkubwa sasa wa kuhakikisha kwamba tunarudi kuwa na viwanda vya kutengeneza nguo ili pamba iweze kupata bei nzuri zaidi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa kwa siku hizi za karibuni Watanzania wameshuhudia mauaji ya kutisha katika Mikoa ya Mwanza na Tanga. Je, Serikali ina mkakati gani wa dhati wa kuzuia mauaji haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili lina majibu mapana sana kwa sababu linagusa vyombo kadhaa vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na hususan Jeshi la Polisi. Kwa sababu swali la msingi linahusu Idara ya Uhamiaji, naomba nilijibu kwa mtazamo wa Idara ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Idara ya Uhamiaji suala la udhibiti wa uhalifu nchini inajikita zaidi katika kuhakikisha tunadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu nchini ambao mara nyingi wamekuwa wakihusishwa na kuongeza wimbi la uhalifu katika nchi yetu kwa kuingiza silaha pamoja na kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo, tumeandaa mkakati kabambe ambao utahakikisha kwamba unadhibiti vipenyo vyote vilivyopo mipakani. Mpaka sasa hivi tumefanya uhakiki katika baadhi ya mikoa na kubaini zaidi ya vipenyo 280 na bado tunaendelea katika baadhi ya mikoa ambayo hatujakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatafuta fedha ili tuweze kufanya hiyo kazi ya kudhibiti mipaka yetu ili tuweze kuzuia hawa wahamiaji haramu wasiweze kuingia katika nchi yetu. Hata hivyo, tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba tunawakamata wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua zinazostahiki kwa kufanya misako katika maeneo mbalimbali nchini. Tumefanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa sana na wahamiaji haramu wengi tayari wameshakamatwa na wameshachukuliwa hatua za kisheria kwa kipindi kifupi tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba tu kutoa ufafanuzi tena kwamba Wilaya ya Bunda ina Majimbo matatu. Kuna Mwibara ya Mheshimiwa Kangi Lugola; kuna Bunda Mjini kwa Mheshimiwa Ester Bulaya na kuna Jimbo la Bunda kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini naomba Mawaziri au Manaibu Waziri wanapokuwa wanapata hayo majibu kutoka kwenye Halmashauri wawe wanayatazama vizuri kwa sababu majibu ninayoyaona hapa yanahusu mpango wa Halmashauri siyo swali la Boniphace Mwita kwenye Jimbo la Bunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mimi nimeuliza mambo ya malambo unaniambia kuna gharama za kujenga mnada, sasa hainiletei faida kwenye swali langu hili. Naomba kujua tu, ni lini hizi shilingi milioni 90, shilingi milioni 200 na shilingi milioni 110 ambazo Naibu Waziri amezitaja kwamba zitatumika kukarabati na kujenga malambo hayo zitapelekwa Bunda na zitatoka chanzo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba kujua, malambo hayo sita ya kukarabati ambayo Naibu Waziri ameyataja hapa na matano ya kujengwa, yatajengwa vijiji gani? Maana naona kama hii ni jumla ya Wilaya ya Bunda yote.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala kwamba lini pesa hizo zitapelekwa ni kama nilivyosema katika jibu langu la msingi. Mheshimiwa Getere pia lazima akubali kwamba kama alivyosema awali kwamba Bunda ina Majimbo matatu, Bunda la Mjini, halikadhalika na Jimbo la Mwibara la kaka yangu pale Mheshimiwa Kangi Lugola, mipango yote ya fedha maana yake ninyi mnapokaa katika Halmashauri yenu ndiyo mnafanya maamuzi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Jimbo likatengeneza bajeti yake kama Jimbo isipokuwa kama Halmashauri ambayo ina Majimbo matatu ndiyo inapanga hivyo vipaumbele. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeainisha jinsi gani mlipanga mipango ya miaka mitatu katika ukarabati na ujenzi wa yale malambo mengine matano. Kwa hiyo, lini fedha hizo zitakwenda, ndiyo maana nimesema katika mwaka huu wa fedha mlianza kutenga bajeti ambayo kuanzia Julai ndiyo mwaka wa fedha huwa unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kuweza kusema vijiji specific, Mheshimiwa Mbunge naomba niweze kusema wazi kwamba kwa hapa itakuwa vigumu kwa sababu Halmashauri imepanga mpango wake huu na kuainisha vijiji, nadhani tuwasiliane baadaye tuone jinsi gani tutafanya. Vilevile tuangalie na ninyi kule katika Halmashauri mpango mlioupanga mlisema mtatekeleza mradi huu katika vijiji gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba kilio cha Wanajimbo lake la Bunda kimesikika. Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha sasa Wanabunda katika Jimbo lake wanapata mahitaji yale ambayo wanayakusudia. Mwisho wa siku kama wananchi wa kawaida au kama wafugaji wa kawaida basi waweze kupata maji kwa ajili ya malisho yao na matumizi mengine ya nyumbani.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi naanza kutia mashaka kidogo kwenye miradi hii ya REA kwa sababu Waziri na Naibu Waziri wanasema mwezi wa sita ndiyo itakuwa mwisho wa REA Phase II lakini vijiji vyangu vya Jimbo la Bunda; Sanzati, Mikomahiro na Mihingo mpaka leo transformer iko moja kwenye Kijiji cha Sanzati na sioni kama kuna miradi inayoendelea pale, sioni kama kuna mafundi pale! Ni lini miradi hii itakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulishakaa na Mheshimiwa Mbunge na tukajadiliana kuhusu vijiji vyake vya Sanzati na vingine. Vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mbunge hivi sasa tunapoongea kazi inaendelea. Isipokuwa katika maeneo anayoyataja Mheshimiwa Mbunge nadhani vile vijiji sita kazi ambayo imebakia sasa ni kushusha nyaya chini kabla hawajawasha. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Bunda Vijijini na Bunda Mjini kwa ujumla wake vijiji vyote ambavyo viko kwenye ile Awamu ya II kama ambavyo inatekelezwa itakamilika ndani ya mwezi huu wa Juni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwa vijiji ambavyo itaonekana kazi haitakamilika ndani ya mwezi Juni, tunaendelea kuifanyia kazi kuviwasha katika mradi wa REA Awamu ya III unaoanza Julai, 2016. Kwa hiyo, vijiji vya Bunda vyote vitapata umeme ifikapo mwaka 2017 kama mnavyotarajia.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, je, ni lini Serikali yetu sikivu itafanya tathmini ya hali halisi ya maeneo haya ambayo ukienda kwenye maeneo hayo kuona hali halisi; na kwa bahati nzuri katika eneo hili kwenye Bunge lililopita niliuliza swali na Waziri wa Kilimo enzi hizo, Mheshimiwa Mwigulu na Naibu mwenyewe nashukuru sana kwa kufika kwenye maeneo yangu; hali halisi ya eneo hilo halipo, watu wameshajenga. Sasa je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya hali halisi kujua maeneo haya ambayo wanamiliki hewa kumbe wananchi wote walishakali na kujenga shule za msingi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na Sheria Namba 17 na Namba 10 alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri zimechelewa sana kwa wananchi wa Kijiji cha Mikomalilo, kwa sababu walishajenga na kulima mazao ya kudumu. Je, ushauri wake sasa haoni umechelewa sana ili kuwashauri watu walime mazao ambayo siyo ya kudumu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu na haja ya kufanya tathmini kuangalia hali halisi ya eneo la Holding Ground husika, Serikali inafahamu tosha kwamba ndiyo wananchi wamekuwa wakilitumia hilo eneo tokea miaka ya 1980; lakini kwa sasa hata pamoja na kwamba kuna maeneo ambayo yamevamiwa, hata yale ambayo yamebaki bado sisi tunaona kwamba ni muhimu kwa ajili ya matumizi ya Wizara na tusingependa kutumia kigezo cha kwamba kimevamiwa kuruhusu sasa; kwa sababu itamaanisha kwamba katika maeneo mengine wananchi vilevile wanaweza kuvamia.
Kwa hiyo, jitihada iliyopo sasa ni kuangalia namna gani tunaweza kunusuru maeneo yaliyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tukiruhusu maeneo yote ya Serikali yachukuliwe na wananchi baadaye Serikali ikihitaji maeneo tunaanza tena ugomvi na mgogoro na wananchi kwa sababu Serikali mara kwa mara itahitaji maeneo kwa ajili ya maendeleo ya kiujumla kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu hili la swali la kwanza la nyongeza, vilevile linajibu swali la pili kwamba tamko hili la kusema wananchi wasijenge, halijachelewa. Hata mwaka 1980 waliporuhusiwa, makubaliano ilikuwa ni kwamba wasipande mazao ya muda mrefu na wala wasijenge.
Kwa hiyo, wananchi wamekuwa wakifahamu na ndiyo maana hata Mheshimiwa Mbunge leo analiuliza hili swali wakati anafahamu kwamba huo ndiyo utaratibu uliokuwa ukitumika tokea mwaka 1980.
Kwa hiyo, sisi kama Wizara hatujachelewa, kilichotokea ni kwamba wananchi hawajafuata makubaliano ambayo tuliwekeana tokea eneo hilo lianze kutumika na wananchi mwaka 1980.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujua tu katika Wizara ya Maji kuna miradi sugu katika Jimbo langu la Bunda, kuna mradi wa maji Mgeta Nyang’alanga, Nyamswa Salama na kuna mradi wa maji Kiloreli na fedha zinazodaiwa Mgeta ni milioni 119 na Nyamswa ni milioni 229 na Kiloreli milioni 400. Naomba kujua tu hizi fedha zitaenda lini ili miradi hii ikamilike? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Halmashauri ya Bunda Vijijini kiasi kumekuwa na matatizo na kuna miradi ambayo haijakamilika lakini pili, katika utekelezaji Halmashauri haijatuletea hati ili tuweze kulipa hiyo fedha. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi na yeye tutasaidiana kufuatilia kuangalia kuna tatizo gani kwenye hii Halmashauri. Kwa nini hii miradi imechelewa sana utekelezaji, kuna tatizo gani? Je, ni ni tatizo la kiutaalam au ni uzembe? Mimi pamoja na yeye tutalifuatilia hili kuweza kuhakikisha miradi hii inakamilika.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004, Kifungu cha 182 na 183 (1) (2) na (3) na kifungu cha 36(1) na (2) tunatambua uwepo wa Maafisa Usafi na Mazingira katika Halmashauri zetu nyingi na kwa kuwa wahitumu hao wanamaliza elimu yao ya vyuo vikuu kwa vyuo vyetu hapa kwa wingi sana toka mwaka 1987, je, ni lini Serikali sasa itatangaza ajira ya wataalam hao ili kukidhi mahitaji ya mkakati aliyotaja Waziri? Swali la kwanza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa maeneo mengi ya Nchi yetu mazingira yake yameharibika sana na kupelekea kuwepo ukame mkubwa na kusababisha njaa au uhaba wa chakula na hasa katika Jimbo langu la Bunda na Wilaya nzima ya Bunda. Je, Waziri yuko tayari kuitisha kongamano la kimazingira la kushirikisha Wabunge ili kujua hali halisi ya mazingira katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la Maafisa Mazingira; kama nilivyozungumza wakati nikijibu swali la msingi kwamba Maafisa Mazingira hawa tayari katika Halmashauri zetu wapo. Aidha, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge katika zile Halmashauri ambazo hawajaweza kuajiri watu hawa basi pale nafasi zitakapoanza kutolewa, Serikali itakapoanza kuajiri tena waajiriwe hawa wa Serikali zile Halmashauri zote zihakikishe kwamba zina Maafisa Mazingira katika Halmashauri husika kama maelekezo ambavyo yamekwishakutolewa. Lakini vilevile na Wizara zote ambazo hazina sekta hii ya mazingira wahakikishe kwamba wana hao maafisa katika sekta hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na ukame ambao umepelekea uhaba wa chakula na Mheshimiwa Mbunge kupendekeza kwamba liwepo kongamano. Ninaloweza kusema kwamba wananchi wote na Wabunge wote ni lazima tukubali kwamba sasa tupo katika mabadiliko makubwa na tuko kwenye athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ambapo sasa inatupasa sisi sote kuhusiana na kilimo, kilimo chetu sasa hivi ambacho kimekuwa na mvua ya kusuasua kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanaelezwa namna ya kutumia taarifa sahihi za wataalam wetu, tafiti zinazofanywa kulingana na mabadiliko ya tabianchi waweze kujua mbegu bora zinazohitajika kwa sasa hivi ili kupambana na huu uhimilivu wa tatizo la tabianchi, mbegu bora hizo zinazozungumzwa katika mazao hayo, lakini vilevile na mazao ambayo yanahimili ukame huo kulingana na mvua ambazo zinanyesha kwa kiwango cha chini sana sasa. Ipo mikoa iliyokuwa inapata mvua ambazo zinanyesha kwa kiasi kikubwa sana lakini leo hii mvua hizo zimekuwa za kusuasua, kwa hiyo, wananchi lazima wafundishwe hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makongamano na taarifa mbalimbali za kuwahujisha wananchi; Hizo tutaendelea kuzitoa kwa wananchi ili waweze kuwa na tahadhari na hali hii ya sasa hivi ya mabadiliko ya tabianchi na suala la makongamano hilo litazungumzika kulingana na kwamba tumeshaamua kwamba shughuli yoyote ambayo tutaifanya tuhakikishe tunazidhibiti matumizi ya hovyo ya Serikali na hivyo tutahakikisha kwamba elimu hii tunaifikisha bila gharama kubwa sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tatizo la upatikanaji wa
pembejeo kwa zao la pamba ni la muda mrefu sana karibu miaka 17 au 20. Ni lini sasa Serikali itakuwa na mikakati maalum ya kumaliza tatizo hili la pembejeo kwa wakulima wa pamba kwa sababu limekuwa sugu kwa muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni muda mrefu sana Serikali tumekuwa tukipandisha bei ya pamba kwa kutegemea soko la dunia. Ni lini sasa Serikali itatengeneza mkakati wa kupata bei ya wakulima wa pamba kwa kutegemea soko la ndani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha upatikanaji wa pembejeo za pamba. Hatua mojawapo ambayo imeshafanyika ni kuanzishwa kwa Mfuko Maalum wa Wakfu wa Pamba (CDTF), ambao kazi yake kubwa ni kugawa na kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa bei nafuu kwa wakulima wa pamba, kazi ambayo tayari imekuwa ikiendelea kwa miaka kadhaa sasa.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Serikali inaendelea na mpango wa kuvifufua na kuboresha utendaji wa vyama vya ushirika ili viweze kusimamia upatikanaji wa pembejeo katika maeneo hayo. Jitihada hizi zinahusisha kwa mfano kufufua Chama cha Ushirika cha Nyanza ili kiweze kufanya kazi kuwasaidia wakulima wa pamba lakini vilevile vyama vingine kama SHIRECU, navyo vilevile kazi ya kuvifufua
inaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na namna gani Serikali inaendelea kuboresha soko la ndani, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mkakati tulionao kwa sasa
ni ule wa mwaka 2016-2020 wa kujaribu kuhakikisha tunaboresha mnyororo mzima wa thamani kutoka kwenye pamba hadi kufikia kwenye nguo. Katika mkakati huo, Serikali
inahakikisha kwamba tunajenga viwanda na kuhamasisha ujenzi wa viwanda ndani ili nguvu kubwa isielekezwe tena katika kutafuta soko la nje bali kutumia soko la ndani ambalo tunaamini tunalo. Kwa sababu kwa idadi ya Watanzania
iliyopo kama tutaweza kutengeneza nguo ambazo zitatumika ndani, tunaamini kwamba bei ya pamba itaendelea kuimarika.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Katika Jimbo langu la Bunda kuna vijiji vya Nyabuzume na Nyaburundu. Kuna wachimbaji wadogo wenye PL wa muda mrefu sana. Tatizo wale wachimbaji wanachimba, madini yanapatikana, lakini pale wanaambiwa kwamba wana leseni za utafiti. Serikali ya kijiji iliwaomba kutoa huduma za maendeleo katika maeneo hayo ya Nyabuzuma na Nyaburundu, hawataki kutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni sheria ipi inawataka hawa wachimbaji ambao wanapata madini,
hawataki kusaidia vijiji hivyo vinavyohusika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna sheria inayowakataza
wachimbaji wadogo au wachimbaji wakubwa wasilipe levy au mapato yoyote yanayotokana na uchimbaji wao. Sheria ya Madini pamoja na Sheria ya Fedha inawataka walipe.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Getere kama kuna shida, wasiliana na sisi tukusaidie ili Halmashauri yako iweze kupata
fedha hizo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matukio ya Bunda yanazidi kuwa mengi kidogo, ni lini sasa Waziri au Naibu Waziri atatembelea Bunda ili kuona hali halisi ya mambo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuahidi kwamba tutashauriana na Mheshimiwa Waziri ili kati yangu ama yeye tuweze kwenda Bunda haraka iwezekanavyo. Tutakaa pamoja tushaurine ratiba hiyo ya kutembelea Bunda muda siyo mrefu sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nataka kuuliza kwa mtu ambaye ni Mtanzania aliyezaliwa katika nchi yetu, anayehoji juu ya Mwenge…
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Badala ya kuhoji juu ya mambo mabaya yanayotokea kwenye Mwenge, anayehoji juu ya Mwenge unafanya nini huyu unaweza kumkabidhi hii nchi akaendelea kukaa nayo? Nataka tu kupata ufafanuzi huo.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo linaonyesha jinsi alivyokomaa katika kujua historia ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwaambie Watanzania, falsafa ya Uhuru wa nchi yetu ya Tanzania haiwezi kutenganishwa na Mwenge wa Uhuru. Naomba niwakumbushe, wakati wa Uhuru tarehe 9 Desemba 1961, Marehemu Baba wa Taifa alisema, sisi tutawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu ulete amani, tumaini, upendo, uondoe chuki na dhuluma, sasa jambo hili si dogo. Kwa Mtanzania anayemuenzi Marehemu Baba wa Taifa itashangaza sana kama hatataka kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda tu kuwaomba Watanzania kwa kweli hatuna haja ya kuchukuliana hatua ya namna moja au nyingine lakini wote tutambue Mwenge wa Uhuru ni tunu kubwa ya Uhuru wa nchi yetu na unapaswa kuenziwa na Watanzania wote.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Napenda kujua, kuna barabara ya Nyamswa –Bunda ambayo mwezi wa 12 mwaka jana alifika Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Waziri na kuitembelea barabara hii na kuahidi kwamba ikifika Februari mwaka huu mkandarasi atakuwa site. Kwa bajeti inayoendelea sasa hivi, hiyo barabara ilitengewa bilioni nane. Sasa napenda kujua; ni lini mkandarasi atakuwa site kwa ahadi ya Waziri, kwa maana ya kwamba hii barabara ni ya muda mrefu kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2000?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara anazoziongelea ni kweli zipo katika mpango na fedha zimetengwa na tenda zimetangazwa. Nimwombe tu Mheshimiwa Getere kama ambavyo nimekuwa nikimwomba ofisini, maana amefuatilia sana ofisini, naomba tu yale masuala ya kutaka kupigana ayapunguze, lakini nimhakikishie kwamba kile ambacho nilimuahidi ndani ya ofisi tukiwa pamoja na Katibu Mkuu, tutayatekeleza.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ambayo nimepewa na Mheshimiwa Naibu Waziri kusema kweli sijui Bunda kuna nini hata nashindwa kuelewa. Kwa sababu unapotaja Kijiji cha Karukekere, Mumagunga, Kung’ombe, Ligamba na kama unavyotaja majibu kwenye paper ambayo nimepewa kwa maana ya kujibiwa kama Mbunge, yakaonyesha sehemu kubwa ya miradi inayotajwa sio ya Jimbo lako, hivi Mbunge unajisikiaje!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nafikiri kwamba ni vizuri wakati fulani haya majibu, na nazani hili ni tatizo la Bunda tuna miradi mikubwa iko Bunda na Mabilioni ya hela, viongozi hawafiki pale kuona hela zinaliwa pale hawafiki, sasa naomba kuuliza niache kwa sababu leo ni siku nzuri tunaenda nyumbani tusilete shida huko mbele niseme sasa nimuulize Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuache haya ambayo ameyasema kwa sababu mimi sioni kama yako kwenye maeneo yangu, kuna kilometa nne za mradi wa maji mkubwa kutoka Ziwa Victoria huko Halmashauri jirani ya Butiama, sasa kama ni kilometa nne kuja kwenye maeneo ambayo yana uhaba wa maji ni lini Serikali itachukua mpango wa kuleta yale maji kutoka bomba la Ziwa Victoria kuja Nyamuswa, Bigegu, Tiring’ati na Malambeka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa kuna mradi mkubwa ulikuja wafadhili kutoka SNV wa shilingi milioni 987 kuja Kijiji cha Nyamuswa na mradi ule unaonekana umefanyiwa ubadhirifu mkubwa sana ni lini Serikali itaenda kushughulikia wabadhirifu wa hela hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi tunaitekeleza kihalmashauri, hatutekelezi kijimbo, sasa hii ndiyo maana inawezekana katika programu ya huo mradi ilichukua vijiji vingi vya Jimbo lingine na vijiji vichache vikawa vya Jimbo la Mheshimiwa Getere, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Getere kwamba utekelezaji unaendelea na mwaka huu tumeweka bajeti, kwa hiyo, tutaendelea ili kuhakikisha kwamba na vijiji vingi vilivyo sehemu ya kwako vinapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, umezungumzia kwamba kuna vijiji kama Nyamuswa ambavyo viko kilometa nne tu kutoka ziwani, ninaomba tushirikiane na Wilaya yako tuangalie kwamba ni kitu gani kitafanyika japo katika swali lako la pili umezungumzia fedha zilizotolewa kutoka kwenye hii programu ya Lake Victoria Water and Sanitation Project na mradi huo mkubwa unaendelea kuzunguka Ziwa letu la Victoria. Kwa hiyo, tutaangalia ni namna gani sasa tutaweza tukaweka mradi mwingine kuupeleka maeneo haya ambayo umeyapendekeza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi tuko pamoja na tutahakikisha wananchi wako wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini hili tatizo la hizi kata limekuwa la muda mrefu na hasa ukizingatia kwamba kata zenyewe ziko pembezoni mwa Mji wa Musoma. Nataka kuuliza ni lini haya maji yatawafikia hizo kata kwa sababu wamekuwa na usumbufu wa muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na matatizo ya mji wa Musoma pia kuna matatizo makubwa ya Mji wa Bunda na hasa Jimbo la Bunda ninakotoka mimi. Kuna kata saba zina matatizo makubwa ya uhaba wa maji ambazo ni Unyali, Kitale, Mgeta, Mihingo, Nyamaghunta na Salama; nilitaka kumuomba tu Waziri ni lini atafika? Nimuombe tu afike kwenye hizo kata saba za Jimbo langu ili aweze kujionea hali halisi ya uhaba wa maji katika jimbo hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ni kweli kwamba, ni muda mrefu, lakini nimuahidi kwamba, mara mradi huu ambao umeanza kutekelezwa utakapokamilika wakazi hawa watafaidika na maji hayo. Swali la pili kuhusu Bunda; naomba nimuahidi Mheshimiwa Mwita Getere kwamba mara baada ya Mkutano huu wa Bunge nitatembelea Mkoa wa Mara na nitafika Bunda. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya kuridhisha, lakini naomba tunapouliza maswali haya tuwe tuna kumbukumbu ya majibu. Swali hili nimeshaliuliza zaidi ya mara ya tatu, katika bajeti ya mwaka 2017/2018 nimeuliza swali hili hapa Bungeni, Naibu Waziri wa Maji na sasa Waziri alijibu kwamba kwa mwaka wa bajeti 2016/2017 malambo haya yangefanyiwa ukarabati na bajeti ya Halmashauri ikaletwa hapa Bungeni sasa tena kipindi hiki wanasema bajeti itakuwa 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimshukuru Naibu Waziri wa Maji ambaye sasa ni Waziri alikuja kwenye Jimbo langu akaangalia miradi akamuuliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kwa hali iliyoko hapa Bunda unajua bajeti kiasi gani ya maji unayo. Mkurugenzi akasema haelewi, akatuambia ana bilioni 1.7 ya Halmashauri ya Bunda kwa ajili ya maji. Ni kwa nini hizi hela zisitumike kutengeneza haya malambo wakati yanahitaji shilingi milioni 350? Naomba Waziri atoe tamko la kutengeneza malambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuna mradi mkubwa sana Mkoa wa Mara unatoka Mgango unakwenda Butiama lakini Vijiji vya Kata za Nyamswa, Kitare, Nyamamta na Salama viko jirani kilomita tatu kutoka kwenye mradi huu. Naomba Serikali ione namna gani inaweza kufanya vijiji hivyo viingie kwenye mradi mkubwa kutoka Ziwa Victoria. Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Getere kwa jinsi ambavyo anahudumia jimbo lake na alishawahi kunichukua tukaenda mpaka jimboni kuangalia matatizo ya miradi hii ya maji. Alichokisema ni kweli bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri yake hawakutumia hata senti tano, fedha yote ikarudi wakati wana matatizo ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI aniruhusu niagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bunda na Mwenyekiti, siku ya Jumatano wiki ijayo waje tukutane pamoja na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kutatua matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, tumetangaza tender kwa ajili ya kuweka bomba kubwa jipya la mradi wa Mgango-Kyabakari. Kwa hiyo, wakati wanaweka bomba hilo Mheshimiwa Mbunge nitaomba tuwasiliane ili tuweze kuainisha na hivyo vijiji vitatu alivyovisema navyo vipate maji kutoka Mgango. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wakati fulani ni vizuri haya majibu nayo tukawa tunayaona vizuri kwa sababu, Mheshimiwa Mbunge anauliza Daraja la Mto Mori, Rorya. Majibu ya matumaini yanakuja Daraja la Mto Mori, Tarime inakuwa inapoteza ile ladha ya swali na hasa mtu anapokuwa ameuliza swali kwa muda mrefu katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kujua Halmashauri hazina uwezo wa kujenga hili daraja ndio maana zimeomba Serikali Kuu isaidie kwa maana ya TAMISEMI. Ni lini sasa Serikali Kuu itatoa fedha za kusaidia daraja hilo kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Rorya uchumi wake ni mdogo haiwezi kujenga hilo daraja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Bunda ambalo natoka mimi kuna daraja la Mto Chamtikiti ambalo limeharibika muda mrefu na hivi karibuni tumesikia kwamba kuna fedha ilitoka kwa ajili ya kutengeneza daraja, lakini mpaka leo mvua inanyesha wanafunzi hawaendi shuleni kwa sababu ya hilo daraja. Ni lini Waziri atakuja Bunda kuliona hilo daraja kwa ajili ya kusaidia hali hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niseme ni kweli nafahamu na mimi Mheshimiwa Getere unafahamu nilikuwa kule Rorya na pale changamoto ni kubwa. Na ni kwamba Halmashauri tunafahamu wazi kwamba kwa sasa haitaweza isipokuwa ni kwa kupitia mamlaka yetu tuliyoiunda ya TARURA.
Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba, suala zima la daraja hili na kwa sababu eneo hili ni eneo la kipaumbele, nitawaagiza wataalam wangu wafike katika daraja hilo, lakini na eneo lingine ambalo Mheshimiwa Getere ulilizungumza, lengo kubwa ni kwamba waende kufanya tathmini tujue thamani ya kazi halafu tutaangalia tutalitengeneza kwa kifungu gani. Aidha, kupitia DFAD kwamba eneo hilo saa nyingine ni eneo la vikwazo au kupitia Mfuko wa Barabara kwa kadiri itakavyoonekana inafaa, lakini nikuhakikishie kwamba, nitawatuma wataalam wangu wataenda kufanya study ya kutosha, lengo kubwa kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Bunda na Vijiji vya Honyari, Kihumbu, Maliwanda, Sarakwa, Kyandege mpaka wao kati ya pori la Akiba la Gruneti na Mheshimiwa Naibu Waziri amesema hapa kutoka mpaka wa Mto Lubana kwenda kwa wananchi ni mita 500 ningependa kujua kutoka mpaka mto Lubana kwenda porini ni mita ngapi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika hili eneo la Gruneti kuna mipaka ambayo ipo lakini itakuwa ni vigumu sana kumpa taarifa kamili umbali uliopo kati ya huo mto na hilo eneo analolisema. Kwa hiyo naomba nitumie nafasi hii kuwambia kuwa nitakaa nae, tutaenda kutembelea hilo eneo ili tuone kwamba kuna umbali wa mita ngapi ambazo zinahusisha. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya ndugu yangu Kangi Lugola nuru ya wanyonge, Jimbo la Mwibara, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa chanzo kikubwa cha maji ya binadamu, mifugo na wanyamapori katika eneo hili la vijiji tisa ni Mto Rubana, na kwa kuwa hakuna chanzo kingine mbadala kwa wananchi wa maeneo hayo, na kwa kuwa ardhi haiongezeki na watu wanaongezeka na mifugo inaongezeka. Je, ni lini sasa Serikali kwa kupitia Wizara yake ya Mazingira itapeleka mradi mkubwa wa maji katika vijiji hivi viwili ili kuviokoa na tatizo la maji?
Swali la pili, kwa kuwa Mto Rubana, ndiyo mpaka kati ya vijiji tisa vinavyopakana na pori hilo la akiba, la Grumeti. Je, ni lini agizo lako ulilolitoa miezi miwili iliyopita, ulipotembelea maeneo hayo kwamba mita 500 za eneo la wazi kutoka eneo la mpaka kwenda vijijini na mita 500 kutoka eneo la mpaka kwenda porini wataweka beacon?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Getere wapiga kura wako wanakuita Tingatinga la maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba baada ya uteuzi wangu nilitembelea Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na kuweza kufanya mikutano miwili Maliwanda pamoja na Hunyari, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu tayari kwa kuzingatia kwamba wananchi walikuwa wanatumia maji ya Mto Rubana kunyweshea mifugo, uvuvi pamoja na matumizi ya nyumbani, tayari katika Kijiji cha Kyandege, Kijiji cha Mugeta na Kijiji cha Mariwanda Serikali tulishawajengea malambo ya kunyweshea mifugo na mabirika ya kunyweshea mifugo yanafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna taasisi inaitwa Rubana Corridor Invironmental Development Strategy wako mbioni na wamekamilisha mchoro wa kujenga bwawa moja kubwa katika Kijiji cha Kihumbu. Pia Halmashauri ya Wilaya Bunda, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 wametenga jumla ya milioni 30 kukarabati lambo la Kihumbu na pia Foundation for Civil Society kushirikiana na asasi niliyoitaja mwanzo, tayari wanataka kujenga visima viwili vya maji katika Kijiji cha Kihumbu, ikiwa ni pamoja na kuongeza lambo moja kubwa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uvuvi uliofanyika Rubana usiendelee na kuchafua mazingira, tayari Foundation for Civil Society wameendesha mafunzo ya vijiji vinne kwa ufugaji wa nyuki na sasa watasambaza mizinga 100 kwa ajili ya kuwafanya wananchi wasiende kuchafua mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu changamoto ya mita 500. Ni kweli kabisa Sheria namba 5 ya mwaka 2009 kifungu cha 74 kinazungumzia kuweka buffer zone ya mita 500 kwenda kwa wananchi. Nimhakikishie Mbunge tayari Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshawasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa TAWA pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwamba wanashughulikia masuala ya beacon. Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba beacon zinazohusu wanyama na wanadamu ni beacon ambazo siyo endelevu, leo utaweka beacon ya mita 500 kwa wananchi, na hawa wanyama wao hawajui kama kuna beacon ya mita 500, baadae watasogea tena kwenye mita 500, baadae wananchi watasema wanyama wamesogea tuweke tena beacon za mita 500, mwishowe vijiji vyote vitaisha kwa kuwa beacon ya hifadhi. Hiyo ndiyo changamoto iliyopo. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Bunda kuna miradi ya maji ya Nyamswa, Salama Kati, Mgeta, Nyang’alanga, Kiloleli, Nyabuzume, Kambugu na mradi wa umwagiliaji wa Maliwanda. Miradi yote hii ni ya muda mrefu sana. Nataka kujua tu Waziri kwamba hii miradi ambayo tayari mingi wameshaitolewa fedha na haijakamilika kwa muda mrefu, ni lini sasa hii miradi itakamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mara kama ya nne kuuliza maswali haya kwenye Bunge hili.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikiri, sio kwamba amekuja mara nyingi tu lakini ameandika barua zaidi ya mara tatu kulalamikia utekelezaji wa miradi katika Halmashauri yake ya Bunda, na kwamba fedha nyingi zimepelekwa, sio na Wizara ya Maji tu, zimepelekwa fedha na Wizara ya Maji, zimepelekwa fedha na JICA shilingi milioni 207 nakumbuka, lakini kuna own source pia ya Halmashauri imetoka miradi ile haijakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona nitume watalaam wangu wa Wizara ya Maji waje kwako kuangalia hili baadae mimi pamoja na wewe tutakwenda kuangalia kuna tatizo gani, kama alivyosema Mwenyekiti pengine kuna shida ya makandarasi au kuna shida ya utekelezaji kwenye Halmashauri kama tulivyobaini katika maeneo mengine.