Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni (104 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Kutokana na wizi wa mifugo uliokithiri katika Bonde la Yayeda Chini, Serikali ilianzisha kituo cha polisi na sasa kimeondolewa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukirudisha kituo hicho ili wananchi wapate huduma za ulinzi wa mifugo na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kituo cha polisi cha Bonde la Mto Yayeda Chini kilianzishwa kutokana na matukio ya kukithiri kwa matukio ya wizi wa mifugo. Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi lilipeleka gari PT Na. 1008, Landrover kituo cha polisi cha Hydom kinachotoa huduma ya ulinzi wa eneo hilo na kuanzisha doria za mara kwa mara ili kupambana na wimbi la wizi wa mifugo. Kwa hivi sasa, hali ya wizi wa mifugo na uhalifu mwingine katika eneo hilo umepungua.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kituo hicho hakijaondolewa bali taratibu za kutoa huduma za ulinzi zimebadilika; ambapo askari hupangwa kwa kazi za ulinzi wa doria eneo hilo kwa kipindi maalum na kwa awamu. Jeshi la Polisi litaendelea kutathmini na kuzingatia hali ya uhalifu wa eneo hilo katika kutoa huduma stahiki za ulinzi na usalama.
MHE. DAVID E. SILINDE (K.n.y MHE. FRANK G. MWAKAJOKA) aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina Mpango gani wa kugenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya hapa Tunduma ili kuendana na ongezeko la watu na wageni wanaoingia nchini?
(b) Je, Serikali haioni vema ujenzi wa kituo hicho uende sambamba na ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu kwa Polisi wetu ambao wana shida kubwa ya makazi?
SPIKA: Sasa Mheshimiwa Silinde wewe Tunduma si ulishaondoka, majibu ya swali hilo Mheshimiwa Naibu, Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI YA WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Kituo cha Polisi Tunduma ni kidogo na hakina nyumba za kutosha. Wilaya ya Momba inahitaji nyumba 150 ili kukidhi mahitaji ya makazi ya Askari. Kama ilivyo kwa maeneo mengi hapa nchini, changamoto kubwa ya ujenzi wa vituo vya Polisi na nyumba za askari ni uhaba wa fedha. Aidha, kwa Kituo cha Polisi Tunduma changamoto nyingine ni eneo la kufanya upanuzi wa kituo kilichopo sasa kwani kituo hicho kipo mpakani kando mwa barabara ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha Jeshi la Polisi linaboreshewa makazi na kuwa na ofisi ili kuwezesha utoaji huduma kwa wananchi kuwa mzuri. Jeshi la Polisi chini ya utaratibu wa mikopo nafuu kutoka taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi lina mpango wa kujenga nyumba na ofisi za Polisi maeneo mbalimbali nchini. Kwa hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za kupata mkopo toka Bank ya Exim ya China ili kujenga nyumba 4,136 za makazi ya Askari katika Mikoa 17 hapa nchini.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya ujambazi unaohusiana na uporaji wa fedha na ni muhimu sana Watanzania wakapata ufahamu kwa takwimu kuhusu ukubwa au udogo wa tatizo hilo kuliko kupata taarifa ya tukio moja moja:-
(a) Je, ni zipi takwimu sahihi na mchanganuo wa matukio ya ujambazi unaohusiana na uporaji wa fedha ikiwa ni pamoja na vifo na majeruhi ya matukio hayo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 Kitaifa?
(b) Je, ni mikoa gani miwili inayoongoza na mikoa gani miwili yenye matukio hayo machache?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya ujambazi yanayohusisha uporaji wa fedha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 yalikuwa kama ifuatavyo:-
Mwaka 2013 matukio 1,266; mwaka 2014 matukio 1,127; na mwaka 2015 yalikuwa 913. Jumla ya matukio yalikuwa 3,306 yaliyosababisha jumla ya vifo vya watu 91 na majeruhi 189.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa inayoongoza kwa matukio hayo katika kipindi hicho ni Dar es Salaam iliyokuwa na matukio 733, yaliyopelekea vifo vya watu 65 na majeruhi 43. Mkoa uliofuata ulikuwa ni Mara uliokuwa na matukio 375 ya uporaji yaliyosababisha vifo 11 na majeruhi sita. Aidha, Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na Kusini Unguja haukuwa na matukio ya uporaji wa fedha kabisa.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamezidi kuongezeka siku hadi siku na kusababisha madhara na vifo kwa watu wasio na hatia:-
Je, Serikali inafanya juhudi gani ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili huu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vya mtu ama watu kujichukulia sheria mikononi ni uhalifu ambao umeanza kushamiri katika jamii yetu ikiwemo Visiwa vya Zanzibar katika kipindi cha mwaka 2013/2014. Jumla ya matukio 2,041 yaliripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 kulikuwa na matukio 1,112 ambapo Zanzibar yaliripotiwa matukio 14. Mwaka 2014 yalipungua na kufikia matukio 929, kati ya hayo Zanzibar yalikuwa ni matukio matano. Aidha, matukio yote yalichukuliwa hatua stahiki ikiwemo wahusika kukamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, limekuwa likichukua hatua mbalimbali za kupambana na wimbi la uhalifu huo, miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kufuata sheria. Aidha, Jeshi la Polisi huwakamata na kuwafikisha Mahakamani watu wanaojichukulia sheria mkononi, kutenda makosa mbalimbali ya jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu, kutoa rai kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, naomba Waheshimiwa Wabunge wote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha wananchi kuepuka vitendo hivyo.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kwa kuwa barabara kuu kwenda mikoani zina foleni na tukiangalia barabara hizo zinatumika na magari mengi ya mizigo ambayo mara nyingi huwa ni chanzo cha ajali na Watanzania wengi kupoteza maisha:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizo zinapungua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyowahi kujibiwa swali la msingi namba 13, 74, 75 na 167, katika Mikutano mbalimbali ya Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zipo sababu nyingi za vyanzo vya ajali za barabarani nchini. Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa, sababu hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu:-
Kwanza, sababu za kibinadamu kama vile ulevi na uzembe zinazochangia asilimia 76 ya ajali zote.
Pili, ubovu wa vyombo vya usafiri zikiwemo hitilafu za kiufundi na mfumo wa umeme wa magari unaochangia asilimia 16.
Tatu, mazingira ya barabara yaani ubovu, ufinyu na usanifu mbaya wa barabara zetu unachangia asilimia saba tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa, suala la msongamano wa magari ambao linahusiana zaidi na mazingira ya barabara linachangia kiasi kidogo cha ajali ikilinganishwa na sababu zingine nilizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajali nchini ni tatizo ambalo kutokana na madhara yake kwa umma, Serikali itaendelea kukabiliana nalo kwa nguvu zote. Kwa kuzingatia hali hii, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani likishirikiana na wadau wengine wa usalama barabarani limechukua hatua zifuatazo:-
(1) Kusimamia kwa karibu mifumo ya sheria ukiwemo utaratibu mpya wa malipo ya papo kwa papo (notification) kwa njia ya kielektroniki ulioanzishwa hivi karibuni katika Jiji la Dar es Salaam na baadaye kutumika kwa nchi nzima.
(2) Kunyang‟anya leseni za madereva wazembe wanaorudia kutenda makosa ya usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani pindi wanaposababisha ajali.
(3) Kuwafukuza au kuwabadilisha kazi Askari wa Usalama Barabarani wanaotuhumiwa kujihusisha katika vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikichochea ongezeko la ajali barabarani.
(4) Kutoa elimu na namba za simu za viongozi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa wananchi ili wafahamu haki zao wanapokuwa abiria au watumiaji wa barabara na kutoa taarifa wanapotendewa isivyo halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwaagiza madereva na watumiaji wengine wa barabara kote nchini kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani na kutoa taarifa za dereva, askari au mtu yoyote anayekiuka sheria za barabarani au taratibu za kazi kwa makusudi ili hatua stahiki zichukuliwe.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Pamoja na kwamba polisi ni walinzi wa raia na mali zao, ila wanakabiliwa na changamoto za nyumba za kuishi, maslahi duni na ukosefu wa vitendea kazi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vitendea kazi kama magari na mafuta?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za askari polisi na kuboresha mishahara yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Destery, Mbunge wa Magu lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiboresha hali ya vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi ikiwemo vyombo vya usafiri, mawasiliano na zana nyingine za kazi. Mathalani kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ililipatia Jeshi la Polisi jumla ya magari 387 kati ya magari 777 yanayotarajiwa kununuliwa. Aidha, Serikali inatarajia kuongeza fedha ya mafuta na vilainishi katika bajeti ya mwaka wa fedha ya 2016/2017. Ni kweli kuwa Jeshi la Polisi, linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi ya Askari. Kupitia Mpango Shirikishi wa wadau mbalimbali na mikopo yenye riba nafuu, Serikali inakusudia kujenga nyumba jumla yake ni kama 4,136 katika mikoa 15 pamoja na Mikoa mitano ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la makazi kwa askari. Serikali inaandaa mpango mkakati wa kujenga nyumba zaidi ya 35,000 kufikia mwaka 2025, ikiwa ni wastani wa takriban nyumba 3,500 wa kila mwaka.
Aidha, Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kutatua changamoto za makazi ya askari kwa kudhamini mikopo nafuu kutoka Taasisi ya kifedha na kuchangia ujenzi wa nyumba pale bajeti inaporuhusu. Kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Umma, Serikali imekuwa ikiongeza viwango vya mishahara, kwa Askari wa Jeshi la Polisi kila mwaka.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni kilichoko Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni bado haujakamilika. Hadi sasa kazi ya ujenzi wa kituo hicho imefikia asilimia 80 ikihusisha ujenzi wa jengo lenyewe, kupauwa na kupigia plasta kuta zote. Kazi kubwa iliyobaki ni kufunga milango, madirisha, kuweka sakafu, kupiga rangi na kununua furniture. Serikali inakusudia kumalizia ujenzi wa kituo hicho ndani ya mwaka wa fedha 2016/2017 kulingana na upatikanaji wa fedha za bajeti.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Yamekuwepo malalamiko mengi ya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu wa kupiga watu, kuwatesa, kuchoma mali na kutishia amani katika Kisiwa cha Unguja Wilaya za Magharibi na Mjini na kwamba wahusika wamekuwa hawajulikani:-
(a) Je, ni kwanini hali hiyo imeachwa kuendelea kwa muda mrefu?
(b) Je, ni kwa nini Jeshi la Polisi limeshindwa kuwakamata wahusika?
(c) Je, wananchi hao wategemee lini vitendo hivyo kutoweka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwepo na ongezeko la matukio saba ya uhalifu katika Wilaya ya Magharibi na Mjini kwa mwaka 2015 ambapo jumla ya matukio 139 yaliripotiwa katika Vituo vya Polisi ikilinganishwa matukio 132 ya mwaka 2014. Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa ongezeko hilo takwimu zinaonesha kuwa vitendo hivyo vya makosa ya jinai kwa ujumla Visiwani Zanzibar vinapungua kwa kasi ya kuridhisha. Mathalani, kwa mwaka 2015 jumla ya makosa 1,673 ya jinai yaliripotiwa katika Kituo cha Polisi, ikilinganishwa na makosa 3,227 yaliyoripotiwa mwaka 2014. Hii ni pungufu ya makosa 1,554, sawa na wastani wa asilimia 51.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo vya uhalifu Zanzibar havijafumbiwa macho hata kidogo kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, kwani kutokana na takwimu zilizoainishwa awali, ni dhahiri kuwa uhalifu Zanzibar sio tu wa kutisha na unaendelea kudhibitiwa. Jeshi la Polisi linao wataalam wa kupambana na wahalifu wa aina mbalimbali na litaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote wanaovunja sheria.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Kwa muda mrefu walemavu wa ngozi (albino) wamekuwa wakiishi kwa hofu katika nchi yao kutokana na kuuawa na kukatwa viungo vyao kwa imani za kishirikina ikiwemo kwa ajili ya kushinda uchaguzi au kujipatia mali:-
Je, Serikali ina mpango wa kuwalinda na kuwahakikishia usalama wa maisha yao watu hao wenye ulemavu wa ngozi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyowahi kujibiwa katika swali la msingi namba 99 na swali namba 60 katika mikutano tofauti ya Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usalama wa ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, Serikali kupitia Jeshi la Polisi na wadau wengine imekuwa ikichukua hatua za maksudi kukomesha mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kuwasaka na kuwakamata watuhumiwa pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya pia juhudi za kuanzisha vituo vya kuwahudumia watu wenye ulemavu wa ngozi ambavyo vimesaidia kuimarisha ulinzi. Pia Jeshi la Polisi kwa kutumia falsafa ya Polisi Jamii inatoa elimu kwa umma juu ya madhara ya vitendo vya ukatili na mauaji na kujerui yanayofanywa na baadhi ya watu kwa msukumo wa imani potofu ya ushirikina. Aidha, Jeshi la Polisi limekuwa likifanya operesheni maalum za mara kwa mara zikiwamo za kukamata waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi ambazo ni kichocheo kikubwa cha ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Jeshi la Polisi ikishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama za Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa imeanzisha vikosi kazi hususan kwenye Mikoa na Wilaya zilizojitokeza kukithiri kwa matukio haya ili kuratibu na kusimamia kwa karibu ulinzi wa ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi. Vikosikazi hivyo hufanya kazi kwa kukusanya taarifa za kiintelejensia na kuzifanyia kazi.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR aliulliza:-
Bunge la Jamhuri ya Muungano hupitisha Bajeti ya Serikali kwa kila Wizara kwa mwaka ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani:-
(a) Je, inakuwaje Wilaya yenye vituo saba vya polisi ina gari moja tu na inapatiwa lita tano hadi saba tu za mafuta kwa siku?
(b) Je, Serikali iko tayari kuziongezea mafuta na magari Wilaya za Magharibi A na B zenye vituo vya polisi vya Fumba, Mbweni, Mazizini, Mwanakwerekwe, Kijitoupele, Fuoni, Airport na Mfenesini ambazo ni gari moja tu kila Wilaya ili kukongeza ufanisi na kuendana na kasi ya hapa kazi tu hasa ukizingatia kuwa Zanzibar inajiandaa na marudio ya Uchaguzi Mkuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Wilaya ya Magharibi A na B hazina magari na mafuta ya kutosha kwa shughuli za polisi. Hali hii ni changamoto kwa vituo vingi vya polisi hapa nchini, hata hivyo, mgawo wa vitendea kazi yakiwemo magari huzingatia jiografia ya Wilaya. Hali ya uhalifu na idadi ya watu wanaohudumiwa na kituo husika na siyo idadi ya vituo vidogo vya Polisi vilivyopo katika Wilaya husika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inakusudia kuwasilisha bajeti mbele ya Bunge lako Tukufu ili kuboresha hali ya vyombo vya usafiri, mafuta na vilainishi ili kukidhi mahitaji halisi ya Jeshi la Polisi hapa nchini, vikiwemo Vituo vya Polisi alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD aliuliza:-
Kituo cha Polisi Maruhubi kinakabiliwa na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa askari wa kutosha; kituo hakitoi huduma saa 24, lakini pia majengo yake ni machakavu sana kiasi kwamba hayana hadhi ya kuwa Kituo cha Polisi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari wa kutosha katika kituo hicho na kuhakikisha kuwa kituo kinatoa huduma zake kwa saa 24?
(b) Je, ni lini Serikali itayakarabati majengo ya kituo hicho ili yaendane na hadhi ya Kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Maruhubi ni Kituo cha Daraja “C” ambacho taratibu za utoaji huduma kwa mujibu wa miongozo ya Jeshi la Polisi kitatoa huduma kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni na kuwa na askari wasiozidi 20.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha Maruhubi mara tu fedha zitakapopatikana.
MHE. JOHN P. KADUTU (k.n.y. MHE. RICHARD P. MBOGO) aliuliza:-
Mwaka 2009 Serikali iliwapa uraia wakimbizi toka Burundi walioingia nchini mwaka 1992 na wengine waliozaliana katika makambi ya wakimbizi ya Katumba, Mushamo na Ulyankulu:-
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kuwapa wakimbizi waliosalia?
(b) Ili kuondoa hali ya sintofahamu katika Sheria ya Wakimbizi Na. 20 inayokataza mikusanyiko zaidi ya watu watano, je, ni lini Serikali itafuta hadhi ya makambi ya wakimbizi katika maeneo ya Katumba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, napenda kurekebisha swali hilo kwamba ni kweli mwaka 2009 Serikali iliwapa uraia wakimbizi toka Burundi walioingia nchini mwaka 1972 na siyo mwaka 1992. Pia hakuna Sheria ya Wakimbizi Na. 20 bali ipo Sheria ya Wakimbizi Na. 9 ya mwaka 1998. Vilevile maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge ni makazi ya wakimbizi na siyo makambi ya wakimbizi na hakuna mkimbizi aliyepo kambini aliyepewa uraia.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Wakimbizi (UNHCR) ipo katika hatua za mwisho kufanya uhakiki kamili kwa wakimbizi walengwa ili kutoa uraia kwa wanaostahili, kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi. Tunategemea hadi kufikia mwisho wa mwaka huu kazi hii itakuwa imekamilika ili taratibu za kutoa uraia kwa mujibu wa sheria ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 20 cha Sheria ya Wakimbizi Na. 9 ya mwaka 1998 kinahusu wakimbizi na hasa kililengwa kwa wakimbizi waliopo makambini katika makazi ya Katumba, Ulyankulu na Mishamo. Wengi wa wakazi wake sasa ni raia, sio wakimbizi. Kwa hiyo, kifungu hicho hakiwahusu kwa kuwa sasa wakazi wengi wa Katumba, Ulyankulu na Mishamo wameshapewa uraia. Wizara yangu kwa kushirikiana na TAMISEMI inaandaa utaratibu wa kufuta utengefu wa maeneo haya ili viwe vijiji vya kawaida kwa mujibu wa sheria.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru mauaji ya vikongwe nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeweka mikakati mbalimbali ya kunusuru mauaji ya vikongwe nchini ikiwa ni pamoja na:-
(i) Kufanya operesheni na misako ya mara kwa mara kubaini waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi na wasiofuata sheria;
(ii) Kutoa elimu kupitia Polisi Jamii, wadau mbalimbali wa ulinzi na usalama, madhehebu ya dini na mashirika na taasisi binafsi, lengo likiwa ni kuwaelimisha wananchi madhara ya kujichukulia sheria mkononi; na
(iii) Kuanzishwa kwa vikosi kazi ili kuweza kufuatilia na kutafuta taarifa mbalimbali za watuhumiwa wanaotenda matukio hayo maarufu kama wakata mapanga, kabla na baada ya kufanyika kwa tukio.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kwenye Bunge lako Tukufu kutoa rai kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vinavyosababisha mauaji kwa nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. ALLY K. MOHAMED aliuliza:-
Kituo cha Polisi cha Marine Kipili, hakina usafiri wa nchi kavu:-
(a) Je, ni lini Serikali itakisaidia kitu hicho usafiri wa nchi kavu angalau hata kukipatia pikipiki?
(b) Je, ni lini Serikali itaongeza mgao wa petroli?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally KeissyMohamed, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Karibuni Serikali imegawa vyombo vya usafiri takribani kwa Wilaya zote, ikiwemo Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Kipili kimo ndani ya Wilaya ya Nkasi kikihudumiwa na gari Namba PT 3836 ambayo ni jipya lililotolewa hivi karibuni. Hata hivyo, utaratibu utafanyika ili wapewe pikipiki iweze kusaidia kupunguza tatizo la usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaongeza mgawo wa mafuta kulingana na hali ya uchumi itakavyoimarika.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kuwadhibiti wakimbizi hasa maaskari ambao hutoroka kambini Nduta na kwenda kujumuika na wananchi, hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika, nchi yetu imekuwa ikipokea wakimbizi kwa miaka mingi na kuwahifadhi katika Kambi na Makazi. Kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi Na. 9 ya mwaka 1998 kifungu cha 16 na 17 kinaelekeza kuwa wakimbizi wote wanaishi katika maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili yao na hawaruhusiwi kutoka bila kibali maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kudhibiti wakimbizi hasa maaskari kutoka nje ya kambi, Serikali imejiwekea mikakati ya makusudi ikiwemo kuwagundua wakimbizi/askari kwa kuwafanyia usaili wa awali na wale watakaobainika hupelekwa katika Kituo cha Utenganisho cha Mwisa kilichopo mkoani Kagera ambako huwekwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Serikali kujiridhisha na mienendo yao, hutakiwa kukana uaskari na kuomba hifadhi upya kwa masharti ya kutokujihusisha na harakati zozote za kisiasa na kijeshi zilizopo nchini. Hata hivyo Ofisi za Wakuu wa Kambi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi hukusanya taarifa za kiintelejensia na kufanya doria na misako mara kwa mara kambini na nje ya kambi ili kubaini wakimbizi watoro na wanapobainika hushtakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Baadhi ya Kambi za Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) zina majengo chakavu sana ikiwemo Kambi ya Nyuki Zanzibar:-
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Kambi hizi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kambi za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania zina majengo chakavu ikiwemo Kambi ya Nyuki, Zanzibar. Hali hii imetokana na ukweli kwamba, Kambi nyingi za Jeshi zilirithi majengo yaliyokuwa yanatumiwa na Taasisi nyingine. Hata hivyo, Jeshi lina utaratibu wa kufanyia matengenezo majengo yake mara kwa mara kwa kadri ya upatikanaji wa fedha za bajeti za maendeleo.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Je, Serikali imefanikiwa kwa kiasi gani kuimarisha majengo na vituo vya Polisi sanjari na kulipa madeni ya Wakandarasi waliojenga majengo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu na uhaba wa majengo ya ofisi za Polisi pamoja na nyumba za makazi kwa Askari. Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kukarabati ofisi na vituo vya Polisi na kujenga nyumba za kuishi Askari. Mathalani, mwaka 2012 Serikali ilijenga maghorofa 15, katika maeneo ya Buyekela Mkoa wa Kagera, matatu yenye uwezo wa kuchukua familia 12. Mkoa wa Mwanza Mabatini sita yenye uwezo wa uchukua familia 24 na Mkoa wa Mara Musoma sita yenye uwezo wa kuchukua familia 24.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiwalipa Wakandarasi wa miradi ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Askari kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha za maendeleo. Mathalani katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya maendeleo.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Katika Jimbo la Tumbatu kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa amani kwa wananchi wanaoishi katika kisiwa hicho na katika hali ya namna hiyo inaporipotiwa kwa Jeshi la Polisi inakuwa tabu kwenda kwa haraka kwenye eneo husika kwa sababu kadhaa ikiwemo ya ukosefu wa usafiri:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Kituo cha Polisi katika kisiwa hicho na kuwapatia usafiri wa uhakika kwa kuzingatia jiografia ya maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo matukio ya kihalifu yanayoripotiwa kutokea katika Kisiwa cha Tumbatu. Jeshi la Polisi linafanya jitihada za kukabiliana na uhalifu kwa kutoa huduma za ulinzi na usalama katika maeneo ya Kisiwa cha Tumbatu kwa kila siku kuwapeleka Askari wa doria ili kuimarisha ulinzi. Kwa sasa lipo boti lenye uwezo wa kubeba Askari 10, iwapo uwezo wa kifedha ukiongezeka hitaji letu ni kupata boti kubwa la mwendo kasi lenye uwezo wa kubeba Askari zaidi ya 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona haja ya kuwepo Kituo cha Polisi katika eneo hilo, ili kusogeza huduma za ulinzi na usalama na hali halisi ya kisiwa hicho kilichozungukwa na bahari na uwepo wa matukio ya uhalifu. Katika kutekeleza hilo tayari Serikali imepata kiwanja na makisio ya ujenzi wa kituo hicho yanaendelea. Aidha, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu inapenda kuhamasisha wadau werevu na wananchi, akiwemo Mheshimiwa Mbunge, kutoa msaada wa hali na mali katika ujenzi wa kituo hiki.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR (K.n.y MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOSS NYIMBO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka uzio kwenye vituo vikubwa vya Polisi vilivyopo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Galloss, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango wa kujenga uzio katika Vituo na Makambi yote ya Polisi Tanzania. Aidha, Jeshi la Polisi kwa kutumia rasilimali zilizopo eneo husika, limekuwa likijenga uzio wa muda au wa kudumu katika maeneo mbalimbali na litaendelea kujenga uzio katika vituo zaidi hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar, Serikali imeanza kujenga uzio kwa baadhi ya maeneo ya Kambi ya Ziwani Zanzibar, mathalani eneo la Chuo Ujenzi umeanza kwa kutumia fedha zilizotokana na mapato ya ndani. Aidha, kwa upande wa mbele ujenzi unafanyika sambamba na kujenga maduka ambayo yatasaidia kuendesha shughuli za Polisi na kujiingizia mapato.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Makazi ya askari yamekuwa ya zamani pia mengine yamekuwa mabovu sana, mfano nyumba za Ziwani Zanzibar, Wete, Pemba na Chakechake Pemba hazikaliki kabisa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifanyia marekebisho nyumba hizo?
(b) Je, ni gharama gani Serikali itatumia kwa marekebisho ya nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo lenye sehemu (a), na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nyumba nyingi za makazi ya askari hazijafanyiwa ukarabati zikiwemo za Ziwani Zanzibar, Wete na Chakechake. Serikali ina mpango wa kuzifanyia marekebisho nyumba zote za polisi Unguja na Pemba kwa kadri uwezo wa fedha utakavyoongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi za ukarabati wa nyumba zote za polisi Unguja na Pemba ni bilioni 1.5.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza:-
Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la makazi kwa askari wa Jeshi la Polisi na Mheshimiwa Rais aligusia azma hiyo alipokuwa akilihutubia Bunge hili la Kumi na Moja kwenye kikao cha ufunguzi.
Je, Serikali imepanga kujenga mikoa mingapi majengo hayo ikiwemo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang‟ombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na uhaba wa nyumba za Jeshi la Polisi. Kwa kutumia mifuko ya Hifadhi ya Jamii, chini ya mpango wa mikopo wenye riba nafuu Serikali imeshajenga nyumba 360 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inakusudia kujenga nyumba nyingine 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba za askari kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiimarika.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu utakwenda sambamba na Mipango ya Maendeleo ya Serikali ukilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaotarajiriwa kuajiriwa baadaye.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR (K.n.y. MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN) aliuliza:-
Suala la raia kupigwa na kuharibiwa mali zao kwa upande wa Zanzibar limekuwa likiongezeka siku hadi siku;
Je, Serikali inatambua tatizo hili na kama inatambua inachukua hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba kila inapofika wakati wa Uchaguzi Mkuu hasa katika kisiwa cha Pemba baadhi ya watu hujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wengine na kuharibu mali zao. Aidha, Serikali itaendelea kuongeza vikosi vya ulinzi na usalama katika maeneo yote tete na kuhakikisha utii wa sheria bila shuruti unazingatiwa. Pia Serikali itaendelea kuelimisha wananchi madhara ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya wengine wasio na hatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nitoe wito kwa wananchi wote kuacha mihemko na itikadi za kisiasa wakati na kabla ya uchaguzi kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kumaliza ujenzi wa nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilizoanza kujengwa tangu mwaka 2012 na sasa zinazidi kuwa magofu ili zisaidie hizo familia chache zipatazo 13?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilianza kujengwa mwaka 2012. Kutokana na ufinyu wa bajeti nyumba hizo hazikuweza kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga fedha katika mwaka wa Fedha 2016/2017 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA (K.n.y MHE. MARWA R. CHACHA) aliuliza:-
Kumekuwepo na vifo vyenye utata wa kisiasa lakini inapotokea mpinzani kupoteza maisha havipewi kipaumbele katika upelelezi na hatua zinazochukuliwa:-
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi Tanzania inathamini maisha ya raia wake wote bila kujali rangi, kabila, itikadi za kidini na itikadi za kichama. Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo ambapo katika utekelezaji wa majukumu yake hatua mbalimbali huchukuliwa ili kuhakikisha haki inatendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua stahiki za kisheria kwa kila aina ya mauaji yanayotokea kwa raia na endepo mazingira ya mauaji yatakuwa yanalihusu Jeshi la Polisi basi Tume huru huundwa ili kuchunguza na kutoa ushauri kwa mamlaka husika na hatua stahiki huchukuliwa dhidi ya wahusika hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwalinda wananchi wake pamoja na mali zao bila upendeleo wowote.
MHE. ANTONY C. KOMU (K.n.y. MHE. HAWA S. MWAIFUNGA) aliuliza:-
Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili ya utumishi ndani ya Jeshi la Polisi kutokana na hilo Askari wengi wanaonekana kukosa weledi kwa kujihusisha na matendo yanayokinzana na maadili ya utumishi wa umma:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa Askari wasio na sifa wanachukuliwa hatua?
(b) Je, zoezi la kuhakiki vyeti vya Askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi limefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi lina utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria askari wachache ambao wanachafua taswira na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu pamoja na kujihusisha na vitendo vinavyokinzana na maadili ya utumishi wa umma. Aidha, tumeamua kusitisha kwa muda ajira zote kwenye vyombo vyote vilivyomo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwemo Jeshi la Polisi na kupitia utaratibu wa kutoa ajira ili kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza na kupata ajira ndani ya vyombo vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la uhakiki wa vyeti vya askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi linaendelea. Mpaka sasa jumla ya askari 19 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Wilaya ya Liwale ilipandishwa hadhi kuwa Wilaya kamili tangu mwaka 1975, lakini ni Wilaya ya pekee ambayo haina Kituo cha Polisi wala nyumba za watumishi wa kada hiyo:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga jengo la kituo cha Polisi Wilaya ya Liwale sambamba na nyumba za watumishi ambao wanaishi uraiani kwa sasa?
(b) Je, ni lini Tarafa ya Kibutuka itapata kituo kidogo cha Polisi ili kulinda wafanyabiashara wa mazao ya ufuta wanaokuja Tarafani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba Wilaya ya Liwale ndiyo Wilaya pekee nchini ambayo haina Kituo cha Polisi na nyumba za watumishi. Liwale ni miongoni mwa Wilaya 65 nchini ambazo bado hazijajengewa vituo vya Polisi.
Hata hivyo, Serikali itajitahidi kujenga vituo vya Polisi awamu kwa awamu kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.
(b) Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma za Polisi kwa wananchi ni azma ya Serikali kujenga Kituo cha Polisi kila Tarafa, sanjari na kupeleka Wakaguzi wa Polisi kuongoza vituo hivi, hata hivyo, Kata nne ikiwemo Kibutuka, Mirui, Kiangala na Nangano za Tarafa ya Kibutuka, kuna Askari Kata ambao wanatoa huduma kwa wananchi. Aidha, katika kutekeleza azma hii tayari Jeshi la Polisi limeshapeleka Wakaguzi katika baadhi ya Tarafa. Tunaomba Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira kwani hali ya fedha itakaporuhusu mpango huu utafika kila Tarafa ikiwemo Kibutuka.
MHE. PASCAL Y. HAONGA (K.n.y. MHE. FRANK G. MWAKAJOKA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya Zimamoto katika Mpaka wa Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya moto inapotokea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma lina kituo katika eneo la Mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Momba katika Mkoa wa Songwe kinachohudumia Wilaya zote ukiwemo mpaka wa Tunduma. Kwa sasa kituo hiki kina gari moja lililopo matengenezoni Mjini Mbeya. Hata hivyo, Askari wanaendelea kutoa Elimu ya Kinga na Tahadhari ya Majanga ya Moto na Utumiaji wa Vifaa kwa Huduma za Kwanza, sambamba na ukaguzi wa majengo na kutoa ushauri kwa wakandarasi na makampuni ya ujenzi kuhusu ujenzi bora wa miundombinu yenye usalama kwa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya zimamoto katika maeneo yote nchini ikiwemo Tunduma. Hata hivyo azma hii nzuri inategemea sana upatikanaji wa rasilimali fedha. Serikali itaendelea kusogeza huduma za zimamoto na uokoaji katika maeneo mbalimbali nchini karibu na wananchi kadri hali ya upatikanaji fedha itakavyoruhusu.
MHE.FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Magari yanayobeba abiria nchini yamekuwa yakitozwa faini pindi yanapokamatwa kwa kosa la kujaza abiria zaidi ya uwezo wake badala ya kutakiwa kupunguza abiria waliozidi.
(a) Je, Serikali haioni kuwa kutoza faini na kuacha gari liendelee na safari huku likiwa limejaza ni sawa na kuhalalisha kosa?
(b) Je, Serikali haioni kuwa ikiwashusha abira waliozidi itakuwa imetoa fundisho na kupunguza ajali kwa abiria ambao hupanda gari huku wakijua limejaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabani Sura ya 168, kifungu cha 58 ni kosa kwa abiria au mtu yeyote kutokuwa na kiti cha kukaa ndani ya gari la abiria na hivyo mtu huyo atahesabika kwamba amening‟inia ndani ya gari hilo. Mabasi yanatozwa faini kwa kuzidisha abiria yakiwa kituoni na maeneo salama abiria wote waliozidi huteremshwa na kurudishiwa nauli zao na utaratibu wa kuwatafutia mabasi mengine ambayo yana nafasi. Aidha, pale ambapo mabasi haya yalizidisha abiria yakikamatwa katika maeneo ambayo si salama huachwa na kuendelea na safari kisha mawasiliano hufanyika katika vituo vya polisi vilivyopo mbele ili abiria washushwe kwenye maeneo ambayo ni salama kwa abiria.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani imekuwa ikiwashusha abiria waliozidi ndani ya basi hasa pale inapokuwa imeonekana maeneo wanayoshushwa ni salama kwa maisha na mali za abiria hao na kutafutiwa usafiri mwingine.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. DEVOTHA M. MINJA) aliuliza:-
Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ukilinganisha na kazi zao wanazofanya kwa jamii.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaboreshea makazi.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yalivyowahi kujibiwa maswali kama haya ndani ya Bunge lako Tukufu mara kadhaa kuhusu Askari kuboreshewa makazi yao, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya Askari wa Jeshi la Magereza na Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea na mpango wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba kwenye baadhi ya magereza na kujenga nyumba mpya. Mahitaji ya nyumba hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni 4,221 hivyo kuwepo kwa upungufu wa takribani nyumba 10,279 ambao unalazimisha baadhi ya Askari wa Magereza kuishi nje ya kambi za jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limesaini mkataba na kampuni ya Poly Technologies ya China kwa kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya magereza nchini. Mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo ni Makao Makuu Magereza nyumba 472, Mkoa wa Arusha nyumba 377, Dar es salaam 952, Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo cha KPF 27, Bohari Kuu 82 na Bwawani 84.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika Mikoa 17; hii Mikoa 17 tunayozungumzia, tafsiri yake ni kwamba Mikoa 15 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar, wameichukulia Unguja na Pemba kama Mkoa kitu ambacho siyo sahihi. Kwa hiyo usahihi wake ni kwamba Mikoa 15 ya Tanzania Bara na Mikoa 5 ya Zanzibar inafanya kuwa Mikoa 19 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimeona nifanye marekebisho kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukizungumza hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, miradi shirikishi na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakapokuwa ikiimarika. Mkakati huu unakwenda sambamba na mipango ya maendeleo ya Serikali ikilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaoajiriwa baadaye.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Kwa miaka ya hivi karibuni vifo vya Watanzania kutokana na ajali za barabarani vimekuwa vingi na kuleta hisia kwamba hali hii sasa ni janga la Kitaifa, ni muhimu Watanzania wakafahamu kwa takwimu kuhusu ukubwa wa tatizo la vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani badala ya kusikia taarifa ya tukio moja moja:-
(a) Je, takwimu ni zipi na mchanganuo wa matukio kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 Kitaifa na Mikoa miwili inayoongoza na yenye ajali chache?
(b) Je, mfumo gani endelevu kama upo, wa wazi ambao Serikali inatumia kutoa takwimu hizi kwa Watanzania badala ya taarifa moja moja pindi inapotokea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842 zilizosababisha vifo karibu 4,002 na majeruhi 20,689. Mwaka 2014 kulitokea ajali 14,260 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015 zilitokea ajali 8,337 zilizosababisha vifo 3,464 na majeruhi 9,383.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa ambayo imeongoza kwa ajali kwa mwaka 2013 ni Mikoa ya Kipolisi ya Kinondoni, ambao ulikuwa na ajali 6,589 na Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ambao ulikuwa na ajali 3,464 na mkoa ambao ulikuwa na ajali chache ilikuwa ni Simiyu ambao ulikuwa na ajali 67 na Tanga ajali 96. Mwaka 2014 mikoa iliyoongoza kwa ajali ni Mikoa ya Kipolisi Kinondoni ambapo ajali zilikuwa ni 3,086 na Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ulifuata kwa kuwa na ajali 2,516. Mikoa ambayo ilikuwa na ajali chache kwa mwaka huo ilikuwa ni Kagera ambayo ilikuwa na ajali 29 na Simiyu ajali 55. Mwaka 2015 Mkoa wa Kipolisi ya Ilala ajali 1,431 na Temeke ajali 1,420 ambayo ndiyo iliyokuwa inaongoza kwa mwaka huo. Mikoa ambayo ilikuwa na ajali chache kwa mwaka 2015 ni Mkoa wa Rukwa ambao ulikuwa na ajali 53 pamoja na Mkoa wa Arusha ambao ulikuwa na ajali 53.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo endelevu wa wazi uliopo wa kutoa takwimu za kupitia taarifa za mwaka za Jeshi la Polisi (Police Annual Reports) ambapo kila Mtanzania anaweza kupata taarifa hizo za ajali.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Ni muda mrefu sasa Kikosi cha Polisi Marine Pemba hakina boti ya doria hali inayopelekea polisi kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
(a) Je, Serikali inatambua hilo?
(b) Kama inalitambua, je, ni lini Serikali itakipatia Kikosi cha Polisi Marine Pemba boti za doria ili kuwawezesha polisi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inalitambua tatizo la Polisi Wanamaji Pemba kukosa boti ya doria. Serikali itawapatia Polisi Wanamaji Pemba boti pale uwezo wa kibajeti utakapoongezeka kwani boti zilizopo haziwezi kuhimili mkondo wa maji uliopo Nungwi kuelekea Pemba.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
(a) Je, ni lini askari wa Iringa watajengewa nyumba?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha wanachodai askari wa Mkoa wa Iringa posho na stahiki zao zingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la ukosefu wa nyumba za askari wa Jeshi la Polisi hapa nchini. Lengo la Serikali ni kujenga nyumba hizo kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi huo. Kwa nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa suala hili na pia amekuwa akijitoa sana katika kuboresha mazingira ya askari katika eneo lake.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua madai ya askari ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kama ilivyo kwa Mikoa mingine hapa nchini. Askari wa Mkoa wa Iringa wanaidai Serikali jumla ya shilingi 431,147,410 na uhakiki wake unaendelea chini ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ili Serikali iweze kulipa baada ya ukaguzi huo.
MHE. KHAMIS M. ALI aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa baadhi ya wakuu wa Vituo vya polisi hasa Zanzibar hutumia pesa ao za mishahara kulipa huduma za umeme katika vituo hivyo;
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwalipa au kuwarejeshea pesa wanazotumia kulipa umeme katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamisi Mtumwa Ali Mbunge wa Kiwengwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikirejesha fedha hizo za umeme endapo askari amelipia au amenunua umeme kwa ajili ya kituo cha polisi kwa kupitia utaratibu wa kujaza fomu za madai na kuambatisha risiti ya malipo hayo kisha kuziwasilisha kwa mhasibu kwa ajili ya malipo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Wizara yangu imekuwa ikijitahidi kupeleka fedha za kulipia umeme kwa wakati ili kuondoa usumbufu unaojitokeza kwa askari walioko vituoni na makambini kadri ya hali ya uwezo utakapokuwa unaruhusu.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma umekumbwa na wimbi kubwa la wakimbizi wa kutoka Burundi na Congo (DRC), kutokana na wimbi hilo ujambazi umeongezeka sana.
Je, Serikali iko tayari kuongeza ulinzi wa kutosha na vitendea kazi vya kutosha ili mamlaka husika iweze kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba suala la wakimbizi kuja nchini hutokea mara nchi jirani zinapokuwa katika hali tete ya usalama katika nchi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiongeza ulinzi pamoja na vitendea kazi ikiwemo magari na pikipiki kwa lengo la kudhibiti uhalifu unapojitokeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, hivi karibuni Mkoa wa Kigoma umepokea magari 11 na Serikali itaendelea kuongeza na kuimarisha ulinzi katika Mkoa wa Kigoma na mahali pengine popote nchini ambapo kutakuwa na tatizo kama hilo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Mgodi wa GGM – Geita unaongoza kwa kuwapiga vijana na kuwachapa viboko na pengine kuwasababishia vifo, lakini wahusika hawachukuliwi hatua stahiki.
Je, Serikali inachukua hatua gani sasa dhidi ya wahusika pale inapotokea wameua watu au kujeruhi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na vitendo vya uonevu na matukio kadhaa baina ya wamiliki wa Mgodi wa GGM na wananchi wanaozunguka mgodi huo. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua stahiki kwa watuhumiwa mara tu taarifa zinapotolewa polisi. Mathalani, tarehe 14/2/2016 majira ya saa 07.15 ndani ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita, watu wawili walijeruhiwa kwa kupigwa risasi za mpira wakiwa wanaondolewa na mlinzi ambapo mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi Na. CC67/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kwenye Bunge lako hili Tukufu kutoa rai kwa wananchi wanaozunguka mgodi wa Geita kuheshimu sheria na taratibu ili kuepuka vitendo vya kuvamia mgodi vinavyoweza kusababisha madhara kwao.
MHE. SOPHIA M. SIMBA aliuliza:-
Hali ya magereza nchini ni mbaya hivyo kufanya vigumu katika utoaji wa haki za kibinadamu licha ya kwamba nchi imekuwa ikijali sana utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kikanda na ya kimataifa katika utoaji wa haki hizo za wafungwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha hali hiyo katika magereza nchini?
(b) Je, Serikali imejenga magereza mapya mangapi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita?
NAIBU WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mathayo Simba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kuboresha hali ya magereza nchini kwa awamu kadri ya fedha zitakavyopatikana. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga fedha katika fungu la maendeleo na matumizi mengineyo kwa ajili ya ukarabati, upanuzi, ujenzi wa mabweni mapya, majengo ya utawala na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya malazi katika magereza nchini ili kuboresha huduma kwa mahabusu na wafungwa kukidhi vigezo vya haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita Serikali imejenga magereza mapya 11 kwa mchanganuo ufuatao:-
1. Gereza la Mkuza- 1996;
2. Gereza la Mbarali - 2003;
3. Gereza la Igunga - 2003;
4. Geeza la Meatu - 2003;
5. Gereza la Mgagao - 2004;
6. Gereza la Kinegele - 2005;
7. Gereza la Mbozi - 2005;
8. Gereza la Mbinga - 2007;
9. Gereza la Chato - 2008;
10. Gereza la Kiteto - 2009; na
11. Gereza la Karatu - 2010.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo magereza hayo pamoja na ujenzi kutokamilika yanaendelea kutumika isipokuwa Gereza la Chato na Gereza la Karatu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya kihalifu nchini yanayohusishwa pia na upatikanaji wa hati za kusafiria zaidi ya moja zinazotolewa hapa Tanzania kwa baadhi ya wahalifu kiholela:-
Je, Serikali inachukua hatua gani katika udhibiti wa utoaji hati za kusafiria kiholela?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji hutoa Pasipoti na Hati za Kusafiria kwa raia yeyote wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria Na. 2 ya mwaka 2002 ili mradi amekidhi matakwa ya sheria hiyo. Pasipoti na Hati za Kusafiria hazitolewi kiholela kwa wahalifu kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutolewa Pasipoti au Hati ya Kusafiria, Idara ya Uhamiaji hufanya uchunguzi wa kujiridhisha kama mwombaji ni raia wa Tanzania na kama hana makosa kihalifu. Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji huchukua hatua zifuatazo ili kudhibiti utoaji holela wa Pasipoti pamoja na Hati za Kusafiria:-
(i) Kuwasiliana na idara mbalimbali ili kujiridhisha nyaraka zilizoambatishwa kwenye ombi la Pasipoti au Hati za Kusafiria mfano RITA;
(ii) Kuchukua hatua za kisheria na za kinidhamu kwa watumishi wanaobainika kujihusisha katika utoaji wa Pasipoti au Hati za Kusafiria kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu;
(iii) Kuweka masharti katika utoaji wa Hati za Kusafiria kwa mwombaji aliyeibiwa au kupoteza Hati za Kusafiria;
(iv) Kuwachukulia hatua za kisheria waombaji wa Pasipoti wanaotumia njia za udanganyifu;
(v) Kutuma taarifa za Pasipoti zilizopotea au kuibiwa kwenye Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ili kuwakamata wahusika;
(vi) Kuimarisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu na takwimu za Watanzania walioomba na kupewa Pasipoti Makao Makuu ya Uhamiaji; na
(vii) Kuweka mfumo wa kielektroniki wa utoaji Pasipoti ili kuweza kutambua watu kwa usahihi na kuondokana na tatizo la kughushiwa kwa Pasipoti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Uhamiaji pia hufuta Pasipoti za watu ambao wamepatikana na hatia za makosa ya biashara ya madawa ya kulevya, utakatishaji fedha, usafirishaji haramu wa binadamu, vitendo vya kigaidi au hata shughuli yeyote haramu kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati ya Kusafiria Na. 20 ya mwaka 2002.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mradi wa REA II ulitarajia kuvipatia umeme vijiji vyote vya Jimbo la Busega na kumekuwepo na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo jimboni humo:-
(a) Je, mpaka sasa ni vijiji vingapi vimepatiwa umeme kupitia mradi huo?
(b) Je, ni lini vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya vijiji 13 vimepatiwa umeme katika Jimbo la Busega kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya II unaoendelea kutekelezwa hivi sasa. Mradi huu utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 ambapo vijiji vyote 18 vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme Wilaya ya Busega inayotekelezwa na Mkandarasi Sengerema Engineering Group inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 91.6; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 52; ufungaji wa transfoma 33 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 932.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi umekamilika kwa asilimia 94 ambapo ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 umekamilika kwa asilimia 97; ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 0.4 umekamilika kwa asilimia 93 na transfoma 18 zimefungwa. Wateja 420 wameunganishiwa umeme. Kazi hii itagharimu jumla ya shilingi bilioni 4.88.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo havikujumuishwa katika mradi kabambe wa REA Awamu ya II vitapatiwa umeme katika Mradi wa REA Awamu ya III utakaoanza mwezi Julai, 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo itajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 68; ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 198; na ufungaji wa transfoma 19 za ukubwa mbalimbali. Pamoja na kazi hizo pia wateja 6,096 wataunganishiwa umeme. Kazi hii itagharimu shilingi bilioni 8.6.
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Askari Polisi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kimara wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kwani kituo ni kidogo na maslahi yao yamekuwa duni:-
(a) Je, ni wapi na lini kituo kipya kitajengwa ili kuboresha huduma na usalama Jimboni Kibamba?
(b) Je, hatua gani zimechukuliwa kuboresha maslahi ya Askari hao ikiwa ni pamoja na kuwaongezea motisha?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kipolisi Kimara ilianzishwa kufuatia kuundwa kwa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam chini ya Mpango wa Maboresho ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2006 kwa lengo la kuboresha ufanisi na kuongeza huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi. Kutokana na uhaba wa rasilimali fedha, huduma za polisi zilianza kutolewa katika jengo la kituo kidogo cha Polisi Mbezi Luis.
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hilo halikidhi hadhi ya kuwa Kituo cha Polisi Wilaya na pia lipo kwenye hifadhi ya barabara kuu ya Morogoro. Serikali itajenga kituo kipya eneo la Luguruni muda wowote kuanzia sasa. Aidha, hali ya vitendea kazi imezidi kuboreshwa ambapo hivi karibuni Wilaya ya Kimara imepatiwa gari lingine lenye namba PT 3696 Toyota Land Cruiser kuimarisha ulinzi wa eneo hilo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha maslahi ya kuongeza motisha kwa askari wa Jeshi la Polisi, hivi karibuni Serikali imeongeza posho ya chakula, yaani Ration Allowance toka shilingi 180,000 hadi kufikia shilingi 300,000 kwa mwezi, kupandisha viwango vya mishahara sambamba na kuendelea kutoa huduma ya Bima ya Afya.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Wapo askari polisi kadhaa ambao wamestaafu kwa zaidi ya miaka 20 sasa na wametumikia nchi kwa uadilifu na uzalendo, lakini hawajalipwa stahili zao; Serikali kwa mara ya mwisho iliwasiliana nao kupitia barua CAB/336/394/01/70 ya tarehe 28 Julai, 2015:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali haijawajibu barua yao zaidi ya miezi sita?
(b) Je, ni kwa nini suala hili halimalizwi kwa miaka yote ili wahusika wapate haki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wizari ya Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, (a) siyo kweli kwamba wastaafu hawa hawajajibiwa kwa zaidi ya miezi sita, bali kumbukumbu zinaonyesha kuwa Jeshi la Polisi limeshawaandikia barua ya kuwajibu askari hao tangu tarehe 12/10/2015 yenye kumbukumbu namba PHQ/C.10/8A/VOL.9/90.
Mheshimiwa Naibu Spika, (b) suala hili halina utata wowote kwani wastaafu hawa hawana wanachodai Jeshi la Polisi kwani haki zao walishalipwa kulingana na mikataba yao, kwani walikuwa chini ya mkataba wa bakishishi (gratuity) ambao ulikuwa ni uchaguzi wao.
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Wilaya ya Uyui ni Wilaya mpya ambayo makao yako Isikizya na Jeshi la Polisi tayari limehamia yaliko Makao Makuu ya Wilaya, lakini mazingira ya hapo kwa askari polisi ni magumu sana kwa sababu hakuna maji, hakuna nyumba za kuishi askari hao ambao kwa sasa wanaishi kwenye nyumba za kupanga au kwenye mabanda ya mabati yaliyojengwa karibu na kituo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira hayo kwa askari wetu ili wafanye kazi katika mazingira bora zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wizari ya Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vituo vya polisi, majengo ya utawala na nyumba za kuishi askari ni suala ambalo linahitaji fedha nyingi kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na upungufu mkubwa kwenye Vituo vya Polisi Daraja la A na B ni vituo ambavyo vinatakiwa kujengwa katika Mikoa na Wilaya za Kipolisi na Miji inayokuwa. Vituo vya Daraja A vinavyotakiwa kujengwa nchi nzima ni 94 kwa wastani wa shilingi bilioni 94, Vituo vya Daraja B vinahitajika 382 kwa gharama ya shilingi bilioni 191 na Vituo Daraja C 4,043 kwa gharama ya shilingi bilioni 950.
Mheshimiwa Naibu Spika, majengo yanayotakiwa na Makamanda ni 15 wastani wa shilingi bilioni 15, nyumba za kuishi Askari ni zaidi ya 35,000 wastani wa shilingi trilioni mbili nukta nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kufanya yafuatayo, ili kukabiliana na tatizo hili la miundombinu ya Jeshi la Polisi:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba za kuishi askari Serikali ina mpango wa kujenga nyumba 3,500 kila mwaka kwa nchi nzima. Serikali kwa Awamu hii ya Tano ina mpango wa kujenga nyumba 4,136 za mkopo kutoka Serikali ya China na tayari mpango huo upo Wizara ya Fedha, mkopo utakaogharimu dola za Kimarekani zinazokisiwa kuwa milioni 500.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Vituo vya Polisi Daraja A, B na C na majengo ya makamanda, Serikali itaendelea kujenga vituo hivi kulingana na uwezo na upatikanaji wa fedha.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kuwasiliana na Serikali za Mitaa, ili pale inapoanzishwa Wilaya au Mikoa mipya kuwepo na huduma zinazohusiana na masuala ya ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya polisi na nyumba za kuishi askari.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Askari wa usalama barabarani ndio wenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, lakini kwa sasa askari hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha askari wa usalama barabarani wanakuwa waadilifu na hawajihusishi na vitendo vya rushwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mhehimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi limekuwa na mikakati ya kuhakikisha askari wa usalama barabarani hawapokei rushwa kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Kutoa elimu wa askari wote wakiwemo wa usalama barabarani juu ya madhara ya rushwa katika mabaraza, kwenye komandi na vikosi, ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa askari kabla ya kuingia kazini na baada ya askari kutoka kazini.
(ii) Kutoa namba za simu za viongozi wa polisi, viongozi wa mamlaka nyingine za ulinzi na usalama kwa umma.
(iii) Mfumo wa kutoa notification kwa kutumia mashine za kielektroniki ambayo nimoja wapo ya mkakati wa kukomesha rushwa barabarani.
(iv) Kusambaza mabango katika maeneo mbalimbali yanayopiga vita rushwa.
(v) Kuanzishwa kwa masanduku ya maoni ili kutoa malalamiko katika vituo vya polisi.
(vi) Kuwasimamia na kuwakagua mara kwa mara askari hawa katika maeneo yao ya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mikakati hiyo Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM) aliuliza:-
Kumekuwepo na ajali nyingi zinazosababisha vifo na majeruhi barabarani, baharini na kwenye maziwa.
Je, ni ajali ngapi zimetokea barabarani, baharini na kwenye maziwa kuanzia Januari, 2015 hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Kakunda Joseph, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha Januari, 2015 hadi Februari, 2016 jumla ya ajali zilizotokea ni 9,864 ambazo zimesababisha vifo 3,936 na majeruhi 9,868 katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kama hicho jumla ya ajali 15 za baharini na kwenye maziwa zilizotokea, ambapo tisa zilitokea baharini na sita zilitokea katika maziwa. Katika ajali hizo, jumla ya watu 24 walipoteza maisha na watano walijeruhiwa.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y. MHE. RHODA E. KUNCHELA) aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu katika eneo la Kata ya Misunkumilo, Wilaya ya Mpanda Mjini, Wanajeshi wanadai eneo hilo ni la Jeshi, lakini makazi ya wananchi yalitangulia na wana hati ya maeneo yao:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutatua jambo hili ikiwa Jeshi limewakuta wananchi katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu za kistratejia, JWTZ lilipewa eneo la Misunkumilo lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mwaka 1985 lenye ukubwa wa hekta 3195. Serikali ililipa fidia kwa wananchi waliokuwepo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1992 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilihamisha kombania yake kutoka katika eneo hilo ila eneo alikabidhiwa Mkuu wa Wilaya kwa uangalizi. Kutokana na sababu za kiusalama hasa ukanda wa Ziwa Tanganyika, imebidi Jeshi lirejee kwenye sehemu hiyo tena. Hata hivyo, sehemu ya eneo hili sasa limevamiwa na kupangiwa matumizi mengine na uongozi wa Manispaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 16 Novemba, 2015 kilifanyika kikao cha pamoja kati ya JWTZ na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi. Maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kulipima upya eneo hilo kwa kuzingatia maendeleo yaliyopo, lakini vile vile na mahitaji ya JWTZ.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi eneo hili litapungua kutoka ekari 3,195 za awali hadi 2,235. Zoezi la kupima upya litakuwa shirikishi na litatekelezwa mara fedha zitakapopatikana katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Jeshi la Polisi nchini linafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini linakabiliwa na upungufu mkubwa wa makazi kwa Askari wake:-
(a) Je, Serikali imepanga kujenga majengo mangapi katika Wilaya Mpya ya Itimila na Busega kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuyakamilisha makazi ya Askari Polisi yaliyomo Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka huu wa Fedha 2016/2017, Wilaya Mpya za Itilima na Busega hazikutengewa fedha za ujenzi. Hata hivyo, kwa kuwa Wilaya ya Itilima na Busega ni mpya hivyo kuwa na mahitaji makubwa. Katika mradi wa nyumba 4,136 unaotarajiwa kuanza punde taratibu za mkopo wa ujenzi wa nyumba hizi utakapokamilika kipaumbele ni kwa mikoa mipya ukiwemo Mkoa wa Simiyu wenye Wilaya za Itilima na Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kukamilisha miradi yote ya Makazi ya Askari nchi nzima ambayo ujenzi wake umesimama kutokana na
ukosefu wa fedha. Azma hii nzuri itategemea upatikanaji wa Fedha za Maendeleo katika Bajeti ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Wizara itaendelea na juhudi mbadala zikiwemo kuhamasisha Waheshimiwa Wabunge, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuchangia na kushiriki katika kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza tatizo kubwa la makazi ya Askari nchini pamoja na ofisi.
MHE.ALLY K. MOHAMED aliuliza:-
Vituo vya Polisi vya Kabwe na Kirando vimechakaa sana na hata polisi hawana nyumba za kuishi:-
Je, ni lini Serikali itajenga au kukarabati vituo hivyo na kuwajengea polisi nyumba za kuishi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Keissy, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kukarabati, kujenga makazi na vituo vya Polisi nchi nzima ikiwemo Kabwe na Kirando kwa awamu. Kwa upande wa makazi ya Askari Polisi awamu ya kwanza ya ujenzi itajumuisa nyumba 4,136. Kwa vituo ambavyo ni chakavu Serikali itaendelea kuvifanyia ukarabati kulingana na uwezo wa fedha kadri utakavyoruhusu.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za Askari Polisi katika Wilaya mpya ya Songwe, hasa ikizingatiwa kuwa Maaskari wengi wameripoti ndani ya Wilaya hii mpya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la makazi ya Askari Polisi katika Wilaya mpya ya Songwe na maeneo mengine nchini hususan kwenye mikoa mipya. Nia ya Serikali ni kutatua tatizo la upungufu wa makazi ya Askari Polisi kwa kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima. Mkoa wa Songwe ambao Wilaya ya Songwe inapatikana, ni sehemu ya mpango huo ambao utaanza kutekelezwa baada ya utaratibu wa mikopo kukamilika.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Kazi za Vikosi vya Ulinzi na Usalama ni kulinda raia, mali zao pamoja na mipaka ya nchi, lakini kuna baadhi yao wanakwenda kinyume na sheria kwa kuwapiga wananchi na kuwasababishia ulemavu au vifo:-
(a) Je, mpaka sasa Serikali imeshawachukulia hatua gani?
(b) Je, mpaka sasa ni askari wangapi wamekutwa na hatia na kufukuzwa kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi hufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Hata hivyo, kuna askari wachache ambao wamekuwa wakikiuka maadili na mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi kama ambavyo imeainishwa katika Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi, namba 103.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kinidhamu kwa watumishi wanaoonekana kwenda kinyume na maadili ya kazi za Jeshi la Polisi ikiwemo kuwapiga wananchi wasio na hatia. Mathalan, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2016 Juni, askari 200 walichukuliwa hatua za kinidhamu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya askari 152 walikutwa na hatia na kufukuzwa kazi.
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali kunyanyaswa na kupigwa na vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi na kusababisha matatizo makubwa ya kiafya kwa watuhumiwa:-
Je, Serikali inasema nini juu ya Polisi wanaofanya vitendo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twahir Awesu Mohammed, Mbunge wa Mkoani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa kunawezekana kukawa na malalamiko katika vituo vyetu vya Polisi kwa mujibu wa PGO Na.103 (1) inaelekeza kuwa japokuwa lalamiko ni dogo kiasi gani lazima Kamanda wa eneo afungue jalada na kuchunguza ukweli wa malalamiko hayo na ikibainika Askari aliyefanya kitendo hicho atachukuliwa hatua za kinidhamu dhidi yake kama vile kukatwa mshahara ama kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeweka mfumo madhubuti wa kushughulikia malalamiko hayo kwa Mikoa yote ya Polisi, Makao Makuu ya Polisi na kama haitoshi Wizarani kwangu kuna dawati la kushughulikia malalamiko.
Kwa nafasi hii, nitoe rai kwa wale wote ambao hawatendewi haki wafuate utaratibu huo na hatua zitachukuliwa kikamilifu. Pia, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kupitia mfumo wa mafunzo kazini, vilevile mafunzo ya vitendo ili kuhakikisha kuwa Askari wote wanafanya kazi zao kwa weledi na usasa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:-
Suala la usalama wa raia na mali zao ni moja ya dhamana ya Jeshi la Polisi nchini; ni muda sasa Zanzibar wananchi wamekuwa wakipigwa, kunyanyaswa na kunyang‟anywa mali zao kunakofanywa na vikosi vya SMZ.
Je, nini kauli ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusiana na matukio hayo huko Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa usalama wa raia na mali zao ndiyo dhamana kuu au kazi ya msingi ya Jeshi la Polisi nchini. Taarifa hizo hadi sasa hazijapata uthibitisho sahihi kutoka kwa wale ambao wanadai kutendewa vitendo hivyo, kwani hakuna taarifa yoyote iliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi Visiwani Zanzibar kuhusiana na uhalifu huo. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo ni kwamba mtu yeyote ambaye anafanyiwa kitendo chochote cha uhalifu anapaswa kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi, ili hatua za kiuchunguzi na kiupelelezi zifanyike ili kubaini wahalifu ambao wamehusika na hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bado inasisitiza kuwa haitambui uwepo wa vitendo hivyo na inatoa wito kwa wananchi wote ambao watafanyiwa au wamefanyiwa vitendo kama hivyo, watoe taarifa kwenye vituo vya polisi au kwa viongozi wa polisi waliopo Makao Makuu Zanzibar na Dar es Salaam ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya vitendo hivyo kwa watuhumiwa.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:-
Pamoja na Jimbo la Kigamboni ni Wilaya ya Kipolisi, majengo ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) na kituo chake ni chakavu sana:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha Wilaya hii inakuwa na ofisi nzuri za polisi?
(b) Je, hatua hizi zitaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kigamboni ni moja kati ya Wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam ambayo imeanzishwa mwaka 2006 chini ya mpango wa maboresho ya Jeshi la Polisi kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma za ulinzi na usalama karibu na wananchi. Kutokana na uhaba wa rasilimali fedha na majengo, huduma za kipolisi zilianza kutolewa katika jengo dogo la Kituo cha Polisi Kigamboni chenye hadhi ya Daraja la C.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inakusudia kujenga vituo vyote vya polisi kwenye Wilaya ambazo hazina majengo yenye hadhi stahiki ikiwemo Wilaya ya Kigamboni. Ujenzi wa kituo hicho utafanyika eneo la Kibada mara fedha zitakapopatikana.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI aliuliza:-
Kumekuwa na tabia za watu kupiga watu wengine hovyo kila siku, vipigo hivyo vinafikia kiasi cha utesaji (torture) kama ilivyotokea Mbeya Sekondari kwa walimu kumshambulia mwanafunzi au mtu kumtoa macho kama ilivyotokea huko Buguruni na maeneo mengine:-
(a) Je, Serikali inaona mateso haya wanayopata Watanzania kutoka kwa Watanzania wenzao?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwalinda wananchi na vitendo hivi vya kikatili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hivi karibuni kumekuwepo na vitendo vya kusikitisha katika nchi yetu na kwa jamii ambavyo ni kinyume cha sheria na havikubaliki. Aidha, Serikali haikubaliani na vitendo vya namna hii vinavyofanywa na mtu/watu/ kikundi kwani vitendo hivyo ni kinyume na sheria na utaratibu mzima wa haki za binadamu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuzuia na kuwalinda raia na mali zao. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Polisi hupokea taarifa za matukio mbalimbali na kuyafanyia uchunguzi wa kina na inapobainika upo ushahidi wa kutosha, mtuhumiwa huchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Nichukue fursa hii kuwaasa sana wale wote ambao wanakiuka taratibu, kanuni na sheria za nchi waache tabia hiyo mara moja. Wizara yangu haitakuwa na suluhu na mtu yeyote atakayetenda uhalifu huo.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Jeshi la Zimamoto Mkoani Njombe linakabiliwa na ukosefu wa Ofisi pamoja na vitendea kazi hususan magari jambo linalopelekea Jeshi hilo kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Je, ni lini Serikali italipatia Jeshi hilo ofisi za kudumu pamoja na magari ili liweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina uhaba mkubwa wa ofisi na vitendea kazi katika vituo vyote nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kuongeza bajeti kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji ili liweze kukabiliana na changamoto zilizopo zikiwemo uhaba wa vitendea kazi kama vile magari ya kuzimia moto, magari ya maokozi pamoja na kufanyia ukarabati ofisi zilizopo katika mikoa yote na kuliwezesha Jeshi la Zimamoto kuwa la kisasa ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nia hii njema ya Serikali itakuwa ikitekelezwa kwa mujibu wa upatikanaji mapato ya Serikali na bajeti itakayotengwa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kila mwaka.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Mkoa wa Kagera umezungukwa na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda na mipaka ya nchi hizo imekuwa adhabu kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, kwani hali ya usalama wa raia na mali zao umekuwa mashakani kutokana na kuvamiwa na majambazi toka nje ya Tanzania wakishirikiana na baadhi ya Watanzania wasio na uzalendo na Taifa lao.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo ili wananchi wa Mkoa wa Kagera waweze kuishi kwa amani na utulivu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yako matukio ya ujambazi katika mikoa ya pembezoni ikiwemo Kagera ambapo watu toka nchi jirani wanaingia na silaha kali za kivita na kufanya unyang‟anyi wa mali za wananchi. Hii inatoka na mkoa huu kupakana na nchi ambazo zimekosa amani na kuzalisha wahamiaji haramu kuingia nchini kwetu kwa njia za panya na tukizingatia kwamba mipaka yetu imezungukwa na mapori makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama inafanya mikakati ya kutekeleza yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya operesheni za pamoja katika mipaka yetu; vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu na nchi ya jirani vinafanya operasheni za pamoja na kubadilishana taarifa mbalimbali za uhalifu na wahalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vya ulinzi na usalama hufanya misako ya kushitukiza katika mapori yote yaliyoko Kagera, Kigoma na maeneo yote ya mipakani, kwani ndiyo maficho ya uhalifu; hufanya doria na polisi kusindikiza magari katika baadhi ya maeneo tete; Kamati za Ulinzi na Usalama za maeneo husika zinafanya vikao vya ujirani mwema ili kuwaelimisha wananchi juu ya kutoa taarifa kwenye Mamlaka za Serikali husika wanapoona wageni wasiofahamika wanaingia ama kutoka katika maeneo yao.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wilaya ya Maswa ni moja ya Wilaya kongwe hapa nchini, lakini haina kituo cha Polisi cha Wilaya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayo Wilaya 162 na kati ya hizo tumefanikiwa kujenga vituo vya Polisi katika Wilaya 97. Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya Polisi katika Wilaya 65 zilizosalia kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, tumepata jengo ambalo litafanywa kuwa kituo cha Polisi cha Wilaya wakati tukisubiri utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa vituo vya Polisi nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira hadi hapo hali ya fedha itakapokuwa nzuri tutakamilisha ujenzi wa vituo vya Polisi katika Wilaya zilizosalia Maswa ikiwa miongoni mwao.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia nyumba za makazi Askari Polisi na Magereza katika Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma?
(b) Je, Serikali imejipangaje kufanya ukarabati kwa nyumba za askari zilizopo Wilayani Tunduru ambazo kwa muda mrefu hazijafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za makazi, maafisa na askari, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mpango wa kujenga nyumba mpya kwenye baadhi ya magereza nchini kwa kutumia fedha zinazotengwa katika fungu la bajeti ya maendeleo kila mwaka. Kwa kutambua uhaba na uchakavu wa nyumba za Askari Polisi na Magereza, Serikali ina mpango wa kuwajengea askari nyumba 9,500 nchi nzima ikiwemo kwenye Gereza la Wilaya ya Tunduru pamoja na nyumba 4,136 kwa upande wa polisi, ikijumuisha Wilaya ya Tunduru.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo la uchakavu wa nyumba za makazi za maafisa na askari, Serikali itaendelea kuzifanyia ukarabati nyumba za Askari Magereza na Polisi nchini zikiwemo za Wilaya ya Tunduru kwa kutenga bajeti ya ukarabati kwa kila mwaka wa fedha kutegemeana na bajeti itakavyoruhusu.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na uchakavu wa vitendea kazi pamoja na kukosekana kwa magari ya kutosha:-
(a) Je, ni lini Serikali itawapatia magari Askari Polisi wa Wilaya ya Masasi ili kupunguza ugumu wa mazingira ya kazi?
(b) Je, ni lini Serikali itarekebisha utaratibu uliopo ambapo inafikia wakati askari wanalazimika kutoa pesa zao mfukoni ili kuwapa chakula mahabusu?
(c) Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za askari katika Wilaya ya Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya ya Masasi kina magari mawili yanayohudumia Wilaya nzima. Hata hivyo, Serikali inatambua kuwa magari hayo hayatoshelezi mahitaji ya Wilaya. Aidha, Serikali inatarajia kupokea magari kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi wakati wowote kuanzia sasa na mara magari hayo yatakapowasili, Wilaya ya Masasi itakuwa miongoni mwa Wilaya zitakazogawiwa magari hayo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia mahabusu wanapokuwa mikononi mwa polisi ili kupata huduma muhimu za kijamii. Mathalani katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuhudumia mahabusu walioko vituo vya polisi, mwaka wa 2016/2017, Serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuhudumia mahabusu walioko Vituo vya Polisi Tanzania Bara na Zanzibar.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la ukosefu wa nyumba za askari hapa nchini. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ina mpango wa ujenzi wa nyumba kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha. Ndiyo maana Serikali inao mpango wa kujenga nyumba 4,136 kwa kupitia mkopo wa bei nafuu kutoka Serikali ya China kupitia Kampuni ya Polytech utakaogharimu dola za Kimarekani milioni 500.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA) aliuliza:- Zanzibar kumekuwa na matukio ya uhalifu yanayojitokeza mara kwa mara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia vitendo vya uhalifu visijitokeze Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu kamaifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mipango ya muda mfupi, kati na mrefu wa kukabiliana na wahalifu na uhalifu ndani ya mipaka ya nchi yetu. Mikakati iliyopo ni pamoja na:- (i) Kuwajengea uwezo wa utendaji kazi askari wote ili wawe na uwezo wa kubaini, kupeleleza na kufuatilia mitandao ya kiuhalifu hapa nchini. (ii) Kufanya misako na doria za miguu, pikipiki na magari ili kubaini na kuzuia hali zozote za kihalifu zinazoweza kujitokeza. (iii) Kuimarisha ulinzi maeneo ya mipaka yote ikiwemo ya maji ili kuzuia uhalifu. (iv) Kuimarisha kikosi cha kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya cha polisi sambamba na madawati ya Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya.
(v) Kuimarisha ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine nchini hasa vyombo vya ulinzi na usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, yakifanyika haya pamoja na mambo mengine vitendo vya uhalifu na wahalifu vitapungua nchini ikiwemo na Zanzibar.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la mahabusu katika magereza hapa nchini kutokana na kuchelewa kwa upelelezi wa mashauri mengi.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji huo wa kesi zilizopo mahakamani?
(b) Je, ni muda gani umewekwa kisheria pale upande wa mashtaka unaposhindwa kupeleka ushahidi mahakamani ili mahakama iweze kumuachia huru mshitakiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiri, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali na za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji wa kesi mahakamani ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa majalada ya kesi unaofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuundwa kwa Jukwaa la Haki Jinai na kutembelea mahabusu magerezani na kufanya mahojiano na mahabusu gerezani ili kushirikisha wadau wengine wa sheria katika kesi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa kisheria wa kuondoa shauri mahakamani kama upelelezi haujakamilika ni siku 60 na mtuhumiwa kuachiwa huru.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Katika Jimbo zima la Mlimba kuna kituo kimoja tu cha polisi cha Mngeta jambo linalofanya hali ya usalama kwa wananchi kuwa duni.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya polisi katika Jimbo la Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhaba wa vituo vya polisi nchini na ili kuimarisha usalama nchini Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya polisi hadi ngazi ya kata na tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira hadi hapo hali ya fedha itakapokuwa nzuri na kutuwezesha kutekeleza mpango huo.
MHE. SABREENA H. SUNGURA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza ajali za barabarani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mkakati wa kudhibiti makosa yanayosababisha madhara makubwa ambayo hupelekea ajali za barabarani kuongezeka. Mambo yaliyolengwa katika mkakati pamoja na mambo mengine ni:-
(1) Udhibiti wa madereva walevi na kuendesha kwa uzembe;
(2) Udhibiti wa mwendokasi kwa madereva na wamiliki wa magari , kuwa na madereva wenza kwa mabasi ya safari za zaidi ya masaa manane;
(3) Kuthibiti uendeshaji magari bila sifa/leseni za udereva ama Bima;
(4) Kudhibiti usafirishaji wa abiria kutumia magari madogo yenye muundo wa tairi moja nyuma;
(5) Kusimamia matumizi ya barabara kwa Makundi Maalum mfano watoto, wazee, walemavu na wasiotumia vyombo vya moto ikiwemo mikokoteni na baiskeli;
(6) Kudhibiti ajali za pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na magurudumu dumumatatu (bajaji);
(7) Kuzishauri mamlaka husika kuweka alama za kudumu za utambulisho kwenye maeneo hatarishi ya ajali;
(8) Kusimamia utaratibu wa nukta (Point System) kwenye leseni za udereva;
(9) Marekebisho ya Sheria za Usalama Barabarani;
(10) Abiria kufunga mikanda ya usalama wanapotumia vyombo vya usafiri;
(11) Kubaini maeneo tete na hatarishi ya ajali za barabarani;
(12) Kuthibiti utoaji na upokeaji rushwa barabarani;
(13) Motisha kwa askari wanaosimamia vizuri majukumu yao; na
(14) Kuwajengea uwezo wa kiutendaji askari wa usalama barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nidhahiri kwamba suala la usalama barabarani siyo la kundi au taasisi moja tu ila ni letu sote. Wabunge ni miongoni mwa wahusika wa suala la usalama barabarani, kwa maana kuwa nafasi yao kubwa ni katika kuelimisha umma na kusaidia katika ujenzi wa utamaduni wa kuheshimu alama za usalama barabarani nchini.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI Aliuliza:-
Moja kati ya kazi za Polisi ni ulinzi na usalama wa raia na mahali zao, uzoefu unaonesha kila zinapotokea kampeni za Uchaguzi Jeshi la Polisi hutumika kama Taasisi ya Chama Tawala hivyo husababisha ulinzi na usalama (hasa Wapinzani) kutoweka mikononi mwa Polisi:-
Je, Serikali haioni kwamba inalitumia Jeshi la Polisi kwa lengo la kudhoofisha Upinzani na kurahisisha kukipatia ushindi Chama chake cha CCM?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ambazo zinatoa mwongozo kwa shughuli za Askari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ifahamike kwamba Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya Ulinzi wa raia na mali zao na siyo kwa ajili ya chama fulani cha siasa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema. Ni Jeshi linalowatumikia Watanzania wote pasipo kujali vyama vyao, kabila zao, dini zao ama rangi zao. Hata hivyo, ikitokea Askari wamekiuka taratibu za kiutendaji tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kinidhamu dhidi ya wale ambao Wizara yangu inapata malalamiko rasmi kupitia dawati la malalamiko.
MHE. ESTHER N. MATIKO Aliuliza:-
Kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa leseni za udereva katika Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya kutokana na kutokuwepo kwa huduma hiyo. Hali hiyo inapelekea wananchi kupata adha kubwa ya kufuata huduma za leseni Musoma Mjini ambao ni Mkoa mwingine wa Polisi; kutokana na adha hiyo wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliamua kujenga na kukamilisha jengo la usalama barabarani:-
(a) Je, ni lini Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya utafungiwa mitambo ya kutoa leseni za udereva ili kuondoa usumbufu uliopo sasa wa kutumia gharama na muda kufuata huduma hiyo Musoma Mjini?
(b) Je, ni lini Ofisi za Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya zitajengwa ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania na Jeshi la Polisi Usalama Barabarani imekuwa ikiboresha huduma za utoaji leseni za udereva na ukusanyaji wa ada za leseni ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinawafikia wananchi bila usumbufu. Serikali kupitia taasisi hizi imefunga mitambo ya kutoa leseni za udereva kila Makao Makuu ya Mkoa ambapo wananchi wote wanaohitaji huduma hizi hufika Mkoani na kuhudumiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufunga mitambo hii kunahitajika maandalizi makubwa ya kifedha na uandaaji wa miundombinu ya mtandao, majengo na rasilimali watu. Kwa sasa, mitambo hiyo imefikishwa hadi kwenye Mikoa ya kikodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. Serikali ingependa kufunga mitambo ya kutoa leseni za udereva katika ngazi za Wilaya ikiwemo Wilaya ya Tarime/Rorya. Hata hivyo, kwani gharama za kufunga mitambo hii katika Wilaya zote nchini ni kubwa mno. Serikali inao mkakati wa kufikisha huduma hizi Wilayani ikiwemo Wilaya ya Tarime/Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kipolisi Tarime/ Rorya ni miongoni mwa Mikoa mipya ambayo bado haijajengewa ofisi mpya za kisasa ikiwemo Songwe, Katavi, Simiyu na Geita. Serikali inatambua uhaba huo wa ofisi katika mikoa hiyo na kuna mkakati wa ndani wa kujenga ofisi hizo kwa kutumia rasilimali zilizopo kama nguvu kazi ya wafungwa na kutengeneza matofali ya kujengea ofisi hizo muhimu kwa huduma ya Kipolisi na Idara zingine za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha ndani ya Mji wa Bunda na wahanga wa matukio hayo ni wafanyabiashara wadogo wadogo.
Je, ni hatua zipi za kiusalama zimechukuliwa ili kukabiliana na wimbi la ujambazi na unyang’anyi katika Mji wa Bunda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa hivi karibuni kulikuwa na wimbi la uhalifu kwa Mkoa wa Mara na mikoa mingineyo. Jeshi la Polisi limeendelea kubuni na kutekeleza mikakakati mbalimbali ya kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu, kadri uchambuzi wa uhalifu unavyoonesha mwenendo na mwelekeo wa uhalifu nchini ukitumika kama zana ya kutabiri uhalifu wa baadaye.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kuwajengea uwezo Maafisa Wakaguzi na Askari kwa kuyatambua na kuyaundia mikakati ya utekelezaji mambo yafuatayo:-
(i) Kutabiri mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za uhalifu pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo korofi, wahalifu wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na uhalifu huo.
(ii) Kuyatambua maeneo nyeti yenye vivutio vya uhalifu na kuyapangia ulinzi pamoja na misako na doria.
(iii) Kuendelea kufanya misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchini.
(iv) Kushirikiana na wadau wote wa ulinzi na usalama kubadilishana taarifa za Kiintelijensia pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya zamani.
Mheshimiwa Spika, kwa nafasi hii nitoe rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwabaini, kuwafichua na kuwakamata ili mkondo wa sheria uchukue nafasi yake kwani hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivi viovu nchini.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 19(1) ya Katiba ya nchi, kila
mtu anayo haki na uhuru wa kuamini dini aitakayo, lakini pia chini ya Ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba ni lazima sheria zifuatwe.
Je, ni kwa nini wanawake wa kiislamu wanapovaa hijabu nikabu wanavuliwa na Maafisa Usalama wanaume?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli kuwa wanawake
wa kiislaamu wanapovaa hijabu na ama nikabu wanavuliwa na maafisa wanaume wa Jeshi la Polisi. Aidha, Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza Jeshi hilo na kwa mujibu wa PGO 103(1) ambayo inasema malalamiko yote dhidi ya Polisi lazima taarifa itolewe mara moja kwa Mkuu wa eneo na hatua za uchunguzi upelelezi ifanyike kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaombe wananchi hususani wanawake, pindi wanapofanyiwa vitendo kama hivyo, kupeleka malalamiko yao polisi au kwenye mamlaka nyingine husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-
Katika upande wa kusini mwa Jimbo la Tunduru Kusini wananchi takribani 200 wa Tanzania na Msumbiji huvuka Mto Ruvuma kila siku kutafuta mahitaji yao ya kila siku, upande wa Msumbiji wameweka Askari wa Uhamiaji ambao huwanyanyasa sana Watanzania kwa kuwapiga na kuwanyang’anya mali zao kwa kukosa hati ya kusafiria.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Kituo cha Uhamiaji katika kijiji cha Makande Kazamoyo na Wenje ili kuwapatia Watanzania huduma ya uhamiaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha kuwa inasogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za Uhamiaji. Katika kutekeleza hilo Wilaya zilizo nyingi ikiwemo Tunduru zina Ofisi za Uhamiaji. Aidha, Serikali inatambua umbali mrefu wa takribani kilometa 90 uliopo kutoka vijiji vya Makando, Kazamoyo na Wenje kutoka Mjini Tunduru zilipo ofisi za Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo na uhitaji
wa huduma za uhamiaji katika vijiji hivyo ili kuwawezesha wanakijiji kuingia na kwenda nchini Msumbiji kihalali, tunafanya ufuatiliaji ili kujua gharama za kufungua ofisi za Uhamiaji katika kijiji cha Makando. Kwa kuanzia Ofisi hiyo itahudumia vijiji vya Kazamoyo na Wenje ili kuwawezesha kuvuka mpaka Kihalali. Tunawaomba wananchi na Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira kwa kuzingatia kuwa suala hili linahitaji kutengewa fedha katika bajeti.
MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeimarisha kwa kuweka boti kwa ajili ya Police Marine maeneo mengi ya mito, maziwa na hata baharini ili kuzuia au kudhibiti ajali zinapotokea.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hiyo katika Mikoa au Wilaya ambazo hazijapata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa kupeleka huduma za boti kwa ajili ya Polisi Wanamaji ili kuzuia, kudhibiti ajali kwa awamu katika mikoa yote na Wilaya ambazo hazijapata huduma pale uwezo wa kibajeti utakapoimarika.
Aidha, muda huu ambapo Serikali inaendelea kutafuta fedha ili huduma hizo ziweze kupatikana, huduma hiyo ya Polisi Wanamaji itatolewa na vituo vya Wanamaji waliopo karibu kwa kufanya doria kwenye maeneo husika.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI aliuliza:-
Gereza la Wilaya ya Iringa ambalo lipo jirani na Hospitali ya Mkoa wa Iringa limekuwa likisababisha usumbufu kwa wananchi wanaotembea kwa miguu hasa nyakati za usiku.
Je, Serikali ina mpango gani kwa kuondoa mwingiliano wa shughuli za kijamii na shughuli za gereza hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Nuhu Mwamindi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yalikuwepo malalamiko ya wananchi kupata usumbufu wa kuingia na kutoka Hospitali ya Mkoa wa Iringa ambapo barabara ya kuingia inapita mbele ya lango la Gereza la Iringa. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, hasa baada ya kufungwa kwa barabara inayopita mbele ya gereza kuelekea hospitalini kwa watumiaji wa magari ilikutanisha uongozi wa Manispaa ya Mkoa wa Iringa na uongozi wa Jeshi la Magereza mkoani humo na kutoa maangizo yafuatayo:-
Moja, uongozi wa Manispaa ya Iringa kuandaa barabara mbadala itakayotumiwa na wananchi wanaokwenda hospitalini kwa kutumia gari; pili, uongozi wa Manispaa uandae ramani ya ukuta utakaozuia matumizi ya barabara inayopita gerezani kwa kutumia gari. Ukuta huo ulilengwa kuzuia magari kutoka eneo ambalo waenda kwa miguu wangepita bila kuingilia shughuli za gereza; na tatu, baada ya kupatikana ramani, uongozi wa gereza ulitakiwa kujenga ukuta huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza tayari limeshatekeleza maagizo hayo kwa kujenga ukuta unaotenganisha barabara ya watembea kwa miguu wanaokwenda hospitali kwa kutumia eneo la mbele ya gereza ili wasiingiliane na shughuli za gereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeshatekeleza agizo la kujenga barabara mbadala inayotumiwa na wananchi wanaokwenda hospitalini na magari. Hata hivyo, pamoja na kujengwa kwa barabara mbadala, gereza limeendelea kuruhusu magari yanayokwenda hospitalini kutumia barabara hiyo mbele ya gereza kwa wakati wa dharura.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA aliuliza:-
Wapo wanawake ambao wamefungwa kwenye magerezani wakiwa na watoto wachanga/wadogo ambao bado wanahitaji uangalizi au huduma za mama zao.
(a) Je, Serikali imejipanga vipi katika kuwanusuru watoto hao ambao hawana hatia?
(b) Je, Serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka gerezani watoto hao wasio na makosa?
(c) Je, Serikali inaweza kulipa Bunge takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na wamefungwa kwa miaka mitano iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raisa Abdallah Mussa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b), na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yapo mazingira ambayo watoto wadogo na watoto wachanga huingia gerezani wakiwa wameambatana na mama zao kutokana na mama zao kufungwa gerezani au kuingia mahabusu, ama mama zao kuingia wakiwa wajawazito na baadae kujifungua gerezani. Watoto hao hupokelewa na kuruhusiwa kuwepo gerezani na mama zao kwa mujibu wa Kifungu cha 144(1) cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Kanuni 728 ya Kanuni za Kudumu za Jeshi la Magereza za mwaka 2003.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kuruhusu watoto kuwa na mama zao magerezani unatokana na kuzingatia maslahi ya mtoto kama inavyohimizwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Mtoto (The Convention of Rights of the Child) na mikataba mbalimbali ya kikanda inayohusiana na haki za mtoto. Kwa kuwa mtoto mchanga huwa bado ananyonya, hivyo himaya stahiki ya malezi na makuzi ya awali huwa ni ya mama yake. Hata hivyo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imetoa nafasi kwa mtoto ambae mzazi wake wake yuko katika ukinzani wa sheria kuweza kupata malezi mbadala ambayo yanazingatia mahitaji yote ya mtoto kama ilivyo kwa mtoto yeyote yule chini ya uangalizi wa uongozi wa magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2016, idadi ya wanawake waliofungwa magerezani kutokana na kukinzana na sheria ilikuwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012 ni 364, mwaka 2013 ni 321, mwaka 2014 ni 373, mwaka 2015 walikuwa ni 334 na mwaka 2016 ni 616. Hivyo kufanya jumla yake wote kuwa ni 2008.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi kutokana na sababu mbalimbali.
(a) Je, ni idadi ya watu wangapi waliopoteza maisha katika Jimbo la Ushetu kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015?
(b) Je, mauaji ya makundi haya yanapungua au yanaongezeka katika Jimbo la Ushetu?
(c) Je, Serikali imeshirikisha vipi jamii kupiga vita mauaji haya, vikiwemo vikundi vya dini, walinzi wa jadi (sungusungu) na uongozi wa kimila Jimboni Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010 wazee waliouawa walikuwa wawili, mwaka 2011 wazee wanne, mwaka 2013 wazee watano, mwaka 2014 wazee waliouawa walifikia sita, mwaka 2015 walikuwa wawili, mwaka 2016 wawili na mwaka 2017 alikuwa ni mzee moja. Kwa hiyo, jumla ya wazee ambao wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 2010 hadi 2017 ni wazee 22 katika Jimbo la Ushetu. Kwa upande wa walemavu wa ngozi, katika kipindi hicho hakuna mlemavu aliyeuawa wala kujeruhiwa Jimboni Ushetu ila kwa nchi nzima kwa kipindi cha miaka 2010 mpaka 2017 walemavu wa ngozi waliouawa walikuwa ni sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kuwa mauaji ya makundi haya katika miaka ya karibuni yanapungua kutokana na misako iliyofanywa ya kuwakamata waganga wa kienyeji ambao wanapiga ramli chonganishi na kuchochea imani za kishirikina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukomesha mauaji haya, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kushirikiana na taasisi mbalimbali zisizo za Kiserikali ndani na nje ya Jimbo hilo katika kutoa elimu ya ukatili huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikishirikiana na jamii na taasisi za kidini, vikundi vya ulinzi jamii ndani na nje ya Jimbo la Ushetu kwa kuwapa elimu wananchi ili kudhibiti maujai hayo ya kikatili.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Mara nyingi kumekuwa na taarifa juu ya watu wanaokamatwa na dawa za kulevya kwenye maeneo mbalimbali nchini, lakini hatuambiwi nini kinafanyika:-
Je, baada ya watu hao kukamatwa, ni nini huwa kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali katika kudhibiti dawa za kulevya za mashambani na viwandani. Hatua hizo zinalenga kudhibiti kilimo cha bangi, uingizaji, usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya za viwandani kote nchini kwa kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia Oktoba, 2015 mpaka Mei, 2017 Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watumiaji mbalimbali ambapo watuhumiwa takribani 14,748 kesi zao zinaendelea mahakamani; watuhumiwa zaidi ya 2,000 walipatikana na hatia wakati watuhumiwa wanaozidi 600 waliachiwa huru na mahakama; na watuhumiwa wanaozidi 13,000 kesi zao ziko katika hatua mbalimbali za upelelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu natoa wito kwa wananchi na wageni kuacha kujihusisha na biashara hii haramu kwa kuwa, hakuna atakayebaki salama kwenye mapambano haya. Serikali kupitia vyombo vyake itaendelea kuwasaka wahusika wote ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
MHE. JUMA OTHMANI HIJA aliuliza:-
Kumekuwa na matukio yasiyo ya kawaida na kukaribia kuhatarisha amani katika Kisiwa cha Tumbatu:-
Je, Serikali haioni ipo haja ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kisiwa hicho ili kukabiliana na matukio ya kiuhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO NA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yako matukio ya kihalifu yanayoripotiwa kutoka katika Kisiwa cha Tumbatu na Jeshi la Polisi linafanya jitihada ya kukabiliana na wahalifu kwa kutoa huduma za ulinzi na usalama katika kisiwa hicho kwa kufanya doria kila siku. Pamoja na doria, kumeanzishwa utaratibu wa detach ambapo askari wanakwenda kulinda kisiwa hicho na kubadilishana kwa zamu ili kuimarisha ulinzi. Aidha, ipo boti yenye uwezo wa kubeba Askari kumi. Iwapo uwezo wa kifedha ukiongezeka tutajitahidi kupata boti kubwa ya mwendo kasi na yenye uwezo wa kubeba Askari zaidi ya kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona haja ya kuwepo Kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Tumbatu ili kusogeza huduma za ulinzi na usalama kwa kuzingatia jiografia ya kisiwa hicho na matukio ya uhalifu. Katika kutekeleza hilo, tayari Serikali imepata kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 600 na makisio ya ujenzi wa kituo hicho umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu naomba kutumia fursa hii kuhamasisha wadau na wananchi akiwemo Mheshimiwa Mbunge kushirikiana kuanza ujenzi wa kituo hiki wakati Serikali inakamilisha mipango yake ya kupata fedha.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Polisi wamekuwa wakifanya msako na kamatakamata ya waganga wa kienyeji sehemu nyingi hapa nchini:-
(a) Je, ni waganga wangapi wa kienyeji walikamtwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu?
(b) Je, ni waganga wa kienyeji wangapi walifikishwa Mahakamani na kutiwa hatiani katika kipindi hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, waganga wa kienyeji waliokamatwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ni 26 na kushtakiwa kwa makosa ya kufanya biashara ya uganga bila kibali na kupatikana na nyara za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya waganga 16 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani. Kati ya hao, waganga saba walipatikana na hatia kwa kufungwa miaka miwili kila mmoja au kulipa faini ambapo jumla ya watuhumiwa sita katika kesi tofauti walilipa faini ya jumla ya Sh.1,250,000/=. Mtuhumiwa wa kesi moja alihukumiwa miaka miwili bila yeye kuwepo Mahakamani, juhudi za kumsaka zinaendelea.
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kutatua tatizo la usafiri kwa Jeshi la Polisi bila mafanikio. Kwa mfano, Kituo cha Polisi Mfenesini, Zanzibar hakina gari la uhakika kwa takribani miaka 10 sasa:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka gari Kituo cha Polisi Mfenesini?
(b) Je, ni lini magari ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwa muda mrefu yatawasili nchini ili kuondoa adha ya usafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kanali (Mst) Masoud Ali Khamis, Mbunge wa Mfenesini, lenye sehemu
(a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Mfenesini kipo Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Wilaya ya Kipolisi Mjini Magharibi A. Mkoa wa Kaskazini Unguja una jumla ya magari 13 ambayo yanatoa huduma za doria na kazi nyingine za Polisi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwemo Kituo cha Polisi Mfenesini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha Polisi Mfenesini kitapatiwa gari mara baada ya taratibu za upatikanaji wa magari utakapokamilika. Hata hivyo, gari la Mkuu wa Polisi wa Wilaya hutoa huduma pale inapotokea dharura ikiwa ni pamoja na kuwachukua mahabusu waliopo katika kituo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, magari haya yamekuwa yakiwasili nchini awamu nchini awamu kwa awamu ambapo hadi sasa jumla ya magari 231 yamekwishawasili kati ya magari 777 yaliyokuwa yameagizwa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Kumekuwa na uuzwaji wa silaha kiholela kama vile mapanga na visu katika barabara zetu ikiwemo Ubungo kwenye mataa hali ambayo inaleta hofu kwa raia wema.
Je, Serikali inalichukuliaje suala hilo ambalo ni hatari sana kwa usalama wa raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na uuzaji holela wa silaha za jadi katika maeneo mbalimbali ya barabara zetu ikiwemo katika makutano ya barabara ya Mandela na Morogoro eneo la Ubungo, Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatambua uwepo wa tatizo hilo na tayari hatua mbalimbali za kudhibiti hali hiyo zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kufanya operesheni za mara kwa mara na kukamata wauzaji wa silaha za jadi barabarani kama vile mapanga, mikuki, upinde na mishale. Aidha, elimu inaendelea kutolewa kwa wafanyabiashara wa bidhaa za silaha hizo kutowapatia wauzaji wasio na eneo maalum la kufanyia biashara hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali linaandaa utaratibu maalum wa uuzaji wa bidhaa za aina hii na kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya biashara hii na kuwashauri wananchi waipige vita na kuepuka kujihusisha nayo.
MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Gereza la Wilaya ya Kibondo – Nyamisati limekuwa na ongezeko kubwa sana la wafungwa na mahabusu kwa sababu ya uwepo wa wakimbizi.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati unaofaa kupeleka mradi mkubwa wa maji kwenye gereza hilo ili kulinda afya za raia na askari walioko kwenye gereza hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna tatizo la upatikanaji wa maji katika Gereza la Kibondo. Mwaka 2010, Serikali kupitia Jeshi la Magereza lilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 20 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu na kazi hiyo ilifanywa na Wakala wa Uchimbaji Mabwawa na Visima iliyopo Ubungo Dar es Salaam. Uchimbaji wa kisima hicho ulikamilika tarehe 2 Oktoba 2010 na kilikuwa na uwezo wa kutoa lita 2,300 kwa saa ambayo ni sawa na lita 55,200 kwa siku. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya maji ya Gereza la Kibondo ambayo ni lita 94,870 kwa siku, hivyo kuwa na upungufu wa takriban lita 39,670 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 upembuzi yakinifu ulifanywa na wataalam wa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mhandisi wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Kibondo na kushauri kuwa ili gereza hilo liondokane na tatizo la maji, Jeshi la Magereza linapaswa kuvuta maji kutoka mtandao wa maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo hadi gerezani ambapo gharama zake ilikadiriwa kuwa ni shilingi 330,492,450. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti, mradi huo haujatekelezwa hadi sasa. Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha tatizo la maji Gereza la Kibondo linapata ufumbuzi wa kudumu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y MHE. KABWE Z. R. ZITTO) aliuliza:-
Nchi ya DRC inaitegemea Kigoma kiuchumi kwa kiwango kikubwa hususan katika soko la bidhaa na huduma ya bandari ya Kigoma na hivyo wananchi wengi wa Kigoma kutembelea Congo na wale wa Congo kutembelea Kigoma. Changamoto kubwa ni gharama za biashara kutokana na viza kati ya nchi hizo mbili licha ya kwamba nchi hizo zote ni wanachama wa SADC na nchi za SADC hazina viza kwa raia wake.
Je, ni kwa nini Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haziondoi viza kwa raia wake ili kudumisha biashara kati ya wananchi wake kwa lengo la kukuza Kigoma kuwa Kituo cha Biashara cha Maziwa Makuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge napenda kumfahamisha kuwa suala la kutotozana viza ni la kimakubaliano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na si kwamba nchi za SADC hazina viza kwa raia wanaotaka katika nchi moja kwenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, katika nchi za SADC ilikubaliwa kuwa kila nchi wanachama ziwekeane utaratibu na namna bora ya kuondoa hitaji la viza kwa raia wao. Kwa sasa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wenye pasipoti za kidiplomasia na utumishi hawahitaji kulipia viza kuingia Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Tanzania na DRC zimekuwa katika mazungumzo ya muda mrefu kuhusu namna bora ya kuondoa malipo ya viza kwa raia wake wenye pasipoti za kawaida, lakini mazungumzo hayo yamechelewa kukamilika kutoka na migogoro ya ndani iliyoko katika nchi ya DRC. Hata hivyo, ni mategemeo kuwa kupatikana kwa suluhisho la kudumu la migogoro iliyoko ndani ya nchi ya DRC kutawezesha kukamilishwa kwa taratibu za kuondoa hitaji la viza baina ya hizo nchi hizi mbili kwa haraka.
KITETO Z. KOSHUMA (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Wavuvi wa Wilaya ya Rorya wanaovua katika Ziwa Victoria wamekuwa wakitekwa, kunyang’anywa nyavu zao pamoja na injini za boti. Aidha, majambazi wanaofanya vitendo hivyo hutumia silaha nzito na inasemekana ni wanajeshi kutoka Uganda.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongea na Serikali ya Uganda ili kukomesha uvamizi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na matukio ya uporaji wa nyavu na injini za wavuvi katika Ziwa Victoria. Uporaji huu unafanywa na wahalifu ambao bado Jeshi la Polisi halina ushahidi kuwa wanatoka ndani au nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na matukio ya uhalifu ikiwemo uporaji wa nyavu na injini za wavuvi katika Ziwa Victoria, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina mikakati ya kununua boti zenye uwezo na zenye mwendo kasi mkubwa. Boti hizi zitasaidia askari polisi kufanya doria za mara kwa mara na kufika kwenye matukio haraka. Aidha, Serikali inashirikiana na nchi jirani katika udhibiti wa pamoja kwa matukio ya uhalifu wa majini.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Jeshi la Polisi lina kazi kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini cha kusikitisha ni kwamba askari wanaishi kwenye nyumba duni sana jambo ambalo linashusha hata hadhi zao hasa kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
(i) Je, ni lini askari wetu watatengenezewa nyumba bora nao wajisikie kuwa Serikali yao inawajali?
(ii) Katika Makao Makuu ya Polisi pale Ziwani kuna majengo yaliyoachwa na wakoloni, je, kwa nini yasifanyiwe ukarabati mkubwa ili yaweze kutumiwa na askari wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Jeshi la Polisi linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa nyumba za kuishi askari. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ina mpango wa kujenga nyumba 350 za kuishi Askari Polisi Zanzibar. Katika idadi hiyo, nyumba 150 zitajengwa Pemba na nyumba 200 zitajengwa Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga nyumba mpya na siyo kukarabati nyumba za zamani zilizoachwa na wakoloni. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Tarehe 25/5/2017 Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akijibu swali Na. 274 kuhusu madai ya mkandarasi aliyejenga vituo vya polisi Mkokotoni Unguja na Madungu alisema, deni tayari limeshahakikiwa na kwamba atalipwa mara fedha zitakapotolewa lakini huu ni mwaka wa tano deni hilo halijalipwa:-
(a) Je, Serikali ina nia thabiti ya kumlipa mkandarasi?
(b) Je, Serikali inasubiri ipelekwe Mahakamani ndipo ilipe deni hilo?
(c) Je, huu ndiyo utawala bora ambao nchi yetu ina dhamira ya kuujenga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a), (b), na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua madeni ya wakandarasi wote akiwemo Albatna Building Contractor na ina nia ya dhati ya kuyalipa madeni yote ya wakandarasi na Washauri Elekezi waliohusika katika miradi mbalimbali ikiwemo miradi iliyohusisha Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Jeshi la Polisi limetenga jumla ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni ambao umetengewa jumla ya shilingi milioni 200 ikiwa ni sehemu ya deni ambalo anadai mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa hakuna deni la mzabuni au mtumishi ambalo halitalipwa kwani madeni yote yaliyohakikiwa yanaendelea kulipwa kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Jimbo la Same Mashariki lina Kata 14 lakini lina Kituo kimoja cha Polisi kilichopo Kata ya Maore na vituo vidogo vilivyopo Kata ya Ndungu na Kihurio; vituo vyote hivyo vipo katika tarafa moja yenye kata tano, kata nyingine tisa ambazo zipo katika tarafa mbili zilizoko mlimani na zipo mbali sana na vituo hivyo vya Polisi zinapata shida sana kutoa ripoti za uhalifu. Kwa kuwa wananchi wa tarafa hizo mbili za mlimani tayari wametenga maeneo ya kuweka vituo vya Polisi:-
(a) Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Vituo vya Polisi katika Tarafa ya Mamba/Vunta na Tarafa ya Gonja?
(b) Kama Serikali ipo tayari kuanzisha Vituo hivyo vya Polisi, je, ni lini Polisi hao wataanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, najibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Vituo vya Polisi katika ngazi ya Kata na Tarafa nchi nzima, Mamba/Vunta na Gonja zikiwemo. Katika Tarafa ya Gonja kuna Kituo cha Polisi, Daraja B kinachotoa huduma za kipolisi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tarafa ya Mamba wananchi wamejitolea eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi ambapo kwa sasa majadiliano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi kuhusu ujenzi wa Kituo cha Polisi, Daraja la B yanaendelea. Hata hivyo, kwa sasa Tarafa ya Mamba ina Kituo kidogo Daraja la C ambacho kinatoa huduma kwa wananchi katika Tarafa hiyo. Aidha, Jeshi la Polisi hufanya doria mara kwa mara katika maeneo hayo ya milimani ambayo hafikiwi kirahisi na vyombo vya usafiri kutokana na jiografia yake.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Tatizo la kupotea kwa watoto katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa kubwa. Aidha, taarifa za kupotea kwa watoto hao zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari:-
(a) Je, ni sababu zipi zinazochangia kuongezeka kwa tatizo hilo siku hadi siku?
(b) Je, kwa nini taarifa za upatikanaji wa watoto hao hazitolewi kwenye vyombo vya habari?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani kuondoa tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri ya Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la upoteaji wa watoto katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam. Aidha, sababu za upotevu wa watoto hawa ni pamoja na uangalifu hafifu wa watoto kutoka kwa wazazi au walezi na jamii kwa ujumla, mazingira magumu wanayoishi baadhi ya watoto, imani za kishirikina, visasi kati ya familia na kupotea kwa bahati mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kudhibiti matukio hayo kwa kutoa elimu kupitia programu ya Polisi Jamii kwa watoto mashuleni na wazazi kupitia mihadhara ya kijamii na vyombo vya habari. Jitihada hizo zimekuwa zikizaa matunda kwa kuongeza elimu ya usalama wetu kwanza miongoni mwa jamii na hivyo kuongeza umakini wa kulinda watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Disemba, 2017 kwa Mkoa wa Dar es Salaam walipotea watoto 184, ambapo watoto waliopatikana ni 176 na watoto ambao wanaendelea kutafutwa ni nane. Jeshi la Polisi linaendelea kutoa rai kwa taasisi na idara mbalimbali kama Ustawi wa Jamii kushirikiana na kuwa na programu za pamoja ili kutoa elimu ya kumlinda mtoto wa Tanzania.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Majengo ya Kituo Afya cha Kambi ya Jeshi Migombani Unguja ni chakavu na pia ni siku nyingi sana.
Je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho ili kiwe cha kisasa na kiendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANO YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi wa Jeshi la Kujenga Taifa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Jeshi cha Migombani Zanzibar ni moja ya vituo vya tiba ambavyo huanzishwa katika kila Kikosi cha JWTZ ili kutoa huduma ya mwanzo ya tiba kwa Wanajeshi na familia zao, watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na wananchi wanaishi jirani kabla ya kupelekwa katika hospitali za rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni, kweli majengo ya kituo hicho na vituo vingine vya JWTZ yamechakaa na kwa sababu ni ya muda mrefu. Kutokana na uchakavu huo wa Kituo cha Kambi ya Migombani na sehemu nyingine, ni matazamio ya Wizara kuvi karabati upya vituo vyote katika mwaka wa fedha 2018/2019 kadri hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-
Hali ya nyumba za Polisi na Magereza nchini ni mbovu sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za askari hao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hali ya makazi kwa Askari wetu siyo nzuri, hata hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo husika kujenga makazi mapya na kufanya ukarabati wa majengo yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 12.3 fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa makazi ya askari wetu katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Songwe kwa michango yao wenyewe wamejenga jengo kubwa kwa ajili ya Kituo cha Polisi katika Kata ya Mpona tangu mwaka 2014 ili kupambana na majambazi wanaovamia wananchi hasa wakati wa mavuno ya zao la ufuta.
Je, ni lini Serikali itasaidia kuamlizia jengo hilo na kupeleka askari polisi ili kituo hicho kianze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo kwa uhakika, Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe ni kati ya mikoa mipya iliyoanzishwa hivi karibuni ambayo ina changamoto nyingi ya vituo vya polisi, ofisi pamoja na nyumba za askari kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchini. Aidha, katika mkoa mpya wa Songwe hakuna Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya mbili mpya za Momba na Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada alizofanya yeye na kushirikiana na wananchi wa Kata ya Mpona za kujenga Kituo cha Polisi katika eneo hilo. Aidha, kwa sasa kipaumbele ni ujenzi wa Ofisi ya Kamanda wa Mkoa pamoja na Wilaya mpya. Hata hivyo Serikali inafanya jitihada ili kukamilisha kituo hicho kulingana na upatikanaji rasilimali.
MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:-
Wananchi wa Kata za Mahinda, Ngoyoni, Mengwe na Kirongo – Samanga walifanya uamuzi wa kujenga vituo vya polisi kwa nguvu zao na vituo hivyo vimefikia hatua mbalimbali za ujenzi, lakini kutokana na kuwepo na shughuli nyingine zinazohitaji michango ya wananchi kama vile ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na maabara wameshindwa kumalizia vituo hivyo.
Je, Serikali iko tayari kuchukua hatua za kumalizia ujenzi wa vituo hivyo njia ya kuwatia moyo wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Rombo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kupongeza sana juhudi za wananchi wa Mahida, Ngoyoni, Mengwe na Korongo kwa uamuzi wao wa kujenga vituo vya polisi kwa nguvu zao wenyewe. Kutokana na ujenzi wa vituo hivyo kuwa katika hatua mbalimbali. Serikali kupitia jeshi la polisi itafanya ukaguzi wa vituo hivyo ili kupata tathmini ya gharama zitakazohitajika katika kukamilisha ujenzi huo. (Makofi)
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16 inatoa uhuru wa faragha kwa raia.
Je, kwa nini Jeshi la Polisi linapokwenda kupekua kwenye nyumba yenye mume na mke hutumia askari wa kiume peke yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upekuzi ni jukumu ambalo sheria imelipa Jeshi la Polisi na utaratibu wake umeainishwa wazi namna ambavyo upekuzi utafanyika kwenye maeneo mbalimbali. Kifungu cha 38 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 inatoa masharti na utaratibu wa kuweza kufanya upekuzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba, majengo na vyombo vya usafiri kama magari, boti na kadhalika endapo Afisa wa Polisi atakuwa amehisi na amejiridhisha pasipo na shaka kwamba kuna sababu ya kutosheleza kuwa kuna uwezekano wa kosa kutendeka au ushahidi kupatikana kuthibitisha kosa lililotendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, upekuzi wa makazi ya nyumba yenye mke na mume sheria haijaweka masharti ya ni askari wa jinsia gani anatakiwa kufanya upekuzi. Hata hiyo, Jeshi la Polisi kwa kutumia Kanuni ya Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) pia kwa kuzingatia busara na utu wa mwanadamu huwa inazingatia utaratibu wa kupeleka askari wa kike na wa kiume pale upekuzi unapofanyika kwenye makazi ya mume na mke.
MHE. AIDA J. KHENAN (k.n.y MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA) aliuliza
(a) Je, kuna sheria yoyote ya nchi inayomruhusu askari polisi kumkatamata mtuhumiwa, kumpiga na kumtesa kabla hajajua kosa lake na kabla ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi?
(b) Je, Serikali inachukua hatua zipi za kuhakikisha kuwa askari wanaofanya vitendo kama hivyo wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi?
(c) Je, mpaka sasa ni askari wangapi wameshachukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa ya kujichukulia hatua mkononi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum lenye shemu (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 kifungu cha 11 kinaeleza namna ya ukamataji. Aidha, kifungu hiki mahsusi cha ukamataji hakimruhusu askari kumpiga na kumtesa raia wakati wowote anapokuwa kizuizini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO) askari yoyote anapobainika kufanya vitendo vya kupiga au kutesa raia huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi na au hata kufikishwa mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha januari mpaka Desemba, 2017 jumla ya askari 105 waliotenda makosa mbalimbali walichukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Je, nini mipango ya Serikali ya kumaliza tatizo kubwa la nyumba za askari hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna tatizo kubwa sana la nyumba za Askari za kuishi. Kwa kufahamu hilo Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya ujenzi wa makazi ya Askari kwa awamu kulingana na uwezo uliopo. Aidha pamoja na kutenga fedha hizo Wizara yangu itajielekeza zaidi kutumia rasilimali zilizopo na teknolojia rahisi ya ujenzi wa nyumba ili kupunguza tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia ubia baina ya Serikali na sekta binafsi Jeshi la Polisi limefanikiwa kujenga nyumba 353 Kunduchi na Mikocheni, Dar es Salaam kwa ajili ya askari wa kawaida na maafisa. Aidha, Jeshi la Magereza linaendelea na ujenzi wa nyumba 320 Ukonga, Dar es Salaam kwa fedha za Serikali na lipo katika mazungumzo ya ubia na Shirika la Nyumba la Taifa utakaowawezesha kujenga nyumba 100 Msalato, Dodoma. Kadhalika, Idara ya Uhamiaji inafanya makubaliano na Shirika la Nyumba la Taifa kwa ajili ya ununuzi wa nyumba 103 Dodoma, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la kuhamia Dodoma. Utaratibu huu utaendelezwa katika Mikoa mingine ili kupunguza changamoto hii kwa Askari wetu. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA) aliuliza:-
Baadhi ya vituo vya Polisi na Magereza nchini vina majengo chakavu sana vikiwemo Kituo cha Polisi Bagamoyo na Gereza la Kigongoni Bagamoyo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kujenga nyumba za Polisi na Askari Magereza Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli baadhi ya Vituo vya Polisi na Magereza nchini vina majengo chakavu ambayo yalijengwa miaka mingi iliyopita na kituo cha Polisi na Magereza Bagamoyo kikiwa miongoni mwao.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga Kituo cha Polisi, Gereza na nyumba za kuishi za Askari katika Wilaya ya Bagamoyo na Wilaya nyingine nchini zisizo na majengo hayo, ujenzi huo utajengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za bajeti. Sambamba na hilo, Wizara imeweka msisitizo katika matumizi ya rasilimali zilizopo kama vile ardhi ili kupunguza tatizo hili kwa kujenga vituo vya Polisi katika Wilaya 25 na Magereza katika Wialaya 52 kote nchini.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Charles Kitwanga alikaririwa na vyombo vya habari mwezi Desemba, 2015, akiliagiza Jeshi la Polisi kumkabidhi majina ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ambazo ongezeko lake nchini lina athari hasi dhidi ya vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa:-
(a) Je, ni hatua gani zimechukuliwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani katika kuwabaini, kuwachunguza na hatimaye kuwafikisha Mahakamani wale wote waliobainika kujihusisha na mtandao wa biashara za dawa za kulevya?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wanaojiingiza kwenye dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya nchini?
(c) Je, ni vijana wangapi kwa nchi nzima ambao kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita wamepatiwa tiba kusaidiwa kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athumani Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kati ya Oktoba, 2015 hadi Aprili, 2017 Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 9,140 wa dawa za kulevya ambapo watuhumiwa 14,410 kesi zao zinaendelea Mahakamani na zipo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 2,401 walikutwa na hatia, watuhumiwa 615 waliachiwa huru na watuhumiwa wengine 13,071 kesi zao ziko chini ya upelelezi.
(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kupitia Programu ya kuzuia uhalifu limeendelea kutoa huduma ya urekebishaji kwa waaathirika wa dawa za kulevya. Kwa kutumia vikundi mbalimbali vya michezo chini ya miradi ya kuzuia uhalifu kama vile familia yangu haina mhalifu na klabu ya usalama wetu kwanza.
(c) Mheshimiwa Spika, vijana 3,000 walipatiwa tiba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa kushirikiana na wadau.
MHE: RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Tanzania imeridhia na kuingia mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwemo diplomasia na mahusiano.
Je, ni nchi ngapi na zipi ambazo Watanzania wanaweza kuzitembelea moja kwa moja kwa utaratibu wa visa on entry wakati wa kuingia ukiondoa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa maelezo kwa kuwa visa ni ruhusa inayoambatana na masharti ambayo hutolewa na nchi husika ili kuwaruhusu raia wa kigeni kuingia, kuondoka au kuwepo nchini katika muda maalum. Ruhusa hiyo inapotolewa katika vituo vya kuingilia nchini inajulikana kama visa on arrival.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa utoaji visa on arrival uko katika sura ya makubaliano ama mikataba baina ya nchi na nchi au taratibu zinazotokana na matengamano na ushirikiano wa kimataifa na kikanda. Utaratibu huu unaweza kubadilika kulingana na mahusianao na hali ya usalama kati ya nchi na nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi 16 ambazo Watanzania wanaweza kuzitembelea katika utaratibu wa visa on arrival. Nchi hizo ni Benin, Burkina Faso, Cape Verde, Cote d’voire, Djibout, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Guinea – Bessau, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Sierra Leone huu wa visa on arrival, pia zipo nchi 67 duniani ambazo Watanzania wanaweza kuzitembelea bila hitajio la visa.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA aliuliza:-
Wapo wanawake ambao wamefungwa kwenye magerezani wakiwa na watoto wachanga/wadogo ambao bado wanahitaji uangalizi au huduma za mama zao.
(a) Je, Serikali imejipanga vipi katika kuwanusuru watoto hao ambao hawana hatia?
(b) Je, Serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka gerezani watoto hao wasio na makosa?
(c) Je, Serikali inaweza kulipa Bunge takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na wamefungwa kwa miaka mitano iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raisa Abdallah Mussa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b), na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yapo mazingira ambayo watoto wadogo na watoto wachanga huingia gerezani wakiwa wameambatana na mama zao kutokana na mama zao kufungwa gerezani au kuingia mahabusu, ama mama zao kuingia wakiwa wajawazito na baadae kujifungua gerezani. Watoto hao hupokelewa na kuruhusiwa kuwepo gerezani na mama zao kwa mujibu wa Kifungu cha 144(1) cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Kanuni 728 ya Kanuni za Kudumu za Jeshi la Magereza za mwaka 2003.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa kuruhusu watoto kuwa na mama zao magerezani unatokana na kuzingatia maslahi ya mtoto kama inavyohimizwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Mtoto (The Convention of Rights of the Child) na mikataba mbalimbali ya kikanda inayohusiana na haki za mtoto. Kwa kuwa mtoto mchanga huwa bado ananyonya, hivyo himaya stahiki ya malezi na makuzi ya awali huwa ni ya mama yake. Hata hivyo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imetoa nafasi kwa mtoto ambae mzazi wake wake yuko katika ukinzani wa sheria kuweza kupata malezi mbadala ambayo yanazingatia mahitaji yote ya mtoto kama ilivyo kwa mtoto yeyote yule chini ya uangalizi wa uongozi wa magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2016, idadi ya wanawake waliofungwa magerezani kutokana na kukinzana na sheria ilikuwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012 ni 364, mwaka 2013 ni 321, mwaka 2014 ni 373, mwaka 2015 walikuwa ni 334 na mwaka 2016 ni 616. Hivyo kufanya jumla yake wote kuwa ni 2008.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA aliuliza:-
Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi kutokana na sababu mbalimbali.
(a) Je, ni idadi ya watu wangapi waliopoteza maisha katika Jimbo la Ushetu kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015?
(b) Je, mauaji ya makundi haya yanapungua au yanaongezeka katika Jimbo la Ushetu?
(c) Je, Serikali imeshirikisha vipi jamii kupiga vita mauaji haya, vikiwemo vikundi vya dini, walinzi wa jadi (sungusungu) na uongozi wa kimila Jimboni Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias John Kwandikwa, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010 wazee waliouawa walikuwa wawili, mwaka 2011 wazee wanne, mwaka 2013 wazee watano, mwaka 2014 wazee waliouawa walifikia sita, mwaka 2015 walikuwa wawili, mwaka 2016 wawili na mwaka 2017 alikuwa ni mzee moja. Kwa hiyo, jumla ya wazee ambao wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 2010 hadi 2017 ni wazee 22 katika Jimbo la Ushetu. Kwa upande wa walemavu wa ngozi, katika kipindi hicho hakuna mlemavu aliyeuawa wala kujeruhiwa Jimboni Ushetu ila kwa nchi nzima kwa kipindi cha miaka 2010 mpaka 2017 walemavu wa ngozi waliouawa walikuwa ni sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kuwa mauaji ya makundi haya katika miaka ya karibuni yanapungua kutokana na misako iliyofanywa ya kuwakamata waganga wa kienyeji ambao wanapiga ramli chonganishi na kuchochea imani za kishirikina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukomesha mauaji haya, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kushirikiana na taasisi mbalimbali zisizo za Kiserikali ndani na nje ya Jimbo hilo katika kutoa elimu ya ukatili huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikishirikiana na jamii na taasisi za kidini, vikundi vya ulinzi jamii ndani na nje ya Jimbo la Ushetu kwa kuwapa elimu wananchi ili kudhibiti maujai hayo ya kikatili.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Kituo cha Polisi Bububu ni kikongwe sana na pia kimechakaa sana na kinahitaji ukarabati mkubwa. Je, ni lini kituo hicho kitafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, na mimi naomba niungane na Waheshimiwa wengine kumshukuru Mwenyezi Mungu kukujalia kuungana na sisi leo ukiwa mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa vituo vya polisi vikongwe nchini kikiwemo Kituo cha Polisi cha Bububu. Jeshi la Polisi lina mpango wa kuvikarabati vituo hivyo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, ukarabati wa vituo hivyo vya Polisi kikiwemo Kituo cha Polisi Bububu utafanyika ili kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wetu ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
• Je, Serikali inatumia pesa kiasi gani kuhudumia mfungwa mmoja kwa siku kwa huduma ya chakula tu?
• Vitendo kama kulala chini, kulala bila blanketi au shuka, kulala bila neti vimekuwa vya kawaida kabisa katika Magereza yetu nchini; je, hii nayo ni sehemu ya adhabu ambayo wafungwa wanapewa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza katika kutekeleza jukumu lake la kuwapokea na kuwahifadhi wahalifu kisheria, pia hutoa huduma ya chakula kwa wahalifu kupitia bajeti inayotengwa na Serikali kila mwaka wa fedha. Gharama ya chakula kwa mfungwa mmoja kwa siku ni wastani wa shilingi 1,342.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za wafungwa na mahabusu Magerezani kwa kununua vifaa mbalimbali vya malazi ikiwemo magodoro, shuka, mablanketi na madawa ya kuua wadudu kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha. Kwa msingi huo inapotokea ukosefu wa huduma hizo, inakuwa siyo sehemu ya adhabu kwa wafungwa bali hutokea kutokana na idadi kubwa ya wafungwa gerezani.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kuchelewesha haki ni kunyima haki.
Je, Jeshi la Polisi limejitathmini juu ya utendaji wake, hususan katika Idara ya Upelelezi wa Makosa mbalimbali kabla ya kuyafikisha mashtaka mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upelelezi wa makosa ya jinai unafanywa kwa kuzingatia sheria mbalimbali kama vile Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 Marejeo ya mwaka 2002, Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo mwaka 2002 na Sheria ya Ushahidi Sura ya 6 Marejeo ya mwaka 2002, pamoja na kuzingatia kanuni za kiutendaji za Jeshi la Polisi (Police General Orders) na sheria nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya lengo la upelelezi wa makosa ya jinai ni kukusanya ushahidi utakaothibitisha kosa lililotendeka na kuripotiwa kituoni. Aidha, kuna baadhi ya makosa yaliyotendeka huhitaji muda mrefu ili ushahidi wake kuweza kupatikana, mathalani makosa ya mauaji na yanayofanana na hayo. Inapodhihirika kuwa kuna ushahidi uliopatikana unaweza kuthibitisha kosa, jalada hupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za kusomwa na kuandaa mashtaka pale ambapo wanaona ushahidi umejitosheleza na kupeleka mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi hufanya tathmini ya kutosha katika utendaji wake kupitia Kitengo cha Ndani cha Tathmini na Uangalizi (Internal Monitoring and Evaluation) na kutoka kwa Waangalizi wa Nje (External Oversight) ambao hulisaidia Jeshi la Polisi kurekebisha kasoro mbalimbali za kiutendaji.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Wilaya ya Chemba haina Kituo cha Polisi; je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Polisi na nyumba za askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Jeshi la Polisi lina uhaba wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi Askari kote nchini ikiwemo Wilaya ya Chemba. Ili kutatua changamoto hii Jeshi la Polisi linashirikisha wadau wa eneo husika pamoja na wadau wengine wa maeneo kwa maendeleo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga vituo vya kisasa vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilayani Chemba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, wananchi na wadau wengine wapo kwenye hatua za awali za kuanza ujenzi wa kituo cha polisi. Aidha, kwa sasa mchoro wa ramani ya kituo na gharama za ujenzi (BOQ) zimeshakamilika na ukusanyaji wa mahitaji ya ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini jitihada hizi zitaungwa mkono na Mheshimiwa Mbunge ili kuhakikishia wananchi wake usalama wao pamoja na mali zao.
MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:-
Katika miaka ya 1980 wanakijiji wa Kijiji cha Mwanchumu, Salaliya na Matongo walitoa maeneo yao kwa Serikali ili yatumike kwa shughuli za kilimo zilizokusudiwa na Gereza la Matongo lakini kwa sasa maeneo hayo hayatumiwi na Magereza kikamilifu.
Je, Serikali ipo tayari kurejesha eneo hilo ambalo halitumiki kikamilifu kwa wananchi wa vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Gereza la Matongo liko Mkoani Simiyu katika Wilaya ya Bariadi na lina ukubwa wa hekari 2472.62. Gereza hili lilianzishwa mwaka 1975 kwa kuchukua eneo lililokuwa la Mbunge wa zamani wa eneo hilo, Marehemu Edward Ng’wani ambapo alifidiwa eneo hilo kwa kupewa eneo lingine na Serikali. Aidha, wananchi wa Vijiji vya Mwanchumu, Salaliya kwa asili ni wahamiaji kutoka maeneo mengine na siyo wenyeji wa Matongo.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa Serikali iko kwenye mpango wa kuboresha kilimo kupitia Jeshi la Magereza kwa kuliwezesha kuzalisha chakula cha kutosheleza kulisha wafungwa na mahabusu. Eneo la Gereza la Matongo lipo kwenye orodha ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika kilimo cha mahindi, alizeti, pamba, ufugaji wa nyuki na mifugo pamoja na upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitwa eneo hilo ili kuwezesha Magereza kuendeleza shughuli za urekebishaji wafungwa kwa kutumia kilimo cha ufugaji ambapo mazao mbalimbali ya kilimo hustawi. Kwa sasa eneo hilo limeshapimwa na taratibu za kufuatilia upatikanaji wa hati unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kutokana na eneo hilo kuwa kwenye mpango mkakati wa Jeshi la Magereza wa kujitosheleza kwa chakula na shughuli nyingine, Serikali haina mpango wa kulirejesha eneo hilo kwa vijiji tajwa.
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMED aliuliza:-
Jeshi la Polisi lina dhamana kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao na ni msimamizi mkuu katika haki za binadamu:-
(a) Je, ni lini Jeshi hilo litafanya kazi zake kisayansi zaidi na kuondokana na kutumia nguvu zisizo za lazima wakati wa kutekeleza majukumu yake?
(b) Je, suala la weledi kwa watendaji wa polisi linasimamiwa vipi ili polisi waweze kupambana na uhalifu unaokua kitalaam kila siku?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twahir Awesu Mohamed, Mbunge wa Mkoani lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa Katiba kusimamia usalama wa raia na mali zao na katika utendaji wake linaongozwa na sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali. Aidha, Jeshi la Polisi limejiwekea kanuni za kudumu (PGO) ambazo zimetafsiri na kutoa mwongozo wa utekelezaji wa sheria zote zinazoongoza utendaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa kazi zake askari anaruhusiwa kutumia nguvu inayoendana na mazingira ya tukio. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu namba 11(2) kinamruhusu askari kutumia nguvu katika ukamataji iwapo mkamatwaji atakaidi. Pia PGO 274 inaeleza mazingira ya matumizi ya nguvu na aina ya nguvu inayopaswa kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wa kiutendaji askari kwa kutoa mafunzo mbalimbali sehemu za kazi yenye lengo la kuwakumbusha taratibu za kazi, pia limekuwa likitoa mafunzo ya weledi ya ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha linafanya kazi zake kwa weledi Jeshi la Polisi limekuwa likiajiri wasomi wenye taaluma mbalimbali kama vile TEHAMA, maabara, uchunguzi wa nyaraka na taaluma zingine zinazohusiana na makosa yanayosababishwa na ukuaji wa teknolojia.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-
Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kiliungua mnamo tarehe 27/12/2010 na ujenzi wake ulianza mara moja.
Je, ni lini ujenzi huu utakamilika na kituo hicho kuendelea na shughuli zake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kituo cha polisi cha Mkokotoni kilipata ajali ya moto mwaka 2010. Baada ya kuungua kwa kituo hichi, wananchi wa eneo husika waliendelea kupata huduma za kipolisi kupitia jingo lililokuwa pembeni na kituo kilichoungua moto. Serikali kupitia Jeshi la Polisi ilitafuta mkandarasi ambaye alianza kujenga upya kituo hicho na kwa sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80. Aidha, shughuli za Kituo cha Polisi cha Mkokotoni zitaanza katika jengo jipya baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Mlele?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uhitaji wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari kote nchini ikiwemo Wilaya ya Mlele. Ili kutatua changamoto hii, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inashirikisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wengine wa maendeleo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga vituo vya polisi vya kisasa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti na uhitaji wa vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini kuwa mkubwa, namwomba Mheshimiwa Mbunge kushiriki katika jitihada hizi kwa kuhamasisha wananchi wake kushiriki katika mpango huu ili kuhakikisha huduma za Kipolisi zinaimarika karika eneo hilo. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Wilaya ya Itilima haina Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Itilima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi lina jumla ya Wilaya za Kipolisi 168 nchi nzima ambapo kati ya hizo, Wilaya 127 zina majengo kwa ajili ya Ofisi na Vituo vya Polisi vya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhaba wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari nchini umesababishwa na kukosekana kwa rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji ambayo ni makubwa. Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi linafanya jitihada mbalimbali kama vile kutumia rasilimali zilizopo katika eneo husika pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa vituo vya polisi nchini. (Makofi)

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Moja ya majukumu makubwa ya Serikali ni kulinda raia na mali zao kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ikiwemo Polisi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukirejesha Kituo cha Polisi katika Tarafa ya Kipatimu Wilayani Kilwa ambacho kilihamishwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Kituo cha Polisi cha Kipatimu kilifungwa mwaka 1998 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu na mahusiano mabaya kati ya raia na Askari kiasi cha kutishia usalama wa Askari na mali za Serikali zilizoko kituoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wananchi wameona umuhimu wa kurejesha huduma za Polisi katika eneo husika ambapo wameanza ujenzi wa kituo kipya cha Polisi. Aidha, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kuwasiliana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi ili kuona namna bora ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.