Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na wote walioshiriki katika kusababisha nikawa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutumia fursa hii adhimu kabisa kuchangia katika mjadala huu na napenda nianze na wenzangu wa TAMISEMI. Nimepitia vitabu vilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati lakini kwa masikitiko makubwa ukiangalia vitabu hivi, nyuma kabisa huku vinasomeka Kamati ya Bunge ya Utawala na Sheria za Serikali za Mitaa Aprili, 2015. Kile kingine cha Utawala Bora nacho hivyo hivyo kinasomeka Aprili, 2015. Tunaweza tukasema labda ni makosa ya uandishi lakini kwa mujibu wa taarifa ambazo ninazo bahati mbaya sana hata Kamati yenyewe haikupitia taarifa hii. Kwa hiyo, yawezekana makosa haya yapo wazi ni kwa sababu Kamati nayo kwa bahati mbaya sana haikushirikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msingi uleule wa Bunge kuishauri na kuisimamia Serikali itategemea zaidi kama Kamati zako zitatimiza wajibu wake na zitafanya kazi kwa mujibu wa Kanuni. Tukiwa na utaratibu huu kwamba zinaletwa taarifa zinasomwa hapa halafu wanakamati hawashirikishwi sidhani kama ni utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye mapendekezo ya Kamati, pendekezo namba 13, linasema kwa kuwa ukusanyaji wa ushuru na majengo katika Halmashauri za Manispaaa utatekelezwa na TRA, ni vyema Serikali ikawa makini na uamuzi huo hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka hiyo haikupata mafanikio huko nyuma ikilinganishwa na mafanikio yaliyoonyeshwa na Serikali za Mitaa. Naamini kabisa kama Kamati ingekuwa imeipitia taarifa hii naamini wasingekubali kuunga mkono kwa sababu taarifa inaonyesha ufanisi umepatikana kwenye Manispaa lakini vilevile wanakubaliana kupeleka TRA, mantiki haikubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika ukusanyaji wa mapato takwimu zinaonyesha Manispaa wamekusanya vizuri sana na mimi nikiangalia takwimu za Manispaa yangu ya Kinondoni miaka mitatu imekusanya vizuri sana, asilimia 75, asilimia 80, asilimia 116. Sasa leo kuamua kodi hii kurudishwa tena TRA watu ambao watategemea watendaji wale wale wa Manispaa kwa kweli hili ni jambo ambalo linanifanya kwa namna moja ama nyingine nisiunge mkono hoja hii. Nashauri Serikali wafanye marekebisho kodi hii ikusanywe na Manispaa kwa sababu imeonekana bado wanaendelea kukusanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la milioni 50 au tunaweza tukaziita mamilioni ya Mheshimiwa Rais kwa kila kijiji na kwa sisi watu wa mjini kila Manispaa na kila mtaa. Katika Jimbo langu nina mitaa 52, tafsiri yake mapesa haya tunatarajiwa kupewa bilioni 2.6 wakati Mfuko wa Jimbo wa Mheshimiwa Mbunge wengine milioni 70, wengine milioni 50. Mbaya zaidi pesa hizo wakati tunazipeleka tuna historia ya mapesa ya mabilioni ya Kikwete ambapo hakukuwa na utaratibu mzuri wa pesa zile kuwafikia walengwa. Wasiwasi wangu ni kwamba hizi pesa tunazipeleka kisiasa na bahati nzuri nashukuru hatujaona kwenye maandishi hizi pesa zimetengwa wapi. Ni bora sasa kabla pesa hizi hazijapelekwa huko tukaonyeshwa kama Bunge utaratibu gani utatumika kuhakikisha walengwa wanazipata pesa hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu, nimepata tabu sana wakati mwingine tunatamani kupongeza Serikali lakini kwa hali ilivyo tunashindwa. Mfano uhaba wa matundu ya vyoo kwamba mpaka hapa tulipo Serikali yetu haijaweza kumudu kuchimba vyoo kwenye shule zetu. Serikali inatupa taarifa kwamba mwaka 2010 mpaka mwaka 2016 tofauti ya vyoo tulivyochimba ni 57,092 wakati mahitaji ya vyoo ni 464,676. Tunapokuwa na Serikali ambayo ina upungufu wa mashimo ya vyoo katika shule zetu 464,000 unakosa cha kupongeza. Kama tunashindwa kuchimba walau matundu ya choo maana yake tusistaajabu tunapopata kipindupindu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili nitamuomba Waziri ajitahidi tuondokane na aibu hii. Haiwezekani tukaja bajeti ya mwaka ujao tukaendelea kusema tuna matatizo au tuna upungufu wa matundu ya vyoo. Serikali iliyopata uhuru miaka 50 hili ni jambo haliwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi katika elimu, tuna programu ya elimu bure, tunasema alhamdullilah lakini kama mwenzangu alivyosema siyo elimu bure ni elimu kwa kodi. Hata hivyo, tujue kwamba ruzuku ya elimu tunayotoa mashuleni ya mtoto mmoja Sh. 500/=, shule yenye watoto 1,000 mwalimu anapewa Sh. 500,000/= kwa mwezi. Shilingi 500,000 kwa mwezi hata matumizi ya Mbunge ndani ya nyumba yake hayapatikani. Wizara lazima ije na suluhisho na katika nafasi yangu ya kushauri angalau basi tuweke sh. 2,000/=, hii sh. 500/= ni pesa ndogo sana. Leo imefika mtu anaogopa kuwa Mwalimu Mkuu kwa sababu ni mateso, ni presha, turekebishe hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya, akina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee hawahudumiwi bure kama tulivyoahidi. Nina ushahidi, mimi katika Jimbo langu tuna Hospitali yetu ya Mwananyamala, kama hiyo haitoshi hospitali zetu tumeweka viingilio kama kwa waganga wa kienyeji kwamba ukitaka kwenda hospitali lazima uwe na sh. 6,000/=. Kwa hiyo, Serikali iondoe hili tozo la kiingilio na kama kuna ulazima wa kuweka basi isizidi sh. 1,000/= ili mwananchi aweze kwenda hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora. Tunaposema utawala bora kwa kweli inatupa tabu sana hasa tukiangalia uchaguzi wa Zanzibar, tunakuwaje na utawala bora katika uchaguzi ule tulioufanya? Uchaguzi ule umetutia aibu, nafikiri Serikali imefika mahali sasa warudi, siyo vibaya mtu kulamba matapishi yako. Uchaguzi ule ulivyofanywa watu wanajua, bahati nzuri niliongea na kaka yangu Mheshimiwa Keissy, msema kweli sana kaka Keissy yeye anajua kabisa kwamba uchaguzi ule wamepiga kura watu 48, hatuwezi kuwa na uchaguzi kama huu, ni aibu. Lazima tujitahidi turudi nyuma tutazame tulipokosea ili tusonge mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utumbuaji wa majipu. Hatuwezi kwenda kwa mtindo huu Rais ndiyo akawa anatumbua majipu. Rais ana kazi nyingi, vyombo vyake vinafanya kazi gani? Tume ya Maadili inafanya kazi gani? Imetengewa pesa hapa shilingi bilioni 6 sijui bilioni ngapi ya kazi gani, wanashughulikia Maadili gani, kwa nini wasitumbuliwe wao? TAKUKURU hawapewi uwezo na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi gani mpaka Rais leo ndiyo anatumbua majipu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuruka live, kama kuonekana usiku ndiyo watu wanapatikana na siye tubadilishe muda.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Tubadili Kanuni tufanye kikao usiku.
MWENYEKITI: Muda wako umemalizika.
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Ili tuonekane. Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Pili, nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba siku ya Alhamisi sawa na tarehe 19 kaka yangu Iddi Mohamed Azzan kwa hiari yake aliamua kufuta kesi ya uchaguzi ya Jimbo la Kinondoni. Namshukuru sana Mungu, namshukuru naye kaka yangu kwa ukomavu, maana sisi watu wa Pwani tunasema “mtu mzima akivuliwa nguo, basi huchutama.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia wametoa sifa nyingi sana kwa Mzee wangu, Mzee Lukuvi. Imenipa tabu hata mimi mchangiaji nisije nikaharibu shughuli hii nikaonekana kituko. Kabla sijafika huko, nianze na maswali mawili ambayo naomba Mheshimiwa Lukuvi wakati akifanya majumuisho ayagusie. La kwanza, ujenzi wa mji wetu mpya wa Kinondoni status yake ikoje? Wananchi wa Kigamboni wana mashaka, hawajui. Nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri atuondoe shaka hii katika majumuisho atakayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, anaonaje; mimi nina mashaka kidogo na hasa ukizingatia sasa tunatarajia au tumeshapitisha kuwa na Manispaa au Wilaya ya Kigamboni. Sasa tutakuwa na Kigamboni Municipal Council, lakini vile vile kuna kitu kinaitwa Kigamboni Development Agency: Je, hatutakuwa na vyombo viwili vyenye mvutano ili kuhakikisha Kigamboni yetu inakuwa nzuri? Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kinondoni, nimekumbwa na suala la bomoa bomoa. Bomoa bomoa ile imenikuta kwenye Kata yangu ya Magomeni, Mtaa wa Kwasuna, Kata yangu ya Hananasif Mtaa wa Kawawa; tena Mtaa umepewa jina la Mzee wetu, namheshimu sana; amepewa Mtaa wa Mabondeni ambapo Serikali wameona pale hawastahili kukaa watu, wakaenda kuvunja bila kujali jina lake walilompa yule mzee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, siku mbili, tatu nimemsikia kaka yangu Mheshimiwa Waziri January Makamba alikuwa na mkutano wa hadhara kule Segerea, amesema Serikali haina mpango tena wa kuendelea na bomoa bomoa. Vile vile ikasemwa kwamba Serikali ina mpango wa kufanya mabadiliko ya sheria ya mazingira ya kupunguza mita 60 baada ya kuona kwamba utekelezaji wake umekuwa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo siyo hoja yangu. Hoja yangu ya msingi; hawa wapiga kura wangu wa Jimbo la Kinondoni nyumba zao zimevunjwa na mbaya zaidi kuna wengine mpaka leo wanaishi pale kwenye vile vibanda. Mheshimiwa Waziri, kibinadamu Serikali lazima ije na suluhisho. Kwa sababu ninavyojua, jukumu la Serikali pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha watu wake wanapata mahali pazuri pa kuishi. Sasa wale watu wanaishi kwenye vijumba vibovu pale. Tumevunja nyumba zao nzuri, tumewabakishia vijumba vya mabati. Lazima Serikali itumie au itekeleze wajibu wake kuhakikisha wale watu wanapata mahali pazuri pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wale watu waliovunjiwa nyumba zao, lazima Serikali ije na mpango, tunawapeleka wapi? Hatuwezi kuwa na Serikali ambayo inapomkuta mtu ana nyumba ya vyumba vitatu na sitting room, inamvunjia halafu anabaki kwenye kibanda cha bati. Tulisema tunawavunjia nyumba zao kwa ajili ya usalama, lakini leo wanaishi katika mazingira magumu zaidi kuliko zile tulizovunja. Mheshimiwa Waziri kama atapenda, nina takwimu za watu waliopata maradhi ya shinikizo la damu kutokana tu na nyumba zao kuwekewa X na waliopoteza maisha. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inatakiwa ihakikishe wananchi hao wanapata mahali pazuri pa kuishi. Nami napenda kushirikiana na Mheshimiwa Waziri katika maeneo yafuatayo:-
Moja, tuna maeneo ya squatters kwenye Kata ya Hananasif na Kata ya Tandale. Tukiamua kufanya maendeleo tukabadilisha kutoka squatters tukafanya mji wa kisasa tukajenga majumba marefu, maana yake hawa watu wote waliokaa mabondeni wanaweza kupata mahali pazuri pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafikiri Serikali ifike mahali hasa sisi Wabunge wa Mjini ambao hatuna mashamba ya kupewa na Serikali wala sitakuja hapa nikaomba shamba Mheshimiwa Waziri, najua hana shamba la kunipa. Ninachokitaka, ni lazima Serikali tuje na mpango wa namna gani ya kubadilisha makazi yetu haya ya squatter tuwe na majumba yaliyokuwa kwenye mpango na majumba ya kwenda juu. Aliweza Mheshimiwa Mzee Karume! Mzee Karume kafanya Zanzibar, sisi tunashindwa kwa sababu gani? Kama tutashindwa kufanya Kinondoni, tunataka tukafanye wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana Shirika lake la Nyumba. Hili Shirika limebadilishwa kabisa kutoka kutengeneza nyumba kwa ajili ya wananchi wanyonge, mpaka sasa wanatengeneza nyumba za kibiashara. Unaambiwa nyumba ya bei nafuu ni sh. 40,000,000 ya bei nafuu ni sh. 60,000,000. Kwa wananchi wetu wenyewe wana uwezo wa kujenga nyumba kwa sh. 30,000,000 ikawa bora kuliko hiyo ya sh. 40,000,000 inayojengwa na Shirika. Sasa kama Shirika hili nalo limekuwa kama la kibepari ambalo lengo lake ni kupata faida, imetokana na lengo la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, tena wananchi wanyonge. Kwa kweli Shirika limetoka kwenye mwelekeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliwahi kusema Shirika lisijenge tena nyumba za kibiashara, lakini lazima Shirika lirudi lijenge nyumba za bei nafuu kweli ambazo wananchi wa hali ya chini wanaweza kukaa. Siyo nyumba za bei nafuu za kiini macho za sh. 30,000,000 au sh. 40,000,000 ambazo wananchi hawawezi kukaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikiamua kutekeleza haya naogopa kusema, Mheshimiwa Lukuvi namheshimu sana mzee wangu, lakini namwomba sana, wale watu wanaoishi pale Kinondoni Mkwajuni wanaiaibisha Serikali yetu. Siyo wa kwenda kuwafukuza! Lazima sasa Serikali ionane na mwakilishi wa wananchi; tuje na mpango wa namna gani tutawaondoa pale ili nao wapate mahali pa kuishi, wasikie. Wakisikia Mheshimiwa Lukuvi ana roho nzuri, anapendwa, anapigiwa makofi na Waheshimiwa Wabunge, nao waone sababu ya Mheshimiwa Lukuvi kupigiwa makofi na Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni niko tayari kushirikiana na Serikali, niko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Waziri kuhakikisha tunalitatua tatizo hili ambalo naamini linanitia aibu kama Mbunge, linamtia aibu yeye kama Waziri na linaitia aibu Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Serikali ya wananchi, madaraka yake imepata kutoka kwa wananchi na lazima itumike kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana na naunga mkono hoja ya Upinzani.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa na kuchangia jambo hili. Pili, nikushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwanza, nianze kusema naunga mkono taarifa zetu hizi nzuri kabisa zilizoandaliwa na Kamati zetu hizi kubwa mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuweka rekodi sawa lakini kubwa kuliko yote kuonesha kwamba sisi watu wa Kinondoni tuliwahi kuonja matunda ya UKAWA. Matunda yale tuliyaonja katika gogoro kubwa linaloonekana kwamba Manispaa na Halmashauri hazichangii 10% za vijana na wanawake. Chini ya aliyekuwa Meya wetu wa UKAWA, Ndugu Boniface Jacob, Manispaa yetu ya Kinondoni ambayo imeitwa manispaa sugu imefanikiwa kutoa pesa shilingi bilioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie wenzangu kama sisi Wabunge tukishirikiana na Madiwani wetu na Wenyeviti wetu wa Halmashauri au Mameya tukawa na nia ya dhati, hizi pesa zinatoka na sisi kwetu Kinondoni zimetoka. Niwaahidi wananchi wa Kinondoni vyovyote itakavyokuwa bila kujali mabadiliko yoyote yaliyotokea tutahakikisha mwaka huu wa fedha 2016/2017 tutatoa pesa shilingi bilioni 6.4 kwa sababu makusanyo yetu ya ndani ni takribani shilingi bilioni 64. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masikitiko hapa, tulikuwa tumekadiria kukusanya property tax shilingi bilioni 10 kwa Manispaa yetu ya Kinondoni. Leo Mheshimiwa Waziri ameondoa kodi hii kutoka manispaa ameipeleka TRA na mpaka sasa ndiyo kwanza wamepeleka vibarua vya kuwataarifu watu kwamba wanadaiwa, tuna masikitiko makubwa sana. Kwa kuondoa hii shilingi bilioni 10 maana yake wananchi wa Kinondoni, vijana na wanawake mmewakosesha shilingi bilioni moja ambayo kama wangegaiwa shilingi milioni hamsini, hamsini, ni wananchi 20,000 mmewakosesha pesa hizi. Ni hasara kubwa sana kwetu sisi watu wa Kinondoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri kama atashindwa kurejesha hii property tax kukusanywa katika Halmashauri basi walau arejeshe katika Manispaa. Kwa sababu kwenye Manispaa pesa nyingi zitapotea, kwa sababu Majiji yana majengo makubwa yenye thamani kubwa tofauti wakati mwingine na Halmashauri yenye majengo madogo. Kwa hiyo, tusije tukaipoteza hii fursa kwa kupoteza mapato mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda niishauri Serikali kama wajibu wetu wa msingi, imeelezwa hapa katika ripoti ya PAC tuna Shirika letu la NSSF. Katika mashirika yetu ya hifadhi hili ni shirika kubwa sana. Hili shirika lina utajiri wa shilingi trilioni 3.8. Shirika hili lina miradi 40 ambayo tayari iko kwenye utekelezaji. Shirika hili limepata mabadiliko, limepata Mkurugenzi mpya na ni mtu mwenye uwezo, Profesa, lakini kwa masikitiko makubwa Wakurugenzi nane ambao walikuwa wanafanya kazi na Mkurugenzi huyu wamesimamishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, yawezekana kuna mambo yamesemwa na nashukuru ripoti imeeleza vizuri, lakini imekuja kueleza vizuri suala la Dege Eco Village na imeeleza kwamba si kweli ardhi imenunuliwa kwa milioni 800 kama inavyoandikwa kwenye magazeti wakati mwingine, kilichotokea pale ni kwamba ardhi ile heka 300 imeingizwa kama capital na yule mwekezaji Azimio amepata 20% ya mradi kwa kutoa viwanja 300; siyo kapewa pesa milioni 800 kwa heka, siyo kweli. Kwa thamani ya mradi share atakayopata 20% wameigawanya kwa viwanja ikaonekana milioni 800 wakati siyo utaratibu. Utaratibu na huu sio mgeni, hata National Housing wamewahi kuingia mkataba na TPDC na wamepata 25% katika jengo lile kubwa pale la Mkapa Tower na kiwanja cha heka moja ni sawasawa na bilioni 4.5. Sasa huu ni utaratibu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masikitiko yangu au ushauri wangu naotaka kumpa dada yangu pale Mheshimiwa Waziri mhusika ni kwamba shirika kubwa kama hili akapewa Director mgeni, Wakurugenzi wake nane ambao walikuwa wanasaidiana na Mkurugenzi aliyeondoka, wanaojua uendeshaji wa shirika hili wakakaa pembeni akawa Mkurugenzi mpya anachukua na Wakurugenzi wake wengine wapya, tunapoteza pesa zetu, yaani shilingi trilioni 3.8 tunaziweka rehani. Hawa watu wanatakiwa wawepo wamsaidie, kuna kaka yangu Magoli, kaka yangu Kidula, Wakurugenzi wapo pale waende wakamsaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunapata hasara kwenye mashirika yetu ni kwa sababu hatujali thamani ya kile kitu tulichonacho. Hii inatuletea matatizo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afanye kila hali Wakurugenzi hawa wamsaidie Mkurugenzi wetu Mkuu ili uchumi wetu usiyumbe.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza shukrani kwa Allah (S.W.) kwa kuniwezesha kuchangia hoja hii ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/2018. Nikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri katika maeneo yafuatayo:-
(a) Kupambana na wafanyakazi hewa, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na Idara zake zote;
(b) Kuendelea na mapambano dhidi ya ufisadi uliokuwa ukifanyika katika nchi yetu; na
(c) Kupambana na kuzuia mfumuko wa bei katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mpango kuandaliwa vizuri na kitaalam, bado kuna upungufu ufuatao:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza msingi wenyewe wa viwanda ni jambo linalohitaji maandalizi makubwa na mapema. Kwa kweli, dhana ya viwanda inataka fedha za kutosha kama mtaji, rasilimali watu wenye ujuzi na miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mawazo yangu, Serikali bado haijawa kwenye wakati mzuri kutoa fedha kwenye viwanda. Badala yake fedha zipelekwe kwenye miundombinu ya kuwezesha viwanda, badala ya kuanzisha viwanda na hasa ukizingatia Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kwenye sekta hii ya viwanda.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kuwa na mahusiano mabaya na wafanyabiashara wakubwa na wadogo, hatuwezi kujenga nchi bila kushirikiana kati ya Serikali na wafanyabiashara.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wafanyakazi wa Serikali ni watu muhimu sana kwa ujenzi wa Taifa letu. Naomba Serikali yetu iwaangalie kwa jicho la huruma.
(d) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na mkakati wa kubadilisha watendaji wake. Jambo hilo ni zuri, lakini linahitaji umakini na hasa watendaji wawe na weledi wa kutosha na hasa wasiwe wakereketwa wa Chama, bali wawe watu wanaoweza kufanya kazi bila ya kuathiriwa na siasa na upendeleo wa kivyama.
(e) Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu amejikita katika usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali za kila siku. Kwa mawazo yangu, kazi hii inaweza pia ikafanywa na Waziri Mkuu na hasa baada ya Rais kuonesha nini anataka katika utendaji wa Serikali na Waziri Mkuu ameona nini Rais anataka ili naye aige.
(f) Mheshimiwa Naibu Spika, demokrasia ni dhana kubwa katika maendeleo ya nchi. Mfano Uchaguzi wa Meya, Tanga, Kinondoni na uchaguzi wa Zanzibar. Kama demokrasia ikiheshimiwa itaongeza mahusiano ya ndani, pia itatoa fursa ya kupata fedha za MCC za Marekani, mfano Dola milioni 698.1 kwa mwaka.
(g) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi ya majengo kukusanywa na TRA. Jambo hili lilikuwa linafanywa na Manispaa vizuri sana, hivyo tunaiomba Serikali jambo hili la Kodi ya Majengo lirejeshwe kwa Manispaa na Halmashauri, kama ilivyokuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kwa Serikali yetu:-
(a) Kujenga miundombinu ya viwanda na siyo kujenga viwanda na kuendesha mashirika ya ndege;
(b) Pesa ya Sekta ya Kilimo kufikia 10% ya bajeti ya nchi;
(c) Serikali ihakikihe mchango wa madini kwa pato la Taifa mpaka kufikia 10% ya pato la Taifa;
(d) Kuleta utengamano wa kisiasa kwa Zanzibar, Tanga na Kinondoni;
(e) Ajira kwa vijana, hasa tuongeze fedha kwenye mabenki, kilimo, uvuvi na ufugaji; na
(f) Kuondoa VAT katika mizigo ya nje na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi kwa kunijalia uzima. Lakini pili nikushukuru sana Mwenyekiti kwa kuamua kuwa mimi niwe mchangiaji wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Kamati hasa hii Kamati ya Serikali za Mitaa kwa kueleza na kwa kutimiza wajibu wao wa kuishauri Serikali; kueleza mambo kwa kina sana, nawashukuru sana muwasilishaji na wanakamati kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kamati ya Katiba na Sheria. Katika Wizara yetu ya dada yangu pale anayeshughulikia ajira na walemavu; dada Jenista. Ukiangalia Kamati imejikita sana kwenye mambo ya kisheria, lakini mahali pengine kwenye taarifa hawajagusa chochote kwenye suala la vijana na walemavu. Ukiambatanisha vijana, walemavu na ajira maana yake hili ni kundi muhimu sana; vijana ni kundi muhimu ambalo linahitaji ajira na walemavu ni kundi muhimu ambalo linahitaji uwezeshaji. Lakini sijui kutokana na Kamati kuwa na mambo mengi bahati mbaya sana sikuona kwamba suala la ajira limepewa uzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, tuna tatizo kubwa sana la ajira na hasa kwa vijana. Mimi kama mwakilishi wa Jimbo la Mjini, Jimbo la Kinondoni linapambana sana na tatizo la vijana na hasa vijana kukosa ajira. Nilitegemea ama wakati mwingine Kamati itueleze Wizara yetu imefanya jambo gani katika ajira; katika kupitia utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji ndani ya mwaka mzima wa Kamati, ningefurahi sana kama Kamati ingetuonesha. Tuna tatizo kubwa sana la ajira, vijana wetu hawana ajira, Serikali lazima ijitahidi ihakikishe inatoa ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiliunganisha hilo la ajira na mikopo ya vijana, kwamba watendaji wetu wa Halmashauri na Serikali za Mitaa hawatoi umuhimu unaostahiki katika ile asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo inatakiwa iende kwa wanawake na vijana. Wakati mwingine wawakilishi tunagombana na watendaji kuonesha kwamba lazima tutenge hizi pesa, lakini wakati mwingine watendaji wanaona kwamba pesa ikibaki ndipo ipelekwe kwenye kundi lile la asilimia 10 ya wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe na niishauri Serikali na nikubaliane na Kamati utengenezwe utaratibu au waraka maalum wa kuwasisitiza watendaji wote wa Halmashauri kwamba suala la asilimia kumi si hisani ni suala la sheria; kwamba Halmashauri zote zitenge asilimia kumi; kiwe ni kipaumbele na isiwe mpaka matatizo au bajeti inapoonekana inaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TAMISEMI napenda kutoa ushauri kwa Serikali. Suala la TAMISEMI kuwa chini ya Ofisi ya Rais sisi wananchi bado halijatunufaisha na nadhani ni busara sasa kama Mheshimiwa Rais ataiona ni vizuri hii TAMISEMI ikarudishwa tena kwa Waziri Mkuu, ili Waziri Mkuu aweze kulisimamia. Kwa sababu kwa mtazamo wangu naamini Mheshimiwa Rais ana majukumu mengi sana na hili jambo linahusu Halmashauri na Manispaa zetu, hivyo Mheshimiwa Rais abaki katika kujikita kwenye kusimamia Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zisimamiwe na Waziri Mkuu. Huu ni ushauri ambao naamini mtani wangu ataupokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, leo Makao Makuu yamehamia Dodoma, Dar es Salaam tunabaki kama jiji. Serikali ifike mahali sasa itambue kwamba ina wajibu wa kuyajenga majiji. Tuna Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, na Mbeya. Haya ni majiji, ukiachilia mbali Tanga na mengineyo, ni majiji ambayo Serikali lazima ije na mpango wa kuhakikisha majiji haya yanakuwa ni majiji kweli yanafanana na majiji mengine na hasa ukizingatia kwa sisi watu wa Dar es Salaam baada ya Serikali kuhama yote tutabaki sisi kama sisi watu wa Jiji la Dar es Salaam na tunatakiwa tujengewe uwezo wa kutosha ili kuhakikisha Jiji letu la Dar es Salaam ambalo ndilo jiji kubwa kuliko majiji yote liwe ni jiji la mfano katika East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utawala bora. Tuna tatizo la utawala bora. Kamati imesema vizuri sana na mimi naipongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukianza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, Mheshimiwa Rais alisema magari yote ambayo sio ya mwendo kasi yanayopita katika njia ya mwendokasi yakikamatwa yang‟olewe matairi. Mheshimiwa Rais mtani wangu, mimi najua Kiswahili yeye hajui na mara nyingi anapenda kutumia Kiswahili kwa lugha ya picha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwamba kwa kusema magari yang‟olewe matairi nilivyomfahamu mimi, kwa kuwa hajui Kiswahili, nilitegemea kwamba anaonesha ni tatizo gari zisipite na gari itakayopita ikamatwe ipelekwe kwenye vyombo vya sheria, ipewe hukumu kali kwa mujibu wa sheria. Si kwamba wang‟oe matairi kama walivyong‟oa. Kwa sababu hata akisema mtu anatumbua naamini huwa anatumia lugha ya picha, hatumbui kwa maana ya kutumbua, anamwajibisha mtu aliyefanya makosa kwa kutokufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuaje leo vyombo vya dola, polisi wanashindwa kumfahamu Mheshimiwa Rais kwamba ana matatizo ya kutofahamu vizuri Kiswahili badala yake wanawakamata mapikipiki wanayang‟oa matairi kisha wanawapeleka mahakamani, sasa huyu mtu umeshang‟oa matairi umemuadhibu, unampeleka mahakamani kwenda kufanya nini? Jeshi la Polisi lazima lielewe lugha ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alipoambiwa kule njaa, aliwaambia mimi niwapikie, alikuwa na maana kwamba hii njaa ya Tanzania kila mtu atimize wajibu wake kuhakikisha anaepukana na njaa. Niwaombe watu wa Jeshi la Polisi wamwelewe sana mtani wangu huyu kwamba hakukusudia wang‟oe matairi ya watu na wale vijana waliong‟olewa matairi yao warudishiwe. Mahakama ndiyo yenye uwezo wa kumtia mtu hatiani, si Jeshi la Polisi wala si tamko la Mheshimiwa Rais ambalo watu hawakulielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Kinondoni tuna tatizo na wakati mwingine ndiyo maana hatupendi sana Mheshimiwa Rais kuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru kaka yangu Mheshimiwa Kuchauka kwa kukubali kunipa nafasi hii badala yake. Pili, nakushukuru wewe Mheshimiwa Mtemi Chenge, kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa na namna bora unavyotuendesha katika mjadala wetu huu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, kwanza, napenda nianze na kuelezea hali halisi ya uchumi na hasa nikichukua Jimbo langu la Kinondoni kama case study. Mimi kama mwakilishi nilijitahidi kupita kwa watu wangu; hali ni mbaya sana kwa wananchi wetu. Imefika mahali katika Manispaa yetu ya Kinondoni, mahoteli yanafungwa, nyumba za wageni zinafungwa, saluni watu hawaendi; hata sasa hivi tumerudi mtu ananunua nyembe anamtafuta mwenzie anampa kitana, anamnyoa nywele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale waliokwenda saluni sasa hivi hawafanyi tena scrub. Akiambiwa afanyiwe scrub, anasema hana muda, ana jambo anawahi. Hali imekuwa mbaya zaidi mpaka kwa akinamama lishe. Dar es Salaam imefikia sasa vijana hawali mchana. Mimi mwenyewe nimeshawahi kukaa na vijana nikawakuta wamechanga, wamesonga ugali wenyewe na samaki wa kukaanga wanakula. Wanakwepa mpaka kwenda kula kwa mama lishe. Hawa akinamama lishe wamekopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza hapa, mzunguko wetu wa pesa kwa wananchi ni mdogo sana. Nimesikitika umetolewa mchango hapa na Mbunge mwenzangu kijana, nimekatishwa tamaa sana. Kwa sababu sisi vijana tunategemewa kuja kuwa viongozi wa baadaye na inapofikia kijana haamini, analeta porojo kwenye suala la kiuchumi, mimi imenikatisha tamaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme suala la bajeti ya nchi yetu siyo suala la vyama, ni suala la Kitaifa. Tunapolichukua suala hili tukalifanya ni la vyama matokeo yake inakuwa mchezo wenu ni mauti yetu. Napenda tuangalie kwanza msingi wa bajeti yetu, kwa sababu inaonekana tulipotoka na tulipo ni tofauti. Hivi msingi wa bajeti yetu ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeambiwa msingi wa bajeti yetu ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi; wakati mwingine ni hotuba ya Mheshimiwa Rais; Mpango wa Miaka 25 wa Maendeleo na mengine mengi yanaingizwa hapa. Turudi tuangalie misingi yetu tunayoitumia katika kutengeneza bajeti zetu. Kama utaratibu ndiyo huu, hatuwezi kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bajeti ya nchi tukaikabidhi kuwa eti kigezo kikubwa ni ilani ya chama wakati hili jambo linahusu nchi nzima; nafikiri hapa ni mahali pa kuanza kubadilika. Lazima suala la uchumi wa nchi yetu liwe ni suala la kitaifa, tukubaliane tunataka kwenda wapi na kwa namna gani. Vyama vya siasa vipimwe kwa kutekeleza mpango kwa ufanisi, visiwe vyama vya siasa vinatuletea mipango hapa ya kila siku ya kuibuka. Leo ikipangwa ilani hii, nasi tunaitikia ilani hii, kesho akija Mheshimiwa Rais akatoa hotuba hii, nasi tunafuata hotuba hii. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima mpango wa uchumi wa nchi yetu usiwe wa kikundi cha watu wachache, tukubaliane; halafu vyama vya siasa vipimwe utekelezaji wa mpango wetu wa uchumi tuliokubaliana. Wananchi watamchagua mtu kwa kutekeleza mpango wetu tuliokubaliana. Isiwe mtu akipata nafasi ya kuongoza nchi hii, basi yeye ndio awapangie watu waende wapi. Hili nafikiri kuna mjadala hapa inabidi tufanye ili tupate muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna tatizo kubwa la nidhamu ya bajeti yetu. Ukiangalia bajeti yetu tulichokubaliana na watekelezaji wetu, watu wetu wa Serikali wanavyotekeleza, ni tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye bajeti, tulikubaliana hapa tutanunua ndege nne; lakini leo unaweza ukasikia mtu anajigamba eti tumeshalipa hela ya ndege sita. Msingi wa bajeti uko wapi? Kwa nini bajeti inapitishwa kama sheria? Leo nchi ya Tanzania imekuwa kama genge; mtu anaamua kufanya matumizi kwenye genge lake na siyo suala la Tanzania kuendeshwa kwa msingi wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaweza ukamsikia kiongozi wetu anakwenda mahali anasema nyie nitawapeni shilingi bilioni 10 hapa mjenge; nyie Magereza nawapa shilingi bilioni moja hapa mjenge; nyie Magomeni, nawapa shilingi bilioni 10 hapa mjenge; nyie sijui Katavi au wapi, nitawapeni hapa mjenge TRA ya shilingi bilioni ngapi! Hatuwezi kwenda kwa mtindo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nidhamu yetu ya matumizi ni muhimu sana na lazima Bunge liheshimiwe kwa kuwa linapitisha bajeti na inakuwa sheria na ihakikishe inafanya kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti. Hili ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli wa mipango yetu; hivi tumeongeza mipango yetu ya maendeleo ya bajeti kutoka 26% au 27% tukaweka asilimia 40; ni kweli tulikuwa tunakusudia kutekeleza? Hivi kweli tunachokipanga tunakusudia kukitekeleza? Kwa nini hatuwi wakweli? Imefika mahali na sisi Wabunge tunapenda kuongopewa. Inafika mahali sisi Wabunge wenyewe tunataka Serikali ije kutuletea muujiza hapa. Nitafanya hivi asilimia 200, nitafanya hivi asilimia 300 mpaka mtu mmoja siku moja akasema kwanza asilimia mwisho 100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatuwi wakweli katika mipango yetu? Hivi wachumi wetu hawa hawajui projection ya mapato yetu? Leo inafika bajeti yetu, tumepeleka mipango yetu, fungu la maendeleo asilimia 20, tena inapelekwa kwenye quarter ya tatu mwezi wa 12. Hivi kweli watendaji wetu, wapangaji wetu wa mipango hawajui uhalisia wa hali yetu? Kama tunataka tubadilike tutoke hapa tulipo, tuwe wakweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono sana Kamati ya Bajeti, imeeleza mambo mengi mazuri sana na kwa kweli kama Serikali itayafanyia kazi tutatoka. Nawaomba Wabunge wenzangu, bajeti ijayo na mipango ijayo; mpango ambao siyo realistic tuukatae. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mapato tuliyotegemea kutoka kwa wafadhili imekuja asilimia 16 tu na mapato tuliyokuwa tunayategemea kutoka kwa wafadhili ni zaidi ya shilingi trilioni 10.08. Asilimia sita ni sawasawa na shilingi trilioni moja. Kamati inatuambia kwamba hawajui kwa nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali na kuliomba Bunge lako Tukufu; tuna tatizo sisi na tatizo letu hatutaki kuambizana ukweli. Kuna jambo linasemwa kwamba sisi Zanzibar hatuko vizuri. Sisi ni Watanzania, ni wenyewe kwa wenyewe; hivi Wazanzibari wale wakikaa pamoja kuna tatizo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Mheshimiwa Rais aliyepita Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alitumia nguvu kubwa sana na muda wake mwingi kuwaunganisha Wazanzibari, Wazanzibari wakafika wakawa na Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa. Hivi jamani sisi kama Taifa tunakwenda mbele au tunarudi nyuma? Baada ya kufika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, leo tunakwenda tunarudi nyuma? Naomba hili jambo lizungumzwe wale wenzetu wakae pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naamini kabisa, hizi pesa za nje zinakawia; miongoni mwa sababu ni pamoja na huu utengamano wa Zanzibar, inaweza ikawa ni sababu. Hili jambo tusilichukulie kishabiki; ni jambo la Kitaifa, ni letu; sisi ni wenyewe kwa wenyewe, kwa nini tusikae kama Taifa tukatatua tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wote wapo na wote walikuwa ma-senior katika uongozi wa nchi hii. Nani asiyemjua Mheshimiwa Maalim Seif, nani asiyemjua Mheshimiwa Mzee Shein? Wote hawa wanajua na wote wana malengo ya kuhakikisha Wazanzibari wanafika mahali pazuri. Tukizungumza kama Taifa, naamini tutatoka na pesa hizo tutazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kwamba mipango yetu haizingatii hali yetu ya kimazingira. Hivi sisi tangu nchi hii imeumbwa, kuna samaki kule baharini wanapita, wanavuliwa huku juu Somalia, South Africa, wanapita wale samaki kila siku. Nimeongea na wataalam wa samaki wanasema, wale wanakua na wakishakua wanakufa. Sisi tangu tumepata uhuru nchi hii hatujawahi kutumia resource ile ya samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kuna kipindi aliikamata ile meli, wakapatikana samaki wengi, yule mtaalam anawaambia Watanzania hawajui hata resources zilizopo kwenye bahari yao, wananchi waliambiwa waende wakachukue samaki watu wamekwenda na mabeseni, kumbe samaki mmoja beseni halitoshi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, kwa nini hatuangalii mazingira yetu, Tanzania kwa jiografia yetu tunapokuwa maskini wenzetu hawatuamini, hawatuelewi, hawaelewi kwa nini tumekuwa maskini sisi, lakini sisi tukipanga mipango hatuangalii jiografia yetu, hatuangalii vitu gani sisi tunavyo wengine hawana, tunataka kufanya vitu wanavyofanya watu wasiokuwa na vitu kama vya kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaimba tu hapa viwanda, hivi sisi kweli tunaweza kwenda kwenye viwanda, kwa nini tusiende kwa yale tunayoyaweza. Sisi tunaweza kulima na watu wetu wanakuwa kwenye kilimo na tuliambizana hapa kilimo ndiyo uti wa mgongo, hayo ni majina – Kilimo Kwanza, kilimo cha kusonga mbele, majina yalikuwa mengi, lakini kimsingi kilimo ni uti wa mgongo. Kwa nini hatu-invest kwenye kilimo? Leo tunategemea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa salama kuonana na wenzangu hapa lakini pili nishukuru kwa kupata fursa hii adhimu kabisa ya kuchangia katika sheria hii muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sheria hii ni miongoni mwa sheria zilizokuwa zinahitajika sana katika ustawi wa Taifa letu. Hata ukisikiliza michango ya wenzangu waliotangulia wote wanaonesha umuhimu wa sheria hii. Kubwa kuliko yote wanajaribu kuonesha sehemu ambapo kuna upungufu ili yafanyiwe marekebisho hatimaye tupate sheria ambayo italeta ustawi kwa jamii yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijakwenda mbali, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa hili lakini nataka nirudi nyuma zaidi. Jumatatu tulikuwa Dar-es-Salaam pale na Mheshimiwa Waziri, tulikuwa na shughuli moja kubwa sana ambayo ilimjumuisha na Mheshimiwa Rais, ilikuwa ni kuja kuzindua mpango wa kuhakikisha zilizokuwa nyumba kongwe za Magomeni zinajengwa na wananchi wale ambao walikuwa hawana mahali pa kukaa, wanakaa kwa shida, wanarudishwa katika nyumba zao zile kongwe. Kwa hili nasema nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu wanufaika ni watu wa Jimbo langu moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niongeze hapa kwamba wale wananchi wa Magomeni wa zilizokuwa nyumba kongwe, nyumba zao zilivunjwa kwa lengo la kuboresha zile nyumba, wajengewe nyumba nzuri na ikiwezekana Manispaa waweke miradi pale kwa ajili ya mapato. Kilichofanya nyumba zile zisijengwe hakisemwi ni kwamba baada ya kupatikana yule mwekezaji TAMISEMI hawakutoa ridhaa ya ule mradi kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa namna moja ama nyingine isije ikaonekana ni Manispaa ya Kinondoni ilikuwa haitaki wale watu wajengewe nyumba kumbe ilikuwa ni mipango kutoka TAMISEMI haijakamilika. Sasa mambo kama haya ya watu wa TAMISEMI kuzuia jambo halafu burden yake au hasara yake kwa Manispaa ya Kinondoni na juzi Meya wangu amesulubiwa sana kwamba alishindwa kuwatetea wananchi wale, napenda record ziwekwe wazi kwamba TAMISEMI ndiyo ilikuwa haijatoa idhini au ridhaa ya kuendelea kwa ule mradi, ndiyo maana wananchi wale wameshindwa kupatiwa zile nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine niseme kwamba, wakati tunawarudisha wale waliokuwa wapangaji wa nyumba kongwe walikuwa wanaishi kwa kulipa kodi tukumbuke tuna wananchi tumewavunjia nyumba zao mabondeni. Kwangu mimi hawa kama ni wapiga kura wangu vilevile naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri amshauri Rais kwamba nyumba zile zinazojengwa Magomeni kipaumbele cha pili baada ya wale waliokuwa wamevunjiwa nyumba zao hawajarudi kiende kwa wale wakazi wa mabondeni waliovunjiwa nyumba zao. Ikiwa tunaona huruma kwa wapangaji wetu kurudi kwenye nyumba zetu, basi kwa hisia hiyo hiyo tuwaonee huruma na wale tuliowavunjia nyumba za kwao wenyewe ili nao warudi pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shughuli ile kwa masikitiko makubwa na Mzee wangu Lukuvi, nampenda sana baba yangu anatuelekeza, sisi vijana tunajifunza kazi kutoka kwa wakubwa, lakini kuna tukio limetokea pale sikulipenda kwa kweli. Sisi tumekwenda pale wawakilishi wa wananchi na mimi ni mwakilishi wa Kinondoni na tukio linafanyika Kinondoni, lakini Wizara ya Mzee wangu Lukuvi na uongozi uliokuwepo pale umeshindwa kutambua uwepo wa mwakilishi wa Jimbo husika, hii inatukatisha tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisafiri umbali mrefu kwenda kushiriki shughuli ile nikifahamu kiongozi wetu wa nchi atakuwepo pale na viongozi wetu watakuwepo pale. Kwa sababu mimi ni mwakilishi wa wananchi na nilivyolelewa kwenye chama changu kwamba natakiwa niheshimu uongozi, sasa inapofika wenzetu wakubwa hawa ambao tunategemea tujifunze kutoka kwao anafika Mbunge wa Jimbo husika, Mheshimiwa Lukuvi yeye ni mgeni pale, anashindwa ku-recognise kuwepo kwa Mbunge, imenisikitisha sana. Nafikiri sio namna nzuri, itatukatisha tamaa sisi kama vijana, itatukatisha tamaa sisi kama wapinzani kushirikiana na Serikali katika matukio ya Kitaifa. Kwa kweli, sikuipenda nimeona niieleze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukirudi sasa kwenye jambo letu hili, sheria hii pamoja na uzuri wake lakini kuna mambo yanayotakiwa yafanyiwe marekebisho. Siku za nyuma kulikuwa na kawaida, mfano, hawa wathamini wanaweza wakathamini jengo au mali inayotaka kuuzwa na baada ya kuthamini TRA wanapokuwa wanataka kwenda kuchukua kodi yao nao huwa wanapeleka watu wengine kwenda kufanya tathmini. Hii ni repetition isiyokuwa na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sasa itambulike kwamba huu uthamini utakaokuwa unafanywa na hawa Wathamini wetu, ile document itakayotokea iwe ni document ya kisheria asitokee mtu mwingine tena akamtafuta mthamini wake, tafsiri yake itakuwa wale waliofanya kazi ile hawaaminiki na tutakuwa tunapoteza nguvu bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, katika huu Muswada kuna suala la Wajumbe wa Bodi, tumeambiwa kutakuwa na Wajumbe wa Bodi tisa na Kamati nne. Muswada haujaeleza moja kwa moja wajumbe wa Kamati hizi nne wote watakuwa wanatoka kwenye ile Bodi ya watu tisa? Kama itakuwa ndivyo, idadi yao itakuwaje? Kila Kamati itakuwa na Wajumbe wa Bodi wawili au vipi? Kwa hiyo, naomba ufafanuzi ili tujue hawa wajumbe wa hizi Kamati nne ni walewale wa Bodi tu peke yao au wengine wanatoka wapi kwa sababu sheria haijaeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna hii stop order. Mara nyingi wananchi wetu wanapowekewa stop order wanatakiwa wasifanye maendelezo yoyote. Hii stop order ni kwa muda gani kwa maana ni muda gani mwananchi anatakiwa asiendeleze? Tukisema hiyo miaka mitatu maana yake mwananchi huyu atapata athari kubwa. Kwa hiyo, mawazo yangu mimi ni bora basi ile stop order isizidi miaka mitatu kwa sababu mwananchi akishapewa ile haruhusiwi kufanya maendeleo yoyote. Kwa hiyo, tuipunguze irudi angalau iwe mwaka mmoja badala ya miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napata tabu sana, ardhi Tanzania imekuwa mali ya Serikali au mali ya Rais. Sisi Kinondoni pale tuna eneo letu kubwa sana, Mheshimiwa Waziri amemshauri Rais walichukue, nilitegemea TAMISEMI kuwa chini ya Rais hata ile ardhi angeweza kuisimamia akiwa kulekule TAMISEMI, sasa hivi imeporwa imepelekwa Serikali Kuu, sasa hii ardhi maana yake inakuwa haina mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar-es-Salaam unapowapora ardhi Manispaa, leo Manispaa ya Kinondoni ikiamua kufanya maendeleo, ikiamua hata kubadilisha ofisi yake inabidi ikamwombe Mheshimiwa Lukuvi kuchukua ile ardhi, nafikiri hili si sawa. Ifike mahali hizi Manispaa ziachiwe ziwe na ardhi na ifike mahali hata wananchi ardhi za kwao ziwe ni za kwao. Isiwe leo mwekezaji anaenda Wizarani anachagua eneo halafu mwananchi hapewi taarifa analazimishwa tu kufanyiwa tathmini.