Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia (2 total)

MHE. MAULID S. MTULIA Aliuliza:-
Taifa lina tatizo kubwa la ukosefu wa ajira rasmi kwa vijana. Vijana wa Jimbo la Kinondoni wameamua kujiajiri katika sanaa mbalimbali kama vile maigizo, maonesho ya mitindo na michezo mbalimbali:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea vijana hawa vifaa, mitaji na menejimenti ili kuongeza tija katika kazi zao;
(b) Je, Serikali imefikia wapi katika suala la hatimiliki ili Wasanii, Wanamichezo na Wanamitindo wetu waweze kupata haki zao.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA
MICHEZO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, nianze wa kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kutambua mchango wa sanaa mbalimbali kama sehemu ya chanzo cha ajira kwa vijana wetu kama Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge ambaye amelionesha hilo katika Jimbo lake la Kinondoni. Wizara yangu kwa sasa iko katika mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa, ambapo dhima kubwa ya mfuko huo ni kusaidia kuinua kipato, kuongeza tija, kukuza uwezo na weledi kupitia utaratibu wa upatikanaji fedha utakaowekwa na hivyo kuwawezesha wasanii kuzalisha kazi bora za sanaa zenye kukidhi viwango vya masoko ya ndani na ya nje.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa unaandaliwa, Serikali inashauri Halmashauri zote ziwasaidie vijana wanaojishughulisha na sanaa kwa kuwapa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa ajili ya mitaji kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato ya kila Halmashauri kwa kuwa sanaa pia ni sehemu ya ujasiriamali na ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wetu kwa sasa. Aidha, sekta binafsi, mashirika, Serikali za Mitaa na taasisi mbalimbali zinaombwa kushirikiana nasi katika kuinua, kukuza na kuboresha vipaji kwa wasanii ili
waweze kujikwamua kiuchumi.
(b) Kuhusu Hakimiliki, Wizara yangu kupitia Bodi ya Filamu, COSOTA na BASATA zimeendelea kuwaelimisha wasanii wa fani mbalimbali kuzisajili kazi zao ili ziweze kutambuliwa, kupata udhibiti na ulinzi kutokana na wizi wa kazi za sanaa. Aidha, Serikali imeendelea kushughulikia migogoro na biashara haramu ya kudurufu kazi za sanaa ili wasanii waweze kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Spika, haki na maslahi ya wasanii yanalindwa kwa Sheria Na. 7 ya mwaka 1999 ya Hakimiliki na Hakishiriki, Sheria Na. 4 ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya 1976 na Sheria Na. 23 ya Baraza la Sanaa la Taifa ya 1984. Serikali inaendelea na urasimishaji wa tasnia ya filamu na muziki ambapo kazi za wasanii hawa zinawekwa stempu za TRA ambazo huwezesha kubaini nakala halisi. Serikali na taasisi zake itaendeleza zoezi la urasimishaji kwa fani nyingine.
MHE. MAULID S.A. MTULIA aliuliza:-
Sera yetu ya Afya ni kuchangia gharama ili kupata huduma ya afya isipokuwa kwa wazee, mama na mtoto:-
Je, ni fedha kiasi gani zimekusanywa kutokana na tozo za uchangiaji gharama ndani ya miaka mitano na ni nini matumizi ya fedha hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kulingana na Mwongozo, fedha za uchangiaji zinakusanywa katika vituo vya kutolea huduma na zinatumika mahali zilipokusanywa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma. Katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015, jumla ya Sh.62,244,000,000 zimekusanywa kutoka katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini.
Mheshimiwa Spika, kulingana na mwongozo huo, fedha hizi zinapaswa kutumika kwa kuweka kipaumbele katika ununuzi wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba lakini pia ukarabati mdogo, kulipia maji, umeme na matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa.