Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia (5 total)

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mimi katika maeneo yangu ya Jimbo langu la Kinondoni, hasa Magomeni Mtaa wa Kwa Suna, Hananasifu
Mtaa wa Mkunguni na mitaa mingine, nyumba za wananchi zilifanyiwa urasimishaji, lakini kwa masikitiko makubwa watu wakatumia fursa ile wengine kwenda kukopa. Nasikitika kwamba Serikali imeenda kuvunja nyumba zile bila kulipa fidia kwa wananchi wale.
Je, kwa nini Serikali inavunja nyumba zilizofanyiwa urasimishaji na kupata leseni za makazi bila kulipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, anachokizungumza ni kweli, kuna maeneo yalifanyika hivyo, lakini suala la msingi hapa kupewa leseni ya makazi haina maana ya kwamba pale ambapo utaratibu wa mipango miji umeyapanga vinginevyo yale maeneo hautavunjiwa. Kwa sababu Dar es Salaam yenyewe sasa hivi iko katika mchakato na ninadhani imekamilisha mpango wa master plan ya mji ule.
Sasa pale ambapo inaonekana kabisa kwamba kuna suala zima la kutaka kuweka miundombinu inayofaa katika
eneo lile watu hawa wanaweza kuvunjiwa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, lakini Wizara ilishatoa tangazo kwa wale ambao walikuwa na umiliki halali na wana hati
kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wamevunjiwa kimakosa, tulisema walete orodha yao na watu wa mipango miji watakwenda kuhakiki waone kweli walivunjiwa kimakosa. Lakini kwa wale ambao waliendelea na ujenzi bila kuzingatia mipango miji imepanga nini katika ule mji hao hawatalipwa na itakuwa ni tatizo. Watu wa Hananasifu na Mkunguni kama alivyosema, kama hao wapo kulingana na maelezo niliyoyatoa, basi tupate wakiwa na hati zao kutoka Wizarani kwetu au kutoka kwenye ma nispaa inayohusika, tutawa-consider kulingana na malalamiko watakavyokuwa wameyaleta.
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu hivi sasa imekuwa soko holela la kazi za wasanii ambazo zinaingizwa kiujanja ujanja
bila kufuata taratibu wala Serikali yetu kupata kodi kwa mujibu wa sheria, pia wasanii wengi wana malalamiko makubwa kwamba kazi zao zinazotumiwa na makampuni ya simu hawalipwi ipasavyo. Vilevile, wasanii wana
manung’uniko mengi kwamba kazi zao za sanaa wanapokwenda kuziuza wanadhulumiwa na wanapewa kwa bei chee. Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuleta mabadiliko ya sheria hizi ambazo Naibu Waziri amezitaja, Sheria Na. 7 ya Mwaka 1999, Sheria Na. 4 ya Mwaka 1976 na Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984. Sheria hizi zote zinaonekana zina miaka mingi haziendi sawa na mabadiliko ya kasi yanayokwenda katika sanaa yetu Tanzania. (Makofi) Swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami kwenda kukaa na wasanii ili tuwasikilize matatizo yao na tuweze kushirikiana nao ili kuwapatia ufumbuzi na kuhakikisha kazi zao zinaleta tija kama ilivyokuwa kwa wasanii wa nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ni kweli
kwamba sheria zetu hizi zinazohusiana na usimamizi wa masuala ya sanaa na wasanii kwa ujumla zimepitwa na
wakati, kwa sasa tunachokifanya ni kuandaa sera kwanza kwa sababu tulikuwa hatuna Sera ya Sanaa, tulikuwa na Sheria ya Filamu lakini hatukuwa na Sera. Kwa hiyo, kwa sasa tunaandaa Sera ya Filamu na vilevile tunaandaa Sera ya Maendeleo ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha sera hizi ambapo Sera ya Filamu tunatarajia kufikia mwishoni mwa mwezi wa Sita tuwe tumekamilisha kuandaa rasimu yake na baada ya kukamilisha sasa tutahuisha hizi sheria ili kusudi ziweze kuendana na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na niseme kwamba tuna kila
sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kuanzisha Idara ya Sanaa katika Wizara yetu. Nia hasa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza kasi ya maendeleo ya tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuambatana naye kwenda katika Jimbo lake, nimekubaliana na hili. Hata hivyo
napenda kumjulisha kwamba Wizara yetu imeanzisha utaratibu kupitia utaratibu wa wadau tuzungumze. Kila
Jumanne tunaongea na wadau wa sekta zetu nne; Sekta ya Habari, Sekta ya Sanaa, Sekta ya Utamaduni pamoja na Sekta ya Michezo. Kwa hiyo, huwa tunaongea na wadau ili kupata changamoto na kupanga ni jinsi gani tuweze kutatua changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, hivyo nichukue nafasi hii kuwaalika wasanii wote pale ambapo tutakuwa tukizungumzia masuala yao siku ya Jumanne fulani kwa mwezi basi waweze kuhudhuria pale Dar es Salaam na hapa Dodoma. Maalum kwa Jimbo lake la Kinondoni, Wizara yangu iko tayari na binafsi niko tayari kuambatana naye ili tuweze kusikiliza matatizo ya wasanii. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MAULID S.A MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, naungana naye katika umuhimu wa watu wetu kuchangia gharama, lakini anaonaje sasa Serikali dhana ya kuchangia gharama ikabaki katika kuchangia dawa pamoja na vipimo lakini wananchi wetu wakapata fursa ya kwenda kumwona Daktari bila kulipa pesa ya kumwona Daktari ili kuongeza idadi ya watu wanaokwenda kwenye vituo vya afya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna makundi yetu maalum ambayo kwa mujibu wa sheria yetu wanatakiwa wapate huduma za afya bure na kwa kuwa Wabunge wengi wamesimama hapa na mimi mmojawapo tunaonesha kwamba bado makundi haya hayapatiwi huduma ya afya bure. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa yuko tayari sasa kufuatana na mimi kwenda katika hospitali zangu za Jimbo la Kinondoni kwenda kusisitiza na kuhakikisha wananchi hawa wanapata huduma bure?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali lake la kwanza kuhusu wananchi kupewa ruhusa ya kwenda kununua dawa na vifaa tiba katika hospitali lakini wakaonwa bure na Madaktari, sisi kama Serikali hatuna utaratibu huo kwa sababu tunafanya kazi kwa mujibu wa sera lakini pia mipango mbalimbali ya kimkakati ya kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika, tunafuata Sera ya Afya ya mwaka 2007 pia Mpango wa Kimkakati wa Huduma za Afya Na.4 ambao unaanza 2015 - 2020. Pamoja na mikakati mbalimbali kama Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na yote haizungumzii uelekeo huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, mwongozo ambao tunaufuata sisi kama Serikali ni kuwahudumia wananchi zaidi kwa kutazama mipango hiyo na uelekeo wetu kwenye mipango yote hii ni kuelekea kwenye universal health coverage ambapo kutakuwa kuna bima ya lazima ya kila Mtanzania. Tukianza kutekeleza mpango huo kama Bunge lako Tukufu litatupitishia sheria ambayo tunakusudia kuileta muda si mrefu basi kila Mtanzania atalazimika kuwa na kadi ya bima ya afya ya namna moja ama nyingine iwe ni CHF ama iwe ni Social Health Insurance kama NHIF.
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania akishakuwa na hiyo kadi yake maana yake sasa atakuwa anatibiwa kwa kutumia kadi ya bima ya afya. Huo ndiyo uelekeo na sio uelekeo anaouzungumzia Mheshimiwa Mtulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu makundi maalum, hata hili suala la makundi maalum kuhudumiwa chini ya kiwango japokuwa tunalikubali, lakini dawa yake hasa ni huu mfumo wa kuwa na bima ya afya ya lazima kwa kila Mtanzanzia ambapo yale makundi maalum ambayo yanapewa msamaha kisera maana yake yatakuwa yanakatiwa bima kabla hayajaenda kutafuta huduma.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, wazee wote ambao wanastahili kupewa msamaha wa kupata huduma za afya basi wanakatiwa kadi za bima ya afya na Serikali kwa sababu wao wanapewa msamaha anapokwenda pale kutibiwa huwezi kubagua yupi ana kadi na yupi hana kadi, kila mtu ana kadi. Yupi kadi yake ni ya msamaha na yupi kadi yake ni ya kulipia, kila mtu atakuwa ana kadi na kila kadi itaheshimiwa na kituo chochote kile cha kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa msingi huo hata haya makundi maalum anayoyazungumzia yatapata huduma zilizo bora. Kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa kuwa tunaelekezwa kufanya hivyo, namhakikishia miaka hii mitano haitakwisha kabla hatujaleta hapa Bungeni mapendekezo yetu ya Sheria ya Single National Health Insurance ambayo ni compulsory kwa kila Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kufuatana naye, anajua yeye ni rafiki yangu halina shida, tutafute muda twende Kinondoni tukatembelee, japokuwa mimi nimeshafika Kinondoni mara nyingi sana. Ahsante.
MHE. MAULID SAID A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokanana taarifa zilizotolewa na TMA wameeleza kwamba baadhi ya mikoa yetu katika Tanzania itapata chini ya wastani wa kiwango cha mvua, kwa maana ya Pwani, Tanga, Zanzibar na Morogoro Kaskazini. Je, Serikali ina mpango gani kukabiliana na tatizo litakalotokana na upungufu huo wa mvua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali yetu kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali duniani tunaanza kuandaa miradi ambayo itakuwa na efficiency kubwa kwa maana ya kutumia maji kidogo kwenye uzalishaji wa mimea. Teknolojia hiyo tunazidi kuichukua na kuiendeleza ili maji kidogo yanayopatikana yaweze kutumika vizuri na uzalishaji uwe mkubwa. Kwa hiyo, tumejiandaa, taarifa ya TMA tunayo na sisi tunaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba production ya mazao hasa ya chakula itaendelea kuwa kama ambavyo matarajio yapo.
MHE. MAULUD S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana kwamba maji ni uhai na kila mwananchi anahitaji maji; lakini tunakubaliana pia kwamba zamani tulikuwa na mabomba yetu ya Serikali ambayo wananchi walikuwa wanapata maji bure, lakini sasa hayapo.
Je, Serikali ian mpango gani kuyarejesha yale mabomba yetu ili wananchi wetu wapate maji bure kwa wale ambao hawana uwezo ukizingatia kwamba kuhitaji maji hakutegemei uwezo wa fedha za mtu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba zamani kulikuwa na mabomba ambayo yalikuwa yanatoa maji bure na hivyo kusaidia wale watu wasiojiweza, lakini kwa sasa mamlaka zote zimepewa maelekezo na zina sheria kwamba kila mamlaka kwenye mkoa inashirikiana na uongozi wa mkoa kubaini wananchi wote ambao hawana uwezo kama wazee na wagonjwa, kwa hiyo wakiorodheshwa wanaendelea kupata kupata huduma ya maji bure.